GEN 1:1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.
GEN 1:2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.
GEN 1:3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo.
GEN 1:4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema; ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza.
GEN 1:5 Mungu akaiita nuru “mchana”, na giza akaliita “usiku”. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.
GEN 1:6 Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji, igawe maji na maji.”
GEN 1:7 Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo.
GEN 1:8 Mungu akaiita hiyo nafasi “anga”. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.
GEN 1:9 Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo.
GEN 1:10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi”, nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.
GEN 1:11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo.
GEN 1:12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema.
GEN 1:13 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.
GEN 1:14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka,
GEN 1:15 nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo.
GEN 1:16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota.
GEN 1:17 Mungu akaiweka hiyo mianga katika nafasi ya anga iangaze dunia,
GEN 1:18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
GEN 1:19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.
GEN 1:20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.”
GEN 1:21 Kwa hiyo Mungu akaumba wanyama wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
GEN 1:22 Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.”
GEN 1:23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.
GEN 1:24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: mifugo, viumbe vinavyotambaa ardhini na wanyama pori, kila kiumbe kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo.
GEN 1:25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, mifugo kulingana na aina zake, na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
GEN 1:26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini na ndege wa angani, na mifugo na wanyama pori wote, na dunia yote, na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini.”
GEN 1:27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba.
GEN 1:28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
GEN 1:29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu.
GEN 1:30 Nao wanyama wote wa nchi, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
GEN 1:31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, vilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.
GEN 2:1 Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.
GEN 2:2 Kufikia siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya; hivyo siku hiyo ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote.
GEN 2:3 Mungu akaibariki siku ya saba, akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika baada ya kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.
GEN 2:4 Haya ndio maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa. Bwana Mwenyezi Mungu alipoziumba mbingu na dunia,
GEN 2:5 hapakuwa na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwa na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwa na mtu wa kuilima ardhi,
GEN 2:6 lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi.
GEN 2:7 Bwana Mwenyezi Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai.
GEN 2:8 Basi Bwana Mwenyezi Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni; huko akamweka huyo mtu aliyemuumba.
GEN 2:9 Bwana Mwenyezi Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Mti wa uzima ulikuwa katikati ya bustani, na pia mti wa kujua mema na mabaya.
GEN 2:10 Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni; kuanzia hapo ukagawanyika kuwa mito minne.
GEN 2:11 Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu.
GEN 2:12 (Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri; bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.)
GEN 2:13 Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi.
GEN 2:14 Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki mwa Ashuru. Mto wa nne ni Frati.
GEN 2:15 Bwana Mwenyezi Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza.
GEN 2:16 Bwana Mwenyezi Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani;
GEN 2:17 lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”
GEN 2:18 Bwana Mwenyezi Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”
GEN 2:19 Basi Bwana Mwenyezi Mungu alikuwa ametengeneza kutoka ardhi wanyama pori wote, na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa jina lake.
GEN 2:20 Hivyo Adamu akawapa majina mifugo wote, ndege wa angani, na wanyama pori wote. Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa.
GEN 2:21 Hivyo Bwana Mwenyezi Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama.
GEN 2:22 Kisha Bwana Mwenyezi Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwa ule ubavu alioutoa kwa mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa mwanaume.
GEN 2:23 Huyo mwanaume akasema, “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu, na nyama ya nyama yangu, ataitwa ‘mwanamke’, kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”
GEN 2:24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
GEN 2:25 Adamu na mkewe wote walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.
GEN 3:1 Basi nyoka alikuwa mjanja kuliko wanyama pori wote ambao Bwana Mwenyezi Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”
GEN 3:2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyo katika bustani,
GEN 3:3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”
GEN 3:4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa.
GEN 3:5 Kwa maana Mungu anajua kwamba mtakapokula tunda hilo, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
GEN 3:6 Mwanamke alipotambua kwamba tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma matunda yake, akala. Pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, akala.
GEN 3:7 Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika.
GEN 3:8 Yule mwanaume na mkewe waliposikia sauti ya Bwana Mwenyezi Mungu akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka kwa Bwana Mwenyezi Mungu katikati ya miti ya bustani.
GEN 3:9 Lakini Bwana Mwenyezi Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?”
GEN 3:10 Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.”
GEN 3:11 Mungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?”
GEN 3:12 Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa matunda ya huo mti, nami nikala.”
GEN 3:13 Ndipo Bwana Mwenyezi Mungu akamuuliza mwanamke, “Umefanya jambo gani?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
GEN 3:14 Hivyo Bwana Mwenyezi Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili, “Umelaaniwa kuliko mifugo wote na wanyama pori wote! Utatambaa kwa tumbo lako na kula mavumbi siku zote za maisha yako.
GEN 3:15 Nami nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke, na kati ya uzao wako na wake; yeye atakuponda kichwa, nawe utamuuma kisigino.”
GEN 3:16 Kwa mwanamke akasema, “Nitakuzidishia sana uchungu wakati wa kuzaa kwako; kwa uchungu utazaa watoto. Tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.”
GEN 3:17 Akamwambia Adamu, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’ “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako; kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo siku zote za maisha yako.
GEN 3:18 Itakuzalia miiba na mibaruti, nawe utakula mimea ya shambani.
GEN 3:19 Kwa jasho la uso wako utakula chakula chako hadi utakaporudi ardhini, kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo; wewe u mavumbi na mavumbini utarudi.”
GEN 3:20 Adamu akamwita mkewe jina Hawa, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.
GEN 3:21 Bwana Mwenyezi Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.
GEN 3:22 Kisha Bwana Mwenyezi Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyoosha mkono wake na kuchuma pia kutoka mti wa uzima akala, naye akaishi milele.”
GEN 3:23 Hivyo Bwana Mwenyezi Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa.
GEN 3:24 Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki mwa Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika kila upande kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.
GEN 4:1 Adamu akakutana kimwili na mkewe Hawa, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu nimemzaa mtoto wa kiume.”
GEN 4:2 Baadaye akamzaa Habili ndugu yake. Basi Habili akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima.
GEN 4:3 Baada ya muda, Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba ikiwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu.
GEN 4:4 Lakini Habili akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Mwenyezi Mungu akamkubali Habili pamoja na sadaka yake,
GEN 4:5 lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.
GEN 4:6 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni?
GEN 4:7 Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, ikikutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”
GEN 4:8 Basi Kaini akamwambia ndugu yake Habili, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Habili ndugu yake, akamuua.
GEN 4:9 Kisha Mwenyezi Mungu akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
GEN 4:10 Mwenyezi Mungu akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini.
GEN 4:11 Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako.
GEN 4:12 Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.”
GEN 4:13 Kaini akamwambia Mwenyezi Mungu, “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili.
GEN 4:14 Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.”
GEN 4:15 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue.
GEN 4:16 Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Mwenyezi Mungu, akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni.
GEN 4:17 Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Idrisi. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Idrisi, jina la mtoto wake.
GEN 4:18 Idrisi akamzaa Iradi; Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; naye Methushaeli akamzaa Lameki.
GEN 4:19 Lameki alioa wanawake wawili: mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila.
GEN 4:20 Ada akamzaa Yabali; huyu akawa baba wa wale wanaoishi katika mahema na kufuga wanyama.
GEN 4:21 Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi.
GEN 4:22 Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini, ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini.
GEN 4:23 Lameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila, nisikilizeni mimi; wake wa Lameki sikieni maneno yangu. Nimemuua mtu kwa kunijeruhi, kijana mdogo kwa kuniumiza.
GEN 4:24 Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba, basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”
GEN 4:25 Adamu akakutana kimwili na mke wake tena, akamzaa mwana, akamwita jina Sethi, akisema, “Mungu amenijalia mwana mwingine badala ya Habili, kwa kuwa Kaini alimuua.”
GEN 4:26 Naye Sethi akamzaa mwana, akamwita jina Enoshi. Wakati huo watu wakaanza kuliitia jina la Mwenyezi Mungu.
GEN 5:1 Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu. Mungu alipomuumba mwanadamu, alimfanya kwa sura ya Mungu.
GEN 5:2 Aliwaumba mwanaume na mwanamke, akawabariki. Walipokwisha kuumbwa, akawaita “Binadamu.”
GEN 5:3 Adamu alipokuwa ameishi miaka mia moja na thelathini, alimzaa mwana aliyekuwa na sura yake, mwenye kufanana naye. Akamwita jina Sethi.
GEN 5:4 Baada ya Sethi kuzaliwa, Adamu aliishi miaka mia nane, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:5 Adamu aliishi jumla ya miaka mia tisa na thelathini, ndipo akafa.
GEN 5:6 Sethi alipokuwa ameishi miaka mia moja na tano, akamzaa Enoshi.
GEN 5:7 Baada ya kumzaa Enoshi, Sethi aliishi miaka mia nane na saba (807), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:8 Sethi aliishi jumla ya miaka mia tisa na kumi na mbili (912), ndipo akafa.
GEN 5:9 Enoshi alipokuwa ameishi miaka tisini, akamzaa Kenani.
GEN 5:10 Baada ya kumzaa Kenani, Enoshi aliishi miaka mia nane na kumi na tano (815), naye alikuwa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:11 Enoshi aliishi jumla ya miaka mia tisa na tano (905), ndipo akafa.
GEN 5:12 Kenani alipokuwa ameishi miaka sabini, akamzaa Mahalaleli.
GEN 5:13 Baada ya kumzaa Mahalaleli, Kenani aliishi miaka mia nane na arobaini, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:14 Kenani aliishi jumla ya miaka mia tisa na kumi, ndipo akafa.
GEN 5:15 Mahalaleli alipokuwa ameishi miaka sitini na tano, akamzaa Yaredi.
GEN 5:16 Baada ya kumzaa Yaredi, Mahalaleli aliishi miaka mia nane na thelathini, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:17 Mahalaleli aliishi jumla ya miaka mia nane tisini na tano (895), ndipo akafa.
GEN 5:18 Yaredi alipokuwa ameishi miaka mia moja na sitini na mbili (162), akamzaa Idrisi.
GEN 5:19 Baada ya kumzaa Idrisi, Yaredi aliishi miaka mia nane, naye akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:20 Yaredi aliishi jumla ya miaka mia tisa na sitini na mbili (962), ndipo akafa.
GEN 5:21 Idrisi alipokuwa ameishi miaka sitini na tano, akamzaa Methusela.
GEN 5:22 Baada ya kumzaa Methusela, Idrisi alitembea na Mungu miaka mia tatu, na akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:23 Idrisi aliishi jumla ya miaka mia tatu sitini na tano (365).
GEN 5:24 Idrisi akatembea na Mungu, kisha akatoweka, kwa sababu Mungu alimchukua.
GEN 5:25 Methusela alipokuwa ameishi miaka mia moja na themanini na saba (187), akamzaa Lameki.
GEN 5:26 Baada ya kumzaa Lameki, Methusela aliishi miaka mia saba na themanini na mbili (782), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:27 Methusela aliishi jumla ya miaka mia tisa sitini na tisa (969), ndipo akafa.
GEN 5:28 Lameki alipokuwa ameishi miaka mia moja na themanini na mbili (182), alimzaa mwana.
GEN 5:29 Akamwita jina Nuhu. Naye akasema, “Huyu ndiye atakayetufariji katika kazi ngumu ya mikono yetu yenye maumivu makali yaliyosababishwa na ardhi iliyolaaniwa na Mwenyezi Mungu.”
GEN 5:30 Baada ya Nuhu kuzaliwa, Lameki aliishi miaka mia tano na tisini na tano (595), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 5:31 Lameki aliishi jumla ya miaka mia saba sabini na saba (777), ndipo akafa.
GEN 5:32 Baada ya Nuhu kuishi miaka mia tano, aliwazaa Shemu, Hamu, na Yafethi.
GEN 6:1 Idadi ya watu ilipoanza kuongezeka duniani, na watoto wa kike wakazaliwa kwao,
GEN 6:2 wana wa Mungu wakawaona kuwa hao binti za wanadamu walikuwa wazuri wa sura, wakaoa yeyote miongoni mwao waliyemchagua.
GEN 6:3 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa; siku zake zitakuwa miaka mia moja na ishirini.”
GEN 6:4 Wanefili walikuwa duniani siku hizo, na hata baadaye, hao wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu na kuzaa nao. Wanefili walikuwa mashujaa wa zamani, na watu mashuhuri.
GEN 6:5 Mwenyezi Mungu akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu.
GEN 6:6 Mwenyezi Mungu akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, na moyo wa Mungu ukasikitika sana.
GEN 6:7 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vinavyotambaa ardhini, na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”
GEN 6:8 Lakini Nuhu akapata kibali machoni pa Mwenyezi Mungu.
GEN 6:9 Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, na mkamilifu miongoni mwa watu wa wakati wake, tena alitembea na Mungu.
GEN 6:10 Nuhu alikuwa na wana watatu: Shemu, Hamu na Yafethi.
GEN 6:11 Wakati huu dunia ilikuwa imejaa uharibifu na ukatili machoni pa Mungu.
GEN 6:12 Mungu akaona jinsi dunia ilivyoharibika, kwa maana watu wote duniani walikuwa wameharibu njia zao.
GEN 6:13 Kwa hiyo Mungu akamwambia Nuhu, “Nitawaangamiza watu wote, kwa kuwa dunia imejaa ukatili kwa sababu yao. Hakika nitaangamiza watu pamoja na dunia.
GEN 6:14 Kwa hiyo jitengenezee safina kubwa kwa mbao za mvinje; tengeneza vyumba ndani yake na uipake lami ndani na nje.
GEN 6:15 Hivi ndivyo utakavyoitengeneza: Safina iwe na urefu wa dhiraa mia tatu, upana wake dhiraa hamsini, na kimo chake dhiraa thelathini.
GEN 6:16 Itengenezee paa na umalizie safina kwa kuacha nafasi ya dhiraa moja juu. Weka mlango ubavuni mwa safina, na uifanye ya ghorofa ya chini, ya kati na ya juu.
GEN 6:17 Nitaleta gharika ya maji juu ya dunia ili kuangamiza kila chenye uhai chini ya mbingu, kila kiumbe chenye pumzi ya uhai ndani yake. Kila kitu juu ya dunia kitaangamia.
GEN 6:18 Lakini mimi nitaweka agano langu na wewe, nawe utaingia ndani ya Safina, wewe pamoja na mke wako, wanao na wake zao.
GEN 6:19 Utaingiza ndani ya Safina kila aina ya kiumbe hai wawili wawili, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja na wewe.
GEN 6:20 Wawili wa kila aina ya ndege, wa kila aina ya mnyama, na wa kila aina ya kiumbe kinachotambaa ardhini watakuja kwako ili wahifadhiwe hai.
GEN 6:21 Utachukua kila aina ya chakula kitakacholiwa, na ukiweke akiba kama chakula kwa ajili yako na yao.”
GEN 6:22 Nuhu akafanya kila kitu kama vile Mungu alimwamuru.
GEN 7:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Nuhu, “Ingia katika safina, wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki.
GEN 7:2 Chukua wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike; na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi, wa kiume na wa kike.
GEN 7:3 Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote.
GEN 7:4 Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya dunia kwa siku arobaini, usiku na mchana; nami nitafutilia mbali kutoka uso wa dunia kila kiumbe hai nilichokiumba.”
GEN 7:5 Nuhu akafanya yote Mwenyezi Mungu aliyomwamuru.
GEN 7:6 Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia sita gharika ilipokuja juu ya dunia.
GEN 7:7 Nuhu na mkewe, na wanawe na wake zao, wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika.
GEN 7:8 Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vinavyotambaa ardhini,
GEN 7:9 wa kiume na wa kike, walikuja kwa Nuhu, wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Nuhu.
GEN 7:10 Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia.
GEN 7:11 Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, siku hiyo chemchemi zote za vilindi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa.
GEN 7:12 Mvua ikanyesha juu ya dunia siku arobaini usiku na mchana.
GEN 7:13 Siku hiyo Nuhu na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao, wakaingia katika ile safina.
GEN 7:14 Nao walikuwa pamoja na kila mnyama pori kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa.
GEN 7:15 Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai vikaja kwa Nuhu viwili viwili, vikaingia katika safina.
GEN 7:16 Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Nuhu; ndipo Mwenyezi Mungu akamfungia ndani.
GEN 7:17 Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani; maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka uso wa dunia.
GEN 7:18 Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya dunia, na safina ikaelea juu ya maji.
GEN 7:19 Maji yakazidi kujaa juu ya dunia, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote.
GEN 7:20 Maji yakaendelea kujaa, yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano.
GEN 7:21 Kila kiumbe hai kinachotambaa juu ya dunia kikaangamia: ndege, mifugo, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi, na wanadamu wote.
GEN 7:22 Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa.
GEN 7:23 Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali; watu, wanyama pori, viumbe vinavyotambaa ardhini, na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Nuhu peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.
GEN 7:24 Maji yakaifunika dunia kwa siku mia moja na hamsini.
GEN 8:1 Mungu akamkumbuka Nuhu na wanyama pori na mifugo wote waliokuwa naye ndani ya safina; akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakapungua.
GEN 8:2 Chemchemi za vilindi zikawa zimefungwa, na malango ya mafuriko ya mbinguni pia yakawa yamefungwa; nayo mvua ikawa imekoma kunyesha.
GEN 8:3 Maji yakaendelea kupungua taratibu katika dunia. Mwishoni mwa siku ya mia moja na hamsini, maji yakawa yamepungua.
GEN 8:4 Na katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati.
GEN 8:5 Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi. Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.
GEN 8:6 Baada ya siku arobaini, Nuhu akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina,
GEN 8:7 akamtoa kunguru, naye akawa akiruka kwenda na kurudi hadi maji yalipokwisha kukauka juu ya dunia.
GEN 8:8 Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya ardhi.
GEN 8:9 Lakini hua hakupata mahali pa kutua, kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Nuhu ndani ya safina. Nuhu akanyoosha mkono akamchukua yule hua, akamrudisha ndani ya safina.
GEN 8:10 Nuhu akangojea siku saba zaidi, kisha akamtoa tena hua kutoka safina.
GEN 8:11 Jioni hua aliporudi kwa Nuhu alikuwa amebeba jani bichi la mzeituni lililochumwa wakati ule ule katika mdomo wake! Ndipo Nuhu akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya dunia.
GEN 8:12 Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Nuhu.
GEN 8:13 Kufikia siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa mia sita na moja (601) wa maisha ya Nuhu, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Nuhu akatoa kifuniko juu ya safina, akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka.
GEN 8:14 Kufikia siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili, dunia ilikuwa imekauka kabisa.
GEN 8:15 Ndipo Mungu akamwambia Nuhu,
GEN 8:16 “Toka katika safina, wewe na mkeo, na wanao na wake zao.
GEN 8:17 Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe, wakiwamo ndege, wanyama na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
GEN 8:18 Kwa hiyo Nuhu akatoka nje pamoja na mkewe, na wanawe na wake zao.
GEN 8:19 Wanyama wote na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, na ndege wote, kila kitu kinachoenda juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina.
GEN 8:20 Kisha Nuhu akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.
GEN 8:21 Mwenyezi Mungu akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.
GEN 8:22 “Kwa muda dunia idumupo, majira ya kupanda na ya kuvuna, wakati wa baridi na wa joto, wakati wa kiangazi na wa masika, usiku na mchana kamwe havitakoma.”
GEN 9:1 Ndipo Mungu akawabariki Nuhu na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, mkaongezeke kwa idadi, na mkaijaze tena dunia.
GEN 9:2 Wanyama wote wa nchi, na ndege wote wa angani, na kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu.
GEN 9:3 Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.
GEN 9:4 “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu, kwa maana damu ni uhai.
GEN 9:5 Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa binadamu mwenzake.
GEN 9:6 “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu, damu yake itamwagwa na mwanadamu; kwa kuwa katika mfano wa Mungu, Mungu alimuumba mwanadamu.
GEN 9:7 Bali ninyi, zaeni mwongezeke kwa idadi; zidini duniani na kuijaza.”
GEN 9:8 Ndipo Mungu akamwambia Nuhu na wanawe pamoja naye:
GEN 9:9 “Sasa mimi ninaweka agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu,
GEN 9:10 pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: ndege, mifugo, na wanyama pori wote, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi: kila kiumbe hai duniani.
GEN 9:11 Ninaweka agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika; kamwe hakutakuwa tena gharika ya kuangamiza dunia.”
GEN 9:12 Mungu akasema, “Hii ni ishara ya agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, agano kwa vizazi vyote vijavyo:
GEN 9:13 Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano nifanyalo kati yangu na dunia.
GEN 9:14 Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukatokea mawinguni,
GEN 9:15 nitakumbuka agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote.
GEN 9:16 Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”
GEN 9:17 Hivyo Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”
GEN 9:18 Wana wa Nuhu waliotoka ndani ya safina walikuwa: Shemu, na Hamu, na Yafethi. (Hamu ndiye alikuwa baba wa Kanaani.)
GEN 9:19 Hao walikuwa wana watatu wa Nuhu, na kutokana nao watu walienea katika dunia.
GEN 9:20 Nuhu akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu.
GEN 9:21 Alipokunywa huo mvinyo wake, akalewa na akalala uchi kwenye hema lake.
GEN 9:22 Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.
GEN 9:23 Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo, wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.
GEN 9:24 Nuhu alipolevuka na kujua lile mwanawe mdogo alilomtendea,
GEN 9:25 akasema, “Alaaniwe Kanaani! Atakuwa mtumwa wa chini kabisa kwa ndugu zake.”
GEN 9:26 Pia akasema, “Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Shemu! Kanaani na awe mtumwa wa Shemu.
GEN 9:27 Mungu na apanue mipaka ya Yafethi; Yafethi na aishi katika mahema ya Shemu, na Kanaani na awe mtumwa wake.”
GEN 9:28 Baada ya gharika, Nuhu aliishi miaka mia tatu na hamsini.
GEN 9:29 Nuhu aliishi jumla ya miaka mia tisa na hamsini, ndipo akafa.
GEN 10:1 Hivi ndivyo vizazi vya wana wa Nuhu, yaani Shemu, Hamu na Yafethi, ambao walizaa wana baada ya gharika.
GEN 10:2 Wana wa Yafethi walikuwa: Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi.
GEN 10:3 Wana wa Gomeri walikuwa: Ashkenazi, Rifathi na Togarma.
GEN 10:4 Wana wa Yavani walikuwa: Al-Yasa, Tarshishi, Kitimu na Rodanimu.
GEN 10:5 (Kutokana na hawa mataifa ya pwani yalienea katika nchi zao, kwa koo zao katika mataifa yao, kila moja kwa lugha yake.)
GEN 10:6 Wana wa Hamu walikuwa: Kushi, Misri, Putu na Kanaani.
GEN 10:7 Wana wa Kushi walikuwa: Seba, Havila, Sabta, Raama na Sabteka. Wana wa Raama walikuwa: Sheba na Dedani.
GEN 10:8 Kushi akamzaa Nimrodi, ambaye alikua akawa shujaa mwenye nguvu duniani.
GEN 10:9 Alikuwa mwindaji hodari mbele za Mwenyezi Mungu; Ndiyo maana watu husema, “Kama Nimrodi, mwindaji hodari mbele za Mwenyezi Mungu.”
GEN 10:10 Vituo vya kwanza katika ufalme wake vilikuwa Babeli, Ereki, Akadi na Kalne, katika nchi ya Shinari.
GEN 10:11 Kutoka nchi ile alienda Ashuru, ambako alijenga miji ya Ninawi, na Rehoboth-Iri, na Kala,
GEN 10:12 na Reseni, mji ulio kati ya Ninawi na Kala; huo ndio mji mkubwa.
GEN 10:13 Misri alikuwa baba wa: Waludi, Waanami, Walehabi, Wanaftuhi,
GEN 10:14 Wapathrusi, Wakasluhi (hao ndio asili ya Wafilisti), na Wakaftori.
GEN 10:15 Kanaani alikuwa baba wa: Sidoni mzaliwa wake wa kwanza, Hethi,
GEN 10:16 Wayebusi, Waamori, Wagirgashi,
GEN 10:17 Wahivi, Waarki, Wasini,
GEN 10:18 Waarvadi, Wasemari na Wahamathi. (Baadaye koo za Wakanaani zilitawanyika,
GEN 10:19 na mipaka ya Kanaani ikaenea kutoka Sidoni kuelekea Gerari hadi Gaza, kisha kuelekea Sodoma, Gomora, Adma na Seboimu, hadi kufikia Lasha.)
GEN 10:20 Hawa ni wana wa Hamu kwa koo zao na lugha zao, katika nchi zao na mataifa yao.
GEN 10:21 Shemu, ndugu mkubwa wa Yafethi, alizaa wana pia. Shemu alikuwa baba wa wana wote wa Eberi.
GEN 10:22 Wana wa Shemu walikuwa: Elamu, Ashuru, Arfaksadi, Ludi na Aramu.
GEN 10:23 Wana wa Aramu walikuwa: Usi, Huli, Getheri na Mashi.
GEN 10:24 Arfaksadi alikuwa baba wa Shela, naye Shela akamzaa Eberi.
GEN 10:25 Eberi akapata wana wawili: Mmoja wao aliitwa Pelegi, kwa kuwa wakati wake dunia iligawanyika; nduguye aliitwa Yoktani.
GEN 10:26 Yoktani alikuwa baba wa: Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera,
GEN 10:27 Hadoramu, Uzali, Dikla,
GEN 10:28 Obali, Abimaeli, Seba,
GEN 10:29 Ofiri, Havila na Yobabu. Hawa wote walikuwa wana wa Yoktani.
GEN 10:30 (Eneo waliloishi lilienea kutoka Mesha kuelekea Sefari, kwenye nchi ya vilima iliyo mashariki.)
GEN 10:31 Hao ndio wana wa Shemu kwa koo zao na lugha zao, katika nchi zao na mataifa yao.
GEN 10:32 Hizi ndizo koo za wana wa Nuhu, kufuatana na vizazi vyao, katika mataifa yao. Kutokana na hawa mataifa yalienea duniani kote baada ya gharika.
GEN 11:1 Wakati huo dunia yote ilikuwa na lugha moja na msemo mmoja.
GEN 11:2 Watu walipoelekea upande wa mashariki, wakafika kwenye tambarare katika nchi ya Shinari, nao wakaishi huko.
GEN 11:3 Wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tufyatue matofali na tuyachome vizuri kwa moto.” Walitumia matofali badala ya mawe, na lami kuunganisha hayo matofali.
GEN 11:4 Ndipo wakasema, “Njooni, tujijengee mji wenye mnara ambao utafika hadi mbinguni, ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.”
GEN 11:5 Lakini Mwenyezi Mungu akashuka ili auone mji na mnara ambao wanadamu walikuwa wanaujenga.
GEN 11:6 Mwenyezi Mungu akasema, “Ikiwa kama taifa moja wanaozungumza lugha moja wameanza kufanya hili, basi hakuna lolote watakalopanga kufanya ambalo halitawezekana kwao.
GEN 11:7 Njooni, tushuke tuvuruge lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.”
GEN 11:8 Hivyo Mwenyezi Mungu akawatawanya kutoka mahali pale waende duniani kote; nao wakaacha kuujenga huo mji.
GEN 11:9 Ndiyo maana pakaitwa Babeli, kwa sababu hapo ndipo Mwenyezi Mungu alipoivuruga lugha ya dunia nzima. Kutoka hapo Mwenyezi Mungu akawatawanya duniani kote.
GEN 11:10 Hivi ndivyo vizazi vya Shemu. Miaka miwili baada ya gharika, Shemu alipokuwa na umri wa miaka mia moja, akamzaa Arfaksadi.
GEN 11:11 Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka mia tano, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:12 Arfaksadi alipokuwa ameishi miaka thelathini na tano, akamzaa Shela.
GEN 11:13 Baada ya kumzaa Shela, Arfaksadi aliishi miaka mia nne na tatu (403), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:14 Shela alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Eberi.
GEN 11:15 Baada ya kumzaa Eberi, Shela aliishi miaka mia nne na tatu (403), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:16 Eberi alipokuwa ameishi miaka thelathini na nne, akamzaa Pelegi.
GEN 11:17 Baada ya kumzaa Pelegi, Eberi aliishi miaka mia nne na thelathini (430), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:18 Pelegi alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Reu.
GEN 11:19 Baada ya kumzaa Reu, Pelegi aliishi miaka mia mbili na tisa (209), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:20 Reu alipokuwa ameishi miaka thelathini na mbili, akamzaa Serugi.
GEN 11:21 Baada ya kumzaa Serugi, Reu aliishi miaka mia mbili na saba (207), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:22 Serugi alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Nahori.
GEN 11:23 Baada ya kumzaa Nahori, Serugi aliishi miaka mia mbili, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:24 Nahori alipokuwa ameishi miaka ishirini na tisa, akamzaa Tera.
GEN 11:25 Baada ya kumzaa Tera, Nahori aliishi miaka mia moja na kumi na tisa (119), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
GEN 11:26 Tera alipokuwa ameishi miaka sabini, akamzaa Abramu, na baadaye akawazaa Nahori na Harani.
GEN 11:27 Hivi ndivyo vizazi vya Tera. Tera aliwazaa Abramu, Nahori na Harani. Harani akamzaa Lutu.
GEN 11:28 Tera alipokuwa bado hai, Harani akafa katika Uru ya Wakaldayo, nchi aliyozaliwa.
GEN 11:29 Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai, naye mke wa Nahori aliitwa Milka; Milka na Iska walikuwa watoto wa Harani.
GEN 11:30 Sarai alikuwa tasa, hakuwa na watoto.
GEN 11:31 Tera akawachukua Abramu mwanawe, mjukuu wake Lutu mwana wa Harani, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka Uru ya Wakaldayo pamoja, wakaenda nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakaishi huko.
GEN 11:32 Tera aliishi miaka mia mbili na mitano (205), akafa huko Harani.
GEN 12:1 Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonesha.
GEN 12:2 “Nitakufanya taifa kubwa na nitakubariki, Nitalikuza jina lako, nawe utakuwa baraka.
GEN 12:3 Nitawabariki wale wanaokubariki, na yeyote akulaaniye nitamlaani; na kupitia kwako mataifa yote duniani yatabarikiwa.”
GEN 12:4 Hivyo Abramu akaondoka kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwambia; naye Lutu akaondoka pamoja naye. Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na umri wa miaka sabini na tano.
GEN 12:5 Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Lutu mwana wa ndugu yake, mali yote waliyokuwa nayo, pamoja na watu aliokuwa amewapata huko Harani, wakasafiri kwenda nchi ya Kanaani, na wakafika huko.
GEN 12:6 Abramu akasafiri katika nchi hiyo hadi huko Shekemu, mahali penye mwaloni wa More. Wakati huo Wakanaani walikuwa wanaishi katika nchi hiyo.
GEN 12:7 Mwenyezi Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Hivyo hapo akamjengea madhabahu Mwenyezi Mungu aliyekuwa amemtokea.
GEN 12:8 Kutoka huko Abramu akasafiri kuelekea kwenye vilima mashariki mwa Betheli, naye akapiga hema huko, Betheli ikiwa upande wa magharibi na Ai upande wa mashariki. Huko alimjengea Mwenyezi Mungu madhabahu na akaliitia jina la Mwenyezi Mungu.
GEN 12:9 Kisha Abramu akasafiri kuelekea upande wa Negebu.
GEN 12:10 Basi kulikuwa na njaa katika nchi hiyo, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali.
GEN 12:11 Alipokaribia kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “Ninajua kwamba wewe ni mwanamke mzuri wa sura.
GEN 12:12 Wamisri watakapokuona, watasema, ‘Huyu ni mke wake.’ Kisha wataniua, lakini wewe watakuacha hai.
GEN 12:13 Sema wewe ni dada yangu, ili nitendewe mema kwa ajili yako, na maisha yangu yahifadhiwe kwa sababu yako.”
GEN 12:14 Abramu alipoingia Misri, Wamisri wakamwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana wa sura.
GEN 12:15 Maafisa wa Farao walipomwona, wakamsifia kwa Farao; ndipo Sarai akapelekwa kwa nyumba ya mfalme.
GEN 12:16 Kwa ajili ya Sarai, Farao akamtendea Abramu mema, naye Abramu akapata kondoo, ng’ombe, punda, ngamia, na watumishi wa kiume na wa kike.
GEN 12:17 Lakini Mwenyezi Mungu akamwadhibu Farao na nyumba yake kwa maradhi ya kufisha kwa sababu ya kumchukua Sarai, mke wa Abramu.
GEN 12:18 Ndipo Farao akamwita Abramu, akamuuliza, “Umenifanyia nini? Kwa nini hukuniambia yeye ni mke wako?
GEN 12:19 Kwa nini ulisema, ‘Yeye ni dada yangu,’ hata nikamchukua kuwa mke wangu? Sasa basi, mke wako huyu hapa. Mchukue uende zako!”
GEN 12:20 Kisha Farao akawapa watu wake amri kuhusu Abramu, wakamsindikiza pamoja na mke wake na kila alichokuwa nacho.
GEN 13:1 Hivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho; pia Lutu akaenda pamoja naye.
GEN 13:2 Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu.
GEN 13:3 Kutoka Negebu, akasafiri sehemu mbalimbali hadi akafika Betheli, mahali ambapo mwanzoni alipiga hema lake kati ya Betheli na Ai,
GEN 13:4 pale alipokuwa amejenga madhabahu ya kwanza. Huko Abramu akaliitia jina la Mwenyezi Mungu.
GEN 13:5 Basi Lutu, aliyekuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na mifugo na mahema.
GEN 13:6 Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali yao.
GEN 13:7 Ukazuka ugomvi kati ya wafugaji wa wanyama wa Abramu na wale wa Lutu. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi pia waliishi katika nchi hiyo.
GEN 13:8 Hivyo Abramu akamwambia Lutu, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu.
GEN 13:9 Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Ukielekea kushoto, nitaenda kulia; ukielekea kulia, mimi nitaenda kushoto.”
GEN 13:10 Lutu akatazama, akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya Mwenyezi Mungu, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi Mungu hajaharibu Sodoma na Gomora.)
GEN 13:11 Hivyo Lutu akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana.
GEN 13:12 Abramu aliishi nchi ya Kanaani, naye Lutu akaishi miongoni mwa miji ya lile bonde na kupiga mahema yake karibu na Sodoma.
GEN 13:13 Basi watu wa Sodoma walikuwa waovu, wakitenda dhambi nyingi dhidi ya Mwenyezi Mungu.
GEN 13:14 Baada ya Lutu kuondoka, Mwenyezi Mungu akamwambia Abramu, “Ukiwa hapo ulipo, inua macho yako utazame kaskazini na kusini, mashariki na magharibi.
GEN 13:15 Nchi yote unayoiona nitakupa wewe na uzao wako hata milele.
GEN 13:16 Nitaufanya uzao wako uwe mwingi kama mavumbi ya nchi, hivyo ikiwa kuna yeyote awezaye kuhesabu mavumbi, basi uzao wako utahesabika.
GEN 13:17 Ondoka, tembea katika marefu na mapana ya nchi, kwa maana ninakupa wewe.”
GEN 13:18 Basi Abramu akaondoa mahema yake, akaenda kuishi karibu na mialoni ya Mamre huko Hebroni. Naye akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu huko.
GEN 14:1 Wakati huo Amrafeli mfalme wa Shinari, Arioko mfalme wa Elasari, Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu
GEN 14:2 walienda kupigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari).
GEN 14:3 Wafalme wa kundi hili la pili waliunganisha majeshi yao katika Bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi).
GEN 14:4 Walikuwa wametawaliwa na Mfalme Kedorlaoma kwa miaka kumi na mbili, lakini mwaka wa kumi na tatu wakaasi.
GEN 14:5 Mwaka wa kumi na nne, Mfalme Kedorlaoma na wafalme waliojiunga naye walienda vitani na wakawashinda Warefai katika Ashtaroth-Kanaimu, Wazuzi katika Hamu, Waemi katika Shawe-Kiriathaimu,
GEN 14:6 na Wahori katika nchi ya vilima ya Seiri, hadi El-Parani karibu na jangwa.
GEN 14:7 Kisha wakarudi, wakaenda En-Misfati (yaani Kadeshi), wakashinda nchi yote ya Waamaleki, pamoja na Waamori walioishi Hasason-Tamari.
GEN 14:8 Ndipo mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari) wakatoka kupanga majeshi yao kwenye Bonde la Sidimu
GEN 14:9 dhidi ya Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari; yaani wafalme wanne dhidi ya wafalme watano.
GEN 14:10 Basi Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, nao wafalme wa Sodoma na wa Gomora walipokimbia, baadhi ya watu walitumbukia huko na wengine wakakimbilia vilimani.
GEN 14:11 Wale wafalme wanne wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora pamoja na vyakula vyao vyote, kisha wakaenda zao.
GEN 14:12 Pia walimteka Lutu, mwana wa ndugu yake Abramu, pamoja na mali yake, kwa kuwa alikuwa akiishi Sodoma.
GEN 14:13 Mtu mmoja aliyekuwa ametoroka akaja kumpa Abramu Mwebrania taarifa. Abramu alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mamre Mwamori, ndugu ya Eshkoli na Aneri, ambao wote walikuwa wameungana na Abramu.
GEN 14:14 Abramu alipopata habari kwamba jamaa yake amechukuliwa mateka, akawaita watu mia tatu na kumi na nane (318) wa nyumbani mwake waliokuwa wamefunzwa kupigana vita, wakawafuatilia hadi Dani.
GEN 14:15 Wakati wa usiku, Abramu aliwapanga watu wake katika vikosi, wakawashambulia na kuwashinda, wakawafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Dameski.
GEN 14:16 Abramu akarudisha mali yote, na akamrudisha Lutu jamaa yake na mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.
GEN 14:17 Abramu aliporudi baada ya kumshinda Mfalme Kedorlaoma na wale wafalme waliojiunga naye, mfalme wa Sodoma akatoka kwenda kumlaki katika Bonde la Shawe (yaani Bonde la Mfalme).
GEN 14:18 Ndipo Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai. Alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana.
GEN 14:19 Naye akambariki Abramu, akisema, “Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na nchi.
GEN 14:20 Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana, ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.” Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu.
GEN 14:21 Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, nawe uchukue hizo mali.”
GEN 14:22 Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua mkono wangu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na dunia, na nimeapa
GEN 14:23 kwamba sitapokea kitu chochote kilicho chako, hata kama ni uzi au gidamu ya kiatu, ili kamwe usije ukasema, ‘Nimemtajirisha Abramu.’
GEN 14:24 Sitapokea chochote, ila kile tu watu wangu walichokula, na sehemu ambayo ni fungu la watu walioenda pamoja nami, ambao ni Aneri, Eshkoli na Mamre. Wao na wapewe fungu lao.”
GEN 15:1 Baada ya jambo hili, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Abramu katika maono, akaambiwa: “Usiogope, Abramu. Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”
GEN 15:2 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina mtoto, na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?”
GEN 15:3 Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”
GEN 15:4 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu lilipomjia, likanena: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.”
GEN 15:5 Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”
GEN 15:6 Abramu akamwamini Mwenyezi Mungu, naye kwake jambo hili likahesabiwa kuwa haki.
GEN 15:7 Pia akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niliyekutoa Uru ya Wakaldayo nikupe nchi hii uimiliki.”
GEN 15:8 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, nitawezaje kujua kwamba nitaimiliki?”
GEN 15:9 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, “Niletee ndama jike, mbuzi, na kondoo dume, kila mmoja wa miaka mitatu, pamoja na hua na kinda la njiwa.”
GEN 15:10 Abramu akamletea hivi vyote, akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga kila kimoja kuelekea mwenzake, lakini hata hivyo ndege hakuwapasua vipande viwili.
GEN 15:11 Kisha ndege walao nyama wakatua juu ya mizoga, lakini Abramu akawafukuza.
GEN 15:12 Jua lilipokuwa linatua, Abramu akashikwa na usingizi mzito, na giza nene na la kutisha likaja juu yake.
GEN 15:13 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni katika nchi isiyo yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne.
GEN 15:14 Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi.
GEN 15:15 Wewe hata hivyo utaenda kwa baba zako kwa amani, na kuzikwa katika uzee mwema.
GEN 15:16 Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana uovu wa Waamori bado haujafikia kipimo.”
GEN 15:17 Jua lilipokuwa limezama na giza limeingia, tanuru la moshi na mwali wa moto unaowaka vikatokea na kupita kati ya vile vipande vya nyama.
GEN 15:18 Siku hiyo Mwenyezi Mungu akafanya agano na Abramu, na kumwambia, “Nitawapa wazao wako nchi hii, kuanzia Kijito cha Misri hadi mto ule mkubwa, Frati:
GEN 15:19 yaani nchi ya Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni,
GEN 15:20 Wahiti, Waperizi, Warefai,
GEN 15:21 Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”
GEN 16:1 Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mjakazi Mmisri jina lake Hajiri.
GEN 16:2 Hivyo Sarai akamwambia Abramu, “Mwenyezi Mungu amenizuilia kupata watoto. Basi nenda ukutane kimwili na mjakazi wangu; huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.” Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema.
GEN 16:3 Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mjakazi wake Mmisri aliyeitwa Hajiri, na kumpa mumewe awe mke wake.
GEN 16:4 Abramu akakutana kimwili na Hajiri, naye akapata mimba. Hajiri alipojua kuwa ana mimba, akaanza kumdharau Sarai.
GEN 16:5 Ndipo Sarai akamwambia Abramu, “Unawajibika na mateso ninayoyapata. Nilimweka mtumishi wangu mkononi mwako. Sasa kwa vile anajua kwamba ana mimba, ananidharau mimi. Mwenyezi Mungu na aamue kati yako na mimi!”
GEN 16:6 Abramu akamwambia, “Haya, mtumishi wako yuko mkononi mwako. Mtendee lolote utakalo!” Ndipo Sarai akamtesa Hajiri, naye akamtoroka.
GEN 16:7 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamkuta Hajiri karibu na chemchemi huko jangwani; chemchemi hiyo ilikuwa kando ya barabara iendayo Shuri.
GEN 16:8 Malaika akamwambia, “Hajiri, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi, na unaenda wapi?” Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.”
GEN 16:9 Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.”
GEN 16:10 Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.”
GEN 16:11 Pia malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia: “Wewe sasa una mimba nawe utamzaa mwana. Utamwita jina lake Ishmaeli, kwa sababu Mwenyezi Mungu amesikia kuhusu huzuni yako.
GEN 16:12 Atakuwa kama punda-mwitu kati ya wanadamu; mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu, na mkono wa kila mtu utakuwa dhidi yake, naye ataishi kwa uhasama na ndugu zake wote.”
GEN 16:13 Hajiri akampa Mwenyezi Mungu aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.”
GEN 16:14 Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi; bado kipo hata leo kati ya Kadeshi na Beredi.
GEN 16:15 Hivyo Hajiri akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hajiri aliyemzalia jina la Ishmaeli.
GEN 16:16 Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita Hajiri alipomzalia Ishmaeli.
GEN 17:1 Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi Mungu akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; nenda mbele zangu na uishi kwa unyofu.
GEN 17:2 Nitafanya agano kati yangu na wewe, nami nitakuzidisha sana.”
GEN 17:3 Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia,
GEN 17:4 “Kwangu mimi, hili ndilo agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi.
GEN 17:5 Hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Ibrahimu, kwa maana nimekufanya baba wa mataifa mengi.
GEN 17:6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana; kwako yatatoka mataifa, na wafalme watatoka kwako.
GEN 17:7 Nitalithibitisha agano langu kama agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo, nami nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazao wako.
GEN 17:8 Nchi yote ya Kanaani, unayoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na ya uzao wako; nami nitakuwa Mungu wao.”
GEN 17:9 Ndipo Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwako wewe, lazima ushike agano langu, wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo.
GEN 17:10 Hili ni agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa.
GEN 17:11 Mtatahiriwa, na hii itakuwa ni alama ya agano kati yangu na ninyi.
GEN 17:12 Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio wa uzao wako.
GEN 17:13 Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima atahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni agano la milele.
GEN 17:14 Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.”
GEN 17:15 Pia Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwa upande wa Sarai mkeo, hutamwita tena Sarai, bali jina lake litakuwa Sara.
GEN 17:16 Nitambariki, na hakika nitakupatia mwana kwake. Nitambariki ili awe mama wa mataifa; wafalme wa mataifa watatoka kwake.”
GEN 17:17 Ibrahimu akaanguka kifudifudi, akacheka na kusema moyoni mwake, “Je, mtu wa miaka mia moja aweza kuzaa mwana? Je, Sara atazaa mtoto katika umri wa miaka tisini?”
GEN 17:18 Ibrahimu akamwambia Mungu, “Laiti Ishmaeli naye angeshiriki baraka yako!”
GEN 17:19 Ndipo Mungu akasema, “Ndiyo, lakini mkeo Sara atakuzalia wewe mwana, nawe utamwita jina lake Isaka. Nitalithibitisha agano langu naye kama agano la milele kwa ajili yake na wazao wake baada yake.
GEN 17:20 Kuhusu Ishmaeli, nimekusikia. Hakika nitambariki; nitamfanya awe na uzao mwingi na nitaongeza sana idadi yake. Atakuwa baba wa watawala kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kubwa.
GEN 17:21 Lakini agano langu nitalithibitisha kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia mwaka ujao majira kama haya.”
GEN 17:22 Alipomaliza kuzungumza na Ibrahimu, Mungu akaondoka kwa Ibrahimu.
GEN 17:23 Siku hiyo hiyo, Ibrahimu akamchukua Ishmaeli mwanawe na wote waliozaliwa nyumbani mwake, pamoja na wale walionunuliwa kwa fedha zake; kila mwanaume wa nyumbani mwake akawatahiri, kama Mungu alivyomwagiza.
GEN 17:24 Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka tisini na tisa alipotahiriwa;
GEN 17:25 naye Ishmaeli mwanawe alitahiriwa akiwa na umri wa miaka kumi na tatu.
GEN 17:26 Ibrahimu na Ishmaeli mwanawe walitahiriwa siku hiyo hiyo.
GEN 17:27 Wanaume wote nyumbani mwa Ibrahimu, waliozaliwa nyumbani mwake na walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa wageni, walitahiriwa pamoja naye.
GEN 18:1 Mwenyezi Mungu akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri.
GEN 18:2 Ibrahimu akainua macho, akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, akaharakisha kutoka ingilio la hema lake, akawalaki na kusujudu hadi chini.
GEN 18:3 Ibrahimu akasema, “Bwana wangu, ikiwa nimepata kibali machoni mwako, usimpite mtumishi wako.
GEN 18:4 Acha yaletwe maji kidogo, nanyi mnawe miguu yenu, na mpumzike chini ya mti huu.
GEN 18:5 Niruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.” Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.”
GEN 18:6 Hivyo Ibrahimu akaharakisha akaingia kwenye hema kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”
GEN 18:7 Kisha Ibrahimu akakimbia kwenye kundi, akachagua ndama mzuri laini, na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha.
GEN 18:8 Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.
GEN 18:9 Wakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?” Akasema, “Yuko ndani ya hema.”
GEN 18:10 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Hakika nitakurudia majira kama haya mwaka ujao, na Sara mkeo atakuwa na mwana.” Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema lililokuwa nyuma ya Ibrahimu.
GEN 18:11 Ibrahimu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amepita umri wa kuzaa mtoto.
GEN 18:12 Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”
GEN 18:13 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’
GEN 18:14 Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu? Nitakurudia majira kama haya mwaka ujao, naye Sara atakuwa na mwana.”
GEN 18:15 Sara akaogopa, hivyo akadanganya na kusema, “Mimi sikucheka.” Lakini Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, ulicheka!”
GEN 18:16 Watu hao waliposimama ili waondoke, walielekeza nyuso zao Sodoma, naye Ibrahimu akatembea nao ili awasindikize.
GEN 18:17 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Je, nimfiche Ibrahimu jambo ninalokusudia kufanya?
GEN 18:18 Hakika Ibrahimu atakuwa taifa kubwa na lenye nguvu, na kupitia kwake mataifa yote ya dunia yatabarikiwa.
GEN 18:19 Kwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili Mwenyezi Mungu atimize ahadi yake kwa Ibrahimu.”
GEN 18:20 Basi Mwenyezi Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi zao zinanisikitisha sana,
GEN 18:21 hivyo nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.”
GEN 18:22 Basi wale watu wakageuka, wakaelekea Sodoma, lakini Ibrahimu akabaki amesimama mbele za Mwenyezi Mungu.
GEN 18:23 Ibrahimu akamsogelea, akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu?
GEN 18:24 Je, ikiwa watakuwepo watu hamsini wenye haki katika mji huo, kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo?
GEN 18:25 Na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo: kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Liwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya haki?”
GEN 18:26 Mwenyezi Mungu akajibu, “Nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitauacha huo mji wote kwa ajili yao.”
GEN 18:27 Kisha Ibrahimu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu.
GEN 18:28 Je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?” Bwana akamjibu, “Nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.”
GEN 18:29 Ibrahimu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?” Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.”
GEN 18:30 Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?” Akajibu, “Sitauangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.”
GEN 18:31 Ibrahimu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, wakipatikana huko watu ishirini tu?” Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”
GEN 18:32 Ibrahimu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?” Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.”
GEN 18:33 Mwenyezi Mungu alipomaliza kuzungumza na Ibrahimu, akaondoka, naye Ibrahimu akarudi nyumbani.
GEN 19:1 Malaika wale wawili walifika Sodoma wakati wa jioni, naye Lutu alikuwa ameketi kwenye lango la mji. Alipowaona, alienda kuwalaki, akasujudu, uso wake ukagusa chini.
GEN 19:2 Akasema, “Bwana zangu, tafadhali karibuni kwenye nyumba ya mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala hapa, kisha asubuhi na mapema mwendelee na safari yenu.” Wakamjibu, “La, tutalala hapa uwanjani.”
GEN 19:3 Lakini aliwasihi sana hadi wakaingia nyumbani mwake. Akawaandalia chakula, mikate isiyotiwa chachu, nao wakala.
GEN 19:4 Kabla hawajaenda kulala, wanaume wote kutoka kila sehemu ya mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, waliizunguka nyumba.
GEN 19:5 Wakamwita Lutu wakisema, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako jioni hii? Watoe nje kwetu ili tuwalawiti.”
GEN 19:6 Lutu akatoka nje kuongea nao, akaufunga mlango nyuma yake.
GEN 19:7 Akawaambia, “La hasha, rafiki zangu! Msifanye jambo hili ovu.
GEN 19:8 Tazama, ninao binti zangu wawili ambao ni bikira. Acha niwatoe kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lolote mnalotaka. Lakini msiwafanyie chochote wanaume hawa, kwa sababu wako chini ya ulinzi wa dari langu.”
GEN 19:9 Wakamjibu, “Tuondokee mbali!” Wakaendelea kusema, “Huyu mtu alikuja hapa kama mgeni na sasa anataka kuwa mwamuzi wetu! Tutakutenda vibaya kuliko wao.” Waliendelea kumlazimisha Lutu na kuusogelea mlango ili kuuvunja.
GEN 19:10 Lakini wanaume wale waliokuwa ndani wakanyoosha mikono yao, wakamvuta Lutu ndani ya nyumba na kuufunga mlango.
GEN 19:11 Kisha wakawapiga kwa upofu wale wanaume waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango.
GEN 19:12 Wale wanaume wawili wakamwambia Lutu, “Una mtu mwingine yeyote hapa: wakwe, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa,
GEN 19:13 kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.”
GEN 19:14 Kwa hiyo Lutu alitoka ili kuzungumza na wakwe wake waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa Mwenyezi Mungu yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe wake walifikiri kwamba alikuwa akitania.
GEN 19:15 Kulipopambazuka, malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walio huku, la sivyo utaangamizwa mji huu utakapoadhibiwa.”
GEN 19:16 Alipositasita, wale wanaume wakamshika mkono wake, na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwahurumia.
GEN 19:17 Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!”
GEN 19:18 Lakini Lutu akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini!
GEN 19:19 Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani; janga hili litanikumba, nami nitakufa.
GEN 19:20 Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo: Ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.”
GEN 19:21 Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja.
GEN 19:22 Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote hadi ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari.)
GEN 19:23 Lutu alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi.
GEN 19:24 Ndipo Mwenyezi Mungu akanyesha moto wa kiberiti juu ya Sodoma na Gomora kutoka kwake Mwenyezi Mungu mbinguni.
GEN 19:25 Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote walioishi katika miji hiyo, hata pia mimea yote katika nchi.
GEN 19:26 Lakini mke wa Lutu akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi.
GEN 19:27 Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Ibrahimu akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za Mwenyezi Mungu.
GEN 19:28 Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka nchi, kama moshi unaotoka katika tanuru.
GEN 19:29 Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare, alimkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu kutoka lile janga lililoharibu miji ile ambamo Lutu alikuwa ameishi.
GEN 19:30 Lutu na binti zake wawili waliondoka Soari na kufanya makao yao kule milimani, kwa maana aliogopa kukaa Soari. Yeye na binti zake wawili waliishi katika pango.
GEN 19:31 Siku moja binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Baba yetu ni mzee, na hakuna mwanaume mahali hapa atakayekutana na sisi kimwili, kama ilivyo desturi ya mahali pote duniani.
GEN 19:32 Tumnyweshe baba yetu mvinyo, kisha tukutane naye kimwili ili tuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.”
GEN 19:33 Usiku ule walimnywesha baba yao mvinyo; alipolewa, binti yake mkubwa akaingia na kukutana naye kimwili. Baba yao hakujua binti yake alipoingia kulala naye wala alipotoka.
GEN 19:34 Siku iliyofuata binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Usiku uliopita mimi nilikutana kimwili na baba yangu. Tumnyweshe divai tena, usiku huu nawe ukutane naye kimwili ili tuweze kuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.”
GEN 19:35 Kwa hiyo wakamnywesha baba yao mvinyo tena usiku ule, naye binti yake mdogo akaingia, akakutana naye kimwili. Kwa mara nyingine baba yao hakujua binti yake alipolala naye wala alipoondoka.
GEN 19:36 Hivyo binti wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao.
GEN 19:37 Binti mkubwa akamzaa mwana, akamwita jina Moabu; ndiye baba wa Wamoabu hata leo.
GEN 19:38 Binti mdogo pia akamzaa mwana, naye akamwita jina Benami; ndiye baba wa Waamoni hata leo.
GEN 20:1 Basi Ibrahimu akaondoka huko akaenda hadi nchi ya Negebu, akaishi kati ya Kadeshi na Shuri. Kwa muda mfupi alikaa Gerari.
GEN 20:2 Huko Ibrahimu akasema kuhusu Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu.” Kisha Abimeleki mfalme wa Gerari akaagiza Sara aletwe, naye akamchukua awe mkewe.
GEN 20:3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.”
GEN 20:4 Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia?
GEN 20:5 Hakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu’; naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri safi na mikono safi.”
GEN 20:6 Kisha Mungu akamwambia katika ndoto ile, “Ndiyo, najua kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse.
GEN 20:7 Sasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.”
GEN 20:8 Kesho yake asubuhi na mapema, Abimeleki akawaita maafisa wake wote, na baada ya kuwaambia yote yaliyotukia, waliogopa sana.
GEN 20:9 Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu na kumwambia, “Wewe umetufanyia nini? Nimekukosea nini hata ukaleta hatia kubwa namna hii kwangu na kwa ufalme wangu? Umenifanyia mambo ambayo hayakupasa kufanyika.”
GEN 20:10 Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ulikuwa na kusudi gani kufanya hivi?”
GEN 20:11 Ibrahimu akajibu, “Niliwaza kwamba, ‘Hakika hakuna hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa sababu ya mke wangu.’
GEN 20:12 Pamoja na hayo, ni kweli kwamba yeye ni dada yangu, binti ya baba yangu ingawa si mtoto wa mama yangu; basi akawa mke wangu.
GEN 20:13 Mungu aliponifanya nisafiri mbali na nyumbani mwa baba yangu, nilimwambia, ‘Hivi ndivyo utakavyoonesha pendo lako kwangu: Kila mahali tutakapoenda, sema hivi kunihusu, “Huyu ni kaka yangu.” ’ ”
GEN 20:14 Kisha Abimeleki akatwaa kondoo na ng’ombe, na watumwa wa kiume na wa kike, akampa Ibrahimu, na akamrudisha Sara kwa mumewe.
GEN 20:15 Abimeleki akasema, “Nchi yangu iko mbele yako; ishi popote unapotaka.”
GEN 20:16 Akamwambia Sara, “Ninampa kaka yako shekeli elfu moja za fedha. Hii ni kufidia kosa lililofanyika dhidi yako mbele ya wote walio pamoja nawe; haki yako imethibitishwa kabisa.”
GEN 20:17 Kisha Ibrahimu akamwomba Mungu, naye Mungu akamponya Abimeleki, mke wake, na wajakazi wake ili waweze kupata watoto tena,
GEN 20:18 kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amefunga tumbo za wanawake wote wa nyumba ya Abimeleki kwa sababu ya Sara, mke wa Ibrahimu.
GEN 21:1 Wakati huu Mwenyezi Mungu akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, na Mwenyezi Mungu akamtendea Sara kama alivyoahidi.
GEN 21:2 Sara akapata mimba, na akamzalia Ibrahimu mwana katika uzee wake, katika majira yale Mungu alikuwa amemwahidi.
GEN 21:3 Ibrahimu akampa huyo mwana ambaye Sara alimzalia jina Isaka.
GEN 21:4 Isaka alipokuwa na umri wa siku nane, Ibrahimu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru.
GEN 21:5 Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka mia moja Isaka mwanawe alipozaliwa.
GEN 21:6 Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, na kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.”
GEN 21:7 Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Ibrahimu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Lakini nimemzalia mwana katika uzee wake.”
GEN 21:8 Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya. Siku ile Isaka aliyoachishwa kunyonya, Ibrahimu alifanya sherehe kubwa.
GEN 21:9 Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hajiri Mmisri alimzalia Ibrahimu alikuwa anadhihaki.
GEN 21:10 Hivyo Sara akamwambia Ibrahimu, “Mwondoe mjakazi huyu mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mjakazi huyo kamwe hatarithi na mwanangu Isaka.”
GEN 21:11 Jambo hili lilimhuzunisha sana Ibrahimu kwa sababu lilimhusu mwanawe.
GEN 21:12 Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana huyo na mjakazi wako. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka.
GEN 21:13 Nitamfanya huyu mwana wa mjakazi wako kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”
GEN 21:14 Kesho yake asubuhi na mapema, Ibrahimu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hajiri. Akaviweka begani mwa Hajiri, akamwondoa pamoja na kijana. Hajiri akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.
GEN 21:15 Maji yalipokwisha kwenye kiriba, Hajiri akamwacha kijana chini ya kichaka.
GEN 21:16 Kisha akaenda akaketi kama umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Akiwa ameketi pale, akaanza kulia kwa huzuni.
GEN 21:17 Mungu akamsikia kijana akilia. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini, Hajiri? Usiogope, Mungu amesikia kijana akilia akiwa amelala pale.
GEN 21:18 Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
GEN 21:19 Ndipo Mungu akamfumbua Hajiri macho, akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.
GEN 21:20 Mungu akawa pamoja na huyo kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde.
GEN 21:21 Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akamtwalia mke kutoka Misri.
GEN 21:22 Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Ibrahimu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya.
GEN 21:23 Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”
GEN 21:24 Ibrahimu akasema, “Ninaapa hivyo.”
GEN 21:25 Ndipo Ibrahimu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyang’anya.
GEN 21:26 Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ametenda hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”
GEN 21:27 Hivyo Ibrahimu akaleta kondoo na ng’ombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano.
GEN 21:28 Ibrahimu akatenga kondoo jike saba kutoka kwa kundi.
GEN 21:29 Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ni nini maana ya hawa kondoo jike saba uliowatenga peke yao?”
GEN 21:30 Ibrahimu akamjibu, “Pokea hawa kondoo jike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”
GEN 21:31 Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu hao wawili waliapiana hapo.
GEN 21:32 Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi nchi ya Wafilisti.
GEN 21:33 Ibrahimu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa milele.
GEN 21:34 Naye Ibrahimu akakaa nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.
GEN 22:1 Baadaye Mungu akamjaribu Ibrahimu. Akamwambia, “Ibrahimu!” Ibrahimu akamjibu, “Mimi hapa.”
GEN 22:2 Kisha Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, mwana wako wa pekee umpendaye, Isaka, uende nchi ya Moria. Mtoe kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima nitakaokuambia.”
GEN 22:3 Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia.
GEN 22:4 Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali.
GEN 22:5 Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunaenda kule. Tutaabudu na kisha tutawarudia.”
GEN 22:6 Ibrahimu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, naye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja,
GEN 22:7 Isaka akamwambia Ibrahimu baba yake, “Baba yangu!” Ibrahimu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.” Isaka akasema, “Moto na kuni zipo. Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”
GEN 22:8 Ibrahimu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.
GEN 22:9 Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni.
GEN 22:10 Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe.
GEN 22:11 Lakini malaika wa Mwenyezi Mungu akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Ibrahimu! Ibrahimu!” Akajibu, “Mimi hapa.”
GEN 22:12 Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”
GEN 22:13 Ibrahimu akainua macho, akaona nyuma yake kondoo dume akiwa amenaswa pembe zake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
GEN 22:14 Ibrahimu akapaita mahali pale Yehova-Yire. Hadi leo inasemekana, “Katika mlima wa Mwenyezi Mungu itapatikana.”
GEN 22:15 Basi malaika wa Mwenyezi Mungu akamwita Ibrahimu kutoka mbinguni mara ya pili,
GEN 22:16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Mwenyezi Mungu, kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee:
GEN 22:17 Hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga wa pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao,
GEN 22:18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”
GEN 22:19 Ndipo Ibrahimu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wote, wakaenda hadi Beer-Sheba. Naye Ibrahimu akaishi huko Beer-Sheba.
GEN 22:20 Baada ya muda, Ibrahimu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto; amemzalia ndugu yako Nahori wana:
GEN 22:21 Usi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye, Kemueli (baba wa Aramu),
GEN 22:22 Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.”
GEN 22:23 Bethueli akamzaa Rebeka.
GEN 22:24 Suria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alizaa wana: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.
GEN 23:1 Sara aliishi miaka mia moja na ishirini na saba (127).
GEN 23:2 Sara akafa huko Kiriath-Arba (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani, naye Ibrahimu akalia na kumwomboleza Sara.
GEN 23:3 Ndipo Ibrahimu akainuka kutoka pale penye maiti ya mke wake. Akazungumza na Wahiti, akasema,
GEN 23:4 “Mimi ni mpitaji na mgeni miongoni mwenu. Niuzieni sehemu ya ardhi yenu ili niweze kumzika maiti wangu.”
GEN 23:5 Wahiti wakamjibu Ibrahimu,
GEN 23:6 “Bwana, tusikilize. Wewe ni mtawala mkuu sana miongoni mwetu. Zika maiti wako katika kaburi unalolipenda kati ya makaburi yetu. Hakuna mtu wa kwetu atakayekuzuia kaburi lake ili kuzika maiti wako.”
GEN 23:7 Ibrahimu akainuka, akasujudu mbele ya Wahiti, wenyeji wa nchi hiyo.
GEN 23:8 Akawaambia, “Kama mnaniruhusu kumzika maiti wangu, basi nisikilizeni, mkamsihi Efroni mwana wa Sohari kwa niaba yangu
GEN 23:9 ili aniuzie pango la Makpela, lililo mali yake, nalo liko mwisho wa shamba lake. Mwambieni aniuzie kwa bei kamili atakayosema ili liwe mahali pangu pa kuzikia miongoni mwenu.”
GEN 23:10 Efroni Mhiti alikuwa ameketi miongoni mwa watu wake; akamjibu Ibrahimu mbele ya Wahiti wote waliokuwa katika lango la mji:
GEN 23:11 “La, bwana wangu, nisikilize. Nakupa shamba, na pia nakupa pango lililo ndani yake. Nakupa mbele ya watu wangu, uzike maiti wako.”
GEN 23:12 Ibrahimu akasujudu tena mbele ya wenyeji wa nchi,
GEN 23:13 akamwambia Efroni wale watu wakiwa wanasikia, “Tafadhali nisikilize. Nitakulipa fedha za hilo shamba. Kubali kuzipokea ili niweze kumzika maiti wangu.”
GEN 23:14 Efroni akamjibu Ibrahimu,
GEN 23:15 “Nisikilize, bwana wangu, thamani ya ardhi hiyo ni shekeli mia nne za fedha, lakini hiyo ni nini kati yako na mimi? Mzike maiti wako.”
GEN 23:16 Ibrahimu akakubali masharti ya Efroni, akampimia ile fedha aliyotaja masikioni mwa Wahiti: shekeli mia nne za fedha kulingana na viwango vya uzito vilivyokuwa vikitumika wakati huo na wafanyabiashara.
GEN 23:17 Hivyo shamba la Efroni huko Makpela karibu na Mamre, yaani shamba pamoja na pango lililokuwamo, nayo miti yote iliyokuwa ndani ya mipaka ya shamba hilo, vilikabidhiwa
GEN 23:18 kwa Ibrahimu kuwa mali yake mbele ya Wahiti wote waliokuwa wamekuja kwenye lango la mji.
GEN 23:19 Baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe kwenye pango ndani ya shamba la Makpela karibu na Mamre (huko Hebroni) katika nchi ya Kanaani.
GEN 23:20 Hivyo Wahiti wakamkabidhi Ibrahimu shamba pamoja na pango lililokuwa humo kuwa mahali pa kuzikia.
GEN 24:1 Wakati huu Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye Mwenyezi Mungu alikuwa amembariki katika mambo yote.
GEN 24:2 Ibrahimu akamwambia mtumishi wake mkuu katika nyumba yake, aliyekuwa msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako chini ya paja langu.
GEN 24:3 Ninataka uape kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao.
GEN 24:4 Bali nenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaka mwanangu mke.”
GEN 24:5 Yule mtumishi akamuuliza, “Je, itakuwaje huyo mwanamke akikataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimrudishe mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?”
GEN 24:6 Ibrahimu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko.
GEN 24:7 Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbingu, alinitoa nyumbani mwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa. Ndiye alisema nami na akaniahidi kwa kiapo, akasema, ‘Nitawapa uzao wako nchi hii.’ Yeye atatuma malaika wake akutangulie ili umtwalie mwanangu mke kutoka huko.
GEN 24:8 Huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.”
GEN 24:9 Basi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Ibrahimu, akamwapia kuhusu shauri hili.
GEN 24:10 Ndipo huyo mtumishi akachukua ngamia kumi miongoni mwa ngamia wa bwana wake, akaondoka, akiwa amechukua aina zote za vitu vizuri kutoka kwa bwana wake. Akaelekea Mesopotamia, akaenda hadi mji wa Nahori.
GEN 24:11 Akawapigisha ngamia magoti karibu na kisima cha maji nje ya mji; ilikuwa inaelekea jioni, wakati wanawake huteka maji.
GEN 24:12 Kisha akaomba, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nipatie ushindi leo, uoneshe ukarimu kwa bwana wangu Ibrahimu.
GEN 24:13 Tazama, nimesimama karibu na kisima hiki cha maji, nao binti za watu wa mji huu wanakuja kuteka maji.
GEN 24:14 Basi na iwe hivi, nitakapomwambia binti mmoja, ‘Tafadhali tua mtungi wako nipate kunywa maji’; naye akisema, ‘Kunywa, nitawanywesha na ngamia wako pia’: basi na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Kwa hili nitajua umemtendea bwana wangu ukarimu.”
GEN 24:15 Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka, aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Ibrahimu.
GEN 24:16 Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mwanaume aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake, tena akapanda juu.
GEN 24:17 Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”
GEN 24:18 Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.
GEN 24:19 Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitawatekea ngamia wako maji pia hadi wote watosheke.”
GEN 24:20 Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine, na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote.
GEN 24:21 Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kama Mwenyezi Mungu ameifanikisha safari yake, au la.
GEN 24:22 Ikawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka moja, na bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi.
GEN 24:23 Kisha akamuuliza, “Wewe ni binti ya nani? Tafadhali niambie. Je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tunapoweza kulala?”
GEN 24:24 Yule msichana akamjibu, “Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.”
GEN 24:25 Akaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.”
GEN 24:26 Yule mtumishi akasujudu na kumwabudu Mwenyezi Mungu,
GEN 24:27 akisema, “Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami, Mwenyezi Mungu ameniongoza safarini, akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.”
GEN 24:28 Yule msichana akakimbia, akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya.
GEN 24:29 Rebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani; huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani.
GEN 24:30 Mara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima.
GEN 24:31 Akamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.”
GEN 24:32 Hivyo yule mtumishi akaingia nyumbani, nayo mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia, na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu.
GEN 24:33 Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula hadi niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.” Labani akasema, “Basi tuambie.”
GEN 24:34 Hivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Ibrahimu.
GEN 24:35 Mwenyezi Mungu amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ng’ombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda.
GEN 24:36 Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho.
GEN 24:37 Naye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao,
GEN 24:38 ila uende hadi kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’
GEN 24:39 “Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’
GEN 24:40 “Akanijibu, ‘Mwenyezi Mungu, ambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu.
GEN 24:41 Kisha, utakapoenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu. Hata wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’
GEN 24:42 “Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia.
GEN 24:43 Tazama, ninasimama kando ya kisima hiki. Mwanamwali akija kuteka maji, nami nikimwambia: Tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka mtungi wako.
GEN 24:44 Naye akiniambia, “Kunywa, nami nitawatekea ngamia wako maji pia,” basi huyo awe ndiye mke Mwenyezi Mungu amemchagulia mwana wa bwana wangu.’
GEN 24:45 “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani, akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’
GEN 24:46 “Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa, na nitawanywesha ngamia wako pia.’ Basi nikanywa, naye akawanywesha na ngamia pia.
GEN 24:47 “Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti ya nani?’ “Akasema, ‘Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’ “Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake,
GEN 24:48 nikasujudu na nikamwabudu Mwenyezi Mungu. Nikamtukuza Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake.
GEN 24:49 Ikiwa mtaonesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie; la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.”
GEN 24:50 Labani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi Mungu; hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema.
GEN 24:51 Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa na Mwenyezi Mungu alivyoongoza.”
GEN 24:52 Ikawa huyo mtumishi wa Ibrahimu aliposikia waliyosema, alisujudu, uso wake ukagusa chini mbele za Mwenyezi Mungu.
GEN 24:53 Ndipo huyo mtumishi akatoa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na kwa fedha, pamoja na mavazi, akampa Rebeka; pia akawapa zawadi za thamani kubwa nduguye na mamaye.
GEN 24:54 Kisha yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye wakala, wakanywa na kulala palepale. Walipoamka asubuhi, yule mtumishi akasema, “Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
GEN 24:55 Lakini ndugu yake Rebeka pamoja na mama yake wakajibu, “Acha binti akae kwetu siku kumi au zaidi, ndipo mwondoke.”
GEN 24:56 Lakini yule mtumishi akawaambia, “Msinicheleweshe, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amefanikisha safari yangu. Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
GEN 24:57 Ndipo wakasema, “Acha tumwite huyo binti tumuulize, tusikie atakavyosema.”
GEN 24:58 Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je, utaenda na mtu huyu?” Akasema, “Nitaenda.”
GEN 24:59 Hivyo wakamwaga ndugu yao Rebeka aondoke, pamoja na mjakazi wake, na mtumishi wa Ibrahimu na watu wake.
GEN 24:60 Wakambariki Rebeka, wakamwambia, “Ndugu yetu, uwe wewe kumi elfu, mara elfu nyingi; nao wazao wako wamiliki malango ya adui zao.”
GEN 24:61 Rebeka na vijakazi wake wakajiandaa, wakapanda ngamia wao, wakafuatana na yule mtu. Hivyo yule mtumishi akamchukua Rebeka, wakaondoka.
GEN 24:62 Basi Isaka alikuwa ametoka Beer-Lahai-Roi, kwa kuwa alikuwa akiishi nchi ya Negebu.
GEN 24:63 Isaka akaenda shambani kutafakari wakati wa jioni; alipoinua macho yake, akaona ngamia wanakuja.
GEN 24:64 Rebeka pia akainua macho, akamwona Isaka. Akashuka kutoka ngamia wake,
GEN 24:65 akamuuliza yule mtumishi, “Ni nani mtu yule kule shambani anayekuja kutulaki?” Yule mtumishi akajibu, “Huyu ndiye bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake, akajifunika.
GEN 24:66 Kisha yule mtumishi akamweleza Isaka mambo yote aliyoyatenda.
GEN 24:67 Isaka akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake. Isaka akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaka akampenda; akafarijika baada ya kifo cha mama yake.
GEN 25:1 Ibrahimu alioa mke mwingine aliyeitwa Ketura.
GEN 25:2 Huyu alimzalia Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua.
GEN 25:3 Yokshani alikuwa baba wa Sheba na Dedani; wazao wa Dedani walikuwa Waashuru, Waletushi na Waleumi.
GEN 25:4 Wana wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa. Hawa wote walikuwa uzao wa Ketura.
GEN 25:5 Ibrahimu akamwachia Isaka kila kitu alichokuwa nacho.
GEN 25:6 Lakini Ibrahimu alipokuwa bado hai, akawapa watoto wa masuria wake zawadi, kisha akawaondoa waende kuishi pande za mashariki mbali na mwanawe Isaka.
GEN 25:7 Kwa jumla, Ibrahimu aliishi miaka mia moja na sabini na tano (175).
GEN 25:8 Ndipo Ibrahimu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku; naye akakusanywa pamoja na watu wake.
GEN 25:9 Watoto wake Isaka na Ishmaeli wakamzika katika pango la Makpela karibu na Mamre, katika shamba lililokuwa la Efroni mwana wa Sohari Mhiti,
GEN 25:10 shamba ambalo Ibrahimu alilinunua kwa Wahiti. Hapo ndipo Ibrahimu alipozikwa pamoja na mkewe Sara.
GEN 25:11 Baada ya kifo cha Ibrahimu, Mungu akambariki mwanawe Isaka, ambaye baadaye aliishi karibu na Beer-Lahai-Roi.
GEN 25:12 Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ambaye Hajiri Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Ibrahimu.
GEN 25:13 Haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, walioorodheshwa kulingana na jinsi walivyozaliwa: Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli ni Nebayothi, akafuatia Kedari, Adbeeli, Mibsamu,
GEN 25:14 Mishma, Duma, Masa,
GEN 25:15 Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema.
GEN 25:16 Hawa walikuwa wana wa Ishmaeli, na haya ni majina ya viongozi wa makabila yao kumi na mbili, kufuatana na makazi yao na kambi zao.
GEN 25:17 Kwa jumla Ishmaeli aliishi miaka mia moja na thelathini na saba (137). Akapumua pumzi ya mwisho, akafa, naye akakusanywa pamoja na watu wake.
GEN 25:18 Wazao wa Ishmaeli waliishi kuanzia nchi ya Havila hadi Shuri, karibu na mpaka wa Misri, kuelekea Ashuru. Hao waliishi kwa uhasama na ndugu zao wote.
GEN 25:19 Hivi ndivyo vizazi vya Isaka mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu akamzaa Isaka.
GEN 25:20 Isaka alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu.
GEN 25:21 Isaka akamwomba Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. Mwenyezi Mungu akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba.
GEN 25:22 Watoto wakashindana tumboni mwake, naye akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza Mwenyezi Mungu.
GEN 25:23 Mwenyezi Mungu akamjibu, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako, na mataifa hayo mawili kutoka ndani yako watatenganishwa. Mmoja atakuwa na nguvu kuliko mwingine, na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”
GEN 25:24 Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake.
GEN 25:25 Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, na mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina Esau.
GEN 25:26 Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina Yakobo. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini Rebeka alipowazaa.
GEN 25:27 Watoto wakakua. Esau akawa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, naye Yakobo akawa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani.
GEN 25:28 Isaka, aliyekuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo.
GEN 25:29 Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu. Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali.
GEN 25:30 Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.)
GEN 25:31 Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”
GEN 25:32 Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?”
GEN 25:33 Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
GEN 25:34 Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu, naye akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake. Kwa hiyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
GEN 26:1 Basi njaa kubwa ikatokea katika nchi hiyo, mbali na njaa iliyotokea wakati wa Ibrahimu. Isaka akaenda kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti huko Gerari.
GEN 26:2 Mwenyezi Mungu akamtokea Isaka, akamwambia, “Usiende Misri, bali ukae katika nchi nitakayokuambia.
GEN 26:3 Kaa katika nchi hii kwa kitambo; mimi nitakuwa pamoja na wewe na nitakubariki. Kwa maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote, na nitatimiza kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.
GEN 26:4 Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote, na kupitia uzao wako mataifa yote yatabarikiwa,
GEN 26:5 kwa sababu Ibrahimu alinitii mimi, na akatenda yote niliyomwagiza, akahifadhi amri zangu, na hukumu zangu, pamoja na sheria zangu.”
GEN 26:6 Hivyo Isaka akaishi huko Gerari.
GEN 26:7 Wanaume wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Wanaume wa huku wanaweza kuniua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa ni mzuri wa sura.”
GEN 26:8 Isaka alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona Isaka akimpapasa Rebeka, mke wake.
GEN 26:9 Abimeleki akamwita Isaka, akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu’?” Isaka akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.”
GEN 26:10 Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotutendea? Ingewezekana mtu yeyote akakutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia kwetu.”
GEN 26:11 Hivyo Abimeleki akatoa amri kwa watu wote, akisema, “Yeyote atakayemnyanyasa mtu huyu au mkewe hakika atauawa.”
GEN 26:12 Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo, na kwa mwaka huo huo akavuna mara mia, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimbariki.
GEN 26:13 Isaka akawa tajiri, nayo mali yake ikaendelea kuongezeka hata akawa tajiri sana.
GEN 26:14 Akawa na mifugo ya kondoo na ng’ombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu.
GEN 26:15 Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Ibrahimu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo.
GEN 26:16 Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.”
GEN 26:17 Basi Isaka akatoka huko, akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko.
GEN 26:18 Ndipo Isaka akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Ibrahimu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya Ibrahimu kufa, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa.
GEN 26:19 Watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakagundua huko kisima chenye maji safi.
GEN 26:20 Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.
GEN 26:21 Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania; akakiita Sitna.
GEN 26:22 Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa Mwenyezi Mungu ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.”
GEN 26:23 Kutoka pale akaenda Beer-Sheba.
GEN 26:24 Usiku ule Mwenyezi Mungu akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Ibrahimu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe. Nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.”
GEN 26:25 Isaka akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Mwenyezi Mungu. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima.
GEN 26:26 Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake.
GEN 26:27 Isaka akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu, na ninyi mlinichukia na kunifukuza?”
GEN 26:28 Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu,’ yaani kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe,
GEN 26:29 kwamba hutatudhuru, kama vile nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote, na tukawaaga kwa amani. Tena sasa umebarikiwa na Mwenyezi Mungu.”
GEN 26:30 Basi Isaka akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa.
GEN 26:31 Kesho yake asubuhi na mapema wakaapiana. Kisha Isaka akawaruhusu waende zao, wakamwacha kwa amani.
GEN 26:32 Siku hiyo watumishi wa Isaka wakaja, wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!”
GEN 26:33 Naye akakiita Shiba; hadi leo mji huo unaitwa Beer-Sheba.
GEN 26:34 Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti.
GEN 26:35 Hawa walikuwa chanzo cha huzuni kwa Isaka na Rebeka.
GEN 27:1 Isaka alipokuwa mzee na macho yake yakapofuka kwa kukosa nguvu, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.” Akajibu, “Mimi hapa.”
GEN 27:2 Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kufa kwangu.
GEN 27:3 Sasa basi chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukaniwindie mawindo.
GEN 27:4 Uniandalie chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili nikubariki kabla sijafa.”
GEN 27:5 Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka akizungumza na mwanawe Esau. Basi Esau alipoenda nyikani kuwinda mawindo ayalete,
GEN 27:6 Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau,
GEN 27:7 ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili nikubariki mbele za Mwenyezi Mungu kabla sijafa.’
GEN 27:8 Sasa mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia:
GEN 27:9 Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili nimwandalie baba yako chakula kitamu kile anachokipenda.
GEN 27:10 Kisha umpelekee baba yako ale, ili akubariki kabla hajafa.”
GEN 27:11 Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, nami nina ngozi nyororo.
GEN 27:12 Itakuwaje baba yangu akinigusa? Ataona kama ninamfanyia ujanja, nami nijiletee laana badala ya baraka.”
GEN 27:13 Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia: nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.”
GEN 27:14 Kwa hiyo alienda akawaleta, akampa mama yake, naye Rebeka akaandaa chakula kitamu, kile alichokipenda baba yake.
GEN 27:15 Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo.
GEN 27:16 Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi.
GEN 27:17 Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.
GEN 27:18 Yakobo akaenda kwa baba yake, akasema, “Baba yangu.” Akajibu, “Naam, mwanangu. Wewe ni nani?”
GEN 27:19 Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili unibariki.”
GEN 27:20 Isaka akamuuliza mwanawe, “Umepataje mawindo haraka hivi, mwanangu?” Akajibu, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”
GEN 27:21 Kisha Isaka akamwambia Yakobo, “Mwanangu, tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”
GEN 27:22 Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaka, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.”
GEN 27:23 Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki.
GEN 27:24 Akamuuliza, “Kweli wewe ni mwanangu Esau?” Akajibu, “Ni mimi.”
GEN 27:25 Kisha Isaka akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nikubariki.” Yakobo akamletea, naye akala; kisha akamletea na divai akanywa.
GEN 27:26 Ndipo Isaka baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”
GEN 27:27 Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaka aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema, “Aha, harufu ya mwanangu ni kama harufu ya shamba ambalo Mwenyezi Mungu amelibariki.
GEN 27:28 Mungu na akupe umande wa mbinguni na utajiri wa duniani: wingi wa nafaka na divai mpya.
GEN 27:29 Mataifa yakutumikie, na mataifa yakusujudie. Uwe bwana juu ya ndugu zako, na wana wa mama yako wakusujudie. Walaaniwe wale wanaokulaani, na wabarikiwe wale wanaokubariki.”
GEN 27:30 Baada ya Isaka kumbariki Yakobo, na punde tu alipoondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni.
GEN 27:31 Naye pia akaandaa chakula kitamu, akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”
GEN 27:32 Isaka baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?” Akamjibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”
GEN 27:33 Isaka akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”
GEN 27:34 Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia kwa sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki! Nibariki mimi pia, baba yangu!”
GEN 27:35 Lakini akamjibu, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu, akachukua baraka yako.”
GEN 27:36 Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”
GEN 27:37 Isaka akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako; pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, na nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”
GEN 27:38 Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.
GEN 27:39 Baba yake Isaka akamjibu, “Makao yako yatakuwa mbali na utajiri wa dunia, mbali na umande wa mbinguni.
GEN 27:40 Utaishi kwa upanga, nawe utamtumikia ndugu yako. Lakini utakapokuwa umejikomboa, utatupa nira yake kutoka shingoni mwako.”
GEN 27:41 Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia; ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”
GEN 27:42 Rebeka alipoambiwa yale Esau mwanawe mkubwa aliyoyasema, akamtumania Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua.
GEN 27:43 Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani.
GEN 27:44 Ukae naye kwa muda hadi ghadhabu ya ndugu yako itulie.
GEN 27:45 Ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze nyote wawili siku moja?”
GEN 27:46 Kisha Rebeka akamwambia Isaka, “Nimechukia maisha kwa sababu ya hawa wanawake Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake Wahiti kama hawa, sitaona haja ya kuendelea kuishi.”
GEN 28:1 Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke Mkanaani.
GEN 28:2 Nenda mara moja hadi Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli, baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako.
GEN 28:3 Mungu Mwenyezi na akubariki, uwe na uzao, uongezeke idadi yako hadi upate kuwa jamii kubwa ya watu.
GEN 28:4 Akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Ibrahimu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu.”
GEN 28:5 Kisha Isaka akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
GEN 28:6 Basi Esau akajua kuwa Isaka amembariki Yakobo na kumtuma Padan-Aramu ili achukue mke huko, na kwamba alipombariki alimwamuru, akisema, “Usioe mke katika binti za Wakanaani,”
GEN 28:7 tena kwamba Yakobo amewatii baba yake na mama yake, naye ameenda Padan-Aramu.
GEN 28:8 Esau akatambua jinsi baba yake Isaka alivyowachukia binti za Wakanaani.
GEN 28:9 Ndipo Esau akaenda kwa Ishmaeli, akamwoa Mahalati, ndugu wa Nebayothi na binti ya Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, kuongezea wale wake wengine aliokuwa nao.
GEN 28:10 Yakobo akatoka Beer-Sheba kwenda Harani.
GEN 28:11 Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake, akajinyoosha na akalala usingizi.
GEN 28:12 Akaota ndoto, na katika ndoto hiyo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni. Nao malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka kwa ngazi hiyo.
GEN 28:13 Juu yake alisimama Mwenyezi Mungu, akasema, “Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba yako Ibrahimu, na Mungu wa Isaka. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako.
GEN 28:14 Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako, mataifa yote ya duniani yatabarikiwa.
GEN 28:15 Niko pamoja nawe, nami nitakulinda popote utakapoenda, na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha hadi nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”
GEN 28:16 Yakobo alipoamka kutoka usingizi, akawaza, “Hakika Mwenyezi Mungu yuko mahali hapa, wala mimi sikujua.”
GEN 28:17 Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo; hili ni lango la mbinguni.”
GEN 28:18 Kesho yake asubuhi na mapema, Yakobo akalichukua lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake.
GEN 28:19 Mahali pale akapaita Betheli, ingawa mji ule hapo awali uliitwa Luzu.
GEN 28:20 Kisha Yakobo akaweka nadhiri, akisema, “Mungu akiwa pamoja nami na kunilinda katika safari hii, akinipa chakula nile na nguo nivae,
GEN 28:21 na nirudi salama nyumbani mwa baba yangu, hapo ndipo Mwenyezi Mungu atakuwa Mungu wangu.
GEN 28:22 Nalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu, na katika yote utakayonipa nitakutolea sehemu ya kumi.”
GEN 29:1 Kisha Yakobo akaendelea na safari yake, na akafika nchi ya watu wa mashariki.
GEN 29:2 Huko akaona kisima katika shamba, pamoja na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu na kisima hicho, kwa sababu walikuwa wakinyweshwa kutoka kisima hicho. Jiwe lililokuwa juu ya mdomo wa kisima lilikuwa kubwa.
GEN 29:3 Kondoo walipokusanyika hapo, wachungaji walilivingirisha jiwe hilo kutoka mdomo wa kisima. Kisha walilirudisha jiwe mahali pake juu ya mdomo wa kisima.
GEN 29:4 Yakobo aliwauliza wachungaji, “Ndugu zangu, ninyi mmetoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka Harani.”
GEN 29:5 Akawauliza, “Je, mnamfahamu Labani, mjukuu wa Nahori?” Wakamjibu, “Ndiyo, tunamfahamu.”
GEN 29:6 Kisha Yakobo akawauliza, “Je, yeye ni mzima?” Wakasema, “Ndiyo, ni mzima; na hapa yuaja Raheli binti yake akiwa na kondoo.”
GEN 29:7 Akawaambia, “Tazama, jua bado liko juu, si wakati wa kukusanya mifugo. Nywesheni kondoo na mwarudishe malishoni.”
GEN 29:8 Wakamjibu, “Haiwezekani, hadi kondoo wote wakusanyike, nalo jiwe livingirishwe kutoka mdomo wa kisima. Ndipo tutawanywesha kondoo.”
GEN 29:9 Alipokuwa akizungumza nao, Raheli akaja na kondoo wa baba yake, kwa maana alikuwa mchunga kondoo.
GEN 29:10 Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mama yake, pamoja na kondoo wa Labani, alienda na kulivingirisha jiwe kutoka mdomo wa kisima na kuwanywesha kondoo wa mjomba wake.
GEN 29:11 Kisha Yakobo akambusu Raheli, na akaanza kulia kwa sauti.
GEN 29:12 Yakobo alikuwa amemwambia Raheli kuwa yeye alikuwa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Basi Raheli alikimbia na kumweleza baba yake.
GEN 29:13 Mara Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo, mwana wa ndugu yake, aliharakisha kwenda kumlaki. Akamkumbatia na kumbusu, halafu akamleta nyumbani mwake, naye Yakobo akamwambia mambo hayo yote.
GEN 29:14 Ndipo Labani akamwambia, “Wewe ni mwili wangu na damu yangu mwenyewe.” Baada ya Yakobo kukaa kwa Labani mwezi mzima,
GEN 29:15 Labani akamwambia, “Kwa vile wewe ni jamaa yangu, ndiyo sababu unifanyie kazi bila ujira? Niambie ujira wako utakuwa nini.”
GEN 29:16 Labani alikuwa na binti wawili; binti mkubwa aliitwa Lea, naye binti mdogo aliitwa Raheli.
GEN 29:17 Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa na umbo la kupendeza na mzuri wa sura.
GEN 29:18 Yakobo akampenda Raheli; akamwambia Labani, “Nitakutumikia kwa miaka saba kwa ajili ya kumpata Raheli binti yako mdogo.”
GEN 29:19 Labani akasema, “Ni bora zaidi nikupe Raheli kuliko kumpa mtu mwingine yeyote. Kaa pamoja na mimi hapa.”
GEN 29:20 Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.
GEN 29:21 Ndipo Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu. Muda wangu umekamilika, nami nataka niingie kwake.”
GEN 29:22 Basi Labani akaalika watu wote wa mahali pale na akafanya karamu.
GEN 29:23 Lakini ilipofika jioni, akamchukua Lea binti yake, akampa Yakobo, naye Yakobo akakutana naye kimwili.
GEN 29:24 Naye Labani akamtoa Zilpa mjakazi wake kuwa mtumishi wa Lea, binti yake.
GEN 29:25 Kesho yake asubuhi, Yakobo akagundua kuwa amepewa Lea! Basi Yakobo akamwambia Labani, “Ni jambo gani hili ulilonitendea? Nilikutumikia kwa ajili ya Raheli, sivyo? Kwa nini umenidanganya?”
GEN 29:26 Labani akajibu, “Si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya kumwoza binti mkubwa.
GEN 29:27 Maliza juma la arusi ya binti huyu, kisha pia nitakupa huyu binti mdogo, kwa kutumika miaka mingine saba.”
GEN 29:28 Naye Yakobo akafanya hivyo. Akamaliza juma na Lea, kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake.
GEN 29:29 Labani akamtoa Bilha mjakazi wake kwa Raheli ili kuwa mtumishi wake.
GEN 29:30 Pia Yakobo akakutana na Raheli kimwili, naye akampenda Raheli kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.
GEN 29:31 Mwenyezi Mungu alipoona kwamba Lea hapendwi, akamwezesha kupata watoto, lakini Raheli alikuwa tasa.
GEN 29:32 Lea akapata mimba, akazaa mwana. Akamwita jina Reubeni, kwa maana alisema, “Ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameona huzuni yangu. Hakika mume wangu sasa atanipenda.”
GEN 29:33 Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana akasema, “Kwa sababu Mwenyezi Mungu alisikia kwamba sipendwi, amenipa tena huyu mwana.” Kwa hiyo akamwita jina Simeoni.
GEN 29:34 Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana akasema, “Sasa mume wangu ataambatana na mimi, kwa sababu nimemzalia wana watatu.” Kwa hiyo akamwita jina Lawi.
GEN 29:35 Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana akasema, “Wakati huu nitamsifu Mwenyezi Mungu.” Kwa hiyo akamwita jina Yuda. Kisha akaacha kuzaa watoto.
GEN 30:1 Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea dada yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”
GEN 30:2 Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia kuzaa watoto?”
GEN 30:3 Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mjakazi wangu. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto, na kupitia kwake mimi pia niweze kuwa na uzao.”
GEN 30:4 Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili,
GEN 30:5 naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana.
GEN 30:6 Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu; amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa hiyo akamwita jina Dani.
GEN 30:7 Bilha mjakazi wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili.
GEN 30:8 Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita jina Naftali.
GEN 30:9 Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mjakazi wake Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake.
GEN 30:10 Zilpa mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana.
GEN 30:11 Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita jina Gadi.
GEN 30:12 Mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili.
GEN 30:13 Ndipo Lea akasema, “Nina furaha kiasi gani! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita jina Asheri.
GEN 30:14 Msimu wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akachuma tunguja ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
GEN 30:15 Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kuninyang’anya mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?” Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”
GEN 30:16 Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.
GEN 30:17 Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano.
GEN 30:18 Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mjakazi wangu.” Kwa hiyo akamwita jina Isakari.
GEN 30:19 Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita.
GEN 30:20 Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Sasa mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita jina Zabuloni.
GEN 30:21 Baadaye akamzaa mtoto wa kike, akamwita jina Dina.
GEN 30:22 Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake.
GEN 30:23 Akapata mimba na akamzaa mwana; akasema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”
GEN 30:24 Akamwita jina Yusufu, akasema, “Mwenyezi Mungu na anipe mwana mwingine.”
GEN 30:25 Baada ya Raheli kumzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu.
GEN 30:26 Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua kazi niliyokufanyia.”
GEN 30:27 Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa uaguzi kwamba Mwenyezi Mungu amenibariki kwa sababu yako.”
GEN 30:28 Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.”
GEN 30:29 Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi nimekutumikia na jinsi wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu.
GEN 30:30 Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, naye Mwenyezi Mungu amekubariki popote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?”
GEN 30:31 Labani akamuuliza, “Nikupe nini?” Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote, lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako.
GEN 30:32 Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabaka mabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi, na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabaka mabaka. Hawa watakuwa ujira wangu.
GEN 30:33 Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabaka mabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.”
GEN 30:34 Labani akasema, “Ninakubali; na iwe kama ulivyosema.”
GEN 30:35 Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa, na mbuzi jike wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao), na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe.
GEN 30:36 Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu, naye Yakobo akaendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki.
GEN 30:37 Lakini Yakobo akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo.
GEN 30:38 Kisha akaweka fito hizo katika mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu,
GEN 30:39 wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao. Wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabaka mabaka.
GEN 30:40 Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe, wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani.
GEN 30:41 Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito,
GEN 30:42 lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama wadhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo.
GEN 30:43 Hivyo Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, mjakazi na watumishi, na ngamia na punda.
GEN 31:1 Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu, naye amepata utajiri huu wote kutokana na mali ya baba yetu.”
GEN 31:2 Yakobo akatambua kwamba moyo wa Labani kwake umebadilika.
GEN 31:3 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.”
GEN 31:4 Hivyo Yakobo akatuma ujumbe kwa Raheli na Lea waje malishoni kwenye makundi yake.
GEN 31:5 Akawaambia, “Naona moyo wa baba yenu kwangu umebadilika, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.
GEN 31:6 Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote,
GEN 31:7 lakini baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru.
GEN 31:8 Aliposema, ‘Wenye madoadoa watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye madoadoa. Aliposema, ‘Wenye mistari watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye mistari.
GEN 31:9 Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi.
GEN 31:10 “Majira ya kuzaliana niliota ndoto. Niliinua macho na kuona kwamba wale beberu waliokuwa wakiwapanda mbuzi walikuwa wana mistari, madoadoa na mabaka mabaka.
GEN 31:11 Malaika wa Mungu akaniita katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’
GEN 31:12 Akaniambia, ‘Inua macho yako uone wale beberu wote wanaowapanda mbuzi wana mistari, madoadoa au mabaka mabaka, kwa maana nimeona yale yote Labani amekutendea.
GEN 31:13 Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia nguzo mafuta, na ukaniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’ ”
GEN 31:14 Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu?
GEN 31:15 Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata mali tuliyolipiwa.
GEN 31:16 Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.”
GEN 31:17 Ndipo Yakobo akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia.
GEN 31:18 Naye akawaswaga wanyama wote mbele yake, pamoja na mali yote aliyokuwa amepata huko Padan-Aramu ili aende kwa baba yake Isaka katika nchi ya Kanaani.
GEN 31:19 Labani alipokuwa ameenda kukata kondoo wake manyoya, Raheli aliiba miungu ya nyumbani mwa baba yake.
GEN 31:20 Zaidi ya hayo, Yakobo alimdanganya Labani Mwaramu kwa kutokumwambia kwamba anakimbia.
GEN 31:21 Hivyo akakimbia pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo na kuvuka Mto, akaelekea nchi ya vilima ya Gileadi.
GEN 31:22 Siku ya tatu, Labani akaambiwa kwamba Yakobo amekimbia.
GEN 31:23 Akiwachukua jamaa zake, akamfuatia Yakobo kwa siku saba na kumkuta kwenye nchi ya vilima ya Gileadi.
GEN 31:24 Ndipo Mungu akamjia Labani Mwaramu katika ndoto usiku na kumwambia, “Jihadhari usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.”
GEN 31:25 Yakobo alikuwa amepiga hema lake katika nchi ya vilima ya Gileadi wakati Labani alimfikia; naye Labani na jamaa yake wakapiga kambi huko pia.
GEN 31:26 Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Umenidanganya na umewachukua binti zangu kama mateka katika vita.
GEN 31:27 Kwa nini ulikimbia kwa siri na kunidanganya? Kwa nini hukuniambia ili nikuage kwa furaha na nyimbo za matari na vinubi?
GEN 31:28 Hata hukuniruhusu niwabusu wajukuu zangu na kuwaaga binti zangu. Umefanya kitu cha kipumbavu.
GEN 31:29 Nina uwezo wa kukudhuru, lakini usiku uliopita Mungu wa baba yako alisema nami, akaniambia, ‘Jihadhari, usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.’
GEN 31:30 Sasa umeondoka kwa sababu umetamani kurudi nyumbani mwa baba yako. Lakini kwa nini umeiiba miungu yangu?”
GEN 31:31 Yakobo akamjibu Labani, “Niliogopa, kwa sababu nilifikiri ungeweza kuninyang’anya binti zako kwa nguvu.
GEN 31:32 Lakini ukimkuta yeyote na miungu yako, huyo mtu hataishi. Mbele ya jamaa zetu, angalia mwenyewe uone kama kuna chochote chako hapa nilicho nacho; kama kipo, kichukue.” Basi Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiiba hiyo miungu.
GEN 31:33 Kwa hiyo Labani akaingia ndani ya hema la Yakobo, na ndani ya hema la Lea, na ndani ya hema la wajakazi wale wawili, lakini hakuipata hiyo miungu. Baadaye alipotoka hema la Lea, akaingia hema la Raheli.
GEN 31:34 Basi Raheli ndiye alikuwa ameichukua ile miungu ya nyumbani mwao na kuiweka katika matandiko ya ngamia, na kukalia. Labani akatafuta kila mahali kwenye hema lakini hakupata chochote.
GEN 31:35 Raheli akamwambia baba yake, “Usikasirike bwana wangu, kwa kuwa siwezi kusimama ukiwepo, niko katika hedhi.” Labani akatafuta lakini hakuweza kuipata miungu ya nyumbani mwake.
GEN 31:36 Yakobo akakasirika na kumshutumu Labani, akisema, “Uhalifu wangu ni nini?” Akamuuliza Labani, “Ni dhambi gani niliyofanya hata unaniwinda?
GEN 31:37 Sasa kwa kuwa umepekua vitu vyangu vyote, umepata nini kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya jamaa yako na yangu, nao waamue kati yetu.
GEN 31:38 “Hadi sasa nimekuwa pamoja nawe miaka ishirini. Kondoo wako na mbuzi wako hawajaharibu mimba, wala sijala kondoo dume kutoka makundi yako.
GEN 31:39 Sijakuletea mfugo aliyeraruliwa na wanyama pori, bali nimegharimia hasara mwenyewe. Tena umenidai malipo kwa chochote kilichoibwa mchana au usiku.
GEN 31:40 Hali yangu imekuwa hivi: Nimechomwa kwa joto la mchana, na kupigwa na baridi usiku, pia usingizi ulinipotea.
GEN 31:41 Imekuwa hivi kwa miaka ile ishirini niliyokuwa nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka ile kumi na nne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita kwa ajili ya makundi yako, nawe ulibadilisha ujira wangu mara kumi.
GEN 31:42 Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hakuwa pamoja nami, hakika ungenifukuza mikono mitupu. Lakini Mungu ameona taabu yangu na kazi ngumu ya mikono yangu, naye usiku uliopita amekukemea.”
GEN 31:43 Labani akamjibu Yakobo, “Wanawake hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, na makundi haya ni makundi yangu. Vyote unavyoviona ni vyangu. Lakini hata hivyo ninaweza kufanya nini kuhusu hawa binti zangu, au kuhusu watoto waliowazaa?
GEN 31:44 Njoo sasa na tufanye agano, wewe na mimi, na liwe kama shahidi kati yetu.”
GEN 31:45 Hivyo Yakobo akachukua jiwe, akalisimamisha kama nguzo.
GEN 31:46 Akawaambia jamaa yake, “Kusanyeni mawe.” Hivyo wakachukua mawe na kuyakusanya yakawa lundo; wakala chakula hapo karibu na hilo lundo.
GEN 31:47 Labani akaliita Yegar-Sahadutha na Yakobo akaliita Galeedi.
GEN 31:48 Labani akasema, “Lundo hili ni shahidi kati yako na mimi leo.” Ndiyo maana likaitwa Galeedi.
GEN 31:49 Pia liliitwa Mispa, kwa sababu alisema, “Mwenyezi Mungu na aweke ulinzi kati yako na mimi wakati hatuko pamoja.
GEN 31:50 Ukiwatenda mabaya binti zangu au ukioa wake wengine zaidi ya binti zangu, hata ingawa hakuna hata mmoja aliye pamoja nasi, kumbuka kwamba Mungu ni shahidi kati yako na mimi.”
GEN 31:51 Pia Labani akamwambia Yakobo, “Hili ndilo lundo, na hii ndiyo nguzo niliyoisimamisha kati yako na mimi.
GEN 31:52 Lundo hili ni shahidi na nguzo hii ni shahidi, kwamba sitavuka lundo hili kuja upande wako kukudhuru, nawe kwamba hutavuka lundo hili na nguzo hii kuja upande wangu kunidhuru.
GEN 31:53 Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba zao, aamue kati yetu.” Hivyo Yakobo akaapa kwa jina la Hofu ya baba yake Isaka.
GEN 31:54 Yakobo akatoa dhabihu huko nchi ya vilima na akawaalika jamaa zake kula chakula. Baada ya kula, wakalala huko.
GEN 31:55 Kesho yake asubuhi na mapema, Labani akawabusu wajukuu zake na binti zake, na kuwabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani.
GEN 32:1 Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye.
GEN 32:2 Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu.
GEN 32:3 Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu.
GEN 32:4 Akawaagiza, akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema: nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwa huko hadi sasa.
GEN 32:5 Ninao ng’ombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ”
GEN 32:6 Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulienda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume mia nne.”
GEN 32:7 Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili; pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ng’ombe na ngamia.
GEN 32:8 Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litanusurika.”
GEN 32:9 Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, Mungu wa baba yangu Isaka, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi.’
GEN 32:10 Sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi, mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa nimekuwa makundi mawili.
GEN 32:11 Nakuomba uniokoe kutoka kwa mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia kina mama pamoja na watoto wao.
GEN 32:12 Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ”
GEN 32:13 Akalala pale usiku ule. Miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake:
GEN 32:14 beberu ishirini na mbuzi jike mia mbili, kondoo dume ishirini na kondoo jike mia mbili,
GEN 32:15 ngamia jike thelathini pamoja na ndama zao, ng’ombe arobaini na mafahali kumi, punda jike ishirini, na punda wa kiume kumi.
GEN 32:16 Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake, na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”
GEN 32:17 Akamwagiza yule aliyetangulia hivi, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unaenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’
GEN 32:18 utamjibu hivi, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi iliyotumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”
GEN 32:19 Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, na wa kundi la tatu, na kila mtumishi wa yale mengine yaliyofuata, hivi: “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye.
GEN 32:20 Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza; hatimaye nitakapomwona, huenda atanikubali.”
GEN 32:21 Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.
GEN 32:22 Usiku ule Yakobo akaamka, akawachukua wake zake wawili, wajakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Mto Yaboki.
GEN 32:23 Baada ya kuwavusha ng’ambo ya kijito, alivusha pia mali yake yote.
GEN 32:24 Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake; naye mtu mmoja akashikana naye mweleka hadi mapambazuko.
GEN 32:25 Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo; kwa hiyo nyonga yake ikateguka alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu.
GEN 32:26 Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.” Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”
GEN 32:27 Yule mtu akamuuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Ni Yakobo.”
GEN 32:28 Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”
GEN 32:29 Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.” Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.
GEN 32:30 Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli, akisema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso, na bado uhai wangu umehifadhiwa.”
GEN 32:31 Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake.
GEN 32:32 Kwa hiyo hadi leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.
GEN 33:1 Yakobo akainua macho, akamwona Esau akija na watu wake mia nne. Kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wake wawili.
GEN 33:2 Akawaweka wale wajakazi na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, nao Raheli na Yusufu wakaja nyuma.
GEN 33:3 Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu hadi chini mara saba alipomkaribia ndugu yake.
GEN 33:4 Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia.
GEN 33:5 Esau akainua macho, akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa waliofuatana nawe ni nani?” Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”
GEN 33:6 Kisha wale wajakazi na watoto wao wakakaribia na kusujudu.
GEN 33:7 Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yusufu na Raheli, nao pia wakasujudu.
GEN 33:8 Esau akauliza, “Makundi hayo yote niliyokutana nayo yana maana gani?” Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”
GEN 33:9 Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”
GEN 33:10 Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa kibali kikubwa.
GEN 33:11 Tafadhali kubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.
GEN 33:12 Ndipo Esau akasema, “Tuendelee na safari; nitakusindikiza.”
GEN 33:13 Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa ng’ombe na kondoo wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa.
GEN 33:14 Hivyo bwana wangu, mtangulie mtumishi wako, nami nije polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, hadi nifike kwa bwana wangu huko Seiri.”
GEN 33:15 Esau akamwambia, “Basi kubali nikuachie baadhi ya watu wangu.” Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo? Niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.”
GEN 33:16 Hivyo siku hiyo Esau akashika njia, akarudi Seiri.
GEN 33:17 Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi. Akajijengea makazi na pia vibanda vya mifugo yake. Hii ndiyo sababu mahali pale panaitwa Sukothi.
GEN 33:18 Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani, na kuweka kambi yake karibu na mji huo.
GEN 33:19 Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia moja vya fedha, akapiga hema lake hapo.
GEN 33:20 Akajenga madhabahu pale na kupaita El-Elohe-Israeli.
GEN 34:1 Basi Dina, binti Yakobo aliyezaliwa na Lea, akaenda kuwatembelea wanawake wa nchi ile.
GEN 34:2 Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile, alipomwona, akamchukua na kumnajisi.
GEN 34:3 Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza.
GEN 34:4 Shekemu akamwambia Hamori, baba yake, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.”
GEN 34:5 Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake. Kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo hadi waliporudi nyumbani.
GEN 34:6 Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo.
GEN 34:7 Basi wana wa Yakobo wakarudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotukia. Walijawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti Yakobo, jambo ambalo halikupasa kutendwa.
GEN 34:8 Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake.
GEN 34:9 Oaneni na sisi; tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu.
GEN 34:10 Mwaweza kuishi nasi, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, mfanye biashara humu na mjipatie mali.”
GEN 34:11 Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Naomba nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema.
GEN 34:12 Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.”
GEN 34:13 Kwa sababu dada yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na Hamori, baba yake.
GEN 34:14 Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili. Hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hajatahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu.
GEN 34:15 Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote.
GEN 34:16 Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi.
GEN 34:17 Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua dada yetu na kuondoka.”
GEN 34:18 Pendekezo lao likakubalika kwa Hamori na Shekemu mwanawe.
GEN 34:19 Kijana huyo, aliyekuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo.
GEN 34:20 Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe walienda kwenye lango la mji kuzungumza na wanaume wa mji wao.
GEN 34:21 Wakasema, “Hawa wanaume ni rafiki zetu. Tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake; nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao, nao wanaweza kuoa binti zetu.
GEN 34:22 Lakini wanaume hawa watakubali kuishi nasi kama watu wamoja nao kwa sharti kwamba wanaume wetu watahiriwe, kama wao.
GEN 34:23 Je, si mifugo yao, mali yao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi tukubali sharti lao, nao wataishi miongoni mwetu.”
GEN 34:24 Wanaume wote waliotoka nje ya lango la mji walikubaliana na Hamori na Shekemu mwanawe, na kila mwanaume katika mji ule akatahiriwa.
GEN 34:25 Baada ya siku tatu, wakati wote wakiwa wangali katika maumivu, wana wawili wa Yakobo, yaani Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua panga zao na kuvamia mji ambao haukutazamia vita, wakaua kila mwanaume.
GEN 34:26 Wakawaua Hamori na Shekemu mwanawe kwa panga, kisha wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka.
GEN 34:27 Wana hao wengine wa Yakobo wakaingia mji uliojaa maiti na kuteka nyara katika mji huo dada yao alikuwa amenajisiwa.
GEN 34:28 Wakateka kondoo na mbuzi, ng’ombe, punda, na kila kitu kilichokuwa ndani ya mji ule na mashambani.
GEN 34:29 Waliteka utajiri wao wote, pamoja na wanawake na watoto wao, wakapora kila kitu ndani ya nyumba zao.
GEN 34:30 Kisha Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, “Mmenitaabisha kwa kunifanya ninuke kama uvundo kwa Wakanaani na Waperizi, watu wanaoishi nchi hii. Sisi ni wachache; wakiunganisha nguvu zao dhidi yangu na kunishambulia, mimi na nyumba yangu tutaangamizwa.”
GEN 34:31 Lakini wakamjibu, “Je, ilikuwa vyema kumtendea dada yetu kama kahaba?”
GEN 35:1 Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko. Ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.”
GEN 35:2 Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mjitakase na mkabadilishe nguo zenu.
GEN 35:3 Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipoenda.”
GEN 35:4 Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mwaloni ulio Shekemu.
GEN 35:5 Kisha wakaondoka, na utisho wa Mungu ukaipata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo.
GEN 35:6 Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani.
GEN 35:7 Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli, kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alijifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake.
GEN 35:8 Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mwaloni ulio nje ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi.
GEN 35:9 Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki.
GEN 35:10 Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo. Lakini hutaitwa tena Yakobo; jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli.
GEN 35:11 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako.
GEN 35:12 Nchi niliyowapa Ibrahimu na Isaka nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.”
GEN 35:13 Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye.
GEN 35:14 Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake.
GEN 35:15 Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.
GEN 35:16 Kisha wakaondoka Betheli. Kabla hawajafika Efrata, Raheli akaanza kujifungua na akapata shida kuu.
GEN 35:17 Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.”
GEN 35:18 Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe jina Benoni. Lakini babaye akamwita jina Benyamini.
GEN 35:19 Kwa hiyo Raheli akafa, na akazikwa kando ya njia iendayo Efrata (ndio Bethlehemu).
GEN 35:20 Yakobo akasimamisha nguzo juu ya kaburi lake, ambayo hadi leo inatambulisha kaburi la Raheli.
GEN 35:21 Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema baada ya kupita Mnara wa Ederi.
GEN 35:22 Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aliyeitwa Bilha, naye Israeli akasikia jambo hilo.
GEN 35:23 Wana wa Lea walikuwa: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni.
GEN 35:24 Wana wa Raheli walikuwa: Yusufu na Benyamini.
GEN 35:25 Wana waliozaliwa na Bilha mjakazi wa Raheli walikuwa: Dani na Naftali.
GEN 35:26 Wana waliozaliwa na Zilpa mjakazi wa Lea walikuwa: Gadi na Asheri.
GEN 35:27 Yakobo akarudi nyumbani mwa baba yake Isaka huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Ibrahimu na Isaka.
GEN 35:28 Isaka aliishi miaka mia moja na themanini.
GEN 35:29 Kisha Isaka akapumua pumzi yake ya mwisho, akafa; akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee aliyeshiba siku. Nao Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.
GEN 36:1 Hivi ndivyo vizazi vya Esau (yaani Edomu).
GEN 36:2 Esau akaoa wake kutoka miongoni mwa wanawake wa Kanaani: Ada binti Eloni Mhiti, Oholibama binti Ana, mjukuu wa kike wa Sibeoni Mhivi;
GEN 36:3 pia akaoa Basemathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.
GEN 36:4 Ada akamzalia Esau Elifazi; Basemathi akamzaa Reueli;
GEN 36:5 Oholibama akawazaa Yeushi, Yalamu na Kora. Hawa ndio wana wa Esau waliozaliwa kwake huko Kanaani.
GEN 36:6 Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike, na watu wote wa nyumbani mwake, mifugo yake pamoja na wanyama wake wengine wote, na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata akiwa Kanaani, akahamia katika nchi iliyo mbali na Yakobo ndugu yake.
GEN 36:7 Mali yao ilikuwa nyingi sana kiasi kwamba haikuwa rahisi wao kuishi pamoja; nchi waliyokuwa wakiishi isingewatosha wote kwa ajili ya mifugo yao.
GEN 36:8 Kwa hiyo Esau (ambaye ni Edomu) aliishi katika nchi ya vilima ya Seiri.
GEN 36:9 Hivi ndivyo vizazi vya Esau, baba wa Waedomu, katika nchi ya vilima ya Seiri.
GEN 36:10 Haya ndiyo majina ya wana wa Esau: Elifazi, mwana wa Esau ambaye mkewe Ada alimzalia; na Reueli, mwana wa Esau ambaye mkewe Basemathi alimzalia.
GEN 36:11 Wana wa Elifazi ni: Temani, Omari, Sefo, Gatamu na Kenazi.
GEN 36:12 Elifazi mwana wa Esau alikuwa pia na suria aliyeitwa Timna, aliyemzalia Amaleki. Hao walikuwa wajukuu wa Ada mke wa Esau.
GEN 36:13 Wana wa Reueli ni: Nahathi, Zera, Shama na Miza. Hao walikuwa wajukuu wa Basemathi mkewe Esau.
GEN 36:14 Wana wa Oholibama binti Ana, mkewe Esau, aliyekuwa mjukuu wa Sibeoni, aliomzalia Esau ni: Yeushi, Yalamu na Kora.
GEN 36:15 Hawa walikuwa wakuu miongoni mwa wazao wa Esau: Wakuu wa wana wa Elifazi, mzaliwa wa kwanza wa Esau ni: Temani, Omari, Sefo, Kenazi,
GEN 36:16 Kora, Gatamu na Amaleki. Hao walikuwa wakuu waliotoka kwa Elifazi huko Edomu; walikuwa wajukuu wa kiume wa Ada.
GEN 36:17 Wakuu wa wana wa Reueli, mwana wa Esau ni: Nahathi, Zera, Shama na Miza. Hawa ndio wakuu waliotoka kwa Reueli huko Edomu; walikuwa wajukuu wa kiume wa Basemathi mkewe Esau.
GEN 36:18 Wakuu wa wana wa Esau ambao mkewe Oholibama alimzalia ni: Yeushi, Yalamu na Kora. Hawa ndio wakuu waliotoka kwa mke wa Esau, Oholibama binti Ana.
GEN 36:19 Hao walikuwa wana wa Esau (ndiye Edomu), na hao walikuwa wakuu wao.
GEN 36:20 Hawa walikuwa wana wa Seiri Mhori, walioishi katika nchi ile: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,
GEN 36:21 Dishoni, Eseri na Dishani. Hawa ndio wana wa Seiri huko Edomu waliokuwa wakuu kwa Wahori.
GEN 36:22 Wana wa Lotani walikuwa: Hori na Homamu. Timna alikuwa dada yake Lotani.
GEN 36:23 Wana wa Shobali walikuwa: Alvani, Manahathi, Ebali, Shefo na Onamu.
GEN 36:24 Wana wa Sibeoni walikuwa: Aya na Ana. (Huyu Ana ndiye aligundua chemchemi ya maji moto jangwani alipokuwa akichunga punda wa Sibeoni, baba yake.)
GEN 36:25 Watoto wa Ana walikuwa: Dishoni na Oholibama binti Ana.
GEN 36:26 Wana wa Dishoni walikuwa: Hemdani, Eshbani, Ithrani na Kerani.
GEN 36:27 Wana wa Eseri walikuwa: Bilhani, Zaavani na Akani.
GEN 36:28 Wana wa Dishani walikuwa: Usi na Arani.
GEN 36:29 Hawa walikuwa wakuu wa Wahori: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,
GEN 36:30 Dishoni, Eseri na Dishani.
GEN 36:31 Wafuatao ni wafalme waliotawala Edomu kabla ya mfalme yeyote wa Israeli kutawala:
GEN 36:32 Bela mwana wa Beori alikuwa mfalme wa Edomu. Mji wake uliitwa Dinhaba.
GEN 36:33 Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra akawa mfalme baada yake.
GEN 36:34 Yobabu alipofariki, Hushamu kutoka nchi ya Watemani akawa mfalme baada yake.
GEN 36:35 Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi, aliyeshinda Midiani katika nchi ya Moabu, akawa mfalme baada yake. Mji wake uliitwa Avithi.
GEN 36:36 Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka akawa mfalme baada yake.
GEN 36:37 Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi ng’ambo ya Mto Frati akawa mfalme baada yake.
GEN 36:38 Shauli alipofariki, Baal-Hanani mwana wa Akbori akawa mfalme baada yake.
GEN 36:39 Baal-Hanani mwana wa Akbori alipofariki, Hadadi akawa mfalme baada yake. Mji wake uliitwa Pau, na mkewe aliitwa Mehetabeli binti Matredi, binti Me-Zahabu.
GEN 36:40 Hawa ndio wakuu waliotokana na Esau, kwa majina, kufuatana na koo zao na nchi zao: Timna, Alva, Yethethi,
GEN 36:41 Oholibama, Ela, Pinoni,
GEN 36:42 Kenazi, Temani, Mibsari,
GEN 36:43 Magdieli na Iramu.
GEN 37:1 Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.
GEN 37:2 Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake, yaani wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake za baba yake, naye akamletea baba yao taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.
GEN 37:3 Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko ndugu zake wote, kwa sababu alikuwa mwanawe wa uzeeni; akamshonea joho lililofumwa vizuri sana.
GEN 37:4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yusufu kuliko yeyote kati yao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.
GEN 37:5 Yusufu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi.
GEN 37:6 Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota:
GEN 37:7 Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani. Ghafula mganda wangu ukasimama wima, nayo miganda yenu ikauzunguka na kuuinamia.”
GEN 37:8 Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto yake, pamoja na yale aliyowaambia.
GEN 37:9 Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akisema, “Sikilizeni: nimeota ndoto nyingine. Wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”
GEN 37:10 Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako, na mimi, na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe?”
GEN 37:11 Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.
GEN 37:12 Basi ndugu zake walikuwa wameenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu.
GEN 37:13 Israeli akamwambia Yusufu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.” Yusufu akajibu, “Vema sana, niko tayari.”
GEN 37:14 Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama ndugu zako wako salama, na makundi pia, kisha uniletee habari.” Basi akamtuma Yusufu kutoka Bonde la Hebroni. Yusufu alipofika Shekemu,
GEN 37:15 mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani, akamuuliza, “Unatafuta nini?”
GEN 37:16 Akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”
GEN 37:17 Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twendeni Dothani.’ ” Kwa hiyo Yusufu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani.
GEN 37:18 Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga njama za kumuua.
GEN 37:19 Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja!
GEN 37:20 Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo, na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”
GEN 37:21 Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao, akasema, “Tusimuue.
GEN 37:22 Msimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani mwa baba yake.
GEN 37:23 Kwa hiyo Yusufu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililofumwa vizuri alilokuwa amevaa.
GEN 37:24 Kisha wakamchukua, wakamtupa katika shimo. Hilo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji.
GEN 37:25 Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.
GEN 37:26 Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini tukimuua ndugu yetu na kuificha damu yake?
GEN 37:27 Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, mwili wetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.
GEN 37:28 Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yusufu kutoka lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri.
GEN 37:29 Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yusufu hayupo, alirarua nguo zake.
GEN 37:30 Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”
GEN 37:31 Kisha wakalichukua lile joho la Yusufu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu.
GEN 37:32 Wakalichukua lile joho lililofumwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”
GEN 37:33 Baba yao akalitambua, akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yusufu ameraruliwa vipande vipande.”
GEN 37:34 Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi.
GEN 37:35 Wanawe wote wa kiume na wa kike wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu hadi nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.
GEN 37:36 Basi Wamidiani wakamuuza Yusufu huko Misri kwa Potifa, mmoja wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa walinzi.
GEN 38:1 Wakati ule, Yuda akawaacha ndugu zake, akaenda kuishi na Hira Mwadulami.
GEN 38:2 Huko Yuda akakutana na binti ya Mkanaani aitwaye Shua. Akamwoa na akakutana naye kimwili,
GEN 38:3 naye akapata mimba, na akamzaa mwana, aliyeitwa jina Eri.
GEN 38:4 Akapata mimba tena, akamzaa mwana na kumwita jina Onani.
GEN 38:5 Akamzaa mwana mwingine tena, akamwita jina Shela. Huyu alimzalia huko Kezibu.
GEN 38:6 Yuda akamtwalia Eri, mzaliwa wake wa kwanza, mke aliyeitwa Tamari.
GEN 38:7 Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamuua.
GEN 38:8 Kisha Yuda akamwambia Onani, “Kutana kimwili na mke wa ndugu yako, na utimize wajibu wako kwake kama mke wa ndugu yako, ili umpatie ndugu yako uzao.”
GEN 38:9 Lakini Onani alijua kwamba uzao haungekuwa wake, kwa hiyo kila alipokutana kimwili na mke wa ndugu yake, alimwaga mbegu chini ili asimpatie ndugu yake uzao.
GEN 38:10 Alichofanya kilikuwa kiovu machoni pa Mwenyezi Mungu, hivyo Mwenyezi Mungu akamuua Onani pia.
GEN 38:11 Kisha Yuda akamwambia Tamari mkwewe, “Ishi kama mjane nyumbani mwa baba yako hadi mwanangu Shela atakapokua.” Kwa maana alifikiri, “Anaweza kufa pia kama ndugu zake.” Kwa hiyo Tamari akaenda kuishi nyumbani mwa baba yake.
GEN 38:12 Baada ya muda mrefu, mke wa Yuda, binti Shua, akafariki. Baada ya msiba, Yuda alienda Timna kwa watu waliokuwa wakikata kondoo wake manyoya, naye alifuatana na rafiki yake Hira Mwadulami.
GEN 38:13 Tamari alipoambiwa, “Baba mkwe wako yuko njiani akielekea Timna kukata kondoo wake manyoya,”
GEN 38:14 alivua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa shela ili asifahamike. Akaketi kwenye mlango wa Enaimu, njiani ya kuelekea Timna. Akafanya hivyo kwa sababu aliona kwamba ingawa Shela sasa alikuwa mtu mzima, bado hajakabidhiwa kwake kuwa mkewe.
GEN 38:15 Yuda alipomwona alifikiri ni kahaba, kwa sababu alikuwa amefunika uso wake.
GEN 38:16 Pasipo kutambua kwamba alikuwa mkwe wake, akamwendea kando ya njia na kumwambia, “Njoo sasa, nikutane na wewe kimwili.” Yule mkwewe akamuuliza, “Utanipa nini nikikutana nawe kimwili?”
GEN 38:17 Akamwambia, “Nitakutumia mwana-mbuzi kutoka kundi langu.” Akamuuliza, “Utanipa amana hadi utakapompeleka?”
GEN 38:18 Akamuuliza, “Nikupe amana gani?” Akamjibu, “Pete yako na kamba yake pamoja na fimbo iliyo mkononi mwako.” Kwa hiyo akampa vitu hivyo, kisha akakutana naye kimwili, naye akapata mimba yake.
GEN 38:19 Tamari akaondoka, akavua shela yake, akavaa tena nguo zake za ujane.
GEN 38:20 Baadaye Yuda akamtuma rafiki yake Mwadulami apeleke yule mwana-mbuzi ili arudishiwe amana yake kutoka kwa yule mwanamke, lakini yule rafiki yake hakumkuta yule mwanamke.
GEN 38:21 Akawauliza watu walioishi mahali pale, “Yuko wapi yule kahaba wa mahali pa ibada za sanamu aliyekuwa kando ya barabara hapa Enaimu?” Wakamjibu, “Hakujawahi kuwa kahaba wa mahali pa ibada za sanamu hapa.”
GEN 38:22 Kwa hiyo akamrudia Yuda na kumwambia, “Sikumpata. Zaidi ya hayo, watu wanaoishi mahali pale walisema, ‘Hakujawahi kuwa kahaba wa mahali pa ibada za sanamu hapa.’ ”
GEN 38:23 Kisha Yuda akasema, “Mwache avichukue vitu hivyo, ama sivyo tutaaibika. Hata hivyo, nilimpelekea mwana-mbuzi, lakini hukumkuta.”
GEN 38:24 Baada ya miezi mitatu, Yuda akaambiwa, “Tamari mkweo ana hatia ya kuwa kahaba, na sasa ana mimba.” Yuda akasema, “Mtoeni nje, achomwe moto hadi afe!”
GEN 38:25 Alipokuwa akitolewa nje, akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake kusema, “Nina mimba ya mtu mwenye vitu hivi.” Akaongeza kusema, “Angalia kama utatambua pete hii na kamba yake pamoja na fimbo hii ni vya nani.”
GEN 38:26 Yuda akavitambua na kusema, “Yeye ana haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumkabidhi kwa mwanangu Shela ili awe mkewe.” Tangu hapo hakukutana naye kimwili tena.
GEN 38:27 Wakati ulipofika wa kujifungua, kukawa na wana mapacha tumboni mwake.
GEN 38:28 Alipokuwa akijifungua, mmoja akatoa mkono wake nje, kwa hiyo mkunga akachukua uzi mwekundu na kuufunga mkononi mwa yule mtoto, akasema, “Huyu ametoka kwanza.”
GEN 38:29 Lakini alipourudisha mkono wake, ndugu yake akatangulia kutoka, naye mkunga akasema, “Hivi ndivyo ulivyotoka kwa nguvu!” Akaitwa Peresi.
GEN 38:30 Kisha ndugu yake, aliyekuwa na uzi mwekundu mkononi, akatoka, naye akaitwa Zera.
GEN 39:1 Wakati huu Yusufu alikuwa amechukuliwa hadi Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa, mmoja wa maafisa wa Farao, na aliyekuwa mkuu wa walinzi, akamnunua Yusufu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.
GEN 39:2 Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yusufu, naye akastawi. Yusufu akaishi nyumbani mwa bwana wake Mmisri.
GEN 39:3 Potifa alipoona kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yusufu, na kwamba Mwenyezi Mungu alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya,
GEN 39:4 Yusufu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamweka kuwa mwangalizi wa mali yake yote.
GEN 39:5 Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yusufu kuwa msimamizi wa nyumba na mali yake yote aliyokuwa nayo, Mwenyezi Mungu aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yusufu. Baraka ya Mwenyezi Mungu ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani.
GEN 39:6 Kwa hiyo Potifa akamwachia Yusufu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. Yusufu alipokuwa msimamizi wa mali yake, Potifa hakujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula. Yusufu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia.
GEN 39:7 Baada ya kitambo, mke wa Potifa akamtamani Yusufu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”
GEN 39:8 Lakini Yusufu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa msimamizi, bwana wangu hajishughulishi na kitu chochote katika nyumba hii; kila kitu alicho nacho amenikabidhi.
GEN 39:9 Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?”
GEN 39:10 Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yusufu siku baada ya siku, Yusufu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.
GEN 39:11 Siku moja Yusufu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwa mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba.
GEN 39:12 Mke wa Potifa akashika vazi Yusufu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yusufu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.
GEN 39:13 Yule mwanamke alipoona kwamba Yusufu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba,
GEN 39:14 akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga yowe.
GEN 39:15 Aliposikia nikipiga yowe, akaacha vazi lake kando yangu, akakimbilia nje.”
GEN 39:16 Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye hadi Potifa aliporudi nyumbani.
GEN 39:17 Mwanamke akamweleza mumewe kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kunidhihaki.
GEN 39:18 Lakini mara nilipopiga yowe kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu, akakimbia nje ya nyumba.”
GEN 39:19 Potifa aliposikia kisa alichosimuliwa na mkewe, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda,” hasira yake ikawaka.
GEN 39:20 Potifa akamchukua Yusufu na kumtia gerezani, mahali wahalifu wa mfalme walipokuwa wamefungwa. Lakini Yusufu alipokuwa huko gerezani,
GEN 39:21 Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza.
GEN 39:22 Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yusufu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani.
GEN 39:23 Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yusufu, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yusufu, akimfanikisha kwa kila alichofanya.
GEN 40:1 Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri.
GEN 40:2 Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu.
GEN 40:3 Akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa walinzi, katika gereza lile lile alimofungwa Yusufu.
GEN 40:4 Mkuu wa walinzi akawakabidhi kwa Yusufu, naye akawahudumia. Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda,
GEN 40:5 kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.
GEN 40:6 Yusufu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni.
GEN 40:7 Ndipo Yusufu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake hivi, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?”
GEN 40:8 Wakamjibu, “Sisi sote tumeota ndoto, lakini hakuna wa kuzifasiri.” Ndipo Yusufu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si ni kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”
GEN 40:9 Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yusufu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu,
GEN 40:10 nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva.
GEN 40:11 Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu. Nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”
GEN 40:12 Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu.
GEN 40:13 Baada ya siku tatu, Farao atakutoa gerezani na kukurudisha kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mkononi mwake, jinsi ulivyofanya ulipokuwa mnyweshaji wake awali.
GEN 40:14 Lakini mambo yako yatakapokuwa mazuri, unikumbuke, unifanyie wema. Useme mema kunihusu kwa Farao ili unitoe huku gerezani.
GEN 40:15 Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.”
GEN 40:16 Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yusufu amefasiri vizuri, akamwambia Yusufu, “Mimi pia niliota ndoto. Kichwani mwangu kulikuwa vikapu vitatu vya mikate.
GEN 40:17 Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kikapu nilichobeba kichwani.”
GEN 40:18 Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu.
GEN 40:19 Baada ya siku tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”
GEN 40:20 Siku ya tatu ilikuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Farao, naye akawaandalia maafisa wake wote karamu. Akawatoa gerezani mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka mbele ya maafisa wake.
GEN 40:21 Ndipo akamrudisha mnyweshaji mkuu kwenye nafasi yake, ili aweke kikombe mkononi mwa Farao tena.
GEN 40:22 Lakini akamwangika yule mwokaji mkuu, kama Yusufu alivyowafasiria.
GEN 40:23 Lakini mnyweshaji mkuu hakumkumbuka Yusufu, bali alimsahau.
GEN 41:1 Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto. Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Naili,
GEN 41:2 wakati ng’ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye matete.
GEN 41:3 Baada yao ng’ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea Mto Naili, wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto.
GEN 41:4 Wale ng’ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka.
GEN 41:5 Farao akaingia usingizini tena, akaota ndoto ya pili. Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja.
GEN 41:6 Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyokaushwa na upepo wa mashariki.
GEN 41:7 Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, na kumbe ilikuwa ndoto.
GEN 41:8 Kesho yake asubuhi, alifadhaika akilini. Hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.
GEN 41:9 Ndipo mnyweshaji mkuu alimwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kosa langu.
GEN 41:10 Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa walinzi.
GEN 41:11 Katika usiku mmoja, kila mmoja wetu aliota ndoto, na kila ndoto ilikuwa na maana yake.
GEN 41:12 Basi kuna kijana Mwebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, mtumishi wa mkuu wa walinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupatia kila mtu tafsiri ya ndoto yake.
GEN 41:13 Nayo mambo yakawa jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu, naye huyo mwingine akaangikwa.”
GEN 41:14 Basi, Farao akatuma Yusufu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake, akaenda mbele ya Farao.
GEN 41:15 Farao akamwambia Yusufu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia habari yako kwamba unapoelezwa ndoto unaweza kuifasiri.”
GEN 41:16 Yusufu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”
GEN 41:17 Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Naili.
GEN 41:18 Nikawaona ng’ombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni, wakaja kujilisha kwenye matete.
GEN 41:19 Baada ya hao, ng’ombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ng’ombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri.
GEN 41:20 Hao ng’ombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ng’ombe saba walionona waliojitokeza kwanza.
GEN 41:21 Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini.
GEN 41:22 “Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja.
GEN 41:23 Baada ya hayo, masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki.
GEN 41:24 Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna yeyote aliyeweza kunifasiria.”
GEN 41:25 Ndipo Yusufu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto hiyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni.
GEN 41:26 Ng’ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba; ni ndoto hiyo hiyo moja.
GEN 41:27 Ng’ombe saba waliokonda na wabaya waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki: Ni miaka saba ya njaa.
GEN 41:28 “Ni kama nilivyomwambia Farao. Mungu amemwonesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni.
GEN 41:29 Miaka saba ya shibe inakuja katika nchi yote ya Misri,
GEN 41:30 lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo shibe yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.
GEN 41:31 “Shibe iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno.
GEN 41:32 Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.
GEN 41:33 “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri.
GEN 41:34 Farao na aweke wasimamizi nchini kote, wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya shibe.
GEN 41:35 Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji.
GEN 41:36 Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”
GEN 41:37 Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote.
GEN 41:38 Hivyo Farao akawauliza, “Je, tunaweza kumpata yeyote kama mtu huyu, aliye na Roho wa Mungu ndani yake?”
GEN 41:39 Ndipo Farao akamwambia Yusufu, “Maadamu Mungu amekufunulia haya yote, hakuna yeyote mwenye akili na hekima kama wewe.
GEN 41:40 Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”
GEN 41:41 Kwa hiyo Farao akamwambia Yusufu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.”
GEN 41:42 Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yusufu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
GEN 41:43 Akampandisha katika gari lake la vita kama msaidizi wake; watu wakamtangulia wakipaza sauti na kusema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alimweka Yusufu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.
GEN 41:44 Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.”
GEN 41:45 Farao akamwita Yusufu jina Safenath-Panea; pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, kuwa mke wake. Ndipo Yusufu akaitembelea nchi yote ya Misri.
GEN 41:46 Yusufu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao, mfalme wa Misri. Naye Yusufu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri.
GEN 41:47 Katika ile miaka saba ya shibe nchi ilizaa mazao kwa wingi sana.
GEN 41:48 Yusufu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya shibe nchini Misri, akakihifadhi katika miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo.
GEN 41:49 Yusufu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari; ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi kipimo.
GEN 41:50 Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili wa kiume.
GEN 41:51 Yusufu akamwita mzaliwa wake wa kwanza jina Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.”
GEN 41:52 Mwana wa pili akamwita jina Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.”
GEN 41:53 Ile miaka saba ya shibe huko Misri ikaisha,
GEN 41:54 nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yusufu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula.
GEN 41:55 Nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao aliwaagiza Wamisri wote, “Nendeni kwa Yusufu, nanyi mfanye anachowaambia.”
GEN 41:56 Njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yusufu akafungua maghala ya vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri.
GEN 41:57 Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yusufu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.
GEN 42:1 Yakobo alipofahamu kuwa kuna nafaka kule Misri, akawaambia wanawe, “Mbona mnakaa tu hapa mkitazamana?”
GEN 42:2 Akaendelea kuwaambia, “Nimesikia kuwa huko Misri kuna nafaka. Teremkeni huko mkatununulie chakula, ili tuweze kuishi wala tusife.”
GEN 42:3 Ndipo ndugu kumi wa Yusufu wakateremka huko Misri kununua nafaka.
GEN 42:4 Lakini Yakobo hakumtuma Benyamini, ndugu yake Yusufu, pamoja na wengine, kwa sababu aliogopa asije akapatwa na madhara.
GEN 42:5 Hivyo wana wa Israeli walikuwa miongoni mwa wale walioenda Misri kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa katika nchi ya Kanaani pia.
GEN 42:6 Wakati huo Yusufu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, na ndiye aliwauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yusufu walifika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi.
GEN 42:7 Mara Yusufu alipowaona ndugu zake, akawatambua. Lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.”
GEN 42:8 Ingawa Yusufu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua.
GEN 42:9 Ndipo Yusufu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali nchi yetu haina ulinzi.”
GEN 42:10 Wakamjibu, “Sivyo, bwana. Watumishi wako wamekuja kununua chakula.
GEN 42:11 Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.”
GEN 42:12 Akawaambia, “La, hasha! Mmekuja kuangalia mahali nchi yetu haina ulinzi.”
GEN 42:13 Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu, na mwingine alikufa.”
GEN 42:14 Yusufu akawaambia, “Kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi!
GEN 42:15 Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa hadi ndugu yenu mdogo aje hapa.
GEN 42:16 Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu. Wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!”
GEN 42:17 Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu.
GEN 42:18 Siku ya tatu, Yusufu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu:
GEN 42:19 Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa.
GEN 42:20 Lakini lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo.
GEN 42:21 Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuokoa maisha yake, lakini hatukumsikiliza. Hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.”
GEN 42:22 Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.”
GEN 42:23 Hawakujua kuwa Yusufu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani.
GEN 42:24 Yusufu akajitenga nao, akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akaamuru Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao.
GEN 42:25 Yusufu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe chakula cha njiani. Baada ya kutendewa hayo yote,
GEN 42:26 wakapakiza nafaka juu ya punda wao, wakaondoka.
GEN 42:27 Walipofika mahali pa kulala huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake; akakuta fedha yake ndani ya gunia lake.
GEN 42:28 Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.” Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”
GEN 42:29 Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema,
GEN 42:30 “Huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi.
GEN 42:31 Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi.
GEN 42:32 Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’
GEN 42:33 “Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu hapa kwangu, kisha nendeni mpeleke chakula kwa jamaa yenu inayoteseka kwa njaa.
GEN 42:34 Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu. Ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ”
GEN 42:35 Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, tazama! Wakapata ndani ya gunia la kila mtu mfuko wa fedha. Wakati wao na baba yao waliona mifuko ya fedha, wakaogopa.
GEN 42:36 Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yusufu hayupo na Simeoni hayupo; tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!”
GEN 42:37 Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Unaweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.”
GEN 42:38 Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa, naye ndiye peke yake aliyebaki. Akipatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.”
GEN 43:1 Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi.
GEN 43:2 Hivyo wakati walikuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine.”
GEN 43:3 Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena hadi mje na ndugu yenu.’
GEN 43:4 Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutaenda kuwanunulia chakula.
GEN 43:5 Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutaenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena hadi mje na ndugu yenu.’ ”
GEN 43:6 Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?”
GEN 43:7 Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado angali hai? Je, mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo yenu hapa’?”
GEN 43:8 Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara moja, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife.
GEN 43:9 Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake; mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Nisipomrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote.
GEN 43:10 Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumeenda na kurudi mara mbili.”
GEN 43:11 Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni sehemu ya bidhaa bora za nchi katika mifuko yenu, na mmpelekee yule mtu kama zawadi: zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi.
GEN 43:12 Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa.
GEN 43:13 Mchukueni ndugu yenu pia, mrudi kwa huyo mtu mara moja.
GEN 43:14 Naye Mungu Mwenyezi awajalie rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi, kama nikufiwa, nimefiwa.”
GEN 43:15 Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na wakajionesha kwa Yusufu.
GEN 43:16 Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani mwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula, kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
GEN 43:17 Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani mwa Yusufu.
GEN 43:18 Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani mwa Yusufu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda wetu.”
GEN 43:19 Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yusufu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumba.
GEN 43:20 Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula.
GEN 43:21 Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake katika gunia lake, kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha.
GEN 43:22 Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.”
GEN 43:23 Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.
GEN 43:24 Msimamizi akawapeleka wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji ya kunawa miguu, na kuwapa punda wao majani.
GEN 43:25 Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yusufu atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko.
GEN 43:26 Yusufu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia.
GEN 43:27 Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?”
GEN 43:28 Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama, wakamsujudia.
GEN 43:29 Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.”
GEN 43:30 Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yusufu akaondoka kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo.
GEN 43:31 Baada ya kunawa uso wake, akarudi; huku akijizuia kulia, akasema, “Pakueni chakula.”
GEN 43:32 Wakampakulia Yusufu peke yake, nao ndugu zake peke yao, na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri.
GEN 43:33 Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao.
GEN 43:34 Walipopelekewa sehemu ya chakula kutoka meza ya Yusufu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.
GEN 44:1 Kisha Yusufu akampa yule msimamizi wa nyumbani mwake maagizo haya: “Jaza magunia ya watu hawa kiasi cha chakula ambacho wanaweza kuchukua, na uweke fedha ya kila mtu katika gunia lake.
GEN 44:2 Kisha weka kikombe changu kile cha fedha katika gunia la yule mdogo wa wote, pamoja na fedha zake ambazo alinunulia nafaka yake.” Naye akafanya kama Yusufu alivyosema.
GEN 44:3 Kulipopambazuka, hao watu wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda wao.
GEN 44:4 Kabla hawajafika mbali kutoka mjini, Yusufu akamwambia mtumishi wake, “Wafuatilie wale watu mara moja; utakapowakuta, waambie, ‘Kwa nini mmelipiza wema kwa ubaya?
GEN 44:5 Je, kikombe hiki sicho anachonywea bwana wangu, na pia hukitumia kwa kubashiri? Hili ni jambo ovu mlilolitenda.’ ”
GEN 44:6 Alipowafikia, akarudia maneno haya kwao.
GEN 44:7 Lakini wakamwambia mtumishi, “Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Liwe mbali na watumishi wako kufanya jambo kama hilo!
GEN 44:8 Tazama, tulikurudishia zile fedha kutoka nchi ya Kanaani ambazo tulizikuta kwenye magunia yetu. Hivyo, kwa nini tuibe fedha au dhahabu kutoka nyumbani mwa bwana wako?
GEN 44:9 Ikiwa yeyote miongoni mwa watumishi wako atapatikana nacho, auawe, na sisi wengine tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”
GEN 44:10 Akajibu, “Vema sana; na iwe kama msemavyo. Yeyote atakayekutwa nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine mtakuwa hamna lawama.”
GEN 44:11 Kila mmoja wao akafanya haraka kushusha gunia lake chini na kulifungua.
GEN 44:12 Ndipo msimamizi akaendelea kutafuta, akianzia kwa mkubwa wa wote na akaishia kwa mdogo wa wote. Basi kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini.
GEN 44:13 Kwa hilo, wakararua nguo zao. Ndipo wote wakapakiza mizigo yao juu ya punda wao na kurudi mjini.
GEN 44:14 Yusufu alikuwa bado yuko nyumbani mwake Yuda na ndugu zake walipoingia. Wote wakajitupa chini mbele yake.
GEN 44:15 Yusufu akawaambia, “Ni jambo gani hili mlilolifanya? Hamjui kuwa mtu kama mimi anaweza kufahamu mambo kwa njia ya kubashiri?”
GEN 44:16 Yuda akajibu, “Tuseme nini kwa bwana wangu? Tutaweza kuzungumza nini? Tutawezaje kuthibitisha kwamba hatuna hatia? Mungu amefunua hatia ya watumishi wako. Sasa sisi tu watumwa wa bwana wangu, sisi pamoja na yule aliyepatikana na kikombe.”
GEN 44:17 Lakini Yusufu akasema, “Liwe mbali nami kufanya jambo kama hili! Mtu yule tu aliyekutwa na kikombe ndiye atakuwa mtumwa wangu. Ninyi wengine rudini kwa baba yenu kwa amani.”
GEN 44:18 Ndipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe.
GEN 44:19 Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’
GEN 44:20 Nasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’
GEN 44:21 “Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’
GEN 44:22 Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’
GEN 44:23 Lakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’
GEN 44:24 Tuliporudi kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema.
GEN 44:25 “Ndipo baba yetu alisema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’
GEN 44:26 Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri hadi ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutaenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu hadi ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’
GEN 44:27 “Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili.
GEN 44:28 Mmoja alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo.
GEN 44:29 Ikiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’
GEN 44:30 “Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu,
GEN 44:31 akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni.
GEN 44:32 Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sitamrudisha kwako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’
GEN 44:33 “Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi wako abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake.
GEN 44:34 Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”
GEN 45:1 Basi Yusufu hakuweza kujizuia tena mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye. Akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwa mtu mwingine na Yusufu alipojitambulisha kwa ndugu zake.
GEN 45:2 Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari.
GEN 45:3 Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yusufu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.
GEN 45:4 Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yusufu, yule ambaye mlimuuza Misri!
GEN 45:5 Sasa msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi.
GEN 45:6 Kwa miaka miwili sasa njaa imekuwa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwa na kulima wala kuvuna.
GEN 45:7 Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuwahifadhia mabaki katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.
GEN 45:8 “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kama baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote.
GEN 45:9 Sasa rudini haraka kwa baba yangu, mkamwambie, ‘Hili ndilo mwanao Yusufu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa mtawala wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie.
GEN 45:10 Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami: wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na vyote ulivyo navyo.
GEN 45:11 Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’
GEN 45:12 “Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi.
GEN 45:13 Mwambieni baba yangu kuhusu heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.”
GEN 45:14 Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia.
GEN 45:15 Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo, ndugu zake wakazungumza naye.
GEN 45:16 Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yusufu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi.
GEN 45:17 Farao akamwambia Yusufu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi hadi nchi ya Kanaani,
GEN 45:18 mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri, nanyi mtafurahia unono wa nchi.’
GEN 45:19 “Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje.
GEN 45:20 Msijali kamwe kuhusu mali yenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ”
GEN 45:21 Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yusufu akawapa magari ya kukokotwa kama Farao alivyoagiza, na pia akawapa chakula cha safari yao.
GEN 45:22 Akampa kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli mia tatu za fedha, na jozi tano za nguo.
GEN 45:23 Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliobeba vitu vizuri vya Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari.
GEN 45:24 Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!”
GEN 45:25 Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani.
GEN 45:26 Wakamwambia baba yao, “Yusufu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki.
GEN 45:27 Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yusufu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yusufu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa.
GEN 45:28 Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yusufu bado yu hai. Nitaenda nikamwone kabla sijafa.”
GEN 46:1 Hivyo Israeli akaondoka na mali yake yote. Alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaka baba yake.
GEN 46:2 Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!” Akamjibu, “Mimi hapa.”
GEN 46:3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako. Usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa.
GEN 46:4 Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yusufu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”
GEN 46:5 Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba, nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo, na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao alikuwa amempelekea kumsafirisha.
GEN 46:6 Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani; Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri.
GEN 46:7 Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote hadi Misri.
GEN 46:8 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), walioenda Misri: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.
GEN 46:9 Wana wa Reubeni ni: Hanoki, Palu, Hesroni, na Karmi.
GEN 46:10 Wana wa Simeoni ni: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
GEN 46:11 Wana wa Lawi ni: Gershoni, Kohathi, na Merari.
GEN 46:12 Wana wa Yuda ni: Eri, Onani, Shela, Peresi, na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi ni: Hesroni na Hamuli.
GEN 46:13 Wana wa Isakari ni: Tola, Puva, Yashubu, na Shimroni.
GEN 46:14 Wana wa Zabuloni ni: Seredi, Eloni, na Yaleeli.
GEN 46:15 Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu, pamoja na binti yake Dina. Jumla ya hawa wanawe wa kiume na wa kike walikuwa thelathini na watatu.
GEN 46:16 Wana wa Gadi ni: Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi, na Areli.
GEN 46:17 Wana wa Asheri ni: Imna, Ishva, Ishvi, na Beria. Dada yao alikuwa Sera. Wana wa Beria ni: Heberi na Malkieli.
GEN 46:18 Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.
GEN 46:19 Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni: Yusufu na Benyamini.
GEN 46:20 Huko Misri, Asenathi binti Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili: Manase na Efraimu.
GEN 46:21 Wana wa Benyamini ni: Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu, na Ardi.
GEN 46:22 Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.
GEN 46:23 Mwana wa Dani ni: Hushimu.
GEN 46:24 Wana wa Naftali ni: Yaseeli, Guni, Yeseri, na Shilemu.
GEN 46:25 Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.
GEN 46:26 Wote walioenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe wake, walikuwa watu sitini na sita.
GEN 46:27 Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yusufu huko Misri, jumla ya jamaa ya Yakobo walioenda Misri walikuwa sabini.
GEN 46:28 Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yusufu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni,
GEN 46:29 Yusufu aliandaa gari lake la vita, na akaenda Gosheni kumlaki baba yake, Israeli. Mara Yusufu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.
GEN 46:30 Israeli akamwambia Yusufu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”
GEN 46:31 Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, walioishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu.
GEN 46:32 Watu hao ni wafugaji; wao huchunga mifugo, na wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na kila kitu walicho nacho.’
GEN 46:33 Farao atakapowaita na kuwauliza, ‘Kazi yenu ni nini?’
GEN 46:34 mjibuni, ‘Watumishi wako wamekuwa wafugaji wa wanyama tangu ujana wetu hadi sasa, kama baba zetu walivyokuwa.’ Ndipo mtaruhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wafugaji wote ni chukizo kwa Wamisri.”
GEN 47:1 Yusufu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na kila kitu walicho nacho, nao sasa wako Gosheni.”
GEN 47:2 Akawachagua ndugu zake watano na kuwapeleka mbele ya Farao.
GEN 47:3 Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?” Wakamjibu, “Watumishi wako ni wafugaji, kama baba zetu walivyokuwa.”
GEN 47:4 Pia wakamwambia Farao, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.”
GEN 47:5 Farao akamwambia Yusufu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako,
GEN 47:6 nayo nchi ya Misri ipo mbele yako; wakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unawafahamu walio na uwezo maalum miongoni mwao, wafanye kuwa wasimamizi wa mifugo yangu.”
GEN 47:7 Ndipo Yusufu akamleta Yakobo baba yake na kumtambulisha mbele ya Farao. Baada ya Yakobo kumbariki Farao,
GEN 47:8 Farao akamuuliza, “Je, una umri gani?”
GEN 47:9 Naye Yakobo akamwambia Farao, “Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni miaka mia moja na thelathini. Miaka yangu imekuwa michache na ya taabu, wala haikufikia miaka ya maisha ya baba zangu.”
GEN 47:10 Yakobo akambariki Farao, kisha akaondoka mbele yake.
GEN 47:11 Ndipo Yusufu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri, akawapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, ile wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza.
GEN 47:12 Pia Yusufu akampa baba yake, na ndugu zake, na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kulingana na hesabu ya watoto wao.
GEN 47:13 Hata hivyo, hapakuwa na chakula katika eneo lote; kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa.
GEN 47:14 Yusufu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao.
GEN 47:15 Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yusufu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.”
GEN 47:16 Yusufu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu. Nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.”
GEN 47:17 Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yusufu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi, kondoo na mbuzi, ng’ombe, na punda wao. Katika mwaka huo wote Yusufu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.
GEN 47:18 Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna chochote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu.
GEN 47:19 Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Tununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.”
GEN 47:20 Kwa hiyo Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao,
GEN 47:21 naye Yusufu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine.
GEN 47:22 Hata hivyo hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walipokea mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao.
GEN 47:23 Yusufu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha.
GEN 47:24 Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba, na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe, na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.”
GEN 47:25 Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.”
GEN 47:26 Basi Yusufu akaiweka iwe sheria ya ardhi katika nchi ya Misri, ambayo inatumika hata leo, kwamba sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni ardhi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao.
GEN 47:27 Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko, wakastawi na kuongezeka kwa idadi.
GEN 47:28 Yakobo akaishi Misri miaka kumi na saba, nayo miaka ya maisha yake ilikuwa mia moja na arobaini na saba (147).
GEN 47:29 Wakati ulipokaribia wa Israeli kufa, akamwita mwanawe Yusufu na kumwambia, “Kama nimepata kibali machoni pake, weka mkono wako chini ya paja langu na uniahidi kuwa utanifanyia fadhili na uaminifu. Usinizike Misri,
GEN 47:30 lakini nitakapopumzika na baba zangu, unichukue kutoka Misri, ukanizike walipozikwa.” Yusufu akamwambia, “Nitafanya kama unavyosema.”
GEN 47:31 Akamwambia, “Niapie.” Ndipo Yusufu akamwapia, naye Israeli akaabudu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.
GEN 48:1 Baada ya muda Yusufu akaambiwa, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu pamoja naye.
GEN 48:2 Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yusufu amekuja kukuona,” Israeli akajitia nguvu, akaketi kitandani.
GEN 48:3 Yakobo akamwambia Yusufu, “Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani. Akanibariki,
GEN 48:4 naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na uongezeke kwa idadi. Nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele, wewe na wazao wako baada yako.’
GEN 48:5 “Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu.
GEN 48:6 Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao.
GEN 48:7 Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, nilihuzunika sana kwa sababu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrata. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrata” (yaani Bethlehemu).
GEN 48:8 Israeli alipowaona wana wa Yusufu, akauliza, “Hawa ni nani?”
GEN 48:9 Yusufu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.” Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.”
GEN 48:10 Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yusufu akawaleta wanawe karibu na baba yake, naye Israeli akawabusu na kuwakumbatia.
GEN 48:11 Israeli akamwambia Yusufu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.”
GEN 48:12 Ndipo Yusufu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli, naye akasujudu, uso wake ukagusa chini.
GEN 48:13 Yusufu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao.
GEN 48:14 Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa ndiye alikuwa mdogo; nao mkono wake wa kushoto, ukipishana na mkono wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase ndiye alikuwa mzaliwa wa kwanza.
GEN 48:15 Ndipo akambariki Yusufu akisema, “Mungu ambaye baba zangu Ibrahimu na Isaka walimtii, Mungu ambaye amekuwa mchungaji wa maisha yangu yote hadi leo,
GEN 48:16 Malaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote, yeye na awabariki vijana hawa. Na waitwe kwa jina langu na kwa majina ya baba zangu Ibrahimu na Isaka, wao na waongezeke kwa wingi katika dunia.”
GEN 48:17 Yusufu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase.
GEN 48:18 Yusufu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.”
GEN 48:19 Lakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.”
GEN 48:20 Akawabariki siku ile na kusema, “Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii: ‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ” Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase.
GEN 48:21 Ndipo Israeli akamwambia Yusufu, “Ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu.
GEN 48:22 Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”
GEN 49:1 Ndipo Yakobo akawaita wanawe na kusema: “Kusanyikeni, mnizunguke ili niweze kuwaambia yale yatakayowatokea siku zijazo.
GEN 49:2 “Kusanyikeni na msikilize, enyi wana wa Yakobo; msikilizeni baba yenu Israeli.
GEN 49:3 “Reubeni, wewe ni mzaliwa wangu wa kwanza, nguvu zangu, tunda la kwanza la nguvu zangu; umepita kwa heshima, umepita kwa uwezo.
GEN 49:4 Usiyezuiwa kama maji, basi hutakuwa mkuu tena, kwa kuwa ulipanda kwenye kitanda cha baba yako, kwenye kitanda changu na kukinajisi.
GEN 49:5 “Simeoni na Lawi ni ndugu: panga zao ni silaha za jeuri.
GEN 49:6 Mimi na nisiingie katika baraza lao, nami nisiunganike katika kusanyiko lao, kwa kuwa wamewaua watu katika hasira yao, na kukata mishipa ya miguu ya mafahali kama walivyopenda.
GEN 49:7 Hasira yao na ilaaniwe, kwa kuwa ni kali mno, nayo ghadhabu yao ni ya ukatili! Nitawatawanya katika Yakobo, na kuwasambaza katika Israeli.
GEN 49:8 “Yuda, ndugu zako watakusifu; mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako; wana wa baba yako watakusujudia.
GEN 49:9 Ee Yuda, wewe ni mwana simba; unarudi toka mawindoni, mwanangu. Kama simba hunyemelea na kulala chini, kama simba jike: nani athubutuye kumwamsha?
GEN 49:10 Fimbo ya ufalme haitaondoka kwa Yuda, wala fimbo ya mtawala kati ya miguu yake, hadi aje yeye ambaye milki ni yake, ambaye utii wa mataifa ni wake.
GEN 49:11 Atamfunga punda wake katika mzabibu, naye mwana-punda wake kwenye tawi lililo bora zaidi; atafua mavazi yake katika divai, majoho yake katika damu ya mizabibu.
GEN 49:12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa divai, meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.
GEN 49:13 “Zabuloni ataishi pwani ya bahari na kuwa bandari za kuegesha meli; mpaka wake utapanuka kuelekea Sidoni.
GEN 49:14 “Isakari ni punda mwenye nguvu ambaye amelala kati ya mizigo yake.
GEN 49:15 Aonapo palivyo pazuri mahali pake pa kupumzika na jinsi nchi yake inavyopendeza, atainamisha bega lake kwenye mzigo na kujitolea kwa ajili ya kazi ngumu.
GEN 49:16 “Dani atahukumu watu wake kwa haki kama mmoja wa makabila ya Israeli.
GEN 49:17 Dani atakuwa nyoka kando ya barabara, nyoka mwenye sumu kando ya njia, yule aumaye visigino vya farasi ili yule ampandaye aanguke chali.
GEN 49:18 “Ee Mwenyezi Mungu, nautafuta wokovu wako.
GEN 49:19 “Gadi atashambuliwa ghafula na kundi la washambuliaji, lakini yeye atawageukia na kuwashinda kabisa.
GEN 49:20 “Chakula cha Asheri kitakuwa kinono, naye atatoa chakula kitamu kinachomfaa mfalme.
GEN 49:21 “Naftali ni kulungu jike aliyeachiwa huru azaaye watoto wazuri.
GEN 49:22 “Yusufu ni mzabibu uzaao, mzabibu uzaao ulio kando ya chemchemi, ambao matawi yake hutanda ukutani.
GEN 49:23 Kwa uchungu wapiga mshale walimshambulia, wakampiga mshale kwa ukatili.
GEN 49:24 Lakini upinde wake ulibaki imara, mikono yake ikatiwa nguvu, na mkono wa Mwenye Nguvu wa Yakobo, kwa sababu ya Mchungaji, Mwamba wa Israeli,
GEN 49:25 kwa sababu ya Mungu wa baba yako, anayekusaidia, kwa sababu ya Mwenyezi, yeye anayekubariki kwa baraka za juu mbinguni, baraka za kilindi kilichoko chini, baraka za matitini na za tumbo la uzazi.
GEN 49:26 Baraka za baba yako ni kubwa kuliko baraka za milima ya kale, nyingi kuliko vilima vya kale. Baraka hizo zote na zikae juu ya kichwa cha Yusufu, juu ya paji la yule mkuu miongoni mwa ndugu zake.
GEN 49:27 “Benyamini ni mbwa-mwitu mwenye njaa kuu; asubuhi hurarua mawindo yake, jioni hugawa nyara.”
GEN 49:28 Haya yote ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hivi ndivyo baba yao alivyowaambia alipowabariki, akimpa kila mmoja baraka iliyomfaa.
GEN 49:29 Ndipo alipowapa maelekezo haya: “Mimi niko karibu kukusanywa kwa watu wangu. Mnizike pamoja na baba zangu kwenye pango katika shamba la Efroni, Mhiti,
GEN 49:30 pango lililoko katika shamba la Makpela, karibu na Mamre huko Kanaani, ambalo Ibrahimu alinunua liwe mahali pa kuzikia kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba.
GEN 49:31 Huko ndiko Ibrahimu na Sara mkewe walikozikwa, huko akazikwa Isaka na Rebeka mkewe, na huko nilimzika Lea.
GEN 49:32 Shamba hilo na pango lililo ndani yake lilinunuliwa kutoka kwa Wahiti.”
GEN 49:33 Baada ya Yakobo kumaliza kutoa maelekezo hayo kwa wanawe, akarudisha miguu yake kitandani, akapumua pumzi ya mwisho, na akakusanywa kwa watu wake.
GEN 50:1 Basi Yusufu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu.
GEN 50:2 Ndipo Yusufu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze,
GEN 50:3 wakatumia siku arobaini, muda uliohitajika kutia dawa asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini.
GEN 50:4 Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yusufu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni,
GEN 50:5 ‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’ ”
GEN 50:6 Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.”
GEN 50:7 Hivyo Yusufu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake, na watu mashuhuri wote wa Misri.
GEN 50:8 Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani mwa Yusufu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni.
GEN 50:9 Magari ya vita na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana.
GEN 50:10 Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu. Yusufu akakaa huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake.
GEN 50:11 Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu.
GEN 50:12 Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza:
GEN 50:13 Wakamchukua hadi nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Ibrahimu alilinunua kutoka kwa Efroni Mhiti pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia.
GEN 50:14 Baada ya Yusufu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wameenda naye kumzika baba yake.
GEN 50:15 Ndugu zake Yusufu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yusufu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?”
GEN 50:16 Kwa hiyo wakampelekea Yusufu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya:
GEN 50:17 ‘Hili ndilo mtakalomwambia Yusufu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yusufu akalia.
GEN 50:18 Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.”
GEN 50:19 Lakini Yusufu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu?
GEN 50:20 Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi.
GEN 50:21 Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawafariji na kusema nao kwa wema.
GEN 50:22 Yusufu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka mia moja na kumi,
GEN 50:23 naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yusufu walipozaliwa.
GEN 50:24 Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Ibrahimu, Isaka na Yakobo.”
GEN 50:25 Naye Yusufu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.”
GEN 50:26 Kwa hiyo Yusufu akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Baada ya kumtia dawa asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.
EXO 1:1 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, kila mmoja na jamaa yake:
EXO 1:2 Reubeni, Simeoni, Lawi na Yuda;
EXO 1:3 Isakari, Zabuloni na Benyamini;
EXO 1:4 Dani na Naftali, Gadi na Asheri.
EXO 1:5 Wazao wote wa Yakobo walikuwa watu sabini; Yusufu alikuwa tayari yuko Misri.
EXO 1:6 Basi Yusufu na kaka zake wote na kizazi kile chote walikufa,
EXO 1:7 lakini Waisraeli walikuwa wamezaana na kuongezeka sana, idadi yao ikawa kubwa mno, hadi wakaijaza nchi.
EXO 1:8 Kisha mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri.
EXO 1:9 Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kuliko sisi.
EXO 1:10 Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana nasi, na kuondoka katika nchi hii.”
EXO 1:11 Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao.
EXO 1:12 Lakini walivyozidi kuteswa, ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi. Wamisri wakawaogopa Waisraeli,
EXO 1:13 kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili.
EXO 1:14 Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.
EXO 1:15 Mfalme wa Misri akawaita wakunga waliowazalisha Waebrania, ambao majina yao yalikuwa Shifra na Pua, akawaambia,
EXO 1:16 “Mtakapowazalisha wanawake Waebrania, chunguzeni wanapojifungua. Ikiwa ni mtoto wa kiume, muueni; lakini ikiwa ni msichana, mwacheni aishi.”
EXO 1:17 Lakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi.
EXO 1:18 Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?”
EXO 1:19 Wakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Waebrania ni tofauti na wanawake wa Misri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.”
EXO 1:20 Kwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi.
EXO 1:21 Kwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe.
EXO 1:22 Kisha Farao akatoa agizo hili kwa watu wake wote: “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania lazima atupwe katika Mto Naili, bali kila mtoto wa kike aachwe aishi.”
EXO 2:1 Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi,
EXO 2:2 naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu.
EXO 2:3 Lakini alipoona hawezi kuendelea kumficha, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha kwenye matete kando ya ukingo wa Mto Naili.
EXO 2:4 Dada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto.
EXO 2:5 Ndipo binti Farao akateremka kwenye Mto Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti Farao akaona kisafina kwenye matete, akamtuma mmoja wa wajakazi wake kukichukua.
EXO 2:6 Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Waebrania.”
EXO 2:7 Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Waebrania akulelee huyu mtoto?”
EXO 2:8 Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto.
EXO 2:9 Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea.
EXO 2:10 Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina Musa, akisema, “Nilimtoa kwenye maji.”
EXO 2:11 Siku moja, Musa alipokuwa mtu mzima, alienda mahali walipokuwa ndugu zake, na akaona jinsi walivyokuwa wakifanyishwa kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmoja wa watu wake.
EXO 2:12 Musa akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha kwenye mchanga.
EXO 2:13 Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?”
EXO 2:14 Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.”
EXO 2:15 Farao aliposikia jambo hili, alijaribu kumuua Musa, lakini Musa akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima.
EXO 2:16 Kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza birika kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao.
EXO 2:17 Baadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Musa akainuka, akawasaidia kunywesha mifugo yao.
EXO 2:18 Wasichana hao waliporudi nyumbani, baba yao Reueli akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?”
EXO 2:19 Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikono ya wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.”
EXO 2:20 Akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.”
EXO 2:21 Musa akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Musa binti yake aliyeitwa Sipora amwoe.
EXO 2:22 Sipora alizaa mtoto wa kiume, naye Musa akamwita jina Gershomu, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
EXO 2:23 Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu.
EXO 2:24 Mungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka agano alilofanya na Ibrahimu pamoja na Isaka na Yakobo.
EXO 2:25 Kwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.
EXO 3:1 Basi Musa alikuwa anachunga mifugo ya Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani. Musa akapeleka mifugo mbali nyuma ya jangwa, naye akafika Horebu, mlima wa Mungu.
EXO 3:2 Huko malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea Musa katika mwali wa moto kutoka kichakani. Musa akaona kwamba ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei.
EXO 3:3 Ndipo Musa akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.”
EXO 3:4 Mwenyezi Mungu alipoona kuwa amegeuka ili aone, Mungu akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, “Musa! Musa!” Naye Musa akajibu, “Mimi hapa.”
EXO 3:5 Mungu akamwambia, “Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.”
EXO 3:6 Kisha akamwambia, “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.” Musa aliposikia hayo, akafunika uso wake kwa sababu aliogopa kumtazama Mungu.
EXO 3:7 Mwenyezi Mungu akamwambia, “Hakika nimeona mateso ya watu wangu katika Misri. Nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, nami nimeguswa na mateso yao.
EXO 3:8 Basi nimeshuka niwaokoe kutoka mkono wa Wamisri, niwatoe na kuwapandisha kutoka nchi hiyo, niwapeleke katika nchi nzuri na kubwa, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
EXO 3:9 Sasa kilio cha Waisraeli kimenifikia, nami nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa.
EXO 3:10 Basi, sasa nenda. Ninakutuma kwa Farao ili kuwatoa watu wangu Waisraeli kutoka Misri.”
EXO 3:11 Lakini Musa akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata niende kwa Farao kuwatoa Waisraeli nchini Misri?”
EXO 3:12 Naye Mungu akasema, “Mimi nitakuwa pamoja nawe. Hii itakuwa ishara kwako kwamba ni Mimi nimekutuma: Utakapokuwa umewatoa watu Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.”
EXO 3:13 Musa akamwambia Mungu, “Ikiwa nitawaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa baba zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani?’ Nitawaambia nini?”
EXO 3:14 Mungu akamwambia Musa, “Mimi niko ambaye niko. Hivyo ndivyo utakavyowaambia Waisraeli: ‘Mimi niko amenituma kwenu.’ ”
EXO 3:15 Vilevile Mungu akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo amenituma kwenu.’ “Hili ndilo Jina langu milele, Jina ambalo mtanikumbuka kwalo kizazi hadi kizazi.
EXO 3:16 “Nenda, ukawakusanye wazee wa Israeli, uwaambie, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, alinitokea akaniambia: Nimewatazama, nami nimeona mliyotendewa huku Misri.
EXO 3:17 Nami nimeahidi kuwapandisha kutoka kwenye mateso yenu katika nchi ya Misri, niwapeleke nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, nchi inayotiririka maziwa na asali.’
EXO 3:18 “Wazee wa Israeli watakusikiliza. Kisha wewe na wazee mtaenda kwa mfalme wa Misri na kumwambia, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania, ametutokea. Turuhusu twende safari ya siku tatu huko jangwani kutoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.’
EXO 3:19 Lakini nafahamu kwamba mfalme wa Misri hatawaruhusu kwenda, hadi mkono wenye nguvu umlazimishe.
EXO 3:20 Kwa hiyo nitaunyoosha mkono wangu na kuwapiga Wamisri kwa maajabu yote nitakayofanya miongoni mwao. Baada ya hayo, atawaruhusu mwondoke.
EXO 3:21 “Nami nitawapa hawa watu upendeleo mbele ya Wamisri, kwa hiyo mtakapoondoka nchini hamtaondoka mikono mitupu.
EXO 3:22 Kila mwanamke Mwisraeli atamwomba jirani yake Mmisri na mwanamke yeyote anayeishi nyumbani mwake ampe vyombo vya fedha, dhahabu na mavazi, ambavyo mtawavika wana wenu wa kiume na wa kike. Hivyo mtawateka nyara Wamisri.”
EXO 4:1 Musa akamjibu, “Itakuwaje wasiponiamini au kunisikiliza, waseme, ‘Mwenyezi Mungu hakukutokea’?”
EXO 4:2 Ndipo Mwenyezi Mungu akamuuliza, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?” Akamjibu, “Ni fimbo.”
EXO 4:3 Mwenyezi Mungu akasema, “Itupe chini.” Musa akaitupa fimbo chini, nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia.
EXO 4:4 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate kwenye mkia.” Basi Musa akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake.
EXO 4:5 Mwenyezi Mungu akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.”
EXO 4:6 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Musa akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji.
EXO 4:7 Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Musa akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake.
EXO 4:8 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili.
EXO 4:9 Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.”
EXO 4:10 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha hapo awali, wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.”
EXO 4:11 Mwenyezi Mungu akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu uwezo wa kuona au upofu? Je, si mimi, Mwenyezi Mungu?
EXO 4:12 Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.”
EXO 4:13 Lakini Musa akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.”
EXO 4:14 Ndipo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Musa, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Haruni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona.
EXO 4:15 Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya.
EXO 4:16 Haruni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake.
EXO 4:17 Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”
EXO 4:18 Kisha Musa akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.” Yethro akamwambia, “Nenda, nami nakutakia mema.”
EXO 4:19 Basi Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.”
EXO 4:20 Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.
EXO 4:21 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili asiwaruhusu watu waende.
EXO 4:22 Kisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza,
EXO 4:23 nami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu aende; basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ”
EXO 4:24 Musa alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, Mwenyezi Mungu akakutana naye, akataka kumuua.
EXO 4:25 Lakini Sipora akachukua kisu cha gumegume, akakata govi la mwanawe na kugusa miguu ya Musa nalo. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.”
EXO 4:26 (Sipora alipomwita Musa, “Bwana arusi wa damu”, alikuwa anamaanisha ile tohara.) Baada ya hayo Mwenyezi Mungu akamwacha.
EXO 4:27 Mwenyezi Mungu akamwambia Haruni, “Nenda jangwani ukamlaki Musa.” Basi akakutana na Musa kwenye mlima wa Mungu, akambusu.
EXO 4:28 Kisha Musa akamwambia Haruni kila kitu Mwenyezi Mungu alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya.
EXO 4:29 Musa na Haruni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli,
EXO 4:30 naye Haruni akawaambia kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amemwambia Musa. Pia akafanya ishara mbele ya watu,
EXO 4:31 nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa Mwenyezi Mungu anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.
EXO 5:1 Baadaye Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Waruhusu watu wangu waende, ili waweze kunifanyia sikukuu huko jangwani.’ ”
EXO 5:2 Farao akasema, “Huyo Mwenyezi Mungu ni nani, hata nimtii na kuruhusu Waisraeli waende? Simjui huyo Mwenyezi Mungu wala sitawaruhusu Waisraeli waende.”
EXO 5:3 Ndipo Musa na Haruni wakasema, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Sasa turuhusu tuwe na safari ya siku tatu ya jangwani ili tukamtolee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, dhabihu, la sivyo aweza kutupiga sisi kwa tauni au kwa upanga.”
EXO 5:4 Lakini mfalme wa Misri akasema, “Mbona ninyi Musa na Haruni mnawaondoa watu kutoka kwenye kazi zao? Rudini kwenye kazi zenu!”
EXO 5:5 Kisha Farao akasema, “Tazama, sasa watu hawa ni wengi, nanyi mnawazuia kufanya kazi.”
EXO 5:6 Siku hiyo hiyo, Farao akatoa amri hii kwa viongozi wa watumwa na wasimamizi wa watu, akawaambia:
EXO 5:7 “Tangu sasa msiwape hawa watu nyasi za kutengenezea matofali; wakusanye nyasi zao wenyewe.
EXO 5:8 Lakini watakeni kutengeneza matofali kiasi kile kile cha mwanzo, kiwango kisipunguzwe. Wao ni wavivu, ndiyo sababu wanalia, wakisema, ‘Turuhusiwe twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.’
EXO 5:9 Fanyeni kazi kuwa ngumu zaidi kwa watu hao ili wakazane na kazi na kuacha kusikiliza uongo.”
EXO 5:10 Basi viongozi wa watumwa na wasimamizi wakaenda kuwaambia watu, “Hivi ndivyo Farao asemavyo: ‘Sitawapa nyasi tena.
EXO 5:11 Nendeni mkatafute nyasi wenyewe popote mnapoweza kuzipata, lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’ ”
EXO 5:12 Basi watu wakatawanyika kote nchini Misri kukusanya mabua ya kutumia badala ya nyasi.
EXO 5:13 Viongozi wa watumwa wakasisitiza wakisema, “Timizeni kazi mnayotakiwa kwa kila siku, kama wakati ule mlipokuwa mkipewa nyasi.”
EXO 5:14 Wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa na viongozi wa watumwa wa Farao walipigwa na kuulizwa, “Kwa nini hamkutimiza kiwango chenu cha kutengeneza matofali jana na leo, kama mwanzoni?”
EXO 5:15 Ndipo wasimamizi wa Waisraeli wakaenda kumlilia Farao, wakisema: “Mbona umewatendea watumishi wako hivi?
EXO 5:16 Watumishi wako hawapewi nyasi, hata hivyo tumeambiwa, ‘Tengenezeni matofali!’ Watumishi wako wanapigwa, lakini kosa ni la watu wako wenyewe.”
EXO 5:17 Farao akasema, “Ninyi ni wavivu ndiyo sababu mnasema, ‘Turuhusu twende tukamtolee Mwenyezi Mungu dhabihu.’
EXO 5:18 Sasa nendeni kazini. Hamtapewa nyasi zozote, nanyi ni lazima mtengeneze matofali.”
EXO 5:19 Wasimamizi wa Waisraeli walitambua kuwa wako taabani walipoambiwa, “Hamtakiwi kupunguza idadi ya matofali mliotakiwa kutengeneza kila siku.”
EXO 5:20 Walipoondoka kwa Farao, wakawakuta Musa na Haruni wakingojea kukutana nao,
EXO 5:21 wakawaambia Musa na Haruni, “Mwenyezi Mungu na awaangalie awahukumu ninyi! Mmetufanya tuwe chukizo kwa Farao na maafisa wake, nanyi mmeweka upanga mikononi mwao ili kutuua sisi.”
EXO 5:22 Musa akarudi kwa Mwenyezi Mungu na kumwambia, “Ee Bwana, mbona umewaletea watu hawa taabu? Kwa nini basi ukanituma mimi?
EXO 5:23 Tangu nilipokwenda kuzungumza na Farao kwa jina lako, amewaletea watu hawa taabu, nawe kamwe hujawakomboa watu wako.”
EXO 6:1 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sasa utaona kitu nitakachomfanyia Farao: Kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawaachia watu waende; kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.”
EXO 6:2 Pia Mungu akamwambia Musa, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EXO 6:3 Nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo kama Mungu Mwenyezi, ingawa kwa Jina langu, Yehova, sikujitambulisha kwao.
EXO 6:4 Pia niliweka agano langu nao kuwapa nchi ya Kanaani, ambako waliishi kama wageni.
EXO 6:5 Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha huzuni cha Waisraeli ambao Wamisri wamewatia utumwani, nami nimelikumbuka agano langu.
EXO 6:6 “Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nami nitawatoa katika nira ya Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu.
EXO 6:7 Nitawachukua ninyi kuwa watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa chini ya nira ya Wamisri.
EXO 6:8 Nami nitawaleta hadi nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EXO 6:9 Musa akawaarifu Waisraeli jambo hili, lakini hawakumsikiliza kwa sababu ya kuvunjika moyo na kazi yao ngumu.
EXO 6:10 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 6:11 “Nenda, mwambie Farao mfalme wa Misri awaachie Waisraeli waondoke nchini mwake.”
EXO 6:12 Lakini Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Ikiwa Waisraeli hawatanisikiliza, kwa nini yeye Farao anisikilize mimi, ambaye huzungumza kwa kigugumizi?”
EXO 6:13 Ndipo Mwenyezi Mungu akanena na Musa na Haruni kuhusu Waisraeli na Farao mfalme wa Misri, naye akawaamuru wawatoe Waisraeli kutoka Misri.
EXO 6:14 Hawa walikuwa wakuu wa jamaa zao: Wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli walikuwa: Hanoki na Palu, Hesroni na Karmi.
EXO 6:15 Wana wa Simeoni walikuwa: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
EXO 6:16 Haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, kulingana na orodha zao: Gershoni, Kohathi na Merari.
EXO 6:17 Wana wa Gershoni kwa koo walikuwa: Libni na Shimei.
EXO 6:18 Wana wa Kohathi walikuwa: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Kohathi aliishi miaka mia moja na thelathini na tatu (133).
EXO 6:19 Wana wa Merari walikuwa: Mahli na Mushi.
EXO 6:20 Amramu akamwoa Yokebedi, shangazi yake, aliyemzalia Haruni na Musa.
EXO 6:21 Wana wa Ishari walikuwa: Kora, Nefegi na Zikri.
EXO 6:22 Wana wa Uzieli walikuwa: Mishaeli, Elisafani na Sithri.
EXO 6:23 Haruni akamwoa Elisheba binti Aminadabu, ndugu yake Nashoni, naye akamzalia Nadabu na Abihu, Eleazari na Ithamari.
EXO 6:24 Wana wa Kora walikuwa: Asiri, Elkana na Abiasafu.
EXO 6:25 Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi.
EXO 6:26 Hawa walikuwa Haruni na Musa, wale wale ambao Mwenyezi Mungu aliwaambia, “Watoeni Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.”
EXO 6:27 Hao ndio waliozungumza na Farao, mfalme wa Misri kuhusu kuwatoa Waisraeli Misri. Ilikuwa ni huyo Musa na huyo Haruni.
EXO 6:28 Mwenyezi Mungu aliponena na Musa huko Misri,
EXO 6:29 akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. Mwambie Farao mfalme wa Misri kila kitu nikuambiacho.”
EXO 6:30 Lakini Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Kwa kuwa mimi huzungumza kwa kigugumizi, Farao atanisikiliza mimi?”
EXO 7:1 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tazama, nimekufanya kama Mungu kwa Farao, naye Haruni ndugu yako atakuwa nabii wako.
EXO 7:2 Utasema kila kitu nitakachokuagiza, naye Haruni ndugu yako atamwambia Farao awaachie Waisraeli watoke katika nchi yake.
EXO 7:3 Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri,
EXO 7:4 hatawasikiliza. Kisha nitaupeleka mkono wangu juu ya Misri, na kwa matendo makuu ya hukumu nitavitoa vikosi vyangu, watu wangu Waisraeli.
EXO 7:5 Nao Wamisri watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya Misri na kuwatoa Waisraeli humo.”
EXO 7:6 Musa na Haruni wakafanya sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaamuru.
EXO 7:7 Musa alikuwa na umri wa miaka themanini na Haruni alikuwa na umri wa miaka themanini na tatu walipozungumza na Farao.
EXO 7:8 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni,
EXO 7:9 “Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Haruni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.”
EXO 7:10 Ndipo Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakafanya sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyoagiza. Haruni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka.
EXO 7:11 Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Misri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao.
EXO 7:12 Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Haruni ikazimeza zile fimbo zao.
EXO 7:13 Hata hivyo, moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
EXO 7:14 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Moyo wa Farao ni mgumu; anakataa kuwaacha watu waondoke.
EXO 7:15 Nenda kwa Farao asubuhi anapoenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Mto Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka.
EXO 7:16 Kisha umwambie, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza.
EXO 7:17 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu: Kwa fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga maji ya Mto Naili, nayo yatabadilika kuwa damu.
EXO 7:18 Samaki walio katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya; Wamisri hawataweza kunywa maji yake.’ ”
EXO 7:19 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.”
EXO 7:20 Musa na Haruni wakafanya kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu.
EXO 7:21 Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri.
EXO 7:22 Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
EXO 7:23 Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni.
EXO 7:24 Nao Wamisri wote wakachimba kandokando ya Mto Naili kupata maji ya kunywa, kwa sababu hawakuweza kunywa maji ya mto.
EXO 7:25 Zilipita siku saba baada ya Mwenyezi Mungu kuyapiga maji ya Mto Naili.
EXO 8:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
EXO 8:2 Ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura.
EXO 8:3 Mto Naili utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga.
EXO 8:4 Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ”
EXO 8:5 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Nyoosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ”
EXO 8:6 Ndipo Haruni akaunyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi.
EXO 8:7 Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri.
EXO 8:8 Ndipo Farao akamwita Musa na Haruni na kusema, “Mwombeni Mwenyezi Mungu awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.”
EXO 8:9 Musa akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako, na watu wako ili vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu, isipokuwa wale walio katika Mto Naili.”
EXO 8:10 Farao akasema, “Kesho.” Musa akamjibu, “Itakuwa kama unavyosema, ili upate kujua kwamba hakuna yeyote kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
EXO 8:11 Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Naili tu.”
EXO 8:12 Baada ya Musa na Haruni kuondoka kwa Farao, Musa akamlilia Mwenyezi Mungu kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao.
EXO 8:13 Naye Mwenyezi Mungu akafanya lile Musa alilomwomba. Vyura wakafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani.
EXO 8:14 Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka.
EXO 8:15 Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
EXO 8:16 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Nyoosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.”
EXO 8:17 Wakafanya hivyo, Haruni aliponyoosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto.
EXO 8:18 Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama.
EXO 8:19 Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
EXO 8:20 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Amka asubuhi na mapema, usimame mbele ya Farao wakati anapoenda mtoni, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
EXO 8:21 Usipowaruhusu watu wangu waondoke, nitatuma makundi ya inzi juu yako na maafisa wako, juu ya watu wako, na ndani ya nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajaa inzi; hata ardhi itafunikwa na inzi.
EXO 8:22 “ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwa na makundi ya inzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, Mwenyezi Mungu, niko katika nchi hii.
EXO 8:23 Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ”
EXO 8:24 Naye Mwenyezi Mungu akafanya hivyo. Makundi makubwa ya inzi walimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na inzi.
EXO 8:25 Ndipo Farao akamwita Musa na Haruni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.”
EXO 8:26 Lakini Musa akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe?
EXO 8:27 Ni lazima twende mwendo wa siku tatu hadi tufike jangwani ili tumtolee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, dhabihu, kama alivyotuagiza.”
EXO 8:28 Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.”
EXO 8:29 Musa akajibu, “Mara tu nitakapoondoka, nitamwomba Mwenyezi Mungu na kesho inzi wataondoka kwa Farao, kwa maafisa wake, na kwa watu wake. Ila hakikisha kwamba Farao hatatenda kwa udanganyifu tena kwa kutokuwaachia watu waende kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.”
EXO 8:30 Ndipo Musa akamwacha Farao na kumwomba Mwenyezi Mungu,
EXO 8:31 naye Mwenyezi Mungu akafanya lile Musa alilomwomba. Inzi wakaondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake, wala hakuna hata inzi aliyebakia.
EXO 8:32 Lakini wakati huu pia Farao akaufanya moyo wake kuwa mgumu, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.
EXO 9:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania, asemalo: “Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu.”
EXO 9:2 Usipowaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia,
EXO 9:3 mkono wa Mwenyezi Mungu utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ng’ombe wako, kondoo na mbuzi.
EXO 9:4 Lakini Mwenyezi Mungu ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ ”
EXO 9:5 Mwenyezi Mungu akaweka wakati na kusema, “Kesho Mwenyezi Mungu atalitenda hili katika nchi.”
EXO 9:6 Siku iliyofuata Mwenyezi Mungu akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa.
EXO 9:7 Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende.
EXO 9:8 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni, “Chukueni majivu ya tanuru, naye Musa ayarushe angani mbele ya Farao.
EXO 9:9 Yatakuwa vumbi jepesi juu ya nchi yote ya Misri, pia yatatokea majipu yenye kufura kwenye miili ya watu na ya wanyama katika nchi yote.”
EXO 9:10 Basi wakachukua majivu kwenye tanuru na kusimama mbele ya Farao. Musa akayarusha hewani, nayo majipu yenye kufura yakatokea kwenye miili ya watu na ya wanyama.
EXO 9:11 Waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya majipu yaliyokuwa kwenye miili yao, na kwenye miili ya Wamisri wote.
EXO 9:12 Lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwambia Musa.
EXO 9:13 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Amka asubuhi na mapema, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili waweze kuniabudu,
EXO 9:14 au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama mimi duniani kote.
EXO 9:15 Kwa kuwa hadi sasa ningekuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi.
EXO 9:16 Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nikuoneshe uwezo wangu, na jina langu litangazwe duniani kote.
EXO 9:17 Bado unaendelea kujiinua dhidi ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende.
EXO 9:18 Hivyo basi, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa hadi leo.
EXO 9:19 Sasa toa amri mifugo yako na kila kitu ulicho nacho shambani, kipelekwe mahali pa usalama. Kwa sababu mvua ya mawe itamwangukia kila mtu na mnyama ambaye hajaletwa ndani, na ambaye bado yuko nje shambani; nao watakufa.’ ”
EXO 9:20 Wale maafisa wa Farao ambao waliliogopa neno la Mwenyezi Mungu wakafanya haraka kuwaleta watumwa wao na mifugo yao ndani.
EXO 9:21 Lakini wale waliopuuza neno la Mwenyezi Mungu wakawaacha watumwa wao na mifugo yao shambani.
EXO 9:22 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili mvua ya mawe inyeshe Misri yote: juu ya watu, wanyama, na juu ya kila kitu kinachoota katika mashamba ya Misri.”
EXO 9:23 Musa alipoinyoosha fimbo yake kuelekea angani, Mwenyezi Mungu akatuma ngurumo na mvua ya mawe; mwanga wa radi ukamulika hadi nchi. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi ya Misri;
EXO 9:24 mvua ya mawe ikanyesha, na radi ikamulika pote. Ikawa dhoruba ya kutisha zaidi, ambayo haijawahi kutokea katika Misri tangu nchi hiyo iwe taifa.
EXO 9:25 Mvua ya mawe ikaharibu kila kitu katika nchi ya Misri kilichokuwa katika mashamba: watu na wanyama; ikaharibu kila kitu kilichoota mashambani na kung’oa kila mti.
EXO 9:26 Mahali pekee ambapo mvua ya mawe haikunyesha ni nchi ya Gosheni, ambako Waisraeli waliishi.
EXO 9:27 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, “Wakati huu nimetenda dhambi. Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, mimi na watu wangu ni wakosaji.
EXO 9:28 Mwombeni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa tumepata ngurumo na mvua za mawe za kutosha. Nitawaachia mwondoke; hamtahitaji kungoja zaidi.”
EXO 9:29 Musa akamjibu, “Nitakapokuwa nimetoka nje ya mji, nitanyoosha mikono yangu juu kumwomba Mwenyezi Mungu. Ngurumo zitakoma na hapatakuwa mvua ya mawe tena, ili upate kujua kuwa nchi ni mali ya Mwenyezi Mungu.
EXO 9:30 Lakini ninajua kuwa wewe na maafisa wako bado hammwogopi Bwana Mwenyezi Mungu.”
EXO 9:31 (Kitani na shayiri viliharibiwa, kwa kuwa shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa imechanua maua.
EXO 9:32 Hata hivyo, ngano na kusemethi hazikuharibiwa kwa sababu zilikuwa hazijakomaa.)
EXO 9:33 Kisha Musa akaondoka kwa Farao, akaenda nje ya mji. Musa akanyoosha mikono yake kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, ngurumo na mvua ya mawe vikakoma, mvua haikuendelea tena kunyesha nchini.
EXO 9:34 Farao alipoona kwamba mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akafanya dhambi tena. Yeye na maafisa wake wakafanya mioyo yao kuwa migumu.
EXO 9:35 Kwa hiyo, moyo wa Farao ukawa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waende, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema kupitia Musa.
EXO 10:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake kuwa mgumu na mioyo ya maafisa wake ili nipate kutenda ishara hizi zangu za ajabu miongoni mwao,
EXO 10:2 ili upate kuwaeleza watoto wako na wajukuu wako jinsi nilivyowatendea Wamisri kwa ukali, na jinsi nilivyofanya ishara zangu miongoni mwao, nanyi mpate kujua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
EXO 10:3 Kwa hiyo Musa na Haruni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania, asemalo: ‘Utaendelea hata lini kukataa kunyenyekea mbele yangu? Waachie watu wangu waende, ili waniabudu.
EXO 10:4 Ukikataa kuwaachia waende, kesho nitaleta nzige katika nchi yako.
EXO 10:5 Nao watafunika uso wa ardhi hata usionekane. Watatafuna mabaki machache yaliyobakizwa baada ya ile mvua ya mawe, yaani pamoja na kila mti unaoota katika mashamba yenu.
EXO 10:6 Nzige hao watajaza nyumba zako, za maafisa wako wote na za Wamisri wote. Jambo ambalo baba zenu wala babu zenu hawajapata kuona tangu siku ile walipoanza kuishi katika nchi hii hadi leo.’ ” Ndipo Musa akageuka na kumwacha Farao.
EXO 10:7 Maafisa wa Farao wakamwambia, “Hadi lini huyu mtu atakuwa tanzi kwetu? Waachie hao watu waende zao, ili wapate kumwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Je, bado hutambui kuwa Misri imeangamia?”
EXO 10:8 Ndipo Musa na Haruni wakaletwa kwa Farao. Farao akawaambia, “Nendeni, mkamwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Lakini ni nani hasa watakaoenda?”
EXO 10:9 Musa akajibu, “Tutaenda na vijana wetu na wazee, pamoja na wana wetu na binti zetu, pia pamoja na mbuzi, kondoo, na ng’ombe wetu kwa sababu tutaadhimisha sikukuu kwa Mwenyezi Mungu.”
EXO 10:10 Farao akasema, “Kama kweli nitawaruhusu mwondoke pamoja na wanawake wenu na watoto wenu, Mwenyezi Mungu awe pamoja nanyi! Ni wazi kwamba mna makusudi mabaya.
EXO 10:11 La hasha! Wanaume peke yao na waende, wakamwabudu Mwenyezi Mungu, kwa kuwa hilo ndilo mmekuwa mkiomba.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakaondolewa mbele ya Farao.
EXO 10:12 Basi Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako juu ya Misri, ili kundi la nzige liweze kuvamia nchi na kutafuna kila kitu kinachoota katika mashamba na kila kitu kilichosazwa na ile mvua ya mawe.”
EXO 10:13 Kwa hiyo Musa akanyoosha fimbo yake juu ya Misri, Mwenyezi Mungu akauleta upepo wa mashariki ukavuma katika nchi yote mchana wote na usiku kucha, kufikia asubuhi upepo ukawa umeleta nzige.
EXO 10:14 Wakaivamia Misri yote na kukaa katika kila eneo la nchi kwa wingi. Kamwe halijapata kutokea pigo la nzige kama hilo, wala halitakuwa tena.
EXO 10:15 Wakafunika ardhi yote hata ardhi ikawa nyeusi. Wakatafuna kila kilichokuwa kimebakizwa na ile mvua ya mawe: kila kitu kilichoota shambani, pamoja na matunda kwenye miti. Hakuna kitu chochote cha kijani kilichosalia katika miti au mmea katika nchi yote ya Misri.
EXO 10:16 Farao akawaita Musa na Haruni kwa haraka na kuwaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na dhidi yenu pia.
EXO 10:17 Sasa unisamehe dhambi yangu mara moja tena na umwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aondoe pigo hili baya kwangu.”
EXO 10:18 Kisha Musa akaondoka kwa Farao akamwomba Mwenyezi Mungu.
EXO 10:19 Naye Mwenyezi Mungu akaugeuza upepo kuwa upepo mkali sana kutoka magharibi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka kwenye Bahari ya Shamu. Hakuna nzige hata mmoja aliyebaki popote katika nchi ya Misri.
EXO 10:20 Lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke.
EXO 10:21 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.”
EXO 10:22 Kwa hiyo Musa akaunyoosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu.
EXO 10:23 Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo waliyokuwa wanaishi.
EXO 10:24 Ndipo Farao akamwita Musa na kusema, “Nendeni, mkamwabudu Mwenyezi Mungu. Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ng’ombe wenu waacheni.”
EXO 10:25 Lakini Musa akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu, na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
EXO 10:26 Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa kuwa hadi tutakapofika huko, hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu Mwenyezi Mungu.”
EXO 10:27 Lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke.
EXO 10:28 Farao akamwambia Musa, “Ondoka mbele yangu! Hakikisha kuwa hutakuja mbele yangu tena! Siku ile utakapouona uso wangu utakufa.”
EXO 10:29 Musa akamjibu, “Iwe kama ulivyosema! Kamwe sitauona uso wako tena.”
EXO 11:1 Basi Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Nitaleta pigo moja zaidi kwa Farao na katika nchi ya Misri. Baada ya hilo, atawaacha mwondoke hapa na atakapofanya hivyo, atawafukuza mtoke kabisa.
EXO 11:2 Waambie watu wote kwamba kila mwanaume na kila mwanamke amwombe jirani yake vitu vya fedha na vya dhahabu.”
EXO 11:3 (Mwenyezi Mungu akawafanya Wamisri wawe na moyo wa ukarimu kwa Waisraeli, naye Musa mwenyewe akaheshimiwa sana na maafisa wa Farao na watu wote katika nchi ya Misri.)
EXO 11:4 Kwa hiyo Musa akasema, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Usiku wa manane, Mimi nitapita katika nchi yote ya Misri.
EXO 11:5 Kila mwanaume kifungua mimba katika Misri atakufa, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Farao, anayeketi kwenye kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mjakazi, anayesaga nafaka kwa jiwe, pamoja na kila mzaliwa wa kwanza wa mifugo.
EXO 11:6 Kutakuwa na kilio kikubwa katika nchi yote ya Misri, kilio ambacho hakijakuwa, wala kamwe hakitakuwa tena.
EXO 11:7 Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna hata mbwa atakayembwekea mwanadamu wala mnyama yeyote.’ Ndipo mtajua kuwa Mwenyezi Mungu huweka tofauti kati ya Misri na Israeli.
EXO 11:8 Maafisa hawa wako wote watanijia, wakisujudu mbele yangu, wakisema, ‘Ondoka, wewe pamoja na watu wako wote wanaokufuata!’ Baada ya haya nitaondoka.” Kisha Musa, akiwa amewaka hasira, akamwacha Farao.
EXO 11:9 Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Farao atakataa kukusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka katika nchi ya Misri.”
EXO 11:10 Musa na Haruni wakafanya maajabu haya yote mbele ya Farao, lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke katika nchi yake.
EXO 12:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni katika nchi ya Misri,
EXO 12:2 “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu.
EXO 12:3 Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya jamaa yake, mmoja kwa kila nyumba.
EXO 12:4 Ikiwa nyumba yoyote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu.
EXO 12:5 Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi.
EXO 12:6 Tunzeni wanyama hao hadi siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni.
EXO 12:7 Ndipo watakapochukua sehemu ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu, na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao.
EXO 12:8 Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu.
EXO 12:9 Msile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani.
EXO 12:10 Msibakize nyama yoyote hadi asubuhi; nazo kama zitabakia hadi asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto.
EXO 12:11 Hivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka ya Mwenyezi Mungu.
EXO 12:12 “Usiku huo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumuua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EXO 12:13 Damu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.
EXO 12:14 “Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu, mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwa Mwenyezi Mungu, katika vizazi vyenu vyote: mtalishika kuwa agizo la kudumu.
EXO 12:15 Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtaondoa chachu yote ndani ya nyumba zenu, kwa maana yeyote atakayekula chochote chenye chachu kuanzia siku ya kwanza hadi ya saba lazima akatiliwe mbali kutoka Israeli.
EXO 12:16 Katika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, na kusanyiko jingine katika siku ya saba. Katika siku hizo msifanye kazi kamwe isipokuwa kutayarisha chakula cha kila mmoja; hilo ndilo tu mtakalofanya.
EXO 12:17 “Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa agizo la kudumu.
EXO 12:18 Katika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja.
EXO 12:19 Kwa muda wa siku saba isionekane chachu yoyote katika nyumba zenu. Yeyote alaye chochote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa.
EXO 12:20 Msile chochote kilichotiwa chachu. Popote mnapoishi, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”
EXO 12:21 Ndipo Musa akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka.
EXO 12:22 Chukueni kitawi cha hisopo, mkichovye kwenye damu iliyopo kwenye sinia, na kuipaka sehemu ya hiyo damu kwenye vizingiti, na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake hadi asubuhi.
EXO 12:23 Mwenyezi Mungu apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.
EXO 12:24 “Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu.
EXO 12:25 Mtakapoingia katika nchi Mwenyezi Mungu atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii.
EXO 12:26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’
EXO 12:27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Mwenyezi Mungu, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri, na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo Waisraeli walisujudu na kuabudu.
EXO 12:28 Waisraeli wakafanya kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa na Haruni.
EXO 12:29 Ilipofika usiku wa manane, Mwenyezi Mungu akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia.
EXO 12:30 Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa hapakuwa nyumba hata moja ambayo hakufa mtu.
EXO 12:31 Wakati huo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni kwa watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu Mwenyezi Mungu kama mlivyoomba.
EXO 12:32 Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ng’ombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”
EXO 12:33 Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!”
EXO 12:34 Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika mavazi na kuyabeba mabegani mwao.
EXO 12:35 Waisraeli wakafanya kama Musa alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na mavazi.
EXO 12:36 Basi Mwenyezi Mungu alikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.
EXO 12:37 Waisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi hadi Sukothi. Walikuwa wanaume wapatao elfu mia sita waliotembea kwa miguu, bila kuhesabu wanawake na watoto.
EXO 12:38 Watu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo, wakiwemo kondoo, mbuzi na ng’ombe.
EXO 12:39 Wakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kujiandalia chakula.
EXO 12:40 Waisraeli waliishi Misri kwa muda wa miaka mia nne na thelathini (430).
EXO 12:41 Siku ya mwisho ya hiyo miaka mia nne na thelathini (430), vikosi vyote vya Mwenyezi Mungu viliondoka Misri.
EXO 12:42 Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri, basi Waisraeli wote wanapaswa kuadhimisha usiku huu kwa kukesha ili kumheshimu Mwenyezi Mungu katika vizazi vijavyo.
EXO 12:43 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni, “Haya ndio masharti kwa ajili ya Pasaka: “Mgeni hataruhusiwa kula Pasaka.
EXO 12:44 Mtumwa yeyote ambaye mmemnunua aweza kuila kama mmemtahiri,
EXO 12:45 lakini kibarua yeyote au msafiri haruhusiwi kula.
EXO 12:46 “Sharti iliwe ndani ya nyumba; msichukue nyama yoyote nje ya nyumba hiyo. Msiuvunje mfupa wowote.
EXO 12:47 Jumuiya yote ya Israeli ni lazima waiadhimishe Pasaka hiyo.
EXO 12:48 “Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu ni lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume yeyote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila.
EXO 12:49 Sheria hiyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”
EXO 12:50 Waisraeli wote walifanya kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa na Haruni.
EXO 12:51 Siku ile ile Mwenyezi Mungu akawatoa Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.
EXO 13:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 13:2 “Niwekeeni wakfu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. Kila mtoto wa kwanza aliye kifungua mimba miongoni mwa Waisraeli ni mali yangu, akiwa wa mwanadamu au wa mnyama.”
EXO 13:3 Ndipo Musa akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii, siku ambayo mlitoka katika nchi ya Misri, katika nchi ya utumwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwatoa humo kwa mkono wenye nguvu. Msile chochote kilichotiwa chachu.
EXO 13:4 Leo, katika mwezi wa Abibu, mnatoka.
EXO 13:5 Mwenyezi Mungu atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi aliyowaapia baba zako kukupa, nchi inayotiririka maziwa na asali, utaiadhimisha sikukuu hii katika mwezi huu:
EXO 13:6 Kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu na katika siku ya saba utamfanyia Mwenyezi Mungu sikukuu.
EXO 13:7 Kwa muda wa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu, pasionekane kitu chochote kilicho na chachu miongoni mwako, wala chachu yoyote isionekane popote ndani ya mipaka yako.
EXO 13:8 Siku ile utamwambia mwanao, ‘Nafanya hivi kwa sababu ya jambo ambalo Mwenyezi Mungu alinitendea nilipotoka katika nchi ya Misri.’
EXO 13:9 Adhimisho hili, litakuwa kama alama kwenye mkono wako na ukumbusho katika paji lako la uso, kwamba sheria ya Mwenyezi Mungu inapaswa iwe kinywani mwako. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.
EXO 13:10 Ni lazima ulishike agizo hili kwa wakati uliopangwa mwaka baada ya mwaka.
EXO 13:11 “Baada ya Mwenyezi Mungu kukuingiza katika nchi ya Wakanaani na kukupa nchi hiyo, kama alivyokuahidi kwa kiapo na kwa baba zako,
EXO 13:12 inakupasa kumtolea Mwenyezi Mungu kila mzaliwa wa kwanza. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa mifugo yako ni mali ya Mwenyezi Mungu.
EXO 13:13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo, lakini kama hutamkomboa, utamvunja shingo yake. Kila mzaliwa wa kwanza mwanaume miongoni mwa wana wenu utamkomboa.
EXO 13:14 “Katika siku zijazo, mwanao akikuuliza, ‘Hii ina maana gani?’ Mwambie, ‘Kwa mkono wenye nguvu Mwenyezi Mungu alitutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
EXO 13:15 Farao alipokataa kwa ukaidi kuturuhusu kuondoka, Mwenyezi Mungu aliua kila mzaliwa wa kwanza wa Wamisri, mwanadamu na wa mnyama. Hii ndiyo sababu ninatoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu mzaliwa wa kwanza wa kiume wa kila tumbo, na kumkomboa kila mzaliwa wa kwanza wa wana wangu.’
EXO 13:16 Jambo hili litakuwa kama ishara kwenye mkono wako na kama alama kwenye paji la uso wako, kwamba Mwenyezi Mungu alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.”
EXO 13:17 Farao alipowaachia watu waende, Mungu hakuwaongoza kufuata njia ipitayo katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa fupi zaidi. Kwa maana Mungu alisema, “Wakikabiliana na vita, wanaweza kubadili mawazo yao na kurudi Misri.”
EXO 13:18 Kwa hiyo Mungu akawaongoza watu kupitia njia ya kuzunguka kupitia jangwani, kuelekea Bahari ya Shamu. Waisraeli walipanda kutoka nchi ya Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.
EXO 13:19 Musa akachukua mifupa ya Yusufu kwa sababu Yusufu alikuwa amewaapisha wana wa Israeli. Alikuwa amewaambia, “Hakika Mungu atakuja kuwasaidia, nanyi ni lazima mwichukue mifupa yangu mwende nayo kutoka mahali hapa.”
EXO 13:20 Baada ya Waisraeli kuondoka Sukothi wakapiga kambi huko Ethamu pembeni mwa jangwa.
EXO 13:21 Wakati wa mchana Mwenyezi Mungu aliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku.
EXO 13:22 Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.
EXO 14:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 14:2 “Waambie Waisraeli wageuke nyuma na wapige kambi karibu na Pi-Hahirothi, kati ya Migdoli na bahari. Watapiga kambi kando ya bahari, mkabala na Baal-Sefoni.
EXO 14:3 Farao atafikiri kwamba, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga katika nchi kwa kuchanganyikiwa, nalo jangwa limewafungia.’
EXO 14:4 Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo.
EXO 14:5 Mfalme wa Misri alipoambiwa kuwa Waisraeli wamekimbia, Farao na maafisa wake wakabadili nia zao kuhusu Waisraeli, wakasema, “Tumefanya nini? Tumewaachia Waisraeli waende zao na tumeukosa utumishi wao!”
EXO 14:6 Kwa hiyo akaandaliwa gari lake la vita, naye akaenda pamoja na jeshi lake.
EXO 14:7 Akachukua magari ya vita mia sita bora, pamoja na magari ya vita mengine yote ya Misri, pamoja na maafisa wa magari hayo yote.
EXO 14:8 Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, kwa hiyo akawafuatia Waisraeli, waliokuwa wakiondoka Misri kwa ujasiri.
EXO 14:9 Nao Wamisri, yaani farasi wote wa Farao na magari ya vita, wapanda farasi na vikosi vya askari, wakawafuatia Waisraeli, wakawakuta karibu na Pi-Hahirothi, mkabala na Baal-Sefoni walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari.
EXO 14:10 Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia Mwenyezi Mungu.
EXO 14:11 Wakamwambia Musa, “Je, ni kwamba hakukuwa na makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri?
EXO 14:12 Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, ‘Tuache tuwatumikie Wamisri’? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!”
EXO 14:13 Musa akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Mwenyezi Mungu atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena.
EXO 14:14 Mwenyezi Mungu atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”
EXO 14:15 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.
EXO 14:16 Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, ili Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini.
EXO 14:17 Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake.
EXO 14:18 Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”
EXO 14:19 Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma,
EXO 14:20 ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.
EXO 14:21 Ndipo Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi Mungu akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika,
EXO 14:22 nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.
EXO 14:23 Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi.
EXO 14:24 Kukaribia mapambazuko, Mwenyezi Mungu akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha.
EXO 14:25 Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao ya vita, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! Mwenyezi Mungu anawapigania dhidi ya Misri.”
EXO 14:26 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudi yawafunike Wamisri, magari yao ya vita, na wapanda farasi wao.”
EXO 14:27 Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari, kulipopambazuka bahari ikarudi mahali pake. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini Mwenyezi Mungu akawasukumia ndani ya bahari.
EXO 14:28 Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika.
EXO 14:29 Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.
EXO 14:30 Siku ile Mwenyezi Mungu akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa.
EXO 14:31 Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwa Mwenyezi Mungu aliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakaweka tumaini lao kwake na kwa Musa mtumishi wake.
EXO 15:1 Ndipo Musa na Waisraeli wakamwimbia Mwenyezi Mungu wimbo huu: “Nitamwimbia Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ametukuzwa sana. Farasi na mpanda farasi amewatosa baharini.
EXO 15:2 “Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na wimbo wangu; amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu, Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
EXO 15:3 Mwenyezi Mungu ni shujaa wa vita; Mwenyezi Mungu ndilo jina lake.
EXO 15:4 Magari ya vita ya Farao na jeshi lake amewatosa baharini. Maafisa wa Farao walio bora sana wamezamishwa katika Bahari ya Shamu.
EXO 15:5 Maji yenye kina yamewafunika, wamezama vilindini kama jiwe.
EXO 15:6 Mkono wako wa kuume, Ee Mwenyezi Mungu ulitukuka kwa uweza. Mkono wako wa kuume, Ee Mwenyezi Mungu, ukamponda adui.
EXO 15:7 “Katika ukuu wa utukufu wako, ukawaangusha chini wale waliokupinga. Uliachia hasira yako kali, ikawateketeza kama kapi.
EXO 15:8 Kwa pumzi ya pua yako maji yalijilundika. Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta, vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.
EXO 15:9 Adui alijivuna, ‘Nitawafuatia, nitawapata. Nitagawanya nyara; nitajishibisha kwao. Nitafuta upanga wangu na mkono wangu utawaangamiza.’
EXO 15:10 Lakini ulipuliza kwa pumzi yako, bahari ikawafunika. Wakazama kama risasi kwenye maji makuu.
EXO 15:11 Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu? Ni nani kama Wewe: uliyetukuka katika utakatifu, utishaye katika utukufu, ukitenda maajabu?
EXO 15:12 “Uliunyoosha mkono wako wa kuume na nchi ikawameza.
EXO 15:13 Katika upendo wako usiokoma utawaongoza watu uliowakomboa. Katika nguvu zako utawaongoza hadi makao yako matakatifu.
EXO 15:14 Mataifa watasikia na kutetemeka, uchungu utawakamata Wafilisti.
EXO 15:15 Wakuu wa Edomu wataogopa, viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu, Wakanaani watayeyuka,
EXO 15:16 vitisho na hofu vitawaangukia. Kwa nguvu ya mkono wako watatulia kama jiwe, hadi watu wako wapite, Ee Mwenyezi Mungu, hadi watu uliowanunua wapite.
EXO 15:17 Utawaingiza na kuwapandikiza juu ya mlima wa urithi wako: hapo mahali, Ee Mwenyezi Mungu, ulipopafanya kuwa makao yako, mahali patakatifu, Ee Mwenyezi Mungu, ulipopajenga kwa mikono yako.
EXO 15:18 “Mwenyezi Mungu atatawala milele na milele.”
EXO 15:19 Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini, Mwenyezi Mungu aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini Waisraeli walipita baharini mahali pakavu.
EXO 15:20 Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Haruni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza.
EXO 15:21 Miriamu akawaimbia: “Mwimbieni Mwenyezi Mungu, kwa maana ametukuka sana. Farasi na mpanda farasi amewatosa baharini.”
EXO 15:22 Kisha Musa akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji.
EXO 15:23 Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara.)
EXO 15:24 Kwa hiyo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, “Tunywe nini?”
EXO 15:25 Ndipo Musa akamlilia Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akamwonesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu. Huko Mwenyezi Mungu akawapa amri na sheria na huko akawajaribu.
EXO 15:26 Mungu akasema, “Mkisikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuyafanya yaliyo mema machoni pake, na mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niwaponyaye.”
EXO 15:27 Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.
EXO 16:1 Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri.
EXO 16:2 Huko jangwani, jumuiya yote wakawanung’unikia Musa na Haruni.
EXO 16:3 Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungekufa kwa mkono wa Mwenyezi Mungu huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”
EXO 16:4 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tazama! Nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu.
EXO 16:5 Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.”
EXO 16:6 Kwa hiyo Musa na Haruni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliwatoa Misri,
EXO 16:7 kisha asubuhi mtauona utukufu wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunung’unikie?”
EXO 16:8 Kisha Musa akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Mwenyezi Mungu wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnung’uniki dhidi yetu, bali dhidi ya Mwenyezi Mungu.”
EXO 16:9 Kisha Musa akamwambia Haruni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake Mwenyezi Mungu, kwa maana amesikia manung’uniko yenu.’ ”
EXO 16:10 Haruni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa Mwenyezi Mungu ukitokeza katika wingu.
EXO 16:11 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 16:12 “Nimesikia manung’uniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
EXO 16:13 Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na utando wa umande kuzunguka kambi.
EXO 16:14 Umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya mchanga wa jangwa.
EXO 16:15 Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani. Musa akawaambia, “Huu ndio mkate ambao Mwenyezi Mungu amewapa mle.
EXO 16:16 Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu ameamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema lenu.’ ”
EXO 16:17 Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa; baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu.
EXO 16:18 Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.
EXO 16:19 Kisha Musa akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote hadi asubuhi.”
EXO 16:20 Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Musa, wakahifadhi kiasi fulani hadi asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Musa akawakasirikia.
EXO 16:21 Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka.
EXO 16:22 Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Musa.
EXO 16:23 Musa akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Mwenyezi Mungu: ‘Kesho itakuwa Sabato ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke hadi asubuhi.’ ”
EXO 16:24 Kwa hiyo wakavihifadhi hadi asubuhi, kama Musa alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu.
EXO 16:25 Musa akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu. Hamtapata chochote juu ya nchi leo.
EXO 16:26 Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwa chochote.”
EXO 16:27 Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote.
EXO 16:28 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu hadi lini?
EXO 16:29 Fahamuni kuwa Mwenyezi Mungu amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.”
EXO 16:30 Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.
EXO 16:31 Waisraeli wakaita ile mikate mana. Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama, na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali.
EXO 16:32 Musa akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza Mwenyezi Mungu: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ”
EXO 16:33 Kwa hiyo Musa akamwambia Haruni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za Mwenyezi Mungu ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.”
EXO 16:34 Kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa, hatimaye Haruni aliiweka ile mana ndani ya Sanduku la Ushuhuda ili aweze kuihifadhi.
EXO 16:35 Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani.
EXO 16:36 (Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efa.)
EXO 17:1 Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa.
EXO 17:2 Kwa hiyo wakagombana na Musa wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Musa akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu Mwenyezi Mungu?”
EXO 17:3 Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanung’unika dhidi ya Musa, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?”
EXO 17:4 Kisha Musa akamlilia Mwenyezi Mungu, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.”
EXO 17:5 Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Nenda mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, na uchukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende.
EXO 17:6 Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Musa akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli.
EXO 17:7 Naye akapaita mahali pale Masa na Meriba, kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Mwenyezi Mungu wakisema, “Je, Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi au la?”
EXO 17:8 Waamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu.
EXO 17:9 Musa akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”
EXO 17:10 Kwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Musa alivyomwagiza, nao Musa, Haruni na Huri wakapanda juu ya kilima.
EXO 17:11 Ikawa wakati wote Musa alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda.
EXO 17:12 Mikono ya Musa ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Haruni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Musa, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki thabiti hadi jua lilipozama.
EXO 17:13 Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.
EXO 17:14 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Andika mambo haya katika kitabu ili yakumbukwe, na uhakikishe kwamba Yoshua amesikia, kwa sababu nitafuta kabisa kumbukumbu la Amaleki chini ya mbingu.”
EXO 17:15 Musa akajenga madhabahu na kuiita Yehova Nisi.
EXO 17:16 Musa akasema, “Kwa maana mikono iliinuliwa dhidi ya kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu, sasa Mwenyezi Mungu atakuwa na vita dhidi ya Waamaleki kizazi hadi kizazi.”
EXO 18:1 Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Musa, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Musa na watu wake wa Israeli, pia jinsi Mwenyezi Mungu alivyowatoa Israeli Misri.
EXO 18:2 Baada ya Musa kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea
EXO 18:3 pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Musa alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
EXO 18:4 Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.”
EXO 18:5 Yethro, baba mkwe wa Musa, pamoja na wana wawili wa Musa na mkewe, wakamjia Musa huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu.
EXO 18:6 Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Musa, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.”
EXO 18:7 Kwa hiyo Musa akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia kwenye hema.
EXO 18:8 Musa akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu Mwenyezi Mungu alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani, na jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaokoa.
EXO 18:9 Yethro akafurahishwa sana kusikia kuhusu mambo yote mazuri Mwenyezi Mungu aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri.
EXO 18:10 Yethro akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri.
EXO 18:11 Sasa najua ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.”
EXO 18:12 Kisha Yethro, baba mkwe wa Musa, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Haruni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Musa mbele za Mungu.
EXO 18:13 Siku iliyofuata, Musa akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni.
EXO 18:14 Baba mkwe wake alipoona yote Musa anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi hadi jioni?”
EXO 18:15 Musa akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu.
EXO 18:16 Kila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwaeleza hukumu na sheria zake Mungu.”
EXO 18:17 Baba mkwe wa Musa akamjibu, “Unachofanya sio kizuri.
EXO 18:18 Wewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe.
EXO 18:19 Sasa nisikilize mimi, nitakupa ushauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake.
EXO 18:20 Wafundishe hukumu na sheria zake, na uwaoneshe jinsi wanavyopaswa kuishi, na jinsi wanavyopaswa kuenenda.
EXO 18:21 Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi.
EXO 18:22 Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe.
EXO 18:23 Ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.”
EXO 18:24 Musa akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema.
EXO 18:25 Musa akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya wawe viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi.
EXO 18:26 Wakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Musa, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe.
EXO 18:27 Kisha Musa akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi kwa nchi yake.
EXO 19:1 Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kuondoka Misri, walifika Jangwa la Sinai siku hiyo hiyo.
EXO 19:2 Baada ya kuondoka Refidimu, waliingia katika Jangwa la Sinai na Israeli wakapiga kambi pale jangwani mbele ya mlima.
EXO 19:3 Kisha Musa akakwea kwenda kwa Mungu, naye Mwenyezi Mungu akamwita kutoka ule mlima, akasema, “Hivi ndivyo utakavyosema na nyumba ya Yakobo na utakachowaambia Waisraeli:
EXO 19:4 ‘Ninyi wenyewe mmeona nililofanya huko Misri, jinsi nilivyowabeba kwenye mabawa ya tai na kuwaleta kwangu.
EXO 19:5 Sasa, mkinitii kikamilifu na kutunza agano langu, basi ninyi mtakuwa hazina yangu ya pekee miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu,
EXO 19:6 ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndio maneno utakayosema kwa Waisraeli.”
EXO 19:7 Kwa hiyo Musa akarudi, akawaita wazee wa watu na kuwaambia maneno yote ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amemwamuru ayaseme.
EXO 19:8 Watu wote wakajibu kwa pamoja, “Tutafanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichokisema.” Naye Musa akarudisha majibu yao kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 19:9 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nitakujia katika wingu zito, ili watu wanisikie nikinena nawe na kila mara waweke tumaini lao kwako.” Kisha Musa akamwambia Mwenyezi Mungu yale ambayo watu walikuwa wamesema.
EXO 19:10 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa watu ukawaweke wakfu leo na kesho. Waambie wafue nguo zao
EXO 19:11 na wawe tayari siku ya tatu, kwa sababu siku hiyo, Mwenyezi Mungu atashuka juu ya Mlima Sinai machoni pa watu wote.
EXO 19:12 Weka mipaka kuzunguka mlima kwa ajili ya watu, uwaambie, ‘Mwe waangalifu, msije mkapanda mlimani au kuugusa. Yeyote atakayeugusa mlima atauawa.
EXO 19:13 Hakika atapigwa mawe au kupigwa mishale; mkono wa mtu hautamgusa. Akiwa mwanadamu au mnyama, hataruhusiwa kuishi.’ Ila tu wakati baragumu itakapopigwa kwa mfululizo, ndipo watu wote watakapopanda mlimani.”
EXO 19:14 Baada ya Musa kushuka kutoka mlimani akawaendea watu na kuwaweka wakfu, wakafua nguo zao.
EXO 19:15 Kisha akawaambia watu, “Jitayarisheni kwa ajili ya siku ya tatu. Mwanaume yeyote asimkaribie mwanamke.”
EXO 19:16 Asubuhi ya siku ya tatu kulikuwa na ngurumo na radi pamoja na wingu nene juu ya mlima na mlio mkubwa sana wa tarumbeta. Kila mmoja aliyekuwa kambini akatetemeka.
EXO 19:17 Kisha Musa akawaongoza watu kutoka kambini kukutana na Mungu, nao wakasimama chini ya mlima.
EXO 19:18 Mlima Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi, kwa sababu Mwenyezi Mungu alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi kutoka tanuru kubwa, na mlima wote ukatetemeka kwa kishindo,
EXO 19:19 nayo sauti ya tarumbeta ikawa kubwa zaidi na zaidi. Kisha Musa akazungumza, nayo sauti ya Mungu ikamjibu.
EXO 19:20 Mwenyezi Mungu akashuka juu ya Mlima Sinai na akamwita Musa apande juu mlimani. Kwa hiyo Musa akapanda juu,
EXO 19:21 naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Shuka ukawaonye watu ili wasijipenyeze kutafuta kumwona Mwenyezi Mungu, na wengi wao wakaangamia.
EXO 19:22 Hata makuhani, watakaomkaribia Mwenyezi Mungu ni lazima wajiweke wakfu, la sivyo Mwenyezi Mungu atawaadhibu.”
EXO 19:23 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Watu hawawezi kupanda Mlima Sinai kwa sababu wewe mwenyewe ulituonya ukisema, ‘Wekeni mipaka kuuzunguka mlima na kuutenga kama patakatifu.’ ”
EXO 19:24 Mwenyezi Mungu akajibu, “Shuka ukamlete Haruni pamoja nawe. Lakini makuhani pamoja na watu wasije wakalazimisha kuja kwa Mwenyezi Mungu, nisije nikawaadhibu.”
EXO 19:25 Basi Musa akashuka kwa watu na kuwaambia lile aliloambiwa.
EXO 20:1 Ndipo Mungu akasema maneno haya yote:
EXO 20:2 “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.
EXO 20:3 “Usiwe na miungu mingine ila mimi.
EXO 20:4 Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji.
EXO 20:5 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanaonichukia,
EXO 20:6 lakini ninaonesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaonipenda na kuzishika amri zangu.
EXO 20:7 Usilitaje bure jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
EXO 20:8 Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase.
EXO 20:9 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote,
EXO 20:10 lakini siku ya saba ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
EXO 20:11 Kwa kuwa kwa siku sita, Mwenyezi Mungu aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.
EXO 20:12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
EXO 20:13 Usiue.
EXO 20:14 Usizini.
EXO 20:15 Usiibe.
EXO 20:16 Usimshuhudie jirani yako uongo.
EXO 20:17 Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ng’ombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.”
EXO 20:18 Watu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali
EXO 20:19 na wakamwambia Musa, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.”
EXO 20:20 Musa akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili hofu ya Mungu iwe nanyi kuwasaidia msitende dhambi.”
EXO 20:21 Watu wakabaki mbali, wakati Musa alipolisogelea lile giza nene mahali pale Mungu alipokuwa.
EXO 20:22 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli hivi: ‘Mmejionea wenyewe kwamba nimesema nanyi kutoka mbinguni:
EXO 20:23 Msijifanyizie miungu yoyote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu.
EXO 20:24 “ ‘Utanitengenezea madhabahu ya udongo, na juu yake utoe sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani, kondoo na mbuzi, na ng’ombe wako. Popote nitakapofanya Jina langu liheshimiwe, nitakuja kwenu na kuwabariki.
EXO 20:25 Ikiwa unanitengenezea madhabahu ya mawe, usiijenge kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia chombo cha kuchongea mtaitia unajisi.
EXO 20:26 Usitumie ngazi kupanda kwenye madhabahu yangu, uchi wako usije ukadhihirika kwa chini.’
EXO 21:1 “Hizi ndizo sheria utakazoweka mbele ya Waisraeli.
EXO 21:2 “Ukimnunua mtumwa Mwebrania, atakutumikia kwa miaka sita. Lakini katika mwaka wa saba, atakuwa huru naye ataenda zake pasipo kulipa chochote.
EXO 21:3 Akija peke yake, ataenda huru peke yake, lakini akija na mke, ataondoka pamoja naye.
EXO 21:4 Ikiwa bwana wake alimpatia mke naye akamzalia wana au binti, mwanamke pamoja na watoto wake watakuwa mali ya bwana wake, na huyo mwanaume ataondoka peke yake.
EXO 21:5 “Lakini mtumishi akisema, ‘Ninampenda bwana wangu, mke wangu pamoja na watoto na sitaki kuwa huru,’
EXO 21:6 basi bwana wake atalazimika kumpeleka mbele ya waamuzi. Kisha atampeleka kwenye mlango, au kizingiti na kutoboa sikio lake kwa shazia. Naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote.
EXO 21:7 “Mtu akimuuza binti yake kuwa mtumwa, hataachwa huru kama watumwa wa kiume wanavyoachiwa.
EXO 21:8 Kama hakumpendeza bwana wake aliyemchagua, huyo bwana atamwacha akombolewe. Hatakuwa na haki ya kumuuza kwa wageni, kwa sababu huyo bwana atakuwa amekosa uaminifu.
EXO 21:9 Akimchagua aolewe na mwanawe, ni lazima ampe haki za kuwa binti yake.
EXO 21:10 Ikiwa huyo mwana aliyeozwa mtumwa mwanamke ataoa mwanamke mwingine, ni lazima aendelee kumtosheleza huyo mke wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zote za ndoa.
EXO 21:11 Iwapo hatamtosheleza kwa mambo hayo matatu, huyo mke wa kwanza ataondoka na kuwa huru bila malipo yoyote ya fedha.
EXO 21:12 “Yeyote anayempiga mtu na kumuua ni lazima auawe.
EXO 21:13 Hata hivyo, kama hakumuua kwa makusudi, lakini Mungu akaruhusu itendeke, basi atakimbilia mahali nitakapomchagulia.
EXO 21:14 Lakini kama mtu akipanga na kumuua mwingine kwa makusudi, mwondoe katika madhabahu yangu na kumuua.
EXO 21:15 “Yeyote anayemshambulia baba yake au mama yake ni lazima auawe.
EXO 21:16 “Yeyote anayemteka nyara mwingine akamuuza au akamweka kwake, akikamatwa ni lazima auawe.
EXO 21:17 “Yeyote atakayemlaani baba yake au mama yake ni lazima auawe.
EXO 21:18 “Watu wakigombana, naye mmoja akampiga mwingine kwa jiwe au kwa ngumi yake na hakufa, bali akaugua na kulala kitandani,
EXO 21:19 yule aliyempiga ngumi hatahesabiwa kuwa na hatia ikiwa mwenzake ataamka na kujikongoja kwa fimbo yake, lakini hata hivyo, ni lazima amlipe fidia ya muda aliopoteza na awajibike hadi apone kabisa.
EXO 21:20 “Mtu akimpiga mtumwa wake wa kiume au wa kike kwa fimbo na mtumwa huyo akafa papo hapo, ni lazima aadhibiwe
EXO 21:21 lakini ikiwa mtumwa ataamka baada ya siku moja au mbili, hataadhibiwa, kwa sababu yule mtumwa ni mali yake.
EXO 21:22 “Watu wawili wakipigana na wakamuumiza mwanamke mjamzito, naye akazaa kabla ya wakati lakini hakuna majeraha makubwa, mhalifu atatozwa mali kiasi cha madai ya mume wa yule mwanamke, na jinsi mahakama itakavyoamua.
EXO 21:23 Lakini kukiwa na jeraha kubwa, ni lazima ulipe uhai kwa uhai,
EXO 21:24 jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu,
EXO 21:25 kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, mchubuko kwa mchubuko.
EXO 21:26 “Mtu akimpiga mtumwa wa kiume au wa kike kwenye jicho na kuliharibu, ni lazima amwache huru yule mtumwa kama fidia ya hilo jicho.
EXO 21:27 Akimvunja jino mtumwa wa kiume au wa kike, ni lazima amwache huru huyo mtumwa kwa kufidia hilo jino.
EXO 21:28 “Fahali akimuua mwanaume au mwanamke kwa kumpiga kwa pembe, fahali huyo ni lazima auawe kwa kupigwa mawe, na nyama yake haitaliwa. Lakini mwenye fahali huyo hatawajibika.
EXO 21:29 Lakini hata hivyo, ikiwa huyo fahali amekuwa na tabia ya kupiga kwa pembe, na mwenyewe ameonywa na hakutaka kumfungia naye akamuua mwanaume au mwanamke, huyo fahali ni lazima auawe kwa mawe na mwenye fahali pia auawe.
EXO 21:30 Lakini ikiwa malipo yatatakiwa kwake, basi anaweza kulipa kinachodaiwa ili kuukomboa uhai wake.
EXO 21:31 Sheria hii pia itatumika ikiwa fahali atampiga kwa pembe mwana au binti.
EXO 21:32 Fahali akimpiga mtumwa wa kike au wa kiume, mwenye fahali atalipa shekeli thelathini za fedha kwa bwana mwenye mtumwa, na fahali ni lazima auawe kwa mawe.
EXO 21:33 “Mtu akiacha shimo wazi, ama akachimba shimo kisha asilifukie, na ng’ombe au punda akatumbukia ndani yake,
EXO 21:34 mwenye shimo ni lazima alipe hasara iliyotokea; ni lazima amlipe mwenye mnyama. Mnyama aliyekufa atakuwa wake.
EXO 21:35 “Fahali wa mtu fulani akimuumiza fahali wa mtu mwingine na akafa, watamuuza yule aliye hai na wagawane sawa fedha pamoja na mnyama aliyekufa.
EXO 21:36 Hata hivyo, ikifahamika kwamba fahali huyo alikuwa na tabia ya kupiga kwa pembe na mwenyewe hakumfunga, ni lazima mwenye fahali alipe mnyama kwa mnyama, na mnyama aliyekufa atakuwa wake.
EXO 22:1 “Mtu yeyote akiiba maksai au kondoo na kumchinja au kumuuza, ni lazima alipe ng’ombe watano badala ya maksai mmoja na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.
EXO 22:2 “Mwizi akishikwa akivunja nyumba akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya kumwaga damu;
EXO 22:3 lakini jambo hilo likitokea wakati jua limechomoza, huyo mtu atakuwa na hatia ya kumwaga damu. “Mwizi huyo sharti alipe, lakini kama hana kitu, lazima auzwe ili alipe kwa ajili ya wizi wake.
EXO 22:4 “Mnyama aliyeibwa akikutwa hai mkononi mwake, iwe ni maksai au punda au kondoo, lazima alipe mara mbili.
EXO 22:5 “Mtu akichunga mifugo yake katika shamba au shamba la mizabibu, na akawaachia walishe katika shamba la mtu mwingine, ni lazima alipe vitu bora kutoka shamba lake mwenyewe au kutoka shamba lake la mizabibu.
EXO 22:6 “Moto ukiwaka na kuenea kwenye vichaka vya miiba na kuteketeza miganda ya nafaka au nafaka ambayo haijavunwa, au kuteketeza shamba lote, mtu yule aliyewasha moto lazima alipe.
EXO 22:7 “Mtu akimpa jirani yake fedha au mali nyingine amtunzie, vitu vile vikiibwa kutoka nyumba ya huyo jirani, kama mwizi akishikwa, lazima alipe mara mbili.
EXO 22:8 Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atafika mbele ya waamuzi ili kuthibitisha kuwa hakuchukua mali ya mwenzake.
EXO 22:9 Pakiwepo jambo lolote la mali isiyo halali, iwe ni maksai, punda, kondoo, mavazi, ama mali yoyote iliyopotea, ambayo mtu fulani atasema, ‘Hii ni mali yangu,’ kila upande utaleta shauri lake mbele ya waamuzi. Yule ambaye waamuzi watathibitisha kuwa ana hatia atamlipa jirani yake mara mbili.
EXO 22:10 “Mtu akimpa jirani yake punda, ng’ombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, yule mnyama akifa, au akijeruhiwa, au akiibiwa bila mtu kuona,
EXO 22:11 jambo hili kati yao wawili litaamuliwa kwa kuapa mbele za Mwenyezi Mungu, kwamba huyo jirani hakuhusika na wizi wa mali ya jirani yake. Mwenye mali itampasa akubali jambo hili, na hakuna malipo yatakayohitajika.
EXO 22:12 Lakini kama mnyama aliibwa kwa jirani, itampasa amlipe mwenye mnyama.
EXO 22:13 Kama ameraruliwa na mnyama pori, ataleta mabaki ya mnyama kama ushahidi, naye hatadaiwa mnyama aliyeraruliwa.
EXO 22:14 “Mtu akiazima mnyama kutoka kwa jirani yake, huyo mnyama akiumia au akafa na mwenye mnyama hayupo, lazima amlipe huyo mnyama.
EXO 22:15 Lakini mwenye mnyama akiwa bado ako na mnyama wake, aliyeazima hatalazimika kumlipa. Kama mnyama alikuwa amekodishwa, fedha iliyolipwa kwa kukodisha inatosha kwa kufidia hasara.
EXO 22:16 “Mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa na akalala naye, lazima alipe mahari, kisha atamwoa msichana huyo.
EXO 22:17 Baba wa msichana akikataa katakata kumpa huyo mtu binti yake, bado ni lazima huyo mtu atalipa mahari kama inavyostahili malipo ya ubikira.
EXO 22:18 “Usiruhusu mwanamke mchawi aishi.
EXO 22:19 “Mtu yeyote aziniye na mnyama lazima auawe.
EXO 22:20 “Mtu yeyote anayemtolea mungu mwingine dhabihu isipokuwa Mwenyezi Mungu, lazima aangamizwe.
EXO 22:21 “Usimtendee mgeni vibaya au kumdhulumu, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri.
EXO 22:22 “Usimdhulumu mjane wala yatima.
EXO 22:23 Ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao.
EXO 22:24 Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima.
EXO 22:25 “Ukimkopesha mmoja wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba.
EXO 22:26 Ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama,
EXO 22:27 kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma.
EXO 22:28 “Usimkufuru Mungu au kumlaani mtawala wa watu wako.
EXO 22:29 “Usiache kutoa sadaka kutoka ghala lako au mapipa yako. “Lazima unipe mzaliwa wa kwanza wa wana wako.
EXO 22:30 Ufanye vivyo hivyo kwa ng’ombe wako na kwa kondoo wako. Waache wakae na mama zao kwa siku saba, lakini siku ya nane unipe.
EXO 22:31 “Ninyi mtakuwa watu wangu watakatifu. Kwa hiyo msile nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama pori; mtupieni mbwa.
EXO 23:1 “Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine.
EXO 23:2 “Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu,
EXO 23:3 nawe usimpendelee mtu maskini katika mashtaka yake.
EXO 23:4 “Ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake.
EXO 23:5 Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia.
EXO 23:6 “Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao.
EXO 23:7 Ujiepushe na mashtaka ya uongo, wala usimuue mtu asiye na hatia au mtu mwaminifu, kwa maana sitamhesabia hana hatia yeye aliye na hatia.
EXO 23:8 “Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki.
EXO 23:9 “Usimdhulumu mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri.
EXO 23:10 “Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao,
EXO 23:11 lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.
EXO 23:12 “Kwa siku sita fanya kazi zako, lakini siku ya saba usifanye kazi, ili maksai wako na punda wako wapate kupumzika, naye mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwako, pamoja na mgeni, wapate kuburudishwa.
EXO 23:13 “Uzingatie kutenda kila kitu nilichokuambia. Usiombe kwa majina ya miungu mingine, wala usiyaruhusu kusikika kinywani mwako.
EXO 23:14 “Mara tatu kwa mwaka utanifanyia sikukuu.
EXO 23:15 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu; kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu kama nilivyokuagiza. Fanya jambo hili kwa wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo ulitoka Misri. “Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.
EXO 23:16 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mavuno kwa malimbuko ya mazao yako uliyopanda katika shamba lako. “Utaadhimisha Sikukuu ya Kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka, unapokusanya mavuno yako toka shambani.
EXO 23:17 “Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakuja mbele za Bwana Mungu Mwenyezi.
EXO 23:18 “Msitoe damu ya dhabihu kwangu pamoja na kitu chochote kilicho na chachu. “Mafuta ya mnyama wa sadaka ya sikukuu yangu yasibakizwe hadi asubuhi.
EXO 23:19 “Utaleta malimbuko bora ya ardhi yako katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
EXO 23:20 “Tazama, ninamtuma malaika akutangulie mbele yako akulinde njiani na kukuleta mahali nilipoandaa.
EXO 23:21 Mtamtii na kusikiliza kile anachokisema. Usiasi dhidi yake; hatakusamehe uasi wako, kwa maana Jina langu limo ndani yake.
EXO 23:22 Ukizingatia atakachosema na kufanya yote ninayosema, nitakuwa adui wa adui zako, na nitawapinga wale wakupingao.
EXO 23:23 Malaika wangu atatangulia mbele yako na kukuleta katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nitawafutilia mbali.
EXO 23:24 Usiisujudie miungu yao, au kuiabudu, wala kufuata desturi yao. Utayabomoa kabisa na kuvunjavunja mawe yao ya ibada vipande vipande.
EXO 23:25 Utamwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na baraka zake zitakuwa juu ya vyakula vyako na maji yako. Nami nitaondoa maradhi miongoni mwako,
EXO 23:26 na hakuna atakayeharibu mimba wala atakayekuwa tasa katika nchi yako. Nami nitakupa maisha makamilifu.
EXO 23:27 “Nitapeleka utisho wangu mbele yako na kufadhaisha kila taifa utakalolifikia. Nitafanya adui zako wote wakupe kisogo na kukimbia.
EXO 23:28 Nitatanguliza nyigu mbele yako kuwafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti waondoke njiani mwako.
EXO 23:29 Lakini sitawafukuza kwa mara moja, kwa sababu nchi itabaki ukiwa na wanyama pori watakuwa wengi mno kwako.
EXO 23:30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hadi uwe umeongezeka kiasi cha kutosha kuimiliki nchi.
EXO 23:31 “Nitaweka mipaka ya nchi yako kuanzia Bahari ya Shamu hadi Bahari ya Wafilisti, na kuanzia jangwani hadi Mto. Nitawatia watu wanaoishi katika nchi hizo mikononi mwako, nawe utawafukuza watoke mbele yako.
EXO 23:32 Usifanye agano lolote nao wala na miungu yao.
EXO 23:33 Usiwaache waishi katika nchi yako, la sivyo watakusababisha utende dhambi dhidi yangu, kwa sababu ibada ya miungu yao hakika itakuwa mtego kwako.”
EXO 24:1 Kisha Mungu akamwambia Musa, “Njooni huku juu kwa Mwenyezi Mungu, wewe na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli. Mniabudu kwa mbali,
EXO 24:2 lakini Musa peke yake ndiye atakayemkaribia Mwenyezi Mungu; wengine wasije karibu. Nao watu wasije wakapanda pamoja naye.”
EXO 24:3 Musa alipoenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za Mwenyezi Mungu, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu tutakifanya.”
EXO 24:4 Ndipo Musa akaandika kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amesema. Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli.
EXO 24:5 Kisha akawatuma vijana wanaume Waisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 24:6 Musa akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli, na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu.
EXO 24:7 Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu, nasi tutatii.”
EXO 24:8 Ndipo Musa akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo Mwenyezi Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”
EXO 24:9 Musa na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani,
EXO 24:10 nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu.
EXO 24:11 Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.
EXO 24:12 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Panda uje kwangu huku mlimani na ukae hapa, nami nitakupa vibao vya mawe, vyenye sheria na amri ambazo nimeziandika ziwe mwongozo wao.”
EXO 24:13 Basi Musa akaondoka na Yoshua mtumishi wake, naye Musa akapanda juu kwenye mlima wa Mungu.
EXO 24:14 Musa akawaambia wazee wa Israeli, “Tungojeni hapa hadi tutakapowarudia. Haruni na Huri wako pamoja nanyi, na kila aliye na shauri aweza kuwaendea wao.”
EXO 24:15 Musa alipopanda juu mlimani, wingu liliufunika huo mlima,
EXO 24:16 nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukatua juu ya Mlima Sinai. Kwa muda wa siku sita wingu lilifunika mlima, na siku ya saba Mwenyezi Mungu akamwita Musa kutoka kati ya lile wingu.
EXO 24:17 Kwa Waisraeli utukufu wa Mwenyezi Mungu ulionekana kama moto uteketezao juu ya mlima.
EXO 24:18 Kisha Musa akaingia ndani ya lile wingu alivyokuwa akipanda mlimani. Naye akakaa huko mlimani kwa muda wa siku arobaini, usiku na mchana.
EXO 25:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 25:2 “Waambie Waisraeli waniletee sadaka. Utapokea sadaka kwa niaba yangu kutoka kwa kila mtu ambaye moyo wake wapenda kutoa.
EXO 25:3 “Hizi ndizo sadaka utakazozipokea kutoka kwao: “dhahabu, fedha na shaba;
EXO 25:4 nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu, pamoja na kitani safi; singa za mbuzi;
EXO 25:5 ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo; mbao za mshita;
EXO 25:6 mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezo kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri;
EXO 25:7 na vito vya shohamu na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kizibau na kile kifuko cha kifuani.
EXO 25:8 “Kisha uwaamuru wanitengenezee mahali patakatifu, nami nitakaa miongoni mwao.
EXO 25:9 Tengeneza Maskani hii na vyombo vyake vyote sawasawa na kielelezo nitakachokuonesha.
EXO 25:10 “Nao watatengeneza Sanduku la mbao za mshita, lenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, upana wa dhiraa moja na nusu, na kimo cha dhiraa moja na nusu.
EXO 25:11 Utalifunika hilo Sanduku kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu juu yake kulizunguka.
EXO 25:12 Utalisubu kwa pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine.
EXO 25:13 Kisha utatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu.
EXO 25:14 Utaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba.
EXO 25:15 Hiyo mipiko itabakia daima katika hizo pete za hilo Sanduku; haitaondolewa.
EXO 25:16 Kisha weka ndani ya hilo Sanduku ule Ushuhuda nitakaokupa.
EXO 25:17 “Tengeneza kifuniko cha upatanisho cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, na upana wa dhiraa moja na nusu.
EXO 25:18 Tengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko.
EXO 25:19 Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; watengeneze makerubi hao wawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili.
EXO 25:20 Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, wakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko.
EXO 25:21 Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku.
EXO 25:22 Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walio juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.
EXO 25:23 “Tengeneza meza ya mbao za mshita yenye urefu wa dhiraa mbili, upana wa dhiraa moja, na kimo cha dhiraa moja na nusu.
EXO 25:24 Ifunike kwa dhahabu safi, na kuitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
EXO 25:25 Kisha tengeneza upapi wenye upana wa nyanda moja, na ufanyie ule upapi ukingo wa dhahabu kuuzunguka pande zote.
EXO 25:26 Tengeneza pete nne za dhahabu kwa ajili ya meza hiyo, na uzifungie kwenye pembe nne, pale penye miguu yake minne.
EXO 25:27 Pete hizo zitakuwa karibu na ukingo ule ili kuishikilia ile mipiko itakayotumika kuibebea hiyo meza.
EXO 25:28 Tengeneza mipiko hiyo kwa mbao za mshita, uifunike na dhahabu, uitumie kubeba hiyo meza.
EXO 25:29 Tengeneza sahani zake na masinia yake kwa dhahabu safi, pamoja na bilauri na bakuli zake kwa ajili ya kumiminia sadaka.
EXO 25:30 Utaweka mikate ya Wonesho juu ya meza hii iwe mbele yangu daima.
EXO 25:31 “Tengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi iliyofuliwa vizuri katika kitako chake na ufito wake; vikombe vyake vinavyofanana na ua, matovu yake na maua yake viwe kitu kimoja.
EXO 25:32 Matawi sita yatatokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matatu upande mwingine.
EXO 25:33 Vikombe vitatu vya mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua vitakuwa katika tawi moja, vikombe vitatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yanayotokeza kwenye kile kinara cha taa.
EXO 25:34 Juu ya kinara chenyewe vitakuwa vikombe vinne vya mfano wa maua ya mlozi, yakiwa na matovu yake na maua yake.
EXO 25:35 Tovu moja litakuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyotokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani matawi sita kwa jumla.
EXO 25:36 Matovu na matawi yote yatakuwa kitu kimoja na kile kinara cha taa, yakifuliwa kwa dhahabu safi.
EXO 25:37 “Kisha tengeneza taa zake saba na uziweke juu ya kinara hicho ili ziangaze mbele yake.
EXO 25:38 Mikasi ya kusawazishia tambi, pamoja na masinia, zote zitakuwa za dhahabu safi.
EXO 25:39 Utatumia talanta moja ya dhahabu safi kutengeneza hicho kinara na vifaa vyake vyote.
EXO 25:40 Hakikisha kuwa umevitengeneza sawasawa na ule mfano uliooneshwa kule mlimani.
EXO 26:1 “Tengeneza maskani ya Mungu kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, naye fundi stadi atatarizi makerubi kwenye mapazia hayo.
EXO 26:2 Mapazia yote yatatoshana kwa ukubwa: kila moja litakuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nane, na upana wa dhiraa nne.
EXO 26:3 Unganisha mapazia matano pamoja; fanya vivyo hivyo kwa hayo mengine matano.
EXO 26:4 Tengeneza vitanzi vya kitambaa cha buluu kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu la kwanza, na ufanye vivyo hivyo na pazia la fungu la mwisho.
EXO 26:5 Fanya vitanzi hamsini katika pazia mmoja, na vitanzi vingine hamsini kwenye pazia la mwisho la fungu hilo lingine, navyo vitanzi vyote vielekeane.
EXO 26:6 Kisha tengeneza vifungo hamsini vya dhahabu ili vitumike kufunga na kuunganisha mapazia pamoja kufanya maskani ya Mungu iwe kitu kimoja.
EXO 26:7 “Tengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya kufunika Maskani.
EXO 26:8 Mapazia hayo kumi na moja yatakuwa na kipimo sawa, yaani urefu wa dhiraa thelathini, na upana wa dhiraa nne.
EXO 26:9 Unganisha hayo mapazia matano yawe fungu moja, na hayo mengine sita yawe fungu lingine. Kunja hilo pazia la sita mara mbili mbele ya Maskani.
EXO 26:10 Tengeneza vitanzi hamsini kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu moja, na vivyo hivyo kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu hilo lingine.
EXO 26:11 Kisha tengeneza vifungo hamsini vya shaba, uviingize katika vile vitanzi ili kukaza hema pamoja kuwa kitu kimoja.
EXO 26:12 Kuhusu kile kipande cha ziada cha pazia za hema, nusu ya hilo pazia lililobaki litaning’inizwa upande wa nyuma wa maskani ya Mungu.
EXO 26:13 Mapazia ya hema yatakuwa na urefu wa dhiraa moja zaidi pande zote, sehemu itakayobaki itaning’inia pande zote za Maskani ili kuifunika.
EXO 26:14 Tengeneza kifuniko cha hema kwa ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.
EXO 26:15 “Tengeneza mihimili ya kusimamisha ya mti wa mshita kwa ajili ya maskani ya Mungu.
EXO 26:16 Kila mhimili uwe na urefu wa dhiraa kumi na upana wa dhiraa moja na nusu,
EXO 26:17 zikiwa na ndimi mbili zilizo sambamba kila mmoja na mwingine. Tengeneza mihimili yote ya Maskani jinsi hii.
EXO 26:18 Tengeneza mihimili ishirini kwa ajili ya upande wa kusini wa Maskani,
EXO 26:19 kisha tengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuweka chini ya hiyo mihimili, vitako viwili kwa kila mhimili, kimoja chini ya kila ulimi.
EXO 26:20 Kuhusu upande wa kaskazini wa Maskani, tengeneza mihimili ishirini
EXO 26:21 na vitako arobaini vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
EXO 26:22 Kisha tengeneza mihimili sita kwa mwisho ulio mbali, yaani upande wa magharibi wa Maskani,
EXO 26:23 na pia utengeneze mihimili miwili ya pembe za upande ulio mbali.
EXO 26:24 Katika pembe hizi mbili ni lazima mihimili yake iwe miwili kuanzia chini hadi juu, na iingizwe kwenye pete moja; mihimili ya pembe hizi mbili itafanana.
EXO 26:25 Kwa hiyo kutakuwa mihimili nane, na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
EXO 26:26 “Pia tengeneza mataruma ya mti wa mshita: matano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa Maskani,
EXO 26:27 matano kwa ajili ya mihimili ya upande mwingine, na matano kwa ajili ya mihimili ya upande wa magharibi, mwisho kabisa mwa Maskani.
EXO 26:28 Taruma la katikati litapenya katikati ya mihimili kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine.
EXO 26:29 Funika hiyo mihimili kwa dhahabu, kisha tengeneza pete za dhahabu ambazo zitashikilia hayo mataruma. Pia funika hayo mataruma kwa dhahabu.
EXO 26:30 “Simamisha maskani ya Mungu sawasawa na mfano uliooneshwa kule mlimani.
EXO 26:31 “Tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi atirizi makerubi kwenye hilo pazia.
EXO 26:32 Litundike kwa kulabu za dhahabu kwenye nguzo nne za mti wa mshita ambazo zimefunikwa kwa dhahabu, zikiwa zimesimamishwa kwenye vitako vinne vya fedha.
EXO 26:33 Ning’iniza pazia hilo kwenye vifungo, kisha weka Sanduku la Ushuhuda nyuma ya pazia. Pazia litatenganisha Mahali Patakatifu kutoka Patakatifu pa Patakatifu.
EXO 26:34 Weka kifuniko cha kiti cha rehema juu ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Patakatifu pa Patakatifu.
EXO 26:35 Weka meza nje ya pazia upande wa kaskazini wa maskani ya Mungu, kisha weka kinara cha taa upande wa kusini wa maskani.
EXO 26:36 “Kwa ajili ya ingilio la hema, tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi.
EXO 26:37 Tengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya hilo pazia, na nguzo tano za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Kisha subu vitako vitano vya shaba kwa ajili yake.
EXO 27:1 “Jenga madhabahu ya mbao za mti wa mshita, kimo chake kiwe dhiraa tatu; itakuwa mraba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano.
EXO 27:2 Tengeneza upembe kwenye kila pembe ya hizo pembe nne, ili zile pembe na madhabahu ziwe zimeungana, na ufunike madhabahu kwa shaba.
EXO 27:3 Tengeneza vyombo vyake vyote kwa shaba: vyungu vyake vya kuondolea majivu, masepetu, mabakuli ya kunyunyizia, uma za nyama, na vyombo vya kuchukulia moto.
EXO 27:4 Kisha tengenezea hayo madhabahu wavu wa shaba, na utengeneze pete za shaba kwenye kila moja ya hizo pembe nne za huo wavu.
EXO 27:5 Weka wavu huo chini ya ukingo wa madhabahu ili ufikie nusu ya kimo cha madhabahu.
EXO 27:6 Tengeneza mipiko ya mti wa mshita kwa ajili ya madhabahu, na uifunike kwa shaba.
EXO 27:7 Hiyo mipiko itaingizwa kwenye zile pete ili iwe pande mbili za madhabahu inapobebwa.
EXO 27:8 Tengeneza madhabahu yawe na uvungu ndani yake ukitumia mbao. Utaitengeneza sawasawa na vile ulivyooneshwa mlimani.
EXO 27:9 “Tengeneza ua kwa ajili ya Hema la Kukutania. Upande wa kusini utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja, na utakuwa na mapazia ya kitani iliyosokotwa vizuri,
EXO 27:10 pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
EXO 27:11 Upande wa kaskazini utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja, nao utakuwa na mapazia, pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
EXO 27:12 “Upande wa magharibi wa ua utakuwa na upana wa dhiraa hamsini, nao utakuwa na mapazia, na nguzo kumi na vitako vyake kumi.
EXO 27:13 Upande wa mwisho wa mashariki jua linakochomoza, ua pia utakuwa na upana wa dhiraa hamsini.
EXO 27:14 Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yatakuwa upande mmoja wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
EXO 27:15 Kutakuwa na mapazia ya dhiraa kumi na tano kwa upande mwingine wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
EXO 27:16 “Kuhusu ingilio la ua, weka pazia lenye urefu wa dhiraa ishirini la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Pazia hilo litashikiliwa na nguzo nne na vitako vinne.
EXO 27:17 Nguzo zote zinazozunguka ua zitakuwa na tepe na kulabu za fedha, na vitako vya shaba.
EXO 27:18 Ua utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja na upana wa dhiraa hamsini, ukiwa na mapazia ya kitani yaliyosokotwa vizuri yenye urefu wa dhiraa tano kwenda juu na vitako vya shaba.
EXO 27:19 Vyombo vingine vyote vinavyotumika katika maskani ya Mungu kwa shughuli yoyote, pamoja na vigingi vyote na hata vile vya ua, vitakuwa vya shaba.
EXO 27:20 “Utawaamuru Waisraeli wakuletee mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa kwa ajili ya mwanga ili zile taa ziwake mfululizo.
EXO 27:21 Katika Hema la Kukutania, nje ya pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda, Haruni na wanawe watahakikisha kuwa taa hizo zinawaka kuanzia jioni hadi asubuhi mbele za Mwenyezi Mungu. Hili litakuwa agizo la milele miongoni mwa Waisraeli kwa vizazi vijavyo.
EXO 28:1 “Mtwae Haruni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
EXO 28:2 Mshonee Haruni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima.
EXO 28:3 Waambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Haruni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani.
EXO 28:4 Haya ndio mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kizibau, kanzu, joho lililofumwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Haruni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
EXO 28:5 Waambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi.
EXO 28:6 “Tengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi.
EXO 28:7 Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kizibau.
EXO 28:8 Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.
EXO 28:9 “Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli
EXO 28:10 kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine.
EXO 28:11 Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu,
EXO 28:12 na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kizibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Haruni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za Mwenyezi Mungu.
EXO 28:13 Tengeneza vijalizo vya dhahabu
EXO 28:14 na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.
EXO 28:15 “Tengeneza kifuko cha kifuani kwa ajili ya kufanya maamuzi, kazi ya fundi stadi. Kitengeneze kama kile kizibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa.
EXO 28:16 Kitakuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja na upana wa shibiri moja, na kikunjwe mara mbili.
EXO 28:17 Kisha weka safu nne za vito vya thamani juu yake. Safu ya kwanza itakuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi;
EXO 28:18 katika safu ya pili itakuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi;
EXO 28:19 safu ya tatu itakuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto;
EXO 28:20 na safu ya nne itakuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Yote yatiwe kwenye vijalizo vya dhahabu.
EXO 28:21 Patakuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kwa jina mojawapo la wana wa Israeli, kila kimoja kichorwe kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.
EXO 28:22 “Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani, tengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba.
EXO 28:23 Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili yake, uzifungie kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani.
EXO 28:24 Funga ile mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete zilizo katika pembe za hicho kifuko cha kifuani,
EXO 28:25 nazo zile ncha nyingine za mkufu zifunge kwenye vile vijalizo viwili, na uziunganishe na vile vipande vya mabega vya kile kizibau upande wa mbele.
EXO 28:26 Tengeneza pete mbili za dhahabu, uziunganishe kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibau.
EXO 28:27 Tengeneza pete nyingine mbili za dhahabu, na uziunganishe sehemu ya chini ya vipande vya mabega, upande wa mbele wa kile kizibau, karibu na pindo, juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kizibau.
EXO 28:28 Pete za kifuko cha kifuani zitafungwa kwenye pete zile za kizibau kwa kamba ya buluu, ziunganishwe na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwa kile kizibau.
EXO 28:29 “Wakati wowote Haruni anapoingia Mahali Patakatifu, atakuwa na yale majina ya wana wa Israeli moyoni mwake juu ya kile kifuko cha kifuani cha uamuzi, kama kumbukumbu ya kudumu mbele za Mwenyezi Mungu.
EXO 28:30 Pia weka Urimu na Thumimu ndani ya kifuko cha kifuani, yawe juu ya moyo wa Haruni kila mara aingiapo mbele za Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo siku zote Haruni atakuwa na uwezo kufanya maamuzi kwa ajili ya Waisraeli mbele za Mwenyezi Mungu.
EXO 28:31 “Shona joho la kizibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu,
EXO 28:32 na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike.
EXO 28:33 Tengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga.
EXO 28:34 Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile.
EXO 28:35 Ni lazima Haruni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za Mwenyezi Mungu, ili asije akafa.
EXO 28:36 “Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: Mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 28:37 Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba.
EXO 28:38 Haruni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Haruni daima ili zikubalike kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 28:39 “Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi.
EXO 28:40 Watengenezee wana wa Haruni makoti, mishipi na kofia, ili kuwapa ukuu na heshima.
EXO 28:41 Baada ya kumvika Haruni ndugu yako pamoja na wanawe nguo hizi, wapake mafuta na kuwabariki. Waweke wakfu ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
EXO 28:42 “Watengenezee nguo za ndani za kitani zitakazofunika mwili, kutoka kiunoni hadi mapajani.
EXO 28:43 Haruni na wanawe ni lazima wavae haya kila wanapoingia katika Hema la Kukutania au wanaposogelea madhabahu wakati wa kutoa huduma katika Mahali Patakatifu, ili wasije wakafanya kosa wakafa. “Haya yawe maagizo ya kudumu kwa Haruni na vizazi vyake.
EXO 29:1 “Hili ndilo utakalofanya ili kuwaweka wakfu makuhani ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani: Chukua fahali mchanga mmoja na kondoo dume wawili wasio na dosari.
EXO 29:2 Kutokana na unga laini wa ngano usiotiwa chachu, tengeneza mikate na maandazi yaliyokandwa kwa mafuta, pamoja na mikate myembamba iliyopakwa mafuta.
EXO 29:3 Viwekwe vyote ndani ya kikapu na kuvitoa pamoja na yule fahali na wale kondoo dume wawili.
EXO 29:4 Kisha mlete Haruni na wanawe kwenye lango la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji.
EXO 29:5 Chukua yale mavazi na umvike Haruni koti, joho la kizibau, na kizibau chenyewe, pamoja na kile kifuko cha kifuani. Mfungie hicho kizibau kwa ule mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi.
EXO 29:6 Weka kilemba kichwani mwake na kuweka taji takatifu lishikamane na hicho kilemba.
EXO 29:7 Chukua yale mafuta ya upako umimine juu ya kichwa chake.
EXO 29:8 Walete wanawe na uwavike makoti,
EXO 29:9 pia uwavike zile tepe za kichwani. Ndipo uwafunge Haruni na wanawe mishipi. Ukuhani ni wao kwa agizo la kudumu. Kwa njia hii utamweka wakfu Haruni na wanawe.
EXO 29:10 “Mlete yule fahali mbele ya Hema la Kukutania, naye Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake.
EXO 29:11 Mchinje huyo fahali mbele za Mwenyezi Mungu kwenye mlango wa Hema la Kukutania.
EXO 29:12 Chukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuipaka kwenye pembe za hayo madhabahu kwa kidole chako, na damu iliyobaki uimwage sehemu ya chini ya madhabahu.
EXO 29:13 Kisha chukua mafuta yote ya huyo mnyama ya sehemu za ndani, na kipande kirefu cha ini, na figo zote mbili pamoja na mafuta yake, uviteketeze juu ya madhabahu.
EXO 29:14 Lakini nyama ya huyo fahali na ngozi yake na matumbo yake utavichoma nje ya kambi. Hii ni sadaka ya dhambi.
EXO 29:15 “Chukua mmoja wa wale kondoo dume, naye Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake.
EXO 29:16 Mchinje huyo kondoo dume, chukua damu yake na uinyunyize pande zote za hayo madhabahu.
EXO 29:17 Mkate huyo kondoo dume vipande vipande na usafishe sehemu za ndani pamoja na miguu, ukiviweka pamoja na kichwa na vipande vingine.
EXO 29:18 Kisha mteketeze huyo kondoo dume mzima juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
EXO 29:19 “Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Haruni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake.
EXO 29:20 Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Haruni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu.
EXO 29:21 Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Haruni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Haruni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu.
EXO 29:22 “Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani, kipande kirefu cha ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.)
EXO 29:23 Kutoka kwa kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za Mwenyezi Mungu, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta, na mkate mwembamba.
EXO 29:24 Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe na uviinue mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa.
EXO 29:25 Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa Mwenyezi Mungu, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
EXO 29:26 Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Haruni, kiinue mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako.
EXO 29:27 “Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Haruni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa.
EXO 29:28 Siku zote hili litakuwa fungu la milele kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Haruni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa Mwenyezi Mungu kutoka sadaka zao za amani.
EXO 29:29 “Mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wazao wake ili waweze kupakwa mafuta na kuwekwa wakfu wakiwa wameyavaa.
EXO 29:30 Mwana atakayeingia mahali pake kuwa kuhani na kuja kwenye Hema la Kukutania kuhudumu katika Mahali Patakatifu atayavaa kwa siku saba.
EXO 29:31 “Chukua nyama ya huyo kondoo dume wa kuwaweka wakfu uipike katika Mahali Patakatifu.
EXO 29:32 Haruni na wanawe wataila ile nyama ya huyo kondoo dume pamoja na ile mikate iliyo kwenye hicho kikapu wakiwa hapo ingilio la Hema la Kukutania.
EXO 29:33 Watakula sadaka hizi ambazo upatanisho ulifanywa kwazo kwa ajili ya kuwaweka wakfu na kuwatakasa. Lakini hakuna mtu mwingine yeyote anayeruhusiwa kuvila, kwa sababu ni vitakatifu.
EXO 29:34 Ikiwa nyama yoyote ya huyo kondoo dume iliyotumika kwa kuwaweka wakfu au mkate wowote umebaki hadi asubuhi, vichomwe. Kamwe visiliwe, kwa sababu ni vitakatifu.
EXO 29:35 “Hivyo utamfanyia Haruni na wanawe kila kitu kama vile nilivyokuamuru: Utachukua muda wa siku saba kuwaweka wakfu.
EXO 29:36 Utatoa dhabihu ya fahali kila siku kuwa sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho. Takasa madhabahu kwa kufanya upatanisho kwa ajili yake, nayo uipake mafuta na kuiweka wakfu.
EXO 29:37 Kwa muda wa siku saba fanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuiweka wakfu. Ndipo madhabahu itakuwa takatifu sana na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
EXO 29:38 “Kwa kawaida hiki ndicho utakachotoa juu ya madhabahu kila siku: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja.
EXO 29:39 Utamtoa mmoja asubuhi na huyo mwingine jioni.
EXO 29:40 Pamoja na mwana-kondoo wa kwanza utatoa efa moja ya unga wa ngano laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta yaliyokamuliwa, pamoja na robo ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji.
EXO 29:41 Huyo mwana-kondoo mwingine mtoe dhabihu wakati wa machweo pamoja na sadaka za unga na za kinywaji kama vile ulivyofanya asubuhi, kuwa harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
EXO 29:42 “Kwa vizazi vijavyo itakuwa kawaida kutoa sadaka hii ya kuteketezwa kila mara kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Mwenyezi Mungu. Hapo ndipo nitakapokutana na ninyi na kusema nanyi,
EXO 29:43 Huko ndipo nitakapokutana na Waisraeli, nalo Hema la Kukutania litatakaswa na utukufu wangu.
EXO 29:44 “Kwa hiyo nitaliweka wakfu Hema la Kukutania pamoja na madhabahu, nami nitamweka wakfu Haruni na wanawe ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani.
EXO 29:45 Ndipo nitakapofanya makao miongoni mwa Waisraeli na kuwa Mungu wao.
EXO 29:46 Nao watajua kuwa Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyewatoa Misri ili nipate kufanya makao miongoni mwao. Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
EXO 30:1 “Tengeneza madhabahu kwa mbao za mshita kwa ajili ya kufukizia uvumba.
EXO 30:2 Madhabahu hayo yawe mraba, urefu na upana wake dhiraa moja, na kimo cha dhiraa mbili, nazo pembe zake zitakuwa kitu kimoja nayo.
EXO 30:3 Funika hayo madhabahu juu na pande zote na pia pembe zake kwa dhahabu safi, na uifanyizie ukingo wa dhahabu kuizunguka.
EXO 30:4 Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, ziwe mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko itumikayo kuibebea madhabahu.
EXO 30:5 Tengeneza mipiko kwa miti ya mshita na uifunike kwa dhahabu.
EXO 30:6 Weka hayo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la ule Ushuhuda, lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ule Ushuhuda, mahali nitakapokutana nawe.
EXO 30:7 “Itampasa Haruni kufukiza uvumba wenye harufu nzuri juu ya madhabahu kila siku asubuhi wakati anapowasha zile taa.
EXO 30:8 Itampasa afukize uvumba tena wakati anapowasha taa wakati wa machweo ili uvumba ufukizwe daima mbele za Mwenyezi Mungu kwa vizazi vijavyo.
EXO 30:9 Usifukize uvumba mwingine wowote juu ya madhabahu haya au sadaka nyingine yoyote ya kuteketezwa wala sadaka ya nafaka, wala usimimine sadaka ya kinywaji juu yake.
EXO 30:10 Mara moja kwa mwaka Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe za hayo madhabahu. Upatanisho huu wa mwaka lazima ufanywe kwa damu ya sadaka ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa vizazi vijavyo. Ni takatifu sana kwa Mwenyezi Mungu.”
EXO 30:11 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 30:12 “Utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja lazima alipe kwa Mwenyezi Mungu fidia kwa ajili ya nafsi yake wakati wa kuhesabiwa kwake. Ndipo hakutakuwa na pigo juu yao unapowahesabu.
EXO 30:13 Kila mmoja anayeenda upande wa wale waliokwisha hesabiwa atatoa nusu shekeli, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini. Hii nusu shekeli ni sadaka kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 30:14 Wote wanaovuka, wenye umri wa miaka ishirini au zaidi, watatoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 30:15 Matajiri hawatalipa zaidi ya nusu shekeli, nao maskini hawatatoa pungufu wakati mnatoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya upatanisho wa nafsi zenu.
EXO 30:16 Utapokea fedha ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli na uzitumie kwa ajili ya huduma ya Hema la Kukutania. Itakuwa ni ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Mwenyezi Mungu kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.”
EXO 30:17 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 30:18 “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake.
EXO 30:19 Haruni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji ya hilo sinia.
EXO 30:20 Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto,
EXO 30:21 watanawa mikono na miguu yao ili wasije wakafa. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Haruni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”
EXO 30:22 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 30:23 “Chukua vikolezo bora vifuatavyo: shekeli mia tano za manemane ya maji, shekeli mia mbili na hamsini za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli mia mbili na hamsini za miwa yenye harufu nzuri,
EXO 30:24 shekeli mia tano za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini ya mafuta ya zeituni.
EXO 30:25 Vitengeneze vikolezo hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako.
EXO 30:26 Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda,
EXO 30:27 meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba,
EXO 30:28 madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake.
EXO 30:29 Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
EXO 30:30 “Mpake Haruni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani.
EXO 30:31 Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo.
EXO 30:32 Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu.
EXO 30:33 Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na kuyamimina juu ya mtu ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ”
EXO 30:34 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Chukua vikolezo vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa,
EXO 30:35 pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu.
EXO 30:36 Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali nitakapokutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu.
EXO 30:37 Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 30:38 Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”
EXO 31:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 31:2 “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda,
EXO 31:3 nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi,
EXO 31:4 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba,
EXO 31:5 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi.
EXO 31:6 Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia.
EXO 31:7 “Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake, pia na vifaa vyote vya kwenye hema:
EXO 31:8 meza na vifaa vyake, kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba,
EXO 31:9 madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, sinia na kinara chake,
EXO 31:10 pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Haruni, na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani,
EXO 31:11 pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu.
EXO 31:12 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
EXO 31:13 “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni lazima mzishike Sabato zangu. Hii itakuwa ni ishara kati yangu na ninyi kwa vizazi vijavyo, ili mpate kujua kwamba Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, niwafanyaye ninyi watakatifu.
EXO 31:14 “ ‘Mtaishika Sabato, kwa sababu ni takatifu kwenu. Yeyote atakayeinajisi lazima auawe, yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.
EXO 31:15 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya mapumziko, takatifu kwa Mwenyezi Mungu. Yeyote afanyaye kazi yoyote siku ya Sabato ni lazima auawe.
EXO 31:16 Waisraeli wataishika Sabato, kuiadhimisha kwa vizazi vijavyo kuwa agano la milele.
EXO 31:17 Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita Mwenyezi Mungu aliumba mbingu na dunia, akapumzika siku ya saba, akastarehe.’ ”
EXO 31:18 Mwenyezi Mungu alipomaliza kusema na Musa juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vile vibao viwili vya Ushuhuda, vibao vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.
EXO 32:1 Watu walipoona kuwa Musa amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimsonga Haruni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.”
EXO 32:2 Haruni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu, na binti zenu wamevaa, mkaniletee.”
EXO 32:3 Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Haruni.
EXO 32:4 Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akasubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”
EXO 32:5 Haruni alipoona hili, akajenga madhabahu mbele ya yule ndama na kutangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa Mwenyezi Mungu.”
EXO 32:6 Kwa hiyo siku iliyofuata watu wakaamka asubuhi na mapema na kutoa sadaka za kuteketeza na sadaka za amani. Baadaye watu wakaketi kula na kunywa, nao wakasimama, wakajizamisha katika sherehe.
EXO 32:7 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka.
EXO 32:8 Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kusubu yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ”
EXO 32:9 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu.
EXO 32:10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”
EXO 32:11 Lakini Musa akamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akasema, “Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu?
EXO 32:12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako.
EXO 32:13 Wakumbuke watumishi wako Ibrahimu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote niliyowaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ”
EXO 32:14 Kisha Mwenyezi Mungu akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.
EXO 32:15 Musa akageuka, akateremka kutoka mlimani akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma.
EXO 32:16 Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao.
EXO 32:17 Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Musa, “Kuna sauti ya vita kambini.”
EXO 32:18 Musa akajibu: “Si sauti ya ushindi, wala si sauti ya kushindwa; ni sauti ya kuimba ninayosikia.”
EXO 32:19 Musa alipoikaribia kambi na kuona yule ndama na ile michezo, hasira yake ikawaka, akatupa vile vibao vilivyokuwa mikononi mwake, akavipasua vipande vipande pale chini ya mlima.
EXO 32:20 Kisha akamchukua yule ndama waliokuwa wamemtengeneza na kumchoma kwenye moto, kisha akamsaga kuwa unga, akanyunyiza kwenye maji na kuwafanya Waisraeli wanywe.
EXO 32:21 Musa akamwambia Haruni, “Watu hawa walikufanyia nini, hata ukawaongoza kufanya dhambi kubwa hivyo?”
EXO 32:22 Haruni akamwambia, “Usikasirike bwana wangu. Unajua jinsi watu hawa walivyo tayari kwa maovu.
EXO 32:23 Waliniambia, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza. Kwa kuwa huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.’
EXO 32:24 Kwa hiyo nikawaambia, ‘Yeyote aliye na kito chochote cha dhahabu avue.’ Kisha wakanipa hiyo dhahabu, nami nikaitupa motoni, akatokea huyu ndama!”
EXO 32:25 Musa akaona kuwa watu wameasi, kwa kuwa Haruni alikuwa amewaacha waasi, na hivyo kuwa kichekesho kwa adui zao.
EXO 32:26 Kwa hiyo Musa akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa Mwenyezi Mungu, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.
EXO 32:27 Ndipo alipowaambia, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’ ”
EXO 32:28 Walawi wakafanya kama Musa alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao elfu tatu.
EXO 32:29 Kisha Musa akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.”
EXO 32:30 Siku iliyofuata Musa akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa Mwenyezi Mungu, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”
EXO 32:31 Hivyo Musa akarudi kwa Mwenyezi Mungu na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu.
EXO 32:32 Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kitabu ulichoandika.”
EXO 32:33 Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kitabu changu.
EXO 32:34 Sasa nenda, uongoze hao watu hadi mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”
EXO 32:35 Ndipo Mwenyezi Mungu akawapiga watu kwa ugonjwa wa tauni kwa sababu ya yale waliyoyafanya na ndama yule ambaye alitengenezwa na Haruni.
EXO 33:1 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande hadi nchi niliyomwahidi Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’
EXO 33:2 Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
EXO 33:3 Pandeni mwende katika nchi inayotiririka maziwa na asali. Lakini mimi sitaenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.”
EXO 33:4 Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yoyote.
EXO 33:5 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ”
EXO 33:6 Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima Horebu.
EXO 33:7 Basi Musa alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania”. Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa Mwenyezi Mungu, angeenda hadi Hema la Kukutania, nje ya kambi.
EXO 33:8 Wakati wowote Musa alipoenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Musa hadi aingie kwenye Hema.
EXO 33:9 Kila mara Musa alipoingia ndani ya Hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mwenyezi Mungu akizungumza na Musa.
EXO 33:10 Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la Hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake.
EXO 33:11 Mwenyezi Mungu angezungumza na Musa uso kwa uso, kama vile mtu anavyozungumza na rafiki yake. Kisha Musa angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka kwenye Hema.
EXO 33:12 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’
EXO 33:13 Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.”
EXO 33:14 Mwenyezi Mungu akajibu, “Uso wangu utaenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.”
EXO 33:15 Kisha Musa akamwambia, “Kama Uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa.
EXO 33:16 Mtu yeyote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipoenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”
EXO 33:17 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nitakufanyia jambo lile uliloomba, kwa sababu ninapendezwa nawe, nami ninakujua kwa jina lako.”
EXO 33:18 Kisha Musa akasema, “Basi nioneshe utukufu wako.”
EXO 33:19 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, Mwenyezi Mungu, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”
EXO 33:20 Lakini Mungu akasema, “Hutaweza kuuona uso wangu, kwa kuwa hakuna mtu yeyote awezaye kuniona akaishi.”
EXO 33:21 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Kuna mahali karibu nami ambapo unaweza kusimama juu ya mwamba.
EXO 33:22 Utukufu wangu unapopita, nitakuweka gengeni kwenye mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hadi nitakapokuwa nimepita.
EXO 33:23 Kisha nitaondoa mkono wangu nawe utaona mgongo wangu; lakini kamwe uso wangu hautaonekana.”
EXO 34:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitaandika juu yake maneno yale yaliyokuwa kwenye vile vibao vya kwanza, ulivyovivunja.
EXO 34:2 Uwe tayari asubuhi, kisha upande juu ya Mlima Sinai. Uje mbele zangu kukutana nami huko juu ya mlima.
EXO 34:3 Mtu yeyote asije nawe, wala asionekane mtu popote mlimani; wala kondoo na mbuzi au ng’ombe wasilishe mbele ya huo mlima.”
EXO 34:4 Kwa hiyo Musa akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, naye akapanda juu ya Mlima Sinai asubuhi na mapema, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwagiza, akachukua vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake.
EXO 34:5 Kisha Mwenyezi Mungu akashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake, Mwenyezi Mungu.
EXO 34:6 Mwenyezi Mungu akapita mbele ya Musa, akitangaza, “Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu,
EXO 34:7 akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”
EXO 34:8 Mara Musa akasujudu na kuabudu.
EXO 34:9 Musa akasema, “Ee Bwana, kama nimepata kibali mbele zako, basi Bwana uende pamoja nasi. Ingawa watu hawa ni wenye shingo ngumu, samehe uovu wetu na dhambi yetu, tuchukue kuwa urithi wako.”
EXO 34:10 Kisha Mwenyezi Mungu akasema: “Tazama, ninafanya agano nanyi. Mbele ya watu wako wote nitafanya maajabu ambayo hayajafanyika katika taifa lolote katika ulimwengu wote. Watu wale mnaoishi miongoni mwao wataona jinsi ilivyo ya kushangaza kazi nitakayowafanyia Mimi, Mwenyezi Mungu wenu.
EXO 34:11 Tii yale ninayokuamuru leo. Tazama nawafukuza mbele yako Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
EXO 34:12 Uwe mwangalifu, usifanye agano na wale wanaokaa katika nchi ile unayoiendea, la sivyo watakuwa mtego katikati yako.
EXO 34:13 Bomoa madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia, na ukatekate nguzo zao za Ashera.
EXO 34:14 Usiabudu mungu mwingine, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye jina lake ni Wivu, ni Mungu mwenye wivu.
EXO 34:15 “Uwe mwangalifu usifanye agano na wale watu wanaoishi katika nchi, kwa maana wakati wanapojifanyia ukahaba kwa miungu yao na kuwatolea kafara, watakualika wewe, nawe utakula sadaka za matambiko yao.
EXO 34:16 Unapowachagua baadhi ya binti zao kuwa wake wa wana wenu na binti hao wakajifanyia ukahaba kwa miungu yao, watawaongoza wana wenu kufanya vivyo hivyo.
EXO 34:17 “Usijifanyie sanamu za kusubu.
EXO 34:18 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, kama nilivyokuamuru. Fanya hivi kwa wakati ulioamriwa, katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa kuwa katika mwezi huo ndipo wewe ulipotoka Misri.
EXO 34:19 “Mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo ni mali yangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wote wa kiume wa mifugo yako, ikiwa ni wa ng’ombe au wa kondoo au mbuzi.
EXO 34:20 Utakomboa mzaliwa wa kwanza wa punda kwa mwana-kondoo, lakini kama humkomboi, utavunja shingo yake. Utakomboa wazaliwa wako wa kwanza wote wa kiume. “Mtu yeyote asije mbele zangu mikono mitupu.
EXO 34:21 “Kwa siku sita utafanya kazi, lakini siku ya saba utapumzika, hata ikiwa ni majira ya kulima au ya kuvuna lazima upumzike.
EXO 34:22 “Utaadhimisha Sikukuu ya Majuma kwa malimbuko ya mavuno ya ngano, na Sikukuu ya Mavuno mwishoni mwa mwaka.
EXO 34:23 Mara tatu kwa mwaka wanaume wako wote watakuja mbele za Bwana Mungu Mwenyezi, Mungu wa Israeli.
EXO 34:24 Nitawafukuza mataifa mbele yako na kupanua mipaka ya nchi yako, wala hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yako wakati unapoenda mara tatu kila mwaka kuonana na Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
EXO 34:25 “Usinitolee damu ya dhabihu pamoja na kitu chochote chenye chachu, wala usibakize dhabihu yoyote ya Sikukuu ya Pasaka hadi asubuhi.
EXO 34:26 “Leta matunda ya kwanza yaliyo bora zaidi ya ardhi yako katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.”
EXO 34:27 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Andika maneno haya, kwa maana kulingana na maneno haya, nimefanya agano na wewe pamoja na Israeli.”
EXO 34:28 Musa alikuwa huko pamoja na Mwenyezi Mungu kwa siku arobaini usiku na mchana bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya agano, yaani zile Amri Kumi.
EXO 34:29 Musa alipoteremka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa uking’aa, kwa sababu alikuwa amezungumza na Mwenyezi Mungu.
EXO 34:30 Haruni na Waisraeli wote walipomwona Musa, kuwa uso wake unang’aa, waliogopa kumkaribia.
EXO 34:31 Lakini Musa akawaita, kwa hiyo Haruni na viongozi wote wa jumuiya wakarudi, naye akazungumza nao.
EXO 34:32 Baadaye Waisraeli wote wakamkaribia, naye akawapa amri zote Mwenyezi Mungu alizompa katika Mlima Sinai.
EXO 34:33 Musa alipomaliza kuzungumza nao, akaweka utaji kwenye uso wake.
EXO 34:34 Lakini kila wakati Musa alipoingia mbele za Mwenyezi Mungu kuzungumza naye, aliondoa ule utaji hadi alipotoka nje. Naye alipotoka nje na kuwaambia Waisraeli lile ambalo ameagizwa,
EXO 34:35 waliona kuwa uso wake unang’aa. Kisha Musa angerudisha utaji juu ya uso wake hadi alipoingia ili kuzungumza na Mwenyezi Mungu.
EXO 35:1 Musa akakusanya jumuiya yote ya Waisraeli na kuwaambia, “Haya ndio mambo ambayo Mwenyezi Mungu amewaamuru ninyi mfanye:
EXO 35:2 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba itakuwa takatifu kwenu, Sabato ya mapumziko kwa Mwenyezi Mungu. Yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe.
EXO 35:3 Msiwashe moto mahali popote katika makazi yenu siku ya Sabato.”
EXO 35:4 Musa akaiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloamuru:
EXO 35:5 Toeni sadaka kwa Mwenyezi Mungu kutoka mali mliyo nayo. Kila mmoja aliye na moyo wa kupenda atamletea Mwenyezi Mungu sadaka ya: “dhahabu, fedha na shaba;
EXO 35:6 nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi; singa za mbuzi;
EXO 35:7 ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo; mbao za mshita;
EXO 35:8 mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezo kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri;
EXO 35:9 vito vya shohamu, na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kizibau na kile kifuko cha kifuani.
EXO 35:10 “Wote wenye ujuzi miongoni mwenu inawapasa kuja na kutengeneza kila kitu Mwenyezi Mungu alichoamuru:
EXO 35:11 “Maskani ya Mungu pamoja na hema lake na kifuniko chake, vibanio, mihimili, mataruma, nguzo na vitako;
EXO 35:12 Sanduku la Agano pamoja na mipiko yake, kifuniko cha kiti cha rehema na pazia linalokizuia;
EXO 35:13 meza na mipiko yake, pamoja na vyombo vyake vyote, mikate ya Wonesho;
EXO 35:14 kinara cha taa kwa ajili ya mwanga pamoja na vifaa vyake vyote, taa na mafuta kwa ajili ya mwanga;
EXO 35:15 madhabahu ya kufukiza uvumba pamoja na mipiko yake, mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri; pazia la mlangoni mahali pa kuingilia ndani ya Maskani;
EXO 35:16 madhabahu ya sadaka za kuteketeza pamoja na wavu wake wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote; sinia la shaba pamoja na tako lake;
EXO 35:17 pazia la eneo la ua pamoja na nguzo zake na vitako vyake, na pazia la ingilio la ua;
EXO 35:18 vigingi vya hema kwa ajili ya Maskani pamoja na ua na kamba zake;
EXO 35:19 mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu kwa ajili ya kuhani Haruni, na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.”
EXO 35:20 Ndipo jumuiya yote ya Waisraeli ilipoondoka mbele ya Musa,
EXO 35:21 na kila mmoja aliyependa na ambaye moyo wake ulimsukuma alikuja na kuleta sadaka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kazi katika Hema la Kukutania, kwa ajili ya huduma yake yote na kwa ajili ya mavazi matakatifu.
EXO 35:22 Wote waliopenda, wanaume na wanawake, wakaja wakaleta vito vya dhahabu vya kila aina: vipini, vipuli, pete na mapambo. Wote wakatoa dhahabu zao kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 35:23 Kila mmoja aliyekuwa na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi, au singa za mbuzi, ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, au ngozi za pomboo, wakavileta.
EXO 35:24 Wale waliotoa sadaka ya fedha au shaba wakavileta kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, na kila aliyekuwa na mti wa mshita kwa ajili ya kazi yoyote ile akauleta.
EXO 35:25 Kila mwanamke aliyekuwa na ujuzi alisokota kwa mikono yake na alileta kile alichosokota, iwe ni nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi.
EXO 35:26 Wanawake wote waliopenda na waliokuwa na ujuzi wakasokota singa za mbuzi.
EXO 35:27 Viongozi wakaleta vito vya shohamu pamoja na vito vingine vya thamani kwa ajili ya kuweka kwenye kizibau na kwenye kifuko cha kifuani.
EXO 35:28 Wakaleta pia vikolezo na mafuta ya zeituni kwa ajili ya mwanga, kwa ajili ya mafuta ya upako na kwa ajili ya uvumba wenye harufu nzuri.
EXO 35:29 Waisraeli wote, wanaume na wanawake, waliopenda wakaleta mbele za Mwenyezi Mungu kwa hiari yao wenyewe sadaka kwa ajili ya kazi yote ya Mwenyezi Mungu aliyokuwa amewaagiza kuifanya kupitia kwa Musa.
EXO 35:30 Kisha Musa akawaambia Waisraeli, “Tazameni, Mwenyezi Mungu amemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda,
EXO 35:31 naye amemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, na uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi,
EXO 35:32 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba,
EXO 35:33 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi wa kupendeza.
EXO 35:34 Tena amempa yeye pamoja na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, uwezo wa kufundisha wengine.
EXO 35:35 Amewajaza ustadi wa kufanya kazi za aina zote zinazofanywa na mafundi, na wenye kubuni michoro, pia na watarizi kwa rangi za buluu, zambarau, nyekundu na kitani safi, na wafumaji: wote wakiwa mafundi na wabunifu hodari.
EXO 36:1 Kwa hiyo Bezaleli, Oholiabu na kila mtu Mwenyezi Mungu aliyempa ustadi na uwezo wa kujua jinsi ya kufanya kazi zote za kujenga mahali patakatifu wataifanya hiyo kazi kama vile Mwenyezi Mungu alivyoagiza.”
EXO 36:2 Ndipo Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi ambaye Mwenyezi Mungu alikuwa amempa uwezo na mwenye kupenda kuja na kufanya kazi.
EXO 36:3 Wakapokea kutoka kwa Musa sadaka zote ambazo Waisraeli walikuwa wameleta ili kuifanya kazi ya ujenzi wa Mahali Patakatifu. Nao watu wakaendelea kuleta sadaka za hiari kila asubuhi.
EXO 36:4 Ikafika wakati mafundi wote wenye ujuzi waliokuwa wakiifanya kazi yote ya mahali patakatifu wakasimamisha kazi zao,
EXO 36:5 wakaja na kumwambia Musa, “Watu wanaleta vitu vingi kuliko tunavyohitaji kwa ajili ya kazi hii ambayo Mwenyezi Mungu ameagiza ifanyike.”
EXO 36:6 Ndipo Musa akatoa agizo, nao wakapeleka neno hili katika kambi yote: “Mwanaume au mwanamke yeyote asilete tena kitu chochote kwa ajili ya sadaka ya mahali patakatifu.” Hivyo watu wakazuiliwa kuleta zaidi,
EXO 36:7 kwa sababu walivyokuwa navyo tayari vilitosha na kuzidi kuifanya kazi yote.
EXO 36:8 Watu wote wenye ustadi miongoni mwa wafanyakazi wote wakatengeneza maskani ya Mungu kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, naye fundi stadi akatirizi makerubi kwenye mapazia hayo.
EXO 36:9 Mapazia yote yalitoshana kwa ukubwa: kila moja lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nane, na upana wa dhiraa nne.
EXO 36:10 Wakayaunganisha mapazia matano pamoja, pia wakafanya vivyo hivyo kwa hayo mengine matano.
EXO 36:11 Kisha wakatengeneza vitanzi vya kitambaa cha buluu kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu la kwanza, pia wakafanya vivyo hivyo na pazia la fungu la mwisho.
EXO 36:12 Wakatengeneza pia vitanzi hamsini katika pazia mmoja, na vitanzi vingine hamsini kwenye pazia la mwisho la fungu hilo lingine, navyo vitanzi vyote vikaelekeana.
EXO 36:13 Kisha wakatengeneza vifungo hamsini vya dhahabu, na wakavitumia kufunga na kuunganisha zile fungu mbili za mapazia pamoja ili maskani ya Mungu ipate kuwa kitu kimoja.
EXO 36:14 Wakatengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya kufunika Maskani.
EXO 36:15 Mapazia hayo kumi na moja yalikuwa na kipimo sawa, yaani urefu wa dhiraa thelathini, na upana wa dhiraa nne.
EXO 36:16 Wakaunganisha mapazia matano kuwa fungu moja, na hayo mengine sita kuwa fungu lingine.
EXO 36:17 Kisha wakatengeneza vitanzi hamsini kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu moja, na vivyo hivyo kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu hilo lingine.
EXO 36:18 Wakatengeneza vifungo hamsini vya shaba ili kukaza hema pamoja kuwa kitu kimoja.
EXO 36:19 Kisha wakatengeneza kifuniko cha hema kwa ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.
EXO 36:20 Wakatengeneza mihimili ya kusimamisha ya mti wa mshita kwa ajili ya maskani ya Mungu.
EXO 36:21 Kila mhimili ulikuwa na urefu wa dhiraa kumi, na upana wa dhiraa moja na nusu,
EXO 36:22 zikiwa na ndimi mbili zilizokuwa sambamba kila mmoja na mwingine. Wakatengeneza mihimili yote ya Maskani jinsi hii.
EXO 36:23 Wakatengeneza mihimili ishirini kwa ajili ya upande wa kusini wa Maskani,
EXO 36:24 na wakatengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuweka chini ya hiyo mihimili, vitako viwili kwa kila mhimili, kimoja chini ya kila ulimi.
EXO 36:25 Kwa upande wa kaskazini wa Maskani wakatengeneza mihimili ishirini
EXO 36:26 na vitako arobaini vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
EXO 36:27 Wakatengeneza mihimili sita kwa mwisho ulio mbali, yaani upande wa magharibi wa Maskani,
EXO 36:28 na mihimili miwili ikatengenezwa kwa ajili ya pembe za Maskani za upande uliokuwa mbali.
EXO 36:29 Katika pembe hizi mbili mihimili yake ilikuwa miwili kuanzia chini hadi juu, na ikaingizwa kwenye pete moja; mihimili ya pembe hizi mbili ilifanana.
EXO 36:30 Kwa hiyo kulikuwa na mihimili nane, na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.
EXO 36:31 Wakatengeneza pia mataruma kwa mti wa mshita: matano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa Maskani,
EXO 36:32 matano kwa ajili ya mihimili ya upande mwingine, na matano kwa ajili mihimili ya upande wa magharibi, mwisho kabisa mwa Maskani.
EXO 36:33 Wakatengeneza taruma la katikati, likapenya katikati ya mihimili kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine.
EXO 36:34 Wakaifunika hiyo mihimili kwa dhahabu, na wakatengeneza pete za dhahabu za kushikilia hayo mataruma. Pia wakayafunika hayo mataruma kwa dhahabu.
EXO 36:35 Wakatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi akatirizi makerubi kwenye hilo pazia.
EXO 36:36 Wakatengeneza nguzo nne za mti wa mshita kwa ajili yake na kuzifunika kwa dhahabu. Wakatengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya nguzo hizo, na kusubu vitako vinne vya fedha.
EXO 36:37 Kwa ajili ya ingilio la hema wakatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi.
EXO 36:38 Pia wakatengeneza nguzo tano zenye kulabu. Wakafunika ncha za juu za hizo nguzo pamoja na tepe zake kwa dhahabu, na pia wakatengeneza vitako vyake vitano vya shaba.
EXO 37:1 Bezaleli akatengeneza Sanduku la mbao za mshita: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja na nusu.
EXO 37:2 Akalifunika kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulizungushia ukingo wa dhahabu.
EXO 37:3 Akasubu pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine.
EXO 37:4 Kisha akatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu.
EXO 37:5 Akaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba.
EXO 37:6 Akatengeneza kifuniko cha upatanisho kwa dhahabu safi: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu.
EXO 37:7 Kisha akatengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko.
EXO 37:8 Akatengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; akawatengeneza kuwa kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili.
EXO 37:9 Makerubi hao walikuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, wakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao walielekeana, wakitazama hicho kifuniko.
EXO 37:10 Akatengeneza meza ya mbao za mshita yenye urefu wa dhiraa mbili, upana wa dhiraa moja, na kimo cha dhiraa moja na nusu.
EXO 37:11 Kisha akaifunika kwa dhahabu safi, na kuitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
EXO 37:12 Pia akatengeneza upapi wenye upana wa nyanda moja, na kuufanyia ule upapi ukingo wa dhahabu kuuzunguka pande zote.
EXO 37:13 Akasubu pete nne za dhahabu kwa ajili ya meza hiyo, na kuzifungia kwenye pembe nne, pale penye miguu yake minne.
EXO 37:14 Pete hizo ziliwekwa karibu na ukingo ule ili kuishikilia ile mipiko iliyotumika kuibebea hiyo meza.
EXO 37:15 Mipiko hiyo ya kubebea meza ilitengenezwa kwa mti wa mshita, na ilikuwa imefunikwa kwa dhahabu.
EXO 37:16 Vyombo vyote vya mezani vilitengenezwa kwa dhahabu safi: yaani sahani zake, masinia, na bakuli na bilauri zake kwa ajili ya kumiminia sadaka za vinywaji.
EXO 37:17 Akatengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi iliyofuliwa vizuri katika kitako chake na ufito wake; vikombe vyake vilivyofanana na ua, matovu na maua vilikuwa kitu kimoja.
EXO 37:18 Matawi sita yalitokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matatu upande mwingine.
EXO 37:19 Vikombe vitatu vya mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua vilikuwa katika tawi moja, vikombe vitatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yaliyotokeza kwenye kile kinara cha taa.
EXO 37:20 Juu ya kinara chenyewe kulikuwa vikombe vinne vya mfano wa maua ya mlozi yakiwa na matovu yake na maua yake.
EXO 37:21 Tovu moja lilikuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyotokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani matawi sita kwa jumla.
EXO 37:22 Matovu na matawi yote yalikuwa kitu kimoja na kile kinara cha taa, yakiwa yamefuliwa kwa dhahabu safi.
EXO 37:23 Akatengeneza taa zake saba, na pia mikasi ya kusawazishia tambi, pamoja na masinia, zote kwa dhahabu safi.
EXO 37:24 Akatengeneza kinara hicho cha taa pamoja na vifaa vyake vyote kutumia talanta moja ya dhahabu safi.
EXO 37:25 Akatengeneza madhabahu ya kufukizia uvumba kwa mbao za mshita. Ilikuwa ya mraba, urefu na upana wake dhiraa moja, na kimo cha dhiraa mbili, nazo pembe zake zilikuwa kitu kimoja nayo.
EXO 37:26 Akafunika hayo madhabahu juu na pande zote na pia zile pembe zake kwa dhahabu safi, na akayafanyizia ukingo wa dhahabu kuizunguka.
EXO 37:27 Akatengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, zikiwa mbili kila upande, za kushikilia mipiko iliyotumika kubebea madhabahu.
EXO 37:28 Akatengeneza mipiko kwa miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.
EXO 37:29 Pia akatengeneza mafuta matakatifu ya upako, na uvumba safi wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato.
EXO 38:1 Akatengeneza madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa mbao za mti wa mshita, kimo chake dhiraa tatu; nayo ilikuwa mraba, urefu wake dhiraa tano, na upana wa dhiraa tano.
EXO 38:2 Akatengeneza upembe kwenye kila pembe ya hizo pembe nne, ili zile pembe na madhabahu zikawa zimeungana, akafunika madhabahu kwa shaba.
EXO 38:3 Akatengeneza vyombo vyake vyote kwa shaba: vyungu vyake vya kuondolea majivu, masepetu, mabakuli ya kunyunyizia, uma za nyama na vyombo vya kuchukulia moto.
EXO 38:4 Akatengeneza wavu wa shaba chini ya ukingo wa madhabahu ili ufikie nusu ya kimo cha madhabahu.
EXO 38:5 Akasubu pete za shaba za kushikilia ile mipiko kwa ajili ya zile pembe nne za huo wavu wa shaba.
EXO 38:6 Akatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuifunika kwa shaba.
EXO 38:7 Akaiingiza ile mipiko kwenye zile pete, ili iwe pande mbili za madhabahu kwa ajili ya kuibeba. Akaitengeneza madhabahu yenye uvungu ndani yake akitumia mbao.
EXO 38:8 Akatengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kutoka kwa vioo vya shaba vilivyotolewa na wanawake waliohudumu pale ingilio la Hema la Kukutania.
EXO 38:9 Kisha akatengeneza ua. Upande wa kusini ulikuwa na urefu wa dhiraa mia moja, na ulikuwa na mapazia ya kitani iliyosokotwa vizuri,
EXO 38:10 pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
EXO 38:11 Upande wa kaskazini ulikuwa na urefu wa dhiraa mia moja, pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
EXO 38:12 Upande wa mwisho wa magharibi ulikuwa na upana wa dhiraa hamsini, na ulikuwa na mapazia, na nguzo kumi na vitako vyake kumi, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
EXO 38:13 Upande wa mwisho wa mashariki jua linakochomoza, pia ulikuwa na upana wa dhiraa hamsini.
EXO 38:14 Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yalikuwa upande mmoja wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
EXO 38:15 Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yalikuwa upande mwingine wa ingilio la ua, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
EXO 38:16 Mapazia yote yaliyozunguka ua yalikuwa ya kitani iliyosokotwa vizuri.
EXO 38:17 Vitako vya nguzo vilikuwa vya shaba. Kulabu na tepe juu ya nguzo zilikuwa za fedha, na ncha zake zilifunikwa kwa fedha. Kwa hiyo nguzo zote za ua zilikuwa na tepe za fedha.
EXO 38:18 Pazia la ingilio la ua lilikuwa la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Pazia hilo lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini kama zile za kwenye ua, na kimo chake kilikuwa dhiraa tano,
EXO 38:19 likiwa na nguzo nne na vitako vinne vya shaba. Kulabu zake na tepe zake zilikuwa za fedha, na ncha zake zilikuwa zimefunikwa kwa fedha.
EXO 38:20 Vigingi vyote vya maskani ya Mungu na vya ua ulioizunguka vilikuwa vya shaba.
EXO 38:21 Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika kwa ajili ya ujenzi wa maskani ya Mungu, hiyo Maskani ya Ushuhuda, ambavyo vilitayarishwa na Walawi kama alivyoagiza Musa, chini ya usimamizi wa Ithamari, mwana wa kuhani Haruni.
EXO 38:22 (Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru Musa,
EXO 38:23 akiwa pamoja na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kubuni michoro, mtarizi kwa rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi.)
EXO 38:24 Jumla ya dhahabu iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa kwa ajili ya kazi ya mahali patakatifu ilikuwa na uzito wa talanta ishirini na tisa na shekeli mia saba na thelathini (730), kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.
EXO 38:25 Fedha iliyopatikana kutokana na jumuiya ya watu waliohesabiwa ilikuwa yenye uzito wa talanta mia moja na shekeli elfu moja mia saba sabini na tano (1,775), kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.
EXO 38:26 Kila mtu alitoa beka moja, ambayo ni sawa na nusu shekeli ya fedha, kwa kazi ya mahali patakatifu, kutoka kwa kila mtu aliyekuwa amehesabiwa mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi, ambao jumla yao walikuwa wanaume elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550).
EXO 38:27 Talanta hizo mia moja za fedha zilitumika kusubu vile vitako mia moja kwa ajili ya mahali patakatifu na pazia: vitako mia moja kwa talanta mia, yaani talanta moja kwa kila kitako.
EXO 38:28 Akatumia hizo shekeli elfu moja mia saba sabini na tano (1,775) kutengeneza kulabu za nguzo, kufunika ncha za nguzo, na kutengeneza vitanzi vyake.
EXO 38:29 Shaba iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa ilikuwa na uzito wa talanta sabini na shekeli elfu mbili mia nne.
EXO 38:30 Akaitumia hiyo shaba kutengeneza vitako vya ingilio la Hema la Kukutania, madhabahu ya shaba pamoja na ule wavu wake na vyombo vyake vyote,
EXO 38:31 vile vitako vya ule ua uliozunguka na vile vya ingilio, na vigingi vyote vya maskani ya Mungu, pamoja na vigingi vya ule ua uliozunguka.
EXO 39:1 Kutokana na nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu akatengeneza mavazi yaliyofumwa kwa ajili ya kuhudumu katika mahali patakatifu. Pia akamshonea Haruni mavazi matakatifu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:2 Akatengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kitani iliyosokotwa vizuri.
EXO 39:3 Akafua vipande vyembamba vya dhahabu kwa nyundo na kutengeneza nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi, kazi ya fundi stadi.
EXO 39:4 Akatengeneza vipande vya mabegani vya kizibau, vilivyounganishwa kwenye pembe zake mbili kwa ajili ya kufungia.
EXO 39:5 Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi ulifanana nacho: ulikuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao ulitengenezwa kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:6 Akatengeneza vito vya shohamu vilivyowekwa katika vijalizo vya dhahabu, navyo vilichorwa na majina ya wana wa Israeli kama vile muhuri huchorwa.
EXO 39:7 Kisha akavifungia kwenye vipande vya mabega ya kizibau kuwa vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:8 Akatengeneza kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi. Akakitengeneza kama kile kizibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa.
EXO 39:9 Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja na upana wa shibiri moja, nacho kilikunjwa mara mbili.
EXO 39:10 Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za vito vya thamani. Safu ya kwanza ilikuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi;
EXO 39:11 safu ya pili ilikuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi;
EXO 39:12 safu ya tatu ilikuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto;
EXO 39:13 katika safu ya nne ilikuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Vito hivyo vilitiwa kwenye vijalizo vya dhahabu.
EXO 39:14 Kulikuwa na vito kumi na viwili, kimoja kwa kila jina la wana wa Israeli; kila kimoja kilichorwa kama muhuri kwa jina mojawapo la makabila yale kumi na mawili.
EXO 39:15 Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani alitengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba.
EXO 39:16 Akatengeneza vijalizo viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, na kuzifungia pete hizo kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani.
EXO 39:17 Akafunga hiyo mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete katika pembe za hicho kifuko cha kifuani,
EXO 39:18 nazo zile ncha nyingine za mkufu akazifunga kwenye vile vijalizo viwili, na kuziunganisha na vile vipande vya mabega vya kile kizibau upande wa mbele.
EXO 39:19 Akatengeneza pete mbili za dhahabu na kuziunganisha kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibau.
EXO 39:20 Kisha akatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuziunganisha sehemu ya chini ya vipande vya mabega upande wa mbele wa kile kizibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kizibau.
EXO 39:21 Akafunga pete za hicho kifuko cha kifuani kwenye pete za kizibau kwa kamba ya buluu, wakiziunganisha na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwa kile kizibau, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:22 Akashona joho la kizibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, kazi ya mfumaji,
EXO 39:23 na lilikuwa na nafasi ya shingo katikati ya joho lile iliyofanana na ukosi, na utepe ulioshonwa kuizunguka nafasi hiyo ili isichanike.
EXO 39:24 Akatengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na ya kitani iliyosokotwa vizuri kuzunguka pindo la hilo joho.
EXO 39:25 Kisha akatengeneza vikengele vya dhahabu safi na kuviunganisha kuzunguka pindo hilo kati ya hayo makomamanga.
EXO 39:26 Hivyo vikengele na makomamanga vilipishana kuzunguka upindo wa joho ili livaliwe kwa kuhudumu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:27 Pia akamtengenezea Haruni na wanawe makoti ya kitani safi, kazi ya mfumaji,
EXO 39:28 na kilemba cha kitani safi, tepe za kichwani za kitani, na nguo za ndani za kitani iliyosokotwa vizuri.
EXO 39:29 Mshipi ulikuwa wa kitani iliyosokotwa vizuri ya rangi ya buluu, na zambarau, na nyekundu, kazi ya mtarizi, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:30 Kisha akatengeneza lile bamba, taji takatifu, kwa dhahabu safi na kuchora juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: Mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu.
EXO 39:31 Kisha wakalifunga kwa kamba ya rangi ya buluu ili kuliunganisha na kile kilemba, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:32 Kwa hiyo kazi yote ya maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania, ikakamilika. Waisraeli wakafanya kila kitu sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 39:33 Ndipo wakaleta maskani ya Mungu kwa Musa: hema pamoja na vifaa vyake vyote, vibanio vyake, mihimili yake, mataruma yake, nguzo na vitako vyake;
EXO 39:34 kifuniko cha ngozi za kondoo dume kilichotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la kufunikia;
EXO 39:35 Sanduku la Ushuhuda pamoja na mipiko yake na kiti cha rehema,
EXO 39:36 meza pamoja na vyombo vyake vyote, na mikate ya Wonesho;
EXO 39:37 kinara cha taa cha dhahabu safi, safu zake za taa pamoja na vifaa vyake vyote, pamoja na mafuta kwa ajili ya taa;
EXO 39:38 madhabahu ya dhahabu, mafuta ya upako, uvumba wenye harufu nzuri, na pazia la ingilio la hema;
EXO 39:39 madhabahu ya shaba, pamoja na wavu wa shaba, nguzo zake na vyombo vyake vyote, sinia, na tako lake;
EXO 39:40 mapazia ya ua pamoja na nguzo na vitako vyake, pia na pazia la ingilio la ua; kamba zake na vigingi vya hema kwa ajili ya ua; vyombo vyote vilivyohitajiwa kwa ajili ya maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania;
EXO 39:41 na mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Haruni na mavazi ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.
EXO 39:42 Waisraeli walikuwa wamefanya kazi yote sawasawa na vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwagiza Musa.
EXO 39:43 Musa akakagua kazi na kuona kuwa walikuwa wameifanya sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameagiza. Kwa hiyo Musa akawabariki.
EXO 40:1 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
EXO 40:2 “Simika maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza.
EXO 40:3 Weka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake.
EXO 40:4 Kisha ingiza kinara cha taa na uweke taa zake juu yake.
EXO 40:5 Weka madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba mbele ya Sanduku la Ushuhuda kisha uweke pazia kwenye lango la maskani ya Mungu.
EXO 40:6 “Weka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa mbele ya lango la maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania;
EXO 40:7 weka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, na uweke maji ndani yake.
EXO 40:8 Tengeneza ua kuzunguka maskani ya Mungu, na uweke pazia penye ingilio la ua.
EXO 40:9 “Chukua mafuta ya upako, upake maskani ya Mungu pamoja na kila kitu kilicho ndani yake; iweke wakfu pamoja na vitu vyote vilivyomo, nayo itakuwa takatifu.
EXO 40:10 Kisha yapake mafuta hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka pamoja na vifaa vyake vyote; weka wakfu madhabahu nayo yatakuwa takatifu sana.
EXO 40:11 Paka sinia mafuta pamoja na kishikilio chake na uviweke wakfu.
EXO 40:12 “Mlete Haruni na wanawe kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji.
EXO 40:13 Kisha mvike Haruni yale mavazi matakatifu, umpake mafuta na kumweka wakfu ili apate kunitumikia kama kuhani.
EXO 40:14 Walete wanawe na uwavike makoti.
EXO 40:15 Kisha wapake mafuta kama ulivyomtia baba yao, ili nao pia wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Kupakwa mafuta kwao kutakuwa kwa ajili ya ukuhani utakaoendelea kwa vizazi vyote vijavyo.”
EXO 40:16 Musa akafanya kila kitu sawa kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
EXO 40:17 Kwa hiyo maskani ya Mungu ilisimikwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, katika mwaka wa pili.
EXO 40:18 Musa alipoweka wakfu maskani ya Mungu, aliweka vitako mahali pake, akasimamisha mihimili, akatia mataruma na kusimamisha nguzo.
EXO 40:19 Kisha akalitandaza hema juu ya maskani ya Mungu na kuifunika hema, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
EXO 40:20 Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake.
EXO 40:21 Kisha Musa akalileta Sanduku ndani ya maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
EXO 40:22 Musa akaweka meza ndani ya Hema la Kukutania, upande wa kaskazini mwa maskani ya Mungu nje ya pazia
EXO 40:23 na kupanga mikate juu yake mbele za Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
EXO 40:24 Akaweka kinara cha taa ndani ya Hema la Kukutania mkabala na meza upande wa kusini mwa maskani ya Mungu
EXO 40:25 na kuziweka taa mbele za Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
EXO 40:26 Musa akaweka madhabahu ya dhahabu ndani ya Hema la Kukutania mbele ya pazia,
EXO 40:27 na akafukiza uvumba wenye harufu nzuri, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
EXO 40:28 Kisha akaweka pazia kwenye ingilio la maskani ya Mungu.
EXO 40:29 Musa akaweka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa karibu na ingilio la maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
EXO 40:30 Akaweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, akaweka maji ndani yake kwa ajili ya kunawia.
EXO 40:31 Naye Musa, Haruni na wanawe wakayatumia kwa kunawia mikono na miguu yao.
EXO 40:32 Wakanawa kila walipoingia katika Hema la Kukutania au walipoikaribia madhabahu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
EXO 40:33 Kisha Musa akatengeneza ua kuizunguka maskani ya Mungu na madhabahu, na pia akaweka pazia kwenye ingilio la huo ua. Hivyo Musa akaikamilisha kazi.
EXO 40:34 Ndipo wingu likafunika Hema la Kukutania, na utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaijaza maskani ya Mungu.
EXO 40:35 Musa hakuweza kuingia ndani ya Hema la Kukutania kwa sababu wingu lilikuwa limetua juu ya Hema, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaijaza maskani ya Mungu.
EXO 40:36 Katika safari yote ya Waisraeli, kila wakati wingu lilipoinuka kutoka juu ya maskani ya Mungu, wangeondoka;
EXO 40:37 lakini kama wingu halikuinuka, hawakuondoka, hadi siku lilipoinuka.
EXO 40:38 Kwa hiyo wingu la Mwenyezi Mungu lilikuwa juu ya maskani ya Mungu mchana, na moto ulikuwa katika hilo wingu wakati wa usiku, machoni pa nyumba yote ya Israeli siku zote za safari zao.
LEV 1:1 Mwenyezi Mungu akamwita Musa na kusema naye kutoka Hema la Kukutania, akamwambia,
LEV 1:2 “Sema na Waisraeli, uwaambie, ‘Yeyote miongoni mwenu anayeleta sadaka kwa Mwenyezi Mungu, alete mnyama kama sadaka yake kutoka kundi lake la ng’ombe, au la kondoo na mbuzi.
LEV 1:3 “ ‘Ikiwa sadaka hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kutoka kundi la ng’ombe, atamtoa ng’ombe dume asiye na dosari. Ni lazima amlete kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili aweze kukubalika kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 1:4 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya kuteketezwa, nayo itakubaliwa kwa niaba yake ili kufanya upatanisho kwa ajili yake.
LEV 1:5 Atamchinja yule fahali mchanga mbele za Mwenyezi Mungu, kisha wana wa Haruni walio makuhani wataleta damu na kuinyunyiza pande zote za madhabahu yaliyo penye ingilio la Hema la Kukutania.
LEV 1:6 Ataichuna hiyo sadaka ya kuteketezwa na kuikata vipande vipande.
LEV 1:7 Wana wa Haruni kuhani wataweka moto juu ya madhabahu na kupanga kuni juu ya huo moto.
LEV 1:8 Kisha hao wana wa Haruni walio makuhani watapanga vile vipande vya nyama, pamoja na kichwa na mafuta ya huyo mnyama, juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu.
LEV 1:9 Ataziosha sehemu za ndani za yule mnyama pamoja na miguu yake kwa maji; naye kuhani atavichoma vyote juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 1:10 “ ‘Ikiwa sadaka ni sadaka ya kuteketezwa kutoka kundi la kondoo au mbuzi, atamtoa dume asiye na dosari.
LEV 1:11 Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu mbele za Mwenyezi Mungu, nao wana wa Haruni walio makuhani watanyunyizia damu yake pande zote za madhabahu.
LEV 1:12 Atamkata vipande vipande, naye kuhani atavipanga, pamoja na kichwa na mafuta ya mnyama juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu.
LEV 1:13 Ataosha sehemu za ndani na miguu kwa maji, naye kuhani atavileta vyote na kuvichoma juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 1:14 “ ‘Ikiwa sadaka inayotolewa kwa Mwenyezi Mungu ni sadaka ya kuteketezwa ya ndege, atamtoa hua au kinda la njiwa.
LEV 1:15 Kuhani atamleta kwenye madhabahu, naye atamvunja shingo na kumnyofoa kichwa na kumchoma juu ya madhabahu. Damu yake itachuruzishwa ubavuni mwa madhabahu.
LEV 1:16 Ataondoa kifuko cha chakula pamoja na uchafu wake na kuvitupa upande wa mashariki wa madhabahu, mahali pale penye majivu.
LEV 1:17 Atampasua na kumweka wazi katika mabawa yake, lakini asimwachanishe kabisa, kisha kuhani ataichoma juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 2:1 “ ‘Mtu yeyote aletapo sadaka ya nafaka kwa Mwenyezi Mungu, sadaka yake itakuwa ya unga laini. Atamimina mafuta juu yake, aweke uvumba juu yake,
LEV 2:2 naye atapeleka kwa makuhani wana wa Haruni. Kuhani atachukua konzi moja unga laini na mafuta, pamoja na uvumba wote, na kuviteketeza kama sehemu ya kumbukumbu juu ya madhabahu, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 2:3 Sadaka ya nafaka iliyobaki ni ya Haruni na wanawe; ni sehemu ya sadaka iliyo takatifu sana iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
LEV 2:4 “ ‘Kama utaleta sadaka ya nafaka iliyookwa, itakuwa ya unga laini: iwe maandazi yaliyotengenezwa bila kutiwa chachu, yaliyochanganywa na mafuta, au mikate myembamba iliyotengenezwa bila kutiwa chachu na iliyopakwa mafuta.
LEV 2:5 Iwapo sadaka yako ya nafaka imeandaliwa kwenye kikaango, itakuwa ni ya unga laini uliochanganywa na mafuta, bila chachu.
LEV 2:6 Vunjavunja na kumimina mafuta juu yake; hii ni sadaka ya nafaka.
LEV 2:7 Ikiwa sadaka yako ya nafaka imepikwa kwenye sufuria, itatengenezwa kwa unga laini na mafuta.
LEV 2:8 Ilete hiyo sadaka ya nafaka iliyotengenezwa kwa vitu hivi kwa Mwenyezi Mungu; mkabidhi kuhani, ambaye ataipeleka madhabahuni.
LEV 2:9 Naye atatoa ile sehemu ya kumbukumbu katika hiyo sadaka ya nafaka, na kuiteketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 2:10 Sadaka ya nafaka iliyobaki ni ya Haruni na wanawe; ni sehemu ya sadaka takatifu sana kati ya sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
LEV 2:11 “ ‘Kila sadaka ya nafaka unayoleta kwa Mwenyezi Mungu ni lazima ifanywe bila kutiwa chachu, kwa kuwa huna ruhusa kuchoma chachu yoyote au asali katika sadaka inayotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
LEV 2:12 Unaweza kuzileta kwa Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya malimbuko, lakini haziwezi kutolewa juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kupendeza.
LEV 2:13 Koleza sadaka zako zote za nafaka kwa chumvi. Usiache kuweka chumvi ya agano la Mungu wako katika sadaka zako za nafaka; weka chumvi kwenye sadaka zako zote.
LEV 2:14 “ ‘Ukileta malimbuko ya sadaka ya nafaka kwa Mwenyezi Mungu, utatoa masuke yaliyopondwa ya nafaka mpya iliyookwa kwa moto.
LEV 2:15 Weka mafuta na uvumba juu yake; ni sadaka ya nafaka.
LEV 2:16 Kuhani atateketeza ile sehemu ya kumbukumbu katika hiyo sadaka ya nafaka iliyopondwa, na mafuta, pamoja na uvumba wote, kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
LEV 3:1 “ ‘Ikiwa mtu anatoa sadaka ya amani, naye akatoa ng’ombe, akiwa dume au jike, atamleta mnyama asiye na dosari mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 3:2 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka yake na kumchinja penye ingilio la Hema la Kukutania. Ndipo makuhani, wana wa Haruni, watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu.
LEV 3:3 Katika hiyo sadaka ya amani ataleta sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto: sehemu za ndani na mafuta yote yanayoungana nazo,
LEV 3:4 figo zote pamoja na mafuta yaliyozifunika karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini; utayaondoa pamoja na figo.
LEV 3:5 Kisha wana wa Haruni wataiteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa iliyo juu ya kuni zinazowaka; ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 3:6 “ ‘Akitoa kondoo au mbuzi kutoka kundi kuwa sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu, atamtoa dume au jike asiye na dosari.
LEV 3:7 Akimtoa mwana-kondoo, atamleta mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 3:8 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka yake, naye atamchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Haruni watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu.
LEV 3:9 Katika hiyo sadaka ya amani ataleta dhabihu iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto: mafuta yake, mafuta yote ya mkia uliokatwa karibu na uti wa mgongo, mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani au yale yanayounganika nazo,
LEV 3:10 figo mbili pamoja na mafuta yanayozifunika yaliyo karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo utayaondoa pamoja na figo.
LEV 3:11 Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu viwe chakula, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
LEV 3:12 “ ‘Ikiwa sadaka yake ni mbuzi, ataileta mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 3:13 Ataweka mkono wake juu ya kichwa chake na kumchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Haruni watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu.
LEV 3:14 Katika ile sadaka anayotoa, atatoa hii sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu: mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani na yale yanayoungana nazo,
LEV 3:15 figo zote mbili pamoja na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo.
LEV 3:16 Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu viwe chakula, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri. Mafuta yote ya mnyama ni ya Mwenyezi Mungu.
LEV 3:17 “ ‘Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mnapoishi: Msile mafuta yoyote ya mnyama wala damu.’ ”
LEV 4:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 4:2 “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote afanyapo dhambi bila kukusudia na akatenda lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu:
LEV 4:3 “ ‘Ikiwa kuhani aliyepakwa mafuta amefanya dhambi na kuwaletea watu hatia, lazima alete kwa Mwenyezi Mungu fahali mchanga asiye na dosari, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya dhambi aliyotenda.
LEV 4:4 Atamkabidhi huyo fahali kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Mwenyezi Mungu. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo fahali na kumchinja mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 4:5 Kisha kuhani huyo aliyepakwa mafuta atachukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuileta katika Hema la Kukutania.
LEV 4:6 Atachovya kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza sehemu yake mara saba mbele za Mwenyezi Mungu, mbele ya pazia la mahali patakatifu.
LEV 4:7 Kisha kuhani atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri iliyo mbele za Mwenyezi Mungu katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ya huyo fahali ataimwaga chini ya hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
LEV 4:8 Atayaondoa mafuta yote ya fahali huyo wa sadaka ya dhambi: mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani au zile zinazounganika nazo,
LEV 4:9 figo zote mbili na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo zote,
LEV 4:10 kama vile mafuta yanavyoondolewa kutoka kwa ng’ombe aliyetolewa sadaka ya amani. Kisha kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
LEV 4:11 Lakini ngozi ya huyo fahali na nyama zake zote, pamoja na kichwa na miguu yake, sehemu za ndani na matumbo,
LEV 4:12 yaani sehemu nyingine zote zilizobaki za huyo fahali, lazima azitoe nje ya kambi hadi mahali palipo safi, ambapo majivu hutupwa; naye atamchoma kwa moto wa kuni juu ya lundo la majivu.
LEV 4:13 “ ‘Ikiwa jumuiya yote ya Israeli watatenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu, hata kama jumuiya hawafahamu jambo hilo, wana hatia.
LEV 4:14 Wanapotambua dhambi waliyoitenda, lazima kusanyiko walete fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi, na kuikabidhi mbele ya Hema la Kukutania.
LEV 4:15 Wazee wa jumuiya wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali mbele za Mwenyezi Mungu, naye huyo fahali atachinjwa mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 4:16 Kisha kuhani aliyepakwa mafuta ataingiza sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya Hema la Kukutania.
LEV 4:17 Atachovya kidole chake kwenye damu na kuinyunyiza mara saba mbele za Mwenyezi Mungu mbele ya hilo pazia.
LEV 4:18 Atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu yaliyo mbele za Mwenyezi Mungu katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu ya kuteketezea sadaka, penye ingilio la Hema la Kukutania.
LEV 4:19 Atayaondoa mafuta yote ya yule fahali na kuyateketeza juu ya madhabahu,
LEV 4:20 naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa.
LEV 4:21 Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya.
LEV 4:22 “ ‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu, Mungu wake, ana hatia.
LEV 4:23 Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete beberu asiye na dosari kuwa sadaka yake.
LEV 4:24 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za Mwenyezi Mungu. Hii ni sadaka ya dhambi.
LEV 4:25 Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu.
LEV 4:26 Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa.
LEV 4:27 “ ‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia, na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Mwenyezi Mungu, yeye ana hatia.
LEV 4:28 Atakapofahamishwa dhambi aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kuwa sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda.
LEV 4:29 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka.
LEV 4:30 Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu.
LEV 4:31 Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.
LEV 4:32 “ ‘Akileta mwana-kondoo kuwa sadaka yake ya dhambi, atamleta jike asiye na dosari.
LEV 4:33 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo mwana-kondoo na kumchinja kwa ajili ya sadaka ya dhambi mahali ambako sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa.
LEV 4:34 Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia juu ya pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na ile damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu.
LEV 4:35 Ataondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kutoka kwa mwana-kondoo wa sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu juu ya zile sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.
LEV 5:1 “ ‘Ikiwa mtu ametenda dhambi kwa sababu hakusema alipotakiwa kutoa ushahidi hadharani kuhusu jambo aliloona au kujua habari zake, yeye atastahili adhabu.
LEV 5:2 “ ‘Au mtu akitambua kuwa ana hatia, kama vile akigusa kitu chochote ambacho ni najisi, iwe ni mizoga ya wanyama pori walio najisi, au ya wanyama wafugwao walio najisi, au ya viumbe vinavyotambaa ardhini, hata akiwa hana habari, amekuwa najisi na mwenye hatia.
LEV 5:3 “ ‘Au akigusa kitu kilicho kichafu kinachotokana na binadamu, kitu chochote kile kinachoweza kumfanya awe najisi, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia.
LEV 5:4 “ ‘Au kama mtu ameapa kufanya kitu chochote bila kufikiri, kiwe chema au kibaya, kwa vyovyote mtu aweza kuapa bila kujali, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia.
LEV 5:5 “ ‘Mtu yeyote atakapokuwa na hatia katika mojawapo ya haya, ni lazima akiri ni kwa njia gani ametenda dhambi,
LEV 5:6 na kama adhabu ya dhambi aliyoitenda, ni lazima alete kwa Mwenyezi Mungu kondoo jike au mbuzi jike kutoka kundi lake kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yake.
LEV 5:7 “ ‘Lakini kama huyo mtu hataweza kumtoa mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda wawili wa njiwa kwa Mwenyezi Mungu ikiwa ni adhabu kwa ajili ya dhambi yake: mmoja wa hao ndege kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wa pili kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
LEV 5:8 Atawaleta kwa kuhani, ambaye atamtoa kwanza ndege mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Atamvunja shingo na kuacha kichwa chake kikining’inia,
LEV 5:9 naye atanyunyiza sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi kwenye pembe za madhabahu. Damu iliyobaki lazima ichuruzwe chini ya madhabahu. Hii ni sadaka ya dhambi.
LEV 5:10 Kisha kuhani atamtoa yule ndege wa pili kama sadaka ya kuteketezwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa, na hivyo kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.
LEV 5:11 “ ‘Ikiwa basi hawezi kupata hua wawili au makinda wawili wa njiwa, ataleta sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kamwe asiweke mafuta wala uvumba juu yake, kwa sababu ni sadaka ya dhambi.
LEV 5:12 Atauleta unga kwa kuhani, ambaye atachukua konzi moja kama sehemu ya kumbukumbu na atauteketeza kwenye madhabahu juu ya sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. Hii ni sadaka ya dhambi.
LEV 5:13 Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yoyote ya hizo alizotenda, naye atasamehewa. Sadaka iliyobaki itakuwa ya kuhani, kama ilivyokuwa ile sadaka ya nafaka.’ ”
LEV 5:14 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
LEV 5:15 “Mtu anapokiuka na kutenda dhambi pasipo kukusudia kuhusu mojawapo ya mambo matakatifu ya Mwenyezi Mungu, huyo mtu ataleta kwa Mwenyezi Mungu kama adhabu kondoo dume mmoja kutoka kundi lake, asiye na dosari, na mwenye thamani halisi ya fedha kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Hii ni sadaka ya hatia.
LEV 5:16 Ni lazima alipe kwa yale aliyoshindwa kufanya kuhusu vitu vitakatifu, kwa kuongeza sehemu ya tano ya thamani ile na kuitoa yote kwa kuhani, ambaye atamfanyia upatanisho kwa huyo kondoo dume kama sadaka ya dhambi, naye atasamehewa.
LEV 5:17 “Kama mtu akifanya dhambi, na kutenda yaliyokatazwa katika mojawapo ya amri za Mwenyezi Mungu, hata ikiwa hajui, yeye ana hatia na anastahili adhabu.
LEV 5:18 Atamletea kuhani kama sadaka ya hatia kondoo dume kutoka kundi lake, kondoo asiye na dosari na mwenye thamani halisi. Kwa njia hii, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa kosa alilotenda bila kukusudia, naye atasamehewa.
LEV 5:19 Hii ni sadaka ya hatia; amekuwa na hatia kwa kufanya kosa dhidi ya Mwenyezi Mungu.”
LEV 6:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
LEV 6:2 “Mtu yeyote akitenda dhambi, naye si mwaminifu kwa Mwenyezi Mungu kwa kumdanganya jirani yake kuhusu kitu fulani alichokabidhiwa, au kimeachwa chini ya utunzaji wake, au kimeibwa, au kama akimdanganya,
LEV 6:3 au akiokota mali iliyopotea na akadanganya kuihusu, au kuapa kwa uongo, au kama akitenda dhambi yoyote ambayo watu wanaweza kuitenda;
LEV 6:4 wakati akitenda dhambi hizo na kuwa mwenye hatia, ni lazima arudishe kile alichokuwa amekiiba au amekichukua kwa dhuluma, au alichokuwa amekabidhiwa, au mali iliyokuwa imepotea akaipata,
LEV 6:5 au chochote alichokuwa amekiapia kwa uongo. Lazima akirudishe kikamilifu, na aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, vyote ampe mwenye mali siku ile anapeleka sadaka yake ya hatia.
LEV 6:6 Kisha kama adhabu lazima amletee kuhani, yaani kwa Mwenyezi Mungu, kuwa sadaka yake ya hatia, kondoo dume kutoka kundi lake asiye na dosari, mwenye thamani kamili.
LEV 6:7 Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Mwenyezi Mungu, naye atasamehewa kwa kosa lolote katika mambo aliyoyatenda lililomfanya kuwa na hatia.”
LEV 6:8 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
LEV 6:9 “Mpe Haruni na wanawe agizo hili: ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa: Sadaka ya kuteketezwa itabaki kwenye moto juu ya madhabahu usiku kucha, hadi asubuhi, nao moto lazima uwe unaendelea kuwaka juu ya madhabahu.
LEV 6:10 Kisha kuhani atavaa mavazi yake ya kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani mwilini wake, na aondoe majivu ya sadaka ya kuteketezwa ambayo moto umeteketeza juu ya madhabahu, na kuyaweka kando ya madhabahu.
LEV 6:11 Kisha atayavua mavazi haya na kuvaa mengine, naye achukue yale majivu nje ya kambi na kuyapeleka mahali palipo safi.
LEV 6:12 Moto ulio juu ya madhabahu lazima uwe unaendelea kuwaka; kamwe usizimike. Kila asubuhi kuhani ataongeza kuni na kupanga sadaka ya kuteketezwa juu ya moto, na kuteketeza mafuta ya wanyama wa sadaka za amani juu yake.
LEV 6:13 Moto lazima uendelee kuwaka juu ya madhabahu mfululizo, kamwe usizimike.
LEV 6:14 “ ‘Haya ndio masharti ya sadaka ya nafaka: Wana wa Haruni wataileta mbele za Mwenyezi Mungu, mbele za madhabahu.
LEV 6:15 Kuhani atachukua konzi moja ya unga laini na mafuta, pamoja na uvumba wote ulio juu ya sadaka ya nafaka, na kuteketeza sehemu hiyo ya kumbukumbu juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 6:16 Haruni na wanawe watakula sehemu iliyobaki, lakini italiwa bila kutiwa chachu mahali patakatifu, nao wataila katika ua wa Hema la Kukutania.
LEV 6:17 Kamwe haitaokwa na chachu; nimewapa kama fungu lao la sadaka iliyotolewa kwangu kwa moto. Ni takatifu sana, kama vile ilivyo sadaka ya dhambi na ya hatia.
LEV 6:18 Kila mwanaume mzao wa Haruni aweza kuila. Ni fungu lake milele la sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto kwa vizazi vijavyo. Chochote kinachozigusa kitakuwa kitakatifu.’ ”
LEV 6:19 Tena Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 6:20 “Hii ni sadaka ambayo Haruni na wanawe wanapaswa kuleta kwa Mwenyezi Mungu siku atakapopakwa mafuta: sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kama sadaka ya kawaida ya nafaka. Nusu yake ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni.
LEV 6:21 Iandae kwa mafuta kwenye kikaango; ilete ikiwa imechanganywa vizuri, na utoe hiyo sadaka ya nafaka ikiwa imevunjwa vipande vipande kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 6:22 Mwanawe atakayeingia mahali pake kama kuhani aliyepakwa mafuta ndiye atakayeiandaa. Ni fungu la milele la Mwenyezi Mungu, nalo litateketezwa kabisa.
LEV 6:23 Kila sadaka ya nafaka ya kuhani itateketezwa kabisa; kamwe haitaliwa.”
LEV 6:24 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 6:25 “Mwambie Haruni na wanawe: ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya dhambi: Sadaka ya dhambi itachinjiwa mbele za Mwenyezi Mungu mahali sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa; ni takatifu sana.
LEV 6:26 Kuhani anayeitoa ndiye atakayeikula; itakuliwa katika mahali patakatifu, katika ua wa Hema la Kukutania.
LEV 6:27 Chochote kitakachogusa nyama yoyote ya hiyo sadaka kitakuwa kitakatifu; na kama damu ya hiyo sadaka itadondokea juu ya vazi, lazima ulifulie mahali patakatifu.
LEV 6:28 Chungu cha udongo kitakachopikiwa nyama lazima kivunjwe, lakini kama imepikiwa kwenye chombo cha shaba, chombo hicho kitasuguliwa na kusuuzwa kwa maji.
LEV 6:29 Kila mwanaume katika jamaa ya kuhani aweza kula nyama hiyo; ni takatifu sana.
LEV 6:30 Lakini kila sadaka ya dhambi ambayo damu yake imeletwa ndani ya Hema la Kukutania kufanya upatanisho katika Mahali Patakatifu kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe.
LEV 7:1 “ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya hatia, ambayo ni takatifu sana:
LEV 7:2 Sadaka ya hatia itachinjiwa mahali pale sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa, nayo damu yake itanyunyizwa pande zote za madhabahu.
LEV 7:3 Mafuta yake yote yatatolewa sadaka: mafuta ya mkia, na mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani,
LEV 7:4 figo zote mbili pamoja na mafuta yanayozifunika karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo yataondolewa pamoja na hizo figo.
LEV 7:5 Kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. Hii ni sadaka ya hatia.
LEV 7:6 Mwanaume yeyote katika jamaa ya kuhani aweza kuila, lakini lazima iliwe mahali patakatifu; ni takatifu sana.
LEV 7:7 “ ‘Sheria hii ya sadaka ya hatia ni sawasawa na ile ya sadaka ya dhambi: Nyama ya yule mnyama aliyetolewa sadaka ni ya yule kuhani anayesimamia ibada ya upatanisho.
LEV 7:8 Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya mtu yeyote anaweza kuichukua ngozi ya mnyama yule aliyetolewa iwe yake.
LEV 7:9 Kila sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni au kupikwa katika sufuria au katika kikaango itakuwa ya kuhani anayeitoa.
LEV 7:10 Nayo kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au iko kavu, itakuwa ya wana wa Haruni, nayo itagawanywa sawa kati yao.
LEV 7:11 “ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya amani ambayo mtu aweza kuileta kwa Mwenyezi Mungu:
LEV 7:12 “ ‘Ikiwa mtu atatoa sadaka ya amani kwa ajili ya kuonesha shukrani, pamoja na sadaka hii ya shukrani, atatoa maandazi yasiyotiwa chachu yaliyochanganywa na mafuta, mikate myembamba isiyotiwa chachu na iliyopakwa mafuta, na maandazi ya unga laini uliokandwa vizuri na kuchanganywa na mafuta.
LEV 7:13 Pamoja na sadaka yake ya amani ya shukrani, ataleta sadaka ya maandazi yaliyotengenezwa kwa chachu.
LEV 7:14 Ataleta moja ya kila aina ya andazi kuwa sadaka, matoleo kwa Mwenyezi Mungu; hii ni ya kuhani anayenyunyiza damu ya sadaka ya amani.
LEV 7:15 Nyama ya sadaka ya amani kwa ajili ya shukrani lazima iliwe siku hiyo hiyo inapotolewa; hutabakiza kitu chochote hadi asubuhi.
LEV 7:16 “ ‘Lakini ikiwa sadaka yake ni kwa ajili ya nadhiri au ni sadaka ya hiari, sadaka hiyo italiwa siku hiyo inapotolewa, lakini chochote kinachobakia kinaweza kuliwa kesho yake.
LEV 7:17 Nyama yoyote ya sadaka inayobaki hadi siku ya tatu lazima iteketezwe kwa moto.
LEV 7:18 Kama nyama yoyote ya sadaka ya amani italiwa siku ya tatu, Mwenyezi Mungu hataikubali. Haitahesabiwa kwake huyo aliyeitoa, kwa kuwa ni najisi. Mtu atakayekula sehemu yake yoyote atahesabiwa hatia.
LEV 7:19 “ ‘Nyama inayogusa chochote kilicho najisi kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe kwa moto. Kuhusu nyama nyingine, mtu yeyote aliyetakaswa anaweza kuila.
LEV 7:20 Lakini kama mtu yeyote najisi akila nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu, huyo mtu lazima akatiliwe mbali na watu wake.
LEV 7:21 Kama mtu yeyote akigusa kitu kilicho najisi, iwe ni uchafu wa mwanadamu, au mnyama najisi, au kitu chochote kilicho najisi, kitu cha kuchukiza, kisha akala nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”
LEV 7:22 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 7:23 “Waambie Waisraeli: ‘Msile mafuta yoyote ya ng’ombe, kondoo wala mbuzi.
LEV 7:24 Mafuta ya mnyama aliyekutwa amekufa au ameraruliwa na wanyama pori yanaweza kutumika kwa kazi nyingine yoyote, lakini kamwe msiyale.
LEV 7:25 Mtu yeyote alaye mafuta ya mnyama ambaye ametolewa sadaka kwa Mwenyezi Mungu kwa moto ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
LEV 7:26 Popote mtakapoishi, kamwe msile damu ya ndege yeyote wala ya mnyama.
LEV 7:27 Mtu yeyote atakayekula damu lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”
LEV 7:28 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 7:29 “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote aletaye sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu ataleta sehemu ya sadaka hiyo kama dhabihu yake kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 7:30 Ataleta sadaka kwa mikono yake mwenyewe iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto; ataleta mafuta ya huyo mnyama pamoja na kidari, naye atainua hicho kidari mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa.
LEV 7:31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Haruni na wanawe.
LEV 7:32 Paja la kulia la sadaka zako za amani utampa kuhani kama matoleo.
LEV 7:33 Mwana wa Haruni atoaye damu na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani ndiye atakayepewa paja hilo la kulia kuwa fungu lake.
LEV 7:34 Kutoka kwa sadaka za amani za Waisraeli, mimi Mungu nimepokea kidari kile kilichoinuliwa, pamoja na lile paja lililotolewa, nami nimevitoa kwa kuhani Haruni na wanawe kuwa fungu lao la milele kutoka kwa Waisraeli.’ ”
LEV 7:35 Hii ndiyo sehemu ya sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, ambazo zilitengwa kwa ajili ya Haruni na wanawe siku ile walipowekwa wakfu ili kumtumikia Mwenyezi Mungu katika kazi ya ukuhani.
LEV 7:36 Siku ile walipopakwa mafuta, Mwenyezi Mungu aliagiza kwamba Waisraeli wawape hili kama fungu lao la milele kwa vizazi vijavyo.
LEV 7:37 Basi haya ndio masharti kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia, sadaka ya kuwekwa wakfu, na sadaka ya amani,
LEV 7:38 ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Musa juu ya Mlima Sinai siku ile alipowaagiza Waisraeli walete sadaka zao kwa Mwenyezi Mungu, katika Jangwa la Sinai.
LEV 8:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 8:2 “Waletee Haruni na wanawe mavazi yao, mafuta ya upako, fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume wawili na kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu.
LEV 8:3 Kisha kusanya watu wote kwenye ingilio la Hema la Kukutania.”
LEV 8:4 Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza, na watu wakakusanyika kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
LEV 8:5 Musa akawaambia kusanyiko, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu ameagiza lifanyike.”
LEV 8:6 Kisha Musa akamleta Haruni na wanawe mbele, akawaosha kwa maji.
LEV 8:7 Akamvika Haruni koti, akamfunga mshipi, akamvika joho, na kumvalisha kizibau. Pia akamfunga hicho kizibau kiunoni mwake kwa mshipi uliofumwa kwa ustadi.
LEV 8:8 Akaweka kifuko cha kifuani juu yake, na kuweka Urimu na Thumimu kwenye hicho kifuko.
LEV 8:9 Kisha akamvika Haruni kilemba kichwani pake, akaweka lile bamba la dhahabu, lile taji takatifu, upande wa mbele wa kilemba, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
LEV 8:10 Kisha Musa akachukua mafuta ya upako, na kuipaka maskani ya Mungu na kila kitu kilichokuwamo; hivyo akaviweka wakfu.
LEV 8:11 Akanyunyiza sehemu ya mafuta juu ya madhabahu mara saba, akaipaka madhabahu mafuta na vyombo vyake vyote, pamoja na sinia na kinara chake, ili kuviweka wakfu.
LEV 8:12 Akamimina sehemu ya hayo mafuta ya upako kichwani mwa Haruni, akampaka mafuta ili kumweka wakfu.
LEV 8:13 Kisha akawaleta wana wa Haruni mbele, akawavika makoti, akawafunga mishipi na kuwavika vilemba, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
LEV 8:14 Kisha akamtoa fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nao Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
LEV 8:15 Musa akamchinja yule fahali na akachukua sehemu ya hiyo damu, kisha kwa kidole chake akaitia kwenye pembe zote za madhabahu ili kutakasa madhabahu. Akaimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Kwa hiyo akayaweka wakfu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu.
LEV 8:16 Pia Musa akachukua mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani, na kipande kirefu cha ini, na figo zote mbili pamoja na mafuta yake, akayateketeza juu ya madhabahu.
LEV 8:17 Lakini fahali, ikiwa pamoja na ngozi yake na nyama yake na sehemu zake za ndani na matumbo, akaiteketeza nje ya kambi, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
LEV 8:18 Kisha Musa akamleta kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
LEV 8:19 Ndipo Musa akamchinja yule kondoo dume na kunyunyiza damu yake pande zote za madhabahu.
LEV 8:20 Musa akamkata yule kondoo dume vipande vipande na kukiteketeza kichwa, vile vipande na yale mafuta.
LEV 8:21 Kisha akamsafisha sehemu za ndani na miguu kwa maji, na kumteketeza yule kondoo dume mzima juu ya madhabahu kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
LEV 8:22 Kisha Musa akamleta yule kondoo dume wa pili, ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
LEV 8:23 Musa akamchinja yule kondoo dume, akaichukua sehemu ya damu yake na kuipaka juu ya ncha ya sikio la kuume la Haruni, na juu ya kidole gumba cha mkono wake wa kuume na juu ya kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
LEV 8:24 Pia Musa akawaleta hao wana wa Haruni mbele, akaipaka sehemu ya hiyo damu kwenye ncha za masikio yao ya kuume, juu ya vidole gumba vya mikono yao ya kuume, na juu ya vidole vikubwa vya miguu yao ya kuume. Kisha akanyunyiza damu pande zote za madhabahu.
LEV 8:25 Akachukua mafuta ya mnyama, mafuta ya mkia, mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani, kipande kirefu cha ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, na paja la kulia.
LEV 8:26 Kisha kutoka kwa kikapu cha mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichokuwa mbele za Mwenyezi Mungu, akachukua andazi moja, na jingine lililotengenezwa kwa mafuta, na mkate mwembamba; akaviweka hivi vyote juu ya mafungu ya mafuta ya mnyama, na juu ya lile paja la kulia.
LEV 8:27 Akaviweka hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe, na kuviinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa.
LEV 8:28 Kisha Musa akavichukua kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kuwa sadaka ya kuwekwa wakfu, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
LEV 8:29 Kisha akachukua kidari, kilicho fungu la Musa la kondoo dume kwa ajili ya kuwekwa wakfu, na kukiinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
LEV 8:30 Kisha Musa akachukua sehemu ya mafuta ya upako, na sehemu ya damu kutoka madhabahu, na kuvinyunyiza juu ya Haruni na mavazi yake, na juu ya wanawe na mavazi yao. Kwa hiyo akamweka Haruni na mavazi yake wakfu, pamoja na wanawe na mavazi yao.
LEV 8:31 Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe, “Pikeni hiyo nyama kwenye ingilio la Hema la Kukutania, na muile hapo pamoja na mkate kutoka kikapu cha sadaka ya kuweka wakfu, kama nilivyoagiza: ‘Haruni na wanawe wataila.’
LEV 8:32 Kisha mteketeze nyama na mikate iliyobaki.
LEV 8:33 Msitoke kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa muda wa siku saba, hadi siku zenu za kuwekwa wakfu ziwe zimetimia, kwa kuwa muda wenu wa kuwekwa wakfu utakuwa siku saba.
LEV 8:34 Lile lililofanyika leo liliagizwa na Mwenyezi Mungu ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
LEV 8:35 Lazima mkae kwenye ingilio la Hema la Kukutania usiku na mchana kwa siku saba, na kufanya lile Mwenyezi Mungu analolitaka, ili msife; kwa kuwa hilo ndilo nililoamriwa.”
LEV 8:36 Kwa hiyo Haruni na wanawe wakafanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichoamuru kupitia kwa Musa.
LEV 9:1 Katika siku ya nane, Musa akawaita Haruni na wanawe, na wazee wa Israeli.
LEV 9:2 Akamwambia Haruni, “Chukua ndama dume kwa ajili ya sadaka yako ya dhambi, na kondoo dume kwa sadaka yako ya kuteketezwa, wote wawili wasiwe na dosari, nao uwalete mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 9:3 Kisha waambie Waisraeli: ‘Chukueni beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na ndama na mwana-kondoo, wote wawili wawe wa umri wa mwaka mmoja, na wasio na dosari, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa,
LEV 9:4 na pia maksai na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya amani, ili kutoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka ya nafaka iliyochanganywa na mafuta. Kwa kuwa leo Mwenyezi Mungu atawatokea.’ ”
LEV 9:5 Wakavileta vile vitu Musa alivyowaagiza mbele ya Hema la Kukutania, na kusanyiko lote wakakaribia na kusimama mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 9:6 Ndipo Musa akasema, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu alilowaagiza mlifanye, ili utukufu wa Mwenyezi Mungu upate kuonekana kwenu.”
LEV 9:7 Musa akamwambia Haruni, “Njoo madhabahuni utoe dhabihu ya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, kuwa upatanisho kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya watu. Kisha utoe sadaka ya upatanisho kwa ajili ya watu, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoagiza.”
LEV 9:8 Hivyo Haruni akaja madhabahuni na kumchinja yule ndama kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe.
LEV 9:9 Wanawe wakamletea damu, naye akachovya kidole chake katika hiyo damu, akaitia kwenye pembe za madhabahu, nayo damu iliyobaki akaimwaga chini ya madhabahu.
LEV 9:10 Juu ya madhabahu akateketeza mafuta, figo na kipande kirefu cha ini kutoka hiyo sadaka ya dhambi, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
LEV 9:11 Akateketeza nyama na ngozi nje ya kambi.
LEV 9:12 Kisha Haruni akachinja sadaka ya kuteketezwa. Wanawe wakamletea damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu.
LEV 9:13 Wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, pamoja na kichwa, naye akaviteketeza juu ya madhabahu.
LEV 9:14 Akasafisha sehemu za ndani na miguu, akaviteketeza juu ya sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu.
LEV 9:15 Kisha Haruni akaleta sadaka ile iliyokuwa kwa ajili ya watu. Akachukua yule mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, akamchinja na kumtoa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kama alivyofanya kwa ile ya kwanza.
LEV 9:16 Haruni akaleta sadaka ya kuteketezwa na kuitoa kama ilivyoelekezwa.
LEV 9:17 Pia akaleta sadaka ya nafaka, akachukua konzi moja na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.
LEV 9:18 Akachinja maksai na kondoo dume kuwa sadaka ya amani kwa ajili ya watu. Wanawe Haruni wakampa ile damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu.
LEV 9:19 Lakini sehemu zile za mafuta ya yule maksai na ya yule kondoo dume, yaani mafuta ya mkia, yaliyofunika tumbo, ya figo na kipande kirefu cha ini,
LEV 9:20 hivi vyote wakaviweka juu ya vidari, kisha Haruni akayateketeza hayo mafuta ya wanyama juu ya madhabahu.
LEV 9:21 Haruni akaviinua vile vidari na paja la kulia mbele za Mwenyezi Mungu ili viwe sadaka ya kuinuliwa, kama Musa alivyoagiza.
LEV 9:22 Kisha Haruni akainua mikono yake kuwaelekea watu na kuwabariki. Naye baada ya kutoa dhabihu ya sadaka ya dhambi, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya amani, akashuka chini.
LEV 9:23 Kisha Musa na Haruni wakaingia kwenye Hema la Kukutania. Walipotoka nje, wakawabariki watu. Nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukawatokea watu wote.
LEV 9:24 Moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu, ukaiteketeza ile sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sehemu ya mafuta yaliyokuwa juu ya madhabahu. Watu wote walipoona jambo hili, wakashangilia kwa furaha na kusujudu.
LEV 10:1 Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea Mwenyezi Mungu moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu.
LEV 10:2 Hivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu na kuwateketeza, nao wakafa mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 10:3 Kisha Musa akamwambia Haruni, “Hili ndilo alilonena Mwenyezi Mungu, aliposema: “ ‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia nitajionesha kuwa mtakatifu; machoni pa watu wote nitaheshimiwa.’ ” Haruni akanyamaza.
LEV 10:4 Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjomba wake Haruni, akawaambia, “Njooni hapa. Ondoeni miili ya ndugu zenu mbele ya mahali patakatifu, mkaipeleke nje ya kambi.”
LEV 10:5 Hivyo wakaja na kuwaondoa, wakiwa bado wamevalia makoti yao ya ibada, wakawapeleka nje ya kambi, kama Musa alivyoamuru.
LEV 10:6 Ndipo Musa akamwambia Haruni pamoja na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msifunue vichwa vyenu wala msirarue mavazi yenu, la sivyo mtakufa na Mwenyezi Mungu ataikasirikia jumuiya nzima. Lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, wanaweza kuwaombolezea wale ambao Mwenyezi Mungu amewaangamiza kwa moto.
LEV 10:7 Msitoke nje ya ingilio la Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa, kwa sababu mafuta ya Mwenyezi Mungu ya upako yako juu yenu.” Hivyo wakafanya kama vile Musa alivyosema.
LEV 10:8 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Haruni,
LEV 10:9 “Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo.
LEV 10:10 Ni lazima mtenganishe kati ya kilicho kitakatifu na kilicho cha kawaida, kati ya kilicho najisi na kilicho safi,
LEV 10:11 na lazima mwafundishe Waisraeli amri zote ambazo Mwenyezi Mungu aliwapa kupitia Musa.”
LEV 10:12 Musa akamwambia Haruni pamoja na wanawe waliosalia, Eleazari na Ithamari, “Chukueni sadaka ya nafaka iliyobaki kutoka kwa sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, muile hapo kando ya madhabahu ikiwa imeandaliwa bila chachu, kwa sababu ni takatifu sana.
LEV 10:13 Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu ni fungu lenu na fungu la wana wenu la sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoamriwa.
LEV 10:14 Lakini wewe na wanao na binti zako mwaweza kula kidari kile kilichoinuliwa na paja lile lililotolewa. Mtavila katika mahali patakatifu; mmepewa wewe na wanao kuwa fungu lenu la sadaka za amani za Waisraeli.
LEV 10:15 Paja lile lililotolewa na kidari kile kilichoinuliwa lazima viletwe pamoja na sehemu za mafuta ya wanyama wa sadaka za kuteketezwa kwa moto, ili kuinuliwa mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. Hili litakuwa fungu lako na wanao milele, kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza.”
LEV 10:16 Musa alipouliza kuhusu mbuzi aliyetolewa sadaka ya dhambi na kugundua kwamba ameteketezwa, aliwakasirikia Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni waliobaki. Akawauliza,
LEV 10:17 “Kwa nini hamkula sadaka ya dhambi katika eneo la mahali patakatifu? Ni takatifu sana. Mlipewa ninyi ili kuondoa hatia ya jumuiya kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 10:18 Kwa kuwa damu yake haikuletwa ndani ya Mahali Patakatifu, mngemla mbuzi huyo katika sehemu ya mahali patakatifu kama nilivyoagiza.”
LEV 10:19 Haruni akamjibu Musa, “Leo wanangu wametoa sadaka zao za dhambi na sadaka zao za kuteketezwa mbele za Mwenyezi Mungu, lakini mambo kama haya yamenitokea mimi. Je, Mwenyezi Mungu angependezwa kama ningekuwa nimekula sadaka ya dhambi leo?”
LEV 10:20 Musa aliposikia haya, akaridhika.
LEV 11:1 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni,
LEV 11:2 “Waambieni Waisraeli: ‘Kati ya wanyama wote wanaoishi juu ya nchi, hawa ndio mtakaowala:
LEV 11:3 Mwaweza kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua.
LEV 11:4 “ ‘Kuna wanyama wengine ambao hucheua tu au wenye kwato zilizogawanyika tu, lakini hao kamwe msiwale. Ngamia ingawa hucheua, hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu.
LEV 11:5 Pelele ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu.
LEV 11:6 Sungura ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu.
LEV 11:7 Naye nguruwe ingawa anazo kwato zilizogawanyika sehemu mbili, hacheui; huyo ni najisi kwenu.
LEV 11:8 Kamwe msile nyama yao wala kugusa mizoga yao; wao ni najisi kwenu.
LEV 11:9 “ ‘Kuhusu viumbe wote wanaoishi ndani ya maji ya bahari na vijito, mtakula wale wote wenye mapezi na magamba.
LEV 11:10 Lakini viumbe wote ndani ya bahari au vijito wasio na mapezi na magamba, wakiwa miongoni mwa makundi au viumbe wote ndani ya maji, hao ni machukizo kwenu.
LEV 11:11 Nao watakuwa machukizo kwenu. Msile nyama yao, nayo mizoga yao itakuwa machukizo.
LEV 11:12 Chochote kinachoishi ndani ya maji ambacho hakina mapezi na magamba kitakuwa chukizo kwenu.
LEV 11:13 “ ‘Wafuatao ndio ndege watakaokuwa machukizo kwenu, hivyo msiwale kwa sababu ni chukizo: tai, furukombe, kipungu,
LEV 11:14 mwewe mwekundu, aina zote za mwewe mweusi,
LEV 11:15 aina zote za kunguru,
LEV 11:16 mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga, shakwe, aina zote za kipanga,
LEV 11:17 bundi, mnandi, bundi mkubwa,
LEV 11:18 mumbi, mwari, nderi,
LEV 11:19 korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.
LEV 11:20 “ ‘Wadudu wote warukao ambao hutembea kwa miguu minne watakuwa chukizo kwenu.
LEV 11:21 Lakini kuna viumbe wenye mabawa ambao hutembea kwa miguu minne mtakaowala: wale wenye vifundo katika miguu yao ya kurukaruka juu ya ardhi.
LEV 11:22 Miongoni mwa hawa, mtakula nzige wa aina zote, senene, parare au panzi.
LEV 11:23 Lakini viumbe wengine wote wenye mabawa na wenye miguu minne ni machukizo kwenu.
LEV 11:24 “ ‘Mtajinajisi kwa wanyama hawa. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 11:25 Yeyote atakayebeba mizoga ya viumbe hawa ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 11:26 “ ‘Kila mnyama mwenye ukwato ulioachana lakini haukugawanyika kabisa, au yule asiyecheua, huyo ni najisi kwenu; yeyote agusaye mzoga wowote wa hao atakuwa najisi.
LEV 11:27 Miongoni mwa wanyama wote wanaotembea kwa miguu minne, wale wanaotembea kwa vitanga vyao ni najisi kwenu; yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 11:28 Yeyote atakayebeba mizoga yao ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni. Wanyama hawa ni najisi kwenu.
LEV 11:29 “ ‘Kuhusu wanyama watambaao juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu: kicheche, panya, aina yoyote ya mijusi mikubwa,
LEV 11:30 guruguru, kenge, mijusi ya ukutani, goromoe na kinyonga.
LEV 11:31 Miongoni mwa wanyama wote wanaotambaa juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 11:32 Ikiwa mmoja wao atakufa na kuangukia juu ya kitu fulani, chombo hicho, hata kikiwa cha matumizi gani, kitakuwa najisi, kiwe kimetengenezwa kwa mti, nguo, ngozi au gunia. Kiweke ndani ya maji; kitakuwa najisi hadi jioni, kisha kitakuwa safi tena.
LEV 11:33 Ikiwa mmoja wa wanyama aliyekufa ataangukia ndani ya chungu, kila kilichomo katika chungu hicho kitakuwa najisi, nawe ni lazima uvunje chungu hicho.
LEV 11:34 Chakula chochote ambacho chaweza kuliwa lakini kikawa kimeingia maji kutoka chungu hicho ni najisi, na kitu chochote cha majimaji ambacho chaweza kunyweka kutoka chungu hicho ni najisi.
LEV 11:35 Chochote ambacho mzoga utaangukia kitakuwa najisi. Jiko au chungu cha kupikia ni lazima kivunjwe. Ni najisi, nawe ni lazima uvihesabu kuwa najisi.
LEV 11:36 Lakini chemchemi au kisima, mahali yanapokusanyika maji, patakuwa safi; lakini yeyote atakayegusa moja ya mizoga hii ni najisi.
LEV 11:37 Kama mzoga ukianguka juu ya mbegu zozote ambazo ni za kupanda, zinabaki safi.
LEV 11:38 Lakini kama mbegu imetiwa maji na mzoga ukaanguka juu yake, hiyo mbegu ni najisi kwenu.
LEV 11:39 “ ‘Kama mnyama ambaye mnaruhusiwa kumla akifa, yeyote atakayeugusa mzoga wake atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 11:40 Yeyote atakayekula sehemu ya mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni. Yeyote atakayebeba mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 11:41 “ ‘Kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi ni chukizo; kisiliwe.
LEV 11:42 Msile kiumbe chochote kinachotambaa juu ya ardhi, kiwe kinachotambaa kwa tumbo lake, au kinachotambaa kwa miguu minne au kwa miguu mingi; ni chukizo.
LEV 11:43 Msijitie unajisi kwa kiumbe chochote kati ya hivi. Msijitie unajisi kwa viumbe hivyo au kutiwa unajisi navyo.
LEV 11:44 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; jitakaseni mwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu. Msijitie unajisi kwa kiumbe chochote kile kiendacho juu ya ardhi.
LEV 11:45 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu niliyewapandisha mtoke Misri ili niwe Mungu wenu. Kwa hiyo kuweni watakatifu kwa sababu Mimi ni mtakatifu.
LEV 11:46 “ ‘Haya ndio masharti kuhusu wanyama, ndege, kila kiumbe hai kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kiendacho juu ya ardhi.
LEV 11:47 Ni lazima mpambanue kati ya kilicho najisi na kilicho safi, kati ya viumbe hai vinavyoweza kuliwa na vile visivyoweza kuliwa.’ ”
LEV 12:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 12:2 “Waambie Waisraeli: ‘Mwanamke ambaye atapata mimba na kuzaa mtoto wa kiume atakuwa najisi kwa siku saba, kama anavyokuwa najisi wakati wa siku zake za hedhi.
LEV 12:3 Naye huyo mtoto atatahiriwa siku ya nane.
LEV 12:4 Kisha ni lazima huyo mwanamke asubiri kwa siku thelathini na tatu, ndipo atakaswe kutoka damu kwake. Hataruhusiwa kugusa kitu chochote kilicho kitakatifu au kuingia mahali patakatifu, hadi siku za kutakaswa kwake zimetimia.
LEV 12:5 Kama alimzaa mtoto wa kike, mwanamke huyo atakuwa najisi kwa majuma mawili, kama wakati wake wa hedhi. Kisha atasubiri kwa siku sitini na sita, ndipo atatakaswa kutoka damu kwake.
LEV 12:6 “ ‘Siku zake za utakaso kwa ajili ya mwana au binti zitakapotimia, mwanamke huyo atamletea kuhani kwenye ingilio la Hema la Kukutania mwana-kondoo mwenye umri wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, na kinda la njiwa au hua kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
LEV 12:7 Atavitoa mbele za Mwenyezi Mungu ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na kisha atatakasika kutokana na kutokwa na damu. “ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya mwanamke atakayezaa mtoto wa kiume au wa kike.
LEV 12:8 Kama huyo mwanamke hana uwezo wa kumpata mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda wawili wa njiwa, mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na mwingine kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kwa njia hii, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.’ ”
LEV 13:1 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni,
LEV 13:2 “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe, au upele, au alama nyeupe juu ya ngozi yake, ambayo yaweza kuwa ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani Haruni, au kwa mmoja wa wanawe, hao makuhani.
LEV 13:3 Kuhani atachunguza hicho kidonda kilichopo juu ya ngozi yake, na kama nywele za mahali palipo na kidonda zimebadilika kuwa nyeupe, na ikiwa kidonda kimeingia ndani ya ngozi, basi ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma. Kuhani atakapomchunguza, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi.
LEV 13:4 Kama alama juu ya ngozi yake ni nyeupe, lakini haionekani kuingia ndani ya ngozi, na nywele kwenye alama hiyo hazijageuka kuwa nyeupe, kuhani atamtenga mtu aliyeambukizwa kwa siku saba.
LEV 13:5 Siku ya saba, kuhani atamchunguza, na kama hakuona badiliko kwenye kile kidonda na hakijaenea juu ya ngozi, atamtenga kwa siku nyingine saba.
LEV 13:6 Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama kidonda kimepungua na hakijaenea juu ya ngozi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa ni safi; ni upele tu. Ni lazima mtu huyo afue mavazi yake, naye atakuwa safi.
LEV 13:7 Lakini ikiwa ule upele utaenea katika ngozi yake baada ya yeye kujionesha kwa kuhani na kutangazwa kuwa safi, ni lazima aende tena kwa kuhani.
LEV 13:8 Kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, atamtangaza kuwa najisi, kwani ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
LEV 13:9 “Wakati mtu yeyote ana ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani.
LEV 13:10 Kuhani atamchunguza na kama kuna uvimbe mweupe katika ngozi ambao umefanya nywele kuwa nyeupe, na kama kuna nyama mbichi ndani ya uvimbe,
LEV 13:11 ni ugonjwa sugu wa ngozi, na kuhani atamtangaza kuwa najisi. Hatamtenga tena kwa sababu ni najisi tayari.
LEV 13:12 “Ikiwa ugonjwa utakuwa umeenea kwenye ngozi yake yote kwa kadiri kuhani atakavyoweza kuona, kwamba umeenea kwenye ngozi yote ya huyo mgonjwa kutoka kichwani hadi wayo,
LEV 13:13 kuhani atamchunguza, na kama ugonjwa umeenea mwili mzima, atamtangaza huyo mtu kuwa safi. Kwa kuwa mwili wote umekuwa mweupe, yeye ni safi.
LEV 13:14 Lakini itokeapo nyama mbichi kwenye ngozi yake, atakuwa najisi.
LEV 13:15 Kuhani atakapoiona hiyo nyama mbichi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hiyo nyama mbichi ni najisi, ana ugonjwa wa kuambukiza.
LEV 13:16 Hiyo nyama mbichi ikigeuka na kuwa nyeupe, ni lazima amwendee kuhani.
LEV 13:17 Kuhani atamchunguza, na kama vidonda vimekuwa vyeupe, kuhani atamtangaza mgonjwa huyo kuwa safi; kisha atakuwa safi.
LEV 13:18 “Wakati mtu ana jipu juu ya ngozi yake nalo likapona,
LEV 13:19 napo mahali palipokuwa na jipu pakatokea uvimbe mweupe, au alama yenye wekundu na weupe, ni lazima akajioneshe kwa kuhani.
LEV 13:20 Kuhani atapachunguza, na kama uvimbe umeingia ndani ya ngozi, na nywele zimegeuka kuwa nyeupe, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza uliojitokeza pale jipu lilipokuwa.
LEV 13:21 Lakini ikiwa kuhani anapopachunguza pakawa hapana nywele nyeupe ndani yake, wala hapakuingia ndani ya ngozi, na pameanza kupungua, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
LEV 13:22 Kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
LEV 13:23 Lakini ikiwa ile alama haijabadilika wala kuenea, ni kovu tu kutokana na jipu, kuhani atamtangaza kuwa safi.
LEV 13:24 “Wakati mtu ameungua kwenye ngozi yake, pakatokea alama yenye wekundu na weupe, au alama nyeupe ikaonekana penye nyama mbichi pale palipoungua,
LEV 13:25 kuhani ataichunguza ile alama, na kama nywele zilizo juu yake zimegeuka kuwa nyeupe, na panaonekana kuingia ndani ya ngozi, basi huo ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza ambao umetokea katika jeraha la moto. Kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
LEV 13:26 Lakini kuhani akipachunguza na akaona kwamba hakuna nywele nyeupe kwenye alama ile, wala hapakuingia ndani ya ngozi, na pamepungua, basi kuhani atamtenga kwa siku saba.
LEV 13:27 Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
LEV 13:28 Lakini, kama alama ile haikubadilika na wala haijaenea kwenye ngozi, napo pamepungua, ni uvimbe kutokana na jeraha la moto, na kuhani atamtangaza kuwa safi; ni kovu tu kutokana na kuungua.
LEV 13:29 “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana kidonda juu ya kichwa au juu ya kidevu,
LEV 13:30 kuhani atakichunguza kile kidonda, na kama ataona kuwa kimeingia ndani ya ngozi, na nywele zilizo juu yake ni njano na nyembamba, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza wa kichwa au kidevu.
LEV 13:31 Lakini kama kuhani akichunguza aina hii ya kidonda, kionekane kuwa hakijaingia ndani ya ngozi, na hakuna nywele nyeusi juu yake, basi atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
LEV 13:32 Siku ya saba kuhani atachunguza kidonda kile, na kama hakijaenea, na hakuna nywele za manjano juu yake, wala haukuingia ndani ya ngozi,
LEV 13:33 mtu huyo ni lazima anyolewe, isipokuwa mahali palipo na ugonjwa, naye kuhani atamtenga kwa siku nyingine saba.
LEV 13:34 Siku ya saba kuhani atachunguza tena kidonda kile; ikiwa hakijaenea kwenye ngozi na hakikuingia ndani ya ngozi, kuhani atamtangaza kuwa safi. Lazima afue nguo zake, naye atakuwa safi.
LEV 13:35 Lakini ikiwa kidonda kitaenea katika ngozi baada ya kutangazwa kuwa safi,
LEV 13:36 kuhani atamchunguza, na kama kidonda kimeenea kwenye ngozi, kuhani hana haja ya kutazama kama kuna nywele za manjano; mtu huyo ni najisi.
LEV 13:37 Hata hivyo, katika uchunguzi wake akiona hapajabadilika, na nywele nyeusi zimeota juu yake, huyo mtu amepona. Yeye si najisi; kuhani atamtangaza kuwa safi.
LEV 13:38 “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana alama nyeupe juu ya ngozi yake,
LEV 13:39 kuhani atamchunguza, na kama alama hizo zina weupe uliofifia, ni vipele visivyo na madhara vilivyojitokeza kwenye ngozi; mtu huyo ni safi.
LEV 13:40 “Wakati mwanaume hana nywele naye ana upara, yeye ni safi.
LEV 13:41 Ikiwa hana nywele kwenye ngozi ya kichwa chake, na ana upara kwenye paji, ni safi.
LEV 13:42 Lakini kama ana kidonda chenye wekundu na weupe kwenye kichwa chake chenye upara, au kwenye paji la uso, ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza unaojitokeza kichwani au kwenye paji lake la uso.
LEV 13:43 Kuhani atamchunguza, na kama kidonda kilichovimba juu ya kichwa chake au kwenye paji la uso ni chekundu au cheupe kama ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza,
LEV 13:44 mtu huyo ni mgonjwa, na ni najisi. Kuhani atamtangaza kuwa najisi kwa sababu ya kidonda kwenye kichwa chake.
LEV 13:45 “Mtu mwenye ugonjwa kama huo wa kuambukiza ni lazima avae nguo zilizoraruka, awachilie nywele zake bila kuzichana, afunike sehemu ya chini ya uso wake, na apige kelele, ‘Najisi! Najisi!’
LEV 13:46 Kwa muda wote atakaokuwa na ugonjwa huo wa kuambukiza atabaki kuwa najisi. Ni lazima aishi peke yake; ni lazima aishi nje ya kambi.
LEV 13:47 “Kuhusu vazi lolote lililoharibiwa na maambukizo ya ukoma, liwe ni vazi la sufu au kitani,
LEV 13:48 vazi lolote lililofumwa au kusokotwa la kitani au sufu, ngozi yoyote au chochote kilichotengenezwa kwa ngozi:
LEV 13:49 ikiwa maambukizo kwenye vazi, ngozi, au vazi lililofumwa au kusokotwa la kitani au sufu, au kitu chochote cha ngozi, ni rangi ya kijani au nyekundu, huo ni ukoma unaoenea, na ni lazima kuhani aoneshwe.
LEV 13:50 Kuhani atachunguza ukoma huo na kulitenga vazi hilo kwa siku saba.
LEV 13:51 Siku ya saba atalichunguza, na kama ukoma umeenea kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au ngozi, kwa vyovyote vile itumikavyo, ni ukoma wa kuangamiza; vazi hilo ni najisi.
LEV 13:52 Ni lazima achome vazi hilo, liwe ni la sufu au kitani kilichofumwa au kusokotwa, au kitu chochote cha ngozi chenye maambukizo; kwa kuwa ni ukoma wa kuangamiza, vazi lote ni lazima lichomwe moto.
LEV 13:53 “Lakini kuhani akilichunguza na akaona kuwa ule ukoma haujaenea kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au kitu cha ngozi,
LEV 13:54 ataagiza kwamba vazi lenye maambukizo lisafishwe. Kisha atalitenga kwa siku nyingine saba.
LEV 13:55 Baada ya vazi lenye maambukizo kusafishwa, kuhani atalichunguza, na kama ukoma haujaonesha badiliko lolote, hata kama haujaenea, ni najisi. Lichome kwa moto, iwe ukoma umeenea upande mmoja au mwingine.
LEV 13:56 Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kuoshwa, basi atararua sehemu iliyoambukizwa ya vazi, au ngozi, au vazi lililofumwa au kusokotwa.
LEV 13:57 Lakini ikijitokeza tena kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, ama kitu cha ngozi, ule ni ukoma unaoenea; chochote chenye ukoma ni lazima kichomwe kwa moto.
LEV 13:58 Vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au kitu chochote cha ngozi, baada ya kusafishwa na kuondolewa ukoma, ni lazima lioshwe tena, ili liwe safi.”
LEV 13:59 Haya ndio masharti kuhusu maambukizo ya ukoma kwenye mavazi ya sufu au kitani, mavazi yaliyofumwa au kusokotwa, ama kitu chochote cha ngozi, kwa ajili ya kuvitangaza kuwa safi au najisi.
LEV 14:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 14:2 “Haya ndio masharti yanayomhusu mtu mgonjwa wakati wa ibada yake ya utakaso, anapoletwa kwa kuhani:
LEV 14:3 Kuhani ataenda kumchunguza nje ya kambi. Kama mtu huyo atakuwa amepona ugonjwa wake wa ngozi wa kuambukiza,
LEV 14:4 kuhani ataagiza vitu vifuatavyo viletwe kwa ajili ya mtu atakayetakaswa: ndege wawili safi walio hai, mti wa mwerezi, kitani nyekundu, na hisopo.
LEV 14:5 Kisha kuhani ataagiza kwamba mmoja wa ndege wale achinjwe kwenye chungu chenye maji safi.
LEV 14:6 Kisha kuhani atamchukua ndege aliye hai na kumtumbukiza pamoja na mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo ndani ya damu ya yule ndege aliyechinjiwa kwenye maji safi.
LEV 14:7 Atamnyunyizia yule mwenye ugonjwa wa kuambukiza maji hayo mara saba, na kumtangaza kuwa safi. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai aende zake kwenye mashamba.
LEV 14:8 “Huyo mtu atakayetakaswa ni lazima afue nguo zake, anyoe nywele zake zote, na aoge kwa maji; ndipo atakapotakasika. Baada ya hili anaweza kuingia kambini, lakini ni lazima akae nje ya hema lake kwa siku saba.
LEV 14:9 Siku ya saba ni lazima anyoe nywele zake zote; yaani anyoe nywele za kichwa, ndevu zake, kope zake na nywele nyingine zote. Ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa safi.
LEV 14:10 “Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta, kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi moja ya mafuta.
LEV 14:11 Kuhani anayemtangaza kuwa safi atamkabidhi mtu huyo atakayetakaswa pamoja na sadaka zake zote mbele za Mwenyezi Mungu katika ingilio la Hema la Kukutania.
LEV 14:12 “Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia, pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa.
LEV 14:13 Atamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjiwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; ni takatifu sana.
LEV 14:14 Kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
LEV 14:15 Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, ayamimine kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto,
LEV 14:16 na achovye kidole chake cha shahada cha mkono wake wa kuume kwenye mafuta yaliyo kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho anyunyize mafuta hayo mara saba mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 14:17 Kuhani atampaka yule anayetakaswa sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio lake la kuume, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia.
LEV 14:18 Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 14:19 “Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa
LEV 14:20 na kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi.
LEV 14:21 “Hata hivyo, kama ni maskini na hawezi kupata vitu hivi, lazima achukue mwana-kondoo wa kiume mmoja kuwa sadaka ya hatia ipate kuinuliwa ili kumfanyia upatanisho, pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka, logi moja ya mafuta,
LEV 14:22 na hua wawili au makinda wawili wa njiwa, kile atakachoweza kupata, mmoja kwa sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa.
LEV 14:23 “Katika siku ya nane, lazima avilete vitu hivyo kwa kuhani, kwa ajili ya kutakaswa kwake kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 14:24 Kuhani atamchukua mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia, pamoja na ile logi ya mafuta ya kuinuliwa mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa.
LEV 14:25 Atamchinja huyo mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia. Kisha ataichukua sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, na aipake pia kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume wa huyo mtu, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
LEV 14:26 Kuhani atamiminia sehemu ya mafuta kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto,
LEV 14:27 na kwa kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume, atamnyunyizia yule anayetakaswa yale mafuta yaliyo kwenye kiganja chake mara saba mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 14:28 Atampaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake katika sehemu zote, kama alivyompaka damu ya sadaka ya hatia: yaani kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
LEV 14:29 Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki katika kiganja chake kwenye kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 14:30 Kisha atatoa dhabihu wale hua ama makinda wa njiwa ambao yule mtu ataweza kuwapata,
LEV 14:31 mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya nafaka. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya yule anayetakaswa.”
LEV 14:32 Haya ndio masharti kwa mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, na ambaye hana uwezo wa kutoa sadaka za kawaida kwa ajili ya kutakaswa kwake.
LEV 14:33 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni,
LEV 14:34 “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ninayowapa kuwa milki yenu, nami nikaweka ukoma unaoenea kwenye nyumba katika nchi ile,
LEV 14:35 ni lazima mwenye nyumba hiyo akamwambie kuhani, ‘Nimeona kitu fulani kinachofanana na ukoma kwenye nyumba yangu.’
LEV 14:36 Kuhani ataagiza vitu vyote vitolewe ndani ya nyumba, kabla hajaenda kuchunguza kama ina ukoma huo, ili kitu chochote ndani ya nyumba kisitangazwe kuwa najisi. Baada ya hili, kuhani ataingia ndani na kuikagua hiyo nyumba.
LEV 14:37 Atachunguza ukoma huo katika kuta za nyumba hiyo, nazo kama zina rangi ya kijani kibichi au wekundu, na kuna mibonyeo ndani ya ukuta,
LEV 14:38 kuhani atatoka na kufunga mlango wa nyumba hiyo kwa siku saba.
LEV 14:39 Siku ya saba, kuhani atarudi kuikagua nyumba. Kama ukoma umeenea juu ya kuta,
LEV 14:40 ataagiza kwamba mawe yote yaliyoambukizwa yaondolewe na kutupwa katika eneo lililo najisi nje ya mji.
LEV 14:41 Kuta zote za ndani ya nyumba hiyo ni lazima zikwanguliwe, na kifusi chake kitupwe mahali najisi nje ya mji.
LEV 14:42 Kisha watachukua mawe mengine na kujenga palipobomolewa kwa udongo mpya wa mfinyanzi, na wapake nyumba hiyo chokaa.
LEV 14:43 “Ikiwa ukoma huo utatokea tena ndani ya ile nyumba baada ya mawe kuondolewa, na nyumba kukwanguliwa na kupakwa chokaa,
LEV 14:44 kuhani ataenda kuikagua, na kama ukoma umeenea ndani ya nyumba, basi ni ukoma unaoharibu; nyumba hiyo ni najisi.
LEV 14:45 Ni lazima ibomolewe: mawe yake, mbao na chokaa yote; vyote vikatupwe nje ya mji mahali palipo najisi.
LEV 14:46 “Yeyote atakayeingia katika nyumba hiyo ikiwa imefungwa, atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 14:47 Yeyote atakayelala au kula ndani ya nyumba hiyo ni lazima afue nguo zake.
LEV 14:48 “Lakini ikiwa kuhani atakuja kuikagua na kukuta kuwa ukoma haujaenea tena baada ya nyumba kupakwa chokaa, ataitangaza nyumba ile kuwa safi, kwa sababu ukoma umekwisha.
LEV 14:49 Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili, mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo.
LEV 14:50 Atamchinja mmoja wa wale ndege kwenye chungu chenye maji safi.
LEV 14:51 Kisha atachukua mti wa mwerezi, hisopo, kitani nyekundu na ndege aliye hai, na kuvitumbukiza ndani ya damu ya ndege aliyechinjwa pamoja na maji safi, na kuinyunyizia nyumba ile mara saba.
LEV 14:52 Ataitakasa nyumba kwa damu ya yule ndege, maji safi, ndege aliye hai, mti wa mwerezi, hisopo na uzi mwekundu.
LEV 14:53 Kisha atamwachia yule ndege aliye hai huru mashambani nje ya mji. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ile, nayo itakuwa safi.”
LEV 14:54 Haya ndio masharti kuhusu aina yoyote ya ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, kidonda chochote,
LEV 14:55 ukoma katika vazi au ndani ya nyumba,
LEV 14:56 kwa uvimbe, upele, au alama nyeupe katika ngozi,
LEV 14:57 kupambanua wakati kitu fulani ni safi au najisi. Haya ndio masharti kuhusu magonjwa ya ngozi ya kuambukiza na ukoma.
LEV 15:1 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni,
LEV 15:2 “Semeni na Waisraeli mwaambie: ‘Mtu yeyote anapotokwa na usaha mwilini, usaha huo ni najisi.
LEV 15:3 Iwe unaendelea kutiririka kutoka mwilini mwake au umeziba, utamfanya najisi. Hivi ndivyo usaha wake utakavyomletea unajisi:
LEV 15:4 “ ‘Kitanda chochote atakacholalia mtu mwenye kutokwa na usaha kitakuwa najisi, na chochote atakachokalia kitakuwa najisi.
LEV 15:5 Yeyote atakayegusa kitanda chake ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:6 Yeyote atakayeketi juu ya kitu chochote alichokalia mwenye kutokwa na usaha, ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:7 “ ‘Yeyote atakayemgusa mtu mwenye kutokwa na usaha, ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:8 “ ‘Ikiwa mtu mwenye kutokwa na usaha atamtemea mate mtu ambaye ni safi, mtu huyo ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:9 “ ‘Kila tandiko ambalo mtu huyo atalikalia wakati wa kupanda mnyama litakuwa najisi,
LEV 15:10 na yeyote atakayegusa kitu chochote alichokuwa amekalia atakuwa najisi hadi jioni. Yeyote atakayeinua vitu hivyo ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:11 “ ‘Yeyote atakayeguswa na mtu anayetokwa na usaha bila kunawa mikono yake kwa maji, ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:12 “ ‘Chungu cha udongo kitakachoguswa na mtu huyo ni lazima kivunjwe, na kifaa chochote cha mbao kitaoshwa kwa maji.
LEV 15:13 “ ‘Mtu atakapotakasika kutoka usaha wake, atahesabu siku saba kwa utakaso wake. Ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji safi, naye atatakasika.
LEV 15:14 Siku ya nane, atachukua hua wawili au makinda wawili wa njiwa, aje mbele za Mwenyezi Mungu kwenye ingilio la Hema la Kukutania, na kumpa kuhani.
LEV 15:15 Kuhani atawatoa dhabihu, mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na huyo mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Kwa njia hii atafanya upatanisho mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huyo mtu kwa sababu ya kutokwa usaha kwake.
LEV 15:16 “ ‘Mtu akitokwa na shahawa, ni lazima aoge mwili mzima kwa maji, na atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:17 Vazi lolote ama ngozi yoyote yenye shahawa juu yake ni lazima ioshwe kwa maji, na itakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:18 Ikiwa mtu atalala na mwanamke, na kukawa na kutoka kwa shahawa, ni lazima wote waoge kwa maji, nao watakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:19 “ ‘Ikiwa mwanamke atatokwa na damu ya kawaida ya mwezi, atakuwa najisi kwa siku saba, na yeyote atakayemgusa atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:20 “ ‘Chochote atakacholalia wakati wake wa hedhi kitakuwa najisi, na chochote atakachokikalia kitakuwa najisi.
LEV 15:21 Yeyote atakayegusa kitanda chake ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:22 Yeyote atakayegusa chochote atakachokalia ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:23 Kiwe ni kitanda ama chochote alichokuwa amekikalia, ikiwa mtu yeyote atakigusa, atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:24 “ ‘Ikiwa mwanaume atalala naye na ile damu ya mwezi ikamgusa, atakuwa najisi kwa siku saba; kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanaume kitakuwa najisi.
LEV 15:25 “ ‘Ikiwa mwanamke atatokwa na damu kwa siku nyingi zaidi ya siku zake za mwezi, au amekuwa na damu inayoendelea zaidi ya kipindi chake, atakuwa najisi kwa kipindi chote cha shida hiyo, kama ilivyokuwa katika siku za hedhi yake.
LEV 15:26 Kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanamke wakati anaendelea kutokwa na damu kitakuwa najisi, kama kilivyokuwa kitanda chake wakati wa siku zake za hedhi, na chochote atakachokalia kitakuwa najisi, kama wakati wake wa hedhi.
LEV 15:27 Yeyote agusaye vitu hivyo atakuwa najisi; ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni.
LEV 15:28 “ ‘Atakapotakasika kutoka hedhi yake, ni lazima ahesabu siku saba, na baada ya hapo atakuwa ametakasika kabisa.
LEV 15:29 Siku ya nane ni lazima achukue hua wawili au makinda wawili wa njiwa, na kumletea kuhani kwenye mlango wa Hema la Kukutania.
LEV 15:30 Kuhani atatoa dhabihu, mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na huyo mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Kwa njia hii, atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Mwenyezi Mungu kwa sababu ya unajisi wa kutokwa damu kwake.
LEV 15:31 “ ‘Ni lazima uwatenge Waisraeli kutokana na vitu ambavyo vinawafanya najisi, ili wasife katika unajisi wao kwa kunajisi makao yangu yaliyo katikati yao.’ ”
LEV 15:32 Haya ni masharti kwa ajili ya mtu mwenye kutokwa na usaha, kwa ajili ya yeyote atakayetokwa na shahawa,
LEV 15:33 kwa ajili ya mwanamke katika siku zake za hedhi, kwa ajili ya mwanaume au mwanamke atokwaye na usaha, na kwa ajili ya mwanaume alalaye na mwanamke ambaye ni najisi.
LEV 16:1 Mwenyezi Mungu akasema na Musa baada ya kifo cha wale wana wawili wa Haruni waliokufa walipokaribia mbele za Mwenyezi Mungu.
LEV 16:2 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: “Mwambie ndugu yako Haruni asije wakati wowote anaotaka ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, nyuma ya pazia pale mbele ya kiti cha rehema kile kilicho juu ya Sanduku la Agano, la sivyo atakufa, kwa sababu huwa ninatokea ndani ya wingu juu ya kile kiti cha rehema.
LEV 16:3 “Hivi ndivyo Haruni atakavyoingia katika Mahali Patakatifu: atachukua fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
LEV 16:4 Atavaa koti takatifu la kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani; atafunga mshipi wa kitani kiunoni, na kuvaa kilemba cha kitani. Haya ni mavazi matakatifu, kwa hiyo ni lazima aoge kwa maji kabla ya kuyavaa mavazi hayo.
LEV 16:5 Atachukua beberu wawili kutoka kwa jumuiya ya Israeli kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
LEV 16:6 “Haruni atamtoa huyo fahali kwa ajili ya sadaka yake ya dhambi ili afanye upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na nyumba yake.
LEV 16:7 Kisha atawachukua wale beberu wawili na kuwaleta mbele za Mwenyezi Mungu kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
LEV 16:8 Haruni atapiga kura kwa ajili ya hao mbuzi wawili, mmoja kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na mwingine kwa ajili ya kubebeshwa dhambi za Israeli.
LEV 16:9 Haruni atamleta yule mbuzi ambaye kura ya Mwenyezi Mungu imemwangukia na kumtoa dhabihu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
LEV 16:10 Lakini mbuzi aliyechaguliwa kwa kura kuwa wa kubebeshwa dhambi atatolewa akiwa hai mbele za Mwenyezi Mungu, atumike kwa kufanya upatanisho kwa kumwacha aende jangwani akiwa amebebeshwa dhambi.
LEV 16:11 “Haruni atamleta yule fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake na nyumba yake, naye atamchinja huyo fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe.
LEV 16:12 Atachukua chetezo kilichojaa makaa yanayowaka kutoka madhabahuni mbele za Mwenyezi Mungu, na konzi mbili za uvumba laini uliosagwa vizuri wenye harufu, na kuvipeleka nyuma ya pazia.
LEV 16:13 Ataweka uvumba juu ya moto mbele za Mwenyezi Mungu, na moshi wa uvumba utafunika kile kiti cha rehema kilicho juu ya Ushuhuda, ili asife.
LEV 16:14 Atachukua sehemu ya damu ya fahali, na kwa kidole chake atanyunyiza sehemu ya mbele ya kiti cha rehema; kisha atanyunyiza sehemu ya hiyo damu kwa kidole chake mara saba mbele ya kiti cha rehema.
LEV 16:15 “Kisha atamchinja mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, na kuichukua damu yake nyuma ya pazia, na aifanyie kama alivyofanya kwa damu ya fahali: Atanyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele yake.
LEV 16:16 Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu kwa sababu ya unajisi na uasi wa Waisraeli, kwa dhambi zao zozote. Atafanya hivyo kwa ajili ya Hema la Kukutania, ambalo liko miongoni mwao katikati ya unajisi wao.
LEV 16:17 Mtu yeyote haruhusiwi kuwa ndani ya Hema la Kukutania, kuanzia wakati Haruni anapoingia kufanya upatanisho katika Patakatifu pa Patakatifu, hadi atakapotoka nje, baada ya kujifanyia upatanisho yeye mwenyewe na nyumba yake, pamoja na jumuiya yote ya Israeli.
LEV 16:18 “Kisha atatoka aje kwenye madhabahu yaliyo mbele za Mwenyezi Mungu na kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atachukua sehemu ya damu ya fahali na sehemu ya damu ya mbuzi, na kuiweka kwenye pembe za madhabahu.
LEV 16:19 Atanyunyiza sehemu ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.
LEV 16:20 “Haruni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai.
LEV 16:21 Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, ili kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo.
LEV 16:22 Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote hadi mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani.
LEV 16:23 “Kisha Haruni ataenda ndani ya Hema la Kukutania na kuvua yale mavazi ya kitani aliyoyavaa kabla ya kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu, naye atayaacha pale.
LEV 16:24 Ataoga kwa maji katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake ya kawaida. Kisha atatoka na kutoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yake na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya watu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, na kwa ajili ya watu.
LEV 16:25 Pia atachoma mafuta ya mnyama wa sadaka ya dhambi juu ya madhabahu.
LEV 16:26 “Yule mtu anayemwachia yule mbuzi wa kubebeshwa dhambi ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji; baadaye anaweza kuingia kambini.
LEV 16:27 Yule fahali na mbuzi waliotolewa kwa ajili ya sadaka za dhambi, ambao damu yao ilikuwa imeletwa Patakatifu pa Patakatifu kwa ajili ya kufanya upatanisho, ni lazima watolewe nje ya kambi. Ngozi zao, nyama, na matumbo vitateketezwa kwa moto.
LEV 16:28 Mtu atakayevichoma ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji; baadaye ataweza kuingia kambini.
LEV 16:29 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ni lazima mfunge, wala msifanye kazi yoyote, iwe mzawa au mgeni anayeishi miongoni mwenu,
LEV 16:30 kwa sababu siku hii upatanisho utafanyika kwa ajili yenu ili kuwatakasa. Kisha mtakuwa safi mbele za Mwenyezi Mungu kutokana na dhambi zenu zote.
LEV 16:31 Ni Sabato ya mapumziko, na lazima mfunge; ni agizo la kudumu.
LEV 16:32 Kuhani ambaye amepakwa mafuta na kuwekwa wakfu ili kuingia mahali pa baba yake kama kuhani mkuu atafanya upatanisho. Atavaa mavazi matakatifu ya kitani,
LEV 16:33 na kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, na pia kwa ajili ya makuhani, pamoja na jumuiya yote ya watu.
LEV 16:34 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Upatanisho utafanywa mara moja tu kwa mwaka kwa ajili ya dhambi zote za Waisraeli.” Ndivyo ilivyofanyika, kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
LEV 17:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 17:2 “Sema na Haruni na wanawe, pamoja na Waisraeli wote, uwaambie: ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloagiza:
LEV 17:3 Mwisraeli yeyote atakayetoa dhabihu ya ng’ombe, mwana-kondoo au mbuzi ndani ya kambi au nje yake,
LEV 17:4 badala ya kuileta kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili kuileta kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu mbele ya Maskani ya Mwenyezi Mungu, mtu huyo atahesabiwa kuwa na hatia ya kumwaga damu; amemwaga damu, na ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
LEV 17:5 Hii ni ili Waisraeli wamletee Mwenyezi Mungu dhabihu wanazozifanya sasa mahali pa wazi mashambani. Ni lazima wazilete kwa makuhani, yaani kwa Mwenyezi Mungu, katika ingilio la Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu kuwa sadaka za amani.
LEV 17:6 Kuhani atanyunyiza damu kwenye madhabahu ya Mwenyezi Mungu katika ingilio la Hema la Kukutania, na kuyateketeza mafuta ya hiyo dhabihu kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 17:7 Kamwe wasitoe tena dhabihu zao kwa sanamu za mbuzi ambazo wamekuwa wakijifanyia nazo ukahaba. Hili litakuwa agizo la kudumu kwao na kwa vizazi vijavyo.’
LEV 17:8 “Waambie: ‘Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote anayeishi miongoni mwao atakayetoa sadaka ya kuteketezwa au dhabihu
LEV 17:9 bila kuileta kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili kutoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
LEV 17:10 “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwao ambaye atakula damu yoyote, nitakuwa kinyume chake, na nitamkatilia mbali na watu wake.
LEV 17:11 Kwa kuwa uhai wa kiumbe uko ndani ya damu, nami nimewapa hiyo damu ili mfanyie upatanisho kwa ajili yenu wenyewe juu ya madhabahu; damu ndiyo ifanyayo upatanisho kwa ajili ya maisha ya mtu.
LEV 17:12 Kwa hiyo, ninawaambia Waisraeli, “Hakuna hata mmoja wenu anayeruhusiwa kula damu, wala mgeni anayeishi miongoni mwenu haruhusiwi kula damu.”
LEV 17:13 “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye atamwinda mnyama au ndege anayeruhusiwa kuliwa ni lazima aimwage damu na kuifunika kwa udongo,
LEV 17:14 kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni damu yake. Ndiyo sababu nimewaambia Waisraeli, “Kamwe msile damu ya kiumbe chochote, kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni damu yake; yeyote atakayekula damu lazima akatiliwe mbali.”
LEV 17:15 “ ‘Mtu yeyote, awe mzawa au mgeni, ambaye atakula mzoga wa kitu chochote ama kilichouawa na wanyama mwitu ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi hadi jioni; kisha atakuwa ametakaswa.
LEV 17:16 Lakini kama hakufua nguo zake na kuoga, atakuwa na hatia kwa kosa hilo.’ ”
LEV 18:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 18:2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
LEV 18:3 Msifanye kama wafanyavyo huko Misri, mahali mlipokuwa mnaishi, wala msifanye kama wanavyofanya katika nchi ya Kanaani, mahali ninapowapeleka. Msifuate matendo yao.
LEV 18:4 Ni lazima mzitii sheria zangu, na mwe waangalifu kuzifuata amri zangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
LEV 18:5 Zishikeni amri zangu na sheria zangu, kwa maana mtu anayezitii ataishi kwa hizo. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 18:6 “ ‘Hakuna mtu yeyote atakayemsogelea ndugu wa karibu ili kukutana naye kimwili. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 18:7 “ ‘Usimvunjie heshima baba yako kwa kukutana kimwili na mama yako. Yeye ni mama yako; usiwe na mahusiano kama hayo naye.
LEV 18:8 “ ‘Usikutane kimwili na mke wa baba yako; hiyo itamvunjia heshima baba yako.
LEV 18:9 “ ‘Usikutane kimwili na dada yako, wala binti ya baba yako, au binti ya mama yako, awe amezaliwa katika nyumba hiyo au mahali pengine.
LEV 18:10 “ ‘Usikutane kimwili na binti ya mwanao ama binti ya binti yako; utajivunjia heshima.
LEV 18:11 “ ‘Usikutane kimwili na binti ya mke wa baba yako, aliyezaliwa na baba yako; huyo ni dada yako.
LEV 18:12 “ ‘Usikutane kimwili na dada wa baba yako; ni ndugu wa karibu wa baba yako.
LEV 18:13 “ ‘Usikutane kimwili na dada wa mama yako, kwa sababu ni ndugu wa mama yako wa karibu.
LEV 18:14 “ ‘Usimvunjie heshima ndugu wa baba yako, kwa kukutana kimwili na mke wake; yeye ni shangazi yako.
LEV 18:15 “ ‘Usikutane kimwili na mkwe wako, yeye ni mke wa mwanao; usiwe na mahusiano kama hayo naye.
LEV 18:16 “ ‘Usikutane kimwili na mke wa kaka yako; utamvunjia heshima kaka yako.
LEV 18:17 “ ‘Usikutane kimwili na mwanamke kisha na binti yake. Usikutane kimwili na binti ya mwanawe au binti ya binti yake; hao ni ndugu zake wa karibu. Huo ni uovu.
LEV 18:18 “ ‘Usimchukue dada wa mke wako kuwa mke mwenza, na kukutana naye kimwili wakati bado mke wako anaishi.
LEV 18:19 “ ‘Usimsogelee mwanamke ili kukutana naye kimwili wakati wa unajisi wa siku zake za mwezi.
LEV 18:20 “ ‘Usikutane kimwili na mke wa jirani yako na kujitia naye unajisi.
LEV 18:21 “ ‘Usimtoe kafara mtoto wako yeyote kwa Moleki, kwani hutalinajisi kamwe jina la Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 18:22 “ ‘Usikutane kimwili na mwanaume vile mwanaume anavyokutana kimwili na mwanamke; hilo ni chukizo.
LEV 18:23 “ ‘Usikutane kimwili na mnyama na kujitia unajisi kwake. Mwanamke asijipeleke kwa mnyama ili kukutana naye kimwili; huo ni upotovu.
LEV 18:24 “ ‘Msijitie unajisi kwa njia yoyote katika hizi, kwa sababu hivi ndivyo mataifa nitakayoyafukuza mbele yenu yalivyojitia unajisi.
LEV 18:25 Hata nchi ilitiwa unajisi, hivyo nikaiadhibu kwa dhambi zake, nayo nchi ikawatapika wakazi wake.
LEV 18:26 Lakini ni lazima mzitunze amri zangu na sheria zangu. Wazawa na wageni wanaoishi miongoni mwenu kamwe wasifanye mambo yoyote ya machukizo haya,
LEV 18:27 kwa kuwa mambo haya yote yalifanywa na watu walioishi katika nchi hii kabla yenu, na nchi ikawa najisi.
LEV 18:28 Mkiinajisi nchi, itawatapika kama ilivyowatapika mataifa yaliyowatangulia.
LEV 18:29 “ ‘Kila mtu atakayefanya mojawapo ya machukizo haya, watu hao ni lazima wakatiliwe mbali na watu wao.
LEV 18:30 Shikeni maagizo yangu, wala msifuate desturi za machukizo yoyote yaliyofanywa kabla hamjafika katika nchi hii, na kujitia unajisi kwa hayo. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
LEV 19:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 19:2 “Sema na kusanyiko lote la Waisraeli, uwaambie: ‘Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni mtakatifu.
LEV 19:3 “ ‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
LEV 19:4 “ ‘Msiabudu sanamu, wala msijitengenezee miungu ya kusubu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
LEV 19:5 “ ‘Mnapotoa dhabihu ya sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu, toeni kwa namna ambayo itakubaliwa kwa niaba yenu.
LEV 19:6 Sadaka hiyo italiwa siku hiyo hiyo mnayoitoa, au kesho yake; chochote kitakachobaki hadi siku ya tatu lazima kiteketezwe kwa moto.
LEV 19:7 Kama sehemu yoyote ya sadaka hiyo italiwa siku ya tatu, itakuwa si safi, nayo haitakubaliwa.
LEV 19:8 Yeyote atakayekula atawajibishwa, kwa sababu amenajisi kitu kilicho kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu; mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.
LEV 19:9 “ ‘Unapovuna mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako.
LEV 19:10 Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
LEV 19:11 “ ‘Usiibe. “ ‘Usiseme uongo. “ ‘Msidanganyane.
LEV 19:12 “ ‘Usiape kwa uongo kwa Jina langu, na hivyo kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 19:13 “ ‘Usimdhulumu wala kumwibia jirani yako. “ ‘Usishikilie mshahara wa kibarua usiku kucha hadi asubuhi.
LEV 19:14 “ ‘Usimlaani kiziwi, wala usiweke kikwazo mbele ya kipofu, lakini umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 19:15 “ ‘Usipotoshe haki; usioneshe kumpendelea maskini, wala upendeleo kwa mwenye cheo, bali mwamulie jirani yako kwa haki.
LEV 19:16 “ ‘Usieneze uchochezi miongoni mwa watu wako. “ ‘Usifanye kitu chochote kile kinachohatarisha maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 19:17 “ ‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake.
LEV 19:18 “ ‘Usijilipizie kisasi wala kuwa na kinyongo dhidi ya mmoja wa jamaa yako, lakini mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 19:19 “ ‘Mtazishika amri zangu. “ ‘Usiwaache mifugo wako wakazaana na wa aina tofauti. “ ‘Usipande mbegu za aina mbili katika shamba lako. “ ‘Usivae vazi lililofumwa kwa nyuzi za aina mbili tofauti.
LEV 19:20 “ ‘Kama mwanaume anakutana kimwili na mjakazi aliyeposwa na mwanaume mwingine, ambaye hajakombolewa wala hajapewa uhuru, lazima iwepo adhabu inayofaa. Hata hivyo hawatauawa, kwa sababu msichana alikuwa bado hajaachwa huru.
LEV 19:21 Lakini huyo mtu lazima alete kondoo dume kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa ajili ya sadaka ya hatia kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 19:22 Kupitia kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya dhambi aliyotenda, naye atasamehewa dhambi yake.
LEV 19:23 “ ‘Mtakapoingia katika hiyo nchi na kupanda aina yoyote ya mti wa matunda, hesabuni matunda yake kama yaliyokatazwa. Kwa miaka mitatu mtayahesabu kwamba yamekatazwa; hayaruhusiwi kuliwa.
LEV 19:24 Katika mwaka wa nne matunda yote ya mti huo yatakuwa matakatifu, sadaka ya sifa kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 19:25 Bali katika mwaka wa tano mnaweza kula matunda ya mti huo. Kwa njia hii mavuno yenu yataongezewa. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
LEV 19:26 “ ‘Msile nyama yoyote yenye damu ndani yake. “ ‘Msifanye uaguzi wala uchawi.
LEV 19:27 “ ‘Msikate nywele za kichwa denge, wala kunyoa pembe za ndevu zenu.
LEV 19:28 “ ‘Msichanje chale miili yenu kwa ajili ya mfu, wala msijichore alama juu ya miili yenu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 19:29 “ ‘Usimdhalilishe binti yako kwa kumfanya kahaba, la sivyo nchi itageukia ukahaba na kujaa uovu.
LEV 19:30 “ ‘Shika Sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 19:31 “ ‘Msiende kwa waaguzi, wala msitafute wapunga pepo, kwa maana watawanajisi. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
LEV 19:32 “ ‘Ukiwa mbele ya mzee, simama ili kuonesha heshima kwa wazee, nawe umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 19:33 “ ‘Wakati mgeni anaishi pamoja nawe katika nchi yako, usimnyanyase.
LEV 19:34 Mgeni anayeishi pamoja nawe ni lazima umtendee kama mmoja wa wazawa wa nchi yako. Mpende kama unavyojipenda mwenyewe, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
LEV 19:35 “ ‘Usitumie vipimo vya udanganyifu unapopima urefu, kupima uzito, wala kupima wingi.
LEV 19:36 Tumia mizani halali, mawe ya kupimia uzito halali, efa halali, na hini halali. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye alikutoa katika nchi ya Misri.
LEV 19:37 “ ‘Shika amri zangu zote na sheria zangu zote, nawe uzifuate. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
LEV 20:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 20:2 “Waambie Waisraeli: ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi Israeli atakayemtoa kafara mtoto wake yeyote kwa Moleki lazima auawe. Watu wa jumuiya hiyo watampiga kwa mawe.
LEV 20:3 Mimi nitauelekeza uso wangu dhidi ya mtu huyo, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa maana kwa kumtoa kafara mmoja wa watoto wake kwa Moleki, amenajisi madhabahu yangu na kulinajisi Jina langu takatifu.
LEV 20:4 Ikiwa watu wa jumuiya watafumba macho yao wakati mtu huyo anapomtoa kafara mmoja wa watoto wake kwa Moleki, nao wakaacha kumuua,
LEV 20:5 mimi nitauelekeza uso wangu dhidi ya mtu huyo pamoja na jamaa yake, nami nitawakatilia mbali yeye na watu wote waliofanya ukahaba na Moleki.
LEV 20:6 “ ‘Mimi nitauelekeza uso wangu dhidi ya mtu anayeenda kwa waaguzi na wenye pepo, na hivyo kujifanyia ukahaba kwa kuwafuata, nami nitamkatilia mbali na watu wake.
LEV 20:7 “ ‘Jitakaseni basi, nanyi kuweni watakatifu, kwa sababu mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
LEV 20:8 Shikeni amri zangu na kuzifuata. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niwafanyaye ninyi watakatifu.
LEV 20:9 “ ‘Ikiwa mtu yeyote atamlaani baba yake au mama yake, lazima auawe. Amemlaani baba yake au mama yake, nayo damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
LEV 20:10 “ ‘Ikiwa mtu atazini na mke wa mtu mwingine, yaani mke wa jirani yake, wazinzi hao wawili lazima wauawe.
LEV 20:11 “ ‘Kama mtu atakutana kimwili na mke wa baba yake, hakumheshimu baba yake. Mwanaume huyo na mwanamke huyo wote wauawe; damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao wenyewe.
LEV 20:12 “ ‘Ikiwa mtu atakutana kimwili na mke wa mwanawe, lazima wote wawili wauawe. Walichokifanya ni upotovu; damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao wenyewe.
LEV 20:13 “ ‘Kama mwanaume akikutana kimwili na mwanaume mwenzake kama vile mwanaume afanyavyo na mwanamke, wanaume hao wawili wamefanya lililo chukizo sana. Lazima wauawe; nayo damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao wenyewe.
LEV 20:14 “ ‘Ikiwa mwanaume ataoa binti pamoja na mama yake, huo ni uovu. Wote watatu ni lazima wachomwe moto, ili pasiwepo na uovu kati yenu.
LEV 20:15 “ ‘Kama mwanaume akikutana kimwili na mnyama, ni lazima auawe, na pia ni lazima mnyama huyo auawe.
LEV 20:16 “ ‘Kama mwanamke atamsogelea mnyama kukutana naye kimwili, muueni mwanamke huyo pamoja na mnyama pia. Lazima wauawe; damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao wenyewe.
LEV 20:17 “ ‘Ikiwa mtu atamwoa dada yake, binti aliyezaliwa na baba yake au mama yake, nao wakakutana kimwili, ni aibu. Lazima wakatiliwe mbali machoni pa watu wao. Huyo mwanaume amemwaibisha dada yake, hivyo atawajibika kwa ajili ya uovu huo.
LEV 20:18 “ ‘Ikiwa mwanaume atakutana kimwili na mwanamke aliye katika hedhi yake, amefunua mtiririko wa hedhi yake, naye huyo mwanamke amejifunua uchi wake. Wote wawili lazima wakatiliwe mbali na watu wao.
LEV 20:19 “ ‘Usikutane kimwili na dada wa mama yako wala wa baba yako, kwa maana hilo litamwaibisha jamaa wa karibu; ninyi wawili mtawajibika kwa ajili ya uovu huo.
LEV 20:20 “ ‘Ikiwa mwanaume atakutana kimwili na shangazi yake, amemwaibisha mjomba wake. Nao watawajibika kwa ajili ya uovu huo; watakufa bila kuzaa mtoto.
LEV 20:21 “ ‘Ikiwa mwanaume ataoa mke wa ndugu yake, hili ni tendo chafu; amemwaibisha ndugu yake. Nao hawatazaa mtoto.
LEV 20:22 “ ‘Zishikeni amri na sheria zangu zote na kuzifuata, ili nchi ninayowaleta kuishi isiwatapike.
LEV 20:23 Kamwe msiishi kwa kufuata desturi za mataifa nitakayoyafukuza mbele yenu. Kwa sababu walifanya mambo haya yote, nilichukizwa sana nao.
LEV 20:24 Lakini niliwaambia ninyi, “Mtaimiliki nchi yao; nitawapa ninyi kuwa urithi, nchi inayotiririka maziwa na asali.” Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye amewatenga kutoka mataifa.
LEV 20:25 “ ‘Kwa hiyo, ninyi lazima mweze kutofautisha kati ya wanyama walio safi na wasio safi, pia kati ya ndege wasio safi na walio safi. Msijitie unajisi kutokana na mnyama yeyote, au ndege, wala kiumbe chochote kinachotambaa juu ya ardhi, ambavyo nimevitenga kuwa najisi kwa ajili yenu.
LEV 20:26 Mtakuwa watakatifu kwangu, kwa sababu Mimi, Mwenyezi Mungu, ni mtakatifu, nami nimewatenga kutoka mataifa kuwa wangu mwenyewe.
LEV 20:27 “ ‘Mwanaume au mwanamke ambaye ni mchawi, mwaguzi au mwenye kupunga pepo miongoni mwenu lazima auawe. Mtawapiga kwa mawe; nayo damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao wenyewe.’ ”
LEV 21:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sema na makuhani, wana wa Haruni, uwaambie: ‘Kamwe kuhani asijitie unajisi kwa ajili ya mtu wake yeyote anayekufa,
LEV 21:2 isipokuwa jamaa wake wa karibu, kama vile mama yake au baba yake, mwanawe au binti yake, ndugu yake,
LEV 21:3 au dada yake asiyeolewa ambaye anamtegemea kwa kuwa hana mume, kwa ajili ya hao aweza kujitia unajisi.
LEV 21:4 Kamwe asijitie unajisi mwenyewe kutokana na wale watu ambao anahusiana nao kwa kuoana, na hivyo kujitia unajisi.
LEV 21:5 “ ‘Kamwe makuhani wasinyoe nywele za vichwa vyao wala wasinyoe pembeni mwa ndevu zao, au kuweka chale kwenye miili yao.
LEV 21:6 Lazima wawe watakatifu kwa Mungu wao, na kamwe wasilinajisi jina la Mungu wao. Kwa sababu ndio wanaotoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu, chakula cha Mungu wao, hivyo lazima wawe watakatifu.
LEV 21:7 “ ‘Kamwe wasioe wanawake waliojinajisi kwa ukahaba, au waliopewa talaka na waume wao, kwa sababu makuhani ni watakatifu kwa Mungu wao.
LEV 21:8 Waoneni kuwa watakatifu, kwa sababu ndio wanaotoa chakula cha Mungu wenu. Kumbukeni kuwa ni watakatifu, kwa sababu Mimi Mwenyezi Mungu ni mtakatifu, Mimi niwafanyaye ninyi kuwa watakatifu.
LEV 21:9 “ ‘Ikiwa binti ya kuhani anajitia unajisi kwa kufanya ukahaba, anamwaibisha baba yake; lazima achomwe kwa moto.
LEV 21:10 “ ‘Kuhani mkuu, yule miongoni mwa ndugu zake ambaye amekwisha kupakwa mafuta kwa kumiminiwa juu ya kichwa chake, na ambaye amewekwa wakfu kuvaa mavazi ya ukuhani, kamwe asiache nywele zake bila kufunikwa, wala asirarue nguo zake.
LEV 21:11 Kamwe asiingie mahali palipo maiti ndani. Kamwe asijitie unajisi, hata kwa ajili ya baba yake au mama yake,
LEV 21:12 wala asiondoke mahali patakatifu pa Mungu wake au kupanajisi, kwa sababu amewekwa wakfu kwa mafuta ya Mungu wake. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 21:13 “ ‘Mwanamke atakayeolewa na kuhani lazima awe bikira.
LEV 21:14 Kamwe asimwoe mjane, au mwanamke aliyepewa talaka, wala mwanamke aliyejinajisi kwa ukahaba, bali atamwoa tu bikira kutoka miongoni mwa watu wake,
LEV 21:15 na hivyo hatawatia unajisi wazao wake miongoni mwa watu wake. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nimfanyaye mtakatifu.’ ”
LEV 21:16 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 21:17 “Mwambie Haruni: ‘Kwa vizazi vijavyo, hakuna mzao wako mwenye dosari atakayekaribia kutoa chakula cha Mungu wake.
LEV 21:18 Hakuna mtu mwenye dosari yoyote awezaye kukaribia: hakuna mtu aliye kipofu au kiwete, au aliyeharibika uso au asiye na viungo kamili,
LEV 21:19 hakuna mtu mwenye mguu au mkono uliolemaa,
LEV 21:20 au mwenye kibiongo au aliyedumaa, au aliye na tatizo la macho, au aliye na uvimbe wenye usaha au majipu, au aliyehasiwa.
LEV 21:21 Hakuna mzao wa kuhani Haruni mwenye kilema chochote atakayekaribia kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. Kama ana kilema, kamwe asikaribie kutoa chakula cha Mungu wake.
LEV 21:22 Anaweza kula chakula kitakatifu sana cha Mungu wake, pia hata chakula kitakatifu.
LEV 21:23 Lakini kwa sababu ya kilema chake, kamwe asikaribie pazia wala kukaribia madhabahu, asije akanajisi mahali patakatifu pangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niwafanyaye watakatifu.’ ”
LEV 21:24 Basi Musa akanena na Haruni, na wanawe, na Waisraeli wote.
LEV 22:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 22:2 “Mwambie Haruni na wanawe kushughulikia kwa uangalifu sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwangu, ili wasilinajisi Jina langu takatifu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 22:3 “Waambie: ‘Katika vizazi vijavyo, ikiwa yeyote wa wazao wako ni najisi, naye akakaribia sadaka takatifu zile Waisraeli wanazoweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na uso wangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 22:4 “ ‘Ikiwa mzao wa Haruni ana ugonjwa wa ngozi unaoambukiza au anatokwa na usaha mwilini, hawezi kula sadaka takatifu hadi atakasike. Pia atakuwa najisi akigusa kitu chochote kilicho najisi kutokana na kugusa maiti, au akigusa mtu aliyetokwa na shahawa,
LEV 22:5 au akigusa kitu chochote kinachotambaa kimfanyacho mtu najisi, au mtu yeyote awezaye kumtia unajisi, hata unajisi uwe gani.
LEV 22:6 Mtu anayegusa kitu chochote cha aina hiyo atakuwa najisi hadi jioni. Kamwe hatakula sadaka yoyote takatifu hadi yeye mwenyewe awe ameoga kwa maji.
LEV 22:7 Jua linapotua, atakuwa safi, na baadaye anaweza kula sadaka takatifu, kwa kuwa ni vyakula vyake.
LEV 22:8 Kamwe asile nyama ya mzoga wala iliyoraruliwa na wanyama pori, naye akatiwa unajisi kwa hilo. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 22:9 “ ‘Makuhani lazima washike maagizo yangu ili wasiwe na hatia, wakafa kwa kuyadharau. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ninayewafanya watakatifu.
LEV 22:10 “ ‘Hakuna mtu yeyote asiye wa jamaa ya kuhani anayeruhusiwa kula sadaka takatifu, hata mgeni wa kuhani au mfanyakazi wake haruhusiwi kuila.
LEV 22:11 Lakini ikiwa kuhani amenunua mtumwa kwa fedha, au mtumwa amezaliwa katika nyumba ya kuhani huyo, mtumwa huyo aweza kula chakula cha huyo kuhani.
LEV 22:12 Ikiwa binti ya kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, binti huyo haruhusiwi kula chochote cha matoleo matakatifu.
LEV 22:13 Lakini ikiwa binti ya kuhani amekuwa mjane au amepewa talaka, naye hana watoto, na akarudi kuishi na jamaa ya baba yake kama wakati wa usichana wake, binti huyo anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mtu asiyeruhusiwa hawezi kula chochote katika chakula hiki.
LEV 22:14 “ ‘Ikiwa mtu yeyote amekula sadaka takatifu kwa makosa, lazima atoe malipo ya sadaka hiyo kwa kuhani na kuongeza sehemu ya tano ya thamani ya sadaka hiyo.
LEV 22:15 Kamwe makuhani wasiinajisi sadaka takatifu ambayo Waisraeli wameitoa kwa Mwenyezi Mungu
LEV 22:16 kwa kuwaruhusu kuzila sadaka hizo takatifu, na hivyo kuwaletea hatia ya kudaiwa malipo. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu niwafanyaye watakatifu.’ ”
LEV 22:17 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 22:18 “Sema na Haruni na wanawe, na Waisraeli wote uwaambie: ‘Ikiwa mmoja wenu, aliye Mwisraeli au mgeni anayeishi katika nchi ya Israeli, atatoa matoleo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu, iwe kutimiza nadhiri au kuwa sadaka ya hiari,
LEV 22:19 lazima amtoe mnyama dume asiye na dosari, akiwa ng’ombe, mbuzi au kondoo, ili aweze kukubalika kwa niaba yako.
LEV 22:20 Kamwe usitoe kitu chochote chenye dosari kwa sababu hakitakubaliwa kwa niaba yako.
LEV 22:21 Mtu yeyote aletapo sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu kutoka kundi la ng’ombe au la mbuzi ili kutimiza nadhiri maalum au sadaka ya hiari, lazima sadaka hiyo isiwe na dosari au waa ili ikubalike.
LEV 22:22 Kamwe usimtolee Mwenyezi Mungu mnyama aliye kipofu, aliyejeruhiwa wala aliye kilema, au chochote kilicho na uvimbe, au chenye upele au vidonda vinavyotoka usaha. Kamwe chochote cha aina hii kisiwekwe juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu ya kuteketezwa kwa moto.
LEV 22:23 Lakini unaweza ukamtoa ng’ombe au kondoo mwenye kilema au aliyedumaa kuwa sadaka ya hiari, lakini hii haitakubalika kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri.
LEV 22:24 Kamwe usimtolee Mwenyezi Mungu mnyama ambaye mapumbu yake yamejeruhiwa, au kuhasiwa, au kuraruliwa au kukatwa. Kamwe usifanye hivi katika nchi yako mwenyewe,
LEV 22:25 na kamwe usikubali wanyama wa aina hii kutoka mkono wa mgeni ili kuwatoa wanyama hao kuwa chakula kwa Mungu wako. Wanyama hao hawatakubaliwa kwa niaba yako, kwa sababu wana vilema, nao wana dosari.’ ”
LEV 22:26 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 22:27 “Ndama, mwana-kondoo au mwana-mbuzi anapozaliwa, atabaki na mama yake kwa siku saba. Kuanzia siku ya nane na kuendelea anaweza kukubaliwa kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto.
LEV 22:28 Usimchinje ng’ombe na ndama wake, au kondoo na kitoto chake siku moja.
LEV 22:29 “Unapomtolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya shukrani, itoe kwa namna ambayo itakubalika kwa niaba yako.
LEV 22:30 Ni lazima iliwe siku hiyo hiyo, pasipo kubakiza chochote hadi asubuhi. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 22:31 “Shikeni maagizo yangu na kuyafuata. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 22:32 Msilinajisi Jina langu takatifu. Lazima nikubalike kuwa mtakatifu kwa Waisraeli. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ninayewafanya watakatifu,
LEV 22:33 na niliyewatoa katika nchi ya Misri niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
LEV 23:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 23:2 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Hizi ndizo sikukuu zangu zilizoamriwa, sikukuu zilizoamriwa za Mwenyezi Mungu, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu.
LEV 23:3 “ ‘Kuna siku sita mnazoweza kufanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, siku ya kusanyiko takatifu. Hamtafanya kazi yoyote. Popote mnapoishi, ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 23:4 “ ‘Hizi ni sikukuu za Mwenyezi Mungu zilizoamriwa, makusanyiko matakatifu mtakayoyatangaza kwa nyakati zilizoamriwa:
LEV 23:5 Pasaka ya Mwenyezi Mungu huanza jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.
LEV 23:6 Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa kwanza, Sikukuu ya Mwenyezi Mungu ya Mikate Isiyotiwa Chachu huanza; kwa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu.
LEV 23:7 Katika siku ya kwanza, mtakuwa na kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida.
LEV 23:8 Kwa siku saba mtamletea Mwenyezi Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku hiyo ya saba mtafanya kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida.’ ”
LEV 23:9 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 23:10 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi nitakayowapa na kuvuna mazao ya nchi hiyo, leteni kwa kuhani mganda wa nafaka ya kwanza mtakayovuna.
LEV 23:11 Naye atauinua huo mganda mbele za Mwenyezi Mungu ili ukubaliwe kwa niaba yenu; kuhani ataupunga siku inayofuata Sabato.
LEV 23:12 Siku hiyo mtakapoinua huo mganda, lazima mtoe kwa Mwenyezi Mungu dhabihu ya kuteketezwa kwa moto ya mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari,
LEV 23:13 pamoja na sadaka yake ya nafaka ya sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto; hii itakuwa sadaka iliyo harufu nzuri ya kupendeza, na sadaka yake ya kinywaji ya robo ya hini ya divai.
LEV 23:14 Kamwe msile mkate wowote, au nafaka iliyokaangwa au nafaka mpya, hadi siku ile mtakayomletea Mungu wenu sadaka hii. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mnapoishi.
LEV 23:15 “ ‘Tangu siku ile iliyofuata Sabato, siku mliyotoa sadaka ya mganda wa kuinuliwa, hesabuni majuma saba kamili.
LEV 23:16 Mtahesabu siku hamsini hadi siku inayofuata Sabato ya saba, ndipo mtatoa sadaka ya nafaka mpya kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 23:17 Kutoka popote mnapoishi, mtaleta mikate miwili iliyotengenezwa kwa sehemu mbili za kumi ya efa moja ya unga laini, uliookwa kwa chachu, kuwa sadaka ya kuinuliwa ya malimbuko kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 23:18 Toeni pamoja na hiyo mikate wana-kondoo saba, kila mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari, na fahali mchanga, na kondoo dume wawili. Watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, sadaka iliyotolewa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
LEV 23:19 Kisha toeni dhabihu ya beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili, kila mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya amani.
LEV 23:20 Kuhani atawainua hao wana-kondoo wawili mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, pamoja na mkate wa malimbuko. Ni sadaka takatifu kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuhani.
LEV 23:21 Siku hiyo hiyo mtatangaza kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mtakapoishi.
LEV 23:22 “ ‘Mnapovuna mavuno ya ardhi yenu, msivune hadi mpakani mwa shamba lenu, au kukusanya masazo ya mavuno yenu. Hayo utayaacha kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
LEV 23:23 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 23:24 “Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtakuwa na Sabato ya mapumziko, kusanyiko takatifu la ukumbusho litakaloadhimishwa kwa kupiga tarumbeta.
LEV 23:25 Msifanye kazi zenu zozote za kawaida, lakini toeni sadaka kwa Mwenyezi Mungu iliyoteketezwa kwa moto.’ ”
LEV 23:26 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 23:27 “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 23:28 Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, ambapo upatanisho unafanyika kwa ajili yenu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
LEV 23:29 Mtu ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
LEV 23:30 Mtu atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake.
LEV 23:31 Hamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo popote mnapoishi.
LEV 23:32 Ni Sabato ya mapumziko kwenu, na lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.”
LEV 23:33 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 23:34 “Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, Sikukuu ya vibanda itaanza, nayo itaadhimishwa kwa siku saba kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 23:35 Siku ya kwanza ni kusanyiko takatifu, msifanye kazi zenu za kawaida.
LEV 23:36 Kwa siku saba toeni sadaka kwa Mwenyezi Mungu za kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku ya nane fanyeni kusanyiko takatifu, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. Ni kusanyiko la mwisho, msifanye kazi zenu za kawaida.
LEV 23:37 (“ ‘Hizi ni sikukuu za Mwenyezi Mungu zilizoamriwa, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu kwa kuleta sadaka kwa Mwenyezi Mungu za kuteketeza kwa moto: sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, dhabihu na sadaka za vinywaji zitahitajika kila siku.
LEV 23:38 Sadaka hizi ni nyongeza ya zile mnazozitoa katika Sabato za Mwenyezi Mungu, na pia ni nyongeza ya matoleo yenu ya chochote mlichoweka nadhiri, na sadaka zenu zote za hiari mnazozitoa kwa Mwenyezi Mungu.)
LEV 23:39 “ ‘Basi kuanzia siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, baada ya kuvuna mazao yote ya nchi, mtaadhimisha sikukuu kwa Mwenyezi Mungu kwa siku saba; siku ya kwanza ni Sabato ya mapumziko, na pia siku ya nane ni Sabato ya mapumziko.
LEV 23:40 Siku ya kwanza mtachukua matunda mazuri ya miti, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi, na matawi ya mirebi, nanyi mtashangilia mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa siku saba.
LEV 23:41 Mtaadhimisha siku hii kuwa sikukuu kwa Mwenyezi Mungu kwa siku saba kila mwaka. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo; iadhimisheni mwezi wa saba.
LEV 23:42 Mtaishi katika vibanda kwa siku saba: Wazawa wote wa Waisraeli wataishi katika vibanda,
LEV 23:43 ili wazao wenu wajue kuwa niliwafanya Waisraeli waishi kwenye vibanda nilipowatoa Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
LEV 23:44 Kwa hiyo Musa akawatangazia Waisraeli sikukuu zilizoamriwa na Mwenyezi Mungu.
LEV 24:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 24:2 “Waagize Waisraeli wakuletee mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa kwa ajili ya mwanga ili taa ziwe zinawaka daima.
LEV 24:3 Nje ya pazia la Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, Haruni ataziwasha taa mbele za Mwenyezi Mungu kuanzia jioni hadi asubuhi daima. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo.
LEV 24:4 Taa zilizo juu ya kinara cha dhahabu safi mbele za Mwenyezi Mungu lazima zihudumiwe daima.
LEV 24:5 “Chukua unga laini, uoke mikate kumi na miwili, ukitumia sehemu mbili za kumi ya efa ya unga kwa kila mkate.
LEV 24:6 Iweke katika mistari miwili, kila mstari mikate sita, uiweke mbele za Mwenyezi Mungu juu ya meza iliyotengenezwa kwa dhahabu safi.
LEV 24:7 Kando ya kila mstari, weka uvumba safi kama sehemu ya kumbukumbu ili kuwakilisha mikate kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto.
LEV 24:8 Mikate hii itawekwa mbele za Mwenyezi Mungu kila wakati, Sabato baada ya Sabato, kwa niaba ya Waisraeli, kuwa agano la kudumu.
LEV 24:9 Hii ni mali ya Haruni na wanawe, watakaoila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni sehemu takatifu sana ya fungu lao milele la sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto.”
LEV 24:10 Basi mwana wa mama Mwisraeli na baba Mmisri alienda miongoni mwa Waisraeli, nayo mapigano yakatokea ndani ya kambi kati yake na Mwisraeli.
LEV 24:11 Huyu mwana wa mwanamke Mwisraeli akalikufuru Jina la Mwenyezi Mungu kwa kulaani; kwa hiyo wakamleta kwa Musa. (Mama yake aliitwa Shelomithi binti Dibri, wa kabila la Dani.)
LEV 24:12 Nao wakamweka mahabusu hadi mapenzi ya Mwenyezi Mungu yawe wazi kwao.
LEV 24:13 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
LEV 24:14 “Mchukue huyo aliyekufuru nje ya kambi. Wale wote waliomsikia akikufuru wataweka mikono juu ya kichwa chake, kisha kusanyiko lote watampiga mawe.
LEV 24:15 Waambie Waisraeli: ‘Ikiwa mtu yeyote atamlaani Mungu wake, atakuwa na hatia kwa uovu wake.
LEV 24:16 Yeyote atakayekufuru Jina la Mwenyezi Mungu ni lazima auawe. Kusanyiko lote watampiga kwa mawe. Iwe ni mgeni au mzawa, atakapolikufuru Jina la Mwenyezi Mungu, ni lazima auawe.
LEV 24:17 “ ‘Kama mtu yeyote atamuua mtu mwingine, ni lazima auawe.
LEV 24:18 Mtu yeyote auaye mnyama wa mtu mwingine lazima afidie, uhai kwa uhai.
LEV 24:19 Ikiwa mtu yeyote atamjeruhi jirani yake, chochote alichomtenda naye atatendewa:
LEV 24:20 iwapo amemvunja mfupa atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kama alivyomjeruhi mwenzake, vivyo hivyo ndivyo atakavyojeruhiwa.
LEV 24:21 Yeyote auaye mnyama wa mtu lazima alipe fidia, lakini yeyote auaye mtu, lazima auawe.
LEV 24:22 Mtakuwa na sheria hiyo hiyo kwa mgeni na kwa mzawa. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
LEV 24:23 Kisha Musa akasema na Waisraeli, nao wakamchukua yule aliyekufuru nje ya kambi na kumpiga mawe. Waisraeli wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
LEV 25:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa katika Mlima Sinai,
LEV 25:2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapa ninyi, nchi yenyewe ni lazima ishike sabato kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
LEV 25:3 Kwa miaka sita mtapanda mazao katika mashamba yenu, nanyi kwa miaka sita mtaikata mizabibu yenu matawi na kuvuna mazao yake.
LEV 25:4 Lakini katika mwaka wa saba, nchi lazima iwe na sabato ya mapumziko, sabato kwa Mwenyezi Mungu. Msipande mbegu katika mashamba yenu, wala msikate mizabibu yenu matawi.
LEV 25:5 Msivune chochote kinachoota chenyewe, wala kuvuna zabibu zenu ambazo hamkuzihudumia. Nchi lazima iwe na mwaka wa mapumziko.
LEV 25:6 Chochote nchi itoacho katika mwaka wa sabato kitakuwa chakula chenu wenyewe, watumishi wenu wa kiume na wa kike, mfanyakazi aliyeajiriwa, na mkazi wa muda anayeishi miongoni mwenu,
LEV 25:7 vilevile malisho ya mifugo yenu na wanyama pori katika nchi yenu. Chochote nchi itakachozalisha kinaweza kuliwa.
LEV 25:8 “ ‘Hesabu sabato saba za miaka saba, yaani miaka saba mara saba, ili sabato saba za miaka saba ziwe muda wa miaka arobaini na tisa.
LEV 25:9 Ndipo tarumbeta itapigwa kila mahali katika siku ya kumi ya mwezi wa saba. Katika Siku ya Upatanisho, piga tarumbeta katika nchi yako yote.
LEV 25:10 Mwaka wa hamsini mtauweka wakfu na kutangaza uhuru katika nchi kwa wakazi wake wote. Itakuwa ni Yubile kwenu; kila mmoja wenu atairudia mali ya jamaa yake, na kila mmoja kurudi kwenye ukoo wake.
LEV 25:11 Mwaka wa hamsini utakuwa Yubile kwenu, msipande wala msivune kile kinachoota chenyewe, au kuvuna zabibu zisizohudumiwa.
LEV 25:12 Kwa kuwa ni Yubile, nayo itakuwa takatifu kwenu; mtakula tu kile kilichotoka moja kwa moja mashambani.
LEV 25:13 “ ‘Katika huu Mwaka wa Yubile, kila mmoja atarudi kwenye mali yake mwenyewe.
LEV 25:14 “ ‘Ikiwa utauza ardhi kwa mmoja wa wazawa wa nchi yako, au ukinunua ardhi kutoka kwake, mmoja asimpunje mwingine.
LEV 25:15 Utanunua ardhi kwa mzawa wa nchi yako kulingana na hesabu ya miaka baada ya Yubile. Naye muuzaji ataiuza kwako kulingana na hesabu ya miaka iliyobaki ya kuvuna mavuno.
LEV 25:16 Miaka inapokuwa mingi, utaongeza bei, nayo miaka ikiwa michache, utapunguza bei, kwa sababu kile anachokuuzia kwa hakika ni hesabu ya mazao.
LEV 25:17 Mmoja asimpunje mwingine, bali utamcha Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
LEV 25:18 “ ‘Fuateni amri zangu na mwe waangalifu kutii amri zangu, nanyi mtaishi salama katika nchi.
LEV 25:19 Kisha nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba na kuishi humo kwa salama.
LEV 25:20 Mwaweza kuuliza, “Tutakula nini katika mwaka wa saba ikiwa hatutapanda wala kuvuna mazao yetu?”
LEV 25:21 Nitawaletea baraka ya pekee katika mwaka wa sita, ili nchi iweze kuzalisha mazao ya kuwatosha kwa miaka mitatu.
LEV 25:22 Mnapopanda mwaka wa nane, mtakula mavuno ya miaka iliyopita, na mtaendelea kuyala mazao hayo hadi mvune mavuno ya mwaka wa tisa.
LEV 25:23 “ ‘Kamwe ardhi isiuzwe kwa mkataba wa kudumu, kwa sababu nchi ni mali yangu, nanyi ni wageni na wapangaji wangu.
LEV 25:24 Katika nchi yote mtakayoshika kuwa milki yenu, ni lazima mtoe ukombozi wa ardhi.
LEV 25:25 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini na akauza baadhi ya mali yake, ndugu yake wa karibu atakuja na kukomboa kile ndugu yake alichokiuza.
LEV 25:26 Iwapo mtu huyo hana jamaa wa karibu wa kukomboa mali hiyo kwa ajili yake, lakini yeye mwenyewe akafanikiwa na kupata mali itoshayo kuikomboa,
LEV 25:27 ataamua tena thamani yake kwa miaka tangu alipoiuza, na kurudisha kiasi kilichobaki cha thamani kwa mtu aliyekuwa amemuuzia mali hiyo, naye ataweza kuirudia mali yake.
LEV 25:28 Lakini kama hatapata njia ya kumlipa mnunuzi, ile mali aliyouza itabaki kumilikiwa na mnunuzi hadi Mwaka wa Yubile. Mali hiyo itarudishwa Mwaka wa Yubile, naye ataweza kuirudia mali yake.
LEV 25:29 “ ‘Ikiwa mtu atauza nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta, yeye anayo haki ya kuikomboa mwaka mzima baada ya mauzo ya hiyo nyumba. Wakati huo anaweza kuikomboa.
LEV 25:30 Ikiwa haikukombolewa kabla ya mwaka mmoja kamili kupita, nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta itakuwa mali ya kudumu ya mnunuzi na wazao wake. Haitarudishwa Mwaka wa Yubile.
LEV 25:31 Lakini nyumba zilizo vijijini bila ya kuwa na kuta zilizozizunguka zitahesabiwa kama mashamba. Zinaweza kukombolewa, nazo zirudishwe Mwaka wa Yubile.
LEV 25:32 “ ‘Walawi siku zote wana haki ya kukomboa nyumba zao katika miji ya Walawi wanayoimiliki.
LEV 25:33 Kwa hiyo mali ya Mlawi inaweza kukombolewa, yaani nyumba iliyouzwa katika mji wowote wanaoushikilia itarudishwa Mwaka wa Yubile, kwa sababu nyumba zilizo katika miji ya Walawi ni mali yao miongoni mwa Waisraeli.
LEV 25:34 Lakini maeneo ya malisho yaliyo mali ya miji yao kamwe yasiuzwe, ni milki yao ya kudumu.
LEV 25:35 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe kati yako, msaidie vile ungemsaidia mgeni au mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi kati yako.
LEV 25:36 Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi kati yako.
LEV 25:37 Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida.
LEV 25:38 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekuleta kutoka nchi ya Misri nikupe nchi ya Kanaani, nami niwe Mungu wako.
LEV 25:39 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini kati yako, naye akajiuza kwako, usimfanye atumike kama mtumwa.
LEV 25:40 Atatendewa kama mfanyakazi aliyeajiriwa, au kama mkazi wa muda katikati yako; naye atatumika hadi Mwaka wa Yubile.
LEV 25:41 Ndipo yeye na watoto wake wataachiwa, naye atarudi kwa watu wa ukoo wake, na kwenye mali ya baba zake.
LEV 25:42 Kwa sababu Waisraeli ni watumishi wangu niliowaleta kutoka nchi ya Misri, kamwe wasiuzwe kama watumwa.
LEV 25:43 Usiwatawale kwa ukatili, lakini utamcha Mungu wako.
LEV 25:44 “ ‘Watumwa wako wa kiume na wa kike watatoka katika mataifa yanayokuzunguka; unaweza kununua watumwa kutoka kwao.
LEV 25:45 Pia unaweza kununua baadhi ya wakazi wa muda wanaoishi kati yako, na jamaa ya koo zao waliozaliwa katika nchi yako; nao watakuwa mali yako.
LEV 25:46 Unaweza kuwafanya hao kuwa urithi wa watoto wako, na unaweza kuwafanya watumwa kwa maisha yao yote. Lakini usiwatawale ndugu zako Waisraeli kwa ukatili.
LEV 25:47 “ ‘Ikiwa mgeni au mkazi wa muda katikati yako atakuwa tajiri, na mmoja wa wazawa wa nchi yako akawa maskini, naye akajiuza kwa yule mgeni anayeishi katikati yako, au kwa mmoja wa jamaa wa koo za wageni,
LEV 25:48 anayo haki ya kukombolewa baada ya kujiuza. Mmoja wa jamaa zake aweza kumkomboa:
LEV 25:49 Mjomba wake, au binamu yake, au yeyote aliye ndugu wa damu katika ukoo wake aweza kumkomboa. Au akifanikiwa, anaweza kujikomboa mwenyewe.
LEV 25:50 Yeye na huyo aliyemnunua watahesabu muda kuanzia mwaka aliojiuza hadi Mwaka wa Yubile. Bei ya kuachiwa kwake itakadiriwa kulingana na ujira unaolipwa mfanyakazi wa kuajiriwa kwa idadi ya hiyo miaka.
LEV 25:51 Ikiwa imebaki miaka mingi, ni lazima atalipia ukombozi wake fungu kubwa la bei iliyolipwa kumnunua.
LEV 25:52 Ikiwa miaka iliyobaki ni michache kufikia Mwaka wa Yubile, atafanya hesabu yake, naye atalipa malipo yanayostahili kwa ajili ya ukombozi wake.
LEV 25:53 Atatendewa kama mtu wa kuajiriwa mwaka hadi mwaka; lazima uone kwamba yule aliyemnunua hamtawali kwa ukatili.
LEV 25:54 “ ‘Hata ikiwa hakukombolewa kwa njia mojawapo ya hizi, yeye na watoto wake wataachiwa katika Mwaka wa Yubile,
LEV 25:55 kwa kuwa kwangu, Waisraeli ni watumishi. Ni watumishi wangu niliowatoa kutoka nchi ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
LEV 26:1 “ ‘Msijitengenezee sanamu, au kusimamisha sanamu ya kuchonga, au jiwe la kuabudia, na pia msijiwekee jiwe lililochongwa katika nchi yenu ili kulisujudia. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
LEV 26:2 “ ‘Zishikeni Sabato zangu na kuheshimu mahali patakatifu pangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
LEV 26:3 “ ‘Ikiwa mtafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii maagizo yangu,
LEV 26:4 nitawanyeshea mvua katika majira yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.
LEV 26:5 Kupura nafaka kwenu kutaendelea hadi wakati wa kuvuna zabibu. Na kuvuna zabibu kutaendelea hadi wakati wa kupanda mbegu, nanyi mtakula na kushiba, na mtaishi salama katika nchi yenu.
LEV 26:6 “ ‘Nitawapa amani katika nchi, mpate kulala pasipo kutiwa hofu na yeyote. Nitawaondoa wanyama wakali watoke kwenye nchi, nao upanga hautapita katika nchi yenu.
LEV 26:7 Mtawafukuza adui zenu, nanyi mtawaua kwa upanga mbele yenu.
LEV 26:8 Watu wenu watano watafukuza adui mia moja, na watu wenu mia moja watafukuza adui elfu kumi, nao adui zenu wataanguka kwa upanga mbele yenu.
LEV 26:9 “ ‘Nitawaangalia kwa upendeleo na kuwafanya mzae na kuzidisha idadi yenu, nami nitalishika agano langu na ninyi.
LEV 26:10 Wakati wa kuvuna mtakuwa bado mnakula mavuno ya mwaka uliopita, na itawalazimu kuyaondoa ghalani ili mpate nafasi ya mavuno mapya.
LEV 26:11 Nitafanya makao yangu miongoni mwenu, nami sitawachukia.
LEV 26:12 Nitatembea kati yenu niwe Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu.
LEV 26:13 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili msiendelee kuwa watumwa wa Wamisri, nikavunja nira yenu, na kuwawezesha kutembea mkiwa mmeinua vichwa vyenu.
LEV 26:14 “ ‘Lakini kama hamtanisikiliza na kutimiza maagizo haya yote,
LEV 26:15 nanyi kama mtazikataa amri zangu na kuzichukia sheria zangu, tena mkishindwa kutimiza amri zangu zote, na hivyo mkavunja agano langu,
LEV 26:16 ndipo nitakapowafanyia hili: Nitawaletea juu yenu hofu ya ghafula, magonjwa ya kudhoofisha, na homa itakayopofusha macho yenu na kuwaondolea uhai wenu. Mtapanda mbegu bila mafanikio, kwa sababu adui zenu watazila.
LEV 26:17 Nitauelekeza uso wangu dhidi yenu ili mshindwe na adui zenu; wale wanaowachukia watawatawala, nanyi mtakimbia ingawa hakuna mtu anayewafukuza.
LEV 26:18 “ ‘Kama baada ya haya yote hamtanisikiliza, nitawaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.
LEV 26:19 Nitakivunja kiburi chenu cha ukaidi, na kuifanya anga iliyo juu yenu iwe kama chuma, na ardhi yenu kama shaba.
LEV 26:20 Nguvu zenu zitatumika bila ya mafanikio, kwa sababu ardhi yenu haitawazalia mazao yake, wala miti ya nchi yenu haitazaa matunda yake.
LEV 26:21 “ ‘Kama mtaendelea kuwa na uadui nami, na kukataa kunisikiliza, nitawazidishia mateso yenu mara saba zaidi, kama dhambi zenu zinavyostahili.
LEV 26:22 Nitawatuma wanyama mwitu dhidi yenu, nao watawaibieni watoto wenu, watawaangamiza ng’ombe wenu, na kuifanya idadi yenu kuwa ndogo, hivi kwamba barabara zenu zitakuwa hazina watu.
LEV 26:23 “ ‘Ikiwa pamoja na mambo haya hamtakubali maonyo yangu lakini mkaendelea kuweka uadui nami,
LEV 26:24 mimi mwenyewe nitaweka uadui nanyi, na kuwatesa kwa ajili ya dhambi zenu mara saba zaidi.
LEV 26:25 Nitawaletea upanga juu yenu ili kuwapatiliza kwa kuvunja agano langu. Mtakapokimbilia mijini mwenu, nitatuma tauni kati yenu, nanyi mtatiwa mikononi mwa adui zenu.
LEV 26:26 Nitakapowaondolea upatikanaji wa mkate wenu, wanawake kumi wataoka mkate wenu katika tanuru moja, nao wataugawa mkate kidogo kwa kupima. Mtakula, lakini hamtashiba.
LEV 26:27 “ ‘Kama hata baada ya haya bado hamtanisikiliza lakini mkaendelea kuweka uadui nami,
LEV 26:28 ndipo katika hasira yangu nitaweka uadui nanyi, nami mwenyewe nitawaadhibu mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.
LEV 26:29 Mtakula nyama ya wana wenu na nyama ya binti zenu.
LEV 26:30 Nitaharibu mahali penu pa juu pa kuabudia, nibomoe madhabahu yenu ya kufukizia uvumba, na kuzilundika maiti zenu juu ya sanamu zenu zisizo na uhai, nami nitawachukia ninyi.
LEV 26:31 Nitaifanya miji yenu kuwa magofu, na kuharibu mahali patakatifu penu pa kuabudia, nami sitapendezwa na harufu nzuri ya sadaka zenu.
LEV 26:32 Nitaiharibu nchi, ili adui zenu watakaoishi humo washangae.
LEV 26:33 Nitawatawanya ninyi miongoni mwa mataifa, na kuufuta upanga wangu na kuwafuatia. Nchi yenu itaharibiwa, nayo miji yenu itakuwa magofu.
LEV 26:34 Ndipo nchi itafurahia sabato zake muda wote ule itakapokuwa ukiwa, nanyi mkiwa katika nchi ya adui zenu. Ndipo nchi itapumzika na kufurahia sabato zake.
LEV 26:35 Wakati wote nchi itakapobaki ukiwa, itapumzika na kufurahia sabato zake ambazo haikuzipata mlipokuwa mnaishi humo.
LEV 26:36 “ ‘Kwa habari ya wenzenu wale watakaobaki, nitaifanya mioyo yao kuwa na hofu kuu katika nchi za adui zao, kiasi kwamba sauti ya jani linalopeperushwa na upepo itawafanya wakimbie. Watakimbia kana kwamba wanakimbia upanga, nao wataanguka, ijapokuwa hakuna anayewafukuza.
LEV 26:37 Watajikwaa mmoja juu ya mwingine kama watu wakimbiao upanga, hata ingawa hakuna anayewafuatia. Hivyo hamtaweza kusimama mbele ya adui zenu.
LEV 26:38 Mtaangamia kati ya mataifa; nchi ya adui zenu itawala.
LEV 26:39 Wenzenu watakaobaki wataangamia katika nchi za adui zao kwa sababu ya dhambi zao; pia kwa sababu ya dhambi za baba zao wataangamia.
LEV 26:40 “ ‘Lakini kama watatubu dhambi zao na dhambi za baba zao, udanganyifu wao dhidi yangu na uadui wao kwangu,
LEV 26:41 ambao ulinifanya niwe na uadui nao hata nikawapeleka katika nchi ya adui zao, wakati mioyo yao isiyotahiriwa itanyenyekea na kutubu dhambi yao,
LEV 26:42 nami nitakumbuka agano langu na Yakobo, na agano langu na Isaka, na agano langu na Ibrahimu, nami nitaikumbuka nchi.
LEV 26:43 Kwa kuwa wataiacha nchi ukiwa, nayo itafurahia sabato zake wakati itakuwa ukiwa bila wao. Wataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao, kwa sababu walizikataa sheria zangu na kuzichukia amri zangu.
LEV 26:44 Lakini pamoja na hili, wakati watakuwa katika nchi ya adui zao, sitawakataa wala kuwachukia kiasi cha kuwaangamiza na kuvunja agano langu nao. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
LEV 26:45 Lakini kwa ajili yao nitalikumbuka agano langu na baba zao, ambao niliwatoa Misri mbele ya mataifa ili niwe Mungu wao. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
LEV 26:46 Hizi ndizo amri, sheria na pia masharti ambazo Mwenyezi Mungu alifanya kati yake mwenyewe na Waisraeli katika Mlima Sinai kupitia kwa Musa.
LEV 27:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
LEV 27:2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kama mtu yeyote ataweka nadhiri maalum ili kuweka watu wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutoa kiasi cha thamani inayolingana,
LEV 27:3 thamani ya kukomboa mwanaume mwenye kati ya umri wa miaka ishirini na miaka sitini itakuwa shekeli hamsini za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu;
LEV 27:4 ikiwa ni mwanamke, weka thamani yake kwa shekeli thelathini.
LEV 27:5 Kama ni mtu mwenye umri wa miaka kati ya mitano na ishirini, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli ishirini, na mwanamke shekeli kumi.
LEV 27:6 Kama ni mtu mwenye umri kati ya mwezi mmoja na miaka mitano, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli tano za fedha, na ile ya mwanamke kuwa shekeli tatu za fedha.
LEV 27:7 Kama ni mtu mwenye miaka sitini na zaidi, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli kumi na tano, na mwanamke shekeli kumi.
LEV 27:8 Kama mtu yeyote anayeweka nadhiri ni maskini mno kuweza kulipa kiasi kilichowekwa, atampeleka huyo mtu kwa kuhani, ambaye ataweka thamani yake kulingana na kile yule anayeweka nadhiri anaweza kulipa.
LEV 27:9 “ ‘Kama kile mtu alichokiwekea nadhiri ni mnyama anayekubalika kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, mnyama huyo aliyetolewa kwa Mwenyezi Mungu anakuwa mtakatifu.
LEV 27:10 Mtu haruhusiwi kumbadilisha au kutoa mnyama mzuri kwa mbaya, au mnyama mbaya kwa mzuri. Kama atatoa mnyama badala ya mwingine, wanyama wote wawili, yaani yule aliyetolewa na yule aliyebadiliwa, ni watakatifu.
LEV 27:11 Kama alichokiwekea nadhiri ni mnyama aliye najisi, yaani yule asiyekubalika kuwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu, huyo mnyama lazima aletwe kwa kuhani,
LEV 27:12 ambaye ataamua ubora wa mnyama huyo, kama ni mzuri au mbaya. Thamani yoyote atakayoweka kuhani, hivyo ndivyo itakavyokuwa.
LEV 27:13 Kama mwenye mnyama atapenda kumkomboa mnyama huyo, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake.
LEV 27:14 “ ‘Kama mtu ataweka nyumba yake wakfu kama kitu kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu, kuhani ataamua ubora wa nyumba hiyo, kama ni nzuri au mbaya. Thamani yoyote kuhani atakayoweka, basi hivyo ndivyo itakavyokuwa.
LEV 27:15 Kama mtu aliyeweka nyumba yake wakfu ataikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nayo nyumba itakuwa yake tena.
LEV 27:16 “ ‘Ikiwa mtu ataweka sehemu ya ardhi ya jamaa yake wakfu kwa Mwenyezi Mungu, thamani yake itawekwa kulingana na kiasi cha mbegu inayohitajiwa kupandwa katika ardhi hiyo, yaani homeri moja ya mbegu za shayiri kwa shekeli hamsini za fedha.
LEV 27:17 Akiweka shamba lake wakfu katika Mwaka wa Yubile, ile thamani iliyokwisha wekwa itakuwa hiyo hiyo.
LEV 27:18 Lakini akiliweka shamba lake wakfu baada ya Yubile, kuhani ataweka thamani kulingana na idadi ya miaka iliyobaki kufikia Mwaka wa Yubile unaofuata, na thamani yake iliyoamuliwa itapunguzwa.
LEV 27:19 Kama mtu anayeweka wakfu shamba anataka kulikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nalo shamba litakuwa lake tena.
LEV 27:20 Kama pengine halikomboi shamba hilo, au kama ameliuza kwa mtu mwingine, kamwe haliwezi kukombolewa.
LEV 27:21 Shamba hilo litakapoachiwa Mwaka wa Yubile, litakuwa takatifu, kama shamba lililotolewa kwa Mwenyezi Mungu, nalo litakuwa mali ya makuhani.
LEV 27:22 “ ‘Kama mtu ameweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu shamba alilonunua, ambalo si sehemu ya ardhi ya jamaa yake,
LEV 27:23 kuhani ataamua thamani yake hadi Mwaka wa Yubile, naye huyo mtu lazima alipe thamani yake siku hiyo kama kitu kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 27:24 Katika Mwaka wa Yubile, shamba litarudishwa kwa mtu yule ambaye lilinunuliwa kutoka kwake, yule ambaye ardhi ilikuwa mali yake.
LEV 27:25 Kila thamani lazima iwekwe kulingana na shekeli ya mahali patakatifu: gera ishirini kwa shekeli.
LEV 27:26 “ ‘Hata hivyo, hakuna mtu atakayemweka wakfu mzaliwa wa kwanza wa mnyama, kwa kuwa mzaliwa wa kwanza tayari ni mali ya Mwenyezi Mungu; awe ng’ombe au kondoo, ni wa Mwenyezi Mungu.
LEV 27:27 Kama ni mmoja wa wanyama walio najisi, aweza kumnunua kwa bei iliyowekwa, akiongeza sehemu ya tano ya thamani yake. Kama hatamkomboa, mnyama huyo atauzwa kwa bei iliyowekwa.
LEV 27:28 “ ‘Lakini chochote kile mtu alicho nacho na akakiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu, iwe ni binadamu, au mnyama, au ardhi ya jamaa, hakiwezi kuuzwa au kukombolewa. Chochote kilichowekwa wakfu ni kitakatifu sana kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 27:29 “ ‘Mtu yeyote aliyewekwa wakfu ili kuangamizwa, hawezi kukombolewa. Mtu kama huyo lazima auawe.
LEV 27:30 “ ‘Zaka ya kila kitu kutoka shambani, iwe ni nafaka kutoka kwa ardhi, au tunda kutoka kwa miti, ni mali ya Mwenyezi Mungu; ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 27:31 Kama mtu akikomboa chochote cha zaka yake, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake.
LEV 27:32 Zaka yote ya kundi la ng’ombe au la kondoo na mbuzi, kila mnyama wa kumi apitaye chini ya fimbo ya yule awachungaye, atakuwa kitu kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu.
LEV 27:33 Yule mnyama wa kumi hatachaguliwa kwa kigezo cha uzuri au ubaya, naye haruhusiwi kubadiliwa. Akimbadili, basi mnyama yule wa kwanza na huyo aliyebadiliwa wote watahesabiwa kuwa watakatifu, na haiwezekani kuwakomboa.’ ”
LEV 27:34 Haya ndio maagizo Mwenyezi Mungu aliyompa Musa juu ya Mlima Sinai kwa ajili ya Waisraeli.
NUM 1:1 Mwenyezi Mungu alisema na Musa katika Jangwa la Sinai, katika Hema la Kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri. Akamwambia,
NUM 1:2 “Hesabu watu wa jumuiya yote ya Waisraeli kwa kufuata koo zao na jamaa zao, ukiorodhesha kila mwanaume kwa jina lake, mmoja mmoja.
NUM 1:3 Wewe na Haruni mtawahesabu kwa migawanyo yao wanaume wote katika Israeli wenye miaka ishirini na kuendelea wanaoweza kutumika katika jeshi.
NUM 1:4 Mwanaume mmoja kutoka kila kabila, kila aliye kiongozi wa jamaa yake, atawasaidia.
NUM 1:5 “Haya ndiyo majina ya wanaume watakaowasaidia: “kutoka Reubeni, ni Elisuri mwana wa Shedeuri;
NUM 1:6 kutoka Simeoni, ni Shelumieli mwana wa Surishadai;
NUM 1:7 kutoka Yuda, ni Nashoni mwana wa Aminadabu;
NUM 1:8 kutoka Isakari, ni Nethaneli mwana wa Suari;
NUM 1:9 kutoka Zabuloni, ni Eliabu mwana wa Heloni;
NUM 1:10 kutoka wana wa Yusufu: kutoka Efraimu, ni Elishama mwana wa Amihudi; kutoka Manase, ni Gamalieli mwana wa Pedasuri;
NUM 1:11 kutoka Benyamini, ni Abidani mwana wa Gideoni;
NUM 1:12 kutoka Dani, ni Ahiezeri mwana wa Amishadai;
NUM 1:13 kutoka Asheri, ni Pagieli mwana wa Okrani;
NUM 1:14 kutoka Gadi, ni Eliasafu mwana wa Deueli;
NUM 1:15 kutoka Naftali, ni Ahira mwana wa Enani.”
NUM 1:16 Hawa walikuwa wanaume walioteuliwa kutoka jumuiya, viongozi wa makabila ya baba zao. Walikuwa wakuu wa koo za Israeli.
NUM 1:17 Musa na Haruni wakawachukua wanaume hao waliokuwa wamepewa majina yao,
NUM 1:18 wakaita jumuiya yote pamoja katika siku ya kwanza ya mwezi wa pili. Watu wakaonesha nasaba zao kwa koo zao na jamaa zao, nao wanaume waliokuwa na miaka ishirini au zaidi waliorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja,
NUM 1:19 kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa. Hivyo aliwahesabu katika Jangwa la Sinai:
NUM 1:20 Kutoka wazao wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:21 Idadi kutoka kabila la Reubeni ilikuwa watu elfu arobaini na sita na mia tano.
NUM 1:22 Kutoka wazao wa Simeoni: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi walihesabiwa na kuorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:23 Idadi kutoka kabila la Simeoni walikuwa watu elfu hamsini na tisa na mia tatu.
NUM 1:24 Kutoka wazao wa Gadi: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:25 Idadi kutoka kabila la Gadi walikuwa watu elfu arobaini na tano, mia sita na hamsini.
NUM 1:26 Kutoka wazao wa Yuda: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:27 Idadi kutoka kabila la Yuda walikuwa watu elfu sabini na nne na mia sita.
NUM 1:28 Kutoka wazao wa Isakari: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:29 Idadi kutoka kabila la Isakari walikuwa watu elfu hamsini na nne na mia nne.
NUM 1:30 Kutoka wazao wa Zabuloni: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:31 Idadi kutoka kabila la Zabuloni walikuwa watu elfu hamsini na saba na mia nne.
NUM 1:32 Kutoka wana wa Yusufu: Kutoka wazao wa Efraimu: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:33 Idadi kutoka kabila la Efraimu walikuwa watu elfu arobaini na mia tano.
NUM 1:34 Kutoka wazao wa Manase: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:35 Idadi kutoka kabila la Manase walikuwa watu elfu thelathini na mbili na mia mbili.
NUM 1:36 Kutoka wazao wa Benyamini: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:37 Idadi kutoka kabila la Benyamini walikuwa watu elfu thelathini na tano na mia nne.
NUM 1:38 Kutoka wazao wa Dani: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:39 Idadi kutoka kabila la Dani walikuwa watu elfu sitini na mbili na mia saba.
NUM 1:40 Kutoka wazao wa Asheri: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:41 Idadi kutoka kabila la Asheri walikuwa watu elfu arobaini na moja na mia tano.
NUM 1:42 Kutoka wazao wa Naftali: Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao.
NUM 1:43 Idadi kutoka kabila la Naftali walikuwa watu elfu hamsini na tatu na mia nne.
NUM 1:44 Hawa walikuwa wanaume waliohesabiwa na Musa, Haruni na viongozi kumi na wawili wa Israeli, kila mmoja akiwakilisha jamaa yake.
NUM 1:45 Wanaume wote Waisraeli waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi la Israeli walihesabiwa kufuatana na jamaa zao.
NUM 1:46 Jumla ya hesabu yao ilikuwa watu elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550).
NUM 1:47 Hata hivyo, jamaa ya kabila la Lawi hawakuhesabiwa pamoja na wengine.
NUM 1:48 Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa:
NUM 1:49 “Kamwe usihesabu kabila la Lawi wala kuwaweka pamoja katika hesabu ya Waisraeli wengine.
NUM 1:50 Badala yake, waweke Walawi kuwa viongozi wa Maskani ya Ushuhuda, juu ya samani zake na kila kitu kilicho ndani yake. Wao watabeba Maskani na samani zake zote; wataitunza na kupiga kambi kuizunguka.
NUM 1:51 Wakati wowote Maskani inapohamishwa, Walawi wataifungua, na wakati wowote Maskani inapotakiwa kusimamishwa, Walawi watafanya kazi hiyo. Mtu yeyote mwingine ambaye atasogea karibu nayo atauawa.
NUM 1:52 Waisraeli watapiga mahema yao kwa makundi makundi, kila mwanaume katika kambi yake mwenyewe chini ya bendera yake.
NUM 1:53 Hata hivyo, Walawi watapiga mahema yao kuzunguka Maskani ya Ushuhuda ili ghadhabu isiipate jumuiya ya Waisraeli. Walawi watawajibika kwa utunzaji wa Maskani ya Ushuhuda.”
NUM 1:54 Waisraeli walifanya haya yote kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 2:1 Mwenyezi Mungu aliwaambia Musa na Haruni:
NUM 2:2 “Waisraeli watapiga kambi zao kuzunguka Hema la Kukutania kwa umbali kiasi, kila mwanaume akiwa chini ya beramu yake, pamoja na bendera ya jamaa yake.”
NUM 2:3 Kwa upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua, kambi ya makundi ya Yuda watapiga kambi chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Yuda ni Nashoni mwana wa Aminadabu.
NUM 2:4 Kundi lake lina watu elfu sabini na nne na mia sita.
NUM 2:5 Kabila la Isakari watapiga kambi karibu na Yuda. Kiongozi wa watu wa Isakari ni Nethaneli mwana wa Suari.
NUM 2:6 Kundi lake lina watu elfu hamsini na nne na mia nne.
NUM 2:7 Kabila la Zabuloni litafuata. Kiongozi wa watu wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni.
NUM 2:8 Kundi lake lina watu elfu hamsini na saba na mia nne.
NUM 2:9 Wanaume wote walio katika kambi ya Yuda, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja themanini na sita na mia nne. Wao watatangulia kuondoka.
NUM 2:10 Kwa upande wa kusini kutakuwa na kambi ya makundi ya Reubeni chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Reubeni ni Elisuri mwana wa Shedeuri.
NUM 2:11 Kundi lake lina watu elfu arobaini na sita na mia tano.
NUM 2:12 Kabila la Simeoni watapiga kambi karibu na Reubeni. Kiongozi wa watu wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Surishadai.
NUM 2:13 Kundi lake lina watu elfu hamsini na tisa na mia tatu.
NUM 2:14 Kabila la Gadi litafuata. Kiongozi wa watu wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli.
NUM 2:15 Kundi lake lina watu elfu arobaini na tano mia sita na hamsini.
NUM 2:16 Wanaume wote walio katika kambi ya Reubeni, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja hamsini na moja na mia nne na hamsini (151,450). Nao watakuwa nafasi ya pili kuondoka.
NUM 2:17 Kisha Hema la Kukutania na kambi ya Walawi vitakuwa katikati ya kambi zote. Wao watasafiri kwa utaratibu ule ule kama walivyopiga kambi, kila mmoja mahali pake mwenyewe chini ya beramu yake.
NUM 2:18 Upande wa magharibi kutakuwa na kambi ya makundi ya Efraimu chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Efraimu ni Elishama mwana wa Amihudi.
NUM 2:19 Kundi lake lina watu elfu arobaini na mia tano.
NUM 2:20 Kabila la Manase litafuata baada ya Efraimu. Kiongozi wa watu wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri.
NUM 2:21 Kundi lake lina watu elfu thelathini na mbili na mia mbili.
NUM 2:22 Kabila la Benyamini litafuata baada ya Manase. Kiongozi wa watu wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni.
NUM 2:23 Kundi lake lina watu elfu thelathini na tano na mia nne.
NUM 2:24 Wanaume wote walio katika kambi ya Efraimu kufuatana na makundi yao ni elfu mia moja na nane na mia moja. Nao watakuwa nafasi ya tatu kuondoka.
NUM 2:25 Upande wa kaskazini kutakuwa na makundi ya kambi ya Dani, chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Dani ni Ahiezeri mwana wa Amishadai.
NUM 2:26 Kundi lake lina watu elfu sitini na mbili na mia saba.
NUM 2:27 Kabila la Asheri watapiga kambi karibu na Dani. Kiongozi wa watu wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani.
NUM 2:28 Kundi lake lina watu elfu arobaini na moja na mia tano.
NUM 2:29 Kabila la Naftali litafuata. Kiongozi wa watu wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani.
NUM 2:30 Kundi lake lina watu elfu hamsini na tatu na mia nne.
NUM 2:31 Wanaume wote walio katika kambi ya Dani ni elfu mia moja hamsini na saba na mia sita. Wao watakuwa wa mwisho kuondoka chini ya beramu yao.
NUM 2:32 Hawa ndio Waisraeli, wakiwa wamehesabiwa kufuatana na jamaa zao. Wote walio kambini kwa makundi yao ni watu elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550).
NUM 2:33 Hata hivyo, Walawi hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
NUM 2:34 Kwa hiyo Waisraeli wakafanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru Musa. Hivyo ndivyo walivyopiga kambi chini ya beramu zao. Pia hivyo ndivyo walivyoondoka, kila mmoja akiwa na ukoo wake na jamaa yake.
NUM 3:1 Hivi ndivyo vizazi vya Haruni na Musa kwa wakati ambao Mwenyezi Mungu alizungumza na Musa katika Mlima Sinai.
NUM 3:2 Majina ya wana wa Haruni yalikuwa: Nadabu mzaliwa wa kwanza na Abihu, Eleazari na Ithamari.
NUM 3:3 Hayo yalikuwa majina ya wana wa Haruni, makuhani wapakwa mafuta, waliokuwa wamesimikwa kuhudumu kama makuhani.
NUM 3:4 Hata hivyo Nadabu na Abihu walikufa mbele za Mwenyezi Mungu walipotoa sadaka kwa moto usioruhusiwa mbele zake katika Jangwa la Sinai. Hawakuwa na wana; kwa hiyo Eleazari na Ithamari walihudumu peke yao kama makuhani wakati wote wa maisha ya Haruni baba yao.
NUM 3:5 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 3:6 “Walete kabila la Lawi mbele ya Haruni kuhani ili wamsaidie.
NUM 3:7 Watafanya huduma kwa ajili yake na kwa jumuiya yote katika Hema la Kukutania kwa kufanya kazi za Maskani.
NUM 3:8 Watatunza samani zote za Hema la Kukutania, wakitimiza wajibu wa kuhudumia Waisraeli kwa kufanya kazi ya Maskani.
NUM 3:9 Wakabidhi Walawi kwa Haruni na wanawe; hao ndio Waisraeli ambao wanakabidhiwa kwake kabisa.
NUM 3:10 Waweke Haruni na wanawe kuhudumu kama makuhani; mtu mwingine yeyote atakayesogea mahali patakatifu atauawa.”
NUM 3:11 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 3:12 “Nimewatwaa Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli badala ya mzaliwa wa kwanza wa kiume wa kila mwanamke wa Mwisraeli. Walawi ni wangu,
NUM 3:13 kwa kuwa wazaliwa wote wa kwanza ni wangu. Nilipowaua wazaliwa wa kwanza huko Misri, nilimtenga kila mzaliwa wa kwanza katika Israeli awe wangu, akiwa mwanadamu au mnyama. Watakuwa wangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
NUM 3:14 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa katika Jangwa la Sinai,
NUM 3:15 “Wahesabu Walawi kwa jamaa zao na koo zao. Mhesabu kila mwanaume mwenye umri wa mwezi mmoja au zaidi.”
NUM 3:16 Kwa hiyo Musa akawahesabu, kama alivyoamriwa na neno la Mwenyezi Mungu.
NUM 3:17 Haya yalikuwa majina ya wana wa Lawi: Gershoni, Kohathi na Merari.
NUM 3:18 Haya ndio yaliyokuwa majina ya koo za Wagershoni: Libni na Shimei.
NUM 3:19 Koo za Wakohathi zilikuwa ni: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli.
NUM 3:20 Koo za Wamerari zilikuwa ni: Mahli na Mushi.
NUM 3:21 Kulikuwa na koo za Walibni na Washimei kwa Gershoni; hizo zilikuwa koo za Wagershoni.
NUM 3:22 Idadi ya wanaume wote wa umri wa mwezi mmoja au zaidi waliohesabiwa walikuwa elfu saba na mia tano.
NUM 3:23 Ukoo wa Wagershoni walitakiwa kuweka kambi zao upande wa magharibi, nyuma ya Maskani.
NUM 3:24 Kiongozi wa jamaa za Wagershoni alikuwa Eliasafu mwana wa Laeli.
NUM 3:25 Katika Hema la Kukutania, Wagershoni walikuwa na wajibu wa kutunza Maskani na hema, vifuniko vyake, pazia katika mlango wa kuingilia ndani ya Hema la Kukutania,
NUM 3:26 mapazia ya ua, pazia katika ingilio la ua unaozunguka Maskani na madhabahu, pamoja na kamba, na kila kinachohusika kwa matumizi yake.
NUM 3:27 Kwa Kohathi kulikuwa koo za Waamrami, Waishari, Wahebroni na Wauzieli; hizo zilikuwa koo za Wakohathi.
NUM 3:28 Hesabu ya wanaume wote wenye umri wa mwezi mmoja au zaidi, walikuwa elfu nane na mia sita. Wakohathi waliwajibika kutunza mahali patakatifu.
NUM 3:29 Koo za Wakohathi zilitakiwa kuweka kambi zao upande wa kusini wa Maskani.
NUM 3:30 Kiongozi wa jamaa za koo za Wakohathi alikuwa Elisafani mwana wa Uzieli.
NUM 3:31 Waliwajibika kutunza Sanduku la Agano, meza, kinara cha taa, madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu vinavyotumika kuhudumu, pazia, na kila kitu kinachohusika na matumizi yake.
NUM 3:32 Kiongozi mkuu wa Walawi alikuwa Eleazari mwana wa kuhani, Haruni. Aliwekwa juu ya wale waliowajibika kutunza mahali patakatifu.
NUM 3:33 Kwa Merari kulikuwa na koo za Wamahli na Wamushi; hizi zilikuwa koo za Merari.
NUM 3:34 Hesabu ya wanaume wote wenye umri wa mwaka mmoja au zaidi waliohesabiwa, walikuwa elfu sita na mia mbili.
NUM 3:35 Kiongozi wa jamaa za koo za Wamerari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili. Hawa walitakiwa kuweka kambi zao upande wa kaskazini mwa Maskani.
NUM 3:36 Wamerari waliwekwa kutunza miimo ya Maskani, mataruma yake, nguzo, vitako na vifaa vyake vyote na kila kitu kilichohusika na matumizi yake,
NUM 3:37 na pia nguzo za ua unaozunguka pamoja na vitako vyake, vigingi vya hema na kamba zake.
NUM 3:38 Musa, na Haruni na wanawe walitakiwa kuweka kambi zao mashariki mwa Maskani, kuelekea mawio ya jua, mbele ya Hema la Kukutania. Wao walihusika na utunzaji wa mahali patakatifu kwa niaba ya Waisraeli. Mtu mwingine yeyote aliyepasogelea mahali patakatifu angeuawa.
NUM 3:39 Jumla ya hesabu ya Walawi waliohesabiwa na Musa na Haruni kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kufuatana na koo zao, pamoja na kila mwanaume mwenye umri wa mwezi mmoja au zaidi, walikuwa elfu ishirini na mbili.
NUM 3:40 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Wahesabu wazaliwa wa kwanza wa kiume wote wa Waisraeli wenye umri wa mwezi mmoja au zaidi na uorodheshe majina yao.
NUM 3:41 Nitwalie Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli, nayo mifugo ya Walawi badala ya wazaliwa wa mifugo ya Waisraeli. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
NUM 3:42 Hivyo Musa akawahesabu wazaliwa wa kwanza wote wa Waisraeli, kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru.
NUM 3:43 Jumla ya hesabu ya wazaliwa wa kwanza wanaume wenye umri wa mwezi mmoja au zaidi, walioorodheshwa kwa majina, walikuwa elfu ishirini na mbili na mia mbili na sabini na watatu (22,273).
NUM 3:44 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 3:45 “Watwae Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, nayo mifugo ya Walawi badala ya mifugo yao. Walawi watakuwa wangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
NUM 3:46 Ili kukomboa wazaliwa wa kwanza mia mbili na sabini na watatu (273) wa Waisraeli ambao wamezidi hesabu ya Walawi,
NUM 3:47 kusanya shekeli tano kwa kila mmoja, kufuatana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini.
NUM 3:48 Mpe Haruni na wanawe hizo fedha kwa ajili ya ukombozi wa idadi ya Waisraeli waliozidi.”
NUM 3:49 Kwa hiyo Musa akakusanya fedha za ukombozi kutoka kwa wale ambao hesabu yao ilizidi wale waliokombolewa na Walawi.
NUM 3:50 Kutokana na wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli alikusanya fedha yenye uzito wa shekeli elfu moja na mia tatu sitini na tano (1,365) kufuatana na shekeli ya mahali patakatifu.
NUM 3:51 Musa akampa Haruni na wanawe ile fedha ya ukombozi, kama alivyoamriwa na neno la Mwenyezi Mungu.
NUM 4:1 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni,
NUM 4:2 “Wahesabu Wakohathi walio sehemu ya Walawi kwa koo zao na jamaa zao.
NUM 4:3 Wahesabu wanaume wote wenye umri wa miaka thelathini hadi hamsini wanaokuja kutumika katika kazi ya Hema la Kukutania.
NUM 4:4 “Hii ndiyo kazi ya Wakohathi katika Hema la Kukutania: Watatunza vitu vilivyo vitakatifu sana.
NUM 4:5 Kambi inapohamishwa, Haruni na wanawe wataingia ndani na kushusha lile pazia la kuzuilia na kufunika nalo Sanduku la Ushuhuda.
NUM 4:6 Kisha watafunika juu yake na ngozi za pomboo, na kutandaza juu yake kitambaa cha rangi ya buluu iliyokolea na kuingiza mipiko mahali pake.
NUM 4:7 “Juu ya meza ya mikate ya Wonesho watatandaza kitambaa cha buluu na waweke sahani juu yake, masinia, bakuli na magudulia kwa ajili ya sadaka za kinywaji; mkate ule ambao upo hapa daima utabaki juu yake.
NUM 4:8 Juu ya hivyo vitu watatandaza kitambaa chekundu na kufunika kwa ngozi za pomboo na kuweka mipiko yake mahali pake.
NUM 4:9 “Watachukua kitambaa cha buluu na kufunika kinara cha taa kilicho kwa ajili ya nuru, pamoja na taa zake, mikasi yake, sinia zake, magudulia yake yote yaliyotumika kuwekea mafuta.
NUM 4:10 Kisha watakisokotea pamoja na vifaa vyake vyote katika ngozi za pomboo na kukiweka kwenye jukwaa lake.
NUM 4:11 “Juu ya madhabahu ya dhahabu watatandaza kitambaa cha buluu na kukifunika kwa ngozi za pomboo na kuweka mipiko yake mahali pake.
NUM 4:12 “Watavichukua vyombo vyote vinavyotumika kuhudumia mahali patakatifu, watavisokotea kwenye kitambaa cha buluu na kufunika kwa ngozi za pomboo, na kuviweka juu ya miti ya kuchukulia.
NUM 4:13 “Wataondoa majivu kutoka madhabahu ya shaba na kutandaza kitambaa cha zambarau juu yake.
NUM 4:14 Kisha wataweka vyombo vyote juu yake vinavyotumika kwa kuhudumia madhabahuni pamoja na vyombo vya kutolea moto, nyuma, miiko na mabakuli ya kunyunyizia. Juu yake watatandaza ngozi za pomboo ya kufunika, na kuweka mipiko mahali pake.
NUM 4:15 “Baada ya Haruni na wanawe kumaliza kazi ya kufunika samani takatifu na vyombo vyake vyote, watu watakapokuwa tayari kung’oa kambi, Wakohathi watakuja kufanya kazi ya kubeba. Lakini wasije wakagusa vitu vitakatifu la sivyo watakufa. Wakohathi ndio watakaobeba vile vitu vilivyomo katika Hema la Kukutania.
NUM 4:16 “Eleazari mwana wa Haruni, kuhani, ndiye atakayesimamia mafuta kwa ajili ya taa, uvumba wenye harufu nzuri, sadaka za kila siku za nafaka na mafuta ya upako. Ndiye atakayekuwa msimamizi wa maskani yote ya Mungu na kila kitu kilicho ndani yake, pamoja na samani takatifu na vyombo vyake.”
NUM 4:17 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni,
NUM 4:18 “Hakikisheni kwamba koo za kabila la Wakohathi hawatengwi kutoka Walawi.
NUM 4:19 Ili wapate kuishi wala wasife wanapokaribia vitu vitakatifu sana, uwafanyie hivi: Haruni na wanawe wataenda mahali patakatifu na kumgawia kila mtu kazi yake, na kwamba ni nini atakachochukua.
NUM 4:20 Lakini Wakohathi hawaruhusiwi kuingia ndani ili kuangalia vitu vitakatifu, hata kwa kitambo kidogo, la sivyo watakufa.”
NUM 4:21 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 4:22 “Wahesabu pia Wagershoni kwa jamaa zao na koo zao.
NUM 4:23 Wahesabu wanaume wote wenye umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao huja kutumika katika Hema la Kukutania.
NUM 4:24 “Hii ndiyo huduma ya koo za Wagershoni wakati wanapofanya kazi na kubeba mizigo.
NUM 4:25 Watabeba mapazia ya maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, kifuniko chake na kifuniko cha nje cha ngozi za pomboo, mapazia ya maingilio ya Hema la Kukutania,
NUM 4:26 mapazia ya ua unaozunguka Maskani na madhabahu, pazia la maingilio, kamba na vifaa vyote vinavyotumika katika huduma yake. Wagershoni watafanya yote yatakiwayo kufanyika na vitu hivi.
NUM 4:27 Utumishi wao wote ukiwa ni kuchukua au wa kufanya kazi nyingine, utafanyika chini ya maelekezo ya Haruni na wanawe. Mtawapangia kama wajibu wao yote watakayoyafanya.
NUM 4:28 Hii ndiyo huduma ya koo za Wagershoni katika Hema la Kukutania. Wajibu wao utakuwa chini ya maelekezo ya Ithamari mwana wa kuhani Haruni.
NUM 4:29 “Wahesabu Wamerari kwa koo zao na jamaa zao.
NUM 4:30 Wahesabu wanaume wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao watakuja kutumika katika Hema la Kukutania.
NUM 4:31 Huu ndio wajibu wao wanapofanya huduma katika Hema la Kukutania: kubeba miimo ya Maskani, mataruma yake, nguzo na vitako,
NUM 4:32 nguzo za ua unaozunguka pamoja na vitako vyake, vigingi vya hema, kamba, vifaa vyake vyote na kila kitu kinachohusiana na matumizi yake. Kila mtu mpangie vitu maalum vya kubeba.
NUM 4:33 Huu ndio utumishi wa koo za Merari kama watakavyofanya kazi katika Hema la Kukutania, chini ya maelekezo ya Ithamari mwana wa kuhani, Haruni.”
NUM 4:34 Musa, Haruni na viongozi wa jumuiya wakawahesabu Wakohathi kwa koo zao na jamaa zao.
NUM 4:35 Wanaume wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao walikuja kutumika katika Hema la Kukutania,
NUM 4:36 waliohesabiwa kwa koo zao, walikuwa elfu mbili na mia saba hamsini (2,750).
NUM 4:37 Hii ilikuwa ndiyo jumla ya wote wale wa koo za Wakohathi ambao walitumika katika Hema la Kukutania. Musa na Haruni waliwahesabu kufuatana na amri ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Musa.
NUM 4:38 Wagershoni walihesabiwa kwa koo zao na jamaa zao.
NUM 4:39 Watu wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao walikuja kutumika katika Hema la Kukutania,
NUM 4:40 waliohesabiwa kwa koo zao na jamaa zao, walikuwa elfu mbili na mia sita na thelathini (2,630).
NUM 4:41 Hii ilikuwa ndiyo jumla ya wale wa koo za Gershoni ambao walitumika katika Hema la Kukutania. Musa na Haruni waliwahesabu kufuatana na amri ya Mwenyezi Mungu.
NUM 4:42 Wamerari walihesabiwa kwa koo zao na jamaa zao.
NUM 4:43 Wanaume wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi miaka hamsini ambao walikuja kutumika katika Hema la Kukutania,
NUM 4:44 waliohesabiwa kwa koo zao, walikuwa elfu tatu na mia mbili.
NUM 4:45 Hii ilikuwa ndiyo jumla ya wale wa koo za Wamerari. Musa na Haruni waliwahesabu kufuatia amri ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Musa.
NUM 4:46 Hivyo Musa, Haruni na viongozi wa Israeli waliwahesabu Walawi wote kwa koo zao na jamaa zao.
NUM 4:47 Wanaume wote wenye umri wa kuanzia miaka thelathini hadi hamsini waliokuja kufanya kazi ya kuhudumu na kubeba Hema la Kukutania
NUM 4:48 walikuwa elfu nane na mia tano themanini (8,580).
NUM 4:49 Kwa amri ya Mwenyezi Mungu kupitia Musa, kila mmoja aligawiwa kazi yake na kuambiwa kitu cha kubeba. Hivyo ndivyo walivyohesabiwa kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 5:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 5:2 “Waamuru Waisraeli kumtoa nje ya kambi mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi uambukizao, au anayetokwa na majimaji ya aina yoyote, au ambaye ni najisi kwa sababu ya maiti.
NUM 5:3 Hii itakuwa ni kwa wote, yaani wanaume na wanawake; watoeni nje ya kambi ili wasije wakanajisi kambi yao, ambamo ninaishi miongoni mwao”.
NUM 5:4 Waisraeli wakafanya hivyo; wakawatoa nje ya kambi. Wakafanya kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwelekeza Musa.
NUM 5:5 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 5:6 “Waambie Waisraeli, ‘Mwanaume au mwanamke akimkosea mwenzake kwa njia yoyote, na kwa hivyo akawa si mwaminifu kwa Mwenyezi Mungu, mtu huyo ana hatia,
NUM 5:7 na ni lazima atubu dhambi aliyoifanya. Ni lazima atoe malipo kamili kwa ajili ya kosa lake, aongeze sehemu ya tano juu ya malipo hayo na kutoa yote kwa mtu aliyemkosea.
NUM 5:8 Lakini ikiwa mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye malipo yanaweza kufanywa kwa ajili ya kosa, malipo yatakuwa mali ya Mwenyezi Mungu, nayo ni lazima apewe kuhani, pamoja na kondoo dume ambaye anatumika kufanyia upatanisho kwa ajili yake.
NUM 5:9 Matoleo yote matakatifu ya Waisraeli wanayoleta kwa kuhani yatakuwa yake.
NUM 5:10 Kila kitu cha mtu kilichowekwa wakfu ni chake mwenyewe, lakini kile atoacho kwa kuhani kitakuwa cha kuhani.’ ”
NUM 5:11 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 5:12 “Nena na Waisraeli uwaambie: ‘Ikiwa mke wa mtu amepotoka na si mwaminifu kwa mumewe,
NUM 5:13 kwa kukutana kimwili na mwanaume mwingine, tendo hili likafichika kwa mumewe na unajisi wake usigundulike (kwa kuwa hakuna ushahidi dhidi yake, naye hakukamatwa katika tendo hilo),
NUM 5:14 nazo hisia za wivu zikamjia mumewe na kumshuku mkewe, naye mke yule ni najisi, au mumewe ana wivu na akamshuku ingawa si najisi,
NUM 5:15 basi atampeleka mkewe kwa kuhani. Huyo mume itampasa apeleke pia sadaka ya unga wa shayiri kiasi cha sehemu ya kumi ya efa kwa niaba ya mkewe. Huyo mwanaume kamwe asimimine mafuta juu ya huo unga wala asiweke uvumba juu yake, kwa sababu ni sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu, sadaka ya ukumbusho ili kukumbushia uovu.
NUM 5:16 “ ‘Kuhani atamleta huyo mwanamke na kumsimamisha mbele za Mwenyezi Mungu.
NUM 5:17 Kisha kuhani atachukua sehemu ya maji matakatifu ndani ya gudulia la udongo na kuchanganya na baadhi ya vumbi kutoka sakafu ya Maskani.
NUM 5:18 Baada ya kuhani kumsimamisha huyo mwanamke mbele za Mwenyezi Mungu, atazifungua nywele za huyo mwanamke na kuweka sadaka ya ukumbusho mikononi mwake, ile sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu, huku kuhani mwenyewe akishikilia yale maji machungu yaletayo laana.
NUM 5:19 Kisha kuhani atamwapiza huyo mwanamke, akimwambia, “Ikiwa hakuna mwanaume mwingine aliyekutana kimwili nawe, wala hujapotoka na kuwa najisi wakati ukiwa umeolewa na mumeo, maji haya machungu yaletayo laana na yasikudhuru.
NUM 5:20 Lakini ikiwa umepotoka wakati ukiwa umeolewa na mume wako na umejinajisi mwenyewe kwa kukutana kimwili na mwanaume mwingine asiyekuwa mumeo”;
NUM 5:21 hapa kuhani atamweka huyo mwanamke chini ya laana ya kiapo akisema: “Mwenyezi Mungu na awafanye watu wako wakulaani na kukukataa, wakati Mwenyezi Mungu atakapolifanya paja lako kupooza na tumbo lako kuvimba.
NUM 5:22 Maji haya yaletayo laana na yaingie ndani ya mwili wako ili tumbo lako livimbe na paja lako lipooze.” “ ‘Kisha mwanamke atasema, “Amen. Iwe hivyo.”
NUM 5:23 “ ‘Kuhani ataandika laana hizi kwenye kitabu, kisha atazioshea laana hizo kwenye yale maji machungu.
NUM 5:24 Kuhani atamnywesha yule mwanamke yale maji machungu yaletayo laana, nayo maji haya yatamwingia na kumsababishia maumivu makali.
NUM 5:25 Kuhani atachukua sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu kutoka mikononi mwa huyo mwanamke, naye ataipunga mbele za Mwenyezi Mungu na kuileta madhabahuni.
NUM 5:26 Kisha kuhani atachota sadaka ya nafaka mkono uliojaa kama sehemu ya kumbukumbu na kuiteketeza juu ya madhabahu, baada ya hayo, atamtaka huyo mwanamke anywe yale maji.
NUM 5:27 Kama amejitia unajisi na kukosa uaminifu kwa mumewe, wakati anapotakiwa anywe maji yale yaletayo laana, yatamwingia na kusababisha maumivu makali; tumbo lake litavimba na paja lake litapooza, naye atakuwa amelaaniwa miongoni mwa watu wake.
NUM 5:28 Hata hivyo, ikiwa huyo mwanamke hakujitia unajisi, naye ni safi, atasafishwa hatia na ataweza kuzaa watoto.
NUM 5:29 “ ‘Basi, hii ndiyo sheria ya wivu mwanamke anapopotoka na kujitia unajisi akiwa ameolewa na mumewe,
NUM 5:30 au hisia za wivu zinapomjia mwanaume kwa sababu ya kumshuku mkewe. Kuhani atamfanya huyo mwanamke kusimama mbele za Mwenyezi Mungu na atatumia sheria hii yote kwa huyo mwanamke.
NUM 5:31 Mume atakuwa hana hatia ya kosa lolote, bali mwanamke atayachukua matokeo ya dhambi yake.’ ”
NUM 6:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 6:2 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Ikiwa mwanaume au mwanamke anataka kuweka nadhiri maalum, nadhiri ya kutengwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama Mnadhiri,
NUM 6:3 ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine chochote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu.
NUM 6:4 Kwa muda wote atakaokuwa Mnadhiri, kamwe hatakula chochote kitokanacho na mzabibu, sio mbegu wala maganda.
NUM 6:5 “ ‘Kwa muda wote wa nadhiri yake ya kujitenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wembe hautapita kichwani mwake. Ni lazima awe mtakatifu hadi kipindi cha kujitenga kwake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kiishe; ni lazima aache nywele za kichwa chake zirefuke.
NUM 6:6 Kwa kipindi chochote cha kujitenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mnadhiri hatakaribia maiti.
NUM 6:7 Hata kama baba yake mwenyewe au mama au kaka au dada akifa, hatajinajisi mwenyewe kwa ajili yao, kwa sababu ishara ya kujiweka wakfu kwake kwa Mungu ipo katika kichwa chake.
NUM 6:8 Kwa kipindi chote cha kujitenga kwake, yeye ni wakfu kwa Mwenyezi Mungu.
NUM 6:9 “ ‘Kama mtu yeyote akifa ghafula karibu na Mnadhiri, atakuwa ametiwa unajisi nywele zake alizoziweka wakfu, hivyo ni lazima anyoe nywele zake siku ya utakaso wake, yaani siku ya saba.
NUM 6:10 Kisha siku ya nane ni lazima alete hua wawili au makinda wawili wa njiwa kwa kuhani katika mlango wa Hema la Kukutania.
NUM 6:11 Kuhani atatoa mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Mnadhiri kwa sababu ametenda dhambi kwa kuwa mbele ya maiti. Siku hiyo hiyo atakiweka wakfu tena kichwa chake.
NUM 6:12 Ni lazima ajitoe kabisa kwa Mwenyezi Mungu kwa kipindi cha kujitenga kwake, na ni lazima atoe mwana-kondoo wa kiume wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya hatia. Siku zilizopita hazitahesabiwa kwa sababu alijitia unajisi katika siku zake za kujitenga.
NUM 6:13 “ ‘Basi hii ndiyo sheria kwa ajili ya Mnadhiri baada ya kipindi chake cha kujitenga kupita. Ataletwa kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
NUM 6:14 Hapo atatoa sadaka zake kwa Mwenyezi Mungu: mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya amani,
NUM 6:15 pamoja na sadaka zake za nafaka na za vinywaji, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, yaani maandazi yaliyotengenezwa kwa unga laini uliochanganywa na mafuta, na mikate myembamba iliyopakwa mafuta.
NUM 6:16 “ ‘Kuhani atavileta vitu hivyo mbele za Mwenyezi Mungu na kufanya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa.
NUM 6:17 Ataleta pia kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, na atatoa dhabihu kondoo dume kuwa sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka yake ya nafaka, na ya kinywaji.
NUM 6:18 “ ‘Kisha kwenye ingilio la Hema la Kukutania, Mnadhiri ni lazima anyoe nywele zake ambazo alikuwa ameziweka wakfu. Atazichukua hizo nywele na kuziweka ndani ya moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka ya amani.
NUM 6:19 “ ‘Baada ya Mnadhiri kunyoa hizo nywele zake za kujitenga kwake, kuhani atampa mikononi mwake bega la kondoo dume lililochemshwa, na pia andazi na mkate mwembamba kutoka kikapu, vyote vikiwa vimetengenezwa bila kuwekwa chachu.
NUM 6:20 Kisha kuhani ataviinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa; ni vitakatifu na ni mali ya kuhani, pamoja na kile kidari kilichoinuliwa, na lile paja lililotolewa. Baada ya hayo, Mnadhiri anaweza kunywa divai.
NUM 6:21 “ ‘Hii ndiyo sheria ya Mnadhiri ambaye anaweka nadhiri kwa matoleo yake kwa Mwenyezi Mungu kufuatana na kujitenga kwake, zaidi ya chochote kile anachoweza kupata. Ni lazima atimize nadhiri aliyoiweka kufuatana na sheria ya Mnadhiri.’ ”
NUM 6:22 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 6:23 “Mwambie Haruni na wanawe, ‘Hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli. Waambieni:
NUM 6:24 “ ‘ “Mwenyezi Mungu akubariki na kukulinda;
NUM 6:25 Mwenyezi Mungu akuangazie nuru ya uso wake na kukufadhili;
NUM 6:26 Mwenyezi Mungu akugeuzie uso wake na kukupa amani.” ’
NUM 6:27 “Hivyo wataliweka Jina langu juu ya Waisraeli, nami nitawabariki.”
NUM 7:1 Musa alipomaliza kuisimamisha Maskani, aliipaka mafuta na kuiweka wakfu pamoja na samani zake zote. Pia alitia madhabahu mafuta na kuiweka wakfu, pamoja na vyombo vyake vyote.
NUM 7:2 Ndipo viongozi wa Israeli, wale wakuu wa jamaa waliokuwa viongozi wa kabila wasimamizi wa wale waliohesabiwa, wakatoa sadaka.
NUM 7:3 Walizileta kama matoleo yao mbele za Mwenyezi Mungu: magari sita ya kukokotwa yaliyofunikwa, pamoja na maksai kumi na wawili; yaani maksai mmoja kutoka kwa kila kiongozi, na gari moja la kukokotwa kutoka kwa kila viongozi wawili. Haya waliyaleta mbele ya Maskani.
NUM 7:4 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 7:5 “Vikubali vitu hivi kutoka kwao, ili viweze kutumika katika kazi kwenye Hema la Kukutania. Wapatie Walawi kama kazi ya kila mtu itakavyohitaji.”
NUM 7:6 Hivyo Musa akachukua yale magari ya kukokotwa pamoja na maksai, na kuwapa Walawi.
NUM 7:7 Aliwapa Wagershoni magari mawili ya kukokotwa na maksai wanne, kama walivyohitaji kwa kazi yao,
NUM 7:8 na pia aliwapa Wamerari magari manne ya kukokotwa na maksai wanane, kama kazi yao ilivyohitaji. Wote walikuwa chini ya maelekezo ya Ithamari mwana wa kuhani, Haruni.
NUM 7:9 Lakini Musa hakuwapa Wakohathi chochote kati ya hivyo, kwa sababu walitakiwa kubeba vitu vitakatifu mabegani mwao, vile walikuwa wanawajibika.
NUM 7:10 Madhabahu yalipopakwa mafuta, viongozi walileta sadaka zao kwa ajili ya kule kuwekwa wakfu kwake na kuziweka mbele ya madhabahu.
NUM 7:11 Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Kila siku kiongozi mmoja ataleta sadaka yake ili kuwekwa wakfu madhabahu.”
NUM 7:12 Yule ambaye alileta sadaka yake siku ya kwanza alikuwa Nashoni, mwana wa Aminadabu, wa kabila la Yuda.
NUM 7:13 Sadaka yake ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:14 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:15 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:16 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:17 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:18 Siku ya pili yake Nethaneli mwana wa Suari, kiongozi wa Isakari, alileta sadaka yake.
NUM 7:19 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:20 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:21 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:22 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:23 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:24 Siku ya tatu Eliabu mwana wa Heloni, kiongozi wa watu wa Zabuloni, alileta sadaka yake.
NUM 7:25 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:26 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:27 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:28 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:29 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:30 Siku ya nne Elisuri mwana wa Shedeuri, kiongozi wa watu wa Reubeni, alileta sadaka yake.
NUM 7:31 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:32 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:33 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:34 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:35 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:36 Siku ya tano Shelumieli mwana wa Surishadai, kiongozi wa watu wa Simeoni, alileta sadaka yake.
NUM 7:37 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:38 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:39 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:40 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:41 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:42 Siku ya sita Eliasafu mwana wa Deueli, kiongozi wa watu wa Gadi, alileta sadaka yake.
NUM 7:43 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:44 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:45 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:46 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:47 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:48 Siku ya saba Elishama mwana wa Amihudi, kiongozi wa watu wa Efraimu, alileta sadaka yake.
NUM 7:49 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:50 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:51 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:52 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:53 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:54 Siku ya nane Gamalieli mwana wa Pedasuri, kiongozi wa watu wa Manase, alileta sadaka yake.
NUM 7:55 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:56 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:57 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:58 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:59 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:60 Siku ya tisa Abidani mwana wa Gideoni, kiongozi wa watu wa Benyamini, alileta sadaka yake.
NUM 7:61 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:62 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:63 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:64 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:65 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:66 Siku ya kumi Ahiezeri mwana wa Amishadai, kiongozi wa watu wa Dani, alileta sadaka yake.
NUM 7:67 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:68 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:69 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:70 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:71 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:72 Siku ya kumi na moja Pagieli mwana wa Okrani, kiongozi wa watu wa Asheri, alileta sadaka yake.
NUM 7:73 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:74 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:75 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:76 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:77 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:78 Siku ya kumi na mbili Ahira mwana wa Enani, kiongozi wa watu wa Naftali, alileta sadaka yake.
NUM 7:79 Sadaka aliyoleta ilikuwa: sahani moja ya fedha yenye uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na bakuli moja la fedha la kunyunyizia lenye uzito wa shekeli sabini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya nafaka;
NUM 7:80 sinia moja la dhahabu lenye uzito wa shekeli kumi, likiwa limejazwa uvumba;
NUM 7:81 fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja na mwana-kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
NUM 7:82 beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi;
NUM 7:83 maksai wawili, kondoo dume watano, beberu watano na wana-kondoo dume watano wa mwaka mmoja, ili vitolewe dhabihu kama sadaka ya amani.
NUM 7:84 Hizi ndizo sadaka zilizotolewa na viongozi wa Israeli madhabahu yalipowekwa wakfu, wakati yalipakwa mafuta: sahani kumi na mbili za fedha, bakuli kumi na mbili za fedha za kunyunyizia, na masinia kumi na mawili ya dhahabu.
NUM 7:85 Kila sahani ya fedha ilikuwa na uzito wa shekeli mia moja na thelathini, na kila bakuli la fedha la kunyunyizia lilikuwa na uzito wa shekeli sabini. Masinia yote kumi na mawili yalikuwa na uzito wa shekeli elfu mbili na mia nne kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.
NUM 7:86 Sahani kumi na mbili za dhahabu zilizojazwa uvumba zilikuwa na uzito wa shekeli kumi kila moja, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Kwa jumla, sahani za dhahabu zilikuwa na uzito wa shekeli mia moja na ishirini.
NUM 7:87 Jumla ya wanyama waliotolewa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa walikuwa fahali kumi na wawili wachanga, kondoo dume kumi na wawili, na wana-kondoo dume kumi na wawili wa mwaka mmoja, pamoja na sadaka zao za nafaka. Beberu kumi na wawili walitolewa kwa ajili ya sadaka za dhambi.
NUM 7:88 Jumla ya wanyama kwa ajili ya dhabihu ya sadaka ya amani walikuwa maksai ishirini na wanne, kondoo dume sitini, beberu wa mwaka mmoja sitini, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja sitini.
NUM 7:89 Musa alipoingia kwenye Hema la Kukutania kuzungumza na Mwenyezi Mungu, alisikia sauti ikisema naye kutoka kati ya wale makerubi wawili waliokuwa juu ya kile kiti cha rehema, juu ya Sanduku la Ushuhuda. Musa akazungumza na Mwenyezi Mungu.
NUM 8:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 8:2 “Sema na Haruni umwambie, ‘Utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’ ”
NUM 8:3 Haruni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 8:4 Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Mwenyezi Mungu alikuwa amemwonesha Musa.
NUM 8:5 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
NUM 8:6 “Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase.
NUM 8:7 Ili kuwatakasa, fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe.
NUM 8:8 Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
NUM 8:9 Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli.
NUM 8:10 Utawaleta Walawi mbele za Mwenyezi Mungu, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi.
NUM 8:11 Haruni atawaweka Walawi mbele za Mwenyezi Mungu wawe sadaka ya kuinuliwa kutoka kwa Waisraeli, ili wawe tayari kuifanya kazi ya Mwenyezi Mungu.
NUM 8:12 “Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Mwenyezi Mungu, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.
NUM 8:13 Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Haruni na wanawe, kisha wawatoe wawe sadaka ya kuinuliwa kwa Mwenyezi Mungu.
NUM 8:14 Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.
NUM 8:15 “Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa wawe sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania.
NUM 8:16 Wao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke Mwisraeli.
NUM 8:17 Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe.
NUM 8:18 Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli.
NUM 8:19 Kati ya Waisraeli wote, nimempa Haruni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”
NUM 8:20 Musa, Haruni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 8:21 Walawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Haruni akawasogeza mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa.
NUM 8:22 Baada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Haruni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 8:23 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 8:24 “Hili linawahusu Walawi: Wanaume wenye umri wa miaka ishirini na tano au zaidi watakuja kushiriki katika kazi kwenye Hema la Kukutania,
NUM 8:25 lakini watakapofika umri wa miaka hamsini, ni lazima waache kazi zao za kawaida wala wasiendelee.
NUM 8:26 Wanaweza kuwasaidia ndugu zao kufanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, lakini wao wenyewe kamwe hawatafanya hiyo kazi. Basi, hivi ndivyo utakavyogawa wajibu kwa Walawi.”
NUM 9:1 Mwenyezi Mungu akasema na Musa katika Jangwa la Sinai katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri. Akasema,
NUM 9:2 “Waamuru Waisraeli waadhimishe Pasaka katika wakati ulioamriwa.
NUM 9:3 Adhimisheni wakati ulioamriwa, yaani wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi huu, kulingana na desturi zake zote na masharti yake.”
NUM 9:4 Hivyo Musa akawaambia Waisraeli waiadhimishe Pasaka,
NUM 9:5 nao wakafanya hivyo kwenye Jangwa la Sinai wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Waisraeli wakafanya kila kitu kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 9:6 Lakini baadhi yao hawakuweza kuadhimisha Pasaka siku ile kwa sababu walikuwa najisi kwa ajili ya kugusa maiti. Kwa hiyo wakamwendea Musa na Haruni siku ile ile,
NUM 9:7 wakamwambia Musa, “Tumekuwa najisi kwa sababu tumegusa maiti, lakini kwa nini tuzuiliwe kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka yake pamoja na Waisraeli wengine katika wakati ulioamriwa?”
NUM 9:8 Musa akawajibu, “Ngojeni hadi nitafute kile Mwenyezi Mungu anachoagiza kuwahusu ninyi.”
NUM 9:9 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 9:10 “Waambie Waisraeli: ‘Mmoja wenu au wazao wenu wanapokuwa najisi kwa sababu ya maiti au wakiwa safarini, hata hivyo wanaweza kuadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu.
NUM 9:11 Wataiadhimisha wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Watamla mwana-kondoo, pamoja na mkate usiotiwa chachu, na mboga chungu.
NUM 9:12 Wasibakize chochote hadi asubuhi wala wasivunje mifupa ya mwana-kondoo. Wanapoiadhimisha Pasaka, hawana budi kufuata masharti yote.
NUM 9:13 Lakini mtu aliyetakasika na hayuko safarini asipoiadhimisha Pasaka, mtu huyo hana budi kukatiliwa mbali na watu wake kwa sababu hakutoa sadaka ya Mwenyezi Mungu kwa wakati ulioamriwa. Mtu huyo atawajibika kubeba matokeo ya dhambi yake.
NUM 9:14 “ ‘Mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye anataka kuiadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu, lazima afanye hivyo kwa kufuata desturi na masharti. Lazima masharti yawe sawasawa kwa mgeni na mzawa.’ ”
NUM 9:15 Katika siku hiyo ambayo Maskani, Hema la Ushuhuda, iliposimamishwa, wingu liliifunika. Kuanzia jioni hadi asubuhi wingu lililokuwa juu ya Maskani lilionekana kama moto.
NUM 9:16 Hivyo ndivyo lilivyoendelea kuwa; wingu liliifunika wakati wa mchana, na usiku lilionekana kama moto.
NUM 9:17 Wakati wowote wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, nao Waisraeli waliondoka; mahali popote wingu lilipotua, Waisraeli walipiga kambi.
NUM 9:18 Kwa amri ya Mwenyezi Mungu Waisraeli waliondoka, na kwa amri yake walipiga kambi. Kwa muda wote wingu lilipokaa juu ya Maskani, Waisraeli walibaki kambini.
NUM 9:19 Wingu lilipobaki juu ya Maskani kwa muda mrefu, Waisraeli walitii amri ya Mwenyezi Mungu nao hawakuondoka.
NUM 9:20 Wakati mwingine wingu lilikuwa juu ya Maskani kwa siku chache tu; kwa amri ya Mwenyezi Mungu wangepiga kambi na kisha kwa amri yake wangeondoka.
NUM 9:21 Wakati mwingine wingu lilikaa kuanzia jioni hadi asubuhi tu; lilipoinuka asubuhi, nao waliondoka. Iwe ni mchana au usiku, wakati wowote wingu lilipoinuka, waliondoka.
NUM 9:22 Ikiwa wingu lilikaa juu ya Maskani kwa siku mbili au mwezi au mwaka, Waisraeli wangebaki wamepiga kambi na hawakuondoka; lakini lilipoinuka, wangeondoka.
NUM 9:23 Kwa amri ya Mwenyezi Mungu walipiga kambi, na kwa amri ya Mwenyezi Mungu waliondoka. Walitii amri ya Mwenyezi Mungu, kufuatana na agizo lake kupitia Musa.
NUM 10:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
NUM 10:2 “Tengeneza tarumbeta mbili za fedha ya kufua, uzitumie kwa kuita jumuiya pamoja na wakati wa kuvunja makambi ili kuondoka.
NUM 10:3 Tarumbeta zote mbili zikipigwa, jumuiya yote itakusanyika mbele yako katika ingilio la Hema la Kukutania.
NUM 10:4 Kama tarumbeta moja tu ikipigwa, viongozi, yaani wakuu wa koo za Israeli, ndio watakaokusanyika mbele yako.
NUM 10:5 Mlio wa kujulisha hatari ukipigwa, makabila yaliyo na makambi upande wa mashariki yataondoka.
NUM 10:6 Mlio wa pili ukipigwa, walio kwenye makambi ya kusini wataondoka. Mlio huo wa kujulisha hatari utakuwa ishara ya kuondoka.
NUM 10:7 Ili kuwakusanya watu, piga tarumbeta zote, lakini siyo kwa mlio wa kujulisha hatari.
NUM 10:8 “Wana wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu na kwa vizazi vijavyo.
NUM 10:9 Mtakapopigana vita katika nchi yenu wenyewe dhidi ya adui anayewaonea, piga tarumbeta kwa mlio wa kujulisha hatari. Ndipo utakumbukwa na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuokolewa kutoka kwa adui zenu.
NUM 10:10 Pia nyakati za furaha yenu, yaani sikukuu zenu zilizoamriwa na sikukuu za Mwezi Mwandamo, mtapiga tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani, nazo zitakuwa ukumbusho kwa ajili yenu mbele za Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
NUM 10:11 Katika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya Maskani ya Ushuhuda.
NUM 10:12 Ndipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine hadi wingu lilipotua katika Jangwa la Parani.
NUM 10:13 Waliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la Mwenyezi Mungu kupitia kwa Musa.
NUM 10:14 Vikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya beramu yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao.
NUM 10:15 Nethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari,
NUM 10:16 naye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni.
NUM 10:17 Ndipo Maskani iliposhushwa, nao wana wa Gershoni na wana wa Merari ambao waliibeba wakaondoka.
NUM 10:18 Vikosi vya kambi ya Reubeni vilifuata, chini ya beramu yao. Elisuri mwana wa Shedeuri alikuwa kiongozi wao.
NUM 10:19 Shelumieli mwana wa Surishadai aliongoza kikosi cha kabila la Simeoni,
NUM 10:20 naye Eliasafu mwana wa Deueli aliongoza kikosi cha kabila la Gadi.
NUM 10:21 Kisha Wakohathi wakaondoka, wakichukua vitu vitakatifu. Maskani ilipaswa kusimamishwa kabla wao hawajafika.
NUM 10:22 Vikosi vya kambi ya Efraimu vilifuata, chini ya beramu yao. Elishama mwana wa Amihudi alikuwa kiongozi wao.
NUM 10:23 Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kikosi cha kabila la Manase,
NUM 10:24 naye Abidani mwana wa Gideoni alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Benyamini.
NUM 10:25 Mwishowe, kama kikosi cha nyuma cha ulinzi wa vikosi vyote, vikosi vya kambi ya Dani viliondoka chini ya beramu yao. Ahiezeri mwana wa Amishadai alikuwa kiongozi wao.
NUM 10:26 Pagieli mwana wa Okrani aliongoza kikosi cha kabila la Asheri,
NUM 10:27 naye Ahira mwana wa Enani aliongoza kikosi cha kabila la Naftali.
NUM 10:28 Huu ndio ulikuwa utaratibu wa kuondoka wa vikosi vya Waisraeli walipokuwa wanaondoka.
NUM 10:29 Basi Musa akamwambia Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwewe Musa, “Tunaondoka kwenda mahali ambapo Mwenyezi Mungu amesema ‘Nitawapa ninyi mahali hapo.’ Twende pamoja, nasi tutakutendea mema, kwa maana Mwenyezi Mungu ameahidi mambo mema kwa Israeli.”
NUM 10:30 Akajibu, “Hapana, sitaenda; nitarudi kwenye nchi yangu mwenyewe na watu wangu mwenyewe.”
NUM 10:31 Lakini Musa akasema, “Tafadhali usituache. Wewe unajua mahali yatupasa kupiga kambi jangwani, nawe unaweza kuwa macho yetu.
NUM 10:32 Ikiwa utafuatana nasi, tutashirikiana nawe mema yoyote tutakayopewa na Mwenyezi Mungu.”
NUM 10:33 Hivyo waliondoka kutoka mlima wa Mwenyezi Mungu, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika.
NUM 10:34 Wingu la Mwenyezi Mungu lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini.
NUM 10:35 Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Musa alisema, “Ee Mwenyezi Mungu, inuka! Watesi wako na watawanyike; adui zako na wakimbie mbele zako.”
NUM 10:36 Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema, “Ee Mwenyezi Mungu, rudi, kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika.”
NUM 11:1 Basi watu wakalalamika kwa habari ya taabu zao masikioni mwa Mwenyezi Mungu, naye alipowasikia, hasira yake ikawaka. Ndipo moto kutoka kwa Mwenyezi Mungu ukawaka miongoni mwao na kuteketeza baadhi ya viunga vya kambi.
NUM 11:2 Watu walipomlilia Musa, akamwomba Mwenyezi Mungu, nao moto ukazimika.
NUM 11:3 Hivyo mahali pale pakaitwa Tabera, kwa sababu moto kutoka kwa Mwenyezi Mungu uliwaka miongoni mwao.
NUM 11:4 Umati wa watu wenye zogo waliokuwa miongoni mwao walitamani sana chakula kingine, Waisraeli wakaanza kulia tena na kusema, “Laiti tungekuwa na nyama tule!
NUM 11:5 Tunakumbuka wale samaki tuliokula huko Misri bila gharama, pia yale matango, matikitimaji, mboga, vitunguu, na vitunguu saumu.
NUM 11:6 Lakini sasa tumepoteza hamu ya chakula; hatuoni kitu kingine chochote isipokuwa hii mana!”
NUM 11:7 Mana ilifanana kama mbegu za giligilani, nayo ilikuwa na rangi ya manjano iliyopauka.
NUM 11:8 Hao watu walienda kukusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia ya mkono au kuitwanga kwenye vinu. Waliipika vyunguni au kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama kitu kilichotengenezwa kwa mafuta ya zeituni.
NUM 11:9 Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, pia mana ilianguka pamoja nao.
NUM 11:10 Musa akasikia watu wa kila jamaa wakilia, kila mmoja kwenye mlango wa hema lake. Mwenyezi Mungu akakasirika mno, naye Musa akafadhaika.
NUM 11:11 Akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Kwa nini umeleta taabu hii juu ya mtumishi wako? Nimekufanyia nini cha kukuchukiza hata ukaweka mzigo huu wa watu hawa wote juu yangu?
NUM 11:12 Je, watu hawa wote mimi ndiye niliyewatungisha mimba? Je, ni mimi niliyewazaa? Kwa nini unaniambia niwachukue mikononi mwangu, kama vile mlezi abebavyo mtoto mchanga, hadi kwenye nchi uliyowaahidi baba zao?
NUM 11:13 Nitapata wapi nyama kwa ajili ya watu wote hawa? Wanaendelea kunililia wakisema, ‘Tupe nyama tule!’
NUM 11:14 Mimi siwezi kuwabeba watu hawa wote peke yangu, mzigo ni mzito sana kwangu.
NUM 11:15 Kama hivi ndivyo unavyonitendea, uniue sasa hivi, yaani kama nimepata kibali machoni pako, wala usiniache nione maangamizi yangu mwenyewe.”
NUM 11:16 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: “Niletee wazee sabini wa Israeli, unaowafahamu kama viongozi na maafisa miongoni mwa watu. Walete katika Hema la Kukutania, ili waweze kusimama huko pamoja nawe.
NUM 11:17 Nami nitashuka na kusema nawe huko. Nami nitachukua sehemu ya Roho yangu iliyo juu yako na kuiweka juu yao. Watakusaidia kubeba mzigo wa watu hao ili usije ukaubeba peke yako.
NUM 11:18 “Waambie hao watu: ‘Jiwekeni wakfu wenyewe kwa ajili ya kesho, wakati mtakapokula nyama. Mwenyezi Mungu aliwasikia mlipolia, mkisema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tulikuwa na hali nzuri zaidi katika nchi ya Misri!” Sasa Mwenyezi Mungu atawapa nyama, nanyi mtaila.
NUM 11:19 Hamtaila kwa siku moja tu, au siku mbili, au tano, kumi au siku ishirini,
NUM 11:20 bali kwa mwezi mzima hadi iwatokee puani, nanyi mtaichukia kabisa, kwa kuwa mmemkataa Mwenyezi Mungu, ambaye yupo miongoni mwenu, nanyi mmelia mbele zake, mkisema, “Hivi kwa nini tulitoka Misri?” ’ ”
NUM 11:21 Lakini Musa alisema, “Mimi niko hapa miongoni mwa watu elfu mia sita wanaotembea kwa miguu, nawe umesema, ‘Nitawapa nyama ya kula kwa mwezi mzima!’
NUM 11:22 Je, wangeweza kupata nyama ya kuwatosha hata kama makundi ya kondoo na ya ng’ombe yangechinjwa kwa ajili yao? Je, wangetosheka hata kama samaki wote wa baharini wangevuliwa kwa ajili yao?”
NUM 11:23 Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Je, mkono wa Mwenyezi Mungu ni mfupi sana? Sasa utaona kama jambo nililolisema litatimizwa kwa ajili yako au la.”
NUM 11:24 Kwa hiyo Musa akatoka na kuwaambia watu lile ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amesema. Akawakusanya wazee wao sabini, akawasimamisha kuzunguka Hema.
NUM 11:25 Kisha Mwenyezi Mungu akashuka katika wingu na kunena na Musa, naye akachukua sehemu ya Roho yake iliyokuwa juu ya Musa na kuiweka juu ya wale wazee sabini. Roho wa Mungu aliposhuka juu yao, wakatoa unabii, lakini hawakufanya hivyo tena.
NUM 11:26 Lakini watu wawili, ambao majina yao ni Eldadi na Medadi, walibaki kambini. Walikuwa wameorodheshwa miongoni mwa wale wazee sabini, lakini hawakutoka kwenda kwenye Hema. Lakini Roho wa Mungu pia alishuka juu yao, nao wakatabiri huko kambini.
NUM 11:27 Mwanaume mmoja kijana alikimbia na kumwambia Musa, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”
NUM 11:28 Yoshua mwana wa Nuni, aliyekuwa msaidizi wa Musa tangu ujana wake, akajibu, akasema, “Musa bwana wangu, wanyamazishe!”
NUM 11:29 Lakini Musa akajibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Ningetamani watu wote wa Mwenyezi Mungu wangekuwa manabii na kwamba Mwenyezi Mungu angeweka Roho yake juu yao!”
NUM 11:30 Ndipo Musa na wale wazee wa Israeli wakarudi kambini.
NUM 11:31 Kisha ukatokea upepo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nao ukawaletea kware kutoka baharini. Ukawaangusha kwenye eneo lote linalozunguka kambi na kujaa ardhini kimo cha mita moja hivi kutoka ardhini kwenye eneo la umbali wa mwendo wa siku moja kila upande.
NUM 11:32 Mchana kutwa na usiku kucha pamoja na siku nzima iliyofuata watu walitoka kwenda kuokota kware. Hakuna mtu yeyote aliyekusanya chini ya homeri kumi. Kisha wakazianika kuzunguka kambi yote.
NUM 11:33 Lakini walipokuwa wakila nyama, ilipokuwa ingali kati ya meno yao na kabla hawajamaliza kula, hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya watu, naye akawapiga kwa tauni.
NUM 11:34 Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Kibroth-Hataava, kwa sababu huko ndiko walipowazika watu ambao walitamani sana chakula kingine.
NUM 11:35 Kutoka Kibroth-Hataava watu wakasafiri hadi Haserothi na kukaa huko.
NUM 12:1 Miriamu na Haruni walianza kuzungumza dhidi ya Musa kwa sababu ya mke wake Mkushi, kwa kuwa alikuwa ameoa Mkushi.
NUM 12:2 Waliuliza, “Je, Mwenyezi Mungu amesema kupitia Musa peke yake? Je, hajasema kutupitia sisi pia?” Naye Mwenyezi Mungu akasikia hili.
NUM 12:3 (Basi Musa alikuwa mtu mnyenyekevu sana, mnyenyekevu kuliko mtu mwingine yeyote katika uso wa dunia.)
NUM 12:4 Ghafula Mwenyezi Mungu akawaambia Musa, Haruni na Miriamu, “Njooni katika Hema la Kukutania, ninyi nyote watatu.” Kwa hiyo wote watatu wakaenda.
NUM 12:5 Kisha Mwenyezi Mungu akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye ingilio la Hema, akawaita Haruni na Miriamu. Waliposogea mbele,
NUM 12:6 Mwenyezi Mungu akawaambia, “Sikilizeni maneno yangu: “Akiwepo nabii wa Mwenyezi Mungu miongoni mwenu, nitajifunua kwake kwa maono, nitanena naye katika ndoto.
NUM 12:7 Lakini sivyo kwa mtumishi wangu Musa; yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.
NUM 12:8 Kwake nitanena naye uso kwa uso, waziwazi wala si kwa mafumbo; yeye ataona umbo la Mwenyezi Mungu. Kwa nini basi ninyi hamkuogopa kuzungumza kinyume cha mtumishi wangu Musa?”
NUM 12:9 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi yao, akawaacha.
NUM 12:10 Hilo wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, Miriamu akawa tayari ana ukoma, mweupe kama theluji. Haruni akamgeukia, akaona ana ukoma.
NUM 12:11 Kisha Haruni akamwambia Musa, “Tafadhali, bwana wangu, usituhesabie dhambi hii ambayo tumeifanya kwa upumbavu.
NUM 12:12 Usimwache awe kama mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa mfu, ambaye nusu ya mwili wake imeharibika hapo atokapo katika tumbo la mama yake.”
NUM 12:13 Hivyo Musa akamlilia Mwenyezi Mungu akisema, “Ee Mungu, nakuomba umponye!”
NUM 12:14 Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Je, kama baba yake angemtemea usoni, asingeona aibu kwa siku saba? Mfungie nje ya kambi kwa siku saba; baada ya hapo anaweza kurudishwa kambini.”
NUM 12:15 Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya kambi kwa siku saba, nao watu hawakuendelea na safari hadi aliporudishwa kambini.
NUM 12:16 Baada ya hayo, watu waliondoka Haserothi, wakapiga kambi katika Jangwa la Parani.
NUM 13:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 13:2 “Watume baadhi ya watu wakaipeleleze nchi ya Kanaani, ninayowapa Waisraeli. Kutoka kwa kila kabila la baba zao, tuma mwanaume aliye mmoja wa viongozi wao.”
NUM 13:3 Hivyo kwa agizo la Mwenyezi Mungu Musa akawatuma kutoka Jangwa la Parani. Wote walikuwa viongozi wa Waisraeli.
NUM 13:4 Haya ndiyo majina yao: kutoka kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri;
NUM 13:5 kutoka kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori;
NUM 13:6 kutoka kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune;
NUM 13:7 kutoka kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu;
NUM 13:8 kutoka kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni;
NUM 13:9 kutoka kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu;
NUM 13:10 kutoka kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi,
NUM 13:11 kutoka kabila la Manase (kabila la Yusufu), Gadi mwana wa Susi;
NUM 13:12 kutoka kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali;
NUM 13:13 kutoka kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli;
NUM 13:14 kutoka kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi;
NUM 13:15 kutoka kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki.
NUM 13:16 Haya ndiyo majina ya watu ambao Musa aliwatuma kuipeleleza nchi. (Musa akampa Hoshea mwana wa Nuni jina Yoshua.)
NUM 13:17 Musa alipowatuma wakaipeleleze Kanaani, alisema, “Pandeni kupitia Negebu, mwende hadi nchi ya vilima.
NUM 13:18 Mwone nchi ni ya namna gani, na kama watu wanaoishi humo wana nguvu au ni wadhaifu, iwapo ni wachache au wengi.
NUM 13:19 Wanaishi katika nchi ya namna gani? Je, ni nzuri au mbaya? Wanaishi katika miji ya namna gani? Je, haina kuta au ngome?
NUM 13:20 Ardhi ikoje? Ina rutuba au la? Je, kuna miti ndani yake au la? Jitahidini kadiri mnavyoweza kuleta baadhi ya matunda ya nchi.” (Ulikuwa msimu wa kuiva zabibu za kwanza.)
NUM 13:21 Hivyo wakapanda na kuipeleleza nchi kutoka Jangwa la Sini hadi Rehobu, kuelekea Lebo-Hamathi.
NUM 13:22 Wakapanda kupitia Negebu hadi wakafika Hebroni, mahali ambapo Ahimani, Sheshai na Talmai, wazao wa Anaki, waliishi. (Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko Misri.)
NUM 13:23 Walipofika katika Bonde la Eshkoli, walikata tawi lililokuwa na kishada kimoja cha zabibu. Wawili wao wakalichukua lile tawi kwenye mti, pamoja na komamanga na tini.
NUM 13:24 Eneo lile likaitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya kile kishada cha zabibu ambacho Waisraeli walikikata huko.
NUM 13:25 Baada ya siku arobaini, wakarudi kutoka kuipeleleza nchi.
NUM 13:26 Wakarudi kwa Musa, Haruni na jumuiya yote ya Waisraeli huko Kadeshi kwenye Jangwa la Parani. Hapo ndipo walipotoa habari kwao na kwa kusanyiko lote na kuwaonesha matunda ya hiyo nchi.
NUM 13:27 Wakampa Musa taarifa hii: “Tuliingia katika nchi uliyotutuma, nayo inatiririka maziwa na asali! Hili hapa tunda lake.
NUM 13:28 Lakini watu wanaoishi huko ni wenye nguvu, na miji yao ina ngome na ni mikubwa sana. Huko tuliona hata wazao wa Anaki.
NUM 13:29 Waamaleki wanaishi Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanaishi katika nchi ya vilima; nao Wakanaani wanaishi karibu na bahari na kando ya Yordani.”
NUM 13:30 Kisha Kalebu akawanyamazisha watu mbele ya Musa na kusema, “Imetupasa kupanda na kuimiliki nchi, kwa maana hakika tunaweza kufanya hivyo.”
NUM 13:31 Lakini watu waliokuwa wamepanda pamoja naye wakasema, “Hatuwezi kuwashambulia wale watu; wana nguvu kuliko sisi.”
NUM 13:32 Wakaeneza taarifa mbaya miongoni mwa Waisraeli kuhusu nchi waliyoipeleleza. Wakasema, “Nchi tuliyoipeleleza hula watu wanaoishi ndani yake. Watu wote tuliowaona huko ni majitu.
NUM 13:33 Tuliwaona Wanefili huko (wazao wa Anaki wanatokana na Wanefili). Tulijiona kama panzi machoni petu wenyewe, nao ndivyo walivyotuona.”
NUM 14:1 Usiku ule watu wote wa jumuiya walipaza sauti zao na kulia kwa sauti kuu.
NUM 14:2 Waisraeli wote wakanung’unika dhidi ya Musa na Haruni, na kusanyiko lote wakawaambia, “Laiti tungekuwa tumefia humo nchi ya Misri! Au humu kwenye hili jangwa!
NUM 14:3 Kwa nini Mwenyezi Mungu anatuleta katika nchi hii ili tufe kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watachukuliwa kama nyara. Je, isingekuwa bora kwetu kurudi Misri?”
NUM 14:4 Wakasemezana wao kwa wao, “Inatupasa kumchagua kiongozi na kurudi Misri.”
NUM 14:5 Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko lote la Waisraeli waliokusanyika hapo.
NUM 14:6 Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale walioenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao,
NUM 14:7 wakasema na kusanyiko lote la Waisraeli, wakawaambia, “Nchi tuliyopita kati yake kuipeleleza ni nzuri sana.
NUM 14:8 Ikiwa Mwenyezi Mungu anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi inayotiririka maziwa na asali, naye atatupatia nchi hiyo.
NUM 14:9 Ila tu msimwasi Mwenyezi Mungu. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini Mwenyezi Mungu yupo pamoja nasi. Msiwaogope.”
NUM 14:10 Lakini kusanyiko lote wakazungumza kuhusu kuwapiga kwa mawe. Ndipo utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaonekana katika Hema la Kukutania kwa Waisraeli wote.
NUM 14:11 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Watu hawa watanidharau hadi lini? Wataendelea kukataa kuniamini mimi hadi lini, ingawa nimetenda ishara za miujiza miongoni mwao?
NUM 14:12 Nitawapiga kwa tauni na kuwaangamiza, lakini nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa lenye nguvu kuliko wao.”
NUM 14:13 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Ndipo Wamisri watasikia juu ya jambo hili! Kwa uweza wako uliwapandisha watu hawa kutoka miongoni mwao.
NUM 14:14 Nao watawaambia wenyeji wa nchi hii jambo hili. Wao tayari wameshasikia kwamba wewe, Ee Mwenyezi Mungu, upo pamoja na watu hawa, na kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeonekana uso kwa uso, nalo wingu lako hukaa juu yao. Tena wewe unawatangulia kwa nguzo ya wingu mchana na kwa nguzo ya moto usiku.
NUM 14:15 Ikiwa utawaua watu hawa wote mara moja, mataifa ambayo yamesikia taarifa hii kukuhusu wewe watasema,
NUM 14:16 ‘Mwenyezi Mungu alishindwa kuwaingiza watu hawa katika nchi aliyowaahidi kwa kiapo; hivyo akawaua jangwani.’
NUM 14:17 “Basi sasa nguvu za Bwana na zionekane, sawasawa na ulivyosema:
NUM 14:18 ‘Mwenyezi Mungu si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo na mwenye kusamehe dhambi na uasi. Lakini haachi kumwadhibu mwenye hatia, huadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne.’
NUM 14:19 Kwa kadiri ya upendo wako mkuu, usamehe dhambi ya watu hawa, kama vile ulivyowasamehe tangu walipotoka Misri hadi sasa.”
NUM 14:20 Mwenyezi Mungu akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba.
NUM 14:21 Hata hivyo, kwa hakika kama niishivyo, na kwa hakika kama utukufu wa Mwenyezi Mungu uijazavyo dunia yote,
NUM 14:22 hakuna hata mmoja wa watu hawa ambao waliuona utukufu wangu na ishara za miujiza niliyotenda huko Misri na huko jangwani, lakini ambaye hakunitii na akanijaribu mara hizi kumi,
NUM 14:23 hakuna hata mmoja wao atakayeona nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo. Hakuna hata mmoja ambaye amenidharau atakayeiona.
NUM 14:24 Lakini kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ana roho ya tofauti na ananifuata kwa moyo wote, nitamwingiza katika nchi aliyoiendea, nao wazao wake watairithi.
NUM 14:25 Kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani wanaishi katika mabonde, kesho geukeni mwelekee jangwani kwa kufuata njia iendayo Bahari ya Shamu.”
NUM 14:26 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni:
NUM 14:27 “Jumuiya hii ovu itanung’unika dhidi yangu hadi lini? Nimesikia malalamiko ya hawa Waisraeli wanaonung’unika.
NUM 14:28 Hivyo waambie, ‘Hakika kama niishivyo, asema Mwenyezi Mungu, nitawafanyia vitu vilevile nilivyosikia mkisema:
NUM 14:29 Kila mmoja wenu mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi ambaye alihesabiwa na amenung’unika dhidi yangu, miili yenu itaanguka katika jangwa hili.
NUM 14:30 Hakuna hata mmoja wenu atakayeingia katika nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kuwa makao yenu, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.
NUM 14:31 Lakini watoto wenu ambao mlisema watachukuliwa mateka, nitawaingiza humo ili waifurahie nchi ambayo ninyi mmeikataa.
NUM 14:32 Bali ninyi, miili yenu itaanguka katika jangwa hili.
NUM 14:33 Watoto wenu watakuwa wachungaji wa mifugo hapa kwa miaka arobaini, wakiteseka kwa ajili ya kukosa uaminifu kwenu, hadi mwili wa mtu wenu wa mwisho ulale katika jangwa hili.
NUM 14:34 Kwa miaka arobaini, mwaka mmoja kwa kila siku katika zile siku arobaini mlizoipeleleza nchi, mtateseka kwa ajili ya dhambi zenu, na kujua jinsi ilivyo vibaya kunifanya mimi kuwa adui yenu.’
NUM 14:35 Mimi Mwenyezi Mungu nimesema, na hakika nitafanya mambo haya kwa jumuiya hii yote ovu, ambayo imefungamana pamoja dhidi yangu. Watakutana na mwisho wao katika jangwa hili; hapa ndipo watafia.”
NUM 14:36 Hivyo watu wale ambao Musa alikuwa amewatuma kuipeleleza nchi, waliorudi na kuifanya jumuiya nzima kunung’unika dhidi ya Musa kwa kueneza taarifa mbaya kuhusu hiyo nchi:
NUM 14:37 watu hawa waliohusika kueneza taarifa mbaya kuhusu hiyo nchi walipigwa na kuanguka kwa tauni mbele za Mwenyezi Mungu.
NUM 14:38 Miongoni mwa watu walioenda kuipeleleza hiyo nchi, ni Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune peke yao waliosalia.
NUM 14:39 Musa alipotoa taarifa hii kwa Waisraeli wote, waliomboleza kwa uchungu.
NUM 14:40 Asubuhi na mapema siku iliyofuata, walipanda kilele kirefu cha nchi ya vilima, wakasema, “Tumetenda dhambi. Tutakwea hadi mahali Mwenyezi Mungu alipotuahidi.”
NUM 14:41 Lakini Musa akasema, “Kwa nini hamtii amri ya Mwenyezi Mungu? Jambo hili halitafanikiwa!
NUM 14:42 Msipande juu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hayupo pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu,
NUM 14:43 kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani watapambana nanyi huko. Kwa sababu mmemwacha Mwenyezi Mungu, hatakuwa pamoja nanyi, ninyi mtaanguka kwa upanga.”
NUM 14:44 Hata hivyo, kwa kiburi chao walipanda juu kuelekea nchi ya vilima virefu, ijapokuwa Musa hakutoka kambini wala Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu.
NUM 14:45 Ndipo Waamaleki na Wakanaani walioishi katika hiyo nchi ya vilima wakateremka na kuwashambulia, wakawapiga njia yote hadi Horma.
NUM 15:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 15:2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Baada ya ninyi kuingia katika nchi ninayowapa kama nyumbani,
NUM 15:3 nanyi mkitoa sadaka za kuteketezwa kwa moto, kutoka makundi ya ng’ombe au kondoo, kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu, ikiwa ni sadaka za kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum ama sadaka ya hiari au sadaka ya sikukuu zenu,
NUM 15:4 ndipo yeye aletaye sadaka yake ataiweka mbele za Mwenyezi Mungu sadaka ya nafaka, sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta.
NUM 15:5 Pamoja na kila mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, andaa robo ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji.
NUM 15:6 “ ‘Pamoja na kondoo dume, andaa sadaka ya nafaka ya sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na theluthi moja ya hini ya mafuta,
NUM 15:7 na theluthi moja ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Vitoe kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 15:8 “ ‘Unapoandaa fahali mchanga kama sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum au sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu,
NUM 15:9 leta pamoja na huyo fahali sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi ya efa uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.
NUM 15:10 Pia utaleta nusu ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Itakuwa sadaka iliyoteketezwa kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 15:11 Kila fahali au kondoo dume, kila mwana-kondoo au mbuzi mchanga, atatayarishwa kwa njia hii.
NUM 15:12 Fanyeni hivi kwa ajili ya kila mmoja, kwa kadiri ya wingi wa mtakavyoandaa.
NUM 15:13 “ ‘Kila mmoja ambaye ni mzawa ni lazima afanye vitu hivi kwa njia hii hapo aletapo sadaka ya kuteketezwa kwa moto kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 15:14 Kwa vizazi vijavyo, wakati wowote mgeni au mtu mwingine yeyote anayeishi miongoni mwenu aletapo sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu, ni lazima afanye sawasawa kabisa na jinsi mnavyofanya ninyi.
NUM 15:15 Jumuiya itakuwa na sheria hizo hizo kwenu na kwa mgeni aishiye miongoni mwenu; hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Ninyi na mgeni mtakuwa sawa mbele za Mwenyezi Mungu:
NUM 15:16 Sheria hizo na masharti hayo vitawahusu ninyi na pia mgeni aishiye miongoni mwenu.’ ”
NUM 15:17 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 15:18 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapeleka,
NUM 15:19 nanyi mkala chakula cha nchi hiyo, toeni sehemu ya chakula hicho kuwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu.
NUM 15:20 Toeni andazi kutoka kwa malimbuko ya chakula chenu kitokacho katika ardhi, na mkitoe kama sadaka kutoka sakafu ya kupuria nafaka.
NUM 15:21 Kwa vizazi vyote vijavyo hamna budi kutoa sadaka hii kwa Mwenyezi Mungu kutoka kwa malimbuko ya unga wenu.
NUM 15:22 “ ‘Basi kama pasipo kukusudia umeshindwa kushika mojawapo katika amri hizi ambazo Mwenyezi Mungu alimpa Musa,
NUM 15:23 amri yoyote ya Mwenyezi Mungu kwenu kupitia Musa, tangu siku ile Mwenyezi Mungu alipowapa na inaendelea hadi vizazi vyote vijavyo;
NUM 15:24 ikiwa hili limefanyika pasipo kukusudia bila jumuiya kuwa na habari nalo, basi jumuiya yote itatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa ikiwa harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji zilizoamriwa kwayo, na beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
NUM 15:25 Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Waisraeli, nao watasamehewa, kwa kuwa haikuwa makusudi nao wamemletea Mwenyezi Mungu sadaka iliyoteketezwa kwa moto na sadaka ya dhambi kwa ajili ya kosa lao.
NUM 15:26 Jumuiya yote ya Waisraeli pamoja na wageni wanaoishi miongoni mwao watasamehewa, kwa sababu watu wote walihusika katika kosa lile lisilokusudiwa.
NUM 15:27 “ ‘Lakini kama mtu mmoja peke yake akitenda dhambi pasipo kukusudia, ni lazima alete mbuzi jike wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
NUM 15:28 Kuhani atafanya upatanisho mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya yule aliyekosa kwa kufanya dhambi pasipo kukusudia, upatanisho utakapofanywa kwa ajili yake, atasamehewa.
NUM 15:29 Sheria hiyo moja itamhusu kila mmoja ambaye ametenda dhambi pasipo kukusudia, awe Mwisraeli mzawa ama mgeni.
NUM 15:30 “ ‘Lakini yeyote ambaye amefanya dhambi kwa dharau awe mzawa au mgeni, anamkufuru Mwenyezi Mungu, naye mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
NUM 15:31 Kwa sababu amelidharau neno la Mwenyezi Mungu na kuvunja amri zake, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali; hatia yake inabaki juu yake.’ ”
NUM 15:32 Waisraeli walipokuwa jangwani, mtu mmoja alikutwa akikusanya kuni siku ya Sabato.
NUM 15:33 Wale waliomkuta akikusanya kuni wakamleta kwa Musa, na Haruni na kusanyiko lote,
NUM 15:34 nao wakamweka kifungoni, kwa sababu haikufahamika kwa wazi kwamba afanyiwe nini.
NUM 15:35 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Huyo mtu ni lazima afe. Kusanyiko lote lazima wampige mawe nje ya kambi.”
NUM 15:36 Hivyo kusanyiko wakamtoa nje ya kambi na kumpiga mawe hadi akafa, kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 15:37 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 15:38 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo.
NUM 15:39 Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote za Mwenyezi Mungu, ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu.
NUM 15:40 Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu.
NUM 15:41 Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa Misri niwe Mungu wenu. Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
NUM 16:1 Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Pelethi, wakachukua baadhi ya watu,
NUM 16:2 wakainuka dhidi ya Musa. Pamoja nao walikuwa wanaume Waisraeli mia mbili na hamsini, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko.
NUM 16:3 Wakaja kama kikundi kuwapinga Musa na Haruni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili wote ni watakatifu, kila mmoja wao, naye Mwenyezi Mungu yu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko la Mwenyezi Mungu?”
NUM 16:4 Musa aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi.
NUM 16:5 Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “Asubuhi Mwenyezi Mungu ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye.
NUM 16:6 Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo,
NUM 16:7 kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele za Mwenyezi Mungu. Mtu ambaye Mwenyezi Mungu atamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!”
NUM 16:8 Pia Musa akamwambia Kora, “Enyi Walawi! Sasa nisikilizeni.
NUM 16:9 Haiwatoshi ninyi kwamba Mungu wa Israeli amewateua ninyi kutoka kusanyiko lote la Israeli, na kuwaleta karibu naye mpate kufanya kazi kwenye Maskani ya Mwenyezi Mungu, na kusimama mbele ya kusanyiko ili kuwahudumia?
NUM 16:10 Amekuleta wewe na ndugu zako Walawi mwe karibu naye; lakini sasa unajaribu kuchukua ukuhani pia.
NUM 16:11 Wewe na wafuasi wako wote mmekusanyika pamoja kinyume cha Mwenyezi Mungu. Haruni ni nani kwamba ninyi mnung’unike dhidi yake?”
NUM 16:12 Kisha Musa akawaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu. Lakini wao wakasema, “Sisi hatuji!
NUM 16:13 Haitoshi tu kwamba wewe umetuleta kutoka nchi inayotiririka maziwa na asali ili kutuua sisi jangwani? Nawe sasa pia unataka kuwa mkuu juu yetu?
NUM 16:14 Zaidi ya hayo, hujatuingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, wala hujatupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Je, utayang’oa macho ya watu hawa? Hapana, sisi hatuji!”
NUM 16:15 Ndipo Musa akakasirika sana na kumwambia Mwenyezi Mungu, “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua chochote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.”
NUM 16:16 Musa akamwambia Kora, “Wewe na wafuasi wako wote kesho mtatokea mbele za Mwenyezi Mungu: wewe na hao wenzako, pamoja na Haruni.
NUM 16:17 Kila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani, vyetezo mia mbili na hamsini kwa jumla, na kukileta mbele za Mwenyezi Mungu. Wewe na Haruni mtaleta vyetezo vyenu pia.”
NUM 16:18 Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani, na kusimama pamoja na Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania.
NUM 16:19 Kora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu wa Mwenyezi Mungu ukatokea kwa kusanyiko lote.
NUM 16:20 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni,
NUM 16:21 “Jitengeni na kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.”
NUM 16:22 Lakini Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?”
NUM 16:23 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 16:24 “Waambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ”
NUM 16:25 Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye.
NUM 16:26 Musa akawaonya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu chochote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.”
NUM 16:27 Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao.
NUM 16:28 Ndipo Musa akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Mwenyezi Mungu amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu.
NUM 16:29 Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi Mwenyezi Mungu hakunituma mimi.
NUM 16:30 Lakini ikiwa Mwenyezi Mungu ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi Mungu.”
NUM 16:31 Mara Musa alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka,
NUM 16:32 nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali yao yote.
NUM 16:33 Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kwa kusanyiko.
NUM 16:34 Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”
NUM 16:35 Moto ukaja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ukawateketeza wale watu mia mbili na hamsini waliokuwa wakifukiza uvumba.
NUM 16:36 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 16:37 “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Haruni, atoe vyetezo kwenye mabaki ya moto na kutawanya makaa mbali kiasi, kwa maana vyetezo ni vitakatifu:
NUM 16:38 vyetezo vya watu waliofanya dhambi iliyowagharimu maisha yao. Fua vyetezo hivyo kuwa bamba ili kufunika madhabahu, kwa maana vimeletwa mbele za Mwenyezi Mungu na vimekuwa vitakatifu. Navyo viwe ishara kwa Waisraeli.”
NUM 16:39 Hivyo kuhani Eleazari akavikusanya vile vyetezo vya shaba vilivyoletwa na wale waliokuwa wameteketezwa kwa moto, naye akavifua kufunika madhabahu,
NUM 16:40 kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwelekeza kupitia Musa. Hili lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba hakuna mtu hata mmoja, isipokuwa mzao wa Haruni, awezaye kuja kufukiza uvumba mbele za Mwenyezi Mungu, la sivyo, angekuwa kama Kora na wafuasi wake.
NUM 16:41 Siku iliyofuata jumuiya yote ya Waisraeli wakanung’unika dhidi ya Musa na Haruni, wakisema, “Mmewaua watu wa Mwenyezi Mungu.”
NUM 16:42 Lakini kusanyiko walipokusanyika kupingana na Musa na Haruni, nao wakageuka kuelekea Hema la Kukutania, ghafula wingu likafunika Hema, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukatokea.
NUM 16:43 Ndipo Musa na Haruni wakaenda mbele ya Hema la Kukutania,
NUM 16:44 naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 16:45 “Jitenge mbali na kusanyiko hili ili niweze kuwaangamiza mara moja.” Wakaanguka kifudifudi.
NUM 16:46 Kisha Musa akamwambia Haruni, “Chukua chetezo chako na uweke uvumba ndani, pamoja na moto kutoka madhabahuni, nawe uende haraka kwenye kusanyiko ili kufanya upatanisho kwa ajili yao. Ghadhabu imekuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na tauni imeanza.”
NUM 16:47 Hivyo Haruni akafanya kama Musa alivyosema, akakimbilia katikati ya kusanyiko. Tauni ilikuwa tayari imeanza miongoni mwa watu, lakini Haruni akafukiza uvumba na kufanya upatanisho kwa ajili yao.
NUM 16:48 Haruni akasimama kati ya waliokuwa hai na waliokufa, nayo tauni ikakoma.
NUM 16:49 Lakini walikufa watu elfu kumi na nne na mia saba kutokana na tauni hiyo, licha ya wale waliokuwa wamekufa kwa sababu ya Kora.
NUM 16:50 Ndipo Haruni akamrudia Musa kwenye mlango wa Hema la Kukutania, kwa maana tauni ilikuwa imekoma.
NUM 17:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 17:2 “Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa makabila ya baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake.
NUM 17:3 Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Haruni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao.
NUM 17:4 Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe.
NUM 17:5 Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manung’uniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako.”
NUM 17:6 Hivyo Musa akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Haruni ikiwa miongoni mwa hizo.
NUM 17:7 Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Mwenyezi Mungu ndani ya Hema la Ushuhuda.
NUM 17:8 Siku iliyofuata Musa aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Haruni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi.
NUM 17:9 Ndipo Musa akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za Mwenyezi Mungu. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.
NUM 17:10 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Rudisha fimbo ya Haruni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manung’uniko yao dhidi yangu, ili wasife.”
NUM 17:11 Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru.
NUM 17:12 Waisraeli wakamwambia Musa, “Tutakufa! Tumepotea, sote tumepotea!
NUM 17:13 Yeyote akaribiaye Maskani ya Mwenyezi Mungu atakufa. Je, sisi sote tutakufa?”
NUM 18:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Haruni, “Wewe, wanao na jamaa ya baba yako mtawajibika kwa makosa dhidi ya mahali patakatifu, na wewe na wanao peke yenu ndio mtakaowajibika kwa makosa dhidi ya ukuhani.
NUM 18:2 Walete Walawi wenzako kutoka kabila la baba zako ili waungane nanyi na kuwasaidia wakati wewe na wanao mnapohudumu mbele ya Hema la Ushuhuda.
NUM 18:3 Watawajibika kwenu na watafanya kazi zote za Hema, lakini kamwe wasisogelee vifaa vya patakatifu au madhabahu, la sivyo wao na ninyi mtakufa.
NUM 18:4 Watajiunga nanyi na watawajibika kwa utunzaji wa Hema la Kukutania, yaani kazi zote kwenye Hema, wala hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kusogea karibu hapo mlipo.
NUM 18:5 “Mtawajibika katika utunzaji wa mahali patakatifu na madhabahu, ili ghadhabu isiwaangukie Waisraeli tena.
NUM 18:6 Mimi mwenyewe nimewachagua Walawi wenzenu kutoka miongoni mwa Waisraeli kama zawadi kwenu, waliowekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu ili kufanya kazi katika Hema la Kukutania.
NUM 18:7 Lakini ni wewe tu na wanao mtakaoweza kutumika kama makuhani kuhusiana na kila kitu kwenye madhabahu na ndani ya pazia. Ninawapa utumishi wa ukuhani kama zawadi. Mtu mwingine yeyote atakayekaribia mahali patakatifu ni lazima auawe.”
NUM 18:8 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Haruni, “Mimi mwenyewe nimekuweka kuwa mwangalizi wa sadaka zote zitakazotolewa kwangu; matoleo yote matakatifu Waisraeli wanayonipa ninakupa wewe na wanao kuwa sehemu yenu na fungu lenu la milele.
NUM 18:9 Mtachukua sehemu ya yale matoleo matakatifu sana ambayo hayateketezwi kwa moto. Kutoka kwa matoleo yote wanayoniletea kama sadaka takatifu sana, ziwe za nafaka, au za dhambi, au za makosa, sehemu ile itakuwa yako na wanao.
NUM 18:10 Mtaila kama kitu kilicho kitakatifu sana; kila mwanaume ataila. Ni lazima mtaiheshimu kama takatifu.
NUM 18:11 “Hiki pia ni chako: chochote kilichotengwa kutoka matoleo yote ya sadaka za kuinuliwa za Waisraeli. Haya ninakupa wewe, na wanao wa kiume na wa kike kuwa sehemu yenu ya milele. Kila mmoja wa nyumba yako ambaye ametakasika anaweza kuyala.
NUM 18:12 “Ninawapa mafuta ya zeituni yaliyo bora kuliko yote, na divai mpya iliyo bora kuliko zote na nafaka wanazompa Mwenyezi Mungu kama malimbuko katika mavuno yao.
NUM 18:13 Malimbuko yote ya nchi ambayo wanamletea Mwenyezi Mungu yatakuwa yenu. Kila mmoja nyumbani mwako ambaye ametakasika anaweza kula.
NUM 18:14 “Kila kitu katika Israeli ambacho kimetolewa kwa Mwenyezi Mungu ni chenu.
NUM 18:15 Kila mzaliwa wa kwanza wa mwanadamu na wa mnyama, ambaye ametolewa kwa Mwenyezi Mungu ni wenu. Lakini ni lazima mtamkomboa kila mwana mzaliwa wa kwanza na kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wasio safi.
NUM 18:16 Watakapokuwa na umri wa mwezi mmoja, ni lazima mtawakomboa kwa bei ya ukombozi iliyowekwa, kwa shekeli tano za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, yenye uzito wa gera ishirini.
NUM 18:17 “Lakini kamwe usimkomboe mzaliwa wa kwanza wa maksai, kondoo au mbuzi; hawa ni watakatifu. Nyunyizia damu yao juu ya madhabahu na uchome mafuta yao kuwa sadaka inayotolewa kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 18:18 Nyama zao zitakuwa chakula chenu, kama ilivyokuwa kidari cha kuinuliwa na paja la mguu wa kulia.
NUM 18:19 Chochote kitakachotengwa kutoka sadaka takatifu ambazo Waisraeli wanamtolea Mwenyezi Mungu, ninakupa wewe, na wanao wa kiume na wa kike kuwa fungu lenu la milele. Ni agano la milele la chumvi mbele za Mwenyezi Mungu, kwako na wazao wako.”
NUM 18:20 Mwenyezi Mungu akamwambia Haruni, “Hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala hutakuwa na sehemu miongoni mwao; Mimi ni fungu lako na urithi wako miongoni mwa Waisraeli.
NUM 18:21 “Ninawapa Walawi zaka yote katika Israeli kama urithi wao kuwa kama malipo kwa kazi wanayoifanya wakati wanapohudumu katika Hema la Kukutania.
NUM 18:22 Kuanzia sasa, kamwe Waisraeli wasisogelee karibu na Hema la Kukutania, la sivyo watabeba matokeo ya dhambi zao, nao watakufa.
NUM 18:23 Ni Walawi watakaofanya kazi katika Hema la Kukutania na kubeba wajibu wa makosa dhidi yake. Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Hawatapokea urithi wowote miongoni mwa Waisraeli.
NUM 18:24 Badala yake, ninawapa Walawi zaka zote zinazotolewa na Waisraeli kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu kuwa urithi wao. Hiyo ndiyo sababu nimesema hivi kuwahusu: ‘Hawatakuwa na urithi miongoni mwa Waisraeli.’ ”
NUM 18:25 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 18:26 “Sema na Walawi na uwaambie: ‘Mtakapopokea zaka kutoka kwa Waisraeli ninayowapa kama urithi wenu kutoka kwao, ni lazima mtoe sehemu ya kumi ya hiyo zaka kuwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu, iwe zaka ya hiyo zaka.
NUM 18:27 Sadaka yenu itahesabiwa kwenu kama nafaka kutoka sakafu ya kupuria, au divai kutoka shinikizo la kukamulia zabibu.
NUM 18:28 Kwa njia hii, ninyi pia mtatoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu kutoka zaka zote mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Kutoka kwa zaka hizi, ni lazima mtoe sehemu ya Mwenyezi Mungu kwa Haruni, kuhani.
NUM 18:29 Ni lazima mtoe kama sehemu ya Mwenyezi Mungu iliyo nzuri sana tena ile sehemu iliyo takatifu sana kuliko zote ya kile kitu mlichopewa.’
NUM 18:30 “Waambie Walawi: ‘Mtakapotoa sehemu zilizo bora sana, itahesabiwa kwenu kama mazao ya sakafu ya kupuria nafaka, au ya shinikizo la kukamulia zabibu.
NUM 18:31 Ninyi na watu wa nyumbani mwenu mnaweza kula sehemu iliyobaki mahali popote, kwani ndio ujira wenu kwa ajili ya kazi yenu katika Hema la Kukutania.
NUM 18:32 Kwa kutoa sehemu zake zilizo bora sana, hamtakuwa na hatia katika jambo hili; ndipo hamtatia unajisi sadaka takatifu za Waisraeli, nanyi hamtakufa.’ ”
NUM 19:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni:
NUM 19:2 “Hivi ndivyo sheria ambayo Mwenyezi Mungu ameagiza itakavyo: Waambie Waisraeli wakuletee mtamba mwekundu asiye na dosari wala waa, na ambaye hajapata kufungwa nira.
NUM 19:3 Mpeni kuhani Eleazari huyo mtamba; naye atatolewa nje ya kambi na kuchinjwa mbele yake huyo kuhani.
NUM 19:4 Kisha kuhani Eleazari atachukua sehemu ya damu yake kwenye kidole chake, na kuinyunyiza mara saba kuelekea upande wa mbele ya Hema la Kukutania.
NUM 19:5 Wakati angali akitazama, mtamba huyo atateketezwa: ngozi yake, nyama yake, damu na sehemu zake za ndani.
NUM 19:6 Kuhani atachukua kuni za mti wa mwerezi, hisopo na sufu nyekundu, na kuvitupa kwenye huyo mtamba anayeungua.
NUM 19:7 Baada ya hayo, kuhani lazima afue nguo zake, na aoge mwili wake kwa maji. Kisha anaweza kurudi kambini, lakini atakuwa najisi hadi jioni.
NUM 19:8 Mtu amchomaye huyo mtamba lazima naye pia afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye pia atakuwa najisi hadi jioni.
NUM 19:9 “Mtu ambaye ametakaswa atakusanya majivu ya mtamba huyo na kuyaweka mahali nje ya kambi palipo safi. Yatahifadhiwa na jumuiya ya Waisraeli kwa matumizi katika maji ya utakaso; ni kwa ajili ya kutakasa kutoka dhambini.
NUM 19:10 Mtu akusanyaye majivu ya huyo mtamba ni lazima pia afue nguo zake, kadhalika naye pia atakuwa najisi hadi jioni. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Waisraeli na kwa wageni wanaoishi miongoni mwao.
NUM 19:11 “Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote atakuwa najisi kwa siku saba.
NUM 19:12 Ni lazima ajitakase mwenyewe kwa maji katika siku ya tatu na siku ya saba, ndipo atakuwa safi. Lakini kama hatajitakasa mwenyewe katika siku ya tatu na ya saba, hatakuwa safi.
NUM 19:13 Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote na kushindwa kujitakasa mwenyewe hunajisi Maskani ya Mwenyezi Mungu. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na Israeli. Kwa sababu hajanyunyiziwa maji ya utakaso, yeye ni najisi; unajisi wake unabaki juu yake.
NUM 19:14 “Hii ndiyo sheria itumikayo wakati mtu amekufa ndani ya hema: Yeyote aingiaye ndani ya hema hilo na yeyote aliye ndani yake watakuwa najisi kwa muda wa siku saba,
NUM 19:15 nacho kila chombo kisicho na kifuniko juu yake kitakuwa najisi.
NUM 19:16 “Mtu yeyote aliye nje mahali pa wazi agusaye mtu aliyeuawa kwa upanga au mtu aliyekufa kwa kifo cha kawaida, au mtu yeyote agusaye mfupa wa mtu aliyekufa au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba.
NUM 19:17 “Kwa mtu aliye najisi, weka majivu ya sadaka ya utakaso wa dhambi ndani ya chombo, umimine maji safi juu yao.
NUM 19:18 Kisha mtu aliyetakasika atachukua hisopo, achovye ndani ya maji, na kunyunyizia hema na vifaa vyote pamoja na watu ambao walikuwamo. Pia ni lazima amnyunyizie mtu yeyote ambaye amegusa mfupa wa mtu aliyekufa, au kaburi, au mtu aliyeuawa, au mtu ambaye amekufa kifo cha kawaida.
NUM 19:19 Mtu ambaye ni safi ndiye atakayemnyunyizia yeyote ambaye ni najisi siku ya tatu na siku ya saba, na katika siku ya saba atamtakasa mtu huyo. Mtu ambaye ametakaswa lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, na jioni ile atakuwa safi.
NUM 19:20 Lakini ikiwa mtu ambaye ni najisi hakujitakasa mwenyewe, ni lazima akatiliwe mbali na jumuiya, kwa sababu ameinajisi Maskani ya Mwenyezi Mungu. Maji ya utakaso hayajanyunyizwa juu yake, naye ni najisi.
NUM 19:21 Hili ni agizo la kudumu kwao. “Mtu anayenyunyiza yale maji ya utakaso lazima pia afue nguo zake, na yeyote anayegusa maji ya utakaso atakuwa najisi hadi jioni.
NUM 19:22 Kitu chochote anachogusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi, na yeyote akigusaye huwa najisi hadi jioni.”
NUM 20:1 Katika mwezi wa kwanza, jumuiya yote ya Waisraeli walifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa.
NUM 20:2 Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Musa na Haruni.
NUM 20:3 Watu wakagombana na Musa, na kusema, “Laiti tungekufa ndugu zetu walipokufa mbele za Mwenyezi Mungu!
NUM 20:4 Kwa nini mmewaleta jumuiya ya Mwenyezi Mungu kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu?
NUM 20:5 Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri hadi mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”
NUM 20:6 Musa na Haruni wakaondoka pale kwenye kusanyiko hadi kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukawatokea.
NUM 20:7 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 20:8 “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Haruni mkawakusanye watu wote. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”
NUM 20:9 Kwa hiyo Musa akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Mwenyezi Mungu kama alivyomwagiza.
NUM 20:10 Musa na Haruni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Musa akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?”
NUM 20:11 Ndipo Musa akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.
NUM 20:12 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”
NUM 20:13 Haya yalikuwa maji ya Meriba, ambapo Waisraeli waligombana na Mwenyezi Mungu, naye akajionesha kuwa mtakatifu kati yao.
NUM 20:14 Musa akawatuma wajumbe kutoka Kadeshi kwenda kwa mfalme wa Edomu, akisema: “Hili ndilo ndugu yako Israeli asemalo: Wewe unafahamu juu ya taabu zote ambazo zimetupata.
NUM 20:15 Baba zetu walishuka Misri, nasi tumeishi huko miaka mingi. Wamisri walitutesa sisi na baba zetu,
NUM 20:16 lakini tulipomlilia Mwenyezi Mungu, alisikia kilio chetu na akamtuma malaika akatutoa Misri. “Sasa tupo hapa Kadeshi, mji ulio mpakani mwa nchi yako.
NUM 20:17 Tafadhali turuhusu tupite katika nchi yako. Hatutapita katika shamba lolote, wala shamba la mizabibu, au kunywa maji kwenye kisima chochote. Tutasafiri kufuata njia kuu ya mfalme, na hatutageuka kulia wala kushoto hadi tuwe tumeshapita nchi yako.”
NUM 20:18 Lakini mfalme wa Edomu akajibu: “Hamtapita hapa. Mkijaribu kupita, tutatoka na kuwashambulia kwa upanga.”
NUM 20:19 Waisraeli wakajibu: “Sisi tutafuata njia kuu; tena ikiwa sisi au mifugo yetu tutakunywa tone la maji yenu, tutalilipia. Sisi tunataka tu kupita kwa miguu, wala si kitu kingine chochote.”
NUM 20:20 Watu wa Edomu wakajibu tena: “Hamwezi kupita hapa.” Ndipo watu wa Edomu wakatoka dhidi ya Waisraeli, jeshi kubwa lenye nguvu.
NUM 20:21 Kwa kuwa Waedomu waliwakatalia Waisraeli kupita katika nchi yao, Israeli wakageuka, wakawaacha.
NUM 20:22 Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori.
NUM 20:23 Kwenye Mlima Hori, karibu na mpaka wa Edomu, Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni,
NUM 20:24 “Haruni atakusanywa pamoja na watu wake. Hataingia katika nchi ninayowapa Waisraeli, kwa sababu ninyi wawili mliasi dhidi ya agizo langu kwenye maji ya Meriba.
NUM 20:25 Watwae Haruni na Eleazari mwanawe, na uwapandishe juu katika Mlima Hori.
NUM 20:26 Mvue Haruni mavazi yake, na umvike Eleazari mwanawe, kwa maana Haruni atakusanywa pamoja na watu wake; atakufa huko.”
NUM 20:27 Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza: Wakapanda Mlima Hori mbele ya macho ya jumuiya yote ya Waisraeli.
NUM 20:28 Musa akamvua Haruni mavazi yake na kumvika mwanawe Eleazari mavazi hayo. Naye Haruni akafia pale juu ya mlima. Kisha Musa na Eleazari wakateremka kutoka mlimani.
NUM 20:29 Jumuiya yote walipofahamu kwamba Haruni amekufa, Waisraeli wote wakamwomboleza kwa siku thelathini.
NUM 21:1 Mfalme wa Aradi, aliyekuwa Mkanaani aliyeishi huko Negebu, aliposikia kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, aliwashambulia Waisraeli na kuwateka baadhi yao.
NUM 21:2 Ndipo Israeli akaweka nadhiri hii kwa Mwenyezi Mungu: “Ikiwa utawatia watu hawa mikononi mwetu, tutaiangamiza kabisa miji yao.”
NUM 21:3 Mwenyezi Mungu akasikiliza ombi la Waisraeli, naye akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Wakawaangamiza kabisa na miji yao; hivyo mahali pale pakaitwa Horma.
NUM 21:4 Waisraeli wakasafiri kutoka Mlima Hori kupitia njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kuizunguka Edomu. Lakini watu wakakosa uvumilivu njiani,
NUM 21:5 wakamnung’unikia Mungu na Musa, wakisema, “Kwa nini umetupandisha kutoka Misri ili tufe jangwani? Hakuna mkate! Hakuna maji! Nasi tunachukia sana chakula hiki duni!”
NUM 21:6 Ndipo Mwenyezi Mungu akapeleka nyoka wenye sumu kati yao; wakawauma watu, nao Waisraeli wengi wakafa.
NUM 21:7 Watu wakamjia Musa na kusema, “Tumetenda dhambi wakati tuliponena dhidi ya Mwenyezi Mungu na dhidi yako. Mwombe Mwenyezi Mungu ili atuondolee hawa nyoka.” Hivyo Musa akawaombea hao watu.
NUM 21:8 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti; yeyote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.”
NUM 21:9 Kwa hiyo Musa akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu yeyote aliumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.
NUM 21:10 Waisraeli waliendelea na safari yao na wakapiga kambi huko Obothi.
NUM 21:11 Kisha wakaondoka Obothi na kupiga kambi huko Iye-Abarimu, katika jangwa linalotazamana na Moabu kuelekea mawio ya jua.
NUM 21:12 Kutoka hapo waliendelea mbele wakapiga kambi kwenye Bonde la Zeredi.
NUM 21:13 Wakasafiri kutoka hapo na kupiga kambi kando ya Mto Arnoni, ambao uko katika jangwa lililoenea hadi nchi ya Waamori. Mto Arnoni ni mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori.
NUM 21:14 Ndiyo sababu Kitabu cha Vita vya Mwenyezi Mungu kinasema: “Wahebu nchini Sufa, na mabonde, Mto Arnoni,
NUM 21:15 na miteremko ya mabonde inayofika hadi makazi ya Ari, na kuegemea mpakani mwa Moabu.”
NUM 21:16 Kutoka hapo waliendelea mbele hadi kisima cha Beeri; kwenye kisima ambacho Mwenyezi Mungu alimwambia Musa, “Wakusanye watu pamoja, nami nitawapa maji.”
NUM 21:17 Kisha Israeli akaimba wimbo huu: “Bubujika, ee kisima! Imba kuhusu maji,
NUM 21:18 kuhusu kisima ambacho kilichimbwa na wakuu, ambacho watu mashuhuri walikifukua, watu mashuhuri wakiwa na fimbo za utawala na bakora.” Kisha wakatoka jangwani kwenda Matana,
NUM 21:19 kutoka Matana wakafika Nahalieli, kutoka Nahalieli wakafika Bamothi,
NUM 21:20 na kutoka Bamothi wakafika kwenye bonde lililoko Moabu, mahali kilele cha Pisga kinatazamana na nyika.
NUM 21:21 Israeli akawatuma wajumbe kumwambia Sihoni mfalme wa Waamori:
NUM 21:22 “Uturuhusu tupite katika nchi yako. Hatutageuka kando kwenda katika mashamba au mashamba ya mizabibu, ama kunywa maji kutoka kisima chochote. Tutasafiri kwenye njia kuu ya mfalme hata tutakapokuwa tumekwisha kupita katika nchi yako.”
NUM 21:23 Lakini Sihoni hakumruhusu Israeli apite katika nchi yake. Alilikutanisha jeshi lake lote, wakaondoka kwenda jangwani ili kupigana na Israeli. Alipofika huko Yahazi, akapigana na Israeli.
NUM 21:24 Hata hivyo, Israeli walimshinda kwa upanga na kuimiliki nchi yake kutoka Mto Arnoni hadi Mto Yaboki, lakini ni kufikia nchi ya Waamoni tu, kwa sababu mipaka yake ilikuwa imezungushwa ukuta.
NUM 21:25 Israeli wakaiteka miji yote ya Waamori na kuimiliki, pamoja na Heshboni na makazi yote yanayoizunguka.
NUM 21:26 Heshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa amepigana dhidi ya mfalme wa Moabu aliyetangulia, na akawa amechukua ardhi yake yote hadi Mto Arnoni.
NUM 21:27 Ndiyo sababu watunga mashairi husema: “Njoo Heshboni na ujengwe tena; mji wa Sihoni na ufanywe upya.
NUM 21:28 “Moto uliwaka kutoka Heshboni, mwali wa moto kutoka mji wa Sihoni. Uliteketeza Ari ya Moabu, raia wa mahali pa Arnoni palipoinuka.
NUM 21:29 Ole wako, ee Moabu! Umeharibiwa, enyi watu wa Kemoshi! Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi, na binti zake kama mateka kwa Mfalme Sihoni wa Waamori.
NUM 21:30 “Lakini tumewashinda; Heshboni umeharibiwa hadi Diboni. Tumebomoa hadi kufikia Nofa, ulioenea hadi Medeba.”
NUM 21:31 Kwa hiyo Israeli akaishi katika nchi ya Waamori.
NUM 21:32 Baada ya Musa kutuma wapelelezi kwenda mji wa Yazeri, Waisraeli waliteka makazi ya mji huo, na kuwafukuza Waamori walioishi huko.
NUM 21:33 Kisha wakageuka na kwenda katika njia inayoelekea Bashani, naye Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote wakatoka kupigana nao huko Edrei.
NUM 21:34 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Usimwogope Ogu, kwa sababu nimeshamkabidhi mikononi mwako, pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Mtendee kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”
NUM 21:35 Kwa hiyo wakamuua, pamoja na wanawe na jeshi lake lote, bila ya kumwacha hata mtu mmoja hai. Nao wakaimiliki nchi yake.
NUM 22:1 Kisha Waisraeli wakasafiri katika tambarare za Moabu na kupiga kambi kando ya Mto Yordani, ng’ambo ya Yeriko.
NUM 22:2 Basi Balaki mwana wa Sipori, aliona mambo yale yote ambayo Israeli aliwatendea Waamori,
NUM 22:3 Moabu aliogopa, kwa kuwa walikuwa watu wengi sana. Hakika, Moabu alijawa na hofu kubwa kwa sababu ya Waisraeli.
NUM 22:4 Wamoabu wakawaambia wazee wa Midiani, “Umati huu wa watu unaenda kuramba kila kitu kinachotuzunguka, kama maksai anavyoramba majani ya shambani.” Kwa hiyo Balaki mwana wa Sipori, aliyekuwa mfalme wa Moabu wakati huo,
NUM 22:5 akatuma wajumbe kwenda kumwita Balaamu mwana wa Beori, aliyekuwa huko Pethori, karibu na Mto, katika nchi yake ya kuzaliwa. Balaki akasema: “Taifa limekuja kutoka Misri, nao wamefunika uso wa nchi, nao wamekaa karibu nami.
NUM 22:6 Sasa uje kuwalaani watu hawa, kwa kuwa wana nguvu sana kuliko mimi. Kisha huenda nikaweza kuwashinda na kuwatoa nje ya nchi. Kwa kuwa ninajua kwamba, wale unaowabariki wanabarikiwa na wale unaowalaani wanalaaniwa.”
NUM 22:7 Wazee wa Moabu na wa Midiani wakaondoka, wakiwa wamechukua ada ya uaguzi. Walipoenda kwa Balaamu, wakamweleza kile Balaki alikuwa amesema.
NUM 22:8 Balaamu akawaambia, “Mlale hapa usiku huu, nami nitawaletea jibu lile Mwenyezi Mungu atakalonipa.” Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakakaa naye.
NUM 22:9 Mungu akamjia Balaamu na kumuuliza, “Watu gani hawa walio pamoja nawe?”
NUM 22:10 Balaamu akamwambia Mungu, “Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alinipelekea ujumbe huu:
NUM 22:11 ‘Taifa ambalo limekuja kutoka Misri limefunika uso wa nchi. Sasa uje unilaanie hao watu. Kisha huenda nitaweza kupigana nao na kuwafukuza.’ ”
NUM 22:12 Lakini Mungu akamwambia Balaamu, “Usiende pamoja nao. Hupaswi kulaani watu hao, kwa kuwa wamebarikiwa.”
NUM 22:13 Asubuhi iliyofuata Balaamu akaamka, akawaambia wakuu wa Balaki, “Rudini katika nchi yenu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenikataza nisiende pamoja nanyi.”
NUM 22:14 Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakarudi kwa Balaki na kumwambia, “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.”
NUM 22:15 Kisha Balaki akatuma wakuu wengine, wengi zaidi na wanaoheshimiwa kuliko wale wa kwanza.
NUM 22:16 Wakafika kwa Balaamu na kumwambia: “Balaki mwana wa Sipori amesema hivi: Usiruhusu kitu chochote kikuzuie kuja kwangu,
NUM 22:17 kwa sababu nitakulipa vizuri sana na kufanya lolote usemalo. Njoo unilaanie watu hawa.”
NUM 22:18 Lakini Balaamu akawajibu, “Hata kama Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, singeweza kufanya kitu chochote kikubwa au kidogo ili kutenda kitu nje ya agizo la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
NUM 22:19 Mlale hapa usiku huu kama wale wengine walivyofanya, nami nitatafuta ni nini kingine Mwenyezi Mungu atakachoniambia.”
NUM 22:20 Usiku ule Mungu akamjia Balaamu na kumwambia, “Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita wewe, nenda nao, lakini ufanye tu lile nitakalokuambia.”
NUM 22:21 Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.
NUM 22:22 Lakini Mungu alikasirika sana alipoenda, naye malaika wa Mwenyezi Mungu akasimama barabarani kumpinga. Balaamu alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.
NUM 22:23 Punda alipomwona malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama barabarani, na upanga ukiwa mkononi mwake, punda akageukia upande kuelekea shambani. Balaamu akampiga ili amrudishe barabarani.
NUM 22:24 Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akasimama katika njia nyembamba iliyo kati ya mashamba mawili ya mizabibu, yakiwa na kuta pande zote mbili.
NUM 22:25 Punda alipomwona malaika wa Mwenyezi Mungu, alijisukumiza karibu na ukuta, na kugandamiza mguu wa Balaamu ukutani. Ndipo Balaamu akampiga tena punda.
NUM 22:26 Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akaendelea mbele na kusimama mahali pembamba ambapo hapakuwa na nafasi ya kugeuka mkono wa kulia wala wa kushoto.
NUM 22:27 Punda alipomwona malaika wa Mwenyezi Mungu, alilala chini Balaamu angali amempanda, naye Balaamu akakasirika na kumpiga kwa fimbo yake.
NUM 22:28 Kisha Mwenyezi Mungu akakifungua kinywa cha punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini kinachokufanya unipige mara hizi tatu?”
NUM 22:29 Balaamu akamjibu punda, “Umenifanya mjinga! Kama ningekuwa na upanga mkononi mwangu, ningekuua sasa hivi.”
NUM 22:30 Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si punda wako mwenyewe, ambaye umenipanda siku zote, hadi leo? Je, nimekuwa na tabia ya kufanya hivi kwako?” Akajibu, “Hapana.”
NUM 22:31 Kisha Mwenyezi Mungu akafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi Mungu amesimama barabarani akiwa ameufuta upanga wake. Balaamu akainama, akaanguka kifudifudi.
NUM 22:32 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamuuliza Balaamu, “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu hizi? Nimekuja kukuzuia kwa sababu njia yako imepotoka mbele yangu.
NUM 22:33 Punda aliniona na kunikwepa mara hizi tatu. Kama punda hangenikwepa, hakika ningekuwa nimeshakuua sasa, lakini ningemwacha punda hai.”
NUM 22:34 Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi Mungu, “Nimetenda dhambi. Sikutambua kuwa umesimama barabarani kunizuia. Basi kama haikupendezi, nitarudi.”
NUM 22:35 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Balaamu, “Uende na watu hao, lakini useme tu lile nikuambialo.” Kwa hiyo Balaamu akaenda na wale wakuu wa Balaki.
NUM 22:36 Balaki aliposikia kuwa Balaamu anakuja, akatoka kumlaki katika mji wa Moabu, katika mpaka wa Mto Arnoni, ukingoni mwa nchi yake.
NUM 22:37 Balaki akamwambia Balaamu, “Je, sikukupelekea jumbe za haraka? Kwa nini hukuja kwangu? Hivi kweli mimi siwezi kukulipa?”
NUM 22:38 Balaamu akajibu, “Vema, sasa nimekuja kwako. Lakini kwani nina uwezo wa kusema tu chochote? Ni lazima niseme tu kile ambacho Mungu ataweka kinywani mwangu.”
NUM 22:39 Kisha Balaamu alienda na Balaki hadi Kiriath-Husothi.
NUM 22:40 Balaki akatoa dhabihu ya ng’ombe na kondoo; baadhi yake akampa Balaamu na wakuu waliokuwa pamoja naye.
NUM 22:41 Asubuhi iliyofuata Balaki akamchukua Balaamu hadi Bamoth-Baali, na kutoka huko Balaamu akawaona baadhi ya watu.
NUM 23:1 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, mnitayarishie mafahali saba na kondoo dume saba.”
NUM 23:2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema; hao wawili kila mmoja wao akatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
NUM 23:3 Kisha Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati mimi ninaenda kando. Huenda Mwenyezi Mungu atakuja kukutana nami. Lolote atakalonifunulia, nitakuambia.” Basi akaenda hata mahali peupe palipoinuka.
NUM 23:4 Mungu akakutana naye, kisha Balaamu akasema, “Nimekwisha kutengeneza madhabahu saba, na juu ya kila madhabahu nimetoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja.”
NUM 23:5 Mwenyezi Mungu akaweka ujumbe katika kinywa cha Balaamu na kusema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
NUM 23:6 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake akiwa na wakuu wote wa Moabu.
NUM 23:7 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake: “Balaki amenileta kutoka Aramu, mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki. Akasema, ‘Njoo, unilaanie Yakobo; njoo unishutumie Israeli.’
NUM 23:8 Nitawezaje kuwalaani, hao ambao Mungu hajawalaani? Nitawezaje kuwashutumu hao ambao Mwenyezi Mungu hakuwashutumu?
NUM 23:9 Kutoka vilele vya miamba ninawaona, kutoka mahali palipoinuka ninawatazama. Ninaliona taifa ambalo wanaishi peke yao, nao hawahesabiwi kama mojawapo ya mataifa.
NUM 23:10 Ni nani awezaye kuhesabu mavumbi ya Yakobo, au kuhesabu robo ya Israeli? Mimi na nife kifo cha mtu mwenye haki, na mwisho wangu na uwe kama wao!”
NUM 23:11 Balaki akamwambia Balaamu, “Ni nini ulichonitendea? Nimekuleta ulaani adui zangu, lakini wewe badala yake umewabariki!”
NUM 23:12 Balaamu akajibu, “Je, hainipasi kusema kile Mwenyezi Mungu anachoweka katika kinywa changu?”
NUM 23:13 Ndipo Balaki akamwambia, “Twende pamoja mahali pengine ambapo unaweza kuwaona; utawaona baadhi tu wala si wote. Nawe kutoka huko, unilaanie hao.”
NUM 23:14 Basi akampeleka kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Pale akajenga madhabahu saba na kutoa sadaka ya fahali na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
NUM 23:15 Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati ninapoenda kuonana na Mungu kule.”
NUM 23:16 Mwenyezi Mungu akakutana na Balaamu, akaweka ujumbe katika kinywa chake akasema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
NUM 23:17 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake, akiwa na wakuu wa Moabu. Balaki akamuuliza, “Je, Mwenyezi Mungu amesema nini?”
NUM 23:18 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake: “Balaki, inuka na usikilize, nisikie mimi, wewe mwana wa Sipori.
NUM 23:19 Mungu si mtu, hata aseme uongo, wala yeye si mwanadamu, hata ajute. Je, anasema, kisha asitende? Je, anaahidi, asitimize?
NUM 23:20 Nimepokea agizo kubariki; amebariki, nami siwezi kubadilisha.
NUM 23:21 “Haijaonekana bahati mbaya katika Yakobo, wala taabu katika Israeli. Mwenyezi Mungu, Mungu wao, yu pamoja nao, nayo sauti kuu ya Mfalme imo kati yao.
NUM 23:22 Mungu aliwatoa kutoka Misri; wao wana nguvu kama za nyati.
NUM 23:23 Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo, wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli. Sasa itasemwa kuhusu Yakobo na Israeli, ‘Tazama yale Mungu aliyotenda!’
NUM 23:24 Taifa lainuka kama simba jike; linajiinua kama simba ambaye hatulii hadi amalize kurarua mawindo yake na kunywa damu ya mawindo yake.”
NUM 23:25 Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa!”
NUM 23:26 Balaamu akajibu, “Je, sikukuambia ni lazima nifanye lolote analosema Mwenyezi Mungu?”
NUM 23:27 Basi Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo, nikupeleke mahali pengine. Huenda itampendeza Mungu kukuruhusu unilaanie hao watu kutoka mahali hapo.”
NUM 23:28 Balaki akamchukua Balaamu juu ya Mlima Peori, unaotazamana na nyika.
NUM 23:29 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, uandae mafahali saba na kondoo dume saba kwa ajili yangu.”
NUM 23:30 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, kisha akatoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
NUM 24:1 Basi Balaamu alipoona imempendeza Mwenyezi Mungu kubariki Israeli, hakuendelea tena kutafuta uchawi kama nyakati nyingine, bali aligeuza uso wake kuelekea nyikani.
NUM 24:2 Balaamu alipotazama nje na kuona Israeli amepiga kambi kabila kwa kabila, Roho wa Mungu akawa juu yake,
NUM 24:3 naye akatoa ujumbe wake: “Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori, ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;
NUM 24:4 ujumbe wake yeye anayesikia maneno ya Mungu, anayeona maono kutoka kwa Mwenyezi, ambaye husujudu, na macho yake yamefunguka:
NUM 24:5 “Tazama jinsi yalivyo mazuri mahema yako, ee Yakobo, maskani zako, ee Israeli!
NUM 24:6 “Kama mabonde, yanaenea, kama bustani kando ya mto, kama miti ya udi iliyopandwa na Mwenyezi Mungu, kama mierezi kando ya maji.
NUM 24:7 Maji yatatiririka kutoka ndoo zake; mbegu yake itakuwa na maji tele. “Mfalme wake atakuwa mkuu kuliko Mfalme Agagi; ufalme wake utatukuka.
NUM 24:8 “Mungu alimleta kutoka Misri; yeye ana nguvu kama nyati. Anayararua mataifa yaliyo adui zake, na kuvunja mifupa yao vipande vipande; huwachoma kwa mishale yake.
NUM 24:9 Hujikunyata na kuvizia kama simba, kama simba jike; nani anayethubutu kumwamsha? “Abarikiwe kila akubarikiye, na alaaniwe kila akulaaniye!”
NUM 24:10 Ndipo hasira ya Balaki ikawaka dhidi ya Balaamu. Akapiga mikono yake pamoja, akamwambia Balaamu, “Nilikuita uje kuwalaani adui zangu, lakini umewabariki mara hizi tatu.
NUM 24:11 Sasa ondoka upesi uende nyumbani! Mimi nilisema nitakuzawadia vizuri sana, lakini Mwenyezi Mungu amekuzuia usizawadiwe.”
NUM 24:12 Balaamu akamwambia Balaki, “Je, hukumbuki jinsi nilivyowaambia wajumbe uliowatuma kwangu? Niliwaambia hivi,
NUM 24:13 ‘Hata ikiwa Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, nisingeweza kufanya kitu chochote kwa matakwa yangu, kikiwa kizuri au kibaya, kwenda kinyume na agizo la Mwenyezi Mungu, nami imenipasa kusema tu kile Mwenyezi Mungu atakachosema’?
NUM 24:14 Sasa ninarudi kwa watu wangu. Lakini njoo, nikuonye kuhusu kile watu hawa watakachowatenda watu wako siku zijazo.”
NUM 24:15 Kisha Balaamu akatoa ujumbe wake: “Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori, ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;
NUM 24:16 ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu, mwenye maarifa kutoka kwa Aliye Juu Sana, aonaye maono kutoka kwa Mwenyezi, na kuanguka kifudifudi nayo macho yake yamefunguliwa:
NUM 24:17 “Namwona yeye, lakini si sasa; namtazama yeye, lakini si karibu. Nyota itatoka kwa Yakobo, fimbo ya ufalme itainuka kutoka kwa Israeli. Atawaponda Wamoabu paji za nyuso, na mafuvu yote ya wana wa Shethi.
NUM 24:18 Edomu itamilikiwa, Seiri, adui yake, itamilikiwa, lakini Israeli atakuwa na nguvu.
NUM 24:19 Mtawala atakuja kutoka kwa Yakobo na kuangamiza walionusurika katika mji.”
NUM 24:20 Kisha Balaamu akawaona watu wa Amaleki, na kutoa ujumbe wake: “Amaleki alikuwa ya kwanza miongoni mwa mataifa, lakini mwisho wake ataangamizwa milele.”
NUM 24:21 Kisha akawaona Wakeni, akatoa ujumbe wake: “Makao yenu ni salama, kiota chenu kiko kwenye mwamba.
NUM 24:22 Hata hivyo ninyi Wakeni mtaangamizwa Ashuru atakapowachukua mateka.”
NUM 24:23 Ndipo akatoa ujumbe wake: “Ole wao! Ni nani ataweza kuishi Mungu atakapofanya hili?
NUM 24:24 Meli zitakuja kutoka pwani za Kitimu, zitaitiisha Ashuru na Eberi, lakini nao pia wataangamizwa.”
NUM 24:25 Kisha Balaamu akainuka na kurudi nyumbani mwake, naye Balaki akashika njia yake.
NUM 25:1 Israeli alipokuwa akikaa Shitimu, wanaume wa Israeli walianza kuzini na wanawake wa Moabu,
NUM 25:2 ambao waliwaalika kushiriki katika sadaka kwa miungu yao. Watu wakala na kusujudu mbele ya miungu hiyo.
NUM 25:3 Kwa hiyo Israeli akaungana katika kumwabudu Baali wa Peori. Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi yao.
NUM 25:4 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Uwachukue viongozi wote wa watu hawa, uwaue hadharani mbele za Mwenyezi Mungu, ili hasira kali ya Mwenyezi Mungu iweze kuondoka kwa Israeli.”
NUM 25:5 Kwa hiyo Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, “Kila mmoja wenu lazima awaue wale wanaume wenu, walioshiriki katika kumwabudu Baali wa Peori.”
NUM 25:6 Ndipo mwanaume Mwisraeli akamleta mwanamke Mmidiani katika jamaa yake palepale mbele ya Musa na mkutano wote wa Israeli walipokuwa wakilia kwenye lango la Hema la Kukutania.
NUM 25:7 Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Haruni, alipoona jambo hili, akaondoka kwenye kusanyiko, akachukua mkuki mkononi mwake,
NUM 25:8 akamfuata yule Mwisraeli ndani ya hema. Akawachoma mkuki wote wawili kwa pamoja, ukapenya kwenye mwili wa yule Mwisraeli na mwili wa yule mwanamke. Ndipo tauni dhidi ya Waisraeli ikakoma.
NUM 25:9 Lakini wale waliokufa kwa hiyo tauni walikuwa watu elfu ishirini na nne.
NUM 25:10 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 25:11 “Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Haruni, amegeuza hasira yangu mbali na Waisraeli, kwa sababu alikuwa na wivu kama nilio nao kwa heshima yangu miongoni mwao, hata kwamba kwa wivu wangu sikuwaangamiza.
NUM 25:12 Kwa hiyo mwambie Finehasi ninafanya agano langu la amani naye.
NUM 25:13 Yeye pamoja na wazao wake watakuwa na agano la ukuhani milele, kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya heshima ya Mungu wake, na akafanya upatanisho kwa Waisraeli.”
NUM 25:14 Jina la Mwisraeli ambaye aliuawa pamoja na mwanamke Mmidiani ni Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa ya Simeoni.
NUM 25:15 Jina la mwanamke Mmidiani aliyeuawa ni Kozbi binti Suri, aliyekuwa mkuu wa kabila la jamaa ya Wamidiani.
NUM 25:16 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 25:17 “Watendeeni Wamidiani kama adui na mwaue,
NUM 25:18 kwa sababu wao waliwatendea kama adui wakati waliwadanganya katika tukio la Peori na dada yao Kozbi, binti ya kiongozi Mmidiani, mwanamke ambaye aliuawa wakati tauni ilikuja kama matokeo ya tukio la Peori.”
NUM 26:1 Baada ya hiyo tauni, Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Eleazari mwana wa kuhani Haruni,
NUM 26:2 “Hesabu jumuiya yote ya Waisraeli kufuatana na jamaa zao, wale wote wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, wanaoweza kutumika katika jeshi la Israeli.”
NUM 26:3 Hivyo Musa na kuhani Eleazari wakazungumza na watu kwenye nchi tambarare ya Moabu, ng’ambo ya Yordani kutokea Yeriko, wakasema,
NUM 26:4 “Hesabuni wanaume wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.”
NUM 26:5 Wazao wa Reubeni, mwana mzaliwa wa kwanza wa Israeli, walikuwa: kutoka kwa Hanoki, ukoo wa Wahanoki; kutoka kwa Palu, ukoo wa Wapalu;
NUM 26:6 kutoka kwa Hesroni, ukoo wa Wahesroni; kutoka kwa Karmi, ukoo wa Wakarmi.
NUM 26:7 Hizi zilikuwa ndizo koo za Reubeni; wale waliohesabiwa walikuwa elfu arobaini na tatu mia saba na thelathini (43,730).
NUM 26:8 Mwana wa Palu alikuwa Eliabu,
NUM 26:9 nao wana wa Eliabu walikuwa Nemueli, Dathani na Abiramu. Hawa wawili Dathani na Abiramu ndio walikuwa maafisa wa jumuiya ambao walimwasi Musa na Haruni, na walikuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora wakati walimwasi Mwenyezi Mungu.
NUM 26:10 Ardhi ilifunua kinywa chake na kuwameza pamoja na Kora, ambaye wafuasi wake walikufa wakati moto ulipowateketeza wanaume mia mbili na hamsini. Nao walikuwa kama alama ya onyo.
NUM 26:11 Pamoja na hayo, hao ukoo wa Kora hawakufa.
NUM 26:12 Wazao wa Simeoni kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Nemueli, ukoo wa Wanemueli; kutoka kwa Yamini, ukoo wa Wayamini; kutoka wa Yakini, ukoo wa Wayakini;
NUM 26:13 kutoka kwa Zera, ukoo wa Wazera; kutoka kwa Shauli, ukoo wa Washauli.
NUM 26:14 Hizi ndizo koo za Simeoni; walikuwa watu elfu ishirini na mbili na mia mbili.
NUM 26:15 Wazao wa Gadi kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Sifoni, ukoo wa Wasifoni; kutoka kwa Hagi, ukoo wa Wahagi; kutoka kwa Shuni, ukoo wa Washuni;
NUM 26:16 kutoka kwa Ozni, ukoo wa Waozni; kutoka kwa Eri, ukoo wa Waeri;
NUM 26:17 kutoka kwa Arodi, ukoo wa Waarodi; kutoka kwa Areli, ukoo wa Waareli.
NUM 26:18 Hizo zilikuwa koo za Gadi; wale waliohesabiwa walikuwa elfu arobaini na mia tano.
NUM 26:19 Eri na Onani walikuwa wana wa Yuda, lakini walifia huko Kanaani.
NUM 26:20 Wazao wa Yuda kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Shela, ukoo wa Washela; kutoka kwa Peresi, ukoo wa Waperesi; kutoka kwa Zera, ukoo wa Wazera.
NUM 26:21 Wazao wa Peresi walikuwa: kutoka kwa Hesroni, ukoo wa Wahesroni; kutoka kwa Hamuli, ukoo wa Wahamuli.
NUM 26:22 Hizo zilikuwa koo za Yuda; wale waliohesabiwa walikuwa elfu sabini na sita na mia tano.
NUM 26:23 Wazao wa Isakari kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Tola, ukoo wa Watola; kutoka kwa Puva, ukoo wa Wapuva;
NUM 26:24 kutoka kwa Yashubu, ukoo wa Wayashubu; kutoka kwa Shimroni, ukoo wa Washimroni.
NUM 26:25 Hizo zilikuwa koo za Isakari; wale waliohesabiwa walikuwa elfu sitini na nne na mia tatu.
NUM 26:26 Wazao wa Zabuloni kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Seredi, ukoo wa Waseredi; kutoka kwa Eloni, ukoo wa Waeloni; kutoka kwa Yaleeli, ukoo wa Wayaleeli.
NUM 26:27 Hizo zilikuwa koo za Zabuloni; wale waliohesabiwa walikuwa elfu sitini na mia tano.
NUM 26:28 Wazao wa Yusufu kwa koo zao kutoka kwa Manase na kwa Efraimu walikuwa:
NUM 26:29 Wazao wa Manase: kutoka kwa Makiri, ukoo wa Wamakiri (Makiri alikuwa baba wa Gileadi); kutoka kwa Gileadi, ukoo wa Wagileadi.
NUM 26:30 Hawa walikuwa wazao wa Gileadi: kutoka kwa Iezeri, ukoo wa Waiezeri; kutoka kwa Heleki, ukoo wa Waheleki;
NUM 26:31 kutoka kwa Asirieli, ukoo wa Waasirieli; kutoka kwa Shekemu, ukoo wa Washekemu;
NUM 26:32 kutoka kwa Shemida, ukoo wa Washemida; kutoka kwa Heferi, ukoo wa Waheferi.
NUM 26:33 (Selofehadi mwana wa Heferi hakuzaa wana, bali alikuwa na watoto wa kike tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa.)
NUM 26:34 Hizo zilikuwa koo za Manase; wale waliohesabiwa walikuwa elfu hamsini na mbili na mia saba.
NUM 26:35 Hawa walikuwa wazao wa Efraimu kwa koo zao: kutoka kwa Shuthela, ukoo wa Washuthela; kutoka kwa Bekeri, ukoo wa Wabekeri; kutoka kwa Tahani, ukoo wa Watahani;
NUM 26:36 Hawa walikuwa wazao wa Shuthela: kutoka kwa Erani, ukoo wa Waerani.
NUM 26:37 Hizo zilikuwa koo za Efraimu; wale waliohesabiwa walikuwa elfu thelathini na mbili na mia tano.
NUM 26:38 Wazao wa Benyamini kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Bela, ukoo wa Wabela; kutoka kwa Ashbeli, ukoo wa Waashbeli; kutoka kwa Ahiramu, ukoo wa Waahiramu;
NUM 26:39 kutoka kwa Shufamu, ukoo wa Washufamu; kutoka kwa Hufamu, ukoo wa Wahufamu.
NUM 26:40 Wazao wa Bela kutoka kwa Ardi na Naamani walikuwa: kutoka kwa Ardi, ukoo wa Waardi; kutoka kwa Naamani, ukoo wa Wanaamani.
NUM 26:41 Hizo zilikuwa koo za Benyamini; wale waliohesabiwa walikuwa elfu arobaini na tano na mia sita.
NUM 26:42 Hawa walikuwa wazao wa Dani kwa koo zao: kutoka kwa Shuhamu, ukoo wa Washuhamu.
NUM 26:43 Wote walikuwa koo za Washuhamu; wale waliohesabiwa walikuwa elfu sitini na nne na mia nne.
NUM 26:44 Wazao wa Asheri kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Imna, ukoo wa Waimna; kutoka kwa Ishvi, ukoo wa Waishvi; kutoka kwa Beria, ukoo wa Waberia;
NUM 26:45 kutoka kwa wazao wa Beria: kutoka kwa Heberi, ukoo wa Waheberi; kutoka kwa Malkieli, ukoo wa Wamalkieli.
NUM 26:46 Asheri alikuwa na binti aliyeitwa Sera.
NUM 26:47 Hizo zilikuwa koo za Asheri; wale waliohesabiwa walikuwa elfu hamsini na tatu na mia nne.
NUM 26:48 Wazao wa Naftali kwa koo zao walikuwa: kutoka kwa Yaseeli, ukoo wa Wayaseeli; kutoka kwa Guni, ukoo wa Waguni;
NUM 26:49 kutoka kwa Yeseri, ukoo wa Wayeseri; kutoka kwa Shilemu, ukoo wa Washilemu.
NUM 26:50 Hizo zilikuwa koo za Naftali; wale waliohesabiwa walikuwa elfu arobaini na tano na mia nne.
NUM 26:51 Jumla ya hesabu ya wanaume wa Israeli ilikuwa elfu mia sita na moja mia saba na thelathini (601,730).
NUM 26:52 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 26:53 “Watagawiwa nchi kama urithi kulingana na hesabu ya majina.
NUM 26:54 Kundi kubwa zaidi lipe urithi mkubwa zaidi, na kundi dogo zaidi lipewe urithi mdogo zaidi; kila kundi litapokea urithi wake kulingana na hesabu ya wale walioorodheshwa.
NUM 26:55 Hakikisha kuwa nchi inagawanywa kwa kura. Kile kitakachorithiwa na kila kikundi kitakuwa kwa kulingana na majina ya kabila la babu yao.
NUM 26:56 Kila urithi utagawanywa kwa kura miongoni mwa makundi makubwa na madogo.”
NUM 26:57 Hawa walikuwa Walawi ambao walihesabiwa kwa koo zao: kutoka kwa Gershoni, ukoo wa Wagershoni; kutoka kwa Kohathi, ukoo wa Wakohathi; kutoka kwa Merari, ukoo wa Wamerari.
NUM 26:58 Hizi pia zilikuwa koo za Walawi: ukoo wa Walibni; ukoo wa Wahebroni; ukoo wa Wamahli; ukoo wa Wamushi; ukoo wa wana wa Kora. (Kohathi alikuwa baba aliyemzaa Amramu;
NUM 26:59 jina la mke wa Amramu ni Yokebedi, naye pia alikuwa mzao wa Lawi, ambaye alizaliwa kwa Walawi nchini Misri. Alimzalia Amramu: Haruni, Musa na dada yao Miriamu.
NUM 26:60 Haruni alikuwa baba yake Nadabu na Abihu, Eleazari na Ithamari.
NUM 26:61 Lakini Nadabu na Abihu walikufa wakati walitoa sadaka mbele za Mwenyezi Mungu kwa moto usioruhusiwa.)
NUM 26:62 Wanaume wote wa Walawi wa umri wa mwezi mmoja na zaidi walikuwa elfu ishirini na tatu. Wao hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine kwa sababu hawakupokea urithi miongoni mwao.
NUM 26:63 Hawa ndio walioorodheshwa na Musa na kuhani Eleazari wakati waliwahesabu Waisraeli kwenye nchi tambarare ya Moabu, kando ya Yordani, ng’ambo ya Yeriko.
NUM 26:64 Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa miongoni mwa wale waliohesabiwa na Musa na kuhani Haruni wakati waliwahesabu Waisraeli katika Jangwa la Sinai.
NUM 26:65 Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amewaambia hao Waisraeli hakika wangekufa huko jangwani, wala hakuna mmoja wao aliyeachwa, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune na Yoshua mwana wa Nuni.
NUM 27:1 Binti za Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, walikuwa wa koo za Manase mwana wa Yusufu. Majina ya hao binti yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Walikaribia
NUM 27:2 ingilio la Hema la Kukutania na kusimama mbele ya Musa, kuhani Eleazari, viongozi na kusanyiko lote, wakasema,
NUM 27:3 “Baba yetu alikufa jangwani. Hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora, ambao walifungamana pamoja dhidi ya Mwenyezi Mungu, lakini alikufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe na hakuacha wana.
NUM 27:4 Kwa nini jina la baba yetu lifutike kutoka ukoo wake kwa sababu hakuwa na mwana? Tupatie milki miongoni mwa ndugu za baba yetu.”
NUM 27:5 Kwa hiyo Musa akaleta shauri lao mbele za Mwenyezi Mungu,
NUM 27:6 naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 27:7 “Wanachosema binti za Selofehadi ni sawa. Ni lazima kwa hakika uwape milki kama urithi miongoni mwa ndugu za baba yao, na kubadili urithi wa baba yao uwe wao.
NUM 27:8 “Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake.
NUM 27:9 Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake.
NUM 27:10 Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake.
NUM 27:11 Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.’ ”
NUM 27:12 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Kwea mlima huu katika safu za Abarimu uione nchi ninayowapa Waisraeli.
NUM 27:13 Baada ya kuiona, wewe pia utakusanywa pamoja na watu wako kama ndugu yako Haruni alivyokusanywa,
NUM 27:14 kwa kuwa jumuiya ilipoasi amri yangu kwenye maji katika Jangwa la Sini, wakati jumuiya ilipogombana nami, nyote wawili mliacha kuitii amri yangu ya kuniheshimu kama mtakatifu mbele ya macho yao.” (Haya yalikuwa maji ya Meriba huko Kadeshi, katika Jangwa la Sini.)
NUM 27:15 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu,
NUM 27:16 “Mwenyezi Mungu, Mungu wa roho zote za wanadamu, na amteue mtu juu ya jumuiya hii
NUM 27:17 ili atoke na kuingia mbele yao, atakayewaongoza katika kutoka kwao na kuingia kwao, ili watu wa Mwenyezi Mungu wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.”
NUM 27:18 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mchukue Yoshua mwana wa Nuni, mtu ambaye Roho wa Mungu yuko ndani yake, uweke mkono juu yake.
NUM 27:19 Msimamishe mbele ya kuhani Eleazari pamoja na kusanyiko lote, umpe maagizo mbele yao.
NUM 27:20 Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli wapate kumtii.
NUM 27:21 Atasimama mbele ya kuhani Eleazari, ambaye atapokea maamuzi kwa ajili yake, kwa kuuliza mbele za Mwenyezi Mungu kwa Urimu. Kwa amri yake, yeye na jumuiya yote ya Waisraeli watatoka, na kwa amri yake, wataingia.”
NUM 27:22 Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza. Akamtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na kusanyiko lote.
NUM 27:23 Kisha akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Yoshua na kumpa maagizo, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoelekeza kupitia kwa Musa.
NUM 28:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 28:2 “Wape Waisraeli agizo hili, uwaambie: ‘Hakikisheni kwamba mnaniletea mimi kwa wakati uliowekwa chakula kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, kama harufu nzuri ya kupendeza.’
NUM 28:3 Waambie: ‘Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto mnayomtolea Mwenyezi Mungu: wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasio na dosari, kuwa sadaka ya kawaida ya kuteketezwa kila siku.
NUM 28:4 Andaa mwana-kondoo mmoja asubuhi na mwingine jioni,
NUM 28:5 kila mmoja atolewe pamoja na sadaka ya nafaka sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa pamoja na robo ya hini ya mafuta ya zeituni.
NUM 28:6 Hii ni sadaka ya kawaida ya kuteketezwa iliyoanzishwa katika Mlima Sinai kama harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto.
NUM 28:7 Sadaka ya kinywaji itakayotolewa pamoja na kila mwana-kondoo ni robo ya hini ya kinywaji kilichochachuka. Mimina sadaka ya kinywaji kwa Mwenyezi Mungu mahali patakatifu.
NUM 28:8 Andaa yule mwana-kondoo wa pili jioni, pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka ya kinywaji kama ulivyofanya kwa ile sadaka nyingine ya asubuhi. Hii ni sadaka iliyotolewa kwa kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 28:9 “ ‘Siku ya Sabato, utatoa sadaka ya wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari pamoja na sadaka yake ya kinywaji na sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta.
NUM 28:10 Hii ni sadaka ya kuteketezwa itakayotolewa kwa ajili ya kila Sabato, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 28:11 “ ‘Siku ya kwanza ya kila mwezi, mtamletea Mwenyezi Mungu sadaka ya kuteketezwa ya fahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo saba wa mwaka mmoja, wote wasiokuwa na dosari.
NUM 28:12 Pamoja na kila fahali, kutakuwa na sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi ya efa, uliochanganywa na mafuta, pamoja na kondoo dume mmoja, sadaka ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta;
NUM 28:13 pamoja na kila mwana-kondoo, sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta. Hii ni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri, sadaka ya kuteketezwa iliyotolewa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu.
NUM 28:14 Pamoja na kila fahali kutakuwa na sadaka ya kinywaji nusu ya hini ya divai; pamoja na kila kondoo dume, theluthi moja ya hini; na pamoja na kila mwana-kondoo, robo hini. Hii ni sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi itakayotolewa kila mwandamo wa mwezi kwa mwaka.
NUM 28:15 Zaidi ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya kinywaji, mbuzi mmoja dume atatolewa kwa Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya dhambi.
NUM 28:16 “ ‘Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, itafanyika Pasaka ya Mwenyezi Mungu.
NUM 28:17 Katika siku ya kumi na tano ya mwezi huo itakuwa sikukuu; kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu.
NUM 28:18 Katika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, msifanye kazi za kawaida.
NUM 28:19 Leteni mbele za Mwenyezi Mungu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo dume saba wenye umri wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 28:20 Pamoja na kila fahali, andaa sadaka ya nafaka sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi ya efa;
NUM 28:21 pia pamoja na kila mmoja wa wale wana-kondoo saba, andaa sehemu ya kumi ya efa.
NUM 28:22 Pia mtoe beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi ambaye atafanya upatanisho kwa ajili yenu.
NUM 28:23 Andaa hizi licha ya zile sadaka za kawaida za kuteketezwa za kila asubuhi.
NUM 28:24 Kwa njia hii andaa chakula cha sadaka ya kuteketezwa kila siku, kwa siku saba kama harufu nzuri impendezayo Mwenyezi Mungu. Hii itaandaliwa licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa ya kila siku pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 28:25 Siku ya saba mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida.
NUM 28:26 “ ‘Siku ya malimbuko, mnapomletea Mwenyezi Mungu sadaka ya nafaka mpya wakati wa Sikukuu ya Majuma, mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida.
NUM 28:27 Mlete sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja, na pia wana-kondoo saba wenye umri wa mwaka mmoja, kama harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 28:28 Pamoja na kila fahali itatolewa sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi ya efa uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini;
NUM 28:29 na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa kila mmoja wa wana-kondoo saba.
NUM 28:30 Ongeza beberu mmoja kwa kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
NUM 28:31 Andaa hizi sadaka pamoja na sadaka zake za vinywaji, kuwa nyongeza ya sadaka za kawaida za kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka. Hakikisha kuwa wanyama hao hawana dosari.
NUM 29:1 “ ‘Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu na msifanye kazi ya kawaida. Ni siku kwa ajili yenu ya kupiga tarumbeta.
NUM 29:2 Mtatayarisha sadaka ya kuteketezwa kama harufu nzuri impendezayo Mwenyezi Mungu ya fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, na wana-kondoo saba wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:3 Pamoja na fahali, andaeni sadaka ya nafaka sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kwa kondoo dume, andaa unga sehemu mbili za kumi ya efa;
NUM 29:4 na pamoja na wana-kondoo saba kila mmoja aandaliwe na sehemu ya kumi ya efa ya unga.
NUM 29:5 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
NUM 29:6 Hivi ni nyongeza ya sadaka za kuteketezwa kila mwezi na kila siku, pamoja na sadaka zake za nafaka, na sadaka za vinywaji kama ilivyoainishwa. Ni sadaka zinazotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, harufu inayopendeza.
NUM 29:7 “ ‘Kwenye siku ya kumi ya mwezi huu wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu. Mtajikana wenyewe na msifanye kazi.
NUM 29:8 Toeni sadaka ya kuteketezwa ya fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, na wana-kondoo saba wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari, kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 29:9 Pamoja na fahali, andaeni sadaka ya nafaka sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini;
NUM 29:10 na kwa kila mmoja wa wana-kondoo saba andaa sehemu ya kumi ya unga laini kwa kila mmoja.
NUM 29:11 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, katika nyongeza ya sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho, na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka, na sadaka zake za vinywaji.
NUM 29:12 “ ‘Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, mtakuwa na kusanyiko takatifu, na hamtafanya kazi za kawaida. Adhimisheni sikukuu kwa Mwenyezi Mungu kwa siku saba.
NUM 29:13 Toeni sadaka ya kuteketezwa mafahali wachanga kumi na watatu, kondoo dume wawili, na wana-kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari, kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
NUM 29:14 Pamoja na hao mafahali kumi na watatu, kila mmoja aandaliwe na sadaka ya nafaka sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kwa kondoo dume wawili, kila mmoja aandaliwe sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini;
NUM 29:15 na kwa wana-kondoo kumi na wanne, kila mmoja aandaliwe sehemu ya kumi ya efa ya unga laini.
NUM 29:16 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, kwa nyongeza ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka, na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 29:17 “ ‘Katika siku ya pili, andaeni mafahali wachanga kumi na wawili, kondoo dume wawili, na wana-kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:18 Pamoja na mafahali, kondoo dume, na wana-kondoo, andaeni sadaka zao za nafaka na sadaka za vinywaji, kulingana na idadi iliyoainishwa.
NUM 29:19 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, kwa nyongeza ya kawaida ya sadaka ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka, pamoja na sadaka zake za vinywaji.
NUM 29:20 “ ‘Katika siku ya tatu, andaeni mafahali wachanga kumi na wawili, kondoo dume wawili, na wana-kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:21 Pamoja na mafahali, kondoo dume, na wana-kondoo, andaeni sadaka zao za nafaka na sadaka za vinywaji, kulingana na idadi iliyoainishwa.
NUM 29:22 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, kwa nyongeza ya kawaida ya sadaka ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 29:23 “ ‘Katika siku ya nne, andaeni mafahali wachanga kumi na wawili, kondoo dume wawili, na wana-kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:24 Pamoja na mafahali, kondoo dume, na wana-kondoo, andaeni sadaka zao za nafaka na sadaka za vinywaji, kulingana na idadi iliyoainishwa.
NUM 29:25 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, kwa nyongeza ya kawaida ya sadaka ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 29:26 “ ‘Katika siku ya tano, andaeni mafahali tisa, kondoo dume wawili na wana-kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:27 Pamoja na mafahali, kondoo dume na wana-kondoo, andaeni sadaka zao za nafaka na sadaka za kinywaji kulingana na idadi iliyoainishwa.
NUM 29:28 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, kwa nyongeza ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 29:29 “ ‘Katika siku ya sita, andaeni mafahali wachanga kumi na wawili, kondoo dume wawili, na wana-kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:30 Pamoja na mafahali, kondoo dume, na wana-kondoo, andaeni sadaka zao za nafaka na sadaka za vinywaji, kulingana na idadi iliyoainishwa.
NUM 29:31 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, kwa nyongeza ya kawaida ya sadaka ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 29:32 “ ‘Katika siku ya saba, andaeni mafahali wachanga kumi na wawili, kondoo dume wawili, na wana-kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:33 Pamoja na mafahali, kondoo dume, na wana-kondoo, andaeni sadaka zao za nafaka na sadaka za vinywaji, kulingana na idadi iliyoainishwa.
NUM 29:34 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, kwa nyongeza ya kawaida ya sadaka ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 29:35 “ ‘Katika siku ya nane, mtakuwa na kusanyiko, na msifanye kazi ya kawaida.
NUM 29:36 Toeni sadaka ya kuteketezwa kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu, sadaka ya kuteketezwa ya fahali mmoja, kondoo dume mmoja, na wana-kondoo dume saba wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
NUM 29:37 Pamoja na fahali, kondoo dume na wana-kondoo, andaeni sadaka zao za nafaka, na sadaka za vinywaji, kulingana na idadi iliyoainishwa.
NUM 29:38 Ongeza beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, katika nyongeza ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
NUM 29:39 “ ‘Zaidi ya kile unachoweka nadhiri na sadaka zenu za hiari, andaeni hizi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwenye sikukuu zenu zilizoamriwa: sadaka zenu za kuteketezwa, sadaka za nafaka, sadaka za vinywaji, pamoja na sadaka zenu za amani.’ ”
NUM 29:40 Musa akawaambia Waisraeli yale yote Mwenyezi Mungu alimwagiza.
NUM 30:1 Musa akawaambia viongozi wa makabila ya Israeli: “Hili ndilo Mwenyezi Mungu analoagiza:
NUM 30:2 Mwanaume awekapo nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, au anapoapa kujifunga kwa ahadi, kamwe asitangue neno lake, bali ni lazima afanye kila kitu alichosema.
NUM 30:3 “Mwanamwali anayeishi bado nyumbani mwa baba yake atakapoweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, ama akajifunga mwenyewe kwa ahadi,
NUM 30:4 na baba yake akasikia kuhusu nadhiri au ahadi yake lakini asimwambie lolote, ndipo nadhiri zake zote na kila ahadi aliyoiweka na kujifunga kwayo itathibitika.
NUM 30:5 Lakini kama baba yake akimkataza wakati anapoisikia, hakuna nadhiri wala ahadi yake yoyote aliyojifunga kwayo itakayosimama; Mwenyezi Mungu atamweka huru huyo mwanamwali kwa sababu baba yake amemkataza.
NUM 30:6 “Akiolewa baada ya kuweka nadhiri au baada ya midomo yake kutamka ahadi fulani bila kufikiri akawa amejifunga hivyo,
NUM 30:7 na mume wake akasikia habari hiyo asimwambie neno lolote, ndipo nadhiri zake ama ahadi zake ambazo alikuwa amejifunga nazo zitathibitika.
NUM 30:8 Lakini ikiwa mume wake atamkataza atakaposikia kuhusu hilo, atakuwa ametangua nadhiri ambazo zilikuwa zimemfunga mkewe, ama ahadi aliyotamka pasipo kufikiri ambayo amejifunga kwayo, naye Mwenyezi Mungu atamweka huru yule mwanamke.
NUM 30:9 “Nadhiri yoyote ama patano ambalo limefanywa na mjane ama mwanamke aliyeachwa vitakuwa vimemfunga.
NUM 30:10 “Ikiwa mwanamke anayeishi na mumewe ataweka nadhiri ama kujifunga mwenyewe kwa ahadi chini ya kiapo,
NUM 30:11 na mumewe akasikia kuhusu jambo hili lakini asimwambie lolote wala hakumkataza, ndipo viapo vyake vyote au ahadi zinazomfunga zitakapothibitika.
NUM 30:12 Lakini ikiwa mumewe atabatilisha nadhiri hizo baada ya kuzisikia, basi hakuna nadhiri au ahadi zozote alizoziweka kwa midomo yake zitakazothibitika. Mumewe atakuwa amezibatilisha, na Mwenyezi Mungu atamweka huru yule mwanamke.
NUM 30:13 Mumewe anaweza kuthibitisha au kutangua nadhiri yoyote anayoweka, au ahadi yoyote aliyoweka kwa kuapa ili kujikana mwenyewe.
NUM 30:14 Lakini ikiwa mumewe hasemi lolote kwake kuhusu jambo hilo siku baada ya siku, basi mumewe atakuwa amethibitisha nadhiri zote, na ahadi zote zinazomfunga mkewe. Anavithibitisha kwa kutokusema lolote kwa mkewe anapoyasikia hayo.
NUM 30:15 Hata hivyo, ikiwa mumewe atavibatilisha baada ya kusikia hayo, basi atawajibika kwa hatia ya mkewe.”
NUM 30:16 Haya ndio masharti ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Musa kuhusu mahusiano kati ya mtu na mkewe, na kati ya baba na binti yake ambaye bado anaishi nyumbani mwa baba yake.
NUM 31:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 31:2 “Uwalipize kisasi Wamidiani kwa ajili ya Waisraeli. Halafu baada ya hayo, utakufa.”
NUM 31:3 Kwa hiyo Musa akawaambia watu, “Waandaeni baadhi ya wanaume wenu waende vitani kupigana na Wamidiani ili wawalipize kisasi cha Mwenyezi Mungu.
NUM 31:4 Peleka wanaume elfu moja vitani kutoka kila kabila la Israeli.”
NUM 31:5 Kwa hiyo waliandaliwa wanaume elfu kumi na mbili kwa vita, wanaume elfu moja kutoka kila kabila, walitolewa kutoka koo za Israeli.
NUM 31:6 Musa aliwatuma vitani, watu elfu moja kutoka kila kabila, pamoja na Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, ambaye alichukua vyombo vya mahali patakatifu na tarumbeta za kuashiria.
NUM 31:7 Walipigana dhidi ya Wamidiani, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa, nao waliua kila mwanaume.
NUM 31:8 Miongoni mwa watu waliouawa walikuwa wafalme watano wa Midiani: Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba. Vilevile walimuua Balaamu mwana wa Beori kwa upanga.
NUM 31:9 Waisraeli waliwateka wanawake wa Midiani pamoja na watoto wao, na wakachukua makundi ya ng’ombe, kondoo na mali yao kama nyara.
NUM 31:10 Walichoma moto miji yote ambayo Wamidiani walikuwa wanaishi, pamoja na kambi zao zote.
NUM 31:11 Walichukua nyara zote na mateka, pamoja na watu na wanyama,
NUM 31:12 nao waliwaleta wafungwa mateka na nyara kwa Musa na kwa kuhani Eleazari, nao Waisraeli walikusanyika kwenye kambi zao katika tambarare za nchi ya Moabu, kando ya Yordani, ng’ambo ya Yeriko.
NUM 31:13 Musa, kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya wakatoka kuwalaki nje ya kambi.
NUM 31:14 Musa aliwakasirikia maafisa wa jeshi, yaani hao wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, ambao walirudi kutoka vitani.
NUM 31:15 Musa akawauliza, “Je, mmewaacha wanawake wote hai?
NUM 31:16 Wanawake hao ndio waliofuata ushauri wa Balaamu, nao ndio waliowasababisha Waisraeli wamwasi Mwenyezi Mungu kwa kile kilichotokea kule Peori, na kwa hiyo pigo liliwapata watu wa Mwenyezi Mungu.
NUM 31:17 Sasa waue wavulana wote. Pia muue kila mwanamke ambaye alikwisha fanya tendo la ndoa,
NUM 31:18 lakini mwacheni hai kwa ajili yenu kila msichana ambaye hajawahi kulala na mwanaume.
NUM 31:19 “Ninyi nyote ambao mmeua mtu yeyote au kumgusa mtu ambaye ameuawa, lazima mkae nje ya kambi kwa muda wa siku saba. Katika siku ya tatu na ya saba lazima mjitakase wenyewe pamoja na wafungwa wenu.
NUM 31:20 Takaseni kila vazi pamoja na kila kitu kilichotengenezwa kwa ngozi, kwa singa za mbuzi au kwa mti.”
NUM 31:21 Kisha kuhani Eleazari aliwaambia askari waliokuwa wameenda vitani, “Haya ndio matakwa ya sheria ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Musa:
NUM 31:22 Dhahabu, fedha, shaba, chuma, bati, risasi,
NUM 31:23 na kitu kingine chochote ambacho kinaweza kuhimili moto lazima mkipitishe kwenye moto, kisha kitakuwa safi. Lakini ni lazima pia kitakaswe kwa maji ya utakaso. Kitu chochote kisichoweza kuhimili moto lazima kipitishwe kwenye yale maji ya utakaso.
NUM 31:24 Katika siku ya saba fueni nguo zenu, nanyi mtakuwa safi. Kisha mtaweza kuingia kambini.”
NUM 31:25 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 31:26 “Wewe na kuhani Eleazari pamoja na viongozi wa jamaa ya jumuiya mtahesabu watu wote na wanyama ambao walitekwa.
NUM 31:27 Gawanyeni hizo nyara kati ya askari ambao walishiriki katika vita na kwa jumuiya.
NUM 31:28 Kutoka fungu la wale walioenda kupigana vitani, tenga kama ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kitu kimoja kati ya kila mia tano, ikiwa ni wanadamu, ng’ombe, punda, kondoo au mbuzi.
NUM 31:29 Chukua ushuru huu kutoka fungu lao, umpe kuhani Eleazari kuwa sehemu ya Mwenyezi Mungu.
NUM 31:30 Kutoka fungu la Waisraeli, chukua kitu kimoja kati ya kila hamsini, ikiwa ni wanadamu, ng’ombe, punda, kondoo, mbuzi au wanyama wengine. Hivyo uwape Walawi, ambao wanawajibika kutunza Maskani ya Mwenyezi Mungu.”
NUM 31:31 Kwa hiyo Musa na kuhani Eleazari wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
NUM 31:32 Nyara zilizobaki kutoka mateka ambayo askari walichukua ni kondoo elfu mia sita na sabini na tano,
NUM 31:33 ng’ombe elfu sabini na mbili,
NUM 31:34 punda elfu sitini na moja,
NUM 31:35 na wanawake elfu thelathini na mbili ambao hawakuwahi kulala na mwanaume.
NUM 31:36 Nusu ya fungu la wale waliopigana vitani lilikuwa: Kondoo elfu mia tatu na thelathini na saba na mia tano,
NUM 31:37 ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa kondoo mia sita na sabini na watano (675);
NUM 31:38 ng’ombe elfu thelathini na sita, ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa ng’ombe sabini na wawili;
NUM 31:39 punda elfu thelathini na mia tano, ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa punda sitini na mmoja;
NUM 31:40 Watu elfu kumi na sita, ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa watu thelathini na wawili.
NUM 31:41 Musa alimpa kuhani Eleazari ushuru kuwa sehemu ya Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
NUM 31:42 Ile nusu iliyokuwa ya Waisraeli, ambayo Musa aliitenga kutoka kwa ile ya watu waliopigana vitani,
NUM 31:43 nusu iliyokuwa ya jumuiya, ilikuwa kondoo elfu mia tatu na thelathini na saba na mia tano,
NUM 31:44 ng’ombe elfu thelathini na sita,
NUM 31:45 punda elfu thelathini na mia tano,
NUM 31:46 na wanadamu elfu kumi na sita.
NUM 31:47 Kutoka hiyo nusu iliyokuwa ya Waisraeli, Musa alichagua moja kati ya kila hamsini ya wanadamu na wanyama, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza, naye aliwapa Walawi, ambao waliwajibika kutunza Maskani ya Mwenyezi Mungu.
NUM 31:48 Kisha maafisa waliokuwa juu ya vikosi vya jeshi, wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, walimwendea Musa
NUM 31:49 na kumwambia, “Watumishi wako wamehesabu askari walio chini ya amri yetu na hakuna hata mmoja aliyekosekana.
NUM 31:50 Kwa hiyo tumeleta sadaka kwa Mwenyezi Mungu ya vyombo vya dhahabu kila mmoja wetu alivyopata, yaani vikuku, bangili, pete za muhuri, vipuli na mikufu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yetu mbele za Mwenyezi Mungu.”
NUM 31:51 Musa na kuhani Eleazari wakapokea kutoka kwao dhahabu, yaani vyombo vyote vilivyonakshiwa.
NUM 31:52 Dhahabu yote kutoka kwa wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia ambavyo Musa na kuhani Eleazari walimletea Mwenyezi Mungu kama zawadi ilikuwa shekeli elfu kumi na sita, mia saba na hamsini (16,750).
NUM 31:53 Kila askari alikuwa amejichukulia nyara zake binafsi.
NUM 31:54 Musa na kuhani Eleazari walipokea dhahabu kutoka kwa wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, wakazileta katika Hema la Kukutania kama ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Mwenyezi Mungu.
NUM 32:1 Basi Wareubeni na Wagadi, waliokuwa na makundi makubwa ya ng’ombe, kondoo na mbuzi, waliona kuwa nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi ni nzuri kwa mifugo.
NUM 32:2 Hivyo walimjia Musa, na kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, na kuwaambia,
NUM 32:3 “Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni,
NUM 32:4 nchi ambayo Mwenyezi Mungu ameishinda mbele ya Waisraeli, inafaa kwa mifugo, nao watumishi wako wana mifugo.
NUM 32:5 Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, nchi hii na ipewe watumishi wako kama milki yetu. Usitufanye tuvuke Yordani.”
NUM 32:6 Musa akawaambia Wagadi na Wareubeni, “Je, watu wa nchi yenu wataenda vitani wakati ninyi mmeketi hapa?
NUM 32:7 Kwa nini mmewakatisha Waisraeli tamaa wasivuke katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu amewapa?
NUM 32:8 Hivi ndivyo baba zenu walivyofanya wakati nilipowatuma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza nchi.
NUM 32:9 Baada ya kufika kwenye Bonde la Eshkoli na kuitazama nchi, waliwakatisha tamaa Waisraeli wasiingie katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amewapa.
NUM 32:10 Siku ile hasira ya Mwenyezi Mungu iliwaka naye akaapa kiapo hiki:
NUM 32:11 ‘Kwa kuwa hawakunifuata kwa moyo wote, hakuna mtu yeyote mwenye miaka ishirini au zaidi ambaye alikuja kutoka Misri atakayeona nchi niliyoahidi kwa kiapo kwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo;
NUM 32:12 hakuna hata mmoja isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, kwa sababu walimfuata Mwenyezi Mungu kwa moyo wote.’
NUM 32:13 Hasira ya Mwenyezi Mungu iliwaka dhidi ya Waisraeli na akawafanya watangetange katika jangwa kwa miaka arobaini, hadi kizazi chote cha wale waliofanya maovu mbele yake kimeangamia.
NUM 32:14 “Nanyi mko hapa, uzao wa wenye dhambi, mkisimamia mahali pa baba zenu na mkimfanya Mwenyezi Mungu kuwakasirikia Waisraeli hata zaidi.
NUM 32:15 Mkigeuka na kuacha kumfuata, atawaacha tena watu hawa wote jangwani, na mtakuwa sababu ya maangamizi yao.”
NUM 32:16 Ndipo wakamjia Musa na kumwambia, “Tungetaka kujenga mazizi hapa kwa ajili ya mifugo yetu na miji kwa ajili ya wanawake wetu na watoto.
NUM 32:17 Lakini sisi tuko tayari kuchukua silaha zetu na kutangulia mbele ya Waisraeli hadi tutakapowaleta mahali pao. Wakati huo wanawake wetu na watoto wataishi katika miji yenye ngome, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya wenyeji wa nchi.
NUM 32:18 Hatutarudi nyumbani mwetu hadi kila Mwisraeli apokee urithi wake.
NUM 32:19 Hatutapokea urithi wowote pamoja nao ng’ambo ya Yordani, kwa sababu urithi wetu umekuja kwetu upande wa mashariki mwa Yordani.”
NUM 32:20 Kisha Musa akawaambia, “Kama mtafanya jambo hili, kama mtajivika silaha mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya vita,
NUM 32:21 na kama ninyi nyote mtaenda mmejivika silaha ng’ambo ya Yordani mbele za Mwenyezi Mungu hadi awe amewafukuza adui zake mbele zake,
NUM 32:22 hadi wakati nchi itakapokuwa imeshindwa mbele za Mwenyezi Mungu, ndipo mtaweza kurudi na kuwa huru kutoka masharti yenu kwa Mwenyezi Mungu na Israeli. Nayo nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Mwenyezi Mungu.
NUM 32:23 “Lakini mkishindwa kufanya hili, mtakuwa mnatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu; nanyi kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata.
NUM 32:24 Jengeni miji kwa ajili ya wanawake na watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya mbuzi na kondoo wenu, lakini fanyeni yale mliyoahidi.”
NUM 32:25 Wagadi na Wareubeni wakamwambia Musa, “Sisi watumishi wako tutafanya kama bwana wetu anavyotuagiza.
NUM 32:26 Watoto na wake zetu, makundi ya mbuzi na kondoo, na makundi ya ng’ombe wetu, watabaki hapa katika miji ya Gileadi.
NUM 32:27 Lakini watumishi wenu, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, watavuka ng’ambo kupigana mbele za Mwenyezi Mungu, sawa kama bwana wetu asemavyo.”
NUM 32:28 Kisha Musa akatoa amri kuwahusu kwa kuhani Eleazari, na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa za makabila ya Israeli.
NUM 32:29 Musa akawaambia, “Ikiwa Wagadi na Wareubeni, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, atavuka Yordani pamoja nanyi mbele za Mwenyezi Mungu, basi mtakapoishinda nchi iliyo mbele yenu, wapeni nchi ya Gileadi kama milki yao.
NUM 32:30 Lakini kama hawatavuka pamoja nanyi wakiwa wamevaa silaha za vita, lazima wakubali kupokea milki yao pamoja nanyi katika nchi ya Kanaani.”
NUM 32:31 Wagadi na Wareubeni wakajibu, “Watumishi wako watafanya lile Mwenyezi Mungu alilosema.
NUM 32:32 Tutavuka mbele za Mwenyezi Mungu kuingia Kanaani tukiwa tumevaa silaha za vita, lakini mali tutakayoirithi itakuwa ng’ambo hii ya Yordani.”
NUM 32:33 Kisha Musa akawapa Wagadi, Wareubeni, na nusu ya kabila la Manase mwana wa Yusufu ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, nchi yote pamoja na miji yake, na nchi inayowazunguka.
NUM 32:34 Wagadi wakajenga Diboni, Atarothi, Aroeri,
NUM 32:35 Atroth-Shofani, Yazeri, Yogbeha,
NUM 32:36 Beth-Nimra na Beth-Harani kama miji iliyozungushiwa ngome, tena wakajenga mazizi kwa ajili ya makundi yao ya mbuzi na kondoo.
NUM 32:37 Nao Wareubeni wakajenga upya miji ya Heshboni, Eleale na Kiriathaimu,
NUM 32:38 pia Nebo na Baal-Meoni (majina ya hiyo miji yalibadilishwa) na Sibma. Miji waliyoijenga upya waliipa majina.
NUM 32:39 Wazao wa Makiri mwana wa Manase walienda Gileadi, wakaiteka nchi na kuwafukuza Waamori waliokuwa huko.
NUM 32:40 Kwa hiyo Musa akawapa Wamakiri, wazao wa Manase, nchi ya Gileadi, nao wakakaa huko.
NUM 32:41 Yairi, mzao wa Manase, akateka makazi yao, akayaita Hawoth-Yairi.
NUM 32:42 Naye Noba akateka Kenathi na makazi yaliyoizunguka, akayaita Noba kwa jina lake.
NUM 33:1 Hivi ndivyo vituo katika safari ya Waisraeli walipotoka Misri kwa vikosi chini ya uongozi wa Musa na Haruni.
NUM 33:2 Kwa agizo la Mwenyezi Mungu, Musa aliweka kumbukumbu ya vituo katika safari yao. Hivi ndivyo vituo katika safari yao:
NUM 33:3 Waisraeli walisafiri kutoka Ramesesi katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, siku iliyofuata Pasaka. Walitembea kwa ujasiri wazi mbele ya Wamisri wote,
NUM 33:4 waliokuwa wakizika wazaliwa wao wa kwanza wote, ambao Mwenyezi Mungu alikuwa amewaua kati yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa ameleta hukumu juu ya miungu yao.
NUM 33:5 Waisraeli waliondoka Ramesesi na kupiga kambi huko Sukothi.
NUM 33:6 Wakaondoka Sukothi na kupiga kambi huko Ethamu, pembeni mwa jangwa.
NUM 33:7 Wakaondoka Ethamu, wakageuka wakarudi Pi-Hahirothi, hadi mashariki mwa Baal-Sefoni, wakapiga kambi yao karibu na Migdoli.
NUM 33:8 Wakaondoka Pi-Hahirothi wakapita katikati ya bahari hadi jangwani, na baada ya kusafiri kwa siku tatu katika Jangwa la Ethamu, walipiga kambi huko Mara.
NUM 33:9 Wakaondoka Mara wakaenda Elimu, mahali ambapo palikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende sabini, huko wakapiga kambi.
NUM 33:10 Wakaondoka Elimu na kupiga kambi kando ya Bahari ya Shamu.
NUM 33:11 Wakaondoka kando ya Bahari ya Shamu na kupiga kambi katika Jangwa la Sini.
NUM 33:12 Wakaondoka katika Jangwa la Sini, wakapiga kambi huko Dofka.
NUM 33:13 Wakaondoka Dofka, wakapiga kambi huko Alushi.
NUM 33:14 Wakaondoka Alushi, wakapiga kambi Refidimu, mahali ambapo hapakuwa na maji ya watu kunywa.
NUM 33:15 Wakaondoka Refidimu na kupiga kambi katika Jangwa la Sinai.
NUM 33:16 Wakaondoka katika Jangwa la Sinai na kupiga kambi huko Kibroth-Hataava.
NUM 33:17 Wakaondoka Kibroth-Hataava na kupiga kambi huko Haserothi.
NUM 33:18 Wakaondoka Haserothi na kupiga kambi huko Rithma.
NUM 33:19 Wakaondoka Rithma na kupiga kambi huko Rimon-Peresi.
NUM 33:20 Wakaondoka Rimon-Peresi na kupiga kambi huko Libna.
NUM 33:21 Wakaondoka Libna na kupiga kambi huko Risa.
NUM 33:22 Wakaondoka Risa na kupiga kambi huko Kehelatha.
NUM 33:23 Wakaondoka Kehelatha na kupiga kambi kwenye mlima Sheferi.
NUM 33:24 Wakaondoka kwenye mlima Sheferi na kupiga kambi huko Harada.
NUM 33:25 Wakaondoka Harada na kupiga kambi huko Makelothi.
NUM 33:26 Wakaondoka Makelothi na kupiga kambi huko Tahathi.
NUM 33:27 Wakaondoka Tahathi na kupiga kambi huko Tera.
NUM 33:28 Wakaondoka Tera na kupiga kambi huko Mithka.
NUM 33:29 Wakaondoka Mithka na kupiga kambi huko Hashmona.
NUM 33:30 Wakaondoka Hashmona na kupiga kambi Moserothi.
NUM 33:31 Wakaondoka Moserothi na kupiga kambi huko Bene-Yaakani.
NUM 33:32 Wakaondoka Bene-Yaakani na kupiga kambi huko Hor-Hagidgadi.
NUM 33:33 Wakaondoka Hor-Hagidgadi na kupiga kambi huko Yotbatha.
NUM 33:34 Wakaondoka Yotbatha na kupiga kambi huko Abrona.
NUM 33:35 Wakaondoka Abrona na kupiga kambi huko Esion-Geberi.
NUM 33:36 Wakaondoka Esion-Geberi na kupiga kambi huko Kadeshi katika Jangwa la Sini.
NUM 33:37 Wakaondoka Kadeshi na kupiga kambi kwenye Mlima Hori, mpakani mwa Edomu.
NUM 33:38 Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kuhani Haruni alipanda Mlima Hori, mahali alipofia katika siku ya kwanza ya mwezi wa tano, mwaka wa arobaini baada ya Waisraeli kutoka Misri.
NUM 33:39 Haruni alikufa juu ya Mlima Hori akiwa na umri wa miaka mia moja ishirini na tatu (123).
NUM 33:40 Mfalme Mkanaani wa Aradi, ambaye aliishi huko Negebu ya Kanaani, akasikia kwamba Waisraeli wanakuja.
NUM 33:41 Wakaondoka kwenye mlima Hori na kupiga kambi huko Salmona.
NUM 33:42 Wakaondoka Salmona, wakapiga kambi huko Punoni.
NUM 33:43 Wakaondoka Punoni, wakapiga kambi huko Obothi.
NUM 33:44 Wakaondoka Obothi, wakapiga kambi huko Iye-Abarimu, mipakani mwa Moabu.
NUM 33:45 Wakaondoka Iye-Abarimu, wakapiga kambi huko Dibon-Gadi.
NUM 33:46 Wakaondoka Dibon-Gadi na kupiga kambi huko Almon-Diblathaimu.
NUM 33:47 Wakaondoka Almon-Diblathaimu na kupiga kambi katika milima ya Abarimu, karibu na Nebo.
NUM 33:48 Wakaondoka kwenye milima ya Abarimu na kupiga kambi kwenye tambarare ya Moabu, kando ya Yordani, ng’ambo ya Yeriko.
NUM 33:49 Huko kwenye tambarare za Moabu walipiga kambi kandokando ya Mto Yordani, kuanzia Beth-Yeshimothi hadi Abel-Shitimu.
NUM 33:50 Katika tambarare za Moabu kando ya Yordani, ng’ambo ya Yeriko, Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 33:51 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mtakapovuka Mto Yordani kuingia Kanaani,
NUM 33:52 wafukuzeni wakazi wote wa nchi iliyo mbele yenu. Haribuni sanamu zao zote za kuchongwa, na sanamu zilizotengenezwa kwa kusubu, na kubomoa mahali pao pa juu pa kuabudia.
NUM 33:53 Mtaimiliki nchi hiyo na kukaa huko, kwa kuwa nimewapeni ninyi kuimiliki.
NUM 33:54 Mtaigawanya nchi hiyo kwa kupiga kura, kufuatana na koo zenu. Kwa kundi kubwa zaidi toa urithi mkubwa zaidi, na kwa kundi dogo zaidi urithi mdogo zaidi. Chochote kinachowaangukia kwa kura kitakuwa chao. Mtaigawanya nchi kufuatana na makabila ya babu zenu.
NUM 33:55 “ ‘Lakini kama hamkuwafukuza wenyeji wa nchi hiyo, wale mtakaowaruhusu wabaki watakuwa kama sindano kwenye macho yenu na miiba kwenu kila upande. Watawasumbua katika nchi mtakayoishi.
NUM 33:56 Kisha nitawatenda ninyi kile ambacho nimepanga kuwatenda wao.’ ”
NUM 34:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 34:2 “Waamuru Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia nchi ya Kanaani, nchi ambayo itagawanywa kwenu kama urithi itakuwa na mipaka ifuatayo:
NUM 34:3 “ ‘Upande wenu wa kusini utajumuisha sehemu ya Jangwa la Sini kufuata mpaka wa Edomu. Upande wa mashariki mpaka wenu wa kusini utaanzia mwisho wa Bahari ya Chumvi,
NUM 34:4 katiza kusini mwa Pito la Akrabimu, kuendelea hadi Sini na kwenda kusini mwa Kadesh-Barnea. Kisha mpaka huo utaenda hadi Hasar-Adari hadi Azmoni,
NUM 34:5 mahali mpaka utapinda, na kuunganika na Kijito cha Misri, na kumalizikia kwenye Bahari ya Kati.
NUM 34:6 Mpaka wenu wa magharibi utakuwa Bahari ya Kati. Huu utakuwa mpaka wenu upande wa magharibi.
NUM 34:7 Kwa mpaka wenu wa kaskazini, wekeni alama kuanzia Bahari ya Kati hadi mlima Hori,
NUM 34:8 na kutoka mlima Hori hadi Pito la Hamathi. Kisha mpaka utaenda hadi Sedadi,
NUM 34:9 kuendelea hadi Zifroni, na kuishia Hasar-Enani. Huu utakuwa mpaka wenu upande wa kaskazini.
NUM 34:10 Kwa mpaka wenu wa mashariki, wekeni alama kuanzia Hasar-Enani hadi Shefamu.
NUM 34:11 Mpaka utaelekea kusini kuanzia Shefamu hadi Ribla upande wa mashariki wa Aini, na kuendelea kwenye miteremko mashariki mwa Bahari ya Kinerethi.
NUM 34:12 Kisha mpaka utashuka kuelekea Mto Yordani na kuishia katika Bahari ya Chumvi.
NUM 34:13 Musa akawaamuru Waisraeli: “Gawanyeni nchi hii kwa kura kama urithi. Mwenyezi Mungu ameagiza kwamba itolewe kwa yale makabila tisa na nusu,
NUM 34:14 kwa sababu jamaa ya kabila la Reubeni, kabila la Gadi, na nusu ya kabila la Manase wamekwishapokea urithi wao.
NUM 34:15 Haya makabila mawili na nusu wamekwishapokea urithi wao upande wa mashariki wa Yordani ng’ambo ya Yeriko, kuelekea mawio ya jua.”
NUM 34:16 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
NUM 34:17 “Haya ndiyo majina ya watu ambao watakusaidia kugawanya nchi kama urithi: Eleazari kuhani na Yoshua mwana wa Nuni.
NUM 34:18 Tena uteue kiongozi mmoja kutoka kila kabila kusaidia kuigawanya nchi.
NUM 34:19 “Haya ndiyo majina yao: “Kalebu mwana wa Yefune, kutoka kabila la Yuda;
NUM 34:20 Shemueli mwana wa Amihudi, kutoka kabila la Simeoni;
NUM 34:21 Elidadi mwana wa Kisloni, kutoka kabila la Benyamini;
NUM 34:22 Buki mwana wa Yogli, kiongozi kutoka kabila la Dani;
NUM 34:23 Hanieli mwana wa Efodi, kiongozi kutoka kabila la Manase mwana wa Yusufu;
NUM 34:24 Kemueli mwana wa Shiftani, kiongozi kutoka kabila la Efraimu mwana wa Yusufu;
NUM 34:25 Elisafani mwana wa Parnaki, kiongozi kutoka kabila la Zabuloni;
NUM 34:26 Paltieli mwana wa Azani, kiongozi kutoka kabila la Isakari;
NUM 34:27 Ahihudi mwana wa Shelomi, kiongozi kutoka kabila la Asheri;
NUM 34:28 Pedaheli mwana wa Amihudi, kiongozi kutoka kabila la Naftali.”
NUM 34:29 Hawa ndio watu ambao Mwenyezi Mungu aliamuru wagawanye urithi kwa Waisraeli katika nchi ya Kanaani.
NUM 35:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa katika nchi tambarare ya Moabu, kando ya Mto Yordani kuvukia Yeriko,
NUM 35:2 “Waagize Waisraeli kuwapa Walawi miji ya kuishi kutoka urithi ambao Waisraeli wataumiliki. Wape maeneo ya malisho kuzunguka hiyo miji.
NUM 35:3 Kisha watakuwa na miji ya kuishi na maeneo ya malisho kwa ajili ya ng’ombe wao, mbuzi na kondoo wao, na mifugo yao mingine yote.
NUM 35:4 “Maeneo ya malisho kuzunguka miji hiyo ambayo mtawapa Walawi yataenea dhiraa elfu moja kutoka ukuta wa miji.
NUM 35:5 Nje ya mji, pima dhiraa elfu mbili upande wa mashariki, upande wa kusini dhiraa elfu mbili, upande wa magharibi dhiraa elfu mbili, na upande wa kaskazini dhiraa elfu mbili, na mji utakuwa katikati. Eneo hili litakuwa lao la malisho.
NUM 35:6 “Miji sita mtakayowapa Walawi itakuwa ya makimbilio, ambayo mtu anayemuua mwenzake aweza kukimbilia humo. Zaidi ya hiyo, wapeni miji mingine arobaini na mbili.
NUM 35:7 Kwa jumla inawapasa kuwapa Walawi miji arobaini na nane, pamoja na maeneo ya malisho yao.
NUM 35:8 Miji ambayo mtawapa Walawi kutoka nchi ambayo Waisraeli wanamiliki itatolewa kwa uwiano wa urithi wa kila kabila. Chukua miji mingi kutoka lile kabila lenye miji mingi, lakini uchukue miji michache kutoka kwa kabila lile lenye miji michache.”
NUM 35:9 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:
NUM 35:10 “Sema na Waisraeli, uwaambie: ‘Mtakapovuka Yordani kuingia Kanaani,
NUM 35:11 chagueni baadhi ya miji iwe miji yenu ya makimbilio, ambayo mtu ambaye ameua mwenzake bila kukusudia aweza kukimbilia humo.
NUM 35:12 Itakuwa mahali pa kukimbilia kutoka mlipiza kisasi, ili mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji asife kabla ya kujitetea mbele ya mkutano.
NUM 35:13 Miji hii sita mtakayoitoa itakuwa miji yenu ya makimbilio.
NUM 35:14 Mtatoa miji mitatu ng’ambo hii ya Yordani na miji mingine mitatu upande wa Kanaani kama miji ya makimbilio.
NUM 35:15 Miji hii sita itakuwa mahali pa makimbilio kwa ajili ya Waisraeli, wageni na watu wengine wanaoishi kati yenu, ili mtu ambaye ameua mtu mwingine pasipo kukusudia aweze kukimbilia humo.
NUM 35:16 “ ‘Kama mtu akimpiga mwenzake kwa chuma naye mtu huyo akafa, mtu huyo ni muuaji; muuaji sharti atauawa.
NUM 35:17 Au kama mtu analo jiwe mkononi mwake, naye akampiga mwenzake nalo akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa.
NUM 35:18 Au kama mtu ana chombo cha mti mkononi mwake ambacho chaweza kuua, naye akampiga mwenzake akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa.
NUM 35:19 Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji; wakati akikutana naye, atamuua.
NUM 35:20 Ikiwa mtu ana chuki ya siku nyingi na mwenzake akamsukuma au akamtupia kitu kwa kukusudia naye akafa,
NUM 35:21 au ikiwa katika uadui akampiga ngumi naye akafa, mtu yule sharti atauawa; yeye ni muuaji. Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji atakapokutana naye.
NUM 35:22 “ ‘Lakini kama mtu akimsukuma mwenziwe ghafula pasipo chuki, au kumtupia kitu pasipo kukusudia,
NUM 35:23 au, pasipo kumwona, akimwangushia jiwe ambalo laweza kumuua naye akafa, basi kwa kuwa hakuwa adui yake naye hakukusudia kumuumiza,
NUM 35:24 kusanyiko lazima waamue kati yake na mlipiza kisasi wa damu kufuatana na sheria hizi.
NUM 35:25 Kusanyiko lazima wamlinde yule anayeshtakiwa kuua kutoka kwa mlipiza kisasi wa damu, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alikokuwa amekimbilia. Lazima akae humo hadi atakapokufa kuhani mkuu aliyekuwa amepakwa mafuta matakatifu.
NUM 35:26 “ ‘Lakini kama mshtakiwa atatoka nje ya mipaka ya mji wa makimbilio ambao amekimbilia,
NUM 35:27 na mlipiza kisasi wa damu akamkuta nje ya mji, mlipiza kisasi wa damu anaweza kumuua mshtakiwa huyo bila kuwa na hatia ya kuua.
NUM 35:28 Mshtakiwa lazima akae katika mji wake wa makimbilio hadi atakapokufa kuhani mkuu; atarudi tu kwenye mali yake baada ya kifo cha kuhani mkuu.
NUM 35:29 “ ‘Hizi ndizo kanuni za sheria zitakazohitajiwa kwenu na katika vizazi vyenu vijavyo, popote mtakapoishi.
NUM 35:30 “ ‘Yeyote anayeua mtu atauawa kama muuaji ikiwa tu kuna ushuhuda wa mashahidi. Lakini hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu.
NUM 35:31 “ ‘Usikubali fidia yoyote ya kuokoa uhai wa muuaji ambaye anastahili kufa. Mtu huyo hakika lazima auawe.
NUM 35:32 “ ‘Usikubali fidia ya mtu ambaye amekimbilia katika mji wa makimbilio, na hivyo kumruhusu kurudi kuishi katika nchi yake kabla ya kifo cha kuhani mkuu.
NUM 35:33 “ ‘Msiinajisi nchi mnayoishi. Umwagaji damu hunajisi nchi, na upatanisho hauwezekani kufanyika katika nchi ambayo damu imemwagwa, isipokuwa tu kwa damu ya yule aliyeimwaga damu.
NUM 35:34 Msiinajisi nchi mnayoishi, ambayo nami ninakaa, kwa kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, ninakaa katikati ya Waisraeli.’ ”
NUM 36:1 Viongozi wa jamaa ya ukoo wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase, waliokuwa wametoka katika koo za wazao wa Yusufu, walikuja na kuzungumza mbele ya Musa na viongozi, wakuu wa jamaa ya Waisraeli.
NUM 36:2 Wakasema, “Mwenyezi Mungu alipomwamuru bwana wangu kuwapa Waisraeli nchi kama urithi kwa kura, alikuamuru kutoa urithi wa ndugu yetu Selofehadi kwa binti zake.
NUM 36:3 Sasa ikiwa wataolewa na wanaume wa makabila mengine ya Israeli, itakuwa kwamba urithi wao utaondolewa kutoka urithi wa mababu zetu na kuongezwa katika urithi wa kabila ambalo dada hao wameolewa. Kwa hiyo sehemu ya urithi tuliyogawiwa itachukuliwa kutoka kwetu.
NUM 36:4 Mwaka wa Yubile kwa Waisraeli utakapofika, urithi wao utaongezwa kwa lile kabila ambalo wameolewa, na mali yao itaondolewa kutoka urithi wa kabila la mababu zetu.”
NUM 36:5 Ndipo kwa agizo la Mwenyezi Mungu Musa akatoa amri ifuatayo kwa Waisraeli: “Kile wazao wa kabila la Yusufu wanachosema ni kweli.
NUM 36:6 Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyoamuru kwa binti za Selofehadi: Wanaweza kuolewa na mtu yeyote wampendaye, mradi tu waolewe miongoni mwa koo za kabila la baba yao.
NUM 36:7 Hakuna urithi katika Israeli utakaohamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila Mwisraeli atatunza ardhi ya kabila lake aliyoirithi kutoka kwa baba zake.
NUM 36:8 Kila binti atakayerithi ardhi katika kabila lolote la Israeli ni lazima aolewe na mtu kutoka kabila na ukoo wa baba yake, ili kila Mwisraeli amiliki urithi wa baba zake.
NUM 36:9 Hakuna urithi uwezao kuhamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila kabila la Israeli litatunza nchi linayorithi.”
NUM 36:10 Kwa hiyo binti za Selofehadi wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
NUM 36:11 Binti za Selofehadi, ambao ni Mahla, Tirsa, Hogla, Milka na Noa, wakaolewa na wana wa ndugu za baba yao.
NUM 36:12 Waliolewa ndani ya koo za wazao wa Manase mwana wa Yusufu, na urithi wao ukabaki katika ukoo na kabila la baba yao.
NUM 36:13 Haya ndio maagizo na masharti ambayo Mwenyezi Mungu aliwapa Waisraeli kupitia Musa katika tambarare za Moabu, karibu na Yordani ng’ambo ya Yeriko.
DEU 1:1 Haya ni maneno aliyosema Musa kwa Waisraeli wote jangwani mashariki mwa Yordani, ambayo iko Araba, inayokabiliana na Sufu, kati ya Parani na Tofeli, Labani, Haserothi na Dizahabu.
DEU 1:2 (Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya Mlima Seiri hadi Kadesh-Barnea.)
DEU 1:3 Katika mwaka wa arobaini, siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja, Musa aliwatangazia Waisraeli yale yote Mwenyezi Mungu aliyomwamuru kuwahusu.
DEU 1:4 Hii ilikuwa baada ya kumshinda Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni, na pia huko Edrei alikuwa amemshinda Ogu mfalme wa Bashani, ambaye alitawala huko Ashtarothi.
DEU 1:5 Huko mashariki mwa Yordani katika nchi ya Moabu, Musa alianza kuielezea sheria hii, akisema:
DEU 1:6 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alisema nasi huko Horebu, “Mmekaa muda wa kutosha katika mlima huu.
DEU 1:7 Vunjeni kambi, msonge mbele kuelekea nchi ya vilima ya Waamori; nendeni kwa watu wote ambao ni majirani wa Araba, katika milima, Shefela, katika Negebu na kandokando ya pwani, hadi nchi ya Wakanaani na hadi Lebanoni, na kufika mto mkubwa Frati.
DEU 1:8 Tazama, nimewapa ninyi nchi hii. Ingieni mkaimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliapa kuwa angewapa baba zenu, Ibrahimu, Isaka na Yakobo, pamoja na uzao wao baada yao.”
DEU 1:9 Wakati ule niliwaambia, “Ninyi mmekuwa mzigo mzito sana kwangu kuwachukua peke yangu.
DEU 1:10 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ameongeza hesabu yenu, hivi kwamba leo ninyi ni wengi kama nyota za angani.
DEU 1:11 Naye Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, na awaongeze mara elfu na kuwabariki kama alivyoahidi!
DEU 1:12 Lakini mimi nitawezaje kubeba matatizo yenu, na mizigo yenu, na magomvi yenu peke yangu?
DEU 1:13 Chagueni baadhi ya watu wenye hekima, wenye ufahamu na wanaoheshimika kutoka kila kabila lenu, nami nitawaweka juu yenu.”
DEU 1:14 Mlinijibu, “Shauri ulilolitoa ni zuri.”
DEU 1:15 Kwa hiyo niliwachukua wanaume viongozi wa makabila yenu, wenye hekima na wanaoheshimika, nami nikawateua wawe na mamlaka juu yenu kama majemadari wa maelfu, wa mamia, wa hamsini, na wa makumi, na kama maafisa wa makabila.
DEU 1:16 Nami wakati ule nikawaagiza waamuzi wenu: “Sikilizeni magomvi kati ya ndugu zenu na mwamue kwa haki, hata kama shauri ni kati ya ndugu Waisraeli, au kati ya mmoja wa ndugu Mwisraeli na mgeni.
DEU 1:17 Msioneshe upendeleo katika maamuzi; wasikilizeni wote sawasawa, wadogo kwa wakubwa. Msimwogope mtu yeyote, kwa kuwa hukumu ni ya Mungu. Mniletee mimi shauri lolote lililo gumu sana kwenu, nami nitalisikiliza.”
DEU 1:18 Nami wakati ule niliwaambia kila kitu ambacho mngefanya.
DEU 1:19 Kisha, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru, tuliondoka kutoka Horebu na kwenda kuelekea nchi ya vilima ya Waamori, kupitia jangwa lile kubwa lote la kutisha, lile mliloliona, nasi tukafika Kadesh-Barnea.
DEU 1:20 Kisha niliwaambia, “Mmefika katika nchi ya vilima ya Waamori, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anatupatia.
DEU 1:21 Tazama, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa nchi. Pandeni mkaimiliki kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, alivyowaambia. Msiogope, wala msikate tamaa.”
DEU 1:22 Ndipo ninyi nyote mkanijia na kusema, “Tupeleke watu watutangulie kuipeleleza nchi kwa ajili yetu, na kutuletea taarifa kuhusu njia tutakayopita, na miji tutakayoiendea.”
DEU 1:23 Wazo hilo lilionekana zuri kwangu; kwa hiyo niliwachagua watu wenu kumi na wawili, mwanaume mmoja kutoka kila kabila.
DEU 1:24 Waliondoka na kukwea katika nchi ya vilima, wakafika katika Bonde la Eshkoli na kuipeleleza.
DEU 1:25 Wakachukua baadhi ya matunda ya nchi, wakatuletea na kutuarifu, “Ni nchi nzuri ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anatupatia.”
DEU 1:26 Lakini hamkuwa tayari kukwea, mkaasi dhidi ya amri ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 1:27 Mkanung’unika ndani ya mahema yenu na kusema, “Mwenyezi Mungu anatuchukia, kwa hiyo alitutoa Misri ili kututia mikononi mwa Waamori kutuangamiza.
DEU 1:28 Twende wapi? Ndugu zetu wametufanya kufa moyo. Wanasema, ‘Watu wa huko wana nguvu zaidi na ni warefu kuliko sisi tulivyo; miji ni mikubwa, yenye kuta zilizofika juu angani. Zaidi ya hayo, tumewaona Waanaki huko.’ ”
DEU 1:29 Ndipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope.
DEU 1:30 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayewatangulia, atawapigania, kama alivyofanya kwa ajili yenu huko Misri, mbele ya macho yenu hasa,
DEU 1:31 na pia huko jangwani. Huko mliona jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowachukua, kama baba amchukuavyo mwanawe, katika njia yote mliyoiendea hadi mkafika mahali hapa.”
DEU 1:32 Pamoja na hili, hamkumtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,
DEU 1:33 ambaye aliwatangulia katika safari yenu, kwa moto usiku na kwa wingu mchana, kuwatafutia mahali penu pa kupiga kambi na kuwaonesha njia mtakayoiendea.
DEU 1:34 Mwenyezi Mungu aliposikia lile mlilosema, alikasirika, akaapa kwamba:
DEU 1:35 “Hakuna mtu wa kizazi hiki kiovu atakayeona nchi nzuri niliyoapa kuwapa baba zenu,
DEU 1:36 isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune. Yeye ataiona, nami nitampa yeye na wazao wake nchi aliyoikanyaga kwa miguu, kwa sababu alimfuata Mwenyezi Mungu kwa moyo wote.”
DEU 1:37 Kwa sababu yenu Mwenyezi Mungu pia alinikasirikia mimi, akasema, “Hutaingia hiyo nchi pia.
DEU 1:38 Lakini msaidizi wako, Yoshua mwana wa Nuni, ataingia. Mtie moyo, kwa sababu atawaongoza Waisraeli kuirithi hiyo nchi.
DEU 1:39 Watoto ambao mlisema wangechukuliwa mateka, yaani watoto wenu ambao bado hawajui jema na baya, wataingia katika nchi. Nitawapa hiyo nchi, nao wataimiliki.
DEU 1:40 Bali ninyi geukeni, mwondoke kuelekea jangwani kwa kufuata njia ya Bahari ya Shamu.”
DEU 1:41 Ndipo mkanijibu, “Tumemtenda Mwenyezi Mungu dhambi. Tutaenda kupigana, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru.” Hivyo kila mmoja wenu akachukua silaha zake, huku mkifikiri kuwa ni rahisi kukwea katika nchi ya vilima.
DEU 1:42 Lakini Mwenyezi Mungu aliniambia, “Waambie, ‘Msipande kupigana, kwa sababu sitakuwa pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu.’ ”
DEU 1:43 Hivyo niliwaambia, lakini hamkutaka kusikia. Mliasi dhidi ya amri ya Mwenyezi Mungu, na katika kiburi chenu mlienda katika nchi ya vilima.
DEU 1:44 Waamori ambao waliishi katika vilima hivyo waliinuka dhidi yenu, wakawafukuza kama kundi la nyuki wakiwapiga njia yote ya Seiri hadi Horma.
DEU 1:45 Mlirudi na kulia mbele za Mwenyezi Mungu, lakini Mungu hakusikiliza kilio chenu, wala hakuwajali.
DEU 1:46 Hivyo mlikaa Kadeshi kwa siku nyingi, kwa muda ule wote mliokaa huko.
DEU 2:1 Kisha tukageuka nyuma na kusafiri kuelekea jangwani kwa njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kama Mwenyezi Mungu alivyonielekeza. Kwa muda mrefu tulitembea kuzunguka nchi ya vilima ya Seiri.
DEU 2:2 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia,
DEU 2:3 “Umetembea kuzunguka hii nchi ya vilima kwa muda wa kutosha; sasa geukia kaskazini.
DEU 2:4 Wape watu maagizo haya: ‘Mko karibu kupita katikati ya nchi ya ndugu zako ambao ni wazao wa Esau, ambao wanaishi Seiri. Watawaogopa, lakini mwe waangalifu.
DEU 2:5 Msiwachokoze kwa vita kwa maana sitawapa ninyi sehemu yoyote ya nchi yao, hata sehemu ya kutosha kuweka wayo wenu juu yake. Nimempa Esau nchi ya vilima ya Seiri kama yake mwenyewe.
DEU 2:6 Mtawalipa fedha kwa chakula mtakachokula na maji mtakayokunywa.’ ”
DEU 2:7 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewabariki kwa kazi yote ya mikono yenu. Amewalinda katika safari yenu katikati ya jangwa hili kubwa. Kwa miaka hii arobaini Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amekuwa pamoja nanyi, na hamkupungukiwa na kitu chochote.
DEU 2:8 Basi tulipita kwa ndugu zetu wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri. Tuligeuka kutoka njia ya Araba ambayo inatokea Elathi na Esion-Geberi, tukasafiri kufuata njia ya jangwa la Moabu.
DEU 2:9 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Usiwasumbue Wamoabu kwa vita, kwa kuwa sitawapa sehemu yoyote ya nchi yao. Nimetoa nchi ya Ari kwa wazao wa Lutu kama milki yao.”
DEU 2:10 (Waemi walikuwa wakiishi huko hapo zamani, watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki.
DEU 2:11 Kama walivyokuwa Waanaki, hao pia walikuwa kama Warefai, lakini Wamoabu waliwaita Waemi.
DEU 2:12 Wahori waliishi Seiri, lakini wazao wa Esau waliwafukuza. Waliwaangamiza Wahori na kukaa mahali pao, kama Waisraeli walivyofanya katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliwapa kama milki yao.)
DEU 2:13 Mwenyezi Mungu akasema, “Sasa ondokeni mvuke Bonde la Zeredi.” Hivyo tukavuka bonde.
DEU 2:14 Miaka thelathini na nane ilipita tangu wakati tuliondoka Kadesh-Barnea hadi tulipovuka Bonde la Zeredi. Kwa wakati huo kile kizazi chote cha wanaume walioweza kwenda vitani kilikuwa kimekufa, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amewaapia.
DEU 2:15 Mkono wa Mwenyezi Mungu uliwakabili hadi alipowaangamiza wote huko kambini.
DEU 2:16 Ikawa baada ya mtu wa mwisho wa wale walioweza kwenda vitani kufa,
DEU 2:17 Mwenyezi Mungu akaniambia,
DEU 2:18 “Leo utapita katika nchi ya Moabu huko Ari.
DEU 2:19 Utakapokuja kwa Waamoni, msiwasumbue wala kuwachokoza kwa vita, kwa kuwa sitawapa ardhi yoyote iliyo ya Waamoni kuwa milki yenu. Nimeitoa kama milki ya wazao wa Lutu.”
DEU 2:20 (Hiyo pia ilidhaniwa kuwa nchi ya Warefai walioishi huko, lakini Waamoni waliwaita Wazamzumi.
DEU 2:21 Walikuwa watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki. Mwenyezi Mungu akawaangamiza kutoka mbele ya Waamoni, ambao waliwafukuza na kukaa mahali pao.
DEU 2:22 Mwenyezi Mungu alikuwa amefanya vivyo hivyo kwa wazao wa Esau, ambao waliishi Seiri, alipowaangamiza Wahori watoke mbele yao. Waliwafukuza na wao wakaishi mahali pao hadi leo.
DEU 2:23 Nao Waavi ambao waliishi katika vijiji hadi Gaza, Wakaftori waliokuja kutoka Kaftori waliwaangamiza na kukaa mahali pao.)
DEU 2:24 “Ondoka sasa na uvuke Bonde la Arnoni. Tazama, nimemweka mikononi mwako Sihoni Mwamori, mfalme wa Heshboni na nchi yake. Anza kuimiliki nchi hiyo na umwingize katika vita.
DEU 2:25 Siku hii ya leo nitaanza kuwatia hofu na woga mataifa yote chini ya mbingu wawaogope ninyi. Watakaposikia taarifa zenu, watatetemeka na kufadhaika kwa sababu yenu.”
DEU 2:26 Kutoka jangwa la Kedemothi nilituma wajumbe wenye maneno ya amani kwa Sihoni mfalme wa Heshboni kusema,
DEU 2:27 “Turuhusu tupite katika nchi yako. Tutapita katika barabara kuu, hatutageuka kuume wala kushoto.
DEU 2:28 Tuuzie chakula tule na maji tunywe kwa thamani yake katika fedha. Turuhusu tu tupite kwa miguu,
DEU 2:29 kama wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri na Wamoabu ambao wanaishi Ari walivyotufanyia, hadi tuvuke Yordani kuingia nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anatupatia.”
DEU 2:30 Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni alikataa kuturuhusu kupita. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alikuwa ameifanya roho yake kuwa ngumu na moyo wake kuwa mkaidi ili amweke kwenye mikono yenu, kama alivyofanya sasa.
DEU 2:31 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Tazama, nimeanza kuwapa Mfalme Sihoni na nchi yake kwako. Sasa anzeni kuishinda na kuimiliki nchi yake.”
DEU 2:32 Sihoni pamoja na jeshi lake lote walipokuja kukutana nasi katika vita huko Yahazi,
DEU 2:33 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alimweka mikononi mwetu, nasi tukamwangamiza pamoja na wanawe na jeshi lake lote.
DEU 2:34 Kwa wakati ule tuliteka miji yake yote na kuiangamiza kabisa: wanaume, wanawake na watoto. Hatukumwacha yeyote.
DEU 2:35 Lakini mifugo na nyara tulizoziteka kutoka ile miji tulijichukulia wenyewe.
DEU 2:36 Kutoka Aroeri kwenye ukingo wa Bonde la Arnoni, kutoka mji ulio ndani ya bonde, hadi kufika Gileadi, hapakuwa na mji hata mmoja uliokuwa na nguvu kutushinda. Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alitupatia yote.
DEU 2:37 Lakini kulingana na amri ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, hamkujiingiza katika nchi yoyote ya Waamoni, wala katika sehemu yoyote iliyo kandokando ya Mto Yaboki, wala katika miji iliyo vilimani.
DEU 3:1 Kisha tukageuka tukakwea kufuata njia iliyoelekea Bashani, Ogu mfalme wa Bashani akaondoka na jeshi lake lote kupigana na sisi huko Edrei.
DEU 3:2 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Usimwogope kwa kuwa nimekwisha mkabidhi mikononi mwako pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Umfanyie sawasawa na ulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”
DEU 3:3 Hivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, pia akamweka Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote mikononi mwetu. Tuliwaangamiza wote, hakubakia hata mmoja.
DEU 3:4 Wakati huo tuliteka miji yake yote. Hakuna mji hata mmoja kati ya ile sitini ambao hatukuuteka, yaani eneo lote la Argobu, utawala wa Mfalme Ogu katika Bashani.
DEU 3:5 Miji yote hii ilijengewa ngome zenye kuta ndefu zenye malango na makomeo; pia kulikuwa na vijiji vingi ambavyo havikujengewa kuta.
DEU 3:6 Tuliwaangamiza kabisa, kama tulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Heshboni, tukiangamiza kila mji, yaani wanaume, wanawake na watoto.
DEU 3:7 Lakini wanyama wote wa kufuga pamoja na nyara kutoka miji yao tulichukua vikawa vyetu.
DEU 3:8 Hivyo kwa wakati huo tukachukua kutoka kwa wafalme hawa wawili wa Waamori nchi ya mashariki mwa Yordani, kutoka Bonde la Arnoni hadi kufika kwenye Mlima Hermoni.
DEU 3:9 (Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri.)
DEU 3:10 Tuliteka miji yote kwenye uwanda wa juu, Gileadi yote, Bashani yote hadi Saleka na Edrei, miji ya utawala wa Ogu huko Bashani.
DEU 3:11 (Mfalme Ogu wa Bashani ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa mabaki ya Warefai. Kitanda chake kilikuwa cha chuma chenye urefu wa dhiraa tisa na upana wa dhiraa nne. Hata sasa kinaweza kuonekana katika mji wa Waamoni wa Raba.)
DEU 3:12 Katika nchi tuliyoiteka wakati ule, niliwapa kabila la Reubeni na Gadi eneo lililoko kaskazini la Aroeri kando ya Bonde la Arnoni, na nusu ya eneo la nchi ya vilima ya Gileadi, pamoja na miji yake.
DEU 3:13 Kisha nusu ya kabila la Manase niliwapa sehemu ya Gileadi iliyobaki pamoja na Bashani yote, ambayo ilikuwa utawala wa Ogu. (Eneo lote la Argobu katika Bashani lilikuwa linajulikana kama nchi ya Warefai.
DEU 3:14 Yairi, mzao wa kabila la Manase, alichukua eneo lote la nchi ya Argobu hadi kufikia mpaka wa Wageshuri na Wamaaka, ukaitwa kwa jina lake; kwa hiyo hadi leo Bashani inaitwa Hawoth-Yairi.)
DEU 3:15 Nikampa Makiri nchi ya Gileadi.
DEU 3:16 Lakini niliwapa Wareubeni na Wagadi eneo kuanzia Gileadi hadi Bonde la Arnoni (katikati ya bonde ulikuwa ndio mpaka), kuelekea hadi Mto Yaboki, ambao ndio mpaka wa Waamoni.
DEU 3:17 Kwa upande wa magharibi mpaka wao ulikuwa Yordani katika Araba, toka ziwa Galilaya hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), kwenye miteremko ya Pisga upande wa mashariki.
DEU 3:18 Wakati huo nilikuamuru: “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekupa nchi hii uimiliki. Lakini ni lazima wanaume wenu wote wenye uwezo, wakiwa wamejiandaa tayari kwa vita, wavuke ng’ambo wakiwatangulia ndugu zako Waisraeli.
DEU 3:19 Lakini wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu (kwani najua mnayo mifugo mingi) wanaweza kukaa katika miji niliyowapa,
DEU 3:20 hadi hapo Mwenyezi Mungu atakapowapa ndugu zenu kupumzika kama alivyowapa ninyi, wao pia wamiliki ile nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, ng’ambo ya Yordani. Baada ya hapo, kila mmoja wenu anaweza kurudi kwenye milki niliyowapa.”
DEU 3:21 Wakati huo nilimwamuru Yoshua, “Umejionea kwa macho yako mwenyewe yale yote ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewafanyia wafalme hawa wawili. Mwenyezi Mungu atazifanyia falme zote huko mnakoenda vivyo hivyo.
DEU 3:22 Msiwaogope, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atapigana kwa ajili yenu.”
DEU 3:23 Wakati huo nilimsihi Mwenyezi Mungu:
DEU 3:24 “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, umemwonesha mtumishi wako ukuu wako na mkono wako wenye uweza. Kwa kuwa ni mungu yupi aliye mbinguni au duniani anayeweza kufanya kazi na matendo makuu kama ufanyayo wewe?
DEU 3:25 Acha niende nikaione hiyo nchi nzuri ng’ambo ya Yordani, ile nchi nzuri ya vilima na Lebanoni.”
DEU 3:26 Lakini kwa sababu yenu Mwenyezi Mungu alinikasirikia na hakutaka kunisikiliza. Mwenyezi Mungu aliniambia, “Hilo latosha; usiseme nami jambo hili tena.
DEU 3:27 Kwea juu ya kilele cha Pisga uangalie magharibi, kaskazini, kusini na mashariki. Iangalie hiyo nchi kwa macho yako, kwa vile wewe hutavuka Yordani.
DEU 3:28 Lakini mwagize Yoshua, mtie moyo na umtie nguvu, kwa kuwa yeye atawaongoza watu hawa hadi ng’ambo na kuwarithisha nchi utakayoiona.”
DEU 3:29 Kwa hiyo tulikaa kwenye bonde karibu na Beth-Peori.
DEU 4:1 Sikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zako, anawapa.
DEU 4:2 Usiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambayo nawapa.
DEU 4:3 Mliona kwa macho yenu wenyewe kile Mwenyezi Mungu alichokifanya kule Baal-Peori. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori,
DEU 4:4 lakini ninyi nyote mlioshikamana na Mwenyezi Mungu kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai hadi leo.
DEU 4:5 Tazama, nimewafundisha amri na sheria kama Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki.
DEU 4:6 Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.”
DEU 4:7 Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba?
DEU 4:8 Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?
DEU 4:9 Mwe waangalifu na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke mioyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.
DEU 4:10 Kumbuka siku uliyosimama mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kule Horebu aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.”
DEU 4:11 Mlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto hadi juu mbinguni, pamoja na mawingu meusi na giza nene.
DEU 4:12 Ndipo Mwenyezi Mungu alipozungumza nanyi kutoka kati ya moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu.
DEU 4:13 Aliwatangazia agano lake, hizo Amri Kumi ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe.
DEU 4:14 Naye Mwenyezi Mungu alinielekeza wakati huo kuwafundisha ninyi sheria na amri ambazo mnapaswa kuzifuata katika nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki.
DEU 4:15 Hamkuona umbo la aina yoyote siku ambayo Mwenyezi Mungu alizungumza nanyi kule Horebu kutoka kati ya moto. Kwa hiyo mjihadhari kwa uangalifu sana,
DEU 4:16 ili msije mkajichafua na kujitengenezea sanamu au kinyago chenye umbo lolote kama la mwanaume au mwanamke,
DEU 4:17 au kama mnyama aliye juu ya nchi au ndege yeyote arukaye angani,
DEU 4:18 au kama kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi, au samaki yeyote aliye ndani ya maji.
DEU 4:19 Na utazamapo juu angani na ukaliona jua, mwezi na nyota na vyote vinavyoipamba mbingu, usije ukashawishiwa kuviinamia na kuviabudu vitu ambavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivigawia mataifa yote chini ya mbingu.
DEU 4:20 Lakini ninyi, Mwenyezi Mungu amewatoa kutoka tanuru la kuyeyushia chuma, kutoka Misri, kuwa watu wa urithi wake, kama mlivyo sasa.
DEU 4:21 Mwenyezi Mungu alinikasirikia kwa sababu yenu na akaapa kwamba sitavuka Yordani kuingia katika nchi nzuri Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayowapa kuwa urithi wenu.
DEU 4:22 Nitakufa katika nchi hii; sitavuka Yordani, lakini ninyi ni karibu mvuke mkaimiliki ile nchi nzuri.
DEU 4:23 Jihadharini msilisahau agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, lile alilofanya nanyi; msijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewakataza.
DEU 4:24 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.
DEU 4:25 Baada ya kuwa na watoto na wajukuu na kuishi katika nchi hiyo siku nyingi, tena mkijichafua na kutengeneza sanamu ya aina yoyote, mkifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kumfanya awe na hasira,
DEU 4:26 ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yenu siku hii kwamba mtaangamia mara moja kutoka katika nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki. Hamtaishi kule kwa muda mrefu bali kwa hakika mtaangamizwa.
DEU 4:27 Mwenyezi Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa, na ni wachache wenu tu watakaosalia miongoni mwa mataifa hayo ambayo Mwenyezi Mungu atawafukuzia.
DEU 4:28 Huko mtaabudu miungu ya miti na mawe iliyotengenezwa na watu, ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kula au kunusa.
DEU 4:29 Lakini kama mtamtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mtampata; kama mtamtafuta kwa moyo wote na kwa roho yote.
DEU 4:30 Mnapokuwa katika dhiki, nayo mambo haya yote yamewatokea siku hizo, ndipo mtamrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kumtii.
DEU 4:31 Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mungu mwenye huruma, hatawaacha au kuwaangamiza wala kusahau agano alilofanya na baba zenu, alilowathibitishia kwa kiapo.
DEU 4:32 Sasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa?
DEU 4:33 Je, kuna watu wengine wowote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi?
DEU 4:34 Je, kuna mungu yeyote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu ya kutisha, kama yale ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu?
DEU 4:35 Mlioneshwa mambo haya ili mpate kujua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu; hakuna mwingine ila yeye.
DEU 4:36 Kutoka mbinguni amewasikizisha sauti yake ili kuwaadilisha. Hapa duniani aliwaonesha moto wake mkubwa, nanyi mlisikia maneno yake kutoka kati ya ule moto.
DEU 4:37 Kwa sababu aliwapenda baba zenu na alichagua wazao wao baada yao, aliwatoa katika nchi ya Misri kwa Uwepo wake na kwa uwezo wake mkuu,
DEU 4:38 aliwafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi na kuwaleta ninyi katika nchi yao na akawapa ninyi kuwa urithi wenu, kama ilivyo leo.
DEU 4:39 Kubalini na mweke moyoni leo kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu mbinguni juu na duniani chini. Hakuna mwingine.
DEU 4:40 Mshike amri na maagizo yake ninayowapa leo, ili mpate kufanikiwa ninyi na watoto wenu baada yenu, na mpate kuishi maisha marefu katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, siku zote.
DEU 4:41 Kisha Musa akatenga miji mitatu mashariki mwa Yordani,
DEU 4:42 ambayo mtu yeyote aliyemuua mtu angeweza kukimbilia ikiwa amemuua jirani yake bila kukusudia na bila kuwa na chuki naye siku zilizopita. Angeweza kukimbilia katika mmoja ya miji hii na kuokoa maisha yake.
DEU 4:43 Miji hiyo ilikuwa: Bezeri katika tambarare ya jangwa kwa ajili ya Wareubeni; Ramothi katika nchi ya Gileadi kwa ajili ya Wagadi; nao mji wa Golani katika nchi ya Bashani kwa ajili ya Wamanase.
DEU 4:44 Hii ndiyo sheria Musa aliyoweka mbele ya Waisraeli.
DEU 4:45 Haya ndio masharti, amri na sheria Musa alizowapa Waisraeli walipotoka Misri,
DEU 4:46 nao walikuwa katika bonde karibu na Beth-Peori mashariki mwa Yordani, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni; naye alishindwa na Musa na Waisraeli walipotoka Misri.
DEU 4:47 Waliimiliki nchi yake na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, wafalme wawili Waamori waliotawala mashariki mwa Yordani.
DEU 4:48 Nchi hii ilienea kutoka Aroeri ukingoni mwa Bonde la Arnoni hadi Mlima Sioni (yaani Hermoni),
DEU 4:49 pamoja na eneo lote la Araba mashariki mwa Yordani, na kuenea hadi Bahari ya Araba kwenye miteremko ya Pisga.
DEU 5:1 Musa akawaita Israeli wote, akawaambia: Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata.
DEU 5:2 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika mlima wa Horebu.
DEU 5:3 Si kwamba Mwenyezi Mungu alifanya agano na baba zetu, bali alifanya nasi, nasi sote ambao tuko hai hapa leo.
DEU 5:4 Mwenyezi Mungu alisema nanyi uso kwa uso kutoka kati ya moto juu ya mlima.
DEU 5:5 (Wakati huo nilisimama kati ya Mwenyezi Mungu na ninyi kuwatangazia neno la Mwenyezi Mungu, kwa sababu mliogopa ule moto, nanyi hamkupanda mlimani.) Naye Mungu alisema:
DEU 5:6 “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
DEU 5:7 “Usiwe na miungu mingine ila mimi.
DEU 5:8 Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji.
DEU 5:9 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanaonichukia,
DEU 5:10 lakini ninaonesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaonipenda na kuzishika amri zangu.
DEU 5:11 Usilitaje bure jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
DEU 5:12 Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alivyokuagiza.
DEU 5:13 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote.
DEU 5:14 Lakini siku ya saba ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au wa kike, wala ng’ombe wako, punda wako au mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye malangoni mwako, ili mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika kama wewe.
DEU 5:15 Kumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato.
DEU 5:16 Waheshimu baba yako na mama yako, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anayokupa.
DEU 5:17 Usiue.
DEU 5:18 Usizini.
DEU 5:19 Usiibe.
DEU 5:20 Usimshuhudie jirani yako uongo.
DEU 5:21 Usitamani mke wa jirani yako. Usitamani nyumba ya jirani yako au shamba lake, mtumishi wake wa kiume au wa kike, ng’ombe au punda wake, wala kitu chochote cha jirani yako.”
DEU 5:22 Hizi ndizo amri alizozitangaza Mwenyezi Mungu kwa sauti kubwa kwa kusanyiko lenu lote huko mlimani kutoka kati ya moto na wingu na giza nene, wala hakuongeza chochote zaidi. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, naye akanipa mimi.
DEU 5:23 Mliposikia sauti kutoka kati ya giza, mlima ulipokuwa ukiwaka moto, viongozi wenu wote wa makabila yenu na wazee wenu walinijia mimi.
DEU 5:24 Nanyi mkasema, “Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ametuonesha utukufu na enzi yake, nasi tumesikia sauti yake kutoka kati ya moto. Leo tumeona kwamba mwanadamu anaweza kuishi hata kama Mungu akizungumza naye.
DEU 5:25 Lakini sasa, kwa nini tufe? Moto huu mkubwa utatuteketeza sisi na tutakufa tukiendelea kusikia sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, zaidi.
DEU 5:26 Ni mtu yupi mwenye mwili ambaye amewahi kuisikia sauti ya Mungu aliye hai akizungumza kutoka kati ya moto, kama sisi tulivyoisikia, naye akaishi?
DEU 5:27 Sogea karibu usikie yale yote asemayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Kisha utuambie chochote kile ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anakuambia. Tutasikiliza na kutii.”
DEU 5:28 Mwenyezi Mungu aliwasikia wakati mlipozungumza nami, na Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nimesikia kile hawa watu walichokuambia. Kila kitu walichokisema ni kizuri.
DEU 5:29 Laiti kama mioyo yao ingekuwa na mwelekeo wa kuniogopa na kuzishika amri zangu zote daima, ili wafanikiwe wao pamoja na watoto wao milele!
DEU 5:30 “Nenda uwaambie warudi kwenye mahema yao.
DEU 5:31 Lakini wewe baki hapa pamoja nami ili niweze kukupa maagizo yote, amri na sheria ambazo utawafundisha wazifuate katika nchi ninayoenda kuwapa waimiliki.”
DEU 5:32 Hivyo kuweni waangalifu kuyafanya yale Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyowaagiza; msigeuke upande wa kuume wala wa kushoto.
DEU 5:33 Fuateni yale yote ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaagiza, ili mpate kuishi, kustawi na kuziongeza siku zenu katika nchi mtakayoimiliki.
DEU 6:1 Haya ndio maagizo, amri na sheria ambazo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliniagiza niwafundishe ninyi ili mpate kuyashika katika nchi ambayo ninyi mnavuka Yordani kuimiliki,
DEU 6:2 ili ninyi, watoto wenu na watoto wao baada yao wamche Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, siku zote kwa kushika amri na maagizo yake yote ninayowapa, ili mweze kuyafurahia maisha marefu.
DEU 6:3 Sikia, ee Israeli, nawe uwe mwangalifu kutii ili upate kufanikiwa na kuongezeka sana katika nchi inayotiririka maziwa na asali, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi ninyi.
DEU 6:4 Sikia, ee Israeli: Mwenyezi Mungu, Mungu wako, Mwenyezi Mungu ni mmoja.
DEU 6:5 Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.
DEU 6:6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako.
DEU 6:7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo.
DEU 6:8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako.
DEU 6:9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
DEU 6:10 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, Isaka na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, yenye miji inayopendeza ambayo hukuijenga,
DEU 6:11 nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba,
DEU 6:12 jihadhari usije ukamwacha Mwenyezi Mungu, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
DEU 6:13 Utamcha Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake.
DEU 6:14 Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka;
DEU 6:15 kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi.
DEU 6:16 Usimjaribu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kama ulivyomjaribu huko Masa.
DEU 6:17 Utayashika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa bidii, na masharti na amri alizokupa.
DEU 6:18 Fanya lililo haki na jema mbele za Mwenyezi Mungu, ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayo Mwenyezi Mungu aliahidi kwa kiapo kwa baba zako,
DEU 6:19 kuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kama Mwenyezi Mungu alivyosema.
DEU 6:20 Siku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alikuagiza wewe?”
DEU 6:21 Mwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakini Mwenyezi Mungu alitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu.
DEU 6:22 Machoni petu, Mwenyezi Mungu alitenda ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno dhidi ya Misri, na dhidi ya Farao na nyumba yake yote.
DEU 6:23 Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupatia nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo.
DEU 6:24 Mwenyezi Mungu akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo.
DEU 6:25 Tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”
DEU 7:1 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, akuletapo katika nchi unayoingia kuimiliki, na awafukuzapo mbele yako mataifa mengi, yaani Wahiti, Wagirgashi, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, mataifa saba makubwa tena yenye nguvu kuliko wewe,
DEU 7:2 pia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapowatia mkononi mwako na ukawashinda, basi ni lazima uwaangamize wote kabisa. Usifanye agano nao, wala usiwahurumie.
DEU 7:3 Usioane nao. Usimtoe binti yako kuolewa na mwanawe, au kumchukua binti yake aolewe na mwanao.
DEU 7:4 Kwa maana watamgeuza mwanao aache kunifuata, ili aitumikia miungu mingine, nayo hasira ya Mwenyezi Mungu itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza ghafula.
DEU 7:5 Hili ndilo utakalowafanyia: Vunja madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia, katakata nguzo zao za Ashera, na kuchoma sanamu zao kwa moto;
DEU 7:6 kwa kuwa wewe ni taifa takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekuchagua kutoka mataifa yote duniani uwe taifa lake, hazina yake ya pekee.
DEU 7:7 Mwenyezi Mungu hakuweka upendo wake juu yenu na kuwachagua kwa sababu mlikuwa wengi mno kuliko watu wengine, kwa maana ninyi ndio mliokuwa wachache sana kuliko mataifa yote.
DEU 7:8 Lakini ni kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwapenda ninyi na kutunza kiapo alichowaapia babu zenu kwamba atawatoa ninyi kwa mkono wenye nguvu na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa, kutoka nguvu za Farao mfalme wa Misri.
DEU 7:9 Basi ujue kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake.
DEU 7:10 Lakini kwa wale wanaomchukia atawalipiza kwenye nyuso zao kwa maangamizi; hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao wale wamchukiao.
DEU 7:11 Kwa hiyo, kuweni waangalifu kufuata maagizo, amri na sheria ninazowapa leo.
DEU 7:12 Mkizingatia sheria hizi na kuzifuata kwa uangalifu, basi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atatunza agano lake la upendo nanyi, kama alivyowaapia baba zenu.
DEU 7:13 Atawapenda ninyi na kuwabariki na kuongeza idadi yenu. Atabariki uzao wa tumbo lenu, mazao ya nchi yenu, nafaka, divai mpya na mafuta, ndama za ng’ombe wa makundi yenu, na kondoo wa makundi yenu katika nchi ile aliyoapa kuwapa baba zenu.
DEU 7:14 Mtabarikiwa kuliko mataifa mengine yote, hakuna wanaume wala wanawake kwenu watakaokosa watoto, wala mifugo yenu haitakuwa tasa.
DEU 7:15 Mwenyezi Mungu atawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wowote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia.
DEU 7:16 Ni lazima mwangamize watu wote ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawatia mikononi mwenu. Msiwatazame kwa kuwahurumia na msiitumikie miungu yao, kwa kuwa itakuwa mtego kwenu.
DEU 7:17 Mnaweza kujiuliza wenyewe: “Mataifa haya ni yenye nguvu kuliko sisi. Tutawezaje kuwafukuza?”
DEU 7:18 Lakini msiwaogope. Kumbukeni vyema jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyofanya kwa Farao na kwa wote huko Misri.
DEU 7:19 Mliona kwa macho yenu wenyewe majaribu makubwa, ishara za miujiza na maajabu, mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, ambao kwa huo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwatoa mtoke Misri. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawafanyia hivyo watu wote ambao mnawaogopa sasa.
DEU 7:20 Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atatuma nyigu miongoni mwao hadi yale mabaki watakaojificha waangamie.
DEU 7:21 Msiingiwe na hofu kwa sababu yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye yupo miongoni mwenu ni mkuu naye ni Mungu wa kutisha.
DEU 7:22 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawafukuza mataifa hayo mbele yenu kidogo kidogo. Hamtaruhusiwa kuwaondoa wote kwa mara moja, la sivyo wanyama pori wataongezeka na kuwa karibu nanyi.
DEU 7:23 Lakini Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawatia watu hao mikononi mwenu, akiwatia katika machafuko makubwa hadi waangamizwe.
DEU 7:24 Atawatia wafalme wao mikononi mwenu, nanyi mtayafuta majina yao chini ya mbingu. Hakuna hata mmoja atakayeweza kusimama dhidi yenu bali mtawaangamiza.
DEU 7:25 Sanamu za miungu yao mtazichoma moto. Msitamani fedha wala dhahabu iliyo juu ya vinyago hivyo, wala msiichukue iwe yenu, la sivyo mtakuwa mmetekwa nayo. Kwa kuwa ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 7:26 Msilete vitu vya machukizo katika nyumba zenu kwani ninyi, mtatengwa kama vitu hivyo kwa maangamizi. Ukichukie kabisa kitu hicho kwa kuwa kimetengwa kwa maangamizi.
DEU 8:1 Uwe mwangalifu kufuata kila agizo ninalokupa wewe leo, ili mweze kuishi, kuongezeka na mweze kuingia mkamiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliahidi kwa kiapo kwa baba zenu.
DEU 8:2 Kumbuka jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la.
DEU 8:3 Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mwenyezi Mungu.
DEU 8:4 Nguo zenu hazikuchakaa wala miguu yenu haikuvimba kwa miaka hii arobaini.
DEU 8:5 Mjue basi ndani ya mioyo yenu kama mtu anavyomwadibisha mwanawe, ndivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atawaadibisha ninyi.
DEU 8:6 Shikeni maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mtembee katika njia zake na kumheshimu.
DEU 8:7 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawaleta katika nchi nzuri, nchi yenye vijito na mabwawa ya maji, yenye chemchemi zinazotiririka mabondeni na katika vilima;
DEU 8:8 nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu na mitini, mikomamanga, mafuta ya zeituni na asali;
DEU 8:9 nchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa chochote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kwenye vilima.
DEU 8:10 Mtakapokwisha kula na kushiba, msifuni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa ajili ya nchi nzuri aliyowapa.
DEU 8:11 Jihadharini msimsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mkashindwa kushika maagizo yake, sheria na amri zake ambazo ninawapa leo.
DEU 8:12 Angalia wakati mtakapokuwa mmekula na kushiba, mkajenga nyumba nzuri na kukaa humo,
DEU 8:13 na wakati makundi yenu ya ng’ombe na mbuzi na kondoo yatakapoongezeka na fedha na dhahabu yenu itakapoongezeka na vyote mlivyo navyo vitakapozidishwa,
DEU 8:14 basi mioyo yenu isiwe na kiburi mkamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
DEU 8:15 Aliwaongoza kupitia jangwa lile kubwa na la kutisha, nchi ile ya kiu isiyo na maji, yenye nyoka wa sumu na nge. Aliwatolea maji katika mwamba mgumu.
DEU 8:16 Aliwapa mana ya kula jangwani, kitu ambacho baba zenu hawakukijua, ili kuwanyenyekeza na kuwajaribu ninyi, na mwishoni apate kuwatendea mema.
DEU 8:17 Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.”
DEU 8:18 Lakini kumbukeni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.
DEU 8:19 Ikiwa mtamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mkaifuata miungu mingine, mkaiabudu na kuisujudia, ninashuhudia dhidi yenu leo kwamba hakika mtaangamizwa.
DEU 8:20 Kama mataifa Mwenyezi Mungu aliyoyaangamiza mbele yenu, ndivyo ninyi mtakavyoangamizwa kwa kutokumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 9:1 Sikiliza, ee Israeli. Sasa mnakaribia kuvuka Yordani mwingie na kuwafukuza mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi pamoja na miji mikubwa yenye kuta zilizofika juu angani.
DEU 9:2 Watu ni wenye nguvu na warefu, ni wana wa Waanaki! Mnafahamu habari zao na mmesikia inavyosemekana: “Ni nani awezaye kusimama dhidi ya Waanaki?”
DEU 9:3 Kuweni na hakika leo kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayetangulia kuvuka mbele yenu kama moto uteketezao. Atawaangamiza; atawatiisha mbele yenu. Nanyi mtawafukuza na kuwaangamiza mara moja, kama Mwenyezi Mungu alivyowaahidi.
DEU 9:4 Baada ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kuwafukuza mbele yenu, msiseme mioyoni mwenu, “Mwenyezi Mungu ametuleta hapa kuimiliki nchi hii kwa sababu ya haki yetu.” La, ni kwa sababu ya uovu wa mataifa haya ndio Mwenyezi Mungu anawafukuza mbele yenu.
DEU 9:5 Si kwa sababu ya haki yenu wala uadilifu wenu kwamba mtaimiliki nchi yao; lakini kwa sababu ya uovu wa mataifa haya, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawafukuza mbele yenu, ili kutimiza lile alilowaapia baba zenu Ibrahimu, Isaka na Yakobo.
DEU 9:6 Basi mjue, si kwa sababu ya haki yenu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa nchi hii nzuri kuimiliki, kwa kuwa ninyi ni taifa lenye shingo ngumu.
DEU 9:7 Kumbukeni hili, kamwe msisahau jinsi mlivyomkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa hasira huko jangwani. Tangu siku mlipotoka Misri hadi mlipofika hapa, mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi Mungu.
DEU 9:8 Kule Horebu mliamsha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo alikasirika sana hata akataka kuwaangamiza.
DEU 9:9 Nilipopanda mlimani kupokea vibao vya mawe, vile vibao vya agano ambalo Mwenyezi Mungu alilifanya nanyi, nilikaa mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula mkate wala sikunywa maji.
DEU 9:10 Mwenyezi Mungu alinipa vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu. Juu ya vibao hivyo kulikuwa amri zote Mwenyezi Mungu alizowatangazia kule mlimani kutoka kati ya moto siku ya kusanyiko.
DEU 9:11 Mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, Mwenyezi Mungu alinipa vibao viwili vya mawe, vile vibao vya agano.
DEU 9:12 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Shuka chini mara moja, kwa sababu watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamepotoka. Wamegeukia mbali haraka kutoka lile nililowaagiza, wamejitengenezea sanamu ya kusubu.”
DEU 9:13 Naye Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nimewaona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu sana!
DEU 9:14 Niache, ili nipate kuwaangamiza na kufuta jina lao chini ya mbingu. Nami nitakufanya kuwa taifa lenye nguvu zaidi na kuwa wengi kuliko wao.”
DEU 9:15 Kwa hiyo, niligeuka na kuteremka kutoka mlimani kwani mlima ulikuwa ukiwaka moto. Pia vile vibao viwili vya agano vilikuwa mikononi mwangu.
DEU 9:16 Nilipotazama, niliona kuwa mmefanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; mmejifanyia sanamu ya kusubu katika umbo la ndama. Mmegeuka upesi kutoka njia ile Mwenyezi Mungu aliyowaagiza.
DEU 9:17 Kwa hiyo nilichukua vile vibao viwili, nikavitupa na kuvipasua vipande vipande mbele ya macho yenu.
DEU 9:18 Ndipo tena nikasujudu hadi chini mbele za Mwenyezi Mungu kwa siku arobaini usiku na mchana. Sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi yote mliyoifanya, mkifanya lile lililo ovu mbele za Mwenyezi Mungu na kumkasirisha.
DEU 9:19 Niliogopa hasira na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa aliwakasirikia ninyi sana na kutaka kuwaangamiza. Bali Mwenyezi Mungu alinisikiliza tena.
DEU 9:20 Lakini Mwenyezi Mungu alimkasirikia Haruni kiasi cha kutaka kumwangamiza, nami wakati huo nilimwombea Haruni pia.
DEU 9:21 Kisha nikachukua ile sanamu ya ndama mliyoitengeneza na kuichoma kwenye moto. Nikaiponda na kuisaga ikawa unga laini kama vumbi, nikatupa lile vumbi kwenye kijito kilichotiririka toka mlimani.
DEU 9:22 Pia mlimkasirisha Mwenyezi Mungu huko Tabera, Masa na Kibroth-Hataava.
DEU 9:23 Vilevile wakati Mwenyezi Mungu alipowatuma kutoka Kadesh-Barnea, alisema, “Kweeni, mkaimiliki nchi niliyowapa.” Lakini mliasi dhidi ya agizo la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Hamkumtegemea wala kumtii.
DEU 9:24 Mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi Mungu tangu nilipowajua ninyi.
DEU 9:25 Nilianguka kifudifudi mbele za Mwenyezi Mungu kwa zile siku arobaini usiku na mchana kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amesema angewaangamiza ninyi.
DEU 9:26 Nilimwomba Mwenyezi Mungu na kusema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, usiangamize watu wako, urithi wako mwenyewe ule ulioukomboa kwa uweza wako mkuu na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu.
DEU 9:27 Wakumbuke watumishi wako Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Usiangalie ukaidi wa watu hawa, uovu wao wala dhambi yao.
DEU 9:28 Watu wa nchi ile uliyotutoa sisi wasije wakasema, ‘Ni kwa sababu Mwenyezi Mungu hakuweza kuwachukua hadi nchi aliyokuwa amewaahidia, kwa sababu aliwachukia, akawaleta ili aje kuwaua jangwani.’
DEU 9:29 Bali wao ni watu wako, urithi wako ule ulioutoa Misri kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyooka.”
DEU 10:1 Wakati ule Mwenyezi Mungu aliniambia, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza uje kwangu juu mlimani. Pia utengeneze Sanduku la mbao.
DEU 10:2 Nitaandika juu ya vibao maneno yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza, ambavyo ulivivunja. Kisha utaviweka ndani ya Sanduku.”
DEU 10:3 Hivyo nikatengeneza Sanduku kwa mti wa mshita, nikachonga pia vibao vya mawe kama vile vya kwanza, kisha nikakwea mlimani nikiwa na vile vibao viwili mikononi mwangu.
DEU 10:4 Mwenyezi Mungu akaandika juu ya hivi vibao kile alichokuwa amekiandika kabla, Amri Kumi alizokuwa amewatangazia huko mlimani, kutoka kati ya moto siku ile ya kusanyiko. Mwenyezi Mungu akanikabidhi.
DEU 10:5 Kisha nikashuka kutoka mlimani na kuweka vibao ndani ya Sanduku nililokuwa nimelitengeneza, kama Mwenyezi Mungu alivyoniagiza, navyo viko huko sasa.
DEU 10:6 (Waisraeli walisafiri kutoka visima vya Bene-Yaakani hadi Mosera. Huko Haruni alifariki na kuzikwa, naye Eleazari mwanawe akachukua nafasi yake kama kuhani.
DEU 10:7 Kutoka pale, walisafiri hadi Gudgoda wakaendelea hadi Yotbatha, nchi yenye vijito vya maji.
DEU 10:8 Wakati huo Mwenyezi Mungu aliteua kabila la Lawi kulibeba Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, kusimama mbele za Mwenyezi Mungu ili kutoa huduma, na kutangaza baraka kwa Jina lake, kama wanavyofanya hadi leo.
DEU 10:9 Hiyo ndiyo sababu ya Walawi kutokuwa na sehemu wala urithi miongoni mwa ndugu zao; Mwenyezi Mungu ndiye urithi wao, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wao, alivyowaambia.)
DEU 10:10 Basi nilikaa mlimani kwa siku arobaini usiku na mchana, kama nilivyofanya mara ya kwanza, pia Mwenyezi Mungu alinisikiliza hata wakati huu. Haikuwa nia yake kuwaangamiza.
DEU 10:11 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nenda, ukawaongoze watu katika njia yao ili waweze kuingia na kuimiliki nchi ile niliyowaapia baba zao kuwapa.”
DEU 10:12 Na sasa, ee Israeli, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anataka nini kwako ila kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote,
DEU 10:13 na kuyashika maagizo ya Mwenyezi Mungu na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?
DEU 10:14 Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo, ni mali ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
DEU 10:15 Hata hivyo Mwenyezi Mungu alikuwa na shauku na baba zako, akawapenda na akawachagua ninyi, wazao wao, kuliko mataifa yote, kama ilivyo leo.
DEU 10:16 Kwa hiyo tahirini mioyo yenu, na msiwe na shingo ngumu tena.
DEU 10:17 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa.
DEU 10:18 Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi.
DEU 10:19 Nanyi wapendeni wageni, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni huko Misri.
DEU 10:20 Mche Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye. Shikamana naye kwa uthabiti na kuapa kwa jina lake.
DEU 10:21 Yeye ni sifa yako; yeye ni Mungu wako, ambaye alikutendea yale maajabu makubwa na ya kutisha uliyoyaona kwa macho yako mwenyewe.
DEU 10:22 Baba zako walioshuka kwenda Misri jumla yao walikuwa sabini, na sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekufanya taifa la watu wengi kama nyota za angani.
DEU 11:1 Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kushika masharti yake, amri zake, sheria zake na maagizo yake siku zote.
DEU 11:2 Kumbuka hivi leo kwamba sio watoto wako walioona na kujua adhabu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako: utukufu wake, mkono wake wenye nguvu, mkono wake ulionyooshwa;
DEU 11:3 ishara alizozifanya na mambo aliyoyafanya katikati ya Misri, kwa Farao mfalme wa Misri na kwa nchi yake yote;
DEU 11:4 lile alilolifanyia jeshi la Wamisri, farasi na magari yake ya vita, jinsi alivyowafurikisha na maji ya Bahari ya Shamu walipokuwa wakiwafuatilia ninyi, na jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaletea angamizi la kudumu juu yao.
DEU 11:5 Sio watoto wenu walioyaona yale Mungu aliyowafanyia huko jangwani hadi mkafika mahali hapa,
DEU 11:6 wala lile Mungu alilowafanyia Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu wa kabila la Reubeni, wakati ardhi ilipofungua kinywa chake katikati ya Israeli yote, ikawameza pamoja na walio nyumbani mwao, mahema yao na kila kitu hai kilichokuwa mali yao.
DEU 11:7 Bali ni macho yenu wenyewe yaliyoyaona mambo haya yote makuu Mwenyezi Mungu aliyoyatenda.
DEU 11:8 Kwa hiyo fuateni maagizo yote ninayowapa leo, ili mpate kuwa na nguvu za kuingia na kuiteka nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki,
DEU 11:9 ili mpate kuishi siku nyingi katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliapa kuwapa baba zenu na wazao wao, nchi inayotiririka maziwa na asali.
DEU 11:10 Nchi mnayoiingia kuimiliki haifanani na nchi ya Misri mlikotoka, ambako mlipanda mbegu zenu na kunyunyizia maji kwa miguu kama bustani ya mboga.
DEU 11:11 Lakini nchi mnayovuka Yordani kuimiliki ni nchi ya milima na mabonde inayokunywa maji ya mvua ya mbinguni.
DEU 11:12 Ni nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anaitunza; macho ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, yanaitazama daima kutoka mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka.
DEU 11:13 Hivyo mkiyatii maagizo yangu ninayowapa leo kwa uaminifu, yaani kwa kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kumtumikia kwa moyo wako wote na kwa roho yenu yote,
DEU 11:14 ndipo atawanyeshea mvua katika nchi yenu kwa majira yake, mvua ya masika na ya vuli, ili mpate kuvuna nafaka zenu, divai mpya na mafuta.
DEU 11:15 Nitawapa majani katika malisho yako kwa ajili ya ng’ombe wenu, nanyi mtakula na kushiba.
DEU 11:16 Jihadharini, la sivyo mtashawishika kugeuka na kuabudu miungu mingine na kuisujudia.
DEU 11:17 Ndipo hasira ya Mwenyezi Mungu itawaka dhidi yenu, naye atafunga mbingu ili mvua isinyeshe nayo ardhi haitatoa mazao, nanyi mtaangamia upesi katika nchi nzuri ambayo Mwenyezi Mungu anawapa.
DEU 11:18 Yawekeni haya maneno yangu katika mioyo yenu na akili zenu, yafungeni kama alama juu ya mikono yenu na kwenye paji za nyuso zenu.
DEU 11:19 Wafundisheni watoto wenu, yazungumzeni mnapoketi nyumbani na mnapotembea njiani, mnapolala na mnapoamka.
DEU 11:20 Yaandikeni juu ya miimo ya nyumba zenu na juu ya malango yenu,
DEU 11:21 ili siku zenu na siku za watoto wenu zipate kuwa nyingi katika nchi ile Mwenyezi Mungu aliyoapa kuwapa baba zenu, kama zilivyo nyingi siku za mbingu juu ya nchi.
DEU 11:22 Mkizingatia kwa makini maagizo haya yote ninayowapa kuyafuata, ya kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kuenenda katika njia zake zote na kushikamana naye kwa uthabiti,
DEU 11:23 ndipo Mwenyezi Mungu atawafukuza mataifa haya yote mbele yako, nawe utawafukuza mataifa yaliyo makubwa na yenye nguvu kuliko wewe.
DEU 11:24 Kila mahali mtakapoweka mguu wenu patakuwa penu: Nchi yenu itaenea kutoka jangwa la Lebanoni, na kutoka Mto Frati hadi bahari ya magharibi.
DEU 11:25 Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama dhidi yenu. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama alivyoahidi, ataweka juu ya nchi yote utisho na hofu kwa ajili yenu popote mtaenda.
DEU 11:26 Tazama, leo ninaweka mbele yenu baraka na laana:
DEU 11:27 baraka kama mtatii maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ninayowapa leo;
DEU 11:28 laana kama hamtatii maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuacha njia ninayowaamuru leo kwa kufuata miungu mingine, ambayo hamkuijua.
DEU 11:29 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapokuwa amewaleta katika nchi mnayoiingia kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka Mlima Gerizimu, na kutangaza laana kutoka Mlima Ebali.
DEU 11:30 Kama mnavyofahamu, milima hii ipo ng’ambo ya Yordani, magharibi mwa barabara, kuelekea machweo ya jua, karibu na mialoni ya More, katika nchi ya wale Wakanaani wanaoishi Araba, jirani na Gilgali.
DEU 11:31 Karibu mvuke ng’ambo ya Yordani kuingia na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa. Mtakapokuwa mmeimiliki na mnaishi humo,
DEU 11:32 hakikisheni kwamba mnatii amri na sheria zote ninazoziweka mbele yenu leo.
DEU 12:1 Hizi ndizo amri na sheria ambazo ni lazima mwe waangalifu kuzifuata katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, amewapa kumiliki, kwa muda wote mtakaoishi katika nchi.
DEU 12:2 Haribuni kabisa kila mahali pao pa kuabudia kwenye milima mirefu, vilima na chini ya kila mti mkubwa ambamo mataifa haya mnayoenda kuchukua ardhi yao huabudia miungu yao.
DEU 12:3 Bomoeni madhabahu zao, vunjeni yale mawe wanayoabudu, chomeni moto nguzo zao za Ashera; katilieni mbali sanamu za miungu yao na mfute majina yao mahali hapo.
DEU 12:4 Kamwe msimwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama wanavyoabudu wao.
DEU 12:5 Bali mtatafuta mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua katika makabila yenu yote ili aliweke jina lake huko kuwa makao yake. Mahali hapo ndipo iwapasapo kwenda;
DEU 12:6 hapo ndipo mtakapoleta sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo zenu, kile ulichoweka nadhiri kutoa, sadaka zenu za hiari na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe, na ya mbuzi na kondoo.
DEU 12:7 Hapo, katika uwepo wa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ninyi pamoja na jamaa zenu, mtakula na kufurahia kila kitu ambacho mmegusa kwa mikono yenu, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewabariki.
DEU 12:8 Msifanye kama tunavyofanya hapa leo, kila mtu anavyopenda mwenyewe,
DEU 12:9 kwa kuwa bado hamjafikia mahali pa mapumziko na urithi ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa.
DEU 12:10 Lakini mtavuka Yordani na kuishi katika nchi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayowapa kama urithi, naye atawapa pumziko kutokana na adui zenu wote wanaowazunguka ili ninyi mpate kuishi kwa salama.
DEU 12:11 Kisha kuhusu mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua kuwa makao ya Jina lake, hapo ndipo inapowapasa kuleta kila kitu ninachowaamuru: sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo, pamoja na vitu vyote vyenye thamani ambavyo mmeweka nadhiri kumtolea Mwenyezi Mungu.
DEU 12:12 Hapo furahini mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, pamoja na Walawi kutoka miji yenu ambao hawana mgawo wala urithi wao wenyewe.
DEU 12:13 Kuweni waangalifu, msitoe dhabihu zenu za kuteketezwa mahali popote mnapopapenda.
DEU 12:14 Mtazitoa tu mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu katika mojawapo ya makabila yenu, nanyi hapo zingatieni kila jambo ninalowaamuru.
DEU 12:15 Hata hivyo, mnaweza kuwachinja wanyama wenu katika miji yenu yoyote ile na kula nyama nyingi mpendavyo kama vile mmemchinja paa au kulungu, kulingana na baraka mtakazojaliwa na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Watu walio najisi na walio safi wanaweza kula.
DEU 12:16 Lakini kamwe usile damu; imwage ardhini kama maji.
DEU 12:17 Hamruhusiwi kula katika miji yenu zaka yenu ya nafaka, ya divai mpya na ya mafuta, au mzaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na makundi yenu ya mbuzi na kondoo, wala chochote ambacho mmeweka nadhiri kukitoa, au sadaka zako za hiari, wala matoleo maalum.
DEU 12:18 Badala yake, mtakula vitu hivyo katika uwepo wa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua: wewe, wana wako na binti zako, watumishi wako wa kiume na wa kike, na Walawi kutoka miji yenu. Mnatakiwa mfurahi mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa kula kitu mtakachoweka mikono yenu.
DEU 12:19 Mwe waangalifu msiwapuuze Walawi kwa muda wote mnaoishi katika nchi yenu.
DEU 12:20 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapokuwa ameongeza nchi yenu kama alivyowaahidi, nanyi mkitamani nyama na mkisema, “Ningependa nyama,” hapo unaweza kula nyingi upendavyo.
DEU 12:21 Kama mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua kuweka Jina lake ni mbali sana kutoka kwenu, unaweza kuchinja wanyama kutoka makundi yenu ya ng’ombe, ya mbuzi na ya kondoo ambayo Mwenyezi Mungu amewapa, kama nilivyokuamuru, na mkiwa katika miji yenu wenyewe mnaweza kula nyingi mtakavyo.
DEU 12:22 Mle kama vile mngekula paa na kulungu. Wote walio najisi na walio safi mnaweza kula.
DEU 12:23 Lakini hakikisheni kwamba hamkula damu, kwa sababu damu ni uhai, kamwe msile uhai pamoja na nyama.
DEU 12:24 Hamruhusiwi kamwe kula damu; imwageni ardhini kama maji.
DEU 12:25 Msile damu, ili mweze kufanikiwa ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo haki machoni pa Mwenyezi Mungu.
DEU 12:26 Lakini vichukueni vitu vyenu vilivyowekwa wakfu pamoja na vile mlivyoweka nadhiri, mwende mahali pale Mwenyezi Mungu atakapopachagua.
DEU 12:27 Leteni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, vyote nyama na damu. Damu ya dhabihu zenu lazima imiminwe kando ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, lakini nyama mnaweza kula.
DEU 12:28 Mwe waangalifu kutii masharti haya yote ninayowapa, ili siku zote mweze kufanikiwa, ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo jema na sahihi mbele za macho ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 12:29 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atayakatilia mbali mbele yenu mataifa ambayo punde kidogo mtayavamia na kuyaondoa. Lakini mtakapokuwa mmeyafukuza na kuishi katika nchi yao,
DEU 12:30 na baada ya kuangamizwa mbele yenu, mwe waangalifu msijiingize katika tanzi kwa kuuliza habari za miungu yao, mkisema, “Je, mataifa haya hutumikiaje miungu yao? Nasi tutafanya vivyo hivyo.”
DEU 12:31 Kamwe msimwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa njia wanayoabudu miungu yao, kwa sababu katika kuabudu miungu yao, wanafanya aina zote za machukizo anayoyachukia Mwenyezi Mungu. Hata huwateketeza watoto wao wa kiume na wa kike motoni kama kafara kwa miungu yao.
DEU 12:32 Hakikisheni kwamba mnafanya yote niliyowaamuru; msiongeze kitu wala msipunguze kitu.
DEU 13:1 Kama nabii, au yule anayetabiri kupitia ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu,
DEU 13:2 ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,”
DEU 13:3 kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wote na kwa roho yote.
DEU 13:4 Ni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye.
DEU 13:5 Huyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
DEU 13:6 Kama ndugu yako hasa, au mwanao au binti yako, au mke umpendaye, au rafiki yako wa karibu sana akikushawishi kwa siri, akisema, “Na twende tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo ninyi wala baba zenu hamkuifahamu,
DEU 13:7 miungu ya watu wanaowazunguka, ikiwa karibu au mbali, kutoka mwisho mmoja wa nchi hadi mwingine),
DEU 13:8 usikubali wala usimsikilize. Usimhurumie! Usimwache wala usimkinge.
DEU 13:9 Hakika ni lazima auawe. Ni lazima mkono wako uwe wa kwanza katika kumuua kisha mikono ya watu wengine wote.
DEU 13:10 Mpigeni kwa mawe hadi afe, kwa sababu alijaribu kuwageuza mtoke kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye aliwatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.
DEU 13:11 Kisha Israeli wote watasikia na kuogopa, wala hakuna mmoja miongoni mwenu atakayefanya uovu tena.
DEU 13:12 Mkisikia ikisemwa kwamba moja ya miji ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa mkae ndani yake
DEU 13:13 kuna wanaume waovu wameinuka miongoni mwenu na wamewapotosha watu wa mji, wakisema, “Twendeni tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo hamkuifahamu),
DEU 13:14 ndipo itakubidi kuuliza, kupima na kuchunguza kwa makini. Kama ni kweli, tena ikihakikishwa kwamba jambo hili linalochukiza limefanyika miongoni mwenu,
DEU 13:15 kwa hakika ni lazima mwaue kwa upanga wale wote wanaoishi katika mji ule. Uharibuni kabisa, pamoja na watu wake na mifugo yake.
DEU 13:16 Kusanyeni nyara zote za mji katika uwanja wa wazi na kuuchoma mji kabisa pamoja na nyara zake zote kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Utabaki kuwa magofu milele na hautajengwa tena.
DEU 13:17 Hakuna kimoja kati ya vitu vilivyolaaniwa kitakachokutwa mikononi mwenu, ili Mwenyezi Mungu ageuze hasira yake kali. Atawahurumia na kuwa na rehema kwenu pia kuongeza idadi yenu, kama alivyowaahidi baba zenu,
DEU 13:18 kwa sababu mnamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mkizishika amri zake zote ninazowapa leo na kufanya lililo jema machoni pake.
DEU 14:1 Ninyi ni watoto wa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Msijichanje ama kujinyoa upara kwenye paji la uso kwa ajili ya aliyekufa,
DEU 14:2 kwa kuwa ninyi ni taifa takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Mwenyezi Mungu amewachagua ninyi kuwa taifa lake la pekee kutoka mataifa yote duniani.
DEU 14:3 Msile kitu chochote ambacho ni machukizo.
DEU 14:4 Hawa ndio wanyama mtakaokula: ng’ombe, kondoo, mbuzi,
DEU 14:5 kulungu, paa, kongoni, paa mweupe, mbuzi-mwitu, pofu na kondoo wa mlimani.
DEU 14:6 Mnaweza kumla mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika mara mbili, pia yule anayecheua.
DEU 14:7 Hata hivyo, miongoni mwa wale wanaocheua au wale walio na kwato zilizogawanyika kamwe msile ngamia, sungura na pelele. Iwapo wanacheua, lakini hawana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu.
DEU 14:8 Nguruwe pia ni najisi; ingawa ana kwato zilizogawanyika, hacheui. Msile nyama yake wala kugusa mzoga wake.
DEU 14:9 Katika viumbe hai vyote viishivyo kwenye maji, mnaweza kula yeyote aliye na mapezi na magamba.
DEU 14:10 Lakini chochote kisicho na mapezi na magamba msile; kwenu ni najisi.
DEU 14:11 Mnaweza kula ndege yeyote aliye safi.
DEU 14:12 Lakini wafuatao msiwale: tai, furukombe, kipungu,
DEU 14:13 kengewa mwekundu, kengewa mweusi, mwewe wa aina yoyote,
DEU 14:14 kunguru wa aina yoyote,
DEU 14:15 mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga wa aina yoyote,
DEU 14:16 bundi, mumbi, bundi mkubwa,
DEU 14:17 mwari, nderi, mnandi,
DEU 14:18 korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.
DEU 14:19 Wadudu wote warukao kwa makundi ni najisi kwenu, msiwale.
DEU 14:20 Lakini viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi mwaweza kula.
DEU 14:21 Msile kitu chochote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni yeyote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
DEU 14:22 Hakikisheni mmetenga sehemu ya kumi ya mazao yote ya mashamba yenu kila mwaka.
DEU 14:23 Mtakula zaka za nafaka yenu, divai mpya, mafuta na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na ya kondoo na mbuzi mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, pale mahali atakapopachagua kama maskani kwa ajili ya Jina lake, ili mpate kujifunza kumheshimu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, daima.
DEU 14:24 Lakini ikiwa mahali pale ni mbali sana nanyi mmebarikiwa na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na hamwezi kubeba zaka yenu (kwa sababu mahali pale Mwenyezi Mungu atakapopachagua kuliweka Jina lake ni mbali sana),
DEU 14:25 basi badilisheni zaka yenu kuwa fedha, mkaichukue hiyo fedha mwende nayo mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua.
DEU 14:26 Tumieni hiyo fedha kununua chochote ukitakacho: ng’ombe, kondoo, divai au kinywaji chochote chenye chachu au chochote mnachotaka. Kisha ninyi na watu wa nyumbani mwenu mtaila mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kufurahi.
DEU 14:27 Msiache kuwajali Walawi wanaoishi katika miji yenu, kwa kuwa hao hawana shamba wala urithi wao wenyewe.
DEU 14:28 Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu,
DEU 14:29 ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.
DEU 15:1 Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni.
DEU 15:2 Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Mwenyezi Mungu wa kufuta madeni umetangazwa.
DEU 15:3 Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako.
DEU 15:4 Hata hivyo, hapatakuwa na maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana,
DEU 15:5 ikiwa tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo.
DEU 15:6 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi.
DEU 15:7 Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini.
DEU 15:8 Bali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji.
DEU 15:9 Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Mwenyezi Mungu dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi.
DEU 15:10 Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako.
DEU 15:11 Siku zote watakuwa watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe wakarimu kwa ndugu zenu walio maskini na wahitaji katika nchi yenu.
DEU 15:12 Kama Mwebrania mwenzako, mwanaume au mwanamke, akijiuza kwako na kukutumikia miaka sita, katika mwaka wa saba ni lazima umwache aende zake akiwa huru.
DEU 15:13 Nawe wakati utakapomwachia usimwache aende mikono mitupu.
DEU 15:14 Mpe kwa hiari kutoka kundi lako la kondoo na mbuzi, kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka, na kutoka shinikizo lako la kukamulia zabibu. Mpe kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alivyokubariki.
DEU 15:15 Kumbukeni kuwa ninyi mlikuwa watumwa huko Misri naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwakomboa. Ndiyo sababu nimewapa agizo hili leo.
DEU 15:16 Lakini mtumishi wako akikuambia, “Sitaki kukuacha,” kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako naye anaridhika nawe,
DEU 15:17 ndipo utachukua chuma kidogo utoboe sikio lake hadi hicho chuma kiingie kwenye ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako wa maisha. Ufanye vivyo hivyo kwa mjakazi wako.
DEU 15:18 Usifikiri kuwa kuna ugumu kumwacha mtumishi wako huru, kwa sababu utumishi wake kwako kwa miaka hii sita umekuwa wa thamani mara mbili ya ujira wa mtumishi wa kuajiriwa. Naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakubariki kwa kila kitu utakachofanya.
DEU 15:19 Wekeni wakfu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa makundi yenu ya ng’ombe na ya mbuzi na kondoo. Maksai walio wazaliwa wa kwanza msiwafanyize kazi, wala msinyoe manyoya ya wazaliwa wa kwanza wa kondoo.
DEU 15:20 Kila mwaka ninyi na jamaa zenu mtapaswa kuwala mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, pale mahali atakapopachagua.
DEU 15:21 Kama mnyama ana dosari, akiwa ni kilema au kipofu au kama ana kilema kibaya, kamwe usimtoe dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 15:22 Itawapasa kumla ninyi wenyewe katika miji yenu. Wote walio najisi na waliotakasika mwaweza kula kama vile mnavyokula paa au kulungu.
DEU 15:23 Lakini kamwe msile damu; imwageni ardhini kama maji.
DEU 16:1 Shikeni mwezi wa Abibu, na kuiadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa sababu katika mwezi wa Abibu, Mungu aliwatoa Misri usiku.
DEU 16:2 Mtatoa dhabihu ya Pasaka ya mnyama kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kutoka kundi lenu la mbuzi na kondoo, au la ng’ombe, mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu kuwa makao kwa ajili ya Jina lake.
DEU 16:3 Msile nyama hiyo pamoja na mikate iliyotiwa chachu, lakini kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, mikate ya kujitesa, kwa sababu mliondoka Misri kwa haraka, ili siku zote za maisha yenu mpate kukumbuka wakati wenu wa kuondoka Misri.
DEU 16:4 Chachu isionekane kwenu katika nchi yenu yote kwa siku saba. Nyama yoyote ya dhabihu mtakayotoa jioni ya siku ya kwanza isibakizwe hadi asubuhi.
DEU 16:5 Kamwe msitoe dhabihu ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa,
DEU 16:6 isipokuwa mahali atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake. Hapo lazima mtoe dhabihu ya Pasaka jioni jua litakapotua, iwe kumbukumbu yenu ya kutoka Misri.
DEU 16:7 Okeni na mle mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kisha asubuhi mrudi kwenye mahema yenu.
DEU 16:8 Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu na siku ya saba fanyeni kusanyiko kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na msifanye kazi.
DEU 16:9 Mhesabu majuma saba tangu wakati mnapoanza kuchukua mundu kuvuna nafaka.
DEU 16:10 Kisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa.
DEU 16:11 Shangilieni mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua kuwa makao ya Jina lake, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi walio katika miji yenu, na wageni, yatima na wajane wanaoishi miongoni mwenu.
DEU 16:12 Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa kule Misri na mfuate amri hizi kwa uangalifu.
DEU 16:13 Adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa siku saba baada ya kukusanya mazao kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka, na kutoka shinikizo lako la kukamulia zabibu.
DEU 16:14 Mfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu.
DEU 16:15 Kwa siku saba mtaiadhimisha sikukuu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, katika mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawabariki katika mavuno yenu na katika kazi zote za mikono yenu na furaha yenu itakamilika.
DEU 16:16 Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Mwenyezi Mungu mikono mitupu:
DEU 16:17 Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowabariki.
DEU 16:18 Wateue waamuzi na maafisa kwa kila kabila lenu katika kila mji ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, nao watawaamua watu kwa usawa.
DEU 16:19 Msipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki.
DEU 16:20 Mfuate haki na haki peke yake, ili mweze kuishi na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa.
DEU 16:21 Msisimamishe nguzo yoyote ya Ashera kando ya madhabahu mliyomjengea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,
DEU 16:22 wala msisimamishe jiwe la kuabudu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anavichukia vitu hivi.
DEU 17:1 Msimtolee Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, dhabihu ya maksai au kondoo aliye na dosari yoyote au hitilafu ndani yake, kwa kuwa hilo litakuwa chukizo kwake.
DEU 17:2 Ikiwa mwanaume au mwanamke anayeishi kati ya mojawapo ya miji anayokupa Mwenyezi Mungu, anakutwa anafanya uovu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa kuvunja agano lake,
DEU 17:3 naye ameenda kinyume na agizo langu kuabudu miungu mingine na kuisujudia, kama vile jua, mwezi au nyota za angani,
DEU 17:4 hili likiwa limeletwa mbele yenu, ni lazima kulichunguza kikamilifu. Ikiwa ni kweli na kuwa limehakikishwa kwamba hili ni chukizo lililofanyika katika Israeli,
DEU 17:5 mchukueni huyo mwanaume au mwanamke ambaye amelifanya tendo hili ovu kwenye lango la mji wenu na kumpiga mawe mtu huyo hadi afe.
DEU 17:6 Kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu mtu huyo atauawa, bali hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu.
DEU 17:7 Ni lazima kwanza mikono ya mashahidi itangulie kumuua huyo mtu, kisha mikono ya watu wote. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
DEU 17:8 Kama mashauri yanaletwa katika mahakama zenu ambayo ni magumu zaidi kwenu kuyaamua, ikiwa ni umwagaji wa damu, madai au mashambulio, yapelekeni mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua.
DEU 17:9 Nendeni kwa makuhani, ambao ni Walawi, na kwa mwamuzi ambaye atakuwa kazini wakati huo. Ulizeni kwao nao watawapa maamuzi.
DEU 17:10 Ni lazima mtende sawasawa na maamuzi watakayowapa mahali Mwenyezi Mungu atakapopachagua. Kuweni waangalifu kufanya kila kitu watakachowaongoza kufanya.
DEU 17:11 Fanyeni sawasawa na sheria wanayowafundisha na maamuzi wanayowapa. Msigeuke mkono wa kuume au kushoto kuacha kufanya yale wanayowaambia.
DEU 17:12 Mwanaume atakayeonesha dharau kwa mwamuzi au kwa kuhani ambaye amewekwa kumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, lazima auawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli.
DEU 17:13 Watu wote watasikia na kuogopa, nao hawatakuwa wenye kudharau tena.
DEU 17:14 Utakapoingia katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kuimiliki na kukaa humo, nanyi mkasema, “Na tumweke mfalme juu yetu kama mataifa yanayotuzunguka,”
DEU 17:15 kuweni na uhakika wa kumweka mfalme juu yenu ambaye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atamchagua. Ni lazima atoke miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msimweke mgeni juu yenu ambaye si ndugu Mwisraeli.
DEU 17:16 Hata hivyo, kamwe mfalme asijipatie hesabu kubwa ya farasi kwa ajili yake mwenyewe, au kuwafanya watu warudi Misri ili kupata farasi wengi, kwa maana Mwenyezi Mungu amekuambia, “Hamtairudia njia ile tena.”
DEU 17:17 Kamwe asioe wake wengi, la sivyo moyo wake utapotoka. Kamwe asijilimbikizie kiasi kikubwa cha fedha na dhahabu.
DEU 17:18 Atakapokuwa amekalia kiti cha ufalme wake, ajiandikie kwenye kitabu nakala ya sheria kwa ajili yake mwenyewe kutoka zile sheria za makuhani ambao ni Walawi.
DEU 17:19 Atakuwa na nakala hiyo, naye ataisoma siku zote za maisha yake ili ajifunze kumheshimu Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kufuata kwa uangalifu maneno yote ya sheria hii na amri hizi,
DEU 17:20 naye asijione kuwa ni bora kuliko ndugu zake na kuipotosha sheria. Ndipo yeye na wazao wake watatawala katika ufalme wake kwa muda mrefu katika Israeli.
DEU 18:1 Makuhani ambao ni Walawi, yaani kabila lote la Lawi, hawatakuwa na mgawo wala urithi pamoja na Israeli. Wataishi kwa sadaka zitolewazo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu za kuteketezwa kwa moto, kwa maana huo ndio urithi wao.
DEU 18:2 Hawatakuwa na urithi miongoni mwa ndugu zao; Mwenyezi Mungu ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.
DEU 18:3 Hili ndilo fungu la makuhani kutoka kwa watu watakaotoa dhabihu ya fahali au kondoo: mguu wa mbele, mataya na matumbo.
DEU 18:4 Mtawapa malimbuko ya nafaka zenu, divai mpya, mafuta na sufu ya kwanza kutoka manyoya ya kondoo wenu,
DEU 18:5 kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewachagua pamoja na wazao wao kutoka makabila yenu kusimama na kuhudumu katika jina la Mwenyezi Mungu siku zote.
DEU 18:6 Ikiwa Mlawi atahama kutoka mojawapo ya miji yenu popote katika Israeli ambapo anaishi, akaja kwa moyo wote mahali Mwenyezi Mungu atakapopachagua,
DEU 18:7 anaweza akahudumu katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama Walawi wenzake wote wanaohudumu hapo mbele za Mwenyezi Mungu.
DEU 18:8 Atashiriki sawa katika mafao yao, hata kama amepokea fedha kutoka mauzo ya mali ya jamaa yake.
DEU 18:9 Mtakapoingia katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, msijifunze kuiga njia za machukizo za mataifa ya huko.
DEU 18:10 Asionekane mtu yeyote miongoni mwenu ampitishaye mwanawe au binti yake katika moto, atakayefanya uaguzi, ulozi, anayetabiri nyakati, anayejishughulisha na uchawi,
DEU 18:11 wala arogaye kwa kupiga mafundo, wala mwaguzi au anayeabudu mizimu, wala awaombaye wafu.
DEU 18:12 Mtu yeyote afanyaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, tena ni kwa sababu ya matendo haya ya kuchukiza wayafanyayo ndiyo maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atayafukuza mataifa hayo mbele yenu.
DEU 18:13 Kamwe msilaumiwe mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 18:14 Mataifa mtakayowafukuza husikiliza wale wafanyao ulozi na uaguzi. Lakini ninyi, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hajawaruhusu kufanya hivyo.
DEU 18:15 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msikilizeni yeye.
DEU 18:16 Kwa kuwa hivi ndivyo mlivyomwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kule Horebu siku ile ya kusanyiko, wakati mliposema, “Na tusiisikie sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, wala kuuona moto huu mkubwa tena, ama sivyo tutakufa.”
DEU 18:17 Mwenyezi Mungu akaniambia: “Wanachosema ni vyema.
DEU 18:18 Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni mwa ndugu zao; nitaweka maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia kila kitu nitakachomwamuru.
DEU 18:19 Kama mtu yeyote hatasikiliza maneno yangu ambayo huyo nabii atayasema kwa Jina langu, mimi mwenyewe nitamwajibisha.
DEU 18:20 Lakini nabii ambaye atathubutu kusema kwa Jina langu kitu chochote ambacho sikumwamuru akiseme, au nabii ambaye husema kwa jina la miungu mingine ni lazima auawe.”
DEU 18:21 Mnaweza kuulizana wenyewe, “Tutawezaje kujua wakati ujumbe haukusemwa na Mwenyezi Mungu?”
DEU 18:22 Ikiwa kile nabii anachotangaza kwa jina la Mwenyezi Mungu hakikutendeka au kutimia, huo ni ujumbe ambao Mwenyezi Mungu hakusema. Nabii huyo amesema kwa ujuaji. Msimwogope huyo.
DEU 19:1 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapokuwa amewaangamiza mataifa ambayo nchi yao anawapa ninyi, wakati mtakuwa mmewafukuza na kuishi katika miji yao na nyumba zao,
DEU 19:2 ndipo mtenge miji mitatu iliyopo katikati ya nchi kwa ajili yenu, katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kuimiliki.
DEU 19:3 Jengeni barabara katika miji hiyo na kuigawa mara tatu, nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama urithi, ili yeyote amuuaye mtu aweze kukimbilia humo.
DEU 19:4 Hii ndiyo kanuni kuhusu mtu amuuaye mwingine na kukimbilia humo kuokoa maisha yake, yaani yeye amuuaye jirani yake bila kukusudia, wala hakumchukia kabla ya hapo.
DEU 19:5 Kwa mfano, mtu aweza kwenda msituni na jirani yake kukata miti, naye anapozungusha shoka kuangusha mti, shoka linaweza kuchomoka kutoka mpini na kumpiga jirani yake na kumuua. Yule mtu anaweza kukimbilia katika mojawapo ya miji hii na kuokoa maisha yake.
DEU 19:6 Kama sivyo, mlipiza kisasi cha damu anaweza kumfuatilia kwa hasira kali, naye akamkamata na kumuua kama umbali ni mrefu sana hata ingawa hastahili kifo, kwa sababu amemuua jirani yake bila kukusudia.
DEU 19:7 Hii ndiyo sababu nimewaagiza ninyi kutenga miji mitatu ya makimbilio kwa ajili yenu.
DEU 19:8 Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, akipanua nchi yenu, kama alivyoahidi kwa kiapo kwa baba zenu na kuwapa nchi yote aliyowaahidi,
DEU 19:9 kwa sababu mmefuata kwa uangalifu sheria zote ninazowaamuru leo, kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuenenda siku zote katika njia zake, ndipo mtenge miji mingine mitatu.
DEU 19:10 Fanyeni hivi ili damu isiyo na hatia isimwagwe katika nchi yenu, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi wenu, ili msije mkawa na hatia ya kumwaga damu.
DEU 19:11 Lakini kama mtu anamchukia ndugu yake, akamvizia, akamshambulia na kumuua, kisha akakimbilia katika mojawapo ya miji hii,
DEU 19:12 wazee wa mji wake watatuma ujumbe kwake, kumleta kutoka mji ule na kumkabidhi mlipiza kisasi cha damu kumuua.
DEU 19:13 Msimwonee huruma. Lazima mwondoe katika Israeli hatia ya umwagaji damu isiyo na hatia ili mpate kufanikiwa.
DEU 19:14 Usisogeze jiwe la mpaka wa jirani yako ambao uliwekwa na wale waliokutangulia katika urithi upokeao katika nchi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anayowapa kuimiliki.
DEU 19:15 Shahidi mmoja hatoshi kumtia hatiani mtu kwa uhalifu au kosa lolote ambalo anaweza kuwa amelitenda. Lazima shauri lolote lithibitishwe kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu.
DEU 19:16 Kama shahidi mwenye nia ya kumdhuru mwingine akisimama kumshtaki mtu kwa uhalifu,
DEU 19:17 watu wawili wanaohusika katika mabishano lazima wasimame mbele za Mwenyezi Mungu na mbele ya makuhani na waamuzi ambao wako kazini wakati huo.
DEU 19:18 Waamuzi lazima wafanye uchunguzi kwa makini na shahidi akionekana kuwa ni mwongo, akitoa ushuhuda wa uongo dhidi ya ndugu yake,
DEU 19:19 basi mtende kama alivyotaka kumtendea ndugu yake. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
DEU 19:20 Watu watakaosalia watasikia hili na kuogopa, uovu kama huo kamwe hautatendeka tena miongoni mwenu.
DEU 19:21 Msioneshe huruma, uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.
DEU 20:1 Mtakapoenda vitani kupigana na adui zenu na mkaona farasi na magari ya vita na jeshi kubwa kuliko lenu, msiwaogope, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa kutoka Misri, atakuwa pamoja nanyi.
DEU 20:2 Mtakapokaribia kwenda vitani, kuhani atakuja mbele na kuhutubia jeshi.
DEU 20:3 Atasema: “Sikia, ee Israeli, leo unaenda vitani kupigana na adui zako. Usife moyo wala usiogope, usitishwe wala usitiwe hofu mbele yao.
DEU 20:4 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ndiye huenda pamoja nanyi kuwapigania dhidi ya adui zenu na kuwapatia ushindi.”
DEU 20:5 Maafisa wataliambia jeshi: “Je, kuna yeyote aliyejenga nyumba mpya ambayo haijawekwa wakfu? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akaiweka wakfu.
DEU 20:6 Je, kuna yeyote aliyepanda shamba la mizabibu na hajaanza kulifurahia? Yeye na arudi nyumbani, au sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akalifurahia.
DEU 20:7 Je, kuna yeyote aliyeposa mwanamke na hajamwoa? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akamwoa.”
DEU 20:8 Kisha maafisa wataongeza haya, “Je, kuna mtu anayeogopa ama kufa moyo? Yeye na arudi nyumbani ili ndugu zake nao wasije wakafa moyo pia.”
DEU 20:9 Maafisa watakapomaliza kuzungumza na jeshi, watawateua wakuu wa vikosi.
DEU 20:10 Mtakapoenda kushambulia mji, wapeni watu wake masharti ya amani.
DEU 20:11 Wakikubali na kuwafungulia malango yao, watu wake wote watakuwa watumwa wa kufanya kazi ngumu, na watawatumikia ninyi.
DEU 20:12 Ikiwa watakataa kufanya mapatano ya amani na wakiwaingiza katika vita, basi mtauzingira mji huo.
DEU 20:13 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapouweka mji huo mkononi mwenu, waueni kwa upanga wanaume wote waliomo.
DEU 20:14 Kwa upande wa wanawake, watoto, mifugo na kila kitu kingine chochote ndani ya huo mji, mnaweza kuvichukua kama nyara kwa ajili yenu. Nanyi mnaweza kuzitumia hizo nyara ambazo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa kutoka kwa adui zenu.
DEU 20:15 Hivi ndivyo mtakavyofanya kwa miji yote iliyo mbali nanyi, ambayo haimilikiwi na mataifa ya karibu.
DEU 20:16 Hata hivyo, katika miji ya mataifa ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi, msiache kitu chochote hai kinachopumua.
DEU 20:17 Waangamizeni kabisa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowaamuru.
DEU 20:18 La sivyo, watawafundisha kufuata mambo yote ya machukizo wanayofanya wakiabudu miungu yao, nanyi mtatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 20:19 Mtakapouzunguka mji kwa vita kwa muda mrefu, mkipigana dhidi yake ili kuuteka, msiharibu miti yake kwa kuikata kwa shoka, kwa sababu mtaweza kula matunda yake. Hivyo msiikate. Je, miti hiyo ya mashambani ni watu, hata muizingire?
DEU 20:20 Hata hivyo, mnaweza kuikata miti isiyo ya matunda na kuitumia kuuzingira, hadi mji unaofanya vita na ninyi utakapoanguka.
DEU 21:1 Kama mtu akikutwa ameuawa, naye amelala kwenye shamba katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kuimiliki, wala haijulikani ni nani aliyemuua,
DEU 21:2 wazee wenu na waamuzi watatoka na kupima umbali kutoka maiti alipolala hadi kwenye miji iliyo jirani.
DEU 21:3 Kisha wazee wa ule mji ulio karibu zaidi na yule maiti watamchukua mtamba ambaye hajapata kufanyishwa kazi na ambaye hajafungwa nira,
DEU 21:4 na kumpeleka kwenye bonde ambalo halijapata kulimwa au kupandwa mazao na ambapo kuna chemchemi inayotiririka. Huko kwenye hilo bonde, wazee watamvunja yule mtamba shingo.
DEU 21:5 Makuhani, hao wana wa Lawi, watasogea mbele, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewachagua kuhudumu na kutoa baraka katika jina la Mwenyezi Mungu, na kuamua mashauri yote ya mabishano na mashambulio.
DEU 21:6 Ndipo wazee wote wa mji ulio karibu zaidi na huyo maiti watanawa mikono yao juu ya huyo mtamba ambaye shingo yake imevunjwa huko kwenye bonde,
DEU 21:7 nao watatangaza: “Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona likifanyika.
DEU 21:8 Ee Mwenyezi Mungu, ukubali upatanisho kwa watu wako Israeli ambao umewakomboa, wala usiwahesabie watu wako hatia ya damu ya mtu asiyekuwa na hatia.” Nayo damu iliyomwagika itakuwa imefanyiwa upatanisho.
DEU 21:9 Hivyo mtakuwa mmejitakasa wenyewe kutoka hatia ya kumwaga damu isiyokuwa na hatia, kwa kuwa mmefanya lile lililo sawa mbele za macho ya Mwenyezi Mungu.
DEU 21:10 Mkienda vitani kupigana na adui zenu, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, akawatia adui mikononi mwenu, nanyi mkachukua mateka,
DEU 21:11 kama ukiona miongoni mwa mateka mwanamke mzuri wa sura nawe ukavutiwa naye, unaweza kumtwaa awe mke wako.
DEU 21:12 Mlete nyumbani mwako, anyoe nywele na kukata kucha zake,
DEU 21:13 avue nguo alizokuwa amevaa alipotekwa. Baada ya kuishi nyumbani mwako na kumwombolezea baba yake na mama yake kwa mwezi mzima, ndipo utakapomwendea, uwe mume wake naye atakuwa mke wako.
DEU 21:14 Lakini kama hutaendelea kupendezwa naye, mwache aende popote anapotaka. Kamwe huwezi kumuuza au kumtendea kama mtumwa, kwa sababu utakuwa umemvunjia heshima.
DEU 21:15 Kama mwanaume ana wake wawili, naye anampenda mmoja na mwingine hampendi na wote wawili wamemzalia wana wa kiume, lakini mwana mzaliwa wa kwanza ni wa yule mke asiyempenda,
DEU 21:16 wakati anapotoa wosia wa mali yake kwa wanawe, kamwe asitoe haki za mzaliwa wa kwanza kwa mwana wa mke ampendaye kwa upendeleo, badala ya mzaliwa hasa wa kwanza, ambaye ni mwana wa mke ambaye hampendi.
DEU 21:17 Ni lazima amkubali mwana wa mke asiyempenda kama mzaliwa wa kwanza kwa kumpa sehemu ya vile vyote alivyo navyo maradufu. Mwana huyo ni ishara ya kwanza ya nguvu za baba yake. Haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye.
DEU 21:18 Kama mtu ana mwana mkaidi na mwasi ambaye hamtii baba yake na mama yake, na hasikii wazazi wanapomkanya,
DEU 21:19 baba yake na mama yake watamleta kwa wazee kwenye lango la mji wake.
DEU 21:20 Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.”
DEU 21:21 Kisha wanaume wote wa mjini mwake watampiga kwa mawe hadi afe. Ndivyo imewapasa kuondoa maovu kati yenu. Israeli yote itasikia hili na kuogopa.
DEU 21:22 Kama mtu ana hatia ya kosa linalompasa kuuawa naye akauawa, mwili wake utaangikwa mtini,
DEU 21:23 kamwe msiuache mwili wake mtini usiku kucha. Hakikisheni mnauzika mwili wake siku ile ile, kwa sababu kila mtu anayeangikwa mtini yupo chini ya laana ya Mungu. Msiinajisi nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi wenu.
DEU 22:1 Ukimwona ng’ombe au kondoo wa ndugu yako anapotea, usipuuze, bali uhakikishe unamrudisha kwa mwenyewe.
DEU 22:2 Ikiwa huyo ndugu haishi karibu nawe au kama wewe hufahamu yeye ni nani, mchukue nyumbani kwako huyo mnyama, umweke hadi mwenyewe aje kumtafuta. Nawe umrudishie.
DEU 22:3 Fanya vivyo hivyo ukimkuta punda wa nduguyo au joho lake au chochote alichopoteza. Usipuuze jambo hilo.
DEU 22:4 Ukimwona punda wa nduguyo au ng’ombe wake ameanguka barabarani, usipuuze jambo hilo. Msaidie asimame kwa miguu yake.
DEU 22:5 Haimpasi mwanamke kuvaa mavazi ya kiume wala mwanaume kuvaa mavazi ya kike, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anachukia yeyote anayefanya hivi.
DEU 22:6 Ukikuta kiota cha ndege kando ya barabara, iwe juu ya mti au chini, naye ndege amelala juu ya makinda au mayai, usimchukue huyo ndege pamoja na makinda yake.
DEU 22:7 Unaweza kuchukua makinda, lakini hakikisha unamwachilia huyo ndege, ili upate kufanikiwa na kuishi maisha marefu.
DEU 22:8 Unapojenga nyumba mpya, fanya ukuta wa kuzuia kandokando ya dari ili usijiletee hatia ya kumwaga damu juu ya nyumba yako ikiwa yeyote ataanguka kutoka humo.
DEU 22:9 Usipande aina mbili za mbegu katika shamba lako la mizabibu; ikiwa utafanya hivyo, si mazao utakayopanda tu yatakuwa najisi, bali nayo matunda ya shamba la mizabibu pia.
DEU 22:10 Usilime kwa maksai aliyefungwa nira pamoja na punda.
DEU 22:11 Usivae nguo za sufu na kitani zilizofumwa pamoja.
DEU 22:12 Fanya vishada kwenye pembe nne za joho unalovaa.
DEU 22:13 Ikiwa mtu atamwoa mke na baada ya kufanya naye tendo la ndoa, akamchukia,
DEU 22:14 akimsingizia na kumwita jina baya, akisema, “Nilimwoa mwanamke huyu, lakini nilipomkaribia sikupata uthibitisho wa ubikira wake”
DEU 22:15 ndipo baba na mama wa msichana wataleta uthibitisho kwamba alikuwa bikira kwa wazee wa mji kwenye lango.
DEU 22:16 Baba wa msichana atawaambia wazee, “Nilimwoza binti yangu kwa huyu mwanaume, lakini hampendi.
DEU 22:17 Sasa amemsingizia na kusema, ‘Sikumkuta huyu binti akiwa bikira.’ Lakini hapa kuna uthibitisho wa ubikira wa binti yangu.” Kisha wazazi wake wataonesha nguo zake kwa wazee wa mji,
DEU 22:18 nao wazee watamchukua huyo mwanaume na kumwadhibu.
DEU 22:19 Watamtoza shekeli mia moja za fedha na kupewa wazazi wa msichana, kwa sababu mwanaume huyu amempa bikira Mwisraeli jina baya. Ataendelea kuwa mke wake; kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake.
DEU 22:20 Hata hivyo, kama shtaka ni la kweli na hakuna uthibitisho kuhusu ubikira wa huyo msichana uliopatikana,
DEU 22:21 huyo msichana ataletwa kwenye mlango wa nyumba ya baba yake, na hapo wanaume wa mji wake watampiga kwa mawe hadi afe. Amefanya kitu cha aibu katika Israeli kwa kufanya ukahaba akiwa nyumbani mwa babaye. Lazima mwondoe uovu kati yenu.
DEU 22:22 Ikiwa mwanaume atakutwa akizini na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanaume na mwanamke aliyezini naye, lazima wauawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli.
DEU 22:23 Ikiwa mwanaume atakutana na bikira mjini ambaye ameposwa na mtu akazini naye,
DEU 22:24 utawachukua wote wawili kwenye lango la mji na kuwapiga kwa mawe hadi wafe; yule msichana kwa kuwa alikuwa mjini na hakupiga yowe kuomba msaada, na yule mwanaume kwa sababu amemtenda jeuri mke wa mtu mwingine. Lazima mwondoe uovu kati yenu.
DEU 22:25 Lakini ikiwa itatokea mwanaume akakutana na msichana aliyeposwa huko mashambani, akambaka, mwanaume aliyefanya hivi peke yake ndiye atakayeuawa.
DEU 22:26 Usimtendee msichana yule jambo lolote; hajafanya dhambi inayostahili kifo. Shauri hili ni kama lile la yeyote ambaye anamshambulia na kumuua kwa makusudi jirani yake,
DEU 22:27 kwa maana mwanaume huyo alimkuta msichana huko mashambani, na ingawa msichana aliyeposwa alipiga yowe, hapakuwa na mtu wa kumwokoa.
DEU 22:28 Ikiwa itatokea mwanaume akutane na bikira ambaye hajaposwa na kumbaka nao wakakutwa,
DEU 22:29 mwanaume atamlipa baba wa msichana shekeli hamsini za fedha. Ni lazima amwoe huyo msichana, kwa maana amemfanyia jeuri. Kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake.
DEU 22:30 Mwanaume asimwoe mke wa baba yake; kamwe asidhalilishe kitanda cha baba yake.
DEU 23:1 Asiingie mtu yeyote aliyehasiwa kwa kupondwa makende au kwa kukatwa uume wake katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu.
DEU 23:2 Mtu ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hata kizazi cha kumi.
DEU 23:3 Hapatakuwa na Mwamoni au Mmoabu au yeyote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hata kizazi cha kumi.
DEU 23:4 Kwa kuwa hawakuja kuwalaki wakiwa na mkate na maji mlipokuwa njiani mkitoka Misri; tena walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia ili awalaani.
DEU 23:5 Hata hivyo, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hakumsikiliza Balaamu bali aligeuza laana kuwa baraka kwenu kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapenda.
DEU 23:6 Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote.
DEU 23:7 Usimchukie Mwedomu, kwa kuwa yeye ni ndugu yako. Usimchukie Mmisri, kwa sababu uliishi kama mgeni katika nchi yake.
DEU 23:8 Kizazi cha tatu cha watoto watakaozaliwa nao wanaweza kuingia katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu.
DEU 23:9 Unapokuwa umepiga kambi dhidi ya adui zako, jitenge na kitu chochote kisicho safi.
DEU 23:10 Ikiwa mtu amechafuka kwa sababu ya kutokwa na shahawa usiku, inampasa atoke nje ya kambi na kukaa huko.
DEU 23:11 Lakini jioni ikikaribia ataoga, na baada ya jua kuzama ataingia tena kambini.
DEU 23:12 Tengeni mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda kujisaidia.
DEU 23:13 Kama sehemu ya vifaa vyenu kuweni na kitu cha kulimia, nanyi mnapojisaidia, chimba shimo na kisha funika kinyesi chako.
DEU 23:14 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hutembea katika kambi yenu ili kuwalinda na kuwaweka adui zenu mikononi mwenu. Kambi yenu ni lazima iwe takatifu, ili asione kitu chochote miongoni mwenu kilicho kichafu, akageuka na kuwaacha.
DEU 23:15 Ikiwa mtumwa amekimbilia kwako, usimrudishe kwa bwana wake.
DEU 23:16 Mwache aishi miongoni mwenu mahali popote anapopapenda na katika mji wowote anaochagua. Usimdhulumu.
DEU 23:17 Asiwepo Mwisraeli mwanamke kahaba au mwanaume hanithi wa mahali pa ibada za sanamu.
DEU 23:18 Kamwe usilete mapato ya ukahaba ikiwa ni ya mwanamke au ni ya mwanaume katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yoyote, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anachukizwa na yote mawili.
DEU 23:19 Usimtoze ndugu yako riba, iwe ni fedha ama chakula ama kitu kingine chochote ambacho unaweza kupata riba juu yake.
DEU 23:20 Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoingia kuimiliki.
DEU 23:21 Ukiweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, usichelewe kuitimiza, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakudai, nawe utakuwa na hatia ya dhambi.
DEU 23:22 Lakini ukijizuia kuweka nadhiri, hutakuwa na hatia.
DEU 23:23 Chochote kitakachotamkwa kwa midomo yako ni lazima uhakikishe umekifanya, kwa sababu uliweka nadhiri yako kwa hiari mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa kinywa chako mwenyewe.
DEU 23:24 Ukiingia katika shamba la mizabibu la jirani yako, unaweza kula zabibu kadiri utakavyo, lakini usiweke chochote kwenye kikapu chako.
DEU 23:25 Ukiingia katika shamba la nafaka la jirani yako, unaweza kukwanyua kwa mikono yako, lakini usikate kwa mundu nafaka iliyosimama.
DEU 24:1 Mtu akimwoa mke na akamchukia kwa sababu ya kuona jambo baya kwake, inawezekana akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani mwake.
DEU 24:2 Baada ya mwanamke huyo kuondoka kwake, inawezekana akaolewa na mtu mwingine.
DEU 24:3 Mume wake wa pili akichukizwa naye, akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani mwake, au huyo mume wa pili akifa,
DEU 24:4 basi yule mume wake wa kwanza, ambaye alimpa talaka, haruhusiwi kumwoa tena baada ya mwanamke huyo kuwa najisi. Hayo yatakuwa machukizo machoni pa Mwenyezi Mungu. Usilete dhambi juu ya nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakupa kama urithi.
DEU 24:5 Kama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wowote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.
DEU 24:6 Usitoe jozi ya mawe ya kusagia, hata ikiwa lile la juu, kuweka rehani kwa ajili ya deni, kwa sababu itakuwa ni kuweka uhai wa mtu kama dhamana.
DEU 24:7 Kama mtu akikamatwa akiiba yeyote miongoni mwa ndugu zake wa Waisraeli na kumtenda kama mtumwa au akimuuza, mwizi huyo ni lazima auawe. Nawe utaondoa uovu kutoka miongoni mwenu.
DEU 24:8 Pakitokea magonjwa ya ngozi ya kuambukiza, mwe waangalifu sana kufanya sawasawa na maagizo ya makuhani, ambao ni Walawi. Ni lazima mfuate kwa uangalifu yale niliyowaamuru.
DEU 24:9 Kumbukeni kile Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alichomfanyia Miriamu njiani baada ya ninyi kutoka Misri.
DEU 24:10 Unapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani mwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani.
DEU 24:11 Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani.
DEU 24:12 Ikiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako.
DEU 24:13 Rudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
DEU 24:14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu.
DEU 24:15 Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Mwenyezi Mungu dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.
DEU 24:16 Baba wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
DEU 24:17 Usipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani.
DEU 24:18 Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa huko Misri, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, akawakomboa kutoka huko. Hii ndiyo sababu ninawaamuru kutenda hili.
DEU 24:19 Unapovuna shamba lako na ukasahau mganda, usirudi kuuchukua. Acha kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane, ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aweze kukubariki wewe katika kazi zote za mikono yako.
DEU 24:20 Unapovuna zeituni kutoka miti yako, usirudie matawi mara ya pili. Acha kilichobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane.
DEU 24:21 Unapochuma zabibu katika shamba lako la mizabibu usirudie tena. Acha zinazobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane.
DEU 24:22 Kumbuka kwamba mlikuwa watumwa katika nchi ya Misri. Ndiyo sababu ninawaamuru kufanya hili.
DEU 25:1 Watu wanapokuwa na ugomvi, wapeleke mahakamani na waamuzi wataamua shauri hilo; watawaachia wasio na kosa na kuwahukumu wenye hatia.
DEU 25:2 Kama mtu mwenye hatia anastahili kupigwa, mwamuzi atamwamuru alale chini ili apigwe mbele yake idadi ya mijeledi kulingana na kosa lake,
DEU 25:3 lakini kamwe asipigwe zaidi ya mijeledi arobaini. Akipigwa zaidi ya mijeledi arobaini, nduguyo atadhalilika machoni pako.
DEU 25:4 Usimfunge maksai kinywa anapopura nafaka.
DEU 25:5 Ikiwa ndugu wanaishi pamoja, naye mmoja wao akafa bila kuacha mwana, kamwe mjane wake asiolewe nje ya jamaa hiyo. Ndugu wa mumewe atamchukua, amwoe na kutimiza wajibu wa shemeji kwake.
DEU 25:6 Mwana wa kwanza atakayemzaa atapewa jina la ndugu aliyekufa ili jina lake lisifutike katika Israeli.
DEU 25:7 Hata hivyo, ikiwa ndugu huyo wa mume hataki kuoa huyo mke wa nduguye, mjane atawaendea wazee kwenye lango la mji na kusema, “Ndugu wa mume wangu anakataa kuendeleza jina la nduguye katika Israeli. Hataki kutimiza wajibu wa shemeji kwangu.”
DEU 25:8 Ndipo wazee wa mji wake watamwita na kuzungumza naye. Kama atashikilia kukataa akisema, “Sitaki kumwoa,”
DEU 25:9 mjane wa nduguye atamwendea mbele ya wazee, atamvua kiatu kimoja na kumtemea mate usoni, na kusema, “Hivi ndivyo ambavyo hufanywa kwa mtu ambaye atakataa kuendeleza jamaa ya ndugu yake.”
DEU 25:10 Jamaa ya mtu huyo itafahamika katika Israeli kama Jamaa ya Aliyevuliwa Kiatu.
DEU 25:11 Ikiwa watu wawili wanapigana na mke wa mmoja wao akaja kumwokoa mumewe na yule anayemshambulia, naye mke huyo akifika na kumkamata sehemu za siri,
DEU 25:12 huyo mwanamke utamkata mkono wake. Usimhurumie.
DEU 25:13 Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi.
DEU 25:14 Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo.
DEU 25:15 Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
DEU 25:16 Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wako, humchukia yeyote ambaye hufanya mambo kama haya, yeyote anayetenda kwa udanganyifu.
DEU 25:17 Kumbuka kile Waamaleki walichowatendea mlipokuwa njiani mkitoka Misri.
DEU 25:18 Mlipokuwa mmechoka na kuishiwa nguvu kwa safari yenu, waliwalaki njiani, wakawapiga wale wote waliokuja nyuma. Waamaleki hawakumwogopa Mungu.
DEU 25:19 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokupa pumziko mbali na adui zako wote wanaokuzunguka katika nchi anayokupa kuimiliki kuwa urithi, utafutilia mbali kumbukumbu lote la Waamaleki chini ya mbingu. Usisahau!
DEU 26:1 Mtakapokuwa mmeingia nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi na mtakapokuwa mmeimiliki na kukaa ndani yake,
DEU 26:2 chukueni baadhi ya mavuno ya kwanza ya yale yote mtakayozalisha kutoka udongo wa nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa na mweke kwenye kapu. Kisha uende mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake,
DEU 26:3 na umwambie kuhani atakayekuwepo wakati huo, “Ninatangaza leo kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwamba nimekuja katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliwaapia baba zetu kwamba atatupa.”
DEU 26:4 Kuhani atapokea lile kapu mikononi mwako na kuliweka chini mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
DEU 26:5 Kisha utatangaza mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako: “Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyekuwa anatangatanga, akaenda Misri pamoja na watu wachache, akaishi huko hadi akawa taifa kubwa, lenye nguvu na watu wengi.
DEU 26:6 Lakini Wamisri walituonea na kututaabisha, wakitufanyisha kazi ngumu.
DEU 26:7 Kisha tulimlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu, naye Mwenyezi Mungu akasikia sauti yetu na akaona huzuni yetu, taabu yetu na mateso yetu.
DEU 26:8 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akatutoa nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, pamoja na utisho mkuu, ishara za miujiza na maajabu.
DEU 26:9 Akatuleta mahali hapa akatupatia nchi hii, nchi inayotiririka maziwa na asali;
DEU 26:10 nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umenipa.” Weka kapu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na usujudu mbele zake.
DEU 26:11 Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walio miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.
DEU 26:12 Utakapokuwa umeshatoa zaka zote za mazao yako katika mwaka wa tatu, ambao ni mwaka wa zaka, utampa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, ili waweze kula katika miji yenu na kushiba.
DEU 26:13 Kisha umwambie Mwenyezi Mungu, Mungu wako: “Nimeondoa katika nyumba yangu ile sehemu iliyowekwa wakfu na nimempa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, kulingana na yote uliyoamuru. Sijazihalifu amri zako wala kusahau hata mojawapo.
DEU 26:14 Sijala sehemu iliyowekwa wakfu wakati nilipokuwa nikiomboleza, wala sijaondoa mojawapo wakati nilipokuwa najisi, wala sijatoa sehemu yake yoyote kwa wafu. Nimemtii Mwenyezi Mungu, Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoniamuru.
DEU 26:15 Angalia chini kutoka mbinguni, maskani yako takatifu, uwabariki watu wako Israeli pamoja na nchi uliyotupatia kama ulivyoahidi kwa kiapo kwa baba zetu, nchi inayotiririka maziwa na asali.”
DEU 26:16 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakuagiza leo kufuata amri hizi na sheria; zingatia kwa makini kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.
DEU 26:17 Umetangaza leo kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wako na kwamba utafuata njia zake, kwamba utayashika maagizo yake, amri zake na sheria zake nawe utamtii.
DEU 26:18 Naye Mwenyezi Mungu ametangaza leo kwamba ninyi ni taifa lake, hazina yake ya pekee kama alivyoahidi, ili mpate kuyashika maagizo yake yote.
DEU 26:19 Ametangaza kwamba atawaweka juu kuliko mataifa mengine aliyoyafanya katika sifa, kuwa fahari na heshima, na kwamba mtakuwa taifa takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama alivyoahidi.
DEU 27:1 Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza watu: “Yashikeni maagizo haya yote ninayowaagiza leo.
DEU 27:2 Mtakapokuwa mmevuka Mto Yordani na kuingia katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, msimamishe mawe makubwa na myapake chokaa.
DEU 27:3 Andikeni juu yake maneno yote ya sheria hii wakati mtakapokuwa mmevuka na kuingia katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, nchi inayotiririka maziwa na asali, kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi.
DEU 27:4 Mtakapokuwa mmevuka Yordani, simamisheni mawe haya juu ya Mlima Ebali, kama ninavyowaagiza leo, na myapake chokaa.
DEU 27:5 Huko mjengeeni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, madhabahu, madhabahu ya mawe. Msitumie kifaa chochote cha chuma juu yake.
DEU 27:6 Jengeni madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa mawe ya shambani, na mtoe sadaka za kuteketezwa juu yake kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 27:7 Toeni sadaka za amani juu yake, mkizila na kufurahia mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 27:8 Nanyi mtaandika maneno yote ya sheria hii kwa wazi sana juu ya mawe haya ambayo mmesimamisha.”
DEU 27:9 Kisha Musa na makuhani, ambao ni Walawi, wakawaambia Israeli wote, “Nyamaza ee Israeli, sikiliza! Sasa umekuwa taifa la Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
DEU 27:10 Mtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kufuata amri zake na maagizo ninayokupa leo.”
DEU 27:11 Siku ile ile Musa akawaagiza watu:
DEU 27:12 Mtakapovuka Mto Yordani, makabila haya yatasimama juu ya Mlima Gerizimu kubariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yusufu na Benyamini.
DEU 27:13 Makabila haya yatasimama juu ya Mlima Ebali kwa kutamka laana: Reubeni, Gadi, Asheri, Zabuloni, Dani na Naftali.
DEU 27:14 Nao Walawi watawasomea watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa:
DEU 27:15 “Alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga au mwenye kusubu sanamu, kitu ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, kazi ya mikono ya fundi stadi, na kuisimamisha kwa siri.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:16 “Alaaniwe mtu amdharauye baba yake na mama yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:17 “Alaaniwe mtu asogezaye jiwe la mpaka wa jirani yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:18 “Alaaniwe mtu ampotoshaye kipofu njiani.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:19 “Alaaniwe mtu apotoshaye haki ya mgeni, yatima au mjane.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:20 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mke wa baba yake, kwa maana anadharau malazi ya baba yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:21 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mnyama yeyote.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:22 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na dada yake, binti ya baba yake au binti ya mama yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:23 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mama mkwe wake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:24 “Alaaniwe mtu amuuaye jirani yake kwa siri.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:25 “Alaaniwe mtu apokeaye rushwa ili kumuua mtu asiye na hatia.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 27:26 “Alaaniwe mtu yule ambaye hatashikilia maneno ya sheria hii kwa kuyatekeleza.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”
DEU 28:1 Ukimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ukamilifu na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa makini, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia.
DEU 28:2 Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako:
DEU 28:3 Utabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.
DEU 28:4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na mifugo wako wachanga, yaani ndama wa makundi yako ya ng’ombe, na wana-kondoo wa makundi yako.
DEU 28:5 Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.
DEU 28:6 Utabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.
DEU 28:7 Mwenyezi Mungu atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
DEU 28:8 Mwenyezi Mungu ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakubariki katika nchi anayokupa.
DEU 28:9 Mwenyezi Mungu atakufanya kuwa taifa lake takatifu, kama alivyokuahidi kwa kiapo, ukishika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kwenda katika njia zake.
DEU 28:10 Kisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la Mwenyezi Mungu, nao watakuogopa.
DEU 28:11 Mwenyezi Mungu atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kukupa wewe.
DEU 28:12 Mwenyezi Mungu atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote.
DEU 28:13 Mwenyezi Mungu atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa makini, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini.
DEU 28:14 Usihalifu amri zangu zozote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.
DEU 28:15 Lakini kama hutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika kwa makini amri zake zote na maagizo ninayokupa leo, laana hizi zote zitakuja juu yako na kukupata:
DEU 28:16 Utalaaniwa mjini na utalaaniwa mashambani.
DEU 28:17 Kapu lako na chombo chako cha kukandia kitalaaniwa.
DEU 28:18 Uzao wa tumbo lako utalaaniwa, mazao ya ardhi yako, ndama wa makundi yako ya ng’ombe na wana-kondoo wa makundi yako.
DEU 28:19 Utalaaniwa uingiapo na utokapo.
DEU 28:20 Mwenyezi Mungu ataleta laana juu yako, fadhaa na kukaripiwa katika kila kitu unachokigusa kwa mkono wako, hadi uwe umeharibiwa na kuangamizwa ghafula kwa ajili ya maovu uliyoyafanya kwa kumwacha yeye.
DEU 28:21 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa magonjwa hadi akuangamize kutoka nchi unayoingia kuimiliki.
DEU 28:22 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa magonjwa ya kudhoofisha, kwa homa na kuwashwa, hari na kwa ukame, kutu na kuwa na uchungu ambavyo vitakupiga hadi uangamie.
DEU 28:23 Anga juu yako itakuwa shaba, na ardhi chini yako itakuwa chuma.
DEU 28:24 Mwenyezi Mungu atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga; vitakujia kutoka angani hadi uangamie.
DEU 28:25 Mwenyezi Mungu atakufanya ushindwe mbele ya adui zako. Utawajia kwa njia moja lakini utawakimbia mbele yao kwa njia saba, nawe utakuwa kitu cha kuchukiza kwa falme zote za dunia.
DEU 28:26 Mizoga yenu itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwa na mtu yeyote wa kuwafukuza.
DEU 28:27 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa majipu ya Misri na kwa vidonda vinavyotoa usaha na kuwashwa, ambavyo huwezi kuponywa.
DEU 28:28 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa wazimu, upofu na kuchanganyikiwa kwa akili.
DEU 28:29 Adhuhuri utapapasapapasa kama kipofu gizani. Hutafanikiwa katika lolote ufanyalo; siku baada ya siku utadhulumiwa na kunyang’anywa, wala hakuna yeyote atakayekuokoa.
DEU 28:30 Utaposa mke, lakini mtu mwingine atakutana naye kimwili. Utajenga nyumba, lakini hutaishi ndani yake. Utapanda shamba la mizabibu, lakini hutakula matunda yake.
DEU 28:31 Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako lakini hutakula nyama yake. Punda wako atachukuliwa kwa nguvu kutoka kwako wala hatarudishwa. Kondoo wako watapewa adui zako, wala hakuna mtu yeyote wa kuwaokoa.
DEU 28:32 Wanao wa kiume na wa kike watatolewa kwa mataifa mengine, nawe utayachosha macho yako ukiwatazamia siku baada ya siku, hutakuwa na nguvu kuinua mkono.
DEU 28:33 Taifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na chochote, bali kuonewa kikatili siku zako zote.
DEU 28:34 Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu.
DEU 28:35 Mwenyezi Mungu atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini.
DEU 28:36 Mwenyezi Mungu atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe.
DEU 28:37 Utakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko Mwenyezi Mungu atakakokupeleka.
DEU 28:38 Utapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila.
DEU 28:39 Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila.
DEU 28:40 Utakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika.
DEU 28:41 Utakuwa na wana wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka.
DEU 28:42 Makundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako.
DEU 28:43 Mgeni anayeishi miongoni mwako atazidi kuinuka juu yako, lakini wewe utaendelea kushuka chini zaidi.
DEU 28:44 Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.
DEU 28:45 Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata hadi uangamizwe, kwa sababu hukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa.
DEU 28:46 Zitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele.
DEU 28:47 Kwa sababu hukumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako,
DEU 28:48 kwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao Mwenyezi Mungu atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza.
DEU 28:49 Mwenyezi Mungu ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukavyo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake,
DEU 28:50 taifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana.
DEU 28:51 Watakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako hadi umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wowote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako hadi umekuwa magofu.
DEU 28:52 Nao wataizingira miji yote katika nchi yako, hata kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakupa.
DEU 28:53 Utakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako wa kiume na wa kike, ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira.
DEU 28:54 Hata yule mtu muungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia,
DEU 28:55 naye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingirwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote.
DEU 28:56 Mwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake,
DEU 28:57 kondoo wa nyuma kutoka tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile adui yako atazileta juu yako na miji yako.
DEU 28:58 Kama hutazingatia maneno yote ya sheria hii, ambayo yameandikwa katika kitabu hiki na kama hutalicha hili jina la fahari na la kutisha, yaani la Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
DEU 28:59 Mwenyezi Mungu ataleta mapigo ya kutisha juu yako na kwa wazao wako, maafa makali na ya kudumu, magonjwa mazito na ya kudumu.
DEU 28:60 Atakuletea juu yako magonjwa yote ya Misri yale uliyoyaogopa, nayo yataambatana nawe.
DEU 28:61 Pia Mwenyezi Mungu atakuletea kila aina ya ugonjwa na maafa ambayo hayakuandikwa humu katika kitabu hiki cha sheria, hadi utakapokuwa umeangamizwa.
DEU 28:62 Ninyi ambao mlikuwa wengi kama nyota za angani mtaachwa wachache tu, kwa sababu hamkumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 28:63 Kama ilivyompendeza Mwenyezi Mungu kuwafanya ninyi mstawi na kuongezeka kwa idadi, ndivyo itakavyompendeza kuwaharibu na kuwaangamiza ninyi. Mtang’olewa kutoka nchi mnayoiingia kuimiliki.
DEU 28:64 Kisha Mwenyezi Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwingine. Huko mtaabudu miungu mingine, miungu ya miti na ya mawe, ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua.
DEU 28:65 Miongoni mwa mataifa hayo hamtapata amani, wala mahali pa kupumzisha wayo wa mguu wenu. Huko Mwenyezi Mungu atawapa mahangaiko ya mawazo, macho yaliyochoka kwa kungojea na moyo uliokata tamaa.
DEU 28:66 Utaishi katika mahangaiko siku zote, ukiwa umejaa hofu usiku na mchana, wala hutakuwa kamwe na uhakika wa maisha yako.
DEU 28:67 Asubuhi utasema hivi, “Laiti ingekuwa jioni!” Jioni utasema, “Laiti ingekuwa asubuhi,” kwa sababu ya hofu ile itakayojaza moyo wako na vitu vile macho yako yatakavyoviona.
DEU 28:68 Mwenyezi Mungu atawarudisha tena Misri kwa meli, safari niliyosema kamwe hamngeenda tena. Huko mtajiuza ninyi wenyewe kwa adui zenu kama watumwa wa kiume na wa kike, lakini hakuna yeyote atakayewanunua.
DEU 29:1 Haya ndio maneno ya agano Mwenyezi Mungu alilomwagiza Musa kufanya na Waisraeli huko Moabu, yakiwa nyongeza ya agano alilofanya nao huko Horebu.
DEU 29:2 Musa akawaita Waisraeli wote, akawaambia: Macho yenu yameona yale yote Mwenyezi Mungu aliyofanya kwa Mfalme Farao huko Misri, kwa maafisa wake wote na kwa nchi yake yote.
DEU 29:3 Kwa macho yenu wenyewe mliona yale majaribu makubwa, ishara zile za miujiza na maajabu makubwa.
DEU 29:4 Lakini hadi leo Mwenyezi Mungu hajawapa akili ya kuelewa au macho yanayoona au masikio yanayosikia.
DEU 29:5 Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu.
DEU 29:6 Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
DEU 29:7 Mlipofika mahali hapa, Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani walikuja kupigana dhidi yetu, lakini tuliwashinda.
DEU 29:8 Tuliichukua nchi yao na kuwapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kama urithi wao.
DEU 29:9 Zingatieni masharti ya agano hili, ili mweze kustawi katika kila kitu mnachofanya.
DEU 29:10 Ninyi nyote leo mnasimama mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; mkiwa viongozi na wakuu wenu, wazee na maafisa wenu, na wanaume wengine wote wa Israeli,
DEU 29:11 pamoja na watoto wenu, wake zenu na pia wageni wanaoishi katika kambi zenu wanaowapasulia kuni na kuwachotea maji.
DEU 29:12 Mnasimama hapa ili kufanya agano na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, agano ambalo Mungu analifanya nanyi siku hii ya leo na kulitia muhuri kwa kiapo,
DEU 29:13 kuwathibitisha ninyi siku hii ya leo kama taifa lake, ili aweze kuwa Mungu wenu kama alivyowaahidi na kama alivyowaapia baba zenu Ibrahimu, Isaka na Yakobo.
DEU 29:14 Ninafanya agano hili pamoja na kiapo chake, sio na ninyi tu
DEU 29:15 mnaosimama hapa na sisi leo mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali pia pamoja na wale ambao hawapo hapa leo.
DEU 29:16 Ninyi wenyewe mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyopita katikati ya nchi hadi tukafika hapa.
DEU 29:17 Mliona miongoni mwao machukizo yao, na sanamu za miti na mawe, za fedha na dhahabu.
DEU 29:18 Hakikisheni kwamba hakuna mwanaume au mwanamke, ukoo au kabila miongoni mwenu leo ambalo moyo wake utamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwenda kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisheni hakuna mzizi miongoni mwenu unaotoa sumu chungu ya namna hii.
DEU 29:19 Mtu wa namna hii asikiapo maneno ya kiapo hiki, hujibariki mwenyewe, na kisha hufikiri, “Nitakuwa salama, hata nikiendelea kuifuata njia yangu mwenyewe.” Hili litaleta maafa juu ya nchi iliyoneshewa sawasawa na nchi kame.
DEU 29:20 Mwenyezi Mungu kamwe hatakuwa radhi kumsamehe, ghadhabu na wivu wa Mungu vitawaka dhidi ya mtu huyo. Laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamwangukia na Mwenyezi Mungu atafuta jina lake chini ya mbingu.
DEU 29:21 Mwenyezi Mungu atamtwaa peke yake kutoka makabila ya Israeli kwa maangamizi, kulingana na laana zote za agano zilizoandikwa kwenye Kitabu hiki cha Torati.
DEU 29:22 Watoto wako watakaofuata baada yako katika vizazi vya baadaye na wageni ambao watakuja kutoka nchi za mbali, wataona maafa, yaliyoipata nchi na magonjwa ambayo Mwenyezi Mungu aliyaleta juu yake.
DEU 29:23 Nchi yote itakuwa jaa linaloungua la chumvi na kiberiti: hakutakuwa kilichopandwa, hakutakuwa kinachochipua, wala hakutakuwa na mimea inayoota juu yake. Itakuwa kama maangamizi ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambazo Mwenyezi Mungu aliangamiza kwa hasira kali.
DEU 29:24 Mataifa yote yatauliza: “Kwa nini Mwenyezi Mungu ameifanya hivi nchi hii? Kwa nini hasira hii kali ikawaka?”
DEU 29:25 Na jibu litakuwa: “Ni kwa sababu watu hawa waliacha agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, agano alilofanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri.
DEU 29:26 Walienda zao na kuabudu miungu mingine na kuisujudia, miungu wasioijua, miungu ambayo Mungu hakuwapa.
DEU 29:27 Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya nchi hii, hivyo Mungu akaleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki.
DEU 29:28 Katika hasira kali na katika ghadhabu kuu Mwenyezi Mungu aliwang’oa kutoka nchi yao na kuwasukumia katika nchi nyingine, kama ilivyo sasa.”
DEU 29:29 Mambo ya siri ni ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.
DEU 30:1 Baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokutawanya miongoni mwa mataifa,
DEU 30:2 hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo,
DEU 30:3 ndipo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya.
DEU 30:4 Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka huko Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakukusanya na kukurudisha.
DEU 30:5 Yeye Mwenyezi Mungu atakurudisha katika nchi iliyokuwa mali ya baba zako, nawe utaimiliki. Naye atakufanya ufanikiwe sana na kukuzidisha kwa idadi kuliko baba zako.
DEU 30:6 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ataitahiri mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi.
DEU 30:7 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ataweka laana hizi zote juu ya adui zako ambao wanakuchukia na kukutesa.
DEU 30:8 Utamtii tena Mwenyezi Mungu na kuzishika amri zake zote ninazokupa leo.
DEU 30:9 Ndipo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokufanikisha sana katika kazi zote za mikono yako na katika uzao wa tumbo lako, wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako. Mwenyezi Mungu atakufurahia tena na kukufanikisha, kama alivyowafurahia baba zako,
DEU 30:10 kama utamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake ambayo yameandikwa katika Kitabu hiki cha Torati, na kumgeukia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.
DEU 30:11 Ninachokuagiza leo sio kigumu sana kwako au usichokiweza.
DEU 30:12 Hakiko juu mbinguni, ili uulize, “Ni nani atakayepanda mbinguni kukileta na kututangazia ili tuweze kutii?”
DEU 30:13 Wala hakiko ng’ambo ya bahari, ili uulize, “Ni nani atakayevuka bahari kwenda kukichukua na kututangazia ili tupate kutii?”
DEU 30:14 La hasha! Lile neno liko karibu sana nawe; liko kinywani mwako na ndani ya moyo wako ili uweze kulitii.
DEU 30:15 Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizi.
DEU 30:16 Ninakuamuru leo kwamba umpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.
DEU 30:17 Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu,
DEU 30:18 nakutangazia siku ya leo kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.
DEU 30:19 Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi,
DEU 30:20 na ili upate kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Ibrahimu, Isaka na Yakobo.
DEU 31:1 Kisha Musa akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote:
DEU 31:2 “Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. Mwenyezi Mungu ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’
DEU 31:3 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama Mwenyezi Mungu alivyosema.
DEU 31:4 Naye Mwenyezi Mungu atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao.
DEU 31:5 Mwenyezi Mungu atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mkawatendee yale yote niliyowaamuru.
DEU 31:6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anaenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”
DEU 31:7 Kisha Musa akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Mwenyezi Mungu aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao.
DEU 31:8 Mwenyezi Mungu mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”
DEU 31:9 Kwa hiyo Musa akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na wazee wote wa Israeli.
DEU 31:10 Kisha Musa akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda,
DEU 31:11 Waisraeli wote wanapokuja mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao.
DEU 31:12 Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuzingatia maneno yote ya sheria hii.
DEU 31:13 Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
DEU 31:14 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sasa siku ya kifo chako imekaribia. Mwite Yoshua, mkajihudhurishe katika Hema la Kukutania, mahali nitakapompa maagizo ya kazi.” Kwa hiyo Musa na Yoshua wakaja na kujihudhurisha kwenye Hema la Kukutania.
DEU 31:15 Kisha Mwenyezi Mungu akatokea katika Hema katika nguzo ya wingu, nalo wingu likasimama juu ya ingilio la Hema.
DEU 31:16 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: “Unaenda kupumzika na baba zako, nao watu hawa hivi karibuni watazini na miungu migeni ya nchi wanayoingia. Wataniacha na kuvunja agano nililofanya nao.
DEU 31:17 Siku hiyo nitawakasirikia na kuwaacha; nitawaficha uso wangu, nao wataangamizwa. Maafa mengi na shida nyingi zitakuja juu yao, nao siku hiyo watauliza, ‘Je, maafa haya hayakuja juu yetu kwa sababu Mungu wetu hayuko pamoja nasi?’
DEU 31:18 Nami hakika nitauficha uso wangu siku hiyo kwa sababu ya maovu yao yote kwa kugeukia miungu mingine.
DEU 31:19 “Sasa ujiandikie wimbo huu, uwafundishe Waisraeli na uwaamuru wauimbe, ili upate kuwa ushahidi wangu dhidi yao.
DEU 31:20 Nitakapokwisha kuwaingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja agano langu.
DEU 31:21 Maafa na shida zitakapokuja juu yao, wimbo huu utashuhudia dhidi yao, kwa sababu hautasahauliwa na wazao wao. Ninajua lile wanaloandaa kufanya, hata kabla sijawaingiza katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo.”
DEU 31:22 Hivyo Musa akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.
DEU 31:23 Mwenyezi Mungu akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”
DEU 31:24 Baada ya Musa kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho,
DEU 31:25 akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu agizo hili, akawaambia:
DEU 31:26 “Chukueni Kitabu hiki cha Torati mkakiweke kando ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu.
DEU 31:27 Kwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi ya Mwenyezi Mungu nikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu!
DEU 31:28 Kusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao.
DEU 31:29 Kwa kuwa ninajua, baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata, kwa sababu mtafanya maovu mbele za macho ya Mwenyezi Mungu, na kuchochea hasira yake kwa kazi za mikono yenu.”
DEU 31:30 Musa akayasoma maneno ya wimbo huu kutoka mwanzo hadi mwisho katika masikio ya kusanyiko lote la Israeli:
DEU 32:1 Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitasema; sikia, ee nchi, maneno ya kinywa changu.
DEU 32:2 Mafundisho yangu na yanyeshe kama mvua, na maneno yangu na yashuke kama umande, kama manyunyu juu ya majani mabichi, kama mvua tele juu ya mimea myororo.
DEU 32:3 Nitalitangaza jina la Mwenyezi Mungu. Naam, sifuni ukuu wa Mungu wetu!
DEU 32:4 Yeye ni Mwamba, kazi zake ni kamilifu, njia zake zote ni haki. Mungu mwaminifu ambaye hakosei, yeye ni mnyofu na mwenye haki.
DEU 32:5 Wamefanya mambo ya upotovu mbele zake; kwa aibu yao, wao si watoto wake tena, lakini ni kizazi kilicho kiovu na kilichopotoka.
DEU 32:6 Je, hii ndiyo njia ya kumlipa Mwenyezi Mungu, enyi watu wajinga na wasio na busara? Je, yeye siye Baba yenu, Muumba wenu, aliyewafanya ninyi na kuwaumba?
DEU 32:7 Kumbuka siku za kale; tafakari vizazi vya zamani vilivyopita. Uliza baba yako, naye atakuambia, wazee wako, nao watakueleza.
DEU 32:8 Aliye Juu Sana alipowapa mataifa urithi wao, alipogawanya wanadamu wote, aliweka mipaka kwa ajili ya mataifa sawasawa na hesabu ya wana wa Israeli.
DEU 32:9 Kwa kuwa fungu la Mwenyezi Mungu ni watu wake, Yakobo kura yake ya urithi.
DEU 32:10 Katika nchi ya jangwa alimkuta, katika nyika tupu ivumayo upepo. Alimhifadhi na kumtunza; akamlinda kama mboni ya jicho lake,
DEU 32:11 kama tai avurugaye kiota chake, na kurukaruka juu ya makinda yake, ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka, na huwachukua kwenye mabawa yake.
DEU 32:12 Mwenyezi Mungu peke yake alimwongoza; hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.
DEU 32:13 Akamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi, akamlisha kwa mavuno ya mashamba. Akamlea kwa asali toka mwambani, na kwa mafuta kutoka mwamba wa gumegume,
DEU 32:14 kwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ng’ombe na kutoka makundi ya mbuzi, kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi, kwa kondoo dume wazuri wa Bashani, na kwa ngano nzuri. Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.
DEU 32:15 Yeshuruni alinenepa na kupiga teke; alikuwa na chakula tele, akawa mzito na akapendeza sana. Akamwacha Mungu aliyemuumba, na kumkataa Mwamba Mwokozi wake.
DEU 32:16 Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni, na kumkasirisha kwa sanamu zao za machukizo.
DEU 32:17 Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu: miungu wasiyoijua, miungu iliyojitokeza siku za karibuni, miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.
DEU 32:18 Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi; mkamsahau Mungu aliyewazaa.
DEU 32:19 Mwenyezi Mungu akaona hili, akawakataa, kwa sababu alikasirishwa na wanawe wa kiume na wa kike.
DEU 32:20 Akasema, “Nitawaficha uso wangu, nami nione mwisho wao utakuwa nini, kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka, watoto ambao si waaminifu.
DEU 32:21 Wamenifanya niwe na wivu kwa kile ambacho si mungu, na kunikasirisha kwa sanamu zao batili. Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa. Nitawafanya wakasirishwe na taifa lile lisilo na ufahamu.
DEU 32:22 Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu, ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti. Utateketeza dunia pamoja na mazao yake, na kuwasha moto katika misingi ya milima.
DEU 32:23 “Nitalundika majanga juu yao na kutumia mishale yangu dhidi yao.
DEU 32:24 Nitatuma njaa ya kudhoofisha dhidi yao, maradhi mabaya yateketezayo, na tauni ya kufisha; nitawapelekea wanyama mwitu wenye meno makali, na nyoka wenye sumu watambaao mavumbini.
DEU 32:25 Barabarani upanga utawakosesha watoto; nyumbani mwao hofu itatawala. Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia, pia watoto wachanga na wazee wenye mvi.
DEU 32:26 Nilisema ningewatawanya na kufuta kumbukumbu lao katika mwanadamu.
DEU 32:27 Lakini nilihofia dhihaka za adui, adui asije akashindwa kuelewa, na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda; Mwenyezi Mungu hakufanya haya yote.’ ”
DEU 32:28 Wao ni taifa lisilo na akili, hakuna busara ndani yao.
DEU 32:29 Laiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili, na kutambua mwisho wao utakuwaje!
DEU 32:30 Mtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja, au wawili kufukuza elfu kumi, kama si kwamba Mwamba wao amewauza, kama si kwamba Mwenyezi Mungu amewaacha?
DEU 32:31 Kwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu, sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri.
DEU 32:32 Mzabibu wao unatoka mzabibu wa Sodoma, na kutoka mashamba ya Gomora. Zabibu zake zimejaa sumu, na vishada vyake vimejaa uchungu.
DEU 32:33 Mvinyo wao ni sumu ya nyoka, sumu yenye kufisha ya swila.
DEU 32:34 “Je, hili sikuliweka akiba na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina?
DEU 32:35 Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza. Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza; siku yao ya maafa ni karibu, na maangamizi yao yanawajia haraka.”
DEU 32:36 Mwenyezi Mungu atawahukumu watu wake, na kuwahurumia watumishi wake atakapoona nguvu zao zimekwisha wala hakuna yeyote aliyebaki, mtumwa au aliye huru.
DEU 32:37 Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao, mwamba walioukimbilia,
DEU 32:38 miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji? Wainuke basi, wawasaidie! Wawapeni basi ulinzi!
DEU 32:39 “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye! Hakuna mungu mwingine ila Mimi. Mimi ninaua na Mimi ninafufua, Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya, wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.
DEU 32:40 Ninainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema: Hakika kama niishivyo milele,
DEU 32:41 wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu, nitalipiza kisasi juu ya adui zangu na kuwalipiza wale wanaonichukia.
DEU 32:42 Nitailevya mishale yangu kwa damu, wakati upanga wangu ukitafuna nyama: damu ya waliochinjwa pamoja na mateka, vichwa vya viongozi wa adui.”
DEU 32:43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake, kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake, atalipiza kisasi juu ya adui zake na kufanya upatanisho kwa ajili ya nchi na watu wake.
DEU 32:44 Musa na Yoshua mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia.
DEU 32:45 Musa alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote,
DEU 32:46 akawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii.
DEU 32:47 Siyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
DEU 32:48 Siku hiyo hiyo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
DEU 32:49 “Kwea katika safu za Abarimu hadi kilima cha Nebo kilicho Moabu, ng’ambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe.
DEU 32:50 Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Haruni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake.
DEU 32:51 Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli.
DEU 32:52 Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”
DEU 33:1 Hii ndiyo baraka Musa mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake.
DEU 33:2 Alisema: “Mwenyezi Mungu alikuja kutoka Mlima Sinai, akachomoza kama jua juu yao kutoka Mlima Seiri, akaangaza kutoka Mlima Parani. Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu kutoka kusini, kutoka miteremko ya mlima wake.
DEU 33:3 Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu, watakatifu wako wote wamo mkononi mwako. Miguuni pako wote wanasujudu, na kutoka kwako wanapokea mafundisho,
DEU 33:4 sheria ile Musa aliyotupatia sisi, tulio milki ya kusanyiko la Yakobo.
DEU 33:5 Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni wakati viongozi wa watu walipokusanyika, pamoja na makabila ya Israeli.
DEU 33:6 “Reubeni na aishi, asife, wala watu wake wasiwe wachache.”
DEU 33:7 Akasema hili kuhusu Yuda: “Ee Mwenyezi Mungu, sikia kilio cha Yuda, mlete kwa watu wake. Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea. Naam, uwe msaada wake dhidi ya adui zake!”
DEU 33:8 Kuhusu Lawi alisema: “Thumimu yako na Urimu yako ulimpa, mtu yule uliyemfadhili. Ulimjaribu huko Masa na kushindana naye kwenye maji ya Meriba.
DEU 33:9 Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake, ‘Mimi siwahitaji kamwe.’ Akawasahau jamaa zake, asiwatambue hata watoto wake, lakini akaliangalia neno lako na kulilinda agano lako.
DEU 33:10 Humfundisha Yakobo mausia yako na Israeli sheria yako. Hufukiza uvumba mbele zako na sadaka nzima za kuteketezwa juu ya madhabahu yako.
DEU 33:11 Ee Mwenyezi Mungu, bariki ustadi wake wote, nawe upendezwe na kazi ya mikono yake. Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake; wapige adui zake hata wasiinuke tena.”
DEU 33:12 Kuhusu Benyamini akasema: “Mwache mpendwa wa Mwenyezi Mungu apumzike salama kwake, kwa maana humkinga mchana kutwa, na yule Mwenyezi Mungu ampendaye hupumzika kati ya mabega yake.”
DEU 33:13 Kuhusu Yusufu akasema: “Mwenyezi Mungu na aibariki nchi yake kwa umande wa thamani kutoka juu mbinguni, na vilindi vya maji vilivyotulia chini;
DEU 33:14 pamoja na vitu vilivyo bora sana viletwavyo na jua, na vitu vizuri sana vinavyoweza kutolewa na mwezi;
DEU 33:15 pamoja na zawadi bora sana za milima ya zamani na kwa wingi wa baraka za vilima vya milele;
DEU 33:16 pamoja na baraka nzuri mno za ardhi na ukamilifu wake, na upendeleo wake yeye aliyeishi kwenye kichaka kilichokuwa kinawaka moto. Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, juu ya paji la uso la aliye mkuu miongoni mwa ndugu zake.
DEU 33:17 Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza; pembe zake ni pembe za nyati, na kwa pembe hizo atapiga mataifa, hata yaliyo miisho ya dunia. Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu; hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.”
DEU 33:18 Kuhusu Zabuloni akasema: “Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje, nawe Isakari, katika mahema yako.
DEU 33:19 Watawaita mataifa kwenye mlima, na huko mtatoa dhabihu za haki; watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari, kwa hazina zilizofichwa mchangani.”
DEU 33:20 Kuhusu Gadi akasema: “Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi! Gadi huishi huko kama simba, akirarua kwenye mkono au kichwa.
DEU 33:21 Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote kwa ajili yake mwenyewe; fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa kwa ajili yake. Viongozi wa watu walipokusanyika, alitimiza haki ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu, na hukumu zake kuhusu Israeli.”
DEU 33:22 Kuhusu Dani akasema: “Dani ni mwana simba, akiruka kutoka Bashani.”
DEU 33:23 Kuhusu Naftali akasema: “Naftali amejaa tele upendeleo wa Mwenyezi Mungu, naye amejaa baraka yake; atarithi magharibi na kusini.”
DEU 33:24 Kuhusu Asheri akasema: “Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri; yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake, yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.
DEU 33:25 Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba, nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.
DEU 33:26 “Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni, ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie, na juu ya mawingu katika utukufu wake.
DEU 33:27 Mungu wa milele ni kimbilio lako, na chini kuna mikono ya milele. Atamfukuza adui yako mbele yako, akisema, ‘Mwangamize yeye!’
DEU 33:28 Hivyo Israeli ataishi salama peke yake. Mzao wa Yakobo ni salama katika nchi ya nafaka na divai mpya, mahali mbingu hudondosha umande.
DEU 33:29 Ee Israeli, wewe umebarikiwa! Ni nani kama wewe, taifa lililookolewa na Mwenyezi Mungu? Yeye ni ngao yako na msaada wako, na upanga wako uliotukuka. Adui zako watatetemeka mbele yako, nawe utapakanyaga mahali pao pa juu.”
DEU 34:1 Kisha Musa akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu hadi kilele cha Pisga, ng’ambo ya Yeriko. Huko Mwenyezi Mungu akamwonesha nchi yote: kutoka Gileadi hadi Dani,
DEU 34:2 Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda hadi bahari ya magharibi,
DEU 34:3 Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari.
DEU 34:4 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Ibrahimu na Isaka na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”
DEU 34:5 Naye Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu akafa huko Moabu, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
DEU 34:6 Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo hadi leo.
DEU 34:7 Musa alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika.
DEU 34:8 Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Musa kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, hadi wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.
DEU 34:9 Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Musa alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amemwagiza Musa.
DEU 34:10 Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Musa, ambaye Mwenyezi Mungu alimjua uso kwa uso,
DEU 34:11 aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Mwenyezi Mungu alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote.
DEU 34:12 Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Musa aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.
JOS 1:1 Baada ya kifo cha Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Musa:
JOS 1:2 “Mtumishi wangu Musa amekufa. Sasa basi, wewe na watu wote hawa jiandaeni kuvuka Mto Yordani kuingia nchi nitakayowapa Waisraeli karibuni.
JOS 1:3 Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Musa.
JOS 1:4 Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa iliyo upande wa magharibi.
JOS 1:5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.
JOS 1:6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utawaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa.
JOS 1:7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Musa mtumishi wangu; usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote utakapoenda.
JOS 1:8 Usiache Kitabu hiki cha Torati kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi.
JOS 1:9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakuwa pamoja nawe popote utakapoenda.”
JOS 1:10 Ndipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema,
JOS 1:11 “Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Tayarisheni vyakula vyenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa iwe yenu.’ ”
JOS 1:12 Lakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema,
JOS 1:13 “Kumbukeni agizo lile Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alilowapa: ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa ninyi utulivu kwa kuwapa nchi hii.’
JOS 1:14 Wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ambayo Musa aliwapa mashariki mwa Yordani, lakini wapiganaji wenu wote, wakiwa wamejiandaa kwa vita, lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu,
JOS 1:15 hadi Mwenyezi Mungu awape nao utulivu, kama alivyowatendea ninyi, hadi wao pia watakapokuwa wamemiliki nchi ile Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kuimiliki nchi yenu wenyewe, ambayo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa mashariki mwa Yordani kuelekea linakochomoza jua.”
JOS 1:16 Ndipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutaenda.
JOS 1:17 Kama vile tulivyomtii Musa kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Musa.
JOS 1:18 Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”
JOS 2:1 Kisha Yoshua mwana wa Nuni akawatuma wapelelezi wawili kutoka Shitimu kwa siri, akawaambia, “Nendeni mkaikague hiyo nchi, hasa Yeriko.” Nao wakaenda na kuingia kwenye nyumba ya kahaba mmoja aliyeitwa Rahabu na kukaa humo.
JOS 2:2 Mfalme wa Yeriko akaambiwa, “Tazama! Baadhi ya Waisraeli wamekuja huku usiku huu kuipeleleza nchi.”
JOS 2:3 Hivyo, mfalme wa Yeriko akatuma huu ujumbe kwa Rahabu: “Watoe wale watu waliokujia na kuingia nyumbani mwako, kwa sababu wamekuja kuipeleleza nchi yote.”
JOS 2:4 Lakini huyo mwanamke alikuwa amewachukua hao watu wawili na kuwaficha. Akasema, “Naam, watu hao walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka.
JOS 2:5 Giza lilipoingia, wakati wa kufunga lango la mji, watu hao waliondoka. Sijui walikokwenda. Wafuatilieni haraka. Huenda mkawapata.”
JOS 2:6 (Lakini alikuwa amewapandisha darini, na kuwafunika kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandika darini.)
JOS 2:7 Basi hao watu wakaondoka kuwafuatilia wale wapelelezi katika njia inayoelekea vivuko vya Yordani. Mara wafuatiliaji walipotoka nje, lango likafungwa.
JOS 2:8 Kabla wale wapelelezi hawajalala, Rahabu akawaendea huko juu darini,
JOS 2:9 akawaambia, “Ninajua kuwa Mwenyezi Mungu amewapa nchi hii na hofu kuu imetuangukia kwa sababu yenu, kiasi kwamba wote wanaoishi katika nchi hii wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yenu.
JOS 2:10 Tumesikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyokausha maji ya Bahari ya Shamu kwa ajili yenu mlipotoka Misri, pia lile mlilowatendea Sihoni na Ogu, wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani, ambao mliwaangamiza kabisa.
JOS 2:11 Tuliposikia kuhusu hili, mioyo yetu iliyeyuka na kila mmoja alikosa ujasiri kwa sababu yenu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mungu juu mbinguni na chini duniani.
JOS 2:12 Sasa basi, tafadhali niapieni kwa Mwenyezi Mungu, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu
JOS 2:13 kwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo.”
JOS 2:14 Wale watu wakamhakikishia Rahabu, “Uhai wetu kwa uhai wenu! Ikiwa hutatoa habari ya nini tunachofanya, Mwenyezi Mungu atakapotupatia nchi hii, tutawatendea kwa hisani na kwa uaminifu.”
JOS 2:15 Kisha akawateremsha dirishani kwa kamba, kwa kuwa nyumba yake aliyokuwa anaishi ilikuwa sehemu ya ukuta wa mji.
JOS 2:16 Alikuwa amewaambia, “Nendeni vilimani ili wale wafuatiliaji wasiwapate. Jificheni huko kwa siku tatu hadi watakaporudi, hatimaye mwende zenu.”
JOS 2:17 Wale watu wakamwambia, “Hiki kiapo ulichotuapisha hakitatufunga,
JOS 2:18 isipokuwa, tutakapoingia katika nchi hii, utakuwa umefunga hii kamba nyekundu dirishani pale ulipotuteremshia na kama utakuwa umewaleta baba yako na mama yako, ndugu zako na jamaa yako yote ndani ya nyumba yako.
JOS 2:19 Ikiwa mtu yeyote atatoka nje ya nyumba yako akaenda mtaani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, hatutawajibika. Lakini yule ambaye atakuwa ndani pamoja nawe, mkono wa mtu yeyote ukiwa juu yake, damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu.
JOS 2:20 Lakini ikiwa utatoa habari ya shughuli yetu tunayofanya, tutakuwa tumefunguliwa kutoka kiapo hiki ulichotufanya tuape.”
JOS 2:21 Naye akajibu, “Nimekubali. Na iwe kama mnavyosema.” Kwa hiyo akaagana nao, nao wakaondoka. Yeye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.
JOS 2:22 Walipoondoka, wakaelekea vilimani na kukaa huko siku tatu, hadi wale waliokuwa wakiwafuatilia wakawa wamewatafuta njia nzima na kurudi pasipo kuwapata.
JOS 2:23 Ndipo wale watu wawili wakaanza kurudi. Wakashuka kutoka kule vilimani, wakavuka mto na kuja kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kumweleza kila kitu kilichowapata.
JOS 2:24 Wakamwambia Yoshua, “Hakika Mwenyezi Mungu ametupatia nchi yote mikononi mwetu; watu wote wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yetu.”
JOS 3:1 Yoshua na Waisraeli wote wakaondoka asubuhi na mapema kutoka Shitimu, wakaenda hadi Mto Yordani, ambako walipiga kambi kabla ya kuvuka.
JOS 3:2 Baada ya siku tatu maafisa wakapita katika kambi yote,
JOS 3:3 wakitoa maagizo kwa watu, wakiwaambia: “Mtakapoona Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, likichukuliwa na Walawi ambao ndio makuhani, mtaondoka hapo mlipo na kulifuata.
JOS 3:4 Ndipo mtakapotambua njia mtakayoiendea, kwa kuwa hamjawahi kuipita kabla. Lakini msisogee karibu, bali kuwe na umbali wa dhiraa elfu mbili kati yenu na Sanduku.”
JOS 3:5 Ndipo Yoshua akawaambia hao watu, “Jitakaseni, kwa kuwa kesho Mwenyezi Mungu atatenda mambo ya kushangaza kati yenu.”
JOS 3:6 Yoshua akawaambia makuhani, “Liinueni Sanduku la Agano mkatangulie mbele ya watu.” Hivyo wakaliinua na kutangulia mbele yao.
JOS 3:7 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Leo nitaanza kukutukuza machoni pa Israeli yote, ili wapate kujua kuwa niko pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Musa.
JOS 3:8 Uwaambie makuhani wanaochukua Sanduku la Agano, ‘Mnapofika kwenye ukingo wa maji ya Yordani, nendeni mkasimame ndani ya mto.’ ”
JOS 3:9 Yoshua akawaambia Waisraeli, “Njooni hapa msikilize maneno ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
JOS 3:10 Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Mungu aliye hai yupo kati yenu, na kwamba kwa hakika atawaondoa mbele yenu hao Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi.
JOS 3:11 Tazameni, Sanduku la Agano la Bwana wa dunia yote litaingia ndani ya Mto Yordani likiwa limewatangulia.
JOS 3:12 Sasa basi, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, mtu mmoja kutoka kila kabila.
JOS 3:13 Mara tu nyayo za makuhani walichukualo Sanduku la Mwenyezi Mungu, Bwana wa dunia yote, zitakapokanyaga ndani ya Mto Yordani, maji hayo yanayotiririka kutoka juu yatatindika na kusimama kama chuguu.”
JOS 3:14 Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia.
JOS 3:15 Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji,
JOS 3:16 maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.
JOS 3:17 Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.
JOS 4:1 Taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua,
JOS 4:2 “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja,
JOS 4:3 uwaambie wachukue mawe kumi na mbili katikati ya Mto Yordani, pale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu.”
JOS 4:4 Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila,
JOS 4:5 naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kulingana na idadi ya makabila ya Israeli,
JOS 4:6 kuwa ishara miongoni mwenu. Siku zijazo, watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’
JOS 4:7 waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka, yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. Sanduku lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”
JOS 4:8 Hivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mbili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na idadi ya makabila ya Israeli, kama Mwenyezi Mungu alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini.
JOS 4:9 Yoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mbili yaliyokuwa katikati ya Mto Yordani, mahali miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko hadi leo.
JOS 4:10 Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani hadi kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimekamilishwa na watu, sawasawa na vile Musa alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka,
JOS 4:11 na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Mwenyezi Mungu na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama.
JOS 4:12 Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamejiandaa kwa vita, kama Musa alivyowaamuru.
JOS 4:13 Idadi ya wanaume elfu arobaini waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za Mwenyezi Mungu hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita.
JOS 4:14 Siku ile Mwenyezi Mungu akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Musa.
JOS 4:15 Basi Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua,
JOS 4:16 “Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.”
JOS 4:17 Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.”
JOS 4:18 Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. Mara tu walipoiweka miguu yao ukingoni mwa mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.
JOS 4:19 Siku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki wa Yeriko.
JOS 4:20 Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mbili waliyokuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani.
JOS 4:21 Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’
JOS 4:22 Basi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’
JOS 4:23 Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka.
JOS 4:24 Alifanya hivi ili mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa Mwenyezi Mungu ni wenye nguvu, na ili kila wakati mpate kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
JOS 5:1 Basi wafalme wote wa Waamori magharibi mwa Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri tena wa kukabiliana na Waisraeli.
JOS 5:2 Wakati huo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya gumegume na uwatahiri Waisraeli tena.”
JOS 5:3 Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya gumegume na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi.
JOS 5:4 Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri.
JOS 5:5 Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini kutoka Misri hawakuwa wametahiriwa.
JOS 5:6 Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini hadi wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii Mwenyezi Mungu. Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali.
JOS 5:7 Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini.
JOS 5:8 Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini hadi walipopona.
JOS 5:9 Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo.
JOS 5:10 Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa wamepiga kambi huko Gilgali kwenye nchi tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka.
JOS 5:11 Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi: mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga.
JOS 5:12 Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.
JOS 5:13 Basi Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi. Yoshua akamwendea na kumuuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?”
JOS 5:14 Akajibu, “La, siko upande wowote, lakini mimi nimekuja nikiwa jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu.” Yoshua akasujudu, uso wake ukigusa chini, akamuuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?”
JOS 5:15 Jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali uliposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.
JOS 6:1 Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa sababu ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.
JOS 6:2 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na wapiganaji wake.
JOS 6:3 Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita.
JOS 6:4 Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo.
JOS 6:5 Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na wapiganaji watapanda, kila mtu akielekea mbele yake.”
JOS 6:6 Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake.”
JOS 6:7 Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu.”
JOS 6:8 Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba waliozibeba zile baragumu saba mbele za Mwenyezi Mungu, wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu likawafuata.
JOS 6:9 Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa.
JOS 6:10 Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige ukelele wa vita; msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote hadi siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!”
JOS 6:11 Basi akalipeleka Sanduku la Mwenyezi Mungu kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala.
JOS 6:12 Yoshua akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, nao makuhani wakalichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu.
JOS 6:13 Wale Makuhani saba waliobeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la Mwenyezi Mungu, huku baragumu hizo zikiendelea kulia.
JOS 6:14 Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita.
JOS 6:15 Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba.
JOS 6:16 Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipiga baragumu kwa sauti kubwa, naye Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana Mwenyezi Mungu amewapa mji huu!
JOS 6:17 Mji huu pamoja na vyote vilivyomo utatengewa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuangamizwa. Rahabu yule kahaba atasalimishwa, pamoja na wote walio naye nyumbani mwake, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma.
JOS 6:18 Lakini mjiepushe na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, msije mkajiletea maangamizi kwa kuchukua chochote katika hivyo; la sivyo, mtailetea kambi ya Israeli maangamizi na taabu.
JOS 6:19 Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi Mungu, lazima viletwe katika hazina yake.”
JOS 6:20 Baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele; kwa ile sauti ya baragumu na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji.
JOS 6:21 Wakauweka mji wakfu kwa Mwenyezi Mungu, na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga: wanaume na wanawake, vijana kwa wazee, ng’ombe, kondoo na punda.
JOS 6:22 Yoshua akawaambia wale watu wawili waliokuwa wameipeleleza nchi, “Nendeni nyumbani mwa yule kahaba; mleteni pamoja na wote walio nyumbani mwake, kulingana na kiapo chenu kwake.”
JOS 6:23 Basi wale vijana waliofanya upelelezi wakaenda kumleta Rahabu, baba yake na mama yake, na ndugu zake na watu wote waliokuwa pamoja naye. Wakaleta jamaa yake yote na kuwaweka mahali nje ya kambi ya Israeli.
JOS 6:24 Kisha wakauchoma mji wote na kila kitu kilichokuwa ndani yake. Lakini fedha, dhahabu, na vyombo vya shaba na vya chuma wakaviweka katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi Mungu.
JOS 6:25 Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu yule kahaba, jamaa yake yote na vyote alivyokuwa navyo, kwa sababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko, naye anaishi miongoni mwa Waisraeli hata leo.
JOS 6:26 Wakati ule Yoshua akatamka kiapo hiki akasema, “Na alaaniwe mbele za Mwenyezi Mungu mtu atakayeinuka kuujenga tena mji huu wa Yeriko: “Kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza wa kiume ataiweka misingi yake; kwa gharama ya mtoto wake wa mwisho atayaweka malango yake.”
JOS 6:27 Hivyo Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yoshua, na sifa zake zikaenea katika nchi yote.
JOS 7:1 Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa; Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alivichukua baadhi ya hivyo vitu. Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Israeli.
JOS 7:2 Basi Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko waende Ai, karibu na Beth-Aveni mashariki mwa Betheli, akawaambia, “Pandeni mkaipeleleze nchi.” Basi wale watu wakapanda wakaipeleleza Ai.
JOS 7:3 Waliporudi kwa Yoshua, wakasema, “Si lazima watu wote waende kupigana na Ai. Watume watu elfu mbili au tatu wakauteke huo mji. Usiwachoshe watu wote, kwa sababu huko kuna watu wachache tu.”
JOS 7:4 Basi wakapanda kama wanaume elfu tatu tu, lakini wakashambuliwa na wanaume wa Ai,
JOS 7:5 ambao waliwaua wanaume kama thelathini na sita miongoni mwao. Wakawafukuza Waisraeli kutoka lango la mji hadi Shebarimu, nao wakawauwa huko kwenye miteremko. Kutokana na hili mioyo ya watu ikayeyuka kwa hofu, ikawa kama maji.
JOS 7:6 Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu, na akabakia hapo hadi jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo, wakatia mavumbi vichwani mwao.
JOS 7:7 Yoshua akasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ng’ambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeridhika kukaa ng’ambo ile nyingine ya Yordani!
JOS 7:8 Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake?
JOS 7:9 Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?”
JOS 7:10 Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Unafanya nini ukilala kifudifudi?
JOS 7:11 Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa; wameiba, wamesema uongo, na wameviweka pamoja na mali yao.
JOS 7:12 Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena hadi mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi.
JOS 7:13 “Nenda, ukawatakase watu. Waambie, ‘Jitakaseni mjiandae kwa ajili ya kesho; kwa sababu hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa vimo kati yenu, ee Israeli. Hamwezi kusimama dhidi ya adui zenu hadi mtakapoviondoa.
JOS 7:14 “ ‘Asubuhi, mtakuja kabila kwa kabila. Kisha kabila atakalolichagua Mwenyezi Mungu watakuja mbele kufuatana na koo zao; nao ukoo atakaouchagua Mwenyezi Mungu watakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa atakayoichagua Mwenyezi Mungu watakuja mbele mtu kwa mtu.
JOS 7:15 Yule atakayekutwa na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, atateketezwa kwa moto pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la Mwenyezi Mungu na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’ ”
JOS 7:16 Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na kabila la Yuda likachaguliwa.
JOS 7:17 Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawachagua Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikachaguliwa.
JOS 7:18 Yoshua akaamuru jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akachaguliwa.
JOS 7:19 Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.”
JOS 7:20 Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya:
JOS 7:21 Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.”
JOS 7:22 Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakakimbia hadi kwenye hema. Tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa kwenye hema lake, pamoja na ile fedha chini yake.
JOS 7:23 Wakavichukua vile vitu toka kwenye hema, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, wakavitandaza mbele za Mwenyezi Mungu.
JOS 7:24 Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe wa kiume na wa kike, ng’ombe, punda na kondoo wake, hema lake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori.
JOS 7:25 Yoshua akasema, “Kwa nini umetuletea taabu hii? Mwenyezi Mungu atakuletea taabu leo.” Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto.
JOS 7:26 Wakakusanya lundo la mawe juu ya Akani, ambalo lipo hadi leo. Naye Mwenyezi Mungu akageuka kutoka hasira yake kali. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Bonde la Akori tangu siku hiyo.
JOS 8:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake.
JOS 8:2 Utautendea mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyotendea Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kunyakua mali zao na mifugo yao kuwa nyara zenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.”
JOS 8:3 Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku,
JOS 8:4 akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho.
JOS 8:5 Mimi na watu walio pamoja nami tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo awali, sisi tutawakimbia.
JOS 8:6 Watatufuatilia hadi tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia,
JOS 8:7 ninyi mtainuka mtoke mafichoni na kuuteka mji. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atautia mkononi mwenu.
JOS 8:8 Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile Mwenyezi Mungu alivyoamuru. Tazameni, nimewaagiza.”
JOS 8:9 Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.
JOS 8:10 Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Yoshua akakusanya jeshi lake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawaongoza kwenda Ai.
JOS 8:11 Wanajeshi wote waliokuwa pamoja na Yoshua walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji.
JOS 8:12 Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka mafichoni kusubiri kushambulia, kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji.
JOS 8:13 Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.
JOS 8:14 Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na wanaume wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema kukutana na Israeli katika vita mahali palipotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji.
JOS 8:15 Yoshua na Waisraeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani.
JOS 8:16 Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji.
JOS 8:17 Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Waisraeli.
JOS 8:18 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai.
JOS 8:19 Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mafichoni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.
JOS 8:20 Wanaume wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani, lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wakiwakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao.
JOS 8:21 Basi Yoshua na Waisraeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kwenye mji, wakawageukia wanaume wa Ai na kuwashambulia.
JOS 8:22 Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka.
JOS 8:23 Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.
JOS 8:24 Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini.
JOS 8:25 Wanaume na wanawake elfu kumi na mbili waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai.
JOS 8:26 Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai.
JOS 8:27 Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwamuru Yoshua.
JOS 8:28 Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo.
JOS 8:29 Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo hadi jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe mengi makubwa juu yake, ambayo yamesalia hadi leo.
JOS 8:30 Kisha Yoshua akajenga madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, katika Mlima Ebali,
JOS 8:31 kama Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alivyokuwa amewaamuru Waisraeli. Akaijenga sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Musa: madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo juu yake hakuna chombo cha chuma kilichotumika. Hapo juu yake wakamtolea Mwenyezi Mungu sadaka za kuteketezwa na kutoa sadaka za amani.
JOS 8:32 Pale mbele ya Waisraeli, Yoshua akanakili juu ya hayo mawe Torati ya Musa, aliyokuwa ameiandika.
JOS 8:33 Waisraeli wote, wakiwa na wazee wao, maafisa na waamuzi, walikuwa wamesimama pande zote mbili za Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, wakiwaelekea makuhani Walawi waliokuwa wamelibeba. Wageni walioishi miongoni mwao, pamoja na wazawa, walikuwa hapo. Nusu ya watu walisimama mbele ya Mlima Gerizimu, na nusu nyingine wakasimama mbele ya Mlima Ebali, kama vile Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameamuru hapo mwanzo alipotoa maagizo ya kuwabariki watu wa Israeli.
JOS 8:34 Hatimaye, Yoshua akasoma maneno yote ya sheria, yaani baraka na laana, kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati.
JOS 8:35 Hakuna neno lolote katika yale yote ambayo Musa alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakuwasomea kusanyiko lote la Waisraeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na wageni walioishi miongoni mwao.
JOS 9:1 Basi ikawa wafalme wote waliokuwa magharibi mwa Yordani waliposikia haya yote, na wale waliokuwa katika nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika pwani yote ya Bahari Kuu hadi kufikia Lebanoni (wafalme wa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi),
JOS 9:2 waliungana ili kupigana vita dhidi ya Yoshua na Israeli.
JOS 9:3 Hata hivyo, watu wa Gibeoni waliposikia kuhusu yote Yoshua aliyowatendea watu wa Yeriko na Ai,
JOS 9:4 waliamua kufanya hila: Wakajifanya kama wajumbe wakiwa na punda waliobebeshwa mizigo ya magunia yaliyochakaa, na viriba vikuukuu vya mvinyo, vyenye nyufa zilizozibwa.
JOS 9:5 Walivaa miguuni mwao viatu vilivyoraruka na kushonwa, kisha wakavaa nguo kuukuu. Chakula chao kilikuwa mkate uliokauka na kuingia koga.
JOS 9:6 Ndipo wakamwendea Yoshua kambini huko Gilgali, wakamwambia yeye pamoja na Waisraeli, “Tumetoka katika nchi ya mbali; fanyeni mkataba nasi.”
JOS 9:7 Basi Waisraeli wakawaambia hao Wahivi, “Lakini huenda mnakaa karibu nasi. Twawezaje basi kufanya mkataba nanyi?”
JOS 9:8 Wakamwambia Yoshua, “Sisi ni watumishi wako.” Yoshua akawauliza, “Ninyi ni nani, na mnatoka wapi?”
JOS 9:9 Nao wakamjibu: “Watumishi wako wametoka nchi ya mbali sana kwa ajili ya umaarufu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Kwa kuwa tumesikia taarifa zake: hayo yote aliyofanya huko Misri,
JOS 9:10 pia yale yote aliyowatendea wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani; huyo Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani, aliyetawala huko Ashtarothi.
JOS 9:11 Basi wazee wetu na wale wote wanaoishi katika nchi yetu walituambia, ‘Chukueni chakula cha safari; nendeni mkakutane na watu hao na kuwaambia, “Sisi tu watumishi wenu, fanyeni mapatano nasi.” ’
JOS 9:12 Mkate huu wetu ulikuwa wa moto tulipoufunga siku tulipoanza safari kuja kwenu, lakini sasa angalia jinsi ulivyokauka na kuota ukungu.
JOS 9:13 Viriba hivi vya mvinyo vilikuwa vipya tulipovijaza, lakini ona jinsi vilivyo na nyufa. Nguo zetu na viatu vimechakaa kwa ajili ya safari ndefu.”
JOS 9:14 Basi Waisraeli wakavikagua vyakula vyao bila kupata shauri kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
JOS 9:15 Ndipo Yoshua akafanya nao mkataba wa amani ili kuwaacha waishi, na viongozi wa kusanyiko wakauthibitisha kwa kiapo.
JOS 9:16 Siku ya tatu baada ya kufanya mkataba na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa watu hao ni majirani zao, walioishi karibu nao.
JOS 9:17 Ndipo Waisraeli wakasafiri, na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao: yaani Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu.
JOS 9:18 Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Kusanyiko lote wakanung’unika dhidi ya hao viongozi,
JOS 9:19 lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa.
JOS 9:20 Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.”
JOS 9:21 Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo.
JOS 9:22 Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ ilhali mnaishi karibu nasi?
JOS 9:23 Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”
JOS 9:24 Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili.
JOS 9:25 Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwenu.”
JOS 9:26 Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuwaua.
JOS 9:27 Siku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu mahali pale Mwenyezi Mungu angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.
JOS 10:1 Baada ya haya Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu alisikia kuwa Yoshua alikuwa ameteka mji wa Ai na kuuangamiza kabisa, tena alikuwa ameua mfalme wake, kama alivyofanya huko Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa watu wa Gibeoni walikuwa wamefanya mapatano ya amani na Waisraeli, na walikuwa wakiishi karibu yao.
JOS 10:2 Yeye na watu wake wakataharuki mno kwa kuwa Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mmoja wa miji ya kifalme; ulikuwa mkubwa kuliko Ai, na watu wake wote walikuwa mashujaa wa vita.
JOS 10:3 Hivyo Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu akaomba msaada kwa Hohamu mfalme wa Hebroni, Piramu mfalme wa Yarmuthi, Yafia mfalme wa Lakishi, na Debiri mfalme wa Egloni.
JOS 10:4 Akawaambia, “Njooni mnisaidie kuipiga Gibeoni, kwa sababu imefanya mkataba wa amani na Yoshua na Waisraeli.”
JOS 10:5 Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, ambao ni wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni, wakaunganisha majeshi yao. Wakapanda na vikosi vyao vyote, nao wakajipanga dhidi ya Gibeoni na kuishambulia.
JOS 10:6 Nao Wagibeoni wakatuma ujumbe kwa Yoshua kwenye kambi ya Gilgali na kumwambia, “Usiwatelekeze watumishi wako. Panda haraka uje kwetu utuokoe! Tusaidie, kwa sababu wafalme wote wa Waamori wanaokaa nchi ya vilima wameunganisha majeshi yao pamoja dhidi yetu.”
JOS 10:7 Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo mashujaa wote.
JOS 10:8 Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.”
JOS 10:9 Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, akawashambulia ghafula.
JOS 10:10 Mwenyezi Mungu akawafadhaisha mbele ya Waisraeli, naye Yoshua na Waisraeli wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Waisraeli wakawafukuza kwa njia inayopanda kwenda Beth-Horoni, huku wakiwaua hadi kufikia Azeka na Makeda.
JOS 10:11 Walipokuwa wanawakimbia Waisraeli kwenye barabara inayoteremka kutoka Beth-Horoni hadi Azeka, Mwenyezi Mungu akawavurumishia mawe makubwa kama mvua kutoka mbinguni, na wengi wao walikufa kwa mawe kuliko wale waliokufa kwa panga za Waisraeli.
JOS 10:12 Siku ile Mwenyezi Mungu alipowakabidhi Waamori kwa Waisraeli, Yoshua akanena na Mwenyezi Mungu akiwa mbele ya Waisraeli, akasema: “Wewe jua, simama juu ya Gibeoni, wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.”
JOS 10:13 Hivyo jua likasimama, nao mwezi ukatulia, hadi taifa hilo lilipokwisha kujilipizia kisasi kwa adui zake, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari. Jua likasimama katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku nzima.
JOS 10:14 Hakujakuwa na siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo Mwenyezi Mungu alimsikiliza mwanadamu. Hakika Mwenyezi Mungu alikuwa akiwapigania Israeli.
JOS 10:15 Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Israeli yote.
JOS 10:16 Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda.
JOS 10:17 Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda,
JOS 10:18 akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mlango wa pango, tena mweke walinzi wa kulilinda.
JOS 10:19 Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewatia mkononi mwenu.”
JOS 10:20 Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza, isipokuwa wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye ngome.
JOS 10:21 Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua kule kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli.
JOS 10:22 Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.”
JOS 10:23 Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni.
JOS 10:24 Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita wanaume wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita walioenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni.
JOS 10:25 Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Mwenyezi Mungu atakalowatendea adui zenu wote mnaoenda kupigana nao.”
JOS 10:26 Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakining’inia juu ya ile miti hadi jioni.
JOS 10:27 Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, ambayo yapo hadi leo.
JOS 10:28 Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamuua kila mmoja katika ule mji, pamoja na mfalme wake kwa upanga. Hakubakiza mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
JOS 10:29 Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli yote hadi mji wa Libna na kuushambulia.
JOS 10:30 Mwenyezi Mungu pia akautia huo mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
JOS 10:31 Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.
JOS 10:32 Mwenyezi Mungu akautia Lakishi mikononi mwa Israeli, hivyo Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilichokuwa ndani yake kwa upanga, kama tu vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna.
JOS 10:33 Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda pamoja na jeshi lake, hadi hapakubakia mtu yeyote.
JOS 10:34 Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.
JOS 10:35 Wakauteka mji huo siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi.
JOS 10:36 Kisha Yoshua na Waisraeli wote wakapanda kutoka Egloni hadi Hebroni, na kuushambulia.
JOS 10:37 Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza mtu yeyote. Kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake.
JOS 10:38 Ndipo Yoshua na Waisraeli wote wakageuka na kushambulia Debiri.
JOS 10:39 Wakauteka mji, mfalme wake na vijiji vyake, na kuupiga kwa upanga. Kila mmoja aliyekuwa ndani yake wakamwangamiza kabisa. Hawakubakiza mtu yeyote. Wakaufanyia Debiri na mfalme wake kama vile walivyokuwa wameifanyia miji ya Libna na Hebroni na wafalme wao.
JOS 10:40 Hivyo Yoshua akalishinda eneo hilo lote, ikiwa ni pamoja na nchi ya vilima, na Negebu, na Shefela, miteremko ya milima, pamoja na wafalme wake wote. Hakubakiza mtu yeyote. Akaangamiza kabisa kila kitu chenye pumzi, kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alivyokuwa ameamuru.
JOS 10:41 Yoshua akawashinda kuanzia Kadesh-Barnea hadi Gaza na kutoka eneo lote la Gosheni hadi Gibeoni.
JOS 10:42 Wafalme hawa wote pamoja na nchi zao Yoshua aliwashinda kwa wakati mmoja, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliwapigania Israeli.
JOS 10:43 Ndipo Yoshua akarudi pamoja na Israeli yote kwenye kambi huko Gilgali.
JOS 11:1 Yabini mfalme wa Hazori aliposikia habari hizo, akatuma ujumbe kwa Yobabu mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na kwa mfalme wa Akshafu,
JOS 11:2 na pia kwa wafalme wa upande wa kaskazini wale waliokuwa milimani, katika Araba upande wa kusini mwa Kinerethi, katika Shefela, na katika miinuko ya Nafoth-Dori upande wa magharibi;
JOS 11:3 kwa Wakanaani upande wa mashariki na magharibi; kwa Waamori, Wahiti, Waperizi na Wayebusi katika nchi ya vilima; na kwa Wahivi chini ya Hermoni katika eneo ya Mispa.
JOS 11:4 Wakaja na vikosi vyao vyote na idadi kubwa ya farasi na magari ya vita: jeshi kubwa, kama wingi wa mchanga ulio pwani ya bahari.
JOS 11:5 Wafalme hawa wote wakaunganisha majeshi yao na kupiga kambi pamoja kwenye Maji ya Meromu, ili kupigana dhidi ya Israeli.
JOS 11:6 Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope, kwa sababu kesho saa kama hii nitawatia wote mikononi mwa Israeli, wakiwa wameuawa. Utakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuyachoma moto magari yao ya vita.”
JOS 11:7 Hivyo Yoshua na jeshi lake lote wakaja dhidi yao ghafula kwenye Maji ya Meromu na kuwashambulia,
JOS 11:8 naye Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Israeli. Wakawashinda na kuwafukuza hadi Sidoni Kuu na kuwafikisha Misrefoth-Maimu, hadi Bonde la Mispa upande wa mashariki, hata pakawa hakuna yeyote aliyebaki.
JOS 11:9 Yoshua akawatendea kama Mwenyezi Mungu alivyoamuru. Akakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuchoma moto magari yao ya vita.
JOS 11:10 Wakati huo Yoshua akarudi na kuuteka mji wa Hazori na kumuua mfalme wake kwa upanga. (Hazori ulikuwa mji mkuu wa falme hizo zote.)
JOS 11:11 Kila aliyekuwa ndani yake wakamuua kwa upanga. Wakawaangamiza kabisa, wala hawakusaza chochote chenye pumzi, na akauchoma Hazori kwa moto.
JOS 11:12 Yoshua akaiteka hii miji yote ya kifalme pamoja na wafalme wake, na akawaua kwa upanga. Akawaangamiza kabisa wote, jinsi Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alivyowaagiza.
JOS 11:13 Lakini Israeli hawakuichoma moto hata mojawapo ya miji iliyojengwa katika vilima vyao vidogo, isipokuwa mji wa Hazori, ambao Yoshua aliuchoma kwa moto.
JOS 11:14 Waisraeli wakajichukulia nyara zote na mifugo yote ya miji hii, bali waliwaua watu wote kwa upanga hadi walipowaangamiza kabisa, pasipo kumbakiza yeyote mwenye pumzi.
JOS 11:15 Kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa mtumishi wake, vivyo hivyo Musa alimwagiza Yoshua, naye Yoshua akafanya vivyo hivyo; hakukosa kufanya lolote katika yale yote Mwenyezi Mungu aliyomwagiza Musa.
JOS 11:16 Yoshua akaiteka nchi hii yote: nchi ya vilima, Negebu yote, eneo yote ya Gosheni, na Shefela, Araba na milima ya Israeli pamoja na materemko yake,
JOS 11:17 kuanzia Mlima Halaki ambao umeinuka kuelekea Seiri hadi Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni chini ya Mlima Hermoni. Akawateka wafalme wake wote, akawapiga na kuwaua.
JOS 11:18 Yoshua akapigana vita dhidi ya wafalme hawa wote kwa muda mrefu.
JOS 11:19 Hakuna mji wowote katika eneo hili uliofanya mkataba wa amani na Israeli, isipokuwa hao Wahivi wa Gibeoni. Wengine wote walishindwa katika vita.
JOS 11:20 Kwa maana Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliifanya mioyo yao iwe migumu, ili kupigana vita dhidi ya Israeli, ili apate kuwaangamiza kabisa, awafutilie mbali pasipo huruma, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
JOS 11:21 Wakati huo Yoshua akaenda kuwaangamiza Waanaki kutoka nchi ya vilima: kuanzia Hebroni, Debiri na Anabu, na kutoka nchi yote ya vilima ya Yuda, na kutoka nchi yote ya vilima ya Israeli. Yoshua akawaangamiza kabisa pamoja na miji yao.
JOS 11:22 Hakuna Waanaki waliosalia katika eneo la Waisraeli; ila tu, kuna wachache waliosalia katika maeneo ya Gaza, Gathi na Ashdodi.
JOS 11:23 Hivyo Yoshua akaiteka nchi hiyo yote kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwagiza Musa, naye Yoshua akawapa Israeli kuwa urithi wao, kulingana na walivyogawanyika katika makabila yao. Ndipo nchi ikawa na amani bila vita.
JOS 12:1 Hawa ndio wafalme wa nchi ambao Waisraeli waliwashinda na kumiliki maeneo yao upande wa mashariki mwa Yordani, kuanzia Bonde la Arnoni hadi Mlima Hermoni, pamoja na eneo lote la upande wa mashariki mwa Araba:
JOS 12:2 Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni. Alitawala kuanzia Aroeri kwenye ukingo wa Bonde la Arnoni, kuanzia katikati ya bonde, hadi kwenye Mto Yaboki, ambao ni mpaka wa Waamoni. Hii ilijumlisha nusu ya Gileadi.
JOS 12:3 Pia alitawala Araba ya mashariki kuanzia Bahari ya Kinerethi hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), hadi Beth-Yeshimothi, kisha kuelekea kusini chini ya miteremko ya Pisga.
JOS 12:4 Nayo nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa mmoja wa mabaki ya Warefai, aliyetawala Ashtarothi na Edrei.
JOS 12:5 Naye alitawala katika Mlima Hermoni, Saleka, Bashani yote hadi mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka na nusu ya Gileadi, hadi kwenye mpaka wa Sihoni mfalme wa Heshboni.
JOS 12:6 Musa, mtumishi wa Bwana, na Waisraeli wakawashinda. Naye Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu akawapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase nchi ya hao wafalme ili iwe milki yao.
JOS 12:7 Hawa ndio wafalme ambao Yoshua na Waisraeli waliwashinda upande wa magharibi mwa Yordani, kuanzia Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni hadi kufikia Mlima Halaki, unaoinuka ukielekea Seiri. Yoshua alitoa nchi zao kwa makabila ya Israeli iwe urithi wao sawasawa na mgawanyiko wa makabila yao.
JOS 12:8 Nchi hizi ni: nchi ya vilima, Shefela, Araba, miteremko ya milima, jangwa, na Negebu; yaani nchi za Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
JOS 12:9 mfalme wa Yeriko; mfalme wa Ai (karibu na Betheli);
JOS 12:10 mfalme wa Yerusalemu; mfalme wa Hebroni;
JOS 12:11 mfalme wa Yarmuthi; mfalme wa Lakishi;
JOS 12:12 mfalme wa Egloni; mfalme wa Gezeri;
JOS 12:13 mfalme wa Debiri; mfalme wa Gederi;
JOS 12:14 mfalme wa Horma; mfalme wa Aradi;
JOS 12:15 mfalme wa Libna; mfalme wa Adulamu;
JOS 12:16 mfalme wa Makeda; mfalme wa Betheli;
JOS 12:17 mfalme wa Tapua; mfalme wa Heferi;
JOS 12:18 mfalme wa Afeki; mfalme wa Lasharoni;
JOS 12:19 mfalme wa Madoni; mfalme wa Hazori;
JOS 12:20 mfalme wa Shimron-Meroni; mfalme wa Akshafu;
JOS 12:21 mfalme wa Taanaki; mfalme wa Megido;
JOS 12:22 mfalme wa Kedeshi; mfalme wa Yokneamu katika Karmeli;
JOS 12:23 mfalme wa Dori (katika Nafoth-Dori); mfalme wa Goimu katika Gilgali;
JOS 12:24 mfalme wa Tirsa;
JOS 13:1 Yoshua alipokuwa mzee, umri wake ukiwa umesogea sana, Mwenyezi Mungu akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado imesalia sehemu kubwa sana ya nchi ambayo haijatwaliwa.
JOS 13:2 “Nchi iliyosalia ni hii: “maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri:
JOS 13:3 kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani, maeneo yale matano ya watawala wa Wafilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni; nchi ya Waavi
JOS 13:4 kuanzia kusini; nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori,
JOS 13:5 eneo la Wagebali; na Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi.
JOS 13:6 “Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza, niwaondoe kwa ajili ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza,
JOS 13:7 sasa basi, ligawanye eneo hili kwa yale makabila tisa na ile nusu ya kabila la Manase kuwa urithi.”
JOS 13:8 Ile nusu nyingine ya Manase, Wareubeni na Wagadi, walishapokea urithi Musa aliokuwa amewapa mashariki mwa Yordani, sawasawa na mtumishi wa Mwenyezi Mungu alivyowagawia.
JOS 13:9 Eneo lao lilienea toka Aroeri, iliyo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, kuanzia mji ulio katikati ya bonde, likijumlisha nchi ya uwanda wa juu wote wa Medeba hadi Diboni,
JOS 13:10 nayo miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, hadi mpakani mwa Waamoni.
JOS 13:11 Vilevile ilijumlisha Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaaka, mlima wote wa Hermoni na Bashani yote ikienea hadi Saleka:
JOS 13:12 yaani ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyekuwa ametawala katika Ashtarothi na Edrei, na ndiye pekee alisalia kwa Warefai. Musa alikuwa amewashinda na kuteka nchi yao.
JOS 13:13 Lakini Waisraeli hawakuwafukuza Wageshuri na Wamaaka, kwa hiyo wanaendelea kuishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo.
JOS 13:14 Lakini kwa kabila la Lawi, Musa hakupeana urithi, kwa kuwa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ndizo zilikuwa urithi wao, kama alivyowaahidi.
JOS 13:15 Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa kabila la Reubeni kufuatana na koo zao:
JOS 13:16 Eneo la Aroeri lililo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, na kuanzia mji ulio katikati ya bonde, pia uwanda wote wa juu kupita Medeba
JOS 13:17 hadi Heshboni na miji yake yote kwenye uwanda wa juu, ikijumlishwa miji ya Diboni, Bamoth-Baali, Beth-Baal-Meoni,
JOS 13:18 Yahasa, Kedemothi, Mefaathi,
JOS 13:19 Kiriathaimu, Sibma, Sereth-Shahari juu ya kilima kilicho katika bonde,
JOS 13:20 Beth-Peori, miteremko ya Pisga na Beth-Yeshimothi:
JOS 13:21 miji yote ya uwanda wa juu na eneo lote la utawala wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni. Musa alikuwa amemshinda Sihoni, pia watawala wakuu wa Wamidiani, ambao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, waliokuwa wameungana na Sihoni, ambao waliishi katika nchi ile.
JOS 13:22 Pamoja na wale waliouawa katika vita, Waisraeli walikuwa wamemuua kwa upanga Balaamu mwana wa Beori aliyekuwa mwaguzi.
JOS 13:23 Mpaka wa Wareubeni ulikuwa ni ukingo wa Mto Yordani. Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa Wareubeni kufuatana na koo zao.
JOS 13:24 Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa kabila la Gadi, kufuatana na koo zao:
JOS 13:25 Nchi ya Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Amoni iliyoenea hadi Aroeri, karibu na Raba;
JOS 13:26 na kuanzia Heshboni hadi Ramath-Mispa na Betonimu, na kutoka Mahanaimu hadi eneo la Debiri;
JOS 13:27 na katika bonde, Beth-Haramu, Beth-Nimra, Sukothi na Safoni na sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Sihoni mfalme wa Heshboni (upande wa mashariki mwa Mto Yordani, eneo inayoishia kwenye Bahari ya Kinerethi).
JOS 13:28 Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Gadi kufuatana na koo zao.
JOS 13:29 Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa nusu ya kabila la Manase, yaani kwa nusu ya jamaa ya uzao wa Manase, kufuatana na koo zao:
JOS 13:30 Eneo lililoenea kuanzia Mahanaimu, na kujumlisha Bashani yote, ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, makazi yote ya Yairi huko Bashani, miji sitini,
JOS 13:31 nusu ya Gileadi, na Ashtarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani).
JOS 13:32 Huu ndio urithi Musa alipeana alipokuwa katika tambarare za Moabu, ng’ambo ya Yordani, mashariki mwa Yeriko.
JOS 13:33 Lakini kwa kabila la Walawi, Musa hakuwapa urithi; Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.
JOS 14:1 Basi haya ndio maeneo Waisraeli waliyapokea kama urithi katika nchi ya Kanaani, ambayo kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa koo za makabila ya Israeli waliwagawia.
JOS 14:2 Urithi wao uligawanywa kwa kura kwa yale makabila tisa na nusu, kama Mwenyezi Mungu alivyoamuru Musa.
JOS 14:3 Musa alikuwa amewapa yale makabila mawili na nusu urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, lakini Walawi hawakupewa urithi miongoni mwa hao wengine,
JOS 14:4 kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa makabila mawili; Manase na Efraimu. Walawi hawakupata mgawo wa ardhi, bali walipewa miji tu kwa ajili ya kuishi, pamoja na maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao na mali zao.
JOS 14:5 Kwa hiyo Waisraeli wakagawana ile nchi, kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
JOS 14:6 Kisha watu wa Yuda wakamwendea Yoshua huko Gilgali, naye Kalebu mwana wa Yefune yule Mkenizi, akamwambia, “Unajua jambo ambalo Mwenyezi Mungu alimwambia Musa mtu wa Mungu huko Kadesh-Barnea kukuhusu wewe na mimi.
JOS 14:7 Nilikuwa na umri wa miaka arobaini, wakati Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu, aliponituma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza hiyo nchi. Nami nikamletea taarifa kama kulingana na nilivyosadiki moyoni.
JOS 14:8 Lakini ndugu zangu tuliopanda nao waliifanya mioyo ya watu iyeyuke kwa hofu. Bali mimi, nilimfuata Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kwa moyo wote.
JOS 14:9 Hivyo katika siku ile, Musa akaniapia, ‘Nchi ambayo umeikanyaga kwa miguu yako itakuwa urithi wako na wa watoto wako milele, kwa sababu umemfuata Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kwa moyo wote.’
JOS 14:10 “Sasa basi, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoahidi, ameniweka hai kwa miaka arobaini na tano tangu alipomwambia Musa jambo hili, Waisraeli walipokuwa wanazunguka jangwani. Hivyo mimi hapa leo nina umri wa miaka themanini na tano!
JOS 14:11 Bado nina nguvu kama siku ile Musa aliponituma; nina nguvu za kwenda vitani sasa kama nilivyokuwa wakati ule.
JOS 14:12 Basi nipe nchi hii ya vilima, ambayo Mwenyezi Mungu aliniahidi siku ile. Wewe mwenyewe ulisikia wakati ule kwamba Waanaki walikuwa huko na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye ngome, lakini, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, nitawafukuza watoke huko kama vile alivyonena.”
JOS 14:13 Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune, na akampa Hebroni kama urithi wake.
JOS 14:14 Hivyo Hebroni imekuwa mali ya Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi tangu wakati ule, kwa sababu alimwandama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wote.
JOS 14:15 (Hebroni uliitwa Kiriath-Arba hapo mwanzo, kuitanishwa na Arba aliyekuwa mtu mkuu kupita wote miongoni mwa Waanaki.) Kisha nchi ikawa na amani bila vita.
JOS 15:1 Mgawo kwa kabila la Yuda, ulienea kufuatana na koo zao, ukishuka kufikia eneo la Edomu, hadi Jangwa la Sini mwisho kabisa upande wa kusini.
JOS 15:2 Mpaka wao wa kusini ulianzia ghuba iliyo kwenye ncha ya kusini mwa Bahari ya Chumvi,
JOS 15:3 ukakatiza kusini mwa Akrabimu, ukaendelea hadi Sini, kisha ukaenda hadi kusini mwa Kadesh-Barnea. Tena ukapitia Hesroni, ukapanda hadi Adari, na ukapinda hadi Karka.
JOS 15:4 Kisha ukaendelea hadi Azmoni, na kuunganika na Kijito cha Misri, na kuishia baharini. Huu ndio mpaka wao wa upande wa kusini.
JOS 15:5 Mpaka wa upande wa mashariki ni Bahari ya Chumvi ukienea mahali Mto Yordani unapoingilia. Mpaka wa upande wa kaskazini ulianzia ghuba ya bahari mahali Mto Yordani unapoingilia,
JOS 15:6 ukapanda hadi Beth-Hogla, na kuendelea kaskazini mwa Beth-Araba hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni.
JOS 15:7 Kisha mpaka ulipanda hadi Debiri kutoka Bonde la Akori, na kugeuka kaskazini hadi Gilgali inayotazamana na miteremko ya Adumimu, kusini mwa bonde. Ukaendelea sambamba hadi maji ya En-Shemeshi na kutokeza huko En-Rogeli.
JOS 15:8 Kisha ukapanda kwa kufuata Bonde la Ben-Hinomu sambamba na mteremko wa kusini wa mji mkubwa wa Wayebusi (yaani Yerusalemu). Kutoka hapo ukapanda juu ya kilima magharibi mwa Bonde la Hinomu mwisho wa ncha ya kaskazini mwa Bonde la Warefai.
JOS 15:9 Kutoka juu ya kilima, mpaka ule ukaendelea hadi kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa, ukatokea kwenye miji ya Mlima Efroni na kuteremka kuelekea Baala (yaani Kiriath-Yearimu).
JOS 15:10 Kisha ukapinda upande wa magharibi kutoka Baala hadi Mlima Seiri, ukafuatia sambamba mteremko wa kaskazini mwa Mlima Yearimu (yaani Kesaloni), ukashuka hadi Beth-Shemeshi, na kukatiza hadi Timna.
JOS 15:11 Ukaelekea hadi mteremko wa kaskazini mwa Ekroni, ukageuka kuelekea Shikeroni, ukapita hadi Mlima Baala na kufika Yabineeli. Mpaka ule ukaishia baharini.
JOS 15:12 Mpaka wa magharibi ni pwani ya Bahari Kuu.
JOS 15:13 Kwa kufuata maagizo ya Mwenyezi Mungu kwake, Yoshua alimpa Kalebu mwana wa Yefune sehemu katika Yuda: Kiriath-Arba, yaani Hebroni. (Arba alikuwa baba wa zamani wa Anaki.)
JOS 15:14 Kutoka Hebroni, Kalebu alifukuza hao Waanaki watatu: Sheshai, Ahimani na Talmai, wana wa Anaki.
JOS 15:15 Kutoka hapo akaondoka kupigana dhidi ya watu walioishi Debiri (mji wa Debiri hapo uliitwa Kiriath-Seferi).
JOS 15:16 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.”
JOS 15:17 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu yake Kalebu, akauteka; hivyo Kalebu akamtoa Aksa binti yake, akaolewa naye.
JOS 15:18 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”
JOS 15:19 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Basi Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
JOS 15:20 Huu ndio urithi wa kabila la Yuda, kufuatana na koo zao:
JOS 15:21 Miji ya kusini kabisa ya kabila la Yuda katika Negebu kuelekea mpaka wa Edomu ilikuwa: Kabseeli, Ederi, Yaguri,
JOS 15:22 Kina, Dimona, Adada,
JOS 15:23 Kedeshi, Hazori, Ithnani,
JOS 15:24 Zifu, Telemu, Bealothi,
JOS 15:25 Hazor-Hadata, Kerioth-Hezroni (yaani Hazori),
JOS 15:26 Amamu, Shema, Molada,
JOS 15:27 Hasar-Gada, Heshmoni, Beth-Peleti,
JOS 15:28 Hasar-Shuali, Beer-Sheba, Biziothia,
JOS 15:29 Baala, Iyimu, Esemu,
JOS 15:30 Eltoladi, Kesili, Horma,
JOS 15:31 Siklagi, Madmana, Sansana,
JOS 15:32 Lebaothi, Shilhimu, Aini na Rimoni; hiyo yote ni miji ishirini na tisa, pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:33 Katika Shefela: Eshtaoli, Sora, Ashna,
JOS 15:34 Zanoa, En-Ganimu, Tapua, Enamu,
JOS 15:35 Yarmuthi, Adulamu, Soko, Azeka,
JOS 15:36 Shaaraimu, Adithaimu na Gedera (au Gederothaimu); yote ni miji kumi na nne, pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:37 Senani, Hadasha, Migdal-Gadi,
JOS 15:38 Dileani, Mispa, Yoktheeli,
JOS 15:39 Lakishi, Boskathi, Egloni,
JOS 15:40 Kaboni, Lamasi, Kitlishi,
JOS 15:41 Gederothi, Beth-Dagoni, Naama na Makeda; yote ni miji kumi na sita pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:42 Libna, Etheri, Ashani,
JOS 15:43 Yifta, Ashna, Nesibu,
JOS 15:44 Keila, Akzibu na Maresha; yote ni miji tisa pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:45 Ekroni, pamoja na makazi yake na vijiji vyake;
JOS 15:46 magharibi mwa Ekroni, maeneo yote yaliyokuwa karibu na Ashdodi, pamoja na vijiji vyake;
JOS 15:47 Ashdodi, makazi yake na vijiji vyake, na Gaza, makazi yake na vijiji vyake, hadi kufikia Kijito cha Misri na Pwani ya Bahari Kuu.
JOS 15:48 Katika nchi ya vilima: Shamiri, Yatiri, Soko,
JOS 15:49 Dana, Kiriath-Sana (yaani Debiri),
JOS 15:50 Anabu, Eshtemoa, Animu,
JOS 15:51 Gosheni, Holoni na Gilo; miji kumi na moja pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:52 Arabu, Duma, Ashani,
JOS 15:53 Yanimu, Beth-Tapua, Afeka,
JOS 15:54 Humta, Kiriath-Arba (yaani Hebroni), na Siori; miji tisa pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:55 Maoni, Karmeli, Zifu, Yuta,
JOS 15:56 Yezreeli, Yokdeamu, Zanoa,
JOS 15:57 Kaini, Gibea na Timna; miji kumi pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:58 Halhuli, Beth-Suri, Gedori,
JOS 15:59 Maarathi, Beth-Anothi na Eltekoni; miji sita pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:60 Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu) na Raba; miji miwili pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:61 Huko jangwani: Beth-Araba, Midini, Sekaka,
JOS 15:62 Nibshani, Mji wa Chumvi, na En-Gedi; miji sita pamoja na vijiji vyake.
JOS 15:63 Yuda hakuweza kuwafukuza Wayebusi, walioishi Yerusalemu; hadi leo Wayebusi huishi huko pamoja na watu wa Yuda.
JOS 16:1 Mgawanyo wa Yusufu ulianzia Yordani ya Yeriko, mashariki mwa miji ya Yeriko na kutoka hapo ulipanda kupitia jangwani na kuingia katika nchi ya vilima ya Betheli.
JOS 16:2 Ukaendelea kutoka Betheli (ndiyo Luzu), ukavuka kuingia eneo la Waarki huko Atarothi,
JOS 16:3 ukateremkia kuelekea magharibi hadi eneo la Wayafleti ukienea hadi eneo la Beth-Horoni ya Chini hadi Gezeri, ukiishia baharini.
JOS 16:4 Kwa hiyo Manase na Efraimu, wazao wa Yusufu, walipokea urithi wao.
JOS 16:5 Hili ndilo lilikuwa eneo la Efraimu, kufuatana na koo zao: Mpaka wa urithi wao ulianzia Ataroth-Adari upande wa mashariki hadi Beth-Horoni ya Juu,
JOS 16:6 na kuendelea mpaka baharini. Kutoka Mikmeta upande wa kaskazini ulipinda kuelekea mashariki hadi Taanath-Shilo, ukiupita hadi Yanoa upande wa mashariki.
JOS 16:7 Kisha uliteremka kutoka Yanoa hadi Atarothi na Naara, ukagusa Yeriko na kutokea katika Mto Yordani.
JOS 16:8 Kutoka Tapua, mpaka ulienda magharibi hadi Bonde la Kana na kuishia baharini. Huu ulikuwa ndio urithi wa kabila la Waefraimu, kufuatana na koo zao.
JOS 16:9 Pia ulijumuisha miji yote na vijiji vyake ambavyo vilitengwa kwa ajili ya Waefraimu ndani ya urithi wa kabila la Manase.
JOS 16:10 Hawakuwatoa Wakanaani walioishi Gezeri; hadi leo Wakanaani wanaishi miongoni mwa watu wa Efraimu, lakini wanatumikishwa kwa kazi ngumu.
JOS 17:1 Huu ndio mgawo wa kabila la Manase, mzaliwa wa kwanza wa Yusufu. Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase, aliyekuwa baba wa Wagileadi, alipewa Gileadi na Bashani kwa sababu alikuwa hodari katika vita.
JOS 17:2 Kwa hiyo mgawo huu ulikuwa kwa ajili ya watu wa Manase waliokuwa wamebaki, ambao ni koo za Abiezeri, Heleki, Asirieli, Shekemu, Heferi na Shemida. Hawa ndio wanaume wale wengine wa uzao wa Manase mwana wa Yusufu kwa koo zao.
JOS 17:3 Basi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana wa kiume ila binti tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa.
JOS 17:4 Wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “Mwenyezi Mungu alimwagiza Musa atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo la Mwenyezi Mungu.
JOS 17:5 Zaidi ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani, fungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi,
JOS 17:6 kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi pamoja na wana wa kiume. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wazao wa Manase waliobaki.
JOS 17:7 Eneo la Manase lilienea kuanzia Asheri hadi Mikmeta mashariki mwa Shekemu. Mpaka ule ulielekea upande wa kusini kutoka pale kujumuisha watu walioishi En-Tapua.
JOS 17:8 (Nchi ya Tapua ilikuwa mali ya Manase, lakini Tapua yenyewe iliyo mpakani mwa nchi ya Manase ilikuwa ya Waefraimu.)
JOS 17:9 Kisha mpaka ule uliendelea kuelekea kusini hadi Bonde la Kana. Kulikuwa na miji ya Efraimu iliyokuwa miongoni mwa miji ya Manase, lakini mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa lile bonde, na kuishia kwenye bahari.
JOS 17:10 Nchi ya kusini ilikuwa ya Efraimu, na ile iliyokuwa upande wa kaskazini ilikuwa ya Manase. Eneo la Manase lilifika bahari na likapakana na Asheri upande wa kaskazini, na Isakari upande wa mashariki.
JOS 17:11 Katika Isakari na Asheri Manase alikuwa na miji pia: Beth-Shani, Ibleamu na watu wa Dori, Endori, Taanaki na Megido, pamoja na makazi yote ya miji hiyo (ya tatu katika orodha ni Nafothi).
JOS 17:12 Lakini Wamanase hawakuweza kuimiliki miji hii, kwa kuwa Wakanaani walikazana kuishi katika maeneo hayo.
JOS 17:13 Hata hivyo, Waisraeli walivyoendelea kupata nguvu waliwatumikisha Wakanaani na kuwatia katika kazi za kulazimishwa, lakini hawakuwafukuza kabisa.
JOS 17:14 Wana wa Yusufu wakamwambia Yoshua, “Kwa nini umetupatia sisi mgawo mmoja tu na sehemu moja tu kuwa urithi? Sisi tu watu wengi sana, na Mwenyezi Mungu ametubariki kwa wingi.”
JOS 17:15 Yoshua akajibu, “Kama ninyi ni wengi sana, na kama nchi ya vilima ya Efraimu ni ndogo sana kwenu, pandeni msituni mkafyeke eneo kwa ajili yenu wenyewe huko kwenye nchi ya Waperizi na Warefai.”
JOS 17:16 Wana wa Yusufu wakajibu, “Hiyo nchi ya vilima haitutoshi, nao Wakanaani wote wanaoishi katika tambarare wana magari ya vita ya chuma, yaani wale walio Beth-Shani na makazi yake, na wale walio katika Bonde la Yezreeli.”
JOS 17:17 Lakini Yoshua akanena na nyumba ya Yusufu, yaani Efraimu na Manase: “Ninyi ni wengi sana na wenye nguvu sana. Hamtakuwa na mgawo mmoja tu,
JOS 17:18 bali pia nchi hii ya vilima yenye msitu. Ifyekeni, nayo mipaka yake itakuwa yenu umbali mtakaoweza kufika. Ingawa Wakanaani wana magari ya vita ya chuma, na wana nguvu, mtaweza kuwafukuza humo.”
JOS 18:1 Kusanyiko lote la Waisraeli wakakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema la Kukutania. Nchi ikawa chini ya utawala wao,
JOS 18:2 lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao.
JOS 18:3 Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, amewapa?
JOS 18:4 Chagueni watu watatu kutoka kila kabila. Nitawatuma kukagua nchi hiyo na kuandika taarifa kuhusu mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Kisha watarudi kwangu.
JOS 18:5 Mtaigawanya hiyo nchi katika sehemu saba. Yuda atabaki katika eneo lake upande wa kusini na nyumba ya Yusufu katika nchi yake upande wa kaskazini.
JOS 18:6 Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, yaleteni kwangu, nami nitawapigia kura mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
JOS 18:7 Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, kwa maana huduma ya ukuhani kwa Mwenyezi Mungu ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa.”
JOS 18:8 Watu hao walipokuwa wanaondoka kwenda kuikagua hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo yake. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za Mwenyezi Mungu.”
JOS 18:9 Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi. Wakaandika maelezo yake kwenye kitabu, mji kwa mji, katika sehemu saba na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo.
JOS 18:10 Basi Yoshua akawapigia kura huko Shilo mbele za Mwenyezi Mungu, na hapo akawagawia Waisraeli nchi kulingana na makabila yao.
JOS 18:11 Kura ya kwanza iliangukia kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao. Eneo lao walilogawiwa lilikuwa kati ya kabila la Yuda na la Yusufu.
JOS 18:12 Upande wa kaskazini, mpaka wao ulianzia pale Yordani, kupitia kaskazini mwa mteremko wa Yeriko, na kuendelea magharibi kuingia katika nchi ya vilima, ukitokea kwenye jangwa la Beth-Aveni.
JOS 18:13 Kutoka hapo ulikatiza kwenye mteremko wa kusini mwa Luzu (yaani Betheli) na kushuka hadi Ataroth-Adari katika kilima kusini mwa Beth-Horoni ya Chini.
JOS 18:14 Kutoka kilima kinachotazamana na Beth-Horoni upande wa kusini mpaka ule ukazunguka kusini kufuatia upande wa magharibi, na ukatokezea Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu), mji wa watu wa Yuda. Huu ndio uliokuwa upande wa magharibi.
JOS 18:15 Upande wa kusini mpaka ulianzia kwenye viunga vya Kiriath-Yearimu kwa upande wa magharibi, nao ukatokeza kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa.
JOS 18:16 Mpaka ukateremka hadi shefela inayotazamana na Bonde la Ben-Hinomu, kaskazini mwa Bonde la Warefai. Ukaendelea chini kwenye Bonde la Hinomu sambamba na mteremko wa kusini mwa mji mkubwa wa Wayebusi na kisha hadi En-Rogeli.
JOS 18:17 Kisha ukapinda kuelekea kaskazini, ukaenda hadi En-Shemeshi na kuendelea hadi Gelilothi, inayotazamana na Njia ya Adumimu, ukateremka hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni.
JOS 18:18 Ukaendelea upande wa mteremko wa kaskazini wa Beth-Araba ukateremka hadi Araba.
JOS 18:19 Kisha ukaenda mpaka kwenye mteremko wa kaskazini wa Beth-Hogla na kujitokeza kwenye ghuba ya kaskazini mwa Bahari ya Chumvi, kwenye maingilio ya Yordani upande wa kusini. Huo ulikuwa mpaka wa kusini.
JOS 18:20 Nayo Yordani ikawa ndio mpaka wa upande wa mashariki.
JOS 18:21 Kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao, lilikuwa na miji ifuatayo: Yeriko, Beth-Hogla, Emeki-Kesisi,
JOS 18:22 Beth-Araba, Semaraimu, Betheli,
JOS 18:23 Avimu, Para na Ofra,
JOS 18:24 Kefar-Amoni, Ofni, na Geba; miji kumi na mbili pamoja na vijiji vyake.
JOS 18:25 Gibeoni, Rama na Beerothi,
JOS 18:26 Mispa, Kefira, Moza,
JOS 18:27 Rekemu, Irpeeli, Tarala,
JOS 18:28 Zela, Elefu, mji wa Wayebusi (yaani Yerusalemu), Gibea na Kiriathi; miji kumi na nne, pamoja na vijiji vyake.
JOS 19:1 Kura ya pili ikaangukia kabila la Simeoni, kufuatana na koo zao. Urithi wao ulikuwa ndani ya eneo la Yuda.
JOS 19:2 Ulijumuisha: Beer-Sheba (au Sheba), Molada,
JOS 19:3 Hasar-Shuali, Bala, Esemu,
JOS 19:4 Eltoladi, Bethuli, Horma,
JOS 19:5 Siklagi, Beth-Markabothi, Hasar-Susa,
JOS 19:6 Beth-Lebaothi na Sharuheni; hii ilikuwa miji kumi na tatu pamoja na vijiji vyake.
JOS 19:7 Pia Aini, Rimoni, Etheri, na Ashani; hii ilikuwa miji minne na vijiji vyake,
JOS 19:8 pamoja na vijiji vyote vinavyoizunguka miji hii hadi Baalath-Beeri (ambayo ndiyo Rama iliyo katika Negebu).
JOS 19:9 Urithi wa Wasimeoni ulitolewa kutoka fungu la Yuda, kwa kuwa fungu la Yuda lilikuwa kubwa kuliko walivyohitaji. Hivyo kabila la Simeoni lilipewa urithi wao ndani ya eneo la Yuda.
JOS 19:10 Kura ya tatu ikaangukia kabila la Zabuloni, kufuatana na koo zao: Mpaka wa urithi wao uliendelea hadi Saridi.
JOS 19:11 Kuelekea upande wa magharibi ukafika Marala, ukagusa Dabeshethi, na kuendelea hadi kwenye bonde karibu na Yokneamu.
JOS 19:12 Ukageuka mashariki, kuanzia Saridi kuelekea mawio ya jua hadi kwenye nchi ya Kisiloth-Tabori, na kwenda hadi Daberathi, kupanda Yafia.
JOS 19:13 Kisha ukaendelea mashariki hadi Gath-Heferi na kufika Eth-Kasini, ukatokea Rimoni na kugeuka kuelekea Nea.
JOS 19:14 Huko mpaka ukazungukia upande wa kaskazini hadi Hanathoni na kuishia katika Bonde la Ifta-Eli.
JOS 19:15 Miji mingine iliyojumuishwa ni Katathi, Nahalali, Shimroni, Idala na Bethlehemu. Kulikuwa na miji kumi na mbili pamoja na vijiji vyake.
JOS 19:16 Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa Zabuloni, kufuatana na koo zao.
JOS 19:17 Kura ya nne ikaangukia kabila la Isakari, kufuatana na koo zao.
JOS 19:18 Eneo lao lilijumuisha: Yezreeli, Kesulothi, Shunemu,
JOS 19:19 Hafaraimu, Shioni, Anaharathi,
JOS 19:20 Rabithi, Kishioni, Ebesi,
JOS 19:21 Remethi, En-Ganimu, En-Hada na Beth-Pasesi.
JOS 19:22 Mpaka ule ukagusa Tabori, Shahasuma na Beth-Shemeshi, na ukaishia kwenye Yordani. Ilikuwa miji kumi na sita, pamoja na vijiji vyake.
JOS 19:23 Miji hii pamoja na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Isakari, kufuatana na koo zao.
JOS 19:24 Kura ya tano ikaangukia kabila la Asheri, kufuatana na koo zao.
JOS 19:25 Eneo lao lilijumuisha: Helkathi, Hali, Beteni, Akshafu,
JOS 19:26 Alameleki, Amadi na Mishali. Upande wa magharibi mpaka uligusa Karmeli na Shihor-Libnathi.
JOS 19:27 Tena ukageuka mashariki kuelekea Beth-Dagoni, ukagusa Zabuloni na Bonde la Ifta-Eli, ukaenda upande wa kaskazini hadi Beth-Emeki na Neyeli, ukipitia Kabul upande wa kushoto.
JOS 19:28 Ukaendelea hadi Abdoni, Rehobu, Hamoni na Kana, na kufika Sidoni Kuu.
JOS 19:29 Mpaka huo ukageukia nyuma kuelekea Rama na kwenda hadi kwenye mji wenye ngome wa Tiro, ukageuka kuelekea Hosa na kutokeza baharini katika eneo la Akzibu,
JOS 19:30 Uma, Afeki na Rehobu. Ilikuwa miji ishirini na mbili, pamoja na vijiji vyake.
JOS 19:31 Miji hii pamoja na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Asheri, kufuatana na koo zao.
JOS 19:32 Kura ya sita ikaangukia kabila la Naftali, kufuatana na koo zao:
JOS 19:33 Mpaka wao uliendelea kutoka Helefi na kwenye mwaloni ulio Saananimu, ukipitia Adami-Nekebu na Yabineeli hadi Lakumu, na kuishia katika Mto Yordani.
JOS 19:34 Mpaka ukaendelea magharibi kupitia Aznoth-Tabori na kutokea Hukoki. Ukagusa Zabuloni upande wa kusini, Asheri upande wa magharibi, na Yordani upande wa mashariki.
JOS 19:35 Miji yenye ngome ilikuwa Sidimu, Seri, Hamathi, Rakathi, Kinerethi,
JOS 19:36 Adama, Rama, Hazori,
JOS 19:37 Kedeshi, Edrei, na En-Hasori,
JOS 19:38 Ironi, Migdal-Eli, Horemu, Beth-Anathi na Beth-Shemeshi. Kulikuwa na miji kumi na tisa na vijiji vyake.
JOS 19:39 Miji hiyo pamoja na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Naftali, kufuatana na koo zao.
JOS 19:40 Kura ya saba ikaangukia kabila la Dani, kufuatana na koo zao.
JOS 19:41 Eneo la urithi wao lilijumuisha: Sora, Eshtaoli, Iri-Shemeshi,
JOS 19:42 Shaalabini, Aiyaloni, Ithla,
JOS 19:43 Eloni, Timna, Ekroni,
JOS 19:44 Elteke, Gibethoni, Baalathi,
JOS 19:45 Yehudi, Bene-Beraki, Gath-Rimoni,
JOS 19:46 Me-Yarkoni na Rakoni, pamoja na eneo linalotazamana na Yafa.
JOS 19:47 (Lakini Wadani walipata shida kulimiliki eneo lao; kwa hiyo walipanda kuishambulia Leshemu, wakaitwaa, wakawaua watu wake kwa upanga na kuukalia. Walikaa Leshemu na kuuita Dani kufuatana na jina la baba yao.)
JOS 19:48 Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Dani, kufuatana na koo zao.
JOS 19:49 Walipomaliza kuigawa nchi kulingana na sehemu zilizowaangukia, Waisraeli walimpa Yoshua mwana wa Nuni urithi kati yao,
JOS 19:50 kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameamuru. Walimpa mji alioutaka, ambao ni Timnath-Sera ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu. Naye akajenga mji, akakaa huko.
JOS 19:51 Haya ndio maeneo ambayo kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa koo za makabila ya Israeli waliyagawanya kwa kura huko Shilo mbele za Mwenyezi Mungu, penye ingilio la Hema la Kukutania. Hivyo wakamaliza kuigawanya nchi.
JOS 20:1 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua,
JOS 20:2 “Waambie Waisraeli, watenge miji ya kukimbilia, kama nilivyokuagiza kupitia Musa,
JOS 20:3 ili mtu yeyote atakayemuua mtu kwa bahati mbaya na pasipo kukusudia aweze kukimbilia huko na kujiepusha na mlipiza kisasi wa damu.
JOS 20:4 “Anapokimbilia mojawapo ya hii miji, atasimama kwenye maingilio ya lango la mji mkuu na kueleza wazee wa mji kuhusu shauri lake. Kisha watampokea katika mji wao na kumpa mahali pa kuishi nao.
JOS 20:5 Kama mlipiza kisasi wa damu akimfuatilia, wasimkabidhi yule mshtakiwa, kwa sababu alimuua jirani yake bila kukusudia, na bila kuwa na nia ya kudhuru.
JOS 20:6 Huyu aliyeua atakaa kwenye mji huo hadi awe amesimama kukabili mashtaka yake mbele ya kusanyiko na hadi kuhani mkuu anayehudumu kwa wakati huo atakapokufa. Ndipo atakapoweza kurudi nyumbani mwake katika mji ambao aliukimbia.”
JOS 20:7 Basi wakatenga Kedeshi katika Galilaya kwenye nchi ya vilima ya Naftali, Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-Arba (yaani Hebroni) kwenye nchi ya vilima ya Yuda.
JOS 20:8 Katika upande wa mashariki mwa Yordani (ng’ambo ya Yeriko) wakatenga Bezeri katika jangwa katika uwanda wa juu katika kabila la Reubeni, Ramothi katika Gileadi katika kabila la Gadi, na Golani huko Bashani katika kabila la Manase.
JOS 20:9 Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote aishiye miongoni mwao aliyemuua mtu kwa bahati mbaya, angeweza kukimbilia katika miji hiyo iliyotengwa na asiuawe na mlipiza kisasi wa damu kabla hajasimama kukabili mashtaka mbele ya kusanyiko.
JOS 21:1 Basi viongozi wa jamaa ya Walawi, wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa nyingine za makabila ya Israeli
JOS 21:2 huko Shilo katika Kanaani na kuwaambia, “Mwenyezi Mungu aliamuru kupitia Musa kuwa mtupe miji ya kuishi yenye maeneo ya malisho kwa mifugo yetu.”
JOS 21:3 Hivyo kama vile Mwenyezi Mungu alivyoamuru, Waisraeli wakawapa Walawi miji ifuatayo, na maeneo ya malisho ya kila mji kutoka urithi wao wenyewe.
JOS 21:4 Kura ya kwanza ikaangukia Wakohathi, kufuatana na koo zao. Walawi waliokuwa wazao wa kuhani Haruni walipewa miji kumi na tatu kutoka makabila ya Yuda, Simeoni na Benyamini.
JOS 21:5 Wazao wengine waliobaki wa Wakohathi walipewa miji kumi kutoka koo za makabila ya Efraimu, Dani na nusu ya Manase.
JOS 21:6 Wazao wa Gershoni walipewa miji kumi na tatu kutoka koo za makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na nusu ya Manase huko Bashani.
JOS 21:7 Wazao wa Merari, kufuatana na koo zao, walipewa miji kumi na mbili kutoka makabila ya Reubeni, Gadi na Zabuloni.
JOS 21:8 Kwa hiyo Waisraeli wakawapa Walawi miji hii na maeneo ya malisho ya kila mji, kama Mwenyezi Mungu alivyoamuru kupitia kwa Musa.
JOS 21:9 Kutoka makabila ya Yuda na Simeoni waligawa miji ifuatayo kwa majina
JOS 21:10 (miji hii walipewa wazao wa Haruni ambao walitokana na koo za Wakohathi wa Walawi, kwa sababu kura ya kwanza iliwaangukia):
JOS 21:11 Waliwapa Kiriath-Arba (yaani Hebroni), pamoja na eneo lake la malisho lililouzunguka, katika nchi ya vilima ya Yuda. (Arba alikuwa baba wa Anaki.)
JOS 21:12 Lakini mashamba na vijiji vilivyouzunguka mji walikuwa wamempa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake.
JOS 21:13 Kwa hiyo wazao wa kuhani Haruni wakapewa Hebroni (mji mkuu wa makimbilio kwa ajili ya yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji), Libna,
JOS 21:14 Yatiri, Eshtemoa,
JOS 21:15 Holoni, Debiri,
JOS 21:16 Aini, Yuta na Beth-Shemeshi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji tisa kutoka kwa makabila haya mawili.
JOS 21:17 Kutoka kabila la Benyamini wakawapa Gibeoni, Geba,
JOS 21:18 Anathothi na Almoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
JOS 21:19 Miji yote waliyopewa makuhani, wazao wa Haruni, ilikuwa kumi na tatu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
JOS 21:20 Koo nyingine za Wakohathi, ambao pia ni Walawi, walipewa miji kutoka kabila la Efraimu:
JOS 21:21 Katika nchi ya vilima ya Efraimu, walipewa: Shekemu (mji wa makimbilio kwa yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji) na Gezeri,
JOS 21:22 Kibsaimu na Beth-Horoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
JOS 21:23 Pia kutoka kabila la Dani, wakapokea: Elteke, Gibethoni,
JOS 21:24 Aiyaloni na Gath-Rimoni pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
JOS 21:25 Kutoka nusu ya kabila la Manase, wakapokea: Taanaki na Gath-Rimoni pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji miwili.
JOS 21:26 Miji hii kumi, na maeneo ya malisho ya kila mji, ilipewa koo za Wakohathi zilizobaki.
JOS 21:27 Koo za Walawi za Wagershoni walipewa: kutoka nusu ya kabila la Manase: Golani katika Bashani (mji wa makimbilio kwa yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji) na Beeshtera, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji miwili;
JOS 21:28 kutoka kabila la Isakari, walipewa: Kishioni, Daberathi,
JOS 21:29 Yarmuthi na En-Ganimu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne;
JOS 21:30 kutoka kabila la Asheri, walipewa: Mishali, Abdoni,
JOS 21:31 Helkathi na Rehobu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
JOS 21:32 Kutoka kabila la Naftali, walipewa: Kedeshi katika Galilaya (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji), Hamoth-Dori na Kartani, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji mitano.
JOS 21:33 Miji yote ya koo za Wagershoni ilikuwa kumi na tatu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
JOS 21:34 Koo za Wamerari (Walawi waliobaki) walipewa: kutoka kabila la Zabuloni: Yokneamu, Karta,
JOS 21:35 Dimna na Nahalali, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne;
JOS 21:36 kutoka kabila la Reubeni, walipewa: Bezeri, Yahasa,
JOS 21:37 Kedemothi na Mefaathi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne;
JOS 21:38 kutoka kabila la Gadi, walipewa: Ramothi katika Gileadi (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa ajili ya mauaji), Mahanaimu,
JOS 21:39 Heshboni na Yazeri, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
JOS 21:40 Miji yote waliyopewa koo za Wamerari, waliokuwa mabaki ya Walawi, ilikuwa ni kumi na mbili.
JOS 21:41 Miji yote ya Walawi katika eneo lililomilikiwa na Waisraeli ilikuwa arobaini na nane, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
JOS 21:42 Kila mji kati ya miji hii ulikuwa na maeneo ya malisho kuuzunguka; ndivyo ilivyokuwa kwa miji hii yote.
JOS 21:43 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawapa Israeli nchi yote aliyokuwa ameapa kuwapa baba zao, nao wakaimiliki na kukaa humo.
JOS 21:44 Mwenyezi Mungu akawapa pumziko kila upande, kama vile alivyokuwa amewaapia baba zao, hakuna hata mmoja wa adui zao aliyeweza kusimama mbele yao, Mwenyezi Mungu akawatia adui zao wote mikononi mwao.
JOS 21:45 Hakuna hata mojawapo ya ahadi nzuri ya Mwenyezi Mungu kwa nyumba ya Israeli ambayo haikutimia; kila moja ilitimia.
JOS 22:1 Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase,
JOS 22:2 naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru.
JOS 22:3 Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyowapa.
JOS 22:4 Sasa kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu pumziko kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ambayo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa ng’ambo ya Yordani.
JOS 22:5 Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria ambazo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa: yaani kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.”
JOS 22:6 Ndipo Yoshua akawabariki na kuwaaga waende zao, nao wakaenda nyumbani kwao.
JOS 22:7 (Kwa nusu ya kabila la Manase, Musa alikuwa amewapa eneo katika Bashani na ile nusu nyingine ya hilo kabila Yoshua aliwapa eneo upande wa magharibi mwa Yordani pamoja na ndugu zao.) Yoshua alipowaaga waende zao nyumbani, aliwabariki,
JOS 22:8 akisema, “Rudini nyumbani kwenu na utajiri wenu mwingi, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia mavazi mengi; nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.”
JOS 22:9 Kwa hiyo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakawaacha Waisraeli huko Shilo katika nchi ya Kanaani ili kurudi Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoipata sawasawa na agizo la Mwenyezi Mungu kupitia Musa.
JOS 22:10 Walipofika Gelilothi karibu na Yordani, katika nchi ya Kanaani, Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakajenga madhabahu ya fahari kubwa huko kando ya Yordani.
JOS 22:11 Waisraeli hao wengine waliposikia kwamba Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walikuwa wamejenga madhabahu kwenye mpaka wa Kanaani huko Gelilothi karibu na Yordani kwenye upande wa Israeli,
JOS 22:12 Waisraeli hao wengine walikusanyika huko Shilo ili wapigane nao.
JOS 22:13 Kwa hiyo Waisraeli wengine wakamtuma Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, aende katika nchi ya Gileadi kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase.
JOS 22:14 Wakatuma viongozi kumi pamoja naye, mmoja kutoka kwa kila kabila la Israeli, kila mmoja akiwa kiongozi katika jamaa miongoni mwa koo za Israeli.
JOS 22:15 Walipofika Gileadi, kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, wakawaambia:
JOS 22:16 “Kusanyiko lote la Mwenyezi Mungu wasema hivi: ‘Je, mmewezaje kuacha kumwamini Mungu wa Israeli jinsi hii? Mmewezaje kumwacha Mwenyezi Mungu na kujijengea madhabahu dhidi yake na kumwasi?
JOS 22:17 Je, dhambi ya Peori haikutosha? Hata ingawa kulikuja tauni juu ya kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hadi leo hatujatakasika kutokana na dhambi hiyo!
JOS 22:18 Je, sasa ndiyo mnamwacha Mwenyezi Mungu? “ ‘Mkimwasi Mwenyezi Mungu leo, kesho atawakasirikia kusanyiko lote la Israeli.
JOS 22:19 Ikiwa nchi mnayomiliki imenajisika, vukeni mje katika nchi ya Mwenyezi Mungu, mahali Maskani ya Mwenyezi Mungu ilipo, nanyi mkajitwalie sehemu miongoni mwetu, lakini msije mkaasi dhidi ya Mwenyezi Mungu wala dhidi yetu sisi kwa kujijengea madhabahu, isipokuwa madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
JOS 22:20 Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu kwa vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, je, ghadhabu haikuwapata kusanyiko lote la Israeli? Si yeye pekee aliyekufa kwa ajili ya dhambi yake.’ ”
JOS 22:21 Ndipo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walipowajibu viongozi wa koo za Israeli, wakisema:
JOS 22:22 “Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Mwenyezi Mungu! Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Mwenyezi Mungu! Yeye anajua! Israeli na wajue! Kama huu umekuwa ni uasi au kukosa utii kwa Mwenyezi Mungu, msituache hai siku hii ya leo.
JOS 22:23 Kama tumejijengea madhabahu yetu wenyewe ili kumwacha Mwenyezi Mungu, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, au kutoa sadaka za amani juu yake, Mwenyezi Mungu mwenyewe na atupatilize leo.
JOS 22:24 “Sivyo! Tulifanya hivyo kwa hofu kwamba siku zijazo wazao wenu wanaweza wakawaambia wazao wetu, ‘Mna uhusiano gani na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli?
JOS 22:25 Mwenyezi Mungu ameifanya Yordani kuwa mpaka kati yetu na ninyi, ninyi Wareubeni na Wagadi! Hamna fungu kwa Mwenyezi Mungu.’ Kwa hiyo wazao wenu wanaweza wakawasababisha wazao wetu wakaacha kumcha Mwenyezi Mungu.
JOS 22:26 “Hii ndiyo sababu tulisema, ‘Tujiweke tayari na tujenge madhabahu, lakini si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa au dhabihu.’
JOS 22:27 Badala yake, itakuwa ni ushahidi kati yetu na ninyi na vizazi vijavyo, kwamba tutamwabudu Mwenyezi Mungu katika mahali patakatifu pake pamoja na sadaka zetu za kuteketezwa, dhabihu na sadaka za amani. Ndipo katika siku zijazo, wazao wenu hawataweza kuwaambia wazao wetu, ‘Ninyi hamna fungu katika Mwenyezi Mungu.’
JOS 22:28 “Nasi tulisema, ‘Wakati wowote wakituambia hilo, au kuwaambia uzao wetu, tutawajibu hivi: Angalieni nakala hii ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, ambayo baba zetu waliijenga, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu, bali kama ushahidi kati yetu na ninyi.’
JOS 22:29 “Hili jambo la kumwasi Mwenyezi Mungu na kumwacha siku hii ya leo kwa kujenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na dhabihu, isipokuwa madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, iliyo mbele ya Maskani yake na liwe mbali nasi.”
JOS 22:30 Kuhani Finehasi na viongozi wa kusanyiko, hao wakuu wa koo za Israeli, waliposikia hayo waliyosema Wareubeni, Wagadi na Manase, wakaridhika.
JOS 22:31 Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akawaambia Wareubeni, Wagadi na Manase, “Leo tunajua kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi, kwa sababu hamkukosa uaminifu kwa Mwenyezi Mungu katika jambo hili. Sasa mmewaokoa Waisraeli kutoka kwa mkono wa Mwenyezi Mungu.”
JOS 22:32 Ndipo Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, na viongozi wakarudi Kanaani kutoka mkutano wao na Wareubeni na Wagadi huko Gileadi, nao wakatoa taarifa kwa Waisraeli.
JOS 22:33 Walifurahi kusikia taarifa hiyo, na wakamhimidi Mungu. Wala hawakuzungumza tena habari za kupigana vita dhidi yao ili kuharibu nchi ambayo Wareubeni na Wagadi waliishi.
JOS 22:34 Nao Wareubeni na Wagadi wakaita madhabahu hayo Edi: kwa kuwa itakuwa shahidi kati yetu na ninyi kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu.
JOS 23:1 Baada ya muda mrefu kupita, naye Mwenyezi Mungu akawa amewapa Israeli pumziko mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo akiwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana,
JOS 23:2 akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa. Yoshua akawaambia: “Mimi ni mzee na umri wangu umeendelea sana.
JOS 23:3 Ninyi wenyewe mmeona kila kitu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alichowatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Ilikuwa ni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyewapigania.
JOS 23:4 Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari kuu upande wa magharibi.
JOS 23:5 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mwenyewe atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowaahidi.
JOS 23:6 “Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Musa, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto.
JOS 23:7 Msishirikiane na mataifa yaliyobakia kati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia.
JOS 23:8 Bali mtashikamana kwa uthabiti na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama vile mmefanya hadi sasa.
JOS 23:9 “Mwenyezi Mungu amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, hadi leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu.
JOS 23:10 Mtu mmoja miongoni mwenu anafukuza watu elfu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapigania, kama alivyoahidi.
JOS 23:11 Kwa hiyo kuweni waangalifu sana kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
JOS 23:12 “Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia kati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao,
JOS 23:13 basi mwe na hakika kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mwangamie kutoka nchi hii nzuri, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa.
JOS 23:14 “Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia.
JOS 23:15 Lakini kama vile kila ahadi njema ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, imekuwa kweli, vivyo hivyo Mwenyezi Mungu ataleta maovu yote kama alivyoonya, hadi awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa.
JOS 23:16 Mkilivunja agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya Mwenyezi Mungu itawaka dhidi yenu, basi nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”
JOS 24:1 Ndipo Yoshua akaita pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maafisa wa Israeli, nao wakaja mbele za Mungu.
JOS 24:2 Yoshua akawaambia watu wote, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Hapo zamani baba zenu, pamoja na Tera baba yake Ibrahimu na Nahori, waliishi ng’ambo ya Mto, nao waliiabudu miungu mingine.
JOS 24:3 Lakini nilimwondoa baba yenu Ibrahimu kutoka nchi hiyo ng’ambo ya Mto, nami nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani, nikampa wazao wengi. Nikampa Isaka,
JOS 24:4 naye Isaka nikampa Yakobo na Esau. Esau nikampa nchi ya vilima ya Seiri, lakini Yakobo pamoja na wanawe wakashuka Misri.
JOS 24:5 “ ‘Kisha nikawatuma Musa na Haruni, nami nikawapiga Wamisri kwa kile nilichokitenda huko, tena nikawatoa ninyi huko.
JOS 24:6 Nilipowatoa baba zenu Misri, mlifika kwenye bahari, nao Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari ya vita na wapanda farasi hadi Bahari ya Shamu.
JOS 24:7 Lakini wakamlilia Mwenyezi Mungu wakitaka msaada, naye akaweka giza kati yenu na Wamisri, akaileta bahari juu yao ikawafunika. Ninyi mliona kwa macho yenu wenyewe kile nilichowatendea Wamisri. Kisha mliishi jangwani kwa muda mrefu.
JOS 24:8 “ ‘Nikawaleta katika nchi ya Waamori ambao waliishi mashariki mwa Yordani. Wakapigana nanyi, lakini nikawatia mikononi mwenu. Nikawaangamiza mbele yenu nanyi mkaimiliki nchi yao.
JOS 24:9 Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipojiandaa kupigana dhidi ya Israeli, alimwita Balaamu mwana wa Beori apate kuwalaani.
JOS 24:10 Lakini sikumkubali Balaamu, kwa hiyo aliwabariki tena na tena, nami niliwaokoa toka mkononi mwake.
JOS 24:11 “ ‘Ndipo mlipovuka Yordani mkafika Yeriko. Raia wa Yeriko wakapigana nanyi, kama walivyofanya Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi, lakini niliwatia mikononi mwenu.
JOS 24:12 Nikatuma nyigu mbele yenu, ambao pia waliwafukuza mbele yenu, hao wafalme wawili wa Waamori. Siyo upanga au upinde wenu wenyewe vilivyowapatia ushindi.
JOS 24:13 Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia, na miji ambayo hamkuijenga, na mnaishi ndani yake, na kula kutoka mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’
JOS 24:14 “Sasa basi mcheni Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ng’ambo ya Mto na huko Misri, nanyi mtumikieni Mwenyezi Mungu.
JOS 24:15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Mwenyezi Mungu, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Mwenyezi Mungu.”
JOS 24:16 Ndipo hao watu wakajibu, “Hili jambo liwe mbali nasi la kumsahau Mwenyezi Mungu na kuitumikia miungu mingine!
JOS 24:17 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mwenyewe ndiye alitutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao.
JOS 24:18 Mwenyezi Mungu akayafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikia Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.”
JOS 24:19 Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu.
JOS 24:20 Ikiwa mkimwacha Mwenyezi Mungu na kuitumikia miungu migeni, atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.”
JOS 24:21 Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikia Mwenyezi Mungu.”
JOS 24:22 Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikia Mwenyezi Mungu.” Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.”
JOS 24:23 Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni mliyo nayo, nanyi mtoleeni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.”
JOS 24:24 Nao watu wakamwambia Yoshua, “Tutamtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na kumtii yeye.”
JOS 24:25 Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria.
JOS 24:26 Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Torati ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko chini ya mwaloni, karibu na mahali patakatifu pa Mwenyezi Mungu.
JOS 24:27 Yoshua akawaambia watu wote, “Tazameni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yote Mwenyezi Mungu aliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.”
JOS 24:28 Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe.
JOS 24:29 Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mwenyezi Mungu akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi.
JOS 24:30 Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Sera katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi.
JOS 24:31 Israeli wakamtumikia Mwenyezi Mungu siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, ambao waliona kila kitu Mwenyezi Mungu alichowatendea Israeli.
JOS 24:32 Nayo ile mifupa ya Yusufu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yusufu.
JOS 24:33 Naye Eleazari mwana wa Haruni akafariki, akazikwa huko Gibea, mlima aliokuwa amepewa mtoto wake Finehasi, kwenye nchi ya vilima ya Efraimu.
JDG 1:1 Baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli wakamuuliza Mwenyezi Mungu, “Ni nani atakayetangulia apande mbele yetu kutupigania dhidi ya Wakanaani?”
JDG 1:2 Mwenyezi Mungu akajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia; nimewapa hiyo nchi mikononi mwao.”
JDG 1:3 Ndipo wanaume wa Yuda wakawaambia Wasimeoni ndugu zao, “Pandeni pamoja nasi katika nchi tuliyopewa, ili tupate kupigana na Wakanaani. Sisi pia tutaenda pamoja nanyi katika sehemu yenu mliyopewa.” Basi Wasimeoni wakaenda pamoja nao.
JDG 1:4 Yuda aliposhambulia, Mwenyezi Mungu akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, nao wakawaua watu elfu kumi huko Bezeki.
JDG 1:5 Huko ndiko walipomkuta huyo Adoni-Bezeki, nao wakapigana naye na kuwafukuza Wakanaani na Waperizi.
JDG 1:6 Adoni-Bezeki pia alikimbia, nao wakamfuata na kumkamata, wakamkata vidole vyake gumba vya mikono na vya miguu.
JDG 1:7 Ndipo Adoni-Bezeki akasema, “Wafalme sabini waliokuwa wamekatwa vidole vyao vya gumba vya mikono na vya miguu walikuwa wakiokota makombo chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa haya kwa yale niliyowatendea.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko.
JDG 1:8 Wanaume wa Yuda wakashambulia pia Yerusalemu na kuiteka. Wakaupiga mji kwa upanga na kuuchoma kwa moto.
JDG 1:9 Baada ya hayo, watu wa Yuda wakateremka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, na Negebu, na nchi ya Shefela.
JDG 1:10 Yuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (mji huu hapo awali uliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai.
JDG 1:11 Kutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (mji huu hapo awali uliitwa Kiriath-Seferi).
JDG 1:12 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayepigana dhidi ya Kiriath-Seferi na kuuteka.”
JDG 1:13 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda; kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa, akaolewa naye.
JDG 1:14 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”
JDG 1:15 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
JDG 1:16 Wazao wa yule Mkeni, baba mkwe wa Musa, wakapanda pamoja na watu wa Yuda kutoka Mji wa Mitende, wakaenda kuishi miongoni mwa watu wa jangwa la Yuda huko Negebu karibu na mji wa Aradi.
JDG 1:17 Basi wanaume wa Yuda wakaenda na Wasimeoni ndugu zao, wakawashambulia Wakanaani walioishi Sefathi, nao wakauangamiza huo mji kabisa. Kwa hiyo huo mji ukaitwa Horma.
JDG 1:18 Watu wa Yuda wakatwaa pia Gaza, Ashkeloni na Ekroni, kila mji na vijiji vyake vinavyouzunguka.
JDG 1:19 Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na watu wa Yuda. Wakaimiliki nchi ya vilima, lakini hawakuweza kuwafukuza watu waliokaa katika hiyo tambarare, kwa sababu walikuwa na magari ya vita ya chuma.
JDG 1:20 Kama vile Musa alivyoahidi, Kalebu alipewa Hebroni, naye akawafukuza wana watatu wa Anaki.
JDG 1:21 Hata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, walioishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini.
JDG 1:22 Basi nyumba ya Yusufu wakashambulia Betheli, naye Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja nao.
JDG 1:23 Walipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo awali uliitwa Luzu),
JDG 1:24 wale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuoneshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.”
JDG 1:25 Hivyo akawaonesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote.
JDG 1:26 Yule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambalo ndilo jina lake hadi leo.
JDG 1:27 Lakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na makazi yake, au watu wa Taanaki na makazi yake, au watu wa Dori na makazi yake, au watu wa Ibleamu na makazi yake, au watu wa Megido na makazi yake, kwa kuwa Wakanaani walikuwa wameamua kuishi katika nchi ile.
JDG 1:28 Israeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa.
JDG 1:29 Wala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi miongoni mwao.
JDG 1:30 Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, na walioishi Nahaloli, bali Wakanaani hao walibaki miongoni mwao; lakini waliwatia katika kazi ya kulazimishwa.
JDG 1:31 Wala Asheri hawakuwafukuza wale walioishi huko Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeki wala Rehobu,
JDG 1:32 na kwa sababu ya jambo hili Waasheri wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi.
JDG 1:33 Wala Naftali hawakuwafukuza wale walioishi Beth-Shemeshi wala wale walioishi Beth-Anathi; lakini Naftali nao pia wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi, nao wale walioishi Beth-Shemeshi na Beth-Anathi wakawa watumishi wao katika kazi ya kulazimishwa.
JDG 1:34 Waamori wakawazuilia Wadani kwenye nchi ya vilima, na hawakuwaacha washuke kuingia kwenye sehemu tambarare.
JDG 1:35 Waamori pia walikuwa wameamua kuendelea kuishi katika Mlima Heresi, Aiyaloni na Shaalbimu; lakini nguvu ya nyumba ya Yusufu ilipoongezeka, wao pia wakashindwa na wakalazimika kuingia katika kazi ya kulazimishwa.
JDG 1:36 Mpaka wa Waamori ulikuwa kuanzia Genge la Akrabimu, kuendelea hadi Sela na kuelekea juu.
JDG 2:1 Malaika wa Mwenyezi Mungu akakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja agano langu nanyi.
JDG 2:2 Msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtabomoa madhabahu yao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili?
JDG 2:3 Sasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke kati yenu, ila watakuwa mitego kwenu, nayo miungu yao itakuwa tanzi kwenu.”
JDG 2:4 Malaika wa Mwenyezi Mungu alipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu.
JDG 2:5 Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtolea Mwenyezi Mungu sadaka.
JDG 2:6 Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao.
JDG 2:7 Watu wakamtumikia Mwenyezi Mungu siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, wale waliokuwa wameona mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli.
JDG 2:8 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mwenyezi Mungu, akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi.
JDG 2:9 Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresi katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi.
JDG 2:10 Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjua Mwenyezi Mungu, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli.
JDG 2:11 Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kuwatumikia Mabaali.
JDG 2:12 Wakamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yaliyowazunguka. Wakamkasirisha Mwenyezi Mungu,
JDG 2:13 kwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi.
JDG 2:14 Hivyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao.
JDG 2:15 Wakati wowote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa kinyume nao ili awashinde, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa.
JDG 2:16 Ndipo Mwenyezi Mungu akawainua waamuzi, ambao waliwaokoa kutoka mikononi mwa hao wavamizi.
JDG 2:17 Lakini hawakuwasikiliza hata waamuzi wao, bali walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine na kuiabudu. Waligeuka upesi na kuiacha njia ambayo baba zao waliiendea, yaani njia ya kutii amri za Mwenyezi Mungu.
JDG 2:18 Kila mara Mwenyezi Mungu alipowainulia mwamuzi, Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na huyo mwamuzi, naye aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao kwa kipindi chote alichoishi yule mwamuzi. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwahurumia kwa sababu ya kilio chao cha huzuni kwa ajili ya wale waliokuwa wakiwatesa na kuwataabisha.
JDG 2:19 Lakini kila mara mwamuzi alipofariki, watu walirudia katika hali mbaya ya uovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine, ili kuitumikia na kuiabudu. Walikataa kuacha matendo yao maovu na njia zao za ukaidi.
JDG 2:20 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawakasirikia sana Israeli na kusema, “Kwa kuwa taifa hili limevunja agano lile nililofanya na baba zao na hawakunisikiliza,
JDG 2:21 mimi nami sitafukuza taifa lolote ambalo Yoshua aliliacha alipofariki.
JDG 2:22 Nitawatumia mataifa hao ili nipate kuwapima Israeli, nione kama wataishika njia ya Mwenyezi Mungu na kuenenda kwa njia hiyo jinsi baba zao walivyofanya.”
JDG 2:23 Mwenyezi Mungu alikuwa ameyaacha hayo mataifa yabaki; hakuyaondoa mara moja kwa kuyatia mikononi mwa Yoshua.
JDG 3:1 Haya ndio mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyaacha ili kuwajaribu Waisraeli wote ambao hawakushiriki vita yoyote huko Kanaani
JDG 3:2 (alifanya hivi ili tu kuwafundisha vita wazao wa Waisraeli ambao hawakuwa na uzoefu wa vita hapo awali):
JDG 3:3 watawala watano wa Wafilisti, pamoja na Wakanaani wote, Wasidoni, na Wahivi walioishi katika milima ya Lebanoni kuanzia Mlima wa Baal-Hermoni hadi Lebo-Hamathi.
JDG 3:4 Waliachwa ili kuwajaribu Waisraeli, kuona kama wangetii amri za Mwenyezi Mungu, alizokuwa amewapa baba zao kwa mkono wa Musa.
JDG 3:5 Waisraeli wakaishi miongoni mwa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
JDG 3:6 Wakaoa binti za hao mataifa, na wakawatoa binti zao wenyewe waolewe na wana wa hao mataifa, na wakaitumikia miungu yao.
JDG 3:7 Waisraeli wakafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, wakamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na kutumikia Mabaali na Maashera.
JDG 3:8 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Israeli. Hivyo akawauza mikononi mwa Kushan-Rishathaimu mfalme wa Mesopotamia, nao Waisraeli wakamtumikia kwa muda wa miaka nane.
JDG 3:9 Waisraeli walipomlilia Mwenyezi Mungu, yeye akawainulia mkombozi, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu, ambaye aliwaokoa.
JDG 3:10 Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu yake; hivyo akawa mwamuzi wa Israeli, na akaenda vitani. Mwenyezi Mungu akamtia Kushan-Rishathaimu mfalme wa Mesopotamia mikononi mwa Othnieli, naye akamshinda.
JDG 3:11 Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arobaini, hadi Othnieli mwana wa Kenazi alipofariki.
JDG 3:12 Waisraeli wakafanya maovu mbele za Mwenyezi Mungu tena; na kwa kuwa walifanya maovu hayo, Mwenyezi Mungu akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli.
JDG 3:13 Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki kwake, wakashambulia Israeli, na wakatwaa Mji wa Mitende.
JDG 3:14 Waisraeli wakawa chini ya Egloni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka kumi na nane.
JDG 3:15 Waisraeli wakamlilia tena Mwenyezi Mungu, naye akawapa mkombozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi.
JDG 3:16 Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga ukatao kuwili, ukiwa na urefu wa kama dhiraa moja, naye akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake, kwenye paja lake la mkono wa kuume.
JDG 3:17 Akamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, aliyekuwa mtu mnene sana.
JDG 3:18 Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, akawatuma wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru waende zao.
JDG 3:19 Ehudi akafuatana nao hadi kwenye sanamu za mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwako.” Mfalme akasema, “Nyamazeni kimya!” Nao wale waliomhudumia wote wakamwacha, wakatoka nje.
JDG 3:20 Ndipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kiti chake,
JDG 3:21 Ehudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia, akamdunga Mfalme Egloni tumboni mwake.
JDG 3:22 Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya upanga.
JDG 3:23 Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu, na kuifunga kwa funguo.
JDG 3:24 Baada yake kuondoka, watumishi wakaja na kupata milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka anajisaidia chumba cha ndani.”
JDG 3:25 Wakangoja hadi wakawa na fadhaa, na wakati hakuifungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama, wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.
JDG 3:26 Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira.
JDG 3:27 Alipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.
JDG 3:28 Akawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakateremka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakumwacha mtu yeyote kuvuka.
JDG 3:29 Wakati huo wakawaua Wamoabu wapatao elfu kumi wenye nguvu na mashujaa; hakuna yeyote aliyetoroka.
JDG 3:30 Siku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.
JDG 3:31 Baada ya Ehudi akaja Shamgari mwana wa Anathi, aliyewapiga Wafilisti mia sita kwa fimbo ya ng’ombe. Naye pia akawaokoa Waisraeli.
JDG 4:1 Baada ya Ehudi kufa, Waisraeli wakafanya tena maovu machoni pa Mwenyezi Mungu.
JDG 4:2 Hivyo Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori. Jemadari wa jeshi lake alikuwa Sisera, aliyeishi huko Haroshethi-Hagoyimu.
JDG 4:3 Kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya vita ya chuma yapatayo mia tisa, naye alikuwa amewatesa Waisraeli kwa ukatili kwa muda wa miaka ishirini, Waisraeli wakamlilia Mwenyezi Mungu wakaomba msaada.
JDG 4:4 Debora, nabii mwanamke, mkewe Lapidothi, ndiye alikuwa anaamua Israeli wakati ule.
JDG 4:5 Debora alikuwa akiketi chini ya Mtende wa Debora uliokuwa kati ya Rama na Betheli katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakaja kwake ili awaamue.
JDG 4:6 Akatuma wamwite Baraka mwana wa Abinoamu kutoka Kedeshi huko Naftali na kumwambia, “Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, anakuagiza: ‘Nenda, chukua wanaume elfu kumi toka Naftali na Zabuloni, mwende Mlima Tabori.
JDG 4:7 Nitamshawishi Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, pamoja na magari yake ya vita na jeshi lake, hadi Mto Kishoni na kumtia mikononi mwako.’ ”
JDG 4:8 Baraka akamwambia, “Ukienda pamoja nami nitaenda, lakini usipoenda pamoja nami, sitaenda.”
JDG 4:9 Debora akamwambia, “Hakika nitaenda pamoja nawe, lakini njia unayoiendea haitakupa heshima wewe, kwa kuwa Mwenyezi Mungu atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Hivyo Debora akaenda pamoja na Baraka hadi Kedeshi,
JDG 4:10 ambapo Baraka aliwaita Zabuloni na Naftali. Watu elfu kumi wakamfuata Baraka, na Debora pia akaenda naye.
JDG 4:11 Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wale wengine, yaani wazao wa Hobabu, mkwewe Musa, naye akapiga hema lake karibu na ule mti mkubwa wa mwaloni ulio Saananimu, karibu na Kedeshi.
JDG 4:12 Sisera alipoambiwa kuwa Baraka mwana wa Abinoamu alikuwa amepanda Mlima Tabori,
JDG 4:13 Sisera akakusanya magari yake ya vita ya chuma mia tisa, na watu wote waliokuwa pamoja naye, kuanzia Haroshethi-Hagoyimu hadi Mto wa Kishoni.
JDG 4:14 Ndipo Debora akamwambia Baraka, “Nenda! Hii ndiyo siku ambayo Mwenyezi Mungu amemtia Sisera mikononi mwako. Je, Mwenyezi Mungu hakukutangulia mbele yako?” Hivyo Baraka akashuka kutoka Mlima Tabori, akifuatwa na watu elfu kumi.
JDG 4:15 Mwenyezi Mungu akamfadhaisha Sisera na magari yake ya vita yote, pamoja na jeshi lake lote kwa upanga mbele ya Baraka, naye Sisera akaliacha gari lake la vita na kukimbia kwa miguu.
JDG 4:16 Lakini Baraka akafuata magari ya vita pamoja na jeshi hadi Haroshethi-Hagoyimu. Jeshi lote la Sisera likaanguka kwa upanga, wala hakuna hata mtu mmoja aliyesalia.
JDG 4:17 Sisera, hata hivyo, akakimbia kwa miguu hadi kwenye hema la Yaeli, mkewe Heberi, Mkeni, kwa sababu palikuwa na uhusiano wa kirafiki kati ya Yabini mfalme wa Hazori na ukoo wa Heberi, Mkeni.
JDG 4:18 Yaeli akaenda kumlaki Sisera na kumwambia, “Karibu, bwana wangu, karibu ingia ndani kabisa. Usiogope.” Basi Sisera akaingia ndani ya hema la Yaeli, naye akamfunika kwa blanketi nene.
JDG 4:19 Akamwambia, “Nina kiu, tafadhali nipe maji ya kunywa.” Ndipo akafungua kiriba cha maziwa na kumpa akanywa, kisha akamfunika.
JDG 4:20 Naye Sisera akamwambia, “Simama mlangoni pa hema na mtu yeyote akija na kukuuliza, ‘Je, kuna mtu yeyote hapa?’ sema, ‘Hapana.’ ”
JDG 4:21 Lakini Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akachukua nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akiwa amelala usingizi kwa kuchoka. Akakipigilia kile kigingi kwenye paji la uso wake, kikapenya hata kuingia ardhini, naye akafa.
JDG 4:22 Baraka akakaribia akimfuatia Sisera, Yaeli akatoka kumlaki. Akamwambia, “Njoo, nitakuonesha mtu unayemtafuta.” Hivyo wakaingia ndani ya hema, na tazama, Sisera alikuwa amelala humo akiwa amekufa, na hicho kigingi cha hema kikiwa kimepigiliwa kupitia paji la uso wake.
JDG 4:23 Basi siku ile Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani, mbele ya Israeli.
JDG 4:24 Nao mkono wa Waisraeli ukaendelea kuwa na nguvu zaidi na zaidi dhidi ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hadi wakamwangamiza.
JDG 5:1 Siku hiyo Debora na Baraka mwana wa Abinoamu wakaimba wimbo huu:
JDG 5:2 “Wakuu katika Israeli wanapoongoza, wakati watu wanapojitoa kwa hiari yao wenyewe: mhimidini Mwenyezi Mungu!
JDG 5:3 “Sikieni hili, enyi wafalme! Sikilizeni, enyi watawala! Nitamwimbia Mwenyezi Mungu, nitaimba; kwa wimbo nitamhimidi Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
JDG 5:4 “Ee Mwenyezi Mungu, ulipotoka katika Seiri, ulipopita katika mashamba ya Edomu, nchi ilitetemeka, mbingu nazo zikamwaga, naam, mawingu yakamwaga maji.
JDG 5:5 Milima ilitetemeka mbele za Mwenyezi Mungu, Yule wa Sinai, mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
JDG 5:6 “Katika siku za Shamgari mwana wa Anathi, katika siku za Yaeli, barabara kuu hazikuwa na watu; wasafiri walipita njia za kando.
JDG 5:7 Mashujaa walikoma katika Israeli, walikoma hadi mimi, Debora, nilipoinuka, nilipoinuka kama mama katika Israeli.
JDG 5:8 Mungu alichagua viongozi wapya vita vilipokuja malangoni ya mji; lakini hapakuonekana ngao wala mkuki miongoni mwa watu elfu arobaini katika Israeli.
JDG 5:9 Moyo wangu u pamoja na wakuu wa Israeli, u pamoja na wale wanaojitoa kwa hiari yao miongoni mwa watu. Mhimidini Mwenyezi Mungu!
JDG 5:10 “Ninyi mpandao punda weupe, mkiketi juu ya matandiko ya thamani, nanyi mnaotembea barabarani, fikirini
JDG 5:11 kuhusu sauti za waimbaji mahali pa kunyweshea maji. Wanasimulia matendo ya haki ya Mwenyezi Mungu, matendo ya haki ya mashujaa wake katika Israeli. “Ndipo watu wa Mwenyezi Mungu walipoteremka malangoni pa mji.
JDG 5:12 ‘Amka, amka! Debora! Amka, amka, uimbe! Ee Baraka! Inuka, chukua mateka wako uliowateka, ee mwana wa Abinoamu.’
JDG 5:13 “Ndipo mabaki ya watu wakashuka dhidi ya wakuu, watu wa Mwenyezi Mungu wakashuka kwangu dhidi ya wenye nguvu.
JDG 5:14 Baadhi yao walitoka Efraimu, ambao chimbuko lao ni Amaleki; Benyamini alikuwa miongoni mwa watu waliokufuata. Kutoka Makiri wakashuka viongozi, na kutoka Zabuloni wale washikao fimbo ya jemadari.
JDG 5:15 Wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora; naam, Isakari alikuwa pamoja na Baraka, wakija nyuma yake kwa mbio wakielekea bondeni. Katika jamaa za Reubeni, palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.
JDG 5:16 Kwa nini ulikaa katikati ya mazizi ya kondoo kusikiliza sauti ya filimbi zinazoita makundi? Kwa jamaa za Reubeni, palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.
JDG 5:17 Gileadi alikaa ng’ambo ya Yordani. Naye Dani, kwa nini alikaa kwenye merikebu siku nyingi? Asheri alikaa kwa utulivu ufuoni mwa bahari, akikaa kwenye ghuba zake ndogo.
JDG 5:18 Watu wa Zabuloni walihatarisha maisha yao, vilevile nao watu wa Naftali.
JDG 5:19 “Wafalme walikuja na kufanya vita; wafalme wa Kanaani walipigana huko Taanaki, karibu na maji ya Megido, lakini hawakuchukua nyara za fedha.
JDG 5:20 Kutoka mbinguni nyota zilipigana, nyota kutoka njia zake zilipigana na Sisera.
JDG 5:21 Mto wa Kishoni uliwasomba, ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Songa mbele, ee nafsi yangu, kwa ujasiri!
JDG 5:22 Ndipo kwato za farasi zikafanya mshindo: farasi wake wenye nguvu huenda mbio kwa kurukaruka.
JDG 5:23 Malaika wa Mwenyezi Mungu akasema, ‘Laani Merozi. Laani watu wake kwa uchungu, kwa kuwa hawakuja kumsaidia Mwenyezi Mungu, kumsaidia Mwenyezi Mungu dhidi ya hao wenye nguvu.’
JDG 5:24 “Yaeli abarikiwe kuliko wanawake wote, mkewe Heberi, Mkeni, abarikiwe kuliko wanawake wote wanaoishi kwenye mahema.
JDG 5:25 Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa; kwenye bakuli la heshima akamletea maziwa mgando.
JDG 5:26 Akanyoosha mkono wake akashika kigingi cha hema, mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi. Akampiga Sisera kwa nyundo, akamponda kichwa chake, akamvunjavunja na kumtoboa paji lake la uso.
JDG 5:27 Aliinama miguuni pa Yaeli, akaanguka; akalala hapo. Alipoinama miguuni pake, alianguka; pale alipoinamia, ndipo alipoanguka, akiwa amekufa.
JDG 5:28 “Kupitia dirishani mamaye Sisera alichungulia; nyuma ya dirisha alilia, akasema, ‘Mbona gari lake la vita linachelewa kufika? Mbona vishindo vya magari yake ya vita vimechelewa?’
JDG 5:29 Wajakazi wale wenye busara kuliko wengine wote wanamjibu; naam, naye anasema moyoni mwake,
JDG 5:30 ‘Je, hawapati na kugawanya nyara: msichana mmoja au wawili kwa kila mtu, mavazi ya rangi mbalimbali kwa Sisera kuwa nyara, mavazi ya rangi mbalimbali yaliyotariziwa, mavazi yaliyotariziwa vizuri kwa ajili ya shingo yangu: haya yote yakiwa nyara?’
JDG 5:31 “Adui zako wote na waangamie hivyo, Ee Mwenyezi Mungu! Bali wote wanaokupenda na wawe kama jua linavyochomoza kwa nguvu zake.” Hivyo nchi ikawa na amani kwa miaka arobaini.
JDG 6:1 Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba.
JDG 6:2 Kwa kuwa Wamidiani walikuwa na nguvu juu yao, Waisraeli walijitengenezea maficho milimani, kwenye mapango, na katika ngome.
JDG 6:3 Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao.
JDG 6:4 Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ng’ombe au punda.
JDG 6:5 Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia wao; wakavamia nchi ili kuiharibu.
JDG 6:6 Wamidiani wakaifanya Israeli kuwa maskini sana, hata Waisraeli wakamlilia Mwenyezi Mungu kumwomba msaada.
JDG 6:7 Waisraeli walipomlilia Mwenyezi Mungu kwa sababu ya Wamidiani,
JDG 6:8 Mwenyezi Mungu akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa.
JDG 6:9 Nikawaokoa kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu, nami nikawapa ninyi nchi yao.
JDG 6:10 Nikawaambia, ‘Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”
JDG 6:11 Malaika wa Mwenyezi Mungu akaja akaketi chini ya mwaloni ulio Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi Mwabiezeri, pale Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione.
JDG 6:12 Malaika wa Mwenyezi Mungu alipomtokea Gideoni, akamwambia, “Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe, ewe shujaa mwenye nguvu.”
JDG 6:13 Gideoni akajibu, “Nisamehe, Ee Bwana wangu. Kama Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi yale matendo yake makuu ambayo baba zetu walitusimulia juu yake waliposema, ‘Je, Mwenyezi Mungu hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa Mwenyezi Mungu ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”
JDG 6:14 Mwenyezi Mungu akamgeukia na kusema “Nenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”
JDG 6:15 Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”
JDG 6:16 Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”
JDG 6:17 Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonesha kuwa kweli ni wewe unayesema nami.
JDG 6:18 Tafadhali nakuomba usiondoke hapa hadi nitakaporudi, nilete sadaka yangu na kuiweka mbele yako.” Naye Mwenyezi Mungu akamwambia, “Nitangoja hadi utakaporudi.”
JDG 6:19 Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mwaloni, akampa.
JDG 6:20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.
JDG 6:21 Malaika wa Mwenyezi Mungu akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Mwenyezi Mungu akatoweka machoni pake.
JDG 6:22 Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Mwenyezi Mungu, akapaza sauti, akasema, “Ole wangu, Bwana Mungu Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Mwenyezi Mungu uso kwa uso!”
JDG 6:23 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”
JDG 6:24 Hivyo Gideoni akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu mahali pale na kupaita Yehova-Shalomu. Hata leo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.
JDG 6:25 Usiku ule ule Mwenyezi Mungu akamwambia, “Mchukue ng’ombe dume wa baba yako, yule wa pili mwenye miaka saba, ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate nguzo ya Ashera iliyo karibu nayo.
JDG 6:26 Kisha mjengee Mwenyezi Mungu, Mungu wako, madhabahu kwa taratibu zake juu ya mwamba katika ngome hii. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”
JDG 6:27 Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.
JDG 6:28 Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa, na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa, na yule ng’ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu iliyojengwa upya!
JDG 6:29 Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?” Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”
JDG 6:30 Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”
JDG 6:31 Lakini Yoashi akaambia umati wa watu waliomzunguka wakiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.”
JDG 6:32 Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.
JDG 6:33 Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ng’ambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli.
JDG 6:34 Ndipo Roho wa Mwenyezi Mungu akamjia Gideoni, naye Gideoni akapiga tarumbeta kuwaita Waabiezeri ili wamfuate.
JDG 6:35 Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.
JDG 6:36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi:
JDG 6:37 tazama, nitaweka manyoya ya kondoo kwenye sakafu ya kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya manyoya tu, na ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.”
JDG 6:38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akayakamua yale manyoya yenye umande, yakatoka maji kiasi cha kujaa bakuli.
JDG 6:39 Kisha Gideoni akamwambia Mwenyezi Mungu, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa manyoya haya. Wakati huu uyafanye manyoya kuwa kavu, na ardhi yote ifunikwe na umande.”
JDG 6:40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Manyoya yakawa kavu, na ardhi yote ikafunikwa na umande.
JDG 7:1 Ndipo Yerub-Baali (yaani Gideoni) na lile jeshi lililokuwa pamoja naye, wakaondoka asubuhi na mapema na kupiga kambi kando ya chemchemi ya Harodi. Kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao katika bonde, karibu na kilima cha More.
JDG 7:2 Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Jeshi lililo pamoja nawe ni kubwa sana kwangu kuwatia Wamidiani mikononi mwao, Israeli asije akajisifu juu yangu, akisema, ‘Mkono wangu ndio uliniokoa.’
JDG 7:3 Kwa hiyo sasa tangaza jeshi lote likiwa linasikia, kwamba: ‘Yeyote anayeogopa na kutetemeka, yeye na arudi nyumbani, aondoke katika Mlima Gileadi.’ ” Hivyo, watu elfu ishirini na mbili wakarudi nyumbani, wakabaki elfu kumi.
JDG 7:4 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Idadi ya jeshi bado ni kubwa. Wapeleke kwenye maji, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako. Nikikuambia, ‘Huyu ataenda pamoja nawe,’ yeye ataenda; lakini nikisema, ‘Huyu hataenda pamoja nawe,’ yeye hataenda.”
JDG 7:5 Gideoni akalipeleka lile jeshi kwenye maji, naye Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Watenganishe watakaoramba maji kwa ulimi kama mbwa, na wale watakaopiga magoti ili kunywa.”
JDG 7:6 Waliokunywa kwa kuramba maji kutoka mikononi mwao walikuwa watu mia tatu. Wengine wote walipiga magoti ili kunywa.
JDG 7:7 Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Kupitia hao watu mia tatu walioramba maji nitawaokoa ninyi, nami nitawatia Wamidiani mkononi mwako. Waache hao watu wengine wote warudi kila mmoja nyumbani mwake.”
JDG 7:8 Hivyo Gideoni akawaruhusu wale Waisraeli wengine kila mmoja aende kwenye hema lake. Akabakia na wale mia tatu, nao wakachukua vyakula na tarumbeta za wenzao. Basi kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake bondeni.
JDG 7:9 Usiku ule ule Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke ushambulie kambi, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako.
JDG 7:10 Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura,
JDG 7:11 nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura, mtumishi wake, wakashuka na kuwafikia walinzi wa mbele wa kambi.
JDG 7:12 Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia wao hawangehesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.
JDG 7:13 Gideoni alifika mara tu mtu mmoja alipokuwa akimweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Tazama, niliota ndoto, mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukaipiga hema kwa nguvu, na kusababisha hema hilo kupinduka na kuporomoka.”
JDG 7:14 Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine isipokuwa upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.”
JDG 7:15 Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akasujudu na kuabudu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! Mwenyezi Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”
JDG 7:16 Akawagawa wale watu mia tatu katika makundi matatu, akawakabidhi tarumbeta mikononi mwao wote, na mitungi mitupu, na mienge ikawekwa ndani yake.
JDG 7:17 Akawaambia, “Nitazameni, fanyeni kama nitakavyofanya. Nitakapofika mwisho wa kambi, mfanye kama nitakavyofanya.
JDG 7:18 Mimi na wote walio pamoja nami tutakapopiga tarumbeta zetu, ninyi nanyi pigeni tarumbeta pande zote za kambi na mpige kelele, mseme, ‘Upanga wa Mwenyezi Mungu na wa Gideoni.’ ”
JDG 7:19 Gideoni na wale watu mia moja waliokuwa pamoja naye wakafika mwisho wa kambi usiku mwanzoni mwa zamu ya kati, mara tu walipokuwa wamebadili zamu. Wakapiga zile tarumbeta zao, na kuvunja ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao.
JDG 7:20 Yale makundi matatu wakapiga tarumbeta na kuvunja mitungi. Wakashika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga. Wakapaza sauti zao, wakisema, “Upanga wa Mwenyezi Mungu, na wa Gideoni!”
JDG 7:21 Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote, Wamidiani wote wakakimbia, huku wakipiga kelele.
JDG 7:22 Walipozipiga zile tarumbeta mia tatu, Mwenyezi Mungu akafanya watu katika kambi yote kugeukiana kila mmoja na mwenziwe kwa upanga. Jeshi likakimbia hadi Beth-Shita kuelekea Serera, hadi mpakani mwa Abel-Mehola karibu na Tabathi.
JDG 7:23 Wanaume Waisraeli wakaitwa kutoka Naftali, Asheri na Manase yote, nao wakawafuatia Wamidiani.
JDG 7:24 Gideoni akatuma wajumbe katika nchi yote ya vilima ya Efraimu, akisema, “Teremkeni dhidi ya Wamidiani na mkazuie vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani.” Hivyo wanaume wote wa Efraimu wakakutanika pamoja na kuzingira vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani.
JDG 7:25 Wakawakamata Orebu na Zeebu, wakuu wawili wa Midiani. Wakamuua Orebu pale penye mwamba wa Orebu, na Zeebu wakamuua pale penye shinikizo la kukamulia zabibu la Zeebu. Wakawafuatia Wamidiani na kuleta vichwa vya Orebu na Zeebu kwa Gideoni, huko ng’ambo ya Yordani.
JDG 8:1 Basi Waefraimu wakamuuliza Gideoni, “Mbona umetutenda hivi? Kwa nini hukutuita ulipoenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali sana.
JDG 8:2 Gideoni akawajibu, “Nilichofanya mimi ni nini kulinganisha na kile ninyi mlichofanya? Je, kuokoa masazo ya zabibu za Efraimu si bora kuliko mavuno kamili ya zabibu ya Abiezeri?
JDG 8:3 Mungu amewatia Orebu na Zeebu, hao viongozi wa Wamidiani, mikononi mwenu. Je, mimi niliweza kufanya nini kulinganisha na mlichofanya ninyi?” Aliposema hili, hasira yao dhidi yake ikatulia.
JDG 8:4 Gideoni pamoja na watu wake mia tatu, wakiwa wamechoka sana lakini bado wakiwafuatia, wakafika Yordani na kuuvuka.
JDG 8:5 Akawaambia wanaume wa Sukothi, “Tafadhali lipatieni jeshi langu mikate, kwa maana wamechoka, nami ningali ninawafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.”
JDG 8:6 Lakini viongozi wa Sukothi wakasema, “Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?”
JDG 8:7 Gideoni akajibu, “Kwa ajili ya hilo tu, Mwenyezi Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, nitaichana nyama ya miili yenu kwenye miiba ya nyikani na kwenye michongoma.”
JDG 8:8 Kutoka hapo alikwea hadi Penieli na kutoa ombi lile lile, lakini nao wanaume wa Penieli wakamjibu kama wanaume wa Sukothi walivyokuwa wamemjibu.
JDG 8:9 Hivyo akawaambia wanaume wa Penieli, “Nitakaporudi kwa ushindi, nitaubomoa mnara huu.”
JDG 8:10 Wakati huu Zeba na Salmuna walikuwa Karkori, wakiwa na jeshi la watu wapatao elfu kumi na tano waliokuwa wamesalia wa mataifa ya mashariki, kwa kuwa watu wapatao elfu mia moja na ishirini wenye panga walikuwa wameuawa.
JDG 8:11 Basi Gideoni akakwea kwa njia ya wafugaji wahamaji mashariki mwa Noba na Yogbeha, na kulishambulia jeshi ambalo halikushuku lolote.
JDG 8:12 Zeba na Salmuna, hao wafalme wawili wa Midiani, wakakimbia lakini yeye Gideoni akawafuata na kuwakamata, akalishinda hilo jeshi lao lote kabisa.
JDG 8:13 Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kupitia Mwinuko wa Heresi.
JDG 8:14 Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali, naye yule kijana akamwandikia majina ya viongozi sabini na saba wa Sukothi, ambao ni wazee wa mji.
JDG 8:15 Ndipo Gideoni akaja na kuwaambia wanaume wa Sukothi, “Tazameni Zeba na Salmuna mlionisimanga kwa ajili yao mkisema, ‘Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?’ ”
JDG 8:16 Akawachukua hao wazee wa mji, na kuwaadhibu wanaume wa Sukothi kwa kuwachapa kwa miiba na michongoma ya nyikani.
JDG 8:17 Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua wanaume wa huo mji.
JDG 8:18 Kisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni wanaume wa aina gani mliowaua huko Tabori?” Wakajibu, “Ni wanaume kama wewe, kila mmoja wao akiwa anafanana na mwana wa mfalme.”
JDG 8:19 Gideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.”
JDG 8:20 Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu.
JDG 8:21 Zeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mwanaume, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo, Gideoni akajitokeza na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia wao.
JDG 8:22 Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, mwanao, na mjukuu wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”
JDG 8:23 Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitawatawala ninyi, wala mwanangu hatawatawala. Mwenyezi Mungu ndiye atakayewatawala ninyi.”
JDG 8:24 Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.)
JDG 8:25 Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka fungu lake la nyara.
JDG 8:26 Uzito wa pete za dhahabu alizoomba ulikuwa shekeli elfu moja na mia saba, bila kuhesabu mapambo mengine, vidani, na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao.
JDG 8:27 Gideoni akatengeneza kizibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.
JDG 8:28 Hivyo Midiani wakashindwa mbele ya Waisraeli, nao hawakuinua vichwa vyao tena. Wakati wa siku za uhai wa Gideoni, nchi ikafurahia amani miaka arobaini.
JDG 8:29 Yerub-Baali mwana wa Yoashi akarudi kwenda kuishi katika nyumba yake.
JDG 8:30 Alikuwa na wana sabini wa kwake mwenyewe, kwa kuwa alikuwa na wake wengi.
JDG 8:31 Suria wake, aliyekuwa anaishi huko Shekemu, pia alimzalia mwana, akamwita jina Abimeleki.
JDG 8:32 Gideoni mwana wa Yoashi akafa akiwa na umri mzuri wa uzee, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake huko Ofra ya Waabiezeri.
JDG 8:33 Mara tu alipofariki Gideoni, Waisraeli wakarudia hali ya uovu na kufanya uasherati kwa kuabudu Mabaali. Wakamsimamisha Baal-Berithi kuwa mungu wao na
JDG 8:34 wala hawakumkumbuka Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyewaokoa kutoka mikononi mwa adui zao wote kutoka kila upande.
JDG 8:35 Pia wakashindwa kuitendea mema jamaa ya Yerub-Baali (yaani Gideoni) kwa ajili ya mambo yote mema aliyokuwa amefanyia Israeli.
JDG 9:1 Siku moja Abimeleki mwana wa Yerub-Baali akaenda kwa ndugu za mama yake huko Shekemu, akawaambia wao na ukoo wote wa mama yake,
JDG 9:2 “Waulizeni watu wote wa Shekemu, ‘Lipi lililo bora kwenu: Kutawaliwa na wana wote sabini wa Yerub-Baali, au mtu mmoja peke yake?’ Kumbukeni kwamba mimi ni mwili wenu na damu yenu.”
JDG 9:3 Ndugu za mama yake walipowaeleza watu wote wa Shekemu, wakaelekea kumkubali Abimeleki, kwa kuwa walisema, “Yeye ni ndugu yetu.”
JDG 9:4 Wakampa shekeli sabini za fedha kutoka hekalu la Baal-Berithi, naye Abimeleki akazitumia kuajiri watu ovyo na wasiojali, wakawa ndio wafuasi wake.
JDG 9:5 Akaenda nyumbani mwa baba yake huko Ofra, na juu ya jiwe moja akawaua ndugu zake sabini, ambao ni wana wa Yerub-Baali. Lakini Yothamu, mwana mdogo kwa wote wa Yerub-Baali, akaokoka kwa kujificha.
JDG 9:6 Ndipo wenyeji wa Shekemu na Beth-Milo wakakusanyika pamoja chini ya mwaloni mkubwa, penye nguzo iliyo Shekemu, wakamtawaza Abimeleki kuwa mfalme.
JDG 9:7 Yothamu alipoambiwa hayo, akapanda juu ya kilele cha mlima Gerizimu, akapaza sauti, akawaambia, “Nisikilizeni enyi wenyeji wa Shekemu, ili Mungu naye apate kuwasikiliza.
JDG 9:8 Siku moja miti ilitoka ili kwenda kujitawazia mfalme. Ikauambia mzeituni, ‘Wewe uwe mfalme wetu.’
JDG 9:9 “Lakini mzeituni ukaijibu, ‘Je, niache kutoa mafuta yangu ambayo kwake miungu na wanadamu huheshimiwa, ili nikatawale miti?’
JDG 9:10 “Kisha miti ikauambia mtini, ‘Njoo na uwe mfalme wetu!’
JDG 9:11 “Lakini mtini ukaijibu, ‘Je, niache kutoa matunda yangu mazuri na matamu, ili nikatawale miti?’
JDG 9:12 “Ndipo miti ikauambia mzabibu, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’
JDG 9:13 “Lakini mzabibu ukaijibu, ‘Je, niache kutoa divai yangu inayofurahisha miungu na wanadamu ili nikatawale miti?’
JDG 9:14 “Mwishoni miti yote ikauambia mchongoma, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’
JDG 9:15 “Nao mchongoma ukaijibu, ‘Kama kweli mnataka kunitawaza niwe mfalme wenu, basi njooni mpate kupumzika chini ya kivuli changu. Lakini kama sivyo, moto na utoke kwenye mchongoma ukateketeze mierezi ya Lebanoni!’
JDG 9:16 “Basi, je, mmetenda kwa uaminifu na heshima kwa kumtawaza Abimeleki kuwa mfalme? Je, mmetendea mema Yerub-Baali na jamaa yake, na mkamtendea kama alivyostahili?
JDG 9:17 Baba yangu aliwapigania na kuhatarisha nafsi yake ili kuwaokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani,
JDG 9:18 lakini leo mmeasi dhidi ya jamaa ya baba yangu, na kuwaua wanawe sabini juu ya jiwe moja. Nanyi mmemtawaza Abimeleki mwana wa mjakazi wake kuwa mfalme juu ya wenyeji wa Shekemu, kwa kuwa yeye ni ndugu yenu.
JDG 9:19 Ikiwa kweli mmemtendea Yerub-Baali na jamaa yake kwa heshima na uaminifu, basi Abimeleki na awe furaha yenu, nanyi mwe furaha yake pia!
JDG 9:20 Lakini kama sivyo, moto na utoke kwa Abimeleki na uwateketeze, ninyi wenyeji wa Shekemu na Beth-Milo; nao moto utoke kwenu, wenyeji wa Shekemu na Beth-Milo, na umteketeze Abimeleki!”
JDG 9:21 Ndipo Yothamu akakimbia, akatoroka akaenda Beeri, akaishi huko, kwa sababu alimwogopa ndugu yake Abimeleki.
JDG 9:22 Baada ya Abimeleki kutawala Israeli kwa muda wa miaka mitatu,
JDG 9:23 Mungu akaruhusu roho mbaya kati ya Abimeleki na wenyeji wa Shekemu, nao wenyeji wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa hila.
JDG 9:24 Hili lilitendeka ili ule ukatili waliotendewa hao wana sabini wa Yerub-Baali upatilizwe, na damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao aliyewaua, na pia iwe juu ya wenyeji wa Shekemu, ambao walimsaidia kuua ndugu zake.
JDG 9:25 Hivyo, kutokana na uadui juu yake, wenyeji wa Shekemu wakaweka watu wa kumvizia katika vilele vya milima. Wakawanyang’anya watu wote waliopita karibu nao, nayo haya yakaarifiwa kwa Abimeleki.
JDG 9:26 Basi Gaali mwana wa Ebedi akaenda pamoja na ndugu zake wakaingia Shekemu, nao wenyeji wa huko wakawa na imani naye.
JDG 9:27 Wakaenda mashambani mwao kuvuna zabibu na kuzisindika hizo zabibu, baadaye wakafanya sherehe katika hekalu la mungu wao. Walipokuwa wakila na kunywa, wakamlaani Abimeleki.
JDG 9:28 Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerub-Baali? Naye Zebuli si ndiye msaidizi wake? Basi watumikieni watu wa Hamori, babaye Shekemu. Kwa nini tumtumikie Abimeleki?
JDG 9:29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu! Basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ondoa jeshi lako lote.’ ”
JDG 9:30 Zebuli aliyekuwa mtawala wa mji aliposikia aliyosema Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana.
JDG 9:31 Akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, na kusema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wamekuja Shekemu, na wanauchochea mji huu kinyume chako.
JDG 9:32 Sasa basi, usiku huu wewe uondoke na watu wako ili mje kuwavizia mashambani.
JDG 9:33 Kisha asubuhi wakati wa kuchomoza jua, amka mapema na ujipange dhidi ya huo mji. Gaali na jeshi lililo pamoja naye watakapotoka kukabiliana nanyi, mwaweza kuwatendea kwa kadiri mnavyoweza.”
JDG 9:34 Kwa hiyo Abimeleki pamoja na jeshi lake lote wakaondoka usiku na kujificha karibu na Shekemu wakiwa vikosi vinne.
JDG 9:35 Basi Gaali mwana wa Ebedi alikuwa ametoka nje akawa amesimama katika ingilio la mji wakati ule ule ambao Abimeleki na watu wake walipokuwa wanatoka sehemu zao za maficho.
JDG 9:36 Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka vilele vya milima!” Zebuli akajibu, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.”
JDG 9:37 Lakini Gaali akasema tena, “Tazama, watu wanashuka kutoka katikati ya nchi na kikosi kimoja kinakuja kutoka Tabur-Ezeri na kikosi kingine kutoka upande wa mwaloni wa Meonenimu.”
JDG 9:38 Ndipo Zebuli akamwambia, “Kuko wapi kujivuna kwako sasa, wewe uliyesema, ‘Huyo Abimeleki ni nani hata tumtumikie?’ Hawa si wale watu uliowadharau? Toka nje sasa ukapigane nao!”
JDG 9:39 Basi Gaali akawaongoza wenyeji wa Shekemu kupigana na Abimeleki.
JDG 9:40 Abimeleki akamfukuza, naye akatoroka. Nao watu wengi wakaanguka njia yote hadi kwenye ingilio la lango, wakiwa wamejeruhiwa katika kule kutoroka.
JDG 9:41 Abimeleki akaishi Aruma, naye Zebuli akawafukuza Gaali na ndugu zake watoke Shekemu.
JDG 9:42 Kesho yake watu wa Shekemu wakatoka wakaenda mashambani, Abimeleki akaambiwa jambo hilo.
JDG 9:43 Hivyo akawachukua watu wake, akawagawanya katika vikosi vitatu na kuwaweka waviziaji huko mashambani. Alipowaona watu wanatoka kwenda nje ya mji, akainuka dhidi yao na kuwashambulia.
JDG 9:44 Abimeleki pamoja na vikosi vyake wakaharakisha kwenda mbele kwenye nafasi iliyokuwa katika ingilio la lango la mji. Vikosi viwili vikawashambulia wale waliokuwa mashambani, na kuwaua.
JDG 9:45 Siku hiyo nzima Abimeleki akazidisha mashambulizi yake dhidi ya mji hadi akawa ameuteka na kuwaua watu wa mji huo. Kisha akauangamiza mji na kusambaza chumvi juu yake.
JDG 9:46 Kwa kusikia jambo hilo, watu wote katika mnara wa Shekemu wakaingia kwenye ngome ya hekalu la El-Berithi.
JDG 9:47 Abimeleki aliposikia kuwa wamekusanyika huko,
JDG 9:48 yeye na watu wake wote wakakwea kwenye Mlima Salmoni. Abimeleki akachukua shoka, akakata baadhi ya matawi, ambayo aliyachukua begani mwake. Akawaagiza wale watu waliokuwa pamoja naye kuwa, “Haraka! Fanyeni kile mmeona nikifanya!”
JDG 9:49 Basi watu wote wakakata matawi na kumfuata Abimeleki. Wakayakusanya hayo matawi juu ya ngome, na kuitia moto ili kuwachoma watu wote waliokuwa ndani. Hivyo watu wote katika mnara wa Shekemu, yamkini wanaume na wanawake elfu moja, pia wakafa.
JDG 9:50 Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka.
JDG 9:51 Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji, wanaume na wanawake, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani, na kupanda juu ya paa la mnara.
JDG 9:52 Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia. Lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto,
JDG 9:53 mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia kwa kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake.
JDG 9:54 Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa.
JDG 9:55 Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani mwake.
JDG 9:56 Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini.
JDG 9:57 Mungu akawapatiliza wanaume wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.
JDG 10:1 Baada ya Abimeleki, Tola mwana wa Pua mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, aliyeishi huko Shamiri, katika nchi ya vilima ya Efraimu, akainuka kuokoa Israeli.
JDG 10:2 Akawa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na tatu. Ndipo akafa, naye akazikwa huko Shamiri.
JDG 10:3 Baada yake akafuatiwa na Yairi, Mgileadi, aliyekuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na mbili.
JDG 10:4 Alikuwa na wana thelathini waliopanda punda thelathini. Nao walikuwa na miji thelathini huko Gileadi, inayoitwa Hawoth-Yairi hadi leo.
JDG 10:5 Yairi akafa, naye akazikwa huko Kamoni.
JDG 10:6 Tena Waisraeli wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Wakaabudu Mabaali na Maashtorethi, na miungu ya Aramu, miungu ya Sidoni, miungu ya Moabu, miungu ya Waamoni, na miungu ya Wafilisti. Na kwa kuwa Waisraeli walimwacha Mwenyezi Mungu wala hawakuendelea kumtumikia,
JDG 10:7 hivyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Waisraeli. Naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni,
JDG 10:8 ambao waliowaonea na kuwatesa mwaka huo. Kwa miaka kumi na nane wakawatesa Waisraeli wote upande wa mashariki mwa Mto Yordani huko Gileadi, katika nchi ya Waamori.
JDG 10:9 Waamoni nao wakavuka Yordani ili kupigana na Yuda, Benyamini na nyumba ya Efraimu, nayo nyumba ya Israeli ikawa katika taabu kubwa.
JDG 10:10 Ndipo Waisraeli wakamlilia Mwenyezi Mungu wakasema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, kumwacha Mungu wetu na kutumikia Mabaali.”
JDG 10:11 Mwenyezi Mungu akawaambia, “Wamisri, Waamori, Waamoni, Wafilisti,
JDG 10:12 Wasidoni, Waamaleki na Wamaoni walipowadhulumu ninyi, nanyi mkanililia na kuomba msaada, je, sikuwaokoa mikononi mwao?
JDG 10:13 Lakini ninyi mmeniacha na kuitumikia miungu mingine, kwa hiyo sitawaokoa tena.
JDG 10:14 Nendeni mkaililie ile miungu mlioichagua. Hiyo miungu na iwaokoe mnapokuwa katika taabu!”
JDG 10:15 Lakini Waisraeli wakamwambia Mwenyezi Mungu, “Tumetenda dhambi. Ututendee lile unaloona kuwa jema kwako, lakini twakusihi utuokoe sasa.”
JDG 10:16 Nao wakaiondoa hiyo miungu migeni kati yao nao wakamtumikia Mwenyezi Mungu. Naye akahuzunika kwa sababu ya taabu ya Israeli.
JDG 10:17 Waamoni walipoitwa vitani na kupiga kambi kule Gileadi, Waisraeli walikusanyika na kupiga kambi huko Mispa.
JDG 10:18 Viongozi wa watu wa Gileadi wakaambiana wao kwa wao, “Yeyote atakayeanzisha mashambulizi dhidi ya Waamoni atakuwa kiongozi wa wote wanaoishi Gileadi.”
JDG 11:1 Basi Yefta Mgileadi alikuwa shujaa mwenye nguvu. Baba yake alikuwa Gileadi, naye mama yake alikuwa kahaba.
JDG 11:2 Mke wa Gileadi pia akamzalia wana, nao walipokua, wakamfukuza Yefta, na kumwambia, “Wewe huwezi kupata urithi katika jamii yetu, kwa sababu wewe ni mwana wa mwanamke mwingine.”
JDG 11:3 Basi Yefta akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu, mahali ambako watu waasi walijiunga naye na kumfuata.
JDG 11:4 Baada ya muda Waamoni wakafanya vita na Israeli,
JDG 11:5 viongozi wa Gileadi wakaenda kumchukua Yefta katika nchi ya Tobu.
JDG 11:6 Wakamwambia Yefta, “Njoo, uwe jemadari wetu, ili tuweze kupigana na Waamoni.”
JDG 11:7 Yefta akawaambia viongozi wa Gileadi, “Je, si mlinichukia na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Kwa nini mwanijia sasa, wakati mko taabuni?”
JDG 11:8 Viongozi wa Gileadi wakamwambia Yefta, “Lakini sasa tumegeuka kukuelekea wewe, ili uende pamoja nasi kupigana na Waamoni, nawe utakuwa kiongozi wetu juu ya watu wote wa Gileadi.”
JDG 11:9 Yefta akawaambia viongozi wa Gileadi, “Ikiwa mtanirudisha kwetu kupigana na Waamoni, naye Mwenyezi Mungu akanisaidia kuwashinda, je, ni kweli nitakuwa kiongozi wenu?”
JDG 11:10 Viongozi wa Gileadi wakamjibu Yefta, “Mwenyezi Mungu ndiye shahidi wetu. Kwa hakika tutafanya kama usemavyo.”
JDG 11:11 Basi Yefta akaenda na viongozi wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi na jemadari wao. Naye akarudia maneno yake yote mbele za Mwenyezi Mungu huko Mispa.
JDG 11:12 Ndipo Yefta akatuma wajumbe kwa mfalme wa Waamoni akisema, “Una nini nasi, hata umekuja kushambulia nchi yetu?”
JDG 11:13 Mfalme wa Waamoni akawajibu wajumbe wale wa Yefta, “Waisraeli walipopanda kutoka Misri, waliichukua nchi yangu kuanzia Mto Arnoni hadi Mto Yaboki, hadi kufikia Mto Yordani. Sasa irudishe kwa amani.”
JDG 11:14 Yefta akarudisha wajumbe kwa mfalme wa Waamoni,
JDG 11:15 kusema: “Hili ndilo asemalo Yefta: Waisraeli hawakuchukua nchi ya Moabu wala nchi ya Waamoni.
JDG 11:16 Lakini walipopanda kutoka Misri, Waisraeli walipitia katika jangwa hadi Bahari ya Shamu na wakafika Kadeshi.
JDG 11:17 Ndipo Waisraeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu, wakisema, ‘Tupe ruhusa kupita katika nchi yako.’ Lakini mfalme wa Edomu hakutusikia. Wakatuma wajumbe pia kwa mfalme wa Moabu, naye akakataa. Kwa hiyo Waisraeli wakakaa huko Kadeshi.
JDG 11:18 “Baadaye wakasafiri kupitia jangwa, wakiambaa na nchi za Edomu na Moabu, wakapitia upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, na kupiga kambi upande ule mwingine wa Mto Arnoni. Hawakuingia katika nchi ya Moabu, kwa kuwa Mto Arnoni ulikuwa mpaka wake.
JDG 11:19 “Kisha Waisraeli wakatuma wajumbe kwa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, na kumwambia, ‘Tupe ruhusa kupita katika nchi yako ili kufikia mahali petu.’
JDG 11:20 Hata hivyo, Sihoni hakuwaamini Waisraeli kupita katika nchi yake. Akaandaa jeshi lake lote na kupiga kambi huko Yahasa, nao wakapigana na Waisraeli.
JDG 11:21 “Ndipo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Waisraeli, nao wakawashinda. Waisraeli wakaimiliki nchi yote ya Waamori walioishi nchi hiyo,
JDG 11:22 wakiiteka nchi yote kuanzia Mto Arnoni hadi Mto Yaboki, na kutoka jangwani hadi Mto Yordani.
JDG 11:23 “Basi kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, amewafukuza Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, wewe unayo haki gani ya kuitamalaki?
JDG 11:24 Je, haikupasi kuchukua kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa? Vivyo hivyo, chochote kile Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alichotupatia sisi, tutakimiliki.
JDG 11:25 Je, wewe ni bora kuliko Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu? Je, yeye alishagombana na Waisraeli au kupigana nao wakati wowote?
JDG 11:26 Kwa maana kwa miaka mia tatu, Waisraeli wameishi Heshboni na makazi yake, Aroeri na makazi yake, na katika miji yote iliyo kando ya Mto Arnoni. Kwa nini wewe hukuyachukua wakati huo?
JDG 11:27 Mimi sijakukosea, bali wewe ndiwe unanikosea kwa kufanya vita nami. Basi Mwenyezi Mungu, aliye Mwamuzi, leo na aamue ugomvi kati ya Waisraeli na Waamoni.”
JDG 11:28 Hata hivyo, mfalme wa Waamoni hakuyajali maneno ya ujumbe wa Yefta.
JDG 11:29 Ndipo Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Yefta. Akapita katikati ya Gileadi na Manase, pia akapita katika Mispa ya Gileadi, na kutokea huko akasonga mbele kushambulia Waamoni.
JDG 11:30 Naye Yefta akaweka nadhiri mbele za Mwenyezi Mungu akisema, “Ikiwa utawatia Waamoni mikononi mwangu,
JDG 11:31 chochote kile kitakachotoka katika mlango wa nyumba yangu cha kwanza ili kunilaki nirudipo kwa amani katika kuwashinda Waamoni, kitakuwa ni cha Mwenyezi Mungu na nitakitoa kuwa sadaka ya kuteketezwa.”
JDG 11:32 Ndipo Yefta akavuka kupigana na hao Waamoni, naye Mwenyezi Mungu akawatia mkononi mwake.
JDG 11:33 Akaharibu kabisa miji ishirini kuanzia Aroeri hadi karibu na Minithi, na kuendelea hadi Abel-Keramimu. Hivyo, Waisraeli wakawashinda Waamoni.
JDG 11:34 Yefta aliporudi nyumbani mwake huko Mispa, tazama, binti yake akatoka ili kumlaki kwa matari na kucheza. Alikuwa mwanawe wa pekee, hakuwa na mwana wala binti mwingine.
JDG 11:35 Alipomwona akararua mavazi yake akalia, “Ee! Binti yangu! Umenifanya niwe na huzuni na kunyong’onyea sana, kwa kuwa nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, ambayo siwezi kuivunja.”
JDG 11:36 Akajibu, “Baba yangu, umetoa neno lako kwa Mwenyezi Mungu. Nitendee mimi kama vile ulivyoahidi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekupa ushindi dhidi ya adui zako Waamoni.”
JDG 11:37 Naye akamwambia baba yake, “Naomba nifanyiwe jambo hili. Nipewe miezi miwili ili kuzunguka vilimani nikaulilie ubikira wangu, mimi na wenzangu.”
JDG 11:38 Baba yake akamwambia, “Unaweza kwenda.” Naye akamwacha aende kwa miezi miwili. Hivyo akaondoka pamoja na wenzake, naye akaulilia ubikira wake huko vilimani kwa sababu hangeolewa kamwe.
JDG 11:39 Baada ya hiyo miezi miwili, alirejea kwa baba yake, naye baba yake akamtendea kama alivyokuwa ametoa nadhiri yake. Naye alikuwa bikira. Nayo ikawa desturi katika Israeli,
JDG 11:40 kwamba kila mwaka binti za Israeli huenda kwa siku nne ili kumkumbuka huyo binti Yefta Mgileadi.
JDG 12:1 Watu wa Efraimu wakaita majeshi yao, wakavuka kwenda Zafoni. Wakamwambia Yefta, “Kwa nini mmeenda kupigana na Waamoni bila kutuita ili twende pamoja nawe? Basi tutaichoma moto nyumba yako, pamoja nawe ukiwa ndani yake.”
JDG 12:2 Yefta akajibu, “Mimi na watu wangu tulikuwa na ugomvi mkubwa na Waamoni. Ingawa niliwaita, hamkuniokoa kutoka mkono wao.
JDG 12:3 Nilipoona kuwa hamniokoi, nikauhatarisha uhai wangu, nikavuka kupigana na Waamoni. Naye Mwenyezi Mungu akanipatia ushindi dhidi yao. Sasa kwa nini mnanijia leo ili kupigana nami?”
JDG 12:4 Ndipo Yefta akakusanya wanaume wa Gileadi pamoja na kupigana na Efraimu. Wagileadi wakawashinda Waefraimu, kwa kuwa Waefraimu walisema, “Ninyi Wagileadi ni waasi mliotoroka toka Efraimu na Manase.”
JDG 12:5 Wagileadi wakaviteka vivuko vya Mto Yordani kuelekea Efraimu. Kisha ilikuwa yeyote aliyenusurika kutoka Efraimu aliposema, “Niache nivuke,” hao wanaume wa Gileadi walimuuliza, “Je wewe ni Mwefraimu?” Akijibu “Hapana,”
JDG 12:6 walimwambia, “Sawa, sema ‘Shibolethi’.” Iwapo alitamka, “Sibolethi”, kwa sababu hakuweza kutamka hilo neno sawasawa, walimkamata na kumuua hapo kwenye vivuko vya Mto Yordani. Waefraimu elfu arobaini na mbili waliuawa wakati huo.
JDG 12:7 Yefta akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa muda wa miaka sita. Kisha Yefta akafa, akazikwa katika mmoja wa miji ya Gileadi.
JDG 12:8 Baada yake, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli.
JDG 12:9 Alikuwa na wana thelathini na binti thelathini. Akawaoza binti zake kwa watu wengine nje ya ukoo wake, na kuwatwalia wanawe wanawake thelathini toka nje ya ukoo wake. Ibzani akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka saba.
JDG 12:10 Kisha Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.
JDG 12:11 Baada yake, Eloni Mzabuloni akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka kumi.
JDG 12:12 Kisha Eloni akafa, akazikwa huko Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.
JDG 12:13 Baada yake, Abdoni mwana wa Hileli Mpirathoni akawa mwamuzi wa Israeli.
JDG 12:14 Naye alikuwa na wana arobaini, na wajukuu thelathini waliopanda punda sabini. Akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka nane.
JDG 12:15 Kisha Abdoni mwana wa Hileli Mpirathoni akafa, akazikwa Pirathoni huko Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.
JDG 13:1 Waisraeli wakafanya maovu tena mbele za Mwenyezi Mungu. Hivyo Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini.
JDG 13:2 Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, aliyeitwa Manoa, wa ukoo wa Wadani, naye alikuwa na mke aliyekuwa tasa, asiyeweza kuzaa watoto.
JDG 13:3 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea huyo mwanamke na kumwambia, “Wewe ni tasa na huna mtoto, lakini utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume.
JDG 13:4 Lakini ujihadhari sana usinywe divai wala kileo kingine chochote, wala usile kitu chochote kilicho najisi,
JDG 13:5 kwa kuwa utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume. Wembe usipite kwenye kichwa chake, kwa kuwa huyo mwana atakuwa Mnadhiri aliyetengwa kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yake. Naye atawaongoza na kuwaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wafilisti.”
JDG 13:6 Ndipo huyo mwanamke akamwendea mumewe na kumwambia, “Mtu wa Mungu alinijia. Alionekana kama malaika wa Mungu, wa kutisha sana. Sikumuuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake.
JDG 13:7 Lakini aliniambia, ‘Utachukua mimba na utazaa mtoto wa kiume. Basi sasa, usinywe divai wala kileo kingine chochote, wala usile kitu kilicho najisi, kwa kuwa huyo mtoto atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake hadi kufa kwake.’ ”
JDG 13:8 Ndipo Manoa akamwomba Mwenyezi Mungu, akasema: “Ee Bwana, nakusihi huyo mtu wa Mungu uliyemtuma kwetu aje tena, ili atufundishe jinsi ya kumlea huyo mwana atakayezaliwa.”
JDG 13:9 Mungu akamsikia Manoa, naye malaika wa Mungu akamjia tena huyo mwanamke alipokuwa shambani; lakini mumewe Manoa hakuwa naye.
JDG 13:10 Basi yule mwanamke akaenda haraka na kumwambia mumewe, “Tazama mtu yule aliyenitokea siku ile yupo hapa!”
JDG 13:11 Manoa akainuka akaandamana na mkewe. Alipomfikia yule mtu akamuuliza, “Je, wewe ndiwe ulisema na mke wangu?” Akasema, “Ni mimi.”
JDG 13:12 Basi Manoa akamuuliza, “Maneno yako yatakapotimia, je, masharti ya maisha ya mtoto huyu yatakuwa ni yapi, na kazi yake itakuwa ni ipi?”
JDG 13:13 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamjibu, “Mke wako hana budi kufanya yale yote niliyomwambia.
JDG 13:14 Kamwe asile kitu chochote kitakachotoka katika mzabibu, wala asinywe divai yoyote wala kileo chochote, wala asile kitu chochote kilicho najisi. Hana budi kufanya kila kitu nilichomwagiza.”
JDG 13:15 Manoa akamjibu yule malaika wa Mwenyezi Mungu, “Twakuomba usubiri kwanza ili tuweze kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.”
JDG 13:16 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamjibu, “Hata kama utanizuia, sitakula chochote kwako. Lakini ukitaka kuandaa sadaka ya kuteketezwa, mtolee Mwenyezi Mungu.” (Manoa hakumtambua kuwa huyu alikuwa malaika wa Mwenyezi Mungu.)
JDG 13:17 Kisha Manoa akamuuliza yule malaika wa Mwenyezi Mungu, “Jina lako ni nani, ili tuweze kukupa heshima wakati maneno uliyonena yatakapotimia?”
JDG 13:18 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamjibu, “Kwa nini unauliza jina langu? Ni jina la ajabu.”
JDG 13:19 Ndipo Manoa akamchukua mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, naye akamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu hapo juu ya mwamba. Naye yule malaika wa Mwenyezi Mungu akafanya jambo la ajabu wakati Manoa na mkewe wakiwa wanaangalia:
JDG 13:20 Mwali wa moto kutoka hapo madhabahuni ulipowaka kuelekea mbinguni, malaika wa Mwenyezi Mungu akapaa ndani ya huo mwali. Manoa na mkewe, kwa kuona jambo hili, wakaanguka kifudifudi.
JDG 13:21 Malaika wa Mwenyezi Mungu hakumtokea tena Manoa na mkewe. Ndipo Manoa akatambua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi Mungu.
JDG 13:22 Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, kwa kuwa tumemwona Mungu.”
JDG 13:23 Lakini mkewe akamwambia, “Ikiwa Mwenyezi Mungu alikuwa amekusudia kutuua, hangepokea sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya unga kutoka mikononi mwetu, wala hangetuonesha mambo haya yote wala kututangazia mambo haya wakati huu.”
JDG 13:24 Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume, akamwita jina Samsoni. Kijana akakua, naye Mwenyezi Mungu akambariki.
JDG 13:25 Roho wa Mwenyezi Mungu akaanza kumpa msukumo alipokuwa huko Mahane-Dani, kati ya Sora na Eshtaoli.
JDG 14:1 Samsoni akateremka Timna, na huko akamwona mwanamke Mfilisti.
JDG 14:2 Alipopanda kutoka huko, akawaambia baba yake na mama yake, “Nimemwona mwanamke Mfilisti huko Timna; basi mnitwalie awe mke wangu.”
JDG 14:3 Baba yake na mama yake wakamjibu, “Je, hakuna mwanamke miongoni mwa jamaa yako au miongoni mwa watu wetu wote, hata ulazimike kwenda kujitwalia mke kutoka kwa hao Wafilisti wasiotahiriwa?” Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Nipatieni huyo kwa maana ndiye alinipendeza.”
JDG 14:4 (Baba yake na mama yake hawakujua kuwa jambo hili limetoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani alikuwa akitafuta sababu ya kukabiliana na Wafilisti; kwa kuwa wakati huo walikuwa wakiwatawala Waisraeli.)
JDG 14:5 Samsoni akateremka Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia.
JDG 14:6 Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Samsoni kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono mitupu kama ambavyo angempasua mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake alichokifanya.
JDG 14:7 Basi akateremka na kuongea na yule mwanamke, naye akampendeza Samsoni.
JDG 14:8 Baada ya muda, Samsoni aliporudi ili akamwoe, akageuka kando ili kuutazama mzoga wa yule simba. Tazama! Ndani ya ule mzoga akaona kundi la nyuki na asali kiasi.
JDG 14:9 Akachukua asali mkononi mwake, akala huku akitembea. Alipowafikia baba yake na mama yake, akawapa kiasi cha ile asali, nao wakala. Lakini hakuwaambia kuwa aliitwaa asali katika mzoga wa simba.
JDG 14:10 Basi baba yake akateremka kumwona huyo mwanamke. Samsoni akafanya karamu huko, kama ilivyokuwa desturi ya vijana.
JDG 14:11 Watu walipomwona, wakaleta vijana wenzake thelathini ili kuwa pamoja naye.
JDG 14:12 Samsoni akawaambia, “Niwape kitendawili, mkiweza kunipa jibu katika muda wa siku hizi saba za karamu, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.
JDG 14:13 Lakini msipoweza kufumbua, ndipo ninyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.” Wakamwambia, “Tuambie hicho kitendawili, hebu na tukisikie.”
JDG 14:14 Akawaambia, “Ndani ya mlaji, kulitoka kitu cha kuliwa, ndani ya mwenye nguvu, kulitoka kitu kitamu.” Kwa muda wa siku tatu hawakuweza kutoa jibu.
JDG 14:15 Siku ya nne, wakamwambia mkewe Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atutegulie hicho kitendawili, la sivyo tutakuchoma moto wewe na wa nyumba ya baba yako. Je, mmetualika ili mpate kutunyang’anya kile tulicho nacho?”
JDG 14:16 Basi mke wa Samsoni akalia mbele yake na kumwambia, “Unanichukia! Hunipendi kabisa. Umewategea watu wangu kitendawili, lakini mimi hujaniambia jibu.” Samsoni akamwambia, “Tazama, sijamweleza baba yangu wala mama yangu, kwa nini nikufumbulie?”
JDG 14:17 Mkewe akalia kwa muda wa zile siku zote saba za karamu. Hivyo siku ya saba Samsoni akamweleza, kwa kuwa aliendelea kumsisitiza sana. Naye mkewe akawaeleza watu wake kile kitendawili.
JDG 14:18 Siku ya saba, kabla ya jua kutua, wanaume wa mji wakamwambia Samsoni, “Ni nini kilicho kitamu kuliko asali? Ni nini chenye nguvu kuliko simba?” Samsoni akawaambia, “Kama hamkulima na mtamba wangu, msingekitegua kitendawili changu.”
JDG 14:19 Ndipo Roho wa Mwenyezi Mungu akamjia Samsoni kwa nguvu. Samsoni akateremka hadi Ashkeloni, akawaua wanaume thelathini wa mji huo, akatwaa mali yao, akawapa watu wale waliotegua kile kitendawili nguo zao. Akiwa amejaa hasira, akakwea kurudi nyumbani kwa baba yake.
JDG 14:20 Naye mke wa Samsoni akakabidhiwa kwa rafiki yake Samsoni aliyekuwa msaidizi wake siku ya arusi.
JDG 15:1 Baada ya kitambo kidogo, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni akachukua mwana-mbuzi, kwenda kumzuru mkewe. Akasema, “Nataka kuingia chumbani kwa mke wangu.” Lakini baba yake huyo mwanamke hakumruhusu kuingia.
JDG 15:2 Baba mkwe wake akamwambia, “Nilikuwa na hakika kwamba ulimchukia, hivyo nikampeana kwa rafiki yako. Je, dada yake mdogo si mzuri kuliko yeye? Mchukue huyo badala yake.”
JDG 15:3 Samsoni akawaambia, “Wakati huu, nitakapowadhuru Wafilisti, sitakuwa na lawama.”
JDG 15:4 Hivyo Samsoni akaondoka na kuwakamata mbweha mia tatu, akawafunga wawili wawili, mikia kwa mikia. Kisha akafungia mwenge wa moto kwenye kila jozi la mikia hiyo.
JDG 15:5 Akawasha ile mienge na kuwaachia wale mbweha katika mashamba ya Wafilisti ya nafaka zilizosimamishwa katika matita. Akateketeza matita ya nafaka, pamoja na mashamba ya mizabibu na mashamba ya mizeituni.
JDG 15:6 Wafilisti walipouliza, “Ni nani aliyetenda jambo hili?” Wakaambiwa, “Ni Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu mkewe alipeanwa kwa rafiki yake.” Hivyo Wafilisti wakapanda, wakamteketeza kwa moto yeye huyo mwanamke pamoja na baba yake.
JDG 15:7 Samsoni akawaambia, “Kwa kuwa mmetenda hivyo, hakika sitatulia hadi niwe nimelipiza kisasi juu yenu.”
JDG 15:8 Akawashambulia kwa ukali na kuwaua watu wengi sana. Kisha akateremka na kukaa kwenye pango katika mwamba wa Etamu.
JDG 15:9 Wafilisti wakapanda na kupiga kambi huko Yuda na kuenea huko Lehi.
JDG 15:10 Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kupigana nasi?” Wakawajibu, “Tumekuja ili kumkamata Samsoni na kumtenda kama alivyotutendea.”
JDG 15:11 Ndipo watu elfu tatu wa Yuda waliteremka hadi kwenye pango katika mwamba wa Etamu, wakamwambia Samsoni, “Je, hujatambua kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hiki ulichotutendea?” Akawajibu, “Nimewatendea tu kile walichonitendea.”
JDG 15:12 Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga na kukutia mikononi mwa Wafilisti.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kuwa hamtaniua ninyi wenyewe.”
JDG 15:13 Wakamjibu, “Sisi hatutakuua, bali tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumchukua toka huko kwenye pango katika mwamba.
JDG 15:14 Alipokaribia Lehi, Wafilisti wakamjia wakipiga kelele. Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu yake kwa nguvu. Kamba zilizomfunga mikono zikawa kama kitani iliyochomwa kwa moto, na vifungo vyake vikaanguka chini toka mikononi mwake.
JDG 15:15 Ndipo akaona mfupa mpya wa taya la punda, akanyoosha mkono, akauchukua na kuua nao Wafilisti wapatao elfu moja.
JDG 15:16 Ndipo Samsoni akasema, “Kwa taya la punda malundo juu ya lundo, kwa taya la punda nimeua watu elfu moja.”
JDG 15:17 Alipomaliza kusema, akautupa ule mfupa wa taya; na mahali pale pakaitwa Ramath-Lehi.
JDG 15:18 Kwa kuwa alihisi kiu sana, akamlilia Mwenyezi Mungu, akisema, “Umempa mtumishi wako ushindi huu mkuu. Je, sasa nife kwa kiu na kuangukia mikononi mwa hawa watu wasiotahiriwa?”
JDG 15:19 Ndipo Mungu akafunua shimo huko Lehi, na maji yakatoka. Samsoni alipoyanywa maji hayo, nguvu zikamrudia, akahuika. Hivyo chemchemi ile ikaitwa En-Hakore, nayo iko hadi leo huko Lehi.
JDG 15:20 Samsoni akawa mwamuzi wa Waisraeli katika siku za Wafilisti kwa muda wa miaka ishirini.
JDG 16:1 Siku moja Samsoni alienda Gaza, akamwona mwanamke kahaba, naye akaingia kwake.
JDG 16:2 Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni amekuja huku!” Hivyo, wakapazingira mahali pale, nao wakamvizia usiku kucha penye lango la mji. Wakakaa kimya usiku kucha, wakiwaza, “Kutakapopambazuka, tutamuua.”
JDG 16:3 Samsoni akalala tu hadi usiku wa manane. Akaamka, na kushika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing’oa pamoja na makomeo yake. Akaviweka mabegani mwake na kuvipeleka hadi kilele cha mlima unaokabili Hebroni.
JDG 16:4 Baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika Bonde la Soreki aliyeitwa Delila.
JDG 16:5 Viongozi wa Wafilisti wakamwendea yule mwanamke na kumwambia, “Mshawishi ili upate kujua siri ya nguvu zake zilizo nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda ili tuweze kumfunga na kumtiisha. Kila mmoja wetu atakupa shekeli elfu moja na mia moja za fedha.”
JDG 16:6 Hivyo Delila akamwambia Samsoni, “Naomba uniambie siri ya hizi nguvu zako nyingi, na jinsi unavyoweza kufungwa ili kukutiisha.”
JDG 16:7 Samsoni akamjibu, “Kama nikifungwa kwa kamba saba za upinde ambazo hazijakauka, hapo ndipo nitakapokuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”
JDG 16:8 Basi viongozi wa Wafilisti wakamletea yule mwanamke kamba saba za upinde ambazo hazijakauka, naye akamfunga Samsoni.
JDG 16:9 Wakati watu wakiwa wanamvizia katika chumba cha ndani, yule mwanamke akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini yeye akazikata zile kamba za upinde, kama vile uzi wa pamba unapoguswa na moto. Hivyo siri ya nguvu zake haikujulikana.
JDG 16:10 Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Tafadhali niambie unaweza kufungwa kwa kitu gani?”
JDG 16:11 Akamwambia, “Kama nikifungwa kwa uthabiti kwa kamba mpya ambazo hazijatumika, basi nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”
JDG 16:12 Hivyo, Delila akachukua kamba mpya na kumfunga nazo. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Wale watu waliokuwa wanamvizia walikuwa katika chumba cha ndani. Lakini akazikata zile kamba zilizokuwa zimefunga mikono yake kama nyuzi.
JDG 16:13 Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Hata sasa umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Nieleze ni jinsi gani unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Kama ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu kwa nguo iliyo katika mtande, na kuukaza kwa msumari, ndipo nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.” Hivyo, Samsoni alipokuwa amelala, Delila akachukua vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake na kuvifuma pamoja na nguo kwenye mtande,
JDG 16:14 na kuukaza kwa msumari. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Samsoni akaamka kutoka usingizini na kung’oa msumari na mtande, pamoja na ile nguo.
JDG 16:15 Ndipo Delila akamwambia, “Wawezaje kusema, ‘Nakupenda,’ wakati moyo wako haupo pamoja nami? Umenifanyia mzaha mara hizi tatu na hujaniambia siri ya hizi nguvu zako nyingi.”
JDG 16:16 Hatimaye, baada ya kusumbuliwa kwa maneno kwa siku nyingi na kuudhiwa, roho yake ikataabika kiasi cha kufa.
JDG 16:17 Hivyo, akamwambia yule mwanamke siri yake yote, akisema, “Wembe haujapita kamwe kichwani mwangu, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nywele za kichwa changu zikinyolewa, nguvu zangu zitanitoka, na nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote!”
JDG 16:18 Delila alipoona kuwa amemweleza siri yake yote, akatuma ujumbe kwa viongozi wa Wafilisti na kusema, “Njooni tena mara nyingine, maana amenieleza siri yake yote.” Basi viongozi wa Wafilisti wakarudi kwa Delila, wakiwa na fedha mikononi mwao.
JDG 16:19 Delila akamfanya alale usingizi magotini pake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake. Delila akaanza kumnyong’onyesha Samsoni, nazo nguvu zake zikamtoka.
JDG 16:20 Yule mwanamke akamwita, “Samsoni! Hao, Wafilisti wanakujia!” Akaamka toka usingizini, akisema, “Nitatoka nje kama hapo awali; nitajinyoosha, niwe huru.” Lakini hakujua kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa amemwacha.
JDG 16:21 Basi Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho yake, wakamteremsha hadi Gaza. Wakamfunga kwa pingu za shaba, wakamweka gerezani ili asage ngano.
JDG 16:22 Wakati huo nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa.
JDG 16:23 Basi viongozi wa Wafilisti wakakusanyika pamoja ili kutoa kafara kuu kwa mungu wao Dagoni, wakisherehekea na kusema, “Mungu wetu amemtia adui yetu Samsoni mikononi mwetu.”
JDG 16:24 Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao, wakisema: “Sasa mungu wetu amemtia adui yetu mikononi mwetu, yule aliyeharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.”
JDG 16:25 Mioyo yao ilipokuwa imefurahishwa, wakapaza sauti, wakisema, “Mleteni Samsoni aje ili atutumbuize.” Basi wakamleta Samsoni kutoka gerezani, naye akawatumbuiza. Wakamsimamisha katikati ya nguzo mbili.
JDG 16:26 Samsoni akamwambia mtumishi aliyeushika mkono wake, “Niweke mahali ambapo ninaweza kuzigusa nguzo ambazo zinategemeza jengo ili nipate kuziegemea.”
JDG 16:27 Basi lile jengo lilikuwa na wanaume na wanawake wengi; viongozi wote wa Wafilisti walikuwa humo, na kwenye dari walikuwepo watu wapatao elfu tatu, wanaume kwa wanawake, wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza.
JDG 16:28 Ndipo Samsoni akamwomba Mwenyezi Mungu, akasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, unikumbuke. Ee Mungu, nakusihi ukanitie nguvu mara hii moja tu, ili kwa tendo hili nipate kulipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa sababu ya macho yangu mawili.”
JDG 16:29 Ndipo Samsoni akazikaribia zile nguzo mbili za katikati zilizokuwa zimelisimamisha lile jengo. Akazishika moja kwa mkono wa kuume, na nyingine kwa mkono wa kushoto.
JDG 16:30 Samsoni akasema, “Acha nife pamoja na Wafilisti!” Ndipo akazisukuma zile nguzo kwa nguvu zake zote, nalo jengo lile likaanguka juu ya viongozi na watu wote waliokuwamo ndani. Hivyo, akawaua watu wengi wakati wa kufa kwake kuliko siku za uhai wake.
JDG 16:31 Basi ndugu zake na jamaa yote ya baba yake wakateremka kwenda kumchukua. Wakampandisha na kumzika kati ya Sora na Eshtaoli, kwenye kaburi la Manoa baba yake. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.
JDG 17:1 Palikuwa na mtu aliyeitwa Mika kutoka nchi ya vilima ya Efraimu.
JDG 17:2 Akamwambia mama yake, “Zile shekeli elfu moja na mia moja za fedha zilizochukuliwa kwako, ambazo nilisikia ukizinenea maneno ya laana, hizi hapa; mimi ndiye niliyezichukua.” Ndipo mama yake akamwambia, “Mwenyezi Mungu na akubariki, mwanangu.”
JDG 17:3 Alipozirudisha zile shekeli elfu moja na mia moja za fedha kwa mama yake, mama yake akamwambia, “Mimi nimeiweka fedha hii wakfu kwa Mwenyezi Mungu ili mwanangu atengeneze sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu. Mimi nitakurudishia wewe.”
JDG 17:4 Hivyo akamrudishia mama yake ile fedha, naye mama yake akachukua shekeli mia mbili za hiyo fedha na kumpa mfua fedha, ambaye aliifanyiza kinyago na sanamu. Navyo vikawekwa ndani ya nyumba ya Mika.
JDG 17:5 Basi Mika alikuwa na mahali pa ibada za sanamu. Akatengeneza kizibau, pamoja na miungu ya nyumbani, na kumweka mmoja wa wanawe kuwa kuhani wake.
JDG 17:6 Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme; kila mtu alifanya alivyoona ni vyema machoni pake.
JDG 17:7 Palikuwa na kijana Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, aliyekuwa akiishi miongoni mwa watu wa kabila la Yuda.
JDG 17:8 Huyu kijana akatoka mji huo wa Bethlehemu ya Yuda na kutafuta mahali pengine pa kuishi. Alipokuwa akisafiri, akafika nyumbani kwa Mika katika nchi ya vilima ya Efraimu.
JDG 17:9 Mika akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?” Akamjibu, “Mimi ni Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, ninatafuta mahali pa kuishi.”
JDG 17:10 Ndipo Mika akamwambia, “Ishi pamoja nami, uwe baba yangu na kuhani wangu, nami nitakupa shekeli kumi za fedha kila mwaka, pamoja na nguo na chakula.”
JDG 17:11 Hivyo yule Mlawi akakubali kuishi pamoja na Mika, naye akawa kama mmoja wa wanawe.
JDG 17:12 Basi Mika akamweka wakfu huyo kijana Mlawi, naye huyo akawa kuhani wake na kuishi nyumbani mwake.
JDG 17:13 Mika akasema, “Sasa najua Mwenyezi Mungu atanitendea mema, kwa kuwa Mlawi huyu amekuwa kuhani wangu.”
JDG 18:1 Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme. Katika siku hizo, watu wa kabila la Dani walikuwa wanatafuta mahali pao wenyewe pa kuishi, kwa sababu walikuwa hawajafika kwenye urithi wao miongoni mwa makabila ya Israeli.
JDG 18:2 Hivyo Wadani wakatuma mashujaa watano kutoka Sora na Eshtaoli ili kupeleleza nchi na kuichunguza. Hawa mashujaa waliwakilisha koo zao zote. Waliwaambia, “Nendeni mkaichunguze hiyo nchi.” Wanaume hao wakaingia katika nchi ya vilima ya Efraimu, wakafika nyumba ya Mika, ambako walilala usiku huo.
JDG 18:3 Walipofika karibu na nyumba ya Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi; hivyo wakaingia humo na kumuuliza, “Ni nani aliyekuleta hapa? Unafanya nini mahali hapa? Kwa nini uko hapa?”
JDG 18:4 Akawaeleza yale Mika aliyomtendea, akasema, “Ameniajiri, nami ni kuhani wake.”
JDG 18:5 Kisha wakamwambia, “Tafadhali tuulizie kwa Mungu kama safari yetu itafanikiwa.”
JDG 18:6 Yule kuhani akawajibu, “Nendeni kwa amani. Safari yenu ina kibali cha Mwenyezi Mungu.”
JDG 18:7 Basi hao wanaume watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa amani na utulivu. Nchi yao haikupungukiwa kitu, hivyo wakastawi. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote.
JDG 18:8 Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?”
JDG 18:9 Wakajibu, “Twendeni, tukawavamie! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki.
JDG 18:10 Mtakapofika huko, mtawakuta watu walio salama, na nchi kubwa ambayo Mungu ameitia mikononi mwenu, isiyopungukiwa kitu chochote duniani.”
JDG 18:11 Ndipo wanaume mia sita kutoka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli.
JDG 18:12 Walipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Dani hadi leo.
JDG 18:13 Kutoka hapo wakaenda hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika.
JDG 18:14 Ndipo wale wanaume watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mnajua kuwa katika mojawapo ya nyumba hizi kuna kizibau, miungu ya nyumbani, sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Sasa basi, fikirini mtakalofanya.”
JDG 18:15 Basi wakaelekea huko, wakafika kwa yule kijana Mlawi, katika nyumba ya Mika, wakamsalimu.
JDG 18:16 Wale Wadani mia sita, wakiwa wamejifunga silaha, wakasimama penye ingilio la lango.
JDG 18:17 Wale watu watano walioenda kupeleleza nchi wakaingia ndani na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, kile kizibau, na ile miungu ya nyumbani, na ile sanamu ya kusubu, wakati yule kuhani akiwa amesimama pale penye ingilio la lango pamoja na wale watu mia sita waliojifunga silaha.
JDG 18:18 Hao watu walipoingia katika nyumba ya Mika na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, kile kizibau, na ile miungu ya nyumbani, na ile sanamu ya kusubu, yule kuhani akawauliza, “Mnafanya nini?”
JDG 18:19 Wakamjibu, “Nyamaza! Weka mkono wako juu ya kinywa chako na ufuatane nasi, uwe baba yetu na kuhani wetu. Si ni afadhali utumikie kabila na ukoo katika Israeli kama kuhani kuliko kumtumikia mtu mmoja na watu wa nyumbani mwake?”
JDG 18:20 Yule kuhani akafurahi. Akachukua kile kizibau, ile miungu ya nyumbani, na sanamu ya kuchonga, naye akaenda pamoja na wale watu.
JDG 18:21 Ndipo wakageuka na kuondoka, wakiwatanguliza mbele watoto wao wadogo, mifugo na mali yao.
JDG 18:22 Walipokuwa wamefika mbali toka nyumbani kwa Mika, watu walioishi karibu na Mika walikusanywa pamoja, nao wakawakimbiza Wadani.
JDG 18:23 Walipofuatilia huku wakipiga kelele, Wadani wakageuka, wakamwambia Mika, “Una nini wewe hata ukawaita watu waje kupigana nasi?”
JDG 18:24 Akawajibu, “Mmechukua miungu niliyoitengeneza, mkamchukua kuhani wangu, nanyi mkaondoka. Nimebaki na nini kingine? Mnawezaje kuniuliza, ‘Una nini wewe?’ ”
JDG 18:25 Wadani wakamjibu, “Usibishane nasi, la sivyo watu wenye hasira watakushambulia, nawe na watu wa nyumbani mwako mtapoteza maisha yenu.”
JDG 18:26 Basi Wadani wakaenda zao, naye Mika alipoona kuwa wana nguvu kuliko yeye, akageuka na kurudi nyumbani mwake.
JDG 18:27 Kisha wakachukua vitu vile Mika alikuwa amevitengeneza, na kuhani wake, wakaendelea hadi Laishi, dhidi ya watu walioishi na amani na utulivu. Wakawashambulia kwa upanga na kuuteketeza mji wao.
JDG 18:28 Hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa, kwa kuwa waliishi mbali na Sidoni, na hawakuwa na ushirikiano na mtu mwingine yeyote. Mji huo ulikuwa kwenye bonde karibu na Beth-Rehobu. Wadani wakaujenga upya huo mji na kuishi humo.
JDG 18:29 Wakauita ule mji Dani kwa kufuata jina la baba yao aliyezaliwa na Israeli, ingawa mji huo uliitwa Laishi hapo awali.
JDG 18:30 Kule Wadani wakajisimamishia ile sanamu ya kuchonga, naye Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa pamoja na wanawe walikuwa makuhani kwa kabila la Dani hadi nchi hiyo ilipotekwa.
JDG 18:31 Wakaendelea kuiabudu ile sanamu ambayo Mika alizitengeneza, wakati wote ule nyumba ya Mungu ilikuwa huko Shilo.
JDG 19:1 Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme. Basi Mlawi mmoja aliyeishi sehemu za mbali katika nchi ya vilima ya Efraimu, akamchukua suria mmoja kutoka Bethlehemu ya Yuda.
JDG 19:2 Lakini suria wake akafanya ukahaba, akamwacha na kurudi nyumbani mwa baba yake huko Bethlehemu ya Yuda. Baada ya kukaa huko kwa muda wa miezi minne,
JDG 19:3 mume wake akaenda kumsihi arudi. Alienda na mtumishi wake na punda wawili. Yule mwanamke akamkaribisha nyumbani mwa baba yake, naye baba yake alipomwona akamkaribisha kwa furaha.
JDG 19:4 Baba mkwe wake, yaani baba yake yule msichana, akamsihi akae. Hivyo akakaa na huyo baba mkwe wake kwa siku tatu, wakila na kunywa, na kulala huko.
JDG 19:5 Siku ya nne wakaamka mapema naye akajiandaa kuondoka, lakini baba wa yule msichana akamwambia mkwewe, “Ujiburudishe kwa kitu cha kula, ndipo uweze kwenda.”
JDG 19:6 Basi wakaketi wote wawili ili kula na kunywa pamoja. Baadaye baba wa msichana akamwambia, “Tafadhali ubakie usiku huu upate kujifurahisha.”
JDG 19:7 Basi yule mtu alipotaka kuondoka, baba mkwe wake akamsihi, hivyo akabaki usiku ule.
JDG 19:8 Asubuhi ya siku ya tano, alipoamka ili aondoke, baba wa yule msichana akamwambia, “Jiburudishe nafsi yako. Ngoja hadi alasiri!” Kwa hiyo wote wawili wakala chakula pamoja.
JDG 19:9 Kisha yule mtu alipoinuka aende zake pamoja na suria wake na mtumishi wake, baba mkwe wake, yaani baba wa yule msichana, akamwambia, “Tazama sasa jioni inakaribia. Ulale hapa, usiku unakaribia. Ukae, ukajifurahishe nafsi yako. Kesho unaweza kuamka asubuhi na mapema uende nyumbani kwako.”
JDG 19:10 Lakini akakataa kulala tena, akaondoka na kuelekea Yebusi (ndio Yerusalemu), akiwa na punda wake wawili waliotandikwa, pamoja na suria wake.
JDG 19:11 Alipokaribia Yebusi na usiku ukiwa umekaribia, mtumishi akamwambia bwana wake, “Haya sasa natuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo.”
JDG 19:12 Lakini bwana wake akamjibu, “Hapana. Hatutaingia kwenye mji wa kigeni, ambao watu wake si Waisraeli. Tutaendelea hadi Gibea.”
JDG 19:13 Tena akasema, “Haya, tujitahidi tufike Gibea au Rama, nasi tutalala katika mji huo.”
JDG 19:14 Hivyo wakaendelea na safari, nalo jua likazama walipokaribia Gibea ya Benyamini.
JDG 19:15 Wakageuka ili kuingia na kulala Gibea. Wakaingia humo, wakaketi kwenye uwanja wa mji, wala hakuna mtu yeyote aliyewakaribisha kwake ili wapate kulala.
JDG 19:16 Jioni ile, mzee mmoja toka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyekuwa anaishi huko Gibea (watu wa sehemu ile walikuwa Wabenyamini), akarudi kutoka kwenye kazi zake za shamba.
JDG 19:17 Alipotazama na kuwaona hao wasafiri katika uwanja wa mji, yule mzee akawauliza, “Ninyi mnaenda wapi? Nanyi mmetoka wapi?”
JDG 19:18 Akamwambia, “Tumepita kutoka Bethlehemu ya Yuda, tunaelekea katika nchi ya vilima ya Efraimu ninakoishi. Nilienda Bethlehemu ya Yuda na sasa ninaenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu yeyote aliyenikaribisha katika nyumba yake.
JDG 19:19 Tunazo nyasi na chakula cha punda wetu, pia mkate na divai kwa ajili yetu sisi watumishi wako: mimi, mtumishi wako mwanamke, pamoja na huyu kijana tuliye naye. Hatuhitaji kitu zaidi.”
JDG 19:20 Yule mzee akawaambia, “Amani iwe kwenu! Karibuni nyumbani mwangu. Nitawapa mahitaji yenu yote, ila tu msilale katika uwanja huu.”
JDG 19:21 Hivyo akamwingiza nyumbani mwake na kuwalisha punda wake. Baada ya kunawa miguu yao, wakala na kunywa.
JDG 19:22 Walipokuwa wakijiburudisha, wanaume waovu wa mji huo wakaizingira ile nyumba. Wakagonga mlango na kusema kwa sauti kuu kwa yule mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanaume aliyeingia kwako, tupate kumlawiti.”
JDG 19:23 Yule mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Hapana, ndugu zangu, msiwe waovu namna hii, ninawasihi. Kwa kuwa huyu mwanaume ni mgeni wangu, msifanye jambo hili la aibu.
JDG 19:24 Tazameni, hapa yupo binti yangu ambaye ni bikira, na suria wa mtu huyu. Nitawatoleeni hawa sasa, mkawatwae kwa nguvu na kuwafanyia lolote mtakalo. Lakini kwa mwanaume huyu msimfanyie jambo ovu hivyo.”
JDG 19:25 Lakini wale wanaume hawakumsikiliza. Hivyo yule mwanaume akamtoa yule suria wake nje kwa wale watu, nao wakambaka na kumnajisi usiku kucha hadi asubuhi. Kulipoanza kupambazuka, wakamwachia aende.
JDG 19:26 Alfajiri yule mwanamke akarudi kwenye ile nyumba bwana wake alikokuwa, akaanguka chini mlangoni, akalala pale hata kulipopambazuka.
JDG 19:27 Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua mlango wa nyumba na kutoka nje ili kuendelea na safari yake, tazama, yule suria wake alikuwa ameangukia penye ingilio la nyumba, mikono yake ikiwa penye kizingiti.
JDG 19:28 Akamwambia yule suria, “Inuka, twende.” Lakini hakujibu. Yule bwana akamwinua, akampandisha juu ya punda wake, na wakaondoka kwenda nyumbani.
JDG 19:29 Alipofika nyumbani, akachukua kisu na kumkatakata yule suria kiungo kwa kiungo, vipande kumi na mbili, na kuvipeleka katika sehemu zote za Israeli.
JDG 19:30 Kila mtu aliyeona akasema, “Jambo la namna hii halijaonekana wala kutendeka, tangu Waisraeli walipopanda kutoka Misri. Fikirini juu ya jambo hili! Tafakarini juu ya jambo hili! Tuambieni tufanye nini!”
JDG 20:1 Ndipo Waisraeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na wa kutoka nchi ya Gileadi wakatoka kama mtu mmoja, wakakusanyika mbele za Mwenyezi Mungu huko Mispa.
JDG 20:2 Viongozi wote wa makabila ya Israeli wakakaa kwenye nafasi zao katika kusanyiko la watu wa Mungu, ambao walikuwa askari elfu mia nne walioenda kwa miguu wenye panga.
JDG 20:3 (Wabenyamini wakasikia kuwa Waisraeli wamepanda kwenda Mispa.) Ndipo Waisraeli wakasema, “Tuelezeni jinsi jambo hili ovu lilivyotendeka.”
JDG 20:4 Hivyo yule Mlawi, mume wa yule mwanamke aliyeuawa, akasema, “Mimi na suria wangu tulifika Gibea ya Benyamini ili tulale huko.
JDG 20:5 Wakati wa usiku wanaume wa Gibea wakanijia na kuizingira nyumba, wakitaka kuniua. Wakambaka suria wangu hata akafa.
JDG 20:6 Ndipo nikamchukua suria wangu, nikamkatakata vipande vipande na kuvipeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli, kwa kuwa wametenda uasherati mkubwa na jambo la aibu katika Israeli.
JDG 20:7 Sasa, ninyi Waisraeli wote, semeni na mtoe uamuzi wenu.”
JDG 20:8 Watu wote wakainuka wakasema, kama mtu mmoja, “Hakuna hata mmoja wetu atakayeenda nyumbani. Hakuna hata mmoja wetu atakayerudi nyumbani kwake.
JDG 20:9 Sasa hili ndilo tutakaloitendea Gibea: Tutaikabili jinsi kura itakavyotuongoza.
JDG 20:10 Tutatoa watu kumi katika kila mia moja kutoka kwenye makabila yote ya Israeli, watu mia moja katika kila elfu moja, na watu elfu moja katika kila elfu kumi, ili waende wakalete mahitaji kwa ajili ya jeshi. Basi wakati jeshi litakapofika Gibea ya Benyamini, watawatendea yale wanayostahili, kwa ajili ya uovu huu walioutenda katika Israeli.”
JDG 20:11 Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakutanika pamoja na kujiunga kama mtu mmoja dhidi ya huo mji.
JDG 20:12 Makabila ya Israeli yakatuma watu kwenda katika kabila la Benyamini lote na kuwaambia, “Ni uovu gani huu wa kutisha uliotendeka kati yenu?
JDG 20:13 Basi watoeni hao wanaume waovu wa Gibea, ili tupate kuwaua na kuuondoa uovu katika Israeli.” Lakini Wabenyamini hawakuwasikia ndugu zao, Waisraeli.
JDG 20:14 Wakatoka katika miji yao, wakakutanika Gibea ili kupigana na Waisraeli.
JDG 20:15 Siku ile Wabenyamini wakakusanya watu elfu ishirini na sita kutoka miji yao waliojifunga panga, mbali na hao vijana wenye uwezo mia saba kutoka wale walioishi Gibea.
JDG 20:16 Miongoni mwa askari hao, palikuwa na askari mia saba waliochaguliwa waliotumia mkono wa kushoto; kila mmoja wao angetupa jiwe kwa kombeo na kulenga unywele bila kukosa.
JDG 20:17 Nao wanaume wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, wakakusanya wanaume elfu mia nne hodari wenye panga.
JDG 20:18 Waisraeli wakapanda Betheli na kumuuliza Mungu, “Ni nani miongoni mwetu atakayetangulia mbele yetu ili kupigana na Wabenyamini?” Mwenyezi Mungu akawajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia.”
JDG 20:19 Kesho yake asubuhi, Waisraeli wakaamka na kupiga kambi karibu na Gibea.
JDG 20:20 Waisraeli wakaondoka ili kupigana na Wabenyamini, nao Waisraeli wakachukua nafasi zao katika vita huko Gibea.
JDG 20:21 Wabenyamini wakatoka Gibea na kuwaua Waisraeli elfu ishirini na mbili siku hiyo.
JDG 20:22 Lakini Waisraeli wakatiana moyo kila mmoja na mwenzake, nao wakachukua tena nafasi zao katika vile vita mahali pale walipokuwa siku ya kwanza.
JDG 20:23 Waisraeli wakapanda mbele za Mwenyezi Mungu na kulia mbele zake hadi jioni. Nao wakamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, tupande tena kupigana vita na Wabenyamini, ndugu zetu?” Mwenyezi Mungu akajibu, “Pandeni mkapigane nao.”
JDG 20:24 Ndipo Waisraeli wakawakaribia Wabenyamini siku ya pili.
JDG 20:25 Wakati huu, Wabenyamini walipotoka Gibea ili kupigana na Waisraeli, wakawaua wanaume elfu kumi na nane wenye panga.
JDG 20:26 Ndipo jeshi lote, na Waisraeli wote, wakapanda Betheli, na huko wakakaa mbele za Mwenyezi Mungu wakilia. Wakafunga siku hiyo hadi jioni na kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu.
JDG 20:27 Nao Waisraeli wakauliza ushauri kwa Mwenyezi Mungu. (Katika siku hizo Sanduku la Agano la Mungu lilikuwa huko,
JDG 20:28 na Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anahudumu mbele za hilo Sanduku.) Wakauliza, “Je, tupande tena kwenda vitani kupigana na Wabenyamini, ndugu zetu, au la?” Mwenyezi Mungu akajibu, “Nendeni, kwa kuwa kesho nitawatia mikononi mwenu.”
JDG 20:29 Basi Waisraeli wakaweka waviziaji kuizunguka Gibea.
JDG 20:30 Kisha Waisraeli wakapanda kupigana na Wabenyamini katika siku ya tatu na kuchukua nafasi zao dhidi ya Gibea kama walivyokuwa wamefanya hapo awali.
JDG 20:31 Wabenyamini wakatoka ili kukabiliana na Waisraeli, ambao waliwavuta Wabenyamini watoke katika mji. Wakaanza kupigana na wakawaua watu wapatao thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika uwanja na katika njia kuu, moja iendayo Betheli na nyingine Gibea.
JDG 20:32 Wabenyamini walipokuwa wakiambiana, “Wanapigwa mbele yetu kama hapo awali,” nao Waisraeli waliambiana, “Turudini nyuma ili tuwavute wauache mji, waende kuelekea barabarani.”
JDG 20:33 Wanaume wote wa Israeli wakaondoka kwenye nafasi zao na kujipanga huko Baal-Tamari, nao wale waviziaji wa Waisraeli wakatoka ghafula walipokuwa kwenye uwanda wa magharibi mwa Gibea.
JDG 20:34 Ndipo vijana wenye uwezo elfu kumi katika Israeli wakaja kuishambulia Gibea. Vita vilikuwa vikali sana, hata Wabenyamini hawakutambua kuwa maangamizi yalikuwa karibu nao.
JDG 20:35 Mwenyezi Mungu akawashinda Wabenyamini mbele ya Waisraeli, na siku hiyo Waisraeli wakawaua Wabenyamini elfu ishirini na tano na mia moja wenye panga.
JDG 20:36 Hivyo Wabenyamini wakaona kuwa wameshindwa. Basi Waisraeli walikuwa wamewaondokea Wabenyamini, kwa sababu Waisraeli waliwategemea hao waviziaji waliokuwa wamewaweka karibu na Gibea.
JDG 20:37 Wale waviziaji wakafanya haraka kuingia Gibea, wakasambaa na kuwaua watu wote wa mji kwa upanga.
JDG 20:38 Waisraeli walikuwa wamekubaliana na hao waviziaji kuwa wangesababisha wingu kubwa la moshi lipande kutoka huo mji,
JDG 20:39 ndipo Waisraeli wangegeuka kupigana. Wabenyamini walikuwa wameanza kuwapiga na kuwaua Waisraeli (wapatao thelathini), hivyo wakasema, “Hakika tunawashinda kama tulivyowashinda katika vita hapo awali.”
JDG 20:40 Lakini nguzo ya moshi ilipoanza kupanda kutoka mji ule, Wabenyamini wakageuka, na tazama: katika mji mzima, moshi ulikuwa ukipaa angani.
JDG 20:41 Ndipo Waisraeli wakawageukia, nao Wabenyamini wakatiwa hofu, kwa kuwa walitambua kwamba maafa yamewajia.
JDG 20:42 Basi wakakimbia mbele ya Waisraeli kuelekea nyikani, lakini hawakuweza kukwepa vile vita. Nao Waisraeli waliotoka katika ile miji wakawaua huko.
JDG 20:43 Wakawazingira Wabenyamini pande zote, wakawafuatia na kuwafikia karibu na Gibea upande wa mashariki.
JDG 20:44 Wakaanguka Wabenyamini elfu kumi na nane, wote wapiganaji hodari.
JDG 20:45 Walipogeuka na kukimbia kuelekea nyikani hata kufikia mwamba wa Rimoni, Waisraeli wakawaua watu elfu tano huko njiani. Wakawafuatia kwa karibu hadi Gidomu, na huko wakawaua wanaume wengine elfu mbili.
JDG 20:46 Siku hiyo wakawaua Wabenyamini elfu ishirini na tano wenye panga, wapiganaji hodari.
JDG 20:47 Lakini watu mia sita wakakimbia kuelekea nyikani katika mwamba wa Rimoni, na kukaa huko muda wa miezi minne.
JDG 20:48 Waisraeli wakarudi na kuwaua kwa upanga Wabenyamini wote, pamoja na wanyama na kila walichokipata. Pia kila mji waliouona wakauchoma kwa moto.
JDG 21:1 Wanaume wa Israeli walikuwa wameapa kiapo kule Mispa, wakasema: “Hapana mtu yeyote wetu atakayemwoza binti yake kwa Mbenyamini.”
JDG 21:2 Watu wakaenda Betheli, wakaketi mbele za Mungu hadi jioni, wakapaza sauti zao wakilia kwa uchungu.
JDG 21:3 Wakasema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limewapata Waisraeli? Kwa nini kabila moja la Israeli limekosekana?”
JDG 21:4 Kesho yake asubuhi na mapema watu wakajenga madhabahu na kuleta sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
JDG 21:5 Ndipo Waisraeli wakauliza, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikukusanyika mbele za Mwenyezi Mungu?” Kwa kuwa walikuwa wameapa kiapo kikuu kuwa yeyote asiyefika mbele za Mwenyezi Mungu huko Mispa, kwa hakika angeuawa.
JDG 21:6 Basi Waisraeli wakahuzunika kwa ajili ya ndugu zao Wabenyamini, wakasema, “Leo kabila moja limekatiliwa mbali na Israeli.
JDG 21:7 Sasa tutawezaje kuwapa binti zetu kuwa wake zao, hao waliobaki, na tumeapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hatutawapa binti zetu kuwa wake zao?”
JDG 21:8 Ndipo wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikukusanyika mbele za Mwenyezi Mungu huko Mispa?” Wakagundua kuwa hakuna hata mmoja kutoka Yabesh-Gileadi aliyefika kambini kwa kusanyiko.
JDG 21:9 Kwa kuwa walipohesabu waliona hapakuwa mtu yeyote wa Yabesh-Gileadi.
JDG 21:10 Ndipo mkutano wakatuma wapiganaji elfu kumi na mbili, wakawaamuru kwenda Yabesh-Gileadi na kuua kwa panga wale wote walioishi huko, wakiwemo wake na watoto.
JDG 21:11 Wakasema, “Hili ndilo mtakalofanya: Ueni kila mwanaume na kila mwanamke ambaye si bikira.”
JDG 21:12 Wakapata kati ya watu walioishi Yabesh-Gileadi wanawali mia nne, mabikira, nao wakawachukua kwenye kambi huko Shilo katika nchi ya Kanaani.
JDG 21:13 Ndipo mkutano ukatuma ujumbe wa amani kwa Wabenyamini huko katika mwamba wa Rimoni.
JDG 21:14 Basi Wabenyamini wakarudi wakati ule, nao wakapewa wale wanawali wa Yabesh-Gileadi waliohifadhiwa. Lakini hawakuwatosha wanaume wote.
JDG 21:15 Waisraeli wakahuzunika kwa ajili ya Wabenyamini, kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa ameweka ufa katika makabila ya Israeli.
JDG 21:16 Viongozi wa kusanyiko wakasema, “Kwa kuwa wanawake wa Wabenyamini wameangamizwa, tufanyeje ili kuwapatia wake wale wanaume waliosalia?”
JDG 21:17 Wakaendelea kusema, “Lazima tuwape Wabenyamini waliopona wake ili wawe na warithi, nalo kabila lolote katika Israeli lisifutike.
JDG 21:18 Hatuwezi kuwapa binti zetu kuwa wake, kwa kuwa sisi Waisraeli tumeapa kiapo hiki: ‘Alaaniwe mtu yeyote ampaye Mbenyamini mke.’ ”
JDG 21:19 Ndipo waliposema, “Tazama iko sikukuu ya kila mwaka ya Mwenyezi Mungu katika Shilo, kaskazini mwa Betheli na mashariki mwa ile barabara inayotoka Betheli kwenda Shekemu, upande wa kusini wa Lebona.”
JDG 21:20 Hivyo wakawaelekeza Wabenyamini, wakisema, “Nendeni mkajifiche kwenye mashamba ya mizabibu,
JDG 21:21 na mkae macho. Wasichana wa Shilo watakapojiunga kwenye kucheza, tokeni kwenye hayo mashamba ya mizabibu, na kila mmoja ajinyakulie mke kutoka miongoni mwa hao wasichana wa Shilo, nanyi mwende nao katika nchi ya Benyamini.
JDG 21:22 Baba zao au ndugu zao watakapotulalamikia, tutawaambia, ‘Kuweni wakarimu kwetu, nanyi mturuhusu tuwe nao kwa kuwa hatukuweza kumpa kila mtu mke tulipopigana. Lakini ninyi pia hamna hatia, kwa kuwa hamkuwapa wao binti zenu kuwa wake.’ ”
JDG 21:23 Basi hivyo ndivyo Wabenyamini walivyofanya. Wasichana walipokuwa wakicheza, kila mtu akanyakua msichana mmoja, akaenda naye ili awe mke wake. Kisha wakarudi katika urithi wao na kuijenga upya miji na kuishi humo.
JDG 21:24 Wakati huo Waisraeli wakaondoka sehemu ile na kwenda nyumbani kwao, kwa makabila yao na kwa jamaa zao, kila mmoja kwenye urithi wake mwenyewe.
JDG 21:25 Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme; kila mtu alifanya alivyoona ni vyema machoni pake.
RUT 1:1 Waamuzi walipotawala Israeli, kulikuwa na njaa katika nchi. Mtu mmoja kutoka nchi ya Bethlehemu ya Yuda, pamoja na mke wake na wanawe wawili, akaenda kuishi katika nchi ya Moabu.
RUT 1:2 Mtu huyu aliitwa Elimeleki, mkewe aliitwa Naomi, na hao wanawe wawili waliitwa Maloni na Kilioni. Walikuwa Waefrathi kutoka Bethlehemu ya Yuda. Wakaenda katika nchi ya Moabu, wakaishi huko.
RUT 1:3 Elimeleki mumewe Naomi akafa, hivyo Naomi akabaki na wanawe wawili.
RUT 1:4 Nao wakaoa wanawake Wamoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na wa pili aliitwa Ruthu. Baada ya kuishi huko miaka kumi,
RUT 1:5 Maloni na Kilioni pia wakafa. Basi Naomi akabaki hana mume wala wanawe wawili.
RUT 1:6 Aliposikia akiwa huko Moabu kwamba Mwenyezi Mungu amewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakwe wake wakajiandaa kurudi nyumbani.
RUT 1:7 Yeye na wakwe wake wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda.
RUT 1:8 Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe wake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani mwa mama yake. Mwenyezi Mungu na awatendee mema kama mlivyowatendea hao waliofariki, na mimi pia.
RUT 1:9 Mwenyezi Mungu na amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani mwa mume mwingine.” Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa,
RUT 1:10 wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe kwa watu wako.”
RUT 1:11 Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Je, mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine ambao wataweza kuwaoa ninyi?
RUT 1:12 Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana,
RUT 1:13 je, mngesubiri hadi wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa Mwenyezi Mungu umekuwa kinyume nami!”
RUT 1:14 Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye.
RUT 1:15 Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”
RUT 1:16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakoenda nami nitaenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu.
RUT 1:17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Mwenyezi Mungu na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.”
RUT 1:18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
RUT 1:19 Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?”
RUT 1:20 Akawaambia, “Msiniite tena Naomi; niiteni Mara, kwa sababu Mwenyezi amenitendea mambo machungu sana.
RUT 1:21 Mimi niliondoka hali nimejaa, lakini Mwenyezi Mungu amenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi? Mwenyezi Mungu amenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”
RUT 1:22 Kwa hiyo Naomi alirudi pamoja na Ruthu Mmoabu mkwe wake, nao wakafika Bethlehemu mwanzoni mwa kuvuna shayiri.
RUT 2:1 Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi.
RUT 2:2 Ruthu, Mmoabu, akamwambia Naomi, “Nitaenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.” Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.”
RUT 2:3 Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka mashambani nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta akifanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alikuwa wa ukoo wa Elimeleki.
RUT 2:4 Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi Mungu awe nanyi!” Nao wakamjibu, “Mwenyezi Mungu akubariki.”
RUT 2:5 Boazi akamuuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule mwanamwali ni wa nani?”
RUT 2:6 Msimamizi akamjibu, “Ni yule Mmoabu aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi.
RUT 2:7 Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.”
RUT 2:8 Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa wajakazi wangu.
RUT 2:9 Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.”
RUT 2:10 Aliposikia hili, akasujudu, uso wake ukagusa chini, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?”
RUT 2:11 Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali.
RUT 2:12 Mwenyezi Mungu na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.”
RUT 2:13 Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa wajakazi wako.”
RUT 2:14 Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.” Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza.
RUT 2:15 Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie.
RUT 2:16 Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.”
RUT 2:17 Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja.
RUT 2:18 Akaibeba na kuelekea mjini, naye mama mkwe wake akaona jinsi alivyoweza kuokota nafaka nyingi. Pia Ruthu akachukua kile alichobakiza baada ya kula na kushiba, akampa.
RUT 2:19 Basi mkwewe akamuuliza, “Je, umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Abarikiwe mtu yule aliyekujali.” Ndipo Ruthu akamwambia mama mkwe wake kuhusu mtu ambaye alikuwa amemfanyia kazi katika shamba lake. Akasema, “Yule mtu niliyefanyia kazi kwake leo, anaitwa Boazi.”
RUT 2:20 Naye Naomi akamwambia mkwewe, “Mwenyezi Mungu ambariki! Hakuacha kuonesha fadhili zake kwa walio hai na kwa waliokufa.” Pia akamwambia, “Huyo mtu ni mmoja wa jamaa yetu wa karibu anayestahili kutukomboa.”
RUT 2:21 Kisha Ruthu, Mmoabu, akasema, “Hata aliniambia, ‘Kaa pamoja na watumishi wangu hadi watakapomaliza kuvuna nafaka yangu yote.’ ”
RUT 2:22 Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, “Binti yangu, itakuwa vyema wewe ufuatane na wajakazi wake, kwa sababu katika shamba la mtu mwingine wanaweza kukudhuru.”
RUT 2:23 Kwa hivyo Ruthu akafuatana na wajakazi wa Boazi, akaokota hadi mwisho wa mavuno ya shayiri na ya ngano. Naye aliishi na mama mkwe wake.
RUT 3:1 Kisha Naomi akamwambia mkwewe, “Binti yangu, nitakutafutia pumziko ili upate mema.
RUT 3:2 Je, Boazi, ambaye umekuwa pamoja na wajakazi wake, si ni jamaa yetu wa karibu? Usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri kwenye sakafu ya kupuria.
RUT 3:3 Basi oga na ukajipake marashi, ujivalie nguo zako nzuri. Kisha uende kwenye sakafu ya kupuria, lakini angalia asijue kwamba upo pale hadi atakapomaliza kula na kunywa.
RUT 3:4 Atakapoenda kulala, angalia mahali atakapolala. Kisha uende ufunue miguu yake, ulale. Naye atakuambia utakalofanya.”
RUT 3:5 Ruthu akajibu, “Lolote usemalo nitatenda.”
RUT 3:6 Basi akashuka hadi kwenye sakafu ya kupuria, akafanya kila kitu mama mkwe wake alichomwambia kufanya.
RUT 3:7 Boazi alipomaliza kula na kunywa, naye akawa amejawa na furaha, alienda kulala mwisho wa lundo la nafaka. Ruthu akanyemelea polepole, akafunua miguu yake, na akalala.
RUT 3:8 Usiku wa manane, kitu kilimshtua Boazi, akajigeuza, akagundua yupo mwanamke amelala miguuni pake.
RUT 3:9 Akauliza, “Wewe ni nani?” Akajibu, “Ni mimi Ruthu, mjakazi wako. Uitande nguo yako juu yangu, kwa sababu wewe ndiwe jamaa wa karibu wa kutukomboa.”
RUT 3:10 Akamwambia, “Binti yangu, ubarikiwe na Mwenyezi Mungu. Wema huu wa sasa ni mkuu kushinda hata ule ulioonesha mwanzoni. Hukuwakimbilia vijana, wakiwa matajiri au maskini.
RUT 3:11 Sasa, binti yangu, usiogope. Nitakufanyia yote uliyoomba. Kwa maana mji wote wa watu wangu wanakujua kwamba wewe ni mwanamke mwenye tabia nzuri.
RUT 3:12 Ingawa ni kweli kwamba mimi ndiye jamaa aliye karibu, bado kuna mtu mwingine wa jamaa aliye karibu zaidi wa kukomboa kuliko mimi.
RUT 3:13 Wewe kaa hapa usiku huu, kisha asubuhi akikubali kukukomboa, vyema, na akomboe. La sivyo, kama hayuko tayari, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo nitafanya hivyo. Lala hapa hadi asubuhi.”
RUT 3:14 Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hadi asubuhi, akaondoka mapema pasipo mtu kuweza kumtambua mwenzake, maana Boazi alisema, “Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika kwenye sakafu ya kupuria.”
RUT 3:15 Pia akamwambia, “Leta shela yako uliyoivaa, uitandaze.” Naye alipoitandaza, akamimina vipimo sita vya shayiri, akamtwika. Kisha Ruthu akarudi zake mjini.
RUT 3:16 Basi Ruthu alipofika kwa mama mkwe wake Naomi, akamuuliza, “Je, binti yangu, ilikuwaje huko?” Ndipo akamwelezea kila kitu Boazi alichomfanyia.
RUT 3:17 Akaendelea kusema, “Amenipa shayiri vipimo sita, akaniambia, ‘Usiende kwa mama mkwe wako mikono mitupu.’ ”
RUT 3:18 Kisha Naomi akasema, “Subiri binti yangu, hadi utakapojua kwamba hili jambo limeendaje. Kwa sababu mtu huyu hatatulia hadi akamilishe jambo hili leo.”
RUT 4:1 Boazi akakwea hadi lango la mji, akaketi pale. Yule mtu wa jamaa aliyekuwa wa karibu wa kukomboa, ambaye Boazi alimtaja, akaja. Boazi akasema, “Njoo hapa, rafiki yangu. Karibu uketi.” Naye akakaribia, akaketi.
RUT 4:2 Boazi akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, “Ketini hapa.” Nao wakaketi.
RUT 4:3 Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki.
RUT 4:4 Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa, na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.” Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.”
RUT 4:5 Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.”
RUT 4:6 Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.”
RUT 4:7 (Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.)
RUT 4:8 Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe inunue mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake.
RUT 4:9 Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni.
RUT 4:10 Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali yake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”
RUT 4:11 Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi. Mwenyezi Mungu na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata na uwe mashuhuri katika Bethlehemu.
RUT 4:12 Kupitia kwa uzao ambao Mwenyezi Mungu atakupa kutokana na huyu mwanamwali, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.”
RUT 4:13 Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake, Mwenyezi Mungu akamjalia Ruthu, naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume.
RUT 4:14 Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote!
RUT 4:15 Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda, na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye alimzaa.”
RUT 4:16 Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake.
RUT 4:17 Wanawake waliokuwa jirani zake wakasema, “Naomi ana mtoto wa kiume.” Wakamwita jina Obedi. Yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.
RUT 4:18 Hivi ndivyo vizazi vya Peresi: Peresi alimzaa Hesroni,
RUT 4:19 Hesroni akamzaa Ramu, Ramu akamzaa Aminadabu,
RUT 4:20 Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni,
RUT 4:21 Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi,
RUT 4:22 Obedi akamzaa Yese, na Yese akamzaa Daudi.
1SA 1:1 Kulikuwa na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyeitwa Elkana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu Mwefraimu.
1SA 1:2 Alikuwa na wake wawili; mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto.
1SA 1:3 Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa Mwenyezi Mungu.
1SA 1:4 Kila mara ilipofika siku ya Elkana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote wa kiume na wa kike.
1SA 1:5 Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunga tumbo.
1SA 1:6 Kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi.
1SA 1:7 Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipoenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha hadi analia na kushindwa kula.
1SA 1:8 Elkana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”
1SA 1:9 Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1SA 1:10 Kwa uchungu wake mwingi Hana alimwomba Mwenyezi Mungu, akilia kwa uchungu.
1SA 1:11 Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa Mwenyezi Mungu kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”
1SA 1:12 Alipokuwa anaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu, Eli alichunguza kinywa chake.
1SA 1:13 Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa
1SA 1:14 naye akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achilia mbali mvinyo wako.”
1SA 1:15 Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa Mwenyezi Mungu.
1SA 1:16 Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa kutokana na uchungu mkuu na huzuni.”
1SA 1:17 Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.”
1SA 1:18 Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena.
1SA 1:19 Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za Mwenyezi Mungu na kisha wakarudi nyumbani mwao huko Rama. Elkana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye Mwenyezi Mungu akamkumbuka.
1SA 1:20 Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina Samweli, akisema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa Mwenyezi Mungu.”
1SA 1:21 Huyo mtu Elkana alipopanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwa Mwenyezi Mungu na kutimiza nadhiri yake,
1SA 1:22 Hana hakuenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele za Mwenyezi Mungu, naye ataishi huko daima.”
1SA 1:23 Elkana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa hadi utakapomwachisha kunyonya, Mwenyezi Mungu na akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe hadi alipomwachisha kunyonya.
1SA 1:24 Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya unga na kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Shilo.
1SA 1:25 Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli,
1SA 1:26 naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa Mwenyezi Mungu.
1SA 1:27 Niliomba mtoto huyu, naye Mwenyezi Mungu amenijalia kile nilichomwomba.
1SA 1:28 Hivyo sasa ninamtoa kwa Mwenyezi Mungu. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa Mwenyezi Mungu.” Naye akamwabudu Mwenyezi Mungu huko.
1SA 2:1 Kisha Hana akaomba na kusema: “Moyo wangu wamshangilia Mwenyezi Mungu, katika Mwenyezi Mungu pembe yangu imeinuliwa juu. Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu, kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
1SA 2:2 “Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Mwenyezi Mungu, hakuna mwingine zaidi yako; hakuna Mwamba kama Mungu wetu.
1SA 2:3 “Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu ajuaye, na yeye hupima matendo.
1SA 2:4 “Pinde za mashujaa zimevunjika, lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu.
1SA 2:5 Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe ili kupata chakula, lakini wale waliokuwa na njaa hawana njaa tena. Mwanamke yule aliyekuwa tasa amezaa watoto saba, lakini yule aliyekuwa na wana wengi amedhoofika.
1SA 2:6 “Mwenyezi Mungu huua na huhuisha; yeye hushusha hadi kaburini na hufufua.
1SA 2:7 Mwenyezi Mungu humfanya mtu maskini naye hutajirisha, hushusha na hukweza.
1SA 2:8 Humwinua maskini kutoka mavumbini na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu; huwaketisha pamoja na wakuu, na kuwafanya warithi kiti cha utawala cha heshima. “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Mwenyezi Mungu; juu yake ameuweka ulimwengu.
1SA 2:9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake, lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza. “Si kwa nguvu mtu hushinda;
1SA 2:10 wale wampingao Mwenyezi Mungu wataharibiwa kabisa. Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni; Mwenyezi Mungu ataihukumu miisho ya dunia. “Atampa nguvu mfalme wake, na kuitukuza pembe ya mpakwa mafuta wake.”
1SA 2:11 Kisha Elkana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele za Mwenyezi Mungu chini ya kuhani Eli.
1SA 2:12 Wana wa Eli walikuwa watu waovu kabisa, hawakumheshimu Mwenyezi Mungu.
1SA 2:13 Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angekuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake.
1SA 2:14 Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angejichukulia chochote uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo.
1SA 2:15 Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angekuja na kusema kwa mtu aliyekuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.”
1SA 2:16 Mtu yule akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka,” mtumishi angejibu, “Hapana, nipe sasa; kama hunipi, nitaichukua kwa nguvu.”
1SA 2:17 Hii dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya Mwenyezi Mungu kwa dharau.
1SA 2:18 Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za Mwenyezi Mungu, kijana akivaa kizibau cha kitani.
1SA 2:19 Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumpelekea alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka.
1SA 2:20 Eli alikuwa akiwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi Mungu na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa Mwenyezi Mungu.” Kisha wakawa wanaenda nyumbani.
1SA 2:21 Mwenyezi Mungu akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana wa kiume watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za Mwenyezi Mungu.
1SA 2:22 Basi Eli, aliyekuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
1SA 2:23 Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote kuhusu haya matendo yenu maovu.
1SA 2:24 Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ninayosikia ikienea miongoni mwa watu wa Mwenyezi Mungu.
1SA 2:25 Mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu alitaka kuwaua.
1SA 2:26 Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza Mwenyezi Mungu na wanadamu.
1SA 2:27 Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walikuwa huko Misri chini ya Farao?
1SA 2:28 Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kizibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli.
1SA 2:29 Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?’
1SA 2:30 “Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasa Mwenyezi Mungu anasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa.
1SA 2:31 Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika jamaa yenu atakayeishi kuuona uzee,
1SA 2:32 nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watatendewa mema, katika jamaa yenu kamwe hapatakuwa na mtu atakayeishi hadi kuwa mzee.
1SA 2:33 Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi.
1SA 2:34 “ ‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja.
1SA 2:35 Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaiimarisha nyumba yake ya ukuhani, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima.
1SA 2:36 Kisha kila mmoja aliyeachwa katika jamaa yenu atakuja na kusujudu mbele yake kwa ajili ya kipande cha fedha na ganda la mkate, akisema, “Niteue katika baadhi ya ofisi ya ukuhani ili niweze kupata chakula.” ’ ”
1SA 3:1 Kijana Samweli alihudumu mbele za Mwenyezi Mungu chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwa na maono mengi.
1SA 3:2 Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida.
1SA 3:3 Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala hekaluni mwa Mwenyezi Mungu, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwa.
1SA 3:4 Kisha Mwenyezi Mungu akamwita Samweli. Samweli akajibu, “Mimi hapa.”
1SA 3:5 Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala.
1SA 3:6 Mwenyezi Mungu akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.”
1SA 3:7 Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua Mwenyezi Mungu. Neno la Mwenyezi Mungu lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.
1SA 3:8 Mwenyezi Mungu akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” Ndipo Eli akatambua kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa akimwita kijana.
1SA 3:9 Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale; akikuita, sema, ‘Nena Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake.
1SA 3:10 Mwenyezi Mungu akaja, akasimama pale, akiita kama hapo awali, “Samweli! Samweli!” Kisha Samweli akasema, “Nena Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.”
1SA 3:11 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe.
1SA 3:12 Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo hadi mwisho.
1SA 3:13 Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia.
1SA 3:14 Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ”
1SA 3:15 Samweli akalala hadi asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya Mwenyezi Mungu. Aliogopa kumwambia Eli yale maono,
1SA 3:16 lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.” Samweli akamjibu, “Mimi hapa.”
1SA 3:17 Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. Mwenyezi Mungu na akuadhibu vikali zaidi kama utanificha chochote alichokuambia.”
1SA 3:18 Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni Mwenyezi Mungu; na afanye lile lililo jema machoni pake!”
1SA 3:19 Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha neno lolote la Samweli lianguke chini.
1SA 3:20 Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa Mwenyezi Mungu.
1SA 3:21 Mwenyezi Mungu akaendelea kutokea huko Shilo, na huko alijidhihirisha kwa Samweli kupitia neno lake.
1SA 4:1 Nalo neno la Samweli likaja kwa Israeli yote. Basi Waisraeli walitoka kwenda kupigana dhidi ya Wafilisti. Waisraeli wakapiga kambi huko Ebenezeri, nao Wafilisti wakapiga kambi huko Afeki.
1SA 4:2 Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao elfu nne kwenye uwanja wa vita.
1SA 4:3 Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, “Kwa nini Mwenyezi Mungu ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu.”
1SA 4:4 Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, walikuwa huko na Sanduku la Agano la Mungu.
1SA 4:5 Wakati Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika.
1SA 4:6 Wafilisti waliposikia makelele, wakauliza, “Kwa nini kuna makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?” Walipofahamu kuwa Sanduku la Mwenyezi Mungu limekuja kambini,
1SA 4:7 Wafilisti wakaogopa, wakasema, “Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo awali.
1SA 4:8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani.
1SA 4:9 Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!”
1SA 4:10 Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia kwenye hema lake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari elfu thelathini walioenda kwa miguu.
1SA 4:11 Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.
1SA 4:12 Siku ile ile mtu mmoja wa kabila la Benyamini akakimbia kutoka uwanja wa vita na kwenda Shilo, nguo zake zikiwa zimeraruka na akiwa na mavumbi kichwani mwake.
1SA 4:13 Alipofika, Eli alikuwa ameketi kwenye kiti chake kando ya barabara akiangalia, kwa sababu moyo wake ulikuwa na hofu kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kueleza kilichokuwa kimetokea, mji wote ukalia.
1SA 4:14 Eli akasikia kelele za kilio, naye akauliza, “Ni nini maana ya makelele haya?” Yule mtu akafanya haraka kwenda kwa Eli,
1SA 4:15 wakati huu Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane, nayo macho yake yalikuwa yamepofuka hadi hakuweza kuona.
1SA 4:16 Akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi, nimekimbia kutoka huko siku ya leo.” Eli akamuuliza, “Je, mwanangu, ni nini kimetokea huko?”
1SA 4:17 Yule mtu aliyeleta habari akajibu, “Waisraeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, na wanajeshi wengi sana wameuawa. Pia wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa, na Sanduku la Mungu limetekwa.”
1SA 4:18 Mara alipotaja Sanduku la Mungu, Eli alianguka kwa nyuma kutoka kiti chake kando ya lango. Shingo yake ikavunjika naye akafa, kwa kuwa alikuwa mzee tena mzito. Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka arobaini.
1SA 4:19 Mkwewe, mke wa Finehasi, alikuwa mjamzito na alikaribia wakati wa kujifungua. Aliposikia habari kwamba Sanduku la Mungu limetekwa na ya kuwa baba mkwe wake na mumewe wamekufa, akapata uchungu naye akajifungua lakini akazidiwa na uchungu.
1SA 4:20 Alipokuwa akifa, wanawake waliokuwa wanamhudumia wakamwambia, “Usiogope, umemzaa mwana wa kiume.” Lakini hakujibu wala kuweka maanani.
1SA 4:21 Alimwita yule mtoto Ikabodi, akisema, “Utukufu umeondoka katika Israeli,” kwa sababu ya kutekwa kwa Sanduku la Mungu na vifo vya baba mkwe na mumewe.
1SA 4:22 Akasema, “Utukufu umeondoka katika Israeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu limetekwa.”
1SA 5:1 Baada ya Wafilisti kuteka Sanduku la Mungu, walilichukua kutoka Ebenezeri hadi Ashdodi.
1SA 5:2 Kisha wakaliingiza lile Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni na kuliweka kando ya huyo Dagoni.
1SA 5:3 Watu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema kesho yake, kumbe, wakamkuta Dagoni ameanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu! Wakamwinua Dagoni na kumrudisha mahali pake.
1SA 5:4 Lakini asubuhi iliyofuata, walipoamka kumbe, walimkuta Dagoni ameanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu! Kichwa chake na mikono vilikuwa vimevunjwa, navyo vimelala kizingitini; ni kiwiliwili chake tu kilichokuwa kimebaki.
1SA 5:5 Ndiyo sababu hadi leo makuhani wa Dagoni na wengine wanaoingia katika hekalu la Dagoni huko Ashdodi hawakanyagi kizingiti.
1SA 5:6 Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu.
1SA 5:7 Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, “Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu.”
1SA 5:8 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?” Wakajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi.” Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli.
1SA 5:9 Lakini baada ya kulihamisha, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu.
1SA 5:10 Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni. Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema, “Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu.”
1SA 5:11 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, “Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu.” Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake.
1SA 5:12 Wale ambao hawakufa walipatwa na majipu, na kilio cha mji kilifika hadi mbinguni.
1SA 6:1 Sanduku la Mwenyezi Mungu lilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba,
1SA 6:2 Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mwenyezi Mungu? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake.”
1SA 6:3 Wakajibu, “Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu.”
1SA 6:4 Wafilisti wakawauliza, “Ni sadaka gani ya hatia tutakayompelekea?” Wakajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya wa dhahabu watano, kulingana na idadi ya watawala wa Wafilisti, kwa sababu tauni hiyo hiyo imewadhuru ninyi na watawala wenu.
1SA 6:5 Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mtukuzeni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu.
1SA 6:6 Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao?
1SA 6:7 “Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ng’ombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ng’ombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini.
1SA 6:8 Chukueni hilo Sanduku la Mwenyezi Mungu na mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekea Mwenyezi Mungu kama sadaka ya hatia. Lipelekeni,
1SA 6:9 lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litaenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwamba Mwenyezi Mungu ndiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono wa Mwenyezi Mungu uliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.”
1SA 6:10 Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ng’ombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini.
1SA 6:11 Wakaliweka Sanduku la Mwenyezi Mungu juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu.
1SA 6:12 Kisha hao ng’ombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ng’ombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.
1SA 6:13 Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona.
1SA 6:14 Lile gari la kukokotwa lilikuja kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ng’ombe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu.
1SA 6:15 Walawi walilishusha Sanduku la Mwenyezi Mungu, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Mwenyezi Mungu.
1SA 6:16 Wale watawala watano wa Wafilisti waliona haya yote, nao wakarudi Ekroni siku ile ile.
1SA 6:17 Haya ndio yale majipu ya dhahabu Wafilisti waliyotuma kama sadaka ya hatia kwa Mwenyezi Mungu: moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni.
1SA 6:18 Nayo hesabu ya wale panya wa dhahabu ilikuwa kulingana na idadi ya miji ya Wafilisti ya watawala watano wa Wafilisti: miji yao yenye ngome, pamoja na vijiji vya miji hiyo. Ule mwamba mkubwa, ambao juu yake waliliweka lile Sanduku la Mwenyezi Mungu, ni ushahidi hadi leo katika shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi.
1SA 6:19 Lakini Mungu aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-Shemeshi, akiwaua watu sabini miongoni mwao kwa sababu walichungulia ndani ya Sanduku la Mwenyezi Mungu. Watu wakaomboleza kwa sababu ya pigo zito kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
1SA 6:20 nao watu wa Beth-Shemeshi wakauliza, “Ni nani awezaye kusimama mbele za Mwenyezi Mungu, huyu Mungu aliye mtakatifu? Sanduku litapanda kwenda kwa nani kutoka hapa?”
1SA 6:21 Kisha wakatuma wajumbe kwa watu wa Kiriath-Yearimu, wakisema, “Wafilisti wamerudisha Sanduku la Mwenyezi Mungu. Shukeni na mlipandishe huko kwenu.”
1SA 7:1 Kisha wanaume wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu kilimani, na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Mwenyezi Mungu.
1SA 7:2 Sanduku la Mwenyezi Mungu lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, jumla ya miaka ishirini. Nao watu wote wa Israeli wakamrudia Mwenyezi Mungu.
1SA 7:3 Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia Mwenyezi Mungu kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi, na kujitoa wenyewe kwa Mwenyezi Mungu na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi kutoka kwa mkono wa Wafilisti.”
1SA 7:4 Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi yao, nao wakamtumikia Mwenyezi Mungu peke yake.
1SA 7:5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea kwa Mwenyezi Mungu.”
1SA 7:6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.” Naye Samweli alikuwa kiongozi wa Israeli huko Mispa.
1SA 7:7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti.
1SA 7:8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.”
1SA 7:9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu. Akamlilia Mwenyezi Mungu kwa niaba ya Israeli, naye Mwenyezi Mungu akamjibu.
1SA 7:10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Mwenyezi Mungu alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli.
1SA 7:11 Wanaume wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.
1SA 7:12 Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri, akisema, “Hadi sasa Mwenyezi Mungu ametusaidia.”
1SA 7:13 Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena. Katika maisha yote ya Samweli, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa dhidi ya Wafilisti.
1SA 7:14 Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawa na amani kati ya Israeli na Waamori.
1SA 7:15 Samweli akaendelea kuwa mwamuzi wa Israeli siku zote za maisha yake.
1SA 7:16 Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli hadi Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote.
1SA 7:17 Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani mwake, huko pia aliamua Israeli. Naye huko alimjengea Mwenyezi Mungu madhabahu.
1SA 8:1 Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli.
1SA 8:2 Mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba.
1SA 8:3 Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki.
1SA 8:4 Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama.
1SA 8:5 Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.”
1SA 8:6 Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba Mwenyezi Mungu.
1SA 8:7 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao.
1SA 8:8 Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri hadi siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe.
1SA 8:9 Sasa wasikilize, lakini waonye sana, na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.”
1SA 8:10 Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi Mungu.
1SA 8:11 Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake.
1SA 8:12 Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake ya vita.
1SA 8:13 Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji.
1SA 8:14 Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake.
1SA 8:15 Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake.
1SA 8:16 Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ng’ombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe.
1SA 8:17 Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake.
1SA 8:18 Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye Mwenyezi Mungu hatawajibu.”
1SA 8:19 Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala.
1SA 8:20 Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.”
1SA 8:21 Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele za Mwenyezi Mungu.
1SA 8:22 Mwenyezi Mungu akamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.” Kisha Samweli akawaambia Waisraeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”
1SA 9:1 Kulikuwa na Mbenyamini mmoja, mtu maarufu, ambaye aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia wa Benyamini.
1SA 9:2 Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli, kijana aliyevutia sana, hakuna aliyelingana naye miongoni mwa Waisraeli; alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote.
1SA 9:3 Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.”
1SA 9:4 Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwa huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata.
1SA 9:5 Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo turudi, au baba yangu ataacha kufikiria kuhusu punda na kuanza kufadhaika kutuhusu.”
1SA 9:6 Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho kweli hutukia. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.”
1SA 9:7 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?”
1SA 9:8 Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli. Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia tutapitia njia ipi.”
1SA 9:9 (Zamani katika Israeli, kama mtu alienda kuuliza neno kwa Mungu, angesema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.)
1SA 9:10 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwa huyo mtu wa Mungu.
1SA 9:11 Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wakikuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?”
1SA 9:12 Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu pa kuabudia.
1SA 9:13 Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu pa kuabudia ili kula. Watu hawataanza kula hadi atakapofika, kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.”
1SA 9:14 Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikoenda mahali pa juu pa kuabudia.
1SA 9:15 Basi siku moja kabla Sauli hajaja, Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunulia Samweli jambo hili:
1SA 9:16 “Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umpake mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli; ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.”
1SA 9:17 Samweli alipomwona Sauli, Mwenyezi Mungu akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.”
1SA 9:18 Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, unaweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?”
1SA 9:19 Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu hadi mahali pa juu pa kuabudia, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako.
1SA 9:20 Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?”
1SA 9:21 Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo kama hili?”
1SA 9:22 Kisha Samweli akamleta Sauli na mtumishi wake ukumbini na kuwaketisha mahali pa heshima zaidi miongoni mwa wale waliokuwa wamealikwa; jumla yao walikuwa kama watu thelathini.
1SA 9:23 Samweli akamwambia mpishi, “Leta ile sehemu ya nyama niliyokupa, ile niliyokuambia iweke kando.”
1SA 9:24 Hivyo mpishi akachukua mguu pamoja na kile kilichokuwa juu yake akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, “Hiki ndicho ambacho kimewekwa kwa ajili yako. Ule, kwa sababu kilitengwa kwa ajili yako kwa tukio hili, tangu niliposema, ‘Nimewaalika wageni.’ ” Naye Sauli akala pamoja na Samweli siku ile.
1SA 9:25 Baada ya kushuka kutoka mahali pa juu pa kuabudia na kufika mjini, Samweli alizungumza na Sauli juu ya dari ya nyumba yake.
1SA 9:26 Walipoamka mapema alfajiri, Samweli akamwita Sauli darini, akamwambia, “Jiandae, nami nitakuaga uende zako.” Sauli alipokuwa tayari yeye na Samweli wakatoka nje pamoja.
1SA 9:27 Walipokuwa wakiteremka kuelekea mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi atangulie mbele yetu.” Naye mtumishi akafanya hivyo. “Subiri hapa kidogo ili nipate kukupa ujumbe kutoka kwa Mungu.”
1SA 10:1 Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je, Mwenyezi Mungu hakukupaka mafuta uwe kiongozi juu ya urithi wake?
1SA 10:2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’
1SA 10:3 “Kisha utaenda mbele kutoka hapa hadi uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwenda kumwabudu Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai.
1SA 10:4 Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao.
1SA 10:5 “Baada ya hayo utaenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu pa kuabudia wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii.
1SA 10:6 Roho wa Mwenyezi Mungu atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti.
1SA 10:7 Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.
1SA 10:8 “Tangulia kushuka mbele yangu hadi Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.”
1SA 10:9 Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile.
1SA 10:10 Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao.
1SA 10:11 Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?”
1SA 10:12 Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?”
1SA 10:13 Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alienda mahali pa juu pa kuabudia.
1SA 10:14 Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?” Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulienda kwa Samweli.”
1SA 10:15 Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.”
1SA 10:16 Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme.
1SA 10:17 Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwa Mwenyezi Mungu huko Mispa,
1SA 10:18 naye akawaambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowadhulumu.’
1SA 10:19 Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele za Mwenyezi Mungu kwa makabila yenu na kwa koo zenu.”
1SA 10:20 Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa.
1SA 10:21 Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana.
1SA 10:22 Wakazidi kuuliza kwa Mwenyezi Mungu, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?” Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, amejificha kwenye mizigo.”
1SA 10:23 Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote.
1SA 10:24 Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambaye Mwenyezi Mungu amemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.” Ndipo watu wakasema kwa sauti kuu, “Mfalme aishi maisha marefu.”
1SA 10:25 Samweli akawaeleza watu madaraka ya ufalme. Akayaandika kwenye kitabu na kukiweka mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Samweli akawaruhusu watu kila mmoja aende nyumbani mwake.
1SA 10:26 Sauli pia akaenda nyumbani mwake huko Gibea, akisindikizwa na watu hodari ambao Mungu alikuwa amegusa mioyo yao.
1SA 10:27 Lakini baadhi ya watu wakorofi walisema, “Huyu mtu atawezaje kutuokoa?” Wakamdharau na wala hawakumletea zawadi. Lakini Sauli akakaa kimya.
1SA 11:1 Nahashi Mwamoni akakwea kuuzingira mji wa Yabesh-Gileadi kwa jeshi. Wanaume wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba nasi, na tutakutumikia.”
1SA 11:2 Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitang’oa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.”
1SA 11:3 Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote. Ikies hakuna hata mmoja atayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.”
1SA 11:4 Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa kuhusu masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa.
1SA 11:5 Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza vile wanaume wa Yabeshi walivyokuwa wamesema.
1SA 11:6 Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira.
1SA 11:7 Akachukua maksai wawili na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha kicho cha Mwenyezi Mungu kikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja.
1SA 11:8 Sauli alipowakusanya huko Bezeki, wanaume wa Israeli walikuwa elfu mia tatu, na wanaume wa Yuda elfu thelathini.
1SA 11:9 Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni wanaume wa Yabesh-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’ ” Wajumbe walipoenda na kutoa taarifa hii kwa wanaume wa Yabeshi, wakafurahi.
1SA 11:10 Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.”
1SA 11:11 Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja hadi mchana. Wale walionusurika wakatawanyika, hivi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja.
1SA 11:12 Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatutawala?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.”
1SA 11:13 Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hii Mwenyezi Mungu ameokoa Israeli.”
1SA 11:14 Ndipo Samweli akawaambia watu, “Njooni, twendeni Gilgali na huko tuthibitishe ufalme.”
1SA 11:15 Kwa hiyo watu wote wakaenda Gilgali na kumthibitisha Sauli kuwa mfalme mbele za Mwenyezi Mungu. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele za Mwenyezi Mungu, naye Sauli na Waisraeli wote wakafanya karamu kubwa.
1SA 12:1 Samweli akawaambia Israeli wote, “Nimesikiliza kila kitu mlichoniambia nami nimewawekea mfalme juu yenu.
1SA 12:2 Sasa mnaye mfalme kama kiongozi wenu. Lakini mimi ni mzee na nina mvi, nao wanangu wapo hapa pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu hadi siku hii ya leo.
1SA 12:3 Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni dhidi yangu mbele za Mwenyezi Mungu na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Nimemdhulumu nani? Nimepokea rushwa kutoka kwa nani ili nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, nitawarudishia.”
1SA 12:4 Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutudhulumu. Hujapokea chochote kutoka mkono wa mtu yeyote.”
1SA 12:5 Samweli akawaambia, “Mwenyezi Mungu ni shahidi dhidi yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.” Wakasema, “Yeye ni shahidi.”
1SA 12:6 Kisha Samweli akawaambia watu, “Mwenyezi Mungu ndiye alimchagua Musa na Haruni, na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri.
1SA 12:7 Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu nitakabiliana nanyi kwa ushahidi mbele za Mwenyezi Mungu wa matendo yote ya haki yaliyofanywa na Mwenyezi Mungu kwenu na kwa baba zenu.
1SA 12:8 “Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimlilia Mwenyezi Mungu awasaidie, naye Mwenyezi Mungu akawatuma Musa na Haruni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa.
1SA 12:9 “Lakini wakamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao.
1SA 12:10 Wakamlilia Mwenyezi Mungu na kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwacha Mwenyezi Mungu na kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’
1SA 12:11 Ndipo Mwenyezi Mungu akawatuma Yerub-Baali, Baraka, Yefta na Samweli, naye akawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama.
1SA 12:12 “Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alikuwa mfalme wenu.
1SA 12:13 Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni, Mwenyezi Mungu amemweka mfalme juu yenu.
1SA 12:14 Mkimcha Mwenyezi Mungu, na kumtumikia na kumtii, nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu!
1SA 12:15 Lakini kama hamkumtii Mwenyezi Mungu, nanyi mkaasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu.
1SA 12:16 “Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo Mwenyezi Mungu anaenda kulifanya mbele ya macho yenu!
1SA 12:17 Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba Mwenyezi Mungu ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya Mwenyezi Mungu mlipoomba mfalme.”
1SA 12:18 Kisha Samweli akamwomba Mwenyezi Mungu, na siku ile ile Mwenyezi Mungu akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi Mungu na Samweli.
1SA 12:19 Watu wote wakamwambia Samweli, “Mwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.”
1SA 12:20 Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwache Mwenyezi Mungu, bali mtumikieni Mwenyezi Mungu kwa moyo wote.
1SA 12:21 Msigeukie sanamu batili. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana.
1SA 12:22 Kwa ajili ya jina lake kuu Mwenyezi Mungu hatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendeza Mwenyezi Mungu kuwafanya watu wake mwenyewe.
1SA 12:23 Lakini iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na nyoofu.
1SA 12:24 Lakini hakikisheni mnamcha Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wote; tafakarini mambo makubwa aliyoyatenda kwa ajili yenu.
1SA 12:25 Hata hivyo mkiendelea kufanya uovu, ninyi na mfalme wenu mtafutiliwa mbali!”
1SA 13:1 Sauli alikuwa na umri wa miaka thelathini, alipokuwa mfalme, akatawala Israeli miaka arobaini na mbili.
1SA 13:2 Sauli alichagua watu elfu tatu kutoka Israeli; miongoni mwa hao, watu elfu mbili walikuwa naye huko Mikmashi na katika nchi ya vilima ya Betheli; nao watu elfu moja walikuwa na Yonathani huko Gibea ya Benyamini. Watu waliosalia aliwarudisha nyumbani mwao.
1SA 13:3 Yonathani akashambulia ngome ya Wafilisti huko Geba, nao Wafilisti wakapata habari hizo. Kisha Sauli akaamuru tarumbeta ipigwe nchi yote na kusema, “Waebrania na wasikie!”
1SA 13:4 Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, na sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali.
1SA 13:5 Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita elfu tatu, waendesha magari ya vita elfu sita, na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki mwa Beth-Aveni.
1SA 13:6 Waisraeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katika miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki.
1SA 13:7 Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani hadi nchi ya Gadi na Gileadi. Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu.
1SA 13:8 Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika.
1SA 13:9 Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa.
1SA 13:10 Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki.
1SA 13:11 Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?” Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi,
1SA 13:12 nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwa Mwenyezi Mungu.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.”
1SA 13:13 Samweli akamwambia Sauli, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aliyokupa. Kama ungetii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote.
1SA 13:14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Mwenyezi Mungu amemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo ya Mwenyezi Mungu.”
1SA 13:15 Kisha Samweli akaondoka Gilgali, akapanda Gibea ya Benyamini, naye Sauli akawahesabu watu aliokuwa nao. Jumla yao walikuwa watu mia sita.
1SA 13:16 Sauli, mwanawe Yonathani na watu waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiishi huko Gibea ya Benyamini, wakati Wafilisti wakiwa wamepiga kambi huko Mikmashi.
1SA 13:17 Makundi ya wavamiaji walikuja kutoka kambi ya Wafilisti katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra karibu na Shuali,
1SA 13:18 kikosi kingine kilielekea Beth-Horoni, nacho kikosi cha tatu kilielekea kwenye nchi ya mpakani ielekeayo Bonde la Seboimu linalotazamana na jangwa.
1SA 13:19 Hapakuwa na mhunzi ambaye angeweza kupatikana katika nchi yote ya Israeli, kwa sababu Wafilisti walikuwa wamesema, “Waebrania wasije wakatengeneza panga au mikuki!”
1SA 13:20 Hivyo Waisraeli wote waliteremka kwa Wafilisti ili kila mtu kunoa plau yake, jembe lake, shoka lake, au mundu wake.
1SA 13:21 Bei ilikuwa fedha theluthi mbili za shekeli kunoa majembe ya plau na majembe ya mkono, na theluthi moja ya shekeli kunoa uma, na shoka, na mchokoo.
1SA 13:22 Kwa hiyo siku ya vita hakuna askari yeyote kambini na Sauli na Yonathani aliyekuwa na upanga wala mkuki mkononi mwake; Sauli na mwanawe Yonathani tu ndio walikuwa navyo.
1SA 13:23 Basi kikosi cha Wafilisti kilikuwa kimetoka kuelekea njia iendayo Mikmashi.
1SA 14:1 Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake.
1SA 14:2 Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu wapatao mia sita;
1SA 14:3 miongoni mwao alikuwepo Ahiya, aliyekuwa amevaa kizibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi Mungu huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka.
1SA 14:4 Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwa na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene.
1SA 14:5 Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba.
1SA 14:6 Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi Mungu atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia Mwenyezi Mungu kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.”
1SA 14:7 Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.”
1SA 14:8 Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone.
1SA 14:9 Wakituambia, ‘Subirini hapo hadi tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao.
1SA 14:10 Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba Mwenyezi Mungu amewatia mikononi mwetu.”
1SA 14:11 Basi wote wawili wakajionesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.”
1SA 14:12 Wanaume wa kwenye doria wakawapazia sauti Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu, nasi tutawakomesha.” Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; Mwenyezi Mungu amewatia mikononi mwa Israeli.”
1SA 14:13 Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake.
1SA 14:14 Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka.
1SA 14:15 Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo ardhi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu.
1SA 14:16 Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote.
1SA 14:17 Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka kwetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo.
1SA 14:18 Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.)
1SA 14:19 Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.”
1SA 14:20 Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake.
1SA 14:21 Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.
1SA 14:22 Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya vilima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii.
1SA 14:23 Hivyo Mwenyezi Mungu akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni.
1SA 14:24 Basi Waisraeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote atakayekula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula.
1SA 14:25 Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwa na asali juu ya ardhi.
1SA 14:26 Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo.
1SA 14:27 Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakaangaa.
1SA 14:28 Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.”
1SA 14:29 Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi macho yangu yalipata kuangaa nilipoonja asali hii kidogo.
1SA 14:30 Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangekula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?”
1SA 14:31 Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi hadi Aiyaloni, walikuwa wamechoka.
1SA 14:32 Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ng’ombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu.
1SA 14:33 Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kula nyama yenye damu.” Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.”
1SA 14:34 Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ng’ombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ” Hivyo kila mmoja akaleta ng’ombe wake jioni ile na kumchinja hapo.
1SA 14:35 Ndipo Sauli akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu.
1SA 14:36 Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara hadi mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.” Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.” Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.”
1SA 14:37 Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile.
1SA 14:38 Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo.
1SA 14:39 Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa kwa mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno.
1SA 14:40 Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.” Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.”
1SA 14:41 Kisha Sauli akamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kwa nini hujamjibu mtumishi wako leo? Ikiwa makosa ni yangu au ya mwanangu Yonathani, jibu kwa Urimu. Lakini ikiwa makosa ni ya wanaume wa Israeli, jibu kwa Thumimu.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama.
1SA 14:42 Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani.
1SA 14:43 Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.” Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?”
1SA 14:44 Sauli akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.”
1SA 14:45 Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta ukombozi huu mkubwa kwa Israeli? Hasha! Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa.
1SA 14:46 Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao.
1SA 14:47 Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda.
1SA 14:48 Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara.
1SA 14:49 Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali.
1SA 14:50 Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli.
1SA 14:51 Babaye Sauli, yaani Kishi, na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli.
1SA 14:52 Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.
1SA 15:1 Samweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye Mwenyezi Mungu alinituma nikupake mafuta ili uwe mfalme juu ya watu wake Israeli; basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
1SA 15:2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri.
1SA 15:3 Basi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wale wanaonyonya, ng’ombe na kondoo, ngamia na punda.’ ”
1SA 15:4 Ndipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu elfu mia mbili, na elfu kumi kutoka Yuda.
1SA 15:5 Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni.
1SA 15:6 Kisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki.
1SA 15:7 Ndipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila hadi Shuri, mashariki mwa Misri.
1SA 15:8 Akamchukua Agagi mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga.
1SA 15:9 Lakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi, na kondoo na ng’ombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona, na kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa.
1SA 15:10 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Samweli kusema:
1SA 15:11 “Ninasikitika kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme, kwa sababu ameacha kunifuata mimi na hakutimiza maagizo yangu.” Samweli akafadhaika, naye akamlilia Mwenyezi Mungu usiku ule wote.
1SA 15:12 Asubuhi na mapema Samweli akaamka kwenda kukutana na Sauli, lakini akaambiwa, “Sauli ameenda Karmeli. Huko amesimamisha mnara kwa heshima yake mwenyewe, naye ameendelea na kuteremkia Gilgali.”
1SA 15:13 Samweli alipomfikia, Sauli akamwambia, “Mwenyezi Mungu akubariki! Nimetimiza yale Mwenyezi Mungu aliyoniagiza.”
1SA 15:14 Lakini Samweli akasema, “Nini basi huu mlio wa kondoo masikioni mwangu? Huu mlio wa ng’ombe ninaousikia ni kitu gani?”
1SA 15:15 Sauli akajibu, “Askari wamewaleta kutoka kwa Waamaleki, waliwaacha wale kondoo na ng’ombe wazuri ili kuwatoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, lakini tuliwaangamiza kabisa wengine wote.”
1SA 15:16 Samweli akamwambia Sauli, “Ngoja! Nami nitakuambia lile Mwenyezi Mungu aliloniambia usiku huu.” Sauli akajibu, “Niambie.”
1SA 15:17 Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa makabila ya Israeli? Mwenyezi Mungu alikupaka mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli.
1SA 15:18 Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita hadi utakapowaangamiza kabisa.’
1SA 15:19 Kwa nini hukumtii Mwenyezi Mungu? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu?”
1SA 15:20 Sauli akasema, “Lakini nilimtii Mwenyezi Mungu. Nilikamilisha ile kazi ambayo Mwenyezi Mungu alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao.
1SA 15:21 Askari walichukua kondoo na ng’ombe kutoka nyara, kutoka kwa wale wazuri sana katika vitu vilivyotengewa Mungu, ili wavitoe kuwa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, huko Gilgali.”
1SA 15:22 Lakini Samweli akajibu: “Je, Mwenyezi Mungu anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama vile kuitii sauti ya Mwenyezi Mungu? Kutii ni bora kuliko dhabihu, nako kusikia ni bora kuliko mafuta ya kondoo dume.
1SA 15:23 Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi, nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu. Kwa sababu umelikataa neno la Mwenyezi Mungu, naye amekukataa wewe kuendelea kuwa mfalme.”
1SA 15:24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya Mwenyezi Mungu na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka.
1SA 15:25 Sasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Mwenyezi Mungu.”
1SA 15:26 Lakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno la Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu amekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!”
1SA 15:27 Samweli alipogeuka ili aondoke, Sauli akang’ang’ania pindo la joho lake, nalo likararuka.
1SA 15:28 Samweli akamwambia, “Mwenyezi Mungu ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako leo, naye ameutia kwa mmoja wa majirani zako, aliye bora kuliko wewe.
1SA 15:29 Yeye aliye Utukufu wa Israeli hasemi uongo wala hana kigeugeu; kwa kuwa yeye si mwanadamu, hata abadili nia yake.”
1SA 15:30 Sauli akajibu, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali niheshimu mbele ya wazee wa watu wangu na mbele ya Israeli; rudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako.”
1SA 15:31 Hivyo Samweli akarudi pamoja na Sauli, naye Sauli akamwabudu Mwenyezi Mungu.
1SA 15:32 Ndipo Samweli akasema, “Niletee Agagi mfalme wa Waamaleki.” Agagi akaja kwake kwa ujasiri, akifikiri, “Hakika uchungu wa mauti umepita.”
1SA 15:33 Lakini Samweli akasema, “Kama upanga wako ulivyofanya wanawake kufiwa na watoto wao, ndivyo mama yako atakavyokuwa hana mtoto miongoni mwa wanawake.” Naye Samweli akamuua Agagi mbele za Mwenyezi Mungu huko Gilgali.
1SA 15:34 Kisha Samweli akaenda Rama, lakini Sauli akapanda nyumbani mwake huko Gibea ya Sauli.
1SA 15:35 Hadi siku Samweli alipofariki hakuenda kumwona Sauli tena, ingawa Samweli alimwomboleza. Naye Mwenyezi Mungu alihuzunika kwamba alimfanya Sauli kuwa mfalme juu ya Israeli.
1SA 16:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli hadi lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.”
1SA 16:2 Lakini Samweli akasema, “Nitaendaje? Sauli atasikia kuhusu jambo hili na ataniua.” Mwenyezi Mungu akamwambia, “Chukua ndama jike, useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.’
1SA 16:3 Mwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakalofanya. Utanipakia mafuta yule nitakuonesha.”
1SA 16:4 Samweli akafanya kile Mwenyezi Mungu alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?”
1SA 16:5 Samweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu.
1SA 16:6 Walipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu anasimama hapa mbele za Mwenyezi Mungu.”
1SA 16:7 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. Mwenyezi Mungu hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini Mwenyezi Mungu hutazama moyoni.”
1SA 16:8 Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu Mwenyezi Mungu hakumchagua.”
1SA 16:9 Kisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu Mwenyezi Mungu hakumchagua.”
1SA 16:10 Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “Mwenyezi Mungu hajawachagua hawa.”
1SA 16:11 Hivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?” Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.” Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi hadi afike.”
1SA 16:12 Basi akatuma aitwe, naye akaletwa. Aling’aa kwa afya, na mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza. Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Inuka na umpake mafuta; huyu ndiye.”
1SA 16:13 Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumpaka mafuta mbele ya ndugu zake. Kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama.
1SA 16:14 Basi Roho wa Mwenyezi Mungu alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu ili imtese.
1SA 16:15 Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho mbaya imeachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu nayo inakutesa.
1SA 16:16 Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walio hapa watafute mtu anayeweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.”
1SA 16:17 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.”
1SA 16:18 Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. Mwenyezi Mungu yu pamoja naye.”
1SA 16:19 Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.”
1SA 16:20 Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe.
1SA 16:21 Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake.
1SA 16:22 Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.”
1SA 16:23 Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.
1SA 17:1 Wakati huo Wafilisti wakakusanya majeshi yao kwa ajili ya vita, nao wakakusanyika huko Soko katika Yuda. Wakapiga kambi huko Efes-Damimu, kati ya Soko na Azeka.
1SA 17:2 Sauli na Waisraeli wakakusanyika na kupiga kambi katika Bonde la Ela na kupanga jeshi ili kupigana vita na Wafilisti.
1SA 17:3 Wafilisti wakawa katika kilima kimoja, na Waisraeli katika kilima kingine, nalo bonde likiwa kati yao.
1SA 17:4 Shujaa aliyeitwa Goliathi, aliyetoka Gathi, akajitokeza kutoka kambi ya Wafilisti. Alikuwa na urefu dhiraa sita na shibiri moja.
1SA 17:5 Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya shaba kifuani mwake yenye uzito wa shekeli elfu tano.
1SA 17:6 Miguuni mwake alivaa mabamba ya shaba, na alikuwa na mkuki wa shaba mgongoni mwake.
1SA 17:7 Mpini wa huo mkuki ulikuwa kama mti wa mfumaji, na ncha ya chuma yake ilikuwa na uzito wa shekeli mia sita. Mbeba ngao wake alitangulia mbele yake.
1SA 17:8 Goliathi alisimama na kuwaambia majeshi ya Israeli kwa sauti kuu, akisema, “Kwa nini mmetoka kupanga vita? Je, mimi si Mfilisti, na ninyi ni watumishi wa Sauli? Chagueni mtu na anishukie mimi.
1SA 17:9 Kama anaweza kupigana nami na kuniua, tutakuwa chini yenu; lakini nikimshinda na kumuua, ninyi mtakuwa chini yetu, na mtatutumikia.”
1SA 17:10 Kisha yule Mfilisti akasema, “Siku hii ya leo nayatukana majeshi ya Israeli! Nipeni mtu tupigane.”
1SA 17:11 Kwa kusikia maneno ya Wafilisti, Sauli na Waisraeli wote wakafadhaika na kuogopa.
1SA 17:12 Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefrathi jina lake Yese aliyekuwa ametoka Bethlehemu ya Yuda. Yese alikuwa na wana wanane, naye wakati wa Sauli alikuwa mzee sana.
1SA 17:13 Wana wakubwa watatu wa Yese walikuwa wamefuatana na Sauli vitani: Mzaliwa wa kwanza alikuwa Eliabu, wa pili Abinadabu, na wa tatu Shama.
1SA 17:14 Daudi ndiye alikuwa mdogo wa wote. Hao wakubwa watatu wakamfuata Sauli,
1SA 17:15 lakini Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili kuchunga kondoo wa baba yake huko Bethlehemu.
1SA 17:16 Kwa siku arobaini huyo Mfilisti alikuwa akija mbele kila siku asubuhi na jioni na kujionesha.
1SA 17:17 Wakati huo Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Chukua hii efa ya bisi na hii mikate kumi kwa ajili ya ndugu zako uwapelekee upesi kambini mwao.
1SA 17:18 Chukua pamoja na hizi jibini kumi kwa jemadari wa kikosi chao. Ujue hali ya ndugu zako na uniletee taarifa za uhakika kutoka kwao.
1SA 17:19 Wao wako pamoja na Sauli na wanaume wote wa Israeli huko kwenye Bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.”
1SA 17:20 Asubuhi na mapema Daudi akaondoka, akaliacha kundi la kondoo pamoja na mchungaji, akapakia vitu vile na kuondoka, kama vile Yese alivyokuwa amemwagiza. Akafika kambini wakati jeshi lilikuwa likitoka kwenda kwenye sehemu yake ya kupigania, huku wakipiga ukelele wa vita.
1SA 17:21 Israeli na Wafilisti walikuwa wakipanga safu zao wakitazamana.
1SA 17:22 Daudi akaacha vile vitu vyake kwa mtunza vifaa, akakimbilia katika safu za vita na kuwasalimu ndugu zake.
1SA 17:23 Alipokuwa akisema nao, Goliathi, yule Mfilisti shujaa kutoka Gathi, akajitokeza mbele ya safu zake na kupiga ile kelele yake ya kawaida ya matukano, naye Daudi akayasikia.
1SA 17:24 Waisraeli walipomwona yule mtu, wote wakamkimbia kwa woga mkuu.
1SA 17:25 Basi Waisraeli walikuwa wakisema, “Je, mnaona jinsi mtu huyu anavyoendelea kujitokeza. Hujitokeza ili kutukana Israeli. Mfalme atatoa utajiri mwingi kwa yule mtu atakayemuua. Pia atamwoza binti yake na atasamehe jamaa ya baba yake kulipa kodi katika Israeli.”
1SA 17:26 Daudi akauliza watu waliokuwa wamesimama karibu naye, “Je, atatendewa nini mtu atakayemuua huyu Mfilisti na kuondoa aibu hii katika Israeli? Ni nani huyu Mfilisti asiyetahiriwa hata atukane majeshi ya Mungu aliye hai?”
1SA 17:27 Wakarudia yale yaliyokuwa yamesemwa na kumwambia kuwa, “Hili ndilo atakalotendewa mtu yule atakayemuua.”
1SA 17:28 Eliabu nduguye mkubwa Daudi alipomsikia akizungumza na watu hasira ikawaka juu yake akamuuliza, “Kwa nini umeteremka kuja hapa? Nao wale kondoo wachache kule nyikani umewaacha na nani? Ninajua jinsi ulivyo na kiburi na jinsi moyo wako ulivyo mwovu; umekuja hapa kutazama vita tu.”
1SA 17:29 Daudi akasema, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi hata kuongea.”
1SA 17:30 Daudi akamgeukia mtu mwingine na kumuuliza jambo lilo hilo, nao watu wakamjibu vilevile kama mwanzo.
1SA 17:31 Lile Daudi alilosema likasikiwa na kuelezwa kwa Sauli, naye Sauli akatuma aitwe.
1SA 17:32 Daudi akamwambia Sauli, “Mtu yeyote asife moyo kwa habari ya huyu Mfilisti; mtumishi wako ataenda kupigana naye.”
1SA 17:33 Sauli akamjibu Daudi, “Wewe hutaweza kwenda kupigana dhidi ya huyu Mfilisti; wewe ni kijana tu, naye amekuwa mtu wa vita tangu ujana wake.”
1SA 17:34 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako amekuwa akichunga kondoo wa baba yake. Simba au dubu alipokuja na kuchukua kondoo kutoka kundi,
1SA 17:35 nilifuatia, nikampiga na nikampokonya kondoo kwenye kinywa chake. Aliponigeukia, nilimkamata nywele zake, nikampiga na kumuua.
1SA 17:36 Mtumishi wako ameshaua simba na dubu pia; huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa hao, kwa sababu ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai.
1SA 17:37 Mwenyezi Mungu ambaye aliniokoa toka katika makucha ya simba na makucha ya dubu ataniokoa kutoka mikono ya huyu Mfilisti.” Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, naye Mwenyezi Mungu na awe pamoja nawe.”
1SA 17:38 Ndipo Sauli akamvika Daudi silaha zake mwenyewe za vita. Akamvika dirii na chapeo ya shaba kichwani mwake.
1SA 17:39 Daudi akajifunga upanga juu ya hayo mavazi na kujaribu kutembea kwa sababu alikuwa hana uzoefu navyo. Daudi akamwambia Sauli, “Siwezi kwenda nikiwa nimevaa hivi, kwa sababu sina uzoefu navyo.” Hivyo akavivua.
1SA 17:40 Kisha akachukua fimbo yake mkononi, akachagua mawe laini matano katika kijito, akayaweka kwenye kifuko ndani ya mfuko wake wa kichungaji, akiwa na kombeo yake mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
1SA 17:41 Wakati ule ule, yule Mfilisti, akiwa na mbeba ngao wake mbele yake, akaendelea kujongea karibu na Daudi.
1SA 17:42 Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau.
1SA 17:43 Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.
1SA 17:44 Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.”
1SA 17:45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana.
1SA 17:46 Siku hii Mwenyezi Mungu atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli.
1SA 17:47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Mwenyezi Mungu haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Mwenyezi Mungu, naye atawatia ninyi wote mikononi mwetu.”
1SA 17:48 Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye.
1SA 17:49 Daudi akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka kifudifudi.
1SA 17:50 Basi Daudi akamshinda huyo Mfilisti kwa kombeo na jiwe; bila kuwa na upanga mkononi mwake akampiga huyo Mfilisti na kumuua.
1SA 17:51 Daudi akakimbia na kusimama juu yake. Akaushika upanga wa huyo Mfilisti na kuuvuta toka kwenye ala yake. Baada ya kumuua, akakata kichwa chake kwa ule upanga. Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao amekufa, wakageuka na kukimbia.
1SA 17:52 Ndipo wanaume wa Israeli na Yuda wakainuka kwenda mbele wakipiga kelele na kufuatia Wafilisti hadi kwenye ingilio la Gathi kwenye malango ya Ekroni. Maiti zao zilitawanyika kando ya barabara ya Shaaraimu hadi Gathi na Ekroni.
1SA 17:53 Waisraeli waliporudi kutoka kuwafukuza Wafilisti, waliteka nyara kutoka kambi yao.
1SA 17:54 Daudi akachukua kichwa cha yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu, naye akaweka silaha za huyo Mfilisti katika hema lake mwenyewe.
1SA 17:55 Sauli alipomwona Daudi anaenda kukabiliana na huyo Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, “Abneri, yule kijana ni mwana wa nani?” Abneri akajibu, “Hakika kama uishivyo, ee mfalme, mimi sifahamu.”
1SA 17:56 Mfalme akasema, “Uliza huyu kijana ni mwana wa nani.”
1SA 17:57 Mara Daudi aliporudi kutoka kumuua huyo Mfilisti, Abneri akamchukua na kumleta mbele ya Sauli. Daudi alikuwa bado anakishikilia kichwa cha yule Mfilisti.
1SA 17:58 Sauli akamuuliza, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?” Daudi akasema, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese wa Bethlehemu.”
1SA 18:1 Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe.
1SA 18:2 Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani mwa baba yake.
1SA 18:3 Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe.
1SA 18:4 Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.
1SA 18:5 Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alifanikiwa sana, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia.
1SA 18:6 Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze.
1SA 18:7 Walipokuwa wanacheza, wakaimba: “Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake.”
1SA 18:8 Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?”
1SA 18:9 Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi.
1SA 18:10 Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake;
1SA 18:11 akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili.
1SA 18:12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Daudi, lakini alikuwa amemwacha yeye.
1SA 18:13 Kwa hiyo Sauli akamwondoa Daudi mbele yake na kumpa kuwa kiongozi wa watu elfu moja, naye Daudi akatoka na kuingia akiongoza vikosi katika vita.
1SA 18:14 Katika kila kitu alichofanya, Daudi alipata mafanikio makubwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye.
1SA 18:15 Sauli alipoona jinsi alivyokuwa akifanikiwa, akamwogopa.
1SA 18:16 Lakini Israeli wote na Yuda walimpenda Daudi, kwa sababu ndiye alikuwa akiwaongoza katika vita vyao.
1SA 18:17 Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupa umwoe, endapo tu utanitumikia kwa ushujaa na kupigana vita vya Mwenyezi Mungu.” Kwa maana Sauli alisema moyoni mwake, “Sitainua mkono wangu dhidi yake. Acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.”
1SA 18:18 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?”
1SA 18:19 Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi.
1SA 18:20 Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli kuhusu jambo hili, likampendeza.
1SA 18:21 Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.”
1SA 18:22 Ndipo Sauli akawaagiza watumishi wake, akisema, “Zungumzeni na Daudi kwa siri na kumwambia, ‘Tazama, mfalme amependezwa nawe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Basi na uwe mkwewe mfalme.’ ”
1SA 18:23 Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.”
1SA 18:24 Watumishi wa Sauli walipomweleza vile Daudi alivyosema,
1SA 18:25 Sauli akajibu, “Mwambieni Daudi, ‘Mfalme hataki zawadi nyingine kuwa mahari, isipokuwa magovi mia moja ya Wafilisti, ili kulipiza kisasi juu ya adui zake.’ ” Mawazo ya Sauli yalikuwa Daudi akaanguke mikononi mwa Wafilisti.
1SA 18:26 Watumishi walipomwambia Daudi mambo haya, ikampendeza kuwa mkwewe mfalme. Basi kabla siku iliyopangwa haijafika,
1SA 18:27 Daudi na watu wake walitoka na kuwaua Wafilisti mia mbili. Akayaleta magovi yao na kupeleka hesabu kamilifu kwa mfalme, ili apate kuwa mkwewe mfalme. Ndipo Sauli akamwoza Daudi Mikali binti yake.
1SA 18:28 Sauli alipotambua kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Daudi na kwamba Mikali binti yake anampenda Daudi,
1SA 18:29 Sauli akazidi kumwogopa Daudi, naye Sauli akabaki kuwa adui yake siku zote za maisha yake.
1SA 18:30 Majemadari wa jeshi la Wafilisti waliendelea kupigana vita na kadiri walivyoendelea kupigana, Daudi akazidi kutenda kwa hekima kuliko maafisa wengine wa Sauli, nalo jina lake likajulikana sana.
1SA 19:1 Sauli akamwambia mwanawe Yonathani na watumishi wake wote wamuue Daudi. Lakini Yonathani mwana wa Sauli alimpenda sana Daudi.
1SA 19:2 Yonathani akamwonya Daudi, akisema, “Baba yangu Sauli anatafuta nafasi ya kukuua. Ujilinde kesho asubuhi, nenda mahali pa siri na ukae huko.
1SA 19:3 Nitatoka na kukaa na baba yangu shambani mahali uliko. Nitazungumza naye juu yako, nami nitakueleza nitakachogundua.”
1SA 19:4 Yonathani akanena mema kuhusu Daudi kwa Sauli baba yake na kumwambia, “Mfalme asitende mabaya kwa mtumishi wake Daudi; hajakukosea, aliyoyafanya yamekuwa ya faida sana kwako.
1SA 19:5 Alihatarisha maisha yake alipomuua yule Mfilisti. Mwenyezi Mungu akajipatia ushindi mkubwa kwa ajili ya Israeli wote, nawe uliuona na ukafurahi. Kwa nini basi utende mabaya kwa mtu asiye na hatia kama Daudi kwa kumuua bila sababu?”
1SA 19:6 Sauli akamsikiliza Yonathani na kuapa hivi: “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, Daudi hatauawa.”
1SA 19:7 Basi Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mazungumzo yote. Akamleta kwa Sauli, naye Daudi akawa pamoja na Sauli kama kwanza.
1SA 19:8 Vita vilitokea tena, naye Daudi akatoka na kupigana na Wafilisti. Akawapiga kwa nguvu nyingi hata wakakimbia mbele yake.
1SA 19:9 Lakini roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu ikaja juu ya Sauli alipokuwa ameketi katika nyumba yake akiwa na mkuki mkononi mwake. Daudi alipokuwa anampigia kinubi,
1SA 19:10 Sauli akajaribu kumchomea Daudi ukutani kwa huo mkuki wake, lakini Daudi akauhepa huo mkuki wa Sauli ukakita ukutani. Usiku ule ule Daudi akakimbia na kuokoka.
1SA 19:11 Sauli akatuma watu nyumbani mwa Daudi wailinde hiyo nyumba na kumuua asubuhi. Lakini Mikali, mkewe Daudi, akamwonya akisema, “Usipokimbia kuokoa maisha yako usiku huu, kesho utauawa.”
1SA 19:12 Basi Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akakimbia na kuokoka.
1SA 19:13 Kisha Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani, akakifunika kwa vazi na kukiwekea singa za mbuzi kichwani.
1SA 19:14 Sauli alipotuma watu kumkamata Daudi, Mikali akasema, “Yeye ni mgonjwa.”
1SA 19:15 Kisha Sauli akatuma watu tena kumwona Daudi naye akawaambia, “Mleteni kwangu juu ya kitanda chake ili nipate kumuua.”
1SA 19:16 Lakini wale watu walipoingia, kumbe ni kinyago tu kilichokuwa kitandani, na kwenye kichwa kulikuwa na singa za mbuzi.
1SA 19:17 Sauli akamwambia Mikali, “Kwa nini umenidanganya mimi hivi na kumwacha adui yangu aende zake ili apate kuokoka?” Mikali akamwambia, “Yeye aliniambia, ‘Niache niende zangu. Kwa nini nikuue?’ ”
1SA 19:18 Daudi alipokuwa amekimbia na kuokoka, alimwendea Samweli huko Rama na kumwambia yale yote Sauli alimfanyia. Ndipo Daudi na Samweli wakaenda Nayothi kukaa huko.
1SA 19:19 Habari zikamfikia Sauli kusema: “Daudi yuko Nayothi huko Rama.”
1SA 19:20 Basi Sauli akatuma watu kumkamata Daudi, lakini walipoona kundi la manabii wakitoa unabii, wakiwa pamoja na Samweli akiwa amesimama hapo kama kiongozi wao, Roho wa Mungu akaja juu ya watu wa Sauli, nao pia wakatoa unabii.
1SA 19:21 Sauli akaelezwa hilo, naye akapeleka watu wengine zaidi, nao wakatoa unabii pia. Sauli akatuma watu mara ya tatu, nao pia wakatoa unabii.
1SA 19:22 Mwishowe, yeye mwenyewe akaondoka kwenda Rama na kwenda hadi kwenye kile kisima kikubwa kilichoko huko Seku. Naye akauliza, “Wako wapi Samweli na Daudi?” Wakasema, “Wako Nayothi huko Rama.”
1SA 19:23 Hivyo Sauli akaenda Nayothi huko Rama. Lakini Roho wa Mungu akaja juu yake hata yeye, akawa anatembea huku anatoa unabii hadi akafika Nayothi.
1SA 19:24 Akavua majoho yake na pia akatoa unabii mbele ya Samweli. Akalala hali hiyo ule mchana kutwa na usiku kucha. Hii ndiyo sababu watu husema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?”
1SA 20:1 Kisha Daudi akakimbia kutoka Nayothi huko Rama akamwendea Yonathani na kumuuliza, “Kwani nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemkosea baba yako kwa jinsi gani, hata kwamba anajaribu kuniua?”
1SA 20:2 Yonathani akajibu, “La hasha! Hutakufa! Tazama, baba yangu hafanyi kitu chochote, kikubwa au kidogo, bila kuniambia mimi. Kwa nini anifiche hili? Sivyo ilivyo!”
1SA 20:3 Lakini Daudi akaapa na kusema, “Baba yako anajua kabisa kwamba nimepata kibali mbele yako, naye amesema moyoni mwake, ‘Yonathani sharti asilijue hili, la sivyo atahuzunika.’ Lakini hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama uishivyo, kuna hatua moja tu kati yangu na mauti.”
1SA 20:4 Yonathani akamwambia Daudi, “Chochote unachotaka nifanye, nitakufanyia.”
1SA 20:5 Basi Daudi akamwambia Yonathani, “Angalia, kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo, nami inanipasa kula chakula pamoja na mfalme; lakini niache niende kujificha shambani hadi kesho kutwa.
1SA 20:6 Kama baba yako akiona ya kuwa sipo, mwambie, ‘Daudi aliniomba sana ruhusa kuwahi Bethlehemu, mji wake wa nyumbani, kwa sababu dhabihu ya mwaka inafanywa huko kwa ajili ya ukoo wake wote.’
1SA 20:7 Akisema, ‘Ni vyema sana,’ basi mtumishi wako yu salama. Lakini akikasirika, unaweza kuwa na hakika kwamba anakusudia kunidhuru.
1SA 20:8 Kwako wewe, mtende wema mtumishi wako, kwa sababu mmeingia kwenye agano naye mbele za Mwenyezi Mungu. Nikiwa na hatia, basi niue wewe mwenyewe! Kwa nini unikabidhi kwa baba yako?”
1SA 20:9 Yonathani akasema, “La hasha! Kama ningekuwa na kidokezo kidogo kwamba baba yangu amekusudia kukudhuru wewe, je, nisingekuambia?”
1SA 20:10 Daudi akamuuliza Yonathani, “Je, nani atakayeniambia kama baba yako atakujibu kwa ukali?”
1SA 20:11 Yonathani akamwambia, “Njoo, twende shambani.” Basi wakaenda huko pamoja.
1SA 20:12 Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Ninakuahidi kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hakika nitamchunguza baba yangu wakati kama huu kesho kutwa! Kama ameweka utaratibu wa kufaa kukuhusu wewe, je, sitakutumia ujumbe na kukufahamisha?
1SA 20:13 Lakini ikiwa baba yangu amenuia kukudhuru, Mwenyezi Mungu na aniadhibu vikali zaidi iwapo sitakufahamisha na kukuaga uende salama. Mwenyezi Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
1SA 20:14 Lakini nitendee wema usiokoma kama ule wa Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yangu, ili nisije nikauawa,
1SA 20:15 wala usiuondoe wema wako kwa jamaa yangu, hata kama ni wakati ule Mwenyezi Mungu atakapokuwa amekatilia mbali kila adui wa Daudi kutoka uso wa dunia.”
1SA 20:16 Basi Yonathani akafanya agano na nyumba ya Daudi, akisema: “Mwenyezi Mungu na awaangamize adui za Daudi.”
1SA 20:17 Naye Yonathani akamtaka Daudi athibitishe tena kiapo chake cha kumpenda, kwa sababu Yonathani alimpenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe.
1SA 20:18 Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo. Itajulikana kwamba haupo kwa kuwa kiti chako kitakuwa wazi.
1SA 20:19 Kesho kutwa, inapokaribia jioni, nenda mahali pale ulipojificha wakati tatizo hili lilipoanza na usubiri karibu na jiwe la Ezeli.
1SA 20:20 Nitapiga mishale mitatu kando yake, kana kwamba nilienda kulenga shabaha.
1SA 20:21 Kisha nitamtuma mvulana na kumwambia, ‘Nenda ukaitafute mishale.’ Nikimwambia, ‘Tazama mishale iko upande huu wako! Uilete hapa,’ basi uje, kwa sababu hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe ni salama, hakuna hatari.
1SA 20:22 Lakini nikimwambia huyo mvulana, ‘Angalia, mishale iko mbele yako,’ basi inakupasa uondoke, kwa sababu Mwenyezi Mungu amekuruhusu uende zako.
1SA 20:23 Kuhusu yale tuliyozungumza wewe na mimi: kumbuka, Mwenyezi Mungu ndiye shahidi kati yako wewe na mimi milele.”
1SA 20:24 Basi Daudi akajificha shambani, na sikukuu ya Mwezi Mwandamo ilipowadia, mfalme akaketi ili ale.
1SA 20:25 Akaketi mahali pake pa kawaida karibu na ukuta, kuelekeana na Yonathani, naye Abneri akaketi karibu na Mfalme Sauli, lakini kiti cha Daudi kilikuwa wazi.
1SA 20:26 Sauli hakusema chochote siku ile kwa kuwa alifikiri, “Kuna kitu cha lazima kimetokea kwa Daudi ambacho kimemfanya najisi asihudhurie karamu; hakika yeye yu najisi.”
1SA 20:27 Lakini siku iliyofuata, siku ya pili ya mwezi, kiti cha Daudi kilikuwa wazi tena. Kisha Sauli akamwambia mwanawe Yonathani, “Kwa nini mwana wa Yese hajaja chakulani jana wala leo?”
1SA 20:28 Yonathani akamjibu, “Daudi alinisihi sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu.
1SA 20:29 Alisema, ‘Niruhusu niende, kwa sababu jamaa yetu wana dhabihu mjini, na ndugu yangu ameniagiza niwepo huko. Kama nimepata kibali mbele yako, niruhusu niende kuona ndugu zangu.’ Hii ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.”
1SA 20:30 Hasira ya Sauli ikawaka dhidi ya Yonathani na kumwambia, “Wewe mwana wa mwanamke mkaidi na mwasi! Je, sijui kuwa umekuwa upande wa mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe na kwa aibu ya mama yako aliyekuzaa?
1SA 20:31 Maadamu mwana wa Yese angali anaishi katika dunia hii wewe wala ufalme wako hautasimama. Sasa tuma aitwe umlete kwangu, kwa kuwa ni lazima afe!”
1SA 20:32 Yonathani akamuuliza baba yake, “Kwa nini auawe? Kwani amefanya nini?”
1SA 20:33 Lakini Sauli akamtupia Yonathani mkuki wake kwa nguvu ili amuue. Hapo ndipo Yonathani alipotambua kwamba baba yake alikusudia kumuua Daudi.
1SA 20:34 Yonathani akainuka kutoka mezani kwa hasira kali. Siku ile ya pili ya mwezi hakula chakula, kwa kuwa alikuwa amehuzunishwa na vitendo vya aibu ambavyo baba yake alikuwa anamtendea Daudi.
1SA 20:35 Kesho yake asubuhi Yonathani alienda shambani kukutana na Daudi. Alikuwa amefuatana na mvulana mdogo,
1SA 20:36 naye Yonathani akamwambia yule mvulana, “Kimbia ukatafute mishale nitakayorusha.” Mvulana alipokuwa akikimbia, akarusha mishale mbele yake.
1SA 20:37 Yule mvulana alipofika mahali pale mshale wa Yonathani ulikuwa umeanguka, Yonathani akamwita, “Je, mshale hauko mbele yako?”
1SA 20:38 Yonathani akampigia kelele, “Harakisha, nenda haraka! Usisimame!” Mvulana akaokota mshale na kurudi kwa bwana wake.
1SA 20:39 (Mvulana hakujua chochote kuhusu hayo yote; Yonathani na Daudi tu ndio waliojua.)
1SA 20:40 Basi Yonathani akampa yule mvulana silaha zake na kumwambia, “Nenda, zirudishe mjini.”
1SA 20:41 Baada ya mvulana kwenda, Daudi akainuka kutoka upande wa kusini wa lile jiwe, naye akasujudu mara tatu mbele ya Yonathani. Kisha kila mmoja akambusu mwenzake, wakalia pamoja. Lakini Daudi akalia zaidi.
1SA 20:42 Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani, kwa kuwa tumeapiana kiapo cha urafiki kati yetu kwa jina la Mwenyezi Mungu, tukisema, ‘Mwenyezi Mungu ndiye shahidi kati yako na mimi, na kati ya wazao wako na wazao wangu milele.’ ” Kisha Daudi akaondoka, naye Yonathani akarudi mjini.
1SA 21:1 Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?”
1SA 21:2 Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi niliyokutuma kuifanya, wala maagizo niliyokupa!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia mahali pa kukutana.
1SA 21:3 Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.”
1SA 21:4 Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.”
1SA 21:5 Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?”
1SA 21:6 Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonesho, iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za Mwenyezi Mungu na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa.
1SA 21:7 Basi siku hiyo palikuwepo mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za Mwenyezi Mungu; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachungaji wa Sauli.
1SA 21:8 Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.”
1SA 21:9 Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungwa katika kitambaa nyuma ya kizibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.” Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.”
1SA 21:10 Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi.
1SA 21:11 Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema: “ ‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?”
1SA 21:12 Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi.
1SA 21:13 Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango, na kuachia mate kutiririka kwenye ndevu zake.
1SA 21:14 Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu?
1SA 21:15 Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani mwangu?”
1SA 22:1 Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.
1SA 22:2 Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao mia nne walikuwa naye.
1SA 22:3 Kutoka huko Daudi akaenda Mispa iliyoko Moabu na kumwambia mfalme wa Moabu, “Naomba uwaruhusu baba yangu na mama yangu waje kukaa nawe hadi nijue nini Mungu atakachonifanyia.”
1SA 22:4 Hivyo akawaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu, nao wakakaa naye muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni.
1SA 22:5 Ndipo nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae ngomeni. Nenda katika nchi ya Yuda.” Hivyo Daudi akaondoka na kwenda katika msitu wa Herethi.
1SA 22:6 Basi Sauli akasikia kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Sauli akiwa na mkuki mkononi, alikuwa ameketi chini ya mti wa mkwaju kwenye kilima huko Gibea, maafisa wake wote wakiwa wamesimama kumzunguka.
1SA 22:7 Sauli akawaambia, “Sikilizeni enyi Wabenyamini! Je, mwana wa Yese atawapa ninyi nyote mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya ninyi nyote majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia?
1SA 22:8 Je, ndiyo sababu ninyi mkapanga hila mbaya dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu ambaye ameniambia ni lini mwanangu alifanya agano na mwana wa Yese. Hapana hata mmoja wenu anayejishughulisha nami wala anayeniambia kwamba mwanangu amechochea mtumishi wangu kunivizia, kama afanyavyo leo.”
1SA 22:9 Lakini Doegi Mwedomu, aliyekuwa akisimama na maafisa wa Sauli, akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu huko Nobu.
1SA 22:10 Ahimeleki akamuuliza Mwenyezi Mungu kwa ajili yake; pia akampa vyakula na ule upanga wa Goliathi Mfilisti.”
1SA 22:11 Kisha mfalme akatuma watu wamwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, waliokuwa makuhani huko Nobu, nao wote wakaja kwa mfalme.
1SA 22:12 Sauli akasema, “Sikiliza sasa, mwana wa Ahitubu.” Akajibu, “Naam, bwana wangu.”
1SA 22:13 Sauli akamwambia, “Kwa nini umepanga njama dhidi yangu, wewe na mwana wa Yese, ukampa vyakula na upanga, tena, ulimuuliza Mungu kwa ajili yake na kwa sababu hiyo ameasi dhidi yangu na kunivizia, kama afanyavyo leo?”
1SA 22:14 Ahimeleki akamjibu mfalme, “Ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliye mwaminifu kama Daudi, mkwewe mfalme, kiongozi wa walinzi wako na anayeheshimika sana katika watu wa nyumbani mwako?
1SA 22:15 Je, siku hiyo ilikuwa ndiyo ya kwanza kumwomba Mungu kwa ajili yake? La hasha! Mfalme na usiwashutumu watumishi wako wala yeyote wa jamaa ya baba yake, kwa kuwa mtumishi wako hafahamu lolote kabisa kuhusu jambo hili lote.”
1SA 22:16 Lakini mfalme akasema, “Ahimeleki, hakika utakufa, wewe na jamaa yote ya baba yako.”
1SA 22:17 Ndipo mfalme akawaamuru walinzi wake waliokuwa kando yake: “Geukeni na kuwaua makuhani wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu nao pia wamejiunga na Daudi. Walijua kuwa alikuwa anakimbia, wala hawakuniambia.” Lakini maafisa wa mfalme hawakuwa radhi kuinua mkono kuwaua makuhani wa Mwenyezi Mungu.
1SA 22:18 Kisha mfalme akamwagiza Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Hivyo basi Doegi Mwedomu, akageuka na kuwaua. Siku ile aliwaua watu themanini na watano waliovaa vizibau vya kitani.
1SA 22:19 Pia akaupiga Nobu, mji wa makuhani kwa upanga, wakiwemo wanaume na wanawake, watoto na wale watoto wanaonyonya, ng’ombe, punda na kondoo wake.
1SA 22:20 Lakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi.
1SA 22:21 Abiathari akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa Mwenyezi Mungu.
1SA 22:22 Kisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli kuwa mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa yote ya baba yako.
1SA 22:23 Kaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.”
1SA 23:1 Daudi alipoambiwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila, nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,”
1SA 23:2 akauliza kwa Mwenyezi Mungu, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?” Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.”
1SA 23:3 Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Je, si zaidi tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!”
1SA 23:4 Daudi akauliza kwa Mwenyezi Mungu tena, naye Mwenyezi Mungu akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.”
1SA 23:5 Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila.
1SA 23:6 Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kizibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.
1SA 23:7 Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa ameenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.”
1SA 23:8 Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi.
1SA 23:9 Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kizibau.”
1SA 23:10 Daudi akasema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu.
1SA 23:11 Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.” Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, atashuka.”
1SA 23:12 Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?” Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.”
1SA 23:13 Basi Daudi na watu wake wapatao mia sita wakaondoka Keila, wakawa wanaenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakuenda huko.
1SA 23:14 Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mkononi mwake.
1SA 23:15 Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue.
1SA 23:16 Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu.
1SA 23:17 Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.”
1SA 23:18 Wote wawili wakafanya agano mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi.
1SA 23:19 Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni?
1SA 23:20 Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.”
1SA 23:21 Sauli akajibu, “Mwenyezi Mungu awabariki kwa kunifikiria.
1SA 23:22 Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali Daudi huenda mara kwa mara, na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mjanja sana.
1SA 23:23 Jueni kila mahali anapojificha, kisha mrudi na kunipa taarifa kamili. Nami nitaenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.”
1SA 23:24 Basi wakaondoka na kwenda hadi Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni.
1SA 23:25 Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka hadi mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi.
1SA 23:26 Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake,
1SA 23:27 mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.”
1SA 23:28 Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi.
1SA 23:29 Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.
1SA 24:1 Baada ya Sauli kurudi kuwafuatia Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika Jangwa la En-Gedi.”
1SA 24:2 Basi Sauli akachukua vijana wenye uwezo elfu tatu kutoka Israeli yote kwenda kumtafuta Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu.
1SA 24:3 Akaja kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi.
1SA 24:4 Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena Mwenyezi Mungu akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli.
1SA 24:5 Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli.
1SA 24:6 Akawaambia watu wake, “Mwenyezi Mungu na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.”
1SA 24:7 Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake.
1SA 24:8 Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kumsujudia, uso wake ukigusa chini.
1SA 24:9 Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’?
1SA 24:10 Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi Mwenyezi Mungu alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.’
1SA 24:11 Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuniua.
1SA 24:12 Mwenyezi Mungu na ahukumu kati yangu na wewe. Naye Mwenyezi Mungu alipize mabaya unayonitendea, lakini mkono wangu hautakugusa.
1SA 24:13 Kama msemo wa kale usemavyo, ‘Kutoka kwa watenda maovu hutoka matendo maovu,’ kwa hiyo mkono wangu hautakugusa wewe.
1SA 24:14 “Je, mfalme wa Israeli ametoka dhidi ya nani? Ni nani unayemfuatia? Je, ni mbwa mfu? Ni kiroboto?
1SA 24:15 Mwenyezi Mungu na awe mwamuzi wetu, yeye na aamue kati yetu. Yeye na anitetee shauri langu; anihesabie haki kwa kuniokoa mkononi mwako.”
1SA 24:16 Daudi alipomaliza kusema haya, Sauli akamuuliza, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Ndipo Sauli akalia kwa sauti kuu.
1SA 24:17 Akamwambia Daudi, “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi; umenitendea mema, lakini mimi nimekutendea mabaya.
1SA 24:18 Sasa umeniambia kuhusu mema uliyonitendea. Mwenyezi Mungu alinitia mikononi mwako, lakini wewe hukuniua.
1SA 24:19 Je, mtu ampatapo adui yake, humwacha aende zake bila kumdhuru? Mwenyezi Mungu na akulipe mema kwa jinsi ulivyonitenda leo.
1SA 24:20 Ninajua kwamba hakika utakuwa mfalme na kwamba ufalme wa Israeli utakuwa imara mikononi mwako.
1SA 24:21 Sasa niapie kwa Mwenyezi Mungu kwamba hutakatilia mbali uzao wangu wala kulifuta jina langu kutoka jamaa ya baba yangu.”
1SA 24:22 Basi Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akarudi zake nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.
1SA 25:1 Basi Samweli akafa, nao Waisraeli wote wakakusanyika na kumwombolezea; wakamzika nyumbani mwake huko Rama. Kisha Daudi akateremka kwenye Jangwa la Parani.
1SA 25:2 Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na makao huko Karmeli, alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli.
1SA 25:3 Jina la mtu huyo lilikuwa Nabali, naye mkewe aliitwa Abigaili. Alikuwa mwanamke mwenye busara na mzuri wa sura, lakini mumewe, aliyekuwa wa ukoo wa Kalebu, alikuwa mwenye hasira na mchoyo katika utendaji wake.
1SA 25:4 Daudi alipokuwa huko jangwani, akasikia kuwa Nabali alikuwa anakata kondoo manyoya.
1SA 25:5 Basi akatuma vijana kumi na kuwaambia, “Pandeni kwa Nabali huko Karmeli, mkamsalimie kwa jina langu.
1SA 25:6 Mwambieni: ‘Amani iwe kwako! Amani iwe kwako pamoja na wa nyumbani mwako! Pia amani iwe pamoja na vyote ulivyo navyo!
1SA 25:7 “ ‘Nasikia kuwa huu ni wakati wa kukata kondoo manyoya. Wafugaji wako walipokuwa pamoja nasi, hatukuwatendea mabaya na wakati wote waliokuwa huko Karmeli hakuna chochote chao kilipotea.
1SA 25:8 Waulize watumishi wako nao watakuambia. Kwa hiyo uwatendee wema vijana wangu, kwani tumekuja wakati wa furaha. Tafadhali wape watumishi wako na mwanao Daudi chochote kitakachokuja mkononi mwako kwa ajili yao.’ ”
1SA 25:9 Watu wa Daudi walipofika wakampa Nabali ujumbe huu kwa jina la Daudi. Kisha wakangojea.
1SA 25:10 Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Huyu Daudi ni nani? Huyu mwana wa Yese ni nani? Watumishi wengi wanakimbia kutoka kwa bwana zao siku hizi.
1SA 25:11 Kwa nini nichukue mkate wangu, maji yangu na nyama niliyochinja kwa ajili ya wakata manyoya wangu, na kuwapa watu ambao hakuna anayejua wanakotoka?”
1SA 25:12 Watu wa Daudi wakageuka na kurudi. Walipofika, wakaarifu kila neno.
1SA 25:13 Daudi akawaambia watu wake, “Jifungeni panga zenu!” Basi wakajifunga panga zao, naye Daudi akajifunga upanga wake. Watu kama mia nne hivi wakapanda pamoja na Daudi, na watu mia mbili wakabaki na vifaa.
1SA 25:14 Mmoja wa watumishi akamwambia Abigaili, mkewe Nabali: “Daudi alituma wajumbe kutoka jangwani kumpa bwana wetu salamu zake, lakini akawatukana.
1SA 25:15 Hata hivyo watu hawa walikuwa wema sana kwetu. Hawakututendea mabaya, na wakati wote tulipokuwa nje huko mashambani karibu nao, hatukupotewa na kitu chochote.
1SA 25:16 Usiku na mchana walikuwa ukuta wa ulinzi wakati wote tulipokuwa tukichunga kondoo wetu karibu nao.
1SA 25:17 Sasa fikiri juu ya jambo hili na uone unaweza kufanya nini, kwa sababu maafa yanakaribia juu ya bwana wetu na nyumba yake yote. Yeye ni mtu mwovu kiasi kwamba hakuna mtu awezaye kuzungumza naye.”
1SA 25:18 Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate mia mbili, viriba viwili vya divai, kondoo watano waliochinjwa vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu kavu, mikate mia mbili ya tini, akavipakia juu ya punda.
1SA 25:19 Kisha akawaambia watumishi wake, “Tangulieni; mimi nitakuja nyuma yenu.” Lakini hakumwambia Nabali mumewe.
1SA 25:20 Ikawa alipokuwa amepanda punda wake kwenye bonde la mlima, tazama, Daudi na watu wake wakawa wanateremka kumwelekea, naye akakutana nao.
1SA 25:21 Daudi alikuwa amesema, “Ilikuwa ni kazi bure kuchunga kwangu kote mali ya huyu mtu huko jangwani hivi kwamba hakuna chochote chake kilichopotea. Yeye amenilipa baya kwa ajili ya wema.
1SA 25:22 Mwenyezi Mungu na amwadhibu Daudi vikali zaidi, ikiwa kesho asubuhi nitambakizia mwanaume hata mmoja hai miongoni mwa watu wake wote!”
1SA 25:23 Abigaili alipomwona Daudi, akashuka haraka kwenye punda wake, akamsujudia Daudi.
1SA 25:24 Akamwangukia miguuni pake na kusema: “Bwana wangu, kosa hili na liwe juu yangu mwenyewe. Tafadhali mruhusu mtumishi wako aseme nawe. Sikia kile mtumishi wako atakachosema.
1SA 25:25 Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake; jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye. Lakini kwangu mimi, mtumishi wako, sikuwaona hao watu waliotumwa na bwana wangu.
1SA 25:26 “Basi sasa, bwana wangu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuzuia kumwaga damu na kulipiza kisasi kwa mikono yako mwenyewe, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama uishivyo, adui zako na wote wanaokusudia kumdhuru bwana wangu wawe kama Nabali.
1SA 25:27 Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe.
1SA 25:28 Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa Mwenyezi Mungu kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya Mwenyezi Mungu.
1SA 25:29 Hata ingawa kuna mtu anayekufuatia ili akuue, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako utavurumishwa kama vile jiwe kutoka kombeo.
1SA 25:30 Mwenyezi Mungu atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli,
1SA 25:31 bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. Mwenyezi Mungu atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.”
1SA 25:32 Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekutuma kunilaki leo.
1SA 25:33 Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu.
1SA 25:34 La sivyo, hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna mwanaume hata mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.”
1SA 25:35 Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani mwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.”
1SA 25:36 Abigaili alipoenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote hadi asubuhi yake.
1SA 25:37 Basi asubuhi, ulevi ulipokuwa umemtoka Nabali, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe.
1SA 25:38 Baada ya siku kumi, Mwenyezi Mungu akampiga Nabali, naye akafa.
1SA 25:39 Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, ambaye amenitetea dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na Mwenyezi Mungu ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.” Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake.
1SA 25:40 Watumishi wa Daudi wakaenda Karmeli na kumwambia Abigaili, wakisema, “Daudi ametutuma kwako kukuchukua uwe mkewe.”
1SA 25:41 Akasujudu uso wake ukielekea chini, akasema, “Mjakazi wako yuko hapa, tayari kuwatumikia na kuwanawisha miguu watumishi wa bwana wangu.”
1SA 25:42 Abigaili akainuka kwa haraka, akapanda punda wake, akihudumiwa na wajakazi wake watano, akaenda pamoja na wajumbe wa Daudi, naye akawa mkewe.
1SA 25:43 Pia Daudi alikuwa amemwoa Ahinoamu wa Yezreeli, wote wawili wakawa wake zake.
1SA 25:44 Lakini Sauli alikuwa amemwoza Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka Galimu.
1SA 26:1 Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?”
1SA 26:2 Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na wapiganaji wake elfu tatu wa Israeli waliochaguliwa, ili kumtafuta Daudi huko.
1SA 26:3 Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko,
1SA 26:4 Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili.
1SA 26:5 Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali ambapo Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka.
1SA 26:6 Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?” Abishai akajibu, “Nitaenda pamoja nawe.”
1SA 26:7 Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli.
1SA 26:8 Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome hadi ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.”
1SA 26:9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu na asiwe na hatia?”
1SA 26:10 Daudi akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, Mwenyezi Mungu mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au ataenda vitani na kuangamia.
1SA 26:11 Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.”
1SA 26:12 Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.
1SA 26:13 Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima, mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao.
1SA 26:14 Daudi akapaza sauti kwa jeshi na kwa Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?” Abneri akajibu, “Nani wewe unayemwita mfalme?”
1SA 26:15 Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako.
1SA 26:16 Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?”
1SA 26:17 Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.”
1SA 26:18 Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia?
1SA 26:19 Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama Mwenyezi Mungu amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za Mwenyezi Mungu! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa Mwenyezi Mungu wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’
1SA 26:20 Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa Mwenyezi Mungu. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.”
1SA 26:21 Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.”
1SA 26:22 Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua.
1SA 26:23 Mwenyezi Mungu humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. Mwenyezi Mungu alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.
1SA 26:24 Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwa Mwenyezi Mungu na kuniokoa kutoka taabu zote.”
1SA 26:25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.” Basi Daudi akaenda zake, naye Sauli akarudi nyumbani.
1SA 27:1 Daudi akasema moyoni mwake, “Katika mojawapo ya siku hizi nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli. Jambo lililo bora ni kutorokea kwenye nchi ya Wafilisti. Hivyo Sauli atakata tamaa ya kunisaka popote katika Israeli, nami nitakuwa nimeponyoka mkononi mwake.”
1SA 27:2 Hivyo Daudi akaondoka na hao watu mia sita waliokuwa pamoja naye na kwenda kwa Akishi mwana wa Maoki mfalme wa Gathi.
1SA 27:3 Daudi na watu wake wakakaa huko Gathi pamoja na Akishi. Kila mtu alikuwa pamoja na jamaa yake, naye Daudi pamoja na wakeze wawili: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali.
1SA 27:4 Sauli alipokuwa ameambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbilia Gathi, hakuendelea kumsaka tena.
1SA 27:5 Ndipo Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, unipe sehemu katika mojawapo ya miji katika nchi nikae huko. Kwa nini mtumwa wako akae pamoja nawe katika mji huu wa kifalme?”
1SA 27:6 Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi mji wa Siklagi, nao Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda tangu wakati huo.
1SA 27:7 Daudi akaishi katika nchi ya Wafilisti muda wa mwaka mmoja na miezi minne.
1SA 27:8 Basi Daudi na watu wake wakapanda na kuwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki. (Tangu zamani haya mataifa yalikuwa yameishi kwenye eneo lililotanda kuanzia Telemu katika njia iteremkayo Shuri hadi kufikia nchi ya Misri.)
1SA 27:9 Kila mara Daudi aliposhambulia eneo, hakubakiza hai mwanaume wala mwanamke, lakini alichukua kondoo na ng’ombe, punda na ngamia, na nguo. Kisha akarudi kwa Akishi.
1SA 27:10 Akishi alipomuuliza, “Je leo umeshambulia wapi?” Daudi humjibu, “Dhidi ya Negebu ya Yuda,” au wakati mwingine husema, “Dhidi ya Negebu ya Yerameeli,” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.”
1SA 27:11 Daudi hakumwacha hai mwanaume au mwanamke ili apate kuletwa Gathi, kwa maana aliwaza, “Wanaweza kujulisha habari zetu na kusema, ‘Hivi ndivyo alivyofanya Daudi.’ ” Hii ndiyo ilikuwa desturi yake wakati wote aliishi katika nchi ya Wafilisti.
1SA 27:12 Akishi akamsadiki Daudi na kuwaza moyoni mwake, akasema, “Daudi amekuwa kitu cha kuchukiza kabisa kwa watu wake, Waisraeli, hivi kwamba atakuwa mtumishi wangu milele.”
1SA 28:1 Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.”
1SA 28:2 Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.”
1SA 28:3 Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi.
1SA 28:4 Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa.
1SA 28:5 Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu.
1SA 28:6 Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kupitia manabii.
1SA 28:7 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.” Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.”
1SA 28:8 Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.”
1SA 28:9 Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?”
1SA 28:10 Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Mwenyezi Mungu, akasema, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.”
1SA 28:11 Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?” Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.”
1SA 28:12 Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.”
1SA 28:13 Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?” Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.”
1SA 28:14 Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?” Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.” Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu, uso wake ukagusa chini.
1SA 28:15 Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?” Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena kupitia manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.”
1SA 28:16 Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, kuona Mwenyezi Mungu amekuacha na kuwa adui yako?
1SA 28:17 Mwenyezi Mungu ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Mwenyezi Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa majirani zako, yaani Daudi.
1SA 28:18 Kwa sababu wewe hukumtii Mwenyezi Mungu, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Mwenyezi Mungu amekutendea mambo haya leo.
1SA 28:19 Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Mwenyezi Mungu pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.”
1SA 28:20 Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku.
1SA 28:21 Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye.
1SA 28:22 Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.”
1SA 28:23 Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.” Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.
1SA 28:24 Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu.
1SA 28:25 Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.
1SA 29:1 Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki, nao Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyo Yezreeli.
1SA 29:2 Watawala wa Wafilisti walipokuwa wakipita pamoja na vikosi vyao vya mamia na vya maelfu, Daudi na watu wake walikuwa wakitembea huko nyuma pamoja na Akishi.
1SA 29:3 Majemadari wa Wafilisti wakauliza, “Vipi kuhusu hawa Waebrania?” Akishi akajibu, “Huyu si Daudi, aliyekuwa afisa wa Sauli mfalme wa Israeli? Ameshakuwa pamoja nami kwa zaidi ya mwaka, naye tangu alipomwacha Sauli hadi sasa, sikuona kosa lolote kwake.”
1SA 29:4 Lakini majemadari wa Wafilisti wakamkasirikia na kusema, “Mrudishe mtu huyu, apate kurudi mahali pale ulipompangia. Haimpasi kufuatana pamoja nasi vitani, asije akageuka, akawa kinyume chetu vitani. Ni kwa njia ipi bora zaidi angeweza kujipatia tena kibali kwa bwana wake, isipokuwa kwa vichwa vya watu wetu wenyewe?
1SA 29:5 Je, huyu si ndiye Daudi walioimba kumhusu katika ngoma zao, wakisema: “ ‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?”
1SA 29:6 Basi Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe umekuwa mtu mwaminifu, nami ningependa utumike pamoja nami katika jeshi. Tangu siku ile uliyofika kwangu hadi sasa, sijaona kosa lolote kwako, lakini hao watawala hawakukubali.
1SA 29:7 Rudi na uende kwa amani; usifanye chochote cha kuwakasirisha watawala wa Wafilisti.”
1SA 29:8 Daudi akamuuliza Akishi, “Lakini mimi nimefanya nini? Je, umeona nini kibaya juu ya mtumishi wako tangu siku ile niliyokuja kwako hadi leo? Kwa nini nisirudi na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?”
1SA 29:9 Akishi akamjibu Daudi, “Mimi ninajua ya kuwa wewe umekuwa wa kupendeza machoni pangu kama vile malaika wa Mungu. Lakini hao majemadari wa Wafilisti wamesema, ‘Huyu haimpasi kwenda vitani pamoja nasi.’
1SA 29:10 Sasa amka mapema, pamoja na watumishi wa bwana wako waliofuatana nawe, nanyi ondokeni asubuhi mara kutakapopambazuka.”
1SA 29:11 Hivyo Daudi na watu wake wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda zao kurudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Yezreeli.
1SA 30:1 Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto,
1SA 30:2 nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakumuua yeyote, bali waliwachukua wakaenda zao.
1SA 30:3 Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao wa kiume na wa kike wamechukuliwa mateka.
1SA 30:4 Hivyo Daudi na watu wake wakapaza sauti na kulia hadi wakaishiwa na nguvu za kulia.
1SA 30:5 Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.
1SA 30:6 Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana kuhusu kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe wa kiume na wa kike. Lakini Daudi akajitia nguvu katika Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
1SA 30:7 Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibau.” Abiathari akamletea,
1SA 30:8 naye Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?” Mwenyezi Mungu akajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.”
1SA 30:9 Daudi pamoja na watu wake mia sita wakafika kwenye Bonde la Besori, ambapo wengine waliachwa nyuma,
1SA 30:10 kwa kuwa watu mia mbili walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu mia nne wakaendelea kufuatia.
1SA 30:11 Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula;
1SA 30:12 kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula chochote wala kunywa maji kwa siku tatu usiku na mchana.
1SA 30:13 Daudi akamuuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?” Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita.
1SA 30:14 Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.”
1SA 30:15 Daudi akamuuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?” Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.”
1SA 30:16 Akamwongoza Daudi hadi mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda.
1SA 30:17 Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana mia nne waliopanda ngamia na kutoroka.
1SA 30:18 Daudi akarudisha kila kitu ambacho Waamaleki walikuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili.
1SA 30:19 Hakuna chochote kilichopotea: kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine chochote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu.
1SA 30:20 Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya mifugo wengine, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”
1SA 30:21 Kisha Daudi akafika kwa wale watu mia mbili waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu.
1SA 30:22 Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakuenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.”
1SA 30:23 Daudi akajibu, “La, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu ametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu.
1SA 30:24 Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyeenda vitani. Wote watashiriki sawa.”
1SA 30:25 Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo.
1SA 30:26 Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka nyara za adui za Mwenyezi Mungu.”
1SA 30:27 Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri;
1SA 30:28 kwa wale walio Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa
1SA 30:29 na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni;
1SA 30:30 na kwa wale walio Horma, Bori-Ashani, Athaki,
1SA 30:31 na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea.
1SA 31:1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika Mlima Gilboa.
1SA 31:2 Wafilisti wakawafuatilia Sauli na wanawe kwa karibu, na wakawaua Yonathani, Abinadabu, na Malki-Shua.
1SA 31:3 Mapigano yakawa makali sana dhidi ya Sauli, nao wapiga upinde wakampata na kumjeruhi vibaya.
1SA 31:4 Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja wanichome na kunidhalilisha.” Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe, akauangukia.
1SA 31:5 Mbeba silaha wake alipoona Sauli amekufa, pia akaangukia upanga wake, akafa pamoja naye.
1SA 31:6 Basi Sauli, wanawe watatu, mbeba silaha wake na watu wake wote wakafa pamoja siku ile ile.
1SA 31:7 Waisraeli waliokuwa kando ya bonde na wale waliokuwa ng’ambo ya Yordani walipoona kuwa jeshi la Waisraeli limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, wakaacha miji yao na kukimbia. Nao Wafilisti wakaenda na kukaa humo.
1SA 31:8 Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe watatu wameanguka katika Mlima Gilboa.
1SA 31:9 Wakamkata Sauli kichwa na kumvua silaha zake, nao wakatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari katika hekalu la sanamu zao na miongoni mwa watu wao.
1SA 31:10 Wakaweka silaha zake katika hekalu la Maashtorethi, na kukifunga kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-Shani.
1SA 31:11 Watu wa Yabesh-Gileadi waliposikia yale Wafilisti waliyomfanyia Sauli,
1SA 31:12 mashujaa wao wote wakaenda usiku hadi Beth-Shani. Wakauchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Beth-Shani na kurudi hadi Yabeshi, ambapo waliiteketeza miili kwa moto.
1SA 31:13 Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga kwa siku saba.
2SA 1:1 Baada ya kifo cha Sauli, Daudi alirudi kutoka kuwashinda Waamaleki, na akakaa siku mbili huko Siklagi.
2SA 1:2 Siku ya tatu akaja mtu mwenye nguo zilizoraruka na mavumbi kichwani mwake kutoka kambi ya Sauli. Alipomjia Daudi, akajitupa chini ili kumpa heshima.
2SA 1:3 Daudi akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?” Akamjibu, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.”
2SA 1:4 Daudi akamuuliza, “Ni nini kilichotokea? Niambie.” Akasema, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wao walianguka na kufa. Naye Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa.”
2SA 1:5 Ndipo Daudi akamwambia huyo kijana aliyemletea taarifa, “Je, umefahamu vipi kwamba Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”
2SA 1:6 Yule kijana akasema, “Nilijipata huko Mlima Gilboa, naye Sauli alikuwa huko akiegemea mkuki wake, na magari ya vita na wapanda farasi wa upande wa adui wakawa wamemkaribia sana.
2SA 1:7 Alipogeuka na kuniona, akaniita, nami nikasema, ‘Je, nifanye nini?’
2SA 1:8 “Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’ “Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’
2SA 1:9 “Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’
2SA 1:10 “Kwa hiyo nikamkaribia na kumuua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.”
2SA 1:11 Ndipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua.
2SA 1:12 Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga hadi jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi la Mwenyezi Mungu na nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga.
2SA 1:13 Daudi akamwambia yule kijana aliyemletea taarifa, “Wewe unatoka wapi?” Akamjibu, “Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.”
2SA 1:14 Daudi akamuuliza, “Kwa nini hukuogopa kuinua mkono wako ili kumwangamiza mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu?”
2SA 1:15 Kisha Daudi akamwita mmoja wa watu wake na kumwambia, “Nenda ukamuue!” Kwa hiyo akampiga, naye akafa.
2SA 1:16 Kwa maana Daudi alikuwa amemwambia, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako mwenyewe. Kinywa chako mwenyewe kimeshuhudia dhidi yako uliposema, ‘Nilimuua mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.’ ”
2SA 1:17 Daudi akafanya maombolezo haya kuhusu Sauli na Yonathani mwanawe,
2SA 1:18 naye akaagiza kwamba watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hili la upinde (ambalo limeandikwa katika Kitabu cha Yashari):
2SA 1:19 “Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa juu ya mahali pako palipoinuka. Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka!
2SA 1:20 “Msilisimulie hili katika Gathi, msilitangaze hili katika barabara za Ashkeloni, binti za Wafilisti wasije wakafurahia, binti za hao wasiotahiriwa wasije wakashangilia.
2SA 1:21 “Enyi milima ya Gilboa, msipate umande wala mvua, wala mashamba yanayozaa sadaka ya nafaka. Kwa maana huko ndiko ngao ya mwenye nguvu iliponajisiwa, ngao ya Sauli haitapakwa tena mafuta.
2SA 1:22 “Kutokana na damu ya waliouawa, kutokana na miili ya wenye nguvu, ule upinde wa Yonathani haukugeuka nyuma. Upanga wa Sauli haukurudi bure.
2SA 1:23 Sauli na Yonathani: maishani walipendwa na kuneemeka, na katika kifo hawakutengana. Walikuwa wepesi kuliko tai, walikuwa na nguvu kuliko simba.
2SA 1:24 “Enyi binti za Israeli, lieni kwa ajili ya Sauli, ambaye aliwavika nguo nyekundu na maridadi, ambaye alirembesha mavazi yenu kwa mapambo ya dhahabu.
2SA 1:25 “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka vitani! Yonathani ameuawa mahali pako palipoinuka.
2SA 1:26 Nahuzunika kwa ajili yako, Yonathani ndugu yangu, kwangu ulikuwa mpendwa sana. Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, wa ajabu kuliko ule wa wanawake.
2SA 1:27 “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka! Silaha za vita zimeangamia!”
2SA 2:1 Ikawa baada ya mambo haya, Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, nipande kwenda katika mojawapo ya miji ya Yuda?” Mwenyezi Mungu akasema, “Panda.” Daudi akauliza, “Je, niende wapi?” Mwenyezi Mungu akajibu, “Nenda Hebroni.”
2SA 2:2 Basi Daudi akakwea kwenda huko pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.
2SA 2:3 Daudi akawachukua pia watu waliokuwa pamoja naye, kila mmoja na jamaa yake, nao wakaishi huko Hebroni na miji yake.
2SA 2:4 Ndipo wanaume wa Yuda wakaja Hebroni, huko wakampaka Daudi mafuta awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda. Daudi alipoambiwa kuwa ni wanaume wa Yabesh-Gileadi waliomzika Sauli,
2SA 2:5 akatuma wajumbe kwa wanaume wa Yabesh-Gileadi, kuwaambia, “Mwenyezi Mungu awabariki kwa kuonesha wema huu kwa kumzika Sauli bwana wenu.
2SA 2:6 Sasa Mwenyezi Mungu na awaoneshe wema na uaminifu, nami pia nitawaonesha wema ule ule kwa kuwa mmefanya jambo hili.
2SA 2:7 Sasa basi, kuweni hodari na mashujaa, kwa maana bwana wenu Sauli amekufa, nao watu wa nyumba ya Yuda wamenipaka mafuta niwe mfalme juu yao.”
2SA 2:8 Wakati huo Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Sauli, alikuwa amemchukua Ish-Boshethi mwana wa Sauli na kumleta hadi Mahanaimu.
2SA 2:9 Akamweka awe mfalme juu ya nchi ya Gileadi, Waasheri, Yezreeli, Efraimu, Benyamini na Israeli yote.
2SA 2:10 Ish-Boshethi mwana wa Sauli alikuwa na umri wa miaka arobaini alipoanza kutawala Israeli, naye akatawala miaka miwili. Hata hivyo, nyumba ya Yuda ikamfuata Daudi.
2SA 2:11 Muda ambao Daudi alikuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda huko Hebroni ilikuwa miaka saba na miezi sita.
2SA 2:12 Abneri mwana wa Neri, pamoja na watumishi wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni.
2SA 2:13 Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wa Daudi wakatoka na kukutana nao kwenye bwawa la Gibeoni. Kikundi kimoja kiliketi upande mmoja wa bwawa, na kikundi kingine upande wa pili.
2SA 2:14 Ndipo Abneri akamwambia Yoabu, “Tuwaweke baadhi ya vijana wasimame, wapigane ana kwa ana mbele yetu.” Yoabu akasema, “Sawa, na wafanye hivyo.”
2SA 2:15 Kwa hiyo vijana wakasimama, wakahesabiwa: watumishi wa Benyamini na wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli kumi na wawili, na upande wa Daudi kumi na wawili.
2SA 2:16 Kisha kila mwanaume akamkamata mpinzani wake kichwani na kumchoma kwa upanga, nao wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale katika Gibeoni pakaitwa Helkath-Hasurimu.
2SA 2:17 Siku hiyo vita vilikuwa vikali sana, naye Abneri na Waisraeli wakashindwa na watumishi wa Daudi.
2SA 2:18 Wana watatu wa Seruya walikuwa huko: Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa.
2SA 2:19 Asaheli akamfukuza Abneri, pasipo kugeuka kulia wala kushoto wakati alimfuata.
2SA 2:20 Abneri akaangalia nyuma na kumuuliza, “Ni wewe, Asaheli?” Akamjibu, “Ndiyo.”
2SA 2:21 Ndipo Abneri akamwambia, “Geuka upande wa kulia au kushoto. Mchukue mmoja wa vijana, umvue silaha zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfukuza.
2SA 2:22 Abneri akamwonya tena Asaheli akimwambia, “Acha kunifukuza! Kwa nini nikuue? Je, nitawezaje kumtazama ndugu yako Yoabu usoni?”
2SA 2:23 Lakini Asaheli alikataa kuacha kumfuatia, kwa hiyo Abneri akamchoma Asaheli tumboni kwa ncha butu ya mkuki wake, mkuki ukamtoboa ukatokea mgongoni mwake. Akaanguka na kufa papo hapo. Ikawa kila mtu alisimama alipofika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa.
2SA 2:24 Lakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni.
2SA 2:25 Ndipo Wabenyamini wakakusanyika tena nyuma ya Abneri. Wakaunda kikosi na kujiimarisha juu ya kilima.
2SA 2:26 Abneri akamwita Yoabu, akamwambia, “Je, ni lazima upanga uendelee kuangamiza milele? Hutambui kwamba jambo hili litaishia katika uchungu? Utaacha kuwaagiza watu wako waache kuwafuatilia ndugu zao hata lini?”
2SA 2:27 Yoabu akajibu, “Hakika kama aishivyo Mungu, kama hukusema, hawa watu wangeendelea kuwafuatia ndugu zao hadi asubuhi.”
2SA 2:28 Basi Yoabu akapiga tarumbeta, nao watu wote wakasimama, hawakuwafuata Waisraeli tena, wala hawakuwapiga tena.
2SA 2:29 Usiku ule wote Abneri na watu wake wakatembea kupitia Araba. Wakavuka Mto Yordani, wakaendelea wakipitia nchi yote ya Bithroni wakafika Mahanaimu.
2SA 2:30 Basi Yoabu akarudi kutoka kumfuatia Abneri, na kuwakusanya watu wake wote. Pamoja na Asaheli, watumishi kumi na tisa wa Daudi walikuwa wamepotea.
2SA 2:31 Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua Wabenyamini mia tatu na sitini waliokuwa pamoja na Abneri.
2SA 2:32 Wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake huko Bethlehemu. Kisha Yoabu na vijana wake wakatembea usiku kucha na kufika huko Hebroni wakati wa mapambazuko.
2SA 3:1 Vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi.
2SA 3:2 Wana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni: Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli;
2SA 3:3 mzaliwa wake wa pili alikuwa Danieli mwana wa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli; wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri;
2SA 3:4 wa nne, Adoniya mwana wa Hagithi; wa tano, Shefatia mwana wa Abitali;
2SA 3:5 wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi.
2SA 3:6 Wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli.
2SA 3:7 Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake Rispa binti Aya. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?”
2SA 3:8 Abneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke!
2SA 3:9 Mungu na amwadhibu Abneri vikali zaidi ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kile Mwenyezi Mungu alichomwahidi kwa kiapo,
2SA 3:10 na kuuhamisha ufalme kutoka nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani hadi Beer-Sheba.”
2SA 3:11 Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri.
2SA 3:12 Ndipo Abneri akatuma wajumbe kwa niaba yake kwa Daudi, kumwambia, “Nchi hii ni ya nani? Fanya mapatano na mimi, nami nitakusaidia kuiweka Israeli yote juu yako.”
2SA 3:13 Daudi akasema, “Vyema, nitafanya mapatano nawe. Lakini nahitaji jambo moja kwako: Usije mbele yangu hadi umemleta Mikali binti Sauli wakati utakapokuja kuniona.”
2SA 3:14 Kisha Daudi akapeleka wajumbe kwa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, kudai, “Nipe Mikali mke wangu, ambaye nilimposa mwenyewe kwa mahari ya magovi mia moja ya Wafilisti.”
2SA 3:15 Kwa hiyo Ish-Boshethi akatoa amri kwamba Mikali achukuliwe kutoka kwa Paltieli mumewe, mwana wa Laishi.
2SA 3:16 Hata hivyo, mumewe alienda pamoja naye, akilia nyuma ya mkewe njia yote hadi Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani!” Kwa hiyo akarudi.
2SA 3:17 Abneri akafanya shauri pamoja na wazee wa Israeli, akasema, “Muda mrefu mmetaka kumfanya Daudi mfalme wenu.
2SA 3:18 Sasa fanyeni hivyo! Kwa maana Mwenyezi Mungu alimwahidi Daudi akisema, ‘Kupitia Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka mikononi mwa Wafilisti na kutoka mikononi mwa adui zako wote.’ ”
2SA 3:19 Pia Abneri mwenyewe akazungumza na kabila la Benyamini. Kisha akaenda Hebroni kumwambia Daudi kila kitu ambacho Israeli na nyumba yote ya Benyamini walichotaka kufanya.
2SA 3:20 Abneri, aliyekuwa na watu ishirini pamoja naye, alipokuja kwa Daudi huko Hebroni, Daudi akamwandalia karamu pamoja na watu wake.
2SA 3:21 Ndipo Abneri akamwambia Daudi, “Niache niende mara moja nikakusanye Israeli yote kwa ajili ya mfalme bwana wangu, ili waweze kufanya mapatano na wewe, ili uweze kutawala yale yote moyo wako unaonea shauku.” Basi Daudi akamuaga Abneri, naye akaenda kwa amani.
2SA 3:22 Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani.
2SA 3:23 Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme, na kwamba mfalme alikuwa amemruhusu aende zake, na kwamba alikuwa ameondoka kwa amani.
2SA 3:24 Basi Yoabu alienda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikuja kwako. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa ameenda!
2SA 3:25 Unajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza mienendo yako, na kugundua kila kitu unachokifanya.”
2SA 3:26 Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili.
2SA 3:27 Basi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Ili kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni palepale, naye akafa.
2SA 3:28 Baadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele za Mwenyezi Mungu kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri.
2SA 3:29 Damu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane yeyote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha au ukoma, au mwenye kuegemea fimbo, au aangukaye kwa upanga, au kupungukiwa na chakula.”
2SA 3:30 (Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.)
2SA 3:31 Kisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae gunia, mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza.
2SA 3:32 Wakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia.
2SA 3:33 Mfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri: “Je, ilipasa Abneri afe kama anavyokufa mpumbavu?
2SA 3:34 Mikono yako haikufungwa, miguu yako haikufungwa pingu. Ulianguka kama yeye aangukaye mbele ya watu waovu.” Nao watu wote wakamlilia tena.
2SA 3:35 Kisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale chochote kulipokuwa bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi, nikionja mkate au kitu kingine chochote kabla ya jua kutua!”
2SA 3:36 Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza.
2SA 3:37 Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri.
2SA 3:38 Kisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mtu mkuu na mashuhuri ameanguka katika Israeli leo?
2SA 3:39 Nami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu. Mwenyezi Mungu na amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”
2SA 4:1 Ish-Boshethi mwana wa Sauli aliposikia kwamba Abneri amekufa huko Hebroni, akakosa ujasiri, nayo Israeli yote wakatiwa hofu kuu.
2SA 4:2 Basi mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili waliokuwa viongozi wa vikundi vya uvamizi. Mmoja aliitwa Baana na mwingine Rekabu, waliokuwa wana wa Rimoni, Mbeerothi, kutoka kabila la Benyamini. Beerothi alihesabiwa kuwa sehemu ya Benyamini,
2SA 4:3 kwa sababu watu wa Beerothi walikimbilia huko Gitaimu na wameishi huko kama wageni hadi leo.
2SA 4:4 (Yonathani mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa mlemavu miguu yote miwili. Alikuwa na umri wa miaka mitano wakati habari kuhusu Sauli na Yonathani zilipofika kutoka Yezreeli. Yaya wake akambeba ili kukimbia, lakini yaya alipokuwa anaharakisha kuondoka, mtoto alianguka akawa kiwete. Jina lake aliitwa Mefiboshethi.)
2SA 4:5 Basi Rekabu na Baana, wana wa Rimoni Mbeerothi wakaenda nyumbani mwa Ish-Boshethi; walifika huko alipokuwa kwenye mapumziko yake ya mchana.
2SA 4:6 Wakaingia kwenye chumba cha ndani kana kwamba wanachukua ngano, wakamchoma Ish-Boshethi mkuki tumboni. Ndipo Rekabu na Baana nduguye wakatoroka.
2SA 4:7 Walikuwa wameingia ndani ya nyumba alipokuwa amelala kitandani chumbani kwake. Baada ya kumchoma mkuki na kumuua, walikata kichwa chake. Walikibeba na kutembea usiku kucha kwa njia ya Araba.
2SA 4:8 Wakamletea Daudi kichwa cha Ish-Boshethi huko Hebroni, wakamwambia mfalme, “Hiki hapa kichwa cha Ish-Boshethi mwana wa Sauli, adui yako, aliyejaribu kukuua. Siku hii ya leo Mwenyezi Mungu amemlipizia kisasi mfalme bwana wangu dhidi ya Sauli na uzao wake.”
2SA 4:9 Daudi akawajibu Rekabu na Baana nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi, akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka taabu zote,
2SA 4:10 yule mtu aliponiambia, ‘Sauli amekufa,’ akadhani ananiletea habari njema, nilimkamata, nikamuua huko Siklagi. Hiyo ndiyo zawadi niliyompa kwa ajili ya taarifa yake!
2SA 4:11 Je, ni mara ngapi zaidi wakati watu waovu wamemuua mtu asiye na hatia akiwa ndani ya nyumba yake mwenyewe na kwenye kitanda chake mwenyewe? Je, sasa nisidai damu yake mikononi mwenu na kuwaondoa duniani?”
2SA 4:12 Kwa hiyo Daudi akawaamuru watu wake, wakawaua. Wakakata mikono yao na miguu, na kutundika viwiliwili vyao kando ya dimbwi huko Hebroni. Lakini wakakichukua kichwa cha Ish-Boshethi na kukizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.
2SA 5:1 Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu mwili wako na damu yako.
2SA 5:2 Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye Mwenyezi Mungu alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”
2SA 5:3 Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Mwenyezi Mungu, nao wakampaka Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.
2SA 5:4 Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli kwa miaka arobaini.
2SA 5:5 Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na tatu.
2SA 5:6 Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.”
2SA 5:7 Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.
2SA 5:8 Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”
2SA 5:9 Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo kuelekea ndani.
2SA 5:10 Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, alikuwa pamoja naye.
2SA 5:11 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi.
2SA 5:12 Naye Daudi akafahamu kuwa Mwenyezi Mungu amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake.
2SA 5:13 Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana wengi wa kiume na wa kike walizaliwa kwake.
2SA 5:14 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani,
2SA 5:15 Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia,
2SA 5:16 Elishama, Eliada na Elifeleti.
2SA 5:17 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome.
2SA 5:18 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai,
2SA 5:19 kwa hiyo Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
2SA 5:20 Ndipo Daudi akaenda Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yanavyofurika, Mwenyezi Mungu amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu.
2SA 5:21 Wafilisti wakaziacha sanamu zao huko, naye Daudi na watu wake wakazichukua.
2SA 5:22 Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai.
2SA 5:23 Kwa hiyo Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi.
2SA 5:24 Mara utakaposikia sauti ya kutembea kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa Mwenyezi Mungu ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.”
2SA 5:25 Basi Daudi akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba hadi Gezeri.
2SA 6:1 Tena Daudi akakusanya vijana wenye uwezo wote wa Israeli: watu elfu thelathini.
2SA 6:2 Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yuda kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka huko, linaloitwa kwa Jina, naam, jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi walio juu ya hilo Sanduku.
2SA 6:3 Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa
2SA 6:4 likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake.
2SA 6:5 Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele za Mwenyezi Mungu kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi.
2SA 6:6 Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa.
2SA 6:7 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu.
2SA 6:8 Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ilifurika dhidi ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza.
2SA 6:9 Daudi akamwogopa Mwenyezi Mungu siku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku la Mwenyezi Mungu litakavyoweza kunijia?”
2SA 6:10 Hakuwa radhi kulichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu kwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti.
2SA 6:11 Sanduku la Mwenyezi Mungu likakaa katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye Mwenyezi Mungu akambariki pamoja na nyumba yake yote.
2SA 6:12 Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Mwenyezi Mungu ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe.
2SA 6:13 Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Mwenyezi Mungu walipotembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa.
2SA 6:14 Daudi, akiwa amevaa kizibau cha kitani, alicheza mbele za Mwenyezi Mungu kwa nguvu zake zote,
2SA 6:15 wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
2SA 6:16 Sanduku la Mwenyezi Mungu lilipokuwa linaingia Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Mwenyezi Mungu, akamdharau moyoni mwake.
2SA 6:17 Wakaleta Sanduku la Mwenyezi Mungu na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mwenyezi Mungu.
2SA 6:18 Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
2SA 6:19 Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani.
2SA 6:20 Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo kwa kuvua mavazi yake machoni pa vijakazi wa watumishi wake, vile mtu asiye na adabu angefanya!”
2SA 6:21 Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele za Mwenyezi Mungu ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine yeyote kutoka nyumba yake aliponiweka niwe mtawala wa Israeli, watu wa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo nitacheza mbele za Mwenyezi Mungu.
2SA 6:22 Nitakuwa asiye na heshima kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.”
2SA 6:23 Naye Mikali binti Sauli hakuwa na watoto hadi siku ya kufa kwake.
2SA 7:1 Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye Mwenyezi Mungu akiwa amempa amani pande zote kutoka kwa adui zake,
2SA 7:2 akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa ninaishi katika jumba la kifalme la mwerezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.”
2SA 7:3 Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe.”
2SA 7:4 Usiku ule neno la Mwenyezi Mungu likamjia Nathani, kusema:
2SA 7:5 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake?
2SA 7:6 Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine na hema kama makao yangu.
2SA 7:7 Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mwerezi?” ’
2SA 7:8 “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Nilikutoa malishoni na kutoka kulisha mifugo, ili uwaongoze watu wangu Israeli.
2SA 7:9 Nimekuwa pamoja nawe popote ulipoenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani.
2SA 7:10 Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzoni,
2SA 7:11 na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa amani mbele ya adui zenu wote. “ ‘Mwenyezi Mungu akuambia kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe atakujengea nyumba.
2SA 7:12 Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake.
2SA 7:13 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitakiimarisha kiti cha ufalme wake milele.
2SA 7:14 Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu.
2SA 7:15 Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako.
2SA 7:16 Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha utawala kitaimarishwa milele.’ ”
2SA 7:17 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.
2SA 7:18 Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Mwenyezi Mungu, akasema: “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa?
2SA 7:19 Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee Bwana Mungu Mwenyezi?
2SA 7:20 “Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi.
2SA 7:21 Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako.
2SA 7:22 “Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee Bwana Mungu Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe,
2SA 7:23 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri?
2SA 7:24 Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee Mwenyezi Mungu, umekuwa Mungu wao.
2SA 7:25 “Basi sasa, Bwana Mwenyezi Mungu, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Fanya kama ulivyoahidi,
2SA 7:26 ili jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako.
2SA 7:27 “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hili.
2SA 7:28 Ee Bwana Mungu Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri.
2SA 7:29 Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”
2SA 8:1 Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akatwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.
2SA 8:2 Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili, hilo kundi waliuawa, na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea ushuru.
2SA 8:3 Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipoenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati.
2SA 8:4 Daudi akateka magari yake ya vita elfu moja, waendesha hayo magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu ishirini. Daudi akawakata mishipa farasi wa magari ya vita, akabakiza farasi mia moja.
2SA 8:5 Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua watu elfu ishirini na mbili miongoni mwao.
2SA 8:6 Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kote alipoenda.
2SA 8:7 Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu.
2SA 8:8 Kutoka miji ya Tibathi na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.
2SA 8:9 Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri,
2SA 8:10 akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.
2SA 8:11 Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda:
2SA 8:12 yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.
2SA 8:13 Naye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi.
2SA 8:14 Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Mwenyezi Mungu alimpatia Daudi ushindi kila alipoenda.
2SA 8:15 Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote.
2SA 8:16 Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu;
2SA 8:17 Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi;
2SA 8:18 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.
2SA 9:1 Daudi akauliza, “Je, hakuna mtu hata mmoja wa nyumba ya Sauli aliyebaki ambaye naweza kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani?”
2SA 9:2 Basi palikuwa na mtumishi wa nyumba ya Sauli aliyeitwa Siba. Wakamwita aje mbele ya Daudi, naye mfalme akamuuliza, “Wewe ndiwe Siba?” Akamjibu, “Naam, mimi ndiye mtumishi wako.”
2SA 9:3 Mfalme akamuuliza, “Je, hakuna yeyote ambaye amebaki wa nyumba ya Sauli ninayeweza kumwonesha wema wa Mungu?” Siba akamjibu mfalme, “Bado yupo mwana wa Yonathani; yeye ni kiwete kwenye miguu yote.”
2SA 9:4 Mfalme akauliza, “Yuko wapi?” Siba akajibu, “Yuko nyumbani mwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-Debari.”
2SA 9:5 Basi Mfalme Daudi akamtaka aletwe kutoka Lo-Debari, kutoka nyumbani mwa Makiri mwana wa Amieli.
2SA 9:6 Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, alipofika kwa Daudi, akainama kumpa mfalme heshima. Daudi akamwita, “Mefiboshethi!” Mefiboshethi akajibu, “Ndimi mtumishi wako.”
2SA 9:7 Daudi akamwambia, “Usiogope, kwa maana hakika nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Nitakurudishia ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli baba yako, nawe daima utakula chakula mezani pangu.”
2SA 9:8 Mefiboshethi akasujudu, akasema, “Mimi mtumishi wako ni nini hata uangalie mbwa mfu kama mimi?”
2SA 9:9 Ndipo mfalme akamwita Siba mtumishi wa Sauli na kumwambia, “Nimempa mwana wa bwana wako kila kitu kilichokuwa mali ya Sauli na jamaa yake.
2SA 9:10 Wewe, wanao na watumishi wako mtamlimia mashamba Mefiboshethi na kumletea mavuno, ili mwana wa bwana wako apate mahitaji yake. Naye Mefiboshethi mwana wa bwana wako atakula chakula mezani pangu daima.” (Siba alikuwa na wana kumi na watano, na watumishi ishirini.)
2SA 9:11 Ndipo Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya chochote bwana wangu mfalme atakachoagiza mtumishi wake kufanya.” Basi Mefiboshethi akala chakula mezani pa Daudi kama mmoja wa wana wa mfalme.
2SA 9:12 Mefiboshethi alikuwa na mwanawe mdogo aliyeitwa Mika, nao watu wote wa nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi.
2SA 9:13 Naye Mefiboshethi akaishi huko Yerusalemu, kwa sababu daima alikula mezani pa mfalme, naye alikuwa kiwete kwenye miguu yote.
2SA 10:1 Baada ya muda, mfalme wa Waamoni akafa, naye Hanuni mwanawe akawa mfalme baada yake.
2SA 10:2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kama vile baba yake alivyonitendea mimi wema.” Hivyo Daudi akatuma wajumbe kuonesha wema wake kwa Hanuni kuhusu baba yake. Watu wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamoni,
2SA 10:3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “Unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kukutumia watu ili kuonesha masikitiko? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kuchunguza na kuupeleleza mji ili kuupindua?”
2SA 10:4 Basi Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa kila mmoja ndevu zake nusu, akakata mavazi yao nyuma katikati kwenye matako, akawaachia waende zao.
2SA 10:5 Daudi alipoambiwa jambo hili, akatuma wajumbe ili kwenda kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko hadi ndevu zenu ziote, ndipo mje.”
2SA 10:6 Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, wakaajiri askari wa miguu elfu ishirini, Waaramu kutoka Beth-Rehobu na Soba, pia mfalme wa Maaka na watu elfu moja, na vilevile watu elfu kumi na mbili kutoka Tobu.
2SA 10:7 Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji.
2SA 10:8 Waamoni wakatoka wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati Waaramu wa Soba na wa Rehobu, na wanaume wa Tobu na Maaka walikuwa peke yao kwenye eneo la wazi.
2SA 10:9 Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu.
2SA 10:10 Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni.
2SA 10:11 Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itawabidi mje kunisaidia. Lakini kama Waamoni watawazidi nguvu, basi nitakuja kuwasaidia.
2SA 10:12 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Mwenyezi Mungu atafanya lile lililo jema machoni pake.”
2SA 10:13 Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake.
2SA 10:14 Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.
2SA 10:15 Baada ya Waaramu kuona wameshindwa na Israeli, wakajikusanya tena.
2SA 10:16 Hadadezeri akaagiza Waaramu walioletwa kutoka ng’ambo ya Mto, wakaenda Helamu pamoja na Shobaki jemadari wa jeshi la Hadadezeri akiwaongoza.
2SA 10:17 Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote, wakavuka Mto Yordani, wakaenda Helamu. Waaramu wakapanga vikosi vyao vya askari kukabiliana na kupigana dhidi ya Daudi.
2SA 10:18 Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari ya vita mia saba na askari wao wa miguu elfu arobaini. Vilevile alimpiga Shobaki jemadari wa jeshi lao, naye akafa huko.
2SA 10:19 Wafalme wote waliokuwa wanamtumikia Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya amani na Waisraeli na wakawa chini yao. Hivyo Waaramu wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.
2SA 11:1 Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme hutoka kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu.
2SA 11:2 Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Akiwa kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura,
2SA 11:3 naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria Mhiti?”
2SA 11:4 Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani mwake.
2SA 11:5 Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.”
2SA 11:6 Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.
2SA 11:7 Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje.
2SA 11:8 Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani mwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akatoka jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme.
2SA 11:9 Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakuteremka kwenda nyumbani mwake.
2SA 11:10 Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakuenda nyumbani,” Daudi akamuuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukuenda nyumbani?”
2SA 11:11 Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani mwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo kama hilo!”
2SA 11:12 Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata.
2SA 11:13 Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakuenda nyumbani.
2SA 11:14 Kesho yake asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka.
2SA 11:15 Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.”
2SA 11:16 Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali alipojua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana.
2SA 11:17 Wanaume wa mji walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa; zaidi ya hayo, Uria Mhiti akafa.
2SA 11:18 Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita.
2SA 11:19 Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita,
2SA 11:20 hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani?
2SA 11:21 Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Akikuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria Mhiti amekufa.’ ”
2SA 11:22 Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema.
2SA 11:23 Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma hadi ingilio la mji.
2SA 11:24 Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria Mhiti, mtumishi wako, amekufa.”
2SA 11:25 Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.”
2SA 11:26 Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea.
2SA 11:27 Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akatumana aletwe nyumbani mwake. Naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi Mungu.
2SA 12:1 Mwenyezi Mungu akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwa na watu wawili; mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini.
2SA 12:2 Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ng’ombe,
2SA 12:3 lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake, hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake.
2SA 12:4 “Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri hakuchukua mmoja wa kondoo au ng’ombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.”
2SA 12:5 Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa!
2SA 12:6 Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.”
2SA 12:7 Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli.
2SA 12:8 Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba yote ya Israeli na ya Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi.
2SA 12:9 Kwa nini ulilidharau neno la Mwenyezi Mungu kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria Mhiti kwa upanga, na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni.
2SA 12:10 Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe, kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria Mhiti kuwa mkeo.’
2SA 12:11 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Kutoka kwa nyumba yako mwenyewe nitaleta maafa juu yako. Mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako mchana mwangavu.
2SA 12:12 Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu mbele ya Israeli yote.’ ”
2SA 12:13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.” Nathani akamjibu, “Mwenyezi Mungu amekuondolea dhambi yako. Hutakufa.
2SA 12:14 Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Mwenyezi Mungu kuonesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”
2SA 12:15 Baada ya Nathani kurudi nyumbani mwake, Mwenyezi Mungu akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua.
2SA 12:16 Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha.
2SA 12:17 Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao.
2SA 12:18 Ilipotimia siku ya saba, yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”
2SA 12:19 Daudi akaona kuwa watumishi wake wananong’onezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?” Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.”
2SA 12:20 Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani mwake, akaomba wamwandalie chakula, naye akala.
2SA 12:21 Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.”
2SA 12:22 Akajibu, “Mtoto alipokuwa angali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Mwenyezi Mungu aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’
2SA 12:23 Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitaenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”
2SA 12:24 Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe; akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina Sulemani. Mwenyezi Mungu alimpenda Sulemani.
2SA 12:25 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
2SA 12:26 Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome ya kifalme.
2SA 12:27 Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji.
2SA 12:28 Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.”
2SA 12:29 Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka.
2SA 12:30 Akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nalo lilizungushiwa vito vya thamani. Likawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo.
2SA 12:31 Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.
2SA 13:1 Ikawa baada ya hayo, Amnoni mwana wa Daudi akampenda Tamari, dada yake Absalomu mwana wa Daudi, aliyekuwa mzuri wa sura.
2SA 13:2 Amnoni akasumbuka sana kuhusu Tamari hata akaugua, kwa kuwa Tamari alikuwa bikira, na ilionekana kwamba haiwezekani Amnoni kumfanyia jambo lolote.
2SA 13:3 Basi Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi. Yonadabu alikuwa mtu wa hila nyingi sana.
2SA 13:4 Akamuuliza Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme; kwa nini siku baada ya siku unaonekana kukonda? Hutaniambia?” Amnoni akamwambia, “Ninampenda Tamari, dada yake Absalomu ndugu yangu.”
2SA 13:5 Yonadabu akamwambia, “Nenda ukalale kitandani na ujifanye kuwa mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona mwambie, ‘Ningependa Tamari dada yangu aje kunipatia chochote ili nile. Tafadhali mruhusu aje na kuniandalia chakula mbele yangu ningali ninamwona, ili nipate kula kutoka mkononi mwake.’ ”
2SA 13:6 Kwa hiyo Amnoni akalala kitandani kujifanya mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia, “Ningependa dada yangu Tamari aje na kuniandalia mikate maalum mbele yangu, ili nipate kula toka mkononi mwake.”
2SA 13:7 Daudi akampelekea Tamari ujumbe huko kwenye jumba la kifalme, kusema: “Nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni ukamwandalie chakula.”
2SA 13:8 Kwa hiyo Tamari akaenda nyumbani mwa nduguye Amnoni, ndugu aliyekuwa amelala. Tamari akachukua unga uliotiwa chachu akaukanda, akaiandaa mikate mbele yake na kuioka.
2SA 13:9 Tamari akaondoa mikate kwenye kikaango ili ampatie Amnoni, lakini akakataa kula. Amnoni akamwambia, “Mtoe nje kila mtu aliye hapa.” Kwa hiyo kila mmoja akaondoka.
2SA 13:10 Ndipo Amnoni akamwambia Tamari, “Leta mkate hapa ndani ya chumba changu ili nipate kula kutoka mkononi mwako.” Basi Tamari akachukua mikate aliyoiandaa na kumletea Amnoni ndugu yake ndani ya chumba chake.
2SA 13:11 Lakini alipompelekea ili ale, akamkamata kwa nguvu na kumwambia, “Njoo ulale nami, dada yangu.”
2SA 13:12 Akamwambia, “Usifanye hivyo, ndugu yangu! Usinitende jeuri! Jambo la namna hii halistahili kufanyika katika Israeli! Usitende jambo hili ovu.
2SA 13:13 Kwa upande wangu je, itakuwaje? Nitaipeleka wapi aibu yangu? Pia kwa upande wako, itakuwaje? Utakuwa kama mmoja wa wapumbavu waovu katika Israeli. Tafadhali zungumza na mfalme; hatakukatalia wewe kunioa.”
2SA 13:14 Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, na kwa kuwa alikuwa na nguvu kuliko Tamari, akamtenda jeuri.
2SA 13:15 Kisha Amnoni akamchukia Tamari, kwa machukio makuu sana. Kwa kweli, Amnoni alimchukia kuliko alivyokuwa amempenda. Amnoni akamwambia, “Inuka na utoke nje!”
2SA 13:16 Tamari akamwambia, “Hapana! Kunifukuza itakuwa vibaya kuliko yale uliyonitendea.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza.
2SA 13:17 Akamwita mtumishi wake mahsusi na kumwambia, “Mtoe huyu mwanamke hapa na ufunge mlango nyuma yake.”
2SA 13:18 Kwa hiyo, mtumishi wake akamtoa nje na kufunga mlango nyuma yake. Tamari alikuwa amevaa joho lililopambwa vizuri, kwa maana lilikuwa aina ya mavazi yaliyovaliwa na binti za mfalme waliokuwa mabikira.
2SA 13:19 Tamari akajitia majivu kichwani mwake na kurarua lile joho alilokuwa amevaa. Akaweka mkono wake kichwani, akaenda zake akilia kwa sauti.
2SA 13:20 Absalomu nduguye akamuuliza, “Je, huyo Amnoni ndugu yako, amekutana nawe kimwili? Sasa nyamaza dada yangu; yeye ni ndugu yako. Usilitie jambo hili moyoni.” Naye Tamari akaishi nyumbani mwa Absalomu nduguye, akiwa mwanamke mwenye huzuni.
2SA 13:21 Mfalme Daudi aliposikia mambo haya yote, akakasirika sana.
2SA 13:22 Absalomu hakusema neno lolote, zuri au baya, kwa Amnoni; alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake.
2SA 13:23 Miaka miwili baadaye, wakati wakata manyoya ya kondoo wa Absalomu walipokuwa huko Baal-Hasori karibu na mpaka wa Efraimu, alialika wana wote wa mfalme kuja huko.
2SA 13:24 Absalomu akaenda kwa mfalme na kumwambia, “Mtumishi wako ninao wakata manyoya ya kondoo waliokuja. Tafadhali, je, mfalme na maafisa wake wanaweza kuungana nami?”
2SA 13:25 Mfalme akajibu, “La, mwanangu. Si lazima sote tuje, tutakuwa tu mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alimsihi sana, mfalme alikataa kwenda, lakini akambariki.
2SA 13:26 Basi Absalomu akasema, “Kama hutakuja, tafadhali mruhusu ndugu yangu Amnoni twende pamoja naye.” Mfalme akamuuliza, “Kwa nini aende pamoja nawe?”
2SA 13:27 Lakini Absalomu alimsihi, kwa hiyo mfalme akamtuma Amnoni pamoja na wana wengine wa mfalme waliobaki.
2SA 13:28 Absalomu aliagiza watu wake, “Sikilizeni! Amnoni atakapokuwa amekunywa mvinyo na kulewa sana nami nikiwaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ basi muueni. Msiogope. Je, si mimi niliyewapa amri hii? Kuweni hodari na wenye ushujaa.”
2SA 13:29 Kwa hiyo watu wa Absalomu wakamtendea Amnoni kama vile Absalomu alivyokuwa amewaagiza. Ndipo wana wote wa mfalme wakainuka, wakapanda nyumbu zao, wakakimbia.
2SA 13:30 Wakiwa njiani, taarifa ilimjia Daudi, kusema: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme; hakuna hata mmoja aliyesalia.”
2SA 13:31 Mfalme akasimama, akararua nguo zake, akalala chini ardhini; nao watumishi wake wote wakasimama kando yake na nguo zao zikiwa zimeraruliwa.
2SA 13:32 Lakini Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akasema, “Bwana wangu asifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme; ni Amnoni peke yake ndiye alikufa. Hili limekuwa kusudi la moyo wa Absalomu tangu siku ile Amnoni alipomtendea jeuri Tamari, dada yake.
2SA 13:33 Mfalme bwana wangu asisumbuliwe na taarifa kwamba wamewaua wana wote wa mfalme. Ni Amnoni peke yake aliyekufa.”
2SA 13:34 Wakati huo, Absalomu akawa amekimbia. Basi mlinzi akaangalia, naye akaona watu wengi barabarani magharibi yake, wakishuka kutoka upande wa kilima. Mlinzi akaenda akamwambia mfalme, “Naona watu wakitokea upande wa Horonaimu, huko upande wa kilimani.”
2SA 13:35 Yonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wako hapa; imekuwa kama vile mtumishi wako alivyosema.”
2SA 13:36 Mara alipomaliza kusema, wana wa mfalme wakaingia ndani wakiomboleza kwa makelele. Pia mfalme na watumishi wake wote wakalia sana kwa uchungu.
2SA 13:37 Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Lakini Mfalme Daudi akaomboleza kwa ajili ya mwanawe kila siku.
2SA 13:38 Baada ya Absalomu kukimbia na kwenda Geshuri, akakaa huko miaka mitatu.
2SA 13:39 Roho ya Mfalme Daudi ikatamani kumwendea Absalomu, kwa maana mfalme alikuwa amefarijika kuhusu kifo cha Amnoni.
2SA 14:1 Yoabu mwana wa Seruya akafahamu kuwa moyo wa mfalme ulikuwa na shauku ya kumwona Absalomu.
2SA 14:2 Kwa hiyo Yoabu akamtuma mtu kwenda Tekoa na kumleta mwanamke mwenye hekima kutoka huko. Akamwambia huyo mwanamke, “Jifanye uko katika maombolezo. Vaa nguo za kuomboleza, nawe usitumie mafuta yoyote ya urembo. Jifanye kama mwanamke ambaye amekuwa na huzuni kwa siku nyingi kwa ajili ya kufiwa.
2SA 14:3 Kisha nenda kwa mfalme ukazungumze maneno haya.” Naye Yoabu akaweka maneno kinywani mwa yule mwanamke.
2SA 14:4 Huyo huyo mwanamke kutoka Tekoa alipofika kwa mfalme, akaanguka kifudifudi kumpa mfalme heshima, akasema, “Ee mfalme, nisaidie!”
2SA 14:5 Mfalme akamuuliza, “Una shida gani?” Akamwambia, “Mimi ni mjane, mume wangu amekufa.
2SA 14:6 Mimi mtumishi wako nilikuwa na wana wawili. Wakapigana wao kwa wao huko shambani wala huko hapakuwa na mtu hata mmoja wa kuwatenganisha. Mmoja akampiga mwenzake na kumuua.
2SA 14:7 Sasa ukoo wote umeinuka dhidi ya mtumishi wako, wakisema, ‘Utukabidhi huyo aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa ajili ya uhai wa ndugu yake aliyemuua, nasi hapo tutakuwa tumekatilia mbali na mrithi pia.’ Wakifanya hivyo, watakuwa wamezima tumaini langu lililobaki, mume wangu hataachiwa jina wala mzao katika uso wa dunia.”
2SA 14:8 Mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Nenda nyumbani, nami nitatoa agizo kwa ajili yako.”
2SA 14:9 Lakini huyo mwanamke kutoka Tekoa akamwambia, “Mfalme bwana wangu, lawama na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, naye mfalme na kiti chake cha utawala asiwe na hatia.”
2SA 14:10 Mfalme akajibu, “Ikiwa mtu yeyote atakusemesha lolote, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena.”
2SA 14:11 Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wake, ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili mwanangu asije akaangamizwa.” Mfalme akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.”
2SA 14:12 Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.” Mfalme akajibu, “Sema.”
2SA 14:13 Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali?
2SA 14:14 Kama vile maji yaliyomwagika ardhini hayawezi kuzoleka, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini hivyo sivyo Mungu anataka; bali hupanga njia ili mtu aliyefukuzwa asibaki akiwa ametengwa naye.
2SA 14:15 “Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba.
2SA 14:16 Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka urithi Mungu aliotupatia.’
2SA 14:17 “Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na awe pamoja nawe.’ ”
2SA 14:18 Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu la kile nitakalokuuliza.” Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.”
2SA 14:19 Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?” Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako.
2SA 14:20 Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, anafahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.”
2SA 14:21 Mfalme akamwambia Yoabu, “Vyema sana, nitalifanya jambo hili. Nenda, ukamlete kijana Absalomu.”
2SA 14:22 Yoabu akasujudu uso wake ukielekea chini ili kumpa mfalme heshima, na akambariki mfalme. Yoabu akasema, “Leo mtumishi wako anajua kuwa amepata kibali machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa sababu mfalme amemjalia mtumishi wake ombi lake.”
2SA 14:23 Ndipo Yoabu akaenda hadi Geshuri akamrudisha Absalomu Yerusalemu.
2SA 14:24 Lakini mfalme akasema, “Lazima Absalomu aende kwenye nyumba yake mwenyewe; kamwe asiuone uso wangu.” Kwa hiyo Absalomu akaenda kwenye nyumba yake na hakuuona uso wa mfalme.
2SA 14:25 Katika Israeli yote hakuna mtu yeyote aliyesifiwa kwa uzuri wa sura kama Absalomu. Kuanzia utosi wa kichwa chake hadi wayo wa mguu wake hakuwa na kasoro.
2SA 14:26 Kila mara aliponyoa nywele za kichwa chake, kwa kuwa alizinyoa nywele zake mara moja kwa mwaka kwa sababu zilikuwa nzito sana kwake, alizipima; uzito wake ulikuwa shekeli mia mbili kwa kipimo cha kifalme.
2SA 14:27 Walizaliwa wana watatu na binti mmoja kwa Absalomu. Jina la binti yake aliitwa Tamari, naye akawa mwanamke mzuri wa sura.
2SA 14:28 Absalomu akaishi miaka miwili huko Yerusalemu pasipo kuuona uso wa mfalme.
2SA 14:29 Basi Absalomu akamtumania Yoabu kwa kusudi la kumtuma kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja kwa Absalomu. Ndipo akamtumania mara ya pili, lakini pia akakataa kuja.
2SA 14:30 Ndipo akawaambia watumishi wake, “Tazama, shamba la Yoabu liko jirani na langu, naye ana shayiri humo. Nendeni mkaitie moto.” Kisha watumishi wa Absalomu wakalitia moto shamba hilo.
2SA 14:31 Basi Yoabu akaenda nyumbani mwa Absalomu, akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wametia moto shamba langu?”
2SA 14:32 Absalomu akamwambia Yoabu, “Tazama, nilikutumia ujumbe na kusema, ‘Njoo ili niweze kukutuma kwa mfalme kuuliza, “Kwa nini nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa bora zaidi kwangu kama ningebaki huko!” ’ Sasa basi, nataka kuuona uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia ya jambo lolote, basi na aniue.”
2SA 14:33 Basi Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia jambo hili. Kisha mfalme akamwita Absalomu, naye akaingia ndani, akasujudu, uso wake ukigusa chini mbele ya mfalme. Naye mfalme akambusu Absalomu.
2SA 15:1 Baada ya muda, Absalomu akajipatia magari ya vita na farasi pamoja na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake.
2SA 15:2 Akawa anaamka asubuhi na mapema na kusimama kando ya barabara inayoelekea kwenye lango la mji. Wakati wowote alipokuja mtu yeyote mwenye mashtaka yanayohitaji kuletwa mbele ya mfalme kwa maamuzi, Absalomu naye angemwita na kumuuliza, “Wewe unatoka mji upi?” Naye angejibu, “Mtumishi wako anatoka katika mojawapo ya makabila ya Israeli.”
2SA 15:3 Kisha Absalomu angemwambia, “Tazama, malalamiko yako ni ya haki na sawasawa, lakini hakuna mwakilishi wa mfalme wa kukusikiliza.”
2SA 15:4 Absalomu aliongeza, “Laiti tu ningeteuliwa kuwa mwamuzi katika nchi. Ndipo kila mmoja mwenye mashtaka au shauri angekuja kwangu nami ningeona kwamba anapata haki.”
2SA 15:5 Pia, wakati mtu yeyote alipomkaribia ili kusujudu mbele yake, Absalomu alinyoosha mkono wake, na kumkumbatia na kumbusu.
2SA 15:6 Absalomu akaendelea na tabia hii mbele ya Waisraeli wote waliomjia mfalme kumwomba awape haki; kwa hiyo Absalomu akavutia mioyo ya watu wa Israeli.
2SA 15:7 Hapo mwisho wa mwaka wa nne, Absalomu akamwambia mfalme, “Naomba unipe ruhusa niende Hebroni nikatimize nadhiri niliyomwekea Mwenyezi Mungu.
2SA 15:8 Mtumishi wako alipokuwa huko Geshuri katika nchi ya Aramu, niliweka nadhiri hii: ‘Ikiwa Mwenyezi Mungu atanirudisha Yerusalemu, nitamwabudu Mwenyezi Mungu huko Hebroni.’ ”
2SA 15:9 Mfalme akamwambia, “Nenda kwa amani.” Hivyo akaenda Hebroni.
2SA 15:10 Kisha Absalomu akatuma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, kusema, “Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta basi semeni, ‘Absalomu ni mfalme huko Hebroni.’ ”
2SA 15:11 Watu mia mbili kutoka Yerusalemu walikuwa wamefuatana na Absalomu. Walikuwa wamealikwa kama wageni nao walienda kwa nia njema, pasipo kujua lolote.
2SA 15:12 Absalomu alipokuwa anatoa dhabihu, pia akatuma aitwe Ahithofeli Mgiloni, mshauri wa Daudi, aje kutoka Gilo, ambao ndio mji wake wa nyumbani. Kwa hiyo mpango wa hila ukapata nguvu, na idadi ya waliofuatana na Absalomu ikaongezeka.
2SA 15:13 Mjumbe akaja na kumwambia Daudi, “Mioyo ya watu wa Israeli inaambatana na Absalomu.”
2SA 15:14 Ndipo Daudi akawaambia maafisa wake wote waliokuwa pamoja naye huko Yerusalemu, “Njooni! Ni lazima tukimbie, la sivyo hakuna hata mmoja wetu atakayeokoka kutoka mkononi mwa Absalomu. Ni lazima tuondoke kwa haraka, la sivyo atakuja mbio na kutupata, atatuangamiza na kuupiga mji kwa upanga.”
2SA 15:15 Maafisa wa mfalme wakamjibu, “Watumishi wako tu tayari kufanya lolote mfalme bwana wetu analochagua.”
2SA 15:16 Mfalme akatoka, pamoja na watu wa nyumbani mwake wakimfuata; lakini akawaacha masuria kumi ili la kile jumba la kifalme.
2SA 15:17 Hivyo mfalme akaondoka, pamoja na watu wote wakimfuata, wakatua mahali mbali kiasi.
2SA 15:18 Watu wake wote wakatembea, wakampita wakiwa wamefuatana na Wakerethi na Wapelethi wote; pia Wagiti wote mia sita waliokuwa wamefuatana naye kutoka Gathi wakapita mbele ya mfalme.
2SA 15:19 Mfalme akamwambia Itai, Mgiti, “Kwa nini ufuatane na sisi? Rudi ukakae pamoja na Mfalme Absalomu. Wewe ni mgeni, mkimbizi kutoka nchini mwako.
2SA 15:20 Ulikuja jana tu. Nami leo nikufanye utangetange pamoja nasi, wakati sijui niendako? Rudi, nawe ukawachukue watu wa kwenu. Wema na uaminifu na viwe pamoja nawe.”
2SA 15:21 Lakini Itai akamjibu mfalme, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama mfalme bwana wangu aishivyo, popote mfalme bwana wangu atakapokuwa, ikiwa ni kuishi au kufa, hapo ndipo mtumishi wako atakapokuwa.”
2SA 15:22 Daudi akamwambia Itai, “Songa mbele, endelea.” Kwa hiyo Itai, Mgiti, akaendelea pamoja na watu wake wote, pia jamaa zote waliokuwa pamoja naye.
2SA 15:23 Watu wote wa nje ya mji wakalia kwa sauti wakati watu wote walipokuwa wakipita. Mfalme naye akavuka Bonde la Kidroni, nao watu wote wakaelekea jangwani.
2SA 15:24 Sadoki pia alikuwako, kadhalika Walawi wote waliokuwa pamoja naye walikuwa wamechukua Sanduku la Agano la Mungu. Wakaweka chini Sanduku la Mungu, naye Abiathari akatoa dhabihu hadi watu wote walipokuwa wameondoka mjini.
2SA 15:25 Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Rudisha Sanduku la Mungu mjini. Ikiwa nitapata kibali mbele za Mwenyezi Mungu, atanirudisha, nami nitaliona Sanduku hili tena pamoja na Maskani yake.
2SA 15:26 Lakini kama yeye atasema, ‘Mimi sipendezwi nawe,’ basi mimi niko tayari; yeye na anifanye chochote aonacho chema kwake.”
2SA 15:27 Pia mfalme alimwambia kuhani Sadoki, “Je, wewe si mwonaji? Rudi mjini kwa amani pamoja na mwanao Ahimaasi na Yonathani mwana wa Abiathari. Wewe na Abiathari wachukueni wana wenu wawili.
2SA 15:28 Nitasubiri kwenye vivuko katika jangwa hadi neno litakapotoka kwenu kuniarifu.”
2SA 15:29 Kwa hiyo Sadoki na Abiathari wakarudisha Sanduku la Mungu hadi Yerusalemu na kukaa huko.
2SA 15:30 Bali Daudi akaendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni, akaenda huku analia, akiwa amefunika kichwa chake, bila viatu miguuni. Watu wote waliokuwa pamoja naye nao wakafunika vichwa vyao, wakawa wanapanda mlima huku wanalia.
2SA 15:31 Basi Daudi alikuwa ameambiwa, “Ahithofeli alikuwa miongoni mwa washiriki wa njama ya Absalomu.” Ndipo Daudi akaomba, akisema, “Ee Mwenyezi Mungu, geuza ushauri wa Ahithofeli kuwa ujinga.”
2SA 15:32 Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali watu walikuwa wamezoea kumwabudu Mungu, Hushai Mwarki alikuwako kumlaki, akiwa amerarua joho lake, na akiwa na mavumbi kichwani.
2SA 15:33 Daudi akamwambia, “Ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu.
2SA 15:34 Lakini ukirudi mjini na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; nilikuwa mtumishi wa baba yako wakati uliopita, lakini sasa nitakuwa mtumishi wako,’ basi utaweza kunisaidia kwa kupinga ushauri wa Ahithofeli.
2SA 15:35 Je, makuhani Sadoki na Abiathari hawatakuwa pamoja nawe? Waambie lolote utakalosikia katika jumba la mfalme.
2SA 15:36 Wana wao wawili, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao huko. Watume kwangu na lolote utakalosikia.”
2SA 15:37 Kwa hiyo Hushai, rafiki wa Daudi, akafika Yerusalemu wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini.
2SA 16:1 Daudi alipokuwa ameenda umbali mfupi kupita kilele cha mlima, akamkuta huko Siba, msimamizi wa shughuli za Mefiboshethi, akingojea kumlaki Daudi. Alikuwa na punda wawili wakiwa wametandikwa na kupakiwa mikate mia mbili, maandazi mia ya zabibu kavu, maandazi mia ya tini, na kiriba cha divai.
2SA 16:2 Mfalme Daudi akamuuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?” Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya watu wa nyumba ya mfalme kupanda, mikate na matunda ni kwa ajili ya watu kula, nayo divai ni kwa kuwaburudisha watakaochoka jangwani.”
2SA 16:3 Kisha mfalme akauliza, “Yuko wapi mwana wa bwana wako?” Siba akamwambia, “Anakawia Yerusalemu, kwa sababu anafikiri, ‘Leo nyumba ya Israeli itanirudishia utawala wa baba yangu.’ ”
2SA 16:4 Ndipo mfalme akamwambia Siba, “Yote yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akasema, “Nasujudu kwa unyenyekevu. Naomba nipate kibali mbele yako, bwana wangu mfalme.”
2SA 16:5 Mfalme Daudi alipokuwa anakaribia Bahurimu, mtu mmoja wa ukoo wa jamaa ya Sauli, akatoka humo. Jina lake ni Shimei mwana wa Gera; akawa analaani alipokuwa akitoka.
2SA 16:6 Akamtupia Daudi na maafisa wote wa mfalme mawe, ingawa vikosi vyote na walinzi maalum walikuwa kulia na kushoto mwa Daudi.
2SA 16:7 Shimei alivyokuwa akilaani, akasema, “Toka hapa, toka hapa, wewe mtu wa damu, wewe mtu mbaya kabisa!
2SA 16:8 Mwenyezi Mungu amekulipiza kwa ajili ya damu yote uliyomwaga ya watu wa nyumba ya Sauli, ambaye nafasi yake umeimiliki wewe. Mwenyezi Mungu amekabidhi ufalme mkononi mwa mwanao Absalomu. Maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mtu wa damu!”
2SA 16:9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu amlaani bwana wangu mfalme? Niruhusu nivuke nikatilie mbali kichwa chake.”
2SA 16:10 Lakini mfalme akamwambia, “Mna nini nami, enyi wana wa Seruya? Ikiwa analaani kwa sababu Mwenyezi Mungu amemwambia, ‘Mlaani Daudi,’ nani awezaye kuuliza, ‘Kwa nini unafanya hivi?’ ”
2SA 16:11 Ndipo Daudi akamwambia Abishai na maafisa wake wote, “Mwanangu, ambaye ametoka viunoni mwangu mwenyewe, anajaribu kuniua. Je, si zaidi sana huyu Mbenyamini! Mwacheni; acha alaani, kwa maana Mwenyezi Mungu amemwambia afanye hivyo.
2SA 16:12 Inawezekana kwamba Mwenyezi Mungu ataona dhiki yangu na kunilipa mema kwa ajili ya laana ninayopokea leo.”
2SA 16:13 Kwa hiyo Daudi na watu wake wakaendelea na safari yao barabarani, huku Shimei akiwa anatembea pembezoni mwa kilima sambamba na Daudi, huku akimlaani na kumtupia Daudi mawe na kumrushia mavumbi.
2SA 16:14 Mfalme na watu wote aliokuwa pamoja nao wakafika kwenye kituo chao wakiwa wamechoka. Mfalme akajiburudisha hapo.
2SA 16:15 Wakati huo, Absalomu pamoja na wanaume wote wa Israeli wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye.
2SA 16:16 Ndipo Hushai Mwarki, rafiki wa Daudi, akamwendea Absalomu na kumwambia, “Mfalme aishi maisha marefu! Mfalme aishi maisha marefu!”
2SA 16:17 Absalomu akamuuliza Hushai, “Je, huu ndio upendo unaomwonesha rafiki yako? Kwa nini hukufuatana na rafiki yako?”
2SA 16:18 Hushai akamwambia Absalomu, “La hasha! Yeye aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu, aliyechaguliwa na watu hawa, atakayechaguliwa tena na wanaume wote wa Israeli, huyu ndiye nitakayekuwa wake, nami nitabakia pamoja naye.
2SA 16:19 Zaidi ya hayo, nimtumikie nani? Je, nisimtumikie mwana? Kama vile nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokutumikia wewe.”
2SA 16:20 Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe ushauri wako. Tufanye nini?”
2SA 16:21 Ahithofeli akamjibu Absalomu, “Kutana kimwili na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza jumba la kifalme. Ndipo Israeli yote itakaposikia kwamba umejifanya chukizo kwa baba yako, nayo mikono ya kila mmoja aliye pamoja nawe itatiwa nguvu.”
2SA 16:22 Kwa hiyo wakamtengenezea Absalomu hema juu ya dari, naye akakutana kimwili na masuria wa baba yake machoni pa Israeli wote.
2SA 16:23 Ilikuwa katika siku hizo shauri lililotolewa na Ahithofeli lilikuwa kama lile ambalo limeulizwa kwa Mungu. Ndivyo Daudi na Absalomu walivyoyaheshimu mashauri yote ya Ahithofeli.
2SA 17:1 Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Nipe ruhusa niwachague watu elfu kumi na mbili, nao waanze safari usiku huu huu kumfuatia Daudi.
2SA 17:2 Nitamshambulia wakati akiwa amechoka na ni dhaifu. Nitampiga na hofu, na kisha watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake
2SA 17:3 na kuwarudisha watu wote kwako. Kifo cha mtu yule unayemtafuta kitamaanisha kurudi kwa wote, hakuna hata mtu mmoja atakayeumizwa.”
2SA 17:4 Mpango huu ulionekana mzuri kwa Absalomu na kwa wazee wote wa Israeli.
2SA 17:5 Lakini Absalomu akasema, “Pia mwiteni Hushai, Mwarki, ili tuweze kusikia anachokisema.”
2SA 17:6 Hushai alipokuja, Absalomu akasema, “Ahithofeli ametoa ushauri huu. Je, tufanye anavyosema? Kama sivyo, tupe maoni yako.”
2SA 17:7 Hushai akamjibu Absalomu, “Ushauri alioutoa Ahithofeli haufai kwa wakati huu.
2SA 17:8 Unamfahamu baba yako na watu wake, ni wapiganaji hodari, nao ni wakali kama dubu aliyepokonywa watoto wake. Zaidi ya hayo, baba yako ni mpiganaji jasiri, usiku hatalala pamoja na vikosi.
2SA 17:9 Hata sasa, amefichwa ndani ya pango au mahali pengine. Kama atatangulia kushambulia vikosi vyako, yeyote asikiaye habari hii atasema, ‘Kuna machinjo makubwa miongoni mwa vikosi vinavyomfuata Absalomu.’
2SA 17:10 Basi hata yule askari hodari kuliko wengine wote, ambaye moyo wake ni kama wa simba, atayeyuka kwa hofu, kwa maana Israeli yote wanajua kwamba baba yako ni mpiganaji na kwamba wale walio pamoja naye ni watu hodari.
2SA 17:11 “Kwa hiyo nakushauri: Israeli wote na wakusanyike kwako, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, wakiwa wengi kama mchanga wa ufuo wa bahari; wakusanyike kwako, nawe ukiwaongoza vitani.
2SA 17:12 Ndipo tutakapomshambulia popote atakapoonekana, nasi tutamwangukia kama umande unavyoshuka juu ya ardhi. Yeye mwenyewe na watu wake hakuna atakayeachwa hai.
2SA 17:13 Kama atakimbilia katika mji wowote, basi Israeli wote watazungushia mji ule kamba, nasi tutauburuta mji huo hadi bondeni, wala isionekane hata changarawe ya huo mji.”
2SA 17:14 Absalomu na wanaume wote wa Israeli wakasema, “Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ule wa Ahithofeli.” Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amekusudia kupinga ushauri mwema wa Ahithofeli, ili kuleta maafa kwa Absalomu.
2SA 17:15 Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari, “Ahithofeli amemshauri Absalomu na wazee wa Israeli kufanya hivi na hivi, lakini mimi nimewashauri wao kufanya lile na lile.
2SA 17:16 Sasa tumeni ujumbe haraka na kumwambia Daudi, ‘Usiku huu usilale kwenye vivuko katika jangwa; vuka bila kukosa, la sivyo, mfalme pamoja na watu wote waliofuatana naye watamezwa.’ ”
2SA 17:17 Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakingoja huko En-Rogeli. Naye mjakazi mmoja alipaswa kuwapasha habari nao wakawa waende kumwambia Mfalme Daudi, kwa maana wasingetaka kujihatarisha kuonekana wakiingia mjini.
2SA 17:18 Lakini kijana mmoja mwanaume akawaona, naye akamwambia Absalomu. Basi wote wawili wakaondoka haraka, wakaenda hadi kwenye nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu. Mtu huyo alikuwa na kisima uani mwake, nao Yonathani na Ahimaasi wakateremka ndani ya kisima hicho.
2SA 17:19 Mkewe akachukua kifuniko, akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima na kuanika nafaka juu yake. Hakuna mtu yeyote aliyefahamu chochote kuhusu jambo hilo.
2SA 17:20 Watu wa Absalomu walipofika kwa huyo mwanamke, wakamuuliza, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Huyo mwanamke akawajibu, “Walivuka kijito.” Watu wa Absalomu wakapekua lakini hawakuwaona hata mmoja, hivyo wakarudi Yerusalemu.
2SA 17:21 Baada ya watu hao kuondoka, wale watu wawili yaani Yonathani na Ahimaasi wakapanda kutoka mle kisimani na kwenda kumpasha Mfalme Daudi habari. Wakamwambia, “Ondoka, uvuke mto haraka. Ahithofeli ameshauri hivi na hivi dhidi yako.”
2SA 17:22 Kwa hiyo Daudi na watu wote aliokuwa nao waliondoka na kuvuka Yordani. Kufika wakati wa mapambazuko, hapakuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa hajavuka Mto Yordani.
2SA 17:23 Ahithofeli alipoona kwamba ushauri wake haukufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani mwake kwenye mji wake. Akaiweka nyumba yake katika utaratibu, kisha akajinyonga mwenyewe. Hivyo akafa na akazikwa katika kaburi la baba yake.
2SA 17:24 Daudi akaenda Mahanaimu, naye Absalomu akavuka Yordani pamoja na wanaume wote wa Israeli.
2SA 17:25 Absalomu alikuwa amemweka Amasa awe mkuu wa jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa mtu mmoja aliyeitwa Yetheri, Mwishmaeli aliyekuwa amemwoa Abigaili binti Nahashi, dada yake Seruya mamaye Yoabu.
2SA 17:26 Waisraeli na Absalomu wakapiga kambi huko nchi ya Gileadi.
2SA 17:27 Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni, Makiri mwana wa Amieli kutoka Lo-Debari, na Barzilai Mgileadi kutoka Rogelimu
2SA 17:28 wakaleta matandiko ya kitanda, mabakuli na vyombo vya mfinyanzi. Walileta pia ngano na shayiri, unga na bisi, maharagwe na kunde,
2SA 17:29 asali na maziwa yaliyoganda, kondoo na jibini kutoka maziwa ya ng’ombe kwa ajili ya Daudi na watu wake ili wale. Kwa maana walisema, “Watu wameona njaa, tena wamechoka na wamepata kiu huko jangwani.”
2SA 18:1 Daudi akakusanya watu aliokuwa nao, na kuteua juu yao majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia.
2SA 18:2 Daudi akatuma vikosi vya askari: theluthi moja ilikuwa chini ya amri ya Yoabu, theluthi ya pili chini ya Abishai mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya Itai, Mgiti. Mfalme akaviambia vikosi, “Hakika mimi mwenyewe nitaenda pamoja nanyi.”
2SA 18:3 Lakini watu wakasema, “Haikupasi kwenda, ikiwa sisi tutalazimika kukimbia, wao hawatatujali. Hata kama nusu yetu tukifa hawatajali, lakini wewe una thamani ya watu kama sisi kumi elfu. Ingekuwa bora zaidi kwako basi kutupatia msaada kutoka mjini.”
2SA 18:4 Mfalme akajibu, “Nitafanya lolote linaloonekana jema zaidi kwenu.” Kwa hiyo mfalme akasimama kando ya lango wakati watu wote wakitoka nje kwa makundi ya mamia na maelfu.
2SA 18:5 Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Kuweni wapole kwa kijana Absalomu kwa ajili yangu.” Vikosi vyote vikasikia mfalme akitoa amri kwa kila jemadari kumhusu Absalomu.
2SA 18:6 Jeshi likatoka kwenda kwenye uwanja wa vita kupigana na Israeli, hivyo vita vikapiganwa katika msitu wa Efraimu.
2SA 18:7 Huko jeshi la Israeli likashindwa na watu wa Daudi; siku hiyo majeruhi walikuwa wengi, idadi ya watu elfu ishirini.
2SA 18:8 Vita vikaenea nchi nzima, watu wengi zaidi wakifia msituni siku hiyo kuliko waliouawa kwa upanga.
2SA 18:9 Basi ikawa Absalomu alikutana na watu wa Daudi. Yeye alikuwa amepanda nyumbu wake, naye nyumbu alipopita chini ya matawi yaliyosongamana ya mwaloni mkubwa, kichwa cha Absalomu kilinaswa kwenye mti. Akaachwa akining’inia hewani, wakati nyumbu aliyekuwa amempanda aliendelea kwenda.
2SA 18:10 Mtu mmoja alipoona hivyo, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akining’inia kwenye mwaloni.”
2SA 18:11 Yoabu akamwambia huyo mtu, “Nini! Ulimwona Absalomu? Kwa nini hukumpiga papo hapo hadi chini? Ndipo ningekupa shekeli kumi za fedha na mkanda wa askari shujaa.”
2SA 18:12 Lakini huyo mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepimiwa shekeli elfu moja mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’
2SA 18:13 Nami kama ningekuwa nimemtendea kwa hila, na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme, wewe mwenyewe ungejitenga nami.”
2SA 18:14 Yoabu akasema, “Mimi sitapoteza muda hapa pamoja nawe.” Hivyo akachukua mikuki mitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu nayo moyoni alipokuwa angali hai akining’inia katika ule mwaloni.
2SA 18:15 Nao wabeba silaha kumi wa Yoabu wakamzunguka Absalomu, wakampiga na kumuua.
2SA 18:16 Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, navyo vikosi vikaacha kuwafuata Israeli, kwa maana Yoabu aliwasimamisha.
2SA 18:17 Wakamchukua Absalomu, wakamtupa katika shimo kubwa huko msituni na kulundika lundo kubwa la mawe juu yake. Huko nyuma, Waisraeli wote wakakimbilia nyumbani mwao.
2SA 18:18 Wakati wa uhai wake, Absalomu alikuwa amechukua nguzo na kuisimamisha katika Bonde la Mfalme, kwa maana alifikiri, “Sina mwana atakayeendeleza kumbukumbu ya jina langu.” Akaita nguzo hiyo kwa jina lake mwenyewe. Nayo inaitwa Mnara wa Ukumbusho wa Absalomu hadi leo.
2SA 18:19 Basi Ahimaasi mwana wa Sadoki akasema, “Niruhusu mimi nikimbie na kumpelekea mfalme habari kwamba Mwenyezi Mungu amemwokoa mfalme kutoka mikononi mwa adui zake.”
2SA 18:20 Yoabu akamwambia Ahimaasi, “Leo si wewe utakayepeleka habari. Unaweza kupeleka habari wakati mwingine, lakini leo haikupasi kupeleka, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa.”
2SA 18:21 Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja Mkushi, “Nenda, ukamwambie mfalme kile ulichoona.” Mkushi akasujudu mbele ya Yoabu, akaondoka mbio.
2SA 18:22 Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia tena Yoabu, “Liwalo na liwe, tafadhali niruhusu nikimbie nyuma ya huyo Mkushi.” Lakini Yoabu akajibu, “Mwanangu, mbona wataka kwenda? Wewe huna habari yoyote itakayokupa tuzo.”
2SA 18:23 Ahimaasi akasema, “Liwalo na liwe, nataka kukimbia.” Kwa hiyo Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia!” Ndipo Ahimaasi akakimbia kufuata njia ya kupitia tambarare, akafika kabla ya huyo Mkushi.
2SA 18:24 Daudi alipokuwa ameketi kati ya lango la ndani na la nje, mlinzi akapanda juu ya paa la lango kupitia ukutani. Alipotazama nje, akaona mtu mmoja akikimbia peke yake.
2SA 18:25 Mlinzi akampazia mfalme sauti na kumpa taarifa. Mfalme akasema, “Ikiwa yuko peke yake, lazima atakuwa na habari njema.” Naye yule mtu akazidi kusogea karibu.
2SA 18:26 Kisha mlinzi akaona mtu mwingine anakuja akikimbia, akamwita bawabu, “Tazama, mtu mwingine anakuja akikimbia peke yake!” Mfalme akasema, “Lazima atakuwa analeta habari njema pia.”
2SA 18:27 Mlinzi akasema, “Ninaona kuwa yule wa kwanza anakimbia kama Ahimaasi mwana wa Sadoki.” Mfalme akasema, “Yeye ni mtu mwema. Analeta habari njema.”
2SA 18:28 Ndipo Ahimaasi akamwita mfalme, akasema, “Mambo yote ni mema!” Akasujudu mbele ya mfalme, uso wake ukigusa chini, akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wako! Yeye aliyewatoa watu wale walioinua mikono yao dhidi ya mfalme bwana wangu.”
2SA 18:29 Mfalme akauliza, “Je, huyo kijana Absalomu yuko salama?” Ahimaasi akajibu, “Kulikuwa na machafuko mengi mara tu Yoabu alipokuwa anataka kumtuma mtumishi wa mfalme pamoja nami mtumishi wako, lakini sijui ilikuwa nini.”
2SA 18:30 Mfalme akasema, “Simama kando na usubiri hapa.” Basi akasogea kando na kusimama hapo.
2SA 18:31 Ndipo huyo Mkushi akawasili na kusema, “Mfalme bwana wangu, sikia habari njema! Leo Mwenyezi Mungu amekuokoa kutoka kwa wale wote walioinuka dhidi yako.”
2SA 18:32 Mfalme akamuuliza huyo Mkushi, “Je, kijana Absalomu yuko salama?” Huyo Mkushi akajibu, “Adui wa mfalme bwana wangu na wote wale walioinuka kukudhuru na wawe kama huyo kijana.”
2SA 18:33 Mfalme akatetemeka. Akapanda chumbani juu kupitia langoni akilia. Alipokuwa akienda, akasema, “Ee mwanangu Absalomu! Mwanangu, mwanangu Absalomu! Laiti ningekufa badala yako: Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”
2SA 19:1 Yoabu akaambiwa, “Mfalme analia na kumwombolezea Absalomu.”
2SA 19:2 Kwa jeshi lote, ushindi wa siku ile ukageuka kuwa maombolezo, kwa sababu siku ile vikosi vilisikia ikisemwa, “Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.”
2SA 19:3 Siku ile watu wakaingia mjini kimya kama vile waingiavyo kwa aibu watu waliokimbia kutoka vitani.
2SA 19:4 Mfalme akafunika uso wake akalia kwa sauti, akisema, “Ee mwanangu Absalomu! Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”
2SA 19:5 Kisha Yoabu akaingia ndani ya nyumba ya mfalme na kusema, “Leo umewaaibisha watu wako wote, waliookoa maisha yako, maisha ya wanao wa kiume na wa kike, maisha ya wake zako na masuria wako.
2SA 19:6 Unawapenda wale wanaokuchukia, na unawachukia wale wanaokupenda. Leo umeonesha wazi kwamba majemadari wako na watu wao hawana maana kwako. Naona kwamba ungefurahi kama Absalomu angekuwa hai leo na sisi sote tuwe tumekufa.
2SA 19:7 Sasa utoke nje ukawatie moyo watu wako. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba ikiwa hutatoka nje, hakuna mtu atakayesalia pamoja nawe ifikapo leo jioni. Hii itakuwa mbaya zaidi kwako kuliko maafa yote yaliyokupata tangu ujana wako hadi sasa.”
2SA 19:8 Kwa hiyo, mfalme akaondoka na kuketi kwenye kiti chake langoni. Watu walipoambiwa, “Mfalme ameketi langoni,” watu wote wakamjia. Wakati huo, Waisraeli walikuwa wamekimbilia nyumbani mwao.
2SA 19:9 Katika makabila yote ya Israeli, watu walikuwa wanabishana wao kwa wao, wakisema, “Mfalme alituokoa kutoka mikononi mwa adui zetu; ndiye alituokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa mfalme ameikimbia nchi kwa sababu ya Absalomu,
2SA 19:10 naye Absalomu, tuliyempaka mafuta atutawale, amekufa vitani. Basi mbona hamsemi lolote kuhusu kumrudisha mfalme?”
2SA 19:11 Mfalme Daudi akapeleka ujumbe huu kwa makuhani Sadoki na Abiathari, kusema: “Waulizeni wazee wa Yuda, ‘Kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme katika jumba lake la kifalme, maadamu kile kinachosemwa katika Israeli yote kimemfikia mfalme katika makao yake?
2SA 19:12 Ninyi ni ndugu zangu, mwili wangu na damu yangu mwenyewe. Kwa hiyo kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme?’
2SA 19:13 Nanyi mwambieni Amasa, ‘Je, wewe si mwili wangu mwenyewe na damu yangu? Mungu na aniadhibu vikali zaidi, kama kuanzia sasa na kuendelea wewe si jemadari wa jeshi langu mahali pa Yoabu.’ ”
2SA 19:14 Alivutia mioyo ya watu wote wa Yuda, kama vile walikuwa mtu mmoja. Wakapeleka ujumbe kwa mfalme, kusema, “Rudi, wewe na watumishi wako wote.”
2SA 19:15 Ndipo mfalme akarudi, akaenda hadi kufikia Mto Yordani. Basi watu wa Yuda walikuwa wamekuja Gilgali ili kutoka kwenda kumlaki mfalme na kumvusha Mto Yordani.
2SA 19:16 Shimei mwana wa Gera, wa kabila la Benyamini kutoka Bahurimu, akaharakisha kuteremka pamoja na wanaume wa Yuda ili kumlaki Mfalme Daudi.
2SA 19:17 Pamoja naye walikuwa Wabenyamini elfu moja wakiwa wamefuatana na Siba, msimamizi wa nyumba ya Sauli, pia wanawe kumi na watano, na watumishi ishirini. Wakaharakisha kwenda Yordani, mahali mfalme alipokuwa.
2SA 19:18 Wakavuka kivuko ili kuwachukua watu wa nyumbani mwa mfalme ili kuwavusha na kufanya kila kitu alichotaka. Shimei mwana wa Gera alipovuka Yordani, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme,
2SA 19:19 na kumwambia, “Bwana wangu na asinihesabie hatia. Usikumbuke jinsi mtumishi wako alivyofanya kosa siku ile bwana wangu mfalme alipoondoka Yerusalemu. Mfalme aliondoe moyoni mwake.
2SA 19:20 Kwa maana mimi mtumishi wako najua nimefanya dhambi, lakini leo nimekuja hapa kama wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu kushuka na kumlaki bwana wangu mfalme.”
2SA 19:21 Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, Shimei hapaswi kuuawa kwa ajili ya hili? Alimlaani mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.”
2SA 19:22 Daudi akajibu, “Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya? Siku ya leo mmekuwa adui zangu! Je, leo kuna yeyote atakayeuawa katika Israeli? Je, mimi sijui kuwa leo ndimi mfalme katika Israeli yote?”
2SA 19:23 Basi mfalme akamwambia Shimei, “Hutakufa.” Naye mfalme akamwahidi kwa kiapo.
2SA 19:24 Pia Mefiboshethi mwana wa Sauli akashuka kwenda kumlaki mfalme. Hakuwa amenawa miguu, wala kunyoa ndevu zake, wala kufua nguo zake tangu siku mfalme alipoondoka Yerusalemu hadi siku aliporudi salama.
2SA 19:25 Alipotoka Yerusalemu kuja kumlaki mfalme, basi mfalme akamuuliza, “Mefiboshethi, kwa nini hukufuatana nami?”
2SA 19:26 Akasema, “Bwana wangu mfalme, maadamu mimi mtumishi wako ni kiwete, nilisema, ‘Nitandikiwe punda wangu, nimpande, ili niweze kwenda pamoja na mfalme.’ Lakini Siba mtumishi wangu akanisaliti.
2SA 19:27 Naye amemchongea mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme. Bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu, kwa hiyo fanya lolote linalokupendeza.
2SA 19:28 Wazao wote wa baba yangu hawastahili kitu kingine isipokuwa kifo kutoka kwa bwana wangu mfalme, lakini ulimpa mtumishi wako nafasi miongoni mwa wale waliokula mezani pako. Je, ninayo haki gani kumwomba mfalme zaidi ya hayo?”
2SA 19:29 Mfalme akamwambia, “Kwa nini useme zaidi? Naamuru wewe na Siba mgawanye mashamba.”
2SA 19:30 Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu achukue kila kitu, kwa kuwa sasa bwana wangu mfalme amerudi nyumbani salama.”
2SA 19:31 Barzilai, Mgileadi, pia akashuka kutoka Rogelimu ili kuvuka Yordani pamoja na mfalme na kumsindikiza kutoka huko.
2SA 19:32 Basi Barzilai alikuwa mzee sana mwenye umri wa miaka themanini. Alikuwa amempatia mfalme mahitaji alipokuwa anaishi huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa mtu tajiri sana.
2SA 19:33 Mfalme akamwambia Barzilai, “Vuka pamoja nami na ukae nami huko Yerusalemu, nami nitakupatia mahitaji yako.”
2SA 19:34 Lakini Barzilai akamjibu mfalme, “Je, nitaishi miaka mingine mingapi, hata nipande kwenda Yerusalemu pamoja na mfalme?
2SA 19:35 Sasa nina miaka themanini. Je, naweza kutofautisha kati ya lililo jema na lililo baya? Je, mtumishi wako anaweza kujua ladha ya kile anachokula au anachokunywa? Je, bado naweza kusikiliza sauti za waimbaji wa kiume na za wanawake? Kwa nini mtumishi wako aongeze mzigo kwa bwana wangu mfalme?
2SA 19:36 Mtumishi wako atavuka Yordani pamoja na mfalme kwa umbali mfupi tu, lakini kwa nini mfalme anizawadie kwa namna hii?
2SA 19:37 Mruhusu mtumishi wako arudi, ili mimi nikafie katika mji wangu mwenyewe karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini yupo hapa mtumishi wako Kimhamu. Mruhusu avuke pamoja na bwana wangu mfalme. Mtendee lolote linalokupendeza.”
2SA 19:38 Mfalme akamwambia Barzilai, “Kimhamu atavuka Yordani pamoja nami, nami nitamtendea lolote litakalokupendeza. Nawe kitu chochote unachotaka kutoka kwangu nitakutendea.”
2SA 19:39 Kwa hiyo watu wote wakavuka Yordani, kisha mfalme akavuka. Mfalme akambusu Barzilai na kumbariki; Barzilai akarudi nyumbani mwake.
2SA 19:40 Mfalme alipovuka kwenda Gilgali, Kimhamu akavuka pamoja naye. Vikosi vyote vya Yuda na nusu ya vikosi vya Israeli vilimvusha mfalme.
2SA 19:41 Baada ya kitambo kidogo, wanaume wote wa Israeli wakaja kwa mfalme na kumwambia, “Kwa nini ndugu zetu, wanaume wa Yuda, wamemrudisha mfalme kwa siri bila kutushirikisha, na kumvusha ng’ambo ya Yordani, yeye na nyumba yake, pamoja na watu wake wote?”
2SA 19:42 Wanaume wote wa Yuda wakawajibu wanaume wa Israeli, “Tulifanya hivi kwa sababu mfalme ni jamaa yetu wa karibu. Kwa nini mnakasirikia jambo hili? Je, tumekula kitu chochote cha mfalme? Je, tumejichukulia kitu chochote kwa ajili yetu wenyewe?”
2SA 19:43 Ndipo wanaume wa Israeli wakawajibu wanaume wa Yuda, “Tunayo haki mara kumi kwa mfalme; sisi tunahusika zaidi na Daudi kuliko ninyi. Kwa nini basi mnatudharau? Je, hatukuwa wa kwanza kuzungumza kuhusu kumrudisha mfalme nyumbani?” Lakini wanaume wa Yuda wakajibu kwa ukali hata kuliko wanaume wa Israeli.
2SA 20:1 Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Hatuna fungu katika Daudi, wala hatuna sehemu katika mwana wa Yese! Kila mtu aende kwenye hema lake, enyi Israeli!”
2SA 20:2 Kwa hiyo wanaume wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini wanaume wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani hadi Yerusalemu.
2SA 20:3 Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kutunza jumba la kifalme, na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane hadi kifo chao.
2SA 20:4 Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite wanaume wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.”
2SA 20:5 Lakini Amasa alipoenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea.
2SA 20:6 Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara kuliko Absalomu. Wachukue watumishi wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.”
2SA 20:7 Hivyo watumishi wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na mashujaa wenye nguvu wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri.
2SA 20:8 Walipokuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kiunoni wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka ala.
2SA 20:9 Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu.
2SA 20:10 Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
2SA 20:11 Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!”
2SA 20:12 Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani hadi kwenye shamba na kutupia nguo juu yake.
2SA 20:13 Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
2SA 20:14 Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walikusanyika na kumfuata.
2SA 20:15 Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumzingira Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wakijaribu kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini,
2SA 20:16 mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.”
2SA 20:17 Yoabu alienda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?” Akamjibu, “Ndiye mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.”
2SA 20:18 Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri.
2SA 20:19 Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa Mwenyezi Mungu?”
2SA 20:20 Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu.
2SA 20:21 Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Mkabidhini mtu huyu mmoja kwangu, nami nitajiondoa katika mji huu.” Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.”
2SA 20:22 Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani mwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu.
2SA 20:23 Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi;
2SA 20:24 Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa; Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu;
2SA 20:25 Sheva alikuwa mwandishi; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;
2SA 20:26 na Ira Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.
2SA 21:1 Wakati wa utawala wa Daudi kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu mfululizo, kwa hiyo Daudi akautafuta uso wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akasema, “Ni kwa sababu ya Sauli na nyumba yake iliyotiwa madoa ya damu, kwa sababu aliwaua Wagibeoni.”
2SA 21:2 Mfalme akawaita Wagibeoni na kuzumgumza nao. (Wagibeoni hawakuwa sehemu ya Israeli, ila walikuwa mabaki ya Waamori. Waisraeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Sauli katika wivu wake kwa ajili ya Israeli na Yuda, alikuwa amejaribu kuwaangamiza.)
2SA 21:3 Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitawaridhishaje ili mbariki urithi wa Mwenyezi Mungu?”
2SA 21:4 Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumuua mtu yeyote katika Israeli.” Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
2SA 21:5 Wakamjibu mfalme, “Kwa habari ya mtu aliyetuangamiza na kupanga njama dhidi yetu ili tuangamizwe na tusiwe na yeyote katika Israeli,
2SA 21:6 tupatieni wazao wake saba wa kiume, tuwaue hadharani mbele za Mwenyezi Mungu huko Gibea ya Sauli, aliyekuwa amechaguliwa na Mwenyezi Mungu.” Basi mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”
2SA 21:7 Mfalme akamhifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa sababu ya kile kiapo mbele za Mwenyezi Mungu kati ya Daudi na Yonathani.
2SA 21:8 Lakini mfalme akamchukua Armoni na Mefiboshethi, wana wawili wa Rispa binti Aya, ambao alikuwa amemzalia Sauli, pamoja na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliokuwa amemzalia Adrieli mwana wa Barzilai, Mmeholathi.
2SA 21:9 Akawakabidhi kwa Wagibeoni, ambao waliwaua na kuwaweka wazi juu ya kilima mbele za Mwenyezi Mungu. Wote saba walianguka kwa pamoja; waliuawa katika siku za kwanza za mavuno, mara tu uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza.
2SA 21:10 Rispa binti Aya akachukua gunia, akajitandikia juu ya mwamba. Kuanzia mwanzo wa mavuno hadi mvua ziliponyesha juu ya miili ya hao waliouawa, Rispa hakuruhusu ndege wa angani kuwagusa wakati wa mchana, wala wanyama mwitu wakati wa usiku.
2SA 21:11 Daudi alipoambiwa kile Rispa binti Aya, suria wa Sauli, alichokuwa amekifanya,
2SA 21:12 alienda akachukua mifupa ya Sauli na mwanawe Yonathani kutoka kwa watu wa Yabesh-Gileadi. (Walikuwa wameichukua kwa siri kutoka uwanja wa watu wote huko Beth-Shani, ambapo Wafilisti walikuwa wamewatundika baada ya kumuua Sauli huko Gilboa.)
2SA 21:13 Daudi akaileta mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani kutoka huko, pia mifupa ya wale waliokuwa wameuawa na kutupwa ilikusanywa.
2SA 21:14 Wakazika mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani katika kaburi la Kishi, babaye Sauli, huko Sela katika nchi ya Benyamini, nao wakafanya kila kitu mfalme alichoagiza. Baada ya hayo, Mungu akajibu maombi kwa ajili ya nchi.
2SA 21:15 Kwa mara nyingine tena kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Israeli. Daudi akashuka pamoja na watu wake ili kupigana dhidi ya Wafilisti, naye akawa amechoka sana.
2SA 21:16 Naye Ishbi-Benobu, mmoja wa wazao wa Warefai, ambaye mkuki wake ulikuwa na uzito wa shekeli mia tatu za shaba, alikuwa amejifunga upanga mpya, naye akasema atamuua Daudi.
2SA 21:17 Lakini Abishai mwana wa Seruya akaja kumwokoa Daudi; akampiga huyo Mfilisti, akamwangusha chini na kumuua. Ndipo watu wakamwapia Daudi, wakisema, “Kamwe hutaenda tena nasi vitani, ili taa ya Israeli isije ikazimwa.”
2SA 21:18 Baada ya muda, kukawa na vita nyingine na Wafilisti, huko Gobu. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Safu, mmoja wa wazao wa Warefai.
2SA 21:19 Katika vita vingine na Wafilisti huko Gobu, Elhanani mwana wa Yaare-Oregimu, Mbethlehemu, alimuua nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.
2SA 21:20 Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwa na mtu mmoja mkubwa mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita kila mguu: jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai.
2SA 21:21 Alipowadhihaki Israeli, Yonathani mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua.
2SA 21:22 Hawa wanne walikuwa wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.
2SA 22:1 Daudi alimwimbia Mwenyezi Mungu maneno ya wimbo huu Mwenyezi Mungu alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli.
2SA 22:2 Akasema: “Mwenyezi Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu,
2SA 22:3 Mungu wangu ni mwamba wangu, ninayemkimbilia, ngao yangu na pembe ya wokovu wangu. Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu na mwokozi wangu, huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.
2SA 22:4 “Ninamwita Mwenyezi Mungu, anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
2SA 22:5 Mawimbi ya mauti yalinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
2SA 22:6 Kamba za Kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili.
2SA 22:7 “Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu, nilimlilia Mungu wangu. Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika masikioni mwake.
2SA 22:8 Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya mbingu ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
2SA 22:9 Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yaliyowaka yakatoka ndani yake.
2SA 22:10 Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
2SA 22:11 Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mabawa ya upepo.
2SA 22:12 Alifanya giza hema lake la kujifunika: mawingu meusi ya mvua ya angani.
2SA 22:13 Kutokana na mwanga wa uwepo wake mwanga wa radi ukatoka.
2SA 22:14 Mwenyezi Mungu alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
2SA 22:15 Aliipiga mishale na kutawanya adui, akawafukuza kwa umeme mkubwa wa radi.
2SA 22:16 Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwake Mwenyezi Mungu, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.
2SA 22:17 “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
2SA 22:18 Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
2SA 22:19 Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini Mwenyezi Mungu alikuwa msaada wangu.
2SA 22:20 Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
2SA 22:21 “Mwenyezi Mungu alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
2SA 22:22 Kwa maana nimezishika njia za Mwenyezi Mungu; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
2SA 22:23 Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake.
2SA 22:24 Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi.
2SA 22:25 Mwenyezi Mungu amenilipa sawasawa na uadilifu wangu, sawasawa na usafi wangu machoni pake.
2SA 22:26 “Kwa yeye aliye mwaminifu unajionesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia unajionesha kutokuwa na hatia,
2SA 22:27 kwa aliye mtakatifu unajionesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka unajionesha kuwa mkaidi.
2SA 22:28 Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi ili uwashushe.
2SA 22:29 Wewe ni taa yangu, Ee Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hulifanya giza langu kuwa mwanga.
2SA 22:30 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta.
2SA 22:31 “Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu; neno la Mwenyezi Mungu halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake.
2SA 22:32 Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya Mwenyezi Mungu? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu?
2SA 22:33 Mungu ndiye anivikaye nguvu, na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
2SA 22:34 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
2SA 22:35 Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
2SA 22:36 Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu; msaada wako umeniinua niwe mkuu.
2SA 22:37 Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze.
2SA 22:38 “Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta, sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
2SA 22:39 Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu.
2SA 22:40 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
2SA 22:41 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu.
2SA 22:42 Walipiga yowe, lakini hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu.
2SA 22:43 Niliwaponda kama mavumbi ya nchi; niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani.
2SA 22:44 “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu; umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa. Watu ambao sikuwajua wananitumikia,
2SA 22:45 nao wageni huja wakininyenyekea, mara wanisikiapo, hunitii.
2SA 22:46 Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
2SA 22:47 “Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu!
2SA 22:48 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, ayawekaye mataifa chini yangu,
2SA 22:49 aniwekaye huru toka kwa adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
2SA 22:50 Kwa hiyo nitakusifu, Ee Mwenyezi Mungu, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.
2SA 22:51 “Humpa mfalme wake ushindi mkuu; huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.”
2SA 23:1 Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi: “Neno la Daudi mwana wa Yese, neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana, mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo, mwimbaji wa nyimbo wa Israeli:
2SA 23:2 “Roho wa Mwenyezi Mungu alinena kupitia kwangu, neno lake lilikuwa katika ulimi wangu.
2SA 23:3 Mungu wa Israeli alinena, mwamba wa Israeli akaniambia: ‘Mtu anatawala watu kwa haki, wakati anapotawala akiwa na hofu ya Mungu,
2SA 23:4 yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo asubuhi isiyo na mawingu, kama mwanga baada ya mvua unaochipuza majani kutoka ardhini.’
2SA 23:5 “Je, si hivyo ilivyo nyumba yangu mbele za Mungu? Je, hajafanya agano la milele nami, lililopangwa na kuimarishwa kila sehemu? Je, hatanifanya niufurahie wokovu wangu na kunijalia matakwa yangu yote?
2SA 23:6 Lakini watu waovu wote watatupwa kando kama miiba, ambayo haikusanywi kwa mkono.
2SA 23:7 Yeyote agusaye miiba hutumia chombo cha chuma au mpini wa mkuki, nayo huchomwa pale ilipo.”
2SA 23:8 Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi: Yosheb-Bashebethi Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia nane, aliowaua katika pambano moja.
2SA 23:9 Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai Mwahohi. Akiwa mmoja wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha Waisraeli wakarudi nyuma,
2SA 23:10 lakini yeye alisimama imara, akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na kugandamana na upanga. Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari kuteka tu nyara za waliokufa.
2SA 23:11 Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia.
2SA 23:12 Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalipigania na kuwaua Wafilisti, naye Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa.
2SA 23:13 Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya wale mashujaa thelathini wakuu walimwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai.
2SA 23:14 Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu.
2SA 23:15 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!”
2SA 23:16 Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Mwenyezi Mungu.
2SA 23:17 Akasema, “Iwe mbali nami, Ee Mwenyezi Mungu, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walienda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa. Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu.
2SA 23:18 Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu.
2SA 23:19 Je, hakupata heshima kubwa kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.
2SA 23:20 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba.
2SA 23:21 Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe.
2SA 23:22 Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu.
2SA 23:23 Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.
2SA 23:24 Miongoni mwa wale Thelathini walikuwa: Asaheli ndugu wa Yoabu; Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu;
2SA 23:25 Shama Mharodi; Elika Mharodi;
2SA 23:26 Helesi Mpalti; Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa;
2SA 23:27 Abiezeri kutoka Anathothi; Mebunai Mhushathi;
2SA 23:28 Salmoni Mwahohi; Maharai Mnetofathi;
2SA 23:29 Heledi mwana wa Baana Mnetofathi; Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini;
2SA 23:30 Benaya Mpirathoni; Hidai kutoka mabonde ya Gaashi;
2SA 23:31 Abi-Alboni Mwaribathi; Azmawethi Mbarhumi;
2SA 23:32 Eliaba Mshaalboni; wana wa Yasheni; Yonathani
2SA 23:33 mwana wa Shama Mharari; Ahiamu mwana wa Sharari Mharari;
2SA 23:34 Elifeleti mwana wa Ahasbai Mmaakathi; Eliamu mwana wa Ahithofeli Mgiloni;
2SA 23:35 Hezro Mkarmeli; Paarai Mwarbi;
2SA 23:36 Igali mwana wa Nathani kutoka Soba; Bani Mgadi;
2SA 23:37 Seleki Mwamoni; Naharai Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha za Yoabu mwana wa Seruya;
2SA 23:38 Ira Mwithiri; Garebu Mwithiri;
2SA 23:39 na Uria Mhiti.
2SA 24:1 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.”
2SA 24:2 Kwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.”
2SA 24:3 Lakini Yoabu akamjibu mfalme, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?”
2SA 24:4 Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi; kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli.
2SA 24:5 Baada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini mwa mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri.
2SA 24:6 Walienda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni.
2SA 24:7 Kisha wakaelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walienda Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda.
2SA 24:8 Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini.
2SA 24:9 Yoabu akamtolea mfalme idadi ya wapiganaji: Katika Israeli kulikuwa wanaume wenye uwezo elfu mia nane ambao wangeweza kutumia upanga, na katika Yuda watu elfu mia tano.
2SA 24:10 Dhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambia Mwenyezi Mungu, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Ee Mwenyezi Mungu, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
2SA 24:11 Kabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno la Mwenyezi Mungu lilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema:
2SA 24:12 “Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”
2SA 24:13 Basi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.”
2SA 24:14 Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.”
2SA 24:15 Basi Mwenyezi Mungu akatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi hadi muda ulioamriwa, wakafa watu elfu sabini kuanzia Dani hadi Beer-Sheba.
2SA 24:16 Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, Mwenyezi Mungu akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Mwenyezi Mungu alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.
2SA 24:17 Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia Mwenyezi Mungu, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”
2SA 24:18 Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengee Mwenyezi Mungu madhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.”
2SA 24:19 Kwa hiyo Daudi akakwea kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi.
2SA 24:20 Arauna alipotazama na kumwona mfalme na maafisa wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu, uso wake ukagusa chini mbele ya mfalme.
2SA 24:21 Arauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?” Daudi akajibu, “Nimekuja kununua sakafu yako ya kupuria, niweze kumjengea Mwenyezi Mungu madhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.”
2SA 24:22 Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ng’ombe kwa ajili ya kuni.
2SA 24:23 Ee mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na akukubali.”
2SA 24:24 Lakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha! Nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, isiyonigharimu chochote.” Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha.
2SA 24:25 Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha Mwenyezi Mungu akajibu kwa ajili ya nchi, nayo tauni ikakoma katika Israeli.
1KI 1:1 Mfalme Daudi alipokuwa mzee umri ukiwa umesogea, hakuweza kupata joto hata walipomfunika kwa nguo.
1KI 1:2 Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, “Turuhusu tumtafute mwanamwali bikira amhudumie mfalme na kumtunza. Anaweza kulala pembeni mwake ili bwana wetu mfalme apate joto.”
1KI 1:3 Kisha wakatafuta katika Israeli yote ili kumpata msichana mzuri wa sura na wakampata Abishagi Mshunami, wakamleta kwa mfalme.
1KI 1:4 Msichana huyo alikuwa mzuri sana wa sura. Akamtunza mfalme na kumhudumia, lakini mfalme hakufanya naye tendo la ndoa.
1KI 1:5 Basi Adoniya mwana wa Hagithi akajigamba na kusema, “Mimi nitakuwa mfalme.” Hivyo akaweka tayari magari ya vita na wapanda farasi, pamoja na watu hamsini wa kumtangulia wakikimbia.
1KI 1:6 (Baba yake hakuwa ameingilia na kumuuliza, “Kwa nini unafanya hivyo?” Alikuwa pia kijana mzuri sana wa sura, na alizaliwa baada ya Absalomu.)
1KI 1:7 Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari, nao wakamsaidia.
1KI 1:8 Lakini kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, nabii Nathani, Shimei, Rei na walinzi maalum wa Daudi hawakujiunga na Adoniya.
1KI 1:9 Ndipo Adoniya akatoa dhabihu ya kondoo, ng’ombe na ndama walionona kwenye Jiwe la Zohelethi karibu na En-Rogeli. Akawaalika ndugu zake wote wana wa mfalme, na wanaume wote wa Yuda waliokuwa maafisa wa mfalme,
1KI 1:10 lakini hakumwalika nabii Nathani, wala Benaya, wala walinzi maalum wa mfalme, wala ndugu yake Sulemani.
1KI 1:11 Ndipo Nathani akamuuliza Bathsheba, mama yake Sulemani, “Je, hujasikia kwamba Adoniya mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme pasipo bwana wetu Daudi kujua jambo hili?
1KI 1:12 Sasa basi, acha nikushauri jinsi utakavyookoa uhai wako mwenyewe na uhai wa mwanao Sulemani.
1KI 1:13 Ingia kwa Mfalme Daudi na umwambie, ‘Bwana wangu mfalme, je hukuniapia mimi mtumishi wako: “Hakika mwanao Sulemani atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme”? Kwa nini basi Adoniya amekuwa mfalme?’
1KI 1:14 Utakapokuwa ukizungumza na mfalme, nitaingia na kuthibitisha hayo uliyoyasema.”
1KI 1:15 Hivyo Bathsheba akaenda kumwona mfalme chumbani mwake, ambapo Abishagi Mshunami alikuwa akimhudumia; naye mfalme alikuwa mzee sana.
1KI 1:16 Bathsheba akainama na kusujudu, uso wake ukagusa chini mbele ya mfalme. Mfalme akauliza, “Ni nini unachokitaka?”
1KI 1:17 Akamwambia, “Bwana wangu, wewe mwenyewe uliniapia mimi mtumishi wako kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwamba: ‘Sulemani Mwanao atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme.’
1KI 1:18 Lakini sasa Adoniya amekuwa mfalme, nawe, bwana wangu mfalme huna habari kuhusu jambo hilo.
1KI 1:19 Ametoa dhabihu idadi kubwa ya ng’ombe, ndama walionona na kondoo, naye amewaalika wana wa mfalme wote, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini hakumwalika Sulemani mtumishi wako.
1KI 1:20 Bwana wangu mfalme, macho ya Israeli yote yanakutazama wewe wajue kutoka kwako kuwa ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake.
1KI 1:21 Kama sivyo, mara tu bwana wangu mfalme atakapopumzishwa pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutatendewa kama wahalifu.”
1KI 1:22 Alipokuwa angali anazungumza na mfalme, nabii Nathani akafika.
1KI 1:23 Wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Kisha akaenda mbele ya mfalme na kumsujudia hadi uso wake ukagusa chini.
1KI 1:24 Nathani akasema, “Je, bwana wangu mfalme, umetangaza kuwa Adoniya atakuwa mfalme baada yako na kwamba ataketi kwenye kiti chako cha ufalme?
1KI 1:25 Leo ameshuka na kutoa dhabihu idadi kubwa ya ng’ombe, ndama walionona na kondoo. Amewaalika wana wote wa mfalme, jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari. Sasa hivi, wanakula na kunywa pamoja naye wakisema, ‘Aishi maisha marefu, Mfalme Adoniya!’
1KI 1:26 Lakini mimi mtumishi wako, na kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, na mtumishi wako Sulemani hakutualika.
1KI 1:27 Je, hili ni jambo ambalo bwana wangu mfalme amelifanya pasipo kuwajulisha watumishi wake ili wapate kujua ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake?”
1KI 1:28 Ndipo Mfalme Daudi akasema, “Mwite Bathsheba, aingie ndani.” Hivyo akaingia mbele ya mfalme na kusimama mbele yake.
1KI 1:29 Ndipo mfalme akaapa: “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka kila taabu,
1KI 1:30 hakika nitatekeleza leo kile nilichokuapia kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwanao Sulemani atakuwa mfalme baada yangu, naye ataketi kwenye kiti changu cha ufalme baada yangu.”
1KI 1:31 Kisha Bathsheba akasujudu, uso wake ukigusa chini mbele ya mfalme, akasema, “Bwana wangu Mfalme Daudi na aishi milele!”
1KI 1:32 Mfalme Daudi akasema, “Mwite kuhani Sadoki ndani, na nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Walipofika mbele ya mfalme,
1KI 1:33 akawaambia: “Wachukueni watumishi wa bwana wenu pamoja nanyi na mkamkalishe mwanangu Sulemani juu ya nyumbu wangu mwenyewe, kisha mkamteremshe hadi Gihoni.
1KI 1:34 Huko kuhani Sadoki na nabii Nathani wampake mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Pigeni tarumbeta na mpaze sauti, mkisema, ‘Mfalme Sulemani aishi maisha marefu!’
1KI 1:35 Kisha mtapanda pamoja naye, atakuja na kuketi kwenye kiti changu cha ufalme na kutawala baada yangu. Nimemweka atawale juu ya Israeli na Yuda.”
1KI 1:36 Benaya mwana wa Yehoyada akamjibu mfalme, “Amen! Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu mfalme, na aamuru vivyo hivyo.
1KI 1:37 Kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa na bwana wangu mfalme, vivyo hivyo na awe na Sulemani kukifanya kiti chake cha utawala kuwa kikuu kuliko kile cha bwana wangu Mfalme Daudi!”
1KI 1:38 Hivyo kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi wakaenda na kumpandisha Sulemani juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi, nao wakamsindikiza hadi Gihoni.
1KI 1:39 Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta kutoka hema takatifu na kumtia Sulemani mafuta. Kisha wakapiga tarumbeta na watu wote wakapaza sauti wakisema, “Mfalme Sulemani aishi maisha marefu!”
1KI 1:40 Na watu wote wakakwea wakimfuata, huku wakipiga filimbi na kushangilia sana, hata ardhi ikatikisika kwa ile sauti.
1KI 1:41 Adoniya pamoja na wageni wote waliokuwa pamoja naye wakasikia sauti hiyo walipokuwa wakimalizia karamu yao. Waliposikia sauti ya tarumbeta, Yoabu akauliza, “Nini maana ya makelele haya yote katika mji?”
1KI 1:42 Hata alipokuwa anaongea, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akafika. Adoniya akasema, “Ingia ndani. Mtu wa maana kama wewe ni lazima awe amelete habari njema.”
1KI 1:43 Yonathani akamjibu, “La hasha! Mfalme Daudi bwana wetu amemfanya Sulemani kuwa mfalme.
1KI 1:44 Mfalme ametuma pamoja naye kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme,
1KI 1:45 nao kuhani Sadoki na nabii Nathani wamempaka mafuta huko Gihoni kuwa mfalme. Kutoka hapo wamepanda wakishangilia, na sauti zimeenea kote katika mji. Hizo ndizo kelele unazosikia.
1KI 1:46 Zaidi ya hayo, Sulemani ameketi kwenye kiti chake cha ufalme.
1KI 1:47 Pia, maafisa wa mfalme wamekuja ili kumpongeza bwana wetu Mfalme Daudi, wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Sulemani kuwa mashuhuri kuliko lako, na kiti chake cha ufalme kiwe na ukuu kuliko chako!’ Naye mfalme akasujudu akiabudu kitandani mwake,
1KI 1:48 akasema, ‘Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye ameruhusu macho yangu kuona mrithi kwenye kiti changu cha ufalme leo.’ ”
1KI 1:49 Waliposikia haya, wageni wote wa Adoniya wakainuka kwa hofu na kutawanyika.
1KI 1:50 Lakini Adoniya kwa kumwogopa Sulemani, akaenda na kushika pembe za madhabahu.
1KI 1:51 Kisha Sulemani akaambiwa, “Adoniya anamwogopa Mfalme Sulemani na ameshikilia pembe za madhabahu. Anasema, ‘Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hatamuua mtumishi wake kwa upanga.’ ”
1KI 1:52 Sulemani akajibu, “Akijionesha kuwa mtu muungwana, hakuna unywele wake utakaoanguka juu ya ardhi; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa.”
1KI 1:53 Ndipo Mfalme Sulemani akawatuma watu, nao wakamshusha kutoka madhabahuni. Naye Adoniya akaja akamwinamia Mfalme Sulemani, naye Sulemani akamwambia, “Nenda nyumbani mwako.”
1KI 2:1 Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Sulemani agizo.
1KI 2:2 Akasema, “Ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jioneshe kuwa mwanaume,
1KI 2:3 shika lile Mwenyezi Mungu, Mungu wako, analokuagiza: Nenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote utakapoenda,
1KI 2:4 na ili Mwenyezi Mungu aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’
1KI 2:5 “Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake.
1KI 2:6 Mtendee kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani.
1KI 2:7 “Lakini uwaoneshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu.
1KI 2:8 “Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, aliyenilaani kwa laana kali siku niliyoenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa Mwenyezi Mungu: ‘Sitakuua kwa upanga!’
1KI 2:9 Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.”
1KI 2:10 Kisha Daudi akalala na baba zake, naye akazikwa katika Mji wa Daudi.
1KI 2:11 Daudi alikuwa ametawala Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na tatu.
1KI 2:12 Kwa hiyo Sulemani akaketi kwenye kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana.
1KI 2:13 Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Sulemani. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?” Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.”
1KI 2:14 Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.” Akajibu, “Unaweza kulisema.”
1KI 2:15 Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, na ufalme umeenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
1KI 2:16 Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.” Bathsheba akasema, “Unaweza kuliomba.”
1KI 2:17 Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Sulemani, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.”
1KI 2:18 Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.”
1KI 2:19 Bathsheba alipoenda kwa Mfalme Sulemani kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akamketisha mkono wake wa kuume.
1KI 2:20 Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.” Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.”
1KI 2:21 Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.”
1KI 2:22 Mfalme Sulemani akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Mwombee na ufalme pia kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa ajili ya kuhani Abiathari, na Yoabu mwana wa Seruya!”
1KI 2:23 Mfalme Sulemani akaapa kwa Mwenyezi Mungu, akasema: “Mungu na aniadhibu vikali zaidi ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili!
1KI 2:24 Basi sasa, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!”
1KI 2:25 Hivyo Mfalme Sulemani akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.
1KI 2:26 Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la Bwana Mungu Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.”
1KI 2:27 Hivyo Sulemani akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa Mwenyezi Mungu, akilitimiza neno la Mwenyezi Mungu alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli.
1KI 2:28 Habari zilipomfikia Yoabu, aliyekuwa amepanga njama na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la Mwenyezi Mungu na kushika pembe za madhabahu.
1KI 2:29 Mfalme Sulemani akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la Mwenyezi Mungu naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Sulemani akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!”
1KI 2:30 Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la Mwenyezi Mungu na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ” Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.” Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.”
1KI 2:31 Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga.
1KI 2:32 Mwenyezi Mungu atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye.
1KI 2:33 Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya Mwenyezi Mungu milele.”
1KI 2:34 Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akamgonga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika shamba lake mwenyewe jangwani.
1KI 2:35 Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu, na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.
1KI 2:36 Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote.
1KI 2:37 Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.”
1KI 2:38 Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu.
1KI 2:39 Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wameenda Gathi.”
1KI 2:40 Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi.
1KI 2:41 Sulemani alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi,
1KI 2:42 mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa Mwenyezi Mungu na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa’? Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’
1KI 2:43 Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa Mwenyezi Mungu na kutii amri niliyokupa?”
1KI 2:44 Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua moyoni mwako makosa yote uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa Mwenyezi Mungu atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda.
1KI 2:45 Lakini Mfalme Sulemani atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitaimarishwa mbele za Mwenyezi Mungu milele.”
1KI 2:46 Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akamgonga Shimei na kumuua. Sasa ufalme ukawa umeimarika mikononi mwa Sulemani.
1KI 3:1 Sulemani akafanya mapatano na Mfalme Farao wa Misri na akamwoa binti yake. Akamleta huyo binti Farao katika Mji wa Daudi hadi alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la Mwenyezi Mungu, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu.
1KI 3:2 Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye mahali pa juu pa kuabudia, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu.
1KI 3:3 Sulemani akaonesha upendo wake kwa Mwenyezi Mungu kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu pa kuabudia.
1KI 3:4 Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia pakuu, naye Sulemani akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu.
1KI 3:5 Mwenyezi Mungu akamtokea Sulemani huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”
1KI 3:6 Sulemani akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.
1KI 3:7 “Sasa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme mahali pa baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu.
1KI 3:8 Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao.
1KI 3:9 Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”
1KI 3:10 Bwana akapendezwa kwamba Sulemani ameliomba jambo hili.
1KI 3:11 Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba busara katika kutoa haki,
1KI 3:12 nitafanya uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwa mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwa baada yako.
1KI 3:13 Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba: utajiri na heshima; siku za maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme.
1KI 3:14 Nawe ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu vile baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.”
1KI 3:15 Ndipo Sulemani akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto. Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.
1KI 3:16 Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake.
1KI 3:17 Mmoja wao akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami.
1KI 3:18 Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine yeyote katika nyumba isipokuwa sisi wawili.
1KI 3:19 “Usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia.
1KI 3:20 Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu.
1KI 3:21 Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia kwa makini katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyemzaa.”
1KI 3:22 Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.” Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako; aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme.
1KI 3:23 Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’ ”
1KI 3:24 Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga.
1KI 3:25 Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.”
1KI 3:26 Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimuue!” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!”
1KI 3:27 Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimuue; ndiye mama yake.”
1KI 3:28 Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.
1KI 4:1 Basi Mfalme Sulemani akatawala Israeli yote.
1KI 4:2 Hawa walikuwa maafisa wake wakuu: Kuhani: Azaria mwana wa Sadoki;
1KI 4:3 Elihorefu na Ahiya, wana wa Shisha: waandishi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi: karani;
1KI 4:4 Benaya mwana wa Yehoyada: jemadari mkuu wa jeshi; Sadoki na Abiathari: makuhani;
1KI 4:5 Azaria mwana wa Nathani: kiongozi wa maafisa wa wilaya; Zabudi mwana wa Nathani: kuhani na mshauri binafsi wa mfalme;
1KI 4:6 Ahishari: msimamizi wa jumba la kifalme; Adoniramu mwana wa Abda: msimamizi wa kazi za kulazimisha.
1KI 4:7 Pia Sulemani alikuwa na watawala kumi na wawili wa wilaya katika Israeli yote, walioshughulikia mahitaji ya mfalme na ya watu wa nyumbani kwa mfalme. Kila mmoja alitoa chakula kwa mwezi mmoja katika mwaka.
1KI 4:8 Majina yao ni haya: Ben-Huri: katika nchi ya vilima ya Efraimu;
1KI 4:9 Ben-Dekari: katika Makasi, Shaalbimu, Beth-Shemeshi na Elon-Beth-Hanani;
1KI 4:10 Ben-Hesedi: katika Arubothi (Soko na nchi yote ya Heferi zilikuwa zake);
1KI 4:11 Ben-Abinadabu: katika Nafoth-Dori (alimwoa Tafathi binti Sulemani);
1KI 4:12 Baana mwana wa Ahiludi: katika Taanaki na Megido, na katika Beth-Shani yote karibu na Sarethani chini ya Yezreeli, kuanzia Beth-Shani hadi Abel-Mehola kupita hadi Yokmeamu;
1KI 4:13 Ben-Geberi: katika Ramoth-Gileadi (makazi ya Yairi mwana wa Manase katika Gileadi ilikuwa yake, kadhalika wilaya ya Argobu katika Bashani na miji yake mikubwa sitini iliyozungukwa na kuta zenye makomeo ya shaba);
1KI 4:14 Ahinadabu mwana wa Ido: katika Mahanaimu;
1KI 4:15 Ahimaasi: katika Naftali (alikuwa amemwoa Basemathi binti Sulemani);
1KI 4:16 Baana mwana wa Hushai: katika Asheri na katika Bealothi;
1KI 4:17 Yehoshafati mwana wa Parua: katika Isakari;
1KI 4:18 Shimei mwana wa Ela: katika Benyamini;
1KI 4:19 Geberi mwana wa Uri: katika Gileadi (nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani). Naye alikuwa mtawala pekee katika eneo hilo.
1KI 4:20 Watu wa Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani; walikula, wakanywa na kufurahi.
1KI 4:21 Mfalme Sulemani akatawala katika falme zote kuanzia Mto hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Sulemani, siku zote za maisha yake.
1KI 4:22 Mahitaji ya Sulemani ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida.
1KI 4:23 Ng’ombe kumi wa zizini, ng’ombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana.
1KI 4:24 Kwa kuwa Sulemani alitawala falme zote magharibi ya Mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote.
1KI 4:25 Wakati wa maisha ya Sulemani, watu wa Yuda na Israeli, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, waliishi salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake.
1KI 4:26 Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne ya magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili.
1KI 4:27 Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Sulemani na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua.
1KI 4:28 Pia walileta kiasi walichopangiwa cha shayiri na majani kwa ajili ya farasi wa magari ya vita na farasi wengine mahali palipostahili.
1KI 4:29 Mungu akampa Sulemani hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari.
1KI 4:30 Hekima ya Sulemani ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri.
1KI 4:31 Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi; kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka.
1KI 4:32 Akanena mithali elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano (1,005).
1KI 4:33 Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wanaotambaa na samaki.
1KI 4:34 Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Sulemani, wakiwa wametumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia kuhusu hekima yake.
1KI 5:1 Hiramu mfalme wa Tiro aliposikia kuwa Sulemani amepakwa mafuta awe mfalme mahali pa Daudi baba yake, akatuma wajumbe kwa Sulemani, kwa sababu Hiramu siku zote alikuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na Daudi.
1KI 5:2 Sulemani akapeleka ujumbe huu kwa Hiramu:
1KI 5:3 “Unajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyopiganwa dhidi yake kutoka pande zote, hadi Mwenyezi Mungu alipowaweka adui zake chini ya miguu yake.
1KI 5:4 Lakini sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, amenipa utulivu kila upande hakuna adui wala maafa.
1KI 5:5 Kwa hiyo, ninakusudia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwambia baba yangu Daudi, aliposema, ‘Mwanao nitakayemweka kwenye kiti cha ufalme mahali pako, ndiye atajenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’
1KI 5:6 “Hivyo toa amri ili mierezi ya Lebanoni ikatwe kwa ajili yangu. Watu wangu watafanya kazi na watu wako, nami nitakulipa kwa ajili ya watu wako kwa ujira wowote utakaoupanga. Unajua kwamba hatuna mtu yeyote mwenye ustadi katika kukata miti kama Wasidoni.”
1KI 5:7 Hiramu aliposikia ujumbe wa Sulemani, akafurahishwa sana akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu leo, kwa kuwa amempa Daudi mwana mwenye hekima ya kutawala taifa hili kubwa.”
1KI 5:8 Hivyo Hiramu akapeleka ujumbe kwa Sulemani: “Nimepokea ujumbe ulionipelekea na nitafanya yote unayohitaji katika kukupatia magogo ya mwerezi na misunobari.
1KI 5:9 Watu wangu watayakokota kutoka Lebanoni hadi kwenye bahari, nami nitayafunga katika mafungu yaelee juu ya maji hadi utakapoelekeza. Huko nitayatenganisha, nawe utaweza kuyachukua. Wewe utakidhi haja yangu kwa kunipatia chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.”
1KI 5:10 Kwa njia hii Hiramu akampa Sulemani miti yote ya mierezi na magogo ya misunobari kama alivyohitaji,
1KI 5:11 naye Sulemani akampa Hiramu kori elfu ishirini za ngano kama chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, pamoja na mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa bathi elfu ishirini. Sulemani aliendelea kumfanyia Hiramu hivyo mwaka baada ya mwaka.
1KI 5:12 Mwenyezi Mungu akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidi. Palikuwa na uhusiano wa amani kati ya Hiramu na Sulemani, na wote wawili wakafanya mkataba.
1KI 5:13 Mfalme Sulemani akakusanya wafanyakazi elfu thelathini kutoka Israeli yote.
1KI 5:14 Akawapeleka Lebanoni kwa zamu za watu elfu kumi kila mwezi. Hivyo walikaa Lebanoni kwa mwezi mmoja, na miezi miwili wakakaa nyumbani. Adoniramu ndiye alikuwa kiongozi wa shokoa.
1KI 5:15 Sulemani alikuwa na wachukuzi wa mizigo elfu sabini, na wachonga mawe elfu themanini huko vilimani,
1KI 5:16 pamoja na wasimamizi elfu tatu mia tatu ambao walisimamia mradi huo na kuwaelekeza wafanyakazi.
1KI 5:17 Kwa amri ya mfalme, walitoa mawe makubwa na bora kwenye machimbo ya mawe kwa kujengea msingi wa mawe yaliyochongwa kwa ajili ya Hekalu.
1KI 5:18 Mafundi wa Sulemani, wa Hiramu na watu wa Gebali walikata na kuandaa mbao na mawe kwa ajili ya ujenzi wa Hekalu.
1KI 6:1 Katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Sulemani katika Israeli, katika mwezi wa Zivu, uliokuwa mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1KI 6:2 Hekalu ambalo Mfalme Sulemani alilijenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu lilikuwa na urefu wa dhiraa sitini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa thelathini kwenda juu.
1KI 6:3 Baraza iliyokuwa mbele ya ukumbi mkuu wa Hekalu iliongeza upana wa Hekalu kwa dhiraa ishirini, na kuchomoza dhiraa kumi mbele ya Hekalu.
1KI 6:4 Akatengeneza madirisha membamba katika Hekalu.
1KI 6:5 Akajenga vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote, vikishikamana na kuta za ukumbi wa Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu.
1KI 6:6 Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano, ya kati ilikuwa dhiraa sita, na ya tatu ilikuwa dhiraa saba. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu.
1KI 6:7 Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa.
1KI 6:8 Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu; ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutoka hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu.
1KI 6:9 Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mwerezi.
1KI 6:10 Mfalme Sulemani akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mwerezi.
1KI 6:11 Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Sulemani kusema:
1KI 6:12 “Kuhusu Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, nitatimiza kupitia kwako ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako.
1KI 6:13 Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.”
1KI 6:14 Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha.
1KI 6:15 Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mwerezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari, na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari.
1KI 6:16 Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mwerezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu.
1KI 6:17 Ukumbi mkuu uliokuwa mbele ya chumba hiki ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini.
1KI 6:18 Ndani, Hekalu lilipambwa na mbao za mwerezi zilizonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi; hakuna jiwe ambalo lilionekana.
1KI 6:19 Ndani ya Hekalu akatengeneza mahali patakatifu pa kuliweka Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu.
1KI 6:20 Mahali patakatifu palikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa ishirini. Akapafunika upande wa ndani, na madhabahu ya mwerezi pia, kwa dhahabu safi.
1KI 6:21 Sulemani akalifunika Hekalu upande wa ndani kwa dhahabu safi, na akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande mmoja hadi ule mwingine mbele ya mahali patakatifu, palipofunikwa kwa dhahabu.
1KI 6:22 Basi akafunika upande wote wa ndani kwa dhahabu. Pia akafunika kwa dhahabu yale madhabahu yaliyokuwa ndani ya mahali patakatifu.
1KI 6:23 Katika mahali patakatifu, akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi kwenda juu.
1KI 6:24 Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi.
1KI 6:25 Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, kwa kuwa makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo.
1KI 6:26 Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi.
1KI 6:27 Aliwaweka makerubi hao katika chumba cha ndani kabisa cha Hekalu, mabawa yao yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta wa upande mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba.
1KI 6:28 Akafunika wale makerubi kwa dhahabu.
1KI 6:29 Kuta zote za Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi za makerubi, mitende na maua yaliyochanua.
1KI 6:30 Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu.
1KI 6:31 Katika ingilio la mahali patakatifu sana, alitengeneza milango ya mbao za mzeituni, yenye miimo ya sehemu moja ya tano ya upana wa madhabahu.
1KI 6:32 Kwenye milango hiyo miwili ya mbao za mzeituni, alinakshi makerubi, mitende, pamoja na maua yaliyochanua, na kufunika makerubi na mitende kwa dhahabu iliyofuliwa.
1KI 6:33 Kwa namna hiyo hiyo, alitengeneza miimo kwa mbao za mzeituni yenye upana wa robo ya upana wa ukumbi mkuu kwa ajili ya ingilio la ukumbi huo.
1KI 6:34 Pia akatengeneza milango miwili kwa mbao za msunobari, kila mmoja ukiwa na vipande viwili ambavyo vilikunjwa kwa bawaba.
1KI 6:35 Akanakshi makerubi, mitende na maua yaliyochanua juu yake, na kufunika kwa dhahabu iliyonyoshwa vizuri juu ya michoro.
1KI 6:36 Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa.
1KI 6:37 Msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu.
1KI 6:38 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Sulemani. Alilijenga kwa miaka saba.
1KI 7:1 Ilimchukua Sulemani miaka kumi na tatu kukamilisha ujenzi wa jumba lake la kifalme.
1KI 7:2 Alijenga jumba lililoitwa Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni. Lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja, upana wa dhiraa hamsini, na kimo cha dhiraa thelathini, na safu nne za nguzo za mwerezi zilizoshikilia boriti za mwerezi zilizosawazishwa.
1KI 7:3 Lilipauliwa kwa mbao za mwerezi juu ya boriti arobaini na tano zilizolalia nguzo, boriti kumi na tano kwa kila safu.
1KI 7:4 Madirisha yake yaliwekwa juu kwa safu tatu, yakielekeana.
1KI 7:5 Milango yenye miimo ya mstatili ilikuwa upande wa mbele katika safu tatu, ikielekeana.
1KI 7:6 Akajenga safu ya nguzo, yenye urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa thelathini. Mbele ya jengo hilo kulikuwa na baraza. Mbele ya baraza kulikuwa na nguzo na paa lililoning’inia.
1KI 7:7 Akajenga ukumbi wa kiti cha ufalme, yaani Ukumbi wa Hukumu, mahali ambapo angetolea hukumu, akaufunika kwa mbao za mwerezi kutoka sakafu hadi dari.
1KI 7:8 Jumba la kifalme ambamo angeishi, aliliweka nyuma kidogo, na lilijengwa kama jumba hilo la hukumu. Pia Sulemani akajenga jumba la kifalme lililofanana na hilo kwa ajili ya binti Farao, aliyekuwa amemwoa.
1KI 7:9 Majengo haya yote, kuanzia nje hadi kwenye ua mkuu, na kuanzia msingi hadi upenuni, yalijengwa kwa mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo kwa msumeno, na nyuso zake za ndani na za nje zililainishwa.
1KI 7:10 Misingi ilijengwa kwa mawe makubwa yaliyo bora, yenye urefu wa dhiraa kumi, na mengine urefu wa dhiraa nane.
1KI 7:11 Sehemu za juu kulikuwa na boriti za mwerezi, na mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo.
1KI 7:12 Ule ua mkuu ulizungukwa na ukuta wa safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa, kama ulivyokuwa ua wa ndani wa Hekalu la Mwenyezi Mungu na baraza yake.
1KI 7:13 Mfalme Sulemani akatuma watu Tiro kumleta Hiramu,
1KI 7:14 ambaye mama yake alikuwa mjane kutoka kabila la Naftali na baba yake alikuwa mtu wa Tiro tena fundi wa shaba. Hiramu alikuwa na ustadi wa hali ya juu na mzoefu katika aina zote za kazi ya shaba. Alikuja kwa Mfalme Sulemani na kufanya kazi zake zote alizopangiwa.
1KI 7:15 Hiramu akasubu nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, na mzingo wa dhiraa kumi na mbili kwa mstari.
1KI 7:16 Pia alitengeneza mataji mawili ya shaba ya kusubu ili kuyaweka juu ya hizo nguzo; kila taji lilikuwa na kimo cha dhiraa tano kwenda juu.
1KI 7:17 Wavu wa mikufu iliyosokotewa kwenye zile taji juu ya zile nguzo, saba kwa kila taji.
1KI 7:18 Akatengeneza makomamanga katika safu mbili kuzunguka kila wavu kuremba mataji yaliyo juu ya nguzo. Alifanya hivyo kwa kila nguzo.
1KI 7:19 Mataji yaliyokuwa juu ya nguzo kwenye baraza, yalikuwa katika umbo la yungiyungi, kimo chake ni dhiraa nne.
1KI 7:20 Juu ya mataji ya zile nguzo mbili, juu ya ile sehemu yenye umbo kama bakuli, karibu na ule wavu, kulikuwa na yale makomamanga mia mbili katika safu kuzunguka pande zote.
1KI 7:21 Hiramu akazisimamisha zile nguzo barazani pa Hekalu. Nguzo iliyokuwa upande wa kusini akaiita Yakini, na ile ya upande wa kaskazini akaiita Boazi.
1KI 7:22 Mataji yaliyokuwa juu yalikuwa na umbo la yungiyungi. Hivyo kazi ya nguzo ikakamilika.
1KI 7:23 Hiramu akasubu Bahari ya chuma, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo, na kimo cha dhiraa tano. Mzunguko wake ulikuwa dhiraa thelathini.
1KI 7:24 Chini ya ukingo, ilizungukwa na mapambo ya maboga kumi kwa kila dhiraa. Maboga hayo yalikuwa yamesubiwa katika safu mbili ili kuwa kitu kimoja na hiyo Bahari.
1KI 7:25 Ile Bahari iliwekwa juu ya mafahali kumi na wawili, watatu wakielekea kaskazini, watatu wakielekea magharibi, watatu wakielekea kusini, na watatu wakielekea mashariki. Hiyo Bahari iliwekwa juu yao, na sehemu zao za nyuma zilielekeana.
1KI 7:26 Bahari hiyo ilikuwa na unene wa nyanda moja, na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi lililochanua; nayo ingejazwa na bathi elfu mbili.
1KI 7:27 Pia akatengeneza vitako kumi vya shaba vinavyoweza kuhamishika, kila kimoja kilikuwa na urefu wa dhiraa nne, upana dhiraa nne na kimo chake dhiraa tatu.
1KI 7:28 Hivi ndivyo vile vitako vilivyotengenezwa: Vilikuwa na mbao za pembeni zilizounganishwa na mihimili.
1KI 7:29 Juu ya mbao kati ya hiyo mihimili kulikuwa na simba, mafahali na makerubi, pia kwenye mihimili yake. Juu na chini ya simba na mafahali kulikuwa na shada za maua yaliyofuliwa.
1KI 7:30 Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya kuyazungusha. Kila kitako kilikuwa na sinia iliyowekwa juu ya vishikizo vinne viliyosubiwa shada za maua kila upande.
1KI 7:31 Ndani ya kitako kulikuwa na nafasi ya wazi iliyokuwa na umbile la mviringo lenye kina cha dhiraa moja. Nafasi hii ya wazi ilikuwa ya mviringo, pamoja na kitako chake ilikuwa dhiraa moja na nusu. Kuzunguka huo mdomo wake kulitiwa nakshi. Papi za vitako zilikuwa mraba na si za mviringo.
1KI 7:32 Yale magurudumu manne yalikuwa chini ya papi, na vyuma vya kuyazungushia viliunganishwa kwenye kitako. Kipenyo cha kila gurudumu kilikuwa dhiraa moja na nusu.
1KI 7:33 Magurudumu hayo yalitengenezwa kama ya magari ya kukokotwa na farasi; vyuma vya kuzungushia magurudumu, duara zake, matindi yake na vitovu vyake, vyote vilikuwa vya kusubu.
1KI 7:34 Kila kitako kilikuwa na mikono minne, moja kwenye kila pembe, ukichomoza kutoka kile kitako.
1KI 7:35 Juu ya kitako kulikuwa na utepe wa mviringo wenye kina cha nusu dhiraa. Vishikio na papi vilishikamana upande wa juu wa kitako.
1KI 7:36 Aliweka nakshi za makerubi, simba na mitende juu ya vishikio na juu ya papi, katika kila nafasi, na shada za maua kuzunguka.
1KI 7:37 Hivi ndivyo Hiramu alivyotengeneza vile vitako kumi. Vyote vilisubiwa kwenye kalibu moja na vilifanana kwa vipimo na kwa umbo.
1KI 7:38 Kisha akatengeneza masinia kumi ya shaba, kila moja likiwa na ujazo wa bathi arobaini, yakiwa na kipenyo cha dhiraa nne kila sinia moja kwa kila kimoja cha vile vitako kumi.
1KI 7:39 Aliweka vitako vitano upande wa kusini wa Hekalu na vingine vitano upande wa kaskazini. Akaweka ile Bahari upande wa kusini, katika pembe ya kusini-mashariki ya Hekalu.
1KI 7:40 Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi zote katika Hekalu la Mwenyezi Mungu kama vile Mfalme Sulemani alikuwa amemwagiza:
1KI 7:41 nguzo mbili; mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo; nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo;
1KI 7:42 makomamanga mia nne kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo);
1KI 7:43 vitako kumi pamoja na masinia yake kumi;
1KI 7:44 ile Bahari ya chuma na wale mafahali kumi na wawili chini yake;
1KI 7:45 masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Vyombo hivi vyote ambavyo Huramu alimtengenezea Mfalme Sulemani kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu vilikuwa vya shaba iliyong’arishwa.
1KI 7:46 Mfalme akaamuru wavisubu katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani ulio kati ya Sukothi na Sarethani.
1KI 7:47 Sulemani hakupima vitu hivi vyote kwa sababu vilikuwa vingi sana; hivyo, uzani wa shaba haukukadiriwa.
1KI 7:48 Sulemani pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu: madhabahu ya dhahabu; meza ya dhahabu za kuweka mikate ya Wonesho;
1KI 7:49 vinara vya taa vya dhahabu safi (vitano upande wa kuume na vitano upande wa kushoto, mbele ya mahali patakatifu); shada za maua, na taa, na makoleo, vyote vikiwa vya dhahabu;
1KI 7:50 vyombo vya dhahabu safi: masinia, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, vyano na vyetezo; na bawaba za dhahabu kwa ajili ya milango ya chumba cha ndani sana, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na pia kwa ajili ya milango ya ukumbi mkuu wa Hekalu.
1KI 7:51 Hivyo, Mfalme Sulemani alipomaliza kazi zote za Hekalu la Mwenyezi Mungu, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1KI 8:1 Kisha Mfalme Sulemani akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Sayuni, Mji wa Daudi.
1KI 8:2 Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Sulemani wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.
1KI 8:3 Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakajitwika lile Sanduku,
1KI 8:4 nao wakalipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, na Hema la Kukutania, pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba,
1KI 8:5 naye Mfalme Sulemani na kusanyiko lote la Israeli waliokuwa wamemzunguka wakasimama mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu za kondoo na ng’ombe nyingi kiasi kwamba idadi yao haikuweza kuandikwa au kuhesabika.
1KI 8:6 Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu hadi mahali pake ndani ya mahali patakatifu sana humo Hekaluni, ndipo Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi.
1KI 8:7 Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea.
1KI 8:8 Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilionekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo.
1KI 8:9 Ndani ya Sanduku hapakuwa na kitu kingine isipokuwa vile vibao viwili vya mawe ambavyo Musa aliviweka ndani yake huko Horebu, mahali Mwenyezi Mungu alipofanya agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
1KI 8:10 Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1KI 8:11 Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulijaza Hekalu lake.
1KI 8:12 Ndipo Sulemani akasema, “Mwenyezi Mungu alisema kwamba ataishi katika giza nene;
1KI 8:13 naam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.”
1KI 8:14 Kusanyiko lote la Israeli walipokuwa wamesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki.
1KI 8:15 Kisha akasema: “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema,
1KI 8:16 ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo na Jina langu liwe humo, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’
1KI 8:17 “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
1KI 8:18 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako.
1KI 8:19 Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni mwili wako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’
1KI 8:20 “Mwenyezi Mungu ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu, na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
1KI 8:21 Nimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuna lile Agano la Mwenyezi Mungu alilofanya na baba zetu alipowatoa Misri.”
1KI 8:22 Kisha Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu machoni pa kusanyiko lote la Israeli, akanyoosha mikono yake kuelekea mbinguni,
1KI 8:23 na kusema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote.
1KI 8:24 Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.
1KI 8:25 “Sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, ikiwa wanao watakuwa waangalifu kwa yote wayafanyayo ili kuenenda mbele zangu kama ulivyofanya.’
1KI 8:26 Sasa, Ee Mungu wa Israeli, ruhusu neno lako ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie.
1KI 8:27 “Je, hakika Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga!
1KI 8:28 Hata hivyo, sikiliza dua la mtumishi wako na maombi yake ya kuhurumiwa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambalo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo.
1KI 8:29 Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwa humo,’ ili upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa.
1KI 8:30 Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia ukiwa mbinguni, makao yako, na unaposikia, samehe.
1KI 8:31 “Mtu akimkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili,
1KI 8:32 basi, sikia ukiwa mbinguni, ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimhukumu yule mwenye hatia na kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake.
1KI 8:33 “Watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, nao wakakugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili,
1KI 8:34 basi usikie ukiwa mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.
1KI 8:35 “Mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu,
1KI 8:36 basi usikie ukiwa mbinguni, usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi, na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.
1KI 8:37 “Njaa au tauni itakapotokea katika nchi, koga au ukungu, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia,
1KI 8:38 kila dua au ombi litakalotolewa na yeyote kati ya watu wako Israeli, akitambua taabu za moyo wake mwenyewe, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili,
1KI 8:39 basi usikie ukiwa mbinguni, makao yako. Usamehe na utende; umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote),
1KI 8:40 ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
1KI 8:41 “Kuhusu mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako,
1KI 8:42 kwa maana watu watasikia kuhusu Jina lako kuu na kuhusu mkono wako wenye nguvu na mkono wako ulionyooshwa, atakapokuja na kuomba kuelekea Hekalu hili,
1KI 8:43 basi na usikie ukiwa mbinguni, makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli, na pia wapate kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.
1KI 8:44 “Watu wako watakapoenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa Mwenyezi Mungu kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako,
1KI 8:45 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, ukawape haki yao.
1KI 8:46 “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu;
1KI 8:47 na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowashinda na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda uovu’;
1KI 8:48 wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako;
1KI 8:49 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, makao yako, ukawape haki yao.
1KI 8:50 Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako; uwasamehe makosa yote waliyoyatenda dhidi yako, na ukawafanye wale waliowashinda kuwaonea huruma;
1KI 8:51 kwa maana ni watu wako na urithi wako, uliowatoa Misri, kutoka lile tanuru la kuyeyushia chuma.
1KI 8:52 “Macho yako na yafumbuke kwa ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako Israeli, nawe uwasikilize wakati wowote wanapokulilia.
1KI 8:53 Kwa maana uliwachagua kati ya mataifa yote ya ulimwengu wawe urithi wako mwenyewe, kama ulivyotangaza kupitia mtumishi wako Musa wakati wewe, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, ulipowatoa baba zetu kutoka Misri.”
1KI 8:54 Sulemani alipomaliza dua na maombi haya yote kwa Mwenyezi Mungu, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiwa amenyoosha mikono yake kuelekea mbinguni.
1KI 8:55 Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa, akisema:
1KI 8:56 “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Musa.
1KI 8:57 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa.
1KI 8:58 Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kushika amri, maagizo, na masharti aliyowapa baba zetu.
1KI 8:59 Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za Mwenyezi Mungu, yawe karibu na Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, usiku na mchana, ili awape haki mtumishi wake na watu wake Israeli, kulingana na mahitaji yao ya kila siku,
1KI 8:60 ili mataifa yote ya dunia wajue kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine.
1KI 8:61 Lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mwishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.”
1KI 8:62 Kisha mfalme na Waisraeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu.
1KI 8:63 Sulemani akatoa dhabihu sadaka za amani kwa Mwenyezi Mungu: ng’ombe elfu ishirini na mbili, pamoja na kondoo na mbuzi elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na Waisraeli wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1KI 8:64 Siku hiyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za Mwenyezi Mungu ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani.
1KI 8:65 Hivyo Sulemani akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Waisraeli wote pamoja naye: walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Wakaiadhimisha mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani jumla siku kumi na nne.
1KI 8:66 Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani wakiwa na mashangilio na furaha moyoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo Mwenyezi Mungu alimtendea kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.
1KI 9:1 Sulemani alipomaliza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme, na alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya,
1KI 9:2 Mwenyezi Mungu akamtokea mara ya pili, vile alivyomtokea huko Gibeoni.
1KI 9:3 Mwenyezi Mungu akamwambia: “Nimesikia dua na maombi uliyofanya mbele zangu, nimeliweka wakfu Hekalu hili ambalo umelijenga, kwa kuweka Jina langu humo milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwa humo siku zote.
1KI 9:4 “Kwako wewe, kama ukienenda kwa unyofu wa moyo na uadilifu, kama baba yako Daudi alivyofanya na kutenda yote ninayoyaagiza kwa kutunza maagizo yangu na sheria,
1KI 9:5 nitakiimarisha kiti chako cha utawala juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe kuwa na mtu kwenye kiti cha utawala cha Israeli.’
1KI 9:6 “Lakini ninyi au wana wenu mkinigeukia mbali na kuziacha amri na maagizo yangu niliyowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
1KI 9:7 basi nitakatilia mbali Israeli kutoka nchi niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Ndipo Israeli itakuwa kitu cha kudharauliwa na watu na kuwa kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote.
1KI 9:8 Ingawa hekalu hili linavutia sasa, wote watakaolipita watashangaa na kudhihaki wakisema, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’
1KI 9:9 Watu watajibu, ‘Kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyewatoa baba zao Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu Mwenyezi Mungu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”
1KI 9:10 Miaka ishirini ilipopita, muda ambao Sulemani alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme,
1KI 9:11 Mfalme Sulemani akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi na misunobari yote na dhahabu yote kama alivyohitaji.
1KI 9:12 Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Sulemani alikuwa amempa, hakupendezwa nayo.
1KI 9:13 Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?” Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo.
1KI 9:14 Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu.
1KI 9:15 Haya ni maelezo kuhusu kazi za kulazimishwa ambazo Mfalme Sulemani aliwafanyiza watu ili kulijenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, na jumba lake la kifalme, na Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri.
1KI 9:16 (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameushambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Sulemani, kama zawadi ya arusi.
1KI 9:17 Sulemani akaujenga tena Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini,
1KI 9:18 akajenga Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake.
1KI 9:19 Vilevile, alijenga miji ya ghala na ya magari yake ya vita na kwa ajili ya farasi wake na wapanda farasi: alijenga kila alichotaka katika Yerusalemu, katika Lebanoni, na katika eneo lote alilotawala.
1KI 9:20 Watu wote waliosalia miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi (watu wasiokuwa Waisraeli),
1KI 9:21 yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwaangamiza kabisa, Sulemani akawalazimisha kuwa shokoa, kama ilivyo hadi leo.
1KI 9:22 Lakini Sulemani hakumfanya Mwisraeli yeyote kuwa mtumwa; hao ndio walikuwa wapiganaji wake, viongozi wa serikali yake, maafisa wake, wakuu wake wa jeshi, majemadari wa magari yake ya vita, na wapanda farasi wake.
1KI 9:23 Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Sulemani: maafisa mia tano na hamsini waliwasimamia watu waliofanya kazi.
1KI 9:24 Baada ya binti Farao kuja kutoka Mji wa Daudi na kuingia jumba la kifalme ambalo Sulemani alikuwa amemjengea, Sulemani akajenga Milo.
1KI 9:25 Sulemani akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani mara tatu kwa mwaka juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi Mungu. Pamoja na hizo dhabihu, akafukiza uvumba mbele za Mwenyezi Mungu, hivyo kutimiza kanuni za Hekalu.
1KI 9:26 Mfalme Sulemani pia akatengeneza meli huko Esion-Geberi, iliyo karibu na Elathi katika Edomu, kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu.
1KI 9:27 Naye Hiramu akawatuma watu wake; mabaharia walioijua bahari, kuhudumu katika hizo meli pamoja na watu wa Sulemani.
1KI 9:28 Wakasafiri kwa bahari hadi Ofiri na kurudi na talanta mia nne na ishirini (420) za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Sulemani.
1KI 10:1 Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Sulemani na uhusiano wake na jina la Mwenyezi Mungu, akaja kumjaribu kwa maswali magumu.
1KI 10:2 Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana wenye ngamia waliobeba vikolezo, dhahabu nyingi, na vito vya thamani. Akaenda kwa Sulemani na kuzungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.
1KI 10:3 Sulemani alimjibu maswali yake yote; hapakuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme hata asiweze kumwelezea.
1KI 10:4 Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na jumba la kifalme alilokuwa amejenga,
1KI 10:5 chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, alipatwa na mshangao mkubwa.
1KI 10:6 Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli.
1KI 10:7 Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia.
1KI 10:8 Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wanaosimama mbele yako daima na kusikia hekima yako!
1KI 10:9 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka kwenye kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake Mwenyezi Mungu wa milele kwa Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.”
1KI 10:10 Naye akampa mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezo na vito vya thamani. Kamwe havijawahi kuletwa tena vikolezo vingi kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Sulemani.
1KI 10:11 (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena zikaleta shehena kubwa ya miti ya msandali, na vito vya thamani kutoka huko.
1KI 10:12 Mfalme alitumia miti ya msandali kutengenezea nguzo za Hekalu la Mwenyezi Mungu na za jumba la kifalme, na kutengenezea vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Miti mingi ya msandali kiasi hicho haijawahi kuletwa au kuonekana tangu wakati ule.)
1KI 10:13 Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
1KI 10:14 Uzito wa dhahabu ambayo Sulemani alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta mia sita sitini na sita (666),
1KI 10:15 mbali na mapato kutoka kwa wafanyabiashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Waarabu na watawala wa nchi.
1KI 10:16 Mfalme Sulemani akatengeneza ngao kubwa mia mbili kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli mia sita.
1KI 10:17 Akatengeneza pia ngao ndogo mia tatu za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.
1KI 10:18 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.
1KI 10:19 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita, na egemeo lenye mviringo juu yake. Kila upande wa kiti ulikuwa na mahali pa kuegemeza mkono, na simba aliyesimama kando kila upande.
1KI 10:20 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kiti kama hicho kiliwahi kutengenezwa katika ufalme mwingine wowote.
1KI 10:21 Vyombo vyote vya Mfalme Sulemani vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo siku za Sulemani.
1KI 10:22 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Mara moja katika kila miaka mitatu zilirudi zikiwa zimebeba dhahabu, fedha na pembe za ndovu, na sokwe na nyani.
1KI 10:23 Mfalme Sulemani alikuwa na utajiri mkubwa na mwenye hekima kuliko wafalme wote wa dunia.
1KI 10:24 Dunia yote ikatafuta kukutana na Sulemani ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake.
1KI 10:25 Kila mwaka, kila mtu aliyekuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezo, farasi na nyumbu.
1KI 10:26 Sulemani alikusanya magari ya vita na farasi. Akawa na magari ya vita elfu moja mia nne, na farasi elfu kumi na mbili, ambayo aliyaweka katika miji ya magari ya vita, na mengine akawa nayo huko Yerusalemu.
1KI 10:27 Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima.
1KI 10:28 Farasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue.
1KI 10:29 Walinunua magari ya vita kutoka Misri kwa shekeli mia sita za fedha kila moja, na kila farasi kwa shekeli mia moja na hamsini; na wakawauzia wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu.
1KI 11:1 Mbali na binti Farao, Mfalme Sulemani aliwapenda wanawake wengi wa kigeni: Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti.
1KI 11:2 Walitoka katika mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Sulemani akakaza kuwapenda.
1KI 11:3 Alikuwa na wake mia saba, binti za uzao wa kifalme, na masuria mia tatu; nao wake zake wakampotosha.
1KI 11:4 Kadiri Sulemani alivyozidi kuzeeka, wake zake wakaugeuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukujitoa kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake.
1KI 11:5 Sulemani akafuata Ashtorethi, mungu wa kike wa Wasidoni, na Moleki mungu wa Waamoni, aliyekuwa chukizo.
1KI 11:6 Kwa hiyo Sulemani akafanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu; hakumfuata Mwenyezi Mungu kikamilifu kama alivyofanya Daudi baba yake.
1KI 11:7 Kwenye kilima mashariki mwa Yerusalemu, Sulemani alijenga mahali pa juu pa kuabudia Kemoshi mungu wa Wamoabu, aliyekuwa chukizo, na pa kuabudia Moleki mungu wa Waamoni, aliyekuwa chukizo.
1KI 11:8 Akafanya vivyo hivyo kwa wake zake wote wa kigeni, ambao walifukiza uvumba na kutoa dhabihu kwa miungu yao.
1KI 11:9 Mwenyezi Mungu akamkasirikia Sulemani kwa sababu moyo wake uligeuka mbali na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekuwa amemtokea mara mbili.
1KI 11:10 Ingawa alikuwa amemkataza Sulemani kufuata miungu mingine, Sulemani hakutii amri ya Mwenyezi Mungu.
1KI 11:11 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamwambia Sulemani, “Kwa kuwa huu ndio msimamo wako, na hukushika agano langu na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitakunyang’anya ufalme na kumpa mmoja wa walio chini yako.
1KI 11:12 Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi baba yako, sitafanya jambo hili wakati wa uhai wako. Nitaurarua kutoka mikononi mwa mwanao.
1KI 11:13 Lakini pia sitaurarua ufalme wote kutoka kwake, bali nitampa kabila moja kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu na kwa ajili ya Yerusalemu, ambao nimeuchagua.”
1KI 11:14 Kisha Mwenyezi Mungu akamwinua adui dhidi ya Sulemani, Hadadi, Mwedomu, kutoka ukoo wa ufalme wa Edomu.
1KI 11:15 Hapo awali Daudi alipokuwa akipigana na Edomu, Yoabu jemadari wa jeshi, aliyekuwa ameenda kuzika waliouawa, alikuwa amewaua wanaume wote katika Edomu.
1KI 11:16 Yoabu na Waisraeli wote walikaa huko kwa miezi sita, hadi walipomaliza kuwaangamiza wanaume wote huko Edomu.
1KI 11:17 Lakini Hadadi, akiwa bado mvulana mdogo, alikimbilia Misri akiwa na baadhi ya maafisa wa Edomu waliokuwa wamemhudumia baba yake.
1KI 11:18 Wakatoka Midiani wakaenda hadi Parani. Wakawachukua watu kutoka Parani, wakaenda nao Misri kwa Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimpa Hadadi nyumba na shamba, na pia chakula.
1KI 11:19 Farao akapendezwa sana na Hadadi, hata akampa dada ya mkewe, Malkia Tapenesi, awe mke wake.
1KI 11:20 Huyo dada yake Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi, ambaye alilelewa na Tapenesi katika jumba la kifalme. Huko, Genubathi akaishi pamoja na watoto wa Farao.
1KI 11:21 Alipokuwa huko Misri, Hadadi alisikia kwamba Daudi amelala na baba zake, na kwamba Yoabu aliyekuwa jemadari wa jeshi pia amekufa. Ndipo Hadadi akamwambia Farao, “Niruhusu niende ili nirudi nchi yangu.”
1KI 11:22 Farao akauliza, “Umekosa nini hapa, kwamba unataka kurudi katika nchi yako?” Hadadi akajibu, “Hakuna, lakini niruhusu niende!”
1KI 11:23 Mungu akamwinua adui mwingine dhidi ya Sulemani, Rezoni mwana wa Eliada, aliyekuwa amemkimbia bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba.
1KI 11:24 Akawakusanya watu, naye akawa kiongozi wa kundi la waasi, wakati Daudi alipoangamiza majeshi ya Soba; waasi walienda Dameski, mahali walipokaa na kumiliki.
1KI 11:25 Rezoni alikuwa adui wa Israeli kwa muda wote alioishi Sulemani, kuongezea matatizo yaliyosababishwa na Hadadi. Kwa hiyo Rezoni akatawala katika Aramu na akawa mkatili kwa Israeli.
1KI 11:26 Pia, Yeroboamu mwana wa Nebati aliasi dhidi ya mfalme. Alikuwa mmoja wa maafisa wa Sulemani, Mwefraimu kutoka Sereda, ambaye mama yake alikuwa mjane aliyeitwa Serua.
1KI 11:27 Haya ndio maelezo ya jinsi alivyomwasi mfalme: Sulemani alikuwa amejenga Milo naye akawa ameziba mwanya katika ukuta wa mji wa Daudi baba yake.
1KI 11:28 Basi Yeroboamu alikuwa mtu mwenye nguvu na hodari; naye Sulemani alipoona jinsi kijana alivyofanya kazi yake, akamweka kuwa kiongozi wa kazi yote ya mikono ya nyumba ya Yusufu.
1KI 11:29 Karibu na wakati ule Yeroboamu alikuwa anatoka nje ya Yerusalemu, Ahiya nabii Mshiloni akakutana naye njiani, akiwa amevaa joho jipya. Hawa wawili walikuwa peke yao mashambani,
1KI 11:30 naye Ahiya akachukua joho jipya alilokuwa amevaa akalirarua vipande kumi na viwili.
1KI 11:31 Kisha akamwambia Yeroboamu, “Jichukulie vipande kumi, kwa kuwa hivi ndivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemavyo: ‘Tazama, ninaenda kumnyang’anya Sulemani ufalme na kukupa makabila kumi.
1KI 11:32 Lakini kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi na mji wa Yerusalemu, ambao nimeuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli, atakuwa na kabila moja.
1KI 11:33 Nitafanya haya kwa sababu wameniacha na kuabudu Ashtorethi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi mungu wa Wamoabu, na Moleki mungu wa Waamoni, nao hawakuenda katika njia zangu wala kufanya yaliyo sawa machoni pangu, wala kushika amri na sheria zangu kama Daudi, babaye Sulemani, alivyofanya.
1KI 11:34 “ ‘Lakini sitauondoa ufalme wote mkononi mwa Sulemani; nimemfanya mtawala siku zote za maisha yake kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, niliyemchagua na ambaye aliyatunza maagizo na amri zangu.
1KI 11:35 Nitauondoa ufalme kutoka mikononi mwa mwanawe na kukupa wewe makabila kumi.
1KI 11:36 Nitampa mwanawe kabila moja ili Daudi mtumishi wangu awe na taa mbele zangu daima katika Yerusalemu, mji ambao nimeuchagua kuweka Jina langu.
1KI 11:37 Lakini wewe, Yeroboamu, nitakutwaa, nawe utatawala yale yote moyo wako unayotamani; utakuwa mfalme wa Israeli.
1KI 11:38 Ikiwa utafanya kila nitakalokuamuru, kuenenda katika njia zangu na kufanya yaliyo sawa mbele za macho yangu kwa kushika amri zangu na maagizo yangu kama alivyofanya Daudi mtumishi wangu, nitakuwa pamoja nawe. Nitakujengea ufalme utakaodumu kama ule niliomjengea Daudi, nami nitakupa Israeli.
1KI 11:39 Nitawatesa wazao wa Daudi kwa ajili ya haya, lakini siyo milele.’ ”
1KI 11:40 Sulemani akajaribu kumuua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akakimbilia Misri, kwa Mfalme Shishaki, naye akakaa huko hadi Sulemani alipofariki.
1KI 11:41 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Sulemani, yote aliyoyafanya na hekima aliyoionesha, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za Sulemani?
1KI 11:42 Sulemani alitawala Israeli yote miaka arobaini, akiwa Yerusalemu.
1KI 11:43 Kisha Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 12:1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wameenda huko kumfanya mfalme.
1KI 12:2 Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Sulemani), akarudi kutoka Misri.
1KI 12:3 Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu; yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia,
1KI 12:4 “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”
1KI 12:5 Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.
1KI 12:6 Kisha Mfalme Rehoboamu akataka ushauri kwa wazee ambao walimtumikia Sulemani baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri niwajibu nini watu hawa?”
1KI 12:7 Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”
1KI 12:8 Lakini Rehoboamu akakataa ushauri aliopewa na wazee, na akataka ushauri kwa vijana wa rika lake waliokuwa wakimtumikia.
1KI 12:9 Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu’?”
1KI 12:10 Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Watu hawa walikuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi.’ Wewe waambie, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.
1KI 12:11 Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.’ ”
1KI 12:12 Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.”
1KI 12:13 Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Alikataa ushauri alilopewa na wazee,
1KI 12:14 akafuata ushauri wa vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.”
1KI 12:15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kutimiza neno ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amenena na Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia kwa Ahiya Mshiloni.
1KI 12:16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme: “Je, tuna fungu gani kwa Daudi? Tuna urithi gani kwa mwana wa Yese? Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli! Angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!” Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao.
1KI 12:17 Lakini kwa habari ya Waisraeli walioishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.
1KI 12:18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu, akafanikiwa kuingia kwenye gari lake la vita na kutorokea Yerusalemu.
1KI 12:19 Hivyo, Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.
1KI 12:20 Waisraeli wote waliposikia kwamba Yeroboamu amerudi, wakatuma watu na kumwita kwenye kusanyiko na kumfanya mfalme juu ya Israeli yote. Ni kabila la Yuda peke yake lililobaki kuwa tiifu kwa nyumba ya Daudi.
1KI 12:21 Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda na kabila la Benyamini, vijana wenye uwezo elfu mia moja na themanini, ili kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani.
1KI 12:22 Lakini neno la Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu:
1KI 12:23 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na nyumba yote ya Yuda na Benyamini, na watu wengine wote,
1KI 12:24 ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu, Waisraeli. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Mwenyezi Mungu na kurudi nyumbani, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameagiza.
1KI 12:25 Kisha Yeroboamu akaimarisha Shekemu, na kuuzungushia ngome katika nchi ya vilima ya Efraimu, na akaishi huko. Kutoka huko, akaenda akajenga Penueli.
1KI 12:26 Yeroboamu akawaza moyoni mwake, “Kuna uwezekano wa ufalme kurudia nyumba ya Daudi.
1KI 12:27 Kama watu hawa watapanda kwenda kutoa dhabihu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu, mioyo yao itamrudia bwana wao, Rehoboamu mfalme wa Yuda. Wataniua mimi na kurudi kwa Mfalme Rehoboamu.”
1KI 12:28 Baada ya kutafuta ushauri, mfalme akatengeneza ndama wawili wa dhahabu. Akawaambia watu, “Ni gharama kubwa kwenu kukwea kwenda Yerusalemu. Hii hapa miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”
1KI 12:29 Ndama mmoja akamweka Betheli, na mwingine akamweka Dani.
1KI 12:30 Nalo jambo hili likawa dhambi, watu wakawa wanaenda hadi Dani kumwabudu huyo aliyewekwa huko.
1KI 12:31 Yeroboamu akajenga nyumba za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia, na kuwateua makuhani kutoka watu wa aina zote, ijapokuwa hawakuwa Walawi.
1KI 12:32 Pia Yeroboamu akaanzisha sikukuu katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, kama sikukuu iliyokuwa ikifanyika huko Yuda, na akatoa dhabihu juu ya madhabahu. Haya aliyafanya huko Betheli, akitoa dhabihu kwa ndama alizotengeneza. Huko Betheli akawaweka makuhani katika mahali pa juu pa kuabudia miungu aliyotengeneza.
1KI 12:33 Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouchagua mwenyewe, alitoa dhabihu juu ya madhabahu aliyokuwa amejenga huko Betheli. Kwa hiyo akaanzisha sikukuu kwa ajili ya Waisraeli, na akapanda madhabahuni kutoa sadaka.
1KI 13:1 Kwa neno la Mwenyezi Mungu, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka.
1KI 13:2 Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la Mwenyezi Mungu: “Ee madhabahu, ee madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia ambao hutoa sadaka hapa, nayo mifupa ya wanadamu itateketezwa juu yako.’ ”
1KI 13:3 Siku hiyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Mwenyezi Mungu aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”
1KI 13:4 Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamateni!” Lakini mkono aliounyoosha kumwelekea yule mtu ukakauka kiasi kwamba hakuweza kuurudisha.
1KI 13:5 Pia, madhabahu yakapasuka na majivu yakamwagika, sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Mwenyezi Mungu.
1KI 13:6 Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Mwenyezi Mungu, nao mkono wa mfalme ukapona na kurudi ulivyokuwa hapo awali.
1KI 13:7 Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani mwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”
1KI 13:8 Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali yako, nisingeenda pamoja nawe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa.
1KI 13:9 Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la Mwenyezi Mungu: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ”
1KI 13:10 Hivyo, akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia aliyokuwa ameijia Betheli.
1KI 13:11 Basi kulikuwa na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme.
1KI 13:12 Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita.
1KI 13:13 Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda
1KI 13:14 na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na kumuuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?” Akamjibu, “Mimi ndiye.”
1KI 13:15 Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi, ule.”
1KI 13:16 Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa.
1KI 13:17 Nimeambiwa kwa neno la Mwenyezi Mungu: ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’ ”
1KI 13:18 Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno la Mwenyezi Mungu: ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’ ” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.)
1KI 13:19 Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.
1KI 13:20 Walipokuwa wameketi mezani, neno la Mwenyezi Mungu likamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu.
1KI 13:21 Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Umeasi neno la Mwenyezi Mungu na hukushika amri uliyopewa na Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
1KI 13:22 Ulirudi, ukala mkate na kunywa maji mahali alipokuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’ ”
1KI 13:23 Huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake.
1KI 13:24 Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, huku punda wake na simba wakiwa wamesimama kando yake.
1KI 13:25 Watu waliopita pale, waliona maiti iliyokuwa imebwagwa, simba akiwa amesimama kando yake. Nao wakaenda kutoa habari katika mji ambao nabii mzee alikuwa anaishi.
1KI 13:26 Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu aliyeliasi neno la Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu lilivyokuwa limemwonya.”
1KI 13:27 Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo.
1KI 13:28 Akaondoka na akakuta maiti imetupwa barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda.
1KI 13:29 Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika.
1KI 13:30 Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”
1KI 13:31 Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.
1KI 13:32 Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Mwenyezi Mungu dhidi ya madhabahu huko Betheli, na dhidi ya nyumba zote za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia ndani ya miji ya Samaria, hakika utatimia.”
1KI 13:33 Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia kutoka watu wa aina zote. Yeyote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia.
1KI 13:34 Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.
1KI 14:1 Wakati ule, Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua,
1KI 14:2 naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme wa watu hawa, yuko huko.
1KI 14:3 Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.”
1KI 14:4 Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama mumewe alivyosema, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo. Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake.
1KI 14:5 Lakini Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.”
1KI 14:6 Hivyo, Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini unajifanya kuwa si wewe? Nimetumwa kwako kukupa habari mbaya.
1KI 14:7 Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli.
1KI 14:8 Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu.
1KI 14:9 Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunigeuka.
1KI 14:10 “ ‘Kwa sababu hii, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu hadi iteketee yote kama mtu anavyochoma kinyesi.
1KI 14:11 Mbwa watawala walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani. Mwenyezi Mungu amenena!’
1KI 14:12 “Lakini wewe, rudi nyumbani. Utakapofika mji wako, kijana atakufa.
1KI 14:13 Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye tu ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambaye Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ameona kitu chema kwake.
1KI 14:14 “Mwenyezi Mungu atajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku hiyo itakuwa lini? Hata sasa yameanza kutokea.
1KI 14:15 Naye Mwenyezi Mungu ataipiga Israeli, hata iwe kama mwanzi unaoyumbayumba kwenye maji. Ataing’oa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ng’ambo ya Mto, kwa sababu wamemghadhibisha Mwenyezi Mungu kwa kutengeneza nguzo za Ashera.
1KI 14:16 Naye atawaacha Israeli kwa sababu ya dhambi Yeroboamu alizozitenda na kuisababisha Israeli kuzitenda.”
1KI 14:17 Kisha, mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirsa. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa.
1KI 14:18 Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema kupitia kwa mtumishi wake, nabii Ahiya.
1KI 14:19 Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
1KI 14:20 Yeroboamu akawatawala kwa miaka ishirini na mbili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 14:21 Rehoboamu mwana wa Sulemani alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kuwa mfalme, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi Mungu alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni.
1KI 14:22 Yuda wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu kuliko baba zao walivyofanya.
1KI 14:23 Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia, mawe ya kuabudiwa, na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda.
1KI 14:24 Kulikuwa na hata mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi. Watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli.
1KI 14:25 Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu.
1KI 14:26 Akachukua hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza.
1KI 14:27 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme.
1KI 14:28 Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.
1KI 14:29 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
1KI 14:30 Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.
1KI 14:31 Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama; alikuwa Mwamoni. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 15:1 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya akawa mfalme wa Yuda,
1KI 15:2 naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka binti Abishalomu.
1KI 15:3 Alitenda dhambi zote baba yake alizotenda kabla yake; moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake ulivyokuwa.
1KI 15:4 Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi, Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akampa taa katika Yerusalemu kwa kumwinua mwana atawale baada yake ili kuifanya Yerusalemu kuwa imara.
1KI 15:5 Kwa kuwa Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, wala hakushindwa kuzishika amri zote za Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yake, isipokuwa kwa suala la Uria, Mhiti.
1KI 15:6 Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote wa maisha ya Abiya.
1KI 15:7 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Abiya na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.
1KI 15:8 Naye Abiya akalala na baba zake akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 15:9 Katika mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa akawa mfalme wa Yuda,
1KI 15:10 naye akatawala katika Yerusalemu miaka arobaini na moja. Bibi yake aliitwa Maaka binti Abishalomu.
1KI 15:11 Asa akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama alivyokuwa ametenda Daudi, baba yake.
1KI 15:12 Akawafukuza mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu kutoka nchi, na kuondoa sanamu zote ambazo baba zake walikuwa wametengeneza.
1KI 15:13 Hata akamwondoa bibi yake Maaka kwenye wadhifa wake kama mama malkia, kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni.
1KI 15:14 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Mwenyezi Mungu kikamilifu maisha yake yote.
1KI 15:15 Akaleta ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu fedha na dhahabu na vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.
1KI 15:16 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha, mfalme wa Israeli siku zote za utawala wao.
1KI 15:17 Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome katika mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia katika nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.
1KI 15:18 Kisha Asa akachukua fedha yote na dhahabu zilizokuwa zimeachwa katika hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika jumba lake la kifalme. Kisha akawakabidhi maafisa wake na kuwatuma kwa Ben-Hadadi mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Aramu, aliyekuwa akitawala Dameski.
1KI 15:19 Akasema, “Na tufanye mkataba kati yangu na wewe, kama ilivyokuwa kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea zawadi ya fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha, mfalme wa Israeli ili aniondokee.”
1KI 15:20 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Akaishinda miji ya Iyoni, Dani, Abel-Beth-Maaka na Kinerethi yote, pamoja na Naftali.
1KI 15:21 Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha ujenzi wa Rama, akaenda kuishi Tirsa.
1KI 15:22 Kisha Mfalme Asa akatoa amri kwa Yuda yote, pasipo kumwacha hata mmoja, kubeba mawe na mbao kutoka Rama, ambazo Baasha alikuwa akizitumia huko. Mfalme Asa akazitumia kujengea Geba iliyo Benyamini na Mispa.
1KI 15:23 Kwa matukio yote ya utawala wa Asa, mafanikio yake yote, yote aliyofanya na miji aliyoijenga, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Hata hivyo, katika uzee wake alishikwa na ugonjwa wa miguu.
1KI 15:24 Kisha Asa akalala na baba zake, naye akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 15:25 Nadabu mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika mwaka wa pili wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, naye akatawala Israeli kwa miaka miwili.
1KI 15:26 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akienenda katika njia za baba yake na katika dhambi yake, aliyoisababisha Israeli kutenda.
1KI 15:27 Baasha mwana wa Ahiya wa nyumba ya Isakari akapanga njama dhidi ya Nadabu, naye akamuua huko Gibethoni, mji wa Wafilisti, wakati Nadabu na Israeli yote walikuwa wameuzingira.
1KI 15:28 Baasha akamuua Nadabu katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, naye Baasha akawa mfalme baada yake.
1KI 15:29 Mara tu alipoanza kutawala, aliwaua watu wote wa nyumba ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu hata mtu mmoja akiwa hai, bali aliwaangamiza wote, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu kupitia kwa mtumishi wake Ahiya Mshiloni.
1KI 15:30 Haya yalitendeka kwa sababu ya dhambi alizozitenda Yeroboamu, zilizosababisha Israeli kutenda dhambi, na kwa sababu alimkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
1KI 15:31 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Nadabu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
1KI 15:32 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli wakati wote wa utawala wao.
1KI 15:33 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya akawa mfalme wa Israeli yote huko Tirsa, naye akatawala kwa miaka ishirini na nne.
1KI 15:34 Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akienenda katika njia ya Yeroboamu na dhambi yake, aliyosababisha Israeli kuitenda.
1KI 16:1 21 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yehu mwana wa Hanani dhidi ya Baasha, kusema:
1KI 16:2 “Nilikuinua kutoka mavumbini na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli, lakini ukaenenda katika njia za Yeroboamu na kusababisha watu wangu Israeli kutenda dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao.
1KI 16:3 Basi nitamwangamiza Baasha pamoja na nyumba yake, nami nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwanawe Nebati.
1KI 16:4 Mbwa watawala walio wa nyumba ya Baasha watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani.”
1KI 16:5 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Baasha, aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
1KI 16:6 Baasha akalala na baba zake naye akazikwa huko Tirsa. Naye Ela mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 16:7 Zaidi ya hayo, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Baasha pamoja na nyumba yake kupitia kwa nabii Yehu mwana wa Hanani, kwa sababu ya maovu yote aliyokuwa ametenda machoni pa Mwenyezi Mungu, akimkasirisha kwa mambo aliyotenda, na kuwa kama nyumba ya Yeroboamu aliyoiangamiza.
1KI 16:8 Katika mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala huko Tirsa kwa miaka miwili.
1KI 16:9 Zimri, mmoja wa maafisa wake, aliyekuwa na amri juu ya nusu ya magari yake ya vita, akapanga njama dhidi ya Ela. Wakati huo Ela alikuwa Tirsa, akilewa katika nyumba ya Arsa, aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme huko Tirsa.
1KI 16:10 Zimri akaingia, akampiga na kumuua katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Kisha Zimri akawa mfalme baada yake.
1KI 16:11 Mara tu alipoanza kutawala na kukalia kiti chake cha kifalme, aliua jamaa yote ya Baasha. Hakumwacha mwanaume hata mmoja, akiwa ni ndugu au rafiki.
1KI 16:12 Hivyo, Zimri akawaangamiza jamaa yote ya Baasha, kama Mwenyezi Mungu alivyonena dhidi ya Baasha kupitia kwa nabii Yehu:
1KI 16:13 kwa sababu ya dhambi zote Baasha na mwanawe Ela walizokuwa wametenda na wakasababisha Israeli kuzitenda, basi wakamkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili.
1KI 16:14 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ela, na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
1KI 16:15 Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala huko Tirsa siku saba. Jeshi lilikuwa limepiga kambi karibu na Gibethoni, mji wa Wafilisti.
1KI 16:16 Waisraeli waliokuwa kambini waliposikia kuwa Zimri amepanga njama ya kumuua mfalme, wakamtangaza Omri, jemadari wa jeshi, kuwa mfalme wa Israeli yote siku hiyo hiyo huko kambini.
1KI 16:17 Ndipo Omri na Waisraeli wote pamoja naye wakaondoka Gibethoni na kuizingira Tirsa.
1KI 16:18 Zimri alipoona kuwa mji umechukuliwa, alienda ndani ya ngome ya jumba la kifalme na kulichoma moto hilo jumba na kujiteketeza ndani yake. Kwa hiyo akafa,
1KI 16:19 kwa sababu ya dhambi alizotenda, akifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia za Yeroboamu na katika dhambi alizotenda na kusababisha Israeli kuzifanya.
1KI 16:20 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Zimri, na uasi alioutenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
1KI 16:21 Kisha, watu wa Israeli wakagawanyika katika makundi mawili, nusu wakamuunga mkono Tibni mwana wa Ginathi ili awe mfalme, na nusu nyingine wakamuunga mkono Omri.
1KI 16:22 Lakini wafuasi wa Omri wakajionesha kuwa wenye nguvu kuliko wale wa Tibni, mwana wa Ginathi. Hivyo Tibni akafa, na Omri akawa mfalme.
1KI 16:23 Katika mwaka wa thelathini na moja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala kwa miaka kumi na mbili, sita kati ya hiyo katika Tirsa.
1KI 16:24 Alinunua kilima cha Samaria kutoka kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha na akajenga mji juu ya hicho kilima, akiuita Samaria, kutokana na Shemeri, jina la mmiliki wa kwanza wa kilima hicho.
1KI 16:25 Lakini Omri akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kutenda dhambi kuliko wote waliomtangulia.
1KI 16:26 Akaenenda katika njia zote za Yeroboamu mwana wa Nebati na katika dhambi zake, ambazo alisababisha Israeli kutenda, hivyo basi wakamkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili.
1KI 16:27 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Omri, yale aliyofanya na mafanikio aliyokuwa nayo, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
1KI 16:28 Omri akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Ahabu mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 16:29 Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na mbili.
1KI 16:30 Ahabu mwana wa Omri akafanya maovu zaidi machoni pa Mwenyezi Mungu kuliko yeyote aliyemtangulia.
1KI 16:31 Kama vile haikutosha kuishi kama Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, naye akaanza kumtumikia Baali na kumwabudu.
1KI 16:32 Akatengeneza madhabahu kwa ajili ya Baali katika hekalu la Baali alilolijenga huko Samaria.
1KI 16:33 Pia Ahabu alitengeneza nguzo ya Ashera na kufanya mengi ili kumkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuliko walivyofanya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.
1KI 16:34 Wakati wa Ahabu, Hieli ule Mbetheli, akaijenga Yeriko upya. Aliweka misingi yake kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, na kuweka malango yake kwa gharama ya mwanawe mdogo Segubu, kama Mwenyezi Mungu alivyonena kupitia kwa Yoshua, mwana wa Nuni.
1KI 17:1 Basi Ilya Mtishbi, kutoka Tishbi katika Gileadi, akamwambia Ahabu, “Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli ninayemtumikia, aishivyo, hapatakuwa na umande wala mvua katika miaka kadhaa ijayo, isipokuwa kwa neno langu.”
1KI 17:2 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya, kusema,
1KI 17:3 “Ondoka hapa, elekea upande wa mashariki ukajifiche karibu na Kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yordani.
1KI 17:4 Utakunywa maji kutoka kile kijito, nami nimeagiza kunguru wakulishe huko.”
1KI 17:5 Naye akafanya kama alivyoambiwa na Mwenyezi Mungu. Akaenda katika Kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yordani na akakaa huko.
1KI 17:6 Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, naye akanywa maji kutoka kile kijito.
1KI 17:7 Baada ya muda, kile kijito kikakauka kwa sababu mvua haikuwa imenyesha katika nchi.
1KI 17:8 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya, kusema,
1KI 17:9 “Ondoka, uende Sarepta ya Sidoni, ukae huko. Nimemwagiza mjane wa huko ili akuhudumie.”
1KI 17:10 Hivyo akaenda Sarepta. Alipofika kwenye lango la mji, alimkuta mjane akiokota kuni pale. Akamwita na kumwambia, “Naomba uniletee maji kidogo kwenye gudulia ili niweze kunywa.”
1KI 17:11 Alipokuwa anaenda kumletea, akamwita akasema, “Tafadhali niletee pia kipande cha mkate.”
1KI 17:12 Akamjibu, “Hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aishivyo, sina mkate wowote, isipokuwa konzi moja ya unga kwenye chungu, na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili tule, kiishe, tukafe.”
1KI 17:13 Ilya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao.
1KI 17:14 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Kile chungu cha unga hakitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile Mwenyezi Mungu atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ”
1KI 17:15 Akaondoka na kufanya kama Ilya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Ilya, yule mwanamke na jamaa yake.
1KI 17:16 Kwa kuwa kile chungu hakikuisha unga na ile chupa ya mafuta haikukauka sawasawa na lile neno la Mwenyezi Mungu lililonenwa na Ilya.
1KI 17:17 Baada ya muda, mwana wa yule mwanamke mwenye nyumba akaugua. Hali yake ikaendelea kuwa mbaya sana, na hatimaye akaacha kupumua.
1KI 17:18 Yule mjane akamwambia Ilya, “Una nini dhidi yangu, ewe mtu wa Mungu? Umekuja ili kunikumbusha dhambi yangu, na kusababisha kifo cha mwanangu?”
1KI 17:19 Ilya akamjibu, “Nipe mwanao.” Ilya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba hadi chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani pake.
1KI 17:20 Kisha akamlilia Mwenyezi Mungu, akasema “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi kwake, kwa kusababisha mwanawe kufa?”
1KI 17:21 Kisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia Mwenyezi Mungu, akisema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!”
1KI 17:22 Mwenyezi Mungu akasikia kilio cha Ilya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka.
1KI 17:23 Ilya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumba chake cha juu, akamshusha, akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!”
1KI 17:24 Ndipo yule mwanamke akamwambia Ilya, “Sasa ninajua kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la Mwenyezi Mungu kutoka kinywani mwako ni kweli.”
1KI 18:1 Baada ya muda mrefu, katika mwaka wa tatu, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya kusema, “Nenda ukajioneshe kwa Ahabu nami nitaleta mvua juu ya nchi.”
1KI 18:2 Kwa hiyo Ilya akaenda kujionesha kwa Ahabu. Wakati huo njaa ilikuwa kali sana katika Samaria,
1KI 18:3 naye Ahabu alikuwa amemwita Obadia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme. (Obadia alimcha Mwenyezi Mungu sana.
1KI 18:4 Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Mwenyezi Mungu, Obadia alikuwa amewachukua manabii mia moja na kuwaficha katika mapango mawili, hamsini kwenye kila moja, na akawa akiwapa chakula na maji.)
1KI 18:5 Ahabu alikuwa amemwambia Obadia, “Nenda katika nchi yote kwenye vijito vyote na mabonde. Huenda tunaweza kupata majani ya kuwalisha farasi na nyumbu ili wapate kuishi, tusilazimike kumuua hata mmoja wa wanyama wetu.”
1KI 18:6 Kwa hiyo wakagawanya nchi waliyokusudia kutafuta majani, Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.
1KI 18:7 Obadia alipokuwa akitembea njiani, Ilya akakutana naye. Obadia akamtambua, akasujudu, uso wake ukigusa chini, na kusema, “Je, hivi kweli ni wewe, bwana wangu Ilya?”
1KI 18:8 Ilya akamjibu, “Ndiyo, nenda ukamwambie bwana wako, ‘Ilya yuko hapa.’ ”
1KI 18:9 Obadia akamuuliza, “Ni kosa gani nimefanya, hata ukaamua kumkabidhi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu ili aniue?
1KI 18:10 Hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa hata moja au ufalme ambapo bwana wangu hajamtuma mtu kukutafuta. Kila wakati taifa au ufalme walipodai kwamba haupo huko, aliwafanya waape kwamba hawakuweza kukupata.
1KI 18:11 Lakini sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kusema, ‘Ilya yuko hapa.’
1KI 18:12 Sijui ni wapi Roho wa Mwenyezi Mungu ataamua kukupeleka wakati nitakapokuacha. Nikienda kumwambia Ahabu na asikupate, ataniua; lakini mimi mtumishi wako nimekuwa nikimwabudu Mwenyezi Mungu tangu ujana wangu.
1KI 18:13 Je, hukusikia, bwana wangu, nilifanya nini Yezebeli alipokuwa akiua manabii wa Mwenyezi Mungu? Niliwaficha manabii wa Mwenyezi Mungu mia moja katika mapango mawili, hamsini katika kila moja, na nikawapatia chakula na maji.
1KI 18:14 Nawe sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kumwambia, ‘Ilya yuko hapa.’ Yeye ataniua!”
1KI 18:15 Ilya akasema, “Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aishivyo, yeye ninayemtumikia, hakika nitajionesha kwa Ahabu leo.”
1KI 18:16 Basi Obadia akaenda kukutana na Ahabu na kumwambia; naye Ahabu akaenda kukutana na Ilya.
1KI 18:17 Ahabu alipomwona Ilya, akamwambia, “Je, ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?”
1KI 18:18 Ilya akamjibu, “Mimi sijaitaabisha Israeli. Lakini wewe na jamaa ya baba yako ndio mnaofanya hivyo. Mmeziacha amri za Mwenyezi Mungu na mkafuata Mabaali.
1KI 18:19 Sasa waite watu kutoka Israeli yote tukutane nao juu ya Mlima Karmeli. Nawe uwalete hao manabii wa Baali mia nne na hamsini na hao manabii mia nne wa Ashera, walao chakula mezani mwa Yezebeli.”
1KI 18:20 Ndipo Ahabu akatuma ujumbe katika Israeli yote na kuwakusanya manabii hao juu ya Mlima Karmeli.
1KI 18:21 Ilya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtayumbayumba katikati ya mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.” Lakini watu hawakusema kitu.
1KI 18:22 Kisha Ilya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa Mwenyezi Mungu aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini.
1KI 18:23 Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na wamweke juu ya kuni, lakini wasimwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni, lakini sitamwashia moto.
1KI 18:24 Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Mwenyezi Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.” Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”
1KI 18:25 Ilya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.”
1KI 18:26 Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa. Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.
1KI 18:27 Wakati wa adhuhuri, Ilya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.”
1KI 18:28 Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja kwa visu na vyembe, hadi damu ikachuruzika.
1KI 18:29 Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu hadi wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na itikio, hakuna aliyejibu, na hakuna aliyezingatia.
1KI 18:30 Kisha Ilya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Wakamkaribia, naye akaikarabati madhabahu ya Mwenyezi Mungu, iliyokuwa imeharibiwa.
1KI 18:31 Ilya akachukua mawe kumi na mbili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la Mwenyezi Mungu lilimjia, kusema, “Jina lako litakuwa Israeli.”
1KI 18:32 Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la Mwenyezi Mungu, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu.
1KI 18:33 Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.”
1KI 18:34 Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena. Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu.
1KI 18:35 Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki.
1KI 18:36 Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Ilya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kama ulivyoagiza.
1KI 18:37 Unijibu, Ee Mwenyezi Mungu! Unijibu ili watu hawa wajue kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”
1KI 18:38 Kisha moto wa Mwenyezi Mungu ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.
1KI 18:39 Watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Mwenyezi Mungu: yeye ndiye Mungu! Mwenyezi Mungu: yeye ndiye Mungu!”
1KI 18:40 Kisha Ilya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Ilya akawaleta Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.
1KI 18:41 Ilya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.”
1KI 18:42 Hivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Ilya akapanda kileleni mwa Karmeli, akainama hadi chini, na kuweka kichwa chake katikati ya magoti.
1KI 18:43 Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama. Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.” Mara saba Ilya akasema, “Nenda tena.”
1KI 18:44 Mara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.” Hivyo Ilya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako la vita, ushuke kabla mvua haijakuzuia.’ ”
1KI 18:45 Wakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli.
1KI 18:46 Nguvu za Mwenyezi Mungu zikamjia Ilya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi ingilio la Yezreeli.
1KI 19:1 Ahabu akamwambia Yezebeli kila kitu Ilya alichokuwa amefanya na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.
1KI 19:2 Hivyo Yezebeli akamtuma mjumbe kwa Ilya, kusema, “Miungu waniadhibu vikali zaidi, ikiwa kesho wakati kama huu sitakuwa nimeondoa uhai wako kama mmoja wa hao manabii.”
1KI 19:3 Ilya aliogopa, na akatoroka kuokoa maisha yake. Alipofika Beer-Sheba katika Yuda, akamwacha mtumishi wake huko,
1KI 19:4 lakini yeye mwenyewe akatembea mwendo wa kutwa nzima katika jangwa. Akafika kwenye mti wa mretemu, akakaa chini yake na kuomba ili afe. Akasema, “Yatosha sasa, Mwenyezi Mungu, ondoa roho yangu, kwani mimi si bora kuliko baba zangu.”
1KI 19:5 Kisha akajinyoosha chini ya mti, akalala usingizi. Mara malaika akamgusa na kumwambia, “Inuka ule.”
1KI 19:6 Akatazama pande zote, na hapo karibu na kichwa chake palikuwa na mkate uliookwa kwenye makaa ya moto, na gudulia la maji. Akala na kunywa, kisha akajinyoosha tena.
1KI 19:7 Yule malaika wa Mwenyezi Mungu akaja tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Inuka ule, kwa kuwa bado una safari ndefu mbele yako.”
1KI 19:8 Kwa hiyo akainuka, akala na kunywa. Akiwa ametiwa nguvu na kile chakula, akasafiri siku arobaini usiku na mchana hadi akafika Horebu, mlima wa Mungu.
1KI 19:9 Huko akaingia katika pango, akalala humo usiku ule. Nalo neno la Mwenyezi Mungu likamjia, kusema, “Unafanya nini hapa, Ilya?”
1KI 19:10 Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.”
1KI 19:11 Mwenyezi Mungu akasema, “Toka nje ukasimame juu ya mlima mbele za Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu yu karibu kupita hapo.” Kisha upepo mzito na wenye nguvu ukapasua milima ile na kuvunjavunja miamba mbele za Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo katika ule upepo. Baada ya upepo palikuwa na tetemeko la ardhi, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo kwenye lile tetemeko.
1KI 19:12 Baada ya tetemeko la ardhi moto ukaja, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo katika ule moto. Baada ya moto ikaja sauti ya utulivu ya kunong’ona.
1KI 19:13 Ilya alipoisikia, akafunika uso kwa vazi lake, akatoka na kusimama kwenye mlango wa pango. Kisha ile sauti ikamwambia, “Ilya, unafanya nini hapa?”
1KI 19:14 Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.”
1KI 19:15 Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Utakapofika huko, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu.
1KI 19:16 Pia mpake mafuta Yehu, mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umpake mafuta Al-Yasa mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola awe nabii baada yako.
1KI 19:17 Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Al-Yasa atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu.
1KI 19:18 Hata sasa nimeweka akiba ya watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.”
1KI 19:19 Hivyo Ilya akaondoka huko na kumkuta Al-Yasa mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliiongoza ile jozi ya kumi na mbili. Ilya akamwendea, na kumvisha vazi lake.
1KI 19:20 Kisha Al-Yasa akawaacha maksai wake, akamkimbilia Ilya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.” Ilya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekufanya nini?”
1KI 19:21 Basi Al-Yasa akamwacha Ilya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Ilya, akamtumikia.
1KI 20:1 Basi, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira Samaria na kuishambulia kwa jeshi.
1KI 20:2 Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi:
1KI 20:3 ‘Fedha yako na dhahabu yako ni vyangu; nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ”
1KI 20:4 Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.”
1KI 20:5 Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimewatuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako.
1KI 20:6 Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ”
1KI 20:7 Mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi, akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochochea matatizo! Alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.”
1KI 20:8 Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.”
1KI 20:9 Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’ ” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi.
1KI 20:10 Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema, “Miungu waniadhibu vikali zaidi ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wanaofuatana nami.”
1KI 20:11 Mfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’ ”
1KI 20:12 Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati yeye na wafalme walikuwa wakinywa katika mahema yao, akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kushambulia mji.
1KI 20:13 Wakati huo huo nabii akamjia Ahabu, mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe utajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
1KI 20:14 Ahabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?” Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’ ” Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?” Nabii akamjibu, “Ni wewe.”
1KI 20:15 Hivyo, Ahabu akawaita maafisa vijana wapatao mia mbili thelathini na wawili (232) waliokuwa chini ya majemadari wa majimbo. Kisha akawakusanya Waisraeli waliobaki, ambao idadi yao walikuwa elfu saba.
1KI 20:16 Wakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa.
1KI 20:17 Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza. Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.”
1KI 20:18 Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.”
1KI 20:19 Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao,
1KI 20:20 kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi, mfalme wa Aramu akapanda farasi na kutoroka pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake.
1KI 20:21 Mfalme wa Israeli akasonga mbele, akawashinda farasi na magari ya vita ya adui, na kuwasababishia Waaramu hasara kubwa.
1KI 20:22 Baadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja tena kukushambulia.”
1KI 20:23 Wakati huo, maafisa wa mfalme wa Aramu wakamshauri, wakamwambia, “Miungu yao ni miungu ya vilimani. Ndiyo sababu walikuwa na nguvu sana kutuzidi. Lakini tukipigana nao katika nchi tambarare, hakika tutawashinda.
1KI 20:24 Fanya hivi: Waondoe hao wafalme wote kutoka nafasi zao na uweke maafisa wengine mahali pao.
1KI 20:25 Ni lazima pia uandae jeshi lingine kama lile ulilopoteza, farasi kwa farasi, gari la vita kwa gari la vita, ili tuweze kupigana na Israeli katika nchi tambarare. Kisha kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.” Akakubaliana nao naye akashughulika ipasavyo.
1KI 20:26 Mwaka uliofuata, majira kama hayo, Ben-Hadadi akawakusanya Waaramu, akaenda Afeki kupigana dhidi ya Israeli.
1KI 20:27 Baada ya Waisraeli kukusanywa na kupewa mahitaji, walienda kukabiliana nao. Waisraeli wakapiga kambi mkabala nao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, Waaramu wakiwa wameenea katika nchi.
1KI 20:28 Yule mtu wa Mungu akaja na kumwambia mfalme wa Israeli, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Kwa sababu Waaramu wanafikiri Mwenyezi Mungu ni Mungu wa vilimani na sio Mungu wa mabondeni, nitalitia jeshi hili kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
1KI 20:29 Kwa siku saba walipiga kambi wakitazamana, na siku ya saba vita vikaanza. Waisraeli wakawajeruhi askari wa miguu wa Waaramu wapatao elfu mia moja kwa siku moja.
1KI 20:30 Waliobaki walikimbilia mji wa Afeki ambako elfu ishirini na saba kati yao waliangukiwa na ukuta. Naye Ben-Hadadi alikimbilia mjini na kujificha kwenye chumba cha ndani.
1KI 20:31 Maafisa wake wakamwambia, “Tazama, tumesikia kwamba wafalme wa nyumba ya Israeli wana huruma. Twendeni kwa mfalme wa Israeli tukiwa tumevaa gunia viunoni mwetu na kamba kuzunguka vichwa vyetu. Huenda akakuacha hai.”
1KI 20:32 Wakiwa wamevaa magunia viunoni mwao na kamba kuzunguka vichwa vyao, wakaenda kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Mtumishi wako Ben-Hadadi anasema: ‘Tafadhali, naomba uniache hai.’ ” Mfalme akajibu, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”
1KI 20:33 Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!” Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita. Ben-Hadadi akajitolea, akisema,
1KI 20:34 “Nitairudisha miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Nawe utaweka mitaa yako katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya kule Samaria.” Ahabu akasema, “Kwa makubaliano, nitakuacha huru.” Hivyo, akaweka mkataba naye, kisha akamruhusu aende zake.
1KI 20:35 Kwa neno la Mwenyezi Mungu, mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.
1KI 20:36 Kwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtii Mwenyezi Mungu, mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.
1KI 20:37 Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige, tafadhali!” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi.
1KI 20:38 Ndipo nabii akaenda na kusimama barabarani akimsubiri mfalme. Akajibadilisha kwa kushusha kitambaa cha kichwani mwake hadi kwenye macho.
1KI 20:39 Mfalme alipopita pale, yule nabii akamwita, “Mtumishi wako alienda vitani mahali vilikuwa kali. Mtu mmoja akanijia akiwa na mateka, akasema, ‘Mlinde mtu huyu. Akitoroka, itakuwa uhai wako kwa uhai wake, ama utalipa talanta ya fedha.’
1KI 20:40 Mtumishi wako alipokuwa na shughuli nyingi hapa na pale, yule mtu akatoweka.” Mfalme wa Israeli akasema, “Hiyo ndiyo hukumu yako. Wewe umeitaja mwenyewe.”
1KI 20:41 Kisha yule nabii akajifunua macho yake haraka, na mfalme wa Israeli akamtambua kama mmoja wa manabii.
1KI 20:42 Akamwambia mfalme, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Umemwacha huru mtu niliyekusudia afe. Kwa hivyo ni uhai wako kwa uhai wake, watu wako kwa watu wake.’ ”
1KI 20:43 Kwa uchungu na hasira, mfalme wa Israeli akaenda kwenye jumba lake huko Samaria.
1KI 21:1 Baada ya hayo, pakawa na tukio lililohusisha shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Shamba hilo lilikuwa Yezreeli, karibu na jumba la kifalme la Ahabu, mfalme wa Samaria.
1KI 21:2 Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu liwe langu, nilime bustani ya mboga kwa kuwa liko karibu na jumba langu. Nitakupa shamba jingine la mizabibu lililo zuri zaidi, au kama utapenda, nitakulipa kulingana na thamani ya shamba lako.”
1KI 21:3 Lakini Nabothi akamjibu, “Mwenyezi Mungu na apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.”
1KI 21:4 Basi Ahabu akaenda nyumbani kwa uchungu na hasira kwa sababu Nabothi Myezreeli alikuwa amemwambia, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula.
1KI 21:5 Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?”
1KI 21:6 Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’ ”
1KI 21:7 Yezebeli mke wake akamuuliza, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme wa Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.”
1KI 21:8 Kwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu, akaweka muhuri wa Ahabu juu ya hizo barua; kisha akazituma kwa wazee na kwa watu wenye vyeo walioishi na Nabothi katika mji wake.
1KI 21:9 Katika barua hizo aliandika: “Tangazeni siku ya watu kufunga, na mkamketishe Nabothi mbele ya watu.
1KI 21:10 Waketisheni walaghai wawili mkabala naye, nao washuhudie dhidi yake kuwa amemlaani Mungu na mfalme pia. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.”
1KI 21:11 Hivyo wazee na watu wenye vyeo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua alizowaandikia.
1KI 21:12 Wakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mbele ya watu.
1KI 21:13 Kisha walaghai wawili wakaja wakaketi mkabala naye; nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme pia.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa.
1KI 21:14 Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.”
1KI 21:15 Mara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na umiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.”
1KI 21:16 Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka, kisha akashuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi.
1KI 21:17 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya Mtishbi, kusema:
1KI 21:18 “Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambalo ameenda kulimiliki.
1KI 21:19 Umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Mahali mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako pia; naam, yako wewe!’ ”
1KI 21:20 Ahabu akamwambia Ilya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!” Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kwa kufanya uovu mbele za macho ya Mwenyezi Mungu.
1KI 21:21 ‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kila mwanaume wa jamaa ya Ahabu katika Israeli, awe mtumwa au mtu huru.
1KI 21:22 Nitaifanya nyumba yako kuwa kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kusababisha Israeli kutenda dhambi.’
1KI 21:23 “Pia Mwenyezi Mungu anasema kumhusu Yezebeli: ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’
1KI 21:24 “Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.”
1KI 21:25 (Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe.
1KI 21:26 Alitenda uovu sana kwa kuzifuata sanamu, kama Waamori ambao Mwenyezi Mungu aliowafukuza mbele ya Israeli.)
1KI 21:27 Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa gunia na kufunga. Akalala na kujifunika gunia na kwenda kwa unyenyekevu.
1KI 21:28 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu lilipomjia Ilya Mtishbi kusema,
1KI 21:29 “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”
1KI 22:1 Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli.
1KI 22:2 Lakini katika mwaka wa tatu, Yehoshafati mfalme wa Yuda akateremka kwenda kumwona mfalme wa Israeli.
1KI 22:3 Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu, na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?”
1KI 22:4 Kwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
1KI 22:5 Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta ushauri wa Mwenyezi Mungu.”
1KI 22:6 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii, wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?” Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”
1KI 22:7 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Mwenyezi Mungu hapa ambaye tunaweza kumuuliza?”
1KI 22:8 Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia kwake twaweza kuuliza ushauri wa Mwenyezi Mungu, lakini namchukia kwa sababu hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila hunitabiria mabaya kila mara. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.” Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”
1KI 22:9 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”
1KI 22:10 Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, huku manabii wote wakitabiri mbele yao.
1KI 22:11 Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma. Naye akatangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Kwa hizi pembe utawapiga Waaramu hadi waangamizwe.’ ”
1KI 22:12 Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ataitia mkononi mwa mfalme.”
1KI 22:13 Mjumbe aliyekuwa ameenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”
1KI 22:14 Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, nitamwambia kile tu Mwenyezi Mungu atakachoniambia.”
1KI 22:15 Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?” Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa Mwenyezi Mungu atawatia mkononi mwa mfalme.”
1KI 22:16 Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Mwenyezi Mungu?”
1KI 22:17 Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”
1KI 22:18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila mabaya tu?”
1KI 22:19 Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Mwenyezi Mungu: Nilimwona Mwenyezi Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka upande wa kulia na wa kushoto.
1KI 22:20 Naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’ “Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.
1KI 22:21 Hatimaye, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za Mwenyezi Mungu na kusema, ‘Nitamshawishi.’
1KI 22:22 “Mwenyezi Mungu akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitaenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “Mwenyezi Mungu akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’
1KI 22:23 “Kwa hiyo sasa Mwenyezi Mungu ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Mwenyezi Mungu ameamuru maafa kwa ajili yako.”
1KI 22:24 Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Mwenyezi Mungu alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”
1KI 22:25 Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapoenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”
1KI 22:26 Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme.
1KI 22:27 Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji hadi nitakaporudi salama.’ ”
1KI 22:28 Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Mwenyezi Mungu hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”
1KI 22:29 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi.
1KI 22:30 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.
1KI 22:31 Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.”
1KI 22:32 Wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati alipopiga kelele,
1KI 22:33 wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, wakaacha kumfuatilia.
1KI 22:34 Lakini mtu mmoja akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake la vita, “Geuza gari na uniondoe katika mapigano, nimejeruhiwa.”
1KI 22:35 Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari lake la vita kuelekea Waaramu. Damu kutoka jeraha lake ikatiririka ndani ya gari lake, na jioni yake akafa.
1KI 22:36 Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!”
1KI 22:37 Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko.
1KI 22:38 Wakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu lilivyokuwa limesema.
1KI 22:39 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ahabu, pamoja na yote aliyoyafanya, jumba la kifalme alilojenga na kupambwa kwa pembe za ndovu, nayo miji aliyoijengea ngome, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
1KI 22:40 Ahabu akalala na baba zake. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 22:41 Yehoshafati mwana wa Asa akawa mfalme wa Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.
1KI 22:42 Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka ishirini na tano. Mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi.
1KI 22:43 Katika kila jambo alitembea katika njia za Asa baba yake wala hakuenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
1KI 22:44 Yehoshafati pia alikuwa na amani na mfalme wa Israeli.
1KI 22:45 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, mafanikio aliyokuwa nayo na uhodari wake katika vita, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
1KI 22:46 Aliondolea mbali katika nchi mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu waliobaki huko hata baada ya utawala wa baba yake Asa.
1KI 22:47 Wakati ule, hakukuwa na mfalme katika Edomu; naibu ndiye alitawala.
1KI 22:48 Wakati huu Yehoshafati akaunda merikebu nyingi za biashara ili kwenda Ofiri kuchukua dhahabu; lakini kamwe hazikusafiri, kwa maana zilivunjikia huko Esion-Geberi.
1KI 22:49 Wakati ule, Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Waache watu wangu wasafiri baharini pamoja na watu wako,” lakini Yehoshafati akakataa.
1KI 22:50 Kisha Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Yehoramu mwanawe akawa mfalme baada yake.
1KI 22:51 Ahazia mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda. Naye akatawala katika Israeli kwa miaka miwili.
1KI 22:52 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu kwa sababu alienenda katika njia za baba yake na mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye alisababisha Israeli itende dhambi.
1KI 22:53 Alimtumikia na kumwabudu Baali na kumghadhibisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
2KI 1:1 Baada ya kifo cha Mfalme Ahabu, nchi ya Moabu iliasi dhidi ya Israeli.
2KI 1:2 Basi Ahazia alikuwa ameanguka huko Samaria kutoka baraza ya chumba chake cha juu, akaumia. Hivyo akatuma wajumbe, akiwaambia, “Nendeni mkaulize kwa Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni, mkaone kama nitapona kutokana na kuumia huku.”
2KI 1:3 Lakini malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Ilya Mtishbi, “Panda uende ukakutane na wajumbe wa mfalme wa Samaria, uwaulize, ‘Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli ndiyo maana mnaenda kumuuliza Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni?’
2KI 1:4 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, ‘Hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!’ ” Hivyo Ilya akaenda.
2KI 1:5 Wajumbe waliporudi kwa mfalme, akawauliza, “Kwa nini mmerudi?”
2KI 1:6 Wakamjibu, “Mtu mmoja alikuja kukutana nasi, naye akatuambia, ‘Rudini kwa mfalme aliyewatuma na mkamwambie, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli ndiyo maana unawatuma watu kwenda kuuliza kwa Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa hiyo hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!” ’ ”
2KI 1:7 Mfalme akawauliza, “Alikuwa mtu wa namna gani ambaye mlikutana naye, akawaambia hili?”
2KI 1:8 Wakamjibu, “Alikuwa mtu aliyekuwa na vazi la manyoya na mkanda wa ngozi kiunoni mwake.” Mfalme akasema, “Huyo alikuwa ni Ilya Mtishbi.”
2KI 1:9 Ndipo mfalme akamtuma mkuu mmoja wa kikosi pamoja na kikosi chake cha askari hamsini kwa nabii Ilya. Yule mkuu wa kikosi akamwendea Ilya, aliyekuwa ameketi juu ya kilima, na kumwambia, “Mtu wa Mungu, mfalme anasema, ‘Shuka chini!’ ”
2KI 1:10 Ilya akamjibu yule mkuu wa kikosi, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza yule mkuu wa kikosi pamoja na watu wake.
2KI 1:11 Aliposikia hili, mfalme akatuma kwa Ilya mkuu wa kikosi mwingine na askari wake hamsini. Yule mkuu wa kikosi akamwambia Ilya, “Mtu wa Mungu, hili ndilo asemalo mfalme, ‘Shuka chini mara moja!’ ”
2KI 1:12 Ilya akajibu, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza yeye na watu wake hamsini.
2KI 1:13 Hivyo mfalme akatuma mkuu wa kikosi wa tatu na watu wake hamsini. Huyu mkuu wa kikosi wa tatu akapanda na kupiga magoti mbele ya Ilya, akiomba, “Mtu wa Mungu, tafadhali niachie uhai wangu na uhai wa hawa watu hamsini, watumishi wako!
2KI 1:14 Tazama, moto umeshuka kutoka mbinguni na kuwateketeza wale wakuu wa vikosi viwili vya kwanza pamoja na watu wao. Lakini sasa niachie uhai wangu!”
2KI 1:15 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Ilya, “Shuka pamoja naye, usimwogope.” Hivyo Ilya akainuka na kushuka pamoja naye kwa mfalme.
2KI 1:16 Akamwambia mfalme, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli wa kumuuliza habari, ndiyo maana ukatuma wajumbe kuuliza Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa sababu umefanya hili, kamwe hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!”
2KI 1:17 Hivyo akafa, sawasawa na lile neno la Mwenyezi Mungu ambalo Ilya alikuwa amesema. Kwa kuwa Ahazia hakuwa na mwana, Yoramu akawa mfalme baada yake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.
2KI 1:18 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ahazia na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 2:1 Mwenyezi Mungu alipokuwa karibu kumchukua Ilya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Ilya na Al-Yasa walikuwa njiani wakitoka Gilgali.
2KI 2:2 Ilya akamwambia Al-Yasa, “Kaa hapa. Mwenyezi Mungu amenituma Betheli.” Lakini Al-Yasa akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja.
2KI 2:3 Wana wa manabii waliokuwa Betheli wakamjia Al-Yasa na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mwenyezi Mungu atakuondolea bwana wako leo?” Al-Yasa akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze kuhusu jambo hilo.”
2KI 2:4 Kisha Ilya akamwambia, “Baki hapa, Al-Yasa. Mwenyezi Mungu amenituma Yeriko.” Naye akajibu, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko.
2KI 2:5 Wana wa manabii waliokuwa Yeriko wakamwendea Al-Yasa na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mwenyezi Mungu atakuondolea bwana wako leo?” Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”
2KI 2:6 Kisha Ilya akamwambia, “Kaa hapa. Mwenyezi Mungu amenituma kwenda Yordani.” Naye akamjibu, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja.
2KI 2:7 Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali Ilya na Al-Yasa waliposimama kando ya Mto Yordani.
2KI 2:8 Ilya akatoa vazi lake, akalikunja na kupiga maji nalo. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.
2KI 2:9 Walipokwisha kuvuka, Ilya akamwambia Al-Yasa, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?” Al-Yasa akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.”
2KI 2:10 Ilya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hutalipata.”
2KI 2:11 Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la farasi la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Ilya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli.
2KI 2:12 Al-Yasa aliliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Al-Yasa hakumwona tena. Kisha akaishika nguo yake na kuirarua vipande viwili.
2KI 2:13 Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Ilya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani.
2KI 2:14 Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Ilya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Ilya?” Al-Yasa alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.
2KI 2:15 Wale wana wa manabii kutoka Yeriko waliokuwa wakitazama wakasema, “Roho ya Ilya inamkalia Al-Yasa.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi chini mbele yake.
2KI 2:16 Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa Mwenyezi Mungu amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.” Al-Yasa akajibu, “Hapana, msiwatume.”
2KI 2:17 Lakini wakasisitiza, hata akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata.
2KI 2:18 Walipomrudia Al-Yasa, aliyekuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?”
2KI 2:19 Watu wa mji wakamwambia Al-Yasa, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu anavyoona, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haina mazao.”
2KI 2:20 Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.
2KI 2:21 Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ”
2KI 2:22 Nayo yale maji yakaponywa hadi leo, sawasawa na neno la Al-Yasa alilokuwa amesema.
2KI 2:23 Kutoka huko Al-Yasa akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakasema, “Paa, wewe mwenye upara! Paa, wewe mwenye upara!”
2KI 2:24 Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la Mwenyezi Mungu. Kisha dubu jike wawili wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.
2KI 2:25 Naye akaondoka huko, akaenda Mlima Karmeli, na kutoka huko akarudi Samaria.
2KI 3:1 Yehoramu mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, naye akatawala kwa miaka kumi na mbili.
2KI 3:2 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini sio kama baba yake na mama yake walivyokuwa wamefanya. Akaondoa nguzo ya ibada ya Baali ambayo baba yake alikuwa ameitengeneza.
2KI 3:3 Hata hivyo akashikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, wala hakuziacha.
2KI 3:4 Basi Mesha mfalme wa Moabu alikuwa mfuga kondoo; naye akatakiwa kumlipa mfalme wa Israeli ushuru wa wana-kondoo elfu mia moja, na sufu ya kondoo dume elfu mia moja.
2KI 3:5 Lakini baada ya Ahabu kufa, mfalme wa Moabu aliasi dhidi ya mfalme wa Israeli.
2KI 3:6 Kwa hiyo wakati ule Mfalme Yehoramu akaondoka kutoka Samaria na kukusanya Israeli yote tayari kwenda vitani.
2KI 3:7 Akapeleka pia ujumbe ufuatao kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda: “Mfalme wa Moabu ameasi dhidi yangu. Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Moabu?” Akajibu, “Nitaenda pamoja nawe. Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
2KI 3:8 Akauliza, “Je, tutashambulia kupitia njia gani?” Akajibu, “Kupitia Jangwa la Edomu.”
2KI 3:9 Hivyo mfalme wa Israeli akaondoka akiwa pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kuzunguka kwa siku saba, jeshi likawa limeishiwa maji kwa matumizi yao na kwa ajili ya wanyama waliokuwa nao.
2KI 3:10 Mfalme wa Israeli akapaza sauti, akasema, “Nini! Je, Mwenyezi Mungu ametuita sisi wafalme watatu ili tu kututia mikononi mwa Moabu?”
2KI 3:11 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Mwenyezi Mungu hapa, ili tuweze kumuuliza Mwenyezi Mungu kupitia kwake?” Afisa mmoja wa mfalme wa Israeli akajibu, “Al-Yasa mwana wa Shafati yuko hapa. Ndiye alikuwa akimimina maji juu ya mikono ya Ilya.”
2KI 3:12 Yehoshafati akasema, “Neno la Mwenyezi Mungu liko pamoja naye.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli na Yehoshafati pamoja na mfalme wa Edomu wakamwendea.
2KI 3:13 Al-Yasa akamwambia mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda kwa manabii wa baba yako na manabii wa mama yako.” Mfalme wa Israeli akajibu, “La, sivyo, kwa sababu ni Mwenyezi Mungu ametuita pamoja sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa Moabu.”
2KI 3:14 Al-Yasa akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aishivyo, ninayemtumikia, kama si kwa heshima niliyo nayo kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, nisingekujali hata kidogo.
2KI 3:15 Lakini sasa, nileteeni mpiga kinubi.” Mpiga kinubi alipokuwa akipiga, mkono wa Mwenyezi Mungu ukaja juu ya Al-Yasa,
2KI 3:16 naye akasema, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Chimbeni bonde hili lijae mahandaki.’
2KI 3:17 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Hamtaona upepo wala mvua, lakini bonde hili litajaa maji, nanyi pamoja na ng’ombe wenu na wanyama wenu wengine mtakunywa.
2KI 3:18 Hili ni jambo rahisi machoni pa Mwenyezi Mungu. Pia ataitia Moabu mikononi mwenu.
2KI 3:19 Mtaushinda kila mji wenye ngome na kila mji mkubwa. Mtakata kila mti ulio mzuri, mtaziba chemchemi zote, na kuharibu kila shamba zuri kwa mawe.”
2KI 3:20 Kesho yake asubuhi, karibu na wakati wa kutoa dhabihu ya asubuhi, tazama, maji yakawa yanatiririka kutoka upande wa Edomu! Nayo nchi ikajaa maji.
2KI 3:21 Basi Wamoabu wote walikuwa wamesikia kuwa wale wafalme wamekuja kupigana dhidi yao. Hivyo kila mtu, kijana na mzee, ambaye angeweza kushika silaha akaitwa na kuwekwa mpakani.
2KI 3:22 Walipoamka asubuhi na mapema, jua likawa linamulika juu ya maji. Wamoabu waliokuwa upande wa pili wakaona maji ni mekundu, kama damu.
2KI 3:23 Wamoabu wakasema, “Ile ni damu! Lazima hao wafalme wamepigana na kuchinjana wao kwa wao. Sasa Moabu, twendeni tukateke nyara!”
2KI 3:24 Lakini Wamoabu walipofika kwenye kambi ya Israeli, Waisraeli wakainuka na kuwapiga hata wakakimbia. Nao Waisraeli wakaivamia nchi na kuwachinja Wamoabu.
2KI 3:25 Wakaiharibu miji, kila mtu akatupa jiwe juu ya kila shamba zuri hadi likafunikwa. Wakaziba chemchemi zote na kukata kila mti mzuri. Kir-Haresethi peke yake ndio uliobaki na mawe yake yakiwa mahali pake. Lakini hata hivyo watu waliokuwa na makombeo wakauzunguka na kuushambulia.
2KI 3:26 Mfalme wa Moabu alipoona kuwa vita vimekuwa vikali dhidi yake, akachukua watu mia saba wenye panga ili kuingia kwa mfalme wa Edomu, lakini wakashindwa.
2KI 3:27 Ndipo akamchukua mwanawe mzaliwa wake wa kwanza, ambaye angekuwa mfalme baada yake, akamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Ghadhabu ikawa kubwa dhidi ya Israeli; wakajiondoa kwake na kurudi katika nchi yao wenyewe.
2KI 4:1 Mke wa mmoja wa wana wa manabii akamlilia Al-Yasa, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu, amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha Mwenyezi Mungu. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.”
2KI 4:2 Al-Yasa akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?” Akasema, “Mtumishi wako hana kitu chochote kabisa, isipokuwa mafuta kidogo.”
2KI 4:3 Al-Yasa akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache.
2KI 4:4 Kisha ingia ndani na ujifungie mlango, wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, na kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.”
2KI 4:5 Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo, naye akaendelea kumimina mafuta.
2KI 4:6 Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.” Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka.
2KI 4:7 Yule mwanamke akaenda akamwambia yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”
2KI 4:8 Siku moja Al-Yasa akaenda Shunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo, naye akamsisitiza Al-Yasa aje kula chakula. Kwa hiyo kila mara alipitia pale, akaingia humo ili ale.
2KI 4:9 Akamwambia mumewe, “Ninajua kwamba huyu mtu ambaye anakuja kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu.
2KI 4:10 Tutengeneze chumba kidogo juu darini na tuweke ndani yake kitanda na meza, kiti na taa kwa ajili yake. Kisha anaweza kukaa humo kila mara akija kwetu.”
2KI 4:11 Siku moja Al-Yasa alipofika, akapanda chumbani kwake na kulala humo.
2KI 4:12 Akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyo Mshunami.” Hivyo akamwita, naye akaja akasimama mbele yake.
2KI 4:13 Al-Yasa akamwambia mtumishi wake, “Mwambie huyu mwanamke, ‘Umetaabika sana kwa ajili yetu. Sasa utendewe nini? Je, tunaweza kuzungumza na mfalme au jemadari wa jeshi kwa niaba yako?’ ” Akajibu, “Mimi ninaishi kwangu miongoni mwa watu wangu.”
2KI 4:14 Al-Yasa akamuuliza mtumishi wake, “Je, ni nini kinachoweza kufanyika kwa ajili yake?” Gehazi akasema, “Hakika, hana mwana, na mume wake ni mzee.”
2KI 4:15 Ndipo Al-Yasa akasema, “Mwite huyo mwanamke.” Kwa hiyo akamwita, naye akaja akasimama mlangoni.
2KI 4:16 Al-Yasa akamwambia, “Mwaka ujao, wakati kama huu utabeba mwana mikononi mwako.” Yule mama akapinga, akasema, “La hasha, bwana wangu! Usimdanganye mtumishi wako, ee mtu wa Mungu!”
2KI 4:17 Lakini yule mwanamke akapata mimba, na mwaka uliofuata wakati kama ule ule akamzaa mwana, kama vile Al-Yasa alivyokuwa amemwambia.
2KI 4:18 Mtoto akakua, naye siku moja akamwendea baba yake, aliyekuwa pamoja na wavunaji.
2KI 4:19 Akamwambia baba yake, “Kichwa changu! Kichwa changu!” Baba yake akamwambia mtumishi, “Mchukue umpeleke kwa mama yake.”
2KI 4:20 Baada ya mtumishi kumbeba na kumpeleka kwa mama yake, mtoto akaketi mapajani mwa mama yake hadi adhuhuri, kisha akafa.
2KI 4:21 Mama akampandisha na kumlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, kisha akafunga mlango, akatoka nje.
2KI 4:22 Akamwita mume wake na kusema, “Tafadhali mtume mmoja miongoni mwa mtumishi pamoja na punda ili niweze kwenda kwa mtu wa Mungu haraka na kurudi.”
2KI 4:23 Mume wake akamuuliza, “Kwa nini uende kwake leo? Leo si mwandamo wa mwezi, wala si Sabato.” Mwanamke akasema, “Yote ni sawa.”
2KI 4:24 Akatandika punda na kumwambia mtumishi wake, “Mwongoze huyo punda. Usinipunguzie mwendo hadi nikuambie.”
2KI 4:25 Kwa hiyo akaenda na kumfikia huyo mtu wa Mungu katika Mlima Karmeli. Alipomwona kwa mbali, huyo mtu wa Mungu akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Tazama, yule Mshunami!
2KI 4:26 Kimbia ukamlaki, umuulize, ‘Je, wewe hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto wako ni mzima?’ ” Akasema, “Kila kitu ni sawasawa.”
2KI 4:27 Alipomfikia huyo mtu wa Mungu pale mlimani, akashika miguu yake. Gehazi akaja ili amwondoe, lakini yule mtu wa Mungu akasema, “Mwache! Yuko katika uchungu mkubwa, lakini Mwenyezi Mungu amenificha jambo hili na hajaniambia kwa nini.”
2KI 4:28 Yule mwanamke akasema, “Je, bwana wangu, mimi nilikuomba mwana? Je, sikukuambia, ‘Usiamshe matumaini yangu’?”
2KI 4:29 Al-Yasa akamwambia Gehazi, “Jikaze viuno, chukua fimbo yangu mkononi mwako na ukimbie. Ikiwa utakutana na mtu yeyote, usimsalimie, na mtu yeyote akikusalimu, usimjibu. Ilaze fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.”
2KI 4:30 Lakini mama mtoto akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo Al-Yasa akainuka, akafuatana naye.
2KI 4:31 Gehazi akatangulia mbele na kuilaza fimbo juu ya uso wa mtoto, lakini hapakuwa na sauti wala itikio. Hivyo Gehazi akarudi kukutana na Al-Yasa, na kumwambia, “Mtoto hajaamka.”
2KI 4:32 Al-Yasa alipofika kwenye ile nyumba, mtoto alikuwa amelala juu ya kitanda chake angali amekufa.
2KI 4:33 Akaingia ndani, akajifungia yeye na yule mtoto, akamwomba Mwenyezi Mungu.
2KI 4:34 Kisha akapanda kitandani, akalala juu ya yule mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, macho yake juu ya macho ya mtoto, mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Naye alipojinyoosha juu yake, mwili wa mtoto ukapata joto.
2KI 4:35 Al-Yasa akajiondoa juu yake na kuanza kutembeatembea ndani ya chumba, kisha akarudi tena kitandani na kujinyoosha tena juu ya mtoto mara nyingine. Mtoto akapiga chafya mara saba, akafungua macho yake.
2KI 4:36 Al-Yasa akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite huyo Mshunami.” Naye akafanya hivyo. Yule Mshunami alipokuja, Al-Yasa akasema, “Mchukue mwanao.”
2KI 4:37 Akaingia ndani, akaanguka miguuni pa Al-Yasa na kusujudu hadi chini. Kisha akamchukua mwanawe na kutoka nje.
2KI 4:38 Al-Yasa akarudi Gilgali, nako huko kulikuwa na njaa katika eneo lile. Wana wa kundi la manabii walipokuwa wanakutana naye, akamwambia mtumishi wake, “Teleka chungu kikubwa jikoni uwapikie manabii.”
2KI 4:39 Mmoja wao akatoka kwenda mashambani kuchuma mboga na akapata mtango-mwitu. Akachuma matango na kujaza nguo yake aliyoikunja ili kubebea. Aliporudi, akayakatakata na kuyatumbukiza ndani ya chungu, ingawa hakuna aliyejua ni nini.
2KI 4:40 Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula.
2KI 4:41 Al-Yasa akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu chochote chenye madhara ndani ya chungu.
2KI 4:42 Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutoka kwa nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Al-Yasa akasema, “Wape watu ili wale.”
2KI 4:43 Mtumishi wake akamuuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia moja?” Lakini Al-Yasa akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Watakula na kusaza.’ ”
2KI 4:44 Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu.
2KI 5:1 Wakati huu, Naamani alikuwa jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu. Alikuwa mtu mkuu mbele ya bwana wake na aliyeheshimiwa sana, kwa sababu kupitia kwake, Mwenyezi Mungu alikuwa amewapa Aramu ushindi. Alikuwa askari hodari, lakini alikuwa na ukoma.
2KI 5:2 Siku hizo vikosi kutoka Aramu vilikuwa vimeenda na vikawa vimemteka msichana kutoka Israeli, naye akamtumikia mkewe Naamani.
2KI 5:3 Akamwambia bibi yake, “Kama bwana wangu angemwona nabii aliye huko Samaria! Angemponya ukoma wake.”
2KI 5:4 Naamani akaenda kwa bwana wake na kumwambia alichosema yule msichana kutoka Israeli.
2KI 5:5 Mfalme wa Aramu akamjibu, “Hakika, nenda. Nitatuma barua kwa mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaondoka, akiwa amechukua talanta kumi za fedha, shekeli elfu sita za dhahabu, na mavazi kumi.
2KI 5:6 Barua aliyopelekea mfalme wa Israeli iliandikwa hivi: “Pamoja na barua hii ninamtuma mtumishi wangu, Naamani, kwako ili uweze kumponya ukoma wake.”
2KI 5:7 Mara mfalme wa Israeli alipomaliza kuisoma ile barua, akararua mavazi yake na kusema, “Je, mimi ni Mungu? Je, mimi naweza kuua na kufufua tena? Kwa nini huyu mtu anamtuma mtu ili mimi nipate kumponya ukoma wake? Tazama jinsi anavyotafuta kuanzisha ugomvi nami!”
2KI 5:8 Al-Yasa mtu wa Mungu aliposikia kwamba mfalme wa Israeli alikuwa amerarua mavazi yake, akamtumia ujumbe huu: “Kwa nini umerarua mavazi yako? Mwamuru mtu huyo aje kwangu, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.”
2KI 5:9 Kwa hiyo Naamani akaenda, akiwa na farasi wake na magari yake ya vita, na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Al-Yasa.
2KI 5:10 Al-Yasa akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.”
2KI 5:11 Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kupitisha mkono wake juu ya mahali penye ugonjwa ili aniponye ukoma wangu.
2KI 5:12 Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu.
2KI 5:13 Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, hungelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ”
2KI 5:14 Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.
2KI 5:15 Kisha Naamani na wahudumu wake wote wakarudi kwa yule mtu wa Mungu. Akasimama mbele yake na kusema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu katika ulimwengu wote isipokuwa katika Israeli. Tafadhali sasa upokee zawadi kutoka kwa mtumishi wako.”
2KI 5:16 Nabii akajibu, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, ninayemtumikia, sitapokea kitu hata kimoja.” Ingawa Naamani alimsihi sana, yeye alikataa.
2KI 5:17 Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea, tafadhali mtumishi wako na apewe udongo kiasi cha mzigo wa kuweza kubebwa na punda wawili, kwa sababu mtumishi wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu.
2KI 5:18 Lakini Mwenyezi Mungu na amsamehe mtumishi wake kwa kitu hiki kimoja: Bwana wangu atakapoingia kwenye hekalu la Rimoni ili kusujudu, naye akiwa anauegemea mkono wangu, nami nikasujudu huko pia, wakati nitakaposujudu ndani ya hekalu la Rimoni, Mwenyezi Mungu na amsamehe mtumishi wako kwa ajili ya jambo hili.”
2KI 5:19 Al-Yasa akamwambia, “Nenda kwa amani.” Baada ya Naamani kusafiri umbali fulani,
2KI 5:20 Gehazi, mtumishi wa Al-Yasa mtu wa Mungu, akajiambia mwenyewe, “Bwana wangu amemwachia kirahisi sana Naamani, huyu Mwaramu, kwa kutokupokea kutoka kwake vile alivyovileta. Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, nitamkimbilia na kupata kitu kutoka kwake.”
2KI 5:21 Hivyo Gehazi akaharakisha kumfuatilia Naamani. Naamani alipomwona akikimbia kumwelekea, akashuka chini kutoka gari lake la vita na kwenda kumlaki. Akauliza, “Je, mambo yote ni sawa?”
2KI 5:22 Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedha na mavazi mawili.’ ”
2KI 5:23 Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mavazi mawili. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi.
2KI 5:24 Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka.
2KI 5:25 Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Al-Yasa bwana wake. Al-Yasa akamuuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?” Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakuenda popote.”
2KI 5:26 Lakini Al-Yasa akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka gari lake la vita ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ng’ombe, au watumishi wa kiume na wa kike?
2KI 5:27 Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Al-Yasa, mwenye ukoma, mweupe kama theluji.
2KI 6:1 Wana wa manabii wakamwambia Al-Yasa, “Tazama, mahali hapa tunapokutana nawe ni padogo sana kwetu.
2KI 6:2 Twendeni Yordani, ambapo kila mmoja wetu anaweza kupata nguzo moja, nasi tujenge huko mahali petu pa kuishi.” Naye akawaambia, “Nendeni.”
2KI 6:3 Kisha mmoja wao akasema, “Je, tafadhali, huwezi kufuatana na watumishi wako?” Al-Yasa akajibu, “Nitakuja.”
2KI 6:4 Naye akaenda pamoja nao. Basi wakaenda Yordani, nao wakaanza kukata miti.
2KI 6:5 Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akalia, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!”
2KI 6:6 Mtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonesha mahali penyewe, Al-Yasa akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea.
2KI 6:7 Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyoosha mkono wake, akalichukua.
2KI 6:8 Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.”
2KI 6:9 Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.”
2KI 6:10 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Al-Yasa alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo.
2KI 6:11 Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?”
2KI 6:12 Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Al-Yasa, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.”
2KI 6:13 Mfalme akaagiza akisema, “Nendeni, mkatafute aliko, ili niweze kutuma watu kumkamata.” Taarifa ikarudi kwamba, “Yuko Dothani.”
2KI 6:14 Ndipo akatuma farasi na magari ya vita na jeshi lenye nguvu huko. Walienda usiku na kuuzunguka mji.
2KI 6:15 Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”
2KI 6:16 Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”
2KI 6:17 Kisha Al-Yasa akaomba, “Ee Mwenyezi Mungu, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Mwenyezi Mungu akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya vita yaliyowaka moto yamemzunguka Al-Yasa pande zote.
2KI 6:18 Adui waliposhuka kumwelekea, Al-Yasa akamwomba Mwenyezi Mungu: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Al-Yasa alivyoomba.
2KI 6:19 Al-Yasa akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria.
2KI 6:20 Baada ya kuingia mjini, Al-Yasa akasema, “Mwenyezi Mungu, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo Mwenyezi Mungu akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.
2KI 6:21 Wakati mfalme wa Israeli aliwaona, akamuuliza Al-Yasa, “Je, baba yangu, niwaue?”
2KI 6:22 Naye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.”
2KI 6:23 Basi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.
2KI 6:24 Baada ya kitambo kidogo, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akaandaa jeshi lake lote akapanda kwenda kuizingira Samaria.
2KI 6:25 Kukawa na njaa kuu katika mji. Samaria ilizingirwa kwa muda mrefu, kiasi kwamba kichwa cha punda kiliuzwa kwa shekeli themanini za fedha, na robo ya kibaba cha mavi ya njiwa kiliuzwa kwa shekeli tano za fedha.
2KI 6:26 Mfalme wa Israeli alipokuwa anapita juu ya ukuta, mwanamke mmoja akamlilia, “Bwana wangu mfalme, nisaidie!”
2KI 6:27 Mfalme akajibu, “Ikiwa Mwenyezi Mungu hakusaidii, nitakutolea wapi msaada? Je, ni kwenye sakafu ya kupuria? Au ni kwenye shinikizo la kukamulia zabibu?”
2KI 6:28 Kisha akamuuliza, “Kwani kuna nini?” Yule mwanamke akamjibu, “Huyu mwanamke aliniambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla leo, na kesho tutamla mwanangu.’
2KI 6:29 Basi tukampika mwanangu na kumla. Siku iliyofuata nikamwambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla.’ Lakini akawa amemficha.”
2KI 6:30 Mfalme aliposikia maneno ya yule mwanamke, akararua mavazi yake. Naye alipoendelea kutembea ukutani, watu wakamtazama, na ndani ya mavazi yake alikuwa amevaa gunia mwilini mwake.
2KI 6:31 Akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi ikiwa kichwa cha Al-Yasa mwana wa Shafati kitabaki juu ya mabega yake leo!”
2KI 6:32 Wakati huu, Al-Yasa alikuwa ameketi ndani ya nyumba yake, akiwa pamoja na wazee. Mfalme akatuma mjumbe kumtangulia, lakini kabla hajafika, Al-Yasa akawaambia wale wazee, “Hammwoni huyu muuaji jinsi anavyotuma mtu kukata kichwa changu? Tazama, wakati mjumbe huyo atakapofika, fungeni mlango na mzuieni asiingie. Je, vishindo vya nyayo za bwana wake haviko nyuma yake?”
2KI 6:33 Alipokuwa angali bado anazungumza nao, mjumbe akamfikia. Naye mfalme akasema, “Maafa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa nini niendelee kumngoja Mwenyezi Mungu zaidi?”
2KI 7:1 Al-Yasa akasema, “Sikiliza neno la Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.”
2KI 7:2 Yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake akamwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama Mwenyezi Mungu atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Al-Yasa akajibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!”
2KI 7:3 Basi kulikuwa na watu wanne wenye ukoma katika ingilio la lango la mji. Wakaambiana, “Kwa nini tukae hapa hadi tufe?
2KI 7:4 Tukisema, ‘Tutaingia mjini,’ mjini kuna njaa, nasi tutakufa humo. Tukikaa hapa, tutakufa. Kwa hiyo twende kambi ya Waaramu, tujisalimishe. Wakituacha hai, tutaishi; wakituua, basi na tufe.”
2KI 7:5 Wakati wa mapambazuko, wakaondoka na kwenda kwenye kambi ya Waaramu. Walipofika mwanzo wa kambi, hapakuwa na mtu,
2KI 7:6 kwa kuwa Bwana alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya magari ya vita, farasi na jeshi kubwa, kiasi kwamba waliambiana, “Tazama, mfalme wa Israeli ameajiri mfalme wa Wahiti na mfalme wa Wamisri kuja kutushambulia sisi!”
2KI 7:7 Kwa hiyo wakaondoka na kukimbia wakati wa giza la jioni na kuacha mahema yao, farasi wao na punda wao. Wakakimbia kuokoa maisha yao na kuacha kila kitu ndani ya kambi kama kilivyokuwa.
2KI 7:8 Wale watu wenye ukoma walipofika mwanzoni mwa kambi, wakaingia kwenye mojawapo ya mahema. Wakala na kunywa, na kuchukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuvificha. Wakarudi na kuingia katika hema lingine, na kuchukua baadhi ya vitu kutoka ndani yake na kuvificha pia.
2KI 7:9 Kisha wakaambiana, “Hili tunalolifanya sio jema. Hii ni siku ya habari njema, nasi tunakaa kimya. Tukisubiri hadi mapambazuko, maafa yatatupata. Twendeni mara moja tukatoe habari hizi katika jumba la mfalme.”
2KI 7:10 Hivyo wakaenda mjini na kuwaita walinzi wa langoni, wakawaambia, “Tulienda katika kambi ya Waaramu lakini hapakuwa na mtu huko, hata sauti ya mtu yeyote, ila farasi na punda waliofungwa, na mahema yaliyoachwa kama yalivyokuwa.”
2KI 7:11 Walinzi wa langoni wakatangaza habari ile kwa sauti kuu, na taarifa hii ikatolewa ndani ya jumba la mfalme.
2KI 7:12 Mfalme akaamka usiku na kuwaambia maafisa wake, “Nitawaambia kile Waaramu walichotufanyia. Wanajua kwamba tuna njaa, hivyo wameacha kambi yao ili kujificha mashambani, wakifikiri, ‘Kwa hakika watatoka nje ya mji, nasi tutawakamata wakiwa hai na kuingia ndani ya mji.’ ”
2KI 7:13 Mmoja wa maafisa wake akajibu, “Waamuru watu wachache wakawachukue farasi watano kati ya wale waliobaki katika mji. Hatima yao itakuwa kama ya Waisraeli wote walio hapa. Watakuwa tu kama Waisraeli hawa ambao wanangoja kifo. Hivyo tuwatumeni wajue kumetendeka nini.”
2KI 7:14 Ndipo wakachagua magari mawili ya vita pamoja na farasi wake, naye mfalme akawatuma wafuatilie jeshi la Waaramu. Akawaamuru waendeshaji akisema, “Nendeni mkaone ni nini kilichotokea.”
2KI 7:15 Wakawafuatia hadi Yordani, nao wakakuta barabara yote ikiwa imetapakaa mavazi na vyombo Waaramu walivyokuwa wamevitupa walipokuwa wakitoroka. Basi wale wajumbe wakarudi na kutoa taarifa kwa mfalme.
2KI 7:16 Kisha watu wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kwa hiyo kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
2KI 7:17 Basi mfalme alikuwa amemweka yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake awe msimamizi wa lango. Nao watu wakamkanyaga walipoingia langoni, naye akafa, kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa ametangulia kusema wakati mfalme alipofika nyumbani mwake.
2KI 7:18 Ikatokea kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia mfalme: “Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.”
2KI 7:19 Yule afisa alikuwa amemwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama Mwenyezi Mungu atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Naye yule mtu wa Mungu alikuwa amemjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!”
2KI 7:20 Ndivyo hasa ilivyotokea kwake, kwa kuwa watu walimkanyaga langoni, naye akafa.
2KI 8:1 Basi Al-Yasa alikuwa amemwambia yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa, “Ondoka wewe na jamaa yako ukaishi mahali popote unapoweza kwa kitambo kidogo, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameamuru njaa katika nchi hii ambayo itadumu kwa miaka saba.”
2KI 8:2 Yule mwanamke akafanya kama vile yule mtu wa Mungu alivyosema. Yeye na jamaa yake wakaondoka na kwenda kuishi katika nchi ya Wafilisti kwa miaka saba.
2KI 8:3 Baada ya miaka saba, yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti, akaenda kwa mfalme kumsihi kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.
2KI 8:4 Mfalme alikuwa anazungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, naye alikuwa amesema, “Hebu niambie mambo yote makuu yaliyofanywa na Al-Yasa.”
2KI 8:5 Gehazi alipokuwa akimweleza mfalme jinsi Al-Yasa alivyomfufua mtu, yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa na Al-Yasa akaja ili amsihi mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake. Gehazi akasema, “Huyu ndiye huyo mwanamke, bwana wangu mfalme, na huyu ndiye mwanawe ambaye Al-Yasa alimfufua.”
2KI 8:6 Mfalme akamuuliza yule mwanamke kuhusu mambo hayo, naye akamweleza. Ndipo akaamuru afisa amshughulikie, kwa kumwambia, “Mrudishie huyu mwanamke kila kitu kilichokuwa mali yake, pamoja na mapato yote yaliyotokana na shamba lake tangu siku alipoondoka nchini hadi sasa.”
2KI 8:7 Al-Yasa akaenda Dameski, naye Ben-Hadadi mfalme wa Aramu alikuwa mgonjwa. Mfalme alipoambiwa, “Mtu wa Mungu amekuja hadi hapa,”
2KI 8:8 mfalme akamwambia Hazaeli, “Chukua zawadi na uende kumlaki mtu wa Mungu. Muulize Mwenyezi Mungu kupitia yeye, kwamba, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”
2KI 8:9 Hazaeli akaenda kumlaki Al-Yasa, akiwa amechukua zawadi ya kila kitu kizuri kilichopatikana Dameski, mizigo iliyobebwa na ngamia arobaini. Akaingia ndani na kusimama mbele yake, akasema, “Mwanao Ben-Hadadi mfalme wa Aramu amenituma niulize, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”
2KI 8:10 Al-Yasa akajibu, “Nenda ukamwambie, ‘Hakika utapona’; lakini Mwenyezi Mungu amenifunulia kwamba kweli atakufa.”
2KI 8:11 Al-Yasa akamkazia Hazaeli macho kwa nguvu hata akaona aibu. Kisha mtu wa Mungu akaanza kulia.
2KI 8:12 Hazaeli akauliza “Kwa nini bwana wangu analia?” Al-Yasa akajibu, “Kwa sababu najua mabaya utakayowatendea Waisraeli. Utachoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, kuwatupa chini kwa nguvu watoto wachanga, na kuwatumbua wanawake wenye mimba.”
2KI 8:13 Hazaeli akasema, “Itawezekanaje mtumishi wako, aliye mbwa tu, kufanya tendo la ajabu hivyo?” Al-Yasa akamjibu, “Mwenyezi Mungu amenionesha kuwa utakuwa mfalme wa Aramu.”
2KI 8:14 Kisha Hazaeli akamwacha Al-Yasa na kumrudia bwana wake. Ben-Hadadi akamuuliza, “Al-Yasa alikuambia nini?” Hazaeli akajibu, “Aliniambia kwamba hakika utapona.”
2KI 8:15 Lakini kesho yake Hazaeli akachukua nguo nzito, akailoweka ndani ya maji, akaitandaza juu ya uso wa mfalme, hivyo akafa. Kisha Hazaeli akawa mfalme baada yake.
2KI 8:16 Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, wakati huo Yehoshafati akiwa mfalme wa Yuda, Yehoramu mwana wa Yehoshafati akaanza kutawala kama mfalme wa Yuda.
2KI 8:17 Alikuwa na umri wa miaka thelathini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka nane.
2KI 8:18 Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti Ahabu. Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu.
2KI 8:19 Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi mtumishi wake, Mwenyezi Mungu hakutaka kuiangamiza Yuda. Alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili ya Daudi na wazao wake milele.
2KI 8:20 Wakati wa utawala wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kujiwekea mfalme wao wenyewe.
2KI 8:21 Basi Yehoramu akaenda Sairi pamoja na magari yake yote ya vita. Waedomu wakamzunguka yeye na majemadari wake wa magari yake ya vita, lakini akaondoka, akapenya usiku na kuwashambulia Waedomu. Hata hivyo, jeshi lake likatorokea nyumbani mwao.
2KI 8:22 Hadi leo Edomu wameasi dhidi ya Yuda. Libna pia wakaasi wakati huo huo.
2KI 8:23 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoramu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 8:24 Yehoramu akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 8:25 Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2KI 8:26 Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri mfalme wa Israeli.
2KI 8:27 Akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, na kutenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alikuwa ameoa kutoka nyumba ya Ahabu.
2KI 8:28 Ahazia akaenda vitani na Yoramu mwana wa Ahabu kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu.
2KI 8:29 Hivyo Mfalme Yoramu akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa na Waaramu huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu. Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.
2KI 9:1 Nabii Al-Yasa akamwita mtu mmoja kutoka kwa wana wa manabii na kumwambia, “Jikaze viuno, uichukue hii chupa ya mafuta, na uende Ramoth-Gileadi.
2KI 9:2 Ukifika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi. Nenda kwake, umtenge na wenzake, na umpeleke katika chumba cha ndani.
2KI 9:3 Kisha chukua hii chupa na umimine mafuta juu ya kichwa chake, nawe utangaze, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Ninakupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ Kisha ufungue mlango na ukimbie; usikawie!”
2KI 9:4 Basi yule kijana nabii akaenda Ramoth-Gileadi.
2KI 9:5 Alipofika, akawakuta maafisa wa jeshi wameketi pamoja, akasema, “Nina ujumbe wako, ee jemadari.” Yehu akauliza, “Kwa yupi miongoni mwetu?” Akamjibu, “Kwako wewe, jemadari.”
2KI 9:6 Yehu akainuka na kuingia ndani ya nyumba. Ndipo yule nabii akamimina mafuta juu ya kichwa cha Yehu, na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Ninakupaka mafuta uwe mfalme juu ya watu wa Mwenyezi Mungu, yaani Israeli.
2KI 9:7 Inakupasa uiangamize nyumba ya bwana wako Ahabu, nami nitalipiza kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii na damu ya watumishi wote wa Mwenyezi Mungu iliyomwagwa na Yezebeli.
2KI 9:8 Nyumba yote ya Ahabu itaangamia. Nitamkatilia mbali kila mzaliwa wa kiume wa Ahabu katika Israeli, aliye mtumwa ama aliye huru.
2KI 9:9 Nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama ile nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ile nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.
2KI 9:10 Kuhusu Yezebeli, mbwa watamla kwenye kiwanja huko Yezreeli, wala hakuna mtu atakayemzika.’ ” Kisha akafungua mlango na kukimbia.
2KI 9:11 Yehu alipotoka nje na kurudi kwenda kwa maafisa wenzake, mmoja wao akamuuliza, “Je, kila kitu ni salama? Kwa nini huyu mwenye wazimu alikuja kwako?” Yehu akajibu, “Wewe unamfahamu huyo mtu, na aina ya mambo ambayo yeye husema.”
2KI 9:12 Wakasema, “Hiyo siyo kweli! Tuambie.” Yehu akasema, “Haya ndio aliyoniambia: ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Ninakupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ ”
2KI 9:13 Wakaharakisha kuvua mavazi yao, na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupaza sauti wakisema, “Yehu ni mfalme!”
2KI 9:14 Basi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akapanga njama dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Waisraeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu,
2KI 9:15 lakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.”
2KI 9:16 Ndipo Yehu akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameenda kumwona.
2KI 9:17 Mlinzi aliyesimama juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.” Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”
2KI 9:18 Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ” Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.” Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”
2KI 9:19 Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ” Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”
2KI 9:20 Yule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”
2KI 9:21 Yoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli, na Ahazia mfalme wa Yuda, wakaondoka kila mmoja kwenye gari lake ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli.
2KI 9:22 Yoramu alipomwona Yehu, akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?” Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli bado ziko?”
2KI 9:23 Yoramu akageuka nyuma na kukimbia, akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini, Ahazia!”
2KI 9:24 Kisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake, naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake la vita.
2KI 9:25 Yehu akamwambia Bidkari, mwendeshaji wa gari lake la vita, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu ya vita nyuma ya Ahabu baba yake, wakati Mwenyezi Mungu alitoa unabii huu kumhusu:
2KI 9:26 ‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asema Mwenyezi Mungu.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu.”
2KI 9:27 Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake la vita kwenye njia inayoelekea Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido, akafia huko.
2KI 9:28 Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi.
2KI 9:29 (Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda.)
2KI 9:30 Kisha Yehu akaenda Yezreeli. Yezebeli aliposikia habari hii, akayapaka macho yake wanja, akatengeneza nywele zake na kutazama nje dirishani.
2KI 9:31 Yehu alipokuwa akiingia langoni, Yezebeli akasema, “Je, umekuja kwa amani, Zimri, wewe muuaji wa bwana wako?”
2KI 9:32 Yehu akaangalia juu dirishani na kuita, “Je, ni nani aliye upande wangu? Ni nani?” Matowashi wawili au watatu wakamtazama.
2KI 9:33 Yehu akasema, “Mtupeni huyo mwanamke chini!” Kwa hiyo wakamtupa chini, nayo sehemu ya damu yake ikatapanyika ukutani, na nyingine juu ya farasi walipokuwa wakimkanyaga kwa miguu yao.
2KI 9:34 Yehu akaingia ndani, akala na akanywa. Akasema, “Mshughulikieni huyo mwanamke aliyelaaniwa. Mzikeni, kwa sababu alikuwa binti ya mfalme.”
2KI 9:35 Lakini walipotoka kwenda kumzika, hawakukuta kitu chochote isipokuwa fuvu la kichwa, miguu yake na mikono.
2KI 9:36 Wakarudi na kumwambia Yehu, ambaye alisema, “Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu alilosema kwa kinywa cha mtumishi wake Ilya Mtishbi, kwamba: Katika kiwanja cha Yezreeli, mbwa wataila nyama ya Yezebeli.
2KI 9:37 Maiti ya Yezebeli itakuwa kama kinyesi juu ya ardhi katika uwanja wa Yezreeli, kwamba hakutakuwa mtu atakayeweza kusema, ‘Huyu ni Yezebeli.’ ”
2KI 10:1 Basi huko Samaria walikuwepo wana sabini wa nyumba ya Ahabu. Kwa hiyo Yehu akaandika barua na kuzituma Samaria: kwa maafisa wa Yezreeli, kwa wazee, na kwa walezi wa watoto wa Ahabu. Akasema,
2KI 10:2 “Mara tu barua hii itakapokufikia, kwa kuwa wana wa bwana wako wapo pamoja nawe, nawe una magari ya vita na farasi, mji wenye ngome na silaha,
2KI 10:3 mchague mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa bwana wako, na umweke kwenye kiti cha utawala cha baba yake. Kisha upigane kwa ajili ya nyumba ya bwana wako.”
2KI 10:4 Lakini wakaogopa sana na kusema, “Ikiwa wafalme wawili hawakuweza kupambana na Yehu, sisi tutawezaje?”
2KI 10:5 Basi msimamizi wa jumba la mfalme, mtawala wa mji, na wazee na walezi wakatuma ujumbe huu kwa Yehu: “Sisi tu watumishi wako, na tutafanya kila kitu utakachosema. Hatutamteuwa mtu yeyote kuwa mfalme. Wewe fanya uonalo kuwa ni bora.”
2KI 10:6 Kisha Yehu akawaandikia barua ya pili, akisema, “Ikiwa ninyi mko upande wangu na mtanitii mimi, twaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, na mnijie huku Yezreeli kesho wakati kama huu.” Wakati huo wana sabini wa mfalme walikuwa wakiishi pamoja na viongozi wa mji wa Samaria, waliokuwa wakiwalea.
2KI 10:7 Hiyo barua ilipowafikia, watu hawa wakawachukua wale wana sabini wa mfalme na kuwachinja wote. Wakaweka vichwa vyao ndani ya makapu na kumpelekea Yehu huko Yezreeli.
2KI 10:8 Mjumbe alipofika, akamwambia Yehu, “Wameleta vichwa vya wana wa mfalme.” Ndipo Yehu akaagiza, “Viwekeni malundo mawili katika ingilio la lango la mji hadi asubuhi.”
2KI 10:9 Kesho yake asubuhi, Yehu akatoka nje. Akasimama mbele ya watu wote na akasema, “Hamna hatia. Ni mimi niliyepanga njama dhidi ya bwana wangu na kumuua, lakini ni nani aliyewaua wote hawa?
2KI 10:10 Fahamuni basi kwamba, hakuna neno ambalo Mwenyezi Mungu amesema dhidi ya nyumba ya Ahabu ambalo halitatimia. Mwenyezi Mungu amefanya lile aliloahidi kupitia mtumishi wake Ilya.”
2KI 10:11 Hivyo Yehu akaua kila mtu huko Yezreeli aliyekuwa amebaki wa nyumba ya Ahabu, ikiwa ni pamoja na wakuu wake, rafiki zake wa karibu, na makuhani wake. Hakuacha yeyote anusurike.
2KI 10:12 Kisha Yehu akaondoka kuelekea Samaria. Alipokuwa njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya ya kondoo, yaani Beth-Ekedi ya wachunga kondoo,
2KI 10:13 Yehu akakutana na watu wa jamaa ya Ahazia mfalme wa Yuda, akauliza, “Ninyi ni nani?” Wao wakasema, “Sisi ni jamaa ya Ahazia, nasi tumeshuka kuwasalimu jamaa ya mfalme na ya mama malkia.”
2KI 10:14 Yehu akaagiza, “Wakamateni wakiwa hai!” Kwa hiyo wakawachukua wakiwa hai, watu arobaini na wawili, na kuwachinja kando ya kisima cha Beth-Ekedi. Hakuacha yeyote anusurike.
2KI 10:15 Baada ya kuondoka hapo, alimkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu, aliyekuwa akienda kumlaki. Yehu akamsalimu na kusema, “Je, moyo wako ni mnyofu kwangu kama moyo wangu ulivyo kwako?” Yehonadabu akajibu, “Ndiyo.” Yehu akasema, “Kama ndivyo, nipe mkono wako.” Yeye akampa mkono, naye Yehu akampandisha kwenye gari lake la vita.
2KI 10:16 Yehu akasema, “Twende pamoja ukaone wivu wangu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.” Hivyo wakasafiri pamoja kwenye gari lake la vita.
2KI 10:17 Yehu alipofika Samaria, akawaua wale wote waliokuwa wamesalia wa jamaa ya Ahabu, akawaangamiza, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu alilosema kupitia Ilya.
2KI 10:18 Kisha Yehu akawaleta watu wote pamoja na kuwaambia, “Ahabu alimtumikia Baali kidogo. Lakini Yehu atamtumikia zaidi.
2KI 10:19 Sasa waiteni manabii wote wa Baali, watumishi wake wote na makuhani wake wote. Hakikisheni kwamba hakuna hata mmoja atakayekosekana, kwa sababu ninaenda kutoa kafara kubwa sana kwa Baali. Yeyote atakayeshindwa kuja hataendelea kuishi.” Lakini Yehu alifanya hivyo kwa hila ili apate kuwaangamiza watumishi wote wa Baali.
2KI 10:20 Yehu akasema, “Itisheni kusanyiko kwa heshima ya Baali.” Basi wakatangaza jambo hilo.
2KI 10:21 Kisha Yehu akapeleka ujumbe katika Israeli yote, nao watumishi wote wa Baali wakaja, hakuna hata mmoja ambaye hakufika. Wakasongamana ndani ya hekalu la Baali hadi likajaa tangu mlango hadi mwisho wake.
2KI 10:22 Naye Yehu akamwambia yule aliyekuwa mtunza chumba cha mavazi, “Leta majoho kwa ajili ya watumishi wote wa Baali.” Basi akawaletea majoho.
2KI 10:23 Kisha Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu wakaingia ndani ya hekalu la Baali. Yehu akawaambia watumishi wa Baali, “Tazameni kila mahali mhakikishe kwamba hakuna hata mtumishi mmoja wa Mwenyezi Mungu aliye hapa pamoja nanyi, ila ni watumishi wa Baali tu.”
2KI 10:24 Kwa hiyo wakaingia ndani ili kutoa kafara na sadaka ya kuteketezwa. Wakati huu, Yehu alikuwa amewaweka watu wake themanini akiwa amewapa onyo kwamba, “Ikiwa mmoja wenu atamwachia mtu yeyote ninayemweka mikononi mwenu atoroke, itakuwa uhai wako kwa uhai wake.”
2KI 10:25 Mara baada ya Yehu kutoa sadaka ya kuteketezwa, akawaamuru walinzi na maafisa: “Ingieni ndani, waueni; asitoroke hata mmoja.” Basi wakawakatakata kwa upanga. Walinzi na maafisa wakazitupa zile maiti nje, kisha wakaingia mahali pa ndani pa ibada katika hekalu la Baali.
2KI 10:26 Wakaileta ile nguzo ya kuabudiwa nje ya hekalu la Baali, na wakaichoma moto.
2KI 10:27 Wakabomoa ile nguzo ya kuabudiwa ya Baali pamoja na hekalu la Baali, nao watu wakapafanya kuwa choo hadi leo.
2KI 10:28 Kwa hiyo Yehu akaangamiza kuabudiwa kwa Baali katika Israeli.
2KI 10:29 Hata hivyo, Yehu hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, yaani kuabudu ndama za dhahabu huko Betheli ya Dani.
2KI 10:30 Mwenyezi Mungu akamwambia Yehu, “Kwa kuwa umefanya vyema kwa kutimiza yaliyo sawa machoni pangu, na umetenda kwa nyumba ya Ahabu yale yote niliyokuwa nimekusudia kutenda, wazao wako wataketi kwenye kiti cha utawala cha Israeli hadi kizazi cha nne.”
2KI 10:31 Lakini Yehu hakuwa mwangalifu kushika sheria za Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda.
2KI 10:32 Katika siku hizo, Mwenyezi Mungu akaanza kupunguza ukubwa wa Israeli. Hazaeli akawashinda Waisraeli sehemu zote za nchi yao
2KI 10:33 mashariki mwa Yordani, katika nchi yote ya Gileadi (eneo la Gadi, Reubeni na Manase), kutoka Aroeri karibu na Bonde la Arnoni kupitia Gileadi hadi Bashani.
2KI 10:34 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehu, yote aliyofanya na mafanikio yake yote, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 10:35 Yehu akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 10:36 Muda Yehu aliotawala Israeli huko Samaria ulikuwa miaka ishirini na nane.
2KI 11:1 Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuangamiza jamaa yote ya mfalme.
2KI 11:2 Lakini Yehosheba, binti ya Mfalme Yehoramu, aliyekuwa pia dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa.
2KI 11:3 Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake katika Hekalu la Mwenyezi Mungu kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.
2KI 11:4 Katika mwaka wa saba, Yehoyada akatumania wakuu wa vikundi vya mamia, na Wakari na walinzi, nao wakaletwa kwake katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Alifanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Ndipo akawaonesha mwana wa mfalme.
2KI 11:5 Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda jumba la kifalme,
2KI 11:6 theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu.
2KI 11:7 Nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika siku ya Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme.
2KI 11:8 Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”
2KI 11:9 Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada.
2KI 11:10 Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 11:11 Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.
2KI 11:12 Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakampaka mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”
2KI 11:13 Athalia aliposikia kelele za walinzi pamoja na watu, akawaendea watu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 11:14 Akaangalia, na tazama, mfalme alikuwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”
2KI 11:15 Kuhani Yehoyada akawaamuru majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, “Mtoeni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.”
2KI 11:16 Basi wakamkamata Athalia alipofika mahali farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuua hapo.
2KI 11:17 Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Mwenyezi Mungu na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi Mungu. Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu.
2KI 11:18 Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu. Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 11:19 Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamteremsha mfalme kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu na kwenda kwenye jumba la mfalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha ufalme;
2KI 11:20 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga nyumbani mwa mfalme.
2KI 11:21 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.
2KI 12:1 Katika mwaka wa saba wa utawala wa Yehu, Yoashi alianza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia, kutoka Beer-Sheba.
2KI 12:2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu miaka yote ambayo Yehoyada kuhani alikuwa akimwelekeza.
2KI 12:3 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
2KI 12:4 Yoashi akawaambia makuhani, “Kusanyeni fedha zote zitakazoletwa kama sadaka takatifu kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu, yaani fedha zilizokusanywa watu walipohesabiwa, fedha zilizopokelewa kutokana na nadhiri za watu binafsi, na fedha zilizoletwa kwa hiari hekaluni.
2KI 12:5 Kila kuhani na apokee fedha kutoka kwa mmoja wa watunza hazina, nazo zitumike kukarabati uharibifu wowote unaoonekana katika Hekalu.”
2KI 12:6 Lakini ikawa kufikia mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Mfalme Yoashi, makuhani walikuwa bado hawajalikarabati Hekalu.
2KI 12:7 Kwa hiyo Mfalme Yoashi akamwita Yehoyada kuhani na makuhani wengine, akawauliza, “Kwa nini hamtengenezi uharibifu uliofanyika hekaluni? Msichukue fedha zaidi kutoka kwa watunza hazina wenu kwa ajili ya matumizi yenu, lakini kuanzia sasa ni lazima fedha yote itumike kwa ajili ya kukarabati Hekalu.”
2KI 12:8 Makuhani wakakubali kuwa hawatakusanya tena fedha kutoka kwa watu na kwamba hawatakarabati Hekalu wenyewe.
2KI 12:9 Yehoyada kuhani akachukua kisanduku na akatoboa tundu kwenye kifuniko chake. Akakiweka kando ya madhabahu upande wa kulia unapoingia hekaluni mwa Mwenyezi Mungu. Makuhani waliolinda ingilio wakaweka ndani ya kisanduku fedha zote ambazo zililetwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 12:10 Kila mara walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani ya kisanduku, mwandishi wa mfalme na kuhani mkuu walikuja, wakazihesabu fedha hizo zilizoletwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, na kuziweka katika mifuko.
2KI 12:11 Walipothibitisha kiasi cha hizo fedha, waliwapa watu walioteuliwa kusimamia kazi katika Hekalu. Kwa fedha hizo, wakawalipa wale watu waliofanya kazi katika Hekalu la Mwenyezi Mungu: maseremala na wajenzi,
2KI 12:12 waashi na wakata mawe. Walinunua mbao na mawe ya kuchongwa kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu la Mwenyezi Mungu, na kulipia gharama nyingine zote za kulitengeneza.
2KI 12:13 Fedha zilizoletwa kwenye Hekalu hazikutumiwa kutengenezea masinia ya fedha, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, tarumbeta wala vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au fedha kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu;
2KI 12:14 zililipwa kwa wafanyakazi, ambao walizitumia kwa kukarabati Hekalu.
2KI 12:15 Wao hawakudai hesabu ya fedha kutoka kwa wale waliowapa ili kuwalipa wafanyakazi, kwa sababu walifanya kwa uaminifu wote.
2KI 12:16 Fedha zilizopatikana kutokana na sadaka za hatia na sadaka za dhambi hazikuletwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu; zilikuwa mali ya makuhani.
2KI 12:17 Basi Hazaeli mfalme wa Aramu akapanda kuishambulia Gathi, akaiteka. Kisha akageuka ili kuishambulia Yerusalemu.
2KI 12:18 Lakini Yoashi mfalme wa Yuda akavichukua vyombo vyote vitakatifu vilivyowekwa wakfu na baba zake, yaani Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, wafalme wa Yuda, na vyombo vyake vyote ambavyo alikuwa ameviweka wakfu, pamoja na dhahabu yote iliyokuwa katika hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika jumba la kifalme; akazipeleka kwa Hazaeli mfalme wa Aramu, ambaye hatimaye aliondoka Yerusalemu.
2KI 12:19 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yoashi na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 12:20 Maafisa wake wakapanga njama dhidi yake, nao wakamuua Yoashi huko Beth-Milo, kwenye barabara inayoteremka kuelekea Sila.
2KI 12:21 Maafisa waliomuua walikuwa Yozabadi mwana wa Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa Shomeri. Akafa na akazikwa na baba zake katika Mji wa Daudi. Naye Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 13:1 Katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wa Yoashi mwana wa Ahazia mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka kumi na saba.
2KI 13:2 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu kwa kufuata dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, na wala hakuziacha.
2KI 13:3 Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Israeli na kwa muda mrefu akawaweka chini ya utawala wa Hazaeli mfalme wa Aramu, na Ben-Hadadi mwanawe.
2KI 13:4 Ndipo Yehoahazi akamsihi Mwenyezi Mungu ampe rehema, naye Mwenyezi Mungu akamsikiliza, kwa maana aliona jinsi mfalme wa Aramu alivyokuwa akiwatesa Israeli vikali.
2KI 13:5 Mwenyezi Mungu akamtoa mwokozi kwa ajili ya Israeli, nao wakaokoka kutoka mamlaka ya Aramu. Hivyo Waisraeli wakaishi katika nyumba zao wenyewe kama ilivyokuwa hapo awali.
2KI 13:6 Lakini hawakuziacha dhambi za nyumba ya Yeroboamu, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, bali wakaendelea kuzitenda. Nguzo ya Ashera pia iliendelea kusimama katika Samaria.
2KI 13:7 Hapakubaki kitu chochote katika jeshi la Yehoahazi isipokuwa wapanda farasi hamsini, magari kumi ya vita na askari wa miguu elfu kumi, kwa kuwa mfalme wa Aramu alikuwa amewaangamiza hao wengine na kuwafanya kama mavumbi wakati wa kupura nafaka.
2KI 13:8 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoahazi, yote aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 13:9 Yehoahazi akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoashi mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 13:10 Katika mwaka wa thelathini na saba wa utawala wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala Israeli huko Samaria, naye akatawala miaka kumi na sita.
2KI 13:11 Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, na hakuacha dhambi yoyote kati ya zile za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, bali aliendelea kuzitenda.
2KI 13:12 Na kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, yote aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 13:13 Yehoashi akalala na baba zake, naye Yeroboamu akawa mfalme baada yake. Yehoashi akazikwa Samaria na wafalme wa Israeli.
2KI 13:14 Wakati huu, Al-Yasa alikuwa anaugua ugonjwa ambao baadaye ulimuua. Yehoashi mfalme wa Israeli akashuka kwenda kumwona na kumlilia. Akalia, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!”
2KI 13:15 Al-Yasa akasema, “Leta upinde na baadhi ya mishale,” naye mfalme akafanya hivyo.
2KI 13:16 Al-Yasa akamwambia mfalme wa Israeli, “Shika upinde mikononi mwako.” Alipokwisha kuuchukua, Al-Yasa akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
2KI 13:17 Al-Yasa akasema, “Fungua dirisha la mashariki,” naye akalifungua. Al-Yasa akasema, “Piga mshale!” Naye akapiga mshale. Al-Yasa akasema, “Mshale wa ushindi wa Mwenyezi Mungu, mshale wa ushindi juu ya Aramu! Utawaangamiza Waaramu kabisa huko Afeki.”
2KI 13:18 Kisha akasema, “Chukua mishale,” naye mfalme akaichukua. Al-Yasa akamwambia, “Piga ardhi kwa hiyo mishale.” Akaipiga mara tatu, halafu akaacha.
2KI 13:19 Mtu wa Mungu akamkasirikia na akasema, “Ungepiga chini mara tano au sita, ndipo ungeishinda Aramu na kuiangamiza kabisa. Lakini sasa utaishinda mara tatu tu.”
2KI 13:20 Al-Yasa akafa, nao wakamzika. Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli.
2KI 13:21 Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Al-Yasa. Ile maiti ilipogusa mifupa ya Al-Yasa, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake.
2KI 13:22 Hazaeli mfalme wa Aramu aliwatesa Israeli wakati wote wa utawala wa Yehoahazi.
2KI 13:23 Lakini Mwenyezi Mungu akawarehemu na akawahurumia, akaonesha kujishughulisha nao kwa sababu ya agano lake na Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Hadi leo, hajawaangamiza wala kuwafukuza mbele zake.
2KI 13:24 Hazaeli mfalme wa Shamu akafa, naye Ben-Hadadi mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 13:25 Kisha Yehoashi mwana wa Yehoahazi akateka tena kutoka kwa Ben-Hadadi mwana wa Hazaeli ile miji aliyokuwa ameitwaa kwa vita kutoka kwa baba yake Yehoahazi. Yehoashi alimshinda mara tatu, hivyo akaweza kuiteka tena ile miji ya Waisraeli.
2KI 14:1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2KI 14:2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu.
2KI 14:3 Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake.
2KI 14:4 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
2KI 14:5 Baada ya ufalme kuimarika mkononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake.
2KI 14:6 Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Musa, ambako Mwenyezi Mungu aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”
2KI 14:7 Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.
2KI 14:8 Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tukabiliane uso kwa uso.”
2KI 14:9 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti.
2KI 14:10 Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani mwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
2KI 14:11 Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda.
2KI 14:12 Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani mwake.
2KI 14:13 Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa mia nne.
2KI 14:14 Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria.
2KI 14:15 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 14:16 Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa Samaria na wafalme wa Israeli. Naye Yeroboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 14:17 Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na tano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli.
2KI 14:18 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amazia, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 14:19 Wakapanga njama dhidi ya Amazia huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuua huko.
2KI 14:20 Akarudishwa kwa farasi, akazikwa huko Yerusalemu pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi.
2KI 14:21 Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, na kumfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake.
2KI 14:22 Ndiye aliijenga upya Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala na baba zake.
2KI 14:23 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, naye akatawala kwa miaka arobaini na moja.
2KI 14:24 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, na hakuacha dhambi hata moja ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda.
2KI 14:25 Ndiye alirudishia mipaka ya Israeli kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bahari ya Araba, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, lililosemwa kupitia mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii kutoka Gath-Heferi.
2KI 14:26 Mwenyezi Mungu alikuwa ameona jinsi kila mmoja katika Israeli, awe mtumwa au aliye huru, alivyoteseka kwa uchungu; hapakuwa na yeyote wa kuwasaidia.
2KI 14:27 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa hajasema kuwa atafuta jina la Israeli chini ya mbingu, akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.
2KI 14:28 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, yote aliyoyafanya na mafanikio yake ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyorudisha Dameski na Hamathi kwa Israeli, ambayo ilikuwa mali ya Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 14:29 Yeroboamu akalala na baba zake, wafalme wa Israeli. Naye Zekaria mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 15:1 Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Azaria mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2KI 15:2 Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na mbili. Mama yake aliitwa Yekolia, kutoka Yerusalemu.
2KI 15:3 Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama Amazia baba yake alivyofanya.
2KI 15:4 Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
2KI 15:5 Mwenyezi Mungu akampiga mfalme kwa ukoma hadi siku aliyokufa, naye aliishi katika nyumba iliyotengwa peke yake. Yothamu mwana wa mfalme akawa msimamizi wa jumba la mfalme, na akawatawala watu wa nchi.
2KI 15:6 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Azaria na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 15:7 Azaria akalala na baba zake, naye akazikwa karibu nao katika Mji wa Daudi. Naye Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 15:8 Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Zekaria mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miezi sita.
2KI 15:9 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyofanya. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
2KI 15:10 Shalumu mwana wa Yabeshi akapanga njama dhidi ya Zekaria. Akamshambulia mbele ya watu, akamuua, na akawa mfalme baada yake.
2KI 15:11 Matukio mengine ya utawala wa Zekaria yameandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
2KI 15:12 Kwa hiyo neno la Mwenyezi Mungu lililonenwa kwa Yehu likatimia, kwamba, “Wazao wako wataketi kwenye kiti cha utawala cha Israeli hadi kizazi cha nne.”
2KI 15:13 Shalumu mwana wa Yabeshi akawa mfalme katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda, naye akatawala katika Samaria kwa mwezi mmoja.
2KI 15:14 Kisha Menahemu mwana wa Gadi akaenda kutoka Tirsa hadi Samaria. Akamshambulia Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamuua, na akawa mfalme baada yake.
2KI 15:15 Matukio mengine ya utawala wa Shalumu, na njama alizozipanga, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
2KI 15:16 Wakati ule, akianzia Tirsa, Menahemu alishambulia Tifsa na kila mtu ndani yake, na wale waliokuwa maeneo jirani, kwa sababu walikataa kufungua malango yao. Akaiangamiza Tifsa yote, na kuwapasua tumbo wanawake wote wenye mimba.
2KI 15:17 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi akawa mfalme wa Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka kumi.
2KI 15:18 Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Katika wakati wa utawala wake wote, hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
2KI 15:19 Kisha Pulu mfalme wa Ashuru akaishambulia Israeli. Menahemu mfalme wa Israeli akampa talanta elfu moja za fedha ili amsaidie na kumwezesha katika utawala wake.
2KI 15:20 Menahemu akatoza fedha hizi kwa nguvu kutoka kwa Israeli. Kila mtu tajiri alilazimika kuchanga shekeli hamsini za fedha ambazo alipewa mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akajiondoa na hakuendelea kuikalia nchi.
2KI 15:21 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Menahemu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 15:22 Menahemu akalala na baba zake. Naye Pekahia mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 15:23 Katika mwaka wa hamsini wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, akatawala miaka miwili.
2KI 15:24 Pekahia akafanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
2KI 15:25 Mmoja wa maafisa wake wakuu, Peka mwana wa Remalia, akapanga njama dhidi yake. Akachukua watu hamsini wa Gileadi pamoja naye, akamuua Pekahia, pamoja na Argobu na Aria, katika ngome ya jumba la kifalme huko Samaria. Kwa hiyo Peka akamuua Pekahia, naye akawa mfalme baada yake.
2KI 15:26 Matukio mengine ya utawala wa Pekahia na yote aliyoyafanya yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
2KI 15:27 Katika mwaka wa hamsini na mbili wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Peka mwana wa Remalia akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, naye alitawala miaka ishirini.
2KI 15:28 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
2KI 15:29 Wakati wa utawala wa Peka mfalme wa Israeli, Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru alikuja na kuteka Iyoni, Abel-Beth-Maaka, Yanoa, Kedeshi na Hazori. Akateka miji ya Gileadi na Galilaya, pamoja na nchi yote ya Naftali, na kuwahamishia watu wote Ashuru.
2KI 15:30 Kisha Hoshea mwana wa Ela akapanga njama dhidi ya Peka mwana wa Remalia. Hoshea akamshambulia Peka na kumuua, kisha akawa mfalme baada yake katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.
2KI 15:31 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Peka na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
2KI 15:32 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2KI 15:33 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki.
2KI 15:34 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya.
2KI 15:35 Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 15:36 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yothamu na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 15:37 (Katika siku hizo, Mwenyezi Mungu akaanza kuwatuma Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia dhidi ya Yuda.)
2KI 15:38 Yothamu akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi, mji wa baba zake. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 16:1 Katika mwaka wa kumi na saba wa utawala wa Peka mwana wa Remalia, Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2KI 16:2 Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
2KI 16:3 Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, na hata akamtoa kafara mwanawe katika moto, akifuata njia za machukizo za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ameyafukuza mbele ya Waisraeli.
2KI 16:4 Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda.
2KI 16:5 Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli wakaondoka kwenda kupigana dhidi ya Yerusalemu na kumzingira Ahazi kwa jeshi, lakini hawakuweza kumshinda.
2KI 16:6 Wakati ule, Resini mfalme wa Aramu akaurudisha mji wa Elathi kwa Aramu kwa kuwafukuza watu wa Yuda. Kisha Waedomu wakahamia Elathi, nao wanaishi huko hadi leo.
2KI 16:7 Ahazi akatuma wajumbe kumwambia Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru kwamba, “Mimi ni mtumishi na mtumwa wako. Njoo na uniokoe kutoka mkononi mwa mfalme wa Aramu na wa mfalme wa Israeli, ambao wananishambulia.”
2KI 16:8 Naye Ahazi akachukua fedha na dhahabu zilizopatikana ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika hazina ya jumba la mfalme, na kuzituma kama zawadi kwa mfalme wa Ashuru.
2KI 16:9 Mfalme wa Ashuru akamwitikia kwa kushambulia Dameski na kuiteka. Akawahamishia wenyeji wake huko Kiri, na kumuua Resini.
2KI 16:10 Kisha Mfalme Ahazi akaenda Dameski kukutana na Tiglath-Pileseri wa Ashuru. Akaona madhabahu huko Dameski, naye akamtumia Uria kuhani mchoro wa hayo madhabahu, pamoja na maelezo ya mpango kamili wa ujenzi wake.
2KI 16:11 Kwa hiyo Uria kuhani akajenga madhabahu kulingana na mipango yote ambayo Mfalme Ahazi alikuwa ameituma kutoka Dameski, na akamaliza ujenzi kabla ya Mfalme Ahazi kurudi.
2KI 16:12 Mfalme aliporudi kutoka Dameski na kuona hayo madhabahu, akayasogelea na kutoa sadaka juu yake.
2KI 16:13 Akatoa sadaka yake ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, akamimina sadaka ya kinywaji na kunyunyizia damu ya sadaka zake za amani juu ya hayo madhabahu.
2KI 16:14 Mfalme Ahazi akayaondoa madhabahu ya zamani ya shaba kutoka hapo mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, yaliyokuwa yamesimama kati ya ingilio la Hekalu na hayo madhabahu mapya, naye akayaweka upande wa kaskazini mwa hayo madhabahu mapya.
2KI 16:15 Ndipo Mfalme Ahazi akatoa amri zifuatazo kwa Uria kuhani: “Juu ya hayo madhabahu kubwa mapya, toa sadaka ya asubuhi ya kuteketezwa na sadaka ya jioni ya nafaka, sadaka ya mfalme ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, pamoja na sadaka yao ya nafaka na sadaka yao ya kinywaji. Unyunyize juu ya hayo madhabahu damu yote ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu. Lakini mimi nitatumia hayo madhabahu ya zamani ya shaba kwa ajili ya kutafuta uongozi.”
2KI 16:16 Naye Uria kuhani akafanya kama Mfalme Ahazi alivyoagiza.
2KI 16:17 Mfalme Ahazi akaondoa mbao za pembeni na kuondoa masinia kwenye vile vishikilio vilivyohamishika. Akaondoa ile Bahari kutoka mafahali wa shaba walioishikilia, na kuiweka kwenye kitako cha jiwe.
2KI 16:18 Kwa heshima ya mfalme wa Ashuru, akaliondoa pia pazia la Sabato lililokuwa limewekwa ndani ya Hekalu, na akaondoa ile njia ya kifalme ya kuingia kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 16:19 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ahazi na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 16:20 Ahazi akalala na baba zake, naye akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Hezekia mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 17:1 Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka tisa.
2KI 17:2 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia.
2KI 17:3 Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akaenda na kumshambulia Mfalme Hoshea, ambaye hapo awali alikuwa akimlipa ushuru kwa sababu alikuwa mtumishi wake.
2KI 17:4 Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri. Wala hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumfunga gerezani.
2KI 17:5 Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuuzingira kwa miaka mitatu.
2KI 17:6 Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawakalisha huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.
2KI 17:7 Yote haya yalitukia kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyekuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine,
2KI 17:8 na kufuata desturi za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta.
2KI 17:9 Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, walijijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote.
2KI 17:10 Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda.
2KI 17:11 Wakafukiza uvumba kila mahali pa juu pa kuabudia, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha Mwenyezi Mungu.
2KI 17:12 Wakatumikia sanamu, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.”
2KI 17:13 Mwenyezi Mungu akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na Torati yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii, na ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu, manabii.”
2KI 17:14 Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumwamini Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
2KI 17:15 Walizikataa amri zake, na agano alilolifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya.”
2KI 17:16 Wakayaacha maagizo yote ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali.
2KI 17:17 Wakawatoa kafara watoto wao wa kiume na wa kike katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Mwenyezi Mungu, wakamghadhibisha.
2KI 17:18 Basi Mwenyezi Mungu akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki.
2KI 17:19 Hata hivyo, Yuda nao hawakuzishika amri za Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli walikuwa wamezianzisha.
2KI 17:20 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kwenye uwepo wake.
2KI 17:21 Alipokwisha kuwatenga Israeli mbali na nyumba ya Daudi, wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme wao. Yeroboamu akawashawishi Israeli waache kumfuata Mwenyezi Mungu na akawasababisha kutenda dhambi kuu.
2KI 17:22 Nao Israeli wakadumu katika dhambi zote za Yeroboamu mwana wa Nebati, nao hawakuziacha
2KI 17:23 hadi Mwenyezi Mungu alipowaondoa kwenye uwepo wake, kama vile alivyokuwa ameonya kupitia watumishi wake wote manabii. Hivyo watu wa Israeli wakaondolewa kutoka nchi yao kwenda uhamishoni Ashuru, nao wako huko hata leo.
2KI 17:24 Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake.
2KI 17:25 Wakati walianza kuishi humo, hawakumwabudu Mwenyezi Mungu, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu.
2KI 17:26 Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.”
2KI 17:27 Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.”
2KI 17:28 Basi mmoja wa makuhani aliyekuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli, akawafundisha jinsi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu.
2KI 17:29 Hata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka katika nyumba za ibada za sanamu ambazo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu pa kuabudia.
2KI 17:30 Watu kutoka Babeli wakatengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakatengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakatengeneza Ashima;
2KI 17:31 Waavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.
2KI 17:32 Walimwabudu Mwenyezi Mungu, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa ibada kwenye mahali pa juu pa kuabudia.
2KI 17:33 Walimwabudu Mwenyezi Mungu, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka.
2KI 17:34 Hadi leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu Mwenyezi Mungu wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo Mwenyezi Mungu aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli.
2KI 17:35 Mwenyezi Mungu alipofanya agano na Waisraeli, aliwaamuru: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu.
2KI 17:36 Bali imewapasa kumwabudu Mwenyezi Mungu aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu, na kwake yeye mtatoa dhabihu.
2KI 17:37 Imewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine.
2KI 17:38 Msisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine.
2KI 17:39 Bali, mtamwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.”
2KI 17:40 Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali.
2KI 17:41 Hata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu Mwenyezi Mungu, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Hadi leo watoto wao na wajukuu wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.
2KI 18:1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Hezekia mwana wa Ahazi mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2KI 18:2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria.
2KI 18:3 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama Daudi baba yake alivyofanya.
2KI 18:4 Akapaondoa mahali pa juu pa kuabudia, akazivunja sanamu, akakatakata nguzo za Ashera. Akavunja vipande vipande ile nyoka ya shaba Musa aliyotengeneza, kwa kuwa hadi siku hizo Waisraeli walikuwa wanaifukizia uvumba. (Ilikuwa ikiitwa Nehushtani).
2KI 18:5 Hezekia aliweka tumaini lake kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Hapakuwa na mfalme mwingine wa kufanana naye miongoni mwa wafalme wa Yuda, kabla yake au baada yake.
2KI 18:6 Alishikamana na Mwenyezi Mungu kwa bidii wala hakuacha kumfuata; alishika amri ambazo Mwenyezi Mungu alikuwa amempa Musa.
2KI 18:7 Naye Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye, akafanikiwa katika kila alichokifanya. Aliasi dhidi ya mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia.
2KI 18:8 Kuanzia mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, aliwashinda Wafilisti, hadi kufikia Gaza na himaya yake yote.
2KI 18:9 Mwaka wa nne wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa saba wa Hoshea mwana wa Ela kutawala Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alienda kushambulia Samaria na kuuzingira.
2KI 18:10 Baada ya miaka mitatu Waashuru wakautwaa. Kwa hiyo Samaria ulitekwa katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea mfalme wa Israeli.
2KI 18:11 Mfalme wa Ashuru akawahamishia Waisraeli huko Ashuru na akawaweka Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.
2KI 18:12 Hili lilitokea kwa sababu hawakumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wao, lakini walikuwa wamevunja agano lake, yale yote ambayo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwaamuru. Hawakuzisikiliza amri wala kuzitimiza.
2KI 18:13 Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka.
2KI 18:14 Basi Hezekia mfalme wa Yuda akamtumia ujumbe mfalme wa Ashuru huko Lakishi akisema: “Nimefanya makosa. Ondoka katika nchi yangu, nami nitakulipa chochote unachokitaka kwangu.” Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia mfalme wa Yuda talanta mia tatu za fedha, na talanta thelathini za dhahabu.
2KI 18:15 Basi Hezekia akampa fedha yote iliyopatikana ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika hazina ya jumba la mfalme.
2KI 18:16 Wakati huu Hezekia mfalme wa Yuda akabandua dhahabu yote iliyokuwa imefunika milango na miimo ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, akampa mfalme wa Ashuru.
2KI 18:17 Mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wake mkuu, na afisa wake mkuu, na jemadari wa jeshi, pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Wakaja Yerusalemu na kusimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi.
2KI 18:18 Wakaagiza mfalme aitwe. Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakawaendea.
2KI 18:19 Yule jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia: “ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako?
2KI 18:20 Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi?
2KI 18:21 Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea.
2KI 18:22 Nawe ukiniambia, “Tunamtumainia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya katika Yerusalemu”?
2KI 18:23 “ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao!
2KI 18:24 Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi?
2KI 18:25 Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza mahali hapa pasipo neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”
2KI 18:26 Ndipo Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania, watu walio juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”
2KI 18:27 Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mkojo wao wenyewe?”
2KI 18:28 Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru!
2KI 18:29 Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa mkononi mwangu.
2KI 18:30 Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Mwenyezi Mungu kwa kuwaambia, ‘Hakika Mwenyezi Mungu atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’
2KI 18:31 “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe,
2KI 18:32 hadi nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu, nchi ya mizeituni na asali. Chagueni uzima, sio mauti! “Msimsikilize Hezekia, kwa kuwa anawapotosha asemapo, ‘Mwenyezi Mungu atatuokoa.’
2KI 18:33 Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru?
2KI 18:34 Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu?
2KI 18:35 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mwenyezi Mungu aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”
2KI 18:36 Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”
2KI 18:37 Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia vile jemadari wa jeshi alivyosema.
2KI 19:1 Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa gunia, naye akaenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 19:2 Akawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi.
2KI 19:3 Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa.
2KI 19:4 Yamkini Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.”
2KI 19:5 Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya,
2KI 19:6 Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo.
2KI 19:7 Sikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake, naye atakaposikia ujumbe fulani, atarudi nchi yake mwenyewe; nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’ ”
2KI 19:8 Jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.
2KI 19:9 Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka Mkushi, mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Basi akatuma tena wajumbe kwa Hezekia na neno hili:
2KI 19:10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’
2KI 19:11 Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa?
2KI 19:12 Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa, hiyo miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari?
2KI 19:13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”
2KI 19:14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe, naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, akaikunjua mbele za Mwenyezi Mungu.
2KI 19:15 Naye Hezekia akamwomba Mwenyezi Mungu akisema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, unayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi.
2KI 19:16 Tega sikio, Ee Mwenyezi Mungu, usikie; fungua macho yako, Ee Mwenyezi Mungu, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.
2KI 19:17 “Ni kweli, Ee Mwenyezi Mungu, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao.
2KI 19:18 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
2KI 19:19 Sasa basi, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe Mungu pekee.”
2KI 19:20 Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru.
2KI 19:21 Hili ndilo neno ambalo Mwenyezi Mungu amelisema dhidi yake: “ ‘Bikira Binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki. Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.
2KI 19:22 Ni nani uliyemtukana na kumkufuru? Ni nani uliyepaza sauti yako dhidi yake, na kumwinulia macho yako kwa kiburi? Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!
2KI 19:23 Kupitia kwa wajumbe wako umelundika matukano juu ya Bwana. Nawe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita, nimepanda juu ya vilele vya milima, vilele vya juu sana katika Lebanoni. Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu, misunobari yake iliyo bora sana. Nimefikia sehemu zake zilizo mbali sana, misitu yake iliyo mizuri sana.
2KI 19:24 Nimechimba visima katika nchi za kigeni na kunywa maji yake. Kwa nyayo za miguu yangu nimekausha vijito vyote vya Misri.”
2KI 19:25 “ ‘Je, hujasikia? Zamani sana niliamuru hili. Siku za kale nilipanga hili; sasa nimelifanya litokee, kwamba umegeuza miji yenye ngome kuwa malundo ya mawe.
2KI 19:26 Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu, wanavunjika mioyo na kuaibishwa. Wao ni kama mimea katika shamba, kama machipukizi mororo ya kijani, kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba, ambayo hukauka kabla ya kukua.
2KI 19:27 “ ‘Lakini ninajua mahali ukaapo, kutoka kwako na kuingia kwako, na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
2KI 19:28 Kwa sababu unaghadhibika dhidi yangu, na ufidhuli wako umefika masikioni mwangu, nitaweka ndoana yangu puani mwako na hatamu yangu kinywani mwako, nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.’
2KI 19:29 “Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kinachoota chenyewe, na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake. Lakini katika mwaka wa tatu, panda na uvune, panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.
2KI 19:30 Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.
2KI 19:31 Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki, na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika. Wivu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni utatimiza jambo hili.
2KI 19:32 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu wala hatapiga mshale hapa. Hatakuja mbele yake akiwa na ngao, wala kupanga majeshi kuuzingira.
2KI 19:33 Kwa njia ile aliyoijia, ndiyo atakayorudi; hataingia katika mji huu, asema Mwenyezi Mungu.
2KI 19:34 Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.”
2KI 19:35 Usiku ule, malaika wa Mwenyezi Mungu akaenda, akawaua wanajeshi elfu mia moja na themanini na tano katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali!
2KI 19:36 Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.
2KI 19:37 Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 20:1 Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”
2KI 20:2 Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Mwenyezi Mungu:
2KI 20:3 “Ee Mwenyezi Mungu, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.
2KI 20:4 Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati, neno la Mwenyezi Mungu likamjia, akaambiwa:
2KI 20:5 “Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako; nitakuponya. Siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 20:6 Nitakuongezea miaka kumi na tano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’ ”
2KI 20:7 Kisha Isaya akasema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini.” Wakafanya hivyo na kuiweka kwenye jipu, naye akapona.
2KI 20:8 Hezekia alimuuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwamba Mwenyezi Mungu ataniponya mimi, na kwamba nitapanda kwenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu siku ya tatu tangu leo?”
2KI 20:9 Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Mwenyezi Mungu kwako kwamba Mwenyezi Mungu atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”
2KI 20:10 Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”
2KI 20:11 Ndipo nabii Isaya akamwita Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.
2KI 20:12 Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia.
2KI 20:13 Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonesha vitu vyote vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina yake. Hapakuwa na kitu katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonesha.
2KI 20:14 Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?” Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”
2KI 20:15 Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?” Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu. Hakuna kitu katika hazina yangu ambacho sikuwaonesha.”
2KI 20:16 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi Mungu:
2KI 20:17 Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba hadi siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Mwenyezi Mungu.
2KI 20:18 Nao baadhi ya wazao wako, mwili wako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mateka, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
2KI 20:19 Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Mwenyezi Mungu ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”
2KI 20:20 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote, na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ulioleta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 20:21 Hezekia akalala na baba zake. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 21:1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na tano. Mama yake aliitwa Hefsiba.
2KI 21:2 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli.
2KI 21:3 Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia ambapo Hezekia baba yake alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akalisujudia jeshi lote la angani na kuliabudu.
2KI 21:4 Akajenga madhabahu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, ambamo Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.”
2KI 21:5 Katika nyua zote mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani.
2KI 21:6 Akamtoa kafara mwanawe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, na akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa Mwenyezi Mungu na kumghadhibisha.
2KI 21:7 Akachukua nguzo ya Ashera aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu, ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Sulemani, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu, mji niliouchagua kutoka makabila yote ya Israeli, nitaliweka Jina langu milele.
2KI 21:8 Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli itangetange kutoka nchi niliyowapa baba zao, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru, na kuishika Torati yote ambayo walipewa na Musa mtumishi wangu.”
2KI 21:9 Lakini hawa watu hawakusikiliza. Manase akawapotosha, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliangamiza mbele ya Waisraeli.
2KI 21:10 Mwenyezi Mungu akasema kupitia watumishi wake manabii:
2KI 21:11 “Manase mfalme wa Yuda ametenda dhambi hizi za kuchukiza. Amefanya maovu mengi kuliko Waamori waliokuwa kabla yake, na ameiongoza Yuda katika dhambi kwa sanamu zake.
2KI 21:12 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Nitaleta maafa makubwa juu ya Yerusalemu na Yuda, kiasi kwamba masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yatawasha.
2KI 21:13 Nitanyoosha juu ya Yerusalemu kamba ya kupimia iliyotumika dhidi ya Samaria, na timazi iliyotumika dhidi ya nyumba ya Ahabu. Nitaifutilia mbali Yerusalemu kama mtu afutavyo sahani, nikiifuta na kuifunikiza.
2KI 21:14 Nitawakataa mabaki wa urithi wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao. Watapokonywa mali yao na kutekwa nyara na adui zao wote,
2KI 21:15 kwa sababu wametenda uovu machoni pangu na kunighadhibisha tangu siku baba zao walipotoka Misri hadi leo.”
2KI 21:16 Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia, hivi kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, na hivyo wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu.
2KI 21:17 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 21:18 Manase akalala na baba zake, akazikwa katika bustani ya jumba lake la kifalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 21:19 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. Mamaye aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, kutoka Yotba.
2KI 21:20 Akatenda maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba yake Manase alivyofanya.
2KI 21:21 Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia.
2KI 21:22 Akamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za Mwenyezi Mungu.
2KI 21:23 Watumishi wa Amoni wakampangia njama, nao wakamuua ndani ya jumba lake la kifalme.
2KI 21:24 Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamepanga njama dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.
2KI 21:25 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 21:26 Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Naye Yosia mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 22:1 Yosia alikuwa na umri wa miaka nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na moja. Mama yake aliitwa Yedida binti Adaya, kutoka Boskathi.
2KI 22:2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia zote za Daudi baba yake. Hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
2KI 22:3 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, Mfalme Yosia akamtuma mwandishi Shafani mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, kwenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akasema:
2KI 22:4 “Panda uende kwa Hilkia, kuhani mkuu, umwambie ahesabu zile fedha ambazo zimeletwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, ambazo mabawabu wamekusanya kutoka kwa watu.
2KI 22:5 Waambie waikabidhi kwa watu walioteuliwa kusimamia kazi ya Hekalu. Waamuru watu hawa wawalipe wafanyakazi ambao wanakarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu:
2KI 22:6 wale maseremala, wajenzi na waashi. Waambie pia wanunue mbao na mawe yaliyochongwa ili kukarabati Hekalu.
2KI 22:7 Lakini hawahitajiki kutoa maelezo ya fedha walizokabidhiwa, kwa sababu wanafanya kazi kwa uaminifu.”
2KI 22:8 Hilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Torati ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma.
2KI 22:9 Kisha Shafani mwandishi akamwendea mfalme na kumpa taarifa akisema: “Maafisa wako wametoa ile fedha ambayo ilikuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na imekabidhiwa mikononi mwa wasimamizi wa marekebisho ya Hekalu.”
2KI 22:10 Ndipo Shafani mwandishi akampasha mfalme habari, akisema: “Hilkia kuhani amenipa kitabu hiki.” Naye Shafani akakisoma kile kitabu mbele ya mfalme.
2KI 22:11 Mfalme aliposikia maneno ya kile Kitabu cha Torati, akararua mavazi yake.
2KI 22:12 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia kuhani, Ahikamu mwana wa Shafani, Akbori mwana wa Mikaya, Shafani mwandishi, na Asaya mtumishi wa mfalme:
2KI 22:13 “Nendeni mkamuulize Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu na Yuda wote kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Mwenyezi Mungu ni kubwa inayowaka dhidi yetu kwa sababu baba zetu hawakuyatii maneno ya kitabu hiki. Hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa humo kutuhusu.”
2KI 22:14 Hilkia kuhani, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya wakaenda kuongea na nabii mke Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tikwa, mwana wa Harhasi mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu katika Mtaa wa Pili.
2KI 22:15 Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu,
2KI 22:16 ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, kulingana na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho mfalme wa Yuda alichosoma.
2KI 22:17 Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine, na kunighadhibisha kwa sanamu zote zilizotengenezwa kwa mikono yao, hasira yangu itawaka dhidi ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’
2KI 22:18 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Mwenyezi Mungu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia:
2KI 22:19 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mwenyezi Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Mwenyezi Mungu.
2KI 22:20 Kwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ” Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.
2KI 23:1 Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.
2KI 23:2 Akapanda kwenda hekaluni mwa Mwenyezi Mungu pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, kilichokuwa kimepatikana katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 23:3 Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za Mwenyezi Mungu: kwamba atamfuata Mwenyezi Mungu na kuzishika amri zake, maagizo na sheria zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, na hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano.
2KI 23:4 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu hadi Betheli.
2KI 23:5 Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani.
2KI 23:6 Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wasio na cheo.
2KI 23:7 Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, nyumba ambazo wanawake walifumia pazia kwa ajili ya Ashera.
2KI 23:8 Yosia akawaleta makuhani wote wa Mwenyezi Mungu kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji.
2KI 23:9 Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia hawakuhudumu katika madhabahu ya Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu pamoja na ndugu zao.
2KI 23:10 Kisha mfalme akapanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe wa kiume au wa kike katika moto kwa Moleki.
2KI 23:11 Akaondoa kutoka ingilio la Hekalu la Mwenyezi Mungu wale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathan-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari ya vita yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa jua.
2KI 23:12 Alizivunja madhabahu ambazo wafalme wa Yuda walikuwa wamezijenga kwenye paa la ghorofa ya Ahazi, pia madhabahu alizokuwa amezijenga Manase katika nyua mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akaziondoa huko, akazivunja vipande vipande, na kutupa hicho kifusi katika Bonde la Kidroni.
2KI 23:13 Mfalme pia akanajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, zilizokuwa mashariki mwa Yerusalemu upande wa kusini wa Kilima cha Uharibifu, ambapo Sulemani mfalme wa Israeli alikuwa amejenga mahali pa kuabudia kwa ajili ya Ashtorethi mungu wa kike wa Wasidoni, aliyekuwa chukizo; na kwa ajili ya Kemoshi mungu wa Wamoabu, aliyekuwa chukizo; na kwa ajili ya Moleki mungu wa watu wa Amoni, aliyekuwa chukizo.
2KI 23:14 Yosia akapasua yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Ashera. Kisha akafunika hayo maeneo kwa mifupa ya wanadamu.
2KI 23:15 Hata madhabahu yaliyokuwa huko Betheli, mahali pa juu pa kuabudia palipokuwa pamejengwa na Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya Israeli watende dhambi, alibomoa hata hayo madhabahu na mahali pa juu pa kuabudia. Alipateketeza kwa moto hapo mahali pa juu pa kuabudia na kupasaga hadi pakawa vumbi, na kuichoma hiyo nguzo ya Ashera pia.
2KI 23:16 Kisha Yosia akatazama huku na huko, naye alipoona makaburi yaliyokuwa kwenye kilima, akaamuru mifupa itolewe humo na akaichoma juu ya madhabahu ya Betheli ili kupanajisi. Hili lilitendeka kulingana na neno la Mwenyezi Mungu lililosemwa na mtu wa Mungu ambaye alitangulia kusema mambo haya.
2KI 23:17 Mfalme akauliza, “Lile kaburi lenye mnara wa ukumbusho ninaloliona ni kwa ajili gani?” Watu wa mji wakasema, “Hii ni alama ya kaburi la mtu wa Mungu aliyekuja kutoka Yuda, naye akanena dhidi ya madhabahu ya Betheli mambo yale yale uliyoifanyia leo.”
2KI 23:18 Akasema, “Liacheni, msiliguse. Msimruhusu mtu yeyote kuiondoa mifupa yake.” Basi wakaiacha mifupa yake pamoja na ile ya yule nabii aliyekuwa amekuja kutoka Samaria.
2KI 23:19 Kama alivyokuwa amefanya huko Betheli, Yosia akabomoa nyumba za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia, ambazo wafalme wa Israeli walikuwa wamejenga ndani ya miji ya Samaria, na ambazo zilikuwa zimemghadhibisha Mwenyezi Mungu.
2KI 23:20 Yosia akawachinja makuhani wote wa mahali pa juu pa kuabudia katika madhabahu zao wenyewe, na kuchoma mifupa ya wanadamu juu yake. Kisha akarudi Yerusalemu.
2KI 23:21 Mfalme akatoa agizo hili kwa watu wote: “Adhimisheni Pasaka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu hiki cha Agano.”
2KI 23:22 Hapakuwahi kuwa na adhimisho lingine la Pasaka kama hilo tangu nyakati za waamuzi walioamua Israeli, wala katika nyakati zote za wafalme wa Israeli na wafalme wa Yuda.
2KI 23:23 Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia, Pasaka hii iliadhimishwa kwa Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu.
2KI 23:24 Zaidi ya hayo, Yosia akawaondoa waaguzi, waabudu mizimu, miungu ya nyumbani, sanamu za kuabudiwa, na vitu vingine vyote vya machukizo vilivyoonekana huko Yuda na Yerusalemu. Aliyafanya haya ili kutimiza matakwa ya sheria iliyoandikwa katika kile kitabu ambacho Hilkia kuhani alikipata ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 23:25 Hapakuwepo mfalme mwingine kabla na baada ya Yosia aliyempenda Mwenyezi Mungu kama yeye; kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, kulingana na Torati yote ya Musa.
2KI 23:26 Hata hivyo, Mwenyezi Mungu hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha.
2KI 23:27 Hivyo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’ ”
2KI 23:28 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 23:29 Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda hadi Mto Frati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumuua huko Megido.
2KI 23:30 Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake katika gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu, wakamzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakampaka mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake.
2KI 23:31 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna.
2KI 23:32 Akafanya maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyofanya.
2KI 23:33 Farao Neko akamfunga kwa minyororo huko Ribla katika nchi ya Hamathi ili asiweze kutawala huko Yerusalemu, naye akatoza kodi ya talanta mia moja za fedha, na talanta moja ya dhahabu katika Yuda.
2KI 23:34 Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, na kulibadilisha jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini akamchukua Yehoahazi na kumpeleka Misri, naye akafia huko.
2KI 23:35 Yehoyakimu akamlipa Farao Neko ile fedha na dhahabu aliyodai. Ili kuweza kufanya hivyo, Yehoyakimu akatoza nchi kodi na kulipiza fedha na dhahabu kutoka kwa watu wa nchi kulingana na makadirio ya mapato yao.
2KI 23:36 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Zebida binti Pedaya kutoka Ruma.
2KI 23:37 Naye akafanya maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyokuwa wamefanya.
2KI 24:1 Wakati wa utawala wa Yehoyakimu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliishambulia nchi, naye Yehoyakimu akawa mtumwa wake kwa miaka mitatu. Lakini hatimaye akabadili mawazo yake na kuasi dhidi ya Nebukadneza.
2KI 24:2 Mwenyezi Mungu akatuma wavamiaji wa Wakaldayo, Waaramu, Wamoabu na Waamoni ili kumshambulia. Aliwatuma kuiangamiza Yuda sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu lililosemwa na watumishi wake manabii.
2KI 24:3 Hakika mambo haya yalitokea Yuda kulingana na agizo la Mwenyezi Mungu, ili kuwaondoa kutoka machoni pake kwa sababu ya dhambi za Manase na yote aliyoyafanya,
2KI 24:4 ikiwa ni pamoja na kumwaga damu isiyo na hatia. Kwa kuwa aliijaza Yerusalemu kwa damu isiyo na hatia, naye Mwenyezi Mungu hakuwa radhi kusamehe.
2KI 24:5 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
2KI 24:6 Yehoyakimu akalala na baba zake. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.
2KI 24:7 Mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwa sababu mfalme wa Babeli alikuwa ameitwaa himaya yake yote, kuanzia Kijito cha Misri hadi Mto Frati.
2KI 24:8 Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu. Mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani kutoka Yerusalemu.
2KI 24:9 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
2KI 24:10 Wakati huo, maafisa wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walikuja kushambulia Yerusalemu, nao wakauzingira kwa jeshi.
2KI 24:11 Nebukadneza mwenyewe akaupandia mji wakati maafisa wake walipokuwa wameuzingira.
2KI 24:12 Yehoyakini mfalme wa Yuda, mama yake, wahudumu wake, wakuu na maafisa wake wote wakajisalimisha kwa Nebukadneza. Katika mwaka wa nane wa utawala wa mfalme wa Babeli, akamchukua Yehoyakini kuwa mfungwa.
2KI 24:13 Kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema, Nebukadneza akaondoa hazina yote kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu na kutoka jumba la mfalme, akavichukua vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani mfalme wa Israeli alikuwa amevitengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2KI 24:14 Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na wapiganaji, watu wenye ustadi wa ufundi na wahunzi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana tu ndio walibaki katika nchi.
2KI 24:15 Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini hadi Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake, na viongozi wote wa nchi.
2KI 24:16 Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli wapiganaji elfu saba wenye nguvu na tayari kwa vita, na mafundi na wahunzi elfu moja.
2KI 24:17 Akamfanya Matania, ndugu wa baba yake Yehoyakini, kuwa mfalme mahali pake, na akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.
2KI 24:18 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna.
2KI 24:19 Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya Yehoyakimu.
2KI 24:20 Haya yote yalitendeka Yerusalemu na Yuda kwa sababu ya hasira ya Mwenyezi Mungu, naye mwishoni akawaondoa mbele zake. Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.
2KI 25:1 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzingira pande zote.
2KI 25:2 Mji ulizingirwa na jeshi hadi mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.
2KI 25:3 Ilipofika siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.
2KI 25:4 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba.
2KI 25:5 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia mfalme na kumpata katika nchi tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika,
2KI 25:6 naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, ambapo hukumu yake ilitangazwa.
2KI 25:7 Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayang’oa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
2KI 25:8 Siku ya saba ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme, afisa wa mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu.
2KI 25:9 Alichoma moto Hekalu la Mwenyezi Mungu, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu.
2KI 25:10 Jeshi lote la Wakaldayo, chini ya mkuu wa askari walinzi wa mfalme, walivunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu.
2KI 25:11 Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi akawapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli.
2KI 25:12 Lakini yule jemadari wa askari walinzi akawaacha baadhi ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
2KI 25:13 Wakaldayo walivunja vipande vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli.
2KI 25:14 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu.
2KI 25:15 Mkuu wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.
2KI 25:16 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Sulemani alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, ilikuwa na uzito mwingi usioweza kupimika.
2KI 25:17 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane. Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza.
2KI 25:18 Yule mkuu wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu.
2KI 25:19 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji.
2KI 25:20 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.
2KI 25:21 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe. Hivyo Yuda wakaenda utumwani mbali na nchi yao.
2KI 25:22 Nebukadneza mfalme wa Babeli akamteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, awe msimamizi wa watu aliowaacha Yuda.
2KI 25:23 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia kuwa mtawala, wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao.
2KI 25:24 Gedalia akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema, “Msiwaogope maafisa wa Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.”
2KI 25:25 Hata hivyo, katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi, nao wakamuua Gedalia, na pia watu wa Yuda, pamoja na Wakaldayo waliokuwa naye huko Mispa.
2KI 25:26 Baada ya haya, watu wote kuanzia aliye mdogo sana hadi aliye mkubwa kabisa, pamoja na maafisa wa jeshi, wakakimbilia Misri kwa kuwaogopa Wakaldayo.
2KI 25:27 Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodaki alifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini kutoka gerezani siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili.
2KI 25:28 Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima kuliko wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli.
2KI 25:29 Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya gerezani, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme.
2KI 25:30 Siku kwa siku mfalme alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake.
1CH 1:1 Adamu, Sethi, Enoshi,
1CH 1:2 Kenani, Mahalaleli, Yaredi,
1CH 1:3 Idrisi, Methusela, Lameki, Nuhu.
1CH 1:4 Wana wa Nuhu walikuwa: Shemu, Hamu na Yafethi.
1CH 1:5 Wana wa Yafethi walikuwa: Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi.
1CH 1:6 Wana wa Gomeri walikuwa: Ashkenazi, Rifathi na Togarma.
1CH 1:7 Wana wa Yavani walikuwa: Al-Yasa, Tarshishi, Kitimu na Rodanimu.
1CH 1:8 Wana wa Hamu walikuwa: Kushi, Misri, Putu na Kanaani.
1CH 1:9 Wana wa Kushi walikuwa: Seba, Havila, Sabta, Raama na Sabteka. Wana wa Raama walikuwa: Sheba na Dedani.
1CH 1:10 Kushi akamzaa Nimrodi, ambaye alikua shujaa mwenye nguvu duniani.
1CH 1:11 Misri akawazaa: Waludi, Waanami, Walehabi, Wanaftuhi,
1CH 1:12 Wapathrusi, Wakasluhi (hao ndio asili ya Wafilisti) na Wakaftori.
1CH 1:13 Wana wa Kanaani walikuwa: Sidoni, mzaliwa wake wa kwanza, na Hethi,
1CH 1:14 Wayebusi, Waamori, Wagirgashi,
1CH 1:15 Wahivi, Waarki, Wasini,
1CH 1:16 Waarvadi, Wasemari na Wahamathi.
1CH 1:17 Wana wa Shemu walikuwa: Elamu, Ashuru, Arfaksadi, Ludi na Aramu. Wana wa Aramu walikuwa: Usi, Huli, Getheri na Mashi.
1CH 1:18 Arfaksadi akamzaa Shela, Shela akamzaa Eberi.
1CH 1:19 Eberi alipata wana wawili: Mmoja wao aliitwa Pelegi, kwa kuwa wakati wake dunia iligawanyika; nduguye aliitwa Yoktani.
1CH 1:20 Wana wa Yoktani walikuwa: Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera,
1CH 1:21 Hadoramu, Uzali, Dikla,
1CH 1:22 Obali, Abimaeli, Sheba,
1CH 1:23 Ofiri, Havila na Yobabu. Wote hawa walikuwa wana wa Yoktani.
1CH 1:24 Wana wa Shemu walikuwa Arfaksadi, Shela,
1CH 1:25 Eberi, Pelegi, Reu,
1CH 1:26 Serugi, Nahori, Tera,
1CH 1:27 Tera akamzaa Abramu (yaani Ibrahimu).
1CH 1:28 Ibrahimu alikuwa na wana wawili: Isaka na Ishmaeli.
1CH 1:29 Hawa ndio wazao wao: Ishmaeli akazaa Nebayothi mzaliwa wa kwanza; kisha Kedari, Adbeeli, Mibsamu,
1CH 1:30 Mishma, Duma, Masa, Hadadi, Tema,
1CH 1:31 Yeturi, Nafishi na Kedema.
1CH 1:32 Wana waliozaliwa na Ketura suria wa Ibrahimu walikuwa: Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. Wana wa Yokshani walikuwa: Sheba na Dedani.
1CH 1:33 Wana wa Midiani walikuwa: Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa.
1CH 1:34 Ibrahimu alikuwa baba wa Isaka. Wana wa Isaka walikuwa: Esau na Israeli.
1CH 1:35 Wana wa Esau walikuwa: Elifazi, Reueli, Yeushi, Yalamu na Kora.
1CH 1:36 Wana wa Elifazi walikuwa: Temani, Omari, Sefo, Gatamu na Kenazi; Elifazi kwa Timna akamzaa Amaleki.
1CH 1:37 Wana wa Reueli walikuwa: Nahathi, Zera, Shama na Miza.
1CH 1:38 Wana wa Seiri walikuwa: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana, Dishoni, Eseri na Dishani.
1CH 1:39 Wana wa Lotani walikuwa wawili: Hori na Homamu. Lotani alikuwa na dada yake aliyeitwa Timna.
1CH 1:40 Wana wa Shobali walikuwa: Alvani, Manahathi, Ebali, Shefo na Onamu. Wana wa Sibeoni walikuwa: Aya na Ana.
1CH 1:41 Mwana wa Ana alikuwa: Dishoni. Nao wana wa Dishoni walikuwa: Hemdani, Eshbani, Ithrani na Kerani.
1CH 1:42 Wana wa Eseri walikuwa: Bilhani, Zaavani na Akani. Wana wa Dishani walikuwa: Usi na Arani.
1CH 1:43 Hawa ndio wafalme waliotawala Edomu kabla hajatawala mfalme yeyote wa Waisraeli: Bela mwana wa Beori, ambaye mji wake ni Dinhaba.
1CH 1:44 Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra akawa mfalme baada yake.
1CH 1:45 Yobabu alipofariki, Hushamu kutoka nchi ya Watemani akawa mfalme baada yake.
1CH 1:46 Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi, aliyeshinda Midiani katika nchi ya Moabu, akawa mfalme baada yake. Mji wake uliitwa Avithi.
1CH 1:47 Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka akawa mfalme baada yake.
1CH 1:48 Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi ng’ambo ya Mto Frati, akawa mfalme baada yake.
1CH 1:49 Shauli alipofariki, Baal-Hanani mwana wa Akbori akawa mfalme baada yake.
1CH 1:50 Baal-Hanani alipofariki, Hadadi akawa mfalme baada yake. Mji wake uliitwa Pau, na mkewe aliitwa Mehetabeli binti Matredi, binti Me-Zahabu.
1CH 1:51 Naye Hadadi pia akafa. Wakuu wa Edomu walikuwa: Timna, Alva, Yethethi,
1CH 1:52 Oholibama, Ela, Pinoni,
1CH 1:53 Kenazi, Temani, Mibsari,
1CH 1:54 Magdieli na Iramu.
1CH 2:1 Hawa walikuwa wana wa Israeli: Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Zabuloni,
1CH 2:2 Dani, Yusufu, Benyamini, Naftali, Gadi na Asheri.
1CH 2:3 Wana wa Yuda walikuwa: Eri, Onani na Shela. Hawa watatu walizaliwa kwake na mkewe Mkanaani, binti Shua. (Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu alimuua.)
1CH 2:4 Tamari, mkwewe Yuda, alimzalia wana wawili: Peresi na Zera.
1CH 2:5 Wana wa Peresi walikuwa: Hesroni na Hamuli.
1CH 2:6 Wana wa Zera walikuwa: Zimri, Ethani, Hemani, Kalkoli na Darda. Jumla ya wana wa Zera walikuwa watano.
1CH 2:7 Mwana wa Karmi alikuwa: Akari, ambaye alileta taabu kwa Waisraeli kwa kukiuka onyo la kutochukua vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa.
1CH 2:8 Mwana wa Ethani alikuwa: Azariya.
1CH 2:9 Wana wa Hesroni walikuwa: Yerameeli, Ramu na Kalebu.
1CH 2:10 Ramu alimzaa Aminadabu, naye Aminadabu akamzaa Nashoni, kiongozi wa kabila la Yuda.
1CH 2:11 Nashoni akamzaa Salmoni, Salmoni akamzaa Boazi,
1CH 2:12 Boazi akamzaa Obedi, Obedi akamzaa Yese.
1CH 2:13 Yese akawazaa Eliabu mwanawe wa kwanza; wa pili Abinadabu, wa tatu Shimea,
1CH 2:14 wa nne Nethaneli, wa tano Radai,
1CH 2:15 wa sita Osemu, na wa saba Daudi.
1CH 2:16 Dada zao walikuwa Seruya na Abigaili. Wana wa Seruya walikuwa watatu: Abishai, Yoabu na Asaheli.
1CH 2:17 Abigaili alikuwa mama yake Amasa, ambaye baba yake alikuwa Yetheri Mwishmaeli.
1CH 2:18 Kalebu mwana wa Hesroni akazaa wana na mkewe Azuba (na pia na Yeriothi). Hawa ndio wana Azuba aliomzalia Kalebu: Yesheri, Shobabu na Ardoni.
1CH 2:19 Azuba alipofariki, Kalebu akamwoa Efrata, aliyemzalia Huri.
1CH 2:20 Huri akamzaa Uri, naye Uri akamzaa Bezaleli.
1CH 2:21 Hatimaye, Hesroni alipokuwa na umri wa miaka sitini, alimwoa binti Makiri, babaye Gileadi. Akakutana kimwili naye, akamzalia Segubu.
1CH 2:22 Segubu akamzaa Yairi, ambaye alitawala miji ishirini na tatu katika Gileadi.
1CH 2:23 (Lakini Geshuri na Aramu wakateka miji ya Hawoth-Yairi, pamoja na Kenathi na makazi yake; jumla ilikuwa miji sitini.)
1CH 2:24 Baada ya Hesroni kufa huko Kalebu-Efrata, Abiya mjane wa Hesroni akamzalia Ashuru, aliye baba wa Tekoa.
1CH 2:25 Wana wa Yerameeli mzaliwa wa kwanza wa Hesroni walikuwa: Ramu mzaliwa wake wa kwanza, Buna, Oreni, Osemu na Ahiya.
1CH 2:26 Yerameeli alikuwa na mke mwingine, aliyeitwa Atara, aliyekuwa mama yake Onamu.
1CH 2:27 Wana wa Ramu mzaliwa wa kwanza wa Yerameeli walikuwa: Maasi, Yamini na Ekeri.
1CH 2:28 Wana wa Onamu walikuwa: Shamai na Yada. Wana wa Shamai walikuwa: Nadabu na Abishuri.
1CH 2:29 Mke wa Abishuri aliitwa Abihaili, aliyemzalia Abani na Molidi.
1CH 2:30 Wana wa Nadabu walikuwa Seledi na Apaimu, lakini Seledi alikufa bila kuzaa watoto.
1CH 2:31 Apaimu akamzaa: Ishi aliyekuwa baba wa Sheshani. Sheshani akamzaa Alai.
1CH 2:32 Wana wa Yada, nduguye Shamai walikuwa: Yetheri na Yonathani. Yetheri alikufa bila kuzaa watoto.
1CH 2:33 Wana wa Yonathani walikuwa: Pelethi na Zaza.
1CH 2:34 Sheshani hakuwa na watoto wa kiume, ila watoto wa kike tu. Alikuwa na mtumishi Mmisri aliyeitwa Yarha.
1CH 2:35 Sheshani akamwoza huyu mtumishi wake Yarha binti yake, akamzalia mwana jina lake Atai.
1CH 2:36 Atai akamzaa Nathani, Nathani akamzaa Zabadi,
1CH 2:37 Zabadi akamzaa Eflali, Eflali akamzaa Obedi,
1CH 2:38 Obedi akamzaa Yehu, Yehu akamzaa Azaria,
1CH 2:39 Azaria akamzaa Helesi, Helesi akamzaa Eleasa,
1CH 2:40 Eleasa akamzaa Sismai, Sismai akamzaa Shalumu,
1CH 2:41 Shalumu akamzaa Yekamia, naye Yekamia akamzaa Elishama.
1CH 2:42 Wana wa Kalebu nduguye Yerameeli walikuwa: Mesha mzaliwa wake wa kwanza alimzaa Zifu, naye mwanawe Maresha akamzaa Hebroni.
1CH 2:43 Hebroni alikuwa na wana wanne: Kora, Tapua, Rekemu na Shema.
1CH 2:44 Shema alikuwa baba yake Rahamu na Rahamu alikuwa baba wa Yorkeamu na Rekemu alikuwa baba wa Shamai.
1CH 2:45 Shamai akamzaa Maoni, naye Maoni akamzaa Beth-Suri.
1CH 2:46 Efa, suria wa Kalebu aliwazaa: Harani, Mosa na Gazezi. Harani alikuwa baba wa Gazezi.
1CH 2:47 Wana wa Yadai walikuwa: Regemu, Yothamu, Geshani, Peleti, Efa na Shaafu.
1CH 2:48 Maaka suria wa Kalebu alikuwa mamaye Sheberi na Tirhana.
1CH 2:49 Pia Maaka akamzaa Shaafu babaye Madmana, na Sheva babaye Makbena na Gibea. Kalebu alikuwa na binti jina lake Aksa.
1CH 2:50 Hao walikuwa wazao wa Kalebu. Wana wa Huri, mzaliwa wa kwanza wa Efrata, walikuwa: Shobali akamzaa Kiriath-Yearimu,
1CH 2:51 Salma akamzaa Bethlehemu, naye Harefu akamzaa Beth-Gaderi.
1CH 2:52 Wazao wa Shobali, baba yake Kiriath-Yearimu, walikuwa: Haroe, nusu ya Wamenuhothi,
1CH 2:53 pamoja na koo za Kiriath-Yearimu ambazo ni: Waithiri, Waputhi, Washumathi na Wamishrai. Kutokana na watu hawa walizaliwa Wasorathi na Waeshtaoli.
1CH 2:54 Wazao wa Salma walikuwa: Bethlehemu, Wanetofathi, Atroth-Beth-Yoabu, nusu ya Wamanahathi, Wazori,
1CH 2:55 pamoja na koo za waandishi zilizoishi katika mji wa Yabesi: yaani Watirathi, Washimeathi na Wasukathi. Hawa ndio Wakeni waliotokana na Hamathi, baba wa nyumba ya Rekabu.
1CH 3:1 Hawa walikuwa wana wa Daudi waliozaliwa huko Hebroni: Mzaliwa wa kwanza alikuwa Amnoni ambaye mama yake aliitwa Ahinoamu wa Yezreeli; wa pili, Danieli ambaye mama yake aliitwa Abigaili wa Karmeli;
1CH 3:2 wa tatu alikuwa Absalomu, ambaye mama yake aliitwa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri; wa nne, Adoniya, ambaye mama yake aliitwa Hagithi;
1CH 3:3 wa tano alikuwa Shefatia ambaye mama yake aliitwa Abitali; wa sita alikuwa Ithreamu, aliyezaliwa na mke wake Egla.
1CH 3:4 Hawa sita walizaliwa huko Hebroni ambako Daudi alitawala kwa miaka saba na miezi sita.
1CH 3:5 nao hawa ndio wana wa Daudi waliozaliwa huko Yerusalemu: mkewe Bathsheba, binti Amieli, alimzalia wana wanne: Shamua, Shobabu, Nathani na Sulemani.
1CH 3:6 Pia kulikuwa na wana wengine: Ibihari, Elishua, Elifeleti,
1CH 3:7 Noga, Nefegi, Yafia,
1CH 3:8 Elishama, Eliada na Elifeleti; wote walikuwa tisa.
1CH 3:9 Hawa wote walikuwa wana wa Daudi, mbali na wale wana waliozaliwa na masuria. Naye Tamari alikuwa dada yao.
1CH 3:10 Mwana wa Sulemani alikuwa Rehoboamu, mwanawe huyo alikuwa Abiya, mwanawe huyo alikuwa Yehoshafati, mwanawe huyo alikuwa Asa,
1CH 3:11 mwanawe huyo alikuwa Yehoramu, mwanawe huyo alikuwa Ahazia, mwanawe huyo alikuwa Yoashi,
1CH 3:12 mwanawe huyo alikuwa Amazia, mwanawe huyo alikuwa Azaria, mwanawe huyo alikuwa Yothamu,
1CH 3:13 mwanawe huyo alikuwa Ahazi, mwanawe huyo alikuwa Hezekia, mwanawe huyo alikuwa Manase,
1CH 3:14 mwanawe huyo alikuwa Amoni na mwanawe huyo alikuwa Yosia.
1CH 3:15 Wana wa Yosia walikuwa: Yohanani mzaliwa wake wa kwanza, Yehoyakimu mwanawe wa pili, wa tatu Sedekia, wa nne Shalumu.
1CH 3:16 Walioingia mahali pa Yehoyakimu kama wafalme ni: Yekonia mwanawe, na Sedekia.
1CH 3:17 Hawa walikuwa wazao wa Yekonia aliyekuwa mateka: Shealtieli mwanawe,
1CH 3:18 Malkiramu, Pedaya, Shenasari, Yekamia, Hoshama na Nedabia.
1CH 3:19 Wana wa Pedaya walikuwa: Zerubabeli na Shimei. Wana wa Zerubabeli walikuwa: Meshulamu na Hanania. Shelomithi alikuwa dada yao.
1CH 3:20 Kulikuwa na wengine watano: Hashuba, Oheli, Berekia, Hasadia na Yushab-Hesedi.
1CH 3:21 Wazao wa Hanania walikuwa: Pelatia na Yeshaya, na wana wa Refaya, na wana wa Arnani, na wana wa Obadia, na wana wa Shekania.
1CH 3:22 Wazao wa Shekania: Shemaya na wanawe: Hatushi, Igali, Baria, Nearia na Shafati; jumla yao walikuwa sita.
1CH 3:23 Wana wa Nearia walikuwa: Elioenai, Hizkia na Azrikamu; jumla yao watatu.
1CH 3:24 Wana wa Elioenai walikuwa: Hodavia, Eliashibu, Pelaya, Akubu, Yohanani, Delaya na Anani; jumla yao wote saba.
1CH 4:1 Wazao wa Yuda walikuwa: Peresi, Hesroni, Karmi, Huri na Shobali.
1CH 4:2 Reaya mwana wa Shobali akamzaa Yahathi, Yahathi akawazaa Ahumai na Lahadi. Hizo zilikuwa koo za Wasorathi.
1CH 4:3 Hawa walikuwa wana wa Etamu: Yezreeli, Ishma na Idbashi. Dada yao aliitwa Haselelponi.
1CH 4:4 Penueli akamzaa Gedori, naye Ezeri akamzaa Husha. Hawa walikuwa wazao wa Huri, mzaliwa wa kwanza wa Efrata, na baba yake Bethlehemu.
1CH 4:5 Ashuri baba yake Tekoa alikuwa na wake wawili, Hela na Naara.
1CH 4:6 Hawa walikuwa wazao wa Naara: Ahuzamu, Heferi, Temeni na Haahashtari.
1CH 4:7 Wana wa Hela walikuwa: Serethi, Sohari, Ethnani,
1CH 4:8 na Kosi ambaye aliwazaa Anubi, Sobeba na jamaa zote za Aharheli mwana wa Harumu.
1CH 4:9 Yabesi aliheshimiwa kuliko ndugu zake. Mama yake alimwita Yabesi, akisema, “Nilimzaa kwa huzuni.”
1CH 4:10 Yabesi akamlilia Mungu wa Israeli akisema, “Ee Mungu, laiti ungenibariki kweli na kuipanua mipaka yangu! Mkono wako na uwe pamoja nami, uniepushe na uovu ili nisidhurike!” Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.
1CH 4:11 Kelubu, nduguye Shuha, akamzaa Mehiri, naye Mehiri akamzaa Eshtoni.
1CH 4:12 Eshtoni akawazaa Beth-Rafa, Pasea na Tehina. Tehina alikuwa baba wa Iri-Nahashi. Hao walikuwa wazao wa Reka.
1CH 4:13 Wana wa Kenazi walikuwa: Othnieli na Seraya. Wana wa Othnieli walikuwa: Hathathi na Meonothai.
1CH 4:14 Meonothai akamzaa Ofra. Seraya akamzaa Yoabu, baba wa Ge-Harashimu, lililoitwa hivyo kwa sababu watu walioishi humo walikuwa mafundi stadi.
1CH 4:15 Kalebu mwana wa Yefune alikuwa na wana watatu: Iru, Ela na Naamu. Naye mwana wa Ela alikuwa: Kenazi.
1CH 4:16 Wana wa Yahaleleli walikuwa: Zifu, Zifa, Tiria na Asareli.
1CH 4:17 Wana wa Ezra walikuwa: Yetheri, Meredi, Eferi na Yaloni. Mmoja wa wake zake Meredi aliwazaa: Miriamu, Shamai na Ishba aliyekuwa baba yake Eshtemoa.
1CH 4:18 Hawa walikuwa watoto wa Bithia binti Farao, ambaye Meredi alikuwa amemwoa. Meredi alikuwa na mke mwingine wa kabila la Yuda ambaye aliwazaa: Yeredi baba wa Gedori, Heberi baba wa Soko, na Yekuthieli baba wa Zanoa.
1CH 4:19 Wana wa mke wa Hodia aliyekuwa dada yake Nahamu walikuwa: baba yake Keila, Mgarmi na Eshtemoa, Mmaakathi.
1CH 4:20 Wana wa Shimoni walikuwa: Amnoni, Rina, Ben-Hanani na Tiloni. Wazao wa Ishi walikuwa: Zohethi na Ben-Zohethi.
1CH 4:21 Wana wa Shela, mwana wa Yuda, walikuwa: Eri baba yake Leka, Laada baba yake Maresha na jamaa za wafumaji nguo za kitani safi walioishi huko Beth-Ashbea,
1CH 4:22 Yokimu, watu walioishi Kozeba, Yoashi na Sarafi waliotawala huko Moabu na Yashubi-Lehemu. (Taarifa hizi ni za zamani sana.)
1CH 4:23 Hawa walikuwa wafinyanzi walioishi Netaimu na Gedera; waliishi huko wakimtumikia mfalme.
1CH 4:24 Wazao wa Simeoni walikuwa: Nemueli, Yamini, Yaribu, Zera na Shauli.
1CH 4:25 Mwana wa Shauli alikuwa Shalumu, Shalumu akamzaa Mibsamu, na Mibsamu akamzaa Mishma.
1CH 4:26 Wazao wa Mishma walikuwa: Hamueli aliyemzaa Zakuri, Zakuri akamzaa Shimei.
1CH 4:27 Shimei alikuwa na wana kumi na sita, na binti sita, lakini ndugu zake hawakuwa na watoto wengi, hivyo ukoo wao wote haukuwa na watu wengi kama ukoo wa Yuda.
1CH 4:28 Waliishi Beer-Sheba, Molada, Hasar-Shuali,
1CH 4:29 Bilha, Esemu, Toladi,
1CH 4:30 Bethueli, Horma, Siklagi,
1CH 4:31 Beth-Markabothi, Hasar-Susimu, Beth-Biri na Shaaraimu. Hii ilikuwa miji yao hadi wakati wa utawala wa Daudi.
1CH 4:32 Vijiji vya miji hiyo vilikuwa Etamu, Aini, Rimoni, Tokeni na Ashani: miji mitano,
1CH 4:33 pamoja na vijiji vyote kuizunguka miji hii hadi huko Baali.
1CH 4:34 Meshobabu, Yamleki, Yosha mwana wa Amazia,
1CH 4:35 Yoeli, Yehu mwana wa Yoshibia, mwana wa Seraya, mwana wa Asieli.
1CH 4:36 Pia Elioenai, Yaakoba, Yeshohaya, Asaya, Adieli, Yesimieli, Benaya,
1CH 4:37 Ziza mwana wa Shifi, mwana wa Aloni, mwana wa Yedaya, mwana wa Shimri, mwana wa Shemaya.
1CH 4:38 Watu hawa walioorodheshwa hapa juu kwa majina walikuwa viongozi wa koo zao. Jamaa zao ziliongezeka sana,
1CH 4:39 wakaenea wakafika viunga vya Gedori kuelekea mashariki mwa bonde wakitafuta malisho kwa ajili ya mifugo yao.
1CH 4:40 Huko walipata malisho mengi mazuri, nayo nchi ilikuwa na nafasi kubwa, yenye amani na utulivu. Baadhi ya Wahamu walikuwa wameishi huko awali.
1CH 4:41 Watu walioorodheshwa majina walikuja nchi hiyo wakati wa Hezekia mfalme wa Yuda. Wasimeoni wakawashambulia Wahamu katika makao yao pamoja na Wameuni ambao walikuwa huko, nao wakawaangamiza kabisa, kama ilivyo dhahiri hadi leo. Kisha wakaishi huko kwa sababu kulikuwa na malisho mazuri kwa mifugo yao.
1CH 4:42 Watu wa kabila la Simeoni wapatao mia tano, wakiongozwa na Pelatia, Nearia, Refaya na Uzieli wana wa Ishi, wakavamia nchi ya vilima ya Seiri.
1CH 4:43 Wakawaua Waamaleki waliobaki, na waliokuwa wamenusurika; nao wanaishi huko hadi leo.
1CH 5:1 Wana wa Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli (yeye alikuwa mzaliwa wa kwanza, lakini kwa kuwa alikinajisi kitanda cha baba yake, haki zake za mzaliwa wa kwanza walipewa wana wa Yusufu mwana wa Israeli. Hivyo hakuorodheshwa kwenye orodha ya ukoo wao kulingana na haki yake ya kuzaliwa.
1CH 5:2 Na ingawa Yuda alikuwa na nguvu zaidi ya ndugu zake wote, na mtawala alitoka kwake, haki za mzaliwa wa kwanza zilikuwa za Yusufu.)
1CH 5:3 Wana wa Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli walikuwa: Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.
1CH 5:4 Wazao wa Yoeli walikuwa: Shemaya mwanawe, Gogu mwanawe; Shimei mwanawe,
1CH 5:5 Mika mwanawe, Reaya mwanawe, Baali mwanawe,
1CH 5:6 na Beera mwanawe, ambaye Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru alimchukua kwenda uhamishoni. Beera alikuwa kiongozi wa Wareubeni.
1CH 5:7 Jamaa zao kulingana na koo zao, walioorodheshwa kwa koo zao kama ifuatavyo: Yeieli aliyekuwa mkuu wao, Zekaria,
1CH 5:8 Bela mwana wa Azazi, mwana wa Shema, mwana wa Yoeli. Hao waliishi katika eneo lililoanzia Aroeri hadi Nebo na Baal-Meoni.
1CH 5:9 Kwa upande wa mashariki walienea hadi pembeni mwa jangwa linaloenea hadi kwenye Mto Frati, kwa sababu mifugo yao ilikuwa imeongezeka huko Gileadi.
1CH 5:10 Wakati wa utawala wa Mfalme Sauli, walipigana vita dhidi ya Wahagari, wakaanguka kwa mikono yao. Kisha wakaishi katika mahema ya Wahagari katika eneo lote la mashariki mwa Gileadi.
1CH 5:11 Wagadi waliishi jirani nao katika nchi ya Bashani, hadi Saleka.
1CH 5:12 Yoeli ndiye alikuwa mkuu wao, Shafamu wa pili, na wakafuata Yanai na Shafati, huko Bashani.
1CH 5:13 Ndugu zao, kulingana na jamaa zao, walikuwa saba: Mikaeli, Meshulamu, Sheba, Yorai, Yakani, Zia na Eberi.
1CH 5:14 Hao walikuwa wana wa Abihaili mwana wa Huri, mwana wa Yaroa, mwana wa Gileadi, mwana wa Mikaeli, mwana wa Yeshishai, mwana wa Yahdo, mwana wa Buzi.
1CH 5:15 Ahi mwana wa Abdieli, mwana wa Guni, alikuwa kiongozi wa jamaa yao.
1CH 5:16 Wagadi waliishi Gileadi, huko Bashani pamoja na vijiji vyake, na pia katika maeneo yote ya malisho ya Sharoni kote walikofika.
1CH 5:17 Yote haya yaliwekwa katika kumbukumbu za ukoo wao wakati wa utawala wa Yothamu, mfalme wa Yuda na Yeroboamu mfalme wa Israeli.
1CH 5:18 Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walikuwa na wanaume elfu arobaini na nne mia saba na sitini (44,760) waliokuwa tayari kwenda vitani, wanaume wenye uwezo wa kutumia ngao na upanga, ambao wangeweza kutumia upinde, walioandaliwa kwa vita.
1CH 5:19 Walipigana vita dhidi ya Wahagari, Yeturi, Nafishi na Nodabu.
1CH 5:20 Walisaidiwa katika kupigana nao, Mungu akawatia Wahagari pamoja na wote walioungana nao mikononi mwao, kwa sababu walimlilia Mungu wakati wa vita. Alijibu maombi yao, kwa sababu walimtegemea.
1CH 5:21 Walitwaa mifugo ya Wahagari: ngamia elfu hamsini, kondoo elfu mia mbili na hamsini, na punda elfu mbili. Pia wakateka watu elfu mia moja,
1CH 5:22 na wengine wengi waliuawa kwa sababu vita vilikuwa ni vya Mungu. Nao waliendelea kuikalia nchi hiyo hadi wakati wa uhamisho.
1CH 5:23 Idadi ya nusu ya kabila la Manase walikuwa wengi sana, Wakakaa kuanzia Bashani hadi Baal-Hermoni, yaani Seniri (ndio Mlima Hermoni).
1CH 5:24 Hawa walikuwa viongozi wa jamaa za kabila hilo: Eferi, Ishi, Elieli, Azrieli, Yeremia, Hodavia na Yadieli. Walikuwa askari shujaa, watu maarufu, viongozi wa jamaa zao.
1CH 5:25 Lakini hawakuwa waaminifu kwa Mungu wa baba zao, nao wakafanya ukahaba kwa miungu ya mataifa, ambayo Mungu alikuwa ameyaangamiza mbele yao.
1CH 5:26 Kwa hiyo Mungu wa Israeli akaiamsha roho ya Pulu, mfalme wa Ashuru (ambaye pia alijulikana kama Tiglath-Pileseri), ambaye aliwachukua Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kwenda uhamishoni. Akawapeleka huko Hala, Habori, Hara na mto Gozani, ambako wamekaa hadi leo.
1CH 6:1 Wana wa Lawi walikuwa: Gershoni, Kohathi na Merari.
1CH 6:2 Wana wa Kohathi walikuwa: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli.
1CH 6:3 Amramu alikuwa na wana: Haruni, Musa, na Miriamu. Haruni alikuwa na wana: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari.
1CH 6:4 Eleazari akamzaa Finehasi, Finehasi akamzaa Abishua,
1CH 6:5 Abishua akamzaa Buki, Buki akamzaa Uzi,
1CH 6:6 Uzi akamzaa Zerahia, Zerahia akamzaa Merayothi,
1CH 6:7 Merayothi akamzaa Amaria, Amaria akamzaa Ahitubu,
1CH 6:8 Ahitubu akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Ahimaasi,
1CH 6:9 Ahimaasi akamzaa Azaria, Azaria akamzaa Yohanani,
1CH 6:10 Yohanani akamzaa Azaria (ndiye alifanya kazi ya ukuhani katika Hekalu alilojenga Mfalme Sulemani huko Yerusalemu),
1CH 6:11 Azaria akamzaa Amaria, Amaria akamzaa Ahitubu,
1CH 6:12 Ahitubu akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Shalumu,
1CH 6:13 Shalumu akamzaa Hilkia, Hilkia akamzaa Azaria,
1CH 6:14 Azaria akamzaa Seraya, Seraya akamzaa Yehosadaki.
1CH 6:15 Yehosadaki alihamishwa wakati Mwenyezi Mungu aliwapeleka uhamishoni watu wa Yuda na Yerusalemu kwa mkono wa Mfalme Nebukadneza.
1CH 6:16 Wana wa Lawi walikuwa: Gershoni, Kohathi na Merari.
1CH 6:17 Haya ndiyo majina ya wana wa Gershoni: Libni na Shimei.
1CH 6:18 Wana wa Kohathi walikuwa: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli.
1CH 6:19 Wana wa Merari walikuwa: Mahli na Mushi.
1CH 6:20 Wazao wa Gershoni: Gershoni akamzaa Libni, Libni akamzaa Yahathi, Yahathi akamzaa Zima,
1CH 6:21 Zima akamzaa Yoa, Yoa akamzaa Ido, Ido akamzaa Zera, Zera akamzaa Yeatherai.
1CH 6:22 Wazao wa Kohathi: Kohathi akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Kora, Kora akamzaa Asiri,
1CH 6:23 Asiri akamzaa Elkana, Elkana akamzaa Ebiasafu, Ebiasafu akamzaa Asiri,
1CH 6:24 Asiri akamzaa Tahathi, Tahathi akamzaa Urieli, Urieli akamzaa Uzia, Uzia akamzaa Shauli.
1CH 6:25 Wazao wa Elkana walikuwa: Amasai na Ahimothi,
1CH 6:26 Ahimothi akamzaa Elkana, Elkana akamzaa Sofai, Sofai akamzaa Nahathi,
1CH 6:27 Nahathi akamzaa Eliabu, Eliabu akamzaa Yerohamu, Yerohamu akamzaa Elkana, Elkana akamzaa Samweli.
1CH 6:28 Wana wa Samweli walikuwa: Yoeli mzaliwa wake wa kwanza, na Abiya mwanawe wa pili.
1CH 6:29 Wafuatao ndio wazao wa Merari: Merari akamzaa Mahli, Mahli akamzaa Libni, Libni akamzaa Shimei, Shimei akamzaa Uza,
1CH 6:30 Uza akamzaa Shimea, Shimea akamzaa Hagia, Hagia akamzaa Asaya.
1CH 6:31 Hawa ndio watu ambao Daudi aliwaweka kuwa viongozi wa uimbaji katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, baada ya Sanduku la Agano kuletwa ili kukaa huko.
1CH 6:32 Walihudumu kwa kuimba mbele ya Maskani, Hema la Kukutania, hadi hapo Mfalme Sulemani alipojenga Hekalu la Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu. Walitimiza wajibu wao kulingana na taratibu walizokuwa wamewekewa.
1CH 6:33 Wafuatao ni watu waliohudumu pamoja na wana wao: Kutoka koo za Wakohathi walikuwa: Hemani, mpiga kinanda, alikuwa mwana wa Yoeli, mwana wa Samweli,
1CH 6:34 mwana wa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elieli, mwana wa Toa,
1CH 6:35 mwana wa Sufu, mwana wa Elkana, mwana wa Mahathi, mwana wa Amasai,
1CH 6:36 mwana wa Elkana, mwana wa Yoeli, mwana wa Azaria, mwana wa Sefania,
1CH 6:37 mwana wa Tahathi, mwana wa Asiri, mwana wa Ebiasafu, mwana wa Kora,
1CH 6:38 mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, mwana wa Israeli;
1CH 6:39 na msaidizi wa Hemani alikuwa Asafu, aliyesimama mkono wa kuume: Asafu mwana wa Berekia, mwana wa Shimea,
1CH 6:40 mwana wa Mikaeli, mwana wa Baaseya, mwana wa Malkiya,
1CH 6:41 mwana wa Ethni, mwana wa Zera, mwana wa Adaya,
1CH 6:42 mwana wa Ethani, mwana wa Zima, mwana wa Shimei,
1CH 6:43 mwana wa Yahathi, mwana wa Gershoni, mwana wa Lawi.
1CH 6:44 Na kutoka kwa walioshirikiana nao, Wamerari, mkono wake wa kushoto: Ethani mwana wa Kishi, mwana wa Abdi, mwana wa Maluki,
1CH 6:45 mwana wa Hashabia, mwana wa Amazia, mwana wa Hilkia,
1CH 6:46 mwana wa Amzi, mwana wa Bani, mwana wa Shemeri,
1CH 6:47 mwana wa Mahli, mwana wa Mushi, mwana wa Merari, mwana wa Lawi.
1CH 6:48 Ndugu zao wengine Walawi walipewa huduma nyingine za kuhudumia hema takatifu, nyumba ya Mungu.
1CH 6:49 Lakini Haruni na uzao wake ndio walikuwa na wajibu wa kutoa sadaka katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba pamoja na yote yaliyofanyika pa Patakatifu, wakifanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, sawasawa na yale yote aliyoagiza Musa mtumishi wa Mungu.
1CH 6:50 Hawa walikuwa wazao wa Haruni: Haruni akamzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Finehasi, Finehasi akamzaa Abishua,
1CH 6:51 Abishua akamzaa Buki, Buki akamzaa Uzi, Uzi akamzaa Zerahia,
1CH 6:52 Zerahia akamzaa Merayothi, Merayothi akamzaa Amaria, Amaria akamzaa Ahitubu,
1CH 6:53 Ahitubu akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Ahimaasi.
1CH 6:54 Zifuatazo ni sehemu walizopewa ziwe nchi yao kwa ajili ya makazi yao (walipewa wazao wa Haruni waliotoka katika ukoo wa Wakohathi, kwa sababu kura ya kwanza iliwaangukia):
1CH 6:55 Walipewa Hebroni katika nchi ya Yuda pamoja na maeneo ya malisho yanayouzunguka.
1CH 6:56 Lakini mashamba pamoja na vijiji vilivyouzunguka mji alipewa Kalebu mwana wa Yefune.
1CH 6:57 Kwa hiyo wazao wa Haruni walipewa miji ifuatayo: Hebroni (mji wa makimbilio), Libna, Yatiri, Eshtemoa,
1CH 6:58 Hileni, Debiri,
1CH 6:59 Ashani, Yuta na Beth-Shemeshi pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:60 Kutoka kabila la Benyamini, walipewa Gibeoni, Geba, Alemethi na Anathothi, pamoja na maeneo yake ya malisho.
1CH 6:61 Wazao waliobaki wa Wakohathi walipewa miji kumi kutoka koo za nusu ya kabila la Manase.
1CH 6:62 Wazao wa Gershoni, kufuatana na koo zao, walipewa miji kumi na tatu kutoka kwa makabila ya Isakari, Asheri na Naftali, na kutoka sehemu ya kabila la Manase huko Bashani.
1CH 6:63 Wazao wa Merari, kufuatana na koo zao walipewa miji kumi na mbili kutoka makabila ya Reubeni, Gadi na Zabuloni.
1CH 6:64 Kwa hiyo Waisraeli waliwapa Walawi miji hii pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:65 Kutoka makabila ya Yuda, Simeoni na Benyamini walipewa miji iliyotajwa hapo juu.
1CH 6:66 Baadhi ya koo za Wakohathi walipewa kama nchi yao miji kutoka kabila la Efraimu.
1CH 6:67 Katika nchi ya vilima ya Efraimu, walipewa Shekemu (mji wa makimbilio) na Gezeri,
1CH 6:68 Yokmeamu, Beth-Horoni,
1CH 6:69 Aiyaloni na Gath-Rimoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:70 Kutoka nusu ya kabila la Manase, Waisraeli waliwapa koo za Wakohathi waliobaki miji ya Aneri na Bileamu pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:71 Wagershoni walipokea miji ifuatayo: Katika nusu ya kabila la Manase, walipokea Golani katika Bashani, na pia Ashtarothi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:72 Kutoka kabila la Isakari walipokea Kedeshi, Daberathi,
1CH 6:73 Ramothi na Anemu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:74 Kutoka kabila la Asheri, walipokea Mashali, Abdoni,
1CH 6:75 Hukoki na Rehobu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:76 Kutoka kabila la Naftali, walipokea Kedeshi katika Galilaya, Hamoni na Kiriathaimu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:77 Wamerari (Walawi waliobakia) walipokea miji ifuatayo: kutoka kabila la Zabuloni, walipokea Yokneamu, Karta, Rimoni na Tabori, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:78 Kutoka kabila la Reubeni, ng’ambo ya Yordani mashariki mwa Yeriko, walipokea Bezeri ulioko jangwani, Yahasa,
1CH 6:79 Kedemothi na Mefaathi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 6:80 Na kutoka kabila la Gadi, walipokea Ramothi huko Gileadi, Mahanaimu,
1CH 6:81 Heshboni na Yazeri, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
1CH 7:1 Wana wa Isakari walikuwa: Tola, Pua, Yashubu na Shimroni; wote ni wanne.
1CH 7:2 Wana wa Tola walikuwa: Uzi, Refaya, Yerieli, Yahmai, Ibsamu na Samweli waliokuwa viongozi wa jamaa zao. Wakati wa utawala wa Mfalme Daudi, wazao wa Tola walioorodheshwa kama wapiganaji katika ukoo wao walikuwa watu elfu ishirini na mbili na mia sita.
1CH 7:3 Mwana wa Uzi alikuwa: Izrahia. Wana wa Izrahia walikuwa: Mikaeli, Obadia, Yoeli na Ishia. Wote hawa watano walikuwa wakuu wao.
1CH 7:4 Kulingana na ukoo wa jamaa zao, walikuwa na watu elfu thelathini na sita waliokuwa wamejiandaa kwa vita, kwa sababu walikuwa na wanawake na watoto wengi.
1CH 7:5 Jamaa waliokuwa wapiganaji kutoka koo zote za Isakari, kama walivyoorodheshwa katika ukoo wao, walikuwa elfu themanini na saba.
1CH 7:6 Wana watatu wa Benyamini walikuwa: Bela, Bekeri na Yediaeli.
1CH 7:7 Wana wa Bela walikuwa: Esboni, Uzi, Uzieli, Yerimothi na Iri; walikuwa viongozi wa jamaa zao; wote ni watano. Wapiganaji walioorodheshwa katika ukoo wao walikuwa elfu ishirini na mbili na thelathini na wanne (22,034).
1CH 7:8 Wana wa Bekeri walikuwa: Zemira, Yoashi, Eliezeri, Elioenai, Omri, Yeremothi, Abiya, Anathothi na Alemethi. Hawa wote walikuwa wana wa Bekeri.
1CH 7:9 Orodha ya ukoo wao iliyoandikwa viongozi wa jamaa zao walikuwa wapiganaji elfu ishirini na mia mbili.
1CH 7:10 Mwana wa Yediaeli alikuwa: Bilhani. Wana wa Bilhani walikuwa: Yeushi, Benyamini, Ehudi, Kenaana, Zethani, Tarshishi na Ahishahari.
1CH 7:11 Hawa wana wote wa Yediaeli walikuwa viongozi wa jamaa zao. Kulikuwa na wapiganaji elfu kumi na saba na mia mbili waliokuwa tayari kwa vita.
1CH 7:12 Washupimu na Wahupimu walikuwa wazao wa Iri. Wahushimu walikuwa wazao wa Aheri.
1CH 7:13 Wana wa Naftali walikuwa: Yahzieli, Guni, Yeseri na Shalumu; hao walikuwa wazao wa Bilha.
1CH 7:14 Wazao wa Manase walikuwa: Asirieli alikuwa mzao wake kutokana na suria wake Mwaramu. Huyu suria akamzaa Makiri baba wa Gileadi.
1CH 7:15 Makiri akatwaa mke kutoka miongoni mwa Wahupimu na Washupimu. Jina la dada yake Makiri aliitwa Maaka. Mwana mwingine wa Makiri aliitwa Selofehadi, aliyekuwa na watoto wa kike tu.
1CH 7:16 Maaka mkewe Makiri akamzaa mwana aliyemwita Pereshi. Jina la nduguye lilikuwa Shereshi. Wana wa Pereshi walikuwa Ulamu na Rakemu.
1CH 7:17 Mwana wa Ulamu alikuwa: Bedani. Hao walikuwa wana wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase.
1CH 7:18 Dada yake aliyeitwa Hamolekethi aliwazaa Ish-Hodi, Abiezeri na Mahla.
1CH 7:19 Wana wa Shemida walikuwa: Ahiani, Shekemu, Liki na Aniamu.
1CH 7:20 Wazao wa Efraimu walikuwa: Shuthela, ambaye alimzaa Beredi, Beredi akamzaa Tahathi, Tahathi akazaa Eleada, Eleada akamzaa Tahathi,
1CH 7:21 Tahathi akamzaa Zabadi, na Zabadi akamzaa Shuthela. Ezeri na Eladi waliuawa na wenyeji wa Gathi walipokuwa wameenda huko kuwanyang’anya mifugo yao.
1CH 7:22 Baba yao Efraimu akawaombolezea kwa siku nyingi, na jamaa zake wakaja kumfariji.
1CH 7:23 Kisha akakutana kimwili na mke wake tena, naye akachukua mimba, akamzalia mwana. Akamwita jina Beria, kwa sababu ya misiba iliyoipata nyumba yake.
1CH 7:24 Beria alikuwa na binti jina lake Sheera. Huyu ndiye aliijenga miji ya Beth-Horoni ya Juu na Beth-Horoni ya Chini, pamoja na Uzen-Sheera.
1CH 7:25 Beria akamzaa pia Refa, naye Refa akamzaa Reshefu, Reshefu akamzaa Tela, Tela akamzaa Tahani,
1CH 7:26 Tahani akamzaa Ladani, Ladani akamzaa Amihudi, Amihudi akamzaa Elishama,
1CH 7:27 Elishama akamzaa Nuni, Nuni akamzaa Yoshua.
1CH 7:28 Nchi zao na makazi yao yalijumuisha Betheli na vijiji vilivyouzunguka, Naarani ilikuwa upande wa mashariki, Gezeri pamoja na vijiji vyake upande wa magharibi, pia Shekemu na vijiji vyake hadi kufikia Aya na vijiji vyake.
1CH 7:29 Katika mipaka ya Manase kulikuwa na Beth-Shani, Taanaki, Megido na Dori pamoja na vijiji vyake. Wazao wa Yusufu mwana wa Israeli waliishi katika miji hii.
1CH 7:30 Wana wa Asheri walikuwa: Imna, Ishva, Ishvi na Beria. Dada yao alikuwa Sera.
1CH 7:31 Wana wa Beria walikuwa: Heberi na Malkieli, aliyekuwa baba yake Birzaithi.
1CH 7:32 Heberi akawazaa Yafleti, Shomeri na Hothamu, na Shua dada yao.
1CH 7:33 Wana wa Yafleti walikuwa: Pasaki, Bimhali na Ashvathi.
1CH 7:34 Wana wa Shemeri walikuwa: Ahi, Roga, Yehuba na Aramu.
1CH 7:35 Wana wa Helemu ndugu yake walikuwa: Sofa, Imna, Sheleshi na Amali.
1CH 7:36 Wana wa Sofa walikuwa: Sua, Harneferi, Shuali, Beri, Imra,
1CH 7:37 Bezeri, Hodu, Shama, Shilsha, Ithrani na Beera.
1CH 7:38 Wana wa Yetheri walikuwa: Yefune, Pispa na Ara.
1CH 7:39 Wana wa Ula walikuwa: Ara, Hanieli na Risia.
1CH 7:40 Hawa wote ndio walikuwa wazao wa Asheri, viongozi wa jamaa zao, watu bora, mashujaa hodari na viongozi maarufu. Idadi ya watu waliokuwa wamejiandaa kwa vita, kama walivyoorodheshwa katika ukoo wao, walikuwa elfu ishirini na sita.
1CH 8:1 Benyamini akamzaa: Bela mzaliwa wake wa kwanza, Ashbeli mwanawe wa pili, Ahara mwanawe wa tatu,
1CH 8:2 Noha mwanawe wa nne na Rafa mwanawe wa tano.
1CH 8:3 Wana wa Bela walikuwa: Adari, Gera, Abihudi,
1CH 8:4 Abishua, Naamani, Ahoa,
1CH 8:5 Gera, Shefufani na Huramu.
1CH 8:6 Hawa ndio wazao wa Ehudi, waliokuwa viongozi wa jamaa za wale walioishi huko Geba na ambao walihamishiwa Manahathi:
1CH 8:7 Naamani, Ahiya na Gera. Gera ndiye aliwapeleka uhamishoni, na alikuwa baba yao Uza na Ahihudi.
1CH 8:8 Shaharaimu aliwazaa wana katika nchi ya Moabu baada ya kuwapa talaka wake zake wawili yaani Hushimu na Baara.
1CH 8:9 Kwa mkewe Hodeshi, akawazaa wana saba: Yobabu, Sibia, Mesha, Malkamu,
1CH 8:10 Yeuzi, Sakia na Mirma. Hao walikuwa wanawe, viongozi wa jamaa zao.
1CH 8:11 Hushimu alimzalia: Abitubu na Elpaali.
1CH 8:12 Wana wa Elpaali walikuwa: Eberi, Mishamu, Shemedi (aliyeijenga miji ya Ono na Lodi, pamoja na vijiji vyake),
1CH 8:13 na Beria na Shema, waliokuwa viongozi wa zile jamaa zilizokuwa zinaishi katika mji wa Aiyaloni, na ambao waliwafukuza wenyeji wa Gathi.
1CH 8:14 Wana wa Beria walikuwa Ahio, Shashaki, Yeremothi,
1CH 8:15 Zebadia, Aradi, Ederi,
1CH 8:16 Mikaeli, Ishpa, na Yoha.
1CH 8:17 Zebadia, Meshulamu, Hizki, Heberi,
1CH 8:18 Ishmerai, Izlia na Yobabu ndio walikuwa wana wa Elpaali.
1CH 8:19 Yakimu, Zikri, Zabdi,
1CH 8:20 Elienai, Silethai, Elieli,
1CH 8:21 Adaya, Beraya na Shimrathi walikuwa wana wa Shimei.
1CH 8:22 Wana wa Shashaki walikuwa Ishpani, Eberi, Elieli,
1CH 8:23 Abdoni, Zikri, Hanani,
1CH 8:24 Hanania, Elamu, Anthothiya,
1CH 8:25 Ifdeya na Penueli.
1CH 8:26 Shamsherai, Sheharia, Athalia,
1CH 8:27 Yaareshia, Ilya na Zikri walikuwa wana wa Yerohamu.
1CH 8:28 Hawa wote walikuwa viongozi wa jamaa zao wakuu, kama walivyoorodheshwa katika koo zao, nao waliishi Yerusalemu.
1CH 8:29 Yeieli alikuwa baba yake Gibeoni naye aliishi huko Gibeoni. Mke wake aliitwa Maaka.
1CH 8:30 Mwanawe mzaliwa wa kwanza alikuwa Abdoni, akafuatiwa na Suri, Kishi, Baali, Neri, Nadabu,
1CH 8:31 Gedori, Ahio, Zekeri,
1CH 8:32 na Miklothi aliyekuwa baba yake Shimea. Hawa pia waliishi karibu na jamaa zao huko Yerusalemu.
1CH 8:33 Neri akamzaa Kishi, Kishi akamzaa Sauli, Sauli akamzaa Yonathani, Malki-Shua, Abinadabu na Esh-Baali.
1CH 8:34 Yonathani akamzaa: Merib-Baali, naye Merib-Baali akamzaa Mika.
1CH 8:35 Wana wa Mika walikuwa: Pithoni, Meleki, Tarea na Ahazi.
1CH 8:36 Ahazi akamzaa Yehoada. Naye Yehoada akawazaa Alemethi, Azmawethi na Zimri, naye Zimri akamzaa Mosa.
1CH 8:37 Mosa akamzaa Binea; Refaya alikuwa mwanawe Binea, Eleasa mwanawe Refaya, naye Aseli mwanawe Eleasa.
1CH 8:38 Aseli alikuwa na wana sita; haya ndiyo majina yao: Azrikamu, Bokeru, Ishmaeli, Shearia, Obadia na Hanani. Hawa wote ndio walikuwa wana wa Aseli.
1CH 8:39 Wana wa Esheki, nduguye Aseli, walikuwa: Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Ulamu, wa pili Yeushi na wa tatu Elifeleti.
1CH 8:40 Wana wa Ulamu walikuwa mashujaa hodari walioweza kutumia upinde. Alikuwa na wana wengi na wajukuu, jumla yao mia moja na hamsini. Hawa wote ndio walikuwa wazao wa Benyamini.
1CH 9:1 Waisraeli wote waliorodheshwa katika koo zilizoandikwa kwenye kitabu cha wafalme wa Israeli. Watu wa Yuda walichukuliwa mateka kwenda Babeli kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa Mungu.
1CH 9:2 Basi watu wa kwanza kurudi kukaa kwenye milki zao katika miji yao walikuwa baadhi ya Waisraeli, makuhani, Walawi na watumishi wa Hekalu.
1CH 9:3 Wale waliotoka Yuda, Benyamini, Efraimu na Manase ambao waliishi Yerusalemu walikuwa:
1CH 9:4 Uthai mwana wa Amihudi, mwana wa Omri, mwana wa Imri, mwana wa Bani, wa wana wa Peresi, mwana wa Yuda.
1CH 9:5 Wazao wa Washiloni waliorudi ni: Asaya mzaliwa wa kwanza na wanawe.
1CH 9:6 Kwa wana wa Zera: Yeueli.
1CH 9:7 Kwa Benyamini walikuwa: Salu mwana wa Meshulamu, mwana wa Hodavia, mwana wa Hasenua;
1CH 9:8 Ibneya mwana wa Yerohamu, Ela mwana wa Uzi, mwana wa Mikri; na Meshulamu mwana wa Shefatia, mwana wa Reueli, mwana wa Ibniya.
1CH 9:9 Watu kutoka Benyamini, kama walivyoorodheshwa katika koo zao, jumla yao walikuwa mia tisa na hamsini na sita (956). Watu hawa wote walikuwa viongozi wa jamaa zao.
1CH 9:10 Wa jamaa za makuhani walikuwa: Yedaya, Yehoyaribu na Yakini;
1CH 9:11 Azaria mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu aliyekuwa afisa kiongozi wa nyumba ya Mungu.
1CH 9:12 Adaya mwana wa Yerohamu, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya; Maasai, mwana wa Adieli, mwana wa Yahzera, mwana wa Meshulamu, mwana wa Meshilemithi, mwana wa Imeri.
1CH 9:13 Makuhani waliokuwa viongozi wa jamaa zao walikuwa elfu moja na mia saba na sitini (1,760). Walikuwa watu wenye uwezo, waliowajibika kuhudumu katika nyumba ya Mungu.
1CH 9:14 Jamaa za Walawi walikuwa: Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, wa wana wa Merari.
1CH 9:15 Bakbakari, Hereshi, Galali na Matania mwana wa Mika, mwana wa Zikri, mwana wa Asafu.
1CH 9:16 Obadia mwana wa Shemaya, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni. Berekia mwana wa Asa, mwana wa Elkana, ambao waliishi katika vijiji vya Wanetofathi.
1CH 9:17 Mabawabu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu waliorudi walikuwa: Shalumu, Akubu, Talmoni, Ahimani na ndugu zao. Shalumu alikuwa mlinzi wao mkuu.
1CH 9:18 Walikuwa wamewekwa katika lango la mfalme lililokuwa upande wa mashariki, hadi wakati huu. Hawa walikuwa mabawabu kutoka kambi ya Walawi.
1CH 9:19 Shalumu mwana wa Kore, mwana wa Ebiasafu, mwana wa Kora, pamoja na mabawabu wenzake kutoka jamaa yake ya Kora waliwajibika kulinda malango ya Hema, kama baba zao walivyokuwa wamewajibika kulinda ingilio la Maskani ya Mwenyezi Mungu.
1CH 9:20 Hapo zamani Finehasi mwana wa Eleazari alikuwa kiongozi wa mabawabu, naye Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye:
1CH 9:21 Zekaria mwana wa Meshelemia alikuwa bawabu katika ingilio la Hema la Kukutania.
1CH 9:22 Jumla ya waliochaguliwa kuwa mabawabu katika sakafu za kupuria nafaka walikuwa watu mia mbili na kumi na wawili (212). Waliandikishwa kwa koo zao kwenye vijiji vyao. Mabawabu hawa waliwekwa katika nafasi zao za kuaminiwa na Daudi, pamoja na Samweli aliyekuwa mwonaji.
1CH 9:23 Wao na wazao wao walikuwa viongozi wa kulinda malango ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, nyumba iliyoitwa Hema.
1CH 9:24 Mabawabu walikuwa pande zote nne: mashariki, magharibi, kaskazini na kusini.
1CH 9:25 Ndugu zao katika vijiji vyao walikuwa wakija mara kwa mara, na kuwasaidia katika kazi zao kwa vipindi mbalimbali vya siku saba.
1CH 9:26 Lakini mabawabu wanne wakuu, waliokuwa Walawi, walikabidhiwa wajibu wa kusimamia vyumba na hazina katika nyumba ya Mungu.
1CH 9:27 Walikesha mahali walipowekwa kuizunguka nyumba ya Mungu, kwa sababu iliwapasa kuilinda. Pia walitunza funguo kwa ajili ya kufungua mlango kila siku asubuhi.
1CH 9:28 Baadhi yao walikuwa viongozi wa kutunza vifaa vilivyotumika katika huduma ndani ya Hekalu; walivihesabu kila vilipoingizwa ndani na kila vilipotolewa.
1CH 9:29 Wengine walipangiwa kutunza mapambo na vifaa vingine vya patakatifu, pamoja na unga, divai, mafuta, uvumba na vikolezo.
1CH 9:30 Lakini baadhi ya makuhani walifanya kazi ya kuchanganya vikolezo.
1CH 9:31 Mlawi aliyeitwa Matithia, mwana mzaliwa wa kwanza wa Shalumu, wa ukoo wa Kora, alikabidhiwa wajibu kwa ajili ya kuoka mikate ya sadaka.
1CH 9:32 Baadhi ya ndugu zao wa koo za Wakohathi walikuwa viongozi wa kuandaa mikate ya Wonesho kwa ajili ya kila Sabato, mikate iliyokuwa inawekwa mezani.
1CH 9:33 Wale waliokuwa waimbaji, viongozi wa jamaa za Walawi, waliishi katika vyumba vya Hekalu, nao hawakufanya shughuli nyingine yoyote kwa sababu iliwapasa kuwajibika kwa kazi hiyo usiku na mchana.
1CH 9:34 Hawa wote walikuwa viongozi wa jamaa za Walawi, wakuu kama walivyoorodheshwa katika koo zao, nao waliishi Yerusalemu.
1CH 9:35 Yeieli alikuwa baba yake Gibeoni, naye aliishi huko Gibeoni. Mke wake aliitwa Maaka,
1CH 9:36 mwanawe mzaliwa wa kwanza alikuwa Abdoni, akafuatiwa na Suri, Kishi, Baali, Neri, Nadabu,
1CH 9:37 Gedori, Ahio, Zekaria na Miklothi.
1CH 9:38 Miklothi akamzaa Shimeamu. Wao pia waliishi karibu na jamaa zao huko Yerusalemu.
1CH 9:39 Neri akamzaa Kishi, Kishi akamzaa Sauli. Sauli akamzaa Yonathani, Malki-Shua, Abinadabu na Esh-Baali.
1CH 9:40 Yonathani akamzaa Merib-Baali, naye Merib-Baali akamzaa Mika.
1CH 9:41 Wana wa Mika walikuwa: Pithoni, Meleki, Tarea, na Ahazi.
1CH 9:42 Ahazi akamzaa Yara, Yara akawazaa Alemethi, Azmawethi na Zimri, naye Zimri akamzaa Mosa.
1CH 9:43 Mosa akamzaa Binea, Binea akamzaa Refaya, na mwanawe huyo ni Eleasa, na mwanawe huyo ni Aseli.
1CH 9:44 Aseli alikuwa na wana sita, na haya ndiyo majina yao: Azrikamu, Bokeru, Ishmaeli, Shearia, Obadia na Hanani. Hao walikuwa wana wa Aseli.
1CH 10:1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika mlima Gilboa.
1CH 10:2 Wafilisti wakawafuatilia Sauli na wanawe kwa karibu, na wakawaua Yonathani, Abinadabu, na Malki-Shua.
1CH 10:3 Mapigano yakawa makali kumzunguka Sauli na wakati wapiga mishale walipompata, wakamjeruhi.
1CH 10:4 Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja na kunidhalilisha.” Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia.
1CH 10:5 Mbeba silaha wake alipoona kwamba Sauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake akafa.
1CH 10:6 Kwa hiyo Sauli na wanawe watatu wakafa, pamoja na nyumba yake yote.
1CH 10:7 Waisraeli wote waliokuwa bondeni walipoona kwamba jeshi limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, waliacha miji yao wakakimbia. Nao Wafilisti wakaenda na kuyamiliki.
1CH 10:8 Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe wameanguka katika Mlima Gilboa.
1CH 10:9 Wakamvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, wakawatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari hizi miongoni mwa sanamu zao na watu wao.
1CH 10:10 Waliweka silaha zake katika hekalu la miungu yao, na wakatundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.
1CH 10:11 Wakazi wote wa Yabesh-Gileadi waliposikia yale Wafilisti waliyomtendea Sauli,
1CH 10:12 mashujaa wao wote wakaondoka, wakautwaa mwili wa Sauli na miili ya wanawe, wakaileta Yabeshi. Wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni ulio Yabeshi, nao wakafunga kwa siku saba.
1CH 10:13 Sauli alikufa kwa sababu hakuwa mwaminifu kwa Mwenyezi Mungu. Hakulishika neno la Mwenyezi Mungu, hata akataka shauri kwa mwaguzi kwa ajili ya uongozi,
1CH 10:14 hakumuuliza Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu alimuua, na ufalme akampa Daudi mwana wa Yese.
1CH 11:1 Waisraeli wote walimjia Daudi kwa pamoja huko Hebroni, wakamwambia, “Sisi ni mwili wako na damu yako.
1CH 11:2 Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”
1CH 11:3 Wazee wote wa Israeli walipokuwa wamewasili kwa Mfalme Daudi huko Hebroni, alifanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Mwenyezi Mungu, nao wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu aliloahidi kupitia kwa Samweli.
1CH 11:4 Daudi na Waisraeli wote wakaenda Yerusalemu (ndio Yebusi). Nao Wayebusi walioishi humo
1CH 11:5 wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu.” Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.
1CH 11:6 Daudi alikuwa amesema, “Yeyote atakayeongoza mashambulizi dhidi ya Wayebusi atakuwa jemadari mkuu.” Yoabu mwana wa Seruya akawa wa kwanza kukwea, naye akawa mkuu.
1CH 11:7 Daudi akafanya makao yake kwenye ngome, hivyo ukaitwa Mji wa Daudi.
1CH 11:8 Akajenga mji pande zote, kuanzia Milo hadi kwenye ukuta kuzunguka; wakati huo huo Yoabu akajenga sehemu zingine zilizobaki za Yerusalemu.
1CH 11:9 Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni alikuwa pamoja naye.
1CH 11:10 Hawa walikuwa wakuu wa mashujaa wa Daudi: wao pamoja na Waisraeli wote wakauimarisha ufalme wake ili kuenea katika nchi yote, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu aliloahidi.
1CH 11:11 Hii ndio orodha ya mashujaa wa Daudi: Yashobeamu Mhakmoni alikuwa mkuu wa maafisa; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu, aliowaua katika pambano moja.
1CH 11:12 Aliyefuata alikuwa Eleazari, mwana wa Dodai Mwahohi, mmoja wa wale mashujaa watatu.
1CH 11:13 Huyo alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-Damimu, wakati Wafilisti walikusanyika huko kwa ajili ya vita. Mahali palipokuwa na shamba limejaa shayiri, vikosi vya Israeli vikawakimbia Wafilisti.
1CH 11:14 Lakini Eleazari na Daudi wakasimama imara katikati ya lile shamba, nao wakalishindania na kuwaua Wafilisti. Naye Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa.
1CH 11:15 Wakuu watatu miongoni mwa wale thelathini walimwendea Daudi kwenye mwamba, katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti walikuwa wamepiga kambi katika Bonde la Warefai.
1CH 11:16 Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu.
1CH 11:17 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilichoko karibu na lango la Bethlehemu!”
1CH 11:18 Kwa hivyo wale watatu, wakapita katikati ya safu za Wafilisti, wakachota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini yeye akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Mwenyezi Mungu.
1CH 11:19 Akasema, “Mungu apishie mbali kwamba nifanye hivi! Je kweli, niinywe damu ya watu hawa waliohatarisha maisha yao?” Kwa sababu walihatarisha maisha yao kuyaleta yale maji, Daudi hakukubali kuyanywa. Huo ndio uliokuwa ujasiri wa wale mashujaa watatu.
1CH 11:20 Abishai, ndugu yake Yoabu ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu, ambao aliwaua; kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu.
1CH 11:21 Alitunukiwa heshima maradufu ya wale Watatu, akawa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.
1CH 11:22 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba.
1CH 11:23 Alimuua Mmisri aliyekuwa na urefu kama dhiraa tano. Ingawa huyo Mmisri alikuwa na mkuki kama mti wa mfumaji mkononi, Benaya alimwendea na rungu. Akamnyang’anya Mmisri mkuki wake na kumuua nao.
1CH 11:24 Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu.
1CH 11:25 Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu: Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.
1CH 11:26 Wale mashujaa walikuwa: Asaheli nduguye Yoabu, Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu,
1CH 11:27 Shamothi Mharori, Helesi Mpeloni,
1CH 11:28 Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa, Abiezeri kutoka Anathothi,
1CH 11:29 Sibekai Mhushathi, Ilai Mwahohi,
1CH 11:30 Maharai Mnetofathi, Heledi mwana wa Baana Mnetofathi,
1CH 11:31 Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini, Benaya Mpirathoni,
1CH 11:32 Hurai kutoka mabonde ya Gaashi, Abieli Mwaribathi,
1CH 11:33 Azmawethi Mbaharumi, Eliaba Mshaalboni,
1CH 11:34 wana wa Hashemu Mgiloni, Yonathani mwana wa Shagee Mharari,
1CH 11:35 Ahiamu mwana wa Sakari Mharari, Elifale mwana wa Uru,
1CH 11:36 Heferi Mmekerathi, Ahia Mpeloni,
1CH 11:37 Hezro Mkarmeli, Naarai mwana wa Ezbai,
1CH 11:38 Yoeli nduguye Nathani, Mibhari mwana wa Hagri,
1CH 11:39 Seleki Mwamoni, Naharai Mbeerothi, mbeba silaha wa Yoabu mwana wa Seruya,
1CH 11:40 Ira Mwithiri, Garebu Mwithiri,
1CH 11:41 Uria Mhiti, Zabadi mwana wa Alai,
1CH 11:42 Adina mwana wa Shiza Mreubeni, aliyekuwa mkuu wa Wareubeni, akiwa pamoja na watu thelathini,
1CH 11:43 Hanani mwana wa Maaka, Yoshafati Mmithni,
1CH 11:44 Uzia Mwashterathi, Shama na Yeieli wana wa Hothamu Mwaroeri,
1CH 11:45 Yediaeli mwana wa Shimri, nduguye Yoha Mtizi,
1CH 11:46 Elieli Mmahawi, Yeribai na Yoshavia wana wa Elnaamu, Ithma Mmoabu,
1CH 11:47 Elieli, na Obedi na Yaasieli Mmesobai.
1CH 12:1 Hawa ndio watu waliomjia Daudi huko Siklagi, wakati alikuwa amefukuzwa mbele ya Sauli mwana wa Kishi (walikuwa miongoni mwa mashujaa waliomsaidia Daudi vitani.
1CH 12:2 Walikuwa na pinde na walikuwa na uwezo wa kupiga mishale au kutupa mawe kwa kombeo wakitumia mkono wa kushoto au wa kulia. Hawa walikuwa ndugu zake Sauli kutoka kabila la Benyamini):
1CH 12:3 Mkuu wao alikuwa Ahiezeri, na wa pili Yoashi, wote wana wa Shemaa Mgibeathi; pia Yezieli na Peleti wana wa Azmawethi; Beraka, Yehu Mwanathothi,
1CH 12:4 na Ishmaya Mgibeoni, shujaa miongoni mwa wale Thelathini, aliyekuwa kiongozi wa wale Thelathini; Yeremia, Yahazieli, Yohanani, Yozabadi Mgederathi,
1CH 12:5 Eluzai, Yerimothi, Bealia, Shemaria, Shefatia Mharufi;
1CH 12:6 Elkana, Ishia, Azareli, Yoezeri na Yashobeamu wana wa Kora;
1CH 12:7 Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu kutoka Gedori.
1CH 12:8 Baadhi ya Wagadi wakajitenga na kujiunga na Daudi katika ngome yake huko jangwani. Walikuwa mashujaa hodari, wakiwa wamejiandaa kwa vita, na wenye uwezo wa kutumia ngao na mkuki. Nyuso zao zilikuwa nyuso za simba na walikuwa na wepesi kama paa milimani.
1CH 12:9 Ezeri alikuwa mkuu wao, Obadia alikuwa wa pili katika uongozi, Eliabu wa tatu,
1CH 12:10 Mishmana wa nne, Yeremia wa tano,
1CH 12:11 Atai wa sita, Elieli wa saba,
1CH 12:12 Yohanani wa nane, Elzabadi wa tisa,
1CH 12:13 Yeremia wa kumi, na Makbanai wa kumi na moja.
1CH 12:14 Hawa Wagadi walikuwa majemadari. Aliyekuwa mdogo alikuwa kama watu mia moja, naye aliyekuwa mkuu alikuwa kama watu elfu moja.
1CH 12:15 Hao ndio walivuka Mto Yordani katika mwezi wa kwanza ukiwa umefurika hadi kwenye kingo zake zote, wakawatorosha watu wote walioishi kwenye mabonde, kuelekea mashariki na magharibi.
1CH 12:16 Wabenyamini wengine na baadhi ya watu kutoka Yuda pia walikuja kwa Daudi katika ngome yake.
1CH 12:17 Daudi akatoka nje kuwalaki na akawaambia, “Kama mmekuja kwangu kwa amani, kunisaidia, mimi niko tayari kuwaruhusu ninyi kuungana nami. Lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu wakati mikono yangu haina hatia, basi Mungu wa baba zetu aone na awahukumu.”
1CH 12:18 Kisha Roho wa Mungu akaja juu ya Amasai, mkuu wa wale Thelathini, naye akasema: “Sisi tu watu wako, ee Daudi! Nasi tuko pamoja na wewe, ee mwana wa Yese! Amani, naam, amani iwe kwako, pia amani kwa wale walio upande wako, kwa kuwa Mungu wako atakusaidia.” Kwa hiyo Daudi akawapokea na kuwafanya viongozi wa vikosi vyake vya uvamizi.
1CH 12:19 Baadhi ya watu kutoka kabila la Manase wakajiunga na Daudi alipoenda pamoja na Wafilisti kupigana na Sauli. (Daudi na watu wake hawakuwasaidia Wafilisti kwa sababu baada ya ushauri, watawala wao walimrudisha. Wakasema, “Itatugharimu vichwa vyetu kama Daudi atatuasi na kurudi kwa Sauli bwana wake.”)
1CH 12:20 Daudi alipoenda Siklagi, hawa ndio wanaume wa kabila la Manase waliojiunga naye: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai, viongozi wa vikosi vya watu elfu moja katika kabila la Manase.
1CH 12:21 Walimsaidia Daudi dhidi ya makundi ya uvamizi, kwa kuwa wote walikuwa mashujaa hodari na walikuwa majemadari katika jeshi lake.
1CH 12:22 Siku baada ya siku watu walikuja kumsaidia Daudi, hadi akawa na jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu.
1CH 12:23 Hawa ndio watu waliojiandaa kwa ajili ya vita waliokuja kwa Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Sauli, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema:
1CH 12:24 watu wa Yuda, wanaochukua ngao na mikuki walikuwa elfu sita na mia nane wakiwa tayari kwa vita.
1CH 12:25 Watu wa Simeoni, mashujaa waliokuwa wamejiandaa kwa vita, walikuwa elfu saba na mia moja.
1CH 12:26 Watu wa Lawi walikuwa elfu nne na mia sita,
1CH 12:27 pamoja na Yehoyada, kiongozi wa jamaa ya Haruni, aliyekuwa na watu elfu tatu na mia saba,
1CH 12:28 na Sadoki, kijana shujaa hodari, aliyekuwa na maafisa ishirini na wawili kutoka jamaa yake.
1CH 12:29 Watu wa Benyamini, ndugu zake Sauli, walikuwa elfu tatu; wengi wao walikuwa wameendelea kuwa waaminifu kwa Sauli hadi wakati huo.
1CH 12:30 Watu wa Efraimu, mashujaa hodari elfu ishirini na mia nane, watu waliokuwa maarufu katika koo zao.
1CH 12:31 Watu wa nusu ya kabila la Manase, waliotajwa kwa majina ili waje kumweka Daudi kuwa mfalme, watu elfu kumi na nane.
1CH 12:32 Watu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya, walikuwa viongozi mia mbili, pamoja na jamaa zao wote chini ya uongozi wao.
1CH 12:33 Watu wa Zabuloni, wapiganaji hodari, tayari kwa vita wakiwa na silaha za kila aina, ili kumsaidia Daudi kwa uaminifu thabiti, walikuwa elfu hamsini.
1CH 12:34 Watu wa Naftali, maafisa elfu moja, pamoja na watu elfu thelathini na saba wenye ngao na mikuki.
1CH 12:35 Watu wa Dani, elfu ishirini na nane na mia sita waliokuwa wamejiandaa kwa vita.
1CH 12:36 Watu wa Asheri, wapiganaji hodari elfu arobaini waliokuwa wameandaliwa kwa vita.
1CH 12:37 Na pia watu kutoka mashariki mwa Yordani, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakiwa na kila aina ya silaha, walikuwa elfu mia moja na ishirini.
1CH 12:38 Wote hawa walikuwa wapiganaji waliojitolea kutumika katika jeshi. Walikuja Hebroni wakiwa wameamua kikamilifu kumfanya Daudi mfalme juu ya Israeli yote. Waisraeli wengine wote walikuwa pia na nia hiyo moja ya kumfanya Daudi kuwa mfalme.
1CH 12:39 Watu hawa wakakaa huko na Daudi siku tatu, wakila na kunywa, kwa sababu jamaa zao zilikuwa zimewapatia mahitaji yao.
1CH 12:40 Pia, majirani zao hata wale walio mbali hadi Isakari, Zabuloni na Naftali, walikuja wakiwaletea vyakula walivyovibeba kwa punda, ngamia, nyumbu na maksai. Kulikuwa na wingi wa unga, maandazi ya tini, maandazi ya zabibu kavu, divai, mafuta, ng’ombe na kondoo, kwa maana kulikuwa na furaha katika Israeli.
1CH 13:1 Daudi alishauriana na kila kiongozi wake, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia.
1CH 13:2 Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote la Israeli, “Mkiona ni vyema, na kama ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tupeleke ujumbe kwa ndugu zetu wengine walio mbali na walio karibu katika nchi yote ya Israeli, pia kwa makuhani na Walawi walio pamoja nao katika miji yao na maeneo ya malisho ya miji hiyo, waje waungane na sisi.
1CH 13:3 Sisi na tulirudishe Sanduku la Mungu wetu kwetu kwa maana hatukujali wakati wa utawala wa Sauli.”
1CH 13:4 Kusanyiko lote wakakubaliana kufanya hivyo, kwa sababu ilionekana vyema kwa watu wote.
1CH 13:5 Basi Daudi akawakusanya Waisraeli wote, kuanzia Mto Shihori ulioko Misri hadi Lebo-Hamathi, ili kulileta Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu.
1CH 13:6 Daudi akiwa pamoja na Waisraeli wote wakaenda Baala ya Yuda (yaani Kiriath-Yearimu) kulipandisha Sanduku la Mungu Mwenyezi Mungu, yeye anayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi: Sanduku linaloitwa kwa Jina lake.
1CH 13:7 Wakalisafirisha Sanduku la Mungu kwa gari jipya la kukokotwa kutoka nyumba ya Abinadabu; nao Uza na Ahio waliliongoza gari hilo.
1CH 13:8 Daudi pamoja na Waisraeli wote walikuwa wanasifu kwa nguvu zao zote mbele za Mungu, kwa nyimbo na kwa vinubi, zeze, matari, matoazi na tarumbeta.
1CH 13:9 Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza akaunyoosha mkono wake ili kulizuia Sanduku, kwa sababu maksai walijikwaa.
1CH 13:10 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Uza, akampiga kwa sababu aliuweka mkono wake kwenye Sanduku. Kwa hiyo akafa pale mbele za Mungu.
1CH 13:11 Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ilifurika dhidi ya Uza, mahali pale pakaitwa Peres-Uza hadi leo.
1CH 13:12 Siku ile Daudi akamwogopa Mungu naye akauliza. “Nitawezaje kulichukua Sanduku la Mungu kwangu?”
1CH 13:13 Hakulichukua hilo Sanduku akae nalo katika Mji wa Daudi. Badala yake, akalipeleka nyumbani mwa Obed-Edomu, Mgiti.
1CH 13:14 Sanduku la Mungu likakaa kwa jamaa ya Obed-Edomu, nyumbani mwake kwa miezi mitatu, naye Mwenyezi Mungu akaibariki nyumba yake pamoja na kila kitu alichokuwa nacho.
1CH 14:1 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, waashi na maseremala ili kumjengea jumba la kifalme.
1CH 14:2 Naye Daudi akatambua kwamba Mwenyezi Mungu amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake.
1CH 14:3 Huko Yerusalemu Daudi akaoa wake wengine zaidi na akawa baba wa wana wengi wa kiume na wa kike.
1CH 14:4 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani,
1CH 14:5 Ibihari, Elishua, Elpeleti,
1CH 14:6 Noga, Nefegi, Yafia,
1CH 14:7 Elishama, Beeliada na Elifeleti.
1CH 14:8 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli yote, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akatoka ili kwenda kukabiliana nao.
1CH 14:9 Basi Wafilisti walikuwa wameingia na kushambulia Bonde la Warefai,
1CH 14:10 Hivyo Daudi akamuuliza Mungu: “Je, niende kuwashambulia hao Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.”
1CH 14:11 Hivyo Daudi pamoja na watu wake wakakwea hadi Baal-Perasimu, akawashinda huko. Akasema, “Kama maji yanavyofurika, Mungu amewafurikia adui zangu kwa kutumia mkono wangu.” Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Baal-Perasimu.
1CH 14:12 Wafilisti walikuwa wametupa miungu yao huko, naye Daudi akaamuru iteketezwe kwa moto.
1CH 14:13 Kwa mara nyingine Wafilisti wakavamia lile bonde;
1CH 14:14 hivyo Daudi akamuuliza Mungu tena, naye Mungu akamjibu, “Usiwafuate moja kwa moja, bali wazungukie na uwashambulie kutoka mbele ya hiyo miti ya miforosadi.
1CH 14:15 Mara utakaposikia sauti ya kutembea vileleni vya miti ya miforosadi, basi utoke upigane vita, kwa sababu hiyo itaonesha kwamba Mungu amekutangulia ili kupiga jeshi la Wafilisti.”
1CH 14:16 Kwa hiyo Daudi akafanya kama alivyoagizwa na Mungu, wakalipiga jeshi la Wafilisti kuanzia Gibeoni hadi Gezeri.
1CH 14:17 Hivyo umaarufu wa Daudi ukaenea katika kila nchi, naye Mwenyezi Mungu akayafanya mataifa yote kumwogopa Daudi.
1CH 15:1 Baada ya Daudi kujijengea nyumba zake katika Mji wa Daudi, akatengeneza sehemu kwa ajili ya Sanduku la Mungu, na akasimamisha hema kwa ajili yake.
1CH 15:2 Kisha Daudi akasema, “Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulibeba Sanduku la Mungu isipokuwa Walawi peke yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwachagua kulibeba Sanduku la Mwenyezi Mungu na kuhudumu mbele zake milele.”
1CH 15:3 Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu ili kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu na kulileta hadi kwenye sehemu aliyokuwa ametengeneza kwa ajili yake.
1CH 15:4 Kisha Daudi akawakusanya wazao wa Haruni na Walawi:
1CH 15:5 Kutoka wazao wa Kohathi, Urieli kiongozi na ndugu zake mia moja na ishirini.
1CH 15:6 Kutoka wazao wa Merari, Asaya kiongozi na ndugu zake mia mbili na ishirini.
1CH 15:7 Kutoka wazao wa Gershoni, Yoeli kiongozi na ndugu zake mia moja na thelathini.
1CH 15:8 Kutoka wazao wa Elisafani, Shemaya kiongozi na ndugu zake mia mbili.
1CH 15:9 Kutoka wazao wa Hebroni, Elieli kiongozi na ndugu zake themanini.
1CH 15:10 Kutoka wazao wa Uzieli, Aminadabu kiongozi na ndugu zake mia moja na kumi na wawili (112).
1CH 15:11 Kisha Daudi akawaita makuhani Sadoki na Abiathari, pamoja na Walawi Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu.
1CH 15:12 Akawaambia, “Ninyi ndio viongozi wa jamaa za Walawi. Ninyi pamoja na Walawi wenzenu inawapasa mjitakase na kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali pale nimetengeneza kwa ajili yake.
1CH 15:13 Ilikuwa ni kwa sababu hii, ninyi Walawi, hamkulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu mara ya kwanza, hata ikasababisha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kuwaka hasira dhidi yetu. Hatukumuuliza jinsi ya kufanya ili tupate kulileta jinsi alivyoagiza.”
1CH 15:14 Kwa hiyo makuhani pamoja na Walawi wakajitakasa ili kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
1CH 15:15 Nao Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu mabegani mwao wakitumia mipiko, kama vile Musa alivyoamuru sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu.
1CH 15:16 Daudi akawaambia viongozi wa Walawi wawateue ndugu zao waimbaji ili waimbe nyimbo za shangwe, wakiwa na vyombo vya uimbaji: zeze, vinubi na matoazi.
1CH 15:17 Basi Walawi wakawateua Hemani mwana wa Yoeli; kutoka miongoni mwa ndugu zake, Asafu mwana wa Berekia; kutoka miongoni mwa ndugu zao Wamerari, Ethani mwana wa Kushaiya;
1CH 15:18 hawa ndio waliochaguliwa kuwa wasaidizi wao: Zekaria, Yaazieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu, Mikneya, pamoja na mabawabu Obed-Edomu na Yehieli.
1CH 15:19 Waimbaji Hemani, Asafu na Ethani walichaguliwa kupiga matoazi ya shaba;
1CH 15:20 Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya walikuwa wapiga zeze kufuatana na sauti ya alamothi,
1CH 15:21 na Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-Edomu, Yehieli na Azazia walikuwa wapiga vinubi, wakiongozwa kwa kufuata sauti ya sheminithi.
1CH 15:22 Kenania kiongozi wa Walawi alikuwa msimamizi wa uimbaji; huu ndio uliokuwa wajibu wake kwa sababu alikuwa stadi katika hilo.
1CH 15:23 Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya Sanduku.
1CH 15:24 Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, makuhani, walikuwa wapiga tarumbeta mbele ya Sanduku la Mungu. Obed-Edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa mabawabu wa Sanduku.
1CH 15:25 Basi Daudi pamoja na wazee wa Israeli na majemadari wa vikosi vya elfu wakaenda ili kulipandisha Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu kwa shangwe.
1CH 15:26 Kwa sababu Mungu alikuwa amewasaidia Walawi waliokuwa wanalichukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, mafahali saba na kondoo dume saba walitolewa dhabihu.
1CH 15:27 Basi Daudi alikuwa amevaa joho la kitani safi, kama walivyokuwa wamevaa Walawi wote waliokuwa wanalichukua lile Sanduku, waimbaji nao walivaa vivyo hivyo, pamoja na Kenania aliyekuwa anaongoza nyimbo za waimbaji. Daudi alivaa pia kizibau cha kitani safi.
1CH 15:28 Hivyo Israeli wote wakalipandisha Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kwa shangwe, wakipiga pembe za kondoo dume, tarumbeta, na kucheza matoazi, zeze na vinubi.
1CH 15:29 Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu lilipokuwa linaingia Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akicheza na kusherehekea, akamdharau moyoni mwake.
1CH 16:1 Wakaleta Sanduku la Mungu na kuliweka ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, na wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu.
1CH 16:2 Baada ya Daudi kumaliza kutoa hizo sadaka za kuteketezwa na hizo sadaka za amani, akawabariki watu katika jina la Mwenyezi Mungu.
1CH 16:3 Kisha akamgawia kila Mwisraeli mwanaume na mwanamke mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu.
1CH 16:4 Akawaweka pia baadhi ya Walawi ili wahudumu mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu kufanya maombi, kumshukuru na kumsifu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli:
1CH 16:5 Asafu ndiye alikuwa mkuu wao, akisaidiwa na Zekaria, Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Matithia, Eliabu, Benaya, Obed-Edomu na Yeieli. Hawa ndio wangepiga zeze na vinubi, Asafu angepiga matoazi,
1CH 16:6 nao Benaya na Yahazieli makuhani, ndio wangepiga tarumbeta mara kwa mara mbele ya Sanduku la Agano la Mungu.
1CH 16:7 Siku ile, kitu cha kwanza Daudi alichofanya ni kumkabidhi Asafu na wenzake zaburi hii ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu:
1CH 16:8 Mshukuruni Mwenyezi Mungu, liitieni jina lake; wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
1CH 16:9 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa; waambieni matendo yake yote ya ajabu.
1CH 16:10 Lishangilieni jina lake takatifu; mioyo ya wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu na ifurahi.
1CH 16:11 Mtafuteni Mwenyezi Mungu na nguvu zake; utafuteni uso wake siku zote.
1CH 16:12 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka,
1CH 16:13 enyi wazao wa Israeli mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
1CH 16:14 Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mungu wetu; hukumu zake ziko duniani kote.
1CH 16:15 Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
1CH 16:16 agano alilolifanya na Ibrahimu, kiapo alichomwapia Isaka.
1CH 16:17 Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele:
1CH 16:18 “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.”
1CH 16:19 Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake,
1CH 16:20 walitangatanga kutoka taifa moja hadi lingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
1CH 16:21 Hakuruhusu mtu yeyote awadhulumu; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
1CH 16:22 “Msiwaguse niliowapaka mafuta; msiwadhuru manabii wangu.”
1CH 16:23 Mwimbieni Mwenyezi Mungu dunia yote; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
1CH 16:24 Tangazeni utukufu wake katika mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
1CH 16:25 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu, mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
1CH 16:26 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu.
1CH 16:27 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
1CH 16:28 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi jamaa za mataifa, mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu,
1CH 16:29 mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake. Leteni sadaka na mje katika nyua zake. Mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake.
1CH 16:30 Dunia yote na itetemeke mbele zake! Ulimwengu ameuweka imara; hauwezi kusogezwa.
1CH 16:31 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; semeni katika mataifa, “Mwenyezi Mungu anatawala!”
1CH 16:32 Bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake; mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo.
1CH 16:33 Kisha miti ya msituni itaimba, itaimba kwa furaha mbele za Mwenyezi Mungu, kwa maana anakuja kuihukumu dunia.
1CH 16:34 Mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mwema; fadhili zake zadumu milele.
1CH 16:35 Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe. Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako.”
1CH 16:36 Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni Mwenyezi Mungu.”
1CH 16:37 Daudi akamwacha Asafu na wenzake mbele ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, ili wahudumu humo mara kwa mara, kulingana na mahitaji ya kila siku.
1CH 16:38 Pia akamwacha Obed-Edomu pamoja na wenzake sitini na wanane wahudumu pamoja nao. Obed-Edomu mwana wa Yeduthuni na pia Hosa walikuwa mabawabu wa lango.
1CH 16:39 Daudi akamwacha kuhani Sadoki pamoja na makuhani wenzake mbele ya hema la ibada la Mwenyezi Mungu katika mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni
1CH 16:40 ili kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu kwenye madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mara kwa mara, asubuhi na jioni, sawasawa na kila kitu kilichoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu ambayo alikuwa amempa Israeli.
1CH 16:41 Waliohudumu pamoja nao walikuwa Hemani, Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa na kutajwa kwa jina kumpa Mwenyezi Mungu shukrani, “Kwa maana fadhili zake zadumu milele.”
1CH 16:42 Hemani na Yeduthuni walikuwa na wajibu wa kupiga tarumbeta, matoazi na kutumia vyombo vingine kwa ajili ya nyimbo za sifa kwa Mungu. Wana wa Yeduthuni waliwekwa langoni.
1CH 16:43 Kisha watu wote wakaondoka, kila mmoja akarudi nyumbani mwake, naye Daudi akarudi nyumbani kuibariki jamaa yake.
1CH 17:1 Baada ya Daudi kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mwerezi, wakati Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu liko ndani ya hema.”
1CH 17:2 Nathani akamjibu Daudi, “Lolote ulilo nalo moyoni mwako litende, kwa maana Mungu yu pamoja nawe.”
1CH 17:3 Usiku ule neno la Mungu likamjia Nathani, kusema:
1CH 17:4 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Wewe hutanijengea mimi nyumba ili nikae humo.
1CH 17:5 Mimi sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowatoa Israeli kutoka Misri hadi leo. Nimehama kutoka hema moja hadi jingine, na kutoka mahali pamoja hadi pengine.
1CH 17:6 Popote nilipoenda pamoja na Waisraeli wote, je, kuna wakati nilimuuliza kiongozi yeyote niliyemwagiza kuwachunga watu wangu, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mwerezi?” ’
1CH 17:7 “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Nilikutoa malishoni na kutoka kulisha mifugo, ili uwaongoze watu wangu Israeli.
1CH 17:8 Nimekuwa pamoja nawe popote ulipoenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani.
1CH 17:9 Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali na nitawapa ili wawe na mahali pao wenyewe pa kuishi na wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzoni,
1CH 17:10 na ambavyo wamefanya siku zote tangu nilipowachagua viongozi kwa ajili ya watu wangu Israeli. Pia nitawatiisha adui zenu wote. “ ‘Pamoja na hayo ninakuambia kwamba Mwenyezi Mungu atakujengea nyumba:
1CH 17:11 Siku zako zikiisha, nawe ukaenda kulala na baba zako, nitamwinua mzao wako kuwa mfalme baada yako, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitauimarisha ufalme wake.
1CH 17:12 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakiimarisha kiti cha ufalme wake milele.
1CH 17:13 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yule aliyekutangulia.
1CH 17:14 Nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; kiti chake cha utawala nitakiimarisha milele.’ ”
1CH 17:15 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.
1CH 17:16 Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Mwenyezi Mungu, akasema: “Mimi ni nani, Ee Bwana Mwenyezi Mungu, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa?
1CH 17:17 Kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Mungu, umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukuka kuliko watu wote, Ee Bwana Mwenyezi Mungu.
1CH 17:18 “Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako,
1CH 17:19 Ee Mwenyezi Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kuu na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kuu sana.
1CH 17:20 “Hakuna aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe.
1CH 17:21 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya maajabu makubwa na ya kutisha, kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri?
1CH 17:22 Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee Mwenyezi Mungu, umekuwa Mungu wao.
1CH 17:23 “Basi sasa, Ee Mwenyezi Mungu, ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake, na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi,
1CH 17:24 ili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako.
1CH 17:25 “Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya.
1CH 17:26 Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri.
1CH 17:27 Basi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele machoni pako; kwa ajili yako, Ee Mwenyezi Mungu, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”
1CH 18:1 Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akatwaa Gathi pamoja na vijiji vinavyouzunguka kutoka utawala wa Wafilisti.
1CH 18:2 Pia Daudi akawashinda Wamoabu, wakawa watumishi wake, nao wakawa wanamletea ushuru.
1CH 18:3 Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mfalme wa Soba, hadi Hamathi, wakati alienda kuimarisha utawala wake katika Mto Frati.
1CH 18:4 Daudi akateka magari ya vita elfu moja miongoni mwa magari yake, waendesha hayo magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu ishirini. Daudi akakata mishipa ya miguu ya farasi wa magari ya vita, akabakiza farasi mia moja.
1CH 18:5 Waaramu wa Dameski, walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua watu elfu ishirini na mbili miongoni mwao.
1CH 18:6 Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski. Basi Waaramu wakawa watumwa wa Daudi, na kumlipa ushuru. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kote alipoenda.
1CH 18:7 Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu.
1CH 18:8 Kutoka miji ya Tibathi na Kuni, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi sana, ambayo Sulemani aliitumia kutengenezea ile Bahari ya shaba, zile nguzo na vifaa mbalimbali vya shaba.
1CH 18:9 Tou mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba,
1CH 18:10 akamtuma mwanawe Hadoramu kwa Mfalme Daudi, ili kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Mfalme Hadadezeri, kwa maana alikuwa amepigana vita mara nyingi na Tou. Hadoramu akamletea Daudi vifaa mbalimbali vya dhahabu, fedha na shaba.
1CH 18:11 Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu aliyokuwa ameitwaa katika mataifa haya yote: Edomu na Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki.
1CH 18:12 Abishai mwana wa Seruya akawaua Waedomu elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi.
1CH 18:13 Akaweka kambi za askari walinzi huko Edomu, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kila alipoenda.
1CH 18:14 Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote.
1CH 18:15 Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu;
1CH 18:16 Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Shausha alikuwa mwandishi;
1CH 18:17 naye Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa maafisa wakuu katika utumishi wa mfalme.
1CH 19:1 Baada ya muda, Nahashi mfalme wa Waamoni akafa, na mwanawe akawa mfalme baada yake.
1CH 19:2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kwa sababu baba yake alinitendea wema.” Hivyo Daudi akatuma wajumbe ili kumfariji Hanuni kwa ajili ya kifo cha baba yake. Watu wa Daudi walipofika kwa Hanuni katika nchi ya Waamoni ili kumfariji,
1CH 19:3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, “Hivi unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kuwatuma wajumbe kukufariji? Je, hawa watu hawakuja kuipeleleza na kuidadisi nchi ili waishinde?”
1CH 19:4 Kwa hiyo Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa ndevu, akakata nguo zao katikati kwenye matako, akawaachia waende zao.
1CH 19:5 Mtu mmoja alipofika na kumpasha Daudi habari za watu hawa, akawatuma wajumbe wengine kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko hadi ndevu zenu ziote, ndipo mje.”
1CH 19:6 Waamoni walipotambua kwamba wamekuwa machukizo kwa Daudi, basi Hanuni na Waamoni wakatuma talanta elfu moja za fedha ili kukodisha magari ya vita, pamoja na waendeshaji wa hayo magari ya kukokotwa na farasi, kutoka Mesopotamia, Aram-Maaka na Soba.
1CH 19:7 Wakakodisha magari ya vita elfu thelathini na mbili na waendeshaji wake, pamoja na mfalme wa Maaka na vikosi vyake. Wakapiga kambi karibu na Medeba. Waamoni nao wakakusanyika toka miji yao, wakatoka ili kupigana vita.
1CH 19:8 Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji.
1CH 19:9 Waamoni wakatoka, wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati wale wafalme wengine waliokuja nao walijipanga kwa vita uwanjani.
1CH 19:10 Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli, akavipanga dhidi ya Waaramu.
1CH 19:11 Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni.
1CH 19:12 Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itakupasa wewe uniokoe; lakini kama Waamoni watakuzidi nguvu, basi mimi nitakuokoa.
1CH 19:13 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Mwenyezi Mungu atafanya lile lililo jema machoni pake.”
1CH 19:14 Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake.
1CH 19:15 Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi Yerusalemu.
1CH 19:16 Baada ya Waaramu kuona kwamba wameshindwa na Israeli, wakapeleka wajumbe na kuwataka Waaramu wengine kutoka ng’ambo ya Mto, wakiongozwa na Shofaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri.
1CH 19:17 Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote na kuvuka Yordani. Akasonga mbele dhidi yao na akajipanga kuwakabili. Daudi akapanga vita ili kupigana na Waaramu, nao wakapigana dhidi yake.
1CH 19:18 Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu arobaini. Pia akamuua Shofaki, jemadari wa jeshi lao.
1CH 19:19 Raia wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya mapatano ya amani na Daudi, wakawa watumishi wake. Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena.
1CH 20:1 Mwanzoni mwa mwaka mpya, wakati wafalme huenda vitani, Yoabu aliliongoza jeshi. Aliangamiza nchi ya Waamoni, na akaenda Raba na kuuzingira, lakini Daudi alibaki Yerusalemu. Yoabu akashambulia Raba na kuuacha ukiwa magofu.
1CH 20:2 Daudi akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nalo lilizungushiwa vito vya thamani. Likawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mji huo.
1CH 20:3 Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka. Daudi akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.
1CH 20:4 Baada ya muda, kulitokea vita dhidi ya Wafilisti, huko Gezeri. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Sipai, aliyekuwa mmoja wa wazao wa Warefai, nao Wafilisti wakashindwa.
1CH 20:5 Katika vita vingine na Wafilisti, Elhanani mwana wa Yairi alimuua Lahmi nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.
1CH 20:6 Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwa na mtu mmoja mkubwa, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu: jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai.
1CH 20:7 Alipowadhihaki Israeli, Yonathani, mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua.
1CH 20:8 Hao walikuwa wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.
1CH 21:1 Shetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu Waisraeli.
1CH 21:2 Kwa hiyo, Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba hadi Dani. Kisha mniletee taarifa niweze kufahamu wako wangapi.”
1CH 21:3 Yoabu akajibu, “Mwenyezi Mungu na aongeze jeshi lake mara mia na zaidi. Mfalme bwana wangu, kwani hawa wote si raia wa bwana wangu? Kwa nini bwana wangu unataka kufanya hivi? Kwa nini kuleta hatia juu ya Israeli?”
1CH 21:4 Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu; kwa hiyo Yoabu akaondoka na kuzunguka Israeli yote, kisha akarudi Yerusalemu.
1CH 21:5 Yoabu akamtolea Daudi idadi ya wapiganaji: Katika Israeli yote kulikuwa na watu milioni moja na elfu mia moja ambao wangeweza kutumia upanga, wakiwemo watu elfu mia nne sabini wa Yuda.
1CH 21:6 Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme.
1CH 21:7 Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli.
1CH 21:8 Kisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
1CH 21:9 Mwenyezi Mungu akamwambia Gadi, mwonaji wa Daudi,
1CH 21:10 “Nenda ukamwambie Daudi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”
1CH 21:11 Kwa hiyo Gadi akamwendea Daudi akamwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Chagua:
1CH 21:12 miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu ya kushindwa na adui zako, ukipatwa na panga zao; au siku tatu za upanga wa Mwenyezi Mungu: siku tatu za tauni katika nchi na malaika wa Mwenyezi Mungu akiangamiza kila mahali katika Israeli.’ Sasa basi, amua jinsi nitakavyomjibu yeye aliyenituma.”
1CH 21:13 Daudi akamwambia Gadi, “Ninayo mahangaiko makubwa. Mimi na nianguke mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa maana rehema zake ni kuu mno, lakini usiniache niangukie mikononi mwa wanadamu.”
1CH 21:14 Basi Mwenyezi Mungu akatuma tauni katika Israeli, na wanaume elfu sabini wa Israeli wakafa.
1CH 21:15 Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, Mwenyezi Mungu akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Mwenyezi Mungu alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi.
1CH 21:16 Daudi akayainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa gunia, wakaanguka kifudifudi.
1CH 21:17 Daudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.”
1CH 21:18 Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akamwamuru Gadi amwambie Daudi apande na kumjengea Mwenyezi Mungu madhabahu kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi.
1CH 21:19 Kwa hiyo Daudi akakwea, akalitii lile neno ambalo Gadi alikuwa amelisema katika jina la Mwenyezi Mungu.
1CH 21:20 Arauna alipokuwa akipura ngano, akageuka, akamwona yule malaika. Wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha.
1CH 21:21 Kisha Daudi akakaribia, Arauna alipotazama na kumwona, akaondoka kwenye uwanja wa kupuria nafaka akamsujudia Daudi, uso wake ukagusa chini.
1CH 21:22 Daudi akamwambia Arauna, “Nipatie huu uwanja wako wa kupuria nafaka, niweze kujenga madhabahu ya Mwenyezi Mungu, ili tauni ipate kukomeshwa katika watu. Niuzie kwa bei yake kamili.”
1CH 21:23 Arauna akamwambia Daudi, “Uchukue huo uwanja. Mfalme bwana wangu na afanye lolote analopenda. Tazama, nitatoa maksai kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, vifaa vya kupuria kuwa kuni, pamoja na ngano kwa ajili ya dhabihu ya nafaka. Natoa hivi vyote.”
1CH 21:24 Lakini Mfalme Daudi akamjibu Arauna, “La hasha! Lakini ninasisitiza kwamba nitalipa bei yake kamili. Sitachukua kilicho chako kwa ajili ya Mwenyezi Mungu au kutoa sadaka ya kuteketezwa isiyonigharimu chochote.”
1CH 21:25 Basi Daudi akamlipa Arauna shekeli mia sita za dhahabu kwa ajili ya ule uwanja.
1CH 21:26 Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwita Mwenyezi Mungu naye Mwenyezi Mungu akajibu maombi yake kwa moto kutoka mbinguni juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
1CH 21:27 Kisha Mwenyezi Mungu akanena na yule malaika, naye akarudisha upanga wake katika ala yake.
1CH 21:28 Wakati huo, Daudi alipoona kwamba Mwenyezi Mungu amemjibu kule kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna Myebusi, akatoa dhabihu huko.
1CH 21:29 Maskani ya Mwenyezi Mungu ambayo Musa aliitengeneza kule jangwani, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kwa wakati huo vilikuwa viko mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni.
1CH 21:30 Lakini Daudi hakuthubutu kuisogelea ili kumuuliza Mungu, kwa sababu aliuogopa upanga wa yule malaika wa Mwenyezi Mungu.
1CH 22:1 Ndipo Daudi akasema, “Nyumba ya Bwana Mwenyezi Mungu itakuwa mahali hapa, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli.”
1CH 22:2 Kwa hiyo Daudi akatoa amri wakusanyike wageni wote walioishi Israeli, na kutoka miongoni mwao, akaweka waashi ili kuchonga mawe kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu.
1CH 22:3 Daudi akatoa chuma tele ili kutengenezea misumari kwa ajili ya mafungo ya malango ya nyumba na shaba tele isiyopimika.
1CH 22:4 Pia akatoa magogo ya mwerezi yasiyohesabika, kwa kuwa Wasidoni na Watiro walikuwa wamemletea Daudi idadi kubwa ya mierezi.
1CH 22:5 Daudi akasema, “Mwanangu Sulemani bado ni mdogo wa umri na hana uzoefu. Nyumba itakayojengwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu inatakiwa iwe yenye uzuri mwingi na sifa na fahari mbele ya mataifa yote. Kwa hiyo nitaifanyia matayarisho.” Daudi akafanya matayarisho makubwa kabla ya kifo chake.
1CH 22:6 Kisha akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza kujenga nyumba kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
1CH 22:7 Daudi akamwambia Sulemani: “Mwanangu, nilikuwa na jambo hili ndani ya moyo wangu, kujenga nyumba kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
1CH 22:8 Lakini neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema: ‘Wewe umemwaga damu nyingi na kupigana vita vingi. Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu.
1CH 22:9 Lakini utakuwa na mwana ambaye atakuwa mtu wa amani na utulivu, nami nitampa utulivu mbele ya adui zake wote pande zote. Jina lake ataitwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu wakati wa utawala wake.
1CH 22:10 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu. Yeye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nami nitakiimarisha kiti chake cha utawala juu ya Israeli milele.’
1CH 22:11 “Sasa, mwanangu, Mwenyezi Mungu awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kama alivyosema utafanya.
1CH 22:12 Mwenyezi Mungu na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika Torati ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
1CH 22:13 Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Mwenyezi Mungu alizompa Musa kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.
1CH 22:14 “Nimejitaabisha sana ili kupata mahitaji kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu: talanta elfu mia moja za dhahabu, talanta milioni moja za fedha, na kiasi kisichopimika cha shaba na chuma, pia mbao na mawe. Nawe unaweza kuviongeza.
1CH 22:15 Unao wafanyakazi wengi: Wachonga mawe, waashi na maseremala, pamoja na watu walio na ustadi katika kila kazi
1CH 22:16 wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma, mafundi wasiohesabika. Sasa basi anza kazi hii, naye Mwenyezi Mungu awe pamoja nawe.”
1CH 22:17 Kisha Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli wamsaidie Sulemani mwanawe.
1CH 22:18 Akawaambia, “Je, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, si yuko pamoja na ninyi? Pia si amewapa amani pande zote? Kwa maana amewatia wenyeji wa nchi mkononi mwangu, nayo nchi iko chini ya Mwenyezi Mungu na watu wake.
1CH 22:19 Sasa itoeni mioyo yenu na nafsi zenu katika kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Anzeni kujenga Maskani ya Bwana Mwenyezi Mungu, ili mweze kulileta Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na vyombo vitakatifu vya Mungu katika Hekalu litakalojengwa kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu.”
1CH 23:1 Daudi alipokuwa mzee aliyeshiba siku, akamfanya Sulemani mwanawe kuwa mfalme juu ya Israeli.
1CH 23:2 Pia akawakusanya viongozi wote wa Israeli, pamoja na makuhani na Walawi.
1CH 23:3 Walawi waliokuwa na umri wa miaka thelathini au zaidi walihesabiwa, nayo hesabu ya wanaume ilikuwa elfu thelathini na nane.
1CH 23:4 Daudi akasema, “Miongoni mwa hawa, elfu ishirini na nne watasimamia kazi ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na elfu sita watakuwa maafisa na waamuzi,
1CH 23:5 na elfu nne watakuwa mabawabu, na wengine elfu nne watamsifu Mwenyezi Mungu kwa ala za uimbaji nilizotoa kwa ajili ya kusudi hilo.”
1CH 23:6 Daudi akawagawa Walawi katika makundi kufuatana na wana wa Lawi: Gershoni, Kohathi na Merari.
1CH 23:7 Wana wa Wagershoni walikuwa wawili: Ladani na Shimei.
1CH 23:8 Wana wa Ladani walikuwa watatu: Yehieli wa kwanza, Zethamu na Yoeli.
1CH 23:9 Wana wa Shimei walikuwa watatu: Shelomothi, Hazieli na Harani. Hawa watatu walikuwa viongozi wa jamaa za Ladani.
1CH 23:10 Nao wana wa Shimei walikuwa: Yahathi, Zina, Yeushi na Beria. Hawa walikuwa wana wa Shimei: wanne kwa jumla.
1CH 23:11 Yahathi alikuwa wa kwanza na Ziza wa pili, lakini Yeushi na Beria hawakuwa na wana wengi; kwa hiyo walihesabiwa kama jamaa moja, wakapewa wajibu kwa pamoja.
1CH 23:12 Wana wa Kohathi walikuwa: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli: wanne kwa jumla.
1CH 23:13 Wana wa Amramu walikuwa: Haruni na Musa. Haruni waliwekwa wakfu, yeye na wazao wake milele, wawe wakiweka wakfu vitu ambavyo ni vitakatifu mno, kutoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu, kuhudumu mbele zake na kubariki katika Jina la Mwenyezi Mungu milele.
1CH 23:14 Wana wa Musa mtu wa Mungu walihesabiwa kama sehemu ya kabila la Lawi.
1CH 23:15 Wana wa Musa walikuwa: Gershomu na Eliezeri.
1CH 23:16 Wazao wa Gershomu: Shebueli alikuwa wa kwanza.
1CH 23:17 Wazao wa Eliezeri: Rehabia alikuwa wa kwanza. Eliezeri alikuwa na mwana mmoja tu, lakini wana wa Rehabia walikuwa wengi sana.
1CH 23:18 Wana wa Ishari: Shelomithi alikuwa wa kwanza.
1CH 23:19 Wana wa Hebroni walikuwa: Yeria alikuwa wa kwanza, wa pili Amaria, wa tatu Yahazieli, na wa nne Yekameamu.
1CH 23:20 Wana wa Uzieli walikuwa: Mika wa kwanza na Ishia wa pili.
1CH 23:21 Wana wa Merari walikuwa: Mahli na Mushi. Wana wa Mahli walikuwa: Eleazari na Kishi.
1CH 23:22 Eleazari akafa bila ya kuwa na wana: alikuwa na binti tu. Binamu zao, wana wa Kishi, wakawaoa.
1CH 23:23 Wana wa Mushi: Mahli, Ederi na Yeremothi; wote walikuwa watatu.
1CH 23:24 Hawa walikuwa wazao wa Lawi kwa jamaa zao. Wakuu wa jamaa kama walivyoandikwa kwa majina yao na kuhesabiwa kila mmoja, yaani wenye uwezo wa kufanya kazi kuanzia miaka ishirini au zaidi, waliohudumu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1CH 23:25 Kwa maana Daudi alikuwa amesema, “Kwa vile Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, amewapa watu wake amani, na amekuja kuishi Yerusalemu milele,
1CH 23:26 Walawi hawahitaji tena kubeba Maskani wala chombo chochote cha utumishi wake.”
1CH 23:27 Kulingana na maagizo ya mwisho ya Daudi, Walawi walihesabiwa kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi.
1CH 23:28 Wajibu wa Walawi ulikuwa kuwasaidia wazao wa Haruni kuhudumu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu: Kuwa wasimamizi wa nyua, vyumba vya pembeni, kutakasa vyombo vitakatifu na utendaji mwingine wowote katika nyumba ya Mungu.
1CH 23:29 Walikuwa wasimamizi wa mikate iliyowekwa mezani, unga kwa ajili ya sadaka za nafaka, mikate myembamba isiyotiwa chachu, uokaji na uchanganyaji, pamoja na vipimo vyote vya wingi na ukubwa.
1CH 23:30 Pia ulikuwa wajibu wao kila asubuhi kumshukuru na kumsifu Mwenyezi Mungu. Iliwapasa pia kufanya hivyo jioni
1CH 23:31 na wakati wowote sadaka za kuteketezwa zilipotolewa kwa Mwenyezi Mungu siku za Sabato na kwenye sikukuu za Mwezi Mwandamo na katika sikukuu nyingine zilizoamriwa. Iliwapasa kuhudumu mbele za Mwenyezi Mungu mara kwa mara kwa idadi maalum na kwa namna waliyokuwa wamepewa maelekezo.
1CH 23:32 Hivyo Walawi wakafanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, katika Mahali Patakatifu chini ya uongozi wa ndugu zao wazao wa Haruni, kwa ajili ya utumishi katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1CH 24:1 Hii ndiyo migawanyo ya wazao wa Haruni: Haruni alikuwa na wana wanne: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari.
1CH 24:2 Nadabu na Abihu walikufa kabla ya baba yao, nao hawakuwa na wana; kwa hiyo ndugu zao Eleazari na Ithamari wakahudumu kama makuhani.
1CH 24:3 Akisaidiwa na Sadoki mwana wa Eleazari na Ahimeleki mwana wa Ithamari, Daudi aliwapanga wazao wa Haruni katika migawanyo kufuatana na wajibu wa huduma zao.
1CH 24:4 Idadi kubwa ya viongozi walipatikana miongoni mwa wazao wa Eleazari, kuliko miongoni mwa wazao wa Ithamari, nao waligawanywa kwa uwiano: Viongozi kumi na sita kutoka jamaa ya wazao wa Eleazari na viongozi wanane kutoka jamaa ya wazao wa Ithamari.
1CH 24:5 Waliwagawanya bila upendeleo kwa kupiga kura, kwa kuwa kulikuwa na maafisa wa mahali patakatifu na maafisa wa Mungu miongoni mwa wazao wale wa Eleazari na wale wa Ithamari.
1CH 24:6 Mwandishi Shemaya mwana wa Nethaneli, Mlawi, aliorodhesha majina yao mbele ya Mfalme Daudi na maafisa: Kuhani Sadoki, Ahimeleki mwana wa Abiathari, na viongozi wa jamaa za makuhani na za Walawi: jamaa moja ikitoka upande wa Eleazari na nyingine upande wa Ithamari.
1CH 24:7 Kura ya kwanza ilimwangukia Yehoyaribu, ya pili Yedaya,
1CH 24:8 ya tatu Harimu, ya nne Seorimu,
1CH 24:9 ya tano Malkiya, ya sita Miyamini,
1CH 24:10 ya saba Hakosi, ya nane Abiya,
1CH 24:11 ya tisa Yeshua, ya kumi Shekania,
1CH 24:12 ya kumi na moja Eliashibu, ya kumi na mbili Yakimu,
1CH 24:13 ya kumi na tatu Hupa, ya kumi na nne Yeshebeabu,
1CH 24:14 ya kumi na tano Bilga, ya kumi na sita Imeri,
1CH 24:15 ya kumi na saba Heziri, ya kumi na nane Hapisesi,
1CH 24:16 ya kumi na tisa Pethahia, ya ishirini Yehezkeli,
1CH 24:17 ya ishirini na moja Yakini, ya ishirini na mbili Gamuli,
1CH 24:18 ya ishirini na tatu Delaya, ya ishirini na nne Maazia.
1CH 24:19 Huu ulikuwa ndio utaratibu wao uliokubalika wa kuhudumu walipoingia katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, kulingana na masharti waliyoelekezwa na Haruni baba yao, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alivyokuwa amemwamuru.
1CH 24:20 Kuhusu wazao wa Lawi waliobaki: Kutoka kwa wana wa Amramu: alikuwa Shubaeli; kutoka kwa wana wa Shubaeli: alikuwa Yedeya.
1CH 24:21 Kuhusu Rehabia, kutoka kwa wanawe: Ishia alikuwa wa kwanza.
1CH 24:22 Kutoka kwa Waishari: alikuwa Shelomothi, kutoka kwa wana wa Shelomothi: alikuwa Yahathi.
1CH 24:23 Wana wa Hebroni: Yeria alikuwa mkuu, Amaria wa pili, Yahazieli wa tatu, na Yekameamu wa nne.
1CH 24:24 Mwana wa Uzieli: alikuwa Mika; kutoka kwa wana wa Mika: alikuwa Shamiri.
1CH 24:25 Ndugu yake Mika: alikuwa Ishia; na kutoka kwa wana wa Ishia: alikuwa Zekaria.
1CH 24:26 Wana wa Merari: walikuwa Mahli na Mushi. Mwana wa Yaazia: alikuwa Beno.
1CH 24:27 Wana wa Merari: kutoka kwa Yaazia: ni Beno, Shohamu, Zakuri na Ibri.
1CH 24:28 Kutoka kwa Mahli: alikuwa Eleazari, ambaye hakuwa na wana.
1CH 24:29 Kutoka kwa Kishi: mwana wa Kishi alikuwa Yerameeli.
1CH 24:30 Nao wana wa Mushi: walikuwa Mahli, Ederi na Yeremothi.
1CH 24:31 Pia walipiga kura kama vile ndugu zao wazao wa Haruni walivyofanya, mbele ya Mfalme Daudi, Sadoki, Ahimeleki na mbele ya viongozi wa jamaa ya makuhani na ya Walawi. Jamaa za ndugu wakubwa zilitendewa sawasawa na zile za ndugu wadogo.
1CH 25:1 Daudi, pamoja na majemadari wa jeshi, wakawatenga baadhi ya wana wa Asafu, wana wa Hemani, na wana wa Yeduthuni kwa ajili ya huduma ya kutoa unabii, wakitumia vinubi, zeze na matoazi. Hii ndiyo orodha ya watu waliofanya huduma hiyo:
1CH 25:2 Kutoka kwa wana wa Asafu walikuwa: Zakuri, Yusufu, Nethania na Asarela. Wana wa Asafu walikuwa chini ya usimamizi wa Asafu, ambaye alitoa unabii chini ya usimamizi wa mfalme.
1CH 25:3 Wana wa Yeduthuni walikuwa sita: Gedalia, Seri, Yeshaya, Shimei, Hashabia, na Matithia, nao walikuwa chini ya usimamizi wa baba yao Yeduthuni, wao walikuwa wakitoa unabii wakitumia vinubi, wakimshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu.
1CH 25:4 Wana wa Hemani walikuwa: Bukia, Matania, Uzieli, Shebueli na Yeremothi, Hanania, Hanani, Eliatha, Gidalti na Romamti-Ezeri, Yoshbekasha, Malothi, Hothiri na Mahaziothi.
1CH 25:5 Wote hawa walikuwa wana wa Hemani mwonaji wa mfalme. Aliwapata wana hawa kutokana na ahadi ya Mungu ili kumwinua. Mungu alimpa Hemani watoto kumi na wanne wa kiume na binti watatu.
1CH 25:6 Hawa wanaume wote walikuwa chini ya usimamizi wa baba yao kwa ajili ya uimbaji katika Hekalu la Mwenyezi Mungu wakitumia matoazi, zeze na vinubi, kwa ajili ya huduma katika nyumba ya Mungu. Asafu, Yeduthuni na Hemani walikuwa chini ya usimamizi wa mfalme.
1CH 25:7 Pamoja na ndugu zao, wote walikuwa wamefundishwa na kuwa stadi wa uimbaji kwa Mwenyezi Mungu. Idadi yao walikuwa mia mbili na themanini na nane (288).
1CH 25:8 Vijana kwa wazee, walimu kwa wanafunzi, wote walipanga kazi zao kwa kupiga kura.
1CH 25:9 Kura ya kwanza, ambayo ilikuwa kwa ajili ya Asafu, ilimwangukia Yusufu, wanawe na jamaa zake, 12; Ya pili ikamwangukia Gedalia, yeye na wanawe pamoja na jamaa zake, 12;
1CH 25:10 Ya tatu ikamwangukia Zakuri, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:11 ya nne ikamwangukia Isri, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:12 ya tano ikamwangukia Nethania, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:13 ya sita ikamwangukia Bukia, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:14 ya saba ikamwangukia Yesarela, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:15 ya nane ikamwangukia Yeshaya, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:16 ya tisa ikamwangukia Matania, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:17 ya kumi ikamwangukia Shimei, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:18 ya kumi na moja ikamwangukia Azareli, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:19 ya kumi na mbili ikamwangukia Hashabia, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:20 ya kumi na tatu ikamwangukia Shubaeli, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:21 ya kumi na nne ikamwangukia Matithia, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:22 ya kumi na tano ikamwangukia Yeremothi, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:23 Ya kumi na sita ikamwangukia Hanania, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:24 ya kumi na saba ikamwangukia Yoshbekasha, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:25 ya kumi na nane ikamwangukia Hanani, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:26 ya kumi na tisa ikamwangukia Malothi, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:27 ya ishirini ikamwangukia Eliatha, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:28 ya ishirini na moja ikamwangukia Hothiri, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:29 ya ishirini na mbili ikamwangukia Gidalti, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:30 ya ishirini na tatu ikamwangukia Mahaziothi, wanawe na jamaa zake, 12;
1CH 25:31 ya ishirini na nne ikamwangukia Romamti-Ezeri, wanawe na jamaa zake, 12.
1CH 26:1 Hii ndiyo migawanyo ya mabawabu: Kutoka kwa wana wa Kora alikuwa: Meshelemia mwana wa Kore, mmoja wa wana wa Asafu.
1CH 26:2 Meshelemia alikuwa na wana wafuatao: Zekaria mzaliwa wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne,
1CH 26:3 Elamu wa tano, Yehohanani wa sita, na Eliehoenai wa saba.
1CH 26:4 Obed-Edomu naye alikuwa na wana wafuatao: Shemaya mzaliwa wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, Sakari wa nne, Nethaneli wa tano,
1CH 26:5 Amieli wa sita, Isakari wa saba, na Peulethai wa nane. (Kwa kuwa Mungu alikuwa amembariki Obed-Edomu.)
1CH 26:6 Shemaya mwanawe Obed-Edomu pia alikuwa na wana waliokuwa viongozi katika jamaa ya baba yao, kwa sababu walikuwa watu wenye uwezo mkubwa.
1CH 26:7 Wana wa Shemaya ni: Othni, Refaeli, Obedi na Elizabadi; jamaa zake Elihu na Semakia walikuwa pia watu wenye uwezo.
1CH 26:8 Hawa wote walikuwa wazao wa Obed-Edomu; wao na wana wao na jamaa zao walikuwa watu wenye uwezo na nguvu za kufanya kazi. Wazao wa Obed-Edomu jumla yao walikuwa sitini na wawili.
1CH 26:9 Meshelemia alikuwa na wana na jamaa zake, waliokuwa watu wenye uwezo: jumla yao watu kumi na wanane.
1CH 26:10 Hosa, Mmerari, alikuwa na wana wafuatao: Shimri alikuwa mkuu wao (baba yake alikuwa amemweka yeye kuwa mkuu, ijapokuwa hakuwa mzaliwa wa kwanza),
1CH 26:11 Hilkia wa pili, Tabalia wa tatu na Zekaria wa nne.
1CH 26:12 Hii migawanyo ya mabawabu, kupitia wakuu wao, walikuwa na zamu za kuhudumu hekaluni mwa Mwenyezi Mungu kama jamaa zao walivyokuwa nazo.
1CH 26:13 Kura zilipigwa kwa kila lango, kufuatana na jamaa zao, wakubwa kwa wadogo.
1CH 26:14 Kura ya Lango la Mashariki ilimwangukia Shelemia. Kisha wakapiga kura kwa Zekaria mwanawe Shelemia, aliyekuwa mshauri mwenye hekima, nayo kura ya Lango la Kaskazini ikamwangukia.
1CH 26:15 Kura ya Lango la Kusini ikamwangukia Obed-Edomu, nayo kura ya maghala ikawaangukia wanawe.
1CH 26:16 Kura za Lango la Magharibi na Lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu zikawaangukia Shupimu na Hosa.
1CH 26:17 Kulikuwa na Walawi sita kila siku upande wa mashariki, wanne upande wa kaskazini, wanne upande wa kusini, na wawili wawili kwa mara moja kwenye ghala.
1CH 26:18 Kuhusu ukumbi kuelekea magharibi, kulikuwa na wanne barabarani na wawili kwenye ukumbi wenyewe.
1CH 26:19 Hii ilikuwa migawanyo ya mabawabu waliokuwa wazao wa Kora na wa Merari.
1CH 26:20 Katika Walawi, Ahiya alikuwa mwangalizi wa hazina za nyumba ya Mungu na mwangalizi wa hazina za vitu vilivyowekwa wakfu.
1CH 26:21 Wazao wa Ladani, waliokuwa Wagershoni kupitia Ladani na waliokuwa viongozi wa jamaa za Ladani Mgershoni, walikuwa Yehieli,
1CH 26:22 wana wa Yehieli, wana wa Zethamu na wa nduguye Yoeli. Wao walikuwa waangalizi wa hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1CH 26:23 Kutoka kwa Waamrami, Waishari, Wahebroni na Wauzieli:
1CH 26:24 Shebueli, mzao wa Gershomu mwana wa Musa, alikuwa afisa mwangalizi wa hazina.
1CH 26:25 Jamaa zake kutoka kwa Eliezeri, wanawe walikuwa: Rehabia, Yeshaya, Yoramu, Zikri na Shelomithi.
1CH 26:26 Shelomithi na jamaa zake walikuwa waangalizi wa hazina zote za vitu vile vilivyowekwa wakfu na Mfalme Daudi, kwa viongozi wa jamaa waliokuwa majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, na kwa maafisa wengine wa jeshi.
1CH 26:27 Baadhi ya nyara zilizotekwa vitani waliziweka wakfu kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu la Mwenyezi Mungu.
1CH 26:28 Kila kitu kilichokuwa kimewekwa wakfu na Samweli mwonaji, na Sauli mwana wa Kishi, Abneri mwana wa Neri, na Yoabu mwana wa Seruya, pamoja na vitu vingine vyote vilivyokuwa vimewekwa wakfu, vyote vilikuwa chini ya uangalizi wa Shelomithi na jamaa zake.
1CH 26:29 Kutoka kwa wana wa Ishari: Kenania na wanawe walipewa kazi nje ya Hekalu kama maafisa na waamuzi juu ya Israeli.
1CH 26:30 Kutoka kwa wana wa Hebroni: Hashabia na jamaa zake, watu elfu moja na mia saba wenye uwezo, waliwajibika katika Israeli magharibi mwa Yordani kwa ajili ya kazi zote za Mwenyezi Mungu na utumishi wa mfalme.
1CH 26:31 Kuhusu wana wa Hebroni, Yeria alikuwa mkuu wao kufuatana na orodha ya jamaa yao. Katika mwaka wa arobaini wa utawala wa Daudi, uchunguzi ulifanyika katika kumbukumbu, nao watu wenye uwezo miongoni mwa wana wa Hebroni wakapatikana huko Yazeri katika Gileadi.
1CH 26:32 Yeria alikuwa na jamaa ya watu elfu mbili mia saba waliokuwa watu wenye uwezo na viongozi wa jamaa, naye Mfalme Daudi akawaweka kuangalia Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila Manase kuhusu kila jambo lililomhusu Mungu na shughuli za mfalme.
1CH 27:1 Hii ndiyo orodha ya Waisraeli: viongozi wa jamaa, majemadari wa maelfu, majemadari wa mamia na maafisa wao, waliomtumikia mfalme kwa lolote lililohusu vikosi vya jeshi vilivyokuwa zamu mwezi baada ya mwezi katika mwaka mzima. Kila kikosi kimoja kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:2 Msimamizi wa kikosi cha kwanza kwa mwezi wa kwanza alikuwa Yashobeamu mwana wa Zabdieli. Kulikuwa na watu elfu ishirini na nne katika kikosi chake.
1CH 27:3 Yeye alikuwa mzao wa Peresi, na mkuu wa maafisa wote wa jeshi kwa mwezi wa kwanza.
1CH 27:4 Msimamizi wa kikosi kwa mwezi wa pili alikuwa Dodai Mwahohi. Miklothi ndiye alikuwa kiongozi wa kikosi chake. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:5 Jemadari wa kikosi cha tatu kwa mwezi wa tatu alikuwa Benaya mwana wa kuhani Yehoyada. Ndiye alikuwa mkuu wa kikosi chake kilichokuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:6 Huyu ndiye yule Benaya aliyekuwa shujaa miongoni mwa wale Thelathini, na ndiye alikuwa juu ya wale Thelathini. Mwanawe Amizabadi ndiye alikuwa mkuu katika kikosi chake.
1CH 27:7 Jemadari wa nne kwa mwezi wa nne alikuwa Asaheli nduguye Yoabu, mwanawe Zebadia ndiye aliingia mahali pake kwenye uongozi. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:8 Jemadari wa kikosi cha tano kwa mwezi wa tano alikuwa Shamhuthi Mwizrahi. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:9 Jemadari wa kikosi cha sita kwa mwezi wa sita alikuwa Ira, mwana wa Ikeshi Mtekoa. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:10 Jemadari wa kikosi cha saba kwa mwezi wa saba alikuwa Helesi Mpeloni wa Waefraimu. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:11 Jemadari wa nane kwa mwezi wa nane, alikuwa Sibekai Mhushathi wa Wazera. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:12 Jemadari wa tisa kwa mwezi wa tisa alikuwa Abiezeri Mwanathothi wa Wabenyamini. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:13 Jemadari wa kumi kwa mwezi wa kumi alikuwa Maharai Mnetofathi wa Wazera. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:14 Jemadari wa kumi na moja kwa mwezi wa kumi na moja alikuwa Benaya Mpirathoni wa Waefraimu. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:15 Jemadari wa kumi na mbili kwa mwezi wa kumi na mbili alikuwa Heldai Mnetofathi kutoka jamaa ya Othnieli. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne.
1CH 27:16 Viongozi wa makabila ya Israeli walikuwa: Kwa Wareubeni: Eliezeri mwana wa Zikri; kwa Wasimeoni: Shefatia mwana wa Maaka;
1CH 27:17 kwa Walawi: Hashabia mwana wa Kemueli; kwa Haruni: Sadoki;
1CH 27:18 kwa Yuda: Elihu, nduguye Daudi; kwa Waisakari: Omri mwana wa Mikaeli;
1CH 27:19 kwa Wazabuloni: Ishmaya mwana wa Obadia; kwa Wanaftali: Yeremothi mwana wa Azrieli;
1CH 27:20 kwa Waefraimu: Hoshea mwana wa Azazia; kwa nusu ya kabila la Manase: Yoeli mwana wa Pedaya;
1CH 27:21 kwa nusu nyingine ya kabila la Manase huko Gileadi: Ido mwana wa Zekaria; kwa Wabenyamini: Yaasieli mwana wa Abneri;
1CH 27:22 kwa Wadani: Azareli mwana wa Yerohamu.
1CH 27:23 Daudi hakuwahesabu watu waliokuwa chini ya miaka ishirini, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa ameahidi kuwafanya Israeli kuwa wengi kama nyota za angani.
1CH 27:24 Yoabu mwana wa Seruya alianza kuwahesabu watu lakini hakumaliza. Kwa sababu ya kuwahesabu watu, hasira ya Mungu iliwaka juu ya Israeli, nayo hiyo hesabu yao haikuingizwa katika kitabu cha kumbukumbu za Mfalme Daudi.
1CH 27:25 Azmawethi mwana wa Adieli ndiye alikuwa msimamizi wa hazina za mfalme. Msimamizi wa hazina katika mashamba, miji, vijiji na kwenye ngome alikuwa Yonathani mwana wa Uzia.
1CH 27:26 Ezri mwana wa Kelubu alikuwa msimamizi wa wafanyakazi waliolima katika mashamba.
1CH 27:27 Shimei Mramathi alikuwa msimamizi wa mashamba ya mizabibu. Zabdi Mshifmi alikuwa msimamizi wa zabibu, utengenezaji na uhifadhi wa divai katika mapipa makubwa.
1CH 27:28 Baal-Hanani Mgederi ndiye alikuwa mwangalizi wa mashamba ya mfalme ya mizeituni na mikuyu katika tambarare za vilima vya magharibi. Yoashi alikuwa msimamizi wa maghala ya mafuta ya zeituni.
1CH 27:29 Shitrai Msharoni alikuwa msimamizi wa mifugo waliolishwa huko Sharoni. Shafati mwana wa Adlai alikuwa msimamizi wa mifugo iliyokuwa makondeni.
1CH 27:30 Obili Mwishmaeli alikuwa msimamizi wa ngamia. Yedeya Mmeronothi alikuwa msimamizi wa punda.
1CH 27:31 Yazizi Mhagri alikuwa msimamizi wa makundi ya kondoo na mbuzi.
1CH 27:32 Yonathani mjomba wa Daudi alikuwa mshauri, mtu mwenye ufahamu mkubwa na mwandishi. Yehieli mwana wa Hakmoni alikuwa akiwahudumia wana wa mfalme.
1CH 27:33 Ahithofeli alikuwa mshauri wa mfalme. Hushai Mwarki alikuwa rafiki wa mfalme.
1CH 27:34 Baada ya Ahithofeli, Yehoyada mwana wa Benaya aliingia mahali pake kama mshauri wa mfalme, pamoja na Abiathari. Yoabu alikuwa jemadari wa majeshi ya mfalme.
1CH 28:1 Daudi akawaita maafisa wote wa Israeli wakusanyike huko Yerusalemu: yaani maafisa walio juu ya makabila, majemadari wa vikosi katika utumishi wa mfalme, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, maafisa wanaosimamia mali yote na mifugo ya mfalme na wanawe, wakiwemo maafisa wa jumba la kifalme, mashujaa na wapiganaji hodari wote.
1CH 28:2 Mfalme Daudi akainuka na kusema: “Nisikilizeni ndugu zangu, nanyi watu wangu. Nilikuwa na nia ya kujenga nyumba ili iwe mahali pa kukaa Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kuwa mahali pa kuwekea miguu ya Mungu wetu, nami nikafanya maandalizi ya kuijenga.
1CH 28:3 Lakini Mungu akaniambia, ‘Wewe hutajenga nyumba kwa Jina langu, kwa sababu wewe umekuwa mtu wa vita na umemwaga damu.’
1CH 28:4 “Hata hivyo, Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alinichagua mimi kutoka jamaa zangu wote niwe mfalme juu ya Israeli milele. Alimchagua Yuda kuwa kiongozi, na kutoka nyumba ya Yuda akaichagua jamaa yangu, na kutoka wana wa baba yangu ikampendeza kunifanya niwe mfalme juu ya Israeli yote.
1CH 28:5 Miongoni mwa wanangu wote, naye Mwenyezi Mungu amenipa wengi, amemchagua Sulemani mwanangu ili kukikalia kiti cha utawala cha ufalme wa Mwenyezi Mungu juu ya Israeli.
1CH 28:6 Aliniambia, ‘Sulemani mwanao ndiye atakayejenga nyumba yangu na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye kuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake.
1CH 28:7 Nitauimarisha ufalme wake milele kama akiendelea kuzishika amri zangu na sheria zangu, kama afanyavyo hivi leo.’
1CH 28:8 “Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la Mwenyezi Mungu, naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri, na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele.
1CH 28:9 “Nawe Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana Mwenyezi Mungu huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali ukimwacha, yeye atakukataa milele.
1CH 28:10 Angalia basi, kwa maana Mwenyezi Mungu amekuchagua wewe ili ujenge Hekalu kuwa mahali patakatifu. Uwe hodari ukafanye kazi hiyo.”
1CH 28:11 Ndipo Daudi akampa Sulemani mwanawe kielelezo kwa ajili ya ukumbi wa Hekalu, nyumba zake, vyumba vyake vya hazina, ghorofa zake, vyumba vyake vya ndani na mahali pa kufanyia upatanisho.
1CH 28:12 Akampa vielelezo vya yote ambayo Roho wa Mungu alikuwa ameviweka moyoni mwake kwa ajili ya kumbi za Hekalu la Mwenyezi Mungu na vyumba vyote vilivyolizunguka, kwa ajili ya hazina za Hekalu la Mungu na kwa hazina za vitu vilivyowekwa wakfu.
1CH 28:13 Mfalme pia akampa Sulemani maelekezo kwa ajili ya migawanyo ya huduma za makuhani na Walawi, pia kwa ajili ya kazi zote za huduma katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akampa pia maelezo kuhusu vifaa vyote vya kutumika katika huduma ya Hekalu.
1CH 28:14 Akamwagizia uzito wa dhahabu kwa ajili ya vitu vyote vya dhahabu vya kutumika katika huduma mbalimbali, uzito wa fedha kwa ajili ya vitu vyote vya fedha vya kutumika katika huduma mbalimbali.
1CH 28:15 Uzito wa dhahabu kwa ajili ya vinara vya dhahabu na taa zake, kukiwa na uzito kwa ajili ya kila kinara na taa zake, pamoja na uzito wa fedha kwa ajili ya kila kinara cha fedha na taa zake, kulingana na matumizi ya kila kinara;
1CH 28:16 uzito wa dhahabu kwa ajili ya meza ya mikate iliyowekwa wakfu, uzito wa fedha kwa ajili ya meza ya fedha;
1CH 28:17 uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya nyuma, mabakuli ya kunyunyizia na vikombe, masinia; uzito wa dhahabu kwa ajili ya kila bakuli la dhahabu; uzito wa fedha kwa ajili ya kila bakuli la fedha;
1CH 28:18 na uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya madhabahu ya kufukizia uvumba. Pia alimpa kielelezo kwa ajili ya gari la vita, yaani wale makerubi wa dhahabu waliokunjua mabawa yao na kutia kivuli juu ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu.
1CH 28:19 Daudi akasema, “Hii yote, ninayo kwa maandishi kutoka mkononi mwa Mwenyezi Mungu ulio juu yangu, naye amenipa ufahamu kwa ajili ya habari zote za kielelezo hiki.”
1CH 28:20 Daudi pia akamwambia Sulemani mwanawe, “Uwe hodari na moyo mkuu, ukafanye kazi hii. Usiogope wala usifadhaike, kwa maana Bwana Mwenyezi Mungu, aliye Mungu wangu, yu pamoja nawe. Hatakuacha wala hatakupungukia, hadi kazi hii yote kwa ajili ya utumishi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu itakapokamilika.
1CH 28:21 Migawanyo ya makuhani na Walawi iko tayari kwa ajili ya kazi yote katika Hekalu la Mungu, naye kila mtu mwenye moyo wa kujitolea, aliye na ustadi katika aina yoyote ya ufundi, atakusaidia katika kazi yote. Maafisa na watu wote watatii kila agizo lako.”
1CH 29:1 Ndipo Mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote: “Mwanangu Sulemani, yeye ambaye Mungu amemchagua, ni kijana mdogo na asiye na uzoefu. Kazi hii ni kubwa, kwa sababu Hekalu hili la fahari si kwa ajili ya mwanadamu bali ni kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu.
1CH 29:2 Kwa uwezo wangu wote nimetenga mali kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu: dhahabu kwa kazi za dhahabu, fedha kwa ajili ya fedha, shaba kwa kazi za shaba, chuma kwa kazi za chuma na miti kwa kazi za miti, vivyo hivyo vito vya shohamu kwa ajili ya kutia kwenye vijalizo, almasi, mawe ya rangi mbalimbali, aina zote za vito vya thamani na marumaru; haya yote kwa wingi mno.
1CH 29:3 Zaidi ya hayo, kwa kujitolea kwangu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, sasa ninatoa hazina zangu mwenyewe za dhahabu na fedha kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, zaidi ya mali niliyotoa kwa ajili ya Hekalu hili takatifu:
1CH 29:4 talanta elfu tatu za dhahabu (dhahabu ya Ofiri), na talanta elfu saba za fedha safi iliyosafishwa, kwa ajili ya kufunika kuta za Hekalu,
1CH 29:5 kwa kazi ya dhahabu na kazi ya fedha na kwa kazi yote itakayofanywa na mafundi. Basi, ni nani anayependa kujitoa kwa Mwenyezi Mungu leo?”
1CH 29:6 Ndipo viongozi wa jamaa, maafisa wa makabila ya Israeli, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, pamoja na maafisa waliokuwa wasimamizi wa kazi za mfalme wakatoa kwa hiari.
1CH 29:7 Wakatoa kwa ajili ya kazi ya Hekalu la Mungu talanta elfu tano na darkoni elfu kumi za dhahabu, talanta elfu kumi za fedha, talanta elfu kumi na nane za shaba, na talanta elfu mia moja za chuma.
1CH 29:8 Kila mmoja aliyekuwa na vito vya thamani akavitoa katika hazina ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, chini ya uangalizi wa Yehieli Mgershoni.
1CH 29:9 Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Mwenyezi Mungu. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.
1CH 29:10 Daudi akamhimidi Mwenyezi Mungu mbele ya kusanyiko lote, akisema: “Uhimidiwe wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli baba yetu, tangu milele hata milele.
1CH 29:11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Mwenyezi Mungu, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee Mwenyezi Mungu, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.
1CH 29:12 Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe unayetawala vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu,
1CH 29:13 Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu Jina lako tukufu.
1CH 29:14 “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vinavyotoka mkononi mwako.
1CH 29:15 Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini.
1CH 29:16 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako.
1CH 29:17 Ninajua, Mungu wangu, kwamba wewe huujaribu moyo na unapendezwa na unyofu. Vitu hivi vyote nimetoa kwa hiari na kwa moyo mnyofu. Nami sasa nimeona kwa furaha jinsi watu wako walio hapa kwa hiari yao walivyokutolea wewe.
1CH 29:18 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu Ibrahimu, Isaka na Israeli, weka shauku hii ndani ya mioyo ya watu wako daima na uifanye mioyo yao iwe na uaminifu kwako.
1CH 29:19 Nawe umpe mwanangu Sulemani kujitolea kwako kwa moyo wote ili kuzishika amri zako, masharti yako, maagizo yako na kufanya kila kitu ili kujenga Hekalu hili la fahari ambalo kwa ajili yake nimetoa.”
1CH 29:20 Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, “Mhimidini Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao. Wakasujudu, na nyuso zao zikagusa chini mbele za Mwenyezi Mungu na mfalme.
1CH 29:21 Siku ya pili yake, wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali elfu moja, kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo dume elfu moja, pamoja na sadaka za vinywaji, na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli yote.
1CH 29:22 Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za Mwenyezi Mungu siku ile. Wakamtawaza Sulemani mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakampaka mafuta mbele za Mwenyezi Mungu ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani.
1CH 29:23 Sulemani akaketi kwenye kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana, na Waisraeli wote wakamtii.
1CH 29:24 Maafisa wote na mashujaa, pamoja na wana wote wa Daudi, wakaahidi kumtii Mfalme Sulemani.
1CH 29:25 Mwenyezi Mungu akamtukuza sana Sulemani mbele ya Waisraeli wote na kumvika fahari ya kifalme ambayo hakuna mfalme yeyote wa Israeli kabla yake aliwahi kuwa nayo.
1CH 29:26 Daudi mwana wa Yese alikuwa mfalme wa Israeli yote.
1CH 29:27 Alitawala Israeli kwa miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na tatu.
1CH 29:28 Daudi akafa akiwa mzee mwenye umri mwema, akiwa ameshiba siku, utajiri na heshima. Naye Sulemani mwanawe akawa mfalme baada yake.
1CH 29:29 Kuhusu matukio ya utawala wa Mfalme Daudi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kumbukumbu za mwonaji Samweli, na kumbukumbu za nabii Nathani na kumbukumbu za mwonaji Gadi,
1CH 29:30 pamoja na habari zote za utawala wake, nguvu zake na matukio yaliyompata yeye, na Israeli, na falme za nchi nyingine zote.
2CH 1:1 Sulemani mwana wa Daudi alijiimarisha katika ufalme wake, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, naye akamfanya mkuu sana.
2CH 1:2 Ndipo Sulemani akasema na Waisraeli wote, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, waamuzi na viongozi wote katika Israeli, pamoja na wakuu wa jamaa.
2CH 1:3 Naye Sulemani na kusanyiko lote wakakwea hadi mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. Hema la Kukutania la Mungu, ambalo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alikuwa amelitengeneza huko jangwani, lilikuwa Gibeoni.
2CH 1:4 Basi Daudi alikuwa amelipandisha Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu hadi mahali alipokuwa amepatengeneza kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa amesimamisha hema kwa ajili ya hilo Sanduku huko Yerusalemu.
2CH 1:5 Lakini yale madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, alikuwa ametengeneza yalikuwa huko Gibeoni mbele ya Maskani ya Mwenyezi Mungu, hivyo Sulemani na kusanyiko lote walimtafuta Mungu huko.
2CH 1:6 Sulemani akapanda huko yalikokuwa madhabahu ya shaba mbele za Mwenyezi Mungu katika Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu elfu moja za sadaka za kuteketezwa juu yake.
2CH 1:7 Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani na kumwambia, “Omba lolote utakalo nikupe.”
2CH 1:8 Sulemani akamjibu Mungu, “Umemwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake.
2CH 1:9 Sasa, Bwana Mwenyezi Mungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi.
2CH 1:10 Nakuomba unipe hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?”
2CH 1:11 Mungu akamwambia Sulemani, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao,
2CH 1:12 kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.”
2CH 1:13 Ndipo Sulemani akaenda Yerusalemu kutoka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kutoka mbele ya Hema la Kukutania. Naye akatawala Israeli.
2CH 1:14 Sulemani akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari elfu moja mia nne, na farasi elfu kumi na mbili, ambayo aliyaweka katika miji ya magari, na mengine akawa nayo huko Yerusalemu.
2CH 1:15 Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa vitu vya kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima.
2CH 1:16 Farasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue.
2CH 1:17 Waliagiza magari ya vita kutoka Misri kwa bei ya shekeli mia sita za fedha, na farasi kwa shekeli mia moja na hamsini. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu.
2CH 2:1 Sulemani akatoa amri kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe.
2CH 2:2 Sulemani akaandika watu elfu sabini kuwa wachukuzi wa mizigo, na watu elfu themanini kuwa wachonga mawe vilimani, na watu elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.
2CH 2:3 Sulemani akapeleka ujumbe huu kwa Mfalme Hiramu wa Tiro: “Unitumie magogo ya mwerezi kama ulivyomfanyia baba yangu Daudi wakati ulipompelekea mierezi ya kujenga jumba lake la kifalme la kuishi.
2CH 2:4 Sasa ninakaribia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, na kuliweka wakfu kwake kwa ajili ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri mbele zake, mahali pa kuweka mikate ya Wonesho kwa kufuata utaratibu na kwa ajili ya mahali pa kutolea sadaka za kuteketezwa kila siku asubuhi na jioni, siku za Sabato na Mwezi Mwandamo pia katika sikukuu zilizoamriwa za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Hili ni agizo la kudumu kwa ajili ya Waisraeli.
2CH 2:5 “Hekalu nitakalolijenga litakuwa kubwa, kwa sababu Mungu wetu ni mkuu kuliko miungu mingine yote.
2CH 2:6 Lakini ni nani awezaye kumjengea Hekalu, maadamu mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kumtosha? Mimi ni nani basi hata nimjengee Hekalu, isipokuwa liwe tu mahali pa kutolea dhabihu za kuteketezwa mbele zake?
2CH 2:7 “Hivyo basi nitumie mtu mwenye ustadi wa kufanya kazi ya kutengeneza dhahabu na fedha, shaba na chuma, nyuzi za rangi ya zambarau, nyekundu na buluu, mwenye uzoefu wa kutia nakshi, ili afanye kazi Yuda na Yerusalemu pamoja na mafundi wangu wenye ustadi, ambao baba yangu Daudi aliwaweka.
2CH 2:8 “Pia nitumie magogo ya mierezi, misunobari na misandali kutoka Lebanoni kwa maana najua kwamba watu wako wanao ujuzi wa kupasua mbao huko. Watu wangu watafanya kazi pamoja na watu wako
2CH 2:9 ili wanipatie mbao kwa wingi kwa sababu Hekalu nitakalojenga lazima liwe kubwa na zuri kabisa.
2CH 2:10 Nitawapa watumishi wako, yaani maseremala wakatao mbao, kori elfu ishirini za unga wa ngano, kori elfu ishirini za shayiri, bathi elfu ishirini za mvinyo, na bathi elfu ishirini za mafuta ya zeituni.”
2CH 2:11 Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akamjibu Sulemani kwa barua: “Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawapenda watu wake, amekufanya wewe kuwa mfalme wao.”
2CH 2:12 Naye Hiramu akaongeza kusema: “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliyeziumba mbingu na nchi! Amempa Mfalme Daudi mwana mwenye hekima, aliyejaliwa maarifa na busara, ambaye atajenga Hekalu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe.
2CH 2:13 “Mimi nitamtuma kwako Huram-Abi, mtu mwenye ustadi mwingi,
2CH 2:14 ambaye mama yake alitoka Dani na baba yake alitoka Tiro. Yeye ni stadi wa kutengeneza vitu, kufanya kazi zote za dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe na mbao pamoja na kufuma. Ni stadi katika kutia rangi ya zambarau, buluu, nyekundu na nguo za kitani safi. Yeye ana ujuzi katika aina zote za kutia nakshi na anaweza kufuatiliza mchoro wowote wa kazi anayopewa. Atafanya kazi na mafundi wako na wale wa bwana wangu, Daudi baba yako.
2CH 2:15 “Sasa basi bwana wangu na awapelekee watumishi wake ngano, shayiri, mafuta ya zeituni na mvinyo kama alivyoahidi,
2CH 2:16 nasi tutakata magogo yote yale unayohitaji kutoka Lebanoni nasi tutayafunga pamoja na kuyaweka yaelee baharini hadi Yafa. Kisha utaweza kuyapeleka hadi Yerusalemu.”
2CH 2:17 Ndipo Sulemani akaamuru ifanyike hesabu ya wageni wote waliokuwa katika Israeli, baada ya ile hesabu iliyofanywa na Daudi; wakapatikana watu elfu mia moja hamsini na tatu na mia sita.
2CH 2:18 Akawaweka watu elfu sabini miongoni mwao kuwa wachukuzi wa mizigo, na elfu themanini kuwa wachonga mawe vilimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi ili wawahimize watu kufanya kazi.
2CH 3:1 Ndipo Sulemani akaanza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu juu ya Mlima Moria, pale ambapo Mwenyezi Mungu alikuwa amemtokea Daudi baba yake. Ilikuwa katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi, mahali palipotolewa na Daudi.
2CH 3:2 Alianza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa utawala wake.
2CH 3:3 Msingi aliouweka Sulemani kwa ajili ya kulijenga Hekalu la Mungu ulikuwa na urefu wa dhiraa sitini, na upana wa dhiraa ishirini kwa kipimo cha kale.
2CH 3:4 Ukumbi wa mbele wa Hekalu ulikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, yaani kuanzia upande mmoja hadi upande mwingine wa upana wa nyumba hiyo, na kimo chake dhiraa thelathini. Akaufunika ndani kwa dhahabu safi.
2CH 3:5 Akaufunika ukumbi mkuu kwa mbao za msunobari, na kufunikwa kwa dhahabu safi, na kuupamba kwa michoro ya mitende na minyororo.
2CH 3:6 Alilipamba Hekalu kwa vito vya thamani. Hiyo dhahabu aliyotumia ilikuwa dhahabu ya Parvaimu.
2CH 3:7 Akazifunika boriti za dari, miimo na vizingiti vya milango, kuta na milango ya Hekalu kwa dhahabu, naye akatia nakshi ya makerubi kwenye kuta.
2CH 3:8 Akajenga Patakatifu pa Patakatifu, urefu na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini, sawasawa na upana wa Hekalu. Alifunika ndani kwa talanta 600 za dhahabu safi.
2CH 3:9 Misumari ya dhahabu ilikuwa na uzito wa shekeli hamsini. Alivifunika pia vyumba vya juu kwa dhahabu.
2CH 3:10 Katika sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza jozi moja ya makerubi ya kuchongwa na kuyafunika kwa dhahabu.
2CH 3:11 Urefu wa mabawa ya hao makerubi ulikuwa jumla ya dhiraa ishirini. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano, nalo liligusa ukuta wa Hekalu; bawa lake lingine lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano, ambalo liligusa bawa la kerubi mwingine.
2CH 3:12 Vivyo hivyo bawa moja la kerubi wa pili lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na liligusa ukuta mwingine wa pili wa Hekalu, na bawa lake lingine lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano nalo liligusa bawa la kerubi wa kwanza.
2CH 3:13 Mabawa ya makerubi hawa yalitanda dhiraa ishirini. Walisimama kwa miguu yao, nyuso zao zikielekea ukumbi mkubwa.
2CH 3:14 Akatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na za kitani safi, na kutarizi makerubi juu yake.
2CH 3:15 Mbele ya Hekalu Sulemani akatengeneza nguzo mbili, ambazo kwa pamoja zilikuwa na urefu wa dhiraa thelathini na tano kwenda juu, na kila moja ilikuwa na taji juu yake yenye kimo cha dhiraa tano.
2CH 3:16 Akatengeneza minyororo iliyosokotwa, na kuiweka juu ya zile nguzo. Pia akatengeneza makomamanga mia moja, na kuyaunganisha kwenye minyororo.
2CH 3:17 Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya Hekalu, moja upande wa kusini na nyingine upande wa kaskazini. Ile moja ya upande wa kusini akaiita Yakini, na ya upande wa kaskazini akaiita Boazi.
2CH 4:1 Mfalme Sulemani akatengeneza madhabahu ya shaba yenye urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini na kimo chake dhiraa kumi.
2CH 4:2 Akatengeneza Bahari ya kusubu, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo na kimo cha dhiraa tano. Kamba ya urefu wa dhiraa thelathini ingeweza kuizunguka.
2CH 4:3 Chini ya huo ukingo, kulikuwa na mafahali kuizunguka, yaani mafahali kumi katika kila dhiraa moja. Hayo mafahali waliyasubu katika safu mbili yakiwa ya kitu kimoja na hiyo Bahari.
2CH 4:4 Bahari hiyo ilikaa juu ya mafahali kumi na wawili, mafahali watatu walielekeza nyuso zao kaskazini, watatu magharibi, watatu kusini, na watatu mashariki. Bahari hiyo ilikaa juu ya hao mafahali, nazo sehemu zao za nyuma zilielekeana.
2CH 4:5 Unene wake ulikuwa nyanda moja, na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi iliyochanua. Ingejazwa na bathi elfu tatu.
2CH 4:6 Kisha akatengeneza masinia kumi kwa ajili ya kuoshea vifaa, naye akayaweka matano upande wa kusini na matano upande wa kaskazini. Ndani yake ndimo walioshea vifaa vya kutumika katika sadaka za kuteketezwa, lakini ile Bahari ilikuwa ya makuhani kunawia.
2CH 4:7 Akatengeneza vinara kumi vya taa vya dhahabu kama ilivyoainishwa na kuviweka hekaluni, vinara vitano upande wa kusini, na vitano upande wa kaskazini.
2CH 4:8 Akatengeneza meza kumi na kuziweka hekaluni, tano upande wa kusini na tano upande wa kaskazini. Pia akatengeneza mabakuli mia moja ya dhahabu ya kunyunyizia.
2CH 4:9 Akatengeneza ukumbi wa makuhani, na ukumbi mwingine mkubwa na milango yake, naye akaifunika hiyo milango kwa shaba.
2CH 4:10 Akaiweka ile Bahari upande wa kusini, kwenye pembe ya kusini-mashariki mwa nyumba.
2CH 4:11 Huramu pia akatengeneza masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi katika Hekalu la Mungu kama vile Mfalme Sulemani alikuwa amemwagiza:
2CH 4:12 zile nguzo mbili; yale mataji mawili yaliyokuwa juu ya hizo nguzo, zile nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli yaliyowekwa juu ya zile nguzo;
2CH 4:13 yale makomamanga mia nne kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo);
2CH 4:14 vishikio pamoja na masinia yake;
2CH 4:15 hiyo Bahari na hao mafahali kumi na wawili chini yake;
2CH 4:16 pia hayo masufuria, masepetu, uma za nyama na vyombo vingine vyote vilivyohusiana. Vitu vyote ambavyo Huram-Abi alimtengenezea Mfalme Sulemani kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa.
2CH 4:17 Mfalme aliagiza wavisubu vitu hivi kwenye kalibu za udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani kati ya Sukothi na Sereda.
2CH 4:18 Vitu hivi vyote Mfalme Sulemani alivyotengeneza vilikuwa vingi sana hivi kwamba uzani wa shaba haungekadirika.
2CH 4:19 Sulemani pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu: madhabahu ya dhahabu; meza za kuweka mikate ya Wonesho;
2CH 4:20 vinara vya taa vya dhahabu safi pamoja na taa zake ili ziwake mbele ya mahali patakatifu kama ilivyoelekezwa;
2CH 4:21 maua ya dhahabu yaliyofanyizwa, taa na makoleo (vilikuwa vya dhahabu bora kabisa);
2CH 4:22 mikasi ya dhahabu safi, mabakuli ya kunyunyizia, masinia na vyetezo; milango ya dhahabu ya Hekalu: yaani milango ya ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, na milango ya ukumbi mkuu.
2CH 5:1 Hivyo Sulemani alipomaliza kazi ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la Mungu.
2CH 5:2 Kisha Sulemani akawaita huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila, na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Sayuni, Mji wa Daudi.
2CH 5:3 Nao wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa mfalme wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba.
2CH 5:4 Wazee wote wa Israeli walipofika, Walawi wakajitwika Sanduku la Agano,
2CH 5:5 nao wakalipandisha Sanduku na Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani, waliokuwa Walawi, walivibeba vitu hivyo,
2CH 5:6 naye Mfalme Sulemani na kusanyiko lote la Israeli waliokuwa wamemzunguka wakasimama mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu za kondoo na ng’ombe nyingi kiasi kwamba idadi yao haikuweza kuandikwa au kuhesabika.
2CH 5:7 Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu hadi mahali patakatifu ndani ya Hekalu, pale Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi.
2CH 5:8 Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kufunika Sanduku na mipiko yake ya kubebea.
2CH 5:9 Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilizojitokeza kutoka Sanduku, nazo zilionekana ukiwa mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo.
2CH 5:10 Ndani ya Sanduku hapakuwa na kitu kingine chochote isipokuwa vile vibao viwili ambavyo Musa aliviweka ndani yake huko Horebu, mahali Mwenyezi Mungu alipofanya agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
2CH 5:11 Basi makuhani wakaondoka hapo Mahali Patakatifu. Makuhani wote waliokuwa huko walikuwa wamejiweka wakfu, bila kujali migawanyo yao.
2CH 5:12 Walawi wote waliokuwa waimbaji, yaani Asafu, Hemani, Yeduthuni, wana wa ndugu zao, walisimama upande wa mashariki wa madhabahu, wakiwa wamevaa kitani safi huku wakipiga matoazi, vinubi na zeze. Walikuwa pamoja na makuhani mia moja na ishirini wakipiga tarumbeta.
2CH 5:13 Wapiga tarumbeta na waimbaji wakaungana katika sauti linganifu, ikawa kama vile ni sauti moja, wakimsifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Nao wakapaza sauti zao, pamoja na tarumbeta na matoazi na vyombo vingine vya uimbaji, wakamsifu Mwenyezi Mungu, wakisema: “Yeye ni mwema; fadhili zake zadumu milele.” Ndipo Hekalu la Mwenyezi Mungu likajazwa na wingu,
2CH 5:14 nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulijaza Hekalu la Mungu.
2CH 6:1 Ndipo Sulemani akasema, “Mwenyezi Mungu alisema kwamba ataishi katika giza nene.
2CH 6:2 Nimejenga Hekalu zuri kwa ajili yako, mahali pako pa kukaa milele.”
2CH 6:3 Kusanyiko lote la Israeli walipokuwa wamesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki.
2CH 6:4 Kisha akasema: “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mikono yake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema,
2CH 6:5 ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo ili Jina langu lipate kuwamo humo, wala sikumchagua mtu yeyote kuwa kiongozi wa watu wangu Israeli.
2CH 6:6 Lakini sasa nimeuchagua Yerusalemu ili Jina langu lipate kuwamo humo, na nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’
2CH 6:7 “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
2CH 6:8 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako.
2CH 6:9 Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni mwili wako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’
2CH 6:10 “Mwenyezi Mungu ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
2CH 6:11 Nimeliweka humo Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuna lile Agano la Mwenyezi Mungu alilofanya na watu wa Israeli.”
2CH 6:12 Kisha Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu machoni pa kusanyiko lote la Israeli, naye akanyoosha mikono yake.
2CH 6:13 Basi Sulemani alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano na kimo chake dhiraa tatu, naye akaliweka katikati ya ukumbi wa nje. Akapanda juu ya hilo jukwaa kisha akapiga magoti mbele ya kusanyiko lote la Israeli, akanyoosha mikono yake kuelekea mbinguni.
2CH 6:14 Akasema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote.
2CH 6:15 Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.
2CH 6:16 “Sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiwa waangalifu katika yote wanayoyafanya na kuenenda mbele zangu kwa kuzingatia sheria zangu kama ulivyofanya.’
2CH 6:17 Sasa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie.
2CH 6:18 “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani na wanadamu? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga!
2CH 6:19 Hata hivyo sikiliza dua la mtumishi wako na maombi yake ya kuhurumiwa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambalo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo.
2CH 6:20 Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa.
2CH 6:21 Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia ukiwa mbinguni, makao yako, na unaposikia, samehe.
2CH 6:22 “Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili,
2CH 6:23 basi, sikia ukiwa mbinguni, ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimwadhibu yule mwenye hatia kwa kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake.
2CH 6:24 “Watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili,
2CH 6:25 basi usikie ukiwa mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.
2CH 6:26 “Mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu,
2CH 6:27 basi usikie ukiwa mbinguni, usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.
2CH 6:28 “Njaa au tauni vikija katika nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia,
2CH 6:29 kila dua au ombi litakalotolewa na yeyote kati ya watu wako Israeli, akitambua taabu zake na uchungu wake, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili,
2CH 6:30 basi usikie ukiwa mbinguni, makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote),
2CH 6:31 ili wakuogope na kuenenda katika utiifu kwako wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
2CH 6:32 “Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako kuu na mkono wako wenye nguvu ulionyooshwa, atakapokuja kuomba kuelekea Hekalu hili,
2CH 6:33 basi na usikie ukiwa mbinguni, makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli, nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.
2CH 6:34 “Watu wako watakapoenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa Mwenyezi Mungu kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako,
2CH 6:35 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, ukawape haki yao.
2CH 6:36 “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi iliyo mbali au karibu
2CH 6:37 na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya utumwa na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa na tumetenda uovu’;
2CH 6:38 wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako,
2CH 6:39 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, makao yako, ukawape haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako.
2CH 6:40 “Sasa, Mungu wangu, macho yako na yafumbuke na masikio yako yasikie maombi yanayoombwa katika mahali hapa.
2CH 6:41 “Sasa inuka, Ee Bwana Mwenyezi Mungu,
2CH 6:42 Ee Bwana Mwenyezi Mungu, usimkatae
2CH 7:1 Baada ya Sulemani kumaliza kuomba, moto ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukalijaza Hekalu.
2CH 7:2 Makuhani hawakuweza kuingia ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu kwa sababu utukufu wa Mwenyezi Mungu ulilijaza.
2CH 7:3 Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa Mwenyezi Mungu ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu, nyuso zao zikigusa chini, wakamwabudu na kumshukuru Mwenyezi Mungu, wakisema, “Yeye ni mwema; fadhili zake zadumu milele.”
2CH 7:4 Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu.
2CH 7:5 Naye Mfalme Sulemani akatoa dhabihu ya ng’ombe elfu ishirini na mbili pamoja na kondoo na mbuzi elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mungu.
2CH 7:6 Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao, vivyo hivyo Walawi wakiwa na vyombo vya uimbaji vya Mwenyezi Mungu ambavyo Mfalme Daudi alikuwa ametengeneza kwa ajili ya kumsifu Mwenyezi Mungu, navyo vilitumika aliposhukuru, akisema, “Fadhili zake zadumu milele.” Mkabala na Walawi, makuhani walipiga tarumbeta zao, nao Waisraeli wote walikuwa wamesimama.
2CH 7:7 Sulemani akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba aliyokuwa ametengeneza haikutosha kuweka sadaka hizo zote za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na za mafuta.
2CH 7:8 Hivyo Sulemani akaiadhimisha sikukuu wakati ule kwa muda wa siku saba, na Waisraeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri.
2CH 7:9 Katika siku ya nane walifanya kusanyiko, kwa sababu walikuwa wameadhimisha kuwekwa wakfu kwa madhabahu kwa muda wa siku saba, na sikukuu kwa muda wa siku nyingine saba.
2CH 7:10 Katika siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba Sulemani akawaaga watu waende nyumbani mwao, wakishangilia na kufurahi mioyoni mwao, kwa wema mwingi Mwenyezi Mungu aliomtendea Daudi na Sulemani na kwa ajili ya watu wake Israeli.
2CH 7:11 Sulemani alipomaliza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme, naye akiwa amefanikiwa kutenda yale yote aliyokuwa nayo moyoni mwake kufanya katika Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika jumba lake mwenyewe la kifalme,
2CH 7:12 Mwenyezi Mungu akamtokea Sulemani usiku na kumwambia: “Nimesikia maombi yako nami nimechagua mahali hapa kwa ajili yangu mwenyewe kuwa Hekalu kwa ajili ya dhabihu.
2CH 7:13 “Nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu,
2CH 7:14 ikiwa watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekeza na kuomba na kuutafuta uso wangu, na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao, na nitaiponya nchi yao.
2CH 7:15 Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yanayoombwa mahali hapa.
2CH 7:16 Kwa maana sasa nimechagua na kutakasa Hekalu hili ili Jina langu lipate kuwa humo milele. Macho yangu na moyo wangu vitakuwepo daima.
2CH 7:17 “Kwako wewe, ukienenda mbele zangu kama Daudi baba yako alivyoenenda, na kufanya yote ninayokuamuru, nawe ukizishika amri zangu na sheria zangu,
2CH 7:18 nitakiimarisha kiti chako cha ufalme kama nilivyoagana na Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe mtu wa kutawala Israeli.’
2CH 7:19 “Lakini mkigeuka na kuyaacha maagizo na amri nilizowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
2CH 7:20 ndipo nitakapoing’oa Israeli kutoka nchi yangu niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Nitalifanya kitu cha kudharauliwa na kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote.
2CH 7:21 Ingawa Hekalu hili linavutia sana sasa, wote watakaolipita watashangaa na kusema, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’
2CH 7:22 Watu watajibu, ‘Ni kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, aliyewatoa Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”
2CH 8:1 Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alilijenga Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba lake mwenyewe la kifalme,
2CH 8:2 Sulemani akajenga tena vijiji vile ambavyo Hiramu alikuwa amempa, naye akawapa Waisraeli waishi humo.
2CH 8:3 Kisha Sulemani akaenda Hamath-Soba na kuuteka.
2CH 8:4 Pia akajenga mji wa Tadmori katika jangwa, na miji yote ya kuhifadhia vitu katika Hamathi.
2CH 8:5 Akajenga tena Beth-Horoni ya Juu na Beth-Horoni ya Chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo.
2CH 8:6 Sulemani pia akajenga Baalathi na miji yake yote ya kuhifadhia vitu, na miji kwa ajili ya magari yake ya vita na kwa ajili ya farasi wake, chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni na katika nchi yote aliyotawala.
2CH 8:7 Watu wote waliosalia kutoka kwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (haya mataifa hayakuwa Waisraeli),
2CH 8:8 yaani wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwa wamewaangamiza: hawa Sulemani akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo.
2CH 8:9 Lakini Sulemani hakuwafanya Waisraeli watumwa kwa ajili ya kazi yake; hao ndio walikuwa wapiganaji wake, majemadari wake, maafisa wake, majemadari wa magari yake ya vita, na wapanda farasi wake.
2CH 8:10 Pia walikuwa maafisa wakuu wa Mfalme Sulemani, maafisa wakaguzi mia mbili na hamsini waliosimamia watu.
2CH 8:11 Sulemani akampandisha mke wake binti Farao kutoka Mji wa Daudi na kumleta jumba la kifalme alilokuwa amemjengea, kwa kuwa alisema, “Mke wangu hataishi katika jumba la kifalme la Daudi mfalme wa Israeli, kwa sababu mahali ambapo Sanduku la Mwenyezi Mungu limefika ni patakatifu.”
2CH 8:12 Mfalme Sulemani akamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu ambayo alikuwa ameijenga mbele ya ukumbi,
2CH 8:13 kulingana na mahitaji ya kila siku kwa ajili ya sadaka zilizoamriwa na Musa kwa ajili ya Sabato, Mwezi Mwandamo na sikukuu nyingine tatu za mwaka: Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma na Sikukuu ya Vibanda.
2CH 8:14 Kwa kushika maagizo ya Daudi baba yake, aliweka migawanyo ya makuhani kwa ajili ya kazi zao, nao Walawi kuongoza kusifu na kusaidia makuhani kufuatana na mahitaji ya kila siku. Pia akaweka mabawabu katika migawanyo kwa ajili ya malango mbalimbali, kwa sababu hivi ndivyo Daudi mtu wa Mungu alivyokuwa ameagiza.
2CH 8:15 Nao hawakuziacha amri za mfalme alizoamuru makuhani au Walawi katika jambo lolote, ikiwa ni pamoja na zile za hazina.
2CH 8:16 Kazi yote ya Mfalme Sulemani ilifanyika kuanzia siku msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu ulipowekwa hadi kukamilika kwake. Kwa hiyo Hekalu la Mwenyezi Mungu likamalizika kujengwa.
2CH 8:17 Ndipo Sulemani akaenda Esion-Geberi na Elathi katika pwani ya Edomu.
2CH 8:18 Naye Hiramu alimpelekea meli zilizoongozwa na maafisa wake mwenyewe, watu waliokuwa na ujuzi wa baharini. Hawa watu pamoja na wale wa Sulemani wakasafiri kwa bahari hadi Ofiri, wakaleta kutoka huko talanta mia nne na hamsini za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Sulemani.
2CH 9:1 Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Sulemani, akaja Yerusalemu kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika akiwa na msafara mkubwa sana, wenye ngamia waliobeba vikolezo, dhahabu nyingi, na vito vya thamani. Alikuja kwa Sulemani na kuzungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.
2CH 9:2 Sulemani alimjibu maswali yake yote, wala hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwake hata asiweze kumwelezea.
2CH 9:3 Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na jumba la kifalme alilokuwa amejenga,
2CH 9:4 chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, alipatwa na mshangao mkubwa.
2CH 9:5 Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli.
2CH 9:6 Lakini sikuamini mambo yaliyosemwa hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana kuliko ile taarifa niliyoisikia.
2CH 9:7 Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wanaosimama mbele yako daima na kusikia hekima yako!
2CH 9:8 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe, na akakuweka kwenye kiti chake cha ufalme utawale kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Kwa sababu ya upendo wa Mungu wako kwa Israeli na shauku yake ya kuwathibitisha milele, amekufanya wewe mfalme juu yao, ili kudumisha haki na uadilifu.”
2CH 9:9 Naye akampa mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezo na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa vikolezo vizuri kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Sulemani.
2CH 9:10 (Watumishi wa Hiramu na wa Sulemani wakaleta dhahabu kutoka Ofiri, tena wakaleta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani.
2CH 9:11 Mfalme akatumia hiyo miti ya msandali kuwa ngazi kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa Yuda tangu siku ile.)
2CH 9:12 Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, zaidi ya vile alivyokuwa amemletea mfalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
2CH 9:13 Uzito wa dhahabu ambayo Sulemani alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta mia sita sitini na sita (666),
2CH 9:14 mbali na mapato yaliyoletwa na wafanyabiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.
2CH 9:15 Mfalme Sulemani akatengeneza ngao kubwa mia mbili kwa dhahabu iliyofuliwa. Kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli mia sita.
2CH 9:16 Akatengeneza pia ngao ndogo mia tatu za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.
2CH 9:17 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.
2CH 9:18 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na mahali pa kuwekea miguu vyote vya dhahabu. Kila upande wa kiti ulikuwa na mahali pa kuegemeza mkono, na simba aliyesimama kando kila upande.
2CH 9:19 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote.
2CH 9:20 Vikombe vyote vya Mfalme Sulemani vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Sulemani.
2CH 9:21 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizoendeshwa na watu wa Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo.
2CH 9:22 Mfalme Sulemani alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.
2CH 9:23 Wafalme wote wa dunia wakatafuta kukutana na Sulemani ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake.
2CH 9:24 Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja, alileta zawadi, vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezo, farasi na nyumbu.
2CH 9:25 Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne kwa ajili ya farasi na magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita, na wengine akawa nao huko Yerusalemu.
2CH 9:26 Sulemani akatawala juu ya wafalme wote kuanzia Mto hadi kwenye nchi ya Wafilisti na kuendelea hadi mpaka wa Misri.
2CH 9:27 Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima.
2CH 9:28 Farasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka nchi nyingine zote.
2CH 9:29 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Sulemani, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Nathani, katika unabii wa Ahiya Mshiloni na katika maono ya Ido mwonaji kuhusu Yeroboamu mwana wa Nebati?
2CH 9:30 Sulemani alitawala Israeli yote miaka arobaini akiwa Yerusalemu.
2CH 9:31 Kisha Sulemani akalala na baba zake, naye akazikwa katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 10:1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wameenda huko kumfanya mfalme.
2CH 10:2 Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Sulemani), akarudi kutoka Misri.
2CH 10:3 Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu; yeye na Waisraeli wote wakamwendea Rehoboamu na kumwambia,
2CH 10:4 “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”
2CH 10:5 Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.
2CH 10:6 Kisha Mfalme Rehoboamu akataka ushauri kwa wazee ambao walimtumikia Sulemani baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri niwajibu nini watu hawa?”
2CH 10:7 Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”
2CH 10:8 Lakini Rehoboamu akakataa ushauri aliopewa na wazee, na akataka ushauri kwa vijana wa rika lake waliokuwa wakimtumikia.
2CH 10:9 Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu’?”
2CH 10:10 Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Watu hawa walikuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ Wewe waambie, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.
2CH 10:11 Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.’ ”
2CH 10:12 Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.”
2CH 10:13 Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Alikataa ushauri aliopewa na wazee,
2CH 10:14 akafuata ushauri wa vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.”
2CH 10:15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Mungu ili kutimiza neno ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amenena na Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia kwa Ahiya Mshiloni.
2CH 10:16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme: “Je, tuna fungu gani kwa Daudi? Tuna urithi gani kwa mwana wa Yese? Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli, angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!” Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao.
2CH 10:17 Lakini kwa habari ya Waisraeli walioishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.
2CH 10:18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoniramu aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu akafanikiwa kuingia kwenye gari lake la vita, akatorokea Yerusalemu.
2CH 10:19 Hivyo, Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.
2CH 11:1 Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na ya Benyamini, vijana wenye uwezo elfu mia moja na themanini, ili kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli, na kuurudisha ufalme kwa Rehoboamu.
2CH 11:2 Lakini neno hili la Mwenyezi Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu:
2CH 11:3 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani mfalme wa Yuda, na Waisraeli wote walio Yuda na Benyamini,
2CH 11:4 ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Mwenyezi Mungu na kurudi, wakaacha kwenda kupigana dhidi ya Yeroboamu.
2CH 11:5 Rehoboamu akaishi Yerusalemu akajenga miji yenye ngome katika Yuda:
2CH 11:6 Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa,
2CH 11:7 Beth-Suri, Soko, Adulamu,
2CH 11:8 Gathi, Maresha, Zifu,
2CH 11:9 Adoraimu, Lakishi, Azeka,
2CH 11:10 Sora, Aiyaloni na Hebroni. Hii ilikuwa miji yenye ngome katika Yuda na Benyamini.
2CH 11:11 Akaimarisha ulinzi wake na kuweka majemadari ndani yake, pamoja na maghala ya vyakula, ya mafuta ya zeituni, na ya divai.
2CH 11:12 Akaweka ngao na mikuki katika miji na kuifanya iwe imara sana. Kwa hiyo Yuda na Benyamini zikawa zake.
2CH 11:13 Makuhani na Walawi kutoka sehemu zote za Israeli wakawa upande wake.
2CH 11:14 Pia Walawi wakaacha maeneo yao ya malisho na mali yao, wakaja Yuda na Yerusalemu kwa sababu Yeroboamu na wanawe walikuwa wamewakataa wasiwe makuhani wa Mwenyezi Mungu.
2CH 11:15 Naye akawa amechagua makuhani wake mwenyewe kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia sanamu za mbuzi na za ndama ambazo alikuwa ametengeneza.
2CH 11:16 Wale waliotoka katika kila kabila la Israeli ambao walielekeza mioyo yao kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, wakawafuata Walawi huko Yerusalemu kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu, Mungu wa baba zao.
2CH 11:17 Wakaimarisha ufalme wa Yuda na kumuunga mkono Rehoboamu mwana wa Sulemani miaka mitatu, wakienenda katika njia za Daudi na Sulemani katika wakati huu.
2CH 11:18 Rehoboamu alimwoa Mahalati aliyekuwa binti Yeremothi mwana wa Daudi; mamaye alikuwa Abihaili binti Eliabu mwana wa Yese.
2CH 11:19 Mahalati alimzalia Rehoboamu wana: Yeushi, Shemaria na Zahamu.
2CH 11:20 Kisha akamwoa Maaka binti Absalomu, aliyemzalia Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi.
2CH 11:21 Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wengine na masuria wake. Kwa jumla alikuwa na wake kumi na wanane na masuria sitini, wana ishirini na wanane na binti sitini.
2CH 11:22 Rehoboamu akamweka Abiya mwana wa Maaka, kuwa mkuu wa wana wa mfalme miongoni mwa ndugu zake ili amfanye mfalme.
2CH 11:23 Akatenda kwa busara, akiwasambaza baadhi ya wanawe katika wilaya zote za Yuda na Benyamini, pamoja na miji yote yenye ngome. Akawapa mahitaji tele na kuwaoza wake wengi.
2CH 12:1 Baada ya ufalme wa Rehoboamu kuimarika naye akawa na nguvu, yeye na Waisraeli wote waliiacha Torati ya Mwenyezi Mungu.
2CH 12:2 Kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu.
2CH 12:3 Akiwa na magari ya vita elfu moja mia mbili, wapanda farasi elfu sitini, na idadi isiyohesabika ya majeshi ya Walibia, Wasukii na Wakushi waliokuja pamoja naye kutoka Misri.
2CH 12:4 Akateka miji ya Yuda yenye ngome, akaendelea hadi Yerusalemu.
2CH 12:5 Ndipo nabii Shemaya akaja kwa Rehoboamu na kwa viongozi wa Yuda waliokuwa wamekusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya hofu ya Shishaki naye akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Ninyi mmeniacha, kwa hiyo, mimi nami sasa ninawaacha mkononi mwa Shishaki.’ ”
2CH 12:6 Viongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “Mwenyezi Mungu ni mwenye haki.”
2CH 12:7 Mwenyezi Mungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili la Mwenyezi Mungu likamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza, bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kupitia kwa Shishaki.
2CH 12:8 Hata hivyo, watamtumikia Shishaki ili wapate kujifunza tofauti kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa nchi nyingine.”
2CH 12:9 Shishaki mfalme wa Misri alipoishambulia Yerusalemu, alichukua hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza.
2CH 12:10 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme.
2CH 12:11 Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu walinzi walienda pamoja naye wakiwa wamebeba hizo ngao na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.
2CH 12:12 Kwa sababu Rehoboamu alijinyenyekeza, hasira ya Mwenyezi Mungu ikageukia mbali naye, hakuangamizwa kabisa. Kukawa na hali nzuri katika Yuda.
2CH 12:13 Mfalme Rehoboamu akajiweka imara katika Yerusalemu na akaendelea kuwa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na saba, mji ambao Mwenyezi Mungu alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili aliweke Jina lake humo. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni.
2CH 12:14 Rehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafuta Mwenyezi Mungu.
2CH 12:15 Kwa habari ya matukio katika utawala wa Rehoboamu, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Shemaya na mwonaji Ido zinazohusiana na vizazi? Kulikuwa na vita vya mara kwa mara kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.
2CH 12:16 Rehoboamu akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 13:1 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu, Abiya akawa mfalme wa Yuda,
2CH 13:2 naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka, binti Urieli wa Gibea. Basi kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.
2CH 13:3 Abiya aliingia vitani na jeshi la watu elfu mia nne wenye uwezo wa kupigana, naye Yeroboamu akapanga jeshi dhidi ya Abiya akiwa na jeshi la watu elfu mia nane wenye uwezo.
2CH 13:4 Abiya akasimama juu ya Mlima Semaraimu, katika nchi ya vilima ya Efraimu, naye akasema, “Yeroboamu na Waisraeli wote, nisikilizeni!
2CH 13:5 Hamfahamu kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi na wazao wake ufalme juu ya Israeli milele kwa agano la chumvi?
2CH 13:6 Hata hivyo Yeroboamu mwana wa Nebati afisa wa Sulemani mwana wa Daudi, aliasi dhidi ya bwana wake.
2CH 13:7 Baadhi ya watu wasiofaa kitu, wabaya kabisa walimkusanyikia na kumpinga Rehoboamu mwana wa Sulemani alipokuwa kijana mdogo asiyekuwa na uamuzi, asiye na nguvu za kuweza kupingana nao.
2CH 13:8 “Hata sasa unapanga kupingana na ufalme wa Mwenyezi Mungu ambao uko mikononi mwa wazao wa Daudi. Kweli ninyi ni jeshi kubwa nanyi mnazo ndama za dhahabu Yeroboamu alizozitengeneza kuwa miungu yenu.
2CH 13:9 Lakini je, hamkuwafukuza makuhani wa Mwenyezi Mungu, wana wa Haruni na Walawi na kujifanyia makuhani wenu wenyewe kama yafanyavyo mataifa ya nchi nyingine? Yeyote anayekuja kujiweka wakfu akiwa na ndama dume na kondoo dume saba aweza kuwa kuhani wa kile ambacho ni miungu kwenu.
2CH 13:10 “Lakini kwetu sisi, Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wetu, wala hatujamwacha. Makuhani wanaomtumikia Mwenyezi Mungu ni wana wa Haruni, nao Walawi wakiwasaidia.
2CH 13:11 Kila asubuhi na jioni wao hutoa sadaka za kuteketezwa na kufukiza uvumba wa harufu nzuri kwa Mwenyezi Mungu. Wao huweka mikate juu ya meza takatifu, na kuwasha taa kwenye kinara cha dhahabu kila jioni. Sisi tunazishika kanuni za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Lakini ninyi mmemwacha Mungu.
2CH 13:12 Mungu yu pamoja nasi; yeye ndiye kiongozi wetu. Makuhani wake wakiwa na tarumbeta zao watapiga baragumu ya vita dhidi yenu. Watu wa Israeli, msipigane dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, kwa maana hamtashinda.”
2CH 13:13 Basi Yeroboamu alikuwa ametuma jeshi kuzunguka nyuma ya Yuda ili akiwa mbele ya Yuda, jeshi liwavizie kwa nyuma.
2CH 13:14 Basi Yuda wakageuka na kuona kwamba wanashambuliwa mbele na nyuma. Ndipo wakamlilia Mwenyezi Mungu. Makuhani wakapiga tarumbeta zao,
2CH 13:15 nao wanaume wa Yuda wakapiga ukelele wa vita. Walipopiga ukelele wa vita, Mungu akawafukuza Yeroboamu na Waisraeli wote mbele ya Mfalme Abiya na Yuda.
2CH 13:16 Waisraeli wakakimbia mbele ya Yuda, naye Mungu akawatia mikononi mwao.
2CH 13:17 Abiya na askari wake wakawachinja kwa machinjo makuu, hata wakawepo majeruhi elfu mia tano miongoni mwa watu wenye uwezo wa Israeli.
2CH 13:18 Waisraeli walitiishwa katika tukio lile, nao watu wa Yuda wakawa washindi kwa sababu walimtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
2CH 13:19 Abiya akamfuatia Yeroboamu na kuteka miji ya Betheli, Yeshana na Efroni kutoka kwake, pamoja na vijiji vya miji hiyo.
2CH 13:20 Yeroboamu hakupata nguvu tena wakati wa utawala wa Abiya. Naye Mwenyezi Mungu akampiga Yeroboamu akafa.
2CH 13:21 Lakini Abiya akapata nguvu. Alioa wanawake kumi na wanne na alikuwa na wana ishirini na wawili na binti kumi na sita.
2CH 13:22 Matukio mengine ya utawala wa Abiya, pamoja na mambo aliyofanya na aliyosema, yameandikwa katika kitabu cha maelezo cha nabii Ido.
2CH 14:1 Naye Abiya akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika siku zake, nchi ikawa na amani kwa miaka kumi.
2CH 14:2 Asa akatenda yaliyo mema na haki machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
2CH 14:3 Akaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu pa kuabudia, akayavunja yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Maashera.
2CH 14:4 Akawaamuru Yuda kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, na kutii sheria zake na amri zake.
2CH 14:5 Akaondoa mahali pa juu pa kuabudia na madhabahu za kufukizia uvumba kwenye kila mji katika Yuda, nao ufalme ulikuwa na amani katika utawala wake.
2CH 14:6 Akajenga miji yenye ngome katika Yuda, wakati nchi ikiwa na amani. Hakuna mtu yeyote aliyepigana vita naye katika miaka hiyo, kwa kuwa Mwenyezi Mungu alimpa amani.
2CH 14:7 Mfalme akawaambia Yuda, “Tuijenge hii miji na tuizungushie kuta, pamoja na minara, malango na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tumemtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tulimtafuta naye ametupatia amani kila upande.” Hivyo wakajenga na wakafanikiwa.
2CH 14:8 Asa alikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu kutoka Yuda, wenye ngao kubwa na mikuki, na jeshi la watu elfu mia mbili na themanini kutoka Benyamini, wenye ngao ndogo na pinde. Watu hawa wote walikuwa wapiganaji hodari.
2CH 14:9 Zera Mkushi akatoka kupigana dhidi yao akiwa na jeshi la watu maelfu ya maelfu na magari ya vita mia tatu, nao wakaja Maresha.
2CH 14:10 Asa akatoka kumkabili, nao wakapanga vita katika Bonde la Sefatha karibu na Maresha.
2CH 14:11 Kisha Asa akamlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kusema, “Ee Mwenyezi Mungu, hakuna yeyote aliye kama wewe wa kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Mungu wetu, kwa kuwa tunakutumainia wewe, nasi kwa jina lako tumekuja dhidi ya jeshi hili kubwa. Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Mungu wetu, usiwaache wanadamu wakushinde wewe.”
2CH 14:12 Mwenyezi Mungu akawapiga Wakushi mbele ya Asa na Yuda. Wakushi wakakimbia,
2CH 14:13 naye Asa na jeshi lake wakawafuatia hadi Gerari. Idadi kubwa ya Wakushi ilianguka hata wasiweze kuinuka tena, wakapondapondwa mbele za Mwenyezi Mungu na majeshi yake. Watu wa Yuda wakachukua nyara nyingi sana;
2CH 14:14 wakaangamiza vijiji vyote vya Gerari, kwa kuwa kicho cha Mwenyezi Mungu kilikuwa kimewaangukia. Wakateka nyara vijiji hivi vyote, kwani kulikuwa na nyara nyingi huko.
2CH 14:15 Pia wakashambulia kambi za wachunga makundi ya wanyama wakachukua na kuyaswaga makundi ya kondoo, mbuzi na ngamia. Kisha wakarudi Yerusalemu.
2CH 15:1 Roho wa Mungu akamjia Azaria mwana wa Odedi.
2CH 15:2 Akatoka ili kumlaki Asa na kumwambia, “Nisikilizeni, Asa na Yuda wote na Benyamini. Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi mkiwa pamoja naye. Mkimtafuta, ataonekana kwenu, lakini mkimwacha, naye atawaacha.
2CH 15:3 Kwa muda mrefu Israeli walikuwa hawana Mungu wa kweli, walikuwa hawana kuhani wa kuwafundisha na wala hawakuwa na sheria.
2CH 15:4 Lakini katika taabu yao walimrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, na kumtafuta, naye akaonekana kwao.
2CH 15:5 Katika siku hizo hapakuwa na amani kwa yeyote aliyesafiri, kutoka wala kuingia, kwa kuwa wakazi wote wa nchi walikuwa katika machafuko makubwa.
2CH 15:6 Taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ukapigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu alikuwa anawahangaisha kwa taabu za kila aina.
2CH 15:7 Lakini ninyi, kuweni hodari wala msikate tamaa, kwa kuwa mtapata thawabu kwa kazi yenu.”
2CH 15:8 Asa aliposikia maneno haya na unabii wa Azaria mwana wa Odedi yule nabii, akajipa moyo. Akaziondoa sanamu zote zilizokuwa machukizo katika nchi yote ya Yuda na Benyamini, na kutoka miji aliyoiteka katika nchi ya vilima ya Efraimu. Akakarabati madhabahu ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa mbele ya ukumbi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 15:9 Kisha akakutanisha Yuda wote, Benyamini na watu kutoka Efraimu, watu wa Manase na Simeoni walioishi miongoni mwao, kwa maana idadi kubwa walikuwa wamemjia kutoka Israeli walipoona kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.
2CH 15:10 Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Asa.
2CH 15:11 Wakati huo wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu za ng’ombe mia saba, kondoo na mbuzi elfu saba kutoka nyara walizoteka.
2CH 15:12 Wakafanya agano kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote.
2CH 15:13 Wale wote ambao hawangemtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, wangelazimika kuuawa, akiwa mdogo au mkubwa, mwanaume au mwanamke.
2CH 15:14 Wakamwapia Mwenyezi Mungu kwa sauti kuu, kwa kelele, na kupiga tarumbeta na mabaragumu.
2CH 15:15 Yuda wote wakafurahia kile kiapo kwa sababu walikuwa wameapa kwa moyo wao wote. Wakamtafuta Mungu kwa bidii, naye akaonekana kwao. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawapa amani pande zote.
2CH 15:16 Mfalme Asa akamwondolea Maaka, bibi yake, wadhifa wake kama mama malkia kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo, akaivunjavunja na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni.
2CH 15:17 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia katika Israeli, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Mwenyezi Mungu kikamilifu maisha yake yote.
2CH 15:18 Akaleta ndani ya Hekalu la Mungu fedha na dhahabu na vile vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.
2CH 15:19 Hapakuwa na vita tena hadi mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa.
2CH 16:1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa Asa, Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.
2CH 16:2 Ndipo Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka hazina ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na kutoka jumba lake la kifalme na kumpelekea Ben-Hadadi mfalme wa Aramu, aliyekuwa anatawala huko Dameski.
2CH 16:3 Akasema, “Na pawe mkataba kati yangu na wewe, kama palivyokuwa kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee.”
2CH 16:4 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Wakashinda Iyoni, Dani, Abel-Maimu na miji yote ya hazina ya Naftali.
2CH 16:5 Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha kujenga Rama na kuacha kazi yake.
2CH 16:6 Ndipo Mfalme Asa akawaleta watu wote wa Yuda, nao wakachukua mawe na miti ambayo Baasha alikuwa anavitumia huko Rama. Kwa vitu hivyo akajenga Geba na Mispa.
2CH 16:7 Ikawa wakati huo mwonaji Hanani akamjia Mfalme Asa wa Yuda na kumwambia: “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Aramu nawe hukumtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wako, jeshi la mfalme wa Aramu limeponyoka mkononi mwako.
2CH 16:8 Je, hukumbuki lililotendeka kwa Wakushi na Walibia, hawakuwa jeshi lenye nguvu na magari mengi ya vita na wapanda farasi? Hata hivyo, ulipomtegemea Mwenyezi Mungu yeye aliwatia mkononi mwako.
2CH 16:9 Kwa kuwa macho ya Mwenyezi Mungu yanazunguka dunia yote ili kuwatia nguvu wale ambao mioyo yao inamtegemea kwa ukamilifu. Umefanya jambo la upumbavu, na kuanzia sasa na kuendelea utakuwa na vita.”
2CH 16:10 Asa akamkasirikia mwonaji kwa sababu ya jambo hili. Alikuwa ameghadhibika sana hata akamweka gerezani. Wakati huo huo Asa akaanza kuwatesa na kuwaonea baadhi ya watu kwa ukatili.
2CH 16:11 Matukio ya utawala wa Asa, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
2CH 16:12 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wake, Asa alishikwa na ugonjwa kwa miguu yake. Ingawa ugonjwa wake ulimzidia sana, hata katika kuugua kwake hakutafuta msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu bali kwa matabibu tu.
2CH 16:13 Katika mwaka wa arobaini na moja wa utawala wa Asa, alikufa, akalala na baba zake.
2CH 16:14 Nao wakamzika katika kaburi lile alilokuwa amejichongea katika Mji wa Daudi. Wakamzika kwa jeneza lililowekwa vikolezo na mchanganyiko wa manukato ya aina mbalimbali yaliyotengenezwa kwa utaalamu wa mtengeneza marashi, nao wakawasha moto mkubwa kwa heshima yake.
2CH 17:1 Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake na akajiimarisha dhidi ya Israeli.
2CH 17:2 Akaweka jeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, na kuweka askari walinzi katika Yuda na katika miji ya Efraimu ambayo baba yake Asa alikuwa ameiteka.
2CH 17:3 Mwenyezi Mungu alikuwa na Yehoshafati kwa sababu katika miaka yake ya mwanzoni alienenda katika njia za Daudi baba yake. Hakutafuta Mabaali
2CH 17:4 bali alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzifuata amri zake badala ya kufuata desturi za Waisraeli.
2CH 17:5 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akauimarisha ufalme chini ya uongozi wake, nao Yuda wote wakamletea Yehoshafati zawadi, hivyo akawa na utajiri mwingi na heshima.
2CH 17:6 Moyo wake ukawa hodari katika njia za Mwenyezi Mungu na zaidi ya yote, akaondoa mahali pa juu pa kuabudia na nguzo za Maashera katika Yuda.
2CH 17:7 Katika mwaka wa tatu wa utawala wake Yehoshafati, alituma maafisa wake ambao ni Ben-Haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya ili kufundisha katika miji ya Yuda.
2CH 17:8 Pamoja nao walikuwa na Walawi kadhaa: Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia, Tob-Adonia; na pamoja nao makuhani Elishama na Yehoramu.
2CH 17:9 Wakafundisha Yuda yote, wakiwa wamechukua Kitabu cha Torati ya Mwenyezi Mungu; wakazunguka miji yote ya Yuda na kufundisha watu.
2CH 17:10 Kicho cha Mwenyezi Mungu kikawa juu ya falme zote za nchi zilizozunguka Yuda, hivyo hawakufanya vita na Yehoshafati.
2CH 17:11 Baadhi ya Wafilisti wakamletea Yehoshafati zawadi na fedha kama ushuru, nao Waarabu wakamletea mifugo: kondoo dume elfu saba na mia saba, na mbuzi elfu saba na mia saba.
2CH 17:12 Yehoshafati akaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi, akajenga ngome na miji ya hazina katika Yuda,
2CH 17:13 na akawa na vifaa vingi katika miji ya Yuda. Pia aliweka wapiganaji wenye uzoefu huko Yerusalemu.
2CH 17:14 Wakaandikishwa katika jamaa zao kama ifuatavyo: Kutoka Yuda, majemadari wa vikosi vya elfu: Jemadari Adna akiwa na wapiganaji elfu mia tatu;
2CH 17:15 aliyefuata ni jemadari Yehohanani, akiwa na wapiganaji elfu mia mbili na themanini;
2CH 17:16 aliyefuata ni Amasia mwana wa Zikri, ambaye alijitolea kwa ajili ya kazi ya Mwenyezi Mungu, akiwa na wapiganaji elfu mia mbili.
2CH 17:17 Kutoka Benyamini: Eliada, mpiganaji hodari, akiwa na watu elfu mia mbili wenye nyuta na ngao;
2CH 17:18 aliyefuata ni Yehozabadi, akiwa na wapiganaji elfu mia moja na themanini tayari kwa vita.
2CH 17:19 Hawa ndio wapiganaji waliomtumikia mfalme, mbali na ambao mfalme aliwaweka katika miji yenye ngome katika Yuda yote.
2CH 18:1 Basi, Yehoshafati alikuwa na mali nyingi sana na heshima. Naye akafanya urafiki na Ahabu kwa uhusiano wa ndoa.
2CH 18:2 Baada ya miaka kadhaa akateremka kumtembelea Ahabu huko Samaria. Ahabu akachinja ng’ombe na kondoo wengi kwa ajili yake na watu aliokuwa amefuatana nao. Kisha Ahabu akamshawishi Yehoshafati kukwea pamoja naye ili kuishambulia Ramoth-Gileadi.
2CH 18:3 Ahabu mfalme wa Israeli akamuuliza Yehoshafati mfalme wa Yuda, “Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako. Tutakuwa pamoja nawe vitani.”
2CH 18:4 Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta ushauri wa Mwenyezi Mungu.”
2CH 18:5 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii, wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?” Wakajibu, “Naam, nenda kwa kuwa Mungu ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”
2CH 18:6 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Mwenyezi Mungu hapa ambaye tunaweza kumuuliza?”
2CH 18:7 Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia kwake twaweza kuuliza ushauri wa Mwenyezi Mungu, lakini namchukia kwa sababu hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila hunitabiria mabaya kila mara. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.” Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”
2CH 18:8 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”
2CH 18:9 Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, huku manabii wote wakitabiri mbele yao.
2CH 18:10 Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma. Naye akatangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Kwa hizi pembe utawapiga Waaramu hadi waangamizwe.’ ”
2CH 18:11 Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho, wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ataitia mkononi mwa mfalme.”
2CH 18:12 Mjumbe aliyekuwa ameenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”
2CH 18:13 Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, nitamwambia kile tu Mwenyezi Mungu atakachoniambia.”
2CH 18:14 Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?” Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa watatiwa mkononi mwako.”
2CH 18:15 Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Mwenyezi Mungu?”
2CH 18:16 Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”
2CH 18:17 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila mabaya tu?”
2CH 18:18 Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Mwenyezi Mungu: Nilimwona Mwenyezi Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama upande wa kulia na wa kushoto.
2CH 18:19 Naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu, mfalme wa Israeli, ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’ “Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.
2CH 18:20 Hatimaye, roho akajitokeza, akasimama mbele za Mwenyezi Mungu na kusema, ‘Nitamshawishi.’ “Mwenyezi Mungu akauliza, ‘Kwa njia gani?’
2CH 18:21 “Akasema, ‘Nitaenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “Mwenyezi Mungu akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’
2CH 18:22 “Kwa hiyo sasa Mwenyezi Mungu ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Mwenyezi Mungu ameamuru maafa kwa ajili yako.”
2CH 18:23 Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Mwenyezi Mungu alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”
2CH 18:24 Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapoenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”
2CH 18:25 Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme.
2CH 18:26 Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji hadi nitakaporudi salama.’ ”
2CH 18:27 Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Mwenyezi Mungu hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”
2CH 18:28 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi.
2CH 18:29 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.
2CH 18:30 Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.”
2CH 18:31 Wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati, wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele, naye Mwenyezi Mungu akamsaidia. Mungu akawaondoa kwake,
2CH 18:32 wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli nao wakaacha kumfuatilia.
2CH 18:33 Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake la vita, “Geuza gari na uniondoe katika mapigano, nimejeruhiwa.”
2CH 18:34 Vita vikaendelea mchana kutwa, naye mfalme wa Israeli akajitegemeza ndani ya gari lake kuwaelekea Waaramu hadi jioni. Basi jioni yake akafa.
2CH 19:1 Mfalme Yehoshafati wa Yuda akarudi salama kwenye jumba lake la kifalme huko Yerusalemu.
2CH 19:2 Yehu mwonaji, mwana wa Hanani, akapanda kwenda kuonana naye akamwambia Mfalme Yehoshafati, “Je, utawasaidia waovu na kuwapenda wale wanaomchukia Mwenyezi Mungu? Kwa sababu ya jambo hili, ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yako.
2CH 19:3 Hata hivyo, kuna mema yaliyoonekana kwako, kwa kuwa umeondoa katika nchi nguzo za Ashera na umeukaza moyo wako katika kumtafuta Mungu.”
2CH 19:4 Yehoshafati aliishi huko Yerusalemu, naye akatoka akaenda tena miongoni mwa watu, kuanzia Beer-Sheba hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kuwageuza wakamrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
2CH 19:5 Akawaweka waamuzi katika nchi, kwenye miji yote ya Yuda yenye ngome.
2CH 19:6 Akawaambia, “Angalieni kwa makini yale mnayotenda, kwa kuwa hamkuhukumu kwa ajili ya mwanadamu bali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ambaye yu pamoja nanyi kila mtoapo hukumu.
2CH 19:7 Basi sasa kicho cha Mwenyezi Mungu na kiwe juu yenu. Hukumuni kwa uangalifu, kwa kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, hakuna jambo la dhuluma, wala upendeleo, wala rushwa.”
2CH 19:8 Pia huko Yerusalemu, Yehoshafati akaweka baadhi ya Walawi, makuhani na viongozi wa jamaa za Waisraeli ili kutoa hukumu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuamua magomvi. Nao waliishi huko Yerusalemu.
2CH 19:9 Akawapa maagizo haya: “Ni lazima mtumike kwa uaminifu na kwa moyo wote katika kicho cha Mwenyezi Mungu.
2CH 19:10 Katika kila shauri lifikalo mbele yenu kutoka kwa ndugu zenu wanaoishi katika miji, ikiwa ni la umwagaji wa damu au mambo mengine kuhusu sheria, amri, hukumu au maagizo, inawapasa ninyi kuwaonya kwamba wasiingie katika hatia dhidi ya Mwenyezi Mungu, la sivyo ghadhabu yake itakuja juu yenu na ndugu zenu. Tendeni hivyo, nanyi hamtatenda dhambi.
2CH 19:11 “Amaria kuhani mkuu atakuwa juu yenu katika jambo lolote linalomhusu Mwenyezi Mungu naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, kiongozi wa kabila la Yuda, atakuwa juu yenu kwa jambo lolote linalomhusu mfalme, nao Walawi watatumika kama maafisa mbele yenu. Tendeni kwa ujasiri, naye Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja na wale watendao vyema.”
2CH 20:1 Ikawa baada ya jambo hili, Wamoabu na Waamoni, pamoja na baadhi ya Wameuni wakaja ili wapigane vita na Yehoshafati.
2CH 20:2 Watu fulani wakaja wakamwambia Yehoshafati, “Jeshi kubwa linakuja dhidi yako kutoka Shamu tokea ng’ambo ile nyingine ya Bahari. Tayari liko Hasason-Tamari” (yaani En-Gedi).
2CH 20:3 Yehoshafati akaogopa, akaamua kumtafuta Mwenyezi Mungu, na akatangaza kwa Yuda wote kufunga.
2CH 20:4 Watu wa Yuda wakakusanyika pamoja ili kutafuta msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakaja kutoka kila mji wa Yuda ili kumtafuta.
2CH 20:5 Kisha Yehoshafati akasimama katika kusanyiko la Yuda na Yerusalemu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, mbele ya ua mpya,
2CH 20:6 akasema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu, si wewe ndiwe uliye Mungu mbinguni? Si wewe ndiwe unayetawala juu ya falme zote za mataifa? Uweza na nguvu viko mkononi mwako, wala hakuna yeyote anayeweza kushindana nawe.
2CH 20:7 Je, si ni wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, na ukawapa wazao wa rafiki yako Ibrahimu hata milele?
2CH 20:8 Wameishi ndani yake na humo wamekujengea mahali patakatifu kwa ajili ya Jina lako, wakisema:
2CH 20:9 ‘Kama maafa yakitujia, ikiwa ni upanga, hukumu, tauni, au njaa, tutasimama mbele zako, mbele ya Hekalu hili ambalo limeitwa kwa Jina lako na kukulilia katika shida yetu, nawe utatusikia na kutuokoa.’
2CH 20:10 “Lakini sasa hawa watu wa Amoni, Moabu na Mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu Israeli wazivamie nchi zao wakati walitoka Misri; hivyo wakageukia mbali nao na hawakuwaangamiza.
2CH 20:11 Tazama jinsi wanavyotulipa kwa kuja kututupa nje ya milki uliyotupatia sisi kuwa urithi.
2CH 20:12 Ee Mungu wetu, je, wewe hutawahukumu? Kwa kuwa sisi hatuna uwezo wa kukabiliana na jeshi hili kubwa linalokuja kutushambulia. Sisi hatujui la kufanya, bali macho yetu yanakutazama wewe.”
2CH 20:13 Wanaume wote wa Yuda pamoja na wake zao, watoto wao na wadogo wao wakasimama pale mbele za Mwenyezi Mungu.
2CH 20:14 Ndipo Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya mtu mmoja jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, Mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi mzao wa Asafu alipokuwa amesimama katika kusanyiko.
2CH 20:15 Akasema: “Sikilizeni, enyi Yuda wote nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu, nawe Mfalme Yehoshafati! Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwenu, ‘Msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Kwa maana vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu.
2CH 20:16 Kesho shukeni kukabiliana nao. Watakwea kwa kupandia Genge la Sisi, nanyi mtawakuta mwisho wa bonde, kabla ya Jangwa la Yerueli.
2CH 20:17 Hamtahitaji kupigana vita hivi. Kaeni kwenye nafasi zenu, simameni imara na mkaone wokovu Mwenyezi Mungu atakaowapatia, enyi Yuda na Yerusalemu. Msiogope, wala msifadhaike. Kesho tokeni mwende mkawakabili, naye Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja nanyi.’ ”
2CH 20:18 Yehoshafati akasujudu, uso wake ukigusa chini, nao watu wote wa Yuda na Yerusalemu wakasujudu na kuabudu mbele za Mwenyezi Mungu.
2CH 20:19 Ndipo baadhi ya Walawi kutoka kwa Wakohathi na kwa wana wa Kora wakasimama na kumsifu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana.
2CH 20:20 Asubuhi na mapema wakaondoka kuelekea Jangwa la Tekoa. Walipoanza safari, Yehoshafati akasimama akasema, “Nisikilizeni, enyi Yuda, na watu wa Yerusalemu! Mwaminini Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hivyo mtathibitika, wasadikini manabii wake nanyi mtafanikiwa.”
2CH 20:21 Alipomaliza kushauriana na watu, Yehoshafati akawaweka watu wa kumwimbia Mwenyezi Mungu na kumsifu katika utukufu wa utakatifu wake walipokuwa wametangulia mbele ya jeshi, wakisema: “Mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwa fadhili zake zadumu milele.”
2CH 20:22 Walipoanza kuimba na kusifu, Mwenyezi Mungu akaweka waviziaji dhidi ya watu wa Amoni, Moabu na wale wa Mlima Seiri waliokuwa wamekuja kuishambulia Yuda, nao wakashindwa.
2CH 20:23 Watu wa Amoni na Moabu wakawainukia watu wa Mlima Seiri ili kuwaua na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kumaliza kuwachinja watu wa Seiri, wakaangamizana wao kwa wao.
2CH 20:24 Yuda walipofika katika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakaliangalia lile jeshi kubwa, wakaona ni maiti tupu zimetapakaa ardhini, wala hakuna yeyote aliyenusurika.
2CH 20:25 Hivyo Yehoshafati na watu wake wakaenda kujitwalia nyara kutoka kwao, nao wakakuta humo wingi wa mifugo, mali, mavazi na vitu vya thamani, ambavyo vilikuwa vingi zaidi ya vile walivyoweza kuchukua. Wakakusanya nyara kwa siku tatu kwa sababu zilikuwa nyingi mno.
2CH 20:26 Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Beraka, mahali walikomtukuza Mwenyezi Mungu. Ndiyo sababu linaitwa Bonde la Beraka hadi leo.
2CH 20:27 Kisha wanaume wote wa Yuda na Yerusalemu, wakiongozwa na Yehoshafati, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha, kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amewasababisha wafurahi juu ya adui zao.
2CH 20:28 Wakaingia Yerusalemu na kwenda hekaluni mwa Mwenyezi Mungu wakiwa na vinubi, zeze na tarumbeta.
2CH 20:29 Hofu ya Mungu ikazipata falme zote za nchi waliposikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyokuwa amepigana dhidi ya adui za Israeli.
2CH 20:30 Ufalme wa Yehoshafati ukawa na amani, kwa kuwa Mungu wake alikuwa amempa amani pande zote.
2CH 20:31 Hivyo Yehoshafati akatawala Yuda. Alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano alipoanza kutawala, akatawala katika Yerusalemu kwa miaka ishirini na tano. Mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi.
2CH 20:32 Alienenda katika njia za Asa baba yake wala hakuenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu.
2CH 20:33 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa, na watu wakawa bado hawajaelekeza mioyo yao kwa Mungu wa baba zao.
2CH 20:34 Matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha Yehu mwana wa Hanani, ambazo zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli.
2CH 20:35 Hatimaye Yehoshafati mfalme wa Yuda akafanya mapatano na Ahazia mfalme wa Israeli, ambaye alifanya maovu sana.
2CH 20:36 Akaungana naye kutengeneza meli nyingi za kwenda Tarshishi, nazo zilitengenezwa huko Esion-Geberi.
2CH 20:37 Ndipo Eliezeri mwana wa Dodavahu wa Maresha akatoa unabii dhidi ya Yehoshafati, akasema, “Kwa kuwa umeungana na Ahazia, Mwenyezi Mungu ataangamiza vile mlivyotengeneza.” Zile meli zikavunjika na hazikuweza kung’oa nanga ili kwenda Tarshishi.
2CH 21:1 Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mwanawe Yehoramu akawa mfalme baada yake.
2CH 21:2 Ndugu zake Yehoramu, wana wa Yehoshafati walikuwa: Azaria, Yehieli, Zekaria, Azaria, Mikaeli na Shefatia. Hawa wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli.
2CH 21:3 Baba yao alikuwa amewapa zawadi nyingi za fedha na dhahabu na vitu vya thamani, pamoja na miji yenye ngome huko Yuda, bali akampa Yehoramu ufalme kwa sababu alikuwa mzaliwa wake wa kwanza wa kiume.
2CH 21:4 Baada ya Yehoramu kujiimarisha katika ufalme wa baba yake, akawaua kwa upanga ndugu zake wote pamoja na baadhi ya wakuu wa Israeli.
2CH 21:5 Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka nane.
2CH 21:6 Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti Ahabu. Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu.
2CH 21:7 Hata hivyo, kwa sababu ya agano ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amefanya na Daudi, Mwenyezi Mungu hakuwa radhi kuangamiza nyumba ya Daudi. Mungu alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili yake na wazao wake milele.
2CH 21:8 Wakati wa utawala wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kujiwekea mfalme wao wenyewe.
2CH 21:9 Basi Yehoramu akaenda huko pamoja na maafisa wake na magari yake ya vita. Waedomu wakamzunguka yeye na majemadari wake wa magari yake ya vita, lakini akaondoka, akapenya usiku na kuwashambulia Waedomu.
2CH 21:10 Hadi leo Edomu wameasi dhidi ya Yuda. Libna pia wakaasi wakati huo huo kwa sababu Yehoramu alikuwa amemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zake.
2CH 21:11 Alikuwa pia ametengeneza mahali pa juu pa kuabudia katika vilima vya Yuda na akawa amewasababisha watu wa Yerusalemu kufanya uzinzi na akawa amewapotosha watu wa Yuda.
2CH 21:12 Yehoramu akapokea barua kutoka kwa nabii Ilya iliyosema: “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Daudi baba yako, asemalo: ‘Hukuenenda katika njia za Yehoshafati baba yako au za Asa mfalme wa Yuda.
2CH 21:13 Lakini umeenenda katika njia za wafalme wa Israeli, nawe umewaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu kuzini, kama vile nyumba ya Ahabu ilivyofanya. Pia umewaua ndugu zako mwenyewe, watu wa nyumbani mwa baba yako, watu waliokuwa bora kuliko wewe.
2CH 21:14 Hivyo basi Mwenyezi Mungu yu karibu kuwapiga watu wako, wanao, wake zako na kila kitu kilicho chako, kwa pigo zito.
2CH 21:15 Wewe mwenyewe utaugua sana kwa ugonjwa wa tumbo kwa muda mrefu, hadi ugonjwa utakaposababisha matumbo yako kutoka nje.’ ”
2CH 21:16 Mwenyezi Mungu akaamsha chuki ya Wafilisti na ya Waarabu walioishi karibu na Wakushi dhidi ya Yehoramu.
2CH 21:17 Wakaishambulia Yuda, wakaivamia na kuchukua mali yote iliyopatikana katika jumba la mfalme pamoja na wanawe na wake zake. Hakubakiziwa mwana yeyote isipokuwa Ahazia aliyekuwa mdogo wa wote.
2CH 21:18 Baada ya mambo haya yote, Mwenyezi Mungu akampiga Yehoramu kwa ugonjwa wa matumbo usio wa kupona.
2CH 21:19 Ikawa baada ya muda, mwisho wa mwaka wa pili, matumbo yake yakatoka nje kwa sababu ya ugonjwa, naye akafa katika maumivu makali sana. Watu wake hawakuwasha moto kwa heshima yake, kama walivyokuwa wamewafanyia baba zake.
2CH 21:20 Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na mbili alipokuwa mfalme, naye akatawala huko Yerusalemu miaka nane. Akafa, bila kusikitikiwa na mtu yeyote, naye akazikwa katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
2CH 22:1 Watu wa Yerusalemu wakamfanya Ahazia, mdogo wa wote wa wana wa Yerohamu, kuwa mfalme mahali pa baba yake, kwa sababu washambuliaji wa ghafula walioingia kambini pamoja na Waarabu, walikuwa wamewaua wana wakubwa wote wa Yehoramu. Kwa hiyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akaanza kutawala.
2CH 22:2 Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri.
2CH 22:3 Ahazia naye akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, kwa sababu mama yake alimshawishi kutenda uovu.
2CH 22:4 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Mwenyezi Mungu kama walivyokuwa wamefanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa baada ya kufa kwa baba yake, nyumba ya Ahabu ndio walikuwa washauri wake, kwa uangamivu wake.
2CH 22:5 Pia akafuata ushauri wao alipoenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu.
2CH 22:6 Hivyo akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu. Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.
2CH 22:7 Mungu alisababisha anguko la Ahazia kutokana na Ahazia kwenda kumwona Yoramu. Ahazia alipowasili, wakatoka pamoja na Yoramu ili kwenda kukutana na Yehu mwana wa Nimshi, ambaye Mwenyezi Mungu alikuwa amempaka mafuta kuangamiza nyumba ya Ahabu.
2CH 22:8 Yehu alipokuwa anatekeleza hukumu juu ya nyumba ya Ahabu, akawakuta wakuu wa Yuda na wana wa jamaa ya Ahazia waliokuwa wanamhudumia Ahazia, naye akawaua.
2CH 22:9 Ndipo akaenda kumsaka Ahazia, nao watu wake wakamkamata alipokuwa amejificha huko Samaria. Akaletwa kwa Yehu, naye Yehu akamuua. Wakamzika, kwani walisema, “Alikuwa mwana wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta Mwenyezi Mungu kwa moyo wake wote.” Hivyo hapakuwa na mtu mwenye uwezo katika nyumba ya Ahazia aliyeweza kushika ufalme.
2CH 22:10 Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuangamiza jamaa yote ya mfalme ya nyumba ya Yuda.
2CH 22:11 Lakini Yehosheba, binti Mfalme Yehoramu, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala. Kwa kuwa Yehosheba, aliyekuwa binti Mfalme Yehoramu, na pia alikuwa mke wa kuhani Yehoyada, alikuwa dada yake Ahazia, akamficha huyo mtoto ili Athalia asimuue.
2CH 22:12 Alibaki amefichwa pamoja nao katika Hekalu la Mungu kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.
2CH 23:1 Katika mwaka wa saba, Yehoyada akaonesha nguvu zake. Alifanya agano na wakuu wa vikosi vya mamia: yaani Azaria mwana wa Yerohamu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri.
2CH 23:2 Wakazunguka katika Yuda yote na kukusanya Walawi na viongozi wa jamaa za Israeli kutoka miji yote. Walipofika Yerusalemu,
2CH 23:3 kusanyiko lote wakafanya agano na mfalme katika Hekalu la Mungu. Yehoyada akawaambia, “Mwana wa mfalme atatawala, kama Mwenyezi Mungu alivyoahidi kuhusu wazao wa Daudi.
2CH 23:4 Basi hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Theluthi yenu makuhani na Walawi ambao mnaingia zamu siku ya Sabato mtalinda milangoni,
2CH 23:5 theluthi yenu mtalinda jumba la kifalme, na theluthi nyingine mtalinda Lango la Msingi. Walinzi wengine wote mwe ndani ya nyua za Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 23:6 Hakuna mtu yeyote ataingia katika Hekalu la Mwenyezi Mungu isipokuwa makuhani na Walawi walio kwenye zamu. Wao wanaweza kuingia kwa sababu ni watakatifu, lakini watu wengine wote itawapasa kulinda kile walichoamriwa na Mwenyezi Mungu.
2CH 23:7 Walawi watajipanga kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha zake mkononi. Mtu mwingine yeyote aingiaye Hekaluni lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”
2CH 23:8 Walawi na watu wote wa Yuda wakafanya vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, kwa sababu kuhani Yehoyada hakuruhusu kikosi chochote kiondoke.
2CH 23:9 Kisha kuhani Yehoyada akawapa wakuu wa vikosi vya mamia mikuki na ngao kubwa na ndogo zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu.
2CH 23:10 Akawapanga walinzi wote kumzunguka mfalme, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.
2CH 23:11 Yehoyada na wanawe wakamtoa Yoashi mwana wa mfalme nje na kumvika taji. Wakampa nakala ya agano na kumtangaza kuwa mfalme. Wakampaka mafuta na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”
2CH 23:12 Athalia aliposikia kelele za watu wakikimbia na kumsifu mfalme, akawaendea watu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 23:13 Akaangalia, na tazama, mfalme alikuwa amesimama karibu na nguzo yake kwenye ingilio. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta, na waimbaji waliokuwa na vyombo vya uimbaji walikuwa wakiongoza nyimbo za sifa. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”
2CH 23:14 Kuhani Yehoyada akawatuma majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, na kuwaambia: “Mleteni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Msimuulie ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.”
2CH 23:15 Kwa hiyo wakamkamata alipofika kwenye ingilio la Lango la Farasi, katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuua hapo.
2CH 23:16 Kisha Yehoyada akafanya agano kwamba yeye na watu wote na mfalme watakuwa watu wa Mwenyezi Mungu.
2CH 23:17 Watu wote wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu pamoja na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu.
2CH 23:18 Yehoyada akaweka uangalizi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu mikononi mwa makuhani, hao Walawi, ambao Mfalme Daudi alikuwa amewagawa ili wahudumu hekaluni kwa ajili ya kutoa sadaka za kuteketezwa za Mwenyezi Mungu, kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, kwa kushangilia na kuimba, vile Daudi alikuwa ameagiza.
2CH 23:19 Pia akawaweka mabawabu kwenye malango ya Hekalu la Mwenyezi Mungu ili kwa vyovyote asije akaingia mtu yeyote aliye najisi.
2CH 23:20 Akawachukua majemadari wa mamia, watu waheshimiwa, viongozi wa watu pamoja na watu wote wa nchi na kumteremsha mfalme kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Wakaingia kwenye jumba la mfalme kupitia Lango la Juu na kumkalisha mfalme kwenye kiti cha ufalme;
2CH 23:21 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga.
2CH 24:1 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba.
2CH 24:2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu miaka yote ya Yehoyada kuhani.
2CH 24:3 Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike.
2CH 24:4 Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 24:5 Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi.
2CH 24:6 Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema la Ushuhuda?”
2CH 24:7 Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu kwa mabaali.
2CH 24:8 Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 24:9 Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu, kwamba inapasa wamletee Mwenyezi Mungu kodi ambayo Musa, mtumishi wa Mwenyezi Mungu, alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani.
2CH 24:10 Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha hadi likajaa.
2CH 24:11 Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana.
2CH 24:12 Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la Mwenyezi Mungu, pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 24:13 Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la Mwenyezi Mungu likarudi katika hali yake ya awali, na wakaliimarisha.
2CH 24:14 Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu: Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada akiwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 24:15 Basi Yehoyada alikuwa mzee aliyeshiba siku alipofariki. Alikufa akiwa na umri wa miaka mia moja na thelathini.
2CH 24:16 Wakamzika pamoja na wafalme katika Mji wa Daudi, kwa sababu ya mema aliyokuwa ametenda katika Israeli kwa ajili ya Mungu na Hekalu lake.
2CH 24:17 Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walikuja kumpa mfalme heshima, naye akawasikiliza.
2CH 24:18 Wakaacha Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, wakaabudu nguzo za maashera na sanamu. Kwa sababu ya hatia yao, hasira ya Mungu ikawajia Yuda na Yerusalemu.
2CH 24:19 Ingawa Mwenyezi Mungu aliwatuma manabii wawarudishe watu kwake na ingawa waliwaonya, hawakuwasikiliza.
2CH 24:20 Ndipo Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada kuhani. Akasimama mbele ya watu akasema, “Hili ndilo asemalo Mungu, ‘Kwa nini mnakataa kuzitii amri za Mwenyezi Mungu? Hamtafanikiwa kwa kuwa mmemwacha Mwenyezi Mungu, naye amewaacha ninyi.’ ”
2CH 24:21 Lakini wakapanga njama dhidi yake, na kwa amri ya mfalme wakampiga kwa mawe hadi akafa katika ua wa Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 24:22 Mfalme Yoashi hakukumbuka wema aliotendewa na Yehoyada baba yake Zekaria, ila alimuua mwanawe, ambaye alisema wakati akiwa amelala akingojea kufa, “Mwenyezi Mungu na alione hili na alipize kisasi.”
2CH 24:23 Mwishoni mwa ule mwaka, jeshi la Waaramu likaja dhidi ya Yoashi, likavamia Yuda na Yerusalemu na kuwaua viongozi wote wa watu. Wakapeleka nyara zao zote kwa mfalme wao huko Dameski.
2CH 24:24 Ingawa jeshi la Waaramu lilikuwa limekuja na watu wachache tu, Mwenyezi Mungu akatia mikononi mwao jeshi kubwa kuliko lao. Kwa sababu Yuda walikuwa wamemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, hukumu ilitekelezwa juu ya Yoashi.
2CH 24:25 Waaramu walipoondoka, walimwacha Yoashi akiwa mgonjwa sana. Maafisa wake wakapanga njama dhidi yake kwa sababu alikuwa amemuua mwana wa Kuhani Yehoyada, nao wakamuua kitandani mwake. Hivyo akafa, wakamzika katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
2CH 24:26 Wale waliopanga njama dhidi yake walikuwa Zabadi mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, na Yehozabadi mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabu.
2CH 24:27 Kwa habari za wanawe, unabii mwingi kumhusu na kumbukumbu za kutengenezwa upya kwa Hekalu la Mungu, zimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme. Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 25:1 Amazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani kutoka Yerusalemu.
2CH 25:2 Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini sio kwa moyo wake wote.
2CH 25:3 Baada ya ufalme kuimarika mkononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake.
2CH 25:4 Hata hivyo hakuwaua watoto wao, lakini akafanya sawasawa na ilivyoandikwa katika Torati, katika Kitabu cha Musa, ambako Mwenyezi Mungu aliamuru: “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”
2CH 25:5 Amazia akawaita watu wa Yuda pamoja, akawaweka chini ya majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia kufuatana na jamaa zao katika Yuda yote na Benyamini. Kisha akawahesabu wale wenye umri wa miaka ishirini au zaidi na akakuta kwamba walikuwa wanaume elfu mia tatu walio tayari kwa utumishi wa jeshi, wenye uwezo wa kutumia mkuki na ngao.
2CH 25:6 Akawaajiri pia wapiganaji elfu mia moja kutoka Israeli kwa talanta mia moja za fedha.
2CH 25:7 Lakini mtu wa Mungu akamjia na kumwambia, “Ee mfalme, haya majeshi kutoka Israeli kamwe usiyaruhusu yaende pamoja na wewe, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hayuko pamoja na Israeli, wala hayupo pamoja na yeyote wa watu wa Efraimu.
2CH 25:8 Hata ukienda na kupigana kwa ujasiri katika vita, Mungu atakufanya ukimbie mbele ya adui, kwa kuwa Mungu anao uwezo wa kusaidia au wa kuangusha.”
2CH 25:9 Amazia akamuuliza yule mtu wa Mungu, “Lakini itakuwaje kwa zile talanta mia moja za fedha nilizolipa kwa ajili ya haya majeshi ya Israeli?” Yule mtu wa Mungu akajibu, “Mwenyezi Mungu aweza kukupa zaidi ya hizo.”
2CH 25:10 Hivyo Amazia akayaondoa yale majeshi yaliyokuwa yamekuja kutoka Efraimu na kuyarudisha nyumbani. Waliwakasirikia sana Yuda, nao wakarudi nyumbani wakiwa na hasira kali.
2CH 25:11 Ndipo Amazia akajitia nguvu na kuliongoza jeshi lake hadi Bonde la Chumvi, ambako aliwaua watu elfu kumi wa Seiri.
2CH 25:12 Jeshi la Yuda pia likawateka watu elfu kumi wakiwa hai, likawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini kwa nguvu, wote wakavunjika vipande vipande.
2CH 25:13 Wakati huo, wanajeshi waliorudishwa na Amazia, ambao hakuwaruhusu kushiriki katika vita, walivamia miji ya Yuda kuanzia Samaria hata Beth-Horoni. Wakawaua watu elfu tatu na kuchukua nyara nyingi sana.
2CH 25:14 Amazia aliporudi kutoka kuwaua Waedomu, alileta pia kutoka huko miungu ya watu wa Seiri. Akaisimamisha kama miungu yake mwenyewe, akaisujudia na kuitolea sadaka za kuteketezwa.
2CH 25:15 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Amazia, naye akamtuma nabii kwake, ambaye alisema: “Kwa nini unauliza kwa miungu ya hawa watu, ambayo haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mkononi mwako?”
2CH 25:16 Nabii alipokuwa angali anazungumza, mfalme akamwambia, “Je, wewe tumekuchagua kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza! Kwa nini uuawe?” Hivyo nabii akanyamaza lakini akasema, “Najua kuwa Mungu ameazimia kukuangamiza kwa sababu umefanya jambo hili na hukusikiliza ushauri wangu.”
2CH 25:17 Baada ya Amazia mfalme wa Yuda kushauriana na washauri wake, akatuma ujumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, kusema: “Njoo tukabiliane uso kwa uso.”
2CH 25:18 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda, “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti.
2CH 25:19 Wewe unasema moyoni mwako kwamba umemshinda Edomu, nawe sasa unajigamba na kujivuna. Lakini kaa nyumbani mwako! Kwa nini utafute matatizo na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
2CH 25:20 Hata hivyo, Amazia hakutaka kusikia, kwa kuwa Mungu alifanya hivyo ili awatie mikononi mwa Yehoashi, kwa sababu waliitafuta miungu ya Edomu.
2CH 25:21 Hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea kuwashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakabiliana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda.
2CH 25:22 Yuda ikashindwa na Israeli na kila mtu akakimbilia nyumbani mwake.
2CH 25:23 Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akamleta Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa mia nne.
2CH 25:24 Akachukua dhahabu yote, fedha na vyombo vyote vilivyopatikana katika Hekalu la Mungu, ambavyo vilikuwa chini ya uangalizi wa Obed-Edomu, pamoja na hazina za jumba la mfalme na mateka, kisha akarudi Samaria.
2CH 25:25 Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na tano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli.
2CH 25:26 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amazia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na wa Israeli?
2CH 25:27 Kuanzia wakati Amazia alipogeuka na kuacha kumfuata Mwenyezi Mungu, walipanga njama dhidi yake huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi. Lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuua huko.
2CH 25:28 Akarudishwa kwa farasi, akazikwa na baba zake katika Mji wa Yuda.
2CH 26:1 Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake.
2CH 26:2 Ndiye aliijenga upya Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala na baba zake.
2CH 26:3 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na mbili. Mama yake aliitwa Yekolia, kutoka Yerusalemu.
2CH 26:4 Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, vile Amazia baba yake alivyofanya.
2CH 26:5 Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu alimfanikisha.
2CH 26:6 Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi, na mahali pengine katikati ya Wafilisti.
2CH 26:7 Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni.
2CH 26:8 Waamoni wakamletea Uzia ushuru, na umaarufu wake ukaenea hadi mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa na nguvu sana.
2CH 26:9 Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome.
2CH 26:10 Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilima na katika nchi tambarare. Alikuwa na watu waliofanya kazi katika mashamba yake, na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo.
2CH 26:11 Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmoja wa maafisa wa mfalme.
2CH 26:12 Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza wapiganaji walikuwa elfu mbili na mia sita.
2CH 26:13 Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu na saba na mia tano waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake.
2CH 26:14 Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, dirii, pinde na mawe ya kombeo.
2CH 26:15 Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno hadi akawa na nguvu sana.
2CH 26:16 Lakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, naye akaingia hekaluni mwa Mwenyezi Mungu ili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba.
2CH 26:17 Azaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini wa Mwenyezi Mungu wenye ujasiri wakamfuata ndani.
2CH 26:18 Wakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukizia Mwenyezi Mungu uvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Haruni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa na Bwana Mwenyezi Mungu.”
2CH 26:19 Uzia, aliyekuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, ukoma ukamtokea kwenye paji la uso wake.
2CH 26:20 Azaria kuhani mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma pajini lake, wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alitamani kuondoka kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amempiga.
2CH 26:21 Mfalme Uzia alikuwa na ukoma hadi siku ya kufa kwake. Akatengwa katika nyumba ya pekee akiwa mwenye ukoma, naye akawa ametengwa kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Yothamu mwanawe akawa msimamizi wa jumba la mfalme, pia akawaongoza watu wa nchi.
2CH 26:22 Matukio mengine ya utawala wa Uzia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa na nabii Isaya mwana wa Amozi.
2CH 26:23 Uzia akalala na baba zake, akazikwa karibu nao katika shamba la kuzikia lililokuwa mali ya wafalme, kwa kuwa watu walisema, “Alikuwa na ukoma.” Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 27:1 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki.
2CH 27:2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya, lakini tofauti na yeye, hakuingilia huduma za hekaluni mwa Mwenyezi Mungu. Lakini hata hivyo, watu wakaendelea na desturi zao mbaya.
2CH 27:3 Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Mwenyezi Mungu na kufanya kazi kubwa kwenye ukuta katika kilima cha Ofeli.
2CH 27:4 Akajenga miji katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na ngome na minara mwituni.
2CH 27:5 Yothamu akafanya vita na mfalme wa Waamoni na kumshinda. Mwaka ule Waamoni wakamlipa talanta mia moja za fedha, kori elfu kumi za ngano, na kori elfu kumi za shayiri. Waamoni wakamletea kiasi hicho hicho mwaka wa pili na wa tatu.
2CH 27:6 Yothamu akaendelea kuwa na nguvu kwa sababu alienenda kwa ukamilifu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
2CH 27:7 Matukio mengine ya utawala wa Yothamu, pamoja na vita vyake vyote na vitu vingine alivyofanya, vimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.
2CH 27:8 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita.
2CH 27:9 Yothamu akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 28:1 Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala. Akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu.
2CH 28:2 Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, na pia akasubu sanamu kwa ajili ya kuabudu Mabaali.
2CH 28:3 Akatoa sadaka za kuteketezwa katika Bonde la Ben-Hinomu, na kuwatoa kafara watoto wake kwa kuwateketeza kwa moto, akifuata njia za machukizo za yale mataifa Mwenyezi Mungu aliyoyafukuza humo mbele ya Waisraeli.
2CH 28:4 Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda.
2CH 28:5 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akamtia mikononi mwa mfalme wa Aramu. Waaramu wakamshinda, wakachukua watu wake wengi mateka na kuwaleta Dameski. Tena alitiwa mikononi mwa mfalme wa Israeli, ambaye aliwaua watu wake wengi.
2CH 28:6 Kwa siku moja Peka mwana wa Remalia aliwaua askari elfu mia moja na ishirini katika Yuda, kwa kuwa Yuda walikuwa wamemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
2CH 28:7 Zikri, askari shujaa Mwefraimu, akamuua Maaseya mwana wa mfalme, Azrikamu mkuu wa jumba la kifalme na Elkana aliyekuwa wa pili kwa mfalme.
2CH 28:8 Waisraeli wakawachukua mateka kutoka ndugu zao, watu wapatao elfu mia mbili, wakiwa wanawake, pamoja na watoto wa kiume na wa kike. Wakachukua pia kiasi kikubwa cha nyara, ambazo walirudi nazo Samaria.
2CH 28:9 Lakini huko kulikuwa na nabii wa Mwenyezi Mungu aliyeitwa Odedi; akaondoka ili kukutana na jeshi liliporejea Samaria. Akawaambia, “Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, aliwatia mikononi mwenu. Lakini mmewachinja kwa hasira ambayo imefika hadi mbinguni.
2CH 28:10 Nanyi sasa mnakusudia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Lakini ninyi je, hamna pia hatia ya dhambi mliyotenda dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu?
2CH 28:11 Basi nisikilizeni! Mkawarudishe mateka mliowachukua kutoka kwa ndugu zenu, kwa kuwa hasira kali ya Mwenyezi Mungu iko juu yenu.”
2CH 28:12 Ndipo baadhi ya viongozi katika Efraimu, yaani Azaria mwana wa Yehohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, wakawapinga wale waliokuwa wakitoka vitani.
2CH 28:13 Wakamwambia, “Hamna ruhusa kuwaleta hao wafungwa hapa, ama sivyo tutakuwa na hatia mbele za Mwenyezi Mungu. Je, mnataka kuongezea dhambi yetu na hatia yetu? Kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa, nayo hasira kali ya Mwenyezi Mungu iko juu ya Israeli.”
2CH 28:14 Hivyo wale askari wakawaacha wale mateka pamoja na nyara mbele ya hao maafisa na kusanyiko lote.
2CH 28:15 Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukua wale mateka, na kutoka zile nyara wakachukua mavazi, wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.
2CH 28:16 Wakati ule, Mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada.
2CH 28:17 Waedomu walikuwa wamekuja tena na kuwashambulia Yuda na kuchukua mateka.
2CH 28:18 Pia Wafilisti walikuwa wameshambulia miji iliyokuwa chini ya vilima na katika miji ya Negebu ya Yuda. Wakatwaa Beth-Shemeshi, Aiyaloni, Gederothi, Soko pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake, Gimzo pia pamoja na vijiji vyake, wakaishi humo.
2CH 28:19 Mwenyezi Mungu aliishusha Yuda kwa sababu ya Ahazi mfalme wa Israeli, kwa kuwa alikuwa ameongeza uovu katika Yuda na kumkosea Mwenyezi Mungu mno.
2CH 28:20 Hivyo Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru akaja kumtesa badala ya kumsaidia.
2CH 28:21 Ahazi akachukua baadhi ya vitu kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu, jumba la kifalme na kutoka kwa wakuu wake na kumpa mfalme wa Ashuru kama ushuru, lakini hilo halikumsaidia.
2CH 28:22 Katika wakati wake wa mateso Mfalme Ahazi akazidi kukosa uaminifu kwa Mwenyezi Mungu.
2CH 28:23 Akatoa sadaka kwa miungu ya Dameski, waliokuwa wamemshinda, kwa kuwa aliwaza, “Kwa kuwa miungu ya mfalme wa Aramu imewasaidia wao, nitaitolea dhabihu ili inisaidie.” Lakini haya ndio yaliyokuwa maangamizi yake na Waisraeli wote.
2CH 28:24 Ahazi akakusanya vyombo vya nyumba ya Mungu na kuvivunja vipande vipande. Akafunga milango ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na kusimamisha madhabahu katika kila njia panda ya barabara za Yerusalemu.
2CH 28:25 Katika kila mji wa Yuda akajenga mahali pa juu pa kuabudia ili kuitolea miungu mingine sadaka za kuteketezwa na kuchochea hasira ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zake.
2CH 28:26 Matukio mengine ya utawala wake na njia zake nyingine zote, kuanzia mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
2CH 28:27 Ahazi akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Yerusalemu, lakini hawakumleta kwenye makaburi ya wafalme wa Israeli. Naye Hezekia mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 29:1 Hezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria.
2CH 29:2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu kama Daudi baba yake alivyofanya.
2CH 29:3 Katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa utawala wake, alifungua milango ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, na kuikarabati.
2CH 29:4 Akawaingiza makuhani na Walawi ndani na kuwakutanisha katika uwanja upande wa mashariki
2CH 29:5 na kusema: “Nisikilizeni mimi, enyi Walawi! Jitakaseni nafsi zenu sasa, mkalitakase Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu. Ondoeni uchafu wote kutoka mahali patakatifu.
2CH 29:6 Baba zetu hawakuwa waaminifu, walifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na wakamwacha yeye. Wakageuza nyuso zao mbali na Maskani ya Mwenyezi Mungu wakamgeuzia visogo vyao.
2CH 29:7 Pia walifunga milango ya ukumbi wa Hekalu na kuzima taa zake. Hawakufukiza uvumba wala kutoa sadaka yoyote ya kuteketezwa katika mahali patakatifu kwa Mungu wa Israeli.
2CH 29:8 Kwa hiyo, hasira ya Mwenyezi Mungu ikashuka juu ya Yuda na Yerusalemu, naye akawa amewafanya kitu cha kutisha, cha kushangaza na kitu cha kufanyia mzaha kama mnavyoona kwa macho yenu wenyewe.
2CH 29:9 Hii ndiyo sababu baba zetu wameanguka kwa upanga na ndiyo sababu wana wetu wa kiume na wa kike, na pia wake zetu wamekuwa mateka.
2CH 29:10 Sasa ninadhamiria moyoni mwangu kufanya agano na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nasi.
2CH 29:11 Wanangu, basi msipuuze jambo hili sasa, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewachagua ninyi msimame mbele zake na kumtumikia, mkawe watumishi wake na mkamfukizie uvumba.”
2CH 29:12 Ndipo Walawi wafuatao wakaanza kazi: Kutoka kwa Wakohathi, Mahathi mwana wa Amasai na Yoeli mwana wa Azaria; kutoka kwa Wamerari, Kishi mwana wa Abdi na Azaria mwana wa Yahaleleli; kutoka kwa Wagershoni, Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;
2CH 29:13 kutoka kwa wana wa Elisafani, Shimri na Yeieli; kutoka kwa wana wa Asafu, Zekaria na Matania;
2CH 29:14 kutoka kwa wana wa Hemani, Yehieli na Shimei; kutoka kwa wana wa Yeduthuni, Shemaya na Uzieli.
2CH 29:15 Walipomaliza kuwakusanya ndugu zao na kujiweka wakfu, wakaingia ndani ili kutakasa Hekalu la Mwenyezi Mungu, kama vile mfalme alivyokuwa ameagiza, kwa kufuata neno la Mwenyezi Mungu.
2CH 29:16 Makuhani wakaingia patakatifu pa Hekalu la Mwenyezi Mungu ili kupatakasa. Wakatoa nje penye ua wa Hekalu la Mungu kila kitu kichafu walichokikuta kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu. Walawi wakavichukua na kuvipeleka nje katika Bonde la Kidroni.
2CH 29:17 Walianza kazi ya utakaso siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza na kufikia siku ya nane ya mwezi huo wakawa wamefikia kwenye ukumbi wa Mwenyezi Mungu. Kwa siku zingine nane wakalitakasa Hekalu la Mwenyezi Mungu lenyewe, wakakamilisha katika siku ya kumi na sita ya mwezi huo wa kwanza.
2CH 29:18 Kisha wakaingia ndani kwa Mfalme Hezekia kutoa habari na kusema: “Tumelitakasa Hekalu la Mwenyezi Mungu lote, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa pamoja na vyombo vyake vyote, meza ya kupanga mikate iliyowekwa wakfu, pamoja na vyombo vyake vyote.
2CH 29:19 Tumeviandaa na kuvitakasa vyombo vyote ambavyo Mfalme Ahazi, kwa kukosa uaminifu kwake, aliviondoa alipokuwa mfalme. Sasa viko mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu.”
2CH 29:20 Ndipo Mfalme Hezekia akainuka asubuhi na mapema, akakusanya maafisa wa mji wakakwea hekaluni mwa Mwenyezi Mungu.
2CH 29:21 Wakaleta mafahali saba, kondoo dume saba, wana-kondoo dume saba na beberu saba kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, kwa ajili ya mahali patakatifu na kwa ajili ya Yuda. Mfalme akawaamuru makuhani, wazao wa Haruni, kuvitoa vitu hivyo sadaka katika madhabahu ya Mwenyezi Mungu.
2CH 29:22 Hivyo wakachinja wale mafahali, nao makuhani wakachukua ile damu na kuinyunyiza kwenye madhabahu, halafu wakawachinja wale kondoo dume saba na kunyunyiza hiyo damu yao kwenye madhabahu, kisha wakawachinja wale wana-kondoo dume na kunyunyiza damu yao kwenye madhabahu.
2CH 29:23 Wale beberu waliokuwa kwa ajili ya sadaka ya dhambi wakaletwa mbele ya mfalme na kusanyiko nao wakaweka mikono yao juu hao beberu.
2CH 29:24 Ndipo makuhani wakawachinja hao beberu na kuweka damu yao kwenye madhabahu kwa ajili ya sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli wote, kwa sababu mfalme alikuwa ameamuru hiyo sadaka ya kuteketezwa na hiyo sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote.
2CH 29:25 Akawaweka Walawi kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu wakiwa na matoazi, vinubi na zeze kama ilivyoagizwa na Daudi na Gadi mwonaji wa mfalme pamoja na nabii Nathani kwani hili lilikuwa limeamriwa na Mwenyezi Mungu kupitia manabii wake.
2CH 29:26 Hivyo Walawi wakasimama tayari wakiwa na ala za uimbaji za Daudi na makuhani walikuwa na tarumbeta zao.
2CH 29:27 Hezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbia Mwenyezi Mungu pamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli.
2CH 29:28 Kusanyiko lote kusujudu katika kuabudu, huku waimbaji wakiimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea hadi walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.
2CH 29:29 Walipomaliza kutoa sadaka, mfalme na kila mtu aliyekuwa pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu.
2CH 29:30 Mfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifu Mwenyezi Mungu kwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha, nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.
2CH 29:31 Kisha Hezekia akasema, “Sasa mmejiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu. Njooni mlete dhabihu na sadaka za shukrani Hekaluni mwa Mwenyezi Mungu.” Hivyo kusanyiko likaleta dhabihu na sadaka za shukrani, nao wote waliokuwa na mioyo ya hiari wakaleta sadaka za kuteketezwa.
2CH 29:32 Idadi ya sadaka za kuteketezwa zilizoletwa na kusanyiko zilikuwa mafahali sabini, kondoo dume mia moja, na wana-kondoo dume mia mbili. Wote hawa walikuwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu.
2CH 29:33 Wanyama waliowekwa wakfu kwa sadaka ya kuteketezwa walikuwa mafahali mia sita, pamoja na kondoo na mbuzi elfu tatu.
2CH 29:34 Lakini makuhani walikuwa wachache sana kuweza kuchuna wale wanyama wote wa sadaka za kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia hadi kazi ile ikakamilika na hadi makuhani wengine walipowekwa wakfu, kwa kuwa Walawi walikuwa makini kujiweka wakfu kuliko makuhani.
2CH 29:35 Kulikuwa na sadaka nyingi za kuteketezwa, pamoja na mafuta ya wanyama ya sadaka za amani na sadaka za kinywaji ambazo ziliambatana na sadaka za kuteketezwa. Kwa hiyo huduma ya Hekalu la Mwenyezi Mungu ikarudishwa kwa upya.
2CH 29:36 Hezekia pamoja na watu wote wakafurahi kwa sababu ya lile Mungu alilolifanya kwa ajili ya watu wake, kwa kuwa lilitendeka papo hapo.
2CH 30:1 Hezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwa Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
2CH 30:2 Mfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili.
2CH 30:3 Kwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida.
2CH 30:4 Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote.
2CH 30:5 Wakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.
2CH 30:6 Kwa amri ya mfalme, matarishi wakazunguka Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake, zilizoandikwa: “Watu wa Israeli, mrudieni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
2CH 30:7 Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kutisha, kama mnavyoona.
2CH 30:8 Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Mwenyezi Mungu. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi.
2CH 30:9 Mkimrudia Mwenyezi Mungu, ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama mkimrudia yeye.”
2CH 30:10 Matarishi wakaenda mji hadi mji katika Efraimu na Manase, wakafika Zabuloni, lakini watu wakawadharau na kuwadhihaki.
2CH 30:11 Lakini, baadhi ya watu wa Asheri, Manase na Zabuloni, wakajinyenyekeza wakaja Yerusalemu.
2CH 30:12 Pia katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa juu ya watu kuwapa umoja katika kutenda yale ambayo mfalme na maafisa wake waliwaamuru, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu.
2CH 30:13 Basi umati mkubwa wa watu wakakusanyika huko Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu katika mwezi wa pili.
2CH 30:14 Wakajitia kazini kuyaondoa yale madhabahu yaliyokuwa huko Yerusalemu, wakayaondoa pia yale madhabahu ya kufukizia uvumba kwa miungu na kuyatupa Bonde la Kidroni.
2CH 30:15 Kisha wakamchinja mwana-kondoo wa Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketezwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 30:16 Kisha wakachukua nafasi zao za kawaida kama ilivyoelezwa katika Torati ya Musa mtu wa Mungu. Makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa na Walawi.
2CH 30:17 Kwa kuwa wengi waliokuwa katika lile kusanyiko walikuwa hawajajitakasa, iliwapasa Walawi wachinje wana-kondoo wengine wa Pasaka kwa ajili ya wale watu ambao hawakuwa wametakaswa, ili kuwatakasa kwa Mwenyezi Mungu.
2CH 30:18 Ingawa watu wengi miongoni mwa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zabuloni walikuwa hawajajitakasa, hata hivyo walikula Pasaka kinyume na ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, “Mwenyezi Mungu, ambaye ni mwema na amsamehe kila mmoja
2CH 30:19 ambaye anauelekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zake, hata kama yeye si safi kulingana na sheria za mahali patakatifu.”
2CH 30:20 Naye Mwenyezi Mungu akamsikia Hezekia akawaponya watu.
2CH 30:21 Waisraeli waliokuwa Yerusalemu wakaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa muda wa siku saba, nao Walawi na makuhani walikuwa wakiimba kila siku, wakiwa na ala za uimbaji za kumsifu Mwenyezi Mungu.
2CH 30:22 Hezekia akazungumza akiwatia moyo Walawi wote, ambao walionesha ustadi katika kumtumikia Mwenyezi Mungu. Hivyo watu wakala chakula cha sikukuu kwa siku saba, wakitoa sadaka za amani na kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
2CH 30:23 Kisha kusanyiko lote wakakubali kuendelea na sikukuu kwa siku saba zaidi; kwa hiyo, kwa siku saba nyingine wakaendelea kuiadhimisha kwa furaha.
2CH 30:24 Hezekia, mfalme wa Yuda akatoa mafahali elfu moja, kondoo na mbuzi elfu saba kwa ajili ya kusanyiko, nao maafisa wakatoa mafahali elfu moja, pamoja na kondoo na mbuzi elfu kumi. Idadi kubwa ya makuhani wakajiweka wakfu.
2CH 30:25 Kusanyiko la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi, na wote waliokusanyika kutoka Israeli, pamoja na wageni waliotoka Israeli na wale walioishi Yuda, wote wakafurahi.
2CH 30:26 Kulikuwa na furaha kubwa katika Yerusalemu, kwa sababu tangu siku za Mfalme Sulemani mwana wa Daudi mfalme wa Israeli halijakuwepo jambo kama hili huko Yerusalemu.
2CH 30:27 Ndipo makuhani na Walawi wakasimama wakawabariki watu, naye Mungu akawasikia, kwa sababu maombi yao yalifika mbinguni, makao yake matakatifu.
2CH 31:1 Baada ya mambo haya yote kumalizika, Waisraeli ambao walikuwa huko wakaenda kwenye miji ya Yuda, wakayavunja yale mawe ya kuabudia na kuzikatakata zile nguzo za Ashera. Wakabomoa mahali pa juu pa kuabudia pamoja na madhabahu zake kila mahali katika Yuda na Benyamini, na katika Efraimu na Manase. Baada ya kuviharibu hivi vyote, Waisraeli wakarudi miji yao wenyewe na kwenye milki zao.
2CH 31:2 Hezekia akawapanga makuhani na Walawi katika migawanyo, kila mgawanyo kulingana na wajibu wao, kama ni makuhani au Walawi, ili kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, kuhudumu, kushukuru na kuimba sifa katika malango ya makao ya Mwenyezi Mungu.
2CH 31:3 Mfalme akatoa matoleo kutoka mali yake mwenyewe kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni na sadaka za kuteketezwa kwa siku za Sabato, kwa Sikukuu za Mwezi Mwandamo na kwa ajili ya sikukuu zilizoamriwa kama ilivyoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu.
2CH 31:4 Akawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Torati ya Mwenyezi Mungu.
2CH 31:5 Mara tu baada ya kutolewa tangazo hilo, Waisraeli wakatoa kwa ukarimu malimbuko ya nafaka zao, divai mpya, mafuta na asali pamoja na vyote vilivyotoka mashambani. Wakaleta kiasi kikubwa cha fungu la kumi la kila kitu.
2CH 31:6 Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda wakaleta pia fungu la kumi la makundi yao ya ng’ombe na makundi ya kondoo na mbuzi pia na fungu la kumi la vitu vitakatifu vilivyowekwa wakfu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na kuvikusanya katika malundo.
2CH 31:7 Wakaanza kufanya haya katika mwezi wa tatu na kumaliza katika mwezi wa saba.
2CH 31:8 Hezekia na maafisa wake walipokuja na kuona yale malundo, wakamsifu Mwenyezi Mungu na kuwabariki watu wake Israeli.
2CH 31:9 Hezekia akawauliza makuhani na Walawi kuhusu yale malundo,
2CH 31:10 naye Azaria aliyekuwa kuhani mkuu, kutoka jamaa ya Sadoki, akajibu, “Tangu watu walipoanza kuleta sadaka zao katika Hekalu la Mwenyezi Mungu tumekuwa na chakula cha kutosha na vingi vya kuweka akiba kwa sababu Mwenyezi Mungu amewabariki watu wake, hivyo tumekuwa na kiasi kingi kilichobaki.”
2CH 31:11 Hezekia akatoa agizo la kutengeneza vyumba vya ghala katika Hekalu la Mwenyezi Mungu nalo hili likafanyika.
2CH 31:12 Kisha kwa uaminifu wakaleta sadaka zao, mafungu yao ya kumi na vitu vilivyowekwa wakfu. Konania Mlawi, ndiye alikuwa msimamizi wa vitu hivi na Shimei ndugu yake ndiye alikuwa msaidizi wake.
2CH 31:13 Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yeremothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya walikuwa waangalizi chini ya Konania na Shimei ndugu yake, waliokuwa wamewekwa na Mfalme Hezekia na Azaria, afisa msimamizi wa Hekalu la Mungu.
2CH 31:14 Kore mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa Lango la Mashariki, alikuwa msimamizi wa sadaka za hiari zilizotolewa kwa Mungu, akiyagawanya hayo matoleo yaliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu na pia zile sadaka zilizowekwa wakfu.
2CH 31:15 Edeni, Miniamini, Yeshua, Shemaya, Amaria na Shekania walimsaidia kwa uaminifu katika miji ya makuhani, wakiwagawia makuhani wenzao kufuatana na migawanyo yao, wazee kwa vijana sawasawa.
2CH 31:16 Zaidi ya hao wakawagawia wanaume wenye umri wa miaka mitatu au zaidi ambao majina yao yalikuwa kwenye orodha ya vizazi, wale wote ambao wangeingia katika Hekalu la Mwenyezi Mungu ili kufanya kazi zao mbalimbali za kila siku kulingana na wajibu katika mgawanyo wao.
2CH 31:17 Kuandikishwa kwa makuhani kulikuwa kwa kufuata chimbuko la nyumba za baba zao na Walawi kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi ilikuwa kufuatana na huduma zao, kwa migawanyo yao.
2CH 31:18 Makuhani waliandikishwa pamoja na watoto wao wadogo, wake zao, watoto wao wa kiume na wa kike, jamii yote iliandikishwa kwa kufuata orodha ya vizazi vyao. Kwa kuwa walikuwa waaminifu katika kujitakasa.
2CH 31:19 Kuhusu makuhani, wazao wa Haruni walioishi kwenye mashamba yaliyozunguka miji yao au katika miji mingine yoyote, watu walitajwa majina ili kumgawia kila mwanaume miongoni mwao na kwa wote waliokuwa katika orodha ya vizazi vya Walawi.
2CH 31:20 Hivi ndivyo Hezekia alivyofanya katika Yuda yote, akifanya lile lililo jema, sawa na la uaminifu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
2CH 31:21 Katika kila kitu alichofanya katika huduma kwenye Hekalu la Mungu na katika kutii sheria na amri, alimtafuta Mungu wake na kufanya kazi kwa moyo wake wote. Naye hivyo akafanikiwa.
2CH 32:1 Baada ya yale yote aliyokuwa amefanya Hezekia kwa uaminifu mkubwa, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaja na kuvamia Yuda. Akaizingira miji yenye ngome, akikusudia kuiteka iwe yake.
2CH 32:2 Hezekia alipoona kuwa Senakeribu amekuja na kwamba alikusudia kufanya vita juu ya Yerusalemu,
2CH 32:3 akafanya shauri na maafisa wake na mashujaa wake juu ya kuzuia maji kutoka chemchemi zilizo nje ya mji, nao wakamsaidia.
2CH 32:4 Umati mkubwa wa watu wakakusanyika na kuzuia chemchemi zote na vijito vilivyotiririka katika nchi yote, wakisema: “Kwa nini wafalme wa Ashuru waje na kukuta maji tele?”
2CH 32:5 Hezekia akafanya kazi kwa bidii kukarabati sehemu zote zilizokuwa zimebomoka za ukuta na kujenga minara juu yake. Akajenga ukuta mwingine nje ya ule uliokuwako, na kuimarisha Milo katika Mji wa Daudi. Akatengeneza pia silaha nyingi na ngao.
2CH 32:6 Akaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya:
2CH 32:7 “Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye.
2CH 32:8 Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.
2CH 32:9 Hatimaye Senakeribu mfalme wa Ashuru na majeshi yake yote walipokuwa wameuzingira Lakishi, akawatuma maafisa wake kwenda Yerusalemu wakiwa na ujumbe huu kwa Hezekia mfalme wa Yuda, na kwa watu wote wa Yuda waliokuwa humo, kusema:
2CH 32:10 “Hili ndilo asemalo Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mmeweka tumaini lenu wapi, hata mnaendelea kukaa katika Yerusalemu, hali mmezingirwa na jeshi?
2CH 32:11 Hezekia asemapo, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, atatuokoa kutoka mkononi wa mfalme wa Ashuru,’ anawapotosha ninyi, naye atawaacha mfe kwa njaa na kiu.
2CH 32:12 Je, si Hezekia mwenyewe aliyeondoa mahali pa juu pa kuabudia pamoja na madhabahu zake, akiwaambia Yuda wa Yerusalemu, ‘Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu moja na kuteketeza dhabihu juu yake’?
2CH 32:13 “Je, hamjui yale mimi na baba zangu tuliyoyafanya kwa mataifa yote ya nchi zingine? Je, miungu ya mataifa hayo iliweza kuokoa nchi zao kutoka mkononi mwangu?
2CH 32:14 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya mataifa haya ambayo baba zangu waliyaangamiza ameweza kuwaokoa watu wake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mungu wenu kuwaokoa mkononi mwangu?
2CH 32:15 Sasa basi, msikubali Hezekia awadanganye na kuwapotosha namna hii. Msimwamini, kwa kuwa hakuna mungu wa taifa lolote wala wa ufalme wowote aliyeweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu au mkononi mwa baba zangu. Sembuse huyo mungu wenu atawaokoaje kutoka mkononi mwangu!”
2CH 32:16 Maafisa wa Senakeribu wakaendelea kunena dhidi ya Bwana Mwenyezi Mungu na dhidi ya mtumishi wake Hezekia.
2CH 32:17 Mfalme pia aliandika barua akimtukana Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, na kusema haya dhidi yake: “Kama vile miungu ya mataifa ya nchi nyingine ilivyoshindwa kuwaokoa watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu.”
2CH 32:18 Kisha wakawaita kwa Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa juu ya ukuta ili kuwatisha na kuwatia hofu ili waweze kuuteka mji.
2CH 32:19 Wakanena kuhusu Mungu wa Yerusalemu kama vile walivyonena kuhusu miungu ya mataifa mengine ya dunia ambayo ni kazi ya mikono ya wanadamu.
2CH 32:20 Mfalme Hezekia na nabii Isaya mwana wa Amozi wakalilia mbingu katika maombi kuhusu jambo hili.
2CH 32:21 Naye Mwenyezi Mungu akamtuma malaika ambaye aliangamiza wapiganaji wote, na viongozi na maafisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Kwa hiyo, mfalme wa Ashuru akarudi nchini mwake kwa aibu. Naye alipoenda katika hekalu la mungu wake, baadhi ya watoto wake mwenyewe wakamuua kwa upanga.
2CH 32:22 Hivyo Mwenyezi Mungu akamwokoa Hezekia na watu wa Yerusalemu kutoka mkononi mwa Senakeribu mfalme wa Ashuru na kutoka mikononi mwa wengine wote. Mwenyezi Mungu akawapa amani pande zote.
2CH 32:23 Watu wengi wakaleta sadaka Yerusalemu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na zawadi za thamani kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda. Tangu hapo na kuendelea, Hezekia aliheshimiwa sana na mataifa yote.
2CH 32:24 Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Akamwomba Mwenyezi Mungu, ambaye alimjibu na kumpa ishara.
2CH 32:25 Lakini moyo wa Hezekia ukajaa majivuno na hakuonesha itikio kwa wema aliotendewa, kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ikawa juu yake na juu ya Yuda na Yerusalemu.
2CH 32:26 Ndipo Hezekia akatubu kwa ajili ya kiburi cha moyo wake, kama walivyofanya watu wa Yerusalemu, kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi Mungu haikuja juu yao katika siku za Hezekia.
2CH 32:27 Hezekia alikuwa na utajiri mwingi sana na heshima, naye akajifanyia hazina kwa ajili ya fedha yake na dhahabu na kwa ajili ya vito vyake vya thamani, vikolezo, ngao na aina zote za vyombo vya thamani.
2CH 32:28 Akajenga pia maghala ya kuhifadhi mavuno ya nafaka, divai mpya na mafuta. Akatengeneza mabanda kwa ajili ya aina mbalimbali za mifugo, na mazizi kwa ajili ya kondoo na mbuzi.
2CH 32:29 Akajenga vijiji na kujipatia idadi kubwa ya kondoo na mbuzi, pamoja na ng’ombe, kwa kuwa Mungu alikuwa amempa utajiri mwingi sana.
2CH 32:30 Hezekia ndiye aliziba njia za kutolea maji za chemchemi za juu za Gihoni na kuyaelekeza maji kutiririkia upande wa magharibi wa Mji wa Daudi. Akafanikiwa katika kila kitu alichofanya.
2CH 32:31 Lakini wajumbe walipotumwa na watawala wa Babeli kumuuliza kuhusu ishara ambayo ilifanyika nchini, Mungu alimwacha ili kumjaribu na kujua kila kitu kilichokuwa moyoni mwake.
2CH 32:32 Matukio mengine ya utawala wa Hezekia na matendo yake ya kujitoa kwa moyo yameandikwa katika maono ya nabii Isaya mwana wa Amozi kwenye kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
2CH 32:33 Hezekia akalala na baba zake na akazikwa kwenye kilima mahali yalipo makaburi ya wazao wa Daudi. Yuda wote na watu wa Yerusalemu wakamheshimu alipofariki. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 33:1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na tano.
2CH 33:2 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli.
2CH 33:3 Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia ambapo Hezekia baba yake, alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Mabaali na nguzo za Maashera. Akayasujudia majeshi yote ya angani na kuyaabudu.
2CH 33:4 Akajenga madhabahu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu ambamo Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litadumu Yerusalemu milele.”
2CH 33:5 Katika nyua zote mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani.
2CH 33:6 Akawatoa kafara watoto wake kwa kuwapitishia motoni katika Bonde la Ben-Hinomu; akafanya ulozi, uaguzi, na uchawi, akatafuta ushauri kwa wenye pepo wa utambuzi na wenye kuwasiliana na mizimu. Akafanya maovu mengi machoni pa Mwenyezi Mungu, akaichochea hasira yake.
2CH 33:7 Akachukua ile sanamu aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu la Mungu ambalo Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Sulemani, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu, mji niliouchagua kutoka makabila yote ya Israeli, nitaliweka Jina langu milele.
2CH 33:8 Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli iondoke tena katika nchi niliyowapa baba zenu, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru kuhusu sheria zote, maagizo na amri zilizotolewa kwa mkono wa Musa.”
2CH 33:9 Lakini Manase akawaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu katika upotovu, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliangamiza mbele ya Waisraeli.
2CH 33:10 Mwenyezi Mungu akasema na Manase pamoja na watu wake, lakini hawakumjali.
2CH 33:11 Hivyo Mwenyezi Mungu akaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
2CH 33:12 Katika dhiki yake akamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.
2CH 33:13 Naye alipomwomba, Mwenyezi Mungu akaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza dua lake. Kwa hiyo akamrudisha Yerusalemu na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu.
2CH 33:14 Baadaye akajenga ukuta wa nje wa Mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli; pia akaufanya mrefu zaidi. Akawaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome.
2CH 33:15 Akaondolea mbali miungu ya kigeni pamoja na sanamu kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Pia akaondoa madhabahu zote alizojenga katika kilima kilichojengwa Hekalu, na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.
2CH 33:16 Kisha akarudisha madhabahu ya Mwenyezi Mungu na kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikie Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
2CH 33:17 Hata hivyo watu wakaendelea kutoa dhabihu mahali pa juu pa kuabudia, lakini wakawa wakimtolea Mwenyezi Mungu, Mungu wao, peke yake.
2CH 33:18 Matukio mengine ya utawala wa Manase, maombi yake kwa Mungu wake na maneno aliyoambiwa na waonaji walionena naye kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
2CH 33:19 Maombi yake, pamoja na jinsi Mungu alivyoguswa na kusihi kwake, pia dhambi zake zote na kukosa uaminifu kwake, pamoja na sehemu alizojenga mahali pa juu pa kuabudia, na kusimamisha nguzo za Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekeza kwake: haya yote yameandikwa katika kumbukumbu za waonaji.
2CH 33:20 Manase akalala na baba zake, akazikwa katika jumba lake la kifalme. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 33:21 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili.
2CH 33:22 Akatenda maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba yake Manase alivyofanya. Amoni akaabudu na kutoa dhabihu kwa sanamu zote alizokuwa ametengeneza Manase.
2CH 33:23 Lakini tofauti na Manase baba yake, hakujinyenyekeza mbele za Mwenyezi Mungu, badala yake Amoni alijiongeza hatia zaidi.
2CH 33:24 Watumishi wa Amoni wakampangia njama, nao wakamuua ndani ya jumba lake la kifalme.
2CH 33:25 Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamepanga njama dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.
2CH 34:1 Yosia alikuwa na umri wa miaka nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na moja.
2CH 34:2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia za Daudi baba yake, hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
2CH 34:3 Katika mwaka wa nane wa utawala wake, alipokuwa angali bado mdogo, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi baba yake. Katika mwaka wake wa kumi na mbili alianza kutakasa mahali pa juu pa kuabudia pa Yuda na Yerusalemu, akiondoa nguzo za Ashera, sanamu za kuchonga, na sanamu za kusubu.
2CH 34:4 Mbele ya macho yake, wakazibomoa madhabahu za Mabaali, wakazivunja madhabahu za kufukizia uvumba zilizokuwa zimesimama juu yake, wakazivunja nguzo za Ashera, sanamu na vinyago. Hivi alivivunja vipande vipande na kutawanya juu ya makaburi ya waliokuwa wamevitolea sadaka.
2CH 34:5 Akachoma mifupa ya makuhani wao juu ya madhabahu zao na kwa njia hiyo akaitakasa Yuda na Yerusalemu.
2CH 34:6 Katika miji ya Manase, Efraimu na Simeoni, hadi Naftali na kwenye magofu yanayoizunguka,
2CH 34:7 akavunja madhabahu na nguzo za Ashera na kuzipondaponda hizo sanamu hadi zikawa unga na kukata vipande vipande madhabahu zote za kufukizia uvumba katika nchi ya Israeli yote. Kisha akarudi Yerusalemu.
2CH 34:8 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yosia, ili kutakasa nchi na Hekalu, akawatuma Shafani, mwana wa Azalia na Maaseya mtawala wa mji, pamoja na Yoa mwana wa Yoahazi, mwandishi ili kukarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
2CH 34:9 Wakamwendea Hilkia kuhani mkuu na kumpa fedha ambazo zilikuwa zimeletwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu ambazo Walawi waliokuwa mabawabu walikuwa wamezikusanya kutoka kwa watu wa Manase, Efraimu na mabaki wote wa Israeli kutoka kwa watu wote wa Yuda na Benyamini na wakazi wa Yerusalemu.
2CH 34:10 Kisha wakazikabidhi hizo fedha kwa watu waliowekwa ili kusimamia kazi ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hawa watu waliwalipa wafanyakazi waliokarabati na kutengeneza Hekalu lipate kurudi katika hali yake.
2CH 34:11 Wakawapa pia mafundi seremala na waashi fedha ili kununua mawe yaliyochongwa, mbao kwa ajili ya kufungia na boriti kwa ajili ya majengo ambayo wafalme wa Yuda walikuwa wameyaacha yakawa magofu.
2CH 34:12 Watu wakafanya kazi kwa uaminifu. Waliokuwa wamewekwa juu yao ili kuwaelekeza ni Yahathi na Obadia, Walawi wa uzao wa Merari, Zekaria na Meshulamu, waliotoka kwenye uzao wa Kohathi. Walawi wote wenye ujuzi wa kupiga ala za uimbaji,
2CH 34:13 wakawa wasimamizi wa vibarua na kuwaongoza wale waliofanya kila aina ya kazi. Baadhi ya Walawi walikuwa waandishi, maafisa na mabawabu.
2CH 34:14 Wakati walikuwa wakizitoa nje fedha zilizokuwa zimetolewa kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu, kuhani Hilkia akakipata kile Kitabu cha Torati ya Mwenyezi Mungu kilichokuwa kimetolewa kwa mkono wa Musa.
2CH 34:15 Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Torati ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” Akampa Shafani kile Kitabu.
2CH 34:16 Kisha Shafani akakipeleka kile Kitabu kwa mfalme na kumwambia, “Maafisa wako wanafanya kila kitu kama walivyokabidhiwa kufanya.
2CH 34:17 Wamelipa fedha zilizokuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu na wamewakabidhi wasimamizi na wafanyakazi.”
2CH 34:18 Kisha Shafani mwandishi akamwarifu mfalme kuwa, “Kuhani Hilkia amenipa Kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
2CH 34:19 Mfalme aliposikia yale maneno ya Torati, akayararua mavazi yake.
2CH 34:20 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, Shafani mwandishi na Asaya mtumishi wa mfalme,
2CH 34:21 “Nendeni mkamuulize Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu na kwa ajili ya mabaki waliosalia katika Israeli na Yuda, kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Mwenyezi Mungu iliyomwagwa juu yetu ni kubwa mno kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la Mwenyezi Mungu wala hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki.”
2CH 34:22 Hilkia pamoja na wale wote mfalme aliokuwa amewatuma pamoja naye wakaenda kuzungumza na nabii mke aitwaye Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tokhathi, mwana wa Hasra mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu, katika Mtaa wa Pili.
2CH 34:23 Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu,
2CH 34:24 ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Nitaleta maafa mahali hapa na kwa watu wake: laana zote zilizoandikwa ndani ya kitabu hicho, ambazo zimesomwa mbele ya mfalme wa Yuda.
2CH 34:25 Kwa sababu wameniacha na kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kunighadhibisha kwa kazi yote ya mikono yao, hivyo hasira yangu itamwagwa mahali hapa, wala haitatulizwa.’
2CH 34:26 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Mwenyezi Mungu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia:
2CH 34:27 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu na uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Mwenyezi Mungu.
2CH 34:28 Basi nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa na juu ya wote wanaoishi hapa.’ ” Kwa hiyo wakampelekea mfalme jibu lake.
2CH 34:29 Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.
2CH 34:30 Akapanda kwenda hekaluni mwa Mwenyezi Mungu pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na Walawi, watu wote, wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, kilichokuwa kimepatikana katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 34:31 Mfalme akasimama karibu na nguzo yake na kufanya upya agano mbele za Mwenyezi Mungu kwamba atamfuata Mwenyezi Mungu na kuzishika amri zake, maagizo na sheria zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, ili kuyatii maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
2CH 34:32 Ndipo akamtaka kila mmoja katika Yerusalemu na Benyamini kuweka ahadi zao wenyewe kwa hilo agano, watu wa Yerusalemu wakafanya hivyo kwa kufuata agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
2CH 34:33 Yosia akaondoa machukizo yote ya sanamu kutoka nchi yote ya Waisraeli na akawataka wale wote waliokuwa katika Israeli wamtumikie Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Kwa muda wote alioishi, hawakushindwa kumfuata Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.
2CH 35:1 Yosia akaadhimisha Pasaka kwa Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu, mwana-kondoo wa Pasaka akachinjwa siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.
2CH 35:2 Akawaweka makuhani kwenye wajibu wao na kuwatia moyo katika utumishi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2CH 35:3 Akawaambia Walawi, waliowafundisha Waisraeli wote na waliokuwa wamejiweka wakfu kwa ajili ya kazi ya Mwenyezi Mungu, “Liwekeni hilo Sanduku takatifu katika Hekalu lile alilojenga Sulemani mwana wa Daudi mfalme wa Israeli. Halipaswi kubebwa mabegani mwenu. Sasa mtumikieni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na watu wake Israeli.
2CH 35:4 Jiandaeni kwa kufuata jamaa zenu katika migawanyo yenu, kufuatana na maelezo yaliyoandikwa na Daudi mfalme wa Israeli na mwanawe Sulemani.
2CH 35:5 “Simameni mahali patakatifu kwa kufuata migawanyo ya jamaa za baba zenu kulingana na koo zenu na pawepo Walawi kwa ajili ya kila mgawanyo wa nyumba ya baba zenu.
2CH 35:6 Chinjeni mwana-kondoo wa Pasaka, jitakaseni, nanyi kwa niaba ya koo zenu fanyeni maandalizi, mkitenda sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu kwa mkono wa Musa.”
2CH 35:7 Ndipo Yosia akawapa watu wote waliokuwepo wana-mbuzi na kondoo wapatao elfu thelathini kwa ajili ya sadaka ya Pasaka, pia na ng’ombe elfu kumi; wote kutoka kwa mali binafsi ya mfalme.
2CH 35:8 Pia maafisa wake, wakatoa kwa hiari yao wakawapa watu, makuhani na Walawi. Hilkia, Zekaria na Yehieli, waliokuwa maafisa wakuu wa Hekalu la Mungu, wakawapa makuhani sadaka za Pasaka wana-kondoo na wana-mbuzi elfu mbili na mia sita, na mafahali mia tatu.
2CH 35:9 Konania na nduguze wawili, Shemaya na Nethaneli, pamoja na Hashabia, Yeieli na Yozabadi waliokuwa viongozi wa Walawi, nao pia wakawapa Walawi wana-kondoo na wana-mbuzi elfu tano, na mafahali mia tano, kwa ajili ya sadaka za Pasaka.
2CH 35:10 Huduma ilipomalizika kuandaliwa makuhani wakasimama mahali pao na Walawi katika migawanyo yao kama mfalme alivyokuwa ameamuru.
2CH 35:11 Wana-kondoo wa Pasaka wakachinjwa, nao makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa, wakati Walawi wakiwa wanawachuna wale wanyama ngozi.
2CH 35:12 Wakatenga sadaka za kuteketezwa ili waweze kugawia ili migawanyo kwa kufuata jamaa za baba zao ili watoe sadaka kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Musa. Wakafanya vivyo hivyo kwa wale mafahali.
2CH 35:13 Wakawaoka wale wanyama wa Pasaka kwenye moto kama ilivyoamriwa, wakachemsha zile sadaka takatifu kwenye vyungu, masufuria makubwa na vikaango na kuwagawia watu wote upesi.
2CH 35:14 Hatimaye wakafanya maandalizi kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani, kwa sababu wale makuhani, yaani wazao wa Haruni, walikuwa wanatoa sadaka za kuteketezwa pamoja na zile sehemu zilizonona hadi usiku. Hivyo Walawi wakafanya maandalizi kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Haruni.
2CH 35:15 Waimbaji, wazao wa Asafu, walikuwa katika nafasi zao, kama ilivyoagizwa na Mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni mwonaji wa Mfalme. Mabawabu katika kila lango hawakuhitaji kuacha nafasi zao kwa sababu Walawi wenzao walifanya maandalizi kwa ajili yao.
2CH 35:16 Kwa hiyo wakati ule, huduma yote ya Mwenyezi Mungu ilifanyika katika kuadhimisha Pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, kama alivyoamuru Mfalme Yosia.
2CH 35:17 Waisraeli waliokuwepo wakaadhimisha Pasaka wakati huo na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa siku saba.
2CH 35:18 Kulikuwa hakujafanyika Pasaka kama hii katika Israeli tangu siku za nabii Samweli wala hakukuwa na mfalme yeyote wa Israeli ambaye kamwe alishaadhimisha Pasaka kama ile aliyofanya Mfalme Yosia, akiwa na makuhani, Walawi, na watu wote wa Yuda na wa Israeli waliokuwa huko, pamoja na wakaaji wa Yerusalemu.
2CH 35:19 Pasaka iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia.
2CH 35:20 Baada ya haya yote, Yosia alipomaliza kulitengeneza vizuri Hekalu, Neko mfalme wa Misri akapanda ili kupigana huko Karkemishi katika Mto Frati, naye Yosia akatoka kwenda kupigana naye.
2CH 35:21 Lakini Neko akamtumia wajumbe kusema, “Kuna ugomvi gani kati yangu mimi na wewe, ee mfalme wa Yuda? Si wewe ninayekushambulia wakati huu, bali ile nyumba niliyo na vita nayo, Mungu ameniambia niharakishe, kwa hivyo acha kumpinga Mungu, ambaye yuko pamoja nami, la sivyo atakuangamiza.”
2CH 35:22 Lakini hata hivyo, Yosia hakukubali kumwacha, bali alijibadilisha ili kupigana naye vita. Hakusikiliza yale Neko aliyokuwa amemwambia kwa agizo la Mungu bali alienda kupigana naye katika tambarare ya Megido.
2CH 35:23 Wapiga upinde wakampiga Mfalme Yosia, naye akawaambia maafisa wake, “Niondoeni, nimejeruhiwa vibaya sana.”
2CH 35:24 Kwa hiyo wakamshusha kutoka gari lake la vita, wakamweka kwenye gari lingine alilokuwa nalo na kumleta Yerusalemu, ambako alifia. Akazikwa katika makaburi ya baba zake, nayo Yuda yote na Yerusalemu wakamwombolezea Yosia.
2CH 35:25 Nabii Yeremia akatunga maombolezo kwa ajili ya kifo chake, nao waimbaji wote, wanaume kwa wanawake, hufanya ukumbusho wa Yosia katika maombolezo hadi leo. Haya yakafanywa desturi katika Israeli, nayo yameandikwa katika Maombolezo.
2CH 35:26 Matukio mengine ya utawala wa Yosia na matendo yake mema, kulingana na yale yaliyoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu:
2CH 35:27 matukio yote, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.
2CH 36:1 Watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia na kumfanya mfalme mahali pa baba yake huko Yerusalemu.
2CH 36:2 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu.
2CH 36:3 Mfalme wa Misri akamwondoa madarakani huko Yerusalemu, na akatoza Yuda kodi ya talanta mia moja za fedha, na talanta moja ya dhahabu.
2CH 36:4 Mfalme wa Misri akamweka Eliakimu, nduguye Yehoahazi, kuwa mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu na kubadili jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini Neko akamchukua Yehoahazi, nduguye Eliakimu, akampeleka Misri.
2CH 36:5 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
2CH 36:6 Nebukadneza mfalme wa Babeli akamshambulia na kumfunga kwa pingu za shaba akampeleka Babeli.
2CH 36:7 Nebukadneza akachukua pia vyombo kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu na kuviweka katika hekalu lake huko Babeli.
2CH 36:8 Matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu, machukizo aliyoyafanya na yote yaliyoonekana dhidi yake, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.
2CH 36:9 Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi. Akafanya yaliyo maovu machoni pa Mwenyezi Mungu.
2CH 36:10 Majira ya vuli, Mfalme Nebukadneza akatuma watu, nao wakamleta Babeli, pamoja na vyombo vya thamani kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Naye akamfanya Sedekia, ndugu yake Yehoyakimu kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu.
2CH 36:11 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na moja.
2CH 36:12 Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, wala hakujinyenyekeza mbele ya nabii Yeremia, ambaye alinena neno la Mwenyezi Mungu.
2CH 36:13 Pia alimwasi Mfalme Nebukadneza, aliyekuwa amemwapisha kwa jina la Mungu. Akashupaza shingo na akafanya moyo wake kuwa mgumu wala hakutaka kumgeukia Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
2CH 36:14 Zaidi ya hayo viongozi wote wa makuhani pamoja na watu wakazidi kukosa uaminifu zaidi na zaidi, wakafanya machukizo yote kama walivyofanya mataifa wakinajisi Hekalu la Mwenyezi Mungu alilokuwa amelitakasa huko Yerusalemu.
2CH 36:15 Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, akawapelekea neno kupitia wajumbe wake tena na tena, kwa sababu alikuwa anawahurumia watu wake pamoja na mahali pa Maskani yake.
2CH 36:16 Lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mwenyezi Mungu wakayadharau maneno yake na kuwacheka manabii wake hadi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ikawa kubwa dhidi ya watu wake, na hakukuwa na namna ya kuituliza.
2CH 36:17 Mungu akamwinua dhidi yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao wa kiume kwa upanga ndani ya mahali patakatifu. Hakumbakiza kijana wala mwanamwali, mzee wala mnyonge. Mungu akawatia wote mikononi mwa Nebukadneza.
2CH 36:18 Akavichukua kwenda Babeli vyombo vyote kutoka Hekalu la Mungu, vikubwa na vidogo, hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu pamoja na hazina za mfalme na za maafisa wake.
2CH 36:19 Wakalichoma Hekalu la Mungu na kuzibomoa kuta za Yerusalemu, wakachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu kila kitu chake cha thamani.
2CH 36:20 Wale watu walionusurika kuuawa kwa upanga wakachukuliwa kwenda uhamishoni Babeli. Nao wakawa watumishi wake na wa wanawe hadi wakati wa utawala wa ufalme wa Uajemi ulifika.
2CH 36:21 Nchi ikaendelea kufurahia pumziko zake za sabato; wakati wote wa kufanywa kwake ukiwa ilipumzika, hadi ile miaka sabini ilipotimia katika kutimiza neno la Mwenyezi Mungu lililonenwa na Yeremia.
2CH 36:22 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Mwenyezi Mungu lililosemwa na nabii Yeremia, Mwenyezi Mungu aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:
2CH 36:23 “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi: “ ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda. Yeyote kati ya watu wa Mungu miongoni mwenu, Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na awe pamoja naye, wacha apande.’ ”
EZR 1:1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Mwenyezi Mungu lililosemwa na nabii Yeremia, Mwenyezi Mungu aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:
EZR 1:2 “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi: “ ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda.
EZR 1:3 Yeyote kati ya watu wa Mungu miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha apande kwenda Yerusalemu katika Yuda na kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, Mungu aliyeko Yerusalemu.
EZR 1:4 Nao wakazi wa popote manusura wanapoishi sasa, wawape manusura fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, na sadaka za hiari kwa ajili ya Hekalu la Mungu huko Yerusalemu.’ ”
EZR 1:5 Kisha viongozi wa jamaa ya Yuda na Benyamini na makuhani na Walawi kila mmoja ambaye moyo wake ulisukumwa na Mungu, akajiandaa kupanda ili kuijenga nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu.
EZR 1:6 Majirani zao wote wakawasaidia vyombo vya fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, pia na zawadi za thamani, pamoja na sadaka zote za hiari.
EZR 1:7 Zaidi ya hayo, Mfalme Koreshi akavitoa vyombo vilivyokuwa mali ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la mungu wake.
EZR 1:8 Koreshi mfalme wa Uajemi akavitoa kwa mkono wa Mithredathi mtunza hazina, aliyevihesabu mbele ya Sheshbaza mkuu wa Yuda.
EZR 1:9 Hii ilikuwa orodha ya vifaa: masinia ya dhahabu yalikuwa thelathini; masinia ya fedha yalikuwa elfu moja; vyetezo vya fedha vilikuwa ishirini na tisa;
EZR 1:10 mabakuli ya dhahabu yalikuwa thelathini; mabakuli ya fedha yaliyofanana yalikuwa mia nne na kumi; vifaa vingine vilikuwa elfu moja.
EZR 1:11 Kwa jumla, kulikuwa na vyombo elfu tano na mia nne vya dhahabu na vya fedha. Sheshbaza akavileta hivi vyote wakati watu walipotoka uhamishoni Babeli kwenda Yerusalemu.
EZR 2:1 Basi hawa ndio watu wa jimbo waliotoka uhamishoni, ambao Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa amewachukua mateka hadi Babeli (walirudi Yerusalemu na Yuda, kila mmoja kwenye mji wake,
EZR 2:2 wakiwa wamefuatana na Zerubabeli, Yeshua, Nehemia, Seraya, Reelaya, Mordekai, Bilshani, Mispari, Bigwai, Rehumu na Baana):
EZR 2:3 wazao wa Paroshi, elfu mbili mia moja sabini na wawili (2,172);
EZR 2:4 wazao wa Shefatia, mia tatu sabini na wawili (372);
EZR 2:5 wazao wa Ara, mia saba sabini na watano (775);
EZR 2:6 wazao wa Pahath-Moabu (wa jamaa ya Yeshua na Yoabu), elfu mbili mia nane na kumi na wawili (2,812);
EZR 2:7 wazao wa Elamu, elfu moja mia mbili hamsini na wanne (1,254);
EZR 2:8 wazao wa Zatu, mia tisa arobaini na watano (945);
EZR 2:9 wazao wa Zakai, mia saba na sitini (760);
EZR 2:10 wazao wa Bani, mia sita arobaini na wawili (642);
EZR 2:11 wazao wa Bebai, mia sita ishirini na watatu (623);
EZR 2:12 wazao wa Azgadi, elfu moja mia mbili ishirini na wawili (1,222);
EZR 2:13 wazao wa Adonikamu, mia sita sitini na sita (666);
EZR 2:14 wazao wa Bigwai, elfu mbili hamsini na sita (2,056);
EZR 2:15 wazao wa Adini, mia nne hamsini na wanne (454);
EZR 2:16 wazao wa Ateri (kupitia Hezekia), tisini na nane (98);
EZR 2:17 wazao wa Besai, mia tatu ishirini na watatu (323);
EZR 2:18 wazao wa Yora, mia moja na kumi na wawili (112);
EZR 2:19 wazao wa Hashumu, mia mbili na ishirini na watatu (223);
EZR 2:20 wazao wa Gibari, tisini na watano (95);
EZR 2:21 watu wa Bethlehemu, mia moja ishirini na watatu (123);
EZR 2:22 watu wa Netofa, hamsini na sita (56);
EZR 2:23 watu wa Anathothi, watu mia moja ishirini na nane (128);
EZR 2:24 watu wa Azmawethi, arobaini na wawili (42);
EZR 2:25 wazao wa Kiriath-Yearimu, Kefira na Beerothi, mia saba arobaini na watatu (743);
EZR 2:26 wazao wa Rama na Geba, mia sita ishirini na mmoja (621);
EZR 2:27 watu wa Mikmashi, mia moja ishirini na wawili (122);
EZR 2:28 watu wa Betheli na Ai, mia mbili na ishirini na watatu (223);
EZR 2:29 wazao wa Nebo, hamsini na wawili (52);
EZR 2:30 wazao wa Magbishi, mia moja hamsini na sita (156);
EZR 2:31 wazao wa Elamu ile ingine, elfu moja mia mbili hamsini na wanne (1,254);
EZR 2:32 wazao wa Harimu, mia tatu na ishirini (320);
EZR 2:33 wazao wa Lodi, Hadidi na Ono, mia saba ishirini na watano (725);
EZR 2:34 wazao wa Yeriko, mia tatu arobaini na watano (345);
EZR 2:35 wazao wa Senaa, elfu tatu mia sita na thelathini (3,630).
EZR 2:36 Makuhani: wazao wa Yedaya (kwa jamaa ya Yeshua), mia tisa sabini na watatu (973);
EZR 2:37 wazao wa Imeri, elfu moja hamsini na wawili (1,052);
EZR 2:38 wazao wa Pashuri, elfu moja mia mbili arobaini na saba (1,247);
EZR 2:39 wazao wa Harimu, elfu moja na kumi na saba (1,017).
EZR 2:40 Walawi: wazao wa Yeshua na Kadmieli (kupitia jamaa ya Hodavia), sabini na wanne (74).
EZR 2:41 Waimbaji: wazao wa Asafu, mia moja ishirini na nane (128).
EZR 2:42 Mabawabu wa lango la Hekalu: wazao wa Shalumu, Ateri, Talmoni, Akubu, Hatita na Shobai, mia moja thelathini na tisa (139).
EZR 2:43 Watumishi wa Hekalu: wazao wa Siha, Hasufa, Tabaothi,
EZR 2:44 wazao wa Kerosi, Siaha, Padoni,
EZR 2:45 wazao wa Lebana, Hagaba, Akubu,
EZR 2:46 wazao wa Hagabu, Shalmai, Hanani,
EZR 2:47 wazao wa Gideli, Gahari, Reaya,
EZR 2:48 wazao wa Resini, Nekoda, Gazamu,
EZR 2:49 wazao wa Uza, Pasea, Besai,
EZR 2:50 wazao wa Asna, Meunimu, Nefusimu,
EZR 2:51 wazao wa Bakbuki, Hakufa, Harhuri,
EZR 2:52 wazao wa Basluthi, Mehida, Harsha,
EZR 2:53 wazao wa Barkosi, Sisera, Tema,
EZR 2:54 wazao wa Nesia na Hatifa.
EZR 2:55 Wazao wa watumishi wa Sulemani: wazao wa Sotai, Hasaferethi, Peruda,
EZR 2:56 wazao wa Yaala, Darkoni, Gideli,
EZR 2:57 wazao wa Shefatia, Hatili, Pokereth-Hasebaimu na Ami.
EZR 2:58 Watumishi wa Hekalu, na wazao wa watumishi wa Sulemani, mia tatu tisini na wawili (392).
EZR 2:59 Wafuatao walikuja kutoka miji ya Tel-Mela, Tel-Harsha, Kerubu, Adoni na Imeri, lakini hawakuweza kuthibitisha kwamba jamaa zao zilikuwa uzao wa Israeli:
EZR 2:60 wazao wa Delaya, Tobia na Nekoda, mia sita hamsini na wawili (652).
EZR 2:61 Kutoka miongoni mwa makuhani: Wazao wa Hobaya, Hakosi, Barzilai (mtu aliyemwoa binti Barzilai Mgileadi, naye akaitwa kwa jina hilo).
EZR 2:62 Hawa walitafuta orodha za jamaa zao, lakini hawakuonekana humo, kwa hiyo waliondolewa ukuhani kwa kuwa walihesabiwa kuwa najisi.
EZR 2:63 Mtawala aliagiza kuwa wasile chochote miongoni mwa vyakula vitakatifu hadi kuwe kuhani atakayehudumu kwa Urimu na Thumimu.
EZR 2:64 Jumla ya watu wote waliorudi walikuwa elfu arobaini na mbili na mia tatu na sitini (42,360);
EZR 2:65 tena zaidi ya hao walikuwa na watumwa wa kiume na wa kike elfu saba, mia tatu na thelathini na saba (7,337); pia walikuwa na waimbaji wanaume na wanawake mia mbili.
EZR 2:66 Walikuwa na farasi mia saba thelathini na sita (736), nyumbu mia mbili arobaini na watano (245),
EZR 2:67 ngamia mia nne thelathini na watano (435), na punda elfu sita, mia saba na ishirini (6,720).
EZR 2:68 Walipofika kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu, baadhi ya viongozi wa jamaa walitoa sadaka za hiari kwa ajili ya kujenga upya nyumba ya Mungu katika eneo lake.
EZR 2:69 Wakatoa kwa kadiri ya uwezo wao na kutia katika hazina darkoni elfu sitini na moja za dhahabu, mane elfu tano za fedha, na mavazi mia moja ya ukuhani kwa ajili ya kazi hiyo.
EZR 2:70 Makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu, na watumishi wa Hekalu waliishi katika miji yao wenyewe, pamoja na baadhi ya watu wengine, nao Waisraeli waliosalia waliishi katika miji yao.
EZR 3:1 Mwezi wa saba ulipowadia baada ya Waisraeli kukaa katika miji yao, watu wote walikusanyika huko Yerusalemu kama mtu mmoja.
EZR 3:2 Yeshua mwana wa Yosadaki na makuhani wenzake, Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na wenzake walianza kujenga madhabahu ya Mungu wa Israeli ili kumtolea dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto, kulingana na ilivyoandikwa katika Torati ya Musa mtu wa Mungu.
EZR 3:3 Ingawa waliwaogopa watu waliowazunguka, walijenga madhabahu juu ya ule msingi wake, wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu za sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni.
EZR 3:4 Kisha kulingana na kile kilichoandikwa, wakaiadhimisha Sikukuu ya Vibanda wakitoa idadi ya sadaka za kuteketezwa kama ilivyohitajika kila siku sawasawa na ilivyoagizwa.
EZR 3:5 Baada ya hayo, walitoa sadaka za kuteketezwa za kawaida, sadaka za Mwezi Mwandamo na dhabihu zote za sikukuu takatifu za Mwenyezi Mungu zilizoamriwa, pamoja na zile sadaka za hiari zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu.
EZR 3:6 Ingawa bado msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu ulikuwa haujawekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.
EZR 3:7 Kisha watu wakawapa mafundi wa uashi na useremala fedha, wakawapa watu wa Sidoni na Tiro vyakula, vinywaji na mafuta ili waweze kuleta magogo ya mwerezi kupitia bahari kutoka Lebanoni hadi Yafa, kama alivyoagiza Koreshi mfalme wa Uajemi.
EZR 3:8 Katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri wa miaka ishirini na zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu.
EZR 3:9 Yeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu.
EZR 3:10 Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumhimidi Mwenyezi Mungu, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli.
EZR 3:11 Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Mwenyezi Mungu hivi: “Yeye ni mwema; upendo wake kwa Israeli wadumu milele.” Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu msingi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu ulikuwa umewekwa.
EZR 3:12 Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha.
EZR 3:13 Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.
EZR 4:1 Adui za Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanajenga Hekalu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli,
EZR 4:2 wakamjia Zerubabeli na viongozi wa jamaa, nao wakasema, “Turuhusuni tuwasaidie kujenga, kwa sababu sisi tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi na tumekuwa tukimtolea dhabihu tangu wakati wa Esar-Hadoni mfalme wa Ashuru, aliyetuleta hapa.”
EZR 4:3 Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa jamaa ya Israeli wakawajibu, “Ninyi hamna sehemu nasi katika kujenga Hekalu la Mungu wetu. Sisi peke yetu tutajenga Hekalu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kama Mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi alivyotuagiza.”
EZR 4:4 Ndipo watu waliowazunguka wakajipanga kuwakatisha tamaa watu wa Yuda na kuwafanya waogope walipokuwa wakiendelea na ujenzi.
EZR 4:5 Wakaajiri washauri kuwapinga katika kazi yao, nao wakaipinga mipango yao wakati wote wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi hadi wakati wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi.
EZR 4:6 Hapo mwanzo wa utawala wa Ahasuero, hao adui waliandika mashtaka dhidi ya watu wa Yuda na Yerusalemu.
EZR 4:7 Pia katika siku za utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli pamoja na wenzao waliandika barua kwa Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa mwandiko wa Kiaramu na katika lugha ya Kiaramu.
EZR 4:8 Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai waliandika barua kwa Mfalme Artashasta dhidi ya watu wa Yerusalemu kama ifuatavyo:
EZR 4:9 Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai, pamoja na wenzao, yaani mahakimu na maafisa walio juu ya watu kuanzia Tripoli, Uajemi, Ereki na Babeli, Waelami wa Shushani,
EZR 4:10 na watu wengine ambao mheshimiwa Asur-Banipali aliwahamisha na kuwakalisha katika mji wa Samaria na mahali pengine Ng’ambo ya Mto Frati.
EZR 4:11 (Hii ndiyo nakala ya barua waliyompelekea.) Kwa Mfalme Artashasta, Kutoka kwa watumishi wako, watu wa Ng’ambo ya Mto Frati:
EZR 4:12 Yapasa Mfalme ajue kuwa Wayahudi waliopanda kuja kwetu kutoka kwenu, wameenda Yerusalemu nao wanaujenga upya ule mji wa uasi na uovu. Wanajenga kuta upya na kukarabati misingi yake.
EZR 4:13 Zaidi ya hayo, yampasa mfalme ajue kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikafanywa upya, hakutakuwa na ulipaji wa kodi wala ada au ushuru, hivyo hazina za mfalme zitaathirika.
EZR 4:14 Sisi sasa kwa kuwa tunawajibika kwa jumba la kifalme na kwamba siyo sawasawa kwetu kuona mfalme akidharauliwa, basi tunatuma ujumbe huu kumtaarifu mfalme,
EZR 4:15 ili ufanyike uchunguzi kwenye kumbukumbu ya maandishi ya waliokutangulia. Katika kumbukumbu hizi utagundua kwamba mji huu ni mwasi, unaowataabisha wafalme na majimbo, ni mahali pa maasi tangu zamani. Ndiyo maana mji huu uliharibiwa.
EZR 4:16 Tunamjulisha mfalme kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikifanywa upya, hutabakiwa na chochote Ng’ambo ya Mto Frati.
EZR 4:17 Mfalme alirudisha jibu hili: Kwa Rehumu, afisa msimamizi, mwandishi Shimshai na wenzenu wote wanaoishi katika Samaria na penginepo Ng’ambo ya Mto Frati: Salamu.
EZR 4:18 Barua mliyotutumia imesomwa na kutafsiriwa mbele yangu.
EZR 4:19 Nilitoa amri na uchunguzi ukafanyika na imegundulika kwamba mji huu una historia ndefu ya maasi dhidi ya wafalme na pamekuwa mahali pa maasi na uchochezi.
EZR 4:20 Yerusalemu umepata kuwa na wafalme wenye nguvu wakitawala nchi yote iliyo Ng’ambo ya Mto Frati, wakitoza kodi, ada na ushuru huko.
EZR 4:21 Kwa hiyo toeni amri kwa watu hawa wasimamishe ujenzi, ili mji huu usiendelee kujengwa hadi nitakapoagiza.
EZR 4:22 Mwe waangalifu msipuuze jambo hili. Kwa nini kuruhusu tishio hili kuendelea na kusababisha hasara kwa ufalme?
EZR 4:23 Mara waliposomewa nakala ya barua ya Mfalme Artashasta, Rehumu na Shimshai aliyekuwa mwandishi na wenzao, walienda mara moja kwa Wayahudi huko Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu kusimamisha ujenzi.
EZR 4:24 Hivyo kazi ya ujenzi wa nyumba ya Mungu huko Yerusalemu ikasimamishwa kabisa hadi mwaka wa pili wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi.
EZR 5:1 Ndipo nabii Hagai na nabii Zekaria mzao wa Ido, wakawatolea unabii Wayahudi waliokuwa Yuda na Yerusalemu kwa jina la Mungu wa Israeli, aliyekuwa pamoja nao.
EZR 5:2 Ndipo Zerubabeli mwana wa Shealtieli na Yeshua mwana wa Yosadaki wakaanza kujenga tena nyumba ya Mungu huko Yerusalemu. Nao manabii wa Mungu walikuwa pamoja nao, wakiwasaidia.
EZR 5:3 Wakati ule Tatenai mtawala wa ng’ambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao waliwaendea, wakawauliza, “Ni nani aliyewapa ruhusa ya kujenga tena Hekalu hili na kurudishia upya kama lilivyokuwa?”
EZR 5:4 Pia waliwauliza, “Je, majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani?”
EZR 5:5 Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa likiwaangalia wazee wa Wayahudi, nao hawakuzuiliwa kujenga hadi taarifa ikaandikwa kwa Dario na majibu yake kupokelewa.
EZR 5:6 Hii ni nakala ya barua ile Tatenai, mtawala wa ng’ambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao maafisa wa ng’ambo ya mto Frati waliyompelekea Mfalme Dario.
EZR 5:7 Taarifa waliyompelekea ilisomeka kama ifuatavyo: Kwa Mfalme Dario: Salamu kwa moyo mkunjufu.
EZR 5:8 Inampasa Mfalme ajue kwamba tulienda katika eneo la Yuda, kwenye Hekalu la Mungu mkuu. Watu wanalijenga kwa mawe makubwa na kuweka mbao kwenye kuta. Kazi inafanyika kwa bidii na inaendelea kwa haraka chini ya uongozi wao.
EZR 5:9 Tuliwauliza viongozi, “Ni nani aliyewapa ruhusa kujenga upya Hekalu hili na kurejesha hali ya jengo kama lilivyokuwa?”
EZR 5:10 Pia tuliwauliza majina yao, ili tukuandikie kukujulisha majina ya viongozi wao.
EZR 5:11 Hili ndilo jibu walilotupatia: “Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunalijenga upya Hekalu ambalo lilijengwa miaka mingi iliyopita, lile ambalo mfalme mkuu wa Israeli alilijenga na kulikamilisha.
EZR 5:12 Lakini kwa sababu baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbinguni, basi aliwatia mkononi mwa Nebukadneza, Mkaldayo, mfalme wa Babeli, ambaye aliliharibu Hekalu hili na kuwaondoa watu na kuwapeleka uhamishoni huko Babeli.
EZR 5:13 “Pamoja na hayo, katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Babeli, Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujengwa upya nyumba hii ya Mungu.
EZR 5:14 Yeye hata aliviondoa vyombo vya dhahabu na fedha vya nyumba ya Mungu, kutoka Hekalu la Babeli ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka ndani ya Hekalu huko Yerusalemu na kuvileta katika Hekalu la Babeli. “Vyombo hivyo Mfalme Koreshi alimkabidhi mtu aliyeitwa Sheshbaza, ambaye Koreshi alikuwa amemteua awe mtawala,
EZR 5:15 naye akamwambia, ‘Chukua vyombo hivi uende ukaviweke ndani ya Hekalu huko Yerusalemu. Nawe uijenge upya nyumba ya Mungu mahali pake.’
EZR 5:16 “Hivyo huyu Sheshbaza alikuja na kuweka misingi ya nyumba ya Mungu iliyo Yerusalemu. Tangu siku hiyo hadi sasa imekuwa ikiendelea kujengwa lakini bado haijamalizika.”
EZR 5:17 Sasa, ikimpendeza mfalme, uchunguzi na ufanyike katika kumbukumbu za maandishi ya ufalme mjini Babeli, kuona kama kweli Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujenga upya nyumba ya Mungu katika Yerusalemu. Kisha tunaomba mfalme na atutumie uamuzi wake kuhusu jambo hili.
EZR 6:1 Kisha Mfalme Dario alitoa amri, nao wakafanya uchunguzi katika kumbukumbu zilizohifadhiwa katika hazina huko Babeli.
EZR 6:2 Kitabu kilipatikana katika ngome la Ekbatana katika jimbo la Umedi; kilikuwa kimeandikwa hivi: Kumbukumbu:
EZR 6:3 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi, mfalme alitoa amri kuhusu Hekalu la Mungu katika Yerusalemu: Hekalu na lijengwe upya likiwa mahali pa kutolea dhabihu, na misingi yake ijengwe. Iwe na kimo cha mikono sitini, upana wa mikono sitini,
EZR 6:4 kuta zijengwe kwa safu tatu za mawe makubwa kisha ifuate safu moja ya mbao. Gharama zitalipwa kutoka hazina ya mfalme.
EZR 6:5 Pia, vyombo vya dhahabu na vya fedha vya nyumba ya Mungu, ambavyo Nebukadneza alivichukua kutoka Hekalu huko Yerusalemu akavileta Babeli, yapasa virudishwe mahali pake ndani ya Hekalu huko Yerusalemu, yapasa viwekwe ndani ya nyumba ya Mungu.
EZR 6:6 Sasa basi, Tatenai, mtawala wa Ng’ambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai pamoja na ninyi, maafisa wenzao wa jimbo hilo kaeni mbali na mahali hapo.
EZR 6:7 Msiingilie kazi ya Hekalu hili la Mungu. Mwacheni mtawala wa Wayahudi na viongozi Wayahudi wajenge upya nyumba hii ya Mungu mahali pake.
EZR 6:8 Zaidi ya hayo, hapa natoa amri kuhusu mtakalofanya kwa ajili ya wazee wa Wayahudi katika ujenzi wa nyumba hii ya Mungu: Gharama za watu hawa zitalipwa kikamilifu kutoka hazina ya mfalme, kutoka mapato ya Ng’ambo ya Mto Frati, ili ujenzi usisimame.
EZR 6:9 Chochote kinachohitajika kama mafahali wachanga, kondoo dume, wana-kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, ngano, chumvi, divai na mafuta kama vitakavyohitajika na makuhani huko Yerusalemu, lazima wapewe kila siku pasipo kukosa,
EZR 6:10 ili waweze kutoa dhabihu inayompendeza Mungu wa mbinguni na kumwombea mfalme na wanawe hali njema.
EZR 6:11 Zaidi ya hayo, ninaamuru kwamba mtu yeyote atakayebadilisha amri hii, boriti itang’olewa kutoka nyumba yake, ichongwe upande mmoja na atumbuliwe nayo. Kwa ajili ya kosa hili nyumba yake ifanywe lundo la taka.
EZR 6:12 Naye Mungu, aliyeliweka Jina lake huko, amwangushe mfalme yeyote au watu watakaoinua mikono kubadili amri hii au kuharibu Hekalu hili ambalo liko Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Nayo itekelezwe kwa bidii na kwa makini.
EZR 6:13 Kwa sababu ya amri aliyotoa Mfalme Dario, Tatenai mtawala wa Ng’ambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao wakaitekeleza kwa bidii na kwa makini.
EZR 6:14 Hivyo wazee wa Wayahudi waliendelea kujenga na kustawi kutokana na mahubiri ya manabii Hagai na Zekaria, wa uzao wa Ido. Wakakamilisha ujenzi wa Hekalu kulingana na agizo la Mungu wa Israeli na amri ya Koreshi, Dario na Artashasta wafalme wa Uajemi.
EZR 6:15 Hekalu lilikamilika siku ya kumi na mbili ya mwezi wa Adari, ndio mwezi wa tatu, katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Dario.
EZR 6:16 Kisha watu wa Israeli: makuhani, Walawi na wengine wote waliohamishwa, wakaadhimisha kule kuwekwa wakfu nyumba ya Mungu kwa shangwe.
EZR 6:17 Kwa ajili ya kuwekwa wakfu nyumba hii ya Mungu walitoa mafahali mia moja, kondoo dume mia mbili, wana-kondoo mia nne; sadaka kwa ajili ya dhambi ya Israeli wote walitoa beberu kumi na wawili, mmoja kwa ajili ya kila kabila la Israeli.
EZR 6:18 Wakawaweka makuhani katika nafasi zao na Walawi wakawekwa katika makundi yao ya huduma kwa Mungu huko Yerusalemu, kulingana na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Musa.
EZR 6:19 Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, waliorudi kutoka uhamishoni wakaadhimisha Pasaka.
EZR 6:20 Makuhani na Walawi walikuwa wamekwisha kujitakasa na hivyo wakatakasika. Walawi wakachinja kondoo wa Pasaka kwa ajili ya wana wa waliorudi kutoka utumwani uhamishoni, kwa ajili ya ndugu zao makuhani na wao wenyewe.
EZR 6:21 Hivyo Waisraeli waliorudi kutoka uhamishoni wakala Pasaka, pamoja na wale waliokuwa wamejitenga na matendo ya unajisi wa Mataifa jirani ili kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
EZR 6:22 Kwa muda wa siku saba waliiadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa furaha, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amewajaza furaha kwa kubadilisha nia ya mfalme wa Ashuru kwamba awasaidie ujenzi wa nyumba ya Mungu, Mungu wa Israeli.
EZR 7:1 Baada ya mambo haya, wakati wa utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Ezra mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia,
EZR 7:2 mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu,
EZR 7:3 mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi,
EZR 7:4 mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki,
EZR 7:5 mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani mkuu Haruni.
EZR 7:6 Huyu Ezra alipanda kutoka Babeli. Alikuwa mwandishi mwenye ujuzi mwingi katika Torati ya Musa, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alikuwa ametoa. Mfalme alikuwa amempa Ezra kila kitu alichoomba, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.
EZR 7:7 Baadhi ya Waisraeli, wakiwemo makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu na watumishi wa Hekalu, nao walikuja Yerusalemu mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta.
EZR 7:8 Ezra aliwasili Yerusalemu mwezi wa tano wa mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta.
EZR 7:9 Ezra alianza safari yake kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akawasili Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kwa kuwa mkono wa neema wa Mungu wake ulikuwa juu yake.
EZR 7:10 Kwa maana Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza na kushika Torati ya Mwenyezi Mungu na kuwafundisha Waisraeli amri na sheria zake.
EZR 7:11 Hii ni nakala ya barua ambayo Mfalme Artashasta alimpa Ezra aliyekuwa kuhani na mwalimu, mtu aliyeelimika katika mambo kuhusu maagizo na amri za Mwenyezi Mungu kwa Israeli.
EZR 7:12 Artashasta, mfalme wa wafalme, Kwa Ezra kuhani, mwalimu wa Torati ya Mungu wa mbinguni: Salamu.
EZR 7:13 Sasa naamuru kwamba mtu yeyote Mwisraeli katika ufalme wangu, pamoja na makuhani na Walawi, ambaye anataka kwenda Yerusalemu pamoja nawe aweza kwenda.
EZR 7:14 Unatumwa na mfalme na washauri wake saba kuchunguza habari za Yuda na Yerusalemu kulingana na Torati ya Mungu wako, iliyo mkononi mwako.
EZR 7:15 Zaidi ya hayo, uchukue fedha na dhahabu ambazo mfalme na washauri wake wamempa Mungu wa Israeli kwa hiari, Mungu ambaye maskani yake yako Yerusalemu,
EZR 7:16 pia fedha na dhahabu zote unazoweza kupata kutoka jimbo la Babeli, pamoja na sadaka za hiari watakazotoa watu na makuhani kwa ajili ya Hekalu la Mungu wao ambalo liko Yerusalemu.
EZR 7:17 Hakikisha kwamba fedha hizi zimetumika kununua mafahali, kondoo dume na wana-kondoo pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, uvitoe dhabihu juu ya madhabahu ya Hekalu la Mungu wenu katika Yerusalemu.
EZR 7:18 Kisha wewe na Wayahudi ndugu zako mnaweza kufanya lolote linaloonekana jema sana kwa fedha na dhahabu zilizosalia, kulingana na mapenzi ya Mungu wenu.
EZR 7:19 Uvitoe kwa Mungu wa Yerusalemu vyombo vyote ulivyokabidhiwa kwa ajili ya ibada katika Hekalu la Mungu wako.
EZR 7:20 Kitu kingine chochote kinachohitajika kwa ajili ya Hekalu la Mungu wenu ambacho unatakiwa kukitoa, unaweza kukitoa kutoka hazina ya mfalme.
EZR 7:21 Mimi, Mfalme Artashasta, sasa naagiza watunza hazina wote wa Ng’ambo ya Mto Frati kutoa kwa bidii chochote kwa Ezra kuhani na mwalimu wa Torati ya Mungu wa mbinguni atakachohitaji kwenu,
EZR 7:22 talanta mia moja za fedha, ngano kori mia moja, divai bathi mia moja, mafuta ya zeituni bathi mia moja, na chumvi kiasi chochote.
EZR 7:23 Chochote ambacho Mungu wa mbinguni ameagiza, kifanyike kwa ukamilifu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wa mbinguni. Kwa nini pawepo ghadhabu dhidi ya utawala wa mfalme na wanawe?
EZR 7:24 Pia ninyi fahamuni kuwa hamna mamlaka ya kuwatoza kodi, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu, watumishi wa Hekalu au wafanyakazi wengine kwenye nyumba ya Mungu.
EZR 7:25 Nawe Ezra, kufuatana na hekima ya Mungu wenu uliyo nayo, weka mahakimu na waamuzi wote wanaozifahamu sheria za Mungu wenu, ili watoe haki kwa watu wote wa Ng’ambo ya Mto Frati. Nawe inakupasa umfundishe yeyote ambaye hazifahamu.
EZR 7:26 Yeyote ambaye hataitii Torati ya Mungu wenu na pia sheria ya mfalme, hakika lazima aadhibiwe kwa kuuawa, kuhamishwa, kunyang’anywa mali au kufungwa gerezani.
EZR 7:27 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu, Mungu ambaye kwa njia hii ameweka ndani ya moyo wa mfalme kuipa heshima nyumba ya Mwenyezi Mungu iliyo Yerusalemu, kwa namna hii
EZR 7:28 ambaye ameniongezea kibali chake mbele ya mfalme, washauri wake na maafisa wote wa mfalme wenye uwezo. Kwa kuwa mkono wa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, ulikuwa pamoja nami, nilijipa moyo nikakusanya watu walio viongozi kutoka Israeli wakwee pamoja nami.
EZR 8:1 Hawa ndio viongozi wa jamaa pamoja na wale walioandikwa ambao walikuja pamoja nami kutoka Babeli wakati wa utawala wa Mfalme Artashasta:
EZR 8:2 wa wazao wa Finehasi, alikuwa Gershoni; wa wazao wa Ithamari, alikuwa Danieli; wa wazao wa Daudi, alikuwa Hatushi
EZR 8:3 wa wazao wa Shekania; wa wazao wa Paroshi, alikuwa Zekaria, na watu mia moja na hamsini walioandikishwa;
EZR 8:4 wa wazao wa Pahath-Moabu, alikuwa Eliehoenai mwana wa Zerahia na wanaume mia mbili;
EZR 8:5 wa wazao wa Zatu, alikuwa Shekania mwana wa Yahazieli na wanaume mia tatu;
EZR 8:6 wa wazao wa Adini, alikuwa Ebedi mwana wa Yonathani na wanaume hamsini;
EZR 8:7 wa wazao wa Elamu, alikuwa Yeshaya mwana wa Athalia, na wanaume sabini;
EZR 8:8 wa wazao wa Shefatia, alikuwa Zebadia mwana wa Mikaeli na wanaume themanini;
EZR 8:9 wa wazao wa Yoabu, alikuwa Obadia mwana wa Yehieli na wanaume mia mbili kumi na nane;
EZR 8:10 wa wazao wa Bani, alikuwa Shelomithi mwana wa Yosifia na wanaume mia moja na sitini;
EZR 8:11 wa wazao wa Bebai, alikuwa Zekaria mwana wa Bebai na wanaume ishirini na nane;
EZR 8:12 wa wazao wa Azgadi, alikuwa Yohanani mwana wa Hakatani na wanaume mia moja na kumi;
EZR 8:13 wa wazao wa Adonikamu: hawa walikuwa wa mwisho ambao majina yao ni Elifeleti, Yeueli, Shemaya na wanaume sitini;
EZR 8:14 wa wazao wa Bigwai, walikuwa Uthai na Zakuri na wanaume sabini.
EZR 8:15 Niliwakusanya kwenye mto unaotiririka kuelekea Ahava, nasi tukapiga kambi pale siku tatu. Nilipokagua kati ya watu na makuhani, sikuwapata Walawi.
EZR 8:16 Basi niliwaita Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu waliokuwa viongozi na Yoyaribu na Elnathani waliokuwa wasomi,
EZR 8:17 nikawatuma kwa Ido kiongozi huko Kasifia. Niliwaambia watakayomwambia Ido na ndugu zake, watumishi wa Hekalu huko Kasifia, ili waweze kutuletea wahudumu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.
EZR 8:18 Kwa sababu mkono wa neema wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, walituletea Sherebia, mtu mwenye busara kutoka wazao wa Mahli mwana wa Lawi, mwana wa Israeli, na wana wa Sherebia pamoja na ndugu zao wanaume kumi na nane.
EZR 8:19 Naye Hashabia, pamoja na Yeshaya kutoka wazao wa Merari na ndugu zake na wapwa wake, walikuwa wanaume ishirini.
EZR 8:20 Vilevile walileta watumishi wa Hekalu mia mbili na ishirini, kikundi ambacho Daudi na maafisa walikuwa wamekianzisha ili kusaidia Walawi. Wote waliorodheshwa kwa majina.
EZR 8:21 Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeze mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali yetu yote.
EZR 8:22 Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.”
EZR 8:23 Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.
EZR 8:24 Kisha niliwatenga viongozi wa makuhani kumi na wawili, pamoja na Sherebia, Hashabia na ndugu zao kumi,
EZR 8:25 nami nikawapimia fedha, dhahabu na vifaa ambavyo mfalme, washauri wake, maafisa wake na Waisraeli wote waliokuwepo walikuwa wamevitoa sadaka kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.
EZR 8:26 Niliwapimia talanta mia sita na hamsini za fedha, vifaa vingine vya fedha vya uzito wa talanta mia moja, talanta mia moja za dhahabu,
EZR 8:27 mabakuli ishirini ya dhahabu ya thamani ya darkoni elfu moja, na vyombo viwili vya shaba iliyosuguliwa, ya thamani kama dhahabu.
EZR 8:28 Niliwaambia, “Ninyi pamoja na vyombo hivi ni wakfu kwa Mwenyezi Mungu. Fedha na dhahabu ni sadaka ya hiari kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu.
EZR 8:29 Vilindeni kwa uangalifu hadi mtakapovipima ndani ya vyumba vya nyumba ya Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu mbele ya makuhani, viongozi na Walawi pamoja na wakuu wa jamaa za Israeli.”
EZR 8:30 Ndipo makuhani na Walawi wakapokea fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu ambavyo vilipimwa na kupelekwa katika nyumba ya Mungu wetu mjini Yerusalemu.
EZR 8:31 Tulianza safari kutoka Mto Ahava kwenda Yerusalemu siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza. Mkono wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, naye njiani alitulinda dhidi ya adui na wanyang’anyi.
EZR 8:32 Kwa hiyo tuliwasili Yerusalemu ambapo tulipumzika kwa siku tatu.
EZR 8:33 Katika siku ya nne, ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu, tukakabidhi mikononi mwa kuhani Meremothi mwana wa Uria. Eleazari mwana wa Finehasi alikuwa pamoja naye, na pia Walawi wawili, Yozabadi mwana wa Yeshua, na Noadia mwana wa Binui.
EZR 8:34 Kila kitu kilihesabiwa kwa idadi na kupimwa kwa uzito, nao uzito wote uliandikwa wakati ule.
EZR 8:35 Kisha mateka waliokuwa wamerudi kutoka utumwani wakatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mungu wa Israeli: mafahali kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, kondoo dume tisini na sita, wana-kondoo sabini na saba, na beberu kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi. Hii yote ilikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu.
EZR 8:36 Pia walikabidhi manaibu wa mfalme na watawala wa Ng’ambo ya Mto Frati maagizo ya mfalme, ambao baadaye walitoa msaada kwa watu na kwa nyumba ya Mungu.
EZR 9:1 Baada ya mambo haya kutendeka, viongozi walinijia na kusema, “Watu wa Israeli, wakiwemo makuhani na Walawi, hawakujitenga na majirani zao katika kufanya machukizo, kama yale ya Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi, Waamoni, Wamoabu, Wamisri na Waamori.
EZR 9:2 Wamewaoa baadhi ya binti zao kuwa wake zao na wake za wana wao, nao wamechanganya taifa takatifu na watu waliowazunguka. Nao viongozi na maafisa wamekuwa mstari wa mbele katika njia hii potovu.”
EZR 9:3 Niliposikia jambo hili nilirarua koti langu na joho langu, nikazing’oa nywele za kichwa changu na ndevu zangu na kuketi nikishangaa.
EZR 9:4 Kisha kila mmoja aliyetetemeshwa na maneno ya Mungu wa Israeli alikusanyika kunizunguka kwa sababu ya upotovu huu wa hao watu waliorudi kutoka utumwani. Nami niliketi pale nikishangaa hadi wakati wa dhabihu ya jioni.
EZR 9:5 Ndipo wakati wa kutoa dhabihu ya jioni nikainuka kutoka kujidhili kwangu nikiwa na koti na joho langu lililoraruka, nikapiga magoti mikono yangu ikiwa imeinuliwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
EZR 9:6 Nami nikaomba: “Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni.
EZR 9:7 Tokea siku za babu zetu hadi sasa, hatia yetu imekuwa kubwa. Kwa sababu ya dhambi zetu, sisi na wafalme wetu na makuhani wetu tumekabiliwa na vita, utumwa, kutekwa na kudhiliwa katika mikono ya wafalme wa kigeni, kama ilivyo leo.
EZR 9:8 “Lakini sasa, kwa muda mfupi, Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, amekuwa na neema kwa kutuachia mabaki na kutupatia mahali imara katika mahali pake patakatifu, hivyo Mungu wetu anatupatia mwanga machoni petu na unafuu katika utumwa wetu.
EZR 9:9 Ingawa tu watumwa, Mungu wetu hajatuacha katika kufungwa kwetu. Ametuonesha huruma mbele ya wafalme wa Uajemi: Ametujalia maisha mapya kwa kujenga upya nyumba ya Mungu wetu na kukarabati magofu yake, naye ametupatia ukuta wa ulinzi katika Yuda na Yerusalemu.
EZR 9:10 “Lakini sasa, Ee Mungu wetu, tunaweza kusema nini baada ya hili? Kwa maana tumedharau maagizo
EZR 9:11 uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii uliposema: ‘Nchi mnayoiingia kuimiliki ni nchi iliyochafuliwa na uovu wa watu wake. Kwa matendo yao ya machukizo wameijaza nchi kwa unajisi wao kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.
EZR 9:12 Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’
EZR 9:13 “Yale yaliyotupata ni matokeo ya matendo yetu mabaya, pia hatia yetu kubwa. Hata hivyo, wewe Mungu wetu, umetuadhibu kidogo kuliko dhambi zetu zilivyostahili na umetupatia mabaki kama haya.
EZR 9:14 Je, tutavunja maagizo yako tena na kuoana na watu ambao hufanya mambo ya machukizo? Je, hutakuwa na hasira ya kutosha juu yetu na kutuangamiza, bila kutuachia mabaki wala atakayenusurika?
EZR 9:15 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Siku ya leo tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”
EZR 10:1 Ezra alipokuwa anaomba na kuungama, huku akilia na kujitupa chini mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa Waisraeli wakiwemo wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kumzunguka. Nao pia wakalia sana.
EZR 10:2 Kisha Shekania mwana wa Yehieli, mmoja wa wazao wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni kutoka mataifa yanayotuzunguka. Lakini pamoja na hili, bado liko tumaini kwa ajili ya Israeli.
EZR 10:3 Sasa na tufanye agano mbele za Mungu wetu kuwafukuza hawa wanawake wote pamoja na watoto wao, kulingana na maonyo ya bwana wangu pamoja na wale ambao wanaogopa amri za Mungu wetu. Hili na lifanyike sawasawa na hii Torati.
EZR 10:4 Inuka, suala hili lipo mikononi mwako. Sisi tutaungana nawe, uwe na ujasiri ukatende hili.”
EZR 10:5 Basi Ezra akainuka na kuwaapisha makuhani viongozi, Walawi na Waisraeli wote kufanya lile lililokuwa limependekezwa. Nao wakaapa.
EZR 10:6 Ndipo Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu akaenda kwenye chumba cha Yehohanani mwana wa Eliashibu. Alipokuwa hapo, hakula chakula wala hakunywa maji, kwa sababu aliendelea kuomboleza kwa kuwa watu wa uhamishoni walikosa uaminifu kwa Mungu.
EZR 10:7 Ndipo lilipotolewa tangazo Yuda yote na Yerusalemu kwa watu wote waliokuwa uhamishoni kukusanyika Yerusalemu.
EZR 10:8 Yeyote ambaye hangejitokeza kwa muda wa siku tatu angepoteza mali yake yote, kulingana na uamuzi wa maafisa na wazee. Naye mtu huyo angefukuzwa kutoka kusanyiko la watu waliokuwa uhamishoni.
EZR 10:9 Katika muda wa siku tatu, watu wote wa Yuda na Benyamini wakawa wamekusanyika huko Yerusalemu. Kwenye siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walikuwa wameketi ndani ya uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakiwa na majonzi mno kwa tukio hilo na kwa sababu ya mvua kubwa.
EZR 10:10 Ndipo Kuhani Ezra aliposimama akawaambia, “Mmekosa uaminifu, mmeoa wanawake wa kigeni, mkaongezea hatia ya Israeli.
EZR 10:11 Sasa tubuni kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, mkafanye mapenzi yake. Jitengeni na mataifa wanaowazunguka na wake zenu wa kigeni.”
EZR 10:12 Kusanyiko lote wakajibu kwa sauti kubwa: “Uko sawa kabisa! Ni lazima tufanye kama unavyosema.
EZR 10:13 Lakini hapa pana watu wengi na ni wakati wa mvua, hivyo hatuwezi kusimama nje. Hata hivyo, shauri hili haliwezi kumalizika kwa siku moja au mbili, kwa sababu tumetenda dhambi kubwa katika jambo hili.
EZR 10:14 Maafisa wetu na watende kwa niaba ya kusanyiko lote. Kisha kila mmoja katika miji yetu ambaye ameoa mwanamke wa kigeni aje kwa wakati uliopangwa, akiwa pamoja na wazee na waamuzi wa kila mji, hadi hasira kali ya Mungu wetu katika shauri hili itakapoondolewa kwetu.”
EZR 10:15 Yonathani mwana wa Asaheli na Yazeya mwana wa Tikwa peke yao, wakiungwa mkono na Meshulamu na Shabethai Mlawi, ndio waliopinga jambo hili.
EZR 10:16 Basi watu wa uhamishoni wakafanya kama ilivyokuwa imependekezwa. Kuhani Ezra akachagua wanaume waliokuwa viongozi wa jamaa, mmoja kutoka kila mgawanyo wa jamaa, nao wote wakachaguliwa kwa majina. Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kumi waliketi kuchunguza mashauri hayo.
EZR 10:17 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wakawa wamemaliza kushughulikia wanaume wote waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni.
EZR 10:18 Miongoni mwa wazao wa makuhani, wafuatao walikuwa wameoa wanawake wa kigeni: Kutoka wazao wa Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zake: Maaseya, Eliezeri, Yaribu na Gedalia.
EZR 10:19 (Wote walitoa nadhiri kwa kuandika kwa mikono yao kuwafukuza wake zao, kwa hatia yao, kila mmoja akatoa kondoo dume kutoka kundini mwake kuwa sadaka ya hatia.)
EZR 10:20 Kutoka wazao wa Imeri: Hanani na Zebadia.
EZR 10:21 Kutoka wazao wa Harimu: Maaseya, Ilya, Shemaya, Yehieli na Uzia.
EZR 10:22 Kutoka wazao wa Pashuri: Elioenai, Maaseya, Ishmaeli, Nethaneli, Yozabadi na Elasa.
EZR 10:23 Miongoni mwa Walawi: Yozabadi, Shimei, Kelaya (ndiye Kelita), Pethahia, Yuda na Eliezeri.
EZR 10:24 Kutoka waimbaji: Eliashibu. Kutoka mabawabu: Shalumu, Telemu na Uri.
EZR 10:25 Miongoni mwa Waisraeli wengine: Kutoka wazao wa Paroshi: Ramia, Izia, Malkiya, Miyamini, Eleazari, Malkiya na Benaya.
EZR 10:26 Kutoka wazao wa Elamu: Matania, Zekaria, Yehieli, Abdi, Yeremothi na Ilya.
EZR 10:27 Kutoka wazao wa Zatu: Elioenai, Eliashibu, Matania, Yeremothi, Zabadi na Aziza.
EZR 10:28 Kutoka uzao wa Bebai: Yehohanani, Hanania, Zabai na Athlai.
EZR 10:29 Kutoka wazao wa Bani: Meshulamu, Maluki, Adaya, Yashubu, Sheali na Yeremothi.
EZR 10:30 Kutoka wazao wa Pahath-Moabu: Adna, Kelali, Benaya, Maaseya, Matania, Bezaleli, Binui na Manase.
EZR 10:31 Kutoka wazao wa Harimu: Eliezeri, Ishiya, Malkiya, Shemaya, Shimeoni,
EZR 10:32 Benyamini, Maluki, na Shemaria.
EZR 10:33 Kutoka wazao wa Hashumu: Matenai, Matata, Zabadi, Elifeleti, Yeremai, Manase na Shimei.
EZR 10:34 Kutoka wazao wa Bani: Maadai, Amramu, Ueli,
EZR 10:35 Benaya, Bedeya, Keluhi,
EZR 10:36 Vania, Meremothi, Eliashibu,
EZR 10:37 Matania, Matenai na Yaasu.
EZR 10:38 Kutoka wazao wa Binui: Shimei,
EZR 10:39 Shelemia, Nathani, Adaya,
EZR 10:40 Maknadebai, Shashai, Sharai,
EZR 10:41 Azareli, Shelemia, Shemaria,
EZR 10:42 Shalumu, Amaria na Yusufu.
EZR 10:43 Kutoka wazao wa Nebo: Yeieli, Matithia, Zabadi, Zebina, Yadai, Yoeli na Benaya.
EZR 10:44 Hawa wote walikuwa wameoa wanawake wa kigeni, na baadhi yao walikuwa wamezaa nao watoto.
NEH 1:1 Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia: Katika mwezi wa Kislevu katika mwaka wa ishirini, wakati nilikuwa ngomeni katika jumba la kifalme la Shushani,
NEH 1:2 Hanani, mmoja wa ndugu zangu, alikuja kutoka Yuda akiwa na watu wengine, nami nikawauliza kuhusu mabaki ya Wayahudi wale walionusurika kwenda uhamishoni na pia kuhusu Yerusalemu.
NEH 1:3 Wakaniambia, “Wale walionusurika kwenda uhamishoni, wale ambao wamerudi kwenye lile jimbo, wako katika taabu kubwa na aibu. Ukuta wa Yerusalemu umebomoka, na malango yake yamechomwa moto.”
NEH 1:4 Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni.
NEH 1:5 Kisha nikasema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika agano lake la upendo na wale wanaompenda na kutii amri zake,
NEH 1:6 tega masikio yako, na ufungue macho yako, ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako usiku na mchana kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako.
NEH 1:7 Tumetenda uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo na sheria ulizompa Musa mtumishi wako.
NEH 1:8 “Kumbuka agizo ulilompa Musa mtumishi wako, ukisema, ‘Mkikosa uaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa,
NEH 1:9 lakini mkinirudia na kutii amri zangu, ndipo hata kama watu wenu walio uhamishoni katika miisho ya dunia, nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali nilipopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina langu.’
NEH 1:10 “Hawa ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na mkono wako wenye nguvu.
NEH 1:11 Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Nipe leo, mimi mtumishi wako, mafanikio kwa kunipa kibali mbele ya mtu huyu.” Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.
NEH 2:1 Katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa utawala wa Mfalme Artashasta, wakati divai ilipoletwa kwake, niliichukua na kumpa mfalme. Sikuwahi kuonekana mwenye huzuni mbele yake kabla ya hapo.
NEH 2:2 Basi mfalme akaniuliza, “Kwa nini uso wako unaonekana una huzuni wakati wewe si mgonjwa? Jambo hili si kitu kingine bali ni huzuni ya moyo.” Niliogopa sana,
NEH 2:3 lakini nikamwambia mfalme, “Mfalme na aishi milele! Kwa nini uso wangu usiwe na huzuni wakati mji walipozikwa baba zangu umebaki magofu, na malango yake yameteketezwa kwa moto?”
NEH 2:4 Mfalme akaniambia, “Je, haja yako ni nini?” Ndipo nikaomba kwa Mungu wa mbinguni,
NEH 2:5 na nikamjibu mfalme, “Ikimpendeza mfalme, na kama mtumishi wako amepata kibali machoni pake, anitume kule mji wa Yuda, mahali baba zangu walipozikwa, ili niweze kuujenga upya.”
NEH 2:6 Kisha mfalme, huku malkia akiwa ameketi karibu naye, akaniuliza, “Safari yako itachukua muda gani, nawe utarudi lini?” Ilimpendeza mfalme kunituma, kwa hiyo nikapanga muda.
NEH 2:7 Pia nikamwambia, “Ikimpendeza mfalme, naomba nipewe barua kwa watawala wa Ng’ambo ya Frati, ili wanipe ulinzi hadi nifike Yuda.
NEH 2:8 Naomba nipewe barua nipeleke kwa Asafu, mtunzaji wa msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengeneza boriti kwa ajili ya malango ya ngome ya Hekalu, na ukuta wa mji, na makao yangu nitakayoishi.” Kwa kuwa mkono wenye neema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu, mfalme akanijalia ombi langu.
NEH 2:9 Basi nilienda kwa watawala wa Ng’ambo ya Frati na kuwapa barua za mfalme. Pia mfalme alikuwa ametuma maafisa wa jeshi na askari wapanda farasi pamoja nami.
NEH 2:10 Sanbalati Mhoroni na Tobia afisa Mwamoni waliposikia kuhusu jambo hili, waliudhika sana kwamba amekuja mtu kuinua ustawi wa Waisraeli.
NEH 2:11 Nilienda Yerusalemu, na baada ya kukaa huko siku tatu,
NEH 2:12 nikaondoka wakati wa usiku pamoja na watu wachache. Sikuwa nimemwambia mtu yeyote kile ambacho Mungu wangu alikuwa ameweka moyoni mwangu kufanya kwa ajili ya Yerusalemu. Hapakuwa na mnyama yeyote nami isipokuwa yule niliyekuwa nimempanda.
NEH 2:13 Nikatoka nje usiku kupitia Lango la Bondeni, kuelekea Kisima cha Joka na Lango la Samadi, nikikagua kuta za Yerusalemu zilizokuwa zimebomolewa, na malango yake yaliyokuwa yameteketezwa kwa moto.
NEH 2:14 Kisha nikaelekea hadi Lango la Chemchemi na Bwawa la Mfalme, lakini hapakuwa na nafasi ya kutosha mnyama wangu kupita,
NEH 2:15 kwa hiyo nikapandia bondeni usiku nikikagua ukuta. Mwishoni nikarudi na kuingia tena kupitia Lango la Bondeni.
NEH 2:16 Maafisa hawakujua nilikoenda wala nilichokuwa nikifanya, kwa sababu nilikuwa bado sijasema lolote kwa Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala maafisa, wala mtu yeyote ambaye angefanya kazi.
NEH 2:17 Ndipo nilipowaambia, “Mnaona taabu tuliyo nayo: Yerusalemu imebaki magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Njooni tujenge upya ukuta wa Yerusalemu, nasi hatutakuwa tena katika aibu hii.”
NEH 2:18 Pia niliwaambia kuhusu mkono wenye neema wa Mungu wangu uliokuwa juu yangu, na kile mfalme alichokuwa ameniambia. Wakajibu, “Haya! Tuanze kujenga tena.” Kwa hiyo wakaanza kazi hii njema.
NEH 2:19 Lakini Sanbalati Mhoroni, Tobia afisa Mwamoni, na Geshemu Mwarabu waliposikia kuhusu jambo hili, walitudhihaki na kutucheka. Wakauliza, “Ni nini hiki mnachokifanya? Je, mnaasi dhidi ya mfalme?”
NEH 2:20 Nikawajibu kwa kusema, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha. Sisi watumishi wake tutaanza kujenga upya, lakini ninyi hamna sehemu wala dai lolote, wala kumbukumbu la haki katika Yerusalemu.”
NEH 3:1 Eliashibu kuhani mkuu na makuhani wenzake walienda kufanya kazi na kulijenga upya Lango la Kondoo. Waliliweka wakfu na kuweka milango mahali pake, wakajenga hadi kufikia Mnara wa Mia, ambao waliuweka wakfu hadi Mnara wa Hananeli.
NEH 3:2 Wanaume wa Yeriko wakajenga sehemu zilizopakana nao, naye Zakuri mwana wa Imri akajenga karibu nao.
NEH 3:3 Lango la Samaki lilijengwa upya na wana wa Hasenaa. Waliweka boriti zake, na wakaweka milango yake na makomeo na nondo.
NEH 3:4 Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu iliyofuatia. Baada yake Meshulamu mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli, alifanya ukarabati na aliyemfuatia ni Sadoki mwana wa Baana.
NEH 3:5 Sehemu iliyofuatia ilikarabatiwa na watu kutoka Tekoa, lakini wakuu wao walikataa kufanya kazi chini ya wasimamizi wao.
NEH 3:6 Lango la Yeshana lilikarabatiwa na Yoyada mwana wa Pasea, na Meshulamu mwana wa Besodeya. Waliweka boriti zake, na wakaweka milango, makomeo na nondo.
NEH 3:7 Karibu nao ukarabati ulifanywa na watu kutoka Gibeoni na Mispa, yaani Melati Mgibeoni, na Yadoni Mmeronothi, sehemu hizi zikiwa chini ya mamlaka ya mtawala wa Ng’ambo ya Frati.
NEH 3:8 Uzieli mwana wa Harhaya, mmoja wa masonara, alikarabati sehemu iliyofuatia, naye Hanania mmoja wa watengenezaji marashi akakarabati sehemu iliyofuatia. Walitengeneza Yerusalemu kufikia Ukuta Mpana.
NEH 3:9 Refaya mwana wa Huri, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia.
NEH 3:10 Kupakana na sehemu hii, Yedaya mwana wa Harumafu alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba yake, naye Hatushi mwana wa Hashabnea akakarabati sehemu iliyofuatia.
NEH 3:11 Malkiya mwana wa Harimu, na Hashubu mwana wa Pahath-Moabu walikarabati sehemu nyingine pamoja na Mnara wa Matanuru.
NEH 3:12 Shalumu mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia akisaidiwa na binti zake.
NEH 3:13 Lango la Bondeni lilikarabatiwa na Hanuni na wakazi wa Zanoa. Walilijenga upya, na kuweka milango yake na makomeo na nondo mahali pake. Pia walikarabati ukuta wenye urefu wa dhiraa elfu moja hadi Lango la Samadi.
NEH 3:14 Lango la Samadi lilikarabatiwa na Malkiya mwana wa Rekabu, mtawala wa wilaya ya Beth-Hakeremu. Alilijenga upya, na kuweka milango yake, na makomeo na nondo.
NEH 3:15 Lango la Chemchemi lilikarabatiwa na Shalumu mwana wa Kolhoze, mtawala wa wilaya ya Mispa. Alilijenga upya, akaliezeka na kuweka milango yake, na makomeo na nondo mahali pake. Pia alikarabati ukuta wa Bwawa la Siloamu karibu na Bustani ya Mfalme, hadi kwenye ngazi zinazoshuka kutoka Mji wa Daudi.
NEH 3:16 Baada yake, Nehemia mwana wa Azbuki, mtawala wa nusu ya wilaya ya Beth-Suri, alikarabati kufikia mkabala na makaburi ya Daudi, hadi kwenye bwawa lililotengenezwa, na kufikia Nyumba ya Mashujaa.
NEH 3:17 Baada yake, ukarabati ulifanywa na Walawi chini ya uongozi wa Rehumu mwana wa Bani. Aliyefuatia ni Hashabia, mtawala wa nusu ya wilaya ya Keila, aliyekarabati sehemu ya wilaya yake.
NEH 3:18 Baada yake, ukarabati ulifanywa na ndugu zao chini ya usimamizi wa Binui mwana wa Henadadi, mtawala wa nusu hiyo ingine ya wilaya ya Keila.
NEH 3:19 Baada yao, Ezeri mwana wa Yeshua, mtawala wa Mispa, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia ile sehemu inayotazamana na mwinuko wa kuelekea kwenye ghala la kuhifadhia silaha, hadi kwenye pembe ya ukuta.
NEH 3:20 Baada yake, Baruku mwana wa Zakai alikarabati kwa bidii sehemu nyingine kuanzia ile pembe, hadi kwenye lango la nyumba ya Eliashibu kuhani mkuu.
NEH 3:21 Kupakana naye, Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia penye lango la nyumba ya Eliashibu hadi mwisho wake.
NEH 3:22 Baada yake, ukarabati ulifanywa na makuhani waliotoka eneo lililouzunguka mji.
NEH 3:23 Baada yao Benyamini na Hashubu walikarabati mbele ya nyumba zao, na baada yao Azaria mwana wa Maaseya, mwana wa Anania alifanya ukarabati kando ya nyumba yake.
NEH 3:24 Baada yake, Binui mwana wa Henadadi alikarabati sehemu nyingine, kuanzia kwenye nyumba ya Azaria hadi kwenye pembe ya ukuta.
NEH 3:25 Naye Palali, mwana wa Uzai alijenga sehemu iliyokuwa mkabala na pembe ya ukuta, hadi kwenye mnara wa juu ambao unachomoka kuanzia kwenye jumba la kifalme, kando ya ua wa walinzi. Baada yake, Pedaya mwana wa Paroshi,
NEH 3:26 na watumishi wa Hekalu walioishi juu ya kilima cha Ofeli walikarabati hadi kufikia mkabala na Lango la Maji, kuelekea mashariki na ule mnara uliochomoza.
NEH 3:27 Baada yao, watu wa Tekoa walikarabati sehemu nyingine, kuanzia mnara mkubwa unaochomoza hadi ukuta wa Ofeli.
NEH 3:28 Makuhani walifanya ukarabati juu ya Lango la Farasi, kila mmoja mbele ya nyumba yake.
NEH 3:29 Baada yao, Sadoki mwana wa Imeri alifanya ukarabati mkabala na nyumba yake. Baada yake, Shemaya mwana wa Shekania, mlinzi wa Lango la Mashariki, alifanya ukarabati.
NEH 3:30 Baada yake, Hanania mwana wa Shelemia, na Hanuni mwana wa sita wa Salafu walikarabati sehemu nyingine. Baada yao, Meshulamu mwana wa Berekia alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba zake za kuishi.
NEH 3:31 Baada yake Malkiya, mmoja wa masonara, alifanya ukarabati hadi kwenye nyumba za watumishi wa Hekalu na wafanyabiashara, mkabala na Lango la Ukaguzi, hadi kufikia chumba kilicho juu ya pembe.
NEH 3:32 Masonara na wafanyabiashara walifanya ukarabati kutoka chumba kilichoko juu ya pembe hadi Lango la Kondoo.
NEH 4:1 Sanbalati aliposikia kwamba tulikuwa tunajenga ukuta upya, alikasirika na akawa na uchungu sana. Aliwadhihaki Wayahudi
NEH 4:2 mbele ya rafiki zake na jeshi la Samaria, akisema, “Hawa Wayahudi wanyonge wanafanya nini? Je, wataweza kuurudishia ukuta wao? Je, watatoa dhabihu? Je, wataweza kumaliza kuujenga kwa siku moja? Je, wataweza kufufua mawe kutoka malundo ya vifusi yaliyoungua hivyo?”
NEH 4:3 Tobia Mwamoni aliyekuwa upande wake akasema, “Wanachokijenga, hata kama mbweha angepanda juu yake, huo ukuta wao wa mawe angeubomoa!”
NEH 4:4 Ee Mungu wetu, utusikie, kwa kuwa tumedharauliwa. Warudishie matukano yao kwenye vichwa vyao wenyewe. Uwatoe ili wawe nyara katika nchi ya waliowateka.
NEH 4:5 Usiusitiri uovu wao, wala usifute dhambi zao mbele zako, kwa kuwa wamewatukana wajenzi.
NEH 4:6 Basi tuliujenga upya ukuta hadi wote ukafikia nusu ya kimo chake, kwa kuwa watu walifanya kazi kwa moyo wote.
NEH 4:7 Lakini wakati Sanbalati, Tobia, Waarabu, Waamoni na watu wa Ashdodi waliposikia kuwa ukarabati wa kuta za Yerusalemu ulikuwa umeendelea, na mianya ilikuwa inazibwa, walikasirika sana.
NEH 4:8 Wote walifanya shauri pamoja kuja kupigana dhidi ya Yerusalemu, na kuchochea machafuko dhidi yake.
NEH 4:9 Lakini tulimwomba Mungu wetu, na tukaweka ulinzi usiku na mchana kupambana na tishio hili.
NEH 4:10 Wakati ule ule, watu wa Yuda wakasema, “Nguvu za wafanyakazi zinapungua, nacho kifusi ni kingi mno, kiasi kwamba hatuwezi kuujenga upya ukuta.”
NEH 4:11 Pia adui zetu walisema, “Kabla hawajajua au kutuona, tutakuwa pale kati yao, na tutawaua na kuikomesha hiyo kazi.”
NEH 4:12 Kisha Wayahudi ambao waliishi karibu nao walikuja zaidi ya mara kumi na kutuambia, “Popote mtakapoelekea, watatushambulia.”
NEH 4:13 Kwa hiyo nikaweka baadhi ya watu nyuma ya sehemu za chini za ukuta kwenye sehemu zilizo wazi, nikawaweka kufuatana na jamaa zao, wakiwa na panga, mikuki na pinde zao.
NEH 4:14 Baada ya kuona hali ilivyo, nikasimama na kuwaambia wakuu, maafisa na wengine wote, “Msiwaogope. Mkumbukeni Bwana, ambaye ni mkuu na mwenye kuogofya. Piganeni kwa ajili ya ndugu zenu, wana wenu na binti zenu, wake zenu na nyumba zenu.”
NEH 4:15 Adui zetu waliposikia kwamba tumetambua hila yao, na kwamba Mungu ameivuruga hila hiyo, sote tulirudi kwenye ukuta, kila mmoja kwenye kazi yake.
NEH 4:16 Kuanzia siku ile na kuendelea, nusu ya watu wangu walifanya kazi ya ujenzi, na nusu nyingine wakashika mikuki, ngao, pinde na dirii. Maafisa walijipanga nyuma ya watu wote wa Yuda
NEH 4:17 waliokuwa wakijenga ukuta. Wale waliobeba vifaa vya ujenzi walifanya kazi yao kwa mkono mmoja, na kushika silaha kwa mkono mwingine,
NEH 4:18 na kila mjenzi alijifunga upanga wake upande mmoja akiwa anafanya kazi. Lakini mtu wa kupiga baragumu alikaa pamoja nami.
NEH 4:19 Kisha nikawaambia wakuu, maafisa na watu wengine wote, “Kazi hii ni kubwa na imeenea sehemu kubwa, nasi tumetawanyika kila mmoja akiwa mbali na mwenzake katika ukuta.
NEH 4:20 Popote mtakaposikia sauti ya baragumu, jiungeni nasi huko. Mungu wetu atatupigania!”
NEH 4:21 Basi tuliendelea na kazi, nusu ya watu wakishikilia mikuki, kuanzia mawio ya jua hadi nyota zilipoonekana.
NEH 4:22 Wakati huo pia niliwaambia watu, “Kila mtu na msaidizi wake wakae ndani ya Yerusalemu wakati wa usiku, ili waweze kutumika kama walinzi wakati wa usiku, na kufanya kazi wakati wa mchana.”
NEH 4:23 Mimi, wala ndugu zangu, wala watu wangu, wala walinzi waliokuwa pamoja nami hatukuvua nguo zetu. Kila mmoja alikuwa na silaha yake, hata alipoenda kuchota maji.
NEH 5:1 Wakati huu wanaume na wake zao wakalia kilio kikuu dhidi ya ndugu zao Wayahudi.
NEH 5:2 Baadhi yao walikuwa wakisema, “Sisi na wana wetu wa kiume na wa kike tuko wengi. Ili tuweze kula na kuishi, ni lazima tupate nafaka.”
NEH 5:3 Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu, na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.”
NEH 5:4 Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu.
NEH 5:5 Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu wa kiume na wa kike kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya watu wengine.”
NEH 5:6 Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana.
NEH 5:7 Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaita mkutano mkubwa ili kukabiliana nao,
NEH 5:8 nikasema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wasioamini. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Wakanyamaza, kwa sababu hawakupata chochote cha kusema.
NEH 5:9 Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu wasioamini?
NEH 5:10 Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome!
NEH 5:11 Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.”
NEH 5:12 Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu chochote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.” Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi.
NEH 5:13 Pia nikakung’uta makunjo ya vazi langu na kusema, “Kila mtu ambaye hatatimiza ahadi hii, Mungu na amkung’ute hivi kutoka nyumba yake na katika mali yake. Basi mtu kama huyo akung’utiwe nje na aachwe bila kitu!” Waliposikia hili, mkutano wote ukasema, “Amen,” na wakamtukuza Mwenyezi Mungu. Nao watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.
NEH 5:14 Zaidi ya hayo, kutoka mwaka wa ishirini wa Mfalme Artashasta, wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, hadi mwaka wake wa thelathini na mbili, yaani miaka kumi na mbili, mimi wala ndugu zangu hatukula chakula ambacho kwa kawaida hupewa watawala.
NEH 5:15 Lakini watawala wa mwanzoni, wale walionitangulia, waliwalemea watu na kuchukua kutoka kwao shekeli arobaini za fedha, pamoja na chakula na mvinyo. Wasaidizi wao pia walijifanya wakuu juu ya watu. Lakini kwa kumheshimu Mungu sikufanya hivyo.
NEH 5:16 Badala yake, nilijitoa kwa bidii katika kazi ya ukuta huu. Watu wangu wote walikutanika pale kwa ajili ya kazi. Hatukujipatia shamba lolote.
NEH 5:17 Zaidi ya hayo, Wayahudi na maafisa mia moja na hamsini walikula mezani pangu, pamoja na wale waliotujia kutoka mataifa jirani.
NEH 5:18 Kila siku niliandaliwa maksai mmoja, kondoo sita wazuri, na kuku, na mvinyo wa kila aina kwa wingi kila baada ya siku kumi. Licha ya mambo haya yote, sikudai chakula kilichokuwa fungu la mtawala, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana kwa watu hawa.
NEH 5:19 Unikumbuke kwa fadhili, Ee Mungu wangu, kwa yote niliyofanya kwa ajili ya watu hawa.
NEH 6:1 Habari zilipofika kwa Sanbalati, Tobia, Geshemu Mwarabu, na adui zetu wengine kwamba nimejenga tena ukuta na hakuna nafasi iliyobakia ndani yake, ingawa hata wakati huo sikuwa nimeweka milango kwenye malango,
NEH 6:2 Sanbalati na Geshemu wakanitumia ujumbe huu: “Njoo, tukutane katika mojawapo ya vijiji katika nchi tambarare ya Ono.” Lakini walikuwa wakikusudia kunidhuru.
NEH 6:3 Kwa hiyo niliwatuma wajumbe kwao na majibu haya: “Kazi ninayoifanya ni kubwa sana, siwezi kuja. Kwa nini niiache kazi isimame nije kwenu?”
NEH 6:4 Walinitumia ujumbe huo huo mara nne, na kila mara nikawapa jibu lile lile.
NEH 6:5 Basi, mara ya tano, Sanbalati akamtuma msaidizi wake kwangu akiwa na ujumbe ule ule, naye alikuwa amechukua mkononi mwake barua isiyofungwa,
NEH 6:6 iliyokuwa imeandikwa: “Habari imeenezwa miongoni mwa mataifa, naye Geshemu anasema kwamba ni kweli, kuwa wewe na Wayahudi mnapanga njama ya kuasi, ndiyo sababu mnajenga ukuta. Zaidi ya hayo, kufuatana na taarifa hizi, karibuni utakuwa mfalme wao,
NEH 6:7 na hata umewateua manabii wafanye tangazo hili kukuhusu huko Yerusalemu: ‘Yuko mfalme katika Yuda!’ Sasa taarifa hii itarudishwa kwa mfalme. Basi njoo, tufanye shauri pamoja.”
NEH 6:8 Nilimpelekea jibu hili: “Hakuna jambo kama hilo unalosema linalofanyika. Unalitunga tu kwenye kichwa chako.”
NEH 6:9 Wote walikuwa wakijaribu kutuogopesha, wakifikiri hivi: “Mikono ya watu italegea kiasi kwamba hawataweza kufanya kazi, nayo haitakamilika.” Lakini niliomba, “Ee Mungu, sasa nitie mikono yangu nguvu.”
NEH 6:10 Siku moja nilienda nyumbani mwa Shemaya mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa ndani ya nyumba yake. Akasema, “Tukutane katika nyumba ya Mungu, ndani ya Hekalu, na tufunge milango ya Hekalu, kwa sababu watu wanakuja kukuua. Naam, wanakuja usiku kukuua.”
NEH 6:11 Lakini nikasema, “Je, mtu kama mimi akimbie? Au mtu kama mimi aende Hekaluni kuokoa maisha yake? Sitaenda!”
NEH 6:12 Nilitambua kwamba Mungu hakumtuma, bali alitabiri dhidi yangu kwa sababu Tobia na Sanbalati walikuwa wamemwajiri.
NEH 6:13 Alikuwa ameajiriwa kunitisha ili kwa kufanya jambo hili nitende dhambi, kisha waweze kuniharibia jina langu na kuniaibisha.
NEH 6:14 Ee Mungu wangu, wakumbuke Tobia na Sanbalati kwa sababu ya yale waliyotenda. Pia kumbuka nabii mke Noadia na manabii wengine ambao wamekuwa wakijaribu kunitisha.
NEH 6:15 Basi ukuta ukakamilika siku ya ishirini na tano mwezi wa Eluli; kazi ilichukua siku hamsini na mbili.
NEH 6:16 Adui zetu wote waliposikia kuhusu hili, mataifa yote yaliyotuzunguka yakaogopa na kupoteza ujasiri, kwa sababu yalitambua kuwa kazi hii imefanyika kwa msaada wa Mungu wetu.
NEH 6:17 Pia katika siku hizo wakuu wa Yuda walikuwa wakituma barua nyingi kwa Tobia, nayo majibu yaliyotoka kwa Tobia yaliendelea kuwajia.
NEH 6:18 Kwa kuwa watu wengi katika Yuda walikuwa wamemwapia Tobia, kwani alikuwa mkwewe Shekania mwana wa Ara, na Yehohanani mwanawe alikuwa amemwoa binti Meshulamu mwana wa Berekia.
NEH 6:19 Zaidi ya hayo, walikuwa wakiniarifu jinsi Tobia alivyo mtu mwema, nao walimwambia kila kitu nilichosema. Naye Tobia alituma barua za kunitisha.
NEH 7:1 Baada ya ukuta kukamilika kujengwa upya na nikaweka milango, mabawabu wa lango, waimbaji, na Walawi waliteuliwa.
NEH 7:2 Nikamweka Hanani ndugu yangu kuwa kiongozi wa Yerusalemu, pamoja na Hanania jemadari wa ngome, kwa kuwa alikuwa mtu mwadilifu na mwenye kumcha Mungu kuliko watu wengine.
NEH 7:3 Nikawaambia, “Malango ya Yerusalemu yasifunguliwe hadi jua litakapokuwa limepanda. Walinzi wa malango wakiwa bado kwenye zamu, waamuru wafunge milango na waweke makomeo. Pia wateueni wenyeji wa Yerusalemu wawe walinzi, kila mmoja kwenye lindo lake, na wengine karibu na nyumba zao wenyewe.”
NEH 7:4 Mji ulikuwa mkubwa, tena wenye nafasi nyingi, lakini walikuwepo watu wachache ndani yake, nazo nyumba zilikuwa bado ni magofu.
NEH 7:5 Hivyo Mungu wangu akaweka moyoni mwangu kuwakusanya wakuu, maafisa na watu kwa ajili ya kuorodheshwa kulingana na jamaa zao. Nilikuta orodha ya vizazi ya wale waliokuwa wa kwanza kurudi toka utumwani. Haya ndio niliyokuta yameandikwa humo:
NEH 7:6 Hawa ndio watu wa jimbo waliotoka uhamishoni, ambao Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa amewachukua mateka (walirudi Yerusalemu na Yuda, kila mmoja kwenye mji wake,
NEH 7:7 wakiwa wamefuatana na Zerubabeli, Yeshua, Nehemia, Azaria, Raamia, Nahamani, Mordekai, Bilshani, Mispereti, Bigwai, Nehumu na Baana):
NEH 7:8 wazao wa Paroshi, elfu mbili mia moja sabini na wawili (2,172);
NEH 7:9 wazao wa Shefatia, mia tatu sabini na wawili (372);
NEH 7:10 wazao wa Ara, mia sita hamsini na wawili (652);
NEH 7:11 wazao wa Pahath-Moabu (wa jamaa ya Yeshua na Yoabu), elfu mbili mia nane na kumi na nane (2,818);
NEH 7:12 wazao wa Elamu, elfu moja mia mbili hamsini na wanne (1,254);
NEH 7:13 wazao wa Zatu, mia nane arobaini na watano (845);
NEH 7:14 wazao wa Zakai, mia saba na sitini (760);
NEH 7:15 wazao wa Binui, mia sita ishirini na wanne (648);
NEH 7:16 wazao wa Bebai, mia sita ishirini na nane (628);
NEH 7:17 wazao wa Azgadi, elfu mbili mia tatu ishirini na wawili (2,322);
NEH 7:18 wazao wa Adonikamu, mia sita sitini na saba (667);
NEH 7:19 wazao wa Bigwai, elfu mbili na sitini na saba (2,067);
NEH 7:20 wazao wa Adini, mia sita hamsini na watano (655);
NEH 7:21 wazao wa Ateri (kupitia Hezekia), tisini na nane (98);
NEH 7:22 wazao wa Hashumu, mia tatu ishirini na nane (328);
NEH 7:23 wazao wa Besai, mia tatu ishirini na wanne (324);
NEH 7:24 wazao wa Harifu, mia moja na kumi na wawili (112);
NEH 7:25 wazao wa Gibeoni, tisini na watano (95);
NEH 7:26 watu wa Bethlehemu na Netofa, mia moja na themanini na nane (188);
NEH 7:27 watu wa Anathothi, mia moja ishirini na nane (128);
NEH 7:28 watu wa Beth-Azmawethi, arobaini na wawili (42);
NEH 7:29 watu wa Kiriath-Yearimu, Kefira na Beerothi, mia saba arobaini na watatu (743);
NEH 7:30 watu wa Rama na Geba, mia sita ishirini na mmoja (621);
NEH 7:31 watu wa Mikmashi, mia moja ishirini na wawili (122);
NEH 7:32 watu wa Betheli na Ai, mia moja ishirini na watatu (123);
NEH 7:33 watu wa Nebo, hamsini na wawili (52);
NEH 7:34 wazao wa Elamu, elfu moja mia mbili hamsini na wanne (1,254);
NEH 7:35 wazao wa Harimu, mia tatu na ishirini (320);
NEH 7:36 wazao wa Yeriko, mia tatu arobaini na watano (345);
NEH 7:37 wazao wa Lodi, Hadidi na Ono, mia saba ishirini na mmoja (721);
NEH 7:38 wazao wa Senaa, elfu tatu mia tisa na thelathini (3,930).
NEH 7:39 Makuhani: wazao wa Yedaya (kwa jamaa ya Yeshua), mia tisa sabini na watatu (973);
NEH 7:40 wazao wa Imeri, elfu moja hamsini na wawili (1,052);
NEH 7:41 wazao wa Pashuri, elfu moja mia mbili arobaini na saba (1,247);
NEH 7:42 wazao wa Harimu, elfu moja na kumi na saba (1,017).
NEH 7:43 Walawi: wazao wa Yeshua (kupitia Kadmieli kupitia jamaa ya Hodavia), sabini na wanne (74).
NEH 7:44 Waimbaji: wazao wa Asafu, mia moja arobaini na nane (148).
NEH 7:45 Mabawabu wa malango: wazao wa Shalumu, Ateri, Talmoni, Akubu, Hatita na Shobai, mia moja thelathini na nane (138).
NEH 7:46 Watumishi wa Hekalu: wazao wa Siha, Hasufa, Tabaothi,
NEH 7:47 wazao wa Kerosi, Sia, Padoni,
NEH 7:48 wazao wa Lebana, Hagaba, Shalmai,
NEH 7:49 wazao wa Hanani, Gideli, Gahari,
NEH 7:50 wazao wa Reaya, Resini, Nekoda,
NEH 7:51 wazao wa Gazamu, Uza, Pasea,
NEH 7:52 wazao wa Besai, Meunimu, Nefusimu,
NEH 7:53 wazao wa Bakbuki, Hakufa, Harhuri,
NEH 7:54 wazao wa Basluthi, Mehida, Harsha,
NEH 7:55 wazao wa Barkosi, Sisera, Tema,
NEH 7:56 wazao wa Nesia na Hatifa.
NEH 7:57 Wazao wa watumishi wa Sulemani: wazao wa Sotai, Soferethi, Perida,
NEH 7:58 Yaala, Darkoni, Gideli,
NEH 7:59 Shefatia, Hatili, Pokereth-Hasebaimu na Amoni.
NEH 7:60 Watumishi wa Hekalu, na wazao wa watumishi wa Sulemani, mia tatu tisini na wawili (392).
NEH 7:61 Wafuatao walikuja kutoka miji ya Tel-Mela, Tel-Harsha, Kerubu, Adoni na Imeri, lakini hawakuweza kuthibitisha kwamba jamaa zao zilikuwa uzao wa Israeli:
NEH 7:62 wazao wa Delaya, Tobia na Nekoda, mia sita arobaini na wawili (642).
NEH 7:63 Kutoka miongoni mwa makuhani: wazao wa Hobaya, wa Hakosi na wa Barzilai (mtu aliyemwoa binti Barzilai Mgileadi, naye akaitwa kwa jina hilo).
NEH 7:64 Hawa walitafuta orodha za jamaa zao, lakini hawakuonekana humo, kwa hiyo waliondolewa ukuhani, kwa kuwa walihesabiwa kuwa najisi.
NEH 7:65 Kwa hiyo, mtawala aliagiza kuwa wasile chochote miongoni mwa vyakula vitakatifu hadi kuwe kuhani atakayehudumu kwa Urimu na Thumimu.
NEH 7:66 Jumla ya watu wote waliorudi walikuwa elfu arobaini na mbili, mia tatu na sitini (42,360);
NEH 7:67 tena zaidi ya hao walikuwa na watumishi wa kiume na wa kike elfu saba, mia tatu na thelathini na saba (7,337); pia walikuwa na waimbaji wanaume na wanawake mia mbili arobaini na watano (245).
NEH 7:68 Walikuwa na farasi mia saba thelathini na sita (736), nyumbu mia mbili arobaini na watano (245),
NEH 7:69 ngamia mia nne thelathini na watano (435) na punda elfu sita, mia saba na ishirini (6,720).
NEH 7:70 Baadhi ya viongozi wa jamaa walichangia kazi ya ujenzi. Mtawala alikabidhi kwenye hazina darkoni elfu moja za dhahabu, mabakuli hamsini, na mavazi mia tano na thelathini ya makuhani.
NEH 7:71 Baadhi ya viongozi wa jamaa walikabidhi kwenye hazina darkoni elfu ishirini za dhahabu, na mane elfu mbili na mia mbili za fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
NEH 7:72 Jumla ya matoleo ya watu wengine yalikuwa ni darkoni elfu ishirini za dhahabu, mane elfu mbili za fedha, na mavazi sitini na saba ya makuhani.
NEH 7:73 Makuhani, Walawi, mabawabu, waimbaji na watumishi wa Hekalu, pamoja na baadhi ya watu wengine na Waisraeli waliosalia waliishi katika miji yao wenyewe. Ilipotimia miezi saba, nao Waisraeli wakiwa tayari wanaishi katika miji yao,
NEH 8:1 watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja kwenye uwanja mbele ya Lango la Maji. Wakamwambia Ezra mwandishi alete Kitabu cha Torati ya Musa, ambacho Mwenyezi Mungu aliamuru kwa ajili ya Israeli.
NEH 8:2 Basi katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba, kuhani Ezra akaleta Torati mbele ya kusanyiko, ambamo walikuwamo wanaume, wanawake na watu wote walioweza kufahamu.
NEH 8:3 Akaisoma kwa sauti kubwa tangu mapambazuko hadi adhuhuri, akiwa ameuelekea uwanja uliokuwa mbele ya Lango la Maji mbele ya wanaume, wanawake na wengine ambao waliweza kufahamu. Watu wote wakasikiliza kwa makini kile Kitabu cha Torati.
NEH 8:4 Mwandishi Ezra alikuwa amesimama juu ya jukwaa la miti lililojengwa kwa kusudi hilo. Karibu naye upande wa kuume walisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya. Upande wake wa kushoto walikuwa Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu.
NEH 8:5 Ezra akakifungua kile kitabu. Watu wote waliweza kumwona kwa sababu alikuwa amesimama juu zaidi, naye alipokifungua watu wote wakasimama.
NEH 8:6 Ezra akamsifu Mwenyezi Mungu, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu Mwenyezi Mungu, nyuso zao zikigusa chini.
NEH 8:7 Watu wakiwa wamesimama pale, Walawi wafuatao waliwafundisha ile Torati: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya.
NEH 8:8 Walisoma kutoka kile Kitabu cha Torati ya Mungu, wakiifafanua na kuwapa maelezo ili watu waweze kufahamu kile kilichokuwa kikisomwa.
NEH 8:9 Ndipo Nehemia aliyekuwa mtawala, Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliokuwa wakiwafundisha watu wakawaambia wote, “Siku hii ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Msiomboleze wala msilie.” Kwa kuwa watu wote walikuwa wakilia walipokuwa wakisikiliza maneno ya ile Torati.
NEH 8:10 Nehemia akasema, “Nendeni mkafurahie chakula kizuri na vinywaji vitamu, na mpeleke sehemu kwa wale ambao hawana chochote cha kula. Siku hii ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu. Msihuzunike, kwa kuwa furaha ya Mwenyezi Mungu ni nguvu zenu.”
NEH 8:11 Walawi wakawatuliza watu wote wakisema, “Kuweni watulivu, kwa kuwa hii ni siku takatifu. Msihuzunike.”
NEH 8:12 Kisha watu wote wakaondoka kwenda kula na kunywa, na kupeana sehemu ya chakula, na wakaadhimisha kwa furaha kubwa, kwa sababu sasa walifahamu maneno yale waliyokuwa wameelezwa.
NEH 8:13 Katika siku ya pili ya mwezi, wakuu wa jamaa zote, pamoja na makuhani na Walawi, walikusanyika wakimzunguka Ezra mwandishi ili wapate kusikiliza kwa makini maneno ya Torati.
NEH 8:14 Wakakuta imeandikwa katika ile Torati, ambayo Mwenyezi Mungu aliiamuru kupitia kwa Musa, kwamba Waisraeli walipaswa kukaa katika vibanda wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba,
NEH 8:15 na kwamba walipaswa kutangaza neno hili na kulieneza katika miji yao na katika Yerusalemu wakisema: “Nendeni katika nchi ya vilima na kuleta matawi kutoka miti ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti ya kivuli, ili kutengeneza vibanda,” kama ilivyoandikwa.
NEH 8:16 Basi watu wakaenda na kuleta matawi, nao wakajijengea vibanda juu ya paa za nyumba zao, katika nyua zao, katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja karibu na Lango la Maji, na uwanja wa Lango la Efraimu.
NEH 8:17 Jamii yote ya watu waliorudi kutoka utumwani wakajenga vibanda na kuishi ndani yake. Tangu wakati wa Yoshua mwana wa Nuni hadi siku ile, Waisraeli hawakuwahi kuiadhimisha namna hii. Furaha yao ilikuwa kubwa sana.
NEH 8:18 Siku baada ya siku, kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho, Ezra alisoma katika kile Kitabu cha Torati ya Mungu. Wakaiadhimisha sikukuu ile kwa siku saba, nayo siku ya nane, kufuatana na maagizo, kulikuwa na kusanyiko maalum.
NEH 9:1 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi ule ule, Waisraeli walikusanyika pamoja, wakifunga na kuvaa gunia, na kujitia mavumbi vichwani mwao.
NEH 9:2 Wale wa uzao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Wakasimama mahali pao, na kuungama dhambi zao na uovu wa baba zao.
NEH 9:3 Wakasimama pale walipokuwa, wakasoma katika kile Kitabu cha Torati ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, kwa muda wa robo siku, na wakatumia robo nyingine kwa kuungama dhambi na kumwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
NEH 9:4 Walawi wafuatao walikuwa wamesimama kwenye ngazi: Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Hawa walimlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wao, kwa sauti kubwa.
NEH 9:5 Nao Walawi Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabnea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakasema: “Simameni mkamsifu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, yeye ambaye ni Mungu tangu milele hata milele.” “Libarikiwe jina lake tukufu, litukuzwe juu ya baraka zote na sifa.
NEH 9:6 Wewe peke yako ndiwe Mwenyezi Mungu. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.
NEH 9:7 “Wewe ni Bwana Mwenyezi Mungu uliyemchagua Abramu na kumtoa kutoka Uru ya Wakaldayo, nawe ukamwita Ibrahimu.
NEH 9:8 Uliona kuwa moyo wake ni mwaminifu kwako, nawe ukafanya agano naye kuwapa wazao wake nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi. Umetimiza ahadi yako kwa sababu wewe ni mwenye haki.
NEH 9:9 “Uliona mateso ya baba zetu huko Misri, ukasikia kilio chao huko Bahari ya Shamu.
NEH 9:10 Ulituma ishara za miujiza na maajabu dhidi ya Farao, dhidi ya maafisa wake wote na watu wote wa nchi yake, kwa kuwa ulifahamu jinsi Wamisri walivyowafanyia ufidhuli. Ukajifanyia jina linalodumu hadi leo.
NEH 9:11 Ukagawa bahari mbele yao, ili waweze kupita katikati yake penye nchi kavu, lakini uliwatupa Wamisri waliowafuatilia katika vilindi, kama jiwe kwenye maji mengi.
NEH 9:12 Mchana uliwaongoza kwa nguzo ya wingu, na usiku kwa nguzo ya moto kuwamulikia njia iliyowapasa kuiendea.
NEH 9:13 “Ulishuka katika Mlima Sinai, ukanena nao kutoka mbinguni. Uliwapa masharti ya kweli na haki, na sheria za kweli na haki, na pia amri na maagizo mazuri.
NEH 9:14 Uliwafahamisha Sabato yako takatifu na ukawapa amri, maagizo na sheria kupitia mtumishi wako Musa.
NEH 9:15 Katika njaa yao uliwapa mkate kutoka mbinguni, na katika kiu yao uliwatolea maji kwenye mwamba. Uliwaambia waingie na kuimiliki nchi ambayo ulikuwa umeapa kuwapa kwa mkono ulioinuliwa.
NEH 9:16 “Lakini wao, baba zetu, wakawa na kiburi na shingo ngumu, nao hawakutii maagizo yako.
NEH 9:17 Wakakataa kusikiliza na kushindwa kukumbuka miujiza uliyoifanya miongoni mwao. Wakawa na shingo ngumu, na katika uasi wao wakamchagua kiongozi ili warudi kwenye utumwa wao. Lakini wewe ni Mungu mwenye kusamehe, mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo. Kwa hiyo hukuwaacha,
NEH 9:18 hata wakati walijitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu na kusema, ‘Huyu ni mungu wenu, aliyewapandisha kutoka nchi ya Misri,’ au walipokufuru sana.
NEH 9:19 “Kwa sababu ya huruma zako kuu hukuwaacha jangwani. Wakati wa mchana ile nguzo ya wingu haikukoma kuwaongoza katika njia yao, wala nguzo ya moto haikuacha kuwamulikia usiku njia iliyowapasa kuiendea.
NEH 9:20 Uliwapa Roho wako mwema ili kuwafundisha. Hukuwanyima mana yako vinywani mwao, nawe ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.
NEH 9:21 Kwa miaka arobaini uliwatunza jangwani. Hawakukosa chochote, na nguo zao hazikuchakaa wala miguu yao haikuvimba.
NEH 9:22 “Uliwapa falme na mataifa, ukiwagawia hata mipaka ya mbali. Wakaimiliki nchi ya Sihoni mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani.
NEH 9:23 Uliwafanya wana wao kuwa wengi kama nyota za angani, nawe ukawaleta katika nchi ambayo uliwaambia baba zao kuingia na kuimiliki.
NEH 9:24 Wana wao wakaingia na kuimiliki nchi. Uliwatiisha Wakanaani mbele yao, walioishi katika nchi, ukawatia Wakanaani mikononi mwao, pamoja na wafalme wao na watu wa nchi, wawafanyie kama wapendavyo.
NEH 9:25 Wakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.
NEH 9:26 “Lakini hawakukutii nao wakaasi dhidi yako, wakatupa sheria zako nyuma yao. Wakawaua manabii wako, waliowaonya ili wakurudie, na wakakufuru sana.
NEH 9:27 Hivyo ukawatia mikononi mwa adui zao, ambao waliwatesa. Lakini walipoteswa, wakakulilia wewe. Uliwasikia ukiwa mbinguni, nawe kwa huruma zako kuu ukawapa wakombozi, waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.
NEH 9:28 “Lakini mara walipokuwa na amani, wakafanya maovu tena machoni pako. Kisha ukawaacha mikononi mwa adui zao, nao wakawatawala. Walipokulilia tena, ukasikia ukiwa mbinguni, na kwa huruma zako ukawaokoa kila mara.
NEH 9:29 “Ukawaonya warudi katika sheria yako, lakini wakawa na kiburi na hawakutii amri zako. Wakatenda dhambi dhidi ya maagizo yako ambayo kwayo mtu ataishi kama akiyatii. Kwa ukaidi wakakugeuzia kisogo, wakawa na shingo ngumu na wakakataa kusikiliza.
NEH 9:30 Kwa miaka mingi ulikuwa mvumilivu kwao na kwa Roho wako ukawaonya kupitia manabii wako. Hata hivyo hawakujali, basi ukawatia mikononi mwa mataifa jirani.
NEH 9:31 Lakini kwa rehema zako kuu hukuwakomesha wala kuwaacha, kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na rehema.
NEH 9:32 “Basi sasa, Ee Mungu wetu, uliye mkuu, mwenye nguvu na Mungu wa kuogofya, mwenye kushika agano lake la upendo, usiache taabu hizi zote zionekane kuwa kitu kidogo mbele za macho yako, taabu hizi zilizotupata, juu ya wafalme wetu na viongozi, juu ya makuhani wetu na manabii, juu ya baba zetu na watu wako wote, tangu siku za wafalme wa Ashuru hadi leo.
NEH 9:33 Katika hayo yote yaliyotupata, umekuwa mwenye haki, na umetenda kwa uaminifu, wakati sisi tumetenda mabaya.
NEH 9:34 Wafalme wetu, viongozi wetu, makuhani wetu na baba zetu hawakufuata sheria yako. Hawakuzingatia amri zako wala maonyo uliyowapa.
NEH 9:35 Hata walipokuwa wangali katika ufalme wao, wakiufurahia wema wako mkuu katika nchi kubwa na yenye rutuba uliyowapa, hawakukutumikia wala kugeuka kutoka njia zao mbaya.
NEH 9:36 “Lakini tazama, sisi ni watumwa leo, watumwa katika nchi uliyowapa baba zetu ili wapate kula matunda yake na vitu vingine vizuri inayozalisha.
NEH 9:37 Kwa sababu ya dhambi zetu, mavuno yake mengi huenda kwa wafalme uliowaweka watutawale. Wanatawala juu ya miili yetu na mifugo yetu kama wapendavyo. Tuko katika dhiki kuu.
NEH 9:38 “Kwa sababu ya haya yote, tunajifunga katika mapatano, na kuyaandika, nao viongozi wetu, Walawi wetu na makuhani wetu wanatia mihuri yao.”
NEH 10:1 Wale waliotia muhuri walikuwa: Nehemia mtawala, mwana wa Hakalia. Sedekia,
NEH 10:2 Seraya, Azaria, Yeremia,
NEH 10:3 Pashuri, Amaria, Malkiya,
NEH 10:4 Hatushi, Shebania, Maluki,
NEH 10:5 Harimu, Meremothi, Obadia,
NEH 10:6 Danieli, Ginethoni, Baruku,
NEH 10:7 Meshulamu, Abiya, Miyamini,
NEH 10:8 Maazia, Bilgai na Shemaya. Hao walikuwa makuhani.
NEH 10:9 Walawi: Yeshua mwana wa Azania, Binui wa wana wa Henadadi, Kadmieli,
NEH 10:10 na wenzao: Shebania, Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani,
NEH 10:11 Mika, Rehobu, Hashabia,
NEH 10:12 Zakuri, Sherebia, Shebania,
NEH 10:13 Hodia, Bani na Beninu.
NEH 10:14 Viongozi wa watu: Paroshi, Pahath-Moabu, Elamu, Zatu, Bani,
NEH 10:15 Buni, Azgadi, Bebai,
NEH 10:16 Adoniya, Bigwai, Adini,
NEH 10:17 Ateri, Hezekia, Azuri,
NEH 10:18 Hodia, Hashumu, Besai,
NEH 10:19 Harifu, Anathothi, Nebai,
NEH 10:20 Magpiashi, Meshulamu, Heziri,
NEH 10:21 Meshezabeli, Sadoki, Yadua,
NEH 10:22 Pelatia, Hanani, Anaya,
NEH 10:23 Hoshea, Hanania, Hashubu,
NEH 10:24 Haloheshi, Pilha, Shobeki,
NEH 10:25 Rehumu, Hashabna, Maaseya,
NEH 10:26 Ahia, Hanani, Anani,
NEH 10:27 Maluki, Harimu na Baana.
NEH 10:28 “Watu wengine wote, wakiwa ni makuhani, Walawi, mabawabu, waimbaji, watumishi wa Hekalu, na wale wote waliojitenga na mataifa jirani kwa ajili ya Torati ya Mungu, pamoja na wake zao na wana wao wote wa kiume na wa kike waliokuwa na uwezo wa kufahamu,
NEH 10:29 basi hawa wote wanajiunga na ndugu zao na wakuu wao, na kujifunga kwa laana na kwa kiapo kufuata Torati ya Mungu iliyotolewa kupitia kwa Musa mtumishi wa Mungu, na kutii kwa uangalifu amri zote, maagizo na sheria za Mwenyezi Mungu, Bwana wetu.
NEH 10:30 “Tunaahidi kutowaoza binti zetu kwa watu wanaotuzunguka, wala kuwaoza wana wetu binti zao.
NEH 10:31 “Mataifa jirani wanapoleta bidhaa zao au nafaka kuuza siku ya Sabato, hatutazinunua kutoka kwao siku ya Sabato, wala siku nyingine yoyote takatifu. Kila mwaka wa saba, tutaacha kuilima ardhi na tutafuta madeni yote.
NEH 10:32 “Tunakubali wajibu wa kutimiza amri za kutoa theluthi ya shekeli kila mwaka kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu:
NEH 10:33 Kwa ajili ya mikate ya Wonesho, kwa ajili ya sadaka za kawaida za nafaka na sadaka za kuteketezwa, kwa ajili ya sadaka za siku za Sabato, Sikukuu za Mwandamo wa Mwezi na sikukuu nyingine zilizoamriwa, kwa ajili ya sadaka takatifu, kwa ajili ya sadaka za dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, na kwa ajili ya kazi zote za nyumba ya Mungu wetu.
NEH 10:34 “Sisi makuhani, Walawi na watu, tumepiga kura kuamua kuwa kila mmoja wa jamaa zetu lazima alete katika nyumba ya Mungu wetu kwa nyakati maalum kila mwaka mchango wa kuni za kukokea moto katika madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika Torati.
NEH 10:35 “Pia tunachukua wajibu wa kuleta malimbuko ya mazao yetu na matunda ya kwanza ya kila mti wa matunda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu kila mwaka.
NEH 10:36 “Kama pia ilivyoandikwa katika Torati, tutawaleta wazaliwa wetu wa kwanza wa kiume, na wa mifugo yetu, yaani wa ng’ombe wetu na wa makundi yetu ya kondoo na mbuzi, katika nyumba ya Mungu wetu, kwa ajili ya makuhani wanaohudumu huko.
NEH 10:37 “Zaidi ya hayo, tutaleta katika maghala ya nyumba ya Mungu wetu, kwa makuhani, vyakula vya kwanza vya mashamba yetu, sadaka zetu za nafaka, matunda ya miti yetu yote, divai yetu mpya na mafuta. Nasi tutaleta zaka za mazao yetu kwa Walawi, kwa kuwa Walawi ndio ambao hukusanya zaka katika miji yote tunakofanya kazi.
NEH 10:38 Kuhani aliye wa uzao wa Haruni atashirikiana na Walawi wanapopokea zaka. Nao Walawi watapaswa kuleta sehemu ya kumi ya zaka katika maghala ya hazina yaliyo katika nyumba ya Mungu wetu.
NEH 10:39 Watu wa Israeli pamoja na Walawi itawapasa kuleta michango yao ya nafaka, divai mpya na mafuta katika vyumba vya ghala, mahali vifaa vya mahali patakatifu vinapohifadhiwa, na wanapokaa makuhani wanaohudumu, na mabawabu na waimbaji. “Hatutaacha kuijali nyumba ya Mungu wetu.”
NEH 11:1 Basi viongozi wa watu walikaa Yerusalemu, nao watu wale wengine walipiga kura ili kuleta mtu mmoja kati ya watu kumi aje kuishi Yerusalemu, mji mtakatifu, nao wengine tisa waliobaki wakae katika miji yao wenyewe.
NEH 11:2 Watu waliwasifu wale wote waliojitolea kuishi Yerusalemu.
NEH 11:3 Hawa ndio viongozi wa majimbo waliokuja kuishi Yerusalemu (baadhi ya Waisraeli, makuhani, Walawi, watumishi wa Hekalu, na wazao wa watumishi wa Sulemani waliendelea kuishi katika miji ya Yuda, kila mmoja katika milki yake mwenyewe katika miji mbalimbali,
NEH 11:4 ambapo watu wengine kutoka Yuda na Benyamini waliishi Yerusalemu). Kutoka wazao wa Yuda: Athaya mwana wa Uzia, mwana wa Zekaria, mwana wa Amaria, mwana wa Shefatia, mwana wa Mahalaleli, mzao wa Peresi.
NEH 11:5 Naye Maaseya mwana wa Baruku, mwana wa Kolhoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zekaria, mzao wa Mshiloni.
NEH 11:6 Wazao wa Peresi walioishi Yerusalemu walikuwa mia nne sitini na nane (468), wanaume wenye uwezo.
NEH 11:7 Kutoka wazao wa Benyamini: Salu mwana wa Meshulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Maaseya, mwana wa Ithieli, mwana wa Yeshaya
NEH 11:8 na wafuasi wake, Gabai na Salai: wanaume mia tisa ishirini na nane (928).
NEH 11:9 Yoeli mwana wa Zikri alikuwa afisa wao mkuu, naye Yuda mwana wa Hasenua alikuwa msimamizi juu ya Mtaa wa Pili katika mji.
NEH 11:10 Kutoka makuhani: Yedaya; mwana wa Yoyaribu; Yakini;
NEH 11:11 Seraya mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu, msimamizi wa nyumba ya Mungu,
NEH 11:12 pamoja na wenzao waliofanya kazi hekaluni: wanaume mia nane ishirini na wawili (822). Adaya mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amzi, mwana wa Zekaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya,
NEH 11:13 na wenzao, waliokuwa viongozi wa jamaa: wanaume mia mbili arobaini na wawili (242). Amashisai mwana wa Azareli, mwana wa Azai, mwana wa Meshilemothi, mwana wa Imeri,
NEH 11:14 na wenzao waliokuwa wanaume wenye uwezo: mia moja ishirini na nane (128). Afisa wao mkuu alikuwa Zabdieli mwana wa Hagedolimu.
NEH 11:15 Kutoka Walawi: Shemaya mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, mwana wa Buni;
NEH 11:16 Shabethai na Yozabadi, viongozi wawili wa Walawi, ambao walisimamia kazi za nje za nyumba ya Mungu;
NEH 11:17 Matania mwana wa Mika, mwana wa Zabdi, mwana wa Asafu, kiongozi aliyeongoza kutoa shukrani na maombi; Bakbukia aliyekuwa msaidizi wake kati ya wenzake; na Abda mwana wa Shamua, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni.
NEH 11:18 Jumla ya Walawi waliokaa katika mji mtakatifu walikuwa wanaume mia mbili themanini na wanne (284).
NEH 11:19 Mabawabu: Akubu, Talmoni na wenzao, waliolinda malango: wanaume mia moja sabini na wawili (172).
NEH 11:20 Waisraeli waliosalia, pamoja na makuhani na Walawi, walikuwa katika miji yote ya Yuda, kila mmoja katika urithi wa baba yake.
NEH 11:21 Watumishi wa Hekalu waliishi katika kilima cha Ofeli. Siha na Gishpa walikuwa wasimamizi wao.
NEH 11:22 Afisa mkuu wa Walawi huko Yerusalemu alikuwa Uzi mwana wa Bani, mwana wa Hashabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika. Uzi alikuwa mmoja wa wazao wa Asafu, waliokuwa waimbaji wenye kuwajibika kwa ajili ya huduma ya nyumba ya Mungu.
NEH 11:23 Waimbaji walikuwa chini ya amri za mfalme, ambazo pia ziliratibu shughuli zao za kila siku.
NEH 11:24 Pethahia mwana wa Meshezabeli, mmoja wa wazao wa Zera mwana wa Yuda, alikuwa mwakilishi wa mfalme katika mambo yote kuhusu mahusiano na watu.
NEH 11:25 Kuhusu vijiji na mashamba yake, baadhi ya watu wa Yuda waliishi Kiriath-Arba na makazi yaliyouzunguka, katika Diboni na makazi yake, katika Yekabzeeli na vijiji vyake,
NEH 11:26 katika Yeshua, katika Molada, katika Beth-Peleti,
NEH 11:27 katika Hasar-Shuali, katika Beer-Sheba na makazi yake,
NEH 11:28 katika Siklagi, katika Mekona na makazi yake,
NEH 11:29 katika En-Rimoni, katika Sora, katika Yarmuthi,
NEH 11:30 Zanoa, Adulamu na vijiji vyake, katika Lakishi na mashamba yake, na katika Azeka na makazi yake. Hivyo walikuwa wakiishi kuanzia Beer-Sheba hadi Bonde la Hinomu.
NEH 11:31 Wazao wa Wabenyamini kutoka Geba waliishi Mikmashi, Aiya, Betheli na makazi yake,
NEH 11:32 katika Anathothi, Nobu na Anania,
NEH 11:33 katika Hazori, Rama na Gitaimu,
NEH 11:34 katika Hadidi, Seboimu na Nebalati,
NEH 11:35 katika Lodi na Ono, na katika Bonde la Mafundi.
NEH 11:36 Baadhi ya makundi ya Walawi wa Yuda waliishi huko Benyamini.
NEH 12:1 Wafuatao walikuwa makuhani na Walawi ambao walirudi na Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na Yeshua: Seraya, Yeremia, Ezra,
NEH 12:2 Amaria, Maluki, Hatushi,
NEH 12:3 Shekania, Rehumu, Meremothi,
NEH 12:4 Ido, Ginethoni, Abiya,
NEH 12:5 Miyamini, Moadia, Bilga,
NEH 12:6 Shemaya, Yoyaribu, Yedaya,
NEH 12:7 Salu, Amoki, Hilkia na Yedaya.
NEH 12:8 Walawi walikuwa Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda, na pia Matania, ambaye pamoja na wenzake, alikuwa kiongozi wa nyimbo za shukrani.
NEH 12:9 Bakbukia na Uni, wenzao, walisimama mkabala nao wakati wa ibada.
NEH 12:10 Yeshua alikuwa baba wa Yoyakimu, Yoyakimu alikuwa baba wa Eliashibu, Eliashibu alikuwa baba wa Yoyada,
NEH 12:11 Yoyada alikuwa baba wa Yonathani, na Yonathani alikuwa baba wa Yadua.
NEH 12:12 Katika siku za Yoyakimu, kulikuwa na wakuu wa jamaa za kikuhani: wa jamaa ya Seraya, Meraya; wa jamaa ya Yeremia, Hanania;
NEH 12:13 wa jamaa ya Ezra, Meshulamu; wa jamaa ya Amaria, Yehohanani;
NEH 12:14 wa jamaa ya Maluki, Yonathani; wa jamaa ya Shebania, Yusufu;
NEH 12:15 wa jamaa ya Harimu, Adna; wa jamaa ya Meremothi, Helkai;
NEH 12:16 wa jamaa ya Ido, Zekaria; wa jamaa ya Ginethoni, Meshulamu;
NEH 12:17 wa jamaa ya Abiya, Zikri; wa jamaa ya Miyamini na ya Maazia, Piltai;
NEH 12:18 wa jamaa ya Bilgai, Shamua; wa jamaa ya Shemaya, Yehonathani;
NEH 12:19 wa jamaa ya Yoyaribu, Matenai; wa jamaa ya Yedaya, Uzi;
NEH 12:20 wa jamaa ya Salu, Kalai; wa jamaa ya Amoki, Eberi;
NEH 12:21 wa jamaa ya Hilkia, Hashabia; wa jamaa ya Yedaya, Nethaneli.
NEH 12:22 Wakuu wa jamaa za Walawi katika siku za Eliashibu, Yoyada, Yohanani na Yadua, pia wale jamaa za makuhani, waliandikishwa wakati wa utawala wa Dario Mwajemi.
NEH 12:23 Wakuu wa jamaa miongoni mwa wazao wa Lawi hadi wakati wa Yohanani mwana wa Eliashibu waliandikishwa katika kitabu cha kumbukumbu.
NEH 12:24 Viongozi wa Walawi walikuwa: Hashabia, Sherebia, Yeshua mwana wa Kadmieli na wenzao, waliosimama mkabala nao kusifu na kushukuru, sehemu moja ikipokezana na nyingine kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu.
NEH 12:25 Mabawabu waliokuwa wakilinda kwenye malango ya ghala ni: Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni na Akubu.
NEH 12:26 Walihudumu siku za Yoyakimu mwana wa Yeshua, mwana wa Yosadaki, na katika siku za mtawala Nehemia, na za Ezra kuhani na mwandishi.
NEH 12:27 Wakati wa kuwekwa wakfu ukuta wa Yerusalemu, Walawi walitafutwa kule walikokuwa wakiishi, nao wakaletwa Yerusalemu kuadhimisha kwa shangwe kuweka wakfu kwa nyimbo za shukrani na kwa uimbaji wakitumia matoazi, vinubi na zeze.
NEH 12:28 Pia waimbaji walikusanywa pamoja kutoka maeneo yaliyozunguka Yerusalemu, kutoka vijiji vya Wanetofathi,
NEH 12:29 kutoka Beth-Gilgali, na kutoka eneo la Geba na Azmawethi, kwa kuwa waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kuzunguka Yerusalemu.
NEH 12:30 Makuhani na Walawi walipokuwa wamekwisha kujitakasa kulingana na desturi, waliwatakasa watu, malango na ukuta.
NEH 12:31 Niliwaagiza viongozi wa Yuda wapande juu ya ukuta. Pia niliagiza makundi mawili makubwa ya waimbaji waimbe nyimbo za kumshukuru Mungu. Kundi moja lilipanda juu ya ukuta upande wa kuume, kuelekea Lango la Samadi.
NEH 12:32 Hoshaya na nusu ya viongozi wa Yuda wakawafuata,
NEH 12:33 pamoja na Azaria, Ezra, Meshulamu,
NEH 12:34 Yuda, Benyamini, Shemaya, Yeremia,
NEH 12:35 pamoja na baadhi ya makuhani wenye tarumbeta, na pia walikuwa na Zekaria mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu,
NEH 12:36 pamoja na wenzake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, wakiwa na vyombo vya uimbaji, kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu. Mwandishi Ezra aliongoza maandamano.
NEH 12:37 Kwenye Lango la Chemchemi waliendelea moja kwa moja mpaka kwenye ngazi za Mji wa Daudi, kwenye mwinuko wa ukuta, na kupitia juu ya nyumba ya Daudi mpaka kwenye Lango la Maji upande wa mashariki.
NEH 12:38 Kundi la pili la waimbaji lilielekea upande wa kushoto. Niliwafuata juu ya ukuta, pamoja na nusu ya watu kupitia Mnara wa Tanuru hadi kwenye Ukuta Mpana,
NEH 12:39 juu ya Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, na Mnara wa Mia, hadi kwenye Lango la Kondoo. Walipofika kwenye Lango la Ulinzi wakasimama.
NEH 12:40 Kisha yale makundi mawili ya waimbaji yaliyoshukuru yakachukua nafasi zao katika nyumba ya Mungu. Nami pia nikafanya hivyo, pamoja na nusu ya maafisa,
NEH 12:41 na makuhani wafuatao: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania wakiwa na tarumbeta zao,
NEH 12:42 na pia Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Makundi haya yaliimba chini ya uongozi wa Yezrahia.
NEH 12:43 Siku hiyo watu walitoa dhabihu nyingi, wakishangilia kwa sababu Mungu aliwapa furaha kuu. Wanawake na watoto walishangilia pia. Sauti ya kushangilia huko Yerusalemu iliweza kusikika mbali sana.
NEH 12:44 Wakati huo watu walichaguliwa kuwa wasimamizi wa vyumba vya ghala kwa ajili ya matoleo, malimbuko na zaka. Kutoka yale mashamba yaliyozunguka miji walipaswa walete kwenye ghala mafungu kama sheria ilivyoamuru kwa ajili ya makuhani na Walawi, kwa kuwa Yuda alifurahishwa na huduma ya makuhani na Walawi.
NEH 12:45 Walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, nao waimbaji na walinzi wa lango wakafanya hivyo pia, kufuatana na amri za Daudi na Sulemani mwanawe.
NEH 12:46 Muda mrefu uliopita, katika siku za Daudi na Asafu, kulikuwa na viongozi wa waimbaji na wa nyimbo za sifa na za kumshukuru Mungu.
NEH 12:47 Kwa hiyo katika siku za Zerubabeli na za Nehemia, Israeli wote walitoa mafungu kila siku kwa ajili ya waimbaji na mabawabu. Pia walitenga fungu kwa ajili ya Walawi wengine, nao Walawi walitenga fungu kwa ajili ya wazao wa Haruni.
NEH 13:1 Siku hiyo, Kitabu cha Musa kilisomwa kwa sauti kuu, na watu wote wakasikia. Humo ilionekana imeandikwa kwamba hakuna Mwamoni wala Mmoabu atakayeruhusiwa katika kusanyiko la watu wa Mungu,
NEH 13:2 kwa sababu hawakuwalaki Waisraeli kwa chakula na maji. Badala yake walimwajiri Balaamu kuwalaani. (Lakini hata hivyo Mungu wetu aligeuza laana kuwa baraka.)
NEH 13:3 Watu waliposikia sheria hii, waliwatenga watu wote wasio Waisraeli waliokuwa wa uzao wa kigeni.
NEH 13:4 Kabla ya hili, kuhani Eliashibu alikuwa amewekwa kuwa msimamizi wa vyumba vya ghala ya nyumba ya Mungu wetu. Alikuwa na uhusiano wa karibu na Tobia,
NEH 13:5 naye alikuwa amempa Tobia chumba kikubwa ambacho mwanzo kilikuwa kikitumika kuweka sadaka za nafaka, uvumba na vyombo vya Hekalu, pamoja na zaka za nafaka, divai mpya na mafuta waliyoagizwa Waisraeli kwa ajili ya Walawi, waimbaji na mabawabu wa lango, pamoja na matoleo kwa makuhani.
NEH 13:6 Lakini wakati haya yote yalipokuwa yakitendeka, sikuwa Yerusalemu, kwa kuwa katika mwaka wa thelathini na mbili wa utawala wa Artashasta mfalme wa Babeli nilikuwa nimerudi kwa mfalme. Baadaye nilimwomba ruhusa,
NEH 13:7 nikarudi Yerusalemu. Hapo niligundua jambo la uovu alilofanya Eliashibu kwa kumpa Tobia chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.
NEH 13:8 Nilikasirika sana na nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia.
NEH 13:9 Nilitoa amri kutakasa vyumba, kisha nikavirudisha vifaa vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za nafaka na uvumba.
NEH 13:10 Pia niligundua kuwa mafungu yaliyopangwa kupewa Walawi hawakuwa wamepewa, nao Walawi wote na waimbaji waliowajibika kwa huduma walikuwa wamerudi katika mashamba yao.
NEH 13:11 Basi niliwakemea maafisa na kuwauliza, “Kwa nini nyumba ya Mungu imepuuzwa?” Kisha niliwaita pamoja na kuwaweka kwenye nafasi zao.
NEH 13:12 Yuda wote walileta zaka za nafaka, divai mpya na mafuta kwenye ghala.
NEH 13:13 Nikamweka kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki, na Mlawi aliyeitwa Pedaya kuwa wasimamizi wa ghala, na kumfanya Hanani mwana wa Zakuri, mwana wa Matania kuwa msaidizi wao, kwa sababu watu hawa walionekana kuwa waaminifu. Walipewa wajibu wa kugawa mahitaji kwa ndugu zao.
NEH 13:14 Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa hili, wala usifute kile nilichokifanya kwa uaminifu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu na kwa ajili ya huduma yake.
NEH 13:15 Siku hizo nikaona watu katika Yuda wakikanyaga mashinikizo ya divai siku ya Sabato na kuleta nafaka wakiwapakiza punda, pamoja na divai, zabibu, tini na aina nyingine za mizigo. Nao walikuwa wakileta haya yote Yerusalemu siku ya Sabato. Kwa hiyo niliwaonya dhidi ya kuuza vyakula siku hiyo.
NEH 13:16 Watu kutoka Tiro walioishi Yerusalemu walileta samaki na aina nyingi za bidhaa na kuziuza Yerusalemu siku ya Sabato kwa watu wa Yuda.
NEH 13:17 Niliwakemea wakuu wa Yuda na kuwaambia, “Ni uovu gani huu mnaofanya wa kuinajisi siku ya Sabato?
NEH 13:18 Je, baba zenu hawakufanya mambo kama haya, hata wakamsababisha Mungu wetu kuleta maafa haya yote juu yetu na juu ya mji huu? Sasa bado mnazidi kuchochea ghadhabu yake dhidi ya Israeli kwa kuinajisi Sabato.”
NEH 13:19 Vivuli vya jioni vilipoangukia juu ya malango ya Yerusalemu kabla ya Sabato, niliamuru milango ifungwe, wala isifunguliwe hadi Sabato iishe. Nikawaweka baadhi ya watu wangu mwenyewe kwenye malango ili pasiwepo mzigo utakaoingizwa ndani siku ya Sabato.
NEH 13:20 Mara moja au mbili wachuuzi na wauzaji wa bidhaa za aina zote walilala usiku nje ya mji wa Yerusalemu.
NEH 13:21 Lakini niliwaonya na kuwaambia, “Kwa nini mnalala karibu na ukuta? Mkifanya hivi tena, nitawaadhibu.” Kuanzia wakati ule hawakuja tena siku ya Sabato.
NEH 13:22 Kisha nikawaamuru Walawi kujitakasa na kwenda kulinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu. Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa ajili ya hili pia, nawe unioneshe wema wako sawasawa na upendo wako mkuu.
NEH 13:23 Zaidi ya hayo, niliona Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake kutoka Ashdodi, Amoni na Moabu.
NEH 13:24 Nusu ya watoto wao walizungumza lugha ya Kiashidodi au lugha ya watu wengine, bali hawakuweza kuzungumza Kiyahudi.
NEH 13:25 Niliwakemea na kuwalaani. Niliwapiga baadhi ya watu na kung’oa nywele zao. Niliwaapisha kwa jina la Mungu na kusema: “Msiwaoze binti zenu kwa wana wao, wala binti zao wasiolewe na wana wenu wala ninyi wenyewe.
NEH 13:26 Je, Sulemani hakutenda dhambi kwa sababu ya wanawake wa aina hiyo? Miongoni mwa mataifa mengi hapakuwa na mfalme kama yeye. Alipendwa na Mungu wake. Naye Mungu alimweka kuwa mfalme juu ya Israeli yote, lakini hata yeye, wanawake wa mataifa mengine walimfanya atende dhambi.
NEH 13:27 Je, tulazimike sasa kusikia kwamba ninyi pia mmefanya uovu huu mkubwa na kutokuwa waaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni?”
NEH 13:28 Mmoja wa wana wa Yoyada mwana wa Eliashibu kuhani mkuu alikuwa mkwewe Sanbalati Mhoroni. Nami nilimfukuza mbele yangu.
NEH 13:29 Ee Mungu wangu, uwakumbuke, kwa sababu wamenajisi ukuhani, na agano la kikuhani na la Walawi.
NEH 13:30 Kwa hiyo niliwatakasa makuhani na Walawi kutokana na chochote kilichokuwa cha kigeni, na kuwapa wajibu, kila mmoja katika kazi yake.
NEH 13:31 Pia nilihakikisha kwamba matoleo ya kuni yaliletwa kwa wakati unaopaswa, na malimbuko kwa wakati wake. Ee Mungu wangu, unikumbuke, unitendee mema.
EST 1:1 Hili ndilo lililotokea wakati wa utawala wa Mfalme Ahasuero, yule aliyetawala majimbo mia moja na ishirini na saba (127) kutoka Bara Hindi hadi Kushi.
EST 1:2 Wakati huo Mfalme Ahasuero alitawala kwenye kiti chake cha ufalme katika ngome ya mji wa Shushani.
EST 1:3 Katika mwaka wa tatu wa utawala wake, alifanya karamu kwa ajili ya wakuu wake wote pamoja na maafisa. Akawaalika viongozi wa jeshi wa Uajemi na Umedi, wana wa wafalme na wakuu wa majimbo.
EST 1:4 Kwa muda wa siku mia moja na themanini mfalme alionesha utajiri mwingi wa ufalme wake, fahari na utukufu wa enzi yake.
EST 1:5 Siku hizo zilipopita, mfalme alifanya karamu kwa muda wa siku saba, katika bustani ya ndani katika jumba la kifalme, kwa ajili ya watu wote kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliokuwa katika ngome ya mji wa Shushani.
EST 1:6 Bustani ilikuwa na mapazia ya kitani nyeupe na buluu, yaliyofungiwa kamba za kitani nyeupe na kitambaa cha zambarau, kwenye pete za fedha juu ya nguzo za marumaru. Kulikuwa na viti vya dhahabu na vya fedha vilivyokuwa vimewekwa kwenye ile sakafu iliyotengenezwa kwa mawe ya rangi, marumaru, lulumizi na mawe mengine ya thamani.
EST 1:7 Vyombo vya dhahabu vilitumika kwa watu kunywea mvinyo, kila kimoja tofauti na kingine, naye mfalme akatoa mvinyo kwa wingi kwa kadiri ya ukarimu wake.
EST 1:8 Kwa amri ya mfalme kila mgeni aliruhusiwa kunywa alichotaka, kwa kuwa mfalme alitoa maagizo kwa watumishi wote kugawa mvinyo kila mtu kwa jinsi alivyotaka.
EST 1:9 Malkia Vashti pia akawafanyia wanawake karamu katika jumba la kifalme la Mfalme Ahasuero.
EST 1:10 Siku ya saba, wakati Mfalme Ahasuero alikuwa amesisimka roho yake kwa mvinyo, aliamuru matowashi saba waliokuwa wakimhudumia, yaani Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi,
EST 1:11 kumleta Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa amevaa taji lake la kifalme, ili aoneshe uzuri wake kwa watu na wakuu, kwa kuwa alikuwa ni mzuri kumtazama.
EST 1:12 Lakini wakati watumishi walipotoa amri ya mfalme, Malkia Vashti alikataa kuja. Ndipo mfalme alighadhibika, na hasira yake ikawaka.
EST 1:13 Kwa kuwa ilikuwa desturi ya mfalme kupata ushauri kwa wataalamu katika mambo ya sheria na haki, alizungumza na watu wenye busara, ambao walijua nyakati,
EST 1:14 nao waliokuwa karibu na mfalme ni Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena na Memukani, wakuu saba wa Uajemi na Umedi waliokuwa na nafasi ya pekee kwa mfalme nao walikuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake.
EST 1:15 Mfalme akauliza, “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewa nini? Malkia hakutii amri ya Mfalme Ahasuero ambayo matowashi walimpelekea.”
EST 1:16 Kisha Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, “Malkia Vashti si kwamba amemkosea mfalme tu bali pia amewakosea wakuu wote na watu wa himaya yote ya Mfalme Ahasuero.
EST 1:17 Kwa maana tendo hili la malkia litajulikana kwa wanawake wote, kwa hiyo watawadharau waume zao na kusema, ‘Mfalme Ahasuero aliagiza Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini alikataa.’
EST 1:18 Siku ya leo, wanawake wa wakuu wa Uajemi na Umedi ambao wamesikia kuhusu tabia ya malkia watawatendea wakuu wote wa mfalme vivyo hivyo. Hapatakuwa na mwisho wa dharau na ugomvi.
EST 1:19 “Kwa hiyo, kama itampendeza mfalme, atoe amri ya kifalme na iandikwe katika sheria ya Uajemi na Umedi, ambayo haitabadilika, kwamba Vashti kamwe asije tena mbele ya Mfalme Ahasuero. Pia mfalme na atoe hiyo nafasi yake ya umalkia kwa mwanamke mwingine aliye bora kuliko yeye.
EST 1:20 Kisha mbiu hii ya mfalme itakapotangazwa katika himaya yake iliyo kubwa sana, wanawake wote watawaheshimu waume zao, kuanzia mdogo hadi mkubwa.”
EST 1:21 Mfalme na wakuu wake walipendezwa na shauri hili, hivyo basi mfalme akafanya kama Memukani alivyopendekeza.
EST 1:22 Alipeleka barua katika sehemu zote za ufalme wake, kwa kila jimbo kwa maandishi yake mwenyewe na kwa kila watu katika lugha yao wenyewe, akitangaza kwa msemo wa kila watu kwamba inampasa kila mwanaume kuwa mtawala wa nyumba yake mwenyewe.
EST 2:1 Baadaye, wakati hasira ya Mfalme Ahasuero ilikuwa imetulia, alimkumbuka Vashti na kile alichokuwa amekifanya, na alilokuwa ameamuru juu yake.
EST 2:2 Kisha watumishi waliomhudumia mfalme walipendekeza, “Watafutwe wanawali mabikira wazuri wa sura kwa ajili ya mfalme.
EST 2:3 Mfalme na awateue maafisa katika kila jimbo la himaya yake kuwaleta hao wanawali wote wazuri wa sura katika nyumba ya wanawake katika ngome ya mji wa Shushani. Kisha wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi wa mfalme, aliyekuwa msimamizi wa wanawake; na wapewe huduma zote za urembo.
EST 2:4 Kisha yule ambaye atampendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti.” Shauri hili likampendeza mfalme, naye akalifuata.
EST 2:5 Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila la Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi,
EST 2:6 ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda.
EST 2:7 Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki.
EST 2:8 Agizo na amri ya mfalme ilipotangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa kwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake.
EST 2:9 Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya urembo na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake.
EST 2:10 Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wake na asili yake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza kufanya hivyo.
EST 2:11 Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.
EST 2:12 Kabla zamu ya msichana haijafika ya kwenda kwa Mfalme Ahasuero, ilimbidi atimize miezi kumi na mbili ya matunzo ya urembo kama ilivyokuwa imepangwa. Kwa miezi sita walikuwa wajipake mafuta ya manemane, na miezi sita kujipaka manukato na vipodozi.
EST 2:13 Basi hivi ndivyo ambavyo msichana angeingia kwa mfalme: Kila kitu alichohitaji aliruhusiwa kuchukua kutoka nyumba ya wanawake na kwenda navyo katika jumba la mfalme.
EST 2:14 Jioni angeenda pale na asubuhi kurudi sehemu nyingine ya nyumba ya wanawake katika utunzaji wa Shaashgazi, towashi wa mfalme aliyekuwa mkuu wa masuria. Hangeweza kurudi kwa mfalme hadi apendezwe naye na kuagiza aitwe kwa jina lake.
EST 2:15 Zamu ya Esta ilipofika kwenda kwa mfalme (msichana ambaye Mordekai alikuwa amemlea, binti Abihaili, mjomba wake), Esta hakutaka vitu zaidi ya vile Hegai, towashi wa mfalme aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake, alikuwa amemshauri. Naye Esta alipata kibali kwa kila mtu aliyemwona.
EST 2:16 Esta alipelekwa kwa Mfalme Ahasuero katika makao ya mfalme mwezi wa kumi, yaani mwezi wa Tebethi, katika mwaka wake wa saba wa kutawala.
EST 2:17 Basi mfalme alivutiwa na Esta kuliko wanawake wengine wote, naye akapata upendeleo na kibali kuliko mabikira wengine. Kisha akamvika taji la kifalme kichwani mwake na kumfanya malkia badala ya Vashti.
EST 2:18 Mfalme akafanya karamu kubwa, karamu ya Esta, kwa wakuu wake wote na maafisa. Mfalme akatangaza siku ya mapumziko katika majimbo yake yote na kugawa zawadi kwa ukarimu wa kifalme.
EST 2:19 Wakati mabikira walikusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi katika lango la mfalme.
EST 2:20 Lakini Esta alikuwa ameficha siri ya asili yake na uraia wake, kama Mordekai alivyokuwa amemwambia, kwa maana aliendelea kufuata maelekezo ya Mordekai kama alivyokuwa akifanya alipokuwa akimlea.
EST 2:21 Ikawa Mordekai alipokuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero.
EST 2:22 Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai.
EST 2:23 Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.
EST 3:1 Baada ya matukio haya, Mfalme Ahasuero alimheshimu Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, akampandisha na kumpa kiti chake cha heshima cha juu sana kuliko wakuu wengine wote.
EST 3:2 Maafisa wote wa mfalme waliokaa langoni mwa mfalme walipiga magoti na kumpa Hamani heshima, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru hili kuhusu Hamani. Lakini Mordekai hakumpigia magoti wala kumheshimu.
EST 3:3 Kisha maafisa wa mfalme waliokuwa langoni mwa mfalme walimuuliza Mordekai, “Kwa nini hutii agizo la mfalme?”
EST 3:4 Siku baada ya siku walizungumza naye lakini hakukubali. Kwa hiyo walimweleza Hamani kuona kama tabia ya Mordekai itaweza kuvumiliwa, kwa maana alikuwa amewaambia kuwa yeye ni Myahudi.
EST 3:5 Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima, alighadhibika.
EST 3:6 Hata hivyo, baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumuua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahasuero.
EST 3:7 Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.
EST 3:8 Kisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa.
EST 3:9 Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta elfu kumi za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.”
EST 3:10 Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi.
EST 3:11 Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”
EST 3:12 Kisha siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza waandishi wa mfalme waliitwa. Wakaandika barua kwa kila jimbo na katika kila lugha ya watu kama agizo la Hamani lilivyotoka kwa mfalme, kwa watawala wa majimbo mbalimbali, na wakuu wa watu mbalimbali. Hizi ziliandikwa kwa jina la Mfalme Ahasuero mwenyewe na kutiwa muhuri wa pete yake mwenyewe.
EST 3:13 Barua zilipelekwa na tarishi katika majimbo yote ya mfalme zikiwa na amri ya kuharibu, kuua na kuangamiza Wayahudi wote, wadogo kwa wakubwa, wanawake na watoto wadogo, siku moja, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, na pia kuteka nyara vitu vyao.
EST 3:14 Nakala ya andiko la amri ilipaswa kutolewa kama sheria katika kila jimbo, na kufahamishwa kwa watu wa kila taifa ili waweze kuwa tayari kwa siku ile.
EST 3:15 Kwa kuharakishwa na amri ya mfalme, matarishi walienda na andiko lilitolewa katika mji wa ngome ya Shushani. Mfalme na Hamani waliketi na kunywa, lakini mji wa Shushani ulifadhaika.
EST 4:1 Mordekai alipojua yote yaliyokwisha kufanyika, alirarua mavazi yake, akavaa magunia na kujipaka majivu, akaenda mjini akiomboleza kwa sauti na kwa uchungu.
EST 4:2 Alienda na kusimama nje ya lango la mfalme, kwa sababu hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia akiwa amevaa magunia.
EST 4:3 Katika kila jimbo ambapo amri na agizo la mfalme lilifika, kulikuwa na maombolezo makuu miongoni mwa Wayahudi pamoja na kufunga, kulia na kuomboleza. Watu wengi wakalala juu ya magunia na majivu.
EST 4:4 Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya magunia, lakini Mordekai hakuzikubali.
EST 4:5 Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyekuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta kilichokuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini.
EST 4:6 Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme.
EST 4:7 Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi.
EST 4:8 Akampa nakala ya andiko la amri kwa ajili ya maangamizi yao, lililokuwa limechapishwa huko Shushani, kumwonesha Esta na kumwelezea. Mordekai akamwambia towashi amshawishi Esta kwenda mbele ya mfalme kuomba rehema na kumsihi kwa ajili ya watu wake.
EST 4:9 Hathaki akarudi kwa Esta na kumwarifu alilolisema Mordekai.
EST 4:10 Kisha Esta akamwamuru Hathaki amweleze Mordekai,
EST 4:11 “Maafisa wote wa mfalme na watu wa majimbo ya ufalme wanajua kuwa mwanaume au mwanamke yeyote ambaye ataingia kumwona mfalme katika ua wa ndani bila kuitwa, mfalme ana sheria moja tu: Atauawa. Njia pekee kinyume na hili ni mfalme kumnyooshea fimbo ya dhahabu ili aishi. Lakini siku thelathini zimepita tangu nilipoitwa kwenda kwa mfalme.”
EST 4:12 Wakati Mordekai aliarifiwa maneno ya Esta,
EST 4:13 Mordekai alirudisha jibu hili: “Usifikiri kwamba kwa sababu uko katika nyumba ya mfalme wewe pekee katika Wayahudi wote utapona.
EST 4:14 Kwa kuwa kama utakaa kimya wakati huu, msaada na ukombozi kwa Wayahudi utatoka mahali pengine, lakini wewe na jamaa ya baba yako mtaangamia. Nani ajuaye kwamba hukuja kwenye nafasi ya mamlaka kwa ajili ya wakati kama huu?”
EST 4:15 Kisha Esta alituma jibu hili kwa Mordekai:
EST 4:16 “Nenda, wakusanye Wayahudi wote walio Shushani, nanyi mfunge kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu, usiku na mchana. Mimi na wajakazi wangu tutafunga kama mnavyofanya. Baada ya kufanyika hili, nitaenda kwa mfalme, hata ingawa ni kinyume cha sheria. Ikiwa ni kuangamia na niangamie.”
EST 4:17 Kwa hiyo Mordekai alienda zake na kutekeleza maagizo yote ya Esta.
EST 5:1 Siku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni.
EST 5:2 Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme.
EST 5:3 Kisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.”
EST 5:4 Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu niliyomwandalia.”
EST 5:5 Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.” Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta.
EST 5:6 Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”
EST 5:7 Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili:
EST 5:8 Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake, na ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.”
EST 5:9 Hamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai.
EST 5:10 Hata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani. Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe.
EST 5:11 Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine.
EST 5:12 Hamani akaongeza, “Si hayo tu. Mimi ndiye mtu pekee ambaye Malkia Esta amemwalika kumsindikiza mfalme kwenye karamu aliyomwandalia. Naye amenialika pamoja na mfalme kesho.
EST 5:13 Lakini haya yote hayanipi kuridhika iwapo ninaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai akiketi kwenye lango la mfalme.”
EST 5:14 Zereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, “Tengeneza mahali pa kuangika watu kimo chake dhiraa hamsini, kisha kesho asubuhi mwombe mfalme Mordekai aangikwe juu yake. Ndipo uende na mfalme kwenye karamu kwa furaha.” Shauri hili lilimpendeza Hamani, naye akajenga mahali pa kuangika watu.
EST 6:1 Usiku ule mfalme hakupata usingizi, hivyo akaagiza aletewe kitabu cha kumbukumbu za matukio ya utawala wake, asomewe.
EST 6:2 Ikaonekana imeandikwa humo kwamba Mordekai alikuwa amefichua jinsi Bigthana na Tereshi, waliokuwa maafisa wawili wa mfalme, walinzi wa lango walivyokuwa wamepanga hila ya kumuua Mfalme Ahasuero.
EST 6:3 Mfalme akauliza, “Je, ni heshima na shukrani gani Mordekai alipokea kwa ajili ya jambo hili?” Watumishi wake wakajibu, “Hakuna lolote alilotendewa.”
EST 6:4 Mfalme akasema, “Ni nani yuko uani?” Wakati huo huo Hamani alikuwa ameingia kwenye ua wa nje wa jumba la mfalme kusema na mfalme kuhusu kumwangika Mordekai katika mahali pa kuangikia watu alipokuwa amepajenga kwa ajili yake.
EST 6:5 Watumishi wake wakamjibu, “Hamani amesimama uani.” Mfalme akaamuru, “Mleteni ndani.”
EST 6:6 Hamani alipoingia, mfalme alimuuliza, “Afanyiwe nini mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu?” Basi Hamani akawaza moyoni mwake, “Ni nani mwingine ambaye mfalme angemheshimu kuliko mimi?”
EST 6:7 Kwa hiyo akamjibu mfalme, “Kwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu,
EST 6:8 aletewe joho la kifalme ambalo mfalme ameshalivaa na farasi ambaye mfalme alishampanda, ambaye amevikwa taji la kifalme kichwani mwake.
EST 6:9 Kisha joho na farasi vikabidhiwe kwa mmoja wa wakuu wa mfalme anayeheshimika sana. Nao wamvike mtu yule ambaye mfalme anapenda kumheshimu, na aongozwe akiwa juu ya farasi kupitia barabara za mji, wakitangaza mbele yake, ‘Hivi ndivyo anavyotendewa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu!’ ”
EST 6:10 Mfalme akamwamuru Hamani, “Nenda mara moja, chukua joho na farasi na ufanye kama vile ulivyopendekeza kwa Mordekai Myahudi, akaaye langoni mwa mfalme. Usipuuze kufanya kitu chochote ulichoshauri.”
EST 6:11 Hivyo Hamani akachukua joho na farasi. Akamvika Mordekai, na kumpandisha juu ya farasi, akamtembeza katika barabara za mji akitangaza mbele yake, “Hivi ndivyo anavyotendewa mtu ambaye mfalme anapenda kumheshimu!”
EST 6:12 Baadaye Mordekai akarudi kwenye lango la mfalme. Lakini Hamani akakimbia nyumbani, akiwa amejaa huzuni,
EST 6:13 naye akamweleza Zereshi mkewe pamoja na rafiki zake wote kila kitu ambacho kimempata. Washauri wake pamoja na Zereshi mkewe wakamwambia, “Kwa kuwa Mordekai, ambaye mbele yake umeanza kuanguka ni wa asili ya Kiyahudi, huwezi kushindana naye; kwa hakika utaanguka!”
EST 6:14 Walipokuwa bado wakizungumza naye, matowashi wa mfalme wakaja na kumharakisha Hamani aende katika karamu aliyoiandaa Esta.
EST 7:1 Basi mfalme na Hamani wakaenda kula chakula pamoja na Malkia Esta.
EST 7:2 Walipokuwa wakinywa mvinyo katika siku ya pili, mfalme akauliza tena, “Malkia Esta, ni nini haja yako? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”
EST 7:3 Kisha Malkia Esta akajibu, “Kama nimepata kibali kwako, ee mfalme, tena kama inapendeza utukufu wako, nijalie maisha yangu, hii ndiyo haja yangu. Pia uokoe watu wangu, hili ndilo ombi langu.
EST 7:4 Kwa kuwa mimi na watu wangu tumeuzwa ili tuangamizwe, tuchinjwe na tuharibiwe. Tungeuzwa tu kama watumwa wa kiume na wa kike, ningenyamaza, kwa sababu shida kiasi hicho haingetosha kumsumbua mfalme.”
EST 7:5 Mfalme Ahasuero akamuuliza Malkia Esta, “Ni nani huyu? Yuko wapi mtu huyu aliyethubutu kufanya jambo kama hili?”
EST 7:6 Esta akasema, “Mtesi na adui ni huyu mwovu Hamani.” Hamani alifadhaika mbele ya mfalme na malkia.
EST 7:7 Mfalme akainuka kwa ghadhabu, akaacha mvinyo wake, akaenda kwenye bustani ya jumba la kifalme. Lakini Hamani, akitambua kwamba mfalme ameshaamua hatima yake, alibaki nyuma kumsihi Malkia Esta aokoe maisha yake.
EST 7:8 Mara mfalme aliporudi kutoka bustani ya jumba la kifalme na kuingia kwenye ukumbi wa karamu, Hamani alikuwa akijitupa kwenye kiti kile Esta alikuwa akiegemea. Mfalme akasema kwa nguvu, “Je, atamdhalilisha malkia hata huku nyumbani akiwa pamoja nami!” Mara neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, walifunika uso wa Hamani.
EST 7:9 Kisha Harbona, mmoja wa matowashi waliomtumikia mfalme, akasema, “Mahali pa kuangika watu penye urefu wa dhiraa hamsini pako nyumbani mwa Hamani. Alikuwa amepatengeneza kwa ajili ya Mordekai, ambaye alizungumza ili kumsaidia mfalme.” Mfalme akasema, “Mwangikeni juu yake!”
EST 7:10 Kwa hiyo wakamtundika Hamani mahali alipokuwa ameandaa kwa ajili ya Mordekai. Ndipo ghadhabu ya mfalme ikatulia.
EST 8:1 Siku ile ile Mfalme Ahasuero akampa Malkia Esta shamba la Hamani, adui wa Wayahudi. Naye Mordekai akaja mbele ya mfalme, kwa kuwa Esta alikuwa amesema jinsi anavyohusiana naye.
EST 8:2 Mfalme akaivua pete yake ya muhuri, ambayo alikuwa amemnyang’anya Hamani, akampa Mordekai, naye Esta akamweka Mordekai asimamie shamba la Hamani.
EST 8:3 Esta alimsihi tena mfalme, akianguka miguuni pake na kulia. Akamwomba akomeshe mpango mwovu wa Hamani Mwagagi ambao alikuwa ameupanga dhidi ya Wayahudi.
EST 8:4 Kisha mfalme alimnyooshea Esta fimbo yake ya utawala ya dhahabu naye aliinuka na kusimama mbele yake.
EST 8:5 Esta akasema, “Ikimpendeza mfalme, nami nikipata kibali, naye akiona ni jambo lililo sawa kunitendea, na akipendezwa nami, basi iandikwe amri ya kuzitangua barua zile Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, alizotunga na kuandika kuangamiza Wayahudi katika majimbo yote ya mfalme.
EST 8:6 Kwa maana nitawezaje kuvumilia kuona maafa yakiwapata watu wangu? Nitawezaje kuvumilia kuona maangamizi ya jamaa zangu?”
EST 8:7 Mfalme Ahasuero akawajibu Malkia Esta na Mordekai Myahudi, “Kwa sababu Hamani aliwashambulia Wayahudi, nimetoa shamba la Hamani kwa Esta, naye ameangikwa kwenye mti wa kunyongea.
EST 8:8 Basi andika amri nyingine kwa jina la mfalme kwa ajili ya Wayahudi kama unavyoona vyema, kisha uifunge kwa kutia muhuri kwa pete ya mfalme kwa kuwa hakuna andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme linaloweza kutanguliwa.”
EST 8:9 Mara moja waandishi wa mfalme wakaitwa kwenye siku ya ishirini na tatu, mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani. Wakaandika yote Mordekai aliyoamuru kwa Wayahudi, kwa majemadari, watawala na wakuu wa majimbo mia moja na ishirini na saba (127) kuanzia Bara Hindi hadi Kushi. Maagizo haya yaliandikwa kwa maandishi ya kila jimbo na kwa lugha ya kila mtu pia kwa Wayahudi kwa maandishi yao wenyewe na lugha yao.
EST 8:10 Mordekai aliandika nyaraka kwa jina la Mfalme Ahasuero, akazitia muhuri kwa pete ya mfalme na kuzipeleka kwa matarishi, ambao waliendesha farasi wepesi waliozalishwa maalum kwa ajili ya mfalme.
EST 8:11 Waraka wa mfalme uliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kuwa na haki ya kukusanyika na kujilinda wenyewe; kuharibu, kuua na kuangamiza jeshi lolote, taifa lolote au jimbo lile litakalowashambulia wao, wake zao, watoto wao na kuteka mali ya adui zao.
EST 8:12 Siku ambayo iliwekwa kwa Wayahudi kufanya hili katika majimbo yote ya Mfalme Ahasuero ilikuwa siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari.
EST 8:13 Nakala ya tangazo ilikuwa itolewe kama sheria katika kila jimbo na iweze kujulikana kwa watu wa kila taifa, ili Wayahudi wawe tayari siku hiyo kulipiza kisasi kwa adui zao.
EST 8:14 Matarishi, wakiwa wamepanda farasi wa kifalme, walitoka mbio wakichochewa na agizo la mfalme. Tangazo lilitolewa pia katika ngome ya mji wa Shushani.
EST 8:15 Mordekai akaondoka mbele ya mfalme akiwa amevaa mavazi ya kifalme ya buluu na nyeupe, taji kubwa la dhahabu na joho la zambarau la kitani safi. Na mji wa Shushani ukasherehekea kwa furaha.
EST 8:16 Kwa maana kwa Wayahudi ulikuwa wakati wa raha na furaha, shangwe na heshima.
EST 8:17 Katika kila jimbo na katika kila jiji, popote waraka wa mfalme ulipofika, kulikuwa na furaha na shangwe miongoni mwa Wayahudi, pamoja na karamu na kushangilia. Na watu wengi wa mataifa mengine wakajifanya Wayahudi kwa sababu ya kuwahofu Wayahudi.
EST 9:1 Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, amri iliyoagizwa na mfalme ilikuwa itekelezwe. Siku hii adui wa Wayahudi walikuwa wametumaini kuwashinda, lakini sasa mambo yaliwageukia na Wayahudi wakawashinda wale waliokuwa wanawachukia.
EST 9:2 Wayahudi walikusanyika katika miji yao, katika majimbo ya Mfalme Ahasuero kuwashambulia wale waliokuwa wanatafuta kuwaangamiza. Hakuna yeyote aliyeweza kushindana nao, kwa sababu watu wa mataifa mengine yote waliwaogopa.
EST 9:3 Nao wakuu wote wa majimbo, majemadari, watawala na maafisa wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa sababu walimhofu Mordekai.
EST 9:4 Mordekai alikuwa mtu mashuhuri katika jumba la mfalme; sifa zake zilienea katika majimbo yote naye alipata uwezo zaidi na zaidi.
EST 9:5 Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia.
EST 9:6 Katika ngome ya Shushani Wayahudi waliua na kuangamiza wanaume mia tano.
EST 9:7 Pia waliwaua Parshendatha, Dalfoni, Aspatha,
EST 9:8 Poratha, Adalia, Ardatha,
EST 9:9 Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha,
EST 9:10 wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara.
EST 9:11 Mfalme aliarifiwa siku hiyo hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani.
EST 9:12 Mfalme akamwambia Malkia Esta, “Wayahudi wamewaua wanaume mia tano, na wana kumi wa Hamani ndani ya ngome ya Shushani. Wamefanyaje katika majimbo mengine ya mfalme yaliyobaki? Je, sasa haja yako ni nini? Nayo pia utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Nalo utatendewa.”
EST 9:13 Esta akajibu, “Ikimpendeza mfalme, uwape ruhusa Wayahudi walio Shushani warudie amri ya leo kesho pia, na wana wa Hamani kumi wanyongwe mahali pa kunyongea watu.”
EST 9:14 Basi mfalme akaamuru kwamba hili litendeke. Amri ilitolewa huko Shushani, nao wakawanyonga wana kumi wa Hamani.
EST 9:15 Wayahudi huko Shushani wakakusanyika pamoja siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, nao wakawaua wanaume mia tatu huko Shushani, lakini hawakuchukua nyara zao.
EST 9:16 Wakati ule ule, Wayahudi wengine waliokuwa kwenye majimbo ya mfalme, wakakusanyika kujilinda nao wakapata nafuu kutokana na adui zao. Waliua adui zao wapatao elfu sabini na tano, lakini hawakugusa nyara zao.
EST 9:17 Hili lilitendeka siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari na siku ya kumi na nne walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.
EST 9:18 Wayahudi huko Shushani, hata hivyo, walikuwa wamekusanyika siku ya kumi na tatu na ya kumi na nne, pia siku ya kumi na tano walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.
EST 9:19 Ndiyo sababu Wayahudi wanaokaa vijijini na katika miji midogo huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kama siku ya furaha na karamu, siku ambayo wao hupeana zawadi mmoja kwa mwingine.
EST 9:20 Mordekai aliandika matukio haya, naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote walio katika majimbo ya Mfalme Ahasuero, majimbo yaliyo mbali na karibu,
EST 9:21 akiwataka kila mwaka washerehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari
EST 9:22 kama wakati ambao Wayahudi walipata nafuu kutoka kwa adui zao na kama mwezi ambao huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha na kuomboleza kwao kuwa siku ya kusherehekea. Aliwaandikia kushika siku hizo kama siku za karamu na za furaha na kupeana zawadi za vyakula wao kwa wao na zawadi kwa maskini.
EST 9:23 Hivyo Wayahudi walikubali kuendeleza sherehe walizokuwa wamezianza, wakifanya lile Mordekai alilokuwa amewaandikia.
EST 9:24 Kwa maana Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi wote, alikuwa amepanga hila dhidi ya Wayahudi ili kuwaangamiza, na alikuwa amepiga puri (yaani kura) kwa ajili ya maangamizi na uharibifu wao.
EST 9:25 Lakini wakati shauri hilo baya lilipoarifiwa kwa mfalme, alitoa amri iliyoandikwa kwamba mipango mibaya ambayo Hamani ameipanga dhidi ya Wayahudi inapasa imrudie juu ya kichwa chake mwenyewe, na kwamba yeye na wanawe waangikwe mahali pa kunyongea watu.
EST 9:26 (Kwa hiyo siku hizi ziliitwa Purimu, kutokana na neno puri.) Kwa sababu ya kila kitu kilichoandikwa kwenye barua hii na kwa sababu ya yale waliyoyaona na yale yaliyowatokea,
EST 9:27 Wayahudi wakachukua na kuimarisha desturi kwamba wao na wazao wao na wote ambao walijiunga nao wangezishika siku hizi mbili kila mwaka bila kuacha, kwa njia ilivyoelekezwa na kwa wakati wake.
EST 9:28 Siku hizi zinapasa zikumbukwe na kuadhimishwa katika kila kizazi, kila jamaa na katika kila jimbo na kila jiji. Nazo siku hizi za Purimu kamwe zisikome kusherehekewa na Wayahudi, wala kumbukumbu zake zisipotee miongoni mwa wazao wake.
EST 9:29 Basi Malkia Esta binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, waliandika kwa mamlaka yote kuthibitisha barua hii ya pili kuhusu Purimu.
EST 9:30 Naye Mordekai akatuma barua kwa Wayahudi wote katika majimbo mia moja na ishirini na saba (127) ya ufalme wa Ahasuero, barua zenye maneno ya amani na matumaini,
EST 9:31 ili kuimarisha siku hizi za Purimu katika majira yake yaliyowekwa, kama Mordekai Myahudi na Malkia Esta walivyowaamuru, na walivyojiimarisha wenyewe na wazao wao kuhusu nyakati za kufunga na kuomboleza.
EST 9:32 Amri ya Esta ilithibitisha taratibu hizi kuhusu Purimu, nayo ikaandikwa katika kumbukumbu.
EST 10:1 Mfalme Ahasuero alitoza ushuru katika himaya yake yote, hadi miambao yake ya mbali.
EST 10:2 Na kuhusu matendo yake yote ya nguvu na uwezo, pamoja na habari zote za ukuu wa Mordekai ambao mfalme alikuwa amempandisha, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Umedi na Uajemi?
EST 10:3 Mordekai Myahudi alikuwa wa pili kwa cheo baada ya Mfalme Ahasuero, naye alikuwa bora kabisa na mkuu miongoni mwa Wayahudi. Aliheshimiwa sana na Wayahudi wenzake wengi, kwa sababu alifanya kazi kwa manufaa ya watu wake na kutetea ustawi wa Wayahudi wote.
JOB 1:1 Katika nchi ya Usi paliishi mtu ambaye aliitwa Ayubu. Mtu huyu alikuwa hana hatia, naye alikuwa mkamilifu; alimcha Mungu na kuepukana na uovu.
JOB 1:2 Alikuwa na wana saba na binti watatu,
JOB 1:3 naye alikuwa na kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, jozi mia tano za maksai, na punda mia tano, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu maarufu sana miongoni mwa watu wa Mashariki.
JOB 1:4 Wanawe walikuwa na desturi ya kufanya karamu katika nyumba zao kwa zamu, nao wangewaalika dada zao watatu ili kula na kunywa pamoja nao.
JOB 1:5 Kipindi cha karamu kilipomalizika, Ayubu angetuma waitwe na kuwafanyia utakaso. Angetoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao asubuhi na mapema, akifikiri, “Pengine wanangu wametenda dhambi na kumlaani Mungu mioyoni mwao.” Hii ilikuwa ndiyo desturi ya kawaida ya Ayubu.
JOB 1:6 Siku moja wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za Mwenyezi Mungu. Shetani naye akaja pamoja nao.
JOB 1:7 Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?” Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.”
JOB 1:8 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.”
JOB 1:9 Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure?
JOB 1:10 Je, wewe hukumzingira pande zote, yeye na watu wa nyumbani mwake, pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki, na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima.
JOB 1:11 Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
JOB 1:12 Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, kila kitu alicho nacho kiko mikononi mwako, lakini huyo mtu mwenyewe usimguse hata kwa kidole.” Ndipo Shetani akatoka mbele za Mwenyezi Mungu.
JOB 1:13 Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa,
JOB 1:14 akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao,
JOB 1:15 Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!”
JOB 1:16 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!”
JOB 1:17 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari.”
JOB 1:18 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako wa kiume na wa kike walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa,
JOB 1:19 ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!”
JOB 1:20 Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akasujudu na kuabudu,
JOB 1:21 akasema: “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi, nami nitaondoka uchi, Mwenyezi Mungu alinipa, naye Mwenyezi Mungu ameviondoa; jina la Mwenyezi Mungu litukuzwe.”
JOB 1:22 Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa kumlaumu Mungu kwa kufanya ubaya.
JOB 2:1 Siku nyingine wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za Mwenyezi Mungu. Shetani naye akaja pamoja nao kujionesha mbele zake.
JOB 2:2 Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?” Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.”
JOB 2:3 Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.”
JOB 2:4 Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake.
JOB 2:5 Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
JOB 2:6 Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Vema sana; kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”
JOB 2:7 Basi Shetani akatoka mbele za Mwenyezi Mungu, naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa.
JOB 2:8 Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho, huku akiketi kwenye majivu.
JOB 2:9 Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”
JOB 2:10 Akamjibu, “Unazungumza kama mwanamke mpumbavu. Je, tupokee mema kutoka kwa Mungu, bali tusipokee mabaya?” Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.
JOB 2:11 Basi rafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia kuhusu taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga kutoka nyumbani mwao, wakakutana ili kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji.
JOB 2:12 Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao.
JOB 2:13 Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.
JOB 3:1 Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.
JOB 3:2 Kisha akasema:
JOB 3:3 “Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali, na usiku ule iliposemekana, ‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’
JOB 3:4 Siku ile na iwe giza; Mungu juu na asiiangalie; nayo nuru isiiangazie.
JOB 3:5 Giza na kivuli kikuu viikalie tena; wingu na likae juu yake; weusi na uifunike nuru yake.
JOB 3:6 Usiku ule na ushikwe na giza nene; usihesabiwe katika siku za mwaka, wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote.
JOB 3:7 Usiku ule na uwe tasa; sauti ya furaha na isisikike ndani yake.
JOB 3:8 Wale wanaozilaani siku na wailaani hiyo siku, wale walio tayari kumwamsha Lewiathani.
JOB 3:9 Nyota zake za alfajiri na ziwe giza; nao ungojee mwanga bila mafanikio, wala usiione miali ya mapambazuko,
JOB 3:10 kwa sababu huo usiku haukunifungia mlango wa tumbo la mama yangu, ili kuyaficha macho yangu kutokana na taabu.
JOB 3:11 “Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa? Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?
JOB 3:12 Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea na matiti ili nipate kunyonyeshwa?
JOB 3:13 Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani. Ningekuwa nimelala na kupumzika
JOB 3:14 pamoja na wafalme na washauri wa dunia, waliojijengea mahali ambapo sasa ni magofu,
JOB 3:15 pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu, waliozijaza nyumba zao kwa fedha.
JOB 3:16 Au kwa nini sikufichwa ardhini kama mtoto aliyezaliwa mfu, kama mtoto mchanga ambaye kamwe hakuuona mwanga?
JOB 3:17 Huko waovu huacha kusumbua na huko waliochoka hupumzika.
JOB 3:18 Wafungwa nao hufurahia utulivu wao, hawasikii tena sauti ya kukemea ya kiongozi wa watumwa.
JOB 3:19 Wadogo kwa wakubwa wamo humo, na mtumwa ameachiwa huru kutoka kwa bwana wake.
JOB 3:20 “Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni, na hao wenye uchungu kupewa uhai,
JOB 3:21 wale wanaotamani kifo ambacho hakiji, wale wanaotafuta kufa zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,
JOB 3:22 ambao hujawa na furaha, na hushangilia wanapofika kaburini?
JOB 3:23 Kwa nini uhai hupewa mtu ambaye njia yake imefichika, ambaye Mungu amemzingira?
JOB 3:24 Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu kwanijia badala ya chakula; kusononeka kwangu kunamwagika kama maji.
JOB 3:25 Lile nililokuwa nikiogopa limenijia; lile nililokuwa nikihofia limenipata.
JOB 3:26 Sina amani, wala utulivu; sina pumziko, bali taabu tu.”
JOB 4:1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
JOB 4:2 “Kama mtu akithubutu kuzungumza nawe, kutakukasirisha? Lakini ni nani awezaye kujizuia asiseme?
JOB 4:3 Fikiri jinsi umewafundisha watu wengi, jinsi umeitia nguvu mikono iliyokuwa dhaifu.
JOB 4:4 Maneno yako yamewategemeza wale waliojikwaa; umeyatia nguvu magoti yaliyokuwa dhaifu.
JOB 4:5 Lakini sasa hii taabu imekujia wewe, nawe unashuka moyo; imekupiga wewe, nawe unafadhaika.
JOB 4:6 Je, kumcha Mungu kwako hakupaswi kuwa ndiyo matumaini yako na njia zako kutokuwa na lawama ndilo taraja lako?
JOB 4:7 “Fikiri sasa: Ni mtu yupi asiye na hatia ambaye aliwahi kuangamia? Ni wapi wanyofu waliwahi kuangamizwa?
JOB 4:8 Kwa jinsi mimi nimechunguza, wale walimao ubaya na wale hupanda uovu, huvuna hayo hayo.
JOB 4:9 Kwa pumzi ya Mungu huangamizwa; kwa mshindo wa hasira zake huangamia.
JOB 4:10 Simba anaweza kunguruma na kukoroma, lakini bado meno ya simba mkubwa huvunjika.
JOB 4:11 Simba anaweza kuangamia kwa kukosa mawindo, nao wana wa simba jike hutawanyika.
JOB 4:12 “Neno lililetwa kwangu kwa siri, masikio yangu yakasikia mnong’ono wake.
JOB 4:13 Katikati ya ndoto za kutia wasiwasi wakati wa usiku, hapo usingizi mzito uwapatapo wanadamu,
JOB 4:14 hofu na kutetemeka kulinishika na kufanya mifupa yangu yote itetemeke.
JOB 4:15 Kuna roho aliyepita mbele ya uso wangu, nazo nywele za mwili wangu zikasimama.
JOB 4:16 Yule roho akasimama, lakini sikuweza kutambua kilikuwa kitu gani. Umbo fulani lilisimama mbele ya macho yangu, kukawa na ukimya kisha nikasikia sauti:
JOB 4:17 ‘Je, binadamu aweza kuwa mwadilifu kuliko Mungu? Je, mtu aweza kuwa safi kuliko Muumba wake?
JOB 4:18 Ikiwa Mungu hawaamini watumishi wake, ikiwa yeye huwalaumu malaika wake kwa kukosea,
JOB 4:19 ni mara ngapi zaidi wale wanaoishi katika nyumba za udongo wa mfinyanzi, ambazo misingi yake ipo mavumbini, ambao wamepondwa kama nondo!
JOB 4:20 Kati ya mawio na machweo huvunjwa vipande vipande; bila yeyote kutambua, huangamia milele.
JOB 4:21 Je, kamba za hema lao hazikung’olewa, hivyo hufa bila hekima?’
JOB 5:1 “Itana, ukitaka, lakini ni nani atakayekujibu? Ni yupi kati ya hao watakatifu utakayemgeukia?
JOB 5:2 Kuweka uchungu moyoni humuua mpumbavu, nao wivu humchinja mjinga.
JOB 5:3 Mimi mwenyewe nimemwona mpumbavu akistawi, lakini ghafula nyumba yake ikawa imelaaniwa.
JOB 5:4 Watoto wake wako mbali na usalama, hushindwa mahakamani bila mtetezi.
JOB 5:5 Wenye njaa huyala mavuno yake, wakiyatoa hata katikati ya miiba, nao wenye kiu huitamani sana mali yake.
JOB 5:6 Kwa maana taabu haioti kutoka kwa udongo, wala ubaya hauchipui kutoka ardhini.
JOB 5:7 Lakini mwanadamu huzaliwa ili kutaabika, kwa hakika kama cheche za moto zinavyoruka kuelekea juu.
JOB 5:8 “Lakini ingekuwa ni mimi, ningemlalamikia Mungu, ningeweka shauri langu mbele zake.
JOB 5:9 Yeye hutenda maajabu yasiyoweza kutambuliwa, miujiza isiyoweza kuhesabika.
JOB 5:10 Yeye huipa nchi mvua, huyapeleka maji kunyesha mashamba.
JOB 5:11 Huwainua juu wanyonge, nao wale wanaoomboleza huinuliwa wakawa salama.
JOB 5:12 Huipinga mipango ya wenye hila, ili mikono yao isifikie ufanisi.
JOB 5:13 Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao, nayo mipango ya wadanganyifu huifagilia mbali.
JOB 5:14 Giza huwapata wakati wa mchana; wakati wa adhuhuri hupapasa kama vile usiku.
JOB 5:15 Humwokoa mhitaji kutokana na upanga ulioko kinywani mwao; huwaokoa kutokana na makucha ya wenye nguvu.
JOB 5:16 Kwa hiyo maskini analo tarajio, nao udhalimu hufumba kinywa chake.
JOB 5:17 “Heri mtu yule ambaye Mungu humkanya; kwa hiyo usidharau adhabu yake Mwenyezi.
JOB 5:18 Kwa kuwa hutia jeraha, lakini pia huyafunga; huumiza, lakini mikono yake pia huponya.
JOB 5:19 Kutoka majanga sita atakuokoa; naam, hata katika saba hakuna dhara litakalokupata wewe.
JOB 5:20 Wakati wa njaa atakukomboa wewe na kifo, naye katika vita atakukomboa na pigo la upanga.
JOB 5:21 Utalindwa kutokana na kichapo cha ulimi, wala hutakuwa na sababu ya kuogopa maangamizi yatakapokujia.
JOB 5:22 Utayacheka maangamizi na njaa, wala hutakuwa na sababu ya kuwaogopa wanyama wakali wa mwituni.
JOB 5:23 Kwa kuwa utakuwa na agano na mawe ya mashamba, nao wanyama pori watakuwa na amani nawe.
JOB 5:24 Utajua kwamba hema lako li salama; utahesabu mali yako wala hutakuta chochote kilichopungua.
JOB 5:25 Utajua kuwa watoto wako watakuwa wengi, nao wazao wako wengi kama majani ya nchi.
JOB 5:26 Utaingia kaburini ukiwa na umri wa uzee mtimilifu, kama masuke ya ngano yanapokusanywa kwa wakati wake.
JOB 5:27 “Tumelichunguza hili, nalo ni kweli. Hivyo lisikie na ulitendee kazi.”
JOB 6:1 Kisha Ayubu akajibu:
JOB 6:2 “Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa, nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani!
JOB 6:3 Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote, kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.
JOB 6:4 Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu, roho yangu inakunywa sumu yake; vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.
JOB 6:5 Je, punda-mwitu hulia akiwa na majani, au fahali hulia akiwa na chakula?
JOB 6:6 Je, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi, au upo utamu katika ute mweupe wa yai?
JOB 6:7 Ninakataa kuvigusa; vyakula vya aina hii hunichukiza.
JOB 6:8 “Laiti ningepata haja yangu, kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia,
JOB 6:9 kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda, kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali!
JOB 6:10 Ndipo bado ningekuwa na hii faraja, furaha yangu katika maumivu makali: kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.
JOB 6:11 “Nina nguvu gani, hata niendelee kutumaini? Matazamio yangu ni nini, hata niendelee kuwa mvumilivu?
JOB 6:12 Je, mimi nina nguvu za jiwe? Je, mwili wangu ni shaba?
JOB 6:13 Je, ninao uwezo wowote wa kujisaidia mimi mwenyewe, wakati mafanikio yamefukuziwa mbali nami?
JOB 6:14 “Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake, hata akiacha uchaji wa Mwenyezi.
JOB 6:15 Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa, ni kama vijito vya msimu, ni kama vijito ambavyo hufurika
JOB 6:16 wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo, ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,
JOB 6:17 lakini hukauka majira ya ukame, na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.
JOB 6:18 Misafara hugeuka kutoka njia zake; hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.
JOB 6:19 Misafara ya Tema inatafuta maji, wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri hutazama kwa matarajio.
JOB 6:20 Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini; wanafika huko, lakini wanahuzunika kwa kukosa walichotarajia.
JOB 6:21 Sasa nanyi mmethibitika kwamba hamna msaada wowote; mnaona jambo la kutisha, nanyi mnaogopa.
JOB 6:22 Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu, au mnilipie fidia kutoka mali yenu,
JOB 6:23 au niokoeni mikononi mwa adui, au nikomboeni kutoka makucha ya wasio na huruma’?
JOB 6:24 “Nifundisheni, nami nitakaa kimya; nionesheni nilikokosea.
JOB 6:25 Tazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli! Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini?
JOB 6:26 Je, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema, na kuyafanya maneno ya mtu anayekata tamaa kama upepo?
JOB 6:27 Mngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima, na kubadilishana rafiki yenu na mali.
JOB 6:28 “Lakini sasa kuweni na huruma mkaniangalie mimi. Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu?
JOB 6:29 Tulizeni hasira, msiwe wadhalimu; angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu.
JOB 6:30 Je, pana uovu wowote mdomoni mwangu? Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?
JOB 7:1 “Je, mwanadamu hana kazi ngumu duniani? Siku zake si kama zile za mtu aliyeajiriwa?
JOB 7:2 Kama mtumwa anavyovionea shauku vivuli vya jioni, au mtu aliyeajiriwa anavyoungojea mshahara wake,
JOB 7:3 ndivyo nilivyogawiwa miezi ya ubatili, nami nimeandikiwa huzuni usiku hata usiku.
JOB 7:4 Nilalapo ninawaza, ‘Itachukua muda gani kabla sijaamka?’ Usiku huwa mrefu, nami najigeuzageuza hadi mapambazuko.
JOB 7:5 Mwili wangu umevikwa mabuu na uchafu, ngozi yangu imetumbuka na kutunga usaha.
JOB 7:6 “Siku zangu zinapita upesi kuliko mtande wa kufuma, nazo zinafikia mwisho wake bila matumaini.
JOB 7:7 Kumbuka, Ee Mungu, maisha yangu ni kama pumzi; macho yangu kamwe hayataona tena raha.
JOB 7:8 Lile jicho linaloniona sasa halitaniona tena; utanitafuta, wala sitakuwepo.
JOB 7:9 Kama vile wingu liondokavyo na kutoweka, vivyo hivyo yeye ashukaye kaburini harudi tena.
JOB 7:10 Kamwe harudi tena nyumbani mwake; wala mahali pake hapatamjua tena.
JOB 7:11 “Kwa hiyo sitanyamaza; nitanena kutokana na maumivu makuu ya roho yangu, nitalalama kwa uchungu wa nafsi yangu.
JOB 7:12 Je, mimi ni bahari, au yule mnyama mkubwa wa baharini, hata uniweke chini ya ulinzi?
JOB 7:13 Ninapofikiri kwamba kitanda changu kitanifariji, nacho kiti changu cha fahari kitapunguza malalamiko yangu,
JOB 7:14 ndipo wanitisha kwa ndoto na kunitia hofu kwa maono,
JOB 7:15 hivyo ninachagua kujinyonga na kufa, kuliko huu mwili wangu.
JOB 7:16 Ninayachukia maisha yangu; nisingetamani kuendelea kuishi. Niache; siku zangu ni ubatili.
JOB 7:17 “Mwanadamu ni kitu gani hata umjali kiasi hiki, kwamba unamtia sana maanani,
JOB 7:18 kwamba unamwangalia kila asubuhi na kumjaribu kila wakati?
JOB 7:19 Je, hutaacha kamwe kunitazama, au kuniacha japo kwa kitambo kidogo tu?
JOB 7:20 Ikiwa nimetenda dhambi, nimekufanyia nini, Ewe mlinzi wa wanadamu? Kwa nini umeniweka niwe shabaha yako? Je, nimekuwa mzigo kwako?
JOB 7:21 Kwa nini husamehi makosa yangu na kuachilia dhambi zangu? Kwa kuwa hivi karibuni nitalala mavumbini; nawe utanitafuta, wala sitakuwepo.”
JOB 8:1 Kisha Bildadi Mshuhi akajibu:
JOB 8:2 “Hata lini wewe utasema mambo kama haya? Maneno yako ni kama upepo mkuu.
JOB 8:3 Je, Mungu hupotosha hukumu? Je, Mwenyezi hupotosha kile kilicho haki?
JOB 8:4 Watoto wako walipomtenda dhambi, aliwapa adhabu ya dhambi yao.
JOB 8:5 Lakini ukimtafuta Mungu, nawe ukamsihi Mwenyezi,
JOB 8:6 ikiwa wewe ni safi na mnyofu, hata sasa atainuka mwenyewe kwa niaba yako, na kukurudisha katika mahali pako pa haki.
JOB 8:7 Ijapokuwa mwanzo wako ulikuwa mdogo, lakini mwisho wako utakuwa wa mafanikio.
JOB 8:8 “Ukaulize vizazi vilivyotangulia na uone baba zao walijifunza nini,
JOB 8:9 kwa kuwa sisi tumezaliwa jana tu na hatujui lolote, nazo siku zetu duniani ni kama kivuli tu.
JOB 8:10 Je, hawatakufundisha na kukueleza? Je, hawataleta maneno ya ufahamu wao?
JOB 8:11 Je, mafunjo yaweza kumea mahali pasipo na matope? Matete yaweza kustawi bila maji?
JOB 8:12 Wakati bado yanaendelea kukua kabla ya kukatwa, hunyauka haraka kuliko majani mengine.
JOB 8:13 Huu ndio mwisho wa watu wote wanaomsahau Mungu; vivyo hivyo matumaini ya wasiomjali Mungu huangamia.
JOB 8:14 Lile analolitumainia huvunjika upesi; lile analolitegemea ni utando wa buibui.
JOB 8:15 Huutegemea utando wake, lakini hausimami; huung’ang’ania, lakini haudumu.
JOB 8:16 Yeye ni kama mti ulionyeshewa vizuri wakati wa jua, ukieneza machipukizi yake bustanini;
JOB 8:17 huifunganisha mizizi yake kwenye lundo la mawe, na kutafuta nafasi kati ya mawe.
JOB 8:18 Unapong’olewa kutoka mahali pake, ndipo mahali pale huukana na kusema, ‘Mimi kamwe sikukuona.’
JOB 8:19 Hakika uhai wake hunyauka, na kutoka udongoni mimea mingine huota.
JOB 8:20 “Hakika Mungu hamkatai mtu asiye na hatia, wala kuitia nguvu mikono ya mtenda maovu.
JOB 8:21 Bado atakijaza kinywa chako na kicheko, na midomo yako na kelele za shangwe.
JOB 8:22 Adui zako watavikwa aibu, nayo mahema ya waovu hayatakuwepo tena.”
JOB 9:1 Kisha Ayubu akajibu:
JOB 9:2 “Naam, najua hili ni kweli. Lakini mwanadamu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?
JOB 9:3 Ingawa mtu angetaka kushindana naye, hangeweza kumjibu Mungu hata mara moja miongoni mwa elfu moja.
JOB 9:4 Hekima yake ni kubwa sana na ana uwezo mwingi mno. Ni nani aliyempinga naye akawa salama?
JOB 9:5 Aiondoa milima bila yenyewe kujua na kuipindua kwa hasira yake.
JOB 9:6 Aitikisa dunia kutoka mahali pake na kuzifanya nguzo zake zitetemeke.
JOB 9:7 Husema na jua, nalo likaacha kuangaza; naye huizima mianga ya nyota.
JOB 9:8 Yeye peke yake huzitandaza mbingu na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
JOB 9:9 Yeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu, na Orioni, Kilimia, na makundi ya nyota za kusini.
JOB 9:10 Hutenda maajabu yasiyopimika, miujiza isiyoweza kuhesabiwa.
JOB 9:11 Anapopita karibu nami, siwezi kumwona; apitapo mbele yangu, simtambui.
JOB 9:12 Anapochukua kwa ghafula, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwambia, ‘Unafanya nini?’
JOB 9:13 Mungu hataizuia hasira yake; hata jeshi kubwa la Rahabu lenye nguvu linajikunyata miguuni pake.
JOB 9:14 “Ni vipi basi mimi nitaweza kubishana naye? Nawezaje kupata maneno ya kuhojiana naye?
JOB 9:15 Ingawa sikuwa na hatia, sikuweza kumjibu; ningeweza tu kumsihi Mhukumu wangu anihurumie.
JOB 9:16 Hata kama ningemwita kwenye shauri, naye akakubali, siamini kama angenisikiliza.
JOB 9:17 Yeye angeniangamiza kwa dhoruba na kuongeza majeraha yangu pasipo na sababu.
JOB 9:18 Asingeniacha nipumue bali angenifunika kabisa na huzuni kuu.
JOB 9:19 Kama ni suala la nguvu, yeye ni mwenye nguvu! Kama ni suala la haki, ni nani awezaye kumwita mahakamani?
JOB 9:20 Hata kama sikuwa na hatia, kinywa changu kingenihukumu; kama sikuwa na kosa, kingenitangaza kuwa mwenye hatia.
JOB 9:21 “Ingawa mimi sina kosa, haileti tofauti katika nafsi yangu; nauchukia uhai wangu.
JOB 9:22 Hayo yote ni sawa; ndiyo sababu nasema, ‘Yeye huwaangamiza wasio na makosa pamoja na waovu.’
JOB 9:23 Wakati wa pigo liletapo kifo cha ghafula, yeye hudhihaki kule kukata tamaa kwa yule asiye na kosa.
JOB 9:24 Nchi inapoangukia mikononi mwa waovu, yeye huwafunga macho mahakimu wake. Kama si yeye, basi ni nani?
JOB 9:25 “Siku zangu zapita mbio kuliko mkimbiaji; zinapita upesi bila kuona furaha hata kidogo.
JOB 9:26 Zinapita upesi kama mashua ya mafunjo, mfano wa tai ayashukiaye mawindo kwa ghafula.
JOB 9:27 Nikisema, ‘Nitayasahau malalamiko yangu, nitabadili sura ya uso wangu na kutabasamu,’
JOB 9:28 bado ninahofia mateso yangu yote, kwa kuwa ninajua hutanihesabu kuwa sina hatia.
JOB 9:29 Kwa kuwa nimeonekana mwenye hatia, kwa nini basi nitaabishwe bure?
JOB 9:30 Hata kama ningejiosha kwa sabuni na kutakasa mikono yangu kwa magadi,
JOB 9:31 wewe ungenitupa kwenye shimo la utelezi kiasi kwamba hata nguo zangu zingenichukia sana.
JOB 9:32 “Yeye si mwanadamu kama mimi ili niweze kumjibu, ili tuweze kushindana naye mahakamani.
JOB 9:33 Laiti pangekuwa na mtu wa kutupatanisha, aweke mkono wake juu yetu sote wawili,
JOB 9:34 mtu wa kuondoa fimbo ya Mungu juu yangu, ili utisho wake usiendelee kunitia hofu.
JOB 9:35 Ndipo ningenena naye, bila kumwogopa, lakini kama ilivyo kwangu sasa, sitaweza.
JOB 10:1 “Nayachukia sana haya maisha yangu; kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia, nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu.
JOB 10:2 Nitamwambia Mungu: Usinihukumu, bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu.
JOB 10:3 Je, inakupendeza wewe kunidhulumu, kuikataa kazi ya mikono yako, huku ukiunga mkono mipango ya waovu?
JOB 10:4 Je, wewe una macho ya kimwili? Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo?
JOB 10:5 Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu, au miaka yako ni kama ile ya mtu,
JOB 10:6 ili utafute makosa yangu na kuichunguza dhambi yangu;
JOB 10:7 ingawa unajua kuwa mimi sina hatia, na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako?
JOB 10:8 “Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya. Je, sasa utageuka na kuniangamiza?
JOB 10:9 Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi. Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena?
JOB 10:10 Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa, na kunigandisha kama jibini,
JOB 10:11 ukanivika ngozi na nyama, na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa?
JOB 10:12 Umenipa uhai na kunitendea wema, katika uangalizi wako umeilinda roho yangu.
JOB 10:13 “Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako, nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako:
JOB 10:14 Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona, wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa.
JOB 10:15 Kama nina hatia, ole wangu! Hata kama ningekuwa sina hatia, siwezi kukiinua kichwa changu, kwa kuwa nimejawa na aibu, na kuzama katika mateso yangu.
JOB 10:16 Nikiinua kichwa changu juu, unaniwinda kama simba, na kuonesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu.
JOB 10:17 Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu na kuzidisha hasira yako juu yangu; nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine.
JOB 10:18 “Kwa nini basi ulinitoa tumboni? Ninatamani ningekufa kabla jicho lolote halijaniona.
JOB 10:19 Laiti nisingezaliwa, au kama ningepelekwa kaburini moja kwa moja kutoka tumboni!
JOB 10:20 Je, siku zangu chache si zimekaribia kwisha? Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi
JOB 10:21 kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena, katika nchi ya giza na uvuli wa mauti,
JOB 10:22 nchi ya giza nene sana, yenye uvuli wa giza na machafuko, ambapo hata nuru ni giza.”
JOB 11:1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:
JOB 11:2 “Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa? Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?
JOB 11:3 Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya? Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?
JOB 11:4 Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili nami ni safi mbele zako.’
JOB 11:5 Aha! Laiti kwamba Mungu angesema, kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,
JOB 11:6 naye akufunulie siri za hekima, kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili. Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.
JOB 11:7 “Je, unaweza kujua siri za Mungu? Je, unaweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?
JOB 11:8 Ni juu mno kuliko mbingu: unaweza kufanya nini? Kina chake ni kirefu kuliko Kuzimu: wewe unaweza kujua nini?
JOB 11:9 Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia, nacho ni kipana kuliko bahari.
JOB 11:10 “Akija na kukufunga gerezani, na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?
JOB 11:11 Hakika anawatambua watu wadanganyifu; naye aonapo uovu, je, haangalii?
JOB 11:12 Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima, endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.
JOB 11:13 “Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake na kumwinulia mikono yako,
JOB 11:14 ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako, wala usiuruhusu uovu ukae kwenye hema lako,
JOB 11:15 ndipo utainua uso wako bila aibu; utasimama imara bila hofu.
JOB 11:16 Hakika utaisahau taabu yako, utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.
JOB 11:17 Maisha yako yatang’aa kuliko adhuhuri, nalo giza litakuwa kama alfajiri.
JOB 11:18 Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini; utatazama pande zote na kupumzika kwa salama.
JOB 11:19 Utalala, wala hakuna atakayekuogofya, naam, wengi watajipendekeza kwako.
JOB 11:20 Bali macho ya waovu hayataona, wokovu utawaepuka; tarajio lao litakuwa ni hangaiko la mtu anayekata roho.”
JOB 12:1 Ndipo Ayubu akajibu:
JOB 12:2 “Bila shaka ninyi ndio watu, nayo hekima itakoma mtakapokufa!
JOB 12:3 Lakini mimi ninao ufahamu kama ninyi; mimi si duni kwenu. Ni nani asiyejua mambo haya yote?
JOB 12:4 “Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu, ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu: mimi ni mtu wa kuchekwa tu, ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!
JOB 12:5 Wanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau kwa wale wenye msiba kana kwamba ndiyo haki ya wale ambao miguu yao inateleza.
JOB 12:6 Mahema ya wanyang’anyi hayasumbuliwi, wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama: wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.
JOB 12:7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha, au ndege wa angani, nao watawaambia;
JOB 12:8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha, au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.
JOB 12:9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua kwamba mkono wa Mwenyezi Mungu ndio uliofanya hili?
JOB 12:10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe, na pumzi ya wanadamu wote.
JOB 12:11 Je, sikio haliyajaribu maneno kama vile ulimi uonjavyo chakula?
JOB 12:12 Je, hekima haipatikani kwa wazee? Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?
JOB 12:13 “Hekima na nguvu ni vya Mungu; shauri na ufahamu ni vyake yeye.
JOB 12:14 Kile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena; mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.
JOB 12:15 Akizuia maji, huwa pana ukame; akiyaachia maji, huharibu nchi.
JOB 12:16 Kwake kuna nguvu na ushindi; anayedanganywa na anayedanganya, wote wawili ni wake.
JOB 12:17 Yeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara, naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.
JOB 12:18 Huondoa pingu zilizofungwa na wafalme, na kuwafunga mishipi ya kiunoni.
JOB 12:19 Huwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara, na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.
JOB 12:20 Hunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika, na kuondoa busara ya wazee.
JOB 12:21 Huwadharau wanaoheshimika, na kuwavua silaha wenye nguvu.
JOB 12:22 Hufunua mambo ya ndani ya gizani, na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.
JOB 12:23 Huyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza; hufanya mataifa kuwa makubwa, naye huyatawanya.
JOB 12:24 Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao; huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.
JOB 12:25 Hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga; huwafanya wapepesuke kama walevi.
JOB 13:1 “Macho yangu yameona hili lote, masikio yangu yamesikia na kulielewa.
JOB 13:2 Hayo mnayoyajua mimi pia ninayajua; mimi si mtu duni kuliko ninyi.
JOB 13:3 Lakini ninayo shauku ya kuzungumza na Mwenyezi na kuhojiana shauri langu na Mungu.
JOB 13:4 Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo; ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!
JOB 13:5 Laiti wote mngenyamaza! Kwa kuwa kwenu hilo lingekuwa hekima.
JOB 13:6 Sikieni sasa hoja yangu; sikilizeni kusihi kwangu.
JOB 13:7 Je, mtazungumza kwa uovu kwa niaba ya Mungu? Je, mtazungumza kwa udanganyifu kwa niaba yake?
JOB 13:8 Mtamwonesha upendeleo? Mtamtetea Mungu kwenye mashtaka yake?
JOB 13:9 Je, ingekuwa vyema Mungu akiwahoji ninyi? Je, mngeweza kumdanganya kama ambavyo mngeweza kuwadanganya wanadamu?
JOB 13:10 Hakika angewakemea mkiwapendelea watu kwa siri.
JOB 13:11 Je, huo ukuu wake haungewatisha ninyi? Je, hofu yake isingewaangukia ninyi?
JOB 13:12 Maneno yenu ni mithali za majivu; utetezi wenu ni ngome za udongo wa mfinyanzi.
JOB 13:13 “Nyamazeni kimya nipate kusema; kisha na yanipate yatakayonipata.
JOB 13:14 Kwa nini nijiweke mwenyewe kwenye hatari na kuyaweka maisha yangu mikononi mwangu?
JOB 13:15 Ingawa ataniua, bado nitamtumaini; hakika nitazitetea njia zangu mbele zake.
JOB 13:16 Naam, hili litanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa maana hakuna mtu asiyemcha Mungu atakayethubutu kuja mbele yake!
JOB 13:17 Sikilizeni maneno yangu kwa makini; nayo masikio yenu yaingize kile nisemacho.
JOB 13:18 Sasa kwa kuwa nimekwisha tayarisha kesi yangu, ninajua nitahesabiwa kuwa haki.
JOB 13:19 Je, kuna yeyote anayeweza kuleta mashtaka dhidi yangu? Kama ndivyo, nitanyamaza na nife.
JOB 13:20 “Ee Mungu, unijalie tu mimi haya mambo mawili, nami sitajificha uso wako:
JOB 13:21 Ondoa mkono wako uwe mbali nami, uache kuniogofya kwa vitisho vyako.
JOB 13:22 Niite kwenye shauri nami nitajibu, au niache niseme, nawe upate kujibu.
JOB 13:23 Ni makosa na dhambi ngapi nilizotenda? Nioneshe kosa langu na dhambi yangu.
JOB 13:24 Kwa nini kuuficha uso wako na kunihesabu mimi kuwa adui yako?
JOB 13:25 Je, utaliadhibu jani lipeperushwalo na upepo? Je, utayasaka makapi makavu?
JOB 13:26 Kwa kuwa unaandika mambo machungu dhidi yangu na kunifanya nizirithi dhambi za ujana wangu.
JOB 13:27 Umeifunga miguu yangu kwenye pingu. Unazichunga kwa makini njia zangu zote kwa kutia alama kwenye nyayo za miguu yangu.
JOB 13:28 “Hivyo mwanadamu huangamia kama kitu kilichooza, kama vazi lililoliwa na nondo.
JOB 14:1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake ni chache nazo zimejaa taabu.
JOB 14:2 Huchanua kama ua kisha hunyauka; huwa kama kivuli kipitacho upesi, wala hadumu.
JOB 14:3 Je, unamwekea jicho lako mtu kama huyo? Je, utamleta mbele yako katika hukumu?
JOB 14:4 Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka kitu najisi? Hakuna awezaye!
JOB 14:5 Siku za mwanadamu zimewekewa mpaka; umekwisha kutangaza idadi ya miezi yake na kuweka mpaka ambao hawezi kuuvuka.
JOB 14:6 Hivyo angalia mbali umwache, hadi awe amekamilisha muda wake kama mtu aliyeajiriwa.
JOB 14:7 “Kwa maana lipo tumaini kwa mti; kama ukikatwa utachipuka tena, nayo machipukizi yake mapya hayatakoma.
JOB 14:8 Mizizi yake yaweza kuchakaa ardhini na kisiki chake kufa udongoni,
JOB 14:9 lakini kwa kupata dalili ya maji utachipua na kutoa machipukizi kama mche.
JOB 14:10 Lakini mwanadamu hufa, na huo ndio mwisho wake; hutoa pumzi ya mwisho, naye hayuko tena!
JOB 14:11 Kama vile maji yanavyotoweka katika bahari, au mkondo wa mto ukaushwavyo na kuwa mkavu,
JOB 14:12 ndivyo mwanadamu alalavyo chini asiamke; hadi mbingu zitakapokuwa hazipo tena, wanadamu hawataamka au kuamshwa kutoka usingizi wao.
JOB 14:13 “Laiti kama ungenificha kaburini, na kunisitiri hadi hasira yako ipite! Laiti ungeniwekea wakati, na kisha ukanikumbuka!
JOB 14:14 Je, kama mtu akifa, aweza kuishi tena? Siku zote za kazi zangu ngumu nitangojea kufanywa upya kwangu.
JOB 14:15 Utaniita nami nitakuitika; utakionea shauku kiumbe ambacho mikono yako ilikiumba.
JOB 14:16 Hakika ndipo utakapozihesabu hatua zangu, lakini hutazifuatia dhambi zangu.
JOB 14:17 Makosa yangu yatatiwa muhuri kwenye mfuko, nawe utazifunika dhambi zangu.
JOB 14:18 “Lakini kama mlima umomonyokavyo na kufikichika na kama vile mwamba uondolewavyo mahali pake,
JOB 14:19 kama maji yamalizavyo mawe, na mafuriko yachukuavyo udongo, ndivyo unavyoharibu tegemeo la mwanadamu.
JOB 14:20 Humshinda mara moja kwa daima, naye hutoweka; waibadilisha sura yake na kumwondoa.
JOB 14:21 Kama wanawe wakipewa heshima, yeye hafahamu; kama wazao wake wakidharauliwa, yeye haoni.
JOB 14:22 Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe, naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”
JOB 15:1 Kisha Elifazi Mtemani akajibu:
JOB 15:2 “Je, mtu mwenye hekima hujibu kwa mawazo matupu, au kujaza tumbo lake kwa upepo wenye joto wa mashariki?
JOB 15:3 Je, aweza kubishana kwa maneno yasiyofaa, kwa hotuba zisizo na maana?
JOB 15:4 Lakini unadhoofisha hata uchaji wa Mungu na kuzuia ibada mbele za Mungu.
JOB 15:5 Dhambi yako inasukuma kinywa chako, nawe umechagua ulimi wa hila.
JOB 15:6 Kinywa chako mwenyewe kinakuhukumu, wala si changu; midomo yako mwenyewe inashuhudia dhidi yako.
JOB 15:7 “Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa? Ulizaliwa kabla ya vilima?
JOB 15:8 Je, wewe husikiliza mashauri ya siri ya Mungu? Je, wewe unaizuia hekima iwe yako mwenyewe?
JOB 15:9 Wewe unajua kitu gani tusichokijua sisi? Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?
JOB 15:10 Wale wenye mvi na wazee wako upande wetu, watu ambao ni wazee hata kuliko baba yako.
JOB 15:11 Je, faraja za Mungu hazikutoshi, au maneno yaliyosemwa kwako kwa upole si kitu?
JOB 15:12 Kwa nini moyo wako unakudanganya, na kwa nini macho yako yanang’aa,
JOB 15:13 ili upate kutoa hasira yako dhidi ya Mungu, na kumwaga maneno kama hayo kutoka kinywani mwako?
JOB 15:14 “Mwanadamu ni kitu gani, hata aweze kuwa safi, au yeye aliyezaliwa na mwanamke, hata aweze kuwa mwadilifu?
JOB 15:15 Kama Mungu hawaamini watakatifu wake, kama hata mbingu zenyewe si safi machoni pake,
JOB 15:16 sembuse mwanadamu ambaye ni mwovu na mpotovu, ambaye hunywa uovu kama anywavyo maji!
JOB 15:17 “Nisikilize mimi nami nitakueleza, acha nikuambie yale niliyoyaona,
JOB 15:18 ambayo watu wenye hekima wameyanena, bila kuficha lolote walilopokea toka kwa baba zao
JOB 15:19 (wakati ambao wao peke yao ndio walipewa nchi, hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao):
JOB 15:20 Mtu mwovu siku zake zote hupata mateso, miaka yote aliwekewa mkorofi.
JOB 15:21 Sauti za kutisha hujaa masikioni mwake; katika kufanikiwa kwake, wanyang’anyi humshambulia.
JOB 15:22 Hukata tamaa kuokoka gizani; amewekwa kwa ajili ya upanga.
JOB 15:23 Hutangatanga, akitafuta chakula; anajua kwamba siku ya giza iko karibu.
JOB 15:24 Taabu na maumivu makuu vinamtia hofu; humshinda kama mfalme aliye tayari kwa vita,
JOB 15:25 kwa sababu amemkunjia Mungu ngumi yake na kujigamba dhidi ya Mwenyezi,
JOB 15:26 kwa kiburi akishambulia dhidi ya Mungu akiwa na ngao nene, iliyo imara.
JOB 15:27 “Ingawa uso wake umefunikwa na mafuta kwa unene na kiuno chake kimevimba kwa kunenepa,
JOB 15:28 ataishi katika miji ya magofu, na katika nyumba ambazo haziishi mwanadamu yeyote, nyumba zinazokuwa vifusi.
JOB 15:29 Hatatajirika tena, nao utajiri wake hautadumu, wala mali yake haitakuwa nyingi juu ya nchi.
JOB 15:30 Hatatoka gizani; mwali wa moto utanyausha machipukizi yake, nayo pumzi ya kinywa cha Mungu itamwondolea mbali.
JOB 15:31 Asijidanganye mwenyewe kutumainia ubatili, kwa kuwa hatapata malipo yoyote.
JOB 15:32 Atakuwa amelipwa kikamilifu kabla ya wakati wake, nayo matawi yake hayatastawi.
JOB 15:33 Atafanana na mzabibu uliopukutishwa matunda yake kabla hayajaiva, kama mzeituni unaodondosha maua yake.
JOB 15:34 Kwa kuwa jamii ya wasiomcha Mungu watakuwa tasa, nao moto utateketeza mahema ya wale wanaopenda rushwa.
JOB 15:35 Hutunga mimba ya madhara na kuzaa uovu; tumbo zao huumba udanganyifu.”
JOB 16:1 Kisha Ayubu akajibu:
JOB 16:2 “Nimepata kusikia mambo mengi kama haya, nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!
JOB 16:3 Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho? Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?
JOB 16:4 Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi, kama mngekuwa katika hali yangu; ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu, na kuwatikisia ninyi kichwa changu.
JOB 16:5 Lakini kinywa changu kingewatia moyo; faraja kutoka mdomoni mwangu ingewaletea nafuu.
JOB 16:6 “Lakini nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi; na nikijizuia, bado hayaondoki.
JOB 16:7 Ee Mungu, hakika umenichakaza; umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote.
JOB 16:8 Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi; nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu.
JOB 16:9 Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake, na kunisagia meno yake; adui yangu hunikazia macho yake makali.
JOB 16:10 Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki; hunipiga shavuni mwangu kwa dharau, na kuungana pamoja dhidi yangu.
JOB 16:11 Mungu amenigeuzia kwa watu wapotovu, na kunitupa katika makucha ya waovu.
JOB 16:12 Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja; amenikamata shingo na kuniponda. Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;
JOB 16:13 wapiga upinde wake wananizunguka. Bila huruma, huchoma figo zangu, na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.
JOB 16:14 Huniponda tena na tena; hunishambulia kama shujaa wa vita.
JOB 16:15 “Nimejishonea gunia juu ya mwili wangu, nami nimezika paji la uso wangu kwenye vumbi.
JOB 16:16 Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia, macho yangu yamepigwa na giza.
JOB 16:17 Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri, na maombi yangu ni safi.
JOB 16:18 “Ee nchi, usiifunike damu yangu, nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.
JOB 16:19 Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni; wakili wangu yuko juu.
JOB 16:20 Mwombezi wangu ni rafiki yangu macho yangu yanapomwaga machozi kwa Mungu;
JOB 16:21 kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.
JOB 16:22 “Ni miaka michache tu itapita kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.
JOB 17:1 Moyo wangu umevunjika, siku zangu zimefupishwa, kaburi linaningojea.
JOB 17:2 Hakika wenye mizaha wamenizunguka; macho yangu yamebaki kutazama uadui wao.
JOB 17:3 “Ee Mungu, nipe dhamana unayodai. Ni nani mwingine atakayeweka dhamana kwa ajili yangu?
JOB 17:4 Umezifunga akili zao zisipate ufahamu, kwa hiyo hutawaacha wapate ushindi.
JOB 17:5 Kama mtu akiwashutumu rafiki zake ili apate ujira, macho ya watoto wake yatashindwa kuona.
JOB 17:6 “Mungu amenifanya kitu cha dhihaka kwa kila mtu, mtu ambaye watu humtemea mate usoni.
JOB 17:7 Macho yangu yamefifia kwa ajili ya majonzi; umbile langu lote ni kama kivuli.
JOB 17:8 Watu wanyofu wanatishwa na hili; watu wasio na hatia wanasimama dhidi ya wasiomcha Mungu.
JOB 17:9 Hata hivyo, waadilifu watazishika njia zao, nao wale wenye mikono safi wataendelea kupata nguvu.
JOB 17:10 “Lakini ninyi njooni, ninyi nyote, jaribuni tena! Sitampata mtu mwenye hekima miongoni mwenu.
JOB 17:11 Siku zangu zimepita, mipango yangu imevunjika, vivyo hivyo shauku za moyo wangu.
JOB 17:12 Watu hawa hufanya usiku kuwa mchana, kwenye giza wao husema, ‘Mwanga u karibu.’
JOB 17:13 Kama nyumba pekee ninayoitarajia ni kaburi, nikikitandika kitanda changu gizani,
JOB 17:14 nikiuambia uharibifu, ‘Wewe u baba yangu,’ na kuliambia buu, ‘Wewe u mama yangu’ au ‘Dada yangu,’
JOB 17:15 liko wapi basi tarajio langu? Ni nani awezaye kuona tarajio lolote kwa ajili yangu?
JOB 17:16 Je, litashuka chini hadi kwenye malango ya mauti? Je, tutashuka pamoja mavumbini?”
JOB 18:1 Bildadi Mshuhi akajibu:
JOB 18:2 “Je, ni lini utafika mwisho wa maneno haya? Uwe mwenye busara, nasi ndipo tutakapoweza kuongea.
JOB 18:3 Kwa nini sisi tunafikiriwa kama wanyama, na kuonekana wajinga machoni pako?
JOB 18:4 Wewe unayejirarua mwenyewe vipande vipande katika hasira yako, je, dunia iachwe kwa ajili yako wewe? Au ni lazima miamba iondolewe mahali pake?
JOB 18:5 “Taa ya mwovu imezimwa, nao mwali wa moto wake umezimika.
JOB 18:6 Mwanga kwenye hema lake umekuwa giza; taa iliyo karibu naye imezimika.
JOB 18:7 Nguvu za hatua zake zimedhoofishwa; hila zake mwenyewe zinamwangusha.
JOB 18:8 Miguu yake imemsukumia kwenye wavu, naye anatangatanga kwenye matundu ya wavu.
JOB 18:9 Tanzi litamkamata kwenye kisigino; mtego utamshikilia kwa nguvu.
JOB 18:10 Kitanzi kimefichwa ardhini kwa ajili yake; mtego uko kwenye njia yake.
JOB 18:11 Vitisho vimemtia hofu kila upande, na adui zake humwandama kila hatua.
JOB 18:12 Janga linamwonea shauku; maafa yako tayari kwa ajili yake aangukapo.
JOB 18:13 Nayo yatakula sehemu ya ngozi yake; mzaliwa wa kwanza wa mauti atakula maungo yake.
JOB 18:14 Atang’olewa kutoka usalama wa hema lake, na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.
JOB 18:15 Moto utakaa katika hema lake; moto wa kiberiti utamwagwa juu ya makao yake.
JOB 18:16 Mizizi yake chini itakauka na matawi yake juu yatanyauka.
JOB 18:17 Kumbukumbu lake litatoweka katika dunia, wala hatakuwa na jina katika nchi.
JOB 18:18 Ameondolewa nuruni na kusukumiwa gizani, naye amefukuzwa mbali atoke duniani.
JOB 18:19 Hana mtoto wala mzao miongoni mwa watu wake, wala aliyenusurika mahali alipoishi.
JOB 18:20 Watu wa magharibi watashangaa yaliyompata; watu wa mashariki watapatwa na hofu.
JOB 18:21 Hakika ndivyo yalivyo makao ya mtu mwovu; ndivyo palivyo mahali pake mtu asiyemjua Mungu.”
JOB 19:1 Ndipo Ayubu akajibu:
JOB 19:2 “Je, mtaendelea kunitesa hadi lini, na kuniponda kwa maneno yenu?
JOB 19:3 Mara kumi hizi mmenishutumu; bila aibu mnanishambulia.
JOB 19:4 Kama ni kweli nimepotoka, kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe.
JOB 19:5 Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu, na kutumia unyonge wangu dhidi yangu,
JOB 19:6 basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya, naye amekokota wavu wake kunizunguka.
JOB 19:7 “Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu; ingawa ninaomba msaada, hakuna haki.
JOB 19:8 Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita; ameyafunika mapito yangu na giza.
JOB 19:9 Amenivua heshima yangu, na kuniondolea taji kichwani pangu.
JOB 19:10 Amenibomoa kila upande hadi nimeisha; ameling’oa tegemeo langu kama mti.
JOB 19:11 Hasira yake imewaka juu yangu; amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake.
JOB 19:12 Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu; yamenizingira, yamepiga kambi kulizunguka hema langu.
JOB 19:13 “Amewatenga ndugu zangu mbali nami; wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa.
JOB 19:14 Watu wa jamaa zangu wameenda mbali; rafiki zangu wamenisahau.
JOB 19:15 Wageni wangu na wajakazi wangu wananiona kama mgeni; wananitazama kama mgeni.
JOB 19:16 Namwita mtumishi wangu, wala haitiki, ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe.
JOB 19:17 Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu; nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe.
JOB 19:18 Hata watoto wadogo hunidhihaki; ninapojitokeza, hunifanyia mzaha.
JOB 19:19 Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa; wale ninaowapenda wamekuwa kinyume nami.
JOB 19:20 Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu; nimeponea nikiwa karibu kufa.
JOB 19:21 “Nihurumieni, rafiki zangu, kuweni na huruma, kwa kuwa mkono wa Mungu umenipiga.
JOB 19:22 Kwa nini mnanifuatia kama Mungu afanyavyo? Hamtosheki kamwe na mwili wangu?
JOB 19:23 “Laiti maneno yangu yangewekwa kwenye kumbukumbu, laiti kwamba yangeandikwa kwenye kitabu,
JOB 19:24 kwamba yangechorwa kwenye risasi kwa kifaa cha chuma, au kuyachonga juu ya mwamba milele!
JOB 19:25 Ninajua kwamba Mkombozi wangu yu hai, naye kwamba mwishoni atasimama juu ya nchi.
JOB 19:26 Nami baada ya ngozi yangu kuharibiwa, bado nikiwa na mwili huu nitamwona Mungu;
JOB 19:27 mimi nitamwona kwa macho yangu mwenyewe: mimi, wala si mwingine. Tazama jinsi moyo wangu unavyomtamani sana!
JOB 19:28 “Mkisema, ‘Tazama tutakavyomwinda, maadamu mzizi wa tatizo uko ndani yake,’
JOB 19:29 ninyi wenyewe uogopeni upanga, kwa kuwa ghadhabu italeta adhabu kwa upanga, nanyi ndipo mtajua kuwa kuna hukumu.”
JOB 20:1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:
JOB 20:2 “Mawazo yanayonisumbua yananisukuma kujibu, kwa sababu nimehangaika sana.
JOB 20:3 Ninasikia makaripio ambayo yananivunjia heshima, nao ufahamu wangu unanisukuma kujibu.
JOB 20:4 “Hakika unajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani, tangu zamani mwanadamu alipowekwa duniani,
JOB 20:5 macheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi, nayo furaha ya wasiomcha Mungu hudumu kwa kitambo tu.
JOB 20:6 Ingawa kujikweza kwake hufikia mbinguni na kichwa chake hugusa mawingu,
JOB 20:7 ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe. Wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’
JOB 20:8 Kama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena, amefukuziwa mbali kama maono ya usiku.
JOB 20:9 Jicho lililomwona halitamwona tena; mahali pake hapatamwona tena.
JOB 20:10 Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini, nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyang’anya watu.
JOB 20:11 Nguvu za ujana zilizoijaza mifupa yake, zitalala naye mavumbini.
JOB 20:12 “Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake naye huuficha chini ya ulimi wake,
JOB 20:13 ingawa hawezi kukubali kuuachia uende, lakini huuweka kinywani mwake.
JOB 20:14 Hata hivyo chakula chake kitakuwa kichungu tumboni mwake, nacho kitakuwa sumu kali ya nyoka ndani yake.
JOB 20:15 Atatema mali alizozimeza; Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika.
JOB 20:16 Atanyonya sumu za majoka; meno ya nyoka mwenye sumu kali yatamuua.
JOB 20:17 Hatafurahia vijito, mito inayotiririsha asali na siagi.
JOB 20:18 Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila; hatafurahia faida itokanayo na biashara yake.
JOB 20:19 Kwa kuwa aliwadhulumu maskini na kuwaacha bila kitu; amenyang’anya kwa nguvu nyumba asizozijenga.
JOB 20:20 “Hakika hatakuwa na amani katika kutamani kwake; hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake.
JOB 20:21 Hakuna chochote kitakachosalia kwa ajili yake ili ale; kufanikiwa kwake hakutadumu.
JOB 20:22 Katikati ya wingi wa ustawi wake, dhiki itampata; taabu itamjia kwa nguvu zote.
JOB 20:23 Atakapokuwa amelijaza tumbo lake, Mungu ataionesha ghadhabu kali dhidi yake, na kumnyeshea mapigo juu yake.
JOB 20:24 Ijapokuwa aikimbia silaha ya chuma, mshale wa shaba utamchoma.
JOB 20:25 Atauchomoa katika mgongo wake, ncha inayong’aa kutoka ini lake. Vitisho vitakuja juu yake;
JOB 20:26 giza nene linavizia hazina zake. Moto usiopepewa na mtu utamteketeza, na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake.
JOB 20:27 Mbingu zitaweka wazi hatia yake, nayo nchi itainuka kinyume chake.
JOB 20:28 Mafuriko yataichukua nyumba yake, maji yaendayo kasi katika siku ya ghadhabu ya Mungu.
JOB 20:29 Hili ndilo fungu Mungu alilowagawia waovu, urithi uliowekwa kwa ajili yao na Mungu.”
JOB 21:1 Ndipo Ayubu akajibu:
JOB 21:2 “Yasikilizeni maneno yangu kwa makini; hii na iwe faraja mnayonipa mimi.
JOB 21:3 Nivumilieni ninapozungumza, nami nikishazungumza, endeleeni kunidhihaki.
JOB 21:4 “Je, kwani malalamiko yangu yanaelekezwa kwa mwanadamu? Kwa nini nisikose subira?
JOB 21:5 Niangalieni mkastaajabu; mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu.
JOB 21:6 Ninapowaza kuhusu hili, ninaogopa, nao mwili wangu unatetemeka.
JOB 21:7 Kwa nini waovu wanaendelea kuishi, wakifikia umri wa uzee na kuendelea kuwa na nguvu?
JOB 21:8 Huwaona watoto wao wakithibitika wakiwa wamewazunguka, wazao wao mbele za macho yao.
JOB 21:9 Nyumba zao zi salama wala hakuna hofu; fimbo ya Mungu haiko juu yao.
JOB 21:10 Madume yao ya ng’ombe huvyaza bila kushindwa kamwe; ng’ombe wao huzaa wala hawaharibu mimba.
JOB 21:11 Huwatoa watoto wao nje kama kundi; wadogo wao huchezacheza.
JOB 21:12 Huimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi, nao huifurahia sauti ya filimbi.
JOB 21:13 Huitumia miaka yao katika mafanikio nao hushuka kaburini kwa amani.
JOB 21:14 Lakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’ Hatuna haja ya kufahamu njia zako.
JOB 21:15 Mwenyezi ni nani hata tumtumikie? Tutapata faida gani kumwomba?
JOB 21:16 Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe, hivyo najitenga mbali na ushauri wa waovu.
JOB 21:17 “Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa? Ni mara ngapi maafa huwajia, yale yawapatayo ambayo Mungu huwapangia katika hasira yake?
JOB 21:18 Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo, kama makapi yachukuliwayo na dhoruba?
JOB 21:19 Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu kwa ajili ya wanawe.’ Mungu na amlipe mtu mwenyewe, ili apate kulijua!
JOB 21:20 Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake; yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi.
JOB 21:21 Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma, miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho?
JOB 21:22 “Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa, iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?
JOB 21:23 Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili, akiwa salama na mwenye amani,
JOB 21:24 mwili wake ukiwa umenawiri, nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta.
JOB 21:25 Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi, akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri.
JOB 21:26 Hao wote hulala mavumbini, nao mabuu huwafunika wote.
JOB 21:27 “Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri, mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya.
JOB 21:28 Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu, mahema ambayo watu waovu walikaa?’
JOB 21:29 Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri? Je, hamkutafakari taarifa zao:
JOB 21:30 kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa, kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu?
JOB 21:31 Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake? Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda?
JOB 21:32 Hupelekwa kaburini, nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake.
JOB 21:33 Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake; watu wote watamfuata, nao umati wa watu wasiohesabika wamemtangulia.
JOB 21:34 “Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu? Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”
JOB 22:1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
JOB 22:2 “Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu? Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi?
JOB 22:3 Je, Mwenyezi angefurahia nini kama ungekuwa mwadilifu? Au je, yeye angepata faida gani kama njia zako zingekuwa kamilifu?
JOB 22:4 “Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea na kuleta mashtaka dhidi yako?
JOB 22:5 Je, uovu wako si mkuu? Dhambi zako si hazina mwisho?
JOB 22:6 Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu; umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.
JOB 22:7 Hukumpa maji aliyechoka, nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,
JOB 22:8 ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi: mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake.
JOB 22:9 Umewafukuza wajane mikono mitupu na kuzivunja nguvu za yatima.
JOB 22:10 Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote, hatari ya ghafula inakutia hofu,
JOB 22:11 ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona, tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.
JOB 22:12 “Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu? Juu kuliko nyota zilizo juu sana!
JOB 22:13 Hivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’ Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo?
JOB 22:14 Mawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi atembeapo juu ya anga la dunia.
JOB 22:15 Je, utaifuata njia ya zamani, ambayo watu waovu waliikanyaga?
JOB 22:16 Waliondolewa kabla ya wakati wao, misingi yao ikachukuliwa na mafuriko.
JOB 22:17 Walimwambia Mungu, ‘Tuache sisi! Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’
JOB 22:18 Lakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri, hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu.
JOB 22:19 “Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi, nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema,
JOB 22:20 ‘Hakika adui zetu wameangamizwa, nao moto umeteketeza mali yao.’
JOB 22:21 “Mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndipo mema yatakapokujia.
JOB 22:22 Uyapokee mafundisho toka kinywani mwake, na maneno yake uyaweke moyoni mwako.
JOB 22:23 Ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya: Ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,
JOB 22:24 kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi, dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,
JOB 22:25 ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako, naye atakuwa fedha yako iliyo bora.
JOB 22:26 Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi, nawe utamwinulia Mungu uso wako.
JOB 22:27 Utamwomba yeye, naye atakusikia, nawe utazitimiza nadhiri zako.
JOB 22:28 Utakusudia jambo nalo litatendeka, nao mwanga utaangazia njia zako.
JOB 22:29 Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’ ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.
JOB 22:30 Atamwokoa hata yule ambaye ana hatia, ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”
JOB 23:1 Ndipo Ayubu akajibu:
JOB 23:2 “Hata leo malalamiko yangu ni ya uchungu; mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua.
JOB 23:3 Laiti ningefahamu mahali pa kumwona; laiti ningeweza kwenda mahali akaapo!
JOB 23:4 Ningeleta kesi yangu mbele zake, na kukijaza kinywa changu na hoja.
JOB 23:5 Ningejua kwamba angenijibu nini, na kuelewa lile angeniambia.
JOB 23:6 Je, angenipinga kwa nguvu nyingi? La, hangenigandamiza.
JOB 23:7 Hapo mtu mwadilifu angeleta kesi yake mbele zake, nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu.
JOB 23:8 “Lakini nikienda mashariki, hayupo; nikienda magharibi, simpati.
JOB 23:9 Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni; akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.
JOB 23:10 Lakini anaijua njia niiendeayo; akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
JOB 23:11 Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu; nimeishika njia yake bila kukengeuka.
JOB 23:12 Sijaziacha amri zilizotoka mdomoni mwake; nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko chakula changu cha kila siku.
JOB 23:13 “Lakini yeye husimama peke yake; ni nani awezaye kumpinga? Yeye hufanya lolote atakalo.
JOB 23:14 Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu, na bado anayo mipango mingi kama hiyo ambayo ameiweka akiba.
JOB 23:15 Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake; nifikiriapo haya yote ninamwogopa.
JOB 23:16 Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia; yeye Mwenyezi amenitia hofu.
JOB 23:17 Hata hivyo sijanyamazishwa na giza, wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.
JOB 24:1 “Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu? Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio?
JOB 24:2 Watu husogeza mawe ya mpaka; huchunga makundi ya wanyama waliyonyang’anya kwa nguvu.
JOB 24:3 Huwanyang’anya yatima punda wao, na kumchukua rehani fahali wa mjane.
JOB 24:4 Humsukuma mhitaji kutoka njia, na kuwafanya maskini wote wa nchi kulazimika kujificha.
JOB 24:5 Kama punda-mwitu jangwani, maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula; mahali palipo jangwa huwapa chakula cha watoto wao.
JOB 24:6 Hukusanya chakula mashambani na kuokota masazo katika mashamba ya mizabibu ya waovu.
JOB 24:7 Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa uchi; hawana chochote cha kujifunika baridi.
JOB 24:8 Hutota kwa mvua za mlimani, nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri.
JOB 24:9 Mtoto yatima hupokonywa matitini; mtoto mchanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni.
JOB 24:10 Kwa kukosa nguo, hutembea uchi; hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa.
JOB 24:11 Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia; hukanyaga mashinikizo, lakini wanaona kiu.
JOB 24:12 Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini, nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada. Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote kwa kutenda mabaya.
JOB 24:13 “Wako wale wanaoiasi nuru, wasiofahamu njia zake wala hawakai katika mapito yake.
JOB 24:14 Mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka, naye huwaua maskini na mhitaji; wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi.
JOB 24:15 Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza, naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’ naye huuficha uso wake.
JOB 24:16 Katika giza, huvunja nyumba, lakini wakati wa mchana hujifungia ndani; hawataki kufanya lolote nuruni.
JOB 24:17 Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao; hujifanya rafiki na vitisho vya gizani.
JOB 24:18 “Lakini wao ni povu juu ya maji; sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa, hivyo hakuna hata mmoja aendaye kwenye shamba la mizabibu.
JOB 24:19 Kama vile joto na hari vinyakuavyo theluji iliyoyeyuka, ndivyo Kuzimu kuwanyakuavyo waliotenda dhambi.
JOB 24:20 Tumbo lililowazaa huwasahau, nao huwa karamu ya mabuu; watu waovu hawakumbukwi tena, lakini huvunjika kama mti.
JOB 24:21 Huwafanya mawindo wanawake tasa na wasio na watoto, nao hawaoneshi huruma kwa wajane.
JOB 24:22 Lakini Mungu huwakokota wenye nguvu kwa uwezo wake; ingawa wamestawi, hawana hakika ya maisha.
JOB 24:23 Aweza akawaacha wakapumzika wakijihisi salama, lakini macho yake yanaona njia zao.
JOB 24:24 Kwa kitambo kidogo hutukuka, hatimaye hutoweka; hushushwa na kukusanywa kama wengine wote; hukatwa kama masuke ya nafaka.
JOB 24:25 “Kama hili sivyo, ni nani awezaye kunithibitisha kuwa mwongo, na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?”
JOB 25:1 Ndipo Bildadi Mshuhi akajibu:
JOB 25:2 “Mamlaka na kuheshimiwa ni vyake Mungu; yeye huthibitisha amani katika mbingu juu.
JOB 25:3 Je, majeshi yake yaweza kuhesabika? Ni nani asiyeangaziwa na nuru yake?
JOB 25:4 Mtu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu? Awezaje mtu aliyezaliwa na mwanamke kuwa safi?
JOB 25:5 Ikiwa hata mwezi sio mwangavu nazo nyota si safi machoni pake,
JOB 25:6 sembuse mtu ambaye ni funza: mwanadamu ambaye ni buu tu!”
JOB 26:1 Kisha Ayubu akajibu:
JOB 26:2 “Tazama jinsi ulivyomsaidia mtu asiye na uwezo! Jinsi ulivyouokoa mkono ulio dhaifu!
JOB 26:3 Ni shauri gani ulilompa yeye asiye na hekima? Nayo ni busara gani kubwa uliyoonesha!
JOB 26:4 Ni nani aliyekusaidia kutamka maneno hayo? Nayo ni roho ya nani iliyosema kutoka kinywani mwako?
JOB 26:5 “Wafu wako katika maumivu makuu, wale walio chini ya maji, na wale wanaoishi ndani yake.
JOB 26:6 Mauti iko wazi mbele za Mungu; Uharibifu haukufunikwa.
JOB 26:7 Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu; naye huining’iniza dunia mahali pasipo na kitu.
JOB 26:8 Huyafungia maji kwenye mawingu yake, hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.
JOB 26:9 Huufunika uso wa mwezi mpevu, akitandaza mawingu juu yake.
JOB 26:10 Amechora mstari wa upeo juu ya maji, ameweka mpaka wa nuru na giza.
JOB 26:11 Nguzo za mbingu nazo zatetemeka, zinatishika anapozikemea.
JOB 26:12 Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari; kwa hekima yake alimkata Rahabu vipande vipande.
JOB 26:13 Aliisafisha anga kwa pumzi yake; kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio.
JOB 26:14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake; tazama jinsi ulivyo mdogo mnong’ono tunaousikia kumhusu! Ni nani basi awezaye kuelewa ngurumo za nguvu zake?”
JOB 27:1 Ndipo Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:
JOB 27:2 “Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu, Mwenyezi ambaye amenifanya nionje uchungu wa nafsi,
JOB 27:3 kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu, nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu,
JOB 27:4 midomo yangu haitanena uovu, wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.
JOB 27:5 Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi; hadi nife, sitakana uadilifu wangu.
JOB 27:6 Nitadumisha haki yangu wala sitaiacha; dhamiri yangu haitanisuta muda wote ninaoishi.
JOB 27:7 “Watesi wangu wawe kama waovu, nao adui zangu wawe kama wasio haki!
JOB 27:8 Kwa maana mtu asiyemcha Mungu analo tegemeo gani anapokatiliwa mbali, Mungu anapouondoa uhai wake?
JOB 27:9 Je, Mungu husikiliza kilio chake, shida zimjiapo?
JOB 27:10 Je, anaweza kumfurahia Mwenyezi? Je, atamwita Mungu nyakati zote?
JOB 27:11 “Nitawafundisha kuhusu uweza wa Mungu; njia za Mwenyezi sitazificha.
JOB 27:12 Ninyi nyote mmeona hili wenyewe. Ni ya nini basi mazungumzo haya yasiyo na maana?
JOB 27:13 “Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu, urithi ule mtu mdhalimu anapokea kutoka kwa Mwenyezi:
JOB 27:14 Hata watoto wake wawe wengi kiasi gani, fungu lao ni kuuawa kwa upanga; wazao wake hawatakuwa kamwe na chakula cha kuwatosha.
JOB 27:15 Tauni itawazika wale watakaonusurika miongoni mwao, nao wajane wao hawatawaombolezea.
JOB 27:16 Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi, na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi,
JOB 27:17 yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba, mwenye haki atayavaa, naye asiye na hatia ataigawanya fedha yake.
JOB 27:18 Nyumba aijengayo ni kama utando wa buibui, kama kibanda alichotengeneza mlinzi.
JOB 27:19 Yeye hulala akiwa tajiri, lakini ndiyo mara ya mwisho; afunguapo macho yake, yote yametoweka.
JOB 27:20 Vitisho humjia kama mafuriko; dhoruba humkumba ghafula usiku.
JOB 27:21 Upepo mkali wa mashariki humchukua, naye hutoweka; humzoa kutoka mahali pake.
JOB 27:22 Humvurumisha bila huruma, huku akikimbia kasi kukwepa nguvu zake.
JOB 27:23 Upepo humpigia makofi kwa dharau, na kumfukuza atoke mahali pake.”
JOB 28:1 Kuna machimbo ya fedha, na mahali dhahabu inaposafishwa.
JOB 28:2 Chuma hupatikana ardhini, nayo shaba huyeyushwa kutoka mawe ya madini.
JOB 28:3 Mwanadamu hukomesha giza; huyatafuta hadi sehemu iliyo mbali, kwa ajili ya kuchimbua mawe yenye madini katika giza jeusi sana.
JOB 28:4 Huchimba shimo jembamba mbali na makao ya watu, mahali paliposahaulika na nyayo za wanadamu; mbali na wanadamu huning’inia na kubembea.
JOB 28:5 Ardhi, ambako chakula hutoka, chini hugeuzwa kwa moto;
JOB 28:6 yakuti samawi hutoka katika miamba yake, nalo vumbi lake lina vipande vya dhahabu.
JOB 28:7 Hakuna ndege awindaye aijuaye njia ile iliyofichika, wala hakuna jicho la mwewe lililoiona.
JOB 28:8 Wanyama wa porini wanaotamba hawajawahi kupakanyaga, wala simba azungukaye huko.
JOB 28:9 Mikono ya mwanadamu hushambulia miamba ya gumegume, na kuiacha wazi mizizi ya milima.
JOB 28:10 Hutoboa shimo refu la kupenya chini kwa chini kwenye miamba; macho yake huona hazina zake zote.
JOB 28:11 Hutafuta vyanzo vya mito na kuvileta vitu vilivyofichika katika nuru.
JOB 28:12 Lakini hekima inaweza kupatikana wapi? Ufahamu unakaa wapi?
JOB 28:13 Mwanadamu hatambui thamani yake; haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai.
JOB 28:14 Kilindi husema, “Haiko ndani yangu”; bahari nayo husema, “Haiko pamoja nami.”
JOB 28:15 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote, wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha.
JOB 28:16 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri, kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa.
JOB 28:17 Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi hubadilishwa kwa vito vya dhahabu.
JOB 28:18 Marijani na yaspi hazistahili kutajwa; thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu.
JOB 28:19 Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi.
JOB 28:20 Ni wapi basi hekima itokako? Ufahamu hukaa wapi?
JOB 28:21 Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai, imesitiriwa hata kwa ndege wa angani.
JOB 28:22 Uharibifu na Mauti husema, “Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.”
JOB 28:23 Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa,
JOB 28:24 kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia na huona kila kitu chini ya mbingu.
JOB 28:25 Alipoufanyia upepo nguvu zake na kuyapima maji,
JOB 28:26 alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua na njia ya mwali wa radi,
JOB 28:27 ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake, akaithibitisha na kuihakikisha.
JOB 28:28 Naye Mungu akamwambia mwanadamu, “Kumcha Bwana: hiyo ndiyo hekima, nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.”
JOB 29:1 Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:
JOB 29:2 “Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita, zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,
JOB 29:3 wakati taa yake ilinimulika kichwani, na kwa mwanga wa Mungu nikapita katikati ya giza!
JOB 29:4 Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu, urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu,
JOB 29:5 wakati Mwenyezi bado alikuwa pamoja nami, nao watoto wangu wakawa wamenizunguka,
JOB 29:6 wakati njia yangu ilikuwa imenyeshewa siagi, nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.
JOB 29:7 “Wakati nilienda kwenye lango la mji na kuketi katika kiwanja,
JOB 29:8 vijana waliniona, wakakaa kando, nao wazee walioketi, wakasimama;
JOB 29:9 wakuu wakaacha kuzungumza, na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao;
JOB 29:10 wenye vyeo wakanyamazishwa, nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.
JOB 29:11 Yeyote aliyenisikia alinena mema juu yangu, nao walioniona walinisifu,
JOB 29:12 kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada, naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.
JOB 29:13 Mtu aliyekuwa karibu kufa alinibariki, nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.
JOB 29:14 Niliivaa haki kama vazi langu; uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.
JOB 29:15 Nilikuwa macho ya kipofu na miguu kwa kiwete.
JOB 29:16 Nilikuwa baba kwa mhitaji; nilimtetea mgeni.
JOB 29:17 Niliyavunja meno makali ya waovu, na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.
JOB 29:18 “Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe, nazo siku zangu zitakuwa nyingi kama chembechembe za mchanga.
JOB 29:19 Mizizi yangu itafika hata kwenye maji, nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.
JOB 29:20 Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu, upinde wangu daima utaendelea kuwa mpya mkononi mwangu.’
JOB 29:21 “Watu walinisikiliza kwa tumaini, wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.
JOB 29:22 Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi; maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.
JOB 29:23 Waliningojea kama manyunyu ya mvua na kuyapokea maneno yangu kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.
JOB 29:24 Walipokata tamaa niliwaonesha uso wa furaha; nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.
JOB 29:25 Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao; niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake; nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.
JOB 30:1 “Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuliko mimi wananidhihaki, watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.
JOB 30:2 Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu, kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
JOB 30:3 Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa, walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.
JOB 30:4 Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi, nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.
JOB 30:5 Walifukuzwa mbali na watu wao, wakipigiwa kelele kama wezi.
JOB 30:6 Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka, kwenye majabali na mahandaki.
JOB 30:7 Kwenye vichaka walilia kama punda, na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.
JOB 30:8 Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya, waliofukuzwa watoke katika nchi.
JOB 30:9 “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo; nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
JOB 30:10 Wananichukia sana na kujitenga nami, wala hawasiti kunitemea mate usoni.
JOB 30:11 Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa, wamekuwa huru kunitendea wanavyopenda.
JOB 30:12 Kuume kwangu kundi linashambulia; wao huitegea miguu yangu tanzi, na kunizingira.
JOB 30:13 Huizuia njia yangu, nao hufanikiwa katika kuniletea maafa, nami sina yeyote wa kunisaidia.
JOB 30:14 Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana; katikati ya magofu huja na kunishambulia.
JOB 30:15 Vitisho vimenifunika; heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo, salama yangu imetoweka kama wingu.
JOB 30:16 “Sasa maisha yangu yamefikia mwisho; siku za mateso zimenikamata.
JOB 30:17 Usiku mifupa yangu inachoma; maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.
JOB 30:18 Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo; hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.
JOB 30:19 Yeye amenitupa kwenye matope, nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.
JOB 30:20 “Ee Mwenyezi Mungu, ninakulilia wewe lakini hunijibu; ninasimama, nawe unanitazama tu.
JOB 30:21 Wewe unanigeukia bila huruma; unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.
JOB 30:22 Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo; umenirusharusha kwenye dhoruba.
JOB 30:23 Ninajua utanileta hadi kifoni, mahali wenye uhai wote wamewekewa.
JOB 30:24 “Hakika hakuna mtu anayemshambulia mhitaji anapoomba msaada katika shida yake.
JOB 30:25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu? Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
JOB 30:26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia; nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.
JOB 30:27 Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii; siku za mateso zinanikabili.
JOB 30:28 Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua; ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.
JOB 30:29 Nimekuwa ndugu wa mbweha, rafiki wa mabundi.
JOB 30:30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika; mifupa yangu inaungua kwa homa.
JOB 30:31 Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo, nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.
JOB 31:1 “Nimefanya agano na macho yangu yasimtazame msichana kwa kumtamani.
JOB 31:2 Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni lipi kutoka kwa Mungu juu, urithi wake kutoka juu kwa Mwenyezi?
JOB 31:3 Je, si uharibifu kwa watu waovu, maangamizi kwa wale watendao mabaya?
JOB 31:4 Je, yeye hazioni njia zangu na kuihesabu kila hatua yangu?
JOB 31:5 “Kama nimeishi katika uongo au mguu wangu umekimbilia udanganyifu,
JOB 31:6 Mungu na anipime katika mizani za uaminifu, naye atajua kwamba sina hatia:
JOB 31:7 kama hatua zangu zimepotoka kutoka njia, kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu, au kama mikono yangu imetiwa unajisi,
JOB 31:8 basi wengine na wale nilichokipanda, nayo yale yote niliyootesha na yang’olewe.
JOB 31:9 “Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke, au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu,
JOB 31:10 basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine, nao wanaume wengine walale naye.
JOB 31:11 Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu, naam, dhambi ya kuhukumiwa.
JOB 31:12 Ni moto uwakao kwa Uharibifu; ungekuwa umeng’oa mavuno yangu.
JOB 31:13 “Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu, walipokuwa na manung’uniko dhidi yangu,
JOB 31:14 nitafanya nini Mungu atakaponikabili? Nitamjibu nini nitakapoitwa kujitetea?
JOB 31:15 Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu, siye aliyewaumba? Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote ndani ya mama zetu?
JOB 31:16 “Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike,
JOB 31:17 kama nimekula chakula changu mwenyewe, bila kuwashirikisha yatima;
JOB 31:18 lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya, nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane:
JOB 31:19 kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo, au mtu mhitaji asiye na mavazi,
JOB 31:20 ambaye wala moyo wake haukunibariki kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo wangu,
JOB 31:21 na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima, nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani,
JOB 31:22 basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu, nao na uvunjike kutoka kiungio chake.
JOB 31:23 Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu, nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.
JOB 31:24 “Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu, au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’
JOB 31:25 kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu, ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,
JOB 31:26 kama nimelitazama jua katika kung’aa kwake au mwezi ukienda kwa fahari yake,
JOB 31:27 hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri, au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,
JOB 31:28 basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa, kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.
JOB 31:29 “Kama nimeshangilia msiba wa adui yangu, au kutazama kwa furaha taabu iliyomjia,
JOB 31:30 lakini sikuruhusu kinywa changu kufanya dhambi kwa kuomba laana dhidi ya maisha yake;
JOB 31:31 kama watu wa nyumbani mwangu kamwe hawakusema, ‘Ni nani ambaye hajashibishwa na nyama ya Ayubu?’
JOB 31:32 Lakini hakuna mgeni aliyelala njiani, kwa maana mlango wangu ulikuwa wazi kwa msafiri;
JOB 31:33 kama nimeifunika dhambi yangu kama wanadamu wengine wafanyavyo, kwa kuficha hatia yangu moyoni mwangu,
JOB 31:34 kwa sababu ya kuogopa umati wa watu, na hivyo kuwa na hofu ya kudharauliwa na jamaa, nikakaa kimya, nisitoke nje ya mlango.
JOB 31:35 (“Laiti angekuwepo mtu wa kunisikia! Tazama sasa ninatia sahihi kwenye utetezi wangu: Mwenyezi na anijibu; mshtaki wangu na aweke mashtaka yake kwenye maandishi.
JOB 31:36 Hakika ningeyavaa begani mwangu, ningeyavaa kama taji.
JOB 31:37 Ningempa hesabu ya kila hatua yangu, ningemwendea kama mwana wa mfalme.)
JOB 31:38 “Kama nchi yangu inalia dhidi yangu, na mifereji yake yote imelowana kwa machozi,
JOB 31:39 kama nimekula mazao yake bila malipo, au kuvunja mioyo ya wapangaji wake,
JOB 31:40 basi miiba na iote badala ya ngano, na magugu badala ya shayiri.” Mwisho wa maneno ya Ayubu.
JOB 32:1 Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe.
JOB 32:2 Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu.
JOB 32:3 Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu.
JOB 32:4 Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu, kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kuliko yeye.
JOB 32:5 Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka.
JOB 32:6 Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema: “Mimi ni mdogo kwa umri, nanyi ni wazee; ndiyo sababu niliogopa, sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua.
JOB 32:7 Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme, nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’
JOB 32:8 Lakini ni Roho iliyo ndani ya mwanadamu, pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo ufahamu.
JOB 32:9 Sio wazee peke yao walio na hekima, sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa.
JOB 32:10 “Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni; mimi nami nitawaambia ninalolijua.
JOB 32:11 Nilingojea mlipokuwa mnaongea, nilizisikiliza hoja zenu; mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema,
JOB 32:12 niliwasikiliza kwa makini. Lakini hakuna hata mmoja wenu aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa; hakuna hata mmoja wenu aliyeweza kujibu hoja zake.
JOB 32:13 Msiseme, ‘Tumepata hekima; Mungu na amthibitishe kuwa mwongo, wala si mwanadamu.’
JOB 32:14 Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu, nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.
JOB 32:15 “Wametiwa hofu na hawana la zaidi la kusema; maneno yamewaishia.
JOB 32:16 Je, ningoje sasa kwa sababu wamekuwa kimya, kwa vile sasa wanasimama bila kuwa na la kujibu?
JOB 32:17 Mimi nami nitakuwa na la kusema; mimi nami nitasema lile nilijualo.
JOB 32:18 Kwa kuwa nimejawa na maneno, nayo Roho iliyo ndani yangu inanisukuma;
JOB 32:19 ndani yangu niko kama chupa iliyojazwa divai, kama kiriba kipya cha divai kilicho karibu kupasuka.
JOB 32:20 Ni lazima niseme ili niweze kutulia; ni lazima nifumbue midomo yangu nipate kujibu.
JOB 32:21 Sitampendelea mtu yeyote, wala sitajipendekeza kwa mtu yeyote;
JOB 32:22 kwa kuwa kama ningekuwa stadi wa kujipendekeza, Muumba wangu angeniondolea mbali kwa upesi.
JOB 33:1 “Lakini Ayubu, sasa sikiliza maneno yangu; zingatia kila kitu nitakachosema.
JOB 33:2 Karibu nitafungua kinywa changu; maneno yangu yapo katika ncha ya ulimi wangu.
JOB 33:3 Maneno yangu yanatoka katika moyo mnyofu; midomo yangu hunena kwa uaminifu yale niyajuayo.
JOB 33:4 Roho wa Mungu ameniumba; pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.
JOB 33:5 Unijibu basi, kama unaweza; jiandae kunikabili mimi.
JOB 33:6 Mimi ni kama wewe mbele za Mungu; mimi pia nimetolewa kwenye udongo.
JOB 33:7 Huna sababu ya kuniogopa, wala mkono wangu haupaswi kukulemea.
JOB 33:8 “Lakini umesema nikiwa ninakusikia, nami nilisikia maneno yenyewe:
JOB 33:9 ‘Mimi ni safi na sina dhambi; mimi ni safi na sina hatia.
JOB 33:10 Lakini bado Mungu amepata dosari kwangu, naye ananiona kama adui yake.
JOB 33:11 Ananifunga miguu kwa pingu, tena anaziangalia njia zangu zote kwa karibu.’
JOB 33:12 “Lakini mimi ninakuambia, katika jambo hili wewe una makosa, kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.
JOB 33:13 Kwa nini unamlalamikia kwamba yeye hamjibu mwanadamu?
JOB 33:14 Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja, au wakati mwingine kwa njia nyingine, ingawa mwanadamu anaweza asielewe.
JOB 33:15 Mungu husema na mwanadamu katika ndoto, katika maono ya usiku, wakati usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu wasinziapo vitandani mwao,
JOB 33:16 anaweza akasemea masikioni mwao, na kuwatia hofu kwa maonyo,
JOB 33:17 ili kumgeuza mtu kutoka kutenda mabaya na kumwepusha na kiburi,
JOB 33:18 kuiokoa nafsi yake na shimo, uhai wake usiangamizwe kwa upanga.
JOB 33:19 Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake,
JOB 33:20 kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri.
JOB 33:21 Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda, nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika, sasa inatokeza nje.
JOB 33:22 Nafsi yake inakaribia kaburi, nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.
JOB 33:23 “Kama bado kuna malaika upande wake kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu, wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake,
JOB 33:24 kumwonea huruma na kusema, ‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni; nimepata ukombozi kwa ajili yake’:
JOB 33:25 ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto; hurudishwa upya kama siku za ujana wake.
JOB 33:26 Humwomba Mungu, akapata kibali kwake, huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha; Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu.
JOB 33:27 Ndipo huja mbele za watu na kusema, ‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki, lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili.
JOB 33:28 Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni, nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’
JOB 33:29 “Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu; mara mbili hata mara tatu,
JOB 33:30 ili aigeuze nafsi yake toka shimoni, ili nuru ya uzima imwangazie.
JOB 33:31 “Ayubu, zingatia, nisikilize mimi; nyamaza, nami nitanena.
JOB 33:32 Kama unalo lolote la kusema, unijibu; sema, kwa maana ninataka uonekane huna hatia.
JOB 33:33 Lakini kama huna la kusema, basi nisikilize mimi; nyamaza, nami nitakufundisha hekima.”
JOB 34:1 Kisha Elihu akasema:
JOB 34:2 “Sikieni maneno yangu, enyi watu wenye hekima; nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye maarifa.
JOB 34:3 Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno kama vile ulimi uonjavyo chakula.
JOB 34:4 Tujichagulie wenyewe yaliyo sawa, nasi tujifunze pamoja yaliyo mema.
JOB 34:5 “Ayubu anasema, ‘Mimi sina hatia, lakini Mungu ameninyima haki yangu.
JOB 34:6 Ingawa niko sawa, ninaonekana mwongo; nami ingawa sina kosa, kidonda changu hakiponi.’
JOB 34:7 Ni mtu gani aliye kama Ayubu, anywaye dharau kama maji?
JOB 34:8 Hushirikiana na watenda maovu, na kuchangamana na watu waovu.
JOB 34:9 Kwa kuwa anasema, ‘Haimfaidi mwanadamu kitu chochote anapojitahidi kumpendeza Mungu.’
JOB 34:10 “Hivyo nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye ufahamu. Kamwe Mungu hatendi uovu, Mwenyezi hafanyi kosa.
JOB 34:11 Humlipa mwanadamu kwa ajili ya lile alilotenda; huleta juu yake kile ambacho matendo yake yanastahili.
JOB 34:12 Ni jambo lisilofikirika kwamba Mungu angefanya makosa, kwamba Mwenyezi angepotosha hukumu.
JOB 34:13 Je, ni nani aliyemtawaza juu ya dunia? Ni nani aliyemweka kuwa mwangalizi wa ulimwengu wote?
JOB 34:14 Kama lilikuwa kusudi la Mungu, naye akaiondoa Roho yake na pumzi yake,
JOB 34:15 wanadamu wote wangeangamia kwa pamoja, na mtu angerudi mavumbini.
JOB 34:16 “Kama ninyi mnaufahamu, sikieni hili; sikilizeni hili nisemalo.
JOB 34:17 Je, yeye aichukiaye haki aweza kutawala? Je, utamhukumu mwenye haki, yeye Aliye na Nguvu Zote?
JOB 34:18 Je, si ni yeye awaambiaye wafalme, ‘Ninyi hamfai kitu,’ nao watu mashuhuri, ‘Ninyi ni waovu,’
JOB 34:19 yeye asiyependelea wakuu, wala haoneshi upendeleo kwa matajiri kuliko maskini, kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake?
JOB 34:20 Wanakufa ghafula, usiku wa manane; watu wanatikiswa nao hupita; wenye nguvu huondolewa bila mkono wa mwanadamu.
JOB 34:21 “Macho yake yanazitazama njia za wanadamu; anaona kila hatua yao.
JOB 34:22 Hakuna mahali penye giza nene, wala uvuli mkubwa, ambapo watenda maovu wanaweza kujificha.
JOB 34:23 Mungu hana haja ya kumchunguza mtu sana, ili apate kuja mbele zake kwa hukumu.
JOB 34:24 Bila kuuliza huwapondaponda wenye nguvu nyingi na kuwaweka wengine mahali pao.
JOB 34:25 Kwa sababu huyaangalia matendo yao yote, huwaondoa usiku, nao wakaangamia.
JOB 34:26 Anawaadhibu kwa ajili ya uovu wao mahali ambapo kila mmoja ataweza kuwaona,
JOB 34:27 kwa sababu wameacha kumfuata Mungu, nao hawakuiheshimu njia yake hata moja.
JOB 34:28 Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake, hivyo akasikia kilio cha wahitaji.
JOB 34:29 Lakini akikaa kimya, ni nani awezaye kumhukumu? Akiuficha uso wake, ni nani awezaye kumwona? Ikiwa ni taifa au mtu mmoja, kwake ni sawa,
JOB 34:30 ili kumzuia mtu mwovu kutawala, au wale ambao huwategea watu mitego.
JOB 34:31 “Kama mwanadamu akimwambia Mungu, ‘Nimekosa lakini sitatenda dhambi tena.
JOB 34:32 Nifundishe nisichoweza kuona; kama nimekukosea, sitafanya hivyo tena.’
JOB 34:33 Je basi, Mungu atakulipa kwa masharti yako, wakati wewe umekataa kutubu? Yakupasa wewe uamue, wala si mimi; sasa niambie lile ulijualo.
JOB 34:34 “Watu wenye ufahamu husema, wenye hekima wanaonisikia huniambia,
JOB 34:35 ‘Ayubu huongea bila maarifa; maneno yake hayana busara.’
JOB 34:36 Laiti Ayubu angejaribiwa hadi mwisho, kwa sababu anajibu kama mtu mwovu!
JOB 34:37 Kwenye dhambi yake huongeza uasi; kwa dharau hupiga makofi miongoni mwetu, na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.”
JOB 35:1 Ndipo Elihu akasema:
JOB 35:2 “Je, unadhani hili ni haki? Wewe unasema, ‘Nina haki mbele za Mungu.’
JOB 35:3 Bado unamuuliza, ‘Ni faida gani nimepata, na imenifaidi nini kwa kutokutenda dhambi?’
JOB 35:4 “Ningependa nikujibu wewe na rafiki zako walio nawe.
JOB 35:5 Tazama juu mbinguni ukaone; yaangalie mawingu yaliyo juu sana juu yako.
JOB 35:6 Je, ukitenda dhambi, inamdhuruje Mungu? Kama dhambi zako zikiwa nyingi, hilo linamfanyia nini Mungu?
JOB 35:7 Kama wewe ni mwadilifu, unampa nini, au yeye anapokea nini mkononi kwako?
JOB 35:8 Uovu wako unamdhuru tu mtu mwingine kama wewe, nayo haki yako inawafaa wanadamu tu.
JOB 35:9 “Wanadamu hulia kwa kulemewa na mateso; huomba msaada kutoka mkono wenye nguvu.
JOB 35:10 Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu Muumba wangu, yeye anifanyaye niimbe usiku,
JOB 35:11 yeye atufundishaye sisi zaidi ya wanyama wa nchi, na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani?’
JOB 35:12 Yeye hajibu wakati watu waliapo kwa sababu ya kiburi cha watu waovu.
JOB 35:13 Naam, Mungu hasikilizi maombi yao ya ubatili; Mwenyezi hayazingatii.
JOB 35:14 Si zaidi sana kwamba hatakusikiliza wewe usemapo humwoni, tena kwamba kesi yako iko mbele zake na wewe lazima umngojee,
JOB 35:15 pia zaidi, kwamba hasira yake kamwe haiadhibu wala haangalii uovu hata kidogo?
JOB 35:16 Hivyo Ayubu hufumbua kinywa chake kwa maneno yasiyo na maana; anaongea maneno mengi bila maarifa.”
JOB 36:1 Elihu akaendelea kusema:
JOB 36:2 “Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonesha kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.
JOB 36:3 Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali, nami nitamhesabia haki Muumba wangu.
JOB 36:4 Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo; mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.
JOB 36:5 “Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu; ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika kusudi lake.
JOB 36:6 Hawaachi waovu waendelee kuishi, bali huwapa walioteswa haki yao.
JOB 36:7 Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki; huwaketisha penye viti vya utawala pamoja na wafalme, na kuwatukuza milele.
JOB 36:8 Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo, wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,
JOB 36:9 huwaonesha yale waliyoyatenda, kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.
JOB 36:10 Huwafanya wao kusikia maonyo, na huwaagiza kutubu uovu wao.
JOB 36:11 Wakitii na kumtumikia, wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio, na miaka yao katika utoshelevu.
JOB 36:12 Lakini wasiposikiliza, wataangamia kwa upanga, nao watakufa pasipo maarifa.
JOB 36:13 “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki; hata anapowafunga, hawamwombi msaada.
JOB 36:14 Wanakufa wangali vijana, miongoni mwa mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu.
JOB 36:15 Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao, na kuzungumza nao katika dhiki zao.
JOB 36:16 “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki, ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi, hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.
JOB 36:17 Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu; hukumu na haki vimekukamata.
JOB 36:18 Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri; usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.
JOB 36:19 Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?
JOB 36:20 Usiutamani usiku uje, ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.
JOB 36:21 Jihadhari usigeukie uovu, ambao unaupenda zaidi ya mateso.
JOB 36:22 “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake. Ni nani aliye mwalimu kama yeye?
JOB 36:23 Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake, au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?
JOB 36:24 Kumbuka kuzitukuza kazi zake, ambazo watu wamezisifu katika wimbo.
JOB 36:25 Wanadamu wote wameiona; watu wanaikazia macho kwa mbali.
JOB 36:26 Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu, kupita ufahamu wetu! Hesabu ya miaka yake haitafutiki.
JOB 36:27 “Yeye huvuta juu matone ya maji, ayachujayo kama mvua kutoka vijito;
JOB 36:28 mawingu huangusha chini maji yake, nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.
JOB 36:29 Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu, jinsi angurumavyo kutoka kwenye hema lake.
JOB 36:30 Tazama anavyotandaza radi yake kumzunguka, naye huvifunika vilindi vya bahari.
JOB 36:31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa, na kuwapa chakula kwa wingi.
JOB 36:32 Huujaza mkono wake kwa radi, na kuiagiza kulenga shabaha yake.
JOB 36:33 Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja; hata mifugo hujulisha kukaribia kwake.
JOB 37:1 “Kwa hili moyo wangu unatetemeka, nao unaruka kutoka mahali pake.
JOB 37:2 Sikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake, sauti ya ngurumo inayotoka kinywani mwake.
JOB 37:3 Huuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote na kuupeleka hata miisho ya dunia.
JOB 37:4 Baada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake; Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari. Wakati sauti yake inanguruma tena, huuachilia umeme wake wa radi.
JOB 37:5 Sauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu; yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.
JOB 37:6 Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’ nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’
JOB 37:7 Ili wanadamu wote aliowaumba wapate kujua kazi zake, yeye humzuilia kila mtu shughuli zake.
JOB 37:8 Wanyama hujificha; hubakia kwenye mapango yao.
JOB 37:9 Dhoruba hutoka katika chumba chake, baridi hutoka katika upepo uendao kasi.
JOB 37:10 Pumzi ya Mungu hutoa barafu, eneo kubwa la maji huganda.
JOB 37:11 Huyasheheneza mawingu kwa maji, naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.
JOB 37:12 Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake, juu ya uso wa dunia yote, kufanya lolote ayaamuruyo.
JOB 37:13 Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu, au kuinyeshea dunia yake na kuonesha upendo wake.
JOB 37:14 “Ayubu, sikiliza hili; nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.
JOB 37:15 Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu, na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?
JOB 37:16 Je, unajua mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia, hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa?
JOB 37:17 Wewe unayeshindwa na joto katika nguo zako wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini,
JOB 37:18 je, unaweza kuungana naye katika kuzitandaza anga, zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa?
JOB 37:19 “Tuambieni yatupasayo kumwambia; hatuwezi kutayarisha shauri letu kwa sababu ya ujinga wetu.
JOB 37:20 Je, aambiwe kwamba nataka kuongea? Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa?
JOB 37:21 Basi hakuna awezaye kulitazama jua, jinsi linavyong’aa angani, upepo ukishafagia mawingu.
JOB 37:22 Kutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu; Mungu huja katika utukufu wa kutisha.
JOB 37:23 Yeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia, naye ametukuzwa katika uweza; katika hukumu zake na haki yake kuu, hatadhulumu.
JOB 37:24 Kwa hiyo wanadamu humwogopa, kwa kuwa yeye hamstahi yeyote anayejidhania kuwa ana hekima.”
JOB 38:1 Kisha Mwenyezi Mungu akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:
JOB 38:2 “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza kwa maneno yasiyo na maarifa?
JOB 38:3 Jikaze kama mwanaume; nitakuuliza swali, nawe unijibu.
JOB 38:4 “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia? Niambie, kama unafahamu.
JOB 38:5 Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake? Hakika wewe unajua! Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?
JOB 38:6 Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini, au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,
JOB 38:7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na malaika wote walipokuwa wakishangilia kwa furaha?
JOB 38:8 “Ni nani aliyeifungia bahari milango ilipopasuka kutoka tumbo,
JOB 38:9 nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake, na kuyafungia katika giza nene,
JOB 38:10 nilipoamuru mipaka yake, na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,
JOB 38:11 niliposema, ‘Unaweza kufika hapa, wala si zaidi; hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?
JOB 38:12 “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke, au kuyaonesha mapambazuko mahali pake,
JOB 38:13 yapate kushika miisho ya dunia, na kuwakung’uta waovu waliomo?
JOB 38:14 Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya muhuri; sura yake hukaa kama ile ya vazi.
JOB 38:15 Waovu huzuiliwa nuru yao, nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.
JOB 38:16 “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari? Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?
JOB 38:17 Umewahi kuoneshwa malango ya mauti? Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?
JOB 38:18 Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia? Niambie kama unajua haya yote.
JOB 38:19 “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi? Nako maskani mwa giza ni wapi?
JOB 38:20 Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake? Unajua njia za kufika maskani mwake?
JOB 38:21 Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa! Kwani umeishi miaka mingi!
JOB 38:22 “Je, umeshawahi kuingia katika maghala ya theluji, au kuona maghala ya mvua ya mawe,
JOB 38:23 ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu, na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?
JOB 38:24 Njia iendayo mahali miali ya radi inapotawanywa ni ipi, au njia iendayo mahali upepo wa mashariki unaposambazwa juu ya dunia?
JOB 38:25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi na njia ya miali ya radi,
JOB 38:26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu, jangwa lisilo na yeyote ndani yake,
JOB 38:27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa, na majani yaanze kumea ndani yake?
JOB 38:28 Je, mvua ina baba? Ni nani baba azaaye matone ya umande?
JOB 38:29 Barafu inatoka tumbo la nani? Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,
JOB 38:30 wakati maji yanakuwa magumu kama jiwe, wakati uso wa vilindi vya maji unaganda?
JOB 38:31 “Je, unaweza kuufunga mnyororo wa Kilimia? Unaweza kulegeza kamba za Orioni?
JOB 38:32 Unaweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake, au kuongoza Dubu na watoto wake?
JOB 38:33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu? Unaweza kuweka utawala wa Mungu duniani?
JOB 38:34 “Unaweza kuipaza sauti yako hadi mawinguni, na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?
JOB 38:35 Je, wewe hutuma miali ya radi kwenye njia zake? Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?
JOB 38:36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima au kuzipa akili ufahamu?
JOB 38:37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu? Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni
JOB 38:38 mavumbi yanapokuwa magumu, na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?
JOB 38:39 “Je, utamwindia simba jike mawindo, na kuwashibisha simba wenye njaa
JOB 38:40 wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao, au wakivizia kichakani?
JOB 38:41 Ni nani ampaye kunguru chakula wakati makinda yake yanamlilia Mungu, yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?
JOB 39:1 “Je, unajua wakati mbuzi wa mlimani wanapozaa? Je, unatambua wakati kulungu jike anapozaa mtoto wake?
JOB 39:2 Je, unaweza kuhesabu miezi hadi wanapozaa? Je, unajua majira yao ya kuzaa?
JOB 39:3 Wao hujiinamisha na kuzaa watoto wao; uchungu wa kuzaa unakoma.
JOB 39:4 Watoto wao hustawi na kuongezeka nguvu nyikani; huenda zao wala hawarudi tena.
JOB 39:5 “Ni nani aliyemwachia punda-mwitu awe huru? Ni nani aliyezifungua kamba zake?
JOB 39:6 Nimempa nchi isiyokaliwa na watu kuwa masikani yake, nchi ya chumvi kuwa makao yake.
JOB 39:7 Huzicheka ghasia za mji, wala hasikii kelele za mwendesha gari.
JOB 39:8 Huzunguka vilimani kwa ajili ya malisho na kutafuta kila kitu kibichi.
JOB 39:9 “Je, nyati atakubali kukutumikia? Atakaa karibu na hori lako usiku?
JOB 39:10 Je, unaweza kumfungia kwenye matuta kwa kamba? Je, atalima mabonde nyuma yako?
JOB 39:11 Je, utamtumainia kwa ajili ya nguvu zake nyingi? Utamwachia yeye kazi zako nzito?
JOB 39:12 Utaweza kumwamini akuletee nafaka yako nyumbani kutoka shambani na kuikusanya kwenye sakafu yako ya kupuria?
JOB 39:13 “Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa furaha, lakini hayawezi kulinganishwa na mabawa na manyoya ya korongo.
JOB 39:14 Huyataga mayai yake juu ya ardhi, na kuyaacha yapate joto mchangani,
JOB 39:15 bila kujali kuwa mguu unaweza kuyaponda, kwamba baadhi ya wanyama wa porini wanaweza kuyakanyaga.
JOB 39:16 Yeye huyafanyia makinda yake ukatili kama vile si yake; hajali kwamba taabu yake inaweza ikawa bure,
JOB 39:17 kwa kuwa Mungu hakumjalia hekima, wala hakumpa fungu la akili njema.
JOB 39:18 Lakini akunjuapo mabawa yake kukimbia, humcheka farasi pamoja na yeye aliyempanda.
JOB 39:19 “Je, wewe humpa farasi nguvu au kuivika shingo yake manyoya marefu?
JOB 39:20 Je, wewe humfanya farasi aruke kama nzige, akistaajabisha kwa tishio la mlio wake wa majivuno?
JOB 39:21 Huparapara bila woga, akizifurahia nguvu zake, husonga mbele kukabiliana na silaha.
JOB 39:22 Huicheka hofu, haogopi chochote, wala haukimbii upanga.
JOB 39:23 Podo hutoa sauti kando yake, pamoja na mkuki unaong’aa na fumo.
JOB 39:24 Bila woga na kwa ghadhabu huimeza nchi, wala tarumbeta iliapo yeye hawezi kusimama.
JOB 39:25 Asikiapo sauti ya baragumu yeye hulia, ‘Aha!’ Hunusa harufu ya vita toka mbali, husikia sauti ya mtoa amri na kelele za vita.
JOB 39:26 “Je, mwewe huruka kwa hekima yako na kuyakunjua mabawa yake kuelekea kusini?
JOB 39:27 Je, tai hupaa juu kwa amri yako na kujenga kiota chake mahali pa juu?
JOB 39:28 Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku; majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake.
JOB 39:29 Kutoka huko hutafuta chakula chake; macho yake hukiona kutoka mbali.
JOB 39:30 Makinda yake hujilisha damu, na pale palipo na machinjo, ndipo yeye alipo.”
JOB 40:1 Mwenyezi Mungu akamwambia Ayubu:
JOB 40:2 “Je, mwenye kushindana na Mwenyezi aweza kumsahihisha? Mwenye kumlaumu Mungu na ajibu.”
JOB 40:3 Ndipo Ayubu akamjibu Mwenyezi Mungu:
JOB 40:4 “Mimi sistahili kabisa: ninawezaje kukujibu wewe? Nauweka mkono wangu juu ya kinywa changu.
JOB 40:5 Nimesema mara moja, lakini sina jibu; naam, nimesema mara mbili, lakini sitasema tena.”
JOB 40:6 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema na Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli:
JOB 40:7 “Jikaze kama mwanaume; nitakuuliza maswali, nawe yakupasa unijibu.
JOB 40:8 “Je, utabatilisha hukumu yangu? Utanilaumu mimi ili kujihesabia haki mwenyewe?
JOB 40:9 Je, una mkono kama wa Mungu, nawe unaweza kutoa sauti ya ngurumo kama yake?
JOB 40:10 Basi jivike mwenyewe utukufu na fahari, nawe uvae heshima na enzi.
JOB 40:11 Fungulia ukali wa ghadhabu yako, mtafute kila mwenye kiburi umshushe,
JOB 40:12 mwangalie kila mtu mwenye kiburi na umnyenyekeze, waponde waovu mahali wasimamapo.
JOB 40:13 Wazike wote mavumbini pamoja; wafunge nyuso zao kaburini.
JOB 40:14 Ndipo mimi mwenyewe nitakukubalia kuwa mkono wako mwenyewe wa kuume unaweza kukuokoa.
JOB 40:15 “Mwangalie mnyama aitwaye Behemothi, niliyemuumba kama nilivyokuumba wewe, anayekula majani kama ng’ombe.
JOB 40:16 Tazama basi nguvu alizo nazo kwenye viuno vyake, uwezo alio nao kwenye misuli ya tumbo lake!
JOB 40:17 Mkia wake hutikisika kama mwerezi; mishipa ya mapaja yake imesukwa pamoja.
JOB 40:18 Mifupa yake ni bomba za shaba, maungo yake ni kama fito za chuma.
JOB 40:19 Yeye ni wa kwanza miongoni mwa kazi za Mungu, lakini Muumba wake anaweza kumsogelea kwa upanga wake.
JOB 40:20 Vilima humletea yeye mazao yake, nao wanyama pori wote hucheza karibu naye.
JOB 40:21 Hulala chini ya mimea ya yungiyungi, katika maficho ya matete kwenye matope.
JOB 40:22 Hiyo mimea ya yungiyungi humficha kwenye vivuli vyake; miti mirefu karibu na kijito humzunguka.
JOB 40:23 Mto unapofurika, yeye hapati mshtuko wa hofu; yeye yu salama, hata kama Yordani ingefurika hadi kwenye kinywa chake.
JOB 40:24 Je, mtu yeyote anaweza kumkamata yeye akiwa macho, au kumnasa kwa mtego na kutoboa pua yake?
JOB 41:1 “Je, unaweza kumvua Lewiathani kwa ndoana ya samaki, au kufunga ulimi wake kwa kamba?
JOB 41:2 Unaweza kupitisha kamba puani mwake, au kutoboa taya lake kwa kulabu?
JOB 41:3 Je, ataendelea kukuomba umhurumie? Atasema nawe maneno ya upole?
JOB 41:4 Je, atafanya agano nawe ili umtwae awe mtumishi wako maisha yake yote?
JOB 41:5 Je, utamfuga na kumfanya rafiki kama ndege, au kumfunga kamba kwa ajili ya wasichana wako?
JOB 41:6 Je, wafanyabiashara watabadilishana bidhaa kwa ajili yake? Watamgawanya miongoni mwa wafanyao biashara?
JOB 41:7 Je, unaweza kuijaza ngozi yake kwa vyuma vyenye ncha kali, au kichwa chake kwa mkuki wa kuvulia samaki?
JOB 41:8 Ukiweka mkono wako juu yake, utavikumbuka hivyo vita na kamwe hutarudia tena!
JOB 41:9 Tumaini lolote la kumtiisha ni kujidanganya; kule kumwona tu kunamwangusha mtu chini.
JOB 41:10 Hakuna yeyote aliye mkali athubutuye kumchokoza. Ni nani basi awezaye kusimama dhidi yangu?
JOB 41:11 Ni nani mwenye madai dhidi yangu ili nipate kumlipa? Kila kitu kilicho chini ya mbingu ni mali yangu.
JOB 41:12 “Sitashindwa kunena kuhusu maungo yake, nguvu zake na umbo lake zuri.
JOB 41:13 Ni nani awezaye kumvua gamba lake la nje? Ni nani awezaye kumsogelea na lijamu?
JOB 41:14 Nani athubutuye kuufungua mlango wa kinywa chake, kilichozungukwa na meno yake ya kutisha pande zote?
JOB 41:15 Mgongo wake una safu za ngao zilizoshikamanishwa imara pamoja;
JOB 41:16 kila moja iko karibu sana na mwenzake, wala hakuna hewa iwezayo kupita kati yake.
JOB 41:17 Zimeunganishwa imara kila moja na nyingine; zimeng’ang’aniana pamoja wala haziwezi kutenganishwa.
JOB 41:18 Akipiga chafya mwanga humetameta; macho yake ni kama miali ya mapambazuko.
JOB 41:19 Mienge iwakayo humiminika kutoka kinywani mwake; cheche za moto huruka nje.
JOB 41:20 Moshi hufuka kutoka puani mwake, kama kutoka chungu kinachotokota kwa moto wa matete.
JOB 41:21 Pumzi yake huwasha makaa ya mawe, nayo miali ya moto huruka kutoka kinywani mwake.
JOB 41:22 Nguvu hukaa katika shingo yake; utisho hutangulia mbele yake.
JOB 41:23 Mikunjo ya nyama yake imeshikamana imara pamoja; iko imara na haiwezi kuondolewa.
JOB 41:24 Kifua chake ni kigumu kama mwamba, kigumu kama jiwe la chini la kusagia.
JOB 41:25 Ainukapo, mashujaa wanaogopa; wanarudi nyuma mbele ya kishindo chake.
JOB 41:26 Upanga unaomfikia haumdhuru, wala mkuki au mshale wala fumo.
JOB 41:27 Chuma hukiona kama unyasi, na shaba kama mti uliooza.
JOB 41:28 Mishale haimfanyi yeye akimbie; mawe ya kombeo kwake ni kama makapi.
JOB 41:29 Rungu kwake huwa kama kipande cha jani kavu; hucheka sauti za kugongana kwa mkuki.
JOB 41:30 Sehemu zake za chini kwenye tumbo zina menomeno na mapengo kama vigae vya chungu, zikiacha mburuzo kwenye matope kama chombo chenye meno cha kupuria.
JOB 41:31 Huvisukasuka vilindi kama sufuria kubwa ichemkayo, na kukoroga bahari kama chungu cha marhamu.
JOB 41:32 Anapopita nyuma yake huacha mkondo unaometameta; mtu angedhani vilindi vilikuwa na mvi.
JOB 41:33 Hakuna chochote duniani kinacholingana naye: yeye ni kiumbe kisicho na woga.
JOB 41:34 Yeye huwatazama chini wale wote wenye kujivuna; yeye ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.”
JOB 42:1 Ndipo Ayubu akamjibu Mwenyezi Mungu:
JOB 42:2 “Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote, wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.
JOB 42:3 Uliuliza, ‘Ni nani huyu afichaye mashauri yangu bila maarifa?’ Hakika nilisema mambo nisiyoyaelewa, mambo ya ajabu mno kwangu mimi kuyajua.
JOB 42:4 “Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena; nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’
JOB 42:5 Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako, lakini sasa macho yangu yamekuona.
JOB 42:6 Kwa hiyo najidharau mwenyewe, na kutubu katika mavumbi na majivu.”
JOB 42:7 Baada ya Mwenyezi Mungu kusema mambo haya yote na Ayubu, akamwambia Elifazi Mtemani, “Nina hasira nawe na rafiki zako wawili, kwa sababu hamkusema yaliyo sawa kunihusu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.
JOB 42:8 Basi sasa chukueni mafahali saba na kondoo dume saba mkamwendee mtumishi wangu Ayubu nanyi mkatoe sadaka za kuteketezwa kwa ajili yenu wenyewe. Mtumishi wangu Ayubu atawaombea, nami nitayakubali maombi yake ili nisiwatendee sawasawa na upumbavu wenu. Ninyi hamkusema yaliyo sawa kwa habari yangu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.”
JOB 42:9 Kwa hiyo Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyowaambia; naye Mwenyezi Mungu akayakubali maombi ya Ayubu.
JOB 42:10 Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Mwenyezi Mungu akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni.
JOB 42:11 Ndipo ndugu zake na dada zake wote, na kila mtu aliyemfahamu mwanzoni wakaja, wakala pamoja naye katika nyumba yake. Wakamfariji na kumtuliza moyo juu ya taabu yote Mwenyezi Mungu aliyoileta juu yake, nao kila mmoja akampa kipande cha fedha na pete ya dhahabu.
JOB 42:12 Mwenyezi Mungu akaibariki sehemu ya mwisho ya maisha ya Ayubu kuliko ile ya kwanza. Alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, ngamia elfu sita, jozi za mafahali elfu moja, na punda jike elfu moja.
JOB 42:13 Tena alikuwa na wana saba na binti watatu.
JOB 42:14 Binti wa kwanza aliitwa Yemima, wa pili Kesia, na wa tatu Keren-Hapuki.
JOB 42:15 Katika nchi ile yote hakukuwa wanawake wazuri kama binti za Ayubu; naye baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao.
JOB 42:16 Baada ya hili Ayubu akaishi miaka mia moja na arobaini; akawaona wanawe, na wana wa wanawe hata kizazi cha nne.
JOB 42:17 Hivyo Ayubu akafa, akiwa mzee aliyeshiba siku.
PSA 1:1 Heri mtu yule ambaye haendi katika shauri la watu waovu, wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, au kuketi katika baraza la wenye mizaha.
PSA 1:2 Bali huifurahia Torati ya Mwenyezi Mungu, naye huitafakari hiyo Torati usiku na mchana.
PSA 1:3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa.
PSA 1:4 Sivyo walivyo waovu! Wao ni kama makapi yanayopeperushwa na upepo.
PSA 1:5 Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu, wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki.
PSA 1:6 Kwa maana Mwenyezi Mungu huziangalia njia za mwenye haki, bali njia za waovu zitaangamia.
PSA 2:1 Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya, na makabila ya watu kula njama bure?
PSA 2:2 Wafalme wa dunia wanajipanga na watawala wanajikusanya dhidi ya Mwenyezi Mungu na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.
PSA 2:3 Wanasema, “Tuvunje minyororo yao na kuvitupilia mbali vifungo vyao.”
PSA 2:4 Yeye anayetawala mbinguni hucheka, Bwana huwadharau.
PSA 2:5 Kisha huwakemea katika hasira yake na kuwaogopesha katika ghadhabu yake, akisema,
PSA 2:6 “Nimemtawaza Mfalme wangu juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.”
PSA 2:7 Nitatangaza amri ya Mwenyezi Mungu: Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako.
PSA 2:8 Niombe, nami nitayafanya mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yako.
PSA 2:9 Utawapondaponda kwa fimbo ya chuma, na kuwavunjavunja kama chombo cha mfinyanzi.”
PSA 2:10 Kwa hiyo, ninyi wafalme, kuweni na hekima; mwonyeke, enyi watawala wa dunia.
PSA 2:11 Mtumikieni Mwenyezi Mungu kwa hofu na mshangilie kwa kutetemeka.
PSA 2:12 Mbusu Mwana, asije akakasirika nawe ukaangamizwa katika njia yako, kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula. Heri wote wanaomkimbilia.
PSA 3:1 Zaburi ya Daudi. Alipomkimbia mwanawe Absalomu. Ee Mwenyezi Mungu, tazama adui zangu walivyo wengi! Ni wengi kiasi gani wanaoinuka dhidi yangu!
PSA 3:2 Wengi wanasema juu yangu, “Mungu hatamwokoa.”
PSA 3:3 Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ni ngao yangu pande zote; umeniwekea utukufu na kuinua kichwa changu.
PSA 3:4 Ninamlilia Mwenyezi Mungu kwa sauti kuu, naye ananijibu kutoka mlima wake mtakatifu.
PSA 3:5 Ninajilaza na kupata usingizi; naamka tena, kwa maana Mwenyezi Mungu hunitegemeza.
PSA 3:6 Sitaogopa makumi elfu ya adui, wanaojipanga dhidi yangu kila upande.
PSA 3:7 Ee Mwenyezi Mungu, amka! Niokoe, Ee Mungu wangu! Wapige adui zangu wote kwenye taya, vunja meno ya waovu.
PSA 3:8 Kwa maana wokovu watoka kwa Mwenyezi Mungu. Baraka yako na iwe juu ya watu wako.
PSA 4:1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi. Nijibu nikuitapo, Ee Mungu wangu mwenye haki! Nipumzishe katika shida zangu; nirehemu, usikie ombi langu.
PSA 4:2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu kuwa aibu hadi lini? Mtapenda udanganyifu na kufuata miungu ya uongo hadi lini?
PSA 4:3 Fahamuni hakika kwamba Mwenyezi Mungu amewatenga wale wamchao kwa ajili yake; Mwenyezi Mungu atanisikia nimwitapo.
PSA 4:4 Katika hasira yako, usitende dhambi. Tulieni kimya mkiwa vitandani mwenu, mkiichunguza mioyo yenu.
PSA 4:5 Toeni dhabihu zilizo haki; mtegemeeni Mwenyezi Mungu.
PSA 4:6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye kutuonesha jema lolote?” Ee Mwenyezi Mungu, tuangazie nuru ya uso wako.
PSA 4:7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi.
PSA 4:8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani, kwa kuwa wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu, waniwezesha kukaa kwa salama.
PSA 5:1 Kwa mwimbishaji. Kwa filimbi. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, tegea sikio maneno yangu, uangalie kupiga kite kwangu.
PSA 5:2 Sikiliza kilio changu ili unisaidie, Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa maana kwako ninaomba.
PSA 5:3 Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Mwenyezi Mungu; asubuhi naleta haja zangu mbele zako, na kusubiri kwa matumaini.
PSA 5:4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu, kwako mtu mwovu hataishi.
PSA 5:5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako, unawachukia wote watendao mabaya.
PSA 5:6 Unawaangamiza wasemao uongo. Mwenyezi Mungu huwachukia wanaomwaga damu na wadanganyifu.
PSA 5:7 Lakini mimi, kwa rehema zako kuu, nitakuja katika nyumba yako, kwa unyenyekevu, nitasujudu kulielekea Hekalu lako takatifu.
PSA 5:8 Niongoze katika haki yako, Ee Mwenyezi Mungu, kwa sababu ya adui zangu, nyoosha njia yako mbele yangu.
PSA 5:9 Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika, mioyo yao imejaa maangamizi. Koo lao ni kaburi lililo wazi, kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu.
PSA 5:10 Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu! Hila zao ziwe anguko lao wenyewe. Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa kuwa wamekuasi wewe.
PSA 5:11 Lakini wote wanaokimbilia kwako na wafurahi, waimbe kwa shangwe daima. Ueneze ulinzi wako juu yao, ili wale wanaolipenda jina lako wapate kukushangilia.
PSA 5:12 Kwa hakika, Ee Mwenyezi Mungu, unawabariki wenye haki, unawazunguka kwa wema wako kama ngao.
PSA 6:1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako.
PSA 6:2 Unirehemu Mwenyezi Mungu, kwa maana nimedhoofika; Ee Mwenyezi Mungu, uniponye, kwa maana mifupa yangu ina maumivu makali.
PSA 6:3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi. Hadi lini, Ee Mwenyezi Mungu, hadi lini?
PSA 6:4 Geuka, Ee Mwenyezi Mungu, unikomboe, uniokoe kwa sababu ya fadhili zako.
PSA 6:5 Hakuna mtu anayekukumbuka akiwa amekufa. Ni nani awezaye kukusifu akiwa Kuzimu?
PSA 6:6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; usiku kucha natiririsha kitanda changu kwa machozi; nimelowesha kiti changu kwa machozi yangu.
PSA 6:7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote.
PSA 6:8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, kwa maana Mwenyezi Mungu amesikia kulia kwangu.
PSA 6:9 Mwenyezi Mungu amesikia kilio changu kwa huruma, Mwenyezi Mungu amekubali sala yangu.
PSA 6:10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, watarudi nyuma na waaibishwe kwa ghafula.
PSA 7:1 Ombolezo la Daudi kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya Kushi, Mbenyamini. Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, ninakukimbilia wewe, uniokoe na kunikomboa na wote wanaonifuatia,
PSA 7:2 la sivyo watanirarua kama simba na kunichana vipande vipande, asiwepo wa kuniokoa.
PSA 7:3 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kama nimetenda haya na kuna hatia mikononi mwangu,
PSA 7:4 au ikiwa nimemtenda uovu aliye na amani nami, au nimemnyang’anya adui yangu pasipo sababu,
PSA 7:5 basi adui anifuatie na kunipata, auponde uhai wangu ardhini na kunilaza mavumbini.
PSA 7:6 Amka kwa hasira yako, Ee Mwenyezi Mungu, inuka dhidi ya ghadhabu ya adui zangu. Amka, Mungu wangu, uamue haki.
PSA 7:7 Kusanyiko la watu na likuzunguke. Watawale kutoka juu.
PSA 7:8 Mwenyezi Mungu na awahukumu makabila ya watu. Nihukumu Ee Mwenyezi Mungu, kwa kadiri ya haki yangu, kwa kadiri ya uadilifu wangu, Ewe Uliye Juu Sana.
PSA 7:9 Ee Mungu mwenye haki, uchunguzaye mawazo na mioyo, komesha ghasia za waovu na ufanye wenye haki waishi kwa amani.
PSA 7:10 Ngao yangu ni Mungu Aliye Juu Sana, anayewaokoa wanyofu wa moyo.
PSA 7:11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Mungu anayeghadhibika kila siku.
PSA 7:12 Mtu asipotubu, Mungu ataunoa upanga wake, ataupinda na kuufunga uzi upinde wake.
PSA 7:13 Ameandaa silaha zake kali, ameweka tayari mishale yake ya moto.
PSA 7:14 Yeye aliye na mimba ya uovu na anayechukua mimba ya ghasia huzaa uongo.
PSA 7:15 Yeye anayechimba shimo na kulifukua hutumbukia katika shimo alilochimba mwenyewe.
PSA 7:16 Ghasia anazozianzisha humrudia mwenyewe, ukatili wake humrudia kichwani.
PSA 7:17 Nitamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya haki yake, na nitaliimbia sifa jina la Mwenyezi Mungu Aliye Juu Sana.
PSA 8:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote! Umeuweka utukufu wako juu ya mbingu.
PSA 8:2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya umeamuru sifa, kwa sababu ya watesi wako, kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.
PSA 8:3 Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota, ulizoziratibisha,
PSA 8:4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali?
PSA 8:5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni, ukamvika taji la utukufu na heshima.
PSA 8:6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.
PSA 8:7 Mifugo na makundi yote pia, naam, na wanyama wa kondeni,
PSA 8:8 ndege wa angani na samaki wa baharini, naam, kila kinachoogelea katika njia za bahari.
PSA 8:9 Ee Mwenyezi Mungu, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!
PSA 9:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, nitakutukuza kwa moyo wangu wote, nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
PSA 9:2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako. Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.
PSA 9:3 Adui zangu wamerudi nyuma, wamejikwaa na kuangamia mbele zako.
PSA 9:4 Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu; umeketi kwenye kiti chako cha enzi, ukihukumu kwa haki.
PSA 9:5 Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu; umeyafuta majina yao milele na milele.
PSA 9:6 Uharibifu usiokoma umempata adui, umeing’oa miji yao; hata kumbukumbu lao limetoweka.
PSA 9:7 Mwenyezi Mungu anatawala milele, ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
PSA 9:8 Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki, atatawala mataifa kwa haki.
PSA 9:9 Mwenyezi Mungu ni kimbilio la wanaodhulumiwa, ni ngome imara wakati wa shida.
PSA 9:10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe, kwa maana wewe Mwenyezi Mungu, hujawaacha kamwe wanaokutafuta.
PSA 9:11 Mwimbieni Mwenyezi Mungu sifa, amefanywa mtawala Sayuni, tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda.
PSA 9:12 Kwa maana yeye anayelipiza kisasi cha damu hukumbuka, hapuuzi kilio cha wanaoonewa.
PSA 9:13 Ee Mwenyezi Mungu, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa! Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,
PSA 9:14 ili niweze kutangaza sifa zako katika malango ya Binti Sayuni, na huko niushangilie wokovu wako.
PSA 9:15 Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba, miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha.
PSA 9:16 Mwenyezi Mungu anajulikana kwa haki yake, waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao.
PSA 9:17 Waovu wataishia Kuzimu, naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.
PSA 9:18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote, wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.
PSA 9:19 Ee Mwenyezi Mungu, inuka, usimwache binadamu ashinde. Mataifa na yahukumiwe mbele zako.
PSA 9:20 Ee Mwenyezi Mungu, wapige kwa hofu, mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.
PSA 10:1 Kwa nini, Ee Mwenyezi Mungu, unasimama mbali? Kwa nini unajificha wakati wa shida?
PSA 10:2 Katika kiburi chake, mwovu humtesa maskini, waovu na wanaswe katika hila wanazozitunga.
PSA 10:3 Hujivunia tamaa za moyo wake; humbariki mlafi na kumtukana Mwenyezi Mungu.
PSA 10:4 Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu, katika mawazo yake yote hakuna nafasi ya Mungu.
PSA 10:5 Njia zake daima hufanikiwa; hujivuna na amri zako ziko mbali naye, huwacheka kwa dharau adui zake wote.
PSA 10:6 Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa, daima nitakuwa na furaha, kamwe sitakuwa na shida.”
PSA 10:7 Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho; shida na ubaya viko chini ya ulimi wake.
PSA 10:8 Huvizia karibu na vijiji; kutoka mafichoni huwanasa wasio na hatia, akivizia wapitaji.
PSA 10:9 Huvizia kama simba aliye mawindoni; huvizia kumkamata mnyonge, huwakamata wanyonge na kuwaburuza katika wavu wake.
PSA 10:10 Mateka wake hupondwa, huzimia; wanaanguka katika nguvu zake.
PSA 10:11 Anajisemea mwenyewe, “Mungu amesahau, huficha uso wake na haoni kabisa.”
PSA 10:12 Inuka Mwenyezi Mungu! Inua mkono wako, Ee Mungu. Usiwasahau wanyonge.
PSA 10:13 Kwa nini mtu mwovu anamtukana Mungu? Kwa nini anajiambia mwenyewe, “Hataniita nitoe hesabu”?
PSA 10:14 Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni, umekubali kuyapokea mkononi mwako. Mhanga anajisalimisha kwako, wewe ni msaada wa yatima.
PSA 10:15 Vunja mkono wa mtu mbaya na mwovu; mwite mtu mbaya atoe hesabu ya uovu wake ambao usingejulikana vinginevyo.
PSA 10:16 Mwenyezi Mungu ni Mfalme milele na milele, mataifa wataangamia watoke nchini mwake.
PSA 10:17 Unasikia, Ee Mwenyezi Mungu, shauku ya wanaoonewa; wewe huwatia moyo, na kusikiliza kilio chao,
PSA 10:18 ukiwatetea yatima na waliodhulumiwa, ili mwanadamu ambaye ni udongo asiogopeshe tena.
PSA 11:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Kwa Mwenyezi Mungu ninakimbilia. Unawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege utorokee kwenye mlima wako.
PSA 11:2 Hebu tazama, waovu wanapinda nyuta zao; wanaweka mishale kwenye nyuzi zake ili wakiwa gizani, wawapige walio wanyofu wa moyo.
PSA 11:3 Wakati misingi imeharibiwa, mwenye haki anaweza kufanya nini?”
PSA 11:4 Mwenyezi Mungu yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; Mwenyezi Mungu yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. Huwaangalia wana wa watu, macho yake yanawachunguza.
PSA 11:5 Mwenyezi Mungu huwachunguza wenye haki, lakini nafsi yake inachukia waovu na wale wanaopenda mapigano.
PSA 11:6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali na kiberiti kinachowaka; upepo wenye joto kali ndio fungu lao.
PSA 11:7 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, yeye hupenda haki. Wanyofu watauona uso wake.
PSA 12:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Mwenyezi Mungu tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka; waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.
PSA 12:2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo; midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.
PSA 12:3 Mwenyezi Mungu na akatilie mbali midomo yote ya hila na kila ulimi uliojaa majivuno,
PSA 12:4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”
PSA 12:5 “Kwa sababu wanyonge wanaonewa, na wahitaji wanalia kwa uchungu, nitainuka sasa,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawalinda kutokana na wale wenye nia mbaya juu yao.”
PSA 12:6 Maneno ya Mwenyezi Mungu ni safi, kama fedha iliyosafishwa katika tanuru, iliyosafishwa mara saba.
PSA 12:7 Ee Mwenyezi Mungu, utatuweka salama na kutulinda na kizazi hiki milele.
PSA 12:8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali wakati yule aliye mbaya sana ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.
PSA 13:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Hadi lini, Ee Mwenyezi Mungu? Je, utanisahau milele? Utanificha uso wako hadi lini?
PSA 13:2 Nitapambana na mawazo yangu hadi lini, na kila siku kuwa na majonzi moyoni mwangu? Adui zangu watanishinda hadi lini?
PSA 13:3 Nitazame, unijibu, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu. Yatie nuru macho yangu, ama sivyo nitalala usingizi wa mauti.
PSA 13:4 Adui yangu atasema, “Nimemshinda,” nao adui zangu watashangilia nitakapoanguka.
PSA 13:5 Lakini ninategemea upendo wako usiokoma; moyo wangu unashangilia katika wokovu wako.
PSA 13:6 Nitamwimbia Mwenyezi Mungu, kwa kuwa amekuwa mwema kwangu.
PSA 14:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wamepotoka, matendo yao ni maovu kabisa; hakuna hata mmoja atendaye mema.
PSA 14:2 Mwenyezi Mungu anawachungulia wanadamu kutoka mbinguni aone kama kuna mwenye hekima, yeyote anayemtafuta Mungu.
PSA 14:3 Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja!
PSA 14:4 Je, watendao maovu kamwe hawatajifunza: wale ambao huwala watu wangu kama watu walavyo mkate, hao ambao hawamwiti Mwenyezi Mungu?
PSA 14:5 Wako hapo, wameingiwa na hofu kuu, maana Mungu yupo pamoja na wenye haki.
PSA 14:6 Ninyi watenda maovu mnakwamisha mipango ya maskini, bali Mwenyezi Mungu ndiye kimbilio lao.
PSA 14:7 Laiti wokovu wa Israeli ungekuja kutoka Sayuni! Mwenyezi Mungu anaporejesha wafungwa wa watu wake, Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!
PSA 15:1 Zaburi ya Daudi. Mwenyezi Mungu, ni nani awezaye kukaa katika Hekalu lako? Nani awezaye kuishi katika mlima wako mtakatifu?
PSA 15:2 Ni yule aendaye pasipo mawaa, atendaye yaliyo haki, asemaye kweli toka moyoni mwake,
PSA 15:3 na hana masingizio ulimini mwake, asiyemtenda jirani yake vibaya, na asiyemsingizia mwenzake,
PSA 15:4 ambaye humdharau mtu mbaya, lakini huwaheshimu wale wamwogopao Mwenyezi Mungu, yule atunzaye kiapo chake hata kama anaumia.
PSA 15:5 Yeye akopeshaye fedha yake bila riba, na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia. Mtu afanyaye haya kamwe hatatikisika.
PSA 16:1 Utenzi wa Daudi. Ee Mungu, uniweke salama, kwa maana kwako nimekimbilia.
PSA 16:2 Nilimwambia Mwenyezi Mungu, “Wewe ndiwe Bwana wangu; pasipo wewe sina jambo jema.”
PSA 16:3 Kuhusu watakatifu walio duniani, hao ndio wenye fahari, na ninapendezwa nao.
PSA 16:4 Huzuni itaongezeka kwa wale wanaokimbilia miungu mingine. Sitazimimina sadaka za damu kwa miungu kama hiyo, au kutaja majina yao mdomoni mwangu.
PSA 16:5 Mwenyezi Mungu umeniwekea fungu langu na kikombe changu; umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.
PSA 16:6 Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, hakika nimepata urithi mzuri.
PSA 16:7 Nitamsifu Mwenyezi Mungu ambaye hunishauri, hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.
PSA 16:8 Nimemweka Mwenyezi Mungu mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika.
PSA 16:9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika salama,
PSA 16:10 kwa maana hutaniacha Kuzimu, wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu.
PSA 16:11 Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na furaha mbele zako, pamoja na furaha ya milele katika mkono wako wa kuume.
PSA 17:1 Sala ya Daudi. Sikia, Ee Mwenyezi Mungu, kusihi kwangu kwa haki, sikiliza kilio changu. Tega sikio kwa ombi langu, halitoki katika midomo ya udanganyifu.
PSA 17:2 Hukumu yangu na itoke kwako, macho yako na yaone yale yaliyo haki.
PSA 17:3 Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku, ingawa umenijaribu, hutaona chochote. Nimeamua kwamba kinywa changu hakitatenda dhambi.
PSA 17:4 Kuhusu matendo ya wanadamu: kwa neno la midomo yako, nimejiepusha na njia za wenye jeuri.
PSA 17:5 Hatua zangu zimeshikamana na njia zako; nyayo zangu hazikuteleza.
PSA 17:6 Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu, nitegee sikio lako na usikie ombi langu.
PSA 17:7 Uoneshe ajabu ya upendo wako mkuu, wewe unayeokoa kwa mkono wako wa kuume wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.
PSA 17:8 Nilinde kama mboni ya jicho lako, unifiche chini ya kivuli cha mabawa yako
PSA 17:9 kutokana na waovu wanaonishambulia, kutokana na adui wauaji wanaonizunguka.
PSA 17:10 Huifunga mioyo yao iliyo migumu, vinywa vyao hunena kwa majivuno.
PSA 17:11 Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira, wakiwa macho, waniangushe chini.
PSA 17:12 Wamefanana na simba mwenye njaa anayewinda, kama simba mkubwa anayenyemelea mafichoni.
PSA 17:13 Inuka, Ee Mwenyezi Mungu, pambana nao, uwaangushe, niokoe kwa upanga wako kutoka kwa waovu.
PSA 17:14 Ee Mwenyezi Mungu, mkono wako uniokoe na watu kama hawa, kutokana na watu wa ulimwengu huu ambao fungu lao liko katika maisha haya. Na wapate adhabu ya kuwatosha. Watoto wao na wapate zaidi ya hayo, hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao.
PSA 17:15 Bali mimi nitauona uso wako katika haki; niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.
PSA 18:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliyomwimbia Mwenyezi Mungu alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Alisema hivi: Nakupenda wewe, Ee Mwenyezi Mungu, nguvu yangu.
PSA 18:2 Mwenyezi Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu; Mungu wangu ni mwamba wangu, ninayemkimbilia. Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu, ngome yangu.
PSA 18:3 Ninamwita Mwenyezi Mungu anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
PSA 18:4 Kamba za mauti zilinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
PSA 18:5 Kamba za Kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili.
PSA 18:6 Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika mbele zake, masikioni mwake.
PSA 18:7 Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya milima ikatikisika; vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
PSA 18:8 Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yanayowaka yakatoka ndani yake.
PSA 18:9 Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
PSA 18:10 Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mabawa ya upepo.
PSA 18:11 Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika, hema lake kumzunguka: mawingu meusi ya mvua ya angani.
PSA 18:12 Kutokana na mwanga wa uwepo wake mawingu yalisogea, ikashuka mvua ya mawe na miali ya radi.
PSA 18:13 Mwenyezi Mungu alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
PSA 18:14 Aliipiga mishale yake na kutawanya adui, naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza.
PSA 18:15 Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwako, Ee Mwenyezi Mungu, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.
PSA 18:16 Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kilindini cha maji makuu.
PSA 18:17 Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
PSA 18:18 Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini Mwenyezi Mungu alikuwa msaada wangu.
PSA 18:19 Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
PSA 18:20 Mwenyezi Mungu alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; amenilipa sawasawa na usafi wa mikono yangu.
PSA 18:21 Kwa maana nimezishika njia za Mwenyezi Mungu; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
PSA 18:22 Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake.
PSA 18:23 Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi.
PSA 18:24 Mwenyezi Mungu amenilipa sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake.
PSA 18:25 Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia, unajionesha kutokuwa na hatia.
PSA 18:26 Kwa aliye mtakatifu, unajionesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka, unajionesha kuwa mkaidi.
PSA 18:27 Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini huwashusha wenye kiburi.
PSA 18:28 Wewe, Ee Mwenyezi Mungu, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka; Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga.
PSA 18:29 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta.
PSA 18:30 Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu, neno la Mwenyezi Mungu halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake.
PSA 18:31 Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya Mwenyezi Mungu? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu?
PSA 18:32 Mungu ndiye anivikaye nguvu na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
PSA 18:33 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
PSA 18:34 Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
PSA 18:35 Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu, nao mkono wako wa kuume hunitegemeza; msaada wako umeniinua niwe mkuu.
PSA 18:36 Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze.
PSA 18:37 Niliwafuatia adui zangu na nikawapata, sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
PSA 18:38 Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu.
PSA 18:39 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
PSA 18:40 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu.
PSA 18:41 Walipiga yowe, lakini hapakuwa na mtu wa kuwaokoa; walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu.
PSA 18:42 Niliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo; niliwamwaga nje kama tope barabarani.
PSA 18:43 Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu; umenifanya kiongozi wa mataifa; watu ambao sikuwajua wananitumikia.
PSA 18:44 Mara wanisikiapo hunitii, wageni hunyenyekea mbele yangu.
PSA 18:45 Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
PSA 18:46 Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!
PSA 18:47 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, awatiishaye mataifa chini yangu,
PSA 18:48 aniokoaye na adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
PSA 18:49 Kwa hiyo nitakusifu katika mataifa, Ee Mwenyezi Mungu; nitaliimbia sifa jina lako.
PSA 18:50 Humpa mfalme wake ushindi mkuu, huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.
PSA 19:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu, anga zahubiri kazi ya mikono yake.
PSA 19:2 Siku baada ya siku zinatoa habari, usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.
PSA 19:3 Hakuna msemo wala lugha, ambapo sauti zao hazisikiki.
PSA 19:4 Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu. Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,
PSA 19:5 linafanana na bwana arusi akitoka chumbani mwake, kama shujaa anavyofurahia kukamilisha kushindana kwake.
PSA 19:6 Huchomoza upande mmoja wa mbingu, na kufanya mzunguko wake hadi upande mwingine. Hakuna kilichojificha joto lake.
PSA 19:7 Torati ya Mwenyezi Mungu ni kamilifu, ikihuisha nafsi. Shuhuda za Mwenyezi Mungu ni za kuaminika, zikimpa mjinga hekima.
PSA 19:8 Maagizo ya Mwenyezi Mungu ni kamili, nayo hufurahisha moyo. Amri za Mwenyezi Mungu huangaza, zatia nuru machoni.
PSA 19:9 Kumcha Mwenyezi Mungu ni utakatifu, nako kwadumu milele. Amri za Mwenyezi Mungu ni za hakika, nazo zina haki.
PSA 19:10 Ni za thamani kuliko dhahabu, kuliko dhahabu iliyo safi sana, ni tamu kuliko asali, kuliko asali kutoka sega.
PSA 19:11 Kwa hizo mtumishi wako anaonywa, katika kuzishika kuna thawabu kubwa.
PSA 19:12 Ni nani awezaye kutambua makosa yake? Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua.
PSA 19:13 Mlinde mtumishi wako na dhambi za makusudi, nazo zisinitawale. Ndipo nitakapokuwa sina lawama, niwe huru na hatia kubwa.
PSA 19:14 Maneno ya kinywa changu na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee Mwenyezi Mungu, Mwamba wangu na Mkombozi wangu.
PSA 20:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Mwenyezi Mungu na akujibu unapokuwa katika dhiki, jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako.
PSA 20:2 Na akutumie msaada kutoka patakatifu na akupatie msaada kutoka Sayuni.
PSA 20:3 Na azikumbuke dhabihu zako zote, na azikubali sadaka zako za kuteketezwa.
PSA 20:4 Na akujalie haja ya moyo wako, na aifanikishe mipango yako yote.
PSA 20:5 Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda, tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu. Mwenyezi Mungu na akupe haja zako zote.
PSA 20:6 Sasa nafahamu kuwa Mwenyezi Mungu humwokoa mpakwa mafuta wake, humjibu kutoka mbingu yake takatifu kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.
PSA 20:7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi, bali sisi tutalitumainia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
PSA 20:8 Wao wameshushwa chini na kuanguka, bali sisi tunainuka na kusimama imara.
PSA 20:9 Ee Mwenyezi Mungu, mwokoe mfalme! Tujibu tunapokuita!
PSA 21:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, mfalme huzifurahia nguvu zako. Tazama jinsi furaha yake ilivyo kuu kwa ushindi unaompa!
PSA 21:2 Umempa haja ya moyo wake na hukumzuilia maombi ya midomo yake.
PSA 21:3 Ulimkaribisha kwa baraka tele na kumvika taji la dhahabu safi kichwani pake.
PSA 21:4 Alikuomba maisha, nawe ukampa, wingi wa siku milele na milele.
PSA 21:5 Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa, umeweka juu yake fahari na utukufu.
PSA 21:6 Hakika umempa baraka za milele, umemfanya awe na furaha kwa shangwe ya uwepo wako.
PSA 21:7 Kwa kuwa mfalme anamtumaini Mwenyezi Mungu; kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.
PSA 21:8 Mkono wako utawashika adui zako wote, mkono wako wa kuume utawakamata adui zako.
PSA 21:9 Wakati utajitokeza, utawafanya kama tanuru la moto. Katika ghadhabu yake Mwenyezi Mungu atawameza, moto wake utawateketeza.
PSA 21:10 Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani, uzao wao kutoka wanadamu.
PSA 21:11 Ingawa watapanga mabaya dhidi yako na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa,
PSA 21:12 kwa kuwa utawafanya wakimbie utakapowalenga usoni pao kwa mshale kutoka upinde wako.
PSA 21:13 Ee Mwenyezi Mungu, utukuzwe katika nguvu zako, tutaimba na kusifu nguvu zako.
PSA 22:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri”. Zaburi ya Daudi. Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa? Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?
PSA 22:2 Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu, hata usiku, sinyamazi.
PSA 22:3 Hata hivyo umesimikwa kwenye kiti cha enzi, Wewe Uliye Mtakatifu; wewe ni sifa ya Israeli.
PSA 22:4 Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao, walikutumaini nawe ukawaokoa.
PSA 22:5 Walikulilia wewe na ukawaokoa, walikutegemea wewe nao hawakuaibika.
PSA 22:6 Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu, wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau.
PSA 22:7 Wote wanaoniona wananidhihaki; wananivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao:
PSA 22:8 Wanasema, “Amtegemea Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu na amwokoe. Amkomboe basi, kwa maana anapendezwa naye.”
PSA 22:9 Hata hivyo ulinitoa tumboni, ukanifanya nikutegemee, hata nilipokuwa ninanyonya matiti ya mama yangu.
PSA 22:10 Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa, toka tumboni mwa mama yangu umekuwa Mungu wangu.
PSA 22:11 Usiwe mbali nami, kwa maana shida iko karibu na hakuna wa kunisaidia.
PSA 22:12 Mafahali wengi wamenizunguka, mafahali wa Bashani wenye nguvu wamenizingira.
PSA 22:13 Simba wanaonguruma na kurarua mawindo wanapanua vinywa vyao dhidi yangu.
PSA 22:14 Nimemiminwa kama maji, mifupa yangu yote imeteguka viungoni. Moyo wangu umegeuka kuwa nta, umeyeyuka ndani yangu.
PSA 22:15 Nguvu zangu zimekauka kama kigae, ulimi wangu umegandamana na kaakaa la kinywa changu, kwa sababu umenilaza katika mavumbi ya kifo.
PSA 22:16 Mbwa wamenizunguka, kundi la watu waovu limenizingira; wamenidunga mikono na miguu.
PSA 22:17 Naweza kuhesabu mifupa yangu yote, watu wananikodolea macho na kunisimanga.
PSA 22:18 Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura.
PSA 22:19 Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, usiwe mbali. Ee Nguvu yangu, uje haraka unisaidie.
PSA 22:20 Okoa maisha yangu na upanga, uhai wangu wa thamani kutoka nguvu za mbwa.
PSA 22:21 Niokoe kutoka kinywani mwa simba, niokoe kutoka pembe za nyati.
PSA 22:22 Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu, katika kusanyiko nitakusifu wewe.
PSA 22:23 Ninyi ambao mnamcha Mwenyezi Mungu, msifuni! Ninyi nyote wazao wa Yakobo, mheshimuni yeye! Mcheni yeye, ninyi wazao wa Israeli!
PSA 22:24 Kwa maana hakupuuza wala kudharau mateso ya aliyeteswa; hakumficha uso wake bali alisikiliza kilio chake.
PSA 22:25 Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa, nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wanaokucha wewe.
PSA 22:26 Maskini watakula na kushiba, wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu watamsifu: mioyo yenu na iishi milele!
PSA 22:27 Miisho yote ya dunia itakumbuka na kumgeukia Mwenyezi Mungu, nazo jamaa zote za mataifa zitasujudu mbele zake,
PSA 22:28 kwa maana ufalme ni wa Mwenyezi Mungu naye huyatawala mataifa.
PSA 22:29 Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu. Wote wanaoshuka mavumbini watapiga magoti mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao.
PSA 22:30 Wazao wa baadaye watamtumikia yeye; vizazi vijavyo vitajulishwa habari za Bwana.
PSA 22:31 Watatangaza haki yake kwa watu ambao hawajazaliwa bado, kwa maana yeye ametenda hili.
PSA 23:1 Zaburi ya Daudi. Mwenyezi Mungu ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
PSA 23:2 Hunilaza katika malisho ya majani mabichi, kando ya maji matulivu huniongoza,
PSA 23:3 hunihuisha nafsi yangu. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
PSA 23:4 Hata nikipita katikati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami; fimbo yako na mkongojo wako vyanifariji.
PSA 23:5 Waandaa meza mbele yangu machoni pa adui zangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, kikombe changu kinafurika.
PSA 23:6 Hakika wema na upendo vitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi Mungu milele.
PSA 24:1 Zaburi ya Daudi. Dunia ni mali ya Mwenyezi Mungu, na vyote vilivyomo, ulimwengu, na wote wanaoishi ndani yake,
PSA 24:2 maana aliiwekea misingi yake baharini, na kuifanya imara juu ya maji.
PSA 24:3 Nani awezaye kuupanda mlima wa Mwenyezi Mungu? Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake?
PSA 24:4 Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe, yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake au kuapa kwa kitu cha uongo.
PSA 24:5 Huyo atapokea baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hukumu ya haki kutoka kwa Mungu Mwokozi wake.
PSA 24:6 Hiki ndicho kizazi cha wale wanaomtafuta, wale wanaoutafuta uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
PSA 24:7 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, inukeni enyi milango ya kale, ili mfalme wa utukufu apate kuingia.
PSA 24:8 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Ni Mwenyezi Mungu aliye na nguvu na uweza, ni Mwenyezi Mungu aliye hodari katika vita.
PSA 24:9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, viinueni juu enyi milango ya kale, ili Mfalme wa utukufu apate kuingia.
PSA 24:10 Ni nani yeye, huyu Mfalme wa utukufu? Ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni; yeye ndiye Mfalme wa utukufu.
PSA 25:1 Zaburi ya Daudi. Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu, naweka tumaini yangu.
PSA 25:2 Ni wewe ninayekutumainia, Usiniache niaibike, wala adui zangu wanishinde.
PSA 25:3 Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea atakayeaibishwa, bali wataaibishwa wafanyao hila bila sababu.
PSA 25:4 Nioneshe njia zako, Ee Mwenyezi Mungu, nifundishe mapito yako,
PSA 25:5 niongoze katika kweli yako na kunifundisha, kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu, nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.
PSA 25:6 Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, rehema zako kuu na upendo, kwa maana zimekuwepo tangu zamani.
PSA 25:7 Usizikumbuke dhambi za ujana wangu wala njia zangu za uasi, sawasawa na upendo wako unikumbuke, kwa maana wewe ni mwema, Ee Mwenyezi Mungu.
PSA 25:8 Mwenyezi Mungu ni mwema na mwenye adili, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.
PSA 25:9 Huwaongoza wanyenyekevu katika haki, naye huwafundisha njia yake.
PSA 25:10 Njia zote za Mwenyezi Mungu ni za upendo na uaminifu kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake.
PSA 25:11 Ee Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya jina lako, unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi.
PSA 25:12 Ni nani basi, mtu yule anayemcha Mwenyezi Mungu? Atamfundisha katika njia atakayoichagua kwa ajili yake.
PSA 25:13 Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake, nao wazao wake watairithi nchi.
PSA 25:14 Siri ya Mwenyezi Mungu iko kwa wale wamchao, yeye huwajulisha agano lake.
PSA 25:15 Macho yangu humwelekea Mwenyezi Mungu daima, kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa miguu yangu kutoka mtego.
PSA 25:16 Nigeukie na unihurumie, kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka.
PSA 25:17 Shida za moyo wangu zimeongezeka, niokoe katika dhiki yangu.
PSA 25:18 Uangalie mateso na shida zangu na uniondolee dhambi zangu zote.
PSA 25:19 Tazama adui zangu walivyo wengi, pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!
PSA 25:20 Uyalinde maisha yangu na uniokoe, usiniache niaibike, kwa maana nimekukimbilia wewe.
PSA 25:21 Uadilifu na uaminifu vinilinde, kwa sababu tumaini langu ni kwako, Mwenyezi Mungu.
PSA 25:22 Ee Mungu, wakomboe Israeli, katika shida zao zote!
PSA 26:1 Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, nithibitishe katika haki, maana nimeishi maisha yasiyo na lawama; nimemtumainia Mwenyezi Mungu bila kusitasita.
PSA 26:2 Ee Mwenyezi Mungu, unijaribu, unipime, uuchunguze moyo wangu na mawazo yangu;
PSA 26:3 kwa maana upendo wako uko mbele yangu daima, nami natembea siku zote katika kweli yako.
PSA 26:4 Siketi pamoja na watu wadanganyifu, wala siandamani na wanafiki,
PSA 26:5 ninachukia kusanyiko la watenda maovu, na ninakataa kuketi pamoja na waovu.
PSA 26:6 Ninanawa mikono yangu kwa kuwa sina hatia, naikaribia madhabahu yako, Ee Mwenyezi Mungu,
PSA 26:7 nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa, huku nikisimulia matendo yako ya ajabu.
PSA 26:8 Ee Mwenyezi Mungu, naipenda nyumba yako unakoishi, mahali pale utukufu wako hukaa.
PSA 26:9 Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi, wala uhai wangu pamoja na wanaomwaga damu,
PSA 26:10 ambao mikononi mwao kuna mipango miovu, ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa.
PSA 26:11 Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama; nikomboe na unihurumie.
PSA 26:12 Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare; katika kusanyiko kuu nitamsifu Mwenyezi Mungu.
PSA 27:1 Zaburi ya Daudi. Mwenyezi Mungu ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Mwenyezi Mungu ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani?
PSA 27:2 Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wale nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka.
PSA 27:3 Hata jeshi linizingire pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri.
PSA 27:4 Jambo moja ninamwomba Mwenyezi Mungu, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa Mwenyezi Mungu na kumtafuta hekaluni mwake.
PSA 27:5 Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema lake, na kuniweka juu kwenye mwamba.
PSA 27:6 Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia Mwenyezi Mungu na kumsifu.
PSA 27:7 Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Mwenyezi Mungu, unihurumie na unijibu.
PSA 27:8 Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, Mwenyezi Mungu “Nitautafuta.”
PSA 27:9 Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu.
PSA 27:10 Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha, Mwenyezi Mungu atanipokea.
PSA 27:11 Nifundishe njia yako, Ee Mwenyezi Mungu, niongoze katika njia iliyo nyoofu, kwa sababu ya watesi wangu.
PSA 27:12 Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri.
PSA 27:13 Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa Mwenyezi Mungu katika nchi ya walio hai.
PSA 27:14 Mngojee Mwenyezi Mungu; uwe hodari na mwenye moyo mkuu, na umngojee Mwenyezi Mungu.
PSA 28:1 Zaburi ya Daudi. Ninakuita wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mwamba wangu; usikatae kunisikiliza. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni.
PSA 28:2 Sikia kilio changu nikikuomba unihurumie, ninapokuita ili unisaidie, ninapoinua mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako.
PSA 28:3 Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na majirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki.
PSA 28:4 Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili.
PSA 28:5 Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Mwenyezi Mungu, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena.
PSA 28:6 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie.
PSA 28:7 Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo.
PSA 28:8 Mwenyezi Mungu ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
PSA 28:9 Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.
PSA 29:1 Zaburi ya Daudi. Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi mashujaa, mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu.
PSA 29:2 Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake.
PSA 29:3 Sauti ya Mwenyezi Mungu iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Mwenyezi Mungu hupiga radi juu ya maji makuu.
PSA 29:4 Sauti ya Mwenyezi Mungu ina nguvu; sauti ya Mwenyezi Mungu ni tukufu.
PSA 29:5 Sauti ya Mwenyezi Mungu huvunja mierezi; Mwenyezi Mungu huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni.
PSA 29:6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati.
PSA 29:7 Sauti ya Mwenyezi Mungu hupiga kwa miali ya radi.
PSA 29:8 Sauti ya Mwenyezi Mungu hutikisa jangwa; Mwenyezi Mungu hutikisa Jangwa la Kadeshi.
PSA 29:9 Sauti ya Mwenyezi Mungu huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!”
PSA 29:10 Mwenyezi Mungu huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Mwenyezi Mungu ametawazwa kuwa Mfalme milele.
PSA 29:11 Mwenyezi Mungu huwapa watu wake nguvu; Mwenyezi Mungu huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.
PSA 30:1 Utenzi wa kuweka wakfu hekalu. Zaburi ya Daudi. Nitakutukuza wewe, Ee Mwenyezi Mungu, kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi, na hukuacha adui zangu washangilie juu yangu.
PSA 30:2 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nilikuita unisaidie na wewe umeniponya.
PSA 30:3 Ee Mwenyezi Mungu, umenitoa Kuzimu, umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.
PSA 30:4 Mwimbieni Mwenyezi Mungu, enyi watakatifu wake; lisifuni jina lake takatifu.
PSA 30:5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi, bali upendo wake hudumu siku zote. Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha, lakini furaha huja asubuhi.
PSA 30:6 Nilipofanikiwa nilisema, “Sitatikiswa kamwe.”
PSA 30:7 Ee Mwenyezi Mungu, uliponijalia, uliuimarisha mlima wangu, lakini ulipouficha uso wako nilifadhaika.
PSA 30:8 Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu, niliita, niliomba rehema kwa Bwana:
PSA 30:9 “Kuna faida gani katika kuangamia kwangu, katika kushuka kwangu shimoni? Je, mavumbi yatakusifu? Je, yatatangaza uaminifu wako?
PSA 30:10 Ee Mwenyezi Mungu, unisikie na kunihurumia; Ee Mwenyezi Mungu, uwe msaada wangu.”
PSA 30:11 Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza, ulinivua gunia ukanivika shangwe,
PSA 30:12 ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya. Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nitakushukuru milele.
PSA 31:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe, kwa haki yako uniokoe.
PSA 31:2 Nitegee sikio lako, uje uniokoe haraka; uwe kwangu mwamba wa kimbilio, ngome imara ya kuniokoa.
PSA 31:3 Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu, uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako.
PSA 31:4 Uniepushe na mtego niliotegewa, maana wewe ndiwe kimbilio langu.
PSA 31:5 Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako, unikomboe Ee Mwenyezi Mungu, uliye Mungu wa kweli.
PSA 31:6 Ninawachukia wale wanaoshikilia sanamu batili; bali mimi ninamtumaini Mwenyezi Mungu.
PSA 31:7 Nitafurahia na kushangilia upendo wako, kwa kuwa uliona mateso yangu na ulijua maumivu ya nafsi yangu.
PSA 31:8 Hukunikabidhi kwa adui yangu bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi.
PSA 31:9 Ee Mwenyezi Mungu unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida; macho yangu yanafifia kwa huzuni, nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.
PSA 31:10 Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi, naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali; nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso, na mifupa yangu inachakaa.
PSA 31:11 Kwa sababu ya adui zangu wote, nimedharauliwa kabisa na majirani zangu, hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho, wale wanaoniona barabarani wananikimbia.
PSA 31:12 Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa, nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.
PSA 31:13 Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi; vitisho viko pande zote; kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu, na kula njama kuniua.
PSA 31:14 Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu; nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
PSA 31:15 Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako, uniokoe mikononi mwa adui zangu na wale wanifuatiao.
PSA 31:16 Mwangazie mtumishi wako uso wako, uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.
PSA 31:17 Usiniache niaibike, Ee Mwenyezi Mungu, kwa maana nimekulilia wewe, bali waovu waaibishwe na kunyamazishwa Kuzimu.
PSA 31:18 Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe, kwa maana kwa kiburi na dharau wao husema kwa majivuno dhidi ya wenye haki.
PSA 31:19 Tazama jinsi wema wako ulivyo mkuu, uliowawekea akiba wanaokucha, unaowapa wale wanaokukimbilia machoni pa watu wote.
PSA 31:20 Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako kutokana na hila za wanadamu; katika makao yako huwaweka salama kutokana na ndimi za mashtaka.
PSA 31:21 Atukuzwe Mwenyezi Mungu, kwa kuwa amenionesha upendo wake wa ajabu nilipokuwa katika mji uliozingirwa.
PSA 31:22 Katika hofu yangu nilisema, “Nimekatiliwa mbali na macho yako!” Hata hivyo ulisikia kilio changu ukanihurumia nilipokuita unisaidie.
PSA 31:23 Mpendeni Mwenyezi Mungu ninyi watakatifu wake wote! Mwenyezi Mungu huwahifadhi waaminifu, lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.
PSA 31:24 Kuweni hodari na mjipe moyo, ninyi nyote mnaomtumaini Mwenyezi Mungu.
PSA 32:1 Zaburi ya Daudi. Funzo. Heri mtu aliyesamehewa makosa yake, ambaye dhambi zake zimefunikwa.
PSA 32:2 Heri mtu yule ambaye Mwenyezi Mungu hamhesabii dhambi, na ambaye rohoni mwake hamna udanganyifu.
PSA 32:3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.
PSA 32:4 Usiku na mchana mkono wako ulinilemea, nguvu zangu zilinyonywa kama vile katika joto la kiangazi.
PSA 32:5 Kisha nikakiri dhambi yangu kwako, wala sikuficha uovu wangu. Nilisema, “Nitaungama makosa yangu kwa Mwenyezi Mungu.” Ndipo uliponisamehe hatia ya dhambi yangu.
PSA 32:6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe wakati unapopatikana, hakika maji makuu yatakapofurika hayatamfikia yeye.
PSA 32:7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha, utaniepusha na taabu na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
PSA 32:8 Nitakufundisha na kukuonesha njia utakayoiendea; nitakushauri na kukuangalia.
PSA 32:9 Usiwe kama farasi au nyumbu wasio na akili, ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu la sivyo hawatakukaribia.
PSA 32:10 Mtu mwovu ana taabu nyingi, bali upendo usio na kikomo wa Mwenyezi Mungu unamzunguka mtu anayemtumaini.
PSA 32:11 Shangilieni katika Mwenyezi Mungu na mfurahi, enyi wenye haki! Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!
PSA 33:1 Mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa furaha, enyi wenye haki; wanyofu wa moyo wanapaswa kumsifu.
PSA 33:2 Msifuni Mwenyezi Mungu kwa kinubi, mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.
PSA 33:3 Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.
PSA 33:4 Maana neno la Mwenyezi Mungu ni haki na kweli, ni mwaminifu kwa yote atendayo.
PSA 33:5 Mwenyezi Mungu hupenda uadilifu na haki; dunia imejaa upendo wake usiokoma.
PSA 33:6 Kwa neno la Mwenyezi Mungu mbingu ziliumbwa, jeshi lao la angani likaumbwa kwa pumzi ya kinywa chake.
PSA 33:7 Anayakusanya maji ya bahari kama kwenye chungu; vilindi vya bahari anaviweka katika ghala.
PSA 33:8 Dunia yote na imwogope Mwenyezi Mungu, watu wote wa dunia wamche.
PSA 33:9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa, aliamuru na ikasimama imara.
PSA 33:10 Mwenyezi Mungu huzuia mipango ya mataifa, hupinga makusudi ya mataifa.
PSA 33:11 Lakini mipango ya Mwenyezi Mungu inasimama imara milele, makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.
PSA 33:12 Heri taifa ambalo Mwenyezi Mungu ni Mungu wao, watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.
PSA 33:13 Mwenyezi Mungu hutazama chini kutoka mbinguni na kuwaona wanadamu wote;
PSA 33:14 kutoka maskani mwake huwaangalia wote wanaoishi duniani:
PSA 33:15 yeye ambaye huumba mioyo yao wote, ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda.
PSA 33:16 Hakuna mfalme anayeokoka kwa ukubwa wa jeshi lake; hakuna shujaa anayeokoka kwa wingi wa nguvu zake.
PSA 33:17 Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu, licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa.
PSA 33:18 Lakini macho ya Mwenyezi Mungu yako kwa wale wamchao, kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,
PSA 33:19 ili awaokoe na mauti, na kuwahifadhi wakati wa njaa.
PSA 33:20 Sisi tunamngojea Mwenyezi Mungu kwa matumaini, yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
PSA 33:21 Mioyo yetu humshangilia, kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.
PSA 33:22 Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Mwenyezi Mungu, tunapoliweka tumaini letu kwako.
PSA 34:1 Zaburi ya Daudi, alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki, ambaye alimfukuza, naye akaondoka. Nitamtukuza Mwenyezi Mungu nyakati zote, sifa zake zitakuwa mdomoni mwangu siku zote.
PSA 34:2 Nafsi yangu itajisifu katika Mwenyezi Mungu, walioonewa watasikia na wafurahi.
PSA 34:3 Mtukuzeni Mwenyezi Mungu pamoja nami, naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
PSA 34:4 Nilimtafuta Mwenyezi Mungu naye akanijibu, akaniokoa kwenye hofu zangu zote.
PSA 34:5 Wale wamtazamao hutiwa nuru, nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.
PSA 34:6 Maskini huyu alimwita Mwenyezi Mungu, naye akamsikia, akamwokoa katika taabu zake zote.
PSA 34:7 Malaika wa Mwenyezi Mungu hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa.
PSA 34:8 Onjeni mwone kwamba Mwenyezi Mungu ni mwema; heri mtu yule anayemkimbilia.
PSA 34:9 Mcheni Mwenyezi Mungu enyi watakatifu wake, kwa maana wale wamchao hawapungukiwi na chochote.
PSA 34:10 Wana simba wenye nguvu hutindikiwa na kuona njaa, bali wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu hawatakosa kitu chochote kilicho chema.
PSA 34:11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize, nitawafundisha kumcha Mwenyezi Mungu.
PSA 34:12 Yeyote kati yenu anayependa uzima na kutamani kuziona siku nyingi njema,
PSA 34:13 basi auzuie ulimi wake na mabaya, na midomo yake kutokana na kusema uongo.
PSA 34:14 Aache uovu, atende mema, aitafute amani na kuifuatilia.
PSA 34:15 Macho ya Mwenyezi Mungu huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.
PSA 34:16 Uso wa Mwenyezi Mungu uko kinyume na watendao maovu, ili kufuta kumbukumbu lao duniani.
PSA 34:17 Wenye haki hulia, naye Mwenyezi Mungu huwasikia, huwaokoa katika taabu zao zote.
PSA 34:18 Mwenyezi Mungu yu karibu na waliovunjika moyo, na huwaokoa waliopondeka roho.
PSA 34:19 Mwenye haki ana mateso mengi, lakini Mwenyezi Mungu humwokoa nayo yote,
PSA 34:20 huhifadhi mifupa yake yote, hata mmoja hautavunjika.
PSA 34:21 Ubaya utamuua mtu mwovu, nao adui za mwenye haki watahukumiwa.
PSA 34:22 Mwenyezi Mungu huwakomboa watumishi wake, yeyote anayemkimbilia yeye hatahukumiwa kamwe.
PSA 35:1 Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, pingana na wale wanaopingana nami, upigane na hao wanaopigana nami.
PSA 35:2 Chukua ngao na kigao. Inuka unisaidie.
PSA 35:3 Inua mkuki wako na fumo lako dhidi ya hao wanaonifuatia. Iambie nafsi yangu, “Mimi ni wokovu wako.”
PSA 35:4 Wafedheheshwe na waaibishwe wale wanaotafuta uhai wangu. Wanaofanya shauri kuniangamiza wafukuzwe mbali kwa bumbuazi.
PSA 35:5 Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa Mwenyezi Mungu akiwafukuza.
PSA 35:6 Njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa Mwenyezi Mungu akiwafuatilia.
PSA 35:7 Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo,
PSA 35:8 maafa na yawapate ghafula: wavu walionifichia na uwatege wenyewe, na waanguke katika shimo hilo, kwa maangamizi yao.
PSA 35:9 Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Mwenyezi Mungu na kuufurahia wokovu wake.
PSA 35:10 Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale waliowazidi nguvu, unawaokoa maskini na wahitaji kutokana na wanaowanyang’anya!”
PSA 35:11 Mashahidi wakatili wanainuka, wananiuliza mambo nisiyoyajua.
PSA 35:12 Wananilipa baya kwa jema na kuiacha nafsi yangu ukiwa.
PSA 35:13 Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa gunia na nikajinyenyekeza kwa kufunga. Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,
PSA 35:14 niliendelea kuomboleza kama vile wao ni rafiki au ndugu. Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni kama ninayemwombolezea mama yangu.
PSA 35:15 Lakini nilipojikwaa, walikusanyika kwa shangwe; washambuliaji walijikusanya dhidi yangu bila mimi kujua. Walinisingizia pasipo kukoma.
PSA 35:16 Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki, wamenisagia meno.
PSA 35:17 Ee Bwana, utatazama hadi lini? Niokoe maisha yangu na maangamizi yao, okoa uhai wangu wa thamani kutokana na simba hawa.
PSA 35:18 Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa, nitakusifu katikati ya watu wengi.
PSA 35:19 Usiwaache wale wanaonisimanga, wale ambao ni adui zangu bila sababu; usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu wakonyeze jicho kwa hila.
PSA 35:20 Hawazungumzi kwa amani, bali wanatunga mashtaka ya uongo dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi.
PSA 35:21 Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.”
PSA 35:22 Ee Mwenyezi Mungu, umeona hili, usiwe kimya. Usiwe mbali nami, Ee Bwana.
PSA 35:23 Amka, inuka unitetee! Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.
PSA 35:24 Nihukumu kwa haki yako, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, sawasawa na haki yako; usiwaache wakusimange.
PSA 35:25 Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!” Au waseme, “Tumemmeza.”
PSA 35:26 Wote wanaofurahia dhiki yangu waaibishwe na wachanganyikiwe; hao wanaojiinua dhidi yangu wavikwe aibu na dharau.
PSA 35:27 Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “Mwenyezi Mungu atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.”
PSA 35:28 Ulimi wangu utanena haki yako na sifa zako mchana kutwa.
PSA 36:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Mwenyezi Mungu. Kuna neno moyoni mwangu kutoka kwa Mungu kuhusu hali ya dhambi ya mwovu. Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.
PSA 36:2 Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake.
PSA 36:3 Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu, ameacha kuwa mwenye hekima au kutenda mema.
PSA 36:4 Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya, hujitia katika njia ya dhambi na hakatai lililo baya.
PSA 36:5 Upendo wako, Ee Mwenyezi Mungu, unafika hadi mbinguni, uaminifu wako hadi kwenye anga.
PSA 36:6 Haki yako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama kilindi kikuu. Ee Mwenyezi Mungu, wewe huwahifadhi mwanadamu na mnyama.
PSA 36:7 Upendo wako usiokoma ni wa thamani mno! Watu wakuu na wadogo hujificha uvulini wa mabawa yako.
PSA 36:8 Wanajifurahisha katika wingi ulio nyumbani mwako, nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.
PSA 36:9 Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima, katika nuru yako twaona nuru.
PSA 36:10 Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe, haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.
PSA 36:11 Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu, wala mkono wa mwovu usinifukuze.
PSA 36:12 Tazama jinsi watenda maovu walivyoanguka: wametupwa chini, hawawezi kuinuka!
PSA 37:1 Zaburi ya Daudi. Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya,
PSA 37:2 kwa maana watanyauka upesi kama majani, watakufa upesi kama mimea ya kijani.
PSA 37:3 Mtumaini Mwenyezi Mungu na utende yaliyo mema. Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.
PSA 37:4 Jifurahishe katika Mwenyezi Mungu naye atakupa haja za moyo wako.
PSA 37:5 Mkabidhi Mwenyezi Mungu njia yako, mtumaini yeye, naye atatenda hili:
PSA 37:6 Yeye atafanya haki yako ing’ae kama mapambazuko, na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.
PSA 37:7 Tulia mbele za Mwenyezi Mungu na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu.
PSA 37:8 Epuka hasira na uache ghadhabu; usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.
PSA 37:9 Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini Mwenyezi Mungu watairithi nchi.
PSA 37:10 Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana.
PSA 37:11 Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele.
PSA 37:12 Waovu hula njama dhidi ya wenye haki na kuwasagia meno,
PSA 37:13 bali Bwana huwacheka waovu, kwa sababu anajua siku yao inakuja.
PSA 37:14 Waovu hufuta upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwaua wale ambao njia zao ni nyofu.
PSA 37:15 Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa.
PSA 37:16 Bora kidogo walicho nacho wenye haki kuliko wingi wa mali ya waovu wengi;
PSA 37:17 kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini Mwenyezi Mungu humtegemeza mwenye haki.
PSA 37:18 Mwenyezi Mungu anazifahamu siku za wanyofu, na urithi wao utadumu milele.
PSA 37:19 Siku za maafa hawatanyauka, siku za njaa watafurahia wingi wa vitu.
PSA 37:20 Lakini waovu wataangamia: Adui za Mwenyezi Mungu watakuwa kama uzuri wa mashamba, watatoweka, watatoweka kama moshi.
PSA 37:21 Waovu hukopa na hawalipi, bali wenye haki hutoa kwa ukarimu.
PSA 37:22 Wale wanaobarikiwa na Mwenyezi Mungu watairithi nchi, bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali.
PSA 37:23 Kama Mwenyezi Mungu akipendezwa na njia ya mtu, yeye huimarisha hatua zake,
PSA 37:24 ajapojikwaa, hataanguka, kwa maana Mwenyezi Mungu humtegemeza kwa mkono wake.
PSA 37:25 Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa au watoto wao wakiombaomba chakula.
PSA 37:26 Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti. Watoto wao watabarikiwa.
PSA 37:27 Acha ubaya na utende wema, nawe utaishi katika nchi milele.
PSA 37:28 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu huwapenda wenye haki naye hatawaacha waaminifu wake. Watalindwa milele, lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali.
PSA 37:29 Wenye haki watairithi nchi, na kuishi humo milele.
PSA 37:30 Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima, nao ulimi wake huzungumza lililo haki.
PSA 37:31 Torati ya Mungu wake imo moyoni mwake; nyayo zake hazitelezi.
PSA 37:32 Watu waovu huvizia wenye haki, wakitafuta kuwaua;
PSA 37:33 lakini Mwenyezi Mungu hatawaacha mikononi mwao wala hatawaacha wahukumiwe kuwa wakosa wanaposhtakiwa.
PSA 37:34 Mngojee Mwenyezi Mungu, na uishike njia yake. Naye atakutukuza uirithi nchi, waovu watakapokatiliwa mbali, utaliona hilo.
PSA 37:35 Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi kama mwerezi wa Lebanoni,
PSA 37:36 lakini alitoweka upesi na hakuonekana, ingawa nilimtafuta, hakupatikana.
PSA 37:37 Watafakari watu wasio na hatia, wachunguze watu wakamilifu, kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani.
PSA 37:38 Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa, mafanikio yao yatakatiliwa mbali.
PSA 37:39 Wokovu wa wenye haki hutoka kwa Mwenyezi Mungu, yeye ni ngome yao wakati wa shida.
PSA 37:40 Mwenyezi Mungu huwasaidia na kuwaokoa, huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi, kwa maana wanamkimbilia.
PSA 38:1 Zaburi ya Daudi. Maombi. Ee Mwenyezi Mungu, usinikemee katika hasira yako, wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.
PSA 38:2 Kwa kuwa mishale yako imenichoma, na mkono wako umenipiga.
PSA 38:3 Hakuna afya mwilini mwangu kwa sababu ya ghadhabu yako, mifupa yangu haina uzima kwa sababu ya dhambi zangu.
PSA 38:4 Maovu yangu yamenifunika kama mzigo mzito mno.
PSA 38:5 Majeraha yangu yameoza na yananuka, kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
PSA 38:6 Nimeinamishwa chini na kushushwa sana, mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
PSA 38:7 Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo, hakuna afya mwilini mwangu.
PSA 38:8 Nimedhoofika na kupondwa kabisa, nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.
PSA 38:9 Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku yako wazi mbele zako, kutamani kwangu sana hakufichiki mbele zako.
PSA 38:10 Moyo wangu unapigapiga, nguvu zangu zimeniishia; hata macho yangu yametiwa giza.
PSA 38:11 Rafiki na wenzangu wananikwepa kwa sababu ya majeraha yangu; majirani wangu wanakaa mbali nami.
PSA 38:12 Wale wanaotafuta uhai wangu wanatega mitego yao, wale ambao wangetaka kunidhuru huongea kuhusu maangamizi yangu; hupanga hila mchana kutwa.
PSA 38:13 Mimi ni kama kiziwi, asiyeweza kusikia, ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake;
PSA 38:14 nimekuwa kama mtu asiyesikia, ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.
PSA 38:15 Ee Mwenyezi Mungu, ninakungojea wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, utajibu.
PSA 38:16 Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie, wala wajitukuze juu yangu mguu wangu unapoteleza.”
PSA 38:17 Kwa maana ninakaribia kuanguka, na maumivu yangu yananiandama siku zote.
PSA 38:18 Naungama uovu wangu, ninataabishwa na dhambi yangu.
PSA 38:19 Wengi wamekua adui zangu bila sababu; wale wanaonichukia bure ni wengi.
PSA 38:20 Wanaolipa wema wangu kwa maovu hunisingizia ninapofuata lililo jema.
PSA 38:21 Ee Mwenyezi Mungu, usiniache, usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.
PSA 38:22 Ee Bwana Mwokozi wangu, uje upesi kunisaidia.
PSA 39:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi. Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi; nitaweka lijamu kinywani mwangu wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.”
PSA 39:2 Lakini niliponyamaza na kutulia, hata pasipo kusema lolote jema, uchungu wangu uliongezeka.
PSA 39:3 Moyo wangu ulipata moto ndani yangu, nilipotafakari, moto uliwaka, ndipo nikasema kwa ulimi wangu:
PSA 39:4 “Ee Mwenyezi Mungu, nijulishe mwisho wa maisha yangu na hesabu ya siku zangu; nijalie kujua jinsi maisha yangu yanavyopita upesi.
PSA 39:5 Umefanya maisha yangu mafupi kama nyanda; muda wangu wa kuishi ni kama hauna thamani kwako. Maisha ya kila mwanadamu ni kama pumzi.
PSA 39:6 Hakika kila binadamu ni kama njozi aendapo huku na huko: hujishughulisha na mengi, lakini ni ubatili; anakusanya mali nyingi, wala hajui ni nani atakayejifaidi nayo.
PSA 39:7 “Lakini sasa Bwana, nitafute nini? Tumaini langu ni kwako.
PSA 39:8 Niokoe kutoka makosa yangu yote, usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.
PSA 39:9 Nilinyamaza, sikufumbua kinywa changu, kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili.
PSA 39:10 Niondolee mjeledi wako, nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako.
PSA 39:11 Unakemea na kuadhibu wanadamu kwa ajili ya dhambi zao; unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo: kila mwanadamu ni kama pumzi tu.
PSA 39:12 “Ee Mwenyezi Mungu, usikie maombi yangu, usikie kilio changu unisaidie, usiwe kiziwi kwa kulia kwangu. Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni, mhamiaji, kama walivyokuwa baba zangu wote,
PSA 39:13 Tazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena kabla sijaondoka na nisiwepo tena.”
PSA 40:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Nilimngoja Mwenyezi Mungu kwa saburi, naye akanijia na kusikia kilio changu.
PSA 40:2 Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu, kutoka matope na utelezi; akaiweka miguu yangu juu ya mwamba na kunipa mahali imara pa kusimama.
PSA 40:3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa na kuweka tumaini lao kwa Mwenyezi Mungu.
PSA 40:4 Heri mtu yule amfanyaye Mwenyezi Mungu kuwa tumaini lake, asiyewategemea wenye kiburi, wale wenye kugeukia miungu ya uongo.
PSA 40:5 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, umefanya mambo mengi ya ajabu. Mambo uliyopanga kwa ajili yetu hakuna awezaye kukuhesabia; kama ningesema na kuyaelezea, yangekuwa mengi mno kuyatangaza.
PSA 40:6 Dhabihu na sadaka hukuvitaka, lakini umefungua masikio yangu; sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukuzihitaji.
PSA 40:7 Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja: imeandikwa kunihusu katika kitabu.
PSA 40:8 Ee Mungu wangu, natamani kuyafanya mapenzi yako; sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”
PSA 40:9 Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa, sikufunga mdomo wangu, Ee Mwenyezi Mungu, kama ujuavyo.
PSA 40:10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu; ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha upendo wako na kweli yako mbele ya kusanyiko kubwa.
PSA 40:11 Ee Mwenyezi Mungu, usinizuilie huruma zako, upendo wako na kweli yako daima vinilinde.
PSA 40:12 Kwa maana taabu zisizohesabika zimenizunguka, dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona. Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu, nao moyo unazimia ndani yangu.
PSA 40:13 Ee Mwenyezi Mungu, uwe radhi kuniokoa; Ee Mwenyezi Mungu, njoo hima unisaidie.
PSA 40:14 Wote wanaotafuta kuniua, waaibishwe na kufadhaishwa; wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, wafukuzwe mbali kwa aibu.
PSA 40:15 Wale wanaoniambia, “Aha! Aha!” wafadhaishwe na iwe aibu yao.
PSA 40:16 Lakini wote wanaokutafuta washangilie na kukufurahia, wale wanaoupenda wokovu wako siku zote waseme, “Mwenyezi Mungu atukuzwe!”
PSA 40:17 Lakini mimi bado ni maskini na mhitaji; Bwana na anifikirie. Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu; Ee Mungu wangu, usikawie.
PSA 41:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Heri mtu yule anayemjali mnyonge, Mwenyezi Mungu atamwokoa wakati wa shida.
PSA 41:2 Mwenyezi Mungu atamlinda na kuyahifadhi maisha yake, atambariki katika nchi na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.
PSA 41:3 Mwenyezi Mungu atamtegemeza akiwa mgonjwa kitandani, na atamwinua kutoka kitandani mwake.
PSA 41:4 Nilisema, “Ee Mwenyezi Mungu nihurumie, niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”
PSA 41:5 Adui zangu wanasema kwa hila, “Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”
PSA 41:6 Kila anapokuja mtu kunitazama, huzungumza uongo, huku moyo wake ukikusanya masingizio; kisha huondoka na kuyasambaza.
PSA 41:7 Adui zangu wote hunong’onezana dhidi yangu, hao huniwazia mabaya sana, wakisema,
PSA 41:8 “Ugonjwa mbaya sana umempata, kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”
PSA 41:9 Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini, yule aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake.
PSA 41:10 Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, nihurumie, ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.
PSA 41:11 Najua kwamba wapendezwa nami, kwa kuwa adui yangu hanishindi.
PSA 41:12 Katika uadilifu wangu unanitegemeza na kuniweka kwenye uwepo wako milele.
PSA 41:13 Mtukuzeni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele.
PSA 42:1 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora. Kama ayala anavyoonea shauku vijito vya maji, ndivyo nafsi yangu inavyokuonea shauku, Ee Mungu.
PSA 42:2 Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai. Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu?
PSA 42:3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu usiku na mchana, huku watu wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?”
PSA 42:4 Mambo haya nayakumbuka ninapoimimina nafsi yangu: Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu, nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu, kwa kelele za shangwe na za shukrani katikati ya umati wa watu waliosherehekea.
PSA 42:5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa kuwa bado nitamsifu, Mwokozi wangu na Mungu wangu.
PSA 42:6 Nafsi yangu inasononeka ndani yangu; kwa hiyo nitakukumbuka kutoka nchi ya Yordani, katika vilele vya Hermoni, kutoka Mlima Mizari.
PSA 42:7 Kilindi huita kilindi, katika ngurumo za maporomoko ya maji yako; mawimbi yako yote pamoja na viwimbi vimepita juu yangu.
PSA 42:8 Mwenyezi Mungu huelekeza upendo wake mchana, wimbo wake uko nami usiku: maombi kwa Mungu wa uzima wangu.
PSA 42:9 Ninamwambia Mungu Mwamba wangu, “Kwa nini umenisahau? Kwa nini niendelee kuomboleza, nikiteswa na adui?”
PSA 42:10 Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali adui zangu wanaponidhihaki, wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?”
PSA 42:11 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa kuwa bado nitamsifu, Mwokozi wangu na Mungu wangu.
PSA 43:1 Ee Mungu unihukumu, nitetee dhidi ya taifa lisilomcha Mungu, niokoe na watu wadanganyifu na waovu.
PSA 43:2 Wewe ni Mungu ngome yangu. Kwa nini umenikataa? Kwa nini niendelee kuomboleza, nikidhulumiwa na adui?
PSA 43:3 Tuma hima nuru yako na kweli yako viniongoze; na vinilete hadi mlima wako mtakatifu, mahali unapoishi.
PSA 43:4 Ndipo nitaenda madhabahuni pa Mungu, kwa Mungu, furaha yangu na shangwe yangu. Nitakusifu kwa kinubi, Ee Mungu, Mungu wangu.
PSA 43:5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu Mwokozi wangu na Mungu wangu.
PSA 44:1 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora. Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu, baba zetu wametueleza yale uliyotenda katika siku zao, siku za kale.
PSA 44:2 Kwa mkono wako uliwafukuza mataifa na ukawapanda baba zetu, uliangamiza mataifa na kuwastawisha baba zetu.
PSA 44:3 Sio kwa upanga wao waliipata nchi, wala si mkono wao uliwapatia ushindi; ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume, na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwapenda.
PSA 44:4 Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu, unayeamuru ushindi kwa Yakobo.
PSA 44:5 Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu; kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu.
PSA 44:6 Siutumaini upinde wangu, upanga wangu hauniletei ushindi;
PSA 44:7 bali wewe unatupatia ushindi juu ya adui zetu, unawaaibisha watesi wetu.
PSA 44:8 Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa, nasi tutalisifu jina lako milele.
PSA 44:9 Lakini sasa umetukataa na kutudhili, wala huendi tena na jeshi letu.
PSA 44:10 Umetufanya tukimbie mbele ya adui, nao watesi wetu wametuteka nyara.
PSA 44:11 Umetuacha tutafunwe kama kondoo na umetutawanya katika mataifa.
PSA 44:12 Umewauza watu wako kwa fedha kidogo, wala hukupata faida yoyote kwa mauzo yao.
PSA 44:13 Umetufanya lawama kwa majirani zetu, dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka.
PSA 44:14 Umetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa; mataifa hututikisia vichwa vyao.
PSA 44:15 Fedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa, na uso wangu umejaa aibu tele,
PSA 44:16 kwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana, kwa sababu ya adui, ambaye anatamani kulipiza kisasi.
PSA 44:17 Hayo yote yametutokea, ingawa tulikuwa hatujakusahau wala hatujaenda kinyume na agano lako.
PSA 44:18 Mioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma; nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako.
PSA 44:19 Lakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha, na ukatufunika kwa giza nene.
PSA 44:20 Kama tungekuwa tumelisahau jina la Mungu wetu au kunyooshea mikono yetu kwa mungu mgeni,
PSA 44:21 je, si Mungu angegundua hili, kwa kuwa anazijua siri za moyo?
PSA 44:22 Hata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.
PSA 44:23 Amka, Ee Bwana! Kwa nini unalala? Zinduka! Usitukatae milele.
PSA 44:24 Kwa nini unauficha uso wako na kusahau taabu na mateso yetu?
PSA 44:25 Tumeshushwa hadi mavumbini, miili yetu imegandamana na ardhi.
PSA 44:26 Inuka na utusaidie, utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.
PSA 45:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Yungiyungi”. Utenzi wa wana wa Kora. Wimbo wa arusi. Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema ninapomsimulia mfalme mabeti yangu; ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi.
PSA 45:2 Wewe ni bora kuliko watu wengine wote na midomo yako imepakwa neema, kwa kuwa Mungu amekubariki milele.
PSA 45:3 Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu, jivike fahari na utukufu.
PSA 45:4 Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi, kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki, mkono wako wa kuume na uoneshe matendo ya kutisha.
PSA 45:5 Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme, mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako.
PSA 45:6 Ee Mungu, kiti chako cha enzi kitadumu milele na milele, fimbo ya utawala wa haki itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako.
PSA 45:7 Unaipenda haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako, kwa kukupaka mafuta ya furaha.
PSA 45:8 Mavazi yako yote yana harufu nzuri ya manemane, udi na mdalasini; kutoka majumba ya kifalme yaliyopambwa kwa pembe za ndovu, sauti za vinanda vya nyuzi zinakufanya ufurahi.
PSA 45:9 Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa; kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri.
PSA 45:10 Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio: Sahau watu wako na nyumba ya baba yako.
PSA 45:11 Mfalme ameshangazwa na uzuri wako; mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako.
PSA 45:12 Binti Tiro atakuletea zawadi, watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako.
PSA 45:13 Ufahari wote una binti mfalme katika chumba chake; vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.
PSA 45:14 Anaongozwa kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa, mabikira wenzake wanamfuata na wanaletwa kwako.
PSA 45:15 Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha, na kuingia katika jumba la mfalme.
PSA 45:16 Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu, mtawafanya wakuu katika nchi yote.
PSA 45:17 Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote, kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.
PSA 46:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
PSA 46:2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa, na milima ianguke kilindini cha bahari,
PSA 46:3 hata maji yake yakinguruma na kuumuka, na milima itetemeke kwa mawimbi yake.
PSA 46:4 Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu, mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi.
PSA 46:5 Mungu yuko katikati yake, hautaanguka, Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
PSA 46:6 Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka, yeye hupaza sauti yake, dunia ikayeyuka.
PSA 46:7 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni yu pamoja nasi; Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
PSA 46:8 Njooni mkaone kazi za Mwenyezi Mungu jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
PSA 46:9 Anakomesha vita hata miisho ya dunia, anakata upinde na kuvunjavunja mkuki, anateketeza ngao kwa moto.
PSA 46:10 “Tulieni, mjue kwamba mimi ndimi Mungu; nitatukuzwa katikati ya mataifa, nitatukuzwa katika dunia.”
PSA 46:11 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni yu pamoja nasi; Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
PSA 47:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Pigeni makofi, enyi mataifa yote, mpigieni Mungu kelele za shangwe!
PSA 47:2 Jinsi gani alivyo wa kutisha, Mwenyezi Mungu Aliye Juu Sana, Mfalme mkuu juu ya dunia yote!
PSA 47:3 Ametiisha mataifa chini yetu, watu wengi chini ya miguu yetu.
PSA 47:4 Alituchagulia urithi wetu, fahari ya Yakobo, aliyempenda.
PSA 47:5 Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Mwenyezi Mungu kwa sauti za tarumbeta.
PSA 47:6 Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa, mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa.
PSA 47:7 Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote, mwimbieni zaburi za sifa.
PSA 47:8 Mungu anayatawala mataifa, Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi kitakatifu.
PSA 47:9 Wakuu wa mataifa wanakusanyika kama watu wa Mungu wa Ibrahimu, kwa kuwa wafalme wa dunia ni mali ya Mungu; yeye ametukuka sana.
PSA 48:1 Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Mwenyezi Mungu ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, katika mji wa Mungu wetu, mlima wake mtakatifu.
PSA 48:2 Ni mzuri katika kuinuka juu kwake, furaha ya dunia yote. Kama vilele vya juu vya Safoni ni Mlima Sayuni, mji wa Mfalme Mkuu.
PSA 48:3 Mungu yuko katika ngome zake; amejionesha mwenyewe kuwa ngome yake.
PSA 48:4 Wafalme walipounganisha nguvu, waliposonga mbele pamoja,
PSA 48:5 walimwona, wakashangaa, wakakimbia kwa hofu.
PSA 48:6 Kutetemeka kuliwashika huko, maumivu kama ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa.
PSA 48:7 Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi zilizovunjwa na upepo wa mashariki.
PSA 48:8 Kama tulivyokuwa tumesikia, ndivyo tulivyoona katika mji wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, katika mji wa Mungu wetu: Mungu ataufanya uwe salama milele.
PSA 48:9 Ee Mungu, hekaluni mwako tunatafakari upendo wako usiokoma.
PSA 48:10 Ee Mungu, kama jina lako lilivyo, sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia, mkono wako wa kuume umejazwa na haki.
PSA 48:11 Mlima Sayuni unashangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako.
PSA 48:12 Tembeeni katika Sayuni, uzungukeni mji, hesabuni minara yake;
PSA 48:13 yatafakarini vyema maboma yake, angalieni ngome zake, ili mpate kusimulia habari zake kwa kizazi kijacho.
PSA 48:14 Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele; atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.
PSA 49:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Sikieni haya, enyi mataifa yote, sikilizeni, ninyi wote mnaoishi dunia hii.
PSA 49:2 Wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini pamoja:
PSA 49:3 Kinywa changu kitasema maneno ya hekima, usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu.
PSA 49:4 Nitatega sikio langu nisikilize mithali, nitafafanua kitendawili kwa zeze:
PSA 49:5 Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja, wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka,
PSA 49:6 wale wanaotegemea mali yao na kujivunia utajiri wao mwingi?
PSA 49:7 Hakuna mwanadamu yeyote awezaye kuukomboa uhai wa mwingine, au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.
PSA 49:8 Fidia ya uhai ni gharama kubwa, hakuna malipo yoyote yanayotosha,
PSA 49:9 ili aishi milele na asione uharibifu.
PSA 49:10 Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa; wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia na kuwaachia wengine mali yao.
PSA 49:11 Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele, makao yao vizazi vyote; ingawa walikuwa na mashamba na kuyaita kwa majina yao.
PSA 49:12 Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu; anafanana na mnyama aangamiaye.
PSA 49:13 Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe, pia ya wafuasi wao, waliothibitisha misemo yao.
PSA 49:14 Kama kondoo, wamewekewa kwenda kaburini, nacho kifo kitawala. Wanyofu watawatawala asubuhi, maumbile yao yataozea kaburini, mbali na majumba yao makubwa ya fahari.
PSA 49:15 Lakini Mungu atakomboa uhai wangu dhidi ya kaburi; hakika atanichukua kwake.
PSA 49:16 Usitishwe mtu anapotajirika, fahari ya nyumba yake inapoongezeka,
PSA 49:17 kwa maana hatachukua chochote atakapokufa, fahari yake haitashuka pamoja naye.
PSA 49:18 Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri, na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa,
PSA 49:19 atajiunga na kizazi cha baba zake, ambao hawataona kamwe nuru ya uzima.
PSA 49:20 Wanadamu wenye utajiri bila ufahamu ni kama wanyama wanaoangamia.
PSA 50:1 Zaburi ya Asafu. Mwenye Nguvu, Mungu, Mwenyezi Mungu, asema na kuiita dunia, tangu mawio ya jua hadi mahali pake liendapo kutua.
PSA 50:2 Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu, Mungu anaangaza.
PSA 50:3 Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya, moto uteketezao unamtangulia, akiwa amezungukwa na tufani kali.
PSA 50:4 Anaziita mbingu zilizo juu, na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:
PSA 50:5 “Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu, waliofanya agano nami kwa dhabihu.”
PSA 50:6 Nazo mbingu zinatangaza haki yake, kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.
PSA 50:7 “Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema, ee Israeli, nami nitashuhudia dhidi yenu: Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.
PSA 50:8 Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako, au sadaka zako za kuteketezwa, ambazo daima ziko mbele zangu.
PSA 50:9 Sina haja na fahali wa banda lako, au mbuzi wa zizi lako.
PSA 50:10 Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu, na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.
PSA 50:11 Ninamjua kila ndege mlimani, nao viumbe wa kondeni ni wangu.
PSA 50:12 Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi, kwa maana ulimwengu ni wangu, na vyote vilivyomo.
PSA 50:13 Je, mimi hula nyama ya mafahali au kunywa damu ya mbuzi?
PSA 50:14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu, timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,
PSA 50:15 na uniite siku ya taabu; nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”
PSA 50:16 Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema: “Una haki gani kunena sheria zangu au kuchukua agano langu mdomoni mwako?
PSA 50:17 Unachukia mafundisho yangu na kuyatupilia mbali maneno yangu.
PSA 50:18 Unapomwona mwizi, unaungana naye, unapiga kura yako pamoja na wazinzi.
PSA 50:19 Unakitumia kinywa chako kunena maovu, na kuuongoza ulimi wako kwa hila.
PSA 50:20 Unamsengenya ndugu yako bila kukoma, na kumsingizia mwana wa mama yako.
PSA 50:21 Mambo haya unayafanya, nami nimekaa kimya, ukadhani Mimi ni kama wewe kabisa. Lakini nitakukemea na kuweka mashtaka mbele yako.
PSA 50:22 “Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu, ama sivyo nitawararua vipande vipande, wala hapatakuwa na yeyote wa kuwaokoa:
PSA 50:23 Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi, naye aiandaa njia yake ili nimwoneshe wokovu wa Mungu.”
PSA 51:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba. Ee Mungu, unihurumie, kwa kadiri ya upendo wako usiokoma, kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu.
PSA 51:2 Unioshe na uovu wangu wote na unitakase dhambi yangu.
PSA 51:3 Kwa maana najua makosa yangu, na dhambi yangu iko mbele yangu daima.
PSA 51:4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi na kufanya yaliyo mabaya machoni pako, ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena, na kuwa na haki unapotoa hukumu.
PSA 51:5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi, mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu.
PSA 51:6 Hakika wewe wapendezwa na kweli inayotoka moyoni; wanifundisha hekima ndani ya moyo wangu.
PSA 51:7 Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi, unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.
PSA 51:8 Unipe kusikia furaha na shangwe, mifupa uliyoiponda na ifurahi.
PSA 51:9 Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu, na uufute uovu wangu wote.
PSA 51:10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.
PSA 51:11 Usinitupe kutoka mbele zako wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.
PSA 51:12 Unirudishie furaha ya wokovu wako, unipe roho ya utii, ili initegemeze.
PSA 51:13 Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watarejea kwako.
PSA 51:14 Ee Mungu, Mungu uniokoaye, niokoe na hatia ya kumwaga damu, nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.
PSA 51:15 Ee Bwana, fungua midomo yangu, na kinywa changu kitatangaza sifa zako.
PSA 51:16 Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningeileta; hufurahii sadaka za kuteketezwa.
PSA 51:17 Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; moyo uliovunjika wenye toba, ee Mungu, hutaudharau.
PSA 51:18 Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi, ukazijenge upya kuta za Yerusalemu.
PSA 51:19 Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki, sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana, pia mafahali watatolewa madhabahuni mwako.
PSA 52:1 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi ameenda nyumbani mwa Ahimeleki.” Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya? Kwa nini unajivuna mchana kutwa, wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?
PSA 52:2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi. Ni kama wembe mkali, ninyi mnaofanya hila.
PSA 52:3 Unapenda mabaya kuliko mema, uongo kuliko kusema kweli.
PSA 52:4 Unapenda kila neno lenye kudhuru, ewe ulimi wenye hila!
PSA 52:5 Hakika Mungu atakushusha chini kwa maangamizi ya milele: atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu kutoka hema lako, atakung’oa kutoka nchi ya walio hai.
PSA 52:6 Wenye haki wataona na kuogopa; watamcheka, wakisema,
PSA 52:7 “Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake, bali alitumainia wingi wa utajiri wake, na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”
PSA 52:8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni unaostawi katika nyumba ya Mungu, nautegemea upendo wa Mungu usiokoma milele na milele.
PSA 52:9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda, nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema. Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.
PSA 53:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi. Utenzi wa Daudi. Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa, hakuna hata mmoja atendaye mema.
PSA 53:2 Mungu anawachungulia wanadamu chini kutoka mbinguni aone kama wako wenye akili, wowote wanaomtafuta Mungu.
PSA 53:3 Kila mmoja amegeukia mbali, wameharibika wote pamoja, hakuna atendaye mema. Naam, hakuna hata mmoja!
PSA 53:4 Je, watendao maovu kamwe hawatajifunza: wale ambao huwala watu wangu kama watu walavyo mkate, hao ambao hawamwiti Mungu?
PSA 53:5 Hapo waliingiwa na hofu kuu, ambapo hapakuwa na hofu. Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia; uliwaaibisha, kwa sababu Mungu aliwadharau.
PSA 53:6 Laiti wokovu wa Israeli ungekuja kutoka Sayuni! Mungu anaporejesha wafungwa wa watu wake, Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!
PSA 54:1 Kwa mwimbishaji. Na ala za nyuzi za uimbaji. Utenzi wa Daudi. Wakati Wazifu walimwendea Sauli na kumjulisha, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu?” Ee Mungu uniokoe kwa jina lako, unifanyie hukumu kwa uwezo wako.
PSA 54:2 Ee Mungu, sikia maombi yangu, usikilize maneno ya kinywa changu.
PSA 54:3 Wageni wananishambulia, watu wakatili wanayatafuta maisha yangu, watu wasiomjali Mungu.
PSA 54:4 Hakika Mungu ni msaada wangu, Bwana ndiye anayenitegemeza.
PSA 54:5 Mabaya na yawarudie wale wanaonisingizia, kwa uaminifu wako uwaangamize.
PSA 54:6 Nitakutolea dhabihu za hiari; Ee Mwenyezi Mungu, nitalisifu jina lako kwa kuwa ni vyema.
PSA 54:7 Kwa maana ameniokoa katika shida zangu zote, na macho yangu yamewatazama adui zangu kwa ushindi.
PSA 55:1 Kwa mwimbishaji. Na ala za uimbaji. Utenzi wa Daudi. Ee Mungu, sikiliza maombi yangu, wala usidharau hoja yangu.
PSA 55:2 Nisikie na unijibu. Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa
PSA 55:3 kwa sauti ya adui, kwa kukaziwa macho na waovu, kwa sababu wananiletea mateso juu yangu na kunitukana kwa hasira zao.
PSA 55:4 Moyo wangu umejaa uchungu, hofu za mauti zimenishambulia.
PSA 55:5 Woga na kutetemeka vimenizunguka, hofu kuu imenigharikisha.
PSA 55:6 Nilisema, “Laiti ningekuwa na mabawa ya njiwa! Ningeruka niende mbali kupumzika.
PSA 55:7 Ningetorokea mbali sana na kukaa jangwani,
PSA 55:8 ningeharakisha kwenda mahali pa salama, mbali na tufani kali na dhoruba.”
PSA 55:9 Ee Bwana, uwatahayarishe waovu na uwachanganyishie semi zao, maana nimeona jeuri na ugomvi mjini.
PSA 55:10 Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake, uovu na dhuluma vimo ndani yake.
PSA 55:11 Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini, vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake.
PSA 55:12 Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia, kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu, ningejificha asinione.
PSA 55:13 Kumbe ni wewe, mwenzangu, mshiriki na rafiki yangu wa karibu,
PSA 55:14 ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri, tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu.
PSA 55:15 Kifo na kiwajie adui zangu ghafula, na washuke Kuzimu wangali hai, kwa maana uovu uko ndani yao.
PSA 55:16 Lakini ninamwita Mungu, naye Mwenyezi Mungu huniokoa.
PSA 55:17 Jioni, asubuhi na adhuhuri ninalia kwa huzuni, naye husikia sauti yangu.
PSA 55:18 Huniokoa nikawa salama katika vita vilivyopangwa dhidi yangu, ingawa watu wengi hunipinga.
PSA 55:19 Mungu anayemiliki milele, atawasikia na kuwaadhibu, watu ambao hawabadilishi njia zao, wala hawana hofu ya Mungu.
PSA 55:20 Mwenzangu hushambulia rafiki zake, naye huvunja agano lake.
PSA 55:21 Mazungumzo yake ni laini kama siagi, hata hivyo vita vimo moyoni mwake. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.
PSA 55:22 Mtwike Mwenyezi Mungu fadhaa zako, naye atakutegemeza, hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.
PSA 55:23 Lakini wewe, Ee Mungu, utawashusha waovu katika shimo la uharibifu. Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila, hawataishi nusu ya siku zao. Lakini mimi ninakutumaini wewe.
PSA 56:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali”. Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi. Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali; mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.
PSA 56:2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa, wengi wananishambulia kwa kiburi chao.
PSA 56:3 Wakati ninaogopa, nitakutumaini wewe.
PSA 56:4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu, katika Mungu ninatumaini, sitaogopa. Mwanadamu mwenye kufa atanitenda nini?
PSA 56:5 Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu, siku zote wanapanga njama za kunidhuru.
PSA 56:6 Wananifanyia hila, wanajificha, wanatazama hatua zangu, wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.
PSA 56:7 Wasiepuke kwa vyovyote, Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa.
PSA 56:8 Andika maombolezo yangu; andika machozi yangu katika kitabu chako: je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?
PSA 56:9 Ndipo adui zangu watarudi nyuma ninapoita msaada. Kwa hili nitajua kwamba Mungu yuko upande wangu.
PSA 56:10 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu, katika Mwenyezi Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
PSA 56:11 katika Mungu ninatumaini, sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
PSA 56:12 Ee Mungu, nina nadhiri kwako, nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.
PSA 56:13 Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti na miguu yangu kwenye kujikwaa, ili niweze kuenenda mbele za Mungu katika nuru ya uzima.
PSA 57:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi. Baada ya kumponyoka Sauli pangoni. Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie, kwa maana nafsi yangu inakukimbilia. Chini ya uvuli wa mabawa yako nitakimbilia hadi maafa yapite.
PSA 57:2 Namlilia Mungu Aliye Juu Sana, Mungu anayetimiza makusudi yake kwangu.
PSA 57:3 Hutumana msaada kutoka mbinguni na kuniokoa, akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali; Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.
PSA 57:4 Niko katikati ya simba; nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kali, watu ambao meno yao ni mikuki na mishale, ambao ndimi zao ni panga kali.
PSA 57:5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote.
PSA 57:6 Waliitegea miguu yangu nyavu, nikachoshwa na dhiki. Wamechimba shimo katika njia yangu, lakini wametumbukia humo wao wenyewe.
PSA 57:7 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa nyimbo.
PSA 57:8 Amka, nafsi yangu! Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko.
PSA 57:9 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kati ya mataifa; nitaimba habari zako, kati ya jamaa za watu.
PSA 57:10 Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni, uaminifu wako unazifikia anga.
PSA 57:11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni, utukufu wako na uwe duniani pote.
PSA 58:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi. Enyi watawala, je, kweli mwanena kwa haki? Je, mnahukumu kwa unyofu miongoni mwa watu?
PSA 58:2 La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu, na mikono yenu hueneza jeuri duniani.
PSA 58:3 Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao, toka tumboni mwa mama zao ni wakaidi na husema uongo.
PSA 58:4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka, kama ile ya fira ambaye ameziba masikio yake,
PSA 58:5 ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi, hata kama mganga angecheza kwa ustadi kiasi gani.
PSA 58:6 Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao; Ee Mwenyezi Mungu, vunja meno makali ya hao simba!
PSA 58:7 Na watoweke kama maji yanavyotiririka; wanapovuta pinde zao, mishale yao na iwe butu.
PSA 58:8 Na wawe kama konokono anayeyeyuka akitembea, kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu.
PSA 58:9 Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba, zikiwa mbichi au kavu, waovu watakuwa wamefagiliwa mbali.
PSA 58:10 Wenye haki watafurahi wakilipizwa kisasi, watakapochovya nyayo zao katika damu ya waovu.
PSA 58:11 Ndipo wanadamu watasema, “Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu, hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”
PSA 59:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi. Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue. Ee Mungu, uniokoe na adui zangu, unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.
PSA 59:2 Uniponye na watu watendao maovu, uniokoe kutokana na wanaomwaga damu.
PSA 59:3 Tazama wanavyonivizia! Watu wakali wananifanyia hila, ingawa Ee Mwenyezi Mungu, mimi sijakosea wala kutenda dhambi.
PSA 59:4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia. Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!
PSA 59:5 Ee Mungu, Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, uliye Mungu wa Israeli, zinduka uyaadhibu mataifa yote; usioneshe huruma kwa wasaliti waovu.
PSA 59:6 Hurudi wakati wa jioni, wakibweka kama mbwa, wakiuzurura mji.
PSA 59:7 Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao, hutema panga kutoka midomo yao, nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”
PSA 59:8 Lakini wewe, Mwenyezi Mungu, uwacheke; unayadharau mataifa hayo yote.
PSA 59:9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe, wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
PSA 59:10 Mungu wangu unayenipenda. Mungu atanitangulia, naye atanifanya niwachekelee wale wanaonisingizia.
PSA 59:11 Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu, au sivyo watu wangu watasahau. Katika uwezo wako wafanye watangetange na uwashushe chini.
PSA 59:12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao, kwa ajili ya maneno ya midomo yao, waache wanaswe katika kiburi chao. Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,
PSA 59:13 wateketeze katika ghadhabu, wateketeze hadi wasiwepo tena. Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia kwamba Mungu anatawala katika Yakobo.
PSA 59:14 Hurudi jioni, wakibweka kama mbwa, wakiuzurura mji.
PSA 59:15 Wanatangatanga wakitafuta chakula, wasipotosheka hubweka kama mbwa.
PSA 59:16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako, asubuhi nitaimba kuhusu upendo wako; kwa maana wewe ndiwe ngome yangu na kimbilio langu wakati wa shida.
PSA 59:17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa. Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu, Mungu unayenipenda.
PSA 60:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Shushani Eduthi”. Utenzi wa Daudi wa kufundisha. Alipopigana na Waaramu kutoka Aram-Naharaimu na Aram-Soba, na Yoabu aliporudi na kuwaua Waedomu elfu kumi na mbili katika Bonde la Chumvi. Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu, umekuwa na hasira; sasa turejeshe!
PSA 60:2 Umetetemesha nchi na kuipasua; uiponye mavunjiko yake, kwa maana inatetemeka.
PSA 60:3 Umewaonesha watu wako nyakati za kukata tamaa; umetunywesha mvinyo unaotuyumbisha.
PSA 60:4 Kwa wale wanaokucha wewe, umewainulia bendera, ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde.
PSA 60:5 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
PSA 60:6 Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi.
PSA 60:7 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni chapeo yangu, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
PSA 60:8 Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
PSA 60:9 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
PSA 60:10 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu?
PSA 60:11 Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
PSA 60:12 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu.
PSA 61:1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, sikia kilio changu, usikilize maombi yangu.
PSA 61:2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita, ninakuita huku moyo wangu unadhoofika; uniongoze kwenye mwamba ulio juu kuniliko.
PSA 61:3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu, ngome imara dhidi ya adui.
PSA 61:4 Natamani kukaa kwenye hema lako milele, na kukimbilia chini ya uvuli wa mabawa yako.
PSA 61:5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu, umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.
PSA 61:6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake, miaka yake kwa vizazi vingi.
PSA 61:7 Mtawaze mbele za Mungu milele; amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.
PSA 61:8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.
PSA 62:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi. Nafsi yangu inapata pumziko kwa Mungu peke yake; wokovu wangu watoka kwake.
PSA 62:2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.
PSA 62:3 Mtanishambulia hadi lini? Je, ninyi nyote mtanitupa chini: Mimi niliye kama ukuta ulioinama, kama uzio unaotikisika?
PSA 62:4 Walikusudia kikamilifu kumwangusha toka mahali pake pa fahari; wanafurahia uongo. Kwa vinywa vyao hubariki, lakini ndani ya mioyo yao hulaani.
PSA 62:5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake, tumaini langu latoka kwake.
PSA 62:6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; ndiye ngome yangu, sitatikisika.
PSA 62:7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu, ndiye mwamba wangu wenye nguvu na kimbilio langu.
PSA 62:8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote, miminieni mioyo yenu kwake, kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.
PSA 62:9 Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu, nao wa ngazi ya juu ni uongo tu; wakipimwa kwenye mizani, si chochote; wote kwa pamoja ni pumzi tu.
PSA 62:10 Usitumainie udhalimu, wala ujivune kwa vitu vya wizi; ingawa utajiri wako utaongezeka, usiuweke moyoni mwako.
PSA 62:11 Jambo moja Mungu amelisema, mambo mawili nimeyasikia: kwamba, Ee Mungu, wewe una nguvu,
PSA 62:12 na kwamba, Ee Bwana, wewe ni mwenye upendo. Hakika utampa kila mtu thawabu kwa kadiri ya alivyotenda.
PSA 63:1 Zaburi ya Daudi. Alipokuwa katika Jangwa la Yuda. Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo wote; nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu unakuonea wewe shauku, katika nchi kame na iliyochoka, mahali pasipo maji.
PSA 63:2 Nimekuona katika mahali patakatifu na kuuona uwezo wako na utukufu wako.
PSA 63:3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakuadhimisha.
PSA 63:4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu, na kwa jina lako nitainua mikono yangu.
PSA 63:5 Nafsi yangu itatoshelezwa, kama kushiba vyakula vizuri; kwa midomo iimbayo kinywa changu kitakusifu wewe.
PSA 63:6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe; ninakuwaza makesha yote ya usiku.
PSA 63:7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu, chini ya uvuli wa mabawa yako naimba.
PSA 63:8 Nafsi yangu inaambatana nawe, mkono wako wa kuume hunishika.
PSA 63:9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataangamizwa; wataenda chini kwenye vilindi vya dunia.
PSA 63:10 Watatolewa wafe kwa upanga, nao watakuwa chakula cha mbweha.
PSA 63:11 Bali mfalme atafurahi katika Mungu, wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu, bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.
PSA 64:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu, uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.
PSA 64:2 Unifiche kutokana na njama za waovu, kutokana na fitina za kundi la watenda maovu.
PSA 64:3 Wananoa ndimi zao kama panga na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.
PSA 64:4 Hurusha mishale kutoka mavizio kwa mtu asiye na hatia, humrushia ghafula bila woga.
PSA 64:5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake katika mipango mibaya; huzungumza kuhusu kuficha mitego yao, nao husema, “Ni nani ataiona?”
PSA 64:6 Hupanga njama la dhuluma na kusema, “Tumebuni mpango mkamilifu!” Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.
PSA 64:7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale, nao ghafula wataangushwa.
PSA 64:8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao na kuwaleta kwenye maangamizi; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao kwa dharau.
PSA 64:9 Wanadamu wote wataogopa, watatangaza kazi za Mungu na kutafakari yale aliyoyatenda.
PSA 64:10 Wenye haki na wafurahi katika Mwenyezi Mungu, na wakimbilie kwake; wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!
PSA 65:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo. Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni; kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.
PSA 65:2 Ewe usikiaye maombi, watu wote watakuja kwako wewe.
PSA 65:3 Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi, wewe ulisamehe makosa yetu.
PSA 65:4 Heri wale uliowachagua na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, mema ya Hekalu lako takatifu.
PSA 65:5 Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki, Ee Mungu Mwokozi wetu, tumaini la miisho yote ya duniani na la bahari zilizo mbali sana,
PSA 65:6 uliyeumba milima kwa uwezo wako, ukiwa umejivika nguvu,
PSA 65:7 uliyenyamazisha dhoruba za bahari, ngurumo za mawimbi yake, na ghasia za mataifa.
PSA 65:8 Wale wanaoishi mbali sana wanaogopa maajabu yako, kule asubuhi ipambazukiapo na kule jioni inakofifilia umeziita nyimbo za furaha.
PSA 65:9 Waitunza nchi na kuinyeshea, waitajirisha kwa wingi. Vijito vya Mungu vimejaa maji ili kuwapa watu nafaka, kwa maana wewe umeviamuru.
PSA 65:10 Umeilowesha mifereji yake na kusawazisha kingo zake; umeilainisha kwa manyunyu na kuibariki mimea yake.
PSA 65:11 Umeuvika mwaka taji la baraka, magari yako yanafurika kwa wingi.
PSA 65:12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha; vilima vimevikwa furaha.
PSA 65:13 Malisho yamejaa makundi ya wanyama, na mabonde yamepambwa kwa mavuno; vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.
PSA 66:1 Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi. Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!
PSA 66:2 Imbeni utukufu wa jina lake; mpeni sifa zake kwa utukufu!
PSA 66:3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako! Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba adui wanajikunyata mbele zako.
PSA 66:4 Dunia yote yakusujudia, wanakuimbia wewe sifa, wanaliimbia sifa jina lako.”
PSA 66:5 Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda, mambo ya kutisha aliyoyatenda miongoni mwa wanadamu!
PSA 66:6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu, wakapita kati ya maji kwa miguu, njooni, tumshangilie.
PSA 66:7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele, macho yake huangalia mataifa yote: waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.
PSA 66:8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu, sauti ya sifa yake isikike,
PSA 66:9 ameyahifadhi maisha yetu na kuizuia miguu yetu kuteleza.
PSA 66:10 Ee Mungu, wewe ulitujaribu, ukatusafisha kama fedha.
PSA 66:11 Umetuingiza kwenye nyavu na umetubebesha mizigo mizito migongoni mwetu.
PSA 66:12 Uliwaruhusu watu watukalie vichwani, tulipita kwenye moto na kwenye maji, lakini ulituleta kwenye nchi iliyojaa utajiri tele.
PSA 66:13 Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa na kukutimizia nadhiri zangu:
PSA 66:14 nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi na nilizotamka kwa kinywa changu nilipokuwa katika shida.
PSA 66:15 Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono na sadaka za kondoo dume, nitakutolea mafahali na mbuzi.
PSA 66:16 Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami niwaambie aliyonitendea.
PSA 66:17 Nilimlilia kwa kinywa changu, sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.
PSA 66:18 Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu, Bwana asingekuwa amenisikiliza;
PSA 66:19 lakini hakika Mungu amenisikiliza na amesikia sauti yangu katika maombi.
PSA 66:20 Ahimidiwe Mungu, ambaye hakulikataa ombi langu, wala kunizuilia upendo wake!
PSA 67:1 Kwa mwimbishaji. Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi. Wimbo. Mungu aturehemu na kutubariki, na kutuangazia nuru za uso wake,
PSA 67:2 ili njia zako zijulikane duniani, wokovu wako katikati ya mataifa yote.
PSA 67:3 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, mataifa yote na wakusifu.
PSA 67:4 Mataifa yote wafurahi na kuimba kwa shangwe, kwa kuwa unatawala watu kwa haki na kuongoza mataifa ya dunia.
PSA 67:5 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, mataifa yote na wakusifu.
PSA 67:6 Ndipo nchi itatoa mazao yake, naye Mungu, Mungu wetu, atatubariki.
PSA 67:7 Mungu atatubariki na miisho yote ya dunia itamcha yeye.
PSA 68:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo. Mungu na ainuke, watesi wake watawanyike, adui zake na wakimbie mbele zake.
PSA 68:2 Kama moshi unavyopeperushwa na upepo, vivyo hivyo uwapeperushe mbali, kama nta inavyoyeyuka kwenye moto, vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu.
PSA 68:3 Bali wenye haki na wafurahi, washangilie mbele za Mungu, wafurahi na kushangilia.
PSA 68:4 Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake, mtukuzeni yeye anayepita juu ya mawingu: jina lake ni Mwenyezi Mungu, furahini mbele zake.
PSA 68:5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane, ni Mungu katika makao yake matakatifu.
PSA 68:6 Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame.
PSA 68:7 Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako, ulipopita nyikani,
PSA 68:8 dunia ilitikisika, mbingu zikanyesha mvua, mbele za Mungu, Yule wa Sinai, mbele za Mungu, Mungu wa Israeli.
PSA 68:9 Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka.
PSA 68:10 Ee Mungu, watu wako waliishi huko, nawe kwa wingi wa utajiri wako uliwapa maskini mahitaji yao.
PSA 68:11 Bwana analitoa neno, wanawake wanaolitangaza neno hilo ni kundi kubwa:
PSA 68:12 “Wafalme na majeshi walikimbia upesi, wanawake waliobaki nyumbani waligawana nyara.
PSA 68:13 Hata unapolala kati ya mioto ya kambini, mabawa ya njiwa wangu yamefunikwa kwa fedha, manyoya yake kwa dhahabu inayong’aa.”
PSA 68:14 Mwenyezi alipowatawanya wafalme katika nchi, ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Mlima Salmoni.
PSA 68:15 Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka, milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka.
PSA 68:16 Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka, kwa nini mnakazia macho kwa wivu, katika mlima Mungu anaochagua kutawala, ambako Mwenyezi Mungu mwenyewe ataishi milele?
PSA 68:17 Magari ya vita ya Mungu ni makumi ya maelfu, na maelfu ya maelfu; Bwana amekuja kutoka Sinai hadi katika patakatifu pake.
PSA 68:18 Ulipopanda juu, uliteka mateka, ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu, hata kutoka kwa wale walioasi, ili wewe, Ee Bwana Mwenyezi Mungu, upate kuishi huko.
PSA 68:19 Ahimidiwe Bwana, Mungu Mwokozi wetu, ambaye siku kwa siku hutuchukulia mizigo yetu.
PSA 68:20 Mungu wetu ni Mungu anayeokoa, Bwana Mungu Mwenyezi hutuokoa na kifo.
PSA 68:21 Hakika Mungu ataponda vichwa vya adui zake, vichwa vya hao wanaoenda katika njia za dhambi.
PSA 68:22 Bwana alisema, “Nitawarudisha kutoka Bashani; nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari,
PSA 68:23 ili uweze kuchovya miguu yako katika damu ya adui zako, huku ndimi za mbwa wako zikiwa na fungu lake.”
PSA 68:24 Ee Mungu, maandamano yako yameonekana, maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu, yakielekea patakatifu pake.
PSA 68:25 Mbele wako waimbaji, baada yao wapiga vinanda, pamoja nao wako wanawali wakipiga matari.
PSA 68:26 Msifuni Mungu katika kusanyiko kubwa, msifuni Mwenyezi Mungu katika kusanyiko la Israeli.
PSA 68:27 Liko kabila dogo la Benyamini likiwaongoza, wakifuatwa na kundi kubwa la watawala wa Yuda, hatimaye watawala wa Zabuloni na Naftali.
PSA 68:28 Ee Mungu, amuru uwezo wako, Ee Mungu tuoneshe nguvu zako, kama ulivyofanya hapo awali.
PSA 68:29 Kwa sababu ya Hekalu lako Yerusalemu wafalme watakuletea zawadi.
PSA 68:30 Mkemee mnyama aliye kwenye matete, kundi la mafahali kati ya ndama za mataifa. Na walete minara ya madini ya fedha wakinyenyekea. Tawanya mataifa yapendayo vita.
PSA 68:31 Wajumbe watakuja kutoka Misri; Kushi atajisalimisha kwa Mungu.
PSA 68:32 Mwimbieni Mungu, enyi falme za dunia, mwimbieni Bwana sifa,
PSA 68:33 mwimbieni sifa yeye apandaye mbingu za kale zilizo juu, yeye angurumaye kwa sauti kuu.
PSA 68:34 Tangazeni uwezo wa Mungu, ambaye fahari yake iko juu ya Israeli, ambaye uwezo wake uko katika anga.
PSA 68:35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako, Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu. Ahimidiwe Mungu!
PSA 69:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi”. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, niokoe, kwa maana maji yamenifika shingoni.
PSA 69:2 Ninazama kwenye vilindi vya matope, pasipo mahali pa kukanyaga, Nimefika kwenye maji makuu, mafuriko yamenigharikisha.
PSA 69:3 Nimechoka kwa kuomba msaada, koo langu limekauka. Macho yangu yanafifia, nikimtafuta Mungu wangu.
PSA 69:4 Wale wanaonichukia bila sababu ni wengi kuliko nywele za kichwa changu; wengi ni adui kwangu bila sababu, wale wanaotafuta kuniangamiza. Ninalazimishwa kurudisha kitu ambacho sikuiba.
PSA 69:5 Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu, wala hatia yangu haikufichika kwako.
PSA 69:6 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, wanaokutumaini wasiaibishwe kwa ajili yangu; wanaokutafuta wasifedheheshwe kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.
PSA 69:7 Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako, aibu imefunika uso wangu.
PSA 69:8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe.
PSA 69:9 Kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila, matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.
PSA 69:10 Ninapolia na kufunga, lazima nivumilie matusi.
PSA 69:11 Ninapovaa gunia, watu hunidharau.
PSA 69:12 Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga, nimekuwa wimbo wa walevi.
PSA 69:13 Lakini Ee Mwenyezi Mungu, ninakuomba, kwa wakati ukupendezao; katika upendo wako mkuu, Ee Mungu, unijibu kwa wokovu wako wa hakika.
PSA 69:14 Uniokoe katika matope, usiniache nizame; niokoe na hao wanaonichukia, kutoka kwa vilindi vya maji.
PSA 69:15 Usiache mafuriko yanigharikishe au vilindi vinimeze, au shimo lifumbe kinywa chake juu yangu.
PSA 69:16 Ee Mwenyezi Mungu, unijibu, kwa wema wa upendo wako; kwa huruma zako nyingi unigeukie.
PSA 69:17 Usimfiche mtumishi wako uso wako, uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.
PSA 69:18 Njoo karibu uniokoe, nikomboe kwa sababu ya adui zangu.
PSA 69:19 Unajua jinsi ninavyodharauliwa, kufedheheshwa na kuaibishwa, adui zangu wote unawajua.
PSA 69:20 Dharau zimenivunja moyo na nimekata tamaa, nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata, wa kunituliza, lakini sikumpata.
PSA 69:21 Waliweka nyongo katika chakula changu na walinipa siki nilipokuwa na kiu.
PSA 69:22 Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego, nayo iwe upatilizo na tanzi.
PSA 69:23 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona, nayo migongo yao iinamishwe daima.
PSA 69:24 Uwamwagie ghadhabu yako, hasira yako kali na iwapate.
PSA 69:25 Mahali pao na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi katika mahema yao.
PSA 69:26 Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi, na kuzungumza kuhusu maumivu ya wale uliowaumiza.
PSA 69:27 Walipize uovu juu ya uovu, usiwaache washiriki katika wokovu wako.
PSA 69:28 Wafutwe kutoka kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.
PSA 69:29 Lakini mimi niko katika maumivu na dhiki; Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.
PSA 69:30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.
PSA 69:31 Hili litampendeza Mwenyezi Mungu kuliko ng’ombe dume, zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake.
PSA 69:32 Maskini wataona na kufurahi: ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi!
PSA 69:33 Mwenyezi Mungu huwasikia wahitaji wala hadharau watu wake waliotekwa.
PSA 69:34 Mbingu na dunia zimsifu, bahari na vyote viendavyo ndani yake,
PSA 69:35 kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni na kuijenga tena miji ya Yuda. Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki,
PSA 69:36 watoto wa watumishi wake watairithi na wale wote wanaolipenda jina lake wataishi humo.
PSA 70:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Maombi. Ee Mungu, ufanye haraka kuniokoa; Ee Mwenyezi Mungu, njoo hima unisaidie.
PSA 70:2 Wale wanaotafuta kuniua, waaibishwe na kufadhaishwa; wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, warudishwe nyuma kwa aibu.
PSA 70:3 Wale wanaoniambia, “Aha! Aha!” na warudi nyuma kwa sababu ya aibu yao.
PSA 70:4 Lakini wote wanaokutafuta washangilie na kukufurahia, wale wanaoupenda wokovu wako siku zote waseme, “Mwenyezi Mungu ni mkuu!”
PSA 70:5 Lakini mimi bado ni maskini na mhitaji; Ee Mungu, unijie haraka. Wewe ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; Ee Mwenyezi Mungu, usikawie.
PSA 71:1 Ee Mwenyezi Mungu, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe.
PSA 71:2 Kwa haki yako uniponye na kuniokoa, unitegee sikio lako uniokoe.
PSA 71:3 Uwe kwangu mwamba wa kimbilio, mahali nitakapokimbilia kila wakati; toa amri ya kuniokoa, kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu.
PSA 71:4 Ee Mungu wangu uniokoe kutoka mkono wa mwovu, kutoka makucha ya watu wapotovu na wakatili.
PSA 71:5 Kwa kuwa umekuwa tumaini langu, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, tegemeo langu tangu ujana wangu.
PSA 71:6 Tangu kuzaliwa nimekutegemea wewe, ulinitoa tumboni mwa mama yangu. Nitakusifu wewe daima.
PSA 71:7 Nimekuwa ishara mbaya kwa wengi, lakini wewe ni kimbilio langu imara.
PSA 71:8 Kinywa changu kimejazwa sifa zako, nikitangaza utukufu wako mchana kutwa.
PSA 71:9 Usinitupe wakati wa uzee, wala usiniache nguvu zangu zinapopungua.
PSA 71:10 Kwa maana adui zangu wananisengenya, wale wanaotaka kuniua wanapanga njama.
PSA 71:11 Wanasema, “Mungu amemwacha, mkimbilieni mkamkamate, kwani hakuna wa kumwokoa.”
PSA 71:12 Ee Mungu, usiwe mbali nami, njoo haraka kunisaidia, Ee Mungu wangu.
PSA 71:13 Washtaki wangu na waangamie kwa aibu, wale wanaotaka kunidhuru na wafunikwe kwa dharau na fedheha.
PSA 71:14 Lakini mimi nitatumaini siku zote; nitakusifu zaidi na zaidi.
PSA 71:15 Kinywa changu kitasimulia haki yako, wokovu wako mchana kutwa, ingawa sifahamu kipimo chake.
PSA 71:16 Ee Bwana Mungu Mwenyezi, nitakuja na kutangaza matendo yako makuu, nitatangaza haki yako, yako peke yako.
PSA 71:17 Ee Mungu, umenifundisha tangu ujana wangu, hadi leo ninatangaza matendo yako ya ajabu.
PSA 71:18 Ee Mungu, usiniache, hata nikiwa mzee wa mvi, hadi nitangaze uwezo wako kwa kizazi kijacho, nguvu zako kwa wote watakaokuja baadaye.
PSA 71:19 Ee Mungu, haki yako imefika juu Lakini mimi mbingu, wewe ambaye umefanya mambo makuu. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?
PSA 71:20 Ingawa umenifanya nipate taabu nyingi na chungu, utanihuisha tena, kutoka vilindi vya dunia utaniinua tena.
PSA 71:21 Utaongeza heshima yangu na kunifariji tena.
PSA 71:22 Ee Mungu wangu, nitakusifu kwa kinubi kwa ajili ya uaminifu wako; Ee Uliye Mtakatifu wa Israeli, nitakuimbia sifa kwa zeze.
PSA 71:23 Midomo yangu itapaza sauti kwa furaha ninapokuimbia sifa, mimi, ambaye umenikomboa.
PSA 71:24 Ulimi wangu utasimulia matendo yako ya haki mchana kutwa, kwa maana wale waliotaka kunidhuru, wameaibishwa na kufadhaishwa.
PSA 72:1 Zaburi ya Sulemani. Ee Mungu, mjalie mfalme aamue kwa haki yako, mwana wa mfalme kwa haki yako.
PSA 72:2 Atawaamua watu wako kwa haki, watu wako walioonewa kwa haki.
PSA 72:3 Milima italeta mafanikio kwa watu, vilima tunda la haki.
PSA 72:4 Atawatetea walioonewa miongoni mwa watu na atawaokoa watoto wa wahitaji, ataponda mdhalimu.
PSA 72:5 Atadumu kama jua linavyodumu, kama mwezi, vizazi vyote.
PSA 72:6 Atakuwa kama mvua inavyonyesha juu ya shamba lililofyekwa, kama manyunyu yanavyonyeshea ardhi.
PSA 72:7 Katika siku zake wenye haki watastawi; mafanikio yatakuwepo hadi mwezi utakapokoma.
PSA 72:8 Atatawala kutoka bahari hadi bahari na kutoka Mto hadi miisho ya dunia.
PSA 72:9 Makabila ya jangwani watamsujudia, na adui zake wataramba mavumbi.
PSA 72:10 Wafalme wa Tarshishi na wa pwani za mbali watamletea ushuru; wafalme wa Sheba na Seba watampa zawadi.
PSA 72:11 Wafalme wote watamsujudia na mataifa yote yatamtumikia.
PSA 72:12 Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia, aliyeonewa asiye na wa kumsaidia.
PSA 72:13 Atawahurumia wanyonge na wahitaji na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti.
PSA 72:14 Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili, kwani damu yao ni ya thamani machoni pake.
PSA 72:15 Aishi maisha marefu! Na apewe dhahabu ya Sheba. Watu wamwombee daima na kumbariki mchana kutwa.
PSA 72:16 Nafaka ijae tele katika nchi yote, juu ya vilele vya vilima na istawi. Tunda lake na listawi kama Lebanoni, listawi kama majani ya kondeni.
PSA 72:17 Jina lake na lidumu milele, na lidumu kama jua. Mataifa yote yatabarikiwa kupitia kwake, nao watamwita aliyebarikiwa.
PSA 72:18 Ahimidiwe Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye peke yake hutenda mambo ya ajabu.
PSA 72:19 Jina lake tukufu lihimidiwe milele, ulimwengu wote ujae utukufu wake.
PSA 72:20 Huu ndio mwisho wa maombi ya Daudi mwana wa Yese.
PSA 73:1 Zaburi ya Asafu. Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, kwa wale ambao mioyo yao ni safi.
PSA 73:2 Bali mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza; nilikuwa karibu kuanguka.
PSA 73:3 Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna nilipoona kufanikiwa kwa waovu.
PSA 73:4 Wao hawana taabu; miili yao ina afya na nguvu.
PSA 73:5 Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine, wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.
PSA 73:6 Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao, wamejivika jeuri.
PSA 73:7 Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi, majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hayana kikomo.
PSA 73:8 Hudhihaki na kusema kwa ukorofi, katika majivuno yao wanatishia kutesa.
PSA 73:9 Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu, nazo ndimi zao humiliki duniani.
PSA 73:10 Kwa hiyo watu wao huwageukia na kunywa maji tele.
PSA 73:11 Wanasema, “Mungu awezaje kujua? Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”
PSA 73:12 Hivi ndivyo walivyo waovu: siku zote hawajali, wanaongezeka katika utajiri.
PSA 73:13 Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure, ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.
PSA 73:14 Mchana kutwa nimetaabika, nimeadhibiwa kila asubuhi.
PSA 73:15 Kama ningesema, “Nitasema hivi,” ningekuwa nimewasaliti watoto wako.
PSA 73:16 Nilipojaribu kuelewa haya yote, yalikuwa magumu kwangu kuelewa.
PSA 73:17 Hadi nilipoingia patakatifu pa Mungu, ndipo nilitambua mwisho wao.
PSA 73:18 Hakika unawaweka mahali pa utelezi, unawaangusha chini kwa uharibifu.
PSA 73:19 Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula, wanatoweshwa kabisa na vitisho!
PSA 73:20 Kama ndoto mtu aamkapo, hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana, utawatowesha kama ndoto.
PSA 73:21 Moyo wangu ulipohuzunishwa, na roho yangu ilipotiwa uchungu,
PSA 73:22 nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa mnyama mkatili mbele yako.
PSA 73:23 Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote, umenishika mkono wangu wa kuume.
PSA 73:24 Unaniongoza kwa ushauri wako, hatimaye utaniingiza katika utukufu.
PSA 73:25 Nani niliye naye mbinguni ila wewe? Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe.
PSA 73:26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa, bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu na fungu langu milele.
PSA 73:27 Wale walio mbali nawe wataangamia, unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako.
PSA 73:28 Lakini kwangu mimi, ni vyema kuwa karibu na Mungu. Nimemfanya Bwana Mungu Mwenyezi kimbilio langu; nami nitayasimulia matendo yako yote.
PSA 74:1 Utenzi wa Asafu. Ee Mungu, mbona umetukataa milele? Mbona hasira yako inatoka moshi juu ya kondoo wa malisho yako?
PSA 74:2 Kumbuka watu uliowanunua zamani, kabila la urithi wako, ambao uliwakomboa: Mlima Sayuni, ambamo uliishi.
PSA 74:3 Geuza hatua zako kuelekea magofu haya ya kudumu, uharibifu wote huu ambao adui ameuleta pale patakatifu.
PSA 74:4 Adui zako wamenguruma pale ulipokutana nasi, wanaweka bendera zao kama alama.
PSA 74:5 Walifanya kama watu wanaotumia mashoka kukata kichaka cha miti.
PSA 74:6 Walivunjavunja milango yote iliyonakshiwa kwa mashoka na vishoka vyao.
PSA 74:7 Waliteketeza kabisa mahali pako patakatifu, wakayanajisi makao ya Jina lako.
PSA 74:8 Walisema mioyoni mwao, “Tutawaponda kabisa!” Walichoma kila mahali Mungu alipoabudiwa katika nchi.
PSA 74:9 Hatukupewa ishara za miujiza; hakuna manabii waliobaki, hakuna yeyote kati yetu ajuaye hali hii itachukua muda gani.
PSA 74:10 Ee Mungu, mtesi atakudhihaki hadi lini? Je, adui watalitukana jina lako milele?
PSA 74:11 Kwa nini unazuia mkono wako, mkono wako wa kuume? Uutoe kutoka makunjo ya vazi lako na uwaangamize!
PSA 74:12 Lakini wewe, Ee Mungu, ni mfalme wangu tangu zamani, unaleta wokovu duniani.
PSA 74:13 Ni wewe uliyeigawanya bahari kwa uweza wako; ulivunja vichwa vya mnyama mkubwa wa baharini.
PSA 74:14 Ni wewe uliyeponda vichwa vya Lewiathani, nawe ukamtoa kama chakula kwa viumbe vya jangwani.
PSA 74:15 Ni wewe uliyefungua chemchemi na vijito, ulikausha mito iliyokuwa ikitiririka daima.
PSA 74:16 Mchana ni wako, na usiku ni wako pia; uliziweka jua na mwezi.
PSA 74:17 Ni wewe uliyeiweka mipaka yote ya dunia, ulifanya kiangazi na masika.
PSA 74:18 Ee Mwenyezi Mungu, kumbuka jinsi mtesi alivyokudhihaki, jinsi watu wapumbavu walivyolitukana jina lako.
PSA 74:19 Usiukabidhi uhai wa njiwa wako kwa wanyama mwitu; usisahau kabisa uhai wa watu wako wanaoteseka milele.
PSA 74:20 Likumbuke agano lako, maana mara kwa mara mambo ya jeuri yamejaa katika sehemu za giza nchini.
PSA 74:21 Usiruhusu waliodhulumiwa warudi nyuma kwa aibu; maskini na wahitaji hebu walisifu jina lako.
PSA 74:22 Inuka, Ee Mungu, ujitetee; kumbuka jinsi wapumbavu wanavyokudhihaki mchana kutwa.
PSA 74:23 Usipuuze makelele ya watesi wako, ghasia za adui zako, zinazoinuka mfululizo.
PSA 75:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Zaburi ya Asafu. Wimbo. Ee Mungu, tunakushukuru, tunakushukuru wewe, kwa kuwa jina lako li karibu; watu husimulia matendo yako ya ajabu.
PSA 75:2 Unasema, “Ninachagua wakati maalum; ni mimi nihukumuye kwa haki.
PSA 75:3 Dunia inapotetemeka na watu wake wote, ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara.
PSA 75:4 Kwa wale wenye majivuno ninasema, ‘Msijisifu tena,’ kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu.
PSA 75:5 Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu; msiseme kwa kiburi.’ ”
PSA 75:6 Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu.
PSA 75:7 Bali Mungu ndiye ahukumuye: Humshusha huyu na kumkweza mwingine.
PSA 75:8 Mkononi mwa Mwenyezi Mungu kuna kikombe kilichojaa mvinyo unaotoka povu uliochanganywa na vikolezo; huumimina, nao waovu wote wa dunia hunywa hata tone la mwisho.
PSA 75:9 Bali mimi, nitatangaza hili milele; nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo.
PSA 75:10 Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote, bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu.
PSA 76:1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Asafu. Wimbo. Katika Yuda, Mungu anajulikana, jina lake ni kuu katika Israeli.
PSA 76:2 Hema lake liko Salemu, makao yake katika Sayuni.
PSA 76:3 Huko alivunja mishale iliyowaka, ngao na panga, silaha za vita.
PSA 76:4 Wewe unang’aa kwa mwanga, mwenye fahari zaidi ya milima yenye utajiri wa wanyama pori.
PSA 76:5 Mashujaa hulala wametekwa nyara, hulala usingizi wao wa mwisho; hakuna hata mmoja wa watu wa vita anayeweza kuinua mikono yake.
PSA 76:6 Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo, farasi na gari la vita vilikaa kimya.
PSA 76:7 Wewe peke yako ndiye wa kuogopwa. Ni nani awezaye kusimama mbele yako unapokasirika?
PSA 76:8 Ulitamka hukumu kutoka mbinguni, nayo nchi ikaogopa, ikawa kimya:
PSA 76:9 wakati wewe, Ee Mungu, ulipoinuka kuhukumu, kuwaokoa wote walioonewa katika nchi.
PSA 76:10 Hakika ghadhabu yako dhidi ya wanadamu inakuletea sifa, na masalia ya ghadhabu yako unajifunga mshipi.
PSA 76:11 Wekeni nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuzitimiza; nchi zote za jirani na walete zawadi kwa Yule astahiliye kuogopwa.
PSA 76:12 Huvunja roho za watawala; anaogopwa na wafalme wa dunia.
PSA 77:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu. Nilimlilia Mungu ili anisaidie, nilimlilia Mungu ili anisikie.
PSA 77:2 Nilipokuwa katika taabu, nilimtafuta Bwana, usiku nilinyoosha mikono bila kuchoka na nafsi yangu ilikataa kufarijika.
PSA 77:3 Ee Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni; nikatafakari, roho yangu ikadhoofika.
PSA 77:4 Ulizuia macho yangu kufumba; nilikuwa nasumbuka, nikashindwa kusema.
PSA 77:5 Nilitafakari kuhusu siku zilizopita, miaka mingi iliyopita,
PSA 77:6 nilikumbuka nilivyoimba nyimbo usiku. Moyo wangu ulitafakari na roho yangu ikauliza:
PSA 77:7 “Je, Bwana atakataa milele? Je, hatatenda mema tena?
PSA 77:8 Je, upendo wake usio na mwisho umetoweka milele? Je, ahadi yake imekoma nyakati zote?
PSA 77:9 Je, Mungu amesahau kuwa na huruma? Je, katika hasira amezuia fadhili zake?”
PSA 77:10 Ndipo nikawaza, “Huu ndio udhaifu wangu: lakini nitakumbuka miaka ya mkono wa kuume wa Aliye Juu Sana.”
PSA 77:11 Nitayakumbuka matendo ya Mwenyezi Mungu; naam, nitaikumbuka miujiza yako ya zamani.
PSA 77:12 Nitazitafakari kazi zako zote na kuyawaza matendo yako makuu.
PSA 77:13 Ee Mungu, njia zako ni takatifu. Ni mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?
PSA 77:14 Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza, umeonesha uwezo wako kati ya mataifa.
PSA 77:15 Kwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako, uzao wa Yakobo na Yusufu.
PSA 77:16 Maji yalikuona, Ee Mungu, maji yalikuona yakakimbia, vilindi vilitetemeka.
PSA 77:17 Mawingu yalimwaga maji, mbingu zikatoa ngurumo kwa radi; mishale yako ilimetameta huku na huko.
PSA 77:18 Ngurumo yako ilisikika katika upepo wa kisulisuli, umeme wako wa radi ukaangaza dunia, nchi ikatetemeka na kutikisika.
PSA 77:19 Njia yako ilipita baharini, mapito yako kwenye maji makuu, ingawa nyayo zako hazikuonekana.
PSA 77:20 Uliongoza watu wako kama kundi kwa mkono wa Musa na Haruni.
PSA 78:1 Utenzi wa Asafu. Enyi watu wangu, sikieni mafundisho yangu, sikilizeni maneno ya kinywa changu.
PSA 78:2 Nitafungua kinywa changu kwa mafumbo, nitazungumza mambo yaliyofichika, mambo ya kale:
PSA 78:3 yale ambayo tuliyasikia na kuyajua, yale ambayo baba zetu walituambia.
PSA 78:4 Hatutayaficha kwa watoto wao; tutakiambia kizazi kijacho matendo yastahiliyo sifa ya Mwenyezi Mungu, uweza wake, na maajabu aliyoyafanya.
PSA 78:5 Aliagiza amri kwa Yakobo na akaweka sheria katika Israeli, ambazo aliwaamuru baba zetu wawafundishe watoto wao,
PSA 78:6 ili kizazi kijacho kizijue, pamoja na watoto ambao watazaliwa, nao pia wapate kuwaeleza watoto wao.
PSA 78:7 Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu, nao hawangesahau matendo yake, bali wangezishika amri zake.
PSA 78:8 Hawangefanana na baba zao, waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi, ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwa Mungu, ambao roho zao hazikumwamini.
PSA 78:9 Watu wa Efraimu, ingawa walijifunga pinde, walikimbia siku ya vita.
PSA 78:10 Hawakulishika agano la Mungu, na walikataa kuishi kwa sheria yake.
PSA 78:11 Walisahau aliyokuwa ameyatenda, maajabu aliyokuwa amewaonesha.
PSA 78:12 Alitenda miujiza machoni mwa baba zao, huko Soani, katika nchi ya Misri.
PSA 78:13 Aliigawanya bahari akawapitisha, alifanya maji yasimame imara kama ukuta.
PSA 78:14 Aliwaongoza kwa wingu mchana, na kwa nuru ya moto usiku kucha.
PSA 78:15 Alipasua miamba jangwani na akawapa maji tele kama bahari,
PSA 78:16 alitoa vijito kutoka jabali lililochongoka, akayafanya maji yatiririke kama mito.
PSA 78:17 Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana.
PSA 78:18 Kwa makusudi walimjaribu Mungu, wakidai vyakula walivyovitamani.
PSA 78:19 Walinena dhidi ya Mungu, wakisema, “Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani?
PSA 78:20 Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu, vijito vikatiririka maji mengi. Lakini je, aweza kutupatia chakula pia? Je, anaweza kuwapatia watu wake nyama?”
PSA 78:21 Mwenyezi Mungu alipowasikia, alikasirika sana, moto wake ukawa dhidi ya Yakobo, na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli,
PSA 78:22 kwa kuwa hawakumwamini Mungu, wala kuutumainia ukombozi wake.
PSA 78:23 Hata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu na kufungua milango ya mbingu,
PSA 78:24 akawanyeshea mana ili watu wale; aliwapa nafaka ya mbinguni.
PSA 78:25 Watu walikula mkate wa malaika, akawatumia chakula chote ambacho wangeweza kula.
PSA 78:26 Aliachia upepo wa mashariki kutoka mbingu na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake.
PSA 78:27 Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, ndege warukao kama mchanga wa pwani.
PSA 78:28 Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao, kuzunguka mahema yao yote.
PSA 78:29 Walikula na kusaza, kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani.
PSA 78:30 Kabla hawajamaliza kula walichokitamani, hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao,
PSA 78:31 hasira ya Mungu ikawaka juu yao, akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao, akiwaangusha vijana wa Israeli.
PSA 78:32 Licha ya haya yote, waliendelea kutenda dhambi, licha ya maajabu yake, hawakuamini.
PSA 78:33 Kwa hiyo akamaliza siku zao katika ubatili na miaka yao katika vitisho.
PSA 78:34 Kila mara Mungu alipowaua baadhi yao, waliosalia walimtafuta, walimgeukia tena kwa shauku.
PSA 78:35 Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa Mwamba wao, kwamba Mungu Aliye Juu Sana alikuwa Mkombozi wao.
PSA 78:36 Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, wakisema uongo kwa ndimi zao,
PSA 78:37 mioyo yao haikuwa thabiti kwake, wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.
PSA 78:38 Hata hivyo alikuwa na huruma, alisamehe maovu yao na hakuwaangamiza. Mara kwa mara alizuia hasira yake, wala hakuchochea ghadhabu yake yote.
PSA 78:39 Alikumbuka kwamba wao walikuwa nyama tu, upepo upitao ambao haurudi.
PSA 78:40 Mara ngapi walimwasi jangwani na kumhuzunisha nyikani!
PSA 78:41 Walimjaribu Mungu mara kwa mara, wakamkasirisha yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
PSA 78:42 Hawakukumbuka uwezo wake, siku aliyowakomboa kutoka kwa mtesi,
PSA 78:43 siku aliyoonesha ishara zake za ajabu huko Misri, maajabu yake huko Soani.
PSA 78:44 Aligeuza mito yao kuwa damu, hawakuweza kunywa maji kutoka vijito vyao.
PSA 78:45 Aliwapelekea makundi ya inzi wakawala, na vyura wakawaharibu.
PSA 78:46 Aliruhusu tunutu kuharibu mimea yao, mazao yao kwa nzige.
PSA 78:47 Aliharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na mikuyu yao kwa mvua iliyochangamana na theluji.
PSA 78:48 Aliwaachia mifugo yao mvua ya mawe, akayapiga makundi ya wanyama wao kwa radi.
PSA 78:49 Aliwafungulia hasira yake kali, ghadhabu yake, hasira na uadui, na kundi la malaika wa kuharibu.
PSA 78:50 Aliitengenezea njia hasira yake, hakuwaepusha na kifo, bali aliwaachia tauni.
PSA 78:51 Aliwapiga wazaliwa wote wa kwanza wa Misri, matunda ya kwanza ya ujana katika mahema ya Hamu.
PSA 78:52 Lakini aliwatoa watu wake kama kundi, akawaongoza kama kondoo kupitia jangwani.
PSA 78:53 Aliwaongoza salama, wala hawakuogopa, bali bahari iliwameza adui zao.
PSA 78:54 Hivyo akawaleta hadi kwenye mpaka wa nchi yake takatifu, hadi nchi ya vilima ambayo mkono wake wa kuume ulikuwa umeitwaa.
PSA 78:55 Aliyafukuza mataifa mbele yao, na kuwagawia nchi zao kama urithi, aliwakalisha makabila ya Israeli katika makao yao.
PSA 78:56 Lakini wao walimjaribu Mungu, na kuasi dhidi ya Yeye Aliye Juu Sana, wala hawakuzishika sheria zake.
PSA 78:57 Kama baba zao, hawakuwa thabiti wala waaminifu, wakawa wasioweza kutegemewa kama upinde wenye kasoro.
PSA 78:58 Wakamkasirisha Mungu kwa mahali pao pa juu pa kuabudia, wakachochea wivu wake kwa sanamu zao.
PSA 78:59 Mungu alipowasikia, alikasirika sana, akamkataa Israeli kabisa.
PSA 78:60 Akaiacha maskani ya Shilo, hema alilokuwa ameliweka katikati ya wanadamu.
PSA 78:61 Akalipeleka Sanduku la nguvu zake utumwani, utukufu wake mikononi mwa adui.
PSA 78:62 Aliachia watu wake wauawe kwa upanga, akaukasirikia sana urithi wake.
PSA 78:63 Moto uliwaangamiza vijana wao, na wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,
PSA 78:64 makuhani wao waliuawa kwa upanga, wala wajane wao hawakuweza kulia.
PSA 78:65 Ndipo Bwana alipoamka kama kuamka usingizini, kama shujaa anavyoamka kutoka bumbuazi la mvinyo.
PSA 78:66 Aliwapiga na kuwashinda adui zake, akawatia katika aibu ya milele.
PSA 78:67 Ndipo alipoyakataa mahema ya Yusufu, hakulichagua kabila la Efraimu,
PSA 78:68 lakini alilichagua kabila la Yuda, Mlima Sayuni, ambao aliupenda.
PSA 78:69 Alijenga patakatifu pake kama vilele, kama dunia ambayo aliimarisha milele.
PSA 78:70 Akamchagua Daudi mtumishi wake na kumtoa kwenye mazizi ya kondoo.
PSA 78:71 Kutoka kuchunga kondoo alimleta kuwa mchungaji wa watu wake Yakobo, wa Israeli urithi wake.
PSA 78:72 Naye Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo, kwa mikono ya ustadi aliwaongoza.
PSA 79:1 Zaburi ya Asafu. Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako, wamelinajisi Hekalu lako takatifu, wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.
PSA 79:2 Wametoa maiti za watumishi kuwa chakula cha ndege wa angani na nyama ya watakatifu wako kwa wanyama wa nchi.
PSA 79:3 Wamemwaga damu kama maji kuzunguka Yerusalemu yote, wala hakuna yeyote wa kuwazika.
PSA 79:4 Tumekuwa kitu cha aibu kwa majirani zetu, cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.
PSA 79:5 Hata lini, Ee Mwenyezi Mungu? Je, wewe utakasirika milele? Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?
PSA 79:6 Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali, juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,
PSA 79:7 kwa maana wamemrarua Yakobo na kuharibu nchi ya makao yake.
PSA 79:8 Usituhesabie dhambi za baba zetu, huruma yako na itujie hima, kwa maana tu wahitaji mno.
PSA 79:9 Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; tuokoe na kutusamehe dhambi zetu kwa ajili ya jina lako.
PSA 79:10 Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wenu?” Mbele ya macho yetu, dhihirisha kati ya mataifa kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa ya watumishi wako.
PSA 79:11 Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako; kwa nguvu za mkono wako hifadhi wale waliohukumiwa kufa.
PSA 79:12 Walipize majirani zetu mara saba aibu walizovurumisha kwako, Ee Bwana.
PSA 79:13 Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakusifu milele; tutasimulia sifa zako kizazi hadi kizazi.
PSA 80:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi za Agano”. Zaburi ya Asafu. Ee Mchungaji wa Israeli tusikie, wewe umwongozaye Yusufu kama kundi; wewe uketiye kwenye kiti cha enzi katikati ya makerubi, angaza
PSA 80:2 mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase. Uamshe nguvu zako, uje utuokoe.
PSA 80:3 Ee Mungu, uturejeshe, utuangazie uso wako, ili tuweze kuokolewa.
PSA 80:4 Ee Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, hata lini hasira yako itawaka dhidi ya maombi ya watu wako?
PSA 80:5 Umewalisha kwa mkate wa machozi, umewafanya wanywe machozi bakuli tele.
PSA 80:6 Tumekuwa chanzo cha ugomvi kwa majirani zetu, na adui zetu wanatudhihaki.
PSA 80:7 Ee Mungu wa majeshi ya mbinguni, uturejeshe; utuangazie uso wako, nasi tuweze kuokolewa.
PSA 80:8 Ulileta mzabibu kutoka Misri, ukawafukuza mataifa, ukaupanda.
PSA 80:9 Uliandaa shamba kwa ajili yake, mizizi ikawa imara, ukajaza nchi.
PSA 80:10 Milima ilifunikwa kwa kivuli chake, matawi yake yakafunika mierezi mikubwa.
PSA 80:11 Matawi yake yalienea hadi Baharini, machipukizi yake hadi kwenye Mto.
PSA 80:12 Mbona umebomoa kuta zake ili wote wapitao karibu wazichume zabibu zake?
PSA 80:13 Nguruwe mwitu wanauharibu, na viumbe wa kondeni hujilisha humo.
PSA 80:14 Turudie, Ee Mungu wa majeshi ya mbinguni! Tazama chini kutoka mbinguni na uone! Linda mzabibu huu,
PSA 80:15 mche ulioupanda kwa mkono wako wa kuume, mwana uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe.
PSA 80:16 Mzabibu wako umekatwa, umechomwa moto, unapowakemea, watu wako huangamia.
PSA 80:17 Mkono wako na utulie juu ya mtu aliye katika mkono wako wa kuume, mwana wa mtu uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe.
PSA 80:18 Ndipo hatutakuacha tena, utuhuishe, nasi tutaliitia jina lako.
PSA 80:19 Ee Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, uturejeshe; utuangazie uso wako, ili tuweze kuokolewa.
PSA 81:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Asafu. Mwimbieni kwa furaha, Mungu aliye nguvu yetu; mpigieni kelele za shangwe Mungu wa Yakobo!
PSA 81:2 Anzeni wimbo, pigeni matari, pigeni kinubi na zeze kwa sauti nzuri.
PSA 81:3 Pigeni baragumu za pembe za kondoo dume wakati wa Mwandamo wa Mwezi, na wakati wa mwezi mpevu, katika siku ya Sikukuu yetu;
PSA 81:4 hii ni amri kwa Israeli, agizo la Mungu wa Yakobo.
PSA 81:5 Aliiweka iwe kama sheria kwa Yusufu alipotoka dhidi ya Misri, huko tulikosikia lugha ambayo hatukuielewa.
PSA 81:6 Asema, “Nimeondoa mzigo mabegani mwao; mikono yao iliwekwa huru kutoka kwa kikapu.
PSA 81:7 Katika shida yako uliniita nami nikakuokoa, nilikujibu katika mawingu yenye ngurumo; nilikujaribu katika maji ya Meriba.
PSA 81:8 “Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya: laiti kama mngenisikiliza, ee Israeli!
PSA 81:9 Hamtakuwa na mungu mgeni miongoni mwenu; msimsujudie mungu wa kigeni.
PSA 81:10 Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchi ya Misri. Panua sana kinywa chako nami nitakijaza.
PSA 81:11 “Lakini watu wangu hawakunisikiliza; Israeli hakunitii.
PSA 81:12 Basi niliwaacha katika ukaidi wa mioyo yao wafuate mashauri yao wenyewe.
PSA 81:13 “Laiti watu wangu wangenisikiliza, laiti Israeli wangefuata njia zangu,
PSA 81:14 ningewatiisha adui zao kwa haraka, na kuugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao!
PSA 81:15 Wale wanaomchukia Mwenyezi Mungu wangejikunyata mbele zake, na adhabu yao ingedumu milele.
PSA 81:16 Bali ninyi mngelishwa ngano iliyo bora, na kuwatosheleza kwa asali inayotoka kwenye mwamba.”
PSA 82:1 Zaburi ya Asafu. Mungu anaongoza kusanyiko kuu, anatoa hukumu miongoni mwa “miungu”:
PSA 82:2 “Hata lini utaendelea kuwatetea wasio haki na kuonesha upendeleo kwa waovu?
PSA 82:3 Teteeni wanyonge na yatima, tunzeni haki za maskini na waliodhulumiwa.
PSA 82:4 Mwokoeni mnyonge na mhitaji, wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu.
PSA 82:5 “Hawajui lolote, hawaelewi lolote. Wanatembea gizani; misingi yote ya dunia imetikisika.
PSA 82:6 “Nilisema, ‘Ninyi ni “miungu”; ninyi nyote ni wana wa Aliye Juu Sana.’
PSA 82:7 Lakini mtakufa kama wanadamu wa kawaida; mtaanguka kama mtawala mwingine yeyote.”
PSA 82:8 Ee Mungu, inuka uihukumu nchi, kwa kuwa mataifa yote ni urithi wako.
PSA 83:1 Wimbo. Zaburi ya Asafu. Ee Mungu, usikae kimya, usinyamaze, Ee Mungu, usikae mbali.
PSA 83:2 Tazama watesi wako wanafanya fujo, jinsi adui zako wanavyoinua vichwa vyao.
PSA 83:3 Kwa ujanja, wanapanga njama dhidi ya watu wako; wanapanga hila dhidi ya wale unaowapenda.
PSA 83:4 Wanasema, “Njooni, tuwaangamize kama taifa, ili jina la Israeli lisikumbukwe tena.”
PSA 83:5 Kwa nia moja wanapanga njama pamoja, wanafanya muungano dhidi yako,
PSA 83:6 mahema ya Edomu na Waishmaeli, ya Wamoabu na Wahagari,
PSA 83:7 Gebali, Amoni na Amaleki, Ufilisti, pamoja na watu wa Tiro.
PSA 83:8 Hata Ashuru wameungana nao kuwapa nguvu wazao wa Lutu.
PSA 83:9 Uwatendee kama vile ulivyowatendea Midiani, na kama vile ulivyowatendea Sisera na Yabini hapo kijito cha Kishoni,
PSA 83:10 ambao waliangamia huko Endori na wakawa kama kinyesi juu ya ardhi.
PSA 83:11 Wafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, watawala wao kama Zeba na Salmuna,
PSA 83:12 ambao walisema, “Na tumiliki maeneo ya malisho ya Mungu.”
PSA 83:13 Ee Mungu wangu, wapeperushe kama mavumbi ya kisulisuli, kama makapi yapeperushwayo na upepo.
PSA 83:14 Kama vile moto unavyoteketeza msitu au mwali wa moto unavyounguza milima,
PSA 83:15 wafuatilie kwa tufani yako na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.
PSA 83:16 Funika nyuso zao kwa aibu ili watu walitafute jina lako, Ee Mwenyezi Mungu.
PSA 83:17 Wao na waaibishwe na kufadhaishwa milele, na waangamie kwa aibu.
PSA 83:18 Hebu wajue kuwa wewe, ambaye jina lako ni Mwenyezi Mungu, kwamba wewe peke yako ndiwe Uliye Juu Sana ya dunia yote.
PSA 84:1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora. Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, makao yako yapendeza kama nini!
PSA 84:2 Nafsi yangu inatamani sana, naam, hata kuona shauku, kwa ajili ya nyua za Mwenyezi Mungu; moyo wangu na mwili wangu vinamlilia Mungu Aliye Hai.
PSA 84:3 Hata shomoro amejipatia makao, mbayuwayu amejipatia kiota mahali awezapo kuweka makinda yake: mahali karibu na madhabahu yako, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mfalme wangu na Mungu wangu.
PSA 84:4 Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, wanaokusifu wewe daima.
PSA 84:5 Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako, na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.
PSA 84:6 Wanapopita katika Bonde la Baka, hulifanya mahali pa chemchemi, pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi.
PSA 84:7 Huendelea toka nguvu hadi nguvu, hadi kila mmoja afikapo mbele za Mungu huko Sayuni.
PSA 84:8 Ee Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, sikia maombi yangu; nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
PSA 84:9 Ee Mungu, uitazame ngao yetu, mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.
PSA 84:10 Siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu kuliko kukaa katika mahema ya waovu.
PSA 84:11 Kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu ni jua na ngao; Mwenyezi Mungu hutoa wema na heshima; hakuna kitu chema anachowanyima wale ambao hawana hatia.
PSA 84:12 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, heri mtu anayekutumaini wewe.
PSA 85:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Ee Mwenyezi Mungu, ulionesha wema kwa nchi yako. Ulimrejeshea Yakobo baraka zake.
PSA 85:2 Ulisamehe uovu wa watu wako, na kufunika dhambi zao zote.
PSA 85:3 Uliweka kando ghadhabu yako yote na umegeuka na kuiacha hasira yako kali.
PSA 85:4 Ee Mungu Mwokozi wetu, uturejeshe tena, nawe uiondoe chuki yako juu yetu.
PSA 85:5 Je, utatukasirikia milele? Utaendeleza hasira yako kwa vizazi vyote?
PSA 85:6 Je, hutatuhuisha tena, ili watu wako wakufurahie?
PSA 85:7 Utuoneshe upendo wako usiokoma, Ee Mwenyezi Mungu, utupe wokovu wako.
PSA 85:8 Nitasikiliza lile atakalosema Mungu aliye Mwenyezi Mungu; anaahidi amani kwa watu wake, watakatifu wake: lakini nao wasirudie upumbavu.
PSA 85:9 Hakika wokovu wake uko karibu na wale wamchao, ili utukufu wake udumu katika nchi yetu.
PSA 85:10 Upendo na uaminifu hukutana pamoja, haki na amani hubusiana.
PSA 85:11 Uaminifu huchipua kutoka nchi, haki hutazama chini kutoka mbinguni.
PSA 85:12 Naam, hakika Mwenyezi Mungu atatoa kilicho chema, nayo nchi yetu itazaa mavuno yake.
PSA 85:13 Haki itatangulia mbele yake na kutengeneza njia kwa ajili ya hatua zake.
PSA 86:1 Maombi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, sikia na unijibu, kwa maana mimi ni maskini na mhitaji.
PSA 86:2 Linda maisha yangu, kwa maana nimejiweka kwako, wewe ni Mungu wangu, mwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
PSA 86:3 Ee Bwana, nihurumie mimi, kwa maana ninakuita mchana kutwa.
PSA 86:4 Mpe mtumishi wako furaha, kwa kuwa kwako wewe, Ee Bwana, ninainua nafsi yangu.
PSA 86:5 Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe, umejaa upendo kwa wote wakuitao.
PSA 86:6 Ee Mwenyezi Mungu, sikia maombi yangu, sikiliza kilio changu unihurumie.
PSA 86:7 Katika siku ya shida yangu nitakuita, kwa maana wewe utanijibu.
PSA 86:8 Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe, hakuna matendo ya kulinganishwa na yako.
PSA 86:9 Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya yatakuja na kuabudu mbele zako; wataliletea utukufu jina lako.
PSA 86:10 Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu; wewe peke yako ndiwe Mungu.
PSA 86:11 Ee Mwenyezi Mungu, nifundishe njia yako, nami nitaenda katika kweli yako; nipe moyo usiositasita, ili niweze kulicha jina lako.
PSA 86:12 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitaliadhimisha jina lako milele.
PSA 86:13 Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; umeniokoa kutoka vilindi vya kaburi.
PSA 86:14 Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia; kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu: watu wasiokuheshimu wewe.
PSA 86:15 Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.
PSA 86:16 Nigeukie na unihurumie; mpe mtumishi wako nguvu zako, mwokoe mwana wa mjakazi wako.
PSA 86:17 Nipe ishara ya wema wako, ili adui zangu waione nao waaibishwe, kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umenisaidia na kunifariji.
PSA 87:1 Zaburi ya wana wa Kora. Wimbo. Ameuweka msingi wake katika mlima mtakatifu;
PSA 87:2 Mwenyezi Mungu anayapenda malango ya Sayuni kuliko makao yote ya Yakobo.
PSA 87:3 Mambo matukufu yanasemwa juu yako, ee mji wa Mungu:
PSA 87:4 “Nitaweka kumbukumbu ya Rahabu na Babeli miongoni mwa wale wanaonikubali mimi: Ufilisti pia na Tiro, pamoja na Kushi, nami nitasema, ‘Huyu alizaliwa Sayuni.’ ”
PSA 87:5 Kuhusu Sayuni itasemwa hivi, “Huyu na yule walizaliwa humo, naye Aliye Juu Sana mwenyewe atamwimarisha.”
PSA 87:6 Mwenyezi Mungu ataandika katika orodha ya mataifa: “Huyu alizaliwa Sayuni.”
PSA 87:7 Watakapokuwa wanapiga vinanda wataimba, “Chemchemi zangu zote ziko kwako.”
PSA 88:1 Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi leanothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi. Ee Mwenyezi Mungu, Mungu uniokoaye, nimelia mbele zako usiku na mchana.
PSA 88:2 Maombi yangu yafike mbele zako, utegee kilio changu sikio lako.
PSA 88:3 Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu, na maisha yangu yanakaribia kaburi.
PSA 88:4 Nimehesabiwa miongoni mwa wale wanaoshuka shimoni; niko kama mtu asiye na nguvu.
PSA 88:5 Nimetengwa pamoja na wafu, kama waliochinjwa walalao kaburini, ambao huwakumbuki tena, ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.
PSA 88:6 Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana, katika vina vya giza nene.
PSA 88:7 Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu, umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.
PSA 88:8 Umenitenga na rafiki zangu wa karibu na kunifanya chukizo kwao. Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka;
PSA 88:9 nuru ya macho yangu imefifia kwa ajili ya huzuni. Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita kila siku, ninakunyooshea wewe mikono yangu.
PSA 88:10 Je, wewe huwaonesha wafu maajabu yako? Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?
PSA 88:11 Je, upendo wako hutangazwa kaburini, uaminifu wako katika Uharibifu?
PSA 88:12 Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza, au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?
PSA 88:13 Lakini ninakulilia wewe, Ee Mwenyezi Mungu, unisaidie; asubuhi maombi yangu huja mbele zako.
PSA 88:14 Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini unanikataa na kunificha uso wako?
PSA 88:15 Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo; nimepatwa na mapigo yako, nami nimekata tamaa.
PSA 88:16 Ghadhabu yako imepita juu yangu; mapigo yako yameniangamiza.
PSA 88:17 Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko; zimenimeza kabisa.
PSA 88:18 Umeniondolea rafiki na wapendwa wangu; giza limekuwa rafiki yangu wa karibu kuliko wote.
PSA 89:1 Utenzi wa Ethani Mwezrahi. Nitaimba kuhusu upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu milele; kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
PSA 89:2 Nitatangaza kuwa upendo wako unasimama imara milele na uaminifu wako umeuthibitisha mbinguni.
PSA 89:3 Ulisema, “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi,
PSA 89:4 ‘Nitaimarisha uzao wako milele na kudumisha ufalme wako kwa vizazi vyote.’ ”
PSA 89:5 Ee Mwenyezi Mungu, mbingu zinayasifu maajabu yako, uaminifu wako pia katika kusanyiko la watakatifu.
PSA 89:6 Kwa kuwa ni nani katika mbingu anayeweza kulinganishwa na Mwenyezi Mungu? Ni nani miongoni mwa viumbe vya mbinguni aliye kama Mwenyezi Mungu?
PSA 89:7 Katika kusanyiko la watakatifu, Mungu huogopwa sana, anahofiwa kuliko wote wanaomzunguka.
PSA 89:8 Ee Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ni nani aliye kama wewe? Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni mwenye nguvu, na uaminifu wako unakuzunguka.
PSA 89:9 Wewe unatawala bahari yenye msukosuko; mawimbi yake yanapoinuka, wewe unayatuliza.
PSA 89:10 Wewe ulimponda Rahabu kama mmoja wa waliochinjwa; kwa mkono wako wenye nguvu, uliwatawanya adui zako.
PSA 89:11 Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako, uliuwekea ulimwengu msingi pamoja na vyote vilivyomo.
PSA 89:12 Uliumba kaskazini na kusini; Tabori na Hermoni wanaliimbia jina lako kwa furaha.
PSA 89:13 Mkono wako umejaa uwezo; mkono wako una nguvu, mkono wako wa kuume umetukuka.
PSA 89:14 Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako cha enzi; upendo na uaminifu vinakutangulia.
PSA 89:15 Heri ni wale ambao wamejifunza kukusifu kwa shangwe, wanaotembea katika mwanga wa uwepo wako, Ee Mwenyezi Mungu.
PSA 89:16 Wanashangilia katika jina lako mchana kutwa, wanafurahi katika haki yako.
PSA 89:17 Kwa kuwa wewe ni utukufu na nguvu yao, kwa wema wako unatukuza pembe yetu.
PSA 89:18 Naam, ngao yetu ni mali ya Mwenyezi Mungu, na mfalme wetu mali ya Aliye Mtakatifu wa Israeli.
PSA 89:19 Ulizungumza wakati fulani katika maono, kwa watu wako waaminifu, ukasema: “Nimeweka nguvu kwa shujaa, nimemwinua kijana miongoni mwa watu.
PSA 89:20 Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, na nimempaka mafuta yangu matakatifu.
PSA 89:21 Kitanga changu kitamtegemeza, hakika mkono wangu utamtia nguvu.
PSA 89:22 Hakuna adui atakayemtoza ushuru, hakuna mtu mwovu atakayemtesa.
PSA 89:23 Nitawaponda adui zake mbele zake na kuwaangamiza watesi wake.
PSA 89:24 Upendo wangu mkamilifu utakuwa pamoja naye, kwa Jina langu pembe yake itatukuzwa.
PSA 89:25 Nitauweka mkono wake juu ya bahari, mkono wake wa kuume juu ya mito.
PSA 89:26 Naye ataniita kwa sauti, ‘Wewe ni Baba yangu, Mungu wangu, Mwamba na Mwokozi wangu.’
PSA 89:27 Nitamteua pia awe mzaliwa wangu wa kwanza, aliyetukuka kuliko wafalme wote wa dunia.
PSA 89:28 Nitadumisha upendo wangu kwake milele, na agano langu naye litakuwa imara.
PSA 89:29 Nitaudumisha uzao wake milele, kiti chake cha utawala kama mbingu zinavyodumu.
PSA 89:30 “Kama wanawe wataacha amri yangu na wasifuate sheria zangu,
PSA 89:31 wakihalifu maagizo yangu na kutoshika amri zangu,
PSA 89:32 nitaadhibu dhambi yao kwa fimbo, uovu wao kwa kuwapiga;
PSA 89:33 lakini sitauondoa upendo wangu kwake, wala sitausaliti uaminifu wangu kamwe.
PSA 89:34 Mimi sitavunja agano langu wala sitabadili lile ambalo midomo yangu imelitamka.
PSA 89:35 Mara moja na kwa milele, nimeapa kwa utakatifu wangu, nami sitamdanganya Daudi:
PSA 89:36 kwamba uzao wake utaendelea milele, na kiti chake cha enzi kitadumu mbele zangu kama jua;
PSA 89:37 kitaimarishwa milele kama mwezi, shahidi mwaminifu angani.”
PSA 89:38 Lakini wewe umemkataa, umemdharau, umemkasirikia sana mpakwa mafuta wako.
PSA 89:39 Umelikana agano lako na mtumishi wako, na umelinajisi taji lake mavumbini.
PSA 89:40 Umebomoa kuta zake zote, na ngome zake zote umezifanya kuwa magofu.
PSA 89:41 Wote wapitao karibu wamemnyang’anya mali yake; amekuwa dharau kwa majirani zake.
PSA 89:42 Umeutukuza mkono wa kuume wa adui zake, umewafanya watesi wake wote washangilie.
PSA 89:43 Umegeuza makali ya upanga wake, na hukumpa msaada katika vita.
PSA 89:44 Umeikomesha fahari yake, na kukiangusha kiti chake cha enzi.
PSA 89:45 Umezifupisha siku za ujana wake, umemfunika kwa vazi la aibu.
PSA 89:46 Hata lini, Ee Mwenyezi Mungu? Utajificha milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto hata lini?
PSA 89:47 Kumbuka jinsi maisha yangu yanavyopita haraka. Ni kwa ubatili kiasi gani umemuumba mwanadamu!
PSA 89:48 Ni mtu gani awezaye kuishi na asione kifo, au kujiokoa mwenyewe kutoka nguvu za kaburi?
PSA 89:49 Ee Bwana, uko wapi upendo wako mkuu wa mwanzoni, ambao katika uaminifu wako ulimwapia Daudi?
PSA 89:50 Bwana kumbuka jinsi mtumishi wako amesimangwa, jinsi ninavyovumilia moyoni mwangu dhihaka za mataifa yote,
PSA 89:51 dhihaka ambazo kwazo adui zako wamenisimanga, Ee Mwenyezi Mungu, ambazo kwazo wamesimanga kila hatua ya mpakwa mafuta wako.
PSA 89:52 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu milele!
PSA 90:1 Maombi ya Musa, mtu wa Mungu. Bwana, wewe umekuwa makao yetu katika vizazi vyote.
PSA 90:2 Kabla ya kuzaliwa milima au hujaumba dunia na ulimwengu, wewe ni Mungu tangu milele hata milele.
PSA 90:3 Huwarudisha watu mavumbini, ukisema, “Rudini mavumbini, enyi wanadamu.”
PSA 90:4 Kwa maana kwako miaka elfu ni kama siku moja iliyokwisha pita, au kama kesha la usiku.
PSA 90:5 Unawatowesha wanadamu katika usingizi wa kifo, nao ni kama majani machanga ya asubuhi:
PSA 90:6 ingawa asubuhi yanachipua, ifikapo jioni huwa yamenyauka na kukauka.
PSA 90:7 Tumeangamizwa kwa hasira yako na tumetishwa kwa ghadhabu yako.
PSA 90:8 Umeyaweka maovu yetu mbele yako, dhambi zetu za siri katika nuru ya uwepo wako.
PSA 90:9 Tumeishi siku zetu zote chini ya ghadhabu yako, tunamaliza miaka yetu kwa kuomboleza.
PSA 90:10 Siku zetu za kuishi ni miaka sabini, au miaka themanini ikiwa tuna nguvu, lakini yote ni ya shida na taabu, nazo zapita haraka, nasi twatoweka.
PSA 90:11 Ni nani ajuaye nguvu za hasira yako? Kwa maana ghadhabu yako ni kubwa kama hofu tunayopaswa kuwa nayo kwako.
PSA 90:12 Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri, ili tujipatie moyo wa hekima.
PSA 90:13 Ee Mwenyezi Mungu, uwe na huruma! Utakawia hata lini? Wahurumie watumishi wako.
PSA 90:14 Tushibishe asubuhi kwa upendo wako usiokoma, ili tuweze kuimba kwa shangwe na kufurahi siku zetu zote.
PSA 90:15 Utufurahishe kulingana na siku ulizotuadhibu, kulingana na miaka tuliyotaabika.
PSA 90:16 Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, utukufu wako kwa watoto wao.
PSA 90:17 Wema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu; uzithibitishe kazi za mikono yetu: naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu.
PSA 91:1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.
PSA 91:2 Nitasema kumhusu Mwenyezi Mungu, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ninayemtumaini.”
PSA 91:3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua.
PSA 91:4 Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mabawa yake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.
PSA 91:5 Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana,
PSA 91:6 wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri.
PSA 91:7 Ijapo watu elfu wataangukia kando yako, kumi elfu mkono wako wa kuume, lakini haitakukaribia wewe.
PSA 91:8 Utatazama tu kwa macho yako na kuona adhabu ya waovu.
PSA 91:9 Ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako; naam, Mwenyezi Mungu ambaye ni kimbilio langu;
PSA 91:10 basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yatalikaribia hema lako.
PSA 91:11 Kwa kuwa atawaagiza malaika wake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote.
PSA 91:12 Watakuchukua mikononi mwao, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.
PSA 91:13 Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.
PSA 91:14 Mwenyezi Mungu asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.
PSA 91:15 Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu.
PSA 91:16 Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonesha wokovu wangu.”
PSA 92:1 Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato. Ni vyema kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,
PSA 92:2 kuutangaza upendo wako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku,
PSA 92:3 kwa zeze yenye nyuzi kumi na kwa sauti ya kinubi.
PSA 92:4 Ee Mwenyezi Mungu, kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha, nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako.
PSA 92:5 Ee Mwenyezi Mungu, tazama jinsi yalivyo makuu matendo yako, tazama jinsi yalivyo ya kina mawazo yako!
PSA 92:6 Mjinga hafahamu, mpumbavu haelewi,
PSA 92:7 ingawa waovu huchipua kama majani na wote watendao maovu wanastawi, wataangamizwa milele.
PSA 92:8 Bali wewe, Ee Mwenyezi Mungu, utatukuzwa milele.
PSA 92:9 Ee Mwenyezi Mungu, hakika adui zako, hakika adui zako wataangamia. Wote watendao maovu watatawanyika.
PSA 92:10 Umeitukuza pembe yangu kama ile ya nyati dume, mafuta mazuri yamemiminwa juu yangu.
PSA 92:11 Macho yangu yamewaona adui zangu wakishindwa, masikio yangu yamesikia maangamizi ya adui zangu waovu.
PSA 92:12 Wenye haki watastawi kama mtende, watakuwa kama mwerezi wa Lebanoni,
PSA 92:13 waliopandwa katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, watastawi katika nyua za Mungu wetu.
PSA 92:14 Wakati wa uzee watakuwa bado wanazaa matunda, watakuwa wabichi tena wamejaa nguvu,
PSA 92:15 wakitangaza, “Mwenyezi Mungu ni mkamilifu; yeye ni Mwamba wangu, na ndani yake hamna uovu.”
PSA 93:1 Mwenyezi Mungu anatawala, amejivika utukufu; Mwenyezi Mungu amejivika utukufu tena amejivika nguvu. Dunia imewekwa imara, haitaondoshwa.
PSA 93:2 Kiti chako cha enzi kimekuwa thabiti tangu zamani; wewe umekuwa tangu milele.
PSA 93:3 Bahari zimepaza, Ee Mwenyezi Mungu, bahari zimepaza sauti zake; bahari zimepaza sauti za mawimbi yake.
PSA 93:4 Yeye ni mkuu kuliko ngurumo ya maji makuu, ni mkuu kuliko mawimbi ya bahari: Mwenyezi Mungu aishiye juu sana ni mkuu.
PSA 93:5 Ee Mwenyezi Mungu, sheria zako ni imara; utakatifu umepamba nyumba yako pasipo mwisho.
PSA 94:1 Ee Mwenyezi Mungu, ulipizaye kisasi, Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.
PSA 94:2 Ee Mhukumu wa dunia, inuka, uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.
PSA 94:3 Ee Mwenyezi Mungu, hadi lini waovu, hadi lini waovu watashangilia?
PSA 94:4 Wanamimina maneno ya kiburi, watenda maovu wote wamejaa majivuno.
PSA 94:5 Ee Mwenyezi Mungu, wanawaponda watu wako; wanawatesa walio urithi wako.
PSA 94:6 Wanamchinja mjane na mgeni, na kuwaua yatima.
PSA 94:7 Nao husema, “Mwenyezi Mungu haoni, Mungu wa Yakobo hafahamu.”
PSA 94:8 Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu; enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
PSA 94:9 Je, aliyeweka sikio asisikie? Aliyeumba jicho asione?
PSA 94:10 Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu? Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
PSA 94:11 Mwenyezi Mungu anajua mawazo ya mwanadamu; anajua kwamba ni ubatili.
PSA 94:12 Ee Mwenyezi Mungu, heri mtu anayeadhibishwa na wewe, mtu unayemfundisha kwa sheria yako,
PSA 94:13 unampa utulivu siku za shida, hadi shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya mwovu.
PSA 94:14 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu hatawakataa watu wake, hatauacha urithi wake.
PSA 94:15 Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki, wote walio na mioyo minyofu wataifuata.
PSA 94:16 Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu? Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?
PSA 94:17 Kama Mwenyezi Mungu hangenisaidia upesi, ningeishi katika kimya cha kifo.
PSA 94:18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,” Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako ulinishikilia.
PSA 94:19 Wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu, faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.
PSA 94:20 Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe, ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?
PSA 94:21 Huungana kuwashambulia wenye haki, kuwahukumu kufa wasio na hatia.
PSA 94:22 Lakini Mwenyezi Mungu amekuwa ngome yangu, na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.
PSA 94:23 Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao; Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, atawaangamiza.
PSA 95:1 Njooni, tumwimbie Mwenyezi Mungu kwa furaha; tumfanyie kelele za shangwe Mwamba wa wokovu wetu.
PSA 95:2 Tuje mbele zake kwa shukrani, tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.
PSA 95:3 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mungu mkuu, mfalme mkuu juu ya miungu yote.
PSA 95:4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia, na vilele vya milima ni mali yake.
PSA 95:5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliyeifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu.
PSA 95:6 Njooni, tusujudu, tumwabudu, tupige magoti mbele za Mwenyezi Mungu Muumba wetu,
PSA 95:7 kwa maana yeye ndiye Mungu wetu, na sisi ni watu wa malisho yake, kondoo chini ya utunzaji wake. Mkiisikia sauti yake leo,
PSA 95:8 msiifanye mioyo yenu migumu kama mlivyofanya kule Meriba, kama mlivyofanya siku ile kule Masa jangwani,
PSA 95:9 ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu.
PSA 95:10 Kwa miaka arobaini nilikasirikia kizazi kile, nikasema, “Hawa ni taifa ambalo mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.”
PSA 95:11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”
PSA 96:1 Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya; mwimbieni Mwenyezi Mungu dunia yote.
PSA 96:2 Mwimbieni Mwenyezi Mungu, lisifuni jina lake; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
PSA 96:3 Tangazeni utukufu wake katika mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
PSA 96:4 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
PSA 96:5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu.
PSA 96:6 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
PSA 96:7 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi jamaa za mataifa, mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu.
PSA 96:8 Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake; leteni sadaka na mje katika nyua zake.
PSA 96:9 Mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake; dunia yote na itetemeke mbele zake.
PSA 96:10 Semeni katika mataifa kwamba, “Mwenyezi Mungu anatawala.” Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa; atawahukumu watu kwa uadilifu.
PSA 96:11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake;
PSA 96:12 mashamba na yashangilie, pamoja na vyote vilivyomo. Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;
PSA 96:13 itaimba mbele za Mwenyezi Mungu kwa maana anakuja, anakuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa katika kweli yake.
PSA 97:1 Mwenyezi Mungu anatawala, nchi na ifurahi, visiwa vyote vishangilie.
PSA 97:2 Mawingu na giza nene vinamzunguka, haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake cha enzi.
PSA 97:3 Moto hutangulia mbele zake na huteketeza adui zake pande zote.
PSA 97:4 Umeme wake wa radi humulika dunia, nchi huona na kutetemeka.
PSA 97:5 Milima huyeyuka kama nta mbele za Mwenyezi Mungu, mbele za Bwana wa dunia yote.
PSA 97:6 Mbingu zinatangaza haki yake, na mataifa yote huona utukufu wake.
PSA 97:7 Wote waabuduo sanamu waaibishwa, wale wajisifiao sanamu: mwabuduni yeye, enyi miungu yote!
PSA 97:8 Sayuni husikia na kushangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako, Ee Mwenyezi Mungu.
PSA 97:9 Kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe Uliye Juu Sana kuliko dunia yote; umetukuka sana juu ya miungu yote.
PSA 97:10 Wale wanaompenda Mwenyezi Mungu na wauchukie uovu, kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu.
PSA 97:11 Nuru huangaza wenye haki na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
PSA 97:12 Furahini katika Mwenyezi Mungu, enyi wenye haki, lisifuni jina lake takatifu.
PSA 98:1 Zaburi. Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu umemfanyia wokovu.
PSA 98:2 Mwenyezi Mungu ameufanya wokovu wake ujulikane na amedhihirisha haki yake kwa mataifa.
PSA 98:3 Ameukumbuka upendo wake na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
PSA 98:4 Mpigieni Mwenyezi Mungu kelele za shangwe, dunia yote, ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda;
PSA 98:5 mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za kuimba,
PSA 98:6 kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: shangilieni kwa furaha mbele za Mwenyezi Mungu, aliye Mfalme.
PSA 98:7 Bahari na ivume na kila kilicho ndani yake, dunia na wote wanaoishi ndani yake.
PSA 98:8 Mito na ipige makofi, milima na iimbe pamoja kwa furaha,
PSA 98:9 vyote na viimbe mbele za Mwenyezi Mungu, kwa maana yuaja kuhukumu dunia. Atahukumu dunia kwa haki na mataifa kwa haki.
PSA 99:1 Mwenyezi Mungu anatawala, mataifa na yatetemeke; anakalia kiti cha enzi katikati ya makerubi, dunia na itikisike.
PSA 99:2 Mwenyezi Mungu ni mkuu katika Sayuni; ametukuzwa juu ya mataifa yote.
PSA 99:3 Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa: yeye ni mtakatifu!
PSA 99:4 Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki, wewe umethibitisha adili; katika Yakobo umefanya yaliyo haki na sawa.
PSA 99:5 Mtukuzeni Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake; yeye ni mtakatifu.
PSA 99:6 Musa na Haruni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake; walimwita Mwenyezi Mungu, naye aliwajibu.
PSA 99:7 Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu; walizishika sheria zake na amri alizowapa.
PSA 99:8 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu, kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.
PSA 99:9 Mtukuzeni Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.
PSA 100:1 Zaburi ya shukrani. Mpigieni Mwenyezi Mungu kelele za shangwe, dunia yote.
PSA 100:2 Mwabuduni Mwenyezi Mungu kwa furaha; njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe.
PSA 100:3 Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu. Yeye ndiye alituumba, sisi tu mali yake; sisi tu watu wake, kondoo wa malisho yake.
PSA 100:4 Ingieni malangoni mwake kwa shukrani na katika nyua zake kwa kusifu, mshukuruni yeye na kulisifu jina lake.
PSA 100:5 Kwa maana Mwenyezi Mungu ni mwema na fadhili zake zadumu milele; uaminifu wake unadumu kwa vizazi vyote.
PSA 101:1 Zaburi ya Daudi. Nitaimba kuhusu upendo wako na haki yako; kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu, nitaimba sifa.
PSA 101:2 Nitazingatia kuishi maisha yasiyo na lawama: utakuja kwangu lini? Nitatembea nyumbani mwangu kwa moyo usio na lawama.
PSA 101:3 Sitaweka mbele ya macho yangu kitu kiovu. Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani; hawatashikamana nami.
PSA 101:4 Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami; nitajitenga na kila ubaya.
PSA 101:5 Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri, huyo nitamnyamazisha; mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi huyo sitamvumilia.
PSA 101:6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, ili waweze kuishi pamoja nami; yeye ambaye moyo wake hauna lawama atanitumikia.
PSA 101:7 Mdanganyifu hatakaa nyumbani mwangu, yeye asemaye kwa uongo hatasimama mbele yangu.
PSA 101:8 Kila asubuhi nitawanyamazisha waovu wote katika nchi; nitamkatilia mbali kila mtenda maovu kutoka mji wa Mwenyezi Mungu.
PSA 102:1 Maombi ya mtu aliyechoka. Anapoteseka na kumimina malalamiko yake kwa Mwenyezi Mungu. Ee Mwenyezi Mungu, usikie maombi yangu; kilio changu cha kuomba msaada kikufikie.
PSA 102:2 Usinifiche uso wako ninapokuwa katika shida. Unitegee sikio lako; ninapoita, unijibu kwa upesi.
PSA 102:3 Kwa kuwa siku zangu zinatoweka kama moshi; mifupa yangu inaungua kama kaa la moto.
PSA 102:4 Moyo wangu umefifia na kunyauka kama jani; ninasahau kula chakula changu.
PSA 102:5 Kwa sababu ya kusononeka kwangu kwa uchungu, nimebakia ngozi na mifupa.
PSA 102:6 Nimekuwa kama bundi wa jangwani, kama bundi kwenye magofu.
PSA 102:7 Nilalapo sipati usingizi; nimekuwa kama ndege mpweke kwenye paa la nyumba.
PSA 102:8 Mchana kutwa adui zangu hunidhihaki; wanaonizunguka hutumia jina langu kama laana.
PSA 102:9 Ninakula majivu kama chakula changu, nimechanganya kinywaji changu na machozi
PSA 102:10 kwa sababu ya ghadhabu yako kuu, kwa maana umeniinua na kunitupa kando.
PSA 102:11 Siku zangu ni kama kivuli cha jioni, ninanyauka kama jani.
PSA 102:12 Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeketi kwenye kiti chako cha enzi milele; sifa zako za ukuu zaendelea vizazi vyote.
PSA 102:13 Utainuka na kuihurumia Sayuni, kwa maana ni wakati wa kumwonesha wema; wakati uliokubalika umewadia.
PSA 102:14 Kwa maana mawe yake ni ya thamani kwa watumishi wako, vumbi lake lenyewe hulionea huruma.
PSA 102:15 Mataifa wataogopa jina la Mwenyezi Mungu, wafalme wote wa dunia watauheshimu utukufu wako.
PSA 102:16 Kwa maana Mwenyezi Mungu ataijenga tena Sayuni na kutokea katika utukufu wake.
PSA 102:17 Ataitikia maombi ya mtu mkiwa, wala hatadharau hoja yao.
PSA 102:18 Hili na liandikwe kwa ajili ya kizazi kijacho, ili taifa litakaloumbwa baadaye waweze kumsifu Mwenyezi Mungu:
PSA 102:19 “Mwenyezi Mungu alitazama chini kutoka patakatifu pake palipo juu, alitazama dunia kutoka mbinguni,
PSA 102:20 kusikiliza vilio vya uchungu vya wafungwa, na kuwaweka huru wale waliohukumiwa kufa.”
PSA 102:21 Kwa hiyo jina la Mwenyezi Mungu latangazwa huko Sayuni na sifa zake katika Yerusalemu,
PSA 102:22 wakati mataifa na falme zitakapokusanyika ili kumwabudu Mwenyezi Mungu.
PSA 102:23 Katika kuishi kwangu alivunja nguvu zangu, akafupisha siku zangu.
PSA 102:24 Ndipo niliposema: “Ee Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu; miaka yako inaendelea vizazi vyote.
PSA 102:25 Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
PSA 102:26 Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu, zote zitachakaa kama vazi. Utazibadilisha kama nguo nazo zitaondoshwa.
PSA 102:27 Lakini wewe, U yeye yule, nayo miaka yako haikomi kamwe.
PSA 102:28 Watoto wa watumishi wako wataishi mbele zako; wazao wao wataimarishwa mbele zako.”
PSA 103:1 Zaburi ya Daudi. Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu. Vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu.
PSA 103:2 Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu, wala usisahau wema wake wote:
PSA 103:3 akusamehe dhambi zako zote, akuponya magonjwa yako yote,
PSA 103:4 aukomboa uhai wako na kaburi, akuvika taji la upendo na huruma,
PSA 103:5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema, ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
PSA 103:6 Mwenyezi Mungu hutenda haki, naye huwapa hukumu ya haki wote wanaodhulumiwa.
PSA 103:7 Alimjulisha Musa njia zake, na watu wa Israeli matendo yake.
PSA 103:8 Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mwenye neema; si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
PSA 103:9 Yeye hatalaumu siku zote, wala haweki hasira yake milele,
PSA 103:10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
PSA 103:11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;
PSA 103:12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.
PSA 103:13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowahurumia wale wanaomcha;
PSA 103:14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa, anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
PSA 103:15 Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani, anachanua kama ua la kondeni;
PSA 103:16 upepo huvuma juu yake nalo hutoweka, mahali pake hapalikumbuki tena.
PSA 103:17 Lakini kutoka milele hata milele upendo wa Mwenyezi Mungu uko kwa wale wamchao, nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
PSA 103:18 kwa wale walishikao agano lake na kukumbuka kuyatii mausia yake.
PSA 103:19 Mwenyezi Mungu ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake unatawala vitu vyote.
PSA 103:20 Mhimidini Mwenyezi Mungu, enyi malaika wake, ninyi mlio mashujaa, mnaozitii amri zake, ninyi mnaotii neno lake.
PSA 103:21 Mhimidini Mwenyezi Mungu, ninyi jeshi lake lote la mbinguni, ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.
PSA 103:22 Mhimidini Mwenyezi Mungu, enyi kazi zake zote kila mahali katika milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu.
PSA 104:1 Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu. Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, wewe ni mkuu sana, umejivika utukufu na enzi.
PSA 104:2 Mwenyezi Mungu amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi, amezitandaza mbingu kama hema,
PSA 104:3 na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji. Huyafanya mawingu kuwa gari lake la vita, na hupanda kwenye mabawa ya upepo.
PSA 104:4 Huzifanya pepo kuwa wajumbe wake, na miali ya moto kuwa watumishi wake.
PSA 104:5 Ameiweka dunia kwenye misingi yake, haiwezi kamwe kuondoshwa.
PSA 104:6 Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi, maji yalisimama juu ya milima.
PSA 104:7 Lakini kwa kukemea kwako maji yalikimbia, kwa sauti ya radi yako yakatoroka,
PSA 104:8 yakapanda milima, yakateremka mabondeni, hadi mahali pale ulipoyakusudia.
PSA 104:9 Uliyawekea mpaka ambao hayawezi kuuvuka, kamwe hayataifunika dunia tena.
PSA 104:10 Huzifanya chemchemi zimwage maji mabondeni, hutiririka kati ya milima.
PSA 104:11 Huwapa maji wanyama wote wa kondeni, punda-mwitu huzima kiu yao.
PSA 104:12 Ndege wa angani hufanya viota kando ya maji, huimba katika matawi.
PSA 104:13 Huinyeshea milima kutoka orofa zake, dunia inatoshelezwa kwa matunda ya kazi yake.
PSA 104:14 Huyafanya majani ya mifugo yaote, na mimea kwa watu kulima, wajipatie chakula kutoka ardhini:
PSA 104:15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu, mafuta kwa ajili ya kung’arisha uso wake, na mkate wa kutia mwili nguvu.
PSA 104:16 Miti ya Mwenyezi Mungu inanyeshewa vizuri, mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
PSA 104:17 Humo ndege hufanya viota vyao, korongo ana nyumba yake kwenye msunobari.
PSA 104:18 Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu; majabali ni kimbilio la pelele.
PSA 104:19 Mwezi hugawanya majira, na jua hutambua wakati wake wa kutua.
PSA 104:20 Unaleta giza, kunakuwa usiku, wanyama wote wa mwituni huzurura.
PSA 104:21 Simba hunguruma kwa mawindo yao, na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
PSA 104:22 Jua huchomoza, nao huondoka, hurudi na kulala katika mapango yao.
PSA 104:23 Kisha wanadamu wanaenda kazini zao, katika kazi zao hadi jioni.
PSA 104:24 Ee Mwenyezi Mungu, jinsi matendo yako yalivyo mengi! Kwa hekima ulizifanya zote, dunia imejaa viumbe vyako.
PSA 104:25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele, imejaa viumbe visivyo na idadi, vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.
PSA 104:26 Huko meli huenda na kurudi, pia Lewiathani, uliyemuumba acheze ndani yake.
PSA 104:27 Hawa wote wanakutazamia wewe, uwape chakula chao kwa wakati wake.
PSA 104:28 Wakati unawapa, wanakikusanya; unapofumbua mkono wako, wao wanashibishwa mema.
PSA 104:29 Unapoficha uso wako, wanapata hofu, unapoondoa pumzi yao, wanakufa na kurudi mavumbini.
PSA 104:30 Unapopeleka Roho wako, wanaumbwa, nawe huufanya upya uso wa dunia.
PSA 104:31 Utukufu wa Mwenyezi Mungu na udumu milele, Mwenyezi Mungu na azifurahie kazi zake:
PSA 104:32 yeye aitazamaye dunia, nayo ikatetemeka, aigusaye milima, nayo ikatoa moshi.
PSA 104:33 Nitamwimbia Mwenyezi Mungu maisha yangu yote; nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi.
PSA 104:34 Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye, ninapofurahi katika Mwenyezi Mungu.
PSA 104:35 Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia na waovu wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, msifu Mwenyezi Mungu. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 105:1 Mshukuruni Mwenyezi Mungu, liitieni jina lake; wajulisheni mataifa aliyoyatenda.
PSA 105:2 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa, waambieni matendo yake yote ya ajabu.
PSA 105:3 Lishangilieni jina lake takatifu, mioyo ya wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu na ifurahi.
PSA 105:4 Mtafuteni Mwenyezi Mungu na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote.
PSA 105:5 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka,
PSA 105:6 enyi wazao wa Ibrahimu mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
PSA 105:7 Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, hukumu zake ziko duniani kote.
PSA 105:8 Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
PSA 105:9 agano alilolifanya na Ibrahimu, kiapo alichomwapia Isaka.
PSA 105:10 Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele:
PSA 105:11 “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.”
PSA 105:12 Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake,
PSA 105:13 walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
PSA 105:14 Hakuruhusu mtu yeyote awadhulumu; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
PSA 105:15 “Msiwaguse niliowapaka mafuta; msiwadhuru manabii wangu.”
PSA 105:16 Akaiita njaa juu ya nchi na kuharibu chakula chao chote,
PSA 105:17 naye akatuma mtu mbele yao, Yusufu, aliyeuzwa kama mtumwa.
PSA 105:18 Walichubua miguu yake kwa minyororo, shingo yake ilifungwa kwa chuma,
PSA 105:19 hadi yale aliyotangulia kusema yalipotimia, hadi neno la Mwenyezi Mungu lilipomthibitisha.
PSA 105:20 Mfalme alituma watu wakamfungua, mtawala wa watu alimwachia huru.
PSA 105:21 Alimfanya mkuu wa nyumba yake, mtawala wa vyote alivyokuwa navyo,
PSA 105:22 kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo, na kuwafundisha wazee wake hekima.
PSA 105:23 Kisha Israeli akaingia Misri, Yakobo akaishi kama mgeni katika nchi ya Hamu.
PSA 105:24 Mwenyezi Mungu aliwafanya watu wake kuzaana sana; aliwafanya kuwa wengi sana kuliko adui zao.
PSA 105:25 Aliigeuza mioyo yao iwachukie watu wake, wakatenda hila dhidi ya watumishi wake.
PSA 105:26 Akamtuma Musa mtumishi wake, pamoja na Haruni, aliyemchagua.
PSA 105:27 Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao, miujiza yake katika nchi ya Hamu.
PSA 105:28 Alituma giza na nchi ikajaa giza, kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake?
PSA 105:29 Aligeuza maji yao kuwa damu, ikasababisha samaki wao kufa.
PSA 105:30 Nchi yao ilijaa vyura tele, ambao waliingia hadi kwenye vyumba vya kulala vya watawala wao.
PSA 105:31 Alisema, yakaja makundi ya inzi, na viroboto katika nchi yao yote.
PSA 105:32 Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe, yenye miali ya radi nchini yao yote,
PSA 105:33 akaharibu mizabibu yao na miti ya tini, na akaangamiza miti ya nchi yao.
PSA 105:34 Alisema, nzige wakaja, tunutu wasio na idadi,
PSA 105:35 wakala kila jani katika nchi yao, wakala mazao ya ardhi yao.
PSA 105:36 Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza katika nchi yao, matunda ya kwanza ya ujana wao wote.
PSA 105:37 Akawatoa Israeli katika nchi wakiwa na fedha na dhahabu nyingi, wala hakuna hata mmoja kutoka makabila yao aliyejikwaa.
PSA 105:38 Misri ilifurahi walipoondoka, kwa sababu hofu ya Israeli ilikuwa imewaangukia.
PSA 105:39 Alitandaza wingu kama kifuniko, na moto kuwamulikia usiku.
PSA 105:40 Waliomba, naye akawaletea kware, akawashibisha kwa mkate wa mbinguni.
PSA 105:41 Alipasua mwamba, maji yakabubujika, yakatiririka jangwani kama mto.
PSA 105:42 Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Ibrahimu mtumishi wake.
PSA 105:43 Aliwatoa watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za shangwe,
PSA 105:44 akawapa nchi za mataifa, wakawa warithi wa mali ambayo wengine walikuwa wameitaabikia:
PSA 105:45 alifanya haya ili wayashike mausia yake na kuzitii sheria zake. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 106:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ni mwema; fadhili zake zadumu milele.
PSA 106:2 Ni nani awezaye kusimulia matendo makuu ya Mwenyezi Mungu au kutangaza kikamilifu sifa zake?
PSA 106:3 Heri wale wanaodumisha haki, ambao daima wanafanya yaliyo mema.
PSA 106:4 Ee Mwenyezi Mungu, unikumbuke unapowatendea mema watu wako, uwe msaada wangu unapowaokoa,
PSA 106:5 ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako, niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako, na kuungana na urithi wako katika kukusifu.
PSA 106:6 Tumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda, tumekosa na tumetenda uovu.
PSA 106:7 Baba zetu walipokuwa Misri, hawakuzingatia maajabu yako, wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako, bali waliasi kando ya bahari, ile Bahari ya Shamu.
PSA 106:8 Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake, ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu.
PSA 106:9 Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka, akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani.
PSA 106:10 Aliwaokoa mikononi mwa adui; kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.
PSA 106:11 Maji yaliwafunika adui zao, hakunusurika hata mmoja.
PSA 106:12 Ndipo walipoamini ahadi zake, nao wakaimba sifa zake.
PSA 106:13 Lakini walisahau upesi aliyowatendea, wala hawakungojea ushauri wake.
PSA 106:14 Jangwani walitawaliwa na tamaa zao, walimjaribu Mungu nyikani.
PSA 106:15 Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba, lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha.
PSA 106:16 Kambini walimwonea wivu Musa, na pia Haruni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu.
PSA 106:17 Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani, ikawazika Abiramu na kundi lake.
PSA 106:18 Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao, mwali wa moto uliwateketeza waovu.
PSA 106:19 Huko Horebu walitengeneza ndama, na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma.
PSA 106:20 Waliubadilisha Utukufu wao kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani.
PSA 106:21 Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyetenda mambo makuu huko Misri,
PSA 106:22 miujiza katika nchi ya Hamu na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu.
PSA 106:23 Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza: kama Musa mteule wake, asingesimama kati yao na Mungu kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.
PSA 106:24 Kisha waliidharau ile nchi nzuri, hawakuiamini ahadi yake.
PSA 106:25 Walinung’unika ndani ya mahema yao, wala hawakumtii Mwenyezi Mungu.
PSA 106:26 Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba atawafanya waanguke jangwani,
PSA 106:27 kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa, na kuwatawanya katika nchi zote.
PSA 106:28 Walijifunga nira na Baali wa Peori, wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai.
PSA 106:29 Waliichochea hasira ya Mwenyezi Mungu, wakamkasirisha kwa matendo yao maovu, nayo tauni ikazuka katikati yao.
PSA 106:30 Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati, nayo tauni ikazuiliwa.
PSA 106:31 Hili likahesabiwa kwake haki, kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.
PSA 106:32 Kwenye maji ya Meriba, walimkasirisha Mwenyezi Mungu, janga likampata Musa kwa sababu yao;
PSA 106:33 kwa maana walimwasi Roho wa Mungu, na maneno yasiyofaa yakatoka mdomoni kwa Musa.
PSA 106:34 Hawakuyaangamiza yale mataifa kama Mwenyezi Mungu alivyowaagiza,
PSA 106:35 bali walijichanganya na mataifa na wakazikubali desturi zao.
PSA 106:36 Waliabudu sanamu zao, zikawa mtego kwao.
PSA 106:37 Wakawatoa wana wao na binti zao dhabihu kwa mashetani.
PSA 106:38 Walimwaga damu isiyo na hatia, damu za wana wao wa kiume na wa kike, ambao waliwatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani, nayo nchi ikanajisika kwa damu zao.
PSA 106:39 Wakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda; kwa matendo yao wenyewe wakajifanyia ukahaba.
PSA 106:40 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawakasirikia watu wake na akauchukia sana urithi wake.
PSA 106:41 Akawakabidhi kwa mataifa na adui zao wakawatawala.
PSA 106:42 Adui zao wakawadhulumu na kuwatia chini ya mkono wao.
PSA 106:43 Mara nyingi aliwaokoa lakini walizama kwenye uasi, na wakajiharibu katika dhambi zao.
PSA 106:44 Lakini akaangalia mateso yao aliposikia kilio chao;
PSA 106:45 kwa ajili yao akakumbuka agano lake, na kutokana na upendo wake mkuu akapooza hasira yake.
PSA 106:46 Akawafanya wahurumiwe na wote waliowashikilia mateka.
PSA 106:47 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tuokoe. Tukusanye tena kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako.
PSA 106:48 Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Watu wote na waseme, “Amen!” Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 107:1 Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa yeye ni mwema, fadhili zake zadumu milele.
PSA 107:2 Waliokombolewa wa Mwenyezi Mungu na waseme hivi, wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,
PSA 107:3 wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini.
PSA 107:4 Baadhi yao walitangatanga jangwani, hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi.
PSA 107:5 Walikuwa na njaa na kiu, nafsi zao zikadhoofika.
PSA 107:6 Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao.
PSA 107:7 Akawaongoza kwa njia iliyo sawa hadi mji ambao wangeweza kuishi.
PSA 107:8 Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
PSA 107:9 kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu, na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.
PSA 107:10 Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo,
PSA 107:11 kwa sababu waliasi dhidi ya maneno ya Mungu, na kudharau ushauri wa Aliye Juu Sana.
PSA 107:12 Aliwatumikisha kwa kazi ngumu; walijikwaa na hapakuwa na mtu wa kuwasaidia.
PSA 107:13 Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao.
PSA 107:14 Akawatoa katika giza na huzuni kuu na akavunja minyororo yao.
PSA 107:15 Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
PSA 107:16 kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma.
PSA 107:17 Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao, wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao.
PSA 107:18 Wakachukia kabisa vyakula vyote, wakakaribia malango ya mauti.
PSA 107:19 Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao.
PSA 107:20 Akalituma neno lake na kuwaponya, akawaokoa kutoka maangamizi yao.
PSA 107:21 Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
PSA 107:22 Na watoe dhabihu za kushukuru, na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.
PSA 107:23 Wengine walisafiri baharini kwa meli, walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu.
PSA 107:24 Waliziona kazi za Mwenyezi Mungu, matendo yake ya ajabu kilindini.
PSA 107:25 Kwa maana alisema na kuamsha tufani iliyoinua mawimbi juu.
PSA 107:26 Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini; katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka.
PSA 107:27 Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi, ujanja wao ukafikia ukomo.
PSA 107:28 Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao, naye akawatoa kwenye taabu yao.
PSA 107:29 Akatuliza dhoruba kwa mnong’ono, mawimbi ya bahari yakatulia.
PSA 107:30 Walifurahi ilipokuwa shwari, naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani.
PSA 107:31 Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
PSA 107:32 Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu, na wamsifu katika baraza la wazee.
PSA 107:33 Yeye aligeuza mito kuwa jangwa, chemchemi za maji zinazotiririka kuwa ardhi yenye kiu,
PSA 107:34 nchi inayozaa ikawa ya chumvi isiyofaa, kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo.
PSA 107:35 Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji, nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zinazotiririka;
PSA 107:36 aliwaleta wenye njaa wakaishi humo, nao wakajenga mji wangeweza kuishi.
PSA 107:37 Walilima mashamba na kupanda mizabibu, nayo ikazaa matunda mengi,
PSA 107:38 Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana, wala hakuruhusu mifugo yao kupungua.
PSA 107:39 Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa kwa kuonewa, maafa na huzuni.
PSA 107:40 Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu, aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia.
PSA 107:41 Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao, na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo.
PSA 107:42 Wanyofu wataona na kufurahi, lakini waovu wote watafunga vinywa vyao.
PSA 107:43 Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya, na atafakari upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu.
PSA 108:1 Wimbo. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
PSA 108:2 Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko.
PSA 108:3 Nitakusifu wewe, Ee Mwenyezi Mungu, kati ya mataifa; nitaimba habari zako, katika jamaa za watu.
PSA 108:4 Kwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu; uaminifu wako unazifikia anga.
PSA 108:5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote.
PSA 108:6 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale unaowapenda wapate kuokolewa.
PSA 108:7 Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi.
PSA 108:8 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni chapeo yangu, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
PSA 108:9 Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
PSA 108:10 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
PSA 108:11 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu?
PSA 108:12 Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
PSA 108:13 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu.
PSA 109:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, ninayekusifu, usiwe kimya,
PSA 109:2 kwa maana watu waovu na wadanganyifu wamefungua vinywa vyao dhidi yangu; wasema dhidi yangu kwa ndimi za udanganyifu.
PSA 109:3 Wamenizunguka kwa maneno ya chuki, wananishambulia bila sababu.
PSA 109:4 Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki, lakini mimi ninawaombea.
PSA 109:5 Wananilipiza mabaya kwa mema, chuki badala ya urafiki wangu.
PSA 109:6 Agiza mtu mwovu ampinge, mshtaki asimame mkono wake wa kuume.
PSA 109:7 Anapohukumiwa, apatikane na hatia, nayo maombi yake yamhukumu.
PSA 109:8 Siku zake za kuishi na ziwe chache, nafasi yake ya uongozi ichukuliwe na mtu mwingine.
PSA 109:9 Watoto wake na waachwe yatima, mke wake na awe mjane.
PSA 109:10 Watoto wake na watangetange wakiomba, na wafukuzwe kwenye magofu ya nyumba zao.
PSA 109:11 Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo, matunda ya kazi yake yatekwe nyara na wageni.
PSA 109:12 Asiwepo mtu yeyote wa kumtendea mema wala wa kuwahurumia yatima wake.
PSA 109:13 Uzao wake na ukatiliwe mbali, majina yao yafutike katika kizazi kifuatacho.
PSA 109:14 Maovu ya baba zake na yakumbukwe mbele za Mwenyezi Mungu, dhambi ya mama yake isifutwe kamwe.
PSA 109:15 Dhambi zao na zibaki daima mbele za Mwenyezi Mungu, ili apate kukatilia mbali kumbukumbu lao duniani.
PSA 109:16 Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema, bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo.
PSA 109:17 Alipenda kulaani, nayo laana ikampata; hakupenda kubariki, kwa hiyo baraka na ikae mbali naye.
PSA 109:18 Alivaa kulaani kama vazi lake, nayo laana ikamwingia mwilini mwake kama maji, kwenye mifupa yake kama mafuta.
PSA 109:19 Na iwe kama joho alilozungushiwa, kama mshipi aliofungiwa daima.
PSA 109:20 Haya na yawe malipo ya Mwenyezi Mungu kwa washtaki wangu, kwa wale wanaoninenea mabaya.
PSA 109:21 Lakini wewe, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, unitendee wema kwa ajili ya jina lako, uniokoe kwa wema wa pendo lako.
PSA 109:22 Maana mimi ni maskini na mhitaji, moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu.
PSA 109:23 Ninafifia kama kivuli cha jioni, nimerushwa-rushwa kama nzige.
PSA 109:24 Magoti yangu yamelegea kwa kufunga, mwili wangu umedhoofika na kukonda.
PSA 109:25 Nimekuwa kitu cha kudharauliwa kwa washtaki wangu, wanionapo, hutikisa vichwa vyao.
PSA 109:26 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nisaidie, niokoe sawasawa na upendo wako.
PSA 109:27 Watu na wafahamu kuwa ni mkono wako, kwamba wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umetenda hili.
PSA 109:28 Wanaweza kulaani, lakini wewe utabariki, watakaposhambulia wataaibishwa, lakini mtumishi wako atashangilia.
PSA 109:29 Washtaki wangu watavikwa fedheha, na kufunikwa na aibu kama joho.
PSA 109:30 Kwa kinywa changu nitamtukuza sana Mwenyezi Mungu, katika umati mkubwa nitamsifu.
PSA 109:31 Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji, kuokoa maisha yake kutoka kwa wale wanaomhukumu.
PSA 110:1 Zaburi ya Daudi. Mwenyezi Mungu amwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowafanya adui zako kuwa mahali pa kuweka miguu yako.”
PSA 110:2 Mwenyezi Mungu ataeneza fimbo yako ya utawala yenye nguvu kutoka Sayuni; utatawala katikati ya adui zako.
PSA 110:3 Askari wako watajitolea kwa hiari katika siku yako ya vita. Ukiwa umevikwa fahari takatifu, kutoka tumbo la mapambazuko utapokea umande wa ujana wako.
PSA 110:4 Mwenyezi Mungu ameapa, naye hatabadilisha mawazo yake: “Wewe ni kuhani milele, kwa mfano wa Melkizedeki.”
PSA 110:5 Bwana yuko mkono wako wa kuume, atawaponda wafalme siku ya ghadhabu yake.
PSA 110:6 Atawahukumu mataifa, akilundika mizoga na kuwaponda watawala wa dunia nzima.
PSA 110:7 Atakunywa maji katika kijito kando ya njia; kwa hiyo atainua kichwa chake juu.
PSA 111:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Nitamtukuza Mwenyezi Mungu kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.
PSA 111:2 Kazi za Mwenyezi Mungu ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.
PSA 111:3 Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, haki yake hudumu daima.
PSA 111:4 Amefanya maajabu yake yakumbukwe, Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na huruma.
PSA 111:5 Huwapa chakula wale wanaomcha, hulikumbuka agano lake milele.
PSA 111:6 Amewaonesha watu wake uwezo wa kazi zake, akiwapa nchi za mataifa mengine.
PSA 111:7 Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, mausia yake yote ni ya kuaminika.
PSA 111:8 Zinadumu milele na milele, zikifanyika kwa uaminifu na unyofu.
PSA 111:9 Aliwapa watu wake ukombozi, aliamuru agano lake milele: jina lake ni takatifu na la kuogopwa.
PSA 111:10 Kumcha Mwenyezi Mungu ndicho chanzo cha hekima, wote wanaozifuata amri zake wana busara. Sifa zake zadumu milele.
PSA 112:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Heri mtu yule amchaye Mwenyezi Mungu, mtu yule apendezwaye sana na amri zake.
PSA 112:2 Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi, kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa.
PSA 112:3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri, haki yake hudumu milele.
PSA 112:4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu, yule mwenye rehema, huruma na haki.
PSA 112:5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba, anayefanya mambo yake kwa haki.
PSA 112:6 Hakika hatatikisika kamwe, mtu mwenye haki atakumbukwa milele.
PSA 112:7 Hataogopa habari mbaya, moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Mwenyezi Mungu.
PSA 112:8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu, mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.
PSA 112:9 Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele; pembe yake itatukuzwa kwa heshima.
PSA 112:10 Mtu mwovu ataona na kuchukizwa, atasaga meno yake na kutoweka, kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu.
PSA 113:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Enyi watumishi wa Mwenyezi Mungu msifuni, lisifuni jina la Mwenyezi Mungu.
PSA 113:2 Jina la Mwenyezi Mungu na lisifiwe, sasa na hata milele.
PSA 113:3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake, jina la Mwenyezi Mungu linapaswa kusifiwa.
PSA 113:4 Mwenyezi Mungu ametukuka juu ya mataifa yote, utukufu wake juu ya mbingu.
PSA 113:5 Ni nani aliye kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, Yule aliyeketi kwenye kiti cha enzi huko juu,
PSA 113:6 ambaye huinama atazame chini aone mbingu na nchi?
PSA 113:7 Huwainua maskini kutoka mavumbini, na kuwanyanyua wahitaji kutoka lundo la majivu,
PSA 113:8 huwaketisha pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.
PSA 113:9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake, akiwa mama watoto mwenye furaha. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 114:1 Israeli alipotoka Misri, nyumba ya Yakobo kutoka kwa watu wa lugha ngeni,
PSA 114:2 Yuda alifanywa makao matakatifu ya Mungu, Israeli akawa milki yake.
PSA 114:3 Bahari ilitazama ikakimbia, Yordani ulirudi nyuma,
PSA 114:4 milima ilirukaruka kama kondoo dume, vilima kama wana-kondoo.
PSA 114:5 Ee bahari, ni nini kilichokufanya ukakimbia, nawe, ee Yordani, ukarudi nyuma,
PSA 114:6 enyi milima mkarukaruka kama kondoo dume, enyi vilima, kama wana-kondoo?
PSA 114:7 Ee dunia, tetemeka mbele za Bwana, mbele za Mungu wa Yakobo,
PSA 114:8 aliyegeuza mwamba kuwa dimbwi la maji, mwamba mgumu kuwa chemchemi za maji.
PSA 115:1 Sio kwetu sisi, Ee Mwenyezi Mungu, sio kwetu sisi, bali utukufu ni kwa jina lako, kwa sababu ya upendo na uaminifu wako.
PSA 115:2 Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wao?”
PSA 115:3 Mungu wetu yuko mbinguni, naye hufanya lolote limpendezalo.
PSA 115:4 Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
PSA 115:5 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona;
PSA 115:6 zina masikio, lakini haziwezi kusikia, zina pua, lakini haziwezi kunusa;
PSA 115:7 zina mikono, lakini haziwezi kupapasa, zina miguu, lakini haziwezi kutembea; wala koo zao haziwezi kutoa sauti.
PSA 115:8 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
PSA 115:9 Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Mwenyezi Mungu, yeye ni msaada na ngao yao.
PSA 115:10 Ee nyumba ya Haruni, mtumainini Mwenyezi Mungu, yeye ni msaada na ngao yao.
PSA 115:11 Ninyi mnaomcha, mtumainini Mwenyezi Mungu, yeye ni msaada na ngao yao.
PSA 115:12 Mwenyezi Mungu anatukumbuka na atatubariki: ataibariki nyumba ya Israeli, ataibariki nyumba ya Haruni,
PSA 115:13 atawabariki wale wanaomcha Mwenyezi Mungu, wadogo kwa wakubwa.
PSA 115:14 Mwenyezi Mungu na awawezeshe kuongezeka, ninyi na watoto wenu.
PSA 115:15 Mbarikiwe na Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na dunia.
PSA 115:16 Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Mwenyezi Mungu, lakini dunia amempa mwanadamu.
PSA 115:17 Sio wafu wanaomsifu Mwenyezi Mungu, wale wanaoshuka mahali pa kimya,
PSA 115:18 bali ni sisi tunaomtukuza Mwenyezi Mungu, sasa na hata milele. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 116:1 Nampenda Mwenyezi Mungu kwa maana amesikia sauti yangu; amesikia kilio changu ili anihurumie.
PSA 116:2 Kwa sababu amenitegea sikio lake, nitamwita siku zote za maisha yangu.
PSA 116:3 Kamba za mauti zilinizunguka, vitisho vya Kuzimu vilinipata, nikalemewa na taabu na huzuni.
PSA 116:4 Ndipo nikaliitia jina la Mwenyezi Mungu: “Ee Mwenyezi Mungu, niokoe!”
PSA 116:5 Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na haki, Mungu wetu ni mwingi wa huruma.
PSA 116:6 Mwenyezi Mungu huwalinda wanyenyekevu, nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.
PSA 116:7 Ee nafsi yangu, tulia tena, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuwa mwema kwako.
PSA 116:8 Kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeniokoa nafsi yangu na mauti, macho yangu kutokana na machozi, miguu yangu kutokana na kujikwaa,
PSA 116:9 ili niweze kutembea mbele za Mwenyezi Mungu, katika nchi ya walio hai.
PSA 116:10 Nilimwamini Mwenyezi Mungu, niliposema, “Mimi nimeteseka sana.”
PSA 116:11 Katika taabu yangu nilisema, “Wanadamu wote ni waongo.”
PSA 116:12 Nimrudishie Mwenyezi Mungu nini kwa wema wake wote alionitendea?
PSA 116:13 Nitakiinua kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu.
PSA 116:14 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu mbele za watu wake wote.
PSA 116:15 Kifo cha watakatifu kina thamani machoni pa Mwenyezi Mungu.
PSA 116:16 Ee Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mtumishi wako, mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako; umeniweka huru toka katika minyororo yangu.
PSA 116:17 Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru na kuliita jina la Mwenyezi Mungu.
PSA 116:18 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu mbele za watu wake wote,
PSA 116:19 katika nyua za nyumba ya Mwenyezi Mungu, katikati yako, ee Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 117:1 Msifuni Mwenyezi Mungu, enyi mataifa yote; mtukuzeni yeye, enyi watu wote.
PSA 117:2 Kwa kuwa upendo wake kwetu ni mkuu, uaminifu wa Mwenyezi Mungu unadumu milele. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 118:1 Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ni mwema; fadhili zake zadumu milele.
PSA 118:2 Israeli na aseme sasa: “Fadhili zake zadumu milele.”
PSA 118:3 Nyumba ya Haruni na iseme sasa: “Fadhili zake zadumu milele.”
PSA 118:4 Wote wanaomcha Mwenyezi Mungu na waseme sasa: “Fadhili zake zadumu milele.”
PSA 118:5 Wakati wa maumivu yangu makuu, nilimlilia Mwenyezi Mungu, naye akanijibu kwa kuniweka huru.
PSA 118:6 Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami, sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
PSA 118:7 Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami, yeye ni msaidizi wangu. Nitawatazama adui zangu wakiwa wameshindwa.
PSA 118:8 Ni bora kumkimbilia Mwenyezi Mungu kuliko kumtumainia mwanadamu.
PSA 118:9 Ni bora kumkimbilia Mwenyezi Mungu kuliko kuwatumainia wakuu.
PSA 118:10 Mataifa yote yalinizunguka, lakini kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
PSA 118:11 Walinizunguka pande zote, lakini kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
PSA 118:12 Walinizunguka kama kundi la nyuki, lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo; kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
PSA 118:13 Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka, lakini Mwenyezi Mungu alinisaidia.
PSA 118:14 Mwenyezi Mungu ni nguvu yangu na wimbo wangu, yeye amefanyika wokovu wangu.
PSA 118:15 Sauti za shangwe na ushindi zinavuma kwenye hema za wenye haki: “Mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu umetenda mambo makuu!
PSA 118:16 Mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu umeinuliwa juu, mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu umetenda mambo makuu!”
PSA 118:17 Sitakufa, bali nitaishi, nami nitayatangaza matendo ya Mwenyezi Mungu.
PSA 118:18 Mwenyezi Mungu ameniadhibu vikali, lakini hakuniacha nife.
PSA 118:19 Nifungulie malango ya haki, nami nitaingia na kumshukuru Mwenyezi Mungu.
PSA 118:20 Hili ni lango la Mwenyezi Mungu ambalo wenye haki wanaweza kuliingia.
PSA 118:21 Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu, umekuwa wokovu wangu.
PSA 118:22 Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni.
PSA 118:23 Mwenyezi Mungu ametenda hili, nalo ni la kushangaza machoni petu.
PSA 118:24 Hii ndiyo siku Mwenyezi Mungu aliyoifanya, tushangilie na kufurahi ndani yake.
PSA 118:25 Ee Mwenyezi Mungu, tuokoe, Ee Mwenyezi Mungu, utujalie mafanikio.
PSA 118:26 Heri yule ajaye kwa jina la Mwenyezi Mungu. Kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu tunakubariki.
PSA 118:27 Mwenyezi Mungu ndiye Mungu, naye ametuangazia nuru yake. Mkiwa na matawi mkononi, unganeni kwenye maandamano ya sikukuu hadi kwenye pembe za madhabahu.
PSA 118:28 Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru, wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.
PSA 118:29 Mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mwema; fadhili zake zadumu milele.
PSA 119:1 Heri wale walio waadilifu katika njia zao, wanaoenenda katika Torati ya Mwenyezi Mungu.
PSA 119:2 Heri wale wanaozishika shuhuda zake, wanaomtafuta kwa moyo wao wote.
PSA 119:3 Wasiofanya lolote lililo baya, wanaoenenda katika njia zake.
PSA 119:4 Umetoa maagizo yako ili tuyatii kwa ukamilifu.
PSA 119:5 Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara katika kuyatii maagizo yako!
PSA 119:6 Hivyo mimi sitaaibishwa ninapozingatia amri zako zote.
PSA 119:7 Nitakusifu kwa moyo mnyofu ninapojifunza sheria zako za haki.
PSA 119:8 Nitayatii maagizo yako; usiniache kabisa.
PSA 119:9 Kijana aisafishe njia yake jinsi gani? Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.
PSA 119:10 Ninakutafuta kwa moyo wangu wote, usiniache niende mbali na amri zako.
PSA 119:11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu ili nisikutende dhambi.
PSA 119:12 Uhimidiwe, Ee Mwenyezi Mungu; nifundishe maagizo yako.
PSA 119:13 Kwa midomo yangu nitasimulia sheria zote zinazotoka katika kinywa chako.
PSA 119:14 Ninafurahia kufuata sheria zako kama mtu afurahiaye mali nyingi.
PSA 119:15 Ninatafakari maagizo yako na kuziangalia njia zako.
PSA 119:16 Ninafurahia maagizo yako, wala sitalipuuza neno lako.
PSA 119:17 Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi; nitalitii neno lako.
PSA 119:18 Yafungue macho yangu nipate kuona mambo ya ajabu katika sheria yako.
PSA 119:19 Mimi ni mgeni duniani, usinifiche amri zako.
PSA 119:20 Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa kwa sheria zako wakati wote.
PSA 119:21 Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa, wanaoenda mbali na amri zako.
PSA 119:22 Niondolee dharau na dhihaka, kwa kuwa ninazishika sheria zako.
PSA 119:23 Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako.
PSA 119:24 Sheria zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu.
PSA 119:25 Nimelazwa chini mavumbini, yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako.
PSA 119:26 Nilikueleza njia zangu ukanijibu, nifundishe sheria zako.
PSA 119:27 Nijulishe mafundisho ya mausia yako, nami nitatafakari maajabu yako.
PSA 119:28 Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni, uniimarishe sawasawa na neno lako.
PSA 119:29 Niepushe na njia za udanganyifu, kwa neema unifundishe sheria zako.
PSA 119:30 Nimechagua njia ya kweli, nimekaza moyo wangu katika sheria zako.
PSA 119:31 Nimeng’ang’ania sheria zako, Ee Mwenyezi Mungu, usiniache niaibishwe.
PSA 119:32 Nakimbilia katika njia ya maagizo yako, kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru.
PSA 119:33 Ee Mwenyezi Mungu, nifundishe kuyafuata maagizo yako, nami nitayashika hadi mwisho.
PSA 119:34 Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako na kuitii kwa moyo wangu wote.
PSA 119:35 Niongoze kwenye njia ya amri zako, kwa kuwa huko napata furaha.
PSA 119:36 Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi.
PSA 119:37 Geuza macho yangu kutoka mambo yasiyofaa, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako.
PSA 119:38 Mtimizie mtumishi wako ahadi yako, ili upate kuogopwa.
PSA 119:39 Niondolee aibu ninayoiogopa, kwa kuwa sheria zako ni njema.
PSA 119:40 Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako! Hifadhi maisha yangu katika haki yako.
PSA 119:41 Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako usiokoma unijie, wokovu wako sawasawa na ahadi yako,
PSA 119:42 ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki, kwa kuwa ninalitumainia neno lako.
PSA 119:43 Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako.
PSA 119:44 Nitaitii amri yako daima, naam, milele na milele.
PSA 119:45 Nitatembea huru, kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
PSA 119:46 Nitasema sheria zako mbele za wafalme wala sitaaibishwa,
PSA 119:47 kwa kuwa ninazifurahia amri zako kwa sababu ninazipenda.
PSA 119:48 Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu, nami ninatafakari juu ya maagizo yako.
PSA 119:49 Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako, kwa sababu umenipa tumaini.
PSA 119:50 Faraja yangu katika mateso yangu ni hii: Ahadi yako inahifadhi maisha yangu.
PSA 119:51 Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka, hata hivyo sitaiacha sheria yako.
PSA 119:52 Ee Mwenyezi Mungu, ninazikumbuka sheria zako za zamani, nazo zinanifariji.
PSA 119:53 Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu, ambao wameacha sheria yako.
PSA 119:54 Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu popote ninapoishi.
PSA 119:55 Ee Mwenyezi Mungu, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako, nami nitatii sheria yako.
PSA 119:56 Hili limekuwa zoezi langu: nami ninayatii mausia yako.
PSA 119:57 Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni fungu langu, nimeahidi kuyatii maneno yako.
PSA 119:58 Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote, nihurumie sawasawa na ahadi yako.
PSA 119:59 Nimezifikiri njia zangu na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako.
PSA 119:60 Nitafanya haraka bila kuchelewa kuzitii amri zako.
PSA 119:61 Hata waovu wanifunge kwa kamba, sitasahau sheria yako.
PSA 119:62 Usiku wa manane ninaamka kukushukuru kwa sababu ya sheria zako za haki.
PSA 119:63 Mimi ni rafiki kwa wale wote wanaokucha, kwa wote wanaofuata mausia yako.
PSA 119:64 Ee Mwenyezi Mungu, dunia imejaa upendo wako, nifundishe maagizo yako.
PSA 119:65 Mtendee wema mtumishi wako Ee Mwenyezi Mungu, sawasawa na neno lako.
PSA 119:66 Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri, kwa kuwa ninaamini amri zako.
PSA 119:67 Kabla sijapata shida nilipotea njia, lakini sasa ninalitii neno lako.
PSA 119:68 Wewe ni mwema, unalotenda ni jema, nifundishe maagizo yako.
PSA 119:69 Ingawa wenye majivuno wamenisingizia uongo, nitafuata mausia yako kwa moyo wangu wote.
PSA 119:70 Mioyo yao ni katili na migumu, bali mimi napendezwa na sheria yako.
PSA 119:71 Ilikuwa vyema mimi kupata shida ili nipate kujifunza maagizo yako.
PSA 119:72 Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu.
PSA 119:73 Mikono yako iliniumba na kunitengeneza, nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako.
PSA 119:74 Wale wanaokucha na wafurahie wanaponiona, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako.
PSA 119:75 Ee Mwenyezi Mungu, ninajua kwamba sheria zako ni za haki, katika uaminifu wako umeniadhibu.
PSA 119:76 Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu, sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
PSA 119:77 Huruma yako na inijie ili nipate kuishi, kwa kuwa naifurahia sheria yako.
PSA 119:78 Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu, lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako.
PSA 119:79 Wale wanaokucha na wanigeukie mimi, hao ambao wanazielewa sheria zako.
PSA 119:80 Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako, ili nisiaibishwe.
PSA 119:81 Nafsi yangu inazimia kwa kutamani wokovu wako, lakini nimeweka tumaini langu katika neno lako.
PSA 119:82 Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako; ninasema, “Utanifariji lini?”
PSA 119:83 Ingawa nimekuwa kama kiriba kwenye moshi, bado sijasahau maagizo yako.
PSA 119:84 Mtumishi wako itampasa angoje hadi lini? Ni lini utawaadhibu washtaki wangu?
PSA 119:85 Wenye majivuno wananichimbia mashimo, kinyume na sheria yako.
PSA 119:86 Amri zako zote ni za kuaminika; unisaidie, kwa sababu watu wananishtaki bila sababu.
PSA 119:87 Walikaribia kabisa kunifuta kutoka uso wa dunia, lakini sijaacha mausia yako.
PSA 119:88 Yahifadhi maisha yangu sawasawa na upendo wako, nami nitatii sheria za kinywa chako.
PSA 119:89 Ee Mwenyezi Mungu, neno lako ni la milele, linasimama imara mbinguni.
PSA 119:90 Uaminifu wako unaendelea kwa vizazi vyote, umeiumba dunia, nayo inadumu.
PSA 119:91 Sheria zako zinadumu hadi leo, kwa kuwa vitu vyote vinakutumikia.
PSA 119:92 Kama nisingefurahia sheria yako, ningeangamia katika taabu zangu.
PSA 119:93 Sitasahau mausia yako kamwe, kwa maana kwayo umehifadhi maisha yangu.
PSA 119:94 Uniokoe, kwa maana mimi ni wako, kwa kuwa nimetafuta mausia yako.
PSA 119:95 Waovu wanangojea kuniangamiza, bali mimi ninatafakari sheria zako.
PSA 119:96 Katika ukamilifu wote ninaona mna kikomo, lakini amri zako hazina mwisho.
PSA 119:97 Aha! Tazama, sheria yako naipenda mno ajabu. Ninaitafakari mchana kutwa.
PSA 119:98 Amri zako zimenipa hekima kuliko adui zangu, kwa kuwa nimezishika daima.
PSA 119:99 Nina akili kuliko walimu wangu wote, kwa kuwa ninatafakari kuhusu sheria zako.
PSA 119:100 Nina ufahamu kuliko wazee, kwa kuwa ninayatii mausia yako.
PSA 119:101 Nimezuia miguu yangu isiende kwenye kila njia mbaya, ili niweze kutii neno lako.
PSA 119:102 Sijaziacha sheria zako, kwa kuwa umenifundisha wewe mwenyewe.
PSA 119:103 Tazama jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu, matamu kuliko asali katika kinywa changu!
PSA 119:104 Ninapata ufahamu kutoka mausia yako, kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu.
PSA 119:105 Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu.
PSA 119:106 Nimeapa na nimethibitisha, kwamba nitafuata sheria zako za haki.
PSA 119:107 Nimeteseka sana, uhifadhi maisha yangu, Ee Mwenyezi Mungu, sawasawa na neno lako.
PSA 119:108 Ee Mwenyezi Mungu, pokea sifa za hiari za kinywa changu, nifundishe sheria zako.
PSA 119:109 Ingawa maisha yangu yako hatarini siku zote, sitasahau sheria yako.
PSA 119:110 Waovu wamenitegea mtego, lakini sijayakiuka maagizo yako.
PSA 119:111 Sheria zako ni urithi wangu milele, naam ni furaha ya moyo wangu.
PSA 119:112 Nimekusudia moyoni mwangu kuyafuata maagizo yako hadi mwisho.
PSA 119:113 Ninachukia watu wa nia mbili, lakini ninapenda sheria yako.
PSA 119:114 Wewe ni kimbilio langu na ngao yangu, nimeweka tumaini langu katika neno lako.
PSA 119:115 Ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu, ili niweze kushika amri za Mungu wangu!
PSA 119:116 Nihifadhi sawasawa na ahadi yako, nami nitaishi; usiache matumaini yangu yakavunjwa.
PSA 119:117 Nitegemeze, nami nitaokolewa, nami daima nitayaheshimu maagizo yako.
PSA 119:118 Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako, kwa maana udanganyifu wao ni bure.
PSA 119:119 Waovu wa nchi unawatupa kama takataka, kwa hivyo nazipenda sheria zako.
PSA 119:120 Mwili wangu unatetemeka kwa kukuogopa wewe, ninaziogopa sheria zako.
PSA 119:121 Nimetenda yaliyo haki na sawa, usiniache mikononi mwa watesi wangu.
PSA 119:122 Mhakikishie mtumishi wako usalama, usiache wenye kiburi wanidhulumu.
PSA 119:123 Macho yangu yamefifia, yakitazamia wokovu wako, na kuitazamia ahadi yako ya kweli.
PSA 119:124 Mtendee mtumishi wako kulingana na upendo wako na unifundishe maagizo yako.
PSA 119:125 Mimi ni mtumishi wako; nipe busara ili niweze kuelewa sheria zako.
PSA 119:126 Ee Mwenyezi Mungu, wakati wako wa kutenda umewadia, kwa kuwa sheria yako inavunjwa.
PSA 119:127 Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu, naam, zaidi ya dhahabu safi,
PSA 119:128 na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili, nachukia kila njia potovu.
PSA 119:129 Sheria zako ni za ajabu, hivyo ninazitii.
PSA 119:130 Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru, kunampa mjinga ufahamu.
PSA 119:131 Nimefungua kinywa changu na kuhema, nikitamani amri zako.
PSA 119:132 Nigeukie na unihurumie, kama uwafanyiavyo siku zote wale wanaolipenda jina lako.
PSA 119:133 Ongoza hatua zangu kulingana na neno lako, usiache dhambi yoyote initawale.
PSA 119:134 Niokoe na uonevu wa wanadamu, ili niweze kutii mausia yako.
PSA 119:135 Mwangazie mtumishi wako uso wako na unifundishe amri zako.
PSA 119:136 Chemchemi za machozi zinatiririka machoni yangu, kwa kuwa sheria yako haifuatwi.
PSA 119:137 Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni mwenye haki, sheria zako ni sahihi.
PSA 119:138 Sheria ulizoziweka ni za haki, ni za kuaminika kikamilifu.
PSA 119:139 Jitihada yangu imenidhoofisha, kwa kuwa adui zangu wanayapuuza maneno yako.
PSA 119:140 Ahadi zako zimejaribiwa kikamilifu, mtumishi wako anazipenda.
PSA 119:141 Ingawa ni mdogo na ninadharauliwa, sisahau mausia yako.
PSA 119:142 Haki yako ni ya milele, na sheria yako ni kweli.
PSA 119:143 Shida na dhiki zimenipata, lakini amri zako ni furaha yangu.
PSA 119:144 Sheria zako ni sahihi milele, hunipa ufahamu ili nipate kuishi.
PSA 119:145 Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita kwa moyo wangu wote, nami nitayatii maagizo yako.
PSA 119:146 Ninakuita; niokoe nami nitazishika sheria zako.
PSA 119:147 Ninaamka asubuhi na mapema na kukuomba msaada; nimeweka tumaini langu katika neno lako.
PSA 119:148 Sikufumba macho yangu usiku kucha, ili niweze kutafakari juu ya ahadi zako.
PSA 119:149 Usikie sauti yangu sawasawa na upendo wako, Ee Mwenyezi Mungu, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na sheria zako.
PSA 119:150 Wale wanaopanga mipango miovu wako karibu nami, lakini wako mbali na sheria yako.
PSA 119:151 Ee Mwenyezi Mungu, hata hivyo wewe u karibu, na amri zako zote ni za kweli.
PSA 119:152 Tangu zamani nimejifunza kutoka shuhuda zako kwamba umezithibitisha ili zidumu milele.
PSA 119:153 Yaangalie mateso yangu, uniokoe, kwa kuwa sijasahau sheria yako.
PSA 119:154 Nitetee katika hali hii yangu na unikomboe, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na ahadi yako.
PSA 119:155 Wokovu uko mbali na waovu, kwa kuwa hawatafuti maagizo yako.
PSA 119:156 Ee Mwenyezi Mungu, huruma zako ni kuu, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na sheria zako.
PSA 119:157 Adui wanaonitesa ni wengi, lakini mimi sitaziacha sheria zako.
PSA 119:158 Ninawatazama wasioamini kwa chuki, kwa kuwa hawalitii neno lako.
PSA 119:159 Tazama jinsi ninavyopenda mausia yako; Ee Mwenyezi Mungu, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na upendo wako.
PSA 119:160 Maneno yako yote ni kweli, sheria zako zote za haki ni za milele.
PSA 119:161 Watawala wamenitesa bila sababu, lakini moyo wangu unatetemeka kwa neno lako.
PSA 119:162 Nafurahia ahadi zako kama mtu aliyepata mateka mengi.
PSA 119:163 Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo, lakini napenda sheria yako.
PSA 119:164 Ninakusifu mara saba kwa siku, kwa ajili ya sheria zako za haki.
PSA 119:165 Wanaopenda sheria yako wana amani tele, wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza.
PSA 119:166 Ee Mwenyezi Mungu, ninangojea wokovu wako, nami ninafuata amri zako,
PSA 119:167 Ninazitii sheria zako, kwa sababu ninazipenda mno.
PSA 119:168 Nimetii mausia yako na sheria zako, kwa kuwa njia zangu zote zinajulikana kwako.
PSA 119:169 Ee Mwenyezi Mungu, kilio changu na kifike mbele zako, nipe ufahamu sawasawa na neno lako.
PSA 119:170 Maombi yangu na yafike mbele zako, niokoe sawasawa na ahadi yako.
PSA 119:171 Midomo yangu na ibubujike sifa, kwa kuwa unanifundisha maagizo yako.
PSA 119:172 Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, kwa kuwa amri zako zote ni za haki.
PSA 119:173 Mkono wako uwe tayari kunisaidia, kwa kuwa nimechagua mausia yako.
PSA 119:174 Ee Mwenyezi Mungu, ninatamani wokovu wako, na sheria yako ni furaha yangu.
PSA 119:175 Nijalie kuishi ili nipate kukusifu, na sheria zako zinitegemeze.
PSA 119:176 Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea. Mtafute mtumishi wako, kwa kuwa sijasahau amri zako.
PSA 120:1 Wimbo wa kwenda juu. Katika dhiki yangu namwita Mwenyezi Mungu, naye hunijibu.
PSA 120:2 Ee Mwenyezi Mungu, uniokoe kutoka midomo ya uongo na ndimi za udanganyifu.
PSA 120:3 Atakufanyia nini, au akufanyie nini zaidi, ewe ulimi mdanganyifu?
PSA 120:4 Atakuadhibu kwa mishale mikali ya shujaa, kwa makaa yanayowaka ya mti wa mretemu.
PSA 120:5 Ole wangu kwa kuwa naishi Mesheki, kwamba naishi katikati ya mahema ya Kedari!
PSA 120:6 Nimeishi muda mrefu mno miongoni mwa wale wanaochukia amani.
PSA 120:7 Mimi ni mtu wa amani; lakini ninaposema, wao wanataka vita.
PSA 121:1 Wimbo wa kwenda juu. Nayainua macho yangu natazama milima: msaada wangu utatoka wapi?
PSA 121:2 Msaada wangu hutoka kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia.
PSA 121:3 Hatauacha mguu wako uteleze, yeye akulindaye hatasinzia,
PSA 121:4 hakika, yeye alindaye Israeli hatasinzia wala hatalala usingizi.
PSA 121:5 Mwenyezi Mungu anakulinda, Mwenyezi Mungu ni uvuli wako mkono wako wa kuume,
PSA 121:6 jua halitakudhuru mchana, wala mwezi wakati wa usiku.
PSA 121:7 Mwenyezi Mungu atakukinga na madhara yote, atayalinda maisha yako,
PSA 121:8 Mwenyezi Mungu atakulinda unapoingia na unapotoka, tangu sasa na hata milele.
PSA 122:1 Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi. Nilishangilia pamoja na wale walioniambia, “Twende nyumbani mwa Mwenyezi Mungu.”
PSA 122:2 Ee Yerusalemu, miguu yetu imesimama malangoni mwako.
PSA 122:3 Yerusalemu imejengwa vyema kama mji ulioshikamana pamoja.
PSA 122:4 Huko ndiko makabila hukwea, makabila ya Mwenyezi Mungu, kulisifu jina la Mwenyezi Mungu kulingana na maagizo waliopewa Israeli.
PSA 122:5 Huko viti vya hukumu hukaa, viti vya ufalme vya nyumba ya Daudi.
PSA 122:6 Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu: “Wote wanaokupenda na wawe salama.
PSA 122:7 Amani na iwe ndani ya kuta zako, na usalama ndani ya ngome zako.”
PSA 122:8 Kwa ajili ya ndugu na rafiki zangu, nitasema, “Amani iwe ndani yako.”
PSA 122:9 Kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, nitatafuta mafanikio yako.
PSA 123:1 Wimbo wa kwenda juu. Ninayainua macho yangu kwako, kwako wewe unayeketi mbinguni kwenye kiti chako cha enzi.
PSA 123:2 Kama vile macho ya watumwa yatazamavyo mkono wa bwana wao, kama vile macho ya mjakazi yatazamavyo mkono wa bibi yake, ndivyo macho yetu yamtazamavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, hadi atakapotuhurumia.
PSA 123:3 Uturehemu, Ee Mwenyezi Mungu, uturehemu, kwa maana tumevumilia dharau nyingi.
PSA 123:4 Tumevumilia dhihaka nyingi kutoka kwa wenye kiburi, dharau nyingi kutoka kwa wenye majivuno.
PSA 124:1 Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi. Kama Mwenyezi Mungu hangekuwa upande wetu; Israeli na aseme sasa:
PSA 124:2 kama Mwenyezi Mungu hangekuwa upande wetu, watu walipotushambulia,
PSA 124:3 hasira yao ilipowaka dhidi yetu, wangetumeza tukiwa hai,
PSA 124:4 mafuriko yangegharikisha, maji mengi yangetufunika,
PSA 124:5 maji yaendayo kasi yangetuchukua.
PSA 124:6 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao.
PSA 124:7 Tumeponyoka kama ndege kutoka mtego wa mwindaji; mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
PSA 124:8 Msaada wetu ni katika jina la Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia.
PSA 125:1 Wimbo wa kwenda juu. Wale wamtumainio Mwenyezi Mungu ni kama Mlima Sayuni, ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele.
PSA 125:2 Kama milima inavyozunguka Yerusalemu, ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowazunguka watu wake sasa na hata milele.
PSA 125:3 Fimbo ya waovu haitadumu juu ya nchi waliyopewa wenye haki, ili wenye haki wasije wakatumia mikono yao kutenda ubaya.
PSA 125:4 Ee Mwenyezi Mungu, watendee mema walio wema, wale walio wanyofu wa moyo.
PSA 125:5 Bali wale wanaogeukia njia zilizopotoka, Mwenyezi Mungu atawafukuza pamoja na watenda maovu. Amani iwe juu ya Israeli.
PSA 126:1 Wimbo wa kwenda juu. Mwenyezi Mungu alipowarejesha mateka Sayuni, tulikuwa kama watu walioota ndoto.
PSA 126:2 Vinywa vyetu vilijaa kicheko, ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe. Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa, “Mwenyezi Mungu amewatendea mambo makuu.”
PSA 126:3 Mwenyezi Mungu ametutendea mambo makuu, nasi tumejaa furaha.
PSA 126:4 Ee Mwenyezi Mungu, turejeshee watu wetu waliotekwa, kama vijito katika Negebu.
PSA 126:5 Wapandao kwa machozi watavuna kwa nyimbo za shangwe.
PSA 126:6 Yeye azichukuaye mbegu zake kwenda kupanda, huku akilia, atarudi kwa nyimbo za shangwe, akichukua miganda ya mavuno yake.
PSA 127:1 Wimbo wa kwenda juu. Wa Sulemani. Mwenyezi Mungu asipoijenga nyumba, wajengao hufanya kazi bure. Mwenyezi Mungu asipoulinda mji, walinzi wakesha bure.
PSA 127:2 Mnajisumbua bure kuamka mapema na kuchelewa kulala, mkitaabikia chakula: kwa maana yeye huwapa usingizi wapendwa wake.
PSA 127:3 Watoto ni urithi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu, uzao ni zawadi kutoka kwake.
PSA 127:4 Kama mishale mikononi mwa shujaa ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.
PSA 127:5 Heri mtu ambaye podo lake limejazwa nao. Hawataaibishwa wanaposhindana na adui zao langoni.
PSA 128:1 Wimbo wa kwenda juu. Heri wale wote wamchao Mwenyezi Mungu, wanaoenda katika njia zake.
PSA 128:2 Utakula matunda ya kazi yako; baraka na mafanikio vitakuwa vyako.
PSA 128:3 Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao ndani ya nyumba yako; wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni kuizunguka meza yako.
PSA 128:4 Hivyo ndivyo atakavyobarikiwa mtu amchaye Mwenyezi Mungu.
PSA 128:5 Mwenyezi Mungu na akubariki kutoka Sayuni siku zote za maisha yako, na uone mafanikio ya Yerusalemu,
PSA 128:6 nawe ujaliwe kuishi uone watoto wa watoto wako. Amani iwe juu ya Israeli.
PSA 129:1 Wimbo wa kwenda juu. Wamenitesa sana tangu ujana wangu; Israeli na aseme sasa:
PSA 129:2 wamenitesa sana tangu ujana wangu, lakini bado hawajanishinda.
PSA 129:3 Wakulima wamelima mgongo wangu, na kufanya mifereji yao mirefu.
PSA 129:4 Lakini Mwenyezi Mungu ni mwenye haki; amenifungua toka kamba za waovu.
PSA 129:5 Wale wote wanaoichukia Sayuni na warudishwe nyuma kwa aibu.
PSA 129:6 Wawe kama majani juu ya paa, ambayo hunyauka kabla hayajakua;
PSA 129:7 kwa hayo mvunaji hawezi kujaza vitanga vyake, wala akusanyaye kujaza mikono yake.
PSA 129:8 Wale wapitao karibu na wasiseme, “Baraka ya Mwenyezi Mungu iwe juu yako; tunakubariki katika jina la Mwenyezi Mungu.”
PSA 130:1 Wimbo wa kwenda juu. Kutoka vilindini ninakulilia, Ee Mwenyezi Mungu.
PSA 130:2 Ee Bwana, sikia sauti yangu. Masikio yako na yawe masikivu kwa kilio changu unihurumie.
PSA 130:3 Kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ungeweka kumbukumbu ya dhambi, Ee Bwana, ni nani angeweza kusimama?
PSA 130:4 Lakini kwako kuna msamaha, kwa hiyo wewe unaogopwa.
PSA 130:5 Namngojea Mwenyezi Mungu, nafsi yangu inangojea, katika neno lake naweka tumaini langu.
PSA 130:6 Nafsi yangu inamngojea Bwana kuliko walinzi waingojeavyo asubuhi, naam, kuliko walinzi waingojeavyo asubuhi.
PSA 130:7 Ee Israeli, mtumaini Mwenyezi Mungu, maana kwa Mwenyezi Mungu kuna upendo usiokoma, na kwake kuna ukombozi kamili.
PSA 130:8 Yeye mwenyewe ataikomboa Israeli kutoka dhambi zao zote.
PSA 131:1 Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi. Moyo wangu hauna kiburi, Ee Mwenyezi Mungu, macho yangu hayajivuni; sijishughulishi na mambo makuu kunizidi wala mambo ya ajabu mno kwangu.
PSA 131:2 Lakini nimetuliza na kunyamazisha nafsi yangu; kama mtoto aliyeachishwa kunyonya na mama yake, kama mtoto aliyeachishwa kunyonya ndivyo ilivyo nafsi iliyo ndani yangu.
PSA 131:3 Ee Israeli, mtumaini Mwenyezi Mungu tangu sasa na hata milele.
PSA 132:1 Wimbo wa kwenda juu. Ee Mwenyezi Mungu, mkumbuke Daudi na taabu zote alizozistahimili.
PSA 132:2 Aliapa kiapo kwa Mwenyezi Mungu na akaweka nadhiri kwa Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo:
PSA 132:3 “Sitaingia nyumbani mwangu au kwenda kitandani mwangu:
PSA 132:4 sitaruhusu usingizi katika macho yangu, wala kope zangu kusinzia,
PSA 132:5 hadi nitakapompatia Mwenyezi Mungu mahali, makao kwa ajili ya Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
PSA 132:6 Tulisikia habari hii huko Efrata, tulikutana nayo katika mashamba ya Yaara:
PSA 132:7 “Twendeni kwenye makao yake, na tuabudu kwenye kiti cha kuwekea miguu yake;
PSA 132:8 inuka, Ee Mwenyezi Mungu, uje mahali pako pa kupumzikia, wewe na Sanduku la nguvu zako.
PSA 132:9 Makuhani wako na wavikwe haki, watakatifu wako na waimbe kwa furaha.”
PSA 132:10 Kwa ajili ya Daudi mtumishi wako, usimkatae mpakwa mafuta wako.
PSA 132:11 Mwenyezi Mungu alimwapia Daudi kiapo, kiapo cha uhakika ambacho hatakitangua: “Nitamweka mmoja wa wazao wako mwenyewe kwenye kiti chako cha ufalme,
PSA 132:12 kama wanao watashika agano langu na sheria ninazowafundisha, ndipo wana wao watakalia kiti chako cha ufalme milele na milele.”
PSA 132:13 Kwa maana Mwenyezi Mungu ameichagua Sayuni, amepaonea shauku pawe maskani yake:
PSA 132:14 “Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele na milele; hapa ndipo nitakapoketi nikitawala, kwa sababu nimepaonea shauku:
PSA 132:15 Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele: nitashibisha maskini wake kwa chakula.
PSA 132:16 Nitawavika makuhani wake wokovu, nao watakatifu wake watadumu wakiimba kwa furaha.
PSA 132:17 “Hapa nitamchipushia Daudi pembe, na kuweka taa kwa ajili ya masiya wangu.
PSA 132:18 Adui zake nitawavika aibu, bali taji kichwani pake litang’aa sana.”
PSA 133:1 Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi. Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!
PSA 133:2 Ni kama mafuta ya thamani yaliyomiminwa kichwani, yakitiririka kwenye ndevu, yakitiririka kwenye ndevu za Haruni, hadi kwenye upindo wa mavazi yake.
PSA 133:3 Ni kama umande wa Hermoni ukianguka juu ya Mlima Sayuni. Kwa maana huko ndiko Mwenyezi Mungu alikoamuru baraka yake, naam, uzima hata milele.
PSA 134:1 Wimbo wa kwenda juu. Msifuni Mwenyezi Mungu, ninyi nyote watumishi wa Mwenyezi Mungu, ninyi mnaotumika usiku ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu.
PSA 134:2 Inueni mikono yenu katika patakatifu na kumsifu Mwenyezi Mungu.
PSA 134:3 Naye Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia, awabariki kutoka Sayuni.
PSA 135:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Lisifuni jina la Mwenyezi Mungu, msifuni, enyi watumishi wa Mwenyezi Mungu,
PSA 135:2 ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.
PSA 135:3 Msifuni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwema, liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza.
PSA 135:4 Kwa maana Mwenyezi Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe, Israeli kuwa hazina yake ya pekee.
PSA 135:5 Ninajua ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu, kwamba Bwana wetu ni mkuu kuliko miungu yote.
PSA 135:6 Mwenyezi Mungu hufanya lolote apendalo, mbinguni na duniani, katika bahari na vilindi vyake vyote.
PSA 135:7 Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia; hupeleka miali ya radi pamoja na mvua na huleta upepo kutoka ghala zake.
PSA 135:8 Alimuua mzaliwa wa kwanza wa Misri, mzaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama.
PSA 135:9 Alipeleka ishara zake na maajabu katikati yako, ee Misri, dhidi ya Farao na watumishi wake wote.
PSA 135:10 Aliyapiga mataifa mengi, na akaua wafalme wenye nguvu:
PSA 135:11 Mfalme Sihoni na Waamori, Ogu mfalme wa Bashani na wafalme wote wa Kanaani:
PSA 135:12 akatoa nchi yao kuwa urithi, urithi kwa watu wake Israeli.
PSA 135:13 Ee Mwenyezi Mungu, jina lako ladumu milele, kumbukumbu za fahari zako, Ee Mwenyezi Mungu, kwa vizazi vyote.
PSA 135:14 Maana Mwenyezi Mungu atawathibitisha watu wake, na kuwahurumia watumishi wake.
PSA 135:15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
PSA 135:16 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona;
PSA 135:17 zina masikio, lakini haziwezi kusikia, wala hakuna pumzi katika vinywa vyao.
PSA 135:18 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
PSA 135:19 Ee nyumba ya Israeli, msifuni Mwenyezi Mungu; ee nyumba ya Haruni, msifuni Mwenyezi Mungu;
PSA 135:20 ee nyumba ya Lawi, msifuni Mwenyezi Mungu; ninyi mnaomcha, msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 135:21 Msifuni Mwenyezi Mungu kutoka Sayuni, msifuni yeye aishiye Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 136:1 Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ni mwema.
PSA 136:2 Mshukuruni Mungu wa miungu.
PSA 136:3 Mshukuruni Bwana wa mabwana:
PSA 136:4 Kwake yeye pekee atendaye maajabu makuu,
PSA 136:5 Ambaye kwa ufahamu wake aliziumba mbingu,
PSA 136:6 Ambaye aliitandaza dunia juu ya maji,
PSA 136:7 Ambaye aliumba mianga mikubwa,
PSA 136:8 Jua litawale mchana,
PSA 136:9 Mwezi na nyota vitawale usiku,
PSA 136:10 Kwake yeye aliyemuua mzaliwa wa kwanza wa Misri,
PSA 136:11 Na kuwatoa Israeli katikati yao,
PSA 136:12 Kwa mkono wenye nguvu ulionyooshwa,
PSA 136:13 Kwake yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu,
PSA 136:14 Na kuwapitisha Israeli katikati yake,
PSA 136:15 Lakini alimfagia Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu,
PSA 136:16 Kwake yeye aliyewaongoza watu wake katika jangwa,
PSA 136:17 Ambaye aliwapiga wafalme wenye nguvu,
PSA 136:18 Naye aliwaua wafalme wenye nguvu,
PSA 136:19 Sihoni mfalme wa Waamori,
PSA 136:20 Ogu mfalme wa Bashani,
PSA 136:21 Akatoa nchi yao kuwa urithi,
PSA 136:22 Urithi kwa Israeli mtumishi wake,
PSA 136:23 Aliyetukumbuka katika unyonge wetu,
PSA 136:24 Alituweka huru toka adui zetu,
PSA 136:25 Ambaye humpa chakula kila kiumbe.
PSA 136:26 Mshukuruni Mungu wa mbinguni,
PSA 137:1 Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza tulipokumbuka Sayuni.
PSA 137:2 Kwenye miti ya huko tulitundika vinubi vyetu,
PSA 137:3 kwa maana huko hao waliotuteka walitaka tuwaimbie nyimbo; watesi wetu walidai nyimbo za furaha; walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja kati ya nyimbo za Sayuni!”
PSA 137:4 Tutaimbaje nyimbo za Mwenyezi Mungu, tukiwa nchi ya kigeni?
PSA 137:5 Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu, basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake.
PSA 137:6 Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu kama sitakukumbuka wewe, kama nisipokufikiri Yerusalemu kuwa furaha yangu kubwa.
PSA 137:7 Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, walichokifanya Waedomu, siku ile Yerusalemu ilipoanguka. Walisema, “Bomoa, bomoa hata misingi yake!”
PSA 137:8 Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa, heri yeye atakayekulipiza wewe kwa yale uliyotutenda sisi:
PSA 137:9 yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga na kuwaponda juu ya miamba.
PSA 138:1 Zaburi ya Daudi. Nitakusifu wewe, Ee Mwenyezi Mungu, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.
PSA 138:2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa maana umeitukuza ahadi yako zaidi ya jina lako.
PSA 138:3 Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.
PSA 138:4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Mwenyezi Mungu, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.
PSA 138:5 Wao na waimbe kuhusu njia za Mwenyezi Mungu, kwa maana utukufu wa Mwenyezi Mungu ni mkuu.
PSA 138:6 Ingawa Mwenyezi Mungu yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali.
PSA 138:7 Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.
PSA 138:8 Mwenyezi Mungu atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.
PSA 139:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, umenichunguza na kunijua.
PSA 139:2 Unajua ninapoketi na ninapoinuka; unatambua mawazo yangu tokea mbali.
PSA 139:3 Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu; unaelewa njia zangu zote.
PSA 139:4 Kabla neno halijafika katika ulimi wangu, wewe walijua kikamilifu, Ee Mwenyezi Mungu.
PSA 139:5 Umenizingira nyuma na mbele; umeweka mkono wako juu yangu.
PSA 139:6 Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu, ni ya juu sana kwangu kuyafikia.
PSA 139:7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
PSA 139:8 Nikienda juu mbinguni, wewe uko huko; nikifanya vilindi kuwa kitanda changu, wewe uko huko.
PSA 139:9 Nikipanda juu kwa mabawa ya mapambazuko, nikikaa pande za mbali za bahari,
PSA 139:10 hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.
PSA 139:11 Nikisema, “Hakika giza litanificha na nuru inayonizunguka iwe usiku,”
PSA 139:12 hata giza halitakuwa giza kwako, usiku utang’aa kama mchana, kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.
PSA 139:13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.
PSA 139:14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu.
PSA 139:15 Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,
PSA 139:16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwa hata moja.
PSA 139:17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu! Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!
PSA 139:18 Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi kuliko mchanga: niamkapo, bado niko pamoja nawe.
PSA 139:19 Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu! Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!
PSA 139:20 Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya, adui zako wanatumia vibaya jina lako.
PSA 139:21 Ee Mwenyezi Mungu, je, nisiwachukie wanaokuchukia? Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?
PSA 139:22 Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao, ninawahesabu ni adui zangu.
PSA 139:23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu, nijaribu na ujue mawazo yangu.
PSA 139:24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu, uniongoze katika njia ya milele.
PSA 140:1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, niokoe, kutoka kwa watu waovu; nilinde na watu wenye jeuri,
PSA 140:2 ambao hupanga mipango mibaya mioyoni mwao, na kuchochea vita siku zote.
PSA 140:3 Wao hufanya ndimi zao kali kama za nyoka, sumu ya nyoka iko midomoni mwao.
PSA 140:4 Ee Mwenyezi Mungu, niepushe na mikono ya waovu; nilinde na watu wenye jeuri wanaopanga kunikwaza miguu yangu.
PSA 140:5 Wenye kiburi wameficha mtego wa kuninasa, wametandaza kamba za wavu wao, wametega mitego kwenye njia yangu.
PSA 140:6 Ee Mwenyezi Mungu, ninakuambia, “Wewe ni Mungu wangu.” Ee Mwenyezi Mungu, usikie kilio changu na kunihurumia.
PSA 140:7 Ee Bwana Mungu Mwenyezi, Mwokozi wangu mwenye nguvu, unikingaye kichwa changu siku ya vita:
PSA 140:8 Ee Mwenyezi Mungu, usiwape waovu matakwa yao, usiache mipango yao ikafanikiwa, wasije wakajisifu.
PSA 140:9 Vichwa vya wanaonizunguka vifunikwe na shida zilizosababishwa na midomo yao.
PSA 140:10 Makaa ya mawe ya moto na yawaangukie! Na watupwe motoni, katika mashimo ya matope, wasiinuke tena kamwe.
PSA 140:11 Wasingiziaji wasifanikiwe katika nchi; maafa na yawawinde watu wenye jeuri.
PSA 140:12 Najua kwamba Mwenyezi Mungu huwapatia maskini haki, na kuitegemeza njia ya mhitaji.
PSA 140:13 Hakika wenye haki watalisifu jina lako, na waadilifu wataishi mbele zako.
PSA 141:1 Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita, njoo kwangu hima. Sikia sauti yangu ninapokuita.
PSA 141:2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.
PSA 141:3 Ee Mwenyezi Mungu, weka mlinzi kinywani mwangu, weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
PSA 141:4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, nisije nikashiriki katika matendo maovu pamoja na watu watendao mabaya, wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
PSA 141:5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. Kichwa changu hakitalikataa. Hata hivyo, maombi yangu daima ni kinyume cha watenda maovu.
PSA 141:6 Watawala wao watatupwa chini kutoka majabali, waovu watajifunza kwamba maneno yangu yalikuwa kweli.
PSA 141:7 Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”
PSA 141:8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.
PSA 141:9 Niepushe na mitego waliyonitegea, kutokana na mitego iliyotegwa na watenda maovu.
PSA 141:10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, wakati mimi ninapita salama.
PSA 142:1 Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Maombi. Namlilia Mwenyezi Mungu kwa sauti, napaza sauti yangu kwa Mwenyezi Mungu anihurumie.
PSA 142:2 Namimina malalamiko yangu mbele zake, mbele zake naeleza shida zangu.
PSA 142:3 Roho yangu inapozimia ndani yangu, wewe ndiwe unajua njia zangu. Katika njia ninayopita, watu wameniwekea mtego.
PSA 142:4 Tazama kuume kwangu na uone, hakuna hata mmoja anayejihusisha nami. Sina kimbilio, hakuna anayejali maisha yangu.
PSA 142:5 Ee Mwenyezi Mungu, nakulilia wewe, nasema, “Wewe ni kimbilio langu, fungu langu katika nchi ya walio hai.”
PSA 142:6 Sikiliza kilio changu, kwa sababu mimi ni mhitaji sana; niokoe na wale wanaonifuatilia, kwa kuwa wamenizidi nguvu.
PSA 142:7 Nifungue kutoka kifungo changu, ili niweze kulisifu jina lako. Ndipo wenye haki watanizunguka, kwa sababu ya wema wako kwangu.
PSA 143:1 Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, sikia sala yangu, sikiliza kilio changu unihurumie; katika uaminifu na haki yako njoo unisaidie.
PSA 143:2 Usimhukumu mtumishi wako, kwa kuwa hakuna mtu aliye hai mwenye haki mbele zako.
PSA 143:3 Adui hunifuatilia, hunipondaponda chini; hunifanya niishi gizani kama wale waliokufa zamani.
PSA 143:4 Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu, moyo wangu ndani yangu unakata tamaa.
PSA 143:5 Nakumbuka siku za zamani; natafakari juu ya kazi zako zote, naangalia juu ya kazi ambazo mikono yako imezifanya.
PSA 143:6 Nanyoosha mikono yangu kwako, nafsi yangu inakuonea kiu kama ardhi kame.
PSA 143:7 Ee Mwenyezi Mungu, unijibu haraka, roho yangu inazimia. Usinifiche uso wako, ama sivyo nitafanana na wale wanaoshuka shimoni.
PSA 143:8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma, kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako. Nioneshe njia nitakayoiendea, kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
PSA 143:9 Ee Mwenyezi Mungu, uniokoe na adui zangu, kwa kuwa nimejificha kwako.
PSA 143:10 Nifundishe kufanya mapenzi yako, kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu, Roho wako mwema na aniongoze katika nchi tambarare.
PSA 143:11 Ee Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya jina lako, hifadhi maisha yangu, kwa haki yako nitoe katika taabu.
PSA 143:12 Kwa upendo wako usiokoma, nyamazisha adui zangu; waangamize watesi wangu wote, kwa kuwa mimi ni mtumishi wako.
PSA 144:1 Zaburi ya Daudi. Ahimidiwe Mwenyezi Mungu Mwamba wangu, aifundishaye mikono yangu vita, na vidole vyangu kupigana.
PSA 144:2 Yeye ni Mungu wangu wa upendo na ulinzi wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, ngao yangu, ninayemkimbilia, ambaye huwatiisha mataifa chini yangu.
PSA 144:3 Ee Mwenyezi Mungu, mwanadamu ni nini hata umjali, Binadamu ni nini hata umfikirie?
PSA 144:4 Mwanadamu ni kama pumzi, siku zake ni kama kivuli kinachopita.
PSA 144:5 Ee Mwenyezi Mungu, pasua mbingu zako, ushuke, gusa milima ili itoe moshi.
PSA 144:6 Peleka umeme uwatawanye adui, lenga mishale yako uwashinde.
PSA 144:7 Nyoosha mkono wako kutoka juu, nikomboe na kuniokoa kutoka maji makuu, kutoka mikononi mwa wageni
PSA 144:8 ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
PSA 144:9 Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia,
PSA 144:10 kwa Yule awapaye wafalme ushindi, ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake, kutokana na upanga hatari.
PSA 144:11 Nikomboe na uniokoe kutoka mikononi mwa wageni ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
PSA 144:12 Kisha wana wetu wakati wa ujana wao watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri, binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa kurembesha jumba la kifalme.
PSA 144:13 Ghala zetu zitajazwa aina zote za mahitaji. Kondoo wetu watazaa kwa maelfu, kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu;
PSA 144:14 maksai wetu watakokota mizigo mizito. Hakutakuwa na kubomoka kuta, hakuna kuchukuliwa mateka, wala kilio cha taabu katika barabara zetu.
PSA 144:15 Heri watu ambao hili ni kweli; heri wale ambao Mwenyezi Mungu ni Mungu wao.
PSA 145:1 Wimbo wa sifa. Wa Daudi. Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme, nitalisifu jina lako milele na milele.
PSA 145:2 Kila siku nitakusifu na kulitukuza jina lako milele na milele.
PSA 145:3 Mwenyezi Mungu ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, ukuu wake haupimiki.
PSA 145:4 Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine, watasimulia matendo yako makuu.
PSA 145:5 Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako, nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu.
PSA 145:6 Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha, nami nitatangaza matendo yako makuu.
PSA 145:7 Wataadhimisha wema wako mwingi, na wataimba kwa shangwe kuhusu haki yako.
PSA 145:8 Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.
PSA 145:9 Mwenyezi Mungu ni mwema kwa wote, ana huruma kwa vyote alivyovifanya.
PSA 145:10 Ee Mwenyezi Mungu, vyote ulivyovifanya vitakusifu, watakatifu wako watakutukuza.
PSA 145:11 Watasimulia utukufu wa ufalme wako na kusema kuhusu ukuu wako,
PSA 145:12 ili watu wote wajue matendo yako makuu na utukufu wa fahari ya ufalme wako.
PSA 145:13 Ufalme wako ni ufalme wa milele, mamlaka yako hudumu vizazi vyote. Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake zote na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.
PSA 145:14 Mwenyezi Mungu huwategemeza wote waangukao, na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.
PSA 145:15 Macho ya watu wote yanakutazama, nawe huwapa chakula chao wakati wake.
PSA 145:16 Waufumbua mkono wako, watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai.
PSA 145:17 Mwenyezi Mungu ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.
PSA 145:18 Mwenyezi Mungu yu karibu na wote wamwitao, karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.
PSA 145:19 Huwatimizia wamchao matakwa yao, husikia kilio chao na kuwaokoa.
PSA 145:20 Mwenyezi Mungu huwalinda wote wanaompenda, bali waovu wote atawaangamiza.
PSA 145:21 Kinywa changu kitazinena sifa za Mwenyezi Mungu. Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu milele na milele.
PSA 146:1 Msifuni Mwenyezi Mungu! Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi Mungu,
PSA 146:2 Nitamsifu Mwenyezi Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu sifa wakati wote ningali hai.
PSA 146:3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu, kwa wanadamu ambao hufa, ambao hawawezi kuokoa.
PSA 146:4 Roho yao itokapo hurudi mavumbini, siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma.
PSA 146:5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, ambaye tumaini lake ni katika Mwenyezi Mungu, Mungu wake,
PSA 146:6 Muumba wa mbingu na nchi, na bahari na vyote vilivyomo: Mwenyezi Mungu anayedumu kuwa mwaminifu milele na milele.
PSA 146:7 Naye huwapatia haki waliodhulumiwa, na kuwapa wenye njaa chakula. Mwenyezi Mungu huwaweka wafungwa huru,
PSA 146:8 Mwenyezi Mungu huwafumbua vipofu macho, Mwenyezi Mungu huwainua waliolemewa na mizigo yao, Mwenyezi Mungu huwapenda wenye haki.
PSA 146:9 Mwenyezi Mungu huwalinda wageni na kuwategemeza yatima na wajane, lakini hupinga njia za waovu.
PSA 146:10 Mwenyezi Mungu atamiliki milele, Mungu wako, ee Sayuni, kwa vizazi vyote. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 147:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa, jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye!
PSA 147:2 Mwenyezi Mungu hujenga Yerusalemu, huwakusanya Israeli walio uhamishoni.
PSA 147:3 Anawaponya waliovunjika mioyo na kuvifunga vidonda vyao.
PSA 147:4 Huzihesabu nyota na huipa kila moja jina lake.
PSA 147:5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi, ufahamu wake hauna kikomo.
PSA 147:6 Mwenyezi Mungu huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu hadi mavumbini.
PSA 147:7 Mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa shukrani, mpigieni Mungu wetu kinubi.
PSA 147:8 Yeye huzifunika anga kwa mawingu, huinyeshea ardhi mvua, na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima.
PSA 147:9 Huwapa chakula mifugo na pia makinda ya kunguru yanapolia.
PSA 147:10 Furaha yake haipo katika nguvu za farasi, wala furaha yake kwenye miguu ya shujaa.
PSA 147:11 Mwenyezi Mungu hupendezwa na wale wamchao, wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma.
PSA 147:12 Mtukuze Mwenyezi Mungu, ee Yerusalemu, msifu Mungu wako, ee Sayuni,
PSA 147:13 kwa maana huimarisha makomeo ya malango yako na huwabariki watu wako walio ndani yako.
PSA 147:14 Huwapa amani mipakani mwenu na kukushibisha kwa ngano safi kabisa.
PSA 147:15 Hutuma amri yake duniani, neno lake hukimbia kasi.
PSA 147:16 Anatandaza theluji kama sufu na kutawanya umande kama majivu.
PSA 147:17 Huvurumisha mvua yake ya mawe kama changarawe. Ni nani awezaye kustahimili ukali wa baridi yake?
PSA 147:18 Hutuma neno lake na kuviyeyusha, huvumisha upepo wake, nayo maji hutiririka.
PSA 147:19 Amemfunulia Yakobo neno lake, sheria zake na maagizo yake kwa Israeli.
PSA 147:20 Hajafanya hivyo kwa taifa lingine lolote, hawazijui sheria zake. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 148:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Msifuni Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, msifuni juu vileleni.
PSA 148:2 Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.
PSA 148:3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi, msifuni yeye, enyi nyota zote zinazong’aa.
PSA 148:4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana, na ninyi maji juu ya anga.
PSA 148:5 Vilisifu jina la Mwenyezi Mungu kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.
PSA 148:6 Aliviweka mahali pake milele na milele, alitoa amri ambayo haibadiliki milele.
PSA 148:7 Msifuni Mwenyezi Mungu kutoka duniani, ninyi wanyama wakubwa wa baharini, na vilindi vyote vya bahari,
PSA 148:8 miali ya radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu, pepo za dhoruba zinazotimiza amri zake,
PSA 148:9 ninyi milima na vilima vyote, miti ya matunda na mierezi yote,
PSA 148:10 wanyama pori na mifugo yote, viumbe vidogo na ndege warukao,
PSA 148:11 wafalme wa dunia na mataifa yote, ninyi wakuu na watawala wote wa dunia,
PSA 148:12 vijana wa kiume na wanawali, wazee na watoto.
PSA 148:13 Wote na walisifu jina la Mwenyezi Mungu, kwa maana jina lake pekee limetukuka, utukufu wake uko juu ya nchi na mbingu.
PSA 148:14 Amewainulia watu wake pembe, sifa ya watakatifu wake wote, ya Israeli, watu walio karibu na moyo wake. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 149:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya, sifa zake katika kusanyiko la watakatifu.
PSA 149:2 Israeli na washangilie katika Muumba wao, watu wa Sayuni na wafurahi katika Mfalme wao.
PSA 149:3 Na walisifu jina lake kwa kucheza na wampigie muziki kwa matari na kinubi.
PSA 149:4 Kwa maana Mwenyezi Mungu anapendezwa na watu wake, anawavika wanyenyekevu taji la wokovu.
PSA 149:5 Watakatifu washangilie katika heshima hii, na waimbe kwa shangwe vitandani mwao.
PSA 149:6 Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao na upanga ukatao kuwili mikononi mwao,
PSA 149:7 ili walipize mataifa kisasi na adhabu juu ya mataifa,
PSA 149:8 wawafunge wafalme wao kwa minyororo, wakuu wao kwa pingu za chuma,
PSA 149:9 ili kuwafanyia hukumu iliyoandikwa dhidi yao. Huu ndio utukufu wa watakatifu wake wote. Msifuni Mwenyezi Mungu.
PSA 150:1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Msifuni Mungu katika patakatifu pake, msifuni katika mbingu zake kuu.
PSA 150:2 Msifuni kwa matendo yake makuu, msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
PSA 150:3 Msifuni kwa mvumo wa tarumbeta, msifuni kwa kinubi na zeze,
PSA 150:4 msifuni kwa matari na kucheza, msifuni kwa kinanda cha nyuzi na filimbi,
PSA 150:5 msifuni kwa matoazi yaliayo, msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
PSA 150:6 Kila chenye pumzi na kimsifu Mwenyezi Mungu. Msifuni Mwenyezi Mungu!
PRO 1:1 Mithali za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:
PRO 1:2 Kwa kupata hekima na nidhamu; kwa kufahamu maneno ya busara;
PRO 1:3 kwa kujipatia nidhamu na busara, kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;
PRO 1:4 huwapa busara wajinga, maarifa na akili kwa vijana;
PRO 1:5 wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao, wenye kupambanua na wapate mwongozo;
PRO 1:6 kwa kufahamu mithali na mifano, misemo na vitendawili vya wenye hekima.
PRO 1:7 Kumcha Mwenyezi Mungu ni chanzo cha maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.
PRO 1:8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
PRO 1:9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako, na mkufu wa kuipamba shingo yako.
PRO 1:10 Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, usikubaliane nao.
PRO 1:11 Wakisema, “Twende tufuatane; tukamvizie mtu na kumwaga damu, njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;
PRO 1:12 tuwameze wakiwa hai kama kaburi, wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni.
PRO 1:13 Tutapata aina zote za vitu vya thamani na kujaza nyumba zetu kwa nyara.
PRO 1:14 Njoo ushirikiane nasi, vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”
PRO 1:15 Mwanangu, usiandamane nao. Usiweke mguu wako katika njia zao,
PRO 1:16 kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni wepesi kumwaga damu.
PRO 1:17 Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu wakati ndege wote wanakuona!
PRO 1:18 Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe; hujivizia tu wenyewe!
PRO 1:19 Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila; huuondoa uhai wa wale wenye mali.
PRO 1:20 Hekima huita kwa sauti kuu barabarani, hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;
PRO 1:21 kwenye makutano ya barabara za mji zenye makelele mengi hupaza sauti, kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:
PRO 1:22 “Enyi wajinga, mtashikilia ujinga wenu hadi lini? Hadi lini wenye mizaha watafurahia mizaha, na wapumbavu kuchukia maarifa?
PRO 1:23 Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu, ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu na kuwafahamisha maneno yangu.
PRO 1:24 Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita na hakuna yeyote aliyekubali niliponyoosha mkono wangu,
PRO 1:25 kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote na hamkukubali karipio langu,
PRO 1:26 mimi nami nitawacheka katika maafa yenu, nitawadhihaki janga litakapowapata:
PRO 1:27 janga litakapowapata kama tufani, maafa yatakapowazoa kama upepo wa kisulisuli, dhiki na taabu zitakapowalemea.
PRO 1:28 “Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu; watanitafuta lakini hawatanipata.
PRO 1:29 Kwa kuwa walichukia maarifa, wala hawakuchagua kumcha Mwenyezi Mungu,
PRO 1:30 kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu, na kukataa maonyo yangu,
PRO 1:31 watakula matunda ya njia zao, na watashibishwa matunda ya hila zao.
PRO 1:32 Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua, na kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza.
PRO 1:33 Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama, atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”
PRO 2:1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
PRO 2:2 kutega sikio lako kwenye hekima na kuweka moyo wako katika ufahamu,
PRO 2:3 na kama utaiita busara, na kuita kwa sauti upate ufahamu,
PRO 2:4 na ukiitafuta kama fedha na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
PRO 2:5 ndipo utakapoelewa kumcha Mwenyezi Mungu na kupata maarifa ya Mungu.
PRO 2:6 Kwa maana Mwenyezi Mungu hutoa hekima, na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
PRO 2:7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu, yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
PRO 2:8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
PRO 2:9 Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki, na sawa: yaani kila njia nzuri.
PRO 2:10 Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako, nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.
PRO 2:11 Busara itakuhifadhi na ufahamu utakulinda.
PRO 2:12 Hekima itakuokoa kutoka njia za waovu, kutoka kwa watu ambao maneno yao yamepotoka,
PRO 2:13 wale wanaoacha mapito ya unyoofu, wakatembea katika njia za giza,
PRO 2:14 wale wanaopenda kutenda mabaya, na kufurahia upotovu wa ubaya,
PRO 2:15 ambao mapito yao yamepotoka, na ambao ni wapotovu katika njia zao.
PRO 2:16 Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba, kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno ya kushawishi kutenda ubaya,
PRO 2:17 aliyemwacha mwenzi wa ujana wake na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu.
PRO 2:18 Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo na mapito yake kwenye roho za waliokufa.
PRO 2:19 Hakuna yeyote aendaye kwake akarudi, au kufikia mapito ya uzima.
PRO 2:20 Hivyo utatembea katika njia za watu wema na kushikamana na mapito ya wenye haki.
PRO 2:21 Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi, nao wasio na lawama watabakia ndani yake.
PRO 2:22 Bali waovu watakatiliwa mbali kutoka nchi, nao wasio waaminifu watang’olewa kutoka humo.
PRO 3:1 Mwanangu, usisahau mafundisho yangu, bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
PRO 3:2 kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako na kukuletea mafanikio.
PRO 3:3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako.
PRO 3:4 Ndipo utapata kibali na jina zuri mbele za Mungu na mwanadamu.
PRO 3:5 Mtumaini Mwenyezi Mungu kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
PRO 3:6 katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako.
PRO 3:7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe; mche Mwenyezi Mungu ukajiepushe na uovu.
PRO 3:8 Hii itakuletea afya mwilini mwako, na lishe kwenye mifupa yako.
PRO 3:9 Mheshimu Mwenyezi Mungu kwa mali yako na kwa malimbuko ya mazao yako yote;
PRO 3:10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika, viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
PRO 3:11 Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi Mungu na usichukie maonyo yake,
PRO 3:12 kwa sababu Mwenyezi Mungu huwaadibisha wale anaowapenda, kama vile baba afanyavyo kwa mwana apendezwaye naye.
PRO 3:13 Heri mtu yule apataye hekima, mtu yule apataye ufahamu,
PRO 3:14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
PRO 3:15 Hekima ana thamani kuliko marijani; hakuna chochote unachokitamani kinachoweza kulinganishwa naye.
PRO 3:16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto kuna utajiri na heshima.
PRO 3:17 Njia zake zinapendeza, mapito yake yote ni amani.
PRO 3:18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia; wale wamshikao watabarikiwa.
PRO 3:19 Kwa hekima Mwenyezi Mungu aliiweka misingi ya dunia, kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
PRO 3:20 kwa maarifa yake vilindi viligawanywa, nayo mawingu yanadondosha umande.
PRO 3:21 Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara, usiache vitoke machoni pako;
PRO 3:22 ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako na pambo la neema shingoni mwako.
PRO 3:23 Kisha utaenda katika njia yako salama, wala mguu wako hautajikwaa;
PRO 3:24 unapolala, hutaogopa; unapolala, usingizi wako utakuwa mtamu.
PRO 3:25 Usiogope maafa ya ghafula au maangamizi yanayowapata waovu,
PRO 3:26 kwa kuwa Mwenyezi Mungu atakuwa tumaini lako na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.
PRO 3:27 Usizuie wema kwa wale wanaostahili ikiwa katika uwezo wako kutenda.
PRO 3:28 Usimwambie jirani yako, “Njoo baadaye, nitakupa kesho”: wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
PRO 3:29 Usipange mabaya dhidi ya jirani yako, anayeishi karibu nawe kwa uaminifu.
PRO 3:30 Usimshtaki mtu bila sababu, wakati hajakudhuru kwa lolote.
PRO 3:31 Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri wala kuchagua njia yake yoyote,
PRO 3:32 kwa kuwa Mwenyezi Mungu humchukia mtu mpotovu, lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
PRO 3:33 Laana ya Mwenyezi Mungu i juu ya nyumba ya mwovu, lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
PRO 3:34 Huwadhihaki wale wanaodhihaki, lakini huwapa neema wale wanyenyekevu na walioonewa.
PRO 3:35 Wenye hekima hurithi heshima, bali huwaaibisha wapumbavu.
PRO 4:1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba; sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.
PRO 4:2 Ninawapa mafundisho ya maana, kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.
PRO 4:3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,
PRO 4:4 baba alinifundisha akisema, “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote; yashike maagizo yangu na wewe utaishi.
PRO 4:5 Pata hekima, pata ufahamu; usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.
PRO 4:6 Usimwache hekima naye atakuweka salama; mpende, naye atakulinda.
PRO 4:7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.
PRO 4:8 Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu.
PRO 4:9 Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji la utukufu.”
PRO 4:10 Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi.
PRO 4:11 Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito ya unyoofu.
PRO 4:12 Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa.
PRO 4:13 Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako.
PRO 4:14 Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu, wala usitembee katika njia ya wapotovu.
PRO 4:15 Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako.
PRO 4:16 Kwa kuwa hawawezi kulala hadi watende uovu; wanashindwa hata kusinzia hadi wamwangushe mtu.
PRO 4:17 Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri.
PRO 4:18 Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hung’aa zaidi na zaidi hadi mchana mkamilifu.
PRO 4:19 Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae.
PRO 4:20 Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu.
PRO 4:21 Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako;
PRO 4:22 kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.
PRO 4:23 Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
PRO 4:24 Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.
PRO 4:25 Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako.
PRO 4:26 Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika.
PRO 4:27 Usigeuke kulia wala kushoto; epusha mguu wako na ubaya.
PRO 5:1 Mwanangu, sikiliza kwa makini hekima yangu, sikiliza vizuri maneno yangu ya busara,
PRO 5:2 ili uweze kutunza busara na midomo yako ihifadhi maarifa.
PRO 5:3 Kwa maana midomo ya mwanamke kahaba hudondoza asali, na maneno ya kinywa chake ni laini kuliko mafuta;
PRO 5:4 lakini mwisho wake ni mchungu kama nyongo, mkali kama upanga ukatao kuwili.
PRO 5:5 Miguu yake hushuka kuelekea kwenye kifo; hatua zake huelekea moja kwa moja kaburini.
PRO 5:6 Yeye hafikirii kuhusu njia ya uzima; njia zake zimepotoka, lakini yeye hajui.
PRO 5:7 Sasa basi wanangu, nisikilizeni; msiache ninalowaambia.
PRO 5:8 Njia zenu ziwe mbali naye, msiende karibu na mlango wa nyumba yake,
PRO 5:9 usije ukapoteza heshima yako kwa wengine, na miaka yako kwa aliye mkatili,
PRO 5:10 wageni wasije wakasherehekea utajiri wako, na jitihada yako ikatajirisha nyumba ya mwanaume mwingine.
PRO 5:11 Mwishoni mwa maisha yako utalia kwa uchungu, wakati nyama na mwili wako vimechakaa.
PRO 5:12 Utasema, “Tazama jinsi gani nilivyochukia adhabu! Tazama jinsi moyo wangu ulivyodharau maonyo!
PRO 5:13 Sikuwatii walimu wangu, wala kuwasikiliza wakufunzi wangu.
PRO 5:14 Nimefika ukingoni mwa maangamizi katika kusanyiko la watu wa Mungu.”
PRO 5:15 Kunywa maji kwenye kisima chako mwenyewe, maji yanayotiririka kutoka kisima chako mwenyewe.
PRO 5:16 Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji na vijito vyako vya maji viwanjani?
PRO 5:17 Na viwe vyako mwenyewe, kamwe visishirikishwe wageni.
PRO 5:18 Chemchemi yako na ibarikiwe na umfurahie mke wa ujana wako.
PRO 5:19 Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri: matiti yake na yakutosheleze siku zote, nawe utekwe daima na upendo wake.
PRO 5:20 Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba? Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine?
PRO 5:21 Kwa maana njia za mtu ni wazi kabisa mbele za Mwenyezi Mungu, naye huyapima mapito yake yote.
PRO 5:22 Matendo mabaya ya mtu mwovu humnasa yeye mwenyewe; kamba za dhambi yake humkamata kwa nguvu.
PRO 5:23 Atakufa kwa kukosa nidhamu, akipotoshwa kwa upumbavu wake mwenyewe.
PRO 6:1 Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako, ikiwa umeshikana mikono kwa kuweka ahadi kwa ajili ya mwingine,
PRO 6:2 kama umetegwa na ulichosema, umenaswa kwa maneno ya kinywa chako,
PRO 6:3 basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru, kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako: Nenda ukajinyenyekeshe kwake; msihi jirani yako!
PRO 6:4 Usiruhusu usingizi machoni pako, usiruhusu kope zako zisinzie.
PRO 6:5 Jiweke huru, kama paa kutoka mkononi mwa mwindaji, kama ndege kutoka mtego wa mwindaji.
PRO 6:6 Ewe mvivu, mwendee mchwa; zitafakari njia zake ukapate hekima!
PRO 6:7 Kwa maana yeye hana msimamizi, wala mwangalizi, au mtawala,
PRO 6:8 lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
PRO 6:9 Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaamka lini kutoka usingizi wako?
PRO 6:10 Kulala kidogo, kusinzia kidogo, kukunja mikono kidogo upate kupumzika:
PRO 6:11 umaskini utakuja juu yako kama mnyang’anyi, na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.
PRO 6:12 Mtu mbaya sana na mlaghai, ambaye huzungukazunguka na maneno ya upotovu,
PRO 6:13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake, anayetoa ishara kwa miguu yake na kuashiria kwa vidole vyake,
PRO 6:14 ambaye hupanga ubaya kwa udanganyifu moyoni mwake: daima huchochea fitina.
PRO 6:15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula; ataangamizwa mara moja, pasipo msaada.
PRO 6:16 Kuna vitu sita anavyovichukia Mwenyezi Mungu, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:
PRO 6:17 macho ya kiburi, ulimi udanganyao, mikono imwagayo damu isiyo na hatia,
PRO 6:18 moyo uwazao mipango miovu, miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,
PRO 6:19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo, na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.
PRO 6:20 Mwanangu, zishike amri za baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
PRO 6:21 Yafunge katika moyo wako daima, yakaze kuizunguka shingo yako.
PRO 6:22 Unapotembea, yatakuongoza; unapolala, yatakulinda; unapoamka, yatazungumza nawe.
PRO 6:23 Kwa maana amri hii ni taa, mafundisho haya ni mwanga, na maonyo ya nidhamu ni njia ya uzima,
PRO 6:24 yakikulinda na mwanamke aliyepotoka, kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka.
PRO 6:25 Moyo wako usitamani uzuri wake, wala macho yake yasikuteke,
PRO 6:26 kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini, hata ukose kipande cha mkate, naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa.
PRO 6:27 Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake bila nguo zake kuungua?
PRO 6:28 Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto bila miguu yake kuungua?
PRO 6:29 Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine; hakuna yeyote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa.
PRO 6:30 Watu hawamdharau mwizi akiiba ili kukidhi njaa yake akiwa na njaa.
PRO 6:31 Lakini akikamatwa, lazima alipe mara saba, ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake.
PRO 6:32 Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa; yeyote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe.
PRO 6:33 Mapigo na aibu ni fungu lake na aibu yake haitafutika kamwe;
PRO 6:34 kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume, naye hataonesha huruma alipizapo kisasi.
PRO 6:35 Hatakubali fidia yoyote; atakataa malipo, hata yakiwa makubwa kiasi gani.
PRO 7:1 Mwanangu, shika maneno yangu na kuzihifadhi amri zangu ndani yako.
PRO 7:2 Shika amri zangu nawe utaishi; linda mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako.
PRO 7:3 Yafunge katika vidole vyako; yaandike katika kibao cha moyo wako.
PRO 7:4 Mwambie hekima, “Wewe ni dada yangu,” uite ufahamu jamaa yako;
PRO 7:5 watakuepusha na mwanamke mzinzi, kutokana na mwanamke mpotovu na maneno yake ya kubembeleza.
PRO 7:6 Kwenye dirisha la nyumba yangu nilitazama nje kupitia upenyo kwenye mwimo wa dirisha.
PRO 7:7 Niliona miongoni mwa wajinga, nikagundua miongoni mwa wanaume vijana, kijana asiye na akili.
PRO 7:8 Alikuwa akishuka njiani karibu na pembe ya kwake, akielekea kwenye nyumba ya huyo mwanamke
PRO 7:9 wakati wa machweo, jua likipungua nuru yake, giza la usiku lilipokuwa likiingia.
PRO 7:10 Ndipo huyo mwanamke akatoka kumlaki, hali amevaa kama kahaba akiwa na nia ya hila.
PRO 7:11 (Ni mwanamke mwenye makelele na mkaidi, miguu yake haitulii nyumbani;
PRO 7:12 mara kwenye barabara za mji, mara kwenye viwanja vikubwa, kwenye kila pembe huvizia.)
PRO 7:13 Huyo mwanamke alimkumbatia kijana na kumbusu, na kwa uso usio na haya akamwambia:
PRO 7:14 “Nina sadaka za amani nyumbani; leo nimetimiza nadhiri zangu.
PRO 7:15 Kwa hiyo nimetoka nje kukulaki; nimekutafuta na nimekupata!
PRO 7:16 Nimetandika kitanda changu kwa kitani za rangi kutoka Misri.
PRO 7:17 Nimetia manukato kitanda changu kwa manemane, udi na mdalasini.
PRO 7:18 Njoo, tuzame katika mapenzi hadi asubuhi; tujifurahishe wenyewe kwa mapenzi!
PRO 7:19 Mume wangu hayupo nyumbani; ameenda safari ya mbali.
PRO 7:20 Amechukua mkoba uliojazwa fedha na hatakuwa nyumbani karibuni.”
PRO 7:21 Kwa maneno laini yule mwanamke akampotosha; alimshawishi kwa maneno yake laini.
PRO 7:22 Mara huyo kijana alimfuata yule mwanamke kama fahali aendaye machinjoni, kama kulungu aingiaye kwenye kitanzi,
PRO 7:23 hadi mshale umchome ini lake, kama ndege anayenaswa kwenye mtego, bila kujua itamgharimu maisha yake.
PRO 7:24 Sasa basi wanangu, nisikilizeni; sikilizeni kwa makini nisemalo.
PRO 7:25 Usiruhusu moyo wako ugeukie njia za huyo mwanamke, wala usitangetange katika mapito yake.
PRO 7:26 Aliowaangusha ni wengi; aliowachinja ni kundi kubwa.
PRO 7:27 Nyumba yake ni njia kuu iendayo kaburini, ielekeayo chini kwenye vyumba vya mauti.
PRO 8:1 Je, hekima haitani? Je, ufahamu hapazi sauti?
PRO 8:2 Juu ya miinuko karibu na njia, penye njia panda, ndipo asimamapo;
PRO 8:3 kando ya malango yaelekeayo mjini, kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:
PRO 8:4 “Ni ninyi watu, ninaowaita; ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.
PRO 8:5 Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili; ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.
PRO 8:6 Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema; ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.
PRO 8:7 Kinywa changu husema lililo kweli, kwa maana midomo yangu huchukia uovu.
PRO 8:8 Maneno yote ya kinywa changu ni ya haki; hakuna mojawapo lililopotoka au la ukaidi.
PRO 8:9 Kwa wenye kupambanua, yote ni sahihi; hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.
PRO 8:10 Chagua mafundisho yangu badala ya fedha, maarifa badala ya dhahabu safi,
PRO 8:11 kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye.
PRO 8:12 “Mimi hekima, nakaa pamoja na busara; ninamiliki maarifa na busara.
PRO 8:13 Kumcha Mwenyezi Mungu ni kuchukia uovu; ninachukia kiburi na majivuno, tabia mbaya na mazungumzo potovu.
PRO 8:14 Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu; nina ufahamu na nina nguvu.
PRO 8:15 Kwa msaada wangu wafalme hutawala na watawala hutunga sheria zilizo za haki,
PRO 8:16 kwa msaada wangu wakuu hutawala, na wenye vyeo wote watawalao dunia.
PRO 8:17 Nawapenda wale wanaonipenda, na wale wanaonitafuta kwa bidii wataniona.
PRO 8:18 Utajiri na heshima viko kwangu, utajiri unaodumu na mafanikio.
PRO 8:19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi; kile ninachotoa hupita fedha iliyo bora.
PRO 8:20 Natembea katika njia ya unyofu katika mapito ya haki,
PRO 8:21 nawapa utajiri wale wanaonipenda na kuzijaza hazina zao.
PRO 8:22 “Mwenyezi Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, kabla ya matendo yake ya zamani;
PRO 8:23 niliteuliwa tangu milele, tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.
PRO 8:24 Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa, wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji;
PRO 8:25 kabla milima haijawekwa mahali pake, kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa,
PRO 8:26 kabla hajaumba dunia wala mashamba yake au vumbi lolote la dunia.
PRO 8:27 Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake, wakati alichora mstari wa upeo wa macho kwenye uso wa kilindi,
PRO 8:28 wakati aliweka mawingu juu na kuziweka imara chemchemi za bahari,
PRO 8:29 wakati aliiwekea bahari mpaka wake ili maji yasivunje agizo lake, na wakati aliweka misingi ya dunia.
PRO 8:30 Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake. Nilijazwa na furaha siku baada ya siku, nikifurahi daima mbele zake,
PRO 8:31 nikifurahi katika dunia yake yote nami nikiwafurahia wanadamu.
PRO 8:32 “Basi sasa wanangu, nisikilizeni; heri wale wanaozishika njia zangu.
PRO 8:33 Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima; msiyapuuze.
PRO 8:34 Heri mtu yule anisikilizaye mimi, akisubiri siku zote malangoni mwangu, akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.
PRO 8:35 Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima, na kujipatia kibali kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
PRO 8:36 Lakini yeyote ashindwaye kunipata hujiumiza mwenyewe; na wote wanaonichukia mimi hupenda mauti.”
PRO 9:1 Hekima amejenga nyumba yake; amechonga nguzo zake saba.
PRO 9:2 Ameandaa nyama na kuchanganya divai yake; pia ameandaa meza yake.
PRO 9:3 Amewatuma wajakazi wake, naye huita kutoka mahali pa juu sana pa mji.
PRO 9:4 Anawaambia wale wasio na akili, “Wote ambao ni wajinga na waje hapa!
PRO 9:5 Njooni, mle chakula changu na mnywe divai niliyoichanganya.
PRO 9:6 Acheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi; tembeeni katika njia ya ufahamu.
PRO 9:7 “Yeyote anayemkosoa mwenye dhihaka hukaribisha matusi; yeyote anayekemea mtu mwovu hupatwa na matusi.
PRO 9:8 Usimkemee mwenye dhihaka, la sivyo atakuchukia; mkemee mwenye hekima naye atakupenda.
PRO 9:9 Mfundishe mtu mwenye hekima naye atakuwa na hekima zaidi; mfundishe mtu mwadilifu naye atazidi kufundishika.
PRO 9:10 “Kumcha Mwenyezi Mungu ndicho chanzo cha hekima, na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.
PRO 9:11 Kwa maana kwa msaada wangu siku zako zitakuwa nyingi, na miaka itaongezwa katika maisha yako.
PRO 9:12 Kama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo; kama wewe ni mtu wa mzaha, wewe mwenyewe ndiwe utateseka.”
PRO 9:13 Mwanamke aitwaye Mpumbavu ana kelele; hana adabu na hana maarifa.
PRO 9:14 Huketi kwenye mlango wa nyumba yake, kwenye kiti katika mahali pa juu sana pa mji,
PRO 9:15 akiita wale wanaopita karibu, wanaoenda moja kwa moja kwenye njia yao.
PRO 9:16 Anawaambia wale wasio na akili, “Wote ambao ni wajinga na waje hapa ndani!
PRO 9:17 Maji yaliyoibiwa ni matamu; chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!”
PRO 9:18 Lakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo, kwamba wageni wake huyo mwanamke wako katika vilindi vya Kuzimu.
PRO 10:1 Mithali za Sulemani: Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake, lakini mwana mpumbavu huleta huzuni kwa mama yake.
PRO 10:2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai, lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.
PRO 10:3 Mwenyezi Mungu hawaachi waadilifu kukaa njaa, lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.
PRO 10:4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.
PRO 10:5 Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi ni mwana mwenye hekima, lakini yeye alalaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.
PRO 10:6 Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki, lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
PRO 10:7 Kumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka, lakini jina la mwovu litaoza.
PRO 10:8 Mwenye hekima moyoni hupokea maagizo, lakini mpumbavu apayukaye huangamia.
PRO 10:9 Mtu mwadilifu hutembea salama, lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagunduliwa.
PRO 10:10 Yeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni, naye mpumbavu apayukaye huangamia.
PRO 10:11 Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima, lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
PRO 10:12 Chuki huchochea faraka, lakini upendo husitiri mabaya yote.
PRO 10:13 Hekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua, lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.
PRO 10:14 Wenye hekima huhifadhi maarifa, bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.
PRO 10:15 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, bali ufukara ni maangamizi ya maskini.
PRO 10:16 Ujira wa wenye haki huwaletea uzima, lakini mapato ya waovu ni dhambi na mauti.
PRO 10:17 Anayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima, lakini yeyote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.
PRO 10:18 Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo, na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.
PRO 10:19 Dhambi haiondolewi kwa maneno mengi, bali wenye busara huzuia ulimi wao.
PRO 10:20 Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora, bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.
PRO 10:21 Midomo ya mwenye haki hulisha wengi, lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.
PRO 10:22 Baraka ya Mwenyezi Mungu hutajirisha, wala haichanganyi na huzuni.
PRO 10:23 Mpumbavu hufurahia hila, lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.
PRO 10:24 Kile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata; kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.
PRO 10:25 Tufani inapopita, waovu hutoweka, lakini wenye haki husimama imara milele.
PRO 10:26 Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho, ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.
PRO 10:27 Kumcha Mwenyezi Mungu huongeza urefu wa maisha, lakini miaka ya mwovu inafupishwa.
PRO 10:28 Tarajio la mwenye haki ni furaha, bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.
PRO 10:29 Njia ya Mwenyezi Mungu ni kimbilio kwa wenye haki, lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.
PRO 10:30 Kamwe wenye haki hawataondolewa, bali waovu hawatasalia katika nchi.
PRO 10:31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima, bali ulimi wa upotovu utakatwa.
PRO 10:32 Midomo ya wenye haki hujua kile chenye kibali, bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.
PRO 11:1 Mwenyezi Mungu huchukia sana mizani za udanganyifu, bali vipimo sahihi ni furaha yake.
PRO 11:2 Kiburi kinapokuja, ndipo huja aibu, bali unyenyekevu huja na hekima.
PRO 11:3 Uadilifu wa wenye haki huwaongoza, bali wasio waaminifu huangamizwa na hila yao.
PRO 11:4 Utajiri haufaidi kitu katika siku ya ghadhabu, bali haki huokoa kutoka mautini.
PRO 11:5 Haki ya wasio na lawama, huwatengenezea njia iliyo nyofu, bali waovu huangushwa kwa uovu wao wenyewe.
PRO 11:6 Haki ya wanyofu huwaokoa, bali wasio waaminifu hunaswa na tamaa mbaya.
PRO 11:7 Matumaini yaliyo katika wanadamu hufa pamoja nao; ahadi zote za uwezo wao hubatilika.
PRO 11:8 Mtu mwenye haki huokolewa kutoka taabu, naye mtu mwovu huingia humo badala yake.
PRO 11:9 Kwa kinywa chake mtu asiyemwamini Mungu humwangamiza jirani yake, bali kwa maarifa mwenye haki huokolewa.
PRO 11:10 Mwenye haki anapofanikiwa, mji hufurahi; mwovu anapoangamia, kuna shangwe za furaha.
PRO 11:11 Kutokana na baraka ya mtu mnyofu mji hukwezwa, bali kwa kinywa cha mwovu mji huharibiwa.
PRO 11:12 Mtu asiye na akili humdharau jirani yake, bali mtu mwenye ufahamu huuzuia ulimi wake.
PRO 11:13 Masengenyo husaliti uaminifu, bali mtu mwaminifu hutunza siri.
PRO 11:14 Pasipo ushauri wa hekima taifa huanguka, bali washauri wengi hufanya ushindi uwe wa hakika.
PRO 11:15 Yeye amdhaminiye mgeni hakika atateseka, bali yeyote akataaye kuunga mkono dhamana ni salama.
PRO 11:16 Mwanamke mwenye moyo wa huruma hupata heshima, bali wanaume wakorofi hupata mali tu.
PRO 11:17 Mwenye huruma hujinufaisha mwenyewe, bali mkatili hujiletea taabu mwenyewe.
PRO 11:18 Mtu mwovu hupata ujira wa udanganyifu, bali yeye apandaye haki huvuna tuzo ya uhakika.
PRO 11:19 Mtu mwenye haki kweli kweli hupata uzima, bali yeye afuatiliaye ubaya huendea kifo chake.
PRO 11:20 Mwenyezi Mungu huwachukia sana watu wenye moyo wa upotovu, bali hupendezwa na wale ambao njia zao hazina lawama.
PRO 11:21 Uwe na hakika na hili: Waovu hawataepuka kuadhibiwa, bali wenye haki watakuwa huru.
PRO 11:22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe ndivyo alivyo mwanamke mzuri ambaye hana busara.
PRO 11:23 Shauku ya mwenye haki huishia tu kwenye mema, bali tumaini la mwovu huishia tu kwenye ghadhabu.
PRO 11:24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi, mwingine huzuia, lakini huwa maskini.
PRO 11:25 Mtu mkarimu atastawi; yeye awaburudishaye wengine ataburudishwa mwenyewe.
PRO 11:26 Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka, bali baraka itamkalia kichwani kama taji yeye aliye radhi kuiuza.
PRO 11:27 Yeye atafutaye mema hupata ukarimu, bali ubaya huja kwake yeye autafutaye.
PRO 11:28 Yeyote ategemeaye utajiri wake ataanguka, bali mwenye haki atastawi kama jani bichi.
PRO 11:29 Yeye aletaye taabu kwa jamaa yake atarithi tu upepo, naye mpumbavu atakuwa mtumishi wa wenye hekima.
PRO 11:30 Tunda la mwenye haki ni mti wa uzima, naye mwenye hekima huokoa maisha.
PRO 11:31 Kama wenye haki watapokea ujira wao duniani, si zaidi sana mtu asiyemcha Mungu, na mwenye dhambi?
PRO 12:1 Yeyote apendaye kuadibishwa hupenda maarifa, bali yeye achukiaye kuonywa ni mpumbavu.
PRO 12:2 Mtu mwema hupata kibali kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bali Mwenyezi Mungu humhukumu mwenye hila.
PRO 12:3 Mtu hathibitiki kutokana na uovu, bali mwenye haki hataondolewa.
PRO 12:4 Mke mwenye tabia nzuri ni taji la mumewe, bali aaibishaye ni kama uozo katika mifupa ya mumewe.
PRO 12:5 Mipango ya mtu mwadilifu ni ya haki, bali ushauri wa mwovu ni udanganyifu.
PRO 12:6 Maneno ya waovu huotea kumwaga damu, bali maneno ya waadilifu huwaokoa.
PRO 12:7 Watu waovu huondolewa na kutoweka, bali nyumba ya mwenye haki husimama imara.
PRO 12:8 Mtu husifiwa kulingana na hekima yake, bali watu wenye akili zilizopotoka hudharauliwa.
PRO 12:9 Heri mtu wa hali ya chini mwenye mtumishi, kuliko kujifanya mtu wa hali ya juu nawe huna chakula.
PRO 12:10 Mtu mwenye haki hujali mahitaji ya mnyama wake, bali matendo ya huruma ya mwovu ni ukatili.
PRO 12:11 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele, bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili.
PRO 12:12 Waovu hutamani mateka ya wapotovu, bali shina la mwenye haki hustawi.
PRO 12:13 Mtu mwovu hunaswa kwa mazungumzo yake ya dhambi, bali mwenye haki huepuka taabu.
PRO 12:14 Kutokana na tunda la midomo yao, watu hujazwa na mambo mema, na kazi ya mikono yao huwaletea thawabu.
PRO 12:15 Njia ya mpumbavu huonekana sawa machoni pake mwenyewe, bali mtu mwenye hekima husikiliza ushauri.
PRO 12:16 Mpumbavu huonesha kuudhika kwake mara moja, bali mtu wa busara hupuuza matukano.
PRO 12:17 Shahidi wa kweli hutoa ushuhuda wa kuaminika, bali shahidi wa uongo husema uongo.
PRO 12:18 Maneno ya kipumbavu huchoma kama upanga, bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji.
PRO 12:19 Midomo isemayo kweli hudumu milele, bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu.
PRO 12:20 Upo udanganyifu katika mioyo ya wale ambao hupanga mabaya, bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani.
PRO 12:21 Hakuna dhara linalompata mwenye haki, bali waovu wana taabu nyingi.
PRO 12:22 Mwenyezi Mungu anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.
PRO 12:23 Mtu mwenye busara hujihifadhia maarifa yeye mwenyewe, bali moyo wa wapumbavu hububujika upumbavu.
PRO 12:24 Mikono yenye bidii itatawala, bali uvivu huishia katika kazi za utumwa.
PRO 12:25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu, bali neno la fadhili humfurahisha.
PRO 12:26 Mtu mwenye haki ni mwangalifu katika urafiki, bali njia ya waovu huwapotosha.
PRO 12:27 Mtu mvivu haoki mawindo yake, bali mtu mwenye bidii ana mali ya thamani.
PRO 12:28 Katika njia ya haki kuna uzima; katika mapito hayo kuna maisha ya milele.
PRO 13:1 Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye, bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
PRO 13:2 Kutoka tunda la midomo yake, mtu hufurahia mambo mema, bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri.
PRO 13:3 Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake, bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia.
PRO 13:4 Mvivu hutamani sana na hapati kitu, bali nafsi ya mwenye bidii hutoshelezwa kikamilifu.
PRO 13:5 Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha.
PRO 13:6 Haki humlinda mtu mwadilifu, bali uovu humwangusha mwenye dhambi.
PRO 13:7 Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote; mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi.
PRO 13:8 Utajiri wa mtu unaweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho.
PRO 13:9 Nuru ya mwenye haki hung’aa sana, bali taa ya mwovu itazimwa.
PRO 13:10 Kiburi huzalisha magomvi tu, bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri.
PRO 13:11 Fedha isiyo ya halali hupungua, bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.
PRO 13:12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua, bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima.
PRO 13:13 Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi, bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo.
PRO 13:14 Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
PRO 13:15 Ufahamu mzuri hupata upendeleo, bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu.
PRO 13:16 Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa, bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake.
PRO 13:17 Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu, bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji.
PRO 13:18 Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu, bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa.
PRO 13:19 Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi, bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya.
PRO 13:20 Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima, bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara.
PRO 13:21 Balaa humwandama mtenda dhambi, bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki.
PRO 13:22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa kwa ajili ya wenye haki.
PRO 13:23 Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi, bali dhuluma hukifutilia mbali.
PRO 13:24 Yeye asiyetumia fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha.
PRO 13:25 Mwenye haki hula hadi akaridhisha moyo wake, bali tumbo la mwovu hutaabika kwa njaa.
PRO 14:1 Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, bali mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.
PRO 14:2 Yeye ambaye njia zake ni nyofu humcha Mwenyezi Mungu, bali yeye ambaye njia zake zimepotoka humdharau Mungu.
PRO 14:3 Mazungumzo ya mpumbavu huleta fimbo mgongoni mwake, bali mwenye hekima hulindwa na maneno ya midomo yake.
PRO 14:4 Pale ambapo hakuna mafahali, hori ni tupu, bali kutokana na nguvu za fahali huja mavuno mengi.
PRO 14:5 Shahidi mwaminifu hadanganyi, bali shahidi wa uongo humimina uongo.
PRO 14:6 Mwenye mzaha huitafuta hekima na haipati, bali maarifa huja kwa urahisi kwa anayepambanua.
PRO 14:7 Kaa mbali na mtu mpumbavu, kwa maana hutapata maarifa katika midomo yake.
PRO 14:8 Hekima ya mwenye busara ni kufikiria njia zake, bali upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
PRO 14:9 Wapumbavu hudhihaki kujirekebisha kutoka dhambi, bali wema hupatikana miongoni mwa wanyofu.
PRO 14:10 Kila moyo hujua uchungu wake wenyewe, wala hakuna yeyote awezaye kushiriki furaha yake.
PRO 14:11 Nyumba ya mwovu itaangamizwa, bali hema la mnyofu litastawi.
PRO 14:12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu, bali mwisho wake huelekeza mautini.
PRO 14:13 Hata katika kicheko moyo unaweza kuuma, nayo furaha yaweza kuishia katika majonzi.
PRO 14:14 Wasio na imani watapatilizwa kikamilifu kwa ajili ya njia zao, naye mtu mwema atapewa thawabu kwa ajili ya njia yake.
PRO 14:15 Mtu mjinga huamini kila kitu, bali mwenye busara hufikiria hatua zake.
PRO 14:16 Mtu mwenye hekima humcha Mwenyezi Mungu na kuepuka mabaya, bali mpumbavu hukasirika kwa hamaki na uzembe.
PRO 14:17 Mtu anayekasirika kwa haraka hufanya mambo ya upumbavu, naye mtu wa hila huchukiwa.
PRO 14:18 Mjinga hurithi upumbavu, bali wenye busara huvikwa maarifa kichwani kama taji.
PRO 14:19 Wapotovu watasujudu mbele ya watu wema, nao waovu kwenye malango ya wenye haki.
PRO 14:20 Maskini huepukwa hata na majirani zao, bali matajiri wana rafiki wengi.
PRO 14:21 Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi, bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.
PRO 14:22 Je, wale wanaopanga ubaya hawapotoki? Bali wale wanaopanga kilicho chema hupata upendo na uaminifu.
PRO 14:23 Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida, bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.
PRO 14:24 Utajiri wa wenye hekima ni taji lao, bali upumbavu wa wapumbavu huzaa upumbavu.
PRO 14:25 Shahidi wa kweli huokoa maisha, bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu.
PRO 14:26 Yeye amchaye Mwenyezi Mungu ana ngome salama, na kwa watoto wake itakuwa kimbilio.
PRO 14:27 Kumcha Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
PRO 14:28 Wingi wa watu ni utukufu wa mfalme, bali pasipo watu mkuu huangamia.
PRO 14:29 Mtu mwenye subira ana ufahamu mwingi, bali anayekasirika haraka huonesha upumbavu.
PRO 14:30 Moyo wenye amani huupa mwili uzima, bali wivu huozesha mifupa.
PRO 14:31 Yeye anayemdhulumu maskini humdharau Muumba wao, bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu.
PRO 14:32 Waovu huangamizwa kwa matendo yao maovu, bali hata katika kifo wenye haki hupata kimbilio.
PRO 14:33 Hekima hukaa katika moyo wa mwenye ufahamu bali haijulikani miongoni mwa wapumbavu.
PRO 14:34 Haki huinua taifa, bali dhambi ni aibu kwa watu wote.
PRO 14:35 Mfalme hupendezwa na mtumishi mwenye hekima, bali ghadhabu yake humwangukia mtumishi mwenye kuaibisha.
PRO 15:1 Jawabu la upole hugeuza ghadhabu, bali neno liumizalo huchochea hasira.
PRO 15:2 Ulimi wa mwenye hekima husifu maarifa, bali kinywa cha mpumbavu hufoka upumbavu.
PRO 15:3 Macho ya Mwenyezi Mungu yako kila mahali, yakiwaangalia waovu na wema.
PRO 15:4 Ulimi uletao uponyaji ni mti wa uzima, bali ulimi udanganyao huponda roho.
PRO 15:5 Mpumbavu hubeza maonyo ya baba yake, bali yeyote akubaliye maonyo huonesha busara.
PRO 15:6 Nyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa, bali mapato ya waovu huwaletea taabu.
PRO 15:7 Midomo ya mwenye hekima hueneza maarifa, bali sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu.
PRO 15:8 Mwenyezi Mungu huchukia sana dhabihu za waovu, bali maombi ya wanyofu humfurahisha Mungu.
PRO 15:9 Mwenyezi Mungu huchukia sana njia ya waovu, bali huwapenda wale wafuatao haki.
PRO 15:10 Adhabu kali humngoja yeye aachaye njia; yeye achukiaye maonyo atakufa.
PRO 15:11 Mauti na Uharibifu viko wazi mbele za Mwenyezi Mungu: je, si zaidi sana mioyo ya wanadamu!
PRO 15:12 Mwenye mzaha huchukia maonyo; hatataka shauri kwa mwenye hekima.
PRO 15:13 Moyo wenye furaha hufanya uso uchangamke, bali maumivu ya moyoni huponda roho.
PRO 15:14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa, bali kinywa cha mpumbavu hujilisha upumbavu.
PRO 15:15 Siku zote za wanaoteswa ni za taabu, bali moyo mchangamfu una karamu ya kudumu.
PRO 15:16 Afadhali kuwa na kidogo pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu, kuliko mali nyingi pamoja na ghasia.
PRO 15:17 Afadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo, kuliko nyama ya ndama aliyenona pamoja na chuki.
PRO 15:18 Mtu mwepesi wa hasira huchochea ugomvi, bali mtu mvumilivu hutuliza ugomvi.
PRO 15:19 Njia ya mvivu imezibwa na miiba, bali njia ya mwenye haki ni barabara kuu.
PRO 15:20 Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake, bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.
PRO 15:21 Upumbavu humfurahisha mtu ambaye hana akili, bali mtu mwenye ufahamu hushika njia iliyonyooka.
PRO 15:22 Mipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri, bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.
PRO 15:23 Mtu hupata furaha katika kutoa jibu linalofaa: je, ni zuri namna gani neno lililotoka kwa wakati wake!
PRO 15:24 Mapito ya uzima huelekea juu kwa ajili ya wenye hekima kumwepusha asiende chini kaburini.
PRO 15:25 Mwenyezi Mungu hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi, bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe.
PRO 15:26 Mwenyezi Mungu huchukia sana mawazo ya mwovu, bali mawazo ya wale walio safi humfurahisha yeye.
PRO 15:27 Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu, bali yeye achukiaye rushwa ataishi.
PRO 15:28 Moyo wa mwenye haki hupima majibu yake, bali kinywa cha mwovu hufoka ubaya.
PRO 15:29 Mwenyezi Mungu yuko mbali na waovu, bali husikia maombi ya wenye haki.
PRO 15:30 Mtazamo wa tabasamu huleta furaha moyoni, nazo habari njema huipa mifupa afya.
PRO 15:31 Yeye asikilizaye maonyo yatoayo uzima atakuwa miongoni mwa wenye hekima.
PRO 15:32 Yeye anayedharau maonyo hujidharau mwenyewe, bali yeyote anayekubali maonyo hupata ufahamu.
PRO 15:33 Kumcha Mwenyezi Mungu humfundisha mtu hekima, nao unyenyekevu huja kabla ya heshima.
PRO 16:1 Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu, bali jibu la ulimi hutoka kwa Mwenyezi Mungu.
PRO 16:2 Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe, bali makusudi hupimwa na Mwenyezi Mungu.
PRO 16:3 Mkabidhi Mwenyezi Mungu lolote ufanyalo, nayo mipango yako itafanikiwa.
PRO 16:4 Mwenyezi Mungu hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe; hata waovu kwa siku ya maangamizi.
PRO 16:5 Mwenyezi Mungu huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo. Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa.
PRO 16:6 Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa; kwa kumcha Mwenyezi Mungu mtu hujiepusha na ubaya.
PRO 16:7 Njia za mtu zinapompendeza Mwenyezi Mungu, huwafanya hata adui zake waishi naye kwa amani.
PRO 16:8 Afadhali kitu kidogo pamoja na haki kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
PRO 16:9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake, bali Mwenyezi Mungu huelekeza hatua zake.
PRO 16:10 Midomo ya mfalme huzungumza kwa hekima ya kiungu, wala kinywa chake hakipotoshi haki.
PRO 16:11 Vipimo na mizani za halali hutoka kwa Mwenyezi Mungu; mawe yote ya kupimia yaliyo katika mfuko ameyafanya yeye.
PRO 16:12 Wafalme huchukia sana kutenda maovu, kwa maana kiti cha ufalme hufanywa imara kupitia haki.
PRO 16:13 Wafalme hufurahia midomo ya uaminifu; humthamini mtu asemaye kweli.
PRO 16:14 Ghadhabu ya mfalme ni mjumbe wa mauti, bali mtu mwenye hekima ataituliza.
PRO 16:15 Uso wa mfalme ung’aapo, inamaanisha uhai; upendeleo wake ni kama wingu la mvua wakati wa vuli.
PRO 16:16 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu, kuchagua ufahamu kuliko fedha!
PRO 16:17 Njia kuu ya wanyofu huepuka ubaya; yeye aichungaye njia yake, huchunga maisha yake.
PRO 16:18 Kiburi hutangulia maangamizi, roho ya majivuno hutangulia maanguko.
PRO 16:19 Ni afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu miongoni mwa walioteswa kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.
PRO 16:20 Yeyote anayekubali mafundisho hustawi, tena amebarikiwa yeye anayemtumaini Mwenyezi Mungu.
PRO 16:21 Wenye hekima moyoni huitwa wenye ufahamu, na maneno ya kupendeza huchochea mafundisho.
PRO 16:22 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwa wale walio nao, bali upumbavu huleta adhabu kwa wapumbavu.
PRO 16:23 Moyo wa mtu mwenye hekima huongoza kinywa chake, na midomo yake huchochea mafundisho.
PRO 16:24 Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali, ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.
PRO 16:25 Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu, bali mwisho wake huelekeza mautini.
PRO 16:26 Shauku ya mfanyakazi humhimiza kufanya kazi; njaa yake humsukuma aendelee.
PRO 16:27 Mtu mbaya kabisa hupanga mabaya, maneno yake ni kama moto uunguzao.
PRO 16:28 Mtu mpotovu huchochea ugomvi, nayo maongezi ya upuzi huwatenganisha rafiki wa karibu.
PRO 16:29 Mtu mkali humvuta jirani yake na kumwongoza katika mapito yale mabaya.
PRO 16:30 Yeye akonyezaye kwa jicho lake anapanga upotovu; naye akazaye midomo yake amenuia mabaya.
PRO 16:31 Mvi ni taji la utukufu; hupatikana kwa maisha ya uadilifu.
PRO 16:32 Ni afadhali mtu mstahimilivu kuliko shujaa, mtu anayeitawala hasira yake kuliko yule autekaye mji.
PRO 16:33 Kura hupigwa kwa siri, lakini kila uamuzi wake hutoka kwa Mwenyezi Mungu.
PRO 17:1 Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi.
PRO 17:2 Mtumishi mwenye hekima atamtawala mwana aaibishaye, naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.
PRO 17:3 Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu, bali Mwenyezi Mungu huujaribu moyo.
PRO 17:4 Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya; mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.
PRO 17:5 Yeye anaye mdhihaki maskini huonesha dharau kwa Muumba wake; yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.
PRO 17:6 Wana wa wana ni taji la wazee, nao wazazi ni fahari ya watoto wao.
PRO 17:7 Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu: je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala!
PRO 17:8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; kokote kigeukiapo, hufanikiwa.
PRO 17:9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo, bali yeyote arudiaye jambo huwatenganisha rafiki wa karibu.
PRO 17:10 Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.
PRO 17:11 Mwovu hupenda kuasi tu; mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake.
PRO 17:12 Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyang’anywa watoto wake, kuliko mpumbavu katika upumbavu wake.
PRO 17:13 Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema, kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.
PRO 17:14 Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji; kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza.
PRO 17:15 Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki, naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki: Mwenyezi Mungu huwachukia sana wote wawili.
PRO 17:16 Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu, wakati yeye hana haja ya kupata hekima?
PRO 17:17 Rafiki hupenda wakati wote naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.
PRO 17:18 Mtu mjinga huutoa mkono ili kuweka rehani, naye huweka dhamana kwa jirani yake.
PRO 17:19 Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi; naye ainuaye sana lango lake hutafuta uharibifu.
PRO 17:20 Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa; naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu huanguka kwenye taabu.
PRO 17:21 Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni; hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu.
PRO 17:22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri, bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.
PRO 17:23 Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri ili kupotosha njia ya haki.
PRO 17:24 Mtu wa ufahamu huitazama hekima, lakini macho ya mpumbavu huhangaika hadi kwenye miisho ya dunia.
PRO 17:25 Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake na uchungu kwa yeye aliyemzaa.
PRO 17:26 Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia, au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao.
PRO 17:27 Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia, naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.
PRO 17:28 Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima akinyamaza, na mwenye ufahamu akiuzuia ulimi wake.
PRO 18:1 Mtu ajitengaye na wengine hufuata matakwa yake mwenyewe; hupiga vita kila shauri jema.
PRO 18:2 Mpumbavu hafurahii ufahamu, bali hufurahia kutangaza maoni yake mwenyewe.
PRO 18:3 Uovu unapokuja, dharau huja pia; pamoja na aibu huja lawama.
PRO 18:4 Maneno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji, bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika.
PRO 18:5 Sio vizuri kumpendelea mtu mwovu, au kumnyima haki asiye na hatia.
PRO 18:6 Midomo ya mpumbavu humletea ugomvi na kinywa chake hualika kipigo.
PRO 18:7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake.
PRO 18:8 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu; huingia sehemu za ndani sana za mtu.
PRO 18:9 Mtu aliye mlegevu katika kazi yake ni ndugu na yule anayeharibu.
PRO 18:10 Jina la Mwenyezi Mungu ni ngome imara, wenye haki huikimbilia na kuwa salama.
PRO 18:11 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa.
PRO 18:12 Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi, bali unyenyekevu hutangulia heshima.
PRO 18:13 Yeye ajibuye kabla ya kusikiliza, huo ni upumbavu wake na aibu yake.
PRO 18:14 Roho ya mtu itastahimili katika ugonjwa bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili?
PRO 18:15 Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa, masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa.
PRO 18:16 Zawadi humfungulia njia mtoaji, nayo humleta mbele ya wakuu.
PRO 18:17 Yeye aliye wa kwanza kuleta mashtaka huonekana sahihi, hadi mwingine ajitokezapo na kumuuliza maswali.
PRO 18:18 Kupiga kura hukomesha mashindano na kutenganisha wapinzani wakuu wanaopingana.
PRO 18:19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuridhika kuliko mji uliozungushiwa ngome, nayo mabishano ni kama malango ya ngome yenye makomeo.
PRO 18:20 Tumbo la mtu litajaa kutokana na tunda la kinywa chake, atashibishwa mavuno yanayotokana na midomo yake.
PRO 18:21 Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi, nao wanaoupenda watakula matunda yake.
PRO 18:22 Mtu anayepata mke anapata kitu chema, naye anajipatia kibali kwa Mwenyezi Mungu.
PRO 18:23 Mtu maskini huomba kuhurumiwa bali tajiri hujibu kwa ukali.
PRO 18:24 Mtu aliye na rafiki wasioaminika huangamia upesi, bali yuko rafiki anayeambatana na mtu kwa karibu kuliko ndugu.
PRO 19:1 Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama, kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.
PRO 19:2 Sio vizuri kuwa na juhudi bila maarifa, wala kufanya haraka na kuikosa njia.
PRO 19:3 Upumbavu wa mtu mwenyewe huharibu maisha yake hata hivyo moyo wake humkasirikia Mwenyezi Mungu.
PRO 19:4 Mali huleta rafiki wengi, bali rafiki wa mtu maskini humwacha.
PRO 19:5 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo hataachwa huru.
PRO 19:6 Wengi hujipendekeza kwa mtawala na kila mmoja ni rafiki wa mtu atoaye zawadi.
PRO 19:7 Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote: Je, rafiki zake watamkwepa kiasi gani! Ingawa huwafuata kwa kuwasihi, hawapatikani popote.
PRO 19:8 Yeye apataye hekima huipenda nafsi yake mwenyewe, yeye ahifadhiye ufahamu hustawi.
PRO 19:9 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo ataangamia.
PRO 19:10 Haistahili mpumbavu kuishi katika anasa, itakuwa vibaya kiasi gani kwa mtumwa kuwatawala wakuu.
PRO 19:11 Hekima ya mtu humpa uvumilivu, ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.
PRO 19:12 Ghadhabu ya mfalme ni kama mngurumo wa simba, bali wema wake ni kama umande juu ya nyasi.
PRO 19:13 Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye, naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.
PRO 19:14 Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi Mungu.
PRO 19:15 Uvivu huleta usingizi mzito, naye mtu mzembe huona njaa.
PRO 19:16 Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake, bali yeye anayezidharau njia zake atakufa.
PRO 19:17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Mwenyezi Mungu, naye atamtuza kwa aliyotenda.
PRO 19:18 Mkanye mwanao, kwa maana kufanya hivyo kuna tumaini, usiwe mshirika katika mauti yake.
PRO 19:19 Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake, kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.
PRO 19:20 Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho, nawe mwishoni utakuwa na hekima.
PRO 19:21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu, lakini kusudi la Mwenyezi Mungu ndilo litakalosimama.
PRO 19:22 Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho, afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.
PRO 19:23 Kumcha Mwenyezi Mungu huongoza kwenye uzima, kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika, bila kuguswa na shida.
PRO 19:24 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani, lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!
PRO 19:25 Mpige mwenye mzaha, naye mjinga atajifunza busara, mkemee mwenye ufahamu naye atapata maarifa.
PRO 19:26 Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake ni mwana aletaye aibu na fedheha.
PRO 19:27 Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho, utatangatanga mbali na maneno ya maarifa.
PRO 19:28 Shahidi mla rushwa hudhihaki hukumu na kinywa cha mtu mwovu humeza ubaya kwa upesi.
PRO 19:29 Adhabu zimeandaliwa kwa ajili ya wenye dhihaka na mapigo kwa ajili ya migongo ya wapumbavu.
PRO 20:1 Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.
PRO 20:2 Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake.
PRO 20:3 Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi, bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana.
PRO 20:4 Mvivu halimi kwa majira; kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama lakini hapati chochote.
PRO 20:5 Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina, lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.
PRO 20:6 Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma, bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?
PRO 20:7 Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake.
PRO 20:8 Mfalme anapoketi kwenye kiti chake cha ufalme kuhukumu, hupepeta ubaya wote kwa macho yake.
PRO 20:9 Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi; mimi ni safi na sina dhambi?”
PRO 20:10 Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti, Mwenyezi Mungu huchukia vyote viwili.
PRO 20:11 Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na adili.
PRO 20:12 Masikio yasikiayo na macho yaonayo: Mwenyezi Mungu ndiye alivifanya vyote viwili.
PRO 20:13 Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini, uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.
PRO 20:14 “Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake.
PRO 20:15 Kuna dhahabu, na marijani kwa wingi, lakini midomo inayonena maarifa ni kito cha thamani.
PRO 20:16 Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie liwe dhamana kwa ajili ya mgeni.
PRO 20:17 Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.
PRO 20:18 Fanya mipango kwa kutafuta mashauri, ukipigana vita, tafuta maelekezo.
PRO 20:19 Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika, kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi.
PRO 20:20 Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itazimwa katika giza nene.
PRO 20:21 Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni.
PRO 20:22 Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!” Mngojee Mwenyezi Mungu, naye atakuokoa.
PRO 20:23 Mwenyezi Mungu anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu, nazo mizani zisizo halali hazimpendezi.
PRO 20:24 Hatua za mtu huongozwa na Mwenyezi Mungu. Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe?
PRO 20:25 Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake.
PRO 20:26 Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu, hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao.
PRO 20:27 Taa ya Mwenyezi Mungu huchunguza roho ya mwanadamu, huchunguza utu wake wa ndani.
PRO 20:28 Upendo na uaminifu humweka mfalme salama; kiti chake cha ufalme huwa salama kwa upendo.
PRO 20:29 Utukufu wa vijana ni nguvu zao, mvi ni fahari ya uzee.
PRO 20:30 Mapigo na majeraha huusafisha ubaya, nayo michapo hutakasa utu wa ndani.
PRO 21:1 Moyo wa mfalme uko katika mkono wa Mwenyezi Mungu; huuongoza kama mkondo wa maji, popote apendapo.
PRO 21:2 Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake, bali Mwenyezi Mungu huupima moyo.
PRO 21:3 Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko dhabihu.
PRO 21:4 Macho ya kudharau na moyo wa kiburi, ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi!
PRO 21:5 Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.
PRO 21:6 Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.
PRO 21:7 Jeuri ya waovu itawaburuta mbali, kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa.
PRO 21:8 Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu, bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu.
PRO 21:9 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
PRO 21:10 Mtu mwovu hutamani sana ubaya, jirani yake hapati huruma kutoka kwake.
PRO 21:11 Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa, mjinga hupata hekima; wakati mtu mwenye hekima anafundishwa, hupata maarifa.
PRO 21:12 Mwenye Haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu, naye atawaangamiza waovu.
PRO 21:13 Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini, yeye pia atalia, wala hatajibiwa.
PRO 21:14 Zawadi inayotolewa kwa siri hutuliza hasira, na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali.
PRO 21:15 Wakati haki imetendeka, huleta furaha kwa wenye haki, bali hofu kwa watenda maovu.
PRO 21:16 Mtu anayepotea kutoka mapito ya ufahamu, hupumzika katika kundi la waliokufa.
PRO 21:17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini, yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.
PRO 21:18 Waovu huwa fidia kwa ajili ya wenye haki, nao wasio waaminifu kwa ajili ya wanyofu.
PRO 21:19 Ni afadhali kuishi jangwani kuliko kuishi na mke mgomvi na mkorofi.
PRO 21:20 Katika nyumba ya mwenye hekima kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta, lakini mtu mpumbavu hutafuna vyote alivyo navyo.
PRO 21:21 Yeye afuatiaye haki na upendo hupata uzima, mafanikio na heshima.
PRO 21:22 Mtu mwenye hekima huushambulia mji wa wenye nguvu, na kuangusha ngome wanazozitegemea.
PRO 21:23 Yeye alindaye kinywa chake na ulimi wake hujilinda na maafa.
PRO 21:24 Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake; hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi.
PRO 21:25 Kutamani sana kwa mvivu kutakuwa kifo chake, kwa sababu mikono yake haitaki kufanya kazi.
PRO 21:26 Mchana kutwa hutamani zaidi, lakini mnyofu hutoa pasipo kuzuia.
PRO 21:27 Dhabihu ya mtu mwovu ni chukizo; si ni chukizo zaidi ikitolewa kwa nia mbaya!
PRO 21:28 Shahidi wa uongo ataangamia, bali maneno ya mwenye kusikia yatadumu.
PRO 21:29 Mtu mwovu ana uso wa ushupavu, bali mtu mnyofu huzifikiria njia zake.
PRO 21:30 Hakuna hekima, wala akili, wala mpango unaoweza kufaulu dhidi ya Mwenyezi Mungu.
PRO 21:31 Farasi huandaliwa kwa ajili ya siku ya vita, bali ushindi huwa kwa Mwenyezi Mungu.
PRO 22:1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi; kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.
PRO 22:2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili: Mwenyezi Mungu ni Muumba wao wote.
PRO 22:3 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha, bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara.
PRO 22:4 Unyenyekevu na kumcha Mwenyezi Mungu huleta utajiri, heshima na uzima.
PRO 22:5 Katika mapito ya waovu kuna miiba na mitego, bali yeye ailindaye nafsi yake hukaa mbali nayo.
PRO 22:6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea, naye hataiacha hata akiwa mzee.
PRO 22:7 Matajiri huwatawala maskini naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye.
PRO 22:8 Yeye aupandaye uovu huvuna taabu, nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa.
PRO 22:9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.
PRO 22:10 Mfukuze mwenye dhihaka, na mvutano utatoweka; ugomvi na matukano vitakoma.
PRO 22:11 Yeye apendaye moyo safi na yeye ambaye maneno yake ni ya neema, mfalme atakuwa rafiki yake.
PRO 22:12 Macho ya Mwenyezi Mungu hulinda maarifa, bali huyapinga maneno ya asiye mwaminifu.
PRO 22:13 Mvivu husema, “Yuko simba nje!” au, “Nitauawa katika mitaa!”
PRO 22:14 Kinywa cha mwanamke kahaba ni shimo refu; yeye aliye chini ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu atatumbukia ndani yake.
PRO 22:15 Upumbavu umefungwa ndani ya moyo wa mtoto, bali fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali naye.
PRO 22:16 Yeye anayemdhulumu maskini ili kujiongezea mali, naye anayempa tajiri zawadi, wote huwa maskini.
PRO 22:17 Tega sikio na usikie misemo ya wenye hekima, elekeza moyo wako kwenye yale nifundishayo,
PRO 22:18 kwa maana inapendeza unapoyahifadhi moyoni mwako na kuwa nayo yote tayari mdomoni mwako.
PRO 22:19 Ili tumaini lako liwe katika Mwenyezi Mungu, hata wewe, ninakufundisha leo.
PRO 22:20 Je, sijakuandikia misemo thelathini, misemo ya mashauri na maarifa,
PRO 22:21 kukufundisha maneno ya kweli na ya kuaminika, ili uweze kutoa majibu sahihi kwake yeye aliyekutuma?
PRO 22:22 Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini, wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,
PRO 22:23 kwa sababu Mwenyezi Mungu atawatetea naye atawateka hao waliowateka.
PRO 22:24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka, usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,
PRO 22:25 la sivyo utajifunza njia zake na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
PRO 22:26 Usiwe mwenye kupeana mikono katika rehani, au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni;
PRO 22:27 ukikosa njia ya kulipa, kitanda chako kitachukuliwa ukiwa umekilalia.
PRO 22:28 Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani lililowekwa na baba zako.
PRO 22:29 Je, unamwona mtu stadi katika kazi yake? Atahudumu mbele ya wafalme; hatahudumu mbele ya watu duni.
PRO 23:1 Uketipo kula chakula na mtawala, angalia vyema kile kilicho mbele yako,
PRO 23:2 na utie kisu kooni mwako kama ukiwa mlafi.
PRO 23:3 Usitamani vyakula vyake vitamu kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.
PRO 23:4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri, uwe na hekima kuonesha kujizuia.
PRO 23:5 Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka, huwa kama umepata mabawa ghafula, ukaruka na kutoweka angani kama tai.
PRO 23:6 Usile chakula cha mtu mchoyo, usitamani vyakula vyake vitamu,
PRO 23:7 kwa maana yeye ni aina ya mtu ambaye kila mara anafikiri kuhusu gharama. Anakuambia, “Kula na kunywa,” lakini moyo wake hauko pamoja nawe.
PRO 23:8 Utatapika kile kidogo ulichokula, nawe utakuwa umepoteza bure maneno yako ya kumsifu.
PRO 23:9 Usizungumze na mpumbavu, kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.
PRO 23:10 Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani wala kunyemelea kwenye mashamba ya yatima,
PRO 23:11 kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu, atawatetea dhidi yako.
PRO 23:12 Elekeza moyo wako kwenye mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
PRO 23:13 Usimnyime mtoto adhabu, ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.
PRO 23:14 Mwadhibu kwa fimbo na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini.
PRO 23:15 Mwanangu, kama moyo wako una hekima, basi moyo wangu utafurahi,
PRO 23:16 utu wangu wa ndani utafurahi, wakati midomo yako itakapozungumza lililo sawa.
PRO 23:17 Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi, bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Mwenyezi Mungu.
PRO 23:18 Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako, nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali.
PRO 23:19 Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima, weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.
PRO 23:20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa,
PRO 23:21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara.
PRO 23:22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.
PRO 23:23 Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu.
PRO 23:24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa, naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.
PRO 23:25 Baba yako na mama yako na wafurahi, mama aliyekuzaa na ashangilie!
PRO 23:26 Mwanangu, nipe moyo wako, macho yako na yafuate njia zangu,
PRO 23:27 kwa maana kahaba ni shimo refu na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.
PRO 23:28 Kama mnyang’anyi, hungojea akivizia, naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.
PRO 23:29 Ni nani mwenye ole? Ni nani mwenye huzuni? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye malalamiko? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani mwenye macho mekundu?
PRO 23:30 Ni hao wanaokaa sana kwenye mvinyo, hao wanaoenda kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.
PRO 23:31 Usiukodolee macho mvinyo ukiwa mwekundu, unapometameta kwenye bilauri, unaposhuka taratibu!
PRO 23:32 Mwishowe huuma kama nyoka na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.
PRO 23:33 Macho yako yataona mambo mageni, na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.
PRO 23:34 Utakuwa kama alalaye baharini, alalaye juu ya kamba ya merikebu.
PRO 23:35 Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia! Wamenichapa, lakini sisikii! Nitaamka lini ili nikanywe tena?”
PRO 24:1 Usiwaonee wivu watu waovu, usitamani ushirika nao;
PRO 24:2 kwa maana mioyo yao hupanga mambo ya jeuri, nayo midomo yao husema kuhusu kuleta madhara.
PRO 24:3 Kwa hekima nyumba hujengwa, nayo kupitia ufahamu huimarishwa;
PRO 24:4 kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vya thamani na vya kupendeza.
PRO 24:5 Mtu mwenye hekima ana uwezo mkubwa, naye mtu mwenye maarifa huongeza nguvu,
PRO 24:6 kwa kufanya vita unahitaji uongozi na kwa ushindi washauri wengi.
PRO 24:7 Hekima i juu mno kwa mpumbavu, katika kusanyiko langoni hana lolote la kusema.
PRO 24:8 Yeye apangaye mabaya atajulikana kama mtu wa hila.
PRO 24:9 Mipango ya upumbavu ni dhambi, watu huchukizwa na mwenye dhihaka.
PRO 24:10 Ukikata tamaa wakati wa taabu, jinsi gani nguvu zako ni kidogo!
PRO 24:11 Okoa wale wanaoongozwa kwenye kifo; wazuie wote wanaojikokota kuelekea machinjoni.
PRO 24:12 Mkisema, “Lakini hatukujua lolote kuhusu hili,” je, yule apimaye mioyo halitambui hili? Je, yule awalindaye maisha yenu halijui hili? Je, hatamlipa kila mtu kulingana na aliyotenda?
PRO 24:13 Ule asali mwanangu, kwa kuwa ni nzuri; asali kutoka sega ni tamu kwa kuonja.
PRO 24:14 Ujue pia kwamba hekima ni tamu kwa nafsi yako: Ukiipata, kuna matumaini kwako ya siku zijazo, nalo tumaini lako halitakatiliwa mbali.
PRO 24:15 Usivizie kama haramia afanyavyo ili kuyashambulia makao ya mwenye haki, wala usiyavamie makazi yake,
PRO 24:16 kwa maana ingawa mtu mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena; lakini waovu huangushwa chini na maafa.
PRO 24:17 Usitazame kwa kufurahia adui yako aangukapo; wakati anapojikwaa, usiruhusu moyo wako ushangilie.
PRO 24:18 Mwenyezi Mungu asije akaona na kuchukia akaiondoa ghadhabu yake mbali naye.
PRO 24:19 Usikasirike kwa sababu ya wapotovu, wala usiwaonee wivu waovu,
PRO 24:20 kwa maana mpotovu hana tumaini la siku zijazo, nayo taa ya waovu itazimwa.
PRO 24:21 Mwanangu, mche Mwenyezi Mungu na mfalme, wala usijiunge na waasi,
PRO 24:22 kwa maana hao wawili watatuma maangamizi ya ghafula juu yao, naye ni nani ajuaye maafa wawezayo kuleta?
PRO 24:23 Hii pia ni misemo ya wenye hekima: Kuonesha upendeleo katika hukumu si vyema:
PRO 24:24 Yeyote amwambiaye mwenye hatia, “Wewe huna hatia,” makabila ya watu watamlaani, na mataifa watamkana.
PRO 24:25 Bali itakuwa vyema kwa wale watakaowatia hatiani wenye hatia, nazo baraka tele zitawajilia juu yao.
PRO 24:26 Jawabu la uaminifu ni kama busu la mdomoni.
PRO 24:27 Maliza kazi zako za nje, nawe uweke mashamba yako tayari, baada ya hayo, jenga nyumba yako.
PRO 24:28 Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu, au kutumia midomo yako kudanganya.
PRO 24:29 Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; nitamlipiza mtu yule kwa kile alichonitendea.”
PRO 24:30 Nilipita karibu na shamba la mvivu, karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili,
PRO 24:31 miiba ilikuwa imeota kila mahali, ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka.
PRO 24:32 Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona, nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona:
PRO 24:33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:
PRO 24:34 na umaskini utakuja juu yako kama mnyang’anyi, na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.
PRO 25:1 Hizi ni mithali zaidi za Sulemani, zilizonakiliwa na watumishi wa Hezekia mfalme wa Yuda:
PRO 25:2 Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.
PRO 25:3 Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini, ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.
PRO 25:4 Ondoa takataka kwenye madini ya fedha, na ndani yake kutatokea chombo cha mfua fedha.
PRO 25:5 Ondoa waovu mbele ya mfalme, nacho kiti chake cha ufalme kitaimarishwa kupitia kwa haki.
PRO 25:6 Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme, wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu;
PRO 25:7 ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,” kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu. Kile ulichokiona kwa macho yako
PRO 25:8 usiharakishe kukipeleka mahakamani, maana utafanya nini mwishoni kama jirani yako atakuaibisha?
PRO 25:9 Ukifanya shauri na jirani yako, usisaliti siri ya mtu mwingine,
PRO 25:10 ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha, na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.
PRO 25:11 Neno lisemwalo kwa wakati ufaao ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.
PRO 25:12 Kama vile kipuli cha dhahabu au pambo la dhahabu safi, ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima kwa sikio lisikilizalo.
PRO 25:13 Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao, huburudisha roho za bwana zake.
PRO 25:14 Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.
PRO 25:15 Kwa uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa, nao ulimi laini unaweza kuvunja mfupa.
PRO 25:16 Ukipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha, ukila zaidi, utatapika.
PRO 25:17 Nenda nyumbani mwa jirani yako mara chache; ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.
PRO 25:18 Kama vile rungu au upanga au mshale mkali ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.
PRO 25:19 Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa, ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.
PRO 25:20 Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi, au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi, ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.
PRO 25:21 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale; kama ana kiu, mpe maji anywe.
PRO 25:22 Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake, naye Mwenyezi Mungu atakupa thawabu.
PRO 25:23 Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua, ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.
PRO 25:24 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
PRO 25:25 Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.
PRO 25:26 Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au kisima kilichotiwa taka ndivyo alivyo mtu mwenye haki akishiriki na waovu.
PRO 25:27 Si vyema kula asali nyingi sana, wala si heshima kujitafutia heshima yako mwenyewe.
PRO 25:28 Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka ndivyo alivyo mtu ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.
PRO 26:1 Kama theluji wakati wa kiangazi au mvua wakati wa mavuno, ndivyo asivyostahili heshima mpumbavu.
PRO 26:2 Kama shomoro apigapigavyo mabawa yake au mbayuwayu katika kuruka kwake kasi, ndivyo ilivyo laana isiyo na sababu haimpati mtu.
PRO 26:3 Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda, nayo fimbo kwa migongo ya wapumbavu!
PRO 26:4 Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake, ama wewe mwenyewe utakuwa kama yeye.
PRO 26:5 Mjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake, ama atakuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe.
PRO 26:6 Kama vile ilivyo kujikata miguu au kunywa sumu, ndivyo ilivyo kutuma ujumbe kwa mkono wa mpumbavu.
PRO 26:7 Kama miguu ya kiwete inavyoning’inia ndivyo ilivyo mithali katika kinywa cha mpumbavu.
PRO 26:8 Kama kufunga jiwe kwenye kombeo, ndivyo ilivyo kumpa mpumbavu heshima.
PRO 26:9 Kama mwiba kwenye mkono wa mlevi ndivyo ilivyo mithali kinywani mwa mpumbavu.
PRO 26:10 Kama mpiga upinde ambaye hujeruhi ovyo, ndivyo alivyo yeye aajiriye mpumbavu au yeyote apitaye njiani.
PRO 26:11 Kama mbwa ayarudiavyo matapiko yake, ndivyo mpumbavu arudiavyo upumbavu wake.
PRO 26:12 Je, unamwona mtu ajionaye mwenye hekima machoni pake mwenyewe? Liko tumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko kwake.
PRO 26:13 Mvivu husema, “Yuko simba barabarani, simba mkali anazunguka mitaa!”
PRO 26:14 Kama vile mlango ugeukavyo kwenye bawaba zake, ndivyo mvivu ajigeuzavyo kitandani mwake.
PRO 26:15 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani, naye huchoka kuupeleka kwenye kinywa chake.
PRO 26:16 Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake mwenyewe, kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.
PRO 26:17 Kama yeye amkamataye mbwa kwa masikio, ndivyo alivyo mtu apitaye njiani na kujiingiza kwenye ugomvi usiomhusu.
PRO 26:18 Kama mwendawazimu atupaye mishale ya moto ya kufisha,
PRO 26:19 ndivyo alivyo mtu amdanganyaye jirani yake na kusema, “Nilikuwa nikifanya mzaha tu!”
PRO 26:20 Bila kuni moto huzimika; pasipo uchongezi ugomvi humalizika.
PRO 26:21 Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, na kama kuni kwenye moto, ndivyo alivyo mtu mgomvi kwa kuchochea ugomvi.
PRO 26:22 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu; huingia sehemu za ndani sana za mtu.
PRO 26:23 Kama rangi ing’aayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya.
PRO 26:24 Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake, lakini moyoni mwake huficha udanganyifu.
PRO 26:25 Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini, kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake.
PRO 26:26 Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu, lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko.
PRO 26:27 Mtu akichimba shimo, atatumbukia ndani yake; mtu akivingirisha jiwe, litamrudia.
PRO 26:28 Ulimi wa uongo huwachukia wale unaowaumiza, nacho kinywa cha kujipendekeza husababisha uharibifu.
PRO 27:1 Usijisifu kwa ajili ya kesho, kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.
PRO 27:2 Mwache mwingine akusifu, wala si kinywa chako mwenyewe; mtu mwingine afanye hivyo na si midomo yako mwenyewe.
PRO 27:3 Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo, lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito kuliko vyote viwili.
PRO 27:4 Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika, lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?
PRO 27:5 Afadhali karipio la wazi kuliko upendo uliofichika.
PRO 27:6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonesha uaminifu, lakini adui huzidisha busu.
PRO 27:7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali, bali kwa mwenye njaa hata kile kilicho kichungu kwake ni kitamu.
PRO 27:8 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake, ndivyo alivyo mtu atangatangaye mbali na nyumbani mwake.
PRO 27:9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni, nao uzuri wa rafiki huchipuka katika ushauri wake wa uaminifu.
PRO 27:10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako, tena usiende nyumbani mwa ndugu yako wakati umepatwa na maafa. Bora jirani wa karibu kuliko ndugu aliye mbali.
PRO 27:11 Mwanangu, uwe na hekima, nawe ulete furaha moyoni mwangu, ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote anitendaye kwa dharau.
PRO 27:12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha, bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara.
PRO 27:13 Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie liwe dhamana kwa ajili ya mgeni.
PRO 27:14 Mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu asubuhi na mapema, itahesabiwa kuwa ni laana.
PRO 27:15 Mke mgomvi ni kama matone yasiyokoma siku ya mvua.
PRO 27:16 Kumzuia ni kama kuuzuia upepo, au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.
PRO 27:17 Kama vile chuma kinoavyo chuma, ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.
PRO 27:18 Yeye autunzaye mtini atakula tunda lake, naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.
PRO 27:19 Kama uso uonekanavyo kwenye maji, ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonesha alivyo.
PRO 27:20 Kuzimu na Uharibifu havishibi, wala macho ya mwanadamu hayashibi.
PRO 27:21 Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu, bali mtu hupimwa kwa sifa anazopewa na watu.
PRO 27:22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu, ukimtwanga kama nafaka kwa mchi, hutauondoa upumbavu wake.
PRO 27:23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako ya kondoo na mbuzi; angalia ng’ombe wako kwa makini.
PRO 27:24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele, nalo taji halidumu vizazi vyote.
PRO 27:25 Wakati majani makavu yameondolewa na mapya yamechipua, nayo majani toka milimani yamekusanywa,
PRO 27:26 wana-kondoo watakupatia mavazi na mbuzi thamani ya shamba.
PRO 27:27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi kukulisha wewe na jamaa yako, na kuwalisha wajakazi wako.
PRO 28:1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna yeyote anayemfukuza, bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
PRO 28:2 Nchi inapokuwa na uasi, inakuwa na viongozi wengi, bali kiongozi mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utaratibu.
PRO 28:3 Mtawala anayewadhulumu maskini, ni kama mvua ya dhoruba inayoharibu mazao yote.
PRO 28:4 Wale wanaoacha sheria huwasifu waovu, bali wale wanaotii sheria huwapinga.
PRO 28:5 Wapotovu hawaelewi haki, bali wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu wanaielewa kikamilifu.
PRO 28:6 Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama, kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.
PRO 28:7 Yeye anayetii sheria ni mwana mwenye ufahamu, bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.
PRO 28:8 Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno hukusanya kwa ajili ya mwingine, ambaye atawahurumia maskini.
PRO 28:9 Mtu yeyote akikataa kusikia sheria, hata maombi yake ni chukizo.
PRO 28:10 Yeye anayemwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya, ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe, bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.
PRO 28:11 Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu maskini mwenye busara humtambua alivyodanganyika.
PRO 28:12 Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa, bali waovu watawalapo, watu hujificha.
PRO 28:13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.
PRO 28:14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha Mwenyezi Mungu, bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu huanguka kwenye taabu.
PRO 28:15 Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye, ndivyo alivyo mtu mwovu anayetawala wanyonge.
PRO 28:16 Mtawala dhalimu hana akili, bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu atafurahia maisha marefu.
PRO 28:17 Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua atakuwa mtoro hadi kufa; mtu yeyote asimsaidie.
PRO 28:18 Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama hulindwa salama, bali yeye ambaye njia zake ni potovu ataanguka ghafula.
PRO 28:19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele, bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.
PRO 28:20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana, bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka hataacha kuadhibiwa.
PRO 28:21 Kuonesha upendeleo si vizuri, hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.
PRO 28:22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri, naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.
PRO 28:23 Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi, kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.
PRO 28:24 Yeye amwibiaye babaye au mamaye na kusema, “Si kosa,” yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.
PRO 28:25 Mtu mwenye tamaa huchochea fitina, bali yule amtegemeaye Mwenyezi Mungu atafanikiwa.
PRO 28:26 Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu, bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.
PRO 28:27 Yeye ampaye maskini hatapungukiwa na kitu chochote, bali yeye awafumbiaye maskini macho hupata laana nyingi.
PRO 28:28 Wakati waovu wanatawala, watu huenda mafichoni, bali waovu wanapoangamia, wenye haki hufanikiwa.
PRO 29:1 Anayekaza shingo baada ya maonyo mengi, ataangamia ghafula, na kamwe hatapona.
PRO 29:2 Wenye haki wanapostawi, watu hufurahi; waovu watawalapo, watu hulia kwa huzuni.
PRO 29:3 Mtu apendaye hekima huleta furaha kwa baba yake, bali aambatanaye na makahaba hutapanya mali yake.
PRO 29:4 Kwa haki mfalme huipa nchi uthabiti, bali mfalme aliye na tamaa ya rushwa huiangamiza.
PRO 29:5 Yeyote amsifuye jirani yake isivyostahili, anautandaza wavu kuitega miguu yake.
PRO 29:6 Mwovu hutegwa na dhambi yake mwenyewe, bali mwenye haki hushangilia na kufurahi.
PRO 29:7 Mwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini, bali mwovu hajishughulishi na hilo.
PRO 29:8 Wanaodhihaki huuchochea mji, bali wenye hekima huzuia hasira.
PRO 29:9 Mwenye hekima akienda mahakamani na mpumbavu, mpumbavu hukasirika na kudhihaki, wala hakuna amani.
PRO 29:10 Watu wanaomwaga damu humchukia mtu mwadilifu, na hutafuta kumuua mtu mnyofu.
PRO 29:11 Mpumbavu huonesha hasira yake yote, bali mwenye hekima hujizuia.
PRO 29:12 Mtawala akisikiliza uongo, maafisa wake wote huwa waovu.
PRO 29:13 Mtu maskini na mtu mdhalimu wanafanana kwa jambo hili: Mwenyezi Mungu hutia nuru macho yao wote wawili.
PRO 29:14 Kama mfalme akiwaamua maskini kwa haki, kiti chake kitakuwa thabiti daima.
PRO 29:15 Fimbo ya maonyo hutia hekima, bali mtoto asiyeonywa humwaibisha mama yake.
PRO 29:16 Waovu wanapostawi, dhambi huongezeka pia; lakini wenye haki wataliona anguko lao.
PRO 29:17 Mkanye mwanao, naye atakupa amani; atakuletea furaha unayotamani.
PRO 29:18 Mahali pasipo na ufunuo, watu huacha kujizuia, bali ana heri mtu yule anayeitii sheria.
PRO 29:19 Mtumishi hawezi kuonywa kwa maneno matupu, hata akielewa, hataitikia.
PRO 29:20 Je, unamwona mtu azungumzaye kwa haraka? Kuna matumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko yeye.
PRO 29:21 Kama mtu akimdekeza mtumishi wake tangu ujanani, atamletea sikitiko mwishoni.
PRO 29:22 Mtu mwenye hasira huchochea ugomvi, naye mtu mwenye hasira ya haraka hutenda dhambi nyingi.
PRO 29:23 Kiburi cha mtu humshusha, bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu hupata heshima.
PRO 29:24 Anayekubaliana na mwizi ni adui wa nafsi yake mwenyewe; huapishwa lakini hathubutu kushuhudia.
PRO 29:25 Kuwaogopa watu huwa ni mtego, bali yeyote amtumainiaye Mwenyezi Mungu atakuwa salama.
PRO 29:26 Wengi hutafuta kusikilizwa na mtawala, bali mtu hupata haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
PRO 29:27 Mwenye haki huwachukia sana wasio waaminifu; waovu huwachukia sana wenye haki.
PRO 30:1 Misemo ya Aguri mwana wa Yake; usia: Huyu mtu alimwambia Ithieli, naam, kwa Ithieli na Ukali:
PRO 30:2 “Mimi ni mjinga kuliko wanadamu wote; sina ufahamu wa kibinadamu.
PRO 30:3 Sijajifunza hekima, wala sina maarifa ya kumjua yeye Aliye Mtakatifu.
PRO 30:4 Ni nani ameshapanda mbinguni na kushuka? Ni nani ameshakusanya upepo kwenye vitanga vya mikono yake? Ni nani ameshafungia maji kwenye nguo yake? Ni nani ameimarisha miisho yote ya dunia? Jina lake ni nani, na mwanawe anaitwa nani? Niambie kama unajua!
PRO 30:5 “Kila neno la Mungu ni kamilifu; yeye ni ngao kwa wale wanaomkimbilia.
PRO 30:6 Usiongeze kwenye maneno yake, ama atakukemea na kukuthibitisha kuwa mwongo.
PRO 30:7 “Ninakuomba vitu viwili, Ee Mwenyezi Mungu; usininyime kabla sijafa:
PRO 30:8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo; usinipe umaskini wala utajiri, bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.
PRO 30:9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana na kusema, ‘Mwenyezi Mungu ni nani?’ Au nisije nikawa maskini nikaiba, nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.
PRO 30:10 “Usimchongee mtumishi kwa bwana wake, asije akakulaani, ukapatilizwa kwalo.
PRO 30:11 “Kuna wanaowalaani baba zao, wala hawawabariki mama zao;
PRO 30:12 ambao ni safi machoni pao wenyewe lakini hawakuoshwa uchafu wao;
PRO 30:13 ambao daima macho yao ni ya kiburi, na kutazama kwao ni kwa dharau;
PRO 30:14 ambao meno yao ni panga na mataya yao yamewekwa visu ili kuwaangamiza maskini katika nchi, na wahitaji kutoka miongoni mwa wanadamu.
PRO 30:15 “Mruba anao binti wawili. Wao hulia daima: ‘Nipe! Nipe!’ “Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe, naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’:
PRO 30:16 Ni kaburi, tumbo lisilozaa, nchi isiyoshiba maji kamwe, na moto, usiosema kamwe, ‘Yatosha!’
PRO 30:17 “Jicho lile limdhihakilo baba, lile linalodharau kumtii mama, litang’olewa na kunguru wa bondeni, litaliwa na tai.
PRO 30:18 “Kuna vitu vitatu vinavyonishangaza sana, naam, vinne nisivyovielewa:
PRO 30:19 Ni mwendo wa tai katika anga, mwendo wa nyoka juu ya mwamba, mwendo wa meli katika maji makuu ya bahari, nao mwendo wa mtu pamoja na msichana.
PRO 30:20 “Huu ndio mwendo wa mwanamke mzinzi, hula akapangusa kinywa chake na kusema, ‘Sikufanya chochote kibaya.’
PRO 30:21 “Kwa mambo matatu nchi hutetemeka, naam, kwa mambo manne haiwezi kuvumilia:
PRO 30:22 mtumwa anapokuwa mfalme, mpumbavu anaposhiba chakula,
PRO 30:23 mwanamke asiyependwa anapoolewa, na mjakazi anapochukua nafasi ya bibi yake.
PRO 30:24 “Vitu vinne duniani vilivyo vidogo, lakini vina akili nyingi sana:
PRO 30:25 Mchwa ni viumbe wenye nguvu ndogo, hata hivyo hujiwekea akiba ya chakula chao wakati wa kiangazi.
PRO 30:26 Pelele ni viumbe vyenye uwezo mdogo, hata hivyo hujitengenezea nyumba zao kwenye miamba.
PRO 30:27 Nzige hawana mfalme, hata hivyo huenda pamoja vikosi vikosi.
PRO 30:28 Mjusi anaweza kushikwa kwa mkono, hata hivyo huonekana katika majumba ya wafalme.
PRO 30:29 “Viko vitu vitatu ambavyo vinapendeza katika mwendo wao, naam, vinne ambavyo hutembea kwa mwendo wa madaha:
PRO 30:30 simba, mwenye nguvu miongoni mwa wanyama, wala haogopi chochote;
PRO 30:31 jogoo atembeaye kwa maringo, pia beberu, na mfalme jeshi lake linapomzunguka.
PRO 30:32 “Ikiwa umefanya upumbavu na ukajitukuza mwenyewe, au kama umepanga mabaya, basi funika mdomo wako kwa mkono wako.
PRO 30:33 Kwa maana kama vile kusukasuka maziwa hutoa siagi, na pia kule kufinya pua hutoa damu, kadhalika kuchochea hasira huleta ugomvi.”
PRO 31:1 Misemo ya Mfalme Lemueli, usia wa mama yake aliyomfundisha:
PRO 31:2 “Sikiliza, ee mwanangu! Sikiliza, ee mwana wa tumbo langu! Sikiliza, ee mwana wa nadhiri zangu!
PRO 31:3 Usitumie nguvu zako kwa wanawake, uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme.
PRO 31:4 “Ee Lemueli, haifai wafalme, haifai wafalme kunywa mvinyo, haifai watawala kutamani sana kileo,
PRO 31:5 wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuru na kuwanyima haki zao wote waliodhulumiwa.
PRO 31:6 Wape kileo wale wanaoangamia, mvinyo wale walio na uchungu,
PRO 31:7 Wanywe na kusahau umaskini wao na wasikumbuke taabu yao tena.
PRO 31:8 “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea, kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.
PRO 31:9 Sema na uamue kwa haki, tetea haki za maskini na wahitaji.”
PRO 31:10 Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata? Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.
PRO 31:11 Mume wake anamwamini kikamilifu, wala hakosi kitu chochote cha thamani.
PRO 31:12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya, siku zote za maisha yake.
PRO 31:13 Huchagua sufu na kitani, naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
PRO 31:14 Yeye ni kama meli za biashara, akileta chakula chake kutoka mbali.
PRO 31:15 Yeye huamka kukiwa bado giza, naye huwapa jamaa yake chakula na wajakazi wake mafungu yao.
PRO 31:16 Huangalia shamba na kulinunua; kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
PRO 31:17 Hufanya kazi zake kwa nguvu, mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
PRO 31:18 Huona kwamba biashara yake ina faida, wala taa yake haizimiki usiku.
PRO 31:19 Huweka mikono yake kwenye pia, navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
PRO 31:20 Huwanyooshea maskini mikono yake na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.
PRO 31:21 Theluji inaposhuka, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto.
PRO 31:22 Yeye hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake, huvaa kitani safi na urujuani.
PRO 31:23 Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji, aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.
PRO 31:24 Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.
PRO 31:25 Amevikwa nguvu na heshima, anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
PRO 31:26 Huzungumza kwa hekima, na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
PRO 31:27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake wala hali chakula cha uvivu.
PRO 31:28 Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa, mumewe pia humsifu, akisema:
PRO 31:29 “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri, lakini wewe umewapita wote.”
PRO 31:30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu, na uzuri unapita upesi; bali mwanamke anayemcha Mwenyezi Mungu atasifiwa.
PRO 31:31 Mpe thawabu anayostahili, nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.
ECC 1:1 Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu:
ECC 1:2 “Ubatili! Ubatili!” Mhubiri anasema. “Ubatili mtupu! Kila kitu ni ubatili.”
ECC 1:3 Mwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote anayotaabikia chini ya jua?
ECC 1:4 Vizazi huja na vizazi hupita, lakini dunia inadumu milele.
ECC 1:5 Jua huchomoza na jua huzama, nalo huharakisha kurudi mawioni.
ECC 1:6 Upepo huvuma kuelekea kusini na kugeukia kaskazini; hurudia mzunguko huo huo, daima ukirudia njia yake.
ECC 1:7 Mito yote hutiririka baharini, hata hivyo bahari kamwe haijai. Mahali mito inapotoka, huko hurudi tena.
ECC 1:8 Vitu vyote vinachosha, kuliko mtu anavyoweza kusema. Jicho kamwe halitosheki kutazama, wala sikio halishibi kusikia.
ECC 1:9 Kile kilichokuwepo kitakuwepo tena, kile kilichofanyika kitafanyika tena, hakuna kilicho kipya chini ya jua.
ECC 1:10 Kuna kitu chochote ambacho mtu anaweza kusema, “Tazama! Kitu hiki ni kipya”? Kilikuwepo tangu zamani za kale, kilikuwepo kabla ya wakati wetu.
ECC 1:11 Hakuna kumbukumbu ya watu wa zamani, hata na wale ambao hawajaja bado hawatakumbukwa na wale watakaofuata baadaye.
ECC 1:12 Mimi, Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.
ECC 1:13 Nilitumia muda wangu wote kujifunza na kuvumbua kwa hekima yote yanayofanyika chini ya mbingu. Jinsi gani Mungu ameweka mzigo mzito juu ya wanadamu!
ECC 1:14 Nimeshaona mambo yote yanayotendeka chini ya jua, hayo yote ni ubatili, hii ni kukimbiza upepo.
ECC 1:15 Kilichopindika hakiwezi kunyooshwa; kile ambacho hakipo haiwezekani kukihesabu.
ECC 1:16 Niliwaza mwenyewe, “Tazama, nimekua na kuongezeka katika hekima kuliko yeyote aliyewahi kutawala Yerusalemu kabla yangu. Nimekuwa na uzoefu mkubwa wa hekima na maarifa.”
ECC 1:17 Ndipo nilipojitahidi kufahamu kutofautisha hekima, wazimu na upumbavu, lakini nikatambua hata hili nalo ni kukimbiza upepo.
ECC 1:18 Kwa kuwa hekima nyingi huleta huzuni kubwa; maarifa yanapoongezeka, masikitiko yanaongezeka.
ECC 2:1 Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili.
ECC 2:2 Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?”
ECC 2:3 Nikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu.
ECC 2:4 Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu.
ECC 2:5 Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe; nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda.
ECC 2:6 Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri.
ECC 2:7 Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike, nao watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ng’ombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu.
ECC 2:8 Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia.
ECC 2:9 Nikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima.
ECC 2:10 Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani, hakuna anasa niliyounyima moyo wangu. Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote, hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote.
ECC 2:11 Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo mikono yangu ilikuwa imefanya na yale niliyotaabika kukamilisha, kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo; hapakuwa na faida yoyote chini ya jua.
ECC 2:12 Kisha nikageuza mawazo yangu kufikiria hekima, wazimu na upumbavu. Ni nini zaidi mtu anayetawala baada ya mfalme anachoweza kufanya ambacho hakijafanywa?
ECC 2:13 Nikaona kuwa hekima ni bora kuliko upumbavu, kama vile nuru ilivyo bora kuliko giza.
ECC 2:14 Mtu mwenye hekima ana macho katika kichwa chake, lakini mpumbavu anatembea gizani; lakini nikaja kuona kwamba wote wawili hatima yao inafanana.
ECC 2:15 Kisha nikafikiri moyoni mwangu, “Hatima ya mpumbavu itanipata mimi pia. Nitafaidi nini basi kwa kuwa na hekima?” Nikasema moyoni mwangu, “Hili nalo ni ubatili.”
ECC 2:16 Kwa maana kwa mtu mwenye hekima, kama ilivyo kwa mpumbavu, hatakumbukwa kwa muda mrefu, katika siku zijazo wote watasahaulika. Kama vile ilivyo kwa mpumbavu, mtu mwenye hekima pia lazima atakufa!
ECC 2:17 Kwa hiyo nikachukia maisha, kwa sababu kazi inayofanyika chini ya jua ilikuwa masikitiko kwangu. Yote hayo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
ECC 2:18 Nikachukia kila kitu nilichokuwa nimetaabikia chini ya jua, kwa sababu ni lazima nimwachie yule ajaye baada yangu.
ECC 2:19 Nani ajuaye kama atakuwa ni mtu mwenye hekima au mpumbavu? Lakini hata hivyo yeye ndiye atakayetawala kazi zote ambazo nimemiminia juhudi na ustadi chini ya jua. Hili nalo ni ubatili.
ECC 2:20 Kwa hiyo moyo wangu ukaanza kukata tamaa juu ya kazi yangu yote niliyoifanya kwa taabu chini ya jua.
ECC 2:21 Kwa kuwa mtu anaweza kufanya kazi yake kwa hekima, maarifa na ustadi, kisha analazimika kuacha vyote alivyo navyo kwa mtu mwingine ambaye hajavifanyia kazi. Hili nalo pia ni ubatili tena ni balaa kubwa.
ECC 2:22 Mtu atapata nini kwa taabu yote na kuhangaika kwa bidii katika kazi anayotaabikia chini ya jua?
ECC 2:23 Siku zake zote kazi yake ni maumivu na masikitiko, hata usiku akili yake haipati mapumziko. Hili nalo pia ni ubatili.
ECC 2:24 Hakuna kitu bora anachoweza kufanya mtu zaidi ya kula na kunywa na kuridhika katika kazi yake. Hili nalo pia, ninaona, latokana na mkono wa Mungu,
ECC 2:25 kwa sababu pasipo yeye, ni nani awezaye kula na kufurahi?
ECC 2:26 Kwa yule mtu anayempendeza Mungu, Mungu humpa hekima, maarifa na furaha, bali kwa mwenye dhambi Mungu humpa kazi ya kukusanya na kuhifadhi utajiri ili Mungu ampe yule anayempenda. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
ECC 3:1 Kuna wakati kwa ajili ya kila jambo, nayo majira kwa kila tendo chini ya mbingu:
ECC 3:2 wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa, wakati wa kupanda na wakati wa kung’oa yaliyopandwa,
ECC 3:3 wakati wa kuua na wakati wa kuponya, wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga,
ECC 3:4 wakati wa kulia na wakati wa kucheka, wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza,
ECC 3:5 wakati wa kutawanya mawe na wakati wa kukusanya mawe, wakati wa kukumbatia na wakati wa kutokumbatia,
ECC 3:6 wakati wa kutafuta na wakati wa kupoteza, wakati wa kuweka na wakati wa kutupa,
ECC 3:7 wakati wa kurarua na wakati wa kushona, wakati wa kunyamaza na wakati wa kuzungumza,
ECC 3:8 wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia, wakati wa vita na wakati wa amani.
ECC 3:9 Mfanyakazi anapata faida gani kutokana na taabu yake?
ECC 3:10 Nimeona mzigo Mungu alioweka juu ya wanadamu.
ECC 3:11 Amefanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Pia ameiweka hiyo milele katika mioyo ya wanadamu, wala hawawezi kutambua kwa kina yale ambayo Mungu amefanya kuanzia mwanzo hadi mwisho.
ECC 3:12 Ninajua kwamba hakuna kitu bora kwa wanadamu kuliko kuwa na furaha na kutenda mema wakati wanapoishi.
ECC 3:13 Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.
ECC 3:14 Ninajua kwamba kila kitu anachokifanya Mungu kitadumu milele, hakuna kinachoweza kuongezwa au kupunguzwa. Mungu hufanya hivyo ili watu wamche yeye.
ECC 3:15 Chochote kilichopo kilishakuwepo, na kitakachokuwepo kimekwishakuwepo; naye Mungu huyaita yale yaliyopita yarudi tena.
ECC 3:16 Pia nikaona kitu kingine tena chini ya jua: Mahali pa kutolea hukumu, uovu ulikuwepo, mahali pa kupatia haki, uovu ulikuwepo.
ECC 3:17 Nikafikiri moyoni mwangu, “Mungu atawaleta hukumuni wote wawili wenye haki na waovu, kwa maana kutakuwako na wakati kwa ajili ya kila jambo, wakati kwa ajili ya kila tendo.”
ECC 3:18 Pia nikafikiri, “Kuhusu wanadamu, Mungu huwajaribu ili wajione kwamba wao ni kama wanyama.
ECC 3:19 Hatima ya mwanadamu ni kama ile ya wanyama; wote wana mwisho unaofanana: Jinsi anavyokufa mnyama, ndivyo anavyokufa mwanadamu. Wote wana pumzi inayofanana; mwanadamu hana cha kumzidi mnyama. Kila kitu ni ubatili.
ECC 3:20 Wote huenda mahali panapofanana; wote hutoka mavumbini, mavumbini wote hurudi.
ECC 3:21 Ni nani ajuaye kama roho ya mtu huenda juu na roho ya mnyama hushuka chini ardhini?”
ECC 3:22 Kwa hiyo nikaona kwamba hakuna kitu kilicho bora zaidi kwa mwanadamu kuliko kuifurahia kazi yake, kwa sababu hilo ndilo fungu lake. Kwa maana ni nani awezaye kumrudisha ili aje kuona kile kitakachotendeka baada yake?
ECC 4:1 Nikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua: Nikaona machozi ya waliodhulumiwa, wala hawana mfariji; uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowadhulumu, lakini hawakuwa na mfariji.
ECC 4:2 Nami nikasema kwamba wafu, waliokwisha kufa, wana furaha kuliko watu walio hai, ambao bado wanaishi.
ECC 4:3 Lakini aliye bora kuliko hao wawili ni yule ambaye hajazaliwa bado, ambaye hajaona ule uovu unaofanyika chini ya jua.
ECC 4:4 Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
ECC 4:5 Mpumbavu hukunja mikono yake na kujiangamiza mwenyewe.
ECC 4:6 Afadhali konzi moja pamoja na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu na kukimbiza upepo.
ECC 4:7 Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:
ECC 4:8 Kulikuwa na mtu aliye peke yake, hakuwa na mwana wala ndugu. Hapakuwa na mwisho wa kazi yake; hata hivyo macho yake hayakutosheka na utajiri wake. Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani, nami kwa nini ninajinyima kufurahia?” Hili pia ni ubatili, ni shughuli yenye taabu!
ECC 4:9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:
ECC 4:10 Kama mmoja akianguka, mwenzake atamwinua. Lakini ni jambo la kuhuzunisha kwa mtu yule aangukaye naye hana wa kumwinua!
ECC 4:11 Pia, kama wawili wakilala pamoja watapashana joto. Lakini ni vipi mtu aweza kujipasha joto mwenyewe?
ECC 4:12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa, watu wawili wanaweza kumkabili adui na kumshinda. Kamba ya nyuzi tatu haikatiki kwa urahisi.
ECC 4:13 Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo.
ECC 4:14 Kijana huyo angeweza kutokea gerezani akapata ufalme, au angeweza kuwa amezaliwa katika umaskini kwenye huo ufalme.
ECC 4:15 Nikaona kwamba wote walioishi na kutembea chini ya jua walimfuata kijana, aliyepokea ufalme.
ECC 4:16 Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
ECC 5:1 Linda hatua zako uendapo katika nyumba ya Mungu. Karibia usikilize kuliko kutoa dhabihu ya wapumbavu, ambao hawajui kuwa wanafanya kosa.
ECC 5:2 Usiwe mwepesi kuzungumza, usiwe na haraka katika moyo wako kuzungumza lolote mbele za Mungu. Mungu yuko mbinguni nawe uko duniani, kwa hiyo maneno yako na yawe machache.
ECC 5:3 Kama vile ndoto huja wakati kuna shughuli nyingi, ndivyo yalivyo mazungumzo ya mpumbavu wakati kuna maneno mengi.
ECC 5:4 Unapomwekea Mungu nadhiri, usikawie kuitimiza. Yeye hafurahii wapumbavu; timiza nadhiri yako.
ECC 5:5 Ni afadhali usiweke nadhiri kuliko kuiweka na usiitimize.
ECC 5:6 Usiruhusu kinywa chako kukuingiza dhambini. Tena usijitetee mbele ya huyo mjumbe wa hekaluni, ukisema, “Niliweka nadhiri kwa makosa.” Kwa nini Mungu akasirike kwa ajili ya yale unayosema na kuiharibu kazi ya mikono yako?
ECC 5:7 Kuota ndoto kwingi na maneno mengi ni ubatili. Kwa hiyo mche Mungu.
ECC 5:8 Ukiona maskini wanaodhulumiwa katika nchi, na hukumu na haki vikipotoshwa, usishangazwe na mambo hayo; kwa maana afisa mmoja anaangaliwa na aliye juu yake, na juu ya hao wawili kuna wengine walio juu yao.
ECC 5:9 Mafanikio ya nchi ni kwa ajili ya wote, hata mfalme mwenyewe hufaidi kutoka mashambani.
ECC 5:10 Yeyote apendaye fedha kamwe hatosheki na fedha; yeyote apendaye utajiri kamwe hatosheki na kipato chake. Hili nalo pia ni ubatili.
ECC 5:11 Mali ikiongezeka, ndivyo walaji wanavyoongezeka. Hii nayo inamfaidia nini mwenye mali isipokuwa ni kushibisha macho yake?
ECC 5:12 Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe amekula kidogo au kingi, lakini wingi wa mali humnyima tajiri usingizi.
ECC 5:13 Nimeshaona uovu mzito chini ya jua: Utajiri uliolimbikizwa na kuleta madhara kwa mwenye mali;
ECC 5:14 au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya, kiasi kwamba wakati akiwa na mwana hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake.
ECC 5:15 Mtu hutoka tumboni mwa mama yake uchi, naye jinsi alivyokuja vivyo hivyo huondoka. Hachukui chochote kutokana na kazi yake ambacho anaweza kukibeba mkononi mwake.
ECC 5:16 Hili nalo ni baya la kusikitisha: Kama vile mtu ajavyo, vivyo hivyo huondoka, naye anapata faida gani, maadamu hutaabika kwa ajili ya upepo?
ECC 5:17 Siku zake zote hula gizani, pamoja na fadhaa kubwa, mateso na hasira.
ECC 5:18 Ndipo nikatambua kwamba ni vyema na sahihi kwa mtu kula na kunywa na kutosheka katika kazi yake ngumu chini ya jua katika siku chache za maisha yake Mungu alizompa, kwa maana hili ndilo fungu lake.
ECC 5:19 Zaidi ya yote, Mungu anapompa mtu yeyote utajiri na milki, humwezesha kuvifurahia, kukubali fungu lake na kuwa na furaha katika kazi yake, hii ni karama ya Mungu.
ECC 5:20 Mara chache mtu huzifikiri siku za maisha yake, kwa sababu Mungu humfanya ashikwe na furaha ya moyoni.
ECC 6:1 Nimeona ubaya mwingine chini ya jua, nao unalemea sana wanadamu:
ECC 6:2 Mungu humpa mwanadamu utajiri, mali na heshima, hivyo hakukosa chochote moyo wake unachokitamani. Lakini Mungu hamwezeshi kuvifurahia, badala yake mgeni ndiye anayevifurahia. Hili ni ubatili, ni ubaya unaosikitisha.
ECC 6:3 Mtu anaweza kuwa na watoto mia moja naye akaishi miaka mingi, lakini haidhuru kuwa ataishi muda mrefu kiasi gani, kama hawezi kufurahia mafanikio yake na kwamba hapati mazishi ya heshima, ninasema afadhali mtoto aliyezaliwa akiwa amekufa kuliko yeye.
ECC 6:4 Kuzaliwa kwake hakuna maana, huondokea gizani na gizani jina lake hufunikwa.
ECC 6:5 Ingawa hakuwahi kuliona jua wala kujua kitu chochote, yeye ana pumziko kuliko mtu huyo:
ECC 6:6 Hata kama huyo mtu ataishi miaka elfu mara mbili na zaidi, lakini akashindwa kufurahia mafanikio yake, je, wote hawaendi sehemu moja?
ECC 6:7 Juhudi zote za binadamu ni kwa ajili ya kinywa chake, hata hivyo hamu yake kamwe haitoshelezwi.
ECC 6:8 Mtu mwenye hekima ana faida gani zaidi ya mpumbavu? Mtu maskini anapata faida gani kwa kujua jinsi ya kujistahi mbele ya watu wengine?
ECC 6:9 Ni bora kile ambacho jicho linakiona kuliko hamu isiyotoshelezwa. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
ECC 6:10 Lolote lililopo limekwisha kupewa jina, naye mwanadamu alivyo ameshajulikana; hakuna mtu awezaye kushindana na mwenye nguvu kuliko yeye.
ECC 6:11 Maneno yanavyokuwa mengi, ndivyo yanavyokosa maana, Je, hilo linamfaidia vipi yeyote?
ECC 6:12 Kwa maana ni nani anayejua lililo jema kwa ajili ya maisha ya mwanadamu, katika siku chache na za ubatili anazopita kama kivuli? Ni nani awezaye kumwambia yatakayotokea chini ya jua baada ya yeye kuondoka?
ECC 7:1 Afadhali sifa nzuri kuliko manukato safi, nayo siku ya kufa kuliko ya kuzaliwa.
ECC 7:2 Afadhali kwenda kwenye nyumba ya msiba kuliko kwenda kwenye nyumba ya karamu, kwa kuwa kifo ni hatima ya kila mwanadamu, imewapasa walio hai kuliweka hili mioyoni mwao.
ECC 7:3 Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, kwa sababu uso wenye huzuni wafaa kwa moyo.
ECC 7:4 Moyo wa wenye hekima uko katika nyumba ya msiba, lakini moyo wa wapumbavu uko katika nyumba ya anasa.
ECC 7:5 Afadhali kusikia karipio la mtu mwenye hekima, kuliko kusikiliza wimbo wa wapumbavu.
ECC 7:6 Kama ilivyo kuvunjika kwa miiba chini ya sufuria, ndivyo kilivyo kicheko cha wapumbavu. Hili nalo pia ni ubatili.
ECC 7:7 Dhuluma humfanya mtu mwenye hekima kuwa mpumbavu, nayo rushwa huuharibu moyo.
ECC 7:8 Mwisho wa jambo ni bora kuliko mwanzo wake, uvumilivu ni bora kuliko kiburi.
ECC 7:9 Usiwe mwepesi kukasirika rohoni mwako, kwa kuwa hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.
ECC 7:10 Usiseme, “Kwa nini siku za kale zilikuwa bora kuliko siku hizi?” Kwa maana si hekima kuuliza maswali kama hayo.
ECC 7:11 Hekima, kama ulivyo urithi, ni kitu chema na huwafaidia wale walionalo jua.
ECC 7:12 Hekima ni ulinzi kama fedha ilivyo ulinzi, lakini faida ya maarifa ni hii: kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo.
ECC 7:13 Tafakari kile Mungu alichokitenda: Nani awezaye kunyoosha kile ambacho yeye amekipinda?
ECC 7:14 Nyakati zikiwa nzuri, ufurahi, lakini nyakati zikiwa mbaya, tafakari hili: Mungu amefanya hiyo moja; naam, pia na hiyo nyingine. Kwa hiyo, mwanadamu hawezi kugundua kitu chochote kuhusu maisha yake ya baadaye.
ECC 7:15 Katika maisha haya yangu ya ubatili nimeshaona haya mawili: mtu mwadilifu akiangamia katika uadilifu wake, naye mtu mwovu akiishi maisha marefu katika uovu wake.
ECC 7:16 Usiwe mwenye haki kupita kiasi, wala usiwe na hekima kupita kiasi: kwa nini kujiangamiza mwenyewe?
ECC 7:17 Usiwe mwovu kupita kiasi, wala usiwe mpumbavu: kwa nini kufa kabla ya wakati wako?
ECC 7:18 Ni vyema kushika hilo moja na wala usiache hilo jingine likupite. Mtu amchaye Mungu ataepuka huko kupita kiasi.
ECC 7:19 Hekima humfanya yeye aliye nayo kuwa na uwezo kuliko watawala kumi katika mji.
ECC 7:20 Hakuna mtu mwenye haki duniani ambaye hufanya mambo ya haki na kamwe asitende dhambi.
ECC 7:21 Usitie maanani kila neno linalosemwa na watu, la sivyo, unaweza kumsikia mtumishi wako akikulaani:
ECC 7:22 kwa kuwa unafahamu moyoni mwako kwamba wewe mwenyewe mara nyingi umewalaani wengine.
ECC 7:23 Yote haya niliyajaribu kwa hekima, nikasema, “Nimeamua kuwa na hekima”: lakini hii ilikuwa nje ya uwezo wangu.
ECC 7:24 Vyovyote hekima ilivyo, hekima iko mbali sana na imejificha, ni nani awezaye kuigundua?
ECC 7:25 Nikageuza fikira zangu ili kuelewa, kuchunguza na kuitafuta hekima na kusudi la mambo, na ili kuelewa ujinga wa uovu, na wazimu wa upumbavu.
ECC 7:26 Nimeona jambo lililo chungu kuliko mauti, mwanamke ambaye ni mtego, ambaye moyo wake ni wavu wa kutegea na mikono yake ni minyororo. Mtu ampendezaye Mungu atamkwepa, bali mwenye dhambi atanaswa naye.
ECC 7:27 Mhubiri anasema, “Tazama, hili ndilo nililogundua: “Nimegundua kitu kimoja baada ya kingine nilipokuwa katika kusudi la mambo:
ECC 7:28 ningali natafiti lakini sipati: nilimpata mwanaume mmoja mnyofu miongoni mwa elfu, lakini hakuna mwanamke mmoja mnyofu miongoni mwao.
ECC 7:29 Hili ndilo peke yake nililolipata: Mungu amemuumba mwanadamu mnyofu, lakini mwanadamu amebuni mambo mengi.”
ECC 8:1 Ni nani aliye kama mtu mwenye hekima? Ni nani ajuaye maelezo ya mambo? Hekima hung’arisha uso wa mtu na kubadili ugumu wa uso wake.
ECC 8:2 Nawaambia, Tii amri ya mfalme, kwa sababu uliapa mbele za Mungu.
ECC 8:3 Usiharakishe kuondoka mbele ya mfalme. Usiendelee kutenda lililo baya, kwa maana mfalme atafanya lolote apendalo.
ECC 8:4 Kwa kuwa neno la mfalme ndilo lenye mamlaka ya mwisho, nani awezaye kumwambia, “Je, wewe unafanya nini?”
ECC 8:5 Yeyote anayetii agizo lake hatadhurika, moyo wa hekima utajua wakati mwafaka na jinsi ya kutenda.
ECC 8:6 Kwa maana kuna wakati mwafaka na utaratibu wa kila jambo, ingawa huzuni ya mwanadamu huwa nzito juu yake.
ECC 8:7 Kwa vile hakuna mtu ajuaye siku zijazo, ni nani awezaye kumwambia linalokuja?
ECC 8:8 Hakuna mwanadamu awezaye kushikilia roho yake asife, wala hakuna mwenye uwezo juu ya siku ya kufa kwake. Kama vile hakuna yeyote arudishwaye nyuma wakati wa vita, kadhalika uovu hautawaweka huru wale wautendao.
ECC 8:9 Yote haya niliyaona, nilipokuwa natafakari kila kitu kinachotendeka chini ya jua. Kuna wakati mtu hujifanya bwana juu ya wengine kwa madhara yake mwenyewe.
ECC 8:10 Ndipo pia nikaona waovu wakizikwa, wale waliozoea kuingia na kutoka mahali patakatifu na kupewa sifa katika mji ambao waliyafanya haya. Hili nalo ni ubatili.
ECC 8:11 Wakati hukumu juu ya tendo ovu haitekelezwi upesi, mioyo ya watu hujaa mipango ya kutenda maovu.
ECC 8:12 Ingawa mtu mwovu hufanya maovu mia moja na akaendelea kuishi maisha marefu, najua kwamba itakuwa bora zaidi kwa watu wanaomwogopa Mungu, wamchao Mungu.
ECC 8:13 Lakini kwa sababu waovu hawamwogopi Mungu, hawatafanikiwa, maisha yao hayatarefuka kama kivuli.
ECC 8:14 Kuna kitu kingine ambacho ni ubatili kinachofanyika duniani: Watu waadilifu kupata yale yanayowastahili waovu, nao waovu kupata yale yanayowastahili waadilifu. Hili nalo pia, nasema ni ubatili.
ECC 8:15 Kwa hiyo mimi ninasifu kufurahia maisha, kwa sababu hakuna kitu bora zaidi kwa mwanadamu chini ya jua kuliko kula, kunywa na kufurahi. Kisha furaha itafuatana naye kazini mwake siku zote za maisha yake ambazo amepewa na Mungu chini ya jua.
ECC 8:16 Nilipotafakari akilini mwangu ili nijue hekima na kuangalia kazi ya mwanadamu duniani, jinsi macho yake hayapati usingizi mchana wala usiku,
ECC 8:17 ndipo nikaona yale yote ambayo Mungu ameyafanya. Hakuna yeyote awezaye kuelewa yale yanayotendeka chini ya jua. Licha ya juhudi zake zote za kutafuta, mtu hawezi kugundua maana yake. Hata ingawa mtu mwenye hekima anadai kuwa anafahamu, kwa hakika hawezi kutambua.
ECC 9:1 Kwa hiyo niliyatafakari haya yote, nikafikia uamuzi kwamba waadilifu na wenye hekima na yale wanayoyafanya yako mikononi mwa Mungu, lakini hakuna mtu ajuaye kama anangojewa na upendo au chuki.
ECC 9:2 Wote wanayo hatima inayofanana, mwadilifu na mwovu, mwema na mbaya, aliye safi na aliye najisi, wale wanaotoa dhabihu na wale wasiotoa. Kama ilivyo kwa mtu mwema, ndivyo ilivyo kwa mtu mwenye dhambi; kama ilivyo kwa wale wanaoapa, ndivyo ilivyo kwa wale wasioapa.
ECC 9:3 Huu ni ubaya ulio katika kila kitu kinachotendeka chini ya jua: Mwisho unaofanana huwapata wote. Zaidi ya hayo, mioyo ya watu, imejaa ubaya na kuna wazimu mioyoni mwao wangali hai, hatimaye huungana na waliokufa.
ECC 9:4 Yeyote aliye miongoni mwa walio hai analo tumaini, hata mbwa hai ni bora kuliko simba aliyekufa!
ECC 9:5 Kwa maana walio hai wanajua kwamba watakufa, lakini wafu hawajui chochote, hawana tuzo zaidi, hata kumbukumbu yao imesahaulika.
ECC 9:6 Upendo wao, chuki yao na wivu wao vimetoweka tangu kitambo, kamwe hawatakuwa tena na sehemu katika lolote linalotendeka chini ya jua.
ECC 9:7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya.
ECC 9:8 Daima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta.
ECC 9:9 Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua.
ECC 9:10 Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko Kuzimu, unakoenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima.
ECC 9:11 Nimeona kitu kingine tena chini ya jua: Si wenye mbio washindao mashindano au wenye nguvu washindao vita, wala si wenye hekima wapatao chakula au wenye akili nyingi wapatao mali, wala wenye elimu wapatao upendeleo, lakini fursa huwapata wote.
ECC 9:12 Zaidi ya hayo, hakuna mwanadamu ajuaye wakati saa yake itakapokuja: Kama vile samaki wavuliwavyo katika wavu mkatili, au ndege wanaswavyo kwenye mtego, vivyo hivyo wanadamu hunaswa na nyakati mbaya zinazowaangukia bila kutazamia.
ECC 9:13 Pia niliona chini ya jua mfano huu wa hekima ambao ulinivutia sana:
ECC 9:14 Palikuwa na mji mdogo uliokuwa na watu wachache ndani yake. Mfalme mwenye nguvu akainuka dhidi yake, akauzingira kwa jeshi kubwa.
ECC 9:15 Katika mji huo kulikuwa na mtu mmoja maskini lakini mwenye hekima, naye akauokoa ule mji kwa hekima yake. Lakini hakuna aliyemkumbuka yule maskini.
ECC 9:16 Kwa hiyo, nikasema, “Hekima ni bora kuliko nguvu.” Lakini hekima ya maskini imedharauliwa, wala hakuna anayesikiliza maneno yake.
ECC 9:17 Maneno ya utulivu ya mwenye hekima husikiwa kuliko makelele ya mtawala wa wapumbavu.
ECC 9:18 Hekima ni bora kuliko silaha za vita, lakini mwenye dhambi mmoja huharibu mema mengi.
ECC 10:1 Kama vile inzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato, ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima.
ECC 10:2 Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume, lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto.
ECC 10:3 Hata anapotembea barabarani, mpumbavu hukosa ufahamu na kudhihirisha kwa kila mmoja jinsi alivyo mpumbavu.
ECC 10:4 Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako, usiache mahali pako, utulivu huweza kuzuia makosa mengi.
ECC 10:5 Kuna ubaya niliouona chini ya jua, aina ya kosa litokalo kwa mtawala:
ECC 10:6 Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za utawala, hali matajiri wanashika nafasi za chini.
ECC 10:7 Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, wakati wakuu wakitembea kwa miguu kama watumwa.
ECC 10:8 Yeye achimbaye shimo aweza kutumbukia ndani yake, yeyote abomoaye ukuta anaweza kuumwa na nyoka.
ECC 10:9 Yeyote apasuaye mawe inawezekana yakamuumiza, yeyote apasuaye magogo inawezekana yakamuumiza.
ECC 10:10 Kama shoka ni butu na halikunolewa, nguvu nyingi zinahitajika, lakini ustadi utaleta mafanikio.
ECC 10:11 Nyoka akiuma kabla ya kuchezeshwa, mchezeshaji hatahitajika tena.
ECC 10:12 Maneno yanayotoka kinywani mwa mtu mwenye hekima yana neema, bali mpumbavu huangamizwa na midomo yake mwenyewe.
ECC 10:13 Mwanzoni maneno yake ni upumbavu, mwishoni ni wazimu mbaya,
ECC 10:14 naye mpumbavu huzidisha maneno. Hakuna yeyote ajuaye linalokuja, ni nani awezaye kueleza ni jambo gani litakalotokea baada yake?
ECC 10:15 Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe, hajui njia iendayo mjini.
ECC 10:16 Ole wako, ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi.
ECC 10:17 Heri wewe, ee nchi ambayo mfalme wako ni wa uzao wenye kuheshimika, na ambayo wakuu wako hula chakula kwa wakati unaofaa: wao hula ili kupata nguvu na si kwa ajili ya ulevi.
ECC 10:18 Kama mtu ni mvivu, paa la nyumba huinama; kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja.
ECC 10:19 Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, nao mvinyo hufurahisha maisha, lakini fedha ni jawabu la mambo yote.
ECC 10:20 Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako, au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala, kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako, naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.
ECC 11:1 Tupa mkate wako juu ya maji, kwa maana baada ya siku nyingi utaupata tena.
ECC 11:2 Wape sehemu watu saba, naam hata wanane, kwa maana hujui ni baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
ECC 11:3 Kama mawingu yamejaa maji, hunyesha mvua juu ya nchi. Kama mti ukianguka kuelekea kusini au kuelekea kaskazini, mahali ulipoangukia, hapo ndipo utakapolala.
ECC 11:4 Yeyote atazamaye upepo hatapanda, yeyote anayeangalia mawingu hatavuna.
ECC 11:5 Kama vile usivyofahamu njia ya upepo, au jinsi mwili uumbwavyo ndani ya tumbo la mama, vivyo hivyo huwezi kufahamu kazi ya Mungu, Muumba wa vitu vyote.
ECC 11:6 Panda mbegu yako asubuhi, nako jioni usiruhusu mikono yako ilegee, kwa maana hujui ni ipi itakayofanikiwa, kwamba ni hii au ni ile, au kwamba zote zitafanikiwa sawasawa.
ECC 11:7 Nuru ni tamu, tena inafurahisha macho kuona jua.
ECC 11:8 Mtu akiishi miaka mingi kiasi gani, na aifurahie yote. Lakini akumbuke siku za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Kila kitu kitakachokuja ni ubatili.
ECC 11:9 Furahi ewe kijana, ukiwa bado kijana, moyo wako na ukupe furaha siku za ujana wako. Fuata njia za moyo wako na chochote macho yako yanaona, lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote Mungu atakuleta hukumuni.
ECC 11:10 Kwa hiyo, ondoa wasiwasi moyoni mwako na utupilie mbali masumbufu ya mwili wako, kwa kuwa ujana na nguvu ni ubatili.
ECC 12:1 Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku za taabu, wala haijakaribia miaka utakaposema, “Mimi sifurahii hiyo”:
ECC 12:2 kabla jua na nuru, nao mwezi na nyota havijatiwa giza, kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
ECC 12:3 siku ile walinzi wa nyumba watakapotetemeka, nao watu wenye nguvu watakapojiinamisha, wakati wasagao watakapokoma kwa sababu ya uchache, nao wachunguliao madirishani kutiwa giza;
ECC 12:4 wakati milango ya kuingia barabarani itakapofungwa na sauti ya kusaga kufifia; wakati watu wataamshwa kwa sauti ya ndege, lakini nyimbo zao zote zikififia;
ECC 12:5 wakati watu watakapoogopa kilichoinuka juu na hatari zitakazokuwepo barabarani; wakati mlozi utakapochanua maua na panzi kujikokota nawe usiwe na shauku ya kitu chochote. Ndipo mwanadamu aiendea nyumba yake ya milele nao waombolezaji wakizunguka barabarani.
ECC 12:6 Mkumbuke Muumba wako: kabla haijakatika kamba ya fedha, au bakuli la dhahabu halijavunjika; kabla mtungi kuvunjika kwenye chemchemi, au gurudumu kuvunjika kisimani,
ECC 12:7 nayo mavumbi kurudi ardhini yalikotoka, na roho kurudi kwa Mungu aliyeitoa.
ECC 12:8 Mhubiri asema, “Ubatili! Ubatili! Kila kitu ni ubatili!”
ECC 12:9 Mhubiri hakuwa tu na hekima, bali aliwagawia watu maarifa pia. Alitafakari na kutafiti na akaweka katika utaratibu mithali nyingi.
ECC 12:10 Mhubiri alitafiti ili kupata maneno sahihi na kila alichoandika kilikuwa sawa na kweli.
ECC 12:11 Maneno ya wenye hekima ni kama mchokoro, mithali zao zilizokusanywa pamoja ni kama misumari iliyopigiliwa ikawa imara, yaliyotolewa na Mchungaji mmoja.
ECC 12:12 Zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo. Hakuna mwisho wa kutunga vitabu vingi, nako kusoma sana huuchosha mwili.
ECC 12:13 Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa: Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.
ECC 12:14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au baya.
SOL 1:1 Wimbo ulio bora wa Sulemani.
SOL 1:2 Unibusu kwa busu la kinywa chako, kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai.
SOL 1:3 Manukato yako yananukia vizuri, jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa. Ndiyo sababu wanawali wanakupenda!
SOL 1:4 Nichukue twende nawe, na tufanye haraka! Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake. Rafiki Tunakushangilia na kukufurahia, tutasifu upendo wako kuliko divai. Mpendwa Tazama jinsi ilivyo bora wakupende!
SOL 1:5 Mimi ni mweusi, lakini napendeza, enyi binti za Yerusalemu, mweusi kama mahema ya Kedari, kama mapazia ya hema la Sulemani.
SOL 1:6 Usinikazie macho kwa sababu mimi ni mweusi, kwa sababu nimefanywa mweusi na jua. Wana wa mama yangu walinikasirikia na kunifanya niwe mtunza mashamba ya mizabibu. Shamba langu mwenyewe la mizabibu nimeliacha.
SOL 1:7 Niambie, wewe ninayekupenda, unalisha wapi kundi lako la kondoo na ni wapi unapowapumzisha kondoo wako adhuhuri. Kwa nini niwe kama mwanamke aliyefunikwa shela karibu na makundi ya rafiki zako?
SOL 1:8 Kama hujui, ewe mwanamke mzuri kuliko wote, fuata nyayo za kondoo, na kulisha wana-mbuzi wako karibu na mahema ya wachungaji.
SOL 1:9 Mpendwa wangu, ninakufananisha na farasi jike aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao.
SOL 1:10 Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli, shingo yako ikiwa na mikufu ya vito.
SOL 1:11 Tutakufanyia vipuli vya dhahabu, vyenye kupambwa kwa fedha.
SOL 1:12 Mfalme alipokuwa mezani pake, manukato yangu yalisambaza harufu yake nzuri.
SOL 1:13 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane kati ya matiti yangu.
SOL 1:14 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi.
SOL 1:15 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpendwa wangu! Tazama jinsi ulivyo mzuri! Macho yako ni kama ya hua.
SOL 1:16 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu! Ee, tazama jinsi unavyopendeza! Na kitanda chetu ni cha majani mazuri.
SOL 1:17 Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, na mapao yetu ni miberoshi.
SOL 2:1 Mimi ni ua la Sharoni, yungiyungi ya bondeni.
SOL 2:2 Kama yungiyungi kati ya miiba, ndivyo alivyo mpendwa wangu kati ya wanawali.
SOL 2:3 Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni, ndivyo alivyo mpenzi wangu miongoni mwa wanaume vijana. Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu, na tunda lake ni tamu kwangu.
SOL 2:4 Amenichukua hadi ukumbi wa karamu, na bendera ya huyu mwanaume juu yangu ni upendo.
SOL 2:5 Nitie nguvu kwa zabibu kavu, niburudishe kwa matofaa, kwa maana ninazimia kwa mapenzi.
SOL 2:6 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
SOL 2:7 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.
SOL 2:8 Sikiliza! Mpenzi wangu! Tazama! Huyu hapa anakuja, akirukaruka juu milimani akizunguka juu ya vilima.
SOL 2:9 Mpenzi wangu ni kama paa au ayala mchanga. Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu, akitazama kupitia madirishani, akichungulia kimiani.
SOL 2:10 Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia, “Inuka, mpendwa wangu, mrembo wangu, tufuatane.
SOL 2:11 Tazama! Wakati wa masika umepita, mvua imekwisha na ikapita.
SOL 2:12 Maua yanatokea juu ya nchi; majira ya kuimba yamewadia, sauti za njiwa zinasikika katika nchi yetu.
SOL 2:13 Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni, zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri. Inuka, njoo mpenzi wangu. Mrembo wangu, tufuatane.”
SOL 2:14 Hua wangu penye nyufa za majabali, mafichoni pembezoni mwa mlima, nioneshe uso wako, na niisikie sauti yako, kwa maana sauti yako ni tamu, na uso wako unapendeza.
SOL 2:15 Tukamatie mbweha, mbweha wale wadogo wanaoharibu mashamba ya mizabibu, mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.
SOL 2:16 Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake, yeye hujilisha kati ya yungiyungi.
SOL 2:17 Hadi jua linapochomoza, na vivuli vikimbie, rudi, mpenzi wangu, na uwe kama paa, au kama ayala mchanga juu ya vilima vya Betheri.
SOL 3:1 Usiku kucha kwenye kitanda changu nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye; nilimtafuta, lakini sikumpata.
SOL 3:2 Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini, katika barabara zake na viwanja; nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye. Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.
SOL 3:3 Walinzi walinikuta walipokuwa wakizunguka mji. Nikawauliza, “Je, mmemwona yule moyo wangu umpendaye?”
SOL 3:4 Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita nilimpata yule moyo wangu umpendaye. Nilimshika na sikumwachia aende hadi nilipomleta katika nyumba ya mama yangu, katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.
SOL 3:5 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.
SOL 3:6 Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani kama nguzo ya moshi, anayenukia manemane na uvumba iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote vya mfanyabiashara?
SOL 3:7 Tazama! Ni gari la Sulemani likisindikizwa na mashujaa sitini, walio wakuu sana wa Israeli,
SOL 3:8 wote wamevaa panga, wote wazoefu katika vita, kila mmoja na upanga wake pajani, wamejiandaa kwa ajili ya vitisho vya usiku.
SOL 3:9 Mfalme Sulemani alijitengenezea gari; alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.
SOL 3:10 Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha, kitako chake kwa dhahabu. Kiti chake kilipambwa kwa zambarau, gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo na binti za Yerusalemu.
SOL 3:11 Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni, mkamtazame Mfalme Sulemani akiwa amevaa taji, taji ambalo mama yake alimvika siku ya arusi yake, siku ambayo moyo wake ulishangilia.
SOL 4:1 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpendwa wangu! Ee, jinsi ulivyo mzuri! Macho yako nyuma ya shela yako ni kama ya hua. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi wakishuka kutoka Mlima Gileadi.
SOL 4:2 Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi, wanaotoka kuogeshwa. Kila jino lina pacha lake; hakuna hata moja lililo pekee.
SOL 4:3 Midomo yako ni kama uzi mwekundu, kinywa chako kinapendeza. Mashavu yako nyuma ya shela yako ni kama vipande viwili vya komamanga.
SOL 4:4 Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, uliojengwa kwa madaha, juu yake zimetundikwa ngao elfu, zote ni ngao za mashujaa.
SOL 4:5 Matiti yako mawili ni kama wana-paa wawili, kama wana-paa mapacha wajilishao kati ya yungiyungi.
SOL 4:6 Hata kupambazuke na vivuli vikimbie, nitaenda kwenye mlima wa manemane na kwenye kilima cha uvumba.
SOL 4:7 Wewe ni mzuri kote, mpendwa wangu, hakuna hitilafu ndani yako.
SOL 4:8 Nenda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu, nenda nami kutoka Lebanoni. Shuka kutoka ncha ya Amana, kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni, kutoka mapango ya simba na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.
SOL 4:9 Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu; umeiba moyo wangu kwa mtazamo mmoja wa macho yako, kwa kito kimoja cha mkufu wako.
SOL 4:10 Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha, dada yangu, bibi arusi wangu! Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai, na harufu ya marhamu yako zaidi ya manukato yoyote!
SOL 4:11 Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali, bibi arusi wangu; maziwa na asali viko chini ya ulimi wako. Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.
SOL 4:12 Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu, bibi arusi wangu; wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa, chemchemi yangu peke yangu.
SOL 4:13 Mimea yako ni bustani ya mikomamanga yenye matunda mazuri sana, yenye hina na nardo,
SOL 4:14 nardo na zafarani, mchai na mdalasini, pamoja na kila aina ya mti wa uvumba, manemane na udi, na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote.
SOL 4:15 Wewe ni chemchemi ya bustani, kisima cha maji yanayotiririka, yakitiririka kutoka Lebanoni.
SOL 4:16 Amka, upepo wa kaskazini, na uje, upepo wa kusini! Vuma juu ya bustani yangu, ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ng’ambo. Mpenzi wangu na aje bustanini mwake na kuonja matunda mazuri sana.
SOL 5:1 Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu, bibi arusi wangu; nimekusanya manemane yangu pamoja na manukato yangu. Nimekula sega langu la asali na asali yangu; nimekunywa divai yangu na maziwa yangu. Rafiki Kuleni, enyi rafiki, mnywe; kunyweni ya kutosha, ee wapenzi.
SOL 5:2 Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho. Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha: “Nifungulie, dada yangu, mpendwa wangu, hua wangu, usiye na hitilafu. Kichwa changu kimeloa umande, na nywele zangu manyunyu ya usiku.”
SOL 5:3 Nimevua joho langu: je, ni lazima nivae tena? Nimenawa miguu yangu: je, ni lazima niichafue tena?
SOL 5:4 Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo; moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.
SOL 5:5 Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu, mikono yangu ikidondosha manemane, vidole vyangu vikitiririka manemane, penye vipini vya komeo.
SOL 5:6 Nilimfungulia mpenzi wangu, lakini mpenzi wangu alishaondoka; alikuwa ameenda zake. Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake. Nilimtafuta lakini sikumpata. Nilimwita lakini hakunijibu.
SOL 5:7 Walinzi walinikuta walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini. Walinipiga, wakanijeruhi, wakaninyang’anya joho langu, hao walinzi wa kuta!
SOL 5:8 Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza: mkimpata mpenzi wangu, mtamwambia nini? Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.
SOL 5:9 Je, mpenzi wako ni bora kuliko wengine namna gani, wewe uliye mzuri kupita wanawake wote? Je, mpenzi wako ni mzuri kuliko wengine, namna gani, hata unatuagiza hivyo?
SOL 5:10 Mpenzi wangu anang’aa, tena ni mwekundu, wa kuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu.
SOL 5:11 Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote, nywele zake ni za mawimbi na ni nyeusi kama kunguru.
SOL 5:12 Macho yake ni kama ya hua kandokando ya vijito vya maji, aliyeogeshwa kwenye maziwa, yaliyopangwa kama vito vya thamani.
SOL 5:13 Mashavu yake ni kama matuta ya mimea ya manukato. Midomo yake ni kama yungiyungi inayodondosha manemane.
SOL 5:14 Mikono yake ni fimbo za dhahabu iliyopambwa kwa krisolitho. Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyong’arishwa iliyopambwa na yakuti samawi.
SOL 5:15 Miguu yake ni nguzo za marumaru zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi. Sura yake ni kama Lebanoni, bora kama miti yake ya mierezi.
SOL 5:16 Kinywa chake chenyewe ni utamu, kwa ujumla yeye ni wa kupendeza. Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu, ee binti za Yerusalemu.
SOL 6:1 Mpenzi wako ameenda wapi, ewe mzuri kupita wanawake wote? Mpenzi wako amegeukia njia ipi, tupate kumtafuta pamoja nawe?
SOL 6:2 Mpenzi wangu ameenda bustanini mwake, kwenye vitalu vya vikolezo, kujilisha bustanini na kukusanya yungiyungi.
SOL 6:3 Mimi ni wake mpenzi wangu, na mpenzi wangu ni wangu; yeye hujilisha kati ya yungiyungi.
SOL 6:4 Wewe ni mzuri, mpendwa wangu, kama Tirsa, unapendeza kama Yerusalemu, umetukuka kama jeshi lenye bendera.
SOL 6:5 Uyageuze macho yako mbali nami; yananigharikisha. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi wanaoteremka kutoka Gileadi.
SOL 6:6 Meno yako ni kama kundi la kondoo wanaotoka kuogeshwa. Kila mmoja ana pacha lake, hakuna hata mmoja aliye peke yake.
SOL 6:7 Mashavu yako nyuma ya shela yako ni kama vipande viwili vya komamanga.
SOL 6:8 Panaweza kuwa na malkia sitini, masuria themanini, na mabikira wasiohesabika;
SOL 6:9 lakini hua wangu, mkamilifu wangu, ni wa namna ya pekee, binti pekee kwa mama yake, kipenzi cha yeye aliyemzaa. Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa; malkia na masuria walimsifu.
SOL 6:10 Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko, mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua, ametukuka kama nyota zinazofuatana?
SOL 6:11 Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi ili kutazama machipuko ya bondeni, kuona kama mizabibu imechipua au kama mikomamanga imechanua maua.
SOL 6:12 Kabla sijang’amua, shauku yangu iliniweka katikati ya magari ya vita ya wakuu wangu.
SOL 6:13 Rudi, rudi, ee Mshulami; rudi, rudi ili tupate kukutazama! Mpenzi Kwa nini kumtazama Mshulami, kama kutazama ngoma ya Mahanaimu?
SOL 7:1 Ee binti ya mwana wa mfalme, tazama jinsi inavyopendeza miguu yako katika viatu! Miguu yako yenye madaha ni kama vito vya thamani, kazi ya mikono ya fundi stadi.
SOL 7:2 Kitovu chako ni kama bilauri ya mviringo ambayo kamwe haikosi divai iliyochanganywa. Kiuno chako ni kichuguu cha ngano kilichozungukwa kwa yungiyungi.
SOL 7:3 Matiti yako ni kama wana-paa wawili, mapacha wa paa.
SOL 7:4 Shingo yako ni kama mnara wa pembe ya ndovu. Macho yako ni vidimbwi vya Heshboni karibu na lango la Beth-Rabi. Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni ukitazama kuelekea Dameski.
SOL 7:5 Kichwa chako kinakuvika taji kama Mlima Karmeli. Nywele zako ni kama zulia la urujuani; mfalme ametekwa na mashungi yake.
SOL 7:6 Tazama jinsi ulivyo mzuri na unavyopendeza, ee pendo, kwa uzuri wako!
SOL 7:7 Umbo lako ni kama la mtende, nayo matiti yako kama vishada vya matunda.
SOL 7:8 Nilisema, “Nitakwea mtende, nami nitayashika matunda yake.” Matiti yako na yawe kama vishada vya mzabibu, harufu nzuri ya pumzi yako kama matofaa,
SOL 7:9 na kinywa chako kama divai bora kuliko zote. Mpendwa Divai na iende moja kwa moja hadi kwa mpenzi wangu, ikitiririka polepole juu ya midomo na meno.
SOL 7:10 Mimi ni mali ya mpenzi wangu, nayo shauku yake ni juu yangu.
SOL 7:11 Njoo, mpenzi wangu, twende mashambani, twende tukalale huko vijijini.
SOL 7:12 Hebu na twende mapema katika mashamba ya mizabibu tuone kama mizabibu imechipua, kama maua yake yamefunguka, na kama mikomamanga imetoa maua: huko nitakupa penzi langu.
SOL 7:13 Mitunguja hutoa harufu zake nzuri, kwenye milango yetu kuna matunda mazuri, mapya na ya zamani, ambayo nimekuhifadhia wewe, mpenzi wangu.
SOL 8:1 Laiti ungekuwa kwangu kama ndugu wa kiume, ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu! Kisha, kama ningekukuta huko nje, ningekubusu, wala hakuna mtu yeyote angenidharau.
SOL 8:2 Ningekuongoza na kukuleta katika nyumba ya mama yangu, yeye ambaye amenifundisha. Ningekupa divai iliyokolezwa unywe, asali ya maua ya mikomamanga yangu.
SOL 8:3 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
SOL 8:4 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza: msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.
SOL 8:5 Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani akimwegemea mpenzi wake? Mpendwa Nilikuamsha chini ya mtofaa, huko mama yako alipotunga mimba yako, huko yeye alipata uchungu akakuzaa.
SOL 8:6 Nitie kama muhuri moyoni mwako, kama muhuri kwenye mkono wako; kwa maana upendo una nguvu kama mauti, wivu wake ni mkatili kama Kuzimu. Unachoma kama mwali wa moto, kama mwali mkubwa wa moto wa Mwenyezi Mungu hasa.
SOL 8:7 Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, mito haiwezi kuugharikisha. Kama mtu angetoa mali yote ya nyumbani mwake kwa ajili ya upendo, angedharauliwa kabisa.
SOL 8:8 Tunaye dada mdogo, matiti yake hayajakua bado. Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu wakati atakapokuja kuposwa?
SOL 8:9 Kama yeye ni ukuta, tutajenga minara ya fedha juu yake. Na kama yeye ni mlango, tutamzungushia mbao za mwerezi.
SOL 8:10 Mimi ni ukuta, nayo matiti yangu ni kama minara. Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake kama yule anayeleta utoshelevu.
SOL 8:11 Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni; alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji. Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake shekeli elfu moja za fedha.
SOL 8:12 Lakini shamba langu la mizabibu ambalo ni langu mwenyewe ni langu kutoa; hizo shekeli elfu moja ni kwa ajili yako, ee Sulemani, na shekeli mia mbili ni kwa ajili ya wale wanaotunza matunda yake.
SOL 8:13 Wewe ukaaye bustanini pamoja na rafiki mliohudhuria, hebu nisikie sauti yako!
SOL 8:14 Njoo, mpenzi wangu, uwe kama paa au kama ayala mchanga juu ya milima iliyojaa manukato.
ISA 1:1 Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.
ISA 1:2 Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia! Kwa maana Mwenyezi Mungu amesema: “Nimewalisha watoto na kuwalea, lakini wameniasi mimi.
ISA 1:3 Ng’ombe anamjua bwana wake, naye punda anajua hori la mmiliki wake, lakini Israeli hajui, watu wangu hawaelewi.”
ISA 1:4 Ole wa taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, uzao wa watenda mabaya, watoto waliozoelea upotovu! Wamemwacha Mwenyezi Mungu, Wamemkataa kwa dharau yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na kumgeuzia kisogo.
ISA 1:5 Kwa nini mzidi kupigwa? Kwa nini kudumu katika uasi? Kichwa chako chote kimejeruhiwa, moyo wako wote ni mgonjwa.
ISA 1:6 Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako hakuna uzima: ni majeraha matupu na makovu na vidonda vinavyotoa damu, havikusafishwa au kufungwa wala kulainishwa kwa mafuta.
ISA 1:7 Nchi yenu imekuwa ukiwa, miji yenu imeteketezwa kwa moto; mashamba yenu yameachwa tupu na wageni mbele ya macho yenu, yameharibiwa kama yaliyopinduliwa na wageni.
ISA 1:8 Binti Sayuni ameachwa kama kipenu katika shamba la mizabibu, kama kibanda katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa.
ISA 1:9 Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni hakutuachia walionusurika, tungekuwa kama Sodoma, tungefanana na Gomora.
ISA 1:10 Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, ninyi watawala wa Sodoma; sikilizeni Torati ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora!
ISA 1:11 Mwenyezi Mungu anasema, “Wingi wa sadaka zenu, ni kitu gani kwangu? Nina sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi, za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona. Sipendezwi na damu za mafahali wala za wana-kondoo na mbuzi.
ISA 1:12 Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu, ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo, huku kuzikanyaga nyua zangu?
ISA 1:13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana! Uvumba wenu ni chukizo kwangu. Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada: siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
ISA 1:14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa: moyo wangu unazichukia kabisa. Zimekuwa mzigo kwangu, nimechoka kuzivumilia.
ISA 1:15 Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi, nitaficha macho yangu nisiwaone; hata mkiomba maombi mengi sitasikiliza. “Mikono yenu imejaa damu!
ISA 1:16 “Jiosheni na mkajitakase. Yaondoeni matendo yenu maovu mbele zangu; acheni kutenda mabaya.
ISA 1:17 Jifunzeni kutenda mema, tafuteni haki. Wateteeni waliodhulumiwa. Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane.
ISA 1:18 “Njooni basi tujadiliane,” asema Mwenyezi Mungu. “Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu, zitakuwa nyeupe kama theluji; ingawa ni nyekundu sana kama damu, zitakuwa nyeupe kama sufu.
ISA 1:19 Mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi,
ISA 1:20 lakini mkikataa na kuasi, mtaangamizwa kwa upanga.” Kwa kuwa kinywa cha Mwenyezi Mungu kimenena.
ISA 1:21 Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu umekuwa kahaba! Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu, haki ilikuwa inakaa ndani yake, lakini sasa ni wauaji!
ISA 1:22 Fedha yenu imekuwa takataka, divai yenu nzuri imechanganywa na maji.
ISA 1:23 Watawala wenu ni waasi, rafiki wa wezi, wote wanapenda rushwa na kukimbilia hongo. Hawatetei yatima; shauri la mjane haliletwi mbele yao.
ISA 1:24 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi: “Lo! Nitapata faraja kutoka kwa adui zangu, na kujilipizia kisasi kwa watesi wangu.
ISA 1:25 Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu, nitawasafisha takataka zenu zote na kuwaondolea unajisi wenu wote.
ISA 1:26 Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani, nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni. Baadaye utaitwa, Mji wa Haki, Mji Mwaminifu.”
ISA 1:27 Sayuni itakombolewa kwa haki, wale walio ndani yake waliotubu, kwa uaminifu.
ISA 1:28 Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa, nao wanaomwacha Mwenyezi Mungu wataangamia.
ISA 1:29 “Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni ambayo mlifurahia, mtafadhaika kwa sababu ya bustani mlizozichagua.
ISA 1:30 Mtakuwa kama mwaloni ulio na majani yanayonyauka, kama bustani isiyokuwa na maji.
ISA 1:31 Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yanayowaka moto, na kazi yake kama cheche ya moto; vyote vitaungua pamoja, wala hakuna wa kuuzima huo moto.”
ISA 2:1 Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:
ISA 2:2 Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la Mwenyezi Mungu utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote, utainuliwa juu ya vilima, na mataifa yote yatamiminika huko.
ISA 2:3 Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Torati itatoka Sayuni, neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu.
ISA 2:4 Atahukumu kati ya mataifa na ataamua migogoro ya mataifa mengi. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena.
ISA 2:5 Njooni, enyi nyumba ya Yakobo, tutembeeni katika nuru ya Mwenyezi Mungu.
ISA 2:6 Mwenyezi Mungu umewatelekeza watu wako, nyumba ya Yakobo. Wamejaa ushirikina unaotoka Mashariki, wanapiga ramli kama Wafilisti na wanashikana mikono na wapagani.
ISA 2:7 Nchi yao imejaa fedha na dhahabu, hakuna mwisho wa hazina zao. Nchi yao imejaa farasi, hakuna mwisho wa magari yao ya vita.
ISA 2:8 Nchi yao imejaa sanamu; wanasujudia kazi za mikono yao, vitu vile vidole vyao vimevitengeneza.
ISA 2:9 Kwa hiyo mwanadamu atashushwa na binadamu atanyenyekezwa: usiwasamehe.
ISA 2:10 Ingieni kwenye miamba, jificheni ardhini kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa enzi yake!
ISA 2:11 Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa na kiburi cha wanadamu kitashushwa, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.
ISA 2:12 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anayo siku aliyoiweka akiba kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi, kwa wote wanaojikweza (nao watanyenyekezwa),
ISA 2:13 kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana, na mialoni yote ya Bashani,
ISA 2:14 kwa milima yote mirefu na vilima vyote vilivyoinuka,
ISA 2:15 kwa kila mnara ulio mrefu sana na kila ukuta wenye ngome,
ISA 2:16 kwa kila meli ya biashara, na kila mashua ya kifahari.
ISA 2:17 Majivuno ya mwanadamu yatashushwa, na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,
ISA 2:18 nazo sanamu zitatoweka kabisa.
ISA 2:19 Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba, na kwenye mahandaki ardhini kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia.
ISA 2:20 Siku ile, watu watawatupia panya na popo sanamu zao za fedha na za dhahabu, walizozitengeneza ili waziabudu.
ISA 2:21 Watakimbilia kwenye mapango miambani na kwenye nyufa za miamba kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia.
ISA 2:22 Acheni kumtumainia mwanadamu, ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake. Yeye ana thamani gani?
ISA 3:1 Tazama sasa, Bwana, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda upatikanaji wa mahitaji na misaada, upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji,
ISA 3:2 shujaa na mtu wa vita, mwamuzi na nabii, mwaguzi na mzee,
ISA 3:3 jemadari wa kikosi cha watu hamsini na mtu mwenye cheo, mshauri, fundi stadi na msihiri mjanja.
ISA 3:4 Nitawafanya wavulana wawe viongozi wao; watoto ndio watakaowatawala.
ISA 3:5 Watu watadhulumiana: mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake. Kijana atainuka dhidi ya mzee, mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.
ISA 3:6 Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake katika nyumba ya baba yake na kusema, “Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu, tawala lundo hili la magofu!”
ISA 3:7 Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema, “Sina msaada. Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu, msinifanye niwe kiongozi wa watu.”
ISA 3:8 Yerusalemu inapepesuka, Yuda inaanguka; maneno yao na matendo yao ni kinyume na Mwenyezi Mungu, wakiudharau uwepo wake uliotukuka.
ISA 3:9 Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao, hujivunia dhambi yao kama Sodoma, wala hawaifichi. Ole wao! Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.
ISA 3:10 Waambie wanyofu itakuwa heri kwao, kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.
ISA 3:11 Ole kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao! Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda.
ISA 3:12 Vijana wanawatesa watu wangu, wanawake wanawatawala. Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha, wanawapoteza njia.
ISA 3:13 Mwenyezi Mungu anachukua nafasi yake mahakamani, anasimama kuhukumu watu.
ISA 3:14 Mwenyezi Mungu anaingia katika hukumu dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake: “Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu, mali iliyonyang’anywa maskini imo nyumbani mwenu.
ISA 3:15 Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu na kuzisaga nyuso za maskini?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ISA 3:16 Mwenyezi Mungu asema, “Wanawake wa Sayuni wana kiburi, wanatembea na shingo ndefu, wakikonyeza kwa macho yao, wanatembea kwa hatua za madaha, wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.
ISA 3:17 Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni; Mwenyezi Mungu atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
ISA 3:18 Katika siku ile Bwana atawanyang’anya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo,
ISA 3:19 vipuli, vikuku, shela,
ISA 3:20 vilemba, mikufu ya vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi,
ISA 3:21 pete zenye muhuri, pete za puani,
ISA 3:22 majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha,
ISA 3:23 vioo, mavazi ya kitani, taji na shali.
ISA 3:24 Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo; badala ya mishipi, ni kamba; badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara; badala ya mavazi mazuri, ni magunia; badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto.
ISA 3:25 Wanaume wako watauawa kwa upanga, nao mashujaa wako watauawa vitani.
ISA 3:26 Malango ya Sayuni yataomboleza na kulia, ataketi mavumbini akiwa fukara.
ISA 4:1 Katika siku ile wanawake saba watamshika mwanaume mmoja wakisema, “Tutakula chakula chetu wenyewe na kuvaa nguo zetu wenyewe, ila wewe uturuhusu tu tuitwe kwa jina lako. Utuondolee aibu yetu!”
ISA 4:2 Katika siku ile Tawi la Mwenyezi Mungu litakuwa zuri na lenye utukufu, nalo tunda la nchi litakuwa fahari na utukufu wa wale Waisraeli watakaonusurika.
ISA 4:3 Wale watakaoachwa Sayuni, watakaobaki Yerusalemu, wataitwa watakatifu, wale wote ambao wameorodheshwa miongoni mwa walio hai huko Yerusalemu.
ISA 4:4 Bwana atausafisha uchafu wa wanawake wa Sayuni, atatakasa madoa ya damu kutoka Yerusalemu kwa Roho ya hukumu na Roho ya moto.
ISA 4:5 Kisha Mwenyezi Mungu ataumba juu ya Mlima wote wa Sayuni, na juu ya wale wote wanaokusanyika hapo, wingu la moshi wakati wa mchana, na kung’aa kwa miali ya moto wakati wa usiku; nako juu ya huo utukufu wote kutatanda kifuniko cha ulinzi.
ISA 4:6 Utakuwa sitara na kivuli kutokana na joto la mchana, na kuwa mahali pa kujificha kutokana na dhoruba na mvua.
ISA 5:1 Nitaimba wimbo kwa mpenzi wangu, wimbo kuhusu shamba lake la mizabibu: Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu kwenye kilima chenye rutuba.
ISA 5:2 Alililima na kuondoa mawe na akaliotesha mizabibu bora sana. Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake, na kutengeneza shinikizo la kukamulia zabibu pia. Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri, lakini lilizaa matunda mabaya tu.
ISA 5:3 “Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu.
ISA 5:4 Ni nini zaidi ambacho kingefanyika katika shamba langu la mizabibu kuliko yale niliyofanya? Nilipotazamia kupata zabibu nzuri, kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu?
ISA 5:5 Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea shamba langu la mizabibu: Nitaondoa uzio wake, nalo litaharibiwa, nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa.
ISA 5:6 Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu, halitakatiwa matawi wala kulimwa, nayo michongoma na miiba itamea huko, nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”
ISA 5:7 Shamba la mzabibu la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ni nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni bustani yake ya kumpendeza. Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu; alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu.
ISA 5:8 Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.
ISA 5:9 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amesema nikisikia: “Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa, nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.
ISA 5:10 Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja ya divai, na homeri moja ya mbegu zilizopandwa itatoa efa moja tu ya nafaka.”
ISA 5:11 Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema wakikimbilia kunywa vileo, wale wakawiao sana hadi usiku, hata wamewaka kwa mvinyo.
ISA 5:12 Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao, matari, filimbi na mvinyo, lakini hawayajali matendo ya Mwenyezi Mungu, wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.
ISA 5:13 Kwa hiyo watu wangu wataenda uhamishoni kwa sababu ya kukosa maarifa; watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa, nao watu wengi watakauka kwa kiu.
ISA 5:14 Kwa hiyo Kaburi limeongeza hamu yake na kupanua mdomo wake bila kikomo, ndani yake watashuka wakuu wao na wingi wa watu, pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote.
ISA 5:15 Hivyo mwanadamu atashushwa, na binadamu kunyenyekezwa, macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.
ISA 5:16 Lakini Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atatukuzwa kwa ajili ya haki yake, naye Mungu Mtakatifu atajionesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa haki yake.
ISA 5:17 Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe, wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri.
ISA 5:18 Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu na uovu kama kwa kamba za mkokoteni,
ISA 5:19 kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka, aharakishe kazi yake ili tupate kuiona. Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike, tena udhihirike ili tupate kuujua.”
ISA 5:20 Ole wao wanaoita ubaya ni wema, na wema ni ubaya, wawekao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza, wawekao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu.
ISA 5:21 Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe, na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.
ISA 5:22 Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo, nao walio hodari katika kuchanganya vileo,
ISA 5:23 wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo, lakini huwanyima haki wasio na hatia.
ISA 5:24 Kwa hiyo, kama ndimi za moto zinavyoteketeza nyasi, na kama vile majani makavu yanavyozama katika miali ya moto, ndivyo mizizi yao itakavyooza, na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi; kwa kuwa wameikataa Torati ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na kulisukumia mbali neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 5:25 Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu inawaka dhidi ya watu wake, mkono wake umeinuliwa na anawapiga. Milima inatetemeka, maiti ni kama takataka kwenye barabara. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.
ISA 5:26 Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali, anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia. Tazama wamekuja, kwa kasi na kwa haraka!
ISA 5:27 Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa, hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala, hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni, hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika.
ISA 5:28 Mishale yao ni mikali, pinde zao zote zimevutwa, kwato za farasi wao ziko kama gumegume, magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli.
ISA 5:29 Ngurumo yao ni kama ile ya simba, wananguruma kama wana simba, wanakoroma wanapokamata mawindo yao, na kuondoka nayo pasipo yeyote wa kuokoa.
ISA 5:30 Katika siku ile watanguruma juu yake kama ngurumo za bahari. Kama mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki; hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.
ISA 6:1 Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi kwenye kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu.
ISA 6:2 Juu yake walikuwa maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka.
ISA 6:3 Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni; dunia yote imejaa utukufu wake.”
ISA 6:4 Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.
ISA 6:5 Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi kati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
ISA 6:6 Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni.
ISA 6:7 Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”
ISA 6:8 Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayeenda kwa ajili yetu?” Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”
ISA 6:9 Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa: “ ‘Mtaendelea daima kusikiliza, lakini kamwe hamtaelewa; mtaendelea daima kutazama, lakini kamwe hamtatambua.’
ISA 6:10 Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu, fanya masikio yao yasisikie, na upofushe macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, nao wakageuka, wakaponywa.”
ISA 6:11 Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?” Naye akanijibu: “Hadi miji iwe imeachwa magofu na bila wakazi, hadi nyumba zitakapobaki bila watu, na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa,
ISA 6:12 hadi Mwenyezi Mungu atakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana, na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa.
ISA 6:13 Hata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi, itaharibiwa tena. Lakini kama vile mvinje au mwaloni ubakizavyo visiki unapokatwa, ndivyo mbegu takatifu itakavyokuwa kisiki katika nchi.”
ISA 7:1 Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.
ISA 7:2 Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo mioyo ya Ahazi na watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.
ISA 7:3 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu, mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi.
ISA 7:4 Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia.
ISA 7:5 Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga njama ili wakuangamize, wakisema,
ISA 7:6 “Tuishambulie Yuda, naam, tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu, na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.”
ISA 7:7 Lakini Bwana Mungu Mwenyezi asema hivi: “ ‘Jambo hili halitatendeka, halitatukia,
ISA 7:8 kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake. Katika muda wa miaka sitini na tano, Efraimu atakuwa ameharibiwa kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa.
ISA 7:9 Kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia peke yake. Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu, hamtaimarika kamwe.’ ”
ISA 7:10 Mwenyezi Mungu akasema na Ahazi tena,
ISA 7:11 “Mwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ishara, iwe kwenye vina virefu sana, au kwenye vimo virefu sana.”
ISA 7:12 Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribu Mwenyezi Mungu.”
ISA 7:13 Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia?
ISA 7:14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli.
ISA 7:15 Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema.
ISA 7:16 Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa.
ISA 7:17 Mwenyezi Mungu ataleta juu yako pamoja na watu wako na juu ya nyumba ya baba yako, nyakati ambazo hazijawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda: naye Mwenyezi Mungu atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”
ISA 7:18 Katika siku ile Mwenyezi Mungu atawapigia filimbi inzi kutoka vijito vya mbali vya Misri, na nyuki kutoka nchi ya Ashuru.
ISA 7:19 Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye miteremko, na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba, na kwenye mashimo yote ya maji.
ISA 7:20 Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ng’ambo ya Mto, yaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako na malaika ya miguu yako, na kuziondoa ndevu zako pia.
ISA 7:21 Katika siku ile, mtu atahifadhi hai mtamba mmoja na kondoo wawili.
ISA 7:22 Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali.
ISA 7:23 Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli elfu moja za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu.
ISA 7:24 Watu wataenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba.
ISA 7:25 Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtaenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba. Patakuwa mahali ng’ombe wataachiwa huru, na kondoo kukimbia kimbia.
ISA 8:1 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Chukua kitabu kikubwa, uandike kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi.
ISA 8:2 Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”
ISA 8:3 Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi.
ISA 8:4 Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”
ISA 8:5 Mwenyezi Mungu akasema nami tena:
ISA 8:6 “Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yanayotiririka taratibu wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia;
ISA 8:7 kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao mafuriko makubwa ya Mto: yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote. Yatafurika juu ya mifereji yake yote, yatamwagikia juu ya kingo zake zote,
ISA 8:8 na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake, yakipita katikati na yakifika hadi shingoni. Mabawa yake yaliyokunjuliwa yatafunika upana wa nchi yako, Ee Imanueli!”
ISA 8:9 Inueni ukelele wa vita, enyi mataifa, na mkavunjwevunjwe! Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali. Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!
ISA 8:10 Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa; fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa, kwa maana Mungu yu pamoja nasi.
ISA 8:11 Mwenyezi Mungu alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:
ISA 8:12 “Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina, usiogope kile wanachokiogopa, wala usikihofu.
ISA 8:13 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndiye peke yake ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu, ndiye peke yake utakayemwogopa, ndiye peke yake utakayemhofu,
ISA 8:14 naye atakuwa mahali patakatifu; lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa na mwamba wa kuwaangusha. Kwa watu wa Yerusalemu, atakuwa mtego na tanzi.
ISA 8:15 Wengi wao watajikwaa; wataanguka na kuvunjika, watategwa na kunaswa.”
ISA 8:16 Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria miongoni mwa wanafunzi wangu.
ISA 8:17 Nitamngojea Mwenyezi Mungu, ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake. Nitaliweka tumaini langu kwake.
ISA 8:18 Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mwenyezi Mungu amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.
ISA 8:19 Watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunong’ona na kunung’unika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai?
ISA 8:20 Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.
ISA 8:21 Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao.
ISA 8:22 Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.
ISA 9:1 Hata hivyo, hakutakuwa huzuni tena kwa wale waliokuwa katika dhiki. Hapo awali aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataipa heshima Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani:
ISA 9:2 Watu wanaotembea katika giza wameona nuru kuu, wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewazukia.
ISA 9:3 Umelikuza taifa, na kuzidisha furaha yao, wanafurahia mbele zako, kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno, kama mashujaa wanavyofurahia wakigawanya nyara.
ISA 9:4 Kama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani, umevunja nira iliyowalemea, ile gongo mabegani mwao na fimbo ya aliyewadhulumu.
ISA 9:5 Kila kiatu cha shujaa kilichotumiwa vitani, na kila vazi lililovingirishwa katika damu vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa, vitakuwa kuni za kuwasha moto.
ISA 9:6 Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto wa kiume, nao utawala utakuwa begani mwake. Naye ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.
ISA 9:7 Kuongezeka kwa utawala wake na amani hakutakuwa na mwisho. Atatawala kwenye kiti cha utawala cha Daudi na juu ya ufalme wake, akiuthibitisha na kuutegemeza kwa haki na kwa adili, tangu wakati huo na hata milele. Wivu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni utatimiza haya.
ISA 9:8 Bwana ametuma ujumbe dhidi ya Yakobo, utamwangukia Israeli.
ISA 9:9 Watu wote watajua hili: Efraimu na wakazi wa Samaria, wanaosema kwa kiburi na majivuno ya mioyo,
ISA 9:10 “Matofali yameanguka chini, lakini tutajenga tena kwa mawe yaliyochongwa, mikuyu imekatwa, na tutapanda mierezi badala yake.”
ISA 9:11 Lakini Mwenyezi Mungu amemtia nguvu adui wa Resini dhidi yao na kuchochea watesi wao.
ISA 9:12 Waaramu kutoka upande wa mashariki na Wafilisti kutoka upande wa magharibi wameila Israeli kwa kinywa kilichopanuliwa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.
ISA 9:13 Lakini watu hawajamrudia yeye aliyewapiga, wala hawajamtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ISA 9:14 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu atakatilia mbali kutoka Israeli kichwa na mkia, tawi la mtende na tete katika siku moja.
ISA 9:15 Wazee na watu mashuhuri ndio vichwa, nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia.
ISA 9:16 Wale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha, nao wale wanaoongozwa wamepotoka.
ISA 9:17 Kwa hiyo Bwana hatawafurahia vijana, wala hatawahurumia yatima na wajane, kwa kuwa kila mmoja wao hamchi Mungu, nao ni waovu, na kila kinywa kinanena upumbavu. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.
ISA 9:18 Hakika uovu huwaka kama moto; huteketeza michongoma na miiba, huwasha moto vichaka vya msituni, hujiviringisha kuelekea juu kama nguzo ya moshi.
ISA 9:19 Kwa hasira ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni nchi itachomwa kwa moto, nao watu watakuwa kuni za kuchochea moto. Hakuna mtu atakayemhurumia ndugu yake.
ISA 9:20 Upande wa kuume watakuwa wakitafuna, lakini bado wataona njaa; upande wa kushoto watakuwa wakila, lakini hawatashiba. Kila mmoja atajilisha kwa nyama ya uzao wake mwenyewe:
ISA 9:21 Manase atamla Efraimu, naye Efraimu atamla Manase; nao pamoja watakuwa kinyume na Yuda. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.
ISA 10:1 Ole wao wawekao sheria zisizo za haki, kwa wale watoao amri za kuonea,
ISA 10:2 kuwanyima maskini haki zao na kuzuilia haki za watu wangu waliodhulumiwa, kuwafanya wajane mawindo yao na kuwanyang’anya yatima.
ISA 10:3 Mtafanya nini siku ya hukumu, wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali? Mtamkimbilia nani awape msaada? Mtaacha wapi mali yenu?
ISA 10:4 Hakutasalia kitu chochote, isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka, au kuanguka miongoni mwa waliouawa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.
ISA 10:5 “Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu, ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu!
ISA 10:6 Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani.
ISA 10:7 Lakini hili silo analokusudia, hili silo alilo nalo akilini; kusudi lake ni kuangamiza, kuyakomesha mataifa mengi.
ISA 10:8 Maana asema, ‘Je, wafalme wote si majemadari wangu?
ISA 10:9 Je, Kalno hakutendwa kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi, nayo Samaria si kama Dameski?
ISA 10:10 Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu, falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria:
ISA 10:11 je, nisiutendee Yerusalemu na sanamu zake kama nilivyoutendea Samaria na vinyago vyake?’ ”
ISA 10:12 Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.”
ISA 10:13 Kwa kuwa anasema: “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao.
ISA 10:14 Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”
ISA 10:15 Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu kuliko yule anayelitumia, au msumeno kujisifu dhidi ya yule anayeutumia? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye, au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!
ISA 10:16 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa mashujaa wake wanene, katika fahari yake moto utawaka kama mwali wa moto.
ISA 10:17 Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake.
ISA 10:18 Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.
ISA 10:19 Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu.
ISA 10:20 Katika siku ile, mabaki ya Israeli, walionusurika wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, lakini watamtegemea kwa kweli Mwenyezi Mungu Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 10:21 Mabaki watarudi, mabaki wa Yakobo watamrudia Mungu Mwenye Nguvu.
ISA 10:22 Ingawa watu wako, ee Israeli, ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaorudi. Maangamizi yamekwisha amriwa, ni mengi tena ni haki.
ISA 10:23 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, atatekeleza maangamizi yaliyoamriwa juu ya nchi yote.
ISA 10:24 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Enyi watu wangu mnaoishi Sayuni, msiwaogope Waashuru, wanaowapiga ninyi kwa fimbo na kuinua rungu dhidi yenu, kama Misri ilivyofanya.
ISA 10:25 Bado kitambo kidogo sana hasira yangu dhidi yenu itakoma, na ghadhabu yangu itaelekezwa kwenye maangamizi yao.”
ISA 10:26 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atawachapa kwa mjeledi, kama alivyowapiga Wamidiani katika mwamba wa Orebu, naye atainua fimbo yake juu ya maji, kama alivyofanya huko Misri.
ISA 10:27 Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa kutoka mabegani mwenu, na nira yao kutoka shingoni mwenu; nira itavunjwa kwa sababu ya kupakwa mafuta.
ISA 10:28 Wanaingia Ayathi, wanapita katikati ya Migroni, wanahifadhi mahitaji huko Mikmashi.
ISA 10:29 Wanavuka kivukoni, nao wanasema, “Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.” Rama inatetemeka; Gibea ya Sauli inakimbia.
ISA 10:30 Piga kelele, ee Binti Galimu! Sikiliza, ee Laisha! Maskini Anathothi!
ISA 10:31 Madmena inakimbia; watu wa Gebimu wanajificha.
ISA 10:32 Siku hii ya leo watasimama Nobu; watatikisa ngumi zao kwa mlima wa Binti Sayuni, kwa kilima cha Yerusalemu.
ISA 10:33 Tazama, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, atayakata matawi kwa nguvu kuu. Miti mirefu sana itaangushwa, ile mirefu itashushwa chini.
ISA 10:34 Atakata vichaka vya msitu kwa shoka; Lebanoni itaanguka mbele zake yeye Mwenye Nguvu.
ISA 11:1 Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese, kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.
ISA 11:2 Roho wa Mwenyezi Mungu atakaa juu yake, Roho wa hekima na wa ufahamu, Roho wa shauri na wa uweza, Roho wa maarifa na wa kumcha Mwenyezi Mungu
ISA 11:3 naye atafurahia kumcha Mwenyezi Mungu. Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake, wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,
ISA 11:4 bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji, kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia. Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.
ISA 11:5 Haki itakuwa mkanda wake na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.
ISA 11:6 Mbwa-mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo, naye chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ng’ombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza.
ISA 11:7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja, watoto wao watalala pamoja, na simba atakula majani makavu kama maksai.
ISA 11:8 Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka, naye mtoto mdogo ataweka mkono wake kwenye kiota cha fira.
ISA 11:9 Hawatadhuru wala kuharibu juu ya mlima wangu mtakatifu wote, kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Mwenyezi Mungu kama maji yajazavyo bahari.
ISA 11:10 Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu.
ISA 11:11 Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi, na kutoka visiwa vya baharini.
ISA 11:12 Atainua bendera kwa mataifa na kuwakusanya Waisraeli walio uhamishoni; atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika kutoka pembe nne za dunia.
ISA 11:13 Wivu wa Efraimu utatoweka, na adui wa Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamwonea Yuda wivu, wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.
ISA 11:14 Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti hadi upande wa magharibi, kwa pamoja watawateka watu nyara hadi upande wa mashariki. Watawapiga Edomu na Moabu, na Waamoni watatawaliwa nao.
ISA 11:15 Mwenyezi Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Misri; kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake juu ya Mto Frati. Ataugawanya katika vijito saba ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu.
ISA 11:16 Kutakuwa na njia kuu kwa mabaki ya watu wake wale waliosalia kutoka Ashuru, kama ilivyokuwa kwa Israeli walipopanda kutoka Misri.
ISA 12:1 Katika siku ile utasema: “Nitakusifu wewe, Ee Mwenyezi Mungu. Ingawa ulinikasirikia, hasira yako imegeukia mbali nawe umenifariji.
ISA 12:2 Hakika Mungu ni wokovu wangu; nitamtumaini wala sitaogopa. Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu, ni nguvu zangu na wimbo wangu; amekuwa wokovu wangu.”
ISA 12:3 Kwa furaha mtachota maji kutoka visima vya wokovu.
ISA 12:4 Katika siku hiyo mtasema: “Mshukuruni Mwenyezi Mungu, mliitie jina lake; julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya, tangazeni kuwa jina lake limetukuka.
ISA 12:5 Mwimbieni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ametenda mambo makuu, hili na lijulikane duniani kote.
ISA 12:6 Pazeni sauti mwimbe kwa furaha, watu wa Sayuni, kwa maana mkuu ni yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.”
ISA 13:1 Neno la unabii kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:
ISA 13:2 Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu, wapazieni sauti, wapungieni mkono waingie katika malango ya wenye heshima.
ISA 13:3 Nimewaamuru watakatifu wangu; nimewaita mashujaa wangu waitimize hasira yangu: wale wanaoshangilia ushindi wangu.
ISA 13:4 Sikilizeni kelele juu ya milima, kama ile ya umati mkubwa wa watu! Sikilizeni, makelele katika falme, kama mataifa yanayokusanyika pamoja! Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anakusanya jeshi kwa ajili ya vita.
ISA 13:5 Wanakuja kutoka nchi za mbali sana, kutoka miisho ya mbingu, Mwenyezi Mungu na silaha za ghadhabu yake, kuangamiza nchi yote.
ISA 13:6 Ombolezeni, kwa maana siku ya Mwenyezi Mungu i karibu, itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.
ISA 13:7 Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea, moyo wa kila mtu utayeyuka.
ISA 13:8 Hofu itawakamata, uchungu na maumivu makali yatawashika, watagaagaa kama mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa. Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake, nyuso zao zikiwaka kama moto.
ISA 13:9 Tazameni, siku ya Mwenyezi Mungu inakuja, siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali, kuifanya nchi kuwa ukiwa, na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo.
ISA 13:10 Nyota za mbinguni na makundi ya nyota havitatoa mwanga wake. Jua linalochomoza litatiwa giza na mwezi hautatoa nuru yake.
ISA 13:11 Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake, waovu kwa ajili ya dhambi zao. Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi, na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.
ISA 13:12 Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi, watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri.
ISA 13:13 Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke, nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, katika siku ya hasira yake iwakayo.
ISA 13:14 Kama paa awindwaye, kama kondoo wasio na mchungaji, kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe, kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa.
ISA 13:15 Yeyote atakayetekwa atapasuliwa tumbo, wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga.
ISA 13:16 Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande mbele ya macho yao; nyumba zao zitatekwa, na wake zao watanajisiwa.
ISA 13:17 Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao, ambao hawajali fedha wala hawafurahii dhahabu.
ISA 13:18 Mishale yao itawaangusha vijana, hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga wala hawataangalia watoto kwa huruma.
ISA 13:19 Babeli, johari ya falme, utukufu wa kiburi cha Wababeli, utaangushwa na Mungu kama Sodoma na Gomora.
ISA 13:20 Hautakaliwa na watu kamwe, wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote. Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko, hakuna mchungaji atakayepumzisha makundi yake huko.
ISA 13:21 Lakini viumbe wa jangwani watalala huko, mbweha watajaza nyumba zake, bundi wataishi humo nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo.
ISA 13:22 Fisi watalia ndani ya ngome zake, mbweha ndani ya majumba yake ya kifahari. Wakati wake umewadia, na siku zake hazitaongezwa.
ISA 14:1 Mwenyezi Mungu atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe. Wageni wataungana nao na kujiunga na nyumba ya Yakobo.
ISA 14:2 Mataifa watawachukua na kuwaleta mahali pao wenyewe. Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa kama watumishi na wajakazi katika nchi ya Mwenyezi Mungu. Watawafanya watekaji wao kuwa mateka, na kuwatawala waliowadhulumu.
ISA 14:3 Katika siku Mwenyezi Mungu atakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili,
ISA 14:4 utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli: Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho! Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma!
ISA 14:5 Mwenyezi Mungu amevunja fimbo ya mwovu, fimbo ya utawala ya watawala,
ISA 14:6 ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa kwa mapigo yasiyo na kikomo, nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa kwa jeuri pasipo huruma.
ISA 14:7 Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani, wanabubujika kwa kuimba.
ISA 14:8 Hata misunobari na mierezi ya Lebanoni inashangilia mbele yako na kusema, “Basi kwa kuwa umeangushwa chini, hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.”
ISA 14:9 Kuzimu kumetaharuki kukulaki unapokuja, kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea, wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu, kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme: wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa.
ISA 14:10 Wote wataitikia, watakuambia, “Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo; wewe umekuwa kama sisi.”
ISA 14:11 Majivuno yako yote yameshushwa hadi Kuzimu, pamoja na kelele ya vinubi vyako, mafunza yametanda chini yako, na minyoo imekufunika.
ISA 14:12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa!
ISA 14:13 Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha utawala juu ya nyota za Mungu; nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.
ISA 14:14 Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”
ISA 14:15 Lakini umeshushwa chini hadi Kuzimu, hadi kwenye vina vya shimo.
ISA 14:16 Wale wanaokuona wanakukazia macho, wanatafakari hatima yako: “Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia na kufanya falme zitetemeke,
ISA 14:17 yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa, aliyeipindua miji yake, na ambaye hakuwaachia mateka wake waende nyumbani?”
ISA 14:18 Wafalme wote wa mataifa wamelala kwa heshima kila mmoja katika kaburi lake.
ISA 14:19 Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako kama tawi lililokataliwa, umefunikwa na waliouawa pamoja na wale waliochomwa kwa upanga, wale wanaoshuka hadi kwenye mawe ya shimo. Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo,
ISA 14:20 Hutajumuika nao kwenye mazishi, kwa kuwa umeharibu nchi yako na kuwaua watu wako. Mzao wa mwovu hatatajwa tena kamwe.
ISA 14:21 Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe kwa ajili ya dhambi za baba zao, wasije wakainuka ili kuirithi nchi na kuijaza dunia kwa miji yao.
ISA 14:22 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni asema, “Nitainuka dhidi yao, nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli pamoja na watu wake walionusurika, watoto wake na wazao wake,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 14:23 “Nitaifanya kuwa mahali pa bundi, na kuwa nchi ya matope; nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ISA 14:24 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ameapa, “Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa, nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.
ISA 14:25 Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu, juu ya milima yangu nitawakanyagia chini. Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu, nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”
ISA 14:26 Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote, huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.
ISA 14:27 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amekusudia, ni nani awezaye kumzuia? Mkono wake umenyooshwa, ni nani awezaye kuurudisha?
ISA 14:28 Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipofariki:
ISA 14:29 Msifurahi, enyi Wafilisti wote, kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika; kutoka mzizi wa huyo nyoka atachipuka nyoka mwenye sumu kali, uzao wake utakuwa joka lirukalo, lenye sumu kali.
ISA 14:30 Maskini kuliko maskini wote watapata malisho, nao wahitaji watalala salama. Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa, nayo njaa itawaua walionusurika.
ISA 14:31 Piga yowe, ee lango! Bweka, ee mji! Yeyukeni, enyi Wafilisti wote! Wingu la moshi linakuja toka kaskazini, wala hakuna atakayechelewa katika safu zake.
ISA 14:32 Ni jibu gani litakalotolewa kwa wajumbe wa taifa hilo? “Mwenyezi Mungu ameifanya imara Sayuni, na ndani yake watu wake walioonewa watapata kimbilio.”
ISA 15:1 Neno la unabii kuhusu Moabu: Ari iliyo Moabu imeangamizwa: imeharibiwa kwa usiku mmoja! Kiri iliyo Moabu imeangamizwa, imeharibiwa kwa usiku mmoja!
ISA 15:2 Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake, hadi mahali pake pa juu pa kuabudia ili walie, Moabu anaombolezea Nebo na Medeba. Kila kichwa kimenyolewa na kila ndevu limeondolewa.
ISA 15:3 Wamevaa magunia barabarani; juu ya mapaa na kwenye viwanja wote wanaomboleza, wakilala kifudifudi na kulia.
ISA 15:4 Heshboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikika hadi Yahazi. Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele, nayo mioyo yao imezimia.
ISA 15:5 Moyo wangu unamlilia Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Soari, hadi Eglath-Shelishiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhithi, wanaenda huku wanalia; barabarani iendayo Horonaimu wanaombolezea maangamizi yao.
ISA 15:6 Maji ya Nimrimu yamekauka na majani yamenyauka; mimea imekauka wala hakuna kitu chochote kibichi kilichobaki.
ISA 15:7 Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi.
ISA 15:8 Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu, kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu, maombolezo yao hadi Beer-Elimu.
ISA 15:9 Maji ya Dimoni yamejaa damu, lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni: simba juu ya wakimbizi wa Moabu na juu ya wale wanaobaki katika nchi.
ISA 16:1 Pelekeni wana-kondoo kama ushuru kwa mtawala wa nchi, Kutoka Sela, kupitia jangwani, hadi mlima wa Binti Sayuni.
ISA 16:2 Kama ndege wanaopapatika waliofukuzwa kutoka kiota, ndivyo walivyo wanawake wa Moabu kwenye vivuko vya Mto Arnoni.
ISA 16:3 “Tupeni shauri, toeni uamuzi. Wakati wa adhuhuri, fanyeni kivuli chenu kama usiku. Waficheni watoro, msisaliti wakimbizi.
ISA 16:4 Waacheni watoro wa Moabu wakae pamoja nanyi; kuweni mahali pao pa salama ili kuepuka mwangamizi.” Mtesi atafikia mwisho na maangamizi yatakoma, aletaye vita atatoweka kutoka nchi.
ISA 16:5 Kwa upendo kiti cha utawala kitaimarishwa, kwa uaminifu mtu ataketi juu yake, yeye atokaye nyumba ya Daudi: yeye ambaye katika kuhukumu hutafuta haki, na huhimiza njia ya haki.
ISA 16:6 Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu: kiburi chake cha kujivuna na udanganyifu, kiburi chake na ufidhuli wake, lakini majivuno yake si kitu.
ISA 16:7 Kwa hiyo Wamoabu wanaomboleza, wanaiombolezea Moabu kwa pamoja. Wanaomboleza na kuhuzunika kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.
ISA 16:8 Mashamba ya Heshboni yananyauka, pia na mizabibu ya Sibma. Watawala wa mataifa wamekanyaga mizabibu iliyo mizuri sana, ambayo ilipata kufika Yazeri na kuenea kuelekea jangwani. Machipukizi yake yalienea yakafika hadi baharini.
ISA 16:9 Hivyo ninalia kama Yazeri aliavyo, kwa ajili ya mizabibu ya Sibma. Ee Heshboni, ee Eleale, ninakulowesha kwa machozi! Shangwe za furaha kwa ajili ya tunda lako lililoiva na kwa ajili ya mavuno zimekomeshwa.
ISA 16:10 Furaha na shangwe zimeondolewa kutoka mashamba ya matunda; hakuna yeyote aimbaye wala apazaye sauti katika mashamba ya mizabibu; hakuna yeyote akanyagaye zabibu shinikizoni, kwa kuwa nimekomesha makelele.
ISA 16:11 Moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama kinubi, nafsi yangu yote kwa ajili ya Kir-Haresethi.
ISA 16:12 Moabu anapojitokeza mahali pake pa juu pa kuabudia, anajichosha mwenyewe tu; anapoenda mahali pake pa ibada za sanamu ili kuomba, haitamfaidi lolote.
ISA 16:13 Hili ndilo neno ambalo Mwenyezi Mungu ameshasema kuhusu Moabu.
ISA 16:14 Lakini sasa Mwenyezi Mungu anasema: “Katika miaka mitatu, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, fahari ya Moabu na watu wake wengi watadharauliwa, nao walionusurika watakuwa wachache sana, tena wanyonge.”
ISA 17:1 Neno la unabii kuhusu Dameski: “Tazama, Dameski haitakuwa tena mji bali itakuwa lundo la magofu.
ISA 17:2 Miji ya Aroeri itaachwa na itaachiwa mifugo ambayo italala huko, bila yeyote wa kuyaogopesha.
ISA 17:3 Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu, nao uweza wa ufalme kutoka Dameski; mabaki ya Aramu yatakuwa kama utukufu wa Waisraeli,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ISA 17:4 “Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia, unono wa mwili wake utadhoofika.
ISA 17:5 Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka na kuvuna nafaka kwa mikono yake, kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke katika Bonde la Warefai.
ISA 17:6 Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki, kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa, kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi kileleni, nne au tano katika matawi yanayozaa sana,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
ISA 17:7 Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao, na kuelekeza macho yao kwa yule Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 17:8 Hawataziangalia tena madhabahu, kazi za mikono yao, nao hawataheshimu nguzo za Ashera, na madhabahu za kufukizia uvumba zilizofanywa kwa mikono yao.
ISA 17:9 Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.
ISA 17:10 Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu, hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu. Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana na kuotesha mizabibu ya kigeni,
ISA 17:11 hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote na asubuhi ile ile unayoipanda, unaifanya ichipue, hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu katika siku ile ya ugonjwa na maumivu yasiyoponyeka.
ISA 17:12 Ole! Ghadhabu ya mataifa mengi: wanaghadhibika kama bahari iliyochafuka! Ole! Makelele ya mataifa wanaovuma: wanavuma kama ngurumo za maji mengi!
ISA 17:13 Ingawa mataifa yanavuma kama ngurumo za maji yanayofanya mawimbi, wakati anayakemea yanakimbia mbali, yanafukuzwa mbele ya upepo kama makapi juu ya milima, kama jani likivingirishwa na dhoruba.
ISA 17:14 Wakati wa jioni, hofu ya ghafula! Kabla ya asubuhi, wametoweka! Hili ndilo fungu la wale wanaotupora, fungu la wale wanaotunyang’anya mali yetu.
ISA 18:1 Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa, kando ya mito ya Kushi,
ISA 18:2 iwapelekayo wajumbe wake kupitia bahari kwa mashua za mafunjo juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito.
ISA 18:3 Enyi mataifa yote ya ulimwengu, ninyi mnaoishi duniani wakati bendera itakapoinuliwa milimani, mtaiona, nayo tarumbeta itakapolia, mtaisikia.
ISA 18:4 Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Nitatulia kimya na kutazama kutoka maskani yangu, kama joto linalometameta katika mwanga wa jua, kama wingu la umande katika joto la wakati wa mavuno.”
ISA 18:5 Kwa maana, kabla ya mavuno, wakati wa kuchanua ukishapita na maua yakawa zabibu zinazoiva, atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi, naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka.
ISA 18:6 Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani na wanyama pori, ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi, nao wanyama pori wakati wote wa masika.
ISA 18:7 Wakati huo matoleo yataletwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito, matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ISA 19:1 Neno la unabii kuhusu Misri: Tazama, Mwenyezi Mungu amepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka naye anakuja Misri. Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake, nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao.
ISA 19:2 “Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri, ndugu atapigana dhidi ya ndugu, jirani dhidi ya jirani, mji dhidi ya mji, ufalme dhidi ya ufalme.
ISA 19:3 Wamisri watakufa moyo, na nitaibatilisha mipango yao. Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa, kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu.
ISA 19:4 Nitawatia Wamisri mikononi mwa bwana mkatili na mfalme mkali atawatawala,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ISA 19:5 Maji ya mito yatakauka, chini ya mto kutakauka kwa jua.
ISA 19:6 Mifereji itanuka; vijito vya Misri vitapungua na kukauka. Matete na nyasi vitanyauka,
ISA 19:7 pia mimea iliyo kando ya Mto Naili, pale mto unapomwaga maji baharini. Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka, litapeperushwa na kutoweka kabisa.
ISA 19:8 Wavuvi watalia na kuomboleza, wote watupao ndoana katika Mto Naili, na watupao nyavu katika maji watadhoofika kwa majonzi.
ISA 19:9 Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa, wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo.
ISA 19:10 Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa, nao vibarua wataugua moyoni.
ISA 19:11 Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa, washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga. Unawezaje kumwambia Farao, “Mimi ni mmoja wa watu wenye hekima, mwanafunzi wa wafalme wa zamani”?
ISA 19:12 Wako wapi sasa watu wako wenye hekima? Wao wakuoneshe na kukufahamisha ni nini Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amepanga dhidi ya Misri.
ISA 19:13 Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu, viongozi wa Memfisi wamedanganyika, walio mawe ya pembe ya taifa lake wameipotosha Misri.
ISA 19:14 Mwenyezi Mungu amewamwagia roho ya kizunguzungu; wanaifanya Misri iyumbayumbe katika yale yote inayoyafanya, kama vile mlevi ayumbayumbavyo katika kutapika kwake.
ISA 19:15 Misri haiwezi kufanya kitu chochote, cha kichwa wala cha mkia, cha tawi la mtende wala cha tete.
ISA 19:16 Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anaoinua dhidi yao.
ISA 19:17 Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anapanga dhidi yao.
ISA 19:18 Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Mji mmoja utaitwa Mji wa Uharibifu.
ISA 19:19 Katika siku hiyo patakuwa na madhabahu ya Mwenyezi Mungu katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa Mwenyezi Mungu kwenye mpaka wa Misri.
ISA 19:20 Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni katika nchi ya Misri. Watakapomlilia Mwenyezi Mungu kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa.
ISA 19:21 Hivyo Mwenyezi Mungu atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali Mwenyezi Mungu. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea Mwenyezi Mungu nadhiri na kuzitimiza.
ISA 19:22 Mwenyezi Mungu ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia Mwenyezi Mungu, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.
ISA 19:23 Katika siku hiyo kutakuwa na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru wataenda Misri, na Wamisri wataenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja.
ISA 19:24 Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia.
ISA 19:25 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”
ISA 20:1 Mwaka ule jemadari mkuu alitumwa na Mfalme Sargoni wa Ashuru, naye akaja Ashdodi, akaushambulia na kuuteka,
ISA 20:2 wakati huo Mwenyezi Mungu alisema kwa kinywa cha Isaya mwana wa Amozi. Akamwambia, “Vua gunia kutoka mwilini mwako na viatu kutoka miguuni mwako.” Naye akafanya hivyo, akitembea uchi, bila viatu.
ISA 20:3 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Kama mtumishi wangu Isaya alivyotembea uchi na bila viatu kwa miaka mitatu, kama ishara na dalili mbaya dhidi ya nchi ya Misri na Kushi,
ISA 20:4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawaongoza mateka wa Wamisri, na watu wa uhamisho wa Kushi, uchi na bila viatu, vijana hata wazee, wakiwa matako wazi, kwa aibu ya Wamisri.
ISA 20:5 Wale waliotegemea Kushi na kujivunia Misri wataogopa na kuaibika.
ISA 20:6 Katika siku ile watu wanaoishi katika pwani hii watasema, ‘Tazama lililowapata wale tuliowategemea, wale tuliowakimbilia kwa msaada na wokovu kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru! Tutawezaje basi kupona?’ ”
ISA 21:1 Neno la unabii kuhusu Jangwa kando ya Bahari: Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini, mshambuliaji anakuja kutoka jangwani, kutoka nchi inayotisha.
ISA 21:2 Nimeoneshwa maono ya kutisha: Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara. Elamu, shambulia! Umedi, zingira kwa jeshi! Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.
ISA 21:3 Kwa sababu hii, mwili wangu umeteswa na maumivu, maumivu makali ya ghafula yamenishika, kama yale ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa. Nimeduwazwa na lile ninalolisikia, nimeshangazwa na lile ninaloliona.
ISA 21:4 Moyo wangu unababaika, woga unanifanya nitetemeke, gizagiza la jioni nililolitamani sana, limekuwa hofu kuu kwangu.
ISA 21:5 Wanaandaa meza, wanatandaza mazulia, wanakula, wanakunywa! Amkeni, enyi maafisa, zitieni ngao mafuta!
ISA 21:6 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Nenda, weka mlinzi, na atoe taarifa ya kile anachokiona.
ISA 21:7 Anapoona magari ya vita pamoja na kundi la farasi, wapanda punda au wapanda ngamia, na awe macho, awe macho kikamilifu.”
ISA 21:8 Naye mlinzi alipaza sauti, “Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi, kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.
ISA 21:9 Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita pamoja na kundi la farasi. Naye anajibu: ‘Babeli umeanguka, umeanguka! Vinyago vyote vya miungu yake vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ”
ISA 21:10 Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria, ninawaambia kile nilichokisikia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, kutoka kwa Mungu wa Israeli.
ISA 21:11 Neno la unabii kuhusu Duma: Mtu fulani ananiita kutoka Seiri, “Mlinzi, usiku utaisha lini? Mlinzi, usiku utaisha lini?”
ISA 21:12 Mlinzi anajibu, “Asubuhi inakuja, lakini pia usiku. Ukitaka kuuliza, basi uliza; na urudi mara tena.”
ISA 21:13 Neno la unabii kuhusu Arabia: Enyi misafara ya Wadedani, mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,
ISA 21:14 leteni maji kwa wenye kiu, ninyi mnaoishi Tema, leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.
ISA 21:15 Wanaukimbia upanga, upanga uliochomolewa alani, kutoka upinde uliopindwa, na kutoka kwa joto la vita.
ISA 21:16 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho.
ISA 21:17 Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, amesema.
ISA 22:1 Neno la unabii kuhusu Bonde la Maono: Nini kinachokutaabisha sasa, kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?
ISA 22:2 Ewe mji uliojaa ghasia, ewe mji wa makelele na sherehe! Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga, wala hawakufa vitani.
ISA 22:3 Viongozi wako wote wamekimbia pamoja, wamekamatwa bila kutumia upinde. Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja, mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.
ISA 22:4 Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami, niache nilie kwa uchungu. Usijaribu kunifariji juu ya maangamizi ya watu wangu.”
ISA 22:5 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayo siku ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya katika Bonde la Maono, siku ya kuangusha kuta na ya kupiga kelele hadi milimani.
ISA 22:6 Elamu analichukua podo, pamoja na waendesha magari ya vita na farasi. Kiri anaifungua ngao.
ISA 22:7 Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita, nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji.
ISA 22:8 Ulinzi wa Yuda umeondolewa. Nawe ulitazama siku ile silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni.
ISA 22:9 Mkaona kuwa Mji wa Daudi una matundu mengi katika ulinzi wake, mkaweka akiba ya maji kwenye Bwawa la Chini.
ISA 22:10 Mlihesabu majengo katika Yerusalemu nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.
ISA 22:11 Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani, lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza, au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale.
ISA 22:12 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliwaita siku ile ili kulia na kuomboleza, kung’oa nywele zenu na kuvaa magunia.
ISA 22:13 Lakini tazama, kuna furaha na sherehe, kuchinja ng’ombe na kuchinja kondoo, kula nyama na kunywa mvinyo! Mnasema, “Tuleni na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa!”
ISA 22:14 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amelifunua hili nikiwa ninasikia: Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema: “Hadi siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”
ISA 22:15 Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asemalo: “Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna, ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:
ISA 22:16 Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa kujikatia kaburi lako mwenyewe, ukichonga kaburi lako mahali palipo juu, na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?
ISA 22:17 “Jihadhari, Mwenyezi Mungu yu karibu kukukamata thabiti, na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu.
ISA 22:18 Atakuvingirisha uwe kama mpira na kukutupa katika nchi kubwa. Huko ndiko utakakofia, na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia, na kuwa fedheha kwa nyumba ya bwana wako!
ISA 22:19 Nitakuondoa kutoka kazi yako, nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako.
ISA 22:20 “Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia.
ISA 22:21 Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda.
ISA 22:22 Nitaweka begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua.
ISA 22:23 Nitampigilia kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake.
ISA 22:24 Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Wazao wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”
ISA 22:25 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni asema, “Katika siku ile, kigingi kilichopigiliwa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioning’inia juu yake utaanguka chini.” Mwenyezi Mungu amesema.
ISA 23:1 Neno la unabii kuhusu Tiro: Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi! Kwa kuwa Tiro imeangamizwa, imeachwa bila nyumba wala bandari. Kuanzia nchi ya Kitimu neno limewajia.
ISA 23:2 Nyamazeni kimya, enyi watu wa kisiwani, pia ninyi wafanyabiashara wa Sidoni, ambao mabaharia wamewatajirisha.
ISA 23:3 Kwenye maji makuu nafaka za Shihori zilikuja; mavuno ya Mto Naili yalikuwa mapato ya Tiro, naye akawa soko la mataifa.
ISA 23:4 Uaibishwe ee Sidoni, nawe ee ngome la bahari, kwa kuwa bahari imesema: “Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa wala sijapata kuzaa, wala sijapata kulea wana wala kutunza binti.”
ISA 23:5 Habari ifikapo Misri, watakuwa katika maumivu makuu kwa ajili ya taarifa kutoka Tiro.
ISA 23:6 Vukeni hadi Tarshishi, ombolezeni, enyi watu wa kisiwani.
ISA 23:7 Je, huu ndio mji wenu uliojaa sherehe, mji wa zamani, zamani kabisa ambao miguu yake imeuchukua kufanya makao nchi za mbali sana?
ISA 23:8 Ni nani amepanga hili dhidi ya Tiro, mji utoao mataji, ambao wafanyabiashara wake ni wana wa mfalme na wachuuzi wake ni watu mashuhuri wa dunia?
ISA 23:9 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndiye alipanga jambo hili, ili kukishusha kiburi cha utukufu wote na kuwanyenyekeza wale wote ambao ni mashuhuri duniani.
ISA 23:10 Ee Binti Tarshishi, pita katika nchi yako kama vile Mto Naili kwa kuwa huna tena bandari.
ISA 23:11 Mwenyezi Mungu amenyoosha mkono wake juu ya bahari na kuzifanya falme zake zitetemeke. Ametoa amri kuhusu Kanaani kwamba ngome zake ziangamizwe.
ISA 23:12 Alisema, “Usizidi kufurahi, ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa! “Simama, vuka uende Kitimu; hata huko hutapata pumziko.”
ISA 23:13 Tazama katika nchi ya Wakaldayo, watu hawa ambao sasa hawaonekani kama wapo! Waashuru wameifanya nchi hiyo kuwa mahali pa viumbe wa jangwani. Wamesimamisha minara yao ya kuuzingira, wameziteka ngome zake na kuziacha tupu na kuufanya kuwa magofu.
ISA 23:14 Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi; ngome yenu imeangamizwa!
ISA 23:15 Wakati huo Tiro utasahauliwa kwa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Lakini mwisho wa miaka hiyo sabini, itakuwa kwa Tiro kama ilivyo katika wimbo wa kahaba:
ISA 23:16 “Twaa kinubi, tembea mjini kote, ewe kahaba uliyesahauliwa; piga kinubi vizuri, imba nyimbo nyingi, ili upate kukumbukwa.”
ISA 23:17 Mwishoni mwa miaka sabini, Mwenyezi Mungu atatembelea Tiro. Naye Tiro atarudia ajira yake ya ukahaba, na atafanya biashara yake na falme zote duniani.
ISA 23:18 Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu; hayatahifadhiwa wala kufichwa. Faida zake zitaenda kwa wale wanaoishi mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri.
ISA 24:1 Tazama, Mwenyezi Mungu ataifanya dunia kuwa ukiwa na kuiharibu, naye atauharibu uso wake na kutawanya wanaoishi ndani yake:
ISA 24:2 ndivyo itakavyokuwa kwa makuhani na kwa watu, kwa bwana na kwa mtumishi, kwa bibi na kwa mjakazi wake, kwa muuzaji na kwa mnunuzi, kwa mkopaji na kwa mkopeshaji, kwa mdaiwa na kwa mdai.
ISA 24:3 Dunia itaharibiwa kabisa na kutekwa nyara kabisa. Mwenyezi Mungu amesema neno hili.
ISA 24:4 Dunia inakauka na kunyauka, dunia inanyong’onyea na kunyauka, waliotukuzwa wa dunia wananyong’onyea.
ISA 24:5 Dunia imetiwa unajisi na watu wake; wameacha kutii sheria, wamevunja amri na kuvunja agano la milele.
ISA 24:6 Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia, watu wake lazima waichukue hatia yao. Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa, nao waliosalia ni wachache sana.
ISA 24:7 Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka, watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.
ISA 24:8 Furaha ya matoazi imekoma, kelele za wenye furaha zimekoma, shangwe za kinubi zimenyamaza.
ISA 24:9 Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo, kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.
ISA 24:10 Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa, mlango wa kila nyumba umefungwa.
ISA 24:11 Barabarani wanalilia kupata mvinyo, furaha yote imegeuka kuwa majonzi, furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.
ISA 24:12 Mji umeachwa katika uharibifu, lango lake limevunjwa vipande.
ISA 24:13 Ndivyo itakavyokuwa duniani na miongoni mwa mataifa, kama vile wakati mzeituni upigwavyo, au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.
ISA 24:14 Wanapaza sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha, kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Mwenyezi Mungu.
ISA 24:15 Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Mwenyezi Mungu utukufu, liadhimisheni jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.
ISA 24:16 Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji: “Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.” Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika! Ole wangu! Watenda hila wanasaliti! Kwa hila watenda hila wanasaliti!”
ISA 24:17 Hofu, shimo na mtego vinakungojea, ewe mtu ukaaye duniani.
ISA 24:18 Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu atatumbukia shimoni, naye yeyote apandaye kutoka shimoni, atanaswa kwenye mtego. Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika.
ISA 24:19 Dunia imepasuka, dunia imechanika, dunia imetikiswa kabisa.
ISA 24:20 Dunia inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo; imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake na ikianguka kamwe haitainuka tena.
ISA 24:21 Katika siku ile Mwenyezi Mungu ataadhibu mamlaka zilizo juu mbinguni, na wafalme walio chini duniani.
ISA 24:22 Watakusanywa pamoja kama wafungwa waliofungwa gerezani; watafungiwa gerezani na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.
ISA 24:23 Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa; kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atatawala juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu, tena mbele ya wazee wake, kwa utukufu.
ISA 25:1 Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza na kulisifu jina lako, kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu umetenda mambo ya ajabu, mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.
ISA 25:2 Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi, mji wenye ngome kuwa magofu, ngome imara ya wageni kuwa si mji tena, wala hautajengwa tena kamwe.
ISA 25:3 Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu, miji ya mataifa katili itakuogopa wewe.
ISA 25:4 Umekuwa kimbilio la watu maskini, kimbilio la mhitaji katika taabu yake, hifadhi wakati wa dhoruba na kivuli wakati wa hari. Kwa maana pumzi ya wakatili ni kama dhoruba ipigayo ukuta
ISA 25:5 na kama joto la jangwani. Wewe wanyamazisha kelele ya wageni; kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu, ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo.
ISA 25:6 Juu ya mlima huu Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ataandaa karamu ya vinono kwa mataifa yote, karamu ya mvinyo wa zamani, nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.
ISA 25:7 Juu ya mlima huu ataharibu sitara ihifadhiyo mataifa yote, kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,
ISA 25:8 yeye atameza mauti milele. Bwana Mungu Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote; ataondoa aibu ya watu wake duniani kote. Mwenyezi Mungu amesema hili.
ISA 25:9 Katika siku ile watasema, “Hakika huyu ndiye Mungu wetu; tulimtumaini, naye akatuokoa. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, tuliyemtumaini; sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.”
ISA 25:10 Mkono wa Mwenyezi Mungu utatulia juu ya mlima huu, bali Moabu atakanyagwa chini kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea.
ISA 25:11 Watakunjua mikono yao katikati yake, kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee. Mungu atashusha kiburi chao licha ya ujanja wa mikono yao.
ISA 25:12 Atabomoa kuta ndefu za ngome yako na kuziangusha chini, atazishusha chini ardhini, hadi mavumbini kabisa.
ISA 26:1 Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda: Tuna mji ulio na nguvu, Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake.
ISA 26:2 Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia, taifa lidumishalo imani.
ISA 26:3 Utamlinda katika amani kamilifu yeye ambaye moyo wake ni thabiti kwa sababu anakutumaini wewe.
ISA 26:4 Mtumaini Mwenyezi Mungu milele, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu, ni Mwamba wa milele.
ISA 26:5 Huwashusha wale wajikwezao, huushusha chini mji wenye kiburi, huushusha hadi ardhini na kuutupa chini mavumbini.
ISA 26:6 Miguu huukanyagia chini: miguu ya hao waliodhulumiwa, hatua za hao maskini.
ISA 26:7 Mapito ya wenye haki ni nyoofu. Ewe uliye Mwenye Haki, waisawazisha njia ya mtu mnyofu.
ISA 26:8 Naam, Mwenyezi Mungu, tukienenda katika sheria zako, twakungojea wewe, jina lako na sifa zako ndizo shauku za mioyo yetu.
ISA 26:9 Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku, wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku. Hukumu zako zinapokuja juu ya dunia, watu wa ulimwengu hujifunza haki.
ISA 26:10 Ingawa neema yaoneshwa kwa waovu, hawajifunzi haki; hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya wala hawazingatii utukufu wa Mwenyezi Mungu.
ISA 26:11 Ee Mwenyezi Mungu, mkono wako umeinuliwa juu, lakini hawauoni. Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe, moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze.
ISA 26:12 Mwenyezi Mungu, unaamuru amani kwa ajili yetu, yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu.
ISA 26:13 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala, lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu.
ISA 26:14 Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai, roho za waliokufa hazitarudi tena. Uliwaadhibu na kuwaangamiza, umefuta kumbukumbu lao lote.
ISA 26:15 Umeliongeza hilo taifa, Ee Mwenyezi Mungu, umeliongeza hilo taifa. Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe, umepanua mipaka yote ya nchi.
ISA 26:16 Mwenyezi Mungu, walikujia katika taabu yao, wewe ulipowarudi, waliweza kuomba kwa kunong’ona tu.
ISA 26:17 Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee Mwenyezi Mungu.
ISA 26:18 Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu, lakini tulizaa upepo. Hatukuleta wokovu duniani, hatujazaa watu katika ulimwengu huu.
ISA 26:19 Lakini wafu wenu wataishi, nayo miili yao itafufuka. Ninyi mnaokaa katika mavumbi, amkeni mkashangilie kwa furaha. Umande wenu ni kama umande wa asubuhi, dunia itawazaa wafu wake.
ISA 26:20 Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu na mfunge milango nyuma yenu, jificheni kwa kitambo kidogo hadi ghadhabu yake ipite.
ISA 26:21 Tazama, Mwenyezi Mungu anakuja kutoka makao yake ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao. Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake, wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.
ISA 27:1 Katika siku ile, Mwenyezi Mungu ataadhibu kwa upanga wake, upanga wake mkali, mkubwa na wenye nguvu; ataadhibu Lewiathani yule nyoka apitaye kwa mwendo laini, Lewiathani yule nyoka mwenye kujipinda; atamuua yule mnyama mkubwa wa baharini.
ISA 27:2 Katika siku ile: “Imbeni kuhusu shamba la mizabibu lililozaa:
ISA 27:3 Mimi, Mwenyezi Mungu, ninalitunza, ninalinywesha maji mfululizo. Ninalichunga usiku na mchana ili mtu yeyote asije akalidhuru.
ISA 27:4 Mimi sijakasirika. Laiti michongoma na miiba ingenikabili! Ningepambana dhidi yake katika vita, ningeichoma moto yote.
ISA 27:5 Au niwaache waje kwangu kwa ajili ya kupata kimbilio, wao na wafanye amani nami, naam, wafanye amani nami.”
ISA 27:6 Katika siku zijazo, Yakobo atatia mizizi, Israeli atatoa chipukizi na kuchanua maua, naye atajaza ulimwengu wote kwa matunda.
ISA 27:7 Je, Mwenyezi Mungu amempiga vile alivyowapiga wale waliompiga? Je, yeye ameuawa vile walivyouawa wale waliomuua yeye?
ISA 27:8 Kwa vita na kwa kumfukuza unapingana naye: kwa mshindo wake mkali anamfukuza, kama siku ile uvumapo upepo wa mashariki.
ISA 27:9 Kwa hili, basi, hatia ya Yakobo itafanyiwa upatanisho, nalo hili litakuwa matunda ya utimilizo wa kuondolewa kwa dhambi yake: Wakati atayafanya mawe yote ya madhabahu kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa vipande vipande, hakuna nguzo za Ashera au madhabahu za kufukizia uvumba zitakazobaki zimesimama.
ISA 27:10 Mji wenye ngome umebaki ukiwa, makazi yaliyotelekezwa, yaliyoachwa kama jangwa. Huko ndama hulisha, huko hujilaza, wanakwanyua matawi yake.
ISA 27:11 Wakati vijiti vyake vimekauka, huvunjwa nao wanawake huja na kuwasha navyo moto. Kwa kuwa hili ni taifa lisilo na ufahamu, kwa hiyo yeye aliyewafanya hana huruma juu yao, Muumba wao hawaoneshi fadhili.
ISA 27:12 Katika siku ile Mwenyezi Mungu atapura kutoka matiririko ya Mto Frati hadi Kijito cha Misri, nanyi ee Waisraeli, mtakusanywa mmoja mmoja.
ISA 27:13 Katika siku ile tarumbeta kubwa italia. Wale waliokuwa wakiangamia katika nchi ya Ashuru, nao wale waliokuwa uhamishoni katika nchi ya Misri watakuja na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.
ISA 28:1 Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu, kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba: kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!
ISA 28:2 Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu. Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo unaoharibu, kama mvua inayonyesha kwa nguvu na mafuriko yanayoshuka, atakiangusha chini kwa nguvu.
ISA 28:3 Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu, kitakanyagwa chini ya nyayo.
ISA 28:4 Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba, litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno: mara mtu aionapo, huichuma na kuila.
ISA 28:5 Katika siku ile, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atakuwa taji la utukufu, taji zuri la maua kwa mabaki ya watu wake.
ISA 28:6 Atakuwa roho ya haki kwa yeye anayeketi kwenye kiti cha hukumu, chanzo cha nguvu kwa wale wazuiao vita langoni.
ISA 28:7 Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo, wanayumbayumba kwa sababu ya kileo: Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo, wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo; wanapepesuka wanapoona maono, wanajikwaa wanapotoa maamuzi.
ISA 28:8 Meza zote zimejawa na matapishi wala hakuna sehemu hata ndogo isiyokuwa na uchafu.
ISA 28:9 “Yeye anajaribu kumfundisha nani? Yeye anamwelezea nani ujumbe wake? Je, ni kwa watoto walioachishwa kunyonya? Je, ni wale ambao ndipo tu wametolewa matitini?
ISA 28:10 Kwa maana ni: Amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; hapa kidogo, kule kidogo.”
ISA 28:11 Sawa kabisa, kwa midomo migeni na kwa lugha ngeni, Mungu atasema na watu hawa,
ISA 28:12 wale ambao aliwaambia, “Hapa ni mahali pa kupumzika, waliochoka na wapumzike,” na, “Hapa ni mahali pa mapumziko,” lakini hawakutaka kusikiliza.
ISA 28:13 Hivyo basi, neno la Mwenyezi Mungu kwao litakuwa: Amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni, hapa kidogo, kule kidogo: ili waende na kuanguka chali, wakijeruhiwa, wakinaswa na kukamatwa.
ISA 28:14 Kwa hiyo sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi watu wenye dharau mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu.
ISA 28:15 Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti, tumefanya mapatano na Kuzimu. Pigo linalofurika litakapopita, haliwezi kutugusa sisi, kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.”
ISA 28:16 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni la thamani kwa ajili ya msingi thabiti. Yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu.
ISA 28:17 Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia na uadilifu kuwa timazi; mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo, nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha.
ISA 28:18 Agano lenu na kifo litabatilishwa, patano lenu na Kuzimu halitasimama. Pigo linalofurika litakapowakumba, litawaangusha chini.
ISA 28:19 Kila mara lijapo litawachukua, asubuhi baada ya asubuhi, wakati wa mchana na wakati wa usiku, litawakumba tangu mwanzo hadi mwisho.” Kuuelewa ujumbe huu utaleta hofu tupu.
ISA 28:20 Kitanda ni kifupi mno kujinyoosha juu yake, nguo ya kujifunikia ni nyembamba mno mtu hawezi kujifunikia.
ISA 28:21 Mwenyezi Mungu atainuka kama alivyofanya kwenye Mlima Perasimu, ataghadhibika kama alivyofanya katika Bonde la Gibeoni: ili kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu, ili kutimiza kazi yake, kazi yake ngeni.
ISA 28:22 Sasa acheni dharau zenu, la sivyo minyororo yenu itakuwa mizito zaidi. Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ameniambia habari za maangamizi yaliyoamriwa dhidi ya nchi yote.
ISA 28:23 Sikilizeni msikie sauti yangu, tegeni masikio na msikie niyasemayo.
ISA 28:24 Mkulima anapolima ili apande, je, hulima siku zote? Je, huendelea kubomoa ardhi na kusawazisha udongo?
ISA 28:25 Baada ya kusawazisha shamba, je, hatapanyi mbegu za bizari na kutawanya jira? Je, hapandi ngano katika sehemu yake, shayiri katika eneo lake, na nafaka nyingine katika shamba lake?
ISA 28:26 Mungu wake humwelekeza na kumfundisha njia iliyo sahihi.
ISA 28:27 Iliki haipurwi kwa nyundo, wala gurudumu la gari halivingirishwi juu ya jira; iliki hupurwa kwa fimbo, na jira kwa ufito.
ISA 28:28 Nafaka lazima isagwe ili kutengeneza mkate, kwa hiyo mtu haendelei kuipura daima. Ingawa huendesha magurudumu ya gari lake la kupuria juu yake, farasi wake hawasagi.
ISA 28:29 Haya yote pia hutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, mwenye mashauri ya ajabu, na anayepita wote kwa hekima.
ISA 29:1 Ole wako, wewe Arieli, Arieli, mji alimokaa Daudi! Ongezeni mwaka kwa mwaka, na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee.
ISA 29:2 Hata hivyo nitauzingira Arieli kwa jeshi, utalia na kuomboleza, utakuwa kwangu kama mahali pa kuwashia moto madhabahuni.
ISA 29:3 Nitapiga kambi pande zote dhidi yako, nitakuzunguka kwa minara na kujenga ngome yakukuzingira.
ISA 29:4 Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini, utamumunya maneno yako kutoka mavumbini. Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu, utanong’ona maneno yako toka mavumbini.
ISA 29:5 Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini; makundi ya watu wakatili watakuwa kama makapi yanayopeperushwa. Naam, ghafula, mara moja,
ISA 29:6 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu, atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo.
ISA 29:7 Kisha makundi ya mataifa yote yanayopigana dhidi ya Arieli, yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzingira kwa jeshi, watakuwa kama ilivyo ndoto, kama maono wakati wa usiku:
ISA 29:8 kama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula, lakini huamka, bado njaa yake ingalipo, kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji, lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu. Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni.
ISA 29:9 Pigweni na butwaa na mshangae; jifanyeni vipofu wenyewe na msione; leweni, lakini si kwa mvinyo, pepesukeni lakini si kwa kileo.
ISA 29:10 Mwenyezi Mungu amewaleteeni usingizi mzito: Ameziba macho yenu ninyi manabii; amefunika vichwa vyenu ninyi waonaji.
ISA 29:11 Kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa muhuri katika kitabu. Mkimpa mtu yeyote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri.”
ISA 29:12 Au mkimpa mtu yeyote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.”
ISA 29:13 Bwana asema: “Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao na kuniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Ibada yao kwangu inatokana na maagizo waliyofundishwa na wanadamu.
ISA 29:14 Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa, kwa ajabu juu ya ajabu. Hekima ya wenye hekima itapotea, nayo akili ya wenye akili itatoweka.”
ISA 29:15 Ole kwa wale wanaoenda kwenye vilindi virefu kumficha Mwenyezi Mungu mipango yao, wafanyao kazi zao gizani na kufikiri, “Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?”
ISA 29:16 Mnapindua mambo juu chini, kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi! Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga, “Wewe hukunifinyanga mimi”? Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi, “Wewe hujui chochote”?
ISA 29:17 Kwa muda mfupi sana, je, Lebanoni haitageuzwa kuwa shamba lenye rutuba, na shamba lenye rutuba liwe kama msitu?
ISA 29:18 Katika siku ile viziwi watasikia maneno ya kitabu, na katika utusitusi na giza macho ya kipofu yataona.
ISA 29:19 Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika Mwenyezi Mungu, wahitaji watafurahi ndani yake Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 29:20 Wakatili watatoweka na wenye kudhihaki watatokomea, nao wote wenye jicho la uovu watakatiliwa mbali,
ISA 29:21 wale ambao kwa neno humfanya mtu kuwa mwenye hatia, wamtegeao mtego mtetezi katika mahakama, na kwa ushuhuda wa uongo humnyima haki yeye asiye na hatia.
ISA 29:22 Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, aliyemkomboa Ibrahimu, analosema kwa nyumba ya Yakobo: “Yakobo hataaibishwa tena, wala nyuso zao hazitabadilika sura tena.
ISA 29:23 Watakapoona watoto wao miongoni mwao, kazi ya mikono yangu, watalitakasa Jina langu takatifu; wataukubali utakatifu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli.
ISA 29:24 Wale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu, nao wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.”
ISA 30:1 Mwenyezi Mungu asema, “Ole kwa watoto wakaidi, kwa wale wanaotimiza mipango ambayo si yangu, wakifanya makubaliano, lakini si kwa Roho wangu Mtakatifu, wakilundika dhambi juu ya dhambi,
ISA 30:2 wale wanaoshuka kwenda Misri bila kutaka ushauri wangu, wanaotafuta msaada wa ulinzi wa Farao, wanaotafuta kivuli cha Misri kiwe kimbilio.
ISA 30:3 Lakini ulinzi wa Farao utakuwa kwa aibu yenu, kivuli cha Misri kitawaletea fedheha.
ISA 30:4 Ingawa wana maafisa katika Soani na wajumbe wamewasili katika Hanesi,
ISA 30:5 kila mmoja ataaibishwa kwa sababu ya taifa lisilowafaa kitu, ambalo haliwaletei msaada wala faida, bali aibu tu na fedheha.”
ISA 30:6 Neno la unabii kuhusu wanyama wa Negebu: Katika nchi ya taabu na shida, ya simba za dume na jike, ya nyoka mwenye sumu kali na nyoka warukao, wajumbe huchukua utajiri wao juu ya migongo ya punda, hazina zao juu ya nundu za ngamia, kwa lile taifa lisilokuwa na faida,
ISA 30:7 kuvipeleka Misri, ambaye msaada wake haufai kabisa. Kwa hiyo nimemwita “Rahabu Asiyefanya Chochote.”
ISA 30:8 Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo.
ISA 30:9 Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
ISA 30:10 Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo.
ISA 30:11 Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!”
ISA 30:12 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu,
ISA 30:13 dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, mara moja.
ISA 30:14 Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo ukipasuka pasipo huruma ambapo katika vipande vyake hakuna kipande kitakachopatikana kwa kuukulia makaa kutoka jikoni au kuchotea maji kisimani.”
ISA 30:15 Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo: “Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu, katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu, lakini hamkutaka.
ISA 30:16 Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’ Kwa hiyo mtakimbia! Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi wanaoenda kasi.’ Kwa hiyo wanaowafukuza wataenda kasi!
ISA 30:17 Watu elfu moja watakimbia kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja, kwa vitishio vya watu watano wote mtakimbia, hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera juu ya kilele cha mlima, kama bendera juu ya kilima.”
ISA 30:18 Hata hivyo Mwenyezi Mungu anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonesha huruma. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!
ISA 30:19 Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu.
ISA 30:20 Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona.
ISA 30:21 Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.”
ISA 30:22 Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!”
ISA 30:23 Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ng’ombe wenu watalisha katika shamba pana la majani.
ISA 30:24 Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto.
ISA 30:25 Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana.
ISA 30:26 Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utang’aa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati Mwenyezi Mungu atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia.
ISA 30:27 Tazama, Jina la Mwenyezi Mungu linakuja kutoka mbali, likiwa na hasira kali inayowaka pamoja na wingu zito la moshi, midomo yake imejaa ghadhabu na ulimi wake ni moto ulao.
ISA 30:28 Pumzi yake ni kama mkondo wa maji yaendayo kasi, yakipanda hadi shingoni. Hutikisa mataifa katika chujio ya uharibifu, huweka lijamu katika mataya ya mataifa ambayo huwaongoza upotevuni.
ISA 30:29 Nanyi mtaimba kama usiku ule mnaadhimisha sikukuu takatifu. Mioyo yenu itashangilia kama vile watu wanapokwea na filimbi kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu, kwa Mwamba wa Israeli.
ISA 30:30 Mwenyezi Mungu atawasababisha watu waisikie sauti yake ya utukufu, naye atawafanya wauone mkono wake ukishuka pamoja na hasira yake kali na moto ulao, kukiwa na tufani ya mvua, ngurumo za radi na mvua ya mawe.
ISA 30:31 Sauti ya Mwenyezi Mungu itaivunjavunja Ashuru, kwa fimbo yake ya utawala atawapiga.
ISA 30:32 Kila pigo Mwenyezi Mungu atakaloliweka juu yao kwa fimbo yake ya kuadhibu, litakuwa kwa wimbo wa matari na vinubi, anapopigana nao katika vita kwa mapigo ya mkono wake.
ISA 30:33 Tofethi pameandaliwa toka zamani, pamewekwa tayari kwa ajili ya mfalme. Shimo lake la moto limetengenezwa kwa kina kirefu na kwa upana mkubwa, likiwa na moto na kuni tele; pumzi ya Mwenyezi Mungu, kama kijito cha kiberiti, huuwasha moto.
ISA 31:1 Ole wao wale wanaoshuka Misri kutafuta msaada, wale wanaotegemea farasi, wanaoweka tumaini katika wingi wa magari yao ya vita, na katika nguvu nyingi za wapanda farasi, lakini hawamwangalii yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, wala hawatafuti msaada kwa Mwenyezi Mungu.
ISA 31:2 Hata hivyo yeye pia ana hekima na anaweza kuleta maafa, wala hayatangui maneno yake. Yeye atainuka dhidi ya nyumba ya mwovu, dhidi ya wale ambao huwasaidia watenda maovu.
ISA 31:3 Lakini Wamisri ni wanadamu, wala si Mungu, farasi wao ni nyama, wala si roho. Mwenyezi Mungu atakaponyoosha Mkono wake, yeye anayesaidia atajikwaa, naye anayesaidiwa ataanguka, wote wawili wataangamia pamoja.
ISA 31:4 Hili ndilo Mwenyezi Mungu analoniambia: “Kama vile simba angurumavyo, simba mkubwa juu ya mawindo yake: hata ingawa kundi lote la wafugaji huitwa pamoja dhidi yake, hatiwi hofu na kelele zao, wala kusumbuliwa na ghasia zao; ndivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atakavyoshuka kufanya vita juu ya Mlima Sayuni na juu ya vilele vyake.
ISA 31:5 Kama ndege warukao, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ataukinga Yerusalemu; ataukinga na kuuokoa, atapita juu yake na kuufanya salama.”
ISA 31:6 Mrudieni yeye ambaye nyumba ya Israeli imemwasi sana.
ISA 31:7 Kwa kuwa katika siku ile kila mmoja wenu atazikataa sanamu za fedha na za dhahabu zilizotengenezwa kwa mikono yenu yenye dhambi.
ISA 31:8 “Ashuru itaanguka kwa upanga ambao si wa mwanadamu; upanga usio wa kibinadamu utawaangamiza. Watakimbia mbele ya upanga na vijana wao wa kiume watafanyizwa kazi kwa lazima.
ISA 31:9 Ngome zao zitaanguka kwa sababu ya hofu; kwa kuona bendera ya vita, majemadari wao watashikwa na hofu ya ghafula,” asema Mwenyezi Mungu, ambaye moto wake uko Sayuni, nalo tanuru lake liko Yerusalemu.
ISA 32:1 Tazama, mfalme atatawala kwa uadilifu na watawala watatawala kwa haki.
ISA 32:2 Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo na kimbilio kutokana na dhoruba, kama vijito vya maji jangwani na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu.
ISA 32:3 Ndipo macho ya wale wanaoona hayatafumbwa tena, nayo masikio ya wale wanaosikia yatasikiliza.
ISA 32:4 Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa, nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha.
ISA 32:5 Mpumbavu hataitwa tena muungwana, wala mtu mbaya kabisa kupewa heshima ya juu.
ISA 32:6 Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu, moyo wake hushughulika na uovu: Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu, na hueneza habari za makosa kuhusu Mwenyezi Mungu; yeye huwaacha wenye njaa bila kitu, na wenye kiu huwanyima maji.
ISA 32:7 Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu, hufanya mipango miovu ili kumwangamiza maskini kwa uongo, hata wakati hoja za mhitaji ni za haki.
ISA 32:8 Lakini mtu muungwana hufanya mipango ya kiungwana, na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa.
ISA 32:9 Enyi wanawake wenye kuridhika sana, amkeni na mnisikilize. Enyi binti mnaojisikia kuwa salama, sikieni lile ninalotaka kuwaambia!
ISA 32:10 Muda zaidi kidogo ya mwaka mmoja, ninyi mnaojisikia salama mtatetemeka, mavuno ya zabibu yatakoma, na mavuno ya matunda hayatakuwepo.
ISA 32:11 Tetemekeni, enyi wanawake wenye kuridhika, tetemekeni kwa hofu, enyi binti mnaojisikia salama! Vueni nguo zenu, vaeni magunia viunoni mwenu.
ISA 32:12 Pigeni vifua vyenu, mlilie mashamba yenu mazuri, kwa ajili ya mizabibu iliyozaa vizuri
ISA 32:13 na kwa ajili ya nchi ya watu wangu, nchi ambayo miiba na michongoma imemea: naam, ombolezeni kwa ajili ya nyumba zote za furaha na kwa ajili ya mji huu wenye kufanya sherehe.
ISA 32:14 Ngome itaachwa, mji wenye kelele nyingi utahamwa, ngome ndani ya mji na mnara wa ulinzi vitakuwa ukiwa milele, mahali pazuri pa punda-mwitu na malisho ya makundi ya kondoo,
ISA 32:15 hadi Roho wa Mungu amwagwe juu yetu kutoka juu, nalo jangwa kuwa shamba lenye rutuba, na shamba lenye rutuba kuwa kama msitu.
ISA 32:16 Haki itakaa katika jangwa, na uadilifu utakaa katika shamba lenye rutuba.
ISA 32:17 Matunda ya haki yatakuwa amani, matokeo ya haki yatakuwa utulivu na matumaini milele.
ISA 32:18 Watu wangu wataishi katika makao ya mahali pa amani, katika nyumba zilizo salama, katika mahali pa kupumzika pasipo na usumbufu.
ISA 32:19 Hata mvua ya mawe iangushe msitu na mji ubomolewe kabisa,
ISA 32:20 tazama jinsi utakavyobarikiwa, ukipanda mbegu yako katika kila kijito, na kuwaacha ng’ombe wako na punda wajilishe kwa uhuru.
ISA 33:1 Ole wako wewe, ee mharibu, wewe ambaye hukuharibiwa! Ole wako, ee msaliti, wewe ambaye hukusalitiwa! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa; utakapokwisha kusaliti, utasalitiwa.
ISA 33:2 Ee Mwenyezi Mungu, uturehemu, tunakutamani. Uwe nguvu yetu kila asubuhi na wokovu wetu wakati wa taabu.
ISA 33:3 Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia; unapoinuka, mataifa hutawanyika.
ISA 33:4 Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa kama wafanyavyo madumadu, watu huvamia juu yake kama kundi la nzige.
ISA 33:5 Mwenyezi Mungu ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka, ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu.
ISA 33:6 Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu, hazina ya wokovu tele, hekima na maarifa; kumcha Mwenyezi Mungu ni ufunguo wa hazina hii.
ISA 33:7 Angalia, mashujaa wake wanapiga kelele barabarani, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.
ISA 33:8 Njia kuu zimeachwa, hakuna wasafiri barabarani. Mkataba umevunjika, mashahidi wake wamedharauliwa, hakuna anayeheshimiwa.
ISA 33:9 Ardhi inaomboleza na kuchakaa, Lebanoni imeaibika na kunyauka; Sharoni ni kama Araba, nayo Bashani na Karmeli wanapukutisha majani yao.
ISA 33:10 “Sasa nitainuka,” asema Mwenyezi Mungu. “Sasa nitatukuzwa; sasa nitainuliwa juu.
ISA 33:11 Mlichukua mimba ya makapi, mkazaa mabua; pumzi yenu ni moto unaowateketeza.
ISA 33:12 Mataifa watachomwa wawe majivu; kama vichaka vya miiba vilivyokatwa ndivyo watakavyochomwa.”
ISA 33:13 Ninyi mlio mbali sana, sikieni lile nililofanya; ninyi mlio karibu, tambueni uweza wangu!
ISA 33:14 Wenye dhambi katika Sayuni wametiwa hofu, kutetemeka kumewakumba wasiomcha Mungu: “Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto ulao? Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto unaowaka milele?”
ISA 33:15 Yeye aendaye kwa uadilifu na kusema lililo haki, yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma na kuizuia mikono yake isipokee rushwa, yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji, na yeye afumbaye macho yake yasitazame uovu:
ISA 33:16 huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu, ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani. Atapewa mkate wake, na maji yake hayatakoma.
ISA 33:17 Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake na kuiona nchi inayoenea mbali.
ISA 33:18 Katika mawazo yenu mtaifikiria hofu iliyopita: “Yuko wapi yule afisa mkuu? Yuko wapi yule aliyechukua ushuru? Yuko wapi afisa msimamizi wa minara?”
ISA 33:19 Hutawaona tena wale watu wenye kiburi, wale watu wenye usemi wa mafumbo, wenye lugha ngeni, isiyoeleweka.
ISA 33:20 Mtazame Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yenu yatauona Yerusalemu, mahali pa amani pa kuishi, hema ambalo halitaondolewa, nguzo zake hazitang’olewa kamwe, wala hakuna kamba yake yoyote itakayokatika.
ISA 33:21 Huko Mwenyezi Mungu atakuwa Mwenye Nguvu wetu. Patakuwa kama mahali pa mito mipana na vijito. Hakuna jahazi lenye makasia litakalopita huko, wala hakuna meli yenye nguvu itakayopita huko.
ISA 33:22 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwamuzi wetu, Mwenyezi Mungu ndiye mtoa sheria wetu, Mwenyezi Mungu ni mfalme wetu, yeye ndiye atakayetuokoa.
ISA 33:23 Kamba zenu za merikebu zimelegea: Mlingoti haukusimama imara, nalo tanga halikukunjuliwa. Wingi wa mateka yatagawanywa, hata yeye aliye mlemavu atachukua nyara.
ISA 33:24 Hakuna yeyote aishiye Sayuni atakayesema, “Mimi ni mgonjwa”; nazo dhambi za wale wanaoishi humo zitasamehewa.
ISA 34:1 Njooni karibu, enyi mataifa, nanyi msikilize; sikilizeni kwa makini, enyi makabila ya watu! Dunia na isikie, navyo vyote vilivyo ndani yake, ulimwengu na vyote vinavyotoka ndani yake!
ISA 34:2 Mwenyezi Mungu ameyakasirikia mataifa yote; ghadhabu yake ni juu ya majeshi yao yote. Atawaangamiza kabisa, atawatia mikononi mwa wachinjaji.
ISA 34:3 Waliouawa watatupwa nje, maiti zao zitatoa uvundo, milima itatota kwa damu zao.
ISA 34:4 Nyota zote za mbinguni zitayeyuka na mbingu itakunjwa kama kitabu, jeshi lote la angani litaanguka kama majani yaliyonyauka kwenye mzabibu, kama tini iliyonyauka kwenye mtini.
ISA 34:5 Upanga wangu umekunywa na kushiba huko mbinguni, tazama, unashuka katika hukumu juu ya Edomu, wale watu ambao nimeshawahukumu, kuwaangamiza kabisa.
ISA 34:6 Upanga wa Mwenyezi Mungu umeoga katika damu, umefunikwa na mafuta ya nyama: damu ya kondoo na mbuzi, mafuta kutoka figo za kondoo dume. Kwa maana Mwenyezi Mungu ana dhabihu huko Bosra, na machinjo makuu huko Edomu.
ISA 34:7 Nyati wataanguka pamoja nao, ndama dume na mafahali wakubwa. Nchi yao italowana kwa damu, nayo mavumbi yataloa mafuta ya nyama.
ISA 34:8 Kwa sababu Mwenyezi Mungu anayo siku ya kulipiza kisasi, mwaka wa malipo, siku ya kushindania shauri la Sayuni.
ISA 34:9 Vijito vya Edomu vitageuka kuwa lami, mavumbi yake yatakuwa kiberiti kiunguzacho, nchi yake itakuwa lami iwakayo!
ISA 34:10 Haitazimishwa usiku wala mchana, moshi wake utapaa juu milele. Kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa; hakuna mtu yeyote atakayepita huko tena.
ISA 34:11 Bundi wa jangwani na bundi mwenye sauti nyembamba wataimiliki, bundi wakubwa na kunguru wataweka viota humo. Mungu atanyoosha juu ya Edomu kamba ya kupimia ya machafuko matupu, na timazi ya ukiwa.
ISA 34:12 Watu wake wa kuheshimiwa hawatakuwa na chochote kitakachoitwa ufalme huko, nao wakuu wao wote watatoweka.
ISA 34:13 Miiba itaenea katika ngome za ndani, viwawi na michongoma itaota kwenye ngome zake. Itakuwa maskani ya mbweha, makao ya bundi.
ISA 34:14 Viumbe vya jangwani vitakutana na fisi, nao mbuzi-mwitu watalia wakiitana; huko viumbe vya usiku vitastarehe pia na kujitafutia mahali pa kupumzika.
ISA 34:15 Bundi wataweka viota huko na kutaga mayai, atayaangua na kutunza makinda yake chini ya uvuli wa mabawa yake; pia huko vipanga watakusanyika, kila mmoja na mwenzi wake.
ISA 34:16 Angalieni katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na msome: Hakuna hata mmoja katika hawa atakayekosekana, hakuna hata mmoja atakayemkosa mwenzi wake. Kwa kuwa ni kinywa chake Mungu kimeagiza, na Roho wake Mtakatifu atawakusanya.
ISA 34:17 Huwagawia sehemu zao, mkono wake huwagawanyia kwa kipimo. Wataimiliki hata milele na kuishi humo kizazi hadi kizazi.
ISA 35:1 Jangwa na nchi kame vitafurahi; nyika itashangilia na kuchanua maua. Kama waridi,
ISA 35:2 litachanua maua, litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha. Litapewa utukufu wa Lebanoni, fahari ya Karmeli na Sharoni; wataona utukufu wa Mwenyezi Mungu, fahari ya Mungu wetu.
ISA 35:3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea,
ISA 35:4 waambieni wale wenye mioyo ya hofu, “Kuweni hodari, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja kulipa kisasi, pamoja na ujira wake, atakuja na kuwaokoa.”
ISA 35:5 Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa.
ISA 35:6 Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu, nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe. Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika, na vijito katika jangwa.
ISA 35:7 Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji, ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi. Maskani ya mbweha walikolala hapo awali patamea nyasi, matete na mafunjo.
ISA 35:8 Nako kutakuwa na njia kuu, nayo itaitwa Njia ya Utakatifu. Wasio safi hawatapita juu yake; itakuwa ya wale wanaotembea katika Njia Ile; yeye asafiriye juu yake, ajapokuwa mjinga, hatapotea.
ISA 35:9 Huko hakutakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapita njia hiyo; hawatapatikana humo. Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko,
ISA 35:10 waliokombolewa na Mwenyezi Mungu watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao. Watapata furaha na shangwe; huzuni na majonzi vitakimbia.
ISA 36:1 Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka.
ISA 36:2 Kisha mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wa jeshi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Jemadari wa jeshi akasimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi.
ISA 36:3 Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakamwendea.
ISA 36:4 Jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia, “ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako?
ISA 36:5 Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi?
ISA 36:6 Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea.
ISA 36:7 Nawe ukiniambia, “Tunamtumainia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu”: Je, si yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya”?
ISA 36:8 “ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao!
ISA 36:9 Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi?
ISA 36:10 Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza nchi hii bila Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”
ISA 36:11 Ndipo Eliakimu, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walio juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”
ISA 36:12 Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mkojo wao wenyewe?”
ISA 36:13 Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru!
ISA 36:14 Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa!
ISA 36:15 Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Mwenyezi Mungu kwa kuwaambia, ‘Hakika Mwenyezi Mungu atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’
ISA 36:16 “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe,
ISA 36:17 hadi nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na ya mashamba ya mizabibu.
ISA 36:18 “Msikubali Hezekia awapotoshe asemapo, ‘Mwenyezi Mungu atatuokoa.’ Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru?
ISA 36:19 Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu?
ISA 36:20 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mwenyezi Mungu aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”
ISA 36:21 Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”
ISA 36:22 Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia vile jemadari wa jeshi alivyosema.
ISA 37:1 Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa gunia, na akaenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
ISA 37:2 Akawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi.
ISA 37:3 Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa.
ISA 37:4 Yamkini Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.”
ISA 37:5 Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya,
ISA 37:6 Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo.
ISA 37:7 Sikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake ili atakaposikia taarifa fulani, atarudi nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’ ”
ISA 37:8 Jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.
ISA 37:9 Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Aliposikia jambo hili akatuma wajumbe kwa Hezekia na neno hili:
ISA 37:10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’
ISA 37:11 Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa?
ISA 37:12 Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa? Yaani miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari?
ISA 37:13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”
ISA 37:14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, akaikunjua mbele za Mwenyezi Mungu.
ISA 37:15 Naye Hezekia akamwomba Mwenyezi Mungu akisema:
ISA 37:16 “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, unayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi.
ISA 37:17 Tega sikio, Ee Mwenyezi Mungu, usikie; fungua macho yako, Ee Mwenyezi Mungu, uone; sikiliza maneno yote ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.
ISA 37:18 “Ni kweli, Ee Mwenyezi Mungu, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya yote pamoja na nchi zao.
ISA 37:19 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
ISA 37:20 Sasa basi, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe Mungu pekee.”
ISA 37:21 Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Kwa sababu umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru,
ISA 37:22 hili ndilo neno ambalo Mwenyezi Mungu amelisema dhidi yake: “Bikira Binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki. Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.
ISA 37:23 Ni nani uliyemtukana na kumkufuru? Ni nani uliyepaza sauti yako dhidi yake, na kumwinulia macho yako kwa kiburi? Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!
ISA 37:24 Kupitia kwa wajumbe wako umelundika matukano juu ya Bwana. Nawe umesema, ‘Kwa magari yangu mengi ya vita, nimepanda juu ya vilele vya milima, vilele vya juu sana katika Lebanoni. Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu, misunobari yake iliyo bora sana. Nimefikia sehemu zake zilizoinuka juu sana, misitu yake iliyo mizuri sana.
ISA 37:25 Nimechimba visima katika nchi za kigeni na kunywa maji yake. Kwa nyayo za miguu yangu nimekausha vijito vyote vya Misri.’
ISA 37:26 “Je, hujasikia? Zamani sana niliamuru hili. Siku za kale nilipanga hili; sasa nimelifanya litokee, kwamba umegeuza miji yenye ngome kuwa malundo ya mawe.
ISA 37:27 Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu, wanavunjika mioyo na kuaibishwa. Wao ni kama mimea katika shamba, kama machipukizi mororo ya kijani, kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba, ambayo hukauka kabla ya kukua.
ISA 37:28 “Lakini ninajua mahali ukaapo, kutoka kwako na kuingia kwako, na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
ISA 37:29 Kwa sababu unaghadhibika na ufidhuli dhidi yangu, na kwa sababu ufidhuli wako umefika masikioni mwangu, nitaweka ndoana yangu puani mwako na hatamu yangu kinywani mwako, nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.
ISA 37:30 “Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kinachoota chenyewe, na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake. Lakini katika mwaka wa tatu panda na uvune, panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.
ISA 37:31 Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.
ISA 37:32 Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki, na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika. Wivu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ndio utatimiza jambo hili.
ISA 37:33 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu wala hatapiga mshale hapa. Hatakuja mbele yake na ngao wala kupanga majeshi kuuzingira.
ISA 37:34 Kwa njia ile aliyoijia ndiyo atakayorudi; hataingia katika mji huu,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 37:35 “Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu!”
ISA 37:36 Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akaenda, akawaua wanajeshi elfu mia moja na themanini na tano katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali!
ISA 37:37 Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.
ISA 37:38 Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
ISA 38:1 Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”
ISA 38:2 Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Mwenyezi Mungu:
ISA 38:3 “Ee Mwenyezi Mungu, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.
ISA 38:4 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Isaya, kusema:
ISA 38:5 “Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako. Nitakuongezea miaka kumi na tano katika maisha yako.
ISA 38:6 Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu.
ISA 38:7 “ ‘Hii ndiyo ishara ya Mwenyezi Mungu kwako kwamba Mwenyezi Mungu atafanya kile alichoahidi:
ISA 38:8 Nitafanya kivuli cha jua kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi kirudi nyuma madaraja kumi.’ ” Hivyo jua likarudi nyuma madaraja kumi ambayo lilikuwa limeshuka.
ISA 38:9 Maandiko ya Hezekia mfalme wa Yuda baada ya kuugua kwake na kupona:
ISA 38:10 Nilisema, “Katika ustawi wa maisha yangu, je, ni lazima nipite katika malango ya mauti, na kupokonywa miaka yangu iliyobaki?”
ISA 38:11 Nilisema, “Sitamwona tena Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu katika nchi ya walio hai, wala sitamtazama tena mwanadamu, wala kuwa na wale ambao sasa wanakaa katika ulimwengu huu.
ISA 38:12 Kama hema la mchunga mifugo, nyumba yangu imebomolewa na kutwaliwa kutoka kwangu. Kama mfumaji nimevingirisha maisha yangu, naye amenikatilia mbali kutoka kitanda cha mfumi. Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
ISA 38:13 Nilingoja kwa uvumilivu hadi mapambazuko, lakini alivunja mifupa yangu yote kama simba. Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
ISA 38:14 Nililia kama mbayuwayu au korongo, niliomboleza kama hua aombolezaye. Macho yangu yalififia nilipotazama mbinguni. Ee Bwana, ninataabika, njoo unisaidie!”
ISA 38:15 Lakini niseme nini? Amesema nami, naye yeye mwenyewe amelitenda hili. Nitatembea kwa unyenyekevu katika miaka yangu yote kwa sababu ya haya maumivu makali ya nafsi yangu.
ISA 38:16 Bwana, kwa mambo kama haya watu huishi, nayo roho yangu hupata uzima katika hayo pia. Uliniponya na kuniacha niishi.
ISA 38:17 Hakika ilikuwa ya faida yangu ndiyo maana nikapata maumivu makali. Katika upendo wako ukaniokoa kutoka shimo la uharibifu; umeziweka dhambi zangu zote nyuma yako.
ISA 38:18 Kwa maana kaburi haliwezi kukusifu, mauti haiwezi kuimba sifa zako; wale wanaoshuka shimoni hawawezi kuutarajia uaminifu wako.
ISA 38:19 Walio hai, walio hai: hao wanakusifu, kama ninavyofanya leo. Baba huwaambia watoto wao habari za uaminifu wako.
ISA 38:20 Mwenyezi Mungu ataniokoa, nasi tutaimba kwa vyombo vya nyuzi siku zote za maisha yetu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
ISA 38:21 Isaya alikuwa amesema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini, mweke juu ya jipu, naye atapona.”
ISA 38:22 Hezekia alikuwa ameuliza, “Kutakuwa na ishara gani kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Mwenyezi Mungu?”
ISA 39:1 Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua na kupona kwake.
ISA 39:2 Hezekia akawapokea wale wajumbe kwa furaha na kuwaonesha vitu vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha lote, na kila kitu kilichokuwa katika hazina yake. Hapakuwa na kitu katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonesha.
ISA 39:3 Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?” Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kwangu kutoka Babeli.”
ISA 39:4 Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?” Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu. Hakuna kitu katika hazina yangu ambacho sikuwaonesha.”
ISA 39:5 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
ISA 39:6 Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba hadi siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Mwenyezi Mungu.
ISA 39:7 Nao baadhi ya wazao wako, mwili wako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
ISA 39:8 Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Mwenyezi Mungu ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Kutakuwa amani na usalama wakati wa uhai wangu.”
ISA 40:1 Wafarijini, wafarijini watu wangu, asema Mungu wenu.
ISA 40:2 Sema na Yerusalemu kwa upole, umtangazie kwamba kazi yake ngumu imekamilika, kwamba dhambi yake imelipiwa fidia, kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Mwenyezi Mungu maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.
ISA 40:3 Sauti ya mtu aliaye nyikani: “Itengenezeni njia ya Mwenyezi Mungu jangwani, yanyoosheni mapito nyikani kwa ajili ya Mungu wetu.
ISA 40:4 Kila bonde litainuliwa, kila mlima na kilima kitashushwa; penye mabonde patanyooshwa, napo palipoparuza patasawazishwa.
ISA 40:5 Utukufu wa Mwenyezi Mungu utafunuliwa, nao wanadamu wote watauona pamoja. Kwa maana kinywa cha Mwenyezi Mungu kimenena.”
ISA 40:6 Sauti husema, “Piga kelele.” Nami nikasema, “Nipige kelele gani?” “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao wote ni kama maua ya kondeni.
ISA 40:7 Majani hunyauka na maua huanguka, kwa sababu pumzi ya Mwenyezi Mungu huyapuliza. Hakika wanadamu ni majani.
ISA 40:8 Majani hunyauka na maua huanguka, lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
ISA 40:9 Wewe uletaye habari njema Sayuni, panda juu ya mlima mrefu. Wewe uletaye habari njema Yerusalemu, paza sauti yako, piga kelele kwa nguvu, paza sauti, usiogope; iambie miji ya Yuda, “Yuko hapa Mungu wenu!”
ISA 40:10 Tazameni, Bwana Mungu Mwenyezi anakuja na nguvu, nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake. Tazameni, ujira wake u pamoja naye, nayo malipo yake yanafuatana naye.
ISA 40:11 Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo: Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake na kuwachukua karibu na moyo wake, huwaongoza taratibu wale wanaonyonyesha.
ISA 40:12 Ni nani aliyepima maji ya bahari kwenye konzi ya mkono wake, au kuzipima mbingu kwa shibiri yake? Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu, au kupima milima kwenye kipimio na vilima kwenye mizani?
ISA 40:13 Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Mwenyezi Mungu, au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?
ISA 40:14 Ni nani ambaye Mwenyezi Mungu ametaka shauri kwake ili kumwelimisha, naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa? Ni nani aliyemfundisha maarifa au kumwonesha mapito ya ufahamu?
ISA 40:15 Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo, ni kama vumbi jembamba juu ya mizani, huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini.
ISA 40:16 Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa.
ISA 40:17 Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu, yanaonekana yasio na thamani na zaidi ya bure kabisa.
ISA 40:18 Basi, utamlinganisha Mungu na nani? Utamlinganisha na kitu gani?
ISA 40:19 Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu, naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu na kuitengenezea mikufu ya fedha.
ISA 40:20 Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii huuchagua mti usiooza. Humtafuta fundi stadi wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika.
ISA 40:21 Je, hujui? Je, hujasikia? Je, hujaambiwa tangu mwanzo? Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia?
ISA 40:22 Anakaa kwenye kiti cha utawala juu ya duara ya dunia, nao watu wanaoishi humo ni kama panzi. Huzitandaza mbingu kama chandarua, na kuzitandaza kama hema la kuishi.
ISA 40:23 Huwafanya wakuu kuwa si kitu, na kuwashusha watawala wa dunia hii kuwa kitu bure.
ISA 40:24 Mara baada ya kupandwa, mara baada ya kutiwa ardhini, mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini, ndipo huwapulizia nao wakanyauka, nao upepo wa kisulisuli huwapeperusha kama makapi.
ISA 40:25 “Utanilinganisha mimi na nani? Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu.
ISA 40:26 Inueni macho yenu mtazame mbinguni: Ni nani aliyeumba hivi vyote? Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine na kuziita kila moja kwa jina lake. Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu, hakuna hata mojawapo inayokosekana.
ISA 40:27 Kwa nini unasema, ee Yakobo, nanyi ee Israeli, kulalamika, “Njia yangu imefichwa Mwenyezi Mungu asiione, Mungu wangu hajali shauri langu?”
ISA 40:28 Je wewe, hufahamu? Je wewe, hujasikia? Mwenyezi Mungu ni Mungu wa milele, Muumba wa miisho ya dunia. Hatachoka wala kulegea, wala hakuna hata mmoja awezaye kuupima ufahamu wake.
ISA 40:29 Huwapa nguvu waliolegea na huongeza nguvu za wadhaifu.
ISA 40:30 Hata vijana huchoka na kulegea, nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,
ISA 40:31 bali wale wamtumainio Mwenyezi Mungu atafanya upya nguvu zao. Watapaa juu kwa mabawa kama tai; watapiga mbio wala hawatachoka, watatembea kwa miguu wala hawatazimia.
ISA 41:1 “Nyamazeni kimya mbele zangu, enyi visiwa! Mataifa na wafanye upya nguvu zao! Wao na wajitokeze, kisha waseme, tukutane pamoja mahali pa hukumu.
ISA 41:2 “Ni nani aliyemchochea mmoja kutoka mashariki, akimwita katika haki kwa utumishi wake? Huyatia mataifa mkononi mwake, na kuwatiisha wafalme mbele zake. Huwafanya kuwa mavumbi kwa upanga wake, huwafanya makapi yapeperushwayo na upepo kwa upinde wake.
ISA 41:3 Huwafuatia na kuendelea salama, katika njia ambayo miguu yake haijawahi kupita.
ISA 41:4 Ni nani aliyefanya jambo hili na kulitimiliza, akiita vizazi tangu mwanzo? Mimi, Mwenyezi Mungu, ni wa kwanza, nami nitakuwa pamoja na wa mwisho: Mimi ndiye.”
ISA 41:5 Visiwa vimeliona na kuogopa, miisho ya dunia inatetemeka. Wanakaribia na kuja mbele,
ISA 41:6 kila mmoja humsaidia mwingine na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!”
ISA 41:7 Fundi humtia moyo sonara, yeye alainishaye kwa nyundo humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe. Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.” Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike.
ISA 41:8 “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu, Yakobo, niliyemchagua, ninyi wazao wa Ibrahimu rafiki yangu,
ISA 41:9 nilikuchukua toka miisho ya dunia, nilikuita kutoka pembe zake za mbali. Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’; nimekuchagua, wala sikukukataa.
ISA 41:10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu na kukusaidia; nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
ISA 41:11 “Wote walioona hasira dhidi yako hakika wataaibika na kutahayarika, wale wakupingao watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.
ISA 41:12 Ingawa utawatafuta adui zako, hutawaona. Wale wanaopigana vita dhidi yako watakuwa kama vile si kitu kabisa.
ISA 41:13 Kwa maana Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, nikushikaye mkono wako wa kuume na kukuambia, Usiwe na hofu, nitakusaidia.
ISA 41:14 Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu, ee Israeli uliye mdogo, kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Mwenyezi Mungu, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 41:15 “Tazama, nitakufanya chombo cha kupuria, kipya na chenye makali, chenye meno mengi. Utaipura milima na kuiponda na kuvifanya vilima kuwa kama makapi.
ISA 41:16 Utaipepeta, nao upepo utaichukua, dhoruba itaipeperushia mbali. Bali wewe utajifurahisha katika Mwenyezi Mungu na katika utukufu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 41:17 “Maskini na wahitaji wanatafuta maji, lakini hayapo, ndimi zao zimekauka kwa kiu. Lakini Mimi Mwenyezi Mungu nitawajibu, Mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.
ISA 41:18 Nitaifanya mito itiririke juu ya vilima vilivyo kame, nazo chemchemi ndani ya mabonde. Nitaligeuza jangwa liwe mabwawa ya maji, nayo ardhi iliyokauka kuwa chemchemi za maji.
ISA 41:19 Katika jangwa nitaotesha mwerezi, mshita, mhadasi na mzeituni. Nitaweka misunobari, mivinje na misanduku pamoja huko nyikani,
ISA 41:20 ili watu wapate kuona na kujua, wapate kufikiri na kuelewa, kwamba mkono wa Mwenyezi Mungu umetenda hili, kwamba yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ndiye alilifanya.”
ISA 41:21 Mwenyezi Mungu asema, “Leta shauri lako. Toa hoja yako,” asema Mfalme wa Yakobo.
ISA 41:22 “Leteni sanamu zenu zituambie ni nini kitakachotokea. Tuambieni mambo ya zamani yalikuwa nini, ili tupate kuyatafakari na kujua matokeo yake ya mwisho. Au tutangazieni mambo yatakayokuja,
ISA 41:23 tuambieni ni nini kitakachotokea baadaye, ili tupate kujua kuwa ninyi ni miungu. Fanyeni jambo lolote zuri au baya, ili tupate kutishika na kujazwa na hofu.
ISA 41:24 Lakini ninyi ni zaidi ya bure kabisa, na kazi zenu hazifai kitu kabisa; yeye awachaguaye ni chukizo sana.
ISA 41:25 “Nimemchochea mtu mmoja kutoka kaskazini, naye yuaja, mmoja toka mawio ya jua aliitaye Jina langu. Huwakanyaga watawala kana kwamba ni matope, kama mfinyanzi akanyagavyo udongo wa kufinyangia.
ISA 41:26 Ni nani aliyenena hili tokea mwanzoni, ili tupate kujua, au kabla, ili tuweze kusema, ‘Alikuwa mwenye haki’? Hakuna aliyenena hili, hakuna aliyetangulia kusema hili, hakuna yeyote aliyesikia maneno kutoka kwenu.
ISA 41:27 Nilikuwa wa kwanza kumwambia Sayuni, ‘Tazama, wako hapa!’ Nilimpa Yerusalemu mjumbe wa habari njema.
ISA 41:28 Ninatazama, lakini hakuna yeyote: hakuna yeyote miongoni mwao awezaye kutoa shauri, hakuna yeyote wa kutoa jibu wakati ninapowauliza.
ISA 41:29 Tazama, wote ni ubatili! Matendo yao ni bure; vinyago vyao ni upepo mtupu na machafuko.
ISA 42:1 “Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza, mteule wangu, ninayependezwa naye; nitaweka Roho yangu juu yake, naye ataleta haki kwa mataifa.
ISA 42:2 Hatapaza sauti wala kupiga kelele, wala hataipaza sauti yake barabarani.
ISA 42:3 Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima. Kwa uaminifu ataleta haki,
ISA 42:4 hatazimia roho wala kukata tamaa, hadi atakaposimamisha haki juu ya dunia. Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”
ISA 42:5 Hili ndilo asemalo Mungu, Mwenyezi Mungu, yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda, aliyeitandaza dunia na vyote vinavyotoka humo, awapaye watu wake pumzi, na uzima kwa wale wanaoenda humo:
ISA 42:6 “Mimi, Mwenyezi Mungu, nimekuita katika haki; nitakushika mkono wako. Nitakulinda na kukufanya kuwa agano kwa ajili ya watu na nuru kwa Mataifa,
ISA 42:7 kuwafungua macho wale wasioona, kuwaacha huru kutoka kifungoni wale waliofungwa, na kuwafungua kutoka gerezani wale wanaokaa gizani.
ISA 42:8 “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu; hilo ndilo Jina langu! Sitampa mwingine utukufu wangu wala sanamu sifa zangu.
ISA 42:9 Tazama, mambo ya kwanza yametokea, nami natangaza mambo mapya; kabla hayajatokea nawatangazia habari zake.”
ISA 42:10 Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya, sifa zake toka miisho ya dunia, ninyi mshukao chini baharini, na vyote vilivyomo, enyi visiwa na wote wanaoishi humo.
ISA 42:11 Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao; makazi anamoishi Kedari na yashangilie. Watu wa Sela waimbe kwa furaha, na wapige kelele kutoka vilele vya milima.
ISA 42:12 Wampe Mwenyezi Mungu utukufu, na kutangaza sifa zake katika visiwa.
ISA 42:13 Mwenyezi Mungu ataenda kama mtu mwenye nguvu, kama shujaa atachochea shauku yake, kwa kishindo ataamsha ukelele wa vita, naye atashinda adui zake.
ISA 42:14 “Kwa muda mrefu nimenyamaza; nimekaa kimya na kujizuia. Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua, ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi.
ISA 42:15 Nitaharibu milima na vilima na kukausha mimea yako yote; nitafanya mito kuwa visiwa na kukausha mabwawa.
ISA 42:16 Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua, kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao, na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini. Haya ndio mambo nitakayofanya; mimi sitawaacha.
ISA 42:17 Lakini wale wanaotumaini sanamu, wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’ watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.
ISA 42:18 “Sikieni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona!
ISA 42:19 Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu, na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma? Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu, aliye kipofu kama mtumishi wa Mwenyezi Mungu?
ISA 42:20 Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia; masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii chochote.”
ISA 42:21 Ilimpendeza Mwenyezi Mungu kwa ajili ya haki yake kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu.
ISA 42:22 Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara, wote wamenaswa katika mashimo, au wamefichwa katika magereza. Wamekuwa nyara, wala hapana yeyote awaokoaye. Wamefanywa mateka, wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.”
ISA 42:23 Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili, au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao?
ISA 42:24 Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka, na Israeli kwa wateka nyara? Je, hakuwa yeye, Mwenyezi Mungu, ambaye tumetenda dhambi dhidi yake? Kwa kuwa hawakufuata njia zake, hawakutii sheria zake.
ISA 42:25 Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka, ukali wa vita. Iliwazunguka kwa miali ya moto, lakini hata hivyo hawakuelewa; iliwateketeza, lakini hawakuyatia moyoni.
ISA 43:1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyekuumba, ee Yakobo, yeye aliyekuhuluku, ee Israeli: “Usiogope kwa maana nimekukomboa, nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.
ISA 43:2 Unapopita kwenye maji makuu, nitakuwa pamoja nawe, unapopita katika mito ya maji, hayatakugharikisha. Utakapopita katika moto, hutaungua, miali ya moto haitakuunguza.
ISA 43:3 Kwa kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako. Ninaitoa Misri kuwa fidia yako, Kushi na Seba badala yako.
ISA 43:4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu, nami kwa kuwa ninakupenda, nitatoa watu badala yako na mataifa badala ya maisha yako.
ISA 43:5 Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe, nitawaleta watoto wako kutoka mashariki, na kukukusanya kutoka magharibi.
ISA 43:6 Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’ nayo kusini, ‘Usiwazuie.’ Walete wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia:
ISA 43:7 kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu, niliyemuumba kwa utukufu wangu, niliyemhuluku na kumfanya.”
ISA 43:8 Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni, wenye masikio lakini hawasikii.
ISA 43:9 Mataifa yote yanakutanika pamoja, na makabila yanakusanyika. Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya, na kututangazia mambo yaliyopita? Walete mashahidi wao ili kuwathibitisha kuwa walikuwa sahihi, ili wengine waweze kusikia, waseme, “Ni kweli.”
ISA 43:10 “Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Mwenyezi Mungu, “na mtumishi wangu niliyemchagua, ili mpate kunijua na kuniamini, na kutambua kwamba Mimi ndiye. Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa, wala hatakuwepo mwingine baada yangu.
ISA 43:11 Mimi, naam mimi, ndimi Mwenyezi Mungu, zaidi yangu hakuna mwokozi.
ISA 43:12 Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza: Mimi mwenyewe, bali si mungu mgeni kati yenu. Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Mwenyezi Mungu, “kwamba Mimi ndimi Mungu.
ISA 43:13 Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye. Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa kutoka mkononi wangu. Mimi ninapotenda, ni nani awezaye kutangua?”
ISA 43:14 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa ajili yenu nitatumana Babeli na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi, katika meli walizozionea fahari.
ISA 43:15 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, yeye Aliye Mtakatifu wako, Muumba wa Israeli, Mfalme wako.”
ISA 43:16 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyefanya njia baharini, mahali pa kupita kwenye maji mengi,
ISA 43:17 aliyeyakokota magari ya vita na farasi, jeshi pamoja na askari wa msaada, nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe, wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi:
ISA 43:18 “Msiyakumbuke mambo yaliyopita, wala msiyatafakari mambo ya zamani.
ISA 43:19 Tazama, nitafanya jambo jipya! Sasa litachipuka, je, hamtalitambua? Nitafanya njia jangwani na vijito vya maji katika nchi kame.
ISA 43:20 Wanyama pori wataniheshimu, mbweha na bundi, kwa sababu ninawapatia maji jangwani, na vijito katika nchi kame, ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua,
ISA 43:21 watu wale niliowaumba kwa ajili yangu, ili wapate kutangaza sifa zangu.
ISA 43:22 “Hata hivyo hukuniita mimi, ee Yakobo, hujajitaabisha kwa ajili yangu, ee Israeli.
ISA 43:23 Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukulemea kwa sadaka za nafaka wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba.
ISA 43:24 Hukuninunulia uvumba wowote wenye manukato, wala hukunipa kwa ukarimu mafuta ya wanyama wa dhabihu zako. Lakini umenilemea kwa dhambi zako, na kunitaabisha kwa makosa yako.
ISA 43:25 “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako, kwa ajili yangu mwenyewe, wala sizikumbuki dhambi zako tena.
ISA 43:26 Tafakari mambo yaliyopita, njoo na tuhojiane, jitetee uweze kupewa haki yako.
ISA 43:27 Baba yako wa kwanza alitenda dhambi, wasemaji wako wameasi dhidi yangu.
ISA 43:28 Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako, nami nitamtoa Yakobo aangamizwe, na Israeli adhihakiwe.
ISA 44:1 “Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu, Israeli, niliyemchagua.
ISA 44:2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni, yeye atakayekusaidia: Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu, Yeshuruni, niliyekuchagua.
ISA 44:3 Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu, na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka; nitamimina Roho wangu Mtakatifu juu ya watoto wako, nayo baraka yangu juu ya wazao wako.
ISA 44:4 Nao watachipua kama nyasi katika shamba la majani, kama mierezi kando ya vijito vya maji yanayotiririka.
ISA 44:5 Mmoja atasema, ‘Mimi ni wa Mwenyezi Mungu’; mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘Wa Mwenyezi Mungu,’ na kujiita kwa jina la Israeli.
ISA 44:6 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Israeli na Mkombozi, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho; zaidi yangu hakuna Mungu.
ISA 44:7 Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze. Yeye atangaze na kuweka mbele yangu ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale, tena ni nini kitakachotokea: naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.
ISA 44:8 Msitetemeke, msiogope. Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani? Ninyi ni mashahidi wangu. Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hasha, hakuna Mwamba mwingine; mimi simjui mwingine.”
ISA 44:9 Wote wachongao sanamu ni ubatili, navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu. Wale ambao wanazitetea ni vipofu, ni wajinga, nao waaibika.
ISA 44:10 Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu, ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?
ISA 44:11 Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa, mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu. Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao, watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.
ISA 44:12 Muhunzi huchukua kifaa na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto, hutengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake. Huona njaa na kupoteza nguvu zake, asipokunywa maji huzimia.
ISA 44:13 Seremala hupima kwa kutumia kamba, na huuchora mstari kwa kalamu; huchonga kwa patasi na kutia alama kwa bikari. Huitengeneza katika umbo la binadamu, umbo la binadamu katika utukufu wake wote, ili iweze kukaa katika mahali pake pa ibada za sanamu.
ISA 44:14 Hukata miti ya mierezi, huchukua mtiriza au mwaloni. Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni, au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.
ISA 44:15 Ni kuni ya binadamu: yeye huchukua baadhi yake na kuota moto, huwasha moto na kuoka mkate. Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu, huitengeneza sanamu na kuisujudia.
ISA 44:16 Sehemu ya kuni huziweka motoni, akapikia chakula chake, hubanika nyama na kula hadi ashibe. Huota moto na kusema, “Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”
ISA 44:17 Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake; yeye huisujudia na kuiabudu. Huiomba na kusema, “Niokoe; wewe ni mungu wangu.”
ISA 44:18 Hawajui chochote, hawaelewi chochote, macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona, akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.
ISA 44:19 Hakuna anayefikiri, hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema, “Sehemu yake nilitumia kwa kuni; hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake, nikabanika nyama na kuila. Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki? Je, nisujudie gogo la mti?”
ISA 44:20 Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha; hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema, “Je, kitu hiki kilicho mkononi wangu wa kuume si ni uongo?”
ISA 44:21 “Ee Yakobo, kumbuka mambo haya, ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu. Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu. Ee Israeli, sitakusahau.
ISA 44:22 Nimeyafuta makosa yako kama wingu, dhambi zako kama ukungu wa asubuhi. Nirudie mimi, kwa kuwa nimekukomboa wewe.”
ISA 44:23 Enyi mbingu, imbeni kwa furaha, kwa maana Mwenyezi Mungu amefanya jambo hili. Ee vilindi vya dunia, piga kelele. Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo, enyi misitu na miti yenu yote, kwa maana Mwenyezi Mungu amemkomboa Yakobo, ameuonesha utukufu wake katika Israeli.
ISA 44:24 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni: “Mimi ni Mwenyezi Mungu, niliyeumba vitu vyote, niliyezitanda mbingu peke yangu, niliyeitandaza nchi mwenyewe.
ISA 44:25 “Mimi huzipinga ishara za manabii wa uongo, na kuwatia upumbavu waaguzi, niyapinduaye maarifa ya wenye hekima, na kuyafanya kuwa upuzi.
ISA 44:26 Mimi ndimi niyathibitishaye maneno ya watumishi wake, na kutimiza utabiri wa wajumbe wake. “Mimi ndiye niiambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’ niiambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’ na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’
ISA 44:27 niiambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka, nami nitakausha vijito vyako,’
ISA 44:28 nisemaye kuhusu Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu, naye atatimiza yote yanipendezayo; atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,” na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’
ISA 45:1 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa mpakwa mafuta wake, Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume kutiisha mataifa mbele yake na kuwavua wafalme silaha zao, kufungua milango mbele yake ili malango yasije yakafungwa:
ISA 45:2 Nitaenda mbele yako na kusawazisha milima; nitavunjavunja malango ya shaba na kukatakata mapingo ya chuma.
ISA 45:3 Nitakupa hazina za gizani, mali iliyofichwa mahali pa siri, ili upate kujua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako.
ISA 45:4 Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu, Israeli niliyemchagua, nimekuita wewe kwa jina lako, na kukupa jina la heshima, ingawa wewe hunitambui.
ISA 45:5 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, wala hakuna mwingine, zaidi yangu hakuna Mungu. Nitakutia nguvu, ingawa wewe hujanitambua,
ISA 45:6 ili kutoka mawio ya jua hadi machweo yake, watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu wala hakuna mwingine.
ISA 45:7 Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza, ninaleta mafanikio na kusababisha maafa. Mimi, Mwenyezi Mungu, huyatenda haya yote.
ISA 45:8 “Enyi mbingu juu, nyesheni haki, mawingu na yaidondoshe. Dunia na ifunguke sana, wokovu na uchipuke, haki na ikue pamoja nao. Mimi, Mwenyezi Mungu, ndiye niliyeiumba.
ISA 45:9 “Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake, yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi. Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi, ‘Unatengeneza nini wewe?’ Je, kazi yako husema, ‘Hana mikono’?
ISA 45:10 Ole wake amwambiaye baba yake, ‘Umezaa nini?’ Au kumwambia mama yake, ‘Umezaa kitu gani?’
ISA 45:11 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake: Kuhusu mambo yatakayokuja, je, unaniuliza habari za watoto wangu, au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?
ISA 45:12 Mimi ndiye niliyeumba dunia na kumuumba mwanadamu juu yake. Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu, nikayapanga majeshi yake yote ya angani.
ISA 45:13 Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu: nitazinyoosha njia zake zote. Yeye atajenga mji wangu upya, na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni, lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi, asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
ISA 45:14 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi, nao wale Waseba warefu, watakujia na kuwa wako, watakujia wakijikokota nyuma yako, watakujia wamefungwa minyororo. Watasujudu mbele yako, wakikusihi na kusema, ‘Hakika Mungu yu pamoja nawe, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine.’ ”
ISA 45:15 Hakika wewe u Mungu unayejificha, Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli.
ISA 45:16 Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika; wataenda kutahayarika pamoja.
ISA 45:17 Lakini Israeli ataokolewa na Mwenyezi Mungu kwa wokovu wa milele; kamwe hutaaibika wala kutatahayarika, milele yote.
ISA 45:18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyeumba mbingu, ndiye Mungu; yeye aliyeifanya dunia na kuiumba, yeye ndiye aliiwekea misingi imara, hakuiumba ili iwe tupu, bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Anasema: “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, wala hakuna mwingine.
ISA 45:19 Sijasema sirini, kutoka mahali fulani katika nchi ya giza; sijawaambia wazao wa Yakobo, ‘Nitafuteni bure.’ Mimi, Mwenyezi Mungu, nasema kweli; ninatangaza lililo sahihi.
ISA 45:20 “Kusanyikeni pamoja mje, enyi wakimbizi kutoka mataifa. Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili, wale waombao miungu isiyoweza kuokoa.
ISA 45:21 Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo; wao na wafanye shauri pamoja. Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani, aliyelitangaza tangu zamani za kale? Je, haikuwa Mimi, Mwenyezi Mungu? Wala hapana Mungu mwingine zaidi yangu mimi, Mungu mwenye haki na Mwokozi; hapana mwingine ila mimi.
ISA 45:22 “Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe, enyi miisho yote ya dunia; kwa maana mimi ndimi Mungu, wala hapana mwingine.
ISA 45:23 Nimeapa kwa nafsi yangu, kinywa changu kimenena katika uadilifu wote neno ambalo halitatanguka: Kila goti litapigwa mbele zangu, kwangu mimi kila ulimi utaapa.
ISA 45:24 Watasema kunihusu, ‘Katika Mwenyezi Mungu peke yake ndiko kuna haki na nguvu.’ ” Wote ambao wamemkasirikia Mungu watamjia yeye, nao watatahayarika.
ISA 45:25 Lakini katika Mwenyezi Mungu wazao wote wa Israeli wataonekana wenye haki na watashangilia.
ISA 46:1 Beli anasujudu, Nebo anainama; sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo. Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea, mzigo kwa waliochoka.
ISA 46:2 Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini; hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu, wote wanaenda utumwani pamoja.
ISA 46:3 “Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo, ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli, ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba, nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.
ISA 46:4 Hata wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye, Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi. Nimewahuluku, nami nitawabeba, nitawahudumia ninyi na kuwaokoa.
ISA 46:5 “Mtanilinganisha na nani, au mtanihesabu kuwa sawa na nani? Ni nani mtakayenifananisha naye ili tuweze kulinganishwa?
ISA 46:6 Wengine humwaga dhahabu kutoka mifuko yao, na kupima fedha kwenye mizani; huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu, kisha huisujudia na kuiabudu.
ISA 46:7 Huiinua mabegani na kuichukua; huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo. Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale. Ingawa mtu huililia, haimjibu; haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.
ISA 46:8 “Kumbukeni hili, litieni akilini, liwekeni moyoni, enyi waasi.
ISA 46:9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale; mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine; mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine aliye kama mimi.
ISA 46:10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo, naam, tangu zamani za kale, mambo ambayo hayajatendeka. Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.
ISA 46:11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye; kutoka nchi ya mbali, mtu atakayetimiza kusudi langu. Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza; lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.
ISA 46:12 Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu, ninyi mlio mbali na haki.
ISA 46:13 Ninaleta haki yangu karibu, haiko mbali; wala wokovu wangu hautachelewa. Nitawapa Sayuni wokovu, Israeli utukufu wangu.
ISA 47:1 “Shuka uketi mavumbini, ee Bikira Binti Babeli; keti chini pasipo na kiti cha utawala, ee Binti wa Wakaldayo. Hutaitwa tena mwororo wala wa kupendeza.
ISA 47:2 Chukua mawe ya kusagia, usage unga, vua shela yako. Pandisha mavazi yako, ondoa viatu vyako, vuka vijito kwa shida.
ISA 47:3 Uchi wako utafunuliwa na aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; sitamhurumia hata mmoja.”
ISA 47:4 Mkombozi wetu: Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake; ndiye yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 47:5 “Keti kimya, ingia gizani, Binti wa Wakaldayo, hutaitwa tena malkia wa falme.
ISA 47:6 Niliwakasirikia watu wangu na kuaibisha urithi wangu; niliwatia mikononi mwako, nawe hukuwaonea huruma. Hata juu ya wazee uliweka nira nzito sana.
ISA 47:7 Ukasema, ‘Nitaendelea kuwa malkia milele!’ Lakini hukutafakari mambo haya wala hukuwaza juu ya kile kingeweza kutokea.
ISA 47:8 “Sasa basi, sikiliza, ewe kiumbe mpenda anasa, ukaaye mahali pako pa salama, na kujiambia mwenyewe, ‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu. Kamwe sitakuwa mjane, wala sitafiwa na watoto.’
ISA 47:9 Haya mawili yatakupata, kufumba na kufumbua, katika siku moja: kufiwa na watoto, na ujane. Yote yatakupata kwa kipimo kikamilifu, ijapokuwa uchawi wako ni mwingi, na uaguzi wako ni mwingi.
ISA 47:10 Umeutegemea uovu wako, nawe umesema, ‘Hakuna yeyote anionaye.’ Hekima yako na maarifa yako vinakupoteza unapojiambia mwenyewe, ‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.’
ISA 47:11 Maafa yatakujia, nawe hutaweza kuyaondoa kwa uaguzi. Janga litakuangukia, wala hutaweza kulikinga kwa fidia; msiba mkuu usioweza kuutabiri utakujia ghafula.
ISA 47:12 “Endelea basi na uaguzi wako, na wingi wa uchawi wako, ambao umeutumikia tangu utoto wako. Labda utafanikiwa, labda unaweza ukasababisha hofu kuu.
ISA 47:13 Ushauri wote uliopokea umekuchosha bure! Wanajimu wako na waje mbele, wale watazama nyota watabiriao mwezi baada ya mwezi, wao na wawaokoe na lile linalokuja juu yenu.
ISA 47:14 Hakika wako kama mabua makavu; moto utawateketeza. Hawawezi hata kujiokoa wao wenyewe kutokana na nguvu za mwali wa moto. Hapa hakuna makaa ya kumtia mtu yeyote joto; hapa hakuna moto wa kuota.
ISA 47:15 Hayo ndiyo yote wanayoweza kuwatendea ninyi, hawa ambao umetaabika nao na kufanya nao biashara tangu utoto. Kila mmoja atatoroka; hakuna yeyote awezaye kukuokoa.
ISA 48:1 “Sikilizeni hili, ee nyumba ya Yakobo, ninyi mnaoitwa kwa jina la Israeli, na mnaotoka katika ukoo wa Yuda, ninyi mnaoapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, mnaomwomba Mungu wa Israeli, lakini si katika kweli au kwa haki;
ISA 48:2 ninyi mnaojiita raia wa mji mtakatifu, na kumtegemea Mungu wa Israeli, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake:
ISA 48:3 Nilitoa unabii mambo ya kwanza tangu zamani, kinywa changu kiliyatangaza na kuyafanya yajulikane; kisha ghafula nikayatenda, nayo yakatokea.
ISA 48:4 Kwa kuwa nalijua jinsi ulivyokuwa mkaidi; mishipa ya shingo yako ilikuwa chuma, paji la uso wako lilikuwa shaba.
ISA 48:5 Kwa hiyo nilikuambia mambo haya tangu zamani, kabla hayajatokea nilikutangazia ili usije ukasema, ‘Sanamu zangu zilifanya hayo; sanamu yangu ya mti, na mungu wangu wa chuma aliyaamuru.’
ISA 48:6 Umesikia mambo haya; yaangalie hayo yote. Je, hutayakubali? “Kuanzia sasa na kuendelea nitakueleza mambo mapya, juu ya mambo yaliyofichika usiyoyajua.
ISA 48:7 Yameumbwa sasa, wala si tangu zamani; hukupata kuyasikia kabla ya siku ya leo. Hivyo huwezi kusema, ‘Naam, niliyajua hayo.’
ISA 48:8 Hujayasikia wala kuyaelewa, tangu zamani sikio lako halikufunguka. Ninafahamu vyema jinsi ulivyo mdanganyifu, uliitwa mwasi tangu kuzaliwa kwako.
ISA 48:9 Kwa ajili ya Jina langu mwenyewe ninaichelewesha ghadhabu yangu, kwa ajili ya sifa zangu nimeizuia isikupate, ili nisije nikakukatilia mbali.
ISA 48:10 Tazama, nimekusafisha, ingawa si kama fedha, nimekujaribu katika tanuru la mateso.
ISA 48:11 Kwa ajili yangu mwenyewe, kwa ajili yangu mwenyewe, nafanya hili. Jinsi gani niliache Jina langu lichafuliwe? Sitautoa utukufu wangu kwa mwingine.
ISA 48:12 “Ee Yakobo, nisikilize mimi, Israeli, ambaye nimekuita: Mimi ndiye; mimi ndimi mwanzo na mwisho.
ISA 48:13 Mkono wangu mwenyewe uliweka misingi ya dunia, nao mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo, zote husimama pamoja.
ISA 48:14 “Kusanyikeni, ninyi nyote, msikilize: Ni ipi miongoni mwa hizo sanamu ambayo imetabiri vitu hivi? Watu wa Mwenyezi Mungu waliochaguliwa na kuungana watatimiza kusudi lake dhidi ya Babeli; mkono wa Mungu utakuwa dhidi ya Wakaldayo.
ISA 48:15 Mimi, naam, Mimi, nimenena; naam, nimemwita yeye. Nitamleta, naye atafanikiwa katika lile nililomtuma.
ISA 48:16 “Nikaribieni na msikilize hili: “Tangu tangazo la kwanza sikusema kwa siri; wakati litokeapo, nitakuwako hapo.” Sasa Bwana Mungu Mwenyezi amenituma, kwa Roho wake Mtakatifu.
ISA 48:17 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea.
ISA 48:18 Laiti ungesikiliza kwa makini maagizo yangu, amani yako ingekuwa kama mto, haki yako kama mawimbi ya bahari.
ISA 48:19 Wazao wako wangekuwa kama mchanga, watoto wako kama chembe zake zisizohesabika; kamwe jina lao lisingefutiliwa mbali, wala kuangamizwa kutoka mbele zangu.”
ISA 48:20 Tokeni huko Babeli, kimbieni kutoka kwa Wakaldayo! Tangazeni hili kwa kelele za shangwe na kulihubiri. Lipelekeni hadi miisho ya dunia; semeni, “Mwenyezi Mungu amemkomboa mtumishi wake Yakobo.”
ISA 48:21 Hawakuona kiu alipowaongoza kupita jangwani; alifanya maji yatiririke kutoka mwamba kwa ajili yao; akapasua mwamba na maji yakatoka kwa nguvu.
ISA 48:22 “Hakuna amani kwa waovu,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 49:1 Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili, ninyi mataifa mlio mbali: Kabla sijazaliwa, Mwenyezi Mungu aliniita, tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu.
ISA 49:2 Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa, katika uvuli wa mkono wake akanificha; akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa, na kunificha katika podo lake.
ISA 49:3 Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye ndani yake nitaonesha utukufu wangu.”
ISA 49:4 Lakini nilisema, “Nimetumika bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida. Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.”
ISA 49:5 Sasa Mwenyezi Mungu asema: yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake, kumrudisha tena Yakobo kwake na kumkusanyia Israeli, kwa maana nimepata heshima machoni pa Mwenyezi Mungu, naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu;
ISA 49:6 yeye asema: “Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kurejesha makabila ya Yakobo, na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi? Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa, ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.”
ISA 49:7 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa, kwa mtumishi wa watawala: “Wafalme watakuona na kusimama, wakuu wataona na kuanguka kifudifudi, kwa sababu ya Mwenyezi Mungu, aliye mwaminifu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.”
ISA 49:8 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Wakati wangu uliokubalika nitakujibu, nami katika siku ya wokovu nitakusaidia; nitakuhifadhi, nami nitakufanya kuwa agano kwa ajili ya watu, ili kurudisha nchi na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa,
ISA 49:9 kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’ nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’ “Watajilisha kando ya barabara na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu.
ISA 49:10 Hawataona njaa wala kuona kiu, wala hari ya jangwani au jua halitawapiga. Yeye mwenye huruma juu yao atawaonesha njia, na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji.
ISA 49:11 Nitaifanya milima yangu yote kuwa barabara, na njia kuu zangu zitainuliwa.
ISA 49:12 Tazama, watakuja kutoka mbali: wengine kutoka kaskazini, wengine kutoka magharibi, wengine kutoka nchi ya Sinimu.”
ISA 49:13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu; furahi, ee dunia; pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima! Kwa maana Mwenyezi Mungu anawafariji watu wake, naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.
ISA 49:14 Lakini Sayuni alisema, “Mwenyezi Mungu ameniacha, Bwana amenisahau.”
ISA 49:15 “Je, mama aweza kumsahau mtoto aliye matitini mwake akinyonya, wala asiwe na huruma juu ya mtoto aliyemzaa? Ingawa anaweza kusahau, mimi sitakusahau wewe!
ISA 49:16 Tazama, nimekuchora kama muhuri katika vitanga vya mikono yangu, kuta zako zi mbele yangu daima.
ISA 49:17 Wana wako wanaharakisha kurudi, nao wale waliokuteka wanaondoka kwako.
ISA 49:18 Inua macho yako ukatazame pande zote: wana wako wote wanakusanyika na kukujia. Kwa hakika kama vile niishivyo, utawavaa wote kama mapambo, na kujifunga nao kama bibi arusi,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 49:19 “Ingawa uliangamizwa na kufanywa ukiwa, na nchi yako ikaharibiwa, sasa nafasi itakuwa finyu kwa ajili ya watu wako, nao wale waliokuangamiza watakuwa mbali sana.
ISA 49:20 Watoto waliozaliwa wakati wa msiba wako bado watakuambia, ‘Mahali hapa ni finyu sana kwetu, tupe eneo kubwa zaidi la kuishi.’
ISA 49:21 Ndipo utasema moyoni mwako, ‘Ni nani aliyenizalia hawa? Nilikuwa nimefiwa, tena tasa; nilikuwa nimehamishwa na kukataliwa. Ni nani aliyewalea hawa? Niliachwa peke yangu, lakini hawa wametoka wapi?’ ”
ISA 49:22 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa, nitainua bendera yangu kwa mataifa; watawaleta wana wako mikononi yao, na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao.
ISA 49:23 Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea, na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea. Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa chini; wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako. Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu; wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.”
ISA 49:24 Je, nyara zaweza kuchukuliwa kutoka kwa mashujaa wa vita, au mateka kuokolewa kutoka kwa watu wakali?
ISA 49:25 Lakini hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Naam, mateka watachukuliwa kutoka kwa mashujaa, na nyara zitapokonywa kutoka kwa watu wakali. Nitashindana na wale wanaoshindana nawe, nami nitawaokoa watoto wako.
ISA 49:26 Nitawafanya wanaokudhulumu wale nyama yao wenyewe; watalewa kwa damu yao wenyewe, kama vile kwa mvinyo. Ndipo wanadamu wote watajua ya kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, ni Mwokozi wako, Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
ISA 50:1 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Iko wapi hati ya talaka ya mama yako ambayo kwayo niliachana naye? Au nimewauza ninyi kwa nani miongoni mwa watu wanaonidai? Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa, kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa.
ISA 50:2 Nilipokuja, kwa nini hapakuwa hata mtu mmoja? Nilipoita, kwa nini hapakuwa hata mtu mmoja wa kujibu? Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa? Je, mimi sina nguvu za kukuokoa? Kwa kukemea tu naikausha bahari, naigeuza mito ya maji kuwa jangwa; samaki wake wanaoza kwa kukosa maji na kufa kwa ajili ya kiu.
ISA 50:3 Ninalivika anga weusi na kufanya gunia kuwa kifuniko chake.”
ISA 50:4 Bwana Mungu Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa, ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka. Huniamsha asubuhi kwa asubuhi, huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.
ISA 50:5 Bwana Mungu Mwenyezi amezibua masikio yangu, nami sikuwa mwasi, wala sikurudi nyuma.
ISA 50:6 Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao, mashavu yangu wale wang’oao ndevu zangu; sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha na kutemewa mate.
ISA 50:7 Kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi ananisaidia, sitatahayarika. Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami ninajua sitaaibika.
ISA 50:8 Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu. Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu? Tukabiliane uso kwa uso! Mshtaki wangu ni nani? Ni nani aliye mshtaki wangu?
ISA 50:9 Ni Bwana Mungu Mwenyezi anisaidiaye mimi. Ni nani huyo atakayenihukumu? Wote watachakaa kama vazi, nondo watawala wawamalize.
ISA 50:10 Ni nani miongoni mwenu amchaye Mwenyezi Mungu, na kulitii neno la mtumishi wake? Yeye atembeaye gizani, yeye asiye na nuru, na alitumainie jina la Mwenyezi Mungu, na amtegemee Mungu wake.
ISA 50:11 Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto, na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi, nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu na ya mienge mliyoiwasha. Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu: Mtalala chini kwa mateso makali.
ISA 51:1 “Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki na mnaomtafuta Mwenyezi Mungu: Tazameni mwamba ambako mlichongwa, na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;
ISA 51:2 mwangalieni Ibrahimu, baba yenu, na Sara, ambaye aliwazaa. Wakati nilimwita alikuwa mmoja tu, nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.
ISA 51:3 Hakika Mwenyezi Mungu ataifariji Sayuni, naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote; atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni, nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya Mwenyezi Mungu. Shangwe na furaha zitakuwa ndani yake, shukrani na sauti za kuimba.
ISA 51:4 “Nisikilizeni, watu wangu; nisikieni, taifa langu: Torati itatoka kwangu; haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.
ISA 51:5 Haki yangu inakaribia mbio, wokovu wangu unakuja, nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa. Visiwa vitanitegemea na kungojea mkono wangu kwa matumaini.
ISA 51:6 Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame dunia chini; mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake kufa kama inzi. Bali wokovu wangu utadumu milele, haki yangu haitakoma kamwe.
ISA 51:7 “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa, ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu: Msiogope mashutumu ya wanadamu wala msitiwe hofu na matukano yao.
ISA 51:8 Kwa maana nondo atawala kama vazi, nao funza atawatafuna kama sufu. Lakini haki yangu itadumu milele, wokovu wangu kwa vizazi vyote.”
ISA 51:9 Amka, Amka! Jivike nguvu, ewe mkono wa Mwenyezi Mungu, Amka, kama siku zilizopita, kama vile vizazi vya zamani. Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande, uliyemchoma huyo mnyama mkubwa?
ISA 51:10 Si ni wewe uliyekausha bahari, maji ya kilindi kikuu, uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari ili waliokombolewa wapate kuvuka?
ISA 51:11 Wale waliolipiwa fidia na Mwenyezi Mungu watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao. Furaha na shangwe zitawapata, huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.
ISA 51:12 “Mimi, naam mimi, ndimi niwafarijie ninyi. Ninyi ni nani hata kuwaogopa wanadamu wanaokufa, wanadamu ambao ni majani tu,
ISA 51:13 kwamba mnamsahau Mwenyezi Mungu Muumba wenu, aliyezitanda mbingu na kuiweka misingi ya dunia, kwamba mnaishi katika hofu siku zote kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu, ambaye nia yake ni kuangamiza? Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?
ISA 51:14 Wafungwa waliojikunyata kwa hofu watawekwa huru karibuni; hawatafia kwenye gereza lao, wala hawatakosa chakula.
ISA 51:15 Kwa maana Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume: Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.
ISA 51:16 Nimeweka maneno yangu kinywani mwako na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu: Mimi niliyeweka mbingu mahali pake, niliyeweka misingi ya dunia, niwaambiaye Sayuni, ‘Ninyi ni watu wangu.’ ”
ISA 51:17 Amka, amka! Simama, ee Yerusalemu, wewe uliyekunywa kutoka mkono wa Mwenyezi Mungu kikombe cha ghadhabu yake, wewe uliyekunywa hata machujo yake, kikombe kile cha kunywea kiwafanyacho watu kuyumbayumba.
ISA 51:18 Kati ya wana wote aliowazaa hapakuwa na hata mmoja wa kumwongoza; kati ya wana wote aliowalea hapakuwa hata mmoja wa kumshika mkono.
ISA 51:19 Majanga haya mawili yamekuja juu yako: ni nani awezaye kukufariji? Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga: ni nani awezaye kukutuliza?
ISA 51:20 Wana wako wamezimia, wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara, kama swala aliyenaswa kwenye wavu. Wamejazwa na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na makaripio ya Mungu wako.
ISA 51:21 Kwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa, uliyelewa, lakini si kwa mvinyo.
ISA 51:22 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi wako, Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake: “Tazama, nimeondoa mkononi mwako kikombe kilichokufanya uyumbayumbe; kutoka kikombe hicho, kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu, kamwe hutakunywa tena.
ISA 51:23 Nitakiweka mikononi mwa watesi wako, wale waliokuambia, ‘Anguka kifudifudi ili tuweze kutembea juu yako.’ Ukaufanya mgongo wako kama ardhi, kama njia yao ya kupita.”
ISA 52:1 Amka, amka, ee Sayuni, jivike nguvu. Vaa mavazi yako ya fahari, ee Yerusalemu, mji mtakatifu. Asiyetahiriwa na aliye najisi hataingia kwako tena.
ISA 52:2 Jikung’ute mavumbi yako, inuka, uketi kwenye kiti cha utawala, ee Yerusalemu. Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako, ee Binti Sayuni uliye mateka.
ISA 52:3 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Mliuzwa pasipo malipo, nanyi mtakombolewa bila fedha.”
ISA 52:4 Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi, hatimaye, Ashuru wakawadhulumu.
ISA 52:5 “Basi sasa nina nini hapa?” asema Mwenyezi Mungu. “Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo, nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,” asema Mwenyezi Mungu. “Mchana kutwa jina langu limetukanwa bila kikomo.
ISA 52:6 Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu; kwa hiyo katika siku ile watajua kwamba ndimi niliyetangulia kulisema. Naam, ni mimi.”
ISA 52:7 Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema ilivyo mizuri juu ya milima, wale wanaotangaza amani, wanaoleta habari njema, wanaotangaza wokovu, wauambiao Sayuni, “Mungu wako anatawala!”
ISA 52:8 Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao, pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha. Mwenyezi Mungu atakaporejea Sayuni, wataliona kwa macho yao wenyewe.
ISA 52:9 Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja, enyi magofu ya Yerusalemu, kwa maana Mwenyezi Mungu amewafariji watu wake, ameikomboa Yerusalemu.
ISA 52:10 Mkono mtakatifu wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa machoni pa mataifa yote, nayo miisho yote ya dunia itaona wokovu wa Mungu wetu.
ISA 52:11 Ondokeni, ondokeni, tokeni huko! Msiguse kitu chochote kilicho najisi! Tokeni kati yake mwe safi, ninyi mchukuao vyombo vya Mwenyezi Mungu.
ISA 52:12 Lakini hamtaondoka kwa haraka, wala hamtaenda kwa kukimbia; kwa maana Mwenyezi Mungu atatangulia mbele yenu, Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu.
ISA 52:13 Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima; atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana.
ISA 52:14 Kama walivyokuwa wengi walioshangazwa naye, kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote na umbo lake kuharibiwa zaidi ya mfano wa mwanadamu:
ISA 52:15 hivyo atayashangaza mataifa mengi, nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake. Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona, nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu.
ISA 53:1 Ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa kwa nani?
ISA 53:2 Alikua mbele yake kama mche mwororo na kama mzizi katika nchi kavu. Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake, hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.
ISA 53:3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso. Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.
ISA 53:4 Hakika alichukua udhaifu wetu na akajitwika huzuni zetu; tulidhania kuwa ameadhibiwa na Mungu, naye akapigwa sana na kujeruhiwa.
ISA 53:5 Lakini alijeruhiwa kwa ajili ya makosa yetu, alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu; adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake, na kwa majeraha yake sisi tumepona.
ISA 53:6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe, naye Mwenyezi Mungu aliweka juu yake maovu yetu sisi sote.
ISA 53:7 Alionewa na kuteswa, hata hivyo hakufungua kinywa chake; aliongozwa kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake.
ISA 53:8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa. Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake? Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai, alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.
ISA 53:9 Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu, pamoja na matajiri katika kifo chake, ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
ISA 53:10 Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kumchubua na kumsababisha ateseke. Ingawa Mwenyezi Mungu amefanya maisha yake kuwa sadaka ya hatia, ataona uzao wake na kuishi siku nyingi, nayo mapenzi ya Mwenyezi Mungu yatafanikiwa mkononi mwake.
ISA 53:11 Baada ya maumivu ya nafsi yake, ataona nuru ya uzima na kuridhika; kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki, naye atayachukua maovu yao.
ISA 53:12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu, naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu, kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti, naye alihesabiwa pamoja na wakosaji. Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi, na kuwaombea wakosaji.
ISA 54:1 “Imba, ewe mwanamke tasa, wewe ambaye kamwe hukuzaa mtoto; paza sauti kwa kuimba, piga kelele kwa furaha, wewe ambaye kamwe hukupata uchungu; kwa sababu watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi kuliko wa mwanamke mwenye mume,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 54:2 “Panua mahali pa hema lako, tandaza mapazia ya hema lako uyaeneze mbali, wala usiyazuie; ongeza urefu wa kamba zako, imarisha vigingi vyako.
ISA 54:3 Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; wazao wako watayamiliki mataifa na kukaa katika miji yao iliyoachwa ukiwa.
ISA 54:4 “Usiogope, wewe hutaaibika. Usiogope aibu, wewe hutaaibishwa. Wewe utasahau aibu ya ujana wako, wala hutakumbuka tena mashutumu ya ujane wako.
ISA 54:5 Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako, yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.
ISA 54:6 Mwenyezi Mungu atakuita urudi kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni; kama mke aliyeolewa bado angali kijana na kukataliwa,” asema Mungu wako.
ISA 54:7 “Kwa kitambo kidogo nilikuacha, lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.
ISA 54:8 Katika ukali wa hasira nilikuficha uso wangu kwa kitambo, lakini kwa fadhili za milele nitakuwa na huruma juu yako,” asema Mwenyezi Mungu Mkombozi wako.
ISA 54:9 “Kwangu mimi jambo hili ni kama siku za Nuhu, nilipoapa kuwa maji ya Nuhu kamwe hayatafunika tena dunia. Hivyo sasa nimeapa sitawakasirikia ninyi, kamwe sitawakemea tena.
ISA 54:10 Ijapotikisika milima, na vilima viondolewe, hata hivyo upendo wangu usiokoma kwenu hautatikisika, wala agano langu la amani halitaondolewa,” asema Mwenyezi Mungu, mwenye huruma juu yenu.
ISA 54:11 “Ewe mji uliyeteswa, uliyepigwa kwa dhoruba na usiyetulizwa, nitakujenga kwa almasi, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.
ISA 54:12 Nitafanya minara yako ya akiki, malango yako kwa vito ving’aavyo, nazo kuta zako zote za vito vya thamani.
ISA 54:13 Watoto wako wote watafundishwa na Mwenyezi Mungu, nayo amani ya watoto wako itakuwa kuu.
ISA 54:14 Kwa haki utathibitika: Kuonewa kutakuwa mbali nawe; hutaogopa chochote. Hofu itakuwa mbali nawe; haitakukaribia wewe.
ISA 54:15 Kama mtu yeyote akikushambulia, haitakuwa kwa ruhusa yangu; yeyote akushambuliaye atajisalimisha kwako.
ISA 54:16 “Tazama, ni mimi niliyemuumba mhunzi, yeye afukutaye makaa kuwa moto, na kutengeneza silaha inayofaa kwa kazi yake. Tena ni mimi niliyemwambia mharibu kufanya uharibifu mwingi.
ISA 54:17 Hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako itakayofanikiwa, nawe utauthibitisha kuwa mwongo kila ulimi utakaokushtaki. Huu ndio urithi wa watumishi wa Mwenyezi Mungu na hii ndiyo haki yao inayotoka kwangu,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 55:1 “Haya! Njooni, ninyi nyote wenye kiu, njooni kwenye maji; nanyi ambao hamna fedha, njooni, nunueni na mle! Njooni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila gharama.
ISA 55:2 Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula, na kutaabikia kitu kisichoshibisha? Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri, nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.
ISA 55:3 Tegeni sikio mje kwangu, nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi. Nitafanya agano la milele nanyi, pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.
ISA 55:4 Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa, kiongozi na jemadari wa mataifa.
ISA 55:5 Hakika utaita mataifa usiyoyajua, nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia, kwa sababu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwa maana amekutukuza.”
ISA 55:6 Mtafuteni Mwenyezi Mungu maadamu anapatikana; mwiteni maadamu yu karibu.
ISA 55:7 Mtu mwovu na aiache njia yake, na mtu mbaya na ayaache mawazo yake. Yeye na amrudie Mwenyezi Mungu, naye atamrehemu, arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.
ISA 55:8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 55:9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia, ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
ISA 55:10 Kama vile mvua na theluji ishukavyo kutoka mbinguni, nayo hairudi tena huko bila kunywesha dunia na kuichipusha na kuistawisha, ili itoe mbegu kwa mpanzi na mkate kwa mlaji,
ISA 55:11 ndivyo lilivyo neno langu litokalo kinywani mwangu: Halitanirudia tupu, bali litatimiliza lile nililokusudia, na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.
ISA 55:12 Mtatoka nje kwa furaha na kuongozwa kwa amani; milima na vilima vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu, nayo miti yote ya shambani itapiga makofi.
ISA 55:13 Badala ya kichaka cha miiba itaota miti ya misunobari, na badala ya michongoma utaota mhadasi. Hili litakuwa jambo la kumpatia Mwenyezi Mungu jina, kwa ajili ya ishara ya milele, ambayo haitaharibiwa.”
ISA 56:1 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Dumisheni haki na mkatende lile lililo sawa, kwa maana wokovu wangu u karibu na haki yangu itafunuliwa upesi.
ISA 56:2 Amebarikiwa mtu yule atendaye hili, mtu yule alishikaye kwa uthabiti, yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.”
ISA 56:3 Usimwache mgeni aambatanaye na Mwenyezi Mungu aseme, “Hakika Mwenyezi Mungu atanitenga na watu wake.” Usimwache towashi yeyote alalamike akisema, “Mimi ni mti mkavu tu.”
ISA 56:4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa matowashi washikao Sabato zangu, ambao huchagua kile kinachonipendeza na kulishika sana agano langu:
ISA 56:5 hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake kumbukumbu na jina bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike: nitawapa jina lidumulo milele, ambalo halitakatiliwa mbali.
ISA 56:6 Wageni wanaoambatana na Mwenyezi Mungu ili kumtumikia, kulipenda jina la Mwenyezi Mungu, na kumwabudu yeye, wote washikao Sabato bila kuinajisi na ambao hushika sana agano langu:
ISA 56:7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala. Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao zitakubalika juu ya madhabahu yangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.”
ISA 56:8 Bwana Mungu Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye Waisraeli waliohamishwa: “Bado nitawakusanya wengine kwao zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.”
ISA 56:9 Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni, njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni!
ISA 56:10 Walinzi wa Israeli ni vipofu, wote wamepungukiwa na maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kubweka; hulala na kuota ndoto, hupenda kulala.
ISA 56:11 Ni mbwa wenye tamaa kubwa, kamwe hawatosheki. Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu; wote wamegeukia njia yao wenyewe, kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.
ISA 56:12 Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo! Tunywe kileo sana! Kesho itakuwa kama leo, au hata bora zaidi.”
ISA 57:1 Mwenye haki hupotea, wala hakuna hata mmoja awazaye hilo moyoni mwake; watu wanaomcha Mungu huondolewa, wala hakuna hata mmoja anayeelewa kuwa wenye haki wameondolewa ili wasipatikane na maovu.
ISA 57:2 Wale wanaoenda kwa unyofu huwa na amani; hupata pumziko wanapolala mautini.
ISA 57:3 “Lakini ninyi: Njooni hapa, ninyi wana wa wachawi, ninyi wazao wa wazinzi na makahaba!
ISA 57:4 Mnamdhihaki nani? Ni nani mnayemcheka kwa dharau, na kumtolea ndimi zenu? Je, ninyi si watoto wa waasi, uzao wa waongo?
ISA 57:5 Mnawaka tamaa katikati ya mialoni na chini ya kila mti uliotanda matawi; mnawatoa kafara watoto wenu kwenye mabonde na chini ya majabali yenye mianya.
ISA 57:6 “Sanamu zilizo kati ya mawe laini ya mabondeni ndizo fungu lenu; hizo ndizo sehemu yenu. Naam, kwa hizo mmemimina sadaka za vinywaji, na kutoa sadaka za nafaka. Katika haya yote, niendelee kuona huruma?
ISA 57:7 Umeweka kitanda chako juu kwenye kilima kirefu kilichoinuka, huko ulienda kutoa dhabihu zako.
ISA 57:8 Nyuma ya milango yako na miimo yako umeweka alama zako za kipagani. Kwa kuniacha mimi, ulifunua kitanda chako, umepanda juu yake na kukipanua sana; ulifanya patano na wale ambao unapenda vitanda vyao, nawe uliangalia uchi wao.
ISA 57:9 Ulienda kwa Moleki ukiwa na mafuta ya zeituni, na ukaongeza manukato yako. Ukawatuma wajumbe wako mbali sana, ukashuka kwenye kaburi lenyewe!
ISA 57:10 Ulikuwa umechoshwa na njia zako zote, lakini hukusema, ‘Hakuna tumaini.’ Ulipata uhuisho wa nguvu zako, kwa sababu hiyo hukuzimia.
ISA 57:11 “Ni nani uliyemhofu hivyo na kumwogopa hata ukawa mwongo kwangu, wala hukunikumbuka au kutafakari hili moyoni mwako? Si ni kwa sababu nimekuwa kimya muda mrefu hata huniogopi?
ISA 57:12 Nitaifunua haki yako na matendo yako, nayo hayatakufaidi.
ISA 57:13 Utakapolia kwa kuhitaji msaada, sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe! Upepo utazipeperusha zote, pumzi peke yake itazipeperusha, Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake, atairithi nchi na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.”
ISA 57:14 Tena itasemwa: “Jengeni, jengeni, itengenezeni njia! Ondoeni vikwazo katika njia ya watu wangu.”
ISA 57:15 Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana, yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu: “Ninaishi mahali palipoinuka na patakatifu, lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu, na mwenye roho ya unyenyekevu, ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu na kuihuisha mioyo yao waliotubu.
ISA 57:16 Sitaendelea kulaumu milele, wala sitakasirika siku zote, kwa kuwa roho ya mwanadamu ingezimia mbele zangu: yaani pumzi ya mwanadamu niliyemuumba.
ISA 57:17 Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi; nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira, na bado aliendelea katika njia zake za tamaa.
ISA 57:18 Nimeziona njia zake, lakini nitamponya, nitamwongoza na kumrudishia upya faraja,
ISA 57:19 nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji katika Israeli. Amani, amani, kwa wale walio mbali na kwa wale walio karibu,” asema Mwenyezi Mungu. “Nami nitawaponya.”
ISA 57:20 Bali waovu ni kama bahari ichafukayo, ambayo haiwezi kutulia, mawimbi yake hutupa takataka na matope.
ISA 57:21 Mungu wangu asema, “Hakuna amani kwa waovu.”
ISA 58:1 “Piga kelele, usizuie. Paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazieni watu wangu uasi wao, na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.
ISA 58:2 Kwa maana kila siku hunitafuta, wanaonekana kutaka kujua njia zangu, kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa, na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake. Hutaka kwangu maamuzi ya haki, nao hutamani Mungu awakaribie.
ISA 58:3 Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona? Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’ “Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.
ISA 58:4 Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano, na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu. Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.
ISA 58:5 Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua, siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza? Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete, na kwa kujilaza juu ya gunia na majivu? Je, huo ndio mnaouita mfungo, siku iliyokubalika kwa Mwenyezi Mungu?
ISA 58:6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua: kufungua minyororo ya udhalimu, na kufungua kamba za nira, kuwaweka huru waliodhulumiwa, na kuvunja kila nira?
ISA 58:7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi, unapomwona aliye uchi, umvike, wala si kumkimbia mtu wa mwili wako na damu yako mwenyewe?
ISA 58:8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko na uponyaji wako utatokea upesi; ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako, na utukufu wa Mwenyezi Mungu utakuwa mlinzi nyuma yako.
ISA 58:9 Ndipo utaita, naye Mwenyezi Mungu atajibu, utalia kuomba msaada, naye atasema: Mimi hapa. “Ukiiondoa nira ya udhalimu, na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,
ISA 58:10 nanyi mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu na kutosheleza mahitaji ya waliodhulumiwa, ndipo nuru yenu itang’aa gizani, nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.
ISA 58:11 Mwenyezi Mungu atakuongoza siku zote, atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame, naye ataitia nguvu mifupa yako. Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri, kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.
ISA 58:12 Watu wako watajenga tena magofu ya zamani na kuinua misingi ya kale; utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka, Mwenye Kurejesha Barabara za Makao.
ISA 58:13 “Ukitunza miguu yako isivunje Sabato, na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu, ukiita Sabato siku ya furaha na siku takatifu ya Mwenyezi Mungu ya kuheshimiwa, kama utaiheshimu kwa kutoenenda katika njia zako mwenyewe, na kutokufanya yakupendezayo au kusema maneno ya upuzi,
ISA 58:14 ndipo utakapojipatia furaha yako katika Mwenyezi Mungu, nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.” Kinywa cha Mwenyezi Mungu kimenena haya.
ISA 59:1 Hakika mkono wa Mwenyezi Mungu si mfupi hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia.
ISA 59:2 Lakini maovu yenu yamewatenga ninyi na Mungu wenu, dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake, ili asisikie.
ISA 59:3 Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu kwa hatia. Midomo yenu imenena uongo, nazo ndimi zenu zimenong’ona mambo maovu.
ISA 59:4 Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki; hakuna hata mmoja anayetetea kwa haki. Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo, huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu.
ISA 59:5 Huangua mayai ya nyoka wenye sumu kali na kutanda wavu wa buibui. Yeyote alaye mayai yao atakufa, nalo moja likianguliwa, nyoka hutoka humo.
ISA 59:6 Utando wao wa buibui haufai kwa mavazi; hawawezi kujifunika kwa kile walichokitengeneza. Matendo yao ni matendo maovu, vitendo vya jeuri vipo mikononi mwao.
ISA 59:7 Miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni myepesi kumwaga damu isiyo na hatia. Mawazo yao ni mawazo maovu; uharibifu na maangamizi huonekana katika njia zao.
ISA 59:8 Hawajui njia ya amani, hakuna haki katika mapito yao. Wameyageuza kuwa njia za upotovu, hakuna apitaye njia hizo atakayeifahamu amani.
ISA 59:9 Hivyo uadilifu uko mbali nasi, nayo haki haitufikii. Tunatazamia nuru, kumbe! Yote ni giza, tunatazamia mwanga, lakini tunatembea katika giza nene.
ISA 59:10 Tunapapasa ukuta kama vipofu, tunapapasa katika njia zetu kama watu wasio na macho. Adhuhuri tunajikwaa kama wakati wa gizagiza; kati ya wenye nguvu, tuko kama wafu.
ISA 59:11 Wote tunanguruma kama dubu; tunalia kwa maombolezo kama hua. Tunatafuta haki, kumbe hakuna kabisa; tunatafuta wokovu, lakini uko mbali.
ISA 59:12 Kwa sababu makosa yetu ni mengi machoni pako, na dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu. Makosa yetu yako pamoja nasi daima, nasi tunayatambua maovu yetu:
ISA 59:13 Uasi na udanganyifu dhidi ya Mwenyezi Mungu, kumgeuzia Mungu wetu kisogo, tukichochea udhalimu na maasi, tukinena uongo ambao mioyo yetu imeuhifadhi.
ISA 59:14 Hivyo uadilifu umerudishwa nyuma, nayo haki inasimama mbali, kweli imejikwaa njiani, uaminifu hauwezi kuingia.
ISA 59:15 Kweli haipatikani popote, na yeyote aepukaye uovu huwa mawindo. Mwenyezi Mungu alitazama, naye akachukizwa kwamba hapakuwa na haki.
ISA 59:16 Aliona kuwa hapakuwa hata mtu mmoja, akashangaa kwamba hapakuwa hata mtu mmoja wa kuingilia kati. Hivyo mkono wake mwenyewe ndio uliomfanyia wokovu, nayo haki yake mwenyewe ndiyo iliyomtegemeza.
ISA 59:17 Alivaa haki kama dirii kifuani mwake, na chapeo ya wokovu kichwani mwake, alivaa mavazi ya kisasi naye akajifunga wivu kama joho.
ISA 59:18 Kulingana na kile walichokuwa wametenda, ndivyo atakavyolipa ghadhabu kwa watesi wake na kisasi kwa adui zake, atavilipa visiwa sawa na wanavyostahili.
ISA 59:19 Kuanzia magharibi, watu wataliogopa jina la Mwenyezi Mungu na kuanzia mawio ya jua, watauheshimu utukufu wake. Adui atakapokuja kama mafuriko, Roho wa Mwenyezi Mungu atainua kiwango dhidi yake na kumshinda.
ISA 59:20 “Mkombozi atakuja Sayuni, kwa wale wa Yakobo wanaozitubu dhambi zao,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 59:21 “Bali mimi, hili ndilo agano langu nao,” asema Mwenyezi Mungu. “Roho wangu Mtakatifu, aliye juu yenu, na maneno yangu niliyoyaweka vinywani vyenu, havitaondoka vinywani mwenu, wala kutoka vinywani mwa watoto wenu, wala kutoka vinywani mwa wazao wao, kuanzia sasa na hata milele,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 60:1 “Ondoka, angaza, kwa kuwa nuru yako imekuja na utukufu wa Mwenyezi Mungu umezuka juu yako.
ISA 60:2 Tazama, giza litaifunika dunia, na giza nene litayafunika mataifa, lakini Mwenyezi Mungu atazuka juu yako na utukufu wake utaonekana juu yako.
ISA 60:3 Mataifa watakuja kwenye nuru yako na wafalme kwa mwanga wa mapambazuko yako.
ISA 60:4 “Inua macho yako na utazame pande zote: Wote wanakusanyika na kukujia, wana wako wanakuja toka mbali, nao binti zako wanabebwa mikononi.
ISA 60:5 Ndipo utatazama na kutiwa nuru, moyo wako utasisimka na kujaa furaha, mali iliyo baharini italetwa kwako, utajiri wa mataifa utakujilia.
ISA 60:6 Makundi ya ngamia yatajaa katika nchi yako, ngamia vijana wa Midiani na Efa. Nao watu wote wanaotoka Sheba watakuja, wakichukua dhahabu na uvumba na kutangaza sifa za Mwenyezi Mungu.
ISA 60:7 Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako, kondoo dume wa Nebayothi watakutumikia, watakubalika kama sadaka juu ya madhabahu yangu, nami nitalipamba Hekalu langu tukufu.
ISA 60:8 “Ni nani hawa warukao kama mawingu, kama hua kuelekea kwenye viota vyao?
ISA 60:9 Hakika visiwa vinanitazama; merikebu za Tarshishi ndizo zinazotangulia, zikiwaleta wana wenu kutoka mbali, wakiwa na fedha na dhahabu zao, kwa heshima ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwa maana amekujalia utukufu.
ISA 60:10 “Wageni watazijenga upya kuta zako, na wafalme wao watakutumikia. Ingawa katika hasira nilikupiga, lakini katika upendeleo wangu nitakuonesha huruma.
ISA 60:11 Malango yako yatakuwa wazi siku zote, kamwe hayatafungwa, mchana wala usiku, ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa: wafalme wao wakiongoza maandamano ya ushindi.
ISA 60:12 Kwa maana taifa au ufalme ule ambao hautakutumikia utaangamia; utaharibiwa kabisa.
ISA 60:13 “Utukufu wa Lebanoni utakujilia, msunobari, mvinje pamoja na mteashuri, ili kupapamba mahali pangu patakatifu, nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu.
ISA 60:14 Wana wa wale waliokutesa watakuja wakisujudu mbele yako; wote wanaokudharau watasujudu miguuni pako; nao watakuita Mji wa Mwenyezi Mungu, Sayuni ya Aliye Mtakatifu wa Israeli.
ISA 60:15 “Ingawa umeachwa na kuchukiwa, bila yeyote anayesafiri ndani yako, nitakufanya kuwa fahari ya milele, na furaha ya vizazi vyote.
ISA 60:16 Utanyonya maziwa ya mataifa, na kunyonyeshwa matiti ya wafalme. Ndipo utakapojua kwamba Mimi, Mwenyezi Mungu, ni Mwokozi wako, Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.
ISA 60:17 Badala ya shaba nitakuletea dhahabu, na fedha badala ya chuma. Badala ya mti nitakuletea shaba, na chuma badala ya mawe. Nitafanya amani kuwa mtawala wako, na haki kuwa mfalme wako.
ISA 60:18 Jeuri hazitasikika tena katika nchi yako, wala maangamizi au uharibifu ndani ya mipaka yako, lakini utaita kuta zako Wokovu, na malango yako Sifa.
ISA 60:19 Jua halitakuwa tena nuru yako mchana, wala mwangaza wa mwezi hautakuangazia, kwa maana Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yako ya milele, naye Mungu wako atakuwa utukufu wako.
ISA 60:20 Jua lako halitazama tena, nao mwezi wako hautafifia tena; Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yako milele, nazo siku zako za huzuni zitakoma.
ISA 60:21 Ndipo watu wako wote watakuwa waadilifu, nao wataimiliki nchi milele. Wao ni chipukizi nililolipanda, kazi ya mikono yangu, ili kuonesha utukufu wangu.
ISA 60:22 Aliye mdogo kwenu atakuwa elfu, mdogo kuliko wote atakuwa taifa lenye nguvu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu; katika wakati wake nitayatimiza haya upesi.”
ISA 61:1 Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi yu juu yangu, kwa sababu Mwenyezi Mungu amenipaka mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwafariji waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao;
ISA 61:2 kutangaza mwaka wa Mwenyezi Mungu uliokubaliwa, na siku ya kisasi ya Mungu wetu, kuwafariji wote wanaoomboleza,
ISA 61:3 na kuwapa mahitaji wale wanaohuzunika katika Sayuni, ili kuwapa taji za uzuri badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa. Nao wataitwa mialoni ya haki, pando la Mwenyezi Mungu, ili kuonesha utukufu wake.
ISA 61:4 Watajenga upya magofu ya zamani na kupatengeneza mahali palipoachwa ukiwa zamani; watafanya upya miji iliyoharibiwa, iliyoachwa ukiwa kwa vizazi vingi.
ISA 61:5 Wageni watayachunga makundi yenu, wageni watafanya kazi katika mashamba yenu, na kutunza mashamba yenu ya mizabibu.
ISA 61:6 Nanyi mtaitwa makuhani wa Mwenyezi Mungu, mtaitwa watumishi wa Mungu wetu. Mtakula utajiri wa mataifa, nanyi katika utajiri wao mtajisifu.
ISA 61:7 Badala ya aibu yao watu wangu watapokea sehemu maradufu, na badala ya fedheha watafurahia katika urithi wao; hivyo watarithi sehemu maradufu katika nchi yao, nayo furaha ya milele itakuwa yao.
ISA 61:8 “Kwa maana Mimi, Mwenyezi Mungu, napenda haki, na ninachukia unyang’anyi na uovu. Katika uaminifu wangu nitawapa malipo yao na kufanya agano la milele nao.
ISA 61:9 Wazao wao watajulikana miongoni mwa mataifa, na uzao wao miongoni mwa makabila ya watu. Wale wote watakaowaona watatambua kuwa ni taifa ambalo Mwenyezi Mungu amelibariki.”
ISA 61:10 Ninafurahia sana katika Mwenyezi Mungu, nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu. Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu, na kunipamba kwa joho la haki, kama vile bwana arusi apambavyo kichwa chake kama kuhani, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vito vyake vya thamani.
ISA 61:11 Kwa maana kama vile ardhi ifanyavyo chipukizi kuota, na bustani isababishavyo mbegu kuota, ndivyo Bwana Mungu Mwenyezi atafanya haki na sifa zichipuke mbele ya mataifa yote.
ISA 62:1 Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hadi haki yake itakapoangaza kama mapambazuko, wokovu wake kama mwanga wa moto.
ISA 62:2 Mataifa wataona haki yako, nao wafalme wote wataona utukufu wako; wewe utaitwa kwa jina jipya lile ambalo kinywa cha Mwenyezi Mungu kitatamka.
ISA 62:3 Utakuwa taji la fahari mkononi mwa Mwenyezi Mungu, taji la kifalme mkononi mwa Mungu wako.
ISA 62:4 Hawatakuita tena Aliyeachwa, wala nchi yako kuiita Ukiwa. Bali utaitwa Hefsiba, nayo nchi yako itaitwa Beula, kwa maana Mwenyezi Mungu atakufurahia, nayo nchi yako itaolewa.
ISA 62:5 Kama vile kijana aoavyo mwanamwali, ndivyo Mwashi wako atakavyokuoa; kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
ISA 62:6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu, hawatanyamaza mchana wala usiku. Ninyi wenye kumwita Mwenyezi Mungu, msitulie,
ISA 62:7 msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu na kuufanya uwe sifa ya dunia.
ISA 62:8 Mwenyezi Mungu ameapa kwa mkono wake wa kuume na kwa mkono wake wenye nguvu: “Kamwe sitawapa tena adui zenu nafaka zenu kama chakula chao; kamwe wageni hawatakunywa tena divai mpya ambayo mmeitaabikia,
ISA 62:9 lakini wale waivunao nafaka wataila na kumsifu Mwenyezi Mungu, nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake katika nyua za patakatifu pangu.”
ISA 62:10 Piteni, piteni katika malango! Tengenezeni njia kwa ajili ya watu. Jengeni, jengeni njia kuu! Ondoeni mawe. Inueni bendera kwa ajili ya mataifa.
ISA 62:11 Mwenyezi Mungu ametoa tangazo hadi miisho ya dunia: “Mwambie Binti Sayuni, ‘Tazama, mwokozi wako anakuja! Tazama ujira wake uko pamoja naye, na malipo yake yanafuatana naye!’ ”
ISA 62:12 Wataitwa Watu Watakatifu, Waliokombolewa na Mwenyezi Mungu; nawe utaitwa Aliyetafutwa, Mji Usioachwa Tena.
ISA 63:1 Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu, kutoka Bosra, mwenye mavazi yaliyotiwa madoa mekundu? Ni nani huyu, aliyevikwa joho la kifahari, anayetembea kwa ukuu wa nguvu zake? “Mimi ndimi, nisemaye katika haki, mwenye nguvu wa kuokoa.”
ISA 63:2 Kwa nini mavazi yako ni mekundu, kama ya yule akanyagaye shinikizo la zabibu?
ISA 63:3 “Nimekanyaga shinikizo la kukamulia zabibu peke yangu; kutoka mataifa hakuna mtu aliyekuwa pamoja nami. Nimewaponda kwa miguu katika hasira yangu na kuwakanyaga chini katika ghadhabu yangu; damu yao ilitia matone kwenye mavazi yangu, na kutia madoa nguo zangu zote.
ISA 63:4 Kwa kuwa siku ya kisasi ilikuwa moyoni mwangu, mwaka wa ukombozi wangu umefika.
ISA 63:5 Nilitazama, lakini hapakuwa yeyote wa kunisaidia, nilishangaa kwa kuwa hapakuwa yeyote aliyetoa msaada; hivyo mkono wangu wenyewe ndio ulionifanyia wokovu, na ghadhabu yangu mwenyewe ndiyo iliyonitegemeza.
ISA 63:6 Nilikanyaga mataifa kwa miguu katika hasira yangu, katika ghadhabu yangu niliwalewesha, na kumwaga damu yao juu ya ardhi.”
ISA 63:7 Nitasimulia kuhusu wema wa Mwenyezi Mungu, kwa matendo ambayo apaswa kusifiwa, sawasawa na yote ambayo Mwenyezi Mungu ametenda kwa ajili yetu: naam, mambo mengi mema aliyoyatenda kwa ajili ya nyumba ya Israeli, sawasawa na huruma zake na wema wake mwingi.
ISA 63:8 Alisema, “Hakika wao ni watu wangu, wana ambao hawatanidanganya”; hivyo akawa Mwokozi wao.
ISA 63:9 Katika taabu zao zote naye alitaabika, na malaika wa uso wake akawaokoa. Katika upendo wake na rehema zake aliwakomboa, akawainua na kuwachukua siku zote zilizopita.
ISA 63:10 Lakini waliasi, na kumhuzunisha Roho Mtakatifu wa Mungu. Hivyo aligeuka na kuwa adui yao, na yeye mwenyewe akapigana dhidi yao.
ISA 63:11 Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita, siku za Musa na watu wake: yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari, pamoja na wachungaji wa kundi lake? Yuko wapi yule aliyeweka Roho wake Mtakatifu katikati yao,
ISA 63:12 aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu kuwa katika mkono wa kuume wa Musa, aliyegawa maji ya bahari mbele yao, ili kujipatia jina milele,
ISA 63:13 aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi? Kama farasi katika nchi iliyo wazi, wao hawakujikwaa,
ISA 63:14 kama ng’ombe wanaoshuka bondeni, walipewa pumziko na Roho wa Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako ili kujipatia jina tukufu.
ISA 63:15 Tazama chini kutoka mbinguni ukaone kutoka kiti chako cha enzi kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu. Uko wapi wivu wako na uweza wako? Umetuzuilia wema wako na huruma zako.
ISA 63:16 Lakini wewe ni Baba yetu, ingawa Ibrahimu hatufahamu sisi wala Israeli hatutambui; wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe Baba yetu, Mkombozi wetu tangu zamani za kale ndilo jina lako.
ISA 63:17 Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini unatuacha twende mbali na njia zako, na kuifanya mioyo yetu migumu hata hatukukuheshimu? Rudi kwa ajili ya watumishi wako, yale makabila ambayo ni urithi wako.
ISA 63:18 Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki mahali pako patakatifu, lakini sasa adui zetu wamepakanyaga mahali patakatifu pako.
ISA 63:19 Sisi tumekuwa kama wale ambao hujawatawala kamwe, kama wale ambao hawajaitwa kwa jina lako.
ISA 64:1 Laiti ungepasua mbingu na kushuka chini, ili milima itetemeke mbele zako!
ISA 64:2 Kama vile moto unavyoteketeza vijiti na kusababisha maji kuchemka, shuka ukafanye jina lako lijulikane kwa adui zako, na kusababisha mataifa yatetemeke mbele zako!
ISA 64:3 Kwa maana ulipofanya mambo ya kutisha ambayo hatukuyatazamia, ulishuka, nayo milima ikatetemeka mbele zako.
ISA 64:4 Tangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia, hakuna sikio lililotambua, hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe, anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao.
ISA 64:5 Uliwasaidia watu wale watendao yaliyo haki kwa furaha, wale wazikumbukao njia zako. Lakini wakati tulipoendelea kutenda dhambi kinyume na njia zako, ulikasirika. Tutawezaje basi kuokolewa?
ISA 64:6 Sisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi, nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu; sisi sote tunasinyaa kama jani, na kama upepo maovu yetu hutupeperusha.
ISA 64:7 Hakuna yeyote anayeliitia jina lako wala anayejitahidi kukushika, kwa kuwa umetuficha uso wako na kutuacha tudhoofike kwa sababu ya dhambi zetu.
ISA 64:8 Lakini, Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Baba yetu. Sisi ni udongo, na wewe ndiwe mfinyanzi; sisi sote tu kazi ya mkono wako.
ISA 64:9 Ee Mwenyezi Mungu, usikasirike kupita kiasi, usizikumbuke dhambi zetu milele. Ee Bwana, utuangalie, twakuomba, kwa kuwa sisi sote tu watu wako.
ISA 64:10 Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa; hata Sayuni ni jangwa, Yerusalemu ni ukiwa.
ISA 64:11 Hekalu letu takatifu na tukufu, ambako baba zetu walikusifu wewe, limechomwa kwa moto, navyo vitu vyote tulivyovithamini vimeharibika.
ISA 64:12 Ee Mwenyezi Mungu, baada ya haya yote, utajizuia? Je, utanyamaza, na kutuadhibu kupita kiasi?
ISA 65:1 “Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia. Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu, nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’
ISA 65:2 Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu kwa watu wakaidi, wanaoenda katika njia ambazo si nzuri, wafuatao mawazo yao wenyewe:
ISA 65:3 taifa ambalo daima hunikasirisha machoni pangu, wakitoa dhabihu katika bustani na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali;
ISA 65:4 watu waketio katika makaburi na kukesha mahali pa siri, walao nyama za nguruwe, nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi,
ISA 65:5 wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie, kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’ Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu, ni moto uwakao mchana kutwa.
ISA 65:6 “Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu: sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu; nitalipiza mapajani mwao:
ISA 65:7 dhambi zenu na dhambi za baba zenu,” asema Mwenyezi Mungu. “Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima na kunichokoza mimi juu ya vilima, nitawapimia mapajani mwao malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.”
ISA 65:8 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana katika kishada cha zabibu, nao watu husema, ‘Usikiharibu, kwa kuwa bado kuna baraka ndani yake,’ hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu; sitawaangamiza wote.
ISA 65:9 Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo, na kutoka kwa Yuda watakaomiliki milima yangu, nao watu wangu wateule watairithi, nako huko wataishi watumishi wangu.
ISA 65:10 Sharoni itakuwa malisho kwa ajili ya makundi ya kondoo, na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia kwa makundi ya ng’ombe, kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta.
ISA 65:11 “Bali ninyi mnaomwacha Mwenyezi Mungu na kuusahau mlima wangu mtakatifu, ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati, na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa kwa ajili ya Ajali,
ISA 65:12 nitawaagiza mfe kwa upanga, nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa; kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika, nilisema lakini hamkusikiliza. Mlitenda maovu machoni pangu, nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”
ISA 65:13 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Watumishi wangu watakula, lakini ninyi mtaona njaa; watumishi wangu watakunywa lakini ninyi mtaona kiu; watumishi wangu watafurahi, lakini ninyi mtaona haya.
ISA 65:14 Watumishi wangu wataimba kwa furaha ya mioyo yao, lakini ninyi mtalia kutokana na uchungu wa moyoni, na kupiga yowe kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.
ISA 65:15 Mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa; Bwana Mungu Mwenyezi atawaua ninyi, lakini watumishi wake atawapa jina jingine.
ISA 65:16 Yeye aombaye baraka katika nchi atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli; yeye aapaye katika nchi ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika na kufichwa kutoka machoni pangu.
ISA 65:17 “Tazama, nitaumba mbingu mpya na dunia mpya. Mambo ya zamani hayatakumbukwa, wala hayatakuja akilini.
ISA 65:18 Lakini furahini na kushangilia daima katika hivi nitakavyoumba, kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza, nao watu wake wawe furaha.
ISA 65:19 Nami nitaifurahia Yerusalemu na kuwafurahia watu wangu; sauti ya maombolezo na ya kilio haitasikika humo tena.
ISA 65:20 “Kamwe hapatakuwa tena ndani yake mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu, au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake. Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja atahesabiwa kwamba ni kijana tu, yeye ambaye hatafika miaka mia moja, atahesabiwa kuwa amelaaniwa.
ISA 65:21 Watajenga nyumba na kuishi ndani yake; watapanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake.
ISA 65:22 Hawatajenga nyumba, nao watu wengine waishi ndani yake, au kupanda mazao na wengine wale. Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti, ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi kazi za mikono yao.
ISA 65:23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga, kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa na Mwenyezi Mungu, wao na wazao wao pamoja nao.
ISA 65:24 Kabla hawajaita, nitajibu, nao wakiwa katika kunena, nitasikia.
ISA 65:25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, naye simba atakula nyasi kama maksai, lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 66:1 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, “Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Iko wapi nyumba mtakayoijenga kwa ajili yangu? Mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?
ISA 66:2 Je, mkono wangu haukuumba vitu hivi vyote, hivyo vikapata kuwepo?” asema Mwenyezi Mungu. “Mtu huyu ndiye ninayemthamini: yeye ambaye ni mnyenyekevu na mwenye roho yenye toba, atetemekaye asikiapo neno langu.
ISA 66:3 Lakini yeyote atoaye dhabihu ya fahali ni kama yeye auaye mtu, na yeyote atoaye sadaka ya mwana-kondoo, ni kama yule avunjaye shingo ya mbwa. Yeyote atoaye sadaka ya nafaka, ni kama yule aletaye damu ya nguruwe, na yeyote afukizaye uvumba wa kumbukumbu, ni kama yule aabuduye sanamu. Wamejichagulia njia zao wenyewe, nazo nafsi zao zinafurahia machukizo yao.
ISA 66:4 Hivyo, mimi pia nitawachagulia mapigo makali, nami nitaleta juu yao kile wanachokiogopa. Kwa maana nilipoita, hakuna yeyote aliyejibu, niliposema, hakuna yeyote aliyesikiliza. Walifanya maovu machoni pangu na kuchagua lile linalonichukiza.”
ISA 66:5 Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, ninyi mtetemekao kwa neno lake: “Ndugu zenu wanaowachukia ninyi na kuwatenga ninyi kwa sababu ya Jina langu, wamesema, ‘Mwenyezi Mungu na atukuzwe, ili tupate kuona furaha yenu!’ Hata sasa wataaibika.
ISA 66:6 Sikieni hizo ghasia kutoka mjini, sikieni hizo kelele kutoka hekaluni! Ni sauti ya Mwenyezi Mungu ikiwalipa adui zake yote wanayostahili.
ISA 66:7 “Kabla hajasikia uchungu, alizaa; kabla hajapata maumivu, alizaa mtoto wa kiume.
ISA 66:8 Ni nani amepata kusikia jambo kama hili? Ni nani amepata kuona mambo kama haya? Je, nchi yaweza kuzaliwa kwa siku moja, au taifa laweza kutokea mara moja? Mara Sayuni alipoona uchungu, alizaa watoto wake.
ISA 66:9 Je, nilete mwana hadi wakati wa kuzaliwa na nisizalishe?” asema Mwenyezi Mungu. “Je, nifunge tumbo la uzazi wakati mimi ndiye nizalishaye?” asema Mungu wako.
ISA 66:10 “Shangilieni pamoja na Yerusalemu na mfurahi kwa ajili yake, ninyi nyote mnaompenda, shangilieni kwa nguvu pamoja naye, ninyi nyote mnaoomboleza juu yake.
ISA 66:11 Kwa kuwa mtanyonya na kutosheka katika faraja ya matiti yake; mtakunywa sana, na kuufurahia wingi wa mafuriko ya ustawi wake.”
ISA 66:12 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Nitamwongezea amani kama mto, nao utajiri wa mataifa kama kijito kifurikacho; utanyonya na kuchukuliwa mikononi mwake, na kubembelezwa magotini pake.
ISA 66:13 Kama mama anavyomfariji mtoto wake, ndivyo nitakavyokufariji wewe, nawe utafarijiwa huko Yerusalemu.”
ISA 66:14 Mtakapoona jambo hili, mioyo yenu itashangilia, nanyi mtastawi kama majani; mkono wa Mwenyezi Mungu utajulikana kwa watumishi wake, bali ghadhabu yake kali itaoneshwa kwa adui zake.
ISA 66:15 Tazama, Mwenyezi Mungu anakuja na moto, magari yake ya vita ni kama upepo wa kisulisuli, atateremsha hasira yake kwa ghadhabu kali, na karipio lake pamoja na miali ya moto.
ISA 66:16 Kwa maana kwa moto na kwa upanga wake Mwenyezi Mungu atatekeleza hukumu juu ya watu wote, nao wengi watakuwa ni wale waliouawa na Mwenyezi Mungu.
ISA 66:17 “Watu wote wanaojiweka wakfu na kujitakasa wenyewe ili kwenda bustanini, wakimfuata aliye katikati ya wale wanaokula nyama za nguruwe na panya pamoja na vitu vingine vilivyo machukizo, watafikia mwisho wao pamoja,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 66:18 “Nami, kwa sababu ya matendo yao na mawazo yao, niko karibu kuja na kukusanya mataifa yote na lugha zote, nao watakuja na kuuona utukufu wangu.
ISA 66:19 “Nitaweka ishara kati yao, nami nitapeleka baadhi ya hao walionusurika kwa mataifa, hadi Tarshishi, kwa Puli na Waludi (wanaojulikana kama wapiga upinde), kwa Tubali na Uyunani, hadi visiwa vya mbali ambavyo havijasikia kuhusu sifa zangu au kuuona utukufu wangu. Watatangaza utukufu wangu miongoni mwa mataifa.
ISA 66:20 Nao watawaleta ndugu zenu wote, kutoka mataifa yote, hadi mlima wangu mtakatifu huko Yerusalemu kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, juu ya farasi, katika magari ya vita na magari makubwa, juu ya nyumbu na ngamia,” asema Mwenyezi Mungu. “Watawaleta, kama Waisraeli waletavyo sadaka zao za nafaka, katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, katika vyombo vilivyotakaswa.
ISA 66:21 Nami nitachagua baadhi yao pia wawe makuhani na Walawi,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 66:22 “Kama vile mbingu mpya na nchi mpya ninazozifanya zitakavyodumu mbele zangu,” asema Mwenyezi Mungu, “ndivyo jina lenu na wazao wenu watakavyodumu.
ISA 66:23 Kutoka Mwezi Mpya hata mwingine, na kutoka Sabato hadi nyingine, wanadamu wote watakuja na kusujudu mbele zangu,” asema Mwenyezi Mungu.
ISA 66:24 “Nao watatoka nje na kuona maiti za wale walioniasi mimi. Funza wao hawatakufa, wala moto wao hautazimika, nao watakuwa kitu cha kuchukiza sana kwa wanadamu wote.”
JER 1:1 Maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani katika mji wa Anathothi, katika nchi ya Benyamini.
JER 1:2 Neno la Mwenyezi Mungu lilimjia katika mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda,
JER 1:3 na pia wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, hadi mwezi wa tano wa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati watu wa Yerusalemu walipopelekwa uhamishoni.
JER 1:4 Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia, kusema,
JER 1:5 “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua; kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum; nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”
JER 1:6 Nami nikasema, “Aa, Bwana Mungu Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”
JER 1:7 Lakini Mwenyezi Mungu akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza.
JER 1:8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 1:9 Kisha Mwenyezi Mungu akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako.
JER 1:10 Tazama, leo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kung’oa na kubomoa, kuharibu na kuangamiza, kujenga na kupanda.”
JER 1:11 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema, “Je, Yeremia unaona nini?” Nami nikajibu, “Naona tawi la mti wa mlozi.”
JER 1:12 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Umeona vyema kwa maana ninaliangalia neno langu ili kuona kwamba limetimizwa.”
JER 1:13 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia tena, “Unaona nini?” Nikajibu, “Naona chungu kinachochemka, kikiwa kimeinama kutoka kaskazini.”
JER 1:14 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Kutoka kaskazini maafa yatamwagwa kwa wote wanaoishi katika nchi.
JER 1:15 Nitawaita watu wote wa falme za kaskazini,” asema Mwenyezi Mungu. “Wafalme wao watakuja na kuweka viti vyao vya utawala katika maingilio ya malango ya Yerusalemu, watakuja dhidi ya kuta zake zote zinazouzunguka, na dhidi ya miji yote ya Yuda.
JER 1:16 Nitatoa hukumu zangu kwa watu wangu kwa sababu ya uovu wao wa kuniacha mimi, kwa kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kuabudu kazi za mikono yao.
JER 1:17 “Jiandae! Simama useme chochote nitakachokuamuru. Usiwaogope, la sivyo nitakufanya uwaogope wao.
JER 1:18 Leo nimekufanya mji wenye ngome, nguzo ya chuma, na ukuta wa shaba ili kusimama dhidi ya nchi yote: dhidi ya wafalme wa Yuda, maafisa wake, makuhani wake na watu wa nchi hiyo.
JER 1:19 Watapigana nawe lakini hawatakushinda, kwa kuwa niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 2:1 Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia kusema,
JER 2:2 “Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu: “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako, jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi na kunifuata katika jangwa lile lote, katika nchi isiyopandwa mbegu.
JER 2:3 Israeli alikuwa mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu, kama malimbuko ya kwanza ya mavuno yake; wote waliomwangamiza walihesabiwa kuwa na hatia, nayo maafa yaliwakumba,’ ” asema Mwenyezi Mungu.
JER 2:4 Sikia neno la Mwenyezi Mungu, ee nyumba ya Yakobo, nanyi nyote jamaa za nyumba ya Israeli.
JER 2:5 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu, hata wakatangatanga mbali nami hivyo? Walifuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili.
JER 2:6 Hawakuuliza, ‘Yuko wapi Mwenyezi Mungu, aliyetupandisha kutoka Misri na kutuongoza kupitia nyika kame, kupitia nchi ya majangwa na mabonde, nchi ya ukame na giza, nchi ambayo hakuna mtu asafiriye ndani yake wala hakuna mtu aishiye humo?’
JER 2:7 Niliwaleta katika nchi yenye wingi wa vitu ili mpate kula matunda yake na utajiri wa mazao yake. Lakini mkaja na kuinajisi nchi yangu, na kuufanya urithi wangu chukizo.
JER 2:8 Makuhani hawakuuliza, ‘Yuko wapi Mwenyezi Mungu?’ Wale wanaoshughulikia sheria hawakunijua mimi; viongozi waliasi dhidi yangu. Manabii walitabiri kwa jina la Baali, wakifuata sanamu batili.
JER 2:9 “Kwa hiyo naleta tena mashtaka dhidi yako,” asema Mwenyezi Mungu. “Nami nitaleta mashtaka dhidi ya watoto wa watoto wako.
JER 2:10 Vuka, nenda ng’ambo hadi pwani ya Kitimu nawe uangalie, tuma watu waende Kedari, wachunguze kwa makini, uone kama kumeshawahi kuwa kitu kama hiki.
JER 2:11 Je, taifa limebadili miungu yake wakati wowote? (Hata ingawa hao si miungu kamwe.) Lakini watu wangu wamebadili Utukufu wao kwa sanamu batili.
JER 2:12 Shangaeni katika hili, ee mbingu, nanyi tetemekeni kwa hofu kuu,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 2:13 “Watu wangu wametenda dhambi mbili: Wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji yaliyo hai, nao wamejichimbia visima vyao wenyewe, visima vilivyobomoka, visivyoweza kuhifadhi maji.
JER 2:14 Je, Israeli ni mtumishi, yaani mtumwa kwa kuzaliwa? Kwa nini basi amekuwa mateka?
JER 2:15 Simba wamenguruma; wamemngurumia. Wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketezwa, nayo imeachwa haina watu.
JER 2:16 Pia watu wa Memfisi na Tapanesi wamekupiga fuvu la kichwa.
JER 2:17 Je, hukujiletea hili wewe mwenyewe kwa kumwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wako alipowaongoza njiani?
JER 2:18 Sasa kwa nini uende Misri kunywa maji ya Shihori? Nawe kwa nini kwenda Ashuru kunywa maji ya Mto?
JER 2:19 Uovu wako utakuadhibu; kurudi nyuma kwako kutakukemea. Basi kumbuka, utambue jinsi lilivyo jambo ovu na chungu kwako unapomwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kutokuwa na hofu yangu,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
JER 2:20 “Zamani nilivunja nira yako na kukatilia mbali vifungo vyako; ukasema, ‘Sitakutumikia!’ Hakika, kwenye kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda matawi yake ulijilaza kama kahaba.
JER 2:21 Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana, mkamilifu na wa mbegu nzuri. Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami, ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu?
JER 2:22 Hata ujisafishe kwa magadi na kutumia sabuni nyingi, bado doa la hatia yako liko mbele zangu,” asema Bwana Mungu Mwenyezi.
JER 2:23 “Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi, sijawafuata Mabaali’? Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni; fikiri uliyoyafanya. Wewe ni ngamia jike mwenye mbio ukikimbia hapa na pale,
JER 2:24 punda-mwitu aliyezoea jangwa, anayenusa upepo katika tamaa yake kubwa: wakati wake wa kuhitaji mbegu ni nani awezaye kumzuia? Madume yoyote yanayomfuatilia hayana haja ya kujichosha; wakati wa kupandwa kwake yatampata tu.
JER 2:25 Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu, na koo lako liwe limekauka. Lakini ulisema, ‘Haina maana! Ninaipenda miungu ya kigeni, nami lazima niifuatie.’
JER 2:26 “Kama vile mwizi anavyoaibika akikamatwa, hivyo ndivyo nyumba ya Israeli inavyoaibishwa: wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao.
JER 2:27 Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’ nalo jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’ Wamenipa visogo vyao wala hawakunigeuzia nyuso zao; lakini wakiwa katika taabu, wanasema, ‘Njoo utuokoe!’
JER 2:28 Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea? Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa wakati mko katika taabu! Kwa maana mna miungu mingi kama mlivyo na miji, ee Yuda.
JER 2:29 “Kwa nini mnaleta mashtaka dhidi yangu? Ninyi nyote mmeniasi,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 2:30 “Nimeadhibu watu wako bure tu, hawakujirekebisha. Upanga wako umewala manabii wako kama simba mwenye njaa.
JER 2:31 “Enyi wa kizazi hiki, tafakarini neno la Mwenyezi Mungu: “Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli au nchi ya giza nene? Kwa nini watu wangu wanasema, ‘Sisi tuko huru kuzurura, hatutarudi kwako tena’?
JER 2:32 Je, mwanamwali husahau vito vyake, au bibi arusi mapambo yake ya arusi? Lakini watu wangu wamenisahau mimi, tena kwa siku zisizo na hesabu.
JER 2:33 Je, wewe una ustadi kiasi gani katika kufuatia mapenzi! Hata wale wanawake wabaya kuliko wote wanaweza kujifunza kutokana na njia zako.
JER 2:34 Katika nguo zako watu huona damu ya uhai ya maskini wasio na hatia, ingawa hukuwakamata wakivunja nyumba. Lakini katika haya yote
JER 2:35 unasema, ‘Sina hatia; Mungu hajanikasirikia.’ Lakini nitakuhukumu kwa sababu unasema, ‘Mimi sijatenda dhambi.’
JER 2:36 Kwa nini unatangatanga sana, ukibadili njia zako? Utakatishwa tamaa na Misri kama ulivyokatishwa na Ashuru.
JER 2:37 Pia utaondoka mahali hapo ukiwa umeweka mikono kichwani, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewakataa wale unaowatumainia; hutasaidiwa nao.
JER 3:1 “Kama mtu akimpa talaka mkewe, naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine, je, huyo mume aweza kumrudia tena? Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa? Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi: Je, sasa utanirudia tena?” asema Mwenyezi Mungu.
JER 3:2 “Inua macho utazame miinuko iliyo kame na uone. Je, pana mahali ambapo hawajalala nawe? Uliketi kando ya barabara ukiwasubiri wapenzi, ukakaa kama mtu anayehamahama jangwani. Umeinajisi nchi kwa ukahaba wako na uovu wako.
JER 3:3 Kwa hiyo mvua imezuiliwa, nazo mvua za vuli hazikunyesha. Hata hivyo, una uso usio na haya kama wa kahaba; unakataa kutahayari kwa aibu.
JER 3:4 Je, wewe hujaniita hivi punde tu: ‘Baba yangu, rafiki yangu tangu ujana wangu,
JER 3:5 je, utakasirika siku zote? Je, ghadhabu yako itaendelea milele?’ Hivi ndivyo unavyozungumza, lakini unafanya maovu yote uwezayo.”
JER 3:6 Wakati wa utawala wa Mfalme Yosia, Mwenyezi Mungu aliniambia, “Je, umeona yale Israeli asiye mwaminifu ameyatenda? Amepanda juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti uliotanda, na amefanya uzinzi huko.
JER 3:7 Mimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya haya yote angenirudia; lakini hakurudi, na dada yake Yuda mdanganyifu aliona hili.
JER 3:8 Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka, na kumfukuza kwa sababu ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake mdanganyifu hakuogopa. Yeye pia alitoka na kufanya uzinzi.
JER 3:9 Kwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake, Yuda aliinajisi nchi kwa kuzini na mawe na miti.
JER 3:10 Pamoja na hayo yote, Yuda dada yake mdanganyifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 3:11 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda mdanganyifu.
JER 3:12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini: “ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana, kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘Sitashika hasira yangu milele.
JER 3:13 Ungama dhambi zako tu: kwamba umemwasi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni chini ya kila mti unaotanda, nawe hukunitii mimi,’ ” asema Mwenyezi Mungu.
JER 3:14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka mji, na wawili kutoka ukoo, nami nitawaleta Sayuni.
JER 3:15 Kisha nitawapeni wachungaji wanaoupendeza moyo wangu, ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu.
JER 3:16 Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena, ‘Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu,’ ” asema Mwenyezi Mungu. “Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine.
JER 3:17 Wakati huo, wataita Yerusalemu kuwa Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu, nayo mataifa yote watakusanyika Yerusalemu kuliheshimu jina la Mwenyezi Mungu. Hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao miovu.
JER 3:18 Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaungana na nyumba ya Israeli, wao kwa pamoja watakuja kutoka nchi ya kaskazini hadi nchi niliyowapa baba zenu kama urithi.
JER 3:19 “Mimi mwenyewe nilisema, “ ‘Tazama jinsi nitakavyowatunza kwa furaha kama wana na kuwapa nchi nzuri, urithi ulio mzuri kuliko wa taifa jingine lolote.’ Nilidhani mngeniita ‘Baba,’ na msingegeuka, mkaacha kunifuata.
JER 3:20 Lakini kama mwanamke asiye mwaminifu kwa mumewe, vivyo hivyo mmekosa uaminifu kwangu, ee nyumba ya Israeli,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 3:21 Kilio kinasikika juu ya miinuko iliyo kame, kulia na kuomboleza kwa watu wa Israeli, kwa sababu wamepotoka katika njia zao na wamemsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
JER 3:22 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, nami nitawaponya ukengeufu wenu.” “Naam, tutakuja kwako, kwa maana wewe ni Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
JER 3:23 Hakika zile ghasia za kuabudu sanamu kwenye vilima na milimani ni udanganyifu; hakika katika Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, uko wokovu wa Israeli.
JER 3:24 Tangu ujana wetu miungu ya aibu imeyala matunda ya kazi za baba zetu: makundi yao ya kondoo na ng’ombe, wana wao wa kiume na wa kike.
JER 3:25 Sisi na tulale chini katika aibu yetu, na fedheha yetu itufunike. Tumetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, sisi na mababa zetu; tangu ujana wetu hadi leo hatukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
JER 4:1 “Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli, nirudie mimi,” asema Mwenyezi Mungu. “Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu na usiendelee kutangatanga,
JER 4:2 ikiwa utaapa katika kweli, kwa haki na kwa unyofu, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo,’ ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye, na ndani yake watajitukuza.”
JER 4:3 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu: “Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu, wala msipande katikati ya miiba.
JER 4:4 Jitahirini katika Mwenyezi Mungu, tahirini mioyo yenu, enyi wanaume wa Yuda na watu wa Yerusalemu, la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu na kuwaka kama moto kwa sababu ya uovu mliotenda, ikiwaka pasipo wa kuizima.
JER 4:5 “Tangaza katika Yuda na upige mbiu katika Yerusalemu, useme: ‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’ Piga kelele na kusema: ‘Kusanyikeni pamoja! Tukimbilie katika miji yenye ngome!’
JER 4:6 Inueni ishara ili kwenda Sayuni! Kimbilieni usalama pasipo kuchelewa! Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini, maangamizi ya kutisha.”
JER 4:7 Simba ametoka nje ya pango lake, mwangamizi wa mataifa amejipanga. Ametoka mahali pake ili aangamize nchi yenu. Miji yenu itakuwa magofu pasipo mtu wa kuishi humo.
JER 4:8 Hivyo vaeni magunia, ombolezeni na kulia kwa huzuni, kwa kuwa hasira kali ya Mwenyezi Mungu haijaondolewa kwetu.
JER 4:9 “Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu “mfalme na maafisa watakata tamaa, makuhani watafadhaika, na manabii watashangazwa mno.”
JER 4:10 Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mungu Mwenyezi, hakika umewadanganya watu hawa na Yerusalemu kwa kusema, ‘Mtakuwa na amani,’ wakati upanga uko kooni!”
JER 4:11 Wakati huo watu hawa na Yerusalemu wataambiwa, “Upepo wa moto kutoka miinuko iliyo kame jangwani unavuma kuelekea kwa watu wangu, lakini sio upepo wa kupepeta na kutakasa;
JER 4:12 upepo wenye nguvu sana kuliko wa kupepeta na kutakasa utakuja kwa amri yangu. Sasa natangaza hukumu zangu dhidi yao.”
JER 4:13 Tazama! Anakuja kama mawingu, magari yake ya vita yanakuja kama upepo wa kisulisuli, farasi wake wana mbio kuliko tai. Ole wetu! Tunaangamia!
JER 4:14 Ee Yerusalemu, usafishe uovu kutoka moyoni mwako, uokolewe. Utaendelea kuficha mawazo yako potovu hadi lini?
JER 4:15 Sauti inatangaza kutoka Dani, ikipiga mbiu ya maafa kutoka vilima vya Efraimu.
JER 4:16 “Waambie mataifa jambo hili, piga mbiu hii dhidi ya Yerusalemu: ‘Jeshi la kuzingira linakuja kutoka nchi ya mbali, likipiga kelele za vita dhidi ya miji ya Yuda.
JER 4:17 Wamemzunguka kama watu walindao shamba, kwa sababu amefanya uasi dhidi yangu,’ ” asema Mwenyezi Mungu.
JER 4:18 “Mwenendo wako na matendo yako mwenyewe vimeleta haya juu yako. Hii ndiyo adhabu yako. Tazama jinsi ilivyo chungu! Tazama jinsi inavyochoma moyo!”
JER 4:19 Ee mtima wangu, mtima wangu! Ninagaagaa kwa maumivu. Ee maumivu makuu ya moyo wangu! Moyo wangu umefadhaika ndani yangu, siwezi kunyamaza, kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta; nimesikia kelele za vita.
JER 4:20 Maafa baada ya maafa, nchi yote imekuwa magofu. Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa, makazi yangu kwa muda mfupi.
JER 4:21 Hata lini nitaendelea kuona bendera ya vita na kusikia sauti za tarumbeta?
JER 4:22 “Watu wangu ni wapumbavu, hawanijui mimi. Ni watoto wasio na akili, hawana ufahamu. Ni hodari kutenda mabaya, hawajui kutenda yaliyo mema.”
JER 4:23 Niliitazama dunia, nayo haikuwa na umbo tena ni tupu; niliziangalia mbingu, mianga ilikuwa imetoweka.
JER 4:24 Niliitazama milima, nayo ilikuwa ikitetemeka, vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.
JER 4:25 Nilitazama, wala hapakuwa na watu; kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.
JER 4:26 Nilitazama, nayo nchi iliyokuwa imestawi vizuri imekuwa jangwa, miji yake yote ilikuwa magofu mbele za Mwenyezi Mungu, mbele ya hasira yake kali.
JER 4:27 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “Nchi yote itaharibiwa, ingawa sitaiangamiza kabisa.
JER 4:28 Kwa hiyo dunia itaomboleza na mbingu zilizo juu zitakuwa giza, kwa sababu nimesema nami sitarudi nyuma, nimeamua na wala sitageuka.”
JER 4:29 Kwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde kila mji unakimbia. Baadhi wanakimbilia vichakani, baadhi wanapanda juu ya miamba. Miji yote imeachwa, hakuna aishiye ndani yake.
JER 4:30 Unafanya nini, ewe uliyeharibiwa? Kwa nini unajivika vazi jekundu na kuvaa vito vya dhahabu? Kwa nini unapaka macho yako wanja? Unajipamba bure. Wapenzi wako wanakudharau, wanautafuta uhai wako.
JER 4:31 Nasikia kilio kama cha mwanamke katika uchungu wa kuzaa, kilio cha uchungu kama cha anayemzaa mtoto wake wa kwanza: kilio cha Binti Sayuni akitweta ili aweze kupumua, akiinua mikono yake, akisema, “Ole wangu! Ninazimia; maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”
JER 5:1 “Pandeni na kushuka katika mitaa ya Yerusalemu, tazameni pande zote na mtafakari, tafuteni katika viwanja vyake. Kama mtaweza kumpata hata mtu mmoja tu atendaye kwa uaminifu na kutafuta kweli, nitausamehe mji huu.
JER 5:2 Ingawa wanasema, ‘Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo,’ bado wanaapa kwa uongo.”
JER 5:3 Ee Mwenyezi Mungu, je, macho yako hayaitafuti kweli? Uliwapiga, lakini hawakusikia maumivu, uliwapondaponda, lakini walikataa maonyo. Walifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko jiwe nao walikataa kutubu.
JER 5:4 Ndipo nikasema, “Hawa ni maskini tu; wao ni wapumbavu, kwa maana hawaijui njia ya Mwenyezi Mungu, sheria ya Mungu wao.
JER 5:5 Kwa hiyo nitaenda kwa wakuu na kuzungumza nao, hakika wao wanaijua njia ya Mwenyezi Mungu, sheria ya Mungu wao.” Lakini kwa nia moja nao pia walikuwa wameivunja nira na kuvivunja vifungo.
JER 5:6 Kwa hiyo simba wa mwituni atawashambulia, mbwa-mwitu wa jangwani atawaangamiza, chui atawavizia karibu na miji yao, ili kumrarua vipande vipande yeyote atakayethubutu kutoka nje, kwa maana uasi wao ni makubwa, na kukengeuka kwao kumekuwa ni kwingi.
JER 5:7 “Kwa nini niwasamehe? Watoto wenu wameniacha kwa kuapa kwa miungu batili. Niliwapatia mahitaji yao yote, lakini bado wamefanya uzinzi na kusongamana katika nyumba za makahaba.
JER 5:8 Wamelishwa vizuri, kama farasi dume wenye tamaa nyingi, kila mmoja akimlilia mke wa mwanaume mwingine.
JER 5:9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?” asema Mwenyezi Mungu. “Je, nisijilipizie kisasi juu ya taifa kama hili?
JER 5:10 “Piteni katika mashamba yake ya mizabibu na kuyaharibu, lakini msiangamize kabisa. Pogoeni matawi yake, kwa kuwa watu hawa sio wa Mwenyezi Mungu.
JER 5:11 Nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda wamekuwa si waaminifu kwangu kabisa,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 5:12 Wamedanganya kuhusu Mwenyezi Mungu. Wamesema, “Yeye hatafanya jambo lolote! Hakuna dhara litakalotupata; kamwe hatutaona upanga wala njaa.
JER 5:13 Manabii ni upepo tu, wala neno halimo ndani yao; kwa hiyo hayo wayasemayo na yatendeke kwao.”
JER 5:14 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Kwa sababu watu hawa wamesema maneno haya, nitayafanya maneno yangu vinywani mwenu kuwa moto, na watu hawa wawe kuni zinazoliwa na huo moto.
JER 5:15 Ee nyumba ya Israeli,” asema Mwenyezi Mungu, “Ninaleta taifa toka mbali dhidi yako, taifa la kale na linaloendelea kudumu, taifa ambalo lugha yao huijui, wala msemo wao huwezi kuuelewa.
JER 5:16 Podo lao ni kama kaburi lililo wazi, wote ni mashujaa hodari.
JER 5:17 Watayaangamiza mazao yenu na chakula chenu, watawaangamiza wana wenu wa kiume na wa kike; watayaangamiza makundi yenu ya kondoo na ya ng’ombe, wataiangamiza mizabibu yenu na mitini yenu. Kwa upanga wataiangamiza miji yenye ngome mliyoitumainia.
JER 5:18 “Hata hivyo katika siku hizo, sitakuangamiza kabisa,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 5:19 “Nao watu watakapouliza, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ametufanyia mambo haya yote?’ utawaambia, ‘Kama mlivyoniacha mimi kwa kuitumikia miungu migeni katika nchi yenu wenyewe, ndivyo sasa mtakavyowatumikia wageni katika nchi ambayo si yenu.’
JER 5:20 “Itangazie nyumba ya Yakobo hili na ulipigie mbiu katika Yuda:
JER 5:21 Sikieni hili, enyi watu wapumbavu, msio na akili, mlio na macho lakini hamwoni, mlio na masikio lakini hamsikii:
JER 5:22 Je, haiwapasi kuniogopa mimi?” asema Mwenyezi Mungu. “Je, haiwapasi kutetemeka mbele zangu? Niliufanya mchanga kuwa mpaka wa bahari, kizuizi cha milele ambacho bahari haiwezi kuupita. Mawimbi yanaweza kuumuka, lakini hayawezi kuupita; yanaweza kunguruma, lakini hayawezi kuuvuka.
JER 5:23 Lakini watu hawa wana mioyo ya ukaidi na ya uasi, wamegeukia mbali na kwenda zao.
JER 5:24 Wao hawaambiani wenyewe, ‘Sisi na tumwogope Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anayetupatia mvua za masika na za vuli kwa majira yake, anayetuhakikishia majuma ya mavuno kwa utaratibu.’
JER 5:25 Matendo yenu mabaya yamezuia haya yote, dhambi zenu zimewazuia msipate mema.
JER 5:26 “Miongoni mwa watu wangu wamo walio waovu wanaovizia kama watu wanaotega ndege, na kama wale wanaoweka mitego kuwakamata watu.
JER 5:27 Kama vitundu vilivyojaa ndege, nyumba zao zimejaa udanganyifu; wamekuwa matajiri na wenye nguvu,
JER 5:28 wamenenepa na kunawiri. Matendo yao maovu hayana kikomo; hawatetei mashauri ya yatima wapate kushinda, hawatetei haki za maskini.
JER 5:29 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?” asema Mwenyezi Mungu. “Je, nisijilipizie kisasi juu ya taifa kama hili?
JER 5:30 “Jambo la kutisha na kushtusha limetokea katika nchi hii:
JER 5:31 Manabii wanatabiri uongo, makuhani wanatawala kwa mamlaka yao wenyewe, nao watu wangu wanapenda hivyo. Lakini mtafanya nini mwisho wake?
JER 6:1 “Kimbieni kwa usalama wenu, enyi watu wa Benyamini! Kimbieni kutoka Yerusalemu! Pigeni tarumbeta katika Tekoa! Inueni ishara juu ya Beth-Hakeremu! Kwa kuwa maafa yanaonekana yakitoka kaskazini, na uharibifu wa kutisha.
JER 6:2 Nitamwangamiza Binti Sayuni, aliye mzuri sana na mwororo.
JER 6:3 Wachungaji pamoja na makundi yao watakuja dhidi yake; watapiga mahema yao kumzunguka, kila mmoja akichunga kundi lake mwenyewe.”
JER 6:4 “Jiandaeni kwa vita dhidi yake! Inukeni tumshambulie mchana! Lakini, ole wetu, mchana unaisha, na vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.
JER 6:5 Kwa hiyo inukeni, tufanye mashambulizi usiku, na kuharibu ngome zake!”
JER 6:6 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Kateni miti mjenge boma kuzingira Yerusalemu. Mji huu ni lazima uadhibiwe; umejazwa na uonevu.
JER 6:7 Kama vile kisima kinavyomwaga maji yake, ndivyo anavyomwaga uovu wake. Ukatili na maangamizi vyasikika ndani yake, ugonjwa wake na majeraha yake viko mbele yangu daima.
JER 6:8 Pokea onyo, ee Yerusalemu, la sivyo nitageukia mbali nawe na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa, asiweze mtu kuishi ndani yake.”
JER 6:9 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli kwa uangalifu kama kwenye mzabibu; pitisha mkono wako kwenye matawi tena, kama yeye avunaye zabibu.”
JER 6:10 Niseme na nani na kumpa onyo? Ni nani atakayenisikiliza mimi? Masikio yao yameziba, kwa hiyo hawawezi kusikia. Neno la Mwenyezi Mungu ni chukizo kwao, hawalifurahii.
JER 6:11 Lakini nimejaa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, nami siwezi kuizuia. “Wamwagie watoto walio barabarani, na juu ya vijana wa kiume waliokusanyika; mume na mke watakumbwa pamoja ndani yake, hata nao wazee waliolemewa na miaka.
JER 6:12 Nyumba zao zitapewa watu wengine, pamoja na mashamba yao na wake zao, nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya wale wanaoishi katika nchi,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 6:13 “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata faida zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu.
JER 6:14 Wanafunga majeraha ya watu wangu bila uangalifu. Wanasema, ‘Amani, amani,’ wakati hakuna amani.
JER 6:15 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno? Hapana, hawana haya hata kidogo; hawajui hata kuona aibu. Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka, watashushwa chini nitakapowaadhibu,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 6:16 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “Simama kwenye njia panda utazame, ulizia mapito ya zamani, ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo, nanyi mtapata amani nafsini mwenu. Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita njia hiyo.’
JER 6:17 Niliweka walinzi juu yenu na kusema, ‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’ Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’
JER 6:18 Kwa hiyo sikilizeni, enyi mataifa, angalieni, enyi mashahidi, lile litakalowatokea.
JER 6:19 Sikia, ee nchi: Ninaleta maafa juu ya watu hawa, matunda ya mipango yao, kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu na wameikataa sheria yangu.
JER 6:20 Unanifaa nini uvumba kutoka Sheba, au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali? Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki, dhabihu zako hazinifurahishi mimi.”
JER 6:21 Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “Nitaweka vikwazo mbele ya watu hawa. Baba na wana wao watajikwaa juu yake, majirani na rafiki wataangamia.”
JER 6:22 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “Tazama, jeshi linakuja kutoka nchi ya kaskazini, taifa kubwa linaamshwa kutoka miisho ya dunia.
JER 6:23 Wamejifunga pinde na mkuki, ni wakatili na hawana huruma. Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma wanapoendesha farasi wao. Wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita ili kukushambulia, ee Binti Sayuni.”
JER 6:24 Tumesikia taarifa zao, nayo mikono yetu imelegea. Uchungu umetushika, maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
JER 6:25 Usitoke kwenda mashambani au kutembea barabarani, kwa kuwa adui ana upanga, na kuna vitisho kila upande.
JER 6:26 Enyi watu wangu, vaeni magunia mjivingirishe kwenye majivu, ombolezeni kwa kilio cha uchungu kama amliliaye mwana pekee, kwa maana ghafula mharibu atatujia.
JER 6:27 “Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma, nao watu wangu kama mawe yenye madini, ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao.
JER 6:28 Wote ni waasi sugu, wakienda huku na huko kusengenya. Wao ni shaba na chuma, wote wanatenda upotovu.
JER 6:29 Mivuo inavuma kwa nguvu, kinachoungua kwa huo moto ni risasi, lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure; waovu hawaondolewi.
JER 6:30 Wanaitwa fedha iliyokataliwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu amewakataa.”
JER 7:1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
JER 7:2 “Simama kwenye lango la nyumba ya Mwenyezi Mungu, na huko upige mbiu ya ujumbe huu: “ ‘Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi watu wote wa Yuda mliokuja kupitia malango haya ili kumwabudu Mwenyezi Mungu.
JER 7:3 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Tengenezeni njia zenu na matendo yenu, nami nitawaacha mkae mahali hapa.
JER 7:4 Msitumainie maneno ya udanganyifu na kusema, “Hili ni Hekalu la Mwenyezi Mungu, Hekalu la Mwenyezi Mungu, Hekalu la Mwenyezi Mungu!”
JER 7:5 Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu, mkatendeana haki kila mmoja na mwenzake,
JER 7:6 kama hamdhulumu mgeni, yatima wala mjane, na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama hamtafuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe,
JER 7:7 ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele.
JER 7:8 Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana.
JER 7:9 “ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua,
JER 7:10 kisha mje na kusimama mbele yangu katika nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu, mkisema, “Tuko salama.” Salama kwa kufanya mambo haya yote ya kuchukiza?
JER 7:11 Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! asema Mwenyezi Mungu.
JER 7:12 “ ‘Nendeni sasa mahali pangu palipokuwa huko Shilo, ambapo nilipafanya pa kwanza kuwa makao ya Jina langu, nanyi mwone lile nililopafanyia kwa ajili ya uovu wa watu wangu Israeli.
JER 7:13 Mlipokuwa mnafanya haya yote, asema Mwenyezi Mungu, nilisema nanyi tena na tena, lakini hamkusikiliza; niliwaita, lakini hamkujibu.
JER 7:14 Kwa hiyo, nililolifanyia Shilo, nitalifanya sasa kwa nyumba hii iitwayo kwa Jina langu, Hekalu mnalolitumainia, mahali nilipowapa ninyi na baba zenu.
JER 7:15 Nitawafukuza mbele yangu, kama nilivyowafanyia ndugu zenu, watu wa Efraimu.’
JER 7:16 “Kwa hiyo usiombe kwa ajili ya watu hawa, wala usinililie, na usifanye maombi kwa ajili yao; usinisihi, kwa sababu sitakusikiliza.
JER 7:17 Je, huyaoni hayo wanayoyatenda katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu?
JER 7:18 Watoto wanakusanya kuni, baba zao wanawasha moto, na wanawake wanakanda unga na kuoka mikate kwa ajili ya Malkia wa Mbinguni. Wanamimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine ili kunikasirisha.
JER 7:19 Lakini je, mimi ndiye wanayenikasirisha? asema Mwenyezi Mungu. Je, hawajiumizi wenyewe na kujiaibisha?
JER 7:20 “ ‘Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Bwana Mungu Mwenyezi: Hasira yangu na ghadhabu yangu vitamwagwa mahali hapa, juu ya mwanadamu na mnyama, juu ya miti ya shambani na juu ya matunda ya ardhini, nayo itaungua pasipo kuzimwa.
JER 7:21 “ ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Endeleeni, ongezeni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya dhabihu zenu nyingine, mle nyama hiyo wenyewe!
JER 7:22 Kwa kuwa nilipowaleta baba zenu kutoka Misri na kusema nao, sikuwapa amri kuhusu sadaka za kuteketezwa na dhabihu tu,
JER 7:23 lakini niliwapa amri hii nikisema: Nitiini mimi, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Nendeni katika njia zote ninazowaamuru ili mpate kufanikiwa.
JER 7:24 Lakini hawakusikiliza wala kujali. Badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Walirudi nyuma badala ya kusonga mbele.
JER 7:25 Tangu wakati ule baba zenu walipotoka Misri hadi sasa, siku baada ya siku, tena na tena nimewatumia watumishi wangu manabii.
JER 7:26 Lakini hawakunisikiliza wala hawakujali. Walikuwa na shingo ngumu na kufanya maovu kuliko baba zao.’
JER 7:27 “Utakapowaambia haya yote, hawatakusikiliza; utakapowaita, hawatajibu.
JER 7:28 Kwa hiyo waambie, ‘Hili ni taifa ambalo halimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wao, wala kukubali maonyo. Kweli imekufa, imetoweka midomoni mwao.
JER 7:29 Nyoeni nywele zenu na kuzitupa, ombolezeni katika miinuko iliyo kame, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekikataa na kukiacha kizazi hiki kilichomkasirisha.
JER 7:30 “ ‘Watu wa Yuda wamefanya maovu machoni pangu, asema Mwenyezi Mungu. Wameziweka sanamu zao za machukizo ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu, na wameitia unajisi.
JER 7:31 Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia sanamu pa Tofethi kwenye Bonde la Ben-Hinomu ili kuwateketeza watoto wao wa kiume na wa kike kwenye moto, kitu ambacho sikuamuru, wala hakikuingia akilini mwangu.
JER 7:32 Kwa hiyo mjihadhari, siku zinakuja, asema Mwenyezi Mungu, wakati watu watakapokuwa hawapaiti Tofethi au Bonde la Ben-Hinomu, lakini watapaita Bonde la Machinjo, kwa sababu watawazika wafu huko Tofethi hadi pasiwe tena nafasi.
JER 7:33 Ndipo mizoga ya watu hawa itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwa na yeyote wa kuwafukuza.
JER 7:34 Nitazikomesha sauti za shangwe na furaha, na sauti za bwana arusi na bibi arusi katikati ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa.
JER 8:1 “ ‘Wakati huo, asema Mwenyezi Mungu, mifupa ya wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, na mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka makaburi yao.
JER 8:2 Itawekwa wazi kwa jua, na mwezi, na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia, na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama kinyesi juu ya ardhi.
JER 8:3 Popote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.’
JER 8:4 “Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “ ‘Je, watu wanapoanguka hawainuki? Je, mtu anapopotea harudi?
JER 8:5 Kwa nini basi watu hawa waliasi? Kwa nini Yerusalemu wanaasi kila mara? Wanang’ang’ania udanganyifu na wanakataa kurudi.
JER 8:6 Nimewasikiliza kwa makini, lakini hawataki kusema lililo sawa. Hakuna anayetubu makosa yake akisema, “Nimefanya nini?” Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe kama farasi anayeenda vitani.
JER 8:7 Hata korongo aliye angani anayajua majira yake yaliyoamriwa, nao njiwa, mbayuwayu na koikoi hufuata majira yao ya kurudi. Lakini watu wangu hawajui Mwenyezi Mungu anachotaka kwao.
JER 8:8 “ ‘Mwawezaje kusema, “Sisi tuna busara kwa sababu tunayo Torati ya Mwenyezi Mungu,” wakati kwa hakika kalamu ya uongo ya waandishi imeandika kwa udanganyifu?
JER 8:9 Wenye hekima wataaibika, watafadhaika na kunaswa. Kwa kuwa wamelikataa neno la Mwenyezi Mungu, hiyo hekima waliyo nayo ni ya namna gani?
JER 8:10 Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao, na mashamba yao kwa wamiliki wengine. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu.
JER 8:11 Wanafunga majeraha ya watu wangu bila uangalifu. Wanasema, “Amani, amani,” wakati hakuna amani.
JER 8:12 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno? Hapana, hawana haya hata kidogo, hawajui hata kuona aibu. Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka, watashushwa chini watakapoadhibiwa, asema Mwenyezi Mungu.
JER 8:13 “ ‘Nitayaondoa mavuno yao, asema Mwenyezi Mungu. Hapatakuwa zabibu kwenye mzabibu. Hapatakuwa na tini kwenye mtini, na majani yake yatanyauka. Kile nilichowapa watanyang’anywa.’ ”
JER 8:14 Kwa nini tunaketi hapa? Kusanyikeni pamoja! Tukimbilie kwenye miji yenye ngome, tukaangamie huko! Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ametuhukumu kuangamia, na kutupatia maji yenye sumu tunywe, kwa sababu tumemtenda dhambi.
JER 8:15 Tulitegemea amani, lakini hakuna jema lililokuja, tulitegemea wakati wa kupona, lakini kulikuwa hofu tu.
JER 8:16 Mkoromo wa farasi wa adui umesikika kuanzia Dani, kwa mlio wa madume yao ya farasi, nchi yote inatetemeka. Wamekuja kuangamiza nchi na vyote vilivyomo, mji na wote wanaoishi ndani yake.
JER 8:17 “Tazama, nitatuma nyoka wenye sumu kali kati yenu, fira ambao hawawezi kulogwa, nao watawauma,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 8:18 Ee Mfariji wangu katika huzuni, moyo wangu umezimia ndani yangu.
JER 8:19 Sikia kilio cha watu wangu kutoka nchi ya mbali: “Je, Mwenyezi Mungu hayuko Sayuni? Je, Mfalme wake hayuko tena huko?” “Kwa nini wamenikasirisha kwa vinyago vyao, kwa sanamu zao za kigeni zisizofaa?”
JER 8:20 “Mavuno yamepita, kiangazi kimekwisha, nasi hatujaokolewa.”
JER 8:21 Kwa kuwa watu wangu wamepondwa, nami nimepondeka pia; ninaomboleza, nayo hofu kuu imenishika.
JER 8:22 Je, hakuna zeri ya kuponya katika Gileadi? Je, hakuna tabibu huko? Kwa nini basi hakuna uponyaji wa majeraha ya watu wangu?
JER 9:1 Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi! Ningelia usiku na mchana kwa kuuawa kwa watu wangu.
JER 9:2 Laiti ningekuwa na nyumba ya kukaa wasafiri jangwani, ningewaacha watu wangu na kwenda mbali nao, kwa kuwa wote ni wazinzi, kundi la watu wadanganyifu.
JER 9:3 “Huweka tayari ndimi zao kama upinde, ili kurusha uongo; wamekuwa na nguvu katika nchi lakini si katika ukweli. Wanatoka dhambi moja hadi nyingine, hawanitambui mimi,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 9:4 “Jihadhari na rafiki zako; usiwaamini ndugu zako. Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu, na kila rafiki ni msingiziaji.
JER 9:5 Rafiki humdanganya rafiki, hakuna yeyote asemaye kweli. Wamefundisha ndimi zao kudanganya, wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.
JER 9:6 Unakaa katikati ya udanganyifu; katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 9:7 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu, kwani ni nini kingine niwezacho kufanya kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?
JER 9:8 Ndimi zao ni mshale wenye sumu, hunena kwa udanganyifu. Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake, lakini moyoni mwake humtegea mtego.
JER 9:9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?” asema Mwenyezi Mungu. “Je, nisijilipizie kisasi kwa taifa kama hili?”
JER 9:10 Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani. Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo, milio ya ng’ombe haisikiki. Ndege wa angani wametoroka na wanyama wamekimbia.
JER 9:11 “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu, makao ya mbweha; nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, asiwepo atakayeishi humo.”
JER 9:12 Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na Mwenyezi Mungu awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?
JER 9:13 Mwenyezi Mungu akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu.
JER 9:14 Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama baba zao walivyowafundisha.”
JER 9:15 Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu.
JER 9:16 Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuyajua, nikiwafuata kwa upanga hadi niwaangamize kabisa.”
JER 9:17 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezaji waje, waite wale walio na ustadi kati yao.
JER 9:18 Nao waje upesi waomboleze juu yetu, hadi macho yetu yatiririke machozi na kope zetu zibubujike maji.
JER 9:19 Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni: ‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa! Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa! Ni lazima tuihame nchi yetu kwa sababu nyumba zetu zimekuwa magofu.’ ”
JER 9:20 Basi, enyi wanawake, sikieni neno la Mwenyezi Mungu; fungueni masikio yenu msikie maneno ya kinywa chake. Wafundisheni binti zenu kuomboleza; fundishaneni kila mmoja na mwenzake maombolezo.
JER 9:21 Mauti imeingia ndani kupitia madirishani, imeingia kwenye majumba yetu ya fahari; imewakatilia mbali watoto katika barabara na vijana wa kiume kutoka viwanja vya miji.
JER 9:22 Sema, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Mizoga ya watu italala kama kinyesi katika mashamba, kama malundo ya nafaka nyuma ya mvunaji, wala hakuna atakayeikusanya.’ ”
JER 9:23 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake, au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake, wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
JER 9:24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hii: kwamba ananifahamu na kunijua mimi, kwamba mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitendaye wema, hukumu na haki duniani, kwa kuwa napendezwa na haya,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 9:25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema Mwenyezi Mungu,
JER 9:26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”
JER 10:1 Sikieni lile Mwenyezi Mungu anasema nanyi, ee nyumba ya Israeli.
JER 10:2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Usijifunze njia za mataifa wala usitishwe na ishara katika anga, ingawa mataifa yanatishwa nazo.
JER 10:3 Kwa maana desturi za mataifa hazina maana, wanakata mti msituni, na fundi anauchonga kwa patasi.
JER 10:4 Wanauremba kwa fedha na dhahabu, wanaukaza kwa nyundo na misumari ili usitikisike.
JER 10:5 Sanamu zao ni kama kinyago kilichowekwa katika shamba la matango kutishia ndege, nazo haziwezi kuongea; na kwa kuwa haziwezi kutembea zinabebwa. Usiziogope. Haziwezi kudhuru wala kutenda lolote jema.”
JER 10:6 Hakuna aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu; wewe ni mkuu, jina lako ni lenye nguvu na uweza.
JER 10:7 Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe, Ee Mfalme wa mataifa? Hii ni stahili yako. Miongoni mwa watu wote wenye hekima katika mataifa na katika falme zao zote, hakuna aliye kama wewe.
JER 10:8 Wote hawana akili, tena ni wapumbavu; wanafundishwa na sanamu batili za miti.
JER 10:9 Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi na dhahabu kutoka Ufazi. Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani: vyote vikiwa vimetengenezwa na mafundi stadi.
JER 10:10 Lakini Mwenyezi Mungu ni Mungu wa kweli, yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele. Anapokasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
JER 10:11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia duniani na chini ya mbingu.’ ”
JER 10:12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake, akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake, na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
JER 10:13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma; huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia. Hupeleka miali ya radi pamoja na mvua, naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
JER 10:14 Kila mtu ni mjinga na hana maarifa; kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. Vinyago vyake ni vya udanganyifu; havina pumzi.
JER 10:15 Ni ubatili tu, vitu vya kufanyia mzaha; wakati wa hukumu yao, wataangamia.
JER 10:16 Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo, kwani ndiye Muumba wa vitu vyote, pamoja na Israeli, kabila la urithi wake: Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.
JER 10:17 Kusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii, enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.
JER 10:18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu wote wanaoishi katika nchi hii; nitawataabisha ili wapate kutekwa.”
JER 10:19 Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu! Jeraha langu ni kubwa! Lakini nilisema, “Kweli hii ni adhabu yangu, nami sharti niistahimili.”
JER 10:20 Hema langu limeangamizwa; kamba zake zote zimekatwa. Wana wangu wametekwa na hawapo tena; hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu wala wa kusimamisha kibanda changu.
JER 10:21 Wachungaji hawana akili wala hawamuulizi Mwenyezi Mungu, hivyo hawastawi na kundi lao lote la kondoo limetawanyika.
JER 10:22 Sikilizeni! Taarifa inakuja: ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini! Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa, na kuwa makao ya mbweha.
JER 10:23 Ninajua, Ee Mwenyezi Mungu, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe; hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.
JER 10:24 Unirudi, Ee Mwenyezi Mungu, lakini kwa kipimo cha haki: si katika hasira yako, usije ukaniangamiza.
JER 10:25 Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa wasiokujua wewe, juu ya mataifa wasioliitia jina lako. Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo; wamemwangamiza kabisa na kuiharibu nchi yake.
JER 11:1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
JER 11:2 “Sikia maneno ya agano hili, nawe uwaambie watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu.
JER 11:3 Waambie kwamba hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Amelaaniwa mtu ambaye hatayatii maneno ya agano hili,
JER 11:4 maneno niliyowaamuru baba zenu nilipowatoa katika nchi ya Misri, kutoka tanuru la kuyeyushia vyuma.’ Nilisema, ‘Nitiini mimi na mfanye kila kitu ninachowaamuru, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
JER 11:5 Kisha nitatimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi inayotiririka maziwa na asali,’ nchi ambayo mnaimiliki leo.” Nikajibu, “Amen, Mwenyezi Mungu.”
JER 11:6 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Tangaza maneno haya yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu: ‘Sikilizeni maneno ya agano hili na kuyafuata.
JER 11:7 Tangu wakati ule niliwapandisha baba zenu kutoka Misri hadi leo, niliwaonya tena na tena, nikisema, “Nitiini mimi.”
JER 11:8 Lakini hawakusikiliza wala kujali. Badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Hivyo nikaleta juu yao laana zote za agano nililokuwa nimewaamuru wao kulifuata, lakini hawakulishika.’ ”
JER 11:9 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Kuna fitina inayoendelea miongoni mwa watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu.
JER 11:10 Wamerudia dhambi za baba zao waliokataa kusikiliza maneno yangu. Wameifuata miungu mingine na kuitumikia. Nyumba zote mbili za Israeli na Yuda zimelivunja agano nililofanya na baba zao.
JER 11:11 Kwa hivyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Nitaleta juu yao maafa ambayo hawawezi kuyakimbia. Hata wakinililia, sitawasikiliza.
JER 11:12 Miji ya Yuda na watu wa Yerusalemu wataenda kuililia miungu ambayo wameifukizia uvumba, lakini haitawasaidia kamwe wakati maafa yatakapowapiga.
JER 11:13 Mnayo miungu mingi kama miji mliyo nayo, ee Yuda, nazo madhabahu mlizozijenga za kumfukizia uvumba huyo mungu wa aibu, Baali ni nyingi kama barabara za Yerusalemu.’
JER 11:14 “Wewe usiwaombee watu hawa wala kufanya maombezi yoyote au kunisihi kwa ajili yao, kwa sababu sitawasikiliza watakaponiita wakati wa taabu yao.
JER 11:15 “Mpendwa wangu anafanya nini hekaluni mwangu, anapofanya mashauri yake maovu na wengi? Je, nyama iliyowekwa wakfu yaweza kukuondolea uovu wako? Unashangilia unapojiingiza katika uovu wako.”
JER 11:16 Mwenyezi Mungu alikuita jina lako Mzeituni uliostawi, wenye matunda yakupendeza. Lakini kwa ngurumo ya mawimbi makuu atautia moto, nayo matawi yake yatavunjika.
JER 11:17 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliyekupanda, ametamka maafa juu yako, kwa sababu nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda mmefanya maovu na kunikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba.
JER 11:18 Kwa sababu Mwenyezi Mungu alinifunulia na kunionesha hila zao mbaya, na waliyokuwa wanayafanya niliyafahamu.
JER 11:19 Nilikuwa kama mwana-kondoo mpole aliyeongozwa machinjoni; mimi sikutambua kwamba walikuwa wamepanga njama dhidi yangu, wakisema, “Sisi na tuuangamize mti na matunda yake; nasi tumkatilie mbali kutoka nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.”
JER 11:20 Lakini, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, wewe uhukumuye kwa haki, uchunguzaye moyo na akili, acha nione ukiwalipiza wao kisasi, kwa maana kwako nimeweka shauri langu.
JER 11:21 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu watu wa Anathothi wanaotafuta uhai wako, wakisema, ‘Usitoe unabii kwa jina la Mwenyezi Mungu, la sivyo utakufa kwa mikono yetu’:
JER 11:22 kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nitawaadhibu. Vijana wao wa kiume watakufa kwa upanga, wana wao wa kiume na wa kike watakufa kwa njaa.
JER 11:23 Hayatabakizwa mabaki kwao kwa sababu nitaleta maafa kwa watu wa Anathothi katika mwaka wa kuadhibiwa kwao.’ ”
JER 12:1 Wewe daima u mwenye haki, Ee Mwenyezi Mungu, niletapo mashtaka mbele yako. Hata hivyo nitazungumza nawe kuhusu hukumu yako: Kwa nini njia ya waovu inafanikiwa? Kwa nini wasio waaminifu wote wanaishi salama?
JER 12:2 Umewapanda, nao wameota, wanakua na kuzaa matunda. Daima u midomoni mwao, lakini mbali na mioyo yao.
JER 12:3 Hata hivyo unanijua mimi, Ee Mwenyezi Mungu; unaniona na kuyachunguza mawazo yangu kukuhusu wewe. Wakokote kama kondoo wanaoenda kuchinjwa! Watenge kwa ajili ya siku ya kuchinjwa!
JER 12:4 Je, nchi itakaa katika hali ya kuomboleza hadi lini, na majani katika kila shamba kunyauka? Kwa sababu wale wanaoishi ndani yake ni waovu, wanyama na ndege wameangamia. Zaidi ya hayo, watu wanasema, “Mwenyezi Mungu hataona yatakayotupata sisi.”
JER 12:5 “Ikiwa umeshindana mbio na watu kwa mguu na wakakushinda, unawezaje kushindana na farasi? Ikiwa unajikwaa kwenye nchi ambayo ni salama, utawezaje kwenye vichaka kando ya Yordani?
JER 12:6 Ndugu zako na jamaa zako nao wamekusaliti, wameinua kilio kikubwa dhidi yako. Usiwaamini hata wakisema mema juu yako.
JER 12:7 “Nitaiacha nyumba yangu, nitupe urithi wangu; nitamtia yeye nimpendaye mikononi mwa adui zake.
JER 12:8 Urithi wangu umekuwa kwangu kama simba wa msituni. Nauchukia kwa kuwa unaningurumia.
JER 12:9 Je, urithi wangu haukuwa kama ndege wa mawindo wa madoadoa ambaye ndege wengine wawindao humzunguka na kumshambulia? Nenda ukawakusanye pamoja wanyama wote wa mwituni; walete ili wale.
JER 12:10 Wachungaji wengi wataliharibu shamba langu la mizabibu na kulikanyaga shamba langu; watalifanya shamba langu zuri kuwa jangwa la ukiwa.
JER 12:11 Litafanywa kuwa jangwa, lililokauka na kuachwa ukiwa mbele zangu; nchi yote itafanywa jangwa kwa sababu hakuna hata mmoja anayejali.
JER 12:12 Juu ya miinuko yote ilivyo kama jangwani waangamizi watavamia, kwa maana upanga wa Mwenyezi Mungu utawala, kuanzia ncha moja ya nchi hadi nyingine; hakuna hata mmoja atakayekuwa salama.
JER 12:13 Watapanda ngano lakini watavuna miiba; watajitaabisha lakini hawatafaidi chochote. Kwa hiyo beba aibu ya mavuno yako kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi Mungu.”
JER 12:14 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa habari ya majirani zangu wote wabaya wanaonyang’anya urithi ambao ninawapa watu wangu Israeli, nitawang’oa kutoka nchi zao, nami nitaing’oa nyumba ya Yuda kutoka katikati yao.
JER 12:15 Lakini baada ya kuwang’oa, nitawahurumia tena na kumrudisha kila mmoja wao kwenye urithi wake mwenyewe na kwenye nchi yake mwenyewe.
JER 12:16 Ikiwa watajifunza vyema njia za watu wangu na kuapa kwa Jina langu, wakisema, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo,’ hata kama wakati fulani walifundisha watu wangu kuapa kwa Baali, ndipo watafanywa imara katikati ya watu wangu.
JER 12:17 Lakini kama taifa lolote halitasikiliza na kutii, nitaling’oa kabisa na kuliangamiza,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 13:1 Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.”
JER 13:2 Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama Mwenyezi Mungu alivyoniagiza, nikajivika kiunoni.
JER 13:3 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kwa mara ya pili:
JER 13:4 “Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.”
JER 13:5 Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama Mwenyezi Mungu alivyoniamuru.
JER 13:6 Baada ya siku nyingi Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.”
JER 13:7 Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa.
JER 13:8 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia:
JER 13:9 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu.
JER 13:10 Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine wakiitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mshipi huu ambao haufai kabisa!
JER 13:11 Kwa maana kama vile mshipi ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyoifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’
JER 13:12 “Waambie: ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’
JER 13:13 Uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: nitawajaza ulevi wote wanaoishi katika nchi hii, pamoja na wafalme wanaoketi kwenye kiti cha ufalme cha Daudi, makuhani, manabii na wakaaji wote wa Yerusalemu.
JER 13:14 Nitawagombanisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema Mwenyezi Mungu. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ”
JER 13:15 Sikieni na mzingatie, msiwe na kiburi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenena.
JER 13:16 Mpeni utukufu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, kabla miguu yenu haijajikwaa juu ya vilima vitakavyotiwa giza. Mlitarajia nuru, lakini ataifanya kuwa giza nene na kuibadili kuwa huzuni kubwa.
JER 13:17 Lakini kama hamtasikiliza, nitalia sirini kwa ajili ya kiburi chenu; macho yangu yatalia kwa uchungu, yakitiririka machozi, kwa sababu kundi la kondoo la Mwenyezi Mungu litachukuliwa mateka.
JER 13:18 Mwambie mfalme na mama malkia, “Shukeni kutoka viti vyenu vya utawala, kwa kuwa taji zenu za utukufu zitaanguka kutoka vichwani mwenu.”
JER 13:19 Miji ya Negebu itafungwa, wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua. Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni, wakichukuliwa kabisa waende mbali.
JER 13:20 Inua macho yako uone wale wanaokuja kutoka kaskazini. Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa, wale kondoo uliojivunia?
JER 13:21 Utasema nini Mwenyezi Mungu atakapowaweka juu yako wale ulioungana nao kama rafiki zako maalum? Je, hutapatwa na uchungu kama mwanamke aliye katika uchungu wa kuzaa?
JER 13:22 Nawe ukijiuliza, “Kwa nini haya yamenitokea?” Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi marinda yako yameraruliwa na mwili wako umetendewa vibaya.
JER 13:23 Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake au chui kubadili madoadoa yake? Vivyo hivyo, wewe uliyezoea kutenda mabaya huwezi kufanya mema.
JER 13:24 “Nitawatawanya kama makapi yapeperushwayo na upepo wa jangwani.
JER 13:25 Hii ndiyo kura yako, fungu nililokuamulia,” asema Mwenyezi Mungu, “kwa sababu umenisahau mimi na kuamini miungu ya uongo.
JER 13:26 Nitayafunua marinda yako juu ya uso wako ili aibu yako ionekane,
JER 13:27 yaani uzinzi wako na kulia kwako kulikojaa tamaa kama farasi, na ukahaba wako usio na aibu! Nimeyaona matendo yako ya machukizo juu ya vilima na mashambani. Ole wako, ee Yerusalemu! Utaendelea kuwa najisi hadi lini?”
JER 14:1 Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu kwa Yeremia kuhusu ukame:
JER 14:2 “Yuda anaomboleza, kudhoofika kwa miji yake; wanaomboleza kwa ajili ya nchi, nacho kilio kinapanda kutoka Yerusalemu.
JER 14:3 Wakuu wanawatuma watumishi wao maji; nao wanakwenda visimani lakini huko hakuna maji. Wanarudi na vyombo bila maji; wakiwa na hofu na kukata tamaa, wanafunika vichwa vyao.
JER 14:4 Ardhi imepasuka nyufa kwa sababu hakuna mvua katika nchi; wakulima wana hofu na wanafunika vichwa vyao.
JER 14:5 Hata kulungu kondeni anaacha kinda lake lililotoka kutotolewa kwa sababu hakuna majani.
JER 14:6 Punda-mwitu wanasimama juu ya miinuko iliyo kame na kutweta kama mbweha; macho yao yanakosa nguvu za kuona kwa sababu ya kukosa malisho.”
JER 14:7 Ingawa dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu, Ee Mwenyezi Mungu, tenda jambo kwa ajili ya jina lako. Kwa kuwa kukengeuka kwetu ni kukubwa, nasi tumetenda dhambi dhidi yako.
JER 14:8 Ee Tumaini la Israeli, Mwokozi wake wakati wa taabu, kwa nini unakuwa kama mgeni katika nchi, kama msafiri anayekaa kwa usiku mmoja tu?
JER 14:9 Mbona unakuwa kama mtu aliyeshtukizwa, kama shujaa asiye na uwezo wa kuokoa? Wewe uko katikati yetu, Ee Mwenyezi Mungu, nasi tunaitwa kwa jina lako; usituache!
JER 14:10 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu watu hawa: “Wanapenda sana kutangatanga, hawaizuii miguu yao. Hivyo Mwenyezi Mungu hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.”
JER 14:11 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Usiombe kwa ajili ya mafanikio ya watu hawa.
JER 14:12 Ingawa wanafunga, sitasikiliza kilio chao; hata wakitoa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu za nafaka, sitazikubali. Badala yake, nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”
JER 14:13 Lakini nikasema, “Aa, Bwana Mungu Mwenyezi, manabii wanaendelea kuwaambia, ‘Hamtaona upanga wala kukabiliwa na njaa. Naam, nitawapa amani ya kudumu mahali hapa.’ ”
JER 14:14 Ndipo Mwenyezi Mungu akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwachagua, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, uaguzi usio na faida, udanganyifu wa mioyo yao, na ubatili.
JER 14:15 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu manabii wanaotabiri kwa jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na njaa.
JER 14:16 Nao watu hao wanaowatabiria watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu kwa sababu ya njaa na upanga. Hapatakuwa na mtu wa kuwazika wao au wake zao, watoto wao wa kiume au wa kike. Nitawamwagia maafa wanayostahili.
JER 14:17 “Nena nao neno hili: “ ‘Macho yangu na yatiririkwe na machozi usiku na mchana bila kukoma; kwa kuwa binti yangu aliye bikira, yaani watu wangu, amepata jeraha baya, pigo la kuangamiza.
JER 14:18 Ninapokwenda shambani, ninaona wale waliouawa kwa upanga; ninapokwenda mjini, huko ninaona maangamizi ya njaa. Nabii na kuhani kwa pamoja wameenda katika nchi wasiyoijua.’ ”
JER 14:19 Je, umemkataa Yuda kabisa? Umemchukia Sayuni kabisa? Kwa nini umetuumiza hata hatuwezi kuponyeka? Tulitarajia amani, lakini hakuna jema lililotujia; tulitarajia wakati wa kupona lakini kuna hofu kuu tu.
JER 14:20 Ee Mwenyezi Mungu, tunatambua uovu wetu na kosa la baba zetu; kweli tumetenda dhambi dhidi yako.
JER 14:21 Kwa ajili ya jina lako usituchukie kabisa; usikidharau kiti chako cha enzi kilichotukuka. Kumbuka agano lako nasi na usilivunje.
JER 14:22 Je, kuna sanamu batili yoyote ya mataifa iwezayo kuleta mvua? Je, anga peke yake zinaweza kuleta mvua? La hasha! Ni wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Kwa hiyo tumaini letu liko kwako, kwa kuwa wewe ndiwe ufanyaye haya yote.
JER 15:1 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia: “Hata kama Musa na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende!
JER 15:2 Nao wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, na wafe; waliowekewa kufa kwa upanga, kwa upanga; waliowekewa kufa kwa njaa, kwa njaa; na waliowekewa kupelekwa uhamishoni, wapelekwe uhamishoni.’ ”
JER 15:3 Mwenyezi Mungu asema, “Nitatuma aina nne za waangamizi: upanga ili kuua, mbwa ili kukokota mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili wale na waangamize.
JER 15:4 Nitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu.
JER 15:5 “Ni nani atakayekuhurumia, ee Yerusalemu? Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako? Ni nani atakayesimama ili kuuliza kuhusu hali yako?
JER 15:6 Umenikataa mimi,” asema Mwenyezi Mungu. “Unazidi kukengeuka. Hivyo nitanyoosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza, siwezi kuendelea kukuonea huruma.
JER 15:7 Nitawapepeta kwa ungo kwenye malango ya miji ya nchi. Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu, kwa maana hawajabadili njia zao.
JER 15:8 Nitawafanya wajane wao kuwa wengi kuliko mchanga wa bahari. Wakati wa adhuhuri nitamleta mwangamizi dhidi ya mama wa vijana wao wa kiume; kwa ghafula nitaleta juu yao maumivu makuu na hofu kuu.
JER 15:9 Mama mwenye watoto saba atazimia na kupumua pumzi yake ya mwisho. Jua lake litatua kukiwa bado mchana, atatahayarika na kufedheheka. Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga mbele ya adui zao,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 15:10 Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa, mtu ambaye ulimwengu wote unashindana na kugombana naye! Sikukopa wala sikukopesha, lakini kila mmoja ananilaani.
JER 15:11 Mwenyezi Mungu akasema, “Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema, hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada nyakati za maafa na nyakati za dhiki.
JER 15:12 “Je, mtu aweza kuvunja chuma, chuma kinachotoka kaskazini, au avunje shaba?
JER 15:13 “Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara, bila gharama, kwa sababu ya dhambi zako zote katika nchi yako yote.
JER 15:14 Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako katika nchi usiyoijua, kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa utakaowaka juu yako daima.”
JER 15:15 Wewe unafahamu, Ee Mwenyezi Mungu, unikumbuke na unitunze mimi. Lipiza kisasi juu ya watesi wangu. Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali; kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.
JER 15:16 Maneno yako yalipokuja, niliyala; yakawa shangwe yangu na furaha ya moyo wangu, kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
JER 15:17 Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe, wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao; niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu, na wewe ulikuwa umenijaza hasira.
JER 15:18 Kwa nini maumivu yangu hayakomi, na jeraha langu ni la kuhuzunisha, wala haliponyeki? Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu, kama chemchemi iliyokauka?
JER 15:19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Ukitubu, nitakurejesha ili uweze kunitumikia; ukinena maneno yenye maana, wala si ya upuzi, utakuwa mnenaji wangu. Watu hawa ndio watakaokugeukia, wala si wewe utakayewageukia wao.
JER 15:20 Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa, ngome ya ukuta wa shaba; watapigana nawe lakini hawatakushinda, kwa maana mimi niko pamoja nawe kukuponya na kukuokoa,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 15:21 “Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu, na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”
JER 16:1 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia:
JER 16:2 “Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.”
JER 16:3 Kwa maana hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu wana wa kiume na wa kike wanaozaliwa katika nchi hii, na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao, na wale wanaume ambao ni baba zao:
JER 16:4 “Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa, lakini watakuwa kama kinyesi juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa. Mizoga yao itakuwa chakula cha ndege na wanyama wa porini.”
JER 16:5 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga; usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeondoa amani yangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 16:6 “Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, na hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao.
JER 16:7 Hakuna yeyote atakayewapa chakula ili kuwafariji wanaoomboleza kwa ajili ya waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, wala hakuna yeyote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji.
JER 16:8 “Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu, na kuketi humo ili kula na kunywa.
JER 16:9 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako, nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, na pia sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’
JER 16:10 “Utakapowaambia watu hawa mambo haya yote na wakakuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu ameamuru maafa makubwa kama haya dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu?’
JER 16:11 Basi waambie, ‘Ni kwa sababu baba zenu waliniacha mimi, wakafuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Waliniacha mimi na hawakuishika sheria yangu,’ asema Mwenyezi Mungu.
JER 16:12 ‘Lakini ninyi mmetenda uovu kupita baba zenu. Tazama jinsi kila mmoja wenu anafuata ukaidi wa moyo wake mbaya, badala ya kunitii mimi.
JER 16:13 Kwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwatupa katika nchi ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua, na huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, kwa maana sitawapa fadhili zangu.’
JER 16:14 “Hata hivyo, siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “wakati watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’
JER 16:15 bali watasema, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, aliyewatoa Waisraeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia.’ Maana nitawarudisha katika nchi niliyowapa baba zao.
JER 16:16 “Lakini sasa nitawaagiza wavuvi wengi,” asema Mwenyezi Mungu, “nao watawavua. Baada ya hilo, nitawaagizia wawindaji wengi, nao watawawinda kwenye kila mlima na kilima, na katika nyufa za miamba.
JER 16:17 Macho yangu yanaziona njia zao zote, hazikufichika kwangu, wala dhambi yao haikusitirika.
JER 16:18 Nitawalipiza maradufu kwa ajili ya uovu wao na dhambi yao, kwa sababu wameinajisi nchi yangu kwa maumbo yasiyo na uhai ya vinyago vyao vibaya, na kuujaza urithi wangu na sanamu za kuchukiza.”
JER 16:19 Ee Mwenyezi Mungu, nguvu zangu na ngome yangu, kimbilio langu wakati wa taabu, kwako mataifa watakujia kutoka miisho ya dunia na kusema, “Baba zetu hawakuwa na chochote isipokuwa miungu ya uongo, sanamu batili ambazo hazikuwafaidi kitu.
JER 16:20 Je, watu hujitengenezea miungu yao wenyewe? Lakini hiyo si Mungu!”
JER 16:21 “Kwa hiyo nitawafundisha: wakati huu nitawafundisha nguvu zangu na uwezo wangu. Ndipo watajua kuwa Jina langu ndimi Mwenyezi Mungu.
JER 17:1 “Dhambi ya Yuda imechorwa kwa kalamu ya chuma, imeandikwa kwa ncha ya almasi, kwenye vibao vya mioyo yao na kwenye pembe za madhabahu zao.
JER 17:2 Hata watoto wao wanakumbuka madhabahu zao na nguzo za Ashera kandokando ya miti iliyotanda na juu ya vilima virefu.
JER 17:3 Mlima wangu katika nchi pamoja na utajiri na hazina zako zote nitavitoa viwe nyara, pamoja na mahali pako pa juu pa kuabudia kwa sababu ya dhambi katika nchi yako yote.
JER 17:4 Kwa kosa lako mwenyewe utaupoteza urithi niliokupa. Nitakufanya mtumwa wa adui zako katika nchi usiyoijua, kwa kuwa umeiwasha hasira yangu, nayo itawaka milele.”
JER 17:5 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu, amtegemeaye mwenye mwili kwa ajili ya nguvu zake, ambaye moyo wake umemwacha Mwenyezi Mungu.
JER 17:6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani; hataona mafanikio yatakapokuja. Ataishi katika sehemu zisizo na maji, katika nchi ya chumvi ambapo hakuna yeyote aishiye humo.
JER 17:7 “Lakini amebarikiwa mtu anayemtumaini Mwenyezi Mungu, ambaye matumaini yake ni katika Mwenyezi Mungu.
JER 17:8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji. Hauogopi wakati wa joto ujapo; majani yake ni mabichi daima. Hauna hofu katika mwaka wa ukame na hautaacha kuzaa matunda.”
JER 17:9 Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote, ni mwovu kupita kiasi. Ni nani awezaye kuujua?
JER 17:10 “Mimi Mwenyezi Mungu ninauchunguza moyo na kuzijaribu nia, ili kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake, kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”
JER 17:11 Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga, ndivyo alivyo mtu apataye mali kwa njia zisizo za haki. Maisha yake yatakapofika katikati, siku zitamwacha, na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu.
JER 17:12 Kiti cha enzi kilichotukuzwa, kilichoinuliwa tangu mwanzo, ndiyo sehemu yetu ya mahali patakatifu.
JER 17:13 Ee Mwenyezi Mungu, uliye tumaini la Israeli, wote wakuachao wataaibika. Wale wanaogeukia mbali nawe wataandikwa mavumbini kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu, chemchemi ya maji yaliyo hai.
JER 17:14 Uniponye, Ee Mwenyezi Mungu, nami nitaponyeka; uniokoe nami nitaokoka, kwa maana wewe ndiwe ninayekusifu.
JER 17:15 Wao huendelea kuniambia, “Liko wapi neno la Mwenyezi Mungu? Sasa na litimie!”
JER 17:16 Sijakukimbia na kuacha kuwa mchungaji wako; unajua sijaitamani siku ya kukata tamaa. Kile kipitacho mdomoni mwangu ki wazi mbele yako.
JER 17:17 Usiwe kwangu kitu cha kunitia hofu kuu; wewe ndiwe kimbilio langu katika siku ya maafa.
JER 17:18 Watesi wangu na waaibishwe, lakini nilinde mimi nisiaibike; wao na watiwe hofu kuu, lakini unilinde mimi na hofu kuu. Waletee siku ya maafa; waangamize kwa maangamizi maradufu.
JER 17:19 Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Nenda ukasimame kwenye lango la watu, mahali ambako wafalme wa Yuda huingilia na kutokea; simama pia kwenye malango mengine yote ya Yerusalemu.
JER 17:20 Waambie, ‘Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi wafalme wa Yuda, nanyi watu wote wa Yuda, na kila mmoja aishiye Yerusalemu apitaye katika malango haya.
JER 17:21 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Jihadharini msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, wala kuingiza mzigo kupitia malango ya Yerusalemu.
JER 17:22 Msitoe mizigo nje ya nyumba zenu wala kufanya kazi yoyote siku ya Sabato, lakini itakaseni siku ya Sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu.
JER 17:23 Hata hivyo hawakusikiliza wala kujali, walishupaza shingo zao, na hawakutaka kusikia wala kukubali adhabu.
JER 17:24 Lakini mkiwa waangalifu kunitii, asema Mwenyezi Mungu, nanyi msipoleta mzigo wowote kupitia malango ya mji huu wakati wa Sabato, lakini mkaitakasa siku ya Sabato kwa kutofanya kazi siku hiyo,
JER 17:25 ndipo wafalme wanaokaa kwenye kiti cha utawala cha Daudi wataingia kupitia malango ya mji huu, pamoja na maafisa wao. Wafalme na maafisa wao watakuja wakiwa wamepanda magari ya vita na farasi, wakiandamana na watu wote wa Yuda na wakaaji wa Yerusalemu, nao mji huu utakaliwa na watu daima.
JER 17:26 Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini na Shefela, kutoka nchi ya vilima na Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sadaka za nafaka, uvumba na sadaka za shukrani kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu.
JER 17:27 Lakini ikiwa hamtanitii mimi kwa kuitakasa Sabato na kwa kutochukua mzigo wowote mnapoingia katika malango ya Yerusalemu wakati wa Sabato, basi nitawasha moto usiozimika katika malango ya Yerusalemu utakaoteketeza ngome zake.’ ”
JER 18:1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
JER 18:2 “Shuka uende hadi nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.”
JER 18:3 Kwa hiyo nikashuka hadi nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake.
JER 18:4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake; hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kwa namna alivyoona ni vyema machoni pake.
JER 18:5 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
JER 18:6 “Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” asema Mwenyezi Mungu. “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli.
JER 18:7 Wakati wowote nitatangaza kuwa taifa au ufalme utang’olewa, utaangushwa na kuangamizwa,
JER 18:8 Lakini ikiwa taifa nililolionya litatubu na kuacha uovu wake nitaghairi, wala sitaleta maafa niliyokuwa nimekusudia kwa taifa hilo.
JER 18:9 Wakati mwingine nitakapotangaza kuwa taifa au ufalme utasimikwa na kujengwa,
JER 18:10 ikiwa litafanya uovu mbele zangu na halitaitii sauti yangu, nitaghairi kutenda jema nililokuwa nimekusudia.
JER 18:11 “Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tazama! Ninaandaa maafa juu yenu, nami ninapanga mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka njia zenu mbaya, kila mmoja wenu. Tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’
JER 18:12 Lakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’ ”
JER 18:13 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Ulizia miongoni mwa mataifa: Ni nani alishasikia jambo kama hili? Jambo la kutisha sana limefanywa na Bikira Israeli.
JER 18:14 Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka kwenye miteremko yake ya mawe wakati wowote? Je, maji yake baridi kutoka vyanzo vilivyo mbali yaliwahi kukoma kutiririka?
JER 18:15 Lakini watu wangu wamenisahau mimi, wanafukizia uvumba sanamu batili, zilizowafanya wajikwae katika njia zao na katika mapito ya zamani. Zimewafanya wapite kwenye vichochoro na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.
JER 18:16 Nchi yao itakuwa kitu cha kutisha, na cha kudharauliwa daima; wote wapitao karibu nayo watashangaa na kutikisa vichwa vyao.
JER 18:17 Kama upepo unaotoka mashariki, nitawatawanya mbele ya adui zao; nitawapa kisogo wala sio uso, katika siku ya maafa yao.”
JER 18:18 Wakasema, “Njooni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njooni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali chochote asemacho.”
JER 18:19 Nisikilize, Ee Mwenyezi Mungu, sikia wanayosema washtaki wangu!
JER 18:20 Je, mema yalipwe kwa mabaya? Lakini wao wamenichimbia shimo. Kumbuka kwamba nilisimama mbele yako na kunena mema kwa ajili yao, ili wewe ugeuze hasira yako kali mbali nao.
JER 18:21 Kwa hiyo uwaache watoto wao waone njaa; uwaache wauawe kwa makali ya upanga. Wake zao wasiwe na watoto, na wawe wajane; wanaume wao wauawe, nao vijana wao wa kiume wachinjwe kwa upanga vitani.
JER 18:22 Kilio na kisikike kutoka nyumba zao ghafula uwaletapo adui dhidi yao, kwa kuwa wamechimba shimo ili kunikamata na wameitegea miguu yangu mitego.
JER 18:23 Lakini unajua, Ee Mwenyezi Mungu, hila zao zote za kuniua. Usiyasamehe makosa yao wala usifute dhambi zao mbele za macho yako. Wao na waangamizwe mbele zako; uwaadhibu wakati wa hasira yako.
JER 19:1 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Nenda ukanunue gudulia la udongo kutoka kwa mfinyanzi. Wachukue baadhi ya wazee wa watu na wa makuhani
JER 19:2 na mtoke mwende hadi Bonde la Ben-Hinomu, karibu na ingilio la Lango la Vigae. Huko tangaza maneno ninayokuambia,
JER 19:3 nawe useme, ‘Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi wafalme wa Yuda na watu wa Yerusalemu. Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Sikilizeni! Nitaleta maafa mahali hapa, ambayo yatafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yawashe.
JER 19:4 Kwa kuwa wameniacha na kupafanya mahali hapa kuwa pa miungu ya kigeni. Wamefukizia uvumba miungu ambayo wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda kamwe hawakuijua, nao wamelijaza eneo hili kwa damu isiyo na hatia.
JER 19:5 Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia pa Baali ili kuteketeza wana wao katika moto kuwa sadaka kwa Baali, kitu ambacho sikukiamuru wala kukitaja, wala hakikuingia akilini mwangu.
JER 19:6 Hivyo jihadharini, siku zinakuja, asema Mwenyezi Mungu, wakati watu hawatapaita tena mahali hapa Tofethi ama Bonde la Ben-Hinomu, bali Bonde la Machinjo.
JER 19:7 “ ‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale wanaotafuta uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
JER 19:8 Nitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kutisha na cha kudharauliwa. Wote wapitao karibu watashangaa na kuudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote.
JER 19:9 Nitawafanya wao kula nyama ya wana wao wa kiume na wa kike; kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzingirwa na jeshi la adui wanaotafuta uhai wao.’
JER 19:10 “Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia,
JER 19:11 uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi.
JER 19:12 Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale wanaoishi ndani yake, asema Mwenyezi Mungu. Nitaufanya mji huu kama Tofethi.
JER 19:13 Nyumba zilizo Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’ ”
JER 19:14 Kisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali Mwenyezi Mungu alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la Mwenyezi Mungu na kuwaambia watu wote,
JER 19:15 “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu, na hawakuyasikiliza maneno yangu.’ ”
JER 20:1 Ikawa kuhani Pashuri mwana wa Imeri, mkuu wa maafisa wa Hekalu la Mwenyezi Mungu, alipomsikia Yeremia akitoa unabii kuhusu mambo haya,
JER 20:2 akaamuru Yeremia nabii apigwe na kufungwa kwenye mkatale katika Lango la Juu la Benyamini katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
JER 20:3 Siku ya pili Pashuri alipomwachia kwenye mkatale, Yeremia akamwambia, “Mwenyezi Mungu hakukuita jina lako kuwa Pashuri bali Magor-Misabibu.
JER 20:4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Nitakufanya uwe tisho kwako na rafiki wako wote; na macho yako mwenyewe yataona wakianguka kwa upanga wa adui zao. Nitawatia Yuda wote mikononi mwa mfalme wa Babeli, ambaye atawachukua mateka na kuwapeleka Babeli, ama awaue kwa upanga.
JER 20:5 Nitatia utajiri wote wa mji huu kwa adui zao: yaani mazao yao yote, vitu vyao vyote vya thamani, na hazina zote za wafalme wa Yuda. Watavitwaa kwa nyara na kuvipeleka Babeli.
JER 20:6 Nawe Pashuri pamoja na wote wanaoishi katika nyumba yako mtaenda uhamishoni Babeli. Mtafia huko na kuzikwa, wewe na rafiki zako wote ambao umewatabiria uongo.’ ”
JER 20:7 Ee Mwenyezi Mungu, umenidanganya, nami nikadanganyika; wewe una nguvu kuliko mimi, nawe umenishinda. Ninadharauliwa mchana kutwa, kila mmoja ananidhihaki.
JER 20:8 Kila ninenapo, ninapiga kelele nikitangaza ukatili na uharibifu. Kwa hiyo neno la Mwenyezi Mungu limeniletea matukano na mashutumu mchana kutwa.
JER 20:9 Lakini nikisema, “Sitamtaja wala kusema tena kwa jina lake,” neno lake linawaka ndani ya moyo wangu kama moto, moto uliofungwa ndani ya mifupa yangu. Nimechoka sana kwa kulizuia ndani mwangu; kweli, siwezi kujizuia.
JER 20:10 Ninasikia minong’ono mingi, “Hofu iko pande zote! Mshtakini! Twendeni tumshtaki!” Rafiki zangu wote wananisubiri niteleze, wakisema, “Labda atadanganyika; kisha tutamshinda na kulipiza kisasi juu yake.”
JER 20:11 Lakini Mwenyezi Mungu yu pamoja nami kama mpiganaji mwenye nguvu; kwa hiyo watesi wangu watajikwaa, Hawatashinda, nao wataaibika sana; aibu yao haitasahaulika milele.
JER 20:12 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, wewe umjaribuye mwenye haki na kupima moyo na nia, hebu nione ukilipiza kisasi juu yao, kwa maana kwako nimeliweka shauri langu.
JER 20:13 Mwimbieni Mwenyezi Mungu! Mpeni Mwenyezi Mungu sifa! Yeye huokoa uhai wa mhitaji kutoka mikononi mwa waovu.
JER 20:14 Ilaaniwe siku niliyozaliwa! Nayo isibarikiwe ile siku mama yangu aliyonizaa!
JER 20:15 Alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari, yule aliyemfanya afurahi sana, akisema, “Mtoto amezaliwa kwako, tena mtoto wa kiume!”
JER 20:16 Mtu huyo na awe kama ile miji ambayo Mwenyezi Mungu aliiangamiza bila huruma. Yeye na asikie maombolezo asubuhi, na ukelele wa vita adhuhuri.
JER 20:17 Kwa sababu hakuniua nikiwa tumboni, hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu, nalo tumbo lake la uzazi lingebaki kuwa kubwa daima.
JER 20:18 Kwa nini basi nilitoka tumboni ili kuona taabu na huzuni, na kuzimaliza siku zangu katika aibu?
JER 21:1 Neno lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu wakati Mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkiya, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwake, kusema:
JER 21:2 “Tuulizie sasa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Nebukadneza mfalme wa Babeli anatushambulia. Labda Mwenyezi Mungu atatenda maajabu kwa ajili yetu kama nyakati zilizopita, ili Nebukadneza atuondokee.”
JER 21:3 Lakini Yeremia akawajibu, “Mwambieni Sedekia,
JER 21:4 ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kuwageuzia silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo mnatumia kupigana na mfalme wa Babeli na Wakaldayo walio nje ya ukuta wakiwazingira kwa jeshi. Nami nitawakusanya ndani ya mji huu.
JER 21:5 Mimi mwenyewe nitapigana dhidi yenu kwa mkono wangu ulionyooshwa na mkono wa nguvu, kwa hasira na ghadhabu kali na ukali mwingi.
JER 21:6 Nitawaangamiza wakaaji wa mji huu, watu na wanyama, nao watauawa kwa tauni ya kutisha.
JER 21:7 Baada ya hayo, nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake na watu wa mji huu ambao walinusurika tauni, upanga na njaa, mkononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, na kwa adui zao wale wanaotafuta uhai wao. Atawaua kwa upanga; hatakuwa na rehema juu yao au huruma wala kuwasikitikia,’ asema Mwenyezi Mungu.
JER 21:8 “Zaidi ya hayo, waambie watu hawa, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tazama, naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.
JER 21:9 Yeyote atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni. Lakini yeyote atakayeenda na kujisalimisha kwa Wakaldayo, ambao wameuzingira mji huu kwa jeshi, atanusurika, naye ataishi.
JER 21:10 Nimekusudia kuufanyia mji huu jambo baya, wala si jema. Utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto, asema Mwenyezi Mungu.’
JER 21:11 “Zaidi ya hayo, iambie nyumba ya mfalme ya Yuda, ‘Sikia neno la Mwenyezi Mungu,
JER 21:12 Ewe nyumba ya Daudi, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Hukumuni kwa haki kila asubuhi, mwokoeni mikononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara, la sivyo ghadhabu yangu italipuka na kuwaka kama moto kwa sababu ya uovu mlioufanya: itawaka na hakuna wa kuizima.
JER 21:13 Niko kinyume nawe, ee Yerusalemu, wewe uishiye juu ya bonde hili kwenye uwanda wa juu wa miamba, asema Mwenyezi Mungu, wewe usemaye, “Ni nani awezaye kuja kinyume chetu? Nani ataingia mahali pa kimbilio letu?”
JER 21:14 Nitawaadhibu kama istahilivyo matendo yenu, asema Mwenyezi Mungu. Nitawasha moto katika misitu yenu ambao utateketeza kila kitu kinachowazunguka.’ ”
JER 22:1 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Shuka kwenye jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, utangaze ujumbe huu huko:
JER 22:2 ‘Sikia neno la Mwenyezi Mungu, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha utawala cha Daudi: wewe, wakuu wako na watu wako mnaopitia malango haya.
JER 22:3 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa.
JER 22:4 Ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, wafalme watakaokalia kiti cha utawala cha Daudi wataingia kupitia malango ya jumba la kifalme wakiwa wamepanda magari na farasi huku wakifuatana na watumishi wao na watu wao.
JER 22:5 Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema Mwenyezi Mungu, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ”
JER 22:6 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu jumba la kifalme la mfalme wa Yuda: “Ingawa uko kama Gileadi kwangu, kama kilele cha Lebanoni, hakika nitakufanya uwe kama jangwa, kama miji ambayo haijakaliwa na watu.
JER 22:7 Nitawatuma waharibifu dhidi yako, kila mtu akiwa na silaha zake, nao watazikata boriti zako bora za mwerezi na kuzitupa motoni.
JER 22:8 “Watu kutoka mataifa mengi watapita karibu na mji huu na kuulizana, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu amefanya jambo la namna hii kwa mji huu mkubwa?’
JER 22:9 Nalo jibu litakuwa: ‘Kwa sababu wameliacha agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na wameabudu na kuitumikia miungu mingine.’ ”
JER 22:10 Usimlilie yeye aliyekufa, wala usimwombolezee; badala yake, afadhali umlilie kwa uchungu yule aliyepelekwa uhamishoni, kwa sababu kamwe hatairudia wala kuiona tena nchi yake aliyozaliwa.
JER 22:11 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Shalumu mwana wa Yosia, aliyeingia mahali pa baba yake kuwa mfalme wa Yuda, lakini ameondoka mahali hapa: “Yeye kamwe hatarudi tena.
JER 22:12 Atafia huko mahali walipompeleka kuwa mateka; hataiona tena nchi hii.”
JER 22:13 “Ole wake yeye ajengaye jumba lake la kifalme kwa dhuluma, vyumba vyake vya juu kwa udhalimu, akiwatumikisha watu wa nchi yake pasipo malipo, bila kuwalipa kwa utumishi wao.
JER 22:14 Anasema, ‘Nitajijengea jumba kuu la kifalme, na vyumba vya juu vyenye nafasi kubwa.’ Hivyo anaweka ndani yake madirisha makubwa, huweka kuta za mbao za mwerezi, na kuzipaka kwa rangi nyekundu.
JER 22:15 “Je, huko kuongeza idadi ya mierezi kutakufanya uwe mfalme? Je, baba yako hakula na kunywa? Alifanya yaliyo sawa na haki, naye akafanikiwa kwa yote.
JER 22:16 Aliwatetea maskini na wahitaji, hivyo yeye akafanikiwa katika yote. Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?” asema Mwenyezi Mungu.
JER 22:17 “Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu katika mapato ya udhalimu, kumwaga damu isiyo na hatia, na katika uonevu na ukatili.”
JER 22:18 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: “Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, ndugu yangu! Ole, dada yangu!’ Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, bwana wangu! Ole, fahari yake!’
JER 22:19 Atazikwa maziko ya punda: ataburutwa na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.”
JER 22:20 “Panda Lebanoni ukapige kelele, sauti yako na isikike huko Bashani, piga kelele toka Abarimu, kwa kuwa wote waliojiunga nawe wameangamizwa.
JER 22:21 Nilikuonya wakati ulipojisikia kwamba uko salama, lakini ulisema, ‘Mimi sitasikiliza!’ Hii imekuwa kawaida yako tangu ujana wako; hujanitii mimi.
JER 22:22 Upepo utawaondoa wachungaji wako wote, na wandani wako wataenda uhamishoni. Kisha utaaibika na kufedheheka kwa sababu ya uovu wako wote.
JER 22:23 Wewe uishiye Lebanoni, wewe uliyetulia kwenye majengo ya mwerezi, tazama jinsi utakavyoomboleza maumivu makali yatakapokupata, maumivu kama ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa!
JER 22:24 “Hakika kama niishivyo,” asema Mwenyezi Mungu, “hata kama wewe, Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya muhuri katika mkono wangu wa kuume, bado ningekung’oa hapo.
JER 22:25 Nitakutia mikononi mwa wanaoutafuta uhai wako, wale unaowaogopa, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na kwa Wakaldayo.
JER 22:26 Nitakutupa mbali wewe na mama aliyekuzaa mwende katika nchi nyingine, ambayo hakuna hata mmoja wenu aliyezaliwa huko, nanyi mtafia huko.
JER 22:27 Kamwe hamtarudi katika nchi mliyotamani kuirudia.”
JER 22:28 Je, huyu mtu Yekonia ni chungu kilichodharauliwa, chungu kilichovunjika, chombo kisichotakiwa na mtu yeyote? Kwa nini yeye na watoto wake watupwe nje kwa nguvu, na kutupwa kwenye nchi wasioijua?
JER 22:29 Ee nchi, nchi, nchi, sikia neno la Mwenyezi Mungu!
JER 22:30 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Mwandike huyu mtu kama asiye na mtoto, mtu ambaye hatafanikiwa maisha yake yote, kwa maana hakuna mzao wake atakayefanikiwa, wala kukaa kwenye kiti cha utawala cha Daudi wala kuendelea kutawala katika Yuda.”
JER 23:1 “Ole wao wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu!” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:2 Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, analowaambia wachungaji wanaowachunga watu wangu: “Kwa sababu mmelitawanya kundi langu na kuwafukuzia mbali, wala hamkuwatunza, basi mimi nitawaadhibu kwa ajili ya uovu mliofanya,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:3 “Mimi mwenyewe nitayakusanya mabaki ya kundi langu kutoka nchi zote ambazo nimewafukuzia, nami nitawarudisha katika malisho yao, ambapo watazaa na kuongezeka idadi yao.
JER 23:4 Nitaweka wachungaji juu yao ambao watawachunga, nao hawataogopa tena au kutishwa, wala hatapotea hata mmoja,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:5 Mwenyezi Mungu asema, “Siku zinakuja, nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki, Mfalme atakayetawala kwa hekima, na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.
JER 23:6 Katika utawala wake, Yuda ataokolewa, na Israeli ataishi salama. Hili ndilo jina atakaloitwa: Mwenyezi Mungu ni Haki Yetu.”
JER 23:7 Mwenyezi Mungu asema, “Hivyo basi, siku zinakuja, ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’
JER 23:8 bali watasema, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, aliyewatoa wazao wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia.’ Ndipo wataishi katika nchi yao wenyewe.”
JER 23:9 Kuhusu manabii: Moyo wangu umevunjika ndani yangu; mifupa yangu yote inatetemeka. Nimekuwa kama mtu aliyelewa, kama mtu aliyelemewa na divai, kwa sababu ya Mwenyezi Mungu na maneno yake matakatifu.
JER 23:10 Nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya laana, nchi imekauka, na malisho ya nyikani yamekauka. Mwenendo wa manabii ni mbaya na mamlaka yao si ya haki.
JER 23:11 “Nabii na kuhani wote si wacha Mungu; hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:12 “Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi, watafukuziwa mbali gizani na huko wataanguka. Nitaleta maafa juu yao katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:13 “Miongoni mwa manabii wa Samaria nililiona jambo la kuchukiza: Walitabiri kwa Baali na kuwapotosha Israeli watu wangu.
JER 23:14 Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu nimeona jambo baya sana: Wanafanya uzinzi na kuenenda katika uongo. Wanatia nguvu mikono ya watenda maovu, kwa ajili hiyo hakuna yeyote anayeachana na uovu wake. Wote wako kama Sodoma kwangu; watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”
JER 23:15 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni kuhusu manabii: “Nitawafanya wale chakula kichungu na kunywa maji yaliyotiwa sumu, kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”
JER 23:16 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Msisikilize wanachowatabiria manabii, wanawajaza matumaini ya uongo. Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe, hayatoki katika kinywa cha Mwenyezi Mungu.
JER 23:17 Huendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi, ‘Mwenyezi Mungu asema: Mtakuwa na amani.’ Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao, wao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’
JER 23:18 Lakini ni yupi miongoni mwao aliyesimama katika baraza la Mwenyezi Mungu ili kuona au kusikia neno lake? Ni nani aliyesikiliza na kusikia neno lake?
JER 23:19 Tazama, dhoruba ya Mwenyezi Mungu itatokea kwa ghadhabu, kisulisuli kitazunguka na kuanguka juu ya vichwa vya waovu.
JER 23:20 Hasira ya Mwenyezi Mungu haitageuka hadi amelitimiza kusudi la moyo wake. Siku zijazo mtalifahamu kwa wazi.
JER 23:21 Mimi sikuwatuma manabii hawa, lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao. Mimi sikusema nao, lakini wametabiri.
JER 23:22 Lakini kama wangesimama barazani pangu, wangetangaza maneno yangu kwa watu wangu, nao wangewageuza kutoka njia zao mbaya na kutoka matendo yao maovu.
JER 23:23 “Je, mimi ni Mungu aliye karibu tu, wala si Mungu aliye pia mbali?” Mwenyezi Mungu asema.
JER 23:24 “Je, mtu yeyote aweza kujificha mahali pa siri nisiweze kumwona?” Mwenyezi Mungu asema. “Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?” Mwenyezi Mungu asema.
JER 23:25 “Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’
JER 23:26 Mambo haya yataendelea hata lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe?
JER 23:27 Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau kwa kumwabudu Baali.
JER 23:28 Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:29 “Je, neno langu si kama moto,” asema Mwenyezi Mungu, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?
JER 23:30 “Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:31 “Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotumia ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi Mungu asema.’
JER 23:32 Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Mwenyezi Mungu. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 23:33 “Basi watu hawa, au nabii, au kuhani, watakapokuuliza, ‘Ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni nini?’ Wewe utawaambia, ‘Ninyi ndio ujumbe. Nami nitawavua kama vazi, asema Mwenyezi Mungu.’
JER 23:34 Nabii, kuhani, au mtu yeyote akisema, ‘Huu ndio ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ nitamwadhibu huyo na nyumba yake.
JER 23:35 Mnaambiana kila mmoja na mwenzake, au kwa mtu wa nyumba yao: ‘Mwenyezi Mungu amejibu nini?’ au ‘Mwenyezi Mungu amesema nini?’
JER 23:36 Lakini kamwe msiseme tena, ‘Nina ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe, na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wetu.
JER 23:37 Hivi ndivyo utakavyoendelea kumuuliza nabii: ‘Mwenyezi Mungu amekujibu nini?’ au ‘Je, Mwenyezi Mungu amesema nini?’
JER 23:38 Ingawa unadai, ‘Huu ndio ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ asema Mwenyezi Mungu. Ulitumia maneno, ‘Huu ndio ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ Ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu.’
JER 23:39 Kwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutenga mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu.
JER 23:40 Nitaleta juu yako fedheha ya kudumu: yaani aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”
JER 24:1 Baada ya Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na maafisa, mafundi stadi na wahunzi wa Yuda, kuchukuliwa kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli na Nebukadneza, mfalme wa Babeli, Mwenyezi Mungu akanionesha vikapu viwili vya tini vilivyowekwa mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.
JER 24:2 Kikapu kimoja kilikuwa na tini nzuri sana, kama zile za mavuno ya kwanza. Kikapu cha pili kilikuwa na tini dhaifu sana, mbovu mno zisizofaa kuliwa.
JER 24:3 Kisha Mwenyezi Mungu akaniuliza, “Je, Yeremia, unaona nini?” Nikamjibu, “Ninaona tini zilizo nzuri ni nzuri sana, lakini zilizo mbaya, ni mbaya sana zisizofaa kuliwa.”
JER 24:4 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia:
JER 24:5 “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama zilivyo hizi tini nzuri, ndivyo ninavyowaona kuwa bora watu wa uhamisho kutoka Yuda, niliowaondoa kutoka mahali hapa kwenda katika nchi ya Wakaldayo.
JER 24:6 Macho yangu yatakuwa juu yao kwa ajili ya kuwapatia mema, nami nitawarudisha tena katika nchi hii. Nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawang’oa,
JER 24:7 nitawapa moyo wa kunifahamu mimi, kwamba mimi ndimi Mwenyezi Mungu. Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, kwa maana watanirudia kwa moyo wote.
JER 24:8 “ ‘Lakini kama zilivyo zile tini dhaifu, ambazo ni mbovu mno zisizofaa kuliwa,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘ndivyo nitakavyomtendea Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake, na mabaki wengine kutoka Yerusalemu, wawe wamebaki katika nchi hii, au wanaishi Misri.
JER 24:9 Nitawafanya kuwa chukizo kabisa na kitu cha kulaumiwa katika mataifa yote ya dunia, watakuwa aibu na kitu cha kudharauliwa, chombo cha dhihaka na kulaaniwa, popote nitakapowafukuzia.
JER 24:10 Nitautuma upanga, njaa na tauni dhidi yao hadi wawe wameangamia kutoka nchi niliyowapa wao na baba zao.’ ”
JER 25:1 Neno likamjia Yeremia kuhusu watu wote wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.
JER 25:2 Nabii Yeremia akawaambia watu wote wa Yuda na wote wanaoishi Yerusalemu:
JER 25:3 Kwa miaka ishirini na tatu, kuanzia mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda, hadi siku hii ya leo, neno la Mwenyezi Mungu limekuwa likinijia, nami nimesema nanyi mara kwa mara, lakini hamkusikiliza.
JER 25:4 Ingawa Mwenyezi Mungu aliwatuma kwenu mara kwa mara watumishi na manabii wake wote, ninyi hamkusikiliza wala hamkujali.
JER 25:5 Walisema, “Geukeni sasa, kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya na matendo yake maovu, ndipo mtaweza kukaa katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliwapa ninyi na baba zenu milele.
JER 25:6 Msiifuate miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Msinikasirishe kwa vitu mlivyovitengeneza kwa mikono yenu.”
JER 25:7 “Lakini ninyi hamkunisikiliza, tena mkanikasirisha kwa vitu mlivyovitengeneza kwa mikono yenu, nanyi mmejiletea madhara juu yenu wenyewe,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 25:8 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni asema hivi: “Kwa sababu hamkuyasikiliza maneno yangu,
JER 25:9 nitayaita mataifa yote ya kaskazini na mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake wote, na dhidi ya mataifa yote yanayowazunguka. Nitawaangamiza kabisa na kuwafanya kitu cha kuchukiwa na kudharauliwa, na kuwa magofu daima.
JER 25:10 Nitawaondolea sauti ya shangwe na furaha, sauti ya bibi arusi na ya bwana arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na mwanga wa taa.
JER 25:11 Nchi hii yote itakuwa ukiwa na isiyofaa kitu, nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini.
JER 25:12 “Miaka sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli na taifa lake na nchi ya Wakaldayo kwa ajili ya hatia yao,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitaifanya kuwa ukiwa milele.
JER 25:13 Nitaleta juu ya nchi hiyo mambo yote niliyosema dhidi yake, yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki, na kutolewa unabii na Yeremia dhidi ya mataifa yote.
JER 25:14 Wao wenyewe watakuwa watumwa wa mataifa mengi na wafalme wakuu. Nitawalipizia sawasawa na matendo yao na kazi ya mikono yao.”
JER 25:15 Hili ndilo neno ambalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliwaambia: “Chukua kutoka mkononi mwangu kikombe hiki kilichojaa divai ya ghadhabu yangu, na kuyanywesha mataifa yote, ninaokutuma kwao.
JER 25:16 Watakapoinywa, watapepesuka na kukasirika sana kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka katikati yao.”
JER 25:17 Hivyo, nikakichukua kikombe kutoka mkononi mwa Mwenyezi Mungu, na kuyafanya mataifa yote aliyonituma kwao kukinywa:
JER 25:18 Yaani Yerusalemu na miji ya Yuda, wafalme wake na wakuu wake, kuwafanya magofu na kuwa kitu cha kutisha, cha dhihaka na laana, kama walivyo leo;
JER 25:19 Farao mfalme wa Misri, watumishi wake, maafisa wake na watu wake wote,
JER 25:20 na wageni wote walio huko; wafalme wote wa nchi ya Usi; wafalme wote wa Wafilisti (wale wa Ashkeloni, Gaza, Ekroni, na watu walioachwa huko Ashdodi);
JER 25:21 Edomu, Moabu na Amoni;
JER 25:22 wafalme wote wa Tiro na Sidoni; wafalme wa nchi za pwani ng’ambo ya bahari;
JER 25:23 Dedani, Tema, Buzi na wote walio maeneo ya mbali;
JER 25:24 wafalme wote wa Arabuni na wafalme wote wa watu wageni wanaoishi katika jangwa;
JER 25:25 wafalme wote wa Zimri, Elamu na Umedi;
JER 25:26 na wafalme wote wa pande za kaskazini, wa karibu na wa mbali, mmoja baada ya mwingine; yaani falme zote duniani. Baada ya hao wote, mfalme wa Sheshaki atakunywa pia.
JER 25:27 “Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Kunyweni, mlewe na mtapike; angukeni, wala msiinuke tena kwa sababu ya upanga nitakaotuma miongoni mwenu.’
JER 25:28 Lakini wakikataa kupokea kikombe kutoka mikononi mwako na kunywa, waambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Ni lazima mnywe!
JER 25:29 Tazama, nimeanza kuleta maafa juu ya mji ulio na Jina langu, na je, kweli ninyi mtaepuka kuadhibiwa? Hamwezi kuepuka kuadhibiwa, kwa maana nitaleta upanga dhidi ya wote wanaoishi duniani, asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.’
JER 25:30 “Basi sasa toa unabii kwa maneno haya yote dhidi yao, uwaambie: “ ‘Mwenyezi Mungu atanguruma kutoka juu; atatoa sauti ya ngurumo kutoka makao yake matakatifu na kunguruma kwa nguvu sana dhidi ya nchi yake. Atapiga kelele kama wao wakanyagao zabibu, atapiga kelele dhidi ya wote wanaoishi katika nchi.
JER 25:31 Ghasia zitasikika hadi miisho ya dunia, kwa maana Mwenyezi Mungu ataleta hukumu dhidi ya mataifa; ataleta hukumu juu ya wanadamu wote na kuwaua waovu wote kwa upanga,’ ” asema Mwenyezi Mungu.
JER 25:32 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Tazama! Maafa yanaenea kutoka taifa moja hadi jingine; tufani kubwa inainuka kutoka miisho ya dunia.”
JER 25:33 Wakati huo, hao waliouawa na Mwenyezi Mungu watatapakaa kila mahali, kuanzia mwisho mmoja wa dunia hadi mwisho mwingine. Hawataombolezewa wala kukusanywa au kuzikwa, lakini watakuwa kama kinyesi juu ya ardhi.
JER 25:34 Lieni na kuomboleza, enyi wachungaji, mjigaragaze katika majivu, ninyi viongozi wa kundi. Kwa maana wakati wenu wa kuchinjwa umewadia; mtaanguka na kuvunjwavunjwa kama vyombo vizuri vya udongo.
JER 25:35 Wachungaji hawatakuwa na mahali pa kukimbilia, viongozi wa kundi hawatapata mahali pa kutorokea.
JER 25:36 Sikia kilio cha wachungaji, maombolezo ya viongozi wa kundi, kwa maana Mwenyezi Mungu anayaharibu malisho yao.
JER 25:37 Makao yao ya amani yataharibiwa kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi Mungu.
JER 25:38 Kama simba ataacha pango lake, nchi yao itakuwa ukiwa kwa sababu ya upanga wa mdhalimu, na kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi Mungu.
JER 26:1 Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilikuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
JER 26:2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Simama katika ua wa nyumba ya Mwenyezi Mungu na useme na watu wote wa miji ya Yuda wanaokuja kuabudu katika nyumba ya Mwenyezi Mungu. Waambie kila kitu nitakachokuamuru, usipunguze neno.
JER 26:3 Huenda watasikia na kugeuka, kisha kila mmoja kutubu na kuacha njia yake mbaya. Nami nitaghairi kuleta maafa niliyopanga kufanya dhidi yao kwa sababu ya matendo yao maovu.
JER 26:4 Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ikiwa hamtanisikiliza na kuifuata sheria yangu niliyoiweka mbele yenu,
JER 26:5 na msipoyasikiliza maneno ya watumishi wangu manabii, ambao nimewatuma kwenu tena na tena (ijapokuwa hamkuwasikiliza),
JER 26:6 ndipo nitaifanya nyumba hii kama Shilo na mji huu kuwa kitu cha kulaaniwa na mataifa yote ya dunia.’ ”
JER 26:7 Makuhani, manabii na watu wote wakamsikia Yeremia akiyasema maneno haya ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu.
JER 26:8 Lakini mara tu Yeremia alipomaliza kuwaambia watu kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru kukisema, basi makuhani, manabii na watu wote walimkamata wakisema, “Ni lazima ufe!
JER 26:9 Kwa nini unatoa unabii katika jina la Mwenyezi Mungu kwamba nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa na kuachwa tupu?” Nao watu wote wakamkusanyikia na kumzunguka Yeremia ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu.
JER 26:10 Maafisa wa Yuda waliposikia kuhusu mambo haya, wakapanda kutoka jumba la kifalme, wakaenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu na kushika nafasi zao kwenye ingilio la Lango Jipya la nyumba ya Mwenyezi Mungu.
JER 26:11 Kisha makuhani na manabii wakawaambia maafisa pamoja na watu wote, “Mtu huyu anastahili ahukumiwe kifo kwa sababu ametoa unabii mbaya dhidi ya mji huu. Mmesikia kwa masikio yenu wenyewe!”
JER 26:12 Kisha Yeremia akawaambia maafisa wote na watu wote: “Mwenyezi Mungu amenituma kutoa unabii dhidi ya nyumba hii na mji huu mambo yote mliyoyasikia.
JER 26:13 Sasa tengenezeni njia zenu na matendo yenu, na kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Ndipo Mwenyezi Mungu atawahurumia na kuacha kuleta maafa aliyokuwa ameyatamka dhidi yenu.
JER 26:14 Lakini mimi niko mikononi mwenu; nifanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki.
JER 26:15 Hata hivyo, jueni kwa hakika, ikiwa mtaniua, kwa kumwaga damu isiyo na hatia, mtakuwa mmejipatia dhambi juu yenu wenyewe, juu ya mji huu, na juu ya wote wanaoishi ndani yake, kwa kuwa ni kweli Mwenyezi Mungu amenituma kwenu ili niseme maneno haya masikioni mwenu.”
JER 26:16 Kisha maafisa na watu wote wakawaambia makuhani na manabii, “Mtu huyu asihukumiwe kifo! Amesema nasi katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
JER 26:17 Baadhi ya wazee wa nchi wakasogea mbele, wakaliambia kusanyiko lote la watu,
JER 26:18 “Mika Mmoreshethi alitoa unabii katika siku za Hezekia mfalme wa Yuda. Akawaambia watu wote wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “ ‘Sayuni italimwa kama shamba, Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto, na kilima cha Hekalu kitakuwa kichuguu kilichofunikwa na vichaka.’
JER 26:19 Je, Hezekia mfalme wa Yuda au mtu mwingine yeyote katika Yuda alimhukumu Mika kufa? Je, Hezekia hakumcha Mwenyezi Mungu na kuhitaji msaada wake? Je, Mwenyezi Mungu hakuwahurumia na kughairi maafa aliyokuwa ametamka dhidi yao? Tunakaribia sana kujiletea maangamizi ya kutisha sisi wenyewe!”
JER 26:20 Wakati huu, Uria mwana wa Shemaya kutoka mji wa Kiriath-Yearimu alikuwa mtu mwingine aliyetoa unabii kwa jina la Mwenyezi Mungu. Alitoa unabii juu ya mambo yaliyofanana na haya dhidi ya mji huu na nchi hii kama alivyofanya Yeremia.
JER 26:21 Mfalme Yehoyakimu na wakuu wake wote na maafisa waliposikia maneno yake, mfalme alitafuta kumuua. Lakini Uria alipata habari, na kwa kuogopa akakimbilia Misri.
JER 26:22 Hata hivyo, Mfalme Yehoyakimu alimtuma Elnathani mwana wa Akbori huko Misri, pamoja na watu wengine ili kwenda kumkamata Uria.
JER 26:23 Wakamrudisha Uria kutoka Misri na kumpeleka kwa Mfalme Yehoyakimu, ambaye alimuua kwa upanga, na mwili wake kutupwa kwenye eneo la makaburi ya watu wasio na cheo.
JER 26:24 Zaidi ya hayo, Ahikamu mwana wa Shafani akamuunga mkono Yeremia, kwa hiyo hakutiwa tena mikononi mwa watu ili auawe.
JER 27:1 Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
JER 27:2 Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Tengeneza nira, ujivike shingoni mwako, uifunge kwa kamba za ngozi.
JER 27:3 Kisha utume ujumbe kwa wafalme wa Edomu, Moabu, Amoni, Tiro na Sidoni kupitia wajumbe ambao wamekuja Yerusalemu kwa Sedekia mfalme wa Yuda.
JER 27:4 Wape ujumbe kwa ajili ya mabwana zao na uwaambie: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: ‘Waambieni hivi mabwana zenu:
JER 27:5 Kwa uwezo wangu mkuu na kwa mkono wangu ulionyooka nimeumba dunia na watu wake na wanyama walio ndani yake, nami humpa yeyote ninayependa.
JER 27:6 Sasa nitazitia nchi zenu zote mkononi mwa mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli, na nitawafanya hata wanyama pori wamtumikie.
JER 27:7 Mataifa yote yatamtumikia yeye, pamoja na mwanawe, na mjukuu wake, hadi wakati wa nchi yake utakapowadia, kisha mataifa mengi na wafalme wenye nguvu nyingi watamshinda.
JER 27:8 “ ‘ “Lakini kama kukiwa na taifa lolote au ufalme ambao hautamtumikia Nebukadneza mfalme wa Babeli, ama kuinamisha shingo yake chini ya nira yake, nitaliadhibu taifa hilo kwa upanga, njaa na tauni, asema Mwenyezi Mungu, hadi nitakapoliangamiza taifa hilo kwa mkono wake.
JER 27:9 Kwa hiyo msiwasikilize manabii wenu, waaguzi wenu, waota ndoto wenu, watabiri na wachawi wanaowaambia ninyi: Hamtamtumikia mfalme wa Babeli.
JER 27:10 Wanawatabiria uongo ambao utawafanya ninyi mhamishwe mbali kutoka nchi yenu. Nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia.
JER 27:11 Lakini ikiwa taifa lolote litainama na kuweka shingo yake katika nira ya mfalme wa Babeli na kumtumikia, nitaliacha taifa hilo katika nchi yake yenyewe ili wailime na kuishi humo, asema Mwenyezi Mungu.” ’ ”
JER 27:12 Nilitoa ujumbe huo huo kwa Sedekia mfalme wa Yuda. Nilisema, “Ingiza shingo yako katika nira ya mfalme wa Babeli, umtumikie yeye na watu wake, nawe utaishi.
JER 27:13 Kwa nini wewe na watu wako mfe kwa upanga, njaa na tauni, ambazo Mwenyezi Mungu ameonya kuhusu taifa lolote ambalo halitamtumikia mfalme wa Babeli?
JER 27:14 Msiyasikilize maneno ya manabii wanaowaambia kwamba, ‘Hamtamtumikia mfalme wa Babeli,’ kwa sababu wanawatabiria uongo.
JER 27:15 ‘Sikuwatuma hao,’ asema Mwenyezi Mungu. ‘Wanatabiri uongo kwa jina langu. Kwa hiyo, nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia, ninyi pamoja na manabii wanaowatabiria.’ ”
JER 27:16 Kisha nikawaambia makuhani na watu hawa wote, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Msiwasikilize manabii wanaosema, ‘Hivi karibuni sana vyombo vya nyumba ya Mwenyezi Mungu vitarudishwa kutoka Babeli.’ Wanawatabiria ninyi uongo.
JER 27:17 Msiwasikilize. Mtumikieni mfalme wa Babeli, nanyi mtaishi. Kwa nini mji huu uwe magofu?
JER 27:18 Kama wao ni manabii na wanalo neno la Mwenyezi Mungu, basi na wamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ili vyombo vilivyobaki katika nyumba ya Mwenyezi Mungu na katika jumba la kifalme la mfalme wa Yuda na katika Yerusalemu visipelekwe Babeli.
JER 27:19 Kwa maana hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni kuhusu zile nguzo, ile Bahari, vile vishikizo vinavyoweza kuhamishwa, vinara na vyombo vingine vilivyoachwa katika mji huu,
JER 27:20 ambavyo Nebukadneza mfalme wa Babeli hakuvichukua alipomchukua Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda kwenda uhamishoni huko Babeli kutoka Yerusalemu, pamoja na wakuu wote wa Yuda na Yerusalemu.
JER 27:21 Naam, hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu vitu ambavyo vimebaki ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, na ndani ya jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, na katika Yerusalemu:
JER 27:22 ‘Vitachukuliwa kupelekwa Babeli, na huko vitabaki hadi siku nitakayovijilia,’ asema Mwenyezi Mungu. ‘Kisha nitavirudisha na kuvirejesha mahali hapa.’ ”
JER 28:1 Katika mwezi wa tano wa mwaka ule ule, yaani mwaka wa nne, mwanzoni mwa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, nabii Hanania mwana wa Azuri, ambaye alitoka Gibeoni, akaniambia katika nyumba ya Mwenyezi Mungu mbele ya makuhani na watu wote:
JER 28:2 “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.
JER 28:3 Katika muda wa miaka miwili nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya Mwenyezi Mungu ambavyo Nebukadneza mfalme wa Babeli aliviondoa kutoka hapa na kuvipeleka Babeli.
JER 28:4 Pia nitamrudisha mahali hapa Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na wote waliohamishwa kutoka Yuda ambao walienda Babeli,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘kwa kuwa nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.’ ”
JER 28:5 Ndipo nabii Yeremia akamjibu nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu.
JER 28:6 Akasema, “Amen! Mwenyezi Mungu na afanye hivyo! Mwenyezi Mungu na ayatimize maneno ya unabii uliyoyatoa kwa kuvirudisha mahali hapa kutoka Babeli vyombo vya nyumba ya Mwenyezi Mungu na watu wote walio uhamishoni.
JER 28:7 Hata hivyo, nisikilize nikuambie yale nitakayoyasema masikioni mwako na masikioni mwa watu hawa wote:
JER 28:8 Tangu mwanzo, manabii waliokutangulia wewe na mimi walitabiri vita, maafa na tauni dhidi ya nchi nyingi na falme kubwa.
JER 28:9 Lakini nabii atakayetabiri amani atatambuliwa kuwa kweli ametumwa na Mwenyezi Mungu ikiwa unabii wake utatimia.”
JER 28:10 Kisha nabii Hanania akaiondoa nira iliyokuwa shingoni mwa Yeremia na kuivunja,
JER 28:11 naye akasema mbele ya watu wote, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Vivi hivi ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadneza mfalme wa Babeli kutoka shingo za mataifa katika muda huu wa miaka miwili.’ ” Alipofanya hivi, nabii Yeremia akaondoka zake.
JER 28:12 Kitambo kidogo baada ya nabii Hanania kuivunja nira kutoka shingo ya nabii Yeremia, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia:
JER 28:13 “Nenda ukamwambie Hanania, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Umevunja nira ya mti, lakini badala yake utapata nira ya chuma.
JER 28:14 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Nitaweka nira ya chuma kwenye shingo za mataifa haya yote ili kufanya yamtumikie Nebukadneza mfalme wa Babeli, nao watamtumikia. Pia nitampa kutawala hata wanyama pori.’ ”
JER 28:15 Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, “Sikiliza Hanania! Mwenyezi Mungu hajakutuma, lakini wewe umelishawishi taifa hili kuamini uongo.
JER 28:16 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Hivi karibuni nitakuondoa duniani. Mwaka huu utakufa, kwa sababu umetangaza uasi dhidi ya Mwenyezi Mungu.’ ”
JER 28:17 Katika mwezi wa saba wa mwaka ule ule, nabii Hanania akafa.
JER 29:1 Haya ndio maneno ya barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa waliopelekwa uhamishoni, na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu.
JER 29:2 (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia na mama malkia, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.)
JER 29:3 Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani, na kwa Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema:
JER 29:4 Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli:
JER 29:5 “Jengeni nyumba na mwishi humo, pandeni bustani na mle mazao yake.
JER 29:6 Oeni wake na mzae watoto wa kiume na wa kike; watafutieni wake watoto wenu wa kiume, na waozeni binti zenu ili nao wazae watoto wa kiume na wa kike; mkaongezeke huko, wala msipungue idadi.
JER 29:7 Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”
JER 29:8 Naam, hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na waaguzi walio miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota.
JER 29:9 Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 29:10 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa.
JER 29:11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Mwenyezi Mungu, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo.
JER 29:12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza.
JER 29:13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wote.
JER 29:14 Nitaonekana kwenu,” asema Mwenyezi Mungu, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali nilipokuwa nimewatoa walipopelekwa uhamishoni,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 29:15 Mnaweza mkasema, “Mwenyezi Mungu ameinua manabii kwa ajili yetu huku Babeli,”
JER 29:16 lakini hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu mfalme aketiye katika kiti cha utawala cha Daudi, na watu wa kwenu wote wanaobaki katika mji huu, ndugu zenu ambao hawakuenda pamoja nanyi uhamishoni.
JER 29:17 Naam, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Nitatuma upanga, njaa na tauni dhidi yao, nami nitawafanya kuwa kama tini mbovu zilizooza, zisizofaa kuliwa.
JER 29:18 Nitawafukuza kwa upanga, kwa njaa na kwa tauni, nami nitawafanya kuwa chukizo kwa falme zote za dunia, kitu cha laana na cha kutisha, kisichofaa na cha kuzomewa miongoni mwa mataifa nitakakowafukuzia.
JER 29:19 Kwa kuwa hawakuyasikiliza maneno yangu,” asema Mwenyezi Mungu, “maneno niliyoyatuma kwao mara kwa mara kupitia kwa watumishi wangu manabii. Wala ninyi watu wa uhamisho hamkusikiliza pia,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 29:20 Kwa hiyo, sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi nyote mlio uhamishoni, niliowapeleka Babeli kutoka Yerusalemu.
JER 29:21 Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya, na Sedekia mwana wa Maaseya, wanaowatabiria uongo kwa jina langu: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu hasa.
JER 29:22 Kwa ajili yao, watu wote wa Yuda walio uhamishoni Babeli watatumia laana hii: ‘Mwenyezi Mungu na akutendee kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwachoma moto.’
JER 29:23 Kwa kuwa wamefanya mambo maovu kabisa katika Israeli, wamezini na wake za majirani zao, tena kwa Jina langu wamesema uongo, mambo ambayo sikuwaambia kuyafanya. Nami nayajua haya, na ni shahidi wa jambo hilo,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 29:24 Mwambie Shemaya Mnehelami,
JER 29:25 “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Ulituma barua kwa jina lako mwenyewe kwa watu wote wa Yerusalemu, kwa Sefania mwana wa kuhani Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Ulimwambia Sefania,
JER 29:26 ‘Mwenyezi Mungu amekuweka wewe uwe kuhani badala ya Yehoyada ili uwe msimamizi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu. Unapaswa kumfunga kwa mikatale na mnyororo wa shingoni mwendawazimu yeyote anayejifanya nabii.
JER 29:27 Kwa nini basi hukumkemea Yeremia Mwanathothi, aliyejifanya kama nabii miongoni mwenu?
JER 29:28 Ametutumia ujumbe huu huku Babeli: Mtakuwa huko muda mrefu. Kwa hiyo jengeni nyumba mkakae; pandeni mashamba na mle mazao yake.’ ”
JER 29:29 Kuhani Sefania, hata hivyo, akamsomea nabii Yeremia ile barua.
JER 29:30 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema:
JER 29:31 “Tuma ujumbe huu kwa watu wote walio uhamishoni kusema: ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Shemaya Mnehelami: Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, hata ingawa sikumtuma, naye amewafanya kuamini uongo,
JER 29:32 hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Hakika nitamwadhibu Shemaya Mnehelami pamoja na uzao wake. Hapatakuwa na yeyote atakayebaki miongoni mwa watu hawa, wala hataona mema nitakayowatendea watu wangu, asema Mwenyezi Mungu, kwa sababu ametangaza uasi dhidi yangu.’ ”
JER 30:1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
JER 30:2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Andika katika kitabu maneno yote niliyonena na wewe.
JER 30:3 Siku zinakuja,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘nitakapowaleta watu wangu Israeli na Yuda kutoka uhamishoni, na kuwarudisha katika nchi niliyowapa baba zao ili kuimiliki,’ asema Mwenyezi Mungu.”
JER 30:4 Haya ndio maneno aliyoyanena Mwenyezi Mungu kuhusu Israeli na Yuda:
JER 30:5 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Vilio vya woga vinasikika: hofu kuu, wala si amani.
JER 30:6 Ulizeni na mkaone: Je, mwanaume aweza kuzaa watoto? Kwa nini basi ninaona kila mwanaume mwenye nguvu ameweka mikono yake tumboni kama mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa, kila uso ukigeuka rangi kabisa?
JER 30:7 Ole! Kwa kuwa siku ile itakuwa ya kutisha. Hakutakuwa na nyingine kama hiyo. Utakuwa wakati wa dhiki kwa Yakobo, lakini ataokolewa kutoka dhiki hiyo.
JER 30:8 “ ‘Katika siku ile,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nitaivunja nira kutoka shingoni mwao na kuvipasua vifungo vyao; wageni hawatawafanya tena watumwa.
JER 30:9 Badala yake, watamtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na Daudi mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.
JER 30:10 “ ‘Hivyo usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu, usifadhaike, ee Israeli,’ asema Mwenyezi Mungu. ‘Hakika, nitakuokoa kutoka mbali, wazao wako kutoka nchi ya uhamisho wao. Yakobo atakuwa tena na amani na usalama, wala hakuna atakayemtia hofu.
JER 30:11 Mimi niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,’ asema Mwenyezi Mungu. ‘Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote nilikokuwa nimewatawanya, sitawaangamiza ninyi kabisa. Nitawaadhibu, lakini kwa haki. Sitawaacha kabisa bila adhabu.’
JER 30:12 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Kidonda chako hakina dawa, jeraha lako haliponyeki.
JER 30:13 Hakuna yeyote wa kukutetea katika shauri lako, hakuna dawa ya kidonda chako, wewe hutapona.
JER 30:14 Wale walioungana nawe wote wamekusahau, hawajali chochote kukuhusu wewe. Nimekupiga vile adui angekupiga, na kukuadhibu vile mtu mkatili angekuadhibu, kwa sababu hatia yako ni kubwa mno, na dhambi zako ni nyingi sana.
JER 30:15 Kwa nini unalia kwa ajili ya jeraha lako, yale maumivu yako yasiyoponyeka? Kwa sababu ya uovu wako mkubwa na dhambi zako nyingi nimekufanyia mambo haya.
JER 30:16 “ ‘Lakini watu wote wakuangamizao wataangamizwa; adui zako wote wataenda uhamishoni. Wale wote wakutekao nyara watatekwa nyara; wote wakufanyao mateka nitawafanya mateka.
JER 30:17 Lakini nitakurudishia afya yako na kuyaponya majeraha yako,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘kwa sababu umeitwa mwenye kutupwa, Sayuni ambaye hakuna yeyote anayekujali.’
JER 30:18 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Nitarudisha baraka za mahema ya Yakobo, na kuhurumia maskani zake. Mji utajengwa tena juu ya magofu yake, nalo jumba la kifalme litasimama mahali pake halisi.
JER 30:19 Nyimbo za kushukuru zitatoka kwao na sauti ya furaha. Nitaiongeza idadi yao wala hawatapungua, nitawapa heshima na hawatadharauliwa.
JER 30:20 Watoto wao watakuwa kama walivyokuwa siku za zamani, nayo jumuiya yao itaimarishwa mbele yangu; nitawaadhibu wote wanaowadhulumu.
JER 30:21 Mmoja wao atakuwa kiongozi wao; mtawala wao atainuka miongoni mwao. Nitamleta karibu nami, naye atanikaribia mimi, kwa maana ni nani yule atakayejitolea kuwa karibu nami?’ asema Mwenyezi Mungu.
JER 30:22 ‘Kwa hiyo ninyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.’ ”
JER 30:23 Tazama, tufani ya Mwenyezi Mungu italipuka kwa ghadhabu, upepo wa kisulisuli uendao kasi utashuka juu ya vichwa vya waovu.
JER 30:24 Hasira kali ya Mwenyezi Mungu haitarudi nyuma hadi atakapotimiza makusudi yote ya moyo wake. Siku zijazo mtayaelewa haya.
JER 31:1 “Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 31:2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Watu watakaopona upanga watapata upendeleo jangwani; nitakuja niwape Israeli pumziko.”
JER 31:3 Mwenyezi Mungu alitutokea zamani, akisema: “Nimekupenda kwa upendo wa milele, nimekuvuta kwa wema.
JER 31:4 Nitakujenga tena, nawe utajengeka upya, ewe Bikira Israeli. Utachukua tena matari yako na kwenda kucheza na wanaofurahi.
JER 31:5 Utapanda tena shamba la mizabibu juu ya vilima vya Samaria, wakulima watapanda na kufurahia matunda yake.
JER 31:6 Siku inakuja ambapo walinzi watapiga kelele juu ya vilima vya Efraimu, wakisema, ‘Njooni, twendeni juu Sayuni, kwake Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.’ ”
JER 31:7 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mshangilieni aliye mkuu wa mataifa. Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme, ‘Ee Mwenyezi Mungu, okoa watu wako, mabaki ya Israeli.’
JER 31:8 Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia. Miongoni mwao watakuwa vipofu na viwete, mama wajawazito na wenye uchungu wa kuzaa. Umati mkubwa wa watu watarudi.
JER 31:9 Watakuja wakilia; wataomba wakati ninawarudisha. Nitawaongoza kando ya vijito vya maji, katika njia iliyonyooka hawatajikwaa, kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli, naye Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.
JER 31:10 “Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi mataifa, litangazeni katika nchi za pwani ya mbali: ‘Yeye aliyewatawanya Israeli atawakusanya na atalichunga kundi lake la kondoo kama mchungaji.’
JER 31:11 Mwenyezi Mungu atamlipia fidia Yakobo na kuwakomboa mkononi mwa walio na nguvu kuliko wao.
JER 31:12 Watakuja na kupiga kelele kwa furaha katika miinuko ya Sayuni; watashangilia ukarimu wa Mwenyezi Mungu: nafaka, divai mpya na mafuta, wana-kondoo wachanga na ndama wa makundi ya ng’ombe nitakaowapa. Watakuwa kama bustani iliyoneshewa vizuri, wala hawatahuzunika tena.
JER 31:13 Kisha wanawali watacheza na kufurahi, vijana wa kiume na wazee pia. Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha, nitawapa faraja na furaha badala ya huzuni.
JER 31:14 Nitawashibisha makuhani kwa wingi, nao watu wangu watajazwa kwa ukarimu wangu,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 31:15 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Sauti imesikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akiwalilia watoto wake na anakataa kufarijiwa, kwa sababu watoto wake hawako tena.”
JER 31:16 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Izuie sauti yako kulia, na macho yako yasitoe machozi, kwa kuwa kazi yako itapata thawabu,” asema Mwenyezi Mungu. “Watarudi kutoka nchi ya adui.
JER 31:17 Kwa hiyo kuna tumaini kwa siku zijazo,” asema Mwenyezi Mungu. “Watoto wako watarudi nchi yao yenyewe.
JER 31:18 “Hakika nimeyasikia maombolezo ya Efraimu: ‘Ulinirudi kama ndama mkaidi, nami nimekubali kutii. Unirudishe, nami nitarudi, kwa sababu wewe ndiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
JER 31:19 Baada ya kupotea, nilitubu; baada ya kuelewa, nilijipiga kifua. Niliaibika na kuona haya kwa sababu niliibeba aibu ya ujana wangu.’
JER 31:20 Je, Efraimu si mwanangu mpendwa, mtoto ninayependezwa naye? Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake, bado ninamkumbuka. Kwa hiyo moyo wangu unamwonea shauku, nina huruma kubwa kwa ajili yake,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 31:21 “Weka alama za barabara, weka vibao vya kuelekeza. Zingatia vyema njia kuu, barabara ile unayoipita. Rudi, ee Bikira Israeli, rudi kwenye miji yako.
JER 31:22 Utatangatanga hata lini, ee binti usiye mwaminifu? Mwenyezi Mungu ameumba kitu kipya duniani: mwanamke atamlinda mwanaume.”
JER 31:23 Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo, “Nitakapowarudisha toka nchi ya kutekwa kwenu, watu walio katika nchi ya Yuda na miji yake kwa mara nyingine tena watatumia maneno haya: ‘Mwenyezi Mungu akubariki, ee makao ya haki, ee mlima mtakatifu.’
JER 31:24 Watu wataishi pamoja katika Yuda na miji yake yote, wakulima na wote wanaohamahama na mifugo yao.
JER 31:25 Nitawaburudisha waliochoka na kuwatuliza walio na huzuni.”
JER 31:26 Kwa jambo hili niliamka na kuangalia pande zote. Usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.
JER 31:27 Mwenyezi Mungu asema, “Siku zinakuja, nitakapoongeza idadi ya watu, na kuzidisha hesabu ya mifugo katika nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.
JER 31:28 Kama vile nilivyowaangalia ili kung’oa na kubomoa, kuharibu, kuangamiza na kuleta maafa juu yao, vivyo hivyo nitawaangalia ili kujenga na kupanda,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 31:29 “Katika siku hizo, watu hawatasema tena, “ ‘Baba wamekula zabibu chachu, nayo meno ya watoto yakatiwa ganzi.’
JER 31:30 Badala yake, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe; yeyote alaye zabibu chachu, meno yake mwenyewe yatatiwa ganzi.
JER 31:31 “Siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.
JER 31:32 Halitafanana na agano nililofanya na baba zao wakati nilipowashika mkono kuwaongoza watoke Misri, kwa sababu walivunja agano langu, ijapokuwa nilikuwa mume kwao,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 31:33 “Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli baada ya siku zile,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitaweka sheria yangu katika nia zao, na kuiandika mioyoni mwao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
JER 31:34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake, wala mtu kumfundisha ndugu yake, akisema, ‘Mjue Mwenyezi Mungu,’ kwa sababu wote watanijua mimi, kuanzia aliye mdogo hata aliye mkubwa kuliko wote,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”
JER 31:35 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyefanya jua liwake mchana, yeye anayeamuru mwezi na nyota kung’aa usiku, yeye anayeichafua bahari ili mawimbi yake yangurume; Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake:
JER 31:36 “Ikiwa amri hizi zitaondoka machoni pangu,” asema Mwenyezi Mungu, “ndipo wazao wa Israeli watakoma kuwa taifa mbele yangu daima.”
JER 31:37 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika na misingi ya dunia chini ikaweza kuchunguzwa, ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli kwa sababu ya yote waliyoyatenda,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 31:38 “Siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “mji huu utakapojengwa upya kwa ajili yangu, kuanzia mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni.
JER 31:39 Kamba ya kupimia itaanzia hapo kuendelea hadi kwenye kilima cha Garebu, na kisha kugeuka kuelekea Goa,
JER 31:40 wanakotupa maiti na majivu, na maeneo yote kuanzia Bonde la Kidroni upande wa mashariki hadi pembe ya Lango la Farasi patakuwa mahali patakatifu kwa Mwenyezi Mungu. Mji huu kamwe hautang’olewa wala kubomolewa tena.”
JER 32:1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, katika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Nebukadneza.
JER 32:2 Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda.
JER 32:3 Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “Kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka.
JER 32:4 Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo, lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe.
JER 32:5 Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi hadi nitakapomshughulikia, asema Mwenyezi Mungu. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ”
JER 32:6 Yeremia akasema, “Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia kusema:
JER 32:7 Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulikomboa.’
JER 32:8 “Kisha, kama Mwenyezi Mungu alivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, jinunulie.’ “Nilijua kwamba hili lilikuwa neno la Mwenyezi Mungu.
JER 32:9 Hivyo nikalinunua shamba hilo lililoko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nami nikampimia shekeli kumi na saba za fedha.
JER 32:10 Nikatia sahihi na kuweka muhuri hati ya kumiliki, nikaweka mashahidi, na kupima ile fedha kwenye mizani.
JER 32:11 Nikachukua ile hati ya kununulia, nakala iliyotiwa muhuri yenye makubaliano na masharti, pia pamoja na ile nakala isiyo na muhuri,
JER 32:12 nami nikampa Baruku mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, hati hii mbele ya binamu yangu Hanameli, na mbele ya mashahidi waliokuwa wameweka sahihi kwenye hati hii na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ua wa walinzi.
JER 32:13 “Nilimpa Baruku maelezo haya mbele yao:
JER 32:14 ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, yaani nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia, na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu.
JER 32:15 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’
JER 32:16 “Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria hii hati ya kununulia, nilimwomba Mwenyezi Mungu:
JER 32:17 “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza.
JER 32:18 Wewe huonesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
JER 32:19 mashauri yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kwa kadri ya matendo yake.
JER 32:20 Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri, na unafanya hivyo hadi leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo hadi leo.
JER 32:21 Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa utisho mkuu.
JER 32:22 Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi inayotiririka maziwa na asali.
JER 32:23 Waliingia na kuimiliki, lakini hawakukutii wala kuifuata sheria yako. Hawakufanya kile ulichowaamuru kufanya. Hivyo ukaleta maafa haya yote juu yao.
JER 32:24 “Tazama jinsi jeshi lilivyouzingira mji huu ili kuuteka. Kwa sababu ya upanga, njaa, na tauni, mji utatiwa mkononi mwa Wakaldayo wanaoushambulia. Ulilolisema limetokea kama unavyoona.
JER 32:25 Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha mbele ya mashahidi.’ ”
JER 32:26 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema:
JER 32:27 “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wa wote wenye mwili. Je, kuna jambo lolote lililo gumu nisiloliweza?
JER 32:28 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa Wakaldayo, na mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli ambaye atauteka.
JER 32:29 Wakaldayo ambao wanaushambulia mji huu watakuja na kuuchoma moto na kuuteketeza, pamoja na nyumba ambamo watu wamenikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba katika mapaa na kumimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine.
JER 32:30 “Watu wa Israeli na wa Yuda hawakufanya kitu kingine ila uovu mbele zangu tangu ujana wao. Naam, watu wa Israeli hawakufanya kitu kingine ila kunikasirisha kwa kazi ambazo mikono yao imetengeneza, asema Mwenyezi Mungu.
JER 32:31 Tangu siku ulipojengwa hadi sasa, mji huu umenikasirisha na kunighadhibisha kiasi kwamba ni lazima niuondoe machoni pangu.
JER 32:32 Watu wa Israeli na wa Yuda wamenikasirisha kwa uovu wote waliofanya: wao, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao, watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu.
JER 32:33 Walinigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao. Ingawa niliwafundisha tena na tena, hawakupenda kusikiliza wala kuitikia adhabu.
JER 32:34 Waliweka miungu yao ya kuchukiza sana katika nyumba iitwayo kwa Jina langu na kuinajisi.
JER 32:35 Wakajenga mahali pa juu pa kuabudia Baali katika Bonde la Ben-Hinomu, ambapo waliwatoa kafara watoto wao wa kiume na wa kike kwa Moleki, ingawa kamwe sikuwaamuru, wala sikuwaza kwamba watafanya chukizo kama hilo na kumfanya Yuda atende dhambi.
JER 32:36 “Mnasema kuhusu mji huu, ‘Kwa upanga, njaa na tauni, mji utatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli,’ lakini hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo:
JER 32:37 Hakika nitawakusanya kutoka nchi zote nilizowafukuzia katika hasira yangu kali na ghadhabu yangu kuu, nitawarudisha mahali hapa na kuwaruhusu waishi salama.
JER 32:38 Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
JER 32:39 Nitawapa moyo mmoja na kutenda pamoja, ili waniche daima kwa mema yao wenyewe na kwa mema ya watoto wao baada yao.
JER 32:40 Nitafanya nao agano la milele: Kamwe sitaacha kuwatendea mema, nami nitawavuvia kunicha mimi, ili wasinigeuke.
JER 32:41 Nitafurahia kuwatendea mema, na kwa hakika nitawapanda katika nchi hii kwa moyo wangu wote na roho yangu yote.
JER 32:42 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Kama nilivyoleta maafa haya makubwa kwa watu hawa, ndivyo nitakavyowapa mafanikio niliyowaahidi.
JER 32:43 Kwa mara nyingine tena mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo mlisema, ‘Imekuwa ukiwa, isiyo na watu wala wanyama, kwa sababu imetiwa mikononi mwa Wakaldayo.’
JER 32:44 Mashamba yatanunuliwa kwa fedha, na hati zitatiwa sahihi, zitatiwa muhuri na kushuhudiwa katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, katika miji ya Yuda na katika miji ya nchi ya vilima, sehemu za magharibi katika miji ya tambarare na katika Negebu, kwa sababu nitarudisha tena mafanikio yao, asema Mwenyezi Mungu.”
JER 33:1 Yeremia alipokuwa angali amefungwa kwenye ua wa walinzi, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia mara ya pili kusema:
JER 33:2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyeumba dunia, Mwenyezi Mungu aliyeifanya na kuithibitisha, Mwenyezi Mungu ndilo jina lake:
JER 33:3 ‘Niite, nami nitakuitikia, nitakuonesha mambo makubwa, yasiyochunguzika na usiyoyajua.’
JER 33:4 Kwa maana hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu nyumba zilizo mji huu na majumba ya kifalme ya Yuda, zote ambazo zimebomolewa ili zitumiwe kupinga kuzingirwa na jeshi na dhidi ya upanga
JER 33:5 katika kupigana na Wakaldayo: ‘Zitajazwa na maiti za watu nitakaowangamiza kwa hasira na ghadhabu yangu. Nitauficha uso wangu kwa sababu ya maovu yake yote.
JER 33:6 “ ‘Hata hivyo, nitauletea afya na uponyaji, nitawaponya watu wangu na kuwafanya wafurahie amani tele na salama.
JER 33:7 Nitawarudisha Yuda na Israeli kutoka uhamishoni, na kuwajenga tena kama walivyokuwa hapo awali.
JER 33:8 Nitawatakasa dhambi zote walizofanya dhidi yangu, na nitawasamehe dhambi zote za uasi dhidi yangu.
JER 33:9 Kisha mji huu utaniletea utukufu, furaha, sifa na heshima mbele ya mataifa yote ya dunia yatakayosikia mambo yote mazuri ninayoufanyia. Nao watashangaa na kutetemeka kwa ajili ya wingi wa mafanikio na amani nitakayoupatia.’
JER 33:10 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Mnasema kuhusu mahali hapa kwamba, “Ni mahali palipoachwa ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama.” Lakini katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu ambazo zimeachwa, ambazo hazikaliwi na wanadamu wala wanyama, huko kutasikika kwa mara nyingine
JER 33:11 sauti za shangwe na furaha, sauti za bibi arusi na bwana arusi, na sauti za wale waletao sadaka za shukrani katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, wakisema, “ ‘ “Mshukuruni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, kwa maana Mwenyezi Mungu ni mwema; fadhili zake zadumu milele.” Kwa kuwa nitairudishia nchi baraka kama ilivyokuwa hapo awali,’ asema Mwenyezi Mungu.
JER 33:12 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Mahali hapa, palipo ukiwa, bila wanadamu wala wanyama: katika miji yake, yatakuwa tena malisho ya wachungaji kuyalaza makundi yao.
JER 33:13 Katika miji ya nchi ya vilima, ya vilima vya magharibi na ya Negebu, katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mkono wa yeye anayehesabu,’ asema Mwenyezi Mungu.
JER 33:14 “ ‘Siku zinakuja,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘wakati nitakapotimiza ahadi yangu ya rehema niliyoifanya kwa nyumba ya Israeli na kwa nyumba ya Yuda.
JER 33:15 “ ‘Katika siku hizo na wakati huo nitalifanya Tawi la haki lichipuke kutoka ukoo wa Daudi, naye atafanya lile lililo haki na sawa katika nchi.
JER 33:16 Katika siku hizo, Yuda ataokolewa na Yerusalemu ataishi salama. Hili ndilo jina atakaloitwa: Mwenyezi Mungu ni Haki Yetu.’
JER 33:17 Kwa maana hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Daudi kamwe hatakosa mtu wa kukalia kiti cha utawala cha nyumba ya Israeli,
JER 33:18 wala makuhani, ambao ni Walawi, kamwe hawatakosa mtu wa kusimama mbele zangu daima ili kutoa sadaka za kuteketezwa, sadaka ya nafaka, na dhabihu.’ ”
JER 33:19 Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema:
JER 33:20 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Ikiwa mtaweza kuvunja agano langu kuhusu usiku na mchana, ili usiku na mchana visiwepo kwa nyakati zake,
JER 33:21 basi agano langu na Daudi mtumishi wangu, na agano langu na Walawi ambao ni makuhani wanaohudumu mbele zangu, linaweza kuvunjwa, na Daudi hatakuwa tena na mzao wa kutawala kwenye kiti chake cha utawala.
JER 33:22 Nitawafanya wazao wa Daudi mtumishi wangu na Walawi wanaohudumu mbele zangu wengi, wasioweza kuhesabika kama nyota za angani, tena wasiopimika kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.’ ”
JER 33:23 Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema:
JER 33:24 “Je, hujasikia kwamba watu hawa wanasema, ‘Mwenyezi Mungu amezikataa zile falme mbili alizozichagua’? Kwa hiyo wamewadharau watu wangu, na hawawaoni tena kama taifa.
JER 33:25 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Kama sijathibitisha agano langu na usiku na mchana, na kuziweka wakfu sheria za mbingu na nchi,
JER 33:26 basi nitawakataa wazao wa Yakobo na Daudi mtumishi wangu, na sitachagua mmoja wa wanawe kutawala wazao wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Kwa maana nitawarudisha kutoka nchi ya kutekwa kwao na kuwaonea huruma.’ ”
JER 34:1 Wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli na jeshi lake lote, pamoja na falme zote na mataifa katika himaya aliyotawala walikuwa wakipigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na miji yote iliyoizunguka, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
JER 34:2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Nenda kwa Sedekia mfalme wa Yuda umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto.
JER 34:3 Hutaweza kuepuka mkono wake, bali hakika utatekwa na kukabidhiwa kwake. Utamwona mfalme wa Babeli kwa macho yako mwenyewe, naye atazungumza nawe ana kwa ana. Nawe utaenda Babeli.
JER 34:4 “ ‘Lakini sikia ahadi ya Mwenyezi Mungu, ee Sedekia mfalme wa Yuda. Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu wewe: Hutakufa kwa upanga,
JER 34:5 bali utakufa kwa amani. Kama vile watu walivyowasha moto wa maziko kwa heshima ya baba zako, wafalme waliokutangulia, ndivyo watu watakavyowasha moto kwa heshima yako na kuomboleza, wakisema: “Ole, Ee Mwenyezi Mungu!” Mimi mwenyewe ninaweka ahadi hii, asema Mwenyezi Mungu.’ ”
JER 34:6 Ndipo nabii Yeremia akamwambia Sedekia mfalme wa Yuda mambo haya yote huko Yerusalemu,
JER 34:7 wakati jeshi la mfalme wa Babeli lilipokuwa likipigana dhidi ya Yerusalemu na miji mingine ya Yuda iliyokuwa bado imara, yaani Lakishi na Azeka. Hii ilikuwa miji pekee yenye ngome iliyobaki katika Yuda.
JER 34:8 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, baada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu ili kutangaza uhuru kwa watumwa.
JER 34:9 Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake Waebrania, wanawake na wanaume. Hakuna yeyote aliyeruhusiwa kumfanya Myahudi mwenzake kuwa mtumwa.
JER 34:10 Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na hawatawashikilia tena. Wakakubali na wakawaacha huru.
JER 34:11 Lakini baadaye wakabadili mawazo yao, na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru, wakawafanya tena watumwa.
JER 34:12 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema:
JER 34:13 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema,
JER 34:14 ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali.
JER 34:15 Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu.
JER 34:16 Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena.
JER 34:17 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asema Mwenyezi Mungu: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia.
JER 34:18 Watu waliovunja agano langu, na ambao hawakutunza masharti ya agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili, kisha wakatembea kati ya vile vipande vya huyo ndama.
JER 34:19 Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama,
JER 34:20 nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
JER 34:21 “Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu.
JER 34:22 Nitatoa amri, asema Mwenyezi Mungu, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, wautwae na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda ili pasiwe na yeyote atakayeweza kuishi humo.”
JER 35:1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:
JER 35:2 “Nenda kwa jamaa ya Warekabi, uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba ya Mwenyezi Mungu, na uwape divai wanywe.”
JER 35:3 Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi.
JER 35:4 Nikawaleta katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, kilichokuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu, aliyekuwa bawabu.
JER 35:5 Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”
JER 35:6 Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupatia agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu msinywe divai.
JER 35:7 Pia msijenge nyumba wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu. Kamwe msiwe na kitu chochote katika hivi, bali mtaishi katika mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’
JER 35:8 Tumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu alituamuru. Sisi wenyewe, wake zetu, watoto wetu wa kiume na wa kike hatujawahi kunywa divai,
JER 35:9 wala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao.
JER 35:10 Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu.
JER 35:11 Lakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njooni, lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washamu.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”
JER 35:12 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema:
JER 35:13 “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu, na kuyatii maneno yangu?’ asema Mwenyezi Mungu.
JER 35:14 ‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai, na agizo hilo wamelishika. Hadi leo hawanywi divai, kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii.
JER 35:15 Mara kwa mara nimewatuma kwenu watumishi wangu wote, manabii wakisema, “Geukeni, kila mmoja aiache njia yake mbaya, na kutengeneza matendo yake. Msiifuate wala kuitumikia miungu mingine. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza.
JER 35:16 Wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’
JER 35:17 “Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza. Niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”
JER 35:18 Kisha Yeremia akaiambia jamaa ya Warekabi, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: ‘Mmetii amri ya baba yenu Yonadabu, na mmefuata mafundisho yake yote na mmefanya kila kitu alichowaamuru.’
JER 35:19 Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa kamwe kuwa na mtu wa kunitumikia mimi.’ ”
JER 36:1 Katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia nabii Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kusema:
JER 36:2 “Chukua kitabu uandike ndani yake maneno yote niliyonena nawe kuhusu Israeli, Yuda na mataifa mengine yote, tangu nilipoanza kunena nawe wakati wa utawala wa Yosia hadi sasa.
JER 36:3 Labda watu wa Yuda watakaposikia maafa ninayokusudia kuwapiga nayo, kila mmoja wao atageuka kutoka njia zake mbaya, kisha nitasamehe uovu wao na dhambi yao.”
JER 36:4 Hivyo Yeremia akamwita Baruku mwana wa Neria, naye Yeremia alipokuwa akiyakariri maneno yote aliyoyasema Mwenyezi Mungu, Baruku akayaandika katika kitabu.
JER 36:5 Kisha Yeremia akamwambia Baruku, “Nimezuiliwa; mimi siwezi kuingia katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
JER 36:6 Basi wewe nenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu siku ya kufunga, uwasomee watu maneno ya Mwenyezi Mungu kutoka kitabu hiki yale uliyoyaandika kutoka kinywani mwangu. Wasomee watu wote wa Yuda waliofika kutoka miji yao.
JER 36:7 Labda wataomba na kusihi mbele za Mwenyezi Mungu na kila mmoja akageuka kutoka njia zake mbaya, kwa sababu hasira na ghadhabu zilizotamkwa dhidi ya watu hawa na Mwenyezi Mungu ni kubwa.”
JER 36:8 Baruku mwana wa Neria akafanya kila kitu nabii Yeremia alichomwambia kufanya. Alisoma maneno ya Mwenyezi Mungu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu kutoka kile kitabu.
JER 36:9 Katika mwezi wa tisa wa mwaka wa tano wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati wa kufunga mbele za Mwenyezi Mungu, ilitangazwa kwa watu wote waliokuwa Yerusalemu, na wale wote waliokuwa wamekuja kutoka miji ya Yuda.
JER 36:10 Kutoka chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruku akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu maneno ya Yeremia katika kile kitabu.
JER 36:11 Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Mwenyezi Mungu kutoka kile kitabu,
JER 36:12 alishuka hadi chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote: yaani Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na maafisa wengine wote.
JER 36:13 Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruku akiwasomea watu katika kile kitabu,
JER 36:14 maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruku, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu, nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruku mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake.
JER 36:15 Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.” Ndipo Baruku akawasomea kile kitabu.
JER 36:16 Walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruku, “Lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.”
JER 36:17 Kisha wakamuuliza Baruku, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”
JER 36:18 Baruku akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”
JER 36:19 Ndipo wale maafisa wakamwambia Baruku, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu yeyote asijue mahali mlipo.”
JER 36:20 Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu.
JER 36:21 Mfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu. Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka chumba cha Elishama mwandishi, na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme.
JER 36:22 Ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto.
JER 36:23 Hata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni, hadi kitabu chote kikateketea.
JER 36:24 Mfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonesha hofu yoyote, wala hawakuyararua mavazi yao.
JER 36:25 Hata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu, yeye hakuwasikiliza.
JER 36:26 Badala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli, na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruku na nabii Yeremia. Lakini Mwenyezi Mungu alikuwa amewaficha.
JER 36:27 Baada ya mfalme kuchoma kile kitabu kilichokuwa na yale maneno Baruku aliyokuwa ameyaandika kutoka kinywani mwa Yeremia, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Yeremia likisema:
JER 36:28 “Chukua kitabu kingine na uandike juu yake maneno yote yaliyokuwa katika kile kitabu cha kwanza, ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda amekiteketeza kwa moto.
JER 36:29 Mwambie pia Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ulikiteketeza kile kitabu ukasema, “Kwa nini uliandika kwenye kitabu kwamba kwa hakika mfalme wa Babeli angekuja na kuangamiza nchi hii, na kuwakatilia mbali watu na wanyama kutoka humo?”
JER 36:30 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Hatakuwa na mtu yeyote atakayekalia kiti cha utawala cha Daudi; maiti yake itatupwa nje kwenye joto wakati wa mchana na kupigwa na baridi wakati wa usiku.
JER 36:31 Nitamwadhibu yeye, watoto wake na watumishi wake kwa ajili ya uovu wao. Nitaleta juu yao na wote wanaoishi Yerusalemu na watu wa Yuda kila maafa niliyoyasema dhidi yao, kwa sababu hawajasikiliza.’ ”
JER 36:32 Kisha Yeremia akachukua kitabu kingine na kumpa mwandishi Baruku mwana wa Neria, naye kama Yeremia alivyosema, Baruku akaandika juu yake maneno yote ya kile kitabu ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda alikuwa amekichoma moto, na maneno mengine mengi yaliyofanana na hayo yaliyoongezewa humo.
JER 37:1 Sedekia mwana wa Yosia akafanywa kuwa mfalme wa Yuda na Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye akatawala mahali pa Yehoyakini mwana wa Yehoyakimu.
JER 37:2 Lakini sio Sedekia, wala watumishi wake, wala watu wa nchi walisikiliza maneno ya Mwenyezi Mungu aliyonena kupitia kwa nabii Yeremia.
JER 37:3 Hata hivyo, Mfalme Sedekia akamtuma Yehukali mwana wa Shelemia, pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia na ujumbe huu: “Tafadhali utuombee kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
JER 37:4 Wakati huu Yeremia alikuwa huru kuingia na kutoka katikati ya watu, kwa sababu alikuwa bado hajatiwa gerezani.
JER 37:5 Jeshi la Farao lilikuwa limetoka Misri, nao Wakaldayo waliokuwa wameuzingira Yerusalemu kwa majeshi waliposikia taarifa kuhusu jeshi hilo walijiondoa Yerusalemu.
JER 37:6 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia nabii Yeremia kusema:
JER 37:7 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambie mfalme wa Yuda aliyekutuma uniulize mimi, ‘Jeshi la Farao lililokuja kukusaidia litarudi katika nchi yake yenyewe, yaani Misri.
JER 37:8 Kisha Wakaldayo watarudi na kushambulia mji huu, watauteka na kuuchoma moto.’
JER 37:9 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Msijidanganye wenyewe mkifikiri, ‘Hakika Wakaldayo watatuacha na kwenda zao.’ Hakika hawatawaacha!
JER 37:10 Hata kama mngelishinda jeshi lote la Wakaldayo linalowashambulia ninyi, na wakawa ni watu waliojeruhiwa tu waliobaki kwenye mahema yao, wangetoka na kuuchoma mji huu moto.”
JER 37:11 Baada ya jeshi la Wakaldayo kujiondoa kutoka Yerusalemu kwa sababu ya jeshi la Farao,
JER 37:12 Yeremia akaondoka mjini kwenda nchi ya Benyamini ili akapate huko sememu yake ya milki miongoni mwa watu.
JER 37:13 Lakini alipofika kwenye Lango la Benyamini, mkuu wa walinzi aliyeitwa Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, akamkamata Yeremia na kusema, “Wewe unaenda kujiunga na Wakaldayo!”
JER 37:14 Yeremia akasema, “Hiyo si kweli, mimi sijiungi na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakumsikiliza; badala yake, akamkamata Yeremia na kumpeleka kwa maafisa.
JER 37:15 Wakamkasirikia Yeremia, wakaamuru apigwe, na akafungwa katika nyumba ya Yonathani mwandishi waliyokuwa wameifanya kuwa gereza.
JER 37:16 Yeremia akawekwa kwenye chumba kilichofukuliwa chini, kilichojengwa kwa zege ndani ya gereza chini ya ngome, akakaa huko kwa muda mrefu.
JER 37:17 Kisha Mfalme Sedekia akatumana aletwe katika jumba la kifalme, mahali alipomuuliza kwa siri, “Je, kuna neno lolote kutoka kwa Mwenyezi Mungu?” Yeremia akajibu, “Ndiyo, utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli.”
JER 37:18 Kisha Yeremia akamwambia Mfalme Sedekia, “Nimefanya kosa gani dhidi yako na maafisa wako au watu hawa, hata ukanifunga gerezani?
JER 37:19 Wako wapi manabii wako waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babeli hatakushambulia wewe wala nchi hii’?
JER 37:20 Lakini sasa, bwana wangu mfalme, tafadhali sikiliza. Niruhusu nilete maombi yangu mbele yako, usinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani mwandishi, nisije nikafia humo.”
JER 37:21 Ndipo Mfalme Sedekia akatoa maagizo Yeremia awekwe katika ua wa walinzi, na apewe mkate kutoka mitaa ya waokaji kila siku hadi mikate yote katika mji itakapokwisha. Kwa hiyo Yeremia akabaki katika ua wa walinzi.
JER 38:1 Shefatia mwana wa Matani, na Gedalia mwana wa Pashuri, na Yehukali mwana wa Shelemia, na Pashuri mwana wa Malkiya wakasikia kile Yeremia alichokuwa akiwaambia watu wote aliposema,
JER 38:2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Yeyote akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni, lakini yeyote atakayejisalimisha kwa Wakaldayo ataishi. Atakayeyatoa maisha yake kama nyara, ataishi.’
JER 38:3 Tena hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Mji huu kwa hakika utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babeli, ambaye atauteka.’ ”
JER 38:4 Ndipo maafisa wakamwambia mfalme, “Mtu huyu imempasa kuuawa. Anawakatisha tamaa askari waliobaki katika mji huu na watu wote kutokana na mambo anayowaambia. Mtu huyu hawatakii mema watu hawa, bali maangamizi yao.”
JER 38:5 Mfalme Sedekia akajibu, “Yeye yuko mikononi mwenu! Mfalme hawezi kufanya lolote kuwapinga ninyi.”
JER 38:6 Basi wakamchukua Yeremia na kumtia kwenye kisima cha Malkiya, mwana wa mfalme, kilichokuwa katika ua wa walinzi. Wakamteremsha Yeremia kwa kamba ndani ya kisima. Hakikuwa na maji ndani yake, ila tope tu, naye Yeremia akazama ndani ya matope.
JER 38:7 Lakini Ebed-Meleki Mkushi, aliyekuwa afisa katika jumba la kifalme, akasikia kuwa walikuwa wamemtia Yeremia ndani ya kisima. Mfalme alipokuwa ameketi katika Lango la Benyamini,
JER 38:8 Ebed-Meleki akatoka nje ya jumba la kifalme na kumwambia,
JER 38:9 “Mfalme bwana wangu, watu hawa wamefanya uovu kwa yote waliomtendea nabii Yeremia. Wamemtupa ndani ya kisima, ambamo atakufa kwa njaa chakula kitakapokosekana katika mji.”
JER 38:10 Basi mfalme akamwamuru Ebed-Meleki Mkushi, akisema, “Chukua watu thelathini kutoka hapa pamoja nawe, mkamtoe nabii Yeremia huko kwenye kisima kabla hajafa.”
JER 38:11 Basi Ebed-Meleki akawachukua watu pamoja naye, wakaenda kwenye chumba kilicho chini ya hazina, ndani ya jumba la kifalme. Akachukua matambaa makuukuu pamoja na nguo zilizochakaa kutoka huko, na kumshushia Yeremia kwa kamba ndani ya kisima.
JER 38:12 Ebed-Meleki Mkushi akamwambia Yeremia, “Weka haya matambaa makuukuu na hizo nguo zilizochakaa makwapani ili kuzuia kamba.” Yeremia akafanya hivyo,
JER 38:13 nao wakamvuta juu kwa kamba na kumtoa katika kisima. Yeremia akakaa katika ua wa walinzi.
JER 38:14 Ndipo Mfalme Sedekia akatuma watu wamwitie nabii Yeremia wamlete kwake kwenye ingilio la tatu la Hekalu la Mwenyezi Mungu. Mfalme akamwambia Yeremia, “Ninataka kukuuliza jambo fulani, usinifiche kitu chochote.”
JER 38:15 Yeremia akamwambia Sedekia, “Nikikupa jibu, je, hutaniua? Hata nikikupa ushauri, wewe hutanisikiliza.”
JER 38:16 Lakini Mfalme Sedekia akamwapia Yeremia kiapo hiki kwa siri, akisema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, ambaye ametupatia pumzi, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako.”
JER 38:17 Kisha Yeremia akamwambia Sedekia, “Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: ‘Ikiwa utajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, maisha yako yatasalimika, na mji huu hautateketezwa kwa moto. Pia wewe na jamaa yako mtaishi.
JER 38:18 Lakini ikiwa hutajisalimisha kwa maafisa wa jeshi la mfalme wa Babeli, mji huu utatiwa mikononi mwa Wakaldayo; nao watauteketeza kwa moto, nawe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao.’ ”
JER 38:19 Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Ninawaogopa Wayahudi ambao wamekimbilia kwa Wakaldayo, kwa kuwa Wakaldayo wanaweza kunitia mikononi mwao, nao wakanitenda vibaya.”
JER 38:20 Yeremia akajibu, “Hawatakutia mikononi mwao. Mtii Mwenyezi Mungu kwa kufanya kile ninachokuambia. Kisha utafanikiwa na maisha yako yatakuwa salama.
JER 38:21 Lakini ukikataa kujisalimisha, hili ndilo Mwenyezi Mungu alilonifunulia:
JER 38:22 Wanawake wote walioachwa katika jumba la kifalme la mfalme wa Yuda wataletwa mbele ya maafisa wa mfalme wa Babeli. Wanawake hao watakuambia: “ ‘Walikupotosha na kukushinda, wale rafiki zako uliowaamini. Miguu yako imezama matopeni; rafiki zako wamekuacha.’
JER 38:23 “Wake zako wote na watoto wataletwa na kutiwa mikononi mwa Wakaldayo. Wewe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao. Lakini utatekwa na mfalme wa Babeli, na mji huu utateketezwa kwa moto.”
JER 38:24 Kisha Sedekia akamwambia Yeremia, “Usiruhusu mtu yeyote ajue kuhusu haya mazungumzo, la sivyo utakufa.
JER 38:25 Maafisa wakisikia kwamba nimezungumza nawe, nao wakakujia na kusema, ‘Tuambie kile ulichozungumza na mfalme na kile mfalme alichokuambia, usitufiche au sivyo tutakuua,’
JER 38:26 basi waambie, ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme asinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani nisije nikafia humo.’ ”
JER 38:27 Viongozi wote wakamjia Yeremia na kumuuliza, naye Yeremia akawaambia kila kitu mfalme alichomwagiza kusema. Kisha hawakusema lolote zaidi na Yeremia kwa sababu hakuna hata mmoja aliyekuwa amesikia mazungumzo yake na mfalme.
JER 38:28 Naye Yeremia akabaki katika ua wa walinzi hadi siku Yerusalemu ilipotekwa. Hivi ndivyo Yerusalemu ilivyotwaliwa:
JER 39:1 Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Mfalme Sedekia wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu na akauzingira.
JER 39:2 Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne wa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia, ukuta wa mji ulibomolewa.
JER 39:3 Kisha maafisa wote wa mfalme wa Babeli wakaja na kuketi kwenye Lango la Kati: Nergal-Shareza wa Samgari, Nebo-Sarsekimu afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa mwenye cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli.
JER 39:4 Mfalme Sedekia wa Yuda na askari wote walipowaona, wakakimbia na kuondoka mjini usiku kwa njia ya bustani ya mfalme, kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili, wakaelekea Araba.
JER 39:5 Lakini jeshi la Wakaldayo wakawafuatia na kumpata Sedekia katika nchi tambarare za Yeriko. Wakamkamata na kumpeleka kwa Nebukadneza mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ambapo alimtangazia hukumu.
JER 39:6 Huko Ribla, mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake, na pia akawaua wakuu wote wa Yuda.
JER 39:7 Kisha akayang’oa macho ya Sedekia na kumfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
JER 39:8 Jeshi la Wakaldayo likachoma moto jumba la kifalme na nyumba za watu, na kuzibomoa kuta za Yerusalemu.
JER 39:9 Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme akawachukua na kuwapeleka uhamishoni Babeli watu waliokuwa wamebaki ndani ya mji, pamoja na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake, na watu wengine wote.
JER 39:10 Lakini Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi aliwabakiza baadhi ya watu maskini katika nchi ya Yuda, ambao hawakuwa na kitu. Naye wakati huo akawapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
JER 39:11 Basi, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa ametoa maagizo kuhusu Yeremia kupitia Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme akisema:
JER 39:12 “Mchukue umtunze. Usimdhuru, lakini umfanyie chochote anachotaka.”
JER 39:13 Basi Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi, Nebushazbani afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa wa cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli
JER 39:14 wakatuma watu kumwondoa Yeremia kutoka ua wa walinzi. Wakamkabidhi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ili amrudishe nyumbani mwake. Kwa hiyo akabaki miongoni mwa watu wake mwenyewe.
JER 39:15 Yeremia alipokuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia kusema:
JER 39:16 “Nenda ukamwambie Ebed-Meleki Mkushi, ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kutimiza maneno yangu dhidi ya mji huu kwa maafa, wala si kwa mema. Wakati huo, hayo yatatimizwa mbele ya macho yako.
JER 39:17 Lakini siku hiyo nitakuokoa, asema Mwenyezi Mungu; hutatiwa mikononi mwa wale unaowaogopa.
JER 39:18 Nitakuokoa; hutaanguka kwa upanga, maisha yako yatakuwa salama, kwa sababu unanitumaini, asema Mwenyezi Mungu.’ ”
JER 40:1 Neno likamjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu baada ya Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli.
JER 40:2 Mkuu wa askari walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aliamuru maafa haya kutokea mahali hapa.
JER 40:3 Sasa Mwenyezi Mungu ameyaleta haya, amefanya sawasawa na alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu na hamkumtii.
JER 40:4 Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Ukiona ni vema, twende pamoja hadi Babeli; nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.”
JER 40:5 Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.” Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake.
JER 40:6 Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.
JER 40:7 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia mwana wa Ahikamu kuwa mtawala wa nchi, na amemweka kuwa kiongozi wa wanaume, wanawake na watoto waliokuwa maskini zaidi katika nchi ambao hawakuchukuliwa kwenda uhamishoni Babeli,
JER 40:8 wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao.
JER 40:9 Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani akaapa ili kuwatia moyo, wao na watu wao. Akasema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.
JER 40:10 Mimi mwenyewe nitakaa Mispa ili kuwawakilisha mbele ya Wakaldayo wanaotujia, lakini ninyi mtavuna divai, matunda ya kiangazi na mafuta, nanyi mtaweka katika vyombo vyenu vya kuhifadhia, na kuishi katika miji mliyojitwalia.”
JER 40:11 Wayahudi wote waliokuwa Moabu, Amoni, Edomu na nchi nyingine zote waliposikia kwamba mfalme wa Babeli ameacha mabaki ya watu katika Yuda na amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kuwa mtawala wao,
JER 40:12 wakarudi wote katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mispa, kutoka nchi zote ambazo walikuwa wametawanywa. Nao wakavuna divai na matunda tele wakati wa kiangazi.
JER 40:13 Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi wakamjia Gedalia huko Mispa
JER 40:14 na kumwambia, “Je, hujui kwamba Baalisi mfalme wa Waamoni amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania akuue?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu hakuwaamini.
JER 40:15 Kisha Yohanani mwana wa Karea akamwambia Gedalia kwa siri huko Mispa, “Acha niende nikamuue Ishmaeli mwana wa Nethania, wala hakuna atakayejua. Kwa nini akuue na kusababisha Wayahudi wote waliokuzunguka watawanyike, na mabaki wa Yuda waangamie?”
JER 40:16 Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu akamwambia Yohanani mwana wa Karea, “Usifanye jambo hilo! Unalosema kuhusu Ishmaeli si kweli.”
JER 41:1 Katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme, naye alikuwa mmoja wa maafisa wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa. Walipokuwa wakila pamoja huko,
JER 41:2 Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na wale watu kumi waliokuwa pamoja naye waliinuka na kumuua Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kwa upanga; wakamuua yule ambaye mfalme wa Babeli alikuwa amemteua awe mtawala wa nchi.
JER 41:3 Ishmaeli akawaua pia Wayahudi wote waliokuwa na Gedalia huko Mispa, pamoja na askari Wakaldayo waliokuwa huko.
JER 41:4 Siku moja baada ya kuuawa kwa siri kwa Gedalia, kabla mtu yeyote hajafahamu jambo hilo,
JER 41:5 watu themanini waliokuwa wamenyoa ndevu zao, waliorarua nguo zao na kujikatakata walikuja kutoka Shekemu, Shilo na Samaria wakileta sadaka za nafaka na uvumba katika nyumba ya Mwenyezi Mungu.
JER 41:6 Ishmaeli mwana wa Nethania akaondoka Mispa ili kwenda kuwalaki, huku akilia alipokuwa akienda. Alipokutana nao, akasema, “Karibuni kwa Gedalia mwana wa Ahikamu.”
JER 41:7 Walipoingia mjini, Ishmaeli mwana wa Nethania na wale watu waliokuwa pamoja naye wakawachinja na kuwatupa ndani ya kisima.
JER 41:8 Lakini watu kumi miongoni mwao wakamwambia Ishmaeli, “Sisi usituue! Tuna ngano na shayiri, mafuta na asali, vilivyofichwa katika shamba.” Kwa hiyo akawaacha na hakuwaua pamoja na wale wengine.
JER 41:9 Basi kile kisima ambacho alitupa zile maiti za watu aliowaua pamoja na Gedalia kilikuwa ni kile kisima ambacho Mfalme Asa alikifanya kuwa sehemu ya ulinzi wake dhidi ya Baasha mfalme wa Israeli. Ishmaeli mwana wa Nethania akakijaza kisima hicho kwa maiti.
JER 41:10 Ishmaeli akawafanya mateka watu wote ambao Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme alikuwa amewaacha huko Mispa na kumweka Gedalia mwana wa Ahikamu juu yao, yaani, binti za mfalme pamoja na watu wote aliokuwa amewaacha huko. Ishmaeli mwana wa Nethania akawachukua mateka na kuondoka nao, akavuka kwenda kwa Waamoni.
JER 41:11 Yohanani mwana wa Karea na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye waliposikia kuhusu uhalifu wote ambao Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa ameufanya,
JER 41:12 waliwachukua watu wao wote kwenda kupigana na Ishmaeli mwana wa Nethania. Wakakutana naye karibu na bwawa kubwa huko Gibeoni.
JER 41:13 Ikawa watu wote waliokuwa na Ishmaeli walipomwona Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wa jeshi waliokuwa pamoja naye, wakafurahi.
JER 41:14 Watu wote ambao Ishmaeli alikuwa amewachukua mateka huko Mispa wakageuka na kumfuata Yohanani mwana wa Karea.
JER 41:15 Lakini Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na watu wake wanane wakamtoroka Yohanani na kukimbilia kwa Waamoni.
JER 41:16 Ndipo Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye wakawaongoza wote walionusurika kutoka Mispa, ambao walipona kutoka mikononi mwa Ishmaeli mwana wa Nethania baada yake kumuua Gedalia mwana wa Ahikamu. Mabaki yao walikuwa askari, wanawake, watoto na matowashi aliowaleta kutoka Gibeoni.
JER 41:17 Kisha wakasafiri hadi Geruth-Kimhamu karibu na Bethlehemu wakiwa njiani kwenda Misri
JER 41:18 ili kuwatoroka Wakaldayo. Waliwaogopa kwa sababu Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa amemuua Gedalia mwana wa Ahikamu, aliyekuwa amewekwa na mfalme wa Babeli kuwa mtawala wa nchi.
JER 42:1 Ndipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia
JER 42:2 Yeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu.
JER 42:3 Omba ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atuambie twende wapi na tufanye nini.”
JER 42:4 Nabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho Mwenyezi Mungu, wala sitawaficha chochote.”
JER 42:5 Kisha wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi Mungu na awe shahidi mwaminifu na wa kweli dhidi yetu, ikiwa hatutafanya kila kitu jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakachokutuma utuambie.
JER 42:6 Likiwa jema au likiwa baya, tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
JER 42:7 Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia.
JER 42:8 Kwa hiyo akawaita Yohanani mwana wa Karea, maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana.
JER 42:9 Akawaambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu:
JER 42:10 ‘Mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawang’oa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo.
JER 42:11 Msimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema Mwenyezi Mungu, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mkononi mwake.
JER 42:12 Nitawaonea huruma ili naye awe na huruma kwenu na kuwarudisha katika nchi yenu.’
JER 42:13 “Lakini mkisema, ‘Hatutakaa katika nchi hii,’ hivyo mkaacha kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,
JER 42:14 na kama mkisema, ‘Hapana, tutaenda kuishi Misri, mahali ambapo hatutaona vita au kusikia sauti ya tarumbeta, au kuwa na njaa ya chakula,’
JER 42:15 basi sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi mabaki ya Yuda. Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Ikiwa mmekusudia kwenda Misri na kufanya makazi huko,
JER 42:16 basi ule upanga mnaouogopa utawapata huko, na njaa mnayoihofia itawafuata huko Misri, nanyi mtafia huko.
JER 42:17 Naam, wote waliokusudia kwenda kuishi Misri watakufa kwa upanga, njaa na tauni; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika au kuokoka maafa nitakayoyaleta juu yao.’
JER 42:18 Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyomwagwa juu ya wale walioishi Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu mtakapoenda Misri. Mtakuwa kitu cha kulaaniwa na kutishiwa, cha kuhukumiwa, na cha kuaibisha; nanyi hamtapaona mahali hapa tena.’
JER 42:19 “Enyi mabaki ya Yuda, Mwenyezi Mungu amewaambia, ‘Msiende Misri.’ Hakikisheni jambo hili: Ninawaonya leo
JER 42:20 kwamba mmefanya kosa kubwa mioyoni mwenu mliponituma kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kusema, ‘Mwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu, nawe utuambie kila kitu atakachosema, nasi tutafanya.’
JER 42:21 Nimewaambieni leo, lakini bado ninyi hamtaki kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, katika yote aliyonituma niwaambie.
JER 42:22 Basi sasa, hakikisheni jambo hili: Mtakufa kwa upanga, njaa na tauni mahali pale mnataka kwenda kuishi.”
JER 43:1 Yeremia alipomaliza kuwaambia watu maneno yote ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, yaani kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amemtuma kuwaambia,
JER 43:2 Azaria mwana wa Hoshaya, na Yohanani mwana wa Karea, na watu wote wenye kiburi wakamwambia Yeremia, “Wewe unasema uongo! Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, hajakutuma kusema, ‘Kamwe msiende Misri kukaa huko.’
JER 43:3 Lakini Baruku mwana wa Neria anakuchochea dhidi yetu ili ututie mikononi mwa Wakaldayo, ili watuue au watuchukue uhamishoni Babeli.”
JER 43:4 Basi Yohanani mwana wa Karea, na maafisa wote wa jeshi, na watu wote wakakataa kutii amri ya Mwenyezi Mungu ya kukaa katika nchi ya Yuda.
JER 43:5 Badala yake, Yohanani mwana wa Karea na maafisa wote wa jeshi wakawaongoza mabaki yote ya Yuda waliokuwa wamerudi kuishi katika nchi ya Yuda kutoka mataifa yote ambayo walikuwa wametawanywa.
JER 43:6 Pia wakawaongoza wanaume wote, wanawake na watoto, na binti za mfalme ambao Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme alikuwa amewaacha na Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, na nabii Yeremia, na Baruku mwana wa Neria.
JER 43:7 Kwa hiyo wakaingia Misri kwa kutokumtii Mwenyezi Mungu, wakaenda hadi Tapanesi.
JER 43:8 Huko Tapanesi neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema:
JER 43:9 “Wayahudi wakiwa wanaona, chukua baadhi ya mawe makubwa na kuyazika katika udongo wa mfinyanzi katika njia iliyojengwa kwa matofali katika lango la jumba la kifalme la Farao huko Tapanesi.
JER 43:10 Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Nitamtumania mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli, nami nitakiweka kiti chake cha utawala juu ya haya mawe niliyoyazika hapa, naye atatandaza hema lake la ufalme juu yake.
JER 43:11 Atakuja na kuishambulia Misri; atawaua waliokusudiwa kuuawa, atawateka waliokusudiwa kutekwa, na atawaua kwa upanga waliokusudiwa kuuawa kwa upanga.
JER 43:12 Atachoma moto mahekalu ya miungu ya Misri, atachoma mahekalu yao na kuteka miungu yao. Kama mchungaji ajizungushiavyo vazi lake, ndivyo atakavyojizungushia Misri na kuondoka mahali hapo kwa amani.
JER 43:13 Huko, ndani ya hekalu la jua nchini Misri, atabomoa nguzo za ibada, na kuteketeza kwa moto mahekalu ya miungu ya Misri.’ ”
JER 44:1 Neno hili lilimjia Yeremia kuhusu Wayahudi wote walioishi Misri, huko Migdoli, Tapanesi na Memfisi, katika nchi ya Pathrosi, kusema:
JER 44:2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Mliona maangamizi makubwa niliyoyaleta juu ya Yerusalemu na juu ya miji yote ya Yuda. Leo imeachwa ukiwa na magofu
JER 44:3 kwa sababu ya uovu waliokuwa wameufanya. Walinikasirisha kwa kufukiza uvumba na kwa kuabudu miungu mingine ambayo haikuwahi kujulikana kwao, wala kwenu na mababu zenu.
JER 44:4 Tena na tena, niliwatuma watumishi wangu manabii ambao walisema, ‘Msifanye jambo hili la kuchukiza ambalo nalichukia!’
JER 44:5 Lakini hawakusikiliza wala hawakujali, hawakugeuka ili kuuacha uovu wao, wala hawakuacha kufukiza uvumba kwa miungu mingine.
JER 44:6 Kwa hiyo hasira yangu kali ilimwagika, ikawaka dhidi ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, na kuifanya ukiwa na magofu kama ilivyo leo.
JER 44:7 “Basi hili ndilo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Kwa nini kujiletea maafa makubwa kama haya juu yenu kwa kujikatilia mbali kutoka Yuda wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, hata kujiacha bila mabaki?
JER 44:8 Kwa nini kuichochea hasira yangu kwa kazi ya mikono yenu, kuifukizia uvumba miungu mingine huko Misri, mahali mlipokuja kuishi? Mtajiangamiza wenyewe na kujifanya kitu cha kulaania na shutumu miongoni mwa mataifa yote duniani.
JER 44:9 Je, mmesahau uovu uliotendwa na baba zenu, na wafalme na malkia wa Yuda, na uovu uliofanywa na ninyi na wake zenu katika nchi ya Yuda na barabara za Yerusalemu?
JER 44:10 Hadi leo hawajajinyenyekeza au kuonesha heshima, wala hawajafuata sheria yangu na amri nilizoweka mbele yenu na baba zenu.
JER 44:11 “Kwa hiyo, hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Mimi nimekusudia kuleta maafa juu yenu, na kuiangamiza Yuda yote.
JER 44:12 Nitawaondoa mabaki ya Yuda waliokusudia kwenda Misri kukaa huko. Wote wataangamia huko Misri, wataanguka kwa upanga au kufa kwa njaa. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana, watakufa kwa upanga au njaa. Watakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha laumu na shutumu.
JER 44:13 Nitawaadhibu wanaoishi Misri kwa upanga, njaa na tauni kama nilivyoiadhibu Yerusalemu.
JER 44:14 Hakuna hata mmoja wa mabaki ya Yuda ambaye ameenda kuishi Misri atakayeepuka au kunusurika ili kurudi katika nchi ya Yuda, ambayo wanaitamani sana kurudi na kuishi ndani yake, hakuna hata mmoja atakayerudi isipokuwa wakimbizi wachache.”
JER 44:15 Kisha wanaume wote ambao walijua kwamba wake zao walikuwa wakifukiza uvumba kwa miungu mingine, pamoja na wanawake wote waliokuwako, yaani kusanyiko kubwa na watu wote walioishi nchi ya Misri na Pathrosi, wakamwambia Yeremia,
JER 44:16 “Hatutausikiliza ujumbe uliotuambia katika jina la Mwenyezi Mungu!
JER 44:17 Hakika tutafanya kila kitu tulichosema tutakifanya: Tutafukiza uvumba kwa Malkia wa Mbinguni na tutammiminia sadaka zetu za kinywaji kama sisi na baba zetu, wafalme na wakuu wetu tulivyofanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Wakati ule tulikuwa na chakula tele, tulikuwa matajiri wala hatukupata dhara lolote.
JER 44:18 Lakini tangu tulipoacha kumfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka za kinywaji, hatupati chochote, na tumekuwa tukiangamizwa kwa upanga na njaa.”
JER 44:19 Wanawake wakaongeza kusema, “Tulipomfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni, na kummiminia sadaka zetu za kinywaji, je, waume zetu hawakujua kwamba tulikuwa tukitengeneza maandazi kwa mfano wake, na kummiminia yeye sadaka za kinywaji?”
JER 44:20 Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake waliokuwa wakimjibu,
JER 44:21 “Je, Mwenyezi Mungu hakukumbuka na kufikiri kuhusu uvumba uliofukizwa katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu na ninyi pamoja na baba zenu, wafalme wenu, maafisa wenu na watu wa nchi?
JER 44:22 Mwenyezi Mungu alipokuwa hawezi kuendelea kuvumilia matendo yenu maovu na mambo ya machukizo mliyoyafanya, nchi yenu ilikuwa kitu cha kulaaniwa na kuachwa ukiwa pasipo wakazi, kama ilivyo leo.
JER 44:23 Kwa sababu mmefukiza uvumba na kufanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, nanyi hamkumtii wala kufuata sheria yake au amri zake au maagizo yake, maafa haya yamekuja juu yenu, kama mnavyoona sasa.”
JER 44:24 Kisha Yeremia akawaambia watu wote, pamoja na wanawake, “Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi watu wote wa Yuda mlioko Misri.
JER 44:25 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Ninyi na wake zenu mmeonesha kwa matendo yenu kile mlichoahidi mliposema, ‘Hakika tutatimiza nadhiri tulizoziweka za kumfukizia uvumba na kummiminia sadaka za kinywaji Malkia wa Mbinguni.’ “Endeleeni basi, fanyeni yale mliyoahidi! Timizeni nadhiri zenu!
JER 44:26 Lakini sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi Wayahudi wote mnaoishi Misri: ‘Ninaapa kwa Jina langu lililo kuu,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘kwamba hakuna hata mmoja atokaye Yuda anayeishi popote Misri ambaye kamwe ataomba tena kwa Jina langu au kuapa, akisema, “Hakika kama Bwana Mungu Mwenyezi aishivyo.”
JER 44:27 Kwa maana ninawaangalia kwa ajili ya madhara, wala sio kwa mema. Kila Myahudi aliyeko nchi ya Misri ataangamia kwa upanga au kwa njaa, hadi wote waangamie.
JER 44:28 Wale watakaonusurika upanga na kurudi katika nchi ya Yuda kutoka Misri watakuwa wachache sana. Ndipo mabaki wote wa Yuda waliokuja kuishi Misri watajua ni neno la nani litakalosimama: kwamba ni langu au ni lao.
JER 44:29 “ ‘Hii itakuwa ndiyo ishara kwenu kwamba nitawaadhibu mahali hapa, asema Mwenyezi Mungu, ili mpate kujua kuwa onyo langu la madhara dhidi yenu hakika litatimizwa.’
JER 44:30 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Nitamtia Farao Hofra mfalme wa Misri mikononi mwa adui zake wanaoutafuta uhai wake, kama nilivyomtia Sedekia mfalme wa Yuda mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, adui aliyekuwa akiutafuta uhai wake.’ ”
JER 45:1 Hili ndilo nabii Yeremia alilomwambia Baruku mwana wa Neria katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, baada ya Baruku kuandika katika kitabu maneno ambayo yalitoka kinywani mwa Yeremia wakati ule:
JER 45:2 “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akuambialo wewe Baruku:
JER 45:3 Ulisema, ‘Ole wangu! Mwenyezi Mungu ameongeza huzuni juu ya maumivu yangu, nimechoka kwa kulia kwa uchungu wala sipati pumziko.’ ”
JER 45:4 Lakini Mwenyezi Mungu akasema, “Mwambie hivi: ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Nitakibomoa kile nilichokijenga, na kung’oa kile nilichokipanda katika nchi yote.
JER 45:5 Je, utajitafutia mambo makubwa kwa ajili yako mwenyewe? Usiyatafute hayo. Kwa kuwa nitaleta maangamizi juu ya watu wote, asema Mwenyezi Mungu, lakini popote utakapoenda, nitayaokoa maisha yako.’ ”
JER 46:1 Hili ni neno la Mwenyezi Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu mataifa:
JER 46:2 Kuhusu Misri: Huu ni ujumbe dhidi ya jeshi la Farao Neko mfalme wa Misri, lililoshindwa huko Karkemishi kwenye Mto Frati na Nebukadneza mfalme wa Babeli, katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:
JER 46:3 “Wekeni tayari ngao zenu, kubwa na ndogo, mtoke kwa ajili ya vita!
JER 46:4 Fungieni farasi lijamu, pandeni farasi! Shikeni nafasi zenu mkiwa mmevaa chapeo! Isugueni mikuki yenu, vaeni dirii vifuani!
JER 46:5 Je, ninaona nini? Wametiwa hofu, wanarudi nyuma, mashujaa wao wameshindwa. Wanakimbia kwa haraka pasipo kutazama nyuma, tena kuna hofu kuu kila upande,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 46:6 Walio wepesi na wenye mbio hawawezi kukimbia, wala wenye nguvu hawawezi kutoroka. Kaskazini, kando ya Mto Frati, wanajikwaa na kuanguka.
JER 46:7 “Ni nani huyu ajiinuaye kama Mto Naili, kama mito yenye maji yanayofanya mawimbi?
JER 46:8 Misri hujiinua kama Mto Naili, kama mito yenye maji yanayofanya mawimbi. Husema, ‘Nitainuka na kufunika dunia, nitaiangamiza miji na watu wake.’
JER 46:9 Songeni mbele, enyi farasi! Endesheni kwa kasi, enyi mnaoendesha magari ya vita! Endeleeni mbele, enyi mashujaa: wanaume wa Kushi na Putu mnaobeba ngao, wanaume wa Ludi mnaovuta upinde.
JER 46:10 Lakini ile siku ni ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, siku ya kulipiza kisasi, kisasi juu ya adui zake. Upanga utakula hata utakapotosheka, hadi utakapozima kiu yake kwa damu. Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, atatoa dhabihu kwenye nchi ya kaskazini, kando ya Mto Frati.
JER 46:11 “Panda hadi Gileadi ukapate zeri, ee Bikira Binti Misri. Lakini umetumia dawa nyingi bila mafanikio; huwezi kupona.
JER 46:12 Mataifa yatasikia juu ya aibu yako, kilio chako kitaijaza dunia. Shujaa mmoja atajikwaa juu ya mwingine, nao wataanguka chini pamoja.”
JER 46:13 Huu ndio ujumbe ambao Mwenyezi Mungu alimwambia nabii Yeremia kuhusu kuja kwa Nebukadneza, mfalme wa Babeli ili kuishambulia Misri:
JER 46:14 “Tangaza hili katika Misri, nawe ulihubiri katika Migdoli, hubiri pia katika Memfisi na Tapanesi: ‘Shikeni nafasi zenu na mwe tayari, kwa kuwa upanga unawala wanaokuzunguka.’
JER 46:15 Kwa nini mashujaa wako wamesombwa na kupelekwa mbali? Hawawezi kusimama, kwa maana Mwenyezi Mungu atawasukuma awaangushe chini.
JER 46:16 Watajikwaa mara kwa mara, wataangukiana wao kwa wao. Watasema, ‘Amka, turudi kwa watu wetu na nchi yetu, mbali na upanga wa mtesi.’
JER 46:17 Huko watu watatangaza, ‘Farao, mfalme wa Misri, ni makelele tu, muda alioandikiwa umekwisha.’
JER 46:18 “Kwa hakika kama niishivyo,” asema Mfalme, ambaye jina lake ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, “mmoja atakuja ambaye ni kama Tabori miongoni mwa milima, kama Karmeli kando ya bahari.
JER 46:19 Funga mizigo yako kwenda uhamishoni, wewe ukaaye Misri, kwa kuwa Memfisi utaangamizwa na kuwa magofu pasipo mkazi.
JER 46:20 “Misri ni mtamba mzuri, lakini mbung’o anakuja dhidi yake kutoka kaskazini.
JER 46:21 Askari wake waliokodiwa katika safu zake wako kama ndama walionenepeshwa. Wao pia watageuka na kukimbia pamoja, hawataweza kuhimili vita, kwa maana siku ya msiba inakuja juu yao, wakati wao wa kuadhibiwa.
JER 46:22 Misri atatoa sauti kama ya nyoka anayekimbia kadiri adui anavyowasogelea na majeshi, watakuja dhidi yake wakiwa na mashoka, kama watu wakatao miti.
JER 46:23 Wataufyeka msitu wake,” asema Mwenyezi Mungu, “hata kama umesongamana kiasi gani. Ni wengi kuliko nzige, hawawezi kuhesabika.
JER 46:24 Binti Misri ataaibishwa, atatiwa mikononi mwa watu wa kaskazini.”
JER 46:25 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asema: “Ninakaribia kuleta adhabu juu ya Amoni mungu wa Thebesi, na juu ya Farao, juu ya Misri na miungu yake, na wafalme wake, pamoja na wanaomtegemea Farao.
JER 46:26 Nitawatia mikononi mwa wanaoutafuta uhai wao, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na maafisa wake. Mwishowe, hata hivyo, Misri itakaliwa kama nyakati zilizopita,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 46:27 “Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu, usifadhaike, ee Israeli. Hakika nitakuokoa kutoka nchi za mbali, uzao wako kutoka nchi walioishi uhamishoni. Yakobo atakuwa tena na amani na salama, wala hakuna hata mmoja atakayewatia hofu.
JER 46:28 Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu, kwa maana mimi niko pamoja nawe,” asema Mwenyezi Mungu. “Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote ambayo miongoni mwake nimekutawanya, sitakuangamiza wewe kabisa. Nitakurudi, lakini kwa haki tu, wala sitakuacha kabisa bila kukuadhibu.”
JER 47:1 Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza:
JER 47:2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini, yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana. Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyo ndani yake, miji na wanaoishi ndani yake. Watu watapiga kelele; wote wanaoishi katika nchi wataomboleza
JER 47:3 kwa sauti ya kwato za farasi wanaoenda mbio, kwa sauti ya magari ya vita ya adui, na mngurumo wa magurudumu yake. Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao, mikono yao italegea.
JER 47:4 Kwa maana siku imewadia kuwaangamiza Wafilisti wote na kuwakatilia mbali walionusurika wote ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni. Mwenyezi Mungu anakaribia kuwaangamiza Wafilisti, mabaki toka pwani za Kaftori.
JER 47:5 Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza, Ashkeloni atanyamazishwa. Enyi mabaki kwenye tambarare, mtajikatakata wenyewe hadi lini?
JER 47:6 “Mnalia, ‘Aa, upanga wa Mwenyezi Mungu, utaendelea hadi lini ndipo upumzike? Rudi ndani ya ala yako; acha na utulie.’
JER 47:7 Lakini upanga utatuliaje wakati Mwenyezi Mungu ameuamuru, wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni pamoja na pwani yake?”
JER 48:1 Kuhusu Moabu: Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: “Ole wake Nebo, kwa maana utaharibiwa. Kiriathaimu utaaibishwa na kutekwa; Misgabu itaaibishwa na kuvunjavunjwa.
JER 48:2 Moabu haitasifiwa tena; huko Heshboni watu watapanga jinsi ya kumwangusha: ‘Njooni na tuliangamize taifa lile.’ Wewe nawe, ee Madmena, utanyamazishwa; upanga utakufuatia.
JER 48:3 Sikiliza kilio kutoka Horonaimu, kilio cha maangamizi makuu na uharibifu.
JER 48:4 Moabu utavunjwa, wadogo wake watapiga kelele.
JER 48:5 Wanapanda kwenda njia ya kuelekea Luhithi, wakilia kwa uchungu wanapotembea, kwenye njia inayoshuka kwenda Horonaimu, kilio cha uchungu kwa ajili ya uharibifu kinasikika.
JER 48:6 Kimbieni! Okoeni maisha yenu, kuweni kama kichaka jangwani.
JER 48:7 Kwa kuwa mmetumainia matendo yenu na mali yenu, ninyi pia mtachukuliwa mateka, naye Kemoshi ataenda uhamishoni, pamoja na makuhani wake na maafisa wake.
JER 48:8 Mwangamizi atakuja dhidi ya kila mji, wala hakuna mji utakaookoka. Bonde litaangamizwa na uwanda utaharibiwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu amesema.
JER 48:9 Wekeni chumvi kwa ajili ya Moabu, kwa kuwa ataangamizwa; miji yake itakuwa ukiwa, hakutakuwa na mtu atakayeishi ndani yake.
JER 48:10 “Alaaniwe yeye afanyaye kazi ya Mwenyezi Mungu kwa ulegevu! Alaaniwe yeye auzuiaye upanga wake usimwage damu!
JER 48:11 “Moabu amestarehe tangu ujana wake, kama divai iliyoachwa kwenye machujo yake, haikumiminwa kutoka chombo kimoja hadi kingine, hajaenda uhamishoni. Kwa hiyo ana ladha ile ile kama aliyokuwa nayo, nayo harufu yake haijabadilika.
JER 48:12 Lakini siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “nitakapotuma watu wamiminao kutoka magudulia, nao watamimina; wataacha magudulia yake yakiwa matupu na kuvunja mitungi yake.
JER 48:13 Kisha Moabu atamwonea aibu Kemoshi, kama vile nyumba ya Israeli walivyoona aibu walipotegemea Betheli.
JER 48:14 “Mwawezaje kusema, ‘Sisi ni mashujaa, watu hodari katika vita’?
JER 48:15 Moabu ataangamizwa na miji yake itavamiwa, vijana wake wa kiume walio bora sana watachinjwa,” asema Mfalme, ambaye jina lake ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
JER 48:16 “Kuanguka kwa Moabu kumekaribia, janga kubwa litamjia kwa haraka.
JER 48:17 Ombolezeni kwa ajili yake, ninyi nyote mnaomzunguka, ninyi nyote mnaojua sifa zake, semeni, ‘Tazama jinsi ilivyovunjika fimbo ya kifalme yenye nguvu, tazama jinsi ilivyovunjika fimbo iliyotukuka!’
JER 48:18 “Shuka kutoka fahari yako uketi katika ardhi iliyokauka, enyi wenyeji wa Binti Diboni, kwa maana yeye aangamizaye Moabu atakuja dhidi yako, na kuangamiza miji yako yenye ngome.
JER 48:19 Simama kando ya barabara na utazame, wewe unayeishi Aroeri. Muulize mwanaume anayekimbia na mwanamke anayetoroka, waulize, ‘Kumetokea nini?’
JER 48:20 Moabu amefedheheshwa, kwa kuwa amevunjavunjwa. Lieni kwa huzuni na kupiga kelele! Tangazeni kando ya Mto Arnoni kwamba Moabu ameangamizwa.
JER 48:21 Hukumu imefika kwenye uwanda wa juu: katika Holoni, Yahasa na Mefaathi,
JER 48:22 katika Diboni, Nebo na Beth-Diblathaimu,
JER 48:23 katika Kiriathaimu, Beth-Gamuli na Beth-Meoni,
JER 48:24 katika Keriothi na Bosra; kwa miji yote ya Moabu, iliyo mbali na karibu.
JER 48:25 Pembe ya Moabu imekatwa, mkono wake umevunjwa,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 48:26 “Mleweshe, kwa kuwa amemdharau Mwenyezi Mungu. Moabu atagaagaa katika matapishi yake, awe kichekesho.
JER 48:27 Je, Israeli hakuwa kitu chako cha kudhihakiwa? Je, alikamatwa miongoni mwa wezi, kiasi cha kutikisa kichwa chako kwa dharau kila mara unapozungumza juu yake?
JER 48:28 Ondokeni miji yenu, mkaishi katikati ya miamba, enyi mnaoishi Moabu. Kuweni kama njiwa ambaye hutengeneza kiota chake kwenye mlango wa pango.
JER 48:29 “Tumesikia kuhusu kiburi cha Moabu: kutakabari kwake kwa kiburi na majivuno, kiburi chake na ufidhuli wake, na kujivuna kwa moyo wake.
JER 48:30 Ninaujua ujeuri wake, lakini ni bure,” asema Mwenyezi Mungu, “nako kujisifu kwake hakumsaidii chochote.
JER 48:31 Kwa hiyo namlilia Moabu, kwa ajili ya Moabu yote ninalia, ninaomboleza kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.
JER 48:32 Ninalia machozi kwa ajili yenu, kama Yazeri aliavyo, enyi mizabibu ya Sibma. Matawi yako yameenea hadi baharini; yamefika hadi bahari ya Yazeri. Mwangamizi ameyaangukia matunda yako yaliyoiva na mizabibu yako iliyoiva.
JER 48:33 Shangwe na furaha vimetoweka kutoka bustani na mashamba ya Moabu. Nimekomesha kutiririka kwa divai kutoka mashinikizo; hakuna hata mmoja ayakanyagaye kwa kelele za shangwe. Ingawa kuna kelele, sio kelele za shangwe.
JER 48:34 “Sauti ya kilio chao inapanda kutoka Heshboni hadi Eleale na Yahazi, kutoka Soari hadi Horonaimu na Eglath-Shelishiya, kwa kuwa hata maji ya Nimrimu yamekauka.
JER 48:35 Nitakomesha wote katika Moabu watoao sadaka mahali pa juu pa kuabudia, na kufukiza uvumba kwa miungu yao,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 48:36 “Kwa hiyo moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama filimbi; unaomboleza kama filimbi kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi. Utajiri waliojipatia umetoweka.
JER 48:37 Kila kichwa kimenyolewa na kila mwenye ndevu zimekatwa; kila mkono umekatwa na kila kiuno kimevalishwa gunia.
JER 48:38 Juu ya mapaa yote katika Moabu na katika viwanja hakuna kitu isipokuwa maombolezo, kwa kuwa nimemvunja Moabu kama gudulia lisilotakiwa na mtu yeyote,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 48:39 “Tazama jinsi alivyovunjikavunjika! Jinsi wanavyolia kwa huzuni! Tazama jinsi Moabu anavyogeuka kwa aibu! Moabu amekuwa kitu cha kudhihakiwa, kitu cha kutisha kwa wale wote wanaomzunguka.”
JER 48:40 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Tazama! Tai anashuka chini, akitanda mabawa yake juu ya Moabu.
JER 48:41 Miji itatekwa na ngome zake zitatwaliwa. Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Moabu itakuwa kama moyo wa mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
JER 48:42 Moabu ataangamizwa kama taifa kwa sababu amemdharau Mwenyezi Mungu.
JER 48:43 Hofu kuu, shimo na mtego vinawangojea, enyi watu wa Moabu,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 48:44 “Yeyote atakayeikimbia hiyo hofu kuu ataanguka ndani ya shimo, yeyote atakayepanda kutoka shimoni, atanaswa katika mtego, kwa sababu nitailetea Moabu mwaka wa adhabu yake,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 48:45 “Katika kivuli cha Heshboni, wakimbizi wamesimama pasipo msaada, kwa kuwa moto umezimika huko Heshboni, Mwali wa moto kutoka katikati ya Sihoni; unaunguza paji za nyuso za Wamoabu, mafuvu ya wanaojivuna kwa kelele.
JER 48:46 Ole wako, ee Moabu! Watu wa Kemoshi wameangamizwa; watoto wako wa kiume wamepelekwa uhamishoni, na binti zako wamechukuliwa mateka.
JER 48:47 “Lakini nitarudisha mateka wa Moabu, katika siku zijazo,” asema Mwenyezi Mungu. Huu ndio mwisho wa hukumu ya Moabu.
JER 49:1 Kuhusu Waamoni: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Je, Israeli hana wana? Je, hana warithi? Kwa nini basi Moleki amechukua milki ya Gadi? Kwa nini watu wake wanaishi katika miji yake?
JER 49:2 Lakini siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “nitakapopiga ukelele wa vita dhidi ya Raba, mji wa Waamoni; utakuwa kilima cha magofu, navyo vijiji vinavyouzunguka vitateketezwa kwa moto. Kisha Israeli atawafukuza wale waliomfukuza,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 49:3 “Lia kwa huzuni, ee Heshboni, kwa kuwa Ai umeangamizwa! Pigeni kelele, enyi wakazi wa Raba! Vaeni gunia na kuomboleza, kimbieni hapa na pale ndani ya kuta, kwa kuwa Moleki ataenda uhamishoni, yeye pamoja na makuhani na maafisa wake.
JER 49:4 Kwa nini unajivunia mabonde yako, kujivunia mabonde yako yaliyozaa sana? Ee binti usiye mwaminifu, unayeutumainia utajiri wako na kusema, ‘Ni nani atakayenishambulia?’
JER 49:5 Nitaleta hofu kuu juu yako kutoka kwa wale wote wanaokuzunguka,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Kila mmoja wenu ataondolewa, wala hakuna hata mmoja atakayekusanya wakimbizi.
JER 49:6 “Lakini hatimaye, nitarudisha mateka wa Waamoni,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 49:7 Kuhusu Edomu: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Je, hakuna tena hekima katika Temani? Je, shauri limewapotea wenye busara? Je, hekima yao imechakaa?
JER 49:8 Geuka na ukimbie, jifiche katika mapango marefu kabisa, wewe uishiye Dedani, kwa kuwa nitaleta maafa juu ya Esau wakati nitakapomwadhibu.
JER 49:9 Je, kama wachuma zabibu wangekuja kwako, wasingebakiza zabibu chache? Kama wezi wangekujia usiku, je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji?
JER 49:10 Lakini nitamvua Esau nguo abaki uchi, nitayafunua maficho yake, ili asiweze kujificha. Watoto wake, jamaa na majirani wataangamia, naye hatakuwepo tena.
JER 49:11 Waache yatima wako; nitayalinda maisha yao. Wajane wako pia wanaweza kunitumaini mimi.”
JER 49:12 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kama wasiostahili kukinywea kikombe ni lazima wakinywe, kwa nini wewe usiadhibiwe? Hutakwepa kuadhibiwa, ni lazima ukinywe.
JER 49:13 Ninaapa kwa nafsi yangu,” asema Mwenyezi Mungu, “kwamba Bosra utakuwa magofu na kitu cha kutisha, cha aibu na cha kulaania; miji yake yote itakuwa magofu milele.”
JER 49:14 Nimesikia ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Jikusanyeni ili kuushambulia! Inukeni kwa ajili ya vita!”
JER 49:15 “Sasa nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, uliyedharauliwa miongoni mwa watu.
JER 49:16 Vitisho vyako na kiburi cha moyo wako vimekudanganya, wewe unayeishi katika majabali ya miamba, wewe unayedumu katika miinuko ya kilima. Ujapojenga kiota chako juu sana kama cha tai, nitakushusha chini kutoka huko,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 49:17 “Edomu atakuwa kitu cha kutisha; wote wapitao karibu watashangaa na kuzomea kwa sababu ya majeraha yake yote.
JER 49:18 Kama vile Sodoma na Gomora zilivyoangamizwa, pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,” asema Mwenyezi Mungu, “vivyo hivyo hakuna mtu yeyote atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu yeyote atakayekaa humo.
JER 49:19 “Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani kuja kwenye nchi ya malisho mengi, ndivyo nitakavyomfukuza Edomu kutoka nchi yake ghafula. Ni nani aliye mteule nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili? Ni nani aliye kama mimi, na ni nani awezaye kunipinga? Tena ni mchungaji yupi awezaye kusimama kinyume nami?”
JER 49:20 Kwa hiyo, sikia kile Mwenyezi Mungu alichokipanga dhidi ya Edomu, kile alichokusudia dhidi ya wale wanaoishi Temani: Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali; yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.
JER 49:21 Kwa sauti ya anguko lao, dunia itatetemeka. Kilio chao kitasikika hadi Bahari ya Shamu.
JER 49:22 Tazama! Tai atapaa juu angani na kuruka chini kwa ghafula, akitandaza mabawa yake juu ya Bosra. Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Edomu itakuwa kama moyo wa mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
JER 49:23 Kuhusu Dameski: “Hamathi na Arpadi imetahayarika, kwa kuwa wamesikia habari mbaya. Wamevunjika moyo na wametaabika kama bahari iliyochafuka.
JER 49:24 Dameski amedhoofika, amegeuka na kukimbia, hofu ya ghafula imemkamata sana; amepatwa na uchungu na maumivu, maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
JER 49:25 Kwa nini mji unaosifika haujaachwa, mji wenye sifa, na wa furaha yangu?
JER 49:26 Hakika, vijana wake wanaume wataanguka barabarani; askari wake wote watanyamazishwa siku hiyo,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
JER 49:27 “Nitatia moto kuta za Dameski; utaangamiza ngome za Ben-Hadadi.”
JER 49:28 Kuhusu Kedari na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza mfalme wa Babeli alizishambulia: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Inuka, ushambulie Kedari na kuwaangamiza watu wa mashariki.
JER 49:29 Mahema yao na makundi yao ya kondoo yatachukuliwa; vibanda vyao vitatwaliwa, pamoja na mali yao yote na ngamia wao. Watu watawapigia kelele, ‘Hofu kuu iko kila upande!’
JER 49:30 “Kimbieni haraka! Kaeni kwenye mapango marefu sana, ninyi mnaoishi Hazori,” asema Mwenyezi Mungu. “Nebukadneza, mfalme wa Babeli amepanga njama dhidi yenu; amebuni hila dhidi yenu.
JER 49:31 “Inuka na ulishambulie taifa lililostarehe, linaloishi kwa kujiamini,” asema Mwenyezi Mungu, “taifa lisilo na malango wala makomeo; watu wake wanaishi peke yao.
JER 49:32 Ngamia wao watakuwa nyara, nayo mifugo yao itatekwa. Walio maeneo ya mbali nitawatawanya pande zote, nami nitaleta maafa juu yao kutoka kila upande,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 49:33 “Hazori itakuwa makao ya mbweha, mahali pa ukiwa milele. Hakuna atakayeishi humo; hakuna mtu atakayekaa ndani yake.”
JER 49:34 Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mapema katika utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda:
JER 49:35 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Tazama, nitavunja upinde wa Elamu, ulio tegemeo la nguvu zao.
JER 49:36 Nitaleta pepo nne dhidi ya Elamu toka pande nne za mbingu, nitawatawanya katika hizo pande nne, wala hapatakuwa na taifa ambalo watu wa Elamu waliofukuzwa hawataenda.
JER 49:37 Nitamfadhaisha Elamu mbele ya adui zao, mbele yao wanaoutafuta uhai wao; nitaleta maafa juu yao, naam, hasira yangu kali,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawafuatia kwa upanga hadi nitakapowamaliza.
JER 49:38 Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu na kumwangamiza mfalme wake na maafisa wake,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 49:39 “Lakini nitarudisha mateka wa Elamu katika siku zijazo,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 50:1 Hili ndilo neno alilosema Mwenyezi Mungu kupitia nabii Yeremia kuhusu Babeli na nchi ya Wakaldayo:
JER 50:2 “Tangazeni! Hubirini katikati ya mataifa, Inueni bendera na mkahubiri; msiache kitu chochote, bali semeni, ‘Babeli utatekwa; Beli ataaibishwa, Merodaki atajazwa na hofu kuu. Sanamu zake zitaaibishwa na vinyago vyake vitajazwa hofu kuu.’
JER 50:3 Taifa kutoka kaskazini litamshambulia, na kuifanya nchi yake ukiwa. Hakuna atakayeishi ndani yake, watu na wanyama wataikimbia.
JER 50:4 “Katika siku hizo, wakati huo,” asema Mwenyezi Mungu, “watu wa Israeli pamoja na watu wa Yuda wataenda wakilia ili kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
JER 50:5 Wataulizia njia iendayo Sayuni na kuelekeza nyuso zao huko. Watakuja na kuambatana na Mwenyezi Mungu katika agano la milele ambalo halitasahaulika.
JER 50:6 “Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea; wachungaji wao wamewapotosha na kuwafanya wazurure mlimani. Walitangatanga juu ya mlima na kilima, na kusahau mahali pao pa kupumzikia.
JER 50:7 Yeyote aliyewakuta aliwala; adui zao walisema, ‘Sisi hatuna hatia, kwa kuwa wao walitenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, malisho yao halisi, Mwenyezi Mungu, aliye tumaini la baba zao.’
JER 50:8 “Kimbieni kutoka Babeli; ondokeni katika nchi ya Wakaldayo, kuweni kama mbuzi wale waongozao kundi.
JER 50:9 Kwa maana nitaamsha na kuleta dhidi ya Babeli muungano wa mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini. Watashika nafasi zao dhidi yake, naye kutokea kaskazini atatekwa. Mishale yao itakuwa kama mishale ya mashujaa walio hodari, ambao hawawezi kurudi mikono mitupu.
JER 50:10 Kwa hiyo Ukaldayo utatekwa nyara; wote wanaouteka, watapata nyara za kutosha,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 50:11 “Kwa sababu hushangilia na kufurahi, wewe utekaye urithi wangu, kwa sababu unachezacheza kama mtamba anayepura nafaka, na kulia kama farasi dume,
JER 50:12 mama yako ataaibika mno, yeye aliyekuzaa atatahayari. Atakuwa mdogo kuliko mataifa mengine yote, atakuwa nyika, nchi kame na jangwa.
JER 50:13 Kwa sababu ya hasira ya Mwenyezi Mungu hatakaliwa na mtu, lakini ataachwa ukiwa kabisa. Wote watakaopita Babeli watatiwa hofu na kudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote.
JER 50:14 “Shikeni nafasi zenu kuzunguka Babeli, enyi nyote mvutao upinde. Mpigeni! Msibakize mshale wowote, kwa kuwa ametenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.
JER 50:15 Piga kelele dhidi yake kila upande! Anajisalimisha, minara yake inaanguka, kuta zake zimebomoka. Kwa kuwa hiki ni kisasi cha Mwenyezi Mungu, mlipizeni kisasi; mtendeeni kama alivyowatendea wengine.
JER 50:16 Katilieni mbali mpanzi kutoka Babeli, pamoja na mvunaji na mundu wake akivuna. Kwa sababu ya upanga wa mdhalimu kila mmoja na arejee kwa watu wake mwenyewe, kila mmoja na akimbilie kwenye nchi yake mwenyewe.
JER 50:17 “Israeli ni kundi lililotawanyika ambalo simba wamelifukuzia mbali. Wa kwanza kumla alikuwa mfalme wa Ashuru, wa mwisho kuponda mifupa yake alikuwa Nebukadneza mfalme wa Babeli.”
JER 50:18 Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: “Nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yake kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.
JER 50:19 Lakini nitamrudisha Israeli katika malisho yake mwenyewe naye atalisha huko Karmeli na Bashani; njaa yake itashibishwa juu ya vilima vya Efraimu na Gileadi.
JER 50:20 Katika siku hizo, wakati huo,” asema Mwenyezi Mungu, “uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli, lakini halitaonekana, na kwa ajili ya dhambi za Yuda, lakini haitapatikana hata moja, kwa kuwa nitawasamehe mabaki nitakaowaacha.
JER 50:21 “Shambulieni nchi ya Merathaimu na wale wanaoishi huko Pekodi. Wafuatieni, waueni na kuwaangamiza kabisa,” asema Mwenyezi Mungu. “Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.
JER 50:22 Kelele ya vita iko ndani ya nchi, kelele ya maangamizi makuu!
JER 50:23 Tazama jinsi nyundo ya dunia yote ilivyovunjika na kuharibika! Tazama jinsi Babeli ilivyokuwa ukiwa miongoni mwa mataifa!
JER 50:24 Nimetega mtego kwa ajili yako, ee Babeli, nawe ukakamatwa kabla hujafahamu; ulipatikana na ukakamatwa kwa sababu ulimpinga Mwenyezi Mungu.
JER 50:25 Mwenyezi Mungu amefungua ghala lake la silaha na kuzitoa silaha za ghadhabu yake, kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayo kazi ya kufanya katika nchi ya Wakaldayo.
JER 50:26 Njooni dhidi yake kutoka mbali. Zifungueni ghala zake za nafaka; mlundikeni kama lundo la nafaka. Mwangamizeni kabisa na msimwachie mabaki yoyote.
JER 50:27 Waueni mafahali wake wachanga wote; waacheni washuke machinjoni! Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia, wakati wao wa kuadhibiwa.
JER 50:28 Wasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeli wakitangaza katika Sayuni jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wetu alivyolipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
JER 50:29 “Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli, wote wavutao upinde. Pigeni kambi kumzunguka kabisa, asitoroke mtu yeyote. Mlipizeni kwa matendo yake; mtendeeni kama alivyotenda. Kwa kuwa alimdharau Mwenyezi Mungu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
JER 50:30 Kwa hiyo, vijana wake wanaume wataanguka barabarani; askari wake wote watanyamazishwa siku ile,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 50:31 “Tazama, niko kinyume nawe, ewe mwenye majivuno,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, “kwa kuwa siku yako imewadia, yaani wakati wako wa kuadhibiwa.
JER 50:32 Mwenye majivuno atajikwaa na kuanguka, wala hakuna yeyote atakayemuinua; nitawasha moto katika miji yake, utakaowateketeza wote wanaomzunguka.”
JER 50:33 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Watu wa Israeli wamedhulumiwa, hata watu wa Yuda pia. Wote waliowateka wamewashikilia sana, wanakataa kuwaachia waende.
JER 50:34 Lakini Mkombozi wao ana nguvu; Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake. Atatetea shauri lao kwa nguvu ili alete amani nchini mwao, lakini ataleta msukosuko kwa wale wanaoishi Babeli.
JER 50:35 “Upanga dhidi ya Wakaldayo!” asema Mwenyezi Mungu, “dhidi ya wale wanaoishi Babeli, na dhidi ya maafisa wake na wenye busara!
JER 50:36 Upanga dhidi ya manabii wake wa uongo! Watakuwa wapumbavu. Upanga dhidi ya mashujaa wake! Watajazwa na hofu kuu
JER 50:37 Upanga dhidi ya farasi na magari yake ya vita pamoja na askari wake wote wa kigeni katika safu zake! Wao watakuwa kama wanawake. Upanga dhidi ya hazina zake! Hizo zitatekwa nyara.
JER 50:38 Ukame juu ya maji yake! Nayo yatakauka. Kwa kuwa ni nchi ya sanamu, wao wanaenda wazimu kwa ajili ya sanamu.
JER 50:39 “Kwa hiyo, viumbe vya jangwani na fisi wataishi humo, nao bundi watakaa humo. Kamwe haitakaliwa tena wala watu hawataishi humo kizazi hadi kizazi.
JER 50:40 Kama Mungu alivyoangamiza Sodoma na Gomora pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,” asema Mwenyezi Mungu, “vivyo hivyo hakuna mtu atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu atakayekaa humo.
JER 50:41 “Tazama! Jeshi linakuja kutoka kaskazini; taifa kubwa na wafalme wengi wanaamshwa kutoka miisho ya dunia.
JER 50:42 Wamejifunga pinde na mikuki; ni wakatili na hawana huruma. Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma wanapoendesha farasi wao; wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita ili kukushambulia, ee Binti Babeli.
JER 50:43 Mfalme wa Babeli amesikia habari kuwahusu, nayo mikono yake imelegea. Uchungu umemshika, maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
JER 50:44 Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani kuja kwenye nchi ya malisho mengi, ndivyo nitakavyomfukuza Babeli kutoka nchi yake ghafula. Ni nani aliye mteule, nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili? Ni nani aliye kama mimi, na ni nani awezaye kunipinga? Tena ni mchungaji yupi awezaye kusimama kinyume nami?”
JER 50:45 Kwa hiyo, sikia ambacho Mwenyezi Mungu amepanga dhidi ya Babeli, kile alichokusudia dhidi ya nchi ya Wakaldayo: Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali. Yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.
JER 50:46 Kwa sauti ya kutekwa kwa Babeli, dunia itatetemeka; kilio chake kitasikika pote miongoni mwa mataifa.
JER 51:1 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi dhidi ya Babeli na wenyeji wa Leb-Kamai.
JER 51:2 Nitawatuma wageni Babeli kumpepeta na kuiharibu nchi yake; watampinga kila upande katika siku ya maafa yake.
JER 51:3 Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake, wala usimwache avae silaha zake. Usiwaonee huruma vijana wake; angamiza jeshi lake kabisa.
JER 51:4 Wataanguka barabarani waliouawa katika nchi ya Wakaldayo, wakiwa na majeraha ya kutisha.
JER 51:5 Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa na Mungu wao, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ingawa nchi yao imejaa uovu mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
JER 51:6 “Kimbieni kutoka Babeli! Okoeni maisha yenu! Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake. Ni wakati wa kisasi cha Mwenyezi Mungu, atamlipa kile anachostahili.
JER 51:7 Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa Mwenyezi Mungu; aliufanya ulimwengu wote ulewe. Mataifa walikunywa mvinyo wake; kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu.
JER 51:8 Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika. Mwombolezeni! Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake, labda anaweza kupona.
JER 51:9 “ ‘Tungemponya Babeli, lakini hawezi kuponyeka; tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe, kwa kuwa hukumu yake inafika angani, inapanda juu hadi mawinguni.’
JER 51:10 “ ‘Mwenyezi Mungu amethibitisha haki yetu; njooni, tutangaze katika Sayuni kitu ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, amefanya.’
JER 51:11 “Noeni mishale, chukueni ngao! Mwenyezi Mungu amewaamsha wafalme wa Wamedi, kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli. Mwenyezi Mungu atalipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
JER 51:12 Inueni bendera dhidi ya kuta za Babeli! Imarisheni ulinzi, wekeni walinzi, andaeni waviziaji! Mwenyezi Mungu atatimiza kusudi lake, amri yake juu ya watu wa Babeli.
JER 51:13 Wewe uishiye kando ya maji mengi na uliye na wingi wa hazina, mwisho wako umekuja, wakati wako wa kukatiliwa mbali.
JER 51:14 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: ‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige, nao watashangilia kwa ushindi juu yako.’
JER 51:15 “Aliiumba dunia kwa uweza wake; akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake, na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
JER 51:16 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma; huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia. Hupeleka miali ya radi pamoja na mvua, naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
JER 51:17 “Kila mtu ni mjinga na hana maarifa; kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. Vinyago vyake ni vya udanganyifu; havina pumzi.
JER 51:18 Ni ubatili tu, vitu vya kufanyia mzaha; wakati wa hukumu yao, wataangamia.
JER 51:19 Yeye Aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo, kwani ndiye Muumba wa vitu vyote, pamoja na kabila la urithi wake: Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.
JER 51:20 “Wewe ndiwe rungu langu la vita, silaha yangu ya vita: kwa wewe navunjavunja mataifa, kwa wewe naangamiza falme,
JER 51:21 kwa wewe navunjavunja farasi na mpanda farasi, kwa wewe navunjavunja gari la vita na mwendeshaji wake,
JER 51:22 kwa wewe napondaponda mwanaume na mwanamke, kwa wewe napondaponda mzee na kijana, kwa wewe napondaponda kijana wa kiume na mwanamwali,
JER 51:23 kwa wewe nampondaponda mchungaji na kundi, kwa wewe nampondaponda mkulima na maksai, kwa wewe nawapondaponda watawala na maafisa.
JER 51:24 “Mbele ya macho yako nitamlipiza Babeli na wote wanaoishi Ukaldayo kwa ajili ya makosa yote waliyofanya katika Sayuni,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 51:25 “Mimi niko kinyume nawe, ee mlima unaoharibu, wewe uangamizaye dunia yote,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitanyoosha mkono wangu dhidi yako, nikuvingirishe kutoka kilele cha mwamba, na kukufanya mlima ulioteketezwa kwa moto.
JER 51:26 Hakuna jiwe litakalochukuliwa kutoka kwako kwa ajili ya kufanywa jiwe la pembeni, wala jiwe lolote kwa ajili ya msingi, kwa maana utakuwa ukiwa milele,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 51:27 “Inueni bendera katika nchi! Pigeni tarumbeta katikati ya mataifa! Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake, iteni falme hizi dhidi yake: Ararati, Mini na Ashkenazi. Wekeni jemadari dhidi yake, pelekeni farasi wengi kama kundi la nzige.
JER 51:28 Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake, wafalme wa Wamedi, watawala wao na maafisa wao wote, pamoja na nchi zote wanazotawala.
JER 51:29 Nchi inatetemeka na kugaagaa, kwa kuwa makusudi ya Mwenyezi Mungu dhidi ya Babeli yanasimama: yaani kuangamiza nchi ya Babeli ili pasiwepo atakayeishi humo.
JER 51:30 Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana, wamebaki katika ngome zao. Nguvu zao zimekwisha, wamekuwa kama wanawake. Makazi yake yameteketezwa kwa moto, makomeo ya malango yake yamevunjika.
JER 51:31 Tarishi mmoja humfuata mwingine, na mjumbe humfuata mjumbe, kumtangazia mfalme wa Babeli kwamba mji wake wote umetekwa,
JER 51:32 Vivuko vya mito vimekamatwa, mabwawa yenye mafunjo yametiwa moto, nao askari wameingiwa na hofu kuu.”
JER 51:33 Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: “Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria wakati inapokanyagwa; wakati wa kumvuna utakuja upesi.”
JER 51:34 “Nebukadneza mfalme wa Babeli ametula, ametufanya tuchangayikiwe, ametufanya tuwe gudulia tupu. Ametumeza kama mnyama wa baharini, na kujaza tumbo lake kwa vyakula vyetu vizuri, kisha akatutapika.
JER 51:35 Jeuri iliyotendewa miili yetu na iwe juu ya Babeli,” ndivyo wasemavyo wakaaji wa Sayuni. “Damu yetu na iwe juu ya wakaaji wa Babeli,” asema Yerusalemu.
JER 51:36 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Tazama, nitakutetea na kukulipizia kisasi; nitaikausha bahari yake na kuzikausha chemchemi zake.
JER 51:37 Babeli utakuwa lundo la magofu na makao ya mbweha, kitu cha kutisha na kudharauliwa, mahali asipoishi mtu.
JER 51:38 Watu wake wote wananguruma kama simba wadogo, wanakoroma kama wana simba.
JER 51:39 Lakini wakiwa wameamshwa, nitawaandalia karamu na kuwafanya walewe, ili washangilie kwa kicheko, kisha walale milele na wasiamke,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 51:40 “Nitawateremsha kama wana-kondoo wanaoenda machinjoni, kama kondoo dume na mbuzi.
JER 51:41 “Tazama jinsi Sheshaki atakavyokamatwa, majivuno ya dunia yote yatakavyonyakuliwa. Babeli atakuwa mwenye hofu kiasi gani kati ya mataifa!
JER 51:42 Bahari itainuka juu ya Babeli; mawimbi yake yanayonguruma yatamfunika.
JER 51:43 Miji yake itakuwa ukiwa, kame na jangwa, nchi isiyokuwa na mtu anayeishi ndani yake, ambayo hakuna mwanadamu atakayepita humo.
JER 51:44 Nitamwadhibu Beli katika Babeli, na kumfanya atapike kitu alichokimeza. Mataifa hayatamiminika tena kwake. Nao ukuta wa Babeli utaanguka.
JER 51:45 “Tokeni ndani yake, enyi watu wangu! Okoeni maisha yenu! Ikimbieni hasira kali ya Mwenyezi Mungu.
JER 51:46 Msikate tamaa wala msiogope tetesi zitakaposikika katika nchi; tetesi moja inasikika mwaka huu, nyingine mwaka unaofuata; tetesi juu ya jeuri katika nchi, na ya mtawala dhidi ya mtawala.
JER 51:47 Kwa kuwa hakika wakati utawadia nitakapoziadhibu sanamu za Babeli; nchi yake yote itatiwa aibu, na watu wake wote waliouawa wataangukia ndani yake.
JER 51:48 Ndipo mbingu na dunia na vyote vilivyomo vitapiga kelele za shangwe juu ya Babeli, kwa kuwa kutoka kaskazini waangamizi watamshambulia,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 51:49 “Babeli ni lazima aanguke kwa sababu ya kuwaua Waisraeli, kama vile waliouawa duniani kote walivyoanguka kwa sababu ya Babeli.
JER 51:50 Wewe uliyepona upanga, ondoka wala usikawie! Mkumbuke Mwenyezi Mungu ukiwa katika nchi ya mbali, na utafakari juu ya Yerusalemu.”
JER 51:51 “Tumetahayari, kwa sababu tumetukanwa na aibu imefunika nyuso zetu, kwa sababu wageni wameingia mahali patakatifu pa nyumba ya Mwenyezi Mungu.”
JER 51:52 “Lakini siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “nitakapoziadhibu sanamu zake, na katika nchi yake yote waliojeruhiwa watalia kwa maumivu makali.
JER 51:53 Hata kama Babeli ikifika angani na kuziimarisha ngome zake ndefu, nitatuma waangamizi dhidi yake,” asema Mwenyezi Mungu.
JER 51:54 “Sauti ya kilio inasikika kutoka Babeli, sauti ya uharibifu mkuu kutoka nchi ya Wakaldayo.
JER 51:55 Mwenyezi Mungu ataiangamiza Babeli, atanyamazisha makelele ya kishindo chake. Mawimbi ya adui yatanguruma kama maji makuu, ngurumo ya sauti zao itavuma.
JER 51:56 Mwangamizi atakuja dhidi ya Babeli; mashujaa wake watakamatwa, nazo pinde zao zitavunjwa. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mungu wa kisasi, yeye atalipiza kikamilifu.
JER 51:57 Nitawafanya maafisa wake na wenye busara walewe, watawala wao, maafisa, pamoja na mashujaa wao; watalala milele na hawataamka,” asema Mfalme, ambaye jina lake ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
JER 51:58 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Ukuta mnene wa Babeli utasawazishwa, na malango yaliyoinuka yatateketezwa kwa moto; mataifa yanajichosha bure, taabu ya mataifa ni nishati tu ya miali ya moto.”
JER 51:59 Huu ndio ujumbe ambao nabii Yeremia alimpa msimamizi wa nyumba ya mfalme, Seraya mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wake.
JER 51:60 Yeremia alikuwa ameandika ndani ya kitabu kuhusu maafa yote yatakayoipata Babeli, yaani yote yaliyokuwa yameandikwa kuhusu Babeli.
JER 51:61 Yeremia akamwambia Seraya, “Utakapofika Babeli, hakikisha kwamba umesoma maneno haya yote kwa sauti kubwa.
JER 51:62 Kisha sema, ‘Ee Mwenyezi Mungu, umesema utaangamiza mahali hapa ili mtu wala mnyama asiishi ndani yake, napo patakuwa ukiwa milele.’
JER 51:63 Utakapomaliza kusoma hiki kitabu, kifungie jiwe kisha ukitupe ndani ya Mto Frati.
JER 51:64 Kisha sema, ‘Hivi ndivyo Babeli utakavyozama na usiinuke tena, kwa sababu ya maafa nitakayoleta juu yake. Nao watu wake wataanguka.’ ” Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.
JER 52:1 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna.
JER 52:2 Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya Yehoyakimu.
JER 52:3 Haya yote yalitendeka Yerusalemu na Yuda kwa sababu ya hasira ya Mwenyezi Mungu, naye mwishoni akawaondoa mbele zake. Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.
JER 52:4 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Wakapiga kambi nje ya mji na kuuzingira pande zote.
JER 52:5 Mji ulizingirwa na jeshi hadi mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.
JER 52:6 Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.
JER 52:7 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba.
JER 52:8 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia Mfalme Sedekia na kumpata katika nchi tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika,
JER 52:9 naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ambapo alimtangazia hukumu.
JER 52:10 Huko Ribla mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Pia akawaua maafisa wote wa Yuda.
JER 52:11 Kisha akayang’oa macho ya Sedekia, akamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli, alipomweka gerezani hadi siku ya kifo chake.
JER 52:12 Siku ya kumi ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme, aliyemtumikia mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu.
JER 52:13 Alichoma moto Hekalu la Mwenyezi Mungu, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu.
JER 52:14 Jeshi lote la Wakaldayo chini ya mkuu wa askari walinzi wa mfalme walivunja kuta zote zilizoizunguka Yerusalemu.
JER 52:15 Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, akawapeleka uhamishoni baadhi ya watu maskini sana na wale waliobaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli.
JER 52:16 Lakini Nebuzaradani akawaacha mabaki ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
JER 52:17 Wakaldayo walivunja nguzo za shaba, vishikilio vya shaba, na Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Kisha wakaichukua shaba yote wakaipeleka Babeli.
JER 52:18 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika Hekaluni.
JER 52:19 Mkuu wa askari walinzi wa mfalme akachukua yale masinia, vile vyetezo, yale mabakuli ya kunyunyizia, zile sufuria, vile vinara vya taa, zile sahani na yale mabakuli yaliyotumika kwa sadaka za vinywaji, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.
JER 52:20 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na wale mafahali kumi na wawili wa shaba waliokuwa chini yake, pamoja na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Mfalme Sulemani alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, ilikuwa na uzito mwingi usioweza kupimika.
JER 52:21 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kimo chake na mzunguko dhiraa kumi na mbili, na unene wa nyanda nne, na zote zilikuwa wazi ndani.
JER 52:22 Sehemu ya shaba juu ya ile nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tano, na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na makomamanga yake ilifanana na hiyo ya kwanza.
JER 52:23 Kulikuwa na makomamanga tisini na sita pembeni; jumla ya makomamanga juu ya wavu uliokuwa umezunguka yalikuwa mia moja.
JER 52:24 Yule mkuu wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu.
JER 52:25 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri saba wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji.
JER 52:26 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.
JER 52:27 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe. Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.
JER 52:28 Hii ndiyo hesabu ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua kwenda uhamishoni: katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu (3,023);
JER 52:29 katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza, watu mia nane na thelathini na wawili (832) kutoka Yerusalemu;
JER 52:30 katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake, Wayahudi mia saba na arobaini na watano (745) walichukuliwa kwenda uhamishoni na Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi wa mfalme.
JER 52:31 Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodaki alifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini mfalme wa Yuda, na kumfungua kutoka gerezani siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili.
JER 52:32 Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima kuliko wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli.
JER 52:33 Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya gerezani, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme.
JER 52:34 Siku kwa siku mfalme wa Babeli alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake, hadi siku ya kifo chake.
LAM 1:1 Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa, mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu! Jinsi umekuwa kama mama mjane, ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa! Yule aliyekuwa malkia miongoni mwa majimbo sasa amekuwa mtumwa.
LAM 1:2 Kwa uchungu, hulia sana usiku, machozi yapo kwenye mashavu yake. Miongoni mwa wapenzi wake wote hakuna yeyote wa kumfariji. Rafiki zake wote wamemsaliti, wamekuwa adui zake.
LAM 1:3 Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili, Yuda ameenda uhamishoni. Anakaa miongoni mwa mataifa, hapati mahali pa kupumzika. Wote ambao wanamsaka wamemkamata katikati ya dhiki yake.
LAM 1:4 Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza, kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja kwenye sikukuu zake zilizoamriwa. Malango yake yote yamekuwa ukiwa, makuhani wake wanalia kwa uchungu, wanawali wake wanahuzunika, naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu.
LAM 1:5 Adui zake wamekuwa mabwana zake, watesi wake wana amani. Mwenyezi Mungu amemletea huzuni kwa sababu ya dhambi zake nyingi. Watoto wake wameenda uhamishoni, wamekuwa mateka mbele ya adui.
LAM 1:6 Fahari zilizokuwa zake zimeondoka kutoka kwa Binti Sayuni. Wakuu wake wako kama ayala ambaye hapati malisho, wakiwa dhaifu wamekimbia mbele ya aliyewakimbiza.
LAM 1:7 Katika siku za mateso yake na kutangatanga, Yerusalemu hukumbuka hazina zote ambazo zilikuwa zake siku za kale. Watu wake walipoanguka katika mikono ya adui, hapatakuwa na yeyote wa kumsaidia. Watesi wake walimtazama na kumcheka katika maangamizi yake.
LAM 1:8 Yerusalemu ametenda dhambi sana kwa hiyo amekuwa najisi. Wote waliomheshimu wanamdharau, kwa maana wameuona uchi wake. Yeye mwenyewe anapiga kite na kugeukia mbali.
LAM 1:9 Uchafu wake umegandamana na nguo zake; hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye. Anguko lake lilikuwa la kushangaza, hapakuwa na yeyote wa kumfariji. “Tazama, Ee Mwenyezi Mungu, teso langu, kwa maana adui ameshinda.”
LAM 1:10 Adui ametia mikono juu ya hazina zake zote, aliona mataifa ya kipagani wakiingia mahali patakatifu pake, wale uliowakataza kuingia kwenye kusanyiko lako.
LAM 1:11 Watu wake wote wanalia kwa uchungu watafutapo chakula; wanabadilisha hazina zao kwa chakula ili waweze kuendelea kuishi. “Tazama, Ee Mwenyezi Mungu, uangalie; kwa maana nimedharauliwa.”
LAM 1:12 “Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando? Angalieni kote mwone. Je, kuna maumivu kama maumivu yangu yale yaliyotiwa juu yangu, yale Mwenyezi Mungu aliyoyaleta juu yangu katika siku ya hasira yake kali?
LAM 1:13 “Kutoka juu alipeleka moto, akaushusha katika mifupa yangu. Aliitandia wavu miguu yangu na akanirudisha nyuma. Akanifanya mkiwa, na mdhaifu mchana kutwa.
LAM 1:14 “Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira, kwa mikono yake zilifumwa pamoja. Zimefika shingoni mwangu na Bwana ameziondoa nguvu zangu. Amenitia mikononi mwa wale ambao siwezi kushindana nao.
LAM 1:15 “Bwana amewakataa mashujaa wote walio kati yangu; ameagiza jeshi dhidi yangu kuwaponda vijana wangu. Katika shinikizo lake la kukamulia zabibu Bwana amemkanyaga Bikira Binti Yuda.
LAM 1:16 “Hii ndiyo sababu ninalia na macho yangu yanafurika machozi. Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji, hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu. Watoto wangu ni wakiwa kwa sababu adui ameshinda.”
LAM 1:17 Sayuni ananyoosha mikono yake, lakini hakuna yeyote wa kumfariji. Mwenyezi Mungu ametoa amri kwa ajili ya Yakobo kwamba majirani zake wawe adui zake; Yerusalemu umekuwa kitu najisi miongoni mwao.
LAM 1:18 “Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake. Sikilizeni, enyi mataifa yote, tazameni maumivu yangu. Wasichana wangu na wavulana wangu wameenda uhamishoni.
LAM 1:19 “Niliita washirika wangu lakini walinisaliti. Makuhani wangu na wazee wangu waliangamia mjini walipokuwa wakitafuta chakula ili waweze kuishi.
LAM 1:20 “Angalia, Ee Mwenyezi Mungu, jinsi nilivyo katika dhiki! Nina maumivu makali ndani yangu, nami ninahangaika moyoni mwangu, kwa kuwa nimekuwa mwasi sana. Huko nje, upanga unaua watu, ndani, kipo kifo tu.
LAM 1:21 “Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu, lakini hakuna yeyote wa kunifariji. Adui zangu wote wamesikia kuhusu dhiki yangu, wanafurahia lile ulilolitenda. Naomba uilete siku uliyoitangaza ili wawe kama mimi.
LAM 1:22 “Uovu wao wote na uje mbele zako; uwaadhibu vikali kama ulivyoniadhibu kwa sababu ya dhambi zangu zote. Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi na moyo wangu umedhoofika.”
LAM 2:1 Tazama jinsi Bwana alivyomfunika Binti Sayuni kwa wingu la hasira yake! Ameitupa chini fahari ya Israeli kutoka mbinguni hadi duniani, hakukumbuka kiti chake cha kuwekea miguu katika siku ya hasira yake.
LAM 2:2 Bila huruma Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo; katika ghadhabu yake amebomoa ngome za Binti Yuda. Ameuangusha ufalme wake na wakuu wake chini kwa aibu.
LAM 2:3 Katika hasira kali amevunja kila pembe ya Israeli. Ameuondoa mkono wake wa kuume alipokaribia adui. Amemteketeza Yakobo kama moto uwakao ule uteketezao kila kitu kinachouzunguka.
LAM 2:4 Ameupinda upinde wake kama adui, mkono wake wa kuume uko tayari. Kama vile adui amewaua wote waliokuwa wanapendeza jicho, amemwaga ghadhabu yake kama moto juu ya hema la Binti Sayuni.
LAM 2:5 Bwana ni kama adui; amemmeza Israeli. Ameyameza majumba yake yote ya kifalme na kuangamiza ngome zake. Ameongeza huzuni na maombolezo kwa Binti Yuda.
LAM 2:6 Ameharibu maskani yake kama bustani, ameharibu mahali pake pa mkutano. Mwenyezi Mungu amemfanya Sayuni kusahau sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake; katika hasira yake kali amewadharau mfalme na kuhani.
LAM 2:7 Bwana amekataa madhabahu yake na kuacha mahali patakatifu pake. Amemkabidhi adui kuta za majumba yake ya kifalme; wameshangilia katika nyumba ya Mwenyezi Mungu kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa.
LAM 2:8 Mwenyezi Mungu alikusudia kuangusha ukuta uliomzunguka Binti Sayuni. Ameinyoosha kamba ya kupimia na hakuuzuia mkono wake usiangamize. Alifanya maboma na kuta ziomboleze, vyote vikaharibika pamoja.
LAM 2:9 Malango yake yamezama ardhini, makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu. Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni miongoni mwa mataifa, sheria haipo tena, na manabii wake hawapati tena maono kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
LAM 2:10 Wazee wa Binti Sayuni wanaketi chini kimya, wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao na kuvaa gunia. Wanawali wa Yerusalemu wameinamisha vichwa vyao hadi chini.
LAM 2:11 Macho yangu yamedhoofika kwa kulia, nina maumivu makali ndani, moyo wangu umemiminwa ardhini kwa sababu watu wangu wameangamizwa, kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia kwenye barabara za mji.
LAM 2:12 Wanawaambia mama zao, “Wapi mkate na divai?” wazimiapo kama watu waliojeruhiwa katika barabara za mji, maisha yao yadhoofikavyo mikononi mwa mama zao.
LAM 2:13 Ninaweza kusema nini kwa ajili yako? Nikulinganishe na nini, ee Binti Yerusalemu? Nitakufananisha na nini, ili nipate kukufariji, ee Bikira Binti Sayuni? Jeraha lako lina kina kama bahari. Ni nani awezaye kukuponya?
LAM 2:14 Maono ya manabii wako yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu, hawakuifunua dhambi yako ili kukuzuilia kwenda utumwani. Maneno waliyokupa yalikuwa ya uongo na ya kupotosha.
LAM 2:15 Wote wapitiao njia yako wanakupigia makofi, wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao kwa Binti Yerusalemu: “Huu ndio ule mji ulioitwa mkamilifu wa uzuri, furaha ya dunia yote?”
LAM 2:16 Adui zako wote wanapanua vinywa vyao dhidi yako, wanadhihaki na kusaga meno yao na kusema, “Tumemmeza. Hii ndiyo siku tuliyoingojea, tumeishi na kuiona.”
LAM 2:17 Mwenyezi Mungu amefanya lile alilolipanga; ametimiza neno lake aliloliamuru siku za kale. Amekuangusha bila huruma, amewaacha adui wakusimange, ametukuza pembe ya adui yako.
LAM 2:18 Mioyo ya watu inamlilia Bwana. Ee ukuta wa Binti Sayuni, machozi yako na yatiririke kama mto usiku na mchana; usijipe nafuu, macho yako yasipumzike.
LAM 2:19 Inuka, lia usiku, zamu za usiku zianzapo; mimina moyo wako kama maji mbele za Bwana. Mwinulie yeye mikono yako kwa ajili ya maisha ya watoto wako, ambao wanazimia kwa njaa kwenye kila mwanzo wa barabara.
LAM 2:20 “Tazama, Ee Mwenyezi Mungu, ufikirie: Ni nani ambaye umepata kumtendea namna hii? Je, wanawake wale wazao wao, watoto waliowalea? Je, kuhani na nabii auawe mahali patakatifu pa Bwana?
LAM 2:21 “Vijana na wazee hujilaza pamoja katika mavumbi ya barabarani, wasichana wangu na wavulana wangu wameanguka kwa upanga. Umewaua katika siku ya hasira yako, umewachinja bila huruma.
LAM 2:22 “Kama ulivyoita siku ya karamu, ndivyo ulivyoagiza mapigo dhidi yangu kila upande. Katika siku ya hasira ya Mwenyezi Mungu hakuna yeyote aliyekwepa au kupona; wale niliowatunza na kuwalea, adui yangu amewaangamiza.”
LAM 3:1 Mimi ndiye mtu aliyeona mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake.
LAM 3:2 Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee gizani wala si katika nuru;
LAM 3:3 hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu tena na tena, mchana kutwa.
LAM 3:4 Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa na ameivunja mifupa yangu.
LAM 3:5 Amenizingira na kunizunguka kwa uchungu na taabu.
LAM 3:6 Amenifanya niishi gizani kama wale waliokufa.
LAM 3:7 Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka, amenifunga kwa minyororo mizito.
LAM 3:8 Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada, anakataa kupokea maombi yangu.
LAM 3:9 Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe, amepotosha njia zangu.
LAM 3:10 Kama dubu aviziaye, kama simba mafichoni,
LAM 3:11 ameniburuta kutoka njiani, akanirarua na kuniacha bila msaada.
LAM 3:12 Amevuta upinde wake na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake.
LAM 3:13 Alinichoma moyo wangu kwa mishale iliyotoka kwenye podo lake.
LAM 3:14 Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote, wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa.
LAM 3:15 Amenijaza kwa majani machungu na kunishibisha kwa nyongo.
LAM 3:16 Amevunja meno yangu kwa changarawe, amenikanyagia mavumbini.
LAM 3:17 Amani yangu imeondolewa, nimesahau kufanikiwa ni nini.
LAM 3:18 Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu.”
LAM 3:19 Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu, uchungu na nyongo.
LAM 3:20 Ninayakumbuka vyema, nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.
LAM 3:21 Hata hivyo najikumbusha neno hili na kwa hiyo ninalo tumaini.
LAM 3:22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu, hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.
LAM 3:23 Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu.
LAM 3:24 Nimeiambia nafsi yangu, “Mwenyezi Mungu ni fungu langu, kwa hiyo nitamngojea.”
LAM 3:25 Mwenyezi Mungu ni mwema kwa wale wanaomtumaini, na kwa yule anayemtafuta;
LAM 3:26 ni vyema kungojea kwa utulivu kwa ajili ya wokovu wa Mwenyezi Mungu.
LAM 3:27 Ni vyema mtu kuchukua nira bado angali kijana.
LAM 3:28 Na akae peke yake awe kimya, kwa maana Mwenyezi Mungu ameiweka juu yake.
LAM 3:29 Hata azike uso wake mavumbini bado tumaini litakuwepo.
LAM 3:30 Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye, na ajazwe na aibu.
LAM 3:31 Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali na Bwana milele.
LAM 3:32 Ingawa huleta huzuni, ataonesha huruma, kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.
LAM 3:33 Kwa maana hapendi kuwaletea mateso au huzuni watoto wa wanadamu.
LAM 3:34 Kuwaponda chini ya nyayo wafungwa wote katika nchi,
LAM 3:35 Kumnyima mtu haki zake mbele za Aliye Juu Sana,
LAM 3:36 kumnyima mtu haki: Je, Bwana asione mambo kama haya?
LAM 3:37 Nani awezaye kusema nalo likatendeka kama Bwana hajaamuru?
LAM 3:38 Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana ndiko yatokako maafa na mambo mema?
LAM 3:39 Je, mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake?
LAM 3:40 Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu, na tumrudie Mwenyezi Mungu.
LAM 3:41 Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu kwa Mungu mbinguni, na tuseme:
LAM 3:42 “Tumetenda dhambi na kuasi nawe hujasamehe.
LAM 3:43 “Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia; umetuchinja bila huruma.
LAM 3:44 Unajifunika mwenyewe kwa wingu, ili pasiwe na ombi litakaloweza kupenya.
LAM 3:45 Umetufanya takataka na uchafu miongoni mwa mataifa.
LAM 3:46 “Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao wazi dhidi yetu.
LAM 3:47 Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula, uharibifu na maangamizi.”
LAM 3:48 Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu, kwa sababu watu wangu wameangamizwa.
LAM 3:49 Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma, bila kupata nafuu,
LAM 3:50 hadi Mwenyezi Mungu atazame chini kutoka mbinguni na kuona.
LAM 3:51 Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu.
LAM 3:52 Wale waliokuwa adui zangu bila sababu wameniwinda kama ndege.
LAM 3:53 Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo na kunitupia mawe;
LAM 3:54 maji yalifunika juu ya kichwa changu, nami nikafikiri nilikuwa karibu kukatiliwa mbali.
LAM 3:55 Nililiitia jina lako, Ee Mwenyezi Mungu, kutoka vina vya shimo.
LAM 3:56 Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako kilio changu nikuombapo msaada.”
LAM 3:57 Ulikuja karibu nilipokuita, nawe ukasema, “Usiogope.”
LAM 3:58 Ee Bwana, ulichukua shauri langu, ukaukomboa uhai wangu.
LAM 3:59 Umeona, Ee Mwenyezi Mungu, ubaya niliotendewa. Tetea shauri langu!
LAM 3:60 Umeona kina cha kisasi chao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu.
LAM 3:61 Ee Mwenyezi Mungu, umesikia matukano yao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu:
LAM 3:62 kile adui zangu wanachonong’ona na kunung’unikia dhidi yangu mchana kutwa.
LAM 3:63 Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama, wananidhihaki katika nyimbo zao.
LAM 3:64 Uwalipe kile wanachostahili, Ee Mwenyezi Mungu, kwa yale ambayo mikono yao imetenda.
LAM 3:65 Weka pazia juu ya mioyo yao, laana yako na iwe juu yao!
LAM 3:66 Wafuatilie katika hasira na uwaangamize chini ya mbingu za Mwenyezi Mungu.
LAM 4:1 Jinsi dhahabu ilivyopoteza mng’ao wake, dhahabu iliyo safi haing’ai! Vito vya thamani vimetawanywa kwenye mwanzo wa kila barabara.
LAM 4:2 Wana wa Sayuni wenye thamani, ambao mwanzo uzito wa thamani yao ulikuwa wa dhahabu, sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo, kazi ya mikono ya mfinyanzi!
LAM 4:3 Hata mbweha hutoa matiti yao kunyonyesha watoto wao, lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma kama mbuni jangwani.
LAM 4:4 Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga umegandamana na kaakaa la kinywa chake, watoto huomba mkate, lakini hakuna yeyote awapaye.
LAM 4:5 Wale waliokula vyakula vya kifahari ni maskini barabarani. Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau sasa wanalalia majivu.
LAM 4:6 Adhabu ya watu wangu ni kubwa kuliko ile ya Sodoma, ambayo ilipinduliwa ghafula wala hapakuwa na mkono wa msaada.
LAM 4:7 Wakuu wao walikuwa wameng’aa kuliko theluji na weupe kuliko maziwa, miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani, kuonekana kwao kama yakuti samawi.
LAM 4:8 Lakini sasa ni weusi kuliko masizi; hawatambulikani barabarani. Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao, imekuwa mikavu kama fimbo.
LAM 4:9 Wale waliouawa kwa upanga ni bora kuliko wale wanaokufa njaa; wanateseka kwa njaa, wanatokomea kwa kukosa chakula kutoka shambani.
LAM 4:10 Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma wanapika watoto wao wenyewe, waliokuwa chakula chao watu wangu walipoangamizwa.
LAM 4:11 Mwenyezi Mungu ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake; ameimwaga hasira yake kali. Amewasha moto katika Sayuni ambao umeteketeza misingi yake.
LAM 4:12 Wafalme wa dunia hawakuamini, wala mtu yeyote wa duniani, kwamba adui na watesi wangeweza kuingia kwenye malango ya Yerusalemu.
LAM 4:13 Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake, na maovu ya makuhani wake, waliomwaga ndani yake damu ya wenye haki.
LAM 4:14 Sasa wanapapasa papasa barabarani kama watu ambao ni vipofu. Wamenajisiwa kabisa kwa damu, hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.
LAM 4:15 Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi! Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!” Wanapokimbia na kutangatanga, watu miongoni mwa mataifa wanasema, “Hawawezi kukaa hapa zaidi.”
LAM 4:16 Mwenyezi Mungu mwenyewe amewatawanya; hawaangalii tena. Makuhani hawaoneshwi heshima, wazee hawakubaliki.
LAM 4:17 Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka, kwa kutazamia bure msaada; tuliangalia kutoka minara yetu kwa taifa lisiloweza kutuokoa.
LAM 4:18 Watu walituvizia katika kila hatua hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu. Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia, kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.
LAM 4:19 Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai angani; walitusaka juu milimani na kutuvizia jangwani.
LAM 4:20 Mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu, pumzi ya uhai wetu hasa, alinaswa katika mitego yao. Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake tungeishi miongoni mwa mataifa.
LAM 4:21 Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu, wewe unayeishi nchi ya Usi. Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa, Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.
LAM 4:22 Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha, hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni. Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako, na atafunua uovu wako.
LAM 5:1 Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, yaliyotupata, tazama, nawe uione aibu yetu.
LAM 5:2 Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni, na nyumba zetu kwa wageni.
LAM 5:3 Tumekuwa yatima wasio na baba, mama zetu wamekuwa kama wajane.
LAM 5:4 Ni lazima tununue maji tunayokunywa, kuni zetu zapatikana tu kwa kununua.
LAM 5:5 Wanaotufuatilia wapo kwenye visigino vyetu, tumechoka na hakuna pumziko.
LAM 5:6 Tumejitolea kwa Misri na Ashuru tupate chakula cha kutosha.
LAM 5:7 Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena, na sisi tunachukua adhabu yao.
LAM 5:8 Watumwa wanatutawala na hakuna wa kutuokoa mikononi yao.
LAM 5:9 Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu kwa sababu ya upanga jangwani.
LAM 5:10 Ngozi yetu ina joto kama tanuru, kutokana na fadhaa ya njaa.
LAM 5:11 Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni, na mabikira katika miji ya Yuda.
LAM 5:12 Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao, wazee hawapewi heshima.
LAM 5:13 Vijana wanataabika kwenye mawe ya kusagia, wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni.
LAM 5:14 Wazee wameondoka katika lango la mji, vijana wameacha kuimba nyimbo zao.
LAM 5:15 Furaha imeondoka mioyoni mwetu, kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.
LAM 5:16 Taji limeanguka kutoka kichwani petu. Ole wetu, kwa maana tumetenda dhambi!
LAM 5:17 Kwa sababu hiyo, mioyo yetu inazimia, kwa sababu ya hayo, macho yetu yamefifia,
LAM 5:18 kwa sababu Mlima Sayuni umekaa ukiwa, na mbweha wanatembea juu yake.
LAM 5:19 Wewe, Ee Mwenyezi Mungu unatawala milele, kiti chako cha enzi chadumu kizazi hadi kizazi.
LAM 5:20 Kwa nini watusahau siku zote? Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu?
LAM 5:21 Turudishe kwako mwenyewe, Ee Mwenyezi Mungu, ili tupate kurudi. Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale,
LAM 5:22 isipokuwa uwe umetukataa kabisa na umetukasirikia pasipo kipimo.
EZE 1:1 Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa miongoni mwa waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu.
EZE 1:2 Katika siku ya tano ya mwezi, mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehoyakini,
EZE 1:3 neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yake.
EZE 1:4 Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini: wingu kubwa sana likiwa na miali ya radi, likizungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama chuma inavyong’aa ndani ya moto.
EZE 1:5 Ndani ya ule moto kulikuwa na mfano wa viumbe wanne wenye uhai. Kuonekana kwao walikuwa na umbo la mwanadamu,
EZE 1:6 lakini kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne.
EZE 1:7 Miguu yao ilikuwa imenyooka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa.
EZE 1:8 Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa,
EZE 1:9 nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja; hawakugeuka walipotembea.
EZE 1:10 Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa hao wanne alikuwa na uso wa mwanadamu, na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, na kwa upande wa kushoto alikuwa na uso wa ng’ombe; pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai.
EZE 1:11 Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliokunjuliwa kuelekea juu; kila bawa liligusa bawa la mwenzake kila upande; kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake.
EZE 1:12 Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipoenda, walienda pasipo kugeuka.
EZE 1:13 Kuonekana kwa wale viumbe hai kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya wale viumbe; ulikuwa na mwangaza mkali na katika ule moto kulitoka miali ya radi.
EZE 1:14 Wale viumbe walipiga mbio kwenda na kurudi, kama miali ya radi.
EZE 1:15 Nilipokuwa nikitazama wale viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe na nyuso zake nne.
EZE 1:16 Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yalimetameta kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilionekana kuwa na gurudumu lingine ndani yake.
EZE 1:17 Magurudumu yalipoenda, yalielekea upande mmoja wa pande nne walikoelekea wale viumbe; wale viumbe walipoenda, magurudumu hayakugeuka.
EZE 1:18 Kingo za magurudumu zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote.
EZE 1:19 Wale viumbe hai walipoenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea; wakati hao viumbe hai walipoinuka kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka.
EZE 1:20 Popote roho alipoenda, wale viumbe nao walienda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa sababu roho ya wale viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.
EZE 1:21 Viumbe wale waliposogea, nayo magurudumu yalisogea; viumbe waliposimama, nayo pia yalisimama; viumbe walipoinuka juu ya nchi, magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa kuwa roho ya hao viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.
EZE 1:22 Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na la kutisha.
EZE 1:23 Chini ya hiyo nafasi, mabawa yao yalitanda moja kuelekea lingine, na kila mmoja alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake.
EZE 1:24 Viumbe wale waliposogea, nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi, kama kishindo cha jeshi. Waliposimama, walishusha mabawa yao.
EZE 1:25 Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa.
EZE 1:26 Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha utawala cha yakuti samawi. Na juu ya kile kiti cha utawala kulikuwa na umbo, mfano wa mwanadamu.
EZE 1:27 Nikaona kwamba kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea juu, alionekana kama chuma inavyong’aa ikiwa ndani ya moto, na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto; mwanga wenye kung’aa sana ulimzunguka.
EZE 1:28 Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mng’ao uliomzunguka. Hivi ndivyo mfano wa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulionekana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.
EZE 2:1 Akaniambia, “Mwanadamu, simama kwa miguu yako nami nitasema nawe.”
EZE 2:2 Alipokuwa akiongea nami, Roho wa Mungu akanijia na kunisimamisha wima, nikamsikia akisema nami.
EZE 2:3 Akaniambia: “Mwanadamu, ninakutuma kwa Waisraeli, taifa ambalo limeniasi mimi; wao na baba zao wameniasi hadi leo.
EZE 2:4 Watu ninaokutuma kwao ni wakaidi na wabishi. Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mungu Mwenyezi.’
EZE 2:5 Kama watasikiliza au hawatasikiliza, kwa kuwa wao ni nyumba ya uasi, watajua nabii amekuwa miongoni mwao.
EZE 2:6 Nawe mwanadamu, usiwaogope wao wala maneno yao. Usiogope, ijapo michongoma na miiba vinakuzunguka na unaishi katikati ya nge. Usiogope yale wasemayo wala usitishwe nao, ijapo wao ni nyumba ya uasi.
EZE 2:7 Lazima uwaambie maneno yangu, ikiwa watasikiliza au hawatasikiliza, kwa kuwa wao ni waasi.
EZE 2:8 Lakini wewe mwanadamu, sikiliza ninalokuambia. Usiasi kama hiyo nyumba ya uasi. Fungua kinywa chako na ule nikupacho.”
EZE 2:9 Ndipo nikatazama, nami nikaona mkono ulionyooshwa kunielekea. Nao ulikuwa na kitabu,
EZE 2:10 ambacho alikikunjua mbele yangu. Pande zote mbili kilikuwa kimeandikwa maneno ya maombolezo, na vilio na ole.
EZE 3:1 Naye akaniambia, “Mwanadamu, kula kilichoko mbele yako, kula kitabu hiki, kisha uende ukaseme na nyumba ya Israeli.”
EZE 3:2 Hivyo, nikafungua kinywa changu, naye akanipa kile kitabu nikile.
EZE 3:3 Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, kula kitabu hiki ninachokupa, ujaze tumbo lako.” Kwa hiyo nikaula, nao ulikuwa mtamu kama asali kinywani mwangu.
EZE 3:4 Kisha akaniambia, “Mwanadamu, sasa nenda katika nyumba ya Israeli ukawanenee maneno yangu.
EZE 3:5 Hukutumwa kwa taifa lenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli.
EZE 3:6 Sikukutuma kwa mataifa mengi yenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu ambao maneno yao hutayaelewa. Hakika ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza.
EZE 3:7 Lakini nyumba ya Israeli haitakusikiliza, kwa kuwa hawako radhi kunisikiliza mimi, kwa kuwa nyumba yote ya Israeli ni wenye paji gumu na mioyo ya ukaidi.
EZE 3:8 Tazama, nimefanya uso wako mgumu dhidi ya nyuso zao, na paji la uso wako gumu dhidi ya paji za nyuso zao.
EZE 3:9 Kama vile almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyolifanya paji la uso wako. Usiwaogope wala usiwahofu, ijapokuwa ni nyumba ya uasi.”
EZE 3:10 Naye akaniambia, “Mwanadamu, sikiliza kwa makini na uyatie moyoni mwako maneno yote nitakayosema nawe.
EZE 3:11 Kisha nenda kwa watu wa taifa lako walio uhamishoni, ukaseme nao. Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi’; iwe watasikiliza au hawatasikiliza.”
EZE 3:12 Ndipo Roho wa Mungu akaniinua juu, nami nikasikia sauti kubwa ya ngurumo nyuma yangu ikisema, “Utukufu wa Mwenyezi Mungu na utukuzwe katika makao yake!”
EZE 3:13 Ilikuwa ni sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yakigusana moja kwa lingine, na sauti ya magurudumu kando yao, sauti kubwa ya ngurumo.
EZE 3:14 Kisha Roho wa Mungu akaniinua juu na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na hasira moyoni mwangu, nao mkono wenye nguvu wa Mwenyezi Mungu ukiwa juu yangu.
EZE 3:15 Nikafika kwa wale watu waliokuwa uhamishoni huko Tel-Abibu karibu na Mto Kebari. Nikakaa miongoni mwao kwa muda wa siku saba, nikiwa nimejawa na mshangao.
EZE 3:16 Mwishoni mwa hizo siku saba neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 3:17 “Mwanadamu, nimekufanya uwe mlinzi wa nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo, ukawape onyo litokalo kwangu.
EZE 3:18 Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usimwonye mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu akifa katika dhambi yake, damu yake nitaidai mkononi mwako.
EZE 3:19 Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako.
EZE 3:20 “Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako.
EZE 3:21 Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.”
EZE 3:22 Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yangu huko, naye akaniambia, “Simama uende sehemu tambarare, nami nitasema nawe huko.”
EZE 3:23 Kwa hiyo niliinuka nikaenda mahali tambarare. Utukufu wa Mwenyezi Mungu ulikuwa umesimama huko, kama utukufu ule niliouona kando ya Mto Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.
EZE 3:24 Ndipo Roho wa Mungu akaja ndani yangu, akanisimamisha kwa miguu yangu. Akasema nami akaniambia: “Nenda ukajifungie ndani ya nyumba yako.
EZE 3:25 Nawe, ee mwanadamu, watakufunga kwa kamba; utafungwa ili usiweze kuwaendea watu.
EZE 3:26 Nitaufanya ulimi wako ushikamane kwenye kaakaa la kinywa chako, ili uwe kimya usiweze kuwakemea, kwa kuwa wao ni nyumba ya uasi.
EZE 3:27 Lakini nitakaposema nawe, nitafungua kinywa chako nawe utawaambia, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi.’ Yeyote atakayesikiliza na asikilize, na yeyote atakayekataa na akatae; kwa kuwa wao ni nyumba ya uasi.
EZE 4:1 “Mwanadamu, sasa chukua tofali, uliweke mbele yako na uchore juu yake ramani ya mji wa Yerusalemu.
EZE 4:2 Kisha uuzingire: Njenga husuru dhidi yake, na upandishe kilima hadi kuta zake, weka kambi dhidi yake pande zote, pamoja na magogo ya kubomoa.
EZE 4:3 Kisha chukua bamba la chuma, ukalisimamishe liwe kama ukuta wa chuma kati yako na huo mji, nawe uuelekeze uso wako. Huo mji utakuwa katika hali ya kuzingirwa, nawe ndiwe utakayeuzingira. Hii itakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli.
EZE 4:4 “Kisha ulale kwa upande wako wa kushoto na uweke dhambi za nyumba ya Israeli juu yako. Utazibeba dhambi zao kwa idadi ya siku utakazolala kwa huo upande mmoja.
EZE 4:5 Nimekupangia idadi ya siku kama miaka ya dhambi yao. Kwa hiyo kwa siku mia tatu na tisini (390), utabeba dhambi za nyumba ya Israeli.
EZE 4:6 “Baada ya kumaliza hili, lala chini tena, wakati huu ulale chini kwa upande wa kuume, uchukue dhambi za nyumba ya Yuda. Nimekupangia siku arobaini, siku moja kwa kila mwaka.
EZE 4:7 Geuza uso wako uuelekeze Yerusalemu uone jinsi ulivyozingirwa, na kwa mkono wako usiovikwa nguo, tabiri dhidi yake.
EZE 4:8 Nitakufunga kwa kamba ili usiweze kugeuka kutoka upande mmoja hadi upande mwingine, hata utakapotimiza siku za kuzingirwa kwako.
EZE 4:9 “Chukua ngano na shayiri, maharagwe na dengu, mtama na mawele, uviweke na kuvihifadhi vyote kwenye gudulia la kuhifadhia, na uvitumie kujitengenezea mkate. Utaula mkate huo kwa hizo siku mia tatu na tisini (390) utakazokuwa umelala kwa upande mmoja.
EZE 4:10 Pima shekeli ishirini za chakula utakachokula kwa kila siku, nawe utakula kwa wakati uliopangwa.
EZE 4:11 Pia pima maji sehemu ya sita ya hini, nawe utakunywa kwa wakati uliopangwa.
EZE 4:12 Nawe utakula chakula vile ungekula mkate wa shayiri; uoke mkate mbele ya macho ya watu, ukitumia moto wa kinyesi cha mwanadamu.”
EZE 4:13 Mwenyezi Mungu akasema, “Hivi ndivyo watu wa Israeli watakavyokula chakula kilicho najisi miongoni mwa mataifa ninakowapeleka.”
EZE 4:14 Ndipo nikasema, “Sivyo Bwana Mungu Mwenyezi! Kamwe mimi sijajitia unajisi. Tangu ujana wangu hadi sasa sijala kamwe kitu chochote kilichokufa au kilichoraruliwa na wanyama pori. Hakuna nyama yoyote najisi iliyoingia kinywani mwangu.”
EZE 4:15 Akasema, “Vema sana, basi nitakuruhusu uoke mkate wako kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe badala ya kinyesi cha mwanadamu.”
EZE 4:16 Kisha Mungu akaniambia, “Mwanadamu! Mimi nitasababisha uhaba wa chakula katika Yerusalemu. Watu watakula chakula cha mgawo kwa wasiwasi, na maji ya mgawo kwa kukata tamaa,
EZE 4:17 kwa kuwa chakula na maji vitakuwa adimu. Kila mmoja atastaajabu kumwona mwenzake, nao watadhoofika kwa sababu ya dhambi yao.
EZE 5:1 “Mwanadamu, chukua upanga mkali na uutumie kama wembe wa kinyozi ili kunyoa kichwa chako na ndevu zako. Kisha uchukue mizani, uzipime na kuzigawanya nywele hizo.
EZE 5:2 Siku zako za kuzingirwa zitakapokwisha, choma theluthi moja ya nywele ndani ya mji. Chukua theluthi nyingine ya hizo nywele uzikatekate kwa upanga ukiuzunguka mji wote, na theluthi ya mwisho uitawanye kwa upepo, kwa kuwa nitawafuatia kwa upanga uliovutwa.
EZE 5:3 Lakini chukua nywele chache uzifungie ndani ya pindo la vazi lako.
EZE 5:4 Tena chukua nywele nyingine chache uzitupe motoni uziteketeze. Moto utaenea kutoka hapo na kufika katika nyumba yote ya Israeli.
EZE 5:5 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Huu ndio mji wa Yerusalemu, ambao nimeuweka katikati ya mataifa, ukiwa umezungukwa na nchi pande zote.
EZE 5:6 Lakini katika uovu wake umeasi sheria na amri zangu kuliko mataifa na nchi zinazouzunguka. Umeasi sheria zangu wala haukufuata amri zangu.
EZE 5:7 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninyi mmekuwa wakaidi kuliko mataifa yanayowazunguka na hamkufuata maagizo yangu wala kuzishika sheria zangu. Wala hamkuweza hata kuzifuata desturi za mataifa yanayowazunguka.
EZE 5:8 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi mwenyewe niko kinyume nawe, Yerusalemu, na nitakupiga kwa adhabu yangu mbele ya mataifa.
EZE 5:9 Kwa sababu ya sanamu zako zote za machukizo, nitakufanyia kile ambacho kamwe sijafanya kabla wala kamwe sitafanya tena.
EZE 5:10 Kwa hiyo, kati yako baba watakula watoto wao, na watoto watakula baba zao. Nitawapiga kwa adhabu, nami nitawatawanya watu wenu walionusurika pande zote za dunia.
EZE 5:11 Kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, kwa kuwa mmenajisi mahali pangu patakatifu kwa sanamu zenu mbovu na desturi zenu za machukizo, mimi mwenyewe nitaondoa fadhili zangu kwenu.
EZE 5:12 Theluthi ya watu wako watakufa kwa tauni au kwa njaa humu ndani yako; theluthi nyingine itaanguka kwa upanga nje ya kuta zako; nayo theluthi nyingine nitaitawanya kwenye pande nne na kuwafuatia kwa upanga.
EZE 5:13 “Ndipo hasira yangu itakapokoma na ghadhabu yangu dhidi yao kupungua, nami nitakuwa nimejilipizia kisasi. Baada ya kuimaliza ghadhabu yangu juu yao, watajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, nimenena katika bidii yangu.
EZE 5:14 “Nitakuangamiza na kukufanya kitu cha kudharauliwa miongoni mwa mataifa yanayokuzunguka, machoni pa wote wapitao karibu nawe.
EZE 5:15 Utakuwa kitu cha kudharauliwa na cha dhihaka, kitu cha onyo na cha kutisha kwa mataifa yanayokuzunguka, nitakapokupiga kwa adhabu katika hasira na ghadhabu yangu kwa kukukemea kwa ukali. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena.
EZE 5:16 Nitakapokurushia mishale yangu ya kufisha na yenye kuharibu ya njaa, nitairusha ili kukuangamiza. Nitaleta njaa zaidi na zaidi juu yako na kukomesha upatikanaji wa chakula kwako.
EZE 5:17 Nitatuma njaa na wanyama pori dhidi yako, navyo vitakuacha bila watoto. Tauni na umwagaji wa damu vitapita katikati yako, nami nitaleta upanga juu yako. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena.”
EZE 6:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema,
EZE 6:2 “Mwanadamu, elekeza uso wako kukabili milima ya Israeli, utabiri dhidi yake,
EZE 6:3 useme, ‘Ee milima ya Israeli, sikieni neno la Bwana Mungu Mwenyezi. Hili ndilo neno asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa milima na vilima, magenge na mabonde: Nakaribia kuleta upanga dhidi yenu, na nitapaharibu mahali penu pa juu pa kuabudia.
EZE 6:4 Madhabahu yenu yatabomolewa na madhabahu yenu ya kufukizia uvumba yatavunjavunjwa, nami nitawachinja watu wenu mbele ya sanamu zenu.
EZE 6:5 Nitazilaza maiti za Waisraeli mbele ya sanamu zao, nami nitatawanya mifupa yenu kuzunguka madhabahu yenu.
EZE 6:6 Popote mnapoishi, miji itaangamizwa na mahali pa juu patabomolewa, ili madhabahu zenu ziharibiwe na kuteketezwa; sanamu zenu zitavunjwavunjwa na kuharibiwa, madhabahu zenu za kufukizia uvumba zitabomolewa, na kila mlichokifanya kitakatiliwa mbali.
EZE 6:7 Watu wenu watachinjwa kati yenu, nanyi mtatambua Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 6:8 “ ‘Lakini nitawabakiza hai baadhi yenu, kwa kuwa baadhi yenu watanusurika kuuawa kwa upanga watakapokuwa wametawanyika katika nchi na katika mataifa.
EZE 6:9 Ndipo katika mataifa walikochukuliwa mateka, watakaonusurika watanikumbuka. Watakumbuka jinsi nilivyohuzunishwa na mioyo yao ya uzinzi ambayo imegeuka kuwa mbali nami, na kwa macho yao ambayo yametamani sanamu zao. Watajichukia wenyewe kwa sababu ya uovu walioutenda na desturi zao za kuchukiza.
EZE 6:10 Nao watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, sikuwaonya bure kuwa nitaleta maafa hayo yote juu yao.
EZE 6:11 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Piga makofi, pigisha mguu wako chini, na upige kelele useme, “Ole!” kwa sababu ya maovu yote na desturi za kuchukiza za nyumba ya Israeli, wataangamia kwa upanga, njaa na tauni.
EZE 6:12 Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni, naye aliye karibu atauawa kwa upanga, naye yule atakayenusurika na kubaki atakufa kwa njaa. Hivyo ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu dhidi yao.
EZE 6:13 Nao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, wakati maiti za watu wao zitakapokuwa zimelala kati ya sanamu zao kuzunguka madhabahu yao, juu ya kila kilima kilichoinuka na juu ya vilele vyote vya milima, chini ya kila mti uliotanda na kila mwaloni wenye majani, yaani sehemu walizofukizia uvumba kwa sanamu zao zote.
EZE 6:14 Nami nitanyoosha mkono wangu dhidi yao na kuifanya nchi yao ukiwa, kuanzia jangwani hadi Dibla, kila mahali wanapoishi. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 7:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 7:2 “Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa nchi ya Israeli: “ ‘Mwisho! Mwisho umekuja juu ya pembe nne za nchi!
EZE 7:3 Sasa mwisho umekuja juu yenu, nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza.
EZE 7:4 Sitawaonea huruma wala kuwarehemu. Hakika nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’
EZE 7:5 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa! Tazama, yanakuja!
EZE 7:6 Mwisho umewadia! Mwisho umewadia! Umejiinua wenyewe dhidi yenu. Tazama, umewadia!
EZE 7:7 Maangamizi yamekuja juu yenu, ninyi mnaoishi katika nchi. Wakati umewadia! Siku imekaribia! Kuna hofu kuu ya ghafula juu ya milima, wala si furaha.
EZE 7:8 Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu na kumaliza hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo.
EZE 7:9 Sitawaonea huruma wala kuwarehemu. Nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi za machukizo miongoni mwenu. “ ‘Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ambaye huwapiga.
EZE 7:10 “ ‘Tazama, siku imefika! Tazama, imewadia! Maangamizi yamezuka ghafula, fimbo imechanua, nayo majivuno yamechipua!
EZE 7:11 Jeuri imeinuka kuwa fimbo ya kuadhibu waovu. Hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa, hata mmoja wa kundi hilo: hakuna utajiri wao utabaki, wala chochote cha thamani.
EZE 7:12 Wakati umewadia, siku imefika. Mnunuzi na asifurahi wala muuzaji asihuzunike, kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote.
EZE 7:13 Muuzaji hatajipatia tena ardhi aliyoiuza wakati wote wawili wangali hai. Kwa kuwa maono kuhusu kundi lote hayatatanguka. Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja atakayeokoa maisha yake.
EZE 7:14 “ ‘Wajapopiga tarumbeta na kuweka kila kitu tayari, hakuna hata mmoja atakayeenda vitani, kwa maana ghadhabu yangu iko juu ya kundi lote.
EZE 7:15 Nje ni upanga, ndani ni tauni na njaa. Walio shambani watakufa kwa upanga, nao waliomo mjini njaa na tauni vitawala.
EZE 7:16 Wote watakaopona na kutoroka watakuwa milimani, wakiomboleza kama hua wa mabondeni, kila mmoja kwa sababu ya dhambi zake.
EZE 7:17 Kila mkono utalegea na kila goti litakuwa dhaifu kama maji.
EZE 7:18 Watavaa gunia na kufunikwa na hofu. Nyuso zao zitafunikwa na aibu, na vichwa vyao vitanyolewa.
EZE 7:19 “ ‘Watatupa fedha yao barabarani, nayo dhahabu yao itakuwa najisi. Fedha yao na dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Hawatashibisha njaa yao au kujaza tumbo zao kwa hiyo fedha wala dhahabu, kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini.
EZE 7:20 Walijivunia vito vyao vizuri na kuvitumia kutengeneza sanamu za machukizo na vinyago vya upotovu. Kwa hiyo nitavifanya vitu hivyo kuwa najisi kwao.
EZE 7:21 Nitavitia vyote mikononi mwa wageni kuwa nyara na kuwa vitu vilivyotekwa mikononi mwa watu waovu wa dunia, nao watavinajisi.
EZE 7:22 Nitaugeuza uso wangu mbali nao, nao waovu wa dunia watapanajisi mahali pangu pa thamani. Wanyang’anyi watapaingia na kupanajisi.
EZE 7:23 “ ‘Andaa minyororo, kwa sababu nchi imejaa umwagaji wa damu na mji umejaa udhalimu.
EZE 7:24 Nitaleta taifa ovu kuliko yote kumiliki nyumba zao. Nitakomesha kiburi cha wenye nguvu na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.
EZE 7:25 Hofu ya ghafula itakapokuja, watatafuta amani, lakini haitapatikana.
EZE 7:26 Maafa juu ya maafa yatakuja, tetesi ya mabaya juu ya tetesi ya mabaya. Watajitahidi kupata maono kutoka kwa nabii; mafundisho ya sheria toka kwa kuhani yatapotea, vivyo hivyo shauri kutoka kwa wazee.
EZE 7:27 Mfalme ataomboleza, mwana wa mfalme atavikwa kukata tamaa, nayo mikono ya watu wa nchi itatetemeka. Nitawaadhibu kulingana na matendo yao, na kwa kanuni zao wenyewe nitawahukumu. “ ‘Ndipo watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 8:1 Katika mwaka wa sita, siku ya tano ya mwezi wa sita, nilipokuwa nimeketi katika nyumba yangu na wazee wa Yuda wakiwa wameketi mbele yangu, mkono wa Bwana Mungu Mwenyezi ulikuja juu yangu.
EZE 8:2 Nikatazama, nikaona umbo mfano wa mwanadamu. Kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea chini alifanana na moto. Kuanzia kiuno kuelekea juu sura yake iling’aa vile chuma king’aavyo kikiwa ndani ya moto.
EZE 8:3 Akanyoosha kitu kilichofanana na mkono, akaniinua kwa kushika nywele za kichwa changu. Roho wa Mungu akaniinua juu kati ya nchi na mbingu, na nikiwa katika maono ya Mungu, akanichukua hadi Yerusalemu, kwenye ingilio la lango la kaskazini mwa ukumbi wa ndani, mahali iliposimama ile sanamu inayochochea wivu.
EZE 8:4 Tazama! Palikuwa na utukufu wa Mungu wa Israeli, kama utukufu ule niliouona katika maono kule kwenye nchi tambarare.
EZE 8:5 Kisha akaniambia, “Mwanadamu, tazama kuelekea kaskazini.” Hivyo nikatazama na kwenye ingilio la kaskazini mwa lango la madhabahu, nikaona sanamu hii ya wivu.
EZE 8:6 Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, je, unaona yale wanayoyafanya: mambo ya kuchukiza kabisa ambayo nyumba ya Israeli wanayatenda hapa, yatakayonifanya niende mbali na mahali pangu patakatifu? Lakini utayaona mambo yanayochukiza hata zaidi.”
EZE 8:7 Kisha akanileta hadi ingilio la ukumbi. Nikatazama, nami nikaona tundu ukutani.
EZE 8:8 Akaniambia, “Mwanadamu, sasa toboa ukuta huu.” Ndipo nikatoboa ule ukuta, nikaona hapo pana mlango.
EZE 8:9 Naye akaniambia, “Ingia ndani, ukaone maovu na machukizo wanayofanya humu.”
EZE 8:10 Hivyo nikaingia ndani na kutazama. Nikaona kuta zote zimechorwa aina mbalimbali ya viumbe vinavyotambaa, na wanyama wanaochukiza, na sanamu zote za nyumba ya Israeli.
EZE 8:11 Mbele ya hizo kuta walisimama wazee sabini wa nyumba ya Israeli, naye Yaazania mwana wa Shafani alikuwa amesimama miongoni mwao. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi, na moshi wa harufu nzuri ya uvumba ulikuwa unapanda juu.
EZE 8:12 Akaniambia, “Mwanadamu, umeona wanayoyafanya wazee wa Israeli wakiwa gizani, kila mmoja kwenye mahali pa ibada pa sanamu yake? Wao husema, ‘Mwenyezi Mungu hatuoni, Mwenyezi Mungu ameiacha nchi.’ ”
EZE 8:13 Akasema tena, “Utawaona wakifanya mambo yaliyo chukizo zaidi.”
EZE 8:14 Ndipo akanileta kwenye ingilio la lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi Mungu, nami nikaona wanawake wameketi hapo, wakimwombolezea Tamuzi.
EZE 8:15 Akaniambia, “Je, mwanadamu, unaliona hili? Utayaona mambo yanayochukiza hata zaidi.”
EZE 8:16 Ndipo akanileta hadi kwenye ukumbi wa ndani wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, na katika ingilio la Hekalu, kati ya baraza na madhabahu, palikuwa na wanaume wapatao ishirini na watano. Walikuwa wamelipa kisogo Hekalu la Mwenyezi Mungu na kuelekeza nyuso zao upande wa mashariki, wakilisujudia jua upande wa mashariki.
EZE 8:17 Akaniambia, “Je, umeona hili mwanadamu? Je, ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda kufanya machukizo wanayoyafanya hapa? Je, ni lazima pia waijaze nchi dhuluma na kuendelea siku zote kunikasirisha? Watazame wanavyonibania pua kana kwamba ninanuka!
EZE 8:18 Kwa hiyo nitawaadhibu kwa hasira; sitawaonea huruma wala kuwarehemu. Hata wakipiga makelele masikioni mwangu, sitawasikiliza.”
EZE 9:1 Kisha nikamsikia akiita kwa sauti kubwa akisema, “Walete wasimamizi wa mji hapa, kila mmoja akiwa na silaha mkononi mwake.”
EZE 9:2 Nami nikaona watu sita wakija toka upande wa lango la juu linalotazama kaskazini, kila mmoja akiwa na silaha za kuangamiza mkononi mwake. Kati yao palikuwa na mtu aliyevaa mavazi ya kitani safi, naye alikuwa na vifaa vya mwandishi kiunoni mwake. Wakaingia ndani ya Hekalu na kusimama pembeni mwa madhabahu ya shaba.
EZE 9:3 Basi utukufu wa Mungu wa Israeli ukaondoka hapo juu ya makerubi, ulikokuwa umekaa, ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwita yule mtu aliyevaa kitani safi na mwenye vifaa vya mwandishi kiunoni mwake,
EZE 9:4 akamwambia, “Pita katika mji wote wa Yerusalemu ukaweke alama kwenye paji za nyuso za wale watu wanaohuzunika na kuomboleza kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.”
EZE 9:5 Nikiwa ninasikiliza, akawaambia wale wengine, “Mfuateni anapopita katika mji wote mkiua, pasipo huruma wala masikitiko.
EZE 9:6 Waueni wazee, vijana wa kiume na wa kike, wamama na watoto, lakini msimguse mtu yeyote mwenye alama. Anzieni katika mahali pangu patakatifu.” Kwa hiyo wakaanza na wale wazee waliokuwa mbele ya Hekalu.
EZE 9:7 Ndipo akawaambia, “Linajisini Hekalu na mkazijaze ua zake maiti za wale waliouawa. Nendeni!” Kwa hiyo wakaenda, wakaanza kuua watu mjini kote.
EZE 9:8 Walipokuwa wakiwaua watu, nami nikaachwa peke yangu, nilisujudu, nikapaza sauti na kusema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi! Je, utaangamiza mabaki yote ya Israeli, katika kumwagwa huku kwa ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?”
EZE 9:9 Mwenyezi Mungu akanijibu, “Dhambi ya nyumba ya Israeli na Yuda imekuwa kubwa mno kupita kiasi, nchi imejaa umwagaji damu na mjini kumejaa udhalimu. Kwani wamesema, ‘Mwenyezi Mungu ameiacha nchi; Mwenyezi Mungu haoni.’
EZE 9:10 Kwa hiyo sitawahurumia wala kuwarehemu, lakini nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyoyatenda.”
EZE 9:11 Ndipo mtu yule aliyevaa nguo ya kitani na mwenye vifaa vya mwandishi kiunoni mwake akarudi na kutoa taarifa, akisema, “Nimefanya kama ulivyoniagiza.”
EZE 10:1 Nikatazama, nikaona juu ya ile nafasi iliyokuwa juu ya vichwa vya wale makerubi kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha utawala cha yakuti samawi.
EZE 10:2 Mwenyezi Mungu akamwambia mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani, “Ingia kati ya yale magurudumu yaliyo chini ya makerubi. Ukaijaze mikono yako makaa ya mawe ya moto kutoka kati ya makerubi na ukayatawanye juu ya mji.” Nilipokuwa nikiangalia, akaingia ndani.
EZE 10:3 Basi wale makerubi walikuwa wamesimama upande wa kusini wa Hekalu wakati yule mtu alipoingia ndani, wingu likaujaza ule ukumbi wa ndani.
EZE 10:4 Kisha utukufu wa Mwenyezi Mungu ukainuka kutoka juu ya wale makerubi, ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Wingu likajaza Hekalu, nao ukumbi ukajawa na mng’ao wa utukufu wa Mwenyezi Mungu.
EZE 10:5 Sauti ya mabawa ya wale makerubi ilisikika hadi ua wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi anapoongea.
EZE 10:6 Mwenyezi Mungu alimwamuru yule mtu aliyevaa nguo ya kitani, akisema, “Chukua moto toka kati ya magurudumu, miongoni mwa makerubi.” Basi yule mtu aliingia ndani, akasimama pembeni mwa gurudumu.
EZE 10:7 Ndipo mmoja wa wale makerubi akanyoosha mkono wake kwenye moto uliokuwa katikati yao, akauchukua moto. Akautia mikononi mwa yule mtu aliyevaa nguo ya kitani, naye alipoupokea, akatoka nje.
EZE 10:8 (Chini ya mabawa ya makerubi palionekana kitu kilichofanana na mikono ya mwanadamu.)
EZE 10:9 Nikatazama, nikaona magurudumu manne kando ya makerubi, moja kando ya kila kerubi. Magurudumu hayo yalimetameta kama zabarajadi.
EZE 10:10 Kule kuonekana kwake, yote manne yalifanana; kila gurudumu lilikuwa kama linazunguka ndani ya lingine.
EZE 10:11 Magurudumu yalipoenda, yalielekea upande mmoja wa pande nne walikoelekea wale makerubi. Makerubi walipoenda, magurudumu hayakuzunguka. Makerubi walienda upande wowote ule kichwa kilielekea, pasipo kugeuka.
EZE 10:12 Miili yao: migongo yao, mikono na mabawa yao, ilikuwa imejaa macho kote, pamoja na yale magurudumu manne.
EZE 10:13 Nikasikia magurudumu yakiitwa “magurudumu ya kisulisuli”.
EZE 10:14 Kila mmoja wa wale makerubi alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa wa kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba, na uso wa nne ulikuwa wa tai.
EZE 10:15 Kisha makerubi wakapaa juu. Hawa ndio wale viumbe walio hai niliowaona kando ya Mto Kebari.
EZE 10:16 Makerubi walipoenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalienda; na makerubi walipotanda mabawa yao wapate kupaa juu kutoka ardhini, magurudumu yale hayakuondoka pembeni mwa makerubi.
EZE 10:17 Makerubi waliposimama, nayo pia yalitulia; nao makerubi walipoinuka juu, magurudumu nayo yaliinuka juu pamoja nao, kwa sababu roho ya wale viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu hayo.
EZE 10:18 Kisha utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaondoka pale kwenye kizingiti cha Hekalu na kusimama juu ya wale makerubi.
EZE 10:19 Nilipokuwa nikitazama, makerubi wakatanda mabawa yao na kuinuka kutoka ardhini, nao walipokuwa wakienda, yale magurudumu yakaenda pamoja nao. Wakasimama kwenye ingilio la lango la mashariki la nyumba ya Mwenyezi Mungu; nao utukufu wa Mungu wa Israeli ukawa juu yao.
EZE 10:20 Hawa walikuwa viumbe hai niliokuwa nimewaona chini ya Mungu wa Israeli kando ya Mto Kebari, nami nikatambua kuwa hao walikuwa makerubi.
EZE 10:21 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne, na chini ya mabawa yao kulikuwa na kile kilichoonekana kama mikono ya mwanadamu.
EZE 10:22 Nyuso zao zilifanana kama zile nilizokuwa nimeziona kando ya Mto Kebari. Kila mmoja alienda mbele moja kwa moja.
EZE 11:1 Ndipo Roho wa Mungu akaniinua na kunileta hadi kwenye lango la nyumba ya Mwenyezi Mungu linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango palikuwa na wanaume ishirini na watano. Nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu.
EZE 11:2 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu.
EZE 11:3 Wao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’
EZE 11:4 Kwa hiyo tabiri dhidi yao; tabiri, ewe mwanadamu.”
EZE 11:5 Kisha Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Hili ndilo ninyi mnalosema, ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu.
EZE 11:6 Mmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti.
EZE 11:7 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Maiti mlizozitupa huko ndizo nyama, na mji huu ndio chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko.
EZE 11:8 Mnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta dhidi yenu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 11:9 Nitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu.
EZE 11:10 Mtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 11:11 Mji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli.
EZE 11:12 Nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.”
EZE 11:13 Basi nilipokuwa nikitoa unabii, Pelatia mwana wa Benaya akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu, nikasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi! Je, utaangamiza kabisa mabaki ya Israeli?”
EZE 11:14 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema:
EZE 11:15 “Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu nawe pamoja na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema kuwahusu, ‘Wako mbali na Mwenyezi Mungu; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’
EZE 11:16 “Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, hata hivyo, kwa kitambo kidogo, nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizoenda.’
EZE 11:17 “Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitawakusanya kutoka mataifa na kuwarudisha kutoka nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’
EZE 11:18 “Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za kuchukiza.
EZE 11:19 Nitawapa moyo usiogawanyika na kuweka roho mpya ndani yao; nitaondoa ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama.
EZE 11:20 Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao.
EZE 11:21 Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za kuchukiza, nitawalipa kikamilifu kulingana na matendo yao,” asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 11:22 Ndipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.
EZE 11:23 Basi utukufu wa Mwenyezi Mungu ukapaa juu kuanzia katika mji na kutua juu ya mlima ulio mashariki mwa mji.
EZE 11:24 Roho akaniinua na kunileta kwa watu wa uhamisho huko Ukaldayo nikiwa katika yale maono niliyopewa na Roho wa Mungu. Ndipo maono niliyokuwa nimeyaona yakanitoka,
EZE 11:25 nami nikawaeleza wale watu wa uhamisho kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amenionesha.
EZE 12:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 12:2 “Mwanadamu, unaishi miongoni mwa watu waasi. Wana macho ya kuona, lakini hawaoni, na masikio ya kusikia lakini hawasikii, kwa kuwa ni watu waasi.
EZE 12:3 “Kwa hiyo, mwanadamu, funga mizigo yako kwa kwenda uhamishoni tena wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toka nje na uende mahali pengine kutoka hapo ulipo. Huenda wataelewa, ingawa wao ni nyumba ya uasi.
EZE 12:4 Wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toa nje mizigo yako iliyofungwa kwa ajili ya kwenda uhamishoni. Kisha wakati wa jioni, wakiwa wanakutazama toka nje kama wale wanaoenda uhamishoni.
EZE 12:5 Wakiwa wanakutazama, toboa ukuta utolee mizigo yako hapo.
EZE 12:6 Beba mizigo hiyo begani mwako wakikuangalia uichukue nje wakati wa giza la jioni. Funika uso wako ili usione nchi, kwa maana nimekufanya ishara kwa nyumba ya Israeli.”
EZE 12:7 Basi nikafanya kama nilivyoamriwa. Wakati wa mchana nilitoa vitu vyangu nje vilivyofungwa tayari kwa uhamishoni. Kisha wakati wa jioni nikatoboa ukuta kwa mikono yangu. Nikachukua mizigo yangu nje wakati wa giza la jioni, nikiwa nimeibeba mabegani mwangu huku wakinitazama.
EZE 12:8 Asubuhi neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 12:9 “Mwanadamu, je, nyumba ile ya uasi ya Israeli haikukuuliza, ‘Unafanya nini?’
EZE 12:10 “Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Unabii huu unamhusu mkuu aliye katika Yerusalemu na watu wote wa nyumba ya Israeli walio huko.’
EZE 12:11 Waambie, ‘Mimi ni ishara kwenu.’ “Kama vile nilivyotenda, basi litatendeka vivyo hivyo kwao. Wataenda uhamishoni kama mateka.
EZE 12:12 “Mkuu aliye miongoni mwao atabeba mizigo yake begani wakati wa giza la jioni na kuondoka, na tundu litatobolewa ukutani ili apite. Atafunika uso wake ili asiweze kuiona nchi.
EZE 12:13 Nitamtandazia wavu wangu, naye atanaswa kwenye mtego wangu; nitamleta hadi Babeli, nchi ya Wakaldayo, lakini hataiona, naye atafia huko.
EZE 12:14 Wote wanaomzunguka nitawatawanya pande zote: watumishi wake na majeshi yake yote; nami nitawafuatilia kwa upanga.
EZE 12:15 “Wao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapowatawanya miongoni mwa mataifa, na kuwatapanya katika nchi zote.
EZE 12:16 Lakini nitawaokoa wachache wao, wasiuawe kwa upanga, njaa na tauni, ili katika mataifa watakakoenda waweze kukiri matendo yao yote ya kuchukiza. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
EZE 12:17 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 12:18 “Mwanadamu, tetemeka unapokula chakula chako, tetemeka kwa hofu unapokunywa maji yako.
EZE 12:19 Waambie watu wa nchi: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kuhusu wakaaji wa Yerusalemu na katika nchi ya Israeli: Watakula chakula chao kwa wasiwasi na kunywa maji yao kwa kufadhaika, kwa kuwa nchi yao itanyang’anywa kila kitu chake kwa sababu ya udhalimu wa wote wanaoishi humo.
EZE 12:20 Miji inayokaliwa na watu itaharibiwa na nchi itakuwa ukiwa. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 12:21 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 12:22 “Mwanadamu, ni ipi hii mithali mlio nayo katika nchi ya Israeli: ‘Siku zinapita na hakuna maono yoyote yanayotimia’?
EZE 12:23 Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaikomesha mithali hii, nao hawataitumia tena katika Israeli.’ Waambie, ‘Siku zimekaribia ambapo kila ono litatimizwa.
EZE 12:24 Kwa maana hapatakuwa tena na maono ya uongo wala ubashiri wa kujipendekeza miongoni mwa watu wa Israeli.
EZE 12:25 Lakini Mimi Mwenyezi Mungu nitasema neno nitakalo, nalo litatimizwa bila kuchelewa. Kwa kuwa katika siku zako, ewe nyumba ya uasi, nitatimiza kila nisemalo, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 12:26 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 12:27 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli inasema, ‘Maono yale anayoyaona ni kwa ajili ya miaka mingi ijayo, naye hutabiri kuhusu siku zijazo zilizo mbali.’
EZE 12:28 “Kwa hiyo, waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakuna maneno yangu yatakayocheleweshwa tena zaidi, lolote nisemalo litatimizwa, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 13:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 13:2 “Mwanadamu, tabiri dhidi ya manabii wa Israeli wanaotabiri sasa. Waambie hao ambao hutabiri kutokana na mawazo yao wenyewe: ‘Sikia neno la Mwenyezi Mungu!
EZE 13:3 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole wao manabii wapumbavu wafuatao roho yao wenyewe na wala hawajaona chochote!
EZE 13:4 Manabii wako, ee Israeli, ni kama mbweha katikati ya magofu.
EZE 13:5 Hamjakwea kwenda kuziba mahali palipobomoka katika ukuta ili kuukarabati kwa ajili ya nyumba ya Israeli, ili isimame imara kwenye vita katika siku ya Mwenyezi Mungu.
EZE 13:6 Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Mwenyezi Mungu amesema”, wakati Mwenyezi Mungu hakuwatuma; bado wakitarajia maneno yao kutimizwa.
EZE 13:7 Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu, hapo msemapo, “Mwenyezi Mungu asema”, wakati Mimi sijasema?
EZE 13:8 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu ya maneno yenu ya uongo na maono yenu ya udanganyifu, Mimi niko kinyume nanyi, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 13:9 Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuorodheshwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli, wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 13:10 “ ‘Kwa sababu wanapotosha watu wangu, wakisema, “Amani”, wakati hakuna amani; pia kwa sababu, wakati ukuta dhaifu unapojengwa, wanaufunika kwa kupaka chokaa,
EZE 13:11 kwa hiyo waambie hao wanaoupaka chokaa isiyokorogwa vyema kwamba ukuta huo utaanguka. Mvua kubwa ya mafuriko itanyesha, nami nitaleta mvua ya mawe inyeshe kwa nguvu, nao upepo wa dhoruba utavuma juu yake.
EZE 13:12 Ukuta utakapoanguka, je, watu hawatawauliza, “Iko wapi chokaa mliyopaka ukuta?”
EZE 13:13 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika ghadhabu yangu nitauachia upepo wa dhoruba, na katika hasira yangu, mvua ya mawe na ya mafuriko itanyesha, ikiwa na ghadhabu ya kuangamiza.
EZE 13:14 Nitaubomoa ukuta mlioupaka chokaa na kuuangusha chini ili msingi wake uwe wazi. Utakapoanguka, mtaangamizwa ndani yake, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 13:15 Hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu dhidi ya huo ukuta na dhidi yao walioupaka chokaa. Nitawaambia ninyi, “Ukuta umebomoka na vivyo hivyo wale walioupaka chokaa,
EZE 13:16 wale manabii wa Israeli walioitabiria Yerusalemu na kuona maono ya amani kwa ajili yake wakati hakukuwa na amani, asema Bwana Mungu Mwenyezi.” ’
EZE 13:17 “Sasa, mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya binti za watu wako wanaotabiri mambo kutoka mawazo yao wenyewe. Tabiri dhidi yao
EZE 13:18 na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole wao wanawake washonao hirizi za uchawi juu ya viwiko vyao vyote na kutengeneza shela za urefu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufunika vichwa vyao kwa makusudi ya kuwanasa watu. Je, mtatega uhai wa watu wangu lakini ninyi mponye wa kwenu?
EZE 13:19 Ninyi mmeninajisi miongoni mwa watu wangu kwa ajili ya konzi chache za shayiri na chembe za mkate. Kwa kuwanenea uongo watu wangu, ambao husikiliza uongo, mmewaua watu ambao hawakustahili kufa, na kuwaacha hai wale ambao walistahili kufa.
EZE 13:20 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Niko kinyume na hizo hirizi zenu za uchawi mnazotumia kuwatega watu kama ndege, nami nitazirarua mikononi mwenu; nitawaweka huru watu mliowatega kama ndege.
EZE 13:21 Nitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu, nao hawatakuwa tena mawindo ya nguvu zenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 13:22 Kwa sababu mliwavunja moyo wenye haki kwa uongo wenu, wakati mimi sikuwaletea huzuni na kwa kuwa mliwatia moyo waovu ili wasiziache njia zao mbaya na hivyo kuokoa maisha yao,
EZE 13:23 kwa hiyo hamtaona tena maono ya uongo wala kufanya ubashiri. Nitawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu. Nanyi ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 14:1 Baadhi ya wazee wa Israeli walinijia na kuketi mbele yangu.
EZE 14:2 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 14:3 “Mwanadamu, watu hawa wameweka sanamu katika mioyo yao na kuweka vitu viovu vya kukwaza mbele ya macho yao. Je, kweli niwaruhusu waniulize jambo lolote?
EZE 14:4 Kwa hiyo sema nao uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mwisraeli yeyote anapoweka sanamu moyoni mwake na kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akaenda kwa nabii, Mimi Mwenyezi Mungu nitamjibu peke yangu sawasawa na ukubwa wa ibada yake ya sanamu.
EZE 14:5 Nitafanya jambo hili ili kukamata tena mioyo ya watu wa Israeli, ambao wote wameniacha kwa ajili ya sanamu zao.’
EZE 14:6 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Tubuni! Acheni sanamu zenu, na matendo yenu yote ya machukizo!
EZE 14:7 “ ‘Mwisraeli au mgeni yeyote anayeishi Israeli anapojitenga nami, na kujiwekea sanamu moyoni mwake, na hivyo kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake, na kisha akamwendea nabii kuuliza shauri kwangu, Mimi Mwenyezi Mungu nitamjibu mwenyewe.
EZE 14:8 Nitamkabili mtu huyo na kumwadhibu, na kumfanya ishara na mithali. Nitamkatilia mbali kutoka kwa watu wangu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 14:9 “ ‘Na ikiwa nabii ameshawishika kutoa unabii, Mimi Mwenyezi Mungu nitakuwa nimemshawishi nabii huyo; nami nitaunyoosha mkono wangu dhidi yake na kumwangamiza kutoka miongoni mwa watu wangu Israeli.
EZE 14:10 Watawajibika kwa hatia yao: nabii atakuwa na hatia sawa na yule mtu aliyekuja kuuliza neno kwake.
EZE 14:11 “ ‘Ndipo watu wa Israeli hawataniacha tena, wala kujitia unajisi tena kwa dhambi zao zote. Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 14:12 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema,
EZE 14:13 “Mwanadamu, nchi ikinitenda dhambi kwa kutokuwa waaminifu nami nikaunyoosha mkono wangu dhidi yake ili kukatilia mbali upatikanaji wake wa chakula na kuipelekea njaa na kuua watu wake na wanyama wao,
EZE 14:14 hata kama watu hawa watatu: Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani ya nchi hiyo, wangeweza kujiokoa hao wenyewe tu kwa uadilifu wao, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 14:15 “Au nikiwaachilia wanyama pori katika nchi hiyo nao wakaiacha bila watoto, nayo ikawa ukiwa hivi kwamba hakuna mtu apitaye kwa sababu ya wanyama pori,
EZE 14:16 hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao peke yao wangeokolewa, lakini nchi ingekuwa ukiwa.
EZE 14:17 “Au nikileta upanga dhidi ya nchi hiyo na kusema, ‘Upanga na upite katika nchi yote,’ nami nikaua watu wa nchi hiyo na wanyama wao,
EZE 14:18 hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao wenyewe tu wangeokolewa.
EZE 14:19 “Au nikipeleka tauni katika nchi hiyo na kumwaga ghadhabu yangu juu yake kupitia kumwaga damu, kuua watu wa nchi hiyo na wanyama wao,
EZE 14:20 hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kumwokoa mwana wala binti. Wao wangeweza kujiokoa wenyewe tu kwa uadilifu wao.
EZE 14:21 “Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Itakuwa vibaya kiasi gani nitakapopeleka dhidi ya Yerusalemu hukumu zangu nne za kutisha, yaani upanga, njaa, wanyama pori na tauni, ili kuua watu wake na wanyama wao!
EZE 14:22 Lakini patakuwa na watakaookoka: wana wa kiume na wa kike watakaoletwa kutoka nchi hiyo. Watakuja kwenu, nanyi mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, mtafarijika kuhusu maafa niliyoleta juu ya Yerusalemu, kwa ajili ya maafa yale yote niliyoleta juu yake.
EZE 14:23 Mtafarijika mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, kwani mtajua kuwa sikufanya lolote ndani yake bila sababu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 15:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 15:2 “Mwanadamu, je, ni vipi mti wa mzabibu unaweza kuwa bora kuliko tawi la mti mwingine wowote ndani ya msitu?
EZE 15:3 Je, mti wake kamwe huchukuliwa na kutengeneza chochote cha manufaa? Je, watu hutengeneza vigingi vya kuning’inizia vitu kutokana na huo mti wake?
EZE 15:4 Nao baada ya kutiwa motoni kama nishati na moto ukateketeza ncha zote mbili na kuunguza sehemu ya kati, je, unafaa kwa lolote?
EZE 15:5 Kama haukufaa kitu chochote ulipokuwa mzima, je, si zaidi sana sasa ambapo hauwezekani kufanyishwa chochote cha kufaa baada ya moto kuuchoma na kuuacha majivu?
EZE 15:6 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kama nilivyoutoa mti wa mzabibu miongoni mwa miti ya msituni kuwa nishati ya moto, hivyo ndivyo nitakavyowatendea watu wanaoishi Yerusalemu.
EZE 15:7 Nitaukaza uso wangu dhidi yao. Ingawa watakuwa wameokoka kwenye moto, bado moto utawateketeza. Nitakapoukaza uso wangu dhidi yao, ninyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 15:8 Nitaifanya nchi kuwa ukiwa kwa sababu wamekuwa si waaminifu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 16:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 16:2 “Mwanadamu, kabili Yerusalemu kuhusu matendo yake ya kuchukiza,
EZE 16:3 useme, ‘Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi, analomwambia Yerusalemu: Asili na kuzaliwa kwako kulikuwa ni katika nchi ya Wakanaani; baba yako alikuwa Mwamori, naye mama yako alikuwa Mhiti.
EZE 16:4 Siku uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuogeshwa kwa maji ili kukufanya safi, wala hukusuguliwa kwa chumvi wala kufunikwa kwa nguo.
EZE 16:5 Hakuna yeyote aliyekuonea huruma au kukusikitikia kiasi cha kukutendea mojawapo ya mambo haya. Badala yake, ulipozaliwa ulitupwa nje penye uwanja, kwa kuwa katika siku uliyozaliwa ulidharauliwa.
EZE 16:6 “ ‘Nami nikapita karibu nawe nikakuona ukigaagaa kwenye damu yako, nawe ulipokuwa umelala hapo penye hiyo damu nikakuambia, “Ishi!”
EZE 16:7 Nilikufanya uote kama mmea wa shambani. Ukakua na kuongezeka sana, ukawa kito cha thamani kuliko vyote. Matiti yako yakatokeza na nywele zako zikaota, wewe uliyekuwa uchi na bila kitu chochote.
EZE 16:8 “ ‘Baadaye nikapita karibu nawe, nilipokutazama na kukuona kuwa umefikia umri wa kupendwa, niliutandaza upindo wa vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikakuapia na kuingia kwenye agano na wewe, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nawe ukawa wangu.
EZE 16:9 “ ‘Nilikuogesha kwa maji, nikakuosha ile damu na kukupaka mafuta.
EZE 16:10 Nikakuvika vazi lililotariziwa na kukuvalisha viatu vya ngozi. Nikakuvika nguo za kitani safi na kukufunika kwa mavazi ya thamani kubwa.
EZE 16:11 Nikakupamba kwa vito: nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni mwako,
EZE 16:12 nikaweka hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na taji nzuri sana kichwani mwako.
EZE 16:13 Kwa hiyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; nguo zako zilikuwa za kitani safi, na hariri, na nguo iliyokuwa imetariziwa. Chakula chako kilikuwa unga laini, asali na mafuta ya zeituni. Ukawa mzuri sana, ukainuka kuwa malkia.
EZE 16:14 Umaarufu wako ulifahamika miongoni mwa mataifa kwa ajili ya uzuri wako, kwani ulikuwa mkamilifu kwa ajili ya utukufu wangu niliokuwa nimeuweka juu yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 16:15 “ ‘Lakini ulitumainia uzuri wako na kutumia umaarufu wako kuwa kahaba. Ulifanya uasherati na kila mtu aliyepita, nao uzuri wako ukawa wake.
EZE 16:16 Ulichukua baadhi ya mavazi yako, ukayatumia kupamba mahali pako pa juu pa kuabudia, ambapo uliendeleza ukahaba wako. Mambo kama hayo hayastahili kutendeka wala kamwe kufanyika.
EZE 16:17 Pia ulichukua vito vizuri nilivyokupa, vito vilivyotengenezwa kwa dhahabu yangu na fedha yangu, ukajitengenezea navyo sanamu za kiume na ukafanya ukahaba nazo.
EZE 16:18 Ukayachukua mavazi yako yaliyotariziwa, na kuyavalisha hizo sanamu, ukatoa mbele ya hizo sanamu mafuta yangu na uvumba wangu.
EZE 16:19 Pia chakula changu nilichokupa ili ule: unga laini, mafuta ya zeituni na asali, ulivitoa mbele yao kuwa uvumba wa harufu nzuri. Hayo ndiyo yaliyotokea, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 16:20 “ ‘Nawe uliwachukua wanao wa kiume na wa kike ulionizalia na kuwatoa kafara kuwa chakula kwa sanamu. Je, ukahaba wako haukukutosha?
EZE 16:21 Uliwachinja watoto wangu na kuwatoa kafara kwa sanamu.
EZE 16:22 Katika matendo yako yote ya machukizo pamoja na ukahaba wako, hukukumbuka siku za ujana wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa bila kitu chochote, ulipokuwa ukigaagaa kwenye damu yako.
EZE 16:23 “ ‘Ole! Ole wako! Asema Bwana Mungu Mwenyezi. Pamoja na maovu yako yote mengine,
EZE 16:24 Ulijijengea jukwaa na kujifanyia mahali pa fahari pa ibada za sanamu kwenye kila uwanja wa mikutano.
EZE 16:25 Katika kila mwanzo wa barabara ulijenga mahali pa fahari pa ibada za sanamu, na kuuaibisha uzuri wako, ukizidi kuutoa mwili wako kwa uzinzi kwa kila apitaye.
EZE 16:26 Ulifanya ukahaba wako na Wamisri, majirani zako waliojaa tamaa, ukaichochea hasira yangu kwa kuongezeka kwa uzinzi wako.
EZE 16:27 Hivyo niliunyoosha mkono wangu dhidi yako na kuipunguza nchi yako; nikakutia kwenye ulafi wa adui zako, binti za Wafilisti, walioshtushwa na tabia yako ya uasherati.
EZE 16:28 Ulifanya ukahaba na Waashuru pia, kwa kuwa hukuridhika, hata baada ya hayo, ukawa bado hukutosheleka.
EZE 16:29 Ndipo uliuzidisha uzinzi wako kwa kujumuisha Ukaldayo, nchi ya wafanyabiashara; lakini hata katika hili hukutosheka.
EZE 16:30 “ ‘Tazama jinsi ulivyo na dhamiri dhaifu, asema Bwana Mungu Mwenyezi, unapofanya mambo haya yote, unatenda kama kahaba asiye aibu!
EZE 16:31 Ulipojenga jukwaa lako katika mwanzo wa kila barabara, na kutengeneza mahali pako pa fahari pa ibada za sanamu katika kila kiwanja cha wazi, hukuwa kama kahaba, kwa sababu ulidharau malipo.
EZE 16:32 “ ‘Wewe mke mzinzi! Unapenda wageni, kuliko mume wako mwenyewe.
EZE 16:33 Kila kahaba hupokea malipo, lakini wewe hutoa zawadi kwa wapenzi wako wote, ukiwahonga ili waje kwako kutoka kila mahali kwa ajili ya ukahaba wako.
EZE 16:34 Kwa hiyo wewe ulikuwa tofauti na wanawake wengine kwenye ukahaba wako. Hakuna aliyekutongoza ili kuzini naye, bali wewe ulikuwa tofauti kabisa, kwani ulilipa wakati hakuna malipo uliyolipwa wewe.
EZE 16:35 “ ‘Kwa hiyo, wewe kahaba, sikia neno la Mwenyezi Mungu!
EZE 16:36 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa umemwaga tamaa zako na kuonesha uchi wako katika uzinzi wako kwa wapenzi wako na kwa sababu ya sanamu zako zote za machukizo na kwa sababu uliwapa damu ya watoto wako,
EZE 16:37 kwa hiyo nitawakusanya wapenzi wako wote, wale uliojifurahisha nao: wale uliowapenda kadhalika na wale uliowachukia. Nitawakusanya wote dhidi yako kutoka pande zote, na nitakuvua nguo mbele yao, nao wataona uchi wako wote.
EZE 16:38 Nitakuhukumia adhabu wanayopewa wanawake wafanyao uasherati na hao wanaomwaga damu; nitaleta juu yako kisasi cha damu cha ghadhabu yangu na hasira yangu yenye wivu.
EZE 16:39 Kisha nitakutia mikononi mwa wapenzi wako, nao watabomoa majukwaa yako na kuharibu mahali pako pa fahari pa ibada za sanamu. Watakuvua nguo zako na kuchukua vito vyako vya thamani na kukuacha uchi na bila kitu.
EZE 16:40 Wataleta kundi la watu dhidi yako, watakaokupiga kwa mawe na kukukatakata vipande vipande kwa panga zao.
EZE 16:41 Watachoma nyumba zako na kutekeleza adhabu juu yako machoni pa wanawake wengi. Nitakomesha ukahaba wako, nawe hutawalipa tena wapenzi wako.
EZE 16:42 Ndipo ghadhabu yangu dhidi yako itapungua, na hasira yangu yenye wivu itakuondokea. Nitatulia, wala sitakasirika tena.
EZE 16:43 “ ‘Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, lakini ulinighadhibisha kwa mambo haya yote, hakika nitaleta juu ya kichwa chako yale uliyotenda, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Je, hukuongeza uasherati juu ya matendo yako mengine ya kuchukiza?
EZE 16:44 “ ‘Kila mtu anayetumia mithali atatumia mithali hii kukuhusu: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.”
EZE 16:45 Wewe ni binti halisi wa mama yako, ambaye alimdharau mume wake na watoto wake; tena wewe ni dada halisi wa dada zako, waliowadharau waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako alikuwa Mwamori.
EZE 16:46 Dada yako mkubwa alikuwa Samaria, aliyeishi upande wako wa kaskazini na binti zake; naye dada yako mdogo, aliyeishi kusini mwako pamoja na binti zake, alikuwa Sodoma.
EZE 16:47 Hukuenda katika njia zao tu na kuiga matendo yao ya kuchukiza, bali baada ya muda mfupi, ulipotoka zaidi yao katika njia zako zote
EZE 16:48 Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, dada yako Sodoma pamoja na binti zake, kamwe hawakufanya yale ambayo wewe na binti zako mmefanya.
EZE 16:49 “ ‘Sasa hii ndiyo ilikuwa dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa wenye kujigamba, walafi na wasiojali; hawakuwasaidia maskini na wahitaji.
EZE 16:50 Walijivuna na kufanya mambo ya kuchukiza sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona.
EZE 16:51 Samaria hakufanya hata nusu ya dhambi ulizofanya. Wewe umefanya mambo mengi sana ya kuchukiza kuwaliko, nawe umewafanya dada zako waonekane kama wenye haki kwa ajili ya mambo haya yote uliyoyafanya.
EZE 16:52 Chukua aibu yako, kwa kuwa umefanya uovu wa dada zako uwe si kitu, nao waonekane kama wenye haki. Kwa kuwa dhambi zako zilikuwa mbaya kuliko zao, wameonekana wenye haki zaidi yako. Kwa hiyo basi, chukua aibu yako, kwa kuwa umewafanya dada zako waonekane wenye haki.
EZE 16:53 “ ‘Lakini nitarudisha baraka za Sodoma na binti zake na za Samaria na binti zake, nami nitarudisha baraka zako pamoja na zao,
EZE 16:54 ili upate kuchukua aibu yako na kufedheheka kwa ajili ya yote uliyotenda ambayo yamekuwa faraja kwao wakijilinganisha na wewe.
EZE 16:55 Nao dada zako, Sodoma na binti zake na Samaria na binti zake, watarudishwa kama vile walivyokuwa mwanzoni, nawe pamoja na binti zako mtarudishwa kama mlivyokuwa hapo awali.
EZE 16:56 Hukuweza hata kumtaja dada yako Sodoma kwa sababu ya dharau yako katika siku za kiburi chako,
EZE 16:57 kabla uovu wako haujafunuliwa. Hata hivyo, sasa unadhihakiwa na binti za Shamu na majirani zake wote, na binti za Wafilisti, wale wote wanaokuzunguka wanakudharau.
EZE 16:58 Utachukua matokeo ya uasherati wako na matendo yako ya kuchukiza, asema Mwenyezi Mungu.
EZE 16:59 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakutendea kama unavyostahili, kwa kuwa umedharau kiapo changu kwa kuvunja agano.
EZE 16:60 Lakini nitakumbuka agano nililolifanya nawe wakati wa ujana wako, nami nitaweka nawe agano imara la milele.
EZE 16:61 Ndipo utakapozikumbuka njia zako na kuona aibu utakapowapokea dada zako, wale walio wakubwa wako na wadogo wako. Nitakupa hao wawe binti zako, lakini si katika msingi wa agano langu na wewe.
EZE 16:62 Hivyo nitalifanya imara agano langu na wewe, nawe utajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 16:63 Basi, nitakapofanya upatanisho kwa ajili yako, kwa yale yote uliyoyatenda, utakumbuka na kuaibika, nawe kamwe hutafumbua tena kinywa chako kwa sababu ya aibu yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 17:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 17:2 “Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli fumbo.
EZE 17:3 Waambie hivi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Tai mkubwa mwenye mabawa yenye nguvu, yaliyojaa manyoya marefu ya rangi mbalimbali, alikuja Lebanoni. Akatua kwenye kilele cha mwerezi,
EZE 17:4 akakwanyua ncha yake na kuichukua hadi nchi ya wafanyabiashara, akaipanda huko katika mji wa wachuuzi.
EZE 17:5 “ ‘Akachukua baadhi ya mbegu za nchi yako na kuziweka katika udongo wenye rutuba. Akazipanda kama mti umeao kando ya maji mengi,
EZE 17:6 nazo zikaota na kuwa mzabibu mfupi, unaoeneza matawi yake. Matawi yake yakamwelekea huyo tai, mizizi yake ikabaki chini ya huo mzabibu. Kwa hiyo ukawa mzabibu na kutoa matawi na vitawi vyenye majani mengi.
EZE 17:7 “ ‘Lakini kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa yenye nguvu yaliyojaa manyoya. Tazama! Huu mzabibu ukatoa mizizi yake kumwelekea huyo tai kutoka mle kwenye shamba lile ulikopandwa, na kutanda matawi yake kumwelekea ili aunyweshe maji.
EZE 17:8 Ulikuwa umepandwa katika udongo mzuri wenye maji mengi ili uweze kutoa matawi, kuzaa matunda, na uweze kuwa mzabibu mzuri sana.’
EZE 17:9 “Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Je, utastawi? Je, hautang’olewa na kuondolewa matunda yake, ili uweze kunyauka? Majani yake mapya yanayochipua yote yatanyauka. Hautahitaji mkono wenye nguvu au watu wengi kuung’oa na mizizi yake.
EZE 17:10 Hata kama utapandwa pengine, je, utastawi? Je, hautanyauka kabisa wakati upepo wa mashariki utakapoupiga, yaani hautanyauka kabisa katika udongo mzuri ambamo ulikuwa umestawi vizuri?’ ”
EZE 17:11 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 17:12 “Waambie nyumba hii ya uasi, ‘Je, mnajua hii ina maana gani?’ Waambie: ‘Mfalme wa Babeli alienda Yerusalemu na kumchukua mfalme wake na watu wake maarufu, akawaleta Babeli.
EZE 17:13 Ndipo akamchukua mmoja wa jamaa ya mfalme na kufanya mapatano naye, akamfanya aape. Akawachukua pia viongozi wa nchi,
EZE 17:14 ili kuudhoofisha ufalme huo, usiweze kuinuka tena, ila uweze kuendelea tu chini ya mapatano yake.
EZE 17:15 Lakini mfalme aliasi dhidi yake kwa kutuma wajumbe wake kwenda Misri ili kupatiwa farasi na jeshi kubwa. Je, atashinda? Je, atafanikiwa? Je, mtu afanyaye mambo kama hayo ataokoka? Je, atavunja mapatano na bado aokoke?
EZE 17:16 “ ‘Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, atafia huko Babeli, katika nchi ya mfalme aliyemketisha kwenye kiti cha utawala, ambaye alidharau kiapo chake na kuvunja mapatano yake.
EZE 17:17 Farao pamoja na jeshi lake kubwa na watu wake wengi hawataweza kusaidia chochote katika vita, watakapozingirwa na jeshi likitaka kuangamiza watu wengi.
EZE 17:18 Alidharau kiapo kwa kulivunja agano. Kwa sababu aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na bado akafanya mambo haya yote, hataokoka.
EZE 17:19 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakika kama niishivyo, nitamwadhibu kwa kudharau kiapo changu, na kulivunja agano langu.
EZE 17:20 Nitautandaza wavu wangu kwa ajili yake, naye atanaswa katika mtego wangu. Nitamleta Babeli na kutekeleza hukumu juu yake huko kwa kuwa hakuwa mwaminifu kwangu.
EZE 17:21 Askari wake wote wanaotoroka wataanguka kwa upanga, nao watakaonusurika watatawanyika katika pande zote za dunia. Ndipo utakapojua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimesema.
EZE 17:22 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi mwenyewe nitachukua chipukizi kutoka kilele cha juu sana cha mwerezi na kukipanda, nitavunja kitawi kichanga kutoka matawi yake ya juu kabisa na kukipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana.
EZE 17:23 Katika vilele vya mlima mrefu wa Israeli nitakipanda, kitatoa matawi na kuzaa matunda na kuwa mwerezi mzuri sana. Ndege wa kila aina watajenga viota vyao ndani yake, nao watapata makazi katika kivuli cha matawi yake.
EZE 17:24 Miti yote ya kondeni itajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ninaishusha miti mirefu na kuikuza miti mifupi kuwa miti mirefu. Mimi naikausha miti mibichi na kuifanya miti mikavu istawi. “ ‘Mimi Mwenyezi Mungu nimesema, nami nitatenda.’ ”
EZE 18:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 18:2 “Je, ninyi watu mna maana gani kutumia mithali hii inayohusu nchi ya Israeli: “ ‘Baba wamekula zabibu chachu, nayo meno ya watoto yametiwa ganzi’?
EZE 18:3 “Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hamtatumia tena mithali hii katika Israeli.
EZE 18:4 Kwa kuwa kila roho ni mali yangu; kama vile ilivyo roho ya baba, vivyo hivyo roho ya mtoto ni mali yangu. Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.
EZE 18:5 “Mtu aweza kuwa ni mwenye haki atendaye yaliyo haki na sawa.
EZE 18:6 Hakula katika mahali pa ibada za sanamu kwenye milima, wala hakuziinulia macho sanamu za nyumba ya Israeli. Hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakukutana kimwili na mwanamke wakati wa siku zake za hedhi.
EZE 18:7 Hamdhulumu yeyote, bali hurudisha kilichowekwa rehani kwake. Hanyang’anyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi.
EZE 18:8 Hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huuzuia mkono wake usifanye mabaya, naye huhukumu kwa haki kati ya mtu na mtu.
EZE 18:9 Huzifuata amri zangu na kuzishika sheria zangu kwa uaminifu. Huyo mtu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 18:10 “Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya
EZE 18:11 (ingawa baba yake hakufanya mojawapo ya haya): “Hula katika mahali pa ibada za sanamu kwenye milima. Humtia unajisi mke wa jirani yake.
EZE 18:12 Huwadhulumu maskini na wahitaji. Hunyang’anyana. Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake. Huziinulia sanamu macho. Hufanya mambo ya machukizo.
EZE 18:13 Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada. Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
EZE 18:14 “Lakini yawezekana mwana huyo ana mwana aonaye dhambi hizi zote anazofanya baba yake, naye ingawa anaziona, yeye hafanyi mabaya kama haya:
EZE 18:15 “Hakula katika mahali pa ibada za sanamu kwenye milima, wala hainulii macho sanamu za nyumba ya Israeli. Hakumtia unajisi mke wa jirani yake.
EZE 18:16 Hamdhulumu yeyote wala kutaka rehani kwa ajili ya mkopo. Hanyang’anyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi.
EZE 18:17 Huuzuia mkono wake usitende dhambi, hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huzishika amri zangu na kuzifuata sheria zangu. Hatakufa kwa ajili ya dhambi za baba yake; hakika ataishi.
EZE 18:18 Lakini baba yake atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe, kwa sababu alikuwa mnyang’anyi, akampokonya ndugu yake na kufanya yaliyo mabaya miongoni mwa watu wake.
EZE 18:19 “Lakini mnauliza, ‘Kwa nini mwana asiadhibiwe kwa uovu wa baba yake?’ Kwa vile mwana ametenda yaliyo haki na sawa na amekuwa mwangalifu kuzishika amri zangu zote, hakika ataishi.
EZE 18:20 Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa. Mwana hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya baba yake, wala baba hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya mwanawe. Haki ya mtu mwenye haki itahesabiwa juu yake na uovu wa mtu mwovu utalipizwa juu yake.
EZE 18:21 “Lakini mtu mwovu akiacha dhambi zake zote alizozitenda na kushika amri zangu zote na kufanya lililo haki na sawa, hakika ataishi, hatakufa.
EZE 18:22 Hakuna kosa lolote alilotenda litakalokumbukwa juu yake. Kwa ajili ya mambo ya haki aliyoyatenda, ataishi.
EZE 18:23 Je, mimi ninafurahia kifo cha mtu mwovu? Asema Bwana Mungu Mwenyezi. Je, si mimi ninafurahi wanapogeuka kutoka njia zao mbaya na kuishi?
EZE 18:24 “Lakini kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi na kufanya mambo ya machukizo ambayo mtu mwovu hufanya, Je, ataishi? Hakuna hata mojawapo ya matendo ya haki aliyotenda litakalokumbukwa. Kwa sababu ya kukosa uaminifu kwake anayo hatia na kwa sababu ya dhambi alizozitenda, atakufa.
EZE 18:25 “Lakini mnasema, ‘Njia ya Bwana si ya haki.’ Sikia, ee nyumba ya Israeli: Je, njia yangu siyo ya haki? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki?
EZE 18:26 Kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, kwa sababu ya dhambi alizotenda, atakufa.
EZE 18:27 Lakini mtu mwovu akigeuka kutoka maovu aliyoyatenda na kufanya yaliyo haki na sawa, ataokoa maisha yake.
EZE 18:28 Kwa kuwa anayafikiria na kugeuka kutoka makosa yake yote aliyoyatenda na kuyaacha, hakika ataishi, hatakufa.
EZE 18:29 Lakini nyumba ya Israeli inasema, ‘Njia za Bwana si haki.’ Je, njia zangu si za haki, ee nyumba ya Israeli? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki?
EZE 18:30 “Kwa hiyo, ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu, kila mmoja sawasawa na njia zake, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Tubuni! Geukeni kutoka makosa yenu yote, ndipo dhambi haitakuwa anguko lenu.
EZE 18:31 Tupilieni mbali makosa yenu yote mliyoyatenda, nanyi mpate moyo mpya na roho mpya. Kwa nini mfe, ee nyumba ya Israeli?
EZE 18:32 Kwa maana sifurahii kifo cha mtu yeyote, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Tubuni basi, mkaishi!
EZE 19:1 “Wewe fanya maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli
EZE 19:2 na useme: “ ‘Tazama jinsi gani mama yako alivyokuwa simba jike miongoni mwa simba! Alilala katikati ya wana simba na kulisha watoto wake.
EZE 19:3 Alimlea mmoja wa watoto wake, naye akawa simba mwenye nguvu. Akajifunza kurarua mawindo naye akala watu.
EZE 19:4 Mataifa wakasikia habari zake, naye akanaswa katika shimo lao. Wakamwongoza kwa ndoana hadi nchi ya Misri.
EZE 19:5 “ ‘Mama yake alipongoja na kuona tumaini lake halitimiziki, nayo matarajio yake yametoweka, akamchukua mwanawe mwingine na kumfanya simba mwenye nguvu.
EZE 19:6 Alizungukazunguka miongoni mwa simba, kwa kuwa sasa alikuwa simba mwenye nguvu. Akajifunza kurarua mawindo naye akala watu.
EZE 19:7 Akabomoa ngome zao na kuiharibu miji yao. Nchi na wote waliokuwa ndani yake wakatiwa hofu kwa kunguruma kwake.
EZE 19:8 Kisha mataifa wakaja dhidi yake kutoka sehemu zilizomzunguka. Wakatanda nyavu zao kwa ajili yake, naye akanaswa katika shimo lao.
EZE 19:9 Wakamvutia kwenye tundu kwa kutumia ndoana, wakamleta kwa mfalme wa Babeli. Wakamfunga gerezani, hivyo kunguruma kwake hakukusikika tena katika milima ya Israeli.
EZE 19:10 “ ‘Mama yako alikuwa kama mzabibu katika shamba lako la mizabibu uliopandwa kando ya maji, ukiwa unazaa sana na wenye matawi mengi kwa sababu ya wingi wa maji.
EZE 19:11 Matawi yake yalikuwa na nguvu, yaliyofaa kuwa fimbo ya mtawala. Ulikuwa mrefu kupita miti mingine katikati ya matawi manene; ulionekana kwa urahisi kwa ajili ya urefu wake na wingi wa matawi yake.
EZE 19:12 Lakini uling’olewa kwa hasira kali na kutupwa chini. Upepo wa mashariki uliufanya usinyae, matunda yake yakapukutika, matawi yake yenye nguvu yakanyauka na moto ukayateketeza.
EZE 19:13 Sasa umepandwa jangwani katika nchi kame na ya kiu.
EZE 19:14 Moto ulienea kuanzia mojawapo ya matawi yake makubwa na kuteketeza matunda yake. Hakuna tawi lenye nguvu lililobaki juu yake linalofaa kuwa fimbo ya mtawala.’ Hili ndilo ombolezo, na litumike kama ombolezo.”
EZE 20:1 Katika mwaka wa saba, mwezi wa tano siku ya kumi, baadhi ya wazee wa Israeli wakaja ili kutaka ushauri kwa Mwenyezi Mungu, wakaketi mbele yangu.
EZE 20:2 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 20:3 “Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa nini mmekuja? Je, ni kutaka ushauri kwangu? Hakika kama niishivyo, sitawaruhusu mtake ushauri toka kwangu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’
EZE 20:4 “Je, utawahukumu? Je, mwanadamu, utawahukumu? Basi uwakabili kwa ajili ya machukizo ya baba zao
EZE 20:5 na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Siku ile nilipochagua Israeli, niliwaapia wazao wa nyumba ya Yakobo kwa mkono ulioinuliwa nami nikajidhihirisha kwao huko Misri. Kwa mkono ulioinuliwa niliwaambia, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
EZE 20:6 Siku ile niliwaapia kwamba nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwaleta katika nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi nzuri kupita zote.
EZE 20:7 Nami nikawaambia, “Kila mmoja wenu aondolee mbali sanamu za chukizo ambazo mmekazia macho, nanyi msijitie unajisi kwa sanamu za Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
EZE 20:8 “ ‘Lakini waliniasi na hawakunisikiliza, hawakuondolea mbali sanamu za machukizo ambazo walikuwa wamezikazia macho, wala kuondolea mbali sanamu za Misri. Ndipo nikasema, nitawamwagia ghadhabu yangu na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko Misri.
EZE 20:9 Lakini kwa ajili ya Jina langu niliwatoa katika nchi ya Misri. Nilifanya hivyo ili kulinda Jina langu lisinajisiwe machoni mwa mataifa walioishi miongoni mwao, na ambao machoni pao nilikuwa nimejifunua kwa Waisraeli.
EZE 20:10 Kwa hiyo nikawaongoza watoke Misri na kuwaleta jangwani.
EZE 20:11 Nikawapa amri zangu na kuwajulisha sheria zangu, kwa kuwa mtu anayezitii ataishi kwa hizo.
EZE 20:12 Pia niliwapa Sabato zangu kama ishara kati yangu nao, ili wapate kujua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu niliwafanya watakatifu.
EZE 20:13 “ ‘Lakini watu wa Israeli waliniasi Mimi jangwani. Hawakufuata amri zangu, bali walikataa sheria zangu, ingawa mtu yule anayezitii ataishi kwa hizo sheria, nao walizinajisi Sabato zangu kabisa. Hivyo nilisema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwaangamiza huko jangwani.
EZE 20:14 Lakini kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kitalifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli.
EZE 20:15 Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba nisingewaingiza katika nchi niliyowapa, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi nzuri kuliko zote,
EZE 20:16 kwa sababu walikataa sheria zangu na hawakufuata amri zangu, na wakazinajisi Sabato zangu. Kwa kuwa mioyo yao iliandama sanamu zao.
EZE 20:17 Lakini niliwahurumia, wala sikuwaangamiza wala kuwafuta kabisa jangwani.
EZE 20:18 Niliwaambia watoto wao kule jangwani, “Msifuate amri za baba zenu wala kushika sheria zao au kujinajisi kwa sanamu zao.
EZE 20:19 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; fuateni amri zangu, tena kuweni waangalifu kushika sheria zangu.
EZE 20:20 Zitakaseni Sabato zangu ili ziwe ishara kati yangu nanyi. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
EZE 20:21 “ ‘Lakini watoto hao wakaniasi: Hawakufuata amri zangu, wala hawakuwa waangalifu kushika sheria zangu, ingawa mtu anayezitii anaishi kwa hizo sheria, nao wakazinajisi Sabato zangu. Hivyo nikasema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko jangwani.
EZE 20:22 Lakini nikauzuia mkono wangu, na kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile kingezuia Jina langu kunajisiwa machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli.
EZE 20:23 Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba ningewatawanya miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali,
EZE 20:24 kwa sababu hawakutii sheria zangu lakini walikuwa wamekataa amri zangu na kuzinajisi Sabato zangu, nayo macho yao yakatamani sanamu za baba zao.
EZE 20:25 Pia niliwaacha wafuate amri ambazo hazikuwa nzuri na sheria ambazo mtu hawezi kuishi kwa hizo sheria.
EZE 20:26 Nikawaacha wanajisiwe kwa matoleo yao ya kuwatoa kafara wazaliwa wao wa kwanza kwa sanamu, ili nipate kuwajaza na hofu hadi wajue kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’
EZE 20:27 “Kwa hiyo, mwanadamu, sema na watu wa Israeli na uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika jambo hili pia, baba zenu walinikufuru kwa kuniacha mimi:
EZE 20:28 Nilipowaleta katika nchi niliyokuwa nimeapa kuwapa na kuona kilima chochote kirefu au mti wowote wenye majani mengi, huko walitoa dhabihu zao, wakatoa sadaka ambazo zilichochea hasira yangu, wakafukiza uvumba wenye harufu nzuri na kumimina sadaka zao za kinywaji.
EZE 20:29 Ndipo nikawaambia: Ni nini maana yake hapa mahali pa juu pa kuabudia mnapopaendea?’ ” (Basi mahali pale panaitwa Bama hata leo.)
EZE 20:30 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Je, mtajinajisi kama vile baba zenu walivyofanya na kutamani vinyago vyao vya machukizo?
EZE 20:31 Mnapotoa matoleo yenu, yaani kutoa kafara watoto wenu motoni, mnaendelea kujinajisi na sanamu zenu zote hadi leo. Je, niulizwe ushauri na ninyi, ee nyumba ya Israeli? Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, mimi sitaulizwa ushauri na ninyi.
EZE 20:32 “ ‘Lile lililoko mioyoni mwenu kamwe halitatokea, mnaposema, “Tunataka tuwe kama mataifa mengine, kama watu wengine wa dunia, wanaotumikia miti na mawe.”
EZE 20:33 Hakika kama niishivyo asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitawatawala kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyooshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika.
EZE 20:34 Nitawatoa toka katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa, kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa.
EZE 20:35 Nitawaleta katika jangwa la mataifa na huko nitatekeleza hukumu juu yenu uso kwa uso.
EZE 20:36 Kama nilivyowahukumu baba zenu katika jangwa la nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu ninyi, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 20:37 Nitawafanya mpite chini ya fimbo yangu, nami nitawaleta katika mkataba wa agano.
EZE 20:38 Nitawaondoa miongoni mwenu wale wanaohalifu na wale wanaoasi dhidi yangu. Ingawa nitawatoa katika nchi wanazoishi, hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 20:39 “ ‘Kwenu ninyi, ee nyumba ya Israeli, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nendeni mkatumikie sanamu zenu, kila mmoja wenu! Lakini baadaye hakika mtanisikiliza mimi nanyi hamtalinajisi tena Jina langu takatifu, kwa matoleo yenu na sanamu zenu.
EZE 20:40 Kwa kuwa katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hapo katika nchi nyumba yote ya Israeli itanitumikia mimi, nami huko nitawakubali. Huko nitataka sadaka zenu na matoleo ya malimbuko yenu, pamoja na dhabihu zenu takatifu zote.
EZE 20:41 Nitawakubali ninyi kama uvumba wenye harufu nzuri wakati nitakapowatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlipokuwa mmetawanyika, nami nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwenu na machoni mwa mataifa.
EZE 20:42 Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapowaleta katika nchi ya Israeli, nchi niliyokuwa nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu.
EZE 20:43 Hapo ndipo nitakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu yote ambayo kwayo mlijitia unajisi, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya maovu yote mliyokuwa mmetenda.
EZE 20:44 Nanyi mtajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapowatendea kwa ajili ya Jina langu, wala si sawasawa na njia zenu mbaya na matendo yenu maovu, ee nyumba ya Israeli, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 20:45 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 20:46 “Mwanadamu, uelekeze uso wako upande wa kusini, hubiri dhidi ya upande wa kusini, na utoe unabii dhidi ya msitu wa Negebu.
EZE 20:47 Waambie watu wa Negebu: ‘Sikieni neno la Mwenyezi Mungu. Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninakaribia kukuwasha moto, nao utateketeza miti yako yote, mibichi na iliyokauka. Miali ya moto haitaweza kuzimwa na kila uso kutoka kusini mpaka kaskazini utakaushwa kwa moto huo.
EZE 20:48 Kila mmoja ataona kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ndiye niliyeuwasha huo moto; nao hautazimwa.’ ”
EZE 20:49 Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mungu Mwenyezi! Wao hunisema, ‘Huyu si huzungumza mafumbo tu?’ ”
EZE 21:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 21:2 “Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli
EZE 21:3 uiambie: ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu.
EZE 21:4 Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utatolewa alani mwake uwe dhidi ya kila mtu kuanzia kusini hadi kaskazini.
EZE 21:5 Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’
EZE 21:6 “Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi.
EZE 21:7 Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatendeka, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 21:8 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema:
EZE 21:9 “Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: “ ‘Upanga, upanga, ulionolewa na kusuguliwa:
EZE 21:10 umenolewa kwa ajili ya mauaji, umesuguliwa ili ung’ae kama miali ya radi! “ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unadharau kila fimbo kama hiyo.
EZE 21:11 “ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa, ili upate kushikwa mkononi, umenolewa na kusuguliwa, umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji.
EZE 21:12 Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu, kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu; u dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wametolewa wauawe kwa upanga pamoja na watu wangu. Kwa hiyo pigapiga kifua chako.
EZE 21:13 “ ‘Lazima kuwe na kujaribiwa. Itakuwaje basi ikiwa fimbo ya ufalme ya Yuda inayodharauliwa na upanga haitakuwepo tena? asema Bwana Mungu Mwenyezi.’
EZE 21:14 “Hivyo basi, mwanadamu, tabiri na ukapige makofi. Upanga wako na upige mara mbili, naam, hata mara tatu. Ni upanga wa mauaji, upanga wa mauaji makuu, ukiwashambulia kutoka kila upande.
EZE 21:15 Ili mioyo ipate kuyeyuka na wanaouawa wawe wengi, nimeweka upanga wa mauaji kwenye malango yao yote. Lo! Umetengenezwa umetemete kama miali ya radi, umeshikwa kwa ajili ya kuua.
EZE 21:16 Ee upanga, kata upande wa kuume, kisha upande wa kushoto, mahali popote makali yako yatakapoelekezwa.
EZE 21:17 Mimi nami nitapiga makofi, nayo ghadhabu yangu itapungua. Mimi Mwenyezi Mungu nimesema.”
EZE 21:18 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 21:19 “Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini.
EZE 21:20 Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome.
EZE 21:21 Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama.
EZE 21:22 Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka magogo ya kubomoa, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka magogo ya kubomoa dhidi ya malango, kupandisha kilima hadi kuta zako, na kujenga husuru dhidi yako.
EZE 21:23 Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha kuhusu uovu wao na kuwachukua mateka.
EZE 21:24 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa sababu ninyi mmefanya uovu wenu ukumbukwe kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mnayoyafanya: kwa kuwa mmefanya hivi, mtachukuliwa mateka.
EZE 21:25 “ ‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yake imewadia, ambaye wakati wake wa adhabu umefikia kilele chake;
EZE 21:26 hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa vile yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa, na aliyekwezwa atashushwa.
EZE 21:27 Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya hadi aje yule aliye mwenye taji kwa haki; huyo ndiye nitakayempa.’
EZE 21:28 “Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kuhusu Waamoni na matukano yao: “ ‘Upanga, upanga, umefutwa kwa ajili ya kuua, umesuguliwa ili kuangamiza na unametameta kama miali ya radi!
EZE 21:29 Wakati wanatoa maono ya uongo juu yako, na wanapobashiri uongo juu yako, upanga utawekwa kwenye shingo za wapotovu watakaouawa, wale siku yao imewadia, wakati wa adhabu yao ya mwisho.
EZE 21:30 “ ‘Urudishe upanga kwenye ala yake! Katika mahali ulipoumbiwa, katika nchi ya baba zako, huko nitakuhukumu.
EZE 21:31 Nitamwaga ghadhabu yangu juu yako na kupuliza moto wa hasira yangu dhidi yako; nitakutia mikononi mwa watu wakatili, watu stadi katika kuangamiza.
EZE 21:32 Mtakuwa kuni za kuwashia moto, damu yenu itamwagwa katika nchi yenu, wala hamtakumbukwa tena; kwa maana Mimi Mwenyezi Mungu nimesema.’ ”
EZE 22:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 22:2 “Mwanadamu, je, wewe utauhukumu? Je, utauhukumu huu mji unaomwaga damu? Basi uujulishe kuhusu matendo yake yote ya machukizo
EZE 22:3 uuambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ee mji unaojiletea maangamizi wenyewe kwa kumwaga damu ndani yake na kujinajisi wenyewe kwa kutengeneza sanamu,
EZE 22:4 umekuwa na hatia kwa sababu ya damu uliyomwaga, na umetiwa unajisi kwa sanamu ulizotengeneza. Umejiletea mwisho wa siku zako na mwisho wa miaka yako umewadia. Kwa hiyo nitakufanya kitu cha kudharauliwa kwa mataifa na kitu cha mzaha kwa nchi zote.
EZE 22:5 Wale walio karibu na wale walio mbali watakudhihaki, ewe mji wenye sifa mbaya, uliyejaa ghasia.
EZE 22:6 “ ‘Tazama jinsi kila mkuu wa Israeli aliye ndani yako anavyotumia nguvu zake kumwaga damu.
EZE 22:7 Ndani yako wamewadharau baba na mama; ndani yako wamewatendea wageni udhalimu, na kuwadhulumu yatima na wajane.
EZE 22:8 Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu.
EZE 22:9 Ndani yako wako watu wasingiziaji, watu walio tayari kumwaga damu, ndani yako wako wale wanaokula vyakula vilivyotolewa mahali pa ibada za sanamu kwenye milima, na kutenda matendo ya uasherati.
EZE 22:10 Ndani yako wako wale wanaovunjia heshima vitanda vya baba zao, ndani yako wamo wale wanaowatendea wanawake jeuri wakiwa katika hedhi, wakati wakiwa najisi.
EZE 22:11 Ndani yako mtu hufanya mambo ya machukizo na mke wa jirani yake, mwingine kwa aibu kubwa hukutana kimwili na mke wa mwanawe, mwingine humtenda jeuri dada yake, binti ya baba yake hasa.
EZE 22:12 Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa majirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 22:13 “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako.
EZE 22:14 Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokuadhibu? Mimi Mwenyezi Mungu nimesema na nitalifanya.
EZE 22:15 Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako.
EZE 22:16 Baada ya kunajisika mbele ya mataifa, utajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 22:17 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 22:18 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa takataka ya chuma kwangu; wote wamekuwa shaba, bati, chuma na risasi iliyoachwa kalibuni. Wao ni taka ya madini ya fedha tu.
EZE 22:19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa kuwa wote mmekuwa takataka ya chuma, nitawakusanya Yerusalemu.
EZE 22:20 Kama vile watu wakusanyavyo fedha, shaba, chuma, risasi na bati kalibuni ili kuyeyusha kwa moto mkali, ndivyo nitakavyowakusanya katika hasira yangu na ghadhabu yangu kuwaweka ndani ya mji na kuwayeyusha.
EZE 22:21 Nitawakusanya na kupuliza juu yenu moto wa hasira yangu na ghadhabu yangu nanyi mtayeyushwa ndani ya huo mji.
EZE 22:22 Kama fedha iyeyukavyo kalibuni, ndivyo mtakavyoyeyuka ndani ya huo mji, nanyi mtajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.’ ”
EZE 22:23 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia tena kusema:
EZE 22:24 “Mwanadamu, iambie nchi, ‘Wewe ni nchi ambayo haijatakaswa wala kunyeshewa katika siku ya ghadhabu.’
EZE 22:25 Kuna hila mbaya ya wakuu ndani yake kama simba angurumaye akirarua mawindo yake, wanakula watu, wanachukua hazina na vitu vya thamani na kuongeza idadi ya wajane ndani yake.
EZE 22:26 Makuhani wake wameihalifu sheria yangu na kunajisi vitu vyangu vitakatifu, hawatofautishi kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida. Wanafundisha kuwa hakuna tofauti kati ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi, nao wanafumba macho yao katika kutunza Sabato zangu, hivyo katikati yao nimetiwa unajisi.
EZE 22:27 Maafisa wake walio ndani yake ni kama mbwa-mwitu wararuao mawindo yao, wanamwaga damu na kuua watu ili kupata faida ya udhalimu.
EZE 22:28 Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi,’ wakati Mwenyezi Mungu hajasema.
EZE 22:29 Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyang’anyi, wanawadhulumu maskini na wahitaji, na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki.
EZE 22:30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, ambaye angejenga ukuta na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka kwa ajili ya watu wa nchi ili nisije nikaiangamiza, lakini sikumwona mtu yeyote.
EZE 22:31 Hivyo nitaimwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwateketeza kwa moto wa hasira yangu, nikiyaleta juu ya vichwa vyao yale yote waliyotenda, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 23:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 23:2 “Mwanadamu, palikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja.
EZE 23:3 Wakawa makahaba huko Misri, wakajitia kwenye ukahaba tangu ujana wao. Katika nchi ile vifua vyao vya ubikira vikakumbatiwa, na wakapoteza ubikira wao.
EZE 23:4 Mkubwa aliitwa Ohola, na mdogo wake Oholiba. Walikuwa wangu nao wakazaa watoto wa kiume na wa kike. Ohola ni Samaria, Oholiba ni Yerusalemu.
EZE 23:5 “Ohola akajitia kwenye ukahaba alipokuwa bado ni wangu, akatamani sana wapenzi wake, mashujaa Waashuru,
EZE 23:6 waliovaa nguo za buluu, watawala na majemadari, wote walikuwa wanaume vijana wa kuvutia, wapandao farasi.
EZE 23:7 Akafanya ukahaba na wakuu wote wa Ashuru, na kujinajisi kwa sanamu zote za kila mwanaume aliyemtamani.
EZE 23:8 Hakuacha ukahaba wake aliouanza huko Misri, wakati wa ujana wake ambapo wanaume walilala naye, wakikumbatia kifua cha ubikira wake na kumwaga tamaa zao juu yake.
EZE 23:9 “Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa wapenzi wake, Waashuru, kwa kuwa ndio aliowatamani.
EZE 23:10 Wakamvua nguo zake wakamwacha uchi, wakawachukua wanawe wa kiume na wa kike, naye wakamuua kwa upanga. Akawa kitu cha kudharauliwa miongoni mwa wanawake, na adhabu ikatolewa dhidi yake.
EZE 23:11 “Oholiba dada yake aliliona jambo hili, lakini kwa tamaa zake na ukahaba wake, akaharibu tabia zake kuliko Ohola, dada yake.
EZE 23:12 Yeye naye aliwatamani Waashuru, watawala na majemadari, mashujaa waliovalia sare, wapandao farasi, wanaume vijana wote waliovutia.
EZE 23:13 Nikaona kuwa yeye pia alijinajisi, wote wawili wakaelekea njia moja.
EZE 23:14 “Lakini yeye akazidisha ukahaba wake. Akaona wanaume waliochorwa ukutani, picha za Wakaldayo waliovalia nguo nyekundu,
EZE 23:15 wakiwa na mikanda viunoni mwao na vilemba vichwani mwao, wote walifanana na maafisa wa Babeli wapandao magari ya vita, wenyeji wa Ukaldayo.
EZE 23:16 Mara tu alipowaona, aliwatamani, akatuma wajumbe kwao huko Ukaldayo.
EZE 23:17 Ndipo hao Wababeli wakaja kwake kwenye kitanda cha mapenzi, nao katika tamaa zao wakamtia unajisi. Baada ya kutiwa unajisi, akawaacha kwa kuwachukia.
EZE 23:18 Alipofanya ukahaba wake waziwazi na kuonesha uchi wake, nilimwacha kwa kumchukia, kama vile nilivyokuwa nimemwacha dada yake.
EZE 23:19 Lakini akazidisha ukahaba wake alipozikumbuka siku za ujana wake, alipokuwa kahaba huko Misri.
EZE 23:20 Huko aliwatamani wapenzi wake, ambao viungo vyao vya uzazi ni kama vya punda, na kile kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi.
EZE 23:21 Hivyo ulitamani uasherati wa ujana wako wakati ulipokuwa Misri, kifua chako kilipokumbatiwa, na matiti yako machanga yakapapaswa.
EZE 23:22 “Kwa hiyo, Oholiba, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitawachochea wapenzi wako wawe kinyume na wewe, wale uliowaacha kwa kuchukia, nitawaleta dhidi yako kutoka kila upande:
EZE 23:23 Wababeli na Wakaldayo wote, watu kutoka Pekodi, na Shoa na Koa, wakiwa pamoja na Waashuru wote, vijana wazuri, wote wakiwa watawala na majemadari, maafisa wa magari ya vita na watu wa vyeo vya juu, wote wakiwa wamepanda farasi.
EZE 23:24 Watakuja dhidi yako wakiwa na silaha, magari ya vita, magari ya kukokota, pamoja na umati mkubwa wa watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao na vigao na kwa chapeo. Nitakutia mikononi mwao ili wakuadhibu, nao watakuadhibu sawasawa na sheria zao.
EZE 23:25 Nitaelekeza hasira yangu yenye wivu dhidi yako, nao watakuadhibu kwa hasira kali. Watakatilia mbali pua yako na masikio yako, na wale watakaosalia miongoni mwako watauawa kwa upanga. Watachukua wana wako wa kiume na wa kike, na wale watakaosalia miongoni mwenu watateketezwa kwa moto.
EZE 23:26 Watakuvua nguo zako pia, na kuchukua mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito na dhahabu.
EZE 23:27 Hivyo ndivyo nitakavyokomesha uasherati wako na ukahaba wako uliouanza huko Misri. Hutatazama vitu hivi kwa kuvitamani wala kukumbuka Misri tena.
EZE 23:28 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninakaribia kukutia mikononi mwa wale unaowachukia, kwa wale uliojitenga nao kwa kuwachukia.
EZE 23:29 Watakutenda mambo ya chuki na kukunyang’anya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako
EZE 23:30 umekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao.
EZE 23:31 Umeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako.
EZE 23:32 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Utakinywea kikombe cha dada yako, kikombe kikubwa na chenye kina kirefu; kitakuletea dharau na dhihaka, kwa kuwa kimejaa sana.
EZE 23:33 Utalewa ulevi na kujawa huzuni, kikombe cha maangamizi na ukiwa, kikombe cha dada yako Samaria.
EZE 23:34 Utakinywa chote na kukimaliza; utakivunja vipande vipande na kuyararua matiti yako. Nimenena haya, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 23:35 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa ulinisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”
EZE 23:36 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwanadamu, je, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi wakabili kwa ajili ya matendo yao ya machukizo,
EZE 23:37 kwa kuwa wamefanya uzinzi na damu imo mikononi mwao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, hata watoto walionizalia wamewatoa kafara, kuwa chakula kwa sanamu hizo.
EZE 23:38 Pia wamenifanyia hili: wakati huo huo wamenajisi patakatifu pangu na kuzitangua Sabato zangu.
EZE 23:39 Siku ile ile walitoa kafara watoto wao kwa sanamu zao, waliingia patakatifu pangu na kupanajisi. Hilo ndilo walilolifanya katika nyumba yangu.
EZE 23:40 “Hata waliwatuma wajumbe kuwaita watu kutoka mbali, nao walipowasili ulioga kwa ajili yao, ukapaka macho yako wanja, na ukavaa mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito vya dhahabu.
EZE 23:41 Ukaketi kwenye kiti cha anasa, kukiwa na meza iliyoandaliwa mbele yake ambayo juu yake ulikuwa umeweka uvumba na mafuta ambayo yalikuwa yangu.
EZE 23:42 “Kelele za umati wa watu wasiojali zilikuwa zimemzunguka, wakaleta watu wengi waliokuwa wakifanya makelele na walevi kutoka nyikani, ambao walitia bangili kwenye mikono ya yule mwanamke na dada yake na pia taji nzuri za kupendeza kwenye vichwa vyao.
EZE 23:43 Ndipo nikasema kuhusu yule aliyechakazwa na uzinzi, ‘Basi wamtumie kama kahaba, kwa kuwa ndivyo alivyo.’
EZE 23:44 Nao wakazini naye. Kama vile watu wazinivyo na kahaba, ndiyo hivyo walivyozini na hao wanawake waasherati, Ohola na Oholiba.
EZE 23:45 Lakini watu wenye haki, watawahukumia adhabu wanawake wafanyao uzinzi na kumwaga damu, kwa kuwa ni wazinzi na damu iko mikononi mwao.
EZE 23:46 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Leteni watu wengi wenye makelele dhidi yao na uwaache wapate hofu na watekwe nyara.
EZE 23:47 Hao watu wengi watawapiga kwa mawe na kuwaua kwa panga zao, watawaua wana wao wa kiume na wa kike, na kuzichoma nyumba zao.
EZE 23:48 “Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi, ili wanawake wote wapate onyo nao wasije wakafanya uasherati kama ninyi mlivyofanya.
EZE 23:49 Utapata adhabu kwa ajili ya uasherati wako na kuchukua matokeo ya dhambi zako za uasherati. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 24:1 Katika mwaka wa tisa, mwezi wa kumi, siku ya kumi, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 24:2 “Mwanadamu, weka kumbukumbu ya tarehe hii, tarehe hii hasa, kwa kuwa mfalme wa Babeli ameuzingira mji wa Yerusalemu kwa jeshi siku hii ya leo.
EZE 24:3 Nenea nyumba hii ya uasi kwa fumbo, uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Teleka sufuria jikoni; iteleke na umimine maji ndani yake,
EZE 24:4 Weka vipande vya nyama ndani yake, vipande vyote vizuri, vya paja na vya bega. Ijaze hiyo sufuria kwa mifupa hii mizuri;
EZE 24:5 chagua yule aliye bora wa kundi la kondoo. Panga kuni chini ya sufuria kwa ajili ya mifupa; chochea hadi ichemke na uitokose hiyo mifupa ndani yake.
EZE 24:6 “ ‘Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Ole wa mji unaomwaga damu, ole wa sufuria ambayo sasa ina ukoko ndani yake, ambayo ukoko wake hautoki. Kipakue kipande baada ya kipande, bila kuvipigia kura.
EZE 24:7 “ ‘Kwa kuwa damu aliyoimwaga ipo katikati yake: Huyo mwanamke aliimwaga juu ya mwamba ulio wazi; hakuimwaga kwenye ardhi, ambako vumbi lingeifunika.
EZE 24:8 Kuchochea ghadhabu na kulipiza kisasi, nimemwaga damu yake juu ya mwamba ulio wazi, ili isifunikwe.
EZE 24:9 “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Ole wa mji unaomwaga damu! Mimi nami nitalundikia kuni nyingi.
EZE 24:10 Kwa hiyo lundika kuni na uwashe moto. Pika hiyo nyama vizuri, changanya vikolezo ndani yake, na uiache mifupa iungue kwenye moto.
EZE 24:11 Kisha teleka sufuria tupu kwenye makaa hadi iwe na moto sana na shaba yake ing’ae, ili uchafu wake upate kuyeyuka na ukoko wake upate kuungua na kuondoka.
EZE 24:12 Imezuia juhudi zote, ukoko wake mwingi haujaondoka, hata ikiwa ni kwa moto.
EZE 24:13 “ ‘Sasa uchafu wako ni uasherati wako. Kwa sababu nilijaribu kukutakasa lakini haikuwezekana kutakaswa kutokana na huo uchafu wako, hutatakasika tena hadi ghadhabu yangu dhidi yako iwe imepungua.
EZE 24:14 “ ‘Mimi Mwenyezi Mungu nimesema, wakati umewadia wa mimi kutenda. Mimi sitazuia, mimi sitaona huruma wala sitapunguza hasira yangu. Utahukumiwa sawasawa na mwenendo na matendo yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 24:15 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 24:16 “Mwanadamu, kwa pigo moja nakaribia kukuondolea kile kilicho furaha ya macho yako. Lakini usiomboleze au kulia wala kudondosha machozi yoyote.
EZE 24:17 Lia kwa uchungu kimya kimya usimwombolezee mtu aliyekufa. Jifunge kilemba chako na uvae viatu vyako miguuni mwako, usifunike sehemu ya chini ya uso wako, wala usile vyakula vya waombolezaji.”
EZE 24:18 Hivyo nikanena na watu asubuhi na jioni mke wangu akafa. Kesho yake asubuhi nilifanya kama nilivyoamriwa.
EZE 24:19 Ndipo watu wakaniuliza, “Je, jambo hili unalofanya linamaanisha nini kwetu?”
EZE 24:20 Kwa hiyo nikawaambia, “Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia kusema:
EZE 24:21 ‘Sema na nyumba ya Israeli. Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninakaribia kupatia unajisi mahali pangu patakatifu, ngome ambayo ndani yake mnaona fahari, furaha ya macho yenu, kitu mnachokipenda. Wana wenu wa kiume na wa kike mliowaacha nyuma wataanguka kwa upanga.
EZE 24:22 Nanyi mtafanya kama nilivyofanya. Hamtafunika sehemu ya chini ya nyuso zenu wala hamtakula vyakula vya kawaida vya waombolezaji.
EZE 24:23 Mtajifunga vilemba vichwani mwenu na kuvaa viatu vyenu miguuni mwenu. Hamtaomboleza au kulia, lakini mtadhoofika kwa sababu ya dhambi zenu na kulia kwa uchungu kila mtu na mwenzake.
EZE 24:24 Ezekieli atakuwa ishara kwenu, mtafanya kama yeye alivyofanya. Jambo hili litakapotokea, mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.’
EZE 24:25 “Nawe, mwanadamu, siku ile nitakapoondoa ngome yao iliyo furaha yao na utukufu wao, kitu cha kupendeza macho yao, kile kilicho shauku ya mioyo yao, wana wao wa kiume na wa kike vilevile,
EZE 24:26 siku hiyo atakayetoroka atakuja kuwapasha habari.
EZE 24:27 Katika siku ile kinywa chako kitamfumbukia yeye aliyenusurika, nawe utaongea wala hutanyamaza tena. Hivyo wewe utakuwa ishara kwao, nao watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
EZE 25:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 25:2 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Waamoni utabiri dhidi yao.
EZE 25:3 Waambie, ‘Sikieni neno la Bwana Mungu Mwenyezi. Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulisema, “Aha!” juu ya mahali pangu patakatifu palipotiwa unajisi, na juu ya nchi ya Israeli ilipoangamizwa, na juu ya watu wa Yuda walipoenda uhamishoni,
EZE 25:4 kwa hiyo nitawatia mikononi mwa watu wa mashariki mkawe mali yao. Watapiga kambi zao kati yenu na kufanya makazi miongoni mwenu, watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu.
EZE 25:5 Nitaufanya mji wa Raba kuwa malisho ya ngamia na Amoni kuwa mahali pa kondoo pa kupumzikia. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 25:6 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa mmepiga makofi yenu na kufanya kishindo kwa miguu, mkifurahia kwa mioyo yenu miovu juu ya yale mabaya yaliyoipata nchi ya Israeli,
EZE 25:7 hivyo nitaunyoosha mkono wangu dhidi yenu na kuwatoa kuwa nyara kwa mataifa. Nitawakatilia mbali kutoka mataifa na kuwang’oa kutoka nchi. Nitawaangamiza, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 25:8 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa sababu Moabu na Seiri wamesema, “Tazama, nyumba ya Yuda imekuwa kama mataifa mengine yote,”
EZE 25:9 kwa hiyo nitaiondoa ile miji iliyo kando ya Moabu, kuanzia miji iliyo mipakani: Beth-Yeshimothi, Baal-Meoni na Kiriathaimu, iliyo utukufu wa nchi hiyo.
EZE 25:10 Nitaitia Moabu pamoja na Waamoni mikononi mwa watu wa Mashariki kuwa milki yao, ili Waamoni wasikumbukwe miongoni mwa mataifa,
EZE 25:11 nami nitatoa adhabu kwa Moabu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 25:12 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa sababu Edomu walilipiza kisasi juu ya nyumba ya Yuda, wakakosea sana kwa kufanya hivyo,
EZE 25:13 kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaunyoosha mkono wangu dhidi ya Edomu na kuua watu wake na wanyama wao. Nitaufanya ukiwa, na kuanzia Temani hadi Dedani wataanguka kwa upanga.
EZE 25:14 Nitalipiza Edomu kisasi kwa mkono wa watu wangu Israeli, nao watawatendea Edomu sawasawa na hasira yangu na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 25:15 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa sababu Wafilisti wamewalipiza kisasi kwa uovu wa mioyo yao na kwa uadui wa siku nyingi wakataka kuangamiza Yuda,
EZE 25:16 kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi ninakaribia kuunyoosha mkono wangu dhidi ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi na kuwaangamiza wale waliosalia katika pwani.
EZE 25:17 Nitalipiza kisasi kikubwa juu yao na kuwaadhibu katika ghadhabu yangu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapolipiza kisasi juu yao.’ ”
EZE 26:1 Mwaka wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 26:2 “Mwanadamu, kwa sababu Tiro amesema kuhusu Yerusalemu, ‘Aha! Lango la kwenda kwa mataifa limevunjika, nayo milango yake iko wazi mbele yangu, sasa kwa kuwa amekuwa magofu nitastawi.’
EZE 26:3 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi niko kinyume na wewe, ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi dhidi yako, kama bahari inayovurumisha mawimbi yake.
EZE 26:4 Watavunja kuta za Tiro na kuibomoa minara yake, nitakwangua udongo wake na kuufanya mwamba mtupu.
EZE 26:5 Itakuwa huko katikati ya bahari patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki, kwa maana nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Atakuwa nyara kwa mataifa,
EZE 26:6 nayo makazi yake huko bara yataangamizwa kwa upanga. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 26:7 “Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kutoka kaskazini nitamleta dhidi ya Tiro Mfalme Nebukadneza wa Babeli, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi na magari ya vita, wapanda farasi na jeshi kubwa.
EZE 26:8 Atayaharibu makazi yako huko bara kwa upanga; atajenga husuru dhidi yako, na kupandisha kilima hadi kuta zako, na kuinua ngao zake dhidi yako.
EZE 26:9 Ataelekeza mapigo ya magogo ya kubomoa boma dhidi ya kuta zako, na kubomoa minara yako kwa silaha zake.
EZE 26:10 Farasi wake watakuwa wengi sana kiasi kwamba utafunikwa na mavumbi watakayotimua. Kuta zako zitatikisika kwa mshindo wa farasi wa vita, magari ya kukokotwa, na magari ya vita wakati aingiapo malango yako kama watu wanaoingia mji ambao kuta zake zimebomolewa kote.
EZE 26:11 “Kwato za farasi wake zitakanyaga barabara zako zote, atawaua watu wako kwa upanga na nguzo zako zilizo imara zitaanguka chini.
EZE 26:12 Watateka utajiri wako na kuchukua nyara bidhaa zako, watazivunja kuta zako na kuzibomoa nyumba zako nzuri, watatupa baharini mawe yako, mbao zako na kifusi chako.
EZE 26:13 Nitakomesha kelele za nyimbo zako, na uimbaji wako wa kinubi kamwe hautasikika tena.
EZE 26:14 Nitakufanya mwamba mtupu, nawe utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za kuvulia samaki. Kamwe hutajengwa tena, kwa maana Mimi Mwenyezi Mungu nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 26:15 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa Tiro: ‘Je, nchi za pwani hazitatetemeka kwa kishindo cha anguko lako, wakati majeruhi wanapolia kwa maumivu makali na wakati mauaji yanaendelea ndani yako?
EZE 26:16 Ndipo wakuu wote wa mataifa ya pwani watashuka kutoka viti vyao vya utawala, na kuweka kando majoho yao na kuvua nguo zao zilizotariziwa. Wataketi chini ardhini, wakiwa wamevikwa hofu kuu, wakitetemeka kila dakika na kukustaajabia.
EZE 26:17 Ndipo wao watakuombolezea na kukuambia: “ ‘Tazama jinsi ulivyoharibiwa, ee mji uliokuwa na sifa, wewe uliyekaliwa na mabaharia! Ulikuwa na nguvu kwenye bahari, wewe na wakaaji wako; wote walioishi huko, uliwatia hofu kuu.
EZE 26:18 Sasa nchi za pwani zinatetemeka katika siku ya anguko lako; visiwa vilivyomo baharini vinaogopa kwa kuporomoka kwako.’
EZE 26:19 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakapokufanya uwe mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa tena na watu, nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako na maji yake makuu yatakapokufunika,
EZE 26:20 ndipo nitakapokushusha chini pamoja na wale wanaoshuka shimoni, kwa watu wa kale, nami nitakufanya uishi katika pande za chini za nchi kama katika magofu ya kale, pamoja na wale wanaoshuka shimoni, nawe hutarudi au kurejea kwenye makao yako katika nchi ya walio hai.
EZE 26:21 Nitakufikisha mwisho wa kutisha wala hutakuwepo tena. Watu watakutafuta, lakini kamwe hutaonekana tena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 27:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 27:2 “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro.
EZE 27:3 Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Ee Tiro, wewe umesema, “Mimi ni mkamilifu katika uzuri.”
EZE 27:4 Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari, wajenzi wako walikamilisha uzuri wako.
EZE 27:5 Walizifanya mbao zako zote kwa misunobari kutoka Seniri; walichukua mwerezi kutoka Lebanoni kukutengenezea mlingoti.
EZE 27:6 Walichukua mialoni kutoka Bashani wakakutengenezea makasia yako; kwa miti ya msanduku kutoka pwani ya Kitimu wakatengeneza sitaha yako na kuipamba kwa pembe za ndovu.
EZE 27:7 Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako, nacho kilikuwa bendera yako; chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau kutoka visiwa vya Al-Yasa.
EZE 27:8 Wakaaji wa Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako; watu wako wenye ustadi, ee Tiro, ndio walikuwa mabaharia wako.
EZE 27:9 Wazee wa Gebali pamoja na mafundi stadi walikuwa mafundi wako kwenye meli. Meli zote za baharini na mabaharia wao walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako.
EZE 27:10 “ ‘Wanaume wa Uajemi, Ludi na Putu walikuwa askari katika jeshi lako. Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako, wakileta fahari yako.
EZE 27:11 Watu wa Arvadi na wa Heleki walikuwa juu ya kuta zako pande zote; watu wa Gamadi walikuwa kwenye minara yako. Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako; wakaukamilisha uzuri wako.
EZE 27:12 “ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali yako.
EZE 27:13 “ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki walifanya biashara nawe; walibadilisha binadamu na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako.
EZE 27:14 “ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali yako.
EZE 27:15 “ ‘Watu wa Dedani walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo.
EZE 27:16 “ ‘Watu wa Aramu walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, wakibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe na akiki nyekundu.
EZE 27:17 “ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walibadilishana ngano iliyotoka Minithi, mtama, asali, mafuta na zeri kwa bidhaa zako.
EZE 27:18 “ ‘Dameski walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako na ukuu wa utajiri wa mali zako, wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari.
EZE 27:19 “ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali walikuletea mali ya biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai.
EZE 27:20 “ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi.
EZE 27:21 “ ‘Arabuni na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako; walifanya biashara nawe ya kubadilishana wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi.
EZE 27:22 “ ‘Wafanyabiashara wa Sheba na wa Raama walifanya biashara nawe, wakabadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezo, vito vya thamani na dhahabu.
EZE 27:23 “ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe.
EZE 27:24 Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara.
EZE 27:25 “ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo zinazokusafirishia bidhaa zako. Umejazwa shehena kubwa katika moyo wa bahari.
EZE 27:26 Wapiga makasia wako wanakupeleka mpaka kwenye maji makuu. Lakini upepo wa mashariki utakuvunja vipande vipande moyoni mwa bahari.
EZE 27:27 Utajiri wako, bidhaa zako na mali yako, mabaharia wako, manahodha wako, mafundi wako wa meli, wafanyabiashara wako na askari wako wote, na kila mmoja aliye kwenye meli atazama kwenye moyo wa bahari siku ile meli yako itakapovunjika.
EZE 27:28 Nchi za pwani zitatetemeka wakati mabaharia wako watakapopiga kelele.
EZE 27:29 Wote wapigao makasia wataacha meli zao, mabaharia wote na wanamaji wote watasimama pwani.
EZE 27:30 Watapaza sauti zao na kulia sana kwa ajili yako; watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao na kujivingirisha kwenye majivu.
EZE 27:31 Watanyoa nywele zao kwa ajili yako, nao watavaa magunia. Watakulilia kwa uchungu wa moyo na kwa maombolezo makuu.
EZE 27:32 Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako, watafanya maombolezo kukuhusu wakisema: “Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro, katika moyo wa bahari?”
EZE 27:33 Bidhaa zako zilipotoka baharini, ulitosheleza mataifa mengi; kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako ulitajirisha wafalme wa dunia.
EZE 27:34 Sasa umevunjavunjwa na bahari, katika vilindi vya maji, bidhaa zako na kundi lako lote vimezama pamoja nawe.
EZE 27:35 Wote wanaoishi katika nchi za pwani wanakustaajabia; wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu, nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga.
EZE 27:36 Wafanyabiashara miongoni mwa mataifa wanakucheka; umefikia mwisho wa kutisha nawe hutakuwepo tena.’ ”
EZE 28:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 28:2 “Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna na umesema, “Mimi ni mungu; nami ninaketi kwenye kiti cha enzi cha mungu katika moyo wa bahari.” Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu, ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.
EZE 28:3 Je, wewe una hekima kuliko Danieli? Je, hakuna siri iliyofichika kwako?
EZE 28:4 Kwa hekima yako na ufahamu wako, umejipatia utajiri, nawe umejikusanyia dhahabu na fedha katika hazina zako.
EZE 28:5 Kwa werevu wako mwingi katika biashara, umeongeza utajiri wako na kwa sababu ya utajiri wako moyo wako umekuwa na kiburi.
EZE 28:6 “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima, mwenye hekima kama mungu,
EZE 28:7 mimi nitawaleta wageni dhidi yako, taifa katili kuliko yote; watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako, na kuchafua fahari yako inayong’aa.
EZE 28:8 Watakushusha chini shimoni, nawe utakufa kifo cha kikatili katika moyo wa bahari.
EZE 28:9 Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,” mbele ya wale wanaokuua? Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu, mikononi mwa hao wanaokuua.
EZE 28:10 Utakufa kifo cha wasiotahiriwa kwa mkono wa wageni. Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 28:11 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 28:12 “Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu, ukiwa umejaa hekima na mkamilifu katika uzuri.
EZE 28:13 Ulikuwa ndani ya Edeni, bustani ya Mungu; kila kito cha thamani kilikupamba: akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi, krisolitho, shohamu na yaspi, yakuti samawi, almasi na zabarajadi. Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake kulifanywa kwa dhahabu; siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.
EZE 28:14 Ulipakwa mafuta kuwa kerubi mlinzi, kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokuweka wakfu. Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu; ulitembea katikati ya vito vya moto.
EZE 28:15 Ulikuwa mnyofu katika njia zako tangu siku ile ya kuumbwa kwako, hadi uovu ulipoonekana ndani yako.
EZE 28:16 Kutokana na biashara yako iliyoenea, ulijazwa na dhuluma, nawe ukatenda dhambi. Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka mlima wa Mungu, nami nikakufukuza, ee kerubi mlinzi, kutoka katikati ya vito vya moto.
EZE 28:17 Moyo wako ukawa na kiburi kwa ajili ya uzuri wako, nawe ukaiharibu hekima yako kwa sababu ya fahari yako. Kwa hiyo nikakutupa chini; nimekufanya kioja mbele ya wafalme.
EZE 28:18 Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma, umenajisi mahali pako patakatifu. Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako, nao ukakuteketeza, nami nikakufanya majivu juu ya nchi, machoni pa wote waliokuwa wakitazama.
EZE 28:19 Mataifa yote yaliyokujua yanakustaajabia; umefikia mwisho wa kutisha na hutakuwepo tena milele.’ ”
EZE 28:20 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 28:21 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Sidoni, ukatabiri dhidi yake,
EZE 28:22 nawe useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Mimi ni kinyume chako, ee Sidoni, nami nitapata utukufu ndani yako. Nao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapotekeleza hukumu zangu na kuonesha utakatifu wangu ndani yake.
EZE 28:23 Nitapeleka tauni ndani yake na kufanya damu itiririke katika barabara zake. Waliochinjwa wataanguka ndani yake, kwa upanga dhidi yake kila upande. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 28:24 “ ‘Nyumba ya Israeli hawatakuwa tena na majirani wenye nia ya kuwadhuru, wanaoumiza kama michongoma na miiba mikali. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 28:25 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakapoikusanya nyumba ya Israeli kutoka mataifa ambako wametawanyika, nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwao machoni pa mataifa. Ndipo watakapoishi katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu Yakobo.
EZE 28:26 Wataishi humo kwa salama na watajenga nyumba na kupanda mashamba ya mizabibu, wataishi kwa salama nitakapowaadhibu majirani zao wote ambao waliwafanyia uovu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao.’ ”
EZE 29:1 Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 29:2 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao mfalme wa Misri na utabiri dhidi yake na dhidi ya Misri yote.
EZE 29:3 Nena, nawe useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Mimi ni kinyume nawe, Farao, mfalme wa Misri, ewe mnyama mkubwa ulalaye katikati ya vijito vyako. Unasema, “Mto Naili ni wangu mwenyewe; niliufanya kwa ajili yangu mwenyewe.”
EZE 29:4 Lakini nitatia ndoana katika mataya yako nami nitawafanya samaki wa vijito vyako washikamane na magamba yako. Nitakutoa katikati ya vijito vyako, pamoja na samaki wote walioshikamana na magamba yako.
EZE 29:5 Nitakutupa jangwani, wewe pamoja na samaki wote wa vijito vyako. Utaanguka uwanjani, nawe hutakusanywa au kuchukuliwa. Nitakutoa uwe chakula kwa wanyama wa nchi na ndege wa angani.
EZE 29:6 Ndipo wale wote wanaoishi Misri watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. “ ‘Umekuwa fimbo ya tete kwa nyumba ya Israeli.
EZE 29:7 Walipokushika kwa mikono yao, ulivunjika na kuchana mabega yao; walipokuegemea, ulivunjika na migongo yao ikateguka.
EZE 29:8 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaleta upanga juu yako na kuua watu wako na wanyama wao.
EZE 29:9 Misri itakuwa ukiwa na isiyolimwa wala kukaliwa na watu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. “ ‘Kwa sababu ulisema, “Mto Naili ni wangu; mimi niliuumba,”
EZE 29:10 kwa hiyo mimi ni kinyume nawe na kinyume na vijito vyako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa magofu na ukiwa kuanzia Migdoli hadi Aswani, hata kufikia mpaka wa Kushi.
EZE 29:11 Hakuna unyayo wa mtu au mnyama utakaopita ndani yake, wala hakuna yeyote atakayeishi humo kwa muda wa miaka arobaini.
EZE 29:12 Nitaifanya nchi ya Misri ukiwa, miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yake itabaki ukiwa miaka arobaini miongoni mwa miji iliyo magofu. Nami nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi nyingine.
EZE 29:13 “ ‘Lakini hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mwishoni mwa hiyo miaka arobaini, nitawakusanya Wamisri kutoka mataifa walikotawanywa.
EZE 29:14 Nitawarejesha hao Wamisri kutoka kutekwa kwao na kuwaweka Pathrosi, nchi ya baba zao. Huko watakuwa na ufalme usiokuwa na nguvu.
EZE 29:15 Utakuwa ufalme dhaifu kuliko zote na kamwe Misri haitajikweza tena juu ya mataifa mengine. Nitaufanya ufalme wake dhaifu sana kiasi kwamba kamwe hautatawala tena juu ya mataifa mengine.
EZE 29:16 Misri haitakuwa tena tumaini la watu wa Israeli bali itakuwa kumbukumbu ya dhambi yao kwa kuigeukia kuomba msaada. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 29:17 Katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza, neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema:
EZE 29:18 “Mwanadamu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliongoza jeshi lake kufanya kazi ngumu dhidi ya Tiro; kila kichwa kilipata upara na kila bega likachunika. Lakini yeye na jeshi lake hawakupata malipo yoyote kutokana na muda wote aliongoza hiyo vita dhidi ya Tiro.
EZE 29:19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaitia Misri mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atachukua utajiri wa Misri. Atateka mateka na kuchukua nyara mali ya Misri kama ujira kwa ajili ya jeshi lake.
EZE 29:20 Nimempa mfalme wa Babeli nchi ya Misri kuwa ujira kwa juhudi zake kwa sababu yeye na jeshi lake walifanya kwa ajili yangu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 29:21 “Katika siku hiyo nitaifanya nyumba ya Israeli iwe na nguvu nami nitakifungua kinywa chako miongoni mwao. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
EZE 30:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 30:2 “Mwanadamu, toa unabii na useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Ombolezeni ninyi na mseme, “Ole wa siku ile!”
EZE 30:3 Kwa kuwa siku ile imekaribia, siku ya Mwenyezi Mungu imekaribia, siku ya mawingu, siku ya maangamizi kwa mataifa.
EZE 30:4 Upanga utakuja dhidi ya Misri, nayo maumivu makuu yataijia Kushi. Mauaji yatakapoangukia Misri, utajiri wake utachukuliwa na misingi yake itabomolewa.
EZE 30:5 Kushi na Putu, Ludi na Arabia yote, Kubu na watu wa nchi ya agano watauawa kwa upanga pamoja na Misri.
EZE 30:6 “ ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Wale walioungana na Misri wataanguka na kiburi cha nguvu zake kitashindwa. Kutoka Migdoli hadi Aswani, watauawa ndani yake kwa upanga, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 30:7 Hizo nchi zitakua ukiwa miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yao itakuwa magofu miongoni mwa miji iliyo magofu.
EZE 30:8 Ndipo watajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapoiwasha Misri moto na wasaidizi wake wote watapondwa.
EZE 30:9 “ ‘Siku hiyo wajumbe watatoka kwangu kwa merikebu, ili kuwatia hofu Ethiopia, wakiwa katika hali yao ya kuridhika. Maumivu makali yatawapata siku ya maangamizi ya Misri, kwa kuwa hakika itakuja.
EZE 30:10 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Nitakomesha makundi ya Misri kwa mkono wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.
EZE 30:11 Yeye na jeshi lake, taifa lililo katili kuliko mataifa yote, ataletwa ili kuangamiza nchi. Watafuta panga zao dhidi ya Misri na kuijaza nchi kwa waliouawa.
EZE 30:12 Nitakausha vijito vya Mto Naili, na kuiuza nchi kwa watu waovu; kwa mkono wa wageni, nitaifanya nchi ukiwa na kila kitu kilicho ndani yake. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena haya.
EZE 30:13 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Nitaangamiza sanamu na kukomesha vinyago katika Memfisi. Hapatakuwa tena na mkuu katika nchi ya Misri, nami nitaeneza hofu katika nchi nzima.
EZE 30:14 Nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa na kuitia moto Soani, nami nitaipiga Thebesi kwa adhabu.
EZE 30:15 Nitaimwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali makundi ya Thebesi.
EZE 30:16 Nitaitia moto nchi ya Misri; Pelusiumu itagaagaa kwa maumivu makuu. Thebesi itachukuliwa na tufani, Memfisi itakuwa katika taabu daima.
EZE 30:17 Wanaume vijana wa Oni na wa Pi-Besethi wataanguka kwa upanga nayo hiyo miji itatekwa.
EZE 30:18 Huko Tapanesi mchana utatiwa giza nitakapovunja nira ya Misri; hapo kiburi cha nguvu zake kitakoma. Atafunikwa na mawingu na vijiji vyake vitatekwa.
EZE 30:19 Kwa hiyo nitaipiga Misri kwa adhabu, nao watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 30:20 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa kwanza, siku ya saba, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 30:21 “Mwanadamu, nimevunja mkono wa Farao mfalme wa Misri. Haukufungwa ili upone au kuwekewa kipande cha ubao ili upate nguvu za kuweza kuchukua upanga.
EZE 30:22 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi ni kinyume na Farao mfalme wa Misri. Nitavunja mikono yake yote miwili, ule mkono ulio mzima pia na ule uliovunjika na kuufanya upanga uanguke toka mkononi mwake.
EZE 30:23 Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi zote.
EZE 30:24 Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli na kuutia upanga wangu mkononi mwake, lakini nitavunja mikono ya Farao, naye atalia kwa huzuni mbele yake kama mtu aliyetiwa jeraha la kumfisha.
EZE 30:25 Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, lakini mikono ya Farao italegea. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapoutia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye ataunyoosha dhidi ya Misri.
EZE 30:26 Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi nyingine. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
EZE 31:1 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza, neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema:
EZE 31:2 “Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri na makundi yake hivi: “ ‘Je, ni nani awezaye kulinganishwa na wewe katika fahari.
EZE 31:3 Angalia Ashuru, zamani ulikuwa mwerezi huko Lebanoni, ukiwa na matawi mazuri na kutia msitu kivuli; ulikuwa mrefu sana, kilele chake kilipita majani ya miti yote.
EZE 31:4 Maji mengi yaliustawisha, chemchemi zenye maji mengi ziliufanya urefuke; vijito vyake vilitiririka pale ulipoota pande zote na kupeleka mifereji yake kwenye miti yote ya shambani.
EZE 31:5 Hivyo ukarefuka kupita miti yote ya shambani; vitawi vyake viliongezeka na matawi yake yakawa marefu, yakitanda kwa sababu ya wingi wa maji.
EZE 31:6 Ndege wote wa angani wakaweka viota kwenye vitawi vyake, wanyama wote wa shambani wakazaana chini ya matawi yake, mataifa makubwa yote yaliishi chini ya kivuli chake.
EZE 31:7 Ulikuwa na fahari katika uzuri, ukiwa na matawi yaliyotanda, kwa kuwa mizizi yake iliteremka hadi kwenye maji mengi.
EZE 31:8 Mierezi katika bustani ya Mungu haikuweza kushindana nao, wala misunobari haikuweza kulingana na vitawi vyake, wala miaramoni haikulinganishwa na matawi yake, wala hakukuwa na mti katika bustani ya Mungu wa kulinganisha na uzuri wake.
EZE 31:9 Niliufanya kuwa mzuri, ukiwa na matawi mengi; nao ulionewa wivu na miti yote ya Edeni katika bustani ya Mungu.
EZE 31:10 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu ulikuwa mrefu sana, kilele chake kikiwa juu ya majani manene ya miti na kwa sababu ulikuwa na kiburi cha urefu wake,
EZE 31:11 niliutia mikononi mwa mtawala wa mataifa, ili yeye autende sawasawa na uovu wake. Nikaukatilia mbali,
EZE 31:12 nayo mataifa mageni yaliyo makatili sana yaliukata huo mti na kuuacha. Matawi yake yalianguka juu ya milima na kwenye mabonde yote, vitawi vyake vikavunjika na kusambaa katika makorongo yote ya nchi. Mataifa yote ya duniani yakaondoka kutoka kivuli chake na kuuacha.
EZE 31:13 Ndege wote wa angani wakakaa kwenye ule mti ulioanguka na wanyama pori wote wakakaa katikati ya vitawi vyake.
EZE 31:14 Kamwe hakutakuwa na miti mingine kando ya hayo maji itakayorefuka zaidi ya huo, vilele vyake vikiwa juu ya majani yote ya miti. Hakuna miti mingine, hata kama imekunywa maji vizuri namna gani, itakayofikia urefu huo. Yote mwisho wake ni kifo, na kuingia ardhini, kama vile ilivyo kwa wanadamu, pamoja na wale wanaoshuka shimoni.
EZE 31:15 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika siku ile mwerezi uliposhushwa chini kaburini nilizifunika chemchemi zenye maji mengi kwa maombolezo: Nilivizuia vijito vyake na wingi wa maji yake nikauzuia. Kwa sababu yake niliivika Lebanoni huzuni, nayo miti yote ya shambani ikanyauka.
EZE 31:16 Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa kishindo cha kuanguka kwake wakati nilipoushusha chini kaburini pamoja na wale wanaoshuka shimoni. Ndipo miti yote ya Edeni, miti iliyo bora kuliko yote na iliyo mizuri sana ya Lebanoni, miti yote ile iliyokunywa maji vizuri, ilifarijika hapa duniani.
EZE 31:17 Wale walioishi katika kivuli chake, wale walioungana naye miongoni mwa mataifa, nao pia walikuwa wamezikwa pamoja naye, wakiungana na wale waliouawa kwa upanga.
EZE 31:18 “ ‘Ni miti ipi ya Edeni inayoweza kulinganishwa nawe kwa fahari na utukufu? Hata hivyo, wewe pia, utashushwa pamoja na miti ya Edeni hadi chini kabisa; utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga. “ ‘Huyu ni Farao pamoja na makundi yake yote, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 32:1 Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema:
EZE 32:2 “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Farao mfalme wa Misri na umwambie: “ ‘Wewe ni kama simba miongoni mwa mataifa, wewe ni kama mnyama mkubwa baharini, unapiga maji kwa kishindo katika vijito vyako, unayavuruga maji kwa miguu yako, na kuchafua vijito.
EZE 32:3 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Nikiwa pamoja na wingi mkubwa wa watu nitautupa wavu wangu juu yako, nao watakukokota katika wavu wangu.
EZE 32:4 Nitakutupa nchi kavu na kukuvurumisha uwanjani. Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako na wanyama wote wa nchi watajishibisha nyama yako.
EZE 32:5 Nitatawanya nyama yako juu ya milima na kujaza mabonde kwa mabaki yako.
EZE 32:6 Nitailowanisha nchi kwa damu yako inayotiririka njia yote hadi milimani, nayo mabonde yatajazwa na nyama yako.
EZE 32:7 Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu na kuzitia nyota zake giza; nitalifunika jua kwa wingu, nao mwezi hautatoa nuru yake.
EZE 32:8 Mianga yote itoayo nuru angani nitaitia giza juu yako; nitaleta giza juu ya nchi yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 32:9 Nitaifadhaisha mioyo ya mataifa mengi nitakapokuangamiza miongoni mwa mataifa, nikikuleta uhamishoni miongoni mwa nchi ambazo hujapata kuzijua.
EZE 32:10 Nitayafanya mataifa mengi wakustaajabie, wafalme wao watatetemeka kwa hofu kwa ajili yako nitakapotikisa upanga wangu mbele yao. Siku ya anguko lako kila mmoja wao atatetemeka kila dakika kwa ajili ya maisha yake.
EZE 32:11 “ ‘Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Upanga wa mfalme wa Babeli utakuja dhidi yako.
EZE 32:12 Nitayafanya makundi yako kuanguka kwa panga za mashujaa: taifa katili kuliko mataifa yote. Watakivunjavunja kiburi cha Misri, nayo makundi yake yote yatashindwa.
EZE 32:13 Nitaangamiza mifugo yake yote wanaojilisha kando ya maji mengi: hayatavurugwa tena kwa mguu wa mwanadamu wala kwato za mnyama hazitayachafua tena.
EZE 32:14 Kisha nitafanya maji yake yatulie na kufanya vijito vyake vitiririke kama mafuta, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 32:15 Nitakapoifanya Misri kuwa ukiwa, na kuiondolea nchi kila kitu kilichomo, nitakapowapiga wote wanaoishi humo, ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’
EZE 32:16 “Hili ndilo ombolezo watakalomwimbia. Binti za mataifa wataliimba, kwa kuwa Misri na makundi yake yote wataliimba, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 32:17 Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 32:18 “Mwanadamu, omboleza kwa ajili ya makundi ya Misri na uwatupe Kuzimu, yeye na binti za mataifa yenye nguvu, waende huko pamoja nao wanaoshuka shimoni.
EZE 32:19 Je, ninyi mmekubalika zaidi ya wengine? Shukeni chini! Nanyi mkalazwe pamoja na hao wasiotahiriwa!
EZE 32:20 Wataanguka miongoni mwa wale waliouawa kwa upanga. Upanga umefutwa; mwache aburutwe mbali pamoja na hao watu wake wote.
EZE 32:21 Kutoka Kuzimu viongozi hodari watanena kuhusu Misri pamoja na wale walioungana nao, ‘Wameshuka chini, nao wamelala kimya pamoja na hao wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.’
EZE 32:22 “Ashuru yuko huko pamoja na jeshi lake lote, amezungukwa na makaburi ya watu wake wote waliouawa, wale wote walioanguka kwa upanga.
EZE 32:23 Makaburi yao yako kwenye kina cha chini cha shimo na jeshi lake limelala kulizunguka kaburi lake. Wote waliokuwa wameeneza hofu kuu katika nchi ya walio hai wameuawa, wameanguka kwa upanga.
EZE 32:24 “Elamu yuko huko, pamoja na makundi yake yote wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote wameuawa, wameanguka kwa upanga. Wote waliokuwa wameeneza hofu katika nchi ya walio hai walishuka Kuzimu bila kutahiriwa. Wanaichukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni.
EZE 32:25 Kitanda kimetandikwa kwa ajili yake miongoni mwa waliouawa, pamoja na makundi yake yote wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote ni watu wasiotahiriwa, wameuawa kwa upanga. Kwa sababu vitisho vyao vilienea katika nchi ya walio hai, wameichukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni, nao wamewekwa miongoni mwa waliouawa.
EZE 32:26 “Mesheki na Tubali wako humo, pamoja na makundi yao wakiwa wameyazunguka makaburi yao. Wote hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga kwa sababu walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.
EZE 32:27 Je, hawakulala na mashujaa wengine wasiotahiriwa waliouawa, ambao wameshuka kaburini wakiwa na silaha zao za vita, ambao panga zao ziliwekwa chini ya vichwa vyao na uovu wao juu ya mifupa yao? Adhabu kwa ajili ya dhambi zao ilikuwa juu ya mifupa yao, ingawa vitisho vya mashujaa hawa vilikuwa vimeenea hadi kwenye nchi ya walio hai.
EZE 32:28 “Wewe pia, ee Farao, utavunjwa nawe utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.
EZE 32:29 “Edomu yuko humo, wafalme wake wote na wakuu wake wote, ambao ijapokuwa wana nguvu, wamelazwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga. Wamelala pamoja na wasiotahiriwa, pamoja na wale wanaoshuka shimoni.
EZE 32:30 “Wakuu wote wa kaskazini na Wasidoni wote wako huko, wameshuka chini pamoja na waliouawa kwa aibu ijapokuwa kuna vitisho vilivyosababishwa na nguvu zao. Wamelala bila kutahiriwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga na kuchukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni.
EZE 32:31 “Farao, yeye pamoja na jeshi lake lote, atakapowaona atafarijiwa kwa ajili ya makundi yake yote, wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 32:32 Ingawa nilimfanya Farao aeneze vitisho vyake katika nchi ya walio hai, Farao pamoja na makundi yake yote watalazwa miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 33:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 33:2 “Mwanadamu, sema na watu wako uwaambie, ‘Nitakapoleta upanga dhidi ya nchi, nao watu wa nchi wakamchagua mmoja wa watu wao na kumfanya awe mlinzi wao,
EZE 33:3 naye auonapo upanga unakuja dhidi ya nchi na kupiga tarumbeta kuonya watu,
EZE 33:4 kama mtu yeyote asikiapo sauti ya tarumbeta hatakubali kuonywa, basi upanga ujapo na kuutoa uhai wake, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
EZE 33:5 Kwa kuwa alisikia sauti ya tarumbeta lakini hakukubali maonyo, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kama angekubali maonyo, angejiokoa mwenyewe.
EZE 33:6 Lakini kama mlinzi akiona upanga unakuja na asipige tarumbeta kuonya watu na upanga ukija na kutoa uhai wa mmoja wao, yule mtu ataondolewa kwa sababu ya dhambi yake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.’
EZE 33:7 “Mwanadamu, nimekufanya wewe kuwa mlinzi kwa ajili ya nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo na uwape maonyo kutoka kwangu.
EZE 33:8 Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Ewe mtu mwovu, hakika utakufa,’ nawe hukusema neno la kumwonya ili atoke katika njia zake, yule mtu mwovu atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini mimi nitaitaka damu yake mkononi mwako.
EZE 33:9 Lakini kama utamwonya huyo mtu mwovu aache njia zake mbaya naye hafanyi hivyo, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini utakuwa umejiokoa mwenyewe.
EZE 33:10 “Mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo mnalosema: “Makosa yetu na dhambi zetu zimetulemea, nasi tunadhoofika kwa sababu ya hayo. Tutawezaje basi kuishi?” ’
EZE 33:11 Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’
EZE 33:12 “Kwa hiyo, mwanadamu, waambie watu wako, ‘Haki ya mtu mwenye haki haitamwokoa wakati anapoacha kutii, wala uovu wa mtu mwovu hautamsababisha yeye kuanguka anapotubu na kuacha uovu. Mtu mwenye haki akitenda dhambi, hataishi kwa sababu ya uadilifu wake wa awali.’
EZE 33:13 Nikimwambia mtu mwenye haki kwamba hakika ataishi, lakini akategemea hiyo haki yake na kutenda uovu, hakuna tendo lolote la haki alilotenda litakalokumbukwa; atakufa kwa ajili ya uovu alioutenda.
EZE 33:14 Nami nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa,
EZE 33:15 kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa.
EZE 33:16 Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi.
EZE 33:17 “Lakini watu wako wanasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini ni njia zao ambazo si sawa.
EZE 33:18 Kama mtu mwenye haki akigeuka kutoka uadilifu wake na kufanya uovu, atakufa kwa ajili ya huo uovu.
EZE 33:19 Naye mtu mwovu akigeuka kutoka uovu wake na kufanya lile lililo haki na sawa, kwa kufanya hivyo ataishi.
EZE 33:20 Lakini, ee nyumba ya Israeli, unasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini nitamhukumu kila mmoja wenu sawasawa na njia zake mwenyewe.”
EZE 33:21 Mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mwezi wa kumi, siku ya tano, mtu aliyekuwa ametoroka kutoka Yerusalemu akanijia na kusema, “Mji wa Yerusalemu umeanguka!”
EZE 33:22 Basi jioni kabla mtu huyo hajaja, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yangu, naye alifungua kinywa changu kabla ya mtu yule aliyenijia asubuhi hajafika. Basi kinywa changu kilifunguliwa na sikuweza tena kunyamaza.
EZE 33:23 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 33:24 “Mwanadamu, watu wanaoishi katika magofu hayo katika nchi ya Israeli wanasema hivi, ‘Ibrahimu alikuwa mtu mmoja tu, hata hivyo akaimiliki nchi. Lakini sisi ni wengi, hakika tumepewa nchi kuwa milki yetu.’
EZE 33:25 Kwa hiyo waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa mnakula nyama ikiwa na damu, na kuinulia sanamu zenu macho na kumwaga damu, je, mtaimiliki nchi?
EZE 33:26 Mnategemea panga zenu, mnafanya mambo ya machukizo na kila mmoja wenu humnajisi mke wa jirani yake. Je, mtaimiliki nchi?’
EZE 33:27 “Waambie hivi: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakika kama niishivyo, wale waliobaki katika magofu wataanguka kwa upanga, wale walio nje mashambani nitawatoa wararuliwe na wanyama pori, nao wale walio katika ngome na kwenye mapango watakufa kwa tauni.
EZE 33:28 Nitaifanya nchi ukiwa, na kiburi cha nguvu zake kitafikia mwisho, nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa ili mtu yeyote asipite huko.
EZE 33:29 Kisha watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapokuwa nimeifanya nchi ukiwa kwa sababu ya mambo yote ya machukizo waliyotenda.’
EZE 33:30 “Kwako wewe, mwanadamu, watu wako wanaongea habari zako wakiwa karibu na kuta na kwenye milango ya nyumba, wakiambiana kila mmoja na mwenzake, ‘Njooni msikie ujumbe ule unaotoka kwa Mwenyezi Mungu.’
EZE 33:31 Watu wangu wanakujia, kama wafanyavyo, nao wanaketi mbele yako kama watu wangu na kusikiliza maneno yako, lakini hawayatendi. Kwa maana udanganyifu u katika midomo yao, lakini mioyo yao ina tamaa ya faida isiyo halali.
EZE 33:32 Naam, mbele yao umekuwa tu kama yeye aimbaye nyimbo za mapenzi kwa sauti nzuri za kuvutia na kupiga vyombo kwa ustadi, kwa kuwa wanasikia maneno yako lakini hawayatendi.
EZE 33:33 “Mambo haya yote yatakapotimia, kwa kuwa hakika yatatokea, ndipo watajua kuwa nabii amekuwa miongoni mwao.”
EZE 34:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 34:2 “Mwanadamu, tabiri dhidi ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole kwa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo?
EZE 34:3 Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi.
EZE 34:4 Hamkuwatia nguvu walio dhaifu, wala kuwaganga wenye maradhi, wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili.
EZE 34:5 Hivyo walitawanyika kwa sababu hapakuwa na mchungaji, nao walipotawanyika, wakawa chakula cha wanyama mwitu wote.
EZE 34:6 Kondoo wangu walitangatanga kwenye milima yote na kwenye kila kilima kirefu. Kondoo wangu walitawanyika duniani kote, bila yeyote wa kuwaulizia wala kuwatafuta.
EZE 34:7 “ ‘Kwa hiyo, ninyi wachungaji, lisikieni neno la Mwenyezi Mungu:
EZE 34:8 Kwa hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, kwa sababu kondoo wangu wamekosa mchungaji na hivyo wametekwa nyara na kuwa chakula cha wanyama pori wote na kwa sababu wachungaji wangu, hawakuwatafuta kondoo wangu, bali wachungaji wamejitunza wenyewe, nao hawakuwalisha kondoo wangu,
EZE 34:9 kwa hiyo enyi wachungaji, sikieni neno la Mwenyezi Mungu:
EZE 34:10 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi ni kinyume na wachungaji, nami nitawadai kondoo wangu mikononi mwao. Nitawafukuza kutoka kuchunga kundi langu, ili wachungaji wasiendelee kujitunza wenyewe. Nitaokoa kondoo wangu kutoka vinywa vyao, nao kondoo hawatakuwa tena chakula chao.
EZE 34:11 “ ‘Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi mwenyewe nitawaulizia kondoo wangu na kuwatafuta.
EZE 34:12 Kama vile mchungaji atafutavyo kundi lake lililotawanyika wakati akiwa pamoja nalo, hivyo ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawaokoa kutoka mahali pote walipokuwa wametawanyikia katika siku ya mawingu na giza nene.
EZE 34:13 Nitawatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mbalimbali, nami nitawaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawalisha kwenye milima ya Israeli, katika mabonde na pia mahali pote panapokaliwa katika nchi.
EZE 34:14 Nitawachunga kwenye malisho mazuri na miinuko ya mlima wa Israeli patakuwa mahali pao pa malisho. Huko watajipumzisha katika nchi ya malisho mazuri, nao watajilisha huko katika malisho tele katika milima ya Israeli.
EZE 34:15 Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo wangu na kuwafanya wapumzike, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 34:16 Nitawaulizia kondoo waliopotea na kuwaleta waliotangatanga. Nitawafunga waliojeruhiwa na kuwatia nguvu walio dhaifu, lakini wale walionona na wenye nguvu nitawaangamiza. Nitalichunga kundi kwa haki.
EZE 34:17 “ ‘Kwenu ninyi, kundi langu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo, kati ya kondoo dume na mbuzi.
EZE 34:18 Je, haiwatoshi ninyi kujilisha kwenye malisho mazuri? Je, ni lazima ninyi kuyakanyaga pia malisho yenu yaliyobaki kwa miguu yenu? Je, haiwatoshi ninyi kunywa maji safi? Je, ni lazima kuyachafua maji mengine kwa miguu yenu?
EZE 34:19 Je, ni lazima kundi langu wajilishe kwa yale mliyoyakanyaga na kunywa maji mliyoyachafua kwa miguu yenu?
EZE 34:20 “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi awaambialo: Tazama, mimi mwenyewe nitahukumu kati ya kondoo wanono na waliokonda.
EZE 34:21 Kwa sababu mmewapiga kikumbo na kuwapiga kwa pembe zenu kondoo wote walio dhaifu hadi wakawafukuza,
EZE 34:22 nitaliokoa kundi langu na hawatatekwa nyara tena. Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo.
EZE 34:23 Nitaweka juu yao mchungaji mmoja, mtumishi wangu Daudi, naye atawachunga, atawachunga na kuwa mchungaji wao.
EZE 34:24 Mimi Mwenyezi Mungu nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu miongoni mwao. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena.
EZE 34:25 “ ‘Nitafanya nao agano la amani na kuwaondoa wanyama mwitu kutoka nchi yao ili kondoo wangu waweze kupumzika nyikani na msituni kwa salama.
EZE 34:26 Nitawabariki wao pamoja na maeneo yanayozunguka kilima changu. Nitawanyeshea mvua kwa majira yake, kutakuwa na mvua za baraka.
EZE 34:27 Miti ya shambani itatoa matunda yake na ardhi itatoa mazao yake, watu watakaa salama katika nchi yao. Watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapovunja vifungo vya nira zao na kuwaokoa kutoka mikono ya wale waliowafanya watumwa.
EZE 34:28 Hawatatekwa tena nyara na mataifa, wala wanyama pori kuwala tena. Wataishi kwa salama, wala hakuna yeyote atakayewatia hofu.
EZE 34:29 Nitawapa nchi yenye sifa kutokana na mazao yake, na hawatapatwa na njaa katika nchi tena, wala kudharauliwa na mataifa.
EZE 34:30 Ndipo watajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wao, niko pamoja nao, na kwamba wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 34:31 Ninyi ni kondoo wangu, kondoo wa malisho yangu; ninyi ni watu wangu, nami ni Mungu wenu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 35:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 35:2 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Mlima Seiri, utabiri dhidi yake
EZE 35:3 na useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi ni kinyume nawe, ee Mlima Seiri, nami nitanyoosha mkono wangu dhidi yako na kukufanya ukiwa.
EZE 35:4 Nitaifanya miji yako kuwa magofu nawe utakuwa ukiwa. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 35:5 “ ‘Kwa sababu ulificha moyoni uadui wa siku nyingi nawe ukawatoa Waisraeli wauawe kwa upanga wakati wa maafa yao, wakati adhabu yake ilipofikia kilele chake,
EZE 35:6 kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitakutia katika umwagaji damu nao utakufuatia. Kwa kuwa hukuchukia kumwaga damu, kumwaga damu kutakufuatia.
EZE 35:7 Nitaufanya Mlima Seiri ukiwa na kuukatilia mbali na wote wanaokuja na wanaoenda.
EZE 35:8 Nitaijaza milima yenu kwa watu wake waliouawa, wale waliouawa kwa upanga wataanguka juu ya vilima vyako na katika mabonde yako na katika makorongo yako yote.
EZE 35:9 Nitakufanya ukiwa milele, watu hawataishi katika miji yako. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 35:10 “ ‘Kwa sababu umesema, “Mataifa haya mawili na nchi hizi zitakuwa zetu nasi tutazimiliki,” ingawa hata Mimi Mwenyezi Mungu nilikuwa huko,
EZE 35:11 kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitakutenda kwa kadiri ya hasira na wivu uliouonesha katika chuki yako juu yao nami nitafanya nijulikane miongoni mwao wakati nitakapokuhukumu.
EZE 35:12 Ndipo utakapojua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimesikia mambo yote ya dharau uliyosema dhidi ya milima ya Israeli. Ulisema, “Wamefanyika ukiwa na kutiwa mikononi mwetu tuwararue.”
EZE 35:13 Ulijigamba dhidi yangu na kusema maneno dhidi yangu bila kujizuia, nami nikayasikia.
EZE 35:14 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Dunia yote inaposhangilia, nitakufanya ukiwa.
EZE 35:15 Kwa sababu ulishangilia wakati urithi wa nyumba ya Israeli ulipofanyika ukiwa, hivyo ndivyo nitakavyokutendea. Utakuwa ukiwa, ee Mlima Seiri, wewe na Edomu yote. Kisha ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 36:1 “Mwanadamu, itabirie milima ya Israeli na useme, ‘Ee milima ya Israeli, sikieni neno la Mwenyezi Mungu.
EZE 36:2 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Adui alisema kuwahusu, “Aha! Mahali palipoinuka pa zamani pamekuwa milki yetu.” ’
EZE 36:3 Kwa hiyo tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu wamewafanya ukiwa na kuwagandamiza kila upande ili mpate kuwa milki ya mataifa mengine, na mpate kuwa kitu cha kusimangwa na kudhihakiwa na watu;
EZE 36:4 kwa hiyo, ee milima ya Israeli, sikieni neno la Bwana Mungu Mwenyezi: Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa milima na vilima, kwa makorongo na mabonde, kwa mahame yaliyo ukiwa, miji iliyoachwa ambayo imetekwa nyara na kudharauliwa na mataifa mengine yanayowazunguka,
EZE 36:5 hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika wivu wangu uwakao nimenena dhidi ya mataifa mengine na dhidi ya Edomu yote, kwa maana kwa furaha na hila katika mioyo yao waliifanya nchi yangu kuwa milki yao ili wapate kuteka nyara sehemu yake ya malisho.’
EZE 36:6 Kwa hiyo tabiri kuhusu nchi ya Israeli na uiambie milima na vilima, makorongo na vijito na mabonde: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninanena katika wivu wa ghadhabu yangu kwa sababu mmedharauliwa na mataifa.
EZE 36:7 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninaapa kwa mkono wangu ulioinuliwa kwamba mataifa wanaowazunguka nao pia watadharauliwa.
EZE 36:8 “ ‘Lakini ninyi, ee milima ya Israeli, mtatoa matawi na matunda kwa ajili ya watu wangu Israeli, kwa sababu hivi karibuni watakuja nyumbani.
EZE 36:9 Mimi ninawajibika nanyi na nitawaangalia kwa upendeleo, mtalimwa na kupandwa mbegu,
EZE 36:10 nami nitaizidisha idadi ya watu kwenu, naam, nyumba yote ya Israeli. Miji itakaliwa na watu na magofu yatajengwa upya.
EZE 36:11 Nitaongeza idadi ya watu na wanyama juu yenu, nao watazaana sana na kuwa wengi mno. Nitawakalisha watu ndani yenu kama ilivyokuwa wakati uliopita, nami nitawafanya mfanikiwe kuliko mbeleni. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 36:12 Nitawafanya watu, watu wangu Israeli, kuishi juu yenu. Watawamiliki ninyi, nanyi mtakuwa urithi wao; hamtawaondolea tena watoto wao.
EZE 36:13 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu watu wanakuambia, “Unawala watu na kuliondolea taifa lako watoto wake,”
EZE 36:14 kwa hiyo hutakula tena watu wala kulifanya tena taifa lako lisiwe na watoto, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 36:15 Sitakufanya tena usikie dhihaka za mataifa, wala kudharauliwa na makabila ya watu, wala kulifanya taifa lako lianguke, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
EZE 36:16 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia tena, kusema:
EZE 36:17 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokuwa wakiishi katika nchi yao wenyewe, waliinajisi kwa mwenendo wao na matendo yao. Mwenendo wao mbele zangu ulikuwa kama mwanamke aliye katika hedhi.
EZE 36:18 Hivyo nilimwaga ghadhabu yangu juu yao kwa sababu walikuwa wamemwaga damu katika nchi na kwa sababu walikuwa wameitia nchi unajisi kwa sanamu zao.
EZE 36:19 Nikawatawanya miongoni mwa mataifa, nao wakatapanywa katika nchi mbalimbali; nikawahukumu kulingana na mwenendo wao na matendo yao.
EZE 36:20 Tena popote walipoenda miongoni mwa mataifa walilinajisi Jina langu takatifu, kwa kuwa watu walisema kuwahusu, ‘Hawa ndio watu wa Mwenyezi Mungu, lakini imewapasa kuondoka katika nchi yake.’
EZE 36:21 Lakini niliwahurumia kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli imelitia unajisi miongoni mwa mataifa huko walikoenda.
EZE 36:22 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Si kwa ajili yako, ee nyumba ya Israeli, kwamba ninafanya mambo haya, bali ni kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo mmelitia unajisi miongoni mwa mataifa mliyoyaendea.
EZE 36:23 Nitauonesha utakatifu wa Jina langu kuu, ambalo limetiwa unajisi miongoni mwa mataifa, jina ambalo limetiwa unajisi miongoni mwao. Ndipo mataifa watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitakapojionesha mwenyewe kuwa mtakatifu kupitia kwenu mbele ya macho yao.
EZE 36:24 “ ‘Kwa kuwa nitawaondoa ninyi toka mataifa, nitawakusanya kutoka nchi zote na kuwarejesha nchi yenu wenyewe.
EZE 36:25 Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakasa kutoka uchafu wenu wote na kutoka sanamu zenu zote.
EZE 36:26 Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama.
EZE 36:27 Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu.
EZE 36:28 Mtaishi katika nchi niliyowapa baba zenu, ninyi mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu.
EZE 36:29 Nitawaokoa ninyi kutoka unajisi wenu wote. Nitaiita nafaka na kuiongeza iwe nyingi sana nami sitaleta njaa juu yenu.
EZE 36:30 Nitaongeza matunda ya miti na mazao ya mashamba, ili msipate tena aibu miongoni mwa mataifa kwa ajili ya njaa.
EZE 36:31 Ndipo mtakapozikumbuka njia zenu za uovu na matendo yenu maovu, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya dhambi zote na matendo yenu ya kuchukiza.
EZE 36:32 Ninataka ninyi mjue kwamba sifanyi hili kwa ajili yenu, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Oneni aibu na mkatahayari kwa ajili ya mwenendo wenu, ee nyumba ya Israeli!
EZE 36:33 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Siku ile nitakapowasafisha kutoka dhambi zenu zote, nitarudisha watu waishi katika miji yenu na magofu yatajengwa upya.
EZE 36:34 Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa badala ya kukaa ukiwa machoni mwa wale wote wanaopita ndani yake.
EZE 36:35 Watasema, “Hii nchi iliyokuwa imeachwa ukiwa sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, miji ile iliyokuwa magofu, ukiwa na kuangamizwa, sasa imejengewa ngome na kukaliwa na watu.”
EZE 36:36 Ndipo mataifa yanayowazunguka yaliyobakia watajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimejenga tena kile kilichoharibiwa, na nimepanda tena kile kilichokuwa ukiwa. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena, nami nitalifanya.’
EZE 36:37 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mara nyingine tena nitasikia maombi ya nyumba ya Israeli na kuwatendea jambo hili: Nitawafanya watu wake kuwa wengi kama kondoo,
EZE 36:38 kuwa wengi kama kundi la kondoo kwa ajili ya dhabihu huko Yerusalemu wakati wa sikukuu zao za wakati ulioamriwa. Hivyo ndivyo miji iliyokuwa magofu itajazwa na makundi ya watu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
EZE 37:1 Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yangu, naye akanitoa nje kwa Roho wa Mwenyezi Mungu na kuniweka katikati ya bonde lililokuwa limejaa mifupa tele.
EZE 37:2 Akanipitisha pande zote kwenye hiyo mifupa, nami nikaona mifupa mingi sana ndani ya lile bonde, mifupa iliyokuwa imekauka sana.
EZE 37:3 Akaniuliza, “Mwanadamu, mifupa hii yaweza kuishi?” Nikajibu, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, wewe peke yako unajua.”
EZE 37:4 Ndipo akaniambia, “Itabirie mifupa hii na uiambie, ‘Enyi mifupa mikavu, sikieni neno la Mwenyezi Mungu!
EZE 37:5 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa hii mifupa: Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.
EZE 37:6 Nitawawekea mishipa, nami nitaifanya nyama ije juu yenu na kuwafunika kwa ngozi. Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtakuwa hai. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
EZE 37:7 Basi nikatabiri kama nilivyoamriwa. Nilipokuwa nikitabiri, kukawa na sauti, sauti ya kugongana, nayo mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.
EZE 37:8 Nikatazama: mishipa na nyama vikatokea juu ya mifupa na ngozi ikaifunika, lakini haikuwa na pumzi ndani yake.
EZE 37:9 Ndipo aliponiambia, “Utabirie pumzi; tabiri, mwanadamu na uiambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Njoo kutoka pande nne za pepo, ee pumzi, nawe upulizie pumzi ndani ya hawa waliouawa, ili wapate kuishi.’ ”
EZE 37:10 Hivyo nikatabiri kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikawaingia, wakawa hai na wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
EZE 37:11 Ndipo akaniambia: “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli. Nao wanasema, ‘Mifupa yetu imekauka na tumaini letu limetoweka, tumekatiliwa mbali.’
EZE 37:12 Hivyo watabirie na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwatoa ndani yake, nami nitawarudisha tena katika nchi ya Israeli.
EZE 37:13 Ndipo ninyi watu wangu, mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa humo.
EZE 37:14 Nitatia Roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi; nami nitawakalisha katika nchi yenu wenyewe. Ndipo mtajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimenena, nami nitalitenda, asema Mwenyezi Mungu!’ ”
EZE 37:15 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 37:16 “Mwanadamu, chukua fimbo na uandike juu yake, ‘Hii ni kwa ajili ya Yuda na Waisraeli waliofungamana naye.’ Kisha chukua fimbo nyingine, uandike juu yake, ‘Fimbo ya Efraimu, ni kwa ajili ya Yusufu na nyumba yote ya Israeli wanaofungamana naye.’
EZE 37:17 Ziunganishe pamoja kuwa fimbo moja ili ziwe fimbo moja katika mkono wako.
EZE 37:18 “Watu wako watakapokuuliza, ‘Je, hutatuambia ni nini maana ya jambo hili?’
EZE 37:19 Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaichukua fimbo ya Yusufu iliyo mkononi mwa Efraimu, na ya makabila ya Israeli yanayofungamana naye, na kuiunganisha na fimbo ya Yuda, nikizifanya kuwa fimbo moja, nao watakuwa mmoja katika mkono wangu.’
EZE 37:20 Inua mbele ya macho yao zile fimbo ulizoziandika
EZE 37:21 kisha waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitawatoa Waisraeli katika mataifa walikokuwa wameenda. Nitawakusanya popote walipo na kuwarudisha katika nchi yao wenyewe.
EZE 37:22 Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi, katika milima ya Israeli. Patakuwa na mfalme mmoja juu yao wote na kamwe hawatagawanyika tena kuwa mataifa mawili au kugawanyika katika falme mbili.
EZE 37:23 Hawatajitia tena unajisi kwa sanamu zao, au vinyago vyao vinavyochukiza, wala kwa makosa yao yoyote, kwa maana nitawaokoa kutoka dhambi zao zote zilizowarudisha nyuma, nami nitawatakasa. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
EZE 37:24 “ ‘Mtumishi wangu Daudi atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja. Watafuata sheria zangu na kuzishika amri zangu kwa uangalifu.
EZE 37:25 Wataishi katika nchi niliyompa mtumishi wangu Yakobo, nchi ambamo baba zenu waliishi. Wao na watoto wao na watoto wa watoto wao wataishi humo milele, naye Daudi mtumishi wangu atakuwa mkuu wao milele.
EZE 37:26 Nitafanya agano la amani nao; litakuwa agano la milele. Nitawafanya imara na kuongeza idadi yao, nami nitaweka mahali patakatifu pangu miongoni mwao milele.
EZE 37:27 Maskani yangu yatakuwa pamoja nao, nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
EZE 37:28 Ndipo mataifa watajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ndiye ninayeifanya Israeli kuwa takatifu, wakati mahali patakatifu pangu patakuwa miongoni mwao milele.’ ”
EZE 38:1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
EZE 38:2 “Mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya Gogu, katika nchi ya Magogu, mtawala mkuu wa Mesheki na Tubali; tabiri dhidi yake
EZE 38:3 na useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ee Gogu, mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali.
EZE 38:4 Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukutia ndoana kwenye mataya yako na kukutoa nje wewe pamoja na jeshi lako lote, yaani farasi wako, wapanda farasi wako waliojiandaa tayari kwa vita, pamoja na kundi kubwa la wajeuri wakiwa na ngao na vigao, wote wakipunga panga zao.
EZE 38:5 Uajemi, Kushi na Putu watakuwa pamoja nao, wote wakiwa na ngao na chapeo,
EZE 38:6 pia Gomeri pamoja na vikosi vyake vyote, na Beth-Togarma kutoka kaskazini ya mbali pamoja na vikosi vyake vyote, mataifa mengi wakiwa pamoja nawe.
EZE 38:7 “ ‘Jiandae, uwe tayari, wewe na makundi yako yote waliokusanyika pamoja nawe, nawe waamrishe.
EZE 38:8 Baada ya siku nyingi utaitwa vitani. Katika miaka ijayo, utaivamia nchi ambayo imepona kutoka vita, na watu wake walikusanywa kutoka mataifa mengi waje katika milima ya Israeli, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imeachwa ukiwa. Wameletwa kutoka mataifa na sasa wote wanaishi katika hali ya salama.
EZE 38:9 Wewe na vikosi vyako vyote na mataifa mengi yaliyo pamoja nawe mtapanda juu, mtawazoa kama tufani na kuifunika nchi kama wingu.
EZE 38:10 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika siku ile mawazo yataingia moyoni mwako nawe utapanga mipango mibaya.
EZE 38:11 Utasema, “Nitapigana vita na nchi ambayo vijiji vyake havina kuna. Nitawashambulia watu wanaoishi kwa amani na wasiotarajia vita: wote wanaishi bila kuta na bila malango na makomeo.
EZE 38:12 Nitateka mateka na kuchukua nyara mali ya wale waliorudi kuishi katika mahame na wale watu waliokusanywa kutoka kwa mataifa, ambao sasa wana mifugo na mali nyingi, wanaoishi katikati ya nchi.”
EZE 38:13 Sheba na Dedani, pamoja na wafanyabiashara wa Tarshishi na vijiji vyake vyote watakuambia, “Je, umekuja kuteka mateka? Je, umekusanya makundi yako ili kuchukua nyara, kutwaa fedha na dhahabu, kutunyang’anya mifugo na mali, na kuteka nyara nyingi zaidi?” ’
EZE 38:14 “Kwa hiyo, mwanadamu, tabiri na umwambie Gogu: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika siku ile, watu wangu Israeli watakapokuwa wanaishi salama, Je, wewe mwenyewe hutalijua hilo?
EZE 38:15 Utakuja kutoka kwako huko kaskazini ya mbali, ukiwa pamoja na mataifa mengi, wote wakiwa wamepanda farasi, kundi kubwa, jeshi kuu.
EZE 38:16 Utakuja dhidi ya watu wangu Israeli kama wingu lifunikavyo nchi. Siku zijazo, ee Gogu, nitakuleta wewe dhidi ya nchi yangu, ili mataifa wapate kunijua Mimi nitakapojionesha mtakatifu kupitia kwako mbele ya macho yao.
EZE 38:17 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Wewe ni yule niliyenena juu yake siku za zamani kupitia kwa watumishi wangu manabii wa Israeli. Wakati ule walitabiri kwa miaka mingi kwamba ningekuleta upigane nao.
EZE 38:18 Hili ndilo litakalotokea katika siku ile: Gogu atakaposhambulia nchi ya Israeli, hasira yangu kali itaamka, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 38:19 Katika wivu wangu na ghadhabu yangu kali, ninasema kuwa wakati ule kutakuwa na tetemeko kuu katika nchi ya Israeli.
EZE 38:20 Samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kondeni, kila kiumbe kinachotambaa ardhini, na watu wote walio duniani kote watatetemeka mbele zangu. Milima itapinduka, majabali yatapasuka na kila ukuta utaanguka chini.
EZE 38:21 Nitaita upanga wa vita dhidi ya Gogu juu ya milima yangu yote, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Upanga wa kila mtu utakuwa dhidi ya ndugu yake.
EZE 38:22 Nitatekeleza hukumu juu yake kwa tauni na kwa umwagaji wa damu. Nitaifanya mvua ya mafuriko kunyesha, mvua ya mawe na moto wa kiberiti juu yake na juu ya vikosi vyake na juu ya mataifa mengi walio pamoja naye.
EZE 38:23 Nami hivyo ndivyo nitakavyoonesha ukuu wangu na utakatifu wangu, nami nitajijulisha mbele ya macho ya mataifa mengi. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’
EZE 39:1 “Mwanadamu, tabiri dhidi ya Gogu useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ee Gogu mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali.
EZE 39:2 Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukuburuta. Nitakuleta kutoka kaskazini ya mbali na kukupeleka wewe dhidi ya milima ya Israeli.
EZE 39:3 Kisha nitaupiga upinde wako kutoka mkono wako wa kushoto na kuifanya mishale ianguke kutoka mkono wako wa kuume.
EZE 39:4 Utaanguka kwenye milima ya Israeli, wewe pamoja na vikosi vyako vyote na yale mataifa yaliyo pamoja nawe. Nitakutoa uwe chakula cha ndege wa aina zote walao nyama na cha wanyama pori.
EZE 39:5 Utaanguka katika uwanja, kwa kuwa nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 39:6 Nitatuma moto juu ya Magogu na kwa wale wanaoishi kwa salama huko pwani, nao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
EZE 39:7 “ ‘Nitalifanya Jina langu takatifu lijulikane miongoni mwa watu wangu Israeli. Sitaliacha tena Jina langu takatifu litiwe unajisi, nayo mataifa watajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ndimi Aliye Mtakatifu wa Israeli.
EZE 39:8 Hili jambo linakuja! Hakika litatendeka, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Hii ndiyo siku ile niliyosema habari zake.
EZE 39:9 “ ‘Ndipo wale wanaoishi katika miji ya Israeli watakapotoka na kutumia hizo silaha kuwashia moto na kuziteketeza, yaani kigao na ngao, pinde na mishale, rungu za vita na mikuki. Kwa miaka saba watavitumia kama kuni.
EZE 39:10 Hawatahitaji kukusanya kuni kutoka mashambani wala kukata kuni kwenye misitu, kwa sababu watatumia silaha kuwa kuni. Nao watawateka mateka wale waliowateka na kuchukua nyara mali ya wale waliochukua mali yao nyara, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 39:11 “ ‘Siku ile nitampa Gogu mahali pa kuzikia katika Israeli, katika bonde la wale wasafirio upande wa mashariki mwa Bahari. Jambo hili litazuia njia ya wasafiri kwa sababu Gogu na makundi yake yote watazikwa huko. Kwa hiyo litaitwa Bonde la Hamon-Gogu.
EZE 39:12 “ ‘Kwa miezi saba nyumba ya Israeli itakuwa ikiwazika ili kuisafisha nchi.
EZE 39:13 Watu wote wa nchi watawazika, nayo siku nitakayotukuzwa itakuwa siku ya kumbukumbu kwa ajili yao, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 39:14 “ ‘Watu wataajiriwa mara kwa mara kuisafisha nchi. Baadhi yao watapita nchini kote, na, wakiwa na wengine, watawazika wale waliosalia juu ya ardhi. Mwisho wa hiyo miezi saba wataanza upekuzi wao.
EZE 39:15 Wanapopita nchini kote, na mmoja wao akaona mfupa wa mwanadamu, ataweka alama kando yake hadi wachimba kaburi wauzike katika Bonde la Hamon-Gogu.
EZE 39:16 (Pia mji uitwao Hamona utakuwa humo.) Hivyo ndivyo watakavyoisafisha nchi.’
EZE 39:17 “Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ita kila aina ya ndege na wanyama pori wote, waambie: ‘Kusanyikeni mje pamoja kutoka pande zote kwa ajili ya dhabihu ninayowaandalia, dhabihu kuu katika milima ya Israeli. Huko mtakula nyama na kunywa damu.
EZE 39:18 Mtakula nyama za watu mashujaa na kunywa damu za wakuu wa dunia kana kwamba ni za kondoo dume na kondoo wake, mbuzi na mafahali, wote walionona kutoka Bashani.
EZE 39:19 Katika dhabihu ninayoandaa kwa ajili yenu, mtakula mafuta hadi mshibe, na kunywa damu hadi mlewe.
EZE 39:20 Kwenye meza yangu watajishibisha kwa farasi na wapanda farasi, watu mashujaa na askari wa kila aina,’ asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 39:21 “Nitauonesha utukufu wangu miongoni mwa mataifa, nayo mataifa yote wataiona adhabu nitakayotoa na mkono wangu nitakaouweka juu yao.
EZE 39:22 Kuanzia siku ile na kuendelea nyumba ya Israeli itajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
EZE 39:23 Na mataifa watajua kuwa nyumba ya Israeli walienda utumwani kwa ajili ya dhambi yao, kwa sababu hawakuwa waaminifu kwangu. Hivyo niliwaficha uso wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao, nao wote wakaanguka kwa upanga.
EZE 39:24 Niliwatendea sawasawa na uchafu wao na makosa yao, nami nikawaficha uso wangu.
EZE 39:25 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Sasa nitamrudisha Yakobo kutoka utumwani, nami nitawahurumia watu wote wa Israeli, nami nitakuwa na wivu kwa ajili ya Jina langu takatifu.
EZE 39:26 Wataisahau aibu yao na jinsi walivyoonesha kutokuwa waaminifu kwangu mimi wakati waliishi salama katika nchi yao, bila kuwa na mtu yeyote wa kuwatia hofu.
EZE 39:27 Nitakapokuwa nimewarudisha kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi za adui zao, mimi nitajionesha kuwa mtakatifu kupitia kwao machoni mwa mataifa mengi.
EZE 39:28 Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao, ingawa niliwapeleka uhamishoni miongoni mwa mataifa, nitawakusanya tena katika nchi yao wenyewe, bila kumwacha yeyote nyuma.
EZE 39:29 Sitawaficha tena uso wangu, kwa maana nitamimina Roho wangu Mtakatifu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 40:1 Katika mwaka wa ishirini na tano wa uhamisho wetu, mwanzoni mwa huo mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kuanguka kwa mji, siku hiyo hiyo mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yangu, naye akanipeleka huko.
EZE 40:2 Nikiwa katika maono ya Mungu alinichukua hadi nchi ya Israeli, naye akaniweka kwenye mlima mrefu sana, ambako upande wa kusini kulikuwa na baadhi ya majengo ambayo yalionekana kama mji.
EZE 40:3 Akanipeleka huko, nami nikamwona mtu ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba. Alikuwa amesimama kwenye lango akiwa na kamba ya kitani na ufito wa kupimia mkononi mwake.
EZE 40:4 Mtu huyo akaniambia, “Mwanadamu, fungua macho yako uone, na utege masikio yako usikie, nawe uzingatie yote nitakayokuonesha, kwa kuwa ndiyo sababu umeletwa hapa. Iambie nyumba ya Israeli kila kitu utakachoona.”
EZE 40:5 Nikaona ukuta uliozunguka eneo lote la Hekalu. Ule ufito wa kupimia uliokuwa mkononi mwa yule mtu ulikuwa na urefu wa dhiraa ndefu sita, dhiraa ndefu ikiwa sawa na dhiraa na nyanda nne. Akaupima ule ukuta; ulikuwa na unene wa dhiraa ndefu sita, na kimo cha dhiraa ndefu sita.
EZE 40:6 Kisha akaenda kwenye lango linaloelekea mashariki. Akapanda ngazi zake akapima kizingiti cha lango, nacho kilikuwa na kina cha huo ufito.
EZE 40:7 Vyumba vya kupumzikia vya walinzi vilikuwa na urefu wa huo ufito mmoja na upana wa huo ufito, kuta zilizochomoza kati ya vyumba hivyo vya mapumziko zilikuwa na unene wa dhiraa tano. Nacho kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi unaoelekea hekaluni kilikuwa na kina cha huo ufito.
EZE 40:8 Kisha akapima baraza ya njia ya lango,
EZE 40:9 ambayo ilikuwa na kina cha dhiraa nane na miimo yake ilikuwa na unene wa dhiraa mbili. Baraza ya lango ilielekea Hekalu.
EZE 40:10 Ndani ya lango la mashariki kulikuwepo vyumba vitatu vya kupumzikia kila upande; vyote vitatu vilikuwa na vipimo vilivyo sawa, nazo nyuso za kuta zilizochomoza kila upande zilikuwa na vipimo vilivyo sawa.
EZE 40:11 Kisha akapima upana wa ingilio la lango, ilikuwa dhiraa kumi, na urefu wake ulikuwa dhiraa kumi na tatu.
EZE 40:12 Mbele ya kila chumba cha kupumzikia kulikuwa na ukuta uliokuwa na kimo cha dhiraa moja kwenda juu, navyo hivyo vyumba vilikuwa dhiraa sita mraba.
EZE 40:13 Kisha akapima njia ya lango kuanzia juu ya ukuta wa nyuma wa chumba kimoja cha kupumzikia hadi juu ya ukuta wa nyuma wa chumba upande wa pili; kukawa na nafasi ya dhiraa ishirini na tano kuanzia lango la ukuta mmoja hadi lango la ukuta uliokuwa upande mwingine.
EZE 40:14 Akapima pande za mbele za hizo kuta zilizochomoza kuzunguka hadi ndani ya ingilio. Urefu wake ulikuwa dhiraa sitini. Kipimo kilikuwa hadi baraza iliyoangaliana na ua.
EZE 40:15 Umbali kuanzia ingilio la njia ya lango hadi mwisho kabisa wa baraza yake ulikuwa dhiraa hamsini.
EZE 40:16 Kulikuwa na vidirisha kwenye hivyo vyumba vya walinzi, na nguzo za hivyo vyumba zilikuwa kwenye mzunguko wa hilo lango; vivyo hivyo kulikuwa na madirisha yaliyozunguka kuelekeana na ua. Juu ya kila nguzo kulikuwa na nakshi za mitende.
EZE 40:17 Kisha akanileta katika ukumbi wa nje. Huko nikaona vyumba vingine pamoja na njia iliyokuwa imejengwa kuzunguka ukumbi wote, kulikuwa na vyumba thelathini vimepangana kando ya hiyo njia.
EZE 40:18 Njia hii iliyojengwa iliambaa na lango, ikiwa na urefu sawa na lango; hii ilikuwa ni njia ya chini.
EZE 40:19 Kisha akapima umbali kutoka ndani ya lango la chini mpaka nje ya ukumbi wa ndani, nao ulikuwa dhiraa mia moja upande wa mashariki na dhiraa mia moja upande wa kaskazini.
EZE 40:20 Kisha akapima urefu na upana wa lango linaloelekea kaskazini, kukabili ukumbi wa nje.
EZE 40:21 Vyumba vyake vilikuwa vitatu kila upande, kuta zilizochomoza kati ya vyumba na baraza zilikuwa na vipimo sawa na zile kuta za lango la kwanza. Zilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano.
EZE 40:22 Madirisha yake, baraza yake na nakshi yake ya mitende vilikuwa na vipimo sawasawa na vile vya lango linaloelekea mashariki. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo.
EZE 40:23 Kulikuwa na lango kwenye ukumbi wa ndani lililoelekea lile lango la kaskazini, kama vile ilivyokuwa ule upande wa mashariki. Akapima kutoka lango moja hadi lile lililo mkabala nalo, lilikuwa dhiraa mia moja.
EZE 40:24 Ndipo akaniongoza mpaka upande wa kusini, nami nikaona lango linaloelekea kusini. Akaipima miimo yake na baraza yake, navyo vilikuwa na vipimo sawa kama hivyo vingine.
EZE 40:25 Lango na baraza yake vilikuwa na madirisha membamba pande zote, kama madirisha ya huko kwingine. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano.
EZE 40:26 Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo. Ilikuwa na nakshi za mitende kwenye kuta zilizochomoza kati ya vyumba kila upande.
EZE 40:27 Ukumbi wa ndani pia ulikuwa na lango lililoelekea kusini. Naye akapima kutoka lango hili hadi kwenye lango la nje upande wa kusini; ilikuwa dhiraa mia moja.
EZE 40:28 Kisha akanileta mpaka ukumbi wa ndani kupitia lango la kusini, naye akapima lango la kusini, ambalo lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine.
EZE 40:29 Vyumba vyake, kuta zilizochomoza kati ya vyumba, na ukumbi wake vyote vilikuwa na vipimo sawa na vile vingine. Hilo lango na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Navyo vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano.
EZE 40:30 (Baraza za malango zilizozunguka ukumbi wa ndani zilikuwa na upana wa dhiraa ishirini na tano na kina cha dhiraa tano.)
EZE 40:31 Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje; miimo yake ilinakshiwa mitende, na kulikuwa na ngazi nane za kupandia.
EZE 40:32 Kisha akanileta hadi kwenye ukumbi wa ndani ulioko upande wa mashariki, naye akalipima lango hilo; lilikuwa na vipimo vilivyo sawasawa na yale mengine.
EZE 40:33 Vyumba vyake, kuta zake zilizochomoza, na baraza yake vilikuwa na vipimo sawa na vile vingine. Lile lango pamoja na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Urefu wake ulikuwa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano.
EZE 40:34 Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje; miimo yake ilinakshiwa mitende pande zote, na kulikuwa na ngazi nane za kupandia.
EZE 40:35 Kisha akanileta mpaka kwenye lango la kaskazini na kulipima. Lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine,
EZE 40:36 kama vile ilivyokuwa kwa vyumba, kuta zake na baraza yake, tena kulikuwa na madirisha pande zote. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano.
EZE 40:37 Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje; miimo yake ilinakshiwa mitende pande zote, na kulikuwa na ngazi nane za kupandia.
EZE 40:38 Kulikuwa na chumba na mlango karibu na baraza katika kila njia ya ndani ya lango ambamo sadaka za kuteketezwa zilioshwa.
EZE 40:39 Kwenye baraza ya lile lango kulikuwepo meza mbili kila upande, ambako sadaka za kuteketezwa, sadaka za dhambi na sadaka za hatia zilichinjiwa.
EZE 40:40 Karibu na ukuta wa nje wa baraza ya lile lango, karibu na ngazi kwenye ingilio kuelekea kaskazini kulikuwa na meza mbili, nao upande mwingine wa ngazi kulikuwa na meza mbili.
EZE 40:41 Kwa hiyo kulikuwa na meza nne upande mmoja wa lango na nyingine nne upande mwingine, zote zilikuwa meza nane, ambapo dhabihu zilichinjiwa.
EZE 40:42 Pia kulikuwa na meza nne za mawe yaliyochongwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, kila meza ilikuwa na urefu wa dhiraa moja na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo cha dhiraa moja. Juu ya meza hizo viliwekwa vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na dhabihu nyingine mbalimbali.
EZE 40:43 Kulikuwa na kulabu, urefu wake nyanda nne, zilizokuwa zimeshikizwa ukutani pande zote. Meza zilikuwa kwa ajili ya nyama za sadaka.
EZE 40:44 Nje ya lango la ndani, kwenye ukumbi wa ndani, kulikuwa na vyumba viwili, kimoja upande wa lango la kaskazini nacho kilielekea kusini, kingine upande wa lango la kusini nacho kilielekea kaskazini.
EZE 40:45 Akaniambia, “Chumba kinachoelekea upande wa kusini ni kwa ajili ya makuhani ambao wana usimamizi wa hekaluni,
EZE 40:46 nacho chumba kinachoelekea upande wa kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wenye usimamizi wa madhabahuni. Hawa ni wana wa Sadoki, ambao ndio Walawi pekee wanaoweza kumkaribia Mwenyezi Mungu ili kuhudumu mbele zake.”
EZE 40:47 Ndipo alipopima ukumbi: nao ulikuwa mraba wa dhiraa mia moja urefu na upana. Madhabahu yalikuwa mbele ya Hekalu.
EZE 40:48 Akanileta kwenye baraza ya Hekalu naye akaipima miimo ya hiyo baraza, nayo ilikuwa na upana wa dhiraa tatu kila upande. Upana wa ingilio ulikuwa dhiraa kumi na nne na kuta zake zilizochomoza zilikuwa na upana wa dhiraa tatu kila upande.
EZE 40:49 Baraza ilikuwa na dhiraa ishirini kwenda juu na dhiraa kumi na mbili kuanzia mbele hadi nyuma. Kulikuwa na ngazi kumi za kupandia huko, pia kulikuwa na nguzo kwa kila upande wa miimo.
EZE 41:1 Kisha yule mtu akanileta katika ukumbi mkuu, naye akaipima miimo; upana wake ulikuwa dhiraa sita kila upande.
EZE 41:2 Ingilio lilikuwa la upana wa dhiraa kumi, na kuta zilizochomoza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa tano. Pia akapima ukumbi mkuu; ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini, na upana wa dhiraa ishirini.
EZE 41:3 Kisha akaingia mahali patakatifu na kupima miimo ya ingilio, kila mmoja ulikuwa na upana wa dhiraa mbili. Ingilio lilikuwa na upana wa dhiraa sita, na kuta zilizochomoza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa saba.
EZE 41:4 Naye akapima urefu wa mahali patakatifu; ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini hadi mwisho wa sehemu ya nje ya ukumbi mkuu. Akaniambia, “Hapa ndipo Patakatifu pa Patakatifu.”
EZE 41:5 Kisha akapima ukuta wa Hekalu, nao ulikuwa na unene wa dhiraa sita, na kila chumba cha pembeni kuzunguka Hekalu kilikuwa na upana wa dhiraa nne.
EZE 41:6 Vyumba vya pembeni vilikuwa na ghorofa tatu, kimoja juu ya kingine, kila ghorofa ilikuwa na vyumba thelathini. Kulikuwa na boriti katika ukuta wote wa Hekalu ili kuimarisha vyumba vya pembeni; kwa hiyo boriti hizo hazikushikamanishwa kwenye ukuta wa Hekalu.
EZE 41:7 Vyumba vya pembeni vilivyozunguka Hekalu vilizidi kupanuka kulingana na sakafu zilivyoenda juu. Ujenzi uliozunguka Hekalu ulijengwa kukwea juu, kwa hiyo vyumba vilipanuka kwa kadiri ya kila kimoja kilivyoenda juu. Ngazi za kupandia zilianzia sakafu ya chini hadi sakafu ya juu kabisa kupitia kwa sakafu ya kati.
EZE 41:8 Nikaona kwamba Hekalu lilikuwa na kitako kilichoinuliwa pande zote; huu ukawa msingi wa vile vyumba vya pembeni. Ulikuwa na urefu wa ule ufito mmoja wa kupimia, yaani dhiraa ndefu sita.
EZE 41:9 Ukuta wa nje wa vyumba vya pembeni ulikuwa na unene wa dhiraa tano. Eneo la wazi katikati ya vyumba vya pembeni vya Hekalu
EZE 41:10 na vyumba vya makuhani lilikuwa na upana wa dhiraa ishirini kuzunguka Hekalu pande zote.
EZE 41:11 Kulikuwa na maingilio kwenye vyumba vya pembeni kutokea eneo lililo wazi, moja upande wa kaskazini na lingine upande wa kusini, nao msingi uliounganisha lile eneo la wazi ulikuwa na upana wa dhiraa tano ukilizunguka lote.
EZE 41:12 Jengo lililoelekeana na ua wa Hekalu upande wa magharibi lilikuwa na upana wa dhiraa sabini. Ukuta wa jengo hilo ulikuwa na unene wa dhiraa tano, kulizunguka lote, urefu ulikuwa wa dhiraa tisini.
EZE 41:13 Kisha akapima Hekalu; lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na ua wa Hekalu na jengo pamoja na kuta zake vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja pia.
EZE 41:14 Upana wa ua wa Hekalu upande wa mashariki, pamoja na upande wa mbele wa Hekalu ulikuwa dhiraa mia moja.
EZE 41:15 Kisha akapima urefu wa jengo lililoelekeana na ua upande wa nyuma wa Hekalu, pamoja na baraza zake kila upande, kwa kipimo cha dhiraa mia moja. Ukumbi mkuu, na mahali patakatifu, pamoja na baraza inayoelekeana na ukumbi,
EZE 41:16 pamoja na vizingiti, madirisha membamba na vyumba vyote vitatu, kila kimoja pamoja na kizingiti vilifunikwa kwa mbao. Sakafu, ukuta hadi kwenye madirisha, na madirisha yenyewe vilifunikwa kwa mbao.
EZE 41:17 Katika nafasi iliyokuwa juu ya upande wa nje wa ingilio la mahali patakatifu, na katika kuta zilizozunguka mahali patakatifu na sehemu ya nje, kwa nafasi zilizo sawa,
EZE 41:18 kulinakshiwa makerubi na mitende; mtende ulikuwa kati ya kerubi na kerubi. Kila kerubi alikuwa na nyuso mbili:
EZE 41:19 upande mmoja uso wa mwanadamu kuelekea mti wa mtende na upande mwingine uso wa simba ukielekea mti mwingine wa mtende. Ilinakshiwa kuzunguka Hekalu lote.
EZE 41:20 Kuanzia sakafu hadi eneo lililo juu ya ingilio, palinakshiwa makerubi na mitende, pamoja na kwenye ukuta wa nje wa Patakatifu.
EZE 41:21 Mahali patakatifu pa nje palikuwa na miimo ya mlango uliokuwa mraba; na ule uliokuwa katika Patakatifu Pa Patakatifu ulifanana na huo.
EZE 41:22 Kulikuwa na madhabahu ya mbao kimo chake dhiraa tatu na ilikuwa dhiraa mbili mraba pande zote, tako lake na pande zake zilikuwa za mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ni meza iliyo mbele za Mwenyezi Mungu.”
EZE 41:23 Mahali patakatifu pa nje na Patakatifu Pa Patakatifu zilikuwa na milango miwili.
EZE 41:24 Kila mlango ulikuwa na vipande viwili, vipande viwili vilivyoshikwa na bawaba vyenye kufunguka kwa kila mlango.
EZE 41:25 Juu ya hiyo milango ya Patakatifu palinakshiwa makerubi na mitende kama nakshi zilizokuwa kwenye kuta, na kulikuwa na ubao ulioning’inia mbele ya baraza kwa nje.
EZE 41:26 Katika kuta za pembeni za ukumbi kulikuwa na madirisha membamba yaliyonakshiwa mitende kila upande. Vyumba vya pembeni vya Hekalu pia vilikuwa vimefunikwa kwa mbao.
EZE 42:1 Ndipo yule mtu akaniongoza kuelekea kaskazini mpaka kwenye ua wa nje na kunileta mpaka kwenye vyumba vinavyoelekeana na ua wa Hekalu na kuelekeana na ukuta wa nje upande wa kaskazini.
EZE 42:2 Jengo ambalo mlango wake ulielekea kaskazini lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na upana wa dhiraa hamsini.
EZE 42:3 Mbele ya zile dhiraa ishirini za ule ua wa ndani unaoelekeana na ile njia ya ua wa nje, kuliinuka vyumba virefu kimoja baada ya kingine vya ghorofa tatu.
EZE 42:4 Mbele ya hivi vyumba kulikuwa na njia ya ndani yenye upana wa dhiraa kumi na urefu wa dhiraa mia moja. Milango yake ilikuwa upande wa kaskazini.
EZE 42:5 Basi vyumba vya juu vilikuwa vyembamba zaidi, kwa kuwa ujia ulichukua nafasi zaidi ndani yake kuliko katika vyumba vya sakafu ya chini na vya katikati ya jengo.
EZE 42:6 Vyumba katika ghorofa ya tatu havikuwa na nguzo, kama kumbi zilivyokuwa nazo, kwa hiyo eneo la sakafu ya vyumba vya juu lilikuwa ni dogo kuliko la sakafu ya chini na ya kati.
EZE 42:7 Kulikuwa na ukuta wa nje uliokuwa sambamba na vile vyumba na ukumbi wa nje, ulitokeza urefu wa dhiraa hamsini.
EZE 42:8 Wakati safu ya vyumba katika ua wa nje vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini, vile vyumba vilivyokuwa karibu zaidi na Hekalu vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja.
EZE 42:9 Vyumba vya chini vilikuwa na ingilio upande wa mashariki unapoingia kutoka ukumbi wa nje.
EZE 42:10 Upande wa kusini kufuata urefu wa ukuta wa ukumbi wa nje, unaopakana na ukumbi wa Hekalu na kuelekeana na ukuta wa nje, kulikuwa na vyumba
EZE 42:11 vyenye ujia unayopita mbele yake. Hivi vilifanana na vile vyumba vya upande wa kaskazini, vilikuwa na urefu na upana ulio sawa, mahali pa kutokea na vipimo vyake vilikuwa sawa. Kama ilivyokuwa milango ya upande wa kaskazini,
EZE 42:12 ndivyo ilivyokuwa milango ya vyumba vya upande wa kusini. Kulikuwa na ingilio kuanzia mwanzo wa njia ambao ulikuwa sambamba na ukuta wa pili uliokuwa upande wa mashariki, ambako ndiko kwa kuingia vyumbani.
EZE 42:13 Kisha akaniambia, “Vyumba vya upande wa kaskazini na vya upande wa kusini, ambavyo vinaelekeana na ukumbi wa Hekalu, ni vyumba vya makuhani, ambako wale makuhani ambao humkaribia Mwenyezi Mungu watakulia zile sadaka takatifu sana. Huko ndiko wataziweka zile sadaka takatifu sana, yaani sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia, kwa kuwa mahali hapo ni patakatifu.
EZE 42:14 Mara makuhani waingiapo mahali patakatifu, hawaruhusiwi kwenda kwenye ukumbi wa nje hadi wayaache mavazi ambayo walivaa wakiwa wanahudumu, kwa kuwa hayo mavazi ni matakatifu. Inawapasa kuvaa mavazi mengine kabla hawajakaribia eneo lililo wazi kwa ajili ya watu.”
EZE 42:15 Alipomaliza kupima vile vilivyokuwa katika eneo la ndani la Hekalu, akanitoa nje kupitia lango la upande wa mashariki na kupima eneo lote linalozunguka:
EZE 42:16 Akapima upande wa mashariki kwa ule ufito wa kupimia, nao ulikuwa dhiraa mia tano.
EZE 42:17 Akapima upande wa kaskazini, nao ulikuwa dhiraa mia tano kwa ufito ule wa kupimia.
EZE 42:18 Tena akapima upande wa kusini, nao ulikuwa dhiraa mia tano kwa ufito ule wa kupimia.
EZE 42:19 Kisha akageukia upande wa magharibi na kuupima, ulikuwa dhiraa mia tano kwa ufito ule wa kupimia.
EZE 42:20 Hivyo akapima eneo katika pande zote nne. Lilikuwa na ukuta kulizunguka wenye urefu wa dhiraa mia tano na upana wa dhiraa mia tano, uliotenganisha mahali Patakatifu na eneo la watu wote.
EZE 43:1 Kisha yule mtu akanileta kwenye lango linaloelekea upande wa mashariki,
EZE 43:2 nami nikaona utukufu wa Mungu wa Israeli ukija kutoka upande wa mashariki. Sauti yake ilikuwa kama ya ngurumo ya maji yaendayo kasi, nayo nchi ikang’aa kwa utukufu wake.
EZE 43:3 Maono niliyoyaona yalikuwa kama maono yale niliyokuwa nimeyaona wakati Mungu alipokuja kuangamiza mji na kama maono niliyokuwa nimeyaona kando ya Mto wa Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.
EZE 43:4 Utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaingia hekaluni kupitia lango linaloelekea upande wa mashariki.
EZE 43:5 Kisha Roho wa Mungu akanichukua na kunileta katika ule ua wa ndani, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ulilijaza Hekalu.
EZE 43:6 Yule mtu akiwa amesimama kando yangu, nilisikia mtu mmoja akisema nami kutoka ndani ya Hekalu.
EZE 43:7 Akasema, “Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa kuweka nyayo za miguu yangu. Hapa ndipo nitakapoishi miongoni mwa Waisraeli milele. Kamwe nyumba ya Israeli hawatalinajisi tena Jina langu takatifu, yaani wao wala wafalme wao, kwa ukahaba wao na kwa sanamu zao zisizokuwa na uhai za wafalme wao katika mahali pao pa juu pa kuabudia.
EZE 43:8 Walipoweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu na miimo yao ya milango karibu na miimo yangu, pakiwa na ukuta tu kati yangu na wao, walilinajisi Jina langu takatifu kwa matendo yao ya machukizo. Kwa sababu hiyo niliwaangamiza kwa hasira yangu.
EZE 43:9 Basi sasa na waweke mbali nami ukahaba wao na sanamu za wafalme wao zisizo na uhai, nami nitakaa miongoni mwao milele.
EZE 43:10 “Mwanadamu, elezea hilo Hekalu kwa watu wa Israeli, ili wapate kuona aibu kwa ajili ya dhambi zao. Wao na wapime hicho kielelezo.
EZE 43:11 Wakishaona aibu kwa ajili ya yale yote waliyotenda, wafahamishe kielelezo cha hilo Hekalu, yaani mpangilio wake, maingilio yake ya kutoka na kuingia, kielelezo chake chote, na masharti yake yote na sheria zake zote. Yaandike haya mbele yao ili wapate kuwa waaminifu kwa hicho kielelezo chake na kufuata masharti yake yote.
EZE 43:12 “Hii ndiyo sheria ya Hekalu: Eneo lote linalozunguka Hekalu juu ya mlima litakuwa takatifu kuliko yote. Hii ndiyo sheria ya Hekalu.
EZE 43:13 “Hivi ndivyo vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ndefu, yaani dhiraa moja na nyanda nne: Tako lake liwe na kina cha hiyo dhiraa moja, na upana wa hiyo dhiraa moja, ikiwa na ukingo wa shibiri moja kuizunguka pembeni. Hiki kitakuwa ndicho kimo cha madhabahu:
EZE 43:14 Kimo cha msingi kuanzia usawa wa ardhi hadi kwenye mfereji sehemu ya chini kimo chake ni dhiraa mbili na upana wake ni dhiraa moja na kuanzia kwenye ukingo mdogo hadi kwenye ukingo mpana kimo chake ni dhiraa nne na upana wake ni dhiraa moja.
EZE 43:15 Pale panapowashwa moto madhabahuni kimo chake kitakuwa dhiraa nne, na pembe nne zinazoelekeza juu kutoka pale panapowashwa moto.
EZE 43:16 Pale panapowashwa moto pa madhabahu ni mraba, urefu wake ni dhiraa kumi na mbili na upana wa dhiraa kumi na mbili.
EZE 43:17 Pia sehemu ya juu ni mraba, urefu wake dhiraa kumi na nne na upana wa dhiraa kumi na nne, ikiwa na ukingo wa nusu dhiraa na mfereji kuizunguka madhabahu. Ngazi za kupandia madhabahuni zitaelekea upande wa mashariki.”
EZE 43:18 Kisha akaniambia, “Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Haya ndio yatakayokuwa masharti ya kutoa dhabihu za kuteketezwa na kunyunyiza damu juu ya madhabahu itakapokuwa imejengwa.
EZE 43:19 Utatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi kwa makuhani, ambao ni Walawi, wa jamaa ya Sadoki, ndio watakaonikaribia kuhudumu mbele zangu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 43:20 Itakupasa kuchukua sehemu ya hiyo damu ya mnyama huyo, na kuiweka juu ya hizo pembe nne za madhabahu, na juu ya ncha zake nne za sehemu ya juu kuzunguka ukingo wote, ili kuitakasa madhabahu, na kufanya upatanisho kwa ajili yake.
EZE 43:21 Itakupasa kumchukua huyo fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi na kumteketeza mahali palipoagizwa katika eneo la Hekalu nje ya mahali Patakatifu.
EZE 43:22 “Siku ya pili yake utamtoa beberu asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nayo madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa yule fahali.
EZE 43:23 Utakapokuwa umemaliza kazi ya kuitakasa, utamtoa fahali mchanga pamoja na kondoo dume toka kwenye kundi, wote wawe hawana dosari.
EZE 43:24 Utawatoa mbele za Mwenyezi Mungu, nao makuhani watanyunyizia chumvi juu yao na kuwatoa kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu.
EZE 43:25 “Kwa siku saba itakupasa kutoa beberu kila siku kwa ajili ya sadaka ya dhambi, pia itakupasa kutoa fahali mchanga na kondoo dume kutoka zizini, wote wawe hawana dosari.
EZE 43:26 Kwa siku saba itawapasa kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuitakasa; hivyo ndivyo watakavyoiweka wakfu.
EZE 43:27 Mwishoni mwa hizi siku saba, kuanzia siku ya nane na kuendelea, itawapasa makuhani kutoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu. Kisha nitawakubali ninyi, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
EZE 44:1 Ndipo yule mtu akanirudisha mpaka kwenye lango la nje la mahali patakatifu, lile linaloelekea upande wa mashariki, nalo lilikuwa limefungwa.
EZE 44:2 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Lango hili litabaki limefungwa. Haliruhusiwi kufunguliwa, wala hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingilia kwenye lango hili. Litabaki limefungwa kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ameingia kupitia lango hili.
EZE 44:3 Yeye aliye mkuu peke yake ndiye anayeweza kukaa penye njia ya hilo lango na kula chakula mbele za Mwenyezi Mungu. Itampasa aingie kwa njia hiyo ya lango la ukumbini na kutokea njia hiyo hiyo.”
EZE 44:4 Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu wa Mwenyezi Mungu ukilijaza Hekalu la Mwenyezi Mungu, nami nikaanguka kifudifudi.
EZE 44:5 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa uangalifu, usikilize kwa makini na uzingatie kila kitu ninachokuambia kuhusu masharti yote yanayohusu Hekalu la Mwenyezi Mungu. Uwe mwangalifu kuhusu wale wanaoruhusiwa hekaluni na wale wasioruhusiwa kuingia mahali patakatifu.
EZE 44:6 Iambie nyumba ya uasi ya Israeli, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Matendo yenu ya machukizo yatosha, ee nyumba ya Israeli!
EZE 44:7 Zaidi ya matendo yenu yote ya machukizo, mmewaleta wageni wasiotahiriwa mioyo na miili katika patakatifu pangu. Mmelinajisi Hekalu langu, huku mkinitolea chakula, mafuta ya wanyama na damu, nanyi mmevunja agano langu.
EZE 44:8 Badala ya kutimiza wajibu wenu kuhusiana na vitu vyangu vitakatifu, mmeweka watu wengine kuwa viongozi katika patakatifu pangu.
EZE 44:9 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakuna mgeni asiyetahiriwa moyo na mwilini anayeruhusiwa kuingia patakatifu pangu, wala hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli.
EZE 44:10 “ ‘Walawi walioniacha wakati Waisraeli walipopotoka wakatoka kwangu na kutangatanga kwa kufuata sanamu zao, sharti watachukua adhabu ya dhambi zao.
EZE 44:11 Wanaweza wakatumika katika mahali patakatifu pangu, wakiwa na uangalizi wa malango ya Hekalu; wanaweza kuchinja wanyama wa sadaka za kuteketezwa, na kutoa dhabihu kwa ajili ya watu, na kusimama mbele ya watu ili kuwahudumia.
EZE 44:12 Lakini kwa sababu walitumikia watu wakiwa mbele ya sanamu zao, na kuifanya nyumba ya Israeli ianguke kwenye dhambi, kwa hiyo nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba ni lazima wachukue matokeo ya dhambi yao, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 44:13 Hawaruhusiwi kukaribia ili kunitumikia kama makuhani wala kukaribia chochote changu kilicho kitakatifu au sadaka iliyo takatifu kupita zote, bali watachukua aibu ya matendo yao ya kuchukiza.
EZE 44:14 Lakini nitawaweka katika uangalizi wa Hekalu na kazi zote zile zinazotakiwa kufanyika ndani yake.
EZE 44:15 “ ‘Lakini makuhani, ambao ni Walawi na wazao wa Sadoki, ambao walitimiza wajibu wao kwa uaminifu katika patakatifu pangu wakati Waisraeli walipopotoka, watakaribia ili kutumika mbele zangu. Itawapasa wasimame mbele zangu ili kutoa dhabihu za mafuta ya wanyama na damu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 44:16 Wao peke yao ndio wenye ruhusa ya kuingia mahali patakatifu pangu. Wao peke yao ndio watakaokaribia meza yangu ili kuhudumu mbele zangu na kufanya utumishi wangu.
EZE 44:17 “ ‘Watakapoingia kwenye malango ya ukumbi wa ndani, watavaa nguo za kitani safi, hawaruhusiwi kamwe kuvaa mavazi ya sufu wakati wanapokuwa wakihudumu kwenye malango ya ukumbi wa ndani wala ndani ya Hekalu.
EZE 44:18 Watavaa vilemba vya kitani safi vichwani mwao na nguo za ndani za kitani safi viunoni mwao. Hawatavaa chochote kitakachowafanya kutoa jasho.
EZE 44:19 Watakapotoka ili kuingia katika ukumbi wa nje mahali watu walipo, watavua nguo walizokuwa wakihudumu nazo na wataziacha katika vyumba vitakatifu nao watavaa nguo nyingine, ili wasije wakaambukiza watu utakatifu kupitia mavazi yao.
EZE 44:20 “ ‘Hawatanyoa nywele za vichwa vyao wala kuziacha ziwe ndefu, bali watazipunguza.
EZE 44:21 Kuhani yeyote asinywe mvinyo aingiapo katika ukumbi wa ndani.
EZE 44:22 Wasioe wanawake wajane wala walioachika, inawapasa kuoa wanawake bikira wenye heshima wa Israeli au wajane wa makuhani.
EZE 44:23 Watawafundisha watu wangu tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida na kuwaonesha jinsi ya kupambanua kati ya vitu najisi na vitu safi.
EZE 44:24 “ ‘Katika magombano yoyote, makuhani watatumika kama mahakimu na kuamua hilo jambo kufuatana na sheria zangu. Watazishika sheria zangu na maagizo yangu katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa, nao watatakasa Sabato zangu.
EZE 44:25 “ ‘Kuhani asijitie unajisi kwa kukaribia maiti; lakini, ikiwa mtu aliyekufa alikuwa baba yake au mama yake, mwana au binti yake, ndugu yake au dada ambaye hakuolewa, basi anaweza kujitia unajisi kwa hao.
EZE 44:26 Baada ya kujitakasa, atakaa hali hiyo kwa muda wa siku saba.
EZE 44:27 Siku atakapoingia katika ukumbi wa ndani wa mahali patakatifu ili kuhudumu, atatoa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 44:28 “ ‘Mimi ndio nitakuwa urithi pekee wa makuhani katika Israeli. Msiwape wao milki, mimi nitakuwa milki yao.
EZE 44:29 Wao watakula sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia na kila kitu kitakachotolewa kwa Mwenyezi Mungu katika Israeli kitakuwa chao.
EZE 44:30 Yote yaliyo bora ya malimbuko ya vitu vyote na matoleo yenu maalum vitakuwa vya makuhani. Inawapasa kuwapa malimbuko ya kwanza ya unga wenu ili baraka ipate kuwa katika nyumba zenu.
EZE 44:31 Makuhani hawaruhusiwi kula chochote, ikiwa ni ndege au mnyama, aliyekutwa amekufa au aliyeraruliwa na wanyama pori.
EZE 45:1 “ ‘Mtakapogawa nchi kuwa urithi, mtaitoa sehemu ya nchi kwa Mwenyezi Mungu kuwa eneo takatifu, urefu wake dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wake dhiraa elfu ishirini; eneo hili lote litakuwa takatifu.
EZE 45:2 Katika eneo hilo patakuwa na sehemu mraba ambayo ni ya mahali patakatifu; kila upande utakuwa dhiraa mia tano, ikiwa imezungukwa na eneo la wazi lenye upana wa dhiraa hamsini.
EZE 45:3 Katika eneo takatifu, pima sehemu yenye urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Ndani ya hilo eneo kutakuwa mahali patakatifu, ndipo Patakatifu pa Patakatifu.
EZE 45:4 Itakuwa sehemu takatifu ya nchi kwa ajili ya makuhani, wale wanaohudumu ndani ya mahali patakatifu na ambao hukaribia ili kuhudumu mbele za Mwenyezi Mungu. Patakuwa mahali pa nyumba zao pamoja na sehemu kwa ajili ya mahali patakatifu.
EZE 45:5 Eneo la urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi litakuwa la Walawi, wanaohudumu hekaluni, kama milki yao kwa ajili ya miji ya kuishi.
EZE 45:6 “ ‘Utatoa mji kama mali yao, wenye upana wa dhiraa elfu tano, na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano karibu na sehemu takatifu; itakuwa mali ya nyumba yote ya Israeli.
EZE 45:7 “ ‘Mkuu anayetawala atakuwa na eneo linalopakana na lile eneo lililowekwa wakfu kwa upande moja, na eneo la mji upande mwingine. Eneo la mji litaenea upande wa magharibi kuanzia upande wa magharibi, na kuenea mashariki kuanzia upande wa mashariki, likiendelea kwa urefu kutoka magharibi hadi mpaka wa mashariki, sambamba na mojawapo ya sehemu za makabila.
EZE 45:8 Nchi hii itakuwa milki yake katika Israeli. Nao wakuu wangu hawatawadhulumu tena watu wangu, bali watairuhusu nyumba ya Israeli kuimiliki nchi kulingana na makabila yao.
EZE 45:9 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Yatosha, enyi wakuu wa Israeli! Acheni mbali ukatili wenu na uonevu wenu mkafanye lile lililo haki na sawa. Acheni kuwatoza watu wangu isivyo haki, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 45:10 Tumieni mizani sahihi na vipimo sahihi vya efa na bathi.
EZE 45:11 Efa na bathi viwe sawa, bathi iwe sehemu ya kumi ya homeri na efa iwe sehemu ya kumi ya homeri, homeri itakuwa ndicho kiwango cha kukubalika kwa vyote viwili.
EZE 45:12 Shekeli moja itakuwa gera ishirini. Shekeli ishirini, jumlisha na shekeli ishirini na tano, jumlisha na shekeli kumi na tano zitakuwa mina moja.
EZE 45:13 “ ‘Hili ndilo toleo maalum mtakalotoa: sehemu ya sita ya efa kutoka kila homeri ya ngano, na sehemu ya sita ya efa kutoka kila homeri ya shayiri.
EZE 45:14 Sehemu ya mafuta iliyoamriwa, yaliyopimwa kwa bathi, ni sehemu ya kumi ya bathi kutoka kila kori moja (ambayo ina bathi kumi au homeri moja, kwa kuwa bathi kumi ni homeri moja).
EZE 45:15 Pia kondoo mmoja atachukuliwa kutoka kila kundi la kondoo mia mbili katika malisho yenye maji mengi ya Israeli. Hivi vitatumika kwa ajili ya sadaka ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya watu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 45:16 Watu wote wa nchi wataungana pamoja katika kutoa sadaka hii maalum ya kutumiwa na mkuu anayetawala Israeli.
EZE 45:17 Utakuwa wajibu wa mkuu anayetawala kutoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji kwenye sikukuu, Mwezi Mwandamo na Sabato, kwenye sikukuu zote zilizoamriwa za nyumba ya Israeli. Atatoa sadaka za dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.
EZE 45:18 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya huo mwezi utamchukua fahali mchanga asiye na dosari na kutakasa mahali patakatifu.
EZE 45:19 Kuhani itampasa achukue sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi na kuipaka kwenye miimo ya Hekalu, kwenye pembe nne za juu za ukingo wa hayo madhabahu na juu ya miimo ya lango la ukumbi wa ndani.
EZE 45:20 Itakupasa kufanya vivyo hivyo katika siku ya saba ya mwezi huo kwa ajili ya mtu ambaye hutenda dhambi bila kukusudia au bila kujua; ndivyo utafanya upatanisho kwa ajili ya Hekalu.
EZE 45:21 “ ‘Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne utaadhimisha Pasaka. Sikukuu itaendelea kwa siku saba, wakati huo wa hizo siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu.
EZE 45:22 Katika siku hiyo mkuu anayetawala atatoa fahali kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa nchi.
EZE 45:23 Kila siku wakati wa hizo siku saba za sikukuu atatoa mafahali saba na kondoo dume saba wasio na dosari kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu na beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
EZE 45:24 Pia atatoa sadaka ya nafaka efa moja kwa kila fahali, na efa moja kwa kila kondoo dume, pamoja na hini moja ya mafuta kwa kila efa.
EZE 45:25 “ ‘Wakati wa hizo siku saba za sikukuu, ambayo huanza katika mwezi wa saba kwenye siku ya kumi na tano, mkuu anayetawala atatoa mahitaji yale yale kwa ajili ya sadaka za dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta.
EZE 46:1 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa mashariki litakuwa linafungwa kwa siku sita za juma, ila siku ya Sabato na siku ya Mwezi Mwandamo litafunguliwa.
EZE 46:2 Mkuu anayetawala ataingia kupitia baraza ya njia ya lango la ukumbi na kusimama karibu na nguzo ya lango. Makuhani watatoa sadaka za mkuu anayetawala za kuteketezwa na sadaka za amani. Mkuu anayetawala atasujudu kwenye kizingiti cha njia ya lango, kisha atatoka nje, lakini lango halitafungwa hadi jioni.
EZE 46:3 Siku za Sabato na za Mwezi Mwandamo watu wote wa nchi wataabudu mbele za Mwenyezi Mungu penye lile ingilio la ile njia.
EZE 46:4 Sadaka za kuteketezwa aletazo mkuu anayetawala kwa Mwenyezi Mungu siku ya Sabato zitakuwa ni wana-kondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasiwe na dosari.
EZE 46:5 Sadaka ya nafaka inayotolewa pamoja na huyo kondoo dume itakuwa efa moja, na sadaka ya nafaka inayotolewa na hao wana-kondoo itakuwa kiasi apendacho mtu pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.
EZE 46:6 Siku ya Mwezi Mwandamo atatoa fahali mchanga, wana-kondoo sita na kondoo dume, wote wasiwe na dosari.
EZE 46:7 Atatoa sadaka ya nafaka ya: efa moja kwa huyo fahali, na efa moja kwa huyo kondoo dume; na kwa wana-kondoo atatoa nafaka nyingi kama atakavyo kutoa; atatoa hini ya mafuta kwa kila efa.
EZE 46:8 Mkuu anayetawala atakapoingia, atapitia kwenye baraza ya njia ya lango, naye atatoka nje kwa njia hiyo hiyo.
EZE 46:9 “ ‘Watu wa nchi wanapokuja mbele za Mwenyezi Mungu katika sikukuu zilizoamriwa, yeyote aingiaye kwa lango la kaskazini kuabudu atatoka nje kwa lango la kusini; na yeyote aingiaye kwa lango la kusini atatoka nje kwa lango la kaskazini. Hakuna mtu yeyote atakayerudi kupitia lango lile aliloingilia, lakini kila mmoja atatoka nje kwa lango linalokabili lile aliloingilia.
EZE 46:10 Mkuu anayetawala atakuwa miongoni mwao, akiingia nao ndani wanapoingia, na akitoka nao nje wanapotoka.
EZE 46:11 “ ‘Kwenye sikukuu na kwenye sikukuu zilizoamriwa, sadaka ya nafaka itakuwa efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja pamoja na kondoo dume mmoja, pamoja na idadi ya wana-kondoo kama mtu apendavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.
EZE 46:12 Mkuu anayetawala anapotoa sadaka ya hiari kwa Mwenyezi Mungu, iwe ni sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, atafunguliwa lango linaloelekea mashariki. Atatoa sadaka yake ya kuteketezwa au sadaka yake ya amani kama afanyavyo katika siku ya Sabato. Kisha atatoka nje. Baada yake kutoka nje, lango litafungwa.
EZE 46:13 “ ‘Kila siku utamtoa mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiyekuwa na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, utaitoa kila siku asubuhi.
EZE 46:14 Pia kila siku asubuhi pamoja na hiyo sadaka utatoa sadaka ya nafaka, ikiwa na sehemu ya sita ya efa pamoja na theluthi moja ya hini ya mafuta ya kuchanganya na ule unga. Utoaji wa sadaka hii ya nafaka kwa Mwenyezi Mungu ni agizo la kudumu.
EZE 46:15 Kwa hiyo mwana-kondoo na sadaka ya nafaka na mafuta vitatolewa kila siku asubuhi kwa ajili ya sadaka ya daima ya kuteketezwa.
EZE 46:16 “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ikiwa mkuu anayetawala atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa wanawe, hiyo zawadi itakuwa pia kwa wazao wake; itakuwa mali yao kwa urithi.
EZE 46:17 Hata hivyo, kama atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa watumishi wake, mtumishi anaweza kuiweka hadi mwaka wa uhuru, kisha itarudishwa kwa mkuu anayetawala. Urithi wake ni wa wanawe peke yao, ni mali yao.
EZE 46:18 Mkuu anayetawala hafai kuchukua urithi wowote wa watu na kuwaondoa kwenye mali yao. Mkuu huyo atawapa wanawe urithi wao katika mali yake mwenyewe, ili pasiwe na mtu wangu yeyote atakayetengwa na urithi wake.’ ”
EZE 46:19 Kisha mtu yule akanileta kupitia kwenye ingilio lililokuwa kando ya lango hadi kwenye vyumba vitakatifu vilivyoelekea kaskazini, ambavyo ni vya makuhani, naye akanionesha mahali fulani upande wa mwisho wa magharibi.
EZE 46:20 Akaniambia, “Mahali hapa ndipo makuhani watakapotokosea sadaka ya hatia na sadaka ya dhambi, na kuoka sadaka ya nafaka, ili kuepuka kuzileta katika ukumbi wa nje na kushirikisha utakatifu kwa watu.”
EZE 46:21 Baada ya hapo akanileta kwenye ukumbi wa nje na kunizungusha kwenye pembe zake nne, nami nikaona katika kila pembe ya huo ukumbi kulikuwa na ukumbi mwingine.
EZE 46:22 Katika pembe nne za huo ukumbi wa nje kulikuwa na kumbi nyingine, zenye urefu wa dhiraa arobaini na upana wake dhiraa thelathini, ambapo hizo kumbi kwenye hizo pembe nne zilikuwa na vipimo vilivyo sawa.
EZE 46:23 Mzunguko wa ndani wa hizo kumbi nne ulikuwa na ukingo wa jiwe, zikiwa na sehemu zilizojengwa kwa ajili ya moto kuzunguka chini ya huo ukingo.
EZE 46:24 Akaniambia, “Hizi ndizo sehemu za kupikia ambazo wale wanaohudumu kwenye Hekalu watatokosea dhabihu za watu.”
EZE 47:1 Yule mtu akanirudisha kwenye ingilio la Hekalu, nami nikaona maji yakitoka chini ya kizingiti cha Hekalu yakitiririkia upande wa mashariki (kwa maana upande wa mbele wa Hekalu ulielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitoka chini upande wa kusini wa Hekalu, kusini mwa madhabahu.
EZE 47:2 Ndipo akanitoa nje kupitia lango la kaskazini na kunizungusha mpaka kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nayo maji yalikuwa yakitiririka kutoka upande wa kusini.
EZE 47:3 Mtu yule alipoenda upande wa mashariki akiwa na kamba ya kupimia mkononi mwake, akapima dhiraa elfu moja, kisha akanipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kwenye vifundo vya miguu.
EZE 47:4 Akapima dhiraa elfu moja nyingine na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika magotini. Akapima dhiraa nyingine elfu moja na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kiunoni.
EZE 47:5 Akapima tena dhiraa elfu moja nyingine, lakini wakati huu yalikuwa mto ambao sikuweza kuvuka, kwa kuwa maji yalikuwa na kina kirefu ambacho ni cha kuogelea, mto ambao hakuna mtu angeweza kuuvuka.
EZE 47:6 Akaniuliza, “Je, mwanadamu, unaona hili?” Kisha akanirudisha kwenye ukingo wa huo mto.
EZE 47:7 Nilipofika pale, nikaona idadi kubwa ya miti kila upande wa ule mto.
EZE 47:8 Akaniambia, “Haya maji yanatiririka kuelekea nchi ya mashariki na kushuka hadi Araba, ambapo huingia Baharini. Yanapomwagikia kwenye hiyo Bahari, maji hayo huponywa na kuwa safi.
EZE 47:9 Popote mto huu unatakapofika, kila kiumbe hai kinachoingia ndani ya hayo maji kitaishi. Nako kutakuwa na samaki wengi mno, mara maji haya yatakapofika huko. Maji hayo yatakuwa hai, na kila kitu kitaishi popote mto utakapofika.
EZE 47:10 Wavuvi watasimama kando ya bahari; kuanzia En-Gedi hadi En-Eglaimu kutakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki. Samaki watakuwa wa aina nyingi, kama samaki wa Bahari Kuu.
EZE 47:11 Lakini madimbwi yake na mabwawa yake hayatakuwa na maji yanayofaa kunywa, bali yatabakia kuwa maji ya chumvi.
EZE 47:12 Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yanayotoka patakatifu yataitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”
EZE 47:13 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Hii ndiyo mipaka ambayo kwayo mtagawanya hiyo nchi kuwa urithi miongoni mwa hayo makabila kumi na mawili ya Israeli, pamoja na mafungu mawili ya Yusufu.
EZE 47:14 Mtagawa kwa usawa miongoni mwao. Kwa sababu niliapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu, nchi hii itakuwa urithi wenu.
EZE 47:15 “Huu ndio utakuwa mpaka wa hiyo nchi: “Upande wa kaskazini utaanzia Bahari Kuu kwa njia ya Hethloni kupitia Lebo-Hamathi hadi maingilio ya Sedadi.
EZE 47:16 Berotha na Sibraimu (ambao uko kwenye mpaka kati ya Dameski na Hamathi), hadi kufikia Haser-Hatikoni, ambao uko katika mpaka wa Haurani.
EZE 47:17 Hivyo mpaka utaendelea kuanzia Baharini hadi Hasar-Enoni, ukiambaa na mpaka wa kaskazini wa Dameski, pamoja na mpaka wa Hamathi upande wa kaskazini. Huu utakuwa mpaka wa kaskazini.
EZE 47:18 Upande wa mashariki mpaka utapita kati ya Haurani na Dameski, kuambaa Yordani na kati ya Gileadi na nchi ya Israeli, hadi bahari ya mashariki na kufika Tamari. Huu utakuwa mpaka wa mashariki.
EZE 47:19 Upande wa kusini utaanzia Tamari hadi kufikia maji ya Meriba-Kadeshi, kisha utaambaa na Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. Huu utakuwa ndio mpaka wa kusini.
EZE 47:20 Upande wa magharibi, Bahari Kuu itakuwa ndio mpaka hadi kwenye sehemu mkabala na Lebo-Hamathi. Huu utakuwa mpaka wa magharibi.
EZE 47:21 “Mtagawanya nchi hii miongoni mwenu kufuatana na makabila ya Israeli.
EZE 47:22 Mtaigawanya kuwa urithi kwa ajili yenu na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwenu na ambao wana watoto. Wao watakuwa kwenu kama wenyeji wazawa wa Israeli, pamoja na ninyi watagawiwa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli.
EZE 47:23 Katika kabila lolote mgeni atakapoishi, hapo ndipo mtakapompatia urithi wake,” asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 48:1 “Haya ndiyo majina ya makabila na sehemu zao: “Kwenye mpaka wa kaskazini, Dani atakuwa na sehemu moja; mpaka huo utafuata barabara ya Hethloni hadi Lebo-Hamathi; Hasar-Enani hata mpaka wa kaskazini wa Dameski karibu na Hamathi utakuwa sehemu ya huo mpaka wake kuanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.
EZE 48:2 Asheri atakuwa na sehemu moja; itapakana na nchi ya Dani kuanzia mashariki hadi upande wa magharibi.
EZE 48:3 Naftali atakuwa na sehemu moja; itapakana na nchi ya Asheri kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:4 Manase atakuwa na sehemu moja; itapakana na nchi ya Naftali kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:5 Efraimu atakuwa na sehemu moja; itapakana na nchi ya Manase kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:6 Reubeni atakuwa na sehemu moja; itapakana na nchi ya Efraimu kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:7 Yuda atakuwa na sehemu moja; itapakana na nchi ya Reubeni kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:8 “Kupakana na nchi ya Yuda kuanzia mashariki mpaka magharibi itakuwa ndiyo sehemu utakayoitoa ili kuwa toleo maalum. Itakuwa na upana wa dhiraa elfu ishirini na tano, nao urefu wake kuanzia mashariki hadi magharibi utakuwa sawa na sehemu moja ya kabila; mahali patakatifu patakuwa katikati ya eneo hilo.
EZE 48:9 “Hiyo sehemu maalum mtakayotoa kwa Mwenyezi Mungu itakuwa na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi.
EZE 48:10 Hii itakuwa ni sehemu takatifu kwa ajili ya makuhani. Itakuwa na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano upande wa kaskazini, upana wa dhiraa elfu kumi upande wa magharibi, dhiraa elfu kumi upande wa mashariki, na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano upande wa kusini. Katikati yake patakuwa mahali patakatifu pa Mwenyezi Mungu.
EZE 48:11 Hii itakuwa kwa ajili ya makuhani waliowekwa wakfu, Wasadoki, waliokuwa waaminifu katika kunitumikia, nao hawakupotoka kama Walawi walivyofanya wakati Waisraeli walipopotoka.
EZE 48:12 Itakuwa toleo maalum kwao kutoka sehemu takatifu ya nchi, yaani sehemu takatifu sana, inayopakana na nchi ya Walawi.
EZE 48:13 “Kando ya nchi ya makuhani, Walawi watakuwa na mgawo wa urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Urefu wake utakuwa jumla dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi.
EZE 48:14 Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu.
EZE 48:15 “Eneo linalobaki lenye upana wa dhiraa elfu tano, na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano litakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mji, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na maeneo ya malisho. Mji utakuwa katikati yake
EZE 48:16 nao utakuwa na vipimo hivi: upande wa kaskazini dhiraa elfu nne na mia tano, upande wa kusini dhiraa elfu nne na mia tano, upande wa mashariki dhiraa elfu nne na mia tano, na upande wa magharibi dhiraa elfu nne na mia tano.
EZE 48:17 Eneo la malisho kwa ajili ya mji litakuwa na eneo la dhiraa mia mbili na hamsini upande wa kaskazini, dhiraa mia mbili na hamsini upande wa kusini, dhiraa mia mbili na hamsini upande wa mashariki, na dhiraa mia mbili na hamsini upande wa magharibi.
EZE 48:18 Eneo linalobaki, linalopakana na sehemu takatifu likiwa na urefu sawa nalo, litakuwa dhiraa elfu kumi upande wa mashariki, na dhiraa elfu kumi upande wa magharibi. Mazao yake yatawapa watumishi wa mji chakula.
EZE 48:19 Watumishi wa mji wanaolima shamba hili watatoka katika makabila yote ya Israeli.
EZE 48:20 Eneo lote la hiyo sehemu litakuwa mraba, yaani dhiraa elfu ishirini na tano kila upande. Kama toleo maalum mtatenga sehemu takatifu, pamoja na milki ya mji.
EZE 48:21 “Eneo linalobaki pande mbili za eneo linalofanya sehemu takatifu na milki ya mji litakuwa mali ya mkuu anayetawala. Eneo hili litaenea upande wa mashariki, kuanzia kwenye dhiraa elfu ishirini na tano za sehemu takatifu hadi mpaka wa mashariki, na kuelekea upande wa magharibi, kuanzia kwenye dhiraa elfu ishirini na tano hadi mpaka wa magharibi. Maeneo haya mawili yanayoenda sambamba na urefu wa sehemu za makabila yatakuwa ya mkuu anayetawala, na sehemu ile takatifu pamoja na mahali patakatifu pa Hekalu itakuwa katikati yake.
EZE 48:22 Kwa hiyo milki ya Walawi na milki ya mji vitakuwa katikati ya eneo lile ambalo ni mali ya mkuu anayetawala. Eneo la mkuu anayetawala litakuwa kati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini.
EZE 48:23 “Kuhusu makabila yaliyobaki: “Benyamini atakuwa na sehemu moja; itakayoanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.
EZE 48:24 Simeoni atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Benyamini kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:25 Isakari atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Simeoni kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:26 Zabuloni atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Isakari kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:27 Gadi atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Zabuloni kuanzia mashariki hadi magharibi.
EZE 48:28 Mpaka wa kusini wa Gadi utapita kusini kuanzia Tamari hadi maji ya Meriba-Kadeshi, kisha kupitia upande wa Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu.
EZE 48:29 “Hii ndiyo nchi mtakayogawanya kuwa urithi kwa makabila ya Israeli, nazo zitakuwa sehemu zao,” asema Bwana Mungu Mwenyezi.
EZE 48:30 “Haya yatakuwa ndiyo malango ya mji ya kutokea: “Kuanzia upande wa kaskazini, ambayo urefu wake ni dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu,
EZE 48:31 malango hayo ya mji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Malango hayo matatu ya upande wa kaskazini moja litakuwa lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi.
EZE 48:32 Upande wa mashariki, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Yusufu, lango la Benyamini na lango la Dani.
EZE 48:33 Upande wa kusini, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zabuloni.
EZE 48:34 Upande wa magharibi, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali.
EZE 48:35 “Urefu wote kuzunguka utakuwa dhiraa elfu kumi na nane. “Nalo jina la mji huo kuanzia wakati huo na kuendelea litakuwa: ‘Mwenyezi Mungu yupo hapa.’ ”
DAN 1:1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu.
DAN 1:2 Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Nebukadneza akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake.
DAN 1:3 Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu:
DAN 1:4 vijana wa kiume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo.
DAN 1:5 Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.
DAN 1:6 Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria.
DAN 1:7 Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita jina Belteshaza, Hanania akamwita jina Shadraki, Mishaeli akamwita jina Meshaki, na Azaria akamwita jina Abednego.
DAN 1:8 Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajinajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii.
DAN 1:9 Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonesha upendeleo na huruma kwa Danieli.
DAN 1:10 Lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”
DAN 1:11 Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria,
DAN 1:12 “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani tule, na maji ya kunywa.
DAN 1:13 Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.”
DAN 1:14 Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.
DAN 1:15 Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri kuliko yeyote kati ya vijana waliokula chakula cha mfalme.
DAN 1:16 Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.
DAN 1:17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.
DAN 1:18 Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme ili kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza.
DAN 1:19 Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme.
DAN 1:20 Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwapata kuwa bora mara kumi zaidi ya waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.
DAN 1:21 Naye Danieli akabaki huko hadi mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.
DAN 2:1 Katika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto. Mawazo yake yakasumbuka na hakuweza kulala.
DAN 2:2 Hivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi, na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia na kusimama mbele ya mfalme,
DAN 2:3 akawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua, nami nataka nijue maana yake.”
DAN 2:4 Ndipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu, “Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.”
DAN 2:5 Mfalme akawajibu wanajimu, “Nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu ilikuwa ipi na kuifasiri, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa kuwa vifusi.
DAN 2:6 Lakini mkiniambia ndoto yangu na kuifasiri, mtapokea kwangu zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi niambieni ndoto yangu na mnifasirie.”
DAN 2:7 Wakajibu kwa mara nyingine, “Mfalme na awaambie watumishi wake ndoto yake, nasi tutaifasiri.”
DAN 2:8 Ndipo mfalme akajibu, “Nina hakika kuwa mnajaribu kupata muda zaidi, kwa sababu mnatambua kuwa nimeamua hivi kwa uthabiti:
DAN 2:9 Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu, ipo adhabu moja tu kwenu. Mmepanga njama kuniambia habari za kunipotosha na mambo maovu, mkitumaini kwamba hali itabadilika. Hivyo basi, niambieni hiyo ndoto, nami nitajua kuwa mwaweza kunifasiria.”
DAN 2:10 Wanajimu wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu duniani ambaye anaweza kufanya analotaka mfalme! Vilevile, hakuna mfalme, hata awe mkuu na mwenye uweza namna gani, aliyeuliza kitu kama hicho kwa mganga, au kwa msihiri, wala kwa mnajimu yeyote.
DAN 2:11 Anachouliza mfalme ni kigumu mno. Hakuna yeyote awezaye kumfunulia mfalme isipokuwa miungu, nao hawaishi miongoni mwa wanadamu.”
DAN 2:12 Jambo hili lilimkasirisha na kumghadhibisha mfalme mno, hata kuagiza kuuawa kwa wenye hekima wote wa Babeli.
DAN 2:13 Hivyo amri ikatolewa ya kuwaua wenye hekima, nao watu wakatumwa kuwatafuta Danieli na rafiki zake ili wawaue.
DAN 2:14 Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alipokuwa ameenda kuwaua wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara.
DAN 2:15 Akamuuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo.
DAN 2:16 Basi Danieli akawaendea mfalme, akamwomba ampe muda ili aweze kumfasiria ile ndoto.
DAN 2:17 Ndipo Danieli akarudi nyumbani mwake na kuwaeleza rafiki zake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo.
DAN 2:18 Aliwasihi waombe rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hii, ili yeye na rafiki zake wasije wakauawa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli.
DAN 2:19 Wakati wa usiku, lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni,
DAN 2:20 akasema: “Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; hekima na uweza ni vyake.
DAN 2:21 Yeye hubadili nyakati na majira; huwaweka wafalme na kuwaondoa. Huwapa hekima wenye hekima, na maarifa wenye ufahamu.
DAN 2:22 Hufunua siri na mambo yaliyofichika; anajua yale yaliyo gizani, nayo nuru hukaa kwake.
DAN 2:23 Ninakushukuru na kukuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu: Umenipa hekima na uwezo; umenijulisha kile tulichokuomba, umetujulisha ndoto ya mfalme.”
DAN 2:24 Ndipo Danieli akamwendea Arioko, ambaye mfalme alikuwa amemteua kuwaua wenye hekima wa Babeli, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babeli. Nipeleke kwa mfalme, nami nitamfasiria ndoto yake.”
DAN 2:25 Arioko akampeleka Danieli kwa mfalme mara moja na kumwambia, “Nimempata mtu miongoni mwa watu wa uhamisho kutoka Yuda ambaye anaweza kumwambia mfalme maana ya ndoto yake.”
DAN 2:26 Mfalme akamuuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?”
DAN 2:27 Danieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza,
DAN 2:28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita mawazoni mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya:
DAN 2:29 “Ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotokea baadaye, naye mfunuaji wa siri akakuonesha ni kitu gani kitakachotokea.
DAN 2:30 Kwangu mimi, nimefunuliwa siri hii, si kwa sababu nina hekima kubwa kuliko watu wengine wanaoishi, bali ili wewe, ee mfalme, upate kujua tafsiri, na ili uweze kuelewa kile kilichopita mawazoni mwako.
DAN 2:31 “Ee mfalme, ulitazama, na mbele yako ilisimama sanamu kubwa mno, iliyong’aa kupita kiasi na yenye kutisha kwa mwonekano wake.
DAN 2:32 Kichwa cha sanamu hiyo kilikuwa kimetengenezwa kwa dhahabu safi; kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha; tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba;
DAN 2:33 miguu yake ilikuwa ya chuma; na nyayo zake zilikuwa chuma na sehemu nyingine udongo uliochomwa.
DAN 2:34 Ulipokuwa unaangalia, jiwe lilikatwa, lakini si kwa mikono ya mwanadamu. Lile jiwe liliipiga ile sanamu kwenye nyayo zake za chuma na udongo, na kuivunja.
DAN 2:35 Ndipo ile chuma, ule udongo, ile shaba, ile fedha na ile dhahabu vikavunjika vipande vipande kwa wakati mmoja, na vikawa kama makapi katika sakafu ya kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperusha bila kuacha hata alama. Lakini lile jiwe lililoipiga ile sanamu likawa mlima mkubwa mno na kuijaza dunia yote.
DAN 2:36 “Hii ndio ilikuwa ndoto, nasi sasa tutamfasiria mfalme.
DAN 2:37 Ee mfalme, wewe ni mfalme wa wafalme. Mungu wa mbinguni amekupa wewe utawala, uweza, nguvu, na utukufu.
DAN 2:38 Mikononi mwako amewaweka wanadamu, wanyama wa kondeni, na ndege wa angani. Popote wanapoishi, amekufanya wewe kuwa mtawala wa hao wote. Wewe ndiwe kile kichwa cha dhahabu.
DAN 2:39 “Baada yako, ufalme mwingine utainuka, ulio dhaifu kuliko wako. Baadaye utafuata ufalme wa tatu, ule wa shaba, nao utaitawala dunia yote.
DAN 2:40 Hatimaye kutakuwako na ufalme wa nne, wenye nguvu kama chuma, kwa maana chuma huvunja na kupondaponda kila kitu; kama vile chuma ivunjavyo vitu vipande vipande, ndivyo ufalme huo utakavyopondaponda na kuvunjavunja nyingine zote.
DAN 2:41 Kama ulivyoona nyayo na vidole, sehemu moja vikiwa vya udongo uliochomwa na sehemu nyingine vya chuma, kadhalika ufalme huu utakuwa umegawanyika; hata hivyo, utakuwa wenye nguvu ya chuma ndani yake kama ulivyoona chuma kikiwa kimechanganywa na udongo.
DAN 2:42 Kama vile vidole vyake vya miguu vilikuwa kwa sehemu chuma na kwa sehemu udongo, ndivyo ufalme huo kwa sehemu utakuwa na nguvu na kwa sehemu udhaifu.
DAN 2:43 Kama ulivyoona nyayo na vidole, sehemu moja vikiwa vya udongo uliochomwa na sehemu nyingine vya chuma, kadhalika ufalme huu utakuwa umegawanyika; wala hawatabaki wameungana tena, kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo.
DAN 2:44 “Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atauweka ufalme ambao kamwe hautaangamizwa, wala hautaachiwa taifa lingine. Utaziponda zile falme zote na kuzikomesha, bali wenyewe utadumu milele.
DAN 2:45 Hii ndiyo maana ya maono ya jiwe lililochongwa kutoka mlimani, lakini si kwa mikono ya mwanadamu, lile jiwe ambalo lilivunja chuma, shaba, udongo, fedha na dhahabu vipande vipande. “Mungu Mkuu amemwonesha mfalme kile kitakachotendeka wakati ujao. Ndoto hii ni ya kweli, na tafsiri yake ni ya kuaminika.”
DAN 2:46 Ndipo Mfalme Nebukadneza akaanguka kifudifudi mbele ya Danieli kumpa heshima, akaagiza wamtolee Danieli sadaka na uvumba.
DAN 2:47 Mfalme akamwambia Danieli, “Hakika Mungu wako ni Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, na mfunuaji wa siri zote, kwa maana umeweza kufunua siri hii.”
DAN 2:48 Ndipo mfalme akamweka Danieli nafasi ya juu, na kumpa zawadi nyingi tele. Akamfanya mtawala wa jimbo lote la Babeli, na kumweka kuwa mkuu wa wenye hekima wote.
DAN 2:49 Zaidi ya hayo, kwa ombi la Danieli, mfalme akawateua Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa jimbo la Babeli, huku Danieli akibaki katika ukumbi wa mfalme.
DAN 3:1 Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa sitini, na upana wa dhiraa sita, akaisimamisha kwenye tambarare ya Dura katika jimbo la Babeli.
DAN 3:2 Kisha mfalme akaita wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu, na maafisa wengine wote wa jimbo kuja kuizindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.
DAN 3:3 Basi wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu, na maafisa wengine wote wa jimbo wakakusanyika ili kuizindua sanamu ile Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha, nao wakasimama mbele ya hiyo sanamu.
DAN 3:4 Ndipo mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha, hili ndilo mnaloamriwa kulifanya:
DAN 3:5 Mara mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima msujudu na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza ameisimamisha.
DAN 3:6 Mtu ambaye hataanguka chini na kuiabudu sanamu hiyo, atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto.”
DAN 3:7 Kwa hiyo, mara waliposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wakasujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.
DAN 3:8 Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi.
DAN 3:9 Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele!
DAN 3:10 Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima asujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu,
DAN 3:11 na kwamba yeyote ambaye hatasujudu na kuiabudu atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto.
DAN 3:12 Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
DAN 3:13 Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme,
DAN 3:14 naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?
DAN 3:15 Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Naye ni mungu yupi ataweza kuwaokoa ninyi kutoka mkononi mwangu?”
DAN 3:16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili.
DAN 3:17 Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru linalowaka moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme.
DAN 3:18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
DAN 3:19 Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika kwao. Akaagiza tanuru lichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake,
DAN 3:20 na akawaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu zaidi katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego, na kuwatupa ndani ya tanuru lililowaka moto.
DAN 3:21 Hivyo watu hawa walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru hilo wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba, na nguo zao nyingine.
DAN 3:22 Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru lilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego.
DAN 3:23 Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru hilo la moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana.
DAN 3:24 Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?” Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.”
DAN 3:25 Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto; hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.”
DAN 3:26 Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa lile tanuru lililowaka moto na kuita kwa sauti kuu, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!” Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto.
DAN 3:27 Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu ya moto.
DAN 3:28 Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao.
DAN 3:29 Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande, na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”
DAN 3:30 Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.
DAN 4:1 Mfalme Nebukadneza, Kwa watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wanaoishi duniani kote: Mafanikio yawe kwenu sana!
DAN 4:2 Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara za miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia.
DAN 4:3 Ishara zake ni kuu kama nini!
DAN 4:4 Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nyumbani katika jumba langu la kifalme, nikiishi kwa raha na mafanikio.
DAN 4:5 Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita mawazoni mwangu vilinitisha.
DAN 4:6 Hivyo nikaagiza kwamba wenye hekima wote wa Babeli waletwe mbele yangu kunifasiria ndoto yangu.
DAN 4:7 Waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi walipokuja, niliwaambia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunifasiria.
DAN 4:8 Mwishoni, Danieli alikuja mbele yangu, nikamweleza hiyo ndoto. (Danieli anaitwa Belteshaza, kwa jina la mungu wangu, nayo roho ya miungu mitakatifu inakaa ndani yake.)
DAN 4:9 Nikasema, “Belteshaza, mkuu wa waganga, ninajua kuwa roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako, wala hakuna siri iliyo ngumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu, nifasirie.
DAN 4:10 Haya ndio maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana.
DAN 4:11 Mti ule ulikua, ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga; ulionekana hadi miisho ya dunia.
DAN 4:12 Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi, na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo.
DAN 4:13 “Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, na mbele yangu nikaona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni.
DAN 4:14 Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, myafyeke matawi yake; yaondoeni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake, na ndege waondoke kutoka matawi yake.
DAN 4:15 Lakini kiacheni kisiki na mizizi yake, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni. “ ‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia.
DAN 4:16 Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu, na apewe akili ya mnyama, hadi nyakati saba zipite juu yake.
DAN 4:17 “ ‘Uamuzi huu umetangazwa na wajumbe; watakatifu, wametangaza hukumu ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za dunia, naye humpa amtakaye, na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’
DAN 4:18 “Hii ndiyo ndoto niliyoipata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe unaweza, kwa sababu roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako.”
DAN 4:19 Ndipo Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza) alipofadhaika sana kwa muda, nayo mawazo yake yakamtia hofu. Basi mfalme akasema, “Belteshaza, usiruhusu ndoto wala maana yake kukutia hofu.” Belteshaza akajibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii ingewahusu adui zako, na maana yake iwahusu watesi wako!
DAN 4:20 Mti uliouona, uliokua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga na kuonekana duniani kote,
DAN 4:21 ukiwa na majani ya kupendeza na matunda mengi, ukitoa chakula kwa wote, na ukiwapa hifadhi wanyama wa kondeni, na kuwa mahali pa viota katika matawi yake kwa ajili ya ndege wa angani:
DAN 4:22 Ee mfalme, wewe ndiwe ule mti! Umekuwa mkubwa na mwenye nguvu; nao ukuu wako umekua hadi kufika juu angani, nayo mamlaka yako yameenea hadi miisho ya dunia.
DAN 4:23 “Ee mfalme, wewe ulimwona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akasema, ‘Ukateni mti na kuuangamiza, lakini kiacheni kisiki kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kwenye majani ya kondeni, wakati mizizi yake inabaki ardhini. Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, mwacheni aishi kama wanyama pori hadi nyakati saba zipite juu yake.’
DAN 4:24 “Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, na hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme:
DAN 4:25 Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori; utakula nyasi kama ng’ombe, na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita hadi utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.
DAN 4:26 Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejeshwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo hutawala.
DAN 4:27 Kwa hiyo, ee mfalme, uwe radhi kupokea ushauri wangu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako na uwe na huruma kwa waliodhulumiwa. Hivyo itawezekana baada ya hayo, mafanikio yako yataendelea.”
DAN 4:28 Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza.
DAN 4:29 Miezi kumi na mbili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli,
DAN 4:30 alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga uwe makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa, na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”
DAN 4:31 Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya ufalme yameondolewa kwako.
DAN 4:32 Utafukuzwa mbali na wanadamu, ukaishi pamoja na wanyama pori, na utakula nyasi kama ng’ombe. Nyakati saba zitapita juu yako, hadi utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.”
DAN 4:33 Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala nyasi kama ng’ombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni, hadi nywele zake zikakua kama manyoya ya tai, nazo kucha zake kama makucha ya ndege.
DAN 4:34 Mwisho wa wakati huo, mimi Nebukadneza niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, nazo fahamu zangu zikanirudia. Ndipo nikamsifu Yeye Aliye Juu Sana, nikamheshimu na kumhimidi yeye aishiye milele.
DAN 4:35 Mataifa yote ya dunia
DAN 4:36 Wakati huo huo fahamu zangu ziliponirudia, nikarudishiwa heshima yangu na fahari yangu kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na wakuu wangu walikuja kunitafuta, nami nikarudishwa kwenye kiti changu cha ufalme, hata nikawa mkuu kuliko mwanzoni.
DAN 4:37 Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, na humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu anachofanya ni haki, na njia zake zote ni adili. Nao wanaoenda kwa kiburi anaweza kuwashusha.
DAN 5:1 Mfalme Belshaza aliandaa karamu kubwa kwa ajili ya wakuu wake elfu moja, na akanywa mvinyo pamoja nao.
DAN 5:2 Belshaza alipokuwa akinywa divai, aliamuru vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekalu huko Yerusalemu viletwe, ili mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wapate kuvinywea.
DAN 5:3 Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wakavinywea.
DAN 5:4 Walipokuwa wakinywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe.
DAN 5:5 Ghafula vidole vya mkono wa mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya chokaa ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika.
DAN 5:6 Uso wa mfalme ukageuka rangi, naye akaogopa sana, kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.
DAN 5:7 Mfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waaguzi waletwe, naye akawaambia hao wenye hekima wa Babeli, “Yeyote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake atavikwa nguo za zambarau, na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa cheo cha tatu katika ufalme.”
DAN 5:8 Ndipo wenye hekima wote wa mfalme wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake.
DAN 5:9 Basi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu, na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi.
DAN 5:10 Malkia aliposikia sauti za mfalme na wakuu wake, alikuja katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele! Usishtuke! Usibadilike rangi hivyo!
DAN 5:11 Yuko mtu katika ufalme wako mwenye roho ya miungu mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, naam, mfalme baba yako, alimweka kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi.
DAN 5:12 Mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo, na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.”
DAN 5:13 Hivyo Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamuuliza, “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa watu wa uhamisho walioletwa na mfalme baba yangu kutoka Yuda?
DAN 5:14 Nimesikia kwamba roho ya miungu iko ndani yako, na kwamba una ufahamu, akili na hekima ya pekee.
DAN 5:15 Watu wenye hekima na wasihiri waliletwa mbele yangu ili kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, lakini hawakuweza kunifafanulia.
DAN 5:16 Basi nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo magumu. Ikiwa unaweza kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utafanywa mtawala wa tatu katika ufalme.”
DAN 5:17 Ndipo Danieli akamjibu mfalme, “Unaweza kubaki na zawadi zako mwenyewe na kumpa mtu mwingine thawabu zako. Hata hivyo, nitasoma maandishi kwa mfalme na kumwambia maana yake.
DAN 5:18 “Ee mfalme, Mungu Aliye Juu Sana alimpa baba yako Nebukadneza utawala, ukuu, utukufu na fahari.
DAN 5:19 Kwa sababu ya ukuu aliompa baba yako, watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha walimhofu na kumwogopa. Wale ambao mfalme alitaka kuwaua, aliwaua; wale aliotaka kuwaacha hai, aliwaacha hai; wale aliotaka kuwapandisha cheo, aliwapandisha; aliotaka kuwashusha, aliwashusha.
DAN 5:20 Lakini moyo wake ulipokuwa na majivuno na kuwa mgumu kwa kiburi, aliondolewa kutoka kwa kiti chake cha ufalme na kuvuliwa utukufu wake.
DAN 5:21 Akafukuzwa mbali na wanadamu na kupewa akili ya mnyama, akaishi pamoja na punda-mwitu; akala majani kama ng’ombe, nao mwili wake ukaloweshwa kwa umande wa mbingu, hadi alipotambua kwamba Mungu Aliye Juu Sana ndiye mtawala katika falme zote za wanadamu, na kwamba humtawaza juu yao yeyote amtakaye.
DAN 5:22 “Lakini wewe mwanawe, ee Belshaza, hukujinyenyekeza, ingawa ulifahamu haya yote.
DAN 5:23 Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, pamoja na wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea divai. Uliisifu miungu ya fedha na dhahabu, ya shaba, chuma, miti na mawe, miungu ambayo haiwezi kuona, au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake.
DAN 5:24 Kwa hiyo ameutuma mkono ule ulioandika maneno.
DAN 5:25 “Haya ndio maneno yaliyoandikwa: mene, mene, tekeli, na peresi
DAN 5:26 “Hii ndiyo maana ya maneno haya: “Mene: Mungu amezihesabu siku za utawala wako na kuukomesha.
DAN 5:27 “Tekeli: Wewe umepimwa katika mizani na kuonekana umepungua.
DAN 5:28 “Peresi: Ufalme wako umegawanywa na kupewa Wamedi na Waajemi.”
DAN 5:29 Kwa amri ya Belshaza, Danieli akavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni, tena akatangazwa kuwa mtawala wa tatu katika ufalme.
DAN 5:30 Usiku ule ule, Belshaza mfalme wa Wakaldayo akauawa,
DAN 5:31 naye Dario Mmedi akanyakua ufalme akiwa na miaka sitini na mbili.
DAN 6:1 Ilimpendeza Dario kuteua wakuu mia moja na ishirini kutawala katika ufalme wake wote,
DAN 6:2 pamoja na wasimamizi watatu juu yao, Danieli akiwa mmoja wao. Wakuu walitoa hesabu kwa wasimamizi hao ili mfalme asipate hasara.
DAN 6:3 Basi Danieli alijidhihirisha miongoni mwa wasimamizi na wakuu kwa sifa zake za kipekee, hata mfalme akapanga kumweka juu ya ufalme wote.
DAN 6:4 Walipofahamu hilo, wasimamizi na wakuu wakajaribu kutafuta sababu za kumshtaki Danieli kuhusu usimamizi wake wa shughuli za serikali, lakini hawakuweza kufanikiwa. Hawakuweza kupata kosa kwake, kwa sababu alikuwa mwaminifu, wala hakupatikana na upotovu au uzembe.
DAN 6:5 Mwishoni watu hawa wakasema, “Kamwe hatutapata msingi wa mashtaka dhidi ya huyu Danieli, isipokuwa iwe inahusiana na sheria ya Mungu wake.”
DAN 6:6 Basi wasimamizi na wakuu wakaingia kwa mfalme kama kikundi, wakasema, “Ee Mfalme Dario, uishi milele!
DAN 6:7 Wasimamizi wa ufalme, wasaidizi, wakuu, washauri na watawala wote wamekubaliana kwamba mfalme atoe sheria na kukazia amri kuwa yeyote atakayetoa dua kwa mungu au mwanadamu katika muda huu wa siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, ee mfalme, atupwe ndani ya tundu la simba.
DAN 6:8 Sasa, ee mfalme, toa amri na uiandike ili isiweze kubadilishwa: kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.”
DAN 6:9 Hivyo Mfalme Dario akaiweka amri hiyo katika maandishi.
DAN 6:10 Basi Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alienda nyumbani mwake kwenye chumba chake cha ghorofani, ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Akapiga magoti na kuomba mara tatu kwa siku, akimshukuru Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya awali.
DAN 6:11 Ndipo watu hawa wakaenda kama kikundi na kumkuta Danieli akiomba na kumsihi Mungu kwa ajili ya msaada.
DAN 6:12 Basi wakaenda kwa mfalme na kusema naye kuhusu amri ya mfalme: “Je, hukutangaza amri kwamba kwa muda huu wa siku thelathini zijazo mtu ambaye atamwomba mungu au mwanadamu yeyote isipokuwa wewe, ee mfalme, angetupwa ndani ya tundu la simba?” Mfalme akajibu, “Amri ndivyo ilivyo, kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.”
DAN 6:13 Ndipo wakamwambia mfalme, “Danieli, ambaye ni mmoja wa mahamisho kutoka Yuda, hakuheshimu, ee mfalme, wala hajali amri uliyoiweka kwa maandishi. Bado anaomba mara tatu kwa siku.”
DAN 6:14 Mfalme aliposikia hili, akahuzunika mno. Akakusudia kumwokoa Danieli, hivyo akafanya kila jitihada ya kumwokoa hadi jua likatua.
DAN 6:15 Ndipo wale watu wakamwendea mfalme kama kikundi na kumwambia, “Ee mfalme, kumbuka kwamba kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi, hakuna amri wala sheria ambayo mfalme ameitoa inayoweza kubadilishwa.”
DAN 6:16 Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!”
DAN 6:17 Jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mlango wa tundu, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake mwenyewe pamoja na kwa pete za wakuu wake, ili hali ya Danieli isiweze kubadilishwa.
DAN 6:18 Kisha mfalme akarudi kwenye jumba lake la kifalme, naye usiku kucha hakuweza kula wala kutumia viburudisho alivyoletewa, na hakuweza kulala.
DAN 6:19 Asubuhi na mapema, mfalme akaondoka na kuharakisha kwenda kwenye tundu la simba.
DAN 6:20 Alipokaribia lile tundu, mfalme akamwita Danieli kwa sauti ya uchungu: “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai! Je, Mungu wako, unayemtumikia daima, ameweza kukuokoa kwa simba?”
DAN 6:21 Danieli akajibu, “Ee mfalme, uishi milele!
DAN 6:22 Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lolote baya mbele yako, ee mfalme.”
DAN 6:23 Basi Mfalme akafurahi mno, akatoa amri Danieli atolewe kutoka kwa lile tundu. Danieli alipotolewa kutoka kwa lile tundu, hakukutwa na jeraha lolote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake.
DAN 6:24 Kwa amri ya mfalme, wale watu waliokuwa wamemshtaki Danieli kwa uongo waliletwa na kutupwa ndani ya lile tundu la simba, pamoja na wake zao na watoto wao. Nao kabla hawajafika chini kwenye sakafu ya lile tundu, simba wakawakamata na kusaga mifupa yao yote.
DAN 6:25 Kisha Mfalme Dario akawaandikia watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha duniani kote: “Mafanikio yawe kwenu sana!
DAN 6:26 “Natoa amri hii, kwamba katika kila sehemu ya ufalme wangu, lazima watu wamwogope na kumheshimu Mungu wa Danieli.
DAN 6:27 Huponya na kuokoa;
DAN 6:28 Hivyo Danieli akastawi wakati wa utawala wa Dario, na utawala wa Koreshi Mwajemi.
DAN 7:1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita mawazoni mwake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake.
DAN 7:2 Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwa na pepo kutoka pande nne za mbingu, zikivuruga bahari kuu.
DAN 7:3 Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari.
DAN 7:4 “Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa ya tai. Nikatazama hadi mabawa yake yalipong’olewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.
DAN 7:5 “Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, aliyefanana na dubu. Upande wake mmoja alikuwa ameinuka, na alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama, ushibe!’
DAN 7:6 “Baada ya huyo, nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.
DAN 7:7 “Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya, tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; akapondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chini ya nyayo zake chochote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.
DAN 7:8 “Nilipokuwa nikifikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ndogo, iliyojitokeza miongoni mwa zile kumi; pembe tatu za mwanzoni ziling’olewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu, na mdomo ulionena kwa majivuno.
DAN 7:9 “Nilipoendelea kutazama, “viti vya utawala vikawekwa, naye Mzee wa Siku akaketi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama sufu. Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka miali ya moto, nayo magurudumu yake yote yalikuwa yanawaka moto.
DAN 7:10 Mto wa moto ulikuwa unatiririka, ukipita mbele yake. Maelfu elfu wakamhudumia; kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake. Mahakama ikakaa kuhukumu, na vitabu vikafunguliwa.
DAN 7:11 “Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia hadi yule mnyama alipouawa, na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto uliowaka.
DAN 7:12 (Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda.)
DAN 7:13 “Katika maono yangu ya usiku nilitazama, na mbele yangu nikamwona mtu kama Mwana wa Adamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku, na akaongozwa mbele zake.
DAN 7:14 Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu; nao watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.
DAN 7:15 “Mimi Danieli nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya mawazo yangu yalinisumbua.
DAN 7:16 Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale, nikamuuliza maana halisi ya haya yote. “Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi:
DAN 7:17 ‘Hao wanyama wanne wakubwa ni falme nne zitakazoinuka duniani.
DAN 7:18 Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele: naam, milele na milele.’
DAN 7:19 “Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, aliyekuwa tofauti na wale wengine wote, tena wa kutisha sana, na meno yake ya chuma na makucha ya shaba: mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chochote kilichosalia.
DAN 7:20 Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake, na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho kuliko zile nyingine, na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno.
DAN 7:21 Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda,
DAN 7:22 hadi huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipoumiliki ufalme.
DAN 7:23 “Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote, nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda.
DAN 7:24 Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu.
DAN 7:25 Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwatesa watakatifu wake, huku akijaribu kubadili majira na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati.
DAN 7:26 “ ‘Lakini mahakama itakaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele.
DAN 7:27 Ndipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote zitakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’
DAN 7:28 “Huu ndio mwisho wa jambo lile. Mimi Danieli nilitaabika sana katika mawazo yangu, nao uso wangu ukabadilika, lakini nililiweka jambo hilo moyoni mwangu.”
DAN 8:1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Mfalme Belshaza, mimi Danieli nilipata maono, baada ya maono yaliyokuwa yamenitokea awali.
DAN 8:2 Katika maono yangu, nilijiona nikiwa ndani ya ngome ya Shushani katika jimbo la Elamu; katika maono nilikuwa kando ya Mto Ulai.
DAN 8:3 Nikatazama juu, na hapo mbele yangu kulikuwa na kondoo dume mwenye pembe mbili, akiwa amesimama kando ya mto, nazo pembe zake zilikuwa ndefu. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko hiyo nyingine, lakini iliendelea kukua baadaye.
DAN 8:4 Nikamtazama yule kondoo dume alivyokuwa akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyeweza kusimama mbele yake, wala hakuna aliyeweza kuokoa kutoka nguvu zake. Akafanya kama alivyopenda, naye akawa mkuu.
DAN 8:5 Nilipokuwa ninatafakari hili, ghafula beberu mwenye pembe moja kubwa katikati ya macho yake alikuja kutoka magharibi, akiruka kasi juu ya dunia yote bila kugusa ardhi.
DAN 8:6 Alikuja akimwelekea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akisimama kando ya mto, akamshambulia kwa hasira nyingi.
DAN 8:7 Nikamwona akimshambulia yule kondoo dume kwa hasira nyingi, akampiga yule kondoo dume na kuvunja pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuwa na nguvu za kumzuia yule beberu; huyo beberu akamwangusha yule kondoo dume chini na kumkanyaga, wala hakuna aliyeweza kumwokoa yule kondoo dume kutoka nguvu za huyo beberu.
DAN 8:8 Yule beberu akawa mkubwa sana, lakini katika kilele cha nguvu zake, ile pembe yake ndefu ilivunjika, na mahali pake pakaota pembe nne kubwa kuelekea pande nne za dunia.
DAN 8:9 Kutoka mojawapo ya zile pembe nne palitokea pembe ndogo, nayo ikaongezeka nguvu kuelekea kusini, na mashariki, na Nchi ya Kupendeza.
DAN 8:10 Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya nyota za jeshi la angani chini duniani, na kuzikanyaga.
DAN 8:11 Pembe hiyo ikajikweza ili iwe kama Mkuu wa hilo jeshi la Mwenyezi Mungu; ikamwondolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya kila siku, napo mahali pake patakatifu pakashushwa chini.
DAN 8:12 Kwa sababu ya uasi, jeshi la watakatifu na dhabihu za kila siku vikatiwa mkononi mwake. Pembe hiyo ikafanikiwa katika kila kitu ilichofanya, nayo kweli ikatupwa chini.
DAN 8:13 Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mtakatifu mwingine, akamwambia, “Je, itachukua muda gani maono haya yatimie: maono kuhusu dhabihu ya kila siku, uasi unaosababisha ukiwa, kutwaliwa kwa mahali patakatifu, na jeshi litakalokanyagwa chini ya nyayo?”
DAN 8:14 Akaniambia, “Itachukua jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo mahali patakatifu patawekwa wakfu tena.”
DAN 8:15 Mimi Danieli nilipokuwa ninaangalia maono na kujaribu kuelewa, mbele yangu alisimama mmoja aliyefanana na mwanadamu.
DAN 8:16 Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka Mto Ulai ikiita, “Jibraili, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.”
DAN 8:17 Alipokuwa akikaribia pale nilipokuwa nimesimama, niliogopa, nikaanguka kifudifudi. Akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.”
DAN 8:18 Alipokuwa akinena nami, nilikuwa katika usingizi mzito, huku nimelala kifudifudi. Ndipo aliponigusa na kunisimamisha wima.
DAN 8:19 Akaniambia, “Nitakuambia yale yatakayotokea baadaye wakati wa ghadhabu, kwa sababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho ulioamriwa.
DAN 8:20 Kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye ulimwona anawakilisha wafalme wa Umedi na Uajemi.
DAN 8:21 Yule beberu mwenye manyoya mengi ni mfalme wa Uyunani, nayo ile pembe ndefu katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.
DAN 8:22 Zile pembe nne zilizoota badala ya ile pembe iliyovunjika zinawakilisha falme nne ambazo zitatokea kutoka taifa lake, lakini hakuna hata mmoja utakaokuwa na nguvu kama ile pembe iliyovunjika.
DAN 8:23 “Katika sehemu ya mwisho ya utawala wao, waasi watakapokuwa waovu kabisa, atainuka mfalme mwenye uso mkali, aliye stadi wa hila.
DAN 8:24 Atakuwa na nguvu nyingi, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe. Atasababisha uharibifu wa kutisha, na atafanikiwa kwa chochote anachofanya. Atawaangamiza watu maarufu na watu watakatifu.
DAN 8:25 Atasababisha udanganyifu ustawi, naye atajihesabu mwenyewe kuwa bora kuliko wote. Wakati watajisikia kuwa salama, atawaangamiza wengi, na kushindana na Mkuu wa wakuu. Lakini ataangamizwa, isipokuwa si kwa uwezo wa mwanadamu.
DAN 8:26 “Maono kuhusu jioni na asubuhi ambayo umepewa ni kweli, lakini yatie muhuri maono haya, kwa maana yanahusu nyakati za baadaye sana.”
DAN 8:27 Mimi Danieli nilikuwa nimechoka sana, na nikalala nikiwa mgonjwa kwa siku kadhaa. Ndipo nikaamka, nikaendelea na shughuli za mfalme. Nilifadhaishwa na maono hayo; sikuweza kuyaelewa.
DAN 9:1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario mwana wa Ahasuero (mzaliwa wa Umedi), ambaye alifanywa mtawala wa ufalme wa Babeli,
DAN 9:2 katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, mimi Danieli nilielewa kutokana na Maandiko, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu lililopewa nabii Yeremia, kwamba ukiwa wa Yerusalemu ungetimizwa kwa miaka sabini.
DAN 9:3 Kwa hiyo nikamgeukia Mwenyezi Mungu na kumsihi katika maombi na dua, katika kufunga, na kuvaa gunia na kujipaka majivu.
DAN 9:4 Nikamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, na kutubu: “Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake,
DAN 9:5 tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi; tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako.
DAN 9:6 Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu, na watu wote wa nchi.
DAN 9:7 “Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu: watu wa Yuda, na wakaaji wa Yerusalemu, na Waisraeli wote, walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu tulikosa uaminifu kwako.
DAN 9:8 Ee Mwenyezi Mungu, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako.
DAN 9:9 Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake.
DAN 9:10 Hatukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, wala kuzishika sheria alizotupatia kupitia kwa watumishi wake, manabii.
DAN 9:11 Israeli wote wamekosea sheria yako na kugeuka mbali, nao wamekataa kukutii. “Kwa hiyo laana na viapo vya hukumu vilivyoandikwa katika Torati ya Musa, mtumishi wa Mungu, vimemiminwa juu yetu, kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako.
DAN 9:12 Umetimiza maneno uliyosema dhidi yetu na dhidi ya watawala wetu, kwa kuleta maafa makubwa juu yetu. Chini ya mbingu yote kamwe hapajatendeka kitu kama kile kilichotendeka kwa Yerusalemu.
DAN 9:13 Kama vile ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, misiba hii yote imekuja juu yetu, lakini hatujaomba fadhili za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa kuacha kutenda dhambi na kuisikiliza kweli yake.
DAN 9:14 Mwenyezi Mungu hakusita kuleta maafa juu yetu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ni mwenye haki katika kila afanyalo; lakini hata hivyo, hatujamtii.
DAN 9:15 “Sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako Misri kwa mkono wenye nguvu, na kujifanyia Jina linalodumu hadi leo, tumetenda dhambi, tumefanya mabaya.
DAN 9:16 Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki, ondoa hasira yako na ghadhabu yako kwa Yerusalemu, mji wako, mlima wako mtakatifu. Dhambi zetu na maovu ya baba zetu yameifanya Yerusalemu na watu wako kitu cha kudharauliwa kwa wale wote wanaotuzunguka.
DAN 9:17 “Basi Mungu wetu, sasa sikia maombi na dua za mtumishi wako. Ee Bwana, kwa ajili yako angalia kwa huruma ukiwa wa mahali pako patakatifu.
DAN 9:18 Ee Mungu, tega sikio, ukasikie; fumbua macho yako ukaone ukiwa wa mji ule wenye Jina lako. Hatukutolei maombi yetu kwa sababu sisi tuna haki, bali kwa sababu ya rehema zako nyingi.
DAN 9:19 Ee Bwana, sikiliza! Ee Bwana, samehe! Ee Bwana, sikia na ukatende! Kwa ajili yako, Ee Mungu wangu, usikawie, kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa Jina lako.”
DAN 9:20 Basi, nilipokuwa bado nikinena na kuomba, nikiungama dhambi yangu na dhambi ya watu wangu Israeli, na nikifanya maombi yangu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima wake mtakatifu,
DAN 9:21 wakati nilipokuwa bado katika maombi, Jibraili, yule mtu niliyekuwa nimemwona katika maono hapo awali, alinijia kwa kasi karibu wakati wa kutoa dhabihu ya jioni.
DAN 9:22 Akanielimisha na kuniambia, “Danieli, sasa nimekuja kukupa akili na ufahamu.
DAN 9:23 Mara ulipoanza kuomba, jibu lilitolewa, ambalo nimekuja kukupasha habari, kwa maana wewe unapendwa sana. Kwa hiyo, tafakari ujumbe huu na uelewe maono haya:
DAN 9:24 “Majuma sabini yameamriwa kwa ajili ya watu wako na kwa ajili ya mji wako mtakatifu, ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, kuleta haki ya milele, kutia muhuri maono na unabii, na pia kumpaka mafuta yeye aliye mtakatifu sana.
DAN 9:25 “Ujue na kuelewa hili: Tangu kutolewa kwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hadi kuja kwa Mpakwa mafuta, aliye mtawala, kutakuwa na majuma saba, na majuma sitini na mawili. Barabara zitajengwa tena pamoja na mahandaki, lakini katika wakati wa taabu.
DAN 9:26 Baada ya majuma sitini na mawili, Mpakwa Mafuta atakatiliwa mbali, wala hatabaki na kitu. Watu wa mtawala atakayekuja watauharibu mji pamoja na mahali patakatifu. Mwisho utakuja kama mafuriko: Vita vitaendelea hadi mwisho, nao ukiwa umeamriwa.
DAN 9:27 Mtawala huyo atathibitisha agano na watu wengi kwa juma moja. Katikati ya juma hilo atakomesha dhabihu na sadaka. Mahali pa dhabihu katika Hekalu, atasimamisha chukizo la uharibifu, hadi mwisho ulioamriwa utakapomiminwa juu yake yeye aletaye uharibifu.”
DAN 10:1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, Danieli (ambaye aliitwa Belteshaza) alipewa ufunuo. Ujumbe wake ulikuwa kweli, nao ulihusu vita vikubwa. Ufahamu wa ujumbe ulimjia katika maono.
DAN 10:2 Wakati huo, mimi Danieli nikaomboleza kwa majuma matatu.
DAN 10:3 Sikula chakula kizuri; nyama wala divai havikugusa midomo yangu; nami sikujipaka mafuta kamwe hadi majuma matatu yalipotimia.
DAN 10:4 Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilikuwa nimesimama kwenye ukingo wa mto mkubwa Hidekeli.
DAN 10:5 Nikatazama juu, na mbele yangu palikuwa na mtu aliyevaa mavazi ya kitani na mshipi wa dhahabu safi kutoka Ufazi kiunoni mwake.
DAN 10:6 Mwili wake ulikuwa kama zabarajadi safi, uso wake kama radi, macho yake kama miali wa moto, mikono yake na miguu yake kama mng’ao wa shaba iliyosuguliwa, nayo sauti yake kama ya umati mkubwa wa watu.
DAN 10:7 Ni mimi Danieli peke yangu niliyeona hayo maono; watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini waligubikwa na hofu kuu, hata wakakimbia na kujificha.
DAN 10:8 Kwa hiyo niliachwa peke yangu, nikitazama maono hayo makubwa; sikubakiwa na nguvu, na rangi ya uso wangu ikabadilika kama aliyekufa, nikakosa nguvu.
DAN 10:9 Kisha nikamsikia akisema, nami nilipokuwa nikimsikiliza, nikapatwa na usingizi mzito, nikalala kifudifudi.
DAN 10:10 Mkono ulinigusa, ukaninyanyua na kuniweka magotini, mikono yangu ikishika chini, huku nikiwa bado ninatetemeka.
DAN 10:11 Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayoenda kunena nawe; simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Aliponiambia haya, nikasimama nikitetemeka.
DAN 10:12 Ndipo akaendelea kusema, “Danieli, usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.
DAN 10:13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa malaika wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi.
DAN 10:14 Sasa nimekuja kukuelezea mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”
DAN 10:15 Alipokuwa akiniambia haya, nilisujudu, uso wangu ukigusa chini, nikawa bubu.
DAN 10:16 Ndipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nami nimeishiwa nguvu.
DAN 10:17 Bwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia, hata ninashindwa kupumua.”
DAN 10:18 Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu.
DAN 10:19 Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa; jipe nguvu.” Alipozungumza nami, nilipata nguvu, nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.”
DAN 10:20 Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja.
DAN 10:21 Lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wenu.
DAN 11:1 Nami katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario Mmedi, nilisimama kumsaidia na kumlinda.)
DAN 11:2 “Sasa basi, ninakuambia kweli: Wafalme wengine watatu watatokea Uajemi. Kisha atatokea mfalme wa nne, ambaye atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Atakapokuwa amekwisha kujipatia nguvu kwa utajiri wake, atamchochea kila mmoja dhidi ya ufalme wa Uyunani.
DAN 11:3 Ndipo mfalme mwenye nguvu atatokea, atakayetawala kwa nguvu nyingi, na kufanya anavyopenda.
DAN 11:4 Baada ya kujitokeza, himaya yake itavunjwa na kugawanyika katika pande nne za mbinguni. Hautaenda kwa wazao wake, wala hautakuwa na nguvu alizokuwa nazo, kwa sababu himaya yake itang’olewa na kupewa wengine.
DAN 11:5 “Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi yake, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi.
DAN 11:6 Baada ya miaka kadhaa, wataungana. Binti ya mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini nguvu za huyo binti hazitadumu; hata mfalme hatadumu wala nguvu zake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, na baba yake, na yeyote aliyemuunga mkono.
DAN 11:7 “Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake; atapigana dhidi yao, naye atashinda.
DAN 11:8 Tena ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma, na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu, na kuvichukua hadi Misri. Kwa miaka kadhaa atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua.
DAN 11:9 Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia nchi ya mfalme wa Kusini, lakini atarudi hadi kwenye nchi yake mwenyewe.
DAN 11:10 Wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika, na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini.
DAN 11:11 “Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye atakusanya jeshi kubwa, lakini litashindwa.
DAN 11:12 Jeshi litakapotekwa, mfalme wa Kusini atajawa na kiburi, na atachinja maelfu mengi; hata hivyo hatabaki na ushindi.
DAN 11:13 Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; baada ya miaka kadhaa, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri.
DAN 11:14 “Katika nyakati hizo, wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio.
DAN 11:15 Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzingira mji kwa majeshi, na kuuteka mji wa ngome. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu za kumzuia; naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora zaidi, havitakuwa na nguvu za kuwakabili.
DAN 11:16 Huyo mvamia nchi atafanya apendavyo; hakuna yeyote atakayeweza kumpinga. Atajiimarisha katika Nchi ya Kupendeza, na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza.
DAN 11:17 Ataamua kuja na nguvu za ufalme wake wote, na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kuuangusha ufalme, lakini mipango yake haitafanikiwa wala kumsaidia.
DAN 11:18 Ndipo atabadili nia yake na kupigana na nchi za pwani na aziteke nyingi, lakini jemadari mmoja atakomesha ufidhuli wake, na kurudisha ufidhuli wake juu yake.
DAN 11:19 Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.
DAN 11:20 “Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, baada ya miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.
DAN 11:21 “Atakayetawala baada yake atakuwa mtu wa kudharauliwa ambaye hajapewa heshima ya kifalme. Atauvamia ufalme wakati watu wake wanapojiona kuwa salama, naye atautwaa kwa hila.
DAN 11:22 Ndipo jeshi kubwa litafagiliwa mbele yake; jeshi pamoja na mkuu mmoja wa agano wataangamizwa.
DAN 11:23 Baada ya kufanya mapatano naye, atatenda kwa udanganyifu, na ataingia madarakani akitumia watu wachache tu.
DAN 11:24 Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanajiona salama, atayavamia, naye atatimiza kile baba zake na babu zake hawakuweza. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atapanga njama ya kupindua miji yenye ngome, lakini kwa muda mfupi tu.
DAN 11:25 “Atachochea nguvu zake na ushujaa wake kwa jeshi kubwa dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi kubwa lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya hila zilizopangwa dhidi yake.
DAN 11:26 Wale wanaokula kutoka meza ya mfalme watajaribu kumwangamiza; jeshi lake litafagiliwa mbali, nao wengi watakufa vitani.
DAN 11:27 Wafalme hawa wawili, mioyo yao ikiwa imekusudia mabaya, wataketi kwenye meza moja na kudanganyana wao kwa wao, lakini pasipo faida, kwa sababu bado mwisho utakuja katika wakati ulioamriwa.
DAN 11:28 Mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake na utajiri mwingi, lakini atakuwa ameukaza moyo wake kinyume cha agano takatifu. Atachukua hatua dhidi ya hilo agano, kisha arudi nchi yake.
DAN 11:29 “Wakati ulioamriwa, atavamia tena Kusini, lakini wakati huu matokeo yake yatakuwa tofauti na yale ya wakati wa kwanza.
DAN 11:30 Meli za nchi ya Kitimu zitampinga, naye atavunjika moyo. Ndipo atarudi nyuma na kutoa hasira yake dhidi ya agano takatifu. Atarudi na kuonesha fadhili kwa wale wanaoliacha agano takatifu.
DAN 11:31 “Majeshi yake yenye silaha yatainuka ili kunajisi ngome ya Hekalu, na kuondolea mbali sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Ndipo watalisimamisha chukizo la uharibifu linalosababisha ukiwa.
DAN 11:32 Kwa udanganyifu, atapotosha wale walionajisi agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti.
DAN 11:33 “Wenye hekima watawafundisha wengi, ingawa kwa kitambo watauawa kwa upanga au kuchomwa moto, au kukamatwa, au kutekwa nyara.
DAN 11:34 Watakapoanguka, watapokea msaada kidogo, nao wengi wasio waaminifu wataungana nao.
DAN 11:35 Baadhi ya wenye hekima watajikwaa, ili waweze kusafishwa, kutakaswa na kufanywa wasio na waa hadi wakati wa mwisho, kwa maana bado litakuja kwa wakati ulioamriwa.
DAN 11:36 “Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza juu ya kila mungu, naye atasema mambo ambayo hayajawahi kusikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitatukia.
DAN 11:37 Hataonesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu yeyote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote.
DAN 11:38 Badala ya kuwajali miungu, ataheshimu mungu wa ngome; mungu ambaye hakujulikana na baba zake ndiye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani, na zawadi za thamani kubwa.
DAN 11:39 Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni, naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala wa watu wengi, na atagawa nchi kwa gharama.
DAN 11:40 “Wakati wa mwisho, mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita, askari wapanda farasi, na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kuzikumba nchi hizo kama mafuriko.
DAN 11:41 Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu, na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka mkono wake.
DAN 11:42 Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi; hata Misri haitaepuka.
DAN 11:43 Atamiliki hazina za dhahabu na fedha na utajiri wote wa Misri, huku Walibia na Wakushi wakijisalimisha kwake.
DAN 11:44 Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu wengi kabisa.
DAN 11:45 Atasimika mahema yake ya ufalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna yeyote atakayemsaidia.
DAN 12:1 “Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa.
DAN 12:2 Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele.
DAN 12:3 Wale wenye hekima watang’aa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watang’aa kama nyota milele na milele.
DAN 12:4 Lakini wewe Danieli, yafunge na kuyatia muhuri maneno ya kitabu hiki hadi wakati wa mwisho. Wengi wataenda hapa na pale, na maarifa yataongezeka.”
DAN 12:5 Ndipo mimi Danieli nikaangalia, nako mbele yangu walisimama wengine wawili, mmoja katika ukingo huu wa mto, na mwingine ukingo wa pili wa mto.
DAN 12:6 Mmoja wao akamwambia yule mtu aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, “Je, itachukua muda gani kabla mambo haya ya kushangaza hayajatimizwa?”
DAN 12:7 Kisha mtu yule aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, akainua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni, nami nikamsikia akiapa kwa jina lake yeye aishiye milele, akisema, “Itakuwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati. Nguvu za watu watakatifu zitakapokuwa zimevunjwa kabisa, ndipo mambo haya yote yatakapotimizwa.”
DAN 12:8 Nilisikia, lakini sikuelewa. Kwa hiyo nikauliza, “Bwana wangu, matokeo ya haya yote yatakuwa nini?”
DAN 12:9 Akajibu, “Danieli, nenda zako, kwa sababu maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri hadi wakati wa mwisho.
DAN 12:10 Wengi watatakaswa, na kuondolewa mawaa na kufanywa safi, lakini waovu wataendelea kuwa waovu. Hakuna mmoja wa waovu atakayefahamu, lakini wale wenye hekima watafahamu.
DAN 12:11 “Tangu wakati ule wa kukomeshwa kwa dhabihu ya kila siku, na kuanzishwa kwa chukizo la uharibifu, kutakuwepo siku elfu moja na mia mbili na tisini (1,290).
DAN 12:12 Kubarikiwa ni yule atakayevumilia hadi kufikia mwisho wa hizo siku elfu moja mia tatu na thelathini na tano (1,335).
DAN 12:13 “Lakini wewe, nenda zako hadi mwisho. Utapumzika, nawe mwisho wa hizo siku utafufuka ili kuupokea urithi uliowekewa.”
HOS 1:1 Neno la Mwenyezi Mungu lililomjia Hosea mwana wa Beeri wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na wakati wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi, mfalme wa Israeli.
HOS 1:2 Mwenyezi Mungu alipoanza kuzungumza kupitia Hosea, Mwenyezi Mungu alimwambia, “Nenda ukajitwalie mwanamke wa uzinzi na watoto wa uzinzi, kwa sababu nchi ina hatia ya uzinzi wa kupindukia kwa kumwacha Mwenyezi Mungu.”
HOS 1:3 Kwa hiyo alimwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba na kumzalia Hosea mwana.
HOS 1:4 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Hosea, “Mwite jina Yezreeli, kwa kuwa kitambo kidogo nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa ajili ya mauaji ya kule Yezreeli, nami nitaukomesha ufalme wa Israeli.
HOS 1:5 Katika siku ile nitavunja upinde wa Israeli katika Bonde la Yezreeli.”
HOS 1:6 Gomeri akachukua tena mimba akamzaa binti. Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Hosea, “Mwite Lo-Ruhama, kwa maana sitaonesha tena upendo kwa nyumba ya Israeli, kwamba nisije kabisa nikawasamehe.
HOS 1:7 Hata hivyo nitaonesha upendo kwa nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa si kwa upinde, upanga au vita, wala kwa farasi na wapanda farasi, bali kupitia Mwenyezi Mungu, Mungu wao.”
HOS 1:8 Baada ya Gomeri kumwachisha Lo-Ruhama kunyonya, Gomeri alipata mwana mwingine.
HOS 1:9 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Mwite Lo-Ami kwa maana ninyi si watu wangu, nami si Mungu wenu.
HOS 1:10 “Hata hivyo Waisraeli watakuwa kama mchanga kando ya bahari, ambao hauwezi kupimika wala kuhesabiwa. Mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai’.
HOS 1:11 Watu wa Yuda na watu wa Israeli wataunganishwa tena, nao watamchagua kiongozi mmoja nao watakwea watoke katika nchi, kwa kuwa siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.
HOS 2:1 “Waambie ndugu zako, ‘Watu wangu,’ na pia waambie dada zako, ‘Wapendwa wangu.’
HOS 2:2 “Mkemeeni mama yenu, mkemeeni, kwa maana yeye si mke wangu, nami si mume wake. Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake na uzinzi kati ya matiti yake.
HOS 2:3 Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa. Nitamfanya kama jangwa, nitamgeuza awe nchi ya kiu, nami nitamuua kwa kiu.
HOS 2:4 Sitaonesha upendo wangu kwa watoto wake, kwa sababu ni watoto wa uzinzi.
HOS 2:5 Mama yao amekosa uaminifu na amewachukua mimba katika aibu. Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu, ambao hunipa chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na kinywaji changu.’
HOS 2:6 Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake kwa vichaka vya miiba, nitamjengea ukuta ili asiweze kutoka.
HOS 2:7 Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata; atawatafuta lakini hatawapata. Kisha atasema, ‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza, kwa maana nilikuwa na hali njema kuliko sasa.’
HOS 2:8 Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta, niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia kwa kumtumikia Baali.
HOS 2:9 “Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari. Nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu iliyokusudiwa kufunika uchi wake.
HOS 2:10 Basi sasa nitaufunua ufisadi wake mbele ya wapenzi wake; hakuna yeyote atakayemtoa mikononi mwangu.
HOS 2:11 Nitakomesha furaha na macheko yake yote: sikukuu zake za mwaka, sikukuu za Miandamo ya Mwezi, siku zake za Sabato, sikukuu zake zote zilizoamriwa.
HOS 2:12 Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema yalikuwa malipo yake kutoka kwa wapenzi wake; nitaifanya kuwa kichaka, nao wanyama pori wataila.
HOS 2:13 Nitamwadhibu kwa ajili ya siku alizowafukizia uvumba Mabaali; alipojipamba kwa pete na kwa vito vya thamani, na kuwaendea wapenzi wake, lakini mimi alinisahau,” asema Mwenyezi Mungu.
HOS 2:14 “Kwa hiyo sasa nitamshawishi; nitamwongoza hadi jangwani na kuzungumza naye kwa upole.
HOS 2:15 Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu, nami nitalifanya Bonde la Akori mlango wa matumaini. Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake, kama siku zile alizotoka Misri.
HOS 2:16 “Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu, “utaniita mimi ‘Mume wangu’; hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu.’
HOS 2:17 Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka mdomoni mwake, wala hataomba tena kwa majina yao.
HOS 2:18 Katika siku ile nitafanya agano kwa ajili yao na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani, na viumbe vinavyotambaa ardhini. Upinde, upanga na vita, nitaondolea mbali katika nchi, ili wote waweze kukaa salama.
HOS 2:19 Nitakuposa uwe wangu milele; nitakuposa kwa uadilifu na haki, kwa upendo na huruma.
HOS 2:20 Nitakuposa kwa uaminifu, nawe utamkubali Mwenyezi Mungu.
HOS 2:21 “Katika siku ile nitajibu,” asema Mwenyezi Mungu, “nitajibu kwa anga, nazo anga zitajibu kwa nchi;
HOS 2:22 nayo nchi itajibu kwa nafaka, divai mpya na mafuta, navyo vitajibu kwa Yezreeli.
HOS 2:23 Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitaonesha pendo langu kwake yule ambaye nilimwita, ‘Si Mpendwa Wangu.’ Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio Watu Wangu,’ ‘Ninyi ni Watu Wangu’; nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu’.”
HOS 3:1 Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nenda, ukaoneshe upendo wako kwa mke wako tena, ingawa amependwa na mwingine naye ni mzinzi. Mpende kama Mwenyezi Mungu apendavyo Waisraeli, ingawa wanageukia miungu mingine na kupenda mikate mitamu ya zabibu kavu iliyowekwa wakfu.”
HOS 3:2 Basi nilimnunua huyo mwanamke kwa shekeli kumi na tano za fedha, pia kwa kiasi kama cha homeri moja na nusu ya shayiri.
HOS 3:3 Kisha nilimwambia, “Utaishi nami kwa siku nyingi, hupaswi kuwa kahaba au kuwa na uhusiano wa karibu na mtu yeyote, nami nitaishi na wewe.”
HOS 3:4 Kwa maana Waisraeli wataishi siku nyingi bila kuwa na mfalme wala mkuu, bila kuwa na dhabihu wala mawe matakatifu, bila kizibau wala miungu ya nyumbani.
HOS 3:5 Baadaye Waisraeli watarudi na kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na Daudi mfalme wao. Watakuja wakitetemeka kwa Mwenyezi Mungu na kwa baraka zake katika siku za mwisho.
HOS 4:1 Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi Waisraeli, kwa sababu Mwenyezi Mungu analo shtaka dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi: “Hakuna uaminifu, hakuna upendo, hakuna kumjua Mungu katika nchi.
HOS 4:2 Kuna kulaani tu, uongo na uuaji, wizi na uzinzi, bila kuwa na mipaka, nao umwagaji damu mmoja baada ya mwingine.
HOS 4:3 Kwa sababu hii nchi huomboleza, wote wanaoishi ndani yake wanadhoofika; wanyama wa kondeni, ndege wa angani na samaki wa baharini wanakufa.
HOS 4:4 “Lakini mtu yeyote na asilete shtaka, mtu yeyote na asimlaumu mwenzake, kwa maana watu wako ni kama wale waletao mashtaka dhidi ya kuhani.
HOS 4:5 Unajikwaa usiku na mchana, nao manabii hujikwaa pamoja nawe. Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako:
HOS 4:6 watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. “Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeacha kuijali Torati ya Mungu wako mimi nami sitawajali watoto wako.
HOS 4:7 Kadiri makuhani walivyoongezeka, ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu, walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu.
HOS 4:8 Wanajilisha dhambi za watu wangu na kupendezwa na uovu wao.
HOS 4:9 Hata itakuwa: Kama walivyo watu, ndivyo walivyo makuhani. Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao na kuwalipa kwa matendo yao.
HOS 4:10 “Watakula lakini hawatashiba; watajiingiza katika ukahaba lakini hawataongezeka, kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu na kujiingiza wenyewe
HOS 4:11 katika ukahaba; kunywa divai ya zamani na divai mpya huondoa ufahamu
HOS 4:12 wa watu wangu. Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti nao hujibiwa na fimbo ya mti. Roho ya ukahaba imewapotosha, hawana uaminifu kwa Mungu wao.
HOS 4:13 Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima, chini ya mialoni, milibua na miela, ambako kuna vivuli vizuri. Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba na wake za wana wenu uzinzi.
HOS 4:14 “Sitawaadhibu binti zenu wakati wanapogeukia ukahaba, wala wake za wana wenu wanapofanya uzinzi, kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya na kutambikia pamoja na makahaba wa mahali pa ibada za sanamu: watu wasiokuwa na ufahamu wataangamia!
HOS 4:15 “Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli, Yuda naye asije akawa na hatia. “Usiende Gilgali, usipande kwenda Beth-Aveni. Wala usiape, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo!’
HOS 4:16 Waisraeli ni wakaidi, kama ndama jike mkaidi. Ni jinsi gani basi Mwenyezi Mungu anaweza kuwachunga kama wana-kondoo katika shamba la majani?
HOS 4:17 Efraimu amejiunga na sanamu, achana naye!
HOS 4:18 Hata wakati wamemaliza vileo vyao wanaendelea na ukahaba wao, watawala wao hupenda sana njia za aibu.
HOS 4:19 Kisulisuli kitawafagilia mbali na dhabihu zao zitawaletea aibu.
HOS 5:1 “Sikieni hili, enyi makuhani! Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli! Sikieni, ee nyumba ya mfalme! Hukumu hii ni dhidi yenu: Mmekuwa mtego huko Mispa, wavu uliotandwa juu ya Tabori.
HOS 5:2 Waasi wamezidisha sana mauaji. Mimi nitawatiisha wote.
HOS 5:3 Ninajua yote kuhusu Efraimu, Israeli hukufichika kwangu. Efraimu, sasa umegeukia ukahaba, Israeli amenajisika.
HOS 5:4 “Matendo yao hayawaachii kurudi kwa Mungu wao. Roho ya ukahaba iko ndani ya mioyo yao, hawamkubali Mwenyezi Mungu.
HOS 5:5 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao; Waisraeli, hata Efraimu, wanajikwaa katika dhambi zao; pia Yuda atajikwaa pamoja nao.
HOS 5:6 Wanapoenda na makundi yao ya kondoo na ng’ombe kumtafuta Mwenyezi Mungu, hawatampata; yeye amejiondoa kutoka kwao.
HOS 5:7 Wao si waaminifu kwa Mwenyezi Mungu; wamezaa watoto haramu. Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi zitawaangamiza wao pamoja na mashamba yao.
HOS 5:8 “Pigeni tarumbeta huko Gibea, na baragumu huko Rama. Pazeni kelele za vita huko Beth-Aveni; ongoza, ee Benyamini.
HOS 5:9 Efraimu ataachwa ukiwa katika siku ya kuadhibiwa. Miongoni mwa makabila ya Israeli ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.
HOS 5:10 Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaosogeza mawe ya mpaka. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama mafuriko ya maji.
HOS 5:11 Efraimu amedhulumiwa, amekanyagwa katika hukumu kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.
HOS 5:12 Mimi ni kama nondo kwa Efraimu, na kama uozo kwa watu wa Yuda.
HOS 5:13 “Efraimu alipoona ugonjwa wake, naye Yuda vidonda vyake, ndipo Efraimu aligeukia Ashuru, na kuomba msaada kwa mfalme mkuu. Lakini hawezi kukuponya, hawezi kukuponya vidonda vyako.
HOS 5:14 Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu, kama simba mkubwa kwa Yuda. Nitawararua vipande vipande na kuondoka; nitawachukua mbali, na hakuna wa kuwaokoa.
HOS 5:15 Kisha nitarudi mahali pangu hadi watakapokubali kosa lao. Nao watautafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”
HOS 6:1 “Njooni, tumrudie Mwenyezi Mungu. Ameturarua vipande vipande lakini atatuponya; ametujeruhi lakini atatufunga majeraha yetu.
HOS 6:2 Baada ya siku mbili atatufufua; katika siku ya tatu atatuinua, ili tuweze kuishi mbele zake.
HOS 6:3 Tumkubali Mwenyezi Mungu, tukaze kumkubali yeye. Kutokea kwake ni hakika kama vile kuchomoza kwa jua; atatujia kama mvua za masika, kama vile mvua za vuli ziinyweshavyo nchi.”
HOS 6:4 “Nifanye nini nawe, Efraimu? Nifanye nini nawe, Yuda? Upendo wako ni kama ukungu wa asubuhi, kama umande wa alfajiri utowekao.
HOS 6:5 Kwa hiyo nimewakata ninyi vipande vipande nikitumia manabii wangu; nimewaua ninyi kwa maneno ya kinywa changu, hukumu zangu zinawaka kama umeme juu yenu.
HOS 6:6 Kwa maana nataka rehema, wala si dhabihu, na kumkubali Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.
HOS 6:7 Wamevunja agano kama Adamu: hawakuwa waaminifu kwangu huko.
HOS 6:8 Gileadi ni mji wa watenda maovu, umetiwa madoa kwa nyayo za damu.
HOS 6:9 Kama wanyang’anyi wamviziavyo mtu, ndivyo magenge ya makuhani wafanyavyo; wanaulia watu kwenye njia iendayo Shekemu, wakifanya uhalifu wa aibu.
HOS 6:10 Nimeona jambo la kutisha katika nyumba ya Israeli. Huko Efraimu amejitolea kwa ukahaba na Israeli amenajisika.
HOS 6:11 “Pia kwa ajili yako, Yuda, mavuno yameamriwa. “Wakati wowote ningerejesha neema ya watu wangu,
HOS 7:1 kila mara nilipotaka kumponya Israeli, dhambi za Efraimu zinafichuliwa na maovu ya Samaria yanafunuliwa. Wanafanya udanganyifu, wezi huvunja nyumba, maharamia hunyang’anya barabarani,
HOS 7:2 lakini hawafahamu kwamba ninakumbuka matendo yao yote mabaya. Dhambi zao zimewameza, ziko mbele zangu siku zote.
HOS 7:3 “Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao, wakuu wao kwa uongo wao.
HOS 7:4 Wote ni wazinzi, wanawaka kama tanuru ambalo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea kuanzia kukanda unga hadi umekwisha kuumuka.
HOS 7:5 Katika sikukuu ya mfalme wetu wakuu wanawaka kwa mvinyo, naye anawaunga mkono wenye mizaha.
HOS 7:6 Mioyo yao ni kama tanuru, wanamwendea kwa hila. Hasira yao inafoka moshi usiku kucha, wakati wa asubuhi inalipuka kama miali ya moto.
HOS 7:7 Wote ni moto kama tanuru; wanawaangamiza watawala wao. Wafalme wake wote wanaanguka, wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi.
HOS 7:8 “Efraimu anajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate ambao haukuiva.
HOS 7:9 Wageni wananyonya nguvu zake, lakini hafahamu hilo. Nywele zake zina mvi hapa na pale, lakini hana habari.
HOS 7:10 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yake, lakini pamoja na haya yote harudi kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, wala kumtafuta.
HOS 7:11 “Efraimu ni kama hua, hudanganywa kwa urahisi na hana akili: mara anaita Misri, mara anageukia Ashuru.
HOS 7:12 Watakapoenda, nitatupa wavu wangu juu yao; nitawavuta chini waanguke kama ndege wa angani. Nitakaposikia wakikusanyika pamoja, nitawanasa.
HOS 7:13 Ole wao, kwa sababu wamepotoka kutoka kwangu! Maangamizi ni yao kwa sababu wameniasi! Ninatamani kuwakomboa, lakini wanasema uongo dhidi yangu.
HOS 7:14 Hawanililii mimi kutoka mioyoni mwao, bali wanaomboleza vitandani mwao. Hukusanyika pamoja kwa ajili ya nafaka na divai mpya, lakini hugeukia mbali nami.
HOS 7:15 Niliwafundisha na kuwatia nguvu, lakini wanapanga mabaya dhidi yangu.
HOS 7:16 Hawamgeukii Yeye Aliye Juu Sana, wako kama upinde wenye kasoro. Viongozi wao wataanguka kwa upanga kwa sababu ya maneno yao ya jeuri. Kwa ajili ya hili watadhihakiwa katika nchi ya Misri.
HOS 8:1 “Wekeni tarumbeta midomoni mwenu! Tai yuko juu ya nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa sababu watu wamevunja agano langu, wameasi dhidi ya sheria yangu.
HOS 8:2 Israeli ananililia, ‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’
HOS 8:3 Lakini Israeli amekataa lile lililo jema, adui atamfuatia.
HOS 8:4 Wanaweka wafalme bila idhini yangu, wamechagua wakuu bila kibali changu. Kwa fedha zao na dhahabu wamejitengenezea sanamu kwa ajili ya maangamizi yao wenyewe.
HOS 8:5 Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama! Hasira yangu inawaka dhidi yao. Watakuwa najisi hadi lini?
HOS 8:6 Zimetoka katika Israeli! Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu. Atavunjwa vipande vipande, yule ndama wa Samaria.
HOS 8:7 “Wanapanda upepo na kuvuna kisulisuli. Bua halina suke, halitatoa unga. Kama lingetoa nafaka, wageni wangeila yote.
HOS 8:8 Israeli amemezwa; sasa yupo miongoni mwa mataifa kama kitu kisicho na thamani.
HOS 8:9 Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake. Efraimu amejiuza mwenyewe kwa wapenzi.
HOS 8:10 Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa, sasa nitawakusanya pamoja. Wataanza kudhoofika chini ya uonevu wa mfalme mwenye nguvu.
HOS 8:11 “Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi kwa ajili ya sadaka za dhambi, hizi zimekuwa madhabahu za kufanyia dhambi.
HOS 8:12 Niliwaandikia mambo mengi yaliyohusu sheria yangu, lakini waliziangalia kama kitu kigeni.
HOS 8:13 Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi nao wanakula hiyo nyama, lakini Mwenyezi Mungu hapendezwi nao. Sasa ataukumbuka uovu wao na kuadhibu dhambi zao: Watarudi Misri.
HOS 8:14 Israeli amemsahau Muumba wake na kujenga majumba ya kifalme, Yuda amejengea miji mingi ngome. Lakini nitatuma moto kwenye miji yao utakaoteketeza ngome zao.”
HOS 9:1 Usifurahie, ee Israeli; usishangilie kama mataifa mengine. Kwa kuwa hukuwa mwaminifu kwa Mungu wako; umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu ya kupuria nafaka.
HOS 9:2 Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai havitalisha watu, divai mpya itawapungukia.
HOS 9:3 Hawataishi katika nchi ya Mwenyezi Mungu, Efraimu atarudi Misri na atakula chakula kilicho najisi huko Ashuru.
HOS 9:4 Hawatammiminia Mwenyezi Mungu sadaka ya divai wala dhabihu zao hazitampendeza. Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao kama mkate wa waombolezaji; nao wote wazilao watakuwa najisi. Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe; kisije katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
HOS 9:5 Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa, katika siku za sikukuu za Mwenyezi Mungu?
HOS 9:6 Hata ikiwa wataokoka maangamizi, Misri atawakusanya, nayo Memfisi itawazika. Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma, nayo miiba itafunika mahema yao.
HOS 9:7 Siku za adhabu zinakuja, siku za malipo zimewadia. Israeli na afahamu hili. Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana na uadui wenu ni mkubwa sana, nabii anadhaniwa ni mpumbavu, mtu aliyeongozwa na Mungu anaonekana mwendawazimu.
HOS 9:8 Nabii, pamoja na Mungu wangu, ndiye mlinzi juu ya Efraimu, hata hivyo mitego inamngojea katika mapito yake yote, na uadui katika nyumba ya Mungu wake.
HOS 9:9 Wamezama sana katika rushwa, kama katika siku za Gibea. Mungu atakumbuka uovu wao na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.
HOS 9:10 “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama kupata zabibu jangwani; nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona matunda ya kwanza katika mtini. Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu kwa ile sanamu ya aibu, nao wakawa najisi kama kitu kile walichokipenda.
HOS 9:11 Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege: hakuna kuzaa, hakuna kubeba mimba, hakuna kuchukua mimba.
HOS 9:12 Hata wakilea watoto, nitamuua kila mmoja. Ole wao nitakapowapiga kisogo!
HOS 9:13 Nimemwona Efraimu, kama Tiro, aliyeoteshwa mahali pazuri. Lakini Efraimu wataleta watoto wao kwa mchinjaji.”
HOS 9:14 Wape, Ee Mwenyezi Mungu, je, utawapa nini? Wape tumbo zinazoharibu mimba na matiti yaliyokauka.
HOS 9:15 “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, niliwachukia huko. Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, nitawafukuza katika nyumba yangu. Sitawapenda tena, viongozi wao wote ni waasi.
HOS 9:16 Efraimu ameharibiwa, mzizi wao umenyauka, hawazai tunda. Hata kama watazaa watoto, nitawachinja wazao wao waliotunzwa vizuri.”
HOS 9:17 Mungu wangu atawakataa kwa sababu hawakumtii; watakuwa watu wa kutangatanga miongoni mwa mataifa.
HOS 10:1 Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana, alijizalia matunda mwenyewe. Kadiri matunda yake yalivyoongezeka, alijenga madhabahu zaidi; kadiri nchi yake ilivyostawi, alipamba mawe yake ya ibada.
HOS 10:2 Moyo wao ni mdanganyifu, nao sasa lazima wachukue hatia yao. Mwenyezi Mungu atabomoa madhabahu zao na kuharibu mawe yao ya ibada.
HOS 10:3 Kisha watasema, “Hatuna mfalme kwa sababu hatukumheshimu Mwenyezi Mungu. Lakini hata kama tungekuwa na mfalme, angeweza kutufanyia nini?”
HOS 10:4 Wanaweka ahadi nyingi, huapa viapo vya uongo wanapofanya mapatano; kwa hiyo mashtaka huchipuka kama magugu ya sumu katika shamba lililolimwa.
HOS 10:5 Watu wanaoishi Samaria huogopa kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni. Watu wake wataiombolezea, vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu, wale waliokuwa wamefurahia fahari yake, kwa sababu itaondolewa kutoka kwao kwenda uhamishoni.
HOS 10:6 Itachukuliwa kwenda Ashuru kama ushuru kwa mfalme mkuu. Efraimu atafedheheshwa; Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti.
HOS 10:7 Samaria na mfalme wake wataelea kama kijiti juu ya maji.
HOS 10:8 Mahali pa juu pa uovu pataharibiwa: ndiyo dhambi ya Israeli. Miiba na mibaruti itaota na kufunika madhabahu zao. Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!” na vilima, “Tuangukieni!”
HOS 10:9 “Tangu siku za Gibea, umetenda dhambi, ee Israeli, huko ndiko ulibaki. Je, vita havikuwapata watenda maovu huko Gibea?
HOS 10:10 Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu; mataifa yatakusanywa dhidi yao ili kuwaweka katika vifungo kwa ajili ya dhambi zao mbili.
HOS 10:11 Efraimu ni ndama jike aliyefundishwa ambaye hupenda kupura; hivyo nitamfunga nira juu ya shingo yake nzuri. Nitamwendesha Efraimu, Yuda lazima alime, naye Yakobo lazima avunjavunje mabonge ya udongo.
HOS 10:12 Jipandieni wenyewe haki, vuneni matunda ya upendo usio na kikomo, vunjeni ardhi yenu isiyolimwa; kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Mwenyezi Mungu, hadi atakapokuja na kuwanyeshea juu yenu haki.
HOS 10:13 Lakini mmepanda uovu, mkavuna ubaya, mmekula tunda la udanganyifu. Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe na wingi wa mashujaa wenu,
HOS 10:14 mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako, na ngome zako zote zitaharibiwa: kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita, wakati mama pamoja na watoto wao walipotupwa kwa nguvu ardhini.
HOS 10:15 Ndivyo itakavyotokea kwako, ee Betheli, kwa sababu uovu wako ni mkuu. Siku ile itakapopambazuka, mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.
HOS 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda; nilimwita mwanangu kutoka Misri.
HOS 11:2 Lakini kadiri nilivyomwita Israeli, ndivyo walivyoenda mbali nami. Walitoa dhabihu kwa Mabaali na kufukiza uvumba kwa vinyago.
HOS 11:3 Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea, nikiwashika mikono; lakini hawakutambua kuwa ni mimi niliyewaponya.
HOS 11:4 Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu, kwa vifungo vya upendo; niliondoa nira shingoni mwao nami nikainama kuwalisha.
HOS 11:5 “Je, hawatarudi Misri, nayo Ashuru haitawatawala kwa sababu wamekataa kutubu?
HOS 11:6 Upanga utavurumishwa katika miji yao, nao utaharibu makomeo ya malango yao na kukomesha mipango yao.
HOS 11:7 Watu wangu wamedhamiria kuniacha. Hata wakimwita Yeye Aliye Juu Sana, kwa vyovyote hatawainua.
HOS 11:8 “Efraimu, ninawezaje kukuacha? Ee Israeli, ninawezaje kukutoa? Nitawezaje kukutendea kama Adma? Nitawezaje kukufanya kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zote zimeamshwa.
HOS 11:9 Sitatimiza hasira yangu kali, wala sitageuka na kumharibu Efraimu. Kwa kuwa mimi ndimi Mungu, wala si mwanadamu, Aliye Mtakatifu miongoni mwenu. Sitakuja kwa ghadhabu.
HOS 11:10 Watamfuata Mwenyezi Mungu; atanguruma kama simba. Anaponguruma, watoto wake watakuja wakitetemeka kutoka magharibi.
HOS 11:11 Watakuja wakitetemeka kama ndege wakitoka Misri, kama hua wakitoka Ashuru. Nitawafanya waishi katika nyumba zao,” asema Mwenyezi Mungu.
HOS 11:12 Efraimu amenizunguka kwa uongo, nyumba ya Israeli kwa udanganyifu. Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu, hata kinyume cha yule mwaminifu Aliye Mtakatifu.
HOS 12:1 Efraimu anajilisha upepo; hufukuzia upepo wa mashariki kutwa nzima na kuzidisha uongo na jeuri. Anafanya mkataba na Ashuru na kutuma mafuta ya zeituni Misri.
HOS 12:2 Mwenyezi Mungu analo shtaka dhidi ya Yuda, atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake na kumlipa kwa kadiri ya matendo yake.
HOS 12:3 Yakobo akiwa tumboni alishika kisigino cha kaka yake; kama mwanadamu, alishindana na Mungu.
HOS 12:4 Alishindana na malaika na kumshinda; alilia na kuomba upendeleo wake. Alimkuta huko Betheli na kuzungumza naye huko:
HOS 12:5 Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mwenyezi Mungu ndilo jina lake!
HOS 12:6 Lakini ni lazima urudi kwa Mungu wako; dumisha upendo na haki, nawe umngojee Mungu wako siku zote.
HOS 12:7 Mfanyabiashara hutumia vipimo vya udanganyifu; hupenda kupunja.
HOS 12:8 Efraimu hujisifu akisema, “Mimi ni tajiri sana; nimetajirika. Pamoja na utajiri wangu wote hawatakuta ndani yangu uovu wowote au dhambi.”
HOS 12:9 “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewaleta kutoka Misri; nitawafanya mkae tena kwenye mahema, kama vile katika siku za sikukuu zenu zilizoamriwa.
HOS 12:10 Niliongea na manabii, nikawapa maono mengi na kusema mifano kupitia wao.”
HOS 12:11 Je, Gileadi si mwovu? Watu wake hawafai kitu! Je, hawatoi dhabihu za mafahali huko Gilgali? Madhabahu zao zitakuwa kama malundo ya mawe katika shamba lililolimwa.
HOS 12:12 Yakobo alikimbilia katika nchi ya Aramu; Israeli alitumika ili apate mke, ili aweze kulipa kwa ajili yake alichunga kondoo.
HOS 12:13 Mwenyezi Mungu alimtumia nabii kumpandisha Israeli kutoka Misri, kupitia kwa nabii alimtunza.
HOS 12:14 Lakini Efraimu amemchochea sana hasira; Bwana wake ataleta juu yake hatia yake ya kumwaga damu naye atamlipiza kwa ajili ya dharau yake.
HOS 13:1 Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka; alitukuzwa katika Israeli. Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali, naye akafa.
HOS 13:2 Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi; wanajitengenezea sanamu kutokana na fedha yao, vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari, vyote kazi ya fundi stadi. Inasemekana kuhusu hawa watu, “Hutoa dhabihu za binadamu na kubusu sanamu za ndama.”
HOS 13:3 Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi, kama umande wa alfajiri utowekao, kama makapi yapeperushwayo kutoka sakafu ya kupuria nafaka, kama moshi utorokao kupitia dirishani.
HOS 13:4 “Bali mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewaleta ninyi toka Misri. Msimkubali Mungu mwingine ila mimi, hakuna Mwokozi isipokuwa mimi.
HOS 13:5 Niliwatunza huko jangwani, katika nchi yenye joto liunguzalo.
HOS 13:6 Nilipowalisha, walishiba, waliposhiba, wakajivuna, kisha wakanisahau mimi.
HOS 13:7 Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba, kama chui nitawavizia kando ya njia.
HOS 13:8 Kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake, nitawashambulia na kurarua vifua vyenu. Kama simba nitawala; mnyama pori atawararua vipande vipande.
HOS 13:9 “Ee Israeli, umeangamizwa, kwa sababu wewe u kinyume nami, kinyume na msaidizi wako.
HOS 13:10 Yuko wapi mfalme wako, ili apate kukuokoa? Wako wapi watawala wako katika miji yako yote ambao ulisema kuwahusu, ‘Nipe mfalme na wakuu’?
HOS 13:11 Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme na katika ghadhabu yangu nilimwondoa.
HOS 13:12 Kosa la Efraimu limehifadhiwa, dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu.
HOS 13:13 Uchungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia, lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima; wakati utakapowadia hatatoka katika tumbo la mama yake.
HOS 13:14 “Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi, nitawakomboa kutoka mautini. Yako wapi, ee mauti, mateso yako? Uko wapi, ee Kuzimu, uharibifu wako? “Sitakuwa na huruma,
HOS 13:15 hata ingawa Efraimu atastawi miongoni mwa ndugu zake. Upepo wa mashariki kutoka kwa Mwenyezi Mungu utakuja, ukivuma kutoka jangwani, chemchemi yake haitatoa maji na kisima chake kitakauka. Ghala lake litatekwa hazina zake zote.
HOS 13:16 Watu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao, kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao. Wataanguka kwa upanga; watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini, wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”
HOS 14:1 Rudi, ee Israeli, kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Dhambi zako zimekuwa anguko lako!
HOS 14:2 Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Mwenyezi Mungu. Mwambieni: “Samehe dhambi zetu zote na utupokee kwa neema, ili tuweze kutoa matunda yetu kama sadaka za mafahali.
HOS 14:3 Ashuru hawezi kutuokoa, hatutapanda farasi wa vita. Kamwe hatutasema tena ‘miungu yetu’ kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza, kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”
HOS 14:4 “Nitaponya ukaidi wao na kuwapenda kwa hiari yangu, kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.
HOS 14:5 Nitakuwa kama umande kwa Israeli; atachanua kama yungiyungi. Kama mwerezi wa Lebanoni atashusha mizizi yake chini;
HOS 14:6 matawi yake yatatanda. Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni, harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.
HOS 14:7 Watu wataishi tena kwenye kivuli chake. Atastawi kama nafaka. Atachanua kama mzabibu, nao umaarufu wake utakuwa kama divai inayotoka Lebanoni.
HOS 14:8 Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu? Nitamjibu na kumtunza. Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi; kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”
HOS 14:9 Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya. Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa. Njia za Mwenyezi Mungu ni adili; wenye haki huenda katika njia hizo, lakini waasi watajikwaa ndani yake.
JOE 1:1 Neno la Mwenyezi Mungu ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli.
JOE 1:2 Sikilizeni hili, enyi wazee; sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi. Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea katika siku zenu au katika siku za babu zenu?
JOE 1:3 Waelezeni watoto wenu, na watoto wenu wawaambie watoto wao, na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.
JOE 1:4 Kilichosazwa na kundi la tunutu nzige wakubwa wamekula, kilichosazwa na nzige wakubwa parare wamekula, kilichosazwa na parare madumadu wamekula.
JOE 1:5 Amkeni, enyi walevi, mlie! Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, kwa kuwa mmenyang’anywa kutoka midomoni mwenu.
JOE 1:6 Taifa limevamia nchi yangu, lenye nguvu tena lisilo na idadi; lina meno ya simba, magego ya simba jike.
JOE 1:7 Limeharibu mizabibu yangu na kuangamiza mitini yangu. Limebambua magome yake na kuyatupilia mbali, likayaacha matawi yake yakiwa meupe.
JOE 1:8 Omboleza kama bikira aliyevaa gunia akimwomboleza mume wa ujana wake.
JOE 1:9 Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu. Makuhani wanaomboleza, wale wanaohudumu mbele za Mwenyezi Mungu.
JOE 1:10 Mashamba yameharibiwa, ardhi imekauka; nafaka imeharibiwa, mvinyo mpya umekauka, mafuta yamekoma.
JOE 1:11 Kateni tamaa, enyi wakulima, lieni, enyi mlimao mizabibu; huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri, kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.
JOE 1:12 Mzabibu umekauka na mtini umenyauka; mkomamanga, mtende na mtofaa, miti yote shambani, imekauka. Hakika furaha yote ya mwanadamu imeondoka.
JOE 1:13 Vaeni gunia, enyi makuhani, mwomboleze; pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni. Njooni, vaeni gunia usiku kucha, enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu; kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.
JOE 1:14 Tangazeni saumu takatifu; liiteni kusanyiko takatifu. Waiteni wazee na wote wanaoishi katika nchi waende katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, wakamlilie Mwenyezi Mungu.
JOE 1:15 Ole kwa siku hiyo! Kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu; itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.
JOE 1:16 Je, chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu: furaha na shangwe kutoka nyumba ya Mungu wetu?
JOE 1:17 Mbegu zinakauka chini ya mabonge ya udongo. Maghala yameachwa katika uharibifu, maghala ya nafaka yamebomolewa, kwa maana hakuna nafaka.
JOE 1:18 Jinsi gani ng’ombe wanavyolia! Makundi ya mifugo yanahangaika kwa sababu hawana malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka.
JOE 1:19 Kwako, Ee Mwenyezi Mungu, naita, kwa kuwa moto umeteketeza malisho ya mbugani na miali ya moto imeunguza miti yote shambani.
JOE 1:20 Hata wanyama pori wanakuonea shauku; vijito vya maji vimekauka, na moto umeteketeza malisho yote ya mbugani.
JOE 2:1 Pigeni tarumbeta katika Sayuni; pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu. Wote wanaoishi katika nchi na watetemeke, kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu inakuja. Iko karibu,
JOE 2:2 siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na utusitusi. Kama mapambazuko yanavyosambaa toka upande huu wa milima hata upande mwingine, jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja. Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani, wala halitakuwepo tena kamwe kwa vizazi vijavyo.
JOE 2:3 Mbele yao moto unateketeza, nyuma yao miali ya moto inawaka kwa nguvu. Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni, nyuma yao ni jangwa lisilofaa: hakuna kitu kinachowaepuka.
JOE 2:4 Wanaonekana kama farasi; wanaenda mbio kama askari wapanda farasi.
JOE 2:5 Wanatoa sauti kama magari ya vita, wanaporukaruka juu ya vilele vya milima, kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua, kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita.
JOE 2:6 Wanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu; kila uso unabadilika rangi.
JOE 2:7 Wanashambulia kama mashujaa; wanapanda kuta kama askari. Wote wanatembea katika safu, hawapotoshi safu zao.
JOE 2:8 Hakuna anayemsukuma mwenzake; kila mmoja anaenda mbele moja kwa moja. Wanapita katika vizuizi bila kuharibu safu zao.
JOE 2:9 Wanaenda kasi kuingia mjini; wanakimbia ukutani. Wanaingia ndani ya nyumba; kwa kuingilia madirishani kama wezi.
JOE 2:10 Mbele yao dunia inatikisika, anga linatetemeka, jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota hazitoi mwanga wake tena.
JOE 2:11 Mwenyezi Mungu anatoa mshindo wa ngurumo mbele ya jeshi lake; majeshi yake hayana idadi, ni wenye nguvu nyingi wale ambao hutii agizo lake. Siku ya Mwenyezi Mungu ni kuu, ni ya kutisha. Ni nani anayeweza kuistahimili?
JOE 2:12 “Hata sasa,” asema Mwenyezi Mungu, “nirudieni kwa mioyo yenu yote, kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.”
JOE 2:13 Rarueni mioyo yenu na siyo mavazi yenu. Mrudieni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa maana yeye ndiye mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo, huona huruma, hujizuia kuleta maafa.
JOE 2:14 Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma na kuacha baraka nyuma yake: sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
JOE 2:15 Pigeni tarumbeta katika Sayuni, tangazeni saumu takatifu, liiteni kusanyiko takatifu.
JOE 2:16 Wakusanyeni watu, wekeni wakfu kusanyiko; waleteni pamoja wazee, wakusanyeni watoto, wale wanyonyao maziwa. Bwana arusi na atoke chumbani mwake na bibi arusi naye atoke katika chumba chake.
JOE 2:17 Makuhani, ambao wanahudumu mbele za Mwenyezi Mungu, na walie katikati ya ukumbi wa Hekalu na madhabahu. Waseme, “Wahurumie watu wako, Ee Mwenyezi Mungu. Usifanye urithi wako kitu cha kudharauliwa, neno la dhihaka kati ya mataifa. Kwa nini wasemezane miongoni mwao, ‘Yuko wapi Mungu wao?’ ”
JOE 2:18 Kisha Mwenyezi Mungu atakuwa na wivu kwa ajili ya nchi yake na kuwa na huruma juu ya watu wake.
JOE 2:19 Mwenyezi Mungu atawajibu: “Ninawapelekea nafaka, mvinyo mpya na mafuta, vya kuwatosha ninyi hadi mridhike kabisa; kamwe sitawafanya tena kitu cha kudharauliwa na mataifa.
JOE 2:20 “Nitafukuza jeshi la kaskazini likae mbali nanyi, nikilisukuma ndani ya jangwa, askari wa safu za mbele wakienda ndani ya bahari ya mashariki na wale wa safu za nyuma katika bahari ya magharibi. Uvundo wake utapaa juu; harufu yake itapanda juu.” Hakika ametenda mambo makubwa.
JOE 2:21 Usiogope, ee nchi; furahi na kushangilia. Hakika Mwenyezi Mungu ametenda mambo makubwa.
JOE 2:22 Msiogope, enyi wanyama pori, kwa kuwa mbuga za malisho yenu zinarudia ubichi. Miti nayo inazaa matunda, mtini na mzabibu inatoa utajiri wake.
JOE 2:23 Furahini, enyi watu wa Sayuni, shangilieni katika Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa kuwa amewapa mvua za vuli kwa kipimo cha haki. Anawapelekea mvua nyingi, mvua ya vuli na ya masika, kama mwanzoni.
JOE 2:24 Sakafu za kupuria zitajaa nafaka, mapipa yatafurika mvinyo mpya na mafuta.
JOE 2:25 “Nitawalipa kwa ajili ya miaka ile iliyoliwa na nzige: parare, madumadu na tunutu, jeshi langu kubwa ambalo nililituma kati yenu.
JOE 2:26 Mtakuwa na wingi wa vyakula hadi mshibe, na mtalisifu jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye amefanya maajabu kwa ajili yenu; kamwe watu wangu hawataaibishwa tena.
JOE 2:27 Ndipo mtajua kuwa mimi niko katika Israeli, kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kwamba hakuna mwingine; kamwe watu wangu hawataaibika tena.
JOE 2:28 “Hata itakuwa, baada ya hayo, nitamimina Roho wangu Mtakatifu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono.
JOE 2:29 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu Mtakatifu.
JOE 2:30 Nami nitaonesha maajabu katika mbingu na duniani: damu, moto na mawimbi ya moshi.
JOE 2:31 Jua litageuzwa kuwa giza na mwezi kuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ya Mwenyezi Mungu ile kuu na ya kutisha.
JOE 2:32 Na kila mtu atakayeliitia jina la Mwenyezi Mungu ataokolewa. Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu kutakuwa na wokovu, kama Mwenyezi Mungu alivyosema, miongoni mwa walionusurika ambao Mwenyezi Mungu awaita.
JOE 3:1 “Katika siku hizo na wakati huo, nitakaporejesha neema ya Yuda na Yerusalemu,
JOE 3:2 nitayakusanya mataifa yote na kuyaleta katika Bonde la Yehoshafati. Hapo nitaingia kwenye hukumu dhidi yao kuhusu urithi wangu, watu wangu Israeli, kwa kuwa waliwatawanya watu wangu miongoni mwa mataifa na kuigawa nchi yangu.
JOE 3:3 Waliwapigia kura watu wangu na kuwauza wavulana ili kupata makahaba; waliwauza wasichana ili wapate kunywa mvinyo.
JOE 3:4 “Sasa una nini dhidi yangu, ee Tiro na Sidoni, nanyi nchi zote za Ufilisti? Je, mnanilipiza kwa yale niliyoyafanya? Kama mnalipa, mimi nitalipiza juu ya vichwa vyenu kwa kasi na kwa haraka yale mliyoyatenda.
JOE 3:5 Kwa kuwa mlichukua fedha na dhahabu yangu pia mkabeba hazina zangu nzuri sana mkapeleka kwenye mahekalu yenu.
JOE 3:6 Mliwauza watu wa Yuda na Yerusalemu kwa Wayunani, ili mpate kuwapeleka mbali na nchi yao.
JOE 3:7 “Tazama nitawaamsha kutoka zile sehemu mlizowauza, nami nitawalipiza juu ya vichwa vyenu kile mlichofanya.
JOE 3:8 Nitawauza wana wenu wa kiume na wa kike kwa watu wa Yuda, nao watawauza kwa Waseba, taifa lililo mbali.” Mwenyezi Mungu amesema.
JOE 3:9 Tangazeni hili miongoni mwa mataifa: Jiandaeni kwa vita! Amsha mashujaa! Wapiganaji wote wasogee karibu na kushambulia.
JOE 3:10 Majembe yenu yafueni yawe panga, na miundu yenu ya kukatia iwe mikuki. Aliye dhaifu na aseme, “Mimi nina nguvu!”
JOE 3:11 Njooni haraka, ninyi mataifa yote kutoka pande zote, kusanyikeni huko. Shusha mashujaa wako, Ee Mwenyezi Mungu!
JOE 3:12 “Mataifa na yaamshwe; na yasonge mbele kuelekea Bonde la Yehoshafati, kwa kuwa nitaketi mahali pale kuhukumu mataifa yote yaliyo kila upande.
JOE 3:13 Tia mundu, kwa kuwa mavuno yamekomaa. Njooni, mkanyage zabibu, kwa kuwa shinikizo la kukamulia zabibu limejaa na mapipa yanafurika: kwa kuwa uovu wao ni mkubwa!”
JOE 3:14 Umati mkubwa, umati mkubwa katika bonde la uamuzi! Kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu ni karibu katika bonde la uamuzi.
JOE 3:15 Jua na mwezi vitatiwa giza, na nyota hazitatoa mwanga wake tena.
JOE 3:16 Mwenyezi Mungu atanguruma kutoka Sayuni na mshindo wa ngurumo kutoka Yerusalemu; dunia na mbingu vitatikisika. Lakini Mwenyezi Mungu atakuwa kimbilio la watu wake, ngome imara kwa ajili ya watu wa Israeli.
JOE 3:17 “Ndipo mtajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, nakaa Sayuni, mlima wangu mtakatifu. Yerusalemu utakuwa mtakatifu; kamwe wageni hawatauvamia tena.
JOE 3:18 “Katika siku hiyo milima itadondosha divai mpya, na vilima vitatiririka maziwa; mabonde yote ya Yuda yatatiririka maji. Chemchemi itatiririka kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu na kunywesha Bonde la Shitimu.
JOE 3:19 Lakini Misri itakuwa ukiwa, Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya jeuri waliofanya kwa watu wa Yuda, ambao katika nchi yao walimwaga damu isiyo na hatia.
JOE 3:20 Yuda itakaliwa na watu milele na Yerusalemu itadumu vizazi vyote.
JOE 3:21 Hatia yao ya damu, ambayo sijasamehe, nitasamehe.”
AMO 1:1 Maneno ya Amosi, mmoja wa wachungaji wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli.
AMO 1:2 Alisema: “Mwenyezi Mungu ananguruma toka Sayuni, pia ananguruma kutoka Yerusalemu; malisho ya wachungaji yanakauka, kilele cha Karmeli kinanyauka.”
AMO 1:3 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Dameski, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliipura Gileadi kwa vyombo vya chuma vyenye meno.
AMO 1:4 Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi.
AMO 1:5 Nitalivunja lango la Dameski; nitamwangamiza mfalme aliye katika Bonde la Aveni, na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni. Watu wote wa Aramu wataenda uhamishoni huko Kiri,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 1:6 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Gaza, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima na kuwauza kwa Edomu,
AMO 1:7 nitatuma moto juu ya kuta za Gaza ambao utateketeza ngome zake.
AMO 1:8 Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni. Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni, hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,” asema Bwana Mungu Mwenyezi.
AMO 1:9 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Tiro, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu, na kutokujali mapatano ya undugu,
AMO 1:10 Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro ambao utateketeza ngome zake.”
AMO 1:11 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Edomu, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, alikataa kuonesha huruma yoyote, kwa sababu hasira yake kali iliendelea kupanda wakati wote na ghadhabu iliwaka bila kuzuiliwa.
AMO 1:12 Nitatuma moto juu ya Temani ambao utateketeza ngome za Bosra.”
AMO 1:13 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Amoni, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliwatumbua wanawake wajawazito wa Gileadi ili kuongeza mipaka yake.
AMO 1:14 Nitatuma moto kwenye kuta za Raba ambao utateketeza ngome zake katikati ya kelele za vita katika siku ya mapigano, katikati ya upepo mkali katika siku ya dhoruba.
AMO 1:15 Mfalme wake ataenda uhamishoni, yeye pamoja na maafisa wake,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 2:1 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Moabu, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu alichoma mifupa ya mfalme wa Edomu, ikawa kama chokaa.
AMO 2:2 Nitatuma moto juu ya Moabu ambao utateketeza ngome za Keriothi. Moabu ataanguka kwa ghasia kubwa katikati ya kelele za vita, na sauti ya tarumbeta.
AMO 2:3 Nitamwangamiza mtawala wake na kuwaua maafisa wake wote pamoja naye,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 2:4 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Yuda, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu wameikataa Torati ya Mwenyezi Mungu na hawakuzishika amri zake, kwa sababu wamepotoshwa na miungu ya uongo, miungu ambayo babu zao waliifuata.
AMO 2:5 Nitatuma moto juu ya Yuda ambao utateketeza ngome za Yerusalemu.”
AMO 2:6 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Israeli, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Wanawauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu.
AMO 2:7 Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini, kama vile juu ya mavumbi ya nchi, na kukataa haki kwa waliodhulumiwa. Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja, kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu.
AMO 2:8 Watu hulala kando ya kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani. Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu.
AMO 2:9 “Nilimwangamiza Mwamori mbele yao, ingawa alikuwa mrefu kama mierezi, na mwenye nguvu kama mialoni. Niliyaangamiza matunda yake juu na mizizi yake chini.
AMO 2:10 “Niliwapandisha toka Misri, na nikawaongoza miaka arobaini jangwani niwape nchi ya Waamori.
AMO 2:11 “Pia niliinua manabii kutoka miongoni mwa wana wenu na Wanadhiri kutoka miongoni mwa vijana wenu. Je, hii si kweli, enyi watu wa Israeli?” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 2:12 “Lakini mliwafanya Wanadhiri kunywa mvinyo na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.
AMO 2:13 “Sasa basi, nitawaponda kama gari linavyoponda likiwa limejazwa nafaka.
AMO 2:14 Mkimbiaji hodari hatanusurika, wenye nguvu wataishiwa nguvu zao, na shujaa hataweza kuokoa maisha yake.
AMO 2:15 Mpiga upinde atakimbia, askari wapiga mbio hawataweza kutoroka, na mpanda farasi hataokoa maisha yake.
AMO 2:16 Hata askari walio mashujaa sana siku hiyo watakimbia uchi,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 3:1 Sikilizeni neno hili alilosema Mwenyezi Mungu dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri:
AMO 3:2 “Ni ninyi tu niliowachagua kati ya jamaa zote za dunia; kwa hiyo nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi zenu zote.”
AMO 3:3 Je, watu wawili hutembea pamoja wasipokubaliana kufanya hivyo?
AMO 3:4 Je, simba hunguruma katika kichaka wakati hana mawindo? Aweza kuvuma katika pango wakati ambao hajakamata chochote?
AMO 3:5 Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini ambapo hajategewa chambo? Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini wakati hakuna chochote cha kunasa?
AMO 3:6 Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari, watu hawatetemeki? Mji unapopatwa na maafa, je, si Mwenyezi Mungu amesababisha?
AMO 3:7 Hakika Bwana Mungu Mwenyezi hatafanya neno lolote bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.
AMO 3:8 Simba amenguruma: je, ni nani ambaye hataogopa? Bwana Mungu Mwenyezi ametamka: je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii?
AMO 3:9 Tangazeni katika ngome za Ashdodi na katika ngome za Misri: “Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria; angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake, na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.”
AMO 3:10 Mwenyezi Mungu asema: “Hawajui kutenda lililo jema, wale ambao hujilundikia nyara na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.”
AMO 3:11 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Adui ataizingira nchi; ataangusha chini ngome zenu na kuteka nyara maboma yenu.”
AMO 3:12 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba vipande viwili tu vya mfupa wa mguu au kipande cha sikio, hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa, wale wanaokaa Samaria kwenye kingo za vitanda vyao, na katika Dameski kwenye viti vyao vya fahari.”
AMO 3:13 “Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, yeye Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
AMO 3:14 “Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake, nitaharibu madhabahu za Betheli; pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali na kuanguka chini.
AMO 3:15 Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika, pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi; nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 4:1 Sikilizeni neno hili, ninyi ng’ombe wa Bashani mlioko juu ya Mlima Samaria, ninyi wanawake mnaowadhulumu maskini, na kuwagandamiza wahitaji, na kuwaambia wanaume wenu, “Tuleteeni vinywaji!”
AMO 4:2 Bwana Mungu Mwenyezi ameapa kwa utakatifu wake: “Hakika wakati utakuja mtakapochukuliwa na kulabu, na wanaosalia kwa ndoana za samaki.
AMO 4:3 Nanyi mtaenda moja kwa moja kupitia mahali palipobomolewa kwenye ukuta, nanyi mtatupwa nje kuelekea Harmoni,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 4:4 “Nendeni Betheli mkatende dhambi; nendeni Gilgali mkazidi kutenda dhambi. Leteni dhabihu zenu kila asubuhi, zaka zenu kila mwaka wa tatu.
AMO 4:5 Mchome mkate uliotiwa chachu kama sadaka ya shukrani, jisifuni kuhusu sadaka zenu za hiari: jigambeni kwa ajili ya sadaka hizo, enyi Waisraeli, kwa kuwa hili ndilo mnalopenda kulitenda,” asema Bwana Mungu Mwenyezi.
AMO 4:6 “Niliwapa njaa kwenye kila mji, na ukosefu wa chakula katika kila mji, hata hivyo bado hamjanirudia mimi,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 4:7 “Pia niliwazuilia ninyi mvua miezi mitatu kabla ya kufikia mavuno. Nilinyesha mvua kwenye mji mmoja, lakini niliizuia mvua isinyeshe mji mwingine. Shamba moja lilipata mvua, na lingine halikupata, nalo likakauka.
AMO 4:8 Watu walitangatanga mji hata mji kutafuta maji, lakini hawakupata ya kuwatosha kunywa, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 4:9 “Mara nyingi nilizipiga bustani zenu na mashamba ya mizabibu, niliyapiga kwa kutu na ukungu. Nzige walitafuna tini zenu na miti ya mizeituni, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 4:10 “Niliwapelekea tauni miongoni mwenu kama nilivyofanya kule Misri. Niliwaua vijana wenu wa kiume kwa upanga, na nikawachukua farasi wenu. Nilijaza pua zenu kwa uvundo kutoka kambi zenu, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 4:11 “Niliwaangamiza baadhi yenu kama nilivyoangamiza Sodoma na Gomora. Mlikuwa kama kijiti kiwakacho kilichonyakuliwa motoni, hata hivyo hamjanirudia,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 4:12 “Kwa hiyo hili ndilo nitakalowafanyia, Israeli, na kwa sababu nitawafanyia hili, jiandaeni kukutana na Mungu wenu, ee Israeli.”
AMO 4:13 Yeye ambaye hufanya milima, anaumba upepo, na kufunua mawazo yake kwa mwanadamu, yeye ageuzaye asubuhi kuwa giza, na kukanyaga mahali pa juu pa nchi: Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.
AMO 5:1 Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:
AMO 5:2 “Bikira Israeli ameanguka, kamwe hatainuka tena, ameachwa pweke katika nchi yake, hakuna yeyote wa kumwinua.”
AMO 5:3 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli, mia moja tu watarudi; wakati mji utakapopeleka mia moja, kumi tu ndio watarudi hai.”
AMO 5:4 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni mpate kuishi;
AMO 5:5 msitafute Betheli, msiende Gilgali, msisafiri kwenda Beer-Sheba. Kwa maana kwa hakika Gilgali itaenda uhamishoni, na Betheli itafanywa kuwa ubatili.”
AMO 5:6 Mtafuteni Mwenyezi Mungu mpate kuishi, au atafagia nyumba ya Yusufu kama moto; utawateketeza, nayo Betheli haitakuwa na yeyote wa kuuzima.
AMO 5:7 Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu na kuiangusha haki chini
AMO 5:8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni, ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko na mchana kuwa usiku, ambaye huyaita maji ya bahari na kuyamwaga juu ya nchi: Mwenyezi Mungu ndilo jina lake;
AMO 5:9 yeye hufanya maangamizi kwenye ngome na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),
AMO 5:10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani, na kumdharau yule ambaye husema kweli.
AMO 5:11 Mnamgandamiza maskini na kumlazimisha awape nafaka. Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari, hamtaishi ndani yake; ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, hamtakunywa divai yake.
AMO 5:12 Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu. Mmewadhulumu wenye haki na kupokea rushwa na kuzuia haki ya maskini mahakamani.
AMO 5:13 Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza nyakati kama hizo, kwa kuwa nyakati ni mbaya.
AMO 5:14 Tafuteni mema, wala si mabaya, ili mpate kuishi. Ndipo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo yupo nanyi.
AMO 5:15 Yachukieni maovu, yapendeni mema; dumisheni haki mahakamani. Yamkini Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, atawahurumia mabaki ya Yusufu.
AMO 5:16 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, yeye Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asemalo: “Kutakuwa na maombolezo barabarani zote, na vilio vya uchungu katika njia kuu zote. Wakulima wataitwa kuja kulia, na waombolezaji waje kuomboleza.
AMO 5:17 Kutakuwa na kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu, kwa kuwa nitapita kati yenu,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 5:18 Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya Mwenyezi Mungu! Kwa nini mnaitamani siku ya Mwenyezi Mungu? Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.
AMO 5:19 Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba kumbe akakutana na dubu, kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta, kumbe akaumwa na nyoka.
AMO 5:20 Je, siku ya Mwenyezi Mungu haitakuwa giza, na si nuru: giza nene, bila mwali wowote?
AMO 5:21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini; siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.
AMO 5:22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka, sitazikubali. Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani, sitazitambua.
AMO 5:23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu! Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.
AMO 5:24 Lakini acheni haki itiririke kama mto, na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!
AMO 5:25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli?
AMO 5:26 Mmeyainua madhabahu ya Sikuthi mungu wenu mtawala, na Kiuni mungu wenu wa nyota, ambao mliwatengeneza wenyewe.
AMO 5:27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,” asema Mwenyezi Mungu, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi ya mbinguni.
AMO 6:1 Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni, na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria, ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine, ambao watu wa Israeli wanawategemea!
AMO 6:2 Nendeni Kalne mkaone kutoka huko; mwende hadi Hamathi iliyo kuu, kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti. Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili? Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?
AMO 6:3 Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya na kuleta karibu utawala wa kuogofya.
AMO 6:4 Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu, na kujinyoosha juu ya viti vya fahari. Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri na ndama walionenepeshwa.
AMO 6:5 Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi, huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.
AMO 6:6 Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa, na mnajipaka mafuta mazuri, lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yusufu.
AMO 6:7 Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni; karamu zenu na kustarehe kutakoma.
AMO 6:8 Bwana Mungu Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema: “Nachukia kiburi cha Yakobo, nachukia ngome zake; nitautoa mji wao na kila kitu kilicho ndani yake.”
AMO 6:9 Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa.
AMO 6:10 Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza! Haturuhusiwi kutaja jina la Mwenyezi Mungu.”
AMO 6:11 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamuru, naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.
AMO 6:12 Je, farasi wanaweza kukimbia kwenye miamba iliyochongoka? Je, mtu aweza kulima kwa maksai huko? Lakini mmegeuza haki kuwa sumu na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:
AMO 6:13 ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu kwa nguvu zetu wenyewe?”
AMO 6:14 Maana Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema, “Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli, nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bonde la Araba.”
AMO 7:1 Hili ndilo alilonionesha Bwana Mungu Mwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua.
AMO 7:2 Wakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “Bwana Mungu Mwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”
AMO 7:3 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akaghairi. Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Hili halitatokea.”
AMO 7:4 Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi alilonionesha katika maono: Bwana Mungu Mwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi.
AMO 7:5 Ndipo nikalia, “Bwana Mungu Mwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”
AMO 7:6 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akaghairi. Bwana Mungu Mwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.”
AMO 7:7 Hili ndilo alilonionesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake.
AMO 7:8 Naye Mwenyezi Mungu akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?” Nikamjibu, “Uzi wa timazi.” Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena.
AMO 7:9 “Mahali pa Isaka pa juu pa kuabudia pataangamizwa, na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa; kwa upanga wangu nitainuka dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”
AMO 7:10 Kisha Amazia kuhani wa Betheli akatuma ujumbe kwa Yeroboamu mfalme wa Israeli, akisema: “Amosi analeta fitina juu yako katikati ya Israeli. Nchi haiwezi kuvumilia maneno yake yote.
AMO 7:11 Kwa kuwa hili ndilo Amosi analosema: “ ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga, na kwa hakika Israeli wataenda uhamishoni, mbali na nchi yao.’ ”
AMO 7:12 Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Nenda zako, ewe mwonaji! Urudi katika nchi ya Yuda. Ujipatie riziki yako huko na kutoa unabii wako.
AMO 7:13 Usiendelee kutoa unabii katika Betheli, kwa sababu hapa ni mahali pa mfalme pa kuabudia na Hekalu la ufalme huu.”
AMO 7:14 Amosi akamjibu Amazia, “Mimi sikuwa nabii wala mwana wa nabii, lakini nilikuwa mchungaji wa kondoo na mtunza mikuyu.
AMO 7:15 Lakini Mwenyezi Mungu akanitoa kutoka kuchunga kondoo na kuniambia, ‘Nenda, ukawatabirie watu wangu Israeli.’
AMO 7:16 Sasa basi, sikieni neno la Mwenyezi Mungu. Ninyi mnasema, “ ‘Usitabiri dhidi ya Israeli, na uache kuhubiri dhidi ya nyumba ya Isaka.’
AMO 7:17 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “ ‘Mke wako atakuwa kahaba mjini, nao wana wako wa kiume na wa kike watauawa kwa upanga. Shamba lako litapimwa na kugawanywa, na wewe mwenyewe utafia katika nchi ya kipagani. Nayo Israeli kwa hakika itaenda uhamishoni, mbali na nchi yao.’ ”
AMO 8:1 Hili ndilo alilonionesha Bwana Mungu Mwenyezi katika maono: kikapu cha matunda yaliyoiva.
AMO 8:2 Akaniuliza, “Amosi, unaona nini?” Nikajibu, “Kikapu chenye matunda yaliyoiva.” Ndipo Mwenyezi Mungu akaniambia, “Wakati umewadia kwa watu wangu Israeli; sitawahurumia zaidi.”
AMO 8:3 Bwana Mungu Mwenyezi asema, “Katika siku ile, nyimbo katika Hekalu zitageuka kuwa maombolezo. Miili mingi, mingi sana: itatupwa kila mahali! Kimya!”
AMO 8:4 Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji, na kuwaonea maskini wa nchi,
AMO 8:5 mkisema, “Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita ili tupate kuuza nafaka, na Sabato itakwisha lini ili tuweze kuuza ngano?” Mkipunguza vipimo, na kuongeza bei, na kudanganya kwa mizani zisizo sawa,
AMO 8:6 mkiwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu, na mkiuza hata takataka za ngano pamoja na ngano.
AMO 8:7 Mwenyezi Mungu ameapa kwake mwenyewe, aliye Fahari ya Yakobo: “Kamwe sitasahau chochote ambacho wamefanya.
AMO 8:8 “Je, nchi haitatetemeka kwa ajili ya hili, nao wote wanaoishi ndani yake hawataomboleza? Nchi yote itainuka kama Mto Naili; itapanda na kushuka kama mto wa Misri.
AMO 8:9 “Katika siku ile,” asema Bwana Mungu Mwenyezi, “Nitalifanya jua litue alasiri na kuifanya dunia iwe giza wakati wa mchana mwangavu.
AMO 8:10 Nitageuza sikukuu zenu za kidini kuwa maombolezo, na kuimba kwenu kote kuwe kilio. Nitawafanya ninyi nyote mvae magunia na kunyoa nywele zenu. Nitaufanya wakati ule uwe kama wa kuombolezea mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu.
AMO 8:11 “Siku zinakuja,” asema Bwana Mungu Mwenyezi, “wakati nitakapotuma njaa katika nchi yote: si njaa ya chakula wala kiu ya maji, lakini njaa ya kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu.
AMO 8:12 Wanaume watayumbayumba kutoka bahari hadi bahari na kutangatanga kutoka kaskazini mpaka mashariki, wakitafuta neno la Mwenyezi Mungu, lakini hawatalipata.
AMO 8:13 “Katika siku ile “wasichana wazuri na wavulana wenye nguvu watazimia kwa sababu ya kiu.
AMO 8:14 Wale waapao kwa aibu ya Samaria, au kusema, ‘Hakika kama miungu yenu iishivyo, ee Dani,’ au ‘Hakika kama mungu wa Beer-Sheba aishivyo’: wataanguka, wala hawatasimama tena.”
AMO 9:1 Nilimwona Bwana akiwa amesimama kando ya madhabahu, naye akasema: “Piga vichwa vya nguzo ili vizingiti vitikisike. Viangushe juu ya vichwa vya watu wote; na wale watakaosalia nitawaua kwa upanga. Hakuna yeyote atakayekimbia, hakuna atakayetoroka.
AMO 9:2 Wajapojichimbia chini hadi kwenye vina vya Kuzimu, kutoka huko mkono wangu utawatoa. Wajapopanda juu hadi kwenye mbingu, kutoka huko nitawashusha.
AMO 9:3 Wajapojificha juu ya kilele cha Karmeli, huko nitawawinda na kuwakamata. Wajapojificha uso wangu katika vilindi vya bahari, huko nako nitaamuru joka kuwauma.
AMO 9:4 Wajapopelekwa uhamishoni na adui zao, huko nako nitaamuru upanga uwaue. Nitawakazia macho yangu kwa mabaya wala si kwa mazuri.”
AMO 9:5 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, yeye agusaye dunia nayo ikayeyuka, na wote wanaoishi ndani yake wakaomboleza: nayo nchi yote huinuka kama Mto Naili, kisha hushuka kama mto wa Misri;
AMO 9:6 yeye ambaye hujenga jumba lake la kifalme katika mbingu na kuisimika misingi yake juu ya dunia, yeye aitaye maji ya bahari na kuyamwaga juu ya nchi: Mwenyezi Mungu ndilo jina lake.
AMO 9:7 “Je, Waisraeli, ninyi si sawa kwangu kama Wakushi?” asema Mwenyezi Mungu. “Je, sikuleta Israeli kutoka Misri, Wafilisti kutoka Kaftori, na Washamu kutoka Kiri?
AMO 9:8 “Hakika macho ya Bwana Mungu Mwenyezi yako juu ya ufalme wenye dhambi. Nami nitauangamiza kutoka uso wa dunia: hata hivyo sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo,” asema Mwenyezi Mungu.
AMO 9:9 “Kwa kuwa nitatoa amri, na nitaipepeta nyumba ya Israeli miongoni mwa mataifa yote, kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo, na hakuna hata punje moja itakayoanguka chini.
AMO 9:10 Watenda dhambi wote miongoni mwa watu wangu watauawa kwa upanga, wale wote wasemao, ‘Maafa hayatatupata wala kutukuta.’
AMO 9:11 “Katika siku ile “Nitalisimamisha hema la Daudi lililoanguka. Nitakarabati mahali palipobomoka na kujenga upya magofu yake, na kuijenga kama ilivyokuwa awali,
AMO 9:12 ili wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yale yanayobeba Jina langu,” asema Mwenyezi Mungu ambaye atafanya mambo haya.
AMO 9:13 “Siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “wakati mvunaji atatanguliwa na mkulima, naye mpanzi atatanguliwa na yeye akamuaye zabibu. Divai mpya itadondoka kutoka milimani, na kutiririka kutoka vilima vyote.
AMO 9:14 Nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa; wataijenga tena miji iliyoachwa magofu, nao wataishi ndani yake. Watapanda mizabibu na kunywa divai yake; watalima bustani na kula matunda yake.
AMO 9:15 Nitaipanda Israeli katika nchi yao wenyewe, hawatang’olewa tena kutoka nchi niliyowapa,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
OBA 1:1 Maono ya Obadia. Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kuhusu Edomu: Tumesikia ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Inukeni, twendeni tukapigane vita dhidi yake.”
OBA 1:2 “Tazama, nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, utadharauliwa kabisa.
OBA 1:3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, wewe unayeishi katika mapango ya miamba na kufanya makao yako juu, wewe unayejiambia mwenyewe, ‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’
OBA 1:4 Ingawa unapaa juu kama tai na kufanya kiota chako kati ya nyota, nitakushusha chini kutoka huko,” asema Mwenyezi Mungu.
OBA 1:5 “Ikiwa wezi wangekuja kwako, ikiwa wanyang’anyi wangekujia usiku: Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yanakungojea: je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji? Kama wachuma zabibu wangekuja kwako, je, wasingebakiza zabibu chache?
OBA 1:6 Lakini tazama jinsi Esau atakavyotekwa, jinsi hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara!
OBA 1:7 Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani, rafiki zako watakudanganya na kukushinda, wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego, lakini hutaweza kuugundua.
OBA 1:8 “Katika siku hiyo,” asema Mwenyezi Mungu, “je, sitaangamiza wenye hekima wa Edomu, hao wenye ufahamu katika milima ya Esau?
OBA 1:9 Ee Temani, mashujaa wako watatiwa hofu, kila mmoja katika milima ya Esau ataangushwa chini kwa kuchinjwa.
OBA 1:10 Kwa sababu ya jeuri uliyofanya dhidi ya ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika; utaangamizwa milele.
OBA 1:11 Siku ile ulisimama mbali ukiangalia wakati wageni walipojichukulia utajiri wake, na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu, ulikuwa kama mmoja wao.
OBA 1:12 Usingemdharau ndugu yako katika siku ya msiba wake, wala kufurahia juu ya watu wa Yuda katika siku ya maangamizi yao, wala kujigamba sana katika siku ya taabu yao.
OBA 1:13 Usingeingia katika malango ya watu wangu katika siku ya maafa yao, wala kuwadharau katika janga lao katika siku ya maafa yao, wala kunyang’anya mali yao katika siku ya maafa yao.
OBA 1:14 Usingengoja kwenye njia panda na kuwaua wakimbizi wao, wala kuwatoa watu wake waliosalia katika siku ya shida yao.
OBA 1:15 “Siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu kwa mataifa yote. Kama ulivyotenda, nawe utatendewa vivyo hivyo, matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako.
OBA 1:16 Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo; watakunywa na kunywa, nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo.
OBA 1:17 Lakini katika Mlima Sayuni kutakuwa na wale watakaookoka; nao utakuwa mtakatifu, nayo nyumba ya Yakobo itamiliki urithi wake.
OBA 1:18 Nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto; nayo nyumba ya Esau itakuwa bua kavu, nao wataiwasha moto na kuiteketeza. Hakutakuwa na watakaosalimika kutoka nyumba ya Esau.” Mwenyezi Mungu amesema.
OBA 1:19 Watu kutoka nchi ya Negebu wataimiliki milima ya Esau, na watu kutoka Shefela wataimiliki nchi ya Wafilisti. Watayamiliki mashamba ya Efraimu na Samaria, naye Benyamini atamiliki Gileadi.
OBA 1:20 Kundi la Waisraeli walio uhamishoni Kanaani watarudi na kuimiliki nchi hadi Sarepta. Walio uhamishoni Sefaradi kutoka Yerusalemu wataimiliki miji ya Negebu.
OBA 1:21 Waokoaji watakwea juu ya Mlima Sayuni kutawala milima ya Esau. Nao ufalme utakuwa wa Mwenyezi Mungu.
JON 1:1 Neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Yona mwana wa Amitai:
JON 1:2 “Nenda mji mkubwa wa Ninawi ukahubiri dhidi yake, kwa sababu uovu wake umefika kwangu.”
JON 1:3 Lakini Yona alimkimbia Mwenyezi Mungu na kuelekea Tarshishi. Alishuka hadi Yafa, ambapo alikuta meli iliyokuwa imepangwa kuelekea bandari ile. Baada ya kulipa nauli, akapanda kwenye meli na kuelekea Tarshishi ili kumkimbia Mwenyezi Mungu.
JON 1:4 Ndipo Mwenyezi Mungu akatuma upepo mkali baharini, nayo dhoruba kali sana ikavuma hata meli ikawa hatarini ya kuvunjika.
JON 1:5 Mabaharia wote waliogopa na kila mmoja akamlilia mungu wake mwenyewe. Nao wakatupa mizigo baharini ili meli ipungue uzito. Lakini Yona alikuwa ameteremkia chumba cha ndani ya meli, ambapo alilala na kupatwa na usingizi mzito.
JON 1:6 Nahodha akamwendea na kusema, “Wewe unawezaje kulala? Amka ukamwite mungu wako! Huenda akatuangalia, tusiangamie.”
JON 1:7 Kisha mabaharia wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tupige kura tumtafute anayehusika na maafa haya.” Wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.
JON 1:8 Kwa hiyo walimuuliza, “Tuambie, ni nani anayehusika kwa kutuletea tatizo hili lote? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? Nchi yako ni ipi? Wewe ni kutoka taifa lipi?”
JON 1:9 Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.”
JON 1:10 Hili liliwaogopesha nao wakamuuliza, “Umefanya nini?” (Walijua alikuwa anamkimbia Mwenyezi Mungu, kwa sababu alishawaambia hivyo.)
JON 1:11 Bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Kwa hiyo walimuuliza, “Tukutendee nini ili kufanya bahari itulie kwa ajili yetu?”
JON 1:12 Akawajibu, “Niinueni mnitupe baharini, nayo itakuwa shwari. Ninajua mawimbi haya makubwa yamewatokea kwa ajili ya kosa langu.”
JON 1:13 Badala yake, wale watu walijitahidi kupiga makasia walivyoweza ili wapate kurudi pwani. Lakini hawakuweza, kwa kuwa bahari ilizidi kuchafuka kuliko mwanzo.
JON 1:14 Ndipo wakamlilia Mwenyezi Mungu, “Ee Mwenyezi Mungu, tafadhali usituue kwa kumuua mtu huyu. Usituhesabie hatia kwa kumuua mtu asiyekuwa na hatia, kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umefanya kama ilivyokupendeza.”
JON 1:15 Kisha wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari iliyokuwa imechafuka ikatulia.
JON 1:16 Katika jambo hili watu wakamwogopa Mwenyezi Mungu sana, wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu na kumwekea nadhiri.
JON 1:17 Lakini Mwenyezi Mungu akamwandaa samaki mkubwa sana kummeza Yona, naye Yona alikuwa ndani ya tumbo la samaki huyo kwa siku tatu, usiku na mchana.
JON 2:1 Akiwa ndani ya tumbo la samaki, Yona alimwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
JON 2:2 Akasema: “Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu, naye akanijibu. Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada, nawe ukasikiliza kilio changu.
JON 2:3 Ulinitupa kwenye kilindi, ndani kabisa ya moyo wa bahari, mikondo ya maji ilinizunguka; mawimbi yako yote na viwimbi vilipita juu yangu.
JON 2:4 Nikasema, ‘Nimefukuziwa mbali na uso wako, hata hivyo nitatazama tena kuelekea Hekalu lako takatifu.’
JON 2:5 Maji yaliyonimeza yalinitisha, kilindi kilinizunguka; mwani ulijisokota kichwani pangu.
JON 2:6 Nilizama chini sana hata pande za mwisho za milima, makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele. Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
JON 2:7 “Uhai wangu ulipokuwa unatoka, nilikukumbuka wewe, Mwenyezi Mungu, nayo maombi yangu yalikufikia wewe, katika Hekalu lako takatifu.
JON 2:8 “Wale watu wanaoshikilia sanamu batili hupoteza neema yao.
JON 2:9 Lakini mimi nitakutolea dhabihu, kwa sauti za shukrani na shangwe. Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza. Wokovu watoka kwa Mwenyezi Mungu.”
JON 2:10 Basi Mwenyezi Mungu akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.
JON 3:1 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yona mara ya pili:
JON 3:2 “Ondoka uende katika mji mkubwa wa Ninawi, ukautangazie ujumbe ninaokupa.”
JON 3:3 Yona akalitii neno la Mwenyezi Mungu naye akaenda Ninawi. Basi Ninawi ulikuwa mji maarufu sana, ilichukua siku tatu kuuzunguka.
JON 3:4 Siku ya kwanza, Yona aliingia mjini. Akatangaza: “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.”
JON 3:5 Watu wa Ninawi wakamwamini Mungu, wakatangaza kufunga, watu wote kuanzia mkubwa sana hadi yule mdogo kabisa, wakavaa gunia.
JON 3:6 Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha utawala, akavua majoho yake ya mfalme, akajifunika gunia na kuketi mavumbini.
JON 3:7 Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote: “Kwa amri ya mfalme na wakuu wake: “Msiruhusu mtu yeyote au mnyama, makundi ya ng’ombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu chochote, msiwaruhusu kula wala kunywa.
JON 3:8 Bali wanadamu na wanyama wavae gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao.
JON 3:9 Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie.”
JON 3:10 Mungu alipoona walivyofanya na jinsi walivyogeuka kutoka njia zao mbaya, akawa na huruma wala hakuleta maangamizi juu yao kama alivyokuwa ameonya.
JON 4:1 Lakini Yona alichukizwa sana akakasirika.
JON 4:2 Akamwomba Mwenyezi Mungu, “Ee Mwenyezi Mungu, hili si lile nililolisema nilipokuwa ningali nyumbani? Hii ndiyo sababu niliharakisha kukimbilia Tarshishi. Nikifahamu kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na huruma, si mwepesi wa hasira na umejaa upendo, ni Mungu ambaye hughairi katika kupeleka maafa.
JON 4:3 Sasa, Ee Mwenyezi Mungu, niondolee uhai wangu, kwa kuwa ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
JON 4:4 Lakini Mwenyezi Mungu akamjibu, “Je unayo haki yoyote kukasirika?”
JON 4:5 Yona akatoka nje akaketi mahali upande wa mashariki wa mji. Hapo akajitengenezea kibanda, akaketi kwenye kivuli chake na kungojea ni nini kitakachotokea katika mji.
JON 4:6 Ndipo Bwana Mwenyezi Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu.
JON 4:7 Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka.
JON 4:8 Jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona hadi akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
JON 4:9 Lakini Mungu alimwambia Yona, “Je, unayo haki kukasirika kuhusu mzabibu huo?” Akasema, “Ndiyo, ninayo haki. Nimekasirika kiasi cha kufa.”
JON 4:10 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “Wewe unakasirika kwa ajili ya mzabibu huu, nawe hukuusababisha kuota wala kuutunza. Uliota usiku mmoja, nao ukafa usiku mmoja.
JON 4:11 Lakini Ninawi ina zaidi ya watu elfu mia moja na ishirini ambao hawawezi kupambanua kulia au kushoto, pamoja na ng’ombe wengi. Je, hainipasi kufikiri kuhusu mji ule mkubwa?”
MIC 1:1 Neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Mika Mmoreshethi wakati wa utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, ufunuo aliouona kuhusu Samaria na Yerusalemu.
MIC 1:2 Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote, sikilizeni, ee dunia na wote mliomo, ili Bwana Mungu Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu, Bwana kutoka Hekalu lake takatifu.
MIC 1:3 Tazama! Mwenyezi Mungu anakuja kutoka mahali pake; anashuka na kukanyaga mahali palipoinuka juu pa dunia.
MIC 1:4 Milima inayeyuka chini yake na mabonde yanagawanyika kama nta mbele ya moto, kama maji yanayotiririka kasi kwenye mteremko.
MIC 1:5 Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo, ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli. Kosa la Yakobo ni lipi? Je, sio Samaria? Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia ni nini? Je, sio Yerusalemu?
MIC 1:6 “Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto, mahali pa kuotesha mizabibu. Nitayamwaga mawe yake katika bonde na kuacha wazi misingi yake.
MIC 1:7 Sanamu zake zote zitavunjwa vipande vipande; zawadi zake zote za Hekalu zitachomwa kwa moto; nitaharibu vinyago vyake vyote. Kwa kuwa alikusanya zawadi zake kutokana na ujira wa kahaba, nazo zitatumika tena kulipa mishahara ya kahaba.”
MIC 1:8 Kwa ajili ya hili nitalia na kuomboleza; nitatembea bila viatu na tena uchi. Nitabweka kama mbweha na kuomboleza kama bundi.
MIC 1:9 Kwa sababu jeraha lake halitibiki; limekuja kwa Yuda. Limefika hasa kwenye lango la watu wangu, hata Yerusalemu kwenyewe.
MIC 1:10 Usiliseme hili huko Gathi; usilie hata kidogo. Huko Beth-le-Afra gaagaa mavumbini.
MIC 1:11 Piteni mkiwa uchi na wenye aibu, ninyi mnaoishi Shafiri. Wale wanaoishi Saanani hawatatoka nje. Beth-Eseli iko katika maombolezo; kinga yake imeondolewa kwako.
MIC 1:12 Wale wanaoishi Marothi wanagaagaa kwa maumivu wakingoja msaada, kwa sababu maangamizi yamekuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hata katika lango la Yerusalemu.
MIC 1:13 Enyi mnaoishi Lakishi, fungeni farasi kwenye magari ya vita. Mlikuwa chanzo cha dhambi kwa Binti Sayuni, kwa kuwa makosa ya Israeli yalikutwa kwako.
MIC 1:14 Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi zawadi za kuagana. Mji wa Akzibu utaonesha wazi udanganyifu kwa wafalme wa Israeli.
MIC 1:15 Nitawaleteeni atakayewashinda ninyi mnaoishi Maresha. Yeye aliye utukufu wa Israeli atakuja Adulamu.
MIC 1:16 Nyoeni nywele zenu katika kuomboleza kwa ajili ya watoto wenu mnaowafurahia; jifanyieni upara kama tai, kwa kuwa watawaacha na kwenda uhamishoni.
MIC 2:1 Ole kwa wale wapangao uovu, kwa wale wapangao hila vitandani mwao! Kunapopambazuka wanalitimiza kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza.
MIC 2:2 Wanatamani mashamba na kuyakamata, pia nyumba na kuzichukua. Wanamlaghai mwanaume nyumba yake, mwanadamu mwenzake urithi wake.
MIC 2:3 Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu asema: “Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa, ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe. Hamtatembea tena kwa majivuno, kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa.
MIC 2:4 Siku hiyo watu watawadhihaki, watawafanyia mzaha kwa wimbo huu wa maombolezo: ‘Tumeangamizwa kabisa; mali ya watu wangu imegawanywa. Ameninyang’anya! Ametoa mashamba yetu kwa wasaliti.’ ”
MIC 2:5 Kwa hiyo hutakuwa na yeyote katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu wa kugawanya mashamba kwa kura.
MIC 2:6 Manabii wao husema, “Usitabiri. Usitabiri kuhusu vitu hivi; aibu haitatupata.”
MIC 2:7 Je, ingesemwa, ee nyumba ya Yakobo: “Je, Roho wa Mwenyezi Mungu amekasirika? Je, yeye hufanya vitu kama hivyo?” “Je, maneno yangu hayamfanyii mema yeye ambaye njia zake ni nyofu?
MIC 2:8 Siku hizi watu wangu wameinuka kama adui. Unawavua joho la kitajiri wale wanaopita pasipo kujali, kama watu warudio kutoka vitani.
MIC 2:9 Unawahamisha wanawake wa watu wangu kutoka nyumba zao za kupendeza. Unaondoa baraka yangu kwa watoto wao milele.
MIC 2:10 Inuka, nenda zako! Kwa maana hapa sio mahali pako pa kupumzikia, kwa sababu pametiwa unajisi, pameharibiwa, wala hapatengenezeki tena.
MIC 2:11 Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema, ‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’ angekuwa ndiye nabii anayekubalika na watu hawa!
MIC 2:12 “Hakika nitawakusanya ninyi nyote, ee Yakobo, Hakika nitawaleta pamoja mabaki ya Israeli. Nitawaleta pamoja kama kondoo ndani ya zizi, kama kundi kwenye malisho yake, mahali hapa patakuwa na msongamano wa watu.
MIC 2:13 Yeye afunguaye njia atawatangulia; watapita kwenye lango na kutoka nje. Mfalme wao atawatangulia, Mwenyezi Mungu atakuwa kiongozi.”
MIC 3:1 Kisha nikasema, “Sikilizeni enyi viongozi wa Yakobo, enyi watawala wa nyumba ya Israeli. Je, hampaswi kujua hukumu,
MIC 3:2 ninyi mnaochukia mema na kupenda maovu; ninyi mnaowachuna watu wangu ngozi na kuondoa nyama kwenye mifupa yao;
MIC 3:3 ninyi mnaokula nyama ya watu wangu, mnaowachuna ngozi na kuvunja mifupa yao vipande vipande; mnaowakatakata kama nyama ya kuwekwa kwenye sufuria na kama nyama ya kuwekwa kwenye chungu?”
MIC 3:4 Kisha watamlilia Mwenyezi Mungu, lakini hatawajibu. Wakati huo atawaficha uso wake kwa sababu ya uovu waliotenda.
MIC 3:5 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu, mtu akiwalisha, wanatangaza ‘amani’; kama hakufanya hivyo, wanaandaa kupigana vita dhidi yake.
MIC 3:6 Kwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono, na giza, msiweze kubashiri. Jua litawachwea manabii hao, nao mchana utakuwa giza kwao.
MIC 3:7 Waonaji wataaibika na waaguzi watafedheheka. Wote watafunika nyuso zao kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.”
MIC 3:8 Lakini mimi nimejazwa nguvu, nimejazwa Roho wa Mwenyezi Mungu, haki na uweza, kumtangazia Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake.
MIC 3:9 Sikieni hili, enyi viongozi wa nyumba ya Yakobo, enyi watawala wa nyumba ya Israeli, mnaodharau haki na kupotosha kila lililo sawa;
MIC 3:10 mnaojenga Sayuni kwa kumwaga damu na Yerusalemu kwa uovu.
MIC 3:11 Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa, na makuhani wake wanafundisha kwa malipo, nao manabii wake wanatabiri kwa fedha. Hata hivyo wanamwegemea Mwenyezi Mungu na kusema, “Je, Mwenyezi Mungu si yumo miongoni mwetu? Hakuna maafa yatakayotupata.”
MIC 3:12 Kwa ajili yenu, Sayuni italimwa kama shamba, Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto, na kilima cha Hekalu kitakuwa kichuguu kilichofunikwa na vichaka.
MIC 4:1 Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la Mwenyezi Mungu utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote; utainuliwa juu ya vilima, na watu wa mataifa watamiminika humo.
MIC 4:2 Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Torati itatoka Sayuni, neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu.
MIC 4:3 Atahukumu kati ya mataifa mengi, na ataamua migogoro ya mataifa yenye nguvu na yaliyo mbali. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena.
MIC 4:4 Kila mtu ataketi chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakuna mtu atakayewaogopesha, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amesema.
MIC 4:5 Mataifa yote yanaweza kutembea katika jina la miungu yao; sisi tutatembea katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wetu milele na milele.
MIC 4:6 “Katika siku hiyo,” asema Mwenyezi Mungu, “nitawakusanya walemavu; nitawakusanya walio uhamishoni na wale niliowahuzunisha.
MIC 4:7 Nitawafanya walemavu kuwa mabaki, wale waliofukuzwa kuwa taifa lenye nguvu. Mwenyezi Mungu atawatawala katika Mlima Sayuni kuanzia siku hiyo na hata milele.
MIC 4:8 Lakini kwako wewe, ee mnara wa ulinzi wa kundi, ee ngome ya Binti Sayuni, milki ya awali itarudishwa kwako, ufalme utakuja kwa Binti Yerusalemu.”
MIC 4:9 Kwa nini sasa unalia kwa nguvu: kwani huna mfalme? Je, mshauri wako amekufa, hata maumivu yakukamate kama ya mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa?
MIC 4:10 Gaagaa kwa uchungu, ee Binti Sayuni, kama mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa, kwa kuwa sasa ni lazima uuache mji ukapige kambi uwanjani. Utaenda Babeli; huko utaokolewa. Huko Mwenyezi Mungu atakukomboa kutoka mikononi mwa adui zako.
MIC 4:11 Lakini sasa mataifa mengi yamekusanyika dhidi yako. Wanasema, “Mwache anajisiwe, macho yetu na yatazame Sayuni kwa furaha!”
MIC 4:12 Lakini hawayajui mawazo ya Mwenyezi Mungu; hawauelewi mpango wake, yeye awakusanyaye kama miganda kwenye sakafu ya kupuria.
MIC 4:13 “Inuka upure, ee Binti Sayuni, kwa kuwa nitakupa pembe za chuma; nitakupa kwato za shaba na utavunja vipande vipande mataifa mengi.” Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa Mwenyezi Mungu, utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote.
MIC 5:1 Panga majeshi yako, ee mji wa majeshi, kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu. Watampiga mtawala wa Israeli shavuni kwa fimbo.
MIC 5:2 “Lakini wewe, Bethlehemu Efrata, ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda, kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli, ambaye asili yake ni kutoka zamani, kutoka milele.”
MIC 5:3 Kwa hiyo Israeli utaachwa hadi mwanamke aliye na uchungu atakapozaa mwana, na ndugu zake wengine warudi kujiunga na Waisraeli.
MIC 5:4 Atasimama na kulichunga kundi lake katika nguvu ya Mwenyezi Mungu, katika utukufu wa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake. Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia.
MIC 5:5 Naye atakuwa amani yao. Mwashuru atakapovamia nchi yetu na kupita katika ngome zetu, tutawainua wachungaji saba dhidi yake, hata viongozi wanane wa watu.
MIC 5:6 Wataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga, nchi ya Nimrodi kwa upanga. Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru atakapoivamia nchi yetu na kuingia katika mipaka yetu.
MIC 5:7 Mabaki ya Yakobo yatakuwa katikati ya mataifa mengi kama umande kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama manyunyu juu ya majani, ambayo hayamngoji mtu wala kukawia kwa mwanadamu.
MIC 5:8 Mabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa, katikati ya mataifa mengi, kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni, kama mwana simba miongoni mwa makundi ya kondoo, ambaye anaumiza vibaya na kuwararua kila anapopita katikati yao, wala hakuna awezaye kuokoa.
MIC 5:9 Mkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako, nao adui zako wote wataangamizwa.
MIC 5:10 “Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu, “nitaangamiza farasi wenu kati yenu, na kubomoa magari yenu ya vita.
MIC 5:11 Nitaiangamiza miji ya nchi yenu, na kuziangusha chini ngome zenu zote.
MIC 5:12 Nitaangamiza uchawi wenu, na hamtapiga tena ramli.
MIC 5:13 Nitaangamiza sanamu zenu, na mawe yenu ya ibada yatoke kati yenu; hamtasujudia tena kazi ya mikono yenu.
MIC 5:14 Nitang’oa nguzo za Ashera kati yenu, na kubomoa miji yenu.
MIC 5:15 Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu, kwa mataifa ambayo hayajanitii.”
MIC 6:1 Sikiliza asemalo Mwenyezi Mungu: “Simama, jitetee mbele ya milima; vilima na visikie lile unalotaka kusema.
MIC 6:2 “Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya Mwenyezi Mungu, sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ana shauri dhidi ya watu wake; anatoa mashtaka dhidi ya Israeli.
MIC 6:3 “Watu wangu, nimewatendea nini? Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu.
MIC 6:4 Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa. Nilimtuma Musa awaongoze, pia Haruni na Miriamu.
MIC 6:5 Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu alivyofanya shauri na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu. Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu hadi Gilgali, ili mfahamu matendo ya haki ya Mwenyezi Mungu.”
MIC 6:6 Nimjie Mwenyezi Mungu na kitu gani na kusujudu mbele za Mungu aliyetukuka? Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa, nije na ndama za mwaka mmoja?
MIC 6:7 Je, Mwenyezi Mungu atafurahishwa na kondoo dume elfu, au mito elfu kumi ya mafuta? Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, mtoto wangu mwenyewe kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?
MIC 6:8 Amekuonesha yaliyo mema, ee mwanadamu. Mwenyezi Mungu anataka nini kwako? Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.
MIC 6:9 Sikiliza! Mwenyezi Mungu anauita mji: kulicha jina lako ni hekima: “Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru.
MIC 6:10 Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu, hazina yako uliyopata kwa udanganyifu na vipimo vilivyopunguka, ambavyo vimelaaniwa?
MIC 6:11 Je, naweza kuhukumu kuwa mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia, aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo?
MIC 6:12 Matajiri wake ni wajeuri; watu wake ni waongo na ndimi zao zinazungumza kwa udanganyifu.
MIC 6:13 Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu, kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.
MIC 6:14 Mtakula lakini hamtashiba; tumbo zenu bado zitakuwa tupu. Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote, kwa sababu mtakachoweka akiba nitatoa kwa upanga.
MIC 6:15 Mtapanda lakini hamtavuna; mtakamua zeituni lakini hamtatumia mafuta yake. Mtakamua zabibu lakini hamtakunywa hiyo divai.
MIC 6:16 Mmezishika sheria za Omri na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, tena umefuata desturi zao. Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi na watu wako kuwa dhihaka; mtachukua dharau za mataifa.”
MIC 7:1 Taabu gani hii niliyo nayo! Nimefanana na yule akusanyaye matunda ya kiangazi, aokotaye masazo baada ya kuvunwa shamba la mizabibu; hakuna kishada chenye matunda ya kula, hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani.
MIC 7:2 Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi; hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki. Watu wote wanavizia kumwaga damu, kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu.
MIC 7:3 Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya, mtawala anadai zawadi, hakimu anapokea rushwa, wenye nguvu wanaamuru wanachotaka: wote wanapanga njama pamoja.
MIC 7:4 Aliye mwema kupita wote kati yao ni kama mchongoma, anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao ni mbaya kuliko uzio wa miiba. Siku ya walinzi wako imewadia, siku Mungu atakayokutembelea. Sasa ni wakati wao wa kuchanganyikiwa.
MIC 7:5 Usimtumaini jirani; usiweke matumaini kwa rafiki. Hata kwa yule alalaye kifuani mwako uwe mwangalifu kwa maneno yako.
MIC 7:6 Kwa kuwa mwana humdharau baba yake, naye binti huinuka dhidi ya mama yake, mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake: adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.
MIC 7:7 Lakini mimi, namtazama Mwenyezi Mungu kwa matumaini, namngoja Mungu Mwokozi wangu; Mungu wangu atanisikia mimi.
MIC 7:8 Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu! Ingawa nimeanguka, nitainuka. Japo ninaketi gizani, Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yangu.
MIC 7:9 Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake, nitabeba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, hadi atakapotetea shauri langu na kuithibitisha haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaiona haki yake.
MIC 7:10 Kisha adui yangu ataliona naye atafunikwa na aibu, yule aliyeniambia, “Yu wapi Mwenyezi Mungu, Mungu wako?” Macho yangu yataona kuanguka kwake, hata sasa atakanyagwa chini ya mguu kama tope barabarani.
MIC 7:11 Siku ya kujenga kuta zako itawadia, siku ya kupanua mipaka yako.
MIC 7:12 Siku hiyo watu watakuja kwako kutoka Ashuru na miji ya Misri, hata kutoka Misri hadi Mto Frati, na kutoka bahari hadi bahari, na kutoka mlima hadi mlima.
MIC 7:13 Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake, kwa sababu ya matunda ya matendo yao.
MIC 7:14 Wachunge watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, ambalo linaishi peke yake msituni, katika maeneo ya malisho yenye rutuba. Waache walishe katika Bashani na Gileadi kama ilivyokuwa siku za kale.
MIC 7:15 “Kama siku zile mlipotoka Misri, nitawaonesha maajabu yangu.”
MIC 7:16 Mataifa yataona na kuaibika, waliondolewa nguvu zao zote. Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao na masikio yao yatakuwa na uziwi.
MIC 7:17 Wataramba mavumbi kama nyoka, kama viumbe vinavyotambaa ardhini. Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka; watamgeukia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa hofu nao watakuogopa.
MIC 7:18 Ni nani Mungu kama wewe, ambaye anaachilia dhambi na kusamehe makosa ya mabaki ya urithi wake? Wewe huwi na hasira milele, bali unafurahia kuonesha rehema.
MIC 7:19 Utatuhurumia tena, utazikanyaga dhambi zetu chini ya nyayo zako, na kutupa maovu yetu yote katika vilindi vya bahari.
MIC 7:20 Utakuwa wa kweli kwa Yakobo, nawe utamwonesha Ibrahimu rehema, kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu siku za kale.
NAH 1:1 Neno la unabii kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu Mwelkoshi.
NAH 1:2 Mwenyezi Mungu ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi; Mwenyezi Mungu hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu. Mwenyezi Mungu hulipiza kisasi juu ya watesi wake, naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.
NAH 1:3 Mwenyezi Mungu si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu, Mwenyezi Mungu hataacha kuadhibu wenye hatia. Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni vumbi la miguu yake.
NAH 1:4 Anakemea bahari na kuikausha, anafanya mito yote kukauka. Bashani na Karmeli zinanyauka na maua ya Lebanoni hukauka.
NAH 1:5 Milima hutikisika mbele yake na vilima huyeyuka. Nchi hutetemeka mbele yake, dunia na wote wanaoishi ndani yake.
NAH 1:6 Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu? Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali? Ghadhabu yake imemiminwa kama moto, na miamba inapasuka mbele zake.
NAH 1:7 Mwenyezi Mungu ni Mwema, kimbilio wakati wa taabu. Huwatunza wale wanaomtegemea,
NAH 1:8 lakini kwa mafuriko makubwa, ataangamiza Ninawi; atafuatilia adui zake hadi gizani.
NAH 1:9 Kila njama wanayopanga dhidi ya Mwenyezi Mungu yeye atalikomesha; taabu haitatokea mara ya pili.
NAH 1:10 Watasongwa katikati ya miiba na kulewa kwa mvinyo wao. Watateketezwa kama mabua makavu.
NAH 1:11 Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja, ambaye anapanga njama dhidi ya Mwenyezi Mungu na kushauri uovu.
NAH 1:12 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Ingawa wana muungano nao ni wengi sana, watakatiliwa mbali na kuangamia. Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda, sitakutesa tena.
NAH 1:13 Sasa nitavunja nira zao kutoka shingo yako, nami nitazivunjilia mbali pingu zako.”
NAH 1:14 Hii ndiyo amri Mwenyezi Mungu aliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi: “Hutakuwa na wazao watakaoendeleza jina lako. Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kusubu zilizopo katika hekalu la miungu yenu. Nitaandaa kaburi lako, kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”
NAH 1:15 Tazama, huko juu milimani, miguu ya huyo mmoja aletaye habari njema, ambaye anatangaza amani! Ee Yuda, sherehekea sikukuu zako, nawe utimize nadhiri zako. Waovu hawatakuvamia tena; wataangamizwa kabisa.
NAH 2:1 Mshambuliaji anasogea dhidi yako, Ninawi. Linda ngome yako, chunga barabara, jitieni nguvu wenyewe, kusanya nguvu zako zote!
NAH 2:2 Mwenyezi Mungu atarudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli, ingawa waangamizi wamewaacha ukiwa na wameharibu mizabibu yao.
NAH 2:3 Ngao za askari wake ni nyekundu, mashujaa wamevaa nguo nyekundu. Chuma kwenye magari ya vita chametameta, katika siku aliyoyaweka tayari, mikuki ya msunobari inametameta.
NAH 2:4 Magari ya vita yanafanya msukosuko barabarani, yakikimbia nyuma na mbele uwanjani. Yanaonekana kama mienge ya moto; yanaenda kasi kama umeme.
NAH 2:5 Anaita vikosi vilivyochaguliwa, lakini bado wanajikwaa njiani. Wanakimbilia haraka kwenye ukuta wa mji, ile ngao ya kuwakinga imetayarishwa.
NAH 2:6 Malango ya mto yamefunguliwa wazi, na jumba la kifalme limeanguka.
NAH 2:7 Imeagizwa kwamba mji uchukuliwe na upelekwe uhamishoni. Vijakazi wake wanaomboleza kama hua na kupigapiga vifua vyao.
NAH 2:8 Ninawi ni kama dimbwi, nayo maji yake yanakauka. Wanalia, “Simama! Simama!” Lakini hakuna anayegeuka nyuma.
NAH 2:9 Chukueni nyara za fedha! Chukueni nyara za dhahabu! Wingi wake hauna mwisho, utajiri kutoka hazina zake zote!
NAH 2:10 Ameharibiwa, ametekwa nyara, ameachwa uchi! Mioyo inayeyuka, magoti yanalegea, miili inatetemeka, na kila uso umebadilika rangi.
NAH 2:11 Liko wapi sasa pango la simba, ambapo waliwalisha watoto wao, ambapo simba dume na simba jike walienda, na wana simba pia, bila kuogopa chochote?
NAH 2:12 Simba aliua mawindo ya kutosha watoto wake, alinyonga mawindo kwa ajili ya mwenzi wake, akijaza makao yake kwa alivyoua na mapango yake kwa mawindo.
NAH 2:13 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anatangaza, “Mimi ni kinyume na ninyi. Magari yenu ya vita nitayateketeza kwa moto, na upanga utakula wana simba wako. Sitawaachia mawindo juu ya nchi. Sauti za wajumbe wako hazitasikika tena.”
NAH 3:1 Ole wa mji unaomwaga damu, uliojaa uongo, uliojaa nyara, na usiokosa mateka.
NAH 3:2 Kelele za mijeledi, vishindo vya magurudumu, farasi wanaoenda mbio na mshtuo wa magari ya vita!
NAH 3:3 Wapanda farasi wanaenda mbio, panga zinametameta, na mikuki inang’aa! Majeruhi wengi, malundo ya maiti, idadi ya miili isiyohesabika, watu wanajikwaa juu ya mizoga:
NAH 3:4 haya yote kwa sababu ya wingi wa tamaa za kahaba, anayeshawishi, bibi mkuu wa mambo ya uchawi, anayewatia utumwani mataifa kwa ukahaba wake na pia jamaa za watu kwa ulozi wake.
NAH 3:5 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anasema, “Mimi ni kinyume na ninyi. Nitafunika uso wako kwa gauni lako. Nitaonesha mataifa uchi wako na falme aibu yako.
NAH 3:6 Nitakutupia uchafu, nitakufanyia dharau na kukufanya kioja.
NAH 3:7 Wote wanaokuona watakukimbia na kusema, ‘Ninawi inaangamia, nani atakayeomboleza kwa ajili yake?’ Nitampata wapi yeyote wa kukufariji?”
NAH 3:8 Je, wewe ni bora kuliko No-Amoni, uliopo katika Mto Naili, uliozungukwa na maji? Mto ulikuwa kinga yake, nayo maji yalikuwa ukuta wake.
NAH 3:9 Kushi na Misri walikuwa nguvu zake zisizo na mpaka; Putu na Libia walikuwa miongoni mwa wale walioungana naye.
NAH 3:10 Hata hivyo alichukuliwa mateka na kwenda uhamishoni. Watoto wake wachanga walivunjwa vunjwa vipande kwenye mwanzo wa kila barabara. Kura zilipigwa kwa watu wake wenye heshima, na watu wake wote wakuu walifungwa kwa minyororo.
NAH 3:11 Wewe pia utalewa; utaenda mafichoni na kutafuta kimbilio kutoka kwa adui.
NAH 3:12 Ngome zako zote ni kama mitini yenye matunda yake ya kwanza yaliyoiva; wakati inapotikiswa, tini huanguka kwenye kinywa chake alaye.
NAH 3:13 Tazama vikosi vyako: wote ni wanawake! Malango ya nchi yako yamekuwa wazi kwa adui zako; moto umeteketeza mapingo yake.
NAH 3:14 Teka maji kwa ajili ya kuzingirwa kwako, imarisha ulinzi wako, Ufanyie udongo wa mfinyanzi kazi, yakanyage matope, karabati tanuru la kuchomea matofali!
NAH 3:15 Huko moto utakuteketeza, huko upanga utakuangusha chini na kama vile panzi, watakumaliza. Ongezeka kama panzi, ongezeka kama nzige!
NAH 3:16 Umeongeza idadi ya wafanyabiashara wako hata wamekuwa wengi kuliko nyota za angani, lakini kama nzige wanaacha nchi tupu kisha huruka na kwenda zake.
NAH 3:17 Walinzi wako ni kama nzige, maafisa wako kama makundi ya nzige wanaotua kwenye kuta wakati wa siku ya baridi; lakini wakati jua linapotokea wanaruka kwenda zao, na hakuna anayejua wanakoenda.
NAH 3:18 Ee mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wanasinzia; wakuu wako wanalala chini mavumbini kupumzika. Watu wako wametawanyika juu ya milima bila kuwa na mtu yeyote wa kuwakusanya.
NAH 3:19 Hakuna kitu kinachoweza kuponya jeraha lako; jeraha lako ni la kukuua. Kila anayesikia habari zako, hupiga makofi kwa kuanguka kwako, kwa kuwa ni nani ambaye hajaguswa na ukatili wako usio na mwisho?
HAB 1:1 Neno la unabii alilopokea nabii Habakuki.
HAB 1:2 Ee Mwenyezi Mungu, hata lini nitakuomba msaada, lakini wewe husikilizi? Au kukulilia, “Udhalimu!” lakini hutaki kuokoa?
HAB 1:3 Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma? Kwa nini unavumilia makosa? Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu; kuna mabishano na mapambano kwa wingi.
HAB 1:4 Kwa hiyo sheria imepotoshwa, nayo haki haipo kabisa. Waovu wanawazunguka wenye haki, kwa hiyo haki imepotoshwa.
HAB 1:5 “Yatazame mataifa, uangalie na ushangae kabisa. Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu ambacho hungeamini, hata kama ungeambiwa.
HAB 1:6 Tazama! Nitawainua Wakaldayo, watu wakatili na wenye haraka, ambao hupita dunia yote ili kuteka makazi yasiyo yao.
HAB 1:7 Ni watu wanoogopwa na wanaotisha; wenyewe ndio sheria yao, na huinua heshima yao wenyewe.
HAB 1:8 Farasi wao ni wepesi kuliko chui, na wakali kuliko mbwa-mwitu wakati wa machweo. Askari wapanda farasi wao huenda mbio; waendesha farasi wao wanatoka mbali. Wanaruka kasi kama tai ili kurarua mawindo;
HAB 1:9 wote wanakuja tayari kutenda udhalimu. Makundi yao wanasonga mbele kama upepo wa jangwani, na kukusanya wafungwa kama mchanga.
HAB 1:10 Wanawabeza wafalme, na kuwadhihaki watawala. Wanaicheka miji yote yenye ngome; wanalundika udongo na kuiteka hiyo miji.
HAB 1:11 Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele: watu wenye hatia, ambao nguvu zao ndio mungu wao.”
HAB 1:12 Ee Mwenyezi Mungu, je, wewe sio wa tangu milele? Mungu wangu, Uliye Mtakatifu wangu, hatutakufa. Ee Mwenyezi Mungu, umewachagua wao ili watekeleze hukumu; Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.
HAB 1:13 Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu, wala huwezi kuvumilia makosa. Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu? Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu wanawameza wale wenye haki kuliko wao wenyewe?
HAB 1:14 Umewafanya watu kama samaki baharini, kama viumbe wa bahari wasio na mtawala.
HAB 1:15 Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana, anawakamata katika wavu wake, anawakusanya katika juya lake; kwa hiyo anashangilia na anafurahi.
HAB 1:16 Kwa hiyo anatoa sadaka kwa wavu wake, na kuchoma uvumba kwa juya lake, kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe, na anafurahia chakula kizuri.
HAB 1:17 Je, aendelee kuwatoa walio katika wavu wake, akiangamiza mataifa bila huruma?
HAB 2:1 Nitasimama katika zamu yangu, na kujiweka juu ya maboma; nitatazama nione atakaloniambia, na jibu nitakalotoa kuhusu lalamiko hili.
HAB 2:2 Kisha Mwenyezi Mungu akajibu: “Andika ufunuo huu, na ukaufanye wazi juu ya vibao, ili mpiga mbiu akimbie nao.
HAB 2:3 Kwa kuwa ufunuo huu unasubiri wakati uliokubalika; unazungumzia mambo ya mwisho, na kamwe hautakosea. Iwapo utakawia, wewe usubiri; kwa hakika utakuja na hautachelewa.
HAB 2:4 “Tazama, amejaa majivuno; anavyovitamani si vya unyofu: lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake:
HAB 2:5 hakika mvinyo humsaliti; ni mwenye kiburi na hana amani. Kwa sababu ni mlafi kama Kuzimu, na kama kifo kamwe hatosheki; anajikusanyia mataifa yote na kuchukua watu wote mateka.
HAB 2:6 “Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema, “ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu! Ataendelea hivi kwa muda gani?’
HAB 2:7 Je, wadai wako hawatainuka ghafula? Je, hawataamka na kukufanya utetemeke? Kisha utakuwa mhanga kwao.
HAB 2:8 Kwa kuwa umeteka nyara mataifa mengi, watu waliobaki watakuteka nyara wewe. Kwa kuwa umemwaga damu ya watu; umeharibu nchi na miji, na watu wote wanaoishi humo.
HAB 2:9 “Ole wake yeye ajengaye milki yake kwa mapato ya udhalimu, awekaye kiota chake juu, ili kukimbia makucha ya uharibifu!
HAB 2:10 Umepanga njama ya maangamizi ya watu wengi, ukiaibisha nyumba yako mwenyewe, na kupotewa na maisha yako.
HAB 2:11 Mawe ya kuta yatapiga kelele, na mihimili ya kazi ya mbao itarudisha mwangwi wake.
HAB 2:12 “Ole wake yeye ajengaye mji kwa kumwaga damu na kuusimamisha mji kwa uhalifu!
HAB 2:13 Je, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni hakuonesha kwamba kazi ya wanadamu ni mafuta tu kwa ajili ya moto, na kwamba mataifa yanajichosha bure?
HAB 2:14 Kwa kuwa dunia itajazwa na maarifa ya utukufu wa Mwenyezi Mungu, kama maji yaifunikavyo bahari.
HAB 2:15 “Ole wake yeye awapaye majirani zake kileo, akikimimina kutoka kwa kiriba cha mvinyo hadi wamelewa, ili apate kutazama miili yao iliyo uchi.
HAB 2:16 Utajazwa na aibu badala ya utukufu. Sasa ni zamu yako! Kunywa na ujifunue! Kikombe kutoka mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu kinakujia, na aibu itafunika utukufu wako.
HAB 2:17 Ukatili ulioifanyia Lebanoni utakufunika, na uharibifu uliowafanyia wanyama utakutisha. Kwa sababu umemwaga damu ya mtu; umeharibu nchi na miji na kila mmoja aliye ndani yake.
HAB 2:18 “Sanamu ina thamani gani, kwani mwanadamu ndiye alichonga? Ama kinyago kinachofundisha uongo? Kwa kuwa yeye aliyekitengeneza hutegemea kazi ya mikono yake mwenyewe; hutengeneza sanamu zisizoweza kuzungumza.
HAB 2:19 Ole wake yeye auambiaye mti, ‘Uwe hai!’ Ama asemaye na jiwe lisilo na uhai, ‘Amka!’ Je, linaweza kuongoza? Limefunikwa kwa dhahabu na fedha; hakuna pumzi ndani yake.
HAB 2:20 Lakini Mwenyezi Mungu yuko katika Hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze mbele yake.”
HAB 3:1 Sala ya nabii Habakuki iliyoimbwa kwa shigionothi.
HAB 3:2 Mwenyezi Mungu, nimezisikia sifa zako; nami naogopa kwa matendo yako, Ee Mwenyezi Mungu. Fufua kazi yako katika siku hizi zetu, tangaza habari yako wakati huu wetu; katika ghadhabu kumbuka rehema.
HAB 3:3 Mungu alitoka Temani, yeye Aliye Mtakatifu kutoka Mlima Parani. Utukufu wake ulifunika mbingu, na sifa zake zikaifunika dunia.
HAB 3:4 Mng’ao wake ulikuwa kama jua linapochomoza; miali ilimulika kutoka mkononi mwake, ambako nguvu zake zilifichwa.
HAB 3:5 Tauni ilimtangulia; maradhi ya kuambukiza yalifuata nyayo zake.
HAB 3:6 Alisimama, akaitikisa dunia; alitazama, na kuyafanya mataifa yatetemeke. Milima ya zamani iligeuka mavumbi na vilima vilivyozeeka vikaanguka. Njia zake ni za milele.
HAB 3:7 Niliona watu wa Kushani katika dhiki, na makazi ya Midiani katika maumivu makali.
HAB 3:8 Ee Mwenyezi Mungu, uliikasirikia mito? Je, ghadhabu yako ilikuwa dhidi ya vijito? Je, ulighadhibikia bahari ulipoendesha farasi wako na magari yako ya vita ili ushinde?
HAB 3:9 Uliufunua upinde wako na kuitisha mishale mingi. Uliigawa dunia kwa mito;
HAB 3:10 milima ilikuona ikatetemeka. Mafuriko ya maji yakapita huko; vilindi vilinguruma na kuinua mawimbi yake juu.
HAB 3:11 Jua na mwezi vilisimama kimya mbinguni katika mng’ao wa mishale yako inayoruka, na katika mng’ao wa mkuki wako umeremetao.
HAB 3:12 Kwa ghadhabu ulipitia kwenye dunia, na katika hasira ulikanyaga mataifa.
HAB 3:13 Ulikuja kuwaokoa watu wako, kumwokoa uliyempaka mafuta. Ulimponda kiongozi wa nchi ya uovu, ukamvua toka kichwani hadi wayo.
HAB 3:14 Kwa mkuki wake mwenyewe ulitoboa kichwa chake wakati mashujaa wake walifurika nje kwa kishindo kututawanya, wakifurahi kama walio karibu kutafuna wale wanyonge waliokuwa mafichoni.
HAB 3:15 Ulikanyaga bahari kwa farasi wako, ukisukasuka maji makuu.
HAB 3:16 Nilisikia na moyo wangu ukagonga kwa nguvu, midomo yangu ikatetemeka kwa hofu niliposikia sauti; uchakavu ukanyemelea mifupa yangu, na miguu yangu ikatetemeka. Hata hivyo nitasubiri kwa uvumilivu siku ya maafa kuyajilia mataifa yaliyotuvamia.
HAB 3:17 Ingawa mtini hauchanui maua na hakuna zabibu juu ya mizabibu, ingawaje mzeituni hauzai, na hata mashamba hayatoi chakula, iwapo hakuna kondoo katika banda, wala ng’ombe katika zizi,
HAB 3:18 hata hivyo nitashangilia katika Mwenyezi Mungu, nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.
HAB 3:19 Bwana Mungu Mwenyezi ni nguvu yangu; huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala, huniwezesha kupita juu ya vilima. Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.
ZEP 1:1 Neno la Mwenyezi Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda:
ZEP 1:2 Mwenyezi Mungu asema, “Nitafagia kila kitu kutoka uso wa dunia.
ZEP 1:3 Nitafagilia mbali watu na wanyama; nitafagilia mbali ndege wa angani na samaki wa baharini. Wafanyao maovu watapata tu kokoto, nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,” asema Mwenyezi Mungu.
ZEP 1:4 “Nitaiadhibu Yuda na wote wanaoishi Yerusalemu. Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali kila mabaki ya Baali, majina ya wapagani na makuhani waabuduo sanamu:
ZEP 1:5 wale ambao husujudu juu ya mapaa kuabudu jeshi la vitu vya angani, wale ambao husujudu na kuapa kwa Mwenyezi Mungu na ambao pia huapa kwa Malkamu,
ZEP 1:6 wale wanaoacha kumfuata Mwenyezi Mungu, wala hawamtafuti Mwenyezi Mungu wala kutaka shauri lake.
ZEP 1:7 Nyamazeni mbele za Bwana Mungu Mwenyezi, kwa maana siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu. Mwenyezi Mungu ameandaa dhabihu, amewaweka wakfu wale aliowaalika.
ZEP 1:8 Katika siku ya dhabihu ya Mwenyezi Mungu nitawaadhibu wakuu na wana wa mfalme na wale wote wanaovaa nguo za kigeni.
ZEP 1:9 Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao hukwepa kukanyaga kizingiti, ambao hujaza hekalu la miungu yao kwa dhuluma na udanganyifu.”
ZEP 1:10 Mwenyezi Mungu asema, “Katika siku hiyo kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki, maombolezo kutoka mtaa wa pili, na mshindo mkubwa kutoka vilimani.
ZEP 1:11 Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni; wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa, wote ambao wanafanya biashara ya fedha wataangamizwa.
ZEP 1:12 Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa, na kuwaadhibu wale ambao wanakaa katika hali ya kuridhika, ambao ni kama divai iliyobaki kwenye machicha, ambao hudhani, ‘Mwenyezi Mungu hatafanya lolote, jema au baya.’
ZEP 1:13 Utajiri wao utatekwa nyara, nyumba zao zitabomolewa. Watajenga nyumba, lakini hawataishi ndani yake; watapanda mizabibu lakini hawatakunywa divai yake.
ZEP 1:14 “Siku kubwa ya Mwenyezi Mungu iko karibu: iko karibu na inakuja haraka. Sikilizeni! Kilio katika siku ya Mwenyezi Mungu kitakuwa chungu. Shujaa atapiga ukelele wa vita huko.
ZEP 1:15 Siku ile ni siku ya ghadhabu, siku ya fadhaa na dhiki, siku ya uharibifu na ukiwa, siku ya giza na utusitusi, siku ya mawingu na giza nene,
ZEP 1:16 siku ya tarumbeta na kelele za vita dhidi ya miji yenye ngome, na dhidi ya minara mirefu.
ZEP 1:17 Nitawaletea watu dhiki, nao watatembea kama vipofu, kwa sababu wametenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu. Damu yao itamwagwa kama vumbi na matumbo yao kama kinyesi.
ZEP 1:18 Fedha yao wala dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Katika moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa, kwa maana ghafula ataleta mwisho wa wote wanaoishi duniani.”
ZEP 2:1 Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja, enyi taifa lisilo na aibu,
ZEP 2:2 kabla wakati ulioamriwa haujafika na siku ile inayopeperusha kama makapi, kabla hasira kali ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu, kabla siku ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu.
ZEP 2:3 Mtafuteni Mwenyezi Mungu, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi, ninyi ambao hufanya lile analoamuru. Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu; labda mtahifadhiwa siku ya hasira ya Mwenyezi Mungu.
ZEP 2:4 Gaza utaachwa na Ashkeloni utaachwa magofu. Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu, na Ekroni utang’olewa.
ZEP 2:5 Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari, enyi Wakerethi; neno la Mwenyezi Mungu liko dhidi yenu, ee Kanaani, nchi ya Wafilisti. “Mimi nitawaangamiza, na hakuna atakayebaki.”
ZEP 2:6 Nchi iliyo karibu na bahari itakuwa malisho yenye visima vya wachungaji, na mazizi ya kondoo.
ZEP 2:7 Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda, hapo watapata malisho. Wakati wa jioni watajilaza chini katika nyumba za Ashkeloni. Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawatunza, naye atawarudishia wafungwa wao.
ZEP 2:8 “Nimeyasikia matukano ya Moabu nazo dhihaka za Waamoni, ambao waliwatukana watu wangu na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao.
ZEP 2:9 Hakika, kama niishivyo,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, “hakika Moabu itakuwa kama Sodoma, Waamoni kama Gomora: mahali pa magugu na mashimo ya chumvi, nchi ya ukiwa milele. Mabaki ya watu wangu watawateka nyara; mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”
ZEP 2:10 Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao, kwa kutukana na kudhihaki watu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ZEP 2:11 Mwenyezi Mungu atakuwa wa kuhofisha kwao atakapoangamiza miungu yote ya nchi. Mataifa katika kila pwani yatamwabudu, kila moja katika nchi yake.
ZEP 2:12 “Ninyi pia, ee Wakushi, mtauawa kwa upanga wangu.”
ZEP 2:13 Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini na kuangamiza Waashuru, akiiacha Ninawi ukiwa na pakame kama jangwa.
ZEP 2:14 Makundi ya kondoo na ng’ombe yatajilaza pale, viumbe vya kila aina. Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba wataishi juu ya nguzo zake. Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani, kifusi kitakuwa milangoni, boriti za mwerezi zitaachwa wazi.
ZEP 2:15 Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha wakijisikia salama. Ulisema moyoni mwako, “Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.” Jinsi gani umekuwa gofu, mahali pa kulala wanyama pori! Wote wanaopita kando yake wanauzomea na kutikisa mkono kwa dharau.
ZEP 3:1 Ole mji wa wadhalimu, waasi na waliotiwa unajisi!
ZEP 3:2 Hautii mtu yeyote, haukubali maonyo. Haumtumaini Mwenyezi Mungu, haukaribii karibu na Mungu wake.
ZEP 3:3 Maafisa wake ni simba wanaonguruma, watawala wake ni mbwa-mwitu wa jioni, ambao hawabakizi chochote kwa ajili ya asubuhi.
ZEP 3:4 Manabii wake ni wenye kiburi, ni wadanganyifu. Makuhani wake hunajisi patakatifu na kuihalifu sheria.
ZEP 3:5 Mwenyezi Mungu aliye ndani yake ni mwenye haki, hafanyi kosa. Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake, kila kukipambazuka huitimiza, bali mtu dhalimu hana aibu.
ZEP 3:6 “Nimeyaangamiza mataifa, ngome zao zimebomolewa. Nimeziacha barabara ukiwa, hakuna anayepita humo. Miji yao imeharibiwa; hakuna mmoja atakayeachwa: hakuna hata mmoja.
ZEP 3:7 Niliuambia huo mji, ‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’ Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali, wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake. Lakini walikuwa bado na shauku kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”
ZEP 3:8 Mwenyezi Mungu anasema, “Kwa hiyo ningojee mimi, siku nitakayosimama kuteka nyara. Nimeamua kukusanya mataifa, kukusanya falme na kumimina ghadhabu yangu juu yao, hasira yangu kali yote. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa hasira yangu yenye wivu.
ZEP 3:9 “Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa, kwamba wote waweze kuliitia jina la Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa pamoja.
ZEP 3:10 Kutoka ng’ambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniabudu, watu wangu waliotawanyika, wataniletea sadaka.
ZEP 3:11 Siku hiyo hutaaibishwa kwa ajili ya makosa yote uliyonitendea, kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu wale wote wanaoshangilia katika kiburi chao. Kamwe hutajivuna tena katika kilima changu kitakatifu.
ZEP 3:12 Lakini nitakuachia ndani yako wapole na wanyenyekevu, ambao wanatumaini jina la Mwenyezi Mungu.
ZEP 3:13 Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa; hawatasema uongo, wala udanganyifu hautakuwa katika vinywa vyao. Watakula na kulala wala hakuna yeyote atakayewaogopesha.”
ZEP 3:14 Imba, ee Binti Sayuni; paza sauti, ee Israeli! Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee Binti Yerusalemu!
ZEP 3:15 Mwenyezi Mungu amekuondolea adhabu yako, amewarudisha nyuma adui zako. Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe; kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.
ZEP 3:16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu, “Usiogope, ee Sayuni; usiiache mikono yako ilegee.
ZEP 3:17 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, yu pamoja nawe, yeye ni Shujaa mwenye nguvu anayeokoa. Atakufurahia kwa furaha kubwa, atakutuliza kwa pendo lake, atakufurahia kwa kuimba.”
ZEP 3:18 “Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa nitaziondoa kwenu; hizo ni mzigo na fedheha kwenu.
ZEP 3:19 Wakati huo nitawaadhibu wote waliokudhulumu; nitaokoa vilema na kukusanya wale waliotawanywa. Nitawapa sifa na heshima katika kila nchi ambayo waliaibishwa.
ZEP 3:20 Wakati huo nitawakusanya; wakati huo nitawaleta nyumbani. Nitawapa sifa na heshima miongoni mwa mataifa yote ya dunia wakati nitakapowarudishia mateka yenu mbele ya macho yenu hasa,” asema Mwenyezi Mungu.
HAG 1:1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, katika siku ya kwanza ya mwezi wa sita, neno la Mwenyezi Mungu lilikuja kupitia kwa nabii Hagai kwenda kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na kwa Yoshua mwana wa kuhani mkuu Yehosadaki:
HAG 1:2 Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Hawa watu husema, ‘Wakati haujawadia wa kujenga nyumba ya Mwenyezi Mungu.’ ”
HAG 1:3 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likaja kupitia kwa nabii Hagai:
HAG 1:4 “Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki gofu?”
HAG 1:5 Sasa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Zitafakarini vyema njia zenu.
HAG 1:6 Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.”
HAG 1:7 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Zitafakarini vyema njia zenu.
HAG 1:8 Pandeni milimani mkalete miti na kujenga nyumba, ili nipate kuifurahia, na nitukuzwe,” asema Mwenyezi Mungu.
HAG 1:9 “Mlitarajia mengi, kumbe, yametokea kidogo. Ulichokileta nyumbani nilikipeperusha. Kwa nini?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Ni kwa sababu ya nyumba yangu, inayobaki katika hali ya magofu, wakati kila mmoja wenu anajishughulisha na nyumba yake mwenyewe.
HAG 1:10 Kwa hiyo, mbingu zimezuia umande wake na ardhi mavuno yake kwa sababu yenu.
HAG 1:11 Niliita ukame mashambani na milimani, kwenye nafaka, mvinyo mpya, mafuta pamoja na chochote kinachozalishwa na ardhi, juu ya watu na ng’ombe, pamoja na kazi za mikono yenu.”
HAG 1:12 Kisha Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yoshua kuhani mkuu mwana wa Yehosadaki, pamoja na mabaki yote ya watu wakaitii sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, pamoja na ujumbe wa nabii Hagai, kwa sababu alikuwa ametumwa na Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Watu walimwogopa Mwenyezi Mungu.
HAG 1:13 Kisha Hagai, mjumbe wa Mwenyezi Mungu, akawapa watu ujumbe huu wa Mwenyezi Mungu: “Mimi niko pamoja nanyi,” asema Mwenyezi Mungu.
HAG 1:14 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akachochea roho ya Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na roho ya kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, pamoja na roho za mabaki yote ya watu. Walikuja, wakaanza kufanya kazi katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wao,
HAG 1:15 siku ya ishirini na nne ya mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario.
HAG 2:1 Katika siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba, neno la Mwenyezi Mungu lilikuja kupitia nabii Hagai, kusema:
HAG 2:2 “Sema na Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, na mabaki ya watu. Uwaulize,
HAG 2:3 ‘Ni nani miongoni mwenu aliyebaki ambaye aliiona hii nyumba katika utukufu wake wa mwanzo? Sasa inaonekanaje kwenu? Je, haionekani kwenu kama si kitu?
HAG 2:4 Lakini sasa uwe imara, ee Zerubabeli,’ asema Mwenyezi Mungu. ‘Kuwa imara, ee kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Mwe imara, enyi watu wote wa nchi,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘na mfanye kazi. Kwa kuwa mimi nipo pamoja nanyi,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
HAG 2:5 ‘Hili ndilo nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri. Pia Roho wangu Mtakatifu anadumu kati yenu. Msiogope.’
HAG 2:6 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Baada ya muda kidogo kwa mara nyingine nitazitikisa mbingu na nchi, bahari na nchi kavu.
HAG 2:7 Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
HAG 2:8 ‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
HAG 2:9 ‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
HAG 2:10 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilikuja kwa nabii Hagai:
HAG 2:11 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Ulizeni makuhani jinsi sheria inavyosema:
HAG 2:12 Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’ ” Makuhani wakajibu, “La.”
HAG 2:13 Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?” Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.”
HAG 2:14 Kisha Hagai akasema, “ ‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asema Mwenyezi Mungu. ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi.
HAG 2:15 “ ‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
HAG 2:16 Mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu.
HAG 2:17 Kazi zenu zote za mikono nilizipiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, lakini hata hivyo, hamkunigeukia mimi,’ asema Mwenyezi Mungu.
HAG 2:18 ‘Tangu leo na kuendelea, kuanzia siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, tafakarini siku ambayo msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu uliwekwa. Tafakarini:
HAG 2:19 Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Hadi sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda. “ ‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’ ”
HAG 2:20 Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Hagai kwa mara ya pili katika siku ya ishirini na nne ya mwezi kusema:
HAG 2:21 “Mwambie Zerubabeli mtawala wa Yuda kwamba nitazitikisa mbingu na nchi.
HAG 2:22 Nitapindua viti vya falme, na kuziharibu kabisa nguvu za falme za kigeni. Nitapindua magari ya vita pamoja na waendeshaji wake; farasi na wapanda farasi wataanguka, kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake.
HAG 2:23 “ ‘Katika siku ile,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nitakuchukua wewe, mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli,’ asema Mwenyezi Mungu. ‘Nitakufanya kama pete yangu ya muhuri, kwa kuwa nimekuchagua,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
ZEC 1:1 Katika mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kusema:
ZEC 1:2 “Mwenyezi Mungu aliwakasirikia sana baba zako wa zamani.
ZEC 1:3 Kwa hiyo waambie watu: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nirudieni mimi,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nami nitawarudia ninyi,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ZEC 1:4 Msiwe kama baba zenu, ambao manabii waliotangulia waliwatangazia: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Geukeni, mziache njia zenu mbaya na matendo yenu maovu.’ Lakini hawakunisikiliza wala kufuata maelekezo yangu, asema Mwenyezi Mungu.
ZEC 1:5 Wako wapi baba zako sasa? Nao manabii, je, wanaishi milele?
ZEC 1:6 Je, maneno yangu na amri zangu nilizowaagiza manabii watumishi wangu, hayakuwapata baba zenu? “Kisha walitubu na kusema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ametutenda sawasawa na njia zetu na matendo yetu yalivyostahili, kama alivyokusudia kufanya.’ ”
ZEC 1:7 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido.
ZEC 1:8 Wakati wa usiku nilipata maono, na tazama, mbele yangu palikuwa na mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia, na weupe.
ZEC 1:9 Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?” Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonesha kuwa ni nini.”
ZEC 1:10 Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewatuma waende duniani kote.”
ZEC 1:11 Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa Mwenyezi Mungu, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.”
ZEC 1:12 Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akasema, “Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, utazuia hadi lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?”
ZEC 1:13 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami.
ZEC 1:14 Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni,
ZEC 1:15 lakini nimeyakasirikia sana mataifa yanayojisikia kuwa yako salama. Nilikuwa nimewakasirikia Israeli kidogo tu, lakini mataifa hayo yaliwazidishia maafa.’
ZEC 1:16 “Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Nitairudia Yerusalemu kwa rehema na huko nyumba yangu itajengwa tena. Nayo kamba ya kupimia itanyooshwa juu ya Yerusalemu,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ZEC 1:17 “Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na Mwenyezi Mungu atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’ ”
ZEC 1:18 Kisha nikatazama juu, na pale mbele yangu nikaona pembe nne!
ZEC 1:19 Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Ni nini hizi?” Akanijibu, “Hizi ni zile pembe zilizowatawanya Yuda, Israeli na Yerusalemu.”
ZEC 1:20 Kisha Mwenyezi Mungu akanionesha mafundi wanne.
ZEC 1:21 Nikauliza, “Hawa wanakuja kufanya nini?” Akanijibu, “Hizi ndizo pembe zilizowatawanya Yuda ili asiwepo atakayeweza kuinua kichwa chake, lakini mafundi wamekuja kuzitia hofu na kuzitupa chini hizi pembe za mataifa ambayo yaliinua pembe zao dhidi ya nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”
ZEC 2:1 Kisha nikatazama juu: pale mbele yangu palikuwa na mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake!
ZEC 2:2 Nikamuuliza, “Unaenda wapi?” Akanijibu, “Kupima Yerusalemu, kupata urefu na upana wake.”
ZEC 2:3 Kisha malaika aliyekuwa akizungumza nami akaondoka, malaika mwingine akaja kukutana naye
ZEC 2:4 na kumwambia: “Kimbia, umwambie yule kijana, ‘Yerusalemu utakuwa mji usio na kuta kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo.
ZEC 2:5 Mimi mwenyewe nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘nami nitakuwa utukufu wake ndani yake.’
ZEC 2:6 “Njooni! Njooni! Kimbieni mtoke katika nchi ya kaskazini,” asema Mwenyezi Mungu, “kwa kuwa nimewatawanya kwenye pande nne za mbingu,” asema Mwenyezi Mungu.
ZEC 2:7 “Njoo, ee Sayuni! Kimbia, wewe ukaaye ndani ya Binti Babeli!”
ZEC 2:8 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Baada ya yeye kuniheshimu na kunituma mimi dhidi ya mataifa yaliyokuteka nyara, kwa kuwa yeyote awagusaye ninyi, anaigusa mboni ya jicho lake,
ZEC 2:9 hakika nitauinua mkono wangu dhidi yao ili watumwa wao wawateke nyara. Ndipo mtajua kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma.
ZEC 2:10 “Shangilia na ufurahie, ee Binti Sayuni, kwa maana ninakuja, nami nitaishi miongoni mwenu,” asema Mwenyezi Mungu.
ZEC 2:11 “Mataifa mengi yataunganishwa na Mwenyezi Mungu siku hiyo, nao watakuwa watu wangu. Nitaishi miongoni mwenu, nanyi mtajua kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma kwenu.
ZEC 2:12 Mwenyezi Mungu atairithi Yuda kama fungu lake katika nchi takatifu na atachagua tena Yerusalemu.
ZEC 2:13 Tulieni mbele za Mwenyezi Mungu, enyi watu wote, kwa sababu ameinuka kutoka makao yake matakatifu.”
ZEC 3:1 Kisha akanionesha Yoshua, kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa Mwenyezi Mungu, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki.
ZEC 3:2 Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Mwenyezi Mungu akukemee Shetani! Mwenyezi Mungu, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?”
ZEC 3:3 Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika.
ZEC 3:4 Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.” Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.”
ZEC 3:5 Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama karibu.
ZEC 3:6 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamwamuru Yoshua:
ZEC 3:7 “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Ikiwa utatembea katika njia zangu na kushika maagizo yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuzilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa.
ZEC 3:8 “ ‘Sikiliza, ee Yoshua kuhani mkuu, pamoja na wenzako walioketi mbele yako, ambao ni watu walio ishara ya mambo yatakayokuja: Ninaenda kumleta mtumishi wangu, Tawi.
ZEC 3:9 Tazama, jiwe nililoliweka mbele ya Yoshua! Kuna macho saba juu ya jiwe lile moja, nami nitachora maandishi juu yake,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nami nitaiondoa dhambi ya nchi hii kwa siku moja.
ZEC 3:10 “ ‘Katika siku hiyo kila mmoja wenu atamwalika jirani yake akae chini ya mzabibu wake na mtini wake,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
ZEC 4:1 Kisha malaika aliyezungumza nami akarudi na kuniamsha, kama mtu aamshwavyo kutoka usingizini.
ZEC 4:2 Akaniuliza, “Unaona nini?” Nikajibu, “Ninaona kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake na taa saba juu yake, tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwenye taa zote zilizo juu yake.
ZEC 4:3 Pia kuna mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume wa bakuli na mwingine upande wa kushoto.”
ZEC 4:4 Nikamuuliza malaika aliyezungumza nami, “Hivi ni vitu gani, bwana wangu?”
ZEC 4:5 Akanijibu, “Hujui kuwa hivi ni vitu gani?” Nikajibu, “Hapana, bwana wangu.”
ZEC 4:6 Kisha akaniambia, “Hili ni neno la Mwenyezi Mungu kwa Zerubabeli: ‘Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa Roho wangu Mtakatifu,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ZEC 4:7 “Wewe ni kitu gani, ee mlima mkubwa sana? Mbele ya Zerubabeli wewe utakuwa ardhi tambarare. Kisha ataweka jiwe la juu kabisa, na watu wakishangilia na kusema, ‘Mungu libariki! Mungu libariki!’ ”
ZEC 4:8 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia:
ZEC 4:9 “Mikono ya Zerubabeli iliweka msingi wa Hekalu hili, mikono yake pia italimalizia. Kisha mtajua ya kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma mimi kwenu.
ZEC 4:10 “Ni nani atakayeidharau siku ya mambo madogo? Macho saba ya Mwenyezi Mungu, yanayozunguka dunia yote, yatashangilia yatakapoona jiwe la juu kabisa likiwa mkononi mwa Zerubabeli!”
ZEC 4:11 Kisha nikamuuliza yule malaika, “Hii mizeituni miwili iliyo upande wa kuume na wa kushoto wa kinara cha taa ni nini?”
ZEC 4:12 Tena nikamuuliza, “Haya matawi mawili ya mizeituni karibu na hiyo mirija miwili ya dhahabu inayomimina mafuta ya dhahabu ni nini?”
ZEC 4:13 Akajibu, “Hujui kuwa haya ni nini?” Nikamjibu, “Hapana, bwana wangu.”
ZEC 4:14 Kwa hiyo akasema, “Hawa ni wawili ambao wamepakwa mafuta ili kumtumikia Bwana wa dunia yote.”
ZEC 5:1 Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kinachoruka!
ZEC 5:2 Akaniuliza, “Unaona nini?” Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka, chenye urefu wa dhiraa ishirini, na upana wa dhiraa kumi.”
ZEC 5:3 Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali.
ZEC 5:4 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’ ”
ZEC 5:5 Kisha yule malaika aliyekuwa akizungumza nami akanijia na kuniambia, “Tazama juu uone ni nini kile kinachojitokeza.”
ZEC 5:6 Nikamuuliza, “Ni kitu gani?” Akanijibu, “Ni kikapu cha kupimia.” Kisha akaongeza kusema, “Huu ni uovu wa watu katika nchi nzima.”
ZEC 5:7 Kisha kifuniko kilichotengenezwa kwa madini ya risasi kilichokuwa kimefunika kile kikapu, kiliinuliwa na ndani ya kile kikapu alikuwako mwanamke ameketi!
ZEC 5:8 Akasema, “Huu ni uovu,” tena akamsukumia ndani ya kikapu na kushindilia kifuniko juu ya mdomo wa kikapu.
ZEC 5:9 Kisha nikatazama juu: na pale mbele yangu, palikuwa na wanawake wawili, wakiwa na upepo katika mabawa yao! Walikuwa na mabawa kama ya korongo, nao wakainua kile kikapu na kuruka nacho kati ya mbingu na nchi.
ZEC 5:10 Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Wanakipeleka wapi hicho kikapu?”
ZEC 5:11 Akanijibu, “Wanakipeleka katika nchi ya Babeli na kujenga nyumba kwa ajili yake. Itakapokuwa tayari, kikapu kitawekwa pale mahali pake.”
ZEC 6:1 Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba!
ZEC 6:2 Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi,
ZEC 6:3 la tatu lilivutwa na farasi weupe, na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu.
ZEC 6:4 Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani, bwana wangu?”
ZEC 6:5 Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake.
ZEC 6:6 Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi, na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.”
ZEC 6:7 Hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote.
ZEC 6:8 Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaoenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho wangu Mtakatifu katika nchi ya kaskazini.”
ZEC 6:9 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
ZEC 6:10 “Chukua fedha na dhahabu kutoka kwa watu waliohamishwa, yaani Heldai, Tobia na Yedaya ambao wamefika kutoka Babeli. Siku hiyo hiyo nenda nyumbani mwa Yosia mwana wa Sefania.
ZEC 6:11 Chukua fedha na dhahabu utengeneze taji, nawe uliweke kichwani mwa kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki.
ZEC 6:12 Umwambie hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Huyu ndiye mtu anayeitwa Tawi, naye atachipua kutoka mahali pake na kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu.
ZEC 6:13 Ni yeye atakayejenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, naye atavikwa utukufu na ataketi kumiliki kwenye kiti cha enzi. Atakuwa kuhani kwenye kiti chake cha enzi. Hapo patakuwa na amani kati ya hao wawili.’
ZEC 6:14 Taji litatolewa kwa Heldai, Tobia, Yedaya na Heni mwana wa Sefania kama kumbukumbu ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.
ZEC 6:15 Wale walio mbali sana watakuja na kusaidia kulijenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, nanyi mtajua kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma kwenu. Hili litatokea ikiwa mtamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa bidii.”
ZEC 7:1 Katika mwaka wa nne wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Zekaria siku ya nne ya mwezi wa tisa, mwezi wa Kisleu.
ZEC 7:2 Watu wa Betheli walikuwa wamemtuma Shareza na Regem-Meleki pamoja na watu wao, kumsihi Mwenyezi Mungu
ZEC 7:3 kwa kuwauliza makuhani wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na manabii, “Je, imempasa kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwa miaka mingi?”
ZEC 7:4 Kisha neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia kusema:
ZEC 7:5 “Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu?
ZEC 7:6 Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu?
ZEC 7:7 Je, haya sio maneno ya Mwenyezi Mungu aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefela zikiwa zimekaliwa na watu?’ ”
ZEC 7:8 Neno la Mwenyezi Mungu likamjia tena Zekaria:
ZEC 7:9 “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Fanyeni hukumu za haki, onesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi.
ZEC 7:10 Msimdhulumu mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
ZEC 7:11 “Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao.
ZEC 7:12 Wakaifanya mioyo yao migumu kama gumegume, na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aliyatuma kwa Roho wake Mtakatifu kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, alikasirika sana.
ZEC 7:13 “ ‘Nilipoita, hawakusikiliza; kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ZEC 7:14 ‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’ ”
ZEC 8:1 Neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia tena.
ZEC 8:2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Nina wivu sana kwa ajili ya Sayuni, ninawaka wivu kwa ajili yake.”
ZEC 8:3 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Nitarudi Sayuni na kufanya makao Yerusalemu. Kisha Yerusalemu utaitwa mji wa kweli, mlima wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni utaitwa Mlima Mtakatifu.”
ZEC 8:4 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Kwa mara nyingine tena wanaume na wanawake walioshiba umri wataketi katika barabara za Yerusalemu, kila mmoja akiwa na mkongojo wake mkononi kwa sababu ya umri wake.
ZEC 8:5 Barabara za mji zitajaa wavulana na wasichana wanaocheza humo.”
ZEC 8:6 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Mambo haya yanaweza kuonekana ya ajabu kwa mabaki ya watu wakati huo, lakini yaweza kuwa ya ajabu kwangu?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ZEC 8:7 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi za mashariki na magharibi.
ZEC 8:8 Nitawarudisha waje kuishi Yerusalemu, watakuwa watu wangu nami nitakuwa mwaminifu na wa haki kwao kama Mungu wao.”
ZEC 8:9 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Ninyi ambao sasa mnasikia maneno haya yanayozungumzwa na manabii ambao walikuwepo wakati wa kuwekwa kwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, mikono yenu na iwe na nguvu ili Hekalu liweze kujengwa.
ZEC 8:10 Kabla ya wakati huo, hapakuwa na ujira kwa mtu wala mnyama. Hakuna mtu aliyeweza kufanya shughuli yake kwa usalama kwa sababu ya adui yake, kwa kuwa nilikuwa nimemfanya kila mtu adui wa jirani yake.
ZEC 8:11 Lakini sasa sitawatendea mabaki ya watu hawa kama nilivyowatenda zamani,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
ZEC 8:12 “Mbegu itakua vizuri, mzabibu utazaa matunda yake, ardhi itatoa mazao yake, na mbingu zitadondosha umande wake. Vitu hivi vyote nitawapa mabaki ya watu kama urithi wao.
ZEC 8:13 Jinsi mlivyokuwa kitu cha laana katikati ya mataifa, ee Yuda na Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka. Msiogope, bali iacheni mikono yenu iwe na nguvu.”
ZEC 8:14 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Kama nilivyokuwa nimekusudia kuleta maangamizi juu yenu, wakati baba zenu waliponikasirisha na sikuonesha huruma,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
ZEC 8:15 “hivyo sasa nimeazimia kufanya mema tena kwa Yerusalemu na Yuda. Msiogope.
ZEC 8:16 Haya ndio mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu,
ZEC 8:17 usipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia haya yote,” asema Mwenyezi Mungu.
ZEC 8:18 Neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia tena.
ZEC 8:19 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Saumu ya mwezi wa nne, ya mwezi wa tano, ya mwezi wa saba, na ya mwezi wa kumi zitakuwa sikukuu za furaha na za shangwe kwa Yuda. Kwa hiyo uipende kweli na amani.”
ZEC 8:20 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Mataifa mengi na wakazi wa miji mingi watakuja,
ZEC 8:21 na wenyeji wa mji mmoja wataenda kwenye mji mwingine na kusema, ‘Twende mara moja na tukamsihi Mwenyezi Mungu, na kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Mimi mwenyewe ninaenda.’
ZEC 8:22 Pia watu wa kabila nyingi na mataifa yenye nguvu yatakuja Yerusalemu kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na kumsihi.”
ZEC 8:23 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Katika siku hizo watu kumi kutoka lugha zote na mataifa, watang’ang’ania upindo wa joho la Myahudi mmoja na kusema, ‘Twende pamoja nawe kwa sababu tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nawe.’ ”
ZEC 9:1 Neno la unabii: Neno la Mwenyezi Mungu liko kinyume na nchi ya Hadraki na Dameski itakuwa mahali pa kupumzika, kwa kuwa macho ya watu na ya makabila yote ya Israeli yako kwa Mwenyezi Mungu;
ZEC 9:2 pia juu ya Hamathi inayopakana nayo, juu ya Tiro na Sidoni, ingawa wana ujuzi mwingi sana.
ZEC 9:3 Tiro amejijengea ngome imara, amelundika fedha kama mavumbi, na dhahabu kama taka za mitaani.
ZEC 9:4 Lakini Bwana atamwondolea mali yake na kuuangamiza uwezo wake wa baharini, naye atateketezwa kwa moto.
ZEC 9:5 Ashkeloni ataona hili na kuogopa; Gaza atagaagaa kwa maumivu makali, pia Ekroni, kwa sababu matumaini yake yatanyauka. Gaza atampoteza mfalme wake na Ashkeloni ataachwa pweke.
ZEC 9:6 Wageni watakalia mji wa Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.
ZEC 9:7 Nitaondoa damu vinywani mwao, chakula kile walichokatazwa kati ya meno yao. Mabaki yao yatakuwa mali ya Mungu wetu, nao watakuwa viongozi katika Yuda, naye Ekroni atakuwa kama Wayebusi.
ZEC 9:8 Lakini nitailinda nyumba yangu dhidi ya majeshi ya wanyang’anyi. Kamwe mdhalimu hatashambulia watu wangu tena, kwa maana sasa ninawachunga.
ZEC 9:9 Shangilia sana, ee Binti Sayuni! Piga kelele, Binti Yerusalemu! Tazama, Mfalme wako anakuja kwako, ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mpole, naye amepanda punda, mwana-punda, mtoto wa punda.
ZEC 9:10 Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu na farasi wa vita kutoka Yerusalemu, nao upinde wa vita utavunjwa. Atatangaza amani kwa mataifa. Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari, na kutoka Mto hadi mwisho wa dunia.
ZEC 9:11 Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya agano langu nawe, nitawaacha huru wafungwa wako watoke kwenye shimo lisilo na maji.
ZEC 9:12 Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini; hata sasa ninatangaza kwamba nitawarejesheeni maradufu.
ZEC 9:13 Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu, nitamfanya Efraimu mshale wangu. Nitawainua wana wako, ee Sayuni, dhidi ya wana wako, ee Uyunani, na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita.
ZEC 9:14 Kisha Mwenyezi Mungu atawatokea; mshale wake utamulika kama radi. Bwana Mungu Mwenyezi atapiga tarumbeta, naye atatembea katika tufani za kusini,
ZEC 9:15 na Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atawalinda. Wataangamiza na kushinda kwa mawe ya kutupa kwa kombeo. Watakunywa na kunguruma kama waliolewa mvinyo; watajaa kama bakuli linalotumika kunyunyizia kwenye pembe za madhabahu.
ZEC 9:16 Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo kama kundi la watu wake. Watang’ara katika nchi yake kama vito vya thamani kwenye taji.
ZEC 9:17 Jinsi gani watavutia na kuwa wazuri! Nafaka itawastawisha vijana wanaume, nayo divai mpya vijana wanawake.
ZEC 10:1 Mwombeni Mwenyezi Mungu mvua wakati wa vuli; ndiye Mwenyezi Mungu atengenezaye mawingu ya tufani. Huwapa watu manyunyu ya mvua, pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu.
ZEC 10:2 Sanamu huzungumza udanganyifu, waaguzi huona maono ya uongo; husimulia ndoto ambazo si za kweli, wanatoa faraja batili. Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo walioteseka kwa kukosa mchungaji.
ZEC 10:3 “Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atalichunga kundi lake, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kama farasi mwenye kiburi akiwa vitani.
ZEC 10:4 Kutoka Yuda litatokea Jiwe la pembeni, kutoka kwake vitatoka vigingi vya hema, kutoka kwake utatoka upinde wa vita, kutoka kwake atatoka kila mtawala.
ZEC 10:5 Kwa pamoja watakuwa kama mashujaa wanaokanyaga barabara za matope wakati wa vita. Kwa sababu Mwenyezi Mungu yu pamoja nao, watapigana na kuwashinda wapanda farasi.
ZEC 10:6 “Nitaiimarisha nyumba ya Yuda na kuiokoa nyumba ya Yusufu. Nitawarejesha kwa sababu nina huruma juu yao. Watakuwa kama watu ambao sijawahi kuwakataa kwa sababu mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao, nami nitawajibu.
ZEC 10:7 Waefraimu watakuwa kama mashujaa, mioyo yao itafurahi kana kwamba ni kwa divai. Watoto wao wataona na kufurahi, mioyo yao itashangilia katika Mwenyezi Mungu.
ZEC 10:8 Nitawaashiria na kuwakusanya ndani. Hakika nitawakomboa, nao watakuwa wengi kama walivyokuwa mwanzoni.
ZEC 10:9 Ijapokuwa niliwatawanya miongoni mwa mataifa, hata hivyo wakiwa katika nchi za mbali watanikumbuka mimi. Wao na watoto wao watanusurika katika hatari nao watarudi.
ZEC 10:10 Nitawarudisha kutoka Misri na kuwakusanya toka Ashuru. Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni, na hapo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha.
ZEC 10:11 Watapita katika bahari ya mateso; bahari iliyochafuka itatulizwa na vilindi vyote vya Mto Naili vitakauka. Kiburi cha Ashuru kitashushwa, nayo fimbo ya utawala ya Misri itatoweka.
ZEC 10:12 Nitawaimarisha katika Mwenyezi Mungu, na katika jina lake watatembea,” asema Mwenyezi Mungu.
ZEC 11:1 Fungua milango yako, ee Lebanoni, ili moto uteketeze mierezi yako!
ZEC 11:2 Piga yowe, ee msunobari, kwa kuwa mwerezi umeanguka; miti ya fahari imeharibiwa! Piga yowe, enyi mialoni ya Bashani, msitu mnene umefyekwa!
ZEC 11:3 Sikiliza yowe la wachungaji; malisho yao manono yameangamizwa! Sikia ngurumo za simba; kichaka kilichostawi sana cha Yordani kimeharibiwa!
ZEC 11:4 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wangu: “Lilishe kundi lililokusudiwa kuchinjwa.
ZEC 11:5 Wanunuzi wake huwachinja na kuondoka pasipo kuadhibiwa. Wale wanaowauza husema, ‘Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, mimi ni tajiri!’ Wachungaji wao wenyewe hawawahurumii.
ZEC 11:6 Kwa kuwa sitawahurumia tena watu wa nchi,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawakabidhi kila mtu mkononi mwa jirani yake na mfalme wake. Wataitenda jeuri nchi, nami sitawaokoa kutoka mikononi mwao.”
ZEC 11:7 Kwa hiyo nikalilisha kundi lililotiwa alama kwa kuchinjwa, hasa kundi lililodhulumiwa sana. Kisha nikachukua fimbo mbili, moja nikaiita Fadhili na nyingine Umoja, nami nikalilisha kundi.
ZEC 11:8 Katika mwezi mmoja nikawaondoa wachungaji watatu. Kundi la kondoo likanichukia, nami nikachoshwa nao,
ZEC 11:9 nikasema, “Sitakuwa mchungaji wenu. Waache wanaokufa wafe na wanaoangamia waangamie. Wale waliobakia kila mmoja na ale nyama ya mwenzake.”
ZEC 11:10 Kisha nikachukua fimbo yangu inayoitwa Fadhili nikaivunja, kutangua agano nililofanya na mataifa yote.
ZEC 11:11 Likatanguka siku hiyo; kwa hiyo wale waliodhulumiwa katika kundi, waliokuwa wakiniangalia wakajua kuwa hilo lilikuwa neno la Mwenyezi Mungu.
ZEC 11:12 Nikawaambia, “Mkiona kuwa ni vyema, nipeni ujira wangu, la sivyo, basi msinipe.” Kwa hiyo wakanilipa vipande thelathini vya fedha.
ZEC 11:13 Naye Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mtupie mfinyanzi,” hiyo bei nzuri waliyonithaminia! Kwa hiyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha na kumtupia huyo mfinyanzi katika nyumba ya Mwenyezi Mungu.
ZEC 11:14 Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Umoja, kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli!
ZEC 11:15 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Vitwae tena vifaa vya mchungaji mpumbavu.
ZEC 11:16 Kwa maana ninaenda kumwinua mchungaji juu ya nchi ambaye hatamjali aliyepotea, wala kuwatafuta wale wachanga au kuwaponya waliojeruhiwa, wala kuwalisha wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo wanono na kuzirarua kwato zao.
ZEC 11:17 “Ole wa mchungaji asiyefaa, anayeliacha kundi! Upanga na uupige mkono wake na jicho lake la kuume! Mkono wake na unyauke kabisa, jicho lake la kuume lipofuke kabisa!”
ZEC 12:1 Neno la unabii: Hili ni neno la Mwenyezi Mungu kuhusu Israeli. Mwenyezi Mungu, yeye azitandaye mbingu, awekaye misingi ya dunia na aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake, asema:
ZEC 12:2 “Nitaenda kufanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumbisha mataifa yote yanayoizunguka. Yuda utazingirwa kwa vita na Yerusalemu pia.
ZEC 12:3 Katika siku hiyo, wakati mataifa yote ya dunia yatakapokusanyika dhidi yake, nitaufanya Yerusalemu kuwa jabali lisilosogezwa kwa mataifa yote. Wote watakaojaribu kulisogeza watajiumiza wenyewe.
ZEC 12:4 Katika siku hiyo nitampiga kila farasi kwa hofu ya ghafula, naye ampandaye nitampiga kwa wazimu,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitalielekeza jicho langu la ulinzi juu ya nyumba ya Yuda, nami nitawapofusha farasi wote wa mataifa.
ZEC 12:5 Kisha viongozi wa Yuda watasema mioyoni mwao, ‘Watu wa Yerusalemu wana nguvu kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ni Mungu wao.’
ZEC 12:6 “Katika siku hiyo nitawafanya viongozi wa Yuda kuwa kama kigae cha moto ndani ya lundo la kuni, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watateketeza kulia na kushoto mataifa yote yanayowazunguka, lakini Yerusalemu utabaki salama mahali pake.
ZEC 12:7 “Mwenyezi Mungu atayaokoa makao ya Yuda kwanza, ili heshima ya nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu isiwe kubwa kuliko ile ya Yuda.
ZEC 12:8 Katika siku hiyo, Mwenyezi Mungu atawakinga wale wanaoishi Yerusalemu, ili aliye dhaifu kupita wote miongoni mwao awe kama Daudi, nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama Malaika wa Mwenyezi Mungu akiwatangulia.
ZEC 12:9 Katika siku hiyo nitatoka kuangamiza mataifa yote yatakayoshambulia Yerusalemu.
ZEC 12:10 “Nami nitamiminia nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu roho ya neema na maombi. Watanitazama mimi, yule waliyemchoma. Nao watamwombolezea kama mtu anayemwombolezea mwanawe wa pekee na kusikitika kwa uchungu kama anayemsikitikia mzaliwa wake wa kwanza wa kiume.
ZEC 12:11 Katika siku hiyo kilio kitakuwa kikubwa Yerusalemu, kama kilio cha Hadad-Rimoni katika tambarare ya Megido.
ZEC 12:12 Nchi itaomboleza, kila ukoo peke yake, nao wake zao peke yao. Ukoo wa nyumba ya Daudi na wake zao, ukoo wa nyumba ya Nathani na wake zao,
ZEC 12:13 ukoo wa nyumba ya Lawi na wake zao, ukoo wa Shimei na wake zao,
ZEC 12:14 na koo zote zilizobaki na wake zao.
ZEC 13:1 “Katika siku hiyo, chemchemi itafunguliwa kwa nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu, kuwatakasa dhambi na unajisi.
ZEC 13:2 “Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi.
ZEC 13:3 Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la Mwenyezi Mungu.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo.
ZEC 13:4 “Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu.
ZEC 13:5 Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’
ZEC 13:6 Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’
ZEC 13:7 “Amka, ee upanga, dhidi ya mchungaji wangu, dhidi ya mtu aliye karibu nami!” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika, nami nitageuza mkono wangu dhidi ya walio wadogo,
ZEC 13:8 katika nchi yote,” asema Mwenyezi Mungu, “theluthi mbili watapigwa na kuangamia; hata hivyo theluthi moja watabaki ndani yake.
ZEC 13:9 Hii theluthi moja nitaileta katika moto; nitawasafisha kama fedha isafishwavyo na kuwajaribu kama dhahabu. Wataliitia Jina langu nami nitawajibu; nitasema, ‘Hawa ni watu wangu,’ nao watasema, ‘Mwenyezi Mungu ni Mungu wetu.’ ”
ZEC 14:1 Siku ya Mwenyezi Mungu inakuja ambayo nyara zilizotekwa kwenu zitagawanywa miongoni mwenu.
ZEC 14:2 Nitayakusanya mataifa yote huko Yerusalemu kupigana dhidi yake, mji utatekwa, nyumba zitavamiwa na kuporwa na wanawake watanajisiwa. Nusu ya mji wataenda uhamishoni, lakini watakaobaki hawataondolewa kutoka mjini.
ZEC 14:3 Kisha Mwenyezi Mungu atatoka na kupigana dhidi ya watu wa yale mataifa, kama apiganavyo siku ya vita.
ZEC 14:4 Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, mashariki mwa Yerusalemu, nao Mlima wa Mizeituni utagawanyika mara mbili kuanzia mashariki hadi magharibi, ukifanya bonde kubwa, nusu ya mlima ukisogea kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini.
ZEC 14:5 Nanyi mtakimbia kupitia katika bonde hilo la mlima wangu kwa kuwa litaenea hadi Aseli. Mtakimbia kama mlivyokimbia tetemeko la ardhi katika siku za Uzia mfalme wa Yuda. Kisha Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye.
ZEC 14:6 Siku hiyo hakutakuwa na nuru, baridi wala theluji.
ZEC 14:7 Itakuwa siku ya kipekee, isiyo na mchana wala usiku, siku ijulikanayo na Mwenyezi Mungu. Jioni inapofika nuru itakuwepo.
ZEC 14:8 Siku hiyo, maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu, nusu kwenda kwenye bahari ya mashariki, na nusu kwenda kwenye bahari ya magharibi wakati wa kiangazi na wakati wa masika.
ZEC 14:9 Mwenyezi Mungu atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo atakuwa Mwenyezi Mungu mmoja, na jina lake litakuwa jina pekee.
ZEC 14:10 Nchi yote kuanzia Geba, kaskazini mwa Yuda, hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itakuwa kama Araba. Lakini Yerusalemu utainuliwa juu na kubaki mahali pake, toka Lango la Benyamini hadi mahali pa Lango la Kwanza, mpaka kwenye Lango la Pembeni na kutoka Mnara wa Hananeli hadi kwenye mashinikizo ya divai ya mfalme.
ZEC 14:11 Utakaliwa na watu, kamwe hautaharibiwa tena, Yerusalemu utakaa salama.
ZEC 14:12 Hii ndiyo tauni ambayo Mwenyezi Mungu atapiga nayo mataifa yote ambayo yalipigana dhidi ya Yerusalemu: Nyama ya miili yao itaoza wangali wamesimama kwa miguu yao, macho yao yataoza kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza vinywani mwao.
ZEC 14:13 Katika siku hiyo Mwenyezi Mungu atawatia wanaume hofu kuu. Kila mwanaume atakamata mkono wa mwenzake nao watashambuliana.
ZEC 14:14 Yuda pia atapigana katika Yerusalemu. Utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka Yerusalemu utakusanywa, wingi wa dhahabu, fedha na mavazi.
ZEC 14:15 Tauni ya aina hiyo hiyo itapiga farasi na nyumbu, ngamia na punda, nao wanyama wote walio kwenye kambi za adui.
ZEC 14:16 Kisha walionusurika katika mataifa yote ambayo yaliushambulia Yerusalemu watakuwa wakipanda Yerusalemu kila mwaka kumwabudu Mfalme, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
ZEC 14:17 Ikiwa taifa lolote la dunia hawataenda Yerusalemu kumwabudu Mfalme, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, mvua haitanyesha kwao.
ZEC 14:18 Ikiwa watu wa Misri nao hawataenda kushiriki, hawatapata mvua. Mwenyezi Mungu ataleta juu yao tauni ambayo itayapiga mataifa ambayo hayataenda kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
ZEC 14:19 Hii itakuwa adhabu ya Misri na adhabu ya mataifa yote yale ambayo hayataenda Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
ZEC 14:20 Katika siku hiyo, kengele zilizofungwa kwenye farasi zitaandikwa maneno haya: “Takatifu kwa Mwenyezi Mungu”. Navyo vyungu vya kupikia katika nyumba ya Mwenyezi Mungu vitakuwa kama bakuli takatifu mbele ya madhabahu.
ZEC 14:21 Kila chungu kilicho Yerusalemu na Yuda kitakuwa kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, na wote wanaokuja kutoa dhabihu watachukua baadhi ya vyungu hivyo na kupikia. Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyabiashara katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 1:1 Neno la unabii: Neno la Mwenyezi Mungu kwa Israeli kupitia kwa Malaki.
MAL 1:2 Mwenyezi Mungu asema, “Nimewapenda ninyi. “Lakini ninyi mnauliza, ‘Wewe umetupendaje?’ ” Mwenyezi Mungu asema, “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nimempenda Yakobo,
MAL 1:3 lakini nikamchukia Esau, nami nimeifanya nchi yake ya vilima kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa jangwani.”
MAL 1:4 Edomu anaweza kusema, “Ingawa tumepondapondwa, tutajenga upya magofu.” Lakini hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Wanaweza kujenga, lakini nitabomoa. Wataitwa Nchi Ovu, watu ambao siku zote wapo chini ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
MAL 1:5 Mtayaona kwa macho yenu wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi Mungu ni mkuu, hata nje ya mipaka ya Israeli!’
MAL 1:6 “Mwana humheshimu baba yake, naye mtumishi humheshimu bwana wake. Kama mimi ni baba, iko wapi heshima ninayostahili? Kama mimi ni bwana, iko wapi heshima ninayostahili?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Ni ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau Jina langu. “Lakini mnauliza, ‘Tumelidharau Jina lako kwa namna gani?’
MAL 1:7 “Mnatoa sadaka chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu. “Lakini ninyi mnauliza, ‘Tumekutia unajisi kwa namna gani?’ “Kwa kusema kuwa meza ya Mwenyezi Mungu ni ya kudharauliwa.
MAL 1:8 Mnapoleta dhabihu za wanyama walio vipofu, je, hilo si kosa? Mnapoleta dhabihu zilizo vilema au wanyama wagonjwa, je, hilo si kosa? Jaribuni kuvitoa kwa mtawala wenu! Je, angefurahishwa nanyi? Je, atawakubalia?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 1:9 “Basi mwombeni Mungu awe na neema kwetu. Je, kwa sadaka kama hizo kutoka mikononi mwenu, atawapokea?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 1:10 “Laiti mmoja wenu angeifunga milango ya Hekalu, ili msije mkawasha moto usiokuwa na faida juu ya madhabahu yangu! Sina furaha nanyi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, “nami sitaikubali sadaka toka mikononi mwenu.
MAL 1:11 Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa, kuanzia mawio ya jua hata machweo yake. Kila mahali uvumba na sadaka safi zitaletwa kwa Jina langu, kwa sababu Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 1:12 “Lakini mnalinajisi Jina langu kwa kusema kuhusu meza ya Bwana, ‘Imetiwa unajisi pamoja na chakula chake. Ni ya kudharauliwa.’
MAL 1:13 Nanyi mnasema, ‘Mzigo gani huu!’ Nanyi mnaidharau kwa kiburi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Mnapowaleta wanyama mliopokonya kwa nguvu, walio vilema au walio wagonjwa na kuwatoa kama dhabihu, je, niwakubali kutoka mikononi mwenu?” asema Mwenyezi Mungu.
MAL 1:14 “Amelaaniwa yeye adanganyaye, aliye na mnyama wa kiume anayekubalika katika kundi lake na kuweka nadhiri ya kumtoa, lakini akatoa dhabihu ya mnyama aliye na dosari kwa Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa mimi ni Mfalme Mkuu, nalo Jina langu linapaswa kuogopwa miongoni mwa mataifa,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 2:1 “Sasa onyo hili ni kwa ajili yenu, enyi makuhani.
MAL 2:2 Kama hamtasikiliza, na kama hamtaki kuielekeza mioyo yenu kuheshimu Jina langu, nitatuma laana juu yenu, nami nitalaani baraka zenu. Naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamkuielekeza mioyo yenu kuniheshimu mimi,” Asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 2:3 “Kwa sababu yenu nitawakatilia mbali wazao wenu. Nitazipaka nyuso zenu kinyesi, hicho kinyesi cha dhabihu zenu. Nanyi mtafukuzwa pamoja nazo mtoke mbele zangu.
MAL 2:4 Nanyi mtajua kuwa nimewapelekea onyo hili ili agano langu na Lawi lipate kuendelea,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 2:5 “Agano langu lilikuwa pamoja naye, agano la uhai na amani, nami nilimpa yote, ili aniche na kuniheshimu, naye akaniheshimu na kusimama akilicha Jina langu.
MAL 2:6 Fundisho la kweli lilikuwa kinywani mwake, wala hakuna uongo wowote uliopatikana katika midomo yake. Alitembea nami katika amani na unyofu, naye akawageuza wengi kutoka dhambini.
MAL 2:7 “Kwa maana yapasa midomo ya kuhani kuhifadhi maarifa. Tena kutoka kinywani mwake watu wangepaswa kutafuta mafundisho, kwa sababu yeye ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 2:8 Lakini mmegeuka mkaiacha njia, na kwa mafundisho yenu mmesababisha wengi kujikwaa. Mmevunja agano na Lawi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 2:9 “Kwa hiyo nimewasababisha ninyi kudharauliwa na kufedheheshwa mbele ya watu wote, kwa sababu hamkufuata njia zangu, bali mmeonesha upendeleo katika mambo ya sheria.”
MAL 2:10 Je, sote hatuna Baba mmoja? Hatukuumbwa na Mungu mmoja? Kwa nini basi tunalinajisi agano la baba zetu kwa kukosa uaminifu kila mmoja kwa mwenzake?
MAL 2:11 Yuda amevunja uaminifu. Jambo la kuchukiza limetendeka katika Israeli na katika Yerusalemu: Yuda amepanajisi mahali patakatifu apendapo Mwenyezi Mungu, kwa kuoa binti ya mungu mgeni.
MAL 2:12 Kwa maana kwa mtu yeyote atendaye jambo hili, Mwenyezi Mungu na amkatilie mbali kutoka mahema ya Yakobo, hata kama huwa anamletea Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni sadaka.
MAL 2:13 Kitu kingine mnachokifanya: Mnaifurikisha madhabahu ya Mwenyezi Mungu kwa machozi. Mnalia na kuugua kwa sababu yeye haziangalii tena sadaka zenu wala hazikubali kwa furaha kutoka mikononi mwenu.
MAL 2:14 Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa.
MAL 2:15 Je, Mwenyezi Mungu hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake.
MAL 2:16 “Ninachukia kuachana,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.
MAL 2:17 Mmemchosha Mwenyezi Mungu kwa maneno yenu. Nanyi mnauliza, “Tumemchosha kwa namna gani?” Mmemchosha kwa kusema, “Wote watendao mabaya ni wema machoni pa Mwenyezi Mungu, naye anapendezwa nao” au “Mungu wa haki yuko wapi?”
MAL 3:1 “Angalieni, nitamtuma mjumbe wangu, atakayeiandaa njia mbele yangu. Ndipo ghafula Bwana mnayemtafuta atakuja hekaluni mwake. Mjumbe wa agano, ambaye mnamwonea shauku, atakuja,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 3:2 Lakini ni nani atakayeweza kustahimili hiyo siku ya kuja kwake? Ni nani awezaye kusimama atakapotokea? Kwa kuwa atakuwa kama moto wa mfua fedha au kama sabuni ya mfua nguo.
MAL 3:3 Ataketi kama mfuaji na asafishaye fedha. Atawatakasa Walawi, naye atawasafisha kama dhahabu na fedha. Kisha Mwenyezi Mungu atakuwa na watu watakaoleta sadaka katika haki,
MAL 3:4 nazo sadaka za Yuda na Yerusalemu zitakubalika kwa Mwenyezi Mungu, kama katika siku zilizopita, kama katika miaka ya zamani.
MAL 3:5 “Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowadhulumu wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 3:6 “Mimi Mwenyezi Mungu sibadiliki. Kwa hiyo ninyi, enyi uzao wa Yakobo, hamjaangamizwa.
MAL 3:7 Tangu wakati wa baba zenu mmegeukia mbali na amri zangu nanyi hamkuzishika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Lakini mnauliza, ‘Tutarudi kwa namna gani?’
MAL 3:8 “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi. “Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’ “Mnaniibia zaka na dhabihu.
MAL 3:9 Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi.
MAL 3:10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi hata mkose nafasi ya kutosha.
MAL 3:11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 3:12 “Ndipo mataifa yote yatawaita mliobarikiwa, kwa maana nchi yenu itakuwa ya kupendeza sana,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 3:13 “Mmesema vitu vigumu dhidi yangu,” asema Mwenyezi Mungu. “Hata hivyo mnauliza, ‘Tumesema nini dhidi yako?’
MAL 3:14 “Mmesema, ‘Ni bure kumtumikia Mungu. Tumepata faida gani kwa kushika maagizo yake na kwenda kama waombolezaji mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni?
MAL 3:15 Lakini sasa wenye kiburi wanabarikiwa. Hakika watenda maovu wanastawi, pia hata wale wanaoshindana na Mungu ndio wanaosalimika.’ ”
MAL 3:16 Ndipo wale waliomcha Mwenyezi Mungu wakasemezana wao kwa wao, naye Mwenyezi Mungu akasikiliza na akasikia. Kitabu cha kumbukumbu kikaandikwa mbele yake kuhusu wale ambao walimcha Mwenyezi Mungu na kuliheshimu jina lake.
MAL 3:17 “Nao watakuwa watu wangu,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, “katika siku ile nitakapowafanya kuwa hazina yangu ya pekee. Nitawahurumia, kama vile kwa huruma mtu amhurumiavyo mwanawe anayemtumikia.
MAL 3:18 Kwa mara nyingine tena utaona tofauti kati ya wenye haki na waovu, kati ya wale wanaomtumikia Mungu na wale wasiomtumikia.
MAL 4:1 “Hakika siku inakuja, itawaka kama tanuru. Wote wenye kiburi na watenda maovu watakuwa mabua makavu, na siku ile inayokuja itawawasha moto,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Hakuna mzizi wala tawi litakalosalia kwao.
MAL 4:2 Bali ninyi mnaoliheshimu Jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mabawa yake. Nanyi mtatoka nje na kurukaruka kama ndama aliyeachiwa kutoka zizini.
MAL 4:3 Kisha ninyi mtawakanyaga waovu, nao watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu siku ile nitakayofanya mambo haya,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
MAL 4:4 “Kumbukeni Torati ya mtumishi wangu Musa, amri na sheria nilizompa huko Horebu kwa ajili ya Israeli wote.
MAL 4:5 “Tazama, nitawapelekea nabii Ilya kabla ya kuja siku ile iliyo kuu na ya kutisha ya Mwenyezi Mungu.
MAL 4:6 Ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, la sivyo nitakuja na kuipiga nchi kwa laana.”
MAT 1:1 Habari za ukoo wa Isa Al-Masihi mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu:
MAT 1:2 Ibrahimu akamzaa Isaka, Isaka akamzaa Yakobo, Yakobo akawazaa Yuda na ndugu zake,
MAT 1:3 Yuda akawazaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari, Peresi akamzaa Esromu, Esromu akamzaa Aramu,
MAT 1:4 Aramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni,
MAT 1:5 Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu, Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu, Obedi akamzaa Yese,
MAT 1:6 Yese akamzaa Daudi, aliyekuwa mfalme. Daudi akamzaa Sulemani, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria.
MAT 1:7 Sulemani akamzaa Rehoboamu, Rehoboamu akamzaa Abiya, Abiya akamzaa Asa,
MAT 1:8 Asa akamzaa Yehoshafati, Yehoshafati akamzaa Yoramu, Yoramu akamzaa Uzia,
MAT 1:9 Uzia akamzaa Yothamu, Yothamu akamzaa Ahazi, Ahazi akamzaa Hezekia,
MAT 1:10 Hezekia akamzaa Manase, Manase akamzaa Amoni, Amoni akamzaa Yosia,
MAT 1:11 wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.
MAT 1:12 Baada ya uhamisho wa Babeli: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli akamzaa Zerubabeli,
MAT 1:13 Zerubabeli akamzaa Abihudi, Abihudi akamzaa Eliakimu, Eliakimu akamzaa Azori,
MAT 1:14 Azori akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Akimu, Akimu akamzaa Eliudi,
MAT 1:15 Eliudi akamzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Matani, Matani akamzaa Yakobo,
MAT 1:16 naye Yakobo akamzaa Yusufu, aliyekuwa mumewe Mariamu, mama yake Isa, aitwaye Al-Masihi.
MAT 1:17 Hivyo, kulikuwa na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Ibrahimu hadi Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho wa Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho wa Babeli hadi Al-Masihi.
MAT 1:18 Kuzaliwa kwake Isa Al-Masihi kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alikuwa ameposwa na Yusufu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Mariamu alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu wa Mungu.
MAT 1:19 Kwa kuwa Yusufu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Mariamu hadharani, hivyo basi alikusudia kumwacha kwa siri.
MAT 1:20 Lakini alipokuwa akifikiri kufanya jambo hili, malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea katika ndoto na kusema, “Yusufu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho wa Mungu.
MAT 1:21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita jina Isa, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”
MAT 1:22 Haya yote yalitukia ili litimie lile Mwenyezi Mungu alilonena kupitia nabii, aliposema:
MAT 1:23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita jina Imanueli” (maana yake, “Mungu pamoja nasi”).
MAT 1:24 Yusufu alipoamka kutoka usingizini, akafanya jinsi alivyoagizwa na malaika wa Mwenyezi Mungu, akamchukua Mariamu kuwa mke wake.
MAT 1:25 Lakini hawakukutana kimwili hadi Mariamu alipojifungua mwanawe; akamwita jina Isa.
MAT 2:1 Baada ya Isa kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Yudea, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu
MAT 2:2 wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”
MAT 2:3 Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu.
MAT 2:4 Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa Torati, akawauliza ni wapi ambapo Al-Masihi angezaliwa.
MAT 2:5 Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Yudea, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:
MAT 2:6 “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, wewe si mdogo miongoni mwa watawala wa Yuda; kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala atakayekuwa mchungaji wa watu wangu Israeli.’ ”
MAT 2:7 Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana.
MAT 2:8 Kisha akawatuma Bethlehemu na kuwaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto huyo kwa makini. Mara tu mtakapompata, nileteeni taarifa ili nami niende kumwabudu.”
MAT 2:9 Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata hadi iliposimama mahali alipokuwa mtoto.
MAT 2:10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno.
MAT 2:11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mama yake, wakamsujudia na kumwabudu yule mtoto Isa. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.
MAT 2:12 Kwa kuwa walikuwa wameonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi nchi yao kwa njia nyingine.
MAT 2:13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea Yusufu katika ndoto akamwambia, “Amka, umchukue mtoto na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko hadi nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”
MAT 2:14 Kisha Yusufu akaamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri,
MAT 2:15 ambako walikaa hadi Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile neno Mwenyezi Mungu alilosema kupitia kwa nabii: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.”
MAT 2:16 Herode alipogundua kwamba alikuwa amedanganywa na wale wataalamu wa nyota, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kwa mujibu wa ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota.
MAT 2:17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, aliposema:
MAT 2:18 “Sauti ilisikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akilia kwa ajili ya wanawe, akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.”
MAT 2:19 Baada ya Herode kufa, malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea Yusufu katika ndoto huko Misri
MAT 2:20 na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wakijaribu kumuua mtoto wamekufa.”
MAT 2:21 Basi Yusufu, akainuka, akamchukua mtoto na mama yake wakaenda hadi nchi ya Israeli.
MAT 2:22 Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Yudea baada ya Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Kwa kuwa alikuwa ameonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya,
MAT 2:23 akaenda kuishi katika mji ulioitwa Nasiri. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii waliposema, “Ataitwa Mnasiri.”
MAT 3:1 Siku hizo Yahya alikuja akihubiri katika nyika ya Yudea, akisema,
MAT 3:2 “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
MAT 3:3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema: “Sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, yanyoosheni mapito yake.’ ”
MAT 3:4 Basi Yahya alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.
MAT 3:5 Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Yudea yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani.
MAT 3:6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.
MAT 3:7 Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?
MAT 3:8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba.
MAT 3:9 Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Ibrahimu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto kutoka kwa mawe haya.
MAT 3:10 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari katika shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.
MAT 3:11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu wa Mungu na kwa moto.
MAT 3:12 Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”
MAT 3:13 Kisha Isa akaja kutoka Galilaya hadi Mto Yordani ili Yahya ambatize.
MAT 3:14 Lakini Yahya akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”
MAT 3:15 Lakini Isa akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yahya akakubali.
MAT 3:16 Naye Isa alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake.
MAT 3:17 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa; ninapendezwa sana naye.”
MAT 4:1 Kisha Isa akaongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu hadi nyikani ili ajaribiwe na ibilisi.
MAT 4:2 Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa.
MAT 4:3 Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiwe Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”
MAT 4:4 Lakini Isa akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”
MAT 4:5 Ndipo ibilisi akampeleka Isa hadi mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu,
MAT 4:6 akamwambia, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa: “ ‘Atakuagizia malaika wake, nao watakuchukua mikononi mwao ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”
MAT 4:7 Isa akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Mwenyezi Mungu, Mungu wako.’ ”
MAT 4:8 Kwa mara nyingine, ibilisi akampeleka Isa hadi kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonesha falme zote za dunia na fahari zake,
MAT 4:9 kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote ukinisujudia na kuniabudu.”
MAT 4:10 Isa akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ”
MAT 4:11 Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.
MAT 4:12 Isa aliposikia kwamba Yahya alikuwa amefungwa gerezani, alirudi Galilaya.
MAT 4:13 Akaondoka Nasiri akaenda kuishi Kapernaumu, mji ulio karibu na bahari, katika nchi ya Zabuloni na Naftali,
MAT 4:14 ili kutimiza neno lililonenwa na nabii Isaya, aliposema:
MAT 4:15 “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, kwenye njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya Mataifa:
MAT 4:16 watu wale waliokaa gizani wameona nuru kuu; nao wale walioishi katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewazukia.”
MAT 4:17 Tangu wakati huo, Isa alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
MAT 4:18 Isa alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa walikuwa wavuvi.
MAT 4:19 Isa akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.”
MAT 4:20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
MAT 4:21 Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Isa akawaita.
MAT 4:22 Nao mara moja wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.
MAT 4:23 Isa akazunguka Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri Habari Njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu.
MAT 4:24 Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Siria, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya.
MAT 4:25 Makundi makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea, na kutoka ng’ambo ya Yordani.
MAT 5:1 Basi Isa alipoona makundi ya watu, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia.
MAT 5:2 Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:
MAT 5:3 “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
MAT 5:4 Heri wale wanaohuzunika, maana hao watafarijiwa.
MAT 5:5 Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi.
MAT 5:6 Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watatoshelezwa.
MAT 5:7 Heri wenye huruma, maana hao watapata rehema.
MAT 5:8 Heri walio na moyo safi, maana hao watamwona Mungu.
MAT 5:9 Heri walio wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.
MAT 5:10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
MAT 5:11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena mabaya ya aina zote dhidi yenu kwa uongo kwa ajili yangu.
MAT 5:12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.
MAT 5:13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.
MAT 5:14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika.
MAT 5:15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliye ndani ya ile nyumba.
MAT 5:16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
MAT 5:17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Torati au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza.
MAT 5:18 Kwa maana, amin nawaambia, hadi mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwa Torati, hadi kila kitu kiwe kimetimia.
MAT 5:19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika ufalme wa mbinguni.
MAT 5:20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa Torati, kamwe hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.
MAT 5:21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’
MAT 5:22 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa Jehanamu.
MAT 5:23 “Kwa hiyo, ikiwa unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako,
MAT 5:24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Nenda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.
MAT 5:25 “Patana na mshtaki wako upesi wakati mpo njiani kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani.
MAT 5:26 Amin, nakuambia, hutatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.
MAT 5:27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’
MAT 5:28 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.
MAT 5:29 Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, ling’oe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa Jehanamu.
MAT 5:30 Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe Jehanamu.
MAT 5:31 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’
MAT 5:32 Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.
MAT 5:33 “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Mwenyezi Mungu.’
MAT 5:34 Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu;
MAT 5:35 au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu.
MAT 5:36 Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.
MAT 5:37 ‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.
MAT 5:38 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’
MAT 5:39 Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia.
MAT 5:40 Mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia.
MAT 5:41 Mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili.
MAT 5:42 Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.
MAT 5:43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’
MAT 5:44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu, na waombeeni wanaowatesa ninyi,
MAT 5:45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.
MAT 5:46 Mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo?
MAT 5:47 Nanyi mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu hawafanyi hivyo?
MAT 5:48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
MAT 6:1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.
MAT 6:2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msitangaze hadharani kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao.
MAT 6:3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya,
MAT 6:4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.
MAT 6:5 “Nanyi mnaposali, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupokea thawabu yao.
MAT 6:6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako.
MAT 6:7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao.
MAT 6:8 Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.
MAT 6:9 “Hivi ndivyo mnavyopaswa kuomba: “ ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.
MAT 6:10 Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.
MAT 6:11 Utupatie riziki yetu ya kila siku.
MAT 6:12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tulivyokwisha kuwasamehe wadeni wetu.
MAT 6:13 Usitutie majaribuni, bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu [kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amen].’
MAT 6:14 Kwa kuwa mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia.
MAT 6:15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
MAT 6:16 “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao kamilifu.
MAT 6:17 Lakini unapofunga, jipake mafuta kichwani na kunawa uso wako,
MAT 6:18 ili kufunga kwako kusionekane na watu wengine ila Baba yako anayeketi mahali pa siri; naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako kwa wazi.
MAT 6:19 “Msijiwekee hazina duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, nao wezi huvunja na kuiba.
MAT 6:20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wezi hawavunji na kuiba.
MAT 6:21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.
MAT 6:22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru.
MAT 6:23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Hivyo basi, ikiwa nuru iliyo ndani yako ni giza, je, hilo ni giza nene aje!
MAT 6:24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.
MAT 6:25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?
MAT 6:26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani kuliko hao ndege?
MAT 6:27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?
MAT 6:28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi.
MAT 6:29 Lakini nawaambia, hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua.
MAT 6:30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba?
MAT 6:31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’
MAT 6:32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote.
MAT 6:33 Lakini utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.
MAT 6:34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Kila siku ina masumbufu yake ya kutosha.
MAT 7:1 “Usihukumu ili usije ukahukumiwa.
MAT 7:2 Kwa maana jinsi unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa, na kwa kipimo kile upimiacho, ndicho utakachopimiwa.
MAT 7:3 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe?
MAT 7:4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako,’ wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe?
MAT 7:5 Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.
MAT 7:6 “Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu; wala msitupie nguruwe lulu zenu. Mkifanya hivyo, watazikanyagakanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.
MAT 7:7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.
MAT 7:8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
MAT 7:9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe?
MAT 7:10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka?
MAT 7:11 Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?
MAT 7:12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Torati na Manabii.
MAT 7:13 “Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi wanaoingia kupitia lango hilo.
MAT 7:14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.
MAT 7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa-mwitu wakali.
MAT 7:16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma?
MAT 7:17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.
MAT 7:18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.
MAT 7:19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
MAT 7:20 Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.
MAT 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
MAT 7:22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’
MAT 7:23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
MAT 7:24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba.
MAT 7:25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba.
MAT 7:26 Kila anayesikia haya maneno yangu na asiyatende ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga.
MAT 7:27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”
MAT 7:28 Isa alipomaliza kusema maneno haya, umati wa watu wakashangazwa sana na mafundisho yake,
MAT 7:29 kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.
MAT 8:1 Isa aliposhuka kutoka mlimani, makundi ya watu wakamfuata.
MAT 8:2 Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, ukitaka, unaweza kunitakasa.”
MAT 8:3 Isa akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake.
MAT 8:4 Kisha Isa akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajioneshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Musa, ili kuwa ushuhuda kwao.”
MAT 8:5 Isa alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada,
MAT 8:6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”
MAT 8:7 Isa akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”
MAT 8:8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia ndani ya nyumba yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.
MAT 8:9 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliye chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
MAT 8:10 Isa aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii.
MAT 8:11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Ibrahimu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni.
MAT 8:12 Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa kilio na kusaga meno.”
MAT 8:13 Kisha Isa akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona wakati ule ule.
MAT 8:14 Isa alipoingia nyumbani mwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa.
MAT 8:15 Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia.
MAT 8:16 Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote.
MAT 8:17 Haya yalifanyika ili litimie neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya, kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na akachukua magonjwa yetu.”
MAT 8:18 Isa alipoona makundi mengi yamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke hadi ng’ambo ya ziwa.
MAT 8:19 Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Isa na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata popote utakakoenda.”
MAT 8:20 Naye Isa akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
MAT 8:21 Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
MAT 8:22 Lakini Isa akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”
MAT 8:23 Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata.
MAT 8:24 Ghafula, kukatokea dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Isa alikuwa amelala usingizi.
MAT 8:25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”
MAT 8:26 Naye Isa akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nayo bahari ikatulia kabisa.
MAT 8:27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”
MAT 8:28 Walipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile.
MAT 8:29 Wakapaza sauti wakisema, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”
MAT 8:30 Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakila.
MAT 8:31 Wale pepo wachafu wakamsihi Isa, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.”
MAT 8:32 Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji.
MAT 8:33 Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu.
MAT 8:34 Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Isa. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.
MAT 9:1 Isa akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao.
MAT 9:2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Isa alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”
MAT 9:3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa Torati wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”
MAT 9:4 Lakini Isa akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu?
MAT 9:5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’?
MAT 9:6 Lakini nataka mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu ana mamlaka duniani kusamehe dhambi.” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani mwako.”
MAT 9:7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani mwake.
MAT 9:8 Umati wa watu walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu aliyekuwa amewakabidhi wanadamu mamlaka kama haya.
MAT 9:9 Isa alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akasimama, akamfuata.
MAT 9:10 Isa alipokuwa ameketi akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na wenye dhambi wakaja, wakaketi kula pamoja naye na wanafunzi wake.
MAT 9:11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?”
MAT 9:12 Lakini Isa aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu.
MAT 9:13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
MAT 9:14 Wanafunzi wa Yahya wakaja na kumuuliza Isa, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”
MAT 9:15 Isa akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wanawezaje kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.
MAT 9:16 “Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo iliyochakaa, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo, nayo hiyo nguo itachanika zaidi.
MAT 9:17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”
MAT 9:18 Isa alipokuwa akiwaambia mambo haya, kiongozi wa sinagogi akaingia, akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.”
MAT 9:19 Isa akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.
MAT 9:20 Wakati huo huo, mwanamke mmoja, aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, akaja nyuma ya Isa, akagusa upindo wa vazi lake,
MAT 9:21 kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”
MAT 9:22 Isa akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa hiyo.
MAT 9:23 Isa alipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele,
MAT 9:24 akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka.
MAT 9:25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka.
MAT 9:26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.
MAT 9:27 Isa alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
MAT 9:28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Isa akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?” Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”
MAT 9:29 Ndipo Isa akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.”
MAT 9:30 Macho yao yakafunguka. Isa akawaonya vikali, akisema, “Chungeni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.”
MAT 9:31 Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.
MAT 9:32 Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Isa.
MAT 9:33 Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea, na umati wa watu wakastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”
MAT 9:34 Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”
MAT 9:35 Isa akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri Habari Njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi.
MAT 9:36 Alipoona umati wa watu, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji.
MAT 9:37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache.
MAT 9:38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili atume watendakazi katika shamba lake la mavuno.”
MAT 10:1 Ndipo Isa akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, naye akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu, ili waweze kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.
MAT 10:2 Haya ndiyo majina ya hao mitume kumi na wawili: wa kwanza, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye;
MAT 10:3 Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo;
MAT 10:4 Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote aliyemsaliti Isa.
MAT 10:5 Hawa kumi na wawili, Isa aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria.
MAT 10:6 Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea.
MAT 10:7 Mnapoenda, hubirini ujumbe huu, ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’
MAT 10:8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure.
MAT 10:9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu.
MAT 10:10 Msichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtendakazi anastahili posho yake.
MAT 10:11 “Mji wowote au kijiji chochote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake hadi mtakapoondoka.
MAT 10:12 Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani.
MAT 10:13 Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake. La sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi.
MAT 10:14 Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo.
MAT 10:15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.
MAT 10:16 “Tazama ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa-mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.
MAT 10:17 “Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao.
MAT 10:18 Nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na kwa watu wa Mataifa.
MAT 10:19 Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo.
MAT 10:20 Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.
MAT 10:21 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe.
MAT 10:22 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
MAT 10:23 Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.
MAT 10:24 “Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake.
MAT 10:25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli, je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake!
MAT 10:26 “Basi msiwaogope, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana.
MAT 10:27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinong’onwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba.
MAT 10:28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika Jehanamu.
MAT 10:29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua.
MAT 10:30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa.
MAT 10:31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
MAT 10:32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
MAT 10:33 Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
MAT 10:34 “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga.
MAT 10:35 Kwa maana nimekuja kuleta uadui kati ya “ ‘mtu na baba yake, binti na mama yake, mkwe na mama mkwe wake;
MAT 10:36 nao adui za mtu watakuwa ni wale watu wa nyumbani mwake.’
MAT 10:37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu.
MAT 10:38 Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu.
MAT 10:39 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
MAT 10:40 “Mtu yeyote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi, na yeyote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma.
MAT 10:41 Mtu yeyote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii atapokea thawabu ya nabii, naye mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki atapokea thawabu ya mwenye haki.
MAT 10:42 Mtu yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”
MAT 11:1 Baada ya Isa kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji ya Galilaya.
MAT 11:2 Yahya aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Al-Masihi alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake
MAT 11:3 ili wakamuulize, “Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”
MAT 11:4 Isa akajibu, “Rudini mkamwambie Yahya yale mnayosikia na kuyaona:
MAT 11:5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema.
MAT 11:6 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”
MAT 11:7 Wale wanafunzi wa Yahya walipokuwa wanaondoka, Isa akaanza kusema na umati wa watu kuhusu Yahya. Akawauliza, “Mlipoenda kule nyikani, mlienda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?
MAT 11:8 Kama sivyo, mlienda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha! Watu wanaovaa mavazi ya kifahari wako katika majumba ya wafalme.
MAT 11:9 Basi mlienda kuona nini? Mlienda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.
MAT 11:10 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa: “ ‘Tazama nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako.’
MAT 11:11 Amin, nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu kuliko Yahya. Lakini aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko Yahya.
MAT 11:12 Tangu siku za Yahya hadi sasa, ufalme wa mbinguni hunyakuliwa kwa nguvu, nao wenye nguvu wanauteka.
MAT 11:13 Kwa maana manabii wote na Torati walitabiri hadi wakati wa Yahya.
MAT 11:14 Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye ndiye yule Ilya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja.
MAT 11:15 Yeye aliye na masikio, na asikie.
MAT 11:16 “Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,
MAT 11:17 “ ‘Tuliwapigia filimbi, lakini hamkucheza; tuliwaimbia nyimbo za maombolezo, lakini hamkuomboleza.’
MAT 11:18 Kwa maana Yahya alikuja, alikuwa hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’
MAT 11:19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.”
MAT 11:20 Ndipo Isa akaanza kuishutumu miji ambayo alifanya miujiza yake mingi, kwa maana watu wake hawakutubu.
MAT 11:21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.
MAT 11:22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi.
MAT 11:23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha! Utashushwa hadi Kuzimu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungekuwepo hadi leo.
MAT 11:24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”
MAT 11:25 Wakati huo Isa alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo.
MAT 11:26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
MAT 11:27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.
MAT 11:28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
MAT 11:29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha katika nafsi zenu.
MAT 11:30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”
MAT 12:1 Wakati huo Isa alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala.
MAT 12:2 Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”
MAT 12:3 Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa?
MAT 12:4 Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani tu.
MAT 12:5 Au hamjasoma katika Torati kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia?
MAT 12:6 Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa.
MAT 12:7 Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia,
MAT 12:8 kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
MAT 12:9 Isa akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao,
MAT 12:10 na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Isa, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
MAT 12:11 Isa akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa?
MAT 12:12 Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”
MAT 12:13 Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine.
MAT 12:14 Lakini Mafarisayo wakatoka nje na kupanga njama ya kumuua Isa.
MAT 12:15 Lakini Isa alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi walimfuata, naye akawaponya wote waliokuwa wagonjwa miongoni mwao,
MAT 12:16 akiwakataza wasiseme yeye ni nani,
MAT 12:17 ili neno lililonenwa na nabii Isaya litimie, aliposema:
MAT 12:18 “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu Mtakatifu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa.
MAT 12:19 Hatagombana wala kupaza sauti, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.
MAT 12:20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, hadi atakapoifanya haki ishinde.
MAT 12:21 Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.”
MAT 12:22 Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Isa akamponya, hata akaweza kusema na kuona.
MAT 12:23 Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”
MAT 12:24 Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.”
MAT 12:25 Isa alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama.
MAT 12:26 Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama?
MAT 12:27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.
MAT 12:28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.
MAT 12:29 “Au tena, mtu anawezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali yake.
MAT 12:30 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.
MAT 12:31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu wa Mungu hatasamehewa.
MAT 12:32 Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho wa Mungu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.
MAT 12:33 “Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake.
MAT 12:34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake.
MAT 12:35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake.
MAT 12:36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa maelezo kuhusu kila neno walilonena lisilo la maana.
MAT 12:37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”
MAT 12:38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Torati wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”
MAT 12:39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona.
MAT 12:40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la samaki mkubwa sana kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana.
MAT 12:41 Siku ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.
MAT 12:42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Sulemani. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.
MAT 12:43 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati.
MAT 12:44 Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye anaporudi huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri.
MAT 12:45 Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.”
MAT 12:46 Wakati alikuwa angali anazungumza na umati wa watu, mama yake na ndugu zake wakasimama nje wakitaka kuongea naye.
MAT 12:47 Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”
MAT 12:48 Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?”
MAT 12:49 Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu zangu!
MAT 12:50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye kaka yangu, na dada yangu, na mama yangu.”
MAT 13:1 Siku hiyo hiyo Isa akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari.
MAT 13:2 Umati mkubwa mno wa watu wakakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari.
MAT 13:3 Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.
MAT 13:4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila.
MAT 13:5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba.
MAT 13:6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina.
MAT 13:7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea.
MAT 13:8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini.
MAT 13:9 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
MAT 13:10 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”
MAT 13:11 Akawajibu, “Ninyi mmepewa ujuzi wa siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawajapewa.
MAT 13:12 Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.
MAT 13:13 Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano: “Ingawa wanatazama, hawaoni; wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi.
MAT 13:14 Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema: “ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama lakini hamtaona.
MAT 13:15 Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’
MAT 13:16 Lakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia.
MAT 13:17 Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.
MAT 13:18 “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi:
MAT 13:19 Mtu yeyote anaposikia neno la ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia.
MAT 13:20 Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na hulipokea mara moja kwa furaha.
MAT 13:21 Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye anarudi nyuma mara moja.
MAT 13:22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu anayelisikia neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda.
MAT 13:23 Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”
MAT 13:24 Isa akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.
MAT 13:25 Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.
MAT 13:26 Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea.
MAT 13:27 “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’
MAT 13:28 “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’ “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayang’oe?’
MAT 13:29 “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyang’oe, kwa maana wakati mking’oa magugu mnaweza mkang’oa na ngano pamoja nayo.
MAT 13:30 Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja hadi wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”
MAT 13:31 Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake.
MAT 13:32 Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.”
MAT 13:33 Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga hadi wote ukaumuka.”
MAT 13:34 Isa alinena mambo haya yote kwa umati wa watu kwa mifano, wala hakuwaambia lolote pasipo mfano.
MAT 13:35 Hii ilikuwa ili kutimiza neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano; nitahubiri mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.”
MAT 13:36 Kisha Isa akaagana na ule umati, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”
MAT 13:37 Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu.
MAT 13:38 Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu.
MAT 13:39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.
MAT 13:40 “Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia.
MAT 13:41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote.
MAT 13:42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.
MAT 13:43 Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.
MAT 13:44 “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.
MAT 13:45 “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi.
MAT 13:46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.
MAT 13:47 “Tena, ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina.
MAT 13:48 Ulipojaa, wavuvi wakauvuta ufuoni, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa.
MAT 13:49 Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki.
MAT 13:50 Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”
MAT 13:51 Isa akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?” Wakamjibu, “Ndiyo.”
MAT 13:52 Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa Torati aliyefundishwa elimu ya ufalme wa mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”
MAT 13:53 Isa alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka.
MAT 13:54 Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?
MAT 13:55 Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Mariamu, nao ndugu zake si Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda?
MAT 13:56 Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?”
MAT 13:57 Wakachukizwa naye. Lakini Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake.”
MAT 13:58 Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.
MAT 14:1 Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Isa,
MAT 14:2 akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yahya; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
MAT 14:3 Herode alikuwa amemkamata Yahya, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake,
MAT 14:4 kwa kuwa Yahya alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.”
MAT 14:5 Herode alitaka sana kumuua Yahya, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.
MAT 14:6 Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria. Alimfurahisha Herode sana,
MAT 14:7 kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba.
MAT 14:8 Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yahya kwenye sinia.”
MAT 14:9 Mfalme alisikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake.
MAT 14:10 Hivyo akaagiza Yahya akatwe kichwa mle gerezani.
MAT 14:11 Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake.
MAT 14:12 Wanafunzi wa Yahya wakaja na kuuchukua mwili wake, wakamzika. Kisha wakaenda wakamwambia Isa.
MAT 14:13 Isa aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji.
MAT 14:14 Isa alipofika kando ya bahari, aliona makundi makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.
MAT 14:15 Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makundi ya watu ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”
MAT 14:16 Isa akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”
MAT 14:17 Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”
MAT 14:18 Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.”
MAT 14:19 Isa akaagiza umati wa watu wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia ule umati.
MAT 14:20 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.
MAT 14:21 Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.
MAT 14:22 Mara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua wamtangulie kwenda ng’ambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiaga ule umati.
MAT 14:23 Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Isa alikuwa huko peke yake.
MAT 14:24 Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.
MAT 14:25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Isa akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji.
MAT 14:26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.
MAT 14:27 Lakini mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”
MAT 14:28 Petro akamjibu, “Bwana Isa, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”
MAT 14:29 Isa akamwambia, “Njoo.” Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Isa.
MAT 14:30 Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, akapaza sauti na kusema, “Bwana, niokoe!”
MAT 14:31 Mara Isa akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”
MAT 14:32 Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma.
MAT 14:33 Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Isa, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”
MAT 14:34 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti.
MAT 14:35 Watu wa eneo lile walipomtambua Isa, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakamletea wagonjwa wao wote,
MAT 14:36 wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.
MAT 15:1 Ndipo baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Torati wakamjia Isa kutoka Yerusalemu na kumuuliza,
MAT 15:2 “Mbona wanafunzi wako wanakiuka mapokeo ya wazee? Kwa maana wao hawanawi mikono yao kabla ya kula!”
MAT 15:3 Isa akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?
MAT 15:4 Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’
MAT 15:5 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’
MAT 15:6 basi hana tena sababu ya kumheshimu baba yake nacho. Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu.
MAT 15:7 Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba:
MAT 15:8 “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami.
MAT 15:9 Huniabudu bure; nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’ ”
MAT 15:10 Isa akaita umati wa watu waliokuwa hapo, akawaambia, “Sikilizeni na mwelewe:
MAT 15:11 kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”
MAT 15:12 Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”
MAT 15:13 Akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu wa mbinguni hakuupanda utang’olewa.
MAT 15:14 Waacheni; wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”
MAT 15:15 Petro akasema, “Tueleze maana ya huu mfano.”
MAT 15:16 Isa akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu?
MAT 15:17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu?
MAT 15:18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi.
MAT 15:19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio.
MAT 15:20 Haya ndio yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
MAT 15:21 Isa aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni.
MAT 15:22 Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”
MAT 15:23 Lakini Isa hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”
MAT 15:24 Isa akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”
MAT 15:25 Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Isa, akasema, “Bwana, nisaidie!”
MAT 15:26 Isa akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
MAT 15:27 Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwa meza za bwana zao.”
MAT 15:28 Ndipo Isa akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.
MAT 15:29 Isa akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko.
MAT 15:30 Umati mkubwa wa watu wakamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya.
MAT 15:31 Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.
MAT 15:32 Kisha Isa akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga watu wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.”
MAT 15:33 Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kulisha umati mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”
MAT 15:34 Isa akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”
MAT 15:35 Isa akaagiza watu wote waketi chini.
MAT 15:36 Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akamshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu.
MAT 15:37 Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.
MAT 15:38 Idadi ya watu walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.
MAT 15:39 Baada ya kuaga umati wa watu, Isa aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani.
MAT 16:1 Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Isa na kumjaribu kwa kumwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni.
MAT 16:2 Isa akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’
MAT 16:3 Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua ishara za nyakati.
MAT 16:4 Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Isa akawaacha, akaenda zake.
MAT 16:5 Wanafunzi wake walipofika ng’ambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate.
MAT 16:6 Isa akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”
MAT 16:7 Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”
MAT 16:8 Isa, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate?
MAT 16:9 Je, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano kwa watu elfu tano, na idadi ya vikapu vilivyojaa mabaki mlivyokusanya?
MAT 16:10 Au ile mikate saba kwa watu elfu nne na idadi ya vikapu vilivyojaa mabaki mlivyokusanya?
MAT 16:11 Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
MAT 16:12 Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi kuhusu chachu ya kutengeneza mikate, bali kuhusu mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
MAT 16:13 Basi Isa alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”
MAT 16:14 Wakamjibu, “Baadhi husema ni Yahya; wengine husema ni Ilya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmoja wa manabii.”
MAT 16:15 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
MAT 16:16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai.”
MAT 16:17 Naye Isa akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni.
MAT 16:18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitajenga jumuiya ya wafuasi wangu, hata malango ya Kuzimu hayataweza kuwashinda.
MAT 16:19 Nitakupa funguo za ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
MAT 16:20 Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Al-Masihi.
MAT 16:21 Tangu wakati huo, Isa alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa Torati, na kwamba itampasa auawe, lakini siku ya tatu kufufuliwa.
MAT 16:22 Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea, akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”
MAT 16:23 Lakini Isa akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
MAT 16:24 Ndipo Isa akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
MAT 16:25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
MAT 16:26 Kwa maana itamfaidi mtu nini kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
MAT 16:27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
MAT 16:28 Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.”
MAT 17:1 Siku sita baada ya jambo hili, Isa akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao.
MAT 17:2 Wakiwa huko, Isa alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang’aa kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama nuru.
MAT 17:3 Ghafula wakawatokea mbele yao Musa na Ilya, wakizungumza na Isa.
MAT 17:4 Ndipo Petro akamwambia Isa, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.”
MAT 17:5 Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililong’aa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.”
MAT 17:6 Wanafunzi waliposikia haya, wakaanguka kifudifudi, wakajawa na hofu.
MAT 17:7 Lakini Isa akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.”
MAT 17:8 Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Isa.
MAT 17:9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Isa akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, hadi Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”
MAT 17:10 Wale wanafunzi wakamuuliza, “Kwa nini basi walimu wa Torati husema kwamba ni lazima Ilya aje kwanza?”
MAT 17:11 Isa akawajibu, “Ni kweli, Ilya lazima aje kwanza, naye atatengeneza mambo yote.
MAT 17:12 Lakini nawaambia, Ilya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.”
MAT 17:13 Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yahya.
MAT 17:14 Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Isa na kupiga magoti mbele yake, akasema,
MAT 17:15 “Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji.
MAT 17:16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”
MAT 17:17 Isa akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.”
MAT 17:18 Isa akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona tangu saa hiyo.
MAT 17:19 Kisha wanafunzi wakamwendea Isa wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”
MAT 17:20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [
MAT 17:21 Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]”
MAT 17:22 Siku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Isa akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu.
MAT 17:23 Nao watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika sana.
MAT 17:24 Baada ya Isa na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”
MAT 17:25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Isa akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”
MAT 17:26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Isa akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa.
MAT 17:27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”
MAT 18:1 Wakati huo, wanafunzi wakamjia Isa na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika ufalme wa mbinguni?”
MAT 18:2 Isa akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao.
MAT 18:3 Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.
MAT 18:4 Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika ufalme wa mbinguni.
MAT 18:5 “Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi.
MAT 18:6 “Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari.
MAT 18:7 “Ole kwa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha.
MAT 18:8 Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele.
MAT 18:9 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, ling’oe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa katika moto wa Jehanamu.
MAT 18:10 “Chungeni ili msimdharau mmoja wa hawa wadogo. Kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [
MAT 18:11 Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.]
MAT 18:12 “Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea?
MAT 18:13 Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea.
MAT 18:14 Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee.
MAT 18:15 “Ndugu yako akikukosea, nenda ukamwoneshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.
MAT 18:16 Lakini asipokusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno ‘lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu’.
MAT 18:17 Akikataa kuwasikiliza hao, waambieni kundi lenu la waumini. Naye akikataa hata kuwasikiliza kundi la waumini, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.
MAT 18:18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.
MAT 18:19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watatendewa na Baba yangu aliye mbinguni.
MAT 18:20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”
MAT 18:21 Kisha Petro akamwendea Isa na kumuuliza, “Bwana, ni mara ngapi nimsamehe ndugu yangu akinikosea? Hadi mara saba?”
MAT 18:22 Isa akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
MAT 18:23 “Kwa hiyo ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake.
MAT 18:24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta elfu kumi aliletwa kwake.
MAT 18:25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.
MAT 18:26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’
MAT 18:27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.
MAT 18:28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’
MAT 18:29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’
MAT 18:30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni.
MAT 18:31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.
MAT 18:32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi.
MAT 18:33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’
MAT 18:34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe hadi atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.
MAT 18:35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”
MAT 19:1 Isa alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Yudea, ng’ambo ya Yordani.
MAT 19:2 Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akawaponya huko.
MAT 19:3 Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu, wakamuuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?”
MAT 19:4 Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke,
MAT 19:5 naye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’?
MAT 19:6 Hivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
MAT 19:7 Wakamuuliza, “Kwa nini basi Musa aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”
MAT 19:8 Isa akawajibu, “Musa aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo.
MAT 19:9 Mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”
MAT 19:10 Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”
MAT 19:11 Isa akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu.
MAT 19:12 Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo; wengine wamefanywa matowashi na wanadamu; na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”
MAT 19:13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Isa ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.
MAT 19:14 Isa akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wa wale walio kama hawa.”
MAT 19:15 Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko.
MAT 19:16 Mtu mmoja akamjia Isa na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”
MAT 19:17 Isa akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”
MAT 19:18 Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?” Isa akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo,
MAT 19:19 waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.”
MAT 19:20 Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”
MAT 19:21 Isa akamwambia, “Ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
MAT 19:22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
MAT 19:23 Ndipo Isa akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
MAT 19:24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
MAT 19:25 Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
MAT 19:26 Lakini Isa akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
MAT 19:27 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata! Tutapata nini basi?”
MAT 19:28 Isa akawaambia, “Amin, nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake kitukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti kumi na viwili vya utawala, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
MAT 19:29 Kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu zake wa kiume au wa kike, baba au mama, watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele.
MAT 19:30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
MAT 20:1 “Kwa maana ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu.
MAT 20:2 Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinari moja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu.
MAT 20:3 “Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi.
MAT 20:4 Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa chochote kilicho haki yenu.’
MAT 20:5 Hivyo basi wakaenda. “Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo.
MAT 20:6 Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’
MAT 20:7 “Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna yeyote aliyetuajiri.’ “Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’
MAT 20:8 “Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’
MAT 20:9 “Wale vibarua walioajiriwa saa kumi na moja wakaja, na kila mmoja wao akapokea dinari moja.
MAT 20:10 Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja.
MAT 20:11 Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba,
MAT 20:12 wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’
MAT 20:13 “Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja?
MAT 20:14 Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe.
MAT 20:15 Je, sina haki ya kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’
MAT 20:16 “Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
MAT 20:17 Basi Isa alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwaita kando wale wanafunzi kumi na wawili na kuwaambia,
MAT 20:18 “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa Torati. Nao watamhukumu kifo
MAT 20:19 na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!”
MAT 20:20 Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Isa pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Isa amfanyie jambo fulani.
MAT 20:21 Isa akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika ufalme wako.”
MAT 20:22 Isa akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?” Wakajibu, “Tunaweza.”
MAT 20:23 Isa akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”
MAT 20:24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili.
MAT 20:25 Lakini Isa akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao.
MAT 20:26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,
MAT 20:27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu:
MAT 20:28 kama vile Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
MAT 20:29 Isa na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu wakamfuata.
MAT 20:30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Isa alikuwa anapita, wakapaza sauti wakisema, “Bwana Isa, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
MAT 20:31 Umati wa watu wakawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema, “Bwana Isa, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”
MAT 20:32 Isa akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
MAT 20:33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”
MAT 20:34 Isa akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.
MAT 21:1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Isa akawatuma wanafunzi wake wawili,
MAT 21:2 akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu, nanyi mtampata punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee.
MAT 21:3 Mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara moja.”
MAT 21:4 Haya yalitukia ili litimie neno lililonenwa na nabii, aliposema:
MAT 21:5 “Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mpole, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”
MAT 21:6 Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Isa alivyokuwa amewaagiza.
MAT 21:7 Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Isa akaketi juu yake.
MAT 21:8 Umati mkubwa wa watu wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kwenye miti, wakayatandaza barabarani.
MAT 21:9 Wale umati wa watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti na kusema, “Hosana, Mwana wa Daudi!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!” “Hosana juu mbinguni!”
MAT 21:10 Isa alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”
MAT 21:11 Wale umati wa watu wakajibu, “Huyu ni Isa, yule nabii kutoka Nasiri ya Galilaya.”
MAT 21:12 Isa akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.
MAT 21:13 Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.”
MAT 21:14 Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya.
MAT 21:15 Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walipoona mambo ya ajabu aliyofanya, na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu, wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika.
MAT 21:16 Wakamuuliza Isa, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya umeamuru sifa’?”
MAT 21:17 Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.
MAT 21:18 Asubuhi na mapema, Isa alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa.
MAT 21:19 Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.
MAT 21:20 Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”
MAT 21:21 Isa akawajibu, “Amin, nawaambia, mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ litafanyika.
MAT 21:22 Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”
MAT 21:23 Isa alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha, wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka haya?”
MAT 21:24 Isa akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Mkinijibu, nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.
MAT 21:25 Je, ubatizo wa Yahya ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?” Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’
MAT 21:26 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yahya kuwa ni nabii.”
MAT 21:27 Hivyo basi wakamjibu Isa, “Sisi hatujui.” Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.
MAT 21:28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’
MAT 21:29 “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitaenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda.
MAT 21:30 “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine, akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitaenda, bwana,’ lakini hakuenda.
MAT 21:31 “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?” Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.” Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika ufalme wa Mungu.
MAT 21:32 Kwa maana Yahya alikuja kwenu kuwaonesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.
MAT 21:33 “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo la kukamulia zabibu ndani yake, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri hadi nchi nyingine.
MAT 21:34 Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake.
MAT 21:35 “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe.
MAT 21:36 Kisha akawatuma watumishi wengine kwao, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile.
MAT 21:37 Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
MAT 21:38 “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’
MAT 21:39 Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.
MAT 21:40 “Basi huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?”
MAT 21:41 Wakamjibu, “Kwa hasira kuu, atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”
MAT 21:42 Isa akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Mwenyezi Mungu ndiye alitenda jambo hili, nalo ni la kushangaza machoni petu’?
MAT 21:43 “Kwa hiyo ninawaambia, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake.
MAT 21:44 Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”
MAT 21:45 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Isa, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao.
MAT 21:46 Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Isa kuwa ni nabii.
MAT 22:1 Isa akasema nao tena kwa mifano, akawaambia,
MAT 22:2 “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi.
MAT 22:3 Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.
MAT 22:4 “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’
MAT 22:5 “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake.
MAT 22:6 Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua.
MAT 22:7 Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.
MAT 22:8 “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja.
MAT 22:9 Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’
MAT 22:10 Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.
MAT 22:11 “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi.
MAT 22:12 Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.
MAT 22:13 “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’
MAT 22:14 “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”
MAT 22:15 Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Isa katika maneno yake.
MAT 22:16 Wakatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode kwake. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonesha upendeleo.
MAT 22:17 Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”
MAT 22:18 Lakini Isa alifahamu kusudi lao mbaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega?
MAT 22:19 Nionesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari.
MAT 22:20 Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
MAT 22:21 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Basi Isa akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
MAT 22:22 Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.
MAT 22:23 Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Isa na kumuuliza swali, wakisema,
MAT 22:24 “Mwalimu, Musa alisema, ‘Mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’
MAT 22:25 Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane.
MAT 22:26 Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba.
MAT 22:27 Hatimaye, yule mwanamke naye akafa.
MAT 22:28 Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”
MAT 22:29 Isa akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu.
MAT 22:30 Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.
MAT 22:31 Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba,
MAT 22:32 ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”
MAT 22:33 Wale umati wa watu waliposikia hayo, walishangaa sana kwa mafundisho yake.
MAT 22:34 Mafarisayo waliposikia kwamba Isa alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja.
MAT 22:35 Mmoja wao, mtaalamu wa Torati, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema,
MAT 22:36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Torati iliyo kuu kuliko zote?”
MAT 22:37 Isa akamjibu, “ ‘Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’
MAT 22:38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.
MAT 22:39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’
MAT 22:40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Torati na Manabii.”
MAT 22:41 Mafarisayo wakiwa wamekusanyika pamoja, Isa akawauliza,
MAT 22:42 “Mnaonaje kuhusu Al-Masihi? Yeye ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”
MAT 22:43 Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho wa Mungu, anamwita Al-Masihi ‘Bwana’? Kwa maana asema,
MAT 22:44 “ ‘Mwenyezi Mungu alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’
MAT 22:45 Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?”
MAT 22:46 Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Isa neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.
MAT 23:1 Kisha Isa akaambia wale umati wa watu na wanafunzi wake:
MAT 23:2 “Walimu wa Torati na Mafarisayo wameketi kwenye kiti cha Musa,
MAT 23:3 hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri.
MAT 23:4 Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza.
MAT 23:5 “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao.
MAT 23:6 Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi.
MAT 23:7 Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Mwalimu.’
MAT 23:8 “Lakini ninyi msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu.
MAT 23:9 Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni.
MAT 23:10 Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Al-Masihi.
MAT 23:11 Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu.
MAT 23:12 Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa.
MAT 23:13 “Lakini ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya ufalme wa mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [
MAT 23:14 Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo hukumu yenu itakuwa kuu zaidi.]
MAT 23:15 “Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, enyi wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja mwongofu, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa Jehanamu mara mbili kuliko ninyi!
MAT 23:16 “Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’
MAT 23:17 Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi: ni ile dhahabu, au ni lile Hekalu linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?
MAT 23:18 Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu; lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’
MAT 23:19 Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi: ni sadaka, au ni madhabahu yanayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu?
MAT 23:20 Basi, mtu anayeapa kwa madhabahu, anaapa kwa hayo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake.
MAT 23:21 Naye mtu anayeapa kwa Hekalu, anaapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake.
MAT 23:22 Naye anayeapa kwa mbingu, anaapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye anayeketi kwenye kiti hicho.
MAT 23:23 “Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo.
MAT 23:24 Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!
MAT 23:25 “Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi.
MAT 23:26 Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia.
MAT 23:27 “Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu.
MAT 23:28 Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
MAT 23:29 “Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki.
MAT 23:30 Nanyi mwasema, ‘Kama tungeishi wakati wa baba zetu, hatungeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’
MAT 23:31 Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii.
MAT 23:32 Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu!
MAT 23:33 “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya Jehanamu?
MAT 23:34 Kwa sababu hii, tazameni, natuma kwenu manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine.
MAT 23:35 Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Habili, aliyekuwa mwenye haki, hadi damu ya Zakaria mwana wa Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu.
MAT 23:36 Amin, nawaambia, haya yote yatakuja kwa kizazi hiki.
MAT 23:37 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!
MAT 23:38 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa.
MAT 23:39 Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena tangu sasa hadi mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu.’ ”
MAT 24:1 Isa akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya Hekalu.
MAT 24:2 Ndipo Isa akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
MAT 24:3 Isa alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”
MAT 24:4 Isa akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye.
MAT 24:5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Al-Masihi,’ nao watawadanganya wengi.
MAT 24:6 Mtasikia habari za vita na tetesi za vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado.
MAT 24:7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.
MAT 24:8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa uchungu.
MAT 24:9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu.
MAT 24:10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana.
MAT 24:11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi.
MAT 24:12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu, upendo wa watu wengi utapoa,
MAT 24:13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
MAT 24:14 Injili hii ya ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.
MAT 24:15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu),
MAT 24:16 basi wale walio Yudea wakimbilie milimani.
MAT 24:17 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba.
MAT 24:18 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.
MAT 24:19 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!
MAT 24:20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato.
MAT 24:21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwepo tangu mwanzo wa dunia hadi sasa: wala haitakuwepo tena kamwe.
MAT 24:22 “Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna mtu ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupishwa.
MAT 24:23 Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Al-Masihi huyu hapa!’ au, ‘Al-Masihi yuko kule,’ msisadiki.
MAT 24:24 Kwa maana watatokea masihi wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa.
MAT 24:25 Tazameni, nimekwisha kuwaambia mapema.
MAT 24:26 “Basi mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki.
MAT 24:27 Kwa maana kama vile radi itokavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
MAT 24:28 Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.
MAT 24:29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile, “ ‘jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’
MAT 24:30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.
MAT 24:31 Naye atawatuma malaika wake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.
MAT 24:32 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
MAT 24:33 Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yote, mtambue kwamba wakati u karibu, hata malangoni.
MAT 24:34 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
MAT 24:35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
MAT 24:36 “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.
MAT 24:37 Kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
MAT 24:38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile Nuhu alipoingia katika safina.
MAT 24:39 Nao hawakujua lolote hadi gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu.
MAT 24:40 Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
MAT 24:41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga kwa kinu cha mkono, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
MAT 24:42 “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu.
MAT 24:43 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa.
MAT 24:44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.
MAT 24:45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa?
MAT 24:46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.
MAT 24:47 Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote.
MAT 24:48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’
MAT 24:49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi.
MAT 24:50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua.
MAT 24:51 Atamkata vipande vipande na kumweka pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.
MAT 25:1 “Wakati huo, ufalme wa mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi.
MAT 25:2 Watano wao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.
MAT 25:3 Wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta ya akiba,
MAT 25:4 lakini wale wenye busara walichukua taa zao na mafuta ya akiba kwenye vyombo.
MAT 25:5 Bwana arusi alipokawia kuja wale wanawali wote wakasinzia na kulala.
MAT 25:6 “Usiku wa manane pakawa na kelele: ‘Tazameni, huyu hapa bwana arusi! Tokeni nje mkamlaki!’
MAT 25:7 “Ndipo wale wanawali wote wakaamka na kuzitengeneza taa zao.
MAT 25:8 Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, ‘Tupatieni mafuta yenu kidogo; taa zetu zinazimika.’
MAT 25:9 “Lakini wale wenye busara wakawajibu, ‘Sivyo, hayatutoshi sisi na ninyi pia. Afadhali mwende kwa wauzao mkajinunulie mafuta yenu.’
MAT 25:10 “Nao walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana arusi akafika. Wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia ndani pamoja naye kwenye karamu ya arusi na mlango ukafungwa.
MAT 25:11 “Baadaye wale wanawali wengine nao wakaja, wakaita, ‘Bwana! Bwana! Tufungulie mlango!’
MAT 25:12 “Lakini yeye bwana arusi akawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, siwajui ninyi!’
MAT 25:13 “Kwa hiyo kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa.
MAT 25:14 “Tena, ufalme wa mbinguni ni kama mtu aliyetaka kusafiri, naye akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao.
MAT 25:15 Mmoja akampa talanta tano, mwingine talanta mbili, na mwingine talanta moja. Kila mmoja alipewa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri.
MAT 25:16 Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi.
MAT 25:17 Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi.
MAT 25:18 Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alienda akachimba shimo ardhini na kuificha ile talanta ya bwana wake.
MAT 25:19 “Baada ya muda mrefu, yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao.
MAT 25:20 Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta tano zaidi.’
MAT 25:21 “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’
MAT 25:22 “Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’
MAT 25:23 “Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’
MAT 25:24 “Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu.
MAT 25:25 Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’
MAT 25:26 “Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu.
MAT 25:27 Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake.
MAT 25:28 “ ‘Basi mnyang’anyeni hiyo talanta, mkampe yule mwenye talanta kumi.
MAT 25:29 Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.
MAT 25:30 Nanyi mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje, kwenye giza, mahali ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.’
MAT 25:31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi kwenye kiti cha enzi cha utukufu wake.
MAT 25:32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi.
MAT 25:33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.
MAT 25:34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
MAT 25:35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha,
MAT 25:36 nilikuwa uchi mkanivisha nguo, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’
MAT 25:37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha?
MAT 25:38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvisha nguo?
MAT 25:39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’
MAT 25:40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmoja wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’
MAT 25:41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika wake.
MAT 25:42 Kwa maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu nanyi hamkuninywesha,
MAT 25:43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi nanyi hamkunivisha nguo, nilikuwa mgonjwa nanyi hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’
MAT 25:44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’
MAT 25:45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi hamkumtendea mmoja wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’
MAT 25:46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”
MAT 26:1 Isa alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake,
MAT 26:2 “Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.”
MAT 26:3 Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa.
MAT 26:4 Wakapanga kumkamata Isa kwa siri na kumuua.
MAT 26:5 Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.”
MAT 26:6 Isa alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma.
MAT 26:7 Naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa. Akayamimina kichwani mwa Isa alipokuwa ameketi mezani kula chakula.
MAT 26:8 Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini?
MAT 26:9 Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.”
MAT 26:10 Isa, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana.
MAT 26:11 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.
MAT 26:12 Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu.
MAT 26:13 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
MAT 26:14 Kisha mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alienda kwa viongozi wa makuhani
MAT 26:15 na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Isa mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha.
MAT 26:16 Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Isa.
MAT 26:17 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Isa wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
MAT 26:18 Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ”
MAT 26:19 Hivyo wanafunzi wakafanya vile Isa alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.
MAT 26:20 Ilipofika jioni, Isa alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili.
MAT 26:21 Nao walipokuwa wakila, Isa akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”
MAT 26:22 Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”
MAT 26:23 Isa akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti.
MAT 26:24 Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!”
MAT 26:25 Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Mwalimu?” Isa akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”
MAT 26:26 Walipokuwa wanakula, Isa akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”
MAT 26:27 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki.
MAT 26:28 Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.
MAT 26:29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
MAT 26:30 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
MAT 26:31 Kisha Isa akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “ ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’
MAT 26:32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
MAT 26:33 Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”
MAT 26:34 Isa akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
MAT 26:35 Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.
MAT 26:36 Kisha Isa akaenda pamoja na wanafunzi wake hadi kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.”
MAT 26:37 Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika.
MAT 26:38 Kisha Isa akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”
MAT 26:39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”
MAT 26:40 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja?
MAT 26:41 Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”
MAT 26:42 Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”
MAT 26:43 Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito.
MAT 26:44 Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.
MAT 26:45 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.
MAT 26:46 Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
MAT 26:47 Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.
MAT 26:48 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.”
MAT 26:49 Mara Yuda akamjia Isa na kumsalimu, “Salamu, Mwalimu!” Akambusu.
MAT 26:50 Isa akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.” Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Isa.
MAT 26:51 Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Isa alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
MAT 26:52 Ndipo Isa akamwambia, “Rudisha upanga wako alani mwake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga.
MAT 26:53 Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?
MAT 26:54 Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”
MAT 26:55 Wakati huo, Isa akaambia wale umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata?
MAT 26:56 Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.
MAT 26:57 Wale waliomkamata Isa wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa Torati pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika.
MAT 26:58 Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.
MAT 26:59 Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Isa ili wapate kumuua.
MAT 26:60 Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza. Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo
MAT 26:61 na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”
MAT 26:62 Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Isa, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”
MAT 26:63 Lakini Isa akakaa kimya. Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Al-Masihi, Mwana wa Mungu.”
MAT 26:64 Isa akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
MAT 26:65 Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia alivyokufuru.
MAT 26:66 Uamuzi wenu ni gani?” Wakajibu, “Anastahili kufa.”
MAT 26:67 Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi
MAT 26:68 na kusema, “Tutabirie, wewe Al-Masihi! Ni nani aliyekupiga?”
MAT 26:69 Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mjakazi mmoja akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Isa wa Galilaya.”
MAT 26:70 Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”
MAT 26:71 Alipotoka nje kufika kwenye lango, mjakazi mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Isa Al-Nasiri.”
MAT 26:72 Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”
MAT 26:73 Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”
MAT 26:74 Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!” Papo hapo jogoo akawika.
MAT 26:75 Ndipo Petro akakumbuka lile neno Isa alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
MAT 27:1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Isa ili kumuua.
MAT 27:2 Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, aliyekuwa mtawala Mrumi.
MAT 27:3 Yuda, aliyemsaliti Isa, alipoona kuwa Isa amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.
MAT 27:4 Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.” Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”
MAT 27:5 Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.
MAT 27:6 Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.”
MAT 27:7 Hivyo basi, baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni.
MAT 27:8 Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo.
MAT 27:9 Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyowekewa na watu wa Israeli,
MAT 27:10 wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoniagiza.”
MAT 27:11 Wakati huo Isa akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Isa akasema, “Wewe wasema hivyo.”
MAT 27:12 Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno.
MAT 27:13 Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?”
MAT 27:14 Lakini Isa hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.
MAT 27:15 Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu.
MAT 27:16 Palikuwa na mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba.
MAT 27:17 Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza hao watu, “Mnataka niwafungulie yupi: Baraba au Isa aitwaye Al-Masihi?”
MAT 27:18 Kwa kuwa alitambua kwamba walikuwa wamemkabidhi Isa kwake kwa ajili ya wivu.
MAT 27:19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
MAT 27:20 Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakashawishi umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Isa auawe.
MAT 27:21 Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?” Wakajibu, “Baraba.”
MAT 27:22 Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Isa aitwaye Al-Masihi?” Wakajibu wote, “Msulubishe!”
MAT 27:23 Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
MAT 27:24 Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya umati wa watu, akasema, “Sina hatia kwa damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”
MAT 27:25 Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”
MAT 27:26 Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Isa apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
MAT 27:27 Kisha askari wa mtawala wakampeleka Isa kwenye Praitorio, na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.
MAT 27:28 Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha
MAT 27:29 wakasokota taji la miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!”
MAT 27:30 Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena.
MAT 27:31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.
MAT 27:32 Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.
MAT 27:33 Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).
MAT 27:34 Hapo wakampa Isa divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa.
MAT 27:35 Walipokwisha kumsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”]
MAT 27:36 Kisha wakaketi, wakamchunga.
MAT 27:37 Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: Huyu ni Isa Mfalme wa Wayahudi.
MAT 27:38 Wanyang’anyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto.
MAT 27:39 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao,
MAT 27:40 na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka msalabani.”
MAT 27:41 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wakamdhihaki, wakisema,
MAT 27:42 “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni mfalme wa Israeli! Ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini.
MAT 27:43 Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ”
MAT 27:44 Hata wale wanyang’anyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.
MAT 27:45 Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote.
MAT 27:46 Ilipofika saa tisa, Isa akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
MAT 27:47 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Ilya.”
MAT 27:48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe.
MAT 27:49 Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumwokoa.”
MAT 27:50 Isa alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.
MAT 27:51 Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka.
MAT 27:52 Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa.
MAT 27:53 Wakatoka makaburini, na baada ya Isa kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.
MAT 27:54 Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Isa walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa sana, wakapaza sauti na kusema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
MAT 27:55 Wanawake wengi walikuwa pale wakitazama kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Isa tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake.
MAT 27:56 Miongoni mwao walikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.
MAT 27:57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yusufu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Isa.
MAT 27:58 Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Isa. Pilato akaamuru apewe.
MAT 27:59 Yusufu akauchukua mwili wa Isa, akaufunga kwa kitambaa cha kitani safi,
MAT 27:60 na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake.
MAT 27:61 Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walikuwa mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.
MAT 27:62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato
MAT 27:63 na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’
MAT 27:64 Basi uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti hadi baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”
MAT 27:65 Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadiri mnavyoweza.”
MAT 27:66 Hivyo basi wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.
MAT 28:1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walienda kulitazama kaburi.
MAT 28:2 Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Mwenyezi Mungu alishuka kutoka mbinguni, akaenda kwenye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia.
MAT 28:3 Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.
MAT 28:4 Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.
MAT 28:5 Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Isa aliyesulubiwa.
MAT 28:6 Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa.
MAT 28:7 Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko.’ Sasa nimekwisha kuwaambia.”
MAT 28:8 Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, lakini wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo.
MAT 28:9 Ghafula, Isa akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu.
MAT 28:10 Ndipo Isa akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”
MAT 28:11 Wale wanawake wakiwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia.
MAT 28:12 Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kupanga njama, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha,
MAT 28:13 wakawaambia, “Semeni, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’
MAT 28:14 Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.”
MAT 28:15 Hivyo basi, wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi hadi leo.
MAT 28:16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Isa alikuwa amewaagiza.
MAT 28:17 Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka.
MAT 28:18 Isa akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
MAT 28:19 Kwa sababu hii, nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho wa Mungu,
MAT 28:20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
MAR 1:1 Mwanzo wa Injili ya Isa Al-Masihi, Mwana wa Mungu,
MAR 1:2 kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako”:
MAR 1:3 “sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia ya Mwenyezi Mungu, yanyoosheni mapito yake.’ ”
MAR 1:4 Yahya alikuja akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.
MAR 1:5 Watu kutoka Yudea yote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.
MAR 1:6 Yahya alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Alikula nzige na asali ya mwitu.
MAR 1:7 Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake.
MAR 1:8 Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho wa Mungu.”
MAR 1:9 Wakati huo Isa akaja kutoka Nasiri ya Galilaya, naye akabatizwa na Yahya katika Mto Yordani.
MAR 1:10 Isa alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho wa Mungu akishuka juu yake kama hua.
MAR 1:11 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”
MAR 1:12 Wakati huo huo, Roho wa Mungu akamwongoza Isa hadi nyikani,
MAR 1:13 naye Isa akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama pori, nao malaika wakamhudumia.
MAR 1:14 Baada ya Yahya kutiwa gerezani, Isa alienda Galilaya, akaanza kuhubiri Injili ya Mungu,
MAR 1:15 akisema, “Wakati umetimia, ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Injili.”
MAR 1:16 Isa alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa walikuwa wavuvi.
MAR 1:17 Isa akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.”
MAR 1:18 Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.
MAR 1:19 Alipoenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.
MAR 1:20 Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Isa.
MAR 1:21 Wakaenda hadi Kapernaumu. Mara ilipofika siku ya Sabato, Isa akaingia sinagogi, akaanza kufundisha.
MAR 1:22 Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama walimu wa Torati.
MAR 1:23 Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye akapaza sauti akisema,
MAR 1:24 “Tuna nini nawe, Isa Al-Nasiri? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”
MAR 1:25 Lakini Isa akamkemea, akamwamuru, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!”
MAR 1:26 Yule pepo mchafu akamgaragaza huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.
MAR 1:27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”
MAR 1:28 Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.
MAR 1:29 Mara walipotoka katika sinagogi, walienda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani mwa Simoni na Andrea.
MAR 1:30 Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Isa habari zake.
MAR 1:31 Hivyo Isa akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.
MAR 1:32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Isa wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu.
MAR 1:33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo.
MAR 1:34 Isa akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.
MAR 1:35 Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Isa akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba.
MAR 1:36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta,
MAR 1:37 nao walipomwona, wakapaza sauti, wakasema, “Kila mtu anakutafuta!”
MAR 1:38 Isa akawajibu, “Twendeni mahali pengine, kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia. Maana nilikuja kwa kusudi hili.”
MAR 1:39 Kwa hiyo akazunguka Galilaya yote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.
MAR 1:40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Isa, akapiga magoti, akimwomba, “Ukitaka, unaweza kunitakasa.”
MAR 1:41 Isa, akiwa amejawa na huruma, akaunyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!”
MAR 1:42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika.
MAR 1:43 Baada ya Isa kumwonya vikali, akamruhusu aende zake mara moja;
MAR 1:44 akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”
MAR 1:45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Isa hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi bali alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.
MAR 2:1 Baada ya siku kadhaa Isa alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba yupo nyumbani.
MAR 2:2 Watu wengi wakakusanyika, kiasi kwamba hapakubaki nafasi yoyote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno.
MAR 2:3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Isa mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne.
MAR 2:4 Kwa kuwa hawakuweza kumfikisha kwa Isa kwa sababu ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa juu ya mahali Isa alikuwa, wakamshusha mtu aliyepooza akiwa amelalia mkeka wake.
MAR 2:5 Isa alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”
MAR 2:6 Basi baadhi ya walimu wa Torati waliokuwa wameketi pale wakawaza mioyoni mwao,
MAR 2:7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
MAR 2:8 Mara moja Isa akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
MAR 2:9 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’?
MAR 2:10 Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi”: Isa akamwambia yule aliyepooza,
MAR 2:11 “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”
MAR 2:12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”
MAR 2:13 Isa akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akaanza kuwafundisha.
MAR 2:14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Naye Lawi akaondoka, akamfuata Isa.
MAR 2:15 Isa alipokuwa ameketi akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana ni watu wengi waliokuwa wakimfuata.
MAR 2:16 Walimu wa Torati waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Isa anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?”
MAR 2:17 Isa aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
MAR 2:18 Basi wanafunzi wa Yahya pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Watu wakamjia Isa na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yahya na wa Mafarisayo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”
MAR 2:19 Isa akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga.
MAR 2:20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga.
MAR 2:21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi.
MAR 2:22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”
MAR 2:23 Siku moja ya Sabato, Isa pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.
MAR 2:24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”
MAR 2:25 Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi yeye na wenzake walipokuwa na njaa, wakahitaji chakula?
MAR 2:26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, Abiathari alipokuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani tu. Naye pia akawapa wenzake.”
MAR 2:27 Kisha Isa akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.
MAR 2:28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
MAR 3:1 Isa akaingia tena ndani ya sinagogi, na kulikuwa na mtu aliyepooza mkono.
MAR 3:2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya huyo mtu siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki.
MAR 3:3 Isa akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”
MAR 3:4 Kisha Isa akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza.
MAR 3:5 Isa akawatazama kwa hasira watu waliomzunguka pande zote, akahuzunika sana kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukawa umeponywa kabisa!
MAR 3:6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya njama ya kumuua Isa wakishirikiana na Maherode.
MAR 3:7 Isa na wanafunzi wake wakaondoka huko, wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya wakamfuata.
MAR 3:8 Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, makundi ya watu wakamjia kutoka Yudea, Yerusalemu, Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, pamoja na wale wa maeneo ya Tiro na Sidoni.
MAR 3:9 Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake watayarishe mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga.
MAR 3:10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa.
MAR 3:11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”
MAR 3:12 Lakini aliwaonya wasiwaambie wengine kumhusu.
MAR 3:13 Isa akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia.
MAR 3:14 Akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa naye, na awatume kwenda kuhubiri
MAR 3:15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.
MAR 3:16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro);
MAR 3:17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo);
MAR 3:18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo,
MAR 3:19 na Yuda Iskariote aliyemsaliti Isa.
MAR 3:20 Kisha Isa alipoingia ndani ya nyumba, umati wa watu wakakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula.
MAR 3:21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”
MAR 3:22 Walimu wa Torati walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli! Anatoa pepo wachafu kwa nguvu ya mkuu wa pepo wachafu!”
MAR 3:23 Basi Isa akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani?
MAR 3:24 Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.
MAR 3:25 Nayo nyumba ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.
MAR 3:26 Na kama Shetani akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama, bali mwisho wake umetimia.
MAR 3:27 Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali yake.
MAR 3:28 Amin, nawaambia, watu wataweza kusamehewa dhambi na kufuru zao zote;
MAR 3:29 lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu wa Mungu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”
MAR 3:30 Isa alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”
MAR 3:31 Kisha wakaja ndugu zake Isa pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita.
MAR 3:32 Umati wa watu walikuwa wameketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”
MAR 3:33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”
MAR 3:34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.
MAR 3:35 Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye kaka yangu, na dada yangu, na mama yangu.”
MAR 4:1 Isa akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Palikuwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika kumzunguka, hata ikambidi Isa aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari.
MAR 4:2 Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema:
MAR 4:3 “Sikilizeni! Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu
MAR 4:4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila.
MAR 4:5 Nyingine zilianguka kwenye mwamba usio na udongo mwingi. Ziliota haraka kwa kuwa udongo ulikuwa kidogo.
MAR 4:6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina.
MAR 4:7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao.
MAR 4:8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.”
MAR 4:9 Kisha Isa akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
MAR 4:10 Alipokuwa peke yake, watu waliokuwa naye pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili wakamuuliza kuhusu mifano yake.
MAR 4:11 Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa siri ya ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje, kila kitu husemwa kwa mifano,
MAR 4:12 ili, “ ‘kuona waone lakini wasitambue, na kusikia wasikie lakini wasielewe; wasije wakageuka na kusamehewa!’ ”
MAR 4:13 Kisha Isa akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine?
MAR 4:14 Yule mpanzi hupanda neno.
MAR 4:15 Hawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, mara Shetani huja na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao.
MAR 4:16 Nazo zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, ni wale wanaolisikia neno, na mara hulipokea kwa furaha.
MAR 4:17 Lakini kwa kuwa hawana mizizi, wao hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, mara wao huiacha imani.
MAR 4:18 Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno;
MAR 4:19 lakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae.
MAR 4:20 Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kuzaa mazao. Wao huzaa mara thelathini, au mara sitini, au mara mia ya mbegu iliyopandwa.”
MAR 4:21 Akawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake?
MAR 4:22 Kwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lolote la siri ambalo halitaletwa nuruni.
MAR 4:23 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
MAR 4:24 Naye akawaambia, “Kuweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa ninyi, hata na zaidi.
MAR 4:25 Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”
MAR 4:26 Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani.
MAR 4:27 Baada yake kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo.
MAR 4:28 Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke.
MAR 4:29 Mara nafaka inapokuwa imekomaa, mkulima huenda shambani na mundu kuvuna, maana mavuno yamekuwa tayari.”
MAR 4:30 Akawaambia tena, “Tuufananishe ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza?
MAR 4:31 Ni kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini.
MAR 4:32 Lakini ikipandwa, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote katika bustani, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wanaweza kujenga viota kwenye kivuli chake.”
MAR 4:33 Kwa mifano mingine mingi kama hii Isa alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa.
MAR 4:34 Hakusema nao neno lolote pasipo mfano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.
MAR 4:35 Ilipokaribia jioni ya siku hiyo, Isa akawaambia wanafunzi wake, “Tuvukeni hadi ng’ambo ya ziwa.”
MAR 4:36 Wakaacha umati wa watu, na wakamchukua vile alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua zingine nyingi pamoja naye.
MAR 4:37 Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji.
MAR 4:38 Isa alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”
MAR 4:39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.
MAR 4:40 Isa akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”
MAR 4:41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”
MAR 5:1 Isa na wanafunzi wake wakafika upande wa pili wa ziwa, wakaingia katika nchi ya Wagerasi.
MAR 5:2 Isa alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini, akakutana naye.
MAR 5:3 Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo.
MAR 5:4 Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia.
MAR 5:5 Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.
MAR 5:6 Alipomwona Isa kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake.
MAR 5:7 Akapaza sauti kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!”
MAR 5:8 Kwa kuwa Isa alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”
MAR 5:9 Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tuko wengi.”
MAR 5:10 Akamsihi Isa sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
MAR 5:11 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima.
MAR 5:12 Wale pepo wachafu wakamsihi Isa wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.”
MAR 5:13 Basi Isa akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao elfu mbili, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.
MAR 5:14 Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakaenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia.
MAR 5:15 Walipofika kwa Isa, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na legioni ya pepo wachafu akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa.
MAR 5:16 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia.
MAR 5:17 Basi watu wakaanza kumwomba Isa aondoke katika nchi yao.
MAR 5:18 Isa alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Isa waende pamoja.
MAR 5:19 Isa hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Mwenyezi Mungu, na jinsi alivyokuhurumia.”
MAR 5:20 Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Isa aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.
MAR 5:21 Isa alipokwisha kuvuka tena na kufika ng’ambo, umati mkubwa wa watu wakamzunguka hapo kando ya bahari.
MAR 5:22 Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Isa, akapiga magoti miguuni pake,
MAR 5:23 akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye ataishi.”
MAR 5:24 Hivyo Isa akaenda pamoja naye. Umati mkubwa wa watu wakamfuata, nao watu wakawa wanamsonga.
MAR 5:25 Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na mbili.
MAR 5:26 Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya.
MAR 5:27 Alikuwa amesikia habari za Isa, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake,
MAR 5:28 kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitaponywa.”
MAR 5:29 Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.
MAR 5:30 Ghafula Isa akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akageukia umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”
MAR 5:31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi watu wanavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”
MAR 5:32 Lakini Isa akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa.
MAR 5:33 Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote.
MAR 5:34 Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
MAR 5:35 Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani mwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”
MAR 5:36 Aliposikia hayo waliyosema, Isa akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
MAR 5:37 Hakumruhusu mtu yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.
MAR 5:38 Walipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi, Isa akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa.
MAR 5:39 Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.”
MAR 5:40 Wale watu wakamcheka. Baada ya kuwafukuza wote nje, Isa akaenda na baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaingia ndani hadi pale alipokuwa mtoto yule.
MAR 5:41 Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana, nakuambia: amka!”)
MAR 5:42 Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili). Walipoona haya, wakastaajabu sana.
MAR 5:43 Isa akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.
MAR 6:1 Isa akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiandamana na wanafunzi wake.
MAR 6:2 Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa. Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!
MAR 6:3 Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu? Na ndugu zake si Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa kwetu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake, wakakataa kumwamini.
MAR 6:4 Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe, na miongoni mwa jamaa na ndugu zake, na nyumbani mwake.”
MAR 6:5 Hakufanya miujiza yoyote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya.
MAR 6:6 Naye akashangazwa sana kwa kutoamini kwao. Kisha Isa akawa anaenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha.
MAR 6:7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.
MAR 6:8 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu.
MAR 6:9 Vaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada.
MAR 6:10 Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo.
MAR 6:11 Kama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu ili kuwe ushuhuda dhidi yao.”
MAR 6:12 Kwa hiyo wakaenenda na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi.
MAR 6:13 Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.
MAR 6:14 Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Isa lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yahya amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
MAR 6:15 Wengine wakasema, “Yeye ni Ilya.” Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmoja wa manabii wa zamani.”
MAR 6:16 Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yahya, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!”
MAR 6:17 Herode mwenyewe alikuwa ameagiza kwamba Yahya akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa.
MAR 6:18 Yahya alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.”
MAR 6:19 Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yahya kinyongo, akataka kumuua. Lakini hakuweza,
MAR 6:20 kwa sababu Herode alimwogopa Yahya akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.
MAR 6:21 Hatimaye Herodia alipata wakati mwafaka aliokuwa akiutafuta. Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya.
MAR 6:22 Binti Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani. Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.”
MAR 6:23 Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”
MAR 6:24 Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?” Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yahya.”
MAR 6:25 Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yahya kwenye sinia.”
MAR 6:26 Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia.
MAR 6:27 Mara mfalme akatuma askari mmoja wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yahya. Akaenda na kumkata Yahya kichwa humo gerezani,
MAR 6:28 akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake.
MAR 6:29 Wanafunzi wa Yahya walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
MAR 6:30 Wale mitume wakakusanyika kwa Isa na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha.
MAR 6:31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Isa akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”
MAR 6:32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu.
MAR 6:33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika.
MAR 6:34 Isa alipofika kando ya bahari, aliona kundi kubwa la watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
MAR 6:35 Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimeenda sana.
MAR 6:36 Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.”
MAR 6:37 Lakini Isa akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.” Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape watu hawa wale?”
MAR 6:38 Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.” Walipokwisha kujua, wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”
MAR 6:39 Kisha Isa akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani,
MAR 6:40 nao wakaketi kwenye vikundi vya watu mia mia, na wengine hamsini hamsini.
MAR 6:41 Isa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili.
MAR 6:42 Watu wote wakala, wakashiba.
MAR 6:43 Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.
MAR 6:44 Idadi ya wanaume waliokula walikuwa elfu tano.
MAR 6:45 Mara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua wamtangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale watu.
MAR 6:46 Baada ya kuwaaga, akaenda mlimani kuomba.
MAR 6:47 Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Isa alikuwa peke yake katika nchi kavu.
MAR 6:48 Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Isa akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita,
MAR 6:49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe,
MAR 6:50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa. Mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!”
MAR 6:51 Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa,
MAR 6:52 kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu.
MAR 6:53 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga.
MAR 6:54 Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Isa.
MAR 6:55 Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Isa yupo.
MAR 6:56 Kila mahali Isa alipoenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.
MAR 7:1 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Torati waliokuwa wametoka Yerusalemu wakakusanyika mbele ya Isa.
MAR 7:2 Wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula kwa mikono iliyo najisi, yaani bila kunawa kama ilivyotakiwa na Torati ya Wayahudi.
MAR 7:3 (Kwa kuwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali chakula pasipo kunawa kwa kufuata desturi za wazee wao.
MAR 7:4 Wanapotoka sokoni hawawezi kula pasipo kunawa. Pia kuna desturi zingine nyingi wanazofuata kama vile jinsi ya kuosha vikombe, vyungu na vyombo vya shaba.)
MAR 7:5 Hivyo, wale Mafarisayo na walimu wa Torati wakamuuliza Isa, “Mbona wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, na badala yake wanakula kwa mikono najisi?”
MAR 7:6 Isa akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa: “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami.
MAR 7:7 Huniabudu bure, nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’
MAR 7:8 Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.”
MAR 7:9 Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuyashika mapokeo yenu!
MAR 7:10 Kwa mfano, Musa alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’
MAR 7:11 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia ni Korbani’ (yaani kimewekwa wakfu kwa Mungu),
MAR 7:12 basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake.
MAR 7:13 Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya aina hiyo.”
MAR 7:14 Isa akaita tena umati ule wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, na mwelewe jambo hili.
MAR 7:15 Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [
MAR 7:16 Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”
MAR 7:17 Baada ya Isa kuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule.
MAR 7:18 Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi?
MAR 7:19 Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Isa alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni safi.)
MAR 7:20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.
MAR 7:21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi,
MAR 7:22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu.
MAR 7:23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”
MAR 7:24 Ndipo Isa akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha.
MAR 7:25 Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake.
MAR 7:26 Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Isa amtoe binti yake huyo pepo mchafu.
MAR 7:27 Isa akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
MAR 7:28 Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.”
MAR 7:29 Ndipo Isa akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.”
MAR 7:30 Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.
MAR 7:31 Kisha Isa akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli.
MAR 7:32 Huko, watu wakamletea Isa mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu.
MAR 7:33 Isa akampeleka yule kiziwi kando, mbali na watu, akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu.
MAR 7:34 Ndipo Isa akatazama mbinguni, akashusha pumzi kwa nguvu, akamwambia, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”)
MAR 7:35 Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa.
MAR 7:36 Isa akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowakanya, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii.
MAR 7:37 Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”
MAR 8:1 Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu walikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Isa akawaita wanafunzi wake akawaambia,
MAR 8:2 “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula.
MAR 8:3 Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”
MAR 8:4 Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”
MAR 8:5 Isa akawauliza, “Mna mikate mingapi?” Wakajibu, “Tuna mikate saba.”
MAR 8:6 Akawaambia watu waketi chini. Akaichukua ile mikate saba na kushukuru, baadaye akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo.
MAR 8:7 Walikuwa pia na visamaki vichache, Isa akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu.
MAR 8:8 Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.
MAR 8:9 Watu waliokula walikuwa wapata elfu nne. Baada ya kuwaaga,
MAR 8:10 aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.
MAR 8:11 Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Isa. Ili kumtega, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni.
MAR 8:12 Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.”
MAR 8:13 Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ng’ambo.
MAR 8:14 Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua.
MAR 8:15 Isa akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”
MAR 8:16 Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.”
MAR 8:17 Isa, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho?
MAR 8:18 Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki?
MAR 8:19 Nilipoimega ile mikate mitano kwa watu elfu tano, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?” Wakamjibu, “Kumi na viwili.”
MAR 8:20 “Je, nilipoimega ile mikate saba kwa watu elfu nne, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?” Wakamjibu, “Saba.”
MAR 8:21 Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”
MAR 8:22 Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Isa amguse.
MAR 8:23 Isa akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Isa akamuuliza, “Unaona chochote?”
MAR 8:24 Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”
MAR 8:25 Isa akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri.
MAR 8:26 Isa akamtuma nyumbani mwake, akamwambia, “Hata kijijini usiingie.”
MAR 8:27 Isa na wanafunzi wake wakaelekea vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Isa akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
MAR 8:28 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yahya, wengine husema ni Ilya, na bado wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”
MAR 8:29 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi.”
MAR 8:30 Isa akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.
MAR 8:31 Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa Torati, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuliwe.
MAR 8:32 Aliyasema haya waziwazi. Ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea.
MAR 8:33 Lakini Isa akageuka na kuwaangalia wanafunzi wake, na akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
MAR 8:34 Ndipo akawaita umati ule wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
MAR 8:35 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa.
MAR 8:36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?
MAR 8:37 Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
MAR 8:38 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”
MAR 9:1 Isa akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
MAR 9:2 Baada ya siku sita, Isa akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Isa akageuka sura mbele yao.
MAR 9:3 Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko vile mtu yeyote duniani angeweza kuyang’arisha.
MAR 9:4 Musa na Ilya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Isa.
MAR 9:5 Petro akamwambia Isa, “Mwalimu, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.”
MAR 9:6 Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.
MAR 9:7 Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.”
MAR 9:8 Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Isa.
MAR 9:9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, hadi Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu.
MAR 9:10 Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?”
MAR 9:11 Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa Torati husema kwamba ni lazima Ilya aje kwanza?”
MAR 9:12 Isa akawajibu, “Ni kweli, Ilya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa?
MAR 9:13 Lakini nawaambia, Ilya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu.”
MAR 9:14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa Torati wakibishana nao.
MAR 9:15 Mara wale watu walipomwona Isa, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.
MAR 9:16 Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”
MAR 9:17 Mtu mmoja miongoni mwa umati ule wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea.
MAR 9:18 Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
MAR 9:19 Isa akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini! Nitakuwa pamoja nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana kwangu.”
MAR 9:20 Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Isa, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.
MAR 9:21 Isa akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake.
MAR 9:22 Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”
MAR 9:23 Isa akamwambia, “Ati, ‘Kama unaweza kufanya jambo lolote’? Yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”
MAR 9:24 Mara baba yake yule mvulana akapaza sauti akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!”
MAR 9:25 Isa alipoona kwamba umati wa watu wanakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”
MAR 9:26 Baada ya yule pepo mchafu kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.”
MAR 9:27 Lakini Isa akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
MAR 9:28 Baada ya Isa kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”
MAR 9:29 Isa akawajibu, “Pepo aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba [na kufunga].”
MAR 9:30 Wakaondoka huko, wakapitia Galilaya. Isa hakutaka mtu yeyote afahamu mahali walipo,
MAR 9:31 kwa maana alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. Nao watamuua, lakini siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.”
MAR 9:32 Lakini wao hawakuelewa kile alimaanisha, nao waliogopa kumuuliza maana yake.
MAR 9:33 Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?”
MAR 9:34 Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.
MAR 9:35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”
MAR 9:36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia,
MAR 9:37 “Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”
MAR 9:38 Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
MAR 9:39 Isa akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu.
MAR 9:40 Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu.
MAR 9:41 Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Al-Masihi, hakika hataikosa thawabu yake.
MAR 9:42 “Mtu yeyote akimsababisha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini.
MAR 9:43 Mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia Jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [
MAR 9:44 Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.]
MAR 9:45 Mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia Jehanamu. [
MAR 9:46 Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.]
MAR 9:47 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, ling’oe. Ni afadhali kwako kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa Jehanamu.
MAR 9:48 Ni mahali ambako funza wao hawafi, wala moto wao hauzimiki.
MAR 9:49 Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.
MAR 9:50 “Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”
MAR 10:1 Isa akaondoka huko, akavuka Mto Yordani, akaenda sehemu za Yudea. Umati mkubwa wa watu wakaenda kwake tena, naye akawafundisha, kama ilivyokuwa desturi yake.
MAR 10:2 Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?”
MAR 10:3 Isa akawajibu, “Je, Musa aliwaamuru nini?”
MAR 10:4 Wakajibu, “Musa aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”
MAR 10:5 Isa akawaambia, “Musa aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.
MAR 10:6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke’.
MAR 10:7 ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe,
MAR 10:8 na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja.
MAR 10:9 Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
MAR 10:10 Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili.
MAR 10:11 Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye.
MAR 10:12 Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”
MAR 10:13 Watu walikuwa wakimletea Isa watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea.
MAR 10:14 Isa alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.
MAR 10:15 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”
MAR 10:16 Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
MAR 10:17 Isa alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
MAR 10:18 Isa akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake.
MAR 10:19 Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”
MAR 10:20 Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
MAR 10:21 Isa akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
MAR 10:22 Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
MAR 10:23 Isa akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!”
MAR 10:24 Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Isa akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika ufalme wa Mungu.
MAR 10:25 Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
MAR 10:26 Wanafunzi wake wakashangaa sana. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
MAR 10:27 Isa akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
MAR 10:28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha kila kitu na kukufuata wewe!”
MAR 10:29 Isa akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au mama au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili,
MAR 10:30 ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu: nyumba, ndugu wa kiume na wa kike, mama na baba na watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao.
MAR 10:31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”
MAR 10:32 Walikuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu, na Isa alikuwa amewatangulia. Wanafunzi wake walishangaa, nao watu waliowafuata walijawa na hofu. Isa akawachukua tena wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia yatakayompata.
MAR 10:33 Akasema, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atasalitiwa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa Torati. Wao watamhukumu kifo na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa,
MAR 10:34 ambao watamdhihaki na kumtemea mate, watampiga na kumuua. Siku tatu baadaye atafufuka.”
MAR 10:35 Kisha Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakaja kwake na kumwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie lolote tutakalokuomba.”
MAR 10:36 Naye akawaambia, “Je, mwataka niwafanyie jambo gani?”
MAR 10:37 Wakamwambia, “Tupe kukaa mmoja upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”
MAR 10:38 Lakini Isa akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?”
MAR 10:39 Wakajibu, “Tunaweza.” Kisha Isa akawaambia, “Kikombe nikinyweacho mtakinywea na ubatizo nibatizwao mtabatizwa,
MAR 10:40 lakini kuketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto si juu yangu mimi kuwapa. Nafasi hizi ni kwa ajili ya wale walioandaliwa.”
MAR 10:41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana.
MAR 10:42 Lakini Isa akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao.
MAR 10:43 Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,
MAR 10:44 na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote.
MAR 10:45 Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
MAR 10:46 Kisha wakafika Yeriko. Isa alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mmoja, jina lake Bartimayo (maana yake “mwana wa Timayo”), alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.
MAR 10:47 Aliposikia kuwa ni Isa Al-Nasiri aliyekuwa anapita, akaanza kupaza sauti akisema, “Isa, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
MAR 10:48 Watu wengi wakamkemea, wakamwambia akae kimya, lakini yeye akazidi kupaza sauti, akisema, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
MAR 10:49 Isa akasimama na kusema, “Mwiteni.” Hivyo wakamwita yule mtu kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Inuka, anakuita.”
MAR 10:50 Akiwa analivua lile joho lake, alisimama na kumwendea Isa.
MAR 10:51 Isa akamuuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona.”
MAR 10:52 Isa akamwambia, “Nenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona, akamfuata Isa njiani.
MAR 11:1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Isa akawatuma wawili wa wanafunzi wake,
MAR 11:2 akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtampata mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa.
MAR 11:3 Mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”
MAR 11:4 Wakaenda, wakampata mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba.
MAR 11:5 Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwana-punda?”
MAR 11:6 Wakawajibu kama vile Isa alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu.
MAR 11:7 Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Isa na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda.
MAR 11:8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani.
MAR 11:9 Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema, “Hosana!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!”
MAR 11:10 “Umebarikiwa ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!” “Hosana kwake yeye aliye juu!”
MAR 11:11 Isa akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
MAR 11:12 Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Isa alikuwa na njaa.
MAR 11:13 Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini.
MAR 11:14 Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.
MAR 11:15 Walipofika Yerusalemu, Isa akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa,
MAR 11:16 wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu.
MAR 11:17 Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyang’anyi.’ ”
MAR 11:18 Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote walishangazwa na mafundisho yake.
MAR 11:19 Ilipofika jioni, Isa na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.
MAR 11:20 Kesho yake asubuhi walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake.
MAR 11:21 Petro akakumbuka na kumwambia Isa, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”
MAR 11:22 Isa akawajibu, “Mwaminini Mungu.
MAR 11:23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng’oka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa.
MAR 11:24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu.
MAR 11:25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [
MAR 11:26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”
MAR 11:27 Wakafika tena Yerusalemu, na Isa alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wa watu wakamjia.
MAR 11:28 Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”
MAR 11:29 Isa akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.
MAR 11:30 Je, ubatizo wa Yahya ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Niambieni!”
MAR 11:31 Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’
MAR 11:32 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’ ” (waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yahya alikuwa nabii wa kweli);
MAR 11:33 kwa hiyo wakamjibu Isa, “Hatujui.” Naye Isa akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”
MAR 12:1 Isa akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, na ndani yake akachimba shimo la shinikizo la kukamulia zabibu, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha shamba hilo la mizabibu kwa wakulima fulani, kisha akasafiri hadi nchi nyingine.
MAR 12:2 Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili kuchukua sehemu yake ya mavuno ya shamba la mizabibu kutoka kwa hao wapangaji.
MAR 12:3 Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu.
MAR 12:4 Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao; nao wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu.
MAR 12:5 Kisha akamtuma mtumishi mwingine, naye huyo wakamuua. Akawatuma wengine wengi; baadhi yao wakawapiga, na wengine wakawaua.
MAR 12:6 “Mwenye shamba alikuwa bado na mmoja wa kumtuma, mwanawe aliyempenda. Hatimaye akamtuma akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
MAR 12:7 “Lakini wale wapangaji wakasemezana pamoja, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, nao urithi utakuwa wetu.’
MAR 12:8 Hivyo wakamchukua na kumuua, wakamtupa nje ya lile shamba la mizabibu.
MAR 12:9 “Sasa basi yule mwenye shamba atafanya nini? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, kisha atawapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.
MAR 12:10 Je, hamjasoma andiko hili: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni;
MAR 12:11 Mwenyezi Mungu ndiye alitenda jambo hili, nalo ni la kushangaza machoni petu’?”
MAR 12:12 Walipotambua kuwa amesema mfano huo kwa ajili yao, wakataka kumkamata, lakini wakaogopa umati ule wa watu. Wakamwacha, wakaenda zao.
MAR 12:13 Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili wamtege Isa katika maneno yake.
MAR 12:14 Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa huna upendeleo. Lakini wewe huifundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?
MAR 12:15 Je, tulipe kodi au tusilipe?” Lakini Isa alijua unafiki wao. Akawauliza, “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinari niione.”
MAR 12:16 Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
MAR 12:17 Ndipo Isa akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Nao wakamstaajabia sana.
MAR 12:18 Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Isa,
MAR 12:19 wakasema, “Mwalimu, Musa alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto.
MAR 12:20 Basi kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa bila kuacha mtoto yeyote.
MAR 12:21 Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu.
MAR 12:22 Hakuna hata mmoja wa hao ndugu saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa.
MAR 12:23 Basi, wakati wa ufufuo yeye atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”
MAR 12:24 Isa akawajibu, “Je, hampotei kwa sababu hamfahamu Maandiko wala uweza wa Mungu?
MAR 12:25 Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.
MAR 12:26 Basi kuhusu wafu kufufuliwa, je hamjasoma katika Kitabu cha Musa jinsi Mungu alivyosema na Musa kutoka kile kichaka akisema, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’?
MAR 12:27 Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”
MAR 12:28 Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Isa amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”
MAR 12:29 Isa akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.
MAR 12:30 Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’
MAR 12:31 Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
MAR 12:32 Yule mwalimu wa Torati akamwambia Isa, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye.
MAR 12:33 Kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, na kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
MAR 12:34 Isa alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe huko mbali na ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
MAR 12:35 Isa alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa Torati wanasema kwamba Al-Masihi ni Mwana wa Daudi?
MAR 12:36 Kwa maana Daudi mwenyewe, akinena kwa kuongozwa na Roho wa Mungu, alisema: “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’
MAR 12:37 Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?” Umati ule wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.
MAR 12:38 Alipokuwa akifundisha, Isa alisema, “Jihadharini na walimu wa Torati. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni.
MAR 12:39 Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kupewa nafasi za heshima katika karamu.
MAR 12:40 Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”
MAR 12:41 Kisha Isa akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha.
MAR 12:42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
MAR 12:43 Isa akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote.
MAR 12:44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali yao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
MAR 13:1 Isa alipokuwa akitoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu! Tazama jinsi mawe haya yalivyo makubwa, na majengo haya yalivyo mazuri!”
MAR 13:2 Ndipo Isa akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali yote yatabomolewa.”
MAR 13:3 Isa alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamuuliza faraghani,
MAR 13:4 “Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo dalili ya kuwa hayo yote yanakaribia kutimia itakuwa gani?”
MAR 13:5 Isa akawaambia: “Jihadharini mtu yeyote asiwadanganye.
MAR 13:6 Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi.
MAR 13:7 Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.
MAR 13:8 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali na njaa. Haya yatakuwa ndio mwanzo wa uchungu.
MAR 13:9 “Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kupigwa mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao.
MAR 13:10 Nayo Injili lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote.
MAR 13:11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu wa Mungu.
MAR 13:12 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe.
MAR 13:13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
MAR 13:14 “Mtakapoona ‘chukizo la uharibifu’ limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walio Yudea wakimbilie milimani.
MAR 13:15 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua chochote.
MAR 13:16 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.
MAR 13:17 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!
MAR 13:18 Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi.
MAR 13:19 Kwa maana siku hizo zitakuwa za dhiki kuu ambayo haijapata kuwa tangu mwanzo, hapo Mungu alipoumba ulimwengu, hadi leo, na wala haitakuwa tena kamwe.
MAR 13:20 “Kama Mwenyezi Mungu hangefupisha siku hizo, kamwe hakuna mtu yeyote angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo.
MAR 13:21 Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Al-Masihi huyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki.
MAR 13:22 Kwa maana watatokea masihi wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule.
MAR 13:23 Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.
MAR 13:24 “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki, “ ‘jua litatiwa giza nao mwezi hautatoa nuru yake;
MAR 13:25 nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’
MAR 13:26 “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.
MAR 13:27 Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.
MAR 13:28 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
MAR 13:29 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni.
MAR 13:30 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
MAR 13:31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
MAR 13:32 “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.
MAR 13:33 Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia.
MAR 13:34 Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe.
MAR 13:35 “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko,
MAR 13:36 akija ghafula asije akawakuta mmelala.
MAR 13:37 Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’ ”
MAR 14:1 Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Isa kwa hila na kumuua.
MAR 14:2 Lakini walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.”
MAR 14:3 Isa alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Isa.
MAR 14:4 Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na wakasemezana, “Upotevu huu wote wa manukato ni wa nini?
MAR 14:5 Manukato haya yangeuzwa kwa zaidi ya dinari mia tatu, na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke.
MAR 14:6 Lakini Isa akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana.
MAR 14:7 Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.
MAR 14:8 Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu.
MAR 14:9 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
MAR 14:10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Isa kwao.
MAR 14:11 Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti.
MAR 14:12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Isa wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
MAR 14:13 Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni.
MAR 14:14 Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba changu cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’
MAR 14:15 Atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.”
MAR 14:16 Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Isa alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
MAR 14:17 Ilipofika jioni, Isa akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili.
MAR 14:18 Walipoketi mezani wakila, Isa akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.”
MAR 14:19 Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi, Bwana?”
MAR 14:20 Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami.
MAR 14:21 Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.”
MAR 14:22 Walipokuwa wanakula, Isa akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.”
MAR 14:23 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo.
MAR 14:24 Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.
MAR 14:25 Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.”
MAR 14:26 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
MAR 14:27 Isa akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “ ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo watatawanyika.’
MAR 14:28 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
MAR 14:29 Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.”
MAR 14:30 Isa akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, wewe mwenyewe utanikana mara tatu.”
MAR 14:31 Lakini Petro akasisitiza zaidi, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.
MAR 14:32 Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Isa akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.”
MAR 14:33 Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika.
MAR 14:34 Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.”
MAR 14:35 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee.
MAR 14:36 Akasema, “Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.”
MAR 14:37 Akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja?
MAR 14:38 Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”
MAR 14:39 Akaenda tena kuomba, akisema maneno yale yale.
MAR 14:40 Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia.
MAR 14:41 Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.
MAR 14:42 Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
MAR 14:43 Isa alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa Torati, na wazee.
MAR 14:44 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.”
MAR 14:45 Mara Yuda akamjia Isa na kusema, “Mwalimu.” Akambusu.
MAR 14:46 Wale watu wakamkamata Isa, wakamweka chini ya ulinzi.
MAR 14:47 Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
MAR 14:48 Kisha Isa akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang’anyi?
MAR 14:49 Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.”
MAR 14:50 Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.
MAR 14:51 Kijana mmoja, aliyekuwa amevaa nguo ya kitani pekee, alikuwa akimfuata Isa. Walipomkamata,
MAR 14:52 alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.
MAR 14:53 Wakampeleka Isa kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa Torati wote wakakusanyika pamoja.
MAR 14:54 Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto.
MAR 14:55 Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Isa ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote.
MAR 14:56 Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.
MAR 14:57 Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema:
MAR 14:58 “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ”
MAR 14:59 Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.
MAR 14:60 Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Isa, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”
MAR 14:61 Lakini Isa akakaa kimya, hakusema neno lolote. Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Al-Masihi, Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?”
MAR 14:62 Isa akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
MAR 14:63 Kuhani mkuu akayararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi?
MAR 14:64 Ninyi mmesikia alivyokufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo.
MAR 14:65 Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.
MAR 14:66 Petro alipokuwa bado yuko chini uani, tazama akaja mmoja wa wajakazi wa kuhani mkuu.
MAR 14:67 Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Isa, Mnasiri.”
MAR 14:68 Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia.
MAR 14:69 Yule mjakazi alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.”
MAR 14:70 Lakini Petro akakana tena. Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!”
MAR 14:71 Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!”
MAR 14:72 Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Isa alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.
MAR 15:1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa Torati na Baraza la Wayahudi lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Isa, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.
MAR 15:2 Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Isa akajibu, “Wewe umesema.”
MAR 15:3 Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi.
MAR 15:4 Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”
MAR 15:5 Lakini Isa hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa.
MAR 15:6 Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka.
MAR 15:7 Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi.
MAR 15:8 Umati ule wa watu wakamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.
MAR 15:9 Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu mfalme wa Wayahudi?”
MAR 15:10 Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Isa mkononi mwake kwa ajili ya wivu.
MAR 15:11 Lakini viongozi wa makuhani wakachochea umati ule wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.
MAR 15:12 Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita mfalme wa Wayahudi?”
MAR 15:13 Wakapiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
MAR 15:14 Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakapiga kelele zaidi, wakisema, “Msulubishe!”
MAR 15:15 Pilato, akitaka kuridhisha umati ule wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Isa apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
MAR 15:16 Askari wakampeleka Isa hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari.
MAR 15:17 Wakamvalisha Isa joho la zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamvika kichwani.
MAR 15:18 Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!”
MAR 15:19 Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki.
MAR 15:20 Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.
MAR 15:21 Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Iskanda na Rufo, alikuwa anaingia mjini kutoka mashambani, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.
MAR 15:22 Kisha wakampeleka Isa hadi mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).
MAR 15:23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa.
MAR 15:24 Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua.
MAR 15:25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha.
MAR 15:26 Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: Mfalme wa Wayahudi.
MAR 15:27 Pamoja naye walisulubiwa wanyang’anyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [
MAR 15:28 Nalo andiko likatimizwa, lisemalo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.”]
MAR 15:29 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu,
MAR 15:30 basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!”
MAR 15:31 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa Torati wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe!
MAR 15:32 Basi huyu Al-Masihi, huyu mfalme wa Israeli, ashuke sasa msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.
MAR 15:33 Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa.
MAR 15:34 Hapo saa tisa, Isa akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
MAR 15:35 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Ilya.”
MAR 15:36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”
MAR 15:37 Kisha Isa akatoa sauti kuu, akakata roho.
MAR 15:38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini.
MAR 15:39 Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Isa aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
MAR 15:40 Palikuwa na wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwa Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome.
MAR 15:41 Hawa walifuatana na Isa na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwako wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye hadi Yerusalemu.
MAR 15:42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi (yaani siku moja kabla ya Sabato),
MAR 15:43 Yusufu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na alikuwa anautarajia ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Isa.
MAR 15:44 Pilato alikuwa akijiuliza kama Isa alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Isa alikuwa amekwisha kufa.
MAR 15:45 Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yusufu ruhusa ya kuuchukua huo mwili.
MAR 15:46 Hivyo Yusufu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi.
MAR 15:47 Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.
MAR 16:1 Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalene, Mariamu mama yake Yakobo, na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Isa.
MAR 16:2 Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua, walienda kaburini.
MAR 16:3 Njiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka ingilio la kaburi?”
MAR 16:4 Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi.
MAR 16:5 Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.
MAR 16:6 Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Isa, Mnasiri, aliyesulubiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza.
MAR 16:7 Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba, ‘Anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko kama alivyowaambia.’ ”
MAR 16:8 Hivyo wakatoka, wakakimbia kutoka mle kaburini wakiwa na hofu kuu na mshangao. Nao hawakumwambia mtu yeyote neno lolote, kwa sababu waliogopa. [
MAR 16:9 Isa alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, aliyekuwa amemtoa pepo wachafu saba.
MAR 16:10 Mariamu akaenda, naye akawaambia wale waliokuwa wamefuatana na Isa, waliokuwa wanaomboleza na kulia.
MAR 16:11 Lakini waliposikia kwamba Isa yu hai na kwamba Mariamu alikuwa amemwona, hawakusadiki.
MAR 16:12 Baadaye Isa akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine.
MAR 16:13 Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.
MAR 16:14 Baadaye Isa akawatokea wale wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutoamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa kutosadiki wale waliomwona baada yake kufufuka.
MAR 16:15 Akawaambia, “Nendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
MAR 16:16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa.
MAR 16:17 Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya;
MAR 16:18 watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”
MAR 16:19 Baada ya Bwana Isa kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu.
MAR 16:20 Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana Isa akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]
LUK 1:1 Kwa kuwa watu wengi wamekaa ili kuandika habari za mambo yaliyotimizwa katikati yetu,
LUK 1:2 kama vile yalivyokabidhiwa kwetu na wale waliokuwa mashahidi walioyaona na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,
LUK 1:3 mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo, ewe mtukufu Theofilo,
LUK 1:4 ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa.
LUK 1:5 Wakati wa utawala wa Herode mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, aliyekuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Haruni.
LUK 1:6 Zakaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Mwenyezi Mungu na maagizo yote bila lawama.
LUK 1:7 Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana.
LUK 1:8 Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zakaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu,
LUK 1:9 alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Mwenyezi Mungu ili kufukiza uvumba.
LUK 1:10 Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba.
LUK 1:11 Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zakaria.
LUK 1:12 Zakaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu.
LUK 1:13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina Yahya.
LUK 1:14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
LUK 1:15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Mwenyezi Mungu, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu wa Mungu hata kabla ya kuzaliwa kwake.
LUK 1:16 Naye atawageuza wengi wa Waisraeli warudi kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
LUK 1:17 Naye atatangulia mbele za Mwenyezi Mungu katika roho na nguvu ya Ilya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuwaweka tayari watu walioandaliwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.”
LUK 1:18 Zakaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.”
LUK 1:19 Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Jibraili, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema.
LUK 1:20 Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”
LUK 1:21 Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zakaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni.
LUK 1:22 Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono.
LUK 1:23 Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani mwake.
LUK 1:24 Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano.
LUK 1:25 Elizabeti akasema, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu alilonitendea aliponipa kibali na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”
LUK 1:26 Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Jibraili aende Galilaya katika mji wa Nasiri,
LUK 1:27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yusufu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Mariamu.
LUK 1:28 Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe!”
LUK 1:29 Mariamu akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni salamu hii ni ya namna gani.
LUK 1:30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Mariamu; umepata kibali kwa Mungu.
LUK 1:31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume na utamwita jina Isa.
LUK 1:32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Mwenyezi Mungu atampa kiti cha utawala cha Daudi baba yake.
LUK 1:33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
LUK 1:34 Mariamu akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”
LUK 1:35 Malaika akamjibu, “Roho wa Mungu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.
LUK 1:36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa.
LUK 1:37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”
LUK 1:38 Mariamu akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Mwenyezi Mungu. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.
LUK 1:39 Wakati huo Mariamu akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye nchi ya vilima ya Yudea.
LUK 1:40 Akaingia nyumbani mwa Zakaria na kumsalimu Elizabeti.
LUK 1:41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho wa Mungu,
LUK 1:42 akapaza sauti kwa nguvu, akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa.
LUK 1:43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata kibali kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
LUK 1:44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliye tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
LUK 1:45 Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Mwenyezi Mungu alilomwambia litatimizwa.”
LUK 1:46 Naye Mariamu akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Mwenyezi Mungu,
LUK 1:47 nayo roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu,
LUK 1:48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili unyonge wa mtumishi wake. Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,
LUK 1:49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu amenitendea mambo ya ajabu: jina lake ni takatifu.
LUK 1:50 Rehema zake hudumu kizazi hadi kizazi, kwa wale wanaomcha.
LUK 1:51 Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake; amewatawanya wale wenye kiburi ndani ya mioyo yao.
LUK 1:52 Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya utawala, lakini amewainua wanyenyekevu.
LUK 1:53 Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.
LUK 1:54 Amemsaidia mtumishi wake Israeli, kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu
LUK 1:55 Ibrahimu na uzao wake milele, kama alivyowaahidi baba zetu.”
LUK 1:56 Mariamu akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani mwake.
LUK 1:57 Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume.
LUK 1:58 Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.
LUK 1:59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zakaria, ambalo ndilo jina la baba yake.
LUK 1:60 Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yahya.”
LUK 1:61 Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”
LUK 1:62 Basi wakamfanyia Zakaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani.
LUK 1:63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yahya.”
LUK 1:64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kuongea, huku akimsifu Mungu.
LUK 1:65 Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima ya Yudea watu walikuwa wakinena kuhusu mambo haya yote.
LUK 1:66 Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa pamoja naye.
LUK 1:67 Zakaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, naye akatoa unabii, akisema:
LUK 1:68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.
LUK 1:69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,
LUK 1:70 (kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake watakatifu tangu zamani),
LUK 1:71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu, na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:
LUK 1:72 ili kuonesha rehema kwa baba zetu na kukumbuka agano lake takatifu,
LUK 1:73 kiapo alichomwapia baba yetu Ibrahimu:
LUK 1:74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu, tupate kumtumikia yeye pasipo hofu
LUK 1:75 katika utakatifu na haki mbele zake, siku zetu zote.
LUK 1:76 “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana; kwa kuwa utamtangulia Mwenyezi Mungu na kuandaa njia kwa ajili yake,
LUK 1:77 kuwajulisha watu wake wokovu utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,
LUK 1:78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu, nuru inayotoka juu itatuzukia
LUK 1:79 ili kuwaangazia wale wanaoishi gizani na katika uvuli wa mauti, kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”
LUK 1:80 Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionesha hadharani kwa Waisraeli.
LUK 2:1 Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Rumi.
LUK 2:2 (Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Siria.)
LUK 2:3 Kila mtu alienda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.
LUK 2:4 Hivyo Yusufu akapanda kutoka mji wa Nasiri ulioko Galilaya kwenda Yudea, hadi Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi.
LUK 2:5 Alienda huko kujiandikisha pamoja na Mariamu, aliyekuwa amemposa, na alikuwa mjamzito.
LUK 2:6 Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu wa kujifungua ukawa umetimia,
LUK 2:7 naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori la kulia ng’ombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.
LUK 2:8 Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku.
LUK 2:9 Ghafula tazama, malaika wa Mwenyezi Mungu akawatokea, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukawang’aria kotekote, wakaingiwa na hofu.
LUK 2:10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama, nawaletea habari njema ya furaha itakayokuwa kwa watu wote.
LUK 2:11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Al-Masihi, Bwana.
LUK 2:12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori la kulia ng’ombe.”
LUK 2:13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,
LUK 2:14 “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
LUK 2:15 Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya yaliyotukia, ambayo Mwenyezi Mungu ametuambia habari zake.”
LUK 2:16 Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Mariamu na Yusufu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ng’ombe.
LUK 2:17 Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto.
LUK 2:18 Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo.
LUK 2:19 Lakini Mariamu akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari.
LUK 2:20 Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.
LUK 2:21 Hata zilipotimia siku nane, uliokuwa wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Isa, jina alilopewa na malaika kabla hajatungwa mimba.
LUK 2:22 Ulipotimia wakati wa utakaso wake Mariamu kwa mujibu wa Torati ya Musa, basi Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu
LUK 2:23 (kama ilivyoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu”),
LUK 2:24 na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu: “Hua wawili au makinda wawili wa njiwa”.
LUK 2:25 Basi huko Yerusalemu kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simeoni, aliyekuwa mwenye haki na mcha Mungu. Alikuwa akitazamia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu wa Mungu alikuwa juu yake.
LUK 2:26 Roho wa Mungu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Al-Masihi wa Bwana.
LUK 2:27 Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho wa Mungu, alienda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Isa ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Torati,
LUK 2:28 ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:
LUK 2:29 “Bwana Mungu Mwenyezi, kama ulivyoahidi, sasa mruhusu mtumishi wako aende kwa amani.
LUK 2:30 Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,
LUK 2:31 ulioweka tayari machoni pa watu wote,
LUK 2:32 nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”
LUK 2:33 Naye Yusufu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto.
LUK 2:34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake,
LUK 2:35 ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.”
LUK 2:36 Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa.
LUK 2:37 Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na nne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba.
LUK 2:38 Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.
LUK 2:39 Yusufu na Mariamu walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Torati ya Mwenyezi Mungu, walirudi mjini kwao Nasiri huko Galilaya.
LUK 2:40 Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akijawa na hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
LUK 2:41 Kila mwaka Yusufu na Mariamu mama yake Isa walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.
LUK 2:42 Isa alipokuwa na umri wa miaka kumi na mbili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi.
LUK 2:43 Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yusufu na Mariamu mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Isa alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua.
LUK 2:44 Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na rafiki zao.
LUK 2:45 Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta.
LUK 2:46 Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa Torati, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
LUK 2:47 Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa.
LUK 2:48 Yusufu na Mariamu mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”
LUK 2:49 Isa akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”
LUK 2:50 Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.
LUK 2:51 Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nasiri, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote.
LUK 2:52 Naye Isa akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
LUK 3:1 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Yudea, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania akiwa mfalme wa Abilene,
LUK 3:2 nao Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, neno la Mungu likamjia Yahya, mwana wa Zakaria huko jangwani.
LUK 3:3 Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.
LUK 3:4 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia ya Mwenyezi Mungu, yanyoosheni mapito yake.
LUK 3:5 Kila bonde litajazwa, kila mlima na kilima vitashushwa. Njia zilizopinda zitanyooshwa, na zilizoparuza zitasawazishwa.
LUK 3:6 Nao watu wote watauona wokovu wa Mungu.’ ”
LUK 3:7 Yahya akaambia umati ule wa watu waliokuwa wanakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?
LUK 3:8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Ibrahimu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto kutoka mawe haya.
LUK 3:9 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”
LUK 3:10 Umati ule wa watu wakamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”
LUK 3:11 Yahya akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”
LUK 3:12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Mwalimu na sisi inatupasa tufanyeje?”
LUK 3:13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”
LUK 3:14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?” Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”
LUK 3:15 Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yahya angeweza kuwa ndiye Al-Masihi.
LUK 3:16 Yahya akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho wa Mungu na kwa moto.
LUK 3:17 Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”
LUK 3:18 Basi, kwa maonyo mengine mengi Yahya aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema.
LUK 3:19 Lakini Yahya alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya,
LUK 3:20 Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yahya gerezani.
LUK 3:21 Baada ya watu wote kubatizwa, Isa naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka.
LUK 3:22 Roho Mtakatifu wa Mungu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”
LUK 3:23 Isa alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yusufu. Yusufu alikuwa mwana wa Eli,
LUK 3:24 Eli alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi, Lawi alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Yana, Yana alikuwa mwana wa Yusufu,
LUK 3:25 Yusufu alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana wa Amosi, Amosi alikuwa mwana wa Nahumu, Nahumu alikuwa mwana wa Esli, Esli alikuwa mwana wa Nagai,
LUK 3:26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi, Maathi alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana wa Semei, Semei alikuwa mwana wa Yoseki, Yoseki alikuwa mwana wa Yoda,
LUK 3:27 Yoda alikuwa mwana wa Yoanani, Yoanani alikuwa mwana wa Resa, Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli, Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli, Shealtieli alikuwa mwana wa Neri,
LUK 3:28 Neri alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Adi, Adi alikuwa mwana wa Kosamu, Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu, Elmadamu alikuwa mwana wa Eri,
LUK 3:29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua, Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri, Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu, Yorimu alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi,
LUK 3:30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni, Simeoni alikuwa mwana wa Yuda, Yuda alikuwa mwana wa Yusufu, Yusufu alikuwa mwana wa Yonamu, Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu, Eliakimu alikuwa mwana wa Melea,
LUK 3:31 Melea alikuwa mwana wa Mena, Mena alikuwa mwana wa Matatha, Matatha alikuwa mwana wa Nathani, Nathani alikuwa mwana wa Daudi,
LUK 3:32 Daudi alikuwa mwana wa Yese, Yese alikuwa mwana wa Obedi, Obedi alikuwa mwana wa Boazi, Boazi alikuwa mwana wa Salmoni, Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni,
LUK 3:33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu, Aminadabu alikuwa mwana wa Aramu, Aramu alikuwa mwana wa Esromu, Esromu alikuwa mwana wa Peresi, Peresi alikuwa mwana wa Yuda,
LUK 3:34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo, Yakobo alikuwa mwana wa Isaka, Isaka alikuwa mwana wa Ibrahimu, Ibrahimu alikuwa mwana wa Tera, Tera alikuwa mwana wa Nahori,
LUK 3:35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi, Serugi alikuwa mwana wa Ragau, Ragau alikuwa mwana wa Pelegi, Pelegi alikuwa mwana wa Eberi, Eberi alikuwa mwana wa Sala,
LUK 3:36 Sala alikuwa mwana wa Kenani, Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi, Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu, Shemu alikuwa mwana wa Nuhu, Nuhu alikuwa mwana wa Lameki,
LUK 3:37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela, Methusela alikuwa mwana wa Idrisi, Idrisi alikuwa mwana wa Yaredi, Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli, Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani,
LUK 3:38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi, Enoshi alikuwa mwana wa Sethi, Sethi alikuwa mwana wa Adamu, Adamu alikuwa mwana wa Mungu.
LUK 4:1 Isa, akiwa amejaa Roho Mtakatifu wa Mungu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho wa Mungu hadi nyikani,
LUK 4:2 ambako alijaribiwa na ibilisi kwa siku arobaini. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa.
LUK 4:3 Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”
LUK 4:4 Isa akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’ ”
LUK 4:5 Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonesha milki zote za dunia kwa mara moja.
LUK 4:6 Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka.
LUK 4:7 Hivyo ukinisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.”
LUK 4:8 Isa akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ”
LUK 4:9 Kisha ibilisi akampeleka hadi Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa,
LUK 4:10 kwa maana imeandikwa: “ ‘Atakuagizia malaika wake ili wakulinde kwa uangalifu;
LUK 4:11 nao watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”
LUK 4:12 Isa akamjibu, “Imenenwa: ‘Usimjaribu Mwenyezi Mungu, Mungu wako.’ ”
LUK 4:13 Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Isa hadi wakati mwingine ufaao.
LUK 4:14 Kisha Isa akarudi hadi Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho wa Mungu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando.
LUK 4:15 Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao, na kila mmoja akamsifu.
LUK 4:16 Isa akaenda Nasiri, alipolelewa, na siku ya Sabato alienda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome,
LUK 4:17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:
LUK 4:18 “Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi yu juu yangu, kwa sababu amenipaka mafuta kuwahubiria maskini Habari Njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoteswa,
LUK 4:19 na kutangaza mwaka wa Mwenyezi Mungu uliokubalika.”
LUK 4:20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.
LUK 4:21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”
LUK 4:22 Watu wote walimsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yusufu?”
LUK 4:23 Isa akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii: ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’ ”
LUK 4:24 Isa akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika katika mji wake mwenyewe.
LUK 4:25 Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Ilya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima.
LUK 4:26 Hata hivyo Ilya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.
LUK 4:27 Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Al-Yasa, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu.”
LUK 4:28 Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana.
LUK 4:29 Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima ambao mji huo ulikuwa umejengwa juu yake, ili wamtupe chini kutoka mteremko mkali.
LUK 4:30 Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya umati huo wa watu akaenda zake.
LUK 4:31 Kisha Isa akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya, na katika siku ya Sabato akawa anafundisha.
LUK 4:32 Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.
LUK 4:33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu. Naye akapaza sauti kwa nguvu akisema,
LUK 4:34 “Tuache! Tuna nini nawe, Isa Al-Nasiri? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”
LUK 4:35 Basi Isa akamkemea yule pepo mchafu, akamwamuru, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Yule pepo mchafu akamwangusha yule mtu chini mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru.
LUK 4:36 Watu wote wakashangaa, wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Anawaamuru pepo wachafu kwa mamlaka na nguvu, nao wanatoka!”
LUK 4:37 Habari zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu ile.
LUK 4:38 Isa akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani mwa Simoni. Basi huko alimkuta mama mkwe wa Simoni akiwa ameshikwa na homa kali, nao wakamwomba Isa amsaidie.
LUK 4:39 Hivyo Isa akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka mara moja, naye akaanza kuwahudumia.
LUK 4:40 Jua lilipokuwa linatua, watu wakamletea Isa watu wote waliokuwa na maradhi mbalimbali, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, naye akawaponya.
LUK 4:41 Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele, wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Isa akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ndiye Al-Masihi.
LUK 4:42 Kesho yake, kulipopambazuka, Isa alienda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke.
LUK 4:43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”
LUK 4:44 Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Yudea.
LUK 5:1 Siku moja Isa alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti, watu wengi walimsonga ili wapate kusikia neno la Mungu.
LUK 5:2 Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao.
LUK 5:3 Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.
LUK 5:4 Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”
LUK 5:5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”
LUK 5:6 Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika.
LUK 5:7 Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.
LUK 5:8 Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni pa Isa na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!”
LUK 5:9 Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata.
LUK 5:10 Vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia. Ndipo Isa akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.”
LUK 5:11 Hivyo wakasogeza mashua zao hadi ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.
LUK 5:12 Ikawa siku moja Isa alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Isa, alianguka chini hadi uso wake ukagusa ardhi, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, unaweza kunitakasa.”
LUK 5:13 Isa akanyoosha mkono wake, akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Na mara ukoma wake ukatakasika.
LUK 5:14 Isa akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu yeyote, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”
LUK 5:15 Lakini habari zake Isa zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wowote. Makundi makubwa ya watu walikuwa wakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.
LUK 5:16 Lakini mara kwa mara Isa alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.
LUK 5:17 Siku moja Isa alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa Torati, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa.
LUK 5:18 Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Isa.
LUK 5:19 Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya matofali, wakamteremsha yule mgonjwa kwa mkeka wake hadi katikati ya umati ule pale mbele ya Isa.
LUK 5:20 Isa alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”
LUK 5:21 Mafarisayo na wale walimu wa Torati wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
LUK 5:22 Isa akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
LUK 5:23 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’?
LUK 5:24 Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi.” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani mwako.”
LUK 5:25 Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake, akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu.
LUK 5:26 Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”
LUK 5:27 Baada ya haya, Isa alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.”
LUK 5:28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.
LUK 5:29 Kisha Lawi akamfanyia Isa karamu kubwa nyumbani mwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao.
LUK 5:30 Lakini Mafarisayo na walimu wa Torati waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Isa, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”
LUK 5:31 Isa akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa.
LUK 5:32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”
LUK 5:33 Wakamwambia Isa, “Wanafunzi wa Yahya na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”
LUK 5:34 Isa akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati yuko pamoja nao?
LUK 5:35 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.”
LUK 5:36 Isa akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, atakuwa amechana nguo mpya, na kile kiraka hakitalingana na ile nguo iliyochakaa.
LUK 5:37 Hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo yote itamwagika.
LUK 5:38 Divai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya.
LUK 5:39 Wala hakuna mtu anayependelea divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani, bali husema, ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’ ”
LUK 6:1 Ikawa siku moja ya Sabato Isa alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, nao wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake.
LUK 6:2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo yasiyo halali kufanywa siku ya Sabato?”
LUK 6:3 Isa akawajibu, “Je, ninyi hamjasoma alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa?
LUK 6:4 Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua na kuila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani tu. Naye pia akawapa wenzake.”
LUK 6:5 Kisha Isa akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
LUK 6:6 Ikawa siku nyingine ya Sabato, Isa aliingia ndani ya sinagogi na akawa anafundisha. Huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza.
LUK 6:7 Mafarisayo na walimu wa Torati walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Isa. Kwa hivyo wakawa wanamwangalia sana ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato.
LUK 6:8 Lakini Isa alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Inuka usimame mbele ya watu wote.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote.
LUK 6:9 Ndipo Isa akawaambia wale walimu wa Torati na Mafarisayo, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato? Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuyaangamiza?”
LUK 6:10 Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako!” Akaunyoosha, na mkono wake ukawa umeponywa kabisa.
LUK 6:11 Wale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao ni nini watakachomtendea Isa.
LUK 6:12 Ikawa katika siku hizo Isa alienda mlimani kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu.
LUK 6:13 Kulipopambazuka, akawaita wanafunzi wake, naye akachagua kumi na wawili, ambao pia aliwaita mitume:
LUK 6:14 Simoni (aliyemwita Petro) na Andrea nduguye, Yakobo, Yohana, Filipo, Bartholomayo,
LUK 6:15 Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni aliyeitwa Zelote,
LUK 6:16 Yuda mwana wa Yakobo, na Yuda Iskariote, aliyekuwa msaliti.
LUK 6:17 Akashuka pamoja nao, akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Yudea, kutoka Yerusalemu, na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni.
LUK 6:18 Walikuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya.
LUK 6:19 Watu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote.
LUK 6:20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema: “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.
LUK 6:21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashibishwa. Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa, kwa sababu mtacheka.
LUK 6:22 Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia, watakapowatenga na kuwatukana na kulikataa jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu.
LUK 6:23 “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.
LUK 6:24 “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.
LUK 6:25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa, maana mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, maana mtaomboleza na kulia.
LUK 6:26 Ole wenu watu watakapowasifu, kwani ndivyo baba zao walivyowasifu manabii wa uongo.
LUK 6:27 “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia.
LUK 6:28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya.
LUK 6:29 Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyang’anya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia.
LUK 6:30 Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie.
LUK 6:31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.
LUK 6:32 “Mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda.
LUK 6:33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo.
LUK 6:34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote.
LUK 6:35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu.
LUK 6:36 Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.
LUK 6:37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa.
LUK 6:38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”
LUK 6:39 Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni?
LUK 6:40 Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.
LUK 6:41 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe?
LUK 6:42 Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.
LUK 6:43 “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri.
LUK 6:44 Kila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba, wala zabibu kwenye michongoma.
LUK 6:45 Vivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo maovu kutoka hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake.
LUK 6:46 “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia?
LUK 6:47 Nitawaonesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda.
LUK 6:48 Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, mkondo wa maji ukaipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri.
LUK 6:49 Lakini yeye anayesikia maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”
LUK 7:1 Baada ya Isa kumaliza kusema haya yote kwa watu waliokuwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu.
LUK 7:2 Mtumishi wa jemadari mmoja Mrumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu na kufa.
LUK 7:3 Jemadari huyo aliposikia habari za Isa, aliwatuma wazee wa Wayahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari.
LUK 7:4 Wale wazee walipofika kwa Isa, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili,
LUK 7:5 kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.”
LUK 7:6 Hivyo Isa akaongozana nao. Lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Isa, “Bwana, usijisumbue, kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu.
LUK 7:7 Ndiyo maana sikujiona hata ninastahili kuja kwako wewe. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.
LUK 7:8 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
LUK 7:9 Isa aliposikia maneno haya, alishangazwa naye sana. Akageukia umati ule wa watu waliokuwa wanamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.”
LUK 7:10 Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Isa waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.
LUK 7:11 Baadaye kidogo, Isa alienda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walienda pamoja naye.
LUK 7:12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mwanamke.
LUK 7:13 Bwana Isa alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”
LUK 7:14 Kisha akalikaribia jeneza, akaligusa. Nao wale waliokuwa wamelibeba wakasimama. Akasema, “Kijana, nakuambia, inuka.”
LUK 7:15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Isa akamkabidhi kwa mama yake.
LUK 7:16 Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.”
LUK 7:17 Habari hizi za mambo aliyoyafanya Isa zikaenea Yudea yote na sehemu zote za jirani.
LUK 7:18 Wanafunzi wa Yahya wakamweleza Yahya mambo haya yote. Hivyo Yahya akawaita wanafunzi wake wawili
LUK 7:19 na kuwatuma kwa Bwana Isa ili kumuuliza, “Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”
LUK 7:20 Wale watu walipofika kwa Isa wakamwambia, “Yahya ametutuma tukuulize, ‘Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumtazamie mwingine?’ ”
LUK 7:21 Wakati huo huo, Isa aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, na pia akawafungua vipofu wengi macho wakapata kuona.
LUK 7:22 Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yahya yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema.
LUK 7:23 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”
LUK 7:24 Wajumbe wa Yahya walipoondoka, Isa akaanza kusema na umati wa watu kuhusu Yahya. Akawauliza, “Mlipoenda kule nyikani, mlienda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?
LUK 7:25 Kama sivyo, mlienda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha! Watu wanaovaa mavazi ya kifahari na kuishi maisha ya anasa wako katika majumba ya kifalme.
LUK 7:26 Lakini mlienda kuona nini? Mlienda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.
LUK 7:27 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa: “ ‘Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako.’
LUK 7:28 Nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hakuna aliye mkuu kuliko Yahya. Lakini yeye aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yahya.”
LUK 7:29 (Watu wote, hata watoza ushuru, waliposikia maneno ya Isa, walikubali kwamba mpango wa Mungu ni haki, maana walikuwa wamebatizwa na Yahya.
LUK 7:30 Lakini Mafarisayo na wataalamu wa Torati walikataa mpango wa Mungu kwao kwa kutokubali kubatizwa na Yahya.)
LUK 7:31 Isa akawauliza, “Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini?
LUK 7:32 Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao, wakisema: “ ‘Tuliwapigia filimbi, lakini hamkucheza; tuliwaimbia nyimbo za maombolezo, lakini hamkulia.’
LUK 7:33 Kwa maana Yahya alikuja, alikuwa hali mkate wala hanywi divai, nanyi mkasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’
LUK 7:34 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’
LUK 7:35 Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.”
LUK 7:36 Basi Farisayo mmoja alimwalika Isa kwake ale chakula. Hivyo Isa akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kuketi mezani.
LUK 7:37 Palikuwa na mwanamke mmoja katika mji ule aliyekuwa mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Isa alikuwa akila chakula nyumbani mwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato.
LUK 7:38 Yule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Isa akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato.
LUK 7:39 Yule Farisayo aliyemwalika Isa alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa, na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani, na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.”
LUK 7:40 Isa akamjibu, “Simoni, nina jambo la kukuambia.” Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.”
LUK 7:41 “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari mia tano na mwingine dinari hamsini.
LUK 7:42 Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda zaidi yule aliyewasamehe?”
LUK 7:43 Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.” Naye Isa akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.”
LUK 7:44 Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake, na kunifuta kwa nywele zake.
LUK 7:45 Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia.
LUK 7:46 Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato.
LUK 7:47 Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”
LUK 7:48 Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”
LUK 7:49 Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”
LUK 7:50 Isa akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”
LUK 8:1 Baada ya haya Isa alienda, akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri Injili ya ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye,
LUK 8:2 pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa. Miongoni mwao alikuwa Mariamu Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba;
LUK 8:3 Yoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode; Susana; na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali yao.
LUK 8:4 Umati mkubwa wa watu walipokuwa wakikusanyika, nao watu walikuwa wakimjia Isa kutoka kila mji, akawaambia mfano huu:
LUK 8:5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila.
LUK 8:6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu.
LUK 8:7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea.
LUK 8:8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.” Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
LUK 8:9 Wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo.
LUK 8:10 Naye akasema, “Ninyi mmepewa ujuzi wa siri za ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili, “ ‘ingawa wanatazama, wasione; ingawa wanasikiliza, wasielewe.’
LUK 8:11 “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu.
LUK 8:12 Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka.
LUK 8:13 Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani.
LUK 8:14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.
LUK 8:15 Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.
LUK 8:16 “Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale wanaoingia ndani waone mwanga.
LUK 8:17 Kwa maana hakuna jambo lolote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lolote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi.
LUK 8:18 Kwa hiyo, kuweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa zaidi. Lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho atanyang’anywa.”
LUK 8:19 Wakati mmoja mama yake Isa na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu.
LUK 8:20 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”
LUK 8:21 Isa akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulifanya.”
LUK 8:22 Siku moja Isa alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni hadi ng’ambo ya ziwa.” Nao wakaondoka.
LUK 8:23 Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.
LUK 8:24 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!” Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari.
LUK 8:25 Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?” Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?”
LUK 8:26 Basi wakafika katika nchi ya Wagerasi, iliyo upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya.
LUK 8:27 Isa aliposhuka kutoka mashua na kukanyaga ufuoni, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali aliishi makaburini.
LUK 8:28 Alipomwona Isa, alipaza sauti, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!”
LUK 8:29 Wakati huo Isa alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa, na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi, alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.
LUK 8:30 Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Legioni,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno.
LUK 8:31 Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda katika Shimo.
LUK 8:32 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Isa awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu.
LUK 8:33 Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremkia gengeni kwa kasi, likatumbukia ziwani na kuzama.
LUK 8:34 Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani.
LUK 8:35 Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Isa, wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Isa, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa.
LUK 8:36 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa.
LUK 8:37 Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Isa aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua, akaondoka zake.
LUK 8:38 Yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Isa afuatane naye, lakini Isa akamuaga, akamwambia:
LUK 8:39 “Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu ambayo Isa alimtendea.
LUK 8:40 Basi Isa aliporudi, umati mkubwa wa watu wakampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea.
LUK 8:41 Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Isa, akimwomba afike nyumbani mwake,
LUK 8:42 kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na mbili, alikuwa anakufa. Isa alipokuwa akienda, umati wa watu wakamsonga sana.
LUK 8:43 Palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, [na alikuwa amegharimia mali yake yote kwa matibabu] lakini hakuna yeyote aliyeweza kumponya.
LUK 8:44 Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Isa na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.
LUK 8:45 Isa akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, umati huu wa watu wanakusonga na kukusukuma kila upande.”
LUK 8:46 Lakini Isa akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”
LUK 8:47 Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Isa. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara moja.
LUK 8:48 Basi Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”
LUK 8:49 Isa alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani mwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”
LUK 8:50 Isa aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”
LUK 8:51 Walipofika nyumbani mwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yohana na Yakobo, pamoja na baba na mama wa yule binti.
LUK 8:52 Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Isa akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”
LUK 8:53 Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa.
LUK 8:54 Isa akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!”
LUK 8:55 Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula.
LUK 8:56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote kuhusu yale yaliyotukia.
LUK 9:1 Isa kisha akawaita wale kumi na wawili pamoja, akawapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote,
LUK 9:2 kisha akawatuma waende wakahubiri ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.
LUK 9:3 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote safarini: sio fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, hata msichukue kanzu ya ziada.
LUK 9:4 Katika nyumba yoyote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo.
LUK 9:5 Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”
LUK 9:6 Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
LUK 9:7 Basi Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za yote yaliyotendeka. Naye akafadhaika, kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yahya amefufuliwa kutoka kwa wafu.
LUK 9:8 Wengine wakasema Ilya amewatokea, na wengine kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka.
LUK 9:9 Herode akasema, “Yahya nilimkata kichwa. Lakini ni nani huyu ninayesikia mambo kama haya kumhusu?” Akatamani sana kumwona.
LUK 9:10 Mitume wake waliporudi, wakamweleza Isa yote waliyofanya. Kisha akaenda nao faraghani hadi mji uitwao Bethsaida.
LUK 9:11 Lakini umati wa watu wakafahamu alikoenda, wakamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.
LUK 9:12 Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Isa na kumwambia, “Waage watu hawa ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”
LUK 9:13 Isa akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.” Nao wakajibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote.”
LUK 9:14 (Walikuwepo wanaume wapatao elfu tano.) Isa akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni katika vikundi vya watu hamsini hamsini.”
LUK 9:15 Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote.
LUK 9:16 Isa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu.
LUK 9:17 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.
LUK 9:18 Siku moja Isa alipokuwa akiomba faraghani, nao wanafunzi wake wakiwa pamoja naye, akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
LUK 9:19 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yahya, wengine husema ni Ilya, na wengine husema kwamba ni mmoja wa manabii wa kale amefufuka.”
LUK 9:20 Kisha akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi wa Mungu.”
LUK 9:21 Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote jambo hilo.
LUK 9:22 Isa akasema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa Torati, na itampasa auawe, lakini siku ya tatu kufufuliwa kutoka mauti.”
LUK 9:23 Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate.
LUK 9:24 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa.
LUK 9:25 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake?
LUK 9:26 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba, pamoja na malaika watakatifu.
LUK 9:27 “Amin, nawaambia, wako baadhi ya watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona ufalme wa Mungu.”
LUK 9:28 Yapata siku nane baada ya Isa kusema hayo, aliwachukua Petro, Yohana na Yakobo, akaenda nao mlimani kuomba.
LUK 9:29 Alipokuwa akiomba, sura ya uso wake ikabadilika, nayo mavazi yake yakametameta kama miali ya radi.
LUK 9:30 Ghafula wakawaona watu wawili, ndio Musa na Ilya, wakizungumza naye.
LUK 9:31 Walionekana katika utukufu wakizungumza na Isa kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu.
LUK 9:32 Petro na wenzake walikuwa wamelala usingizi mzito. Walipoamka, wakaona utukufu wa Isa na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.
LUK 9:33 Musa na Ilya walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Isa, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.” Lakini Petro hakujua alichosema.
LUK 9:34 Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu, likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu.
LUK 9:35 Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, niliyemchagua. Msikieni yeye.”
LUK 9:36 Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Isa akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu yeyote yale waliyokuwa wameyaona.
LUK 9:37 Kesho yake waliposhuka kutoka mlimani, alikutana na umati mkubwa wa watu.
LUK 9:38 Mtu mmoja katika umati ule akapaza sauti, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, kwani ndiye mtoto wangu wa pekee.
LUK 9:39 Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige mayowe, kisha humwangusha na kumtia kifafa hata akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana, na hamwachi ila mara chache.
LUK 9:40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
LUK 9:41 Isa akawajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia hadi lini? Mlete mwanao hapa.”
LUK 9:42 Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Isa akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, na akamrudisha kwa baba yake.
LUK 9:43 Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu. Wakati bado watu walikuwa wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Isa, yeye akawaambia wanafunzi wake:
LUK 9:44 “Sikilizeni kwa makini haya nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu.”
LUK 9:45 Lakini wao hawakuelewa alimaanisha nini. Maana ya maneno hayo ilifichika kwao, hivyo hawakuyaelewa, nao wakaogopa kumuuliza maana yake.
LUK 9:46 Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote.
LUK 9:47 Lakini Isa akayatambua mawazo yao, naye akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake.
LUK 9:48 Kisha akawaambia, “Yeyote amkaribishaye mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi, na yeyote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma. Kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”
LUK 9:49 Yohana akasema, “Bwana, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamzuia, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
LUK 9:50 Isa akasema, “Msimzuie, kwa sababu yeyote ambaye si kinyume nanyi, yu upande wenu.”
LUK 9:51 Wakati ulipokaribia wa yeye kuchukuliwa mbinguni, alikaza uso wake kwenda Yerusalemu.
LUK 9:52 Akatuma watu wamtangulie, nao wakaenda katika kijiji kimoja cha Samaria kumwandalia kila kitu;
LUK 9:53 lakini watu wa kijiji kile hawakumkaribisha kwa sababu alikuwa anaenda zake Yerusalemu.
LUK 9:54 Wanafunzi wake, yaani Yakobo na Yohana, walipoona hayo, wakasema: “Bwana Isa, unataka tuagize moto kutoka mbinguni ili uwaangamize?”
LUK 9:55 Isa akageuka na kuwakemea.
LUK 9:56 Naye Isa na wanafunzi wake wakaenda kijiji kingine.
LUK 9:57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Isa, “Nitakufuata popote utakakoenda.”
LUK 9:58 Isa akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
LUK 9:59 Isa akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.” Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
LUK 9:60 Isa akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze ufalme wa Mungu.”
LUK 9:61 Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikawaage jamaa zangu.”
LUK 9:62 Isa akamwambia, “Mtu yeyote ashikaye jembe kulima kisha akatazama nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu.”
LUK 10:1 Baada ya hayo, Bwana Isa akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye.
LUK 10:2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.
LUK 10:3 Nendeni! Tazama ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa-mwitu.
LUK 10:4 Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.
LUK 10:5 “Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’
LUK 10:6 Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia.
LUK 10:7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.
LUK 10:8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu,
LUK 10:9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umewakaribia.’
LUK 10:10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme:
LUK 10:11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakung’uta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’
LUK 10:12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.
LUK 10:13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.
LUK 10:14 Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi.
LUK 10:15 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha! Utashushwa hadi Kuzimu.
LUK 10:16 “Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”
LUK 10:17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana Isa, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”
LUK 10:18 Isa akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama radi.
LUK 10:19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru.
LUK 10:20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”
LUK 10:21 Wakati huo Isa akashangilia katika Roho wa Mungu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
LUK 10:22 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”
LUK 10:23 Basi Isa akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona.
LUK 10:24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.”
LUK 10:25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa Torati alisimama ili kumjaribu Isa, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
LUK 10:26 Isa akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?”
LUK 10:27 Akajibu, “ ‘Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”
LUK 10:28 Isa akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”
LUK 10:29 Lakini yule mtaalamu wa Torati, akitaka kujionesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Isa, “Jirani yangu ni nani?”
LUK 10:30 Isa akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa.
LUK 10:31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.
LUK 10:32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.
LUK 10:33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia.
LUK 10:34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka hadi kwenye nyumba ya wageni na kumtunza.
LUK 10:35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’
LUK 10:36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi?”
LUK 10:37 Yule mtaalamu wa Torati akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.” Ndipo Isa akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”
LUK 10:38 Ikawa Isa na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani mwake.
LUK 10:39 Martha alikuwa na dada yake aliyeitwa Mariamu, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana Isa akisikiliza yale alikuwa akisema.
LUK 10:40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Isa na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba dada yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”
LUK 10:41 Lakini Bwana Isa akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi?
LUK 10:42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Mariamu amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”
LUK 11:1 Siku moja, Isa alikuwa mahali fulani akiomba. Alipomaliza kuomba, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana Isa, tufundishe kuomba, kama vile Yahya alivyowafundisha wanafunzi wake.”
LUK 11:2 Akawaambia, “Mnapoomba, semeni: “ ‘Baba yetu [uliye mbinguni], jina lako litukuzwe, ufalme wako uje. [ Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.]
LUK 11:3 Utupatie kila siku riziki yetu.
LUK 11:4 Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea. Wala usitutie majaribuni [bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu].’ ”
LUK 11:5 Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu,
LUK 11:6 kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa ale.’
LUK 11:7 “Kisha yule aliye ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’
LUK 11:8 Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.
LUK 11:9 “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.
LUK 11:10 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
LUK 11:11 “Je, kuna baba yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake?
LUK 11:12 Au mtoto akimwomba yai atampa nge?
LUK 11:13 Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wa Mungu wale wamwombao!”
LUK 11:14 Basi Isa alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu wakashangaa.
LUK 11:15 Lakini wengine wakasema, “Anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, yule mkuu wa pepo wachafu wote.”
LUK 11:16 Wengine ili kumjaribu wakataka awaoneshe ishara kutoka mbinguni.
LUK 11:17 Isa akajua mawazo yao, naye akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Nayo nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe itaanguka.
LUK 11:18 Kama Shetani amegawanyika mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Nawaambia haya kwa sababu ninyi mnadai ya kuwa mimi ninatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli.
LUK 11:19 Kama mimi natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, wafuasi wenu nao je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.
LUK 11:20 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umewajia.
LUK 11:21 “Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha anapoilinda nyumba yake, mali yake iko salama.
LUK 11:22 Lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yeye humnyang’anya silaha zake zote alizozitegemea, na kuchukua nyara.
LUK 11:23 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.
LUK 11:24 “Pepo mchafu anapomtoka mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’
LUK 11:25 Naye anaporudi na kuikuta ile nyumba imefagiwa na kupangwa vizuri,
LUK 11:26 ndipo huenda na kuchukua pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza.”
LUK 11:27 Ikawa Isa alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya umati ule wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”
LUK 11:28 Isa akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”
LUK 11:29 Umati wa watu walipokuwa wanazidi kuongezeka, Isa akaendelea kusema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.
LUK 11:30 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki.
LUK 11:31 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kuwahukumu watu wa kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Sulemani. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.
LUK 11:32 Siku ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.
LUK 11:33 “Hakuna mtu yeyote awashaye taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunikia chini ya bakuli. Badala yake huiweka juu ya kinara chake, ili watu wote wanaoingia waone nuru.
LUK 11:34 Jicho lako ni taa ya mwili wako. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote pia umejaa nuru. Lakini kama jicho ni bovu, mwili wako wote pia umejaa giza.
LUK 11:35 Kwa hiyo, hakikisha kwamba nuru iliyo ndani yako isiwe giza.
LUK 11:36 Basi ikiwa mwili wako wote umejaa nuru, bila sehemu yake yoyote kuwa gizani, basi utakuwa na nuru kama vile taa ikuangazavyo kwa nuru yake.”
LUK 11:37 Isa alipomaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika nyumbani mwake kwa chakula. Isa akaingia na kuketi katika sehemu yake mezani.
LUK 11:38 Yule Farisayo akashangaa kwamba Isa hakunawa kwanza kabla ya kula.
LUK 11:39 Ndipo Bwana Isa akamwambia, “Sasa, enyi Mafarisayo mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyang’anyi na uovu.
LUK 11:40 Enyi wapumbavu! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza nje ndiye alitengeneza na ndani pia?
LUK 11:41 Basi toeni sadaka ya vile mlivyo navyo, na tazama, vitu vyote vitakuwa safi kwenu.
LUK 11:42 “Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kufanya haya ya pili bila kupuuza hayo ya kwanza.
LUK 11:43 “Ole wenu Mafarisayo, kwa sababu ninyi mnapenda kukalia viti vya mbele katika masinagogi, na kusalimiwa kwa heshima masokoni.
LUK 11:44 “Ole wenu, kwa sababu ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.”
LUK 11:45 Mtaalamu mmoja wa Torati akamjibu, akasema, “Mwalimu, unaposema mambo haya, unatutukana na sisi pia.”
LUK 11:46 Isa akamjibu, “Nanyi wataalamu wa Torati, ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja kuwasaidia.
LUK 11:47 “Ole wenu, kwa sababu ninyi mnajenga makaburi ya manabii waliouawa na baba zenu.
LUK 11:48 Hivyo ninyi mwashuhudia na mnathibitisha kile baba zenu walichofanya. Wao waliwaua manabii, nanyi mnawajengea makaburi.
LUK 11:49 Kwa sababu ya jambo hili, Mungu katika hekima yake alisema, ‘Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na wengine watawatesa.’
LUK 11:50 Kwa hiyo kizazi hiki kitawajibika kwa ajili ya damu ya manabii iliyomwagwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu,
LUK 11:51 tangu damu ya Habili hadi damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, nawaambia, kizazi hiki kitawajibika kwa haya yote.
LUK 11:52 “Ole wenu ninyi wataalamu wa Torati, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.”
LUK 11:53 Isa alipoondoka huko, walimu wa Torati na Mafarisayo wakaanza kumpinga vikali na kumsonga kwa maswali,
LUK 11:54 wakivizia kumkamata kwa kitu atakachosema ili wamshtaki.
LUK 12:1 Wakati huo, umati mkubwa wa watu maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Isa akaanza kuzungumza kwanza na wanafunzi wake, akawaambia: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki wao.
LUK 12:2 Hakuna jambo lolote lililositirika ambalo halitafunuliwa, au lililofichwa ambalo halitajulikana.
LUK 12:3 Kwa hiyo, lolote mlilosema gizani litasikiwa nuruni. Na kile mlichonong’ona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa.
LUK 12:4 “Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya lolote zaidi.
LUK 12:5 Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo!
LUK 12:6 Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao.
LUK 12:7 Naam, hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
LUK 12:8 “Ninawaambia kwamba yeyote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu.
LUK 12:9 Lakini yeye atakayenikana mimi mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu.
LUK 12:10 Naye kila atakayenena neno baya dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote atakayemkufuru Roho Mtakatifu wa Mungu hatasamehewa.
LUK 12:11 “Watakapowapeleka katika masinagogi, na mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema.
LUK 12:12 Kwa maana Roho wa Mungu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”
LUK 12:13 Mtu mmoja katika umati ule wa watu akamwambia Isa, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.”
LUK 12:14 Lakini Isa akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?”
LUK 12:15 Ndipo Isa akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”
LUK 12:16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana.
LUK 12:17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’
LUK 12:18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa maghala yangu ya nafaka na kujenga mengine makubwa zaidi na nihifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu.
LUK 12:19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’
LUK 12:20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’
LUK 12:21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”
LUK 12:22 Kisha Isa akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini.
LUK 12:23 Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi.
LUK 12:24 Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani kuliko ndege!
LUK 12:25 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?
LUK 12:26 Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?
LUK 12:27 “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua.
LUK 12:28 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba!
LUK 12:29 Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya.
LUK 12:30 Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote.
LUK 12:31 Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia.
LUK 12:32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi ufalme.
LUK 12:33 Uzeni mali yenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu.
LUK 12:34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.
LUK 12:35 “Kuweni tayari mkiwa mmevikwa kwa ajili ya huduma na taa zenu zikiwa zinawaka,
LUK 12:36 kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka karamu ya arusi, ili ajapo na kubisha mlango waweze kumfungulia mara moja.
LUK 12:37 Heri wale watumishi ambao bwana wao atakapokuja atawakuta wakiwa wanakesha. Amin, nawaambia, atajifunga mkanda wake na kuwaketisha ili wale, naye atakuja na kuwahudumia.
LUK 12:38 Itakuwa heri kwa watumwa hao ikiwa bwana wao atakapokuja atawakuta wamekesha hata kama atakuja usiku wa manane, au karibu na mapambazuko.
LUK 12:39 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua saa mwizi atakuja, hangeiacha nyumba yake kuvunjwa.
LUK 12:40 Ninyi nanyi hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.”
LUK 12:41 Ndipo Petro akamuuliza, “Bwana Isa, mfano huu unatuambia sisi peke yetu au watu wote?”
LUK 12:42 Isa akamjibu, “Ni yupi basi wakili mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamfanya msimamizi juu ya watumishi wake wote, ili awape watumishi wengine chakula chao wakati unaofaa?
LUK 12:43 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.
LUK 12:44 Amin nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote.
LUK 12:45 Lakini kama yule mtumishi atasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga wale watumishi, wa kiume na wa kike, na kula na kunywa na kulewa.
LUK 12:46 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wale wasioamini.
LUK 12:47 “Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi.
LUK 12:48 Lakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi.
LUK 12:49 “Nimekuja kuleta moto duniani; laiti kama ungekuwa tayari umewashwa!
LUK 12:50 Lakini ninao ubatizo ambao lazima nibatizwe, nayo dhiki yangu ni kuu hadi ubatizo huo ukamilike!
LUK 12:51 Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? La, nawaambia sivyo, nimekuja kuleta mafarakano.
LUK 12:52 Kuanzia sasa, kutakuwa na watu watano katika nyumba moja, watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu.
LUK 12:53 Watafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, naye mama mkwe dhidi ya mkwewe na mkwe dhidi ya mama mkwe wake.”
LUK 12:54 Pia Isa akaambia umati ule wa watu, “Mwonapo wingu likitokea magharibi, mara mwasema, ‘Mvua itanyesha,’ nayo hunyesha.
LUK 12:55 Nanyi mwonapo upepo wa kusini ukivuma, ninyi husema, ‘Kutakuwa na joto,’ na huwa hivyo.
LUK 12:56 Enyi wanafiki! Mnajua jinsi ya kutambua kuonekana kwa dunia na anga. Inakuwaje basi kwamba mnashindwa kutambua wakati huu wa sasa?
LUK 12:57 “Kwa nini hamwamui wenyewe lililo haki?
LUK 12:58 Ukiwa njiani na mshtaki wako kwenda kwa hakimu, jitahidi kupatana naye mkiwa njiani. La sivyo, atakupeleka kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa afisa, naye afisa atakutupa gerezani.
LUK 12:59 Nakuambia, hutatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.”
LUK 13:1 Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Isa habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua, na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa.
LUK 13:2 Isa akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo kama hicho walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote?
LUK 13:3 La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo.
LUK 13:4 Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu: mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote walioishi Yerusalemu?
LUK 13:5 Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”
LUK 13:6 Kisha Isa akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja.
LUK 13:7 Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’
LUK 13:8 “Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uuache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea.
LUK 13:9 Nao ukizaa matunda mwaka ujao, vyema! La sivyo, uukate.’ ”
LUK 13:10 Basi Isa alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato.
LUK 13:11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na nane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima.
LUK 13:12 Isa alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.”
LUK 13:13 Isa alipomwekea mikono yake, akasimama wima mara moja, akaanza kumtukuza Mungu.
LUK 13:14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Isa alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia umati ule wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”
LUK 13:15 Lakini Bwana Isa akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ng’ombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato?
LUK 13:16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti ya Ibrahimu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na nane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”
LUK 13:17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.
LUK 13:18 Kisha Isa akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini?
LUK 13:19 Umefanana na punje ya haradali ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti, nao ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”
LUK 13:20 Isa akauliza tena, “Nitaufananisha ufalme wa Mungu na nini?
LUK 13:21 Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga hadi wote ukaumuka.”
LUK 13:22 Isa akapita katika miji na vijiji, akifundisha wakati alisafiri kwenda Yerusalemu.
LUK 13:23 Mtu mmoja akamuuliza, “Bwana Isa, ni watu wachache tu watakaookolewa?” Isa akawaambia,
LUK 13:24 “Jitahidini sana kuingia kupitia mlango mwembamba, kwa maana nawaambia wengi watajaribu kuingia, lakini hawataweza.
LUK 13:25 Mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkibisha mlango na kusema, ‘Bwana! Tufungulie mlango!’ “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako.’
LUK 13:26 “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’
LUK 13:27 “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
LUK 13:28 “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapowaona Ibrahimu, Isaka, Yakobo na manabii wote wakiwa katika ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje.
LUK 13:29 Watu watatoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika ufalme wa Mungu.
LUK 13:30 Tazama, kuna walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”
LUK 13:31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Isa na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”
LUK 13:32 Isa akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’
LUK 13:33 Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa: kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.
LUK 13:34 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!
LUK 13:35 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena hadi wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Mwenyezi Mungu.’ ”
LUK 14:1 Siku moja ya Sabato, Isa alipoenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo, watu walikuwa wakimchunguza kwa makini.
LUK 14:2 Hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili.
LUK 14:3 Isa akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa Torati, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?”
LUK 14:4 Wakakaa kimya. Hivyo Isa akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.
LUK 14:5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ng’ombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?”
LUK 14:6 Nao hawakuwa na la kusema.
LUK 14:7 Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu:
LUK 14:8 “Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe.
LUK 14:9 Mkifanya hivyo, yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa.
LUK 14:10 Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule aliyekualika atakapokuona, atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote.
LUK 14:11 Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”
LUK 14:12 Kisha Isa akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umepata malipo.
LUK 14:13 Bali unapoandaa karamu, waalike maskini, vilema, viwete na vipofu,
LUK 14:14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
LUK 14:15 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Isa, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya ufalme wa Mungu!”
LUK 14:16 Isa akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi.
LUK 14:17 Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’
LUK 14:18 “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’
LUK 14:19 “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ng’ombe wa kulimia, nami ninaenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’
LUK 14:20 “Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’
LUK 14:21 “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’
LUK 14:22 “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’
LUK 14:23 “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyo nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ijae.
LUK 14:24 Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”
LUK 14:25 Umati mkubwa wa watu walikuwa wakisafiri pamoja na Isa, naye akageuka, akawaambia,
LUK 14:26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe.
LUK 14:27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
LUK 14:28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha?
LUK 14:29 La sivyo, baada ya kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki,
LUK 14:30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
LUK 14:31 “Au je, mfalme fulani akienda vita na mfalme mwingine, si yeye huketi chini kwanza na kufikiri: je, akiwa na jeshi la watu elfu kumi, ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu elfu ishirini?
LUK 14:32 Ikiwa hawezi, basi yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma wajumbe na kuomba masharti ya amani.
LUK 14:33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
LUK 14:34 “Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, itafanywaje ili iweze kukolea tena?
LUK 14:35 Haifai ardhi wala kwa lundo la mbolea, bali hutupwa nje. “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
LUK 15:1 Basi watoza ushuru na wenye dhambi wote walikuwa wanakusanyika ili wapate kumsikiliza Isa.
LUK 15:2 Lakini Mafarisayo na walimu wa Torati wakanung’unika wakisema, “Huyu mtu anawakaribisha wenye dhambi na kula nao.”
LUK 15:3 Ndipo Isa akawaambia mfano huu:
LUK 15:4 “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja, naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea hadi ampate?
LUK 15:5 Naye akishampata, humbeba mabegani mwake kwa furaha
LUK 15:6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani, na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimempata kondoo wangu aliyepotea.’
LUK 15:7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.
LUK 15:8 “Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii hadi aipate?
LUK 15:9 Baada ya kuipata, yeye huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’
LUK 15:10 Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”
LUK 15:11 Isa akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili.
LUK 15:12 Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.
LUK 15:13 “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali, na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa.
LUK 15:14 Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana chochote.
LUK 15:15 Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na raia mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.
LUK 15:16 Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa chochote.
LUK 15:17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa!
LUK 15:18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako.
LUK 15:19 Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’
LUK 15:20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake. “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.
LUK 15:21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’
LUK 15:22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake.
LUK 15:23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi.
LUK 15:24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kusherehekea.
LUK 15:25 “Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza.
LUK 15:26 Akamwita mmoja wa watumishi na kumuuliza maana ya mambo yale.
LUK 15:27 Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’
LUK 15:28 “Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumsihi.
LUK 15:29 Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana-mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu.
LUK 15:30 Lakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’
LUK 15:31 “Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako.
LUK 15:32 Lakini ilitubidi tufurahi na kushangilia kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa na sasa yu hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’ ”
LUK 16:1 Isa akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Huyo msimamizi alishitakiwa kwake kwamba alikuwa akitapanya mali ya tajiri yake.
LUK 16:2 Hivyo huyo tajiri akamwita na kumuuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’
LUK 16:3 “Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba.
LUK 16:4 Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani mwao.’
LUK 16:5 “Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamuuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’
LUK 16:6 “Akajibu, ‘Vipimo mia moja vya mafuta ya mizeituni.’ “Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike vipimo hamsini.’
LUK 16:7 “Kisha akamuuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’ “Akajibu, ‘Vipimo elfu moja vya ngano.’ “Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, uandike vipimo mia nane!’
LUK 16:8 “Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru.
LUK 16:9 Nawaambia, tumieni mali ya dunia kujipatia rafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele.
LUK 16:10 “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu katika mambo makubwa. Na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa.
LUK 16:11 Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli?
LUK 16:12 Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
LUK 16:13 “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”
LUK 16:14 Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau.
LUK 16:15 Isa akawaambia, “Ninyi mnajionesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.
LUK 16:16 “Torati na Manabii vilihubiriwa hadi kuja kwa Yahya. Tangu wakati huo Injili ya ufalme wa Mungu inahubiriwa, na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu.
LUK 16:17 Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Torati.
LUK 16:18 “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kumwoa mwanamke mwingine anazini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa anazini.
LUK 16:19 “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku.
LUK 16:20 Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima.
LUK 16:21 Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.
LUK 16:22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa.
LUK 16:23 Kule Kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Ibrahimu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa kifuani mwake.
LUK 16:24 Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’
LUK 16:25 “Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu.
LUK 16:26 Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’
LUK 16:27 “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani mwa baba yangu,
LUK 16:28 maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’
LUK 16:29 “Ibrahimu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Musa na Manabii, wawasikilize hao.’
LUK 16:30 “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Ibrahimu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’
LUK 16:31 “Ibrahimu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Musa na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”
LUK 17:1 Isa akawaambia wanafunzi wake, “Mambo yanayosababisha watu watende dhambi hayana budi kutukia. Lakini ole wake mtu yule anayeyasababisha.
LUK 17:2 Ingekuwa heri kama mtu huyo angefungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa baharini, kuliko kumsababisha mmoja wa hawa wadogo kutenda dhambi.
LUK 17:3 Kwa hiyo, jilindeni. “Ndugu yako akikukosea, mwonye; naye akitubu, msamehe.
LUK 17:4 Akikukosea mara saba kwa siku moja, na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”
LUK 17:5 Mitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
LUK 17:6 Bwana akawajibu, “Kama mngekuwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ng’oka ukaote baharini,’ nao ungewatii.
LUK 17:7 “Ikiwa mmoja wenu ana mtumishi anayelima shambani au anayechunga kondoo, je, mtumishi huyo arudipo atamwambia, ‘Karibu hapa keti ule chakula’?
LUK 17:8 Je, badala yake, hatamwambia, ‘Niandalie chakula, nile, jifunge unitumikie ninapokula na kunywa; baadaye unaweza kula na kunywa’?
LUK 17:9 Je, huyo mtu atamshukuru mtumishi huyo kwa kutimiza yale aliyoamriwa?
LUK 17:10 Vivyo hivyo nanyi mkishafanya mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi tu watumishi tusiostahili; tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.’ ”
LUK 17:11 Isa alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya.
LUK 17:12 Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali,
LUK 17:13 wakapaza sauti, wakasema, “Isa, Bwana, tuhurumie!”
LUK 17:14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.
LUK 17:15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Isa, akimsifu Mungu kwa sauti kuu.
LUK 17:16 Akajitupa miguuni mwa Isa akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.
LUK 17:17 Isa akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa?
LUK 17:18 Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?”
LUK 17:19 Isa akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”
LUK 17:20 Isa alipoulizwa na Mafarisayo ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii,
LUK 17:21 wala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana ufalme wa Mungu umo ndani yenu.”
LUK 17:22 Kisha Isa akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona.
LUK 17:23 Watu watawaambia, ‘Yule kule!’ au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie.
LUK 17:24 Kwa maana kama vile radi imulikavyo katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake.
LUK 17:25 Lakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki.
LUK 17:26 “Kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu.
LUK 17:27 Watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ikaja na kuwaangamiza wote.
LUK 17:28 “Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Lutu: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga.
LUK 17:29 Lakini siku ile Lutu alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote.
LUK 17:30 “Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa.
LUK 17:31 Siku hiyo, mtu yeyote aliye juu ya dari ya nyumba yake, hata vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba, asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote.
LUK 17:32 Mkumbukeni mke wa Lutu!
LUK 17:33 Mtu yeyote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa.
LUK 17:34 Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
LUK 17:35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. [
LUK 17:36 Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]”
LUK 17:37 Kisha wakamuuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana Isa?” Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, huko ndiko tai watakapokusanyika.”
LUK 18:1 Kisha Isa akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa.
LUK 18:2 Akawaambia, “Katika mji mmoja palikuwa hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu.
LUK 18:3 Katika mji huo alikuwako mjane mmoja aliyekuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’
LUK 18:4 “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu,
LUK 18:5 lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ”
LUK 18:6 Bwana Isa akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu.
LUK 18:7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia?
LUK 18:8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”
LUK 18:9 Isa akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine:
LUK 18:10 “Watu wawili walienda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru.
LUK 18:11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyang’anyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
LUK 18:12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’
LUK 18:13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’
LUK 18:14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”
LUK 18:15 Pia, watu walikuwa wakimletea Isa watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea.
LUK 18:16 Lakini Isa akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.
LUK 18:17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”
LUK 18:18 Mtawala mmoja akamuuliza Isa, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
LUK 18:19 Isa akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake.
LUK 18:20 Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”
LUK 18:21 Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
LUK 18:22 Isa aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
LUK 18:23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi.
LUK 18:24 Isa akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu!
LUK 18:25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
LUK 18:26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
LUK 18:27 Isa akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”
LUK 18:28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
LUK 18:29 Isa akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu
LUK 18:30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”
LUK 18:31 Isa akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa.
LUK 18:32 Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua.
LUK 18:33 Naye siku ya tatu atafufuka.”
LUK 18:34 Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Isa alikuwa anazungumzia nini.
LUK 18:35 Isa alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.
LUK 18:36 Kipofu huyo aliposikia umati wa watu wakipita, akauliza nini kilikuwa kikitendeka.
LUK 18:37 Wakamwambia, “Isa Al-Nasiri anapita.”
LUK 18:38 Akapaza sauti, akasema, “Isa, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
LUK 18:39 Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
LUK 18:40 Isa akasimama, akawaamuru wamlete huyo mtu kwake. Alipokaribia, Isa akamuuliza,
LUK 18:41 “Unataka nikufanyie nini?” Akajibu, “Bwana, nataka kuona.”
LUK 18:42 Isa akamwambia, “Basi upate kuona. Imani yako imekuponya.”
LUK 18:43 Akapata kuona mara hiyo, akamfuata Isa, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.
LUK 19:1 Isa akaingia Yeriko, naye alikuwa anapita katikati ya huo mji.
LUK 19:2 Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo.
LUK 19:3 Yeye alikuwa akijitahidi kumwona Isa ni mtu wa namna gani. Lakini kutokana na umati mkubwa wa watu hakuweza, kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo.
LUK 19:4 Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati wa watu akapanda juu ya mkuyu ili amwone Isa, kwa sababu angeipitia njia ile.
LUK 19:5 Isa alipofika pale chini ya huo mkuyu, akatazama juu, akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani mwako!”
LUK 19:6 Hivyo Zakayo akashuka upesi, akamkaribisha Isa nyumbani mwake kwa furaha kubwa.
LUK 19:7 Watu wote walipoona hivyo, wakaanza kunung’unika wakisema, “Ameenda kuwa mgeni wa mtu mwenye dhambi.”
LUK 19:8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana Isa, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”
LUK 19:9 Ndipo Isa akamwambia, “Leo, wokovu umeingia nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.
LUK 19:10 Kwa maana Mwana wa Adamu amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
LUK 19:11 Walipokuwa wanasikiliza haya, Isa akaendelea kuwaambia mfano, kwa sababu alikuwa anakaribia Yerusalemu na watu walikuwa wakidhani ya kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa unakuja saa hiyo.
LUK 19:12 Hivyo akawaambia: “Mtu mmoja mwenye cheo kikubwa alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi.
LUK 19:13 Hivyo akawaita kumi miongoni mwa watumishi wake, na akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Fanyeni biashara na fedha hizi hadi nitakaporudi.’
LUK 19:14 “Lakini raia wa nchi yake walimchukia wakapeleka ujumbe na kusema, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu.’
LUK 19:15 “Hata hivyo alirudi akiwa amekwisha kupokea mamlaka ya ufalme, akawaita wale watumishi wake aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu ni faida kiasi gani kila mmoja wao aliyopata kwa kufanya biashara.
LUK 19:16 “Wa kwanza akaja na kusema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia, nimepata faida mara kumi zaidi.’
LUK 19:17 “Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’
LUK 19:18 “Wa pili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’
LUK 19:19 “Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’
LUK 19:20 “Kisha akaja yule mtumishi mwingine, akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa.
LUK 19:21 Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka, na kuvuna ambapo hukupanda.’
LUK 19:22 “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, ninayechukua nisichoweka, na kuvuna nisichopanda,
LUK 19:23 kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba, ili nitakaporudi nichukue iliyo yangu na riba yake?’
LUK 19:24 “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyang’anyeni fungu lake la fedha, mkampe yule mwenye kumi.’
LUK 19:25 “Wakamwambia, ‘Bwana, mbona; tayari anayo mafungu kumi!’
LUK 19:26 “Akawajibu, ‘Nawaambia kwamba kila aliye na kitu, ataongezewa. Lakini yule asiye na kitu, hata alicho nacho atanyang’anywa.
LUK 19:27 Lakini wale adui zangu ambao hawakutaka mimi niwe mfalme juu yao. Waleteni hapa mkawaue mbele yangu.’ ”
LUK 19:28 Baada ya Isa kusema haya, alitangulia kupanda kwenda Yerusalemu.
LUK 19:29 Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye mlima ulioitwa Mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia,
LUK 19:30 “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtampata mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa.
LUK 19:31 Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ”
LUK 19:32 Wale waliotumwa wakaenda, wakapata kila kitu kama Isa alivyowaambia.
LUK 19:33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?”
LUK 19:34 Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.”
LUK 19:35 Wakamleta kwa Isa, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Isa juu yake.
LUK 19:36 Alipokuwa akienda, watu wakatandaza mavazi yao barabarani.
LUK 19:37 Alipokaribia mahali yanapoanzia miteremko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema:
LUK 19:38 “Amebarikiwa mfalme ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!” “Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.”
LUK 19:39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwamo miongoni mwa umati ule wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.”
LUK 19:40 Isa akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa watanyamaza, mawe yatapaza sauti.”
LUK 19:41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia,
LUK 19:42 akisema, “Laiti ungejua, hata wewe leo, yale yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako.
LUK 19:43 Hakika siku zinakujia, ambazo adui zako watakuzingira, nao watakuzunguka pande zote na kukuzuilia ndani.
LUK 19:44 Watakuponda chini, wewe na watoto walio ndani ya kuta zako. Nao hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kujiliwa kwako.”
LUK 19:45 Ndipo akaingia eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo.
LUK 19:46 Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyang’anyi.’ ”
LUK 19:47 Kila siku alikuwa akifundisha Hekaluni. Lakini viongozi wa makuhani, walimu wa Torati na viongozi wa watu walikuwa wakitafuta njia ili kumuua.
LUK 19:48 Lakini hawakupata nafasi kwa sababu watu wote walimfuata wakiyasikiliza maneno yake kwa usikivu mwingi.
LUK 20:1 Siku moja, Isa alipokuwa akifundisha watu Hekaluni na kuhubiri Habari Njema, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati, pamoja na wazee wa watu wakamjia.
LUK 20:2 Wakamuuliza, “Tuambie, unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Ni nani aliyekupa mamlaka haya?”
LUK 20:3 Akawajibu, “Nami nitawauliza swali. Nijibuni:
LUK 20:4 Je, ubatizo wa Yahya ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”
LUK 20:5 Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’
LUK 20:6 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ watu wote watatupiga mawe, kwa sababu wanaamini kwamba Yahya alikuwa nabii.”
LUK 20:7 Basi wakajibu, “Hatujui ulikotoka.”
LUK 20:8 Isa akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”
LUK 20:9 Akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu.
LUK 20:10 Wakati wa mavuno ulipofika, akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili wampe sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu.
LUK 20:11 Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza.
LUK 20:12 Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba.
LUK 20:13 “Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’
LUK 20:14 “Lakini wale wapangaji walipomwona, wakasemezana wao kwa wao. Wakasema, ‘Huyu ndiye mrithi. Basi na tumuue ili urithi uwe wetu.’
LUK 20:15 Kwa hiyo wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua. “Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wapangaji hawa?
LUK 20:16 Atakuja na kuwaua hao wapangaji, na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!”
LUK 20:17 Lakini Isa akawakazia macho, akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni’?
LUK 20:18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”
LUK 20:19 Walimu wa Torati na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja, kwa sababu walifahamu kwamba amesema mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu.
LUK 20:20 Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa wenye haki. Walitaka kumtega kwa maneno yake, ili wampeane katika uwezo na mamlaka ya mtawala.
LUK 20:21 Hivyo wale wapelelezi wakamuuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu katika kweli.
LUK 20:22 Je, ni halali sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”
LUK 20:23 Lakini Isa akatambua hila yao, akawaambia,
LUK 20:24 “Nionesheni dinari. Je, sura hii na maandishi haya yaliyo juu yake ni vya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
LUK 20:25 Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
LUK 20:26 Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza.
LUK 20:27 Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Isa na kumuuliza,
LUK 20:28 “Mwalimu, Musa alituandikia kwamba kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto.
LUK 20:29 Basi kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa, akafa bila kuzaa mtoto.
LUK 20:30 Kisha yule wa pili akamwoa huyo mjane, naye akafa bila mtoto,
LUK 20:31 naye wa tatu pia akamwoa. Vivyo hivyo ndugu wote saba wakawa wamemwoa huyo mwanamke, na wote wakafa pasipo yeyote kupata mtoto.
LUK 20:32 Mwishowe, yule mwanamke naye akafa.
LUK 20:33 Sasa basi, siku ya ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”
LUK 20:34 Isa akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa.
LUK 20:35 Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi.
LUK 20:36 Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo.
LUK 20:37 Hata Musa alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila kuteketea, alipomwita Mwenyezi Mungu, ‘Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.’
LUK 20:38 Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, kwa kuwa kwake wote ni hai.”
LUK 20:39 Baadhi ya walimu wa Torati wakasema, “Mwalimu, umesema sawasawa kabisa!”
LUK 20:40 Baada ya hayo hakuna mtu aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
LUK 20:41 Kisha Isa akawaambia, “Imekuwaje basi wao husema Al-Masihi ni Mwana wa Daudi?
LUK 20:42 Daudi mwenyewe anasema katika Kitabu cha Zaburi: “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume,
LUK 20:43 hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’
LUK 20:44 Ikiwa Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ basi atakuwaje mwanawe?”
LUK 20:45 Wakati watu wote walikuwa wanamsikiliza, Isa akawaambia wanafunzi wake,
LUK 20:46 “Jihadharini na walimu wa Torati. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. Hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kukaa kwenye nafasi za heshima katika karamu.
LUK 20:47 Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema, wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”
LUK 21:1 Isa alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu.
LUK 21:2 Akamwona pia mjane mmoja maskini akiweka humo sarafu mbili ndogo za shaba.
LUK 21:3 Isa akasema, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo zaidi ya watu wengine wote.
LUK 21:4 Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kutokana na wingi wa mali yao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
LUK 21:5 Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Isa akawaambia,
LUK 21:6 “Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
LUK 21:7 Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonesha kwamba yanakaribia kutendeka?”
LUK 21:8 Isa akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate.
LUK 21:9 Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”
LUK 21:10 Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine.
LUK 21:11 Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
LUK 21:12 “Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu.
LUK 21:13 Hii itawapa nafasi ya kushuhudia.
LUK 21:14 Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka.
LUK 21:15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga.
LUK 21:16 Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na rafiki zenu, na baadhi yenu watawaua.
LUK 21:17 Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu.
LUK 21:18 Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia.
LUK 21:19 Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.
LUK 21:20 “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia.
LUK 21:21 Wakati huo, wale walio Yudea wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo, nao wale walio mashambani wasiingie mjini.
LUK 21:22 Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa.
LUK 21:23 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu.
LUK 21:24 Wataanguka kwa makali ya upanga, na wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote. Nao mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa Mataifa hadi muda wa hao watu wa Mataifa utimie.
LUK 21:25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari.
LUK 21:26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika.
LUK 21:27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu.
LUK 21:28 Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”
LUK 21:29 Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote.
LUK 21:30 Inapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua wenyewe ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia.
LUK 21:31 Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yakitukia, mtambue kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.
LUK 21:32 “Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
LUK 21:33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
LUK 21:34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama mtego unasavyo.
LUK 21:35 Hivyo ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote wanaoishi katika uso wa dunia yote.
LUK 21:36 Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”
LUK 21:37 Kila siku Isa alikuwa akifundisha Hekaluni, na jioni ilipofika, alienda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha.
LUK 21:38 Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.
LUK 22:1 Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia.
LUK 22:2 Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Isa, kwa sababu waliwaogopa watu.
LUK 22:3 Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale kumi na wawili.
LUK 22:4 Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi angeweza kumsaliti Isa.
LUK 22:5 Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha.
LUK 22:6 Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Isa kwao, ambapo hakuna umati wa watu.
LUK 22:7 Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa.
LUK 22:8 Hivyo Isa akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”
LUK 22:9 Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?”
LUK 22:10 Isa akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni hadi kwenye nyumba atakayoingia.
LUK 22:11 Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’
LUK 22:12 Atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.”
LUK 22:13 Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Isa alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
LUK 22:14 Wakati ulipowadia, Isa akaketi mezani pamoja na wale mitume wake.
LUK 22:15 Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu.
LUK 22:16 Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka hadi itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.”
LUK 22:17 Baada ya kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote.
LUK 22:18 Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi ufalme wa Mungu utakapokuja.”
LUK 22:19 Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
LUK 22:20 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu.
LUK 22:21 Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami.
LUK 22:22 Mwana wa Adamu anaenda zake kama ilivyokusudiwa. Lakini ole wake mtu huyo amsalitiye!”
LUK 22:23 Wakaanza kuulizana wenyewe ni nani miongoni mwao angeweza kufanya jambo hilo.
LUK 22:24 Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao.
LUK 22:25 Isa akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’
LUK 22:26 Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye anayetawala na awe kama yeye anayehudumu.
LUK 22:27 Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule anayeketi mezani au ni yule anayehudumu? Si ni yule aliyeketi mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule anayehudumu.
LUK 22:28 Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu.
LUK 22:29 Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, nami ninawapa ninyi,
LUK 22:30 ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya utawala, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.”
LUK 22:31 Isa akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano.
LUK 22:32 Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe baada ya kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”
LUK 22:33 Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata katika kifo.”
LUK 22:34 Isa akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba unanijua.”
LUK 22:35 Kisha Isa akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?” Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.”
LUK 22:36 Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja.
LUK 22:37 Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe kunihusu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu hayana budi kutimizwa.”
LUK 22:38 Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.” Akawajibu, “Inatosha.”
LUK 22:39 Isa akatoka, akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata.
LUK 22:40 Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.”
LUK 22:41 Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba
LUK 22:42 akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.”
LUK 22:43 Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu.
LUK 22:44 Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.
LUK 22:45 Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni.
LUK 22:46 Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.”
LUK 22:47 Isa alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu wakaja. Waliongozwa na Yuda, aliyekuwa mmoja wa wale kumi na wawili. Akamkaribia Isa ili ambusu.
LUK 22:48 Lakini Isa akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
LUK 22:49 Wafuasi wa Isa walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?”
LUK 22:50 Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.
LUK 22:51 Lakini Isa akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.
LUK 22:52 Kisha Isa akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyang’anyi?
LUK 22:53 Kila siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”
LUK 22:54 Kisha wakamkamata Isa, wakamchukua, wakaenda naye hadi nyumbani mwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali.
LUK 22:55 Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao.
LUK 22:56 Mjakazi mmoja akamwona kwa mwanga wa moto akiwa ameketi pale. Akamtazama sana, akasema, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Isa!”
LUK 22:57 Lakini Petro akakana, akasema, “Ewe mwanamke, hata simjui!”
LUK 22:58 Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, “Wewe pia ni mmoja wao!” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!”
LUK 22:59 Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, “Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Isa, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya.”
LUK 22:60 Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sijui unalosema!” Wakati huo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika.
LUK 22:61 Naye Bwana Isa akageuka, akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka lile neno ambalo Bwana alimwambia: “Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu.”
LUK 22:62 Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
LUK 22:63 Watu waliokuwa wanamlinda Isa wakaanza kumdhihaki na kumpiga.
LUK 22:64 Wakamfunga kitambaa machoni na kumuuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?”
LUK 22:65 Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.
LUK 22:66 Kulipopambazuka, Baraza la Wazee, yaani viongozi wa makuhani na walimu wa Torati, wakakutana pamoja, naye Isa akaletwa mbele yao.
LUK 22:67 Wakamwambia, “Kama wewe ndiwe Al-Masihi, tuambie.” Isa akawajibu, “Hata nikiwaambia, hamtaamini.
LUK 22:68 Nami nikiwauliza swali, hamtanijibu.
LUK 22:69 Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu ataketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”
LUK 22:70 Wote wakauliza, “Wewe basi ndiwe Mwana wa Mungu?” Yeye akawajibu, “Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye.”
LUK 22:71 Kisha wakasema, “Tuna haja gani tena ya ushahidi zaidi? Tumesikia wenyewe kutoka kinywani mwake.”
LUK 23:1 Kisha umati wote wa watu wakainuka na kumpeleka Isa kwa Pilato.
LUK 23:2 Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita ni Al-Masihi, mfalme.”
LUK 23:3 Basi Pilato akamuuliza Isa, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Isa akajibu, “Wewe wasema.”
LUK 23:4 Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na umati ule wote, “Sioni msingi wowote wa kumshtaki mtu huyu!”
LUK 23:5 Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Yudea yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”
LUK 23:6 Pilato aliposikia hayo akauliza kama huyo mtu alikuwa Mgalilaya.
LUK 23:7 Alipofahamu kwamba Isa alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.
LUK 23:8 Herode alipomwona Isa alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha.
LUK 23:9 Herode akamuuliza maswali mengi, lakini Isa hakumjibu lolote.
LUK 23:10 Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana.
LUK 23:11 Herode na askari wake wakamdhihaki Isa na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato.
LUK 23:12 Siku hiyo, Herode na Pilato wakapata urafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.
LUK 23:13 Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu,
LUK 23:14 akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami sikupata msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake.
LUK 23:15 Wala Herode hakumpata na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo.
LUK 23:16 Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachilia.” [
LUK 23:17 Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.]
LUK 23:18 Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyu! Tufungulie Baraba!”
LUK 23:19 (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.)
LUK 23:20 Pilato, akitaka kumwachia Isa, akasema nao tena.
LUK 23:21 Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”
LUK 23:22 Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”
LUK 23:23 Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu, wakidai kwamba Isa asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda.
LUK 23:24 Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe.
LUK 23:25 Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Isa mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.
LUK 23:26 Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni Mkirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Isa.
LUK 23:27 Idadi kubwa ya watu wakamfuata Isa, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea.
LUK 23:28 Isa akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu.
LUK 23:29 Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao tumbo zao hazikuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’
LUK 23:30 Ndipo “ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!” na vilima, “Tufunikeni!” ’
LUK 23:31 Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”
LUK 23:32 Watu wawili wahalifu walipelekwa pamoja na Isa ili wakasulubiwe.
LUK 23:33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walimsulubisha Isa pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume, na mwingine upande wake wa kushoto.
LUK 23:34 Isa akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.
LUK 23:35 Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Al-Masihi wa Mungu, Mteule wake.”
LUK 23:36 Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe,
LUK 23:37 na wakamwambia, “Kama wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”
LUK 23:38 Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.
LUK 23:39 Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Al-Masihi? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”
LUK 23:40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu hiyo hiyo?
LUK 23:41 Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”
LUK 23:42 Kisha akasema, “Isa, unikumbuke utakapokuja katika ufalme wako.”
LUK 23:43 Isa akamjibu, “Amin, nakuambia, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.”
LUK 23:44 Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa,
LUK 23:45 kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili.
LUK 23:46 Isa akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.
LUK 23:47 Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.”
LUK 23:48 Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao.
LUK 23:49 Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.
LUK 23:50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yusufu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi,
LUK 23:51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa raia wa Arimathaya huko Yudea, naye alikuwa anaungojea ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa.
LUK 23:52 Yusufu alienda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Isa.
LUK 23:53 Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado.
LUK 23:54 Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.
LUK 23:55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Isa wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Isa ulivyolazwa.
LUK 23:56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.
LUK 24:1 Siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa, wakaenda kaburini.
LUK 24:2 Wakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka mdomo wa kaburi,
LUK 24:3 lakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Isa.
LUK 24:4 Walipokuwa wanashangaa kuhusu jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayong’aa kama umeme wakasimama karibu nao.
LUK 24:5 Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao hadi chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu?
LUK 24:6 Hayuko hapa; amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba:
LUK 24:7 ‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi na waovu ili asulubiwe, na siku ya tatu afufuke.’ ”
LUK 24:8 Ndipo wakayakumbuka maneno ya Isa.
LUK 24:9 Waliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote.
LUK 24:10 Basi Mariamu Magdalene, Yoana, na Mariamu mama yake Yakobo, pamoja na wanawake wengine waliofuatana nao ndio waliwaelezea mitume habari hizi.
LUK 24:11 Lakini hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi.
LUK 24:12 Hata hivyo, Petro akainuka na kukimbia kwenda kule kaburini. Alipoinama kuchungulia, akaona vile vitambaa vya kitani, ila hakuona kitu kingine. Naye akaenda zake akijiuliza nini kilichotokea.
LUK 24:13 Ikawa siku hiyo hiyo, wanafunzi wawili wa Isa walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba kutoka Yerusalemu.
LUK 24:14 Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia.
LUK 24:15 Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Isa mwenyewe akaja akatembea pamoja nao,
LUK 24:16 lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue.
LUK 24:17 Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?” Wakasimama, nyuso zao zikionesha huzuni.
LUK 24:18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, “Je, wewe ndiwe peke yako mgeni huku Yerusalemu, ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?”
LUK 24:19 Akawauliza, “Mambo gani?” Wakamjibu, “Mambo ya Isa Al-Nasiri. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote.
LUK 24:20 Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha.
LUK 24:21 Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatendeke.
LUK 24:22 Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walienda kaburini leo alfajiri,
LUK 24:23 lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Isa yu hai.
LUK 24:24 Kisha baadhi ya wenzetu walienda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.”
LUK 24:25 Isa akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii!
LUK 24:26 Je, haikumpasa Al-Masihi kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?”
LUK 24:27 Naye akianzia na Torati ya Musa na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu.
LUK 24:28 Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Isa akawa kama anaendelea mbele.
LUK 24:29 Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao.
LUK 24:30 Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia.
LUK 24:31 Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena.
LUK 24:32 Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?”
LUK 24:33 Wakaondoka mara hiyo, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao wamekusanyika,
LUK 24:34 wakasema, “Ni kweli! Bwana Isa amefufuka, naye amemtokea Simoni.”
LUK 24:35 Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Isa alipoumega mkate.
LUK 24:36 Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Isa mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”
LUK 24:37 Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka.
LUK 24:38 Lakini Isa akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu?
LUK 24:39 Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi mwenyewe. Niguseni mwone; kwa maana mzuka huna nyama na mifupa, kama mnavyoniona mimi.”
LUK 24:40 Aliposema haya, akawaonesha mikono na miguu yake.
LUK 24:41 Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?”
LUK 24:42 Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa,
LUK 24:43 naye akakichukua na kukila mbele yao.
LUK 24:44 Akawaambia, “Haya ndio yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu katika Torati ya Musa, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”
LUK 24:45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko Matakatifu.
LUK 24:46 Akawaambia, “Haya ndio yaliyoandikwa: Al-Masihi atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu.
LUK 24:47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu.
LUK 24:48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
LUK 24:49 “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo kutoka juu.”
LUK 24:50 Baada ya kuwaongoza hadi Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki.
LUK 24:51 Alipokuwa anawabariki, akawaacha, akachukuliwa mbinguni.
LUK 24:52 Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu.
LUK 24:53 Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu.
JOH 1:1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, naye huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
JOH 1:2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
JOH 1:3 Vitu vyote viliumbwa kupitia kwake, na hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa pasipo yeye.
JOH 1:4 Ndani yake kulikuwa na uzima, nao huo uzima ulikuwa nuru ya watu.
JOH 1:5 Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda.
JOH 1:6 Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yahya.
JOH 1:7 Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kupitia kwake watu wote waweze kuamini.
JOH 1:8 Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru.
JOH 1:9 Nuru halisi inayomwangazia kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
JOH 1:10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni, na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua.
JOH 1:11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea.
JOH 1:12 Bali wote waliompokea, yaani wale walioliamini jina lake, aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu.
JOH 1:13 Hawa hawakuzaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali wamezaliwa kwa mapenzi ya Mungu.
JOH 1:14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
JOH 1:15 Yahya alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ ”
JOH 1:16 Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema.
JOH 1:17 Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Musa, lakini neema na kweli zimekuja kupitia Isa Al-Masihi.
JOH 1:18 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba, ndiye ambaye amemdhihirisha.
JOH 1:19 Huu ndio ushuhuda wa Yahya wakati viongozi wa Wayahudi waliwatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?”
JOH 1:20 Yahya alikiri waziwazi pasipo kuficha, akasema, “Mimi si Al-Masihi.”
JOH 1:21 Wakamuuliza, “Wewe ni nani, basi? Je, wewe ni Ilya?” Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.” “Je, wewe ni yule Nabii?” Akajibu, “Hapana.”
JOH 1:22 Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
JOH 1:23 Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Mwenyezi Mungu.’ ”
JOH 1:24 Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo,
JOH 1:25 wakamuuliza, “Kama wewe si Al-Masihi, wala si Ilya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?”
JOH 1:26 Yahya akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini kati yenu yupo mtu msiyemjua.
JOH 1:27 Yeye anakuja baada yangu, nami sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
JOH 1:28 Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ng’ambo ya Yordani, mahali Yahya alipokuwa akibatiza.
JOH 1:29 Siku iliyofuata, Yahya alimwona Isa akimjia, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
JOH 1:30 Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’
JOH 1:31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
JOH 1:32 Kisha Yahya akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho Mtakatifu wa Mungu akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake.
JOH 1:33 Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho Mtakatifu wa Mungu akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho wa Mungu.’
JOH 1:34 Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
JOH 1:35 Siku iliyofuata, Yahya alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili.
JOH 1:36 Alipomwona Isa akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
JOH 1:37 Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yahya akisema haya, wakamfuata Isa.
JOH 1:38 Isa akageuka, akawaona wakimfuata, akawauliza, “Mnataka nini?” Wakamwambia, “Mwalimu, unaishi wapi?”
JOH 1:39 Isa akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!” Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
JOH 1:40 Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yahya alisema na kumfuata Isa.
JOH 1:41 Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masihi” (yaani Al-Masihi).
JOH 1:42 Naye akamleta kwa Isa. Isa akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro).
JOH 1:43 Siku iliyofuata Isa aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
JOH 1:44 Filipo alikuwa raia wa Bethsaida, mji walikotoka Andrea na Petro.
JOH 1:45 Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Musa aliandika habari zake katika Torati, na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani Isa Al-Nasiri, mwana wa Yusufu.”
JOH 1:46 Nathanaeli akauliza, “Nasiri! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nasiri?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
JOH 1:47 Isa alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake, akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.”
JOH 1:48 Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?” Isa akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
JOH 1:49 Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
JOH 1:50 Isa akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu kuliko hilo.”
JOH 1:51 Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”
JOH 2:1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Isa alikuwepo.
JOH 2:2 Isa pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia.
JOH 2:3 Divai ilipokwisha, mama yake Isa akamwambia, “Wameishiwa na divai.”
JOH 2:4 Isa akamwambia, “Mama, kwa nini unanihusisha? Saa yangu haijawadia.”
JOH 2:5 Mama yake akawaambia wale watumishi, “Fanyeni lolote atakalowaambia.”
JOH 2:6 Basi hapo palikuwa na mitungi sita iliyotengenezwa kwa mawe; iliwekwa hapo kwa ajili ya desturi ya Kiyahudi ya kujitakasa; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.
JOH 2:7 Isa akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi hadi juu.
JOH 2:8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo; mpelekeeni mkuu wa sherehe.” Hivyo wakachota, wakampelekea.
JOH 2:9 Yule mkuu wa sherehe akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilishwa kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando,
JOH 2:10 akamwambia, “Watu wote hutoa divai nzuri kwanza, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa sana; lakini wewe umeiweka ile nzuri zaidi hadi sasa.”
JOH 2:11 Huu ndio muujiza wa kwanza wa Isa; aliufanya huko Kana ya Galilaya. Hivyo Isa alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
JOH 2:12 Baada ya hayo, Isa pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka hadi Kapernaumu, wakakaa huko siku chache.
JOH 2:13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya Wayahudi, Isa alipanda kwenda Yerusalemu.
JOH 2:14 Huko uani la Hekalu aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha.
JOH 2:15 Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka ua la Hekalu, pamoja na kondoo na ng’ombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao.
JOH 2:16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?”
JOH 2:17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”
JOH 2:18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya yote?”
JOH 2:19 Isa akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”
JOH 2:20 Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?”
JOH 2:21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake.
JOH 2:22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Isa alikuwa ameyasema.
JOH 2:23 Ikawa Isa alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, nao wakaamini katika jina lake.
JOH 2:24 Lakini Isa hakujiaminisha kwao, kwa sababu aliwajua wanadamu wote.
JOH 2:25 Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mwanadamu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa kila mtu.
JOH 3:1 Basi palikuwa na mtu mmoja Farisayo, jina lake Nikodemo, mmoja wa Baraza la Wayahudi lililotawala.
JOH 3:2 Huyu alimjia Isa usiku akamwambia, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”
JOH 3:3 Isa akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.”
JOH 3:4 Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!”
JOH 3:5 Isa akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho.
JOH 3:6 Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho.
JOH 3:7 Kwa hiyo usishangae ninapokuambia, ‘Huna budi kuzaliwa mara ya pili.’
JOH 3:8 Upepo huvuma kokote unakopenda. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu unakotoka wala unakoenda. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.”
JOH 3:9 Nikodemo akamuuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?”
JOH 3:10 Isa akamwambia, “Wewe ni mwalimu wa Waisraeli, nawe huelewi mambo haya?
JOH 3:11 Amin, amin ninakuambia, sisi tunazungumza lile tunalolijua na tunashuhudia lile tuliloliona. Lakini ninyi watu hamkubali ushuhuda wetu.
JOH 3:12 Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni?
JOH 3:13 Hakuna mtu yeyote aliyeenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani Mwana wa Adamu.
JOH 3:14 Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu,
JOH 3:15 ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.
JOH 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
JOH 3:17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.
JOH 3:18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
JOH 3:19 Hii ndiyo hukumu: Kwamba nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru, kwa sababu matendo yao ni maovu.
JOH 3:20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe.
JOH 3:21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”
JOH 3:22 Baada ya haya, Isa na wanafunzi wake walienda katika eneo la Yudea, nao wakakaa huko kwa muda na kubatiza watu.
JOH 3:23 Yahya naye alikuwa akibatiza watu huko Ainoni karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji mengi. Watu wakamjia huko ili kubatizwa.
JOH 3:24 (Hii ilikuwa kabla Yahya hajafungwa gerezani.)
JOH 3:25 Mashindano yakazuka kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yahya na Myahudi mmoja kuhusu suala la desturi ya kunawa kwa utakaso.
JOH 3:26 Wakamwendea Yahya wakamwambia, “Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng’ambo ya Yordani, yule uliyeshuhudia habari zake, sasa anabatiza na kila mtu anamwendea!”
JOH 3:27 Yahya akawajibu, “Hakuna mtu yeyote awezaye kupata kitu chochote isipokuwa kile tu alichopewa kutoka mbinguni.
JOH 3:28 Ninyi wenyewe ni mashahidi wangu kwamba nilisema, ‘Mimi si Al-Masihi, ila nimetumwa nimtangulie.’
JOH 3:29 Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika.
JOH 3:30 Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kupungua.
JOH 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu yu juu ya yote, yeye aliye wa duniani ni wa dunia, naye huzungumza mambo ya duniani. Yeye aliyekuja kutoka mbinguni, yu juu ya yote.
JOH 3:32 Yeye hushuhudia yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna yeyote anayekubali ushuhuda wake.
JOH 3:33 Lakini yeyote anayekubali huo ushuhuda anathibitisha kwamba, Mungu ni kweli.
JOH 3:34 Yeye aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, kwa kuwa Mungu humpa Roho wake pasipo kipimo.
JOH 3:35 Baba anampenda Mwana, naye ametia vitu vyote mkononi mwake.
JOH 3:36 Yeyote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”
JOH 4:1 Isa alipata habari kuwa Mafarisayo walisikia kwamba yeye alikuwa akipata wanafunzi kuliko Yahya na kuwabatiza,
JOH 4:2 ingawa kwa kweli si Isa mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake.
JOH 4:3 Bwana Isa alipojua mambo haya, aliondoka Yudea akarudi tena Galilaya.
JOH 4:4 Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria.
JOH 4:5 Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu.
JOH 4:6 Kisima cha Yakobo kilikuwa huko. Naye Isa alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
JOH 4:7 Mwanamke mmoja Msamaria alipokuja kuteka maji, Isa akamwambia, “Naomba maji ninywe.”
JOH 4:8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wameenda mjini kununua chakula.)
JOH 4:9 Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.)
JOH 4:10 Isa akamjibu, “Kama ungeijua karama ya Mungu, na ni nani anakuomba maji ya kunywa, ungemwomba yeye, naye angekupa maji ya uzima.”
JOH 4:11 Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi?
JOH 4:12 Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”
JOH 4:13 Isa akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena.
JOH 4:14 Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.”
JOH 4:15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena, wala nisije tena hapa kuteka maji!”
JOH 4:16 Isa akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”
JOH 4:17 Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.” Isa akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume.
JOH 4:18 Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano, na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.”
JOH 4:19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii.
JOH 4:20 Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”
JOH 4:21 Isa akamjibu, “Mwanamke, niamini: wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu.
JOH 4:22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi.
JOH 4:23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba anawatafuta watu wanaomwabudu kwa namna hii.
JOH 4:24 Mungu ni Roho, na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
JOH 4:25 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Al-Masihi” (yaani Aliyetiwa mafuta) “anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.”
JOH 4:26 Isa akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.”
JOH 4:27 Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au, “Kwa nini unazungumza naye?”
JOH 4:28 Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini, akawaambia watu,
JOH 4:29 “Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Al-Masihi?”
JOH 4:30 Basi wakamiminika watu kutoka mjini, wakamwendea Isa.
JOH 4:31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Mwalimu, kula.”
JOH 4:32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”
JOH 4:33 Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?”
JOH 4:34 Lakini Isa akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake.
JOH 4:35 Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune’? Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa!
JOH 4:36 Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja.
JOH 4:37 Hivyo ule msemo, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa.
JOH 4:38 Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda. Wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”
JOH 4:39 Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Isa kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.”
JOH 4:40 Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili.
JOH 4:41 Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.
JOH 4:42 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kwamba huyu ndiye Al-Masihi, Mwokozi wa ulimwengu.”
JOH 4:43 Baada ya zile siku mbili, Isa aliondoka kwenda Galilaya.
JOH 4:44 (Basi Isa mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.)
JOH 4:45 Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu.
JOH 4:46 Hivyo Isa akafika tena Kana ya Galilaya, kule alikuwa amebadili maji kuwa divai. Kulikuwa na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu.
JOH 4:47 Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumsihi aende akamponye mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.
JOH 4:48 Isa akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”
JOH 4:49 Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”
JOH 4:50 Isa akamjibu, “Nenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaenda zake.
JOH 4:51 Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake, wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima.
JOH 4:52 Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana saa saba, ndipo homa iliisha.”
JOH 4:53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati Isa alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa.
JOH 4:54 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Isa alifanya aliporudi Galilaya kutoka Yudea.
JOH 5:1 Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Isa akapanda kwenda Yerusalemu.
JOH 5:2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa Bethzatha kwa Kiebrania, ambalo lilikuwa limezungukwa na makumbi matano.
JOH 5:3 Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani vipofu, viwete, na waliopooza [wakingojea maji yatibuliwe.
JOH 5:4 Kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji. Yule angekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao].
JOH 5:5 Mtu mmoja aliyekuwa ameugua kwa miaka thelathini na nane alikuwa hapo.
JOH 5:6 Isa alipomwona akiwa amelala hapo, na akijua amekuwa katika hali hiyo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?”
JOH 5:7 Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.”
JOH 5:8 Isa akamwambia, “Inuka! Chukua mkeka wako na uende.”
JOH 5:9 Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea. Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.
JOH 5:10 Kwa hiyo viongozi wa Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato; si halali wewe kubeba mkeka wako.”
JOH 5:11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Chukua mkeka wako na uende.’ ”
JOH 5:12 Wakamuuliza, “Ni mtu gani huyo aliyekuambia uchukue mkeka wako uende?”
JOH 5:13 Basi yule mtu aliyeponywa hakufahamu ni nani aliyemponya, kwa sababu Isa alikuwa amepotea ndani ya umati ule wa watu waliokuwa hapo.
JOH 5:14 Baadaye Isa akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa. Usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo baya zaidi.”
JOH 5:15 Yule mtu akaenda, akawaambia wale viongozi wa Wayahudi kuwa ni Isa aliyemponya.
JOH 5:16 Kwa hiyo viongozi wa Wayahudi wakaanza kumsumbua Isa, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato.
JOH 5:17 Isa akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.”
JOH 5:18 Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumuua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.
JOH 5:19 Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lolote peke yake. Yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lolote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo.
JOH 5:20 Baba ampenda Mwana na kumwonesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa.
JOH 5:21 Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda.
JOH 5:22 Wala Baba hamhukumu mtu yeyote, lakini hukumu yote amempa Mwana,
JOH 5:23 ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeyote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.
JOH 5:24 “Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini na kuingia uzimani.
JOH 5:25 Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai.
JOH 5:26 Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake.
JOH 5:27 Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.
JOH 5:28 “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake,
JOH 5:29 nao watatoka makaburini. Wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima, nao wale waliotenda maovu watafufuka ili wahukumiwe.
JOH 5:30 “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.
JOH 5:31 “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli.
JOH 5:32 Lakini yuko mwingine anishuhudiaye, na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli.
JOH 5:33 “Mlituma wajumbe kwa Yahya, naye akaishuhudia kweli.
JOH 5:34 Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu; la, bali ninalitaja hili ili ninyi mpate kuokolewa.
JOH 5:35 Yahya alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake.
JOH 5:36 “Ninao ushuhuda mkuu kuliko ule wa Yahya. Kazi ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, kazi hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba amenituma.
JOH 5:37 Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake,
JOH 5:38 wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye.
JOH 5:39 Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele. Maandiko haya ndio yanayonishuhudia mimi.
JOH 5:40 Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.
JOH 5:41 “Mimi sikubali kutukuzwa na wanadamu,
JOH 5:42 lakini mimi ninawafahamu. Ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu.
JOH 5:43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei. Lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea.
JOH 5:44 Mnawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamfanyi bidii kupata utukufu unaotoka kwa Mungu?
JOH 5:45 “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba. Mshtaki wenu ni Musa, ambaye mmemwekea tumaini lenu.
JOH 5:46 Kama mngemwamini Musa, mngeniamini na mimi, kwa maana aliandika habari zangu.
JOH 5:47 Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Musa, mtaaminije ninayoyasema?”
JOH 6:1 Baada ya haya, Isa alienda ng’ambo ya Bahari ya Galilaya (ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia).
JOH 6:2 Umati mkubwa wa watu waliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa.
JOH 6:3 Kisha Isa akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake.
JOH 6:4 Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
JOH 6:5 Isa alipotazama na kuona umati ule mkubwa wa watu wakimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?”
JOH 6:6 Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.
JOH 6:7 Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.”
JOH 6:8 Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia,
JOH 6:9 “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa watu hawa wote?”
JOH 6:10 Isa akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi (palikuwa na wanaume wapatao elfu tano).
JOH 6:11 Ndipo Isa akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.
JOH 6:12 Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.”
JOH 6:13 Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.
JOH 6:14 Baada ya watu kuona muujiza ule Isa aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!”
JOH 6:15 Isa akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.
JOH 6:16 Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini.
JOH 6:17 Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Isa alikuwa hajajumuika nao.
JOH 6:18 Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
JOH 6:19 Wanafunzi walipokuwa wameenda mwendo wa maili tatu au nne, walimwona Isa akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana.
JOH 6:20 Lakini Isa akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.”
JOH 6:21 Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.
JOH 6:22 Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ng’ambo waliona kwamba palikuwa na mashua moja tu, na kwamba Isa hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao.
JOH 6:23 Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana Isa kumshukuru Mungu.
JOH 6:24 Mara wale watu wakatambua kwamba Isa hakuwa hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Isa.
JOH 6:25 Walipomkuta Isa ng’ambo ya bahari wakamuuliza, “Mwalimu, umefika lini huku?”
JOH 6:26 Isa akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
JOH 6:27 Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba Mwenyezi amemtia muhuri.”
JOH 6:28 Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”
JOH 6:29 Isa akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”
JOH 6:30 Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani?
JOH 6:31 Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”
JOH 6:32 Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Musa aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni.
JOH 6:33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
JOH 6:34 Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”
JOH 6:35 Isa akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe.
JOH 6:36 Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini.
JOH 6:37 Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuza nje kamwe.
JOH 6:38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.
JOH 6:39 Haya ndio mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho.
JOH 6:40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”
JOH 6:41 Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”
JOH 6:42 Wakasema, “Huyu si Isa, mwana wa Yusufu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?”
JOH 6:43 Hivyo Isa akawaambia, “Acheni kunung’unikiana ninyi kwa ninyi.
JOH 6:44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho.
JOH 6:45 Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu.
JOH 6:46 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba.
JOH 6:47 Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele.
JOH 6:48 Mimi ni mkate wa uzima.
JOH 6:49 Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa.
JOH 6:50 Lakini hapa kuna mkate kutoka mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa.
JOH 6:51 Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
JOH 6:52 Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”
JOH 6:53 Hivyo Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.
JOH 6:54 Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho.
JOH 6:55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
JOH 6:56 Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake.
JOH 6:57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu.
JOH 6:58 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.”
JOH 6:59 Isa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.
JOH 6:60 Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?”
JOH 6:61 Isa alipojua kwamba wafuasi wake wananung’unika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi?
JOH 6:62 Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza?
JOH 6:63 Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima.
JOH 6:64 Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Isa alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti.
JOH 6:65 Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”
JOH 6:66 Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata.
JOH 6:67 Hivyo Isa akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?”
JOH 6:68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
JOH 6:69 Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.”
JOH 6:70 Ndipo Isa akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.”
JOH 6:71 (Hapa alikuwa anasema kuhusu Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Isa.)
JOH 7:1 Baada ya mambo haya, Isa alienda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi huko walitaka kumuua.
JOH 7:2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
JOH 7:3 Hivyo ndugu zake Isa wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya.
JOH 7:4 Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jioneshe kwa ulimwengu.”
JOH 7:5 Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.
JOH 7:6 Isa akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote.
JOH 7:7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu.
JOH 7:8 Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.”
JOH 7:9 Baada ya kusema hayo, akabaki Galilaya.
JOH 7:10 Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alienda lakini kwa siri.
JOH 7:11 Viongozi wa Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”
JOH 7:12 Kulikuwa na minong’ono iliyoenea kumhusu Isa katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.”
JOH 7:13 Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
JOH 7:14 Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Isa alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha.
JOH 7:15 Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”
JOH 7:16 Ndipo Isa akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma.
JOH 7:17 Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe.
JOH 7:18 Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake.
JOH 7:19 Je, Musa hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”
JOH 7:20 Ule umati wa watu wakamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”
JOH 7:21 Isa akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu.
JOH 7:22 Lakini kwa kuwa Musa aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Musa bali kwa baba zetu wa zamani), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato.
JOH 7:23 Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi Torati ya Musa isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato?
JOH 7:24 Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”
JOH 7:25 Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua?
JOH 7:26 Mbona yuko hapa anazungumza hadharani, na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Al-Masihi?
JOH 7:27 Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Al-Masihi atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.”
JOH 7:28 Ndipo Isa, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui.
JOH 7:29 Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.”
JOH 7:30 Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia.
JOH 7:31 Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Al-Masihi atakapokuja, atafanya miujiza mikuu kuliko aliyoifanya mtu huyu?”
JOH 7:32 Mafarisayo wakasikia watu wakinong’ona mambo kama hayo kuhusu Isa, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.
JOH 7:33 Isa akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma.
JOH 7:34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”
JOH 7:35 Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani?
JOH 7:36 Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”
JOH 7:37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Isa akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe.
JOH 7:38 Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yanavyosema, vijito vya maji ya uzima vitatiririka kutoka ndani yake.”
JOH 7:39 Isa aliposema haya, alimaanisha Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye wote waliomwamini wangempokea. Kwa maana hadi wakati huo Roho wa Mungu alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Isa alikuwa bado hajatukuzwa.
JOH 7:40 Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa umati ule wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”
JOH 7:41 Wengine wakasema, “Huyu ndiye Al-Masihi!” Lakini wengine wakauliza, “Je, Al-Masihi kwao ni Galilaya?
JOH 7:42 Je, Maandiko hayasemi kwamba Al-Masihi atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?”
JOH 7:43 Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Isa.
JOH 7:44 Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.
JOH 7:45 Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Isa, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”
JOH 7:46 Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”
JOH 7:47 Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika?
JOH 7:48 Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini?
JOH 7:49 Lakini umati huu wa watu wasiojua Torati ya Musa, wamelaaniwa.”
JOH 7:50 Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Isa siku moja usiku, na alikuwa mmoja wao, akauliza,
JOH 7:51 “Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”
JOH 7:52 Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!” [
JOH 7:53 Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani mwake.
JOH 8:1 Lakini Isa akaenda katika Mlima wa Mizeituni.
JOH 8:2 Alfajiri na mapema Isa akaja tena Hekaluni; watu wote wakakusanyika, naye akaketi, akaanza kuwafundisha.
JOH 8:3 Walimu wa Torati na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote.
JOH 8:4 Wakamwambia Isa, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini.
JOH 8:5 Katika sheria, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, hadi wafe. Sasa wewe wasemaje?”
JOH 8:6 Walimuuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki. Lakini Isa akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole chake.
JOH 8:7 Walipoendelea kumuulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.”
JOH 8:8 Akainama tena na kuandika ardhini.
JOH 8:9 Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Isa akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake.
JOH 8:10 Isa akainuka na kumwambia, “Mwanamke, wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?”
JOH 8:11 Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja, Bwana.” Isa akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako. Kuanzia sasa usitende dhambi tena.”]
JOH 8:12 Kisha Isa akasema nao tena, akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata, hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”
JOH 8:13 Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki, kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.”
JOH 8:14 Isa akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli, kwa sababu najua nilikotoka na ninakoenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakoenda.
JOH 8:15 Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu; mimi simhukumu mtu yeyote.
JOH 8:16 Lakini hata nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma.
JOH 8:17 Imeandikwa katika Torati yenu kwamba ushahidi wa watu wawili ni thabiti.
JOH 8:18 Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.”
JOH 8:19 Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?” Isa akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.”
JOH 8:20 Isa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia.
JOH 8:21 Isa akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kuja.”
JOH 8:22 Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?”
JOH 8:23 Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini; mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu; mimi si wa ulimwengu huu.
JOH 8:24 Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu; kwa maana msipoamini kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.”
JOH 8:25 Wakamuuliza, “Wewe ni nani?” Naye Isa akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo.
JOH 8:26 Nina mambo mengi ya kusema kuwahusu ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kuaminika, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.”
JOH 8:27 Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia kuhusu Baba yake wa Mbinguni.
JOH 8:28 Kisha Isa akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua Mwana wa Adamu juu, ndipo mtajua kuwa mimi ndiye yule niliyesema, na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu, bali ninasema yale tu Baba yangu amenifundisha.
JOH 8:29 Yeye aliyenituma yu pamoja nami; hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.”
JOH 8:30 Wengi waliomsikia Isa akisema maneno haya wakamwamini.
JOH 8:31 Kisha Isa akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli.
JOH 8:32 Ndipo mtaijua kweli, nayo kweli itawaweka huru.”
JOH 8:33 Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Ibrahimu, nasi hatujakuwa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?”
JOH 8:34 Isa akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.
JOH 8:35 Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima.
JOH 8:36 Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli.
JOH 8:37 Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Ibrahimu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu.
JOH 8:38 Ninasema yale niliyoyaona nikiwa mbele za Baba yangu, nanyi mnafanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.”
JOH 8:39 Wakajibu, “Baba yetu ni Ibrahimu.” Isa akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Ibrahimu, mngefanya mambo yale aliyofanya Ibrahimu.
JOH 8:40 Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya jambo la namna hii.
JOH 8:41 Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.” Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.”
JOH 8:42 Isa akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
JOH 8:43 Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho.
JOH 8:44 Ninyi ni watoto wa baba yenu, ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli, maana hamna kweli ndani yake. Anaposema uongo, yeye husema lugha yake ya asili kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.
JOH 8:45 Lakini kwa sababu nimewaambia kweli, hamkuniamini!
JOH 8:46 Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini?
JOH 8:47 Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”
JOH 8:48 Wayahudi wakamjibu Isa, “Je, hatuko sahihi tunaposema kwamba wewe ni Msamaria, na kwamba una pepo mchafu?”
JOH 8:49 Isa akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau.
JOH 8:50 Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi.
JOH 8:51 Amin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu, hataona mauti milele.”
JOH 8:52 Ndipo Wayahudi wakapaza sauti, wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu! Ibrahimu alikufa, na manabii vilevile, nawe unasema kuwa mtu akitii neno lako hatakufa milele.
JOH 8:53 Je, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu ambaye alikufa, na manabii ambao pia walikufa? Unafikiri wewe ni nani?”
JOH 8:54 Isa akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi.
JOH 8:55 Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake.
JOH 8:56 Baba yenu Ibrahimu alishangilia kwamba angeiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.”
JOH 8:57 Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, nawe wasema umemwona Ibrahimu?”
JOH 8:58 Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Ibrahimu hajakuwa, Mimi niko.”
JOH 8:59 Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Isa akajificha, naye akatoka Hekaluni.
JOH 9:1 Isa alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa.
JOH 9:2 Wanafunzi wake wakamuuliza, “Mwalimu, ni nani aliyetenda dhambi; ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”
JOH 9:3 Isa akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake.
JOH 9:4 Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi.
JOH 9:5 Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”
JOH 9:6 Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule kipofu machoni.
JOH 9:7 Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni Kutumwa). Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.
JOH 9:8 Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?”
JOH 9:9 Wengine wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “Siye, bali anafanana naye.” Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.”
JOH 9:10 Wakamuuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?”
JOH 9:11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Isa alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia, ‘Nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu,’ ndipo nikanawa nami nikapata kuona!”
JOH 9:12 Wale wakamuuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?” Akawajibu, “Sijui.”
JOH 9:13 Wakamleta yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali kwa Mafarisayo.
JOH 9:14 Basi siku hiyo Isa alitengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato.
JOH 9:15 Mafarisayo nao wakaanza kumuuliza yule mtu alivyopata kuona. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”
JOH 9:16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.
JOH 9:17 Hivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho. Wasemaje kuhusu mtu huyo?” Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.”
JOH 9:18 Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu akapata kuona, hadi walipowaita wazazi wake.
JOH 9:19 Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?”
JOH 9:20 Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu.
JOH 9:21 Lakini hatujui jinsi anavyoweza kuona sasa, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni; yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.”
JOH 9:22 Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi, kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Isa kuwa ndiye Al-Masihi atafukuzwa kutoka sinagogi.
JOH 9:23 Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.”
JOH 9:24 Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.”
JOH 9:25 Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.”
JOH 9:26 Wakamuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?”
JOH 9:27 Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?”
JOH 9:28 Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake! Sisi ni wanafunzi wa Musa.
JOH 9:29 Tunajua kwamba Mungu alisema na Musa, lakini mtu huyu hatujui anakotoka.”
JOH 9:30 Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu!
JOH 9:31 Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii.
JOH 9:32 Tangu zamani hatujasikia kwamba mtu amemponya yeyote aliyezaliwa kipofu.
JOH 9:33 Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lolote.”
JOH 9:34 Wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje.
JOH 9:35 Isa aliposikia kuwa wamemfukuza atoke nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta, akamuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”
JOH 9:36 Yule mtu akamjibu, “Yeye ni nani, Bwana? Niambie ili nipate kumwamini.”
JOH 9:37 Isa akamjibu, “Umekwisha kumwona; naye anayezungumza nawe, ndiye.”
JOH 9:38 Yule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu.
JOH 9:39 Isa akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona wawe vipofu.”
JOH 9:40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?”
JOH 9:41 Isa akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.
JOH 10:1 “Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang’anyi.
JOH 10:2 Yeye anayeingia kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo.
JOH 10:3 Mlinzi humfungulia lango, na kondoo huisikia sauti yake. Yeye huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi.
JOH 10:4 Baada ya kuwatoa wote nje, yeye hutangulia mbele yao na kondoo humfuata, kwa kuwa wanaijua sauti yake.
JOH 10:5 Lakini kondoo hawatamfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.”
JOH 10:6 Isa alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia.
JOH 10:7 Kwa hiyo Isa akasema nao tena, akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo.
JOH 10:8 Wote walionitangulia ni wezi na wanyang’anyi, nao kondoo hawakuwasikia.
JOH 10:9 Mimi ndimi lango. Yeyote anayeingia zizini kupitia kwangu ataokoka. Ataingia na kutoka, naye atapata malisho.
JOH 10:10 Mwizi huja ili aibe, aue na aangamize. Mimi nimekuja ili wapate uzima, kisha wawe nao tele.
JOH 10:11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
JOH 10:12 Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Anapomwona mbwa-mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa-mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya.
JOH 10:13 Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.
JOH 10:14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu, nao kondoo wangu wananijua.
JOH 10:15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, ndivyo nami ninautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
JOH 10:16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili. Inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu; hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.
JOH 10:17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena.
JOH 10:18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu, na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”
JOH 10:19 Waliposikia maneno haya, Wayahudi wakagawanyika.
JOH 10:20 Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”
JOH 10:21 Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”
JOH 10:22 Ikafika Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu huko Yerusalemu. Ilikuwa majira ya baridi.
JOH 10:23 Naye Isa alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika Ukumbi wa Sulemani.
JOH 10:24 Wayahudi wakamkusanyikia, wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka hadi lini? Kama wewe ndiwe Al-Masihi, tuambie waziwazi.”
JOH 10:25 Isa akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia.
JOH 10:26 Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu.
JOH 10:27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata.
JOH 10:28 Nami ninawapa uzima wa milele; hawataangamia kamwe, wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu.
JOH 10:29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote, na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake.
JOH 10:30 Mimi na Baba yangu tu umoja.”
JOH 10:31 Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo,
JOH 10:32 lakini Isa akawaambia, “Nimewaonesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni kwa ipi kati ya hiyo miujiza mnataka kunipiga mawe?”
JOH 10:33 Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Ingawa wewe ni mwanadamu, unajifanya kuwa Mungu.”
JOH 10:34 Isa akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Torati yenu kwamba, ‘Nimesema kuwa ninyi ni “miungu” ’?
JOH 10:35 Kama aliwaita ‘miungu’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka,
JOH 10:36 je, mwawezaje kusema kwamba yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru, kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu’?
JOH 10:37 Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini.
JOH 10:38 Lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ni ndani yake.”
JOH 10:39 Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao.
JOH 10:40 Isa akaenda tena ng’ambo ya Yordani hadi mahali Yahya alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko.
JOH 10:41 Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yahya hakufanya muujiza wowote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.”
JOH 10:42 Nao watu wengi wakamwamini Isa huko.
JOH 11:1 Basi mtu mmoja, jina lake Lazaro, alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania, kijiji cha Mariamu na Martha dada yake.
JOH 11:2 (Huyu Mariamu, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye alimpaka Bwana Isa mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake.)
JOH 11:3 Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Isa kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.”
JOH 11:4 Lakini Isa aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti, bali ni wa kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.”
JOH 11:5 Isa aliwapenda Martha, Mariamu na Lazaro ndugu yao.
JOH 11:6 Hata hivyo, baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, alikawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.
JOH 11:7 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Yudea.”
JOH 11:8 Wanafunzi wake wakamwambia, “Mwalimu, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”
JOH 11:9 Isa akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wanaotembea mchana hawawezi kujikwaa, kwa maana wanaona kwa nuru ya ulimwengu huu.
JOH 11:10 Lakini wale wanaotembea usiku hujikwaa kwa sababu hawana nuru ndani yao.”
JOH 11:11 Baada ya kusema haya, Isa akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.”
JOH 11:12 Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.”
JOH 11:13 Hata hivyo, Isa alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.
JOH 11:14 Kwa hiyo Isa akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa.
JOH 11:15 Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwako huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.”
JOH 11:16 Tomaso (aliyeitwa Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”
JOH 11:17 Isa alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne.
JOH 11:18 Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa yamkini maili mbili,
JOH 11:19 na Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Mariamu kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao.
JOH 11:20 Martha aliposikia kwamba Isa anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Mariamu alibaki nyumbani.
JOH 11:21 Martha akamwambia Isa, “Bwana, kama ungekuwa hapa, ndugu yangu hangekufa.
JOH 11:22 Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”
JOH 11:23 Isa akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”
JOH 11:24 Martha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”
JOH 11:25 Isa akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi;
JOH 11:26 na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”
JOH 11:27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Al-Masihi, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”
JOH 11:28 Baada ya kusema haya, Martha alienda akamwita Mariamu dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.”
JOH 11:29 Mariamu aliposikia hivyo, akaondoka upesi, akaenda hadi alipokuwa Isa.
JOH 11:30 Isa alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha.
JOH 11:31 Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Mariamu nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani kwamba alikuwa anaenda kule kaburini kulilia huko.
JOH 11:32 Mariamu alipofika mahali pale Isa alipokuwa, alipiga magoti miguuni pake na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, ndugu yangu hangekufa.”
JOH 11:33 Isa alipomwona Mariamu akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Isa alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana.
JOH 11:34 Akauliza, “Mmemweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”
JOH 11:35 Isa akalia machozi.
JOH 11:36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”
JOH 11:37 Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”
JOH 11:38 Isa akafika penye kaburi akiwa amefadhaika sana kwa mara nyingine. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe liliwekwa kwenye ingilio lake.
JOH 11:39 Isa akasema, “Liondoeni jiwe.” Martha dada yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.”
JOH 11:40 Isa akamwambia, “Sikukuambia kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”
JOH 11:41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Isa akainua macho yake juu, akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia.
JOH 11:42 Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya watu hawa waliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”
JOH 11:43 Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti yake, akaita, “Lazaro, njoo huku!”
JOH 11:44 Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake. Isa akawaambia, “Mfungueni; mwacheni aende zake.”
JOH 11:45 Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Mariamu walipoona yale Isa aliyoyatenda, wakamwamini.
JOH 11:46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Isa aliyoyafanya.
JOH 11:47 Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa Baraza la Wayahudi. Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi.
JOH 11:48 Tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”
JOH 11:49 Mmoja wao aliyeitwa Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote!
JOH 11:50 Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”
JOH 11:51 Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe, bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Isa angekufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi;
JOH 11:52 wala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja.
JOH 11:53 Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Isa.
JOH 11:54 Kwa hiyo Isa akawa hatembei tena hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.
JOH 11:55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu ili wakajitakase kabla ya Pasaka.
JOH 11:56 Watu wakawa wanamtafuta Isa, nao waliposimama kwenye ua la Hekalu, waliulizana, “Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu?”
JOH 11:57 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Isa aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.
JOH 12:1 Siku sita kabla ya Pasaka, Isa alienda Bethania, makao ya Lazaro, aliyekuwa amemfufua kutoka kwa wafu.
JOH 12:2 Wakaandaa karamu kwa heshima ya Isa. Martha akawahudumia, wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Isa.
JOH 12:3 Kisha Mariamu akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Isa na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.
JOH 12:4 Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wanafunzi wa Isa, ambaye baadaye angemsaliti Isa, akasema,
JOH 12:5 “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari mia tatu, na fedha hizo wakapewa maskini?”
JOH 12:6 Yuda hakusema hivi kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi; ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha, na akawa akiiba zile fedha.
JOH 12:7 Isa akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu.
JOH 12:8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.”
JOH 12:9 Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Isa alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Isa, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Isa alikuwa amemfufua.
JOH 12:10 Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakapanga njama ya kumuua Lazaro pia,
JOH 12:11 kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake, Wayahudi wengi walikuwa wanamfuata Isa na kumwamini.
JOH 12:12 Siku iliyofuata umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Isa angekuja Yerusalemu.
JOH 12:13 Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema, “Hosana!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!” “Amebarikiwa mfalme wa Israeli!”
JOH 12:14 Isa akamkuta mwana-punda, akampanda, kama ilivyoandikwa,
JOH 12:15 “Usiogope, ewe Binti Sayuni; tazama, mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda!”
JOH 12:16 Wanafunzi wake Isa mwanzoni hawakuelewa mambo haya. Lakini Isa alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.
JOH 12:17 Wale waliokuwepo Isa alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu waliendelea kushuhudia.
JOH 12:18 Na kwa sababu walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu, umati wa watu wakaenda kumlaki.
JOH 12:19 Hivyo Mafarisayo walipoona hayo, wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”
JOH 12:20 Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wameenda kuabudu wakati wa Sikukuu.
JOH 12:21 Hawa wakaenda kwa Filipo, aliyekuwa raia wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Isa.”
JOH 12:22 Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Isa.
JOH 12:23 Isa akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.
JOH 12:24 Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa, huzaa mbegu nyingi.
JOH 12:25 Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele.
JOH 12:26 Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
JOH 12:27 “Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii’? Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu.
JOH 12:28 Baba, litukuze jina lako.” Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.”
JOH 12:29 Umati ule wa watu waliokuwa mahali pale waliisikia ile sauti, nao wakasema hiyo ilikuwa sauti ya radi; wengine wakasema malaika ameongea naye.
JOH 12:30 Isa akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu.
JOH 12:31 Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
JOH 12:32 Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.”
JOH 12:33 Isa aliyasema haya akionesha ni kifo gani atakachokufa.
JOH 12:34 Umati ule wa watu wakapaza sauti, wakasema, “Tumesikia kutoka Torati kwamba Al-Masihi adumu milele; hivyo wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?”
JOH 12:35 Ndipo Isa akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingali pamoja nanyi. Nendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakoenda.
JOH 12:36 Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Isa aliondoka, akajificha wasimwone.
JOH 12:37 Hata baada ya Isa kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini.
JOH 12:38 Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa kwa nani?”
JOH 12:39 Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine:
JOH 12:40 “Amewafanya vipofu, na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka nami nikawaponya.”
JOH 12:41 Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Isa na kunena habari zake.
JOH 12:42 Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi.
JOH 12:43 Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zinazotoka kwa Mungu.
JOH 12:44 Isa akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali pia yeye aliyenituma.
JOH 12:45 Yeyote anionaye mimi amemwona yeye aliyenituma.
JOH 12:46 Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kila mtu aniaminiye asibaki gizani.
JOH 12:47 “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa.
JOH 12:48 Yuko anayehukumu yule anayenikataa mimi na kuyakataa maneno yangu; yale maneno niliyoyasema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho.
JOH 12:49 Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema.
JOH 12:50 Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”
JOH 13:1 Sikukuu ya Pasaka ilikuwa imekaribia. Isa alijua kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni; naam, aliwapenda hadi mwisho.
JOH 13:2 Isa alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia wazo la kumsaliti Isa ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni.
JOH 13:3 Isa, akijua kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake, na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu,
JOH 13:4 aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni.
JOH 13:5 Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.
JOH 13:6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”
JOH 13:7 Isa akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”
JOH 13:8 Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.” Isa akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”
JOH 13:9 Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!”
JOH 13:10 Isa akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.”
JOH 13:11 Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.
JOH 13:12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi. Akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia?
JOH 13:13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana’; hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo.
JOH 13:14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi.
JOH 13:15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi.
JOH 13:16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma.
JOH 13:17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri kwenu mkiyatenda.
JOH 13:18 “Sisemi hivi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni kutimiza andiko lisemalo, ‘Yeye aliyekula chakula changu ameinua kisigino chake dhidi yangu.’
JOH 13:19 “Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye.
JOH 13:20 Amin, amin nawaambia, yeyote anayempokea yule niliyemtuma anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.”
JOH 13:21 Baada ya kusema haya, Isa alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”
JOH 13:22 Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani.
JOH 13:23 Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Isa alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Isa.
JOH 13:24 Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.”
JOH 13:25 Yule mwanafunzi akamwegemea Isa, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?”
JOH 13:26 Isa akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni.
JOH 13:27 Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia. Isa akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda, litende haraka.”
JOH 13:28 Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Isa alimwambia hivyo.
JOH 13:29 Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Isa alikuwa anamwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini kitu.
JOH 13:30 Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.
JOH 13:31 Baada ya Yuda kutoka nje, Isa akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
JOH 13:32 Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe, naye atamtukuza mara moja.
JOH 13:33 “Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta, na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi: Niendako, ninyi hamwezi kuja.
JOH 13:34 “Amri mpya nawapa: Mpendane. Kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane.
JOH 13:35 Mkipendana ninyi kwa ninyi kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”
JOH 13:36 Simoni Petro akamuuliza, “Bwana, unaenda wapi?” Isa akamjibu, “Ninakoenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.”
JOH 13:37 Petro akamuuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.”
JOH 13:38 Isa akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
JOH 14:1 Isa akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mnamwamini Mungu, mniamini pia.
JOH 14:2 Nyumbani mwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningewaambia. Naenda kuwaandalia makao.
JOH 14:3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo nanyi mpate kuwepo.
JOH 14:4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakoenda.”
JOH 14:5 Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakoenda, tutaijuaje njia?”
JOH 14:6 Isa akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kupitia kwangu.
JOH 14:7 Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”
JOH 14:8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, na hiyo itatutosha.”
JOH 14:9 Isa akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuoneshe Baba’?
JOH 14:10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi.
JOH 14:11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba, na Baba yuko ndani yangu; la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.
JOH 14:12 Amin, amin nawaambia, yeyote anayeniamini mimi, kazi ninazozifanya naye atazifanya. Naam, na atazifanya kazi kubwa kuliko hizi, kwa sababu mimi ninaenda kwa Baba.
JOH 14:13 Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana.
JOH 14:14 Mkiniomba lolote kwa Jina langu, nitalifanya.
JOH 14:15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.
JOH 14:16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele.
JOH 14:17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi, naye anakaa ndani yenu.
JOH 14:18 Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja kwenu.
JOH 14:19 Bado kitambo kidogo na ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona. Kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.
JOH 14:20 Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, na ninyi mko ndani yangu, na mimi niko ndani yenu.
JOH 14:21 Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
JOH 14:22 Ndipo Yuda (siyo Iskariote) akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”
JOH 14:23 Isa akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake.
JOH 14:24 Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu, na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.
JOH 14:25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi.
JOH 14:26 Lakini huyo Msaidizi, yaani huyo Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
JOH 14:27 Amani nawaachia; amani yangu nawapa. Amani hii ninayowapa si kama ile ulimwengu unatoa. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
JOH 14:28 “Mlisikia nikisema, ‘Ninaenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngenipenda, mngefurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuliko mimi.
JOH 14:29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini.
JOH 14:30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu,
JOH 14:31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru. “Haya inukeni; twendeni zetu.
JOH 15:1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.
JOH 15:2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi linalozaa, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi.
JOH 15:3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi.
JOH 15:4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.
JOH 15:5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote.
JOH 15:6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, huyo hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea.
JOH 15:7 Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa.
JOH 15:8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa kwa vile mnavyozaa matunda mengi, nanyi mtajidhihirisha kuwa wanafunzi wangu.
JOH 15:9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu.
JOH 15:10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
JOH 15:11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu iwe kamili.
JOH 15:12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi.
JOH 15:13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
JOH 15:14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.
JOH 15:15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya. Bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu.
JOH 15:16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi.
JOH 15:17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.
JOH 15:18 “Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu.
JOH 15:19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda kama unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia.
JOH 15:20 Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia.
JOH 15:21 Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma.
JOH 15:22 Kama sikuja na kusema nao, hawangekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao.
JOH 15:23 Yeyote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu.
JOH 15:24 Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine yeyote, hawangekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii, na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu.
JOH 15:25 Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Torati kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’
JOH 15:26 “Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.
JOH 15:27 Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.
JOH 16:1 “Nimewaambia mambo haya yote ili msije mkaiacha imani.
JOH 16:2 Watawatenga na masinagogi. Naam, saa yaja ambayo mtu yeyote atakayewaua atadhani kwa kufanya hivyo anamtumikia Mungu.
JOH 16:3 Nao watawatenda haya kwa sababu hawamjui Baba wala mimi.
JOH 16:4 Lakini nimewaambia ninyi mambo haya, ili saa hiyo ikiwadia mpate kukumbuka ya kuwa nilikuwa nimewaambia. Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
JOH 16:5 “Sasa mimi ninaenda kwake yeye aliyenituma, lakini hakuna hata aniulizaye, ‘Unaenda wapi?’
JOH 16:6 Kwa sababu nimewaambia mambo haya, mioyo yenu imejawa na huzuni.
JOH 16:7 Lakini nawaambia kweli, yafaa mimi niondoke, kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; lakini nikienda nitamtuma kwenu.
JOH 16:8 Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu.
JOH 16:9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;
JOH 16:10 kwa habari ya haki, kwa sababu ninaenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena;
JOH 16:11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.
JOH 16:12 “Bado ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili sasa.
JOH 16:13 Atakapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonesha mambo yajayo.
JOH 16:14 Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.
JOH 16:15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.”
JOH 16:16 Isa akaendelea kusema, “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.”
JOH 16:17 Baadhi ya wanafunzi wakaulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona’? Naye ana maana gani asemapo, ‘Kwa sababu ninaenda kwa Baba’?”
JOH 16:18 Wakaendelea kuulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Kitambo kidogo’? Hatuelewi hilo analosema.”
JOH 16:19 Isa akatambua kuwa walitaka kumuuliza kuhusu hilo, hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana nina maana gani niliposema, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona’?
JOH 16:20 Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
JOH 16:21 Mwanamke anapokuwa na uchungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini baada ya mtoto kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha yake ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni.
JOH 16:22 Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye.
JOH 16:23 Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin nawaambia, mkimwomba Baba jambo lolote kwa jina langu, yeye atawapa.
JOH 16:24 Hadi sasa hamjaomba jambo lolote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.
JOH 16:25 “Nimewaambia mambo haya kwa mafumbo. Saa yaja ambapo sitazungumza nanyi tena kwa mafumbo bali nitawaeleza waziwazi kuhusu Baba.
JOH 16:26 Siku hiyo mtaomba kwa Jina langu. Wala sitawaambia kwamba nitamwomba Baba kwa ajili yenu,
JOH 16:27 kwa maana Baba mwenyewe anawapenda, kwa sababu mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.
JOH 16:28 Nilitoka kwa Baba na kuja ulimwenguni; sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”
JOH 16:29 Ndipo wanafunzi wake wakasema, “Sasa unazungumza waziwazi, wala si kwa mafumbo.
JOH 16:30 Sasa tumejua kwamba wewe unajua mambo yote, wala hakuna haja ya mtu kukuuliza maswali. Kwa jambo hili tunaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”
JOH 16:31 Isa akawajibu, “Je, sasa mnaamini?
JOH 16:32 Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani mwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami.
JOH 16:33 “Nimewaambia mambo haya ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”
JOH 17:1 Baada ya Isa kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema: “Baba, saa imewadia. Mtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe.
JOH 17:2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa.
JOH 17:3 Nao uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe uliye Mungu wa pekee wa kweli, na Isa Al-Masihi uliyemtuma.
JOH 17:4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye.
JOH 17:5 Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujaumbwa.
JOH 17:6 “Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako.
JOH 17:7 Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako,
JOH 17:8 kwa kuwa maneno yale uliyonipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma.
JOH 17:9 Ninawaombea wao. Siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako.
JOH 17:10 Wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao.
JOH 17:11 Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.
JOH 17:12 Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia.
JOH 17:13 “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao.
JOH 17:14 Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia, kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu.
JOH 17:15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu.
JOH 17:16 Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu.
JOH 17:17 Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndilo kweli.
JOH 17:18 Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo.
JOH 17:19 Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.
JOH 17:20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao,
JOH 17:21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako. Wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma mimi.
JOH 17:22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.
JOH 17:23 Mimi ndani yao na wewe ndani yangu: ili wawe wamekamilika katika umoja, na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
JOH 17:24 “Baba, shauku yangu ni kwamba wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.
JOH 17:25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma.
JOH 17:26 Nimefanya jina lako lijulikane kwao, nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao, na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”
JOH 18:1 Isa alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake, wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani; yeye na wanafunzi wake wakaingia humo.
JOH 18:2 Basi Yuda, aliyemsaliti, alipafahamu mahali hapo, kwani Isa alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara.
JOH 18:3 Hivyo Yuda akaja kwenye bustani akiongoza kikosi cha askari Warumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha.
JOH 18:4 Isa, akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao, akawauliza, “Mnamtafuta nani?”
JOH 18:5 Wao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.” Isa akawajibu, “Mimi ndiye.” (Yuda, aliyemsaliti, alikuwa amesimama pamoja nao.)
JOH 18:6 Isa alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini!
JOH 18:7 Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.”
JOH 18:8 Isa akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.”
JOH 18:9 Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”
JOH 18:10 Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. (Mtumishi huyo aliitwa Malko.)
JOH 18:11 Isa akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?”
JOH 18:12 Hivyo wale askari, wakiwa na jemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Isa na kumfunga.
JOH 18:13 Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule.
JOH 18:14 Kayafa ndiye alikuwa amewashauri viongozi wa Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.
JOH 18:15 Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Isa. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia uani kwa kuhani mkuu pamoja na Isa.
JOH 18:16 Lakini Petro alisimama nje karibu na lango. Ndipo yule mwanafunzi mwingine, aliyejulikana na kuhani mkuu, akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani.
JOH 18:17 Yule msichana akamuuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akajibu, “Sio mimi.”
JOH 18:18 Wale watumishi na askari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.
JOH 18:19 Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Isa kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake.
JOH 18:20 Isa akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni, mahali Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri.
JOH 18:21 Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale waliosikia yale niliyowaambia. Wanajua niliyoyasema.”
JOH 18:22 Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye akampiga Isa kofi usoni. Kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?”
JOH 18:23 Isa akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?”
JOH 18:24 Ndipo Anasi akampeleka Isa kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa.
JOH 18:25 Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya watu waliokuwepo wakamuuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?” Petro akakana, akasema, “Sio mimi.”
JOH 18:26 Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamuuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Isa?”
JOH 18:27 Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati huo huo.
JOH 18:28 Ndipo viongozi wa Wayahudi wakamchukua Isa kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala Mrumi. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri. Ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani ya jumba kwa sababu walitaka kushiriki katika Pasaka.
JOH 18:29 Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa, akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”
JOH 18:30 Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu, tusingemleta kwako.”
JOH 18:31 Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.”
JOH 18:32 Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Isa kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.
JOH 18:33 Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Isa, akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?”
JOH 18:34 Isa akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu?”
JOH 18:35 Pilato akamjibu, “Je, mimi ni Myahudi? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”
JOH 18:36 Isa akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa viongozi wa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”
JOH 18:37 Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Isa akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni: ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”
JOH 18:38 Pilato akamuuliza Isa, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena, akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Isa, “Sioni msingi wowote wa kumshtaki mtu huyu.
JOH 18:39 Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘mfalme wa Wayahudi’?”
JOH 18:40 Wao wakapiga kelele, wakajibu, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyang’anyi.
JOH 19:1 Ndipo Pilato akamtoa Isa akaamuru apigwe mijeledi.
JOH 19:2 Askari wakasokota taji la miiba, wakamvika Isa kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau.
JOH 19:3 Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.
JOH 19:4 Pilato akatoka tena nje, akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Isa kwenu kuwajulisha kwamba mimi sioni msingi wowote wa kumshtaki.”
JOH 19:5 Kwa hiyo Isa akatoka nje akiwa amevaa lile taji la miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, mtu ndiye huyu!”
JOH 19:6 Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe. Lakini mimi sioni msingi wowote wa kumshtaki.”
JOH 19:7 Viongozi wa Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria, na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.”
JOH 19:8 Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi.
JOH 19:9 Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Isa, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Isa hakumjibu.
JOH 19:10 Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”
JOH 19:11 Ndipo Isa akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”
JOH 19:12 Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Isa, lakini viongozi wa Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”
JOH 19:13 Pilato aliposikia maneno haya, akamtoa Isa nje tena. Akaketi kwenye kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe (kwa Kiebrania ni Gabatha).
JOH 19:14 Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”
JOH 19:15 Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?” Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”
JOH 19:16 Ndipo Pilato akamkabidhi Isa kwao ili wamsulubishe. Kwa hiyo askari wakamchukua Isa.
JOH 19:17 Isa, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha).
JOH 19:18 Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wawili, mmoja kila upande wake, naye Isa katikati.
JOH 19:19 Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Isa; likasema: Isa Al-Nasiri Mfalme wa Wayahudi.
JOH 19:20 Kwa kuwa mahali hapo Isa aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini.
JOH 19:21 Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.”
JOH 19:22 Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”
JOH 19:23 Askari walipokwisha kumsulubisha Isa, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono, bali limefumwa tangu juu hadi chini.
JOH 19:24 Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.” Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema, “Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura.” Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.
JOH 19:25 Karibu na msalaba wa Isa walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Mariamu mke wa Klopa, na Mariamu Magdalene.
JOH 19:26 Isa alipomwona mama yake mahali pale, na yule mwanafunzi aliyempenda akiwa amesimama karibu, Isa akamwambia mama yake, “Mama, huyu hapa ndiye mwanao.”
JOH 19:27 Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyu hapa ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Isa nyumbani mwake.
JOH 19:28 Baada ya haya, akijua kuwa mambo yote yamemalizika, na ili kutimiza Maandiko, Isa akasema, “Naona kiu.”
JOH 19:29 Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni.
JOH 19:30 Baada ya kuionja hiyo siki, Isa akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.
JOH 19:31 Ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, na siku iliyofuata ingekuwa Sabato maalum. Kwa kuwa viongozi wa Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe, na miili iondolewe kwenye misalaba.
JOH 19:32 Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Isa, na ya yule mwingine pia.
JOH 19:33 Lakini walipomkaribia Isa, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake.
JOH 19:34 Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni, na mara pakatoka damu na maji.
JOH 19:35 Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini.
JOH 19:36 Kwa maana mambo haya yalitukia ili andiko litimie, lisemalo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.”
JOH 19:37 Tena andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.”
JOH 19:38 Baada ya mambo haya, Yusufu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Isa, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Isa. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua.
JOH 19:39 Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Isa usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini.
JOH 19:40 Wakauchukua mwili wa Isa, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi.
JOH 19:41 Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado.
JOH 19:42 Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Isa humo.
JOH 20:1 Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa bado giza, Mariamu Magdalene alienda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio.
JOH 20:2 Hivyo akakimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Isa alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!”
JOH 20:3 Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara moja kuelekea kaburini.
JOH 20:4 Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini.
JOH 20:5 Akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani, lakini hakuingia.
JOH 20:6 Ndipo Simoni Petro akaja akimfuata nyuma, akaingia ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini,
JOH 20:7 na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Isa. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda.
JOH 20:8 Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini akaingia ndani, akaona, na akaamini.
JOH 20:9 (Kwa kuwa hadi wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Isa afufuke kutoka kwa wafu.)
JOH 20:10 Kisha hao wanafunzi wakaondoka, wakarudi nyumbani mwao.
JOH 20:11 Lakini Mariamu Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama kuchungulia mle kaburini,
JOH 20:12 naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Isa ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.
JOH 20:13 Wakamuuliza Mariamu, “Mwanamke, mbona unalia?” Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu, na sijui walikomweka.”
JOH 20:14 Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Isa amesimama, lakini hakumtambua.
JOH 20:15 Isa akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?” Mariamu, akidhani alikuwa anaongea na mtunza bustani, akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nioneshe ulikomweka, nami nitamchukua.”
JOH 20:16 Isa akamwita, “Mariamu!” Ndipo Mariamu akamgeukia Isa na kusema naye kwa Kiebrania, “Raboni!” (maana yake “Mwalimu”).
JOH 20:17 Isa akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”
JOH 20:18 Kwa hiyo Mariamu Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Isa, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Isa alikuwa amemweleza mambo hayo yote.
JOH 20:19 Ilipokuwa jioni ya siku hiyo hiyo ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Naye Isa akawatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”
JOH 20:20 Baada ya kusema haya, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana Isa.
JOH 20:21 Isa akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi.”
JOH 20:22 Alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu wa Mungu.
JOH 20:23 Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa; na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”
JOH 20:24 Lakini Tomaso (aliyeitwa Didimasi), mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Isa alipokuja.
JOH 20:25 Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana Isa.” Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari, na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”
JOH 20:26 Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Isa akaja, milango ikiwa imefungwa, na kusimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi.”
JOH 20:27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”
JOH 20:28 Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”
JOH 20:29 Isa akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”
JOH 20:30 Isa alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki.
JOH 20:31 Lakini hii imeandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Isa ndiye Al-Masihi, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.
JOH 21:1 Baada ya haya Isa akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia. Yeye alijionesha kwao hivi:
JOH 21:2 Simoni Petro, Tomaso (aitwaye Didimasi), Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo, na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja.
JOH 21:3 Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutaenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata chochote.
JOH 21:4 Mara baada ya kupambazuka, Isa akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Isa.
JOH 21:5 Isa akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?” Wakamjibu, “La.”
JOH 21:6 Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu, na tazama, wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.
JOH 21:7 Basi yule mwanafunzi aliyependwa na Isa akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana Isa!” Simoni Petro aliposikia kwamba ni Bwana Isa, akajifunga nguo yake (kwa kuwa alikuwa ameitoa), naye akajitosa baharini.
JOH 21:8 Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa mia mbili.
JOH 21:9 Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake, na mikate.
JOH 21:10 Isa akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”
JOH 21:11 Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu ufuoni. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa mia moja hamsini na watatu (153). Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika.
JOH 21:12 Isa akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Walijua kuwa ni Bwana Isa.
JOH 21:13 Isa akaja, akachukua ule mkate, akawapa, na vivyo hivyo akawagawia wale samaki.
JOH 21:14 Hii ilikuwa mara ya tatu Isa kuwatokea wanafunzi wake baada yake kufufuliwa kutoka kwa wafu.
JOH 21:15 Walipokwisha kula, Isa akamuuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?” Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.” Isa akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”
JOH 21:16 Isa akamuuliza tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?” Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.” Isa akamwambia, “Chunga kondoo wangu.”
JOH 21:17 Kwa mara ya tatu Isa akamuuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?” Petro akahuzunika sana kwa kuwa Isa alimuuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.” Isa akamwambia, “Lisha kondoo wangu.
JOH 21:18 Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka. Lakini utakapokuwa mzee, utanyoosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.”
JOH 21:19 Isa alisema haya ili kuashiria aina ya kifo ambacho Petro angemtukuza nacho Mungu. Kisha Isa akamwambia Petro, “Nifuate!”
JOH 21:20 Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Isa akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Isa walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”)
JOH 21:21 Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamuuliza Isa, “Bwana, na huyu je?”
JOH 21:22 Isa akamjibu, “Ikiwa nataka aishi hadi nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!”
JOH 21:23 Kwa sababu ya maneno haya ya Isa, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Isa hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi hadi nitakaporudi, inakuhusu nini?”
JOH 21:24 Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya, na ndiye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
JOH 21:25 Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Isa alifanya. Kama yote yangeandikwa, nadhani hata ulimwengu wote haungekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu ambavyo vingeandikwa.
ACT 1:1 Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, Theofilo, kuhusu mambo yote Isa aliyoyafanya na kufundisha tangu mwanzo,
ACT 1:2 hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wa Mungu wale mitume aliowachagua.
ACT 1:3 Baada ya mateso yake, alijionesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu ufalme wa Mungu.
ACT 1:4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake.
ACT 1:5 Yahya aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho wa Mungu.”
ACT 1:6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Isa, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
ACT 1:7 Isa akawaambia, “Sio wajibu wenu kujua nyakati au majira ambayo Baba ameyaweka kwa mamlaka yake mwenyewe.
ACT 1:8 Lakini mtapokea nguvu, Roho wa Mungu akiwajilia juu yenu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na Yudea yote, na Samaria, na miisho ya dunia.”
ACT 1:9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
ACT 1:10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake mbinguni, ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao.
ACT 1:11 Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Isa aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni, atarudi tena jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.”
ACT 1:12 Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato kutoka mjini.
ACT 1:13 Walipowasili mjini Yerusalemu, walienda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo na Andrea; Filipo na Tomaso; Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo.
ACT 1:14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pia walikuwepo wanawake kadhaa, na Mariamu mama yake Isa, na ndugu zake Isa.
ACT 1:15 Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao walikuwa watu wapatao mia moja na ishirini), akasema,
ACT 1:16 “Ndugu zangu, ilibidi andiko litimie, ambalo Roho wa Mungu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda, aliyewaongoza wale waliomkamata Isa.
ACT 1:17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”
ACT 1:18 (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje.
ACT 1:19 Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu.)
ACT 1:20 “Kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Zaburi, “ ‘Mahali pake na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’ na, “ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’
ACT 1:21 Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Isa alipokuwa akiishi kati yetu,
ACT 1:22 kuanzia ubatizo wa Yahya hadi siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”
ACT 1:23 Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yusufu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya.
ACT 1:24 Kisha wakaomba, wakasema, “Mwenyezi Mungu, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua
ACT 1:25 ili achukue nafasi ya huduma ya utume, ambayo Yuda aliiacha ili aende anapostahili.”
ACT 1:26 Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.
ACT 2:1 Siku ya Pentekoste ilipowadia, waumini wote walikuwa mahali pamoja.
ACT 2:2 Ghafula, sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali ikatoka mbinguni, ikaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi.
ACT 2:3 Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.
ACT 2:4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.
ACT 2:5 Basi walikuwako Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu.
ACT 2:6 Waliposikia sauti hii, umati wa watu walikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
ACT 2:7 Wakiwa wameshangaa na kustaajabu, wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya?
ACT 2:8 Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa?
ACT 2:9 Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na jimbo la Asia,
ACT 2:10 Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni kutoka Rumi
ACT 2:11 (Wayahudi na wale walioongokea dini ya Kiyahudi), Wakrete na Waarabu: sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.”
ACT 2:12 Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”
ACT 2:13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa kwa divai!”
ACT 2:14 Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akapaza sauti yake na kuhutubia umati ule wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na nyote mnaoishi Yerusalemu, nisikilizeni kwa makini, ili jambo hili lijulikane kwenu.
ACT 2:15 Hakika watu hawa hawajalewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi!
ACT 2:16 La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:
ACT 2:17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
ACT 2:18 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri.
ACT 2:19 Nami nitaonesha maajabu juu mbinguni, na ishara chini duniani: damu, moto, na mawimbi ya moshi.
ACT 2:20 Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Mwenyezi Mungu iliyo tukufu.
ACT 2:21 Na kila mtu atakayeliitia jina la Mwenyezi Mungu, ataokolewa.’
ACT 2:22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Isa Al-Nasiri alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo.
ACT 2:23 Baada ya huyu mtu kutolewa kwenu kwa mpango wa Mungu uliokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi mlimuua kwa kumsulubisha msalabani, kwa mikono ya watu waovu.
ACT 2:24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.
ACT 2:25 Kwa maana Daudi asema hivi kumhusu: “ ‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika.
ACT 2:26 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini.
ACT 2:27 Kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.
ACT 2:28 Umenionesha njia za uzima, utanijaza na furaha mbele zako.’
ACT 2:29 “Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu wa zamani Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa hadi leo.
ACT 2:30 Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo, kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha utawala.
ACT 2:31 Daudi, akiona mambo yaliyo mbele, akanena kuhusu kufufuka kwa Al-Masihi, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu.
ACT 2:32 Mungu alimfufua huyu Isa, na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo.
ACT 2:33 Basi yeye ametukuzwa hadi mkono wa kuume wa Mungu, na amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu wa Mungu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia.
ACT 2:34 Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema, “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume,
ACT 2:35 hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’
ACT 2:36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Isa, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Al-Masihi.”
ACT 2:37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
ACT 2:38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Isa Al-Masihi, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho wa Mungu.
ACT 2:39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
ACT 2:40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.”
ACT 2:41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa, na siku ile waliongezeka watu wapatao elfu tatu.
ACT 2:42 Nao wakadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali.
ACT 2:43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume.
ACT 2:44 Waumini wote walikuwa mahali pamoja, nao wakashirikiana katika mambo yote.
ACT 2:45 Waliuza mali yao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
ACT 2:46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe,
ACT 2:47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kundi la waumini wa Isa wale waliokuwa wakiokolewa.
ACT 3:1 Siku moja, Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali, yapata saa tisa alasiri.
ACT 3:2 Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni.
ACT 3:3 Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka.
ACT 3:4 Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.”
ACT 3:5 Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.
ACT 3:6 Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nitakachokupa. Kwa jina la Isa Al-Masihi wa Nasiri, tembea!”
ACT 3:7 Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu.
ACT 3:8 Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu.
ACT 3:9 Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu,
ACT 3:10 wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu kwa yale yaliyomtukia.
ACT 3:11 Aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wakiwakimbilia pale Ukumbi wa Sulemani.
ACT 3:12 Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi Waisraeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemfanya mtu huyu kutembea?
ACT 3:13 Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Isa, ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato, ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake.
ACT 3:14 Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki, mkaomba mpewe yule muuaji.
ACT 3:15 Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya.
ACT 3:16 Kwa imani katika jina la Isa, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni jina la Isa na imani kutoka kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama nyote mnavyoona.
ACT 3:17 “Sasa ndugu zangu, najua ya kuwa ninyi mlitenda bila kujua, kama walivyofanya viongozi wenu.
ACT 3:18 Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Al-Masihi atateswa.
ACT 3:19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kutoka kwake Mwenyezi Mungu,
ACT 3:20 naye apate kumtuma Al-Masihi, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Isa.
ACT 3:21 Ilimpasa mbingu zimpokee hadi wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa manabii wake watakatifu.
ACT 3:22 Kwa maana Musa alisema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu. Itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia.
ACT 3:23 Mtu ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atatupiliwa mbali kabisa na watu wake.’
ACT 3:24 “Naam, manabii wote tangu Samweli na waliokuja baada yake, wote walitabiri kuhusu siku hizi.
ACT 3:25 Ninyi ndio wana wa manabii na wa agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Ibrahimu, ‘Kupitia kwa uzao wako, watu wote wa ulimwengu watabarikiwa.’
ACT 3:26 Mungu alipomfufua Isa Mwanawe, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya.”
ACT 4:1 Petro na Yohana walipokuwa wakisema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masadukayo wakawajia,
ACT 4:2 huku wakiwa wamekasirika sana kwa sababu mitume walikuwa wanawafundisha watu na kuhubiri kwamba kuna ufufuo wa wafu ndani ya Isa.
ACT 4:3 Wakawakamata Petro na Yohana na kuwafunga gerezani hadi kesho yake kwa kuwa ilikuwa jioni.
ACT 4:4 Lakini wengi waliosikia lile neno waliamini, idadi yao ilikuwa yapata wanaume elfu tano.
ACT 4:5 Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na walimu wa Torati walikusanyika Yerusalemu.
ACT 4:6 Walikuwemo kuhani mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda, na wengi wa jamaa ya kuhani mkuu.
ACT 4:7 Baada ya kuwasimamisha Petro na Yohana katikati yao, wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au kwa jina la nani mmefanya jambo hili?”
ACT 4:8 Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu wa Mungu, akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu,
ACT 4:9 kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa,
ACT 4:10 ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Isa Al-Masihi wa Nasiri, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa.
ACT 4:11 Huyu ndiye “ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa, ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’
ACT 4:12 Wala hakuna wokovu katika mwingine yeyote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu linalopasa kutuokoa.”
ACT 4:13 Viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Isa.
ACT 4:14 Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lolote kuwapinga.
ACT 4:15 Wakawaamuru watoke nje ya Baraza la Wayahudi, ili wasemezane jambo hilo wao wenyewe.
ACT 4:16 Wakaulizana, “Tuwafanyie nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha muujiza huu mkubwa walioufanya, ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu.
ACT 4:17 Lakini ili kuzuia jambo hili lisiendelee kuenea zaidi kwa watu, ni lazima tuwaonye watu hawa ili wasiseme tena na mtu yeyote kwa jina la Isa.”
ACT 4:18 Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Isa.
ACT 4:19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu.
ACT 4:20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
ACT 4:21 Baada ya vitisho vingi, wakawaachia waende zao. Hawakuona njia yoyote ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu, kwa kuwa watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetukia.
ACT 4:22 Kwa kuwa umri wa yule mtu aliyekuwa ameponywa kwa muujiza ulikuwa zaidi ya miaka arobaini.
ACT 4:23 Punde Petro na Yohana walipoachiliwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee.
ACT 4:24 Watu waliposikia hayo, wakapaza sauti zao, wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeziumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo.
ACT 4:25 Wewe ulinena kwa Roho wa Mungu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema: “ ‘Mbona mataifa wanaghadhibika, na makabila ya watu kuwaza ubatili?
ACT 4:26 Wafalme wa dunia wamejipanga, na watawala wanakusanyika pamoja dhidi ya Mwenyezi Mungu na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.’
ACT 4:27 Ni kweli Herode na Pontio Pilato, pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu kupanga njama dhidi ya mwanao mtakatifu Isa, uliyempaka mafuta.
ACT 4:28 Wakafanya yale uweza wako na mapenzi yako yalikusudia yatokee tangu zamani.
ACT 4:29 Sasa, Mwenyezi Mungu, angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu.
ACT 4:30 Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Isa.”
ACT 4:31 Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.
ACT 4:32 Waumini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho.
ACT 4:33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Isa kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote.
ACT 4:34 Wala hapakuwa mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa,
ACT 4:35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
ACT 4:36 Yusufu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja),
ACT 4:37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.
ACT 5:1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja.
ACT 5:2 Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.
ACT 5:3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho wa Mungu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja?
ACT 5:4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja, si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, je, fedha ulizozipata, si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.”
ACT 5:5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia.
ACT 5:6 Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakampeleka nje kumzika.
ACT 5:7 Muda wa saa tatu baadaye, mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia.
ACT 5:8 Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”
ACT 5:9 Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakupeleka nje.”
ACT 5:10 Wakati ule ule, akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe.
ACT 5:11 Hofu kuu ikalipata kundi la waumini wa Isa lote, pamoja na watu wote waliosikia kuhusu matukio haya.
ACT 5:12 Mitume walifanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Waumini wote walikuwa wakikusanyika katika Ukumbi wa Sulemani.
ACT 5:13 Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao, ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu.
ACT 5:14 Hata hivyo, waliomwamini Bwana Isa wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake.
ACT 5:15 Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao.
ACT 5:16 Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.
ACT 5:17 Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo, wakajawa na wivu.
ACT 5:18 Wakawakamata mitume na kuwafunga gerezani.
ACT 5:19 Lakini wakati wa usiku, malaika wa Mwenyezi Mungu akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia,
ACT 5:20 “Nendeni, mkasimame Hekaluni, mkawaambie watu maneno yote ya maisha haya mapya.”
ACT 5:21 Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu. Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya Baraza la Wayahudi, yaani wazee wote wa Israeli. Wakatumana wale mitume waletwe kutoka gerezani.
ACT 5:22 Lakini wale walinzi wa Hekalu walipoenda gerezani hawakuwakuta mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari.
ACT 5:23 Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na askari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu yeyote.”
ACT 5:24 Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.
ACT 5:25 Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu mliowafunga gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.”
ACT 5:26 Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na askari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.
ACT 5:27 Waliwaleta mitume, wakawasimamisha mbele ya Baraza la Wayahudi ili kuhani mkuu awahoji.
ACT 5:28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
ACT 5:29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.
ACT 5:30 Mungu wa baba zetu alimfufua Isa kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba.
ACT 5:31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi.
ACT 5:32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu wa Mungu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”
ACT 5:33 Wale wajumbe wa Baraza la Wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua mitume.
ACT 5:34 Lakini Farisayo mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa Torati, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya Baraza la Wayahudi, akaamuru mitume watolewe nje kwa muda.
ACT 5:35 Ndipo alipowaambia wazee wa Baraza, “Enyi wanaume wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa.
ACT 5:36 Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao mia nne walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu.
ACT 5:37 Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika.
ACT 5:38 Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waachieni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa.
ACT 5:39 Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”
ACT 5:40 Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Isa, wakawaachia waende zao.
ACT 5:41 Nao mitume wakatoka nje ya Baraza la Wayahudi, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Isa.
ACT 5:42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri Habari Njema kwamba Isa ndiye Al-Masihi.
ACT 6:1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, Wayahudi wa Kiyunani walinung’unika dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawo wa chakula wa kila siku.
ACT 6:2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani.
ACT 6:3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu wa Mungu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii,
ACT 6:4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na katika huduma ya neno.”
ACT 6:5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho wa Mungu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao kutoka Antiokia, mtu wa Mataifa aliyeongokea dini ya Kiyahudi.
ACT 6:6 Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono.
ACT 6:7 Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu, hata makuhani wengi wakaitii ile imani.
ACT 6:8 Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu.
ACT 6:9 Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa) la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na jimbo la Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano.
ACT 6:10 Lakini hawakuweza kushindana na ile hekima aliyopewa na Roho wa Mungu alipokuwa akisema.
ACT 6:11 Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Musa na dhidi ya Mungu.”
ACT 6:12 Wakawachochea watu, wazee na walimu wa Torati, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya Baraza la Wayahudi.
ACT 6:13 Wakawaleta mashahidi wa uongo ambao walishuhudia, wakasema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Torati.
ACT 6:14 Kwa maana tumemsikia akisema kwamba Isa Al-Nasiri atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Musa.”
ACT 6:15 Watu wote waliokuwa wameketi katika Baraza la Wayahudi wakamkazia macho Stefano, wakaona uso wake unang’aa kama uso wa malaika.
ACT 7:1 Ndipo kuhani mkuu akamuuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?”
ACT 7:2 Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani,
ACT 7:3 akamwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na katika jamii yako, uende hadi nchi nitakayokuonesha.’
ACT 7:4 “Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa.
ACT 7:5 Mungu hakumpa urithi wowote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Ibrahimu hakuwa na mtoto.
ACT 7:6 Mungu akasema naye hivi: ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne.’
ACT 7:7 Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka katika nchi hiyo na wataniabudu mahali hapa.’
ACT 7:8 Ndipo akampa Ibrahimu agano la tohara. Naye Ibrahimu akamzaa Isaka na kumtahiri siku ya nane. Baadaye Isaka akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale baba zetu wa zamani kumi na wawili.
ACT 7:9 “Kwa sababu hao baba zetu wa zamani walimwonea wivu Yusufu ndugu yao, walimuuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye.
ACT 7:10 Akamwokoa kutoka mateso yote yaliyompata. Tena Mungu akampa Yusufu kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Naye Farao akamweka kuwa mtawala wa Misri na wa jumba lote la kifalme.
ACT 7:11 “Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula.
ACT 7:12 Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza.
ACT 7:13 Walipoenda mara ya pili, Yusufu alijitambulisha kwa ndugu zake; naye Farao akapata habari kuhusu ndugu za Yusufu.
ACT 7:14 Ndipo Yusufu akawatuma kumleta Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote; kwa jumla walikuwa watu sabini na watano.
ACT 7:15 Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia.
ACT 7:16 Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Ibrahimu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.
ACT 7:17 “Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Ibrahimu, watu wetu walizidi kuongezeka sana huko Misri.
ACT 7:18 Ndipo ‘mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri’.
ACT 7:19 Huyu mfalme akawatendea watu wetu hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe.
ACT 7:20 “Wakati huo Musa alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani mwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu.
ACT 7:21 Walipomweka nje mtoni, binti Farao akamchukua akamlea kama mtoto wake.
ACT 7:22 Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo.
ACT 7:23 “Musa alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli.
ACT 7:24 Aliona mmoja wao akidhulumiwa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamuua kulipiza kisasi.
ACT 7:25 Musa alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa.
ACT 7:26 Siku iliyofuata Musa aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kudhulumiana?’
ACT 7:27 “Lakini yule mtu aliyekuwa akimdhulumu mwenzake akamsukuma Musa kando, akamuuliza, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?
ACT 7:28 Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’
ACT 7:29 Musa aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume.
ACT 7:30 “Baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Musa jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto.
ACT 7:31 Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Mwenyezi Mungu, ikisema:
ACT 7:32 ‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’ Musa alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama.
ACT 7:33 “Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.
ACT 7:34 Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’
ACT 7:35 “Huyu ndiye Musa waliyemkataa waliposema, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kupitia kwa yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka.
ACT 7:36 Aliwaongoza Waisraeli kutoka Misri baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamu, na katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.
ACT 7:37 “Huyu ndiye yule Musa aliyewaambia Waisraeli, ‘Mungu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe.’
ACT 7:38 Huyu ndiye yule Musa aliyekuwa katika kusanyiko huko jangwani, ambaye malaika alisema naye pamoja na baba zetu kwenye Mlima Sinai, naye akapokea maneno yaliyo hai ili atupatie.
ACT 7:39 “Lakini baba zetu walikataa kumtii Musa, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena.
ACT 7:40 Wakamwambia Haruni, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza, kwa maana mtu huyu Musa aliyetutoa nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.’
ACT 7:41 Huu ni ule wakati walitengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichokitengeneza kwa mikono yao wenyewe.
ACT 7:42 Ndipo Mungu akageuka, akawaachia waabudu jeshi lote la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Manabii: “ ‘Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli?
ACT 7:43 La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki, na nyota ya mungu wenu Refani, vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu. Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli.
ACT 7:44 “Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani, ambalo lilitengenezwa kama Mungu alivyomwelekeza Musa, kulingana na kielelezo alichokiona.
ACT 7:45 Baada ya kupokea Hema, baba zetu waliingia nalo walipokuja na Yoshua wakati walimiliki nchi, Mungu alipoyafukuza mataifa mbele yao. Nalo lilidumu katika nchi hadi wakati wa Daudi,
ACT 7:46 ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.
ACT 7:47 Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.
ACT 7:48 “Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema:
ACT 7:49 “ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani? asema Mwenyezi Mungu. Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?
ACT 7:50 Je, mkono wangu haukuumba vitu hivi vyote?’
ACT 7:51 “Enyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho wa Mungu, kama walivyofanya baba zenu.
ACT 7:52 Je, kuna nabii gani ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji.
ACT 7:53 Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”
ACT 7:54 Wazee wa Baraza la Wayahudi waliposikia haya wakaghadhibika, wakamsagia meno.
ACT 7:55 Lakini Stefano, akiwa amejawa na Roho wa Mungu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, na Isa akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
ACT 7:56 Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”
ACT 7:57 Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja.
ACT 7:58 Wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka mavazi yao miguuni mwa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.
ACT 7:59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Isa, pokea roho yangu.”
ACT 7:60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana, usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.
ACT 8:1 Naye Sauli alikua pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano. Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya waumini wa Isa huko Yerusalemu, nao waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Yudea na Samaria.
ACT 8:2 Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwomboleza sana.
ACT 8:3 Lakini Sauli alianza kuangamiza kundi la waumini. Aliingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani.
ACT 8:4 Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipoenda.
ACT 8:5 Filipo akaenda mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Al-Masihi.
ACT 8:6 Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza alizofanya, wakasikiliza kwa makini yale aliyosema.
ACT 8:7 Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele, na wengi waliopooza na viwete wakaponywa.
ACT 8:8 Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.
ACT 8:9 Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu,
ACT 8:10 nao watu wote, wakubwa kwa wadogo, wakamsikiliza na kustaajabu, wakisema, “Mtu huyu ndiye ajulikanaye kama Uweza Mkuu wa Mungu.”
ACT 8:11 Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake.
ACT 8:12 Lakini watu walipomwamini Filipo akihubiri Injili ya ufalme wa Mungu na jina la Isa Al-Masihi, wakabatizwa, wanaume na wanawake.
ACT 8:13 Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.
ACT 8:14 Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko.
ACT 8:15 Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu wa Mungu,
ACT 8:16 kwa sababu Roho wa Mungu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Isa.
ACT 8:17 Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho wa Mungu.
ACT 8:18 Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho wa Mungu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha
ACT 8:19 akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho wa Mungu.”
ACT 8:20 Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!
ACT 8:21 Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.
ACT 8:22 Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Mwenyezi Mungu. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako.
ACT 8:23 Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.”
ACT 8:24 Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Mwenyezi Mungu, ili hayo mliyosema lolote lisinitokee.”
ACT 8:25 Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana Isa, wakarudi Yerusalemu wakihubiri Injili katika vijiji vingi vya Samaria.
ACT 8:26 Basi malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara inayotoka Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.”
ACT 8:27 Hivyo akaondoka. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa ameenda Yerusalemu ili kuabudu,
ACT 8:28 naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi kwenye gari lake la vita akisoma kitabu cha nabii Isaya.
ACT 8:29 Roho wa Mungu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”
ACT 8:30 Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamuuliza, “Je, unaelewa hayo unayoyasoma?”
ACT 8:31 Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye.
ACT 8:32 Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la Maandiko: “Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni, kama mwana-kondoo anyamazavyo mbele yake yule amkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake.
ACT 8:33 Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake. Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake? Kwa maana maisha yake yaliondolewa kutoka duniani.”
ACT 8:34 Yule towashi akamuuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?”
ACT 8:35 Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la Maandiko, akamweleza Injili ya Isa.
ACT 8:36 Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamuuliza Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” [
ACT 8:37 Filipo akamwambia, “Ukiamini kwa moyo wako wote, unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Isa Al-Masihi ni Mwana wa Mungu.”]
ACT 8:38 Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Filipo na yule towashi wakateremka kwenye maji pamoja, naye Filipo akambatiza.
ACT 8:39 Nao walipotoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi.
ACT 8:40 Filipo akajikuta Azoto; akasafiri akihubiri Injili katika miji yote hadi akafika Kaisaria.
ACT 9:1 Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana Isa, akamwendea kuhani mkuu,
ACT 9:2 naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mfuasi yeyote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu.
ACT 9:3 Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza pande zote.
ACT 9:4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”
ACT 9:5 Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?” Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Isa unayemtesa.
ACT 9:6 Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa unachopaswa kufanya.”
ACT 9:7 Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza.
ACT 9:8 Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza hadi Dameski.
ACT 9:9 Kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu; naye hakula wala kunywa chochote.
ACT 9:10 Huko Dameski kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana Isa alimwita katika maono, “Anania!” Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”
ACT 9:11 Bwana Isa akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba,
ACT 9:12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”
ACT 9:13 Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu.
ACT 9:14 Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”
ACT 9:15 Lakini Bwana Isa akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo nilichochagua kutangaza jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na watu wa Israeli.
ACT 9:16 Nami nitamwonesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”
ACT 9:17 Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Isa aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu wa Mungu.”
ACT 9:18 Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa.
ACT 9:19 Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.
ACT 9:20 Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba Isa Al-Masihi ni Mwana wa Mungu.
ACT 9:21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?”
ACT 9:22 Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Isa ndiye Al-Masihi.
ACT 9:23 Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakapanga njama kumuua Sauli.
ACT 9:24 Lakini Sauli akagundua njama yao. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua.
ACT 9:25 Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.
ACT 9:26 Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi.
ACT 9:27 Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana Isa, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Isa huko Dameski.
ACT 9:28 Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana Isa.
ACT 9:29 Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani, lakini wao walijaribu kumuua.
ACT 9:30 Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.
ACT 9:31 Ndipo waumini katika Yudea yote, Galilaya na Samaria wakawa na wakati wa amani. Likatiwa nguvu; na kwa kuwezeshwa na Roho wa Mungu, idadi yao ikaongezeka, na wakaendelea kudumu katika kumcha Bwana.
ACT 9:32 Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alienda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida.
ACT 9:33 Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, aliyekuwa amepooza na kwa muda wa miaka nane alikuwa hajatoka kitandani.
ACT 9:34 Petro akamwambia, “Ainea, Isa Al-Masihi anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka.
ACT 9:35 Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana Isa.
ACT 9:36 Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini.
ACT 9:37 Wakati huo akaugua, akafa, na wakauosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani.
ACT 9:38 Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”
ACT 9:39 Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao. Alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.
ACT 9:40 Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi.
ACT 9:41 Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai.
ACT 9:42 Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana Isa.
ACT 9:43 Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.
ACT 10:1 Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu aliyeitwa Kornelio, aliyekuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia.
ACT 10:2 Yeye na jamaa yake yote walikuwa wacha Mungu; alitoa kwa ukarimu kwa wale walio na mahitaji na kumwomba Mungu mara kwa mara.
ACT 10:3 Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”
ACT 10:4 Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?” Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
ACT 10:5 Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro.
ACT 10:6 Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”
ACT 10:7 Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia.
ACT 10:8 Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.
ACT 10:9 Siku iliyofuata, walipokuwa wanaukaribia mji, yapata saa sita mchana, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba.
ACT 10:10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana.
ACT 10:11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama kitambaa kikubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne.
ACT 10:12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani.
ACT 10:13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”
ACT 10:14 Petro akajibu, “La hasha, Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”
ACT 10:15 Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”
ACT 10:16 Jambo hili lilitokea mara tatu, na ghafula kile kitambaa kikarudishwa mbinguni.
ACT 10:17 Petro alipokuwa akisumbuka kuhusu maana ya maono hayo, wale watu waliotumwa na Kornelio waliipata nyumba ya Simoni, wakasimama kwenye lango.
ACT 10:18 Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.
ACT 10:19 Wakati Petro akiwa anafikiria kuhusu yale maono, Roho wa Mungu akamwambia, “Simoni, kuna watu watatu wanaokutafuta.
ACT 10:20 Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”
ACT 10:21 Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”
ACT 10:22 Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani mwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.”
ACT 10:23 Basi Petro akawakaribisha ndani wawe wageni wake. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.
ACT 10:24 Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa na rafiki zake wa karibu.
ACT 10:25 Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni mwake kwa heshima.
ACT 10:26 Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”
ACT 10:27 Petro alipokuwa akizungumza naye, akaingia ndani na kuwakuta watu wengi wamekusanyika.
ACT 10:28 Akawaambia, “Mnajua kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi.
ACT 10:29 Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”
ACT 10:30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizong’aa akasimama mbele yangu,
ACT 10:31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na misaada yako kwa maskini imekumbukwa mbele za Mungu.
ACT 10:32 Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’
ACT 10:33 Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”
ACT 10:34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo,
ACT 10:35 lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye.
ACT 10:36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza Injili ya amani kupitia kwa Isa Al-Masihi. Yeye ni Bwana wa wote.
ACT 10:37 Mnajua yale yaliyotukia katika Yudea yote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yahya:
ACT 10:38 Jinsi Mungu alivyompaka mafuta Isa Al-Nasiri katika Roho wa Mungu, na jinsi alivyoenda kila mahali akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
ACT 10:39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Yudea na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani.
ACT 10:40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu.
ACT 10:41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.
ACT 10:42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alipakwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.
ACT 10:43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”
ACT 10:44 Petro alipokuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu wa Mungu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe.
ACT 10:45 Wale waumini waliokuwa wametahiriwa waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho wa Mungu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa.
ACT 10:46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akasema,
ACT 10:47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu wa Mungu kama sisi tulivyompokea.”
ACT 10:48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Isa Al-Masihi. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.
ACT 11:1 Mitume na waumini waliokuwa huko Yudea wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu.
ACT 11:2 Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, waumini waliotahiriwa wakamshutumu,
ACT 11:3 wakisema, “Ulienda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”
ACT 11:4 Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema,
ACT 11:5 “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama kitambaa kikubwa kikishuka kutoka mbinguni, kikashushwa kwa ncha zake nne, nacho kikanikaribia.
ACT 11:6 Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama mwitu, wanyama watambaao, na ndege wa angani.
ACT 11:7 Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’
ACT 11:8 “Nikajibu, ‘La hasha, Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’
ACT 11:9 “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’
ACT 11:10 Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.
ACT 11:11 “Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa.
ACT 11:12 Roho Mtakatifu wa Mungu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio.
ACT 11:13 Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro.
ACT 11:14 Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’
ACT 11:15 “Nami nilipoanza kusema, Roho wa Mungu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo.
ACT 11:16 Nami nikakumbuka yale Bwana Isa aliyosema, ‘Yahya alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho wa Mungu.’
ACT 11:17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupatia sisi tuliomwamini Bwana Isa Al-Masihi, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”
ACT 11:18 Waliposikia haya hawakuwa na lingine la kupinga. Nao wakamsifu Mungu, wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”
ACT 11:19 Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokea Stefano alipouawa walisafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu yeyote isipokuwa Wayahudi.
ACT 11:20 Lakini baadhi yao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakiwahubiria Injili kuhusu Bwana Isa.
ACT 11:21 Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana Isa.
ACT 11:22 Habari hizi zilipofika masikioni mwa waumini wa Isa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia.
ACT 11:23 Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana Isa kwa mioyo yao yote.
ACT 11:24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho wa Mungu, mwenye imani, nayo idadi kubwa ya watu wakaongezeka kwa Bwana Isa.
ACT 11:25 Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli,
ACT 11:26 naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na waumini na kufundisha idadi kubwa ya watu. Wanafunzi waliitwa wafuasi wa Al-Masihi mara ya kwanza huko Antiokia.
ACT 11:27 Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia.
ACT 11:28 Mmoja wao aliyeitwa Agabo akasimama, akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu wa Mungu kwamba njaa kubwa ingeenea ulimwengu mzima. (Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio.)
ACT 11:29 Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Yudea.
ACT 11:30 Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.
ACT 12:1 Wakati huo huo Mfalme Herode Agripa aliwakamata baadhi ya waumini wa Isa.
ACT 12:2 Akaamuru Yakobo, ndugu yake Yohana, auawe kwa upanga.
ACT 12:3 Alipoona jambo hilo limewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamkamata Petro pia. Hii ilitokea wakati wa Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu.
ACT 12:4 Baada ya kumkamata alimfunga gerezani chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari, vyenye askari wanne kila kimoja. Herode alikuwa amekusudia kumfanyia mashtaka mbele ya watu baada ya Pasaka.
ACT 12:5 Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini waumini wa Isa walikuwa wakimwombea kwa Mungu kwa bidii.
ACT 12:6 Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda lango la gereza.
ACT 12:7 Ghafula malaika wa Mwenyezi Mungu akatokea, na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.
ACT 12:8 Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.”
ACT 12:9 Petro akatoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono.
ACT 12:10 Walipita kundi la kwanza la walinzi na la pili, wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo, wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro.
ACT 12:11 Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yoyote kuwa Mwenyezi Mungu amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka makucha ya Herode Agripa na kutoka matazamio yote ya Wayahudi.”
ACT 12:12 Mara Petro alipotambua hili alienda nyumbani mwa Mariamu, mama yake Yohana aliyeitwa pia Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekutana kwa maombi.
ACT 12:13 Petro alipobisha hodi kwenye lango la nje, mjakazi aliyeitwa Roda akaja kumfungulia.
ACT 12:14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi mno akarudi bila kufungua lango, akapaza sauti, akasema, “Petro yuko langoni!”
ACT 12:15 Wakamwambia yule mjakazi, “Umerukwa na akili.” Alipozidi kusisitiza kuwa ni kweli, wakasema, “Lazima awe ni malaika wake.”
ACT 12:16 Lakini Petro aliendelea kugonga langoni, nao walipofungua lango na kumwona Petro, walistaajabu sana.
ACT 12:17 Yeye akawaashiria kwa mkono wake wanyamaze kimya, akawaeleza jinsi Mwenyezi Mungu alivyomtoa gerezani. Naye akaongeza kusema, “Waelezeni Yakobo na ndugu wengine habari hizi.” Kisha akaondoka akaenda sehemu nyingine.
ACT 12:18 Kulipokucha kukawa na fadhaa kubwa miongoni mwa wale askari kuhusu yaliyomtukia Petro.
ACT 12:19 Baada ya Herode kuamuru atafutwe kila mahali na bila kumpata, aliwahoji wale askari walinzi kisha akatoa amri wauawe. Basi Herode Agripa akatoka Yudea akaenda Kaisaria, akakaa huko kwa muda.
ACT 12:20 Basi Herode Agripa alikuwa amekasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Hivyo watu wa miji hiyo miwili wakaungana pamoja wakataka kukutana naye. Baada ya kuungwa mkono na Blasto, mtumishi maalum wa Mfalme Herode Agripa aliyeaminika, wakaomba mapatano ya amani maana nchi zao zilitegemea nchi ya huyo mfalme kwa mahitaji yao ya chakula.
ACT 12:21 Katika siku iliyochaguliwa Herode Agripa akavaa mavazi yake ya kifalme, akaketi kwenye kiti chake cha utawala, akawahutubia watu.
ACT 12:22 Watu waliokuwa wamekusanyika wakapaza sauti, wakisema, “Hii si sauti ya mwanadamu, bali ni ya Mungu!”
ACT 12:23 Ghafula, kwa kuwa Herode hakumpa Mungu utukufu, malaika wa Mwenyezi Mungu akampiga, naye akaliwa na chango, akafa.
ACT 12:24 Lakini neno la Mungu likaendelea mbele na kuenea, nao wengi wakaambatana nalo.
ACT 12:25 Barnaba na Sauli walipomaliza ile huduma yao iliyowapeleka, wakarudi Yerusalemu wakiwa pamoja na Yohana aitwaye Marko.
ACT 13:1 Katika kundi la waumini wa Isa huko Antiokia kulikuwa na manabii na walimu: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli.
ACT 13:2 Walipokuwa wakimwabudu Mwenyezi Mungu na kufunga, Roho Mtakatifu wa Mungu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi niliyowaitia.”
ACT 13:3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.
ACT 13:4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho wa Mungu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini hadi kisiwa cha Kipro.
ACT 13:5 Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kama msaidizi wao.
ACT 13:6 Walipokwisha kupita katika nchi zote hizo wakafika Pafo, ambapo walikutana na Myahudi mmoja mchawi aliyekuwa nabii wa uongo, jina lake Bar-Yesu.
ACT 13:7 Mtu huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mtu mwenye hekima aliyekuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala wa kile kisiwa. Sergio Paulo akawaita Sauli na Barnaba akitaka kusikia neno la Mungu.
ACT 13:8 Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani.
ACT 13:9 Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho wa Mungu, akamkazia macho Elima huyo mchawi,
ACT 13:10 akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Mwenyezi Mungu zilizo nyoofu?
ACT 13:11 Nawe sasa sikiliza, mkono wa Mwenyezi Mungu u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.” Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akapapasa akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwoneshe njia.
ACT 13:12 Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana Isa.
ACT 13:13 Kisha Paulo na wenzake wakasafiri toka Pafo wakafika Perga huko Pamfilia. Lakini, Yohana Marko akawaacha huko, akarejea Yerusalemu.
ACT 13:14 Kutoka Perga wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia. Siku ya Sabato wakaingia ndani ya sinagogi, wakaketi.
ACT 13:15 Baada ya Torati ya Musa na Kitabu cha Manabii kusomwa, viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mna neno la kuwafariji watu hawa, tafadhali lisemeni.”
ACT 13:16 Paulo akasimama, akawapungia mkono na kusema: “Enyi wanaume wa Israeli na ninyi nyote mnaomcha Mungu.
ACT 13:17 Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua baba zetu, akawafanya kustawi walipokuwa huko Misri, kwa uwezo mwingi akawaongoza na kuwatoa katika nchi ile.
ACT 13:18 Kwa muda wa miaka arobaini alivumilia matendo yao walipokuwa jangwani.
ACT 13:19 Naye baada ya kuyaangamiza mataifa saba yaliyokuwa yakiishi katika nchi ya Kanaani, akawapa Waisraeli nchi yao iwe urithi wao.
ACT 13:20 Haya yote yalichukua kama muda wa miaka mia nne na hamsini. “Baada ya haya, Mungu akawapa waamuzi hadi wakati wa nabii Samweli.
ACT 13:21 Ndipo watu wakaomba wapewe mfalme, naye Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini, aliyetawala kwa miaka arobaini.
ACT 13:22 Baada ya kumwondoa Sauli katika ufalme, akawainulia Daudi kuwa mfalme wao. Mungu pia alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayetimiza mapenzi yangu yote.’
ACT 13:23 “Kutoka uzao wa mtu huyu, Mungu amewaletea Israeli Mwokozi Isa, kama alivyoahidi.
ACT 13:24 Kabla ya kuja kwa Isa, Yahya alihubiri toba na ubatizo kwa watu wote wa Israeli.
ACT 13:25 Yahya alipokuwa anakamilisha kazi yake, alisema: ‘Ninyi mnadhani mimi ni nani? Mimi si yeye. La, lakini yeye yuaja baada yangu, ambaye mimi sistahili kufungua kamba za viatu vya miguu yake.’
ACT 13:26 “Ndugu zangu, wana wa Ibrahimu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.
ACT 13:27 Kwa sababu watu wa Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua, wala kuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye.
ACT 13:28 Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe.
ACT 13:29 Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini.
ACT 13:30 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu.
ACT 13:31 Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu.
ACT 13:32 “Nasi tunawaletea Habari Njema: kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu
ACT 13:33 sasa ameyatimiza kwetu sisi, watoto wao, kwa kumfufua Isa, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: “ ‘Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako.’
ACT 13:34 Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya: “ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika nilizomwahidi Daudi.’
ACT 13:35 Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi, “ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’
ACT 13:36 “Basi Daudi alipokwisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa na baba zake, na mwili wake ukaoza.
ACT 13:37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu.
ACT 13:38 “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kupitia kwa huyu Isa msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu.
ACT 13:39 Kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa Torati ya Musa.
ACT 13:40 Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate:
ACT 13:41 “ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka, mkastaajabu, mkaangamie, kwa maana nitatenda jambo wakati wenu ambalo hamtasadiki, hata kama mtu akiwaambia.’ ”
ACT 13:42 Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato iliyofuata.
ACT 13:43 Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na watu wa Mataifa walioongokea dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu.
ACT 13:44 Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Mwenyezi Mungu.
ACT 13:45 Lakini Wayahudi walipoona umati ule mkubwa wa watu, walijawa na wivu, wakayakanusha maneno Paulo aliyokuwa akisema.
ACT 13:46 Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu wa Mataifa.
ACT 13:47 Kwa maana hili ndilo Mwenyezi Mungu alilotuamuru: “ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa, ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’ ”
ACT 13:48 Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Mwenyezi Mungu; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.
ACT 13:49 Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote.
ACT 13:50 Lakini viongozi wa Wayahudi wakawachochea wanawake wenye kumcha Mungu, wenye vyeo pamoja na watu maarufu katika mji, wakachochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwafukuza kutoka eneo hilo.
ACT 13:51 Hivyo Paulo na Barnaba wakakung’uta mavumbi ya miguu yao ili kuwapinga, nao wakaenda Ikonio.
ACT 13:52 Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho wa Mungu.
ACT 14:1 Huko Ikonio Paulo na Barnaba waliingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi kama ilivyokuwa desturi yao. Huko wakahubiri kwa uwezo mkubwa kiasi kwamba Wayahudi pamoja na watu wa Mataifa wakaamini.
ACT 14:2 Lakini wale Wayahudi waliokataa kuamini wakawachochea watu wa Mataifa, wakatia chuki ndani ya mioyo yao dhidi ya waumini.
ACT 14:3 Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri kuhusu Bwana Isa, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza.
ACT 14:4 Lakini watu wa mji ule waligawanyika, wengine wakakubaliana na Wayahudi na wengine na mitume.
ACT 14:5 Watu wa Mataifa na Wayahudi wakajiunga na baadhi ya viongozi, wakafanya mpango wa kuwatendea mitume mabaya na kuwapiga mawe.
ACT 14:6 Lakini mitume walipopata habari hizi wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia na sehemu zilizopakana nayo.
ACT 14:7 Huko wakaendelea kuhubiri Injili.
ACT 14:8 Katika mji wa Listra, kulikuwa na kiwete, aliyekuwa amelemaa tangu kuzaliwa, na hakuwa ametembea kamwe.
ACT 14:9 Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa.
ACT 14:10 Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!
ACT 14:11 Umati ule wa watu walipoona yaliyokuwa yamefanywa na Paulo, wakapaza sauti, wakasema kwa lugha yao ya Kilikaonia, “Miungu imetushukia katika umbo la binadamu!”
ACT 14:12 Wakamwita Barnaba Zeu na Paulo wakamwita Herme kwa kuwa ndiye alikuwa msemaji mkuu.
ACT 14:13 Kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa nje kidogo tu ya mji, akaleta mafahali na mashada ya maua penye lango la mji kwa sababu yeye na umati ule wa watu walitaka kuwatolea dhabihu.
ACT 14:14 Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia haya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema,
ACT 14:15 “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea Habari Njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.
ACT 14:16 Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka.
ACT 14:17 Lakini hakuacha kuwaonesha watu uwepo wake: Ameonesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.”
ACT 14:18 Hata kwa maneno haya yote, ilikuwa vigumu kuzuia umati ule wa watu kuwatolea dhabihu.
ACT 14:19 Ndipo wakaja baadhi ya Wayahudi kutoka Antiokia na Ikonio wakawashawishi wale watu, wakampiga Paulo kwa mawe, wakamburuta hadi nje ya mji, wakidhani amekufa.
ACT 14:20 Lakini baada ya wanafunzi kukusanyika akainuka na kurudi mjini. Kesho yake yeye na Barnaba wakaondoka kwenda Derbe.
ACT 14:21 Wakahubiri Injili katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia,
ACT 14:22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kupitia katika taabu nyingi.”
ACT 14:23 Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kundi la waumini wa Isa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana Isa waliyemwamini.
ACT 14:24 Kisha wakapitia Pisidia wakafika Pamfilia.
ACT 14:25 Baada ya kuhubiri neno la Mungu huko Perga, wakateremkia Atalia.
ACT 14:26 Kutoka Atalia wakasafiri baharini wakarudi Antiokia, ambako walikuwa wamesifiwa kwa ajili ya neema ya Mungu kutokana na ile huduma waliyokuwa wameikamilisha.
ACT 14:27 Walipowasili Antiokia wakawaita waumini pamoja na kutoa taarifa ya yale yote Mungu aliyokuwa ametenda kupitia kwao na jinsi alivyokuwa amefungua mlango wa imani kwa ajili ya watu wa Mataifa.
ACT 14:28 Nao wakakaa huko pamoja na wanafunzi kwa muda mrefu.
ACT 15:1 Baadhi ya watu wakashuka Antiokia kutoka Yudea, nao wakawa wanawafundisha waumini: “Msipotahiriwa kulingana na desturi aliyofundisha Musa, hamwezi kuokoka.”
ACT 15:2 Baada ya Paulo na Barnaba kutokubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kwenda Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee.
ACT 15:3 Hivyo wakatumwa na waumini. Wakapitia Foinike na Samaria, wakielezea jinsi watu wa Mataifa walivyoongoka. Habari hizi zikaleta furaha kubwa kwa ndugu wote.
ACT 15:4 Walipofika Yerusalemu, walipokelewa na kundi la waumini na mitume pamoja na wazee. Ndipo Paulo na Barnaba wakawaarifu kila kitu Mungu alichokuwa amefanya kupitia kwao.
ACT 15:5 Ndipo baadhi ya waumini waliokuwa wa dhehebu la Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hao watu wa Mataifa lazima watahiriwe na waagizwe kutii Torati ya Musa.”
ACT 15:6 Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili.
ACT 15:7 Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu wa Mataifa wapate kusikia ujumbe wa Injili na kuamini.
ACT 15:8 Mungu, ajuaye mioyo ya watu, alionesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu wa Mungu kama vile alivyotupatia sisi.
ACT 15:9 Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani.
ACT 15:10 Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka nira shingoni mwa wanafunzi ambayo baba zetu wala sisi hatukuweza kuibeba?
ACT 15:11 Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi, kama wao wanavyookolewa.”
ACT 15:12 Kusanyiko lote wakakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu wa Mataifa.
ACT 15:13 Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni.
ACT 15:14 Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka watu wa Mataifa kwa ajili ya Jina lake.
ACT 15:15 Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:
ACT 15:16 “ ‘Baada ya mambo haya nitarudi, nami nitajenga upya nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena magofu yake na kuisimamisha,
ACT 15:17 ili wanadamu wengine wote wapate kumtafuta Mwenyezi Mungu, hata wale watu wa Mataifa wote ambao wanaitwa kwa Jina langu, asema Mwenyezi Mungu, anayefanya mambo haya,’
ACT 15:18 ambayo yamejulikana tangu zamani.
ACT 15:19 “Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu.
ACT 15:20 Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu.
ACT 15:21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Musa amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”
ACT 15:22 Mitume na wazee, pamoja na kundi la waumini wote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba, pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu.
ACT 15:23 Wakatumwa na barua ifuatayo: Sisi mitume na wazee, ndugu zenu. Kwa waumini wa Mataifa mlio Antiokia, Siria na Kilikia. Salamu.
ACT 15:24 Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu.
ACT 15:25 Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,
ACT 15:26 watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi.
ACT 15:27 Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia.
ACT 15:28 Kwa maana imempendeza Roho wa Mungu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima:
ACT 15:29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema. Kwaherini.
ACT 15:30 Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kundi la waumini pamoja, wakawapa ile barua.
ACT 15:31 Baada ya hao watu kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo.
ACT 15:32 Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii, wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga waumini katika imani.
ACT 15:33 Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma. [
ACT 15:34 Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.]
ACT 15:35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi walifundisha na kuhubiri neno la Bwana Isa.
ACT 15:36 Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana Isa tuone jinsi wanavyoendelea.”
ACT 15:37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye.
ACT 15:38 Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi naye.
ACT 15:39 Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro.
ACT 15:40 Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana Isa.
ACT 15:41 Akapitia Siria na Kilikia, akiimarisha makundi ya waumini ya huko.
ACT 16:1 Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani.
ACT 16:2 Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio
ACT 16:3 Paulo alitaka Timotheo aandamane naye, hivyo akamtahiri kwa sababu ya Wayahudi walioishi eneo lile, kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani.
ACT 16:4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate.
ACT 16:5 Hivyo makundi ya waumini yakaimarika katika imani, na wakaongezeka kwa idadi kila siku.
ACT 16:6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho wa Mungu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko jimbo la Asia.
ACT 16:7 Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Isa hakuwaruhusu.
ACT 16:8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa.
ACT 16:9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.”
ACT 16:10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri Injili huko.
ACT 16:11 Tukasafiri kwa meli kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, na kesho yake tukafika Neapoli.
ACT 16:12 Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa jimbo hilo la Makedonia, uliokuwa koloni ya Warumi. Nasi tukakaa huko siku kadhaa.
ACT 16:13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, ambapo tulitarajia kupata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko.
ACT 16:14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, raia wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Mwenyezi Mungu akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo.
ACT 16:15 Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani mwake, akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana Isa, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.
ACT 16:16 Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mjakazi aliyekuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri.
ACT 16:17 Huyu mjakazi alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipaza sauti na kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.”
ACT 16:18 Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Isa Al-Masihi, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka mara hiyo.
ACT 16:19 Basi mabwana wa yule mjakazi walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta hadi sokoni mbele ya viongozi wa mji.
ACT 16:20 Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi.
ACT 16:21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”
ACT 16:22 Umati wa watu wakajiunga kuwashambulia Paulo na Sila, na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wapigwe mijeledi.
ACT 16:23 Baada ya kuwapiga sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu.
ACT 16:24 Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.
ACT 16:25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.
ACT 16:26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.
ACT 16:27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka.
ACT 16:28 Lakini Paulo akapaza sauti kwa nguvu, akisema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”
ACT 16:29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila.
ACT 16:30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”
ACT 16:31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Isa Al-Masihi, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.”
ACT 16:32 Wakamwambia neno la Bwana Isa, yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake.
ACT 16:33 Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa.
ACT 16:34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.
ACT 16:35 Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waachie waende zao.”
ACT 16:36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaachie huru, kwa hiyo tokeni na mwende zenu kwa amani.”
ACT 16:37 Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raia wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”
ACT 16:38 Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raia wa Rumi.
ACT 16:39 Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji.
ACT 16:40 Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walienda nyumbani mwa Lidia, ambapo walikutana na waumini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.
ACT 17:1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.
ACT 17:2 Kama ilivyokuwa desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwa Maandiko,
ACT 17:3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Al-Masihi ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Isa ninayewaambia habari zake, ndiye Al-Masihi.”
ACT 17:4 Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.
ACT 17:5 Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani mwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye umati ule wa watu.
ACT 17:6 Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipaza sauti na kusema: “Watu hawa walioupindua ulimwengu wamekuja huku,
ACT 17:7 naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Isa.”
ACT 17:8 Waliposikia haya, umati ule wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia.
ACT 17:9 Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaachia waende zao.
ACT 17:10 Usiku ule ule, wale ndugu wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi.
ACT 17:11 Hawa Waberoya walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli.
ACT 17:12 Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume Wayunani wa tabaka la juu.
ACT 17:13 Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea.
ACT 17:14 Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya.
ACT 17:15 Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye hadi Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.
ACT 17:16 Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu.
ACT 17:17 Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko.
ACT 17:18 Kundi la wenye falsafa, Waepikureo na Wastoiko, wakajibizana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri Injili kuhusu Isa na ufufuo wa wafu.
ACT 17:19 Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini?
ACT 17:20 Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.”
ACT 17:21 (Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya.)
ACT 17:22 Ndipo Paulo akasimama katikati ya mkutano wa Areopago, akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana.
ACT 17:23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa makini vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.
ACT 17:24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo, ndiye Bwana wa mbingu na nchi; hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu.
ACT 17:25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote.
ACT 17:26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi.
ACT 17:27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu.
ACT 17:28 ‘Kwa kuwa ndani yake tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni uzao wake.’
ACT 17:29 “Kwa kuwa sisi ni uzao wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu.
ACT 17:30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu.
ACT 17:31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Al-Masihi kutoka kwa wafu.”
ACT 17:32 Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.”
ACT 17:33 Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao.
ACT 17:34 Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao walikuwemo Dionisio, mmoja wa mkutano wa Areopago, na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari, na wengine wengi.
ACT 18:1 Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho.
ACT 18:2 Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mzawa wa Ponto, aliyekuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona,
ACT 18:3 naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao.
ACT 18:4 Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.
ACT 18:5 Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Isa ndiye Al-Masihi.
ACT 18:6 Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakung’uta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”
ACT 18:7 Kisha akaondoka kwenye sinagogi, akaenda nyumbani mwa Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu; nyumba yake ilikuwa karibu na sinagogi.
ACT 18:8 Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa.
ACT 18:9 Usiku mmoja Bwana Isa akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze,
ACT 18:10 kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa nina watu wengi katika mji huu.”
ACT 18:11 Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha Maandiko ya Mungu.
ACT 18:12 Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani.
ACT 18:13 Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.”
ACT 18:14 Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza.
ACT 18:15 Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.”
ACT 18:16 Akawafukuza kutoka mahakamani.
ACT 18:17 Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali kitendo chao hata kidogo.
ACT 18:18 Baada ya kukaa Korintho kwa muda, Paulo akaagana na ndugu, akasafiri kwa meli kwenda Siria akiwa amefuatana na Prisila na Akila. Walipofika Kenkrea, Paulo alinyoa nywele zake kwa kuwa alikuwa ameweka nadhiri.
ACT 18:19 Walipofika Efeso, Paulo aliwaacha Prisila na Akila huko, lakini yeye akaingia kwenye sinagogi akawa anajadiliana na Wayahudi.
ACT 18:20 Walipomwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi hakukubali.
ACT 18:21 Lakini alipokuwa akiondoka, akaahidi, “Nitarudi kama Mungu akipenda.” Kisha akasafiri kwa meli kutoka Efeso.
ACT 18:22 Alitia nanga Kaisaria, akaenda Yerusalemu na kuwasalimu waumini, kisha akaenda Antiokia.
ACT 18:23 Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote.
ACT 18:24 Basi akaja Efeso Myahudi aliyeitwa Apolo, mzawa wa Iskanderia. Alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa na ujuzi wa Maandiko.
ACT 18:25 Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana Isa, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi kuhusu Isa, ingawa alijua tu ubatizo wa Yahya.
ACT 18:26 Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimwalika kwao na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.
ACT 18:27 Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini.
ACT 18:28 Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akithibitisha kwa Maandiko kwamba Isa ndiye Al-Masihi.
ACT 19:1 Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa,
ACT 19:2 akawauliza, “Je, mlipokea Roho wa Mungu mlipoamini?” Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho wa Mungu.”
ACT 19:3 Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yahya.”
ACT 19:4 Paulo akasema, “Ubatizo wa Yahya ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani Isa.”
ACT 19:5 Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Isa.
ACT 19:6 Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu wa Mungu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.
ACT 19:7 Walikuwa wapatao wanaume kumi na wawili.
ACT 19:8 Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya ufalme wa Mungu.
ACT 19:9 Lakini baadhi yao wakakaidi; walikataa kuamini, na wakakashifu Njia Ile hadharani. Basi Paulo aliachana nao. Akaenda na wanafunzi wale, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano.
ACT 19:10 Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko jimbo la Asia wakawa wamesikia neno la Bwana Isa.
ACT 19:11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kupitia kwa Paulo,
ACT 19:12 hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.
ACT 19:13 Baadhi ya Wayahudi waliotangatanga wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Isa kwa wale wenye pepo, wakisema, “Kwa jina la Isa, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.”
ACT 19:14 Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo.
ACT 19:15 Siku moja pepo mchafu akawajibu, “Isa namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?”
ACT 19:16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.
ACT 19:17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Isa likaheshimiwa sana.
ACT 19:18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.
ACT 19:19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma elfu hamsini za fedha.
ACT 19:20 Hivyo neno la Bwana Isa likaenea sana na kuwa na nguvu.
ACT 19:21 Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.”
ACT 19:22 Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko jimbo la Asia.
ACT 19:23 Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia Ile.
ACT 19:24 Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa,
ACT 19:25 aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii!
ACT 19:26 Mnaona na kusikia jinsi huyu Paulo amewashawishi na kuwapoteza watu wengi hapa Efeso na karibu jimbo lote la Asia. Anasema kwamba miungu iliyofanywa kwa mikono ya wanadamu si miungu hata kidogo.
ACT 19:27 Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu wa kike Artemi aliye mkuu, anayeabudiwa jimbo lote la Asia na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”
ACT 19:28 Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele wakisema, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!”
ACT 19:29 Mara mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia waliokuwa wakisafiri na Paulo, wakakimbilia nao katika ukumbi wa maonesho.
ACT 19:30 Paulo akataka kuingia katikati ya umati, lakini wanafunzi hawakumruhusu.
ACT 19:31 Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi wa maonesho.
ACT 19:32 Umati wa watu walikuwa na taharuki. Walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko.
ACT 19:33 Wayahudi wakamsukumia Iskanda mbele na baadhi ya watu kwenye umati ule wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu.
ACT 19:34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”
ACT 19:35 Baadaye karani wa mji akanyamazisha umati ule wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni?
ACT 19:36 Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka.
ACT 19:37 Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike.
ACT 19:38 Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana mashtaka dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka.
ACT 19:39 Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali.
ACT 19:40 Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.”
ACT 19:41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.
ACT 20:1 Baada ya zile ghasia kumalizika, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia.
ACT 20:2 Alipita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo. Ndipo hatimaye akawasili Uyunani,
ACT 20:3 ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Kwa sababu baadhi ya Wayahudi walikuwa wamepanga njama dhidi yake alipokuwa karibu kusafiri kwa meli kwenda Siria, aliamua kurudi kupitia Makedonia.
ACT 20:4 Paulo aliandamana na Sopatro mwana wa Piro kutoka Beroya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, na Gayo kutoka Derbe, pia Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka jimbo la Asia.
ACT 20:5 Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa.
ACT 20:6 Lakini sisi tukasafiri kwa meli kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba.
ACT 20:7 Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea hadi usiku wa manane.
ACT 20:8 Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi.
ACT 20:9 Kijana mmoja jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akihubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamchukua akiwa amekufa.
ACT 20:10 Paulo akashuka chini, akajitupa juu yake na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, bado yuko hai!”
ACT 20:11 Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea hadi mapambazuko, akaondoka.
ACT 20:12 Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.
ACT 20:13 Tukatangulia kwenye meli, tukasafiri kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Alikuwa amefanya utaratibu huu kwa sababu alikuwa akienda huko kwa miguu.
ACT 20:14 Alipotukuta huko Aso, alijiunga nasi kwenye meli, tukasafiri hadi Mitilene.
ACT 20:15 Kutoka huko tuliendelea kwa meli, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto.
ACT 20:16 Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko jimbo la Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste kama ingewezekana.
ACT 20:17 Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kundi la waumini waje wakutane naye.
ACT 20:18 Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi muda wote nilikuwa nanyi, tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa jimbo la Asia.
ACT 20:19 Nilimtumikia Bwana Isa kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi.
ACT 20:20 Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba.
ACT 20:21 Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Isa Al-Masihi.
ACT 20:22 “Nami sasa nimesukumwa na Roho wa Mungu, ninaenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko.
ACT 20:23 Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu wa Mungu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja.
ACT 20:24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Isa aliyonipa, yaani kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu.
ACT 20:25 “Nami sasa najua kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu niliowahubiria ufalme wa Mungu atakayeniona tena.
ACT 20:26 Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu yeyote.
ACT 20:27 Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu.
ACT 20:28 Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho wa Mungu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Chungeni jumuiya ya waumini ya Mungu, aliowanunua kwa damu yake mwenyewe.
ACT 20:29 Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa-mwitu wakali watakuja kati yenu, ambao hawatalihurumia kundi.
ACT 20:30 Hata kutoka miongoni mwenu watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate.
ACT 20:31 Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.
ACT 20:32 “Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa.
ACT 20:33 Sikutamani fedha wala dhahabu wala vazi la mtu yeyote.
ACT 20:34 Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.
ACT 20:35 Katika kila jambo nimewaonesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Isa mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”
ACT 20:36 Paulo alipomaliza kusema haya akapiga magoti pamoja nao wote akaomba.
ACT 20:37 Wote wakalia, wakamkumbatia Paulo na kumbusu.
ACT 20:38 Kilichowahuzunisha zaidi ni kwa sababu ya yale maneno aliyosema kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Wakaenda naye hadi kwenye meli.
ACT 21:1 Tulipokwisha kujitenga nao, tukasafiri kwa meli moja kwa moja hadi Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo, na kutoka huko tukaenda Patara.
ACT 21:2 Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo.
ACT 21:3 Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri hadi Siria. Tukatia nanga katika bandari ya Tiro, ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake.
ACT 21:4 Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wa Mungu wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.
ACT 21:5 Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba.
ACT 21:6 Baada ya kuagana, tukapanda kwenye meli, nao wakarudi manyumbani mwao.
ACT 21:7 Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja.
ACT 21:8 Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani mwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake.
ACT 21:9 Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.
ACT 21:10 Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo akateremka kutoka Yudea.
ACT 21:11 Alipotufikia, akachukua mshipi wa Paulo, akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe, akasema, “Roho wa Mungu anasema: ‘Hivi ndivyo viongozi wa Wayahudi huko Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’ ”
ACT 21:12 Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu.
ACT 21:13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Isa.”
ACT 21:14 Alipokataa kushawishika, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na yatendeke.”
ACT 21:15 Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu.
ACT 21:16 Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani mwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.
ACT 21:17 Tulipofika Yerusalemu, ndugu wakatukaribisha kwa furaha.
ACT 21:18 Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulienda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwako.
ACT 21:19 Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.
ACT 21:20 Baada ya kusikia mambo haya, wakamsifu Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria.
ACT 21:21 Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote wanaoishi miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Musa, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu.
ACT 21:22 Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu.
ACT 21:23 Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tuna watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri.
ACT 21:24 Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria.
ACT 21:25 Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
ACT 21:26 Ndipo kesho yake Paulo akaenda na wale watu, akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
ACT 21:27 Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka jimbo la Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata.
ACT 21:28 Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.”
ACT 21:29 (Walikuwa wamemwona Trofimo Mwefeso, akiwa mjini pamoja na Paulo, wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)
ACT 21:30 Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa.
ACT 21:31 Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari Warumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko.
ACT 21:32 Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari, wakakimbia kwenye ule umati wa watu. Wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.
ACT 21:33 Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini.
ACT 21:34 Baadhi ya watu katika umati ule wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya taharuki, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi.
ACT 21:35 Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za umati ule wa watu zilikuwa kubwa.
ACT 21:36 Umati wa watu waliofuata waliendelea kupaza sauti na kusema, “Mwondoe huyu!”
ACT 21:37 Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?” Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani?
ACT 21:38 Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi elfu nne wenye silaha jangwani?”
ACT 21:39 Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi kutoka Tarso huko Kilikia, raia wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”
ACT 21:40 Baada ya kupata ruhusa kwa yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi, akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:
ACT 22:1 “Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu.”
ACT 22:2 Waliposikia akisema kwa lugha ya Kiebrania, wakanyamaza kabisa. Ndipo Paulo akasema,
ACT 22:3 “Mimi ni Myahudi, niliyezaliwa Tarso huko Kilikia, lakini nimelelewa katika mji huu. Miguuni mwa Gamalieli, nilifundishwa kikamilifu katika sheria ya baba zetu, na nikawa mwenye juhudi kwa ajili ya Mungu kama nyote mlivyo leo.
ACT 22:4 Niliwatesa wafuasi wa Njia hii hadi kufa, nikiwakamata wanaume na wanawake, na kuwatupa gerezani,
ACT 22:5 kama kuhani mkuu na baraza zima la wazee wanavyoweza kushuhudia kunihusu. Hata nilipokea barua kutoka kwao kwenda kwa ndugu wale wa Dameski, nami nikaenda huko ili kuwaleta watu hawa Yerusalemu kama wafungwa ili waadhibiwe.
ACT 22:6 “Nilipokuwa njiani kuelekea Dameski, yapata saa sita mchana, ghafula nuru kubwa kutoka mbinguni ikanimulika kotekote.
ACT 22:7 Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli! Sauli! Mbona unanitesa?’
ACT 22:8 “Nikajibu, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ “Naye akaniambia, ‘Mimi ni Isa Al-Nasiri unayemtesa.’
ACT 22:9 Basi wale watu waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia sauti ya yule aliyekuwa akisema nami.
ACT 22:10 “Nikauliza, ‘Nifanye nini, Bwana?’ “Naye Bwana Isa akaniambia, ‘Inuka uingie Dameski, huko utaambiwa yote unayopaswa kufanya.’
ACT 22:11 Kwa kuwa nilikuwa siwezi kuona kwa ajili ya mng’ao wa ile nuru, wenzangu wakanishika mkono wakaniongoza kuingia Dameski.
ACT 22:12 “Mtu mmoja mcha Mungu, jina lake Anania, alikuja kuniona. Alizishika sana sheria zetu, na aliheshimiwa sana na Wayahudi walioishi huko Dameski.
ACT 22:13 Akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Sauli, pata kuona tena!’ Nami mara hiyo nikaweza kumwona.
ACT 22:14 “Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe ili ujue mapenzi yake, umwone yeye Aliye Mwenye Haki na upate kusikia maneno kutoka kinywani mwake.
ACT 22:15 Kwa kuwa utakuwa shahidi wake kwa watu kuhusu kile ulichokiona na kukisikia.
ACT 22:16 Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita Jina lake.’
ACT 22:17 “Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula,
ACT 22:18 nikamwona Bwana Isa akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu.’
ACT 22:19 “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyoenda kwenye kila sinagogi ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini.
ACT 22:20 Damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’
ACT 22:21 “Ndipo Bwana Isa akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ”
ACT 22:22 Umati ule wa watu wakamsikiliza Paulo hadi aliposema neno hilo, ndipo wakapaza sauti zao na kupiga kelele wakisema, “Mwondoeni duniani, hafai kuishi!”
ACT 22:23 Walipokuwa wakipiga kelele na kutoa mavazi yao huku wakirusha mavumbi juu hewani,
ACT 22:24 yule jemadari akaamuru Paulo aingizwe kwenye ngome. Akaelekeza kwamba apigwe mijeledi na ahojiwe ili kujua kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna hiyo.
ACT 22:25 Lakini walipokwisha kumfunga kwa kamba za ngozi ili wampige mijeledi, Paulo akamwambia kiongozi wa askari aliyekuwa amesimama pale karibu naye, “Je, ni halali kwenu kwa mujibu wa sheria kumpiga mtu ambaye ni raia wa Rumi hata kabla hajapatikana na hatia?”
ACT 22:26 Yule kiongozi aliposikia maneno haya, alimwendea yule jemadari na kumwambia, “Unataka kufanya nini? Kwa maana huyu mtu ni raia wa Rumi.”
ACT 22:27 Yule jemadari akaja akamuuliza Paulo, “Niambie, wewe ni raia wa Rumi?” Paulo akajibu, “Naam, hakika.”
ACT 22:28 Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.” Paulo akasema “Lakini mimi ni raia wa Rumi kwa kuzaliwa.”
ACT 22:29 Mara wale waliokuwa wanataka kumhoji wakajiondoa haraka, naye yule jemadari akaingiwa na hofu alipotambua ya kuwa amemfunga Paulo, ambaye ni raia wa Rumi, kwa minyororo.
ACT 22:30 Kesho yake, kwa kuwa yule jemadari alitaka kujua hakika kwa nini Paulo alikuwa anashutumiwa na Wayahudi, alimfungua, na akawaagiza viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote likutane. Kisha akamleta Paulo, akamsimamisha mbele yao.
ACT 23:1 Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa Baraza la Wayahudi, akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.”
ACT 23:2 Kwa ajili ya jambo hili kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani.
ACT 23:3 Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!”
ACT 23:4 Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana kuhani mkuu wa Mungu?”
ACT 23:5 Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa kuhani mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’ ”
ACT 23:6 Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo, akapaza sauti kwenye Baraza la Wayahudi, akasema, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.”
ACT 23:7 Aliposema haya, kukazuka mabishano kati ya Mafarisayo na Masadukayo, na baraza lote likagawanyika.
ACT 23:8 (Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)
ACT 23:9 Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa Torati ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lolote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye”
ACT 23:10 Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi.
ACT 23:11 Usiku uliofuata, Bwana Isa akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”
ACT 23:12 Kulipopambazuka Wayahudi wakapanga njama pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa hadi wawe wamemuua Paulo.
ACT 23:13 Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini.
ACT 23:14 Wakaenda kwa viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumeapa kwamba hatutakula chochote hadi tuwe tumemuua Paulo.
ACT 23:15 Sasa basi, wewe pamoja na Baraza la Wayahudi mwombeni jemadari amlete Paulo mbele yenu kwa kisingizio cha kutaka taarifa sahihi zaidi kuhusu kesi yake. Nasi tuko tayari kumuua kabla hajafika hapa.”
ACT 23:16 Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia kuhusu njama hiyo, alienda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo.
ACT 23:17 Ndipo Paulo akamwita mmoja wa viongozi wa askari, akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, ana jambo la kumweleza.”
ACT 23:18 Hivyo yule kiongozi wa askari akampeleka yule kijana kwa jemadari, akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.”
ACT 23:19 Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumuuliza, “Unataka kuniambia nini?”
ACT 23:20 Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye Baraza la Wayahudi kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina kumhusu.
ACT 23:21 Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wameapa kwamba hawatakula wala kunywa hadi wamuue Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ombi lao.”
ACT 23:22 Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu yeyote kwamba umenieleza habari hizi.”
ACT 23:23 Kisha yule jemadari akawaita viongozi wake wawili wa askari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari mia mbili, wapanda farasi sabini, na watu mia mbili wenye mikuki.
ACT 23:24 Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mkampeleke salama kwa mtawala Feliksi.”
ACT 23:25 Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo:
ACT 23:26 Klaudio Lisia. Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi. Salamu.
ACT 23:27 Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumuua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya askari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raia wa Rumi.
ACT 23:28 Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya Baraza la Wayahudi.
ACT 23:29 Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lolote linalostahili kifo au kifungo.
ACT 23:30 Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na njama dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara moja. Niliwaagiza washtaki wake pia waeleze mashtaka yao dhidi yake mbele yako.
ACT 23:31 Hivyo askari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta hadi Antipatri.
ACT 23:32 Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wao wakarudi kwenye ngome ya askari.
ACT 23:33 Askari walipofika Kaisaria, walimpa mtawala ile barua, na kumkabidhi Paulo kwake.
ACT 23:34 Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimuuliza Paulo alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia,
ACT 23:35 alisema, “Nitasikiliza kesi yako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.
ACT 24:1 Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania akateremka hadi Kaisaria pamoja na baadhi ya wazee na mwanasheria aitwaye Tertulo, wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala.
ACT 24:2 Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na mabadiliko mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele.
ACT 24:3 Wakati wote na kila mahali, kwa namna yoyote, mtukufu Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi.
ACT 24:4 Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi.
ACT 24:5 “Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanasiri,
ACT 24:6 na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata. [Tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu.
ACT 24:7 Lakini jemadari Lisia alitujia na nguvu nyingi, akamwondoa mikononi mwetu,
ACT 24:8 akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako.] Kwa kumchunguza mwenyewe utaweza kujua ukweli kuhusu mashtaka haya yote tunayoleta dhidi yake.”
ACT 24:9 Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka haya yote ni kweli.
ACT 24:10 Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha.
ACT 24:11 Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu.
ACT 24:12 Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu yeyote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi au mahali pengine popote mjini.
ACT 24:13 Wala hawawezi kabisa kukuthibitishia mashtaka haya wanayoleta dhidi yangu.
ACT 24:14 Lakini ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu kama mfuasi wa Njia Ile, ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Torati na kile kilichoandikwa katika Manabii,
ACT 24:15 nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wenye haki na wasio na haki.
ACT 24:16 Kwa hiyo ninajitahidi siku zote kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na mbele za wanadamu.
ACT 24:17 “Basi, baada ya miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu.
ACT 24:18 Nilikuwa nimetakaswa waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu pamoja nami, wala sikuhusika katika ghasia yoyote.
ACT 24:19 Lakini kuna Wayahudi fulani kutoka jimbo la Asia ambao walipaswa kuwa hapa mbele yako na kunishtaki kama wana jambo lolote dhidi yangu.
ACT 24:20 Au, watu hawa walio hapa waseme ni kosa gani walilonipata nalo waliponisimamisha mbele ya Baraza la Wayahudi,
ACT 24:21 isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopaza sauti mbele yao na kusema, ‘Mimi nashtakiwa mbele yenu leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’ ”
ACT 24:22 Basi Feliksi, ambaye alifahamu vizuri habari za Njia Ile, akaahirisha kesi ile, akasema, “Jemadari Lisia atakapoteremka huku, nitaamua kesi yenu.”
ACT 24:23 Ndipo akaamuru kiongozi wa askari amweke chini ya ulinzi lakini ampe uhuru na kuwaruhusu rafiki zake wamhudumie.
ACT 24:24 Baada ya siku kadhaa, Feliksi alikuja pamoja na Drusila mkewe, aliyekuwa Myahudi. Alituma aitiwe Paulo, naye akamsikiliza alipokuwa akinena kuhusu imani katika Al-Masihi Isa.
ACT 24:25 Naye Paulo alipokuwa akinena kuhusu haki, kuwa na kiasi na kuhusu hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu, akasema, “Hiyo yatosha sasa! Unaweza kuondoka. Nitakapokuwa na muda, nitakuita.”
ACT 24:26 Wakati huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempa rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye.
ACT 24:27 Baada ya miaka miwili kupita, Porkio Festo akaingia kwenye utawala mahali pa Feliksi, lakini kwa kuwa Feliksi alitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwacha Paulo gerezani.
ACT 25:1 Siku tatu baada ya Festo kuwasili Kaisaria kuchukua wajibu wake mpya, alipanda kwenda Yerusalemu,
ACT 25:2 ambako viongozi wa makuhani na viongozi wa Wayahudi walikuja mbele yake na kuleta mashtaka yao dhidi ya Paulo.
ACT 25:3 Wakamsihi sana Festo, kama upendeleo kwao, aamuru Paulo ahamishiwe Yerusalemu, kwa kuwa walikuwa wanaandaa kumvizia ili wamuue akiwa njiani.
ACT 25:4 Festo akawajibu, “Paulo amezuiliwa huko Kaisaria, nami mwenyewe ninaenda huko hivi karibuni.
ACT 25:5 Baadhi ya viongozi wenu wafuatane nami na kutoa mashtaka dhidi ya mtu huyo huko, kama amekosa jambo lolote.”
ACT 25:6 Baada ya Festo kukaa miongoni mwao kwa karibu siku nane au kumi, akashuka kwenda Kaisaria na siku iliyofuata akaitisha mahakama, akaketi penye kiti chake cha hukumu, akaamuru Paulo aletwe mbele yake.
ACT 25:7 Paulo alipotokea, wale Wayahudi waliokuwa wameteremka toka Yerusalemu wakasimama wakiwa wamemzunguka, wakileta mashtaka mengi mazito dhidi yake ambayo hawakuweza kuyathibitisha.
ACT 25:8 Ndipo Paulo akajitetea, akasema, “Mimi sikufanya jambo lolote kinyume cha sheria ya Wayahudi au dhidi ya Hekalu au kinyume cha Kaisari.”
ACT 25:9 Festo, akitaka kuwapendeza Wayahudi, akamuuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na kukabili mashtaka mbele yangu huko?”
ACT 25:10 Paulo akasema, “Mimi sasa nimesimama mbele ya mahakama ya Kaisari, ambako ninastahili kushtakiwa. Kama vile wewe mwenyewe unavyojua vyema kabisa sijawatendea Wayahudi kosa lolote.
ACT 25:11 Basi kama mimi nina hatia ya kutenda kosa lolote linalostahili kifo, sikatai kufa. Lakini kama mashtaka yaliyoletwa dhidi yangu na hawa Wayahudi si kweli, hakuna yeyote aliye na haki ya kunikabidhi mikononi mwao. Naomba rufaa kwa Kaisari!”
ACT 25:12 Baada ya Festo kufanya shauri pamoja na baraza lake, akatangaza, “Wewe umeomba rufaa kwa Kaisari, nako kwa Kaisari utaenda!”
ACT 25:13 Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo.
ACT 25:14 Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili kesi ya Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani.
ACT 25:15 Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake.
ACT 25:16 “Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa.
ACT 25:17 Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi kwenye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe.
ACT 25:18 Washtaki wake walipoinuka kuzungumza, hawakumshtaki kwa uhalifu wowote kama nilivyotarajia.
ACT 25:19 Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu aitwaye Isa aliyekufa, lakini Paulo alidai kwamba yu hai.
ACT 25:20 Kwa kuwa sikujua jinsi ya kupeleleza jambo hili, nilimuuliza kama angependa kwenda Yerusalemu na kuhojiwa huko kuhusu mashtaka haya.
ACT 25:21 Lakini Paulo alipoomba afadhiliwe ili rufaa yake isikilizwe na Mfalme Agusto, nilimwamuru alindwe hadi nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.”
ACT 25:22 Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.” Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.”
ACT 25:23 Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo Paulo akaletwa ndani kwa amri ya Festo.
ACT 25:24 Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba hapaswi kuendelea kuishi.
ACT 25:25 Sikuona kwamba ametenda jambo lolote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa mfalme, niliamua kumpeleka Rumi.
ACT 25:26 Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia Bwana Mtukufu kumhusu mtu huyu. Hivyo basi, nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika.
ACT 25:27 Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”
ACT 26:1 Ndipo Agripa akamwambia Paulo, “Una ruhusa kujitetea.” Hivyo Paulo akawaashiria kwa mkono wake, akaanza kujitetea, akasema:
ACT 26:2 “Mfalme Agripa, najiona kuwa na heri kusimama mbele yako leo ninapojitetea kuhusu mashtaka yote ya Wayahudi,
ACT 26:3 hasa kwa sababu unajua vyema desturi zote za Kiyahudi na ya kuwa wewe unajua kwa undani mila na masuala ya mabishano. Kwa hiyo, nakusihi unisikilize kwa uvumilivu.
ACT 26:4 “Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu.
ACT 26:5 Wao wamenifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia wakipenda kushuhudia, kwamba kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu, niliishi nikiwa Farisayo.
ACT 26:6 Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo.
ACT 26:7 Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii usiku na mchana. Ee mfalme, ninashtakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hili.
ACT 26:8 Kwa nini yeyote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu?
ACT 26:9 “Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Isa Al-Nasiri.
ACT 26:10 Nami hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwafunga watakatifu wengi gerezani, na walipokuwa wakiuawa nilipiga kura yangu kuunga mkono.
ACT 26:11 Mara nyingi nilienda kutoka sinagogi moja hadi lingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilienda miji ya kigeni ili kuwatesa.
ACT 26:12 “Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninaenda Dameski, nilikuwa na mamlaka na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani.
ACT 26:13 Ilikuwa yapata adhuhuri, ee mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni iliyong’aa kuliko jua, ikatuangaza pande zote, mimi na wale niliokuwa pamoja nao.
ACT 26:14 Wote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’
ACT 26:15 “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’ “Naye Bwana akajibu, ‘Ni mimi Isa unayemtesa.
ACT 26:16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonesha.
ACT 26:17 Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao,
ACT 26:18 uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwa nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’
ACT 26:19 “Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni,
ACT 26:20 bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Yudea na pia kwa watu wa Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao.
ACT 26:21 Ni kwa sababu hii Wayahudi walinikamata nilipokuwa Hekaluni, wakataka kuniua.
ACT 26:22 Hadi leo nimepata msaada kutoka kwa Mungu, na hivyo nasimama hapa nikishuhudia kwa wakubwa na wadogo. Sisemi chochote zaidi ya yale ambayo manabii na Musa walisema yatatukia:
ACT 26:23 kwamba Al-Masihi atateswa, na kwamba yeye atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, na atatangaza nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.”
ACT 26:24 Paulo alipokuwa akifanya utetezi huu, Festo akasema kwa sauti kubwa, “Paulo, wewe umerukwa na akili! Kusoma kwingi kunakufanya uwe kichaa!”
ACT 26:25 Lakini Paulo akajibu, “Mimi sijarukwa na akili, mtukufu sana Festo, bali nanena kweli nikiwa na akili zangu timamu.
ACT 26:26 Naam, mfalme anajua kuhusu mambo haya yote, nami nasema naye kwa uhuru. Kwa sababu nina hakika kwamba hakuna hata mojawapo ya mambo haya asilolijua, kwa kuwa hayakufanyika mafichoni.
ACT 26:27 Mfalme Agripa, je, unaamini manabii? Najua kuwa unaamini.”
ACT 26:28 Agripa akamwambia Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe mfuasi wa Al-Masihi?”
ACT 26:29 Paulo akasema, “Ikiwa ni kwa haraka au la, namwomba Mungu, si wewe peke yako bali pia wale wote wanaonisikiliza leo, wawe kama mimi nilivyo, kasoro minyororo hii.”
ACT 26:30 Baada ya kusema hayo, mfalme akainuka pamoja na mtawala na Bernike na wale waliokuwa wameketi pamoja nao.
ACT 26:31 Walipokuwa wakiondoka, wakaambiana, “Mtu huyu hafanyi jambo lolote linalostahili kifo au kifungo.”
ACT 26:32 Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeachwa huru kama hangekuwa amekata rufaa kwa Kaisari.”
ACT 27:1 Ilipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa meli kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa kiongozi mmoja wa askari aliyeitwa Juliasi, aliyekuwa wa Kikosi cha Walinzi wa Kaisari.
ACT 27:2 Tulipanda meli iliyotoka Adramitio, iliyokuwa inakaribia kusafiri kwenda kwenye bandari zilizopo pwani ya jimbo la Asia, tukaanza safari yetu tukiwa pamoja na Aristarko, Mmakedonia kutoka Thesalonike.
ACT 27:3 Kesho yake tukatia nanga Sidoni, naye Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kwa rafiki zake ili wamtimizie mahitaji yake.
ACT 27:4 Kutoka huko tukaingia baharini tena na tukapita upande wa chini wa kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.
ACT 27:5 Baada ya sisi kuvuka bahari iliyo upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira huko Likia.
ACT 27:6 Huko yule kiongozi wa askari akapata meli ya Iskanderia ikielekea Italia, akatupandisha humo.
ACT 27:7 Tukasafiri polepole kwa siku nyingi na kwa shida, hatimaye tukafika karibu na Nido. Kwa kuwa upepo wa mbisho ulituzuia tusiweze kushika mwelekeo tuliokusudia, tukapita chini ya Krete mkabala na Salmone.
ACT 27:8 Tukaambaa na pwani kwa shida, tukafika sehemu iitwayo Bandari Nzuri, karibu na mji wa Lasea.
ACT 27:9 Muda mwingi ulikuwa umepotea, na kusafiri baharini kulikuwa hatari, kwa sababu wakati huu ulikuwa baada ya Siku ya Kufunga. Hivyo Paulo akawaonya akasema,
ACT 27:10 “Mabwana, naona kuwa hii safari ni yenye maafa na ya kuleta hasara kubwa kwa meli na shehena, pia kwa maisha yetu.”
ACT 27:11 Lakini badala ya yule kiongozi wa askari kusikiliza yale Paulo aliyosema, akafuata zaidi ushauri wa nahodha na mwenye meli.
ACT 27:12 Kwa kuwa ile bandari ilikuwa haifai kukaa wakati wa majira ya baridi, wengi wakashauri kwamba tuendelee na safari wakitarajia kufika Foinike na kukaa huko kwa majira ya baridi. Hii ilikuwa bandari iliyo katika kisiwa cha Krete ikikabili upande wa kusini-magharibi na kaskazini-magharibi.
ACT 27:13 Upepo mtulivu ulipoanza kuvuma toka kusini, wakadhani kuwa wangeweza kufikia lengo lao, hivyo wakang’oa nanga na kusafiri wakipita kandokando ya pwani ya kisiwa cha Krete.
ACT 27:14 Lakini baada ya muda mfupi, ikavuma tufani kubwa iitwayo Eurakilo kutoka kisiwa cha Krete.
ACT 27:15 Meli ikapigwa na dhoruba na haikuweza kushindana na ule upepo, tukarudishwa baharini upepo ulikokuwa unaelekea.
ACT 27:16 Hatimaye tukisafiri kupita chini ya kisiwa kidogo kiitwacho Kauda, ambapo kwa kuwa tulikuwa tumekingiwa upepo na hicho kisiwa, tuliweza kwa shida kuifunga mashua ya kuokolea watu.
ACT 27:17 Watu walipokwisha kuivuta mashua hiyo na kuiingiza katika meli, waliifunga kwa kamba chini ya meli yenyewe ili kuzishikanisha pamoja. Wakiogopa kupelekwa kwenye mchanga karibu na pwani ya Sirti, wakashusha matanga wakaiacha meli isukumwe na huo upepo.
ACT 27:18 Tulikuwa tunapigwa na dhoruba kwa nguvu, kiasi kwamba kesho yake walianza kutupa shehena toka kwenye meli.
ACT 27:19 Siku ya tatu, wakatupa vyombo vya meli baharini kwa mikono yao wenyewe.
ACT 27:20 Wakati jua wala nyota hazikuonekana kwa siku nyingi, na dhoruba iliendelea kuvuma, hatimaye tulikata tamaa ya kuokolewa.
ACT 27:21 Baada ya watu kukaa siku nyingi bila kula chakula, Paulo akasimama mbele yao na kusema: “Enyi watu, kama mngekubali ushauri wangu wa kutosafiri kwa meli kutoka Krete, basi mngejiepusha na uharibifu na hasara hii.
ACT 27:22 Sasa ninawasihi sana, jipeni moyo kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake, ila meli itaangamia.
ACT 27:23 Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ninayemwabudu alisimama karibu nami,
ACT 27:24 akaniambia, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amekupa kwa neema uhai wa wote wanaosafiri pamoja nawe.’
ACT 27:25 Hivyo jipeni moyo, enyi watu, kwa kuwa ninamwamini Mungu kwamba yatakuwa kama vile alivyoniambia.
ACT 27:26 Lakini hata hivyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani.”
ACT 27:27 Usiku wa kumi na nne ulipofika, tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika Bahari ya Adria. Ilipokuwa yapata usiku wa manane, mabaharia wakahisi kwamba walikuwa wanakaribia nchi kavu.
ACT 27:28 Kwa hiyo wakapima kina cha maji na kukuta kilikuwa pima ishirini; baada ya kuendelea mbele kidogo, wakapima tena wakapata kina cha pima kumi na tano.
ACT 27:29 Wakiogopa kwamba meli yetu ingegonga kwenye miamba, wakashusha nanga nne za nyuma ya meli, wakawa wanaomba kupambazuke.
ACT 27:30 Katika jaribio la kutoroka kutoka kwa meli, mabaharia wakashusha mashua ya kuokolea watu baharini, wakijifanya kwamba wanaenda kushusha nanga za omo.
ACT 27:31 Ndipo Paulo akamwambia yule jemadari na askari, “Hawa watu wasipobaki katika meli, hamtaweza kuokoka.”
ACT 27:32 Hivyo basi wale askari wakakata kamba zilizoshikilia ile mashua ya kuokolea watu kwenye meli, wakaiacha ianguke humo baharini.
ACT 27:33 Kabla ya mapambazuko, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi mkiwa mmefunga na bila kula chochote.
ACT 27:34 Kwa hiyo nawasihi mle chakula, kwa maana itawasaidia ili mweze kuishi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza unywele hata mmoja kutoka kichwani mwake.”
ACT 27:35 Baada ya kusema maneno haya, Paulo akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega akaanza kula.
ACT 27:36 Ndipo wote wakatiwa moyo, wakaanza kula chakula.
ACT 27:37 Ndani ya meli tulikuwa jumla ya watu mia mbili na sabini na sita (276).
ACT 27:38 Baada ya watu wote kula chakula cha kutosha, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini.
ACT 27:39 Kulipopambazuka, mabaharia hawakuitambua ile nchi, lakini waliona ghuba yenye ufuko wa mchanga, ambako waliamua kuipweleza meli kama ingewezekana.
ACT 27:40 Kwa hiyo wakatupa nanga zote na kuziacha baharini, na wakati huo huo wakalegeza kamba zilizokuwa zikishikilia usukani wa meli. Kisha wakatweka tanga la mbele lishike upepo na kuisukuma meli kuelekea pwani.
ACT 27:41 Lakini wakafika mahali bahari mbili zinakutana, wakaipweleza meli ufuoni; omo ikakwama sana, ikawa haiwezi kuondolewa; lakini sehemu ya shetri ikavunjika vipande vipande kutokana na kupigwa kwa mawimbi yenye nguvu.
ACT 27:42 Wale askari wakapanga kuwaua wale wafungwa ili kuzuia hata mmoja wao asiogelee na kutoroka.
ACT 27:43 Lakini yule jemadari alitaka kuokoa maisha ya Paulo, basi akawazuia askari wasitekeleze mpango wao. Akaamuru wale wanaoweza kuogelea wajitupe baharini kwanza, waogelee hadi nchi kavu.
ACT 27:44 Waliosalia wangefika nchi kavu kwa kutumia mbao au vipande vya meli iliyovunjika, hivyo wote wakafika nchi kavu salama.
ACT 28:1 Baada ya kufika nchi kavu salama, ndipo tukafahamu kwamba jina la kile kisiwa ni Malta.
ACT 28:2 Wenyeji wa kile kisiwa walituonesha ukarimu usio wa kawaida. Waliwasha moto na kutukaribisha sisi sote kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa na baridi.
ACT 28:3 Paulo alikusanya mzigo wa kuni, na alipokuwa anaweka kuni kwenye moto, nyoka mwenye sumu akatoka humo kwa ajili ya joto na kujisokotea mkononi mwake.
ACT 28:4 Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akining’inia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni muuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.”
ACT 28:5 Lakini Paulo akamkung’utia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yoyote.
ACT 28:6 Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona kwamba hakuna chochote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu.
ACT 28:7 Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la kiongozi mkuu wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio. Alitupokea kwake, na akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu.
ACT 28:8 Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaugua homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya.
ACT 28:9 Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa.
ACT 28:10 Wakatupatia heshima nyingi, nasi tulipokuwa tayari kusafiri kwa meli, wakatupakilia vitu vyote tulivyokuwa tunavihitaji.
ACT 28:11 Miezi mitatu baadaye tukaanza safari kwa meli iliyokuwa imetia nanga kwenye kisiwa hicho kwa ajili ya majira ya baridi. Hii ilikuwa meli ya Iskanderia yenye alama ya miungu pacha waitwao Kasta na Poluksi.
ACT 28:12 Kituo chetu cha kwanza kilikuwa Sirakusa na tukakaa huko siku tatu.
ACT 28:13 Kisha tukang’oa nanga, tukafika Regio. Siku iliyofuata, upepo mkali wa kusi ukavuma, na siku ya pili yake tukafika Puteoli.
ACT 28:14 Huko tukawakuta ndugu, nasi tukakaribishwa tukae nao kwa siku saba. Hivyo tukaendelea na safari hadi Rumi.
ACT 28:15 Ndugu wa huko Rumi waliposikia habari zetu, walikuja hadi Soko la Apio na mahali paitwapo Mikahawa Mitatu kutulaki. Paulo alipowaona, alimshukuru Mungu akatiwa moyo.
ACT 28:16 Tulipofika Rumi, Paulo aliruhusiwa kuishi peke yake akiwa na askari wa kumlinda.
ACT 28:17 Siku tatu baadaye Paulo akawaita pamoja viongozi wa Wayahudi. Walipokwisha kukusanyika akawaambia, “Ndugu zangu, ingawa sikufanya jambo lolote dhidi ya watu wetu au dhidi ya desturi za baba zetu, lakini nilikamatwa huko Yerusalemu nikakabidhiwa kwa Warumi.
ACT 28:18 Wao walipokwisha kunihoji, wakataka kuniachia huru kwa sababu hawakuona kosa lolote nililolifanya linalostahili adhabu ya kifo.
ACT 28:19 Lakini Wayahudi walipopinga uamuzi huo, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, ingawa sikuwa na lalamiko lolote juu ya taifa langu.
ACT 28:20 Basi hii ndiyo sababu nimewatumania, ili niseme nanyi. Kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.”
ACT 28:21 Wakamjibu, “Hatujapokea barua zozote kutoka Yudea zinazokuhusu, wala hapana ndugu yeyote aliyekuja hapa ambaye ametoa taarifa au kuzungumza jambo lolote baya juu yako.
ACT 28:22 Lakini tungependa kusikia kutoka kwako unalofikiri kwa sababu tunajua kwamba kila mahali watu wanazungumza mabaya kuhusu jamii hii.”
ACT 28:23 Baada ya kupanga siku ya kuonana naye, watu wengi wakaja kuanzia asubuhi hadi jioni akawaeleza na kutangaza kuhusu ufalme wa Mungu akijaribu kuwahadithia juu ya Isa kutoka Torati ya Musa na kutoka Manabii.
ACT 28:24 Baadhi wakasadiki yale aliyosema, lakini wengine hawakuamini.
ACT 28:25 Hivyo hawakukubaliana, nao walipokuwa wanaondoka, Paulo akatoa kauli moja zaidi: “Roho wa Mungu alinena kweli na baba zenu aliposema mambo yale yaliyomhusu Bwana Isa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:
ACT 28:26 “ ‘Nenda kwa watu hawa na useme, “Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama, lakini hamtaona.”
ACT 28:27 Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’
ACT 28:28 “Basi na ijulikane kwenu kwamba, huu wokovu wa Mungu umepelekwa kwa watu wa Mataifa, nao watasikiliza.” [
ACT 28:29 Baada yake kusema maneno haya, Wayahudi wakaondoka wakiwa na hoja nyingi miongoni mwao.]
ACT 28:30 Kwa miaka miwili mizima Paulo alikaa huko kwa nyumba aliyokuwa amepanga. Akawakaribisha wote walioenda kumwona.
ACT 28:31 Akahubiri ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yale yaliyomhusu Bwana Isa Al-Masihi, kwa ujasiri wote na bila kizuizi chochote.
ROM 1:1 Paulo, mtumishi wa Al-Masihi Isa, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu,
ROM 1:2 Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika Maandiko Matakatifu,
ROM 1:3 yaani Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi,
ROM 1:4 na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani Isa Al-Masihi, Bwana wetu.
ROM 1:5 Kupitia kwake tumepokea neema na utume ili kuwaita watu wote wa mataifa waje kwenye utii utokanao na imani kwa ajili ya jina lake.
ROM 1:6 Ninyi nyote pia mko miongoni mwa watu walioitwa ili wapate kuwa mali ya Isa Al-Masihi.
ROM 1:7 Kwa wote walio Rumi wanaopendwa na Mungu na kuitwa kuwa watakatifu.
ROM 1:8 Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kupitia kwa Isa Al-Masihi kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote.
ROM 1:9 Kwa maana Mungu ninayemtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Injili ya Mwanawe, ni shahidi wangu jinsi ninavyowakumbuka daima
ROM 1:10 katika maombi yangu siku zote. Nami ninaomba kwamba hatimaye sasa kwa mapenzi ya Mungu, njia ipate kufunguliwa kwa ajili yangu ili nije kwenu.
ROM 1:11 Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuwapa karama za rohoni ili mwe imara,
ROM 1:12 au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi.
ROM 1:13 Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mara nyingi nimekusudia kuja kwenu (ingawa hadi sasa nimezuiliwa), ili nipate kuvuna mavuno miongoni mwenu kama nilivyovuna miongoni mwa watu wa Mataifa wengine.
ROM 1:14 Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima.
ROM 1:15 Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.
ROM 1:16 Mimi siionei haya Injili, kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia.
ROM 1:17 Kwa maana katika Injili haki ya Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”
ROM 1:18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao.
ROM 1:19 Kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao.
ROM 1:20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani uweza wake wa milele na asili yake ya uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.
ROM 1:21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza.
ROM 1:22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga,
ROM 1:23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizotengenezwa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vinavyotambaa.
ROM 1:24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakaivunjia heshima miili yao wao kwa wao.
ROM 1:25 Waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.
ROM 1:26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wazifuate tamaa za aibu. Hata wanawake wao wakabadili mahusiano ya kimwili ya asili kwa mahusiano yasiyokusudiwa.
ROM 1:27 Vivyo hivyo wanaume pia wakaacha mahusiano ya kimwili ya asili na wanawake, wakawakiana kwa tamaa mbaya wao kwa wao. Wanaume wakafanya matendo ya aibu na wanaume wengine, nao wakapata adhabu waliyostahili kwa ajili ya upotovu wao.
ROM 1:28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa.
ROM 1:29 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji,
ROM 1:30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao,
ROM 1:31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili.
ROM 1:32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.
ROM 2:1 Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo.
ROM 2:2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli.
ROM 2:3 Hivyo wewe mwanadamu, unapotoa hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu?
ROM 2:4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?
ROM 2:5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa.
ROM 2:6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu kulingana na matendo yake.
ROM 2:7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele.
ROM 2:8 Lakini kwa wale wanaotafuta mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.
ROM 2:9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia,
ROM 2:10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa.
ROM 2:11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.
ROM 2:12 Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria.
ROM 2:13 Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki.
ROM 2:14 (Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria.
ROM 2:15 Wao wanaonesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.)
ROM 2:16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kupitia kwa Isa Al-Masihi, kama isemavyo Injili yangu.
ROM 2:17 Tazama, wewe ukiwa unajiita Myahudi na kuitegemea Torati na kujisifia uhusiano wako na Mungu,
ROM 2:18 kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo Torati,
ROM 2:19 kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani,
ROM 2:20 mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo Torati,
ROM 2:21 basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba?
ROM 2:22 Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu?
ROM 2:23 Wewe ujivuniaye Torati, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja Torati?
ROM 2:24 Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.”
ROM 2:25 Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii Torati, lakini kama unavunja Torati, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa.
ROM 2:26 Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo Torati inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa?
ROM 2:27 Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii Torati watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana Torati ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja.
ROM 2:28 Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili.
ROM 2:29 Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho wa Mungu, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu kama huyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.
ROM 3:1 Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara?
ROM 3:2 Kuna faida kubwa kwa kila namna! Kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa maneno halisi ya Mungu.
ROM 3:3 Ingekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu?
ROM 3:4 La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa: “Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena, na ukashinde unapotoa hukumu.”
ROM 3:5 Lakini ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.)
ROM 3:6 La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angewezaje kuhukumu ulimwengu?
ROM 3:7 Mtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?”
ROM 3:8 Nasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja”? Wao wanastahili hukumu yao.
ROM 3:9 Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi.
ROM 3:10 Kama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.
ROM 3:11 Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.
ROM 3:12 Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja.”
ROM 3:13 “Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.” “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”
ROM 3:14 “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.”
ROM 3:15 “Miguu yao ina haraka kumwaga damu;
ROM 3:16 maangamizi na taabu viko katika njia zao,
ROM 3:17 wala njia ya amani hawaijui.”
ROM 3:18 “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.”
ROM 3:19 Basi tunajua kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu.
ROM 3:20 Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.
ROM 3:21 Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Torati na Manabii wanaishuhudia.
ROM 3:22 Haki hii inayotoka kwa Mungu hupatikana kwa Isa Al-Masihi kwa wote wanaomwamini. Kwa maana hapo hakuna tofauti,
ROM 3:23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu,
ROM 3:24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kupitia kwa ukombozi ulio katika Al-Masihi Isa.
ROM 3:25 Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kupitia kwa imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake, Mungu aliziachilia bila adhabu zile dhambi zilizotangulia kufanywa.
ROM 3:26 Alifanya hivyo ili kuonesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Isa.
ROM 3:27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La, bali kwa ile sheria ya imani.
ROM 3:28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kupitia kwa imani wala si kwa matendo ya sheria.
ROM 3:29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia.
ROM 3:30 Basi kwa kuwa kuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani hiyo hiyo.
ROM 3:31 Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.
ROM 4:1 Tuseme nini basi, kuhusu Ibrahimu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili?
ROM 4:2 Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu.
ROM 4:3 Kwa maana Maandiko yasemaje? “Ibrahimu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
ROM 4:4 Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili.
ROM 4:5 Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki.
ROM 4:6 Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena kuhusu baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:
ROM 4:7 “Wamebarikiwa wale ambao wamesamehewa makosa yao, ambao dhambi zao zimefunikwa.
ROM 4:8 Heri mtu yule Mwenyezi Mungu hamhesabii dhambi zake.”
ROM 4:9 Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tumesema imani ya Ibrahimu ilihesabiwa kwake kuwa haki.
ROM 4:10 Je, ilihesabiwaje kwake kuwa haki? Ni kabla ya kutahiriwa, au baada yake kutahiriwa? Haikuwa baada yake kutahiriwa, bali kabla hajatahiriwa!
ROM 4:11 Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote waaminio pasipo kutahiriwa, ili wahesabiwe kuwa wenye haki.
ROM 4:12 Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo baba yetu Ibrahimu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.
ROM 4:13 Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Ibrahimu au kwa wazao wake kupitia kwa sheria bali kupitia kwa haki ipatikanayo kwa imani.
ROM 4:14 Kwa maana ikiwa wale wanaoishi kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu,
ROM 4:15 kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria, hakuna makosa.
ROM 4:16 Kwa hiyo, ahadi huja kupitia kwa imani, ili iwe ni kwa neema, na ihakikishiwe wazao wote wa Ibrahimu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Ibrahimu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote.
ROM 4:17 Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anayefufua waliokufa, na kuvitaja vitu ambavyo haviko kana kwamba viko.
ROM 4:18 Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Ibrahimu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”
ROM 4:19 Ibrahimu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri hali ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri hali ya kufa ya tumbo la Sara.
ROM 4:20 Lakini Ibrahimu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu,
ROM 4:21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi.
ROM 4:22 Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”
ROM 4:23 Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake,
ROM 4:24 bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupatia haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Isa Bwana wetu kutoka kwa wafu.
ROM 4:25 Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.
ROM 5:1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi,
ROM 5:2 ambaye kupitia kwake tumepata kuifikia neema hii kupitia kwa imani, neema ambayo tunasimama ndani yake sasa. Nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu.
ROM 5:3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi,
ROM 5:4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini,
ROM 5:5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kupitia kwa Roho wa Mungu ambaye ametupatia.
ROM 5:6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Al-Masihi alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi.
ROM 5:7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema.
ROM 5:8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Al-Masihi alikufa kwa ajili yetu.
ROM 5:9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake!
ROM 5:10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kupitia kwa kifo cha Mwanawe, si zaidi sana baada ya kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake.
ROM 5:11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.
ROM 5:12 Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na kupitia dhambi hii mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi:
ROM 5:13 kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwemo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria.
ROM 5:14 Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Musa, mauti ilitawala watu wote, hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri, kama alivyofanya Adamu, aliye mfano wa yule atakayekuja.
ROM 5:15 Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, basi neema ya Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani Isa Al-Masihi, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi.
ROM 5:16 Tena ile karama ya Mungu haiwezi kulinganishwa na matokeo ya ile dhambi ya mtu mmoja. Kwani hukumu ilikuja kupitia kwa dhambi ya mtu mmoja, ikaleta adhabu; lakini ile karama ilikuja baada ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki.
ROM 5:17 Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kupitia kwa huyo mtu mmoja, yaani Isa Al-Masihi.
ROM 5:18 Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote.
ROM 5:19 Kwa maana kama vile kupitia kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kupitia kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.
ROM 5:20 Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi,
ROM 5:21 ili kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo neema iweze kutawala kupitia kwa haki hata kuleta uzima wa milele katika Isa Al-Masihi Bwana wetu.
ROM 6:1 Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka?
ROM 6:2 La hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi?
ROM 6:3 Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Al-Masihi Isa tulibatizwa katika mauti yake?
ROM 6:4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kupitia kwa ubatizo katika mauti, ili kama vile Al-Masihi alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, nasi pia tupate kuishi maisha mapya.
ROM 6:5 Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake.
ROM 6:6 Kwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi.
ROM 6:7 Kwa maana mtu yeyote aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.
ROM 6:8 Basi ikiwa tulikufa pamoja na Al-Masihi, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye.
ROM 6:9 Kwa maana tunajua kwamba Al-Masihi, kwa sababu alifufuliwa kutoka kwa wafu, hawezi kufa tena; mauti haina tena mamlaka juu yake.
ROM 6:10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu; lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.
ROM 6:11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Al-Masihi Isa.
ROM 6:12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya.
ROM 6:13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki.
ROM 6:14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.
ROM 6:15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha!
ROM 6:16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii? Iwe ni watumwa wa dhambi ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki?
ROM 6:17 Lakini Mungu apewe shukrani kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa.
ROM 6:18 Nanyi baada ya kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.
ROM 6:19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa.
ROM 6:20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki.
ROM 6:21 Lakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti.
ROM 6:22 Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele.
ROM 6:23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Al-Masihi Isa Bwana wetu.
ROM 7:1 Ndugu zangu, sasa ninasema na wale wanaoijua Torati: Je, hamjui kwamba Torati ina mamlaka juu ya mtu wakati akiwa hai tu?
ROM 7:2 Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa.
ROM 7:3 Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.
ROM 7:4 Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia Torati kupitia kwa mwili wa Al-Masihi, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu.
ROM 7:5 Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na Torati zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti.
ROM 7:6 Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na Torati ili tutumike katika njia mpya ya Roho wa Mungu, wala si katika njia ya zamani ya Torati iliyoandikwa.
ROM 7:7 Tuseme nini basi? Kwamba Torati ni dhambi? La, hasha! Lakini singejua dhambi isipokuwa kwa sababu ya Torati. Singejua kutamani ni nini kama Torati haikusema, “Usitamani.”
ROM 7:8 Lakini dhambi ilipata nafasi katika amri, nayo ikazaa kila aina ya tamaa ndani yangu. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa.
ROM 7:9 Mwanzoni nilikuwa hai pasipo sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa.
ROM 7:10 Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti.
ROM 7:11 Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua.
ROM 7:12 Hivyo basi, Torati yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.
ROM 7:13 Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kupitia kwa amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.
ROM 7:14 Kwa maana tunajua kwamba Torati ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi.
ROM 7:15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia.
ROM 7:16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa Torati ni njema.
ROM 7:17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.
ROM 7:18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote linalokaa ndani yangu, yaani katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda.
ROM 7:19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo.
ROM 7:20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.
ROM 7:21 Hivyo naiona Torati ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo.
ROM 7:22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia Torati ya Mungu.
ROM 7:23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.
ROM 7:24 Ole wangu, mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
ROM 7:25 Namshukuru Mungu anayeniokoa kupitia kwa Isa Al-Masihi Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa Torati ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.
ROM 8:1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Al-Masihi Isa.
ROM 8:2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Al-Masihi Isa imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.
ROM 8:3 Kwa maana kile ambacho Torati haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili,
ROM 8:4 ili haki ipatikanayo kwa Torati itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho wa Mungu.
ROM 8:5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho wa Mungu, huziweka nia zao katika mambo ya huyo Roho.
ROM 8:6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho wa Mungu ni uzima na amani.
ROM 8:7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii Torati ya Mungu, wala haiwezi kuitii.
ROM 8:8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.
ROM 8:9 Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu ambaye hana Roho wa Al-Masihi, huyo si wa Al-Masihi.
ROM 8:10 Lakini kama Al-Masihi anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki.
ROM 8:11 Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Isa kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Al-Masihi Isa kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kupitia kwa Roho wake Mtakatifu akaaye ndani yenu.
ROM 8:12 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi tu wadeni, si wa mwili, ili tuishi kwa kuufuata mwili,
ROM 8:13 kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.
ROM 8:14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu.
ROM 8:15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iletayo hofu tena, bali mlipokea Roho wa kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, Baba.”
ROM 8:16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu kwamba sisi tu watoto wa Mungu.
ROM 8:17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Al-Masihi, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.
ROM 8:18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu.
ROM 8:19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu.
ROM 8:20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini,
ROM 8:21 ili viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
ROM 8:22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama uchungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.
ROM 8:23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho wa Mungu, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani ukombozi wa miili yetu.
ROM 8:24 Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana, basi hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari?
ROM 8:25 Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi.
ROM 8:26 Vivyo hivyo, Roho wa Mungu hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa.
ROM 8:27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huyo huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.
ROM 8:28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wanaompenda, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake, ili kuwaletea mema.
ROM 8:29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
ROM 8:30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.
ROM 8:31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu?
ROM 8:32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?
ROM 8:33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Mungu ndiye anayewahesabia haki.
ROM 8:34 Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Hakuna! Al-Masihi Isa aliyekufa, naam, na zaidi ya hayo, akafufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea.
ROM 8:35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Al-Masihi? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga?
ROM 8:36 Kama ilivyoandikwa: “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”
ROM 8:37 Lakini katika mambo haya yote tu zaidi ya washindi kwa yeye aliyetupenda.
ROM 8:38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo,
ROM 8:39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Al-Masihi Isa, Bwana wetu.
ROM 9:1 Ninasema kweli katika Al-Masihi, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho wa Mungu.
ROM 9:2 Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu.
ROM 9:3 Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Al-Masihi kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili,
ROM 9:4 yaani watu wa Israeli. Hao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea Torati, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi.
ROM 9:5 Wao ni wa uzao wa baba zetu wa zamani, ambao kutoka kwao Al-Masihi alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen.
ROM 9:6 Si kwamba neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi.
ROM 9:7 Wala hawawi wazao wa Ibrahimu kwa sababu wao ni watoto wake, lakini: “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka.”
ROM 9:8 Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Ibrahimu.
ROM 9:9 Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”
ROM 9:10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani baba yetu Isaka.
ROM 9:11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama,
ROM 9:12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”
ROM 9:13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”
ROM 9:14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha!
ROM 9:15 Kwa maana Mungu alimwambia Musa, “Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”
ROM 9:16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu.
ROM 9:17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani kote.”
ROM 9:18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.
ROM 9:19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?”
ROM 9:20 Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ”
ROM 9:21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?
ROM 9:22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu?
ROM 9:23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake?
ROM 9:24 Hivi vyombo ni sisi, ambao pia alituita, sio kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa.
ROM 9:25 Kama alivyosema Mungu katika Hosea: “Nitawaita ‘watu wangu’ wale ambao si watu wangu; nami nitamwita ‘mpendwa wangu’ yeye ambaye si mpendwa wangu,”
ROM 9:26 tena, “Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ ”
ROM 9:27 Isaya anapaza sauti na kusema kuhusu Israeli kwamba: “Ingawa idadi ya Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaookolewa.
ROM 9:28 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ataitekeleza hukumu yake duniani kwa haraka na kwa ukamilifu.”
ROM 9:29 Ni kama vile alivyotabiri Isaya, akisema: “Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, hakutuachia uzao, tungekuwa kama Sodoma, tungefanana na Gomora.”
ROM 9:30 Kwa hiyo tuseme nini? Kwamba watu wa Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kupitia kwa imani.
ROM 9:31 Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kupitia kwa sheria, hawakuipata.
ROM 9:32 Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kupitia kwa imani bali kupitia kwa matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza”.
ROM 9:33 Kama ilivyoandikwa: “Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza watu na mwamba wa kuwaangusha. Yeyote atakayemwamini hataaibika kamwe.”
ROM 10:1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe.
ROM 10:2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.
ROM 10:3 Kwa kuwa hawakuijua haki ya Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.
ROM 10:4 Kwa maana Al-Masihi ni ukomo wa sheria ili kila mtu aaminiye ahesabiwe haki.
ROM 10:5 Musa anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”
ROM 10:6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Al-Masihi chini)
ROM 10:7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda Kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Al-Masihi kutoka kwa wafu).
ROM 10:8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani lile neno la imani tunalolihubiri.
ROM 10:9 Kwa sababu, ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Isa ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.
ROM 10:10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.
ROM 10:11 Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.”
ROM 10:12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao.
ROM 10:13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Mwenyezi Mungu, ataokolewa.”
ROM 10:14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria?
ROM 10:15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri Habari Njema!”
ROM 10:16 Lakini si wote waliotii Injili. Kwa maana Isaya asema, “Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”
ROM 10:17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Al-Masihi.
ROM 10:18 Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana: “Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu.”
ROM 10:19 Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Musa asema, “Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale ambao si taifa. Nitawakasirisha kwa taifa lile lisilo na ufahamu.”
ROM 10:20 Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema, “Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakunitafuta.”
ROM 10:21 Lakini kuhusu Israeli anasema, “Mchana kutwa nimewanyooshea watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”
ROM 11:1 Basi nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Ibrahimu kutoka kabila la Benyamini.
ROM 11:2 Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale Maandiko yasemayo kuhusu Ilya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli?
ROM 11:3 Alisema, “Mwenyezi Mungu, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?”
ROM 11:4 Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.”
ROM 11:5 Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu.
ROM 11:6 Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena.
ROM 11:7 Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu,
ROM 11:8 kama ilivyoandikwa: “Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo, macho ili wasiweze kuona, na masikio ili wasiweze kusikia, hadi leo.”
ROM 11:9 Naye Daudi anasema: “Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa, kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao.
ROM 11:10 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona, nayo migongo yao iinamishwe daima.”
ROM 11:11 Hivyo nauliza tena: Je, Waisraeli walijikwaa ili waanguke na kuangamia kabisa? La, hasha! Lakini kwa sababu ya makosa yao, wokovu umewafikia watu wa Mataifa, ili kuwafanya Waisraeli waone wivu.
ROM 11:12 Basi ikiwa kukosa kwao kumekuwa utajiri mkubwa kwa ulimwengu, tena kama kuangamia kwao kumeleta utajiri kwa watu wa Mataifa, kurudishwa kwao kutaleta utajiri mkuu zaidi.
ROM 11:13 Sasa ninasema nanyi watu wa Mataifa. Maadamu mimi ni mtume kwa watu wa Mataifa, naitukuza huduma yangu
ROM 11:14 ili kuwafanya watu wangu waone wivu na hivyo kuwaokoa baadhi yao.
ROM 11:15 Kwa kuwa ikiwa kukataliwa kwao ni kupatanishwa kwa ulimwengu, kukubaliwa kwao si kutakuwa ni uhai baada ya kufa?
ROM 11:16 Kama sehemu ya donge la unga uliotolewa kuwa limbuko ni mtakatifu, basi unga wote ni mtakatifu, nalo shina kama ni takatifu, vivyo hivyo na matawi nayo.
ROM 11:17 Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni,
ROM 11:18 basi usijivune juu ya hayo matawi. Lakini ukijivuna, kumbuka jambo hili: Si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe.
ROM 11:19 Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.”
ROM 11:20 Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa.
ROM 11:21 Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe.
ROM 11:22 Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Ukali kwa wale walioanguka, bali wema wa Mungu kwako wewe, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali.
ROM 11:23 Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina.
ROM 11:24 Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu, na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni wao mwenyewe!
ROM 11:25 Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie.
ROM 11:26 Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa: “Mkombozi atakuja kutoka Sayuni; ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo.
ROM 11:27 Hili ndilo agano langu nao nitakapoziondoa dhambi zao.”
ROM 11:28 Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya baba zao wa zamani;
ROM 11:29 kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake.
ROM 11:30 Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao,
ROM 11:31 hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu.
ROM 11:32 Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.
ROM 11:33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri wa hekima na maarifa ya Mungu! Tazama jinsi hukumu zake hazichunguziki, na ambavyo njia zake hazitafutiki!
ROM 11:34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Mwenyezi Mungu? Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”
ROM 11:35 “Au ni nani aliyempa chochote ili arudishiwe?”
ROM 11:36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake. Utukufu ni wake milele! Amen.
ROM 12:1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana.
ROM 12:2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kujaribu ili kuthibitisha mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza na kamilifu machoni pake.
ROM 12:3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.
ROM 12:4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja,
ROM 12:5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Al-Masihi, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.
ROM 12:6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani.
ROM 12:7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe,
ROM 12:8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.
ROM 12:9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema.
ROM 12:10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine.
ROM 12:11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana Isa.
ROM 12:12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi.
ROM 12:13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.
ROM 12:14 Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani.
ROM 12:15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.
ROM 12:16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.
ROM 12:17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote.
ROM 12:18 Ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote.
ROM 12:19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Mwenyezi Mungu.
ROM 12:20 Badala yake: “Kama adui yako ana njaa, mlishe; kama ana kiu, mpe kinywaji. Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”
ROM 12:21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
ROM 13:1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu.
ROM 13:2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe.
ROM 13:3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu.
ROM 13:4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema yako. Lakini ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya.
ROM 13:5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri.
ROM 13:6 Kwa sababu hii mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu, ambao hutumia muda wao wote kutawala.
ROM 13:7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.
ROM 13:8 Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria.
ROM 13:9 Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”
ROM 13:10 Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa sheria.
ROM 13:11 Nanyi fanyeni hivi, mkiutambua wakati tulio nao. Saa ya kuamka kutoka usingizini imewadia, kwa maana sasa wokovu wetu umekaribia kuliko hapo kwanza tulipoamini.
ROM 13:12 Usiku umeendelea sana, mapambazuko yamekaribia. Kwa hiyo tuyaweke kando matendo ya giza na tuvae silaha za nuru.
ROM 13:13 Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.
ROM 13:14 Bali jivikeni Bwana Isa Al-Masihi, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.
ROM 14:1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake.
ROM 14:2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu.
ROM 14:3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali.
ROM 14:4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.
ROM 14:5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini.
ROM 14:6 Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Mwenyezi Mungu. Naye alaye nyama hula kwa Mwenyezi Mungu, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Mwenyezi Mungu na humshukuru Mungu.
ROM 14:7 Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe.
ROM 14:8 Kama tunaishi, tunaishi kwa Mwenyezi Mungu, nasi pia tukifa tunakufa kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Mwenyezi Mungu.
ROM 14:9 Kwani kwa sababu hii hasa, Al-Masihi alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani waliokufa na walio hai.
ROM 14:10 Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu.
ROM 14:11 Kwa kuwa imeandikwa: “ ‘Kama vile niishivyo,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘kila goti litapigwa mbele zangu, na kila ulimi utakiri kwa Mungu.’ ”
ROM 14:12 Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.
ROM 14:13 Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana. Badala yake mtu aamue kutoweka kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya ndugu mwingine.
ROM 14:14 Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Isa kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi.
ROM 14:15 Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Al-Masihi alikufa kwa ajili yake.
ROM 14:16 Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu.
ROM 14:17 Kwa maana ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho wa Mungu.
ROM 14:18 Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Al-Masihi kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.
ROM 14:19 Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi.
ROM 14:20 Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae.
ROM 14:21 Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.
ROM 14:22 Je, wewe unayo imani? Ile imani uliyo nayo, uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiye na sababu ya kujihukumu nafsi yake kwa ajili ya kile anachokifanya.
ROM 14:23 Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, amehukumiwa, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa chochote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.
ROM 15:1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe.
ROM 15:2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani.
ROM 15:3 Kwa maana hata Al-Masihi hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”
ROM 15:4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.
ROM 15:5 Mungu atoaye saburi na faraja awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Al-Masihi Isa,
ROM 15:6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
ROM 15:7 Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Al-Masihi alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.
ROM 15:8 Kwa maana nawaambia kwamba Al-Masihi amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonesha kweli ya Mungu, na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani,
ROM 15:9 na pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa: “Kwa hiyo nitakutukuza kati ya watu wa Mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.”
ROM 15:10 Tena yasema, “Enyi watu wa Mataifa, furahini pamoja na watu wa Mungu.”
ROM 15:11 Tena, “Msifuni Mwenyezi Mungu, ninyi watu wa Mataifa wote, na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”
ROM 15:12 Tena Isaya anasema, “Shina la Yese litachipuka, yeye atakayeinuka ili kuyatawala mataifa. Watu wa Mataifa watamtumaini.”
ROM 15:13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wa Mungu.
ROM 15:14 Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema, mkijazwa ufahamu wote na mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi.
ROM 15:15 Hata hivyo, nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu ili kuwakumbusha tena kuvihusu, kutokana na ile neema Mungu aliyonipa
ROM 15:16 niwe mhudumu wa Al-Masihi Isa kwa watu wa Mataifa. Alinipa huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubalika na Mungu, kwa kutakaswa na Roho wa Mungu.
ROM 15:17 Kwa hiyo ninajisifu katika Al-Masihi Isa, kwenye utumishi wangu kwa Mungu.
ROM 15:18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Al-Masihi amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya,
ROM 15:19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake hadi Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Al-Masihi kwa ukamilifu.
ROM 15:20 Hivyo imekuwa nia yangu kuhubiri Injili pale ambapo Al-Masihi hajajulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
ROM 15:21 Lakini kama ilivyoandikwa: “Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona, nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”
ROM 15:22 Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.
ROM 15:23 Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi.
ROM 15:24 Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi hadi huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo.
ROM 15:25 Ila sasa niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko.
ROM 15:26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walio miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu.
ROM 15:27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini.
ROM 15:28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania.
ROM 15:29 Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Al-Masihi.
ROM 15:30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi na kwa upendo wa Roho wa Mungu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu.
ROM 15:31 Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walio Yudea, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu,
ROM 15:32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi.
ROM 15:33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.
ROM 16:1 Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mhudumu katika kundi la waumini la Kenkrea.
ROM 16:2 Naomba mpokeeni katika Bwana Isa ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.
ROM 16:3 Wasalimuni Prisila na Akila, watumishi wenzangu katika Al-Masihi Isa.
ROM 16:4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makundi yote ya waumini walio watu wa Mataifa.
ROM 16:5 Salimuni pia kundi la waumini wanaokutana nyumbani mwao. Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Al-Masihi huko jimbo la Asia.
ROM 16:6 Msalimuni Mariamu, aliyefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.
ROM 16:7 Wasalimuni Androniko na Yunia, jamaa zangu ambao wamekuwa gerezani pamoja nami. Wao ni maarufu miongoni mwa mitume, nao walikuwa katika Al-Masihi kabla yangu.
ROM 16:8 Msalimuni Ampliato, yeye nimpendaye katika Bwana Isa.
ROM 16:9 Msalimuni Urbano, mtendakazi mwenzetu katika Al-Masihi, pamoja na rafiki yangu mpendwa Stakisi.
ROM 16:10 Msalimuni Apele aliyejaribiwa na akaithibitisha imani yake katika Al-Masihi. Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Aristobulo.
ROM 16:11 Msalimuni ndugu yangu Herodioni. Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Narkiso walio katika Bwana Isa.
ROM 16:12 Wasalimuni Trifaina na Trifosa, wale wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana Isa. Msalimuni rafiki yangu mpendwa Persisi, mwanamke mwingine aliyefanya kazi kwa bidii katika Bwana Isa.
ROM 16:13 Msalimuni Rufo, mteule katika Bwana Isa, pamoja na mama yake, ambaye amekuwa mama kwangu pia.
ROM 16:14 Wasalimuni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.
ROM 16:15 Wasalimuni Filologo, Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa na watakatifu wote walio pamoja nao.
ROM 16:16 Salimianeni kwa busu takatifu. Makundi yote ya waumini ya Al-Masihi wanawasalimu.
ROM 16:17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza.
ROM 16:18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana wetu Al-Masihi, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.
ROM 16:19 Kila mtu amesikia kuhusu utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.
ROM 16:20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Isa iwe nanyi. Amen.
ROM 16:21 Timotheo, mtendakazi mwenzangu anawasalimu. Vivyo hivyo Lukio, Yasoni, na Sosipatro, ndugu zangu.
ROM 16:22 Mimi, Tertio, niliye mwandishi wa waraka huu, nawasalimu katika Bwana Isa.
ROM 16:23 Gayo, ambaye ni mwenyeji wangu na wa kundi lote la waumini, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto ndugu yetu, pia wanawasalimu. [
ROM 16:24 Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe pamoja nanyi nyote. Amen.]
ROM 16:25 Sasa atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara kwa Injili yangu na kuhubiriwa kwa Isa Al-Masihi, kutokana na kufunuliwa siri zilizofichika tangu zamani za kale.
ROM 16:26 Lakini sasa siri hiyo imefunuliwa na kujulikana kupitia maandiko ya kinabii kutokana na amri ya Mungu wa milele, ili mataifa yote yaweze kumwamini na kumtii:
ROM 16:27 ndiye Mungu, aliye pekee mwenye hekima, ambaye kupitia kwa Isa Al-Masihi utukufu ni wake milele na milele! Amen.
1CO 1:1 Paulo, niliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Al-Masihi Isa, na Sosthene ndugu yetu.
1CO 1:2 Kwa kundi la waumini wa Mungu walioko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Al-Masihi Isa na walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Al-Masihi Isa Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia.
1CO 1:3 Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
1CO 1:4 Ninamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu kwa sababu ya neema yake mliyopewa katika Al-Masihi Isa.
1CO 1:5 Kwa kuwa katika Al-Masihi mmetajirishwa kwa kila hali, katika kusema kwenu na katika maarifa yenu yote,
1CO 1:6 kwa sababu ushuhuda wetu kumhusu Al-Masihi ulithibitishwa ndani yenu.
1CO 1:7 Kwa hiyo hamkupungukiwa na karama yoyote ya kiroho wakati mnangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
1CO 1:8 Atawafanya imara hadi mwisho, ili msiwe na hatia siku ile ya Bwana wetu Isa Al-Masihi.
1CO 1:9 Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Isa Al-Masihi, Bwana wetu ni mwaminifu.
1CO 1:10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano kati yenu, na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi.
1CO 1:11 Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi kati yenu.
1CO 1:12 Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa”; na mwingine, “Mimi ni wa Al-Masihi.”
1CO 1:13 Je, Al-Masihi amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?
1CO 1:14 Nashukuru kwamba sikumbatiza mtu yeyote isipokuwa Krispo na Gayo.
1CO 1:15 Kwa hiyo hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa jina langu.
1CO 1:16 (Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana; lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.)
1CO 1:17 Kwa maana Al-Masihi hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Al-Masihi usije ukakosa nguvu yake.
1CO 1:18 Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.
1CO 1:19 Kwa maana imeandikwa: “Nitaiharibu hekima ya wenye hekima, na kubatilisha akili ya wenye akili.”
1CO 1:20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu?
1CO 1:21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa.
1CO 1:22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima.
1CO 1:23 Lakini sisi tunamhubiri Al-Masihi aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi.
1CO 1:24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Al-Masihi ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu.
1CO 1:25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.
1CO 1:26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika vyeo.
1CO 1:27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima; Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu.
1CO 1:28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko,
1CO 1:29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake.
1CO 1:30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Al-Masihi Isa, aliyefanyika kwetu hekima inayotoka kwa Mungu, yaani haki yetu, na utakatifu na ukombozi.
1CO 1:31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Mwenyezi Mungu.”
1CO 2:1 Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu.
1CO 2:2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote nilipokuwa nanyi, isipokuwa Isa Al-Masihi aliyesulubiwa.
1CO 2:3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana.
1CO 2:4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi, bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho wa Mungu,
1CO 2:5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.
1CO 2:6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika.
1CO 2:7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuumbwa, kwa ajili ya utukufu wetu.
1CO 2:8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangeelewa, hawangemsulubisha Bwana wa utukufu.
1CO 2:9 Lakini ni kama ilivyoandikwa: “Hakuna jicho limepata kuona, wala sikio limepata kusikia, wala hayakuingia moyoni mwa mwanadamu yeyote, mambo ambayo Mungu amewaandalia wale wanaompenda”:
1CO 2:10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake. Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu.
1CO 2:11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho Mtakatifu wa Mungu.
1CO 2:12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure.
1CO 2:13 Haya ndio tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho.
1CO 2:14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yanayotoka kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni.
1CO 2:15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.
1CO 2:16 “Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Mwenyezi Mungu ili apate kumfundisha?” Lakini sisi tunayo mawazo ya Al-Masihi.
1CO 3:1 Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Al-Masihi.
1CO 3:2 Niliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula. Naam, hata sasa hamko tayari.
1CO 3:3 Ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini? Je, si mwaendelea kama watu wa kawaida?
1CO 3:4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?
1CO 3:5 Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kupitia wao mliamini, kama vile Bwana Isa alivyompa kila mtu huduma yake.
1CO 3:6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliikuza.
1CO 3:7 Hivyo mwenye kupanda na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ambaye huifanya ikue.
1CO 3:8 Apandaye mbegu ana lengo sawa na yule atiaye maji na kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake.
1CO 3:9 Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.
1CO 3:10 Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mmoja inampasa awe mwangalifu jinsi anavyojenga.
1CO 3:11 Kwa maana hakuna mtu yeyote awezaye kuweka msingi mwingine wowote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Isa Al-Masihi.
1CO 3:12 Kama mtu yeyote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, miti, majani au nyasi,
1CO 3:13 kazi yake itaonekana ilivyo, kwa kuwa Siku ile itaidhihirisha. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu.
1CO 3:14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu yake.
1CO 3:15 Kama kitateketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini tu kama mtu aliyenusurika kwenye moto.
1CO 3:16 Je, hamjui kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
1CO 3:17 Kama mtu yeyote akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ndio hilo hekalu.
1CO 3:18 Msijidanganye. Kama mtu yeyote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima.
1CO 3:19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,”
1CO 3:20 tena, “Mwenyezi Mungu anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.”
1CO 3:21 Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Vitu vyote ni vyenu,
1CO 3:22 iwe ni Paulo au Apolo au Kefa, au dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au ujao: haya yote ni yenu,
1CO 3:23 na ninyi ni wa Al-Masihi, naye Al-Masihi ni wa Mungu.
1CO 4:1 Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Al-Masihi na mawakili wa siri za Mungu.
1CO 4:2 Tena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu.
1CO 4:3 Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yoyote ya kibinadamu. Naam, hata mimi mwenyewe sijihukumu.
1CO 4:4 Dhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinihesabii kuwa asiye na hatia. Bwana Isa ndiye anihukumuye.
1CO 4:5 Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni hadi Bwana Isa atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.
1CO 4:6 Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine.
1CO 4:7 Kwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?
1CO 4:8 Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi!
1CO 4:9 Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia.
1CO 4:10 Kwa ajili ya Al-Masihi sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Al-Masihi. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa.
1CO 4:11 Hadi saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao.
1CO 4:12 Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki; tunapoteswa, tunastahimili;
1CO 4:13 tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Hadi sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.
1CO 4:14 Siwaandikii mambo haya ili kuwaaibisha, bali ili kuwaonya, kama wanangu wapendwa.
1CO 4:15 Hata kama mnao walimu elfu kumi katika Al-Masihi, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Al-Masihi Isa kwa kuwaletea Injili.
1CO 4:16 Basi nawasihi igeni mfano wangu.
1CO 4:17 Kwa sababu hii ninamtuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana Isa. Yeye atawakumbusha kuhusu njia za maisha yangu katika Al-Masihi Isa, ambayo yanakubaliana na mafundisho yangu ninayofundisha katika kila kundi la waumini.
1CO 4:18 Baadhi yenu mmekuwa na jeuri mkidhani kuwa sitafika kwenu.
1CO 4:19 Lakini kama Bwana Isa akipenda, nitafika kwenu hivi karibuni, nami nitajua, si tu kile wanachosema hawa watu jeuri, bali pia nguvu yao.
1CO 4:20 Kwa kuwa ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu.
1CO 4:21 Ninyi amueni. Je, nije kwenu na fimbo, au nije kwa upendo na kwa roho ya upole?
1CO 5:1 Yamkini habari imeenea ya kuwa miongoni mwenu kuna uzinzi ambao haujafanyika hata miongoni mwa watu wasiomjua Mungu: Kwamba mtu anaishi na mke wa baba yake.
1CO 5:2 Nanyi mwajivuna! Je, haiwapasi kuhuzunika na kumtenga na ushirika wenu mtu huyo aliyefanya mambo hayo?
1CO 5:3 Hata kama siko pamoja nanyi katika mwili, niko nanyi katika roho. Nami nimekwisha kumhukumu mtu huyo aliyetenda jambo hili, kama vile ningekuwepo.
1CO 5:4 Mnapokutana katika Jina la Bwana wetu Isa nami nikiwepo pamoja nanyi katika roho, na uweza wa Bwana Isa ukiwepo,
1CO 5:5 mkabidhini mtu huyu kwa Shetani, ili mwili wake uharibiwe, lakini roho yake iokolewe katika siku ya Mwenyezi Mungu.
1CO 5:6 Majivuno yenu si mazuri. Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge zima la unga?
1CO 5:7 Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Al-Masihi, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu.
1CO 5:8 Kwa hiyo, tusiiadhimishe sikukuu hii kwa chachu ya zamani, chachu ya nia mbaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, ndio weupe wa moyo na kweli.
1CO 5:9 Niliwaandikia katika waraka wangu kuwa msishirikiane na wazinzi.
1CO 5:10 Sina maana kwamba msishirikiane na wazinzi wa ulimwengu huu, au wenye tamaa mbaya, wanyang’anyi au waabudu sanamu. Kwa kufanya hivyo ingewalazimu mtoke ulimwenguni humu.
1CO 5:11 Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye.
1CO 5:12 Yanihusu nini kuwahukumu wale watu walio nje ya kundi la waumini? Je, si mnapaswa kuwahukumu hao walio ndani?
1CO 5:13 Mungu atawahukumu hao walio nje. “Ninyi mwondoeni huyo mtu mwovu miongoni mwenu.”
1CO 6:1 Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu?
1CO 6:2 Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo?
1CO 6:3 Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya?
1CO 6:4 Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, je, mnachagua watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kundi la waumini kuwa waamuzi kati yenu?
1CO 6:5 Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waumini?
1CO 6:6 Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!
1CO 6:7 Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyang’anywa?
1CO 6:8 Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.
1CO 6:9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti,
1CO 6:10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyang’anyi hawataurithi ufalme wa Mungu.
1CO 6:11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Isa Al-Masihi na katika Roho wa Mungu wetu.
1CO 6:12 “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote.
1CO 6:13 “Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili sio kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana Isa, na Bwana Isa kwa ajili ya mwili.
1CO 6:14 Naye Mungu aliyemfufua Bwana Isa kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake.
1CO 6:15 Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Al-Masihi mwenyewe? Je, nichukue viungo vya mwili wa Al-Masihi na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha!
1CO 6:16 Hamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.”
1CO 6:17 Lakini mtu aliyeungwa na Bwana Isa anakuwa roho moja naye.
1CO 6:18 Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe.
1CO 6:19 Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu wa Mungu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe,
1CO 6:20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
1CO 7:1 Basi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: “Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke.”
1CO 7:2 Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe.
1CO 7:3 Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe.
1CO 7:4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe.
1CO 7:5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda, ili mweze kujitoa kwa maombi. Kisha mrudiane tena, ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.
1CO 7:6 Nasema haya kama ushauri na si amri.
1CO 7:7 Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.
1CO 7:8 Kwa wale wasiooa na kwa wajane, nasema hivi, ingekuwa vizuri wasioe.
1CO 7:9 Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
1CO 7:10 Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi, ila ni Bwana Isa): Mke asitengane na mumewe.
1CO 7:11 Lakini akitengana, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.
1CO 7:12 Lakini kwa wengine nasema (si Bwana Isa, ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache.
1CO 7:13 Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache.
1CO 7:14 Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe anayeamini. Kama haingekuwa hivyo watoto wenu wangakuwa si safi; lakini ilivyo sasa, wao ni watakatifu.
1CO 7:15 Lakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani.
1CO 7:16 Wewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume, unajuaje kama utamwokoa mkeo?
1CO 7:17 Lakini kila mtu na aishi maisha aliyopangiwa na Bwana Isa, yale Mungu aliyomwitia. Hii ni sheria ninayoiweka kwa makundi yote ya waumini.
1CO 7:18 Je, mtu alikuwa tayari ametahiriwa alipoitwa? Asijifanye asiyetahiriwa. Je, mtu alikuwa hajatahiriwa alipoitwa? Asitahiriwe.
1CO 7:19 Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu. Lakini kuzitii amri za Mungu ndilo jambo muhimu.
1CO 7:20 Basi kila mtu na abaki katika hali aliyoitwa nayo.
1CO 7:21 Je, wewe ulipoitwa ulikuwa mtumwa? Jambo hilo lisikusumbue. Ingawaje unaweza kupata uhuru, tumia nafasi uliyo nayo sasa kuliko wakati mwingine wowote.
1CO 7:22 Kwa maana yeyote aliyeitwa katika Bwana Isa akiwa mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana Isa, kama vile yeyote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Al-Masihi.
1CO 7:23 Mlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu.
1CO 7:24 Ndugu zangu, kama kila mtu alivyoitwa, akae katika wito wake alioitiwa na Mungu.
1CO 7:25 Basi, kuhusu wale walio bikira, mimi sina amri kutoka kwa Bwana Isa, lakini mimi natoa shauri kama mtu ambaye ni mwaminifu kwa rehema za Bwana Isa.
1CO 7:26 Kwa sababu ya shida iliyopo sasa, naona ni vyema mkibaki kama mlivyo.
1CO 7:27 Je, umeolewa? Basi usitake talaka. Je, hujaoa? Usitafute mke.
1CO 7:28 Lakini kama ukioa, hujatenda dhambi; na kama bikira akiolewa, hajatenda dhambi. Lakini wale wanaooa watakabiliana na matatizo mengi katika maisha haya, nami nataka kuwazuilia hayo.
1CO 7:29 Lakini ndugu zangu, nina maana kwamba muda uliobaki ni mfupi. Tangu sasa wale waliooa waishi kama wasio na wake;
1CO 7:30 nao wanaoomboleza, kama ambao hawaombolezi; wenye furaha kama wasiokuwa nayo; wale wanaonunua, kama vile vitu walivyonunua si mali yao;
1CO 7:31 nao wale wanaoshughulika na vitu vya dunia hii, kama ambao hawahusiki navyo. Kwa maana dunia hii kama tunavyoiona sasa inapita.
1CO 7:32 Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana Isa, jinsi ya kumpendeza Bwana Isa.
1CO 7:33 Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, jinsi ya kumfurahisha mkewe,
1CO 7:34 na mawazo yake yamegawanyika. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana: lengo lake ni awe mtakatifu kimwili na kiroho. Lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe.
1CO 7:35 Ninasema haya kwa faida yenu wenyewe, sio ili kuwawekea vizuizi bali mpate kuishi kwa jinsi ilivyo vyema bila kuvutwa pengine katika kujitoa kwenu kwa Bwana Isa.
1CO 7:36 Kama mtu yeyote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane.
1CO 7:37 Lakini mwanaume ambaye ameamua moyoni mwake kutooa bila kulazimishwa na mtu yeyote, bali anaweza kuzitawala tamaa zake kutomwoa huyo mwanamwali, basi anafanya ipasavyo.
1CO 7:38 Hivyo basi, mwanaume amwoaye mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi.
1CO 7:39 Mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima awe katika Bwana Isa.
1CO 7:40 Lakini kwa maoni yangu, angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.
1CO 8:1 Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga.
1CO 8:2 Mtu yeyote anayedhani kwamba anajua kitu, bado hajui kama impasavyo kujua.
1CO 8:3 Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye Mungu.
1CO 8:4 Hivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu: Tunajua kwamba “Sanamu si kitu chochote kabisa duniani,” na kwamba “Kuna Mungu mmoja tu.”
1CO 8:5 Kwa kuwa hata kama wapo hao wanaoitwa miungu, wakiwa mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi),
1CO 8:6 kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi; na kuna Bwana mmoja tu, Isa Al-Masihi, ambaye kwa yeye vitu vyote vilitoka na kwa yeye tunaishi.
1CO 8:7 Lakini si wote wanaojua jambo hili. Baadhi ya watu bado wamezoea sanamu kuwa halisi hivi kwamba wanapokula chakula kama hicho wanadhani kimetolewa sadaka kwa sanamu na kwa kuwa dhamiri zao ni dhaifu, dhamiri yao inanajisika.
1CO 8:8 Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu, wala hatupotezi chochote tusipokula, wala hatuongezi chochote tukila.
1CO 8:9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu.
1CO 8:10 Kwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu?
1CO 8:11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Al-Masihi alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu.
1CO 8:12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Al-Masihi.
1CO 8:13 Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.
1CO 9:1 Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Isa, Bwana wetu? Je, ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana?
1CO 9:2 Hata kama mimi si mtume kwa wengine, hakika mimi ni mtume kwenu, kwa maana ninyi ni muhuri wa utume wangu katika Bwana Isa.
1CO 9:3 Huu ndio utetezi wangu kwa hao wanaokaa kunihukumu.
1CO 9:4 Je, hatuna haki ya kula na kunywa?
1CO 9:5 Je, hatuna haki ya kusafiri na mke anayeamini, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu zake Bwana Isa na Kefa?
1CO 9:6 Au ni mimi na Barnaba tu inatubidi kufanya kazi ili tuweze kupata mahitaji yetu?
1CO 9:7 Ni askari yupi aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye shamba la mizabibu na asile matunda yake? Ni nani achungaye kundi na asipate maziwa yake.
1CO 9:8 Je, nasema mambo haya katika mtazamo wa kibinadamu tu? Je, Torati haisemi vivyo hivyo?
1CO 9:9 Kwa maana imeandikwa katika Torati ya Musa: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ng’ombe?
1CO 9:10 Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno.
1CO 9:11 Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu?
1CO 9:12 Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi? Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia Injili ya Al-Masihi.
1CO 9:13 Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni?
1CO 9:14 Vivyo hivyo, Bwana Isa ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili.
1CO 9:15 Lakini sijatumia hata mojawapo ya haki hizi. Nami siandiki haya nikitumaini kwamba mtanifanyia mambo hayo. Heri nife kuliko mtu yeyote kuninyima huku kujisifu kwangu.
1CO 9:16 Lakini ninapohubiri Injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili!
1CO 9:17 Nikihubiri kwa hiari, ninayo thawabu. Lakini kama si kwa hiari, basi ninachofanya ni kutekeleza tu uwakili niliowekewa.
1CO 9:18 Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ya kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.
1CO 9:19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadiri iwezekanavyo.
1CO 9:20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya Torati, nilikuwa kama aliye chini ya Torati (ingawa mimi siko chini ya Torati), ili niweze kuwapata wale walio chini ya Torati.
1CO 9:21 Kwa watu wasio na Torati nilikuwa kama asiye na Torati (ingawa siko huru mbali na Torati ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Al-Masihi), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria.
1CO 9:22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao.
1CO 9:23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.
1CO 9:24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano ili mkapata tuzo.
1CO 9:25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji lisilodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji linalodumu milele.
1CO 9:26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa.
1CO 9:27 La, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha, ili nikiisha kuwahubiria wengine, nisije nikakataliwa.
1CO 10:1 Ndugu zangu, sitaki mkose kufahamu ukweli huu kwamba baba zetu walikuwa wote chini ya wingu na kwamba wote walipita katikati ya bahari.
1CO 10:2 Wote wakabatizwa kuwa wa Musa ndani ya lile wingu na ndani ya ile bahari.
1CO 10:3 Wote walikula chakula kile kile cha roho,
1CO 10:4 na wote wakanywa kile kile kinywaji cha roho, kwa maana walikunywa kutoka ule mwamba wa roho uliofuatana nao, nao ule mwamba ulikuwa Al-Masihi.
1CO 10:5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, kwa hiyo miili yao ilitapakaa jangwani.
1CO 10:6 Basi mambo haya yalifanyika kama mifano ili kutuzuia tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya.
1CO 10:7 Msiwe waabudu sanamu, kama baadhi yao walivyokuwa, kama ilivyoandikwa, “Watu waliketi chini kula na kunywa, kisha wakainuka kucheza na kufanya sherehe za kipagani.”
1CO 10:8 Wala tusifanye uzinzi kama baadhi yao walivyofanya, wakafa watu elfu ishirini na tatu kwa siku moja.
1CO 10:9 Wala tusimjaribu Al-Masihi, kama baadhi yao walivyofanya, wakafa kwa kuumwa na nyoka.
1CO 10:10 Msinung’unike kama baadhi yao walivyofanya, wakaangamizwa na malaika mharibifu.
1CO 10:11 Mambo haya yote yaliwapata wao ili yawe mifano kwa wengine, nayo yaliandikwa ili yatuonye sisi ambao mwisho wa nyakati umetufikia.
1CO 10:12 Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke.
1CO 10:13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kushinda ili mweze kustahimili.
1CO 10:14 Kwa hiyo wapendwa wangu, zikimbieni ibada za sanamu.
1CO 10:15 Nasema watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo.
1CO 10:16 Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Al-Masihi? Mkate tunaoumega, si ushirika wa mwili wa Al-Masihi?
1CO 10:17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja.
1CO 10:18 Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni?
1CO 10:19 Je, nina maana kwamba sadaka iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yoyote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yoyote?
1CO 10:20 La hasha! Lakini sadaka za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani.
1CO 10:21 Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana Isa na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika Chakula cha Bwana Isa na katika chakula cha mashetani pia.
1CO 10:22 Je, tunataka kuamsha wivu wa Mwenyezi Mungu? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?
1CO 10:23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga.
1CO 10:24 Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.
1CO 10:25 Kuleni chochote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lolote kwa ajili ya dhamiri.
1CO 10:26 Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Mwenyezi Mungu.”
1CO 10:27 Ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri.
1CO 10:28 Lakini kama mtu yeyote akikuambia, “Hiki kimetolewa sadaka kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri.
1CO 10:29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?
1CO 10:30 Nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa ajili ya kile ambacho ninamshukuria Mungu?
1CO 10:31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.
1CO 10:32 Msiwe kikwazo kwa mtu yeyote, wawe Wayahudi au Wayunani, au kwa kundi la waumini la Mungu,
1CO 10:33 kama hata mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali kwa ajili ya wengi, ili waweze kuokolewa.
1CO 11:1 Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Al-Masihi.
1CO 11:2 Ninawasifu kwa kunikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mapokeo kama nilivyowapatia.
1CO 11:3 Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Al-Masihi, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Al-Masihi ni Mungu.
1CO 11:4 Kila mwanaume anayeomba au kutoa unabii akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake.
1CO 11:5 Naye kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele.
1CO 11:6 Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kukata au kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake.
1CO 11:7 Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu; lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume.
1CO 11:8 Kwa maana mwanaume hakutoka kwa mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume.
1CO 11:9 Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume.
1CO 11:10 Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka juu yake.
1CO 11:11 Lakini katika Bwana Isa, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke.
1CO 11:12 Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu.
1CO 11:13 Hukumuni ninyi wenyewe: Je, inafaa kwa mwanamke kumwomba Mungu bila kufunika kichwa chake?
1CO 11:14 Je, maumbile ya asili hayatufundishi kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu?
1CO 11:15 Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake? Kwa maana mwanamke amepewa nywele ndefu ili kumfunika.
1CO 11:16 Kama mtu anataka kubishana kuhusu jambo hili, sisi wala makundi ya waumini ya Mungu hatutambui desturi nyingine.
1CO 11:17 Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara.
1CO 11:18 Kwanza, mnapokutana kama kundi la waumini, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo.
1CO 11:19 Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonesha ni nani anayekubaliwa na Mungu.
1CO 11:20 Mkutanikapo pamoja si Chakula cha Bwana Isa mnachokula,
1CO 11:21 kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa.
1CO 11:22 Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kundi la waumini la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu kuhusu jambo hili? La, hasha!
1CO 11:23 Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana Isa yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Isa, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate,
1CO 11:24 naye baada ya kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
1CO 11:25 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.”
1CO 11:26 Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana Isa hadi ajapo.
1CO 11:27 Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana Isa isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana Isa.
1CO 11:28 Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe.
1CO 11:29 Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana Isa, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe.
1CO 11:30 Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa.
1CO 11:31 Lakini kama tungejichunguza wenyewe tusingehukumiwa.
1CO 11:32 Tunapohukumiwa na Bwana Isa, tunaadibishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
1CO 11:33 Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo pamoja ili kula, mngojane.
1CO 11:34 Kama mtu akiwa na njaa, ale nyumbani mwake ili mkutanapo pamoja msije mkahukumiwa. Nami nitakapokuja nitawapa maelekezo zaidi.
1CO 12:1 Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu.
1CO 12:2 Mnajua kwamba mlipokuwa watu wasiomjua Mungu, kwa njia moja au nyingine mlishawishika na kupotoshwa mkielekezwa kwa sanamu zisizonena.
1CO 12:3 Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu anayeweza kusema, “Isa na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Isa ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho wa Mungu.
1CO 12:4 Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule.
1CO 12:5 Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana Isa ni yule yule.
1CO 12:6 Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.
1CO 12:7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho wa Mungu kwa faida ya wote.
1CO 12:8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo.
1CO 12:9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja.
1CO 12:10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii, kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine kunena aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha.
1CO 12:11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.
1CO 12:12 Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi; navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Al-Masihi.
1CO 12:13 Kwa maana katika Roho mmoja wa Mungu wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
1CO 12:14 Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi.
1CO 12:15 Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili.
1CO 12:16 Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili.
1CO 12:17 Kama mwili wote ungakuwa jicho tu, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungekuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi?
1CO 12:18 Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda.
1CO 12:19 Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
1CO 12:20 Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja.
1CO 12:21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!”
1CO 12:22 Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana.
1CO 12:23 Navyo vile viungo tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee;
1CO 12:24 wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa,
1CO 12:25 ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake.
1CO 12:26 Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho; kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.
1CO 12:27 Sasa ninyi ni mwili wa Al-Masihi na kila mmoja wenu ni sehemu ya huo mwili.
1CO 12:28 Mungu ameweka katika jumuiya ya waumini kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za kusaidiana, karama za uongozi, na aina mbalimbali za lugha.
1CO 12:29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanatenda miujiza?
1CO 12:30 Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri?
1CO 12:31 Basi tamanini sana karama zilizo kuu. Nami nitawaonesha njia iliyo bora zaidi.
1CO 13:1 Hata kama nikisema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolia au toazi linalovuma.
1CO 13:2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu.
1CO 13:3 Nikitoa mali yote niliyo nayo, na nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.
1CO 13:4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi.
1CO 13:5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya.
1CO 13:6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli.
1CO 13:7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
1CO 13:8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.
1CO 13:9 Kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunatoa unabii kwa sehemu.
1CO 13:10 Lakini ukamilifu ukija, yale yasiyo kamili hutoweka.
1CO 13:11 Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto.
1CO 13:12 Kwa maana sasa tunaona taswira kama kwa kioo, lakini wakati huo tutaona wazi. Sasa nafahamu kwa sehemu, wakati huo nitafahamu kikamilifu, kama vile mimi ninavyofahamika kikamilifu.
1CO 13:13 Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.
1CO 14:1 Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii.
1CO 14:2 Kwa maana mtu yeyote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa roho.
1CO 14:3 Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji.
1CO 14:4 Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii huwajenga waumini.
1CO 14:5 Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha, lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa atafsiri, ili waumini wote wapate kujengwa.
1CO 14:6 Sasa ndugu zangu, nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya, nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho?
1CO 14:7 Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, kama vile filimbi au kinubi, mtu atajuaje ni wimbo gani unaoimbwa kusipokuwa na tofauti ya upigaji?
1CO 14:8 Tena kama tarumbeta haitoi sauti inayoeleweka, ni nani atakayejiandaa kwa ajili ya vita?
1CO 14:9 Vivyo hivyo na ninyi, mkinena maneno yasiyoeleweka katika akili, mtu atajuaje mnalosema? Kwa maana mtakuwa mnasema hewani tu.
1CO 14:10 Bila shaka ziko sauti nyingi ulimwenguni, wala hakuna isiyo na maana.
1CO 14:11 Basi kama sielewi maana ya hiyo sauti, nitakuwa mgeni kwa yule msemaji, naye atakuwa mgeni kwangu.
1CO 14:12 Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kuwajenga waumini.
1CO 14:13 Kwa sababu hii, yeye anenaye kwa lugha na aombe kwamba apate kutafsiri kile anachonena.
1CO 14:14 Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda.
1CO 14:15 Nifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, na pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia.
1CO 14:16 Ikiwa unabariki kwa roho, mtu mwingine atakayejikuta miongoni mwa hao wasiojua, atawezaje kusema “Amen” katika kushukuru kwako, wakati haelewi unachosema?
1CO 14:17 Mnaweza kuwa mnatoa shukrani kweli, sawa, lakini huyo mtu mwingine hajengeki.
1CO 14:18 Namshukuru Mungu kwamba mimi nanena kwa lugha kuliko ninyi nyote.
1CO 14:19 Lakini katika kundi la waumini ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno elfu kumi kwa lugha.
1CO 14:20 Ndugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima.
1CO 14:21 Katika Torati imeandikwa kwamba: “Kupitia kwa watu wenye lugha ng’eni na kupitia midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, lakini hata hivyo hawatanisikiliza, asema Mwenyezi Mungu.”
1CO 14:22 Basi kunena kwa lugha ni ishara, si kwa waaminio, bali kwa wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio.
1CO 14:23 Kwa hiyo kama kundi la waumini wote wakikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioelewa au wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu?
1CO 14:24 Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote,
1CO 14:25 nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko kati yenu!”
1CO 14:26 Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kundi la waumini.
1CO 14:27 Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu, si zaidi, mmoja baada ya mwingine, na lazima awepo mtu wa kutafsiri.
1CO 14:28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya katika kundi la waumini, na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.
1CO 14:29 Manabii wawili au watatu wanene, na wengine wapime kwa makini yale yasemwayo.
1CO 14:30 Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze.
1CO 14:31 Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo.
1CO 14:32 Roho za manabii huwatii manabii.
1CO 14:33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani. Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu,
1CO 14:34 wanawake wanapaswa kuwa kimya katika kundi la waumini. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama Torati isemavyo.
1CO 14:35 Wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza katika kundi la waumini.
1CO 14:36 Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia?
1CO 14:37 Kama mtu yeyote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana Isa.
1CO 14:38 Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.
1CO 14:39 Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha.
1CO 14:40 Lakini kila kitu kitendeke kwa ufasaha na kwa utaratibu.
1CO 15:1 Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama.
1CO 15:2 Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.
1CO 15:3 Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Al-Masihi alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema,
1CO 15:4 ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema,
1CO 15:5 na kwamba alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili.
1CO 15:6 Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya mia tano kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala.
1CO 15:7 Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote.
1CO 15:8 Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.
1CO 15:9 Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu niliwatesa waumini wa Mungu.
1CO 15:10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami.
1CO 15:11 Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.
1CO 15:12 Basi kama tumehubiri kwamba Al-Masihi alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu?
1CO 15:13 Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Al-Masihi hakufufuliwa.
1CO 15:14 Tena ikiwa Al-Masihi hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili.
1CO 15:15 Zaidi ya hayo, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Al-Masihi kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi.
1CO 15:16 Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Al-Masihi hajafufuka.
1CO 15:17 Tena kama Al-Masihi hajafufuliwa, imani yenu ni batili; nanyi bado mko katika dhambi zenu.
1CO 15:18 Hivyo basi, wote waliolala katika Al-Masihi wamepotea.
1CO 15:19 Ikiwa tumaini letu ndani ya Al-Masihi ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wote.
1CO 15:20 Lakini kweli Al-Masihi amefufuliwa kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala.
1CO 15:21 Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kupitia kwa mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kupitia kwa mtu mmoja.
1CO 15:22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Al-Masihi wote watafanywa hai.
1CO 15:23 Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Al-Masihi, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja.
1CO 15:24 Ndipo mwisho utafika, atakapomkabidhi Mungu Baba Mwenyezi ufalme, baada ya kuangamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu.
1CO 15:25 Kwa maana lazima Al-Masihi atawale hadi awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake.
1CO 15:26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti.
1CO 15:27 Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake”. Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Al-Masihi hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa.
1CO 15:28 Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.
1CO 15:29 Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao?
1CO 15:30 Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa?
1CO 15:31 Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Al-Masihi Isa Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku.
1CO 15:32 Kama kwa sababu za kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani? Kama wafu hawafufuliwi, “Tuleni na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa.”
1CO 15:33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”
1CO 15:34 Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.
1CO 15:35 Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?”
1CO 15:36 Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa.
1CO 15:37 Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine.
1CO 15:38 Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake.
1CO 15:39 Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti.
1CO 15:40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari ya ile miili ya mbinguni ni ya aina moja, na fahari ya ile miili ya duniani ni ya aina nyingine.
1CO 15:41 Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.
1CO 15:42 Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika;
1CO 15:43 unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu,
1CO 15:44 unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho. Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia.
1CO 15:45 Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima.
1CO 15:46 Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho.
1CO 15:47 Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni.
1CO 15:48 Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni.
1CO 15:49 Kama vile tulivyochukua mfano wa mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.
1CO 15:50 Ndugu zangu nisemalo ni hili: mwili na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika.
1CO 15:51 Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa:
1CO 15:52 ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa.
1CO 15:53 Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa.
1CO 15:54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”
1CO 15:55 “Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako? Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?”
1CO 15:56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria.
1CO 15:57 Lakini Mungu apewe shukrani, yeye atupaye ushindi kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
1CO 15:58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapendwa, simameni imara. Msitikisike. Mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana Isa, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana Isa si bure.
1CO 16:1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makundi ya waumini ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo.
1CO 16:2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake, na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango.
1CO 16:3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu.
1CO 16:4 Ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.
1CO 16:5 Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia.
1CO 16:6 Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo.
1CO 16:7 Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana Isa akipenda.
1CO 16:8 Lakini nitakaa Efeso hadi wakati wa Pentekoste,
1CO 16:9 kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.
1CO 16:10 Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana Isa, kama mimi nifanyavyo.
1CO 16:11 Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.
1CO 16:12 Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.
1CO 16:13 Kesheni; simameni imara katika imani; kuweni mashujaa na hodari.
1CO 16:14 Fanyeni kila kitu katika upendo.
1CO 16:15 Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio walikuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi,
1CO 16:16 mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii.
1CO 16:17 Nilifurahi Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu.
1CO 16:18 Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.
1CO 16:19 Makundi ya waumini wa jimbo la Asia wanawasalimu. Akila na Prisila pamoja na kundi la waumini walioko nyumbani mwao wanawasalimu sana katika Bwana Isa.
1CO 16:20 Ndugu wote walio hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
1CO 16:21 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.
1CO 16:22 Kama mtu yeyote hampendi Bwana Isa Al-Masihi, na alaaniwe. Bwana wetu Isa, njoo.
1CO 16:23 Neema ya Bwana Isa iwe nanyi.
1CO 16:24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Al-Masihi Isa. Amen.
2CO 1:1 Barua hii ni kutoka kwangu mimi Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu.
2CO 1:2 Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
2CO 1:3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote.
2CO 1:4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu.
2CO 1:5 Kama vile mateso ya Al-Masihi yanavyozidi maishani mwetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kupitia kwa Al-Masihi.
2CO 1:6 Ikiwa tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata.
2CO 1:7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki faraja yetu.
2CO 1:8 Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko jimbo la Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi.
2CO 1:9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu.
2CO 1:10 Yeye ametuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo, na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa,
2CO 1:11 kama vile mnavyoungana kusaidiana nasi katika maombi. Hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.
2CO 1:12 Basi haya ndio majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeishi katika ulimwengu kwa utakatifu na uaminifu unaotoka kwa Mungu, na hasa katika uhusiano wetu na ninyi. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu.
2CO 1:13 Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba,
2CO 1:14 kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Isa.
2CO 1:15 Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili.
2CO 1:16 Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia, na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Yudea.
2CO 1:17 Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?
2CO 1:18 Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajakuwa “Ndiyo” na “Siyo”.
2CO 1:19 Kwa kuwa Isa Al-Masihi, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silvano, na Timotheo tulimhubiri kwenu, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo”, bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo”.
2CO 1:20 Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Al-Masihi ni “Ndiyo”. Kwa sababu hii, ni kwake yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu.
2CO 1:21 Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Al-Masihi. Alitupaka mafuta
2CO 1:22 kwa kututia muhuri wake na kutupatia Roho wake Mtakatifu mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia yote aliyotuahidi.
2CO 1:23 Namwita Mungu awe shahidi wangu kwamba sikurudi Korintho kwa sababu niliwahurumia ninyi.
2CO 1:24 Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi ili mfurahi, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.
2CO 2:1 Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi.
2CO 2:2 Kwa kuwa nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha?
2CO 2:3 Niliwaandikia hivyo ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao walipaswa kunifurahisha. Nilikuwa na uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu.
2CO 2:4 Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana moyoni mwangu, tena kwa machozi mengi; shabaha yangu haikuwa niwahuzunishe, bali niwaoneshe kina cha upendo wangu kwenu.
2CO 2:5 Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote. Nasema hivi ili nisiwe mkali kupita kiasi.
2CO 2:6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha.
2CO 2:7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi.
2CO 2:8 Kwa hiyo, nawasihi mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwake.
2CO 2:9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo.
2CO 2:10 Mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Al-Masihi kwa ajili yenu,
2CO 2:11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatujakosa kuzijua hila zake.
2CO 2:12 Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Al-Masihi na kukuta kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa amenifungulia mlango,
2CO 2:13 bado nilikuwa sina amani kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao, nikaenda Makedonia.
2CO 2:14 Lakini Mungu apewe shukrani, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Al-Masihi. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye.
2CO 2:15 Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Al-Masihi miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea.
2CO 2:16 Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo?
2CO 2:17 Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na neno la Mungu ili tujifaidishe. Bali tunalinena neno lake kwa unyofu katika Al-Masihi tukiwa mbele za Mungu, kama watu waliotumwa na Mungu.
2CO 3:1 Je, tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunahitaji kupata barua za utambulisho kwenu au kutoka kwenu, kama watu wengine?
2CO 3:2 Ninyi wenyewe ndio barua yetu iliyoandikwa katika mioyo yetu, inayojulikana na kusomwa na kila mtu.
2CO 3:3 Nanyi mwadhihirisha wazi kwamba ninyi ni barua inayotoka kwa Al-Masihi, matokeo ya huduma yetu, ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai, si katika vibao vya mawe, bali katika vibao ambavyo ni mioyo ya wanadamu.
2CO 3:4 Hili ndilo tumaini tulilo nalo mbele za Mungu kupitia kwa Al-Masihi.
2CO 3:5 Si kwamba sisi tunafikiri kuwa tunaweza kufanya jambo lolote wenyewe, lakini utoshelevu wetu unatoka kwa Mungu.
2CO 3:6 Ndiye alitutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya: si wa andiko, bali wa Roho wa Mungu; kwa kuwa andiko huua, bali Roho hutia uzima.
2CO 3:7 Basi ikiwa ile huduma iliyoleta mauti, iliyoandikwa kwa herufi juu ya jiwe, ilikuja kwa utukufu hata Waisraeli wakawa hawawezi kuutazama uso wa Musa kwa sababu ya ule utukufu wake, ingawa ulikuwa wa kufifia,
2CO 3:8 je, huduma ya Roho wa Mungu haitakuwa na utukufu zaidi?
2CO 3:9 Ikiwa huduma ile inayowahukumu wanadamu ina utukufu, je, ile huduma iletayo haki haitakuwa ya utukufu zaidi?
2CO 3:10 Kwa maana kile kilichokuwa na utukufu sasa hakina utukufu, kikilinganishwa na huu utukufu unaozidi.
2CO 3:11 Ikiwa kile kilichokuwa kinafifia kilikuja kwa utukufu, je, si zaidi utukufu wa kile kinachodumu!
2CO 3:12 Kwa hiyo, kwa kuwa tunalo tumaini hili, tuna ujasiri sana.
2CO 3:13 Sisi si kama Musa, ambaye ilimpasa kuweka utaji wa kufunika uso wake ili Waisraeli wasiuone ule mng’ao uliokuwa juu yake hadi ulipofifia na hatimaye kutoweka.
2CO 3:14 Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana hadi leo utaji ule ule hufunika Torati inaposomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Al-Masihi peke yake unaondolewa.
2CO 3:15 Hata leo Torati ya Musa inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao.
2CO 3:16 Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana Mungu Mwenyezi, utaji unaondolewa.
2CO 3:17 Basi Bwana Isa ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi, hapo pana uhuru.
2CO 3:18 Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji, tunadhihirisha utukufu wa Bwana Isa kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, unaotoka kwa Bwana Isa, aliye Roho.
2CO 4:1 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa.
2CO 4:2 Lakini tumekataa mambo ya siri na ya aibu; hatufuati njia za udanganyifu, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu.
2CO 4:3 Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea.
2CO 4:4 Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Al-Masihi, aliye sura ya Mungu.
2CO 4:5 Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe, ila tunamhubiri Isa Al-Masihi kuwa ni Bwana, na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Isa.
2CO 4:6 Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ing’ae gizani,” ameifanya nuru yake ing’ae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Al-Masihi.
2CO 4:7 Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu, wala si kwetu.
2CO 4:8 Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa;
2CO 4:9 twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi.
2CO 4:10 Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Isa ili uzima wa Isa uweze kudhihirishwa katika miili yetu.
2CO 4:11 Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Isa, ili uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti.
2CO 4:12 Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.
2CO 4:13 Imeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.” Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema,
2CO 4:14 kwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Isa kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia pamoja na Isa na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake.
2CO 4:15 Haya yote ni kwa faida yenu, ili neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.
2CO 4:16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.
2CO 4:17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi.
2CO 4:18 Kwa hivyo hatuangalii yale yanayoonekana, bali yale yasiyoonekana. Kwa maana yale yanayoonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoonekana ni ya milele.
2CO 5:1 Kwa maana twajua kama hema letu la dunia tunayoishi likiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu.
2CO 5:2 Katika hema hili twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni,
2CO 5:3 kwa kuwa tukishavikwa hatutaonekana tena kuwa uchi.
2CO 5:4 Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hili twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima.
2CO 5:5 Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo, naye ametupatia Roho wa Mungu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.
2CO 5:6 Kwa hiyo siku zote tuna ujasiri, hata ingawa tunajua kwamba tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana Isa.
2CO 5:7 Kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona.
2CO 5:8 Naam, tuna ujasiri, na tunaona ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana Isa.
2CO 5:9 Kwa hiyo, tukiwa katika mwili huu au tukiwa mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana Isa.
2CO 5:10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Al-Masihi, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.
2CO 5:11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Mwenyezi Mungu, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.
2CO 5:12 Sio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu, mweze kuwajibu hao wanaoona fahari kuhusu mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni.
2CO 5:13 Kama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu; kama tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu.
2CO 5:14 Kwa kuwa upendo wa Al-Masihi unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa.
2CO 5:15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.
2CO 5:16 Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Al-Masihi kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo.
2CO 5:17 Kwa hiyo mtu akiwa ndani ya Al-Masihi, amekuwa kiumbe kipya: ya kale yamepita; tazama, yamekuwa mapya.
2CO 5:18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kupitia kwa Isa Al-Masihi, na kutupatia sisi huduma ya upatanisho:
2CO 5:19 kwamba Mungu alikuwa ndani ya Al-Masihi akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho.
2CO 5:20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Al-Masihi, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Al-Masihi: mpatanishwe na Mungu.
2CO 5:21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kupitia kwake Al-Masihi.
2CO 6:1 Kama watendakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msipokee neema ya Mungu bure.
2CO 6:2 Kwa maana asema: “Wakati wangu uliokubalika nilikusikia, siku ya wokovu nilikusaidia.” Tazama, wakati uliokubalika ndio huu, siku ya wokovu ndiyo hii.
2CO 6:3 Hatuweki kikwazo katika njia ya mtu yeyote, ili huduma yetu isionekane kuwa na lawama.
2CO 6:4 Bali tunajidhihirisha kuwa watumishi wa Mungu kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida;
2CO 6:5 katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia; katika kazi ngumu, katika kukesha na katika kufunga;
2CO 6:6 katika utakatifu, katika ufahamu, katika uvumilivu, na katika utu wema; katika Roho wa Mungu na upendo wa kweli;
2CO 6:7 katika maneno ya kweli na katika nguvu za Mungu; kwa silaha za haki mkononi wa kuume na mkononi wa kushoto;
2CO 6:8 katika utukufu na katika kudharauliwa, katika sifa mbaya na katika sifa nzuri; tukionekana kama wadanganyaji, lakini tukiwa wakweli;
2CO 6:9 tukiwa maarufu, lakini tukihesabiwa kama tusiojulikana; tukiwa kama wanaokufa, lakini tunaishi; tukipigwa, lakini hatuuawi;
2CO 6:10 tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote.
2CO 6:11 Tumesema nanyi wazi, enyi Wakorintho na kuwafungulieni mioyo yetu wazi kabisa.
2CO 6:12 Sisi hatujizuii kuwapenda, bali ninyi mmeuzuia upendo wenu kwetu.
2CO 6:13 Sasa nasema kama na watoto wangu: Ninyi pia ifungueni mioyo yenu kabisa.
2CO 6:14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini. Kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza?
2CO 6:15 Kuna mapatano gani kati ya Al-Masihi na Beliari? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini?
2CO 6:16 Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”
2CO 6:17 Kwa hiyo, “Tokeni miongoni mwao, mkatengwe nao, asema Mwenyezi Mungu. Msiguse kitu chochote kilicho najisi, nami nitawakaribisha.”
2CO 6:18 Na, “Mimi nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa wanangu wa kiume na wa kike, asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
2CO 7:1 Wapendwa, kwa kuwa tunazo ahadi hizi, basi na tujitakase nafsi zetu kutokana na kila kitu kitiacho mwili na roho unajisi, tukitimiza utakatifu kwa kumcha Mungu.
2CO 7:2 Tupatieni nafasi mioyoni mwenu. Hatujamkosea mtu yeyote, wala hatujampotosha mtu yeyote, wala hatujamdhulumu mtu yeyote.
2CO 7:3 Sisemi haya ili kuwahukumu, kwa kuwa nilisema mwanzo kwamba ninyi mko mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja au kuishi pamoja.
2CO 7:4 Nina ujasiri mwingi kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.
2CO 7:5 Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na amani. Tulisumbuliwa kila upande; kwa nje kulikuwa na mapigano, na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu.
2CO 7:6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa Tito kufika kwetu.
2CO 7:7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.
2CO 7:8 Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu.
2CO 7:9 Lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike, na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.
2CO 7:10 Kwa maana huzuni ya kiungu huleta toba iletayo wokovu, wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti.
2CO 7:11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kiungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo.
2CO 7:12 Hivyo, ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone mbele za Mungu jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu.
2CO 7:13 Kwa ajili ya haya yote tumefarijika. Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.
2CO 7:14 Nilikuwa nimewasifu ninyi kwake, nanyi hamkuniaibisha. Lakini kama vile yale yote tuliyowaambia yalikuwa kweli, hivyo kule kujisifu kwetu kwa Tito kuwahusu ninyi kumethibitishwa kuwa kweli pia.
2CO 7:15 Upendo wake kwenu unaongezeka sana anapokumbuka jinsi mlivyokuwa watiifu, mkampokea kwa hofu na kutetemeka.
2CO 7:16 Nafurahi kwamba ninaweza kuwatumaini ninyi kabisa.
2CO 8:1 Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa waumini wa Makedonia.
2CO 8:2 Ingawa walikuwa na majaribu makali, furaha yao kubwa na umaskini wao mkuu zilifurika kwa ukarimu mwingi.
2CO 8:3 Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri walivyoweza, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao,
2CO 8:4 wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu.
2CO 8:5 Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana Isa kwanza, na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu kufuatana na mapenzi ya Mungu.
2CO 8:6 Kwa hiyo tulimsihi Tito, kwa kuwa ndiye alianzisha jambo hili, akamilishe tendo hili la neema kwa upande wenu.
2CO 8:7 Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote, iwe ni katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa.
2CO 8:8 Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine.
2CO 8:9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.
2CO 8:10 Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu katika jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo.
2CO 8:11 Sasa ikamilisheni kazi hii, ili shauku yenu ya kuitenda iandamane na kuimaliza, mkijitolea kulingana na uwezo wenu.
2CO 8:12 Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.
2CO 8:13 Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano.
2CO 8:14 Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo utasaidia kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu.
2CO 8:15 Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”
2CO 8:16 Ninamshukuru Mungu ambaye amemtia Tito moyo wa kuwajali ninyi kama mimi ninavyowajali.
2CO 8:17 Si kwamba Tito amekubali tu ombi letu, bali anakuja kwenu akiwa na shauku kuliko wakati mwingine, tena kwa hiari yake mwenyewe.
2CO 8:18 Nasi tunamtuma pamoja naye ndugu ambaye anasifiwa na makundi yote ya waumini kwa huduma yake ya kuhubiri Injili.
2CO 8:19 Zaidi ya hayo, alichaguliwa na makundi ya waumini ili asafiri pamoja nasi tulipokuwa tunapeleka matoleo ya ukarimu, kwa ajili ya utukufu wa Bwana Isa mwenyewe, na ili kuonesha hisani yetu kuwasaidia.
2CO 8:20 Tunataka kuepuka lawama yoyote kuhusu jinsi tunavyosimamia matoleo haya ya ukarimu.
2CO 8:21 Kwa kuwa tunakusudia kufanya kile kilicho haki, si machoni mwa Bwana Isa peke yake, bali pia machoni mwa wanadamu.
2CO 8:22 Pamoja nao, tunamtuma ndugu yetu ambaye mara kwa mara ametuthibitishia kwa njia nyingi kwamba ana shauku, naam, zaidi sana sasa kwa sababu analo tumaini kuu kwenu.
2CO 8:23 Kwa habari ya Tito, yeye ni mwenzangu na mtendakazi pamoja nami miongoni mwenu. Kwa habari za ndugu zetu, wao ni wawakilishi wa makundi ya waumini, na utukufu kwa Al-Masihi.
2CO 8:24 Kwa hiyo waonesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu, na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, ili makundi ya waumini yapate kuuona upendo wenu.
2CO 9:1 Hakuna haja ya kuwaandikia kuhusu huduma hii kwa watakatifu.
2CO 9:2 Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa Wamakedonia, nikiwaambia kwamba ninyi watu wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana. Na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa.
2CO 9:3 Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari.
2CO 9:4 Kwa maana nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamko tayari, sisi, na hata ninyi pia, tungeona haya kwa kuwa na ujasiri hivi katika ninyi.
2CO 9:5 Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu.
2CO 9:6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye haba pia atavuna haba, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu.
2CO 9:7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu.
2CO 9:8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema.
2CO 9:9 Kama ilivyoandikwa: “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele.”
2CO 9:10 Yeye ampaye mpanzi mbegu ya kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu.
2CO 9:11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.
2CO 9:12 Huduma hii mnayofanya si tu ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi kwake Mungu.
2CO 9:13 Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Al-Masihi, na kwa ukarimu wenu wa kuwashirikisha wao na watu wengine wote.
2CO 9:14 Nayo mioyo yao itawaonea shauku wanapowaombea, kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu.
2CO 9:15 Mungu apewe shukrani kwa karama yake isiyoelezeka!
2CO 10:1 Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Al-Masihi, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi!
2CO 10:2 Nawaomba nitakapokuja kwenu nisipaswe kuwa na ujasiri dhidi ya watu fulani kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata mtazamo wa ulimwengu huu.
2CO 10:3 Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo.
2CO 10:4 Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome.
2CO 10:5 Tunaangusha mawazo na kila kitu kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na kuteka nyara kila fikira ipate kumtii Al-Masihi.
2CO 10:6 Tena tunakuwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, hapo kutii kwenu kutakapokamilika.
2CO 10:7 Mnayaangalia yaliyo mbele ya macho yenu tu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Al-Masihi, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Al-Masihi, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo.
2CO 10:8 Basi hata nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana Isa alitupatia ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya.
2CO 10:9 Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu.
2CO 10:10 Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni mdhaifu, na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.”
2CO 10:11 Watu kama hao wajue ya kuwa yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi ndivyo tulivyo, na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.
2CO 10:12 Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonesha ya kuwa hawana busara.
2CO 10:13 Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ya huduma ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi.
2CO 10:14 Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama ambavyo ingekuwa tusingekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Al-Masihi.
2CO 10:15 Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, ndivyo eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi,
2CO 10:16 ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine.
2CO 10:17 Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Mwenyezi Mungu.”
2CO 10:18 Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Mwenyezi Mungu humsifu.
2CO 11:1 Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo.
2CO 11:2 Ninawaonea wivu, wivu wa kiungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Al-Masihi kama mabikira safi.
2CO 11:3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Hawa alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Al-Masihi.
2CO 11:4 Kwa sababu mtu akija na kuwahubiria Isa mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.
2CO 11:5 Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu”.
2CO 11:6 Inawezekana mimi si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.
2CO 11:7 Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo?
2CO 11:8 Niliyanyang’anya makundi mengine ya waumini kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi.
2CO 11:9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nilipopungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walitimiza mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia.
2CO 11:10 Kwa hakika kama vile kweli ya Al-Masihi ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili.
2CO 11:11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda!
2CO 11:12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.
2CO 11:13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Al-Masihi.
2CO 11:14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru.
2CO 11:15 Kwa hiyo basi si ajabu kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.
2CO 11:16 Nasema tena: mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo.
2CO 11:17 Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi vile Bwana Isa angesema, bali kama mjinga.
2CO 11:18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu.
2CO 11:19 Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana!
2CO 11:20 Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida, au akiwanyang’anya, au akijitukuza mwenyewe, au akiwadanganya.
2CO 11:21 Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo! Lakini jambo lolote ambalo mtu mwingine angethubutu kujisifia, ninene kama mjinga, nami nathubutu kujisifu kuhusu hilo.
2CO 11:22 Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Ibrahimu? Mimi pia ni mzao wa Ibrahimu.
2CO 11:23 Je, wao ni watumishi wa Al-Masihi? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii zaidi yao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimepigwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi.
2CO 11:24 Mara tano nimepigwa na Wayahudi mijeledi arobaini kasoro moja.
2CO 11:25 Mara tatu nilipigwa mijeledi, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nilivunjikiwa na meli, nilikaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa;
2CO 11:26 nimekuwa katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyang’anyi, hatari kutoka kwa Wayahudi wenzangu, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo.
2CO 11:27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; nimejua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi.
2CO 11:28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa kila siku na mzigo wa wajibu wangu kwa makundi yote ya waumini.
2CO 11:29 Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?
2CO 11:30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonesha udhaifu wangu.
2CO 11:31 Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo.
2CO 11:32 Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata.
2CO 11:33 Lakini niliteremshwa kwa kapu kubwa kupitia dirisha ukutani, nikaokolewa kutoka mkononi mwake.
2CO 12:1 Yanipasa nijisifu. Ingawa haifaidi kitu, nitanena kuhusu maono na mafunuo kutoka kwa Bwana Isa.
2CO 12:2 Namjua mtu mmoja katika Al-Masihi ambaye miaka kumi na nne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua.
2CO 12:3 Nami najua kwamba mtu huyu, iwe ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua,
2CO 12:4 alinyakuliwa hadi Paradiso. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia.
2CO 12:5 Nitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu mwenyewe, ila nitajisifia udhaifu wangu.
2CO 12:6 Hata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema,
2CO 12:7 au kwa sababu ya mafunuo haya makuu. Ili kunizuia nisijivune, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese.
2CO 12:8 Kwa habari ya jambo hili, nilimsihi Mwenyezi Mungu mara tatu aniondolee mwiba huu.
2CO 12:9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Al-Masihi ukae juu yangu.
2CO 12:10 Hii ndiyo sababu nafurahia katika udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida kwa ajili ya Al-Masihi. Kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.
2CO 12:11 Nimejifanya mjinga, lakini mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ilinipasa kusifiwa na ninyi, kwa sababu mimi si dhalili kuliko wale “mitume walio bora”, ingawa mimi si kitu.
2CO 12:12 Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi.
2CO 12:13 Je, ninyi ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makundi mengine ya waumini, ila tu kwamba mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili!
2CO 12:14 Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara ya tatu. Nami sitawalemea, kwa sababu sihitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi. Kwa kuwa watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao.
2CO 12:15 Hivyo nitafurahi kutumia kila kitu nilicho nacho kwa ajili yenu, hata mwili wangu pia. Je, ninavyozidi kuwapenda, ndivyo upendo wenu kwangu unavyopungua?
2CO 12:16 Iwe iwavyo, kwa vyovyote vile, mimi sikuwalemea. Lakini wengine wanadhani mimi ni mjanja, nami niliwapata kwa hila!
2CO 12:17 Je, nilijipatia faida kwa kumtumia mtu yeyote niliyemtuma kwenu?
2CO 12:18 Nilimshawishi Tito aje kwenu, nami nilimtuma pamoja na ndugu yetu. Je, Tito aliwatumia ninyi ili kujipatia faida? Je, hatukuenenda kwa roho moja, na kwa hatua zile zile?
2CO 12:19 Je, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Al-Masihi. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu.
2CO 12:20 Kwa kuwa nina hofu kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko.
2CO 12:21 Nina hofu kwamba nitakapokuja tena kwenu, Mungu wangu atanidhili mbele yenu, nami nitasikitishwa na wengi waliotenda dhambi mbeleni, na wala hawajatubu kwa uchafu wao, uasherati, na ufisadi walioushiriki.
2CO 13:1 Hii itakuwa mara ya tatu mimi kuja kwenu. “Shtaka lolote lazima lithibitishwe na mashahidi wawili au watatu.”
2CO 13:2 Niliwaonya nilipokuwa pamoja nanyi mara ya pili. Sasa narudia wakati sipo, kwamba nikija tena sitawahurumia wale waliokuwa wametenda dhambi hapo awali au wengine wote,
2CO 13:3 kwa kuwa mnadai uthibitisho kwamba Al-Masihi anazungumza kwa kunitumia mimi. Yeye si dhaifu katika kushughulika nanyi, bali ana nguvu kati yenu.
2CO 13:4 Kwa kuwa alisulubiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Vivyo hivyo, sisi tu dhaifu kupitia kwake, lakini katika kuwashughulikia ninyi tutaishi pamoja naye kwa nguvu za Mungu.
2CO 13:5 Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Isa Al-Masihi yu ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho!
2CO 13:6 Natumaini mtaona kuwa sisi hatukushindwa.
2CO 13:7 Lakini tunamwomba Mungu msije mkatenda kosa lolote, si ili sisi tuonekane kuwa tumeshinda hilo jaribio, bali ili ninyi mtende lililo haki, hata kama tutaonekana kuwa tumeshindwa.
2CO 13:8 Kwa maana hatuwezi kufanya lolote kinyume na kweli, bali kuithibitisha kweli tu.
2CO 13:9 Tunafurahi wakati wowote tunapokuwa dhaifu, lakini ninyi mkawa na nguvu. Nayo maombi yetu ni kwamba mpate kuwa wakamilifu.
2CO 13:10 Hii ndiyo sababu nawaandikia mambo haya wakati sipo, ili nikija nisiwe mkali katika kutumia mamlaka yangu, mamlaka Bwana Isa aliyonipa ya kuwajenga ninyi wala si ya kuwabomoa.
2CO 13:11 Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Kuweni wakamilifu, farijianeni, kuweni na nia moja, na mkae kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.
2CO 13:12 Salimianeni kwa busu takatifu.
2CO 13:13 Watakatifu wote wanawasalimu.
2CO 13:14 Neema ya Bwana Isa Al-Masihi, na upendo wa Mungu, na ushirika wa Roho wa Mungu ukae nanyi nyote.
GAL 1:1 Paulo mtume, si mtume wa wanadamu wala aliyetumwa na mwanadamu, bali na Isa Al-Masihi na Mungu Baba Mwenyezi aliyemfufua Isa kutoka kwa wafu,
GAL 1:2 na ndugu wote walio pamoja nami.
GAL 1:3 Neema na amani zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi,
GAL 1:4 yeye aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu.
GAL 1:5 Utukufu una yeye milele na milele. Amen.
GAL 1:6 Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Al-Masihi na kuifuata Injili nyingine,
GAL 1:7 ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Al-Masihi.
GAL 1:8 Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele!
GAL 1:9 Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!
GAL 1:10 Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Al-Masihi.
GAL 1:11 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu.
GAL 1:12 Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Isa Al-Masihi.
GAL 1:13 Ninyi mmekwisha kusikia kuhusu maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyotesa makundi ya waumini wa Mungu kwa nguvu na kujaribu kuwaangamiza.
GAL 1:14 Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika langu, maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu.
GAL 1:15 Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake,
GAL 1:16 alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote,
GAL 1:17 wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilienda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.
GAL 1:18 Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefa na nilikaa naye siku kumi na tano.
GAL 1:19 Lakini sikumwona mtume mwingine yeyote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana Isa.
GAL 1:20 Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo.
GAL 1:21 Baadaye nilienda sehemu za Siria na Kilikia.
GAL 1:22 Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makundi ya waumini huko Yudea yaliyo katika Al-Masihi.
GAL 1:23 Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo awali alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.”
GAL 1:24 Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.
GAL 2:1 Kisha, baada ya miaka kumi na nne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu, wakati huu pamoja na Barnaba, na nikamchukua Tito pia.
GAL 2:2 Nilienda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure.
GAL 2:3 Lakini hata Tito aliyekuwa nami, na alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa.
GAL 2:4 Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru tulio nao katika Al-Masihi Isa, wapate kututia utumwani,
GAL 2:5 hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili ukweli wa Injili ubaki nanyi.
GAL 2:6 Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote.
GAL 2:7 Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi.
GAL 2:8 Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa.
GAL 2:9 Basi Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za jumuiya ya waumini, walitupatia mkono wa shirika, mimi na Barnaba, walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa, na wao waende kwa Wayahudi.
GAL 2:10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.
GAL 2:11 Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi.
GAL 2:12 Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara.
GAL 2:13 Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.
GAL 2:14 Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?
GAL 2:15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa,
GAL 2:16 bado tunajua kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kupitia kwa imani katika Isa Al-Masihi. Hivyo sisi pia, tumemwamini Al-Masihi Isa ili tupate kuhesabiwa haki kupitia kwa imani katika Al-Masihi, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.
GAL 2:17 “Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Al-Masihi, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Al-Masihi amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha!
GAL 2:18 Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonesha kwamba mimi ni mkosaji.
GAL 2:19 Kwa maana mimi kupitia kwa sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu.
GAL 2:20 Nimesulubiwa pamoja na Al-Masihi, wala si mimi tena ninayeishi, bali Al-Masihi ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani katika Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.
GAL 2:21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kupitia kwa Torati, basi Al-Masihi alikufa bure!”
GAL 3:1 Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Isa Al-Masihi aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa.
GAL 3:2 Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika Torati, au kwa kuyaamini yale mliyosikia?
GAL 3:3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili?
GAL 3:4 Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure!
GAL 3:5 Je, Mungu huwapa Roho wake Mtakatifu na kufanya miujiza kati yenu kwa sababu mnatii Torati, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?
GAL 3:6 Kama vile “Ibrahimu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
GAL 3:7 Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Ibrahimu.
GAL 3:8 Andiko liliona tangu awali kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, hivyo likatangulia kumtangazia Ibrahimu Injili, likisema kwamba, “Kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.”
GAL 3:9 Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Ibrahimu, mtu wa imani.
GAL 3:10 Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya Torati wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Torati.”
GAL 3:11 Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia Torati, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.”
GAL 3:12 Lakini Torati haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”
GAL 3:13 Al-Masihi alitukomboa kutoka laana ya Torati kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.”
GAL 3:14 Alitukomboa ili baraka aliyopewa Ibrahimu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kupitia kwa Al-Masihi Isa, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho wa Mungu.
GAL 3:15 Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii.
GAL 3:16 Ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa uzao”, yakimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako”, yaani mtu mmoja, ndiye Al-Masihi.
GAL 3:17 Ninachotaka kusema ni kwamba, Torati, ambayo ilitolewa miaka mia nne na thelathini (430) baadaye, haitangui agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile.
GAL 3:18 Kwa maana kama urithi hupatikana kwa Torati, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Ibrahimu urithi kupitia kwa ahadi.
GAL 3:19 Kwa nini basi iwepo Torati? Torati iliwekwa kwa sababu ya makosa hadi atakapokuja yule Mzao wa Ibrahimu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Torati iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.
GAL 3:20 Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.
GAL 3:21 Je basi, Torati inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama Torati iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kupitia kwa Torati.
GAL 3:22 Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kupitia kwa imani katika Isa Al-Masihi yapate kupewa wale wanaoamini.
GAL 3:23 Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya Torati, tumefungwa hadi ile imani ifunuliwe.
GAL 3:24 Hivyo, Torati ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Al-Masihi, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani.
GAL 3:25 Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na Torati.
GAL 3:26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Al-Masihi Isa kupitia kwa imani.
GAL 3:27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Al-Masihi, mmemvaa Al-Masihi.
GAL 3:28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Al-Masihi Isa.
GAL 3:29 Nanyi mkiwa ni mali ya Al-Masihi, basi ninyi ni wa uzao wa Ibrahimu na warithi sawasawa na ile ahadi.
GAL 4:1 Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote.
GAL 4:2 Yeye huwa chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini hadi ufike wakati uliowekwa na baba yake.
GAL 4:3 Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu.
GAL 4:4 Lakini wakati uliopangwa ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria,
GAL 4:5 ili awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, nasi tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa wana.
GAL 4:6 Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.”
GAL 4:7 Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mwana. Na kwa kuwa wewe ni mwana, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kupitia kwa Al-Masihi.
GAL 4:8 Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu.
GAL 4:9 Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa?
GAL 4:10 Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka!
GAL 4:11 Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.
GAL 4:12 Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya.
GAL 4:13 Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria Injili.
GAL 4:14 Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Al-Masihi Isa.
GAL 4:15 Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imeenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngeng’oa macho yenu na kunipa mimi.
GAL 4:16 Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia ukweli?
GAL 4:17 Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku.
GAL 4:18 Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu.
GAL 4:19 Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea uchungu, ninatamani kwamba Al-Masihi aumbike ndani yenu.
GAL 4:20 Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu.
GAL 4:21 Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema?
GAL 4:22 Kwa maana imeandikwa kwamba Ibrahimu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru.
GAL 4:23 Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.
GAL 4:24 Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, linalozaa watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hajiri.
GAL 4:25 Basi Hajiri anawakilisha Mlima Sinai ulio Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake.
GAL 4:26 Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu.
GAL 4:27 Kwa maana imeandikwa: “Furahi, ewe mwanamke tasa, wewe usiyezaa; paza sauti, na kuimba kwa furaha, wewe usiyepatwa na uchungu wa kuzaa; kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi kuliko wa mwanamke mwenye mume.”
GAL 4:28 Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaka, tu watoto wa ahadi.
GAL 4:29 Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa uweza wa Roho wa Mungu, ndivyo ilivyo hata sasa.
GAL 4:30 Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.”
GAL 4:31 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.
GAL 5:1 Al-Masihi alitupatia uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na nira ya utumwa.
GAL 5:2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba mkikubali kutahiriwa, basi Al-Masihi hatakuwa na thamani kwenu hata kidogo.
GAL 5:3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika Torati yote.
GAL 5:4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kupitia kwa Torati mmetengwa na Al-Masihi, mko mbali na neema ya Mungu.
GAL 5:5 Kwa maana, kupitia Roho wa Mungu tunangojea kwa shauku tumaini la haki kwa imani.
GAL 5:6 Kwa maana ndani ya Al-Masihi Isa, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kupitia kwa upendo.
GAL 5:7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli?
GAL 5:8 Ushawishi kama huo haukutoka kwa yule anayewaita.
GAL 5:9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.”
GAL 5:10 Nina hakika katika Bwana Isa kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani.
GAL 5:11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa.
GAL 5:12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!
GAL 5:13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo.
GAL 5:14 Kwa maana Torati yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”
GAL 5:15 Lakini mkiumana na kutafunana, angalieni msije mkaangamizana.
GAL 5:16 Kwa hiyo nasema, nendeni kwa Roho wa Mungu, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
GAL 5:17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.
GAL 5:18 Lakini mkiongozwa na Roho wa Mungu, hamko chini ya Torati.
GAL 5:19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi,
GAL 5:20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
GAL 5:21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi ufalme wa Mungu.
GAL 5:22 Lakini tunda la Roho wa Mungu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
GAL 5:23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.
GAL 5:24 Wote walio wa Al-Masihi Isa wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake.
GAL 5:25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho wa Mungu, basi, tuenende kwa Roho.
GAL 5:26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.
GAL 6:1 Ndugu zangu, ikiwa mtu amepatikana akitenda dhambi, basi ninyi mnaoishi kwa Roho wa Mungu mnapaswa kumrejesha mtu huyo kwa upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa.
GAL 6:2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Al-Masihi.
GAL 6:3 Mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe.
GAL 6:4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine.
GAL 6:5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.
GAL 6:6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.
GAL 6:7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna.
GAL 6:8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho wa Mungu, katika Roho atavuna uzima wa milele.
GAL 6:9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.
GAL 6:10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waumini.
GAL 6:11 Angalieni herufi kubwa ninazotumia nikiwaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!
GAL 6:12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Al-Masihi.
GAL 6:13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu.
GAL 6:14 Lakini mimi naomba nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, ambaye kwake ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.
GAL 6:15 Kwa maana katika Al-Masihi Isa, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu!
GAL 6:16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, hata kwa Israeli wa Mungu.
GAL 6:17 Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Isa.
GAL 6:18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe pamoja na roho zenu. Amen.
EPH 1:1 Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa mapenzi ya Mungu.
EPH 1:2 Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
EPH 1:3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Al-Masihi.
EPH 1:4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo
EPH 1:5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kupitia kwa Isa Al-Masihi kwa furaha na mapenzi yake.
EPH 1:6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.
EPH 1:7 Ndani yake tunao ukombozi kupitia kwa damu yake, yaani msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake
EPH 1:8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote.
EPH 1:9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Al-Masihi,
EPH 1:10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Al-Masihi.
EPH 1:11 Katika Al-Masihi sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake,
EPH 1:12 ili, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Al-Masihi, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.
EPH 1:13 Ninyi pia mliingia ndani ya Al-Masihi mliposikia neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Baada ya kuamini, mlitiwa muhuri ndani yake, huyo Roho Mtakatifu wa Mungu mliyeahidiwa,
EPH 1:14 yeye ambaye ni amana yetu ya kutuhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu, kwa sifa ya utukufu wake.
EPH 1:15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Isa na upendo wenu kwa watakatifu wote,
EPH 1:16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu.
EPH 1:17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi.
EPH 1:18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu
EPH 1:19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno
EPH 1:20 aliyoitumia katika Al-Masihi alipomfufua kutoka kwa wafu, na kumketisha mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho,
EPH 1:21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia.
EPH 1:22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake, na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya jumuiya ya waumini,
EPH 1:23 ambayo ni mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.
EPH 2:1 Ninyi mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu,
EPH 2:2 ambazo mlizitenda mlipofuata njia za ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii.
EPH 2:3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulistahili ghadhabu, kama watu wengine wote.
EPH 2:4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema,
EPH 2:5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Al-Masihi Isa, yaani mmeokolewa kwa neema.
EPH 2:6 Mungu alitufufua pamoja na Al-Masihi na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Al-Masihi Isa,
EPH 2:7 ili katika ulimwengu ujao apate kuonesha wingi wa neema yake isiyolinganishwa, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Al-Masihi Isa.
EPH 2:8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kupitia kwa imani, nayo haikutokana na ninyi wenyewe. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu,
EPH 2:9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu.
EPH 2:10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Al-Masihi Isa, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
EPH 2:11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba hapo awali ninyi ambao ni watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu),
EPH 2:12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Al-Masihi, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi hamkuwa na tumaini wala Mungu duniani.
EPH 2:13 Lakini sasa katika Al-Masihi Isa, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kupitia kwa damu ya Al-Masihi.
EPH 2:14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa vikundi viwili tuwe kikundi kimoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu,
EPH 2:15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani,
EPH 2:16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao.
EPH 2:17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu.
EPH 2:18 Kwa maana kupitia kwake sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
EPH 2:19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena na wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu.
EPH 2:20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Al-Masihi Isa ndiye jiwe kuu la pembeni.
EPH 2:21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kuinuliwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Mwenyezi Mungu.
EPH 2:22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kupitia kwa Roho wake Mtakatifu.
EPH 3:1 Kwa sababu hii, mimi Paulo, ni mfungwa wa Al-Masihi Isa kwa ajili yenu ninyi watu wa Mataifa.
EPH 3:2 Kwa hakika mmekwisha kusikia kuhusu ile huduma ya neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu,
EPH 3:3 yaani ile siri iliodhihirishwa kwangu kupitia ufunuo, kama nilivyotangulia kuandika kwa kifupi.
EPH 3:4 Kwa kusoma haya, basi mtaweza kuelewa ufahamu wangu katika siri ya Al-Masihi.
EPH 3:5 Siri hii haikudhihirishwa kwa wanadamu katika vizazi vingine kama vile sasa ilivyodhihirishwa na Roho wa Mungu kwa mitume na manabii watakatifu wa Mungu.
EPH 3:6 Siri hii ni kwamba, kupitia kwa Injili, watu wa Mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Al-Masihi Isa.
EPH 3:7 Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi.
EPH 3:8 Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Al-Masihi,
EPH 3:9 na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote.
EPH 3:10 Ili sasa kupitia kwa jumuiya ya waumini, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho,
EPH 3:11 sawasawa na kusudi lake la milele alilolitimiza katika Al-Masihi Isa Bwana wetu.
EPH 3:12 Ndani yake na kupitia kwa imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri.
EPH 3:13 Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.
EPH 3:14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti,
EPH 3:15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye.
EPH 3:16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kupitia kwa Roho wake Mtakatifu kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake,
EPH 3:17 ili Al-Masihi apate kukaa mioyoni mwenu kupitia kwa imani. Nami ninaomba kwamba mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo,
EPH 3:18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Al-Masihi,
EPH 3:19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.
EPH 3:20 Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu,
EPH 3:21 yeye atukuzwe katika jumuiya ya waumini, na katika Al-Masihi Isa kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.
EPH 4:1 Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana Isa, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa.
EPH 4:2 Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo.
EPH 4:3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho wa Mungu katika kifungo cha amani.
EPH 4:4 Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
EPH 4:5 Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja,
EPH 4:6 Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.
EPH 4:7 Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Al-Masihi.
EPH 4:8 Kwa hiyo husema: “Alipopaa juu zaidi, aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa.”
EPH 4:9 (Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema kwamba Al-Masihi pia alishuka pande za chini sana za dunia?
EPH 4:10 Yeye aliyeshuka ndiye aliyepaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.)
EPH 4:11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu,
EPH 4:12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili mwili wa Al-Masihi upate kujengwa
EPH 4:13 hadi sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima, kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Al-Masihi.
EPH 4:14 Basi hatutakuwa tena watoto wachanga, tukiyumbishwa na mawimbi, na tukipeperushwa hapa na pale na kila upepo wa mafundisho, na kwa ujanja na hila za watu katika njama zao.
EPH 4:15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani Al-Masihi.
EPH 4:16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, huku kila kiungo kikifanya kazi yake.
EPH 4:17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana Isa kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa wanavyoishi, katika ubatili wa mawazo yao.
EPH 4:18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao.
EPH 4:19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kujiingiza katika kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.
EPH 4:20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Al-Masihi.
EPH 4:21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Isa.
EPH 4:22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu,
EPH 4:23 ili mfanywe upya katika roho ya nia zenu,
EPH 4:24 na mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki ya kweli na utakatifu.
EPH 4:25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja.
EPH 4:26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika,
EPH 4:27 wala msimpe ibilisi nafasi.
EPH 4:28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kinachofaa kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.
EPH 4:29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yanayofaa kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao.
EPH 4:30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi.
EPH 4:31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu na hasira, makelele na masingizio, pamoja na kila aina ya uovu.
EPH 4:32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Al-Masihi alivyowasamehe ninyi.
EPH 5:1 Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wanaopendwa,
EPH 5:2 mkiishi maisha ya upendo, kama vile Al-Masihi alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.
EPH 5:3 Lakini uasherati usitajwe miongoni mwenu kamwe, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu wa Mungu.
EPH 5:4 Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu.
EPH 5:5 Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Mwasherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya (mtu kama huyo ni mwabudu sanamu) kamwe hataurithi ufalme wa Al-Masihi na wa Mungu.
EPH 5:6 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama hayo juu ya wale wasiomtii.
EPH 5:7 Kwa hiyo, msishirikiane nao.
EPH 5:8 Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana Isa. Nendeni kama watoto wa nuru
EPH 5:9 (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli),
EPH 5:10 nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana Isa.
EPH 5:11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni.
EPH 5:12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini.
EPH 5:13 Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana,
EPH 5:14 kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana: “Amka, wewe uliyelala, ufufuke kutoka kwa wafu, naye Al-Masihi atakuangazia.”
EPH 5:15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima,
EPH 5:16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu.
EPH 5:17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana Isa.
EPH 5:18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo mna upotovu, bali mjazwe Roho wa Mungu.
EPH 5:19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana Isa mioyoni mwenu,
EPH 5:20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba Mwenyezi kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi.
EPH 5:21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kutokana na kumcha Al-Masihi.
EPH 5:22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama vile mnavyomtii Bwana Isa.
EPH 5:23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Al-Masihi alivyo kichwa cha jumuiya ya waumini, ambayo ni mwili wake, naye Al-Masihi ni Mwokozi wake.
EPH 5:24 Basi, kama vile jumuiya ya waumini wanavyomtii Al-Masihi, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.
EPH 5:25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Al-Masihi alivyoipenda jumuiya ya waumini na akajitoa kwa ajili yake,
EPH 5:26 kusudi aifanye takatifu, akiitakasa kwa kuiosha kwa maji katika neno lake,
EPH 5:27 apate kujiletea jumuiya tukufu isiyo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na isiyo na hatia.
EPH 5:28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.
EPH 5:29 Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Al-Masihi anavyoitunza jumuiya yake ya waumini.
EPH 5:30 Sisi tu viungo vya mwili wake.
EPH 5:31 “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.”
EPH 5:32 Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Al-Masihi na jumuiya ya waumini wake.
EPH 5:33 Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.
EPH 6:1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana Isa, kwa kuwa hili ni jema.
EPH 6:2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi,
EPH 6:3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”
EPH 6:4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana Isa.
EPH 6:5 Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa unyofu wa moyo, kama vile mnavyomtii Al-Masihi.
EPH 6:6 Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Al-Masihi, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo.
EPH 6:7 Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mngemtumikia, wala si wanadamu,
EPH 6:8 mkijua kwamba Bwana Isa atampa kila mtu thawabu kwa lolote jema alilotenda, awe mtumwa au mtu huru.
EPH 6:9 Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi hiyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.
EPH 6:10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana Isa na katika uweza wa nguvu zake.
EPH 6:11 Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kuzipinga hila za ibilisi.
EPH 6:12 Kwa maana kushindana kwetu si dhidi ya mwili na damu, bali dhidi ya falme na mamlaka, dhidi ya wakuu wa ulimwengu huu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
EPH 6:13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja, nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.
EPH 6:14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani,
EPH 6:15 nayo miguu yenu ivalishwe viatu vya utayari tunaopata katika Injili ya amani.
EPH 6:16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
EPH 6:17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho wa Mungu, ambao ni neno la Mungu,
EPH 6:18 mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.
EPH 6:19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri,
EPH 6:20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.
EPH 6:21 Tikiko, aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana Isa, atawaambia kila kitu, ili pia mpate kujua hali yangu na kile ninachofanya.
EPH 6:22 Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali yetu, na awatie moyo.
EPH 6:23 Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Bwana Isa Al-Masihi.
EPH 6:24 Neema iwe na wote wanaompenda Bwana wetu Isa Al-Masihi kwa upendo wa dhati. Amen.
PHI 1:1 Paulo na Timotheo, watumishi wa Al-Masihi Isa.
PHI 1:2 Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
PHI 1:3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi.
PHI 1:4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha,
PHI 1:5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo.
PHI 1:6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Al-Masihi Isa.
PHI 1:7 Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu. Ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami.
PHI 1:8 Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Al-Masihi Isa.
PHI 1:9 Haya ndio maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote,
PHI 1:10 ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Al-Masihi,
PHI 1:11 mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kupitia kwa Isa Al-Masihi, kwa utukufu na sifa za Mungu.
PHI 1:12 Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili.
PHI 1:13 Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Al-Masihi.
PHI 1:14 Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana Isa wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.
PHI 1:15 Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Al-Masihi kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Al-Masihi kwa nia njema.
PHI 1:16 Hawa wa mwisho wanamhubiri Al-Masihi kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili.
PHI 1:17 Hao wa kwanza wanamtangaza Al-Masihi kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu.
PHI 1:18 Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Al-Masihi anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi. Naam, nami nitaendelea kufurahi,
PHI 1:19 kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Isa Al-Masihi, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu.
PHI 1:20 Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Al-Masihi atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa.
PHI 1:21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Al-Masihi, na kufa ni faida.
PHI 1:22 Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini nichague lipi? Mimi sijui!
PHI 1:23 Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Al-Masihi, jambo hilo ni bora zaidi.
PHI 1:24 Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili.
PHI 1:25 Nikiwa na hakika ya jambo hili, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani,
PHI 1:26 ili kwa kuja kwangu kwenu tena, furaha yenu iwe nyingi katika Al-Masihi Isa kwa ajili yangu.
PHI 1:27 Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Al-Masihi, ili nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja,
PHI 1:28 wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu.
PHI 1:29 Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Al-Masihi, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake,
PHI 1:30 kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.
PHI 2:1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Al-Masihi, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho wa Mungu, kukiwa na wema wowote na huruma,
PHI 2:2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja.
PHI 2:3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake.
PHI 2:4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
PHI 2:5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Al-Masihi Isa:
PHI 2:6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa kitu cha kushikilia,
PHI 2:7 bali alijifanya si kitu, akachukua hali hasa ya mtumwa, naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
PHI 2:8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza, akatii hata mauti: naam, mauti ya msalaba!
PHI 2:9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana, na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,
PHI 2:10 ili kwa Jina la Isa, kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi,
PHI 2:11 na kila ulimi ukiri kwamba Isa Al-Masihi ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi.
PHI 2:12 Kwa hiyo, wapendwa wangu, kama vile mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka,
PHI 2:13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.
PHI 2:14 Fanyeni mambo yote bila kunung’unika wala kushindana,
PHI 2:15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnang’aa kama mianga ulimwenguni.
PHI 2:16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Al-Masihi kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.
PHI 2:17 Lakini hata nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma inayotoka katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote.
PHI 2:18 Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.
PHI 2:19 Natumaini katika Bwana Isa kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu.
PHI 2:20 Sina mtu mwingine kama yeye, ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi.
PHI 2:21 Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Isa Al-Masihi.
PHI 2:22 Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana ametumika pamoja nami kwa kazi ya Injili, kama vile mwana kwa baba yake.
PHI 2:23 Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa.
PHI 2:24 Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana Isa kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni.
PHI 2:25 Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtendakazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu.
PHI 2:26 Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa.
PHI 2:27 Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni.
PHI 2:28 Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue.
PHI 2:29 Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana Isa kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa,
PHI 2:30 kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Al-Masihi, akihatarisha maisha yake ili aweze kunihudumia vile ninyi hamkuweza.
PHI 3:1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana Isa! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.
PHI 3:2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao.
PHI 3:3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho wake Mtakatifu, tunaona fahari katika Al-Masihi Isa, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili,
PHI 3:4 ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili. Kama mtu yeyote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi.
PHI 3:5 Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya Torati, ni Farisayo,
PHI 3:6 kwa habari ya juhudi, nilikuwa nikitesa jumuiya ya waumini, kuhusu haki inayopatikana kwa Torati, sikuwa na hatia.
PHI 3:7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Al-Masihi.
PHI 3:8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Al-Masihi Isa Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Al-Masihi.
PHI 3:9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe inayopatikana kwa sheria, bali ile inayopatikana kwa imani katika Al-Masihi, haki ile inayotoka kwa Mungu kupitia kwa imani.
PHI 3:10 Nataka nimjue Al-Masihi na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake,
PHI 3:11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.
PHI 3:12 Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Al-Masihi Isa.
PHI 3:13 Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele.
PHI 3:14 Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Al-Masihi Isa.
PHI 3:15 Hivyo sisi sote tuliokuwa kiroho tuwaze jambo hili, hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu ataliweka wazi hilo nalo.
PHI 3:16 Lakini na tushike sana lile ambalo tumekwisha kulifikia.
PHI 3:17 Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea.
PHI 3:18 Kwa maana, kama nilivyokwisha kuwaambia mara nyingi kabla, nami sasa nasema tena hata kwa machozi, watu wengi wanaishi kama adui wa msalaba wa Al-Masihi.
PHI 3:19 Mwisho wa watu hao ni maangamizi, mungu wao ni tumbo, na utukufu wao ni aibu, na mawazo yao yamo katika mambo ya dunia.
PHI 3:20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani Bwana Isa Al-Masihi,
PHI 3:21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.
PHI 4:1 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji langu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana Isa, ninyi wapendwa wangu.
PHI 4:2 Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana Isa.
PHI 4:3 Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.
PHI 4:4 Furahini katika Bwana Isa siku zote, tena nasema furahini!
PHI 4:5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana Isa yu karibu.
PHI 4:6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
PHI 4:7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Al-Masihi Isa.
PHI 4:8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo.
PHI 4:9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
PHI 4:10 Nina furaha kubwa katika Bwana Isa kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo.
PHI 4:11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote.
PHI 4:12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa.
PHI 4:13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
PHI 4:14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu.
PHI 4:15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kundi lingine la waumini lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi.
PHI 4:16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja.
PHI 4:17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu.
PHI 4:18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu.
PHI 4:19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Al-Masihi Isa.
PHI 4:20 Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen.
PHI 4:21 Msalimuni kila mtakatifu katika Al-Masihi Isa. Ndugu walio pamoja nami wanawasalimu.
PHI 4:22 Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wale watu wa nyumbani mwa Kaisari.
PHI 4:23 Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe pamoja na roho zenu. Amen.
COL 1:1 Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu.
COL 1:2 Kwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Al-Masihi wanaoishi Kolosai.
COL 1:3 Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, tunapowaombea ninyi,
COL 1:4 kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Al-Masihi Isa, na upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote:
COL 1:5 imani na upendo ule unaotoka katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni, na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani ile Injili
COL 1:6 iliyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote.
COL 1:7 Mlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, aliye mhudumu mwaminifu wa Al-Masihi kwa ajili yenu,
COL 1:8 ambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho wa Mungu.
COL 1:9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu.
COL 1:10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana Isa, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu,
COL 1:11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha
COL 1:12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru.
COL 1:13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake Mpendwa,
COL 1:14 ambaye kwake tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.
COL 1:15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.
COL 1:16 Kwake yeye vitu vyote vilivyo mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya utawala au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa kupitia kwake na kwa ajili yake.
COL 1:17 Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.
COL 1:18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani jumuiya ya waumini, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote.
COL 1:19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake,
COL 1:20 na kupitia kwake aweze kuvipatanisha vitu vyote kwake mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake iliyomwagika msalabani.
COL 1:21 Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya.
COL 1:22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kupitia kwa mwili wa Al-Masihi kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama,
COL 1:23 ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake.
COL 1:24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Al-Masihi kwa ajili ya mwili wake, ambao ni jumuiya ya waumini.
COL 1:25 Mimi nimekuwa mtumishi wa jumuiya ya waumini kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi neno la Mungu kwa ukamilifu:
COL 1:26 Hii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu.
COL 1:27 Kwao Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Al-Masihi ndani yenu, tumaini la utukufu.
COL 1:28 Yeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Al-Masihi.
COL 1:29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.
COL 2:1 Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walio Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi.
COL 2:2 Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani Al-Masihi,
COL 2:3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa.
COL 2:4 Nawaambia mambo haya ili mtu yeyote asiwadanganye kwa maneno matamu.
COL 2:5 Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Al-Masihi ulivyo.
COL 2:6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Al-Masihi Isa kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake,
COL 2:7 mkijikita na kujengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.
COL 2:8 Chungeni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu, yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Al-Masihi.
COL 2:9 Maana utimilifu wote wa Mungu unakaa ndani ya Al-Masihi katika umbile la mwili wa kibinadamu,
COL 2:10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Al-Masihi, aliye mkuu juu ya kila nguvu na kila mamlaka.
COL 2:11 Katika Al-Masihi pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Al-Masihi,
COL 2:12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kupitia kwa imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.
COL 2:13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Al-Masihi. Alitusamehe dhambi zetu zote,
COL 2:14 baada ya kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akaigongelea kwenye msalaba wake.
COL 2:15 Baada ya Mungu kuzivua enzi na mamlaka, aliziaibisha hadharani, akishangilia katika ushindi wa msalaba.
COL 2:16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato.
COL 2:17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo yajayo; lakini uhalisi unapatikana kwa Al-Masihi.
COL 2:18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza unyenyekevu wa uongo na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu.
COL 2:19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua jinsi Mungu anavyouwezesha.
COL 2:20 Kwa kuwa mlikufa pamoja na Al-Masihi, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kana kwamba ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri kama hizi:
COL 2:21 “Msishike! Msionje! Msiguse!”?
COL 2:22 Amri hizi zote mwisho wake ni kuharibika zinapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu.
COL 2:23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hazifai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.
COL 3:1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Al-Masihi, yatafuteni yaliyo juu, Al-Masihi alikoketi mkono wa kuume wa Mungu.
COL 3:2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani.
COL 3:3 Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Al-Masihi katika Mungu.
COL 3:4 Al-Masihi, aliye uzima wenu, atakapofunuliwa, ndipo nanyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.
COL 3:5 Basi, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambao ni ibada ya sanamu.
COL 3:6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja.
COL 3:7 Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo.
COL 3:8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu.
COL 3:9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake,
COL 3:10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake.
COL 3:11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Al-Masihi ni yote, na ndani ya yote.
COL 3:12 Basi, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wanaopendwa sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu.
COL 3:13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana Isa alivyowasamehe ninyi.
COL 3:14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
COL 3:15 Amani ya Al-Masihi na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani.
COL 3:16 Neno la Al-Masihi na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.
COL 3:17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Isa, mkimshukuru Mungu Baba Mwenyezi kupitia kwake.
COL 3:18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana Isa.
COL 3:19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe wakali kwao.
COL 3:20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hii inampendeza Bwana Isa.
COL 3:21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.
COL 3:22 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, wala si kwa kujipendekeza tu kwao, bali kwa moyo mnyofu na kumcha Bwana.
COL 3:23 Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote kama watu wanaomtumikia Bwana Isa, na si wanadamu,
COL 3:24 kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Isa Al-Masihi mnayemtumikia.
COL 3:25 Yeyote atendaye mabaya atapewa adhabu ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.
COL 4:1 Ninyi mabwana, watendeeni watumwa wenu yaliyo haki na yanayostahili, mkitambua kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.
COL 4:2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru.
COL 4:3 Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena neno lake, ili tupate kuitangaza siri ya Al-Masihi, ambayo kwa ajili yake nimefungwa.
COL 4:4 Ombeni ili nipate kuitangaza hiyo siri kwa udhahiri kama inipasavyo.
COL 4:5 Nendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.
COL 4:6 Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.
COL 4:7 Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana Isa.
COL 4:8 Nimemtuma kwenu kwa lengo maalum la kuwafahamisha hali yetu, na pia awatie moyo.
COL 4:9 Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.
COL 4:10 Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni.)
COL 4:11 Isa aitwaye Yusto pia anawasalimu. Hawa peke yao ndio Wayahudi miongoni mwa watendakazi wenzangu kwa ajili ya ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu.
COL 4:12 Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Al-Masihi Isa, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti.
COL 4:13 Ninashuhudia kumhusu kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli.
COL 4:14 Rafiki yetu mpendwa, Luka yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu.
COL 4:15 Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kundi la waumini wanaokutana katika nyumba yake.
COL 4:16 Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kundi la waumini wa Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia.
COL 4:17 Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana Isa.”
COL 4:18 Mimi Paulo naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi.
1TH 1:1 Paulo, Silvano na Timotheo.
1TH 1:2 Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima.
1TH 1:3 Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Isa Al-Masihi.
1TH 1:4 Ndugu zetu mnaopendwa na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua,
1TH 1:5 kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho wa Mungu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda kati yenu kwa ajili yenu.
1TH 1:6 Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana Isa, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho wa Mungu.
1TH 1:7 Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya.
1TH 1:8 Kwa maana kutoka kwenu neno la Bwana Isa limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali, kiasi kwamba hatuna haja ya kusema chochote juu yake.
1TH 1:9 Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli,
1TH 1:10 na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani Isa, yeye aliyetuokoa kutoka ghadhabu inayokuja.
1TH 2:1 Ndugu zangu, kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua kwamba kuja kwetu kwenu hakukuwa bure,
1TH 2:2 kama vile mjuavyo, tulikuwa tumeteswa na kutukanwa huko Filipi, lakini hata hivyo, kwa msaada wa Mungu wetu, tulikuwa na ujasiri wa kuwaambia Injili ya Mungu ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa.
1TH 2:3 Kwa maana himizo letu halikutokana na hila wala nia mbaya au udanganyifu.
1TH 2:4 Kinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu.
1TH 2:5 Kama mnavyojua, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya; Mungu ndiye shahidi yetu.
1TH 2:6 Hatukuwa tukitafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine yeyote, ingawa kama mitume wa Al-Masihi tungeweza kuwa mzigo kwenu.
1TH 2:7 Lakini tulikuwa wapole kati yenu, kama vile mama anawatunza watoto wake wadogo.
1TH 2:8 Tuliwapenda sana, kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu.
1TH 2:9 Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote tulipokuwa tukiwahubiria Injili ya Mungu.
1TH 2:10 Ninyi wenyewe ni mashahidi na Mungu pia, jinsi tulivyokuwa watakatifu, wenye haki na wasio na lawama miongoni mwenu ninyi mlioamini.
1TH 2:11 Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake.
1TH 2:12 Tuliwatia moyo, tukiwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yanayompendeza Mungu, anayewaita katika ufalme wake na utukufu wake.
1TH 2:13 Nasi pia tunamshukuru Mungu bila kukoma kwa sababu mlipolipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali mlilipokea kama lilivyo hasa, neno la Mungu, linalotenda kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.
1TH 2:14 Kwa maana ninyi ndugu zetu, mlifanyika wafuasi wa makundi ya waumini wa Mungu walio ndani ya Al-Masihi Isa katika Yudea. Mlipata mateso yale yale kutoka kwa watu wenu wenyewe kama vile waumini hao walivyoteswa na Wayahudi,
1TH 2:15 wale waliomuua Bwana Isa na manabii, nasi wakatufukuza pia. Watu hao walimchukiza Mungu na tena ni adui wa watu wote,
1TH 2:16 wakijitahidi kutuzuia tusizungumze na watu wa Mataifa ili wapate kuokolewa. Kwa njia hii wanazidi kujilundikia dhambi zao hadi kikomo. Lakini hatimaye ghadhabu ya Mungu imewafikia.
1TH 2:17 Lakini ndugu zetu, tulipotenganishwa nanyi kwa muda mfupi (ingawa kutengana huko kulikuwa kwa mwili tu, si kwa moyo), tulizidi kuwa na shauku kubwa kuwaona uso kwa uso.
1TH 2:18 Maana tulitaka kuja kwenu, hasa mimi Paulo, nilitaka kuja tena na tena, lakini Shetani akatuzuia.
1TH 2:19 Kwa maana tumaini letu ni nini, au furaha yetu, au taji letu la kujisifia mbele za Bwana wetu Isa Al-Masihi wakati wa kuja kwake? Je, si ni ninyi?
1TH 2:20 Naam, ninyi ndio fahari yetu na furaha yetu.
1TH 3:1 Kwa hivyo tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliamua tubaki Athene peke yetu.
1TH 3:2 Tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Al-Masihi, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu,
1TH 3:3 ili mtu yeyote asifadhaishwe na mateso haya. Mnajua vyema kwamba tumewekewa hayo mateso.
1TH 3:4 Kwa kweli, tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaambia mara kwa mara kwamba tutateswa na imekuwa hivyo kama mnavyojua.
1TH 3:5 Kwa sababu hii niliposhindwa kuvumilia zaidi, nilimtuma mtu ili nipate habari za imani yenu. Niliogopa kwamba kwa njia fulani yule mjaribu asiwe amewajaribu, nasi tukawa tumejitaabisha bure.
1TH 3:6 Lakini Timotheo amerejea kwetu hivi sasa kutoka kwenu, na ameleta habari njema kuhusu imani yenu na upendo wenu. Ametuambia kwamba siku zote mnatukumbuka kwa wema, na kwamba mna shauku ya kutuona kama vile sisi tulivyo na shauku ya kuwaona ninyi.
1TH 3:7 Kwa hiyo, ndugu zetu, katika dhiki na mateso yetu yote tumefarijika kwa sababu ya imani yenu.
1TH 3:8 Sasa kwa kuwa hakika tunaishi, kwa kuwa ninyi mmesimama imara katika Bwana Isa.
1TH 3:9 Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu?
1TH 3:10 Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaza kile kilichopungua katika imani yenu.
1TH 3:11 Basi Mungu wetu na Baba yetu mwenyewe na Bwana wetu Isa atengeneze njia ya sisi kuja kwenu.
1TH 3:12 Bwana Isa na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu.
1TH 3:13 Tunamwomba Mungu aimarishe mioyo yenu ili msiwe na lawama katika utakatifu mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana wetu Isa pamoja na watakatifu wote.
1TH 4:1 Na kuhusu mambo mengine, ndugu, tuliwafundisha jinsi ya kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi. Sasa tunawaomba na kuwasihi katika Bwana Isa mfanye hivi zaidi na zaidi.
1TH 4:2 Kwa kuwa mnajua maagizo tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Isa.
1TH 4:3 Mapenzi ya Mungu ni ninyi mtakaswe, ili mjiepushe na uasherati,
1TH 4:4 na kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima,
1TH 4:5 bali si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu.
1TH 4:6 Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali.
1TH 4:7 Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu.
1TH 4:8 Kwa hiyo, mtu yeyote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.
1TH 4:9 Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.
1TH 4:10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.
1TH 4:11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza,
1TH 4:12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.
1TH 4:13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala katika mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini.
1TH 4:14 Tunaamini kwamba Isa alikufa na kufufuka. Na kwa hivyo, tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja naye wale waliolala katika Isa.
1TH 4:15 Kulingana na neno la Bwana Isa mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana Isa, hakika hatutawatangulia waliolala katika mauti.
1TH 4:16 Kwa maana Bwana Isa mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Al-Masihi watafufuka kwanza.
1TH 4:17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana Isa hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana Isa milele.
1TH 4:18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.
1TH 5:1 Basi ndugu, hatuna haja ya kuwaandikia kuhusu nyakati na majira,
1TH 5:2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Mwenyezi Mungu itakuja kama mwizi anavyokuja usiku.
1TH 5:3 Watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile uchungu unavyomjia mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.
1TH 5:4 Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi.
1TH 5:5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku.
1TH 5:6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine wanavyolala, bali tukeshe na kuwa na kiasi.
1TH 5:7 Kwa kuwa wote wanaolala, hulala usiku, na wale wanaolewa, hulewa usiku.
1TH 5:8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.
1TH 5:9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
1TH 5:10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye.
1TH 5:11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.
1TH 5:12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana Isa na ambao wanawaonya.
1TH 5:13 Waheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi.
1TH 5:14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote.
1TH 5:15 Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.
1TH 5:16 Furahini siku zote;
1TH 5:17 ombeni bila kukoma;
1TH 5:18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndio mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Al-Masihi Isa.
1TH 5:19 Msiuzime moto wa Roho wa Mungu.
1TH 5:20 Msiyadharau maneno ya unabii.
1TH 5:21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema.
1TH 5:22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.
1TH 5:23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Isa Al-Masihi.
1TH 5:24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.
1TH 5:25 Ndugu, tuombeeni.
1TH 5:26 Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu.
1TH 5:27 Ninawaagiza mbele za Bwana Isa mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.
1TH 5:28 Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe nanyi. Amen.
2TH 1:1 Paulo, Silvano na Timotheo.
2TH 1:2 Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Bwana Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
2TH 1:3 Ndugu, inatupasa kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, na inastahili hivyo kwa sababu imani yenu inazidi kukua sana, nao upendo wa kila mmoja wenu kwa mwenzake unazidi kuongezeka.
2TH 1:4 Ndiyo sababu miongoni mwa makundi ya waumini ya Mungu, tunajivunia saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.
2TH 1:5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili yake.
2TH 1:6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi,
2TH 1:7 na kuwapa ninyi mnaoteseka amani pamoja na sisi, wakati Bwana Isa atadhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu.
2TH 1:8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Isa.
2TH 1:9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa uweza wake,
2TH 1:10 siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.
2TH 1:11 Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu wetu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu.
2TH 1:12 Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Isa lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Isa Al-Masihi.
2TH 2:1 Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Isa Al-Masihi na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi,
2TH 2:2 msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho, wala neno la unabii, au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, kusema kwamba siku ya Mwenyezi Mungu imekwisha kuwepo.
2TH 2:3 Mtu yeyote asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja hadi uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa.
2TH 2:4 Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.
2TH 2:5 Je, hamkumbuki kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya?
2TH 2:6 Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia.
2TH 2:7 Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo hadi atakapoondolewa.
2TH 2:8 Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Isa atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake.
2TH 2:9 Kuja kwa yule mwasi kutalingana na vile Shetani hufanya kazi. Atatumia nguvu za aina mbalimbali katika miujiza, na ishara na ajabu za uongo,
2TH 2:10 na katika njia zote ambazo uovu hudanganya wanaoangamia. Wanaangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli ili wapate kuokolewa.
2TH 2:11 Kwa sababu hii, Mungu anawatumia nguvu ya udanganyifu, ili waamini uongo,
2TH 2:12 na hivyo wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.
2TH 2:13 Lakini inatupasa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana Isa, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho wa Mungu kwa kuiamini kweli.
2TH 2:14 Kwa kusudi hili Mungu aliwaita ninyi kupitia Injili tuliyowahubiria, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
2TH 2:15 Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.
2TH 2:16 Bwana wetu Isa Al-Masihi mwenyewe na Mungu, Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema,
2TH 2:17 awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.
2TH 3:1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana Isa lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu.
2TH 3:2 Ombeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini.
2TH 3:3 Lakini Bwana Isa ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu.
2TH 3:4 Nasi tuna tumaini katika Bwana Isa ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza.
2TH 3:5 Mwenyezi Mungu aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Al-Masihi.
2TH 3:6 Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Isa Al-Masihi, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa.
2TH 3:7 Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi,
2TH 3:8 wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu.
2TH 3:9 Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe mfano wenu wa kufuata.
2TH 3:10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”
2TH 3:11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi, bali hujishughulisha na mambo ya wengine.
2TH 3:12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Isa Al-Masihi, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe.
2TH 3:13 Lakini kwenu ninyi, ndugu, kamwe msichoke katika kutenda mema.
2TH 3:14 Ikiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyo katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu.
2TH 3:15 Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.
2TH 3:16 Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Mwenyezi Mungu awe nanyi nyote.
2TH 3:17 Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.
2TH 3:18 Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe nanyi nyote. Amen.
1TI 1:1 Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu, na ya Al-Masihi Isa aliye tumaini letu.
1TI 1:2 Kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani.
1TI 1:3 Kama nilivyokusihi wakati nilipoenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo
1TI 1:4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani.
1TI 1:5 Kusudi la maagizo haya ni upendo unaotoka katika moyo safi, dhamiri safi na imani ya kweli.
1TI 1:6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa,
1TI 1:7 wanataka kuwa walimu wa Torati, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.
1TI 1:8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa.
1TI 1:9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji,
1TI 1:10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli,
1TI 1:11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.
1TI 1:12 Namshukuru Al-Masihi Isa Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake.
1TI 1:13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu.
1TI 1:14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Al-Masihi Isa.
1TI 1:15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Al-Masihi Isa alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote.
1TI 1:16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Al-Masihi Isa apate kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele.
1TI 1:17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.
1TI 1:18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vita vizuri,
1TI 1:19 ukiishikilia imani na dhamiri safi, ambazo wengine wamevikataa, na hivyo wakaangamia kwa habari ya imani yao.
1TI 1:20 Miongoni mwao wako Himenayo na Iskanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.
1TI 2:1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote:
1TI 2:2 kwa ajili ya wafalme na wale wote walio katika mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu.
1TI 2:3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu,
1TI 2:4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli.
1TI 2:5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Al-Masihi Isa,
1TI 2:6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao.
1TI 2:7 Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Al-Masihi wala sisemi uongo), mwalimu wa watu wa Mataifa katika imani na kweli.
1TI 2:8 Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.
1TI 2:9 Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,
1TI 2:10 bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu.
1TI 2:11 Mwanamke na ajifunze katika utulivu na utiifu wote.
1TI 2:12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya.
1TI 2:13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Hawa.
1TI 2:14 Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji.
1TI 2:15 Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake, wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.
1TI 3:1 Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kuwa mwangalizi wa kundi la waumini, atamani kazi nzuri.
1TI 3:2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha,
1TI 3:3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha.
1TI 3:4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia.
1TI 3:5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kundi la waumini la Mungu?)
1TI 3:6 Asiwe mtu aliyeongoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi.
1TI 3:7 Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.
1TI 3:8 Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali.
1TI 3:9 Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi.
1TI 3:10 Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.
1TI 3:11 Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.
1TI 3:12 Shemasi awe mume wa mke mmoja, na aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema.
1TI 3:13 Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Al-Masihi Isa.
1TI 3:14 Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili,
1TI 3:15 nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo jumuiya ya waumini ya Mungu aliye hai, iliyo nguzo na msingi wa kweli.
1TI 3:16 Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa: Alidhihirishwa katika mwili, akathibitishwa kuwa na haki katika Roho wa Mungu, akaonekana na malaika, akahubiriwa miongoni mwa mataifa, akaaminiwa ulimwenguni, akachukuliwa juu katika utukufu.
1TI 4:1 Roho wa Mungu asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani.
1TI 4:2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto.
1TI 4:3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli.
1TI 4:4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani,
1TI 4:5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.
1TI 4:6 Ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Al-Masihi Isa, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata.
1TI 4:7 Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee; badala yake, jizoeze kuwa mtauwa.
1TI 4:8 Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao.
1TI 4:9 Hili ni neno la kuaminiwa tena lastahili kukubaliwa kabisa.
1TI 4:10 Nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi, kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.
1TI 4:11 Mambo haya yaagize na kuyafundisha.
1TI 4:12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi.
1TI 4:13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, hadi nitakapokuja.
1TI 4:14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.
1TI 4:15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako.
1TI 4:16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.
1TI 5:1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako;
1TI 5:2 nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.
1TI 5:3 Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli.
1TI 5:4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo inavyompendeza Mungu.
1TI 5:5 Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie.
1TI 5:6 Lakini mjane aishiye kwa anasa amekufa, ingawa anaishi.
1TI 5:7 Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo yeyote wa kulaumiwa.
1TI 5:8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.
1TI 5:9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na amekuwa mke wa mume mmoja;
1TI 5:10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.
1TI 5:11 Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Al-Masihi, watataka kuolewa tena.
1TI 5:12 Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza.
1TI 5:13 Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema.
1TI 5:14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu.
1TI 5:15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.
1TI 5:16 Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kundi la waumini, ili lile kundi liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.
1TI 5:17 Wazee wa kundi la waumini wanaoongoza shughuli za kundi hilo vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha.
1TI 5:18 Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.”
1TI 5:19 Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu.
1TI 5:20 Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa.
1TI 5:21 Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Al-Masihi Isa na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo.
1TI 5:22 Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.
1TI 5:23 Acha kunywa maji peke yake, tumia divai kidogo kwa sababu ya tumbo lako na maumivu yako ya mara kwa mara.
1TI 5:24 Dhambi za watu wengine ni dhahiri nazo zinawatangulia kwenda hukumuni; na dhambi za watu wengine zinawafuata nyuma yao.
1TI 5:25 Vivyo hivyo, matendo mema yako dhahiri, na hata yale yasiyo dhahiri hayawezi kufichika.
1TI 6:1 Wale wote walio chini ya nira ya utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu.
1TI 6:2 Wale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu. Badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waumini, ambao ni wapendwa wao. Fundisha mambo haya na uwahimize kuyafuata.
1TI 6:3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Isa Al-Masihi na yale ya utauwa,
1TI 6:4 huyo anajivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya,
1TI 6:5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.
1TI 6:6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa.
1TI 6:7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu.
1TI 6:8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo.
1TI 6:9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi.
1TI 6:10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.
1TI 6:11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.
1TI 6:12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi.
1TI 6:13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Al-Masihi Isa, ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri,
1TI 6:14 uishike amri hii bila dosari wala lawama hadi kufunuliwa kwake Bwana wetu Isa Al-Masihi;
1TI 6:15 ambako Mungu atadhihirisha kwa wakati wake mwenyewe: Mungu ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana,
1TI 6:16 yeye pekee aishiye milele, anayedumu katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.
1TI 6:17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie.
1TI 6:18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali yao na wengine.
1TI 6:19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani ule uzima ambao ni wa kweli.
1TI 6:20 Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu,
1TI 6:21 ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani. Neema iwe nanyi. Amen.
2TI 1:1 Paulo mtume wa Al-Masihi Isa kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima ulio ndani ya Al-Masihi Isa.
2TI 1:2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa.
2TI 1:3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu.
2TI 1:4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha.
2TI 1:5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike, na ninasadiki sasa wewe pia unayo.
2TI 1:6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu.
2TI 1:7 Maana Mungu hakutupatia roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.
2TI 1:8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,
2TI 1:9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema, bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Al-Masihi Isa tangu milele.
2TI 1:10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Al-Masihi Isa, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kupitia kwa Injili.
2TI 1:11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii.
2TI 1:12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.
2TI 1:13 Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Al-Masihi Isa.
2TI 1:14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho wa Mungu akaaye ndani yetu.
2TI 1:15 Unajua ya kuwa watu wote katika jimbo la Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene.
2TI 1:16 Bwana Isa akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara, wala hakuionea aibu minyororo yangu.
2TI 1:17 Badala yake, alipokuwa Rumi alinitafuta kwa bidii hadi akanipata.
2TI 1:18 Bwana Isa na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso.
2TI 2:1 Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Al-Masihi Isa.
2TI 2:2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile.
2TI 2:3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Al-Masihi Isa.
2TI 2:4 Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari.
2TI 2:5 Vivyo hivyo, mwanariadha hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano.
2TI 2:6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno.
2TI 2:7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Mwenyezi Mungu atakupa ufahamu katika mambo haya yote.
2TI 2:8 Mkumbuke Isa Al-Masihi aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu,
2TI 2:9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi.
2TI 2:10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Al-Masihi Isa, pamoja na utukufu wa milele.
2TI 2:11 Hili ni neno la kuaminiwa: Kama tumekufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye.
2TI 2:12 Kama tukistahimili, pia tutatawala pamoja naye. Kama tukimkana, naye atatukana.
2TI 2:13 Tusipoaminika, yeye hudumu akiwa mwaminifu, kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.
2TI 2:14 Endelea kuwakumbusha mambo haya, ukiwaonya mbele za Mungu waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote, bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia.
2TI 2:15 Jitahidi kujionesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli.
2TI 2:16 Jiepushe na maneno machafu yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kutomcha Mungu.
2TI 2:17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto,
2TI 2:18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kupita, nao hupindua imani ya baadhi ya watu.
2TI 2:19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Mwenyezi Mungu anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Mwenyezi Mungu na auache uovu.”
2TI 2:20 Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida.
2TI 2:21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema.
2TI 2:22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana Isa kwa moyo safi.
2TI 2:23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa unajua hayo huzaa magomvi.
2TI 2:24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana Isa kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu.
2TI 2:25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli,
2TI 2:26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.
2TI 3:1 Lakini yakupasa ufahamu jambo hili: kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari.
2TI 3:2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu,
2TI 3:3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema,
2TI 3:4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wanaopenda anasa kuliko kumpenda Mungu:
2TI 3:5 wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu kama hao.
2TI 3:6 Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya.
2TI 3:7 Hawa hujifunza siku zote, lakini kamwe hawawezi kuufikia ujuzi wa kweli.
2TI 3:8 Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo watu hawa hupingana na kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani.
2TI 3:9 Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile upumbavu wa hao watu wawili ulivyokuwa dhahiri.
2TI 3:10 Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu,
2TI 3:11 mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana Isa aliniokoa katika hayo yote.
2TI 3:12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Al-Masihi Isa atateswa.
2TI 3:13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.
2TI 3:14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani,
2TI 3:15 na jinsi tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kupitia kwa imani katika Al-Masihi Isa.
2TI 3:16 Maandiko yote yamevuviwa na Mungu, na yafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki,
2TI 3:17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
2TI 4:1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Al-Masihi Isa, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba:
2TI 4:2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.
2TI 4:3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu watakaowaambia yale masikio yao yanatamani kusikia.
2TI 4:4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.
2TI 4:5 Bali wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.
2TI 4:6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia.
2TI 4:7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda.
2TI 4:8 Sasa nimewekewa taji la haki ambalo Bwana, Mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.
2TI 4:9 Jitahidi kuja kwangu upesi
2TI 4:10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na ameenda Thesalonike. Kreske ameenda Galatia, na Tito ameenda Dalmatia.
2TI 4:11 Ni Luka pekee aliye hapa nami. Mtafute Marko uje naye, kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu.
2TI 4:12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso.
2TI 4:13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.
2TI 4:14 Iskanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana Isa atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda.
2TI 4:15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga maneno yetu vikali.
2TI 4:16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.
2TI 4:17 Lakini Bwana Isa alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba.
2TI 4:18 Bwana Isa ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe milele na milele. Amen.
2TI 4:19 Wasalimu Prisila na Akila, na wote wa nyumbani mwa Onesiforo.
2TI 4:20 Erasto alibaki Korintho, nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa.
2TI 4:21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote.
2TI 4:22 Bwana Isa awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi.
TIT 1:1 Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Isa Al-Masihi kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu na kuijua kweli iletayo utauwa:
TIT 1:2 imani na ujuzi katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu, asiyesema uongo, aliahidi hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu,
TIT 1:3 naye kwa wakati wake aliouweka alilidhihirisha neno lake kupitia kwa mahubiri ambayo mimi nimewekewa amana kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu.
TIT 1:4 Kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tunayoshiriki sote.
TIT 1:5 Sababu yangu ya kukuacha huko Krete ni ili uweke utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwateua wazee wa kundi la waumini katika kila mji, kama nilivyokuagiza.
TIT 1:6 Mzee wa kundi la waumini asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waumini, wala hawashtakiwi kwa ufisadi.
TIT 1:7 Kwa kuwa mwangalizi wa kundi ni wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali.
TIT 1:8 Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake.
TIT 1:9 Lazima alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, ili aweze kuwatia moyo wengine kwa mafundisho yenye uzima na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.
TIT 1:10 Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara.
TIT 1:11 Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu.
TIT 1:12 Hata mmoja wa manabii wao mwenyewe amesema, “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.”
TIT 1:13 Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani,
TIT 1:14 ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli.
TIT 1:15 Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna chochote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka.
TIT 1:16 Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lolote jema.
TIT 2:1 Bali wewe fundisha yale yaliyo sahihi kulingana na mafundisho ya kweli.
TIT 2:2 Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.
TIT 2:3 Vivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema,
TIT 2:4 ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao,
TIT 2:5 wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu yeyote asije akalikufuru neno la Mungu.
TIT 2:6 Vivyo hivyo, himiza vijana wawe na kiasi.
TIT 2:7 Katika kila jambo uwe kielelezo kwa kutenda mema. Katika mafundisho yako uoneshe uadilifu, utaratibu,
TIT 2:8 na usemi sahihi usio na lawama, ili wanaokupinga watahayari, wakose neno lolote baya la kusema kutuhusu.
TIT 2:9 Wafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao,
TIT 2:10 wala wasiwaibie, bali waoneshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu yawe ya kuvutia.
TIT 2:11 Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa.
TIT 2:12 Nayo inatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa,
TIT 2:13 huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Isa Al-Masihi.
TIT 2:14 Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani wale walio na juhudi katika kutenda mema.
TIT 2:15 Basi wewe fundisha mambo haya. Himiza na kukaripia kwa mamlaka yote. Usiruhusu mtu yeyote akudharau.
TIT 3:1 Wakumbushe watu kunyenyekea kwa watawala na kwa wenye mamlaka, na kutii, wakiwa tayari kutenda kila lililo jema,
TIT 3:2 wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi bali wawe wema, wakiwa wapole kwa watu wote.
TIT 3:3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi.
TIT 3:4 Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa,
TIT 3:5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kupitia kwa Roho Mtakatifu wa Mungu,
TIT 3:6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kupitia kwa Isa Al-Masihi Mwokozi wetu,
TIT 3:7 ili, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele.
TIT 3:8 Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.
TIT 3:9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili.
TIT 3:10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena.
TIT 3:11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.
TIT 3:12 Mara nitakapomtuma Artema au Tikiko kwako, jitahidi kuja unione huko Nikopoli, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.
TIT 3:13 Fanya kila uwezalo uwasafirishe Zena yule mwanasheria na Apolo na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji katika safari yao.
TIT 3:14 Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.
TIT 3:15 Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale wanaotupenda katika imani. Neema iwe nanyi nyote. Amen.
PHM 1:1 Paulo, mfungwa wa Al-Masihi Isa, pamoja na Timotheo ndugu yetu.
PHM 1:2 kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kundi la waumini wanaokutana nyumbani mwako.
PHM 1:3 Neema na amani zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
PHM 1:4 Siku zote ninamshukuru Mungu wangu ninapokukumbuka katika maombi yangu,
PHM 1:5 kwa sababu ninasikia kuhusu imani yako katika Bwana Isa na upendo wako kwa watakatifu wote.
PHM 1:6 Naomba utiwe nguvu katika kushiriki imani yako na wengine, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu wa kila kitu chema tunachoshiriki kwa ajili ya Al-Masihi.
PHM 1:7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.
PHM 1:8 Hata hivyo, ingawa katika Al-Masihi ningekuwa na ujasiri wa kukuagiza yale yakupasayo kutenda,
PHM 1:9 lakini ninakuomba kwa upendo. Mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Al-Masihi Isa,
PHM 1:10 nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.
PHM 1:11 Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.
PHM 1:12 Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa.
PHM 1:13 Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili.
PHM 1:14 Lakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari.
PHM 1:15 Huenda sababu ya Onesimo kutengwa nawe kwa muda ni ili uwe naye daima,
PHM 1:16 si kama mtumwa sasa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana Isa.
PHM 1:17 Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika nawe, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe.
PHM 1:18 Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi.
PHM 1:19 Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa hilo deni. Kumbuka kwamba nakudai hata nafsi yako.
PHM 1:20 Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana Isa, yaani uniburudishe moyo wangu katika Al-Masihi.
PHM 1:21 Huku nikiwa na hakika ya kutii kwako, nakuandikia nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.
PHM 1:22 Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.
PHM 1:23 Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Al-Masihi Isa, anakusalimu.
PHM 1:24 Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watendakazi wenzangu wanakusalimu.
PHM 1:25 Neema ya Bwana Isa Al-Masihi iwe pamoja na roho zenu. Amen.
HEB 1:1 Zamani, Mungu alisema na baba zetu kupitia kwa manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali,
HEB 1:2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kupitia kwa Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu.
HEB 1:3 Mwana ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Baada ya kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni.
HEB 1:4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.
HEB 1:5 Kwa maana ni kwa malaika yupi Mungu aliwahi kusema, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako”? Au tena, “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu”?
HEB 1:6 Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema, “Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”
HEB 1:7 Anaponena kuhusu malaika, anasema, “Huwafanya malaika wake kuwa pepo, watumishi wake kuwa miali ya moto.”
HEB 1:8 Lakini kwa habari za Mwana asema, “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, kitadumu milele na milele, nayo haki itakuwa fimbo ya utawala ya ufalme wako.
HEB 1:9 Umependa haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako kwa kukupaka mafuta ya furaha.”
HEB 1:10 Pia asema, “Hapo mwanzo, Ee Mwenyezi Mungu, uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
HEB 1:11 Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu; zote zitachakaa kama vazi.
HEB 1:12 Utazikunjakunja kama joho, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe hubadiliki, nayo miaka yako haikomi kamwe.”
HEB 1:13 Je, ni kwa malaika yupi Mungu aliwahi kusema, “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako”?
HEB 1:14 Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?
HEB 2:1 Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha.
HEB 2:2 Kwa kuwa kama ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara, na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki,
HEB 2:3 je, sisi tutapataje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana Isa, ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia.
HEB 2:4 Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu, na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho wa Mungu alizozigawa kulingana na mapenzi yake.
HEB 2:5 Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika.
HEB 2:6 Lakini kuna mahali mtu mmoja ameshuhudia, akisema: “Mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali?
HEB 2:7 Umemfanya chini kidogo kuliko malaika; ukamvika taji la utukufu na heshima,
HEB 2:8 nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu chochote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake.
HEB 2:9 Lakini twamwona Isa, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji la utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu.
HEB 2:10 Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilifaa kwamba Mungu, ambaye ni kwa ajili yake na kupitia kwake kila kitu kimekuwepo, amkamilishe mwanzilishi wa wokovu wao kupitia kwa mateso yake.
HEB 2:11 Yeye awafanyaye watu kuwa watakatifu, pamoja na hao ambao hufanywa watakatifu, wote hutoka katika jamaa moja. Hivyo Isa haoni aibu kuwaita ndugu zake.
HEB 2:12 Yeye anasema, “Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu; mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.”
HEB 2:13 Tena, “Nitaweka tumaini langu kwake.” Tena anasema, “Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mungu amenipa.”
HEB 2:14 Basi kwa kuwa watoto wana mwili na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi,
HEB 2:15 na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti.
HEB 2:16 Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Ibrahimu.
HEB 2:17 Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu.
HEB 2:18 Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.
HEB 3:1 Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Isa, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu.
HEB 3:2 Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemteua, kama Musa alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.
HEB 3:3 Isa ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Musa, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe.
HEB 3:4 Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu.
HEB 3:5 Musa, kama mtumishi, alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale Mungu angeyasema baadaye.
HEB 3:6 Lakini Al-Masihi ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.
HEB 3:7 Kwa hiyo, kama Roho wa Mungu asemavyo: “Leo, mkiisikia sauti yake,
HEB 3:8 msiifanye mioyo yenu migumu, kama mlivyofanya katika uasi, wakati ule wa kujaribiwa jangwani,
HEB 3:9 ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima, ingawa kwa miaka arobaini walikuwa wameyaona matendo yangu.
HEB 3:10 Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile, nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.’
HEB 3:11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, ‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”
HEB 3:12 Ndugu zangu, chungeni asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.
HEB 3:13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu inaitwa “Leo”, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.
HEB 3:14 Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Al-Masihi, tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.
HEB 3:15 Kama ilivyonenwa: “Leo, mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu migumu kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”
HEB 3:16 Basi ni nani waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?
HEB 3:17 Lakini ni nani Mungu aliwakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani?
HEB 3:18 Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii?
HEB 3:19 Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.
HEB 4:1 Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa.
HEB 4:2 Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia; lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani.
HEB 4:3 Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema, “Kwa hiyo nikaapa katika hasira yangu, ‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ” Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
HEB 4:4 Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika kutoka kazi zake zote.”
HEB 4:5 Tena hapo awali amesema, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”
HEB 4:6 Kwa hiyo inabaki kuwa wazi kwa wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii.
HEB 4:7 Kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita “Leo”, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa: “Leo, mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu migumu”.
HEB 4:8 Kwa maana kama Yoshua angelikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine.
HEB 4:9 Basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu;
HEB 4:10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake.
HEB 4:11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.
HEB 4:12 Kwa maana neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
HEB 4:13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye lazima tutawajibika kwake.
HEB 4:14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Isa Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu.
HEB 4:15 Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi.
HEB 4:16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
HEB 5:1 Kwa maana kila kuhani mkuu anayechaguliwa miongoni mwa wanadamu anawekwa kuwawakilisha kwa mambo yanayomhusu Mungu, ili apate kutoa matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi.
HEB 5:2 Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka.
HEB 5:3 Hii ndiyo sababu inampasa kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe na vivyo hivyo kwa ajili ya dhambi za watu.
HEB 5:4 Hakuna anayejitwalia heshima hii mwenyewe; ni lazima aitwe na Mungu, kama vile Haruni alivyoitwa.
HEB 5:5 Pia Al-Masihi hakujitwalia utukufu yeye mwenyewe wa kuwa Kuhani Mkuu, bali Mungu alimwambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako.”
HEB 5:6 Pia mahali pengine asema, “Wewe ni kuhani milele, kwa mfano wa Melkizedeki.”
HEB 5:7 Katika siku za maisha ya Isa hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu.
HEB 5:8 Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utiifu kutokana na mateso aliyoyapata,
HEB 5:9 naye akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii.
HEB 5:10 Naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
HEB 5:11 Tunayo mengi ya kusema kuhusu habari ya ukuhani huu, lakini ni vigumu kuyaeleza, kwa sababu ninyi ni wazito wa kuelewa.
HEB 5:12 Kwa hakika, ingawa hadi wakati huu ingewapasa kuwa walimu, bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu!
HEB 5:13 Kwa maana yeyote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki.
HEB 5:14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.
HEB 6:1 Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Al-Masihi na tukisonga mbele ili tufikie utimilifu, tusiweke tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu,
HEB 6:2 mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele.
HEB 6:3 Mungu akitujalia tutafanya hivyo.
HEB 6:4 Kwa kuwa ni vigumu kwa wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho wa Mungu,
HEB 6:5 ambao wameonja uzuri wa neno la Mungu na nguvu za wakati ujao,
HEB 6:6 kisha wakianguka, kuwarejesha tena katika toba. Kwa kuwa wanamsulubisha Mwana wa Mungu tena na kumdhalilisha hadharani, nayo ikawa hasara kwao.
HEB 6:7 Ardhi inayopokea mvua inayonyesha mara kwa mara juu yake na baadaye inatoa mazao ya kuwanufaisha wale ambao inalimwa kwa ajili yao, hupokea baraka za Mungu.
HEB 6:8 Lakini ardhi ikizaa miiba na mibaruti, haina thamani na iko hatarini kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.
HEB 6:9 Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mema zaidi, mambo kuhusu wokovu.
HEB 6:10 Mungu si mdhalimu: yeye hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na hata sasa mnaendelea kuwahudumia.
HEB 6:11 Nasi twataka kila mmoja wenu aoneshe bidii hiyo hiyo ili mpate kujua uhakika kamili wa lile tumaini hadi mwisho,
HEB 6:12 ili msije mkawa wavivu, bali mpate kuwaiga wale ambao kwa imani na saburi hurithi zile ahadi.
HEB 6:13 Mungu alipompa Ibrahimu ahadi yake, kwa sababu hapakuwa mwingine mkuu kuliko yeye ambaye angeapa naye, aliapa kwa nafsi yake,
HEB 6:14 akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.”
HEB 6:15 Ibrahimu naye, baada ya kungoja kwa saburi, alipokea kile kilichoahidiwa.
HEB 6:16 Wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao, nacho kiapo hicho huthibitisha kile kilichosemwa na hivyo humaliza mabishano yote.
HEB 6:17 Mungu alipotaka kuonesha kwa udhahiri zaidi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake kwa warithi wa ahadi, aliithitibisha kwa kiapo.
HEB 6:18 Mungu alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwavyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia ili tulishike lile tumaini lililowekwa mbele yetu tuwe na faraja thabiti.
HEB 6:19 Tunalo tumaini hili kama nanga ya roho iliyo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika mahali patakatifu nyuma ya pazia,
HEB 6:20 ambapo Isa mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.
HEB 7:1 Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Alipokutana na Ibrahimu akirudi kutoka kuwashinda wafalme, Melkizedeki alimbariki,
HEB 7:2 naye Ibrahimu alimpa sehemu ya kumi ya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake ni “mfalme wa haki”. Na pia “mfalme wa Salemu” maana yake ni “mfalme wa amani”.
HEB 7:3 Hana baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake, kama Mwana wa Mungu. Yeye adumu akiwa kuhani milele.
HEB 7:4 Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Ibrahimu, baba yetu wa zamani, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake.
HEB 7:5 Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi ambao hufanyika makuhani kupokea sehemu ya kumi kutoka kwa watu ambao ni ndugu zao, ingawa ndugu zao ni wazao wa Ibrahimu.
HEB 7:6 Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Ibrahimu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi.
HEB 7:7 Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kuliko yeye.
HEB 7:8 Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na watu ambao hufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai.
HEB 7:9 Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Ibrahimu,
HEB 7:10 kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Ibrahimu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani.
HEB 7:11 Kama ukamilifu ungeweza kupatikana kupitia kwa ukuhani wa Walawi (kwa kuwa katika msingi huo, sheria ilitolewa kwa watu), kwa nini basi kulikuwa na haja ya kuja kuhani mwingine: kuhani kwa mfano wa Melkizedeki, wala si kwa mfano wa Haruni?
HEB 7:12 Kwa kuwa ukuhani ukibadilika, lazima sheria nayo ibadilike.
HEB 7:13 Yeye ambaye mambo haya yanasemwa alikuwa wa kabila lingine, na hakuna mtu wa kabila hilo aliyewahi kuhudumu katika madhabahu.
HEB 7:14 Kwa maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika uzao wa Yuda, tena kuhusu kabila hilo Musa hakusema lolote kwa habari za makuhani.
HEB 7:15 Tena hayo tuliyosema yako wazi zaidi kama akitokea kuhani mwingine kama Melkizedeki,
HEB 7:16 yeye ambaye amefanyika kuhani si kwa misingi ya sheria kama ilivyokuwa kwa baba zake, bali kwa misingi ya uwezo wa uzima usioharibika.
HEB 7:17 Kwa maana imeshuhudiwa kwamba: “Wewe ni kuhani milele, kwa mfano wa Melkizedeki.”
HEB 7:18 Kwa upande mmoja, ile amri ya mwanzo isiyofaa na dhaifu imebatilishwa
HEB 7:19 (kwa maana sheria haikufanya kitu chochote kuwa kikamilifu). Kwa upande mwingine, tumeletewa tumaini lililo bora zaidi ambalo linatuleta karibu na Mungu.
HEB 7:20 Nalo tumaini hilo halikutolewa pasipo kiapo! Wengine walikuwa makuhani pasipo kiapo chochote,
HEB 7:21 lakini Isa alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alimwambia: “Mwenyezi Mungu ameapa, naye hatabadilisha mawazo yake: ‘Wewe ni kuhani milele.’ ”
HEB 7:22 Kwa ajili ya kiapo hiki, Isa amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
HEB 7:23 Basi kumekuwa na makuhani wengi wa aina hiyo, kwa kuwa kifo kiliwazuia kuendelea na huduma yao ya ukuhani.
HEB 7:24 Lakini kwa sababu Isa anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu.
HEB 7:25 Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao.
HEB 7:26 Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu.
HEB 7:27 Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe.
HEB 7:28 Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu; lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.
HEB 8:1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Aliye Mkuu mbinguni,
HEB 8:2 yeye anayehudumu katika patakatifu, hema la kweli lililowekwa na Mwenyezi Mungu, wala si na mwanadamu.
HEB 8:3 Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo, ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa.
HEB 8:4 Kama angekuwa duniani, hangekuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria.
HEB 8:5 Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Musa alionywa alipokaribia kujenga Maskani, akaambiwa: “Hakikisha kuwa unavitengeneza vitu vyote kwa mfano uliooneshwa kule mlimani.”
HEB 8:6 Lakini huduma aliyopewa Isa ni bora kuliko yao, kama vile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake lilivyo bora zaidi ya lile la zamani, nalo limewekwa misingi ya ahadi zilizo bora zaidi.
HEB 8:7 Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine.
HEB 8:8 Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema: “Siku zinakuja, asema Mwenyezi Mungu, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.
HEB 8:9 Agano langu halitakuwa kama lile nililofanya na baba zao nilipowashika mkono kuwaongoza watoke nchi ya Misri, kwa sababu hawakuendelea kuwa waaminifu katika agano langu, nami nikawaacha, asema Mwenyezi Mungu.
HEB 8:10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli baada ya siku zile, asema Mwenyezi Mungu. Nitaziweka sheria zangu katika nia zao na kuziandika mioyoni mwao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
HEB 8:11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake, wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Mwenyezi Mungu,’ kwa sababu wote watanijua mimi, tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.
HEB 8:12 Kwa sababu nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”
HEB 8:13 Kwa kuliita agano hili “jipya”, Mungu amefanya lile agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.
HEB 9:1 Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia.
HEB 9:2 Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu.
HEB 9:3 Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu,
HEB 9:4 ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano.
HEB 9:5 Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi wa Utukufu, wakikitia kivuli kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kujadili vitu hivi kwa undani sasa.
HEB 9:6 Basi vitu hivi vilipokuwa vimepangwa, makuhani waliingia mara kwa mara katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada.
HEB 9:7 Lakini ni kuhani mkuu peke yake aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema. Tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, na hakuingia kamwe bila damu, ambayo alitoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi za watu walizotenda bila kukusudia.
HEB 9:8 Kwa njia hii, Roho wa Mungu alikuwa anaonesha kwamba, maadamu lile hema la kwanza lilikuwa bado limesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakatifu ilikuwa bado haijafunguliwa.
HEB 9:9 Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu.
HEB 9:10 Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya.
HEB 9:11 Al-Masihi alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu.
HEB 9:12 Hakuingia kupitia kwa damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele.
HEB 9:13 Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje.
HEB 9:14 Basi damu ya Al-Masihi, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, si itazisafisha dhamiri zetu zaidi kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!
HEB 9:15 Kwa sababu hii Al-Masihi ni mpatanishi wa agano jipya, ili wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele: kwa vile yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka kwa dhambi walizozitenda chini ya agano la kwanza.
HEB 9:16 Kwa habari ya wosia, ni muhimu kuthibitisha kifo cha yule aliyeutoa,
HEB 9:17 kwa sababu wosia huwa na nguvu tu wakati mtu ameshakufa; kamwe hauwezi kutumika wakati yule aliyeuandika bado yuko hai.
HEB 9:18 Hii ndiyo sababu hata lile agano la kwanza halikuweza kutekelezwa pasipo damu.
HEB 9:19 Musa alipotangaza kila amri kwa watu wote, alichukua damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji, sufu nyekundu na matawi ya mti wa hisopo, akanyunyizia kile kitabu na watu wote.
HEB 9:20 Alisema, “Hii ndiyo damu ya agano, ambalo Mungu amewaamuru kulitii.”
HEB 9:21 Vivyo hivyo alinyunyizia damu hiyo kwenye ile hema pamoja na kila kifaa kilichotumika ndani yake kwa taratibu za ibada.
HEB 9:22 Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.
HEB 9:23 Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi.
HEB 9:24 Kwa maana Al-Masihi hakuingia patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu.
HEB 9:25 Wala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile kuhani mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe.
HEB 9:26 Ingekuwa hivyo, ingempasa Al-Masihi kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu.
HEB 9:27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu,
HEB 9:28 vivyo hivyo Al-Masihi alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.
HEB 10:1 Torati ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kupitia kwa dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu.
HEB 10:2 Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi.
HEB 10:3 Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka,
HEB 10:4 kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.
HEB 10:5 Kwa hiyo, Al-Masihi alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka, bali mwili uliniandalia;
HEB 10:6 sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukupendezwa nazo.
HEB 10:7 Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja, imeandikwa kunihusu katika kitabu: Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ”
HEB 10:8 Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe).
HEB 10:9 Kisha akasema, “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile agano la kwanza ili kuimarisha la pili.
HEB 10:10 Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kupitia kwa sadaka ya mwili wa Isa Al-Masihi alioutoa mara moja tu.
HEB 10:11 Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile, ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi.
HEB 10:12 Lakini huyu kuhani baada ya kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu.
HEB 10:13 Tangu wakati huo anangoja hadi adui zake wawekwe chini ya miguu yake,
HEB 10:14 kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.
HEB 10:15 Pia Roho wa Mungu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema:
HEB 10:16 “Hili ndilo agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Mwenyezi Mungu. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika katika nia zao.”
HEB 10:17 Kisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao sitakumbuka tena.”
HEB 10:18 Basi haya yaliposamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayohitajika kwa ajili ya dhambi.
HEB 10:19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Isa,
HEB 10:20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani mwili wake,
HEB 10:21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu,
HEB 10:22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Al-Masihi na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi.
HEB 10:23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.
HEB 10:24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema.
HEB 10:25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.
HEB 10:26 Tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi.
HEB 10:27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu.
HEB 10:28 Yeyote aliyeikataa Torati ya Musa alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu.
HEB 10:29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema?
HEB 10:30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Mwenyezi Mungu atawahukumu watu wake.”
HEB 10:31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.
HEB 10:32 Kumbukeni siku zile za kwanza, ambazo baada ya kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu.
HEB 10:33 Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliotendwa hivyo.
HEB 10:34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyang’anywa mali yenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.
HEB 10:35 Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno.
HEB 10:36 Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi.
HEB 10:37 Kwa kuwa, “Bado kitambo kidogo tu, yeye ajaye atakuja wala hatakawia.”
HEB 10:38 Na, “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani. Naye akisitasita, sina furaha naye.”
HEB 10:39 Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaositasita na kuangamia, bali tuko miongoni mwa hao wenye imani na hivyo tunaokolewa.
HEB 11:1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana.
HEB 11:2 Maana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya.
HEB 11:3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.
HEB 11:4 Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu bora kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.
HEB 11:5 Kwa imani Idrisi alitwaliwa kutoka maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, “kwa sababu Mungu alimchukua”. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu.
HEB 11:6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wanaomtafuta kwa bidii.
HEB 11:7 Kwa imani, Nuhu alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.
HEB 11:8 Kwa imani Ibrahimu, alipoitwa aende mahali Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakoenda.
HEB 11:9 Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaka na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.
HEB 11:10 Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.
HEB 11:11 Kwa imani Ibrahimu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake.
HEB 11:12 Hivyo kutokana na huyu mtu aliyekuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.
HEB 11:13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani.
HEB 11:14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.
HEB 11:15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangepata nafasi ya kurudi huko.
HEB 11:16 Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.
HEB 11:17 Kwa imani Ibrahimu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaka kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu,
HEB 11:18 hata ingawa Mungu alikuwa amemwambia Ibrahimu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaka.”
HEB 11:19 Ibrahimu alihesabu kuwa Mungu angeweza kumfufua Isaka kutoka kwa wafu. Na kusema kwa mfano, alimpata tena Isaka kutoka kwa wafu.
HEB 11:20 Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.
HEB 11:21 Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yusufu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.
HEB 11:22 Kwa imani, Yusufu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa Waisraeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.
HEB 11:23 Kwa imani, wazazi wa Musa walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
HEB 11:24 Kwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.
HEB 11:25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa muda mfupi.
HEB 11:26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Al-Masihi ni utajiri mkubwa kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye.
HEB 11:27 Kwa imani Musa aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho.
HEB 11:28 Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.
HEB 11:29 Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.
HEB 11:30 Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.
HEB 11:31 Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.
HEB 11:32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii,
HEB 11:33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba,
HEB 11:34 wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni.
HEB 11:35 Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi.
HEB 11:36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani.
HEB 11:37 Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya,
HEB 11:38 watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.
HEB 11:39 Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa.
HEB 11:40 Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
HEB 12:1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu.
HEB 12:2 Basi na tumtazame sana Isa mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
HEB 12:3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili msije mkachoka na kukata tamaa.
HEB 12:4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu.
HEB 12:5 Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema: “Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala usikate tamaa akikukemea,
HEB 12:6 kwa sababu Mwenyezi Mungu huwaadibisha wale anaowapenda, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mwana.”
HEB 12:7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake?
HEB 12:8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto haramu, wala si watoto halali.
HEB 12:9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi?
HEB 12:10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake.
HEB 12:11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.
HEB 12:12 Kwa hiyo, itieni nguvu mikono yenu iliyo dhaifu na magoti yenu yaliyolegea.
HEB 12:13 Sawazisheni mapito ya miguu yenu, ili kitu kilicho kiwete kisidhoofishwe bali kiponywe.
HEB 12:14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao bila kuwa nao hakuna mtu atakayemwona Bwana.
HEB 12:15 Chungeni sana mtu yeyote asiikose neema ya Mungu, na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.
HEB 12:16 Chungeni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza.
HEB 12:17 Baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.
HEB 12:18 Hamjaufikia mlima ule uwezao kuguswa na ambao unawaka moto; wala kwenye giza, utusitusi na dhoruba;
HEB 12:19 kwenye mlio wa tarumbeta, au kwenye sauti isemayo maneno ya kutisha kiasi ambacho wale walioisikia waliomba wasiambiwe neno jingine zaidi,
HEB 12:20 kwa sababu hawangeweza kustahimili neno lile lililoamriwa: “Hata mnyama akigusa mlima huu, atapigwa mawe.”
HEB 12:21 Waliyoyaona yalikuwa ya kutisha kiasi kwamba Musa alisema, “Ninatetemeka kwa hofu.”
HEB 12:22 Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia,
HEB 12:23 kwenye jumuiya ya waumini ya wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa,
HEB 12:24 kwa Isa mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa, ile inenayo mambo mema kuliko damu ya Habili.
HEB 12:25 Angalieni msije mkamkataa yeye anenaye. Ikiwa wao hawakuepuka adhabu walipomkataa yeye aliyewaonya hapa duniani, sisi je, tutaokokaje tusipomsikiliza yeye anayetuonya kutoka mbinguni?
HEB 12:26 Wakati ule sauti yake ilitetemesha dunia, lakini sasa ameahidi, “Kwa mara moja tena nitatetemesha si nchi tu bali na mbingu pia.”
HEB 12:27 Maneno haya “kwa mara moja tena” yanaonesha kuondoshwa kwa vile vitu vinavyoweza kutetemeshwa, yaani vile vitu vilivyoumbwa, kwa kusudi vile vitu visivyoweza kutetemeshwa vibaki.
HEB 12:28 Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani, na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inayompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji,
HEB 12:29 kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao.”
HEB 13:1 Endeleeni kupendana kama ndugu.
HEB 13:2 Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua.
HEB 13:3 Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.
HEB 13:4 Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote.
HEB 13:5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema, “Kamwe sitakuacha, wala sitakupungukia.”
HEB 13:6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri, “Mwenyezi Mungu ni msaada wangu; sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”
HEB 13:7 Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao.
HEB 13:8 Isa Al-Masihi ni yeye yule jana, leo na hata milele.
HEB 13:9 Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria.
HEB 13:10 Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake.
HEB 13:11 Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi.
HEB 13:12 Vivyo hivyo, Isa naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe.
HEB 13:13 Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba.
HEB 13:14 Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.
HEB 13:15 Basi kupitia kwa Isa, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake.
HEB 13:16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.
HEB 13:17 Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa maelezo. Watiini ili wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu.
HEB 13:18 Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia.
HEB 13:19 Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.
HEB 13:20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Isa, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo,
HEB 13:21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni pake, kupitia kwa Isa Al-Masihi, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.
HEB 13:22 Ndugu zangu, nawasihi mchukuliane na maneno yangu ya maonyo, kwa kuwa nimewaandikia waraka mfupi tu.
HEB 13:23 Nataka mjue kwamba ndugu yetu Timotheo amefunguliwa kutoka gerezani. Akifika mapema, nitakuja pamoja naye kuwaona.
HEB 13:24 Wasalimuni viongozi wenu wote na watakatifu wote. Wale wa kutoka Italia wanawasalimu.
HEB 13:25 Neema iwe nanyi nyote. Amen.
JAM 1:1 Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Isa Al-Masihi.
JAM 1:2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali,
JAM 1:3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
JAM 1:4 Acheni saburi ikamilishe kazi yake, ili mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
JAM 1:5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima, basi amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.
JAM 1:6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, linalopeperushwa na upepo na kutupwa huku na huko.
JAM 1:7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana Isa.
JAM 1:8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.
JAM 1:9 Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa.
JAM 1:10 Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani.
JAM 1:11 Kwa maana jua kali huchomoza na kuyakausha majani ya mmea, nalo ua lake linaanguka, na uzuri wake unaharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake.
JAM 1:12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji lile la uzima Mungu alilowaahidia wale wanaompenda.
JAM 1:13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
JAM 1:14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya.
JAM 1:15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa huzaa mauti.
JAM 1:16 Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike.
JAM 1:17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.
JAM 1:18 Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote.
JAM 1:19 Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika.
JAM 1:20 Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu.
JAM 1:21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.
JAM 1:22 Basi kuweni watendaji wa Neno, wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu.
JAM 1:23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo
JAM 1:24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na husahau upesi jinsi alivyo.
JAM 1:25 Lakini yeye anayeangalia kwa makini katika sheria kamilifu iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau, bali akatenda alichosikia, basi atabarikiwa katika kile anachofanya.
JAM 1:26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake haifai kitu.
JAM 1:27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu, Baba yetu, ndiyo hii: ni kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.
JAM 2:1 Ndugu zangu, waumini katika imani ya Bwana wetu wa utukufu, Isa Al-Masihi, hawapaswi kuwa na upendeleo.
JAM 2:2 Je, ikiwa mtu anakuja katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, na kisha akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa.
JAM 2:3 Mkimpa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,”
JAM 2:4 je, hamjabagua kati yenu wenyewe na kuwa mahakimu wenye mawazo maovu?
JAM 2:5 Ndugu zangu, sikilizeni: Je, si Mungu huwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi ufalme aliowaahidi wale wanaompenda?
JAM 2:6 Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani?
JAM 2:7 Je, si wao wanalikufuru jina lile bora sana mliloitiwa?
JAM 2:8 Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko, isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema.
JAM 2:9 Lakini mkiwapendelea watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa wakosaji.
JAM 2:10 Kwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote.
JAM 2:11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.
JAM 2:12 Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru.
JAM 2:13 Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.
JAM 2:14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa?
JAM 2:15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula,
JAM 2:16 naye mmoja wenu akamwambia, “Nenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini?
JAM 2:17 Vivyo hivyo, imani peke yake, kama haikuambatana na matendo, imekufa.
JAM 2:18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.” Nioneshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo.
JAM 2:19 Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani wanaamini hivyo na kutetemeka.
JAM 2:20 Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu?
JAM 2:21 Je, Ibrahimu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaka madhabahuni?
JAM 2:22 Unaona jinsi imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda.
JAM 2:23 Kwa njia hiyo likatimizwa andiko lisemalo, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu.
JAM 2:24 Mnaona kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.
JAM 2:25 Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba: je, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine?
JAM 2:26 Kama vile mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.
JAM 3:1 Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi.
JAM 3:2 Sisi sote tunajikwaa katika mambo mengi. Ikiwa mtu yeyote hakosei kamwe katika yale anayosema, yeye ni mkamilifu, naye anaweza kuuzuia pia na mwili wake wote.
JAM 3:3 Tunapotia lijamu kwenye vinywa vya farasi ili kuwafanya watutii, tunaweza kuigeuza miili yao yote.
JAM 3:4 Au chukua mfano wa meli: ingawa ni kubwa sana, nazo hupelekwa na upepo mkali, zinaelekezwa kwa usukani mdogo sana kokote wanakotaka nahodha.
JAM 3:5 Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa!
JAM 3:6 Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa Jehanamu.
JAM 3:7 Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini hufugika na hufugwa na binadamu,
JAM 3:8 lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.
JAM 3:9 Kwa ulimi tunamhimidi Mwenyezi Mungu na Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu.
JAM 3:10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo.
JAM 3:11 Je, chemchemi moja inaweza kutoa katika tundu moja maji matamu na maji ya chumvi?
JAM 3:12 Je, ndugu zangu, mtini unaweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Wala chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
JAM 3:13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aioneshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima.
JAM 3:14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli.
JAM 3:15 Hekima kama hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani.
JAM 3:16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.
JAM 3:17 Lakini hekima inayotoka mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki.
JAM 3:18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.
JAM 4:1 Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu?
JAM 4:2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu.
JAM 4:3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.
JAM 4:4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.
JAM 4:5 Au mwadhani kwamba Maandiko yasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?
JAM 4:6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Maandiko yasema: “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
JAM 4:7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia.
JAM 4:8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili.
JAM 4:9 Huzunikeni, na mwomboleze, na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni.
JAM 4:10 Jinyenyekezeni mbele za Mwenyezi Mungu, naye atawainua.
JAM 4:11 Ndugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu yeyote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu, anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria, bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria.
JAM 4:12 Yuko Mtoa sheria mmoja tu na yeye peke yake ndiye Hakimu; ndiye awezaye kuokoa au kuangamiza. Lakini wewe ni nani hata umhukumu jirani yako?
JAM 4:13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutaenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.”
JAM 4:14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka.
JAM 4:15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Mwenyezi Mungu akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.”
JAM 4:16 Ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kote kwa namna hii ni uovu.
JAM 4:17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
JAM 5:1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia.
JAM 5:2 Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo.
JAM 5:3 Dhahabu yenu na fedha yenu zimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu, nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho.
JAM 5:4 Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu, na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
JAM 5:5 Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe; mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa.
JAM 5:6 Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, waliokuwa hawapingani nanyi.
JAM 5:7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana Isa. Tazameni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani, na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua ya kwanza na ya mwisho.
JAM 5:8 Ninyi nanyi vumilieni, tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana Isa kumekaribia.
JAM 5:9 Ndugu zangu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!
JAM 5:10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa jina la Mwenyezi Mungu, wakiwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso.
JAM 5:11 Kama mnavyojua, tunawahesabu wale waliovumilia kuwa wabarikiwa. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu, na mmeona kile ambacho hatimaye Mwenyezi Mungu alimtendea. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.
JAM 5:12 Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, iwe kwa mbingu au kwa dunia, au kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, la sivyo mtahukumiwa.
JAM 5:13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu.
JAM 5:14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kundi la waumini wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana Isa.
JAM 5:15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana Isa atamwinua, na kama ametenda dhambi, atasamehewa.
JAM 5:16 Kwa hiyo, ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu, tena yanafaa sana.
JAM 5:17 Ilya alikuwa mwanadamu kama sisi. Aliomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita.
JAM 5:18 Kisha akaomba tena, nazo mbingu zikatoa mvua, nayo ardhi ikatoa mazao yake.
JAM 5:19 Ndugu zangu, yeyote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejeshwa na mtu mwingine,
JAM 5:20 hamna budi kujua kwamba yeyote amrejeshaye mwenye dhambi kutoka upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka mauti na kufunika wingi wa dhambi.
1PE 1:1 Petro, mtume wa Isa Al-Masihi.
1PE 1:2 Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba Mwenyezi kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho wa Mungu, katika utiifu kwa Isa Al-Masihi na kunyunyiziwa damu yake.
1PE 1:3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi! Kwa rehema zake kuu, ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima, kupitia kwa kufufuka kwa Isa Al-Masihi kutoka kwa wafu,
1PE 1:4 ili tuupate urithi usioangamia, usioharibika, na usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
1PE 1:5 Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kupitia kwa imani, hadi utakapokuja ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho.
1PE 1:6 Katika haya yote mnafurahi sana, ijapokuwa kwa muda mfupi sasa mmehuzunishwa kwa majaribu ya aina nyingi.
1PE 1:7 Haya yamewajia ili imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo ingawa inasafishwa kwa moto, ionekane kuwa halisi, na imalizie kwa sifa, utukufu na heshima Isa Al-Masihi atakapodhihirishwa.
1PE 1:8 Ijapokuwa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha yenye utukufu na isiyoelezeka.
1PE 1:9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.
1PE 1:10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewafikia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa.
1PE 1:11 Walijaribu kujua ni wakati upi na ni mazingira yapi ambayo Roho wa Al-Masihi, aliyekuwa ndani yao, alionesha alipotabiri mateso ya Al-Masihi na utukufu ambao ungefuata.
1PE 1:12 Walifunuliwa kwamba walikuwa wanawahudumia ninyi, bali si wao wenyewe, waliponena kuhusu mambo hayo. Mmeambiwa mambo haya sasa na wale waliowahubiria Injili kwa Roho wa Mungu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.
1PE 1:13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Isa Al-Masihi atakapodhihirishwa.
1PE 1:14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga.
1PE 1:15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote.
1PE 1:16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
1PE 1:17 Kwa kuwa mnamlilia Baba anayehukumu kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, kaeni kama wageni wakati wenu duniani, mkiogopa na kumcha Mungu.
1PE 1:18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa, ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu. Hamkukombolewa kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu,
1PE 1:19 bali mlikombolewa kwa damu ya thamani ya Al-Masihi, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa.
1PE 1:20 Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika nyakati hizi za mwisho kwa ajili yenu.
1PE 1:21 Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.
1PE 1:22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni.
1PE 1:23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu inayoharibika, bali kwa mbegu isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele.
1PE 1:24 Maana, “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao wote ni kama maua ya kondeni; majani hunyauka na maua huanguka,
1PE 1:25 lakini neno la Mwenyezi Mungu ladumu milele.” Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.
1PE 2:1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna.
1PE 2:2 Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu,
1PE 2:3 ikiwa kweli mmeonja kwamba Bwana Isa ni mwema.
1PE 2:4 Mnapokuja kwake, yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake,
1PE 2:5 ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kupitia kwa Isa Al-Masihi.
1PE 2:6 Kwa maana imeandikwa katika Maandiko: “Tazama, naweka katika Sayuni, jiwe la pembeni teule lenye thamani, na yeyote atakayemwamini hataaibishwa kamwe.”
1PE 2:7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hili ni la thamani. Lakini kwao wasioamini, “Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni,”
1PE 2:8 tena, “Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae, na mwamba wa kuwaangusha.” Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno, kama walivyowekewa tangu zamani.
1PE 2:9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.
1PE 2:10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.
1PE 2:11 Wapendwa, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu.
1PE 2:12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.
1PE 2:13 Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Awe ni mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi,
1PE 2:14 au wawe maafisa aliowaweka. Kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale wanaotenda mema.
1PE 2:15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema myanyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu.
1PE 2:16 Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu.
1PE 2:17 Mheshimuni kila mtu ipasavyo, wapendeni waumini wote, mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme.
1PE 2:18 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali.
1PE 2:19 Kwa maana ni jambo la sifa kama mtu akivumilia anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya Mungu.
1PE 2:20 Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la kusifiwa mbele za Mungu.
1PE 2:21 Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Al-Masihi naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.
1PE 2:22 “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.”
1PE 2:23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki.
1PE 2:24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, na tupate kuishi katika haki. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa.
1PE 2:25 Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.
1PE 3:1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno,
1PE 3:2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu.
1PE 3:3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi.
1PE 3:4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu.
1PE 3:5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao,
1PE 3:6 kama Sara alivyomtii mumewe Ibrahimu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote.
1PE 3:7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa kuwajali, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu.
1PE 3:8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, mkijaliana, na wanyenyekevu.
1PE 3:9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka.
1PE 3:10 Kwa maana, “Yeyote apendaye uzima na kuona siku njema, basi auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila.
1PE 3:11 Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema; lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.
1PE 3:12 Kwa maana macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza maombi yao. Bali uso wa Mwenyezi Mungu uko kinyume na watendao maovu.”
1PE 3:13 Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema?
1PE 3:14 Lakini hata ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki, mmebarikiwa. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.”
1PE 3:15 Bali mtukuzeni Al-Masihi kama Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima,
1PE 3:16 mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Al-Masihi waaibike kwa ajili ya masingizio yao.
1PE 3:17 Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, ikiwa ni mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.
1PE 3:18 Kwa kuwa Al-Masihi naye aliteswa mara moja tu kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho wa Mungu.
1PE 3:19 Baada ya kufanywa hai, alienda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni:
1PE 3:20 roho ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Nuhu, wakati wa kujenga safina, ambamo watu wachache tu, yaani watu wanane, waliokolewa ili wasiangamie kwa gharika.
1PE 3:21 Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia: si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu. Inatuokoa kupitia kwa ufufuo wa Isa Al-Masihi.
1PE 3:22 Yeye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu; nao malaika, mamlaka na nguvu zote zimetiishwa chini yake.
1PE 4:1 Kwa hiyo, kwa kuwa Al-Masihi aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia hiyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi.
1PE 4:2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki hapa duniani ili kutimiza tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi ili kutimiza mapenzi ya Mungu.
1PE 4:3 Kwa maana wakati uliopita, mmetumia muda mwingi mkifanya yale wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu.
1PE 4:4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika maisha yao ya uovu uliopita kiasi, nao huwatukana ninyi.
1PE 4:5 Lakini itawapasa wao kutoa maelezo kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.
1PE 4:6 Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo.
1PE 4:7 Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo kuweni na tahadhari, mkiwa na akili tulivu na kujidhibiti, mkikesha katika kuomba.
1PE 4:8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.
1PE 4:9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manung’uniko.
1PE 4:10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.
1PE 4:11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote anayehudumu hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kupitia kwa Isa Al-Masihi. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.
1PE 4:12 Wapendwa, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata.
1PE 4:13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Al-Masihi, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
1PE 4:14 Mkitukanwa kwa ajili ya jina la Al-Masihi, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu.
1PE 4:15 Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine.
1PE 4:16 Lakini ukiteseka kwa kuwa mfuasi wa Al-Masihi, usihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali mtukuze Mungu kwa sababu umeitwa kwa jina hilo.
1PE 4:17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje?
1PE 4:18 Basi, “Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka, itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?”
1PE 4:19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.
1PE 5:1 Kwa wazee walio miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Al-Masihi, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa:
1PE 5:2 lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika.
1PE 5:3 Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi.
1PE 5:4 Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji la utukufu lisiloharibika.
1PE 5:5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote jivikeni unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa, “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
1PE 5:6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.
1PE 5:7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye anajishughulisha sana na mambo yenu.
1PE 5:8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza.
1PE 5:9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
1PE 5:10 Nanyi baada ya kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Al-Masihi, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha.
1PE 5:11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.
1PE 5:12 Kwa msaada wa Silvano, ninayemhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo, na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.
1PE 5:13 Kundi la waumini lililoko Babeli, lililochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu; vivyo hivyo mwanangu Marko anawasalimu.
1PE 5:14 Salimianeni kwa busu la upendo. Amani iwe nanyi nyote mlio katika Al-Masihi.
2PE 1:1 Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Isa Al-Masihi.
2PE 1:2 Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Isa Bwana wetu.
2PE 1:3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.
2PE 1:4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.
2PE 1:5 Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa;
2PE 1:6 katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa;
2PE 1:7 katika utauwa, upendano wa kindugu; na katika upendano wa kindugu, upendo.
2PE 1:8 Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yatawasaidia kutokosa bidii wala kutokuzaa matunda katika kumjua Bwana wetu Isa Al-Masihi.
2PE 1:9 Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya, haoni mbali na ni kipofu, naye amesahau kwamba ametakaswa kutoka dhambi zake za zamani.
2PE 1:10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe,
2PE 1:11 na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi.
2PE 1:12 Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo.
2PE 1:13 Naona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niko katika hema hili ambalo ni mwili wangu,
2PE 1:14 kwa sababu najua kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Isa Al-Masihi alivyoliweka wazi kwangu.
2PE 1:15 Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.
2PE 1:16 Tulipowafahamisha kuhusu uweza na kuja kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake.
2PE 1:17 Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba Mwenyezi, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.”
2PE 1:18 Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.
2PE 1:19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama nuru inavyong’aa gizani, hadi kupambazuke na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu.
2PE 1:20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe.
2PE 1:21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu.
2PE 2:1 Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana Mungu Mwenyezi wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka.
2PE 2:2 Nao wengi watafuata njia zao potovu, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa.
2PE 2:3 Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi.
2PE 2:4 Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa Kuzimu katika vifungo vya giza wakae humo hadi ije hukumu;
2PE 2:5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, lakini akamhifadhi Nuhu, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba;
2PE 2:6 kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu;
2PE 2:7 na kama alimwokoa Lutu, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu
2PE 2:8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku):
2PE 2:9 ikiwa hivyo ndivyo, basi Mwenyezi Mungu anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu.
2PE 2:10 Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka. Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni.
2PE 2:11 Lakini hata malaika, ijapokuwa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Mwenyezi Mungu.
2PE 2:12 Lakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia.
2PE 2:13 Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki karamu pamoja nanyi.
2PE 2:14 Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana!
2PE 2:15 Wameiacha njia iliyo nyoofu, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu.
2PE 2:16 Lakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, alipoongea kwa sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.
2PE 2:17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu unaopeperushwa na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao.
2PE 2:18 Kwa maana wao hunena maneno matupu ya kiburi. Nao wanavutia tamaa mbaya za asili ya mwili, ili kuwashawishi watu ambao wanajiondoa kutoka kwa wale wanaoishi katika hatia.
2PE 2:19 Wanawaahidi uhuru wakati wao wenyewe ni watumwa wa upotovu; kwa maana “mtu ni mtumwa wa chochote kinachomtawala.”
2PE 2:20 Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Isa Al-Masihi, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya kuliko ile ya kwanza.
2PE 2:21 Ingekuwa afadhali kwao kama hawangeijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa.
2PE 2:22 Kwao mithali zimetukia kuwa za kweli, zinaposema: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”
2PE 3:1 Wapendwa, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu.
2PE 3:2 Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi wetu mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.
2PE 3:3 Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbovu.
2PE 3:4 Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.”
2PE 3:5 Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwa tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji.
2PE 3:6 Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa.
2PE 3:7 Kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
2PE 3:8 Lakini wapendwa, msisahau neno hili: kwamba kwa Mwenyezi Mungu, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.
2PE 3:9 Mwenyezi Mungu hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
2PE 3:10 Lakini siku ya Mwenyezi Mungu itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilicho ndani yake kitaunguzwa.
2PE 3:11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu,
2PE 3:12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto.
2PE 3:13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.
2PE 3:14 Kwa sababu hii, wapendwa, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute bila mawaa wala dosari, na mkiwa na amani kwake.
2PE 3:15 Hesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpendwa Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu.
2PE 3:16 Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote, akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha, kama wanavyopotosha Maandiko mengine na kujiletea maangamizi yao wenyewe.
2PE 3:17 Basi, ninyi wapendwa, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwa uthabiti wenu.
2PE 3:18 Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.
1JO 1:1 Tunawajulisha lile lililokuwako tangu mwanzo, lile tulilosikia, ambalo tumeliona kwa macho yetu, ambalo tumelitazama na kuligusa kwa mikono yetu, kuhusu Neno la uzima.
1JO 1:2 Uzima huo ulidhihirishwa; nasi tumeuona na kuushuhudia, nasi twawatangazia uzima wa milele, ambao ulikuwa pamoja na Baba, nao ukadhihirishwa kwetu.
1JO 1:3 Twawatangazia lile tuliloliona na kulisikia, ili nanyi mwe na ushirika nasi. Na ushirika wetu hasa ni pamoja na Baba na Mwanawe, Isa Al-Masihi.
1JO 1:4 Tunaandika mambo haya ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.
1JO 1:5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote.
1JO 1:6 Tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli.
1JO 1:7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Isa, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
1JO 1:8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu.
1JO 1:9 Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutokana na udhalimu wote.
1JO 1:10 Tukisema hatujatenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.
1JO 2:1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Isa Al-Masihi, Mwenye Haki.
1JO 2:2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.
1JO 2:3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake.
1JO 2:4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli.
1JO 2:5 Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake:
1JO 2:6 Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Isa alivyoenenda.
1JO 2:7 Wapendwa, siwaandikii ninyi amri mpya bali ile ya zamani, ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ya zamani ni lile neno mlilosikia.
1JO 2:8 Lakini nawaandikia amri mpya, yaani lile neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu, kwa sababu giza linapita na ile nuru ya kweli tayari inang’aa.
1JO 2:9 Yeyote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani.
1JO 2:10 Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu chochote ndani yake cha kumkwaza.
1JO 2:11 Lakini yeyote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakoenda, kwa sababu giza limempofusha macho.
1JO 2:12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa ajili ya Jina lake.
1JO 2:13 Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nawaandikia ninyi watoto wadogo, kwa sababu mmemjua Baba.
1JO 2:14 Nawaandikia ninyi akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.
1JO 2:15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake.
1JO 2:16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu.
1JO 2:17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.
1JO 2:18 Watoto wadogo, huu ni wakati wa mwisho! Kama mlivyosikia kwamba anayempinga Al-Masihi anakuja, hivyo basi wanaompinga Al-Masihi wengi wamekwisha kuja. Kutokana na hili twajua kwamba huu ni wakati wa mwisho.
1JO 2:19 Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa. Kwa maana kama wangekuwa wa kwetu, wangekaa pamoja nasi; lakini kutoka kwao kulionesha kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa wa kwetu.
1JO 2:20 Lakini ninyi mmepakwa mafuta na yeye Aliye Mtakatifu, nanyi nyote mnaijua kweli.
1JO 2:21 Siwaandikii kwa sababu hamuijui kweli, bali kwa sababu mnaijua, nanyi mnajua hakuna uongo unaotoka katika kweli.
1JO 2:22 Je, mwongo ni nani? Mwongo ni mtu yule asemaye kwamba Isa si Al-Masihi. Mtu kama huyo ndiye anayempinga Al-Masihi, yaani yeye humkana Baba na Mwana.
1JO 2:23 Hakuna yeyote amkanaye Mwana aliye na Baba. Yeyote anayemkubali Mwana anaye na Baba pia.
1JO 2:24 Bali ninyi, hakikisheni kwamba lile mlilosikia tangu mwanzo linadumu ndani yenu. Kama lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba.
1JO 2:25 Hii ndiyo ahadi yake kwetu, yaani uzima wa milele.
1JO 2:26 Nawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha.
1JO 2:27 Bali ninyi, upako mlioupata kutoka kwake unadumu ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu yeyote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.
1JO 2:28 Sasa basi, watoto wapendwa, kaeni ndani yake, ili atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake wakati wa kuja kwake.
1JO 2:29 Mkijua kuwa yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa naye.
1JO 3:1 Tazameni ni pendo kuu namna gani alilotupatia Baba, kwamba sisi tuitwe wana wa Mungu! Na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.
1JO 3:2 Wapendwa, sasa tu wana wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.
1JO 3:3 Kila mmoja mwenye matumaini haya ndani yake hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.
1JO 3:4 Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi.
1JO 3:5 Lakini mwajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi, wala ndani yake hamna dhambi.
1JO 3:6 Kila mtu akaaye ndani yake hatendi dhambi. Kila mtu atendaye dhambi hakumwona yeye wala hakumtambua.
1JO 3:7 Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki.
1JO 3:8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi.
1JO 3:9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu.
1JO 3:10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.
1JO 3:11 Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi.
1JO 3:12 Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamuua ndugu yake. Basi kwa nini alimuua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
1JO 3:13 Ndugu zangu, ninyi msistaajabu kama ulimwengu ukiwachukia.
1JO 3:14 Sisi tunajua kwamba tumepita mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini.
1JO 3:15 Yeyote amchukiaye ndugu yake ni muuaji, nanyi mwajua kwamba muuaji hana uzima wa milele ndani yake.
1JO 3:16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Isa Al-Masihi aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu.
1JO 3:17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo?
1JO 3:18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.
1JO 3:19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu
1JO 3:20 kila mara mioyo yetu inapotuhukumu. Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu, naye anajua kila kitu.
1JO 3:21 Wapendwa, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri mbele za Mungu,
1JO 3:22 lolote tuombalo, twalipokea kutoka kwake, kwa sababu tumezitii amri zake na kutenda yale yanayompendeza.
1JO 3:23 Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Isa Al-Masihi, na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru.
1JO 3:24 Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kupitia kwa Roho wa Mungu, yule aliyetupatia.
1JO 4:1 Wapendwa, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni.
1JO 4:2 Hivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Isa Al-Masihi amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu.
1JO 4:3 Lakini kila roho ambayo haimkubali Isa haitoki kwa Mungu. Hii ndiyo roho ya anayempinga Al-Masihi, ambayo mmesikia kwamba inakuja na sasa tayari iko ulimwenguni.
1JO 4:4 Watoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu.
1JO 4:5 Wao wanatokana na ulimwengu na kwa hiyo hunena yaliyo ya ulimwengu, hivyo ulimwengu huwasikiliza.
1JO 4:6 Sisi twatokana na Mungu na yeyote anayemjua Mungu hutusikiliza, lakini asiyetokana na Mungu hatusikilizi. Hivi ndivyo tunavyoweza kutambua Roho wa Kweli na roho ya upotovu.
1JO 4:7 Wapendwa, tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu.
1JO 4:8 Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo.
1JO 4:9 Hivi ndivyo Mungu alivyoonesha pendo lake kwetu: Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kupitia kwake.
1JO 4:10 Hili ndilo pendo: si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu.
1JO 4:11 Wapendwa, kama Mungu alivyotupenda sisi, imetupasa na sisi kupendana.
1JO 4:12 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote. Lakini tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu.
1JO 4:13 Tunajua kwamba twakaa ndani yake na yeye ndani yetu, kwa sababu ametupatia sisi sehemu ya Roho wake Mtakatifu.
1JO 4:14 Nasi tumeona na kushuhudia kwamba Baba amemtuma Mwanawe ili awe Mwokozi wa ulimwengu.
1JO 4:15 Kila akiriye kwamba Isa ni Mwana wa Mungu, basi Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.
1JO 4:16 Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu. Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake.
1JO 4:17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu.
1JO 4:18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.
1JO 4:19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza.
1JO 4:20 Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemwona?
1JO 4:21 Naye ametupatia amri hii: Yeyote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.
1JO 5:1 Kila mtu anayeamini kwamba Isa ndiye Al-Masihi amezaliwa na Mungu, na yeyote ampendaye Baba humpenda pia mtoto aliyezaliwa naye.
1JO 5:2 Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake.
1JO 5:3 Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito.
1JO 5:4 Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani hiyo imani yetu.
1JO 5:5 Ni nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Isa ni Mwana wa Mungu.
1JO 5:6 Huyu ndiye alikuja kwa maji na damu, yaani Isa Al-Masihi. Hakuja kwa maji peke yake, bali kwa maji na damu. Naye Roho wa Mungu ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli.
1JO 5:7 Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni: hao ni Baba, Neno na Roho wa Mungu. Hawa watatu ni umoja.
1JO 5:8 Pia wako mashahidi watatu duniani]: hao ni Roho, Maji na Damu; hawa watatu wanakubaliana katika umoja.
1JO 5:9 Kama tunaukubali ushuhuda wa wanadamu, basi ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa kuwa huu ndio ushuhuda wa Mungu kwamba amemshuhudia Mwanawe.
1JO 5:10 Kila mtu amwaminiye Mwana wa Mungu anao huu ushuhuda moyoni mwake. Kila mtu asiyemwamini Mungu amemfanya yeye kuwa mwongo, kwa sababu hakuamini ushuhuda Mungu alioutoa kuhusu Mwanawe.
1JO 5:11 Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupatia uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe.
1JO 5:12 Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.
1JO 5:13 Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele.
1JO 5:14 Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.
1JO 5:15 Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.
1JO 5:16 Mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo.
1JO 5:17 Jambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.
1JO 5:18 Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hawezi kumdhuru.
1JO 5:19 Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu.
1JO 5:20 Nasi pia twajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupatia sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani ndani ya Isa Al-Masihi Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.
1JO 5:21 Watoto wapendwa, jilindeni nafsi zenu kutokana na sanamu. Amen.
2JO 1:1 Mzee.
2JO 1:2 kwa sababu ya ile kweli inayokaa ndani yetu, na ambayo itaendelea kukaa nasi milele.
2JO 1:3 Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Isa Al-Masihi, Mwanawe Baba, zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.
2JO 1:4 Imenipa furaha kuu kuona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile Baba alivyotuagiza.
2JO 1:5 Sasa, mama mteule mpendwa, si kwamba ninakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Tupendane kila mmoja na mwenzake.
2JO 1:6 Hili ndilo pendo: kwamba tuenende kwa kuzitii amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.
2JO 1:7 Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Isa Al-Masihi amekuja katika mwili, wametawanyika ulimwenguni. Mtu kama huyo ni mdanganyifu na anampinga Al-Masihi.
2JO 1:8 Jihadharini msije mkapoteza kile mlichokitenda, bali mpate kupewa thawabu kamilifu.
2JO 1:9 Mtu yeyote asiyedumu katika mafundisho ya Al-Masihi bali ameyaacha, yeye hana Mungu. Yeyote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia.
2JO 1:10 Msimpokee mtu yeyote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu.
2JO 1:11 Yeyote amkaribishaye mtu kama huyo anashiriki katika matendo yake maovu.
2JO 1:12 Ninayo mengi ya kuwaandikia, lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kwenu na kuongea nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.
2JO 1:13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu. Amen.
3JO 1:1 Mzee.
3JO 1:2 Mpendwa, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya njema kama vile roho yako ifanikiwavyo.
3JO 1:3 Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza kuhusu uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli.
3JO 1:4 Sina furaha kubwa kuliko hii, ya kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.
3JO 1:5 Rafiki mpendwa, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako.
3JO 1:6 Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya jumuiya ya waumini. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu.
3JO 1:7 Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasiomwamini Al-Masihi.
3JO 1:8 Kwa hiyo imetupasa sisi kuonesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.
3JO 1:9 Nililiandikia kundi la waumini, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu.
3JO 1:10 Hivyo nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu, na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke miongoni mwa waumini.
3JO 1:11 Rafiki mpendwa, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Yeyote atendaye mema anatoka kwa Mungu, bali atendaye mabaya hajamwona Mungu.
3JO 1:12 Kila mtu ameshuhudia mema kuhusu Demetrio, vivyo hivyo hata na hiyo kweli yenyewe. Sisi pia twashuhudia mema juu yake, nanyi mwajua kwamba ushuhuda wetu ni kweli.
3JO 1:13 Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kuandika kwa kalamu na wino.
3JO 1:14 Badala yake, nataraji kukuona upesi, nasi tutaongea pamoja ana kwa ana.
3JO 1:15 Amani iwe kwako. Rafiki zetu walio hapa wanakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu walio huko, kila mmoja kwa jina lake.
JUD 1:1 Yuda, mtumwa wa Isa Al-Masihi, na nduguye Yakobo.
JUD 1:2 Rehema, amani na upendo ziwe kwenu kwa wingi.
JUD 1:3 Wapendwa, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwitetee imani iliyokabidhiwa watakatifu kwa nafasi moja itoshayo.
JUD 1:4 Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri kati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wanaopotosha neema ya Mungu, na kuifanya kuwa ruhusa ya kutenda maovu, wakimkana Isa Al-Masihi, ambaye pekee ni Mtawala wetu mkuu na Bwana wetu.
JUD 1:5 Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Mwenyezi Mungu, akiisha kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.
JUD 1:6 Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu.
JUD 1:7 Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.
JUD 1:8 Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka.
JUD 1:9 Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi kuhusu mwili wa Musa, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Mwenyezi Mungu na akukemee!”
JUD 1:10 Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yatakayowaangamiza.
JUD 1:11 Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora.
JUD 1:12 Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha wenyewe tu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kung’olewa kabisa.
JUD 1:13 Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele.
JUD 1:14 Idrisi, mtu wa saba kuanzia Adamu, alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Mwenyezi Mungu anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake,
JUD 1:15 ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.”
JUD 1:16 Watu hawa ni wenye kunung’unika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbovu; hujisifu kwa maneno makuu, na kuwasifu mno watu wengine kwa faida yao wenyewe.
JUD 1:17 Lakini ninyi wapendwa, kumbukeni yale mitume wa Bwana wetu Isa Al-Masihi waliyotabiri awali.
JUD 1:18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.”
JUD 1:19 Hawa ndio watu wanaowagawanya ninyi, wanaofuata tamaa zao za asili, wala hawana Roho wa Mungu.
JUD 1:20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho wa Mungu.
JUD 1:21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia rehema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi, inayowapeleka katika uzima wa milele.
JUD 1:22 Wahurumieni walio na mashaka;
JUD 1:23 okoeni wengine kwa kuwanyakua kutoka motoni; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.
JUD 1:24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi:
JUD 1:25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Isa Al-Masihi Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.
REV 1:1 Ufunuo wa Isa Al-Masihi aliopewa na Mungu ili awaoneshe watumishi wake mambo ambayo ni lazima yatukie hivi karibuni. Alijulisha mambo haya kwa kumtuma malaika wake kwa Yohana mtumishi wake,
REV 1:2 ambaye anashuhudia kuhusu kila kitu alichokiona, yaani neno la Mungu na ushuhuda wa Isa Al-Masihi.
REV 1:3 Amebarikiwa yeye asomaye maneno ya unabii huu, na wamebarikiwa wale wanaoyasikia na kuyatia moyoni yale yaliyoandikwa humo, kwa sababu wakati umekaribia.
REV 1:4 Yohana.
REV 1:5 na kutoka kwa Isa Al-Masihi, aliye shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, mtawala wa wafalme wa dunia. Kwake yeye anayetupenda na aliyetuweka huru kutoka dhambi zetu kwa damu yake,
REV 1:6 na akatufanya sisi kuwa ufalme na makuhani, ili tumtumikie Mungu wake ambaye ni Baba yake. Utukufu na uwezo ni vyake milele na milele! Amen.
REV 1:7 “Tazama! Anakuja na mawingu,” na “kila jicho litamwona, hata wale waliomchoma”; na makabila yote duniani “yataomboleza kwa sababu yake.”
REV 1:8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mwenyezi Mungu, “aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”
REV 1:9 Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Isa na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Isa.
REV 1:10 Katika Siku ya Bwana, nilikuwa katika Roho wa Mungu na nikasikia sauti kubwa kama ya baragumu nyuma yangu
REV 1:11 ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makundi saba ya waumini: kwa Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
REV 1:12 Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu,
REV 1:13 na katikati ya vile vinara vya taa, alikuwamo mtu kama Mwana wa Adamu, akiwa amevaa joho refu, na mkanda wa dhahabu ukiwa umefungwa kifuani mwake.
REV 1:14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto.
REV 1:15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba inayong’aa katika tanuru la moto, nayo sauti yake ilikuwa kama mngurumo wa maji mengi.
REV 1:16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua liking’aa kwa nguvu zake zote.
REV 1:17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho.
REV 1:18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na Kuzimu.
REV 1:19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya.
REV 1:20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makundi saba ya waumini, navyo vile vinara saba ni hayo makundi saba.
REV 2:1 “Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Efeso, andika: Haya ndio maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu.
REV 2:2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewajaribu wale wanaojifanya mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo.
REV 2:3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.
REV 2:4 Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza.
REV 2:5 Kumbuka basi ni wapi ulikoanguka! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake.
REV 2:6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.
REV 2:7 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda ya uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.
REV 2:8 “Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Smirna, andika: Haya ndio maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka.
REV 2:9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani.
REV 2:10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji la uzima.
REV 2:11 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini. Yeye ashindaye hatadhuriwa kamwe na mauti ya pili.
REV 2:12 “Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Pergamo, andika: Haya ndio maneno yake yeye aliye na upanga mkali wenye makali kuwili.
REV 2:13 Ninajua unakoishi: kule Shetani ana kiti chake cha utawala. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu, hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji wenu mkuu, anakoishi Shetani.
REV 2:14 Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu na kufanya uasherati.
REV 2:15 Vivyo hivyo unao wale wanaoyashikilia mafundisho ya Wanikolai.
REV 2:16 Basi tubu! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.
REV 2:17 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa. Nitampa pia jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.
REV 2:18 “Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Thiatira, andika: Haya ndio maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto, na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa.
REV 2:19 Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako, na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.
REV 2:20 Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.
REV 2:21 Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki.
REV 2:22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake.
REV 2:23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makundi yote ya waumini yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.
REV 2:24 Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo yanayoitwa mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wowote juu yenu):
REV 2:25 Lakini shikeni sana mlicho nacho, hadi nitakapokuja.
REV 2:26 Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu hadi mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa:
REV 2:27 ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma, atawavunja vipande vipande kama chombo cha udongo’: kama mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu.
REV 2:28 Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi.
REV 2:29 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.
REV 3:1 “Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Sardi, andika: Haya ndio maneno ya aliye na zile Roho saba za Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa.
REV 3:2 Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu.
REV 3:3 Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia; yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.
REV 3:4 Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili.
REV 3:5 Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.
REV 3:6 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.
REV 3:7 “Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Filadelfia, andika: Haya ndio maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua.
REV 3:8 Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu.
REV 3:9 Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, nitawafanya waje wapige magoti miguuni pako, na wakiri kwamba nimekupenda.
REV 3:10 Kwa kuwa umeshika amri yangu ya kuvumilia katika saburi, nitakulinda katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote, ili kuwajaribu wote wanaoishi duniani.
REV 3:11 Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akalichukua taji lako.
REV 3:12 Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika Hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji mkubwa wa Mungu wangu, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya.
REV 3:13 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.
REV 3:14 “Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Laodikia, andika: Haya ndio maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu.
REV 3:15 Nayajua matendo yako, kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa moto au baridi.
REV 3:16 Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu.
REV 3:17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi.
REV 3:18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.
REV 3:19 Wale ninaowapenda, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.
REV 3:20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.
REV 3:21 Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.
REV 3:22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.”
REV 4:1 Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango uliokuwa wazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo mwanzo ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo huku, nami nitakuonesha yale ambayo hayana budi kutendeka baada ya haya.”
REV 4:2 Ghafula nilikuwa katika Roho wa Mungu, na hapo mbele yangu palikuwa kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu.
REV 4:3 Aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua uliong’aa kama zumaridi.
REV 4:4 Kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti vingine ishirini na vinne vya utawala, na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne. Walivaa mavazi meupe, na walikuwa na taji za dhahabu vichwani mwao.
REV 4:5 Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya kiti cha enzi, taa saba zilikuwa zinawaka. Hizi ndizo roho saba za Mungu.
REV 4:6 Pia mbele ya kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama bilauri. Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wamejaa macho mbele na nyuma.
REV 4:7 Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ng’ombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka.
REV 4:8 Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:
REV 4:9 Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele,
REV 4:10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aliyeketi kwenye kiti cha enzi, na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema:
REV 4:11 “Bwana wetu na Mungu wetu, wewe unastahili kupokea utukufu na heshima na uweza, kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako viliumbwa na vimekuwako.”
REV 5:1 Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nje, kikiwa kimefungwa kwa mihuri saba.
REV 5:2 Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, “Ni nani anayestahili kuivunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu?”
REV 5:3 Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala hata kutazama ndani yake.
REV 5:4 Nikalia sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake.
REV 5:5 Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja mihuri yake saba.”
REV 5:6 Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba za Mungu zilizotumwa duniani pote.
REV 5:7 Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi.
REV 5:8 Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu.
REV 5:9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe unastahili kukitwaa kitabu na kuivunja mihuri yake, kwa sababu ulichinjwa, na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu kutoka kila kabila, kila lugha, kila jamaa na kila taifa.
REV 5:10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani wa kumtumikia Mungu wetu, nao watatawala duniani.”
REV 5:11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu.
REV 5:12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa, kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na sifa!”
REV 5:13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi, na baharini, na vyote vilivyomo, vikiimba: “Sifa na heshima na utukufu na uweza ni vyake yeye aliyeketi juu ya hicho kiti cha enzi, na kwa Mwana-Kondoo, milele na milele!”
REV 5:14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee wakaanguka kifudifudi wakaabudu.
REV 6:1 Nikaangalia Mwana-Kondoo alipofungua ule muhuri wa kwanza miongoni mwa mihuri saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!”
REV 6:2 Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda.
REV 6:3 Alipouvunja ule muhuri wa pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!”
REV 6:4 Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa.
REV 6:5 Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu palikuwa na farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake.
REV 6:6 Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja, na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”
REV 6:7 Alipouvunja ule muhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!”
REV 6:8 Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.
REV 6:9 Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza.
REV 6:10 Wakalia kwa sauti kuu, wakasema, “Hata lini, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi kwa watu wanaoishi duniani kwa ajili ya damu yetu?”
REV 6:11 Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, hadi idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.
REV 6:12 Nikatazama alipouvunja ule muhuri wa sita. Pakatokea tetemeko kuu la ardhi, na jua likawa jeusi kama gunia lililotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu.
REV 6:13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali.
REV 6:14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.
REV 6:15 Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima.
REV 6:16 Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo!
REV 6:17 Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”
REV 7:1 Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wowote.
REV 7:2 Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka mawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema,
REV 7:3 “Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye paji za nyuso za watumishi wa Mungu wetu.”
REV 7:4 Ndipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: elfu mia moja na arobaini na nne kutoka makabila yote ya Israeli.
REV 7:5 Kutoka kabila la Yuda elfu kumi na mbili walitiwa muhuri, kutoka kabila la Reubeni elfu kumi na mbili, kutoka kabila la Gadi elfu kumi na mbili,
REV 7:6 kutoka kabila la Asheri elfu kumi na mbili, kutoka kabila la Naftali elfu kumi na mbili, kutoka kabila la Manase elfu kumi na mbili,
REV 7:7 kutoka kabila la Simeoni elfu kumi na mbili, kutoka kabila la Lawi elfu kumi na mbili, kutoka kabila la Isakari elfu kumi na mbili,
REV 7:8 kutoka kabila la Zabuloni elfu kumi na mbili, kutoka kabila la Yusufu elfu kumi na mbili, na kutoka kabila la Benyamini elfu kumi na mbili.
REV 7:9 Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuwahesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao.
REV 7:10 Nao walikuwa wakipaza sauti kwa nguvu, wakisema: “Wokovu una Mungu wetu, yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo!”
REV 7:11 Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee, na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu,
REV 7:12 wakisema: “Amen! Sifa na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu viwe kwa Mungu wetu milele na milele. Amen!”
REV 7:13 Kisha mmoja wa wale wazee akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”
REV 7:14 Nikamjibu, “Bwana, wewe unajua.” Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa.
REV 7:15 Kwa hiyo, “Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na kumtumikia usiku na mchana katika Hekalu lake; naye aliyeketi katika kile kiti cha enzi atatanda hema lake juu yao.
REV 7:16 Kamwe hawataona njaa wala kiu tena. Jua halitawachoma wala joto lolote liunguzalo.
REV 7:17 Kwa maana Mwana-Kondoo aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi atakuwa Mchungaji wao; naye atawaongoza kwenda kwenye chemchemi za maji yaliyo hai. Naye Mungu atawafuta machozi kutoka machoni mwao.”
REV 8:1 Mwana-Kondoo alipouvunja ule muhuri wa saba, pakawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.
REV 8:2 Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.
REV 8:3 Malaika mwingine, aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote, juu ya yale madhabahu ya dhahabu yaliyo mbele ya kile kiti cha enzi.
REV 8:4 Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika.
REV 8:5 Kisha yule malaika akakichukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwa yale madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi na ngurumo, miali ya radi na tetemeko la ardhi.
REV 8:6 Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.
REV 8:7 Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, navyo vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi. Na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea, na nyasi yote mbichi ikateketea.
REV 8:8 Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu,
REV 8:9 theluthi ya viumbe vyenye uhai vilivyoishi baharini vikafa, na theluthi ya meli zikaharibiwa.
REV 8:10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji.
REV 8:11 Nyota hiyo inaitwa Pakanga. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.
REV 8:12 Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.
REV 8:13 Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipaza sauti kwa nguvu, huku akiruka katikati ya anga, akasema, “Ole! Ole! Ole wa watu wanaoishi duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”
REV 9:1 Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo.
REV 9:2 Alipolifungua hilo Shimo, moshi ukapanda kutoka humo kama moshi wa tanuru kubwa sana. Jua na anga vikatiwa giza na ule moshi uliotoka katika hilo Shimo.
REV 9:3 Ndipo katika ule moshi wakatoka nzige wakaenda juu ya nchi, nao wakapewa nguvu kama zile za nge wa duniani.
REV 9:4 Wakaambiwa wasidhuru majani ya nchi, wala mmea wala mti wowote, bali wawadhuru tu wale watu ambao hawana muhuri wa Mungu kwenye paji za nyuso zao.
REV 9:5 Wakaruhusiwa kuwatesa kwa muda wa miezi mitano, lakini wasiwaue. Uchungu wa kuuma kwao ulikuwa kama ule wa mtu anapoumwa na nge.
REV 9:6 Katika siku hizo watu watatafuta kifo lakini hawatakiona, watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia.
REV 9:7 Wale nzige walikuwa na umbo kama la farasi waliotayarishwa kwa ajili ya vita. Kwenye vichwa vyao kulikuwa na kitu kama taji za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.
REV 9:8 Walikuwa na nywele kama za wanawake, na meno yao yalikuwa kama ya simba.
REV 9:9 Walikuwa na dirii kama za chuma, na sauti za mabawa yao zilikuwa kama ngurumo za farasi wengi na magari ya vita mengi yakikimbia vitani.
REV 9:10 Walikuwa na mikia yenye miiba ya kuumia, kama nge. Nguvu yao ya kutesa watu kwa huo muda wa miezi mitano ilikuwa katika mikia yao.
REV 9:11 Walikuwa na mfalme wao, ambaye ni malaika wa lile Shimo, ambaye jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani ni Apolioni.
REV 9:12 Ole ya kwanza imepita, bado nyingine mbili zinakuja.
REV 9:13 Malaika wa sita akaipiga tarumbeta yake, nami nikasikia sauti ikitoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu.
REV 9:14 Ile sauti ikamwambia yule malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie wale malaika wanne waliofungwa kwenye ule mto mkubwa Frati.”
REV 9:15 Basi wale malaika wanne, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hiyo, na siku hiyo, na mwezi huo, na mwaka huo ili wawaue theluthi ya wanadamu wakafunguliwa.
REV 9:16 Idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili. Nilisikia idadi yao.
REV 9:17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika maono yangu: Wapanda farasi walivaa dirii vifuani zenye rangi nyekundu sana kama ya moto, na yakuti samawi, na kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vichwa vya simba, na moto, moshi na kiberiti vilitoka vinywani mwao.
REV 9:18 Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo hayo matatu, yaani huo moto, moshi na kiberiti, vilivyotoka kwenye vinywa vya hao farasi.
REV 9:19 Nguvu za hao farasi zilikuwa katika vinywa vyao na kwenye mikia yao, kwa sababu mikia yao ilikuwa kama nyoka, yenye vichwa ambayo waliitumia kudhuru.
REV 9:20 Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea.
REV 9:21 Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao.
REV 10:1 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake uling’aa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.
REV 10:2 Mkononi mwake alikuwa ameshika kijitabu kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu.
REV 10:3 Naye akapaza sauti kwa nguvu kama simba anayenguruma. Aliponguruma, zile radi saba zikatoa ngurumo zake.
REV 10:4 Nazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.”
REV 10:5 Kisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni.
REV 10:6 Naye akaapa kwa Yule aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo, akasema, “Hakuna kungoja tena!
REV 10:7 Lakini katika siku zile huyo malaika wa saba atakaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”
REV 10:8 Ndipo ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni ikasema nami tena, ikaniambia, “Nenda, chukua kile kitabu kilichofunguliwa kilichoko mkononi mwa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”
REV 10:9 Basi nikamwendea nikamwomba yule malaika anipe kile kijitabu. Akaniambia, “Chukua na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali.”
REV 10:10 Hivyo nikakichukua kile kijitabu kutoka mkononi mwa yule malaika, nikakila. Kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu, lakini baada ya kukila, tumbo langu likatiwa uchungu.
REV 10:11 Kisha nikaambiwa, “Imekupasa kutoa unabii tena kuhusu makabila mengi, mataifa, lugha na wafalme.”
REV 11:1 Ndipo nikapewa mwanzi uliokuwa kama ufito wa kupimia, nikaambiwa, “Nenda ukapime Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu, nawe uwahesabu wale waabuduo humo.
REV 11:2 Lakini usiupime ua wa nje wa Hekalu; uache, kwa sababu ua huo wamepewa watu wa Mataifa. Hao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na mbili.
REV 11:3 Nami nitawapa mashahidi wangu wawili uwezo, nao watoe unabii kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini, wakiwa wamevaa gunia.”
REV 11:4 Hawa ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili vya taa visimamavyo mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wa dunia yote.
REV 11:5 Kama mtu yeyote akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Hivi ndivyo impasavyo kufa mtu yeyote atakayetaka kuwadhuru.
REV 11:6 Watu hawa wanao uwezo wa kufunga anga ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Nao watakuwa na uwezo wa kuyabadili maji kuwa damu na kuipiga dunia kwa kila aina ya mapigo mara kwa mara kama watakavyo.
REV 11:7 Basi watakapokuwa wamemaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika lile Shimo atapigana nao vita, atawashinda na kuwaua.
REV 11:8 Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkubwa, ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo pia Isa Bwana wao alisulubiwa.
REV 11:9 Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa wataziangalia hizo maiti zao na hawataruhusu zizikwe.
REV 11:10 Watu wanaoishi duniani watazitazama maiti za hao manabii wawili kwa furaha, na kushangilia kwa kupeana zawadi, kwa sababu hao manabii waliwatesa watu wanaoishi duniani.
REV 11:11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu ikawaingia, nao wakasimama kwa miguu yao na wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu.
REV 11:12 Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati adui zao wakiwa wanawatazama.
REV 11:13 Saa hiyo hiyo, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo, nao walionusurika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.
REV 11:14 Ole ya pili imekwisha kupita, tazama ole ya tatu inakuja upesi.
REV 11:15 Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema: “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Al-Masihi wake, naye atatawala milele na milele.”
REV 11:16 Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya utawala, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,
REV 11:17 wakisema: “Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu na ukaanza kutawala.
REV 11:18 Mataifa walikasirika; nao wakati wa ghadhabu yako umewadia. Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa, na kuwapa thawabu watumishi wako manabii, na watakatifu wako pamoja na wale wote wanaoliheshimu Jina lako, wakubwa kwa wadogo: na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”
REV 11:19 Ndipo Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano lake likaonekana humo. Kukatokea miali ya radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la ardhi na mvua kubwa ya mawe.
REV 12:1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na taji lenye nyota kumi na mbili lilikuwa kichwani mwake.
REV 12:2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa.
REV 12:3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi, na taji saba katika vichwa vyake.
REV 12:4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa.
REV 12:5 Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi.
REV 12:6 Yule mwanamke akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini.
REV 12:7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika wake likapigana nao.
REV 12:8 Lakini joka na malaika wake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni.
REV 12:9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika wake.
REV 12:10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema: “Sasa wokovu na uweza na ufalme wa Mungu wetu Mwenyezi umekuja, na mamlaka ya Al-Masihi wake. Kwa kuwa ametupwa chini mshtaki wa ndugu zetu, anayewashtaki mbele za Mungu usiku na mchana.
REV 12:11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao. Wala wao hawakuyapenda maisha yao sana, hata wakawa tayari kufa.
REV 12:12 Kwa hiyo furahini, ninyi mbingu na wote wanaoishi humo! Lakini ole wenu nchi na bahari, kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu, akiwa amejaa ghadhabu, kwa sababu anajua ya kuwa muda wake ni mfupi!”
REV 12:13 Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto wa kiume.
REV 12:14 Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka hadi mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko jangwani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu, ya wakati ambako lile joka haliwezi kufika.
REV 12:15 Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke, achukuliwe na mafuriko.
REV 12:16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao lile joka lilikuwa limeutoa kinywani mwake.
REV 12:17 Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke na likaondoka ili kupigana vita na wazawa waliosalia wa huyo mwanamke, yaani wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Isa Al-Masihi.
REV 13:1 Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari. Nami nikamwona mnyama akitoka ndani ya bahari. Mnyama huyo alikuwa na pembe kumi na vichwa saba, akiwa na taji kumi kwenye hizo pembe zake, na juu ya kila kichwa kulikuwa na jina la kukufuru.
REV 13:2 Mnyama yule niliyemwona alifanana na chui, lakini miguu yake ilikuwa kama ya dubu na kichwa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu zake, kiti chake cha utawala na mamlaka makubwa.
REV 13:3 Mojawapo ya vichwa vya huyo mnyama kilikuwa kama kilichokwisha kupata jeraha la mauti, lakini jeraha hilo la mauti likapona. Ulimwengu wote ukashangaa ukamfuata huyo mnyama.
REV 13:4 Watu wakaliabudu lile joka kwa sababu lilikuwa limempa huyo mnyama mamlaka yake, pia wakamwabudu huyo mnyama na kuuliza, “Ni nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana vita naye?”
REV 13:5 Huyo mnyama akapewa mdomo wa kusema maneno ya kiburi na kukufuru, na uwezo wa kutumia mamlaka yake kwa muda wa miezi arobaini na mbili.
REV 13:6 Akafungua kinywa chake ili kumkufuru Mungu, akilitukana Jina lake na mahali aishipo na wale wanaokaa mbinguni.
REV 13:7 Pia akaruhusiwa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda. Akapewa uwezo juu ya watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa.
REV 13:8 Nao watu wote wanaoishi duniani watamwabudu huyo mnyama: wale wote ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
REV 13:9 Yeye aliye na sikio na asikie.
REV 13:10 “Ikiwa mtu ni wa kuchukuliwa mateka, atachukuliwa mateka. Ikiwa mtu ni wa kuuawa kwa upanga, atauawa kwa upanga.” Hapa ndipo penye wito wa subira na imani ya watakatifu.
REV 13:11 Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka.
REV 13:12 Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akaifanya dunia na wote walioishi duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.
REV 13:13 Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi.
REV 13:14 Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya watu walioishi duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi.
REV 13:15 Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa.
REV 13:16 Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye paji la uso wake,
REV 13:17 ili mtu yeyote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake.
REV 13:18 Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na ufahamu na ahesabu tarakimu za huyo mnyama, kwa maana ni tarakimu za kibinadamu. Tarakimu zake ni mia sita sitini na sita (666).
REV 14:1 Kisha nikatazama, na hapo mbele yangu Mwana-Kondoo alikuwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale elfu mia moja na arobaini na nne wenye jina la Mwana-Kondoo na jina la Baba yake limeandikwa kwenye paji za nyuso zao.
REV 14:2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao.
REV 14:3 Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi, na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai, na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao elfu mia moja na arobaini na nne waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani.
REV 14:4 Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.
REV 14:5 Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.
REV 14:6 Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale wanaoishi duniani: kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa.
REV 14:7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”
REV 14:8 Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, mji ule ulioyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”
REV 14:9 Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye paji la uso wake au kwenye mkono wake,
REV 14:10 yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo.
REV 14:11 Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.”
REV 14:12 Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Isa.
REV 14:13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Isa Bwana tangu sasa.” “Naam,” asema Roho wa Mungu, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”
REV 14:14 Nikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa kama Mwana wa Adamu, akiwa na taji la dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake.
REV 14:15 Kisha malaika mwingine akaja kutoka Hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.”
REV 14:16 Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.
REV 14:17 Malaika mwingine akatoka katika Hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali.
REV 14:18 Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.”
REV 14:19 Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu.
REV 14:20 Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi, kwa umbali wa maili mia moja na themanini.
REV 15:1 Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.
REV 15:2 Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.
REV 15:3 Nao wakaimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema: “Bwana Mungu Mwenyezi, matendo yako ni makuu na ya ajabu. Njia zako wewe ni za haki na za kweli, Mfalme wa nyakati zote!
REV 15:4 Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Mwenyezi Mungu na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu. Mataifa yote yatakuja na kuabudu mbele zako, kwa kuwa matendo yako ya haki yamedhihirishwa.”
REV 15:5 Baada ya haya nikatazama, nalo Hekalu la Hema la Ushuhuda lilikuwa limefunguliwa mbinguni.
REV 15:6 Ndani ya lile Hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani iliyong’aa, na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao.
REV 15:7 Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele.
REV 15:8 Nalo lile Hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna yeyote aliyeweza kuingia mle Hekaluni hadi yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.
REV 16:1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”
REV 16:2 Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake.
REV 16:3 Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa.
REV 16:4 Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu.
REV 16:5 Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema: “Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa, wewe uliyeko, uliyekuwako, Uliye Mtakatifu, kwa sababu umehukumu hivyo;
REV 16:6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako na manabii wako, nawe umewapa damu wanywe kama walivyostahili.”
REV 16:7 Nikasikia madhabahu ikiitikia, “Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni kweli na haki.”
REV 16:8 Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua, nalo likapewa nguvu za kuwaunguza watu kwa moto.
REV 16:9 Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu.
REV 16:10 Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha utawala cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu,
REV 16:11 wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu.
REV 16:12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Frati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme kutoka Mashariki.
REV 16:13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.
REV 16:14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.
REV 16:15 “Tazama, naja kama mwizi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.”
REV 16:16 Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Har-Magedoni kwa Kiebrania.
REV 16:17 Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kubwa ikatoka mle Hekaluni katika kile kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha kuwa!”
REV 16:18 Kukawa na miali ya radi, ngurumo, radi na tetemeko kubwa la ardhi. Hapajawahi kuwa na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu awepo duniani, kwani lilikuwa tetemeko kubwa ajabu.
REV 16:19 Ule mji mkubwa ukagawanyika katika sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikaanguka. Mungu akakumbuka Babeli Mkuu na kumpa kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu ya hasira yake.
REV 16:20 Kila kisiwa kikatoweka wala milima haikuonekana.
REV 16:21 Mvua kubwa ya mawe yenye uzito wa talanta moja ikashuka kutoka mbinguni, ikawaangukia wanadamu. Nao wanadamu wakamlaani Mungu kwa ajili ya hayo mapigo ya mvua ya mawe, kwa sababu pigo hilo lilikuwa la kutisha.
REV 17:1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aliyeketi juu ya maji mengi.
REV 17:2 Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu walioishi duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”
REV 17:3 Kisha yule malaika akanichukua katika Roho wa Mungu, akanipeleka jangwani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.
REV 17:4 Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake.
REV 17:5 Kwenye paji lake la uso palikuwa pameandikwa jina la siri: Babeli Mkuu, Mama wa makahaba na wa machukizo ya dunia.
REV 17:6 Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Isa. Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana.
REV 17:7 Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
REV 17:8 Huyo mnyama ambaye ulimwona awali alikuwako, lakini sasa hayuko, naye atapanda kutoka lile Shimo na kwenda kwenye maangamizi yake. Watu wanaoishi duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwako hapo awali, na sasa hayuko, lakini atakuwako baadaye.
REV 17:9 “Hapa ndipo penye wito wa akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia.
REV 17:10 Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, mmoja yupo, mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja atalazimika kukaa kwa muda mfupi.
REV 17:11 Yule mnyama aliyekuwako hapo awali na sasa hayuko, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anaenda kwenye maangamizi yake.
REV 17:12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama.
REV 17:13 Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.
REV 17:14 Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”
REV 17:15 Kisha yule malaika akaniambia, “Yale maji uliyoyaona yule kahaba akiwa ameketi juu yake ni jamaa, makundi ya watu, mataifa na lugha.
REV 17:16 Zile pembe kumi ulizoziona, pamoja na huyo mnyama, watamchukia huyo kahaba, watamfilisi na kumwacha uchi, watamla nyama yake na kumteketeza kwa moto.
REV 17:17 Kwa maana Mungu ameweka mioyoni mwao kutimiza kusudi lake kwa kukubali kumpa yule mnyama mamlaka yao ya utawala hadi maneno ya Mungu yatakapotimia.
REV 17:18 Yule mwanamke uliyemwona ni ule mji mkubwa unaowatawala wafalme wa dunia.”
REV 18:1 Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka kuu na dunia ikaangazwa kwa mng’ao wake.
REV 18:2 Naye akapaza sauti kwa nguvu, akisema: “ ‘Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu!’ Umekuwa makao ya mashetani na makazi ya kila pepo mchafu, makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.
REV 18:3 Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye, na wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”
REV 18:4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “ ‘Tokeni katikati yake, enyi watu wangu,’ ili msije mkashiriki dhambi zake, ili msije mkapatwa na pigo lake lolote;
REV 18:5 kwa kuwa dhambi zake zimefika hadi mbinguni, naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.
REV 18:6 Mtendee kama yeye alivyotenda; umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda. Katika kikombe chake mchanganyie mara mbili ya kile alichochanganya.
REV 18:7 Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na utukufu na anasa alizojipatia. Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema, ‘Mimi ninatawala kama malkia; mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’
REV 18:8 Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja: mauti, maombolezo na njaa. Naye atateketezwa kwa moto, kwa maana Mwenyezi Mungu amhukumuye ana nguvu.
REV 18:9 “Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea.
REV 18:10 Kwa hofu kubwa ya mateso yake, watasimama mbali na kulia na wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, ee Babeli mji wenye nguvu! Hukumu yako imekuja katika saa moja!’
REV 18:11 “Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena:
REV 18:12 Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marumaru,
REV 18:13 bidhaa za mdalasini na vikolezo, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ng’ombe na kondoo; farasi na magari ya vita; na miili na roho za wanadamu.
REV 18:14 “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’
REV 18:15 Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza,
REV 18:16 wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkuu, uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi, ya rangi ya zambarau na nyekundu, ukimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu!
REV 18:17 Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa kama huu umeangamia!’ “Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali.
REV 18:18 Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’
REV 18:19 Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, mji ambao wote wenye meli baharini walitajirika kupitia kwa mali yake! Katika saa moja tu ameangamizwa!’
REV 18:20 “Furahia kwa ajili yake, ee mbingu! Furahini watakatifu, mitume na manabii! Mungu amemhukumu kwa vile alivyowatendea ninyi.”
REV 18:21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia, akalitupa baharini akisema: “Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli utakavyotupwa chini kwa nguvu, wala hautaonekana tena.
REV 18:22 Nyimbo za wapiga vinubi na waimbaji, wapiga filimbi na wapiga tarumbeta kamwe hazitasikika tena ndani yako. Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi mwenye ujuzi wa aina yoyote. Wala sauti ya jiwe la kusagia kamwe haitasikika tena.
REV 18:23 Mwanga wa taa hautaangaza ndani yako tena. Sauti ya bwana arusi na bibi arusi kamwe haitasikika ndani yako tena. Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia. Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.
REV 18:24 Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu, na wote waliouawa duniani.”
REV 19:1 Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipaza sauti na kusema: “Haleluya! Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu,
REV 19:2 kwa maana hukumu zake ni za kweli na za haki. Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake. Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.”
REV 19:3 Wakasema tena kwa sauti kuu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu milele na milele.”
REV 19:4 Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu: “Amen, Haleluya!”
REV 19:5 Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema: “Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!”
REV 19:6 Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipaza sauti na kusema: “Haleluya! Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala.
REV 19:7 Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu! Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia na bibi arusi wake amejiweka tayari.
REV 19:8 Akapewa kitani safi, inayong’aa na nzuri, ili avae.” (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)
REV 19:9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndio maneno ya kweli ya Mungu.”
REV 19:10 Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Isa. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Isa ndio roho ya unabii.”
REV 19:11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita.
REV 19:12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe.
REV 19:13 Amevaa joho lililoloweshwa katika damu, na Jina lake ni Neno la Mungu.
REV 19:14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri.
REV 19:15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenyezi.
REV 19:16 Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili: Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.
REV 19:17 Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, naye akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njooni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu,
REV 19:18 ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo kwa wakubwa.”
REV 19:19 Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda farasi pamoja na jeshi lake.
REV 19:20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo aliyekuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.
REV 19:21 Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda farasi nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.
REV 20:1 Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile Shimo na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
REV 20:2 Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni ibilisi, au Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka elfu.
REV 20:3 Akamtupa katika lile Shimo, akamfunga humo na kulitia muhuri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa hadi hiyo miaka elfu itimie. Baada ya hayo lazima afunguliwe kwa muda mfupi.
REV 20:4 Kisha nikaona viti vya utawala vilivyokuwa vimekaliwa na wale waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Tena nikaona roho za wale waliokatwa vichwa kwa sababu ya ushuhuda wa Isa na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawakuwa wamemsujudu huyo mnyama wala sanamu yake wala hawakupokea ile chapa yake kwenye paji za nyuso zao au kwenye mikono yao. Wakawa hai na kutawala pamoja na Al-Masihi miaka elfu.
REV 20:5 (Wafu waliosalia hawakufufuka hadi ilipotimia hiyo miaka elfu.) Huu ndio ufufuo wa kwanza.
REV 20:6 Waliobarikiwa na walio watakatifu ni wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Hao mauti ya pili haina nguvu juu yao, bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Al-Masihi, nao watatawala pamoja naye kwa muda wa miaka elfu.
REV 20:7 Hiyo miaka elfu itakapotimia, Shetani atafunguliwa atoke kifungoni mwake,
REV 20:8 naye atatoka ili kuyadanganya mataifa yaliyopo katika pembe nne za dunia, yaani Gogu na Magogu apate kuwakusanya tayari kwa vita. Idadi yao ni kama mchanga ulioko pwani.
REV 20:9 Nao walitembea katika eneo lote la dunia, wakaizunguka kambi ya watakatifu na ule mji unaopendwa. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza.
REV 20:10 Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo usiku na mchana, milele na milele.
REV 20:11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana.
REV 20:12 Nami nikawaona wafu, wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu.
REV 20:13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda.
REV 20:14 Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani hilo ziwa la moto.
REV 20:15 Iwapo mtu yeyote jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.
REV 21:1 Kisha nikaona “mbingu mpya na nchi mpya”, kwa maana mbingu ya kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwa na bahari tena.
REV 21:2 Nikauona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.
REV 21:3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
REV 21:4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”
REV 21:5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”
REV 21:6 Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yoyote.
REV 21:7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.
REV 21:8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”
REV 21:9 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonesha bibi arusi, yaani mke wa Mwana-Kondoo.”
REV 21:10 Naye akanichukua katika Roho wa Mungu hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu.
REV 21:11 Ulikuwa uking’aa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo.
REV 21:12 Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli.
REV 21:13 Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi.
REV 21:14 Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na mbili, na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
REV 21:15 Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na ufito wa dhahabu wa kupimia huo mji, malango yake na kuta zake.
REV 21:16 Mji huo ulikuwa mraba, urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Akaupima huo mji kwa huo ufito akakuta una kama stadioni 12,000; urefu wake na upana wake na kwenda juu kwake vilikuwa sawa.
REV 21:17 Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa mia moja na arobaini na nne (144) kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia.
REV 21:18 Ukuta huo ulijengwa kwa yaspi hali mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi, iking’aa kama kioo.
REV 21:19 Misingi ya kuta za mji huo zilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili yakuti samawi, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi,
REV 21:20 wa tano sardoniki, wa sita akiki, wa saba krisolitho, wa nane zabarajadi, wa tisa yakuti manjano, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho, wa kumi na mbili amethisto.
REV 21:21 Yale malango kumi na mbili yalikuwa ni lulu kumi na mbili, kila lango lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji huo ilikuwa ya dhahabu safi iliyong’aa kama kioo.
REV 21:22 Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio Hekalu lake.
REV 21:23 Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake.
REV 21:24 Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake.
REV 21:25 Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo.
REV 21:26 Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo.
REV 21:27 Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.
REV 22:1 Kisha yule malaika akanionesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwa kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo,
REV 22:2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa.
REV 22:3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia,
REV 22:4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye paji za nyuso zao.
REV 22:5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.
REV 22:6 Kisha yule malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli. Mwenyezi Mungu, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake yale ambayo hayana budi kutukia upesi.”
REV 22:7 “Tazama, naja upesi! Amebarikiwa yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”
REV 22:8 Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionesha mambo hayo.
REV 22:9 Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
REV 22:10 Kisha akaniambia, “Usiyafunge maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, kwa sababu wakati umekaribia.
REV 22:11 Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu, yeye atendaye haki na aendelee kutenda haki, na yeye aliye mtakatifu na aendelee kuwa mtakatifu.”
REV 22:12 “Tazama, naja upesi! Thawabu yangu i mkononi mwangu, nami nitampa kila mtu sawasawa na alivyotenda.
REV 22:13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
REV 22:14 “Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake.
REV 22:15 Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.
REV 22:16 “Mimi, Isa, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya jumuiya ya waumini. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi inayong’aa.”
REV 22:17 Roho wa Mungu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.
REV 22:18 Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza humo chochote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
REV 22:19 Kama mtu yeyote akipunguza humo chochote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule Mji Mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
REV 22:20 Yeye anayeshuhudia mambo haya asema, “Hakika, naja upesi!” Amen. Njoo, Bwana Isa.
REV 22:21 Neema ya Bwana Isa iwe na watakatifu wote. Amen.
