﻿Waefeso.
1.
Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa mapenzi ya Mungu. 
Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi. 
Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Al-Masihi. 
Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 
alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kupitia kwa Isa Al-Masihi kwa furaha na mapenzi yake. 
Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. 
Ndani yake tunao ukombozi kupitia kwa damu yake, yaani msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 
aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 
Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Al-Masihi, 
ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Al-Masihi. 
Katika Al-Masihi sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, 
ili, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Al-Masihi, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake. 
Ninyi pia mliingia ndani ya Al-Masihi mliposikia neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Baada ya kuamini, mlitiwa muhuri ndani yake, huyo Roho Mtakatifu wa Mungu mliyeahidiwa, 
yeye ambaye ni amana yetu ya kutuhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu, kwa sifa ya utukufu wake. 
Kwa sababu hii, tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Isa na upendo wenu kwa watakatifu wote, 
sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 
Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 
Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 
na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 
aliyoitumia katika Al-Masihi alipomfufua kutoka kwa wafu, na kumketisha mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho, 
juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 
Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake, na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya jumuiya ya waumini, 
ambayo ni mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote. 
