﻿Sefania.
2.
Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja, enyi taifa lisilo na aibu, 
kabla wakati ulioamriwa haujafika na siku ile inayopeperusha kama makapi, kabla hasira kali ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu, kabla siku ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu. 
Mtafuteni Mwenyezi Mungu, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi, ninyi ambao hufanya lile analoamuru. Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu; labda mtahifadhiwa siku ya hasira ya Mwenyezi Mungu. 
Gaza utaachwa na Ashkeloni utaachwa magofu. Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu, na Ekroni utang’olewa. 
Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari, enyi Wakerethi; neno la Mwenyezi Mungu liko dhidi yenu, ee Kanaani, nchi ya Wafilisti. “Mimi nitawaangamiza, na hakuna atakayebaki.” 
Nchi iliyo karibu na bahari itakuwa malisho yenye visima vya wachungaji, na mazizi ya kondoo. 
Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda, hapo watapata malisho. Wakati wa jioni watajilaza chini katika nyumba za Ashkeloni. Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawatunza, naye atawarudishia wafungwa wao. 
“Nimeyasikia matukano ya Moabu nazo dhihaka za Waamoni, ambao waliwatukana watu wangu na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao. 
Hakika, kama niishivyo,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, “hakika Moabu itakuwa kama Sodoma, Waamoni kama Gomora: mahali pa magugu na mashimo ya chumvi, nchi ya ukiwa milele. Mabaki ya watu wangu watawateka nyara; mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.” 
Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao, kwa kutukana na kudhihaki watu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. 
Mwenyezi Mungu atakuwa wa kuhofisha kwao atakapoangamiza miungu yote ya nchi. Mataifa katika kila pwani yatamwabudu, kila moja katika nchi yake. 
“Ninyi pia, ee Wakushi, mtauawa kwa upanga wangu.” 
Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini na kuangamiza Waashuru, akiiacha Ninawi ukiwa na pakame kama jangwa. 
Makundi ya kondoo na ng’ombe yatajilaza pale, viumbe vya kila aina. Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba wataishi juu ya nguzo zake. Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani, kifusi kitakuwa milangoni, boriti za mwerezi zitaachwa wazi. 
Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha wakijisikia salama. Ulisema moyoni mwako, “Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.” Jinsi gani umekuwa gofu, mahali pa kulala wanyama pori! Wote wanaopita kando yake wanauzomea na kutikisa mkono kwa dharau. 
