﻿Sefania.
1.
 Neno la Mwenyezi Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda: 
Mwenyezi Mungu asema, “Nitafagia kila kitu kutoka uso wa dunia. 
Nitafagilia mbali watu na wanyama; nitafagilia mbali ndege wa angani na samaki wa baharini. Wafanyao maovu watapata tu kokoto, nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,” asema Mwenyezi Mungu. 
“Nitaiadhibu Yuda na wote wanaoishi Yerusalemu. Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali kila mabaki ya Baali, majina ya wapagani na makuhani waabuduo sanamu: 
wale ambao husujudu juu ya mapaa kuabudu jeshi la vitu vya angani, wale ambao husujudu na kuapa kwa Mwenyezi Mungu na ambao pia huapa kwa Malkamu, 
wale wanaoacha kumfuata Mwenyezi Mungu, wala hawamtafuti Mwenyezi Mungu wala kutaka shauri lake. 
Nyamazeni mbele za Bwana Mungu Mwenyezi, kwa maana siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu. Mwenyezi Mungu ameandaa dhabihu, amewaweka wakfu wale aliowaalika. 
Katika siku ya dhabihu ya Mwenyezi Mungu nitawaadhibu wakuu na wana wa mfalme na wale wote wanaovaa nguo za kigeni. 
Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao hukwepa kukanyaga kizingiti, ambao hujaza hekalu la miungu yao kwa dhuluma na udanganyifu.” 
Mwenyezi Mungu asema, “Katika siku hiyo kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki, maombolezo kutoka mtaa wa pili, na mshindo mkubwa kutoka vilimani. 
Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni; wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa, wote ambao wanafanya biashara ya fedha wataangamizwa. 
Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa, na kuwaadhibu wale ambao wanakaa katika hali ya kuridhika, ambao ni kama divai iliyobaki kwenye machicha, ambao hudhani, ‘Mwenyezi Mungu hatafanya lolote, jema au baya.’ 
Utajiri wao utatekwa nyara, nyumba zao zitabomolewa. Watajenga nyumba, lakini hawataishi ndani yake; watapanda mizabibu lakini hawatakunywa divai yake. 
“Siku kubwa ya Mwenyezi Mungu iko karibu: iko karibu na inakuja haraka. Sikilizeni! Kilio katika siku ya Mwenyezi Mungu kitakuwa chungu. Shujaa atapiga ukelele wa vita huko. 
Siku ile ni siku ya ghadhabu, siku ya fadhaa na dhiki, siku ya uharibifu na ukiwa, siku ya giza na utusitusi, siku ya mawingu na giza nene, 
siku ya tarumbeta na kelele za vita dhidi ya miji yenye ngome, na dhidi ya minara mirefu. 
Nitawaletea watu dhiki, nao watatembea kama vipofu, kwa sababu wametenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu. Damu yao itamwagwa kama vumbi na matumbo yao kama kinyesi. 
Fedha yao wala dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Katika moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa, kwa maana ghafula ataleta mwisho wa wote wanaoishi duniani.” 
