﻿Mika.
6.
Sikiliza asemalo Mwenyezi Mungu: “Simama, jitetee mbele ya milima; vilima na visikie lile unalotaka kusema. 
“Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya Mwenyezi Mungu, sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ana shauri dhidi ya watu wake; anatoa mashtaka dhidi ya Israeli. 
“Watu wangu, nimewatendea nini? Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu. 
Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa. Nilimtuma Musa awaongoze, pia Haruni na Miriamu. 
Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu alivyofanya shauri na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu. Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu hadi Gilgali, ili mfahamu matendo ya haki ya Mwenyezi Mungu.” 
Nimjie Mwenyezi Mungu na kitu gani na kusujudu mbele za Mungu aliyetukuka? Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa, nije na ndama za mwaka mmoja? 
Je, Mwenyezi Mungu atafurahishwa na kondoo dume elfu, au mito elfu kumi ya mafuta? Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, mtoto wangu mwenyewe kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu? 
Amekuonesha yaliyo mema, ee mwanadamu. Mwenyezi Mungu anataka nini kwako? Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako. 
Sikiliza! Mwenyezi Mungu anauita mji: kulicha jina lako ni hekima: “Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru. 
Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu, hazina yako uliyopata kwa udanganyifu na vipimo vilivyopunguka, ambavyo vimelaaniwa? 
Je, naweza kuhukumu kuwa mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia, aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo? 
Matajiri wake ni wajeuri; watu wake ni waongo na ndimi zao zinazungumza kwa udanganyifu. 
Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu, kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu. 
Mtakula lakini hamtashiba; tumbo zenu bado zitakuwa tupu. Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote, kwa sababu mtakachoweka akiba nitatoa kwa upanga. 
Mtapanda lakini hamtavuna; mtakamua zeituni lakini hamtatumia mafuta yake. Mtakamua zabibu lakini hamtakunywa hiyo divai. 
Mmezishika sheria za Omri na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, tena umefuata desturi zao. Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi na watu wako kuwa dhihaka; mtachukua dharau za mataifa.” 
