﻿Mika.
4.
Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la Mwenyezi Mungu utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote; utainuliwa juu ya vilima, na watu wa mataifa watamiminika humo. 
Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Torati itatoka Sayuni, neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu. 
Atahukumu kati ya mataifa mengi, na ataamua migogoro ya mataifa yenye nguvu na yaliyo mbali. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena. 
Kila mtu ataketi chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakuna mtu atakayewaogopesha, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amesema. 
Mataifa yote yanaweza kutembea katika jina la miungu yao; sisi tutatembea katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wetu milele na milele. 
“Katika siku hiyo,” asema Mwenyezi Mungu, “nitawakusanya walemavu; nitawakusanya walio uhamishoni na wale niliowahuzunisha. 
Nitawafanya walemavu kuwa mabaki, wale waliofukuzwa kuwa taifa lenye nguvu. Mwenyezi Mungu atawatawala katika Mlima Sayuni kuanzia siku hiyo na hata milele. 
Lakini kwako wewe, ee mnara wa ulinzi wa kundi, ee ngome ya Binti Sayuni, milki ya awali itarudishwa kwako, ufalme utakuja kwa Binti Yerusalemu.” 
Kwa nini sasa unalia kwa nguvu: kwani huna mfalme? Je, mshauri wako amekufa, hata maumivu yakukamate kama ya mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa? 
Gaagaa kwa uchungu, ee Binti Sayuni, kama mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa, kwa kuwa sasa ni lazima uuache mji ukapige kambi uwanjani. Utaenda Babeli; huko utaokolewa. Huko Mwenyezi Mungu atakukomboa kutoka mikononi mwa adui zako. 
Lakini sasa mataifa mengi yamekusanyika dhidi yako. Wanasema, “Mwache anajisiwe, macho yetu na yatazame Sayuni kwa furaha!” 
Lakini hawayajui mawazo ya Mwenyezi Mungu; hawauelewi mpango wake, yeye awakusanyaye kama miganda kwenye sakafu ya kupuria. 
“Inuka upure, ee Binti Sayuni, kwa kuwa nitakupa pembe za chuma; nitakupa kwato za shaba na utavunja vipande vipande mataifa mengi.” Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa Mwenyezi Mungu, utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote. 
