﻿Amosi.
1.
Maneno ya Amosi, mmoja wa wachungaji wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli. 
Alisema: “Mwenyezi Mungu ananguruma toka Sayuni, pia ananguruma kutoka Yerusalemu; malisho ya wachungaji yanakauka, kilele cha Karmeli kinanyauka.” 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Dameski, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliipura Gileadi kwa vyombo vya chuma vyenye meno. 
Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi. 
Nitalivunja lango la Dameski; nitamwangamiza mfalme aliye katika Bonde la Aveni, na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni. Watu wote wa Aramu wataenda uhamishoni huko Kiri,” asema Mwenyezi Mungu. 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Gaza, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima na kuwauza kwa Edomu, 
nitatuma moto juu ya kuta za Gaza ambao utateketeza ngome zake. 
Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni. Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni, hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,” asema Bwana Mungu Mwenyezi. 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Tiro, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu, na kutokujali mapatano ya undugu, 
Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro ambao utateketeza ngome zake.” 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Edomu, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, alikataa kuonesha huruma yoyote, kwa sababu hasira yake kali iliendelea kupanda wakati wote na ghadhabu iliwaka bila kuzuiliwa. 
Nitatuma moto juu ya Temani ambao utateketeza ngome za Bosra.” 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Amoni, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliwatumbua wanawake wajawazito wa Gileadi ili kuongeza mipaka yake. 
Nitatuma moto kwenye kuta za Raba ambao utateketeza ngome zake katikati ya kelele za vita katika siku ya mapigano, katikati ya upepo mkali katika siku ya dhoruba. 
Mfalme wake ataenda uhamishoni, yeye pamoja na maafisa wake,” asema Mwenyezi Mungu. 
