﻿Hosea.
8.
“Wekeni tarumbeta midomoni mwenu! Tai yuko juu ya nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa sababu watu wamevunja agano langu, wameasi dhidi ya sheria yangu. 
Israeli ananililia, ‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’ 
Lakini Israeli amekataa lile lililo jema, adui atamfuatia. 
Wanaweka wafalme bila idhini yangu, wamechagua wakuu bila kibali changu. Kwa fedha zao na dhahabu wamejitengenezea sanamu kwa ajili ya maangamizi yao wenyewe. 
Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama! Hasira yangu inawaka dhidi yao. Watakuwa najisi hadi lini? 
Zimetoka katika Israeli! Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu. Atavunjwa vipande vipande, yule ndama wa Samaria. 
“Wanapanda upepo na kuvuna kisulisuli. Bua halina suke, halitatoa unga. Kama lingetoa nafaka, wageni wangeila yote. 
Israeli amemezwa; sasa yupo miongoni mwa mataifa kama kitu kisicho na thamani. 
Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake. Efraimu amejiuza mwenyewe kwa wapenzi. 
Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa, sasa nitawakusanya pamoja. Wataanza kudhoofika chini ya uonevu wa mfalme mwenye nguvu. 
“Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi kwa ajili ya sadaka za dhambi, hizi zimekuwa madhabahu za kufanyia dhambi. 
Niliwaandikia mambo mengi yaliyohusu sheria yangu, lakini waliziangalia kama kitu kigeni. 
Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi nao wanakula hiyo nyama, lakini Mwenyezi Mungu hapendezwi nao. Sasa ataukumbuka uovu wao na kuadhibu dhambi zao: Watarudi Misri. 
Israeli amemsahau Muumba wake na kujenga majumba ya kifalme, Yuda amejengea miji mingi ngome. Lakini nitatuma moto kwenye miji yao utakaoteketeza ngome zao.” 
