﻿Hosea.
5.
“Sikieni hili, enyi makuhani! Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli! Sikieni, ee nyumba ya mfalme! Hukumu hii ni dhidi yenu: Mmekuwa mtego huko Mispa, wavu uliotandwa juu ya Tabori. 
Waasi wamezidisha sana mauaji. Mimi nitawatiisha wote. 
Ninajua yote kuhusu Efraimu, Israeli hukufichika kwangu. Efraimu, sasa umegeukia ukahaba, Israeli amenajisika. 
“Matendo yao hayawaachii kurudi kwa Mungu wao. Roho ya ukahaba iko ndani ya mioyo yao, hawamkubali Mwenyezi Mungu. 
Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao; Waisraeli, hata Efraimu, wanajikwaa katika dhambi zao; pia Yuda atajikwaa pamoja nao. 
Wanapoenda na makundi yao ya kondoo na ng’ombe kumtafuta Mwenyezi Mungu, hawatampata; yeye amejiondoa kutoka kwao. 
Wao si waaminifu kwa Mwenyezi Mungu; wamezaa watoto haramu. Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi zitawaangamiza wao pamoja na mashamba yao. 
“Pigeni tarumbeta huko Gibea, na baragumu huko Rama. Pazeni kelele za vita huko Beth-Aveni; ongoza, ee Benyamini. 
Efraimu ataachwa ukiwa katika siku ya kuadhibiwa. Miongoni mwa makabila ya Israeli ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia. 
Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaosogeza mawe ya mpaka. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama mafuriko ya maji. 
Efraimu amedhulumiwa, amekanyagwa katika hukumu kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu. 
Mimi ni kama nondo kwa Efraimu, na kama uozo kwa watu wa Yuda. 
“Efraimu alipoona ugonjwa wake, naye Yuda vidonda vyake, ndipo Efraimu aligeukia Ashuru, na kuomba msaada kwa mfalme mkuu. Lakini hawezi kukuponya, hawezi kukuponya vidonda vyako. 
Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu, kama simba mkubwa kwa Yuda. Nitawararua vipande vipande na kuondoka; nitawachukua mbali, na hakuna wa kuwaokoa. 
Kisha nitarudi mahali pangu hadi watakapokubali kosa lao. Nao watautafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.” 
