﻿Hosea.
4.
Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi Waisraeli, kwa sababu Mwenyezi Mungu analo shtaka dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi: “Hakuna uaminifu, hakuna upendo, hakuna kumjua Mungu katika nchi. 
Kuna kulaani tu, uongo na uuaji, wizi na uzinzi, bila kuwa na mipaka, nao umwagaji damu mmoja baada ya mwingine. 
Kwa sababu hii nchi huomboleza, wote wanaoishi ndani yake wanadhoofika; wanyama wa kondeni, ndege wa angani na samaki wa baharini wanakufa. 
“Lakini mtu yeyote na asilete shtaka, mtu yeyote na asimlaumu mwenzake, kwa maana watu wako ni kama wale waletao mashtaka dhidi ya kuhani. 
Unajikwaa usiku na mchana, nao manabii hujikwaa pamoja nawe. Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako: 
watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. “Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeacha kuijali Torati ya Mungu wako mimi nami sitawajali watoto wako. 
Kadiri makuhani walivyoongezeka, ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu, walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu. 
Wanajilisha dhambi za watu wangu na kupendezwa na uovu wao. 
Hata itakuwa: Kama walivyo watu, ndivyo walivyo makuhani. Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao na kuwalipa kwa matendo yao. 
“Watakula lakini hawatashiba; watajiingiza katika ukahaba lakini hawataongezeka, kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu na kujiingiza wenyewe 
katika ukahaba; kunywa divai ya zamani na divai mpya huondoa ufahamu 
wa watu wangu. Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti nao hujibiwa na fimbo ya mti. Roho ya ukahaba imewapotosha, hawana uaminifu kwa Mungu wao. 
Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima, chini ya mialoni, milibua na miela, ambako kuna vivuli vizuri. Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba na wake za wana wenu uzinzi. 
“Sitawaadhibu binti zenu wakati wanapogeukia ukahaba, wala wake za wana wenu wanapofanya uzinzi, kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya na kutambikia pamoja na makahaba wa mahali pa ibada za sanamu: watu wasiokuwa na ufahamu wataangamia! 
“Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli, Yuda naye asije akawa na hatia. “Usiende Gilgali, usipande kwenda Beth-Aveni. Wala usiape, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo!’ 
Waisraeli ni wakaidi, kama ndama jike mkaidi. Ni jinsi gani basi Mwenyezi Mungu anaweza kuwachunga kama wana-kondoo katika shamba la majani? 
Efraimu amejiunga na sanamu, achana naye! 
Hata wakati wamemaliza vileo vyao wanaendelea na ukahaba wao, watawala wao hupenda sana njia za aibu. 
Kisulisuli kitawafagilia mbali na dhabihu zao zitawaletea aibu. 
