﻿Yeremia.
47.
Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza: 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini, yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana. Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyo ndani yake, miji na wanaoishi ndani yake. Watu watapiga kelele; wote wanaoishi katika nchi wataomboleza 
kwa sauti ya kwato za farasi wanaoenda mbio, kwa sauti ya magari ya vita ya adui, na mngurumo wa magurudumu yake. Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao, mikono yao italegea. 
Kwa maana siku imewadia kuwaangamiza Wafilisti wote na kuwakatilia mbali walionusurika wote ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni. Mwenyezi Mungu anakaribia kuwaangamiza Wafilisti, mabaki toka pwani za Kaftori. 
Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza, Ashkeloni atanyamazishwa. Enyi mabaki kwenye tambarare, mtajikatakata wenyewe hadi lini? 
“Mnalia, ‘Aa, upanga wa Mwenyezi Mungu, utaendelea hadi lini ndipo upumzike? Rudi ndani ya ala yako; acha na utulie.’ 
Lakini upanga utatuliaje wakati Mwenyezi Mungu ameuamuru, wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni pamoja na pwani yake?” 
