﻿Yeremia.
13.
Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.” 
Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama Mwenyezi Mungu alivyoniagiza, nikajivika kiunoni. 
Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kwa mara ya pili: 
“Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.” 
Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama Mwenyezi Mungu alivyoniamuru. 
Baada ya siku nyingi Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.” 
Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa. 
Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia: 
“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu. 
Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine wakiitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mshipi huu ambao haufai kabisa! 
Kwa maana kama vile mshipi ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyoifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’ 
“Waambie: ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’ 
Uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: nitawajaza ulevi wote wanaoishi katika nchi hii, pamoja na wafalme wanaoketi kwenye kiti cha ufalme cha Daudi, makuhani, manabii na wakaaji wote wa Yerusalemu. 
Nitawagombanisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema Mwenyezi Mungu. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ” 
Sikieni na mzingatie, msiwe na kiburi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenena. 
Mpeni utukufu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, kabla miguu yenu haijajikwaa juu ya vilima vitakavyotiwa giza. Mlitarajia nuru, lakini ataifanya kuwa giza nene na kuibadili kuwa huzuni kubwa. 
Lakini kama hamtasikiliza, nitalia sirini kwa ajili ya kiburi chenu; macho yangu yatalia kwa uchungu, yakitiririka machozi, kwa sababu kundi la kondoo la Mwenyezi Mungu litachukuliwa mateka. 
Mwambie mfalme na mama malkia, “Shukeni kutoka viti vyenu vya utawala, kwa kuwa taji zenu za utukufu zitaanguka kutoka vichwani mwenu.” 
Miji ya Negebu itafungwa, wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua. Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni, wakichukuliwa kabisa waende mbali. 
Inua macho yako uone wale wanaokuja kutoka kaskazini. Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa, wale kondoo uliojivunia? 
Utasema nini Mwenyezi Mungu atakapowaweka juu yako wale ulioungana nao kama rafiki zako maalum? Je, hutapatwa na uchungu kama mwanamke aliye katika uchungu wa kuzaa? 
Nawe ukijiuliza, “Kwa nini haya yamenitokea?” Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi marinda yako yameraruliwa na mwili wako umetendewa vibaya. 
Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake au chui kubadili madoadoa yake? Vivyo hivyo, wewe uliyezoea kutenda mabaya huwezi kufanya mema. 
“Nitawatawanya kama makapi yapeperushwayo na upepo wa jangwani. 
Hii ndiyo kura yako, fungu nililokuamulia,” asema Mwenyezi Mungu, “kwa sababu umenisahau mimi na kuamini miungu ya uongo. 
Nitayafunua marinda yako juu ya uso wako ili aibu yako ionekane, 
yaani uzinzi wako na kulia kwako kulikojaa tamaa kama farasi, na ukahaba wako usio na aibu! Nimeyaona matendo yako ya machukizo juu ya vilima na mashambani. Ole wako, ee Yerusalemu! Utaendelea kuwa najisi hadi lini?” 
