﻿Yeremia.
2.
Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia kusema, 
“Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu: “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako, jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi na kunifuata katika jangwa lile lote, katika nchi isiyopandwa mbegu. 
Israeli alikuwa mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu, kama malimbuko ya kwanza ya mavuno yake; wote waliomwangamiza walihesabiwa kuwa na hatia, nayo maafa yaliwakumba,’ ” asema Mwenyezi Mungu. 
Sikia neno la Mwenyezi Mungu, ee nyumba ya Yakobo, nanyi nyote jamaa za nyumba ya Israeli. 
Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: “Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu, hata wakatangatanga mbali nami hivyo? Walifuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili. 
Hawakuuliza, ‘Yuko wapi Mwenyezi Mungu, aliyetupandisha kutoka Misri na kutuongoza kupitia nyika kame, kupitia nchi ya majangwa na mabonde, nchi ya ukame na giza, nchi ambayo hakuna mtu asafiriye ndani yake wala hakuna mtu aishiye humo?’ 
Niliwaleta katika nchi yenye wingi wa vitu ili mpate kula matunda yake na utajiri wa mazao yake. Lakini mkaja na kuinajisi nchi yangu, na kuufanya urithi wangu chukizo. 
Makuhani hawakuuliza, ‘Yuko wapi Mwenyezi Mungu?’ Wale wanaoshughulikia sheria hawakunijua mimi; viongozi waliasi dhidi yangu. Manabii walitabiri kwa jina la Baali, wakifuata sanamu batili. 
“Kwa hiyo naleta tena mashtaka dhidi yako,” asema Mwenyezi Mungu. “Nami nitaleta mashtaka dhidi ya watoto wa watoto wako. 
Vuka, nenda ng’ambo hadi pwani ya Kitimu nawe uangalie, tuma watu waende Kedari, wachunguze kwa makini, uone kama kumeshawahi kuwa kitu kama hiki. 
Je, taifa limebadili miungu yake wakati wowote? (Hata ingawa hao si miungu kamwe.) Lakini watu wangu wamebadili Utukufu wao kwa sanamu batili. 
Shangaeni katika hili, ee mbingu, nanyi tetemekeni kwa hofu kuu,” asema Mwenyezi Mungu. 
“Watu wangu wametenda dhambi mbili: Wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji yaliyo hai, nao wamejichimbia visima vyao wenyewe, visima vilivyobomoka, visivyoweza kuhifadhi maji. 
Je, Israeli ni mtumishi, yaani mtumwa kwa kuzaliwa? Kwa nini basi amekuwa mateka? 
Simba wamenguruma; wamemngurumia. Wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketezwa, nayo imeachwa haina watu. 
Pia watu wa Memfisi na Tapanesi wamekupiga fuvu la kichwa. 
Je, hukujiletea hili wewe mwenyewe kwa kumwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wako alipowaongoza njiani? 
Sasa kwa nini uende Misri kunywa maji ya Shihori? Nawe kwa nini kwenda Ashuru kunywa maji ya Mto? 
Uovu wako utakuadhibu; kurudi nyuma kwako kutakukemea. Basi kumbuka, utambue jinsi lilivyo jambo ovu na chungu kwako unapomwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kutokuwa na hofu yangu,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. 
“Zamani nilivunja nira yako na kukatilia mbali vifungo vyako; ukasema, ‘Sitakutumikia!’ Hakika, kwenye kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda matawi yake ulijilaza kama kahaba. 
Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana, mkamilifu na wa mbegu nzuri. Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami, ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu? 
Hata ujisafishe kwa magadi na kutumia sabuni nyingi, bado doa la hatia yako liko mbele zangu,” asema Bwana Mungu Mwenyezi. 
“Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi, sijawafuata Mabaali’? Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni; fikiri uliyoyafanya. Wewe ni ngamia jike mwenye mbio ukikimbia hapa na pale, 
punda-mwitu aliyezoea jangwa, anayenusa upepo katika tamaa yake kubwa: wakati wake wa kuhitaji mbegu ni nani awezaye kumzuia? Madume yoyote yanayomfuatilia hayana haja ya kujichosha; wakati wa kupandwa kwake yatampata tu. 
Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu, na koo lako liwe limekauka. Lakini ulisema, ‘Haina maana! Ninaipenda miungu ya kigeni, nami lazima niifuatie.’ 
“Kama vile mwizi anavyoaibika akikamatwa, hivyo ndivyo nyumba ya Israeli inavyoaibishwa: wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao. 
Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’ nalo jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’ Wamenipa visogo vyao wala hawakunigeuzia nyuso zao; lakini wakiwa katika taabu, wanasema, ‘Njoo utuokoe!’ 
Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea? Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa wakati mko katika taabu! Kwa maana mna miungu mingi kama mlivyo na miji, ee Yuda. 
“Kwa nini mnaleta mashtaka dhidi yangu? Ninyi nyote mmeniasi,” asema Mwenyezi Mungu. 
“Nimeadhibu watu wako bure tu, hawakujirekebisha. Upanga wako umewala manabii wako kama simba mwenye njaa. 
“Enyi wa kizazi hiki, tafakarini neno la Mwenyezi Mungu: “Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli au nchi ya giza nene? Kwa nini watu wangu wanasema, ‘Sisi tuko huru kuzurura, hatutarudi kwako tena’? 
Je, mwanamwali husahau vito vyake, au bibi arusi mapambo yake ya arusi? Lakini watu wangu wamenisahau mimi, tena kwa siku zisizo na hesabu. 
Je, wewe una ustadi kiasi gani katika kufuatia mapenzi! Hata wale wanawake wabaya kuliko wote wanaweza kujifunza kutokana na njia zako. 
Katika nguo zako watu huona damu ya uhai ya maskini wasio na hatia, ingawa hukuwakamata wakivunja nyumba. Lakini katika haya yote 
unasema, ‘Sina hatia; Mungu hajanikasirikia.’ Lakini nitakuhukumu kwa sababu unasema, ‘Mimi sijatenda dhambi.’ 
Kwa nini unatangatanga sana, ukibadili njia zako? Utakatishwa tamaa na Misri kama ulivyokatishwa na Ashuru. 
Pia utaondoka mahali hapo ukiwa umeweka mikono kichwani, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewakataa wale unaowatumainia; hutasaidiwa nao. 
