﻿Isaya.
52.
Amka, amka, ee Sayuni, jivike nguvu. Vaa mavazi yako ya fahari, ee Yerusalemu, mji mtakatifu. Asiyetahiriwa na aliye najisi hataingia kwako tena. 
Jikung’ute mavumbi yako, inuka, uketi kwenye kiti cha utawala, ee Yerusalemu. Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako, ee Binti Sayuni uliye mateka. 
Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Mliuzwa pasipo malipo, nanyi mtakombolewa bila fedha.” 
Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi, hatimaye, Ashuru wakawadhulumu. 
“Basi sasa nina nini hapa?” asema Mwenyezi Mungu. “Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo, nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,” asema Mwenyezi Mungu. “Mchana kutwa jina langu limetukanwa bila kikomo. 
Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu; kwa hiyo katika siku ile watajua kwamba ndimi niliyetangulia kulisema. Naam, ni mimi.” 
Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema ilivyo mizuri juu ya milima, wale wanaotangaza amani, wanaoleta habari njema, wanaotangaza wokovu, wauambiao Sayuni, “Mungu wako anatawala!” 
Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao, pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha. Mwenyezi Mungu atakaporejea Sayuni, wataliona kwa macho yao wenyewe. 
Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja, enyi magofu ya Yerusalemu, kwa maana Mwenyezi Mungu amewafariji watu wake, ameikomboa Yerusalemu. 
Mkono mtakatifu wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa machoni pa mataifa yote, nayo miisho yote ya dunia itaona wokovu wa Mungu wetu. 
Ondokeni, ondokeni, tokeni huko! Msiguse kitu chochote kilicho najisi! Tokeni kati yake mwe safi, ninyi mchukuao vyombo vya Mwenyezi Mungu. 
Lakini hamtaondoka kwa haraka, wala hamtaenda kwa kukimbia; kwa maana Mwenyezi Mungu atatangulia mbele yenu, Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu. 
Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima; atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana. 
Kama walivyokuwa wengi walioshangazwa naye, kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote na umbo lake kuharibiwa zaidi ya mfano wa mwanadamu: 
hivyo atayashangaza mataifa mengi, nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake. Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona, nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu. 
