﻿Isaya.
30.
Mwenyezi Mungu asema, “Ole kwa watoto wakaidi, kwa wale wanaotimiza mipango ambayo si yangu, wakifanya makubaliano, lakini si kwa Roho wangu Mtakatifu, wakilundika dhambi juu ya dhambi, 
wale wanaoshuka kwenda Misri bila kutaka ushauri wangu, wanaotafuta msaada wa ulinzi wa Farao, wanaotafuta kivuli cha Misri kiwe kimbilio. 
Lakini ulinzi wa Farao utakuwa kwa aibu yenu, kivuli cha Misri kitawaletea fedheha. 
Ingawa wana maafisa katika Soani na wajumbe wamewasili katika Hanesi, 
kila mmoja ataaibishwa kwa sababu ya taifa lisilowafaa kitu, ambalo haliwaletei msaada wala faida, bali aibu tu na fedheha.” 
Neno la unabii kuhusu wanyama wa Negebu: Katika nchi ya taabu na shida, ya simba za dume na jike, ya nyoka mwenye sumu kali na nyoka warukao, wajumbe huchukua utajiri wao juu ya migongo ya punda, hazina zao juu ya nundu za ngamia, kwa lile taifa lisilokuwa na faida, 
kuvipeleka Misri, ambaye msaada wake haufai kabisa. Kwa hiyo nimemwita “Rahabu Asiyefanya Chochote.” 
Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo. 
Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya Mwenyezi Mungu. 
Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo. 
Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!” 
Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu, 
dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, mara moja. 
Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo ukipasuka pasipo huruma ambapo katika vipande vyake hakuna kipande kitakachopatikana kwa kuukulia makaa kutoka jikoni au kuchotea maji kisimani.” 
Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo: “Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu, katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu, lakini hamkutaka. 
Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’ Kwa hiyo mtakimbia! Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi wanaoenda kasi.’ Kwa hiyo wanaowafukuza wataenda kasi! 
Watu elfu moja watakimbia kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja, kwa vitishio vya watu watano wote mtakimbia, hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera juu ya kilele cha mlima, kama bendera juu ya kilima.” 
Hata hivyo Mwenyezi Mungu anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonesha huruma. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye! 
Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. 
Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. 
Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” 
Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!” 
Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ng’ombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. 
Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. 
Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana. 
Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utang’aa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati Mwenyezi Mungu atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia. 
Tazama, Jina la Mwenyezi Mungu linakuja kutoka mbali, likiwa na hasira kali inayowaka pamoja na wingu zito la moshi, midomo yake imejaa ghadhabu na ulimi wake ni moto ulao. 
Pumzi yake ni kama mkondo wa maji yaendayo kasi, yakipanda hadi shingoni. Hutikisa mataifa katika chujio ya uharibifu, huweka lijamu katika mataya ya mataifa ambayo huwaongoza upotevuni. 
Nanyi mtaimba kama usiku ule mnaadhimisha sikukuu takatifu. Mioyo yenu itashangilia kama vile watu wanapokwea na filimbi kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu, kwa Mwamba wa Israeli. 
Mwenyezi Mungu atawasababisha watu waisikie sauti yake ya utukufu, naye atawafanya wauone mkono wake ukishuka pamoja na hasira yake kali na moto ulao, kukiwa na tufani ya mvua, ngurumo za radi na mvua ya mawe. 
Sauti ya Mwenyezi Mungu itaivunjavunja Ashuru, kwa fimbo yake ya utawala atawapiga. 
Kila pigo Mwenyezi Mungu atakaloliweka juu yao kwa fimbo yake ya kuadhibu, litakuwa kwa wimbo wa matari na vinubi, anapopigana nao katika vita kwa mapigo ya mkono wake. 
Tofethi pameandaliwa toka zamani, pamewekwa tayari kwa ajili ya mfalme. Shimo lake la moto limetengenezwa kwa kina kirefu na kwa upana mkubwa, likiwa na moto na kuni tele; pumzi ya Mwenyezi Mungu, kama kijito cha kiberiti, huuwasha moto. 
