﻿Wimbo.
6.
Mpenzi wako ameenda wapi, ewe mzuri kupita wanawake wote? Mpenzi wako amegeukia njia ipi, tupate kumtafuta pamoja nawe? 
Mpenzi wangu ameenda bustanini mwake, kwenye vitalu vya vikolezo, kujilisha bustanini na kukusanya yungiyungi. 
Mimi ni wake mpenzi wangu, na mpenzi wangu ni wangu; yeye hujilisha kati ya yungiyungi. 
Wewe ni mzuri, mpendwa wangu, kama Tirsa, unapendeza kama Yerusalemu, umetukuka kama jeshi lenye bendera. 
Uyageuze macho yako mbali nami; yananigharikisha. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi wanaoteremka kutoka Gileadi. 
Meno yako ni kama kundi la kondoo wanaotoka kuogeshwa. Kila mmoja ana pacha lake, hakuna hata mmoja aliye peke yake. 
Mashavu yako nyuma ya shela yako ni kama vipande viwili vya komamanga. 
Panaweza kuwa na malkia sitini, masuria themanini, na mabikira wasiohesabika; 
lakini hua wangu, mkamilifu wangu, ni wa namna ya pekee, binti pekee kwa mama yake, kipenzi cha yeye aliyemzaa. Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa; malkia na masuria walimsifu. 
Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko, mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua, ametukuka kama nyota zinazofuatana? 
Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi ili kutazama machipuko ya bondeni, kuona kama mizabibu imechipua au kama mikomamanga imechanua maua. 
Kabla sijang’amua, shauku yangu iliniweka katikati ya magari ya vita ya wakuu wangu. 
Rudi, rudi, ee Mshulami; rudi, rudi ili tupate kukutazama! Mpenzi Kwa nini kumtazama Mshulami, kama kutazama ngoma ya Mahanaimu? 
