﻿Zaburi.
144.
Zaburi ya Daudi. Ahimidiwe Mwenyezi Mungu Mwamba wangu, aifundishaye mikono yangu vita, na vidole vyangu kupigana. 
Yeye ni Mungu wangu wa upendo na ulinzi wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, ngao yangu, ninayemkimbilia, ambaye huwatiisha mataifa chini yangu. 
Ee Mwenyezi Mungu, mwanadamu ni nini hata umjali, Binadamu ni nini hata umfikirie? 
Mwanadamu ni kama pumzi, siku zake ni kama kivuli kinachopita. 
Ee Mwenyezi Mungu, pasua mbingu zako, ushuke, gusa milima ili itoe moshi. 
Peleka umeme uwatawanye adui, lenga mishale yako uwashinde. 
Nyoosha mkono wako kutoka juu, nikomboe na kuniokoa kutoka maji makuu, kutoka mikononi mwa wageni 
ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. 
Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia, 
kwa Yule awapaye wafalme ushindi, ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake, kutokana na upanga hatari. 
Nikomboe na uniokoe kutoka mikononi mwa wageni ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. 
Kisha wana wetu wakati wa ujana wao watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri, binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa kurembesha jumba la kifalme. 
Ghala zetu zitajazwa aina zote za mahitaji. Kondoo wetu watazaa kwa maelfu, kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu; 
maksai wetu watakokota mizigo mizito. Hakutakuwa na kubomoka kuta, hakuna kuchukuliwa mateka, wala kilio cha taabu katika barabara zetu. 
Heri watu ambao hili ni kweli; heri wale ambao Mwenyezi Mungu ni Mungu wao. 
