﻿Zaburi.
125.
Wimbo wa kwenda juu. Wale wamtumainio Mwenyezi Mungu ni kama Mlima Sayuni, ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele. 
Kama milima inavyozunguka Yerusalemu, ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowazunguka watu wake sasa na hata milele. 
Fimbo ya waovu haitadumu juu ya nchi waliyopewa wenye haki, ili wenye haki wasije wakatumia mikono yao kutenda ubaya. 
Ee Mwenyezi Mungu, watendee mema walio wema, wale walio wanyofu wa moyo. 
Bali wale wanaogeukia njia zilizopotoka, Mwenyezi Mungu atawafukuza pamoja na watenda maovu. Amani iwe juu ya Israeli. 
