﻿Zaburi.
119.
Heri wale walio waadilifu katika njia zao, wanaoenenda katika Torati ya Mwenyezi Mungu. 
Heri wale wanaozishika shuhuda zake, wanaomtafuta kwa moyo wao wote. 
Wasiofanya lolote lililo baya, wanaoenenda katika njia zake. 
Umetoa maagizo yako ili tuyatii kwa ukamilifu. 
Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara katika kuyatii maagizo yako! 
Hivyo mimi sitaaibishwa ninapozingatia amri zako zote. 
Nitakusifu kwa moyo mnyofu ninapojifunza sheria zako za haki. 
Nitayatii maagizo yako; usiniache kabisa. 
Kijana aisafishe njia yake jinsi gani? Ni kwa kutii, akilifuata neno lako. 
Ninakutafuta kwa moyo wangu wote, usiniache niende mbali na amri zako. 
Nimelificha neno lako moyoni mwangu ili nisikutende dhambi. 
Uhimidiwe, Ee Mwenyezi Mungu; nifundishe maagizo yako. 
Kwa midomo yangu nitasimulia sheria zote zinazotoka katika kinywa chako. 
Ninafurahia kufuata sheria zako kama mtu afurahiaye mali nyingi. 
Ninatafakari maagizo yako na kuziangalia njia zako. 
Ninafurahia maagizo yako, wala sitalipuuza neno lako. 
Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi; nitalitii neno lako. 
Yafungue macho yangu nipate kuona mambo ya ajabu katika sheria yako. 
Mimi ni mgeni duniani, usinifiche amri zako. 
Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa kwa sheria zako wakati wote. 
Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa, wanaoenda mbali na amri zako. 
Niondolee dharau na dhihaka, kwa kuwa ninazishika sheria zako. 
Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako. 
Sheria zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu. 
Nimelazwa chini mavumbini, yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. 
Nilikueleza njia zangu ukanijibu, nifundishe sheria zako. 
Nijulishe mafundisho ya mausia yako, nami nitatafakari maajabu yako. 
Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni, uniimarishe sawasawa na neno lako. 
Niepushe na njia za udanganyifu, kwa neema unifundishe sheria zako. 
Nimechagua njia ya kweli, nimekaza moyo wangu katika sheria zako. 
Nimeng’ang’ania sheria zako, Ee Mwenyezi Mungu, usiniache niaibishwe. 
Nakimbilia katika njia ya maagizo yako, kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru. 
Ee Mwenyezi Mungu, nifundishe kuyafuata maagizo yako, nami nitayashika hadi mwisho. 
Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako na kuitii kwa moyo wangu wote. 
Niongoze kwenye njia ya amri zako, kwa kuwa huko napata furaha. 
Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi. 
Geuza macho yangu kutoka mambo yasiyofaa, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. 
Mtimizie mtumishi wako ahadi yako, ili upate kuogopwa. 
Niondolee aibu ninayoiogopa, kwa kuwa sheria zako ni njema. 
Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako! Hifadhi maisha yangu katika haki yako. 
Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako usiokoma unijie, wokovu wako sawasawa na ahadi yako, 
ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki, kwa kuwa ninalitumainia neno lako. 
Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako. 
Nitaitii amri yako daima, naam, milele na milele. 
Nitatembea huru, kwa kuwa nimejifunza mausia yako. 
Nitasema sheria zako mbele za wafalme wala sitaaibishwa, 
kwa kuwa ninazifurahia amri zako kwa sababu ninazipenda. 
Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu, nami ninatafakari juu ya maagizo yako. 
Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako, kwa sababu umenipa tumaini. 
Faraja yangu katika mateso yangu ni hii: Ahadi yako inahifadhi maisha yangu. 
Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka, hata hivyo sitaiacha sheria yako. 
Ee Mwenyezi Mungu, ninazikumbuka sheria zako za zamani, nazo zinanifariji. 
Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu, ambao wameacha sheria yako. 
Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu popote ninapoishi. 
Ee Mwenyezi Mungu, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako, nami nitatii sheria yako. 
Hili limekuwa zoezi langu: nami ninayatii mausia yako. 
Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni fungu langu, nimeahidi kuyatii maneno yako. 
Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote, nihurumie sawasawa na ahadi yako. 
Nimezifikiri njia zangu na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako. 
Nitafanya haraka bila kuchelewa kuzitii amri zako. 
Hata waovu wanifunge kwa kamba, sitasahau sheria yako. 
Usiku wa manane ninaamka kukushukuru kwa sababu ya sheria zako za haki. 
Mimi ni rafiki kwa wale wote wanaokucha, kwa wote wanaofuata mausia yako. 
Ee Mwenyezi Mungu, dunia imejaa upendo wako, nifundishe maagizo yako. 
Mtendee wema mtumishi wako Ee Mwenyezi Mungu, sawasawa na neno lako. 
Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri, kwa kuwa ninaamini amri zako. 
Kabla sijapata shida nilipotea njia, lakini sasa ninalitii neno lako. 
Wewe ni mwema, unalotenda ni jema, nifundishe maagizo yako. 
Ingawa wenye majivuno wamenisingizia uongo, nitafuata mausia yako kwa moyo wangu wote. 
Mioyo yao ni katili na migumu, bali mimi napendezwa na sheria yako. 
Ilikuwa vyema mimi kupata shida ili nipate kujifunza maagizo yako. 
Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu. 
Mikono yako iliniumba na kunitengeneza, nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako. 
Wale wanaokucha na wafurahie wanaponiona, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako. 
Ee Mwenyezi Mungu, ninajua kwamba sheria zako ni za haki, katika uaminifu wako umeniadhibu. 
Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu, sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. 
Huruma yako na inijie ili nipate kuishi, kwa kuwa naifurahia sheria yako. 
Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu, lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako. 
Wale wanaokucha na wanigeukie mimi, hao ambao wanazielewa sheria zako. 
Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako, ili nisiaibishwe. 
Nafsi yangu inazimia kwa kutamani wokovu wako, lakini nimeweka tumaini langu katika neno lako. 
Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako; ninasema, “Utanifariji lini?” 
Ingawa nimekuwa kama kiriba kwenye moshi, bado sijasahau maagizo yako. 
Mtumishi wako itampasa angoje hadi lini? Ni lini utawaadhibu washtaki wangu? 
Wenye majivuno wananichimbia mashimo, kinyume na sheria yako. 
Amri zako zote ni za kuaminika; unisaidie, kwa sababu watu wananishtaki bila sababu. 
Walikaribia kabisa kunifuta kutoka uso wa dunia, lakini sijaacha mausia yako. 
Yahifadhi maisha yangu sawasawa na upendo wako, nami nitatii sheria za kinywa chako. 
Ee Mwenyezi Mungu, neno lako ni la milele, linasimama imara mbinguni. 
Uaminifu wako unaendelea kwa vizazi vyote, umeiumba dunia, nayo inadumu. 
Sheria zako zinadumu hadi leo, kwa kuwa vitu vyote vinakutumikia. 
Kama nisingefurahia sheria yako, ningeangamia katika taabu zangu. 
Sitasahau mausia yako kamwe, kwa maana kwayo umehifadhi maisha yangu. 
Uniokoe, kwa maana mimi ni wako, kwa kuwa nimetafuta mausia yako. 
Waovu wanangojea kuniangamiza, bali mimi ninatafakari sheria zako. 
Katika ukamilifu wote ninaona mna kikomo, lakini amri zako hazina mwisho. 
Aha! Tazama, sheria yako naipenda mno ajabu. Ninaitafakari mchana kutwa. 
Amri zako zimenipa hekima kuliko adui zangu, kwa kuwa nimezishika daima. 
Nina akili kuliko walimu wangu wote, kwa kuwa ninatafakari kuhusu sheria zako. 
Nina ufahamu kuliko wazee, kwa kuwa ninayatii mausia yako. 
Nimezuia miguu yangu isiende kwenye kila njia mbaya, ili niweze kutii neno lako. 
Sijaziacha sheria zako, kwa kuwa umenifundisha wewe mwenyewe. 
Tazama jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu, matamu kuliko asali katika kinywa changu! 
Ninapata ufahamu kutoka mausia yako, kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu. 
Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu. 
Nimeapa na nimethibitisha, kwamba nitafuata sheria zako za haki. 
Nimeteseka sana, uhifadhi maisha yangu, Ee Mwenyezi Mungu, sawasawa na neno lako. 
Ee Mwenyezi Mungu, pokea sifa za hiari za kinywa changu, nifundishe sheria zako. 
Ingawa maisha yangu yako hatarini siku zote, sitasahau sheria yako. 
Waovu wamenitegea mtego, lakini sijayakiuka maagizo yako. 
Sheria zako ni urithi wangu milele, naam ni furaha ya moyo wangu. 
Nimekusudia moyoni mwangu kuyafuata maagizo yako hadi mwisho. 
Ninachukia watu wa nia mbili, lakini ninapenda sheria yako. 
Wewe ni kimbilio langu na ngao yangu, nimeweka tumaini langu katika neno lako. 
Ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu, ili niweze kushika amri za Mungu wangu! 
Nihifadhi sawasawa na ahadi yako, nami nitaishi; usiache matumaini yangu yakavunjwa. 
Nitegemeze, nami nitaokolewa, nami daima nitayaheshimu maagizo yako. 
Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako, kwa maana udanganyifu wao ni bure. 
Waovu wa nchi unawatupa kama takataka, kwa hivyo nazipenda sheria zako. 
Mwili wangu unatetemeka kwa kukuogopa wewe, ninaziogopa sheria zako. 
Nimetenda yaliyo haki na sawa, usiniache mikononi mwa watesi wangu. 
Mhakikishie mtumishi wako usalama, usiache wenye kiburi wanidhulumu. 
Macho yangu yamefifia, yakitazamia wokovu wako, na kuitazamia ahadi yako ya kweli. 
Mtendee mtumishi wako kulingana na upendo wako na unifundishe maagizo yako. 
Mimi ni mtumishi wako; nipe busara ili niweze kuelewa sheria zako. 
Ee Mwenyezi Mungu, wakati wako wa kutenda umewadia, kwa kuwa sheria yako inavunjwa. 
Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu, naam, zaidi ya dhahabu safi, 
na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili, nachukia kila njia potovu. 
Sheria zako ni za ajabu, hivyo ninazitii. 
Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru, kunampa mjinga ufahamu. 
Nimefungua kinywa changu na kuhema, nikitamani amri zako. 
Nigeukie na unihurumie, kama uwafanyiavyo siku zote wale wanaolipenda jina lako. 
Ongoza hatua zangu kulingana na neno lako, usiache dhambi yoyote initawale. 
Niokoe na uonevu wa wanadamu, ili niweze kutii mausia yako. 
Mwangazie mtumishi wako uso wako na unifundishe amri zako. 
Chemchemi za machozi zinatiririka machoni yangu, kwa kuwa sheria yako haifuatwi. 
Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni mwenye haki, sheria zako ni sahihi. 
Sheria ulizoziweka ni za haki, ni za kuaminika kikamilifu. 
Jitihada yangu imenidhoofisha, kwa kuwa adui zangu wanayapuuza maneno yako. 
Ahadi zako zimejaribiwa kikamilifu, mtumishi wako anazipenda. 
Ingawa ni mdogo na ninadharauliwa, sisahau mausia yako. 
Haki yako ni ya milele, na sheria yako ni kweli. 
Shida na dhiki zimenipata, lakini amri zako ni furaha yangu. 
Sheria zako ni sahihi milele, hunipa ufahamu ili nipate kuishi. 
Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita kwa moyo wangu wote, nami nitayatii maagizo yako. 
Ninakuita; niokoe nami nitazishika sheria zako. 
Ninaamka asubuhi na mapema na kukuomba msaada; nimeweka tumaini langu katika neno lako. 
Sikufumba macho yangu usiku kucha, ili niweze kutafakari juu ya ahadi zako. 
Usikie sauti yangu sawasawa na upendo wako, Ee Mwenyezi Mungu, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na sheria zako. 
Wale wanaopanga mipango miovu wako karibu nami, lakini wako mbali na sheria yako. 
Ee Mwenyezi Mungu, hata hivyo wewe u karibu, na amri zako zote ni za kweli. 
Tangu zamani nimejifunza kutoka shuhuda zako kwamba umezithibitisha ili zidumu milele. 
Yaangalie mateso yangu, uniokoe, kwa kuwa sijasahau sheria yako. 
Nitetee katika hali hii yangu na unikomboe, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na ahadi yako. 
Wokovu uko mbali na waovu, kwa kuwa hawatafuti maagizo yako. 
Ee Mwenyezi Mungu, huruma zako ni kuu, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na sheria zako. 
Adui wanaonitesa ni wengi, lakini mimi sitaziacha sheria zako. 
Ninawatazama wasioamini kwa chuki, kwa kuwa hawalitii neno lako. 
Tazama jinsi ninavyopenda mausia yako; Ee Mwenyezi Mungu, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na upendo wako. 
Maneno yako yote ni kweli, sheria zako zote za haki ni za milele. 
Watawala wamenitesa bila sababu, lakini moyo wangu unatetemeka kwa neno lako. 
Nafurahia ahadi zako kama mtu aliyepata mateka mengi. 
Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo, lakini napenda sheria yako. 
Ninakusifu mara saba kwa siku, kwa ajili ya sheria zako za haki. 
Wanaopenda sheria yako wana amani tele, wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza. 
Ee Mwenyezi Mungu, ninangojea wokovu wako, nami ninafuata amri zako, 
Ninazitii sheria zako, kwa sababu ninazipenda mno. 
Nimetii mausia yako na sheria zako, kwa kuwa njia zangu zote zinajulikana kwako. 
Ee Mwenyezi Mungu, kilio changu na kifike mbele zako, nipe ufahamu sawasawa na neno lako. 
Maombi yangu na yafike mbele zako, niokoe sawasawa na ahadi yako. 
Midomo yangu na ibubujike sifa, kwa kuwa unanifundisha maagizo yako. 
Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, kwa kuwa amri zako zote ni za haki. 
Mkono wako uwe tayari kunisaidia, kwa kuwa nimechagua mausia yako. 
Ee Mwenyezi Mungu, ninatamani wokovu wako, na sheria yako ni furaha yangu. 
Nijalie kuishi ili nipate kukusifu, na sheria zako zinitegemeze. 
Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea. Mtafute mtumishi wako, kwa kuwa sijasahau amri zako. 
