﻿Zaburi.
116.
Nampenda Mwenyezi Mungu kwa maana amesikia sauti yangu; amesikia kilio changu ili anihurumie. 
Kwa sababu amenitegea sikio lake, nitamwita siku zote za maisha yangu. 
Kamba za mauti zilinizunguka, vitisho vya Kuzimu vilinipata, nikalemewa na taabu na huzuni. 
Ndipo nikaliitia jina la Mwenyezi Mungu: “Ee Mwenyezi Mungu, niokoe!” 
Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na haki, Mungu wetu ni mwingi wa huruma. 
Mwenyezi Mungu huwalinda wanyenyekevu, nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa. 
Ee nafsi yangu, tulia tena, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuwa mwema kwako. 
Kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeniokoa nafsi yangu na mauti, macho yangu kutokana na machozi, miguu yangu kutokana na kujikwaa, 
ili niweze kutembea mbele za Mwenyezi Mungu, katika nchi ya walio hai. 
Nilimwamini Mwenyezi Mungu, niliposema, “Mimi nimeteseka sana.” 
Katika taabu yangu nilisema, “Wanadamu wote ni waongo.” 
Nimrudishie Mwenyezi Mungu nini kwa wema wake wote alionitendea? 
Nitakiinua kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu. 
Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu mbele za watu wake wote. 
Kifo cha watakatifu kina thamani machoni pa Mwenyezi Mungu. 
Ee Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mtumishi wako, mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako; umeniweka huru toka katika minyororo yangu. 
Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru na kuliita jina la Mwenyezi Mungu. 
Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu mbele za watu wake wote, 
katika nyua za nyumba ya Mwenyezi Mungu, katikati yako, ee Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi Mungu. 
