﻿Zaburi.
111.
Msifuni Mwenyezi Mungu. Nitamtukuza Mwenyezi Mungu kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko. 
Kazi za Mwenyezi Mungu ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari. 
Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, haki yake hudumu daima. 
Amefanya maajabu yake yakumbukwe, Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na huruma. 
Huwapa chakula wale wanaomcha, hulikumbuka agano lake milele. 
Amewaonesha watu wake uwezo wa kazi zake, akiwapa nchi za mataifa mengine. 
Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, mausia yake yote ni ya kuaminika. 
Zinadumu milele na milele, zikifanyika kwa uaminifu na unyofu. 
Aliwapa watu wake ukombozi, aliamuru agano lake milele: jina lake ni takatifu na la kuogopwa. 
Kumcha Mwenyezi Mungu ndicho chanzo cha hekima, wote wanaozifuata amri zake wana busara. Sifa zake zadumu milele. 
