﻿Zaburi.
102.
Maombi ya mtu aliyechoka. Anapoteseka na kumimina malalamiko yake kwa Mwenyezi Mungu. Ee Mwenyezi Mungu, usikie maombi yangu; kilio changu cha kuomba msaada kikufikie. 
Usinifiche uso wako ninapokuwa katika shida. Unitegee sikio lako; ninapoita, unijibu kwa upesi. 
Kwa kuwa siku zangu zinatoweka kama moshi; mifupa yangu inaungua kama kaa la moto. 
Moyo wangu umefifia na kunyauka kama jani; ninasahau kula chakula changu. 
Kwa sababu ya kusononeka kwangu kwa uchungu, nimebakia ngozi na mifupa. 
Nimekuwa kama bundi wa jangwani, kama bundi kwenye magofu. 
Nilalapo sipati usingizi; nimekuwa kama ndege mpweke kwenye paa la nyumba. 
Mchana kutwa adui zangu hunidhihaki; wanaonizunguka hutumia jina langu kama laana. 
Ninakula majivu kama chakula changu, nimechanganya kinywaji changu na machozi 
kwa sababu ya ghadhabu yako kuu, kwa maana umeniinua na kunitupa kando. 
Siku zangu ni kama kivuli cha jioni, ninanyauka kama jani. 
Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeketi kwenye kiti chako cha enzi milele; sifa zako za ukuu zaendelea vizazi vyote. 
Utainuka na kuihurumia Sayuni, kwa maana ni wakati wa kumwonesha wema; wakati uliokubalika umewadia. 
Kwa maana mawe yake ni ya thamani kwa watumishi wako, vumbi lake lenyewe hulionea huruma. 
Mataifa wataogopa jina la Mwenyezi Mungu, wafalme wote wa dunia watauheshimu utukufu wako. 
Kwa maana Mwenyezi Mungu ataijenga tena Sayuni na kutokea katika utukufu wake. 
Ataitikia maombi ya mtu mkiwa, wala hatadharau hoja yao. 
Hili na liandikwe kwa ajili ya kizazi kijacho, ili taifa litakaloumbwa baadaye waweze kumsifu Mwenyezi Mungu: 
“Mwenyezi Mungu alitazama chini kutoka patakatifu pake palipo juu, alitazama dunia kutoka mbinguni, 
kusikiliza vilio vya uchungu vya wafungwa, na kuwaweka huru wale waliohukumiwa kufa.” 
Kwa hiyo jina la Mwenyezi Mungu latangazwa huko Sayuni na sifa zake katika Yerusalemu, 
wakati mataifa na falme zitakapokusanyika ili kumwabudu Mwenyezi Mungu. 
Katika kuishi kwangu alivunja nguvu zangu, akafupisha siku zangu. 
Ndipo niliposema: “Ee Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu; miaka yako inaendelea vizazi vyote. 
Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako. 
Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu, zote zitachakaa kama vazi. Utazibadilisha kama nguo nazo zitaondoshwa. 
Lakini wewe, U yeye yule, nayo miaka yako haikomi kamwe. 
Watoto wa watumishi wako wataishi mbele zako; wazao wao wataimarishwa mbele zako.” 
