﻿Zaburi.
83.
Wimbo. Zaburi ya Asafu. Ee Mungu, usikae kimya, usinyamaze, Ee Mungu, usikae mbali. 
Tazama watesi wako wanafanya fujo, jinsi adui zako wanavyoinua vichwa vyao. 
Kwa ujanja, wanapanga njama dhidi ya watu wako; wanapanga hila dhidi ya wale unaowapenda. 
Wanasema, “Njooni, tuwaangamize kama taifa, ili jina la Israeli lisikumbukwe tena.” 
Kwa nia moja wanapanga njama pamoja, wanafanya muungano dhidi yako, 
mahema ya Edomu na Waishmaeli, ya Wamoabu na Wahagari, 
Gebali, Amoni na Amaleki, Ufilisti, pamoja na watu wa Tiro. 
Hata Ashuru wameungana nao kuwapa nguvu wazao wa Lutu. 
Uwatendee kama vile ulivyowatendea Midiani, na kama vile ulivyowatendea Sisera na Yabini hapo kijito cha Kishoni, 
ambao waliangamia huko Endori na wakawa kama kinyesi juu ya ardhi. 
Wafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, watawala wao kama Zeba na Salmuna, 
ambao walisema, “Na tumiliki maeneo ya malisho ya Mungu.” 
Ee Mungu wangu, wapeperushe kama mavumbi ya kisulisuli, kama makapi yapeperushwayo na upepo. 
Kama vile moto unavyoteketeza msitu au mwali wa moto unavyounguza milima, 
wafuatilie kwa tufani yako na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako. 
Funika nyuso zao kwa aibu ili watu walitafute jina lako, Ee Mwenyezi Mungu. 
Wao na waaibishwe na kufadhaishwa milele, na waangamie kwa aibu. 
Hebu wajue kuwa wewe, ambaye jina lako ni Mwenyezi Mungu, kwamba wewe peke yako ndiwe Uliye Juu Sana ya dunia yote. 
