﻿Zaburi.
75.
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Zaburi ya Asafu. Wimbo. Ee Mungu, tunakushukuru, tunakushukuru wewe, kwa kuwa jina lako li karibu; watu husimulia matendo yako ya ajabu. 
Unasema, “Ninachagua wakati maalum; ni mimi nihukumuye kwa haki. 
Dunia inapotetemeka na watu wake wote, ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara. 
Kwa wale wenye majivuno ninasema, ‘Msijisifu tena,’ kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu. 
Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu; msiseme kwa kiburi.’ ” 
Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu. 
Bali Mungu ndiye ahukumuye: Humshusha huyu na kumkweza mwingine. 
Mkononi mwa Mwenyezi Mungu kuna kikombe kilichojaa mvinyo unaotoka povu uliochanganywa na vikolezo; huumimina, nao waovu wote wa dunia hunywa hata tone la mwisho. 
Bali mimi, nitatangaza hili milele; nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo. 
Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote, bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu. 
