﻿Zaburi.
64.
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu, uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui. 
Unifiche kutokana na njama za waovu, kutokana na fitina za kundi la watenda maovu. 
Wananoa ndimi zao kama panga na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha. 
Hurusha mishale kutoka mavizio kwa mtu asiye na hatia, humrushia ghafula bila woga. 
Kila mmoja humtia moyo mwenzake katika mipango mibaya; huzungumza kuhusu kuficha mitego yao, nao husema, “Ni nani ataiona?” 
Hupanga njama la dhuluma na kusema, “Tumebuni mpango mkamilifu!” Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila. 
Bali Mungu atawapiga kwa mishale, nao ghafula wataangushwa. 
Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao na kuwaleta kwenye maangamizi; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao kwa dharau. 
Wanadamu wote wataogopa, watatangaza kazi za Mungu na kutafakari yale aliyoyatenda. 
Wenye haki na wafurahi katika Mwenyezi Mungu, na wakimbilie kwake; wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye! 
