﻿Zaburi.
21.
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, mfalme huzifurahia nguvu zako. Tazama jinsi furaha yake ilivyo kuu kwa ushindi unaompa! 
Umempa haja ya moyo wake na hukumzuilia maombi ya midomo yake. 
Ulimkaribisha kwa baraka tele na kumvika taji la dhahabu safi kichwani pake. 
Alikuomba maisha, nawe ukampa, wingi wa siku milele na milele. 
Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa, umeweka juu yake fahari na utukufu. 
Hakika umempa baraka za milele, umemfanya awe na furaha kwa shangwe ya uwepo wako. 
Kwa kuwa mfalme anamtumaini Mwenyezi Mungu; kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa. 
Mkono wako utawashika adui zako wote, mkono wako wa kuume utawakamata adui zako. 
Wakati utajitokeza, utawafanya kama tanuru la moto. Katika ghadhabu yake Mwenyezi Mungu atawameza, moto wake utawateketeza. 
Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani, uzao wao kutoka wanadamu. 
Ingawa watapanga mabaya dhidi yako na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa, 
kwa kuwa utawafanya wakimbie utakapowalenga usoni pao kwa mshale kutoka upinde wako. 
Ee Mwenyezi Mungu, utukuzwe katika nguvu zako, tutaimba na kusifu nguvu zako. 
