﻿Zaburi.
16.
Utenzi wa Daudi. Ee Mungu, uniweke salama, kwa maana kwako nimekimbilia. 
Nilimwambia Mwenyezi Mungu, “Wewe ndiwe Bwana wangu; pasipo wewe sina jambo jema.” 
Kuhusu watakatifu walio duniani, hao ndio wenye fahari, na ninapendezwa nao. 
Huzuni itaongezeka kwa wale wanaokimbilia miungu mingine. Sitazimimina sadaka za damu kwa miungu kama hiyo, au kutaja majina yao mdomoni mwangu. 
Mwenyezi Mungu umeniwekea fungu langu na kikombe changu; umeyafanya mambo yangu yote yawe salama. 
Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, hakika nimepata urithi mzuri. 
Nitamsifu Mwenyezi Mungu ambaye hunishauri, hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha. 
Nimemweka Mwenyezi Mungu mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika. 
Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika salama, 
kwa maana hutaniacha Kuzimu, wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu. 
Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na furaha mbele zako, pamoja na furaha ya milele katika mkono wako wa kuume. 
