﻿Zaburi.
12.
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Mwenyezi Mungu tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka; waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu. 
Kila mmoja humwambia jirani yake uongo; midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu. 
Mwenyezi Mungu na akatilie mbali midomo yote ya hila na kila ulimi uliojaa majivuno, 
ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?” 
“Kwa sababu wanyonge wanaonewa, na wahitaji wanalia kwa uchungu, nitainuka sasa,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawalinda kutokana na wale wenye nia mbaya juu yao.” 
Maneno ya Mwenyezi Mungu ni safi, kama fedha iliyosafishwa katika tanuru, iliyosafishwa mara saba. 
Ee Mwenyezi Mungu, utatuweka salama na kutulinda na kizazi hiki milele. 
Watu waovu huenda wakiringa kila mahali wakati yule aliye mbaya sana ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu. 
