﻿Zaburi.
6.
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Ee Mwenyezi Mungu, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako. 
Unirehemu Mwenyezi Mungu, kwa maana nimedhoofika; Ee Mwenyezi Mungu, uniponye, kwa maana mifupa yangu ina maumivu makali. 
Nafsi yangu ina uchungu mwingi. Hadi lini, Ee Mwenyezi Mungu, hadi lini? 
Geuka, Ee Mwenyezi Mungu, unikomboe, uniokoe kwa sababu ya fadhili zako. 
Hakuna mtu anayekukumbuka akiwa amekufa. Ni nani awezaye kukusifu akiwa Kuzimu? 
Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; usiku kucha natiririsha kitanda changu kwa machozi; nimelowesha kiti changu kwa machozi yangu. 
Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote. 
Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, kwa maana Mwenyezi Mungu amesikia kulia kwangu. 
Mwenyezi Mungu amesikia kilio changu kwa huruma, Mwenyezi Mungu amekubali sala yangu. 
Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, watarudi nyuma na waaibishwe kwa ghafula. 
