﻿Waamuzi.
5.
Siku hiyo Debora na Baraka mwana wa Abinoamu wakaimba wimbo huu: 
“Wakuu katika Israeli wanapoongoza, wakati watu wanapojitoa kwa hiari yao wenyewe: mhimidini Mwenyezi Mungu! 
“Sikieni hili, enyi wafalme! Sikilizeni, enyi watawala! Nitamwimbia Mwenyezi Mungu, nitaimba; kwa wimbo nitamhimidi Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 
“Ee Mwenyezi Mungu, ulipotoka katika Seiri, ulipopita katika mashamba ya Edomu, nchi ilitetemeka, mbingu nazo zikamwaga, naam, mawingu yakamwaga maji. 
Milima ilitetemeka mbele za Mwenyezi Mungu, Yule wa Sinai, mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 
“Katika siku za Shamgari mwana wa Anathi, katika siku za Yaeli, barabara kuu hazikuwa na watu; wasafiri walipita njia za kando. 
Mashujaa walikoma katika Israeli, walikoma hadi mimi, Debora, nilipoinuka, nilipoinuka kama mama katika Israeli. 
Mungu alichagua viongozi wapya vita vilipokuja malangoni ya mji; lakini hapakuonekana ngao wala mkuki miongoni mwa watu elfu arobaini katika Israeli. 
Moyo wangu u pamoja na wakuu wa Israeli, u pamoja na wale wanaojitoa kwa hiari yao miongoni mwa watu. Mhimidini Mwenyezi Mungu! 
“Ninyi mpandao punda weupe, mkiketi juu ya matandiko ya thamani, nanyi mnaotembea barabarani, fikirini 
kuhusu sauti za waimbaji mahali pa kunyweshea maji. Wanasimulia matendo ya haki ya Mwenyezi Mungu, matendo ya haki ya mashujaa wake katika Israeli. “Ndipo watu wa Mwenyezi Mungu walipoteremka malangoni pa mji. 
‘Amka, amka! Debora! Amka, amka, uimbe! Ee Baraka! Inuka, chukua mateka wako uliowateka, ee mwana wa Abinoamu.’ 
“Ndipo mabaki ya watu wakashuka dhidi ya wakuu, watu wa Mwenyezi Mungu wakashuka kwangu dhidi ya wenye nguvu. 
Baadhi yao walitoka Efraimu, ambao chimbuko lao ni Amaleki; Benyamini alikuwa miongoni mwa watu waliokufuata. Kutoka Makiri wakashuka viongozi, na kutoka Zabuloni wale washikao fimbo ya jemadari. 
Wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora; naam, Isakari alikuwa pamoja na Baraka, wakija nyuma yake kwa mbio wakielekea bondeni. Katika jamaa za Reubeni, palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni. 
Kwa nini ulikaa katikati ya mazizi ya kondoo kusikiliza sauti ya filimbi zinazoita makundi? Kwa jamaa za Reubeni, palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni. 
Gileadi alikaa ng’ambo ya Yordani. Naye Dani, kwa nini alikaa kwenye merikebu siku nyingi? Asheri alikaa kwa utulivu ufuoni mwa bahari, akikaa kwenye ghuba zake ndogo. 
Watu wa Zabuloni walihatarisha maisha yao, vilevile nao watu wa Naftali. 
“Wafalme walikuja na kufanya vita; wafalme wa Kanaani walipigana huko Taanaki, karibu na maji ya Megido, lakini hawakuchukua nyara za fedha. 
Kutoka mbinguni nyota zilipigana, nyota kutoka njia zake zilipigana na Sisera. 
Mto wa Kishoni uliwasomba, ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Songa mbele, ee nafsi yangu, kwa ujasiri! 
Ndipo kwato za farasi zikafanya mshindo: farasi wake wenye nguvu huenda mbio kwa kurukaruka. 
Malaika wa Mwenyezi Mungu akasema, ‘Laani Merozi. Laani watu wake kwa uchungu, kwa kuwa hawakuja kumsaidia Mwenyezi Mungu, kumsaidia Mwenyezi Mungu dhidi ya hao wenye nguvu.’ 
“Yaeli abarikiwe kuliko wanawake wote, mkewe Heberi, Mkeni, abarikiwe kuliko wanawake wote wanaoishi kwenye mahema. 
Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa; kwenye bakuli la heshima akamletea maziwa mgando. 
Akanyoosha mkono wake akashika kigingi cha hema, mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi. Akampiga Sisera kwa nyundo, akamponda kichwa chake, akamvunjavunja na kumtoboa paji lake la uso. 
Aliinama miguuni pa Yaeli, akaanguka; akalala hapo. Alipoinama miguuni pake, alianguka; pale alipoinamia, ndipo alipoanguka, akiwa amekufa. 
“Kupitia dirishani mamaye Sisera alichungulia; nyuma ya dirisha alilia, akasema, ‘Mbona gari lake la vita linachelewa kufika? Mbona vishindo vya magari yake ya vita vimechelewa?’ 
Wajakazi wale wenye busara kuliko wengine wote wanamjibu; naam, naye anasema moyoni mwake, 
‘Je, hawapati na kugawanya nyara: msichana mmoja au wawili kwa kila mtu, mavazi ya rangi mbalimbali kwa Sisera kuwa nyara, mavazi ya rangi mbalimbali yaliyotariziwa, mavazi yaliyotariziwa vizuri kwa ajili ya shingo yangu: haya yote yakiwa nyara?’ 
“Adui zako wote na waangamie hivyo, Ee Mwenyezi Mungu! Bali wote wanaokupenda na wawe kama jua linavyochomoza kwa nguvu zake.” Hivyo nchi ikawa na amani kwa miaka arobaini. 
